Taarifa kwa vyombo vya Habari ya zamani
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 21 Desemba, 2018 ametoa heshima za mwisho kwa mwili wa Marehemu Prof. Egid Beatus Mubofu (aliyekuwa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma – UDOM) aliyefariki dunia tarehe 18 Desemba, 2018 huko Pretoria, Afrika Kusini.
Mhe. Rais Magufuli amekwenda kutoa heshima za mwisho nyumbani kwa Marehemu Tabata Jijini Dar es Salaam na kutoa mkono wa pole kwa wafiwa akiwemo Mke wa Marehemu Bi. Joyce Chamhulo Mubofu, Wahadhiri wa Vyuo Vikuu, Wanafunzi, Ndugu, Jamaa na Majirani wa Marehemu.
Katika salamu zake, Mhe. Rais Magufuli ameelezea kusikitishwa na kifo cha Prof. Mubofu ambaye anasema Taifa lilikuwa linamtegemea kutokana na sifa kubwa alizojijengea katika utumishi wake wa umma, ambapo alidhihirisha uchapakazi wa hali ya juu, uadilifu mkubwa, ubunifu, utiifu na kuchukia rushwa.
Mhe. Rais Magufuli amesema alimfahamu Prof. Mubofu tangu akiwa mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, baadaye akiwa Mhadhiri, na utendaji wake mzuri alipokuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) ambalo aliweza kulifanyia mabadiliko, likaongeza tija na kuongeza makusanyo ya maduhuli ya Serikali.
“Prof. Mubofu ametuachia somo kubwa, alikuwa anashika Mabilioni ya fedha za Serikali lakini aliishi maisha ya kawaida, kwa mara nyingine nawapa pole sana wafiwa wote, Wahadhiri wa Vyuo Vikuu mliopo hapa, Wanafunzi, Ndugu, Jamaa na Majirani, tumuombee Prof. Mubofu apumzike mahali pema peponi na sisi tuliobaki tuendelee kushikamana pamoja na familia ya marehemu na kuiombea moyo wa subira na uvumilivu” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
21 Desemba, 2018
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 21 Desemba, 2018 amefunga mafunzo kwa Maafisa na Wakaguzi Wasaidizi wa Jeshi la Polisi Tanzania.
Sherehe za kufunga mafunzo hayo zimefanyika katika Chuo cha Taaluma ya Polisi Dar es Salaam kilichopo Kurasini.
Mafunzo hayo yamefanyika kwa muda wa miezi 6 ambapo jumla Askari 513 wakiwemo Maafisa wa Polisi 120 na Wakaguzi Wasaidizi 393 wamehitimu.
Kabla ya kufunga mafunzo hayo, Mhe. Rais Magufuli amekagua gwaride lililoandaliwa na Maafisa na Wakaguzi Wasaidizi hao ambao pia wamekula kiapo mbele yake, amepokea maelezo na kukagua silaha ambazo Polisi wamefanikiwa kuwanyang’anya wahalifu katika mikoa mbalimbali hapa nchini na ameshuhudia burudani ya ngoma na muziki wa bendi iliyoandaliwa na vikundi vya burudani vya Jeshi la Polisi.
Akizungumza na Maafisa na Askari wa Jeshi la Polisi, viongozi wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama, wageni mbalimbali wakiwemo Maafisa Wakuu wastaafu wa Polisi na wadau wa Polisi, Mhe. Rais Magufuli amewapongeza Maafisa na Wakaguzi Wasaidizi kwa kuhitimu mafunzo hayo na amewataka kwenda kuwahudumia wananchi vizuri na kuwasimamia Askari watakaowaongoza kufanya kazi kwa weledi na kwa kuzingatia sheria na taratibu za nchi.
Mhe. Rais Magufuli amesema hatarajii kuona wanaendeleza mambo yanayotia doa utendaji kazi wa Polisi yakiwemo kupokea rushwa, kunyanyasa watu, kubambikiza kesi na utovu wa nidhamu na hivyo amewataka kuzingatia kiapo chao na ujumbe uliomo kwenye wimbo wa Jeshi la Polisi.
“Mkisikia sisi viongozi tunasema nchi ina amani na utulivu basi mjue tunajivunia uwepo wa Jeshi la polisi, kwa hivyo nawapongeza sana kwa jinsi mnavyopambana na uhalifu, mlipambana kule Kibiti mpaka Askari wenzenu walipoteza maisha, natambua mchango wenu na nawapenda sana” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Mhe. Rais Magufuli amekubali ombi la shilingi Milioni 700 lililotolewa na Mkuu wa chuo hicho DCP Anthony Rutashuburugukwa kwa ajili ya kukarabati majengo ya chuo, na kuagiza fedha hizo pamoja na fedha nyingine kiasi cha shilingi Bilioni 7 ambazo ni kati ya shilingi Bilioni 10 alizoahidi kutoa kwa ajili ya ujenzi wa makazi ya Askari Polisi zitolewe kwa jeshi hilo ndani ya kipindi cha wiki moja.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli amewatia moyo Askari Polisi wanaotekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria na taratibu na amewataka Maafisa wa Polisi waache kuwakatisha tamaa Askari wanapotekeleza majukumu yao ikiwemo kuwaamrisha Askari wa vyeo vya chini wawaachie watuhumiwa wanaowakamata, kuwaweka Askari mahabusu na kuwakataza kutekeleza majukumu yao kwa kigezo cha kutokuwa na kibali.
“Nafahamu kuna Askari walichomwa visu wakati wanawakamata watuhumiwa, naagiza Askari hao watibiwe vizuri hata kama itahitajika kupelekwa nje, na wale watuhumiwa waliowajeruhi wakamatwe na wapelekwe mahakamani” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Halikadhalika Mhe. Rais Magufuli ameelezea kutoridhiwa na utendaji kazi wa kitengo cha fedha cha Jeshi la Polisi Tanzania na amemtaka Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) Simon Sirro na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kurekebisha dosari zilizopo pamoja na kuyalinda maeneo ya Jeshi la Polisi yasimegwe, kuuzwa ama kuingia mikataba isiyokuwa na maslahi kwa jeshi hilo.
Mapema akitoa taarifa kwa Mhe. Rais Magufuli, IGP Simon Sirro amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kupatiwa fedha shilingi Bilioni 10 kwa ajili ya kujenga nyumba 400 za makazi ya Askari, kununuliwa magari 777 ambapo 497 wameshapatiwa, kupatiwa shilingi Bilioni 50.3 za kuwalipa wazabuni, kuboresha maslahi ya askari, kuwapandisha vyeo askari 3,089, kuajiri askari wapya 818 na ameomba nafasi zilizoachwa wazi na Maafisa na Askari waliostaafu zijazwe.
Nae Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhandisi Hamad Masauni amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa usimamizi wake wa karibu kwa Jeshi la Polisi na ameahidi kuwa polisi wataendelea kutekeleza majukumu yao ya usalama wa Raia na mali zao kikamilifu na kwa weledi.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
21 Desemba, 2018
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 20 Desemba, 2018 ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa daraja jipya la Selander linalounganisha eneo la Aga Khan na Coco Beach Jijini Dar es Salaam kwa lengo la kupunguza msongamano wa magari katika barabara ya Ali Hassan Mwinyi.
Daraja hilo lenye urefu wa meta 1,030 na upana wa meta 20.5 litakuwa na njia 4 za magari na njia 2 za watembea kwa miguu, na litajengwa pamoja na barabara unganishi zenye jumla ya kilometa 5.2.
Sherehe za uwekaji jiwe la msingi katika mradi huo zimefanyika katika eneo la Aga Khan na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Mke wa Rais Mhe. Mama Janeth Magufuli, Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, Spika wa Bunge Mhe. Job Yustino Ndugai, Mawaziri, Wabunge, Mabalozi wa nchi mbalimbali, viongozi wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama, viongozi wa Dini, viongozi wa vyama vya siasa na viongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa huo Mhe. Paul Makonda.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mhandisi Patrick Mfugale amesema ujenzi wa daraja hilo utakaochukua muda wa miezi 30 kuanzia tarehe 23 Julai, 2018 utagharimu shilingi Bilioni 256 zilizotolewa kwa mkopo nafuu kutoka Jamhuri ya Korea kupitia Mfuko wa Ushirikiano wa Maendeleo ya Kiuchumi (EDCF) na Serikali ya Tanzania.
Mhandisi Mfugale ameongeza kuwa daraja hilo litadumu kwa muda wa miaka 100 na litajengwa bila kuathiri nyumba zilizopo kando ya barabara za Kenyatta na Toure ambazo miongoni mwake wanaishi Mabalozi.
Mhe. Rais Magufuli ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Korea kwa kufadhili ujenzi wa daraja hilo na amemuomba Balozi Mteule wa Jamhuri ya Korea hapa nchini Mhe. Cho Tae-ick kufikisha ujumbe wake kwa Rais wa Jamhuri ya Korea Mhe. Moon Jae-in kuwa Tanzania itaendeleza na kukuza zaidi uhusiano na ushirikiano wake na nchi hiyo hususani wakati huu ambapo inaendelea kufanya mapinduzi makubwa ya kiuchumi.
“Jamhuri ya Korea ni marafiki wetu wa kweli, wametusaidia kujenga daraja la Kikwete katika mto Malagarasi na wametusaidia kujenga Hospitali ya Taaluma na Sayansi ya Tiba Mloganzila na miradi mingine, tunawashukuru sana, naomba na sisi Watanzania tubadilike, tuchape kazi, tuwe wazalendo, tuwahimize vijana wetu waje wafanye kazi kwenye mradi huu” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Mhe. Rais Magufuli ameitaka Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kutafuta jina la daraja jipya la Selander na amependekeza lipewe jina la Tanzanite linaloakisi Utanzania.
Aidha, ametoa wito kwa Watanzania wote kuchapa kazi kwa juhudi na maarifa huku wakitanguliza uzalendo, kudumisha amani na upendo na kutokukatishana tamaa ili Tanzania ifanikiwe kupiga hatua za kimaendeleo kama ilivyofanya Jamhuri ya Korea ambayo uchumi wake ulikuwa sawa na Tanzania miaka ya 60 wakati Tanzania ikipata uhuru.
Mhe. Rais Magufuli amempongeza Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Isack Kamwelwe kwa juhudi zake za kusimamia ukusanyaji wa mapato ya Serikali ikiwemo kuhakikisha mabasi yote 49,000 yaliyopo nchini yanaanza kutoa tiketi za kielekroniki, kuongeza tija katika ukusanyaji wa mapato ya usafirishaji kwa njia ya reli na kufuatilia meli moja kubwa iliyonunuliwa kwa ushirikiano wa Tanzania na China ili ianze kuja nchini na kuinufaisha Tanzania.
Mapema katika salamu zake Balozi Mteule wa Jamhuri ya Korea Mhe. Cho Tae-ick ameishukuru Tanzania kwa uhusiano na ushirikiano mzuri uliopo kati yake na Jamhuri ya Korea ambapo katika kipindi cha miaka 26 ya uhusiano huo, Jamhuri ya Korea imetoa ufadhili wenye thamani ya zaidi ya shilingi Trilioni 1 na hivyo kuifanya Tanzania kuwa nchi inayoongoza kwa ufadhili wa nchi hiyo Barani Afrika.
Nae mwakilishi wa EDCF Mhe. Hyon-jong Lee amesema kwa umuhimu wa kipekee wa uhusiano ya Tanzania na Jamhuri ya Korea, Serikali za nchi hizo zinaendelea na majadiliano ya ufadhili wa miradi yenye thamani ya shilingi Bilioni 687.6 itakayotekelezwa nchini Tanzania katika kipindi cha kuanzia mwaka 2018 hadi 2020.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
20 Desemba, 2018
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 19 Desemba, 2018 ameweka jiwe la msingi la upanuzi wa barabara ya Morogoro Jijini Dar es Salaam katika sehemu ya kuanzia Kimara hadi Kibaha yenye urefu wa Kilometa 19.2.
Upanuzi huo utahusisha kuongeza njia za magari kutoka 2 zilizopo sasa hadi 8, kujenga madaraja 6 na makalavati 36, na kujenga barabara ya juu (Flyover) katika eneo la Kibamba CCM kwenye makutano ya barabara inayotokea Bunju na barabara ya kwenda hospitali ya Mloganzila.
Sherehe za uwekaji jiwe la msingi la mradi huo zimefanyika katika eneo la Kimara Stopover na kuhudhuriwa na Mke wa Rais Mhe. Mama Janeth Magufuli, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job Yustino Ndugai, Mawaziri, Wabunge, viongozi wa Dini, viongozi wa vyama vya siasa na viongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa huo Mhe. Paul Makonda.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mhandisi Patrick Mfugale amesema barabara ya Morogoro ni lango kuu la usafiri kati ya Jiji la Dar es Salaam lenye bandari kuu na mikoa mingi ya Tanzania Bara na nchi jirani, na kwamba upanuzi wake utasaidia kupunguza msongamano mkubwa wa magari takribani 50,000 yanayopita katika barabara hiyo kwa siku na utaokoa muda kutoka saa tatu zinazotumika kupita eneo hilo kwa sasa hadi nusu saa.
Amebainisha kuwa upanuzi wa barabara hiyo utafanyika kwa muda wa miezi 30 kuanzia tarehe 21 Julai 2018 na utagharimu shilingi Bilioni 141.56, fedha zote zinatolewa na Serikali ya Tanzania.
Akizungumza katika sherehe hizo Mhe. Rais Magufuli amewapongeza wananchi wa Dar es Salaam kwa kupatiwa mradi huo mkubwa na kubainisha kuwa pamoja na barabara hiyo Serikali ya Awamu ya Tano inaendelea kuboresha miundombinu ya Dar es Salaam ambapo barabara zenye jumla ya kilometa 212 zinajengwa kwa gharama ya shilingi Bilioni 660.
Kuhusu fidia kwa nyumba zilizovunjwa wakati wa upanuzi wa barabara hiyo Mhe. Rais Magufuli amewataka wanasiasa kuacha kuwapotosha wananchi kuwa watalipwa fidia, na amesema Serikali haitalipa fidia kwa mtu yeyote aliyejenga katika eneo la hifadhi ya barabara kwa mujibu wa sheria.
“Kuna wanasiasa wanataka waonekane wao ndio wanawatetea wananchi na wanasema Serikali itoe fidia, nataka niwaambie ndugu ukivamia barabara unatafuta umasikini, fidia haipo, fidia haipo, narudia fidia haipo” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli na kuwataka Watanzania kote nchini kuacha kuvamia maeneo ya hifadhi ya barabara na kujenga makazi.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli ametoa wito kwa Watanzania kuendelea kulipa kodi na kwamba Serikali itaendelea kuhakikisha kodi inayokusanywa inasimamiwa vizuri kwa kuelekezwa katika miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa barabara, kuendeleza elimu, afya na kuboresha upatikanaji wa maji ukiwemo mkoa wa Dar es Salaam ambao kwa sasa unapata maji kwa asilimia 75.
Mhe. Rais Magufuli amewaonya Madiwani wa Jiji la Dar es Salaam waliokuwa wakichelewesha kuanza kwa ujenzi wa kituo kikuu cha mabasi kutokana na kubishana juu ya mkandarasi wa kukijenga na kubainisha kuwa “Nilikuwa nawafuatilia jinsi mnavyobishana na leo mngekuwa bado mnabishana nilipanga nitangaze kuondoa fedha hizo (shilingi Bilioni 50) na kupeleka mahali pengine, ndugu zangu viongozi naomba tutangulize maslahi ya wananchi, sio maslahi yetu binafsi”.
Mapema Spika wa Bunge Mhe. Job Yustino Ndugai amempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa namna Serikali inavyosimamia utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo na kumhakikishia kuwa Bunge litaendelea kuunga mkono juhudi hizo zenye maslahi makubwa kwa Taifa.
Wabunge wa Mkoa wa Dar es Salaam wamemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kazi kubwa inayofanywa na Serikali katika Mkoa huo ikiwemo kutatua tatizo la maji, kuimarisha miundombinu ya barabara na reli, kununua ndege na kuboresha uwanja wa ndege na kuboresha huduma za afya na elimu.
Wakati huo huo, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Isack Kamwelwe amesema Serikali itaanza kutekeleza sheria ya kudhibiti uzito wa magari barabarani kuanzia Januari 2019 ili kuokoa uharibifu mkubwa wa barabara unaojitokeza katika barabara nyingi hivi sasa.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
19 Desemba, 2018
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amefuta mara moja maelekezo ya barua yenye kumbukumbu namba CHA.56/193/02/16 ya tarehe 23 Novemba, 2018 iliyoandikwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia (Baada ya kupokea maelekezo ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi) kwenda kwa Wakuu wa Vyuo vya Ualimu, Wakuu wa Vyuo vya Maendeleo ya Jamii, Wakuu wa Vyuo Vikuu na Vyuo Vikuu Vishiriki na Taasisi zilizochini ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.
Mhe. Rais Magufuli amesema barua hiyo yenye kichwa cha habari “MATUMIZI SAHIHI YA BENDERA, NEMBO NA WIMBO WA TAIFA” imetoa maelekezo ambayo yanaathiri uzalendo wa Watanzania na inaleta mkanganyiko wa tafsiri ya rangi na alama zilizomo katika bendera ya Taifa.
“Hata mimi mwenyewe tangu nasoma shule hadi leo nafahamu kuwa Bendera ya Taifa ina rangi ya njano na sio rangi ya dhahabu, na rangi hiyo ya njano inawakilisha madini yote, sio dhahabu pekee yake.
Kwa hiyo nimeamua kuifuta barua hiyo na kama kuna mabadiliko basi ni lazima yafanyike kwa kuzingatia taratibu zote kwa kuwa jambo hili ni la Kitaifa, sio la mtu mmoja” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Mhe. Rais Magufuli ameagiza Bendera, Nembo na Wimbo wa Taifa viendelee kutumika kama ilivyokuwa kabla ya kuandikwa kwa barua hiyo na ametoa wito kwa Watanzania kuendelea kuwa wazalendo, kuipenda nchi yao na kuitangaza popote walipo ilimradi wanazingatia sheria na maslahi mapana ya Taifa.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
14 Desemba, 2018
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 17 Desemba, 2018 ameungana na Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) kuadhimisha miaka 50 ya tangu kuanzishwa kwa Baraza hilo.
Maadhimisho hayo yamefanyika katika ukumbi wa Diamond Jubilee Jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, Waheshimiwa Mabalozi wa Iran na Misri, viongozi wa vyombo vya ulinzi na usalama, viongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa huo Mhe. Paul Makonda, Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja Mhe. Vuai Mwinyi Mohamed, Wajumbe wa Baraza la Ulamaa na Masheikh wa Mikoa na Wilaya zote 26 za Tanzania pamoja na Makatibu wao.
Akizungumza katika maadhimisho hayo, Mhe. Rais Magufuli ameipongeza BAKWATA na Waislamu wote nchini kwa kuendelea kudumisha amani, umoja, mshikamano na kuyashika vizuri mafunzo ya dini, na amebainisha kuwa mambo hayo yana faida kubwa kwa jamii nzima ya Waislamu na Madhehebu mengine.
Mhe. Rais Magufuli amesema katika kipindi cha miaka 50 taasisi mbalimbali zilizo chini ya BAKWATA na Uislamu kwa ujumla zimeendelea kutoa mchango mkubwa katika maendeleo ya Tanzania kwa kuunga mkono juhudi za Serikali katika utoaji wa huduma za elimu, afya, maji na nyingine na kwamba Serikali inatambua mchango huo mkubwa.
Ameahidi kuwa Serikali ya Awamu ya Tano itaendeleza na kukuza zaidi uhusiano wake mzuri na BAKWATA na Madhehebu mengine ya Dini, na ametoa wito kwa Waislamu na Waumini wa Madhahebu mengine ya Dini kuendeleza utamaduni mzuri wa kushirikiana, kuvumiliana, kusameheana na kutunza amani, mambo ambayo yanasaidia kuepusha migogoro.
“Naomba niwahakikishie ndugu zangu, Serikali inawapenda Waislamu na inayapenda Madhehebu yote ya Dini, tutaendelea kuhakikisha tunashirikiana kulisukuma mbele gurudumu la maendeleo la Taifa letu, kwa pamoja tunaweza” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Aidha, Mhe Rais Magufuli ameelezea juhudi mbalimbali zinazofanywa na Serikali kuharakisha maendeleo ikiwemo ununuzi wa ndege, kuanza mradi wa uzalishaji wa umeme katika mto Rufiji, kujenga viwanda, kujenga reli ya kati na kufufua reli ya kaskazini, kujenga meli mpya na kukarabati za zamani, kujenga barabara, kuongeza kasi ya usambazaji umeme vijijini, kujenga hospitali na vituo vya afya na kuongeza ukusanyaji wa kodi.
Amempongeza Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Sheikh Aboubakar Zubeir bin Ally kwa uongozi wake mzuri wa BAKWATA, ushirikiano mzuri na taasisi nyingine ikiwemo Serikali na kutojikweza kwake, na pia ametoa mchango wa shilingi Milioni 30 kwa BAKWATA.
Mapema Mufti wa Tanzania Sheikh Aboubakar Zubeir bin Ally amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kuungana nao katika maadhimisho hayo, amemshukuru kwa kusaidia kujengwa kwa Msikiti mkubwa wa BAKWATA Jijini Dar es Salaam ambao utakuwa na uwezo wa kuchukua Waumini 9,000 kwa mara moja, na pia kwa juhudi alizoanza kufuatilia na kurejesha mali za Waislamu zilizoporwa.
“Mhe. Rais kwa niaba ya BAKWATA tunakushukuru sana na Waislamu wameridhika sana kwa kuhakikisha Msikiti huu unajengwa na ujenzi wake unaendelea vizuri” amesema Sheikh Aboubakar Zubeir bin Ally.
Katika Maadhimisho hayo Mhe. Rais Magufuli pia amekabidhi tuzo kwa Waislamu waliotoa mchango mkubwa katika BAKWATA.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
17 Desemba, 2018
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 13 Desemba, 2018 amekutana na kufanya mazungumzo na Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wote wa Tanzania Bara, Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Kikao hicho kimehudhuriwa na Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. George Huruma Mkuchika na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Selemani Jafo.
Wengine ni Katibu Mkuu Kiongozi Mhe. Balozi John Kijazi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Dkt. Adelardius Kilangi, Katibu Mkuu wa TAMISEMI Mhandisi Musa Iyombe, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Doto James na Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Charles Kichere.
Katika kikao hicho Mhe. Rais Magufuli na viongozi hao wa Mikoa wamezungumza masuala mbalimbali yanayohusu utendaji kazi wa Serikali mikoani hususani usimamizi wa shughuli za maendeleo na utoaji wa huduma kwa wananchi.
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli na Waziri Mkuu wa Misri Mhe. Dkt. Mustafa Madbouly tarehe 12 Desemba, 2018 wameshuhudia utiaji saini mkataba wa ujenzi wa mradi wa kuzalisha umeme katika mto Rufiji utakaotekelezwa kwa muda wa miezi 42 kuanzia sasa.
Mkataba huo umetiwa saini kati ya Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Dkt. Tito Mwinuka na wawakilishi wa kampuni za ujenzi kutoka Misri ambao ni Mwenyekiti wa kampuni ya Arab Contractors Bw. Mohamed Mohsen Salaheldin na Mtendaji Mkuu wa kampuni ya Elsewedy Bw. Ahmed Sadek Elsewedy.
Hafla ya utiaji saini mkataba huo imefanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan, Mke wa Rais Mhe. Mama Janeth Magufuli, Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job Yustino Ndugai, Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Ndg. Bashiru Ally Kakurwa, Katibu Mkuu Kiongozi Mhe. Balozi John Kijazi, Mawaziri na Naibu Mawaziri wa Tanzania na Misri, Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu Wakuu, Mabalozi wa nchi mbalimbali, Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa Mikoa, Wabunge, viongozi wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama, viongozi wa Dini, viongozi wa vyama vya siasa, Wakuu wa Wilaya na viongozi wa taasisi mbalimbali za Serikali.
Akizungumza baada ya kushuhudia utiaji saini wa mkataba huo, Mhe. Rais Magufuli amesema ujenzi wa mradi huo utakaozalisha megawatts 2,115 za umeme utagharimu shilingi Trilioni 6.558, fedha ambazo zinatolewa na Serikali ya Tanzania na katika kipindi cha miaka zaidi ya 60 ya uhai wake mradi huu utaiwezesha Tanzania kupata umeme mwingi, wa uhakika na wa gharama nafuu kwa ajili ya matumizi ya majumbani na biashara ikiwemo viwanda.
“Kwa hivi sasa nchi yetu ina megawatts 1,560 tu za umeme, mradi huu pekee yake utazalisha megawatts 2,115. Uzuri ni kwamba umeme unaozalishwa kwa kutumia maji ni nafuu sana (shilingi 36/- tu kwa uniti moja) ikilinganishwa na umeme wa vyanzo vingine (mfano umeme wa mafuta unaofikia shilingi 446/- kwa uniti moja)” ametoa mfano Mhe. Rais Magufuli.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli amebainisha kuwa mradi huu unatarajiwa kuleta manufaa mengine kama vile kuimarisha uhifadhi wa mazingira katika maeneo ya mradi, mifugo ikiwemo wanyamapori kupata maji ya kutosha, kilimo cha umwagiliaji, kuvutia utalii, uvuvi na kukuza ujenzi wa viwanda, tofauti na madai ya baadhi ya watu wanaodai kuwa utaharibu mazingira.
“Eneo lote la mradi huu ni sawa na asilimia 1.8 hadi 2 tu ya pori zima la hifadhi ya akiba ya Selous, kuwepo kwa mradi huu kutasaidia watu wengi kupika kwa kutumia umeme badala ya kuni na mkaa ambao takwimu zinaonesha umekuwa ukisababisha kukatwa kwa hekta 583 za miti kila siku. Tuna imani kubwa ukikamilika wananchi wengi wataachana na matumizi ya kuni na mkaa na badala yake kutumia umeme utakaopatikana kwa bei nafuu” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Ametoa wito kwa Watanzania wote kuunga mkono juhudi za Serikali kutekeleza mradi huu na amewataka wanaotumiwa na mabeberu kupiga juhudi hizi waache kwa kuwa mradi huu unatekelezwa kwa manufaa ya Watanzania wote bila kubagua itikadi ya siasa, dini ama kabila la mtu.
Pia amewashukuru viongozi wa Dini waliojitokeza kwa wingi kushuhudia tukio hilo na kuomba dua njema kwa mradi na Taifa, pamoja na viongozi wengine wote kwa kutambua umuhimu wa mradi huu mkubwa.
Mhe. Rais Magufuli amemshukuru Waziri Mkuu wa Misri Mhe. Dkt. Mustafa Madbouly kwa ujio wake hapa nchini na amemuomba amfikishie salama za shukrani kwa Rais wa Misri Mhe. Abdel Fattah el-Sisi kwa uhusiano na ushirikiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na Misri na ameahidi kuuendeleza na kuukuza uhusiano huu.
Waziri Mkuu wa Misri Mhe. Dkt. Mustafa Madbouly amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kuendeleza uhusiano na ushirikiano mzuri wa Tanzania na Misri ulioasisiwa na viongozi wa Mataifa haya Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere na Hayati Gamal Abdel Nasser, na ameahidi kuwa pamoja na kutekeleza mradi huu Misri itaendelea kushirikiana na Tanzania katika maeneo mengine ya biashara na uwekezaji pamoja na kuunga mkono juhudi mbalimbali za kuwaletea Watanzania maendeleo.
Nao viongozi mbalimbali waliopata fursa ya kutoa salamu katika tukio hilo wamempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa jitihada kubwa anazozifanya katika uongozi wake ikiwemo kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo, kuhakikisha nchi ina amani, kulinda hadhi ya nchi na kuhakikisha nchi inajenga misingi ya kujitegemea na wameahidi kuendelea kuunga mkono juhudi hizo kwa manufaa ya Taifa.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
12 Desemba, 2018
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 10 Desemba, 2018 amepokea hati za utambulisho za Mabalozi 2 kutoka nchi za Ethiopia na Misri walioteuliwa kuziwakilisha nchi hizo hapa nchini.
Mabalozi waliowasilisha hati zao ni Mhe. Yonas Yosef Sanbe – Balozi wa Ethiopia hapa nchini na Mhe. Mohamed Gaber Mohamed Abulwafa – Balozi wa Misri hapa nchini.
Mabalozi hao wamemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kuwakaribisha hapa nchini na wameahidi kuwa katika kipindi cha uwakilishi wao watahakikisha wanaimarisha na kukuza zaidi uhusiano na ushirikiano wa nchi hizo na Tanzania hususani kusimamia kwa ukaribu ushirikiano katika maeneo ya kiuchumi.
Mhe. Rais Magufuli amewaomba Mabalozi hao kufikisha salamu zake kwa viongozi wakuu wa nchi hizo na kubainisha kuwa Tanzania ipo tayari kwa ushirikiano zaidi utakaoleta manufaa kwa wananchi wa nchi zote.
Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mkuu wa Masuala ya Kimataifa wa Canada Mhe. Marc-Andre Fredette, Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Baada ya mazungumzo hayo Mhe. Fredette ambaye anashughulikia Wizara 3 za Canada (Wizara ya Mambo ya Nje, Wizara ya Biashara za Kimataifa na Wizara ya Maendeleo) amepongeza maendeleo makubwa ambayo Tanzania imeyapata na amesema Tanzania na Canada zinaendelea kushirikiana katika maeneo mbalimbali yakiwemo katika sekta ya afya na elimu kwa ufanisi mkubwa.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
10 Desemba, 2018
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ameiagiza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Wizara ya Fedha na Mipango kushirikiana na viongozi wa taasisi na vyombo mbalimbali vya umma kufanya tathmini ili kupata majawabu yatakayowezesha kuongeza ukusanyaji wa mapato na kudhibiti mianya ya upotevu wa mapato hayo.
Mhe. Rais Magufuli ametoa maagizo hayo tarehe 10 Desemba, 2018 wakati akizungumza katika kikao kilichowakutanisha viongozi wa TRA wakiwemo Mameneja wa Mikoa yote nchini, Baadhi ya Mawaziri na Makatibu Wakuu, Wakuu wa Mikoa yote nchini, Benki Kuu ya Tanzania (BOT), Ofisi ya Takwimu ya Taifa, viongozi wakuu wa taasisi zinazohusika na udhibiti na ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali na wajasiriamali wadogo kilichofanyika katika ukumbi wa Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam.
Mhe. Rais Magufuli amesema mfumo na taratibu zinazotumika kukusanya mapato zina mapungufu makubwa hali iliyosababisha kuwepo kwa uwiano wa chini wa ukusanyaji wa kodi ikilinganishwa na nchi mbalimbali za Afrika, kutokuwepo kwa vyanzo vipya vya mapato, kutowavutia watu wengi kulipa kodi na kusababisha watu kufunga biashara zao.
Ameitaka TRA kuimarisha mifumo ya kielektroniki ya ukusanyaji wa mapato na kuhamasisha zaidi watu kulipa kodi, kushirikiana na vyombo vya dola kubaini na kuwakamata wakwepa kodi wote hususani wanaosafirisha bidhaa mipakani kimagendo na kuacha kuwakatisha tamaa wafanyabiashara kwa kuwafanyia makadirio ya kodi kwa viwango cha juu visicholipika.
“TRA mnakwenda kwa mfanyabiashara mnamkadiria kodi shilingi Bilioni 2, anawaambia nitatoa Bilioni 1 au Milioni 800, mnakataa na mnaamua kumfungia biashara, sasa biashara ikifungwa utakuwa umepata nini? Tunashindwa hata kutumia busara zetu katika ukusanyaji wa kodi” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli amewaonya baadhi ya viongozi wa siasa ambao wamekuwa wakiwakingia kifua wafanyabiashara wanaokwepa kulipa kodi na amewaagiza maafisa wa TRA kukusanya kodi kwa mujibu wa sheria bila kushinikizwa na mtu yeyote.
Katika hatua nyingine, Mhe. Rais Magufuli ametoa vitambulisho vya wajasiriamali 670,000 kwa Wakuu wa Mikoa yote ya Tanzania (kila Mkuu wa Mkoa amekabidhiwa vitambulisho 25,000) kwa ajili ya kuwagawia wajasiriamali wa Mikoa hiyo ambao watavilipia shilingi 20,000 kwa kila kitambulisho kimoja, na ameagiza wajasiriamali watakaopatiwa vitambulisho hivyo wasibughudhiwe wakati wanafanya biashara zao.
“Mfanyabiashara mdogo akivaa kitambulisho hiki asisumbuliwe na mtu yeyote, na niseme kwa dhati ndugu zangu viongozi wa siasa mtu utakayemkuta na kitambulisho hiki na anafanya biashara ya chini ya Milioni 4 usimsumbue” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Kuhusu kodi ya majengo Mhe. Rais Magufuli ameitaka TRA kuweka utaratibu rahisi wa kukusanya kodi ya majengo na ameelekeza nyumba ya kawaida iliyopo kijijini ilipiwe shilingi 10,000/= na nyumba ya ghorofa ilipiwe shilingi 20,000/=, kwa maeneo ya mjini nyumba ya kawaida ilipiwe shilingi 50,000/=, nyumba ya ghorofa kila sakafu ilipiwe shilingi 50,000/= na kodi itozwe kwa kiwanja na sio kila jengo lililopo katika kiwanja hicho.
Mapema Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Dkt. Albina Chuwa ametoa maelezo ya hali ya takwimu za kiuchumi hapa nchini na kubainisha kuwa takwimu za ukuaji wa uchumi kwa kipindi cha Januari hadi Juni 2018 zinaonesha kuwa uchumi wa Tanzania unakua kwa wastani mzuri wa asilimia 7.0 na mfumuko wa bei umeandika rekodi ya chini zaidi kuwahi kutokea katika miaka 10 ambapo ilikuwa wastani wa asilimia 3.0 katika mwezi Novemba 2018.
Nae Gavana wa BOT Prof. Florens Luoga amesema benki hiyo imeendelea kufanya juhudi za kusimamia na kuimarisha sekta ya fedha ambapo ukopeshaji kutoka benki mbalimbali kwenye kwa wafanyabiashara umepanda kutoka asilimia 0.8 mwaka 2017 hadi kufikia asilimia 4.9 Septemba 2018, BOT imepunguza riba kwa mikopo yake kwa benki kutoka asilimia 16-12 mwaka 2017, kutoka asilimia 12 hadi asilimia 7 mwaka 2018 na kwamba inaelekea kufikia asilimia 3.5.
Kamishna Mkuu wa TRA Bw. Charles Kichere ameeleza juhudi mbalimbali za kuongeza ukusanyaji wa mapato zilizofanikisha kukusanya shilingi Trilioni 42.9 katika kipindi cha miaka 3 iliyopita na kwamba hivi sasa inaendelea kuimarisha mifumo hususani bandarini ambapo mfanyabiashara atapata huduma kwa pamoja.
Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango ameahidi kusimamia maelekezo yote yaliyotolewa na Mhe. Rais Magufuli na ameagiza maafisa masuhuli wote kuhakikisha fedha zote zinazokusanywa zinaingizwa katika mfuko mkuu wa Serikali pamoja na kuhakikisha hawaingii mikataba mipya ya misamaha ya kodi bila kupata ridhaa ya Waziri wa Fedha na Mipango.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasilinao ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
10 Desemba, 2018
Taarifa kwa vyombo vya Habari
SALAMU ZA MHE. JOHN POMBE MAGUFULI, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, KWA WANANCHI KATIKA KUMBUKUMBU YA MIAKA 57 YA UHURU, TAREHE 09 DESEMBA, 2018
Ndugu Wananchi na Ndugu Watanzania Wenzangu;
Jumapili, tarehe 9 Disemba 2018, nchi yetu (Tanzania Bara), itatimiza miaka 57 tangu kupata Uhuru wake kutoka Utawala wa Uingereza. Napenda, kwanza kabisa, kutumia fursa hii kuwashukuru na kuwapongeza wazee wetu wote, wakiongozwa na Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, kwa kufanikisha kupatikana kwa uhuru wa nchi yetu. Aidha, nawapongeza Watanzania wote kwa kutimiza miaka hii 57 tukiwa wamoja na nchi yetu ikiwa na amani. Hongereni sana Watanzania wenzangu. “Happy Birthday Tanzania Bara”.
Kama ilivyo ada, maandalizi ya Sherehe za Uhuru mwaka huu yalikwishaanza. Takribani shilingi bilioni moja zilitengwa kuadhimisha sherehe hizo. Hata hivyo, kama mlivyosikia kutoka kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, nilitoa maelekezo kwamba, mwaka huu tusifanye sherehe. Badala yake, Watanzania wapumzike na kuitumia siku hiyo kutafakari Uhuru tulionao; mahali tulipotoka, mahali tulipo sasa na tunakoelekea. Naomba kusisitiza kuwa tarehe 9 Disemba, 2018 itakuwa Siku ya Mapumziko.
Ndugu Wananchi na Ndugu Watanzania Wenzangu;
Uhuru tulioupata tarehe 9 Disemba, 1961 ulikuwa mwanzo tu wa kuanza harakati za kutafuta uhuru mwingine. Uhuru wa kiuchumi, ambao pengine ni mgumu zaidi kuliko ule wa mwanzo. Napenda kutumia fursa hii kuzipongeza Serikali za Awamu zote za nchi yetu pamoja na Watanzania kwa mafanikio makubwa ya kiuchumi yaliyopatikana katika kipindi cha miaka 57 iliyopita. Sio siri kuwa Tanzania ya sasa sio sawa na ile ya mwaka 1961. Mambo mengi makubwa yamefanyika nchini mwetu.
Pamoja na ukweli huo, ni wazi kuwa nchi yetu bado ina safari ndefu ya kufika kule tunakotamani kufika; ambako ni kujenga Tanzania iliyo imara zaidi, yenye amani na umoja. Tanzania yenye maendeleo ya kiuchumi na inayojitegemea. Tanzania ambayo huduma za kijamii zinapatikana kwa urahisi zaidi. Tanzania yenye watu walioelimika. Na Tanzania yenye watu wenye kipato kizuri.
Nafarijika kuona kuwa, katika kipindi cha miaka mitatu tuliyokaa madarakani, Serikali kutekeleza ndoto hiyo. Tumefanikiwa kudumisha Amani, Umoja na Muungano wetu wa Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar. Tumeendeleza juhudi za kukuza uchumi. Hivi sasa nchi yetu ni miongoni mwa nchi tano ambazo uchumi wake unakua kwa kasi Barani Afrika. Tumefanikiwa kuwavutia wawekezaji wengi, ambapo mitaji yenye thamani ya zaidi ya shilingi trilioni 30 imeingia nchini. Tumeimarisha miundombinu mbalimbali na kuboresha huduma nyingine za jamii. Tumepata mafanikio makubwa katika mapambano dhidi ya rushwa na nchi yetu inatajwa kuwa mfano wa kuigwa. Tumelinda rasilimali zetu.
Wito wangu kwa Watanzania wote, endeleeni kuiunga mkono Serikali yenu. Kama nilivyosema, hivi sasa tupo kwenye vita vya kiuchumi. Vita hii ni ngumu. Hivyo, kila Mtanzania ni lazima ashiriki kwa kutimiza jukumu lake la kuendelea kudumisha amani na umoja, kulinda muungano wetu pamoja na kuchapa kazi kwa bidii. Tuache maneno maneno. Ni lazima tujenge dhana ya kujitegemea katika kujenga Uchumi wetu.
Ndugu Wananchi na Ndugu Watanzania Wenzangu;
Katika kuadhimisha Miaka 57 ya Uhuru, nimeagiza kuwa fedha zilizotengwa kwa ajili ya Sherehe zitumike kujenga Hospitali ya Uhuru katika Jiji la Dodoma. Kama mnavyofahamu, ili kutekeleza mawazo ya waasisi wetu, Serikali imeamua kuhamishia rasmi Makao Makuu ya nchi yetu Jijini Dodoma. Hii imefanya mahitaji ya huduma za jamii, ikiwemo afya, kuongezeka. Hivyo, tumeamua kujenga Hospitali nyingine kubwa itakayosaidiana na Hospitali ya Benjamin Mkapa na Hospitali ya Mkoa.
Sambamba na hayo, katika kuadhimisha Miaka 57 ya Uhuru mwaka huu, nimeamua, kwa mujibu wa Mamlaka niliyopewa kwenye Ibara ya 45 (1)(d) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kutoa msamaha kwa wafungwa 4,477, ambapo kati yao wafungwa 1,176 watatoka siku ya Maadhimisho ya Uhuru. Msamaha huu utawahusu wafungwa wagonjwa, wazee kuanzia miaka 70 na zaidi, wafungwa wa kike waliongia gerezani wakiwa wajawazito, na waliongia na watoto wanaonyonya au wasionyonya pamoja na wafungwa wenye ulemavu wa mwili na akili.
Halikadhalika, nimeamua kwa wafungwa waliotumikia robo ya adhabu zao, wapunguziwe robo ya adhabu zao baada ya punguzo la kawaida la theluthi moja linalotolewa kwenye Kifungu 49 (1) cha Sheria ya Magereza Sura ya 58. Hata hivyo, msamaha huu hautawahusu wafungwa wanaotumikia baadhi ya adhabu, zikiwemo kunyongwa, kifungo cha maisha, biashara ya dawa za kulevya na binadamu, makosa ya unyang’anyi, kukutwa na viungo vya binadamu, makosa ya kupatikana na silaha, risasi, milipuko isivyo halali, makosa ya shambulio la aibu, kunajisi, kubaka, kulawiti, kuwapa mimba wanafunzi wa shule za msingi na sekodari, uhujumu uchumi, rushwa, ubadhirifu, ujangili, waliowahi kupunguziwa kifungo kwa msamaha wa Rais, wanaotumikia kifungo chini ya Sheria ya Bodi ya Parole, wenye makosa ya kutoroka au kujaribu ama kusaidia kutoroka chini ya ulinzi halali, waliongia gerezani baada ya tarehe 1 Disemba, 2018 au waliowahi kufungwa na kurudi tena gerezani pamoja na wenye makosa ya kinadhamu magerezani.
Naomba nimalizie salamu zangu kwa kuwatakia tena kila la heri katika Maadhimisho ya Miaka 57 ya Uhuru wa Tanzania Bara.
Mungu Wabariki Watanzania Wote!
Mungu Ibariki Tanzania!
Mungu Ibariki Afrika!
“Ahsanteni Sana kwa kunisikiliza”
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 06 Desemba, 2018 amekutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mkuu Mstaafu wa Idara ya Usalama wa Taifa Bw. Apson Mwang’onda, Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Baada ya mazungumzo hayo Bw. Apson Mwang’onda amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kukubali ombi lake la kumuona na kuzungumza nae na amempongeza kwa uongozi mzuri unaochochea kasi ya maendeleo hususani katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendelo.
Bw. Apson Mwang’onda ameitaja baadhi ya miradi mikubwa ya maendeleo kuwa ni mradi wa uzalishaji wa umeme katika mto Rufiji (Stieglers’ Gorge Power Project) na Ujenzi wa madaraja na barabara ambazo licha ya kurahisisha usafiri zitasaidia kuondoa msongamano wa magari katika Jiji la Dar es Salaam.
“Mabadiliko ni makubwa sana ambayo yametokea, kuna miradi mikubwa mingi inafanyika sasa hivi, kwa hiyo mabadiliko ni makubwa kusema kweli na yote hayo ni kwa manufaa ya nchi, kwa hiyo nachoweza kusema amefanya kazi kubwa kwa maendeleo ya nchi” amesema Bw. Apson Mwang’onda.
Ametoa wito kwa wananchi kutoa ushirikiano kwa Serikali ya Awamu ya Tano ili itekeleza mipango yake kwa ufanisi na kwa manufaa ya Taifa.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
06 Desemba, 2018
Taarifa kwa vyombo vya habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amemteua Balozi Lut. Jen. Mstaafu Wyjones Mathew Kisamba kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Nyumbu (Tanzania Automotive Technology Center).
Balozi Lut. Jen. Mstaafu Kisamba anachukua nafasi ya Prof. Burton Mwamila ambaye amemaliza muda wake.
Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli amemteua Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Magereza (SACP) Mbaraka Sultan Semwanza kuwa Kamishna wa Utawala na Fedha katika Jeshi la Zimamoto na Uokoaji.
SACP Semwanza anachukua nafasi ya CF Michael Shija ambaye amestaafu.
Uteuzi wa viongozi hao umeanza tarehe 04 Desemba, 2018.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
04 Desemba, 2018
Taarifa kwa vyombo vya habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amemteua Jaji Mstaafu Steven Bwana kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Umma kwa kipindi cha miaka 3.
Pamoja na kumteua mwenyekiti wa tume, Mhe. Rais Magufuli amewateua Makamishna 5 wa Tume ya Utumishi wa Umma.
Walioteuliwa ni;
- Bw. George D. Yambesi
- Balozi Mstaafu John Michael Haule
- Bi. Immaculate P. Ngwale
- Bw. Yahaya F. Mbila
- Balozi Mstaafu Daniel Ole Njoolay.
Uteuzi huu wa Mwenyekiti na Makamishna wa Tume ya Utumishi wa Umma umeanza tarehe 22 Novemba, 2018.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
04 Desemba, 2018
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli na Rais wa Jamhuri ya Kenya Mhe. Uhuru Muigai Kenyatta tarehe 01 Desemba, 2018 wamezindua kituo cha huduma kwa pamoja mpakani (Ones Stop Border Post – OSBP) katika eneo la Namanga mpakani mwa Tanzania na Kenya.
Pamoja na kuzindua ofisi za kituo hicho katika pande zote mbili, Waheshimiwa Marais wamepanda miti ya kumbukumbu na kukagua utoaji wa huduma zikiwemo za forodha na uhamiaji.
Kituo hicho ni miongoni mwa vituo 15 vya OSBP vinavyojengwa katika mipaka ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa lengo la kurahisisha ufanyaji wa biashara miongoni mwa nchi hizo, kuharakisha huduma za mpakani, kuongeza mapato na kuimarisha usalama.
Ujenzi wa kituo cha Namanga OSBP umefadhiliwa na Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB), Shirika la Maendeleo la Japan (JICA) na Serikali za Tanzania na Kenya ambapo miundombinu ya upande wa Tanzania imegharimu shilingi Bilioni 22.365.
Tangu kianze kutoa huduma kituo hicho kimesaidia kupunguza muda unaotumiwa kukamilisha huduma za mpakani (clearance) kutoka saa 1 hadi dakika 15, na pia kwa upande wa Tanzania ukusanyaji wa mapato umeongezeka kutoka shilingi Bilioni 41 hadi kufikia shilingi Bilioni 58 zinazotarajiwa mwaka huu.
Wakizungumza baada ya kuzindua kituo hicho Mhe. Rais Magufuli na Mhe. Rais Kenyatta wamewashukuru wafadhili wa mradi wa ujenzi wa kituo hicho (AfDB na JICA) na wametoa wito kwa Watanzania na Wakenya kuongeza biashara kupitia mpaka huo, huku wakitaka wafanyabiashara wadogo wasibughudhiwe.
“Kenya ni ya 3 kati ya nchi 10 zinazoongoza kwa uwekezaji Tanzania kwa hiyo Wafanyabiashara wa Kenya wanapopita hapa msiwaone kuwa ni maadui, halikadhalika Tanzania ni yenye mifugo mingi hasa ng’ombe kwa hiyo Watanzania wanapopeleka nyama Kenya nao wasikwamishwe” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
“Sisi tujione wana Afrika Mashariki, tuzilete nchi zetu pamoja na tuutumie umoja wetu wa watu takribani Milioni 200 kufanya biashara na kunufaika, sisi viongozi wajibu wetu ni kurahisisha biashara sio kukwamisha, na nyie wananchi muwe huru kufanya biashara zenu ilimradi msivunje sheria na kufanya biashara haramu” amesema Mhe. Rais Kenyatta.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli ameahidi kushughulikia tatizo la maji katika eneo la Namanga kwa kuwapeleka maji ya kutoka Longido ambako Serikali imejenga mradi mkubwa wa maji uliogharimu shilingi Bilioni 15.
Pia Mhe. Rais Magufuli ameishukuru AfDB baada ya Mkurugenzi Mkuu wa benki hiyo katika ukanda wa Afrika Mashariki Bw. Gabriel Negatu kueleza kuwa imeridhia kutoa fedha kwa ajili ya kutekeleza mradi wa ujenzi wa barabara ya Malindi – Lungalunga – Tanga – Pangani – Bagamoyo inayounganisha Tanzania na Kenya, na mradi wa barabara ya Rumonge – Manyovu – Kasulu – Kibondo – Nyakanazi inayounganisha Tanzania na Burundi.
Baada ya kuagana na Mhe. Rais Kenyatta ambaye amerejea nchini kwake, Mhe. Rais Magufuli akiwa njiani kwenda Arusha Mjini amekutana na wananchi wa Odonyosamba wilayani Arumeru na kuahidi kushughulikia tatizo la maji linalolikabili eneo hilo ambapo ameagiza fedha zilizotengwa kwa ajili ya mradi wa kusafisha maji kiasi cha shilingi Milioni 500 zitolewe wiki ijayo na pia amemuagiza Waziri wa Maji na Umwagiliaji Prof. Makame Mbarawa kufika katika eneo hilo ili kuangalia namna ya kufikisha maji ya kutoka mradi mkubwa wa maji Arusha Mjini kwa wananchi hao.
Mhe. Rais Magufuli pia amekutana na wananchi wa Mianzini katika Jiji la Arusha ambapo amesema Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuboresha Jiji la Arusha ikiwemo kujenga barabara za kisasa ndani ya Jiji hilo, kuwajali wafanyabiashara wadogo na kwamba kesho ataweka jiwe la msingi la mradi wa maji wa Arusha Mjini utakaogharimu shilingi Bilioni 520.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Arusha
01 Desemba, 2018
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 30 Novemba, 2018 amekutana na Rais wa Jamhuri ya Uganda, Mhe. Yoweri Kaguta Museveni na Rais wa Jamhuri ya Kenya, Mhe. Uhuru Muigai Kenyatta kando ya Mkutano wa 20 wa Wakuu wa Nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC).
Mara baada ya kikao cha ndani kilichofanyika katika moja ya kumbi za watu mashuhuri ndani ya kituo cha AICC, Marais wote watatu wamesafiri kwa gari moja hadi Ikulu ndogo ya Arusha Mjini ambako Mhe. Rais Magufuli amewaalika wageni wake kwa chakula cha mchana.
Baada ya chakula cha mchana Mhe. Rais Museveni ambaye ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki amesema Mkutano wa 20 wa Wakuu wa Nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki umeahirishwa hadi tarehe 27 Desemba, 2018 utakapofanyika tena.
Mhe. Rais Museveni amesema mkutano huo umeahirishwa kutokana na mmoja wa wanachama wa jumuiya hiyo ambaye ni nchi ya Burundi kutohudhuria, ilihali mkataba wa jumuiya hiyo unataka maamuzi yafanywe na wanachama wote kwa pamoja.
“Tuliamua kuahirisha mkutano kwa leo kwa sababu mmoja wetu ambaye ni Burundi hakuja, tumeahirisha mkutano mpaka tarehe 27 Desemba, 2018 wakati sisi wote tutakapokuwepo, kwa sababu mkataba wa Afrika Mashariki unasema mambo mawili, moja lazima tuwe na mkutano mmoja wa kawaida kila mwaka na ndio huu wa leo.
Lakini vile vile uamuzi wowote utakaofanyika lazima wanachama wote wawepo, kwa hiyo kama mmoja hayupo sio vizuri kuendelea, inakuwa inakwenda kinyume na mkataba” amesema Mhe. Rais Museveni.
Akiwa hapa Arusha kesho tarehe 01 Desemba, 2018 Mhe. Rais Magufuli na Mhe. Rais Kenyatta watafungua kituo cha huduma za pamoja mpakani (One Stop Border Post) katika eneo la Namanga mpakani mwa Tanzania na Kenya.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
30 Novemba, 2018
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 28 Novemba, 2018 amekutana na kufanya mazungumzo na Rais Mstaafu wa Afrika Kusini na Mwenyekiti wa jopo la ngazi ya juu lililoundwa na Umoja wa Afrika (AU) kushughulikia tatizo la utoroshaji wa fedha (ikiwemo utakatishaji, wizi, rushwa na biashara haramu) kutoka Afrika Mhe. Thabo Mbeki, Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Mhe. Mbeki amesema mazungumzo hayo yamemwezesha kupata taarifa na uzoefu muhimu kutoka kwa Mhe. Rais Magufuli kuhusu juhudi zinazofanywa na Serikali ya Tanzania kukabiliana na utoroshaji wa fedha katika maeneo mbalimbali yakiwemo sekta ya madini na rushwa, matatizo ambayo yanazikabili nchi zingine za Afrika.
“Ni wazi kwamba juhudi zinazofanywa na Tanzania zina umuhimu mkubwa kufanywa na nchi zingine za Afrika, kwa pamoja Waafrika tunaweza kukabiliana na utoroshaji wa fedha zetu kwenda nje ya nchi zetu, na Mhe. Rais Magufuli amezungumza kwa usahihi kabisa juu ya Matrilioni ya Dola za Marekani zinazopotea kupitia utoroshaji huo” amesisitiza Mhe. Mbeki.
Mhe. Rais Magufuli amempongeza Mhe. Rais Mstaafu Mbeki kwa kuongoza jopo hilo na kubainisha kuwa Tanzania ipo tayari kutoa ushirikiano utakaowezesha kunusuru rasilimali za Afrika, hivyo amemshauri kutenga muda wa kutosha ili apate taarifa za uhakika kutoka kwa viongozi na wataalamu katika mamlaka zinazodhibiti utoroshaji wa fedha hapa nchini.
Ripoti ya taasisi ya kimataifa iitwayo Global Financial Intergrity (GFI) ya mwaka 2014 kuhusu tatizo la utoroshaji wa fedha za Afrika inasema Afrika inapoteza Dola za Marekani kati ya Trilioni 1.4 na Trilioni 2.5 kwa mwaka kutokana na tatizo hilo, na kwamba kwa ujumla Afrika imepoteza Dola za Marekani Trilioni 95 kwa miaka 50 iliyopita, ikiwemo Tanzania iliyoripotiwa kupoteza dola za Marekani Bilioni 19 katika miaka 40 iliyopita.
“Na njia nyingi zinazotumika katika kutupotezea hizo fedha na kuibiwa, wanaweza wakaja kuwekeza lakini kila siku wakawa wanasema wanapata hasara kumbe hawapati hasara, wanatengeneza faida kubwa lakini kwenye vitabu wanawaandikia wanapata hasara, wanaweza wakaja kama wawekezaji na wakawa wanazidisha gharama za uwekezaji kuliko uhalisia” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Maendeleo ya Kimataifa wa Norway Mhe. Nicolai Astrup, Ikulu Jijini Dar es Salaam na kumshukuru kwa mchango mkubwa ambao Norway inautoa katika maendeleo ya Tanzania kwenye sekta mbalimbali zikiwemo elimu, kilimo, nishati na gesi.
Mhe. Rais Magufuli amemhakikishia Mhe. Nicolai Astrup kuwa Serikali ya Awamu ya Tano itaendeleza na kukuza zaidi uhusiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na Norway ikiwemo kushirikiana na kampuni ya Equinor ya Norway katika uwekezaji wa kiwanda cha kusindika gesi asilia (LNG) kwa manufaa ya pande zote mbili, na kushirikiana na kampuni ya Yara ya Norway katika kuwawezesha wakulima kupata mbolea bora na gharama nafuu.
Nae Mhe. Nicolai Astrup amempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali ya Tanzania kupambana na rushwa, kuongeza ukusanyaji wa kodi na kuimarisha uchumi, na kwamba Norway itaendelea kuunga mkono juhudi za Tanzania kufikia uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.
Mhe. Nicolai Astrup amebainisha kuwa pamoja na kufadhili miradi mbalimbali ikiwemo umeme vijijini (REA) na kuimarisha mifumo ya ukusanyaji kodi kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Norway itatoa Dola za Marekani Milioni 56 (sawa na shilingi Bilioni 127) kwa ajili ya miradi ya maendeleo.
Mazungumzo hayo yamehudhuriwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt. Damas Ndumbaro, Naibu Waziri wa Kilimo Mhe. Omary Mgumba na Balozi wa Norway hapa nchini Mhe. Elisabeth Jacobsen.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
28 Novemba, 2018
Taarifa kwa vyombo vya habari
“Kwa masikitiko makubwa nimepokea taarifa ya ajali ya kugongana kwa mabasi madogo ya abiria huko Tarime Mkoani Mara na kusababisha vifo vya watu 16 na wengine watatu kujeruhiwa, magari hayo baada ya kugongana uso kwa uso yaliwaka moto na hivyo miili ya marehemu imeungua kwa kiasi cha kuwa vigumu kuitambua.
“Nawapa pole familia zote zilizopoteza ndugu, jamaa na marafiki katika ajali hii, nakupa pole Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Adam Malima na wote walioguswa na vifo hivi, nawaombea Marehemu wote wapumzike mahali pema peponi na majeruhi wapone haraka”
Ni salamu za rambirambi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli alizozitoa leo tarehe 27 Novemba, 2018 kufuatia ajali ya barabarani iliyohusisha mabasi madogo ya abiria kugongana uso kwa uso katika mteremko wa Komaswa Wilaya ya Tarime Mkoani Mara na kusababisha watu 16 kupoteza maisha na wengine 3 kujeruhiwa.
Ajali hiyo imetokea jana majira ya saa 10:00 jioni ambapo basi moja dogo lililokuwa likitoka Musoma kwenda Tarime liligongana na basi jingine dogo lililokuwa likitoka Tarime kwenda Rorya na kisha kuwaka moto ambapo miili ya watu 15 waliofariki dunia papo hapo iliungua moto, majeruhi 4 wakakimbizwa hospitali na mmoja wao akafariki dunia baadaye.
Mhe. Rais Magufuli amewakumbusha watumiaji wa barabara kuzingatia sheria na kanuni za usalama barabarani ikiwemo kuendesha vyombo vya moto kwa tahadhari na kuhakikisha vinakuwa katika hali ya usalama.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
27 Novemba, 2018
Taarifa kwa vyombo vya habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 27 Novemba, 2018 amefungua maktaba mpya, kubwa na ya kisasa ya Kikuu cha Dar es Salaam iliyojengwa katika Kampasi Mlimani (Mwl. Julius K. Nyerere) Jijini Dar es Salaam.
Maktaba hiyo kubwa Afrika Mashariki na Kati imejengwa kwa gharama ya shilingi Bilioni 93.6 ikiwa ni msaada kutoka Serikali ya China na inakuwa maktaba kubwa kuliko maktaba zote ambazo China imezijenga barani Afrika.
Katika taarifa yake Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Prof. William Anangisye amesema majengo ya maktaba hiyo yenye ghorofa mbili yamechukua eneo lenye ukubwa wa meta za mraba 20,000 yakiwa na uwezo wa kuhifadhi vitabu 800,000, kukalisha watumiaji 2,100 kwa wakati mmoja, yana kompyuta 160 zilizounganishwa na mtandao kwa ajili ya kusoma vitabu kwa njia ya kielektroniki, ofisi za wafanyakazi, eneo la wanafunzi wenye mahitaji maalum na ukumbi wa kisasa wa mihadhara wenye uwezo wa kuchukua watu 600.
Prof. Anangisye ameishukuru Serikali kwa mchango mkubwa uliosaidia kufanikisha ujenzi wa maktaba hiyo, ameishukuru Serikali ya China kwa kutoa msaada wa fedha za ujenzi huo na kampuni ya ujenzi ya Jiangsu Jiangdu ya China kwa kujenga majengo yenye ubora na hadhi ya hali ya juu.
Ameahidi kuwa Jumuiya ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam itahakikisha majengo ya maktaba hiyo yanatunzwa vizuri na maktaba inatumika kuwanufaisha wanafunzi wa chuo hicho pamoja na wanafunzi wa taasisi zingine za vyuo na wananchi wa kawaida.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa namna anavyotoa kipaumbele kwa sekta ya elimu na ameahidi kuwa wizara yake itaendelea kuhakikisha taasisi zote zilizo chini ya wizara hiyo zinaendeshwa kwa kuzingatia maadili na matumizi bora ya rasilimali, pia amemshukuru Balozi wa China hapa nchini Mhe. Wang Ke kwa kusimamia na kufuatilia kwa ukaribu ujenzi wa maktaba hiyo na kwa Serikali ya China kutoa shilingi Bilioni 50.8 kwa ajili ya ujenzi wa chuo cha elimu ya mafunzo ya ufundi stadi (VETA) Mkoani Kagera.
Akizungumza katika sherehe hizo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amemshukuru Balozi wa China hapa nchini Mhe. Wang Ke na kumuomba apeleke shukrani za Tanzania kwa Rais wa China Mhe. Xi Jinping kwa misaada ambayo China imekuwa ikiitoa kwa Tanzania, ikiwemo ujenzi wa Maktaba hiyo na Chuo cha VETA kitakachojengwa Mkoani Kagera.
Mhe. Rais Magufuli amesema urafiki wa China na Tanzania ulioasisiwa na Baba wa Taifa Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere na Mwenyekiti Mao Zedong umeendelea kuleta manufaa makubwa na kwamba Serikali ya Awamu ya Tano na itauendeleza na kuukuza uhusiano na ushirikiano huu mzuri.
“Jambo la kufurahisha ni kwamba misaada yao haiambatani na masharti. Wenyewe wakiamua kukupa wanakupa, walitujengea TAZARA, URAFIKI na pia wametusaidia katika maeneo mengine ya maendeleo” amesema Mhe. Rais Magufuli na kumhakikishia Mhe. Balozi Wang Ke kuwa Serikali itahakikisha kila msaada unaotolewa unatumiwa vizuri.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli amempongeza Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Mstaafu Prof. Rwekaza Mukandala kwa kuandaa mpango wa ujenzi wa maktaba hiyo, na pia amewapongeza Jumuiya ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa kupata maktaba ambayo itawasaidia kuongeza kiwango cha ubora wa elimu.
Amewataka wana Jumuiya ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kuhakikisha maktaba hiyo inatunzwa vizuri na ametoa wito kwa Watanzania kujifunza lugha ya Kichina katika jengo mojawapo la maktaba hiyo litakalokuwa likifundisha lugha hiyo kwa kuwa kuna manufaa makubwa kwa Watanzania kujifunza lugha hiyo.
Sherehe hizo zimehudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Balozi wa China hapa nchini Mhe. Wang Ke, Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, Mawaziri Wakuu Wastaafu Mhe. Jaji Mstaafu Joseph Sinde Warioba na Mhe. Edward Ngoyai Lowassa, Mawaziri, Mabalozi wa nchi mbalimbali na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Paul Makonda.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
27 Novemba, 2018
Taarifa kwa vyombo vya habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 26 Novemba, 2018 ameungana na Maaskofu, Mapadre, Watawa na Waumini wa Kanisa Katoliki kutoa heshima za mwisho kwa aliyekuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Mbeya Mhashamu Askofu Evaristo Chengula aliyefariki dunia tarehe 21 Novemba, 2018 katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete Jijini Dar es Salaam alikokuwa akipatiwa Matibabu.
Misa Takatifu ya kumuaga Marehemu Askofu Chengula iliyoongozwa na Askofu Mkuu Mwandamizi Jude Thadaeus Ruwa’ichi, imefanyika katika Kanisa la Mtakatifu Imakulata lililopo Makao Makuu ya Baraza la Maaskofu, Kurasini Jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu Mhe. Benjamin William Mkapa na Mkewe Mhe. Mama Anna Mkapa.
Akizungumza baada ya Misa hiyo Mhe. Rais Magufuli ametoa salamu za pole kwa Maaskofu wote wa Kanisa Katoliki, Mapadre, Watawa, Waumini wa Kanisa Katoliki Jimbo la Mbeya na Wakatoliki wote nchini kwa kuondokewa na kiongozi aliyekuwa akifanya vyema kazi yake ya kutangaza Injili.
Mhe. Rais Magufuli amesema pamoja na majukumu yake ya kutoa huduma za kiroho Marehemu Askofu Chengula alisimamia ukweli ikiwemo kupinga hadharani ndoa na mapenzi ya jinsia moja licha ya kuwepo mashinikizo mbalimbali.
Akitoa salamu kwa niaba ya Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC) Makamu wa Rais wa TEC Mhashamu Askofu Flavian Kasalla amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa ushirikiano alioutoa wakati wa kuuguza na baada ya kifo cha Askofu Chengula na pia amewashukuru madaktari na wauguzi, viongozi na wote waliokuwa wakimuombea kabla na baada ya kifo.
Mhashamu Askofu Evaristo Chengula amefariki dunia kwa ugonjwa wa moyo na baada ya Misa ya kumuaga mwili wake umesafirishwa kwenda Mbeya.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
26 Novemba, 2018
Taarifa kwa vyombo vya habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amemteua Dkt. Lutengano Undule Mwakahesya kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri wa Wakala wa Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja (Petroleum Bulk Procurement Agency – PBPA).
Taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi imeeleza kuwa uteuzi wa Dkt. Mwakahesya umeanza tarehe 21 Novemba, 2018.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
22 Novemba, 2018
Taarifa kwa vyombo vya habari
Benki ya Dunia imeridhia kutoa Dola za Marekani Milioni 300 sawa na shilingi Bilioni 680.5 kwa Tanzania kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa kuongeza ubora wa elimu ya sekondari unaokusudiwa kujenga vyumba vya madarasa, mabweni, maabara, nyumba za watumishi na kununua vifaa vya kufundishia.
Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia Kanda ya Afrika Dkt. Hafez Ghanem aliyekutana na Mhe. Rais Magufuli tarehe 16 Novemba, 2018 Ikulu Jijini Dar es Salaam amesema pamoja na kuridhia kutoa fedha za mradi huo, Benki hiyo inaendelea kufadhili miradi mbalimbali ya maendeleo nchini Tanzania yenye thamani ya Dola za Marekani Bilioni 5.2 sawa na zaidi ya shilingi Trilioni 13 na kwamba miradi hiyo inatekelezwa kutokana na uhusiano na ushirikiano mzuri uliopo kati yake na Tanzania.
Dkt. Hafez Ghanem amesema katika mazungumzo hayo wamejadili juu ya maendeleo ya miradi hiyo na kazi nzuri ambayo inafanywa na Tanzania kuimarisha uchumi, na pia amempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa matokeo mazuri ya mapambano dhidi ya rushwa na kuimarisha huduma za kijamii.
Kwa upande wake Mhe. Rais Magufuli ameishukuru Benki ya Dunia kwa ushirikiano na uhusiano mzuri na Tanzania na ameahidi kuwa Serikali ya Awamu ya Tano itaendeleza na kukuza uhusiano huo, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha fedha zote zinazotolewa kwa ajili ya miradi ya maendeleo zinatumika kwa miradi iliyokusudiwa.
“Namshukuru Dkt. Hafez Ghanem na Benki ya Dunia kwa kuendelea kutoa fedha kwa ajili ya miradi ya Tanzania, hizo Dola Milioni 300 ambazo baadhi ya watu wasiotutakia mema walisema zimefyekelewa mbali, anasema zitaletwa, na pia Benki ya Dunia imetoa Dola Bilioni 5.2 ambazo zinafadhili miradi mbalimbali ya elimu, nishati, barabara, kilimo, afya na maji, ni miradi mikubwa na mingi.
“Kwa hiyo amekuja kututhibitishia kuwa Benki ya Dunia haitatuacha” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Doto James ameitaja baadhi ya miradi inayoendelea kutekelezwa kwa ushirikiano na Benki ya Dunia kuwa ni mradi wa uboreshaji wa bandari ya Dar es Salaam ambayo ujenzi wake umefikia asilimia 24, ujenzi wa barabara za juu katika makutano ya barabara eneo la Ubungo Jijini Dar es Salaam, mradi wa ujenzi wa miundombinu ya mabasi yaendayo haraka (BRT) kwa awamu kwana na ya pili na miradi mingine mbalimbali.
Mazungumza kati ya Mhe. Rais Magufuli na Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia Dkt. Hafez Ghanem yamehudhuriwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt. Augustine Mahiga, Waziri wa Katiba na Sheria Prof. Palamagamba Kabudi, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu na Mwakilishi wa Benki ya Dunia hapa nchini Bi. Bella Bird.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
16 Novemba, 2018
Taarifa kwa vyombo vya habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 12 Novemba, 2018 ametangaza uamuzi wa Serikali kununua korosho zote za wakulima msimu huu kwa bei ya shilingi 3,300 kwa kilo baada ya wanunuzi binafsi kushindwa kutimiza maagizo ya Serikali kwa kuanza kununua kwa kusuasua na kwa bei isiyoridhisha.
Mhe. Rais Magufuli ametangaza uamuzi huo leo Ikulu Jijini Dar es Salaam muda mfupi baada ya kuwaapisha Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mhe. Joseph George Kakunda, Waziri wa Kilimo Mhe. Japhet Ngailonga Hasunga, Naibu Waziri Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Dkt. Mary Machuche Mwanjelwa, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Constantine John Kanyasu, Naibu Waziri wa Kilimo Mhe. Innocent Lugha Bashungwa, Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Mwita Mwikwabe Waitara na Mwenyekiti wa Tume ya Kurekebisha Sheria Mhe. Jaji Mstaafu January Henry Msoffe.
Pamoja na kutangaza uamuzi huo Mhe. Rais Magufuli ameagiza Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) kutoa fedha za kununulia korosho hizo na ameliagiza Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kupeleka askari katika maghala yote yenye korosho na kuanza ununuzi wa korosho mara moja kwa kushirikiana na Bodi ya Mazao Mchanganyiko.
Mhe. Rais Magufuli pia ameagiza wakulima waanze kulipwa fedha zao mara moja na bila kukatwa fedha yoyote.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli ameagiza kiwanda cha kubangua korosho cha BUCCO Investment Holding kilichopo Mkoani Lindi ambacho hivi karibuni kimechukuliwa na Serikali baada ya aliyeuziwa kiwanda hicho kushindwa kukiendesha, kikabidhiwe kwa JWTZ ili jeshi hilo lianze kukitumia kubangua korosho zitakazonunuliwa katika msimu huu.
Kiwanda hicho kina uwezo wa kubangua tani 20,000 za korosho kwa mwaka na Mhe. Rais ameagiza Bodi ya Mazao Mchanganyiko ianze kutafuta soko la ndani na nje ya nchi kwa ajili ya kuuza korosho zikiwemo zitakazobanguliwa kiwandani hapo.
“Mwaka huu huenda tutazalisha kati ya tani 210,000 na 220,000 za korosho, korosho hizi zinaweza kuzalisha tani takribani 70,000 za korosho zilizobanguliwa, kwa hiyo tutanunua korosho zote, tutatafuta soko tutaziuza na tusipopata soko tutakula sisi wenyewe” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Halikadhalika, Mhe. Rais Magufuli ameagiza Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kilichokuwa chini ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kuhamishiwa Ofisi ya Waziri Mkuu ili kuongeza ufanisi katika kupata wawekezaji wazuri hapa nchini.
Mhe. Rais Magufuli ameionya Bodi ya Pamba na bodi nyingine za mazao kuhakikisha zinatekeleza majukumu yao kwa maslahi ya wakulima badala ya kuwaacha wakikandamizwa na wanunuzi binafsi na amesisitiza kuwa “kilichotokea kwa Bodi ya Korosho, Bodi ya Pamba ijiandae”.
Kwa Mawaziri na Naibu Mawaziri wapya aliowateua, Mhe. Rais Magufuli amewataka kurekebisha dosari zote zilizojitokeza katika usimamizi wa Kilimo, Viwanda, Biashara na Uwekezaji, na ameelezea kutoridhishwa kwake na mwenendo wa wizara hizo mbili hali iliyosababisha afanye mabadiliko ya Mawaziri.
“Wizara ya Kilimo mambo mengi imebidi niwe namtuma Waziri Mkuu kwa sababu kwenye wizara hakuna hatua zinazochukuliwa na hakuna maamuzi, nataka Mawaziri muwe mnafanya maamuzi, haiwezekani wakulima wanapata shida Mawaziri mpo, Makatibu Wakuu wenu wapo na wataalamu wapo. Kule Dodoma wakulima wa zabibu wanapata shida mpaka leo hakuna utatuzi wa shida zao” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Tukio hilo limehudhuriwa na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job Yustino Ndugai na Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma ambao wamewataka viongozi wa Wizara ya Kilimo na Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kufanya kazi kwa kutambua umuhimu wa wizara hizo na uwekezaji mkubwa ambao nchi imeufanya katika kilimo.
Viongozi wengine waliohudhuria tukio hilo ni Mawaziri, Makatibu Wakuu, Viongozi Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama, Viongozi wa Dini, Viongozi wa Siasa, Majenerali wa JWTZ na viongozi wa Taasisi za Serikali.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
12 Novemba, 2018
Taarifa kwa vyombo vya habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amempongeza Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu Mhe. Benjamin William Mkapa kwa mchango wake mkubwa alioutoa wakati wa uongozi wake.
Mhe. Rais Magufuli ametoa pongezi hizo katika Misa Takatifu ya Shukrani ya Uhai kwa Rais Mstaafu Mkapa ambaye leo tarehe 12 Novemba, 2018 ametimiza miaka 80 tangu kuzaliwa iliyofanyika katika Parokia ya Bikira Maria Imakulata, Upanga Jijini Dar es Salaam na kuongozwa Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo.
Mhe. Rais Magufuli amesema wakati akiwa madarakani Rais Mstaafu Mkapa amefanya mambo mengi na muhimu kwa Taifa na amebainisha kuwa Watanzania wataendelea kumkumbuka kwa kazi nzuri aliyoifanya.
“Mhe. Rais Mstaafu Mkapa wakati wa uongozi wako ulifanya kazi kubwa, na kwa miaka 20 ambayo nilifanya kazi na wewe baada ya kuniteua kuwa Naibu Waziri na baadaye Waziri nilijifunza kuwa wewe ni mcha Mungu, muadilifu, mnyenyekevu kwa Mungu na mchapakazi.
“Leo unapotimiza miaka 80 nakushukuru na kukupongeza sana, nakuombea Mwenyezi Mungu aendelee kukupa afya njema wewe na familia yako, na sisi viongozi tuliopo sasa tutaendelea kuyaenzi mazuri yote uliyoyafanya” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Kwa upande wake Mhe. Rais Mstaafu Mkapa amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kumtakia heri, amewashukuru Maaskofu Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, Askofu Mkuu Mwandamizi Jude Thadaeus Ruwai’chi na Askofu Msaidizi Eusebius Nzigirwa walioongoza Misa hiyo pamoja na viongozi wengine na waumini wenzake.
Rais Mstaafu Mkapa amebainisha kuwa anampongeza Mhe. Rais Magufuli kwa uongozi wake kwa kuwa Tanzania imeendelea kuwa na sifa nzuri ya amani na umoja na kwamba hata akiwa nje ya nchi anapoulizwa siri ya Tanzania kuwa na Marais Wastaafu watatu ambao wanaishi vizuri nchini mwao, huwajibu kuwa siri kubwa ni uwepo wa amani, umoja na mshikamano.
Misa hiyo imehudhuriwa na Mke wa Rais Mama Janeth Magufuli na Mke wa Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu Mama Anna Mkapa.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
12 Novemba, 2018
Taarifa kwa vyombo vya habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 10 Novemba, 2018 amefanya mabadiliko madogo katika Baraza la Mawaziri kwa kuteua Mawaziri wawili na Naibu Mawaziri wanne.
Kwanza, Mhe. Rais Magufuli amemteua Mhe. Japhet Ngailonga Hasunga kuwa Waziri wa Kilimo.
Kabla ya uteuzi huo Mhe. Hasunga alikuwa Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, na anachukua nafasi ya Mhe. Dkt. Charles John Tizeba ambaye uteuzi wake umetenguliwa.
Pili, Mhe. Rais Magufuli amemteua Mhe. Joseph George Kakunda kuwa Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji.
Kabla ya uteuzi huo Mhe. Kakunda alikuwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), na anachukua nafasi ya Mhe. Charles John Mwijage ambaye uteuzi wake umetenguliwa.
Tatu, Mhe. Rais Magufuli amemteua Mhe. Constantine John Kanyasu kuwa Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii. Mhe. Kanyasu anachukua nafasi ya Mhe. Hasunga ambaye ameteuliwa kuwa Waziri wa Kilimo.
Nne, Mhe. Rais Magufuli amemteua Mhe. Dkt. Mary Machuche Mwanjelwa kuwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.
Kabla ya uteuzi huo Dkt. Mwanjelwa alikuwa Naibu Waziri wa Kilimo.
Tano, Mhe. Rais Magufuli amemteua Mhe. Mwita Mwikwabe Waitara kuwa Naibu Waziri wa TAMISEMI. Mhe. Waitara anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Mhe. Kakunda ambaye ameteuliwa kuwa Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji.
Sita, Mhe. Rais Magufuli amemteua Mhe. Innocent Lugha Bashungwa kuwa Naibu Waziri wa Kilimo. Mhe. Bashungwa anachukua nafasi ya Mhe. Dkt. Mwanjelwa ambaye ameteuliwa kuwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.
Uteuzi wa viongozi hawa umeanza leo tarehe 10 Novemba, 2018 na wateule wote wataapishwa Jumatatu tarehe 12 Novemba, 2018 saa 3:00 asubuhi, Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli ametengua uteuzi wa Mwenyekiti wa Bodi ya Korosho Mama Anna Margareth Abdallah na kuivunja bodi hiyo kuanzia leo tarehe 10 Novemba, 2018.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
10 Novemba, 2018
Taarifa kwa vyombo vya habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 10 Novemba, 2018 amekagua magari ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) yaliyoandaliwa kwa ajili ya kubeba korosho za wakulima endapo wanunuzi binafsi hawatatii maagizo ya Serikali ifikapo Jumatatu tarehe 12 Novemba, 2018 saa 10:00 Jioni.
Mhe. Rais Magufuli amefanya ukaguzi huo katika Kambi ya Jeshi ya Twalipo, Kikosi cha Usafirishaji cha 95KJ Mgulani Jijini Dar es Salaam ambapo magari 75 yenye uwezo wa kubeba tani 1,500 kwa mpigo yameandaliwa kwa ajili ya kubeba korosho katika mikoa ya Lindi, Mtwara, Ruvuma, Pwani na Tanga.
Akizungumza na Maafisa na Askari wa JWTZ waliokuwepo wakati wa ukaguzi huo, Mhe. Rais Magufuli amesema endapo wanunuzi binafsi hawatatii maagizo ya Serikali ya kununua korosho za wakulima kwa bei isiyopungua shilingi 3,000 kwa kilo sambamba na kutii agizo lililotolewa jana na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, hakuna mnunuzi yeyote atakayeruhusiwa kununua korosho na Serikali itachukua hatua ya kutumia JWTZ na Bodi ya Mazao Mchanganyiko kununua korosho zote za wakulima kwa bei ya zaidi ya shilingi 3,000 kwa kilo.
Mhe. Rais Magufuli amebainisha kuwa baada ya kununua korosho, Serikali itatafuta soko na korosho nyingine zitabanguliwa kwa ajili ya soko la ndani na nje ya nchi.
“Nataka kuwahakikishia wakulima wa korosho Serikali ipo na itaendelea kuwapigania, ikifika Jumatatu saa 10:00 jioni, hawa wanunuzi binafsi hawajajitokeza na kueleza watanunua tani ngapi, Serikali itanunua korosho zote na fedha za kununulia zipo” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Mhe. Rais Magufuli amesema Serikali inalazimika kuchukua hatua hizi baada ya wanunuzi binafsi kufanya mgomo wa kununua korosho kwa kusuasua licha ya kufanya nao mazungumzo na kufikia makubaliano tarehe 28 Oktoba, 2018 Jijini Dar es Salaam.
Katika mazungumzo hayo Serikali iliungana na msimamo wa wakulima wa korosho wa kukataa bei ya kati ya shilingi 1,900 hadi 2,700 kwa kilo, na hivyo kukubaliana kuwa korosho zitanunuliwa kwa bei isiyopungua shilingi 3,000 kwa kilo.
Mhe. Rais Magufuli amesema pamoja na kufikiwa kwa makubaliano hayo wanunuzi binafsi wameendelea kutotii kwani kati ya kampuni 37 zilizoomba kununua korosho ni kampuni 14 tu ndizo zimejitokeza na ununuzi unafanyika kwa kusuasua.
“Nimefurahi sana kwamba Jeshi letu la Ulinzi Tanzania lipo tayari kufanya operesheni hii na tunaweza kuiita OPERESHENI KOROSHO, nimeambiwa kuwa kuna takribani tani 210,000 za korosho, kule Lindi na Mtwara kuna maghala yanayoweza kuhifadhi tani 77,000 na hapa Dar es Salaam kuna maghala yanayoweza kuhifadhi zaidi ya tani 90,000 pamoja na maghala mengine, natarajia kuona zoezi hili linakamilika haraka.
“Na kutokana na jambo hili, sasa JWTZ kupitia Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ianze kufikiria kuanzisha kiwanda kikubwa cha kubangua korosho, hata kama itakuwa ni kwa Serikali kutoa fedha za kujenga kiwanda hicho, tuanze kuachana na uuzaji wa korosho ghafi, huo ni utumwa, tuwe na viwanda vyetu na vijana wetu wapate ajira” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Mapema akitoa taarifa ya maandalizi ya kutekeleza jukumu hilo, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jen. Venance Mabeyo amesema JWTZ imetayarisha magari ya uwezo tofauti 75 yenye uwezo wa kubeba jumla ya tani 1,500 kwa mpigo na kwamba tani nyingine 500 zitabebwa na meli ya kijeshi (Landing Craft) ambayo inaweza kutia nanga mahali popote katika ufukwe wa bahari.
“Mhe. Rais na Amiri Jeshi Mkuu tupo tayari kutekeleza jukumu hili” amesema Jen. Mabeyo.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
10 Novemba, 2018
Taarifa kwa vyombo vya habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 08 Novemba, 2018 amepokea hati za utambulisho za Mabalozi 3 walioteuliwa kuziwakilisha nchi za Hispania, Canada na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) hapa nchini, baada ya Mabalozi waliokuwepo kumaliza muda wao.
Waliowasilisha hati zao za utambulisho ni Mhe. Francisco Pedros Carretero – Balozi wa Hispania hapa nchini, Mhe. Pamela O’donnel – Balozi wa Canada hapa nchini na Mhe. Khalifa Abdulrahaman Mohamed Al-Marzooqi – Balozi wa Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) hapa nchini.
Pamoja na kuwakaribisha Mabalozi hao Mhe. Rais Magufuli amewahakikishia kuwa Tanzania inathamini uhusiano na ushirikiano mzuri kati yake na nchi hizo na ameahidi kuwa Serikali ya Awamu ya Tano itaendeleza na kukuza uhusiano huo kwa manufaa ya wananchi wa nchi zote.
Mhe. Rais Magufuli amewaambia Mabalozi hao kuwa Serikali inatarajia kuona shughuli mbalimbali ikiwemo miradi ya maendeleo iliyokuwa ikisimamiwa na Mabalozi waliotangulia inaendelezwa na kuanzisha maeneo mapya ya ushirikiano ikiwemo uwekezaji katika viwanda, ujenzi wa miundombinu, ufadhili katika miradi ya huduma za kijamii kama vile maji, afya na nishati zikipata msukumo mkubwa zaidi.
Kwa upande wao Mabalozi hao wameahidi kuendeleza na kukuza zaidi uhusiano na ushirikiano wa Tanzania na nchi wanazoziwakilisha na wamempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa juhudi zake za kukuza uchumi, kupiga vita rushwa na kuimarisha ustawi wa jamii.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
08 Novemba, 2018
Taarifa kwa vyombo vya habari
Uamuzi wa Serikali ya Awamu ya Tano kufungua Ubalozi wa Tanzania nchini Israel umeanza kuzaa matunda baada ya timu ya madaktari na wataalamu wa matibabu ya moyo 30 kutoka nchini Israel kuja hapa nchini kwa ajili ya kuokoa maisha ya watoto 51 wanaopatiwa matibabu katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete Jijini Dar es Salaam.
Timu ya Madaktari na wataalamu hao wakiwemo 2 kutoka Marekani na Canada wanatoka shirika la Save a Child’s Heart la Israel wamekutana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete Prof. Mohamed Janabi amesema kati ya watoto 51 wanaopatiwa matibabu katika kampeni hii 10 watafanyiwa upasuaji wa kufungua kifua na 20 watafanyiwa upasuaji kwa kutumia tundu dogo.
Prof. Janabi amebainisha kuwa kwa kipindi cha miaka mitatu iliyopita Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete imetoa matibabu ya moyo kwa wagonjwa 254,881 ambapo kati yake wagonjwa 799 wamefanyiwa upasuaji wa kufungua kifua, 2,056 wamefanyiwa upasuaji kwa kutumia tundu dogo na wengine wamepatiwa matibabu mengine ya moyo.
Ameongeza kuwa ushirikiano wa taasisi hiyo na wataalamu kutoka nje ya nchi umesaidia kuwawezesha wataalamu wa Tanzania kutoa huduma za kibingwa za matibabu ya moyo na pia kuokoa gharama kubwa zilizokuwa zikitumika kupeleka wagonjwa nje ya nchi, ambapo kwa kipindi cha miaka mitatu Tanzania imetumia shilingi Bilioni 22 ikilinganishwa na shilingi Bilioni 87.8 ambazo zingetumika kutoa matibabu hayo nje ya nchi.
Kiongozi wa timu ya Madaktari hao na Mkurugenzi Mtendaji wa Save a Child’s Heart Bw. Simon Fisher na Mkuu wa Kitengo cha upasuaji wa moyo wa shirika hilo Prof. Sasson Lior wamemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa ushirikiano mkubwa ambao timu hiyo inapata kutoka Serikali ya Tanzania na wameahidi kuwa taasisi hiyo itaendelea kushirikiana na Tanzania kuokoa maisha ya watoto.
Kwa upande wake Mhe. Rais Magufuli amewashukuru madaktari na wataalamu hao kwa kuja Tanzania kuokoa maisha ya watoto na pia amemshukuru Waziri Mkuu wa Israel Mhe. Benjamin Netanyahu kwa kuendeleza na kuimarisha uhusiano na ushirikiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na Israel.
Mhe. Rais Magufuli amemuandikia barua ya shukrani Mhe. Netanyahu na kuikabidhi kwa Balozi wa Israel hapa nchini Mhe. Noah Gal Gendler ambapo pamoja na kushukuru kwa msaada wa matibabu pia amemshukuru kwa ushirikiano katika sekta nyingine.
“Israel ni marafiki zetu wa siku nyingi, tunasaidiana na kushirikiana kwa mengi, ndio maana niliona tufungue Ubalozi wetu kule Israel ili kurahisha masuala haya muhimu ya ushirikiano na yenye manufaa kwa watu wetu” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Mhe. Rais Magufuli ametoa wito kwa Balozi wa Israel hapa nchini Mhe. Noah Gal Gendler na wataalamu hao kuwahamasisha wawekezaji wanaoweza kuja kujenga viwanda vya dawa na vifaa tiba hapa nchini na kuwahakikishia kuwa Serikali itanunua dawa na vifaa hivyo, na pia watakuwa na uhakika wa soko la Afrika Mashariki na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC).
Mhe. Rais Magufuli pia amewapongeza Madaktari wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete kwa juhudi kubwa wanazozifanya kuokoa maisha ya watu na amewahakikishia kuwa Serikali inatambua juhudi hizo na itaendelea kuwajengea mazingira bora ya kazi.
Tukio hili limehudhuriwa na Naibu Waziri wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile.
Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli amefanya mazungumzo na Balozi wa Israel hapa nchini Mhe. Noah Gal Gendler na baada ya mazungumzo hayo Mhe. Gendler amesema Israel imetoa nafasi za masomo kwa watanzania 150 watakaogharamiwa na Serikali ya Israel kwa ajili ya kujifunza utaalamu wa kilimo cha kisasa kwa miezi 11.
Halikadharika Mhe. Rais Magufuli amekutana na Daktari Bingwa wa upasuaji wa ubongo na uti wa mgongo Prof. Roger Hartl kutoka nchini Marekani ambaye amepongeza juhudi za Tanzania kuendeleza huduma za matibabu ya kibingwa na ameahidi kuendeleza ushirikiano kati ya taasisi yake ya Weill Cornell Medicine iliyopo nchini Marekani na Tanzania.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
08 Novemba, 2018
Taarifa kwa vyombo vya habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amemteua Lut Jen. Mstaafu Samweli A. Ndomba kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Mzinga.
Lut Jen. Mstaafu Ndomba anachukua nafasi ya Bw. Andrew Severin Nyumayo ambaye amemaliza muda wake.
Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli amemteua Prof. Zacharia M.D. Mganilwa kuwa Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) kwa kipindi kingine cha miaka mitano.
Uteuzi wa viongozi hawa umeanza tarehe 05 Novemba, 2018.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
07 Novemba, 2018
Taarifa kwa vyombo vya habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 04 Novemba, 2018 ameungana na Waumini wa Kanisa Katoliki hapa nchini kuadhimisha Jubilei ya miaka 150 ya Uinjilishaji Tanzania Bara.
Misa Takatifu ya maadhimisho ya Jubilei hiyo ambayo imefanyika Bagamoyo Mkoani Pwani ambako Ukristo uliingia mwaka 1868 imeongozwa na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Nairobi nchini Kenya Mwadhama John Kardinali Njue.
Misa hiyo imehudhuriwa na Mke wa Rais Mhe. Mama Janeth Magufuli, Rais Mstaafu Mhe. Benjamin William Mkapa, Spika Mstaafu Mhe. Anne Makinda, Maaskofu wa Majimbo yote ya Kanisa Katoliki hapa nchini na nchi jirani, Mapadre, Watawa na waumini wa Kanisa hilo kutoka majimbo yote hapa nchini.
Akizungumza katika Misa hiyo, Mhe. Rais Magufuli amelipongeza Kanisa Katoliki kwa mchango lililoutoa kuwahudumia Watanzania kiroho na kutoa huduma za kijamii tangu miaka 150 iliyopita na ameahidi kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na Kanisa katika kudumisha amani na upendo na kuwaletea wananchi maendeleo.
Mhe. Rais Magufuli amewashukuru Maaskofu, Mapadre, Watawa na viongozi wote wa Kanisa Katoliki kwa namna wanavyoshirikiana na Serikali na Madhehebu mengine ya dini katika kuleta maendeleo na kuimarisha ustawi wa jamii bila kubagua na amewaomba waendelee kukemea vitendo viovu vikiwemo uvunjifu wa amani, rushwa, ufisadi na ubakaji.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli amewashukuru wananchi wa Bagamoyo kwa kuupokea Ukristo ambao uwepo wake umeleta manufaa makubwa kwa Watanzania na ameahidi kuwa Serikali itashirikiana na viongozi wa Kanisa hilo kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili.
Rais wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC) Mhashamu Gervas Nyaisonga amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kuungana na Kanisa Katoliki katika Jubilei hiyo, amempongeza kwa kazi nzuri ya kutimiza ahadi alizozitoa kwa Watanzania katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wake na ameahidi kuwa Kanisa Katoliki litaendelea kuliombea Taifa na kushirikiana na Serikali.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
04 Novemba, 2018