Taarifa kwa vyombo vya Habari ya zamani
Taarifa kwa vyombo vya habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 01 Aprili, 2018 ameungana na Wakristo wote Tanzania katika maadhimisho ya Misa Takatifu ya sikukuu ya Pasaka iliyofanyika katika Kanisa la Mtakatifu Joseph, Jimbo Kuu la Dar es Salaam.
Misa hiyo imeongozwa na Paroko Msaidizi wa Parokia ya Mtakatifu Joseph Padre Venance Tegete.
Akizungumza baada ya kukaribishwa na Padre Tegete kutoa salamu, Mhe. Rais Magufuli amewatakia Watanzania wote heri ya Pasaka na ametoa wito kwa Watanzania kuendelea kuishi kwa amani na upendo huku wakishiriki ipasavyo katika ujenzi wa Taifa.
“Kifo na ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo ukafufue matendo yetu, tuendelee kuijenga amani yetu, upendo wetu na tujenge maendeleo ya Watanzania wote, kwani Kristo alifundisha upendo miongoni mwetu.
“Kwa hiyo Baba nakushukuru sana kwa kuongoza Misa hii, naomba ufikishe shukrani zangu kwa Kardinali Pengo, Maaskofu wote na Watanzania wote tuendelee kusimama pamoja ili kulijenga Taifa letu” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Mhe. Rais Magufuli aliongozana na Mkewe Mhe. Mama Janeth Magufuli.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU.
Dar es Salaam
01 Aprili, 2018
Taarifa kwa vyombo vya habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 27 Machi, 2018 amepokea ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha wa 2016/17
Tukio la kukabidhiwa kwa ripoti hiyo limefanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, Naibu Spika Mhe. Dkt. Tulia Ackson, Mawaziri, wenyeviti wa kamati nne za Bunge, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT) Prof. Florens Luoga na viongozi wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama.
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Prof. Mussa Juma Assad amewasilisha kwa Mhe. Rais Magufuli ripoti 6 ambazo ni ripoti ya Serikali Kuu, ripoti ya Mamlaka za Serikali za Mitaa, ripoti ya Mashirika ya Umma, ripoti ya miradi ya maendeleo, ripoti ya Ukaguzi na Ufanisi na ripoti 10 zinazohusu ukaguzi wa ufanisi katika sekta mbalimbali.
Akitoa mchanganuo wa hati za ukaguzi wa hesabu katika Serikali Kuu na taasisi zake, Mamlaka za Serikali za Mitaa na Mashirika ya Umma kwa mwaka 2016/17 Prof. Assad amesema ofisi yake imetoa jumla ya hati 561 ambapo kati yake hati 502 sawa na asilimia 90 zinaridhisha, hati 45 sawa na asilimia 8 zina mashaka, hati 7 sawa na asilimia 1 haziridhishi na hati 7 sawa na asilimia 1 ni mbaya.
Prof. Assad amesema kwa ujumla Serikali imeendelea kufanya vizuri kwani kumekuwa hatua nzuri zaidi ya kuongeza hati zinazoridhisha na kupunguza hati za mashaka na mbaya.
Amebainisha kuwa Mashirika ya Umma yamepata hati safi kwa asilimia 96, Mamlaka ya Serikali za Mitaa asilimia 90 na Serikali Kuu ambayo imepata asilimia 86 kutokana na ndani yake kuwemo vyama vya siasa 7 ambavyo hakukua na makubaliano juu hesabu zake.
Kufuatia ripoti hiyo Mhe. Rais Magufuli amemuagiza Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Selemani Jafo kuwasimamisha kazi Wakurugenzi wa Halmashauri 3 za Kigoma-Ujiji, Kigoma Vijijini na Pangani kutokana na halmashauri zao kupata hati chafu na ameahidi kuwa Serikali itafanyia kazi ripoti hizo na kuchukua hatua stahiki.
Kuhusu kesi za rufaa ya kodi zenye thamani ya Shilingi Trilioni 4.4 ambazo mpaka sasa hazijafanyiwa uamuzi na Mahakama, Mhe. Rais Magufuli amemuagiza Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango kujadiliana na Jaji Mkuu ili kesi hizo ziamliwe haraka.
Baada ya kupokea ripoti hizo Mhe. Rais Magufuli amemkabidhi Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa na kumuagiza aitishe kikao cha Mawaziri wote ili wazijadili na kutafuta majawabu ya hoja zilizomo.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli amempongeza Prof. Mussa Juma Assad na ofisi yake kwa kazi nzuri ya ukaguzi wa hesabu za Serikali na amemhakikishia kuwa ushauri na mapendekezo yote yaliyotolewa katika ripoti hiyo yatafanyiwa kazi.
Katika salamu zao Wenyeviti wa Kamati za Kudumu za Bunge za Hesabu za Serikali (PAC), Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) na Bajeti wamempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa juhudi mbalimbali anazozifanya kuwaletea Watanzania maendeleo na wamemhakikishia kuwa wataendelea kuunga mkono juhudi hizo kwa kushauri na kuisimamia Serikali.
Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa amewahakikishia Wenyeviti hao wa Bunge kuwa Serikali itafanyia kazi ushauri walioutoa ikiwemo kuteua na kuthibitisha uteuzi wa viongozi mbalimbali wa bodi na taasisi, na kuchukua hatua dhidi ya watendaji wenye dosari.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
27 Machi, 2018
Taarifa kwa vyombo vya habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amezindua magari mapya 181 ya bodi ya dawa (MSD) yatakayotumika kusambaza dawa na vifaa tiba hapa nchini.
Sherehe za uzinduzi wa magari hayo zimefanyika tarehe 26 Machi, 2018 Makao Makuu ya MSD Keko Mwanga Jijini Dar es Salaam ambapo pamoja na kuzindua magari Mhe. Rais Magufuli amekagua bohari ya dawa na kuzungumza na wananchi.
Magari yaliyozinduliwa yamejumuisha magari madogo 104 (aina ya Toyota Land Cruiser) na malori makubwa na madogo 77 (aina ya Man) yenye uwezo wa kuchukua kati ya tani 5.5 na 15 kila moja, yote yakiwa na thamani ya Shilingi Bilioni 20.75 na yametolewa kwa msaada kutoka Mfuko wa Dunia wa Kupambana na UKIMWI, Kifua Kikuu na Malaria (Global Fund).
Mkurugenzi Mkuu wa MSD Bw. Laurean Rugambwa Bwanakunu ameeleza kuwa upatikanaji wa magari hayo utasaidia usambazaji wa dawa wa moja kwa moja kuanzia ngazi ya vijiji kila baada ya miezi miwili, utaokoa fedha nyingi zilizokuwa zikitumika kukodi magari na utapunguza tatizo la dawa kuisha muda wake.
“Watu watajiuliza, kwa nini tumepewa msaada wa magari yote haya 181, wengine watajiuliza hawa Global Fund wana mapenzi gani na MSD au Serikali? Jibu ni hawa wana imani na mapenzi na Serikali unayoiongoza wewe Mhe. Rais kwa sababu ya umakini wake” amesema Bw. Bwanakunu.
Ameongeza kuwa tangu taasisi hiyo ianze kutekeleza maagizo ya Mhe. Rais Magufuli hivi sasa inahudumia vituo 7,309 katika kanda zake 10, na kwamba kupitia maduka 7 ya kuwauzia dawa wananchi moja kwa moja, imeshauza dawa zenye thamani ya Shilingi Bilioni 12.6 zikiwa na bei nafuu iliyopungua kwa wastani wa asilimia 40.
Mwakilishi wa Mtendaji Mkuu wa Global Fund Bw. linden Morrison ameipongeza Serikali kwa usambazaji mzuri dawa na vifaa tiba kupitia MSD na amesema mpaka sasa mfuko huo umetumia Dola za Marekani zaidi ya Bilioni 2 (Sawa na takribani Shilingi Trilioni 4.5 za Tanzania) kupambana na UKIMWI, Kifua Kikuu na Malaria hapa nchini zikiwemo Dola Milioni 595 (Sawa na takribani Shilingi Trilioni 1.3 za Tanzania) zilizotolewa Januari 2018 kuendeleza mapambano dhidi ya magonjwa hayo.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa namna alivyotilia mkazo uboreshaji wa huduma za afya hapa nchini kwa kuongeza bajeti hadi kufikia Shilingi Trilioni 2.2, na matokeo yake hatua kubwa imepigwa katika kuboresha huduma za matibabu ya kibingwa ikiwemo kuanza kupandikiza vifaa vya usikivu, kupandikiza figo na upasuaji wa moyo, na kwamba asilimia 42 ya fedha za dawa zinapeleka dawa moja kwa moja katika zahanati na vituo vya afya na hivyo kuwafikia wananchi wengi vijijini.
Katika hotuba yake Mhe. Rais Magufuli ameishukuru Global Fund kwa kutoa magari hayo na kwa kuwa mdau muhimu katika mapambano dhidi ya UKIMWI, Kifua Kikuu na Malaria na pia ameipongeza MSD kwa kazi nzuri ya usambazaji wa dawa.
Hata hivyo Mhe. Rais Magufuli ametoa changamoto kwa MSD, wataalamu wa afya na wafanyabiashara kujenga viwanda vya kutengeneza dawa na vifaa tiba ili Mabilioni ya fedha zinazotengwa kwa ajili ya ununuzi wa dawa na vifaa hivyo zizalishe ajira na dawa za gharama nafuu kutoka viwanda vya hapahapa nchini, badala ya kupelekwa kwenye viwanda nje ya nchi.
“Inauma sana Shilingi Bilioni 500 za Global Fund na fedha za bajeti tulizotenga shilingi Bilioni 269, kwa asilimia 96 zinakwenda nje ya nchi kununua dawa na vifaa tiba, sisi tunabaki na asilimia 4 tu, ndio maana nawaomba wasomi, MSD na hata wafanyabiashara waaminifu mjenge viwanda vya dawa hapahapa” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli ameitaka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kufuatilia utendaji kazi wa kiwanda cha dawa cha Keko Pharmaceuticals ili kama mwekezaji wake ameshindwa wapewe wenye uwezo wa kukiendesha na pia ameionya Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) dhidi ya ucheleweshaji katika ukaguzi wa dawa bandarini.
Sherehe hizo zimehudhuriwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Bw. Paul Makonda, Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile, Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Josephat Kandege na Wabunge.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
26 Machi, 2018
Taarifa kwa vyombo vya habari
“Nimesikitishwa sana na taarifa ya vifo vya watu 26 waliopoteza maisha katika ajali ya barabarani iliyotokea huko Mkuranga Mkoani Pwani, tumepoteza idadi kubwa ya Watanzania wenzetu na nguvu kazi ya Taifa.
“Naungana na wafiwa wote katika kipindi hiki kigumu cha huzuni na majonzi ya kuondokewa na wapendwa wao na watu waliowategemea”
Ni sehemu ya salamu za rambirambi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli alizozituma kwa Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo kufuatia vifo vya watu 26 vilivyotokea tarehe 24 Machi, 2018 saa 3 usiku, baada ya basi dogo (Hiace) lililokuwa limebeba abiria kugongana na lori lililokuwa limebeba chumvi katika kijiji cha Mparange Wilaya ya Mkuranga Mkoani Pwani.
Basi hilo lilikuwa linatoka Mkuranga kuelekea Kimanzichana wakati lori lilikuwa linatoka Lindi kuelekea Dar es Salaam.
Mhe. Rais Magufuli amemtaka Mhandisi Evarist Ndikilo kumfikishia salamu za pole kwa familia za marehemu, ndugu, jamaa, marafiki na wote walioguswa na vifo hivyo na pia amevitaka vyombo vinavyoshughulikia usalama wa barabarani kuchunguza chanzo cha ajali hiyo na kuchukua hatua zinazostahili.
Amewaombea marehemu wote wapumzishwe mahali pema na majeruhi 9 wa ajali hiyo wapone haraka ili waungane na familia na jamaa zao kuendelea na shughuli za kila siku.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
25 Machi, 2018
Taarifa kwa vyombo vya habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amefanya uteuzi wa Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Nguvu za Atomiki (TAEC), Mkurugenzi wa Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC), Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Benjamin Mkapa – Dodoma na Mwenyekiti wa Bodi ya Hospitali ya Benjamini Mkapa - Dodoma.
Taarifa iliyotolewa tarehe 23 Machi, 2018 na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi imeeleza kuwa Mhe. Rais Magufuli amemteua Prof. Lazaro S.P. Busagala kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Nguvu za Atomiki (TAEC) kuanzia tarehe 22 Machi, 2018.
Kabla ya uteuzi huo Prof. Busagala alikuwa Makamu Mkuu wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) – Taaluma na Utafiti.
Mhe. Rais Magufuli amemteua Prof. Damian Gabagambi kuwa Mkurugenzi wa Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) kuanzia tarehe 22 Machi, 2018.
Prof. Gabagambi anachukua nafasi ya Bw. Mlingi Elisha Mkucha ambaye atapangiwa kazi nyingine.
Kabla ya uteuzi huo Prof. Gabagambi alikuwa Mhadhiri wa Uchumi wa Chuo Kikuu cha Kilimo – Sokoine (SUA).
Mhe. Rais Magufuli amemteua Dkt. Deodatus Michael Mutasiwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Hospitali ya Benjamin Mkapa – Dodoma.
Mhe. Rais Magufuli amemteua Dkt. Alphone Bilola Chandika kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Benjamin Mkapa – Dodoma.
Kabla ya Uteuzi huu Dkt. Chandika alikuwa akikaimu nafasi hiyo.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
23 Machi, 2018
Taarifa kwa vyombo vya habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 22 Machi, 2018 amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Ulinzi wa Israel Mhe. Avigdor Lieberman Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Mazungumzo hayo yamehudhuriwa na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Dkt. Hussein Ali Mwinyi, Balozi wa Israel hapa nchini Mhe. Noah Gal Gendler, viongozi wakuu wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ) na Jeshi la Polisi.
Katika mazungumzo hayo Mhe. Rais Magufuli amemshukuru Mhe. Lieberman kwa kuitembelea Tanzania na amemhakikishia kuwa Serikali ya Awamu ya Tano ina dhamira ya dhati ya kuukuza zaidi na kuuimarisha uhusiano na ushirikiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na Israel.
Mhe. Rais Magufuli ametaka makubaliano ya ushirikiano kati ya Tanzania na Israel katika maeneo mbalimbali yakiwemo ulinzi na usalama, mafunzo na masuala ya kiuchumi yatiwe saini haraka ili utekelezaji uanze mara moja.
“Tanzania na Israel ni marafiki wa miaka mingi, nataka kuona urafiki wetu unakuwa zaidi, nawakaribisha wawekezaji kutoka Israel kuja kuwekeza katika kilimo, madini na gesi na pia kuwepo ndege za moja kwa moja kutoka Israel hadi Dar es Salaam na Kilimanjaro ili kukuza utalii” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli amemuomba Mhe. Lieberman kumfikishia ujumbe Waziri Mkuu wa Israel Mhe. Benjamin Netanyahu wa kumualika kutembelea Tanzania na pia kuanzisha ofisi ya ubalozi hapa nchini badala ya kutumia ofisi za ubalozi zilizopo Nairobi nchini Kenya.
Kwa upande wake Mhe. Avigdor Lieberman amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kumkaribisha na kufanya nae mazungumzo na pia amemhakikishia kuwa Israel imejipanga kuongeza uhusiano na ushirikiano wake na Tanzania katika maeneo yote ya makubaliano pamoja na kusaidia kilimo na usindikaji wa chakula.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
22 Machi, 2018
Taarifa kwa vyombo vya habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 21 Machi, 2018 amewaapisha Meja Jenerali Mstaafu Simon Marco Mumwi kuwa Balozi wa Tanzania nchini Urusi na IGP Mstaafu Ernest Jumbe Mangu kuwa Balozi wa Tanzania nchini Rwanda.
Hafla ya kuwaapisha Mabalozi hao imefanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan.
Akizungumza baada ya kuapishwa Mhe. Balozi Mumwi amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa uteuzi huo na ameahidi kuwa katika kipindi chake atahakikisha uhusiano na ushirikiano kati ya Tanzania na Urusi unaimarishwa na Tanzania inanufaika na uhusiano huo hususani katika azma yake ya kuvutia uwekezaji katika viwanda.
Kwa upande wake Mhe. Balozi Mangu pamoja na kumshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kumuamini ameahidi kuongeza msukumo katika utekelezaji wa ajenda muhimu za maendeleo kati ya Tanzania na Rwanda hususani ujenzi na manufaa ya mradi mkubwa wa reli ya kati utakaoiunganisha bandari ya Dar es Salaam na nchi nne za magharibi mwa Tanzania ikiwemo Rwanda.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika ya Mashariki Dkt. Susan Kolimba amewapongeza Mabalozi hao kwa kuteuliwa kuiwakilisha Tanzania nchini Urusi na Rwanda na ameahidi kuwa wizara hiyo itakuwa tayari wakati wote kutoa ushirikiano ili kufanikisha utekelezaji wa majukumu yao ikiwemo diplomasia ya uchumi.
Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan amewataka Mabalozi hao kufuatilia na kusimamia kwa ukaribu makubaliano mbalimbali ambayo Tanzania na nchi hizo wameyafikia ikiwemo miradi ya maendeleo.
Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli amekutana na Mtendaji Mkuu wa kampuni ya Millicom International Services LLC inayomiliki kampuni ya simu za mkononi ya Tigo Bw. Mauricio Ramos, Ikulu Jijini Dar es Salaam ambapo wamezungumza kuhusu uwekezaji wa kampuni hiyo hapa nchini.
Baada ya mazungumzo hayo Bw. Mauricio Ramos amesema amekuja kumweleza Mhe. Rais Magufuli kuhusu maendeleo ya kampuni hiyo ambayo imewekeza Dola za Marekani zaidi ya Bilioni 1 (sawa na zaidi ya Shilingi Trilioni 2.23 za Tanzania) katika miaka mitano iliyopita, imeajiri wafanyakazi zaidi ya 90,000 na kuwafikishia mawasiliano Watanzania kwa takribani asilimia 90.
Bw. Mauricio Ramos amempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa jitihada zake za kupambana na rushwa na amebainisha kuwa juhudi hizo ni muhimu katika kuharakisha maendeleo na kupunguza umasikini.
Nae Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa Mnyaa amesema kampuni ya simu za mkononi ya Tigo ni ya pili kwa ukubwa hapa nchini ikiwa na wateja Milioni 11.06 na imekuwa ikilipa vizuri kodi ambapo mwaka 2017 ililipa kiasi cha Shilingi Bilioni 262.77.
Katika hatua nyingine, Mhe. Rais Magufuli amekutana na watendaji wakuu wa kampuni ya Ferrostaal kutoka nchini Ujerumani na Denmark na Watendaji wakuu wa taasisi zilizo chini ya Wizara ya Fedha na Mipango na Wizara ya Nishati, ambapo wamejadili kuhusu mradi wa ujenzi wa kiwanda cha kuzalisha mbolea Mkoani Lindi.
Mazungumzo hayo yamehudhuriwa na Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mhe. Charles Mwijage, Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Medard Kalemani na Balozi wa Denmark hapa nchini Mhe. Einar Hebogard Jensen.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
21 Machi, 2018
Taarifa kwa vyombo vya habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ametengua uteuzi wa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Nyumba la Taifa (National Housing Corporation - NHC) Bi. Blandina Nyoni kuanzia tarehe 21 Machi, 2018.
Pia Mhe. Rais Magufuli ameivunja Bodi ya NHC kuanzia leo.
Uteuzi wa Mwenyekiti na bodi nyingine utafanyika baadaye.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
21 Machi, 2018
Taarifa kwa vyombo vya habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 21 Machi, 2018 atawaapisha Mabalozi Wateule wawili aliowateua kuiwakilisha Tanzania katika nchi za Rwanda na Urusi.
Taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi imeeleza kuwa Mhe. Rais Magufuli atamuapisha IGP-Mstaafu Ernest Jumbe Mangu kuwa Balozi wa Tanzania nchini Rwanda na Meja Jenerali Mstaafu Simon Marco Mumwi kuwa Balozi wa Tanzania nchini Urusi.
Hafla ya kuapishwa kwa Mabalozi Wateule hao itafanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam kuanzia saa 5:00 asubuhi.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
20 Machi, 2018
Taarifa kwa vyombo vya habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ametoa wiki moja kuanzia tarehe 19 Machi, 2018 kwa Mawaziri kufanyia kazi na changamoto na maoni yaliyotolewa na wafanyabiashara katika mkutano wa 11 wa Baraza la Taifa la Biashara uliofanyika leo Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Mhe. Rais Magufuli ambaye ni Mwenyekiti wa baraza hilo ametoa maagizo hayo wakati akihitimisha mkutano huo ambao wafanyabiashara na wawekezaji kutoka sekta mbalimbali wamepata nafasi ya kueleza maendeleo ya shughuli zao, changamoto zinazowakabili na mapendekezo ya kuimarisha biashara na uwekezaji hapa nchini.
Miongoni mwa changamoto hizo ni utozaji wa kodi unaoathiri biashara na uwekezaji, urasimu wa taasisi za Serikali, udhibiti wa bidhaa za kutoka nje ya nchi zinazoathiri uzalishaji wa bidhaa za ndani, uwepo wa sheria na kanuni kandamizi kwa biashara na uwekezaji na utendaji usioridhisha kwa baadhi ya maafisa wa Serikali.
Mhe. Rais Magufuli amewataka Mawaziri kuandika maelezo yenye majibu ya changamoto na maoni hayo na kuwasilisha kwa Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa ndani ya kipindi cha wiki moja ili Serikali ifanyie kazi na kuimarisha mazingira ya biashara na uwekezaji hapa nchini.
Mhe. Rais Magufuli amewapongeza wafanyabiashara hao kwa mchango mkubwa wanaoutoa katika uchumi wa nchi na amewahakikishia kuwa Serikali itaendelea kuwapa ushirikiano wowote watakaouhitaji hususani katika ujenzi wa viwanda.
“Nataka kuwaambia kwa dhati kabisa, Serikali ninayoiongoza haiwachukii wafanyabiashara, inawapenda na itawaunga mkono, kama nilivyowaambia huko nyuma huu ndio wakati wenu wa kufanya biashara, fanyeni biashara zenu na lipeni kodi, hizi changamoto tumezipokea na tutazifanyia kazi” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli ametoa wito kwa wafanyabiashara hao kuhakikisha wanashiriki katika miradi mikubwa anayotekelezwa na Serikali ikiwemo ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa (Standard Gauge), mradi wa umeme katika maporomoko ya mto Rufiji (Stieglers’ Gorge), mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta la kutoka Hoima - Uganda hadi bandari ya Tanga - Tanzania, na amewataka wafanyabiashara wanaofanya vitendo vya udanganyifu katika kodi na uingizaji wa bidhaa wabadilike.
Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa maelekezo yake ya kutaka utozaji wa kodi uangaliwe ili usiathiri shughuli za uwekezaji na uzalishaji, na amewataka wafanyabiashara kuendelea kufanya shughuli zao kwa amani kwa kuwa Serikali itaendelea kuwalinda.
Mapema Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) Dkt. Reginald Mengi amepongeza juhudi mbalimbali zinazofanywa na Serikali kuimarisha uwekezaji zikiwemo kuimarishwa kwa sekta ya fedha, usimamizi mzuri wa uchumi na kuongezeka kwa mikopo.
Dkt. Mengi ametoa mapendekezo ya sekta binafsi yakiwemo kuiwezesha zaidi sekta binafsi ili iongeze uzalishaji na ulipaji wa kodi, kuweka vivutio vya kodi katika viwanda, kuimarisha miundombinu na vivutio vya kilimo, kupunguza urasimu katika uwekezaji, kuwepo mifumo ya kisasa ya ukusanyaji wa kodi na kuboresha utendaji wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
19 Machi, 2018
Taarifa kwa vyombo vya habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 19 Machi, 2018 amekutana na Rais wa Kanda ya Afrika wa kampuni ya vinywaji ya AB-INBEV inayomiliki asilimia 57.5 ya hisa za kampuni ya bia Tanzania (TBL) Bw. Ricardo Tadeu.
Katika mazungumzo hayo Bw. Ricardo Tadeu amempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa kusimamia vizuri uwekezaji hapa nchini, na kumueleza kuwa uzalishaji katika TBL kuanzia mwaka 2015 hadi sasa, umeendelea kukua na kwamba kampuni hiyo inatarajia kupanua uwekezaji kwa kujenga kiwanda kingine cha kuzalisha bia Mkoani Dodoma ambapo Dola za Marekani Milioni 100 zitawekezwa.
Bw. Ricardo Tadeu amemhakikishia Mhe. Rais Magufuli kuwa kampuni hiyo itaendelea kuwa mlipaji mzuri wa kodi kama ambavyo imekuwa ikifanya na kuongeza ajira kupitia kwa wakulima wanaozalisha mazao ya ngano, mtama na mahindi ambayo hutumika kutengenezea vinywaji.
Mhe. Rais Magufuli amemhakikishia Bw. Ricardo Tadeu kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na TBL na ameipongeza kwa kuwa mlipaji kodi mzuri na kwa uamuzi wake wa kujenga kiwanda cha kuzalisha bia mkoani Dodoma, kitakachoungana na viwanda vingine vilivyopo Dar es Salaam, Mbeya, Mwanza na Arusha.
Mhe. Rais Magufuli ameongeza kuwa Serikali inachukua hatua madhubuti kuvilinda viwanda vya bia na ametoa wito kwa kampuni hiyo na wawekezaji wengine kuendelea kuwekeza hapa nchini kutokana na uwepo wa fursa kubwa ya soko la ndani, Afrika Mashariki na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).
Mazungumzo hayo yamehudhuriwa na Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mhe. Charles Mwijage, Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango na Kamishna Mkuu wa TRA Bw. Charles Kichere.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
19 Machi, 2018
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 15 Machi, 2018 amefungua kiwanda cha kutengeneza sigara cha Philip Morris Tanzania Limited kilichopo Kingolwira Mkoani Morogoro na kuagiza viongozi wote nchini kuwalinda na kuwavutia wawekezaji.
Pamoja na agizo hilo Mhe. Rais Magufuli amewahakikishia wawekezaji wote wanaojenga viwanda kuwa Serikali itaendelea kushirikiana nao kuhakikisha viwanda hivyo vinakuwa na tija ili wakulima waweze kupata masoko ya uhakika ya mazao yao, Watanzania kupata ajira na Serikali kupata kodi kwa ajili ya maendeleo ya nchi.
“Niwaombe wawekezaji msisite, endeleeni kujenga viwanda vya kutosha katika nchi hii, niwaombe viongozi na watendaji wenzangu katika Serikali kuanzia Mawaziri, Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa wilaya mpaka Wakurugenzi mtengeneze mazingira mazuri ya kusaidia wawekezaji kuwekeza, sisi viongozi ndani ya Serikali kamwe tusije kuwa chanzo cha kuzuia wawekezaji kuwekeza” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Mhe. Rais Magufuli ameipongeza kampuni ya Philip Morris Tanzania Limited kwa uwekezaji wa kiwanda hicho uliogharimu Shilingi Bilioni 65 na kampuni ya Mansoor Industries Limited kwa uendeshaji wa kiwanda.
Meneja Mkuu wa kampuni ya Philip Morris Tanzania Bi. Dagmara Piasecka amesema uamuzi wa kampuni hiyo kuwekeza hapa nchini ni uthibitisho wa mtazamo na imani ya muda mrefu iliyonayo kwa Tanzania kutokana na kuwepo kwa mazingira mazuri ya biashara, amani na utulivu, ukuaji mzuri wa uchumi na sera nzuri ya viwanda inayosimamiwa vizuri na Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mansoor Industries Limited Mhe. Mansoor Shanif Hirani amesema kiwanda hicho kilichoanza kujengwa mwaka 2017 kina uwezo wa kutengeneza sigara Milioni 400 na kulipa kodi kiasi cha Shilingi Bilioni 12 kwa mwaka, kimetoa ajira kwa watu 224 na kitaingiza fedha za kigeni kwa kuuza sigara ndani na nje ya nchi.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Steven Kebwe amesema mkoa huo wenye viwanda zaidi ya 3,000 unaendelea na kampeni kubwa ya ujenzi wa viwanda vingine 300 katika mwaka huu.
Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mhe. Charles Mwijage amemhakikishia Mhe. Rais Magufuli kuwa ujenzi wa viwanda unaendelea vizuri katika nchi nzima na amebainisha kuwa vipo viwanda vingi vilivyokamilika na vimeanza uzalishaji.
Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli amejibu ombi la kupatiwa maji lililotolewa na Mbunge wa Jimbo la Morogoro Mjini Mhe. Aziz Abood kwa kumhakikishia kuwa Serikali itafanyia kazi tatizo la uhaba wa maji kwa ajili ya wakazi wa Mji wa Morogoro na maendeleo ya viwanda.
Katika mkutano huo Mhe. Rais Magufuli amesikiliza kero ya wafanyabiashara ndogondogo kunyang’anywa bidhaa zao na Manispaa ya Morogoro kwa madai ya kuendesha shughuli zao katika maeneo yasiyoruhusiwa, na ameiagiza manispaa hiyo kuacha kuwanyanyasa na badala yake waboreshe mazingira yao na kuepusha hatari ya milipuko ya magonjwa.
Mhe. Rais Magufuli amerejea Jijini Dar es Salaam.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Morogoro
15 Machi, 2018
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 14 Machi, 2018 ameweka jiwe la msingi la kipande cha pili cha mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa (Standard Gauge) kinachoanzia Morogoro hadi Makutupora Mkoani Dodoma.
Sherehe za uwekaji jiwe la msingi katika mradi huo zimefanyika katika Kijiji cha Ihumwa nje kidogo ya Mji wa Dodoma na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Tulia Ackson, Mawaziri, Makatibu Wakuu, viongozi wa vyombo vya ulinzi na usalama, Mabalozi wa Uturuki na Uingereza hapa nchini, Wabunge na wananchi wa Dodoma.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Reli Tanzania (TRC) Bw. Masanja Kadogosa amesema ujenzi wa kipande cha pili cha reli chenye urefu wa kilometa 422 utagharimu Shilingi Trilioni 4.3 na ni sehemu ya mradi mkubwa ujenzi wa reli ya kati wa kuanzia Dar es Salaam hadi Mwanza yenye urefu wa kilometa 1,219.
Bw. Kadogosa amesema ujenzi wa kipande cha pili utakaofanyika kwa miezi 36 utakamilika ifikapo tarehe 25 Februari, 2021 na umetanguliwa na ujenzi wa kipande cha kwanza cha kuanzia Dar es Salaam hadi Morogoro utakaokamilika Novemba 2019.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa Mnyaa amesema wakati ujenzi wa kipande cha pili cha reli ya kati ukianza, ujenzi wa kipande cha kwanza umefikia asilimia 9 na kwamba treni zitakazotumia reli hiyo zitakuwa na uwezo wa kubeba tani 10,000 za mzigo kwa wakati mmoja (sawa na malori 500 ambayo yangesafirisha mzigo kwa barabara) na itakuwa na uwezo wa kwenda kasi ya kilometa 120 kwa saa na treni ya abiria kwenda kwa kasi ya kilometa 160 kwa saa.
Kabla ya kumkaribisha Mhe. Rais Magufuli, Waziri Mkuu Mhe Kassim Majaliwa Majaliwa amemshukuru kwa msukumo mkubwa aliouweka katika utekelezaji wa miradi na shughuli kubwa za Serikali ikiwemo ujenzi wa reli na amewataka Watanzania kuunga mkono juhudi hizo.
Katika hotuba yake Mhe. Rais Magufuli ameelezea kufurahishwa na utekelezaji wa mradi huo ambao amesema utasaidia kurahisisha na kupunguza gharama za usafirishaji wa mizigo na abiria, na pia utaokoa barabara ambazo zinaharibika kutokana na kusafirishaji mizigo mizito kwa magari.
“Kwa kutumia reli hii mtu atasafiri kutoka Dar es Salaam hadi hapa Dodoma kwa saa 3 tu ikilinganishwa na saa 5 hadi 6 zinazotumika hivi sasa kusafiri kwa gari, na pia mtu atasafiri kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza kwa saa 9 ikilinganishwa na saa 36 anazotumia sasa kwa kutumia treni” amesema Mhe. Rais Magufuli na kuongeza kuwa reli hiyo itakuwa na uwezo wa kusafirisha tani milioni 17 za mizigo kwa mwaka ikilinganishwa na ya sasa yenye uwezo wa kusafirisha tani milioni 5 tu.
“Bila shaka hii itaongeza mapato katika bandari yetu ya Dar es Salaam na pia itaimarisha biashara hususani kati ya nchi yetu na nchi zinazohudumiwa na ushoroba wa kati wa nchi za Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya kongo (DRC), Rwanda na Uganda” ameongeza Mhe. Rais Magufuli.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli amewataka wananchi wa Dodoma na Watanzania kwa ujumla kuchangamkia fursa zinazoletwa na mradi huu mkubwa ambao utazalisha ajira za moja kwa moja 30,000 na zisizo za moja kwa moja lakini 600,000 pamoja na miradi mingine ya ujenzi wa barabara na madaraja, bomba la mafuta la kuanzia Hoima Uganda hadi bandari ya Tanga nchini Tanzania, ujenzi wa mradi wa umeme katika maporomoko ya mto Rufiji (Stieglers’ Gorge) utakaozalisha megawatts 2,100, upanuzi na ukarabati wa viwanja 11 vya ndege na ujenzi wa meli katika ziwa Victoria.
Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli amemtaka Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango kufuatilia utozaji wa kodi unaofanywa na Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) ili kuepusha utozaji wa viwango ambavyo ni kero na amesisitiza kuwa “Inatakiwa kulipa kodi isiwe kero, iwe ni heshima”.
Hata hivyo Mhe. Rais Magufuli amewataka Watanzania kuendelea kulipa kodi ili fedha zinazopatikana ziendelee kugharamia miradi ya maendeleo ikiwemo kupelekea huduma muhimu za maji, elimu, afya na umeme ambapo Serikali imedhamiria ifikapo mwaka 2021 vijiji vyote nchini vipatiwe umeme.
Kesho tarehe 15 Machi, 2018 Mhe. Rais Magufuli atafungua kiwanda cha kutengeneza sigara cha Philip Moris kilichopo Kingolwira Mkoani Morogoro.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Chamwino
14 Machi, 2018
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Mazungumzo kati ya Kamati Maalum iliyoundwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli na Kampuni ya Bharti Airtel inayomiliki hisa katika kampuni ya simu za mkononi ya Airtel Tanzania yameanza rasmi tarehe 12 Machi, 2018 Jijini Dar es Salaam.
Katika mazungumzo hayo kamati iliyoundwa na Mhe. Rais Magufuli inaongozwa na Waziri wa Katiba na Sheria Prof. Palamagamba Kabudi na timu ya Bharti Airtel inaongozwa na Mwanasheria Mkuu wake Bw. Mukesh Bhavnani.
Mazungumzo hayo yanalengo la kufikia makubaliano yatakayokuwa na tija kwa pande zote mbili (Serikali ya Tanzania na Bharti Airtel) na kuimarisha sekta ya mawasiliano nchini Tanzania.
Kampuni ya Bharti Airtel iliomba kufanyika kwa mazaungumzo hayo baada ya kamati iliyofanya uchunguzi kuhusu umiliki wa kampuni ya Airtel Tanzania kuwasilisha ripoti yake kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli.
Jaffar Haniu
Naibu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
12 Machi, 2018
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ameiagiza Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji na Wizara Fedha na Mipango kutatua vikwazo vinavyosababisha viwanda vya ndani vya kusindika mafuta ya mbegu zinazozalishwa hapa nchini kushindwa kushindana na mafuta yanayoagizwa kutoka nje ya nchi ikiwemo tozo za kodi.
Mhe. Rais Magufuli ametoa agizo hilo tarehe 11 Machi, 2018 katika sherehe za uzinduzi wa kiwanda cha kusindika mafuta ya kula Mjini Singida (Mount Meru Millers Ltd) baada ya kupokea taarifa ya mmiliki wa kiwanda hicho Bw. Atul Mittal aliyeiomba Serikali iondoe kodi ya ongezeko la thamani kwa mafuta ya mbegu zinazolimwa hapa nchini.
Bw. Atul Mittal ameongeza kuwa hatua hiyo itawezesha mafuta yanayozalishwa hapa nchi kumudu ushindani dhidi ya mafuta kutoka nje ya nchi na hivyo kuchochea uzalishaji wa mazao ya mbegu za mafuta yakiwemo alizeti na pamba na kuongeza ajira kupitia kilimo na viwanda.
Pamoja na agizo hilo Mhe. Rais Magufuli pia ameiagiza Wizara ya Fedha na Mipango kuangalia namna nzuri ya kuwapunguzia kodi wafanyabiashara wanaowekeza viwanda hapa nchini na kuongeza viwango vya kodi kwa mafuta yanayoagizwa kutoka nje ya nchi ili kuvilinda viwanda vya kusindika mafuta ya kula vya ndani.
“Mimi chama changu kimeniagiza nizalishe ajira, siwezi kutengeneza ajira za kwenye majukwaa, ni lazima kuwe na viwanda vya kuwajiri hawa watu.
“Kiwanda hiki kinazalisha tani 90,000 za mafuta kwa mwaka wakati uzalishaji wa nchi nzima ni tani 135,000, hii ni asilimia 30 tu ya mahitaji ya tani 450,000 na huenda yakaongezeka hadi kufikia tani 500,000 kwa mwaka kutokana na ongezeko la watu, ni dhahiri tunahitaji viwanda vingi kama hivi, lakini ili viwanda hivi viweze kuhimili ushindani tunahitaji kuvilinda dhidi ya viwanda vya nje, ndio maana nawaomba viongozi wenzangu Mawaziri, Wakuu wa Mikoa, Wakurugenzi na viongozi wengine tuhakikishe tunavilinda viwanda hivi kwa gharama zozote” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Mhe. Rais Magufuli amempongeza mmiliki wa kiwanda cha Mount Meru Millers Bw. Atul Mittal kwa uwekezaji huo uliowezesha kupatikana kwa ajira za kudumu 300 na za muda 900 na ameahidi kuwa Serikali itafanyia kazi mapendekezo aliyoyatoa yenye lengo la kuongeza uzalishaji wa mafuta ya kula hadi kutosheleza mahitaji kwa asilimia 100 katika kipindi cha muda mfupi ujao.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli amewataka wafanyabiashara kuacha kulalamika na badala yake kujenga viwanda vya kuzalisha bidhaa mbalimbali zikiwemo za pamba, dripu za maji ya wagonjwa, dawa za binadamu na viwanda vya kusindika mafuta ya kula badala ya kufanya ujanjaujanja wa kuagiza mafuta kutoka nje ya nchi kwa madai kuwa ni ghafi wakati ni safi.
Mapema leo asubuhi Mhe. Rais Magufuli amezindua viwanda vya kampuni ya Kahama Oil Mills vinavyozalisha bidhaa za plastiki, chuma, mabati na mabomba ya maji.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kahama Oil Mills Bw. Mhoja Nkwabi Kabalo amesema viwanda hivyo vina uwezo wa kuzalisha bidhaa bora kwa ajili ya mahitaji ya ndani ya nchi na ameongeza kuwa hivi karibuni kampuni hiyo inatarajia kufungua viwanda vingine vinne ambavyo ni kiwanda cha kukamua alizeti tani 150 kwa siku huko Kibaigwa Dodoma, Kiwanda cha kuzalisha mikate 4,000 kwa saa huko Miyungi Dodoma, Kiwanda cha Nyama kitakachokuwa na uwezo wa kuchakata ng’ombe 70 na mbuzi 200 kwa saa huko Nyakakarango Mkoani Geita na kiwanda cha maji tiba Mkoani Shinyanga.
Pamoja na kumpongeza Bw. Mhoja Nkwabi kwa uwekezaji huo Mhe. Rais Magufuli amewaagiza viongozi wa Serikali kuhakikisha wakandarasi wanaopata zabuni katika miradi ya Serikali wanatumia bidhaa zinazozalishwa na viwanda vya ndani na amewataka wazalishaji wa bidhaa hizo kuzalisha bidhaa bora.
Akiwa njiani kutoka Kahama Mkoani Shinyanga kuelekea Singida Mhe. Rais Magufuli amewasalimu wananchi wa Tinde na Igunga na kuwahakikishia kuwa Serikali itatekeleza ahadi ilizozitoa na amewataka kuchapa kazi na kulinda amani.
Mhe. Rais Magufuli amewasili katika Ikulu ya Chamwino Mkoani Dodoma.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dodoma
11 Machi, 2018
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 09 Machi, 2018 amefungua tawi la benki ya CRDB - Chato Mkoani Geita na kuiagiza Benki Kuu ya Tanzania (BOT) kuendelea kuchukua hatua ikiwa ni pamoja na kuzifungia benki ambazo zinaendeshwa kwa kusuasua ili kulinda sekta ya benki na uchumi wa nchi.
Pamoja na kutoa agizo hilo Mhe. Rais Magufuli amesema Serikali haitatoa fedha kwa ajili ya kuinusuru benki yeyote itakayoshindwa kujiendesha yenyewe na ameipongeza BOT kwa kuzifungia benki 5 na kuziwekea muda wa matazamio wa miezi 6 benki nyingine 3 ambazo zinaendeshwa kwa kusuasua.
“Benki itakayoshindwa kujisimamia ifungeni, ni afadhali tuwe na benki chache zinazofanya vizuri kuliko kuwa na utitiri wa benki ambazo hazifanyi vizuri, kulikuwa na mchezo benki ikishindwa kujisimamia Serikali inatoa fedha za wananchi na kwenda kuipatia mtaji, matokeo yake huko ndiko wajanja walikuwa wanakula fedha za wananchi kwa kukopa na kutorudisha mikopo, naomba niwaeleze mimi sitatoa fedha kuipatia benki inayoshindwa kujisimamia” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Hata hivyo Mhe. Rais Magufuli ameipongeza benki ya CRDB kwa kujiendesha kwa ufanisi huku ikiwa imewafikia watanzania wengi kupitia matawi yake zaidi ya 250 na ametoa wito kwa CRDB na benki nyingine nchini kupunguza viwango vya riba ili Watanzania waweze kumudu kukopa na kuwekeza katika shughuli za uzalishaji mali.
Mhe. Rais Magufuli amewahakikishia Watanzania kuwa nchi inakwenda vizuri na amewataka kuunga mkono hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali ambazo zimeanza kuimarisha uchumi na kuwezesha utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo kama vile ujenzi wa reli ya kisasa (Standard Gauge), uzalishaji umeme katika maporomoko ya mto Rufiji (Stieglers Gorge), ununuzi wa ndege 6, ujenzi wa barabara na madaraja na hivi karibuni Serikali itasaini mkataba wa ujenzi wa meli katika ziwa Victoria itakayogharimu Shilingi Bilioni 35.
Mhe. Rais Magufuli amemshukuru Balozi wa Denmark hapa nchini Mhe. Einar Jensen ambaye amehudhuria sherehe za ufunguzi wa tawi la CRDB – Chato kwa nchi yake kushirikiana kwa mafanikio na CRDB kwa miaka 25 na pia kuwaleta wafanyabiashara wanaotarajia kuwekeza Dola za Marekani Bilioni 1.92 (Takribani Shiling Trilioni 4.268 za Tanzania) katika ujenzi wa kiwanda cha mbolea Mkoani Mtwara ambacho licha ya kuzalisha mbolea ya kutosheleza mahitaji ya nchi na kuuzwa nje ya nchi, kitazalisha ajira 4,000.
“Sio hicho kiwanda tu, mpaka sasa kuna viwanda vingine 3,060 vimejengwa, tunapofanya yote haya wapo ambao hawatapenda na watataka kutuchonganisha, nawaomba Watanzania tuweke uzalendo mbele” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Aidha, amewataka Watanzania kutokubali kutumiwa katika vitendo vya uvunjifu wa amani ambavyo vinaweza kusababisha machafuko kama yaliyotokea kwa nchi jirani na nyingine duniani, na ameonya kuwa vyombo vya dola havitawavumilia watakaothubutu kuvunja sheria na kuleta vurugu.
Mapema wakitoa maelezo kuhusu benki ya CRDB Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa benki hiyo Bw. Ally Laay na Mkurugenzi Mtendaji Dkt. Charles Kimei wamesema CRDB imeendelea kufanya vizuri ambapo katika miezi mitatu iliyopita amana zimeongezeka kutoka Shilingi Trilioni 4 hadi 4.4, imeanzisha bidhaa iitwayo “Kilimo Fahari” yenye lengo la kuwakopesha wakulima, na inatarajia kuwaunganisha wafanyabiashara wa Tanzania na wawekezaji wakubwa wa viwanda kutoka nchi zenye teknolojia na mitaji mikubwa zaidi ili kuendeleza viwanda nchini.
Viongozi hao wa CRDB wamekabidhi hundi ya Shilingi Milioni 50 kwa ajili ya kusaidia michezo wilayani Chato na wamepokea ombi la Mbunge wa Chato Dkt. Medard Matogolo Kalemani la kujengewa uwanja wa mpira utakaoitwa CRDB Stadium.
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Ashatu Kijaji amesema Tanzania inafanya vizuri katika mpango wa fedha jumuishi ambapo katika miaka 3 mfurulizo imeshika nafasi ya kwanza Barani Afrika na nafasi ya sita duniani na kwamba juhudi zinaendelea kufanywa ili kuongeza idadi ya Watanzania wanaotumia huduma za kifedha.
Sherehe za ufunguzi wa tawi la CRDB Chato zimehudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Waziri wa Nishati na Mbunge wa Chato Dkt. Medard Matogolo Kalemani, Naibu Waziri wa Madini Mhe. Doto Biteko, Wabunge na viongozi mbalimbali wa Mkoa wa Geita wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa Mhandisi. Robert Gabriel Luhumbi.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Chato
09 Machi, 2018
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 10 Machi, 2018 amefungua barabara ya lami ya Uyovu – Bwanga Mkoani Geita na barabara ya lami ya Isaka – Ushirombo Mkoani Shinyanga na kuwataka Watanzania kutumia miundombinu hiyo kuongeza uzalishaji mali utakaosaidia kukuza kipato na kujenga uchumi wa nchi.
Akitoa taarifa katika sherehe za ufunguzi wa barabara ya Uyovu – Bwanga zilizofanyika Runzewe Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara hapa nchini (TANROADS) Mhandisi Patrick Mfugale amesema ujenzi wa barabara hiyo yenye urefu wa kilometa 45 na upana wa meta 11, umegharimu Shilingi Bilioni 47 na Milioni 917, fedha zote zikiwa zimetolewa na Serikali ya Tanzania.
Katika sherehe za ufunguzi wa barabara ya Isaka – Ushirombo zilizofanyika katika Mji wa Kahama, Mhandisi Mfugale amesema ujenzi wa barabara hiyo yenye urefu wa kilometa 132 umegharimu Shilingi Bilioni 193 na Milioni 897.
Naibu Waziri wa Ujenzi Mhandisi Elias John Kwandikwa amesema kujengwa kwa barabara hizo ni muhimu kwa mawasiliano ya ukanda wa mikoa ya Mwanza, Geita, Kagera, Shinyanga na Kigoma ambazo zinaiunganisha Tanzania na nchi jirani za Burundi, Rwanda, Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Mhandisi Kwandikwa amebainisha kuwa miradi hiyo imetekelezwa sambamba na miradi mingine ya barabara za lami za Bwanga – Biharamulo (Km-67), Nyakanazi – Kakonko (Km-50), Ushirombo – Lusahunga (Km-110) na Kidahwe – Kasulu (Km-63) na kwamba kwa sasa maandalizi yanafanywa ili kuanza ujenzi wa barabara nyingine za lami za Geita – Bulyanhulu (Km-58.3), Bulyanhulu – Kahama (Km-61.7), Nyamirembe – Katoke (Km-50) na usanifu wa barabara ya Ushirombo – Lulembera – Katoro (Km-56) na Lutembelumasa – Ipalamasa – Mbogwe – Masumbwe (Km-98).
Akizungumza na wananchi wa Runzewe Mhe. Rais Magufuli amesema Serikali ya Awamu ya Tano inatekeleza miradi hiyo kwa gharama kubwa kutokana na hatua madhubuti inazochukua kujenga uchumi na amewataka wananchi kuunga mkono juhudi hizo kwa kuhakikisha wanalinda amani iliyopo na kuchapa kazi.
Amewasihi wazazi na walezi kuwaeleza vijana wao juu ya athari za kujihusisha na vitendo vya uvunjifu wa amani na amewahakikishia kuwa Serikali itaendelea kutatua kero za wananchi na kuwajengea mazingira bora ya kilimo, ufugaji na biashara ikiwemo kulifanyia kazi ombi la kuongezewa maeneo ya kilimo na ufugaji kutoka kwenye hifadhi kutokana na mahitaji yao kuongezeka.
Akiwa njiani Mhe. Rais Magufuli amesimamishwa na wananchi wa Masumbwe katika Wilaya ya Mbogwe na kuwahakikishia kuwa ahadi yake ya kuwajengea kilometa 5 za barabara ya lami katika Mji huo itatekelezwa.
Akizungumza na wananchi wa Kahama kabla ya kufungua barabara ya Isaka – Ushirombo Mhe. Rais Magufuli amewapongeza wakulima kwa namna walivyoitikia wito wa kuongeza juhudi katika kilimo cha mazao mbalimbali yakiwemo Mpunga na Pamba.
Mhe. Rais Magufuli ameagiza wananchi waliojenga makazi yao katika eneo la ekari 308 kati ya eneo lote la Mwamva lenye ekari 348 lililotengwa kwa ajili ya ujenzi wa Chuo cha Maendeleo ya Jamii, wasiondolewe na kwamba eneo lililobaki la ekari 40 ndilo litumike kujenga chuo hicho na wananchi wasilivamie.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli amewapongeza Wabunge wa Mkoa wa Shinyanga kwa uwakilishi mzuri wa wananchi wao na amewahakikishia kuwa maombi yao ambayo ni kukomesha unyanyasaji dhidi ya wamachinga na wachimbaji wadogo wa madini, kuongeza fedha katika hospitali na kupanua usambazaji wa maji katika maeneo machache yaliyobaki yatafanyiwa kazi.
“Wabunge wenu wanashukuru kuwa sasa maeneo yao mengi yanapata maji safi na salama, naomba wananchi mjipongeze wenyewe kwa kuwa hizo ni kodi zenu, na Serikali ninayoiongoza itaendelea kuhakikisha wananchi mnapata mahitaji mnayostahili, ninachowaomba tuilinde amani yetu na tuchape kazi” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Kesho tarehe 11 Machi, 2018 Mhe. Rais Magufuli ataendelea na ziara yake kwa kufungua kiwanda cha kukamua mafuta ya alizeti cha Kahama Oil Mill kilichopo Mkoani Shinyanga na Kiwanda cha kukamua mafuta ya alizeti cha Mount Meru Millers Limited kilichopo Mkoani Singida.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Kahama
10 Machi, 2018
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 09 Machi, 2018 amefungua tawi la benki ya CRDB - Chato Mkoani Geita na kuiagiza Benki Kuu ya Tanzania (BOT) kuendelea kuchukua hatua ikiwa ni pamoja na kuzifungia benki ambazo zinaendeshwa kwa kusuasua ili kulinda sekta ya benki na uchumi wa nchi.
Pamoja na kutoa agizo hilo Mhe. Rais Magufuli amesema Serikali haitatoa fedha kwa ajili ya kuinusuru benki yeyote itakayoshindwa kujiendesha yenyewe na ameipongeza BOT kwa kuzifungia benki 5 na kuziwekea muda wa matazamio wa miezi 6 benki nyingine 3 ambazo zinaendeshwa kwa kusuasua.
“Benki itakayoshindwa kujisimamia ifungeni, ni afadhali tuwe na benki chache zinazofanya vizuri kuliko kuwa na utitiri wa benki ambazo hazifanyi vizuri, kulikuwa na mchezo benki ikishindwa kujisimamia Serikali inatoa fedha za wananchi na kwenda kuipatia mtaji, matokeo yake huko ndiko wajanja walikuwa wanakula fedha za wananchi kwa kukopa na kutorudisha mikopo, naomba niwaeleze mimi sitatoa fedha kuipatia benki inayoshindwa kujisimamia” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Hata hivyo Mhe. Rais Magufuli ameipongeza benki ya CRDB kwa kujiendesha kwa ufanisi huku ikiwa imewafikia watanzania wengi kupitia matawi yake zaidi ya 250 na ametoa wito kwa CRDB na benki nyingine nchini kupunguza viwango vya riba ili Watanzania waweze kumudu kukopa na kuwekeza katika shughuli za uzalishaji mali.
Mhe. Rais Magufuli amewahakikishia Watanzania kuwa nchi inakwenda vizuri na amewataka kuunga mkono hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali ambazo zimeanza kuimarisha uchumi na kuwezesha utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo kama vile ujenzi wa reli ya kisasa (Standard Gauge), uzalishaji umeme katika maporomoko ya mto rufiji (Stieglers Gorge), ununuzi wa ndege 6, ujenzi wa barabara na madaraja na hivi karibuni Serikali itasaini mkataba wa ujenzi wa meli katika ziwa Victoria itakayogharimu Shilingi Bilioni 35.
Mhe. Rais Magufuli amemshukuru Balozi wa Denmark hapa nchini Bw. Einar Jensen ambaye amehudhuria sherehe za ufunguzi wa tawi la CRDB – Chato kwa nchi yake kushirikiana kwa mafanikio na CRDB kwa miaka 25 na pia kuwaleta wafanyabiashara wanaotarajia kuwekeza Dola za Marekani Bilioni 1.92 katika ujenzi wa kiwanda cha mbolea Mkoani Mtwara ambacho licha ya kuzalisha mbolea ya kutosheleza mahitaji ya nchi na kuuzwa nje ya nchi, kitazalisha ajira 4,000.
“Sio hicho kiwanda tu, mpaka sasa kuna viwanda vingine 3,060 vimejengwa, tunapofanya yote haya wapo ambao hawatapenda na watataka kutuchonganisha, nawaomba Watanzania tuweke uzalendo mbele” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Aidha, amewataka Watanzania kutokubali kutumiwa katika vitendo vya uvunjifu wa amani ambavyo vinaweza kusababisha machafuko kama yaliyotokea kwa nchi jirani na nyingine duniani, na ameonya kuwa vyombo vya dola havitawavumilia watakaothubutu kuvunja sheria na kuleta vurugu.
Mapema wakitoa maelezo kuhusu benki ya CRDB Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa benki hiyo Bw. Ally Laay na Mkurugenzi Mtendaji Dkt. Charles Kimei wamesema CRDB imeendelea kufanya vizuri ambapo katika miezi mitatu iliyopita amana zimeongezeka kutoka Shilingi Trilioni 4 hadi 4.4, imeanzisha bidhaa iitwayo “Kilimo Fahari” yenye lengo la kuwakopesha wakulima, na inatarajia kuwaunganisha wafanyabiashara wa Tanzania na wawekezaji wakubwa wa viwanda kutoka nchi zenye teknolojia na mitaji mikubwa zaidi ili kuendeleza viwanda nchini.
Viongozi hao wa CRDB wamekabidhi hundi ya Shilingi Milioni 50 kwa ajili ya kusaidia michezo wilayani Chato na wamepokea ombi la Mbunge wa Chato Dkt. Medard Matogolo Kalemani la kujengewa uwanja wa mpira utakaoitwa CRDB Stadium.
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Ashatu Kijaji amesema Tanzania inafanya vizuri katika mpango wa fedha jumuishi ambapo katika miaka 3 mfurulizo imeshika nafasi ya kwanza Barani Afrika na nafasi ya sita duniani na kwamba juhudi zinaendelea kufanywa ili kuongeza idadi ya Watanzania wanaotumia huduma za kifedha.
Sherehe za ufunguzi wa tawi la CRDB Chato zimehudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Waziri wa Nishati na Mbunge wa Chato Dkt. Medard Matogolo Kalemani, Naibu Waziri wa Madini Mhe. Doto Biteko, Wabunge na viongozi mbalimbali wa Mkoa wa Geita wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa Mhandisi. Robert Gabriel Luhumbi.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Chato
09 Machi, 2018
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amerejea nchini tarehe 24 Februari, 2018 akitokea nchini Uganda ambako amehudhuria mkutano wa 19 wa wakuu wa nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki uliomalizika jana Mjini Kampala.
Katika uwanja wa ndege wa Mwanza Mhe. Rais Magufuli amepokelewa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Bw. John Mongella aliyeongozana na Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Angeline Mabula na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dkt. Antony Dialo.
Akiwa uwanjani hapo Mhe. Rais Magufuli amezungumza na wafanyakazi wa uwanja wa ndege wa Mwanza ambao wamemuomba asaidie kutatua changamoto mbalimbali zinazoukabili uwanja huo zikiwemo mahitaji ya jengo la abiria kutokana na jengo lililopo kuwa dogo, mahitaji ya ujenzi wa uzio wa kuzunguka uwanja na ndege zinazobeba minofu ya samaki kutotumia uwanja wa Mwanza na badala yake kutumia viwanja vya nchi jirani kutokana na ongezeko la tozo ya kodi kwa ndege hizo.
Katika majibu yake Mhe. Rais Magufuli ameahidi kuwa Serikali itafanyia kazi mahitaji ya kujengwa kwa jengo la abiria pamoja na ujenzi wa uzio ili uwanja wa Mwanza uwe na hadhi ya kimataifa na hivyo kuiwezesha nchi kupata mapato zaidi.
Kuhusu changamoto ya ndege za kubeba minofu ya samaki kutotumia uwanja wa Mwanza Mhe. Rais Magufuli amesema Serikali itafanyia kazi jambo hilo na kulitafutia ufumbuzi haraka ili ndege hizo zitumie uwanja huo na kuiingizia nchi mapato.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli amesema anasubiri ripoti ya Wizara ya Ardhi kuhusu wananchi waliovamia uwanja wa ndege wa Mwanza lakini amebainisha kuwa Serikali haiwezi kukimbilia kuondoa kaya zaidi ya 1,900 zinazodaiwa kuvamia eneo hilo na badala yake itaangalia njia bora ya kufanya.
Hata hivyo ametaka wananchi waliopo katika eneo hilo wasiendeleze makazi yao wakati uamuzi wa Serikali unasubiriwa.
“Bahati nzuri Naibu Waziri wa Ardhi upo hapa, kafanyieni kazi changamoto hii na mnipe ripoti” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Baada ya kutoka uwanja wa ndege wa Mwanza Mhe. Rais Magufuli ameelekea nyumbani kwake Chato Mkoani Geita kwa mapumziko.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Mwanza
24 Februari, 2018
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Mkutano wa 19 wa wakuu wa nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki umemaliza jioni tarehe 23 Februari, 2018 katika hoteli ya Munyonyo mjini Kampala nchini Uganda.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amehudhuria mkutano huo pamoja na Marais wengine Mhe. Yoweri Kaguta Museveni wa Uganda, Mhe. Uhuru Muigai Kenyatta wa Kenya, Mhe. Salva Kiir Mayardit wa Sudani Kusini na Rais wa Burundi Mhe. Pierre Nkurunziza amewakilishwa na Makamu wa Kwanza wa Rais Mhe. Gaston Sindimwo na Rais wa Rwanda Mhe. Paul Kagame amewakilishwa na Waziri wa Miundombinu Mhe. James Musoni.
Mkutano huo umeongozwa na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Mhe. Yoweri Kaguta Museveni na kwa pamoja Waheshimiwa Marais wamemteua Mhe. Jaji Charles Ayako Nyachae kuwa Jaji wa Mahakama ya Awali ya Afrika Mashariki na Mhe. Jaji Faustin Ntezilyayo kuwa Naibu Jaji Mkuu wa Mahakama ya Afrika Mashariki kuanzia tarehe 01 Julai, 2018.
Pia wameamua Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kuwa na Naibu Makatibu Wakuu wawili badala ya mapendekezo ya kuwa na Naibu Makatibu Wakuu watano.
Aidha, wakuu wa nchi wamezindua mkakati wa tano wa maendeleo wa Jumuiya ya Afrika Mashariki unaoanzia 2016/17 hadi 2020/21, wameamua kuendelea na majadiliano kuhusu mkataba wa ubia wa kibiashara kati ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na Umoja wa Ulaya (EPA) na wamepokea ripoti ya maendeleo ya majadiliano ya kutafuta amani ya mgogoro wa Burundi kutoka kwa Mratibu wa mazungumzo hayo Mhe. Rais Mstaafu Benjamin Willian Mkapa.
Halikadhalika wakuu wa nchi wamewahimiza wahusika wote katika mgogoro wa Burundi kushirikiana na Mratibu na Msuluhishi wa mgogoro huo ili kufanikisha mazungumzo hayo.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Kampala
23 Februari, 2018
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ametoa wito kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kusimamia vizuri rasilimali walizonazo na kukusanya kodi vizuri ili waweze kutekeleza miradi mikubwa ya ujenzi wa miundombinu na kuimarisha huduma za afya kwa wananchi.
Mhe. Rais Magufuli ametoa wito huo tarehe 22 Februari, 2018 mjini Kampala nchini Uganda wakati akichangia katika mkutano wa wakuu wa nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki unaojadili maendeleo na upatikanaji wa fedha kwa ajili ya miradi ya sekta ya miundombinu na afya.
Kabla ya Mhe. Rais Magufuli kutoa mchango wake, Marais walioshiriki mkutano huo wamepokea taarifa ya mkutano wa majadiliano ya kisekta (Round Table) kuhusu mahitaji ya fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi ya sekta ya miundombinu na afya ambapo imeelezwa kuwa katika miaka 10 ijayo nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki zitahitaji Dola za Marekani Bilioni 78 kutekeleza miradi ya miundombinu inayopendekezwa.
Taarifa hiyo imechangiwa na wadau mbalimbali wakiwemo Marais, wawakilishi wa sekta binafsi na washirika wa maendeleo ambao wameelezea njia mbalimbali za kupata fedha za kutekeleza miradi hiyo ikiwemo kutumia mfumo wa ushirikiano kati ya Serikali na Sekta binafsi (PPP).
Katika mchango wake Mhe. Rais Magufuli amesema pamoja na kutumia mfumo wa PPP ni muhimu kwa Serikali za kila nchi kusimamia vizuri ukusanyaji wa mapato ya kodi na rasilimali nyingine ili kutekeleza miradi ya miundombinu, afya na sekta nyingine.
Ametahadharisha kuwa japo kuwa mfumo wa PPP ni mzuri, ni vyema wataalamu wakachukua tahadhali za kutosha ili kuepusha Serikali kuingia katika mikataba isiyokuwa na maslahi kwa nchi zao kutokana na baadhi ya wadau wa sekta binafsi kutaka kutengeneza faida kubwa kwa kupandisha gharama za miradi.
Mhe. Rais Magufuli ametolea mfano wa miradi mikubwa iliyoanza kutekelezwa nchini Tanzania ukiwemo ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa (Standard Gauge) na ujenzi wa mradi wa kuzalisha umeme katika maporomoko ya mto Rufiji (Stieglers’ Gorge), kuwa Serikali ya Tanzania imeamua kuanza kutekeleza miradi hiyo kwa kutumia fedha zake baada ya kufanikiwa kusimamia vizuri rasilimali zake na kubana matumizi.
“Mimi naamini tukiamua tunaweza, nchi zetu zina rasilimali nyingi za kuweza kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo, mathalani tafiti zinaonesha kuwa kama nchi zetu zitaweza kukusanya vizuri mapato ya kodi, zinaweza kutekeleza nusu ya miradi yake ya maendeleo.
“Lakini ukiachilia mbali mapato ya kodi, tunapoteza fedha nyingi kupitia utoroshaji wa rasilimali zetu, ripoti ya jopo la Umoja wa Afrika lililoongozwa na Rais Mstaafu wa Afrika Kusini Mhe. Thabo Mbeki imeeleza kuwa nchi za Afrika zinapoteza Dola za Marekani Bilioni 150 kila mwaka kutokana na utoroshaji wa rasilimali” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Marais waliohudhuria mkutano huo ni Rais wa Uganda Mhe. Yoweri Kaguta Museveni, Rais wa Kenya Mhe. Uhuru Muigai Kenyatta, Rais wa Sudan Kusini Mhe. Salva Kiir Mayardit na Marais wa Rwanda na Burundi wamewakilishwa.
Kesho tarehe 23 Februari, 2018 Mhe. Rais Magufuli atahudhuria mkutano wa 19 wa wakuu wa nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Kampala
22 Februari, 2018
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 21 Februari, 2018 amewasili nchini Uganda ambapo atahudhuria mkutano wa 19 wa wakuu wa nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki utakaofanyika Ijumaa tarehe 23 Februari, 2018 Mjini Kampala.
Katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Entebbe Mhe. Rais Magufuli amepokelewa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Uganda Mhe. Sam Kutesa na kisha kuelekea Ikulu ya Entebbe ambako amekutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Uganda Mhe. Yoweri Kaguta Museveni.
Kesho tarehe 22 Februari, 2018 Mhe. Rais Magufuli atahudhuria mkutano maalum katika ngazi ya wakuu wa nchi unaohusu masuala ya miundombinu na afya na keshokutwa tarehe 23 Februari, 2018 na atahudhuria mkutano wa 19 wa wakuu wa nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Kampala
21 Februari, 2018
Taarifa kwa vyombo vya habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 16 Februari, 2018 saa 3:00 asubuhi atawaapisha Mabalozi wawili aliowateua kuiwakilisha Tanzania katika nchi za Nigeria na Sweden.
Taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi imeeleza kuwa watakaoapishwa ni Mhe. Muhidin Ally Mboweto ambaye ameteuliwa kuwa Balozi wa Tanzania nchini Nigeria na Mhe. Dkt. Wilbrod Peter Slaa ambaye ameteuliwa kuwa Balozi wa Tanzania nchini Sweden.
Uteuzi wa Mabalozi hao kuiwakilisha Tanzania katika nchi walizopangiwa umeanza jana tarehe 15 Februari, 2018.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
16 Februari, 2018
Taarifa kwa vyombo vya habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 15 Februari, 2018 amemuapisha Luteni Jenerali Yacoub Hassan Mohamed kuwa Mnadhimu Mkuu wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).
Hafla ya kuapishwa kwa Lut Jen. Yacoub Hassan Mohamed imefanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan, Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Dkt. Hussein Ali Mwinyi, Waziri wa Katiba na Sheria Prof. Palamagamba Kabudi, viongozi wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama, maafisa wa JWTZ na viongozi wengine mbalimbali.
Kabla Lut Jen. Yacoub Hassan Mohamed hajaapishwa kuwa Mnadhimu Mkuu wa JWTZ, Mhe. Rais Magufuli amemvalisha cheo kipya cha Luteni Jenerali.
Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli ameshuhudia Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi nchini Jenerali Venance Salvatory Mabeyo akiwavisha cheo kipya cha Meja Jenerali Maafisa 10 wa JWTZ waliopandishwa vyeo kutoka Brigedia Jenerali jana tarehe 15 Februari, 2018.
Maafisa hao ni Mej Jen. Alfred Fabian Kapinga, Mej Jen. Blasius Kalima Masanja, Mej Jen. Anselm Shigongo Bahati, Mej Jen. Kaisy Philip Njelekela, Mej Jen. Shija Seif Makona, Mej Jen. George Thomas Msongole, Mej Jen. Martin Shiminzi Busungu, Mej Jen. Jacob Gidion Kingu, Mej Jen. Ramadhan Rama Mrangira na Mej Jen. Mathew Eduard Mkingule.
Aidha, Jen. Mabeyo ametangaza kuwa Mhe. Rais Magufuli ameridhia uteuzi wa Majenerali wafuatao kushika madaraka mbalimbali katika JWTZ;
Mej Jen. Jacob Gidion Kingu ameteuliwa kuwa Mkuu wa Chuo cha Ulinzi wa Taifa (NDC), akichukua nafasi ya Lut Jen. Yacoub Hassan Mohamed ambaye ameteuliwa kuwa Mnadhimu Mkuu wa JWTZ.
Mej. Jen. Martin Shiminzi Busungu ameteuliwa kuwa Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), akichukua nafasi ya Mej Jen. Michael Joseph Isamuhyo ambaye amestaafu.
Mej Jen. Blasius Kalima Masanja ameteuliwa kuwa Mkuu wa Utumishi Jeshini.
Mej Jen. Shija Seif Makona ameteuliwa kuwa Mkuu wa Shirika la Mzinga, akichukua nafasi ya Mej Jen. Jacob Gidion Kingu ambaye ameteuliwa kuwa Mkuu wa Chuo cha Ulinzi wa Taifa (NDC).
Mej Jen. George Thomas Msongole ameteuliwa kuwa Mkuu wa Kamandi ya Jeshi la Nchi Kavu akichukua nafasi ya Mej Jen. Sharif Sheikh Othman ambaye ameteuliwa Mkuu wa Kamandi ya Vikosi chini ya Makao Makuu ya Jeshi.
Mej Jen. Ramadhan Rama Mrangira ameteuliwa kuwa Kamishna wa Mipango na Maendeleo wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).
Jen. Mabeyo ameongeza kuwa Mhe. Rais Magufuli ameridhia Majenerali wengine waliopandishwa vyeo na kuwa Meja Jenerali waendelee na nafasi zao kama ifuatavyo;
Mej Jen. Alfred Fabian Kapinga anaendelea kuwa Mkuu wa Mafunzo na Utendaji Kivita.
Mej Jen. Anselm Shigongo Bahati anaendelea kuwa Mkuu wa Shirika wa Nyumbu.
Mej Jen. Kaisy Philip Njelekela anaendelea kuwa Jaji Wakili Mkuu wa JWTZ.
Mej Jen. Mathew Eduardo Mkingule anaendelea kuwa Mdhibiti Mkuu wa JWTZ.
Akizungumza baada ya kuapishwa, Mnadhimu Mkuu wa JWTZ Lut Jen. Yacoub Hassan Mohamed amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kumuamini na ameahidi kutekeleza wajibu wake ipasavyo ikiwemo kusimamia ahadi ya Mkuu wa Majeshi Jen. Mabeyo ya kuiimarisha JWTZ.
Majenerali wastaafu waliowahi kushika nafasi ya Mnadhimu Mkuu wa JWTZ wamempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa kuwapandisha vyeo Majenerali hao na kufanya uteuzi wa Mnadhimu Mkuu wa JWTZ, na wamewasihi Maafisa hao wa Jeshi kuwa watumishi bora watakaoendeleza juhudi za kuliimarisha jeshi na kukabiliana na changamoto za kiusalama vya kisasa.
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Dkt. Hussein Ali Mwinyi amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa uteuzi huo ambao amesema utasaidia kuimarisha zaidi utendaji kazi wa JWTZ ambalo limejipatia sifa kubwa ndani na nje ya nchi kwa viwango vya juu vya weledi na nidhamu kijeshi.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
15 Februari, 2018
Taarifa kwa vyombo vya habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 14 Februari, 2018 amemteua Meja Jenerali Yakubu Hassan Mohamed kuwa Mnadhimu Mkuu wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).
Pamoja na uteuzi huo, Mhe. Rais Magufuli amempandisha cheo kutoka Meja Jenerali na kuwa Luteni Jenerali.
Luteni Jenerali Yakubu Hassan Mohamed anachukua nafasi ya Luteni Jenerali James Alois Mwakibolwa ambaye amestaafu.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli amewapandisha vyeo kutoka Brigedia Jenerali na kuwa Meja Jenerali wafuatao;
- Brig Jen. J.G. Kingu
- Brig Jen. M.S. Busungu
- Brig Jen. R.R. Mrangira
- Brig Jen. B.K. Masanja
- Brig Jen. G.T. Msongole
- Brig Jen. A.F. Kapinga
- Brig Jen. K.P. Njelekela
- Brig Jen. A.S. Bahati
- Brig Jen. M.E. Mkingule
- Brig Jen. S.S. Makona
Mabrigedia Jenerali wote waliopandishwa vyeo watapangiwa vituo vya kazi baadaye.
Mnadhimu Mkuu wa JWTZ Luteni Jenerali Yakubu Hassan Mohamed ataapishwa kesho tarehe 15 Februari, 2018 saa 5:00 asubuhi Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
14 Februari, 2018
Taarifa kwa vyombo vya habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amemteua Dkt. Omari Rashid Nundu kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL Corporation) na Bw. Waziri Waziri Kindamba kuwa Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo.
Uteuzi wa Dkt. Omari Rashid Nundu na Bw. Waziri Waziri Kindamba umeanza tarehe 01 Februari, 2018.
Kabla ya Uteuzi huu Dkt. Omari Rashid Nundu alikuwa Mwenyekiti wa Bodi ya iliyokuwa Kampuni ya Simu Tanzania (Tanzania Telecommunication Company Limited – TTCL) na Bw. Waziri Waziri Kindamba alikuwa Mtendaji Mkuu wa kampuni hiyo.
Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) ilibadilishwa rasmi tarehe 28 Novemba, 2017 na kuwa Shirika la Simu Tanzania (TTCL Corporation) baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kutia saini sheria namba 12 ya mwaka 2017 ya Shirika la Simu Tanzania (TTCL Corporation) na tarehe 01 Februari, 2018 TTCL Corporation ilianza kufanya kazi rasmi.
Pamoja na kufanya uteuzi wa Mwenyekiti wa Bodi na Mkurugenzi Mkuu wa TTCL Corporation, Mhe. Rais Magufuli ameiagiza Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kuwahamisha wafanyakazi wote na maafisa wa umma (Employees and Public Officers) wa iliyokuwa TTCL kwenda TTCL Corporation.
Pia Mhe. Rais Magufuli amemuagiza Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa Mnyaa kutoivunja bodi ya iliyokuwa TTCL, wajumbe wake wote kuendelea na nafasi zao na kujaza nafasi za wajumbe zilizobaki ikiwa ni pamoja na nafasi moja ya mjumbe kutoka Zanzibar.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
12 Februari, 2018
Taarifa kwa vyombo vya habari
China imeridhia kutoa msaada wa Dola za Marekani Milioni 62 sawa na Shilingi Bilioni 138.3 za Tanzania kwa ajili ya ujenzi wa Chuo Kikuu cha Usafirishaji hapa nchini.
Balozi wa China hapa nchini Mhe. Wang Ke amesema hayo tarehe 12 Februari, 2018 muda mfupi baada ya kufanya mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt John Pombe Magufuli na kumkabidhi barua yenye ujumbe wa Rais wa China Mhe. Xi Jinping, Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Mhe. Wang Ke ameeleza kuwa msaada huo ni sehemu ya misaada na miradi mbalimbali ambayo China inaitekeleza hapa nchini Tanzania yenye lengo la kuimarisha uhusiano na ushirikiano kati yake na Tanzania.
Kwa upande wake Mhe. Rais Magufuli amemuomba Mhe. Wang Ke kumfikishia shukrani zake kwa Rais wa China kwa ujumbe na msaada huo ambao amesema utasaidia kuimarisha huduma za usafirishaji hapa nchini.
Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli amepokea taarifa kutoka kwa viongozi wa Shirika la Simu Tanzania kuhusu mwelekeo wa shirika hilo baada ya kuanza kutumika kwa sheria namba 12 ya mwaka 2017 ya Shirika la Simu Tanzania, iliyolibadili kutoka Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) na kuwa Shirika la Simu Tanzania (TTCL Corporation) kuanzia tarehe 01 Februari, 2018.
Pamoja na kupokea taarifa hiyo Mhe. Rais Magufuli amemteua Dkt. Omari Rashid Nundu kuendelea kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya TTCL Corp na Bw. Waziri Waziri Kindamba kuwa Mkurugenzi Mkuu wa TTCL Corp, na amewataka kuchapa kazi kwa juhudi na kuhakikisha TTCL Corp inaongeza ufanisi, na kutoa gawio kwa Serikali.
Dkt. Omari Rashid Nundu na Bw. Waziri Waziri Kindamba wamemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa uteuzi huo na wamesema TTCL itaendelea kujiimarisha kwa kupanua huduma za mawasiliano nchini, kuongeza na kuboresha bidhaa ikiwemo TTCL Pesa, kuzalisha faida zaidi na kuusimamia vizuri mkongo wa Taifa kwa maslahi na usalama wa nchi.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
12 Februari, 2018
Taarifa kwa vyombo vya habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 10 Februari, 2018 amempandisha cheo na kumteua Bw. Mohamed Hassan Haji kuwa Kamishna wa Polisi Zanzibar.
Taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi imefafanua kuwa Mhe. Rais Magufuli amempandisha cheo Bw. Mohamed Hassan Haji kutoka Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) na kuwa Kamishna wa Polisi (CP), na kisha kumteua kuwa Kamishna wa Polisi Zanzibar.
Kamishna wa Polisi Mohamed Hassan Haji amepandishwa cheo na kuteuliwa kuwa Kamishna wa Polisi Zanzibar kuanzia leo tarehe 10 Februari, 2018.
Kabla ya uteuzi huu Kamishna wa Polisi Mohamed Hassan Haji alikuwa Mhasibu Mkuu wa Polisi Zanzibar.
Kamishna wa Polisi Mohamed Hassan Haji anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Kamishna wa Polisi Hamad Omar Makame ambaye amestaafu.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
10 Februari, 2018
Taarifa kwa vyombo vya habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amewahakikishia Mabalozi na wakuu wa mashirika ya kimataifa waliopo hapa nchini kuwa katika mwaka 2018 Serikali ya Awamu ya Tano itaendeleza juhudi za kuboresha mazingira ya uwekezaji ikiwemo mapambano dhidi ya rushwa, kuboresha miundombinu ya barabara, reli na usafiri wa anga, kuongeza uzalishaji wa umeme na kukabiliana na vikwazo vya biashara.
Mhe. Rais Magufuli amesema hayo tarehe 09 Februari, 2018 katika hafla ya mwaka mpya aliyowaandalia Mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini, iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Kutokana na dhamira hiyo Mhe. Rais Magufuli ametoa wito kwa Mabalozi hao kuwahamasisha wawekezaji na wafanyabiashara kutoka nchi zao, kuja hapa nchini kuwekeza na kufanya biashara mbalimbali na kwamba Serikali itatoa ushirikiano wowote utakaohitajika.
Aidha, Mhe. Rais magufuli amesema mwaka 2017 ulikuwa wenye mafanikio makubwa kwa Serikali kitaifa na kimataifa, ambapo iliendelea kutekeleza mpango wa maendeleo wa miaka 5 (2016/17-2020/2012) unaolenga kuiwezesha nchi kuwa ya uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025 na ametaja baadhi ya mafanikio hayo kuwa ni kuziba mianya ya ukwepaji wa kodi kulikowezesha kuongezeka kwa mapato kwa asilimia 7.87, ikiwemo rekodi ya juu kuwahi kufikiwa hapa nchini ya ukusanyaji wa Shilingi Trilioni 1.66 mwezi Desemba 2017.
Mafanikio mengine ni ukuaji mzuri wa uchumi wa asilimia 6.8 katika nusu ya kwanza ya mwaka 2017, kudhibiti mfumuko wa bei uliokuwa chini ya asilimia 5.5, kuongezeka kwa akiba ya fedha za kigeni na kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo pamoja na kuboresha huduma za kijamii zinazowagusa zaidi wananchi kama vile afya, elimu na maji.
Kuhusu azma ya kujenga viwanda, Mhe. Rais Magufuli amesema utekelezaji wa azma hii unakwenda vizuri ambapo katika kipindi cha miaka miwili viwanda 3,500 vimejengwa na vingine vingi vinaendelea kujengwa.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli amesema kama ilivyofanya katika mwaka 2017 Tanzania itaendelea kutekeleza majukumu mbalimbali ya kikanda na kimataifa ikiwemo kushiriki katika juhudi za kutafuta amani, kushiriki harakati za usuluhishi wa migogoro ikiwemo ya Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Jamhuri ya Afrika ya Kati, Lebanon, Sudan na Sudani kusini.
Hata hivyo ameelezea kusikitishwa kwake na uamuzi wa Umoja wa Mataifa kuanza kutekeleza sera ya kupunguza gharama kwenye misheni za kulinda amani kwani kwa kufanya hivyo itadhohofisha jitihada za kutafuta amani kwenye maeneo yenye migogoro na kuhatarisha maisha ya walinda amani pamoja na raia wasio na hatia wanaoishi kwenye maeneo yenye migogoro.
Pia, Mhe. Rais Magufuli amesema pamoja na nia njema ya mpango wa majaribio wa kutafuta suluhu la kudumu ya tatizo la wakimbizi (Comprehensive Refugee Response Framework – CRRF) Tanzania imeamua kujitoa kutokana na changamoto za kiusalama na ukosefu wa fedha za kugharamia mpango huo.
Mhe. Rais Magufuli amezungumzia taarifa za kukamatwa kwa meli zenye kupeperusha bendera ya Tanzania zikiwa zimehusika katika uhalifu na kuwahakikishia Mabalozi hao kuwa meli hizo sio za Tanzania bali zilijipatia usajili wa Tanzania, na kwamba kufuatia hali hiyo Tanzania imechukua hatua ya kusitisha usajili wa meli zote 470 zenye usajili wa Tanzania na kusitisha zoezi la usajili mpya wa meli wakati uchunguzi zaidi ukiendelea kufanyika.
Kwa upande wake Naibu Kiongozi wa Mabalozi na wakuu wa mashirika ya kimataifa hapa nchini ambaye ni Balozi wa Saharawi Mhe. Brahim Salehe El-Mami Buseif amempongeza Mhe. Rais Magufuli na Serikali yake kwa juhudi kubwa zilizofanyika kuimarisha huduma za afya, elimu, maji na kuongeza ukusanyaji wa mapato na ameahidi kuwa Mabalozi na wakuu wa mashirika ya kimataifa wataendelea kushirikiana na Serikali katika kufanikisha miradi mbalimbali.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
09 Februari, 2018
Taarifa kwa vyombo vya habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 06 Februari, 2018 amezindua Kituo cha Mafunzo Maalum ya Kijeshi (Comprehensive Training Center – CTC) kilichopo Mapinga katika Wilaya ya Bagamoyo Mkoani Pwani.
Kituo hicho kimejengwa kwa msaada kutoka Jeshi la Ukombozi la Watu wa China kwa gharama ya Shilingi Bilioni 67.87 na kitatumika kutoa mafunzo ya kijeshi ya kisasa yatakayowawezesha askari kukabiliana na vitisho vya kisasa vya kiusalama.
Kabla ya kuzindua kituo hicho Mhe. Rais Magufuli na Balozi wa China hapa nchini Mhe. Wang Ke wameshuhudia makabidhiano ya kituo hicho kutoka Jeshi la Ukombozi la Wananchi wa China lililowakilishwa na Naibu Mkuu wa Idara ya Mafunzo na Utawala ya Kamisheni Kuu ya Jeshi hilo Jenerali Yang Jian kwenda kwa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) lililowakilishwa na Meja Jenerali Yakub Hassan Mohamed.
Mhe. Rais Magufuli pia ameshuhudia mazoezi ya kijeshi yaliyofanywa katika kituo hicho yakiwemo shambulizi la kutokea baharini (amphibian landing), makomandoo kukabiliana na magaidi na kupiga shabaha kwa kutumia miundombinu ya kisasa.
Akizungumza na Maafisa, Askari na wananchi waliojitokeza kushuhudia tukio la makabidhiano ya kituo hicho Mhe. Rais Magufuli amelishukuru Jeshi la Ukombozi la Watu wa China na Serikali ya China kwa kutoa msaada wa kujengwa kwa kituo hicho na amesema Serikali ya Awamu ya Tano inathamini na kutambua mchango wa China katika Jeshi la Ulinzi la wananchi wa Tanzania.
Mhe. Rais Magufuli amesema China imeendelea kudhihirisha urafiki na udugu wake na Tanzania kwani licha ya kujenga kituo hicho pia imetoa msaada wa kujenga kituo cha mafunzo ya kijeshi ya anga cha Ngerengere Mkoani Morogoro na miradi mingine ya maendeleo ya jamii na hivyo amemuomba Balozi wa China hapa nchini Mhe. Wang Ke kufikisha shukrani zake kwa Rais wa China Mhe. Xi Jinping.
Mhe. Wang Ke na Jen. Yang Jian wamesema China imejenga kituo hicho cha mafunzo maalum ya kijeshi ambacho ni alama nyingine ya uhusiano na ushirikiano wa kirafiki na kidugu kati yake na Tanzania na wameipongeza JWTZ kwa kupata kituo ambacho wanaamini kitatumika kuimarisha ulinzi na usalama wa Tanzania na nchi nyingine za Afrika.
Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi nchini Jenerali Venance Salvatory Mabeyo amesema miundo ya kituo hicho inakifanya kuwa kituo cha kimataifa kilicho bora zaidi Afrika Mashariki na Kati kitakachoweza kutoa mafunzo ya kisasa kwa askari wengi na amemuomba Mhe. Rais Magufuli kusaidia ujenzi wa daraja la mto Mpigi litakalokiunganisha na barabara ya kwenda Dar es Salaam.
Pamoja na kukubali ombi hilo Mhe. Rais Magufuli pia amekubali maombi ya Jen. Mabeyo ya kupeleka maji, umeme na barabara katika eneo ambalo China imekubali kutoa msaada wa kujenga makao makuu ya JWTZ Mkoani Dodoma na ameahidi kuziagiza wizara husika kutekeleza maombi hayo haraka.
Tukio la kukabidhiwa kwa kituo cha mafunzo maalum ya kijeshi limehudhuriwa na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Dkt. Hussein Mwinyi na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt. Augustine Mahiga.
Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli amezungumza na wananchi wa Mapinga waliosimamisha msafara wake na kumuomba awasaidie kulipwa fidia kufuatia maeneo yao kuchukuliwa kwa ajili ya miradi ukiwemo mradi wa ujenzi wa kituo hicho cha mafunzo cha jeshi na kuvunjiwa nyumba zao katika eneo la Makurunge.
Katika majibu yake Mhe. Rais Magufuli amesema Serikali haiwezi kurudia kuwalipa watu ambao tayari walishalipwa fidia na hawezi kuwatetea watu ambao wamevunja sheria kwa kuvamia maeneo yasiyokuwa yao.
Mhe. Rais Magufuli pia amesema Serikali ina dhamira ya dhati ya kutekeleza mradi wa bandari na eneo la uwekezaji la Bagamoyo na amewataka watu wote waliolipwa fidia wakati hawakuwa na maeneo warejeshe fedha za Serikali, waliolipwa fidia kuondoka katika maeneo yaliyolipiwa, na kwa wale ambao hawajalipwa fidia waendelee kutumia maeneo yao kwa shughuli zao mbalimbali.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
06 Februari, 2018