Taarifa kwa vyombo vya Habari ya zamani
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amewatembelea na kuwapa pole majeruhi waliolazwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili Jijini Dar es Salaam ambao wameungua moto katika ajali iliyotokea jana asubuhi Mjini Morogoro baada ya mafuta yaliyokuwa yakimwagika kutoka kwenye lori lililopinduka kulipuka moto. Ajali hiyo imesababisha vifo vya watu 71 mpaka sasa.
Majeruhi 46 wamefikishwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbi kwa magari ya wagonjwa na helkopta na majeruhi wengine wanaendelea kupatiwa matibabu Mkoani Morogoro.
Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya Taifa Muhimbili Prof. Lawrence Museru na Mkuu wa Kitengo cha Wagonjwa wa Dharura cha hospitali hiyo Dkt. Juma Mfinanga wamemueleza Mhe. Rais Magufuli kuwa wagonjwa 46 waliofikishwa hospitalini hapo ni wale walioungua kwa kiwango kikubwa cha hadi takribani asilimia 100 na kwamba 3 kati yao wamefariki dunia baada ya kufika.
Pamoja na kuwapa pole, Mhe. Rais Magufuli amewataka Watanzania kutokuwa wepesi wa kuwahukumu kwa madai walikuwa wakiiba mafuta, kwani baadhi yao walikwenda eneo la tukio kwa lengo la kutoa msaada, wengine walikutwa na moto wakiwa katika maeneo yao ya kazi na wengine walikutwa na moto wakiwa wanasafiri katika magari yao.
Mhe. Rais Magufuli amewashukuru Madaktari na Wauguzi wa Hospitali ya Mkoa wa Morogoro, Hospitali ya Taifa Muhimbili na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kwa juhudi kubwa wanazozifanya kutoa matibabu kwa majeruhi hao na ameagiza kuwa gharama za matibabu na huduma nyingine kwa majeruhi hao zitatolewa na Serikali.
“Nawashukuru sana Madaktari na Manesi, wanafanya kazi kubwa sana, kweli wanafanya kazi kubwa sana, nimewaona wagonjwa wanahudumiwa vizuri, lakini kikubwa sisi Watanzania tumtangulize Mungu mbele, tuwaombee hawa wagonjwa, lakini na wale waliotangulia mbele za haki nao tuwaombee, na niwaombe ndugu zangu Watanzania katika ajali tusiwe wepesi wa kuhukumu, nimefika humu wodini nimemkuta mmoja ni dereva wa lori la mafuta, alipofika pale aliamua kushuka aende akasaidie, lakini nae ameungua na amelazwa hapa, yupo mwingine alikuwa anasafiri kwenda Mtwara, wala hakwenda kuchukua mafuta, nae ameungua” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli alipokuwa akizungumza na wananchi waliokuwa nje ya wodi ya Kibasila.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli ameuagiza uongozi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili kuwatangaza majeruhi wote kwa majina yao na mahali wanakotoka ili ndugu na jamaa zao wapate taarifa.
Katika hatua nyingine, Mhe. Rais Magufuli amemuagiza Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya Taifa Muhimbili Prof. Lawrence Museru kumruhusu Bi. Rahel Kitwai Roita mkazi wa Turiani Morogoro kuuchukua mwili wa Marehemu mama yake, baada ya mwili huo kuzuiwa kutokana na kudaiwa zaidi ya shilingi Milioni 5 ambazo ni gharama za matibabu.
Bi. Rahel Kitwai Roita ametoa ombi hilo akiwa pembezoni mwa njia ya kupita wagonjwa ambapo Mhe. Rais Magufuli ametaka deni hilo la shilingi Milioni 5 adaiwe yeye na ametoa rambirambi ya shilingi laki 5.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
11 Agosti, 2019
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amemteua Jaji Mstaafu Ibrahim Sayida Mipawa kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Maadili ya Viongozi wa Umma.
Jaji Mstaafu Mipawa anachukua nafasi Jaji Mstaafu Januari Msofe ambaye ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Kurekebisha Sheria.
Uteuzi wa Jaji Mstaafu Mipawa umeanza tarehe 07 Agosti, 2019.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
13 Agosti, 2019
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amemuomba Rais wa Jamhuri ya Afrika Kusini, Mhe. Matamela Cyril Ramaphosa kuwahamasisha zaidi wafanyabiashara wa Afrika Kusini kuja kuwekeza hapa nchini kwa kuwa Tanzania inayo dhamira ya dhati ya kuongeza ushirikiano wake na nchi hiyo katika nyanja mbalimbali za kiuchumi.
Mhe. Rais Magufuli amesema hayo leo tarehe 15 Agosti, 2019 Ikulu Jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na wananchi kupitia vyombo vya habari muda mfupi baada ya kufanya mazungumzo na Mhe. Rais Ramaphosa ambaye amewasili hapa nchini jana jioni kwa Ziara ya Kitaifa ya siku 3 na baadaye kuhudhuria Mkutano wa 39 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) unaofanyika Jijini Dar es Salaam.
Katika mazungumzo hayo yaliyotanguliwa na mapokezi rasmi yaliyofanyika katika viwanja vya Ikulu, Mhe. Rais Magufuli amesema katika kutekeleza mipango yake ya maendeleo na dira ya kufikia uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025 Tanzania inawakaribisha wawekezaji mbalimbali, na kwa kuwa Afrika Kusini imepiga hatua kubwa katika viwanda amewaalika wafanyabiashara wa nchi hiyo kuja kujenga viwanda vya kuzalisha bidhaa mbalimbali zikiwemo dawa na vifaa tiba, kuchakata madini na kwamba Serikali itatoa ushirikiano wowote utakaohitajika.
Mhe. Rais Magufuli pia amemuomba Mhe. Rais Ramaphosa kuongeza ushirikiano na Tanzania katika utalii, hasa ikizingatiwa nchi hiyo inapokea watalii zaidi ya Milioni 10 kwa mwaka ikilinganishwa na Watalii Milioni 1.5 wanaoingia hapa nchini, na katika hilo ametoa wito kwa Afrika Kusini kuongeza safari za treni ya watalii na kwa wawekezaji wake kuja kuwekeza katika hoteli na fukwe za Tanzania.
Kwa upande wa biashara, Mhe. Rais Magufuli amesema Afrika Kusini ni nchi inayoongoza kwa kufanya biashara na Tanzania ikilinganishwa na nchi nyingine za SADC ambapo asilimia 70 ya bidhaa za Tanzania zinazokwenda SADC huenda Afrika Kusini na kwamba biashara kati ya Tanzania na Afrika Kusini imeendelea kukua ambapo katika mwaka 2018 ilikuwa na thamani ya shilingi Trilioni 2 na Bilioni 687 ikilinganishwa na mwaka 2017 ilipokuwa na thamani ya shilingi Trilioni 2 na Bilioni 528.
Amempongeza Mhe. Rais Ramaphosa kwa kuja na wafanyabiashara ambao wanajadiliana na wafanyabiashara wa Tanzania juu ya kushirikiana kibiashara, na amemhakikishia kuwa Tanzania itakuwa tayari kuhakikisha ushirikiano huo unafanikiwa.
“Sisi Tanzania tumeamua kuwa tunanunua bidhaa zetu Afrika Kusini badala ya kununua bidhaa hizo huko mbali, na kwa kuanzia pikipiki za kuongozea misafara ya viongozi tutakazotumia wakati huu wa Mkutano wa 39 wa SADC tumenunua Afrika Kusini” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Kwa upande wake Mhe. Rais Ramaphosa amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kumwalika kufanya Ziara ya Kitaifa hapa nchini na amemhakikishia kuwa wananchi Afrika Kusini wanaiona Tanzania ni nyumbani kwao na hivyo Serikali yake ipo tayari kuuendeleza na kuukuza uhusiano mzuri kati yake na Tanzania.
Mhe. Rais Ramaphosa ameelezea kufurahishwa kwake na kuwepo kwa kampuni 228 za Afrika Kusini zilizowekeza nchini Tanzania na kuajiri wa zaidi ya watu 21,000 na ameahidi kwenda kuwahimiza zaidi wafanyabiashara na wawekezaji wa Afrika Kusini kuja kuwekeza nchini Tanzania huku akiwakaribisha wawekezaji wa Tanzania kwenda kuwekeza Afrika Kusini.
Ameipongeza Tanzania kwa kuzalisha mazao mengi ya chakula na ameahidi kuwa Afrika Kusini itaendelea kununua mazao kutoka Tanzania.
Aidha, Mhe. Rais Ramaphosa amesema Afrika Kusini ipo tayari kushirikiana na Tanzania katika nyanja nyingine mbalimbali zikiwemo afya, ulinzi na usalama, utalii na amekubaliana na mapendekezo ya Tanzania juu ya mpango wa kufundisha lugha ya Kiswahili nchini Afrika Kusini hasa wakati huu ambapo SADC inatarajia kuifanya kuwa lugha rasmi ya 4.
Katika ziara hii, Mhe. Rais Ramaphosa ameongozana na Mkewe Mhe. Dkt. Tshepo Motsepe ambaye wakati wa mazungumzo rasmi ya Waheshimiwa Marais amekuwa na mazungumzo na Mke wa Rais wa Tanzania Mhe. Mama Janeth Magufuli.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
15 Agosti, 2019
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Afrika Kusini, Mhe. Matamela Cyril Ramaphosa ameipongeza Tanzania kwa kasi kubwa ya ukuaji wa uchumi wa wastani wa asilimia 7 kwa mwaka na kubainisha kuwa hiyo ni fursa muhimu ya kuhakikisha Tanzania na Afrika Kusini zinakuza zaidi ushirikiano wa kiuchumi kwa manufaa ya pande zote mbili.
Mhe. Rais Ramaphosa amesema hayo leo tarehe 15 Agosti, 2019 katika Dhifa ya Kitaifa iliyoandaliwa kwa heshima yake na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli na kufanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Pamoja na kuhimiza kukuza uhusiano wa kiuchumi, Mhe. Ramaphosa amesema Tanzania na Afrika Kusini ambazo zina uhusiano wa kirafiki, kihistoria na kidugu zinayo changamoto ya kuhakikisha zinaliwezesha na kulitumia vizuri kundi kubwa la vijana ambao ndio nguvu kazi ya Taifa, kwa kuhakikisha sekta binafsi inakuzwa na hivyo kuiwezesha kuajiri vijana wengi.
Ametolea mfano wa hatua zilizochukuliwa na uongozi wake za kuanzisha mpango wa kutoa vivutio kwa kampuni binafsi zinazotoa fursa kwa vijana kufanya kazi ikiwemo kuzipunguzia kodi na kubainisha kuwa mpango huo umesaidia kuwapa fursa vijana takribani 100,000 katika kipindi kifupi, ambapo wanapata fursa ya kujifunza ujuzi mbalimbali na kujenga uwezo wa kufanya shughuli za uzalishaji mali.
Mhe. Rais Ramaphosa amempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa jitihada mbalimbali za kukuza uchumi wa Tanzania anazozifanya na amesema licha ya kumuunga mkono katika kipindi cha Uenyekiti wake wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) atakachokianza tarehe 17 Agosti, 2019 anaamini jitihada hizo pia ataziweka katika SADC.
Kwa upande wake, Mhe. Rais Magufuli amemshukuru Mhe. Rais Ramaphosa kwa dhamira yake ya kuendeleza na kukuza zaidi uhusiano na ushirikiano wa Tanzania na Afrika Kusini hususani katika uchumi na amempongeza kwa mpango wake wa kusaidia vijana ujulikanao kwa jina la YES (Youth Employment Service) ambao ameahidi kuwa Serikali itaufanyia kazi ili kuona namna ya kuutekeleza hapa Tanzania.
Kabla ya Dhifa ya Kitaifa, Mhe. Rais Magufuli na Mhe. Rais Ramaphosa wameshiriki mkutano wa wafanyabiashara wa Afrika Kusini na Tanzania uliofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar es Salaam ambapo Mhe. Rais Magufuli amewataka wafanyabiashara kupuuza kauli zinazodai Tanzania inawachukia wawekezaji na badala yake amewakaribisha kuja kuwekeza katika miradi mbalimbali ya uzalishaji vikiwemo viwanda ili Tanzania iondokane na uagizaji mkubwa wa bidhaa za viwandani kutoka nchi za nje.
Amewataka wafanyabiashara wa Tanzania na Afrika Kusini kujielekeza katika mijadala ya masuala muhimu yatakayosaidia kuinua biashara na uwekezaji baina ya nchi hizo, kupata wabia makini wa biashara, kuainisha maeneo ya biashara na uwekezaji na kujiandaa kwa utekelezaji.
Nae Mhe. Rais Ramaphosa ameishukuru Tanzania kwa mchango mkubwa ilioutoa kwa Afrika Kusini wakati wa harakati za ukombozi na kubainisha kuwa baada ya ukombozi kupatikana nchi hizo zinapaswa kujikita katika kuimarisha uchumi ili kuinua maisha ya wananchi wake ambao ni ndugu.
Mhe. Rais Ramaphosa amezungumzia changamoto mbalimbali zinazokwamisha ufanyaji wa biashara na uwekezaji baina ya nchi za SADC zikiwemo Tanzania na Afrika Kusini na ametoa wito kwa nchi hizo kufanyia kazi changamoto hizo ikiwemo kuongeza imani kwa wafanyabiashara kwa kuondoa vikwazo, urasimu na taratibu ambazo zinawakatisha tamaa wafanyabiashara na wawekezaji.
Amesema Afrika Kusini ipo tayari kushirikiana na sekta binafsi katika kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi na ametoa wito kwa nchi za Afrika kushirikiana kutatua changamoto ili kwa pamoja zipige hatua za kimaendeleo badala ya kuacha nchi zingine zikiwa nyuma.
Mhe. Ramaphosa amesisitiza kuwa kwa hivi sasa Afrika ndio Bara lenye uchumi unaokua vizuri na linazo fursa nyingi za uchumi ikilinganishwa na Mabara mengine, hivyo ni wakati wake sasa kuchangamka na kujiimarisha.
Ijumaa (Tarehe 16 Agosti, 2019), Mhe. Rais Ramaphosa ataendelea na ziara yake hapa nchini kwa kutembelea kambi ya wapigania uhuru wa Afrika Kusini iliyopo Mazimbu Mkoani Morogoro.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
15 Agosti, 2019
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ametangaza uamuzi wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC kuwa lugha Kiswahili inakuwa lugha rasmi ya 4 ya SADC kuanzia leo tarehe 18 Agosti, 2019.
Mhe. Rais Magufuli ametangaza uamuzi huo wakati akifunga Mkutano wa 39 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC uliofanyika kwa siku 2 (tarehe 17-18 Agosti, 2019) katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam.
Mhe. Rais Magufuli ameeleza kuwa uamuzi huo ni heshima kubwa kwa Baba wa Taifa Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere ambaye alitumia lugha ya Kiswahi katika harakati za ukombozi wa Mataifa mbalimbali ya Afrika hususani kwa wapigania uhuru ambao walijifunza na kutumia lugha hiyo katika mapambano dhidi ya wakoloni.
Amemuelezea Hayati Mwl. Nyerere kuwa alikuwa mtu mwenye huruma na upendo mkubwa sio tu kwa nchi yake ya Tanzania bali Afrika nzima kutokana na kujitoa kwake kwa hali na mali katika kusaidia mapambano ya ukombozi tena kwa gharama zilizobebwa na Watanzania.
Mhe. Rais Magufuli amewashukuru viongozi wenzake walioshiriki mkutano huu wa 39 wa SADC Jijini Dar es Salaam kwa majadiliano yenye mafanikio makubwa waliyoyafikia, na ameeleza maazimio kadhaa yaliyofikiwa kuwa ni kuzitaka nchi wanachama kuendelea kutekeleza mkakati na mwongozo wa maendeleo ya viwanda wa SADC wa mwaka 2015-2063, kuendelea kufuatilia hali ya usalama katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), kuitaka Falme ya Lesotho kuharakisha utungwaji wa sheria itakayoanzisha Mamlaka ya Kitaifa ya Kusimamia mabadiliko na kuiagiza Sekretarieti ya SADC kuanzisha chombo cha SADC cha kukabiliana na majanga.
Kuhusu hali ya uchumi, Mhe. Rais Magufuli amesema Wakuu wa Nchi na Serikali wamezitaka nchi wanachama kuendelea kuwekeza kwenye miundombinu itakayochochea ukuaji wa uchumi na kuboresha sera za uchumi na fedha.
Ameongeza kuwa wamejadili maombi ya Burundi kujiunga na SADC ambapo wameitaka Sekretarieti kuiarifu nchi hiyo juu ya maeneo ambayo bado hayajakamilika na kwa vikwazo dhidi ya Zimbabwe wamekubaliana kuendelea kuwasiliana na Jumuiya ya Kimataifa ili kuondoa vikwazo hivyo huku wakisisitiza kuwa wapo pamoja na Zimbabwe.
Mhe. Rais Magufuli ameishukuru Sekretarieti ya SADC kwa mchango wake katika maandalizi ya mkutano huo na ameitaka kutumia vizuri michango ya wanachama ili ilete matokeo katika ustawi wa jamii.
Amewakaribisha nchi wanachama wa SADC kuja kuwekeza nchini Tanzania na kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii.
Katika kipindi cha mwaka mmoja wa uongozi wa Mhe. Rais Magufuli, nchi 4 za SADC zitafanya uchaguzi Mkuu ambazo ni Malawi, Botswana, Mauritius na Msumbiji, hivyo amezitakia nchi hizo uchaguzi mwema wenye amani na utulivu.
Akimaliza muda wa mwaka mmoja wa Uenyekiti wake Mhe. Rais Magufuli atakabidhi Uenyekiti huo kwa Rais wa Jamhuri ya Msumbiji mwezi Agosti 2020.
Baada ya kumalizika kwa mkutano huo, Mhe. Rais Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Ushelisheli Mhe. Danny Faure ambapo viongozi hao wamekubaliana kuimarisha zaidi uhusiano na ushirikiano kati ya Tanzania na Ushelisheli katika biashara na uwekezaji.
Mhe. Rais Magufuli amemualika Mhe. Rais Faure kuja kuwekeza katika viwanda vya samaki na kilimo na kwamba Serikali ya Tanzania ipo tayari kutoa ushirikiano wowote utakaohitajika.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
18 Agosti, 2019
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ameipongeza Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kwa kazi nzuri ya kuchunguza sampuli mbalimbali, kusimamia sheria za usimamizi wa kemikali na kudhibiti vinasaba vya binadamu.
Mhe. Rais Magufuli ametoa pongezi hizo leo tarehe 20 Agosti, 2019 alipotembelea Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali iliyopo Kivukoni Jijini Dar es Salaam ambapo ameona jinsi mitambo ya uchunguzi vya kisasa inavyofanya kazi ikiwemo uchunguzi wa vinasaba vya miili ya watu waliopoteza maisha katika ajali ya moto iliyotokea Mjini Morogoro tarehe 10 Agosti, 2019 baada ya lori lililobeba mafuta kupinduka na kisha kulipuka moto.
Akiwa katika maabara hiyo, Mhe. Rais Magufuli amejionea mitambo mipya ya uchunguzi wa vinasaba vya binadamu, sumu, dawa za kulevya, kemikali na dawa inavyofanya kazi kwa haraka ambapo uchunguzi wa sampuli moja huchukua muda wa dakika 45 na unafanywa na vijana wa Tanzania.
Akizungumza na wafanyakazi wa Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Mhe. Rais Magufuli amewapongeza kwa kazi kubwa ya utambuzi wa vinasaba waliyoifanya kwa miili 10 ya ajali ya kuzama kwa kivuko cha MV Nyerere, miili 14 ya ajali ya moto iliyotokea Tarime Mkoani Mara na miili 50 kati ya 69 ya watu walioungua moto katika ajali ya lori la mafuta Mjini Morogoro.
Pamoja na kufanikisha utambuzi wa vinasaba katika miili hiyo na hivyo kuwawezesha ndugu wa marehemu kutambua ilipozikwa miili ya ndugu zao, Mhe. Rais Magufuli pia amewapongeza kwa uadilifu na uchapakazi wao katika majukumu mengine yakiwemo kutambua dawa za kulevya, kutoa ushahidi mahakamani na kufanya kazi katika mazingira yenye kemikali hatari kwa afya ya binadamu.
Mhe. Rais Magufuli ameeleza kuwa Serikali ya Awamu ya Tano iliamua kuchukua hatua madhubuti za kuimarisha Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali kwa kununua vifaa vipya na vya kisasa, kuongeza wafanyakazi na kuibadili kutoka kuwa Wakala wa Serikali na kuwa Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kwa kutambua umuhimu wake mkubwa na kuiongezea nguvu za kufanya kazi kwa uhuru zaidi ili kupata manufaa yanayotarajiwa.
“Nafahamu kuna wakati mlikuwa mnachunguza jambo na mnaandika ripoti ya uchunguzi wenu lakini hizo ripoti zilikuwa zinazimwa kwa sababu mlikuwa hamna nguvu, sasa mna nguvu nataka mfanye kazi” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Aidha, amewataka wafanyakazi wa Mamlaka ya Mkemia Mkuu wa Serikali kuendelea kufanya kazi kwa uadilifu mkubwa, kutopokea rushwa, kutotoa siri na ameviagiza vyombo vya ulinzi na usalama kuhakikisha watumishi wa ofisi hiyo wanaofanya uchunguzi wa masuala mazito wanakuwa salama na hawaingiliwi katika majukumu yao.
Amemuagiza Mwenyekiti wa Bodi ya mamlaka hiyo Prof. Ester Hellen Jason na Mkemia Mkuu wa Serikali Dkt. Fidelice Mafumiko kusimamia vizuri matumizi ya fedha zinatumika kununua mahitaji mbalimbali vikiwemo vitenganishi vitumikavyo maabara.
Mapema katika taarifa yake, Dkt. Mafumiko amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa Serikali ya Awamu ya Tano kutoa shilingi Bilioni 5.338 kwa ajili ya kununulia mitambo na kuongeza wafanyakazi kutoka 110 hadi 294 hali iliyoongeza ufanisi wa kazi ambapo kwa kipindi cha miaka 4 tangu 2015 vielelezo 204,974 vimechunguzwa sawa na wastani wa vielelezo 51,244 kwa mwaka, kiwango ambacho ni ongezeko la asilimia 510 ikilinganishwa na rekodi za mwaka 2015/16.
Amebainisha kuwa ufanisi wa mamlaka hiyo pia umesaidia kuongeza mahudhurio mahakamani kutoka kesi 35 kwa mwezi (2015) hadi kufikia kesi 220 kwa mwezi mwaka huu (2019) na imeongeza ofisi nyingine 2 za Kanda ya Kati na Kanda ya Kusini hali iliyorahisisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi.
Mhe. Rais Magufuli ambaye amepata nafasi ya kuwasiliza wafanyakazi wa mamlaka hiyo ameahidi kufanyia kazi changamoto mbalimbali zikiwemo mahitaji ya vifaa vya kisasa zaidi vya kufanyia kazi, kuboresha maslahi ya watumishi na kuimarisha miundombinu.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
20 Agosti, 2019
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania katika nchi mbalimbali duniani wamempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kwa utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati ambayo inajengwa kwa fedha za Watanzania.
Mabalozi hao 43 ambao wapo hapa nchini tangu tarehe 13 Agosti, 2019 wametoa pongezi hizo leo tarehe 22 Agosti, 2019 walipokutana na kuzungumza na Mhe. Rais Magufuli Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Wametoa pongezi hizo baada ya kutembelea mradi wa ujenzi wa bwawa la Nyerere litakalozalisha megawati 2,115 katika mto Rufiji, mradi wa ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa (standard gauge railway) unaoanzia Dar es Salaam hadi Dodoma, jengo la 3 la abiria katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam Jijini Dar es Salaam, mradi wa ujenzi wa barabara za juu katika makutano ya barabara ya Morogoro na Sam Nujoma (Ubungo Interchange), mradi wa upanuzi wa bandari ya Dar es Salaam, mradi wa usambazaji wa gesi (Taifa Gas), mradi wa udhibiti wa mawasiliano Tanzania na mradi wa ujenzi wa daraja la Tanzanite (New Selander Bridge) katika bahari ya Hindi.
Kwa upande wa Zanzibar wametembelea mradi wa ujenzi wa jengo la biashara na makazi (shopping mall) eneo la Michenzani, mradi wa ujenzi wa jengo la 3 la abiria katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Sheikh Abeid Amani Karume, mradi wa ujenzi wa nyumba za kisasa wa Fumba Wilaya ya Magharibi, mradi wa ujenzi wa barabara ya Kaskazini - Bububu – Mkokotoni na mradi wa ujenzi wa bandari ya mafuta na gesi katika eneo la Manga Pwani.
Mabalozi hao wameeleza kuwa utekelezaji wa miradi hiyo pamoja na juhudi nyingine kubwa zinazofanywa na Serikali katika nyanja mbalimbali za huduma za jamii zimeleta heshima kwa nchi na machoni mwa Jumuiya ya Kimataifa, na kwamba zimedhihirisha kufikiwa kwa malengo ya Tanzania kuingia katika uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.
Pia wamempongeza kwa kuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kwa kipindi cha mwaka mmoja na wameahidi kuongoza vyema katika mikutano ya Mabalozi wa SADC katika nchi wanazowakilisha kwa kuzingatia mwelekeo ambao Mhe. Rais Magufuli ameutoa katika Mkutano wa 39 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC uliofanyika tarehe 17-18 Agosti, 2019 Jijini Dar es Salaam.
Akizungumza baada ya kuwasilikiza Mabalozi hao, Mhe. Rais Magufuli amewapongeza kwa kazi wanazozifanya katika nchi wanazoiwakilisha Tanzania na amewataka waendelee kutekeleza majukumu yao kizalendo na kwa kutanguliza maslahi ya Tanzania.
Pamoja na kueleza kuhusu hali ya uchumi wa nchi, juhudi za kuwapelekea maendeleo Watanzania na juhudi za kujenga uwezo wa kujitegemea, Mhe. Rais Magufuli amewataka Mabalozi hao kutafuta wawekezaji watakaowekeza katika miradi yenye manufaa hapa nchini.
“Nataka Mabalozi mtuletee miradi ya maendeleo, ifike mahali Balozi ujiulize kwa kuwa kwangu Balozi nimepeleka nini nyumbani? Nimewezesha kujengwa kiwanda? Kujengwa barabara? Kujenga daraja au jengo fulani?” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Mhe. Rais Magufuli amewasisitiza Mabalozi hao kuhakikisha wanasimamia na kufuatilia kwa karibu masuala wanayoamini yana manufaa kwa nchi ikiwemo uwekezaji na kwamba wasikubali kukwamishwa na viongozi ama wizara yoyote.
“Nataka muwe very aggressive, na ukiona mtu anakukwamisha mimi nipo niandikieni uone kama hatakwama yeye, mimi nataka kuona vitu sio maneno maneno” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Kuhusu changamoto mbalimbali walizomueleza, Mhe. Rais Magufuli ametoa wito kwa Mabalozi hao kuzishughulikia pale ambapo wao wenyewe wana uwezo na amemtaka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kufanyia kazi taarifa wanazopelekewa na Mabalozi hao kwa wakati.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
22 Agosti, 2019
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amefungua maadhimisho ya 4 ya wiki ya viwanda ya Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) na kuhimiza nchi wanachama kutilia mkazo utekelezaji wa Mkakati wa SADC wa Maendeleo ya Viwanda wa kuanzia mwaka 2015 – 2063.
Ufunguzi huo umefanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Mawaziri na Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu Wakuu, Mabalozi, Wabunge, Sekretarieti ya SADC, viongozi kutoka sekta binafsi na washiriki wa maonesho ya viwanda kutoka nchi mbalimbali.
Mhe. Rais Magufuli ambaye amengozana na Mkewe Mama Janeth Magufuli amesema pamoja na kuwepo kwa Mkakati wa SADC wa Maendeleo ya Viwanda bado kasi ya ukuaji wa viwanda ni ndogo na hivyo kusababisha viwanda kuendelea kutoa mchango mdogo katika maendeleo ya kiuchumi kwa nchi za SADC.
Amebainisha kuwa nchi za SADC zimeendelea kuwa wazalishaji wa malighafi na nguvu kazi kwa ajili ya mataifa mengine huku zenyewe zikiwa waagizaji wa bidhaa za viwandani kutoka nje ilihali zikipangiwa bei ya kuuza na kununua bidhaa hizo, hali inayodidimiza wakulima na kurudisha nyuma juhudi za kupata maendeleo ya kiuchumi.
Mhe. Rais Magufuli ameongeza kuwa kutokana na kutokuwa na viwanda urari wa biashara kati ya Afrika na mabara mengine umekuwa sio mzuri na ametolea mfano wa mwaka 2017 ambapo thamani ya biashara kati ya Afrika na Umoja wa Ulaya ilikuwa ni shilingi Trilioni 708 (Euro Bilioni 280) ambapo Afrika ilinunua bidhaa za shilingi Trilioni 376.7 (Euro Bilioni 149) na ikauza bidhaa za shilingi Trilioni 331 (Euro Bilioni 131), lakini asilimia 60 ya bidhaa ilizouza zilikuwa ghafi na hivyo kuwa na thamani ndogo.
“Hii inathibitisha kwamba sisi Afrika tunazalisha bidhaa ambazo hatuzitumii na tunatumia bidhaa ambazo hatuzizalishi, ni lazima tubadilishe mwelekeo huu ili tuzalishe bidhaa ghafi, tuzisindike au kutengeneza viwandani na tuzitumie” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Ili kuepukana na changamoto hii inayosababisha upotevu wa fedha za kigeni, Mhe. Rais Magufuli ametoa wito kwa nchi za SADC kutekeleza kwa vitendo nguzo 3 za Mkakati wa SADC wa Maendeleo ya Viwanda ambazo ni kuhimiza maendeleo ya viwanda kama kichocheo cha mageuzi ya kiuchumi na kiteknolojia, kuongeza ushindani wa bidhaa za viwandani na kutumia mtangamano wa kikanda na jiografia yetu (yenye watu takribani Milioni 350) kwa maendeleo ya viwanda na uchumi.
Mhe. Rais Magufuli ametoa wito kwa nchi za SADC kuweka kipaumbele katika uhawilishaji wa teknolojia ya viwanda vya ndani ya Jumuiya na ndani ya Afrika pamoja na kuuziana malighafi na bidhaa zingine miongoni mwa nchi wanachama ili kukuza mitaji na kuendeleza viwanda vya ndani ya SADC na Afrika nzima, kukuza na kuendeleza ubunifu wa watu wa Afrika pamoja na kuhamasisha matumizi ya teknolojia rahisi na kujenga mazingira wezeshi kwa ajili ya kukuza sekta ya viwanda.
Maeneo mengine ni kuondoa vikwazo vyote vinavyochelewesha maendeleo ya sekta ya viwanda na kuhimiza sekta binafsi kuchangamkia fursa za kuwekeza katika viwanda badala ya kubaki ikilalamikia changamoto inazokumbana nazo.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli ameeleza juhudi mbalimbali zilizofanywa na Tanzania katika kuendeleza viwanda kuwa ni pamoja na kuongeza uzalishaji wa umeme ikiwemo mradi mkubwa wa kuzalisha megawati 2,115 katika mto Rufiji, kujenga miundombinu ya reli, barabara, bandari, viwanja vya ndege na kuhamasisha ujenzi wa viwanda ambapo kati ya mwaka 2015 na sasa viwanda zaidi ya 4,000 vimejengwa.
Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Innocent Bashungwa, Katibu Mtendaji wa SADC Dkt. Stergomena Tax na Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF) Bw. Salum Shamte wamempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa jitihada kubwa za kujenga mazingira wezeshi ya ujenzi wa viwanda hapa nchini, na wametoa wito kwa nchi zote za SADC kutilia mkazo uboreshaji wa mazingira wezeshi na wadau mbalimbali kujitokeza kuwekeza katika viwanda.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
05 Agosti, 2019
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amemteua Dkt. Suleiman Magesa Missango kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Dkt. Missango ni Mkurugenzi wa Utafiti na Sera za Uchumi wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT).
Uteuzi wa Dkt. Missango unaanza leo tarehe 30 Julai, 2019.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
30 Julai, 2019
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 01 Agosti, 2019 amefungua Jengo la 3 (Terminali III) la Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam ambalo lina uwezo wa kuhudumia abiria 6,000,000 kwa mwaka.
Sherehe za ufunguzi wa jengo hilo zimefanyika uwanjani hapo na kuhudhuriwa na wananchi na viongozi mbalimbali wakiwemo Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job Yustino Ndugai, Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, Katibu Mkuu Kiongozi Mhe. Balozi John Kijazi, Mawaziri na Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu Wakuu, Mabalozi na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa, Wabunge, Viongozi Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama, Viongozi wa Dini, Viongozi wa Vyama vya Siasa, Wakuu wa Mikoa na viongozi wa taasisi mbalimbali.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Mhandisi Patrick Mfugale amesema ujenzi wa jengo hilo umegharimu jumla ya shilingi Bilioni 722 na kwamba kukamilika kwake kutaufanya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere kuongeza uwezo wa kuhudumia abiria kutoka 2,000 hadi kufikia 8,000.
Akizungumza katika sherehe hizo, Mhe. Rais Magufuli ameipongeza TANROADS kwa kusimamia ukamilishaji wa uwanja huo, hasa baada ya ujenzi wake kukwama mwaka 2016 kutokana na mkandarasi kutolipwa fedha alizokuwa anadai na pia amempongeza Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kwa kuanzisha ujenzi wa uwanja huo.
Mhe. Rais Magufuli amewataka Watanzania kujivunia mafanikio hayo huku akibanisha kuwa kufanikiwa kwa mradi huo na miradi mingine mikubwa ambayo Serikali ya Awamu ya Tano inaitekeleza kutokana na maamuzi thabiti, usimamizi mzuri na nidhamu ya Serikali katika matumizi ya fedha za umma pamoja na kuwabana mafisadi na hivyo fedha kuelekezwa kwa Watanzania wote.
“Ndugu zangu Watanzania tunaweza, kinachotakiwa ni kujiamini na kuamua kufanya, bila kuamua Watanzania tutaendelea kuwa wategemezi katika miradi ya maendeleo ya Taifa letu” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Ameitaja miradi mikubwa ambayo imetokana na uamuzi thabiti uliofanya kuwa ni ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa (SGR) utakaogharimu shilingi Trilioni 7.5, mradi wa umeme katika mto Rufiji (shilingi Trilioni 6.5), ujenzi wa daraja la Kigongo – Busisi (shilingi Bilioni 699), ujenzi wa barabara za juu Ubungo - Dar es Salaam (shilingi Bilioni 247), ujenzi wa daraja la selander (shilingi Bilioni 270), ujenzi wa barabara ya njia 8 kutoka Kimara – Kibaha (shilingi Bilioni 140), ujenzi wa viwanja vya ndege 15 (shilingi Trilioni 1.868), kununua ndege (shilingi Trilioni 1.03) na kwamba Serikali imeamua kununua ndege zingine 3.
Miradi mingine ni ujenzi wa barabara na madaraja (shilingi Trilioni 5.37), ujenzi wa bandari kuu (shilingi Trilioni 1.2), ujenzi wa meli katika maziwa makuu (shilingi Bilioni 172.3), ujenzi wa barabara za lami katika Jiji la Dar es Salaam (shilingi Bilioni 660), ujenzi wa majengo ya halmashauri (shilingi Trilioni 1.35), ujenzi wa hospitali na vituo vya afya (shilingi Bilioni 361), ununuzi vifaa vya hospitali (shilingi Bilioni 64), ujenzi wa lada 4 katika viwanja vya ndege (shilingi Bilioni 67), mikopo kwa elimu ya juu (shilingi Trilioni 1.612), kutoa elimu bure (shilingi Bilioni 348.67), kukarabati shule na vyuo vikongwe (shilingi Bilioni 308.1).
Mhe. Rais Magufuli amesisitiza kuwa Tanzania sio masikini na hivyo amewataka Watanzania kuchangamkia fursa mbalimbali za kujipatia kipato ikiwemo kuutumia uwanja huo vizuri, kuongeza uzalishaji mali katika maeneo mbalimbali na amewashukuru viongozi wa Dini kwa kuliombea Taifa na Wabunge kwa kupitisha bajeti ya kutekeleza miradi mikubwa yenye maslahi kwa Watanzania wote.
Mapema kabla ya hotuba hiyo Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhe. Isack Kamwelwe amesema baada ya kukamilisha uwanja huo, wizara yake inajipanga kukarabati Jengo la 2 la uwanja huo ili kuliongezea uwezo kutoka kuhudumia abiria 1,500,000 kwa mwaka hadi kufikia 3,000,000.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
01 Agosti, 2019
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 26 Julai, 2019 ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa mradi wa kuzalisha umeme katika mto Rufiji Mkoani Pwani ambao utakamilika Juni 2022 na kuzalisha megawati 2,115.
Sherehe za uwekaji wa jiwe la msingi la mradi huo zimefanyika kando ya eneo litakapojengwa bwawa la maji na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Tulia Ackson, Waziri wa Nishati wa Misri Mhe. Dkt. Mohamed Shaker, Mawaziri na Naibu Mawaziri wa Tanzania, Wabunge, Viongozi Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama, Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya, Viongozi wa Dini, Viongozi wa vyama vya siasa na viongozi wa taasisi mbalimbali za Serikali.
Ujenzi wa mradi huo utagharimu shilingi za Kitanzania Trilioni 6.5 na bwawa litakalojengwa litakuwa la kwanza kwa ukubwa Afrika Mashariki na la nne kwa ukubwa Barani Afrika, na Mhe. Rais Magufuli amependekeza bwana hilo liitwe Bwawa la Nyerere ikiwa ni kutambua na kuenzi maono ya Baba wa Taifa Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere aliyetaka kujenga bwawa hilo wakati wa uongozi wake.
Katika hotuba yake, Mhe. Rais Magufuli ameipongeza Wizara ya Nishati kwa kusimamia utekelezaji mradi huo na ameeleza kuwa Serikali imechukua hatua za kujenga bwawa hilo ili kuongeza uzalishaji wa umeme nchini kutoka megawati 1,601 zinazozalishwa hivi sasa, hadi kufikia megawati 10,000 ifikapo mwaka 2025.
Mhe. Rais Magufuli amesema pamoja na kutekeleza mradi huo, Serikali itajenga mradi wa kuzalisha umeme katika mto Ruhudji utakaozalisha megawati 359, mradi wa Lumakali megawati 222, mradi wa kakono megawati 87, Rusumo megawati 80 na mingine itakayotumia nishati ya gesi, makaa ya mawe, jua, jotoardhi, upepo na urani.
Amewataka wakandarasi wanaojenga mradi (Arab Contractors na Elsewedy Electric za Misri) kukamilisha mradi huo kabla ya Juni 2022 hasa ikizingatiwa hakuna tatizo la fedha ili Watanzania waanze kunufaika mapema.
Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt Medard Kalemani amesema tayari wakandarasi wanaojenga mradi huo wamelipwa asilimia 15 ya fedha zote za mradi huo ambayo ni sawa na shilingi Trilioni 1.007 na kwamba ujenzi utahusisha bwawa la maji lenye uwezo wa kukusanya mita za ujazo Bilioni 33.2, Jengo la mitambo ya kuzalisha umeme litakalokuwa na mitambo 9, kituo cha umeme na njia ya kusafirishia umeme yenye urefu wa kilometa 135 hadi kufika Chalinze.
Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Tulia Ackson amesema Wabunge wanampongeza Mhe. Rais Magufuli kwa utekelezaji wa mradi huo na wanaamini kuwa umeme utakaozalishwa utawasaidia Watanzania na pia kufanikisha miradi mikubwa inayotekelezwa katika awamu hii ikiwemo ujenzi wa reli na ujenzi wa viwanda.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa amesema kuanza kwa ujenzi wa mradi huo ni mafanikio makubwa ya Mhe. Rais Magufuli ambaye amedhamiria kuhakikisha kila nyumba ya Mtanzania inapatiwa umeme.
Waziri wa Nishati wa Misri amewasilisha salamu za Rais wa Misri, Mhe. Abdel Fattah El- Sisi ambaye ameahidi kufuatilia ujenzi wa mradi huo unaofanywa na kampuni za Misri na pia ameahidi kuwa nchi hiyo itaendelea kushirikiana na Tanzania katika nyanja mbalimbali ikiwemo kutoa udhamini wa masomo ya nishati jadidifu kwa wanafunzi 50 ambao watasaidia juhudi za kuongeza uzalishaji wa umeme hapa nchini.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli amewataka Watanzania kujivunia mafanikio haya makubwa ya kuongeza uzalishaji wa umeme nchini na kutoyumbishwa na wanaopinga utekelezaji wa mradi huo kwa kigezo cha uharibifu wa mazingira kwani mradi huo utasaidia zaidi kutunza mazingira kwa watu kutumia umeme badala ya kuni na mkaa zinazotokana na ukataji wa miti, na pia utasaidia kuwepo uvuvi, kilimo cha umwagiliaji na kuinua utalii kutokana na Wanyama wengi kupata maji ya uhakika.
“Kwenye hili pori la Selous kuna hoteli za kitalii za gharama kubwa, kuna vitalu vya utalii 47 na kuna uwindaji unaendelea, sasa haiwezekani sisi tukitaka kujenga bwawa la kuzalisha umeme tuambiwe tunaharibu mazingira wakati eneo tunalotumia ni chini ya asilimia 3 ya pori la Selous.
Mradi huu umekumbana na upinzani mkali wa ndani na nje ya nchi, lakini kwa kuwa sisi ni Taifa huru na sio masikini kama watu wanavyodhani, tumeamua kutekeleza mradi huu” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Mhe. Rais Magufuli ameagiza kumegwa kwa sehemu ya Pori la Akiba la Selous ili iwe Hifadhi ya Taifa na amependekeza iitwe Hifadhi ya Nyerere na sehemu yenye vitalu vya uwindaji iendelee, lengo likiwa kuimarisha zaidi uhifadhi wa maliasili katika eneo hilo na kupata manufaa zaidi.
Ameagiza barabara ya kuunganisha eneo la mradi huo mpaka Fuga ianze kujengwa kwa kiwango cha lami hatua kwa hatua ili kurahisisha mawasiliano ya eneo hilo.
Pamoja na kutaka wananchi wa Morogoro na Pwani wapewe kipaumbele katika ajira wakati wa mradi huo, Mhe. Rais Magufuli ameagiza mradi huo kukatiwa bima ya Taifa, utoaji wa vibali vya kazi kwa wafanyakazi wa kutoka nje ya nchi ufanyike haraka na vyombo vya ulinzi na usalama vya Morogoro na Pwani vishirikiane kuulinda.
Pia amewataka viongozi na wananchi wa Mikoa yote yenye vyanzo vya maji vinavyomwaga maji yake katika mto Rufiji kuhakikisha wanavitunza vyanzo hivyo ili viendelee kuchangia maji mengi katika mto Rufiji.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Rufiji
26 Julai, 2019
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ameitaka menejimenti na wafanyakazi wa Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA) kubadilika kwa kufanya kazi kwa tija wakati Serikali ya Tanzania na Zambia zikifanya juhudi za kuimarisha miundominu ikiwemo kununua injini na mabehewa mapya ya treni.
Mhe. Rais Magufuli ametoa maagizo hayo leo wakati akizungumza na wafanyakazi wa TAZARA akiwa safarini kwa treni kutoka Dar es Salaam hadi Kisaki Mkoani Morogoro na baadaye kuelekea Rufiji ambako kesho atakuwa mgeni rasmi katika sherehe za uwekaji jiwe la msingi katika mradi za kuzalisha umeme wa mto Rufiji.
Akizungumza na wafanyakazi wa TAZARA katika Stesheni ya Fuga, Mhe. Rais Magufuli ameelezea kutofurahisha na taarifa za TAZARA kufanya kazi kwa kiwango cha chini ambapo kwa sasa inasafirisha tani 250,000 za mzigo kwa mwaka ikilinganishwa na uwezo wake wa tani 5,000,000 na imebakiwa na injini 5 zinazoendesha mabehewa 100 tu, ikilinganishwa na mahitaji ya injini 15 na mabehewa 700.
Mhe. Rais Magufuli amesema kwa sehemu kubwa matatizo ya TAZARA yamesababishwa na menejimenti na wafanyakazi wa TAZARA ambao wamekuwa wakiiendesha tangu mwaka 1975 walipokabidhiwa baada ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Zambia kwa kushirikiana na China kuwekeza Dola za Marekani Milioni 500 (sawa na shilingi Trilioni 1 na Bilioni 140) na baadaye thamani yake kupanda hadi kufikia zaidi ya shilingi Trilioni 4.
“Nyinyi wafanyakazi wa TAZARA ndio mlioifikisha TAZARA hapa ilipofika, Baba wa Taifa Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere na Mzee Keneth Kaunda wa Zambia waliwekeza kwenye mradi huu kwa kutambua umuhimu mkubwa wa reli hii, lakini nyinyi wafanyakazi mmepukutisha mpaka tumefika hapa, kuna mabehewa na injini hazifanyi kazi, matengenezo hayafanyiki, ni aibu uwekezaji wa TAZARA upotee bure namna hii, nataka mbadilike” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Hata hivyo Mhe. Rais Magufuli amesema Serikali ya Awamu ya Tano itahakikisha TAZARA inaimarishwa na hivyo ameagiza mapendekezo ya mabadiliko ya sheria yatakayoruhusu kila nchi kuwekeza yaharakishwe ili uwekezaji huo utakaohusisha ununuzi wa injini nyingine na mabehewa ya mizigo na abiria ufanyike.
Akiwa katika safari hiyo, Mhe. Rais Magufuli aliyeongozana na Mkewe Mhe. Mama Janeth Magufuli amesimama na kuzungumza na wananchi wa Gwata Wilayani Kisarawe ambapo amewaahidi kuwa Serikali itafanyia kazi maombi yao ya kutengenezewa barabara ya kutoka Gwata hadi Nzenga yenye urefu wa kilometa 32, kupatiwa umeme, kujengewa zahanati na ametoa mchango wa shilingi Milioni 5 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa vya shule ya msingi Gwata.
Halikadhalika, Mhe. Rais Magufuli amezungumza na wananchi wa Kisaki Mkoani Morogoro ambapo ameahidi kuwa Serikali itatoa shilingi Milioni 400 kwa ajili ya kuanza mara moja ujenzi wa Kituo cha Afya Kisaki na ameagiza uwanja wa kujenga kituo hicho upatikane ndani ya siku 7 kuanzia leo.
Pia ameendesha harambee ya kuchangisha fedha za ujenzi wa Kituo cha Polisi Kisaki na kufanikisha kupatikana jumla ya shilingi Milioni 39.1 kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho ambacho Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro ameahidi kukikamilisha ndani ya miezi mitatu kuanzia sasa.
Kuhusu malalamiko wa wakulima kudai wafugaji wamekuwa wakilisha mifugo kwenye mashamba yao, Mhe. Rais Magufuli amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Kebwe Stephen Kebwe kuhakikisha migogoro hiyo inakoma, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wafugaji wanaolisha mazao kwenye mashamba ya wakulima wanakamatwa na wanachukuliwa hatua kali.
“Haiwezekani migogoro hii ya wakulima iendelee wakati viongozi mpo, mnafanya nini na hii migogoro haijaanza leo” ameeleza Mhe. Rais Magufuli.
Ameliagiza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuhakikisha vijiji 2 vya Kata ya Kisaki ambavyo havina umeme vinapatiwa umeme haraka.
Aidha, amewataka wananchi wa Kisaki kuchangamkia fursa za mradi wa kuzalisha umeme wa mto Rufiji kwa kuzalisha mazao mengi na kujipatia ajira wakati wa ujenzi.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
25 Julai, 2019
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 25 Julai, 2019 amesafiri kwa treni ya TAZARA kutoka Jijini Dar es Salaam kuelekea Kisaki Mkoani Morogoro na baadaye atakwenda Rufiji Mkoani Pwani ambako kesho atakuwa Mgeni Rasmi katika sherehe ya kuweka jiwe la msingi mradi wa kuzalisha umeme katika mto Rufiji.
Kabla ya kupanda treni, Mhe. Rais Magufuli ambaye ameongozana na Mkewe Mhe. Mama Janeth Magufuli amezungumza na viongozi wa TAZARA na kuwataka kuwasilisha mapendekezo yao juu ya hatua zinazopaswa kuchukuliwa kuboresha usafirishaji wa mizigo na abiria kupitia TAZARA.
Mhe. Rais Magufuli amesema Serikali inatambua umuhimu wa TAZARA na haiwezi kuiacha ikifanya kazi kwa ufanisi mdogo usiowaleta manufaa Watanzania kama ilivyokusudiwa.
TAZARA iliyojengwa kwa msaada kutoka China, ilianza kutoa huduma mwaka 1975 na inamilikiwa kwa ubia wa asilimia 50 kwa 50 wa nchi ya Tanzania na Zambia.
Reli ya TAZARA yenye urefu wa kilometa 1,860 ina uwezo wa kusafirisha tani Milioni 5 za mizigo kwa mwaka lakini kutokana na uwekezaji mdogo uliosababisha upungufu mkubwa wa injini na mabehewa inasafirisha chini ya tani laki 3 kwa mwaka.
Mkurugenzi Mkuu wa TAZARA Bw. Bruno Chingandu na Meneja Mkuu wa TAZARA Tanzania Bw. Fuad Abdallah wamemueleza Mhe. Rais Magufuli kuwa tayari mapendekezo ya mabadiliko ya sheria yamewasilishwa Serikalini ili kuwezesha kila nchi kuwekeza katika TAZARA kwa lengo la kuboresha usafirishaji wa abiria na mizigo.
Mhe. Rais Magufuli ameagiza mchakato wa kufanya marekebisho ya sheria hiyo uharakishwe ili juhudi za kununua injini na mabehewa zifanyike haraka.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
25 Julai, 2019
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amemteua Bw. Julius S. Mtatiro kuwa Mkuu wa Wilaya ya Tunduru, Mkoani Ruvuma.
Bw. Mtatiro anachukua nafasi ya Bw. Juma Zuberi Homera ambaye ameteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Katavi.
Uteuzi wa Bw. Mtatiro unaanza leo tarehe 14 Julai, 2019.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Chato
14 Julai, 2019
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Uganda, Mhe. Yoweri Kaguta Museveni leo tarehe 13 Julai, 2019 amefanya Ziara Binafsi ya siku 1 hapa nchini kwa kumtembelea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli nyumbani kwake katika Kijiji cha Mlimani Wilaya ya Chato Mkoani wa Geita.
Mhe. Rais Museveni aliyetua katika uwanja wa ndege wa Chato akitokea nchini Angola amepokelewa na Mwenyeji wake Mhe. Rais Magufuli na kisha viongozi hao wakawasalimu wananchi wa Chato na viongozi mbalimbali waliokusanyika uwanjani hapo kwa ajili ya kumlaki.
Katika salamu hizo, Mhe. Rais Magufuli amemshukuru Mhe. Rais Museveni kwa kuja kumtembelea na kuzungumza nae na amebainisha kuwa ziara hiyo inazidi kudhihirisha uhusiano mzuri, wa kidugu, kijirani na kirafiki uliopo kati ya Tanzania na Uganda na kwamba Serikali ya Tanzania itahakikisha uhusiano huo unakuzwa na kuimarishwa zaidi.
Mhe. Rais Magufuli amemuelezea Mhe. Rais Museveni kuwa mmoja wa wanafunzi wazuri wa Baba wa Taifa, Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere kutokana na kutambua juhudi kubwa alizozifanya katika kuzisaidia nchi nyingi za Afrika kupigania ukombozi na kuondoa utawala wa mabavu ikiwemo Uganda, na pia kwa maono yake ya kutaka nchi za Afrika Mashariki na Afrika nzima kujielekeza katika kujenga maendeleo na ustawi wa jamii.
Mhe. Rais Magufuli amemshukuru Mhe. Rais Museveni kwa misaada aliyoitoa kwa Tanzania wakati Mkoa wa Kagera ulipokumbwa na tetemeko la ardhi, ajali ya kivuko cha MV Nyerere na matibabu kwa Mjane wa Baba wa Taifa, Mama Maria Nyerere alipokuwa nchini Uganda hivi karibuni.
Aidha, amemshukuru kwa kufanikisha mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta la kuanzia Hoima nchini Uganda hadi Bandari ya Tanga nchini Tanzania ambalo kwa asilimia 75 ya kilometa zake 1,442 linapita Tanzania, na kubainisha kuwa Tanzania ipo tayari kutoa ushirikiano wa kuhakikisha mradi huo wenye thamani ya takribani shilingi Trilioni 8 unafanikiwa.
Pamoja na shukrani hizo, Mhe. Rais Magufuli amesema licha kuongezeka kwa biashara kati ya Tanzania na Uganda kutoka shilingi Bilioni 178.2 mwaka 2015 hadi kufikia shilingi Bilioni 358.7 mwaka 2018 bado nchi hizo zina fursa nyingi kukuza uchumi kupitia uhusiano wake mzuri.
Amesema katika kufungua fursa zaidi Tanzania imeimarisha bandari ya Dar es Salaam ambayo katika mwaka 2018 ilipitisha mizigo ya Uganda kiasi cha tani 188,591, inajenga meli mpya katika ziwa Victoria na kukarabati meli nyingine 5, imefufua njia ya reli na meli ya kuvusha mabehewa ya treni (MV Umoja) kati ya bandari ya Mwanza na Port Bell nchini Uganda, inashirikiana na Uganda kutekeleza mradi wa kuzalisha umeme wa Murongo-Kikagati na imeanzisha hifadhi 3 za Taifa katika ukanda wa Kaskazini Magharibi ambazo ni Burigi-Chato, Ibanda-Kyerwa na Rumanyika-Karagwe ili kuimarisha utalii katika eneo hilo.
Katika salamu zake, Mhe. Rais Museveni amesema kuja kwake Tanzania ni kama anakuja kufanya Hija kutokana na kutambua mchango mkubwa wa Tanzania wakati wa uongozi wa Hayati Mwl. Nyerere aliyezisaidia nchi nyingi za Afrika kupata uhuru na kuondokana na utawala wa mabavu ambapo yeye na wapigania uhuru wengine Afrika walipata hifadhi na mafunzo Jijini Dar es Salaam.
Mhe. Rais Museveni amesema baada ya kupatikana kwa uhuru na ukombozi wa Mataifa ya Afrika jukumu kubwa kwa sasa ni kujielekeza katika maendeleo ya pamoja, maendeleo ya mtu mmoja mmoja na kutengeneza ajira kwa watu ili wapate kipato cha kuwafaa katika Maisha yao.
Amempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo ukiwemo ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa (standard gauge railway – SGR), ujenzi wa viwanja vya ndege ukiwemo uwanja wa ndege wa Chato, ujenzi wa barabara na usimamizi mzuri wa maliasili utakaosaidia kuchochea uchumi.
Baada ya kusalimiana na wananchi, Mhe. Rais Museveni akiwa na mwenyeji wake, Mhe. Rais Magufuli amemjulia hali Mama wa Mhe. Rais Magufuli, Bibi Susana Magufuli ambaye baada ya kupatiwa matibabu katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete anaendelea na matibabu hayo akiwa nyumbani katika Kijiji cha Mlimani, Wilayani Chato na kisha viongozi hao wamefanya mazungumzo ya faragha.
Baada ya mazungumzo hayo viongozi hao wamesema wamekubaliana kukamilishwa kwa masuala machache hasa yahusuyo kodi katika utekelezaji wa mradi mkubwa wa ujenzi wa bomba la mafuta la Hoima – Tanga na kwamba mradi huo utaanza kutekelezwa hivi karibuni.
“Namshukuru sana Mhe. Rais Museveni kwa kuja kunitembelea hapa Chato, ametoka Angola moja kwa moja hadi hapa Chato na amemuona Mama yangu ambaye ni mgonjwa, huu ni upendo wa pekee, lakini zaidi kwa namna anavyomuenzi Baba wa Taifa Hayati Mwl. Nyerere na anavyoipenda Tanzania, nataka kumhakikishia kuwa Tanzania itahakikisha uhusiano huu na ndugu zetu Waganda unadumishwa” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Kabla ya kuwaaga wananchi wa Chato katika uwanja wa ndege wa Chato na kurejea nchini Uganda, Mhe. Rais Museveni ameahidi kujenga jengo la vyumba 7 vya madarasa katika shule ya msingi Nyamilezi wilayani humo.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Chato
13 Julai, 2019
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 15 Julai, 2019 amezindua nyumba za makazi ya Askari Polisi katika Mkoa wa Geita na kuwahakikishia Askari Polisi wote nchini kuwa Serikali itaendelea kuboresha makazi yao kwa kutambua mchango wao mkubwa katika usalama wa raia na mali zao.
Sherehe za uzinduzi wa nyumba 20 zikiwa miongoni mwa nyumba 114 zilizojengwa katika Mikoa mbalimbali nchi nzima zimefanyika Mjini Geita na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Mawaziri na Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu, Viongozi Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama, Viongozi wa Dini, Viongozi wa Siasa na Viongozi wa Mkoa wa Geita wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa huo Mhandisi Robert Gabriel Luhumbi.
Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) Simon Nyakoro Sirro amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kuagiza kutolewa kwa shilingi Bilioni 10 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba 400 za makazi ya Askari Polisi zikiwemo nyumba hizo 114 zilizokamilika na kwamba nyumba nyingine 286 zitakuwa zimekamilika ifikapo Septemba 2019.
IGP Sirro pia amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa Serikali kulisaidia jeshi hilo kupata shilingi Bilioni 3.5 kwa ajili ya kununua helkopta mpya, shilingi Milioni 700 kwa ajili ya ukarabati na uendelezaji wa Chuo cha Polisi Dar es Salaam, shilingi Bilioni 126.3kwa kulipa malimbikizo ya askari, shilingi Bilioni 5 kununulia vifaa, shilingi Bilioni 10 kwa ajili ya sare za askari na shilingi Bilioni 1.3 kwa ajili ya kuendeleza miradi mbalimbali iliyokuwa imekwama.
Pamoja na kumshukuru Mhe. Rais Magufuli, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Kangi Alphaxard Lugola amemhakikishia kuwa Jeshi la Polisi lipo imara kuhakikisha raia na mali zao ni salama na amebainisha kuwa kujengwa kwa nyumba hizo ni uthibitisho kuwa fedha zinazokusanywa na Serikali ya Awamu ya Tano zinaelekezwa katika Maendeleo.
Akizungumza na katika sherehe hizo, Mhe. Rais Magufuli amelipongeza Jeshi la Polisi kwa kujenga nyumba hizo pamoja wadau waliochangia nyumba 49, na ameagiza nyumba ambazo hazijakamilishwa zikamilishwe haraka.
Mhe. Rais Magufuli ametaka nyumba hizo zitunzwe vizuri na pia ametoa wito kwa wananchi kushirikiana vizuri na Jeshi la Polisi badala ya kufanya vitendo vya kulidhalilisha jeshi hilo pamoja na vyombo vingine vya ulinzi na usalama.
Kwa wachimbaji na wafanyabiashara wa madini nchini wakiwemo wauzaji wa madini ya dhahabu waliopo Mkoani Geita, Mhe. Rais Magufuli amewataka kuuza madini yao katika masomo ya madini yaliyoanzishwa katika Mikoa yote ili Serikali iweze kukusanya kodi inayostahili na kuitumia katika maendeleo.
Akiwa njiani kutoka Chato kwenda Geita, Mhe. Rais Magufuli amewasalimu wananchi wa Bwanga na kisha wananchi wa Buselesele na Katoro ambapo amewaahidi kuwa Serikali itatoa shilingi Bilioni 1.5 kwa ajili ya ujenzi wa hospitali yenye hadhi ya Wilaya katika Mji huo wenye idadi kubwa ya wakazi zaidi ya 300,000.
Akiwa njiani kutoka Geita kwenda Mwanza Mjini, Mhe. Rais Magufuli amewasalimu wananchi wa Sengerema na Busisi na kuwahakikishia kuwa Serikali itajenga daraja Busisi – Kigongo litakalokuwa na urefu wa kilometa 3.2 na litakalokuwa daraja refu kuliko yote haAfrika Mashariki na Kati.
Ametoa wiki mbili kwa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kuhakikisha inatia saini mkataba wa ujenzi na mkandarasi atakayejenga daraja hilo baada ya upembuzi yakinifu na usanifu wake kukamilika, na kwamba katika miezi 2 ijayo mkandarasi huyo akabidhiwe eneo la ujenzi ili aanze kazi kwa kuwa Serikali imeshatenga karibu shilingi Bilioni 700 kwa ajili ya ujenzi huo.
Mhe. Rais Magufuli amesema nchi inakwenda vizuri, mambo mengi yanafanyika na hivyo amewataka Watanzania kudumisha amani, mshikamano na upendo, na kujiandaa kuwachagua viongozi wazuri katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika baadaye mwaka huu.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Mwanza
15 Julai, 2019
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 15 Julai, 2019 amezindua huduma za tiba ya saratani na miradi mingine 6 ya tiba katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando iliyopo Jijini Mwanza.
Miradi hiyo ni ufunguzi wa huduma za tiba ya kutoa mionzi kwa wagonjwa wa saratani, uzinduzi wa mradi wa upanuzi wa vyumba vya kufanyia upasuaji, ufunguzi wa huduma za maabara ya kisasa ya Molecular Baiolojia, uzinduzi wa mradi wa upanuzi wa jengo la huduma za wagonjwa wa dharura na mahututi, ufunguzi wa jengo la tiba kwa wagonjwa walio wanachama wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya na miradi ya mtambo wa kuzalisha oksijeni ya wagonjwa na kiwanda cha kutengeneza maji ya mishipa ya damu (Dripu).
Mkurugenzi Mkuu wa hospitali hiyo Prof. Abel Makubi ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa kuwekeza shilingi Bilioni 5.5 katika ujenzi wa jengo la kutunzia mashine za mionzi na kwa kutenga shilingi Bilioni 1.7 kwa ajili ya ujenzi wa wodi za wagonjwa wa saratani katika mwaka wa fedha wa 2019/20.
Amebainisha kuwa hospitali hiyo imewekeza katika tiba ya saratani kufuatia takwimu zinazoonesha kuwa asilimia 50 ya wagonjwa wa saratani waliokuwa wakipata tiba ya mionzi katika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road Jijini Dar es Salaam walikuwa wakitoka Kanda ya Ziwa, na kwamba tangu hospitali hiyo ianze kutoa tiba ya kemikali na mionzi Aprili 2017 hadi Aprili 2019 jumla ya wagonjwa 47,740 wamepata tiba ya kemikali, wagonjwa 523 wamepata tiba ya mionzi ya nje na wagonjwa 169 wamepata tiba ya mionzi ya ndani.
“Mhe. Rais nafurahi kukujulisha kuwa uzinduzi huu wa huduma ya mionzi kwa wagonjwa wa saratani kwa sasa utaondoa usumbufu wa wagonjwa kwenda Dar es Salaam katika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road na kuokoa shilingi Bilioni 1 na Milioni 900 ambazo zingetoka mifukoni mwao kwa mwaka” amesema Prof. Makubi.
Aidha, Prof. Makubi amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa hospitali hiyo kupatiwa shilingi Bilioni 1 na Milioni 500 kwa mwaka kwa ajili ya dawa za wagonjwa wa saratani na pia amewashukuru Ubalozi wa India kwa kusaidia mashine 2 za mionzi ya nje zenye thamani ya shilingi Bilioni 2 na Milioni 200, Shirika la Nguvu za Atomiki Dunia lililochangia mashine ya mionzi ya ndani yenye thamani ya shilingi Bilioni 1 na Milioni 200 na Taasisi ya Saratani ya Ocean Road ambayo hutoa msaada wa baadhi ya dawa.
Prof. Makubi ameongeza kuwa pamoja na uwekezaji huo mkubwa katika tiba ya saratani hospitali hiyo inayo mitambo 2 ya kuzalisha oksijeni kwa ajili ya matibabu ya wagonjwa mahututi, dharura, watoto wachanga na akina Mama Wajawazito ambapo huzalisha mitungi 70 hadi 80 kwa siku na hivyo kuokoa wastani wa shilingi Milioni 150 kwa mwezi, pia imewekeza mtambo wa kuzalisha aina 17 za dripu za maji na hivyo kuokoa shilingi Milioni 12 kila mwezi.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa maelekezo ya kuitaka wizara hiyo ifanyie kazi tatizo la ukusanyaji wa mapato katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando ambapo baada ya Serikali kuingilia kati makusanyo hayo yameongezeka kutoka shilingi Bilioni 1.2 hadi kufikia shilingi Bilioni 3.9 na baada ya kujengwa kwa jengo la Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya idadi ya wagonjwa imeongezeka kutoka 100 hadi 300 kwa siku na mapato kuongezeka kutoka Milioni 800 hadi Bilioni 2 na Milioni 500 kwa mwezi.
Mhe. Ummy Mwalimu ameongeza kuwa kwa nchi nzima Serikali ya Awamu ya Tano imeongeza fedha za dawa za tiba ya saratani kutoka shilingi Milioni 700 hadi kufikia shilingi Bilioni 10 kwa mwaka na hivyo kuwawezesha wagonjwa wengi wa saratani hasa wenye kipato cha chini kupata matibabu.
Akizungumza na wananchi na viongozi wa Mkoa wa Mwanza waliohudhuria sherehe hizo Mhe. Rais Magufuli amempongeza Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Mwanza ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando Mhashamu Renatus Nkwande kwa maendeleo makubwa yanayofanyika hospitalini hapo, amempongeza Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako kwa kufanikisha upatikanaji wa mashine za tiba ya saratani pamoja na madaktari na wauguzi wote wakiongozwa na Prof. Makubi kwa kuboresha huduma za matibabu kwa wagonjwa.
Mhe. Rais Magufuli ameiagiza Wizara ya Afya kufanya uchambuzi wa madeni yote ambayo Serikali inadaiwa katika hospitali za nje ya nchi ili kubaini watu waliotibiwa maradhi ambayo yangeweza kutibika hapa nchini ili wahusika walipe madeni yao.
Ameipongeza Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando kwa kuanzisha viwanda vya oksijeni na dripu za maji za wagonjwa na ameitaka hospitali hiyo kupanua uzalishaji wake ili kusambaza nchi nzima badala ya kununua bidhaa hizo kutoka nje ya nchi.
Mhe. Rais Magufuli ameyahakikishia Madhehebu ya Dini kote nchini kuwa Serikali itaendelea kushirikiana nayo katika utoaji huduma za kijamii kupitia taasisi zake mbalimbali, lakini ameyataka madhehebu hayo kuvumilia pale Serikali inapochukua hatua za kuingilia kati pale uendeshaji wake na utoaji wa huduma unapokuwa na dosari hasa ikizingatiwa kuwa Serikali huchangia dawa, vifaa, watumishi na fedha za uendeshaji.
Halikadhalika, Mhe. Rais Magufuli ameitaka Wizara ya Afya kufanya utafiti ili kubaini sababu za kuwepo kwa asilimia 50 ya wagonjwa wote wa saratani kutoka Kanda ya Ziwa pamoja na ongezeko kubwa la wagonjwa wa moyo kutoka katika ukanda huo ili kutafuta suluhisho.
Kuhusu uwanja wa ndege wa Mwanza, Mhe. Rais Magufuli ameziagiza Halmashauri za Jiji la Mwanza na Manispaa ya Ilemela kutafuta fedha kiasi shilingi Bilioni 4 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa jengo la abiria katika uwanja wa ndege wa Mwanza ambako halmashauri hizo zitajipatia kipato na kuboresha hali ya uwanja huo.
Katika hatua nyingine, Mhe. Rais Magufuli amemkabidhi Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Geita Alhad Yusuf Kabaju vitabu zaidi ya 17,000 vya Dini ya Kiislamu ambavyo ni Misahafu na Juzuu alivyopewa zawadi kutoka Taasisi ya Al-Hikma.
Mhe. Rais Magufuli amekabidhi vitabu hivyo katika sherehe ya uzinduzi wa nyumba za makazi ya Askari Polisi katika Mkoa wa Geita iliyofanyika mapema leo.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Mwanza
15 Julai, 2019
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ametoa siku 5 kuanzia tarehe 16 Julai, 2019 kwa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano na Wizara ya Fedha na Mipango kuhakikisha vifaa vya ujenzi wa chelezo ya kujengea meli na vifaa vya ukarabati wa meli vilivyokwama katika Bandari ya Dar es Salaam kutokana na mchakato wa kikodi vinafikishwa katika Bandari ya Mwanza.
Mhe. Rais Magufuli ametoa agizo hilo alipotembelea Bandari ya Mwanza kwa lengo la kukagua maendeleo ya ujenzi wa chelezo, ukarabati wa meli 5 na ujenzi wa meli mpya katika Ziwa Victoria yanayofanywa na kampuni 2 za ukarasi kutoka Jamhuri ya Korea kwa gharama ya shilingi Bilioni 152 kwa ajili hiyo.
Akiwa bandarini hapo, Mhe. Rais Magufuli ameeleza kutofurahishwa na ucheleweshaji wa takribani mwezi mmoja wa makontena 58 yenye vifaa vya ujenzi vilivyoagizwa na kampuni za ukandarasi za Korea Total Marine Innovation (KTMI) na STX JV SAEKYUNG Construction Ltd za Korea kwa sababu ya kusubiri msamaha wa kodi na amemtaka mkandarasi huyo aache visingizio.
Meneja wa mradi wa ujenzi wa chelezo na ukarabati wa meli Mhandisi Abel Gwanafyo amesema ujenzi wa chelezo pamoja na ukarabati wa meli ya MV Victoria na Mv Butiama umepangwa kukamilika ifikapo Machi 2020.
Kuhusu ujenzi wa meli mpya Meneja Mradi wa ujenzi wa Meli hiyo Mhandisi Vitus Mapunda amesema maandalizi ya vifaa vya meli hiyo itakayokuwa na uwezo wa kubeba tani 400 za mzigo, abiria 1,200 na magari makubwa na madogo 23 yanayohusisha usanifu, ukataji wa vyuma, injini 2 na majenereta 3 yamefikia asilimia 35 na kwamba makontena 300 yenye vifaa hivyo yatawasili nchini Septemba 2019 kutoka nchini Korea.
Baada ya kukagua hali ya meli ya Mv Victoria na Mv Butiama ambazo ukarabati wake umeanza, Mhe. Rais Magufuli namewasalimu wafanyakazi walioajiriwa katika mradi huo na kuwaagiza wakandarasi kuhakikisha wanalinda maslahi yao na sheria za usalama kazini kuzingatiwa.
Pia Mhe. Rais Magufuli ameagiza mitambo miwili ya kunyanyulia mizigo (Cranes) iliyokuwa imeuzwa na Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) kurejeshwa mara moja.
Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli amefanya ziara ya kushtukiza katika Gereza Kuu la Butimba Jijini Mwanza ambapo amezungumza na wafungwa na Askari Magereza.
Wafungwa wa gereza hilo wamemueleza kero mbalimbali wanazokabiliana nazo na pia Askari Magereza wamemueleza changamoto mbalimbali ambazo ameahidi kuzifanyia kazi.
Akiwa njiani kutoka Butimba, Mhe. Rais Magufuli amesimama na kuwasalimu wananchi waliokuwa wamekusanyika kwa maelfu katika eneo hilo na baada ya kuelezwa kero ya kukosekana kwa wodi ya wanaume katika Hospitali ya Wilaya ya Ilemela amemuagiza Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza kuhakikisha jengo la wodi hiyo ambalo limetengewa shilingi Milioni 300 linakamilika ifikapo tarehe 30 Julai, 2019.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Mwanza
16 Julai, 2019
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ameiagiza Wizara ya Katiba na Sheria pamoja na vyombo vyote vya ulinzi na usalama vinavyohusika na masuala ya Mahakama kupita katika Magereza yote nchini ili kuchambua na kuwaondoa Mahabusu ambao hawastahili ama hawalazimiki kuwa Magerezani.
Mhe. Rais Magufuli ametoa agizo hilo leo wakati akizungumza na wananchi wa Kongwa katika Mkutano wa hadhara uliofanyika Mjini hapo muda mfupi baada kutembelea eneo la maziko ya ukoo wa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Job Yustino Ndugai (ambaye ni Mbunge wa Kongwa) na kuweka shada la maua katika kaburi la Baba yake Mzazi, Marehemu Yustino Ndugai.
Mhe. Rais Magufuli amechukua hatua hiyo ikiwa ni siku 2 tangu atembelee Gereza Kuu la Butimba Mkoani Mwanza na kujionea hali halisi ambapo amekuta Gereza hilo lenye uwezo wa kuchukua wafungwa na mahabusu 900 lina jumla ya wafungwa na mahabusu 1,925 wakiwemo mahabusu wenye makosa madogo yanayoweza kupata dhamana.
Amempongeza Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini (DPP) Bw. Biswalo Mganga kwa kuchukua hatua mara moja ambapo ndani ya siku 2 amepitia Magereza ya Butimba, Bariadi, Mugumu, Tarime, Bunda na Kahama na kuwaachia Mahabusu zaidi ya 325 wakiwemo Askari Polisi waliokamatwa kwa kuhusika na utoroshaji wa dhahabu Mkoani Mwanza, na ameagiza Askari hao warejeshwe kazini.
“Siwezi kutawala nchi ya machozi, machozi haya yataniumiza, siwezi kutawala nchi ya watu wanaosikitika wapo kwenye unyonge na unyonge wao ni wa kuonewa” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Mhe. Rais Magufuli amewapongeza wananchi wa Kongwa kwa kuchapa kazi na kushirikiana vizuri na Mbunge wao katika maendeleo, na amemuelezea Mhe. Ndugai kuwa ni kiongozi mwenye mchango mkubwa kwa Taifa kutokana na kuliongoza Bunge kupitisha bajeti na Sheria mbalimbali zilizoiwezesha Serikali kutetea rasimali za Taifa, kuongeza ukusanyaji wa mapato na kutekeleza miradi mbalimbali mikubwa na yenye manufaa kwa Watanzania wote.
Ameitaja baadhi ya miradi hiyo kuwa ni ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa (Standard Gauge Railway – SGR), kujenga mradi wa uzalishaji wa megawati 2,115 za umeme katika mto Rufiji, miradi ya maji, ujenzi wa barabara, ujenzi wa hospitali na vituo vya afya, kutoa elimu ya msingi na sekondari bila malipo, kutoa shilingi Bilioni 473 za mikopo ya elimu ya juu na kuongeza bajeti ya dawa kutoka shilingi Bilioni 31 (2015/16) hadi shilingi Bilioni 270 hivi sasa.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli amesema kutokana na mafanikio ya kuongeza ukusanyaji wa mapato kutoka shilingi Bilioni 850 (2015/16) hadi kufikia shilingi Trilioni 1 na Bilioni 300 kwa mwezi hivi sasa, Serikali imeweza kufufua Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) kwa kununua ndege mpya 8 zikiwemo 6 zilizowasili nchini na kuanza kutoa huduma ndani na nje ya nchi, na kwamba tayari ameshatoa maelekezo ya kununuliwa kwa ndege zingine 3 (Airbus 2 na Bombardier 1) ili kupanua huduma za usafiri wa anga na kukuza utalii.
Ametoa wito kwa wananchi wa Kongwa kuendelea kuchapa kazi na kudumisha amani, na amewapongeza viongozi wa Mkoa wa Dodoma na Mkoa wa Manyara kwa kukomesha migogoro ya wakulima na wafugaji iliyokuwa ikisababisha mauaji.
Akizungumza katika Mkutano huo, Mhe. Ndugai amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa hatua yake ya kuhamishia Serikali katika Makao Makuu ya Nchi Mkoani Dodoma pamoja na kutekeleza miradi mikubwa ikiwemo ujenzi wa Hospitali ya Uhuru, Uwanja wa Ndege Msalato, barabara za lami za Jiji la Dodoma kilometa 110, kutoa shilingi Bilioni 1.5 kwa ajili ya mradi wa maji wa Kongwa, kujenga Hospitali ya Wilaya ya Kongwa, vituo vya afya vya Ugogoni na Mlali na kujenga chuo cha ufundi.
Mhe. Ndugai amemuomba Mhe. Rais Magufuli kusaidia kujenga barabara ya lami ya Mbande – Kongwa- Mpwapwa hadi kuungana na Barabara Kuu ya Iringa – Dodoma, na kwa ombi lake la kusaidiwa ujenzi wa Shule ya Msingi Sagala iliyoezuliwa na Upepo, Mhe. Rais Magufuli amechangia shilingi Milioni 5 na ameendesha harambee iliyofanikisha kupatikana shilingi Milioni 6.5, mifuko 528 ya saruji na mabati 252.
Kuhusu maombi ya kupelekewa Kikosi cha Jeshi katika Wilaya ya Kongwa ambayo ina historia ya kuwa na kambi ya wapigania uhuru wa nchi nyingi za Afrika, Mhe. Rais Magufuli ameahidi kufanyia kazi maombi hayo.
Akiwa njiani kutoka Kongwa kwenda Ikulu ya Chamwino, Mhe. Rais Magufuli amesimama kuwasalimu wananchi wa Mbande Mnadani na Mbande Njiapanda ambao wamemshukuru kwa kupatiwa vitambulisho vya wajasiriamali vinavyowawezesha kufanya biashara bila bughudha, na amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt. Binilith Mahenge kumega eneo lililo chini ya Tume ya Kurekebisha Mashirika ya Umma (PSRC) kando ya Mbande Njiapanda kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Mabasi, Kituo cha Polisi na Kituo kidogo cha afya, na kuhakikisha eneo la Mbande Mnadani linapatiwa maji na vyoo. Pia amechangia shilingi Milioni 5 kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho cha Polisi.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Chamwino
18 Julai, 2019
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amemteua Mhe. George Boniface Simbachawene kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira.
Mhe. Simbachawene anachukua nafasi ya Mhe. January Yusuf Makamba ambaye uteuzi wake umetenguliwa.
Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli amemteua Bw. Hussein Mohamed Bashe kuwa Naibu Waziri wa Kilimo.
Mhe. Bashe anachukua nafasi ya Mhe. Innocent Lugha Bashungwa ambaye aliteuliwa kuwa Waziri wa Biashara na Uwekezaji.
Katika hatua nyingine, Mhe. Rais Magufuli amemteua Balozi Dkt. Martin Lumbanga kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA).
Balozi Dkt. Lumbanga ameteuliwa kushika nafasi hiyo kwa kipindi cha pili.
Uteuzi wa viongozi hao unaanza leo tarehe 21 Julai, 2019.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
21 Julai, 2019
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ameiagiza Wizara ya Nishati kumrejesha kazini mara moja aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) Dkt. James Mataragio.
Katika agizo hilo, Mhe. Rais Magufuli ameitaka Wizara ya Nishati kumrejesha Dkt. Mataragio katika nafasi yake ya Mkurugenzi Mkuu wa TPDC ili aendelee na majukumu yake.
Dkt. Mataragio alisimamishwa kazi na Bodi ya Wakurugenzi ya TPDC tarehe 20 Agosti, 2016.
Mhe. Rais Magufuli ametoa agizo hilo leo tarehe 22 Julai, 2019.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
22 Julai, 2019
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 22 Julai, 2019 amemuapisha Mhe. George Boniface Simbachawene kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira na Mhe. Hussein Mohamed Bashe kuwa Naibu Waziri wa Kilimo.
Hafla ya kuapishwa kwa viongozi hao imefanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan, Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, Katibu Mkuu Kiongozi Mhe. Balozi John Kijazi, Mawaziri, Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu na Viongozi Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama.
Mhe. Rais Magufuli amewapongeza viongozi hao kwa uteuzi walioupata na amewataka kwenda kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na kurekebisha kasoro zilizopo katika wizara zao ili kuleta matokeo yanayotarajiwa.
Amemtaka Mhe. Simbachawene kuhakikisha fedha nyingi zinazoelekezwa katika masuala ya mazingira zinaleta matokeo ya kuboresha mazingira, vibali vya Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) haviwi kikwazo cha uwekezaji na kutekeleza maagizo yanayotolewa na Serikali kwa wakati.
“Nakumbuka suala la mifuko ya plastiki limechukua muda mrefu, karibu miaka minne, nimetia saini halikutekelezwa, Makamu wa Rais akazungumza weee halikutekelezwa, Waziri Mkuu akazungumza Bungeni halikutekelezwa, mpaka mwishoni mwishoni hapa nilipotoa amri ya lazima ndipo likaanza kutekelezwa, sasa usiende kufanya hivyo wewe (Mhe. Simbachawene)” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Mhe. Rais Magufuli amemtaka Mhe. Bashe kutekeleza kwa vitendo mawazo yake mazuri ambayo amekuwa akiyatoa Bungeni kuhusu sekta ya kilimo ili kukabiliana na changamoto mbalimbali, kuongeza uzalishaji wa mazao kwa kutumia kilimo cha kisasa na kupata masoko ya uhakika ya mazao ya kahawa na pamba ambayo hivi sasa yapo katika msimu wa mauzo.
Mhe. Simbachawene amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa uteuzi huo na ameahidi kushughulikia masuala ya fedha nyingi zinazoelekezwa katika mazingira kutoleta matokeo katika kukabiliana na uharibifu wa mazingira, kuwezesha wizara nyingine kimazingira na kuimarisha Muungano.
Pamoja na kumshukuru Mhe. Rais Magufuli, Mhe. Bashe ameahidi kutekeleza ipasavyo majukumu yake kwa kuhakikisha Ilani ya Uchaguzi Mkuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika kilimo inatekelezwa huku akitambua kuwa kati ya asilimia 60 na 70 ya Watanzania wanategemea kilimo na kwamba uwepo wake Bungeni umemsaidia kujua changamoto nyingi zinazowakabili wakulima.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli ameahidi kukutana na wafugaji wa Tanzania ili kuzungumza nao juu ya changamoto mbalimbali zinazowakabili kwa lengo la kuhakikisha mifugo mingi iliyopo hapa nchini inaleta manufaa yanayostahili.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
22 Julai, 2019
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ameiagiza Wizara ya Katiba na Sheria pamoja na vyombo vyote vya ulinzi na usalama vinavyohusika na masuala ya Mahakama kupita katika Magereza yote nchini ili kuchambua na kuwaondoa Mahabusu ambao hawastahili ama hawalazimiki kuwa Magerezani.
Mhe. Rais Magufuli ametoa agizo hilo leo wakati akizungumza na wananchi wa Kongwa katika Mkutano wa hadhara uliofanyika Mjini hapo muda mfupi baada kutembelea eneo la maziko ya ukoo wa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Job Yustino Ndugai (ambaye ni Mbunge wa Kongwa) na kuweka shada la maua katika kaburi la Baba yake Mzazi, Marehemu Yustino Ndugai.
Mhe. Rais Magufuli amechukua hatua hiyo ikiwa ni siku 2 tangu atembelee Gereza Kuu la Butimba Mkoani Mwanza na kujionea hali halisi ambapo amekuta Gereza hilo lenye uwezo wa kuchukua wafungwa na mahabusu 900 lina jumla ya wafungwa na mahabusu 1,925 wakiwemo mahabusu wenye makosa madogo yanayoweza kupata dhamana.
Amempongeza Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini (DPP) Bw. Biswalo Mganga kwa kuchukua hatua mara moja ambapo ndani ya siku 2 amepitia Magereza ya Butimba, Bariadi, Mugumu, Tarime, Bunda na Kahama na kuwaachia Mahabusu zaidi ya 325 wakiwemo Askari Polisi waliokamatwa kwa kuhusika na utoroshaji wa dhahabu Mkoani Mwanza, na ameagiza Askari hao warejeshwe kazini.
“Siwezi kutawala nchi ya machozi, machozi haya yataniumiza, siwezi kutawala nchi ya watu wanaosikitika wapo kwenye unyonge na unyonge wao ni wa kuonewa” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Mhe. Rais Magufuli amewapongeza wananchi wa Kongwa kwa kuchapa kazi na kushirikiana vizuri na Mbunge wao katika maendeleo, na amemuelezea Mhe. Ndugai kuwa ni kiongozi mwenye mchango mkubwa kwa Taifa kutokana na kuliongoza Bunge kupitisha bajeti na Sheria mbalimbali zilizoiwezesha Serikali kutetea rasimali za Taifa, kuongeza ukusanyaji wa mapato na kutekeleza miradi mbalimbali mikubwa na yenye manufaa kwa Watanzania wote.
Ameitaja baadhi ya miradi hiyo kuwa ni ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa (Standard Gauge Railway – SGR), kujenga mradi wa uzalishaji wa megawati 2,115 za umeme katika mto Rufiji, miradi ya maji, ujenzi wa barabara, ujenzi wa hospitali na vituo vya afya, kutoa elimu ya msingi na sekondari bila malipo, kutoa shilingi Bilioni 473 za mikopo ya elimu ya juu na kuongeza bajeti ya dawa kutoka shilingi Bilioni 31 (2015/16) hadi shilingi Bilioni 270 hivi sasa.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli amesema kutokana na mafanikio ya kuongeza ukusanyaji wa mapato kutoka shilingi Bilioni 850 (2015/16) hadi kufikia shilingi Trilioni 1 na Bilioni 300 kwa mwezi hivi sasa, Serikali imeweza kufufua Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) kwa kununua ndege mpya 8 zikiwemo 6 zilizowasili nchini na kuanza kutoa huduma ndani na nje ya nchi, na kwamba tayari ameshatoa maelekezo ya kununuliwa kwa ndege zingine 3 (Airbus 2 na Bombardier 1) ili kupanua huduma za usafiri wa anga na kukuza utalii.
Ametoa wito kwa wananchi wa Kongwa kuendelea kuchapa kazi na kudumisha amani, na amewapongeza viongozi wa Mkoa wa Dodoma na Mkoa wa Manyara kwa kukomesha migogoro ya wakulima na wafugaji iliyokuwa ikisababisha mauaji.
Akizungumza katika Mkutano huo, Mhe. Ndugai amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa hatua yake ya kuhamishia Serikali katika Makao Makuu ya Nchi Mkoani Dodoma pamoja na kutekeleza miradi mikubwa ikiwemo ujenzi wa Hospitali ya Uhuru, Uwanja wa Ndege Msalato, barabara za lami za Jiji la Dodoma kilometa 110, kutoa shilingi Bilioni 1.5 kwa ajili ya mradi wa maji wa Kongwa, kujenga Hospitali ya Wilaya ya Kongwa, vituo vya afya vya Ugogoni na Mlali na kujenga chuo cha ufundi.
Mhe. Ndugai amemuomba Mhe. Rais Magufuli kusaidia kujenga barabara ya lami ya Mbande – Kongwa- Mpwapwa hadi kuungana na Barabara Kuu ya Iringa – Dodoma, na kwa ombi lake la kusaidiwa ujenzi wa Shule ya Msingi Sagala iliyoezuliwa na Upepo, Mhe. Rais Magufuli amechangia shilingi Milioni 5 na ameendesha harambee iliyofanikisha kupatikana shilingi Milioni 6.5, mifuko 328 ya saruji na mabati 252.
Kuhusu maombi ya kupelekewa Kikosi cha Jeshi katika Wilaya ya Kongwa ambayo ina historia ya kuwa na kambi ya wapigania uhuru wa nchi nyingi za Afrika, Mhe. Rais Magufuli ameahidi kufanyia kazi maombi hayo.
Akiwa njiani kutoka Kongwa kwenda Ikulu ya Chamwino, Mhe. Rais Magufuli amesimama kuwasalimu wananchi wa Mbande Mnadani na Mbande Njiapanda ambao wamemshukuru kwa kupatiwa vitambulisho vya wajasiriamali vinavyowawezesha kufanya biashara bila bughudha, na amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt. Binilith Mahenge kumega eneo lililo chini ya Tume ya Kurekebisha Mashirika ya Umma (PSRC) kando ya Mbande Njiapanda kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Mabasi, Kituo cha Polisi na Kituo kidogo cha afya, na kuhakikisha eneo la Mbande Mnadani linapatiwa maji na vyoo. Pia amechangia shilingi Milioni 5 kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho cha Polisi.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Chamwino
18 Julai, 2019
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amewataka madereva wanaoendesha vyombo vya usafiri wa abiria kuzingatia sheria na taratibu za usalama wa barabarani wakati wote wa safari zao.
Mhe. Rais Magufuli amesema hayo tarehe 10 Julai, 2019 Kijijii cha Kihanga, Wilaya ya Karagwe Mkoani Kagera alipokutana na abiria na dereva wa basi dogo linalofanya safari zake kati ya Bukoba na Karagwe.
Ameeleza kuwa ajali nyingi za barabarani husababishwa na ukiukwaji wa sheria na taratibu za usalama barabarani na kwamba jukumu la kuhakikisha sheria na taratibu hizo zinatekelezwa lipo mikononi mwa watumiaji wote wa barabara hasa madereva wanaoendesha vyombo vya usafiri.
“Poleni na safari ndugu zangu, nimefurahi kuwaona na kuwasalimu, na wewe dereva hongera kwa kazi, fanya kazi zako kwa kuzingatia sheria na taratibu za usalama barabarani, pia kumbuka kusali kabla na baada ya safari” amesema Mhe. Rais Magufuli alipokuwa akizungumza na abiria na dereva wa basi hilo.
Kwa baadhi ya abiria hao ambao ni wanafunzi, Mhe. Rais Magufuli amewataka kusoma kwa juhudi na kufanya vizuri katika masomo yao.
Mhe. Rais Magufuli yuko mapumzikoni Wilayani Karagwe katika Mkoa wa Kagera.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Karagwe
10 Julai, 2019
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amesema Serikali imechukua hatua madhubuti za kuwalinda wakulima wa zao la kahawa kwa kutoa fedha ili kuviwezesha vyama vya ushirika kununua kwa bei nzuri na ameruhusu wanunuzi binafsi wa ndani na nje ya nchi kununua kahawa hiyo ilimradi wazingatie sheria na utaratibu uliowekwa na Serikali.
Mhe. Rais Magufuli amesema hayo leo tarehe 11 Julai, 2019 alipozungumza na wananchi wa Kyaka, Rwamishenye, Kemondo, Muleba na Kyamyorwa Mkoani Kagera wakati akiwa safarini kutoka Karagwe kwenda Chato Mkoani Geita.
Amefafanua kuwa hatua ya Serikali kutoa fedha kupitia Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) ambapo wakulima wanauza kahawa yao kupitia vyama vya ushirika kwa bei ya shilingi 1,100/- kwa kilo imelenga kukabiliana na unyonyaji dhidi ya wakulima uliotokea misimu iliyopita ambapo bei ilishushwa hadi shilingi 300 kwa kilo na amefafanua kuwa kupitia utatatibu huo wakulima watapata malipo ya pili.
“Nataka niwahakikishie Serikali haiwezi kukubali kuona wakulima wake wananyonywa, ndio maana tumetoa fedha ili muuze kahawa yenu kupitia vyama vya ushirika, tunataka mpate fedha nzuri, lakini kama kuna wanunuzi wanaotaka kuja kununua kahawa hapa kwa bei nzuri ya shilingi 1,500 au 1,600 au hata shilingi 2,000 hatuwazuii waje kuanzia hata leo ilimradi wahakikishe wanafuata sheria na taratibu ikiwemo kulipa makato yote yanayopaswa kwa sababu baadhi ya makato hayo ni kwa ajili ya magunia na pia tunataka tuanze kutoa miche ya kahawa bure” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Kuhusu tatizo la upatikanaji wa maji ambalo wananchi wa maeneo hayo wamemuomba Mhe. Rais Magufuli awasaidie kulitatua, Mhe. Rais Magufuli amemuagiza Waziri wa Maji Mhe. Prof. Makame Mbarawa ambaye yupo ziarani Mkoani Kagera kushughulikia haraka iwezekanavyo na kwa Kata ya Kyaka ametoa maelekezo kuwa wizara iwapeleke watalaamu watakaoweka miundombinu ya kuvuta maji ya Mto Kagera na kuyapandisha hadi kwenye mlima uliopigwa bomu wakati wa vita vya Kagera na kisha kuyasambaza kwa wananchi kwa mtiririko kabla ya tarehe 25 Desemba, 2019.
Katika maelekezo yake, Mhe. Prof. Mbarawa amesema wizara itatatua matatizo ya maji katika maeneo hayo kwa kutumia fedha za Mfuko wa Maji lakini kwa Mji wa Muleba tayari Serikali imetenga shilingi Milioni 400 na Nyakabango shilingi Milioni 600 kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maji.
Mhe. Rais Magufuli amewapongeza wananchi wa maeneo hayo kwa hatua kubwa za maendeleo ikiwemo ujenzi wa nyumba, taasisi zinazotoa huduma za kijamii, miundombinu ya barabara na umeme, na amewasihi kuendelea kushirikiana na Serikali kwa kuchapa kazi kwa juhudi na maarifa pamoja na kuhakikisha wanadumisha amani na mshikamano ambavyo ni jambo muhimu katika maendeleo ya Taifa lolote duniani.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli ametoa wito kwa wananchi hao kuzitunza vizuri Hifadhi za Taifa mpya zilizoanzishwa ambazo ni Rumanyika-Karagwe, Ibanda-Kyerwa na Burigi-Chato na pia kutumia vizuri fursa za kujipatia kipato kupitia hifadhi hizo ikiwemo kufanya biashara na watalii ikiwemo kuuza bidhaa zao za kilimo, ufugaji na nyinginezo.
Halikadhalika, Mhe. Rais Magufuli amezungumzia juhudi zinazofanywa na Serikali kuimarisha huduma za usafiri katika Ziwa Victoria ambapo meli kubwa ya abiria inajengwa na meli nyingine 5 zinakarabatiwa kwa gharama ya shilingi Bilioni 152.
Mhe. Rais Magufuli amemuagiza Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Medard Kalemani kwenda katika Mkoa wa Kagera kushughulikia matatizo ya kukosekana kwa umeme yaliyolalamikiwa na wananchi hao.
Akiwa katika Kijiji cha Kibehe Wilayani Chato ambako wananchi wamelalamikia soko la zao la pamba, Mhe. Rais Magufuli amewaagiza viongozi wa Mikoa yote inayozalisha zao la pamba kusimamia vizuri soko la zao hilo na ameelekeza kuwa utaratibu wa kuingia mikataba na wanunuzi uwahusishe wanunuzi wengi badala ya kibali kutolewa kwa mnunuzi mmoja ili kuweka ushindani wa bei.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Chato
11 Julai, 2019
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amemtumia salamu za rambirambi Mwenyekiti wa Kampuni za Said Salim Bakhresa kufuatia vifo vya wafanyakazi 5 wa vyombo vya habari vya Azam Media Limited vilivyotokea tarehe 08 Julai, 2019 katika ajali ya barabarani.
Ajali hiyo imetokea majira ya saa 2:30 asubuhi katika eneo la Kizonzo, katikati ya Igunga (Tabora) na Shelui (Singida) ambapo basi aina ya Coaster lililowabeba wafanyakazi wa Azam Media Limited likielekea Mwanza limegongana uso kwa uso na Lori la mizigo lililokuwa linakwenda Dar es Salaam.
Wafanyakazi wa Azam Media Limited walikuwa safarini kutoka Dar es Salaam kuelekea kwenye sherehe za uzinduzi wa Hifadhi ya Taifa ya Burigi-Chato kwa ajili ya kurusha matangazo ya moja kwa moja ya sherehe hizo.
Katika salamu hizo, Mhe. Rais Magufuli ameelezea kushtushwa na taarifa za ajali iliyosababisha vifo vya watu 7 wakiwemo wafanyakazi hao 5, Dereva na Msaidizi wake na amewaombea Marehemu wote wapumzike mahali pema peponi, Amina.
“Nimeshtushwa sana na vifo hivi, nampa pole Mwenyekiti Ndg. Said Salim Bakhresa, ndugu wa Marehemu wote, Mtendaji Mkuu Ndg. Tido Mhando na wafanyakazi wote wa Azam Media Ltd, waandishi wa habari wote na watu wote walioguswa na vifo hivi” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Mhe. Rais Magufuli amewaombea majeruhi 3 wa ajali hiyo wapone haraka ili waweze kuendelea na majukumu yao ya kila siku.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli amerejea wito wake wa kuwataka watumiaji wa barabara hususani madereva kuwa makini na kuzingatia sheria za usalama barabarani ili kuepusha ajali zinazoweza kuepukika.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Chato
08 Julai, 2019
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amemtumia salamu za rambirambi Mwenyekiti wa Kampuni za Said Salim Bakhresa kufuatia vifo vya wafanyakazi 5 wa vyombo vya habari vya Azam Media Limited vilivyotokea tarehe 08 Julai, 2019 katika ajali ya barabarani.
Ajali hiyo imetokea majira ya saa 2:30 asubuhi katika eneo la Kizonzo, katikati ya Igunga (Tabora) na Shelui (Singida) ambapo basi aina ya Coaster lililowabeba wafanyakazi wa Azam Media Limited likielekea Mwanza limegongana uso kwa uso na Lori la mizigo lililokuwa linakwenda Dar es Salaam.
Wafanyakazi wa Azam Media Limited walikuwa safarini kutoka Dar es Salaam kuelekea kwenye sherehe za uzinduzi wa Hifadhi ya Taifa ya Burigi-Chato kwa ajili ya kurusha matangazo ya moja kwa moja ya sherehe hizo.
Katika salamu hizo, Mhe. Rais Magufuli ameelezea kushtushwa na taarifa za ajali iliyosababisha vifo vya watu 7 wakiwemo wafanyakazi hao 5, Dereva na Msaidizi wake na amewaombea Marehemu wote wapumzike mahali pema peponi, Amina.
“Nimeshtushwa sana na vifo hivi, nampa pole Mwenyekiti Ndg. Said Salim Bakhresa, ndugu wa Marehemu wote, Mtendaji Mkuu Ndg. Tido Mhando na wafanyakazi wote wa Azam Media Ltd, waandishi wa habari wote na watu wote walioguswa na vifo hivi” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Mhe. Rais Magufuli amewaombea majeruhi 3 wa ajali hiyo wapone haraka ili waweze kuendelea na majukumu yao ya kila siku.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli amerejea wito wake wa kuwataka watumiaji wa barabara hususani madereva kuwa makini na kuzingatia sheria za usalama barabarani ili kuepusha ajali zinazoweza kuepukika.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Chato
08 Julai, 2019
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Kenya, Mhe. Uhuru Muigai Kenyatta tarehe 06 Julai, 2019 amerejea nchini Kenya baada ya kumaliza ziara yake binafsi ya siku 2 aliyomtembelea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli katika Wilaya ya Chato Mkoani Geita.
Kabla ya kuruka katika uwanja wa ndege wa Chato, Mhe. Rais Kenyatta amefanya mazungumzo ya faragha na mwenyeji wake, Mhe. Rais Magufuli katika Kijiji cha Mlimani na baada ya mazungumzo hayo viongozi hao wamezungumza na waandishi wa habari.
Viongozi hao wamesema mazungumzo yao yalijikita katika kuimarisha zaidi uhusiano na ushirikiano wa Tanzania na Kenya hususani katika masuala ya kiuchumi ambapo wametaka biashara baina ya nchi hizo ikuzwe zaidi pamoja na kujenga uwiano wa kibiashara wenye maslahi kwa pande zote.
Mhe. Rais Magufuli amesema kwa kuzingatia kuwa Kenya imefanya uwekezaji mkubwa zaidi nchini Tanzania ikilinganishwa na uwekezaji wa Tanzania nchini Kenya, wamekubaliana kuwa kampuni za Kenya zijielekeza kuongeza thamani ya bidhaa kwa kuanzisha viwanda vitakavyosindika mazao na kuchakata bidhaa mbalimbali hapahapa Tanzania badala ya kusafirisha malighafi kwenda Kenya.
Ameongeza kuwa wamekubaliana kuwa Kenya itanunua gesi ya Tanzania badala ya kuagiza kutoka nje ya Bara la Afrika kwa kuwa Tanzania imejaaliwa gesi nyingi, na wamewaagiza Mawaziri wa Tanzania na Kenya kukutana na kujadili namna Kenya itavyonunua gesi hiyo.
Kuhusu ziwa Victoria ambalo kwa asilimia 51 lipo Tanzania na kwa asilimia 5 lipo Kenya, Mhe. Rais Magufuli amesema wamekubaliana kuwa Mawaziri wa nchi hizo wahakikishe meli za Tanzania na Kenya zinaimarishwa na kuondoa vikwazo vinavyokwamisha meli hizo kufanya kazi ya kukuza biashara katika nchi za Tanzania, Kenya na Uganda ambazo zinazunguka ziwa hilo.
Kwa upande wake, Mhe. Rais Uhuru Kenyatta amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa mapokezi mazuri aliyoyapata hapa Chato, na kwa upendo mkubwa uliooneshwa na wananchi wa Chato kwake na ujumbe wake, na ameeleza kuwa huo ni uthibitisho wa uhusiano mzuri, undugu na urafiki wa karibu wa Wakenya na Watanzania.
Amesema pamoja na kuimarisha zaidi uhusiano wa Tanzania na Kenya uliojengwa na Waasisi wa Mataifa hayo Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere na Hayati Mzee Jomo Kenyatta, wamekubaliana kuhakikisha nchi hizo zinakuwa na amani na kuheshimu mkataba wa kukabiliana na uhalifu ambapo Mtanzania atakayekamatwa kwa uhalifu nchini Kenya anashughulikiwa kwa mujibu wa sheria za Kenya na Mkenya atakayekamatwa kwa uhalifu nchini Tanzania anashughulikiwa kwa mujibu wa sheria za Tanzania.
Mhe. Uhuru Kenyatta amesisitiza kuwa Wakenya na Watanzania hawana sababu ya kupoteza muda kwa mambo yasiyo ya msingi bali kuhakikisha uchumi unakua, biashara inaongezeka na uhusiano na ushirikiano katika maeneo mbalimbali unaimarika zaidi.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli na Mhe. Rais Kenyatta wamekubaliana kuwakutanisha wake wa waasisi wa Mataifa ya Tanzania, Kenya na Uganda ambao ni Mama Maria Nyerere, Mama Ngina Kenyatta na Mama Miria Obote kwa siku 3 Jijini Dar es Salaam ili wapate muda wa kujadiliana pamoja na kukumbuka misingi iliyowekwa na waasisi wa Mataifa hayo.
Akiwa nyumbani kwa Mhe. Rais Magufuli katika Kijiji cha Mlimani Wilayani Chato Mhe. Kenyatta ameweka shada la maua katika makaburi ya familia ya Mhe. Rais Magufuli na pia amemtembelea tena Mama Mzazi wa Mhe. Rais Magufuli, Bibi Suzana Magufuli ambaye baada ya kupatiwa matibabu ya kiharusi katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete Jijini Dar es Salaam anaendelea kupata matibabu hayo akiwa nyumbani.
Pamoja na kumshukuru kwa kumtembelea nyumbani kwake Chato, Mhe. Rais Magufuli ametoa zawadi ya ndege wanne aina ya Tausi kwa Mhe. Rais Kenyatta ili akawafuge na kuweka kumbukumbu nyingine ya uhusiano mzuri wa Tanzania na Kenya.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Chato
06 Julai, 2019
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Kenya, Mhe. Uhuru Muigai Kenyatta amekemea vitendo vya baadhi ya watu wanaotoa kauli za uchochezi unaolenga kudhohofisha uhusiano wa kirafiki, kidugu na kijirani uliopo kati ya Kenya na Tanzania na amebainisha kuwa vitendo hivyo haviwezi kuruhusiwa kuwagawa Wakenya na Watanzania.
Mhe. Rais Kenyatta amesema hayo tarehe 05 Julai, 2019 wakati akiwasalimu wananchi muda mfupi baada ya kutua katika uwanja wa ndege wa Chato Mkoani Geita katika siku ya kwanza ya ziara yake binafsi ya kumtembelea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli aliyepo mapumzikoni Chato Mkoani Geita.
Amefafanua kuwa Tanzania na Kenya zimejaaliwa kuwa na mali nyingi, kuongea lugha moja ya Kiswahili na wananchi wake wanashirikiana kwa mambo mengi, hivyo kauli ama vitendo vyovyote vinavyolenga kuharibu uhusiano huu mzuri havikubaliki na havitafanikiwa.
“Nimekuja hapa Chato kama ndugu, jirani na rafiki. Na hii ndio Jumuiya ya Afrika Mashariki ambayo sisi tunataka, sio jumuiya ya watu ambao wana fikira ndogo, za zamani, za kikabila, za ujinga, sisi tunataka jumuiya ya watu wenye maono ya mbele, ambao wanajua kwamba Kenya ikitajirika Tanzania imetajirika, Tanzania ikitajirika Kenya imetajirika, watu ambao hawawagawi watu kwa mambo madogomadogo ambayo hayasaidii” amesema Mhe. Rais Kenyatta.
Mhe. Rais Kenyatta ameongeza kuwa katika uongozi wake anatamani kuona Jumuiya ya Afrika Mashariki inakuwa kitu kimoja, wananchi wake wanakuwa huru kwenda nchi yoyote ndani ya jumuiya na ametoa wito kwa wana Afrika Mashariki kujielekeza katika kuzijenga nchi zao kimaendeleo badala ya kupoteza muda mwingi kwa porojo za kisiasa.
Amempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa juhudi kubwa anazizofanya kujenga uchumi wa Watanzania na pia amepongeza ujenzi wa uwanja wa ndege wa Chato ambao amesema utasaidia kukuza biashara, ujenzi wa viwanda na uwekezaji mwingine katika eneo hilo na nchi jirani.
Kwa upande wake, Mhe. Rais Magufuli amemshukuru Mhe. Rais Kenyatta kwa kuomba kuja kumtembelea akiwa mapumzikoni Chato, na amebainisha kuwa ziara yake ni uthibitisho kuwa uhusiano wa Tanzania na Kenya ni mzuri na Wakenya na Watanzania ni wamoja.
Mhe. Rais Magufuli amefafanua kuwa uhusiano wa Tanzania na Kenya umeanza kabla ya uhuru ambapo Watanzania wanaona Kenya ni nyumbani kwao na Wakenya wanaona Tanzania ni nyumbani kwao, na kwamba nchi hizo zimekuwa zikishirikiana katika maeneo mengi ya kiuchumi, kijamii na kitamaduni.
Ametoa mfano wa ushirikiano katika uchumi kwa kueleza kuwa katika mwaka 2018 biashara kati ya nchi hizo ilikuwa na thamani ya shilingi Trilioni 1.045 ambapo Tanzania iliuza nchini Kenya bidhaa zenye thamani ya shilingi Bilioni 482.43 na iliagiza bidhaa zenye thamani ya shilingi Bilioni 563.07.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli amesema Kenya ni kati ya nchi 5 zinazoongoza kwa uwekezaji nchini Tanzania ambapo inayo miradi ya uwekezaji 504 yenye thamani ya shilingi Trilioni 3 na Bilioni 868 na ambayo imetoa ajira kwa watu 50,927, ilihali Tanzania inazo kampuni 24 zilizowekeza shilingi Bilioni 423 nchini Kenya. Halikadhalika katika utalii amesema kwa mwaka 2018 Watanzania 222,216 walikwenda kutalii nchini Kenya (ambao ni sawa na asilimia 10 ya watalii wote waliotembelea Kenya) na hivyo kuifanya Tanzania kuwa nchi ya pili kwa kupeleka watalii wengi nchini humo ikitanguliwa na Marekani.
Mhe. Rais Magufuli amempongeza Mhe. Rais Kenyatta kwa kukemea na kuchukua hatua dhidi ya kiongozi mmoja wa siasa nchini Kenya aliyetoa kauli za kichochezi zilizolenga kuharibu uhusiano mzuri wa Watanzania na Wakenya na amemhakikishia kuwa Watanzania wanawapenda Wakenya.
Amesisitiza kuwa Tanzania na Kenya zinashirikiana katika miradi mingi ikiwemo ujenzi wa miundombinu kama vile barabara ya Arusha – Namanga – Arthi River nchini Kenya, vituo vya huduma za pamoja vya mipaka ya Holili na Namanga, na hivi sasa mradi wa ujenzi wa barabara ya Arusha – Holili – Taveta, mradi wa kusafirisha umeme kutoka Tanzania kwenda Kenya na maandalizi yanaendelea ya kujenga barabara ya lami ya Bagamoyo (Tanzania) – Mombasa (Kenya).
Pia, Mhe. Rais Magufuli amesema Serikali ya Tanzania inajenga meli mpya 1 na kukarabati meli 5 katika ziwa Victoria ambazo zitatoa huduma za usafiri wa abiria na mizigo kati ya Tanzania, Kenya na Uganda na hivyo amewataka Watanzania na Wakenya kuendelea kushikamana ili kuimarisha uchumi wa nchi zao.
Akiwa nyumbani kwa Mhe. Rais Magufuli, Mhe. Rais Kenyatta amemjulia hali mama wa Mhe. Rais Magufuli, Bibi Suzana Magufuli anayeendelea kupatiwa matibabu nyumbani hapo.
Mhe. Rais Kenyatta leo analala Chato Mkoani Geita na kesho atamaliza ziara yake binafsi ya siku 2 na kurejea nchini Kenya.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Chato
05 Julai, 2019
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Kenya Mhe. Uhuru Muigai Kenyatta keshokutwa Ijumaa tarehe 05 Julai, 2019 atafanya ziara binafsi ya siku 2 hapa nchini kwa mwaliko wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli.
Mhe. Rais Kenyatta atatua katika uwanja wa ndege wa Chato Mkoani Geita saa 4:00 asubuhi na kisha kuelekea nyumbani kwa Mhe. Rais Magufuli katika kijiji cha Mlimani Wilayani Chato.
Akiwa Chato, Mhe. Rais Kenyatta atafanya mazungumzo na mwenyeji wake Mhe. Rais Magufuli.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Chato
03 Julai, 2019