Taarifa kwa vyombo vya Habari ya zamani
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 13 Machi, 2019 amekutana na kufanya mazungumzo na Ujumbe wa Urusi ulioongozwa na Mjumbe Maalum wa Rais wa Urusi katika masuala ya Afrika ambaye ni Naibu Waziri wa Mambo ya Nje, Mhe. Mikhail Bogdanov, Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Mhe. Rais Magufuli amemshukuru Rais wa Urusi Mhe. Vladimir Putin kwa ushirikiano na uhusiano mzuri kati ya Tanzania na nchi hiyo na amemhakikishia kuwa Serikali anayoiongoza inatambua umuhimu wa uhusiano huo na kwamba itauendeleza na kuukuza zaidi hususani katika masuala ya biashara, uwekezaji, utalii na utoaji wa huduma za kijamii kama vile afya, elimu na miundombinu.
“Naomba ufikishe ujumbe wangu kwa Mhe. Rais Putin kuwa Watanzania wanaipenda Urusi na tunamkaribisha kuja kutembelea nchi yetu pamoja na wananchi wengine wa Urusi, tunawakaribisha pia wawekezaji waje wawekeza katika fursa mbalimbali zilizopo hapa Tanzania kwa manufaa yetu sote” Mhe. Rais Magufuli amemueleza Mhe. Bogdanov.
Kwa upande wake Mhe. Bogdanov ambaye amewahi kutembelea Tanzania miaka 8 iliyopita ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa kasi nzuri ya maendeleo iliyoyapata katika kipindi kifupi na amebainisha kuwa Urusi imedhamiria kukuza zaidi uhusiano na ushirikiano mzuri uliopo kati yake na Tanzania.
Mhe. Bogdanov amesema Urusi inao mpango mahususi wa kushirikiana na nchi za Afrika ikiwemo Tanzania katika kuongeza kasi ya maendeleo na kwamba hivi karibu Tanzania na Urusi zitatiliana saini makubaliano ya kuanzisha tume ya pamoja ya ushirikiano (Joint Permanent Commission – JPC) katika biashara, uwekezaji na uchumi ili rasilimali na fursa zilizopo katika pande zote zitumike kwa manufaa ya wananchi wa nchi hizo.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi amesema mazungumzo hayo yamekwenda vizuri na kwamba Tanzania inatarajia tume ya pamoja ya ushirikiano ya Tanzania na Urusi itasaidia kukuza uchumi kupitia madini, gesi na utalii hasa wakati huu ambapo Urusi imeitangaza Tanzania kuwa nchi yenye vivutio bora vya utalii duniani.
Mazungumzo hayo yamehudhuriwa na Balozi Tanzania nchi Urusi Mhe. Mej Jen. Mstaafu Simon Mumwi na Balozi wa Urusi nchini Tanzania Mhe. Yuri Popov.
Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na timu ya wataalamu wa Tanzania na Morocco wanaoshughulikia ujenzi wa uwanja wa michezo katika Jiji la Dodoma, unaotarajiwa kujengwa kwa msaada wa Mfalme wa Morocco Mtukufu Mohammed VI.
Balozi wa Morocco hapa nchini aliyeongoza ujumbe wa wataalamu kutoka Morocco Mhe. Abdelilah Benryane amesema pamoja na kuzungumzia uhusiano mzuri wa Tanzania na Morocco wamejadiliana kuhusu utekelezaji wa miradi iliyokubaliwa wakati wa ziara ya Mfalme wa Morocco hapa nchini mwaka 2016 ikiwemo ujenzi wa Msikiti wa Baraza la Waislamu Tanzania (BAKWATA) unaojengwa Jijini Dar es Salaam na kuanza kwa ujenzi wa uwanja wa mpira wa miguu Jijini Dodoma.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mhandisi Patrick Mfugale amesema uwanja huo utajengwa jirani na eneo la Nanenane kando ya barabara ya Dodoma – Morogoro, utajengwa kwa mfano wa mlima Kilimanjaro na utakuwa na uwezo wa kuchukua watazamaji kati ya 85,000 na 100,005.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
13 Machi, 2019
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Rwanda, Mhe. Paul Kagame tarehe 08 Machi, 2019 amemaliza ziara yake ya kikazi ya siku 2 hapa nchini Tanzania na kurejea nchini kwake, baada ya hapo jana kufanya mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam, Mhe. Rais Kagame ameagwa na mwenyeji wake Mhe. Rais Magufuli.
Mara baada ya kuagana na mgeni wake, Mhe. Rais Magufuli amesalimiana na wananchi wa Dar es Salaam waliojitokeza kumuaga Mhe. Rais Kagame ambao wengi wao walikuwa ni wanawake na kuwatakia heri ya Siku ya Wanawake ambayo huadhimishwa tarehe 08 Machi, kila mwaka duniani kote.
Katika salamu hizo, Mhe. Rais Magufuli amewashukuru wanawake wote hapa nchini kwa mchango wao mkubwa kwa Taifa na amesema Serikali inatambua na kuthamini juhudi zao mbalimbali.
“Mungu awabariki sana akina Mama, mnafanya kazi nzuri kwa ajili ya Taifa hili, endeleeni kuimarisha umoja wa Watanzania wote, Serikali ninayoiongoza inathamini sana kazi nzuri zinazofanywa na akina Mama, endeleeni kutembea kifua mbele, Mungu atawalinda, na mimi sasa hivi naondoka kwenda kumuona Mama yangu hospitalini katika siku yake hii, pia natoa shukrani nyingi kwenu na kwa viongozi wa Mkoa na Wilaya kwa jinsi mnavyojitolea kuwapokea na kuwaaga vizuri wageni wetu” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
08 Machi, 2019
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Rwanda, Mhe. Paul Kagame tarehe 07 Machi, 2019 amefanya ziara ya kikazi ya siku 2 hapa nchini ambapo amekutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Baada ya mazungumzo hayo Mhe. Rais Magufuli amemshukuru Mhe. Rais Kagame ambaye ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kufanya ziara yake ya kwanza hapa nchini tangu alipochukua kijiti cha kuwa Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo.
Mhe. Rais Magufuli ameeleza kuwa mazungumzo yao yamejikita katika masuala ya kiuchumi kati ya Tanzania na Rwanda pamoja na ukanda wa Jumuiya ya Afrika wenye watu zaidi ya Milioni 165, na kusisitiza umuhimu wa wana Afrika Mashariki kutilia mkazo maendeleo ya kiuchumi yenye manufaa makubwa kwa wananchi.
“Mhe. Rais Kagame nimefurahishwa sana na ujio wako, hii ni dalili nzuri ya kuendeleza na kukuza uhusiano na ushirikiano wetu, nakukaribisha tena utembelee hapa Tanzania Bara na Zanzibar pia” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Kwa upande wake Mhe. Rais Kagame amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kumkaribisha na kufanya nae mazungumzo na kwamba anatarajia mazungumzo yao kuhusu biashara, siasa na ushirikiano yatasaidia kuzijenga zaidi nchi hizo pamoja na nchi nyingine za Jumuiya ya Afrika Mashariki.
“Nakushukuru kama ndugu kama rafiki, Watanzania na Wanyarwanda ni marafiki, ni ndugu, tukijijenga hapo tutaijenga Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla, kwa hiyo asante sana Mhe. Rais” amesema Mhe. Rais Kagame.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
07 Machi, 2019
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 03 Machi, 2019 amefanya mabadiliko madogo ya Baraza la Mawaziri.
Katika mabadiliko hayo Mhe. Rais Magufuli amemteua Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga kuwa Waziri wa Katiba na Sheria.
Kabla ya uteuzi huo, Mhe. Dkt. Mahiga alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Mhe. Rais Magufuli amemteua Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Kabla ya uteuzi huo Mhe. Prof. Kabudi alikuwa Waziri wa Katiba na Sheria.
Mawaziri Wateule hao wataapishwa kesho tarehe 04 Machi, 2019 saa 3:30 Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
03 Machi, 2019
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 04 Machi, 2019 amewaapisha Mawaziri 2, Balozi 1 na kushuhudia Naibu Makamishna wa Polisi 5 wakivishwa vyeo vipya vya Kamishna wa Polisi (CP) na kuapishwa kuongoza Kamisheni za Polisi.
Mhe. Rais Magufuli amemuapisha Mhe. Balozi Dkt. Augustine Phillip Mahiga kuwa Waziri wa Katiba na Sheria na Mhe. Prof. Palamagamba John Aidan Mwaluko Kabudi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Mhe. Rais Magufuli amemuapisha Mhe. Hassan Simba Yahya kuwa Balozi wa Tanzania nchini Zambia. Mhe. Balozi Simba amechukua nafasi ya Mhe. Balozi Abdulrahman Kaniki ambaye amemaliza muda wake.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli ameshuhudia Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) Simon Sirro akiwavisha cheo cha Kamishna wa Polisi na kuwaapisha, Naibu Makamishna wa Polisi 5.
Walioapishwa ni CP - Charles Omari Mkumbo ambaye ameteuliwa kuwa Kamishna wa Intelijensia ya Jinai, CP - Liberatus Materu Sabas aliyeteuliwa kuwa Kamishna wa Operesheni na Mafunzo, CP - Shabani Mrai Hiki aliyeteuliwa kuwa Kamishna wa Maabara ya Uchunguzi wa Kisayansi, CP - Leonard Paul Lwabuzala aliyeteuliwa kuwa Kamishna wa Fedha na Lojistiki na CP - Benedict Michael Wakulyamba aliyeteuliwa kuwa Kamishna wa Utawala na Menejimenti ya Utumishi.
Akizungumza katika tukio hilo Mhe. Rais Magufuli amewapongeza Mawaziri, Balozi na Makamishna wa Polisi kwa kuteuliwa kwao na amewataka kwenda kutekeleza majukumu yao vizuri ikiwa ni pamoja na kufanya mabadiliko ya kuondoa dosari zilizopo katika maeneo yao ya kazi na kuongeza ufanisi zaidi huku wakiweka mbele maslahi ya Taifa.
Mhe. Rais Magufuli amelipongeza Jeshi la Polisi kwa kazi nzuri linayoifanya lakini ametaka lijitafakari juu ya baadhi ya matukio ambayo yanaacha maswali mengi kwa wananchi juu ya hatua zinazochukuliwa na polisi, na ametolea mfano wa tukio la kutekwa kwa mfanyabiashara Mohammed Dewji, vitendo vya rushwa, Polisi kuhusishwa na magendo, vitendo vya rushwa na dawa za kulevya, pamoja na hatua zinazochukuliwa dhidi ya Maafisa wa Polisi wanaoshindwa kufanya kazi kwa tija.
Mhe. Rais Magufuli amemtaka IGP - Simon Sirro kutosita kuwaondoa Maafisa wa Polisi wanaoshindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo na kuteua ama kupendekeza Maafisa wapya wenye uwezo wa kufanya kazi vizuri, na pia ametaka Polisi iondokane na utamaduni wa kuwapeleka Makao Makuu ya Polisi Maafisa ambao wanashindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo kwenye vituo vya kazi wanavyopangiwa.
Hafla ya kuapishwa kwa Mawaziri, Balozi na Makamishna wa Polisi imefanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job Yustino Ndugai, Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Tulia Ackson, Katibu Mkuu Kiongozi Mhe. Balozi John Kijazi, Mawaziri na Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu Wakuu, Viongozi Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama, Viongozi wa Madhehebu ya Dini na Majaji wa Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufani.
Viongozi walioapishwa pia wamekula kiapo cha uadilifu kwa viongozi wa umma kilichoongozwa na Kamishna wa Maadili Mhe. Jaji Mstaafu Harold Nsekela.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
04 Machi, 2019
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ameonya kuwa hatamvumilia kiongozi yeyote wa Mkoa, Wilaya ama Halmashauri ya Wilaya, Mji, Manispaa na Jiji atakayebainika kuhusika kuwatoza ushuru ama tozo yoyote wajasiriamali wadogo waliopatiwa vitambulisho.
Mhe. Rais Magufuli ametoa onyo hilo leo tarehe 01 Machi, 2019 wakati akizungumza na wananchi katika Mtaa wa Lumumba Jijini Dar es Salaam, muda mfupi baada ya kutoka katika Ofisi Ndogo za Chama Cha Mapinduzi (CCM) alikoongoza kikao cha viongozi wenzake wa CCM.
Mhe. Rais Magufuli amefafanua kuwa kiongozi yeyote atakayebainika kuwatoza wajasiriamali wadogo wenye vitambulisho atachukuliwa hatua ikiwa ni pamoja na kuvuliwa madaraka, na hivyo ametaka wajasiliamali hao wasibughudhiwe.
Katika tukio hilo Mhe. Rais Magufuli ambaye ni Mwenyekiti wa CCM, akiwa na baadhi ya Wajumbe wa Kamati Kuu ya CCM ambao ni Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara) Ndg. Philip Mangula na Katibu Mkuu wa CCM Ndg. Bashiru Ally Kakurwa, wamempokea Waziri Mkuu Mstaafu Mhe. Edward Lowassa ambaye ametangaza kurudi CCM ikiwa ni zaidi ya miaka mitatu tangu alipotangaza kujiunga na chama cha upinzani.
Mhe. Rais Magufuli ametoa wito kwa Watanzania kudumisha amani, umoja, udugu na mshikamano na kujielekeza katika ajenda kuu ya ujenzi wa Taifa, badala ya kupoteza muda mwingi kwa marumbano yasiyo na tija.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
01 Machi, 2019
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 28 Februari, 2019 amekutana na kufanya mazungumzo na Makamu wa Rais wa Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Japan (JICA) Bw. Kazuhiko Koshikawa.
Mazungumzo hayo yamefanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt. Damas Ndumbaro na Balozi wa Japan hapa nchini Mhe. Shinichi Goto.
Mhe. Rais Magufuli ameishukuru JICA kwa kuwa mdau muhimu wa maendeleo ya Tanzania na amemhakikishia Bw. Kazuhiko Koshikawa kuwa Tanzania itaendeleza na kukuza zaidi ushirikiano huo hususani katika ujenzi wa miundombinu.
Ameelezea kufurahishwa kwake na kutiwa saini kwa miradi miwili ya upanuzi wa barabara ya Mwenge – Morocco (kilometa 4.3) na Daraja la Gerezani Jijini Dar es Salaam ambayo ujenzi wake utaanza wakati wowote kuanzia sasa, pamoja na msaada wa shilingi Bilioni 57 kwa ajili ya uboreshaji wa bandari ya Kigoma.
Kwa upande wake Bw. Kazuhiko Koshikawa amempongeza Mhe. Rais Magufuli na Serikali ya Awamu ya Tano kwa juhudi kubwa za kukuza maendeleo ya Tanzania na kuendeleza ushirikiano mzuri na JICA uliowezesha miradi mingi ya maendeleo kutekelezwa.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt. Damas Ndumbaro amesema ushirikiano mzuri wa Serikali ya Tanzania na JICA unathibitisha rekodi nzuri ya uhusiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na nchi mbalimbali ambao una manufaa makubwa katika uchumi.
Katika mazungumzo hayo Mhe. Rais Magufuli ameagana na Mwakilishi Mkazi wa JICA hapa nchini aliyemaliza muda wake Bw. Toshio Nagase na kumkaribisha Mwakilishi Mkazi mpya wa JICA Bw. Naofumi Yamamura.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
28 Februari, 2019
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 26 Februari, 2019 amekutana na kufanya mazungumzo na Mkuu wa Idara ya Upasuaji wa Ubongo na Mishipa kutoka Hospitali ya Kimataifa ya Chuo Kikuu cha Peking (PUIH) iliyopo Beijing nchini China Prof. Zhao Yuanil ambaye ameongoza timu ya wataalamu wanaoshirikiana na Taasisi ya Tiba ya Mifupa, Upasuaji wa Ubongo na Mishipa ya Fahamu ya Muhimbili (MOI).
Mazungumzo hayo yamefanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Balozi wa China hapa nchini Mhe. Wang Ke, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu na Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili Prof. Lawrence Mseru.
Katika mazungumzo hayo Mhe. Rais Magufuli ameishukuru Hospitali ya Kimataifa ya Chuo Kikuu cha Peking kwa kukubali ombi lake la kuanzisha ushirikiano na MOI na amemhakikishia Prof. Yuanil kuwa Serikali ipo tayari kutoa ushirikiano zaidi utakaowezesha MOI kuongeza uwezo wake wa kutoa huduma za upasuaji wa ubongo na mishipa ya fahamu kwa Watanzania ambao wamekuwa wakikosa huduma hiyo ama kulazimika kutumia gharama kubwa kwenda nje ya nchi.
Mhe. Rais Magufuli ameelezea kufurahishwa kwake na taarifa za kufanyika kwa mafanikio kwa upasuaji wa kwanza uliofanywa na Daktari Bingwa Prof. Yuanil hapo jana na kwamba anaamini wataalamu zaidi wataendelea kuja hapa nchini kutoka PUIH kwa ajili ya kutoa huduma na kuwafundisha madaktari wa Tanzania, na pia Watanzania wengi watakwenda nchini China kujifunza upasuaji wa ubongo na mishipa ya fahamu.
Kwa upande wake Prof. Yuanil amempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa juhudi zake kubwa za kuhakikisha MOI inaimarishwa ikiwemo kufanya uwekezaji mkubwa katika miundombinu na amemhakikishia kuwa PUIH itahakikisha makubaliano yaliyotiwa saini mwaka jana kati ya hospitali hiyo na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto yanatekelezwa kikamilifu.
“Tanzania kuna watu zaidi ya Milioni 50 na kuna idadi kubwa ya watu wenye magonjwa ya ubongo, wanaopata majeraha kichwani, uvimbe wa ubongo, matatizo ya mishipa ya damu ya ubongo na magonjwa ya uti wa mgongo ambao wanahitaji kupata matibabu mazuri hapahapa, lakini naambiwa kuna wataalamu 10 tu ambao hawatoshelezi mahitaji, ndio maana tupo hapa kuangalia mnafanya nini na tuone namna ya kusaidia kuwaongezea uwezo” amesema Prof. Yuanil.
Nae Mhe. Ummy Mwalimu amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa jitihada zake za kuwatafuta Madaktari Bingwa kutoka PUIH na kutoa maelekezo ya kuanzishwa kwa ushirikiano na MOI, pamoja na kuhakikisha Serikali inatoa zaidi ya Shilingi Bilioni 12.5 za kuimarisha miundombinu ya MOI ili itoe matibabu ya kibingwa ya upasuaji wa ubongo na mishipa ya fahamu kwa Watanzania wengi.
“Kwa kweli Watanzania wawe na matumaini makubwa kuwa huduma zile za kibobezi zitapatikana ndani ya nchi na hakuna kwenda nje, mambo yote ndani ya nchi, kwa hiyo tunashukuru sana kwa maono haya ya Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli, yeye ndio alipata taarifa kuwa kuna Daktari Bingwa huyu wa upasuaji wa ubongo na kisha akatupa maelekezo kuwa daktari huyo ameweza kutoa matibabu kwa wagonjwa walioshindikana katika nchi nyingi, kwa hiyo tukafanya mawasiliano kupitia Ubalozi wetu wa China na baadaye tukasaini mkataba Septemba 2018 nilipokwenda China na sasa tumeanza kutekeleza” amesema Mhe. Ummy Mwalimu.
Mkurugenzi Mtendaji wa MOI Dkt. Respicious Boniface amesema kupitia ushirikiano huu Tanzania inatarajia kupata wataalamu wengi wa upasuaji wa ubongo na mishipa ya fahamu na amebainisha kuwa pamoja na kufanya upasuaji wa mafanikio kwa mgonjwa mmoja hapo jana, wagonjwa wengine wawili watafanyiwa upasuaji leo na kwamba ushirikiano huu utaiwezesha MOI kuwa kituo bora cha upasuaji wa ubongo na mishipa ya fahamu Barani Afrika.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
26 Februari, 2019
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ametuma salamu za rambirambi kwa familia zilizopoteza jamaa zao katika ajali ya barabarani iliyotokea katika Wilaya ya Mbozi Mkoani Songwe na kusababisha vifo vya watu 19.
Ajali hiyo imetokea jana tarehe 21 Februari, 2019 majira ya saa 3:15 usiku katika mteremko wa mlima Senjele ambapo lori (Semi-trailer) lililokuwa likisafiri kutoka Tunduma kwenda Mbeya Mjini lililigonga basi la abiria kwa nyuma, kisha basi hilo likaminywa katikati baada ya kuligonga lori jingine (Semi-trailer) lililokuwa mbele yake na kusababisha vifo vya watu wote 18 waliokuwemo ndani ya basi pamoja na dereva wa lori lililogonga basi la abiria.
Mhe. Rais Magufuli amemtaka Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brig. Jen. Mstaafu Nicodemas Elias Mwangela kufikisha salamu zake za pole kwa ndugu, jamaa, marafiki na wote walioguswa na vifo vya watu hao na amewaombea kwa Mwenyezi Mungu aziweke roho za Marehemu wote mahali pema peponi, Amina.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli amezitaka mamlaka zinazohusika na usalama wa barabarani Mkoani Songwe kufanya uchunguzi wa ajali hiyo na kuchukua hatua zinazostahili pamoja na kujipanga vizuri kukabiliana na matukio ya ajali za barabarani.
Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli ametoa mkono wa pole kwa familia ya Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Hamisi Kigwangalla ambaye amefiwa na mwanae aitwaye Zul Hamis Kigwangalla jana tarehe 21 Februari, 2019 Jijini Dar es Salaam.
Mhe. Rais Magufuli akiwa na Mkewe Mhe. Mama Janeth Magufuli wamefika nyumbani kwa familia hiyo Mikocheni Jijini Dar es Salaam na kukutana na baadhi ya wanafamilia wakiongozwa na Mama wa Marehemu Dkt. Bayoum Kigwangalla wakiwa katika maandalizi ya kusafirisha mwili wa marehemu kwenda Nzega Mkoani Tabora. Dkt. Hamis Kigwangalla ameshatangulia Nzega ambako mazishi yatafanyika baadaye leo.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
22 Februari, 2019
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 20 Februari, 2019 amekutana na kufanya mazungumzo na Afisa Mwendeshaji Mkuu wa Kampuni ya Barrick Gold anayeshughulikia Afrika na Mashariki ya Kati Dkt. Willem Jacobs, Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Baada ya mazungumzo hayo Dkt. Willem Jacobs aliyeongozana na washauri wa Barrick Gold Corporation ambao ni Rich Haddock, Duncan Bullivant na Wicus du Preez amesema wamekutana na Mhe. Rais Magufuli ili kumhakikishia kuwa makubaliano yaliyofikiwa tarehe 19 Oktoba, 2017 watayatekeleza kikamilifu hasa baada ya kampuni kubwa ya uchimbaji dhahabu ya Rand Gold ya Afrika Kusini kuungana na Barrick Gold Corporation katika umiliki, uwekezaji na menejimenti.
Dkt. Willem Jacobs amebainisha kuwa hakuna kitakachokuwa tofauti na makubaliano yaliyofikiwa awali ambayo yaliongozwa na Mwenyekiti Mtendaji wa Barrick Gold Corporation Prof. John Thornton ikiwemo Barrick Gold Corporation kuilipa Serikali ya Tanzania kifuta machozi cha Dola za Marekani Milioni 300 (sawa na shilingi Bilioni 682.5), kuendelea na uwekezaji kwa ubia kati ya Serikali ya Tanzania na Kampuni ya Barrick Gold na mgawanyo wa mapato ya kiuchumi kwa uwiano wa asilimia 50 kwa 50 kati ya Serikali ya Tanzania na kampuni ya Barrick Gold.
Dkt. Willem Jacobs amempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa jitihada zake za kusimamia maslahi ya Watanzania katika rasilimali za nchi yao na amesema pamoja na ukweli kwamba Mhe. Rais Magufuli yupo katika njia sahihi, yeye akiwa Mwafrika anaunga mkono juhudi hizo kwa kuwa ndio mwelekeo sahihi ambao nchi za Afrika zinapaswa kuufuata.
“Mimi ni Mwafrika na sisi sote ni Waafrika, anachokifanya Mhe. Rais Magufuli ni sahihi kabisa, anahakikisha utajiri wa rasilimali uliopo unabainishwa na unawanufaisha Watanzania, na ndio maana tupo hapa kwa sababu tunakubaliana na Mhe. Rais.
Na hivi ndivyo sisi Waafrika tunapaswa kufanya kwa rasilimali zetu, na sisi tunahakikisha tunafanya kazi vizuri na Serikali na jamii kulinda rasilimali hizi, kumbuka rasilimali hizi ni za wananchi, jukumu langu kama mwekezaji ni kubadili hayo madini kuwa kodi na ajira kwa Tanzania na pia kampuni yangu kupata faida yake halali” amesema Dkt. Willem Jacobs.
Amebainisha kuwa baada ya muungano huo wa Rand Gold na Barrick Gold, sasa Kampuni mpya ya Barrick Gold imekuwa kampuni kubwa inayoongoza kwa umiliki wa rasilimali za dhahabu duniani ikimiliki rasilimali 5 kati ya 10, na kwamba kutokana na uwezo huo Barrick Gold Corporation sasa imeweza kujiimarisha zaidi kiuwekezaji na utaalamu na ipo tayari kushirikiana na Tanzania kuhakikisha rasilimali ya dhahabu iliyopo inaleta manufaa kwa pande zote mbili yaani Watanzania na mwekezaji.
Waziri wa Katiba na Sheria Prof. Palamagamba Kabudi ambaye ameongoza timu ya majadiliano kwa niaba ya Serikali ya Tanzania na Kampuni ya Barrick Gold amesema nyaraka za makubaliano hayo zimekamilika na kwamba sasa kinachosubiriwa ni utekelezaji wa makubaliano hayo unaotarajiwa kukamilika ifikapo mwisho wa mwezi Machi 2019.
“Baada ya muungano wao (Rand Gold na Barrick Gold Corporation) hii sasa ni timu mpya na tumewaona ni watu ambao sasa wapo tayari kutekeleza yale yote yaliyokubaliwa, na sasa ni kwa kila upande kwenda kwenye vyombo vyake vinavyohusika kufanya maamuzi ya mwisho ili utekelezaji ufanyike” amesema Prof. Kabudi.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
20 Februari, 2019
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amemteua Dkt. Michael Wilfred Ng’umbi kuwa Mkurugenzi wa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW).
Kabla ya uteuzi huo Dkt. Ng’umbi alikuwa Mhadhiri Mwandamizi wa Kitivo cha Elimu cha Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (Open University of Tanzania – OUT)
Dkt. Ng’umbi amechukua nafasi ya Dkt. Fidelice Mafumiko ambaye ameteuliwa kuwa Mkemia Mkuu wa Serikali.
Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli amemteua Mhe. Jaji Stephen Mrimi Magoiga kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Ushindani (Fair Competition Tribunal – FCT)
Jaji Magoiga amechukua nafasi ya Mhe. Jaji Barke Mbaraka Sehel ambaye ameteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani.
Taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi Mhe. Balozi John Kijazi imeeleza kuwa uteuzi wa viongozi hawa umeanza tarehe 19 Februari, 2019.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
20 Februari, 2019
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 19 Februari, 2019 amemteua Bw. Hosea Ezekiel Kashimba kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (Public Service Social Security Fund - PSSSF).
Bw. Kashimba anachukua nafasi ya Bw. Eliud Sanga ambaye uteuzi wake umetenguliwa.
Kabla ya uteuzi huo Bw. Kashimba alikuwa Mkurugenzi wa Ukaguzi wa Ndani wa Shirika la Hifadhi ya Jamii la NSSF.
Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli amefanya uteuzi wa viongozi wengine 2 kama ifuatavyo;
Kwanza, Mhe. Rais Magufuli amemteua Bw. Augustine Emmanuel Mbokella kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Benki ya Biashara ya TIB (TIB Corporate Bank Limited).
Na pili, Mhe. Rais Magufuli amemteua Bi. Latifa Mohammed Khamis kuwa Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Biashara za Nje (TANTRADE).
Taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi Mhe. Balozi John Kijazi imeeleza kuwa uteuzi wa viongozi hawa umeanza leo tarehe 19 Februari, 2019.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
19 Februari, 2019
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amemteua Dkt. Lucas Luhende Kija kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Ushauri la Taifa kwa Watu Wenye Ulemavu.
Dkt. Kija ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu (DUCE).
Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli amemteua Bw. Michael Pius Nyagoga kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Wakala wa Umeme Vijijini (REA).
Bw. Nyagoga ni Kaimu Kamishna Msaidizi wa Sera, Idara ya Maendeleo ya Sekta ya Fedha, Wizara ya Fedha na Mipango.
Taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi Mhe. Balozi John Kijazi imeeleza kuwa uteuzi wa wenyeviti hao umeanza tarehe 13 Februari, 2019.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
14 Februari, 2019
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 07 Februari, 2019 amekutana na kufanya mazungumzo na Mjumbe Maalum wa Rais wa Zimbabwe ambaye ni Waziri wa Ardhi, Kilimo, Maji, Mazingira na Makazi Vijijini Mhe. Pretence Shiri.
Mazungumzo hayo yamefanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam ambapo Mhe. Shiri amekabidhi barua kutoka kwa Rais wa Zimbabwe Mhe. Emmerson Mnangagwa.
Mhe. Shiri ameishukuru Tanzania kwa mchango mkubwa ilioutoa kwa Zimbabwe wakati wa kupigania uhuru uliopatikana mwaka 1980, na amebainisha kuwa Wazimbabwe wanaichukulia Tanzania kuwa ni nyumbani.
“Tunafurahi sana kuwa hapa Tanzania, tunajisikia ni nyumbani kwetu, bila Tanzania Zimbabwe isingepata uhuru mwaka 1980, ingechukua muda mrefu sana, lakini tunafurahi kuwa Watanzania walijitolea kwa kiasi kikubwa kuhakikisha Zimbabwe inakuwa nchi huru” amesema Mhe. Shiri.
Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na Kaimu Balozi wa Jumuiya ya Ulaya Bw. Charles Stuart na baada ya mazungumzo hayo Bw. Stuart amesema mazungumzo baina yao yalikuwa mazuri na yamehusu uhusiano wa muda mrefu wa Tanzania na Umoja wa Ulaya na dhamira ya umoja huo kuisadia Tanzania.
“Uhusiano wa Tanzania na Umoja wa Ulaya umekuwa imara siku zote, na kumekuwa na maeneo mengi ya uhusiano yenye maslahi muhimu kwa pande zote na kwa miaka mingi” amesema Mhe. Stuart.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
07 Februari, 2019
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 06 Februari, 2019 amekutana na kufanya mazungumzo na Kamishna Mkuu wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) Mhe. Filippo Grandi, Ikulu Jijini Dar es Salaam na kumhakikishia kuwa Serikali itaendeleza ushirikiano na shirika hilo katika kutekeleza jukumu la kuhudumia wakimbizi.
Mhe. Rais Magufuli amesema Tanzania imekuwa ikipokea wakimbizi kutoka nchi mbalimbali baada ya kutokea machafuko katika nchi hizo, na imekuwa ikiwapa hifadhi na kuwaruhusu watumie rasilimali za Watanzania licha ya wakati mwingine kutopata misaada kutoka Jumuiya ya Kimataifa.
“Nchi yetu kwa sasa ina wakimbizi 350,000 waliopo katika maeneo mbalimbali wakiwemo 40,000 wa kutoka nchini Burundi, tunawapa hifadhi na wanatumia huduma za kijamii na miundombinu ya Watanzania katika maeneo wanayoishi.
Nimefurahi Mhe. Grandi anasema tutaendelea kushirikiana na kwamba sasa wapo tayari kusaidia gharama za kuhudumia wakimbizi pamoja na jamii katika maeneo wanayoishi wakimbizi, maana tangu miaka 10 iliyopita UNHCR imekuwa ikiahidi kutoa fedha za kusaidia wakimbizi lakini haitekelezi ahadi zake” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Hata hivyo Mhe. Rais Magufuli amesema pamoja na dhamira njema ya kuwapa hifadhi wakimbizi na kuwapa uraia baadhi ya wakimbizi, Serikali inaendelea kuwahimiza kurejea makwao wakimbizi ambao katika nchi zao machafuko yamekwisha ili wakaungane na familia, ndugu, jamaa na kujenga nchi zao.
Kwa upande wake Mhe. Grandi amemshukuru Mhe. Rais Magufuli na Serikali yake kwa kuendelea kuwapokea na kuwapa hifadhi wakimbizi kutoka nchi zenye matatizo mbalimbali, na amesema UNHCR inatambua mchango mkubwa ambao kwa miaka mingi Tanzania inautoa kuwapa hifadhi na kuwahudumia wakimbizi kutoka kwenye nchi zinazoizunguka ambazo zimekuwa na machafuko ya mara kwa mara.
Mhe. Grandi ameahidi kuwa UNHCR itahakikisha inatekeleza ahadi zake za kusaidia jukumu la kuwapa hifadhi wakimbizi, kusaidia vyombo vya ulinzi na usalama ambavyo vimekuwa vikifanya kazi kubwa ya kuhudumia wakimbizi hao kwa kuvipatia teknolojia na vitendea kazi pamoja na kusaidia jamii katika maeneo yanayokaliwa na wakimbizi.
Aidha, Mhe. Grandi ameomba radhi kufuatia Serikali ya Tanzania kukamata makontena yaliyoingizwa nchini yakiwa na nguo zinazofanana na sare za jeshi hali iliyolazimu nguo hizo kuchomwa moto, na kubainisha kuwa jambo hilo halitajirudia.
“Ilitokea kampuni moja ya Japan ilitoa msaada wa nguo kwa ajili ya wafanyakazi wetu, nguo zile kwa bahati mbaya zilikuwa zinafanana kama sare za jeshi, na tulizipokea ili tuzisambaze kwenye maeneo ambayo tunawahudumia wakimbizi, hili ni kosa, hatukupaswa kufanya hivyo na hatujawahi kufanya hivyo, lakini wakati mwingine vitu hivi vinatokea, namuomba radhi Mhe. Rais na namuahidi kuwa haitatokea tena” amesema Bw. Grandi.
Mhe. Rais Magufuli amempongeza Bw. Grandi kwa uungwana wake wa kuomba radhi kwa kitendo cha kuingiza nguo zinazofanana na sare za jeshi na amesema anaamini UNHCR haitarudia kufanya hivyo.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
05 Februari, 2019
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amemteua Dkt. Islam Seif Salum Mchenga kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Uvuvi wa Bahari Kuu (Deep Sea Fishing Authority – DSFA).
Taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi, Mhe. Balozi John Kijazi imeeleza kuwa uteuzi wa Dkt. Mchenga umeanza tarehe 01 Desemba, 2018 na kwamba kabla ya uteuzi huo alikuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi - Zanzibar.
Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli amemteua Dkt. Emmanuel Andrew Sweke kuwa Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Uvuvi wa Bahari Kuu (DSFA).
Uteuzi wa Dkt. Sweke umeanza tarehe 01 Desemba, 2018 na kabla ya uteuzi huo alikuwa Afisa Utafiti wa Uvuvi Mwandamizi na Kaimu Mkurugenzi wa Kituo cha Utafiti wa Uvuvi Tanzania (Tanzania Livestock Research Institute - TAFIRI) – Kigoma.
Katika hatua nyingine, Mhe. Rais Magufuli amemteua Prof. Sebastian W. Chenyambuga kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya Utafiti wa Mifugo (TALIRI).
Uteuzi wa Prof. Chenyambuga umeanza tarehe 26 Januari, 2019.
Halikadhalika, Mhe. Rais Magufuli amemteua Prof. Justinian Rwezaula Ikingura kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (Geological Survey of Tanzania - GST).
Uteuzi wa Prof. Ikingura umeanza tarehe 18 Januari, 2019.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
30 Januari, 2019
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 23 Januari, 2019 amezungumza na viongozi wa Madhehebu mbalimbali ya Dini hapa nchini ambapo amewashukuru kwa mchango wao mkubwa wa kutoa huduma za kiroho na kijamii kupitia taasisi wanazoziongoza.
Mkutano huo umefanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Kangi Lugola, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Selemani Jafo, Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake, Wazee na Watoto Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile na Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhe. Jumaa Aweso.
Akizungumza baada ya kupokea maoni, ushauri na mapendekezo ya viongozi hao wa Dini, Mhe. Rais Magufuli amesema Serikali inatambua kazi kubwa na nzuri inayofanywa na Madhehebu ya Dini katika kuihudumia jamii na ameahidi kuwa itaendeleza ushirikiano huo mzuri kwa kuwa una manufaa makubwa kwa wananchi na katika ujenzi wa Taifa.
Mhe. Rais Magufuli ameahidi kuwa Serikali itafanyia kazi maoni, ushauri na mapendekezo yote yaliyotolewa na viongozi hao wa Dini, na amewahakikishia kuwa Serikali itaendelea kutekeleza majukumu yake ya kuimarisha huduma za kijamii zikiwemo kuongeza usambazaji wa maji kwa wananchi, kujenga miundombinu ya elimu, afya na usafiri, kutoa elimu bila malipo kwa shule za msingi hadi sekondari, kutoa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu kwa vyuo vya Serikali na visivyo vya Serikali na kulinda amani na usalama wa nchi.
Kuhusu usimamizi wa ubora wa huduma zinazotolewa na baadhi ya taasisi zilizo chini ya Madhehebu ya Dini kama vile vyuo na hospitali, Mhe. Rais Magufuli amesema Serikali inachukua hatua hizo ili kuhakikisha Watanzania wanapata elimu na matibabu bora kwa gharama nafuu, na kwamba haifanyi hivyo kwa lengo kuziumiza taasisi hizo.
Kwa upande wa misamaha ya kodi, Mhe. Rais Magufuli amesema Serikali haijafuta misamaha ya kodi kwa taasisi za Dini huku akibainisha kuwa mwaka 2016 ilitoa misamaha yenye thamani ya shilingi Bilioni 19.66, mwaka 2017 ilitoa misamaha yenye thamani ya shilingi Bilioni 17.6 na mwaka 2018 ilitoa misamaha yenye thamani ya shilingi Bilioni 46.84 na kwamba pamoja na kutoa misamaha hiyo kumekuwa na changamoto ya baadhi ya taasisi kuuza bidhaa zinawekewa misamaha ama kutumia bidhaa za misahama ya kodi kufanyia kibiashara.
Kuhusu zoezi la uhakiki wa wakulima wa korosho kwenda polepole na hivyo kusababisha wakulima wengi kutolipwa fedha zao, Mhe. Rais Magufuli amewaagiza viongozi wa Mikoa, Wilaya na Tarafa kuondoa urasimu katika uhakiki huo na hivyo kuharakisha zoezi ili wakulima walipwe mapema kwa kuwa fedha za malipo ya korosho zao zipo.
Mhe. Rais Magufuli amekubaliana na maoni ya viongozi wa Dini kwa kuwataka viongozi wa Serikali katika ngazi mbalimbali kuweka utaratibu wa kukutana na kuzungumza na Viongozi wa Madhehebu ya Dini katika maeneo yao, na amemuagiza Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa kuhakikisha kero za Viongozi wa Dini zinatatuliwa.
Halikadhalika Mhe. Rais Magufuli amesema Serikali itafanyia kazi ushauri wa kudhibiti michezo ya kamali ambayo inazidi kushika kasi na kusababisha wananchi hasa vijana kutumia muda mwingi kucheza kamali badala ya kufanya kazi za uzalishaji mali kwa ajili ya ujenzi wa Taifa.
Pamoja na kutoa maoni hayo viongozi hao wa Dini wamempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa uongozi wake mzuri, uzalendo, ukweli na kutekeleza kwa vitendo ahadi alizozitoa kwa Watanzania, na wamemuahidi kuwa wataendelea kushirikiana na Serikali anayoiongoza na kumuombea.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
23 Januari, 2019
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 27 Januari, 2019 amefanya uteuzi wa Majaji 6 wa Mahakama ya Rufani, Majaji 15 wa Mahakama Kuu, Wakuu wa Wilaya 2 na Wakurugenzi 10 wa Halmashauri za Wilaya hapa nchini.
Uteuzi wa viongozi hao umetangazwa na Katibu Mkuu Kiongozi Mhe. Balozi John Kijazi, Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Walioteuliwa kuwa Majaji wa Mahakama ya Rufani ni;
- Mhe. Jaji Sahel Barke
- Mhe. Jaji Dkt. Mary Levira
- Mhe. Jaji Rehema Kerefu Sameji
- Mhe. Jaji Winnie Korosso
- Mhe. Jaji Ignus Kitusi
- Mhe. Jaji Lugano Samson Mwandambo
Walioteuliwa kuwa Majaji wa Mahakama Kuu ni;
- Cyprian Phocas Mkeha
- Dunstan Beda Ndunguru
- Seif Mwinshehe Kulita
- Dkt. Ntemi Nimilwa Kilikamajenga
- Zepherine Nyalugenda Galeba
- Dkt. Juliana Laurent Masabo
- Mustapha Kambona Ismail
- Upendo Elly Madeha
- Willbard Richard Mashauri
- Yohane Bokobora Masara
- Dkt. Lilian Mihayo Mongella
- Fahamu H. Mtulya
- John Rugalema Kahyoza
- Athumani Matuma Kirati
- Susan Bernard Mkapa
Wakuu wa Wilaya.
- Mhe. Rais Magufuli amemteua Bw. Charles Francis Kabeho kuwa Mkuu wa Wilaya ya Tarime.
Bw. Kabeho anachukua nafasi ya Bw. Glorious Luoga ambaye uteuzi wake umetenguliwa.
- Mhe. Rais Magufuli amemteua Bw. Thomas Cornel Apson kuwa Mkuu wa Wilaya ya Mwanga.
Bw. Apson anachukua nafasi ya Bw. Aaron Mbogho ambaye uteuzi wake umetenguliwa.
Wakurugenzi wa Halmashauri za Wilaya walioteuliwa kujaza nafasi zilizokuwa wazi ni.
- Isaya M. Mbenje - Pangani
- Dkt. Fatuma Ramadhani Mganga - Bahi
- Regina Bieda – Tunduma
- Jonas Emmanuel Mallosa – Ulanga
- Ally Juma Ally – Njombe
- Misana Kalela Kwangura - Nkasi
- Diodes M. Rutema – Kibondo
- Netho Ndilito - Mufindi
- Elizabeth Mathias Gumbo – Itilima
- Stephen Mhoja Mashauri Ndaki – Kishapu
Uteuzi wa viongozi hawa unaanza leo tarehe 27 Januari, 2019.
Majaji Wateule wa Mahakama ya Rufani na Majaji Wateule wa Mahakama Kuu wataapishwa Jumanne tarehe 29 Januari, 2019 kuanzia saa 3:00 asubuhi Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Aidha, Wakuu wa Wilaya 2 na Wakurugenzi 10 wa Halmashauri za Wilaya walioteuliwa leo, wanatakiwa kufika Ikulu Jijini Dar es Salaam tarehe 29 Januari, 2019 saa 3:00 asubuhi kwa ajili ya kupata maelekezo ya kikazi na kula kiapo cha uadilifu kwa viongozi wa umma.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
27 Januari, 2019
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amewaagiza viongozi wa Wazira ya Madini na Wizara ya Fedha na Mpango kujadiliana na kukubaliana na wadau wa madini kuhusu utaratibu mzuri utakaowezesha kuongezeka kwa mapato yatokanayo na madini yote yanayozalishwa hapa nchini ikiwemo kupendekeza viwango vya tozo za kodi na ushuru vitakavyowavutia wadau kulipa tozo hizo badala ya kukwepa.
Mhe. Rais Magufuli ametoa maagizo hayo tarehe 22 Januari, 2019 katika kituo cha kimataifa cha mikutano cha Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam baada ya kupokea maoni ya wachimbaji wadogo, wafanyabiashara na wadau wengine wa sekta ya madini wanaokutana kwa siku mbili kituo hapo kwa lengo la kujadili masuala mbalimbali yahusuyo madini.
Katika maoni yao wadau hao wa madini wamemueleza Mhe. Rais Magufuli kuwa tozo kubwa na nyingi zilizowekwa katika madini hasa dhahabu zimesababisha wachimbaji wadogo na kati na wafanyabiashara wengi kukwepa kuuza madini yao katika utaratibu rasmi, hali inayosababisha zaidi ya asilimia 90 ya dhahabu inayozalishwa hapa nchini kutoroshwa na hivyo kusababisha Serikali kukosa mapato.
Wamezitaja tozo hizo kuwa ni kodi ya ongezeko la thamani (VAT) inayotozwa kwa asilimia 18, kodi ya zuio ya asilimia 5, kodi ya ukaguzi ya asilimia 1, ushuru wa huduma wa asilimia 0.3, mrahaba wa asilimia 6 na hivyo kufanya jumla ya tozo kuwa asilimia 30.3, na baadaye wanatozwa kodi ya kampuni kwa mwaka ambayo ni asilimia 30 ya faida.
Aidha, wadau hao wameomba wataalamu na viongozi wa madini wawe karibu na wachimbaji ili kujua uhalisia uchimbaji na biashara yake, kutafuta suluhisho la madini yaliyozuiliwa kusafirishwa nje ya nchi kutokana na kukosekana kwa mitambo ya kuchakatia, kupunguza gharama za leseni, kuanzisha vituo vya masoko ya madini, kupata bei elekezi ya madini ya viwanda na ujenzi na Benki Kuu ya Tanzania (BOT) kununua dhahabu.
Mhe. Rais Magufuli amesema Serikali itakuwa tayari kufanyia kazi mapendekezo ya wadau hao yenye lengo la kuongeza ukusanyaji wa mapato ikiwemo kupeleka Bungeni marekebisho ya sheria zinazohusu tozo za madini ili nchi iweze kunufaika na rasilimali hiyo, tofauti na sasa ambapo utoroshaji wa madini, ukwepaji wa kodi na wizi vinasababisha madini ya Tanzania kuzinufaisha nchi nyingine.
Amemtaka Waziri wa Madini Mhe. Doto Biteko kuhakikisha anachukua hatua za haraka za kufanya mabadiliko katika maeneo yote yaliyoonesha udhaifu ndani ya wizara hiyo ikiwemo kuwaondoa viongozi na wataalamu ambao wamekuwa chanzo cha upotevu wa mapato ya Serikali, kutafuta wawekezaji watakaojenga viwanda vya kuchenjua na kuchakata madini na kuanzisha vituo vya kuuzia madini.
Mhe. Rais Magufuli ametoa siku 30 kwa Waziri Biteko kuhakikisha ukuta wa kuzunguka madini ya Tanzanite wa Mererani unawekewa kamera za ulinzi na vifaa vya ukaguzi kwa wanaoingia na kutoka katika eneo hilo, pamoja na kuondoa sharti linalowataka vijana wenye ajira ndio waruhusiwe kuingia, hali iliyosababisha kuwepo malalamiko kuwa linasababisha vijana wasio na ajira kuingia kwa kuruka ukuta na kuwepo uhaba wa wachimbaji migodini.
Pia amemuagiza Waziri Biteko kuhakikisha maeneo yote ya madini ambayo yanashikiliwa na watu bila kufanyiwa kazi yananyang’anywa ili wapewe wachimbaji ambao wapo tayari kuchimba madini, kwa kutoa kipaumbele kwa wachimbaji wadogo na wa kati ambao wametajwa kufikia Milioni 6.
Mkutano huo umehudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Makamu wa Rais, Mhe. Samia Suluhu Hassan, Waziri wa Madini Mhe. Doto Biteko, Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Philip Mpango, Baadhi ya Wakuu wa Mikoa, Makatibu Wakuu, viongozi wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama, Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Viongozi wa Dini na viongozi wa vyama vya siasa.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
22 Januari, 2019
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 16 Januari, 2019 amekutana na kufanya mazungumzo na Rais Mstaafu wa Nigeria Mhe. Dkt. Olusegun Obasanjo Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Baada ya mazungumzo hayo Mhe. Dkt. Obasanjo amempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa kazi nzuri anayoifanya katika uongozi wake ikiwemo kupambana na rushwa, kuimarisha utoaji wa elimu, kuimarisha miundombinu, kuongeza nishati ya umeme, kuboresha usafiri wa ardhini na angani na jinsi wadau mbalimbali wa ndani na nje wanavyopaswa kuelewa juhudi zinazofanyika.
Mhe. Dkt. Obasanjo amesema Mhe. Rais Magufuli amedhihirisha kuwa kiongozi imara wa kusimamia mambo muhimu yenye maslahi kwa nchi yake na amebainisha kuwa licha ya kwamba maendeleo ya nchi hayapatikani mara moja lakini kwa muda mfupi Mhe. Rais Magufuli amefanya juhudi kubwa za kuimarisha maeneo ya huduma za kijamii, kukiimarisha chama chake cha siasa (Chama Cha Mapinduzi – CCM) na kwamba ameonesha kuwa anakijua anachokifanya katika maeneo ya uchumi.
“Tusijisahau kwamba ukoloni mamboleo bado upo na mabeberu bado wanaendelea kufanya juhudi za kuhakikisha wanatunyonya, na kiongozi yeyote wa Afrika anayethubutu kuwazui hawezi kuwa rafiki wa hao ambao walikuwa wakinufaika kwa kutunyonya” amesisitiza Mhe. Dkt. Obasanjo.
Mapema kabla ya kukutana na Mhe. Dkt. Obasanjo, Mhe. Rais Magufuli amepokea hati za utambulisho za Mabalozi watatu walioteuliwa kuziwakilisha nchi za Jamhuri ya Korea, Malawi na Brazil hapa nchini, baada ya waliokuwa Mabalozi wa nchi hizo kumaliza muda wao.
Waliowasilisha hati hizo ni Balozi wa Jamhuri ya Korea hapa nchini Mhe. Cho Tae-ics aliyechukua nafasi ya Mhe. Song Geum-young, Balozi wa Malawi hapa nchini Mhe. Glad Chembe Munthali aliyechukua nafasi ya Mhe. Hawa Olga Ndilowe na Balozi wa Brazil hapa nchini Mhe. Antonio Augusto Martins Cesar aliyechukua nafasi ya Mhe. Carlos Alfonso Iglesias Puente.
Mabalozi wote wamemhakikishia Mhe. Rais Magufuli kuwa katika kipindi chao watakahakikisha wanaendeleza na kukuza zaidi uhusiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na nchi hizo na matunda ya uhusiano na ushirikiano huo yanawanufaisha wananchi wa pande zote.
Mhe. Rais Magufuli amempongeza Mhe. Cho Tae-ics kwa kuteuliwa kuiwakilisha Jamhuri ya Korea hapa nchini na amemtaka apelekee salamu zake za shukrani kwa Rais wa Korea Mhe. Moon Jae-in kwa ushirikiano mzuri ambao Tanzania inaupata kutoka Korea ikiwemo kujengwa kwa miundombinu kama vile Daraja la Kikwete lililopo mto Malagarasi Mkoani Kigoma, Hospitali ya Mafunzo na Tiba Mloganzila na Daraja la Tanzanite linalounganisha ufukwe wa Aga Khan na Coco Beach Jijini Dar es Salaam, na pia amemuomba kushiriki katika ujenzi wa miundombinu ya Makao Makuu Jijini Dodoma ili kuweka alama ya ushirikiano kati ya Tanzania na Korea.
Kwa Mhe. Glad Chembe Munthali, Mhe. Rais Magufuli amemuomba afikishe salamu zake kwa Rais wa Malawi Mhe. Prof. Arthur Peter Muthalika na kumhakikishia kuwa Tanzania itadumisha na kukuza zaidi uhusiano wa kirafiki na kidugu uliopo kati yake na Malawi na kwamba endapo Malawi itahitaji kununua chakula, Tanzania ipo tayari wakati wowote kutoa chakula hicho.
Mhe. Rais Magufuli amemtaka Balozi wa Brazil hapa nchini Mhe. Antonio Augusto Martins Cesar kufikisha salamu zake kwa Rais wa Brazil Mhe. Jair Bolsonaro na kumshukuru kwa ushirikiano mzuri uliopo kati ya Brazil na Tanzania na pia ameiomba nchi hiyo ishiriki katika uzalishaji wa nishati ya umeme kwa ajili ya kuendeleza viwanda hapa nchini ikiwemo kuwekeza katika mradi wa kuzalisha umeme katika mto Luhuji Mkoani Njombe wenye uwezo wa kuzalisha Megawatts kati ya 350 na 400.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
16 Januari, 2019
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 15 Januari, 2019 ameshuhudia utiaji saini wa makubaliano kati ya Serikali ya Tanzania na kampuni ya Bharti Airtel ya India juu ya umiliki wa hisa za kampuni Airtel Tanzania na maslahi mengine ya Tanzania kutokana na biashara ya kampuni hiyo.
Hafla ya utiaji saini makubaliano hayo imefanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam ambapo Waziri wa Katiba na Sheria Prof. Palamagamba Kabudi ametia saini kwa niaba ya Serikali ya Tanzania na Mwenyekiti wa Bharti Airtel Bw. Sunil Mittal ametia saini kwa niaba ya kampuni ya Bharti Aitel.
Waziri wa Katiba na Sheria Prof. Kabudi amesema katika makubaliano hayo kampuni ya Bharti Airtel imekubali kupunguza umiliki wa hisa zake za kampuni ya simu za mkononi ya Airtel Tanzania kutoka asilimia 60 hadi 51 na hivyo kuongeza hisa za Serikali kutoka asilimia 40 hadi 49 bila malipo yoyote kutoka Serikalini.
Prof. Kabudi amebainisha maeneo mengine ya makubaliano kuwa ni Serikali kupata gawio la kila mwaka kutokana na umiliki wake wa asilimia 49 ambapo inakadiriwa itakuwa ikipata shilingi Bilioni 10, kufutwa kwa madeni yote ya kampuni ya Airtel yaliyokuwa yamefikia shilingi Trilioni 1, Bharti Airtel itatoa shilingi Bilioni 1 kila mwezi kwa kipindi cha miaka 5 kuanzia Aprili 2019 ili kuonesha nia njema na Bharti Airtel itatoa shilingi Bilioni 2.3 kwa ajili ya kuchangia huduma za kijamii.
Maeneo mengine ya makubaliano ni Bodi ya Wakurugenzi wa Airtel Tanzania kuundwa na wajumbe 7 ambapo Serikali ya Tanzania itawakilishwa na wajumbe 3 (akiwemo Mwenyekiti atakayeteuliwa na Serikali) na Bharti Airtel itawakilishwa na wajumbe 4, Menejimenti ya Airtel Tanzania itaongozwa na Bharti Airtel lakini Afisa Mkuu wa Ufundi atateuliwa na Serikali ya Tanzania, pande zote mbili zitashirikiana kuandaa upya nyaraka muhimu za kusaidia uendeshaji wa kampuni, pande zote mbili zitashirikiana kuongeza tija na ufanisi wa Airtel Tanzania na pande zote mbili zitashirikiana kutumia miundombinu ya Shirika la Simu Tanzania (TTCL) ikiwa kuna hoja za kibiashara.
Kwa upande wake Bw. Sunil Mittal amesema amefurahishwa na kufikiwa kwa makubaliano katika mazungumzo hayo na amebainisha kuwa awali aliona kuna ugumu wa kufikia makubaliano lakini baadaye alielewa kuwa lengo la Mhe. Rais Magufuli ni kuhakikisha anaweka mwelekeo mzuri wenye manufaa kwa Tanzania.
Bw. Mittal ameongeza kuwa makubaliano hayo yameandika historia mpya kwa hisa nyingi kumilikiwa na Watanzania katika kampuni ya Airtel Tanzania na kwamba anatarajia kuwa Airtel Tanzania itaendelea kufanya vizuri katika soko la Tanzania ambayo ni nchi yenye uwekezaji mkubwa wa Bharti Airtel Barani Afrika.
Akizungumza baada ya kushuhudia utiaji saini makubaliano hayo Mhe. Rais Magufuli ameipongeza timu iliyoiwakilisha Serikali ya Tanzania chini ya Prof. Kabudi na timu ya Bw. Mittal kwa kufikia makubaliano hayo yaliyochukua muda wa miezi 8 na ameelezea furaha yake kuwa sasa Airtel Tanzania itaanza kutoa manufaa kwa Serikali ikiwemo gawio na maslahi mengine yanayostahili, mambo ambayo hayakufanyika kwa miaka zaidi ya 8 tangu kampuni hiyo ianzishwe hapa nchini.
Amempongeza Bw. Mittal kwa kuridhia kuongeza hisa za Serikali, kutoa shilingi Bilioni 1 kila mwezi kwa miaka 5 na kutoa mchango wa Shilingi Bilioni 2.3 ambazo ameagiza ziungane na shilingi Bilioni 1 iliyotengwa kwa ajili ya sherehe za siku ya Uhuru za mwaka 2018 (na kufanya jumla shilingi Bilioni 3.3) kwenda kujenga hospitali katika makao makuu ya nchi Jijini Dodoma.
“Huu ndio uwekezaji ninaoutaka, uwekezaji ambao tuna faida nao, Airtel ilikuwepo tangu miaka 8, 9 iliyopita lakini tulikuwa hatupati kitu, sasa tutapata fedha, na hili liwe somo kwetu Watanzania wote kuwa Serikali inapotetea maslahi ya Watanzania haizungumzi kutoka hewani, tujifunze kuwaheshimu watalaamu wetu” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Mhe. Rais Magufuli amemhakikishia Bw. Mittal na wawekezaji wote hapa nchini kuwa Tanzania ni nchi nzuri ya kuwekeza na itadumisha utamaduni wa kuboresha mazingira ya uwekezaji kwa kutambua kuwa uwekezaji huo unasaidia kuzalisha ajira na kuiwezesha Serikali kupata mapato.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
15 Januari, 2019
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ameagiza kusitishwa mara moja kwa zoezi la kuviondoa vijiji na vitongoji vinavyodaiwa kuwepo katika maeneo ya hifadhi na amewataka viongozi wa wizara zote zinazohusika kukutana ili kubainisha na kuanza mchakato wa kurasimisha maeneo ya vijiji na vitongoji hivyo.
Mhe. Rais Magufuli ametoa agizo hilo tarehe 15 Januari, 2019 Ikulu Jijini Dar es Salaam alipokutana na Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Dkt. Hamis Kigwangallah, Katibu Mkuu Kiongozi Mhe. Balozi John Kijazi, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhandisi Joseph Nyamhanga na Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Bi. Dorothy Mwanyika.
Pamoja na agizo hilo Mhe. Rais Magufuli ametaka viongozi wa wizara husika kubainisha maeneo ya hifadhi za wanyamapori na misitu ambayo hayana wanyamapori ama misitu ili yagawiwe kwa wafugaji na wakulima ambao kwa sasa wanataabika kupata maeneo ya kufugia wanyama na kuzalisha mazao.
Mhe. Rais Magufuli pia ameitaka Wizara ya Maliasili na Utalii kuangalia upya zoezi la uwekaji wa mipaka ya hifadhi na makazi, na kutumia busara katika uwekaji wa mawe ya mipaka hiyo ili kutowaondoa wananchi katika maeneo ambayo hayana ulazima wa kuwaondoa.
“Mimi sifurahii kuona wafugaji kila mahali wanafukuzwa, kama kuna eneo ambalo tunafikiri lilikuwa hifadhi ya wanyama lakini halitumiki, tutabadilisha sheria, tunalimega na tunaligawa kwa wafugaji, vivyo hivyo hata kwa wakulima kama kuna eneo tunaona ni hifadhi lakini halina msitu wala wanyamapori, na lina rutuba, na wakulima wanataka kulima nalo tunalimega tunawapa wakulima.
Baadaye tutajua kabisa eneo hili ni la hifadhi, hili ni la mifugo, hili ni la wakulima, hili ni la makazi. Kwa hiyo nyinyi Mawaziri na Makatibu Wakuu mkakae mkatangulize maslahi ya hawa tunaowaongoza ambao ni wakulima, wafugaji, wavuvi nakadhalika, lakini pia tunahitaji wanyamapori, sijasema sasa hifadhi zote za wanyama tunazimaliza, hapana, hifadhi za wanyama lazima tuzihifadhi” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Mhe. Rais Magufuli ameagiza vijiji vyote 366 vilivyoainishwa kuwepo ndani ya maeneo ya hifadhi hapa nchini visiondolewe katika maeneo hayo na badala yake ametoa mwezi mmoja kwa viongozi wa wizara zote zinazohusika kubainisha maeneo ya vijiji hivyo na kuanzisha mchakato wa mabadiliko ya sheria ili yawasilishwe katika kikao kijacho cha Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Amefafanua kuwa ni lazima Serikali ifanye maamuzi haya sasa kwa kuwa idadi ya Watanzania imeongezeka hadi kufikia Milioni 55, idadi ya mifugo imeongeza hadi kufikia Milioni 35 na hivyo kuna ongezeko kubwa la mahitaji ya maeneo ya ardhi ikilinganishwa na wakati nchi inapata uhuru ambapo Watanzania walikuwa Milioni 9 na mifugo ilikuwa Milioni 10.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli ameagiza sheria ya vyanzo vya maji pia iangaliwe upya ili kutowazuia Watanzania wanaozalisha mazao kandokando mwa mito na ameelezea kutofurahishwa kwake na vitendo vya kufyeka mazao ya wakulima kwa madai kuwa wamelima ndani ya mita 60.
Halikadhalika Mhe. Rais Magufuli ameipongeza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kuwasilisha kwake mapendekezo ya kufutwa kwa mashamba ambayo hayajaendelezwa na ameagiza wizara hiyo iendelee kumpelekea mapendekezo ya mashamba yote yaliyotelekezwa ili ayafute na wananchi wagawiwe kwa ajili ya kuyatumia kwa uzalishaji wa mazao na mifugo.
Hata hivyo Mhe. Rais Magufuli amesema maagizo hayo hayana maana kuwa sasa wananchi waruhusiwe kuvamia maeneo ya hifadhi, na ametaka zoezi la uwekaji wa mipaka lifanyike haraka na kwa uwazi.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
15 Januari, 2019
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 11 Januari, 2019 ameongoza mapokezi ya ndege mpya aina ya Airbus A220-300 iliyonunuliwa na Serikali ya Tanzania kwa ajili ya kuimarisha huduma za usafiri wa anga kupitia Shirika la Ndege Tanzania (ATCL).
Ndege hiyo ni ya pili ya aina ya Airbus 220-300 kununuliwa na Serikali kwa ajili ya ATCL na ni ndege ya 6 kuwasili hapa nchini kati ya ndege 7 ambazo Serikali ya Awamu ya Tano imezinunua kwa lengo la kuimarisha usafiri wa anga, kukuza utalii, kuimarisha mazingira ya biashara na uwekezaji na kukuza uchumi wa nchi.
Sherehe za mapokezi ya ndege hiyo zimefanyika katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere (Terminal One) Jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, Naibu Spika Mhe. Dkt. Tulia Ackson, Balozi wa Canada hapa nchini Mhe. Pamela O’donnel, Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dkt. Bashiru Ally Kakurwa, Mawaziri, Makatibu Wakuu, Wabunge, viongozi wa Dini, viongozi wa siasa, wafanyabiashara, viongozi na wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa huo Mhe. Paul Makonda.
Akizungumza baada ya kuipokea na kuizindua ndege hiyo, Mhe. Rais Magufuli amewapongeza Watanzania wote kwa mafanikio makubwa yaliyopatikana kwa kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wake ikiwemo kununua ndege 7 zilizowezesha kuimarishwa kwa ATCL pamoja kutekelezwa kwa miradi mikubwa kama vile ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa (standard gauge) na mradi wa kuzalisha umeme katika mto Rufiji, na kwamba kwa mwendo huu mambo mengine mengi makubwa yanakuja.
Mhe. Rais Magufuli amempongeza Mkurugenzi Mtendaji wa ATCL Mhandisi Ladislaus Matindi na wafanyakazi wote wa ATCL kwa kazi nzuri wanayofanya wakiwemo Marubani vijana wa Kitanzania watatu walioendesha ndege hiyo kutoka Montreal nchini Canada hadi Jijini Dar es Salaam Tanzania, na amebainisha kuwa hayo ni matunda ya kununua ndege mpya na kuimarisha ATCL.
“Tumeambiwa hapa tangu tuanze kununua ndege hizi ATCL imeongeza idadi ya Marubani kutoka 11 hadi 50, walioajiriwa ni vijana wetu wa Kitanzania, na kwa ujumla wafanyakazi wapya wa ATCL walioajiriwa ni 380, hivi kama tusingenunua ndege hizi vijana hawa wangeendesha nini? Wangeendesha matoroli? Lakini sasa wamepata ajira wananufaika wao na familia zao au jamaa zao” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Mhe. Rais Magufuli amesisitiza kuwa ndege hizi zote zimenunuliwa kwa fedha za Watanzania kwa asilimia 100, na amewataka Watanzania wote kuelewa kuwa maendeleo ya Tanzania yataletwa na Watanzania wenyewe na kwamba hakuna nchi yoyote duniani iliyoendelea kwa kutegemea misaada.
“Tunahitaji misaada lakini iwe ni misaada ya kutuwezesha kusonga mbele kimaendeleo na kujitegemea na sio kutulemaza, sekta binafsi pia tunaihitaji lakini iwe ni sekta binafsi ya manufaa kwa Taifa.
Hata leo amekuja mwenyekiti wa Bharti Airtel, tumezungumza na amekubali kuongeza hisa za Serikali katika airtel kutoka 40 hadi 49 na kupunguza hisa kwenye kampuni yake kutoka asilimia 60 hadi 51 bila kutudai malipo yoyote, pia Airtel itatoa gawio kwa Serikali wakati miaka minane yote ya nyuma haikuwahi kutoa hata senti tano” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli ameagiza ndege mbili za Serikali (Fokker 28 na Fokker 50) zilizokuwa zikitumiwa kusafirisha viongozi zipigwe rangi za ATCL na kuanza kusafirisha abiria ili kuiongezea uwezo ATCL na kuwawezesha Watanzania wote kupata huduma za usafiri wa anga.
Mapema Naibu Spika Mhe. Tulia Ackson ameipongeza Serikali kwa juhudi kubwa za kuimarisha usafiri wa anga kwa kununua ndege mpya, na amefafanua kuwa anafurahi kuona matunda ya fedha zinazopitishwa na Bunge katika bajeti.
Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kuongoza juhudi za kuleta mageuzi ya kiuchumi hapa nchini na amemhakikishia kuwa Watanzania wanamuunga mkono na wapo tayari kuhakikisha nchi yao inasonga mbele.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
11 Januari, 2019
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 11 Januari, 2019 amekutana na Mwenyekiti wa kampuni ya Bharti Airtel Bw. Sunil Mittal, Ikulu Jijini Dar es Salaam ambapo wamezungumzia maendeleo ya mazungumzo ya umiliki wa hisa za kampuni ya simu za mkononi ya Airtel Tanzania.
Baada ya mazungumzo hayo Bw. Sunil Mittal amesema kampuni yake imekubali kuongeza hisa zinazomilikiwa na Serikali ya Tanzania katika kampuni ya Airtel Tanzania kutoka asilimia 40 hadi asilimia 49 na hivyo kupunguza hisa zilizokuwa zikimilikiwa na Bharti Airtel kutoka asilimia 60 hadi asilimia 51.
Bw. Sunil Mittal ameongeza kuwa mazungumzo kati ya kampuni yake na Serikali ya Tanzania yanakwenda vizuri na kwamba kampuni ya Bharti Airtel imeridhishwa na makubaliano yaliyofikiwa katika masuala yaliyokuwa yakijadiliwa yenye lengo la kuiimarisha kampuni ya Airtel, kuleta manufaa kwa pande zote mbili na kuboresha huduma za mawasiliano za kampuni hiyo.
Kwa upande wake Mhe. Rais Magufuli ameelezea kufurahishwa kwake na hatua iliyofikiwa katika mazungumzo hayo ambapo pamoja na kuongeza hisa za Serikali katika umiliki wa Airtel Tanzania, kampuni hiyo imekubali kutoa gawio kwa Serikali ya Tanzania mara baada ya mazungumzo hayo kukamilika hivi karibuni.
“Masuala mengine ya kumalizia mazungumzo haya yataendelea leo ili kumalizia, lakini jambo zuri ni kuwa sasa wamekubali kutoa gawio kwa Serikali ambapo kwa muda wa miaka minane hadi kumi tulikuwa hatujapata gawio, kiasi cha asilimia za gawio nacho watajadili leo, kwa hiyo mimi naona huu ni mwanga mzuri wa kwenda mbele kati ya kampuni ya Bharti Airtel na Serikali ya Tanzania pamoja na kampuni zingine” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Kwa upande wa Tanzania timu ya majadiliano na kampuni ya Bharti Airtel inaongozwa na Waziri wa Katiba na Sheria Prof. Palamagamba Kabudi.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
11 Januari, 2019
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 09 Januari, 2019 amewaapisha viongozi aliowateua jana pamoja na wajumbe wa Tume ya Utumishi wa Umma aliwateua hivi karibuni.
Hafla ya kuapishwa kwa viongozi hao imefanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job Yustino Ndugai, Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, Katibu Mkuu Kiongozi Mhe. Balozi John Kijazi, Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dkt. Bashiru Ally Kakurwa, Mawaziri na Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu Wakuu, viongozi wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama, viongozi wa Dini na viongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa huo Mhe. Paul Makonda.
Walioapishwa ni Mhe. Doto Mashaka Biteko – Waziri wa Madini, Bi. Zainab Abdi Seraphine Chaula – Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto (Afya), Bi. Dorothy Aidani Mwaluko – Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Uwekezaji), Arch. Elius Asangalwise Mwakalinga – Katibu Mkuu Ujenzi, Bw. Faustine Rweshabura Kamuzora – Katibu Tawala Mkoa wa Kagera, Bi. Dorothy Onesphoro Gwajima – Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) anayeshughulikia afya na Bw. Faustine Kasabubu Michael – Naibu Katibu Mkuu Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.
Wajumbe wa Tume ya Utumishi wa Umma walioapishwa ni Mwenyekiti wa Tume Mhe. Jaji Mstaafu Steven James Bwana, na Makamishna 6 ambao ni Bw. George Daniel Yambesi, Bw.Yahaya Fadhili Mbila, Bi. Hadija Ali Mohamed Mbaraka, Bi. Immaculate Peter Ngwale, Bw. Daniel Ole Njoolay na Bw. John Michael Haule.
Akizungumza baada ya kuwaapisha viongozi hao, Mhe. Rais Magufuli amewapongeza kwa kushika nyadhifa hizo na amewataka kwenda kutekeleza majukumu yao kwa kutanguliza maslahi ya Watanzania wote.
Mhe. Rais Magufuli pia amewapongeza viongozi na watendaji mbalimbali wa Serikali na kueleza kuwa wanafanya kazi kubwa na nzuri huku akibainisha kuwa anatambua kuwa baadhi yao wanashindwa hata kwenda likizo kutokana na kukabiliwa na majukumu mazito ya kuwahudumia wananchi.
Hata hivyo Mhe. Rais Magufuli ameelezea kutorishwa na utendaji wa Wizara ya Madini hususani katika udhibiti wa utoroshaji wa madini na hivyo amemtaka Waziri aliyeteuliwa Mhe. Biteko na taasisi zilizo chini ya wizara yake kushirikiana na Wizara ya Fedha na Mipango na Benki Kuu ya Tanzania kuanzisha vituo vya ununuzi wa madini ili kudhibiti utoroshaji na kuiwezesha Benki Kuu kuwa na hifadhi ya dhahabu.
“Tumewaruhusu wawekezaji na wachimbaji wadogo wachimbe dhahabu, Je Wizara ya Madini mmeshajiuliza dhahabu inayochimbwa inauzwa wapi? Na je kama wanachimba na wanauza sisi tunapata asilimia ngapi? Hili suala ni la Wizara ya Madini, halikuwa suala la Bunge kujiuliza, wala halikuwa suala la Waziri Mkuu au Rais kujiuliza.
“Kwenye sheria ya madini nina hakika kuna mahali imeelekeza kuanzishwa kwa vituo vya kuuzia madini, je vimeanzishwa vituo vingapi? viko wapi? Kwa sababu vingeanzishwa vituo hivi tungejua dhahabu inayosafirishwa, wapi imeuzwa na inawezekana tungekuwa na taarifa za kila wiki, lakini hakuna” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli amempongeza Inspekta Jenerali wa Polisi Simon Sirro kwa kazi nzuri iliyofanywa na Jeshi la Polisi kukamata zaidi ya kilogramu 300 za dhahabu Mkoani Mwanza na ametaka Askari Polisi 8 wanaotuhumiwa kujihusisha na vitendo vya rushwa wakati wa ukamataji wa dhahabu hiyo wachukuliwe hatua za kisheria.
Mhe. Rais Magufuli amewaonya viongozi wa Serikali ambao wamekuwa wakilumbana badala ya kufanya kazi na amesema vitendo hivyo vikiendelea hatasita kutengua uteuzi wao na kuteua viongozi wengine watakaofanya kazi bila malumbano.
Mapema wakitoa salamu, Spika wa Bunge Mhe. Job Yustino Ndugai na Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamisi Juma wamewapongeza viongozi walioteuliwa na wamewataka kwenda kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na kwa kasi ya Serikali ya Awamu ya Tano, na kwamba Bunge na Mahakama zitatoa ushirikiano kwao.
Nae Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa amewapongeza viongozi walioteuliwa na kubainisha kuwa Serikali inaamini kuwa wataongeza nguvu katika utekelezaji wa ahadi ambazo imewaahidi wananchi hadi kufikia 2020.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
09 Januari, 2019
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 08 Januari, 2019 amefanya mabadiliko madogo katika Baraza la Mawaziri na kufanya uteuzi wa viongozi mbalimbali wa wizara na taasisi za Serikali.
Uteuzi wa viongozi hao uliotangazwa na Katibu Mkuu Kiongozi Mhe. Balozi John Kijazi, Ikulu Jijini Dar es Salaam ni kama ifuatavyo;
- Mhe. Rais Magufuli amemteua Mhe. Anjellah Kairuki kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Uwekezaji.
Mhe. Rais Magufuli amefanya uteuzi wa Waziri anayeshughulikia masuala ya uwekezaji kwa lengo la kuongeza msukumo na kuimarisha usimamizi wa masuala ya uwekezaji hasa baada ya kuamua Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kihamishiwe Ofisi ya Waziri Mkuu.
Kabla ya uteuzi huo Mhe. Kairuki alikuwa Waziri wa Madini.
- Mhe. Rais Magufuli amemteua Mhe. Doto Biteko kuwa Waziri wa Madini. Kabla ya uteuzi huo Mhe. Biteko alikuwa Naibu Waziri wa Madini.
Kufuatia uteuzi huo Wizara ya Madini sasa itakuwa na Naibu Waziri mmoja ambapo Mhe. Stanslaus Nyongo anaendelea na wadhifa wake.
- Mhe. Rais Magufuli amemteua Mhandisi Joseph Nyamuhanga kuwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).
Kabla ya uteuzi huo Mhandisi Nyamuhanga alikuwa Katibu Mkuu Ujenzi, na anachukua nafasi ya Mhandisi Mussa Iyombe ambaye amestaafu.
- Mhe. Rais Magufuli amemteua Dkt. Zainabu Chaula kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto (anayeshughulikia afya). Kabla ya Uteuzi huo Dkt. Chaula alikuwa Naibu Katibu Mkuu TAMISEMI (afya).
- Mhe. Rais Magufuli amemteua Arch. Elius Mwakalinga kuwa Katibu Mkuu Ujenzi. Kabla ya uteuzi huo Arch. Mwakalinga alikuwa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) na anachukua nafasi ya Mhandisi Nyamuhanga ambaye ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu TAMISEMI.
- Mhe. Rais Magufuli amemteua Bi. Dorothy Mwaluko kuwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Uwekezaji). Kabla ya Uteuzi huo Bi. Mwaluko alikuwa Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.
- Mhe. Rais Magufuli amemteua Dkt. Dorothy Gwajima kuwa Naibu Katibu Mkuu TAMISEMI (Afya). Kabla ya uteuzi huo Dkt. Gwajima alikuwa Mkurugenzi wa Tiba wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.
- Mhe. Rais Magufuli amemteua Dkt. Francis K. Michael kuwa Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora. Kabla ya uteuzi huo Dkt. Francis K. Michael alikuwa Mhandiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
- Mhe. Rais Magufuli amemteua Dkt. Mpoki Ulisubisya kuwa Balozi.
Kabla ya uteuzi huo Dkt. Ulisubisya alikuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto (akishughulikia afya). Kituo cha kazi cha Dkt. Ulisubisya kitatangazwa baadaye.
- Mhe. Rais Magufuli amemteua Prof. Faustin Kamuzora kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera.
Kabla ya Uteuzi huo Prof. Kamuzora alikuwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera na Uratibu na anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Bw. Athumani Diwani Msuya ambaye ameteuliwa kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).
Uapisho wa viongozi hao utafanyika kesho tarehe 09 Januari, 2019 saa 3:30 asubuhi, Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli ameifuta nafasi ya Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ulinzi. Nafasi hiyo ilikuwa inashikiliwa Bi. Immaculate Ngwalle ambaye amestaafu.
Katika hatua nyingine, Mhe. Rais Magufuli amefanya uamuzi wa kufungua Ubalozi Mpya wa Tanzania nchini Cuba. Balozi wa Tanzania nchini Cuba atateuliwa baadaye.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
08 Januari, 2019
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amewatakia heri ya Mwaka Mpya wa 2019 Watanzania wote na kuwaomba wadumishe umoja, amani na upendo waliouonesha katika mwaka 2018.
Akizungumza kutoka nyumbani kwake Ikulu Jijini Dar es Salaam, Mhe. Rais Magufuli amesema mwaka 2018 ulikuwa wa mafanikio makubwa kwa Watanzania na anatarajia kuwa mwaka 2019 utakuwa wa mafanikio zaidi kulingana na mipango ambayo nchi imejipangia kuitekeleza.
Mhe. Rais Magufuli amewataka watumishi wa umma, viongozi, wakulima, wafanyabiashara, wavuvi na wafugaji kuongeza juhudi za uzalishaji mali katika mwaka 2019 huku wakipiga vita rushwa, wizi, ufisadi, ubadhilifu na kwamba anaamini kuwa uchumi wa Tanzania utazidi kupanda katika mwaka 2019.
“Ujumbe wangu kwa watumishi wa umma, ni kama nilivyotoa ujumbe kwa Watanzania wengine, wachape kazi, wajiamini, waachane na utamaduni wa kila kitu wanachokifanya kudai ni maagizo kutoka juu, huo ni ugonjwa ambao umeanza kuwapata watumishi wa umma ambapo kila wanalolifanya hata kama ni kwa mujibu wa sheria hawataki kujiamini, na wanasema hili ni maagizo kutoka juu” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Amemalizia kwa kusema “Ninaanza kuiona Tanzania mpya inakuja, tusiiachie Tanzania mpya, tuifike, tuikae na tuiishi kwa sababu huu ndio wakati wa kuijenga Tanzania mpya, nina imani kubwa sana Mungu wetu atatusaidia, mwaka 2019 mengi mazuri yatafanyika, kikubwa ni mshikamano wetu sote Watanzania, niwaombe Watanzania wote wa rika zote, wa dini zote, wa makabila yote, mshikamano waliouonesha kwa mwaka 2018 katika Serikali, wauoneshe tena mwaka 2019, na ikiwezekana wauoneshe zaidi na zaidi kwa kutanguliza zaidi uzalendo na Utanzania wetu, tutafanikiwa, Mungu ni mwema, Mungu ibariki Tanzania, Mungu wabariki Watanzania wote na Mungu ubariki mwaka 2019.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
31 Desemba, 2018
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 04 Januari, 2019 ameshuhudia utiaji saini wa mkataba wa mauziano ya mahindi kati ya Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) na Shirika la Chakula Duniani (WFP) uliofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Mkataba huo umetiwa saini na Kaimu Mtendaji Mkuu wa NFRA Bi. Vumilia Zikankuba na Mwakilishi na Mkurugenzi Mkazi wa WFP hapa nchini Bw. Michael Danford, ambapo WFP itanunua tani 36,000 zenye thamani ya shilingi Bilioni 21 kutoka NFRA.
Baada ya kutia saini mkataba huo Bw. Michael Danford amesema mahindi hayo ni sehemu ya tani 160,000 za chakula zenye thamani ya shilingi Bilioni 132.2 zilizonunuliwa na WFP nchini Tanzania katika mwaka 2018, ikiwa ni ongezeko la kutoka shilingi Bilioni 63.6 zilizotumika kununua chakula katika mwaka 2017.
Bw. Michael Danford amebainisha kuwa kutokana na uhusiano mzuri wa Tanzania na WFP uliodumu kwa miaka 40 sasa, mwaka 2017 shirika hilo liliweka mpango mkakati unaoendana na Mpango wa Maendeleo wa Tanzania, ambapo limeamua kuwa mnunuzi mkubwa wa mazao ya chakula nchini Tanzania kwa ajili ya kusaidia wakimbizi na nchi jirani zenye matatizo ya chakula na kwamba WFP inatarajia kuendelea kuongeza kiwango cha chakula kitakachokuwa kikinunuliwa kutoka Tanzania.
Ameahidi kuwa WFP itaendelea kufanya kazi kwa karibu na NFRA na taasisi zingine zinazohusika katika ununuzi wa chakula ikiwemo Shirika la Reli Tanzania (TRC) ambako imetoa msaada wa kuliboresha ili kuhakikisha usafirishaji wa mazao unafanyika vizuri.
Pamoja na kushuhudia utiaji saini wa mkataba huo Mhe. Rais Magufuli ameiagiza Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali za Serikali zikiwemo Jeshi la Polisi, Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Shirika la Reli Tanzania (TRC) na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) kuhakikishia wanaondoa urasimu na kuharakisha ununuzi wa mazao yanayonunuliwa na WFP (ikiwemo tani hizo 36,000 za mahindi) ili wakulima wa Tanzania wanufaike na fursa hiyo.
Mhe. Rais Magufuli ameipongeza WFP kwa uamuzi wake wa kununua chakula kutoka Tanzania kwa ajili ya kusaidia wakimbizi na nchi zenye matatizo ya chakula na ameitaka NFRA kutoa tani zote 45,000 za mahindi ambazo WFP waliomba kununua, ili fedha zitakazopatikana zitumike kununua mahindi mengine kutoka kwa wakulima.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli ameitaka NFRA kujipanga vizuri katika shughuli zake ili kuondokana na utaratibu wa kuwa inapatiwa fedha kutoka Serikalini kila mwaka kwa ajili ya kununua mazao ya hifadhi ya chakula, ilihali mazao yaliyopo hifadhini yakiuzwa kiujanjaujanja kwa wafanyabiashara tena kwa bei ya kutupa.
“Nyinyi NFRA wapeni hawa WFP tani zote 45,000 wanazozihitaji, na hata wakihitaji tani 100,000 wapeni au hata 200,000 wapeni, mkipata hizo fedha nendeni mkanunue mazao ya wakulima wanaohangaika na soko. Lakini pia punguzeni matumizi makubwa ya fedha za kugharamia zoezi la ununuzi wa mazao” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Pia Mhe. Rais Magufuli amewataka wafanyabiashara kuacha kulalamika na badala yake wafanye biashara zao kwa uwazi na kwamba Serikali itawaunga mkono.
Mapema Naibu Waziri wa Kilimo Mhe. Innocent Bashungwa amesema wizara imechukua hatua kadhaa za kuimarisha mazingira kwa WFP kununua mahindi na mazao mengine hapa nchini, na kwamba jambo hilo linafanywa sambamba na mkakati wa kufungamanisha kilimo na viwanda na kuimarisha ushirika ili kupanua zaidi uwigo wa soko la mazao ya wakulima.
Hafla ya utiaji saini mkataba huo imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Naibu Waziri wa Kilimo Mhe. Omary Mgumba, Naibu Waziri wa Ujenzi Mhe. Elias Kwandikwa, Makatibu Wakuu, viongozi wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama na wakuu wa taasisi mbalimbali.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
04 Januari, 2019
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 28 Desemba, 2018 ametengua uteuzi wa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) Dkt. Irene Isaka.
Uteuzi wa Mkurugenzi Mkuu wa SSRA utafanywa baadaye.
Dkt. Irene Isaka atapangiwa kazi nyingine.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
28 Desemba, 2018
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 23 Desemba, 2018 amewaongoza Watanzania kuipokea ndege mpya aina ya Airbus A220-300 iliyonunuliwa na Serikali kwa lengo la kuimarisha huduma za usafiri wa anga kupitia Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL).
Ndege hiyo (A220-300) ni kati ya ndege 2 za aina hiyo zilizonunuliwa na Serikali ya Tanzania kwa kutumia fedha za ndani na ndege ya pili inatarajiwa kuwasili hapa nchini wiki 2 zijazo kutoka nchini Canada ambako zinatengenezwa.
Sherehe ya mapokezi ya ndege hiyo imefanyika katika kituo namba 1 (terminal one) cha Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Mke wa Rais Mhe. Mama Janeth Magufuli, Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, Spika wa Bunge Mhe. Job Yustino Ndugai, Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, Mawaziri na Naibu Mawaziri, Balozi wa Canada hapa nchini Mhe. Pamela O’Donnel, Wabunge, Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu Wakuu, viongozi wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama, viongozi wakuu wa taasisi za umma na binafsi, viongozi wa Dini, viongozi wa vyama vya siasa na viongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa huo Mhe. Paul Makonda.
Kuwasili kwa ndege hiyo (A220-300) kunafanya jumla ya ndege zilizowasili nchini tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani kufikia 5 kati ya ndege 7 zilizonunuliwa.
Akizungumza na Watanzania muda mfupi kabla ya ndege hiyo kuwasili, Mhe. Rais Magufuli amesema Serikali inatekeleza kwa vitendo Ilani ya Uchaguzi Mkuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2015 ambayo inaelekeza kuimarishwa kwa usafiri wa anga na ameagiza kununuliwa kwa ndege ya 8 aina ya Bombardier Dash 8-Q400 ili kutimiza lengo la mpango wa Maendeleo wa ATCL la kufikia ndege 8 ifikapo mwaka 2021/22.
Mhe. Rais Magufuli amewapongeza Watanzania wote, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, ATCL, Wabunge na wadau wengine wote kwa mafanikio ya kununua ndege hiyo na ametoa wito kwa Watanzania kuendelea kulipa kodi ili Serikali iweze kutekeleza mipango mingine mingi ya kuliendeleza Taifa.
Amefafanua kuwa kutokana na kodi Serikali imeweza kununua ndege, kujenga barabara nyingi na nyingine zinaendelea kujengwa, kujenga njia mpya ya reli ya kati na kufufua reli za zamani, kujenga meli mpya na kukarabati meli za zamani, kupanua viwanja vya ndege vya kimataifa vya Dar es Salaam (JNIA) na Kilimanjaro (KIA), kukarabati viwanja vya 11 nchini na kupanua bandari.
Pamoja na kuipongeza ATCL kwa kuzalisha faida ya shilingi Bilioni 28 tangu ianze kupatiwa ndege mpya na Serikali Oktoba 2016, Mhe. Rais Magufuli amelitaka shirika hilo kuhakikisha linazalisha faida na kushughulikia mapungufu yaliyoanza kujitokeza ikiwemo hujuma katika ukatishaji wa tiketi.
Aidha Mhe. Rais Magufuli ameagiza viongozi na wafanyakazi wa Serikali ambao waliwahi kukatiwa tiketi kwa kulipiwa na Serikali na hawakusafiri, kurejesha Serikalini fedha hizo mara moja na ametaka apewe orodha ya viongozi na wafanyakazi hao (wanaokadiriwa kuwa takribani 100).
Halikadharika Mhe. Rais Magufuli amesema Serikali inaendelea kuimarisha Chuo cha Usafirishaji (NIT) ikiwemo kukinunulia ndege 5 kwa ajili ya mafunzo kwa marubani na wahandisi, ikiwa ni juhudi za kuhakikisha nchi inakuwa na marubani na wahandisi wa kutosha pamoja na kujenga uwezo wa kufanya matengenezo ya ndege hapa hapa nchini kupitia karakana ya ndege iliyopo KIA.
Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli ametoa shilingi Milioni 10 kwa Kepteni Mstaafu Narzis Peter Mapunda aliyekuwa rubani wa kwanza wa ndege za ATC na ambaye wakati wa kuvunjika kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki alionesha uzalendo mkubwa wa kuirejesha hapa Tanzania moja ya ndege za shirika la ndege la Afrika Mashariki baada ya kutolewa amri kuwa Ndege zote ziegeshwe Nairobi nchini Kenya.
Pamoja na kutoa fedha hizo Mhe. Rais Magufuli ameiagiza ATCL kumsafirisha bure Kepteni Mstaafu Mapunda pamoja na Mkewe mahali popote watakapohitaji kusafiri kwa ndege za ATCL ikiwa ni kutambua mchango wake mkubwa kwa Taifa na uzalendo aliouonesha bila kujali kama kitendo chake cha kuirejesha ndege hiyo nyumbani Tanzania kingeweza kugharimu maisha yake.
“Naomba kutoa wito kwa Watanzania hasa vijana, tuwe wazalendo kama alivyokuwa Kepteni Mapunda, yeye aliposikia Jumuiya ya Afrika Mashariki imevunjika na kuna agizo ndege zote wazipaki Nairobi Kenya, alijifanya kama anakwenda kupaki badala yake akairusha na kuja nayo moja kwa moja Tanzania, hakujali kutunguliwa ama kukosa mawasiliano ya waongoza ndege, tunakushukuru sana Mzee Mapunda” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Mapema akitoa taarifa ya maendeleo ya ATCL tangu Serikali ikodishe ndege kwa shirika hilo, Katibu Mkuu wa Uchukuzi Dkt. Leonard Chamriho amesema hadi Oktoba 2018 ATCL ilikuwa imelipa Serikalini shilingi Bilioni 6.7 ikiwa ni gharama za ukodishaji wa ndege, imelipa kodi ya shilingi Bilioni 8.6, imeongeza idadi ya abiria waliosafirishwa kutoka 5,600 hadi 34,000, imeongeza umiliki wa soko la ndani kutoka asilimia 2.5 hadi 36 na kuongeza kiwango cha kuruka na kutua kwa wakati kutoka asilimia 22 hadi 87.
Pia Dkt. Chamriho amesema idadi ya marubani imeongezeka kutoka 11 hadi kufikia 50 wengi wao wakiwa ni Watanzania waliofundishwa hapa nchini na nje ya nchi, imeongeza wahandisi na mafundi kutoka 31 hadi kufikia 87 wakiwemo wahandisi wazawa 36 na mafundi 45.
Spika wa Bunge Mhe. Job Yustino Ndugai na Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma wameipongeza Serikali kwa mafanikio makubwa ya kununua ndege na kuimarisha ATCL na wametoa wito kwa wafanyakazi wa ATCL kuhakikisha shirika hilo halirudi katika historia mbaya ya kufirisika.
Nae Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Isack Kamwelwe amesema wizara hiyo imejipanga kuhakikisha ATCL inajiimarisha kwa huduma na ufanisi, na kuhakikisha karakana iliyopo KIA inafufuliwa ili kuondokana na gharama kubwa ya matengenezo ya ndege yanalazimu kuzipeleka ndege nchini Canada.
Katika sherehe hizo Mhe. Rais Magufuli ameshuhudia tukio la kutia saini makubaliano ya kukodisha ndege kwa ATCL ambapo Katibu Mkuu Kiongozi Mhe. Balozi John Kijazi ametia saini na kukabidhi kwa niaba ya Serikali.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
23 Desemba, 2018