Taarifa kwa vyombo vya Habari ya zamani
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ametangaza siku 4 za maombolezo kuanzia leo tarehe 21 Septemba, 2018 kufuatia ajali ya kuzama kwa kivuko cha MV Nyerere katika ziwa Victoria na kusababisha vifo vya watu 131 waliothibitika mpaka sasa.
Kivuko hicho kilipinduka na kisha kuzama majini jana mchana meta chache kabla ya kufika katika kisiwa cha Ukara kikitokea kisiwa cha Bugolora ambapo mpaka sasa watu 40 wameokolewa wakiwa hai, miili 131 imeopolewa na zoezi la uokoaji linaendelea.
Pamoja na kutangaza siku 4 za maombolezo Mhe. Rais Magufuli amewapa pole wote waliopoteza jamaa zao katika ajali hiyo, amewaombea majeruhi wapone haraka na amewapongeza viongozi wa Mkoa wa Mwanza, vyombo vya ulinzi na usalama na wananchi wote wanaoendelea kushiriki katika uokoaji.
“Kwa masikitiko makubwa nawapa pole wote waliopoteza jamaa zao katika ajali hii, huu ni msiba mkubwa uliolikumba Taifa letu, nawaomba Watanzania wote kwa wakati huu ambapo vyombo vyetu vya ulinzi na usalama kwa kushirikiana na wananchi wanaendelea na uokoaji tuwe watulivu na tuendelee na kushikamana kama ilivyo desturi yetu, huu sio wakati wa kulumbana na kukatishana tamaa” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli amewataka Watanzania kuwapuuza wanaotaka kutumia ajali hii kujipatia umaarufu wa kisiasa, na amebainisha kuwa ni vema Watanzania wote tuungane kuwaombea Marehemu wapumzike mahali pema, majeruhi wapone haraka na kuwatia moyo wote wanaoendelea na zoezi la uokoaji.
Mhe. Rais Magufuli amemtuma Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa kwenda eneo la tukio, ameagiza kuundwa tume ya uchunguzi wa chanzo cha ajali hii na ameagiza wote waliohusika kusababisha ajali hii wakamatwe na kufikishwa katika vyombo vya sheria.
“Taarifa za awali zimeonesha dhahiri kuwa kivuko cha MV Nyerere kilikuwa na idadi kubwa ya watu na mizigo kupita uwezo wake, kama kuna mtu yeyote mwenye ushahidi wa chanzo chochote cha ajali hii, tunatarajia kuwa ataupeleka mahakamani” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
21 Septemba, 2018
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amemteua Balozi Mstaafu Ali Idi Siwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF).
Uteuzi wa Balozi Mstaafu Ali Idi Siwa unaanza leo tarehe 20 Septemba, 2018.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
20 Septemba, 2018
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 12 Septemba, 2018 amewaapisha viongozi watatu aliowateua hivi karibuni.
Viongozi walioapishwa ni Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto (anayeshughulikia Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto) Dkt. John Kiang’u Jingu, Balozi wa Tanzania nchini Uganda Dkt. Aziz Ponary Mlima na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) CP Diwani Athumani Msuya.
Hafla ya kuapishwa kwa viongozi hao imefanyika katika Ikulu ya Chamwino Mkoani Dodoma na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job Yustino Ndugai, Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi, Mawaziri, viongozi wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama na viongozi wa Mkoa wa Dodoma wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa huo Dkt. Binilith Satano Mahenge.
Akizungumza baada ya kuwaapisha, Mhe. Rais Magufuli amemtaka Dkt. Jingu kwa kushirikiana na viongozi wengine wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kufuatilia usajili na utendaji kazi wa mashirika yasiyo ya kiserikali (NGO’s), na kuhakikisha yanafanya kazi kwa kuzingatia sheria ambazo pamoja na mambo mengine zinayataka kuendesha shughuli zao kwa uwazi hususani masuala ya mapato na matumizi ya fedha za ufadhili wa shughuli zake.
Mhe. Rais Magufuli amemtaka Balozi wa Tanzania nchini Uganda, Mhe. Dkt. Mlima kusimamia vizuri ushirikiano wa Tanzania na Uganda hasa biashara na uwekezaji unaoendelea kati ya nchi hizi mbili na kuhakikisha Tanzania inanufaika na ushirikiano huo.
Halikadhalika, Mhe. Rais Magufuli amemtaka Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU CP Diwani Athumani Msuya kuongeza kasi ya kushughulikia tatizo la rushwa nchini kwa kuhakikisha wote wanaokabiliwa na tuhuma za kujihusisha na rushwa wanafikishwa mahakamani na sheria inachukua mkondo wake.
Mhe. Rais Magufuli pia amemtaka CP Diwani kuungalia upya muundo wa TAKUKURU ili uweke bayana majukumu ya Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, na kuhakikisha watendaji wa taasisi hiyo wanaoonekana kutofanya kazi kwa tija na kujihusisha na vitendo vya rushwa wanachukuliwa hatua ikiwa ni pamoja na kuondolewa kazini na kufikishwa mahakamani.
“Nataka ukaisafishe TAKUKURU, kuna baadhi ya wafanyakazi wa TAKUKURU wanajihusisha na rushwa, kawaondoe, nataka kuona TAKUKURU inashughulikia rushwa kwelikweli hasa rushwa kubwakubwa, ukipita huko vijijini wananchi wanateseka sana, wananyanyaswa na kuna dhuluma nyingi sana, na tatizo kubwa ni rushwa” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Viongozi walioapishwa na Mhe. Rais Magufuli pia wamekula kiapo cha uadilifu kwa watumishi wa umma kilichoongozwa na Kamishna wa Maadili Mhe. Jaji Mstaafu Harold Nsekela na baada ya viapo vyao wamemshukuru Mhe. Rais kwa kuwateua na wamemuahidi kufanya kazi kwa juhudi, maarifa na kwa kutanguliza maslahi ya Taifa.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Chamwino
12 Septemba, 2018
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amewaagiza viongozi wa Mikoa na Wilaya zote nchini kwa kushirikiana na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuandaa mipango bora itakayowawezesha wafugaji kufuga mifugo yao bila kuwaathiri wakulima, badala ya kuwafukuza wafugaji katika maeneo yao kwa madai kuwa ni wavamizi.
Mhe. Rais Magufuli ametoa agizo hilo leo wakati akizungumza na wananchi wa Itilima na Meatu katika ziara yake inayoendelea hapa Mkoani Simiyu.
Amefafanua kuwa Watanzania wote wana haki ya kuishi mahali popote katika nchi yao hivyo ni wajibu wa viongozi wa Mikoa na Wilaya kutengeneza mipango itakayoainisha maeneo ya malisho na huduma nyingine za mifugo badala ya kufukuza wafugaji kana kwamba sio raia wa Tanzania.
“Wafugaji na wakulima wanahitajiana, wakulima wanawahitaji ng’ombe na wafugaji wanahitaji mazao ya kilimo, kwa hiyo changamoto ni kwenu viongozi wa Mikoa na Wilaya kutengeneza mipango mizuri itayowapa haki makundi yote kuishi bila migogoro” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli ameiagiza Wizara ya Maliasili na Utalii kusimamia vizuri maliasili za Taifa ikiwemo kuzuia uvamizi katika hifadhi za taifa, mapori ya akiba na misitu ya Serikali, pamoja na kuhakikisha wawekezaji na wafanyabiashara wote wanaokuja kuendesha shughuli zao hapa nchini katika sekta ya utalii, wanalipa kodi na tozo zote wanazopaswa kulipa.
Katika ziara ya leo Mhe. Rais Magufuli ambaye ameongozana na baadhi ya Mawaziri amejibu kero za wananchi kuhusiana na maji, huduma za afya na barabara, ambapo Waziri wa Maji na Umwagiliaji Prof. Makame Mbarawa amemhakikishia Mbunge wa Itilima Mhe. Njalu Silanga na wananchi wake kuwa Serikali inachimba visima 40 vya maji kwa gharama ya Shilingi Bilioni 1.55 na mabwawa 2 yatakayogharimu shilingi Bilioni 1.5 kwa ajili ya vijiji vya Nhobora, Sawira na Mwamapalala, na kwa Mji wa Mwanhuzi ambao ni Makao Makuu ya Wilaya ya Meatu, Serikali imetenga shilingi Milioni 318 kwa ajili ya kuchimba visima 8 vya maji na shilingi Milioni 214 kwa ajili ya kuimarisha mfumo wa usambazaji maji katika Mji huo.
Nae Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu amesema mwaka huu Serikali imetenga shilingi Milioni 600 kwa ajili ya ujenzi wa zahanati na kituo cha afya katika Jimbo la Itilima, na kwa Wilaya ya Meatu pamoja na kutoa shilingi Milioni 607 kwa ajili ya kuboresha huduma za afya, Serikali ipo katika mipango ya ujenzi wa kiwanda kikubwa cha kuzalisha bidhaa za hospitali kitakachogharimu shilingi Bilioni 29.3.
Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Selemani Jafo amesema pamoja na kujenga majengo ya Halmashauri ya Itilima katika mwaka huu wa fedha Serikali imetenga shilingi Bilioni 1.5 za kujengea Hospitali ya Wilaya na kwa Jimbo la Kisesa ameahidi kutafuta fedha kwa ajili ya kujenga kituo cha afya.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Isack Kamwelwe amewahakikishia wananchi wa Itilima, Kisesa na Meatu kuwa Serikali itaendelea kuimarisha miundombinu ya barabara na madaraja na kwamba sasa inajiandaa kufanya usanifu wa awali kwa barabara ya Bariadi – Itilima – Kisesa – Mwandoya – Ngoboko ili baadaye ijengwe kwa kiwango cha lami.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Kangi Lugola amesema kama ambavyo Wizara yake kupitia Jeshi la Polisi imefanya juhudi kubwa kukabiliana na mauaji ya vikongwe na wenye ualbino, inaendelea kufanya juhudi kama hizo kuhakikisha ujambazi, uporaji, wizi na unyanyasaji wa raia na mali zao haupati nafasi, na ametoa wito kwa wananchi kutoa taarifa kila wanapobaini vitendo vya uvunjaji wa sheria.
Naibu Mawaziri wa Madini Mhe. Doto Biteko na Mhe. Stanslaus Nyongo wameahidi kuendelea kusimamia vizuri rasilimali ya madini na kwamba ili kuvutia uwekezaji zaidi katika uzalishaji wa chumvi tayari Serikali imefuta kodi 8 kati ya 11 zilizokuwepo.
Katika mkutano wa hadhara uliofanyika Mwanhuzi, Mhe. Rais Magufuli amepokea ombi la Mbunge wa Jimbo la Meatu Mhe. Salum Hamis Salum “Mbuzi” la kujengewa barabara za Mji huo na ameiagiza Wizara ya Ujenzi kuanza ujenzi wa kilometa 3 za barabara hizo ndani ya miezi miwili kuanzia sasa.
Mhe. Rais Magufuli amemshukuru Mwakilishi Mkazi wa Shirika la umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu (UNFPA) Bi. Jacqueline Mahon kwa ufadhili wa shilingi Bilioni 9 za kutekeleza mradi wa Nilinde Nikulinde ambao unaimarisha huduma za afya kwa kupanua zahanati 31, hospitali 2, vituo vya afya 5, kujenga benki ya damu ya Mkoa, kununua magari 9 na kununua vifaa vya hospitali.
Pia Mhe. Rais Magufuli amefungua majengo ya uboreshaji wa utoaji wa huduma za afya katika Hospitali ya Wilaya ya Meatu kwa niaba ya vituo vingine 39 vya kutolea huduma za afya katika Mkoa wa Simiyu na kuzungumza na wafanyakazi wa hosptali hiyo.
Kesho Mhe. Rais Magufuli ataendelea na ziara yake ambapo ataweka jiwe la msingi la ujenzi wa daraja la Sibiti linalounganisha Mkoa wa Simiyu na Mkoa wa Singida.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Mwanhuzi, Meatu
09 Septemba, 2018
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amemteua Ndg. Stephen Masato Wasira kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere.
Ndg. Wasira anachukua nafasi ya Prof. Mark James Mwandosya.
Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli amemteua Dkt. Festus Bulugu Limbu kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (National Economic Empowerment Council – NEEC).
Dkt. Limbu anachukua nafasi ya Dkt. John Jingu ambaye ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto (anayeshughulikia Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto).
Uteuzi wa viongozi hao unaanza leo tarehe 09 Septemba, 2018.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Bariadi
09 Septemba, 2018
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 08 Septemba, 2018 ameendelea na ziara yake katika Kanda ya Ziwa ambapo ameweka jiwe la msingi la mradi wa maji wa Lamadi na kufungua barabara za Mji wa Lamadi katika Wilaya ya Busega, amefungua jengo la wagonjwa wa nje (OPD) la Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Simiyu, na ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa kiwango cha lami wa barabara ya Maswa – Bariadi.
Mradi wa maji wa Lamadi utakaozalisha lita Milioni 3.3 za maji kwa siku ambayo ni mara mbili ya mahitaji ya lita Milioni 1.8 ya wakazi wa mji huo kwa sasa, utatatua kero ya miaka mingi ya uhaba wa maji kwa wakazi hao ambao kwa sasa wanapata maji kwa asilimia 23 tu ya mahitaji yao.
Waziri wa Maji na Umwagiliaji Prof. Makame Mbarawa amemueleza Mhe. Rais Magufuli kuwa mradi huo ambao umepangwa kukamilika mwezi Mei 2019 utagharimu shilingi Bilioni 12.83 na ni sehemu ya mpango wa uboreshaji wa huduma za majisafi na usafi wa mazingira wa ziwa Victoria (LV WATSAN) unaotekelezwa katika miji ya Mwanza, Musoma, Bukoba, Magu, Misungwi na Lamadi kwa gharama ya shilingi Bilioni 276, fedha ambazo zimetolewa kwa mkopo nafuu kutoka Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD), Benki ya Uwekezaji ya Ulaya (EIB) na Serikali ya Tanzania.
Ujenzi wa barabara za Mji wa Lamadi zenye jumla ya kilometa 6.26 umegharimu shilingi Bilioni 9.192 ambapo barabara hizo zimewekewa taa, mifereji, njia za waenda kwa miguu na eneo la kuegesha magari lenye ukubwa wa meta 900.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Selemani Jafo amemueleza Mhe. Rais Magufuli kuwa pamoja na barabara hizo Serikali itajenga kituo cha mabasi na kilometa nyingine 1.5 ya barabara, kununua gari la taka na kuandaa ramani ya mpango mji katika Mji wa Lamadi kwa gharama ya shilingi Bilioni 6.47, na kwamba mradi kama huo unatekelezwa katika miji mingine 17 hapa nchini kwa gharama ya shilingi Bilioni 561 ikiwa ni fedha za mkopo nafuu ktoka Benki ya Dunia.
Jengo la wagonjwa wa nje la Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Simiyu limejengwa katika eneo la Nyaumata kwa ghamara ya shilingi Bilioni 1.8, na ni sehemu ya mradi mzima wa ujenzi wa miundombinu ya hospitali hiyo uliopangwa kugharimu shilingi Bilioni 11. Gharama za ujenzi huo zimepungua kutoka makadirio ya awali ya shilingi Bilioni 46 baada ya Mhe. Rais Magufuli kutembelea mradi huo mwaka juzi na kutoa maelekezo ya kutaka zipunguzwe ili ziendane na gharama halisi za ujenzi.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu amesema Serikali imetenga shilingi Bilioni 3 kwa ajili ya kujenga miundombinu mingine ya hospitali hiyo katika kipindi cha miezi 6, na kwa kuunga mkono ukamilishaji wa haraka wa hospitali hiyo Mhe. Rais Magufuli ameahidi kuongeza fedha nyingine shilingi Bilioni 4.
Ujenzi wa barabara ya Maswa – Bariadi yenye urefu wa kilometa 49.7 utagharimu shilingi Bilioni 88.877, na barabara hii ni sehemu ya barabara ya Mwigumbi – Maswa – Bariadi – Lamadi yenye urefu wa kilometa 171.8.
Akizungumza katika miradi hiyo Mhe. Rais Magufuli amezishukuru taasisi zote za kimataifa zilizotoa mikopo nafuu kwa Tanzania kwa lengo la kufanikisha miradi hiyo, na ameahidi kuwa Serikali itahakikisha miradi hiyo inatekelezwa vizuri na inaleta manufaa yanayotarajiwa kwa wananchi.
Mhe. Rais Magufuli amewapongeza wananchi wa Simiyu kwa kupata miradi hiyo na ametoa wito kwa Watanzania wote kuunga mkono juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali katika kuwaletea maendeleo, ikiwa ni pamoja na kulipa kodi kwa kuwa fedha za kugharamia miradi hiyo zinatokana na kodi zao.
Mhe. Rais Magufuli amempongeza Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Bw. Anthony Mtaka, viongozi na wakulima wa mkoa wa Simiyu kwa juhudi kubwa walizofanya katika kuongeza uzalishaji wa zao la pamba, ambapo katika msimu uliopita kati ya kilo Milioni 226 zilizozalishwa hapa nchini, kilo Milioni 120 zimezalishwa katika Mkoa wa Simiyu.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli ameitaka Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) kufanya kazi usiku na mchana ili kukamilisha haraka ujenzi wa miundombinu ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Simiyu.
Mhe. Rais Magufuli pia ameagiza Wakurugenzi wote wa Halmashauri za Wilaya, Miji, Manispaa na Majiji kuhakikisha fedha za vijana na wanawake (asilimia 10) zinatengwa kama inavyopaswa ili kuwawezesha vijana kupata fedha za kufanya shughuli za ujasiriamali.
Mhe. Rais Magufuli kesho anaendelea na ziara yake hapa Mkoani Simiyu kwa kutembelea Wilaya ya Meatu.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Bariadi
08 Septemba, 2018
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amewataka viongozi wa Wizara, Mikoa na Wilaya kuhakikisha kero na malalamiko wananchi wanyonge yanatafutiwa ufumbuzi haraka badala ya kuwaacha wakipigwa danadana.
Mhe. Rais Magufuli ametoa maagizo hayo tarehe 07 Septemba, 2018 wakati akizungumza na wananchi akiwa njiani kutoka Mugumu kwenda Tarime katika eneo la daraja la mto Mara Wilayani Serengeti, na Nyamongo, Nyamwaga na Tarime Mjini Wilayani Tarime ambako ameendelea na ziara yake katika Mkoa wa Mara.
Kabla ya kutoa maagizo hayo Mhe. Rais Magufuli amekagua maendeleo ya ujenzi wa daraja la mto Mara lililopo katika barabara inayounganisha Mugumu na Tarime ambalo lina urefu wa meta 94, upana meta 9.9, ambalo ujenzi wake umefikia asilimia 75 na litagharimu shilingi Bilioni 8.5 hadi kukamilika.
Akizungumza na wananchi baada ya kukagua ujenzi wa daraja hilo Mhe. Rais Magufuli amesikiliza kilio cha Mama mmoja mwenye upofu aitwaye Nyambura Nyamarasa aliyedai mazao yake yameliwa na mifugo, na kwamba juhudi za kufuatilia haki yake hazijafanikiwa huku akiendelea kuhangaika.
Mhe. Rais Magufuli ameelezea kutofurahishwa na Mkuu wa Wilaya ya Serengeti Bw. Nurdin Babu ambaye hajachukua hatua licha ya Mama huyo kumpelekea kilio chake, na ameagiza vyombo vya dola vimkamate mtu anayedaiwa kulisha mifugo katika shamba la Mama huyo na kumfikisha katika vyombo vya sheria.
“Viongozi niliowachagua na mnaofanya kazi na Serikali ninayoongoza, nataka kuona mnashughulikia matatizo ya watu wanyonge, sitaki kuona watu wenye fedha wanawanyanyasa masikini, na kweli leo nilitaka kukufukuza kazi Mkuu wa Wilaya, nakusamehe lakini kashughulikie haki ya huyo Mama na viongozi wote hakikisheni watu wanyonge hawanyanyaswi” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Katika Mji wa Nyamongo wananchi wamemuomba Mhe. Rais Magufuli awasaidie kutatua tatizo la maji huku wakibainisha kuwa kuna fedha shilingi Milioni 700 za mradi huo zimetumika ilihali maji hakuna, pia wamemuomba awasaidie kulipwa fidia waliopisha uwekezaji wa mgodi wa madini.
Hata hivyo Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime Bw. Apoo Castro Tindwa amesema mradi wa maji wa shilingi Milioni 700 unatekelezwa na mwekezaji ambaye ni kampuni ya Acacia na kwamba Halmashauri ya Wilaya ya Tarime hawajaupokea kutokana na kutotoa maji.
Kuhusu madai ya kulipwa fidia ya ardhi kwa wananchi waliopisha uwekezaji wa kampuni ya madini ya Acacia, Naibu Waziri wa Madini Mhe. Doto Biteko amesema zoezi hilo linakwamishwa na wananchi wenyewe kutokana na baadhi yao kupeleka madai wakati hawana maeneo huku akibainisha kuwa uhakiki uliofanywa na Wizara kwa majina 1,544 umebaini kuwa majina 720 yalikuwa hewa na majina 1,116 wahusika hawakujitokeza kuhakikiwa wakiwemo watumishi wa umma, hivyo akatoa wito kwa wananchi wanaowakwamisha wenzao kulipwa fidia waache kufanya hivyo.
Akizungumza na wananchi wa Nyamongo Mhe. Rais Magufuli amesema atafuatilia utekelezaji wa mradi wa maji unaogharamiwa na kampuni ya Acacia, lakini amewaagiza viongozi wa Tarime na Mkoa wa Mara kumfuatilia mtu anayedaiwa kukusanya asilimia moja ya mapato ya mgodi wa Acacia badala ya malipo hayo kupatiwa vijiji 6 vinavyozungumza mgodi huo ili aeleze fedha zote alizokusanya na zipo wapi.
“Mnaweza mkawa mnabishana na kupoteza muda kwa ajili ya hizo shilingi Milioni 700 wakati hapa kuna mtu anakusanya fedha nyingi zaidi kwa kujifanya yeye ni mbia kwa niaba ya vijiji 6, hizo fedha anazokusanya zingemaliza matatizo yote ya maji hapa Nyamongo na zingesaidia mahitaji mengine ya wananchi” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Kabla ya kuondoka Nyamongo Mhe. Rais Magufuli amesikiliza maombi ya kupatiwa vitabu, mabweni na maabara kutoka kwa wanafunzi wa shule ya Sekondari Ingwe, na papo hapo akaendesha harambee ya kuchangisha fedha ambapo amefanikiwa kupata shilingi Milioni 26 zikiwemo shilingi Milioni 5 alizotoa yeye papo hapo kwa ajili ya kusaidia shule hiyo.
Mhe. Rais Magufuli pia amesalimiana na wananchi wa Nyamwaga ambao wamemuomba Serikali ihamishie Makao Makuu ya Halmashauri ya Wilaya ya Tarime Mjini hapo, na katika majibu yake amesema ombi hilo lifikishwe kwake kupitia hatua zinazostahili.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli amehutubia mkutano wa hadhara Mjini Tarime na kuwahakikishia wananchi wa mji huo kuwa Serikali ya Awamu ya Tano itaendelea kuwahudumia wananchi bila kuwabagua na kwamba kwa Tarime imetenga shilingi Bilioni 14 kwa ajili ya mradi mkubwa wa maji, imeanza ujenzi wa barabara ya Tarime – Mugumu kwa kiwango cha lami, imetoa shilingi milioni 400 za ujenzi wa kituo cha afya, inatoa fedha za elimu bila malipo kila mwezi na inaendelea kusambaza umeme kwa vijiji vyote visivyo na umeme.
Mhe. Rais Magufuli amezungumza uwekezaji wa shamba la miwa na kiwanda cha sukari katika wilaya ya Tarime, na kueleza kuwa Serikali itafanya uchambuzi wa kina kabla ya kuridhia mradi huo huku akiwataka viongozi wa Mkoa na Wilaya kuondoa tofauti zao.
Kwa wilaya jirani ya Rorya Mhe. Rais Magufuli amemuagiza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Selemani Jafo kutafuta fedha kiasi cha shilingi Bilioni 1.5 kwa ajili ya kujenga hospitali.
Kesho tarehe 08 Septemba, 2018 Mhe. Rais Magufuli ataendelea na ziara yake katika Kanda ya Ziwa kwa kutembelea Mkoa wa Simiyu.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Musoma
07 Septemba, 2018
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 06 Septemba, 2018 ameendelea na ziara yake Mkoani Mara ambapo amezindua mradi wa ufugaji wa samaki kwa kutumia mabwawa na vizimba Mjini Musoma na kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa barabara ya lami ya Makutano – Natta (Sanzate).
Mradi wa samaki unaotekelezwa na kikosi cha Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kikosi cha 27KJ una mabwawa 16 na visimba 18, umegharimu shilingi Milioni 213 na unatarajiwa kuzalisha tani 100 za samaki kila baada ya miezi 6 zitakazoingiza mapato ya shilingi milioni 700.
Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jen. Venance Mabeyo amemueleza Mhe. Rais Magufuli kuwa JWTZ kupitia vikosi vyake na kampuni zake za uzalishaji mali inatekeleza mradi huo pamoja na miradi mingine ili kupunguza utegemezi wa bajeti ya Serikali, na kuunga mkono juhudi za Serikali kujenga viwanda kwani mradi huo umepangwa kupanuliwa kwa kuongeza visimba na kujenga kiwanda cha kuchakata minofu ya samaki.
Akizungumza na Maafisa na Askari wa JWTZ baada ya kuzindua mradi huo Mhe. Rais Magufuli ameipongeza JWTZ kwa juhudi kubwa za uzalishaji mali inazozifanya kupitia vikosi na kampuni zake, ametoa shilingi Milioni 40 kwa ajili ya kuongeza vizimba vingine 10 katika mradi huo na ameahidi kuchangia fedha pindi JWTZ itakapoanza kujenga kiwanda cha kuchakata samaki.
Mhe. Rais Magufuli amemuagiza Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Luhaga Mpina kuhakikisha wizara yake inatatua tatizo la upatikanaji wa vifaranga vya samaki kwa ajili ya kuwawezesha Watanzania wengi kufuga samaki ili Tanzania inufaike na mapato ya samaki kama ilivyo kwa nchi nyingine zikiwemo Vietnam, China na Namibia.
Akiwa Butiama Mhe. Rais Magufuli ameongozana na Mke wa Baba wa Taifa Mama Maria Nyerere kuweka jiwe la msingi katika ujenzi wa barabara ya lami ya Makutano - Natta (Sanzate) yenye urefu wa kilometa 50 na ambayo ujenzi wake utagharimu shilingi Bilioni 54.6.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mhandisi Patrick Mfugale amesema barabara hiyo ni sehemu ya kwanza ya barabara ya Makutano – Nyamuswa – Ikoma Gate yenye urefu wa kilometa 135, ambayo inaunganisha mikoa ya Mara na Arusha kupitia mbuga za wanyama za Serengeti, Ngorongoro na Manyara.
Akizungumza na wananchi wa Butiama katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa Mwenge Kijijini Butiama Mhe. Rais Magufuli amewahakikishia wananchi hao kuwa pamoja na kujenga barabara hiyo Serikali itaendelea kujenga barabara nyingine za kuunganisha Butiama, Mugumu na Tarime ili kuimarisha mawasilino na kuipa heshima Butiama na Mkoa mzima wa Mara ambako ndiko alikozaliwa Baba wa Taifa Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere.
Mhe. Rais Magufuli amemshukuru Mama Maria Nyerere na familia yote kwa mchango mkubwa uliotolewa na Hayati Baba wa Taifa katika kupigania uhuru, kujenga Taifa, kupigania ukombozi wa Mataifa mengi ya Afrika na kuipatia Tanzania heshima kubwa duniani, na ameahidi kuwa Serikali ya Awamu ya Tano itahakikisha tatizo la maji lililopo Butiama linatatuliwa haraka iwezekanavyo.
“Nakupongeza Waziri wa Maji Prof. Makame Mbarawa kwa kuwa na mpango wa kuleta maji Butiama, nitafuatilia, haiwezekani mahali alipozaliwa Baba wa Taifa pakakosa maji, na wewe Waziri wa TAMISEMI Mhe. Selemani Jafo hakikisha hospitali ya Butiama inaboreshwa haraka na nimeagiza ile shule ya msingi Mwisenge pale Musoma Mjini aliyosoma Baba wa Taifa inajengewa uzio na majengo yake yanaboreshwa” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Akiwa njiani kuelekea Mugumu Wilayani Serengeti Mhe. Rais Magufuli amesikiliza kero za wananchi wa Nyamuswa, Isenyi, Iharara na Natta ambapo amewahakikishia kuwa Serikali imeanza kufanyia kazi tatizo la maji katika maeneo hayo, amewaagiza viongozi wa Wizara na Mkoa wa Mara kukutana na wananchi ili kutatua migogoro ya ardhi na ubadhilifu wa fedha za vijiji na amechangia shilingi Milioni 10 kwa ajili ya shule za Nyamuswa na Natta.
Mhe. Rais Magufuli amehutubia mkutano wa hadhara katika Mji wa Mugumu ambapo amesema pamoja kutenga shilingi Bilioni 1.9 kwa ajili ya mji huo kupata maji kutoka bwawa la Manchira Serikali imejipanga kutekeleza mradi mkubwa utakaomaliza tatizo la maji la mji huo pamoja na kujenga kwa kiwango cha lami barabara ya Mugumu – Tarime na Mugumu – Butiama.
Mhe. Rais Magufuli ametoa wito kwa wananchi wa Mugumu kujiepusha na migogoro isiyo ya lazima na badala yake wapendane na kuishi kwa amani na utulivu kwa kuwa kufanya hivyo kutawawezesha kutumia muda mwingi katika uzalishaji mali, ujenzi wilaya yao na kulinda heshima ya Baba wa Taifa Hayati Mwl. Nyerere aliyezaliwa katika Mkoa wa Mara.
“Na nyinyi viongozi pendaneni na shirikianeni, matatizo mengine ya wananchi mnaweza kuyamaliza nyinyi wenyewe bila hata kuyaleta kwa Rais, lakini mtafanikiwa kama mtakuwa na upendo miongoni mwenu na kushirikiana” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Mhe. Rais Magufuli kesho tarehe 07 Septemba, 2018 anaendelea na ziara yake hapa Mkoani Mara kwa kutembelea wilaya ya Tarime.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Mugumu, Mara
06 Septemba, 2018
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amemteua Kamishna wa Polisi Diwani Athumani kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).
Uteuzi wa Kamishna Diwani Athumani unaanza tarehe 06 Septemba, 2018.
Kabla ya uteuzi huo Kamishna Diwani Athumani alikuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera.
Kamishna Diwani Athumani anachukua nafasi ya Kamishna wa Polisi Valentino Mlowola ambaye ameteuliwa kuwa Balozi.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Musoma
06 Septemba, 2018
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 04 Septemba, 2018 ameendelea na ziara yake katika mikoa ya Mwanza na Mara kwa kufungua viwanda 3 vya kampuni ya Lakairo, kuzindua ujenzi wa kiwango cha lami kwa barabara ya Bulamba – Kisorya (51km), kufungua mradi wa maji katika kijiji cha Nebuye kwa ajili ya wananchi wa Nansio, kuzindua ujenzi wa chuo cha ualimu cha Murutunguru na kuzungumza na wananchi.
Viwanda vya kampuni ya Lakairo vilivyopo katika eneo la Isangijo Wilaya ya Magu mkoani Mwanza vinajumuisha kiwanda cha kutengeneza vifungashio vya nafaka, kiwanda cha pipi na jojo na kiwanda cha ‘steelwire’ ambavyo ni uwekezaji wa Mbunge wa Jimbo la Rorya Mhe. Lameck Airo (Lakairo), uliogharimu shilingi Bilioni 20.1 na vimeajiri watu 400.
Akizungumza baada ya kufungua viwanda hivyo Mhe. Rais Magufuli amempongeza Mhe. Lameck Airo kwa uwekezaji huo na ametoa wito kwa Mtanzania yeyote mwenye uwezo wa kuwekeza katika viwanda ama biashara kufanya hivyo huku akibainisha kuwa anawapenda wawekezaji na matajiri wanaoendesha shughuli zao kwa kuzingatia sheria na taratibu za nchi.
“Mimi nawapenda wafanyabiashara na matajiri, fanyeni biashara zenu kwa amani lakini zingatieni sheria. Naiagiza Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji pamoja na Wizara ya Fedha na Mipango kujenga mazingira mazuri ya kuwawezesha wawekezaji hawa hasa hawa wazalendo kama akina Lakairo” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Akiwa wilayani Bunda mkoani Mara, Mhe. Rais Magufuli amezindua ujenzi wa kiwango cha lami wa barabara ya Nyamuswa – Bunda – Kisorya katika sehemu ya Bulamba – Kisorya – Nansio yenye urefu wa kilometa 51 ambayo ujenzi wake umepangwa kukamilika Novemba mwaka huu (2018) kwa gharama ya shilingi Bilioni 156.108.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mhandisi Patrick Mfugale amesema ujenzi wa barabara hiyo unaofadhiliwa na Serikali ya Tanzania kwa asilimia 100 umefikia asilimia 54.07 na kwamba itakapokamilika itakuwa kichocheo kikubwa cha uchumi na ustawi wa jamii katika kisiwa cha Ukerewe na maeneo jirani ya wilaya ya Bunda na mkoa wa Mara kwa ujumla.
Mhe. Rais Magufuli ameelezea kutofurahishwa na kasi ya ujenzi ya Mkandarasi Nyanza Road Works Ltd ya Tanzania aliyepewa kazi hiyo tangu mwaka 2014 na ameiagiza Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano na TANROADS kumsimamia kwa karibu ili amalizie kazi ndani ya muda uliopangwa vinginevyo achukuliwe hatua zikiwemo kukatwa fedha na kufukuzwa.
Amewataka viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwabana viongozi wa Serikali katika utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2015 na amewahakikishia wananchi wa Mara kuwa Serikali itahakikisha inakamilisha barabara yote ya Nyamuswa – Bunda – Kisorya – Nansio, inajenga uwanja wa ndege wa Musoma, hospitali ya Musoma na mradi wa Maji.
Akiwa katika kisiwa cha Ukerewe, Mhe. Rais Magufuli amezindua ujenzi wa chuo cha ualimu cha Murutunguru unaohusisha ujenzi wa majengo mawili ya vyumba 8 vya madarasa, mabweni 2 yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 212, jiko, chumba cha mihadhara, bwalo la chakula na miundombinu mingine itakayogharimu shilingi Bilioni 2.3 ikiwa ni ufadhili kutoka Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Sweden (SIDA), Benki ya Dunia (WB) na Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Uingereza (DFID).
Kisiwani Ukerewe Mhe. Rais Magufuli pia amefungua mradi wa maji na usafi wa mazingira katika kijiji cha Nebuye utakaohudumia wakazi wote wa Mji wa Nansio ambao ni makao makuu ya wilaya ya Ukerewe.
Mradi huo uliofadhiliwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) umegharimulimu shilingi Bilioni 10.9 na una uwezo wa kuzalisha lita Milioni 8.647 za maji kwa siku ambayo ni mara mbili ya mahitaji ya wakazi 59,000 wa Nansio.
Mhe. Rais Magufuli amezungumza na wananchi wa Nansio katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja Ukuta Mmoja ambapo pamoja na kuwashukuru kwa kumpigia kura nyingi katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 amesema Serikali imedhamiria kutekeleza dhamira ya Baba wa Taifa Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere ya kukiendeleza kisiwa cha Ukerewe kwa kuhakikisha inajenga miundombinu ya barabara ya uhakika, inaimarisha huduma za elimu, maji, umeme na afya, na hivyo amewataka wananchi kutoa ushirikiano kwa Serikali katika utekelezaji wa dhamira hiyo.
Ameongeza kuwa sambamba na juhudi hizo Serikali ya Awamu ya Tano imechukua hatua madhubuti za kusimamia rasilimali za umma ikiwemo kudhibiti wizi, ufisadi na rushwa pamoja na kutekeleza miradi mikubwa ikiwemo kuongeza uzalishaji wa umeme utakaoiwezesha nchi kuwa na umeme wa gharama nafuu kwa ajili ya maendeleo ya viwanda.
Kuhusu uvuvi, Mhe. Rais Magufuli amempongeza Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Luhaga Mpina kwa juhudi zake za kukabiliana na uvuvi haramu ambazo sasa zimeanza kuzaa matunda kwa samaki kuongezeka katika ziwa Victoria huku akibainisha kuwa uvuvi haramu uliokuwepo umesababisha viwanda vingi vya samaki kufa, ajira kupotea na samaki kupungua kwa kiasi kikubwa kutokana uharibifu mkubwa wa mazalia na uvuvi wa samaki wadogo.
Katika ziara hiyo Mhe. Rais Magufuli ameongozana na Waziri wa Maji na Umwagiliaji Prof. Makame Mbarawa, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Kangi Lugola, Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Luhaga Mpina, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Isack Aloyce Kamwelwe, Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mhe. Charles Mwijage, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. John Mongella na Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Adam Malima.
Kesho Mhe. Rais Magufuli anaendeleo na ziara yake Mkoani Mara.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Ukerewe, Mwanza
04 Septemba, 2018
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 05 Septemba, 2018 ameendelea na ziara yake katika mkoa wa Mara ambapo amezindua mradi wa maji safi na usafi wa mazingira wa Manispaa ya Musoma, kufungua barabara ya Simiyu/Mara – Musoma na kuzungumza na wananchi wa Bunda Mjini, Kiabakari na Bunda Mjini.
Mradi wa maji wa Manispaa ya Musoma umetekelezwa kwa ushirikiano wa Serikali ya Tanzania na Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD) kwa gharama ya Shilingi Bilioni 51.37, una uwezo wa kuzalisha lita Milioni 36 za maji kwa siku ambazo ni karibu mara mbili ya mahitaji ya mji wa Musoma ambao unahitaji lita Milioni 19 kwa siku.
Ukarabati wa barabara ya lami ya kuanzia mpakani mwa mkoa wa Simiyu na Mara hadi Musoma mjini yenye urefu wa kilometa 85.5 umegharimu shilingi Bilioni 123.319 zote zikiwa zimetolewa na Serikali ya Tanzania.
Kabla ya kufungua miradi hiyo Mhe. Rais Magufuli ambaye alitokea kisiwani Ukerewe Mkoani Mwanza amezungumza na wananchi wa Bunda Mjini na kupokea kilio kikubwa cha wananchi kukosa maji licha ya mji huo kupelekewa mradi mkubwa wa maji tangu miaka 8 iliyopita.
Kilio cha maji pia kimetolewa na wananchi wa Kiabakari na wananchi wa Musoma Mjini ambako licha ya kuwepo mradi mkubwa wa maji wananchi bado hawajasambaziwa maji na hivyo kuwanufaisha wananchi 120,000 tu.
Akizungumza na wananchi wa Bunda Mjini Mhe. Rais Magufuli ameahidi kushughulikia tatizo la maji la mji huo kwa kuhakikisha mradi wa maji wa mji huo unaanza kutoa maji na kuchukua hatua dhidi ya mkandarasi Nyakilang’ani ambaye hajakamilisha mradi mpaka sasa.
Kuhusu mradi wa maji wa Manispaa ya Musoma Mhe. Rais Magufuli ambaye amehutubia wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja Mukendo Musoma Mjini amesema licha ya kuwa mradi huo unazalisha maji mara mbili ya mahitaji ya wananchi wa Manispaa hiyo, umeishia kuwanufaisha wananchi 120,000 tu kutokana na kutojengwa kwa tangi na kuwekwa mfumo wa kusambazia maji na hivyo amemuagiza Waziri wa Maji na Umwagiliaji Prof. Makame Mbarawa kupeleka mradi wa kujenga tanki na mfumo wa usambazaji maji kwa wananchi haraka iwezekanavyo.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli ameelezea kutoridhishwa na hatua zinazochukuliwa na viongozi wa Wizara, Mkoa wa Mara na vyombo vya dola dhidi ya mfanyabiashara Nyakilang’ani ambaye amelalamikiwa na wananchi wa Mwisenge katika Manispaa ya Musoma kuwa baada ya kuuziwa hoteli ya Musoma amezuia wananchi kukatiza katika eneo hilo wanapotaka kwenda katika mwambao wa ziwa Victoria na hivyo kulazimika kuzunguka umbali mrefu.
“Hoteli hii imechukuliwa tangu miaka 10 iliyopita, haijaendelezwa, wananchi wanakosa ajira, Serikali inakosa mapato halafu viongozi mpo mnamuangalia tu, huyohuyo Nyakilang’ani amepewa mradi wa maji wa mji wa Bunda huu mwaka wa 8 na mpaka sasa hautoi maji, viongozi mpo hamchukui hatua.
“Sasa nataka hoteli ya Musoma iliyojengwa na Baba wa Taifa kwa nia yake njema ya kuiendeleza Musoma ichukuliwe kwa sababu ameshindwa kuiendeleza” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Kuhusu kero ya maji ya wananchi wa Kiabakari Mhe. Waziri Mbarawa ameeleza kuwa tayari Serikali imeandaa mradi mkubwa utakaogharimu shilingi Bilioni 70 ambao utatatua tatizo la maji la eneo hilo pamoja na maeneo jirani ya Musoma vijijini.
Mhe. Rais Magufuli pia amewahakikishia wananchi wa Mkoa wa Mara kuwa Serikali itahakikisha inaujenga kwa kiwango cha lami uwanja wa ndege wa Musoma ili uweze kupokea ndege kubwa na ndogo, na kukamilisha ujenzi wa hospitali ya Musoma haraka ili ifanane na hadhi ya hospitali iliyopo katika Mkoa aliozaliwa Baba wa Taifa.
Akiwa Musoma Mjini Mhe. Rais Magufuli ametembelea shule ya msingi Mwisenge aliyosoma Baba wa Taifa Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere na kujionea hali ya miundombinu, ambapo licha ya kuchangia shilingi milioni 20 amemuagiza Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako kufika shuleni hapo na kuandaa mpango wa kukarabati majengo ya shule hiyo ili kuhifadhi historia hiyo muhimu kwa Taifa.
Ziara hiyo imehudhuriwa na Waziri wa Maji na Umwagiliaji Prof. Makame Mbarawa, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Isack Aloyce Kamwelwe, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Kangi Lugola, Wabunge wakiwemo wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Maji na Mifugo na Mwakilishi wa AFD hapa nchini Bi. Stéphanie Mouen.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Musoma
05 Septemba, 2018
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 05 Septemba, 2018 amekutana na Spika Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mzee Pius Msekwa na Mkewe Mama Anna Abdallah (Waziri Mstaafu) katika Ikulu Ndogo ya Nansio Ukerewe mkoani Mwanza.
Baada ya mazungumzo yao Mzee Msekwa amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kufanya ziara yake ya kwanza katika kisiwa cha Ukerewe tangu achaguliwe kuwa Rais, na kwa Serikali kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kisiwani humo ikiwemo Maji, ujenzi wa barabara na ununuzi wa meli mpya katika ziwa Victoria.
Mhe. Msekwa pia amezungumzia utendaji kazi wa Mhe. Rais Magufuli na Serikali ya Awamu ya Tano, ambapo amesema mageuzi makubwa yanayofanywa yanaandika historia kama alivyofanya Baba wa Taifa Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere.
“Kwa Nyerere tulisema kama sio juhudi zako Nyerere, maendeleo tungepata wapi, na huyu Rais Magufuli naye tutasema kama sio juhudi zako meli, Dreamliner, reli na mengine mengi tungepata wapi?” amesisitiza Mzee Msekwa.
Kwa upande wake Mama Anna Abdallah amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kazi kubwa ya kujenga uchumi na kuwapa nafasi za uongozi wanawake wengi, na ametoa wito kwa wanawake wote waliopata nafasi za uongozi kuonesha mfano mzuri kwa kuchapa kazi kwa juhudi, uadilifu mkubwa na kujiamini ili wengine wengi zaidi waendelee kupata nafasi.
“Nafurahishwa sana na kazi zinazofanywa na Mhe. Rais Magufuli, kwa hakika anatutendea mazuri mengi sana sisi Watanzania na sisi wanawake” amesema Mama Anna Abdallah.
Mhe. Rais Magufuli amekutana na Mzee Msekwa na Mama Anna Abdallah kando ya ziara yake katika kanda ya ziwa ambayo leo inaendelea mkoani Mara.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Ukerewe, Mwanza
05 Septemba, 2018
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 03 Septemba, 2018 amemteua Dkt. John Antony Kiang’u Jingu kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto (anayeshughulikia Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto).
Kabla ya uteuzi huu Dkt. Jingu alikuwa Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Dkt. Jingu anachukua nafasi ya Bi. Sihaba Nkinga ambaye uteuzi wake umetenguliwa.
Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli amemteua Bw. Gabriel Pascal Malata kuwa Kamishna wa Kazi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu.
Kabla ya uteuzi huo Bw. Malata alikuwa Mkurugenzi Msaidizi Kesi za Madai, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Bw. Malata anachukua nafasi ya Bi. Hilda Nkanda Kabisa ambaye uteuzi wake umetenguliwa.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Mwanza
03 Septemba, 2018
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 03 Septemba, 2018 ameshuhudia utiaji saini wa mkataba wa ujenzi wa meli mpya, chelezo na ukarabati wa meli za Mv Victoria na Mv Butiama katika ziwa Victoria kati ya Kampuni ya Huduma za Meli Tanzania (MSCL) na Kampuni za kutoka nchini Korea ambazo ni M/S Gas Entec Co. Limited, Kangnam Corp, M/S STX Engine Co. Ltd, Saekyung Construction Ltd, KTMI Co. Ltd, zinazoshirikiana na kampuni mbili za Kitanzania ambazo ni Suma JKT na Yuko’s Enterprises.
Hafla ya utiaji saini wa mikataba hiyo imefanyika katika bandari ya Mwanza Kusini Jijini Mwanza na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Mawaziri, Balozi wa Korea hapa nchini Mhe. Song Geum-young, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania Jen. Venance Mabeyo, Viongozi wa Mkoa wa Mwanza na Mara, Wabunge na wananchi.
Meli mpya itajengwa kwa muda wa miezi 24 kwa gharama ya shilingi Bilioni 88.764, ikiwa na urefu wa mita 90, upana mita 17, kimo mita 10.9, uwezo wa kuchukua abiria 1,200, mizigo tani 400, magari madogo 20, na itakuwa na uwezo wa kwenda kasi zaidi (ambapo itatumia saa 6 ikilinganishwa na saa 12 za meli zilizopo) kati ya Mwanza na Bukoba na itakuwa ndio meli kubwa kuliko zote hapa nchini na katika Maziwa Makuu.
Chelezo (mahali pa kujengea na kutengenezea meli) itajengwa kwa muda wa miezi 12 kwa gharama ya shilingi Bilioni 35.99 na itakuwa na urefu wa mita 100.
Katika mradi huu, meli ya Mv Victoria yenye uwezo wa kubeba abiria 1,200 na tani 200 za mizigo ambayo ilisimama kutoa huduma tangu mwaka 2014 kutokana na ubovu itakarabatiwa kwa gharama ya shilingi Bilioni 22.712, na meli ya Mv Butiama yenye uwezo wa kuchukuwa abiria 200 na tani 100 za mizigo ambayo ilisimama tangu mwaka 2010 kutokana na ubovu itakarabatiwa kwa gharama ya shilingi Bilioni 4.897.
Kaimu Meneja Mkuu wa MSCL Bw. Eric Benedict Hamissi amesema pamoja na ukarabati wa meli hizo 2, MSCL itakarabati meli nyingine 3 ambazo ni Mv Serengeti na Mv Umoja katika Ziwa Victoria na Mv Liemba iliyopo katika ziwa Tanganyika.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu Mhe. Selemani Kakoso amempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa dhamira yake ya kuimarisha usafiri wa majini katika maeneo mbalimbali hapa nchini na amewahakikishia Watanzania kuwa miradi na fedha za utekelezaji wa miradi hiyo zimepitishwa na Bunge, na kwamba sio kweli kuwa Serikali inatumia fedha bila kuidhinishwa na Bunge.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Isack Aloyce Kamwelwe ameahidi kusimamia utekelezaji wa mradi huo ipasavyo na kwamba wizara yake imeanza kuchukua hatua za kuongeza ufanisi wa bandari ya Dar es Salaam ikiwemo kuongeza kiwango cha mizigo kutoka tani Milioni 16.2 za mwaka 2017/18.
Akizungumza baada ya kushuhudia utiaji saini wa utekelezaji wa miradi hiyo Mhe. Rais Magufuli ameelezea kufurahishwa kwake na kuanza kwa ujenzi meli mpya na chelezo pamoja na ukarabati wa meli za Mv Victoria na Mv Butiama ambazo ni utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2015.
Mhe. Rais Magufuli amewapongeza Wabunge waliopitisha bajeti ya Serikali iliyowezesha kuanza kwa utekelezaji wa miradi hiyo ambayo itasaidia kukabiliana na tatizo kubwa la usafiri wa majini katika ziwa Victoria baada ya Mv Bukoba kuzama mwaka 1996 na Mv Butiama na Mv Victoria kusimama kutoa huduma.
Kuhusu madai ya wafanyakazi wa MSCL wanaodai kutolipwa mishahara kwa miezi 27, Mhe. Rais Magufuli ameahidi kuwa Serikali itatoa shilingi Bilioni 3.7 za kuwalipa wafanyakazi hao ndani ya wiki mbili lakini amemtaka Kaimu Meneja Mkuu wa MSCL kusimamia vizuri utendaji na mapato ya kampuni hiyo pamoja na kudhibiti wizi wa mafuta ambao hufanywa na wafanyakazi.
“Fedha hizi shilingi Bilioni 152 zilizotolewa kwa ajili ya miradi hii zimetokana na kodi za Watanzania, nataka kampuni hii ifanye kazi kwa ufanisi na izalishe gawio kama mashirika mengine ya Serikali, Kaimu Meneja Mkuu ukadhibiti mapato na wizi wa mafuta, anza kutumia tiketi za kielektroniki” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Mwanza
03 Septemba, 2018
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, atafanya ziara ya kikazi katika mikoa ya Mwanza, Mara na Simiyu kati ya tarehe 03 Septemba, 2018 na tarehe 10 Septemba, 2018.
Katika ziara hiyo Mhe. Rais Magufuli ataweka mawe ya msingi na kufungua miradi mbalimbali ya maendeleo, pamoja na kuzungumza na wananchi katika mikutano ya hadhara.
Taarifa zaidi kuhusu ziara ya Mhe. Rais Magufuli katika mikoa husika zitatolewa na viongozi wa mikoa hiyo.
Aidha, baada ya kumaliza ziara katika mikoa hiyo Mhe. Rais Magufuli anatarajia kufanya ziara katika mikoa ya Katavi, Rukwa, Songwe na Mbeya katika tarehe zitakazopangwa.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Chato, Geita
30 Agosti, 2018
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amewataka viongozi wote nchini kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria sambamba na kuhakikisha wanasimamia ipasavyo matumizi ya rasilimali za umma kwa maslahi ya wananchi.
Mhe. Rais Magufuli ametoa maagizo hayo tarehe 30 Agosti, 2018 katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chato mkoani Geita, wakati akizungumza na viongozi na wafanyakazi wa wilaya hiyo, ambapo amesisitiza kuwa viongozi wote wajenge utaratibu wa kusoma sheria na kujiepusha kutumiwa kwa maslahi ya watu binafsi.
Huku akitolea mfano wa mgogoro wa makontena yanayodaiwa kuwa na fenicha za shule, na yanayoshikiliwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) katika bandari ya Dar es Salaam, Mhe. Rais Magufuli amesema makontena hayo yanapaswa kulipiwa kodi kwa mujibu wa sheria, huku akisisitiza kuwa Waziri wa Fedha na Mipango ndiye mwenye dhamana ya kupokea misaada kwa niaba ya Serikali na sio Mkuu wa Mkoa.
“Kwa mujibu wa sheria ya Madeni, Dhamana na Misaada Namba 30 ya mwaka 1974 (kama ilivyorekebishwa na sheria namba 9 ya mwaka 2003) kifungu cha 3, 6, 13 na 15, Waziri wa Fedha na Mipango ndiye mwenye mamlaka ya kukopa nje na ndani, kutoa dhamana na kupokea misaada kwa niaba ya Serikali.
“Kwa msingi huo, hakuna mtu yoyote mwenye mamlaka ya kukopa, kutoa dhamana na kupokea misaada kwa niaba ya Serikali bila mtu huyo kukasimiwa mamlaka hayo na Waziri wa Fedha kwa mujibu wa sheria hiyo” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli amewataka Madiwani wa halmashauri zote hapa nchini kuhakikisha wanasimamia kwa ukaribu matumizi ya fedha za bajeti ikiwa ni pamoja na kuhakikisha fedha hizo zinaelekezwa katika miradi na huduma zenye kujibu kero na kuboresha maisha ya wananchi badala ya kuacha zikitumiwa kulipana posho za vikao na safari zisizo na tija.
“Nafahamu kuwa hata nyie Madiwani huwa mnakaa kikao siku moja na mnataka kulipwa posho ya siku mbili au tatu, au mtumishi wa halmashauri anasafiri kwa siku mbili lakini anaandikiwa posho za siku nne, nataka mchezo huu ukome, elekezeni fedha kwenye mahitaji muhimu ya wananchi, Wakurugenzi na Wakuu wa Wilaya simamieni hilo” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Katika mkutano huo ambapo alianza kwa kupokea maswali, kero na maoni ya wafanyakazi na viongozi, Mhe. Rais Magufuli amewahakikishia kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kujenga uchumi wa kujitegemea na kutatua kero za wananchi wakiwemo wafanyakazi wote bila kubagua na amewataka viongozi wa Wilaya ya Chato kuwa wabunifu wa namna ya kuharakisha maendeleo ya wananchi badala ya kubweteka kwa kutegemea kupendelewa naye kwa kigezo cha kuwa mwananchi wa Chato.
“Mimi ni Rais wa Tanzania nzima sio Rais wa Chato, nina wajibu wa kuhudumia Tanzania nzima, kwa hiyo mambo ya hapa Chato wabaneni viongozi wa hapa Chato” amebainisha Mhe. Rais Magufuli.
Kuhusu uhaba wa watumishi, Mhe. Rais Magufuli amesema baada ya Serikali kuokoa Shilingi Bilioni 138 zilizokuwa zikilipwa kwa watumishi hewa na wenye vyeti feki, sasa imeanza kuajiri watumishi ambapo watumishi 52,000 wanaajiriwa na kwamba sambamba na hilo katika kipindi kifupi kijacho itaanza kulipa madeni ya watumishi baada ya uhakiki kukamilika.
Amewaagiza viongozi wa wilaya ya Chato ambao wamesikiliza kero za wafanyakazi na Madiwani akiwemo Mbunge wa Jimbo hilo na Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani kufanyia kazi kero zote zilizo ndani ya uwezo wao.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Chato, Geita
30 Agosti, 2018
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amemtuma Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kumwakilisha katika sherehe za uapisho wa Rais Mteule wa Jamhuri ya Zimbabwe Mhe. Emmerson Dambudzo Mnangagwa zitakazofanyika Jumapili tarehe 26 Agosti, 2018 katika uwanja wa michezo wa Taifa Mjini Harare.
Mhe. Rais Mstaafu Dkt. Kikwete atafuatana na Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (Bara) Ndg. Philip Japhet Mangula na Mwenyekiti wa chama cha UDP Ndg. John Momose Cheyo.
Mhe. Rais Mnangagwa ataapishwa kesho kuongoza Zimbabwe baada ya kushinda katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika tarehe 30 Julai, 2018 akiwa anapokea kijiti kutoka kwa aliyekuwa Rais wa nchi hiyo Ndg. Robert Gabriel Mugabe.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Chato, Geita
25 Agosti, 2018
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amewahakikishia Watanzania kuwa juhudi za kujenga Tanzania mpya zinakwenda vizuri kutokana na mafanikio makubwa yaliyoanza kupatikana katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo na utatuzi wa kero za wananchi.
Mhe. Rais Magufuli ametoa kauli hiyo leo tarehe 18 Agosti, 2018 aliposalimiana na wananchi waliokusanyika katika njiapanda ya Bugando Jijini Mwanza na Mjini Sengerema akiwa njiani kuelekea Chato Mkoani Geita kwa mapumziko.
Mhe. Rais Magufuli amesema utekelezaji wa ahadi za Serikali ya Awamu ya Tano unakwenda vizuri ambapo katika kipindi kifupi cha miaka miwili na miezi 8 kumekuwa na kasi kubwa ya ujenzi wa viwanda vilivyofikia 3,060, Shirika la Ndege la Taifa (ATCL) limefufuliwa, miundombinu ya barabara na madaraja inajengwa, watoto wanapata elimu bure na mengine mengi ambayo yamechangia kupanua uwigo wa ajira na kukuza uchumi wa nchi.
“Nataka kuwahakikishia ndugu zangu tunakwenda vizuri, juhudi zetu za kujenga Tanzania mpya zinapata mafanikio makubwa, tumejenga viwanda vingi, nataka tuirudishe Tanzania ya Nyerere ambapo hapa Mwanza kulikuwa na viwanda vingi na vijana wengi walipata ajira” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Akiwa Sengerema Mhe. Rais Magufuli amesikiliza kero za wananchi ambapo amepiga marufuku viongozi wa halmashauri kuwanyang’anya bidhaa zao wafanyabiashara wadogo na badala yake ameagiza viongozi wote nchini kujielekeza kutatua kero zinazowakabili wananchi ikiwemo ukosefu wa soko la mazao yao.
Mhe. Rais Magufuli ametoa agizo hilo baada ya wananchi wa Sengerema kudai Halmashauri ya Wilaya hiyo imekuwa ikiwanyang’anya matunda aina ya nanasi wakulima na wafanyabiashara wanaouza matunda yao mjini hapo.
Amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Bw. John Mongella kufuatilia na kutatua kero hiyo.
“Nilishasema viongozi wote niliowateua mimi msisherehekee uteuzi, mtasherehekea siku mkimaliza uongozi, nataka mchape kazi, tatueni kero za wananchi na waleteeni maendeleo” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Kabla ya kukutana na wananchi wa Mwanza Mhe. Rais Magufuli amewajulia hali wagonjwa waliolazwa katika wodi ya uangalizi maalum (ICU) ya hospitali ya Bugando Jijini Mwanza akiwemo dada yake Bi. Monica Joseph Magufuli.
Mhe. Rais Magufuli amewashukuru madaktari na wauguzi wa hospitali hiyo kwa juhudi kubwa wanazozifanya kuwatibu wagonjwa, na amesema Serikali itaendelea kushirikiana na uongozi wa hospitali hiyo ili kuimarisha huduma za matibabu kwa wananchi.
Mapema leo asubuhi Mhe. Rais Magufuli amesafiri kwa ndege ya Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) aina ya Boeing 787-8 Dreamliner iliyonunuliwa na Serikali kwa lengo la kuimarisha shirika hilo, na akiwa ndani ya ndege abiria waliosafiri nae kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza wamemshangilia na kumpongeza kwa juhudi zake za kuifufua ATCL na wamemuombea dua.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
18 Agosti, 2018.
Taarifa kwa vyombo vya habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 13 Agosti, 2018 amefanya uteuzi wa Mkuu wa Wilaya 1, Wakurugenzi wa Halmashauri za Wilaya, Miji, Manispaa na Majiji 41, na amewahamisha vituo vya kazi Mkuu wa Wilaya 1 na Wakurugenzi wa Wilaya, Miji, Manispaa na Majiji 19.
Taarifa iliyotolewa leo tarehe 13 Agosti, 2018 na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi, Ikulu Jijini Dar es Salaam imeeleza kuwa Mhe. Dkt. Magufuli amemteua Bi. Senyi Simon Ngaga kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kwimba Mkoa wa Mwanza.
Bi. Senyi Simon Ngaga amechukua nafasi ya Mhandisi Mtemi Msafiri Simeon ambaye amehamishwa kituo cha kazi na kuwa Mkuu wa Wilaya ya Chato Mkoani Geita, baada ya Mkuu wa Wilaya ya Chato aliyeteuliwa hivi karibuni Kanali Patrick Norbert Songea kwenda kwenye mafunzo ya kijeshi nje ya nchi.
Uteuzi wa Bi. Senyi Simon Ngaga unaanza leo tarehe 13 Agosti, 2018 na Wakuu wa Wilaya wote wawili wanatakiwa kuripoti katika vituo vyao vya kazi mara moja.
AIDHA, Mhe. Rais Magufuli amefanya uteuzi na uhamisho wa Wakurugenzi wa Halmashauri za Wilaya, Miji, Manispaa na Majiji, kufuatia baadhi ya Wakurugenzi waliokuwa katika nafasi hizo kustaafu, kupangiwa kazi nyingine, kuhamishwa na wengine kuondolewa katika nafasi za ukurugenzi kama ifuatavyo;
- 1. Mkoa wa Arusha.
i. Jiji la Arusha – Dr. Maulid Suleiman Madeni.
ii. Halmashauri ya Wilaya ya Meru – Bw. Emanuel Mkongo.
- 2. Mkoa wa Dar es Salaam.
i. Manispaa ya Temeke – Bw. Lusubilo Mwakabibi (Amehamishiwa kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko Mkoani Kigoma).
ii. Manispaa ya Ubungo – Bi. Beatrice Dominic Kwai (Amehamishiwa kutoka Halmashauri ya Manispaa ya Mtwara).
iii. Manispaa ya Ilala – Bw. Jumanne Kiango Shauri (Amehamishiwa kutoka Halmashauri ya Mji wa Korogwe).
iv. Manispaa ya Kigamboni – Bw. Ng’wilabuzu Ndatwa Ludigija (Amehamishiwa kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa).
- 3. Mkoa wa Dodoma.
i. Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa – Bw. Mustafa S. Yusuph.
ii. Halmashauri ya Mji wa Kondoa – Ndg. Msoleni Juma Dakawa.
iii. Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa – Bw. Paul Mamba Sweya.
iv. Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa – Dkt. Omary A. Nkullo.
- 4. Mkoa wa Geita.
i. Halmashauri ya Wilaya ya Nyang’hwale – Bi. Mariam Khatib Chaurembo.
ii. Halmashauri ya Wilaya ya Chato – Bw. Eliud Leonard Mwaiteleke (Amehamishiwa kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi).
- 5. Mkoa wa Iringa.
i. Halmashauri ya Manispaa ya Iringa – Bw. Hamid Ahmed Njovu (amehamishiwa kutoka Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga).
- 6. Mkoa wa Kagera.
i. Halmashauri ya Wilaya ya Misenyi – Bw. Innocent Mbandwa Mukandala.
ii. Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba – Bw. Limbe Bernard Maurice (amehamishiwa kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Misenyi).
iii. Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba – Bw. Solomon O. Kimilike.
- 7. Mkoa wa Katavi.
i. Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo – Bw. Ramadhan Mohamed.
- 8. Mkoa wa Kigoma.
ii. Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma – Ndg. Mwailwa Smith Pangani (Amehamishiwa kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo).
iii. Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko – Ndg. Masumbuko Stephano Magang’hila.
iv. Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma – Bi. Upendo Erick Mangali.
- 9. Mkoa wa Kilimanjaro.
i. Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga – Ndg. Zefrin Kimolo Lubuva.
ii. Halmashauri ya Wilaya ya Moshi – Tatu Selemani Kikwete (Amehamishiwa kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha).
- 10. Mkoa wa Lindi
i. Halmashauri ya Wilaya ya Liwale – Bw. Nassib Bakari Mmbaga (Amehamishiwa kutoka Halmashauri ya Manispaa ya Temeke).
ii. Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa – Bw. Renatus Blas Mchau.
- 11. Mkoa wa Mara.
i. Halmashauri ya Wilaya ya Musoma – Bw. Kayombo Lipesi John (Amehamishiwa kutoka Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo).
ii. Halmashauri ya Wilaya ya Butiama – Ndg. Magori Mgalani Alphonce.
- 12. Mkoa wa Mbeya.
i. Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya – Bw. Stephan Edward Katemba (Amehamishiwa kutoka Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni).
ii. Halmashauri ya Jiji la Mbeya – Mrakibu Mwandamizi wa Polisi James Cola Kasusura.
iii. Halmashauri ya Wilaya ya Kyela – Bi. Lucy L. Mganga.
- 13. Mkoa wa Morogoro.
i. Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero – Mhandisi Stephano Bulili Kaliwa.
ii. Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro – Ndg. Kayombe Masoud Lyoba.
iii. Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi – Bw. Mussa Elias Mnyeti.
iv. Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa – Asajile Lucas Mwambambale.
- 14. Mkoa wa Mtwara.
i. Halmashauri ya Manispaa ya Mtwara – Kanali Emmanuel Hally Mwaigobeko.
- 15. Mkoa wa Mwanza.
ii. Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi – Ndg. Kisena Magena Mabuba.
iii. Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe – Bi. Ester Anania Chaula.
- 16. Mkoa wa Njombe.
i. Halmashauri ya Wilaya ya Wanging’ombe – Ndg. Edes Philip Lukoa (Amehamishiwa kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze).
ii. Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa – Ndg. Sunday Deogratius George.
- 17. Mkoa wa Pwani.
i. Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze – Bi. Amina Mohamed Kiwanuka (Amehamishiwa kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Wanging’ombe).
ii. Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha – Ndg. Butamo Nuru Ndalahwa (Amehamishiwa kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Moshi).
- 18. Mkoa wa Rukwa.
i. Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi – Bw. Engelus Wilbard Kamugisha.
ii. Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo – Ndg. Msongela Nitu Palela (Amehamishiwa kutoka Halmashauri ya Manispaa ya Ilala).
iii. Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga – Bw. Jacob James Mtalitinya (Amehamishiwa kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Nzega).
- 19. Mkoa wa Ruvuma.
i. Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga – Bw. Juma Ally Mnwele.
ii. Halmashauri ya Mji wa Mbinga – Bi. Grace Stephen Quintine.
iii. Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo – Bw. Evans Nachimbinya.
iv. Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru – Bw. Gasper Zahoro Balyomi.
- 20. Mkoa wa Shinyanga.
i. Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga – Mrakibu Msaidizi wa Uhamiaji Hoja Mahiba.
- 21. Mkoa wa Simiyu.
i. Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi – Mrakibu Msaidizi wa Zimamoto James Marco John Mtembelea.
- 22. Mkoa wa Singida.
i. Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi – Bw. Justice K. Lawrence
- 23. Mkoa wa Songwe.
i. Halmashauri ya Wilaya ya Tunduma – Mhandisi Mussa Natty.
ii. Halmashauri ya Wilaya ya Songwe – Bi. Fauzia Hamidu.
iii. Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi – Ndg. Kazimbaya Makwega. Adeladius (Amehamishiwa kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto).
- 24. Mkoa wa Tabora.
i. Halmashauri ya Wilaya ya Nzega – Ndg. Sekiete Seleman Yahaya.
ii. Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge – Bi. Martha Daudi Luleka.
- 25. Mkoa wa Tanga.
i. Halmashauri ya Mji wa Korogwe – Bw. Nicodemus John Bee.
ii. Halmashauri ya Wilaya ya Kilindi – Ndg. Gracia Max Makota.
iii. Halmashauri ya Wilaya ya Bumbuli – Bw. George Haule.
iv. Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe – Ndg. Kwame Andrew Daftari.
v. Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto – Mrakibu Mwandamizi wa Uhamiaji Ikupa Harrison Mwasyoge.
Wakurugenzi ambao katika mabadiliko haya wamebadilishiwa vituo vya kazi wanapaswa kwenda kuripoti katika vituo vyao vipya vya kazi mara moja, na Wakurugenzi ambao wameteuliwa kwa mara ya kwanza wanatakiwa kuripoti kwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Jijini Dodoma siku ya Jumatano tarehe 15 Agosti, 2018 kwa ajili ya kupata maelekezo zaidi kuhusu majukumu yao na kula kiapo cha uadilifu kwa viongozi wa umma.
Wakurugenzi wateule wanaokwenda TAMISEMI Jijini Dodoma wanapaswa kuwa na vyeti vyao halisi (Originals), pamoja na nakala za vyeti hivyo zilizothibitishwa kisheria (Certified Copies) vinavyoonesha matokeo ya kumaliza elimu ya kidato cha nne, kidato cha sita na elimu ya taaluma walizosomea.
Wakurugenzi ambao vituo vyao vya kazi havikutajwa katika mabadiliko haya wanaendelea na nyadhifa zao katika vituo walivyopo.
WAKATI HUO HUO, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. George Huruma Mkuchika amemteua Ndg. Mnkondo Yesaya Bendera kuwa Katibu Tawala wa Wilaya ya Rungwe ili kujaza nafasi iliyoachwa wazi na Bw. Moses Maurus Mashaka ambaye amepangiwa kazi nyingine.
Bw. Bendera anatakiwa kuripoti kwa Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Jijini Dodoma Jumatano tarehe 15 Agosti, 2018 kwa maelezo zaidi, akiwa na vyeti vyake halisi (Originals) vya elimu ya Sekondari na vya elimu yay a taaluma alizosomea.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
13 Agosti, 2018
Taarifa kwa vyombo vya habari
Uingereza imetoa msaada wa shilingi Bilioni 307.5 kwa Tanzania kwa ajili ya kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli katika elimu, mapambano dhidi ya rushwa na uboreshaji huduma za afya.
Waziri wa Maendeleo ya Kimataifa wa Uingereza Mhe. Penny Mordaunt ametangaza msaada huo tarehe 10 Agosti, 2018 alipokutana na kufanya mazungumzo na Mhe. Rais Magufuli Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Mhe. Penny Mordaunt amesema fedha hizo zinatolewa kwa ajili ya kuunga mkono vipaumbele vya Mhe. Rais Magufuli ambapo kati yake shilingi Bilioni 124.5 zitaelekezwa katika kuinua ubora wa elimu hususani kutoa fursa ya elimu kwa watoto wa kike na wenye ulemavu, shilingi Bilioni 23.5 zitaelekezwa katika kuunga mkono juhudi za kupambana na rushwa, na shilingi Bilioni 160 zitaelekezwa katika kuboresha huduma za afya.
“Tunafanya hivi ili kudhihirisha dhamira yetu ya kuimarisha na kukuza zaidi uhusiano na ushirikiano wetu, tunataka kujielekeza katika kuhakikisha Mhe. Rais Magufuli anafanikisha ahadi zake kwa Watanzania na tunafurahi kuwa wadau muhimu wa hilo” amesema Mhe. Penny Mordaunt.
Ameongeza kuwa pamoja na kuwa wachangiaji wakubwa katika bajeti ya Serikali, Uingereza ni nchi inayoongoza kwa uwekezaji nchini Tanzania na kwamba wanafurahishwa na wito wa Mhe. Rais Magufuli kuwakaribisha wawekezaji na wafanyabiashara zaidi kutoka Uingereza watakaowekeza kwa manufaa ya pande zote (win-win).
Mhe. Rais Magufuli amemshukuru Mhe. Penny Mordaunt kwa msaada huo na amemuomba kufikisha shukrani zake kwa Waziri Mkuu wa Uingereza Mhe. Theresa May kwa mchango mkubwa ambao Uingereza hutoa kuchangia bajeti ya Serikali na kufadhili miradi mbalimbali ya maendeleo.
“Namshukuru sana Waziri Penny Mordaunt kwa kutambua juhudi zetu za kuinua elimu, kupambana na rushwa na ufisadi pamoja na kuboresha huduma za afya, msaada huu utatusaidia kuongeza nguvu kwa sababu watoto wakipata elimu bora, tukikomesha rushwa na watu wetu wakiwa na afya njema tutaweza kujenga viwanda na kukuza uchumi wetu kwa kasi zaidi” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Mhe. Rais Magufuli amemuahidi Mhe. Penny Mordaunt kuwa fedha zilizotolewa kiasi cha shilingi Bilioni 307.5 zitatumika vizuri na kwamba Serikali ya Awamu ya Tano itahakikisha uhusiano wa Tanzania na Uingereza unazidi kuimarishwa kwa kuwa inatambua kuwa Uingereza ndio mwekezaji mkubwa hapa nchini na imekuwa ikitoa misaada mikubwa ya fedha za walipa kodi wa Uingereza kwa ajili ya maendeleo ya Tanzania.
Pia, Mhe. Rais Magufuli amemkabidhi Mhe. Penny Mordaunt albamu ya picha za shule ya sekondari Ihungo mkoani Kagera iliyojengwa upya baada ya kuharibika vibaya kufuatia tetemeko la ardhi lililotokea Septemba 2016, na ameishukuru Uingereza kwa msaada wa shilingi Bilioni 6 zilizotumika kujenga majengo hayo kupitia Wakala wa Majengo Tanzania (TBA).
Mazungumzo hayo yamehudhuriwa na Balozi wa Uingereza hapa nchini Mhe. Sarah Cooke na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Mhe. Dkt. Augustine Mahiga ambaye amesema ziara ya Waziri Penny Mordaunt imezidi kukuza uhusiano wa Tanzania na Uingereza.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
10 Agosti, 2018
Taarifa kwa vyombo vya habari
Rais wa Jamhuri ya Uganda Mhe. Yoweri Kaguta Museveni amefanya ziara ya kikazi ya siku moja hapa nchini ambapo amekutana na kufanya mazungumzo na mwenyeji wake Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli.
Baada ya Mhe. Rais Museveni kupokelewa na Mhe. Rais Magufuli katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere majira ya 3:30 asubuhi na kisha kufanya mazungumzo Ikulu Jijini Dar es Salaam, viongozi hao wamezungumza na wananchi kupitia vyombo vya habari.
Mhe. Rais Museveni amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kumkaribisha na amesema alikuja kumpa taarifa juu ya yaliyojiri katika mkutano wa viongozi wa mataifa yanayoinukia kiuchumi duniani (BRICS) ambayo ni Brazil, Urusi, India, China na Afrika Kusini uliofanyika nchini Afrika Kusini mwishoni mwa mwezi uliopita ambapo yeye aliiwakilisha Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Mhe. Rais Museveni ambaye ni Mwenyekiti wa sasa wa Jumuiya ya Afrika Mashariki amesema katika mkutano huo amewahakikishia viongozi wa mataifa hayo kuwa nchi za Afrika Mashariki zinazo fursa nyingi na kubwa na ametoa wito kwa kampuni za nchi hizo kuja kuwekeza na kufanya biashara ikiwemo kushiriki katika ujenzi wa miundombinu ya barabara, reli, umeme, usafiri wa majini, viwanda, hoteli na kukuza utalii.
Mbali na hayo Mhe. Rais Museveni amesema yeye na Rais Magufuli wamezungumzia hali ya Burundi na Sudani Kusini, na juhudi zinazoendelea kuleta amani na utulivu katika mataifa hayo ya Afrika Mashariki.
Amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kurejesha usafirishaji wa mizigo kwa kutumia reli ya kati kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza na kutoka Mwanza hadi Kampala kupitia kivuko cha Umoja katika ziwa Victoria.
Mhe. Rais Museveni amempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa kufufua Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) baada ya kununua ndege 7 ambazo hivi karibuni zitaanza safari za kwenda Entebbe Uganda, na ameahidi kuwa naye ameanza mchakato wa kufufua Shirika la Ndege la Uganda ili kuimarisha usafiri wa anga.
Kwa upande wake Mhe. Rais Magufuli amemshukuru Mhe. Rais Museveni kwa kufanya ziara ya kikazi ya siku moja hapa nchini na kumpa taarifa kuhusu kikao cha BRICS kilichofanyika Afrika Kusini, na pia amempongeza kwa namna anavyohakikisha uhusiano na ushirikiano wa Tanzania na Uganda unazidi kuimarika.
Mhe. Rais Magufuli ameelezea kufurahishwa na Uganda ilivyotoa ushirikiano katika kurejesha usafirishaji wa mizigo kwa njia ya reli kutoka bandari ya Dar es Salaam hadi Kampala nchini Uganda ambapo safari ya kwanza pekee iliwezesha tani zaidi ya 800 (sawa na malori takribani 50) kubebwa kwa treni kwa mpigo, na kwamba juhudi hizo zinaendelea sambamba na ujenzi wa reli hiyo kwa kiwango cha kisasa (standard gauge).
Mhe. Rais Magufuli amebainisha kuwa wamezungumzia maendeleo ya mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta ghafi la kuanzia Hoima nchini Uganda hadi bandari ya Tanga nchini Tanzania na wamewaagiza Mawaziri husika kuharakisha utekelezaji wa mradi huo, pamoja na tume ya pamoja ya nchi zote mbili kukutana mara kwa mara ili kuongeza kasi ya utekelezaji wa masuala mbalimbali ya maendeleo kwa nchi hizi.
Aidha, viongozi hao wamezungumzia kuhusu dhamira yao ya kuongeza uzalishaji wa nishati ya umeme ikiwemo kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi miwili ya umeme katika mto Kagera ambayo ni Mrongo-Kigagati na Msongezi inayojengwa kwa ushirikiano wa Tanzania na Uganda.
Katika hatua nyingine, Mhe. Rais Magufuli ameungana na wasanii, ndugu, jamaa na marafiki katika kutoa heshima za mwisho kwa msanii mkongwe nchini Mzee Amri Athuman maarufu “King Majuto” ambaye mwili wake umeagwa leo katika ukumbi wa Karimjee Jijini Dar es Salaam na baadaye kusafirishwa kwenda nyumbani kwake Tanga kwa mazishi.
Viongozi wengine waliohudhuria tukio hilo ni Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete, Mufti wa Tanzania Sheikh Aboubakar Zubery Ali na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Paul Makonda.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
09 Agosti, 2018
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ametuma salamu za rambirambi kwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe kufuatia kifo cha msanii mkongwe hapa nchini Mzee Amri Athuman maarufu kwa jina la King Majuto kilichotokea tarehe 08 Agosti, 2018 Jijini Dar es Salaam.
King Majuto amefariki dunia majira ya saa 1:30 Jioni katika Hospitali ya Taifa Muhimbili alikokuwa akipatiwa matibabu.
Katika salamu hizo Mhe. Rais Magufuli amemtaka Dkt. Mwakyembe kufikisha salamu zake za pole kwa familia ya Marehemu, Wasanii wote nchini, wadau wa sanaa, ndugu, jamaa, marafiki na wote walioguswa na kifo cha King Majuto.
Mhe. Rais Magufuli amesema King Majuto atakumbukwa kwa mchango wake mkubwa na wa muda mrefu alioutoa kupitia sanaa ya uigizaji na uchekeshaji, ambapo alishiriki kuelimisha jamii, kuendeleza na kukuza sanaa na kuunga mkono juhudi za chama na Serikali katika kuhimiza maendeleo.
"King Majuto alikuwa kielelezo cha safari ndefu ya sanaa kwa nchi yetu, kwa muda wote amedhihirisha kipaji, ujuzi na uwezo wa hali ya juu katika uigizaji na uchekeshaji na hivyo kuwa kipenzi cha Watanzania na wasanii wenzake, hatutasahau ucheshi wake, upendo na uzalendo kwa nchi yake wakati wote wa uhai wake" amesema Mhe. Rais Magufuli.
Mhe. Rais Magufuli amesema anaungana na familia na wote walioguswa na kifo cha King Majuto katika kipindi hiki cha majonzi na amemuombea kwa Mwenyezi Mungu apumzike mahali pema peponi, Amina.
Inna lillahi wa inna ilaihi raji'un
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
08 Agosti, 2018
Taarifa kwa vyombo vya habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 06 Agosti, 2018 amekutana na Balozi wa China hapa nchini Mhe. Wang Ke ambaye pamoja na kufanya nae mazungumzo amewasilisha barua kutoka kwa Rais wa China Mhe. Xi Jinping.
Katika mazungumzo hayo Mhe. Wang Ke amemueleza Mhe. Rais Magufuli kuwa uhusiano na ushirikiano wa Tanzania na China umeendelea kukua kwa kasi kubwa hususani katika masuala ya kiuchumi, ambapo miradi mbalimbali ya maendeleo imetekelezwa na inaendelea kutekelezwa, na kwamba katika kipindi cha miaka 6 iliyopita uwekezaji wa China nchini Tanzania umekuwa mara kumi kutoka Shilingi Trilioni 1.58 hadi kufikia Shilingi Trilioni 15.82.
Mhe. Wang Ke amemhakikishia Mhe. Rais Magufuli kuwa China itaendelea kuwa mshirika muhimu wa maendeleo ya Tanzania.
Kuhusu ombi alilolitoa Mhe. Rais Magufuli wakati meli ya matibabu ya China ilipokuja hapa nchini mwezi Novemba 2017, Mhe. Wang Ke amesema Mhe. Rais Xi Jinping ameshafanyia kazi ombi hilo kwa kutoa udhamini wa masomo kwa madaktari 20 watakaosomea ngazi ya uzamili na uzamivu katika matibabu ya ini na uboho (bone marrow) katika Chuo Kikuu cha Shandong cha China, na pia nafasi 30 za wataalamu watakaohudhuria semina ya mafunzo ya usimamizi wa hospitali.
Mhe. Rais Magufuli amemshukuru Mhe. Rais Xi Jinping kwa kutoa nafasi hizo za masomo na kwa mchango mkubwa wa China katika maendeleo ya Tanzania, na amemuomba Mhe. Wang Ke kufikisha ujumbe wake kwa Mhe. Rais Xi Jinping kuwa Tanzania itaendeleza na kukuza zaidi uhusiano na ushirikiano wake wa kidugu na kihistoria na China.
Mhe. Rais Magufuli ametoa wito kwa Mhe. Wang Ke kuendelea kuwahimiza wawekezaji zaidi kuja kushirikiana na Tanzania katika uwekezaji kwenye maeneo mbalimbali kwa manufaa ya pande zote mbili na kwamba Serikali ya Tanzania itakuwa tayari kujenga mazingira mazuri ya uwekezaji na biashara.
Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli ameagana na Balozi wa Canada hapa nchini Mhe. Ian Myles na Balozi wa Ubelgiji hapa nchini Mhe. Paul Cartier baada ya Mabalozi hao kumaliza muda wao.
Baada ya mazungumzo hayo Mabalozi hao wameelezea kufurahishwa kwao na uhusiano na ushirikiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na nchi zao na wamempongeza Mhe. Rais Magufuli na Serikali anayoiongoza kwa hatua kubwa za kuleta mageuzi ya kiuchumi, kuboresha utendaji kazi wa watumishi wa umma, kupambana na rushwa na kuboresha huduma za kijamii.
Katika hatua nyingine, Mhe. Rais Magufuli amekutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Burundi Mhe. Ezechiel Nibigira ambaye amewasilisha barua kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Burundi Mhe. Pierre Nkurunziza.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli amefanya mazungumzo na Mhe. Nibigira, mazungumzo ambayo yamehudhuriwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt. Susan Kolimba na Balozi wa Burundi hapa nchini Mhe. Gervais Abayeho.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
06 Agosti, 2018
Taarifa kwa vyombo vya habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli jioni ya tarehe 04 Agosti, 2018 ameungana na viongozi wa Wizara ya Maliasili na Utalii na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii Jinsia na Watoto, kumpokea Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Hamisi Kigwangala ambaye amesafirishwa kwa ndege kutoka Arusha alikopata ajali leo asubuhi, kuja Jijini Dar es Salaam kwa matibabu zaidi.
Dkt. Kigwangalla aliyekuwa akisafiri kutoka Arusha kwenda Dodoma amepata ajali leo majira ya saa 12:15 asubuhi katikati ya vijiji vya Mdolii na Minjingu Wilaya ya Babati Mkoani Manyara baada ya gari lake kupinduka na kusababisha kifo cha Afisa Habari wa Wizara ya Maliasili na Utalii Bw. Hamza Temba na wengine watano akiwemo Dkt. Kigwangalla kuumia.
Baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam, Dkt. Kigwangalla amepelekwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa matibabu.
Katika mapokezi hayo Mhe. Rais Magufuli alikuwa pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mrisho Gambo (aliyemsindikiza Dkt. Kigwangalla), Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Japhet Hasunga, Katibu Mkuu wa Wizara ya Utalii na Maliasili Mej Jen. Gaudence Milanzi na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii Jinsia na Watoto Dkt. Mpoki Ulisubisya.
Akizungumza uwanjani hapo Mhe. Rais Magufuli amempa pole Dkt. Kigwangalla na kumuombea apone haraka na pia amewashukuru madaktari na wauguzi wa Kituo cha afya cha Magugu walioanza kutoa huduma ya kwanza na amewashukuru Madaktari na wauguzi wa hospitali ya Selian iliyopo Mjini Arusha kwa juhudi kubwa walizofanya kuokoa maisha ya Dkt. Kigwangalla na majeruhi wengine wa ajali hiyo.
Mhe. Rais Magufuli ametoa salamu za pole kwa familia, wafanyakazi wa Wizara ya Maliasili na Utalii, ndugu, jamaa na marafiki wote kufuatia kifo cha Bw. Hamza Temba na amemuombea apumzike mahali pema peponi, Amina.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
04 Agosti, 2018
Taarifa kwa vyombo vya habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 01 Agosti, 2018 amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Nchi wa Mambo ya Nje wa Japan Mhe. Masahisa Sato Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Katika mazungumzo hayo Mhe. Sato amesema Japan itaendeleza na kukuza zaidi uhusiano na ushirikiano wa kiuchumi na Tanzania na ameomba kuharakishwa kwa mchakato wa utiaji saini mkataba wa ushirikiano katika kulinda uwekezaji kati ya Tanzania na Japan (Bilateral Investment Protection Agreement – BIPA) ili kuchochea kasi ya uwekezaji.
Mhe. Sato pia ameahidi kufuatilia miradi yote inayofadhiliwa na Japan hapa nchini na ambayo utekelezaji wake unasuasua ili kutatua vikwazo na kutekeleza miradi hiyo.
Kwa upande wake Mhe. Rais Magufuli amempongeza Mhe. Sato kwa kutembelea Tanzania na amemuomba afikishe salamu na shukrani zake za dhati kwa Waziri Mkuu wa Japan Mhe. Shinzo Abe kwa ushirikiano na uhusiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na Japan, uliowezesha kutekelezwa kwa miradi mingi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa barabara na madaraja, umeme, maji na afya.
Mhe. Rais Magufuli amemuomba Mhe. Sato kufikisha mwaliko wake kwa wafanyabiashara na wawekezaji wa Japan wakiwemo wenye viwanda vya magari, kuja nchini Tanzania kuwekeza katika sekta mbalimbali na amemhakikishia kuwa Serikali itawapa ushirikiano wowote watakaouhitaji.
“Mwambie Waziri Mkuu Shinzo Abe kuwa kwa niaba ya Watanzania namshukuru sana na namuomba ushirikiano huu mzuri uendelee, waambie wafanyabiashara wa kampuni za magari waje hata kesho, tutahakikisha wanapata mazingira mazuri ya kuwekeza” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Mazungumzo hayo yamehudhuriwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje Dkt. Susan Kolimba na Balozi wa Japan nchini Tanzania Mhe. Masaharu Yoshida.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
01 Agosti, 2018
Taarifa kwa vyombo vya habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 01 Agosti, 2018 amewaapisha Wakuu wa Mikoa 4, Makatibu Wakuu 2, Makatibu Tawala wa Mikoa 13 na Naibu Makatibu Wakuu 2 aliowateua tarehe 28 Julai, 2018.
Hafla ya kuapishwa kwa viongozi hao imefanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, Mawaziri, Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi, Jaji Kiongozi Mhe. Dkt. Elieza Feleshi, viongozi wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama, Wakuu wa Mikoa wote wa Tanzania Bara, Viongozi wa Dini na Viongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam.
Wakuu wa Mikoa walioapishwa ni Brig. Jen. Nicodemus Elias Mwangela (Songwe), Brig. Jen. Marco Elisha Gaguti (Kagera), Ali Salum Hapi (Iringa) na Albert John Chalamila (Mbeya), wakati Makatibu Wakuu walioapishwa ni Prof. Joseph Rwegasira Buchweishaija (Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji) na Andrew Wilson Massawe (Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Ajira na Wenye Ulemavu).
Makatibu Tawala wa Mikoa walioapishwa ni Eric Katemansimba Shitindi (Njombe), Maduka Paul Kessy (Dodoma), Dr. Jilly Elibariki Maleko (Mtwara), Abubakar Mussa Kunenge (Dar es Salaam), Happiness William Seneda (Iringa), Karolina Albert Mthapula (Mara) na David Zacharia Kafulila (Songwe),
Wengine ni Denis Isidory Bandisa (Geita), Abdalla Mohamed Malela (Katavi), Rashid Kassim Mchatta (Kigoma), Missaile Raymond Musa (Manyara), Christopher Derek Kadio (Mwanza) na Prof. Riziki Silas Shemdoe (Ruvuma).
Naibu Makatibu Wakuu walioapishwa ni Dkt. Jim James Yonazi (Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano {Mawasiliano}) na Edwin Paul Mhede (Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji).
Akizungumza baada ya kuwaapisha Mhe. Rais Magufuli amewataka viongozi hao kwenda kuchapa kazi kwa juhudi na maarifa katika maeneo waliyopangiwa kwa kushirikiana na viongozi na wafanyakazi wengine waliopo katika maeneo hayo.
Mhe. Rais Magufuli amesema amechukua muda mrefu kufanya uteuzi wa viongozi hao pamoja na Wakuu wa Wilaya ambao wanaapishwa na Wakuu wa Mikoa katika mikoa waliyopangiwa, ili kujiridhisha juu ya uwezo wao na kwamba anaamini aliowateua watafanya kazi ya kutatua kero za wananchi na kusukuma mbele gurudumu la maendeleo.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli amewataka Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa Mikoa kwenda kusimamia ipasavyo ukusanyaji wa mapato ya halmashauri na ameelezea kutoridhishwa na ukusanyaji wa kiwango cha chini wa mapato hasa katika Majiji ya Dar es Salaam na Mbeya ambayo yana vyanzo vingi na vikubwa lakini yanakusanya kiasi kidogo huku yakizidiwa na Jiji jipya la Dodoma.
“Mkuu wa Mkoa wewe ndio Rais wa mkoa huo, sasa mkoa wako unapokuwa haukusanyi mapato huwa najiuliza sana kuna sababu gani ya kuendelea na Mkuu wa Mkoa ambaye hasimamii ukusanyaji wa mapato?” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Halikadhalika Mhe. Rais Magufuli amewaonya viongozi wa mikoa wasiokuwa na uhusiano mzuri miongoni mwao na amewataka viongozi hao kuwajibika kutekeleza Ilani ya Uchaguzi Mkuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2015, inayotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Tano.
Mapema kabla ya hotuba ya Mhe. Rais, Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa wamempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa kufanya uteuzi wa viongozi hao na wamewataka viongozi hao kuzingatia viapo vyao, kujifunza kwa umakini yaliyopo katika ofisi zao na kusimamia kwa tija shughuli za Serikali.
Viongozi walioapishwa na Mhe. Rais Magufuli pia wamekula kiapo cha uadilifu kwa viongozi wa umma kilichoongozwa na Kamishna wa Maadili Jaji Mstaafu Harold Nsekela.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
01 Agosti, 2018
Taarifa kwa vyombo vya habari
Wakuu wa Mikoa 4, Makatibu Wakuu 2, Naibu Makatibu Wakuu 2 na Makatibu Tawala wa Mikoa 13 walioteliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli siku ya Jumamosi tarehe 28 Julai, 2018 wataapishwa tarehe 01 Agosti, 2018 saa 4:00 asubuhi, Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Wakuu wa Mikoa yote ya Tanzania Bara mnapaswa kuhudhuria tukio hili.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
30 Julai, 2018
Taarifa kwa vyombo vya habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 30 Julai, 2018 amekabidhi hati miliki za viwanja kwa Mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini na wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa yenye makazi yake hapa nchini kwa ajili ya kujenga ofisi na makazi katika makao makuu ya nchi Jijini Dodoma.
Hafla ya kukabidhi hati hizo imefanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Spika wa Bunge Mhe. Job Yustino Ndugai, Mawaziri, Makatibu Wakuu, viongozi wa vyombo vya ulinzi na usalama na viongozi wa mkoa wa Dodoma wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa huo Dkt. Binilith Satano Mahenge.
Jumla ya hati 67 zimekabidhiwa ambapo 62 kati yake ni za Balozi za nchi mbalimbali na 5 ni za Mashirika ya Kimataifa, na kila kiwanja kina ukubwa wa ekari 5.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt. Binilith Mahenge amewahakikishia Mabalozi hao kuwa mkoa huo umejipanga kuwapokea, kuwapa huduma zote muhimu ikiwemo huduma za afya, maji, umeme, kutengeneza miundombinu ya barabara katika maeneo waliyopatiwa viwanja na usalama wa uhakika.
Nae Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi amesema Serikali imetoa bure viwanja hivyo 67 baada ya kugharamia ulipaji wa fidia, upangaji, upimaji na umilikishaji, na kwamba itakuwa tayari kufanyia kazi mahitaji mengine ya Mabalozi na mashirika hayo kama yatakuwepo.
Kiongozi wa Mabalozi na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa hapa nchini Mhe. Balozi Eugen Kayihura amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa dhamira yake njema ya kutoa bure viwanja vya kujenga ofisi na makazi, na kwamba hati hizo wataziwasilisha katika Serikali za nchi zao na mashirika yao.
Akizungumza kabla ya kukabidhi hati hizo Mhe. Rais Magufuli amesema Serikali iliamua kutoa viwanja vya Ubalozi na Mashirika hayo ya Kimataifa kwa lengo la kurahisisha mchakato wa kuhamia Makao Makuu ya nchi Jijini Dodoma.
“Makamu wa Rais ameshahamia Dodoma, Waziri Mkuu ameshahamia Dodoma, Mawaziri na viongozi wengine wengi tayari wapo Dodoma, nimebaki mimi, na nimepanga kuhamia kabla ya mwaka huu kuisha, sasa nikaona nisiondoke nikawaacha nyinyi wawakilishi wa Marais huku Dar es Salaam” amesema Mhe. Rais Magufuli na kutoa wito kwa Mabalozi hao kuhamia Dodoma.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli amewahakikishia kuwa Serikali inaendelea kuimarisha huduma na miundombinu ya Dodoma ikiwemo ujenzi wa barabara za kuunganisha mikoa jirani na Dodoma ambazo zimekamilika, upanuzi wa uwanja wa ndege wa Dodoma ambao umekamilika na kwamba leo ametoa maelekezo kwa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kutangaza zabuni ya ujenzi wa uwanja mkubwa wa ndege wa Msalato ambao utakuwa na urefu wa kilometa 3 na utaweza kupokea ndege kubwa na ndogo.
“Tunataka kujenga uwanja ambao ndege yetu Boeing 787-7 Dreamliner itaweza kutua, pia ndege zetu mbili aina Bombardier CS-300 zitafika mwezi wa 11 mwaka huu na Kampuni ya Boeing wametuambia ndege yetu nyingine iliyopangwa kuja mwaka 2020 sasa wataileta mwaka ujao mwishoni (2019), kwa hiyo kwenda Dodoma kutakuwa na usafiri wa uhakika” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Mhe. Rais Magufuli amebainisha juhudi mbalimbali zinazofanywa na Serikali katika kujenga uchumi, kuboresha maisha ya watu na kulinda rasilimali za Taifa, na amewaomba Mabalozi na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa kuunga mkono juhudi hizo kwa kuhimiza wawekezaji kuja kushirikiana na Tanzania katika uwekezaji.
Mapema leo asubuhi Mhe. Rais Magufuli amepokea hati za utambulisho za Balozi wa Kenya hapa nchini Mhe. Dan Kazungu, ambaye ameteuliwa na Mhe. Rais Uhuru Kenyatta baada ya Mhe. Chirau Ali Makwere kumaliza muda wake.
Mhe. Rais Magufuli amemuomba Mhe. Balozi Kazungu kumfikishia salamu Mhe. Rais Uhuru Kenyatta na kumhakikishia kuwa Tanzania itaendeleza na kukuza uhusiano na ushirikiano mzuri uliopo kati yake na Kenya ambayo ni nchi inayoongoza kwa kuwekeza nchini Tanzania kati ya nchi zote za Bara la Afrika, na ni nchi ya 5 duniani kwa uwekezaji mkubwa hapa nchini.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
30 Julai, 2018
Taarifa kwa vyombo vya habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amemtumia salamu za rambirambi Mufti wa Tanzania Sheikh Aboubakary Zubeir bin Ally kufuatia kifo cha Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Mwanza na Mwenyekiti wa Baraza la Ulamaa katika Mkoa huo Sheikh Salum Hassani Fereji kilichotokea usiku wa kuamkia tarehe 28 Julai, 2018 katika hospitali ya Bugando Mkoani humo.
Mhe. Rais Magufuli amesema anamkumbuka Sheikh Salum Hassani Fereji wa ucha Mungu wake, ukarimu, upendo kwa wananchi na namna alivyokuwa akiunga mkono juhudi za kudumisha amani na kusukuma mbele maendeleo.
"Nimesikitishwa sana na kifo cha Sheikh Fereji, nilipokuwa nikienda Mwanza alikuwa miongoni mwa viongozi wa dini waliokuja kunipokea na amekuwa akifanya kazi ya Mwenyezi Mungu kwa mapenzi makubwa na nchi yake, pole sana Mufti wa Tanzania na nakuomba unifikishie salamu zangu za pole kwa familia yake, Waislamu wote wa Mkoa wa Mwanza na nchi nzima pamoja na wote walioguswa na msiba huu" amesema Mhe. Rais Magufuli.
Mhe. Rais Magufuli amemuombea Marehemu Sheikh Salum Hassan Fereji apumzike mahali pema, Amina.
Inna lillahi wa inna ilayhi raji'un.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
30 Julai, 2018
Taarifa kwa vyombo vya habari
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) Bw. David Beasley amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kwa uongozi mzuri, na kwamba WFP imedhamiria kutumia fursa hiyo kufanikisha utekelezaji wa mipango yake mbalimbali.
Bw. Beasley ambaye amewahi kuwa Gavana wa Jimbo la Carolina Kusini nchini Marekani amesema hayo tarehe 26 Julai, 2018 Ikulu Jijini Dar es Salaam muda mfupi baada ya kukutana na kufanya mazungumzo na Mhe. Rais Magufuli, kando ya ziara yake ya siku 7 hapa nchini.
“Tumezungumza kuhusu namna Tanzania inavyong’ara kimataifa, kuhusu WFP inavyoweza kushirikiana na Tanzania kuboresha maisha ya wakulima wadogo, kupata masoko na bei nzuri ya mazao ya wakulima wadogo na tunaamini Tanzania inaweza kuwa mzalishaji mkubwa wa chakula kwa ajili ya ukanda wote wa Afrika, hivyo tunataka kutumia fursa ya ukarimu, ushirikiano na uongozi bora wa Mhe. Rais Magufuli na baraza lake la Mawaziri ambalo tunaamini wamedhamiria kuboresha maisha, kuongeza tija na kuondoa rushwa” amesema Bw. Beasley.
Bw. Beasley amebainisha kuwa pamoja na kununua mazao ya chakula kutoka kwa wakulima kila msimu, WFP inaendesha miradi ya kuwawezesha wakulima wadogo kuzalisha mazao bora na kwa tija nchini Tanzania na hivi sasa inao mpango wa kupanua uwigo kwa kuongeza idadi ya wakulima wanaofikiwa na mradi huo kutoka 50,000 hadi 250,000 katika miaka miwili ijayo.
Aidha, Bw. Beasley ameahidi kulifanyia kazi ombi la Mhe. Rais Magufuli la kutaka WFP iongeze kiwango cha mazao inayoyanunua kutoka kwa wakulima kutoka tani 56,000 za msimu uliopita, ikiwa ni juhudi za kukabiliana na changamoto ya wakulima kukosa soko la mazao ya chakula cha ziada kinachozalishwa hapa nchini.
Kwa upande wake Mhe. Rais Magufuli amempongeza Bw. Beasley kwa kutembelea Tanzania na dhamira yake njema ya kushirikiana na Tanzania katika kuwasaidia wakulima wadogo wa mazao ya chakula, kuongeza kiwango cha mahindi yanayonunuliwa na WFP na pia kutumia bandari ya Dar es Salaam kusafirisha mazao na mizigo mbalimbali ya nchi za ukanda huu.
Mhe. Rais Magufuli amesema Serikali ipo tayari kushirikiana na WFP hasa katika kukabiliana na changamoto ya wakulima kukosa soko la mazao ya ziada na amebainisha kuwa katika msimu huu Tanzania ina takribani tani milioni 4 za chakula cha ziada kinachopaswa kuuzwa nje ya nchi.
“Namshukuru sana kwa kuunga mkono juhudi tunazozifanya kwa ajili ya maendeleo ya Watanzania, na hii ndio njia pekee ya kuhakikisha nchi inajikomboa kwa kuwa na uchumi wa kweli, kwani tumedhamiria kujitegemea, na pia namshukuru kwa kuunga mkono ‘Hapa Kazi Tu’ na juhudi zingine zote ikiwemo kupambana na rushwa na kwamba anaiona Tanzania ya pekee na yenye mwelekeo tofauti wa kuleta neema” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Mhe. Rais Magufuli amemhakikishia Bw. Beasley kuwa uchumi wa Tanzania unakuwa vizuri kwa wastani wa asilimia 7 na unatarajiwa kuongezeka hadi asilimia 7.1 katika kipindi kifupi kijacho, mfumuko wa bei umeendelea kuwa kwa tarakimu moja (ukiwa umeshuka hadi kufikia asilimia 3.8), pia amemkaribisha kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii na kuwa balozi wa kuutangaza uzuri wa Tanzania.
Mazungumzo ya Mhe. Rais Magufuli na Bw. Beasley yamehudhuriwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Dkt. Augustine Mahiga, Naibu Waziri wa Kilimo Mhe. Omar Mgumba na Mwakilishi Mkazi wa WFP hapa nchini Bw. Michael Dunford.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
26 Julai, 2018