Taarifa kwa vyombo vya Habari ya zamani
Taarifa kwa vyombo vya habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amewataka viongozi na waumini wa madhehebu ya dini nchini kujiepusha na migogoro ambayo imekuwa ikiharibu sifa na heshima ya taasisi hizo muhimu katika jamii.
Mhe. Rais Magufuli ametoa wito huo tarehe 04 Februari, 2018 mara baada ya kuhudhuria Ibada ya kuwekwa wakfu kwa Askofu wa Tano wa Dayosisi ya Dar es Salaam Baba Askofu Jackson Sosthenes Jackson katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Albano Upanga.
Mhe. Rais Magufuli amesema viongozi wa Serikali husikitishwa na uwepo wa migogoro katika madhehebu ya dini, na hupata mashaka kama kweli viongozi wa madhehebu husika wanazingatia matakwa ya uchungaji.
Amempongeza Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania Dkt. Jacob Chimeledya kwa kuumaliza mgogoro uliokuwa ukilikabili Kanisa hilo na hatimaye kufikia hatua ya kumweka wakfu Baba Askofu Jackson Sosthenes Jackson kuwa Askofu wa Tano wa Dayosisi ya Dar es Salaam.
Mhe. Rais Magufuli amemtaka Baba Askofu Jackson Sosthenes Jackson kuwa Askofu wa wote, kuvunja makundi yaliyokuwepo katika Dayosisi hiyo, kutolipiza kisasi na kusamehe yote yaliyopita na badala yake ajenge Dayosisi imara na aongoze kwa haki na upendo kwa wote.
Mhe. Rais Magufuli amewahakikishia viongozi wa Kanisa la Anglikana Tanzania kuwa Serikali ya Awamu ya Tano itaendelea kushirikiana na kanisa hilo na madhehebu mengine ya dini katika shughuli zao mbalimbali ikiwa ni pamoja na taasisi mbalimbali zinazotoa huduma za kijamii kama vile hospitali, na shule.
Ibada hiyo imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Mke wa Rais Mhe. Mama Janeth Magufuli, Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Tulia Ackson Mwansasu, Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu Mhe. Benjamin William Mkapa na Mkewe Mhe. Mama Anna Mkapa na Waziri Mkuu Mstaafu Mhe. Jaji Mstaafu Joseph Sinde Warioba.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
04 Februari, 2018
Taarifa kwa vyombo vya habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 03 Februari, 2018 amewatunuku kamisheni maafisa wanafunzi 197 wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kundi la 62/17 katika viwanja vya Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Kati ya maafisa hao, 188 wamepata mafunzo ya kijeshi katika Chuo cha Mafunzo ya Kijeshi Monduli Mkoani Arusha (TMA) yaliyoanza tarehe 23 Januari, 2017 na 9 wamepata mafunzo katika nchi za Burundi, Kenya, China na Uingereza, na wote wametunukiwa cheo cha Luteni Usu.
Taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Chuo cha Mafunzo ya Kijeshi Monduli Meja Jen. Paul Peter Massao kwa Mhe. Rais Magufuli, imeeleza kuwa kati ya maafisa wote 197, maafisa 160 ni wanaume ambapo 149 ni Watanzania na 11 wanatoka nchi rafiki na maafisa 28 ni wanawake ambapo 25 ni Watanzania na 3 wanatoka nchi rafiki.
Meja Jen. Massao ameeleza kuwa mafunzo kwa maafisa hao yameendeshwa kwa kuzingatia viwango vilivyowekwa na kukubalika kimataifa, na maendeleo yao yalikuwa mazuri katika nyanja zote yaani darasani na mazoezi katika medani.
Pamoja na kutunuku kamisheni kwa maafisa hao Mhe. Rais Magufuli ametoa zawadi kwa wanafunzi waliofanya vizuri zaidi, ambapo aliyefanya vizuri zaidi kwa ujumla ni Lut Usu. Michael Jimmy Igoti, aliyefanya vizuri zaidi darasani ni Lut Usu. Nsangarufu Obadia Mwamondo, aliyefanya vizuri zaidi katika medani ni Lut Usu. Benson Godfrey Kwembe, aliyefanya vizuri zaidi kutoka nchi rafiki ni Lut Usu. Mukundane Beka (Uganda) na aliyefanya vizuri zaidi katika wanawake ni Lut Usu. Flavia Mavala Baraza (Kenya).
Akizungumza baada ya kushiriki chakula cha mchana pamoja na maafisa hao, Mhe. Rais Magufuli amewapongeza kwa kuhitimu mafunzo salama na kutunukiwa kamisheni na amewahakikishia askari wote wa JWTZ kuwa Serikali ya Awamu ya Tano inathamini kazi zinazofanywa na Jeshi hilo na itaendeleza juhudi zilizofanywa tangu awamu zilizopita za kujenga jeshi imara, linaloheshimika na lililo tayari kutekeleza majukumu yake ya kuilinda nchi wakati wote.
Mhe. Rais Magufuli amelipongeza Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kwa kukamilisha ujenzi wa ukuta katika eneo la machimbo ya madini ya Tanzanite la Mererani Mkoani Manyara, na kwa kuitikia wito wa kujenga viwanda ambapo viwanda vya Maji na nafaka vimeanza kujengwa, na pia Jeshi la Magereza kwa kuimarisha kiwanda cha kutengeneza viatu.
Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli amewaapisha Majaji 2, Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali aliowateua tarehe 01 Februari, 2018.
Walioapishwa kuwa Majaji ni Mhe. George Mcheche Masaju na Mhe. Gerson John Mdemu.
Mhe. Rais Magufuli amemuapisha Mhe. Dkt. Adelardus Lubango Kilangi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Mhe. Paul Joel Ngwembe kuwa Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Matukio yote mawili yamehudhuriwa na Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Tulia Ackson Mwansasu, Katibu Mkuu Kiongozi Mhe. Balozi John Kijazi na viongozi wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
03 Februari, 2018
Taarifa kwa vyombo vya habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amepokea kwa huzuni na masikitiko taarifa za kifo cha mmoja wa waasisi wa Taifa na mwanasiasa mkongwe nchini Mzee Kingunge Ngombale Mwiru kilichotokea tarehe 02 Februari, 2018 saa 10:30 alfajiri katika Hospitali ya Taifa Muhimbili Jijini Dar es Salaam.
Mzee Kingunge Ngombale Mwiru alikuwa akipatiwa matibabu hospitalini hapo baada ya kushambuliwa na mbwa wake nyumbani kwake Jijini Dar es Salaam tarehe 22 Desemba, 2017.
Mhe. Rais Magufuli amesema Taifa limempoteza mtu muhimu ambaye alitoa mchango mkubwa katika juhudi za kupigania uhuru na baada ya kupata uhuru akiwa mtumishi mtiifu wa Chama cha TANU na baadaye Chama Cha Mapinduzi (CCM), na katika nyadhifa mbalimbali za uongozi ndani ya Serikali.
“Mzee Kingunge Ngombale Mwiru ametoa mchango mkubwa sana, sisi kama Taifa hatuwezi kusahau na tutayaenzi mema yote aliyoyafanya wakati wa utumishi wake uliotukuka, ametuachia somo la kupigania maslahi ya nchi wakati wote, kuwa wazalendo wa kweli, kudumisha amani na mshikamano, kuchapa kazi kwa juhudi na maarifa na kuwa na nidhamu” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Kufuatia msiba huu, Mhe. Rais Magufuli amewapa pole wanafamilia wote, wanachama wa CCM, ndugu, jamaa, marafiki na wote walioguswa na msiba huu, na amewaombea kuwa na moyo wa subira, uvumilivu na ustahimilivu katika kipindi hiki cha majonzi.
Mwenyezi Mungu ailaze roho ya Marehemu Kingunge Ngombale Mwiru mahali pema peponi, Amina.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
02 Februari, 2018
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt John Pombe Magufuli amemteua Dkt. Adelardus Kilangi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).
Taarifa iliyotolewa jioni hii na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi imeeleza kuwa uteuzi wa Dkt. Adelardus Kilangi unaanza tarehe 01 Februari, 2018.
Kabla ya uteuzi huu Dkt. Kilangi alikuwa Mkurugenzi wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino (St. Augustine University) kituo cha Arusha, na pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Shughuli za Mkondo wa Juu wa Mafuta (Tanzania Petroleum Upstream Regulatory Authority – PURA).
Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli amemteua Bw. Paul Joel Ngwembe kuwa Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali (DAG) kuanzia leo tarehe 01 Februari, 2018.
Kabla ya Uteuzi huu Bw. Ngwembe alikuwa Mkurugenzi wa masuala ya sheria katika Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (Tanzania Insurance Regulatory Authority – TIRA).
Kufuatia uteuzi huu Mhe. Rais Magufuli amewateua aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. George Mcheche Masaju na aliyekuwa Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Gerson Mdemu kuwa Majaji wa Mahakama Kuu kuanzia leo tarehe 01 Februari, 2018.
Wateule wote wataapishwa Jumamosi tarehe 03 Februari, 2018 saa 9:00 Alasiri.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
01 Februari, 2018
Taarifa kwa vyombo vya habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amesema Serikali inaunga mkono utekelezaji wa matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kwa Mahakama ili kuongeza ufanisi wa majukumu yake.
Mhe. Rais Magufuli ametoa kauli hiyo tarehe 01 Februari, 2018 wakati akihutubia katika siku ya sheria, maadhimisho ambayo yamefanyika katika Mtaa wa Chimala, Wilaya ya Ilala Jijini Dar es Salaam, yakiwa na kauli mbiu “Matumizi ya Tehama katika utoaji wa haki kwa wakati na kuzingatia maadili”.
Pamoja na kuunga mkono matumizi ya TEHAMA kwa Mahakama, Mhe. Rais Magufuli ameipongeza Mahakama kwa kazi inayoifanya ikiwemo kupunguza mrundikano wa kesi na ameahidi kuwa Serikali ipo tayari kusikiliza ushauri wa Mahakama juu ya maslahi ya wafanyakazi utakaotolewa mwezi huu na Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma.
Pia Mhe. Rais Magufuli amesema yupo tayari kufanya uteuzi wa Majaji wengine kadiri atakavyoshauriwa na Mahakama ili kukabiliana na changamoto ya upungufu mkubwa wa Majaji iliyosababisha ongezeko kubwa la mrundikano wa mashauri katika Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufani.
Hata hivyo Mhe. Rais Magufuli ametoa wito kwa Mahakama kuendelea kurekebisha dosari ambazo zimekuwa zikiuchafua mhimili huo wa Dola ikiwemo Majaji na Mahakimu kujihusisha na vitendo vya upokeaji wa rushwa na ucheleweshaji wa kesi ambavyo vinasababisha hasara kubwa kwa Taifa.
“Nilikuuliza Mhe. Jaji Mkuu na mimi nasema kwa uwazi kabisa, katika vibali vingi vya kusafiri nje ya nchi ninavyoombwa na Majaji na ambavyo vyote huwa ninaruhusu, na vimenisaidia kufanya utafiti wangu, wengi huwa wanaomba kwenda likizo nje ya nchi, Afrika Kusini, Uingereza, nakadhalika, na wanaenda na familia zao, wanakaa huko kwa siku 28, na pale chini wanaandika kuwa watajigharamia, hili huwa ni swali ninalojiuliza sana, maana mshahara wa Jaji ninaujua.
“Na ukweli huwa nafuatilia anapokwenda kule anakaa hotel na nani amehusika kulipa hotel hiyo yenye gharama za juu, na kwa nini ni fulani fulani tu, Mhe. Jaji Mkuu majibu hujayapata na mimi sijayapata, sasa Mhe. Jaji Mkuu fuatilia hili” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli amempongeza Mhe. Jaji Mkuu kwa hatua alizochukuwa kuwafukuza kazi watumishi 112 wa Mahakama wakiwemo Mahakimu 17 waliojihusisha na vitendo vya ukiukwaji wa maadili na amevishangaa vyombo vingine ambavyo hushirikiana na Mahakama kama vile Jeshi la Polisi, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Magereza na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) kwa kutowawajibisha watumishi wake wanaokiuka maadili.
“Mwaka jana nililalamika, sasa mwaka huu sitalalamika, nitachukua hatua, tena mwezi huu wa pili hautaisha, pale ofisini kwangu napokea barua nyingi za malalamiko ya ucheleweshaji wa kesi, kila kesi upelelezi haujakamilika, ni lazima kuwe na utatuzi wa jambo hili, hivi sasa kuna kesi za Shilingi Bilioni 169.1 na Dola za Marekani Milioni 38.2 zinasubiri tu na nchi inakosa mapato” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Halikadhalika Mhe. Rais Magufuli amemtaka Waziri wa Katiba na Sheria Prof. Palamagamba Kabudi, kukamilisha kanuni za sheria ya msaada wa kisheria (Legal Aid Act, No.1 of 2017) ambayo imepitishwa na Bunge na kusainiwa na Rais tangu miezi 9 iliyopita, ndani ya kipindi cha mwezi mmoja kuanzia sasa.
Mapema kabla ya hotuba ya Mhe. Rais Magufuli Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma alisema Mahakama imedhamiria kuanza matumizi ya TEHAMA katika shughuli zake na ametaka watumishi hasa Majaji na Mahakimu wajiandae kutumia teknolojia hiyo, na pia ameahidi kuwa Mahakama itaendelea kuchukua hatua dhidi ya vitendo vya ukiukwaji wa maadili na kusimamia uwajibikaji.
Nae Makamu wa Rais wa Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS) Mhe. Godwin Simba Ngwilimi amesema TLS inaunga mkono dhamira ya kutumia TEHAMA katika shughuli za Mahakama na amempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa uongozi wake unaoakisi nia na matarajio ya Watanzania.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
01 Februari, 2018
Taarifa kwa vyombo vya habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 31 Januari, 2018 amewajulia hali wagonjwa waliolazwa katika Hospitali ya Tumaini Jijini Dar es Salaam akiwemo muigizaji mkongwe nchini Mzee Amri Athuman, maarufu kwa jina la “King Majuto”.
Mhe. Rais Magufuli ambaye ameongozana na Mkewe Mhe. Mama Janeth Magufuli, amewajulia hali wagonjwa waliolazwa katika wodi namba 3 hadi namba 8 na baadaye akamuona King Majuto ambaye anaendelea kupata matibabu ya tezi dume.
King Majuto amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kwenda hospitali kumuona na amempongeza kwa namna anavyosimamia huduma za afya nchini, kwani tangu maradhi yalipomuanza amehudumiwa vizuri na ana matumaini ya kupona na kurejea katika majukumu yake ya kila siku.
Aidha, King Majuto amemuombea Mhe. Rais Magufuli ili aendelee kutekeleza majukumu yake ya kuongoza nchi vizuri, na amebainisha kuwa hatua zinazochukuliwa na Serikali ya Awamu ya Tano zimerejesha nidhamu, zimeongeza uchapakazi, zimesaidia kukabiliana na wizi na zimeongeza heshima ya nchi.
“Kiongozi lazima awe namna hii, sio kuleta mzahamzaha, ukisema jambo watu wanatekeleza, wezi wanakamatwa, wala rushwa wanakamatwa, wenye vyeti feki hata kama amefanya kazi miaka 20 fukuza, hii safi, sasa kuna heshima na watu wanachapa kazi, ndio maana mimi hata wakati wa kampeni niliwaambia wasanii wenzangu hapa Rais ni Magufuli” amesema King Majuto.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
31 Januari, 2018
Taarifa kwa vyombo vya habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 31 Januari, 2018 amezindua mfumo wa uhamiaji mtandao (e-Immigration) ambao utasaidia kuimarisha ulinzi na usalama wa mipaka ya nchi, kudhibiti ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali na kuimarisha utoaji wa huduma za kiuhamiaji kwa raia wa Tanzania na wageni wanaoingia na kuishi hapa nchini kwa madhumuni mbalimbali.
Uzinduzi wa mfumo huo umefanyika katika ofisi kuu ya uhamiaji Jijini Dar es salaam na kuhudhuriwa na Mke wa Rais Mhe. Mama Janeth Magufuli, Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Seif Ali Iddi, na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa.
Wengine ni Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, Jaji Mkuu wa Zanzibar Mhe. Omar Othman Makungu, Spika wa Baraza la Wawakilishi Mhe. Zubeir Ali Maulid, Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Tulia Ackson Mwansasu, Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili Mhe. Dkt. Ali Hassan Mwinyi na Rais Mstaafu wa Zanzibar Mhe. Amani Abeid Karume.
Kabla ya kuzindua mfumo wa uhamiaji mtandao Mhe. Rais Magufuli amekagua teknolojia iliyotumika katika mfumo huo ikiwa ni pamoja na kuchukuliwa alama za vidole na baadaye kupatiwa pasipoti mpya ya kielekektronikia (e-Passport) ambayo pia imeanza kutolewa leo.
Mhe. Rais Magufuli amempongeza Waziri wa Mambo ya ndani ya nchi Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba na Idara ya Uhamiaji kwa kufanikisha mchakato uliofanikisha uwepo wa mfumo wa uhamiaji mtandao na kuanza kutoa pasipoti mpya ya kielektronikia kwa gharama nafuu ya Shilingi Bilioni 127.2 ikilinganishwa na makadirio yaliyowekwa awali ya Shilingi Bilioni 400.
“Hapa tumeokoa fedha nyingi za Watanzania, kuna watu walikuwa wamejiandaa kutupiga na kuchukua hizo Shilingi Bilioni 400, lakini tukatumia vyombo vyetu mbalimbali, tukafanya uchunguzi na tumefanikiwa kutekeleza mradi huu kwa gharama nafuu” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Aidha, kwa kutambua kazi nzuri inayofanywa na idara ya uhamiaji baada ya kupokea maelekezo yake ya kutakiwa kufanya mabadiliko makubwa, Mhe. Rais Magufuli ameahidi kutoa Shilingi Bilioni 10 kwa ajili ya kujenga ofisi ya makao makuu ya idara hiyo Mjini Dodoma.
“Kamishna Jenerali Dkt. Anna Makakala na timu yako mnafanya kazi nzuri, ndio maana nimewanunulia nyumba 103 kwa ajili ya wafanyakazi na leo nitawapa fedha nyingine Shilingi Bilioni 10 mkajenge ofisi nzuri ya makao makuu, nyinyi endeleeni kuchapa kazi, endeleeni kukamata wahamiaji haramu na endeleeni kukusanya mapato vizuri” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Mapema akitoa taarifa ya mfumo wa uhamiaji mtandao, Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Dkt. Anna Makakala amesema mfumo huo ni muunganiko wa mifumo mbalimbali ambayo imesanifiwa kufanya kazi kwa pamoja, kutoa taarifa kwa watumiaji na wadau wa huduma za kiuhamiaji na kwamba kupitia mfumo huo idara ya uhamiaji inatarajia kutoa pasipoti za kielektronikia (e-Passport), viza za kielektronikia (e-Visa), vibali vya ukaazi vya kielektronikia (e-Permit) na udhibiti wa mipaka wa kielektronikia (e-Border Management) kwa awamu nne hadi ifikapo mwisho wa mwaka huu 2018, pamoja na kutoa pasipoti ya kielektronikia ya Afrika Mashariki ya Tanzania.
Balozi wa Ireland hapa nchini Mhe. Paul Sherlock ameipongeza Tanzania kwa kufanikisha mradi huu na kueleza kuwa mfumo huu wa uhamiaji mtandao ni alama muhimu ya Taifa.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
31 Januari, 2018
Taarifa kwa vyombo vya habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 29 Januari, 2018 amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi Mteule Mhe. Dkt. Wilbrod Peter Slaa, Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Baada ya Mazungumzo hayo Balozi Mteule Mhe. Dkt. Slaa amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kumuamini na kumteua kuwa Balozi na ameahidi kuwa yupo tayari kutekeleza majukumu atakayopangiwa kwa kutanguliza maslahi ya Taifa.
Mhe. Dkt. Slaa amempongeza Mhe. Rais Magufuli na Serikali yake ya Awamu ya Tano kwa uongozi bora wenye maono na uthubutu wa kutekeleza mambo makubwa yenye maslahi kwa nchi ikiwemo miradi mikubwa kama vile ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa (Standard Gauge), ujenzi wa daraja la juu (Flyover) katika makutano ya barabara ya Nyerere na Mandela (Tazara), mradi wa uzalishaji umeme katika maporomoko ya mto Rufiji (Stieglers’ Gorge) na mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi.
“Kwa kweli naona faraja, ninafurahi Serikali ya Awamu ya Tano inatekeleza hatua kwa hatua karibu yote tuliyokuwa tunayapigania kwa miaka takribani 20 ya huko nyuma, na mimi Dkt. Slaa nilikuwa napiga kelele kwa sababu nilikuwa naona kuna upungufu.
“Leo ninasema ninafurahi yale niliyokuwa napigia kelele yanatekelezwa kwa sababu nimeyaona, sasa kitu kikubwa ni macho, ushabiki katika maendeleo hauna tija, ushabiki katika siasa nao hauna tija, kama nilivyowahi kueleza huko nyuma siasa ni sayansi, wapo wanaofikiri siasa ni upotoshaji na siasa ni udanganyifu lakini siasa ni sayansi, na siasa kama ni sayansi ina misingi yake inayohitaji kusimamiwa, na misingi yake ni nini kilikuwa ni tatizo na tatizo hilo linatatuliwa kwa misingi ipi, sasa haya tunayoyasema ni hivi, tulikuwa na tatizo la umeme, Stieglers’ Gorge inaanza kujengwa, na miradi mingine mikubwa inatekelezwa, haya ndio mambo ya msingi” amesema Mhe. Dkt. Slaa.
Kwa upande wake Mhe. Rais Magufuli amempongeza Mhe. Dkt. Slaa kwa moyo wake wa kizalendo na amesema aliamua kumteua kuwa Balozi kwa kuwa anatambua kuwa ataweza kupigania maslahi ya Tanzania popote atakapopangiwa kuiwakilisha.
“Dkt. Slaa alinijulisha kuwa anakuja na akaomba akija angependa kuja kuniona na nikampangia leo, tumezungumza mambo mengi na ameniahidi kuwa atakwenda kufanya kazi yake vizuri kwenye nchi atakayokwenda kuwa Balozi.
“Mhe. Dkt. Wilbrod Slaa ni mtu safi, anazungumza kutoka moyoni na anaipenda Tanzania na mimi kutokana na moyo wake wa kuchukia ufisadi na kuchukia wizi nikaamua kumteua kuwa Balozi” Amesema Mhe. Rais Magufuli.
Wakati huo huo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ameagana na maafisa wakuu wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) ambao wanastaafu baada ya kutimiza umri.
Walioagana na Mhe. Rais Magufuli ni Luteni Jenerali James Mwakibolwa aliyekuwa Mnadhimu Mkuu wa JWTZ na Meja Jenerali Michael Isamuhyo aliyekuwa Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).
Wengine ni Brigedia Jenerali Aron Lukyaa, Brigedia Jenerali William Kivuyo, Brigedia Jenerali Elizaphani Marembo na Kanali Peter Samegi.
Akizungumza baada ya kuagana, Luteni Jenerali Mwakibolwa amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kumteua kuwa Mnadhimu Mkuu wa JWTZ na amesema anaondoka na kuliacha jeshi likiwa na nidhamu, utii, uzalendo na weledi.
Nae Meja Jenerali Isamuhyo pamoja na kumshukuru Mhe. Rais Magufuli amesema anafurahi kuiacha JKT ikiwa imeimarika katika majukumu yake yakiwemo ujenzi wa viwanda, kilimo na kuimarisha mafunzo kwa vijana wazalendo.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
29 Januari, 2018
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amemtumia salamu za rambirambi Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma kufuatia kifo cha Jaji Mstaafu wa Mahakama ya Rufani Tanzania Mhe. Robert Kisanga kilichotokea jana tarehe 23 Januari, 2018 katika hospitali ya Regency Jijini Dar es Salaam.
Katika salamu hizo Mhe. Rais Magufuli amesema Jaji Mstaafu Robert Kisanga atakumbukwa kwa mchango wake mkubwa alioutoa kwa Taifa wakati wote wa utumishi wake uliojaa umakini, uchapakazi, uzalendo na ushirikiano na wengine, mambo ambayo yalimwezesha kupata mafanikio makubwa.
“Sote tunafahamu kazi nzuri alizofanya akiwa katika majukumu mbalimbali ya kitaifa, mchango wake katika kuijenga taaluma ya uanasheria baada ya uhuru na uanzishaji wa Mahakama ya Rufani baada ya kuvunjika kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki mwaka 1977, kwa hakika mchango wake hautasahaulika.
“Nakuomba Mhe. Jaji Mkuu Prof. Ibrahim Hamis Juma unifikishie salamu zangu za pole kwa familia ya Marehemu Jaji Mstaafu Kisanga, Majaji na wanasheria wote, ndugu, jamaa na marafiki wote walioguswa na msiba huu” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Mhe. Rais Magufuli amewaombea wafiwa wote wawe na moyo wa subira, uvumilivu na ustahimilivu katika kipindi hiki kigumu cha majonzi na amemuombea Marehemu Jaji Mstaafu Kisanga apumzishwe mahali pema peponi, Amina.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
24 Januari, 2018
Taarifa kwa vyombo vya habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 22 Januari, 2018 amepokea hati za utambulisho kutoka kwa Mabalozi 6 walioteuliwa kuziwakilisha nchi zao hapa nchini.
Mabalozi waliowasilisha hati zao ni Mhe. Konstantinos Moatsos – Balozi wa Ugiriki hapa nchini mwenye makazi yake Nairobi nchini Kenya, Mhe. Fafre Camara – Balozi wa Mali hapa nchini mwenye makazi yake Addis Ababa nchini Ethiopia na Mhe. Dina Mufti Sid – Balozi wa Ethiopia hapa nchini mwenye makazi yake Nairobi nchini Kenya.
Wengine ni Mhe. Elizabeth Taylor – Balozi wa Colombia hapa nchini mwenye makazi yake Nairobi nchini Kenya, Mhe. Martin Gomez Bustillo – Balozi wa Argentina hapa nchini mwenye makazi yake Nairobi nchini Kenya na Mhe. Uriel Norman R. Garibay – Balozi wa Ufilipino mwenye makazi yake Nairobi nchini Kenya.
Mhe. Rais Magufuli amewapongeza Mabalozi wote kwa kuteuliwa kuziwakilisha nchi zao hapa nchini na ameahidi kuwapa ushirikiano utakaowezesha uhusiano na ushirikiano kati ya Tanzania na nchi zao kukua zaidi.
Mhe. Rais Magufuli amewahakikishia kuwa Tanzania inatambua uwepo wa fursa mbalimbali za kibiashara na kiuchumi katika nchi hizo pamoja na ujuzi na uzoefu katika nyanja mbalimbali, na kwamba ni matarajio yake kuwa ujio wao utasaidia kuongeza manufaa ya kiuchumi na kubadilishana uzoefu.
Pia Mhe. Rais Magufuli amewaomba Mabalozi hao kufikisha salamu zake kwa viongozi wa nchi zao na amewakaribisha kutembelea Tanzania.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
22 Januari, 2018
Taarifa kwa vyombo vya habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amewaagiza Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasliano Prof. Makame Mbarawa Mnyaa na Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji wa Zanzibar Balozi Ali Abeid Karume kusitisha usajili wa meli mpya hapa nchini mpaka hapo itakapotangazwa vinginevyo.
Mhe. Rais Magufuli ametoa agizo hilo tarehe 19 Januari, 2018 alipokuwa akizungumza na wafanyakazi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki katika ukumbi wa kimataifa wa mikutano wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam, kikao ambacho kimehudhuriwa na Mawaziri hao.
Ametoa agizo hilo ili kujipanga upya kufuatia taarifa za kukamatwa kwa dawa za kulevya katika meli zinazopeperusha bendera ya Tanzania ambazo hadi sasa zimefikia meli 5.
Sambamba na kusitishwa kwa usajili mpya wa meli Mhe. Rais Magufuli amewaagiza Mawaziri hao pamoja na vyombo vya dola kufanya uchunguzi wa kina kwa meli zote 470 ambazo zimesajiliwa hapa nchini na zinapeperusha bendera ya Tanzania.
Pia Mhe. Rais Magufuli amemuagiza Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Augustine Mahiga kusimamia utekelezaji wa maagizo hayo na kuhakikisha jina la Tanzania halichafuliwi ndani na nje na nchi.
“Kafanyeni uchunguzi wa kina kwa meli zote zinazopeperusha bendera ya Tanzania, fanyeni uchunguzi kwa meli zilizokamatwa ambazo ni 5 na pia hizi 470 zilizosajiliwa na zinazoendelea kufanya kazi zichunguzeni, hatuwezi kuacha jina la nchi yetu lichafuliwe na watu wanaofanya mambo kwa maslahi yao” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli ametaka maagizo yote yaliyotolewa na Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan kuhusiana na meli hizo yatekelezwe.
Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli amewataka wafanyakazi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kutilia mkazo utekelezaji wa sera ya diplomasia ya uchumi ili nchi iweze kunufaika na fursa mbalimbali za uhusiano na ushirikiano na mataifa mengine duniani.
Mhe. Rais Magufuli amemuagiza Waziri Mahiga kuhakikisha Mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania nje ya nchi, na Wakurugenzi wa idara za wizara hiyo wanafanya kazi zenye manufaa kwa nchi, ikiwemo kuwataka Mabalozi kutoa taarifa kila baada ya robo mwaka juu ya ukusanyaji wa mapato na utekelezaji wa sera hiyo.
“Wakupe taarifa kila baada ya robo mwaka, na Balozi ambaye atakuwa hakusanyi mapato vizuri na kuinua biashara na uwekezaji atakuwa hafai kuendelea kuwa Balozi, tena kawaambie kabisa kwenye suala hili hakuna mchezo” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Halikadhalika Mhe. Rais Magufuli amemtaka Waziri Mahiga na watendaji wa wizara yake kufuatilia kwa ukaribu na kushirikiana na Mawaziri wanaohusika katika utekelezaji wa mikataba mbalimbali ambayo Tanzania imetiliana saini na nchi mbalimbali duniani, na kwamba hataki kusikia utekelezaji wa mikataba ambayo baadhi yake inahusisha miradi mikubwa yenye manufaa kwa Tanzania, unakwama ama kusuasua.
“Mnapokuwa mnahitaji taarifa kutoka wizara nyingine kama ni Waziri muandikie Waziri mwenzako kama ni Katibu Mkuu muandikie Katibu Mkuu mwenzako halafu nakala ya barua ilete kwangu kupitia kwa Katibu Mkuu Kiongozi, nataka nione huyo atakayechelewesha ama kutotoa taarifa” ameongeza Mhe. Rais Magufuli.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
19 Januari, 2018
Taarifa kwa vyombo vya habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 17 Januari, 2018 amemteua Dkt. Titus Mwinuka kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO).
Kabla ya uteuzi huu Dkt. Titus Mwinuka alikuwa akikaimu nafasi hiyo.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
17 Januari, 2018
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ameagiza kuchukuliwa hatua dhidi ya viongozi na watendaji ambao shule za msingi na sekondari zilizopo katika maeneo yao zinawatoza wanafunzi michango mbalimbali kinyume na muongozo uliotolewa na Serikali wa utoaji wa elimu bila malipo.
Mhe. Rais Magufuli ametoa maagizo hayo leo asubuhi tarehe 17 Januari, 2018 Ikulu Jijini Dar es Salaam alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Lazaro Ndalichako na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Selemani Said Jafo.
Mhe. Rais Magufuli amesema Serikali inatoa Shilingi Bilioni 23.875 kila mwezi kwa ajili ya kuwezesha utoaji wa elimu bila malipo lakini inashangaza kuona bado kuna walimu wanaendelea kuwatoza michango ama kuwarudisha nyumbani wanafunzi ambao wanashindwa kutoa michango hiyo.
“Nawaagiza Mawaziri, sitaki kusikia mwanafunzi anarudishwa nyumbani kwa kushindwa kutoa michango, na fikisheni maagizo haya kwa Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi na wote wanaohusika, nikisikia tena mahali jambo hili linaendelea hawa niliowateua mimi wataondoka.
“Haiwezekani tumefuta ada, halafu walimu wanaamua kuanzisha michango tena mikubwa ambayo watu masikini wanashindwa kusomesha watoto wao, na kama wazazi wanataka kuchangia kitu shuleni wapeleke michango yao kwa Mkurugenzi, lakini sitaki kusikia mwanafunzi anapewa sharti la kutoa mchango ndipo apokelewe shule” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Mhe. Rais Magufuli ametoa maagizo hayo baada ya kupata taarifa kuwa zipo baadhi ya shule ambazo wanafunzi wanadaiwa michango mbalimbali tena kwa kiwango kikubwa ikiwemo chakula, maabara, madawati na ziara za kujifunza, hali iliyosababisha wazazi kushindwa kumudu.
Waziri Prof. Joyce Lazaro Ndalichako ameagiza walimu na viongozi wa halmashauri kuwarudisha shule mara moja wanafunzi wote waliorudishwa nyumbani kwa kutotoa michango na pia kurejesha mara moja michango iliyokusanywa kinyume na mwongozo wa Serikali.
Waziri Mhe. Selemani Said Jafo amewaagiza Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya kuwasilisha taarifa ya shule ambazo zimetoza michango kinyume na mwongozo wa Serikali ifikapo Ijumaa wiki hii (tarehe 19 Januari, 2018) ili hatua zichuliwe dhidi ya walimu na maafisa elimu ambao kwa makusudi wamekiuka mwongozo huo.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
17 Januari, 2018
Taarifa kwa vyombo vya habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 16 Januari, 2018 amepokea hati za utambulisho za Mabalozi 6 walioteuliwa kuziwakilisha nchi zao hapa nchini.
Mabalozi waliowasilisha hati zao za utambulisho ni Balozi wa Nigeria hapa nchini Mhe. Sahabu Isah Gada, Balozi wa Poland hapa nchini Mhe. Krzysztof Buzalski, Balozi wa Uturuki hapa nchini Mhe. Ali Davutoglu, Balozi wa Ufaransa hapa nchini Mhe. Frédéric Clavier, Balozi wa Israel hapa nchini Mhe. Noah Gal Gendler na Balozi wa Australia hapa nchini Mhe. Alison Chartres.
Akizungumza na Mabalozi hao Mhe. Rais Magufuli amewapongeza kwa kuteuliwa kuziwakilisha nchi zao hapa nchini na ameahidi kuwa Tanzania itaendeleza na kukuza zaidi uhusiano na ushirikiano mzuri uliopo kati yake na nchi hizo.
Mhe. Rais Magufuli ametoa wito kwa Mabalozi hao kutilia mkazo ushirikiano katika masuala ya kiuchumi yakiwemo kuwahamasisha wafanyabiashara na wawekezaji wa nchi hizo kuja kufanya biashara na kuwekeza hapa nchini, hususani katika viwanda, kilimo, utalii na utoaji wa huduma mbalimbali za kijamii na kwamba Serikali itakuwa tayari wakati wote kujenga mazingira bora ya kufanikisha biashara na uwekezaji huo.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli amewaomba Mabalozi hao kufikisha salamu zake kwa viongozi wa nchi zao, na kuwakaribisha kuitembelea Tanzania ili kuimarisha zaidi uhusiano na ushirikiano.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
16 Januari, 2018
Taarifa kwa vyombo vya habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amemtumia salamu za rambirambi Mkuu wa Mkoa wa Kagera Meja Jenerali Mstaafu Salum Kijuu kufuatia watu 11 kupoteza maisha katika ajali ya gari iliyotokea katika Kijiji cha Nyangozi, Wilaya ya Biharamulo Mkoani Kagera.
Ajali hii imetokea jana tarehe 14 Januari, 2018 majira ya saa 11 jioni baada ya basi dogo la abiria aina ya Nissan Caravan lililokuwa likitoka Kakonko Mkoani Kigoma kuelekea Kahama Mkoani Shinyanga kuligonga ubavuni lori la mizigo kisha kugongana uso kwa uso na lori jingine na kusababisha vifo vya watu 11 na wengine 6 kujeruhiwa.
Mhe. Rais Magufuli amepokea kwa huzuni na masikitiko makubwa taarifa za vifo vya Watanzania hao na amemtaka Mkuu wa Mkoa wa Kagera Meja Jenerali Mstaafu Salum Kijuu kumfikishia pole kwa familia za Marehemu wote, ndugu, jamaa, marafiki na wote walioguswa na vifo hivyo.
“Nimehuzunishwa na kusikitishwa sana na vifo hivi, nawapa pole wafiwa wote, ninawaombea marehemu wapumzike mahali pema na majeruhi wapone haraka ili waweze kuungana na familia zao na kuendelea na shughuli zao za kila siku” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli amewakumbusha watumiaji wa barabara hasa madereva kuwa makini na kuzingatia sheria za usalama barabarani na ameviagiza vyombo vinavyohusika kuongeza jitihada za kukabiliana na ajali za barabarani ili kuokoa maisha ya watu na mali zinazopotea kutokana na ajali.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
15 Januari, 2018
Taarifa kwa vyombo vya habari
Rais wa Jamhuri ya Rwanda Mhe. Paul Kagame tarehe 14 Januari, 2018 amefanya ziara ya kikazi ya siku moja hapa nchini kwa mwaliko wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli.
Mhe. Rais Kagame amewasili katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam na kupokelewa na mwenyeji wake Mhe. Rais Magufuli na kisha kulakiwa na viongozi mbalimbali wakiongozwa na Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan, na baadaye akaelekea Ikulu ambako pamoja na kufanya mazungumzo ya faragha, viongozi hao wamezungumza na wananchi kupitia vyombo vya habari.
Mhe. Rais Magufuli amesema katika mazungumzo yao wamekubaliana ujenzi wa reli kwa kiwango cha kisasa (Standard Gauge) kati ya Isaka nchini Tanzania na Kigali nchini Rwanda yenye urefu wa takribani kilometa 400 uanze mwaka huu (2018), na wamewaagiza Mawaziri wanaohusika na miundombinu kukutana ndani ya kipindi cha wiki mbili kuanza sasa ili kuweka mipango ya utekelezaji ikiwemo upatikanaji wa fedha.
Mhe. Rais Magufuli ameongeza kuwa wakati uamuzi huo ukifikiwa, Tanzania ambayo tayari imeanza ujenzi wa reli ya kati (Standard Gauge) kuanzia Dar es Salaam – Morogoro hadi Dodoma yenye urefu wa kilometa 726 na itakayogharimu Shilingi Trilioni 7.6, itaanza mchakato wa kuunganisha sehemu iliyobaki ya kutoka Dodoma - Isaka yenye urefu wa takribani kilometa 400 ili mizigo iweze kusafirishwa moja kwa moja kutoka bandari ya Dar es Salaam hadi Kigali nchini Rwanda.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli amebainisha kuwa japo kuwa kumekuwa na ongezeko la mizigo ya Rwanda inayosafirishwa kupitia Tanzania iliyofikia tani 950,000 kwa mwaka, biashara kati ya nchi hizi mbili sio ya kuridhisha na hivyo amesema wamekubaliana kuboresha zaidi mazingira ya biashara ikiwemo kuimarisha miundombinu ya reli na barabara na kuwahamasisha wafanyabiashara wa Tanzania na Rwanda kufanya biashara zaidi.
“Tukijenga reli kutoka Isaka hadi Kigali, na sisi huku tunajenga kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma na tukaunganisha Dodoma hadi Isaka, mizigo mingi ya Rwanda itasafirishwa kupitia bandari ya Dar es Salaam, biashara itakua zaidi na ajira zitaongezeka, kule Lulenge Ngara, Burundi na Rwanda kote kuna madini ya Nickel, tukijenga miundombinu yetu tutasafirisha madini haya na tutaongeza biashara.
“Na reli hii itatumiwa na nchi nyingine za Burundi, DRC na Uganda, kwa hiyo ni jambo muhimu sana kwa uchumi wetu na majirani” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Mhe. Rais Magufuli amemhakikishia Mhe. Rais Kagame kuwa Tanzania itaendeleza na kukuza zaidi uhusiano na ushirikiano wake na Rwanda kwa manufaa ya wananchi, na kwamba ipo tayari kumuunga mkono atakapochaguliwa kuwa mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU) katika kikao cha wakuu wa nchi na Serikali kinachotarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwezi huu wa Januari, 2018 Mjini Addis Ababa nchini Ethiopia.
“Mhe. Rais Kagame nakupongeza sana, unafanya kazi kubwa ya kuwapigania wananchi wako, Watanzania tunajua ulikoitoa Rwanda na tunajua ulipoifikisha, nakuhakikishia tutaendelea kushirikiana katika jukumu la kuwaletea wananchi maendeleo” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Kwa upande wake Mhe. Rais Kagame amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa mwaliko wake na amempongeza kwa kazi nzuri inayofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano na ushirikiano mzuri uliopo kati ya nchi yake na Tanzania.
Mhe. Rais Kagame amesema yeye na Mhe. Rais Magufuli wameamua kufanya kazi ya kuwaletea wananchi maendeleo na ameahidi kuendelea kufanya kazi kwa ushirikiano na Mhe. Rais Magufuli ili mipango yote waliyojiwekea itekelezwe ikiwemo kuinua biashara na kuongeza ajira, na pia ameshukuru kwa Tanzania kuwa tayari kumuunga mkono atakapochaguliwa kuwa Mwenyekiti wa AU.
Mhe. Rais Kagame amemaliza ziara yake ya kikazi ya siku moja hapa nchini na amerejea nchini kwake Rwanda.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
14 Januari, 2018
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 13 Januari, 2018 amekutana na kufanya mazungumzo na Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM, Itikadi na Uenezi Ndg. Humphrey Polepole, Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Baada ya mazungumzo hayo Ndg. Polepole amesema Mhe. Dkt. Magufuli amemuelekeza kuwajulisha wanachama wa CCM na umma wa Watanzania kuwa anasikitishwa na hafurahishwi na mjadala unaoendelea juu kuongezwa kwa kipindi cha Urais kutoka miaka 5 iliyowekwa kwa mujibu wa katiba, hadi miaka 7.
Ndg. Polepole amesema Mhe. Dkt. Magufuli amewataka wanachama wa CCM na umma wa Watanzania kwa ujumla kuupuuza mjadala huo kwa kuwa haujawahi kujadiliwa katika kikao chochote cha chama, na ni kinyume na katiba ya CCM na katiba ya nchi.
Ameongeza kuwa Mhe. Dkt. Magufuli amewataka wana CCM na umma wa Watanzania kutokubali kuyumbishwa ama kupotoshwa na mambo yasiyokuwa ya msingi na badala yake wajielekeze katika ajenda muhimu ya kujenga uchumi na kutekeleza Ilani ya CCM ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
Ndg. Polepole amebainisha kuwa Mhe. Dkt. Magufuli hana mpango wowote na hatarajii kuongeza kipindi cha Urais wakati wote wa uongozi wake.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
13 Januari, 2018
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Isdor Mpango tarehe 11 Januari, 2018 amewasilisha taarifa ya kamati aliyoiunda kuchunguza umiliki wa kampuni ya simu Airtel kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli aliyeagiza kufanyika kwa uchunguzi huo tarehe 20 Desemba, 2017.
Baada ya kuwasilisha taarifa hiyo, Dkt. Mpango amesema Serikali imejiridhisha kuwa ubinafsishaji wa Shirika la Simu Tanzania (TTCL) kwenda Celtel, baadaye kuhamishiwa Zain na sasa Airtel ulifanyika kwa ukiukwaji mkubwa wa sheria, kanuni na taratibu.
Kufuatia ukiukwaji huo Dkt. Mpango amesema Serikali inayomiliki asilimia 40 ya hisa za kampuni ya Airtel imeamua kufanya mazungumzo na kampuni ya Airtel inayomiliki asilimia 60 ya hisa ili nchi iweze kupata haki yake.
“Lakini niwaambie Watanzania yale ambayo tumeyaona ni machafu sana, ni mambo ya hovyo kabisa, nchi yetu kwa kifupi tuliingizwa mkenge, ni fedha nyingi zimepotea kwa hiyo sisi katika majadiliano haya lengo letu litakuwa ni kuhakikisha Watanzania wanapata haki yao” amesema Dkt. Mpango.
Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli amepokea taarifa ya utekelezaji wa maagizo aliyoyatoa tarehe 25 Novemba, 2017 wakati wa ufunguzi wa Hospitali ya Taaluma na Tiba ya Chuo Kikuu cha Tiba na Sayansi Shirikishi (Mloganzila) kutoka kwa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu.
Baadhi ya maagizo hayo ni kupunguza baadhi ya idara na madaktari katika hospitali ya Taifa Muhimbili na kuhamishia Mloganzila na hospitali za mikoa kuhamishwa kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kwenda Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.
Mhe. Ummy Mwalimu amewasilisha taarifa hiyo akiwa ameongozana na viongozi wakuu wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Taasisi ya Mifupa (MOI), Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKHI), Chuo Kikuu cha Tiba na Sayansi Shirikishi (MUHAS).
Katika hatua nyingine, Waziri wa Katiba na Sheria Prof. Palamagamba Kabudi amekamilisha kanuni za sheria ya madini namba 7 ya mwaka 2017 na kuwasilisha vitabu vya kanuni hizo kwa Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi.
Akiwa na Naibu Mawaziri wa Madini Mhe. Stanslaus Haroon Nyongo na Mhe. Doto Mashaka Biteko, Prof. Kabudi amesema kanuni hizo zimekamilika siku moja kabla ya tarehe ya mwisho iliyotolewa na Mhe. Rais Magufuli na kubainisha kuwa sasa sheria inaweza kuanza kutumika.
Kwa upande wao Naibu Mawaziri wa Madini wamewataka Watanzania na wadau wote wa sekta ya madini kushirikiana na Serikali kutekeleza sheria hiyo na wamempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa kutoa msukumo wa kukamilishwa kwa kanuni hizo.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
11 Januari, 2018
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amemteua Bw. Alphayo Kidata kuwa Balozi.
Taarifa iliyotolewa leo tarehe 11 Januari, 2018 na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi imeeleza kuwa uteuzi wa Bw. Alphayo Kidata umeanza tarehe 10 Januari, 2018.
Kabla ya uteuzi huo, Bw. Alphayo Kidata alikuwa Katibu Mkuu, Ikulu.
Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli amemteua Meja Jenerali Mstaafu Simon Mumwi kuwa Balozi.
Mabalozi hawa wateule watapangiwa vituo vya kazi na kuapishwa baada ya taratibu kukamilika.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
11 Januari, 2018
Taarifa kwa vyombo vya habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 09 Januari, 2018 amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri Mkuu Mstaafu Mhe. Edward Ngoyai Lowassa, Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Baada ya mazungumzo hayo Mhe. Edward Ngoyai Lowassa amempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa kazi nzuri anayoifanya na ametaja baadhi ya maeneo ambayo kazi kubwa imefanyika kuwa ni kutoa elimu bila malipo, ujenzi wa mradi wa uzalishaji wa umeme katika maporomoko ya mto Rufiji (Stiegler’s Gorge), ujenzi wa viwanda na ujenzi wa reli kwa kiwango cha kisasa (Standard Gauge) ambavyo vinazalisha ajira nyingi kwa Watanzania.
“Nimepata faraja sana kuja hapa Ikulu kuonana na Mhe. Rais, tumezungumza nae na nimempongeza kwa kazi nzuri anayoifanya, lazima tukiri anafanya kazi nzuri na anahitaji kutiwa moyo.
“Moja kubwa ambalo ni la msingi sana ni la kujenga ajira, katika kuanza ujenzi wa reli ya kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro hapo anajenga ajira, na kwenye nchi yoyote inayoendelea suala muhimu ni kujenga ajira, Stiegler;s Gorge ni kujenga ajira na mingine ya aina hiyo, lazima kuwepo na kipaumbele cha kusema kwamba tunajenga ajira, jingine ni la elimu, ni muhimu sana, hauwezi kuacha elimu katika mambo yako unayofanya, hili nalo lazima lisemwe vya kutosha, kwa kweli nakushukuru Mhe. Rais, you made my day” amesema Mhe. Lowassa.
Kwa upande wake Mhe. Rais Magufuli amempongeza Mhe. Edward Ngoyai Lowassa kwa kutambua kazi kubwa inayofanywa na Serikali na amesema Mhe. Lowassa ni mmoja wa viongozi ambaye kwa wakati wake ametoa mchango wake katika nchi.
Mhe. Rais Magufuli ameongeza kuwa Mhe. Lowassa ni mwanasiasa mzuri kwani hata wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu uliopita ambao naye aligombea kiti cha Urais, hakuwahi kumtukana.
“Mhe. Lowassa ameniomba mara nyingi nikutane nae, na leo nimekutana nae, tumezungumza mambo mengi, ameniambia ya kwake na mimi nimemwambia ya kwangu, kwa ujumla Mhe. Lowassa ni mwanasiasa mzuri na tuendelee kuwaenzi wazee hawa ambao kwa nyakati fulani walifanya mambo mazuri, na mimi napenda kumpongeza Mhe. Lowassa ambaye kama alivyosema hapa kuwa tumefanya mambo mazuri mengi.
“Ametaja miradi mbalimbali tunayotekeleza, ametaja mradi wa Stiegler’s Gorge utakaogharimu zaidi ya Shilingi Trilioni 7, amezungumzia juu ya elimu bure, amezungumzia juu ya maji ambayo kwa bahati nzuri yeye alikuwa Waziri wa Maji na anafahamu sasa tumefikia wapi, amezungumza juu ya umeme tulivyosambaza katika vijiji mbalimbali, elimu bure, huduma za hospitali na mengine” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
09 Januari, 2018
Taarifa kwa vyombo vya habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 08 Januari, 2018 amemuapisha Mhe. Doto Mashaka Biteko kuwa Naibu Waziri wa Madini na kuiagiza Wizara hiyo kwa kushirikiana na Wizara ya Katiba na Sheria kuhakikisha kanuni za sheria mpya ya madini namba 7 ya mwaka 2017 inasainiwa ifikapo Ijumaa tarehe 12 Januari, 2018.
Mhe. Rais Magufuli ametoa agizo hilo muda mfupi baada ya Mhe. Biteko kuapishwa Ikulu Jijini Dar es Salaam na ameelezea kutoridhishwa kwake na namna viongozi na watendaji wa Wizara ya Madini wanavyotekeleza majukumu yao polepole na bila kujali maslahi ya nchi.
“Sheria hii imepitishwa na Bunge na mimi nikaisaini tangu mwezi wa 7 mwaka 2017, mpaka leo ni miezi 7 bado hamjasaini kanuni zake ili sheria ianze kutekelezwa, na wahusika wote wapo, yaani mpaka leo hamjaelewa Watanzania wanataka nini? amesema Mhe. Rais Magufuli.
Amemuagiza Waziri wa Katiba na Sheria Prof. Palamagamba Kabudi kushirikiana na Naibu Mawaziri, Katibu Mkuu na Wakurugenzi wanaohusika katika Wizara ya Madini kuhakikisha kanuni hizo zinasainiwa.
Pamoja na maagizo hayo Mhe. Rais Magufuli ametengua uteuzi wa Kamishna wa Madini Mhandisi Benjamin Mchwampaka na amemteua Prof. Shukrani Elisha Manya kuwa Kamishna wa Madini na pia kukaimu nafasi ya Mtendaji Mkuu wa Kamisheni ya Madini.
Kabla ya uteuzi huu Prof. Shukrani Elisha Manya alikuwa Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Idara ya Jiolojia.
Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli ameiagiza Wizara ya Kilimo kuhakikisha mbolea inafikishwa katika mikoa yote ya uzalishaji wa chakula ukiwemo mkoa wa Rukwa ifikapo Ijumaa tarehe 12 Januari, 2018.
Mhe. Rais Magufuli amemuelekeza Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa kufuatilia jambo hilo na amebainisha kuwa endapo mbolea haitafikishwa katika maeneo hayo ifikapo Ijumaa wahusika waachie ngazi.
“Wakulima wanataka mbolea na muda ni huu, inasikitisha sana, fedha kwenye bajeti zimetengwa lakini mpaka leo mbolea haijawafikia wakulima, sasa Mkoa kama Rukwa ndio tunaoutegemea kwa chakula, Waziri yupo na watendaji wake wapo lakini mpaka leo mbolea haijapelekwa, wakulima watazalishaje chakula?” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Mhe. Rais Magufuli amewataka watendaji wote wa Serikali kutekeleza majukumu yao ipasavyo na ameonya kuwa hatosita kumfukuza kazi mtendaji yeyote atayeshindwa kutekeleza wajibu wake kwa maslahi ya Watanzania.
“Nataka kila mmoja afanye kazi, Watanzania wanataka maendeleo, hakuna muda wa kubembelezana, kila mmoja afanyie kazi mambo yanayomhusu asisubiri kuambiwa, kule bandarini niliunda timu za kuchunguza madudu yaliyopo huko naambiwa kuna makontena 178 ya makinikia hayana mwenyewe, mengine yapo Ubungo, mengine bandari” ameongeza Mhe. Rais Magufuli.
Mhe. Rais Magufuli amempongeza Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Waheshimiwa Wabunge kwa kazi nzuri wanayoifanya zikiwemo kamati zinazoundwa kuchunguza mambo mbalimbali na amekiri kuwa Bunge limekuwa likiisaidia sana Serikali kukabiliana na changamoto mbalimbali.
Hafla ya kuapishwa kwa Naibu Waziri wa Madini Mhe. Doto Mashaka Biteko imehudhuriwa na Spika wa Bunge Mhe. Job Yustino Ndugai na viongozi mbalimbali wa Wizara na vyombo vya ulinzi na usalama.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
08 Januari, 2018
Taarifa kwa vyombo vya habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 06 Januari, 2018 amewajulia hali baadhi ya wagonjwa waliolazwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete Jijini Dar es Salaam wakiwemo Mzee Kingunge Ngombale Mwiru na Mapacha walioungana Maria na Consolata Mwakikuti.
Katika wodi ya Mwaisela, Mhe. Rais Magufuli amemjulia hali Mzee Kingunge Ngombale Mwiru ambaye anatibiwa majeraha baada ya kushambuliwa na mbwa wake, nyumbani kwake Jijini Dar es Salaam.
Dkt. Ibrahim Mkoma wa hospitali hiyo amemueleza Mhe. Rais Magufuli kuwa hali ya Mzee Kingunge inaendelea vizuri.
Mzee Kingunge amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kwenda kumuona hospitalini hapo na amemueleza kuwa sasa anajisikia nafuu baada ya kupata matibabu.
Pamoja na kumpa pole na kumuombea apone haraka Mhe. Rais Magufuli amesema anatambua mchango mkubwa wa Mzee Kingunge katika siasa na maendeleo ya nchi.
Katika wodi ya Sewahaji, Mhe. Rais Magufuli amemjulia hali Bw. Richard Kajumulo ambaye ni Kaka wa Mbunge wa Muleba Kusini Prof. Anna Kajumulo Tibaijuka, Bw. Said Abeid Salim, Bi. Amina Ismail Shirwa, Mzee Hamad Lila na amempa pole Naibu Katibu Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Dkt. Zainab Chaula aliyefiwa na Mama yake mzazi wakati Mhe. Rais akiwa wodini humo.
Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli amewajulia hali mapacha walioungana Maria na Consolata Mwakikuti ambao wamelazwa katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete kwa matibabu ya moyo.
Maria na Consolata wamemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kwenda kuwaona na kuwapa pole na pia wameongoza sala ya kumuombea Mhe. Rais Magufuli na nchi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete Prof. Mohamed Janabi amesema matibabu kwa Maria na Consolata ambao ni wanafunzi mwaka wa kwanza katika Chuo Kikuu cha Kanisa Katoliki Ruaha (RUCU) yanakwenda vizuri.
Aidha, Prof. Janabi amesema taasisi hiyo imefanikiwa kutoa matibabu kwa wagonjwa wa moyo 14,000 katika mwaka uliopita na kwamba inashika nafasi ya tatu barani Afrika kwa utoaji wa huduma bora za matibabu ya moyo.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli amewashukuru na kuwapongeza madaktari wa hospitali ya Taifa Muhimbili na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete kwa kazi kubwa wanayofanya kutibu wagonjwa na amesema Serikali itaendelea kutatua changamoto zinazowakabili ili kuboresha huduma zaidi.
“Nawashukuru sana madaktari na wafanyakazi wote, mnafanya kazi kubwa ya kuwatibu wagonjwa, pia mmeboresha hospitali na inaonekana ni safi, mimi niwaahidi kuwa Serikali itaendelea kuboresha mazingira yenu ya kazi ili muendelee kutoa huduma nzuri” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
06 Januari, 2018
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 06 Januari, 2018 amemteua Mhe. Doto Mashaka Biteko kuwa Naibu Waziri wa Madini.
Mhe. Doto Mashaka Biteko ni Mbunge wa Jimbo la Bukombe na alikuwa Mwenyekiti wa kamati ya muda iliyochunguza madini ya Tanzanite.
Kufuatia uteuzi huu Wizara ya Madini sasa itakuwa na Waziri na Naibu Mawaziri wawili.
Mhe. Rais Magufuli amefanya uteuzi huu kwa lengo la kuongeza nguvu kutokana na uwingi wa majukumu katika Wizara ya Madini.
Mhe. Doto Mashaka Biteko ataapishwa Jumatatu tarehe 08 Januari, 2018 saa 3:00 asubuhi Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
06 Januari, 2018
Taarifa kwa vyombo vya habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 04 Januari, 2018 amepokea barua kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Uganda Mhe. Yoweri Kaguta Museveni iliyowasilishwa na Mjumbe Maalum Mhe. Sam Kutesa ambaye ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Uganda.
Pamoja na kupokea barua hiyo Mhe. Rais Magufuli amefanya mazungumzo na Mhe. Sam Kutesa, Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Baada ya mazungumzo hayo Mhe. Sam Kutesa amesema Mhe. Rais Museveni amemtumia Mhe. Rais Magufuli na Watanzania wote salamu za heri ya mwaka mpya na pia wamezungumzia masuala yahusuyo uhusiano na ushirikiano kati ya Tanzania na Uganda.
Mhe. Sam Kutesa amesema Uganda inafurahishwa na kuridhishwa na uhusiano na ushirikiano mzuri na wa kidugu uliopo kati yake na Tanzania na kwamba mazungumzo ya leo yalijikita kuuimarisha zaidi kwa manufaa ya wananchi wa nchi zote mbili.
“Tumezungumza namna tutakavyoimarisha na kukuza zaidi uhusiano wetu katika maeneo mbalimbali, kama unavyojua kuna miradi ya maendeleo ya ushirikiano ukiwemo mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi Bandari ya Tanga hapa Tanzania, na miradi mingine na masuala mbalimbali ya ushirikiano” amesema Mhe. Sam Kutesa.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
04 Januari, 2018
Taarifa kwa vyombo vya habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, tarehe 03 Januari, 2018 ameagana na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT) anayemaliza muda wake Prof. Benno Ndulu Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Baada ya mazungumzo yao, Prof. Ndulu amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kumuamini na kufanya nae kazi tangu alipoingia madarakani na amebainisha kuwa anafurahi kumaliza kipindi chake huku uchumi wa nchi ukiwa mzuri.
Prof. Ndulu amempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa miongozo muhimu iliyosaidia kuimarisha uchumi ikiwemo kudhibiti mfumuko wa bei ambao mwezi Novemba 2017 ulifikia asilimia 4.4 na kuongezeka kwa akiba ya fedha za kigeni kutoka Dola za Marekani Bilioni 1.8 hadi kufikia Dola za Marekani Bilioni 6 hivi sasa, hali ambayo imeimarisha uwezo wa Serikali kujiendesha na kugharamia miradi mikubwa ya maendeleo.
“Nimekuja kumuaga Mhe. Rais na kumshukuru, nafurahi kuwa naondoka wakati hali ya uchumi ikiwa nzuri, Taifa linakopesheka na kuna mazingira mazuri zaidi ya uchumi kuendelea kukua, nampongeza sana Mhe. Rais kwa kusimamia mambo mbalimbali muhimu ya kuimarisha na kukuza uchumi katika kipindi chote nilichofanya nae kazi” amesema Prof. Ndulu.
Mhe. Rais Magufuli pia amezungumza na Gavana Mteule Prof. Florens Luoga na baada ya mazungumzo hayo, Prof. Luoga amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa uteuzi huo na kumhakikishia kuwa ataisimamia BOT ili iendelee kuwa chombo imara cha kusimamia uchumi wa nchi, kuisimamia fedha ya Tanzania na kuhakikisha nchi inatekeleza miradi mikubwa ya maendeleo kama vile ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa (Standard Gauge), ujenzi wa uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam na mradi wa umeme katika maporomoko ya maji ya mto Rufiji (Stiegler’s Gorge).
Prof. Luoga ameungana na Prof. Ndulu kueleza kuwa taarifa zinazotolewa na BOT kuhusu ukuaji wa uchumi zinaandaliwa kitaalamu na kwa kushirikisha vyombo mbalimbali vikiwemo Benki ya Dunia (WB) na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na ameonya dhidi ya baadhi ya watu ambao wamekuwa wakipotosha ukweli kuhusu takwimu za uchumi zinazotolewa na BOT.
Kwa upande wake Mhe. Rais Magufuli amempongeza Prof. Ndulu kwa utumishi wake wa miaka 10 na kazi nzuri aliyoifanya kusimamia uchumi ambapo katika kipindi hicho kasi ya ukuaji wa uchumi imeongezeka kutoka wastani wa asilimia 5 hadi kufikia asilimia 7, ameimarisha usimamizi wa benki na maduka ya kubadilishia fedha, amesimamia ongezeko la akiba ya fedha za kigeni inayoiwezesha nchi kumudu kuagiza bidhaa na huduma kwa miezi 6 na kuanza kwa utekelezaji wa miradi mikubwa ya ujenzi wa reli, umeme, ununuzi wa ndege na mingine.
“Nakushukuru sana Prof. Ndulu, umefanya kazi nzuri ya kusimamia uchumi wa Taifa letu, ndio maana leo unamaliza muda wako lakini tayari Benki ya Dunia na kamisheni ya dunia inayoshughulikia teknolojia na maendeleo shirikishi wanakuhitaji ufanye nao kazi, na mimi nimeidhinisha uende ukatuwakilishe” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Mhe. Rais Magufuli amempongeza Gavana Mteule Prof. Luoga kwa kupokea uteuzi wake na amemtaka kufanya kazi ya kusimamia uchumi wa Taifa kwa ufanisi mkubwa zaidi ili nchi ipige hatua za maendeleo kwa kasi zaidi.
Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli amesema mwezi ujao Serikali itatoa Shilingi Bilioni 200 kwa ajili ya kulipa madeni ya ndani yatakayokuwa yamehakikiwa yakiwemo ya wazabuni mbalimbali waliotoa huduma katika taasisi za Serikali, madai ya walimu na madai ya wakandarasi.
“Nasisitiza madeni tutakayolipa ni ya ndani, na tutalipa madeni ambayo yamehakikiwa, kwa hiyo maandalizi ya kutoa fedha hizo yaanze mara moja na ni matarajio yangu fedha hizi zitasaidia kuchochea ukuaji wa uchumi wetu” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
03 Januari, 2018
Taarifa kwa vyombo vya habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 02 Januari 2018 amekutana na Mwanamuziki Nguza Viking na watoto wake waliofika Ikulu Jijini Dar es Salaam kwa lengo la kumshukuru kwa kupatiwa msamaha wa kuachiwa huru kwake Nguza Viking (Babu Seya) na Mwanae Papii Nguza (Papii Kocha) waliokuwa wakitumia adhabu ya kifungo cha maisha jela.
Nguza Viking na Papii Nguza wakiwa na wana familia wengine Nguza Mbangu na Francis Nguza wamezungumza na Mhe. Rais Magufuli ambapo wamemshukuru kwa msamaha alioutoa kwao na kwa wafungwa wengine 61 waliokuwa wamehukumiwa adhabu ya kifo, na wamemuahidi kuwa raia wema na watachapa kazi kwa juhudi na maarifa.
“Yaani sijui nisemaje, hapa nina furaha kubwa sana moyoni mwangu, nilikuwa naomba sana tangu muda mrefu nikutane nae, nimeomba sana sana, hatimaye leo nimefanikiwa na nimemwambia namshukuru sana kwa kutusamehe na sasa nipo tayari kuchapa kazi, Hapa Kazi Tu” amesema Nguza Viking na kuungwa mkono na mwanae Papii Nguza.
Nguza Viking na wanae wamemuombea Mhe. Rais Magufuli na wameiombea nchi, na pia msemaji wa familia hii Nguza Mbangu amesema wanajipanga kuendeleza kazi zao za sanaa.
Kwa upande wake Mhe. Rais Magufuli amewashukuru kwa kuja kumuona na kumshukuru lakini amesema shukrani zimwendee Mwenyezi Mungu ambaye ndiye husamehe.
“Najua mmekuwa mkihangaika kutaka kuniona, nikaona wacha niwasikilize, hata hivyo mshukuruni Mwenyezi Mungu ambaye ndiye hutoa msamaha, sasa nendeni mkachape kazi, na mmtangulize Mungu” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli ametia saini kitabu cha maombolezo na kumpa pole Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Kangi Alphaxard Lugola aliyefiwa na Mkewe Kamishna Msaidizi wa Polisi Mary Lugola.
Kamishna Msaidizi wa Polisi Mary Lugola amefariki dunia jana asubuhi tarehe 01 Januari, 2018 katika hospitali ya Rabinisia iliyopo Jijini Dar es Salaam alikokuwa akipatiwa matibabu na msiba upo Gerezani Railway Club Jijini Dar es Salaam.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasilino ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
02 Januari, 2018
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
"Nimepokea kwa mshtuko na masikitiko makubwa taarifa za kutokea kwa ajali iliyosababisha ndugu zetu takribani 36 kupoteza maisha baada ya basi la abiria kugongana na roli katika barabara ya Nakuru - Eldoret nchini Kenya.
Msiba huu umesababisha majonzi makubwa sio tu kwa ndugu zetu wa Kenya bali pia kwetu sote wana Jumuiya ya Afrika Mashariki, tumepoteza wapendwa wetu na nguvu kazi yetu.
Kwa niaba ya Watanzania wote nakupa pole sana ndugu yangu Mhe. Uhuru Kenyatta, Rais wa Jamhuri ya Kenya kwa msiba huu mkubwa ulioupata, nawapa pole wana familia wote waliowapoteza jamaa zao na pia nawapa pole wananchi wote wa Kenya.
Naungana nanyi katika kipindi hiki kigumu cha majonzi, nawaombea majeruhi wote wa ajali hii wapone haraka na Marehemu wote wapumzishwe mahali pema peponi, Amina".
Hizi ni salamu za rambirambi alizozitoa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kwa Rais wa Jamhuri ya Kenya Mhe. Uhuru Kenyatta kufuatia ajali ya barabarani iliyosababisha vifo vya watu takribani 36 baada ya basi la abiria kugongana na roli katika barabara ya Nakuru - Eldoret nchini humo leo tarehe 31 Desemba, 2017.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
31 Desemba, 2017
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 28 Desemba, 2017 amekutana kwa mara ya kwanza na kamati maalum aliyoiunda kwa lengo la kuhakiki mali za chama hicho, Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Kamati hiyo aliitangaza tarehe 20 Desemba, 2017 Mkoani Dodoma na inaongozwa na Dkt. Bashir Ally.
Katika Mazungumzo hayo Mhe. Rais Magufuli amewataka wajumbe wa kamati hiyo kufuatilia na kuhakiki mali zote za chama, kumhoji mtu yeyote ambaye atahitajika kutoa taarifa juu mali za chama na kubaini thamani ya mali, mahali zilipo, makusanyo ya mapato na wanaozishikilia ama kutumia mali hizo.
Mhe. Rais Magufuli pia ametoa wito kwa wanachama wa CCM na wananchi wengine kutoa ushirikiano kwa kutoa taarifa zote zinazohusu mali za chama kwa kamati hiyo, na watakaoitwa kuhojiwa waitikie wito huo.
“Nataka mali za chama zikinufaishe chama, nataka mkamhoji mtu yeyote, awe kiongozi, awe mwanachama, awe mfanyabiashara, mtu yeyote. Mkazihakiki mali zote ili chama kipate haki yake” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Akizungumza kwa niaba ya kamati hiyo, Dkt. Bashiru Ally amesema kamati imeanza kazi rasmi na ametoa wito kwa wanachama, wananchi na wote wanaozitumia mali za chama kutoa ushirikiano watakapoitwa kuhojiwa.
“Tumezungumza na Mwenyekiti kwa karibu saa mbili, katueleza matarajio yake, sababu za kuunda tume hii, kazi zake na faida zake kwa chama na kwa nchi, kwa hiyo ametukabidhi vitendea kazi na taarifa mbalimbali na ametueleza kazi yetu ni kuhakiki mali zote za chama kwa kushirikiana na wanachama na wale wanaoshirikiana na chama kuzitumia hizo mali kama vile wapangaji, wasimamizi, nakadhalika” amesema Dkt. Bashiru Ally.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
28 Desemba, 2017
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 28 Desemba, 2017 amewasilisha fomu yake ya tamko kuhusu rasilimali na madeni katika ofisi ya Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma iliyopo Mtaa wa Ohio, Wilaya ya Ilala Jijini Dar es Salaam.
Baada ya kuwasilisha fomu hiyo Mhe. Rais Magufuli ameipongeza Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kwa kazi inazofanya na amemtaka Kamishna wa Maadili Jaji Mstaafu Harold Nsekela kutopokea fomu ya kiongozi yeyote ambaye atakuwa hajawasilisha tamko lake ifikapo tarehe 31 Desemba, 2017.
“Mhe. Jaji Nsekela ikifika tarehe 31 Desemba, ambayo ni siku ya mwisho kwa Mujibu wa Sheria, weka mstari na usipokee fomu zingine, halafu tuone sheria itafanyaje, nakutakia kazi njema” amesisistiza Mhe. Rais Magufuli.
Kwa upande wake Mhe. Jaji Mstaafu Harold Nsekela amemshukuru na kumpongeza Mhe. Rais Magufuli kwa kutekeleza matakwa ya kisheria yanayomlazimu kujaza fomu hizo na amesisitiza kuwa ujazaji wa fomu hizo kwa viongozi wa umma sio ombi.
“Viongozi hawaombwi kujaza fomu hizi, kuna baadhi wanadhani labda kutuletea hilo tamko ni fadhila, hapana, sheria ya nchi inahitaji hivyo na kuna sababu zake za msingi” amesema Mhe. Jaji Mstaafu Nsekela.
Aidha, Mhe. Jaji Mstaafu Nsekela amempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa kuwasilisha taarifa ya akaunti yake ya benki sambamba na tamko hilo, na amekiri kuwa ameonesha mfano wa kuigwa na viongozi wengine.
Tamko la viongozi wa umma kuhusu rasilimali na madeni linatolewa kwa mujibu wa kifungu cha 9 na cha 11 cha sheria ya maadili ya viongozi wa umma namba 13 ya mwaka 1995.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
28 Desemba, 2017
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amewataka Watanzania na taasisi mbalimbali kutumia takwimu sahihi zinazotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu na kujiepusha na takwimu za upotoshaji zinazosambazwa na baadhi ya watu kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.
Mhe. Rais Magufuli amesema hayo tarehe 20 Desemba, 2017 katika hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi la jengo la Ofisi ya Taifa ya Takwimu inayojengwa katika eneo la Makulu Mjini Dodoma.
Pamoja na wito huo Mhe. Rais Magufuli ameitaka Ofisi ya Taifa ya Takwimu pamoja na vyombo vingine husika kuchukua hatua za kisheria dhidi ya mtu yeyote ama taasisi itakayotoa takwimu za upotoshaji.
“Kwa hiyo ndugu zangu Watanzania tumieni takwimu sahihi kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu, puuzeni takwimu za kupika zinazotolewa na baadhi ya watu kwenye mitandao, wapuuzeni hata wanaosema vyuma vimebana, vyuma vimebana kwa wanaotaka vya bure lakini wanaochapa kazi vyuma havijabana” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Amebainisha kuwa uchumi wa Tanzania unakwenda vizuri ambapo katika nusu ya kwanza ya mwaka huu umekua kwa asilimia 6.8, mfumuko wa bei umeshuka hadi asilimia 4.4 kwa mwezi Novemba 2017 na akiba ya fedha za kigeni imefikia Dola za Marekani Bilioni 5.82 ambayo inaiwezesha nchi kununua bidhaa na huduma kwa miezi mitano, ikilinganishwa na wastani unaopaswa wa miezi miezi 4.
Mhe. Rais Magufuli ameongeza kuwa Serikali imeendelea kufanya mambo makubwa ya maendeleo ya nchi ikiwemo ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa (Standard Gauge) kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma utakaogharimu Shilingi Trilioni 7.6, kutoa fedha za dawa ambazo zimeongezeka kutoka Shilingi Bilioni 31 hadi 269, kutoa Shilingi Bilioni 23.876 kwa ajili ya elimu bila malipo kwa shule za msingi na sekondari kila mwezi, mradi wa kuzalisha umeme katika maporomoko ya mto Rufiji (Stiegler’s Gorge), kuongeza mikopo ya wanafunzi wa vyuo vikuu kutoka Shilingi Bilioni 373 hadi Shilingi Bilioni 483 na mengine mengi.
“Hizi ndio takwimu sahihi, na nyinyi Ofisi ya Taifa ya Takwimu mkiona mtu anapotosha ukweli huu mkamateni mpelekeni mahakamani akajifunze kupata takwimu sahihi”
“Haya tunayoyafanya wale ambao walikuwa wanapata fedha za bure lazima watapiga kelele kuwa vyuma vimebana, lakini tunabana vya bure ili kuwaletea wananchi maendeleo, na kwa kweli tutabana sana” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Mhe. Rais Magufuli amempongeza Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Dkt. Albina Chuwa na wafanyakazi wote wa ofisi hiyo kwa kazi nzuri wanayoifanya na pia ameishukuru Benki ya Dunia, Shirika la Maendeleo la Uingereza (DFID) na Shirika la Maendeleo la Canada kwa ufadhili wake waliowezesha kujengwa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Mjini Dodoma na Ofisi nyingine iliyojengwa Zanzibar pamoja na kusaidia shughuli nyingine za Ofisi hiyo.
Ujenzi wa jengo la Ofisi ya Taifa ya Takwimu Mjini Dodoma lenye ghorofa nne na ukubwa mita za mraba 7,100 ulianza Machi 2017 na unatarajiwa kukamilika Januari 2018 kwa gharama ya Shilingi Bilioni 11.6.
Katika taarifa yake kwa Mhe. Rais Magufuli Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Dkt. Albina Chuwa amesema kwa kutambua umuhimu wa takwimu katika kupanga, kutekeleza na kusimamia masuala mbalimbali ya maendeleo na ustawi wa jamii, ofisi yake imepiga hatua kubwa katika ukusanyaji na utoaji wa takwimu bora na hivyo kuiwezesha kushika nafasi ya pili barani Afrika ikitanguliwa na Ofisi ya Takwimu ya Afrika Kusini.
Hafla hiyo imehudhuriwa na Mke wa Rais Mhe. Mama Janeth Magufuli, Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, Mawaziri, Naibu Mawaziri na Makatibu Wakuu, Mabalozi, Mwakilishi wa Benki ya Dunia kwa nchi za Tanzania, Burundi, Malawi na Somalia Bi. Bella Bird na viongozi mbalimbali wa mkoa wa Dodoma wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa Dkt. Binilith Mahenge.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dodoma
20 Desemba, 2017