Taarifa kwa vyombo vya Habari ya zamani
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amewataka Watanzania kutotishwa na janga la ugonjwa wa homa ya mapafu inayosababishwa na virusi vya Corona (Covid-19) na badala yake waendelee kuchapa kazi na kujenga uchumi huku wakizingatia tahadhari zote za kujikinga kuambukizwa ugonjwa huo kama zilivyotolewa na wataalamu.
Mhe. Rais Magufuli amesema hayo tarehe 22 Machi, 2020 alipohudhuria Ibada ya Jumapili katika Kanisa la Mtakatifu Paulo wa Msalaba, Jimbo Kuu la Jimbo Kuu Katoliki la Dodoma, iliyoongozwa na Paroko wa Parokia hiyo Padre Onesmo Wisi.
Katika salamu zake katika Ibada hiyo, Mhe. Rais Magufuli amesema kuwepo kwa ugonjwa wa Corona isiwe sababu ya kutishana kiasi cha kumsahau Mwenyezi Mungu, hivyo ametoa wito kwa Wakristo na Waumini wa madhehebu mengine kumrudia Mwenyezi Mungu ili aepusha janga hili, badala ya kumwacha shetani atawale.
Mhe. Rais Magufuli amekemea tabia za baadhi ya watu wanaofanya mzaha juu ya ugonjwa huu ama kuwatia hofu wananchi kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii, na badala yake ametaka Watanzania waendelee kuchapa kazi huku wakingatia tahadhari.
“Watu tusitishane, tunatishana mno. Niwaombe ndugu Wakristo na Watanzania kwa ujumla wa Madhehebu yote, huu ndio wakati mzuri sana wa kumtegemea Mungu kuliko wakati wote, tuendelee kuchapa kazi, tuendelee kuujenga uchumi wetu, hatuwezi kusalimu amri kwa ugonjwa huu wa Corona na kushindwa kumtegemea Mungu na tukashindwa kuendeleza uchumi wetu” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Amewashukuru viongozi wa Dini kwa kuungana na Serikali katika kuwahamasisha wananchi kuchukua tahadhari na ametoa wito kwa viongozi hao kuendelea kuliombea Taifa ili Mwenyezi Mungu aepushe balaa hili la Corona.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Chamwino
22 Machi, 2020
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ameahirisha Mbio za Mwenge wa Uhuru za mwaka huu zilizopangwa kuzinduliwa tarehe 02 Aprili, 2020 huko Unguja, Zanzibar kwa lengo la kuchukua tahadhari ya kusambaa kwa virusi vya ugonjwa wa Corona (Covid-19) endapo utaingia hapa nchini.
Mhe. Rais Magufuli ametangaza maamuzi hayo tarehe 16 Machi, 2020 alipokuwa akiwasalimu wananchi wa Ubungo, Mbezi Mwisho na Kibamba Jijini Dar es Salaam, wakati akikagua maendeleo ya upanuzi wa barabara na ujenzi wa barabara za juu katika makutano ya barabara za Morogoro, Sam Nujoma na Mandela eneo la Ubungo (Ubungo Interchange).
Pamoja na kuahirisha Mbio za Mwenge wa Uhuru, Mhe. Rais Magufuli ameagiza fedha zilizoandaliwa kwa ajili ya mbio hizo zipelekwe Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa ajili ya maandalizi ya kujiweka tayari endapo ugonjwa wa Corona utaingia hapa nchini.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli amewasisitiza Watanzania wote kuendelea kuchukua tahadhari ya kuambukizwa virusi vya ugonjwa wa Corona kwa kuepuka misongamano, kutogusana, kunawa mikono kwa sabuni na maji yanayotiririka na kuzingatia maelekezo mengine ya wataalamu wa afya, lakini amesema ugonjwa huo bado haujaingia hapa nchini.
Katika ziara hiyo Mhe. Rais Magufuli ambaye ameongozana na Mkewe Mama Janeth Magufuli amekagua maendeleo ya upanuzi wa barabara ya Mwenge – Morocco yenye urefu wa kilometa 4.1 ambayo inajengwa njia 4 kwa gharama ya shilingi Bilioni 77.5 na ujenzi wa barabara za juu Ubungo ambao umefikia asilimia 70.
Ujenzi wa barabara za juu Ubungo unatarajiwa kukamilika kabla ya Desemba 2020 kwa gharama ya shilingi Bilioni 230 na unatarajiwa kusaidia kwa kiasi kikubwa kukabiliana na msongamano wa magari katika Jiji la Dar es Salaam.
Mhe. Rais Magufuli pia amekagua maendeleo ya upanuzi wa barabara ya Kimara – Kibaha yenye urefu wa kilometa 19.2 ambayo ujenzi wake umefikia asilimia 70 na inatarajiwa kukamilika Januari 2021 kwa gharama ya shilingi Bilioni 140.
Akiwa Mlandizi Mkoani Pwani Mhe. Rais Magufuli amesikiliza malalamiko ya wafanyabiashara ndogondogo wa eneo hilo walioondolewa kandokando mwa barabara na ameagiza wafanyabiashara hao warejee katika maeneo yao lakini wasifanyie biashara barabarani wala wasiwazuie wenye vibanda vya maduka kufanya biashara zao.
Mjini Chalinze, Mhe. Rais Magufuli amewahakikishia wananchi kuwa Serikali itahakikisha tatizo la maji katika Mji huo linamalizika baada ya kukamilika kwa mradi mkubwa ambao unaendelea kutekelezwa.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Pwani
16 Machi, 2020
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 26 Machi, 2020 amepokea ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka 2018/19 na ripoti ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) ya mwaka 2018/19, Ikulu Chamwino, Mkoani Dodoma.
Hafla ya kupokea ripoti hizo imehudhuriwa na Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, Spika wa Bunge na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job Yustino Ndugai, Mwakilishi wa Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Jaji George Mcheche Masaju, Mawaziri na Naibu Waziri, Makatibu Wakuu na Viongozi Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama.
Mhe. Rais Magufuli amempongeza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Bw. Charles Kichere kwa kazi nzuri ya ukaguzi aliyoifanya ambayo imeonesha maeneo mbalimbali ambayo Serikali imefanya vizuri na maeneo ambayo yanahitaji kufanyiwa kazi, na amewaagiza Makamu wa Rais, Waziri Mkuu na Katibu Mkuu Kiongozi Mhe. Balozi John Kijazi kwenda kufanyia kazi dosari zote zilizojitokeza katika utendaji kazi wa Serikali.
Pamoja na kupokea ripoti 19 za ukaguzi kutoka kwa CAG, amempongeza kwa ofisi yake kuanza kukagua mashirika ya umma badala ya kutumia taasisi za ukaguzi za nje ya nchi hali iliyowezesha kuokoa shilingi Bilioni 1.4, kuonesha dosari za matumizi ya fedha katika taasisi mbalimbali ikiwemo vyama vya siasa na Jeshi la Polisi na pia amemuagiza Naibu Waziri wa Utumishi na Utawala Bora Mhe. Mary Mwanjelwa kuhakikisha wakaguzi mahsusi wa ukaguzi 25 waliombwa na CAG kwa ajili ya ukaguzi wa kitaaluma katika miradi mikubwa, taasisi na mashirika wanajiriwa haraka iwezekanavyo ili kudhibiti upotevu wa fedha na mali za umma katika maeneo hayo.
Kwa upande wa TAKUKURU amempongeza Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU ambaye alikuwa Naibu Mkurugenzi Mkuu, Brig. Jen. John Mbungo kwa kazi nzuri inayofanywa na taasisi hiyo katika kudhibiti vitendo vya rushwa, kuokoa fedha na mali za umma zilizokuwa zimepotea, na pia kurejesha shilingi Bilioni 8.8 za wakulima zilizokuwa zimeibwa kupitia vyama vya ushirika vya wakulima hapa nchini.
Kutokana na kazi hiyo nzuri, Mhe. Rais Magufuli amemteua Brig. Jen. John Mbungo kuwa Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU kuanzia leo tarehe 26 Machi, 2020.
Mhe. Rais Magufuli ameelezea kutofurahishwa kwake na viongozi wa Mikoa na Wilaya kutochukua hatua kwa wakati pale wananchi wanapodhulumiwa haki zao, na kwamba haikuwa sawa kwa wakulima kudhulumiwa shilingi Bilioni 8.8 ambazo zimesubiri timu ya TAKUKURU ya kitaifa kuchukua hatua.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli amerejea kauli yake ya kumshukuru Baba wa Taifa, Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere kwa kufanya uamuzi wa kuhamishia Makao Makuu ya Serikali Mkoani Dodoma, na kuamua kujenga Ikulu katika eneo zuri la Chamwino, ukiwemo ukumbi ambao leo umetumiwa kupokea ripoti za CAG na TAKUKURU baada ya kukarabatiwa na Serikali ya Awamu ya Tano.
Amesema ukarabati wa ukumbi huo ni sehemu ya kazi kubwa iliyofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano ya kujenga na kukarabati majengo na miundombinu ya Ikulu ya Chamwino yenye ukuta (fensi) wenye urefu wa kilometa 27 na eneo la ukubwa kilometa za mraba 34.5, hali inayoifanya Ikulu ya Tanzania kuwa na eneo kubwa zaidi duniani.
Nae, CAG Bw. Charles Kichere amesema ripoti za ukaguzi 19 alizoziwasilisha ni za Serikali Kuu, Serikali za Mitaa, Mashirika ya Umma, miradi ya maendeleo, ukaguzi wa ufanisi, ukaguzi wa mifumo ya TEHAMA, ufuatiliaji wa mapandekezo yaliyotolewa katika ripoti za ukaguzi wa ufanisi kwa miaka iliyopita na ripoti 12 za ukaguzi wa ufanisi zinazohusu sekta mbalimbali.
Amebainisha kuwa kwa mwaka wa fedha unaoishia tarehe 30 Juni, 2019 ametoa jumla ya hati 1,082 ambapo kati yake hati zinazoridhisha ni 1,017 (94%), hati zenye mashaka 46 (4.25%), hati zisizoridhisha 7 (0.64%) na hati mbaya 12 (1.11%) ambazo ni za vyama vya siasa.
Kwa upande wake Brig. Jen. Mbungo amesema utafiti uliofanywa kwa mwaka 2018/19 umeonesha kuwa idadi ya Watanzania wanaoamini kuwa vitendo vya rushwa vimepungua imeongezeka kutoka asilimia 37 (2015) hadi kufikia asilimia 71 na pia ripoti ya Jukwaa la Uchumi Duniani (World Economic Forum - WEF) kwa kushirikiana na sekta binafsi imeonesha kuwa Tanzania imeshika nafasi ya 28 kati ya nchi 136 kwa ufanisi katika matumizi mazuri ya fedha za umma.
Ameongeza kuwa katika mwaka 2018/19 operesheni za TAKUKURU zimefanikiwa kuokoa shilingi Bilioni 82.8 ikilinganishwa na shilingi Bilioni 70.3 za mwaka 2017/18 na pia miradi ya maendeleo iliyofuatiliwa imeongezeka kutoka 691 yenye thamani ya shilingi Trilioni 1 na Bilioni 494 hadi kufikia miradi 1,106 yenye thamani ya shilingi Trilioni 1 na Bilioni 668.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Chamwino
26 Machi, 2020
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ameahirisha Mbio za Mwenge wa Uhuru za mwaka huu zilizopangwa kuzinduliwa tarehe 02 Aprili, 2020 huko Unguja, Zanzibar kwa lengo la kuchukua tahadhari ya kusambaa kwa virusi vya ugonjwa wa Corona (Covid-19) endapo utaingia hapa nchini.
Mhe. Rais Magufuli ametangaza maamuzi hayo asubuhi tarehe 16 Machi, 2020 alipokuwa akiwasalimu wananchi wa Ubungo, Mbezi Mwisho na Kibamba Jijini Dar es Salaam, wakati akikagua maendeleo ya upanuzi wa barabara na ujenzi wa barabara za juu katika makutano ya barabara za Morogoro, Sam Nujoma na Mandela eneo la Ubungo (Ubungo Interchange).
Pamoja na kuahirisha Mbio za Mwenge wa Uhuru, Mhe. Rais Magufuli ameagiza fedha zilizoandaliwa kwa ajili ya mbio hizo zipelekwe Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa ajili ya maandalizi ya kujiweka tayari endapo ugonjwa wa Corona utaingia hapa nchini.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli amewasisitiza Watanzania wote kuendelea kuchukua tahadhari ya kuambukizwa virusi vya ugonjwa wa Corona kwa kuepuka misongamano, kutogusana, kunawa mikono kwa sabuni na maji yanayotiririka na kuzingatia maelekezo mengine ya wataalamu wa afya, lakini amesema ugonjwa huo bado haujaingia hapa nchini.
Katika ziara hiyo Mhe. Rais Magufuli ambaye ameongozana na Mkewe Mama Janeth Magufuli amekagua maendeleo ya upanuzi wa barabara ya Mwenge – Morocco yenye urefu wa kilometa 4.1 ambayo inajengwa njia 4 kwa gharama ya shilingi Bilioni 77.5 na ujenzi wa barabara za juu Ubungo ambao umefikia asilimia 70.
Ujenzi wa barabara za juu Ubungo unatarajiwa kukamilika kabla ya Desemba 2020 kwa gharama ya shilingi Bilioni 230 na unatarajiwa kusaidia kwa kiasi kikubwa kukabiliana na msongamano wa magari katika Jiji la Dar es Salaam.
Mhe. Rais Magufuli pia amekagua maendeleo ya upanuzi wa barabara ya Kimara – Kibaha yenye urefu wa kilometa 19.2 ambayo ujenzi wake umefikia asilimia 70 na inatarajiwa kukamilika Januari 2021 kwa gharama ya shilingi Bilioni 140.
Akiwa Mlandizi Mkoani Pwani Mhe. Rais Magufuli amesikiliza malalamiko ya wafanyabiashara ndogondogo wa eneo hilo walioondolewa kandokando mwa barabara na ameagiza wafanyabiashara hao warejee katika maeneo yao lakini wasifanyie biashara barabarani wala wasiwazuie wenye vibanda vya maduka kufanya biashara zao.
Mjini Chalinze, Mhe. Rais Magufuli amewahakikishia wananchi kuwa Serikali itahakikisha tatizo la maji katika Mji huo linamalizika baada ya kukamilika kwa mradi mkubwa ambao unaendelea kutekelezwa.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Pwani
16 Machi, 2020
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amewataka Watanzania kutotishwa na janga la ugonjwa wa homa ya mapafu inayosababishwa na virusi vya Corona (Covid-19) na badala yake waendelee kuchapa kazi na kujenga uchumi huku wakizingatia tahadhari zote za kujikinga kuambukizwa ugonjwa huo kama zilivyotolewa na wataalamu.
Mhe. Rais Magufuli amesema hayo tarehe 22 Machi, 2020 alipohudhuria Ibada ya Jumapili katika Kanisa la Mtakatifu Paulo wa Msalaba, Jimbo Kuu la Jimbo Kuu Katoliki la Dodoma, iliyoongozwa na Paroko wa Parokia hiyo Padre Onesmo Wisi.
Katika salamu zake katika Ibada hiyo, Mhe. Rais Magufuli amesema kuwepo kwa ugonjwa wa Corona isiwe sababu ya kutishana kiasi cha kumsahau Mwenyezi Mungu, hivyo ametoa wito kwa Wakristo na Waumini wa madhehebu mengine kumrudia Mwenyezi Mungu ili aepusha janga hili, badala ya kumwacha shetani atawale.
Mhe. Rais Magufuli amekemea tabia za baadhi ya watu wanaofanya mzaha juu ya ugonjwa huu ama kuwatia hofu wananchi kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii, na badala yake ametaka Watanzania waendelee kuchapa kazi huku wakingatia tahadhari.
“Watu tusitishane, tunatishana mno. Niwaombe ndugu Wakristo na Watanzania kwa ujumla wa Madhehebu yote, huu ndio wakati mzuri sana wa kumtegemea Mungu kuliko wakati wote, tuendelee kuchapa kazi, tuendelee kuujenga uchumi wetu, hatuwezi kusalimu amri kwa ugonjwa huu wa Corona na kushindwa kumtegemea Mungu na tukashindwa kuendeleza uchumi wetu” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Amewashukuru viongozi wa Dini kwa kuungana na Serikali katika kuwahamasisha wananchi kuchukua tahadhari na ametoa wito kwa viongozi hao kuendelea kuliombea Taifa ili Mwenyezi Mungu aepushe balaa hili la Corona.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Chamwino
22 Machi, 2020
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 10 Aprili, 2020 ameungana na Waumini wa Kanisa Katoliki katika Parokia ya Mlimani, Wilaya ya Chato Mkoani Geita kusali Ibada ya Ijumaa Kuu iliyoongozwa na Padre Prof. Innocent Sanga kutoka Jimbo Kuu Katoliki la Mbeya.
Ibada ya Ijumaa Kuu huadhimishwa ikiwa ni kumbukumbu ya kusulubiwa na kufa kwa Bwana Yesu Kristo, zaidi ya miaka 2,000 iliyopita.
Katika salamu zake, Mhe. Rais Magufuli amemshukuru Padre Sanga kwa mahubiri yaliyowakumbusha Wakristo kuwa msalaba unaokoa, na kwamba kupitia msalaba Mungu ataikoa dunia dhidi ya majanga mbalimbali ukiwemo ugonjwa wa homa ya mapafu unaosababishwa na virusi vya Corona (Covid-19).
Mhe. Rais Magufuli amesema mpaka sasa idadi ya Watanzania waliothibitika kuwa na virusi vya Corona ni takribani 29, Watanzania 5 waliopatwa na maambukizi wamepona, Watanzania 3 wamefariki dunia na kwa takribani asilimia 90 ya waliopatwa na virusi hivyo wanaendelea vizuri.
Amebainisha kuwa kutokana na madhara ya ugonjwa huo duniani, upo uwezekano wa kutokea upungufu wa chakula, hivyo ametoa wito kwa Watanzania kuzalisha chakula cha kutosha na pia amewataka Watanzania kuendelea kuchapa kazi kila mahali walipo huku wakichukua tahadhari za kutoambukizwa kama wanavyoelekezwa na wataalamu.
Mhe. Rais Magufuli amesisitiza kuwa Serikali imeamua kutowazuia watu ndani ya nyumba zao wala kufunga mipaka kwa kutambua madhara makubwa yanayoweza kujitokeza kutokana na kufanya hivyo ndani ya nchi na kwa nchi 8 ambazo zinategemea kupata huduma na bidhaa kupitia Tanzania hususani Bandari ya Dar es Salaam.
Amewataka Watanzania wote kuendelea kumuomba Mwenyezi Mungu ili aiepushe dunia na janga la ugonjwa wa Corona.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Chato
10 Aprili, 2020
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ameagiza kusimamishwa kazi mara moja kwa aliyekuwa Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) katika Mkoa wa Morogoro Mhandisi Godwin Andalwisye na wahandisi wake 12 waliokuwa na jukumu la uangalizi wa barabara katika Mkoa huo.
Mhe. Rais Magufuli ametoa agizo hilo leo tarehe 16 Machi, 2020 baada ya kutembelea eneo la daraja la Kiegeya lililosombwa na maji ya mvua tarehe 02 Machi, 2020 na kusababisha kukatika kwa mawasiliano ya barabara ya Dodoma – Morogoro ambayo ni kiunganishi muhimu cha Mikoa ya Kanda ya Kati, Kanda ya Magharibi, Kanda ya Kaskazini Magharibi na nchi jirani za Uganda, Rwanda, Burundi na DRC ambazo husafirisha mizigo na abiria kwenda Dar es Salaam.
Mawasiliano ya barabara hiyo yalirejea baada ya siku 2 na mpaka sasa eneo hilo linapitika kwa madaraja ya muda huku kazi ya kuimarisha ikiendelea.
Mhe. Rais Magufuli ameagiza kusimamishwa kazi kwa Maafisa hao wa TANROADS pamoja na kuwachunguza kama kuna vitendo vya hujuma walivifanya, kutokana na kutochukua tahadhari za kitaalamu za kuzuia maji ya mvua yasisombe daraja lililokuwepo na pia kushindwa kurejesha mawasiliano ya barabara kwa kujenga daraja haraka licha ya fedha za kufanyia kazi hizo kuwepo.
Katika mahojiano na Mkurugenzi wa Matengenezo wa TANROADS Mhandisi Mohamed Ntunda, Mhe. Rais Magufuli ameelezwa kuwa hadi daraja la Kiengeya linasombwa na maji ya mvua, TANROADS katika Mkoa wa Morogoro walikuwa na zaidi ya shilingi Bilioni 3 za matengenezo ya dharura ya barabara.
Akiwa katika eneo hilo Mhe. Rais Magufuli ameliona daraja la muda lililojengwa na Wataalamu wa TANROADS na pia ametembea kwa miguu kuelekea mto unakotirisha maji yake ambapo ameshauri wataalamu hao waangalie uwezekano wa kujenga daraja katika eneo jingine lenye umbali mfupi wa daraja na miinuko inayofaa endapo wataona inafaa kufanya hivyo.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli amemuonya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Aloyce Kamwelwe, Mtendaji Mkuu wa TANROADS Mhandisi Patrick Mfugale na Mkurugenzi wa Matengenezo wa TANROADS Mhandisi Mohamed Ntunda kutokana na kutoridhishwa na juhudi zilizofanywa kurejesha mawasiliano ya uhakika katika eneo hilo na ametaka kosa hilo lisirudie.
Ametoa siku 7 kwa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano pamoja na TANROADS kuhakikisha eneo hilo linakuwa na daraja la uhakika la kupita magari kama ilivyokuwa kabla ya daraja kusombwa na maji ili kutoathiri shughuli za kiuchumi na kijamii kutokana na kukatika kwa mawasiliano ya barabara.
Mhe. Rais Magufuli amewataka Mameneja wa TANROADS wa Mikoa yote hapa nchini kuhakikisha mawasiliano ya barabara kuu katika Mikoa yao hayakatiki vinginevyo meneja husika atavuliwa wadhifa wake.
Wasafiri na wananchi waliokusanyika katika eneo hilo wakati Mhe. Rais Magufuli akikagua eneo hilo wamelalamikia kukatika kwa mawasiliano ya barabara ya kuelekea Hospitali ya Misheni ya Berega kutokana na kusombwa kwa daraja, hivyo amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Loatha Sanare kuhakikisha Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) inajenga daraja hilo ndani ya siku 7 ili wananchi waendelee kupata huduma za matibabu kama kawaida.
Halikadhalika wananchi hao wamelalamikia kutokamilika kwa ujenzi wa chumba cha upasuaji katika Kituo cha Afya Magubike na Mhe. Rais Magufuli amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Morogoro kuhakikisha jengo hilo linajengwa ndani ya miezi 2.
Pia, Wananchi hao wamelalamikia kuchangishwa shilingi 20,000 kwa kila kaya kwa ajili ya kujenga jengo la maabara katika shule yao ya Sekondari, lakini fedha hizo hazijulikani zilikokwenda na badala yake wameanza kuchangishwa fedha nyingine shilingi 5,000 kwa kila kaya, na Mhe. Rais Magufuli amemuagiza Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro Wilbroad Mutafungwa kufuatilia na kuchukua hatua stahiki. Mhe. Rais Magufuli amechangia shilingi Milioni 5 na ameagiza wananchi wasichangishwe fedha za ujenzi wa maabara hiyo.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Morogoro
16 Machi, 2020
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 28 Februari, 2020 amekagua maendeleo ya ujenzi wa Msikiti mkubwa wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) unaojengwa Kinondoni Jijini Dar es Salaam.
Msikiti huo unajengwa kwa ufadhili wa Mfalme Mohammed VI wa Morocco baada ya kuombwa na Mhe. Rais Magufuli alipofanya ziara rasmi hapa nchini Oktoba 2016.
Akiongozwa na Mufti wa Tanzania, Sheikh Aboubakar Zubeir bin Ally, Mhe. Rais Magufuli amejionea kazi za ukamilishaji wa jengo jipya la Msikiti na jengo la ofisi ya Taasisi ya Mfalme Mohammed VI wa Morocco zikiendelea kukamilishwa, na ameelezea kufurahishwa kwake na ubora na uzuri wa Msikiti huo.
Mhe. Rais Magufuli amemshukuru Mfalme Mohammed VI wa Morocco kwa kutekeleza ombi alilomuomba la kuwajengea Waislamu Msikiti mkubwa kuliko yote hapa nchini, na amempongeza Mufti wa Tanzania na Waislamu wote kwa kujengewa nyumba nzuri ya Ibada.
Mufti wa Tanzania, Sheikh Aboubakar Zubeir bin Ally amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kuwajali Waislamu na kuwaombea msaada wa kujengewa Msikiti huo ambao ujenzi wake umefikia asilimia 97.
Akiwa na viongozi wenzake wa BAKWATA, Sheikh Mkuu Aboubakar Zubeir bin Ally ameongoza Dua ya kumuombea Mhe. Rais Magufuli na kuliombea Taifa ili Mwenyezi Mungu aiepushe Tanzania dhidi ya maradhi ya homa ya virusi vya corona, kudumisha amani na utulivu na kuombea Uchaguzi Mkuu utakaofanyika baadaye mwaka huu ufanyike vizuri na kwa amani.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
28 Februari, 2020
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 24 Februari, 2020 amekutana na kufanya mazungumzo na Msomi na Mwanamajumui wa Afrika (Pan-Africanist) Prof. Patrick Loch Otieno Lumumba, Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Dkt. Magufuli na Prof. PLO Lumumba ambaye ni raia wa Kenya wamezungumzia masuala mbalimbali yahusuyo juhudi za Afrika katika kuimarisha uchumi kwa kutumia rasilimali zake na pia wajibu wa Waafrika na viongozi wao katika kuimarisha huduma za kijamii na kukabiliana na changamoto mbalimbali.
Mhe. Rais Magufuli amempongeza Prof. PLO Lumumba kwa juhudi zake za kueleza waziwazi makosa yanayosababisha nchi za Afrika kubaki nyuma kiuchumi, kijamii na kisiasa, wajibu wa viongozi na wananchi wa Afrika katika kukabiliana na changamoto zinazozikabili nchi zao na mapenzi yake makubwa kwa Afrika.
Mhe. Rais Magufuli amemueleza juhudi ambazo Serikali ya Awamu ya Tano inazifanya katika kujenga uchumi imara wa kujitegemea ikiwemo utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati kama vile ujenzi wa reli ya kisasa (standard gauge railway-SGR), ujenzi wa Bwawa la Nyerere litakalozalisha megawati 2,115 za umeme, kuongeza usambazaji wa umeme kutoka vijiji 2,018 hadi kufikia vijiji 8,587, ujenzi wa barabara na madaraja makubwa na madogo, kutoa elimu bila malipo kwa shule za msingi na sekondari, kuongeza mikopo ya elimu ya juu, kuongeza ukusanyaji wa mapato, kudhibiti rasilimali muhimu ya madini na kupambana na rushwa.
“Mimi sijawahi kukutana nawe kabla, lakini nakusikia na kukuona kupitia vyombo vya habari jinsi unavyopaza sauti kuhusu Bara la Afrika, nakupongeza kwa juhudi hizo, na ninafarijika kwamba unaisemea vizuri Afrika” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Kwa upande wake Prof. PLO Lumumba amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kutenga muda wake kuzungumza nae, na amempongeza kwa juhudi kubwa alizozionesha katika kipindi kifupi cha uongozi wake wa miaka 4 ambapo ameonesha mfano wa namna ya kupigania rasilimali za nchi ikiwemo madini, kujenga nidhamu ya utumishi Serikalini, kuimarisha uchumi, kupambana na wizi wa mali za umma, rushwa na ufisadi.
Prof. PLO Lumumba amesema inafaa kwa nchi za Afrika kujifunza mambo yanayofanyika Tanzania kwa sasa, na amesisitiza kuwa ni muhimu kwa Waafrika kujiamini na kuchukua hatua madhubuti za kuwaondoa katika hali ya sasa ambapo rasilimali zake zinachukuliwa na Mataifa ya nje ilihali wananchi wake wakikabiliwa na changamoto mbalimbali.
Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli amekutana na Mwakilishi wa Kansela wa Ujerumani anayeshughulikia masuala ya Afrika Bw. Guenter Nooke, Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Bw. Nooke amewasilisha ujumbe wa Kansela wa Ujerumani Mhe. Angela Merkel na pia ameelezea kufurahishwa kwake na hatua kubwa za maendeleo zilizofikiwa hapa nchini ikilinganishwa na alipokuja miaka iliyopita.
Pia amepongeza juhudi zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano katika kupambana na rushwa na kuimarisha uchumi ambapo ameahidi kuwa Ujerumani itaendelea kushirikiana na Tanzania katika uwekezaji na biashara na masuala mengine ya kijamii.
Kwa upande wake, Mhe. Rais Magufuli amemhakikishia Kansela wa Ujerumani kuwa Serikali ya Awamu ya Tano ipo tayari kuuendeleza na kuukuza zaidi uhusiano mzuri na wa kihistoria uliopo kati yake na Ujerumani, na inawakaribisha wafanyabiashara na wawekezaji kuja kuwekeza hapa nchini.
Katika mazungumzo hayo Bw. Nooke ameongoza na Balozi wa Ujerumani hapa nchini Mhe. Regine Hess.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
24 Februari, 2020
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amewapongeza Madaktari na Wauguzi wote hapa nchini kwa kazi nzuri wanazozifanya na amewahakikishia kuwa Serikali itaendelea kuboresha maslahi na mazingira yao ya kazi.
Mhe. Rais Magufuli amesema hayo leo tarehe 20 Februari, 2020 wakati akihutubia mkutano wa Madaktari uliofanyika katika ukumbi wa Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Madaktari na watoa huduma za afya zaidi ya 1,500 kutoka Mikoa yote ya Tanzania Bara.
Mhe. Rais Magufuli amesema sambamba na juhudi kubwa zilizofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano katika kuimarisha huduma za afya, Madaktari wameonesha ushirikiano mkubwa katika kutekeleza majukumu yao ikiwemo utoaji huduma za matibabu ya kibingwa.
Katika mkutano huo, Mhe. Rais Magufuli amepokea taarifa ya Chama cha Madaktari Tanzania (MAT) iliyotolewa na Rais wa MAT Dkt. Elisha Osati na pia amesikiliza maoni na kero mbalimbali za Madaktari ambapo ameahidi kuwa Serikali itatoa jengo kwa ajili shughuli za MAT na pia ameahidi kuwa Serikali itaanza kuwaajiri Madaktari wapya 1,000 waliohitimu masomo yao.
Kuhusu changamoto zingine zilizotolewa na MAT na Madaktari hao, Mhe. Rais Magufuli amewahakikishia Madaktari na watoa huduma za afya hao kuwa changamoto hizo amezisikia na ameiagiza Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kuanza kuzishughulikia.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli amefafanua kuwa katika miaka 4 iliyopita Serikali ya Awamu ya Tano imefanya juhudi kubwa kuimarisha huduma za afya ambapo Zahanati zimeongezeka kutoka 6,044 hadi 6,467 (zahanati 368 zimejengwa na Serikali), Vituo vya Afya vimeongezeka kutoka 718 hadi 1,169 (Vituo vya Afya 352 vimejengwa na Serikali), Vituo vya Afya vinavyotoa huduma za upasuaji vimeongezeka kutoka 115 hadi kufikia 467 na Hospitali zenye hadhi ya Wilaya zimeongezeka kutoka 77 hadi kufikia 147 (Hospitali mpya 70 zimejengwa na Serikali). Miundombinu hii imegharimu shilingi Bilioni 293.705 na imewekewa vifaa tiba vyenye thamani ya shilingi Bilioni 68.706.
Mhe. Rais Magufuli ameongeza kuwa katika kipindi hiki pia Hospitali za Rufaa za Mikoa 23 zimekarabatiwa kwa gharama ya shilingi Bilioni 89.5, Hospitali za Mloganzila na Benjamin Mkapa zimekamilishwa na kuwekewa vifaa tiba kwa gharama ya shilingi Bilioni 102.9, Hospitali za Rufaa za Mikoa ya Geita, Katavi, Njombe, Simiyu na Songwe zimejengwa kwa shilingi Bilioni 58 na ujenzi wa Hospitali za Rufaa za Musoma, Mtwara, Mwananyamala na Sekou Toure Mwanza unaendelea. Juhudi hizi zimesaidia kuongeza idadi ya vituo vya kutolea tiba kutoka 7,014 mwaka 2015 hadi kufikia 8,446 mwaka 2019.
Pia, Mhe. Rais Magufuli ametaja maeneo mengine ya mafanikio kuwa ni kuongeza bajeti ya dawa kutoka shilingi Bilioni 31 hadi Shilingi Bilioni 270, kupunguza idadi ya wagonjwa wanaokwenda kutibiwa nje ya nchi kutoka wastani wa 200 kwa mwaka hadi 60 kutokana na kuimarika kwa huduma za matibabu ya kibingwa, kuajiri watumishi wapya wa afya 13,479 (kati ya watumishi wote 62,498) wakiwemo Madaktari Bingwa 22 na Madaktari 1,156, imejenga nyumba 832 za watumishi wa afya kwa kushirikiana na Taasisi ya Benjamin Mkapa.
Kutokana na juhudi hizo, Mhe. Rais Magufuli ametoa wito kwa Madaktari kuendelea kuchapa kazi kwa juhudi na maarifa na amewataka kutengeneza mikakati ya kuiwezesha Tanzania kuzalisha dawa na vifaa tiba, badala ya kuendelea kuagiza kutoka nje ya nchi kwa kiasi kikubwa.
Amekemea vitendo vya baadhi ya viongozi wa kisiasa kuwaweka mahabusu Madaktari lakini amewataka Madaktari kujiepusha na vitendo viovu ili wasichuliwe hatua.
Mapema Rais wa MAT Dkt. Elisha Osati na Mkurugenzi wa Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI) Dkt. Respicious Boniface wamemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa uwekezaji mkubwa ambao Serikali imeufanya katika sekta ya afya hususani kuimarisha matibabu ya kibingwa katika hospitali na taasisi zake, na wamemhakikishia kuwa Madaktari wataendelea kumuunga mkono kwa kuchapa kazi zaidi.
Katika Mkutano huo, Mhe. Rais Magufuli amekabidhi tuzo 2 zilizoandaliwa na MAT kwa Dkt. Jesse Mbwambo (Daktari Bingwa wa Magonjwa ya akili) na Wilson Koweli Chotamganga (Afisa Tabibu) kwa kutambua mchango wao mkubwa katika matibabu na pia amepokea tuzo ya MAT kwa kutambua mchango wake katika kuimarisha huduma za afya hapa nchini.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
20 Februari, 2020
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 17 Februari, 2020 amezindua kipindi cha 2 cha awamu ya 3 ya mpango wa kunusuru kaya masikini wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF III), katika ukumbi wa Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam.
Sherehe za uzinduzi huo zimehudhuriwa na Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Balozi Seif Ali Iddi, Spika wa Bunge Mhe. Job Yustino Ndugai, Marais Wastaafu Mhe. Dkt. Ali Hassan Mwinyi, Mhe. Benjamin William Mkapa na Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Mawaziri, Makatibu Wakuu, Mabalozi, Viongozi Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama, Viongozi wa Dini na Viongozi wa vyama vya Siasa.
Akizungumza katika sherehe hizo, Mhe. Rais Magufuli amewapongeza Marais Wastaafu wa kuasisi na kuiendeleza TASAF ambayo imetoa mchango mkubwa katika kupunguza umasikini hapa nchini.
Mhe. Rais Magufuli amebainisha kuwa juhudi za kukabiliana na umasikini hapa nchini ikiwemo mpango wa TASAF zimepata mafanikio makubwa ambapo takwimu za Ofisi ya Taifa ya Takwimu zimeonesha kuwa kati ya mwaka 1990/91 na 2017/18 umasikini wa mahitaji ya msingi (Basic Needs) umepungua kutoka asilimia 39.0 hadi 26.4, umasikini wa chakula umepungua kutoka asilimia 19.7 hadi 9.5, na kwamba takwimu za Benki ya Dunia zinaonesha kuwa Tanzania ni nchi inayoongoza kwa kasi kubwa ya kupambana na umasikini kati ya nchi za Afrika zilizopo kusini mwa Jangwa la Sahara.
Amebainisha kuwa utekelezaji wa TASAF ulioanza mwaka 2000 na ambao kwa sasa upo katika awamu ya 3 na utagharimu shilingi Trilioni 4.109 zikiwemo shilingi Trilioni 2.032 za kipindi cha pili cha awamu ya tatu amepangwa kunufaisha Halmashauri zote 185 za Tanzania Bara na Wilaya 11 za Zanzibar, na kwamba baada ya kufanya maboresho sasa ruzuku imepunguzwa kutoka asilimia 67 hadi 38 na itaelekezwa kwa wazee wasiojiweza, watoto wadogo na kwa wenye kiwango kikubwa cha ulemavu.
Mhe. Rais Magufuli ameongeza kuwa asilimia 60 (sawa na Shilingi Trilioni 1.22) ya fedha hizo zitatumika kutekeleza miradi ya maendeleo takribani 30,000 iliyopo kwenye vijiji na mitaa 16,596 ya Tanzania Bara na Shehia 388 za Zanzibar na miradi hiyo itahusisha afya, elimu, maji, barabara na mazingira. Miradi hii inatarajiwa kuzalisha ajira Milioni 1.2 kwa watu wenye nguvu walio katika kaya masikini.
Amesisitiza kuwa licha ya kuwa sehemu ya fedha hizo ni ufadhili, sehemu kubwa ambayo ni kiasi cha shilingi Trilioni 1.035 ni mkopo kutoka Benki ya Dunia na hivyo amewaagiza viongozi wote wa Mikoa, Wilaya na Halmashauri kuhakikisha wanasimamia utekelezaji mzuri wa mpango huo na kwamba kufanikiwa ama kutofanikiwa kwake itakuwa ni kipimo cha kama wanastahili kuendelea na nyadhifa zao ama laa.
“Mathalani katika zoezi la uhakiki wa kaya masikini lililofanywa kuanzia Novemba 2015 hadi Juni 2017 tuliweza kubaini kaya masikini hewa 73,561. Hii ni aibu sana kwa viongozi wa Mikoa, Wilaya na Halmashauri” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Mapema Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF Bw. Ladslaus Mwamanga amesema TASAF imepata mafanikio makubwa katika awamu zake zote ambapo katika awamu ya 1 kaya 1,704 zilinufaika na ufadhili wa shilingi Bilioni 72, Awamu ya 2 kaya 12,347 zilinufaika na ufadhili wa shilingi Bilioni 430 na kipindi cha 1 cha awamu ya 3 Mamlaka za Serikali za Mitaa 159 za Tanzania Bara na Zanzibar yote zimenufaika na ufadhili ya shilingi Trilioni 1.46.
Mkurugenzi wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Dkt. Albina Chuwa amesema pamoja na takwimu kuonesha Tanzania inafanya vizuri katika kupunguza umasikini, viashiria vya huduma za kijamii navyo vinaonesha Tanzania imepiga hatua kubwa ambapo uandikishaji wanafunzi Shule za Msingi umepanda kutoka asilimia 78 (2012) hadi kufikia asilimia 83 (2018) na huenda imefika zaidi ya asilimia 90 hivi sasa, upatikanaji wa maji kutoka vyanzo bora umepanda hadi kufikia 83, nyumba za Watanzania zimeezekwa mabati kwa asilimia 84.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
17 Dar es Salaam.
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 11 Januari, 2020 ameendelea na ziara yake Visiwani Zanzibar ambapo ameweka jiwe la msingi la Shule ya Sekondari Mwanakwerekwe iliyopo Mjini Magharibi na amefungua hoteli yenye hadhi ya nyota tano iitwayo Hotel Verde – Azam Luxury Resort and Spa iliyopo Mtoni.
Shule ya Sekondari Mwanakwerekwe yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 960 inajengwa kwa gharama ya shilingi Bilioni 2 na Milioni 628, ni moja kati ya shule 24 zinazojengwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa ufadhili wa Benki ya Dunia chini ya mradi wa kuinua kiwango cha elimu Zanzibar kwa gharama ya shilingi Bilioni 79.7.
Akizungumza baada ya kuweka jiwe la msingi na kukagua majengo ya Shule ya Sekondari Mwanakwerekwe, Mhe. Rais Magufuli amempongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein kwa juhudi kubwa za kuiletea maendeleo Zanzibar ikiwemo utekelezaji wa mradi huo na ameeleza kuridhishwa kwake na ubora wa majengo yanayojengwa.
Hata hivyo ametaka Mkandarasi anayejenga majengo hayo kampuni ya CRJE kutoka China ambayo ilipaswa kukamilisha ujenzi huo tangu Agosti 2019 kuhakikisha inakamilisha kazi ifikapo Machi 2020 kama ilivyoahidi, badala ya kutoa visingizio vya mvua na mchanga.
Pia, Mhe. Rais Magufuli ameelezea kutoridhishwa na matokeo ya shule za Zanzibar kushika nafasi za chini katika ufaulu wa mitihani ya Kitaifa na hivyo ametoa wito kwa Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Zanzibar Mhe. Riziki Pembe Juma pamoja na wataalamu wake wa Wizara kufanyia kazi changamoto hiyo ili shule za Zanzibar zifanye vizuri katika mitihani hiyo.
Hotel Verde Azam Luxury Resort and Spa ambayo ujenzi wake ulianza mwaka 2011 kwa gharama ya shilingi Bilioni 65, inamilikiwa na Mtanzania Said Salim Bakhresa ikiwa ni moja ya hoteli za kipekee katika ukanda wa Afrika Mashariki iliyojengwa kwa kuzingatia uhifadhi wa mazingira.
Hotel hii ambayo inachangia jitihada za Zanzibar kuongeza idadi ya watalii hadi kufikia 500,000 kwa mwaka ina vyumba 106, imezalisha ajira za moja kwa moja 250 na katika kipindi cha mwaka mmoja tangu ianze kutoa huduma imeshachangia pato la Serikali ya Zanzibar kupitia kodi kwa kiwango cha shilingi Bilioni 4.6.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Bakhresa Group of Companies Bw. Salim Aziz Salim ameishukuru Serikali kwa kuunga mkono jitihada za wawekezaji ikiwemo ujenzi wa hoteli hiyo.
Akizungumza baada ya kufungua hoteli hiyo, Mhe. Rais Magufuli amempongeza Sheikh Said Salim Bakhresa kwa uwekezaji huo pamoja na uwekezaji mwingine anaoufanya katika sekta za viwanda, kilimo, usafiri na ametoa wito kwake na kwa wafanyabiashara wengine kujitokeza kuwekeza katika sekta mbalimbali za kujenga uchumi na ustawi wa jamii ya Watanzania wote.
Pamoja na kuipongeza Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa kuruhusu uwekezaji huo kufanyika, Mhe. Rais Magufuli amewataka viongozi mbalimbali wa Serikali kutowakatisha tamaa wawekezaji wazalendo wanapotaka kuwekeza katika miradi mbalimbali kama alivyofanya Sheikh Said Salim Bakhresa na badala yake wawatie moyo na kuwaunga mkono ili kufanikisha uwekezaji huo.
Mhe. Rais Magufuli amewapongeza viongozi wa vyombo vya ulinzi na usalama kwa kazi nzuri wanayoifanya kuhakikisha nchi inatulia na amewataka Wazanzibari wote kudumisha amani kwani bila amani nchi haiwezi kufanya maendeleo ikiwemo utalii ambao unachangia asilimia 80 ya fedha za kigeni za Zanzibar na asilimia 27 za Pato la Taifa.
Ameutaka uongozi wa Hotel Verde – Azam Luxury Resort and Spa kuhakikisha hoteli hiyo iliyopo ufukweni mwa Bahari ya Hindi haitumiwi na wahalifu wakiwemo wanaojihusisha na dawa za kulevya.
Kesho tarehe 12 Januari, 2020 Mhe. Rais Magufuli atashiriki sherehe za Maadhimisho ya miaka 56 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar zitakazofanyika katika uwanja wa Amaan.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Zanzibar
11 Januari, 2020
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 08 Februari, 2020 amewatunuku Kamisheni Maafisa wapya 128 wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ) kundi la 67/19, katika viwanja vya Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Maafisa hao walianza mafunzo yao tarehe 28 Januari, 2019 ambapo kati yao Maafisa 100 wamepata mafunzo katika Chuo cha Mafunzo ya Kijeshi – Monduli (TMA) na Maafisa 28 wamepata mafunzo yao katika nchi za China (10), India (2), Kenya (5), Morocco (9), Uingereza (1) na Ujerumani (1). Maafisa hao wametunukiwa cheo cha Luteni Usu.
Sherehe za kutunuku Kamisheni kwa Maafisa hao zimehudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Naibu Spika, Mhe. Tulia Ackson.
Akitoa taarifa ya Mafunzo hayo, Mkuu wa Chuo cha TMA Brig. Jen Ibrahim Michael Mhona amesema kati ya Maafisa hao wapo wenye shahada katika sayansi ya kijeshi, usafiri wa anga, uhandisi wa ndege na mifumo yake, ulinzi na menejimenti ya kijeshi.
Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jen. Venance Salvatory Mabeyo amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kuwatunuku Kamisheni Maafisa hao na kwa jitihada kubwa zinazofanywa na Serikali kuboresha JWTZ. Amewataka Maafisa hao wapya kuheshimu, kuthamini, kuzingatia na kutii kiapo chao.
Mhe. Rais Magufuli amewapongeza Maafisa hao kwa kutunukiwa Kamisheni na ameipongeza JWTZ kwa kutoa mafunzo hayo. Aidha, ameipongeza JWTZ kwa kutoa mafunzo kwa kiwango cha shahada katika chuo cha TMA na amewahakikishia Maafisa na Askari wa JWTZ kuwa Serikali itaendelea kuhakikisha inaliimarisha jeshi hilo ili liendelee kutimiza wajibu wake ipasavyo.
Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli amemuapisha Balozi (Kanali) Wilbert Augustine Ibuge kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliani ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
08 Februari, 2020.
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ameipongeza Mahakama na wadau wake kwa hatua kubwa za kimaendeleo zilizopigwa katika kipindi cha miaka 4 iliyopita na ameahidi kuwa Serikali itaendelea kuhakikisha Mahakama inaboreshwa zaidi.
Mhe. Rais Magufuli ametoa kauli hiyo tarehe 06 Februari, 2020 katika sherehe za kilele cha Wiki ya Elimu na Siku ya Sheria zilizofanyika katika ukumbi wa Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Spika wa Bunge Mhe. Job Yustino Ndugai, Majaji Wakuu Wastaafu, Mabalozi wa nchi mbalimbali, Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama, viongozi wa taasisi mbalimbali, viongozi wa Dini na Viongozi wa Siasa.
Katika hotuba hiyo, Mhe. Rais Magufuli ameelezea kufurahishwa kwake na mafanikio makubwa ya utekelezaji wa ahadi na maelekezo yake juu ya uboreshaji wa Mahakama yakiwemo kumaliza mrundikano wa mashauri mahakamani na kupunguza mrundikano wa mashauri yenye muda wa zaidi ya miaka 2 kutoka asilimia 12 hadi 5.
Mhe. Rais Magufuli amebainisha mafanikio mengine kuwa ni Serikali kuteua Majaji wapya 11 wa Mahakama ya Rufani, Majaji wapya 39 wa Mahakama Kuu na kuajiri Mahakimu wapya 396 ambao wamesaidia kupunguza tatizo la ucheleweshaji wa kesi, na pia amempongeza Waziri wa Katiba na Sheria kwa kuwapa Mahakimu 195 mamlaka ya kusikiliza mashauri ya Mahakama Kuu ambapo Mahakimu 98 walifanya kazi hiyo wamemaliza mashauri 1,132 kwa mwaka jana. Ameahidi kuwaangalia Mahakimu waliofanya kazi hiyo.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli amepongeza hatua kubwa iliyopigwa na Mahakama katika matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ambayo licha ya kupunguza tatizo la ucheleweshaji wa kesi na rushwa, pia imesaidia kuongeza maduhuri ya Serikali kutoka shilingi Bilioni 1.6 hadi kufikia shilingi Bilioni 2.5.
Maeneo mengine ni kuanzishwa kwa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka ambapo katika maeneo inayofanya kazi idadi ya mashauri imepungua (mfano Mahakama ya Kisutu ambayo mashauri yanayofikishwa mahakamani yamepungua kutoka zaidi ya 1,500 kwa mwaka hadi kufikia 300), kutoa msamaha kwa wafungwa 38,801 hali iliyosaidia kupunguza msongamano magerezani na kuanzishwa kwa Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Ufisadi (Mahakama ya Mafisadi) ambapo tangu ianzishwe mwaka 2016 mashauri 119 yamesajiliwa, 89 yamemalizika, faini iliyolipwa ni shilingi Bilioni 13.6 na fidia shilingi Bilioni 30.6.
Kuhusu miundombinu, Mhe. Rais Magufuli amesema kwa miaka 4 Serikali imejenga Mahakama Kuu 2 (Mara na Kigoma), imekarabati Mahakamu Kuu 4 (Dar es Salaam, Shinyanga, Mbeya na Sumbawanga), imejenga Mahakama za Wilaya 15 na Mahakama za Mwanza 11.
Mhe. Rais Magufuli amekiri kuwa pamoja na mafanikio hayo makubwa bado kuna changamoto na ameahidi kuwa Serikali itaendelea kuzishughulikia kadiri uwezo wa kifedha unavyo ruhusu.
Ametoa wito kwa Mahakama na wadau wengine yakiwemo Mabaraza ya Ardhi kutoa kipaumbele katika kushughulikia migogoro ya ardhi na dhuluma dhidi ya wanawake hasa wajane ambayo imekithiri hapa nchini. Amewataka Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya ambao ni wenyeviti wa kamati za mahakama katika maeneo yao kushirikiana vizuri na Mahakama katika kushughulikia kero mbalimbali za wananchi.
Kuhusu kaulimbinu ya mwaka huu isemayo “Uwekezaji na Biashara; Wajibu wa Mahakama na wadau katika kukuza uwekezaji na biashara” Mhe. Rais Magufuli ameipongeza Mahakama kwa kutambua safari ya Tanzania kujenga uchumi wa viwanda inapoelekea katika uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa ushirikiano mkubwa ambao Serikali inautoa kwa Mahakama na ameahidi kuwa Mahakama itaendelea kutekeleza majukumu yake kwa weledi ili kuhakikisha Watanzania wanapata haki yao ipasavyo.
Rais wa Chama cha Wanasheria Tanzania (TLS) Dkt. Rugemeleza Nshala amesema TLS iliyotimiza miaka 65 tangu kuanzishwa kwake ina Mawakili 8,667 ambapo takribani asilimia 75 ni vijana. Hivyo kuna hitaji kubwa la kuwajengea uwezo wa kimaadili na uzoefu wa kazi za uwakili na hivyo TLS inahitaji kupata majengo na fedha za kujiendesha, mambo ambayo Mhe. Rais Magufuli amesema Serikali itayaangalia.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
06 Februari, 2020
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amemteua Balozi (Kanali) Wilbert Augustine Ibuge kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Uteuzi wa Balozi Ibuge unaanza tarehe 06 Februari, 2020.
Kabla ya uteuzi huo Balozi Ibuge alikuwa Mkuu wa Itifaki (Chief of Protocal) katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Balozi Ibuge anachukua nafasi ya Dkt. Faraji Kasidi Mnyepe ambaye amehamishwa wizara kwa kuteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.
Dkt. Mnyepe anachukua nafasi ya Dkt. Frolence Turuka ambaye amestaafu.
Uteuzi wa Mkuu wa Itifaki utafanywa baadaye na tarehe ya kuapishwa kwa Balozi Ibuge itatangazwa baadaye.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
06 Februari, 2020
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 05 Februari, 2020 amekutana na Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) Mhe. Dkt. Stergomena Tax, Balozi wa Umoja wa Ulaya hapa nchini Mhe. Manfred Fanti na Balozi wa China hapa nchini Mhe. Wang Ke, Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Baada ya mazungumzo yake na Mhe. Rais Magufuli ambaye ni Mwenyekiti wa SADC, Dkt. Stergomena Tax amesema alikuja kutoa taarifa ya utekelezaji wa masuala mbalimbali ya SADC ikiwemo uendelezaji wa viwanda na kanda huru ya biashara ambapo wamekubaliana kuendelea kuhamasisha nchi wanachama kuendeleza viwanda ili kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi.
Ameelezea baadhi ya maeneo yaliyopo katika mkakati wa kukuza uchumi wa SADC kuwa ni kuendeleza miundombinu hasa ya usafiri na nishati ambayo bado ni changamoto kwa nchi za SADC, lakini ameipongeza Tanzania kwa hatua madhubuti zinazoendelea kuchukuliwa ikiwemo ujenzi wa barabara, reli na kuongeza uzalishaji wa umeme.
Kwa upande wake Balozi wa EU hapa nchini Mhe. Manfred Fanti amesema mazungumzo yake na Mhe. Rais Magufuli yamekuwa na manufaa makubwa ambapo wamejadili maendeleo mazuri ya kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na EU, na kwamba katika siku za karibuni wamekamilisha mazungumzo yaliyoruhusu kuendelea kwa mpango wa EU kuchangia bajeti ya maendeleo ya Tanzania ambapo shilingi Bilioni 132 zilizokuwa zimezuiwa zimeruhusiwa na sasa wanaandaa mpango mwingine wa miaka 7 utakaoanza mwaka huu.
Mhe. Manfred Fanti amesema kwa jinsi anavyoyaona maendeleo ya Tanzania ana matumaini makubwa kuwa EU itaendelea kufanya kazi kwa ukaribu zaidi na Tanzania ili kufanya vizuri zaidi.
Mhe. Rais Magufuli amemshukuru Mhe. Balozi Fanti kwa juhudi zake za kuimarisha uhusiano wa Tanzania na EU na amemhakikishia kuwa Tanzania itaendelea kushirikiana na EU katika masuala mbalimbali yenye maslahi kwa pande zote mbili.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli amekutana na Balozi wa China hapa nchini Mhe. Wang Ke na kumkabidhi barua aliyomwandikia Rais wa China Mhe. Xi Jinping akimpa pole kwa janga la homa ya virus vya Corona lililolikumba Jiji la Wuhan nchini humo na kusababisha vifo vya mamia ya watu.
Pamoja na kukabidhi barua hiyo, Mhe. Rais Magufuli amesema Tanzania imeguswa na kulipuka kwa janga hilo na ipo tayari kutoa ushirikiano wowote ambao Serikali ya China itahitaji katika jitihada za kukabiliana na homa hiyo.
“China ni ndugu zetu ni marafiki zetu, tunatoa pole kwa Mhe. Rais Xi Jinping na Wachina wote waliopatwa na madhara ya homa hii, daima Tanzania tupo pamoja na China na katika hili tupo pamoja pia” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Kwa upande wake, Balozi Wang Ke amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kuguswa na janga hilo na kuungana na China katika kipindi hiki kigumu. Ametumia nafasi hiyo kueleza hali ilivyo nchini China ambapo amesema Serikali ya China imeanza kupata mafanikio katika kukabiliana na homa hiyo, imefanikiwa kuzuia isienee katika nchi zingine kwa ushirikiano na Shirika la Afya Duniani (WHO) na nchi mbalimbali ikiwemo Tanzania.
Aidha, amemhakikishia Mhe. Rais Magufuli kuwa licha ya Tanzania kutokuwa na mtu yeyote aliyethibitika kuambukizwa homa ya Corona, pia Watanzania 400 waliopo katika Jiji la Wuhan ambao wengi wao ni wanafunzi hawajaambukizwa homa hiyo na jitihada za kuhakikisha wanakuwa salama zinafanyika.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
05 Februari, 2020
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 03 Februari, 2020 amewaapisha viongozi wa Wizara, Mahakama, Majeshi na Mikoa aliowateua tarehe 31 Januari, 2020 kushika nyadhifa mbalimbali.
Makatibu Wakuu wa Wizara walioapishwa ni Bi. Zena Ahmed Said aliyeapishwa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Prof. Riziki Silas Shemdoe aliyeapishwa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Bw. Christopher Derek Kadio aliyeapishwa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Dkt. Hassan Abbas Said aliyeapishwa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Bi. Mary Gasper Makondo aliyeapishwa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Makatibu Tawala wa Mikoa walioapishwa ni Bw. Stephen Muhoja Mashauri aliyeapishwa kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma, Bw. Emmanuel Mpawe Tutuba aliyeapishwa kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza na Bi. Judica Haikase Omari aliyeapishwa kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Tanga.
Mhe. Rais Magufuli amemuapisha Bw. Leonard Robert Masanja kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na amemuapisha Bw. Nathaniel Mathew Nhonge kuwa Kamishna wa Ardhi katika Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Kwa upande wa Mahakama, Mhe. Rais Magufuli amemuapisha Bw. Wilbert Martin Chuma kuwa Msajili Mkuu wa Mahakama, amemuapisha Bw. Kelvin David Mhina kuwa Msajili wa Mahakama ya Rufani na ameshuhudia Jaji Kiongozi Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi akimuapisha Bi. Sharmillah Said Sarwatt kuwa Msajili wa Mahakama Kuu.
Mhe. Rais Magufuli amewaapisha Jaji Dkt. Gerald Alex Ndika, Bw. Julius Bundala Kalolo na Bi. Genoveva Namatovu Kato kuwa Makamishna wa Tume ya Utumishi wa Mahakama.
Mhe. Rais Magufuli amemuapisha Brig. Jen. Suleiman Mungiya Mzee kuwa Kamishna Jenerali wa Magereza na John William Masunga kuwa Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji.
Viongozi wote walioapishwa leo wamekula kiapo cha uadilifu kwa viongozi wa umma kilichoongozwa na Kamishna wa Maadili Jaji Mstaafu Harold Nsekela, mbele ya Mhe. Rais Magufuli.
Akizungumza baada ya kuwaapisha, Mhe. Rais Magufuli amemtaka kila mmoja kwenda kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria na taratibu, na kuchapa kazi kwa manufaa ya Watanzania wote.
Ametoa wito kwa viongozi hao kwenda kushirikiana ipasavyo na viongozi wengine waliopo katika ofisi zao na amewataka viongozi na watendaji wa ofisi hizo kutoa ushirikiano kwa viongozi wapya walioteuliwa kuongoza ofisi hizo.
Hafla ya kuapishwa kwa viongozi hao imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, Mawaziri, Katibu Mkuu Kiongozi Mhe. Balozi John Kijazi, Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu Wakuu, Viongozi Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama, Wakuu wa Mikoa ya Tanga, Ruvuma, Mwanza na Dar es Salaam, viongozi wa Dini, viongozi wa siasa na viongozi wa taasisi mbalimbali.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
03 Februari, 2020
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 31 Januari, 2020 amefanya uteuzi wa viongozi mbalimbali wa Wizara, Mahakama, Mikoa na Majeshi.
Katibu Mkuu Kiongozi, Mhe. Balozi John Kijazi amewataja walioteuliwa kama ifuatavyo;
Wizara.
- Mhe. Rais Magufuli amemteua Bi. Mary Gasper Makondo kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi. Kabla ya uteuzi huo Bi. Mary Gasper Makondo alikuwa Kamishna wa Ardhi katika Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi. Anachukua nafasi ya Bi. Doroth Mwanyika ambaye amestaafu.
- Mhe. Rais Magufuli amemteua Dkt. Hassan Abbas kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo. Kabla ya uteuzi huo Dkt. Hassan Abbas alikuwa Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo. Anachukua nafasi ya Bi. Suzan Mlawi ambaye amestaafu.
- Mhe. Rais Magufuli amemteua Prof. Riziki Silas Shemdoe kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara. Kabla ya uteuzi huo Prof. Riziki Silas Shemdoe alikuwa Katibu Tawala Mkoa wa Ruvuma. Anachukua nafasi ya Prof. Joseph Buchweishaija ambaye amestaafu.
- Mhe. Rais Magufuli amemteua Bi. Zena Ahmed Said kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati. Kabla ya uteuzi huo Bi. Zena Ahmed Said alikuwa Katibu Tawala Mkoa wa Tanga. Anachukua nafasi ya Dkt. Hamis Mwinyimvua ambaye amestaafu.
- Mhe. Rais Magufuli amemteua Bw. Christopher Kadio kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi. Kabla ya uteuzi huo Bw. Christopher Kadio alikuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza. Anachukua nafasi ya Mej. Jen Jacob Kingu ambaye ameteuliwa kuwa Balozi.
- Mhe. Rais Magufuli amemteua Bw. Leonard R. Masanja kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati. Kabla ya uteuzi huo Bw. Leonard R. Masanja alikuwa Kamishna wa Umeme na Nishati Mbadala.
Mikoa.
- Mhe. Rais Magufuli amemteua Bi. Judica Haikase Omari kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Tanga.
- Mhe. Rais Magufuli amemteua Bw. Stephen Mashauri kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma.
- Mhe. Rais Magufuli amemteua Bw. Emmanuel Mpawe Tutuba kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza.
Majeshi.
- Mhe. Rais Magufuli amemteua Brig. Jen. Suleiman Mungiya Mzee kuwa Kamishna Jenerali wa Magereza. Brig. Jen. Suleiman Mungiya Mzee anachukua nafasi ya Phaustine Kasike ambaye ameteuliwa kuwa Balozi.
- Mhe. Rais Magufuli amemteua Naibu Kamishna wa Magereza (DCP) John William Masunga kuwa Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji. DCP John William Hasunga anachukua nafasi ya Thobias Andengenye ambaye uteuzi wake umetenguliwa.
Ardhi.
- Mhe. Rais Magufuli amemteua Bw. Nathaniel Mathew Nhonge kuwa Kamishna wa Ardhi katika Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi. Kabla ya uteuzi huo Bw. Nathaniel Mathew Nhonge alikuwa Kamishna wa Ardhi Msaidizi Kanda ya Dar es Salaam na Pwani.
Mahakama.
- Mhe. Rais Magufuli amemteua Bw. Wilbert M. Chuma kuwa Msajili Mkuu wa Mahakama.
- Mhe. Rais Magufuli amemteua Bw. Kelvin D. Mhina kuwa Msajili wa Mahakama ya Rufani.
- Mhe. Rais Magufuli amemteua Bi. Shamira S. Sarwat kuwa Msajili wa Mahakama Kuu.
==========
- Mhe. Rais Magufuli amewateua Mhe. Jaji Dkt. Gerald Ndika, Wakili - Julius Kalolo Bundala na Wakili – Genoveva M. Kato kuwa Makamishna wa Tume ya Utumishi wa Mahakama.
Tarehe ya kuapishwa kwa viongozi hawa itatangazwa baadaye.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu
Dar es Salaam
31 Januari, 2020
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 02 Februari, 2020 ametuma salamu za rambirambi kwa familia za watu 20 waliopoteza maisha wakati wakitoka katika Ibada huko Moshi Mkoani Kilimanjaro, na kwa familia za watu zaidi ya 20 waliopoteza maisha kutokana na madhara ya mvua kubwa zinazonyesha Mkoani Lindi na Mikoa mingine hapa nchini.
Watu 20 waliofariki dunia Mjini Moshi, walikuwa miongoni mwa watu waliokusanyika katika viwanja vya Majengo kuhudhuria Ibada iliyoongozwa na Mtume Boniface Mwamposa, na wamefariki dunia baada ya kukanyagwa na wenzao wakati wakitoka katika lango moja waliloelekezwa kupita ili kukanyaga mafuta ya upako. Katika tukio hili watu 16 wamejeruhiwa.
Watu wengine zaidi ya 20 wamefariki dunia Mkoani Lindi na katika Mikoa mingine hapa nchini ambayo imekumbwa na madhara yatokanayo na mvua nyingi zinazoendelea kunyesha.
Mhe. Rais ameeleza kusikitishwa na idadi kubwa ya vifo vya Watanzania waliopoteza maisha katika matukio hayo, na amewaombea Marehemu wote wapumzike mahali pema peponi na Majeruhi wote wapone haraka na kurejea katika majukumu yao.
Amemtaka Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Mhe. Anna Mghwira, Mkuu wa Mkoa wa Lindi Mhe. Godfrey Zambi na Wakuu wa Mikoa wengine ambao Mikoa yao imepatwa na madhara ya watu kupoteza maisha kutokana na madhara ya mvua, kufikisha salamu zake za pole kwa familia, ndugu, jamaa, marafiki na wote walioguswa na vifo hivyo.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli ametoa wito kwa Watanzania wote kuchukua tahadhali katika matukio yote yenye viashiria vya hatari ikiwemo mikusanyiko mikubwa ya watu na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha na amevitaka Vyombo vya Ulinzi na Usalama kuhakikisha vinasimamia ipasavyo tahadhali za kiusalama.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
02 Februari, 2020
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amefanya uteuzi wa wenyeviti 3 watakaoongoza bodi za taasisi 2 za Serikali na 1 ya ubia wa Serikali na Sekta Binafsi.
Kwanza, Mhe. Rais Magufuli amemteua Bw. Gabriel Pascal Malata kuwa Mwenyekiti na Mjumbe wa kuiwakilisha Serikali katika Bodi ya Kampuni ya Airtel Tanzania Ltd.
Bw. Malata ni Naibu Wakili Mkuu wa Serikali.
Pili, Mhe. Rais Magufuli amemteua Prof. Martha Qorro kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini (Institute of Rural Development Planning - IRDP).
Prof. Martha Qorro ni Profesa Mshiriki wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
Tatu, Mhe. Rais Magufuli amemteua Prof. Joseph Rwegasira Buchweshaija kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela (NM-AIST).
Taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi, Mhe. Balozi John Kijazi imeeleza kuwa uteuzi wa viongozi hawa umeanza tarehe 30 Januari, 2020.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
31 Januari, 2020
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 28 Januari, 2020 amepokea hati za utambulisho za Mabalozi 9 walioteuliwa kuziwakilisha nchi zao hapa nchini.
Mabalozi waliowasilisha hati zao za utambulisho ni Mhe. Maria Amelia Maio de Paiva (Balozi wa Ureno hapa nchini), Mhe. Douglas Foo Peow Yong (Balozi wa Singapore hapa nchini), Mhe. Alex Chua (Balozi wa Ufilipino hapa nchini), Mhe. Angela Veronica Comfort (Balozi wa Jamaica hapa nchini) na Mhe. Dkt. Christian Fellner (Balozi wa Austria hapa nchini).
Mabalozi wengine waliowasilisha hati zao za utambulisho ni Mhe. Francisca Ashietey-Odunton (Balozi wa Ghana hapa nchini), Mhe. Jesús Agustin Manzanilla Puppo (Balozi wa Venezuela hapa nchini), Mhe. Yacin Elmi Bouh (Balozi wa Djibouti hapa nchini) na Mhe. Oded Joseph (Balozi wa Israel hapa nchini).
Pamoja na kupokea hati za utambulisho za Mabalozi hao, Mhe. Rais Magufuli amepokea salamu kutoka kwa viongozi wakuu wa nchi hizo ambao wameeleza kufurahishwa kwao na uhusiano na ushirikiano mzuri na Tanzania, na dhamira yao ya kuukuza na kuuendeleza zaidi uhusiano huo.
Mhe. Rais Magufuli amewashukuru viongozi wakuu wa nchi hizo kwa salamu, na amewapongeza na kuwakaribisha Mabalozi walioteuliwa kuziwakilisha nchi hapa nchini.
Amewahakikishia kuwa Tanzania ipo tayari kukuza zaidi uhusiano wake na nchi hizo hasa katika diplomasia ya uchumi, na amewataka Mabalozi hao kuwahamasisha wafanyabiashara kuja kuwekeza hapa Tanzania katika sekta mbalimbali zikiwemo kilimo, ufugaji, uvuvi, madini, mafuta na gesi na biashara nyingine mbalimbali kwa manufaa ya pande zote mbili.
Mhe. Rais Magufuli amesisitiza kuwa anatambua kuwa ushirikiano na nchi hizo utasaidia kubadilishana uzoefu, ujuzi, teknolojia na mitaji itakayosaidia kutumia rasilimali zilizopo Tanzania kwa manufaa ya Watanzania na wananchi wa nchi hizo.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
28 Januari, 2020
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 27 Januari, 2020 amewaapisha Mawaziri 2 na Mabalozi 3 aliowateua hivi Karibuni.
Mawaziri walioapishwa ni Mhe. George Boniface Mwataguluvala Simbachawene aliyeapishwa kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi na Mhe. Mussa Azzan Zungu aliyeapishwa kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira.
Mabalozi walioapishwa ni Mhe. Maimuna Kibenga Tarishi aliyeapishwa kuwa Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa Geneva – Uswisi, Mhe. Hussein Athuman Kattanga aliyeapishwa kuwa Balozi wa Tanzania Tokyo – Japan na Mhe. Prof. Kennedy Godfrey Gastorn aliyeapishwa kuwa Mwakilishi wa Kudumu katika Umoja wa Mataifa New York Marekani.
Akizungumza baada ya kuwaapisha na kushuhudia wakila kiapo cha uadilifu kwa viongozi wa umma, Mhe. Rais Magufuli amewataka viongozi hao kwenda kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu, uchapakazi, kutanguliza maslahi ya Tanzania pamoja na kushirikiana vizuri na viongozi na watendaji wengine katika wizara zao.
Amemtaka Mhe. Waziri Simbachawene kushughulikia dosari zilizopo katika Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ikiwemo kuhakikisha watendaji na viongozi ambao ni kikwazo katika ufanisi wa wizara wanaondolewa, pamoja na kushughulikia makubaliano yaliyotiwa saini na viongozi wakuu wa wizara waliopita kuhusu mkataba wa ununuzi wa vifaa vya zimamoto (vyenye thamani ya zaidi ya shilingi Trilioni 1) katika mazingira yasiyokuwa na uadilifu na bila kujali maslahi ya Taifa.
Hafla ya kuapishwa kwa viongozi hao imefanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam na imehudhuriwa na Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi, Katibu Mkuu Kiongozi Mhe. Balozi John Kijazi, Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu Wakuu na Viongozi Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
27 Januari, 2020
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 24 Januari, 2020 ameshuhudia utiaji saini wa mikataba ya makubaliano kati ya Serikali ya Tanzania na Kampuni ya Barrick Gold Corporation ambayo imekuwa katika mazungumzo na Tanzania juu ya biashara ya madini na umiliki wa hisa zake.
Hafla ya utiaji saini mikataba ya makubaliano hayo imefanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, Mawaziri na Naibu Mawaziri, Katibu Mkuu Kiongozi Mhe. Balozi John Kijazi, Makatibu Wakuu, Mwanasheria Mkuu wa Serikali Prof. Adelardus Kilangi, Viongozi Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama, Viongozi wa Dini, Viongozi wa Vyama vya Siasa na viongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa Mhe. Paul Makonda.
Mikataba 9 iliyosainiwa ni mkataba wa msingi wa makubaliano, mkataba wa menejimenti na utoaji wa huduma, Mkataba wa wanahisa wa kampuni ya Twiga Minerals Corporation, Mkataba wa wanahisa wa kampuni ya North Mara, Mkataba wa wanahisa wa kampuni ya Bulyanhulu, Mkataba wa wanahisa wa kampuni Buzwagi, Mkataba wa maendeleo ya mgodi wa North Mara, Mkataba wa maendeleo ya mgodi wa Bulyanhulu na Mkataba wa Maendeleo wa mgodi wa Buzwagi.
Chini ya makubaliano hayo Serikali ya Tanzania ambayo haikuwa na hisa katika migodi ya Barrick Gold Corporation sasa itamiliki hisa kwa asilimia 16 zisizopungua thamani kutokana na ongezeko la mtaji wa mwekezaji (Undiluted Free Carried Interest) na itapata mgawanyo wa asilimia 50 kwa 50 ya mapato ya kiuchumi.
Aidha, kampuni ya Acacia itafutwa na kufungwa kwa ofisi zake zilizopo London (Uingereza) na Johannesburg (Afrika Kusini), Tanzania itashiriki katika utoaji wa huduma mbalimbali zikiwemo za kibenki, kisheria na bima, na pia kampuni za Tanzania zitashiriki kuuza bidhaa mbalimbali katika migodi ya Twiga Minerals Corporation.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Timu ya Serikali ya Tanzania iliyofanya majadiliano na kampuni ya Barrick Gold Corporation amefafanua kuwa kampuni ya Twiga Minerals Corporation ndio itakayokuwa mmiliki wa migodi 3 ya dhahabu ambayo ni Bulyanhulu, North Mara na Buzwagi na kwamba katika kila mgodi Tanzania inamiliki hisa kwa asilimia 16 na itapata mgawanyo wa 50/50 ya mapato ya kiuchumi.
Mhe. Prof. Kabudi amempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa juhudi zake kubwa alizozifanya kupigania maslahi ya Watanzania katika biashara ya madini iliyokuwa ikifanywa na Barrick Gold Corporation hapa nchini licha ya kejeli na kukatishwa tamaa kulikofanywa na baadhi ya Watanzania.
Mtendaji Mkuu na Rais wa Barrick Gold Corporation Dkt. Mark Bristow amekiri kuwa mikataba hii ina maslahi kwa pande zote mbili, imeunda kampuni ya Twiga Minerals Corporation ambayo ina muundo utakaoruhusu Serikali ya Tanzania na Watanzania kuwa na maamuzi na amempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa kusimama kidete huku akibainisha kuwa hatua alizochukua hazifukuzi wawekezaji kama ilivyokuwa inavumishwa bali kutetea maslahi ya pande zote mbili.
Akizungumza baada ya kushuhudia utiaji saini wa mikataba hiyo na Barrick Gold Corporation kukabidhi hati ya umiliki wa asilimia 16 ya hisa za Twiga Minerals Corporation kwa Msajili wa Hazina (kwa niaba ya Serikali ya Tanzania), Mhe. Rais Magufuli amempongeza Prof. Kabudi na timu yake ya Tanzania iliyoshiriki iliyofanya majadiliano hayo katika mazingira magumu tangu ilipoanza mwaka 2017, na baada ya makubaliano hayo ameruhusu makontena ya mchanga wa dhahabu yaliyokuwa yamekamatwa katika Bandari ya Dar es Salaam yauzwe kupitia kampuni ya Twiga Minerals Corporation ili Tanzania nayo inufaike.
“Ndugu zangu mlioshiriki kwenye mazungumzo, Mungu atawalipa, mmeifanya kazi yenu wengine mmetoa machozi lakini nina uhakika Mungu atawalipa, inawezekana historia yenu isijulikane sana kwa Watanzania lakini Mungu anajua, mimi nawapongeza sana sana sana” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Mhe. Rais Magufuli pia ameipongeza timu ya majadiliano ya Barrick Gold Corporation kwa kufikia hatua hiyo, amewahakikishia kuwa Tanzania itaendelea kuwa mahali pazuri pa uwekezaji unaozingatia maslahi ya pande zote mbili na ametoa wito kwa kampuni iliyoundwa ya Twiga Mineral Corporation kuendelea kufanya kazi kwa uadilifu na kwamba Serikali itakuwa karibu nayo.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
24 Januari, 2020
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amesikitishwa na kitendo cha viongozi wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kutia saini makubaliano ya zabuni ya kununua vifaa vya zimamoto na uokoaji vyenye thamani ya Euro Milioni 408.5 (sawa na zaidi ya shilingi Trilioni 1) kutoka kampuni moja ya nchi za nje bila kufuata sheria.
Mhe. Rais Magufuli amesema ameshangazwa kuona viongozi hao wameingia makubaliano hayo ilihali zabuni hiyo haijapangwa kwenye bajeti wala kupitishwa na Bunge, huku kukiwa na mazingira ya ukosefu wa uadilifu kutokana na aina ya vifaa vilivyotajwa katika zabuni hiyo na viongozi hao kusafirishwa kwenda nchi husika kwa kugharamiwa na kampuni waliyokubaliana kusambaza vifaa hivyo.
Mhe. Rais Magufuli amempongeza Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi Meja Jenerali Jacob Kingu kwa kuandika barua ya kujiuzulu wadhifa wake ili kuwajibika kwa dosari hiyo, na amewashangaa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Kangi Lugola na Kamishna Jenerali wa Zimamoto na Uokoaji (CGF) Thobias Andengenye kutowajibika kwa dosari hiyo.
“Nakueleza Mhe. Lugola na Kamishna Jenerali Andengenye, ninawashangaa kuwaona mpo hapa, ninawapenda sana lakini huu ndio ukweli, sitaki kuwa mnafiki, shilingi Trilioni 1 na kitu mtu anasaini wakati sheria zote zinajulikana, mwenye mamlaka ya kukopa fedha ni Wizara ya Fedha pekee yake, wanajua, ikiwa hivyo basi kila wizara itakopa” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli amesema maafisa wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali waliohusika kupitisha makubaliano hayo wakati Mwanasheria Mkuu wa Serikali Prof. Adelardus Kilangi akiwa msibani (alipofiwa na mkewe) pamoja na Maafisa wengine wa Wizara ya Mambo ya Ndani waliohusika katika kashfa hii wajitafakari.
Mhe. Rais Magufuli amesema hayo leo tarehe 23 Januari, 2020 wakati wa sherehe za ufunguzi wa majengo 12 yenye makazi ya familia 172 za Maafisa na Askari Magereza katika Gereza la Ukonga Jijini Dar es Salaam.
Ujenzi wa majengo hayo umegharimu shilingi Bilioni 13 ambapo awali Mhe. Rais Magufuli aliagiza Jeshi la Magereza lipewe shilingi Bilioni 10 lakini baada ya Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) iliyopewa zabuni ya ujenzi kushindwa kumaliza kazi kwa miezi 27 wakiwa wamefikia asilimia 45 tu, aliagiza kazi hiyo ikabidhiwe kwa Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ) kupitia Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ambao walipatiwa shilingi Bilioni 3 na kufanikiwa kukamilisha ujenzi huo kwa muda wa miezi 7.
Ameipongeza JWTZ kupitia JKT kwa kazi nzuri waliyoifanya katika ujenzi huo na ujenzi wa miradi mingine ikiwemo ukuta wa eneo la madini ya Tanzanite Mirerani Mkoani Manyara, kambi ya JWTZ Ngerengere Mkoani Morogoro na ujenzi wa Ikulu Chamwino Mkoani Dodoma.
Hata hivyo amelitaka Jeshi la Magereza kujirekebisha na kujifunza kutoka JKT kwa kuwa linayo nguvu kazi ya wafungwa takribani 13,000 ambao wanaweza kutumika katika uzalishaji mali na kujenga miundombinu ya jeshi hilo yakiwemo makazi ya Maafisa na Askari badala ya kusubiri kujengewa na majeshi mengine ama kutumia wakandarasi.
Mhe. Rais Magufuli ameeleza kusikitishwa kwake na kusuasua kwa ujenzi wa jengo la kiwanda cha kutengeneza viatu cha Gereza Kuu Karanga kilichopo Moshi Mkoani Kilimanjaro ambacho licha ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii wa PSSSF (ambao ni wabia) kutoa shilingi Bilioni 9 tangu Oktoba 2019, hadi sasa Jeshi la Magereza limeshindwa kuharakisha ujenzi huo ambao umefikia asilimia 45 tu, ilihali mitambo inayopaswa kufungwa katika jengo hilo imeshawasili Bandari ya Dar es Salaam.
Amemuagiza Kamishna Jenerali wa Magereza (CGP) Phaustine Kasike kuhakikisha majengo mapya 12 yaliyojengwa katika Gereza la Ukonga yanatunzwa na kuendeleza utaratibu wa kujenga nyumba za Maafisa na Askari wake pamoja na kukarabati zilizopo, kwa kuwa haridhishwi na hali duni ya makazi ya Maafisa na Askari Magereza hapa nchini.
Pia amemtaka CGP Kasike kuhakikisha maji yanaingizwa katika nyumba za makazi ya Maafisa na Askari Magereza katika majengo mapya 12 ya Ukonga, kwa kuwa wakati wa ukaguzi amebaini kuwa makazi hayo hayajaunganishwa na mtandao wa maji ndani ya nyumba.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
23 Januari, 2020
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 14 Januari, 2020 amewaapisha Mabalozi 4 aliowateua hivi karibuni kuiwakilisha Tanzania katika nchi za Afrika Kusini, Namibia, Zimbabwe na Nigeria.
Walioapishwa ni Mej. Jen (Mstaafu) Gaudence Salim Milanzi anayekuwa Balozi wa Tanzania Pretoria - Afrika Kusini, Dkt. Modestus Francis Kipilimba anayekuwa Balozi wa Tanzania Windhoek – Namibia, Prof. Emmanuel David Mwaluko Mbennah anayekuwa Balozi wa Tanzania Harare – Zimbabwe na Dkt. Benson Alfred Bana anayekuwa Balozi wa Tanzania Abuja – Nigeria.
Baada ya kuwaapisha, Mhe. Rais Magufuli amewataka kuripoti katika vituo walivyopangiwa ndani ya wiki 2 kuanzia sasa na amewasisitiza kwenda kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa sheria, kwa kuzingatia maslahi ya Taifa hasa kiuchumi na kuwawezesha Watanzania kupata ajira katika fursa zilizopo katika nchi hizo.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi amewataka Mabalozi hao kufuatilia maeneo yote ambayo Mhe. Rais Magufuli alikubaliana na Waheshimiwa Marais wenzake alipotembelea nchi hizo hivi karibuni, na pia kuitangaza vyema Tanzania ambayo kwa sasa inapiga hatua kubwa katika maeneo mengi.
Hafla ya kuapishwa kwa Mabalozi hao imefanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Makamu wa Rais, Mhe. Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa.
Kabla ya kuwaapisha Mabalozi hao, Mhe. Rais Magufuli ameongoza kikao cha Baraza la Mawaziri kilichofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
14 Januari, 2020
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amemtumia salamu za rambirambi Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job Yustino Ndugai kufuatia kifo cha ghafla cha aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Newala Vijijini Mkoani Mtwara, Mhe. Rashid Ajali Akbar kilichotokea leo huko Mingoyo Mkoani Lindi.
Katika Salamu hizo, Mhe. Rais Magufuli ameelezea kuhuzunishwa na kifo cha Mbunge huyo ambaye wakati wa uhai wake aliwatumikia wananchi wa Newala Vijijini kwa dhati na alifanya kazi kwa ushirikiano mzuri na viongozi wenzake katika Bunge, Chama na Serikali.
“Mhe. Spika naomba unifikishie salamu zangu za pole kwa familia ya Marehemu Akbar, Wabunge, wananchi wa Newala Vijijini na wote walioguswa na msiba huu, nawaombea moyo wa uvumilivu na ustahimilivu katika kipindi hiki cha majonzi” amesema Mhe. Rais Magufuli katika salamu hizo.
Amemuombea Marehemu Rashid Ajali Akbar apumzike mahali pema peponi, Amina.
Inna lillahi wa inna ilayhi raji'un.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
15 Januari, 2020
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amefanya uteuzi wa wenyeviti 5 wa bodi za taasisi za Serikali baada ya bodi za taasisi hizo kumaliza muda wake.
Taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi, Mhe. Balozi John Kijazi imeeleza kuwa wenyeviti hao wameongezewa muda baada ya vipindi vyao vya awali kumalizika;
Kwanza, Mhe. Rais Magufuli amemteua Mhe. Agustino Lyatonga Mrema kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Parole.
Pili, Mhe. Rais Magufuli amemteua Dkt. Harun Ramadhani Kondo kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Posta Tanzania (TPC).
Uteuzi wa Mhe. Mrema na Dkt. Kondo umeanza tarehe 20 Januari, 2020.
Tatu, Mhe. Rais Magufuli amemteua Prof. Mayunga Habibu Hemed Nkunya kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC).
Nne, Mhe. Rais Magufuli amemteua Bw. Fidelis Kashumba Mutakyamilwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Tume ya Taifa Mipango na Matumizi ya Ardhi.
Tano, Mhe. Rais Magufuli amemteua Bw. Peter Maziku Maduki kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA).
Uteuzi wa Prof. Nkunya, Bw. Mutakyamilwa na Bw. Maduki umeanza tarehe 17 Januari, 2020.
Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli amemteua Dkt. Noel Biseko Logwa kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa. Uteuzi wa Dkt. Logwa umeanza tarehe 17 Januari, 2020 na kabla ya uteuzi huo alikuwa Mhadhiri na Mkuu wa Idara ya Akiolojia na Mafunzo ya Urithi (Archeology and Heritage Studies) ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Dkt. Logwa amechukua nafasi ya Prof. Audax Mabula ambaye amestaafu.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
20 Januari, 2020
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amewashukuru Mabalozi wanaoziwakilisha nchi mbalimbali hapa nchini kwa ushirikiano mkubwa walioutoa kwa Serikali ya Awamu ya Tano na hivyo kuwa Sehemu ya mafanikio makubwa ya yaliyopatikana nchini Tanzania katika miaka 4 iliyopita.
Mhe. Rais Magufuli ametoa pongezi hizo leo tarehe 21 Januari, 2020 katika hafla ya kuukaribisha Mwaka Mpya aliyowaandalia Mabalozi na Wakuu wa Mashirika ya Kimataifa (Sherry Party) na kufanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Katika hotuba yake, Mhe. Rais Magufuli amesema miaka 4 ya tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani Tanzania imepiga hatua kubwa katika kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2025, Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2015 – 2020, mipango ya kimataifa na kikanda na Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka 5 (2016/17 – 2020/21) iliyolenga kujenga uchumi wa viwanda utakaochochea mageuzi ya kiuchumi na maendeleo ya watu.
Ametaja baada ya mafanikio hayo kuwa ni kulinda na kudumisha amani na usalama wa nchi, kuimarisha Muungano ambao Aprili 2020 utatimiza miaka 56, ukuaji mzuri wa uchumi wa wastani wa asilimia 7, kudhibiti mfumuko wa bei hadi kufikia asilimia 3.5 na kuongeza akiba ya fedha za kigeni kutoka Dola za Marekani Bilioni 4.123 hadi kufikia Dola za Marekani 5.579 zinazotosheleza kuagiza bidhaa na huduma kwa kipindi kisichopungua miezi 6.3.
Mafanikio mengine ya kiuchumi ni kuongezeka kwa ukusanyaji wa mapato kutoka wastani wa shilingi Bilioni 850 kwa mwezi hadi kufikia shilingi Trilioni 1.5 (ambapo Desemba 2019 ilifikia shilingi Trilioni 1.9), kuvutia uwekezaji wenye thamani ya shilingi Trilioni 30 uliozalisha ajira laki 1, kuogeza biashara ya nje kutoka shilingi Trilioni 11.5 hadi kufikia shilingi Trilioni 16.6, kuongeza uzalishaji wa mazao ya biashara kutoka tani 796,512 hadi kufikia tani 1,141,774 (ongezeko la asilimia 43.3) na kujenga viwanda vipya 4,877.
Aidha, katika kipindi hicho mauzo ya dhahabu nje ya nchi yameongezeka kutoka Dola za Marekani Bilioni 1.469 hadi kufikia Bilioni 1.743, mapato ya Serikali kutokana na madini yameongezeka kutoka shilingi Bilioni 168 hadi kufikia shilingi Bilioni 346, idadi ya watalii imeongezeka kutoka watalii Milioni 1.1 hadi kufikia Milioni 1.5 na mapato yatokanayo na utalii yameongezeka kutoka Dola za Marekani Bilioni 1.9 hadi kufikia Bilioni 2.488.
Mhe. Rais Magufuli ameongeza kuwa katika kipindi hicho Serikali imetekeleza miradi mikubwa ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa reli ya kisasa (standard gauge railway) kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma utakaogharimu zaidi ya shilingi Trilioni 7, ujenzi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere litakalozalisha megawati 2,115 za umeme utakaogharimu shilingi Trilioni 6.5, ujenzi wa kilometa 2,500 za barabara za lami na nyingine 2,400 zikiendelea kujengwa, kilometa 7,087 la barabara za lami zikiwa katika maandalizi ya kuanza kujenzi na kukamilisha ujenzi wa madaraja makubwa 8.
Miradi mingine ni kufufua reli ya Dar es Salaam – Tanga – Moshi iliyokuwa haitoi huduma tangu miaka zaidi ya 20 iliyopita, kupanua bandari za Dar es Salaam, Mtwara na Tanga, kukarabati meli 7 katika maziwa makuu, kukamilisha ujenzi wa jengo la 3 la abiria katika uwanja wa ndege wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam (Terminal III), kujenga viwanja vya ndege 11, kununua rada 4, na kufufua Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) baada ya kununua ndege mpya 11.
Kwa upande wa huduma za kijamii amesema mbali na kujenga Bwawa la Mwalimu Nyerere, Serikali imejenga njia ya umeme ya Iringa – Shinyanga, Makambako – Songea na Lindi – Mtwara, kupeleka umeme vijijini ambapo idadi ya vijiji vilivyofikiwa na umeme imeongezeka kutoka 2,018 hadi kufikia 8,587, kujenga vituo vya afya 352 na Hospitali za Wilaya 69, kuajiri watumishi wa afya 8,000 na kuongeza bajeti ya dawa na vifaa tiba kutoka shilingi Bilioni 31 hadi kufikia shilingi Bilioni 270 kwa mwaka.
Amebainisha kuwa Serikali inatoa elimu bila malipo kwa shule za msingi na sekondari ambapo imeshatumia shilingi Trilioni 1, mikopo ya elimu ya juu imeongezeka kutoka shilingi Bilioni 341 hadi kufikia shilingi Bilioni 450, imetekeleza miradi ya maji yenye thamani ya shilingi Trilioni 3 na hivyo kuongeza upatikanaji wa maji kutoka wastani wa asilimia 56 hadi kufikia asilimia 71, kuongeza mapambano dhidi ya rushwa na Serikali kuhamia Dodoma.
Mhe. Rais Magufuli amesema kwa kuongozwa na sera ya diplomasia ya uchumi, Tanzania imeendeleza na kukuza zaidi uhusiano wake na nchi mbalimbali duniani ambapo pamoja na kufanya ziara katika nchi mbalimbali, Balozi mpya 7 zimefunguliwa na kushiriki katika shughuli na mipango mbalimbali ya kimataifa ikiwemo ulinzi wa amani ambapo kwa sasa askari 2,297 wa Tanzania wapo katika ulinzi wa amani katika nchi mbalimbali.
Ameahidi kuwa katika mwaka 2020 Serikali imejipanga kuendelea kutekeleza Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano, kudumisha amani na usalama, kukuza zaidi uchumi, kuimarisha akiba ya fedha za kigeni, kuongeza ukusanyaji wa mapato, kukuza sekta kuu za uzalishaji yaani kilimo, viwanda, ujenzi, madini na utalii pamoja na kuboresha mazingira ya kufanyia biashara ambapo amewaomba Mabalozi hao kuwashawishi wafanyabiashara wa nchi zao kuja kuwekeza nchini Tanzania.
Pia, amewahakikishia kuwa katika mwaka 2020 ambapo Tanzania inafanya Uchaguzi Mkuu, Serikali imejipanga kuhakikisha unafanyika kwa misingi ya kidemokrasia na katika mazingira ya amani, uhuru na haki, na amezikaribisha nchi na taasisi mbalimbali kuja kuangalia jinsi Tanzania ilivyokomaa kidemokrasia pindi wakati ukifika.
Ameahidi kuwa Tanzania, itaendelea kukuza ujirani mwema, kushirikiana na nchi mbalimbali na kutekeleza majukumu ya kimataifa ikiwemo kuwahudumia wakimbizi na kuwarejesha makwao kwa hiari, lakini ameeleza kusikitishwa na hujuma na propaganda zinafanyika kwa lengo la kukwamisha zoezi hilo.
Akizungumza kwa niaba ya Mabalozi hao, Kiongozi wa Mabalozi (Dean of Diplomatic Corps) Mhe. Ahamada El Badaoui Mohamed Fakih amempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa uongozi mzuri aliouonesha katika kipindi cha miaka minne ambapo miradi mikubwa ya maendeleo imetekelezwa, kukua kwa uchumi, ustawi wa watu na ameahidi kuwa Mabalozi wataendelea kutoa ushirikiano wowote utakaohitajika.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
21 Januari, 2020
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 14 Januari, 2020 amepokea hati za utambulisho za Mabalozi 3 walioteuliwa kuziwakilisha nchi za Ujerumani, Qatar na Algeria hapa nchini.
Mabalozi waliowasilisha hati hizo ni Mhe. Regine Hess – Balozi wa Jamhuri ya Ujerumani hapa nchini, Mhe. Hussein Bin Ahmed Mohamed Ibrahim Al-Homaid – Balozi wa Taifa la Qatar hapa nchini na Mhe. Ahmed Djellal – Balozi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Algeria hapa nchini.
Akizungumza na Mabalozi hao, Mhe. Rais Magufuli amewakaribisha hapa nchini na kuwahakikishia kuwa Serikali ya Awamu ya Tano inayo dhamira ya dhati ya kuukuza na kuuimarisha zaidi uhusiano na ushirikiano mzuri na wa kihistoria uliopo kati ya Tanzania na nchi hizo.
Mhe. Rais Magufuli ametoa wito kwa Mabalozi hao kuwahamasisha wafanyabiashara na wawekezaji mbalimbali kutoka nchini mwao kuja kuwekeza hapa nchini katika sekta mbalimbali hasa kilimo, mafuta, gesi, viwanda na madini kwa kuwa Tanzania imejaaliwa kuwa na rasilimali za kutosha katika sekta hizo ambazo zinahitaji ushirikiano wa pamoja katika uwekezaji.
Amewaomba Mabalozi hao kufikisha shukrani zake kwa viongozi wa nchi zao na kuwakaribisha kutembelea Tanzania kwa ziara rasmi ama kutembelea vivutio vingi vya utalii vilivyopo.
Kwa upande wao, Mabalozi hao wamemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kukubali kuwapokea na katika kipindi cha uwakilishi wao wameahidi kufanya juhudi za kuimarisha zaidi uhusiano na ushirikiano hasa katika masuala ya kiuchumi ambayo Serikali ya Awamu ya Tano inayapa kipaumbele.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
14 Januari, 2020
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 14 Januari, 2020 amewaapisha Mabalozi 4 aliowateua hivi karibuni kuiwakilisha Tanzania katika nchi za Afrika Kusini, Namibia, Zimbabwe na Nigeria.
Walioapishwa ni Mej. Jen (Mstaafu) Gaudence Salim Milanzi anayekuwa Balozi wa Tanzania Pretoria - Afrika Kusini, Dkt. Modestus Francis Kipilimba anayekuwa Balozi wa Tanzania Windhoek – Namibia, Prof. Emmanuel David Mwaluko Mbennah anayekuwa Balozi wa Tanzania Harare – Zimbabwe na Dkt. Benson Alfred Bana anayekuwa Balozi wa Tanzania Abuja – Nigeria.
Baada ya kuwaapisha, Mhe. Rais Magufuli amewataka kuripoti katika vituo walivyopangiwa ndani ya wiki 2 kuanzia sasa na amewasisitiza kwenda kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa sheria, kwa kuzingatia maslahi ya Taifa hasa kiuchumi na kuwawezesha Watanzania kupata ajira katika fursa zilizopo katika nchi hizo.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi amewataka Mabalozi hao kufuatilia maeneo yote ambayo Mhe. Rais Magufuli alikubaliana na Waheshimiwa Marais wenzake alipotembelea nchi hizo hivi karibuni, na pia kuitangaza vyema Tanzania ambayo kwa sasa inapiga hatua kubwa katika maeneo mengi.
Hafla ya kuapishwa kwa Mabalozi hao imefanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Makamu wa Rais, Mhe. Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa.
Kabla ya kuwaapisha Mabalozi hao, Mhe. Rais Magufuli ameongoza kikao cha Baraza la Mawaziri kilichofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
14 Januari, 2020