Taarifa kwa vyombo vya Habari ya zamani
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 05 Mei, 2018 amefungua daraja la mto Kilombero lenye urefu wa mita 384 lililojengwa pamoja na barabara zake zenye urefu wa kilometa 9.142 kwa gharama ya Shilingi Bilioni 61.133 zilizotolewa na Serikali ya Tanzania.
Kabla ya kukata utepe wa ufunguzi Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa Mnyaa amemuomba Mhe. Rais Magufuli daraja hilo liitwe “Daraja la Magufuli” (Magufuli Bridge), na baada ya majadiliano ya muda mfupi na viongozi walioshika utepe wakiwemo Maaskofu, Masheikh, Wabunge na viongozi wa Mkoa wa Morogoro, Mhe. Rais Magufuli akakubali na kulifungua.
Prof. Mbarawa ameamua kutoa jina hilo ikiwa ni kwa mujibu wa sheria, na amebainisha kuwa uamuzi wake huo umezingatia juhudi kubwa zilizofanywa na Mhe. Rais Magufuli tangu akiwa Waziri wa Ujenzi, ambapo baada ya kutokea ajali ya kuzama kivuko iliyosababisha takribani watu 30 kupoteza maisha mwaka 2001 alifika Ifakara, akatoa pole kwa wafiwa na akaagiza kuanza kwa mchakato wa ujenzi na kisha kuufuatilia kwa ukaribu hadi daraja hilo limekamilika.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mhandisi Patrick Mfugale amesema daraja hilo lenye njia mbili litadumu kwa miaka zaidi ya 120, lina uwezo wa kubeba tani 180 kila upande, lina njia za watembea kwa miguu na limefungwa taa zinazotumia nishati ya jua (Solar Power).
Akizungumza na wananchi wa Ifakara katika uwanja wa michezo mjini hapo Mhe. Rais Magufuli aliyeongozana na Mkewe Mhe. Mama Janeth Magufuli amewapongeza wananchi wa Ifakara kwa kujengewa daraja hilo, na pia amewapongeza Watanzania wote kwa kulipa kodi zilizowezesha kutekelezwa kwa mradi huo mkubwa kwa kutumia fedha zao.
Mhe. Rais Magufuli amewataka wananchi wa Ifakara, Malinyi, Kilombero, Kilosa na maeneo mengine yatakayonufaika na kujengwa kwa Daraja la Magufuli na ujenzi wa barabara ya Kidatu – Ifakara kutumia miundombinu hiyo kwa manufaa yaani kuongeza uzalishaji wa mazao ya kilimo na kuyasafirisha kwenda kwenye masoko, na amewahakikishia kuwa Serikali itaendeleza ujenzi wa barabara ya lami kutoka Ifakara – Malinyi – Londo hadi Lumecha Wilayani Songea ambako itaungana na barabara kuu ya Songea – Namtumbo – Tunduru – Mtambaswala.
Mhe. Rais Magufuli amebainisha kuwa ujenzi wa miundombinu hiyo ni sehemu ya juhudi za Serikali ya Awamu ya tano kujenga uchumi na kwamba juhudi kama hizo pia zinafanyika kuongeza uzalishaji wa umeme kupitia miradi ya Kinyerezi 1,2-3 na mradi wa umeme katika mto Rufiji (Stieglers Gorge) itakayoiwezesha Tanzania kuwa na Megawati 5,000 za umeme ifikapo mwaka 2021, kujenga reli, kuimarisha usafiri wa anga, kulinda rasilimali ikiwemo madini na kuboresha huduma za jamii zikiwemo kutoa elimu bure kwa shule za msingi hadi sekondari, kuongeza mikopo ya elimu ya juu, kuimarisha miradi ya maji na kuboresha huduma za afya.
Mhe. Rais Magufuli ambaye akiwa njiani kuelekea Ifakara amesimamishwa na wananchi wa vijiji vya Sande, Misufini, Mkula, Mang’ula, Mang’ula Kona, Kisawasawa, Kiberege na Sululu ambako amesikiliza kero zao na kuchangia fedha katika miradi ya maendeleo, amewataka Wabunge kuwajibika ipasavyo kwa kusikiliza kero za wapiga kura wao na kuzifanyia kazi badala ya kuacha kero hizo ziwasubiri viongozi wa kitaifa.
“Wabunge mna fedha za mfuko wa jimbo, wasaidieni wananchi wenu, haiwezekani wananchi wawe wanamuomba Rais fedha za kujengea matundu ya vyoo vya shule wakati nyinyi mpo” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Kuhusu kero ya wananchi kuendelea kutozwa ushuru wa mazao yasiyozidi tani moja kwa mujibu wa sheria, Mhe. Rais Magufuli amewataka viongozi kote nchini kuwashughulikia wanaotoza ushuru huo na kusisitiza kuwa “Najua viongozi wote Tanzania mnanisikia, nataka mtu atoke na mchele hapa Ifakara apeleke Dar es Salaam, apeleke Moshi, apeleke Tabora na ashuke nao mpaka Mpanda bila kubughudhiwa ilimradi hauzidi tani moja”.
Akiwa katika Vijiji vya Mang’ula na Mang’ula Kona Mhe. Rais Magufuli amesema Serikali imeanza kuchukua hatua za kukirejesha kiwanda kutengeneza vipuri cha Mang’ula ili kuhakikisha kinaendeshwa kwa malengo yaliyokusudiwa na Baba wa Taifa Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Ifakara
05 Mei, 2018
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 04 Mei, 2018 ameweka jiwe la msingi la mradi wa ujenzi wa barabara ya lami ya Kidatu – Ifakara Mkoani Morogoro yenye urefu wa kilometa 66.9 inayojengwa pamoja na daraja la mto Ruaha Mkuu lenye urefu wa mita 130 lililopo katika barabara hiyo.
Sherehe za uwekaji jiwe la msingi zimefanyika katika eneo la Nyandeo – Kidatu na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Mke wa Rais Mhe. Mama Janeth Magufuli, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa Mnyaa, Balozi wa Umoja wa Ulaya hapa nchini Mhe. Roeland Van de Geer, Mwakilishi wa Shirika la Misaada ya Maendeleo la Uingereza (DFID) Bi. Beth Arthy, Wabunge wa Mkoa wa Morogoro na wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu na viongozi wa Mkoa wa Morogoro.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mhandisi Patrick Mfugale amesema ujenzi wa barabara na daraja hilo utagharimu Shilingi Bilioni 104.914 ambapo kati yake asilimia 49.15 zinatolewa na Umoja wa Ulaya, asilimia 40.13 zinatolewa na DFID, asilimia 10.72 zinatolewa na Shirika la Misaada la Marekani (USAID) na fedha nyingine zinatolewa na Serikali ya Tanzania.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa Mnyaa amesema barabara hiyo ni muhimu kwa mikoa ya nyanda za juu kusini kwa kuwa inaunganisha eneo muhimu la ukanda wa kilimo wa kusini (Southern Agricultural Growth Corridor of Tanzania – SAGCOT) na pia inaunganisha barabara kuu ya Dar es Salaam – Tunduma (TANZAM) kuanzia Mikumi – Ifakara – Lupiro – Malinyi – Londo hadi Lumecha katika wilaya ya Songea Mkoani Ruvuma.
Balozi wa Umoja wa Ulaya nchini Mhe. Roeland Van de Geer na Mwakilishi wa DFID Bi. Beth Arthy wamempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa jitihada zake za kuhakikisha mradi huo unatekelezwa na wamebainisha kuwa barabara hiyo itawanufaisha wananchi takribani milioni 9 kwa kurahisisha usafirishaji wa mazao yakiwemo ya chakula na hivyo kuongeza usalama wa chakula nchini.
Nao Wabunge wa Mkoa wa Morogoro wamemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa Serikali kuanza ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami, na wamemuomba kuwasaidia kutatua kero nyingine zilizopo katika majimbo yao zikiwemo uhaba wa maji na upotevu wa fedha za miradi ya maji, uhaba wa ardhi ya kilimo kutokana na mashamba makubwa kushikiliwa na watu ambao hawayaendelezi na ubovu wa barabara katika majimbo yao.
Katika hotuba yake Mhe. Rais Magufuli ameushukuru Umoja wa Ulaya (EU), DFID na USAID kwa kuchangia katika ujenzi wa barabara ya Kidatu – Ifakara pamoja na daraja la mto Ruaha Mkuu na amewaomba washirika hao wa maendeleo watoe ushirikiano kwa Serikali katika kuendeleza ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami kuanzia Ifakara – Lupiro – Malinyi – Londo hadi Lumecha wilayani Songea.
Kuhusu kero zilizotolewa na Wabunge wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Rais Magufuli amewahakikishia kuwa Serikali itaendelea kujenga kwa kiwango cha lami barabara nyingine muhimu za mkoa huo, itaendelea kuwanyang’anya mashamba wamiliki ambao wameyatelekeza na kisha kuwagawia wananchi bure, na pia ameagiza wakandarasi wote waliolipwa fedha kwa ajili ya kujenga miradi ya maji na hawakujenga miradi hiyo, waanze kuijenga mara moja na kama sivyo warejeshe fedha walizolipwa ama vyombo vya dola viwakamate.
“Wakandarasi waliokula fedha za miradi ya maji wajue kuwa wamekula sumu, fedha ya Serikali huwa hailiwi, wakandarasi wanaojijua kuwa wamekula fedha za maji waende wenyewe kujenga miradi na kama sivyo warudishe fedha walizochukua, wasipofanya hivyo wakamwatwe. ameagiza Mhe. Rais Magufuli.
Akiwa njiani kutoka Iringa Mjini Mhe. Rais Magufuli amesalimiana na wananchi wa Ilula na Ruaha Mbuyuni Mkoani Iringa ambako amechangia Shilingi Milioni 5 kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya, na kisha akasalimiana na wananchi Ruaha Darajani Mkoani Morogoro ambako amechangia Shilingi Milioni 3 katika ujenzi wa shule ya msingi Ruaha Darajani na kuagiza shule hiyo isajiliwe ndani ya mwezi huu.
Mhe. Rais Magufuli pia amesalimiana na wananchi wa Mikumi na Kidodi ambako amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji Prof. Kitila Mkumbo kwenda katika maeneo hayo kufuatilia sababu za kukabiliwa na uhaba wa maji licha ya kuwepo mradi wa maji uliogharimu takribani Shilingi Milioni 800.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Kilombero
04 Mei, 2018
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 03 Mei, 2018 amefungua barabara ya Iyovi – Iringa – Mafinga yenye urefu wa kilometa 218.6 ambayo ni sehemu ya barabara kuu ya Dar es Salaam – Tunduma (TANZAM), inayounganisha Bandari ya Dar es Salaam na nchi jirani za kusini mwa Afrika zikiwemo Zambia, Zimbabwe, Kongo-DRC na Malawi.
Sherehe za ufunguzi wa barabara hiyo zimefanyika katika eneo la Ihemi, Iringa Vijijini na kuhudhuriwa na Mke wa Rais Mhe. Mama Janeth Magufuli, Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mhe. Charles Mwijage, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi, Naibu Balozi wa Denmark hapa nchini Bi. Camilla Christensen, Wabunge, viongozi wa dini na viongozi wa siasa.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mhandisi Patrick Mfugale amesema ujenzi wa barabara hiyo umegharimu Shilingi Bilioni 282 zilizotolewa kwa mkopo nafuu kutoka Serikali ya Denmark kupitia Shirika lake la misaada (DANIDA) na Shilingi Bilioni 1.8 zilizotolewa na Serikali ya Tanzania.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa Mnyaa amesema mbali na barabara hiyo Denmark imeshirikiana na Tanzania kukarabati barabara za Ubungo - Mlandizi (kilometa 60.7), Chalinze – Melela (kilometa 129) na Chalinze – Segera – Tanga (kilometa 246.7) na amebainisha kuwa kukamilika kwa barabara hizo kutasaidia kuimarisha usafiri na shughuli za kiuchumi ikiwemo kilimo na biashara.
Naibu Balozi wa Denmark hapa nchini Bi. Camilla Christensen ameelezea kufurahishwa kwake na kukamilika kwa ujenzi huo na amesisitiza kuwa uhusiano wa Tanzania na Denmark ulioanza miaka 50 iliyopita utaendelea kudumishwa hususani katika vipaumbele vinavyohusu uchumi na fedha, afya, ajira na uboreshaji wa biashara.
Mhe. Rais Magufuli ameishukuru Serikali ya Denmark kwa kufadhili miradi mbalimbali ukiwemo ujenzi wa barabara ya Iyovi – Iringa – Mafinga ambayo itasaidia kuboresha maisha ya watu kwa kuwarahisishia kupata masoko ya mazao na bidhaa zao pamoja na kukuza uzalishaji mali.
“Ndugu zangu wananchi wa Iringa, barabara hii imekamilika na ni miongoni mwa barabara bora tulizonazo hapa nchini kwetu, natoa wito kwenu mchangamkie fursa, limeni mazao ya kutosha na myasafirishe kwenda kwenye masoko mbalimbali ya ndani na nje ya nchi” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli ameiomba Denmark kupitia DANIDA kufadhili ujenzi wa barabara ya Igumbiro – Kihesa yenye urefu wa kilometa 11 ambayo itasaidia magari yatokayo kusini mwa Tanzania kwenda Dodoma kutopita katikati ya Mji wa Iringa ili kuepusha msongamano na athari za ajali za magari zinazoweza kutokea.
Mapema asubuhi Mhe. Rais Magufuli amefungua kiwanda cha kutotoresha vifaranga na kuzalisha chakula cha kuku cha Silverlands kilichopo Ihemi, Iringa Vijijini.
Mkurugenzi wa Silverlands Dkt. Ben Moshi amesema kiwanda hicho kina uwezo wa kuzalisha vifaranga 150,000 kwa wiki na tani 40 za chakula cha kuku kwa saa, na kwamba mwaka huu kimezalisha vifaranga 7,200,000 ambavyo vimeuzwa ndani ya nchi na nchi nyingine zikiwemo Ethiopia, Kenya, Nigeria na Uganda.
Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mhe. Charles Mwijage amesema uwepo wa kiwanda hicho utawasaidia wakulima kupata soko la mazao kwani kinahitaji tani 120,000 za mahindi kwa mwaka na tani 40,000 za soya, na amesisitiza kuwa teknolojia inayotumika inamwezesha mfugaji kuzalisha kuku bora wasiokuzwa kwa kutumia dawa na virutubisho vya kikemikali.
Mhe. Rais Magufuli amewapongeza wawekezaji wa kiwanda cha Silverlands kwa uwekezaji mkubwa wa Dola za Marekani Milioni 71 na kutoa ajira kwa watu 938 lakini amewataka kulipa kodi za Serikali kama inavyopaswa badala ya kusingizia kuwa hawapati faida.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Iringa
03 Mei, 2018
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Viongozi wa Mkoa wa Iringa wamemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kwa miradi mikubwa inayotekelezwa na Serikali Mkoani humo na wameahidi kuendelea kumuungano mkono na kumuombea katika majukumu mazito anayoyatekeleza.
Viongozi hao waliojumuisha Waheshimiwa Madiwani, viongozi wa vyama vya siasa, viongozi wa dini na viongozi wa kimila wametoa shukrani hizo katika hafla ya chakula cha jioni iliyoandaliwa na Mhe. Rais Magufuli na kufanyika katika Ikulu ndogo Mjini Iringa.
Wamesema katika kipindi cha miaka miwili na nusu ya Serikali ya Awamu ya Tano Mhe. Rais Magufuli amedhihirisha kutanguliza maslahi ya Watanzania wote bila kubagua vyama vya siasa.
“Mhe. Rais umekuwa ukisisitiza katika hotuba zako kuwa wewe hujali mambo ya vyama, na hii imedhirika kuwa kweli hujali vyama, umesaidia sana, hela za kutoka kwako zimekuja nyingi, kama alivyosema Mhe. Mahiga, kuna barabara nzuri katika kipindi chako ambacho umekuwa Rais, umejenga barabara ya lami kutoka Mlandege mpaka kwa Mkuu wa Wilaya karibu Shilingi Bilioni 3.5, tuna stendi nzuri ipo Ipogolo ya karibu Shilingi Bilioni 3, tuna maji, kwa hiyo kuna vitu vimefanyika kwa kweli Mhe. Rais hupendelei, hela zinakuja hata sisi ambao ni wa CHADEMA unaleta hela, kwa hiyo tunakupongeza sana” amesema Mhe. Peter Msigwa, Mbunge wa Iringa Mjini.
Aidha, Viongozi hao wamempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa jitihada kubwa alizozielekeza katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya kitaifa ikiwemo ununuzi wa ndege kwa ajili ya Shirika la Ndege la Taifa (ATCL) ambalo litaimarisha utalii na kuitangaza nchi kimataifa, ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa (standard gauge), mradi wa umeme wa mto Rufiji (Stieglers’ Gorge), ujenzi wa viwanja vya ndege, bandari, barabara na madaraja, ambavyo vitaimarisha uchumi na kujenga heshima ya nchi.
“Mhe. Rais nchi yetu ina vivutio vya utalii, ina rasilimali nyingi, haya unayofanya sasa yanakwenda kuitangaza nchi yetu, ndege zetu zinaporuka zikiwa zimechorwa mnyama Twiga na zimeandikwa ‘The Wings of Kilimanjaro’ zinaitangaza nchi yetu, treni itainua uchumi wetu, tunakupongeza sana na tunakushukuru sana” amesema Salim Asas, Mjumbe wa NEC na Kaimu Mwenyekiti Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Iringa.
Katika hafla hiyo ambayo ilihudhuriwa na Mke wa Rais Mhe. Mama Janeth Magufuli, Mawaziri, viongozi wa dini, viongozi wa kabila la Wahehe, Wabunge, Madiwani, Viongozi wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA), wafanyabiashara na Viongozi wa Mkoa wa Iringa, Mhe. Rais Magufuli amewashukuru viongozi hao na kuahidi kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na Mkoa wa Iringa kusukuma maendeleo ya Mkoa.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Iringa
02 Mei, 2018
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ameviagiza vyombo vya dola, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kuchunguza mradi wa ujenzi wa jengo la ukumbi wa mihadhara na ofisi za Wahadhiri katika Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Mkwawa (MUCE) kilichopo katika Manispaa ya Iringa.
Mhe. Rais Magufuli ambaye alisoma chuoni hapo wakati ikiwa shule ya sekondari ya Mkwawa, ametoa agizo hilo tarehe 02 Mei, 2018 alipotembelea chuo hicho na kuzungumza na wanafunzi na Wahadhiri katika uwanja wa michezo.
Ujenzi wa jengo la ukumbi wa mihadhara na ofisi za Wahadhiri ulianza mwaka 2010 na tayari Serikali imeshatoa Shilingi Bilioni 8 na Milioni 804, lakini ujenzi wake bado haujakamilika.
Mhe. Rais Magufuli pia ameagiza vyombo vinavyohusika vifuatilie kesi iliyofunguliwa dhidi ya Mkandarasi aliyekuwa akijenga majengo hayo.
Katika Mkutano wake na wanafunzi wa MUCE Mhe. Rais Magufuli amesikiliza kero zao mbalimbali zikiwemo zinazohusu mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu na mazingira ya kusomea, ambapo amewaeleza kuwa Serikali imekuwa ikiongeza fedha za mikopo na kuwakopesha wanafunzi wengi zaidi lakini akasisitiza kuwa sasa haitaweza kutoa mikopo kwa wanafunzi wote wa vyuo vikuu.
“Nataka niwahakikishie Serikali ya Awamu ya Tano inawapenda wanafunzi wa vyuo vikuu, lakini lazima niwaambie ukweli Serikali haiwezi kutoa mikopo kwa wanafunzi wote” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Aidha Mhe. Rais Magufuli ameagiza Wakala wa Barabara Mkoani Iringa (TANROADS) kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa barabara ya kuingia chuoni hapo ili ijengwe kwa kiwango cha lami.
Akisoma taarifa kwa niaba ya Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambacho kinakisimamia Chuo Kikuu cha MUCE, Prof. Bonaventure Rutibwa amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kutembelea UDSM na kukijengea mabweni yanayochukua wanafunzi 4,000 katika kampasi ya Mwl. J.K Nyerere Mlimani Jijini Dar es Salaam ambayo yamepewa jina la “Hosteli za Dkt. John Pombe Magufuli”
Naye Rasi wa MUCE Prof. Esther Dungumaro ameseam chuo hicho kilichoanza mwaka 2005 kimezalisha walimu 7,090 wenye shahada ya kwanza na shahada ya uzamili na kwamba katika mwaka huu kitazalisha walimu 1,365 wakiwemo 641 wa masomo ya sayansi.
Katika ziara hiyo Mhe. Rais Magufuli ameongozana na Mkewe Mhe. Mama Janeth Magufuli, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi na Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Charles Mwijage.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Iringa
02 Mei, 2018
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 02 Mei, 2018 ameweka jiwe la msingi katika mradi wa ujenzi wa hospitali ya Wilaya ya Kilolo Mkoani Iringa na kuwahakikishia wananchi wa Wilaya hiyo kuwa Serikali itahakikisha ujenzi wa hospitali hiyo unakamilika haraka na kupeleka madaktari na wauguzi kwa ajili ya kuanza kutoa huduma.
Majengo ambayo yameanza kujengwa ni jengo la matibabu kwa wagonjwa wa nje (OPD), jengo la mionzi (Radiology), jengo la huduma ya mama na mtoto (RCH), jengo la maabara na jengo la wodi za kulaza wagonjwa, ambapo tayari Serikali imetoa Shilingi Bilioni 4.2 na hospitali inatarajiwa kuanza kutoa huduma ifikapo mwezi Agosti 2018.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Selemani Jafo amemueleza Mhe. Rais Magufuli kuwa ujenzi wa hospitali kama hiyo unaendelea katika wilaya nyingine za Mvomero, Buchosa na Siha.
Mhe. Jafo amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kutilia mkazo ujenzi wa hospitali za wilaya na vituo vya afya na amefafanua kuwa tangu Tanzania ipate uhuru ilifanikiwa kujenga hospitali 77, lakini kwa miaka miwili na nusu Serikali ya Awamu ya Tano imetenga Shilingi Bilioni 105 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa hosptali mpya 67, na pia imechukua hatua madhubuti za kuviimarisha vituo vya afya kwa kuviwezesha vituo vipya 208 kutoa huduma za upasuaji ikilinganishwa na vituo vya afya 115 vilivyokuwa na uwezo huo tangu uhuru.
Akizungumza na wananchi wa Kilolo baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi huo, Mhe. Rais Magufuli amewapongeza wananchi wa Kilolo kwa juhudi zao katika uzalishaji mali na amebainisha kuwa Serikali itaendelea kutekeleza ahadi zote ziliwekwa kwenye Ilani ya Uchaguzi ikiwemo utoaji wa elimu bila malipo ambapo inatoa Shilingi Bilioni 23.8 kila mwezi, kusambaza umeme kwa vijiji vyote Tanzania ifikapo mwaka 2021, kuongeza dawa hospitali ambapo imetenga Shilingi Bilioni 269 katika bajeti hii na kupeleka maji katika maeneo yenye uhaba wa maji.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli amewaahidi wananchi wa Kilolo kuwa sehemu ya barabara ya Iringa - Kilolo yenye kilometa 28 ambayo haijajengwa kwa kiwango cha lami, itaanza kujengwa hatua kwa hatua na amewataka kuongeza juhudi katika kilimo ili waweze kunufaika na barabara hiyo.
Mhe. Rais Magufuli ametoa wito kwa wananchi kujiunga na mifuko ya bima ya afya ili kujihakikishia upatikanaji wa matibabu kwa kuwa Serikali inaboresha huduma za afya, na pia ameagiza halmashauri zote nchini kuhakikisha zinaanzisha mifuko ya dawa (Drug Revolving Fund) ili kuwa na uhakika wa upatikanaji wa dawa.
Mhe. Rais Magufuli ameagiza halmashauri zote zilizoshindwa kutumia fedha za miradi iliyopangwa katika halmashauri hizo, zirejeshwe hazina na zipangiwe kazi nyingine.
Akiwa njiani kuelekea Kilolo Mhe. Rais Magufuli amesalimiana na wananchi wa kijiji cha Kilambo kilichopo Iringa Vijijini ambapo amechangia Shilingi Milioni 10 kwa ajili ya ujenzi wa majengo ya zahanati na shule, na amesalimiana na wananchi wa Kijiji cha Ndiwili ambako amechangia Shilingi Milioni 7 kwa ajili ya ujenzi wa majengo ya shule na zahanati.
Halikadhalika Mhe. Rais amesalimiana na wananchi wa Ipogolo katika Manispaa ya Iringa ambapo amewatahadharisha waliojenga majengo katika hifadhi ya barabara.
Katika ziara hii Mhe. Rais Magufuli ameongozana na Mkewe Mhe. Mama Janeth Magufuli, Waziri wa TAMISEMI Mhe. Selemani Jafo, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi na Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mhe. Charles Mwijage.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Iringa
02 Mei, 2018
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amesema Serikali ya Awamu ya Tano imefanikiwa kuzalisha ajira 1,826,743 katika kipindi kifupi cha miaka miwili na nusu iliyopita.
Mhe. Rais Magufuli amesema hayo tarehe 01 Mei, 2018 katika sherehe za maadhimisho ya sikukuu ya wafanyakazi (Mei Mosi) zilizofanyika kitaifa katika uwanja wa CCM Samora Mjini Iringa na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, Mke wa Rais Mhe. Janeth Magufuli, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job Yastino Ndugai, Naibu Spika Mhe. Dkt. Tulia Ackson, Mawaziri, Makatibu Wakuu, viongozi wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama, Wabunge, Viongozi wa dini na viongozi wa siasa.
Mhe. Rais Magufuli amefafanua kuwa kati ya ajira zilizozalishwa, wafanyakazi 18,101 ni watumishi wa umma wapya walioajiriwa kupitia kada mbalimbali, sekta binafsi imetoa ajira mpya 582,073 na ajira nyingine zimezalishwa kupitia miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa barabara na madaraja, umeme, ujenzi wa shule na vyuo, afya, viwanja vya ndege, viwanda, kilimo, mifugo na madini.
Aidha Mhe. Rais Magufuli amesema katika kipindi hicho Serikali imewapandisha vyeo wafanyakazi 88,016 na wengine 25,504 watakaopandishwa ifikapo Julai 2018 na ameahidi kuwa Serikali itaendelea kuajiri watumishi wapya na kuwapandisha vyeo wafanyakazi kadri bajeti itakavyoruhusu.
Kuhusu malimbikizo ya madeni ya wafanyakazi Mhe. Rais Magufuli amesema Serikali imeshawalipa wafanyakazi 52,851 waliokuwa wakidai Shilingi Bilioni 220.627 za madeni ya mishahara na yasiyo ya mishahara yaliyolimbikizwa tangu mwaka 2007 na amewahakikishia watumishi wote wanaodai madeni halali kuwa watalipwa fedha zao.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli amesema Serikali imeamua kuelekeza fedha nyingi katika kugharamia miradi mikubwa ya maendeleo na amewataka wafanyakazi kuongeza juhudi na maarifa kazini ili kuongeza ufanisi na uzalishaji mali, na pia ameahidi kuwaongeza mshahara kabla kumaliza kipindi chake cha uongozi.
Mhe. Rais Magufuli amemuagiza Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa kuchukua hatua dhidi ya viongozi wanaowahamisha wafanyakazi pasipo kuwalipa stahili zao na ameonya kuwa hatarajii kusisikia mtumishi mwingine amehamishwa bila kulipwa stahili zake.
Mhe. Rais Magufuli pia amemuagiza Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenister Mhagama kuhakikisha mifuko ya hifadhi ya jamii iliyounganishwa kutoka 5 na kubaki 2 ambayo ni Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Sekta Binafsi (NSSF), inaanza kufanya kazi haraka.
Kwa wakazi wa Mkoa wa Iringa Mhe. Rais Magufuli amewahakikishia kuwa Serikali anayoiongoza itaendelea kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo ya mkoa huo ikiwemo kuimarisha miundombinu ya utalii, kujenga barabara na kusambaza umeme katika vijiji 179 vilivyobaki.
Katika taarifa yao iliyowasilishwa na Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) Dkt. Yahya Msigwa, wafanyakazi nchini wamempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa juhudi zake zikiwemo kubana matumizi yasiyo ya lazima, kuunganisha mifuko ya hifadhi ya jamii, kupigania rasimali za Taifa, kuondoa watumishi hewa, vita dhidi ya rushwa na dawa za kulevya na ujenzi wa miundombinu, na wamemuahidi kumuunga mkono na hawatawatetea wafanyakazi wazembe, wavivu, watovu wa nidhamu, jeuri na wala rushwa
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Iringa
01 Mei, 2018
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amefungua barabara ya lami ya Iringa – Migoli – Fufu yenye urefu wa kilometa 189 na ambayo inaunganisha Mkoa wa Iringa na Mkoa wa Dodoma.
Barabara hiyo ambayo ni sehemu ya barabara kuu ya kuanzia Cape Town nchini Afrika Kusini hadi Cairo nchini Misri (The Great North Road) imejengwa kwa gharama ya Shilingi Bilioni 207.457 ikiwa ni ufadhili wa benki ya maendeleo ya Afrika (AfDB) kwa asilimia 65.9, Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Japan (JICA) kwa asilimia 21.3 na Serikali ya Tanzania imetoa asilimia 12.8.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mhandisi Patrick Mfugale amesema kukamilika kwa barabara hiyo kumeondoa adha iliyowakumba wananchi kwa miaka mingi ambapo safari ya Iringa – Dodoma iliyochukua siku nzima ama siku kadhaa wakati wa mvua, sasa inachukua muda wa saa 2:30.
Balozi wa Japan hapa nchini Mhe. Masaharu Yoshida na Mwakilishi wa AfDB Bw. Jeremy Aguma wameipongeza Serikali ya Tanzania kwa utekelezaji mzuri wa miradi inayofadhiliwa na taasisi zao, na wameahidi kukuza zaidi ushirikiano katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo itakayosaidia kukuza uchumi wa wananchi kama inavyoelekezwa katika dira ya maendeleo ya mwaka 2025.
Wabunge wa Mkoa wa Iringa wakiongozwa na Mbunge wa Ismani na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Vangimembe Lukuvi wamemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa juhudi zake zilizoyawezesha majimbo yao kupata miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa barabara, vituo vya afya na zahanati, Maji, uwanja wa ndege wa Nduli, Umeme, ruzuku ya elimu na dawa.
Akizungumza na wananchi waliojitokeza katika ufunguzi wa barabara hiyo Mhe. Rais Magufuli amewapongeza kwa kupata barabara ya uhakika na amewataka kuongeza juhudi katika uzalishaji mali hasa katika kilimo na biashara ili waweze kunufaika nayo.
Mhe. Rais Magufuli amezishukuru AfDB na JICA kwa kuendelea kuwa washirika muhimu wa maendeleo ya Tanzania, na kwa namna ya pekee amempongeza Mtendaji Mkuu wa TANROADS Mhandisi Patrick Mfugale kwa uchapakazi wake, ubunifu, uaminifu na uadilifu uliomwezesha kuiongoza TANROADS kwa mafanikio hasa katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya ujenzi wa barabara na madaraja.
Mhe. Rais Magufuli amesema pamoja na kujenga barabara hiyo, Serikali inauboresha uwanja wa ndege wa Nduli ili uweze kupokea ndege kubwa zitakazoleta watalii wengi na wafanyabiashara katika mkoa wa Iringa na maeneo mengine ya kusini mwa Tanzania ili rasilimali zilizopo katika maeneo hayo ikiwemo Hifadhi ya Taifa ya Ruaha ziwanufaishe wananchi kama wanavyonufaika wananchi wa Kaskazini mwa Tanzania.
“Ruaha ni hifadhi kubwa, nataka hifadhi hii iwe kitovu cha utalii, nataka nyinyi ndugu zangu wa Iringa mnufaike na utalii katika hifadhi hii kama wanavyonufaika kule kaskazini kupitia Serengeti, watalii wakija hapa wenye hoteli watapata wateja, wenye maziwa watauza, wenye matunda watauza, wenye mahindi watauza, mtapata hela” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli amewataka wananchi wa Iringa kuwapuuza wanaodai Serikali inakopa sana, na kueleza kuwa fedha hizo hukopwa kwa masharti nafuu, riba ndogo na hulipwa kwa muda mrefu, na kwamba ndizo zinatumika kujenga miundombinu ya kuchochea uchumi.
Pamoja na Mke wa Rais Mhe. Mama Janeth Magufuli sherehe hizo pia zimehudhuriwa na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job Yustino Ndugai, Mawaziri, Wabunge kutoka kamati ya bajeti na kamati ya miundombinu, Maaskofu na viongozi wa vyama vya siasa.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Iringa
29 Aprili, 2018
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
“Nimepokea kwa masikitiko taarifa ya kifo cha Mkuu wa Mkoa Mstaafu Ndg. Abbas Kandoro, nawapa pole wana familia, ndugu, jamaa na marafiki wote walioguswa na msiba huu, pamoja na wananchi wa mikoa ya Tabora, Arusha, Dar es Salaam, Mwanza na Mbeya ambako aliwahi kuwa Mkuu wa Mkoa.
Tumempoteza mtu muhimu ambaye mchango wake katika utumishi kwa umma katika nyadhifa mbalimbali zikiwemo Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi wa halmashauri hautasahaulika.
Ndg. Abbas Kandoro alikuwa kiongozi shupavu, aliyejiamini na kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia sheria na taratibu, aliwapenda watu aliowaongoza na alidhirisha uzalendo wa kweli.
Nimesikitishwa sana na kifo chake, nawaombea wafiwa wote wawe na moyo wa subira, uvumilivu na ustahilivu katika kipindi hiki cha majonzi na pia namuombea Marehemu Abbas Kandoro apumzike mahali pema peponi, Amina”
Ni sehemu ya salamu za rambirambi alizozitoa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kufuatia kifo cha Mkuu wa Mkoa Mstaafu Ndg. Abbas Kandoro kilichotokea jana jioni tarehe 27 Aprili, 2018 katika Hospitali ya Taifa Muhimbili Jijini Dar es Salaam.
Mhe. Rais Magufuli amemtaka Mkuu wa Mkoa wa Iringa Bi. Amina Masenza kufikisha salamu hizo kwa familia ya Marehemu, ndugu, jamaa, marafiki na wote walioguswa na msiba huo.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dodoma
28 Aprili, 2018
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 27 Aprili, 2018 amefungua barabara ya lami ya Dodoma – Babati yenye urefu wa kilometa 251 ambayo imekamilisha ujenzi ya lami katika barabara kuu ya kaskazini iitwayo “The Great North Road” ambayo inaanzia Cape Town nchini Afrika Kusini hadi Cairo nchini Misri.
Sherehe za ufunguzi wa barabara hiyo zimefanyika katika eneo la Bicha, wilaya ya Kondoa mkoani Dodoma na kuhudhuriwa na Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) Dkt. Akinumwi Adesina na Balozi wa Japan hapa nchini Mhe. Masaharu Yoshida.
Akitoa taarifa ya mradi huo Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mhandisi Patrick Mfugale amesema kazi za ujenzi ziligawanywa katika sehemu 4 ambazo ni Dodoma–Mayamaya (km 43.65), Mayamaya–Mela (km 99.35), Mela–Bonga (km 88.8), Babati–Bonga (km 16.2) na km3 za kuingia Kondoa Mjini, na kwamba mradi huo umegharimu Shilingi Bilioni 378.4.
Rais wa benki ya AfDB ambayo imetoa mkopo wa Shilingi Bilioni 203.14 kuchangia ujenzi huo Dkt. Adesina ameelezea kufurahishwa kwake na kukamilika kwa barabara hiyo na kubainisha kuwa itasaidia kukuza biashara, utalii, kuunganisha familia na kuimarisha utangamano wa nchi za Afrika.
Dkt. Adesina amempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa juhudi zake za kufuatilia upatikanaji wa fedha za miradi kutoka AfDB tangu akiwa Waziri wa Ujenzi, na amesisitiza kuwa AfDB itaendelea kuunga mkono juhudi zake za kuwaletea maendeleo Watanzania ikiwemo kujenga miundombinu ya Jiji la Dodoma.
Akizungumza kabla ya kufungua barabara hiyo Mhe. Rais Magufuli ameishukuru AfDB na Serikali ya Japan kupitia Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Japan (JICA) kwa ufadhili wake katika ujenzi wa barabara ya Dodoma – Babati pamoja na miradi mingine hapa nchini.
Mhe. Rais Magufuli pia amemshukuru Dkt. Adesina kwa kukubali AfDB kufadhili ujenzi wa miundombinu ya Jiji la Dodoma na kutoa Dola za Marekani Milioni 200 kwa ajili ya ujenzi wa uwanja mkubwa wa ndege wa kimataifa katika eneo la Msalato nje kidogo ya Jiji la Dodoma.
Mhe. Rais Magufuli amewaagiza wataalamu wa Wizara ya Fedha na Mipango pamoja na Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kuharakisha mchakato wa kupata fedha hizo ili ujenzi wa uwanja uanze mara moja.
Mhe. Rais Magufuli ameongeza kuwa kujengwa kwa uwanja huo kutaziwezesha ndege kubwa kutua moja kwa moja katika makao makuu ya nchi Jijini Dodoma, na kwamba pamoja na kununua ndege 6 Serikali imenunua ndege nyingine kubwa ya 7 ili kuimarisha Shirika la Ndege la Taifa (ATCL).
Mhe. Rais Magufuli amewashukuru Watanzania wote kwa kulipa kodi na kuiwezesha Serikali kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo ikiwemo barabara ya Dodoma – Babati, na ametoa wito kwa wananchi kuitunza na vyombo vya ulinzi na usalama kuhakikisha vinachukua hatua dhidi ya waharibifu wa barabara na wanaosababisha ajali kwa kuvunja sheria za usalama barabarani.
Katika hatua nyingine Mhe. Rais Magufuli ameviagiza vyombo vya dola kuwatafuta wote waliohusika na upotevu wa Shilingi Bilioni 2 kati ya Shilingi Bilioni 2.8 zilizotolewa na Serikali tangu miaka ya 80 kutekeleza mradi wa maji wa Ntoboko kwa ajili ya wananchi wa Kondoa lakini mpaka leo mradi huo haujatekelezwa.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli amewataka viongozi wa wilaya ya Kondoa kuacha migogoro baina yao na badala yake washughulikie maendeleo na kero za wananchi na amesisitiza kuwa “Nyie viongozi nimewateua mimi, achane migogoro, mkiendelea nitawatoa”.
Akiwa njiani kurejea Ikulu ya Chamwino Mhe. Rais Magufuli amekutana na wananchi wa Veyula katika Jiji la Dodoma na kuchangia Shilingi Milioni 10 zitakazoungana na Shilingi Milioni 5 zitakazotolewa na Mbunge Dodoma Mjini Mhe. Anthony Mavunde na Shilingi Milioni 1 zitakazotolewa na Mkuu wa Wilaya ya Dodoma kwa ajili ya kujenga vyumba vya madarasa vya shule ya msingi Veyula.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dodoma
27 Aprili, 2018
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ameupandisha hadhi Mji wa Dodoma kutoka Halmashauri ya Manispaa na kuwa Halmashauri ya Jiji, na amemteua aliyekuwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma Bw. Godwin Kunambi kuwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Mhe. Rais Magufuli ametangaza uamuzi huo tarehe 26 Aprili, 2018 wakati akihutubia katika sherehe za kuadhimisha miaka 54 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar zilizofanyika katika uwanja wa Jamhuri Jijini Dodoma.
Pamoja na kuupandisha hadhi Mji wa Dodoma Mhe. Rais Magufuli ameagiza taratibu za kisheria zifanyike kukamilisha mchakato huo, na amesisitiza kuwa azma ya Serikali kuhamia Dodoma inaendelea kutekelezwa na kwamba yeye mwenyewe atahamia Dodoma mwaka huu.
Sherehe hizo zimehudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein, Mke wa Rais Mhe. Mama Janeth Magufuli, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Seif Ali Idd na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa.
Viongozi wengine ni Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job Yustino Ndugai, Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Ibrahim Hamis Juma, Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Mhe. Zubeir Ali Maulid, Jaji Mkuu wa Zanzibar Mhe. Omar Othman Makungu na Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu Mhe. Benjamin William Mkapa.
Katika sherehe hizo zilizohudhuriwa na Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) Dkt. Akinumwi Adesina, Mhe. Rais Magufuli ameishukuru AfDB kwa ufadhili wa miradi ya maendeleo yenye thamani ya Dola za Marekani Bilioni 3.457 sawa na Shilingi Trilioni 7 na Bilioni 778 za Tanzania zikiwemo fedha za miradi 25 zilizotolewa kuanzia mwezi Novemba, 2017 yenye thamani ya Dola za Marekani Bilioni 1.986 sawa na Shilingi Trilioni 4 na Bilioni 467 za Kitanzania.
Mhe. Rais Magufuli amewapongeza Watanzania wote kwa kutimiza miaka 54 ya muungano na amesisitiza kuwa yeye na Rais wa Zanzibar Dkt. Ali Mohamed Shein wapo imara na wataendelea kuwa imara kuulinda na kuudumisha muungano, kuilinda amani na kupigania maendeleo ya Tanzania.
“Taifa letu linakwenda vizuri, uchumi wetu unakua vizuri, mwaka jana umekuwa kwa wastani wa asilimia 7 na mwaka huu tunatarajia utakua kwa wastani wa asilimia 7.1, mfumuko wa bei umeendelea kuwa chini kwa wastani wa asilimia 4” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Kabla ya kuhutubia wananchi Mhe. Rais Magufuli amekagua gwaride rasmi lililoandaliwa na majeshi ya ulinzi na usalama na amewaongoza viongozi mbalimbali na wananchi kushuhudia maonesho ya gwaride, mazoezi ya kujihami, halaiki, muziki wa dansi na ngoma za makabila mbalimbali zilizotumbuiza uwanjani hapo.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli amefanya mazungumzo rasmi na Rais wa AfDB Dkt. Adesina yaliyofanyika katika Ikulu ndogo ya Jijini Dodoma na kuhudhuriwa na Rais wa Zanzibar Mhe. Dkt. Shein.
Baada ya Mazungumzo hayo Dkt. Adesina amempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa kazi kubwa anayoifanya kuimarisha uchumi wa Tanzania na amesema wamejadiliana mambo kadhaa yakiwemo namna benki hiyo ilivyosaidia juhudi za maendeleo za Tanzania tangu mwaka 1971 na inavyoendelea kusaidia katika ufadhili wa miradi mbalimbali ya maendeleo.
Ametaja baadhi ya maeneo ambayo AfDB itatoa ufadhili kuwa ni uzalishaji na usambazaji wa nishati, uboreshaji wa miundombinu ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya Jiji la Dodoma hasa barabara.
“Yote kwa yote nimemhakikishia Mhe. Rais Magufuli kuwa AfDB itamuunga mkono katika mipango yake na maono yake ili tuweze kuisaidia Tanzania kukua zaidi, nimefurahi kuzungumza na Mhe. Rais na naona Tanzania ipo katika njia sahihi” amesema Dkt. Adesina.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dodoma
26 Aprili, 2018
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amewataka Wabunge wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kutilia mkazo ajenda zitakazoimarisha zaidi umoja, upendo, ushirikiano na mshikamano baina ya nchi wanachama ili kufanikisha jukumu muhimu la kupambana na umasikini wa wananchi na kukuza uchumi.
Mhe. Rais Magufuli amesema hayo tarehe 24 Aprili, 2018 wakati akihutubia Bunge la Afrika Mashariki kwa mara ya kwanza tangu aingie madarakani, katika ukumbi wa Pius Msekwa uliopo ndani ya viwanja vya Bunge Mjini Dodoma ambako Bunge hilo linafanyia vikao vyake kwa mara ya kwanza katika mji huo.
Mhe. Rais Magufuli amesema Wabunge hao wanao wajibu wa kushughulikia migogoro ambayo imekuwa ikigharimu maisha ya wananchi, vikwazo vya biashara na uwekezaji, na kutilia mkazo ujenzi wa viwanda vitakavyochakata na kuzalisha bidhaa zitokanazo na rasilimali lukuki zilizopo ndani ya Afrika Mashariki ili manufaa ya rasilimali hizo yawanufaishe wananchi.
Ametaja miongoni mwa mambo yanayopaswa kutiliwa mkazo na nchi zote kuwa ni kuimarisha miundombinu ya usafirishaji na uzalishaji wa umeme wakutosha na wenye gharama nafuu, ambavyo ni muhimu katika ujenzi wa viwanda.
“Tafiti zinaonesha gharama za usafiri kwenye ukanda wetu ni mara 4 hadi 5 ukilinganisha na gharama za Asia Mashariki, Marekani na Ulaya na zinachangia kuongezeka kwa gharama za bidhaa kwa asilimia 40.
“Umeme pia umeonekana kuwa sio mwingi, utafiti uliofanywa na taasisi ya Power Africa mwaka 2015 umeonesha kuwa nchi zote 6 za Jumuiya ya Afrika Mashariki zina takribani megawati 6,500 tu za umeme, hiki ni kiwango kidogo mno kuweza kuhimili mahitaji ya uchumi wa kisasa” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Katika kutekeleza azma hiyo Mhe. Rais Magufuli ametoa wito kwa nchi wanachama kubadilishana uzoefu wa namna ya kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazojitokeza na kutekeleza miradi muhimu ya maendeleo, na pia ameshauri nchi wanachama zisitegemee misaada pekee na badala yake zifikirie kutekeleza miradi kwa fedha zake zenyewe ili kuokoa muda na kupunguza gharama za miradi husika.
Mhe. Rais Magufuli amezungumzia juhudi zinazofanywa na Tanzania katika kufikia dhamira hiyo kuwa ni pamoja na kuanza ujenzi wa reli ya kisasa (Standard Gauge) kuanzia Dar es Salaam hadi Dodoma ambayo itaunganisha hadi nchi za Burundi, Rwanda na Uganda, kujenga meli katika ziwa Victoria, kutekeleza mradi wa uzalishaji wa umeme katika mto Rufiji (Stieglers’ Gorge), kununua ndege 6, kujenga barabara, kupanua bandari ya Dar es Salaam, ujenzi wa bomba la kusafirisha mafuta ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi bandari ya Tanga nchini Tanzania, kuboresha viwanja vya ndege 11 na amepongeza juhudi mbalimbali zinazofanywa na nchi nyingine wanachama wa Afrika Mashariki.
“Nataka kuwahakikishia Waheshimiwa Wabunge wa Afrika Mashariki kuwa Serikali ninayoiongoza itaendelea kushirikiana na Bunge hili katika masuala mbalimbali ya kuiunganisha jumuiya yetu, na ninawaomba nanyi mtekeleze wajibu wenu wa kuwaunganisha na kuwaelimisha wananchi ili waone umuhimu wa jumuiya hii” amebainisha Mhe. Rais Magufuli.
Kwa upande wake Spika wa Bunge la Afrika Mashariki Mhe. Martin Ngoga amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kulihutubia Bunge hilo na amempongeza kwa jitihada zake za kujenga nidhamu ya utumishi wa umma, kuzidisha mapambano dhidi ya rushwa, kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo, kukuza uwekezaji na biashara ikiwemo ujenzi wa viwanda na kuonesha uongozi mahiri, na ametoa wito kwa Watanzania kuunga mkono juhudi hizo.
Pamoja na Wabunge wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, viongozi wengine waliohudhuria wakati Mhe. Rais Magufuli akihutubia bunge hilo ni Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, Naibu wa Pili wa Waziri Mkuu wa Uganda Mhe. Kirunda Kivejinja, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job Yustino Ndugai, Katibu Mkuu Kiongozi Mhe. Balozi John Kijazi, Mawaziri, Mabalozi wanaowakilisha nchi mbalimbali hapa nchini, viongozi wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama na Wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dodoma
24 Aprili, 2018
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 23 Aprili, 2018 amefungua jengo la mfuko wa hifadhi ya jamii wa PSPF, ofisi ya makao makuu ya benki ya NMB Mjini Dodoma na matawi mawili ya benki hiyo.
Jengo la PSPF lenye ghorofa 11 lina ukubwa wa mita za mraba 15,741.60, limejengwa kwa gharama ya Shilingi Bilioni 30.56 na ndani ya jengo hilo ndimo benki ya NMB imefungua ofisi zake za makao makuu, tawi la benki kwa wateja maalum, na tawi la benki kwa wateja binafsi lililopewa jina la Kambarage kwa lengo la kumuenzi Baba wa Taifa Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere.
Mkurugenzi Mkuu wa PSPF Bw. Adam Mayingu amesema jengo hilo ambalo tayari limeshapata wapangaji kwa asilimia 98 wengi wao wakiwa ofisi za umma, linatarajiwa kuzalisha Shilingi Bilioni 4.7 kila mwaka na litarejesha fedha za uwekezaji ndani ya miaka 8 na kwamba katika juhudi hizo hizo za kuunga mkono Serikali kuhamia Dodoma PSPF inatekeleza mradi mwingine wa ujenzi wa nyumba 500 za watumishi kwa ushirikiano na mfuko wa hifadhi ya jamii wa Watumishi Housing.
Mkurugenzi Mtendaji wa benki ya NMB Bi. Ineke Bussemaker amesema benki hiyo yenye matawi 218 ndio benki kubwa inayoendeshwa kwa faida hapa nchini na ikiwa na kiwango kidogo cha mikopo chechefu, imekuwa ikichangia katika bajeti ya nchi kupitia kodi na gawio ambapo kwa miaka mitatu mfurulizo imetoa gawio la Shilingi Bilioni 16.525 kila mwaka na katika sherehe hizo amechangia Shilingi Milioni 50 kwa maendeleo ya Dodoma.
Akizungumza kwa niaba ya Mke wa Baba wa Taifa Mhe. Mama Maria Nyerere, Mtoto wa Baba wa Taifa Bw. Makongoro Nyerere ameishukuru benki ya NMB kwa kutambua mchango wa Baba wa Taifa na kuamua tawi hilo liitwe jina lake la “Kambarage” na pia ametoa wito kwa vijana kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Mhe. Rais Magufuli.
“Mhe. Rais wewe chapa kazi, hawa wanaokushambulia na kukupinga hata wakati wa Baba wa Taifa walikuwepo na wengine walikimbilia nchi nyingine, wewe chapa kazi” amesisitiza Bw. Makongoro Nyerere.
Akihutubia kabla ya kufungua rasmi miradi hiyo, Mhe. Rais Magufuli ameipongeza PSPF kwa kuwekeza katika jengo ambalo tayari limeshapata wapangaji na pia ameipongeza mifuko ya hifadhi ya jamii kwa kuitikia wito wa kuwekeza katika viwanda 16 ambavyo vitazalisha ajira na kuchangia katika uchumi wa nchi.
Mhe. Rais Magufuli pia ameipongeza benki ya NMB kwa kazi nzuri inayofanya na kwa kuwafikishia huduma Watanzania wengi, lakini ametaka katika mwaka huu wa 2017/18 benki hiyo inayomilikiwa na Serikali kwa asilimia 32 iongeze gawio.
“Mwaka 2012/13 Benki ya NMB ilitoa gawio kwa Serikali la Shilingi Bilioni 10.805, mwaka 2013/14 ikatoa Shilingi Bilioni 14.301, mwaka 2014/15 ikatoa Shilingi Biliongi 16.525, mwaka 2015/16 ikatoa gawio hilohilo la Shilingi Bilioni 16.525 na mwaka 2016/17 ikatoa tena gawio hilohilo la Shilingi Bilioni 16.525, yaani miaka mitatu mfurulizo mnatoa gawio lilelile wakati mnatuambia faida ya benki imekua, nataka mnaoiwakilisha Serikali kwenye NMB mkaliangalie hili na gawio la mwaka 2017/18 liongezeke” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli amejibu ombi lililotolewa na Mbunge wa Dodoma Mjini Mhe. Anthony Mavunde la kupunguzwa kwa tozo ya kodi katika mchuzi wa zabibu, na amewataka wadau wanaohusika wakiwemo wabunge kufanyia kazi ombi hilo kwa zao la zabibu na mazao mengine ya kilimo na mifugo hapa nchini ili tozo za kodi zisisababishe bidhaa za wazalishaji wa Tanzania kushindwa kushindana na bidhaa zinazoingizwa nchini kutoka nje ya nchi.
Mhe. Rais Magufuli pia amemshukuru Mtoto wa Baba wa Taifa Bw. Makongoro Nyerere kwa ujumbe wake kwa Watanzania hasa vijana na amemhakikishia kuwa Serikali anayoiongoza ipo imara na itaendelea kuwa imara kusimamia misingi ya kulijenga Taifa.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu.
Dodoma
23 Aprili, 2018
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amemteua Dkt. Edmund Bernard Mndolwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya Posta Tanzania (TPB).
Uteuzi wa Dkt. Mndolwa umeanza tarehe 23 Aprili, 2018.
Dkt. Mndolwa anachukua nafasi ya Prof. Lettice Rutashobya ambaye amemaliza muda wake.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dodoma
23 Aprili, 2018
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amemteua Bw. Msalika Robert Makungu kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Tabora.
Bw. Makungu anachukua nafasi ya Dkt. Thea Ntara ambaye amestaafu.
Uteuzi wa Bw. Makungu unaanzia tarehe 20 Aprili, 2018 na tarehe ya kuapishwa kwake itapangwa baadaye.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
20 Aprili, 2018
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 20 Aprili, 2018 amefanya mazungumzo na Kamishna wa amani na usalama wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika Mhe. Balozi Smail Chergui ambaye amewasilisha ujumbe wa Mwenyekiti wa Kamisheni hiyo Mhe. Moussa Faki Mahamat.
Mhe. Chergui amesema katika mazungumzo yake na Mhe. Rais Magufuli yaliyofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam, wamejadili kuhusu masuala yahusuyo amani na usalama barani Afrika hususani ukanda wa maziwa makuu pamoja na masuala ya wakimbizi.
Mhe. Chergui amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa ushauri wake na mchango wake wa mawazo na uzoefu, wenye lengo la kuimarisha amani na usalama.
Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli amekutana na Msaidizi wa Rais wa Misri na Waziri Mkuu Mstaafu wa Misri Mhe. Ibrahim Roshdy Mahlab ambaye amewasilisha ujumbe kutoka kwa Rais wa Misri Mhe. Abdel Fattah el-Sisi.
Baada ya mazungumzo hayo Mhe. Mahlab amesema katika mazungumzo yake na Mhe. Rais Magufuli wamejadili namna ya kuimarisha zaidi uhusiano na ushirikiano kati ya Tanzania na Misri, hasa ikizingatiwa kuwa zipo fursa nyingi ambazo nchi hizi mbili marafiki zinapaswa kuzifanyia kazi.
Mhe. Mahlab amebainisha kuwa utekelezaji wa makubaliano yaliyowekwa wakati wa ziara ya Rais wa Misri Mhe. Abdel Fattah el-Sisi hapa nchini umeanza ambapo tume ya pamoja ya ushirikiano kati ya nchi hizi imeshakutana nchi Misri na kuainisha maeneo yenye fursa na yanayopaswa kufanyiwa kazi.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
20 Aprili, 2018
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 20 Aprili, 2018 amewaapisha Majaji 10 wa Mahakama Kuu, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Wakili Mkuu wa Serikali, Naibu Wakili Mkuu wa Serikali na Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka aliowateua tarehe 15 Aprili, 2018.
Majaji walioapishwa ni Mhe. Elvin Claud Mgeta, Mhe. Elinaza Benjamin Luvanda, Mhe. Yose Joseph Mlyambina, Mhe. Immaculata Kajetan Banzi, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani, Mhe. Paul Joel Ngwembe, Mhe. Agnes Zephania Mgeyekwa, Mhe. Stephen Murimi Magoiga, Mhe. Thadeo Marco Mwenempazi na Mhe. Butamo Kasuka Philip.
Mhe. Rais Magufuli amemuapisha Dkt. Evaristo Emmanuel Longopa kuwa Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Bw. Edson Athanas Makallo kuwa Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka, Dkt. Julius Clement Mashamba kuwa Wakili Mkuu wa Serikali na Dkt. Ally Saleh Possi kuwa Naibu Wakili Mkuu wa Serikali.
Baada ya kuapishwa kwao, Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kufanya uteuzi wa Majaji hao na kwamba uteuzi huo utasaidia kupunguza mrundikano wa mashauri ya Mahakama Kuu ambapo sasa Jaji mmoja atakuwa akisikiliza wastani wa mashauri 460 kwa mwaka ikilinganishwa na Jaji mmoja kusikiliza mashauri 535 kabla ya uteuzi huo.
Mhe. Prof. Juma amewahusia Majaji wapya umuhimu wa kuzingatia majukumu yao, miiko na kuwa mfano bora wa kusimamia sheria na pia ametoa wito kwa wananchi kuwa makini wanapopata taarifa za mahakama kutoka vyanzo visivyo rasmi kwani kumekuwa na upotoshaji wa makusudi.
“Mhe. Rais Bajeti yetu ya mwaka 2017/18 ilikuwa Shilingi Bilioni 125, bajeti tuliyopangiwa sasa 2018/19 ni Shilingi Bilioni 141, sasa wanaosema bajeti imeshuka, imeshuka kwa namna gani? labda ni kushuka kwa kugeuza. Kwa upande wa bajeti ya maendeleo kwa mwaka 2017/18 ilikuwa Shilingi Bilioni 18, mwaka huu tumepangiwa Shilingi Bilioni 35” amesisitiza Mhe. Prof. Juma.
Akizungumza baada ya salamu za Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Rais Magufuli amewapongeza Majaji na viongozi wote walioapishwa na ametoa wito kwao kutekeleza majukumu yao kwa kumtanguliza Mwenyezi Mungu, kuweka mbele maslahi ya Taifa na kutenda haki hasa kwa Watanzania wanyonge wakiwemo wajane na watu masikini ambao hudhulumiwa katika vyombo vya kutolea haki.
Mhe. Rais Magufuli ameungana na Jaji Mkuu wa Tanzania kuwatahadharisha Watanzania dhidi ya watu wanaotumia mitandao ya kijamii kufanya upotoshaji wa taarifa na kuleta madhara katika jamii na ametaka Majaji na mamlaka nyingine zichukue hatua za kisheria dhidi ya wanaofanya upotoshaji huo.
Mhe. Rais Magufuli ametaja upotoshaji mmojawapo kuwa ni madai kwamba Serikali imeiba Shilingi Trilioni 1.5, na akamuuliza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Prof. Mussa Juma Assad ambaye amejibu sio kweli kwamba fedha hizo zimeibwa.
“Nilikuwa nasoma mahali wanasema Serikali imeiba Shilingi Trilioni 1.5, siku moja nikampigia CAG, kwamba mbona kwenye ripoti yako uliyonisomea Ikulu hukunieleza huu wizi wa Trilioni 1.5? Kwa sababu ungenisomea siku hiyo hiyo ningefukuza watu, kama nimefukuza wakurugenzi watatu siku hiyo hiyo kwa sababu ya hati chafu, hawa wa Trilioni 1.5 uliwaficha wapi? Nimejaribu kupita kwenye ripoti siioni mahali palipoandikwa zimepotea Trilioni 1.5, Prof. Assad akaniambia hakuna kitu kama hicho, nikamuuliza Katibu Mkuu akasema hakuna kitu kama hicho” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Viongozi wote walioapishwa pia wamekula kiapo cha uadilifu kwa viongozi wa umma kilichoongozwa na Kamishna wa Maadili Mhe. Jaji Mstaafu Harold Nsekela, na hafla ya kuapishwa kwao imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi, Makatibu Wakuu, wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama na viongozi wa dini.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
20 Aprili, 201
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amemteua Prof. Idris Suleiman Kikula kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Madini.
Taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi imeeleza kuwa uteuzi wa Prof. Kikula umeanzia tarehe 17 Aprili, 2018.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa Mhe. Rais Magufuli amewateua Makamishna wa Tume ya Madini kama ifuatavyo:
- Bw. Doto James – Katibu Mkuu, Fedha na Mipango.
- Bi. Dorothy Mwanyika – Katibu Mkuu, Ardhi na Maendeleo ya Makazi.
- Dkt. Florens Turuka – Katibu Mkuu, Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).
- Mhandisi Musa Iyombe – Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).
- Bw. Haroun Athuman Kinega – Mtendaji Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji wa Madini (FEMATA).
- Dkt. Evaristo Emmanuel Longopa – Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
- Prof. Abdulkarim Hamis Mruma – Mkurugenzi wa Taasisi ya Jiolojia na Utafutaji Madini Tanzania (GST).
- Dkt. Athanas Simon Macheyeki – Katibu Mtendaji wa Taasisi ya Uhamasishaji, Uwazi na Uwajibikaji katika Rasilimali za Madini, Mafuta na Gesi Asilia (TEITI).
Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli amemteua Balozi Mstaafu Daniel Ole Njoolay kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania (MKURABITA).
Uteuzi wa Balozi Mstaafu Njoolay umeanza tarehe 17 Aprili, 2018.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
18 Aprili, 2018
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amewapongeza madaktari na wauguzi wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) iliyopo Jijini Dar es Salaam kwa mafanikio makubwa iliyoyapata katika utoaji wa huduma za matibabu ya moyo.
Mhe. Rais Magufuli aliyeongozana na Mkewe Mhe. Mama Janeth Magufuli ametoa pongezi hizo hizo tarehe 18 Aprili, 2018 alipotembelea taasisi hiyo na kuwajulia hali wagonjwa wanaopatiwa matibabu akiwemo Waziri Mstaafu Dkt. Juma Ngasongwa.
Mhe. Rais Magufuli amesema JKCI ambayo imepata mafanikio katika matibabu ya moyo kwa njia ya upasuaji wa tundu dogo na kufungua kifua imesaidia kuokoa vifo kwa Watanzania wengi waliokuwa wanakosa uwezo wa kifedha wa kwenda kutibiwa nje ya nchi, imepunguza gharama za kutibiwa nje ya nchi na imeijengea heshima Tanzania.
“Prof. Janabi, madaktari wote na wauguzi wa taasisi hii nawapongeza sana kwa kazi nzuri mnayoifanya, natambua kuwa wapo baadhi ya waliokuwa wananufaika na wagonjwa kupelekwa nje ya nchi hawatafurahia kazi mnayoifanya lakini nyinyi chapeni kazi na Serikali ipo na nyinyi” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI Prof. Mohamed Janabi amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kuitembelea taasisi hiyo na kuwatia moyo na ameahidi kuwa wataendelea kuchapa kazi kwa juhudi ili kuimarisha zaidi huduma za matibabu ya moyo.
Amefafanua kuwa JKCI imefanikiwa kupunguza idadi ya wagonjwa waliokuwa wanakwenda kutibiwa nje ya nchi kwa asilimia 83 na kwamba tangu mwaka 2015 idadi ya wagonjwa waliotibiwa katika taasisi hiyo ni zaidi ya 2,420 ambao wangehitaji wastani wa Shilingi Milioni 30 kwa kila mmoja kutibiwa nje ya nchi.
Kabla ya kutembelea JKCI Mhe. Rais Magufuli na Mkewe Mhe. Mama Janeth Magufuli wamekwenda Kariakoo Jijini hapa kutoa pole kwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha Bw. Mrisho Gambo ambaye amefiwa na Mama yake Bi Rehema Paulo Mombuli, ambaye mwili wake unasafirishwa kwenda Arusha na baadaye Moshi mkoani Kilimanjaro kwa mazishi.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
18 Aprili, 2018
Taarifa kwa vyombo vya habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 15 Aprili, 2018 amefanya uteuzi wa Majaji 10 wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali (Deputy Attorney General - DAG), Naibu Mkurugenzi wa Mashitaka (Deputy Director of Public Prosecutions – (DDPP), Wakili Mkuu wa Serikali (Solicitor General), na Naibu Wakili Mkuu wa Serikali (Deputy Solicitor General).
Walioteuliwa ni;
- Bw. Elvin Claud Mugeta
- Bw. Elinaza Benjamin Luvanda
- Bw. Yose Joseph Mlyambina.
- Bi. Immaculata Kajetan Banzi
- Bw. Mustafa Siyani
- Bw. Paul Joel Ngwembe
- Bi. Agnes Zephania Mgeyekwa
- Bw. Stephen Murimi Magoiga
- Bw. Thadeo Mwenempazi
10. Bi. Butamo Kasuka Philip
Kabla ya uteuzi huu, Bi. Butamo Kasuka Philip alikuwa Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Makamu wa Rais.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli amemteua Dkt. Evaristo Emmanuel Longopa kuwa Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali (DAG).
Dkt. Longopa anachukua nafasi ya Bw. Paul Joel Ngwembe ambaye ameteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama Kuu Tanzania.
Mhe. Rais Magufuli amemteua Bw. Edson Athanas Makallo kuwa Naibu Mkurugenzi wa Mashitaka (Deputy Director of Public Prosecutions).
Mhe. Rais Magufuli amemteua Dkt. Julius Clement Mashamba kuwa Wakili Mkuu wa Serikali (Solicitor General).
Mhe. Rais Magufuli amemteua Dkt. Ally Possi kuwa Naibu Wakili Mkuu wa Serikali (Deputy Solicitor General).
Mhe. Rais Magufuli amefafanua kuwa amefanya uteuzi wa Majaji wa Mahakama Kuu kwa lengo kujaza nafasi za Majaji waliostaafu na amefanya uteuzi wa Wakili Mkuu wa Serikali na Naibu Wakili Mkuu wa Serikali kwa lengo la kuhakikisha ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mkurugenzi wa Mashitaka na Wakili Mkuu wa Serikali zinafanya kazi vizuri zaidi katika kushughulikia masuala ya mahakama.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
15 Aprili, 2018
Taarifa kwa vyombo vya habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 12 Aprili, 2018 amewapandisha vyeo maafisa wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) katika vyeo mbalimbali.
Taarifa iliyosomwa na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania Jenerali Venance Salvatory Mabeyo, Ikulu Jijini Dar es Salaam imeeleza kuwa Mhe. Rais Magufuli amempandisha cheo Meja Jenarali Peter Paul Massao kuwa Luteni Jenerali.
Meja Jenerali Massao ni Mkuu wa Chuo cha Mafunzo ya Maafisa Wanafunzi wa Jeshi Monduli (TMA) na kwa uteuzi huo, sasa JWTZ itakuwa na Luteni Jenerali wawili.
Mhe. Rais Magufuli amempandisha cheo Brigedia Jenerali Henry Kamunde kuwa Meja Jenerali.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli amewapandisha vyeo maafisa 27 wa JWTZ kutoka cheo cha Kanali na kuwa Brigedia Jenerali na Afisa 1 kutoka Luteni Kanali na kuwa Kanali.
Waliopandishwa vyeo hivyo ni D.D.M Mullugu, J.J Mwaseba, A.S Mwamy, R.K Kapinda, C.D Katenga, Z.S Kiwenge, M.A Mgambo, A.M Alphonce, A.P Mutta, A.V Chakila, M.G Mhagama, V.M Kisiri, C.E Msolla na S.M Mzee.
Wengine ni C.J Ndiege, I.M Mhona, R.C Ng’umbi, S.J Mnkande, A.C Sibuti, M.M Mumanga, I.S Ismail, M.N Mkeremy, G.S Mhidze, M.A Machanga, S.B Gwaya, P.K Simuli na M.E Gaguti.
Halikadhalika Mhe. Rais Magufuli amempandisha cheo Luteni Kanali Bernard Masala Mlunga kuwa Kanali na ameteuliwa kuwa Mpambe wa Rais (Aide de Camp – ADC)
Kanali Mlunga ameteuliwa kuwa Mpambe wa Rais akichukua nafasi ya Kanali Mbaraka Naziad Mkeremy ambaye amepandishwa cheo kuwa Brigedia Jenerali.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
12 Aprili, 2018
Taarifa kwa vyombo vya habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 11 Aprili, 2018 amezindua Taasisi ya Jakaya Mrisho Kikwete na kuahidi kuwa Serikali itatoa ushirikiano kwa taasisi hiyo ili kufanikisha malengo iliyojiwekea.
Katika hotuba yake wakati wa halfa ya uzinduzi iliyofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam Mhe. Rais Magufuli amempongeza Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete ambaye ni Mwenyekiti wa Taasisi hiyo kwa uamuzi wake wa kuanzisha taasisi itakayosaidiana na Serikali ya Tanzania na nchi zingine za Afrika katika kupambana na umasikini na kuboresha maisha ya watu.
Mhe. Rais Magufuli ametoa wito kwa wadau mbalimbali wa maendeleo zikiwemo nchi mbalimbali na mashirika ya kimataifa kutoa ushirikiano na kuchangia juhudi zinazofanywa na Taasisi ya Jakaya Mrisho Kikwete kwa kuwa anaamini kuwa michango hiyo itatumika kutekeleza malengo yaliyokusudiwa.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli amebainisha kuwa Serikali ya Awamu ya Tano itashirikiana na taasisi zote za kiraia zinazofanya kazi kwa lengo la kuwaletea maendeleo wananchi, na ameonya kuwa Serikali haitashirikiana wala kuzifumbia macho taasisi za kiraia zenye malengo ya kuvuruga amani na kuharibu maadili ya Watanzania.
Mhe. Rais Magufuli amemsifu Mhe. Dkt. Kikwete kwa kazi aliyoifanya akiwa Rais, ya kusimamia vizuri mageuzi ya kiuchumi, ujenzi wa miundombinu, uboreshaji wa huduma mbalimbali za kijamii hususani afya, elimu na maji, ukuzaji wa demokrasia na kuitangaza vyema Tanzania kimataifa, na ameahidi kuwa Serikali ya Awamu ya Tano itaendeleza juhudi hizo.
“Watanzania tutaendelea kukukumbuka kwa kusimamia ujenzi wa shule za kata, Chuo Kikuu cha Dodoma, Hospitali ya Mloganzila, ujenzi wa miundombinu ikiwemo barabara, bomba la gesi nakadhalika, kwa hakika umetufanyia mengi sana, tunakushukuru sana na nina hakika mchango wako utaendelea kukumbukwa vizazi na vizazi” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Kwa upande wake Mhe. Dkt. Kikwete amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kuzindua taasisi hiyo na amemhakikishia kuwa kama ilivyo katika malengo yake itahakikisha inajikita kusaidia juhudi za Serikali katika sekta ya afya hususani afya ya mama na mtoto, kuwaendeleza na kuwalea vijana kuwa raia wema na wazalendo kwa Taifa, kuboresha kilimo chenye tija, kuendeleza utawala bora na kudumisha amani.
Mhe. Dkt. Kikwete amesema taasisi hiyo itafanya kazi kwa ukaribu na Serikali na kwa kushirikiana na wadau wengine na kamwe haitajihusisha na shughuli za kupingana na Serikali wala kushindana na taasisi nyingine zinazofanya shughuli zao hapa nchini.
Hafla ya uzinduzi wa Taasisi ya Jakaya Mrisho Kikwete imehudhuriwa na Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili Mhe. Alhaji Ali Hassan Mwinyi, Mawaziri, Mabalozi wanaoziwakilisha nchi mbalimbali hapa nchini na viongozi wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
11 Aprili, 2018
Taarifa kwa vyombo vya habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amemteua Prof. Isaya Jayambo Jairo kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu (NBAA).
Taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi imeeleza kuwa uteuzi wa Prof. Jairo unaanza tarehe 11 Aprili, 2018.
Prof. Jairo ni Mkuu wa Chuo cha Kodi (ITA) na ameteuliwa kushika wadhifa huo kwa kipindi cha pili baada ya kipindi chake cha kwanza kumalizika.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
11 Aprili, 2018
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 08 Aprili, 2018 ameshiriki Ibada ya kumsimika Mhashamu Askofu Isaac Amani kuwa Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Arusha, iliyofanyika katika viwanja vya Kanisa la Mtakatifu Teresia wa Mtoto Yesu Jijini Arusha.
Mhashamu Askofu Isaac Amani aliyekuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Moshi aliteuliwa na Baba Mtakatifu Francis tarehe 27 Desemba, 2017 kuwa Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Arusha na amesimikwa na Askofu Mkuu Mstaafu wa Jimbo Kuu Katoliki la Arusha Mhashamu Josephat Louis Lebulu na Balozi wa Baba Mtakatifu hapa nchini Askofu Mkuu Marek Solczynski.
Ibada ya kusimikwa kwa Askofu Mkuu Isaac Amani imehudhuriwa na Maaskofu 33 wa Kanisa Katoliki, Mke wa Rais Mhe. Mama Janeth Magufuli, Waziri Mkuu Mstaafu Mhe. Mizengo Pinda, Spika Mstaafu Mhe. Anne Makinda, viongozi wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama, Wabunge, Viongozi wa Mkoa wa Arusha wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa Bw. Mrisho Gambo na wananchi wa Arusha.
Akizungumza baada ya Ibada hiyo Mhe. Rais Magufuli amemshukuru Askofu Mkuu Mstaafu Lebulu kwa utumishi wake na ushirikiano ulioutoa kwa Serikali katika kipindi chote cha miaka 20 aliyokuwa Askofu Mkuu na amempongeza Askofu Mkuu Isaac Amani kwa kusimikwa kuliongoza Jimbo Kuu Katoliki la Arusha.
Mhe. Rais Magufuli amemuahidi Askofu Mkuu Isaac Amani, Maaskofu wote na viongozi wote wa madhehebu ya dini hapa nchini kuwa Serikali ya Awamu ya Tano itaendelea kushirikiana na viongozi hao katika masuala mbalimbali.
Kwa kunukuu vifungu mbalimbali vya Biblia, Mhe. Rais Magufuli amesisitiza umuhimu wa Watanzania wote wakiwemo viongozi wa dini, Serikali na wanasiasa kudumisha amani, na kwamba Serikali anayoiongoza itakuwa tayari wakati wote kutoa ushirikiano katika kuhakikisha amani inakuwepo.
Katika risala iliyosomwa na Padre Alois Kitomari kwa niaba ya familia ya Mungu Jimbo Kuu Katoliki la Arusha, imempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa juhudi zake za kusimamia vizuri nidhamu ya utumishi wa umma na utendaji wa taasisi za umma, kukabiliana na ufisadi, uzembe na ubadhilifu wa mali za umma, vita dhidi ya rushwa, ujenzi wa viwanda, bandari na madini na uboreshaji wa sekta ya usafiri kwa kujenga reli ya kisasa, ununuzi wa ndege na ujenzi wa barabara.
Mhe. Rais Magufuli amechangia mifuko 300 ya saruji kwa ajili ya ujenzi Kanisa Kuu jipya la Mtakatifu Teresia wa Mtoto Yesu ambalo ujenzi wake unaendelea.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Arusha
08 Aprili, 2018
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 07 Aprili, 2018 ameungana na Watanzania wote kuadhimisha siku ya mmoja wa waasisi wa Taifa Hayati Sheikh Abeid Amani Karume, Rais wa Kwanza wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Kwanza wa Baraza la Mapinduzi kwa kuzindua kituo cha polisi, kufungua nyumba 31 za askari polisi na kushuhudia maonesho ya Polisi katika uwanja wa Kumbukumbu ya Sheikh Amri Abeid Jijini la Arusha.
Kituo cha polisi cha watalii na wanadiplomasia kilichopo Naura, kituo cha polisi cha Muriet, na nyumba za 18 kati ya 31 za makazi ya polisi vimejengwa kwa mchango wa wafanyabiashara wa Mkoa wa Arusha na Benki ya CRDB kwa gharama ya Shilingi Milioni 753, wakati nyumba za polisi 13 zimejengwa na Serikali kwa gharama ya Shilingi Milioni 250.
Mhe. Rais Magufuli aliagiza kujengwa kwa nyumba hizo baada ya kutokea ajali ya moto iliyosababisha nyumba 13 za makazi ya askari polisi na mali zao kuungua moto tarehe 27 Septemba, 2017.
Katika kutekeleza agiza hilo Mkuu wa Mkoa wa Arusha Bw. Mrisho Gambo akaamua kuwashirikisha wafanyabiashara na benki ya CRDB kuchangia ujenzi huo na kufanikiwa kujenga nyumba nyingine 18 na vituo hivyo viwili vya polisi.
Pamoja na kuzindua miradi hiyo Mhe. Rais Magufuli ameshuhudia maonesho ya Jeshi la Polisi ya kuzuia na kupambana na uhalifu yakiwemo kukabiliana na waandamanaji haramu, wezi, waporaji watumiao silaha na magaidi, yaliyofanyika katika uwanja wa Kumbukumbu ya Sheikh Amri Abeid.
Akizungumza baada ya maonesho hayo Mhe. Rais Magufuli amesema Taifa litaendelea kumkumbuka Hayati Sheikh Abeid Amani Karume kwa juhudi zake za kujenga nchi ikiwemo kuwajengea makazi wananchi masikini kule Zanzibar na ametoa wito kwa Watanzania kumuenzi kwa kudumisha amani na kuchapa kazi.
Pamoja na kumpongeza Mkuu wa Mkoa wa Arusha Bw. Mrisho Gambo kwa jitihada zake za kuwaunganisha wadau na kisha kufanikiwa kujenga nyumba za askari na vituo vya polisi Mhe. Rais Magufuli ametoa Shilingi Bilioni 10 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za askari polisi wa vyeo vya chini nchini, na amewaagiza viongozi wa mikoa yote kuwashirikisha wadau katika ujenzi huo kama ilivyofanyika mkoani Arusha ili kukabiliana na tatizo la askari kukosa nyumba za makazi.
“Askari polisi mnafanya kazi kubwa sana ya kulinda raia na mali zao, natambua juhudi kubwa mnazofanya na napenda kuwashukuru sana, naomba Watanzania wote tuendelee kuliunga mkono Jeshi la Polisi.
“Wakati naingia madarakani kulikuwa na mauaji kila wakati, kule Kibiti pekee yake waliuawa watu 59 wakiwemo askari polisi 17 na raia 42, Jeshi la Polisi limefanya kazi kubwa na sasa mauaji yale yamedhibitiwa, ni lazima tulipongeze jeshi letu” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli amekubali maombi ya Mkuu wa Jeshi la Polisi IGP Simon Sirro la kuongezewa idadi ya askari na kupandishwa vyeo kwa maafisa wa polisi ambapo ameruhusu Jeshi la Polisi kuajiri askari wapya 1,500 kutoka Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na kumpelekea mapendekezo ya maafisa wanaostahili kupandishwa vyeo.
Mhe. Rais Magufuli amempongeza IGP Sirro kwa hatua ya kuwafukuza kazi askari polisi 458 waliokutwa na makosa ya kinidhamu na uadilifu kuanzia mwaka 2015 hadi sasa, na ametaka hatua hizo ziendelee kuchukuliwa dhidi ya askari wengine wanaokiuka maadili na taratibu za kazi ili kuondoa malalamiko kutoka kwa wananchi yakiwemo upokeaji rushwa na unyanyasaji raia kwa kuwabambikiza kesi.
Halikadhalika Mhe. Rais Magufuli amepiga marufuku askari, maafisa wa polisi na viongozi wengine wa Serikali kushiriki ufyekaji wa mashamba ya bangi na badala yake ametaka mashamba hayo yanapobainika yafyekwe na wanavijiji wenyewe waliohusika kuyalima.
Maadhimisho hayo yamehudhuriwa na Mke wa Rais Mhe. Mama Janeth Magufuli na viongozi mbalimbali wakiwemo Mawaziri, Naibu Mawaziri, viongozi wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama, wabunge na wananchi.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Arusha
07 Aprili, 2018
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 06 Aprili, 2018 amezindua ukuta unaozunguka migodi ya madini ya Tanzanite katika wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara uliojengwa na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kwa lengo la kudhibiti utoroshaji wa madini na ukwepaji wa kodi.
Ukuta huo wenye urefu wa kilometa 24.5 umejengwa kwa gharama ya Shilingi Bilioni 5 na Milioni 646 ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo yaliyotolewa na Mhe. Rais Magufuli tarehe 20 Septemba, 2017 alipokuwa akizindua barabara ya KIA – Mirerani.
Mhe. Rais Magufuli ameipongeza JWTZ kwa kukamilisha kazi hiyo kwa haraka na kwa gharama nafuu na amewapongeza maafisa, askari na vijana 2,356 wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) walioshiriki katika ujenzi kwa uzalendo wao na kujituma ili kulinda rasilimali hiyo muhimu kwa Taifa.
Mhe. Rais Magufuli amelikubali ombi la Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania Jenerali Venance Salvatory Mabeyo na ameagiza vijana wa JKT walioshiriki katika ujenzi wa ukuta huo waajiriwe katika vyombo vya ulinzi na usalama vikiwemo Polisi na JWTZ ilimradi wawe na sifa zinazostahili.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli amewahakikishia wananchi wa Mirerani kuwa watanufaika zaidi na hatua ambazo zinachukuliwa kudhibiti utoroshaji na ukwepaji wa kodi za madini ya Tanzanite na amekabidhi gari jipya la wagonjwa aina ya Toyota Land Cruiser “Hard Top” alilowaahidi wakati akiagiza kujengwa kwa ukuta huo.
“Wananchi wa Mirerani msiwe na wasiwasi, hasa nyinyi wachimbaji, mtaingia mikataba na Serikali na mtafanya kazi zenu vizuri kabisa, tumeamua kuchukua hatua hizi kwa sababu tunataka mali iliyokuwa inapotea hapa isipotee tena.
“Asilimia 40 ya Tanzanite iliyokuwa ikizalishwa hapa ilikuwa inapotea, madini yetu yalikuwa yanatoa ajira kwa watu wengine wa nchi nyingine, wakati nyinyi wananchi wa Mirerani hamna maji wala gari ya wagonjwa, sasa mimi nimewaletea gari la wagonjwa” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli na kuagiza JWTZ iendelee kufanya ulinzi katika eneo hilo.
Halikadhalika Mhe. Rais Magufuli amemshukuru Mzee Jumanne Ngoma aliyevumbua madini ya Tanzanite mwaka 1967 na kutambuliwa na Baba wa Taifa Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere mwaka 1980, na amempa Shilingi Milioni 100 kwa kutambua mchango mkubwa alioutoa kwa Taifa kuvumbua madini hayo, yanayopatikana Tanzania pekee.
Amebainisha kuwa utafiti uliofanywa katika kitalu C umebaini kuwa kuna mashapo ya Tanzanite yatakayochimbwa hadi mwaka 2042 na kwamba lipo eneo jingine lenye Tanzanite nyingi zaidi na ambalo Serikali italizungushia ukuta ili kulinda na kudhibiti utoroshaji madini na ukwepaji wa kodi.
Mhe. Rais Magufuli amewataka Watanzania kuunga mkono juhudi za Serikali kuinua uchumi, kutekeleza miradi ya maendeleo na kudhibiti rasilimali za nchi, na amewasihi kujiepusha na watu wanaoshabikia mabaya kwa nchi wakiwemo wanaowaunga mkono wanyonyaji na uvunjifu wa amani.
Kwa upande wake Mzee Jumanne Ngoma amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kutambua mchango wake wa kuvumbua madini ya Tanzanite na amesema anaamini sasa madini hayo yatapata thamani inayostahili.
Nae Waziri wa Madini Mhe. Angellah Kairuki amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa maelekezo yake ya kujengwa kwa ukuta na kulisimamia vizuri soko la Tanzanite ambapo malipo ya mrabaha kutoka kwa wachimbaji ukiondoa Tanzanite One na STAMICO kwa miezi mitatu tu ya kuanzia Januari hadi Machi mwaka huu yamefikia Shilingi Milioni 714 na hivyo kuzidi malipo ya mwaka mzima wa 2015 (Shilingi Milioni 166.8), 2016 (Shilingi Milioni 71.8) na 2017 (Shilingi Milioni 147.1).
Katika sherehe za uzinduzi wa ukuta huo Mhe. Rais Magufuli amekabidhi tuzo na vyetu kwa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jen. Mabeyo, maafisa na askari wa JWTZ na vijana wa JKT walioshiriki ujenzi huo.
Sherehe hizo zimehudhuriwa na Mke wa Rais Mhe. Mama Janeth Magufuli, Waziri wa Ulinzi na JKT Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Palamagamba Kabudi, Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Hamis Kigwangallah, viongozi wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama, wakuu wa mikoa ya Manyara, Arusha, Dodoma, Tanga, Singida na Kilimanjaro, wajumbe wa kamati ya kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii na kamati ya kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Arusha
06 Aprili, 2018
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
“Nimepokea kwa mshtuko na masikitiko makubwa taarifa ya vifo vya watu 12 waliopoteza maisha katika ajali ya barabarani iliyotokea jana usiku katika wilaya ya Igunga mkoani Tabora, nawapa pole wafiwa wote, ndugu, jamaa na marafiki walioguswa na msiba huu mkubwa.
“Aidha, nalitaka Jeshi la Polisi, Kamati za Ulinzi na Usalama za Mikoa na Wilaya na Mamlaka zote zinazohusika na usalama wa barabarani kujitathmini, na kutafuta majawabu ya kwa nini ajali za barabarani zinaendelea kutokea kwa kusababishwa na uzembe na uvunjaji wa sheria za barabarani?”
Ni sehemu ya salamu za rambirambi na maelekezo aliyoyatoa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 05 Aprili, 2018 kufuatia ajali iliyotokea katika Kijiji cha Makomero, Wilaya ya Igunga Mkoani Tabora jana tarehe 04 Aprili, 2018 saa 2:00 usiku na kusababisha vifo vya watu 12.
Ajali hiyo imetokea baada ya basi la kampuni ya City Boy lililokuwa limebeba abiria kutoka Karagwe Mkoani Kagera kuelekea Dar es Salaam kugongana uso kwa uso na lori aina ya Fuso lililokuwa linatoka Singida kuelekea Igunga.
Pamoja na kutoa pole kwa wafiwa na kutoa maelekezo hayo, Mhe. Rais Magufuli amewataka viongozi wote wanaohusika na usimamizi wa usalama wa barabarani kutafakari kwa nini ajali nyingi zimekuwa zikitokea katika maeneo yaleyale na kutafuta ufumbuzi ili kuepusha madhara ya watu kupoteza maisha, kupata ulemavu wa kudumu na kupoteza mali.
Aidha Mhe. Rais Magufuli amemtaka Mkuu wa Mkoa wa Tabora Bw. Aggrey Mwanri kufikisha salamu zake za pole kwa wafiwa wote, na amewaombea Marehemu wote wapumzishwe mahali pema peponi na majeruhi wote 46 wapone haraka ili waungane na familia zao katika ujenzi wa Taifa.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
05 Aprili, 2018
Taarifa kwa vyombo vya habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amemteua Dkt. Fidelice Mbaruku Simbagungile Mafumiko kuwa Mkemia Mkuu wa Serikali.
Uteuzi wa Dkt. Mafumiko umeanza tarehe 03 Aprili, 2018.
Kabla ya uteuzi huu Dkt. Mafumiko alikuwa Mkurugenzi wa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW)
Dkt. Mafumiko anachukua nafasi ya Prof. Samuel Manyele ambaye amemaliza muda wake.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
03 Aprili, 2018
Taarifa kwa vyombo vya habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 03 Aprili, 2018 amezindua mradi wa kuzalisha megawati 240 za umeme kwa kutumia gesi asilia (Kinyerezi II) uliopo Kinyerezi Jijini Dar es Salaam.
Kabla ya kuzindua mradi huo Mhe. Rais Magufuli amekagua mitambo 6 ya kisasa inayotumia teknolojia mpya na ya kwanza kufungwa Afrika Mashariki iitwayo “Combined Cycle” ambayo inatumia hatua mbili za kuzalisha umeme kwa kutumia gesi na mvuke.
Teknolojia hii itaiwezesha mitambo ya Kinyerezi II kuzalisha megawati 167.82 kwa kutumia gesi asilia na megawati 80.4 kwa kutumia mvuke na mpaka sasa tayari megawati 160 zimeshaanza kuzalishwa na kuingizwa kwenye gridi ya Taifa, megawati 40.2 zitaingizwa kwenye gridi ya Taifa ifikapo mwezi Mei na megawati 48 zitaingizwa kwenye gridi ya Taifa ifikapo mwezi Juni mwaka huu.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Dkt. Tito Mwinuka amesema mradi huu umegharimu Shilingi Bilioni 798, fedha zote zikiwa zimetolewa na Serikali ya Tanzania ambapo kati ya fedha hizo asilimia 15 zimetolewa fedha taslimu na asilimia 85 zimekopwa kutoka benki za Japan.
Waziri wa Nishati Dkt. Medard Matogolo Kalemani amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa jitihada zake za kuimarisha upatikanaji wa umeme hapa nchini ikiwemo kuhakikisha mradi wa uzalishaji wa umeme wa Kinyerezi II unakamilika, upanuzi wa Kinyerezi I kwa kuongeza uzalishaji umeme kutoka megawati 150 hadi kufikia megawati 335 na kutekeleza mradi wa uzalishaji wa umeme megawati 2,100 katika maporomoko ya mto Rufiji (Stieglers Gorge) ambayo ikikamilika itaiwezesha nchi kuwa na uwezo wa kuzalisha jumla ya megawati 5,000 za umeme.
Dkt. Kalemani amebainisha kuwa pamoja na kutekeleza miradi hiyo Serikali ya Awamu ya Tano imetekeleza miradi ya usafirishaji na usambazaji wa umeme mkubwa ya Iringa – Dodoma – Singida – Shinyanga (kilovoti 400, kilometa 679), Singida – Arusha – Namanga (kilovoti 400, kilometa 414), Makambako – Songea (kilovoti 220, kilometa 300) na mradi wa umeme vijijini (REA) umevifikia vijiji vipya 4,916 na wateja wapya 874,984.
Katika hotuba yake Mhe. Rais Magufuli ameipongeza TANESCO kwa kazi nzuri inayoifanya na amempongeza mkandarasi kampuni ya Sumitomo Corporation kwa kukamilisha mradi wa Kinyerezi II siku 45 kabla ya muda uliopangwa na kuwaajiri Watanzania kwa asilimia 80 ya wafanyakazi wote 2,000 waliopata ajira katika mradi huo.
Mhe. Rais Magufuli ameitaka Wizara ya Nishati kuongeza juhudi za kusambaza umeme kwa wananchi ili kuepuka madhara yakiwemo uharibifu wa misitu unaosababisha hekta 400,000 kufyekwa kila mwaka kwa ajili ya kuni na mkaa.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli amewaagiza viongozi wa wizara, idara na taasisi za Serikali kuwasiliana pale kunapokuwa na changamoto zinazokwamisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo ikiwemo vifaa kukwama bandarini kutokana na kudaiwa kodi ili kuepusha ucheleweshaji na ongezeko kubwa la gharama za miradi hiyo.
Mhe. Rais Magufuli amewaondoa shaka wananchi wa Dar es Salaam kuwa japo Serikali inahamia Dodoma Jiji la Dar es Salaam litaendelea kuboreshwa na ameitaja baadhi ya miradi kuwa ni ujenzi wa barabara za juu (Flyover), ujenzi wa uwanja wa ndege (Terminal 3), reli ya kisasa (Standard Gauge), bandari, barabara na mradi wa kujenga vizuri eneo la bonde la Msimbazi.
“Hatutalitelekeza Jiji la Dar es Salaam, ninachowaomba endeleeni kuungana na Serikali katika juhudi hizi za maendeleo na msikubali watu wawashawishi kuvuruga amani kwa kuwa nchi hii ni yetu sote” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
03 Aprili, 2018
Taarifa kwa vyombo vya habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 02 Aprili, 2018 ameongoza mapokezi ya ndege mpya aina ya Bombardier Dash-8 Q400 iliyonunuliwa na Serikali ya Tanzania kwa ajili ya Shirika la Ndege la Taifa (ATCL) ambayo imewasili hapa nchini ikitokea nchini Canada ilikotengenezwa.
Mapokezi ya ndege hiyo yenye uwezo wa kubeba abiria 76 yamefanyika katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Mawaziri, Wabunge, viongozi wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama, viongozi wa dini, wakuu wa mikoa ya Dar es Salaam, Kilimanjaro na Mwanza na wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam.
Akiwa uwanjani hapo Mhe. Rais Magufuli pamoja na viongozi na wananchi waliohudhuria mapokezi hayo wameshuhudia ndege hiyo ikipokea heshima ya kumwagiwa maji (Water Salute) na baadaye kuikagua.
Katika hotuba yake Mhe. Rais Magufuli amewapongeza Watanzania kwa mafanikio haya makubwa ya kununua ndege kwa ajili ya kuliimarisha Shirika la Ndege la Taifa na kukuza utalii, na amewataka kuendelea kushikamana na kushirikiana na Serikali katika juhudi za mbalimbali za maendeleo.
Kabla ya hotuba hiyo viongozi wa dini wameiombea dua Tanzania na viongozi wake, na wamemtaka Mhe. Rais Magufuli kuendelea kufanya kazi zenye manufaa kwa Watanzania bila kujali wanaobeza juhudi hizo.
Hii ni ndege ya 3 kuwasili nchini kati ya ndege 6 zilizonunuliwa na Serikali, ndege nyingine kubwa 2 aina ya Bombardier CS300 yenye uwezo wa kubeba abiria 132 kila moja, na 1 aina ya Boeing 787-8 Dreamliner yenye uwezo wa kubeba abiria 264 zitawasili baadaye mwaka huu.
Mapema kabla ya mapokezi ya ndege hiyo Mhe. Rais Magufuli amezindua mradi wa kusimika mfumo wa rada 4 za kuongozea ndege za kiraia kwenye viwanja vya ndege vya Julius Nyerere, Kilimanjaro, Mwanza na Songwe, sherehe ambazo zimefanyika katika uwanja wa ndege kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam.
Akitoa maelezo ya mradi huo Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCAA) Bw. Hamza Johari amesema mradi huo ambao umeanza kutekelezwa tarehe 22 Agosti, 2017 utakamilika mwezi Mei 2019 kwa gharama Shilingi Bilioni 67.3 fedha zote zikiwa zimetolewa na Serikali ya Tanzania, na kwamba tayari utengenezaji wa rada ya kwanza ya uwanja wa Julius Nyerere umekamilika.
Amebainisha baadhi ya faida za mradi huo kuwa ni kuwezesha anga la Tanzania kuonekana kwa asilimia 100, utaiwezesha TCAA kutoa huduma kwa haraka na kuongeza mapato yatokanayo na tozo kwa ndege zinazopita katika anga la Tanzania, kuimarisha usalama na kuongeza uwezo wa TCAA kuongoza ndege nyingi na kwa haraka.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa Mnyaa amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa dhamira yake ya kuimarisha usafiri wa anga ikiwemo kutoa fedha kwa ajili ya kutekeleza mradi wa usimikaji wa rada 4, kujenga na kuboresha viwanja vya ndege nchini na kununua ndege mpya 6 kwa ajili ya kuimarisha usafiri wa anga.
Akizungumza kabla ya kuzindua mradi huo Mhe. Rais Magufuli ameipongeza TCAA kwa kuchangia asilimia 45 ya gharama za mradi huo kutokana na mapato yake na amemtaka mkandarasi anayejenga mradi huo kuukamilisha haraka ili kuondokana na hali ya sasa ambapo rada iliyopo ina uwezo wa kufanya kazi kwa asilimia 25 tu ya nchi nzima.
Mhe. Rais Magufuli amesema Watanzania wana kila sababu ya kutembea kifua mbele kwa kuwa nchi inakwenda vizuri na amewataka kuendelea kulipa kodi.
“Napenda kuwahakikishia kuwa tunakwenda vizuri, hivi sasa nchi yetu ni kati ya nchi 5 zenye uchumi unaokua kwa kasi Barani Afrika, tumechukua hatua katika sekta ya madini na sasa inachangia asilimia 17 ya pato la Taifa ikilinganishwa na asilimia 11 za huko nyuma.
“Nataka kuwahakikishia kuwa Serikali ipo, haijalala na haitalala” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
02 Aprili, 2018