Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, leo tarehe 14 Julai, 2021 amefungua kongamano la kwanza la kumbukizi ya maisha ya aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tatu, Hayati Benjamin William Mkapa lililofanyika Jijini Dar es Salaam.
Mhe. Rais Samia amesema mchango mkubwa wa Hayati Rais Mkapa wakati wa uhai wake utabaki kama alama katika historia ya taifa letu. Pia alisimamia mageuzi makubwa ya kiuchumi nchini pamoja na hatua kubwa alizochukua za kutoa fursa zaidi kwa sekta binafsi na kukaribisha uwekezaji nchini.
Amesema hatua ya kukaribisha uwekezaji kutoka nje ilisaidia kuongeza mapato ya Serikali kutoka shilingi Bilioni 331.2 mwaka 1995 hadi kufikia shilingi Trilioni 2 mwaka 2005.
Aidha, Mhe. Rais Samia amesema Hayati Rais Mkapa atakumbukwa kwa jitihada zake zilizowezesha nchi yetu kupunguziwa deni la taifa kwa zaidi ya nusu pamoja na nchi wahisani na taasisi za fedha kurejesha imani na Tanzania na kuanza kuisadia tena.
Mhe. Rais Samia amemuelezea Hayati Rais Mkapa kuwa ni kiongozi aliyeasisi taasisi nyingi nyeti ikiwemo Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Wakala wa Barabara nchini (Tanroads), Baraza la Taifa la Biashara (TNBC), Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Tume ya Kupambana na UKIMWI (TACAIDS) na Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge (MKURABITA) ambazo zimewezesha mageuzi makubwa katika maendeleo ya nchi yetu.
Amesema kwa upande wa Kimataifa, Hayati Rais Mkapa ameacha alama katika diplomasia ya kimataifa. Pia alishiriki kikamilifu katika kufufua Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), ushiriki wake katika kurejesha amani nchini Burundi pia alishiriki katika kugeuza uliokua Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU) na kuwa Umoja wa Afrika (AU).
Kama sehemu ya kuunga mkono juhudi za Hayati Rais Mkapa kupitia Taasisi yake ya Benjamin Mkapa, Rais Samia amesema kuwa atachangia uanzishwaji wa Mfuko wa Wakfu wa Hayati Mzee Mkapa ili kuendelea kuenzi kazi kubwa inayofanywa na Taasisi hiyo katika sekta ya afya.
Katika Kongamano hilo, Mhe. Rais Samia ameendelea kusisitiza kuwa kila mwananchi azidi kuchukua tahadhari za kujikinga na ugonjwa wa UVIKO-19 kwa kufuata maelekezo ya wataalamu wa afya.
Baadhi ya viongozi wastaafu wa kimataifa walioshiriki kwa njia ya mtandao katika Kongamano hilo ni Rais Mstaafu wa Marekani Bill Clinton, Rais mstaafu wa Nigeria Olusegun Obasanjo na Waziri Mkuu mstaafu wa Uingereza Tony Blair ambao wote kwa pamoja wamemtaja Hayati Rais Mkapa kama kiongozi aliyekua na maono ya kimageuzi katika uongozi wake.
Kongamano hilo lililofanyika Jijini Dar es Salaam limehudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, Rais mstaafu wa Awamu ya Pili Mhe. Ali Hassan Mwinyi, Rais mstaafu wa Awamu ya nne Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete na Rais mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mhe. Amani Abeid Karume.