Taarifa kwa vyombo vya Habari ya zamani
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 08 Novemba, 2017 ametembelea shamba la miwa na kiwanda cha sukari cha Kagera (Kagera Sugar) kilichopo Wilayani Misenyi na kuagiza viwanda vyote vya kuzalisha sukari nchini kutafuta namna ya kuongeza uzalishaji ili kumaliza tatizo la upungufu wa tani 130,000 unaoikabili nchi kwa sasa.
Mhe. Rais Magufuli ametoa agizo hilo baada ya kutembelea shamba la miwa linalolimwa kwa kutumia teknolojia ya kisasa ya umwagiliaji (Centre Pivot) na kiwanda cha sukari cha Kagera ambacho uzalishaji wake kwa sasa ni tani 75,000 za sukari kwa mwaka ambazo zinaungana na tani nyingine 245,000 kutoka viwanda vingine nchini kufanya uzalishaji wa jumla ya tani 320,000 kiwango ambacho ni pungufu ikilinganishwa na mahitaji ya tani 420,000.
Mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi wa kiwanda hicho Bw. Seif Seif amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa hatua alizochukua kudhibiti uingizaji wa sukari hapa nchini na kueleza kuwa kabla ya kuchukua hatua hizo wazalishaji wa sukari walishaamua kufunga viwanda vyao kutokana na kukithiri kwa uingizaji holela wa sukari kutoka nchi za nje tena bila kuzingatia ubora na usalama kwa walaji.
Bw. Seif amebainisha kuwa hatua zilizochukuliwa na Mhe. Rais Magufuli zimewasaidia wazalishaji wa sukari kuanza kupiga hatua katika uwekezaji ambapo shamba la Kagera linalolima hekta 14,000 kwa mwaka na kuzalisha tani 75,000 za sukari limepanga kuendelea kupanua mashamba yake hadi kufikia hekta 30,000 na uzalishaji wa tani 170,000 za sukari ifikapo mwaka 2022.
Pamoja na kuipongeza Kagera Sugar kwa kufufua kiwanda hicho kilichokufa baada ya kupigwa mabomu wakati wa vita vya Kagera, Mhe. Rais Magufuli ambaye amezungumza na wafanyakazi wa kiwanda hicho, amekubali ombi la kujengwa kwa daraja katika mto Kagera litakalounganisha shamba hilo na Wilaya ya Karagwe ambako upanuzi wa kilimo cha miwa umepangwa kufanywa, na pia ametoa wito kwa mwekezaji huyo kuitumia benki ya kilimo (TAB) kupata mikopo.
“Shamba na kiwanda hiki mnaajiri watu 5,000 nawapongeza sana na sisi Serikali ni lazima tuwaunge mkono, kuhusu ombi la daraja, tutalijenga na nakuagiza Katibu Mkuu wa Ujenzi Bw. Joseph Nyamuhanga ifikapo Januari 2018 muanze kujenga, kwa kuwa Bw. Seif ameshanunua vyuma vya ujenzi, na pia tumepata fedha kutoka benki ya maendeleo Afrika (AfDB) Shilingi Bilioni 242, hizo zote tunazipeleka kwenye benki ya kilimo, Bw. Seif sasa nenda ukakope huko, na ukikopa uelekeze kwenye kilimo” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli amekubali pendekezo la kuwatumia wazalishaji wa sukari wa hapa nchini kuagiza sukari inayopungua ili kukidhi mahitaji ya nchi, lakini ameonya kuwa mwanya huo usitumiwe kuingiza sukari isiyo bora na salama na ametaka utaratibu huo ufanywe kwa muda mfupi wakati viwanda vinaongeza uzalishaji wake ili hatimaye Serikali ipige marufuku uingizaji wa sukari kutoka nje ya nchi.
Pia, amempa siku tatu Waziri wa Kilimo Dkt. Charles Tizeba kuwaondoa mara moja Maafisa wote waliokuwa wakitoa vibali kwa waingizaji wa sukari hapa nchini kutokana na vitendo vyao vya kutoa vibali hovyo na hivyo kudhohofisha viwanda vya ndani.
Kabla ya kufika Kagera Sugar Mhe. Rais Magufuli amezungumza na wananchi wa Bunazi na kusikiliza kero zao ikiwemo ya kuuziwa sukari kwa bei ya juu ikilinganishwa na bei ya Bukoba Mjini, na kufuatia kero hiyo ameitaka Kagera Sugar kumpa uwakala mfanyabiashara wa Bunazi Richard Lulinda ili aweze kuwauzia sukari wananchi wanaozunguka shamba hilo kwa bei nafuu.
Kuhusu kero ya wananchi wa Bunazi kukodishwa mashamba ya kulima mazao katika eneo la kijiji Mhe. Rais Magufuli amepiga marufuku ukodishaji huo na amechangia shilingi Milioni 5 kwa ajili ya kukamilisha majengo ya shule ambayo viongozi wa kijiji walidai wanakamilisha ujenzi huo kwa kutumia fedha za kukodisha maeneo ya kijiji.
Akiwa anarejea Bukoba Mjini Mhe. Rais Magufuli amesimamishwa na wananchi wa Rwamishenye na kupokea kero zao ambapo pamoja na kuwachangia Shilingi Milioni 5 kwa ajili ya ujenzi wa majengo ya shule amewataka wawaambie viongozi wao kata na mitaa kufikisha Serikalini andiko la kujengewa Soko.
Katika ziara hii Mhe. Rais Magufuli ameongozana na Mkewe Mama Janeth Magufuli, Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mhe. Charles Mwijage, Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani na Waziri wa Kilimo Dkt. Charles Tizeba.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Bukoba
08 Novemba, 2017
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 07 Novemba, 2017 amefungua barabara ya lami ya Kyaka – Bugene Mkoani Kagera yenye urefu wa kilometa 59.1 iliyogharimu Shilingi Bilioni 81.597 fedha zote zikiwa zimetolewa na Serikali ya Tanzania.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) Mhandisi Patrick Mfugale amemueleza Mhe. Rais Magufuli kuwa barabara hiyo ni sehemu ya barabara ya Kyaka – Bugene – Kasulo yenye urefu wa kilometa 183.1 ambayo inaiunganisha Tanzania na nchi jirani za Rwanda na Burundi.
Kabla ya kufungua barabara hiyo Mhe. Rais Magufuli akiwa na Mkewe Mama Janeth Magufuli amesafiri kwa barabara hiyo kutoka Kyaka hadi Karagwe zilipofanyika sherehe za ufunguzi na amempongeza mkandarasi, kampuni ya CHICO ya China, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa Mnyaa na timu ya wataalamu wa TANROADS kwa kuusimamia mradi huo wao wenyewe kwa gharama ya shilingi Milioni 519.2 badala ya kuajiri msimamizi ambaye angelipwa zaidi Shilingi Bilioni 4.5.
“Napenda kuwapongeza sana TANROADS kwa kusimamia mradi huu nyinyi wenyewe, zaidi ya Shilingi Bilioni 4 mlizookoa kwa kuwatumia wataalamu wetu kuusimamia mradi huu ni fedha nyingi sana, nataka kitengo hiki cha usimamizi wa miradi tukiimarishe, hivi sasa tunao wahandisi 15,000 wanaoweza kufanya kazi hizi, tuwatumie” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Mhe. Rais Magufuli pia amezungumza na waandishi wa habari waliokuwa wakirekodi na kurusha matangazo ya sherehe hizo ambapo amewashukuru kwa kazi kubwa wanayoifanya na amewahakikishia kuwa Serikali itaendelea kushirikiana nao, na ipo tayari kuwasaidia ikiwa ni pamoja na kuwezesha mafunzo ya kuwaongezea ujuzi.
Sherehe za ufunguzi wa barabara ya Kyaka – Bugene zimehudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mhe. Charles Mwijage, Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani, Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu wakiongozwa na Prof. Norman Sigalla King, Wabunge wa Mkoa wa Kagera na viongozi wa Dini na Siasa.
Akiwa njiani kuelekea Karagwe Mhe. Rais Magufuli amesimamishwa na wananchi wa Kyaka na kusikiliza kero zao ambapo amewaagiza viongozi wa Mkoa wa Kagera kutowabughudhi wananchi wanaojihusisha na shughuli za kilimo, na badala yake wawasaidie kuondoa migogoro ya ardhi, kusajiri mifugo yao na kuinua uzalishaji wa mazao ili Mkoa wa Kagera uwe na malighafi za kutosha kuanzisha viwanda.
“Pale Mtukula tumejenga kituo cha pamoja cha huduma mpakani (One Stop Border Post) kati yetu na Uganda, lengo letu ni kurahisisha biashara kati ya Tanzania na Uganda, kwa hiyo nataka kuona wananchi wa Kagera mnachangamkia fursa hii, anzisheni viwanda kama vya nyama na mazao mengine ya kilimo, fugeni mifugo kisasa ili mnufaike” amebainisha Mhe. Rais Magufuli.
Akiwa Bukoba Mjini kundi kubwa la wananchi wa mji huo limeusimamisha msafara wake ambapo baada ya kupokea kero mbalimbali, Mhe. Rais Magufuli ameahidi kutekeleza ahadi yake ya kutatua tatizo la uhaba wa maji katika mji huo na ametoa wito kwa viongozi wa Manispaa ya Bukoba kuwasilisha Serikalini andiko la kuomba kujengewa kituo cha mabasi kama wananchi walivyomuomba.
“Ndugu zangu mimi nipo pamoja na nyinyi, kero zenu nazijua na tutazishughulikia, ninachowaomba punguzeni kubishana, mnapoteza muda mwingi kubishana badala ya maendeleo, mnajichelewesha, Mji huu hautakiwi uwe hivi ulivyo” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Mhe. Rais Magufuli kesho tarehe 08 Novemba, 2017 ataendelea na ziara yake Mkoani Kagera ambapo atatembelea shamba la miwa na kiwanda cha sukari cha Kagera kilichopo Misenyi na kujionea uwekezaji mkubwa na wa kisasa.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Bukoba
07 Novemba, 2017
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amefungua miundombinu mipya ya uwanja wa ndege wa Bukoba Mkoani Kagera na kuiagiza Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kuachana na mpango wa kujenga uwanja mpya katika eneo la Omukajunguti na badala yake waongeze urefu wa barabara ya kurukia ndege katika uwanja wa ndege wa Bukoba ili ndege kubwa zaidi ziweze kutumia uwanja huo.
Mhe. Rais Magufuli aliyeongozana na Mkewe Mama Janeth Magufuli amesema ujenzi wa uwanja mpya katika eneo la Omukajunguti utasababisha Serikali kutumia fedha nyingi bila sababu zikiwemo Shilingi Bilioni 9.2 za kulipa fidia na gharama kubwa za kujenga uwanja katika eneo hilo chepechepe.
Hata hivyo Mhe. Dkt. Magufuli ameipongeza Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA), Wakandarasi Wazalendo waliojenga uwanja wa ndege Bukoba na wananchi wa Bukoba kwa kufanikisha ujenzi wa uwanja huo ambao utasaidia kuchochea uchumi kwa kuendeleza na kukuza utalii, ujenzi wa viwanda na biashara mbalimbali.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TAA Bw. Richard Mayongela amemueleza Mhe. Rais Magufuli kuwa kazi za ujenzi, upanuzi na ukarabati wa uwanja huo zimehusisha ujenzi wa barabara ya kurukia ndege yenye urefu wa mita 1,500 na upana wa mita 30, ujenzi wa eneo la kuegesha ndege, ujenzi wa eneo la kuegesha magari, ujenzi wa jengo la abiria, kituo cha kuzalisha umeme wa dharula na kufunga mifumo ya kisasa ya ukaguzi, ubebaji mizigo na kurekodi matukio (CCTV).
Bw. Mayongela amesema ujenzi, upanuzi na ukarabati huo umegharimu Shilingi Bilioni 31.95 ambapo kati yake Shilingi Bilioni 6.35 zimetolewa na Serikali ya Tanzania na fedha nyingine zimetolewa kwa mkopo nafuu kutoka Benki ya Dunia.
Nae Mwakilishi wa Benki ya Dunia Bw. Andre Bald amempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa Tanzania kuwa na uchumi unaokuwa vizuri na kwa kasi na ameelezea kufurahishwa na matunda ya ushirikiano kati ya Tanzania na Benki ya Dunia katika kufanikisha miradi mbalimbali nchini ukiwemo mradi wa uwanja wa ndege wa Bukoba.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa Mnyaa amesema mradi wa ujenzi, upanuzi na ukarabati wa uwanja wa ndege wa Bukoba ni moja ya miradi mitatu inayotekelezwa, mingine ikiwa ni viwanja vya ndege vya Tabora na Kigoma ambapo Benki ya Dunia imetoa mkopo nafuu wa Shilingi Bilioni 129 na Serikali ya Tanzania imetoa Shilingi Bilioni 26.
Prof. Mbarawa ameongeza kuwa katika mwaka huu wa fedha Serikali itafanya upembuzi yakinifu katika viwanja vya ndege 11 hapa nchini ambavyo ni Singida, Lindi, Njombe, Iringa, Musoma, Ziwa Manyara, Kilwa Masoko, Songea, Tanga, Moshi na Simiyu na kwamba kati ya viwanja hivyo upanuzi na ukarabati utafanyika katika viwanja vya ndege vya Songea, Iringa na Musoma katika mwaka huu wa fedha.
Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli amesema Serikali itaanza kulipa stahili mbalimbali za wafanyakazi kuanzia mwezi huu na kubainisha kuwa malipo hayo yanafanyika baada ya kufanya uhakiki ambao umesaidia kutambua udanganyifu mkubwa katika baadhi ya madai ya wafanyakazi.
Ametoa mfano wa baadhi ya wadai hao kuwa ni Jakson Kaswahili Robert wa Ukerewe anayedai Shilingi Bilioni 7 na Milioni 626 wakati uhakiki umebaini kuwa hadai kitu, Mwachano Ramadhan Msingwa wa Bagamoyo anayedai Shilingi Bilioni 1 na Milioni 754 wakati uhakiki umebaini kuwa anadai Shilingi Milioni 2 na Gideon Zakayo anayedai Milioni 104, na ameagiza vyombo vya dola kuwachunguza wafanyakazi hao pamoja na watumishi wa Menejimenti ya Utumishi wa Umma ambao waliidhinishi watu hao walipwe madai hayo.
Mhe. Rais Magufuli amesema katika jitihada za kuwajali wafanyakazi Serikali imetoa Shilingi Trilioni 1.2 kulipa madeni ya mifuko ya hifadhi ya jamii na ameeleza kuwa ili kuongeza ufanisi Serikali inapeleka bungeni muswada wa kuunganisha mifuko ya hifadhi ya jamii ili ibaki mifuko miwili, mmoja utakaoshughulikia wafanyakazi wa umma na mwingine utakaoshughulikia wateja kutoka sekta binafsi.
Ametoa wito kwa Watanzania kuendelea kuunga mkono juhudi mbalimbali za Serikali ya Awamu ya Tano na amewataka wanasomi wakiwemo wanasheria kusaidia kupigania maslahi ya nchi ikiwemo kesi mbalimbali zilizofunguliwa katika mahakama za kimataifa na juhudi za kupigania rasilimali za Taifa badala ya kupinga mitandaoni.
Sherehe hizo zimehudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge inayoshughulikia miundombinu, Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani, Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mhe. Charles Mwijage na Wabunge wa Mkoa wa Kagera.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Bukoba
06 Novemba, 2017
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 06 Novemba, 2017 ametengua uteuzi wa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba Bw. Erasto Aron Mfugale na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba Vijijini Bi. Mwantum Kitwana Dau.
Bw. Erasto Aron Mfugale na Bi. Mwantumu Kitwana Dau watapangiwa kazi nyingine.
Kufuatia hatua hiyo uteuzi wa Wakurugenzi wa Halmashauri hizo utafanywa baadaye.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Bukoba
06 Novemba, 2017
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 06 Novemba, 2017 ameanza ziara ya kikazi ya siku 4 katika Mkoa wa Kagera.
Akiwa njiani Kutoka Chato Mkoani Geita alikokuwa mapumzikoni kuelekea Bukoba Mjini Mhe. Rais Magufuli amezungumza na wananchi wa Muleba na Kemondo, Bukoba Vijijini na kuwahakikishia kuwa Serikali itasaini mkataba na kampuni ya kutoka Jamhuri ya Korea kati ya mwezi Desemba mwaka huu na Januari mwakani kwa ajili ya kuanza kuunda meli mpya katika ziwa Victoria itakayokuwa na uwezo wa kubeba idadi kubwa ya abiria na mzigo mkubwa zaidi ikilinganishwa na meli zilizopo
“Tunaunda meli ya kisasa itakayobeba abiria wengi na mizigo mingi, na pia tutakarabati meli zilizopo za MV Victoria na MV Butiama, tunataka pamoja na kujenga barabara, tuhakikishe kuna meli za uhakika ili muweze kusafiri na kusafirisha mazao yenu kwenda kwenye masoko” amesema Rais Magufuli.
Kuhusu ufugaji Mhe. Rais Magufuli amewaagiza viongozi wa Mkoa wa Kagera kuhakikisha mifugo yote inawekwa alama kwa mujibu wa sheria, ili kurahisisha utambuzi wa mifugo inayoingizwa nchini kutoka nchi jirani na pia kudhibiti ruzuku inayotolewa na Serikali kwa dawa za mifugo ya hapa nchini.
“Tanzania sio shamba la kuchungia mifugo ya nchi jirani, ndio maana tumeamua kukamata mifugo na kuchukua hatua kwa mujibu wa kisheria, na hata huko kwenye nchi jirani wakishika mifugo ya kutoka Tanzania wachukue hatua za kisheria za nchi hizo” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Hata hivyo amewataka wananchi wa Kagera kuacha kuvamia maeneo ya hifadhi ikiwemo hifadhi ya Burigi na ameagiza viongozi wa Wilaya ya Muleba kufuatilia madai ya wananchi juu ya kuuzwa kwa ardhi ya kijiji kulikosababisha wananchi kukosa maeneo ya kulima na kulisha mifugo yao.
“Na kuna watu waliouziwa ranchi na Serikali, watu hao hawajaziendeleza ranchi hizo na badala yake wanawakodisha wananchi, wafuatilieni na mkiona hawajaziendeleza nyang’anyeni muwape wananchi wazitumie kwa ufugaji, lakini pia hakikisheni wananchi hawavamii maeneo ya hifadhi yaliyotengwa” ameongeza Mhe. Rais Magufuli.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli amewaagiza viongozi wa Mkoa na Wilaya za Mkoa wa Kagera kuwachukulia hatua maafisa wote wa halmashauri ambao bado wanawatoza ushuru wakulima wanaosafirisha mazao yaliyo chini ya tani moja kwa kuwa tayari Serikali imeshaamua kuondoa adha hiyo na kuwawezesha wakulima wadogo kunufaika na kilimo chao.
Mchana wa leo (06 Novemba, 2017) Mhe. Rais Magufuli atafungua mradi wa upanuzi wa uwanja wa ndege wa Bukoba.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Bukoba
06 Novemba, 2017
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 31 Oktoba, 2017 amefungua kiwanda cha kuzalisha bidhaa za plastiki cha Victoria Moulders na kiwanda cha dawa za binadamu cha Prince Pharmaceuticals Co. Ltd vilivyopo katika wilaya ya Nyamagana Mkoani Mwanza.
Mmiliki wa kiwanda cha Victoria Moulders Bw. Manjit Singn amemueleza Mhe. Rais Magufuli kuwa kiwanda hicho pamoja na kiwanda dada cha Poly Bags vilivyopo katika eneo moja la Igogo vimeajiri watu 500 na vinazalisha bidhaa za plastiki ambazo ni Mabomba ya maji, matanki ya maji, ndoo, nyavu na mifuko ya kuhifadhia nafaka.
Kiwanda cha dawa cha Prince Pharmaceuticals kilichopo Buhongwa kinazalisha aina 26 za dawa na uwezo wake ni kuzalisha kilogram 1,400 na lita 5,000 za aina mbalimbali za dawa kwa siku, ambazo husambwazwa kupitia MSD na wafanyabiashara.
Mkurugenzi wa Kiwanda hicho Bw. Hetal Vithlani amemueleza Mhe. Rais Magufuli kuwa kabla ya Serikali ya Awamu ya Tano kuingia madarakani alipoteza matumaini ya kuendelea na mradi huo lakini sasa amepata matumaini mapya baada ya Serikali kuanza kununua dawa ambapo MSD imeagiza aina 7 za dawa zenye thamani ya Shilingi Bilioni 2.2 na kwamba ifikapo mwaka 2020 kiwanda kitaongeza uzalishaji wa dawa za maji kutoka lita 5,000 hadi kufikia lita 10,000.
Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mhe. Charles Mwijage amesema viwanda hivyo ni muhimu kwa kuwa vipo katika kundi la viwanda vinavyozalisha bidhaa zenye mahitaji makubwa.
Mhe. Mwijage amemueleza Mhe. Rais Magufuli kuwa nchi inahitaji tani Miliomi 15 za mifuko ya kuhifadhia mazao ikilinganishwa na tani milioni 5 zinazozalishwa kwa mwaka hivi sasa, na kwamba juhudi za kuwahamasisha wawekezaji zinaendelea. Kwa dawa za binadamu amesema ndani ya miezi 18 viwanda vitatu vya kutengeneza dawa na kimoja cha kutengeneza dripu za maji ya wagonjwa vitajengwa.
Kwa upande wake Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu amesema ujenzi wa viwanda vya dawa utasaidia kuokoa fedha nyingi ambazo Serikali inazitumia kununua dawa kutoka nje ya nchi ambapo hivi asilimia 80 ya dawa zinaagizwa nje ya nchi.
Pamoja na kumshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa msukumo wake wa kuongeza bajeti ya dawa kutoka Shilingi Bilioni 31 hadi kufikia Shilingi Bilioni 269, Mhe. Ummy Mwalimu amesema Serikali itajenga kiwanda cha kuzalisha dripu za maji ili kuokoa Shilingi Bilioni 12 ambazo hutumika kila mwaka kuagiza dripu kutoka nje ya nchi.
Ameongeza kuwa Serikali imeendelea kuimarisha usambazaji wa dawa na hivi karibuni bodi ya dawa (MSD) itapatiwa magari mapya 190 ya kusambazia dawa nchini na kwamba kutokana na kazi nzuri inayofanywa, MSD imeteuliwa kuwa msambazaji wa dawa katika nchi 15 za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).
Akizungumza baada ya kufungua viwanda hivyo Mhe. Rais Magufuli amezipongeza kampuni za Victoria Moulders na Prince Pharmaceuticals kwa kuwekeza viwanda hivyo na ametoa wito kwa wafanyabiashara kote nchini kujitokeza kuwekeza katika ujenzi wa viwanda kwa kuwa Serikali itawaunga mkono.
“Niwaombe wafanyabiashara wa Tanzania na wasomi, badala ya kulalamika fedha zimepotea jengeni viwanda, huyu mwenye kiwanda cha Prince Pharmaceuticals alikuwa anataka kufunga mradi wa kiwanda hiki lakini baada ya Serikali ya Awamu ya Tano kuingia madarakani anapata fedha, haingii akilini nchi iwe inaagiza dripu kutoka nje ya nchi” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli ametoa wiki mbili kwa wawekezaji waliopewa viwanda vya TPI na Keko Pharmaceuticals ambavyo Serikali ina hisa, kuanza uzalishaji mara moja vinginevyo wanyang’anywe na wapewe wawekezaji ambao wapo tayari kuanza uzalishaji.
“Mhe. Waziri umewapa mwezi mmoja ni muda mrefu mno, mimi nawapa wiki mbili wawe wameanza uzalishaji wa dawa, tumewasubiri imetosha, kama hawawezi kuanza kutengeneza dawa wapewe wengine wenye uwezo” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Akiwa njiani wakati wa kutembelea viwanda hivyo, Mhe. Rais Magufuli amezungumza na wananchi wa Butimba na kuwahakikishia kuwa Serikali imedhamiria kurejesha viwanda vilivyokuwepo kati ya eneo la Mkuyuni na Igogo Mjini Mwanza kikiwemo kiwanda cha kusaga nafaka ambacho Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF) tayari limetenga Shilingi Bilioni 8 kwa ajili ya kukifufua.
Mhe. Rais Magufuli amemaliza ziara yake ya siku mbili Mkoani Mwanza na amewasili Kijijini kwake Chato Mkoani Geita kwa mapumziko.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Chato
31 Oktoba, 2017
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 31 Oktoba, 2017 amefungua kiwanda cha kuzalisha bidhaa za plastiki cha Victoria Moulders na kiwanda cha dawa za binadamu cha Prince Pharmaceuticals Co. Ltd vilivyopo katika wilaya ya Nyamagana Mkoani Mwanza.
Mmiliki wa kiwanda cha Victoria Moulders Bw. Manjit Singn amemueleza Mhe. Rais Magufuli kuwa kiwanda hicho pamoja na kiwanda dada cha Poly Bags vilivyopo katika eneo moja la Igogo vimeajiri watu 500 na vinazalisha bidhaa za plastiki ambazo ni Mabomba ya maji, matanki ya maji, ndoo, nyavu na mifuko ya kuhifadhia nafaka.
Kiwanda cha dawa cha Prince Pharmaceuticals kilichopo Buhongwa kinazalisha aina 26 za dawa na uwezo wake ni kuzalisha kilogram 1,400 na lita 5,000 za aina mbalimbali za dawa kwa siku, ambazo husambwazwa kupitia MSD na wafanyabiashara.
Mkurugenzi wa Kiwanda hicho Bw. Hetal Vithlani amemueleza Mhe. Rais Magufuli kuwa kabla ya Serikali ya Awamu ya Tano kuingia madarakani alipoteza matumaini ya kuendelea na mradi huo lakini sasa amepata matumaini mapya baada ya Serikali kuanza kununua dawa ambapo MSD imeagiza aina 7 za dawa zenye thamani ya Shilingi Bilioni 2.2 na kwamba ifikapo mwaka 2020 kiwanda kitaongeza uzalishaji wa dawa za maji kutoka lita 5,000 hadi kufikia lita 10,000.
Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mhe. Charles Mwijage amesema viwanda hivyo ni muhimu kwa kuwa vipo katika kundi la viwanda vinavyozalisha bidhaa zenye mahitaji makubwa.
Mhe. Mwijage amemueleza Mhe. Rais Magufuli kuwa nchi inahitaji tani Miliomi 15 za mifuko ya kuhifadhia mazao ikilinganishwa na tani milioni 5 zinazozalishwa kwa mwaka hivi sasa, na kwamba juhudi za kuwahamasisha wawekezaji zinaendelea. Kwa dawa za binadamu amesema ndani ya miezi 18 viwanda vitatu vya kutengeneza dawa na kimoja cha kutengeneza dripu za maji ya wagonjwa vitajengwa.
Kwa upande wake Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu amesema ujenzi wa viwanda vya dawa utasaidia kuokoa fedha nyingi ambazo Serikali inazitumia kununua dawa kutoka nje ya nchi ambapo hivi asilimia 80 ya dawa zinaagizwa nje ya nchi.
Pamoja na kumshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa msukumo wake wa kuongeza bajeti ya dawa kutoka Shilingi Bilioni 31 hadi kufikia Shilingi Bilioni 269, Mhe. Ummy Mwalimu amesema Serikali itajenga kiwanda cha kuzalisha dripu za maji ili kuokoa Shilingi Bilioni 12 ambazo hutumika kila mwaka kuagiza dripu kutoka nje ya nchi.
Ameongeza kuwa Serikali imeendelea kuimarisha usambazaji wa dawa na hivi karibuni bodi ya dawa (MSD) itapatiwa magari mapya 190 ya kusambazia dawa nchini na kwamba kutokana na kazi nzuri inayofanywa, MSD imeteuliwa kuwa msambazaji wa dawa katika nchi 15 za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).
Akizungumza baada ya kufungua viwanda hivyo Mhe. Rais Magufuli amezipongeza kampuni za Victoria Moulders na Prince Pharmaceuticals kwa kuwekeza viwanda hivyo na ametoa wito kwa wafanyabiashara kote nchini kujitokeza kuwekeza katika ujenzi wa viwanda kwa kuwa Serikali itawaunga mkono.
“Niwaombe wafanyabiashara wa Tanzania na wasomi, badala ya kulalamika fedha zimepotea jengeni viwanda, huyu mwenye kiwanda cha Prince Pharmaceuticals alikuwa anataka kufunga mradi wa kiwanda hiki lakini baada ya Serikali ya Awamu ya Tano kuingia madarakani anapata fedha, haingii akilini nchi iwe inaagiza dripu kutoka nje ya nchi” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli ametoa wiki mbili kwa wawekezaji waliopewa viwanda vya TPI na Keko Pharmaceuticals ambavyo Serikali ina hisa, kuanza uzalishaji mara moja vinginevyo wanyang’anywe na wapewe wawekezaji ambao wapo tayari kuanza uzalishaji.
“Mhe. Waziri umewapa mwezi mmoja ni muda mrefu mno, mimi nawapa wiki mbili wawe wameanza uzalishaji wa dawa, tumewasubiri imetosha, kama hawawezi kuanza kutengeneza dawa wapewe wengine wenye uwezo” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Akiwa njiani wakati wa kutembelea viwanda hivyo, Mhe. Rais Magufuli amezungumza na wananchi wa Butimba na kuwahakikishia kuwa Serikali imedhamiria kurejesha viwanda vilivyokuwepo kati ya eneo la Mkuyuni na Igogo Mjini Mwanza kikiwemo kiwanda cha kusaga nafaka ambacho Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF) tayari limetenga Shilingi Bilioni 8 kwa ajili ya kukifufua.
Mhe. Rais Magufuli amemaliza ziara yake ya siku mbili Mkoani Mwanza na amewasili Kijijini kwake Chato Mkoani Geita kwa mapumziko.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Chato
31 Oktoba, 2017
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amefungua kiwanda cha vinywaji baridi cha Sayona kilichopo Nyakato Mjini Mwanza kilichojengwa na kampuni ya Kitanzania ya Motisan kwa gharama ya takribani Shilingi Bilioni 11 na Milioni 800.
Kiwanda hiki cha kisasa ambacho kimejengwa kwa muda wa mwaka mmoja na nusu kina uwezo wa kuzalisha chupa 1,200 kwa dakika moja katika mitambo yake minne ya kuzalisha vinywaji baridi pamoja na chupa 100 za maji, kimezalisha ajira za watu 200 na kinaungana na kiwanda kingine cha vinywaji baridi cha Sayona kilichopo Mboga Mkoani Pwani kusindika matunda ya wakulima na kuinua hali zao za maisha.
Akizungumza baada ya Mhe. Rais kufungua kiwanda cha Sayona Mwanza, Mkurugenzi Mkuu wa Motisan Group Bw. Subhash Patel amesema kampuni yake imedhamiria kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano za kujikita katika uchumi wa viwanda na ameahidi kuwa mwaka ujao wa 2018 kampuni hiyo itajenga viwanda vingine vitano.
Mhe. Rais Magufuli amempongeza Bw. Subhash Patel kwa uwekezaji mkubwa anaoufanya katika viwanda na amemtaka yeye pamoja na wafanyabiashara wengine kutumia muda huu kuwekeza zaidi katika viwanda na kwamba Serikali yake itawaunga mkono.
“Bw. Subhash nakupongeza sana, wewe jenga viwanda Serikali itakuunga mkono, na nataka niwaambie wafanyabiashara na wawekezaji, huu ndio wakati wa kuwekeza na mimi nawapenda wafanyabiashara na wawekezaji, hapa kusingekuwa na kiwanda hiki, vijana hawa 200 wasingepata ajira, nataka kukupongeza sana hata kwa mpango wako wa kujenga viwanda vingine vitano mwakani, hii ni safi sana” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Mhe. Dkt. Magufuli amempongeza Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Bw. John Mongella kwa juhudi anazofanya kusimamia utekelezaji wa sera ya viwanda kwa kuhakikisha viwanda vinaanzishwa na ametaka juhudi hizo ziendelee ili Mwanza irejeshe historia yake ya kuwa na viwanda vingi vinavyozalisha ajira na kukuza uchumi wa mkoa.
Wakizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika eneo la Nyakato Mwatex Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mhe. Charles Mwijage, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa Mnyaa na Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Anjelina Mabula wamewahakikishia wananchi wa Mwanza kuwa Serikali ya Awamu ya Tano inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuuendeleza Mkoa wa Mwanza kwa kuhakikisha viwanda zaidi vinajengwa, miundombinu inaimarishwa na migogoro ya ardhi inamalizwa na wamewataka wananchi wajielekeze zaidi katika uzalishaji mali.
Katika mkutano huo, Mbunge wa Nyamagana Mhe. Stanslaus Mabula, Umoja wa Wamachinga na Umoja wa Wanawake wajasiriamali Mkoa wa Mwanza wamemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa juhudi kubwa anazofanya kuwajali wananchi hasa wa hali ya chini na kupigania maendeleo ya Taifa zima.
Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli amezungumzia utekelezaji wa ahadi ya kutoa Shilingi Milioni 50 kwa kila Kijiji ama Mtaa kwa kueleza kuwa Serikali imeona njia bora ni kuelekeza fedha hizo katika miradi mikubwa yenye manufaa na matokeo mapana kwa wananchi na amesisitiza kuwa utekelezaji wa dhamira hiyo umeanza.
Amebainisha kuwa pamoja na hatua hizo Serikali inaendelea kukabiliana na wote waliojihusisha na ufisadi wa mali za umma na kwamba haitasita kuchukua hatua za kisheria hata kama wahusika watakimbia, kujificha ama kutetewa mahali popote.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Mwanza
30 Oktoba, 2017
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 30 Oktoba 2017, ameondoka jijini Dar es salaam kuelekea mkoani Mwanza, ambapo pamoja akiwa mkoani humo atafungua Mradi wa Ujenzi wa daraja la watembea kwa miguu lililopo eneo la Furahisha.
Baadae Rais Magufuli atafungua Kiwanda cha Vinywaji baridi cha Sayona kilichopo Nyakato mkoani humo na kufanya Mkutano wa Hadhara.
Katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalim Julius Nyerere, Mhe. Rais Magufuli ameagwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe. Paul Makonda.
Jaffar Haniu
Naibu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
30 Oktoba, 2017
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 27 Oktoba 2017 amewaapisha Wakuu wa Mikoa 6, Makatibu Wakuu 4 na Naibu Makatibu Wakuu 7 aliowateua jana tarehe 26 Oktoba, 2017.
Hafla ya kuapishwa kwa viongozi hao imefanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan, Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, Spika wa Bunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job Yustino Ndugai, Mawaziri, Wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama na viongozi wengine mbalimbali.
Wakuu wa mikoa walioapishwa ni Mkuu wa Mkoa wa Mara Bw. Adam Kighoma Malima, Mkuu wa Mkoa Manyara Bw. Alexander Pastory Mnyeti, Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Bw. Joackim Leonard Wangabo, Mkuu wa Mkoa wa Geita Bw. Robert Gabriel Lughumbi, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Bw. Gelasius Gasper Byakanwa na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Bi. Christina Solomon Mndeme.
Awali Bi. Christina Solomoni Mndeme aliapishwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma na baada ya kiapo Mhe. Rais Magufuli amefanya mabadiliko kwa kumhamisha kituo cha kazi na kuwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Dkt. Binilith Mahenge amehamishwa na sasa atakuwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma.
Makatibu Wakuu walioapishwa ni Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira Mhandisi Joseph Kizito Malongo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Bi. Suzan Paul Mlawi, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Bi. Dorothy Stanley Mwanyika na Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Prof. Simon Samwel Msanjila.
Naibu Makatibu Wakuu walioapishwa ni Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Bi. Dorothy Aidan Mwaluko, Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Bi. Butamo Kasuka Phillip, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Dkt. Thomas Didimu Kashililah na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango (Utawala) Bi. Susana Bernard Mkapa.
Wengine ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji (Biashara na Uwekezaji) Prof. Joseph Rwegasira Bushweishaija, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Bw. Niclolaus William na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji (Viwanda) Bw. Ludovick James Nduhiye.
Akizungumza baada ya kuwaapisha, Mhe. Rais Magufuli amewataka viongozi hao kuwatumikia wananchi vizuri kwa kutatua kero zinazowakabili na kuleta mabadiliko yatakayosaidia kuboresha maisha yao.
Ametolea mfano wa Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kuwa hatarajii kusikia wanafunzi vyuo vya elimu ya juu wamecheleweshewa mikopo kwa kuwa tayari Hazina imeshapeleka Shilingi Bilioni 147 kwa ajili ya mikopo ya wanafunzi ambao vyuo vinafunguliwa hivi karibuni.
“Nataka kila Mkuu wa Mkoa na Mkuu wa Wilaya ajiulize amefanya nini kubadili maisha ya wananchi wa Mkoa wake ama Wilaya yake, nataka Makatibu Makuu na Naibu Makatibu Wakuu wakatatue kero zilizopo katika wizara zao” Amesema Mhe. Rais Magufuli.
Mhe. Rais Magufuli amemtaka Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Adolf Mkenda kufanya mabadiliko ya kiutendaji katika Wizara hiyo ikiwa ni pamoja na kusimamia vizuri diplomasia ya uchumi, kuhakikisha kila Balozi anayeiwakilisha Tanzania nje ya nchi anafanya kazi yenye kuleta manufaa kwa Tanzania na kuondoa watumishi wa waliopo katika Balozi mbalimbali duniani pasipo sababu za msingi za kuwepo kwao nje ya nchi.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
27 Oktoba, 2017
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 26 Oktoba, 2017 amefanya mabadiliko katika safi ya Makatibu Wakuu, Naibu Makatibu Wakuu na Wakuu wa Mikoa kwa kuteua, kupandisha vyeo na kuhamisha vituo vya kazi.
Taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi Ikulu Jijini Dar es Salaam imeeleza kuwa Mhe. Rais Magufuli ameteua amewapandish Naibu Makatibu Wakuu 4 na kuwa Makatibu Wakuu wapya, ameteua Naibu Makatibu Wakuu wapya 7 na amewahamisha vituo vya kazi Makatibu Wakuu 4 na Naibu Katibu Mkuu 1.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli amefanya uteuzi wa Wakuu wa Mikoa 3 na kufanya mabadiliko katika mikoa mingine 3. Na pia amefanya uteuzi wa Balozi mmoja.
Orodha ya Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu Wakuu ni kama ifuatavyo;
- 1. Ofisi ya Rais Ikulu.
- Katibu Mkuu – Bw. Alphayo Kidata
- 2. Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.
- Katibu Mkuu (Utumishi) – Laurian Ndumbaro
- Naibu Katibu Mkuu - Dorothy Mwaluko
- 3. Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).
- Katibu Mkuu - Mhandisi Mussa Iyombe
- Naibu Katibu Mkuu(Afya) - Dkt. Zainabu Chaula
- Naibu Katibu Mkuu(Elimu) - Bw. Tixon Nzunda
- 4. Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira.
- Katibu Mkuu - Mhandisi Joseph Kizito Malongo
- Naibu Katibu Mkuu - Bi. Butamo Kasuka Phillipo
- 5. Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu.
- Katibu Mkuu(Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) – Bw. Erick Shitindi
- Katibu Mkuu(Bunge na Waziri Mkuu) - Maimuna Tarishi
- Katibu Mkuu(Sera na Uratibu) - Prof. Faustine Kamuzora
- 6. Wizara ya Kilimo.
- Katibu Mkuu - Mhandisi Methew Mtigumwe
- Naibu Katibu Mkuu - Dkt. Thomas Didimu Kashililah
- 7. Wizara ya Mifugo na Uvuvi.
- Katibu Mkuu (Mifugo) - Dkt. Maria Mashingo
- Katibu Mkuu (Uvuvi) - Dkt. Yohana Budeba
- 8. Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.
- Katibu Mkuu (Ujenzi) - Mhandisi Joseph Nyamuhanga
- Katibu Mkuu (Uchukuzi) - Dkt. Leonard Chamriho
- Katibu Mkuu (Mawasiliano) – Dkt. Maria Sassabo
- Naibu Katibu Mkuu (Mawasiliano) – Mhandisi Anjelina Madete
- 9. Wizara ya Fedha na Mipango.
- Katibu Mkuu - Doto James Mgosha
- Naibu Katibu Mkuu (Utawala) - Bi. Susana Mkapa
- Naibu Katibu Mkuu (Fedha za Nje) – Bi. Amina Shaaban
- Naibu Katibu Mkuu (Sera) - Dkt. Khatibu Kazungu
10.Wizara ya Nishati.
- Katibu Mkuu - Dkt. Hamis Mwinyimvua
11.Wizara ya Madini.
- Katibu Mkuu - Prof. Simon S. Msanjila
- 12. Wizara ya Katiba na Sheria.
- Katibu Mkuu - Prof. Sifuni Mchome
- Naibu Katibu Mkuu - Amon Mpanju
- 13. Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
- Katibu Mkuu - Prof. Adolf F. Mkenda
- Naibu Katibu Mkuu - Balozi Ramadhani Muombwa Mwinyi
14.Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.
- Katibu Mkuu - Dkt. Florence Turuka
- Naibu Katibu Mkuu - Bi. Immaculate Peter Ngwale
- 15. Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
- Katibu Mkuu - Meja Jen. Projest A. Rwegasira
- Naibu Katibu Mkuu - Balozi Hassan Simba Yahaya
16.Wizara ya Maliasili na Utalii.
- Katibu Mkuu - Meja Jen. Gaudence S. Milanzi
- Naibu Katibu Mkuu - Dkt. Aloyce K. Nzuki
17.Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
- Katibu Mkuu - Dorothy Mwanyika
- Naibu Katibu Mkuu - Dkt. Moses M. Kusiluka
18.Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji.
- Katibu Mkuu - Prof. Elisante Ole Gabriel
- Naibu Katibu Mkuu (Viwanda) – Ludovick J. Nduhiye
- Naibu Katibu Mkuu (Biashara na Uwekezaji) – Prof. Joseph Buchwaishaija
- 19. Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi.
- Katibu Mkuu - Dkt. Leonard Akwilapo
- Naibu Katibu Mkuu - Prof. James Epiphan Mdoe
- Naibu Katibu Mkuu - Dkt. Ave-Maria Semakafu
- 20. Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.
- Katibu Mkuu (Afya) - Dkt. Mpoki Ulisubisya
- Naibu Katibu Mkuu (Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto) - Bi. Sihaba Nkinga.
- 21. Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.
- Katibu Mkuu - Bi. Suzan Paul Mlawi
- Naibu Katibu Mkuu - Nicholaus B. William
- 22. Wizara ya Maji na Umwagiliaji.
- Katibu Mkuu - Prof. Kitila Mkumbo
- Naibu Katibu Mkuu - Mhandisi Emmanuel Kalobelo
Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli amewapandisha vyeo Wakuu wa Wilaya 3 na kuwateua kuwa Wakuu wa Mikoa kujaza nafasi za Wakuu wa Mikoa waliostaafu.
Mhe. Rais Magufuli amemteua Bw. Alexander Pastory Mnyeti kuwa Mkuu wa Mkoa wa Manyara. Kabla ya uteuzi huu Bw. Mnyeti alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Arumeru na anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Bw. Joel Bendera ambaye amestaafu.
Mhe. Rais Magufuli amemteua Bw. Joackim Leonard Wangabo kuwa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa. Kabla ya uteuzi huu Bw. Wangabo alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Nanyumbu na anachukua nafasi ya Kamishna wa Polisi Zelote Stephen ambaye amestaafu.
Mhe. Rais Magufuli amemteua Bw. Robert Gabriel Luhumbi kuwa Mkuu wa Mkoa wa Geita. Kabla ya uteuzi huu Bw. Luhumbi alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Korogwe na anachukua nafasi ya Meja Jen. Ezekiel Kyunga ambaye amestaafu.
Mhe. Rais Magufuli amemteua Bw. Adam Kigoma Malima kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara. Bw. Adam Kigoma Malima anachukua nafasi ya Dkt. Charles Mlingwa.
Mhe. Rais Magufuli amemteua Bi. Christine Solomon Mndeme kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma. Kabla ya uteuzi huu Bi. Mndeme alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini na anachukua nafasi ya Bw. Jordan Rugimbana.
Mhe. Rais Magufuli amemteua Bw. Gelasius Gasper Byakanwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mtwara. Bw. Byakanwa alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai na anachukua nafasi ya Bi. Halima Dendego.
Katika hatua nyingine, Mhe. Rais Magufuli amemteua aliyekuwa Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP - Mstaafu) Ernest Mangu kuwa Balozi.
IGP – Mstaafu Ernest Mangu pamoja na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Dkt. Aziz Mlima watapangiwa vituo vya kazi baada ya taratibu kukamilika.
Makatibu Wakuu wapya 4, Naibu Makatibu Wakuu wapya 7, na Wakuu wa Mikoa 6 walioteuliwa wataapishwa kesho tarehe 27 Oktoba, 2017 saa 8:00 Mchana, Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
26 Oktoba, 2017
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 25 Oktoba, 2017 amepokea hati za utambulisho za Mabalozi watatu waliopangiwa kuziwakilisha nchi za Oman, Uholanzi na China hapa nchini.
Waliowasilisha hati zao kwa Mhe. Rais Magufuli, Ikulu Jijini Dar es Salaam ni Mhe. Ali Abdullah Al Mahruqi – Balozi wa Oman hapa nchini, Mhe. Jeroen Verheul – Balozi wa Uholanzi hapa nchini na Mhe. Wang Ke – Balozi wa China hapa nchini.
Mhe. Rais Magufuli amewapongeza Mabalozi hao kwa kuteuliwa kuziwakilisha nchi zao hapa nchini na amewahakikishia kuwa Serikali yake itafanya kazi nao kwa ukaribu ili kuendeleza na kukuza zaidi ushirikiano kati ya nchi hizo na Tanzania hususani katika uchumi.
“Nimefurahishwa sana na ziara iliyofanywa na Mawaziri wa Oman hapa nchini, naomba ufikishe shukrani zangu kwa Mfalme wa Oman Mtukufu Sayyid Qaboos bin Said Al Said, naamini yote tuliyozungumza ikiwemo kubadilishana uzoefu katika mafuta na gesi, uwekezaji katika viwanda na ujenzi wa miundombinu tutayatekeleza kwa manufaa ya wananchi wa nchi zetu” amesema Mhe. Rais Magufuli alipozungumza na Balozi Ali Abdullah Al Mahruqi wa Oman.
Mhe. Rais Magufuli amemuambia Balozi Jeroen Verheul wa Uholanzi kuwa Tanzania inayo gesi nyingi na itafurahi kupokea wawekezaji kutoka Uholanzi ikizingatiwa kuwa nchi hiyo ina uzoefu na teknolojia kubwa katika sekta hiyo.
Kwa upande wa Balozi wa China hapa nchini Mhe. Wang Ke, Mhe. Rais Magufuli amesema uhusiano wa Tanzania na China ni wa kihistoria na kidugu, hivyo ametoa wito kwa Balozi huyo kuuendeleza na kuhakikisha fursa zenye manufaa kwa nchi zote zinatumiwa ipasavyo ikiwemo kukuza uwekezaji, biashara, utalii na ushirikiano katika usafiri wa anga.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
25 Oktoba, 2017
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amemteua Prof. Frolens Dominic Andrew Makinyika Luoga kuwa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT).
Prof. Luoga anachukua nafasi ya Prof. Benno Ndulu ambaye anamaliza muda wake.
Prof. Luoga ni Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Taaluma).
Mhe. Rais Magufuli ametangaza uteuzi huu tarehe 23 Oktoba, 2017 katika hafla ya kuwatunuku vyeti vya shukurani na pongezi wajumbe wa kamati zilizofanya uchunguzi wa aina, kiwango na thamani ya madini yaliyokuwemo katika makinikia, iliyofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Katika hafla hiyo Mhe. Rais Magufuli amewatunuku vyeti wajumbe wote 28 wa kamati hizo kwa kutambua mchango mkubwa wa kila mmoja wao katika uchunguzi na majadiliano kuhusu rasilimali za madini na matokeo ya kazi yao ambayo yameiletea nchi na Serikali faida na heshima kubwa.
“Uzalendo wako, jitihada zako binafsi na ushirikiano wako kwa wajumbe wa kamati katika kupigania maslahi makubwa ya nchi yetu ni jambo la kupigiwa mfano na litakaloenziwa daima.
“Kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Wananchi wa Tanzania na mimi binafsi, nakushukuru na kukupongeza sana” imenukuliwa sehemu ya shukurani na pongezi hizo za Rais Magufuli.
Miongoni mwa waliotunukiwa cheti cha shukurani na pongezi ni Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job Yustino Ndugai kwa kutambua uzalendo wake, jitihada zake binafsi na ushirikiano wake mkubwa kwa Bunge na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kupigania maslahi makubwa nchi, jambo ambalo ni la kupigiwa mfano na litakaloenziwa daima.
Mhe. Rais Magufuli amewashukuru Watanzania wote kwa kuunga mkono jitihada za kupigania rasilimali za nchi na amewataka wawapuuze wanaobeza jitihada hizo pamoja na kuzitaka mamlaka husika kuchukua hatua za kisheria dhidi ya wanaotoa takwimu za upotoshaji kwa lengo la kuwagombanisha wananchi na Serikali.
Halikadhalika Mhe. Rais Magufuli amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na wafanyabiashara na wawekezaji na ametoa wito kwa wafanyabiashara na wawekezaji wa ndani kuchangamkia fursa mbalimbali za biashara kwa kuwa Serikali inawapenda na itaendelea kuwaunga mkono.
Katika hafla hiyo, viongozi mbalimbali wakiwemo wa dini, vyama vya siasa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge Mhe. Mussa Azzan Zungu wamempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa jitihada kubwa alizozifanya katika kupigania maslahi ya Watanzania katika biashara ya madini na wameahidi kuendelea kumuunga mkono na kumuombea.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
23 Oktoba, 2017
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 23 Oktoba, 2017 atawatunuku vyeti wajumbe wa kamati zilizofanya uchunguzi wa kiwango, aina na thamani ya madini katika makinikia na baadaye kufanya mazungumzo na kampuni ya Barrick Gold.
Tanzania na Barrick Gold Corporation zilifikia makubaliano tarehe 19 Oktoba, 2017 na kutiliana saini mkataba wa kutekeleza mwelekeo mpya wa namna kampuni hiyo itakavyoendesha biashara ya madini ya dhahabu yanayochimbwa katika migodi yake hapa nchini, pamoja na kulipa takribani Shilingi Bilioni 700 za kuonesha nia njema ya kufidia madai ya upotevu wa mapato yaliyotokana na biashara hiyo.
Tukio hili litafanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam kuanzia saa 5:00 asubuhi na kurushwa moja kwa moja na vyombo vya habari vya redio, televisheni na mitandao mbalimbali.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
23 Oktoba, 2017
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amemteua Bi. Janeth Masaburi kuwa Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mhe. Rais Magufuli amefanya uteuzi huo kwa mujibu wa Ibara ya 66 (1)(e) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayompa mamlaka ya kuteua wabunge 10 watakaokuwa miongoni mwa Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Bi. Janeth Masaburi ataapishwa kulingana na taratibu za Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
21 Oktoba, 2017
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amemtumia salamu za rambirambi Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania Sheikh Aboubakar Zubeir Ally kufuatia kifo cha Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Mkoa wa Morogoro Abdallah Salim Mkanga kilichotokea tarehe 18 Oktoba, 2017.
Sheikh Abdallah Salim Mkanga amefariki dunia katika hospitali ya Muhimbili Jijini Dar es Salaam alikopelekwa kwa ajili ya kupata matibabu.
Katika salamu hizo Mhe. Rais Magufuli amemuomba Sheikh Aboubakar Zubeir Ally kuwapa pole familia ya Marehemu Abdallah Salim Mkanga, Waislamu wote wa Mkoa wa Morogoro, ndugu, jamaa na marafiki walioguswa na msiba huo.
“Namuombea Marehemu Abdallah Salim Mkanga apumzishwe mahali pema na nawaombea wanafamilia wote wawe na subira na moyo wa uvumilivu katika kipindi hiki cha majonzi” amesema Rais Magufuli.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
20 Oktoba, 2017
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amemtumia salamu za rambirambi Rais wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC) Mhashamu Tercisius Ngalalekumtwa kufuatia kifo cha Askofu wa Jimbo Katoliki la Tunduru Masasi Mhashamu Castory Msemwa, kilichotokea jana tarehe 19 Oktoba, 2017 nchini Oman.
Mhashamu Askofu Castory Msemwa amefariki dunia Mjini Muscat akiwa safarini kuelekea nchini India kwa Matibabu.
"Nimepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha Baba Askofu Msemwa, kilichotokea huko Oman, Baba Askofu Msemwa ametoa mchango mkubwa sio tu katika kutimiza majukumu yake ya huduma za kiroho bali pia katika kuisaidia jamii kupata huduma mbalimbali anazostahili binadamu na amekuwa akitoa ushirikiano mkubwa kwa taasisi nyingine zikiwemo za Serikali katika kudumisha amani, upendo, umoja na kuwahudumia wananchi, mchango wake utakumbukwa daima" Amesema Mhe. Rais Magufuli.
Mhe. Rais Magufuli amemuomba Rais wa TEC Mhashamu Tercisius Ngalalekumtwa kumfikishia pole nyingi kwa Maaskofu wote wa TEC, Mapadre, Makatekista na waumini wote wa Jimbo Katoliki la Tunduru Masasi kwa msiba huu mkubwa uliotokea na amesema anaungana nao katika kipindi cha majonzi na maombi kwa Marehemu.
"Raha ya milele umpe ee Bwana na mwanga wa milele umuangazie, Marehemu Askofu Castory Msemwa apumzike kwa amani, Amina" Amemalizia Mhe. Rais Magufuli.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
20 Oktoba, 2017
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Majadiliano kati ya Tanzania na timu ya wawakilishi wa kampuni ya Barrick Gold inayomiliki migodi ya madini hapa nchini yamekamilika na makubaliano kati ya pande hizo yametiwa saini tarehe 19 Oktoba, 2017 mbele ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli Ikulu, Jijini Dar es Salaam.
Timu ya Barrick Gold Corporation ilikuwa imeongozwa na Mwenyekiti Mtendaji wa kampuni hiyo Prof. John Thornton wakati timu iliyowakilisha Serikali ya Tanzania imeongozwa na Waziri wa Katiba na Sheria Prof. Palamagamba John Aidan Mwaluko Kabudi.
Miongozi mwa mambo waliyokubaliana ni kutekeleza mwelekeo mpya wa biashara ya madini ambapo kutakuwa na mgawanyo sawa wa faida (yaani Tanzania kupata asilimia 50 na Barrick Gold Corporation kupata asilimia 50 ya faida) na kuundwa kwa kampuni ya ubia wa usimamizi wa migodi ya madini iliyopo Tanzania ambayo itakuwa na makao makuu yake Mwanza na ofisi ndogo Dar es Salaam nchini Tanzania badala ya nchini Uingereza.
Mengine ni kufunga ofisi za uhasibu na fedha zilizopo Johannesburg Afrika Kusini na kuhamishia Tanzania na kutekeleza masharti yote ya mabadiliko ya sheria mpya ya madini na rasilimali za nchi ya mwaka 2017.
Aidha, Barrick Gold Corporation imekubali kuwepo kwa wawakilishi wa Serikali katika bodi za migodi yake yote hapa nchini, kazi mbalimbali za kwenye migodi kufanywa na kampuni za Kitanzania, Migodi kutoa ajira za kudumu kwa wachimbaji, wachimbaji hao kuishi majumbani kwao badala ya kuishi kwenye makambi ya migodi na mashauri yote ya kesi mbalimbali kufanywa hapa nchini.
Kampuni ya Barrick Gold pia imekubali kutoa Dola za Kimarekani Milioni 300 sawa na takribani Shilingi Bilioni 700 kama malipo ya kuonesha nia njema ya kufidia fedha zilizotokana na upotevu wa mapato kupitia biashara ya kampuni hiyo.
Akizungumza baada ya kutia saini makubaliano hayo Prof. Thornton amempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa msimamo wake unaojenga misingi ya biashara ya kuaminiana na uwazi, ambayo ni muhimu na ya namna yake kwa biashara katika karne hii ya 21.
Prof. Thornton amesema Barrick Gold Corporation watazingatia makubaliano haya na wanaamini kuwa yamefungua ukurasa muhimu utakaowezesha kufanya biashara kisasa.
Kwa upande wake Mhe. Rais Magufuli amezipongeza timu zote mbili yaani Tanzania na Barrick Gold Corporation kwa kazi kubwa ziliyofanya kufikia makubaliano hayo na kwa kipekee amempongeza Prof. Thornton kwa nia yake thabiti ya kukubali kufanyika kwa mazungumzo na kukubali mambo yaliyofikiwa.
Mhe. Rais Magufuli amesema makubaliano hayo yataisaidia nchi kuzalishaji ajira zaidi, kupata manufaa mbalimbali yanayostahili ikiwemo fedha za kugharamia huduma za kijamii kwa wananchi na yanajenga msingi imara ambao utaiwezesha Tanzania kunufaika na rasilimali zake za madini.
Mhe. Dkt. Magufuli amemuagiza Waziri wa Katiba na Sheria Prof. Kabudi kuunda timu zitakazoshughulikia biashara ya madini ya Tanzanite na Almasi pamoja na migodi mingine ya dhahabu haraka iwezekanavyo ili nchi iweze kunufaika ipasavyo.
“Nataka machimbo yote ya dhahabu mchakato kama huu ufanyike, pia nakuagiza Prof. Kabudi biashara ya madini ya Tanzanite na Almasi nako ni lazima kufuate utaratibu huu, asiyetaka aondoke” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Pia Mhe. Rais Magufuli amewataka Watanzania kuunga mkono juhudi hizi badala ya baadhi yao kuzibeza kwa kuwa zina manufaa kwa taifa na wananchi wake.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
19 Oktoba, 2017
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Mfalme wa Oman Mtukufu Sayyid Qaboos bin Said Al Said amemhakikishia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kuwa nchi hiyo ipo tayari kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano kwa kuongeza uwekezaji katika viwanda, uzalishaji wa nishati, kuongeza thamani ya madini, kuendeleza sekta ya gesi na mafuta na kuendeleza ukanda wa uwekezaji wa Bagamoyo ili kukuza uchumi kwa kasi zaidi.
Ujumbe huu wa Mfalme wa Oman umewasilishwa kwa Mhe. Rais Magufuli na Waziri wa Mafuta na Gesi wa Oman Mhe. Dkt. Mohammed Hamad Al Rumhy aliyeongozana na Waziri wa Uwekezaji wa Oman Mhe. Salem Ben Nasser Al Ismaily na Naibu Waziri wa Utalii Mhe. Maitha Saif Majid, Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Dkt. Rumhy ambaye ameongoza watu zaidi 300 waliokuja nchini kwa meli ya Mfalme wa Oman amesema ziara hii imelenga kuimarisha uhusiano kati ya Tanzania na Oman hususani katika masuala ya uchumi, ambapo Oman inabadilishana uzoefu na Tanzania kuhusu biashara ya mafuta na gesi, itajenga kiwanda kikubwa cha kuzalisha mbolea katika ukanda wa uwekezaji wa Bagamoyo, itajenga viwanda vya mazao na kununua mazao ya wakulima na itawekeza katika uchakataji wa madini ili kuongeza thamani.
“Mhe. Rais tunataka kushirikiana nanyi kuendeleza ukanda wa uwekezaji wa Bagamoyo, tunataka Bagamoyo isiwe eneo la bandari tu, bali pia liwe ni eneo ambalo tutajenga viwanda mbalimbali, tuzalishe mbolea na tununue mazao ya wakulima na kuyasafirisha, sisi tupo tayari na kesho tunakwenda kuangalia eneo hilo ili kazi zianze mara moja” amesema Dkt. Rumhy.
Kwa upande wake Mhe. Rais Magufuli amemshukuru Mfalme wa Oman Mtukufu Sayyid Qaboos bin Said Al Said kwa kutuma ujumbe huo na amemhakikishia kuwa Tanzania ipo tayari kuendeleza na kukuza zaidi uhusiano wake na Oman.
Mhe. Rais Magufuli amemtaka Dkt. Rumhy kufikisha ujumbe wake kwa Mfalme na wawekezaji wa Oman kuwa atafurahi kuona uwekezaji huo unaanza mara moja na kwamba Serikali itatoa ushirikiano wowote utakaohitajika kwa manufaa ya pande zote mbili.
“Mhe. Dkt. Mohamed naomba ukamwambie Mfalme kuwa namshukuru kwa ujumbe huu na namkaribisha sana Tanzania, nimefurahi kuona mpo tayari kushirikiana nasi kujenga viwanda, kuzalisha mazao na kuendeleza ukanda wa uwekezaji wa Bagamoyo, sisi tupo tayari hata leo, njooni tushirikiane kwa sababu nyinyi ni ndugu zetu na tutafanya uwekezaji kwa faida yetu sote” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli ametaka Oman iongeze ushirikiano na Tanzania katika masuala ya utalii na usafiri wa anga, kuwekeza katika usindikaji wa nyama na uvuvi na ushirikiano katika kubadilishana wataalamu wa nyanja mbalimbali wakiwemo walimu wa lugha ya Kiswahili na Kiarabu.
Amemshukuru Mfalme wa Oman kwa msaada kujenga visima vya maji 100 hapa nchini na amemuomba kuungana na Serikali katika safari yake ya kuhamia Dodoma kwa kujenga miundombinu itakayoweka kumbukumbu ya ushirikiano wa kidugu na kihistoria kati ya nchi hizi mbili.
Mazungumzo hayo yamehudhuriwa na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Medard Matogoro Kalemani na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Suzan Alphonce Kolimba.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
18 Oktoba, 2017
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 15 Oktoba, 2017 amerejea Jijini Dar es Salaam akitokea Zanzibar ambako jana alikuwa mgeni rasmi katika sherehe za kilele cha mbio za Mwenge wa Uhuru, kumbukumbu ya Hayati Baba wa Taifa Mwl. Julius Kambarage Nyerere na wiki ya vijana zilizofanyika katika uwanja wa Amaan Mjini Magharibi.
Katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Abeid Amani Karume, Mhe. Rais Magufuli ameagwa na viongozi wa Mkoa wa Mjini Magharibi wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa huo Bw. Ayoub Mohamed Mahmoud.
Kabla ya kuondoka Ikulu Zanzibar Mhe. Rais Magufuli amekula chakula cha mchana na wakimbiza Mwenge wa Uhuru mwaka huu walioongozwa na Amour Hamad Amour na kuwahakikishia kuwa Serikali itafanyia kazi taarifa ya Mwenge waliyoiwasilisha kwake katika sherehe za jana.
“Mlipokuwa mkikimbiza Mwenge wa Uhuru nilikuwa nafuatilia miradi mliyokuwa mnatembeleana maelekezo mliyokuwa mkitoa, sehemu zote mlizobaini kuwepo kwa dosari ninawahakikishia kuwa tutazifuatilia na kuchukua hatua” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Mhe. Rais Magufuli amesema anatambua uzalendo waliouonesha wakati wote wa kukimbiza Mwenge wa Uhuru na amewasihi kuendeleza maadili na uzalendo huo kwa manufaa ya taifa.
Kwa upande wao wakimbiza Mwenge hao wamemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa heshima kubwa na upendo aliyowaonesha, kwa kupokea taarifa yao na kuahidi kuifanyia kazi na pia kuwaalika kula nao chakula cha mchana kwa kuwa hii imekuwa ni historia ya kipekee kwa wakimbiza Mwenge wa Uhuru hapa nchini.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Zanzibar
15 Oktoba, 2017
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Askofu wa Jimbo Katoliki la Zanzibar Mhashamu Agustino Shao amewataka Watanzania kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kwa hatua anazochukua kurekebisha mambo muhimu kwa maendeleo ya taifa, licha ya kuwepo kwa changamoto katika kipindi cha mpito.
Baba Askofu Shao amesema hayo tarehe 15 Oktoba, 2017 wakati akihubiri katika Misa Takatifu iliyofanyika katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Joseph, Parokia ya Minaramiwili ambapo Mhe. Rais Magufuli ameungana na waumini wa Kanisa Katoliki kusali Ibada ya Jumapili ya Dominika ya 28 ya mwaka A wa Kanisa.
Akitoa mfano wa nchi ya Zimbabwe ambayo Rais wake Mhe. Robert Mugabe aliamua kuchukua hatua za kupigania maslahi ya Wazimbabwe na sasa wananchi wa nchi hiyo wameanza kuzalisha bidhaa na kuziuza nje ya nchi, Askofu Shao amesema hatua zinazochukuliwa na Mhe. Rais Magufuli kupambana na rushwa, kupigania rasilimali za Watanzania, kuimarisha nidhamu na uwajibikaji, kukabiliana na wizi na ubadhilifu wa mali za umma na kubana matumizi, zinapaswa kuungwa mkono na Watanzania wote.
“Hatutaweza kusema tunaimaliza rushwa wakati tunaendelea kuishi kwa kupata fedha ambazo hujazifanyia kazi, ni lazima tuishi machungu ya kuimaliza rushwa, ni lazima tuishi machungu ya kuweka uadilifu katika utendaji wetu, tusipoishi machungu hayo tutaishi dunia mbili, dunia ya rushwa na dunia ya kujenga uchumi na uadilifu wa Watanzania, tukubali kujikatalia ili tuweze kupata mazuri tuliyotaka” amesema Baba Askofu Shao.
Katika salamu zake baada ya kumalizika kwa Misa Takatifu, Mhe. Rais Magufuli amemshukuru Baba Askofu Shao kwa mahubiri yake na ameungana nae kuwahakikishia Watanzania kuwa Serikali inachukua hatua za kupambana na rushwa na kulinda rasilimali za nchi ili ziweze kuwanufaisha wananchi wenyewe.
Mhe. Rais Magufuli amesema hata Hayati Baba wa Taifa Mwl. Julius Kambarage Nyerere ambaye jana ametimiza miaka 18 tangu afariki dunia, alipiga vita rushwa na alipigania rasilimali za nchi, hivyo ametaka Watanzania wote kuungana katika juhudi hizo.
Mhe. Dkt. Magufuli ambaye ameongozana na Mkewe Mama Janeth Magufuli amewashukuru Watanzania wote kwa maombi yao na amechangia Shilingi Milioni 1 kwa ajili kwaya ya kanisa hilo na Shilingi Milioni 5 kwa ajili ya maendeleo ya Kanisa.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Zanzibar
15 Oktoba, 2017
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amesema Serikali haitafuta mbio za Mwenge wa Uhuru kwa kuwa ni alama ya Uhuru na Utaifa wa nchi na kwamba unatoa mchango mkubwa katika kuchochea maendeleo, kuwaunganisha Watanzania na kuimarisha Muungano.
Mhe. Rais Magufuli amesema hayo tarehe 14 Oktoba, 2017 katika sherehe za kilele cha mbio za Mwenge wa Uhuru, kumbukumbu ya Baba wa Taifa Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere na Wiki ya Vijana zilizofanyika kitaifa katika uwanja wa Amaan uliopo Mjini Magharibi, Zanzibar.
Pamoja na kauli hiyo Mhe. Rais Magufuli amesema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar zitaendeleza mbio za mwenge wa uhuru na kuutetea Muungano kwa nguvu zote.
“Kauli mbiu ya Mwenge wa Uhuru mwaka huu inasema Shiriki Kukuza Uchumi wa Viwanda kwa Maendeleo ya Nchi yetu. Nimefarijika zaidi kusikia kuwa katika Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka huu jumla ya viwanda 148 vimezinduliwa, viwanda hivyo vimejengwa kwa gharama ya Shilingi Bilioni 468.46 na vinatarajiwa kuzalishaji ajira 13,370.
Hii ndio sababu tumekuwa tukihimiza ujenzi wa viwanda na hizi ni baadhi ya faida za Mwenge” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Kuhusu Kumbukumbu ya Mwl. Nyerere, Mhe. Rais Magufuli amewataka Watanzania wote kuendelea kumuenzi Baba wa Taifa kwa kuwa wazalendo, kuthamini utu na usawa wa binadamu na muhimu zaidi kujitathimini ni kwa kiasi gani wanajiepusha na vitendo vinavyoathiri ustawi wa nchi na watu wake kama vile wizi, rushwa, ubinafsi na kukosa uzalendo.
Ametolea mfano wa Mwl. Nyerere ambaye mwanzoni mwa uongozi wake alipochaguliwa kuwa Rais wa Tanzania aliamua kupunguza mshahara wake na kukataa kuongeza mishahara ya wafanyakazi wengine Serikalini kwa maelezo kuwa hawezi kuongeza mishahara ya wachache wakati wananchi wengi ni masikini na hawapati huduma muhimu za afya, elimu na maji.
“Ninaposema hivyo simaanishi kuwa mishahara isiongezwe. La hasha. Ninachosema ni kwamba kabla ya kudai nyongeza ya mishahara ni lazima kwanza kufahamu uwezo wa Serikali, lakini pia tutambue kuwa kuna Watanzania wenzetu wengi tu wanaohitaji kuboreshewa huduma.
Hata hivyo baada ya kukamilisha zoezi la uhakiki wa watumishi hewa na vyeti feki, Serikali imewapandisha vyeo na kuwarekebishia mishahara watumishi 59,967 ambapo kiasi cha Shilingi Bilioni 159.33 zimetengwa kwenye bajeti ya mwaka huu na mishahara mipya itaanza kulipwa kuanzia mwaka huu. Na kwa upande wa Zanzibar kima cha chini cha mshahara kimeongezwa kutoka Shilingi 150,000/- hadi kufikia Shilingi 300,000/-” Amesema Mhe. Rais Magufuli.
Kuhusu vijana Mhe. Rais Magufuli amewataka kuendelea kujielimisha katika Nyanja mbalimbali, kujiepusha na matumizi ya dawa za kulevya na kujikinga dhidi ya maambukizi ya ugonjwa wa Ukimwi.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli amewapongeza na kuwakabidhi vyeti wakimbiza Mwenge wa Uhuru Kitaifa walioongozwa na Amour Hamad Amour kwa kukimbiza mwenge huo kwa siku 195 katika mikoa yote 31 na Halmashauri 195, ambapo jumla ya miradi 1,512 yenye thamani ya jumla ya Shilingi Trilioni 1.1 imepitiwa. Na pia ameahidi kuchukua hatua dhidi ya wote waliohusika kusababisha dosari katika miradi 19 ambayo viongozi wa mwenge wamebaini.
Sherehe hizo zimehudhuriwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein, Makama wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Seif Ali Idd, Mke wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Janeth Magufuli, Mke wa Rais wa Zanzibar Mama Mwanamwema Shein na viongozi wengine wa Tanzania Bara na Zanzibar.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Zanzibar
14 Oktoba, 2017
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 12 Oktoba, 2017 amewasili Zanzibar ambapo keshokutwa tarehe 14 Oktoba atakuwa mgeni rasmi katika sherehe za kilele cha mbio za Mwenge wa Uhuru, Kumbukumbu ya siku ya Baba wa Taifa Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere na kilele cha wiki ya vijana kitaifa zitakazofanyika katika uwanja wa Amaan.
Mhe. Rais Magufuli ambaye ameongozana na mkewe Mama Janeth Magufuli ametua katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Abeid Amani Karume na kupokelewa na Makamu wa Rais wa Pili wa Zanzibar Mhe. Balozi Seif Ali Idd.
Jaffar Haniu
Naibu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Zanzibar
12 Oktoba, 2017
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Kiongozi wa Jumuiya ya Ismailia Mtukufu Karim Al-Hussaini Aga Khan amesema Jumuiya hiyo imedhamiria kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano kwa kupanua hospitali ya Aga Khan iliyopo Jijini Dar es Salaam na kujenga chuo kikuu kikubwa katika Afrika Mashariki, Mkoani Arusha.
Mtukufu Karim Al-Hussaini Aga Khan amesema hayo tarehe 11 Oktoba, 2017 Ikulu Jijini Dar es Salaam alipofanya mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli.
Amesema Upanuzi wa hospitali ya Aga Khan utahusisha kuongeza idadi ya vitanda vya wagonjwa kutoka 72 vya sasa hadi kufikia vitanda 172, utaimarisha matibabu ya moyo na kansa na utaongeza ufundishaji wa madaktari na wataalamu wengine wa afya.
Kuhusu chuo kikuu kitakachojengwa Arusha, Mtukufu Karim Al-Hussaini Aga Khan amesema Jumuiya hiyo imedhamiria kujenga chuo kikuu kikubwa ambacho kitafundisha viongozi sio tu wa Tanzania na Afrika Mashariki, bali pia Afrika nzima ili waweze kuwa chachu ya mabadiliko na maendeleo ya Afrika.
Kwa upande wake Mhe. Rais Magufuli amemshukuru Mtukufu Karim Al-Hussaini Aga Khan kwa taasisi zake kutoa huduma za kijamii hapa nchini, lakini ametoa wito kwa taasisi hizo kupunguza gharama za huduma zake kwa wananchi ili wananchi waweze kumudu hasa ikizingatiwa kuwa zimekuwa zikipata msamaha wa kodi kutoka Serikalini.
Mhe. Rais Magufuli amesema Serikali ya Awamu ya Tano ipo tayari kuendeleza na kuimarisha zaidi ushirikiano na Aga Khan na amemuomba kiongozi huyo kuendelea kupanua uwigo wa huduma za taasisi zake ikiwa ni pamoja na kuwekeza Mjini Dodoma yaliko makao makuu ya Serikali.
Kwa upande wa vyombo vya habari vinavyomilikiwa na Aga Khan Mtukufu Karim Al-Hussaini amesema yeye haamini kuwa ni kipaumbele kwa vyombo vya habari kujikita katika masuala ya siasa na badala yake anaamini kuwa vyombo vya habari vina wajibu mpana zaidi wa kujikita katika masuala ya maendeleo hususani katika nchini zinazoendelea, na kwamba Aga Khan ipo katika mchakato wa kujikita katika wajibu huo kwa kuwa na waandishi wa habari na wachambuzi mahiri.
Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na ujumbe wa Maseneta wa Baraza la Seneti la Marekani ambao ni wajumbe wa kamati ya mazingira inayoshughulikia hifadhi ya taifa, wanyamapori na misitu ya Marekani ambao wamekuwepo hapa nchini kwa siku 3 kwa lengo la kutembelea hifadhi ya taifa ya Ngorongoro.
Maseneta hao ni Mhe. James Inhofe, Mhe. Mike Enzi, Mhe. David Perdue, Mhe. Luther Strange, Mhe. Tim Scott na Mhe. John Thune.
Baada ya Mazungumzo hayo Mhe. Seneta James Inhofe na Mhe. Seneta Mike Enzi wamemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kukutana nao na kuwakaribisha wafanyabiashara na wawekezaji kutoka nchini Marekani kuja kuwekeza hapa nchini na wamekiri kuwa Tanzania inazo rasilimali nyingi ambazo ni fursa muhimu ya kukuza uchumi.
Mazungumzo kati ya Maseneta hao na Mhe. Rais Magufuli yamehudhuriwa na Kaimu Balozi wa Marekani hapa nchini Mhe. Dkt. Inmi Patterson.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
11 Oktoba, 2017
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
“Kwa mshtuko na masikitiko makubwa nimepokea taarifa ya vifo vya watu 12 waliopoteza maisha baada ya gari la abiria walilokuwa wakisafiria kutumbukia katika ziwa Victoria Mkoani Mwanza, nawapa pole sana wote waliopoteza jamaa zao katika ajali hii, nawaomba wawe na moyo wa uvumilivu, ustahimilivu na subira katika kipindi hiki cha majonzi”
Hiyo ni sehemu ya salamu za rambirambi alizozitoa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Bw. John Mongella kufuatia ajali ya basi la abiria (Daladala) lililozama katika ziwa Victoria baada ya kugonga vizuizi vya kivuko cha Kigongo Wilayani Misungwi na kisha kutumbukia na kuzama majini.
Mhe. Rais Magufuli amemtuma Bw. Mongella kufikisha salamu zake za pole kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki wote waliopatwa na msiba huu na amesema anaungana nao katika maombolezo.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli amewaombea marehemu wote wapumzishwe mahali pema peponi na majeruhi 3 walionusurika katika ajali hii wapone haraka ili waweze kuendelea na shughuli zao za kila siku.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
09 Oktoba, 2017
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 09 Oktoba, 2017 amewaapisha Mawaziri 8, Naibu Mawaziri 16 na Katibu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, aliowateua tarehe 07 Oktoba, 2017.
Mawaziri walioapishwa ni George Huruma Mkuchika – Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Selemani Said Jafo – Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Dkt. Charles John Tizeba – Waziri wa Kilimo, Luhaga Joelson Mpina – Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Dkt. Medard Matogoro Chananja Kalemani – Waziri wa Nishati, Anjellah Kairuki – Waziri wa Madini, Dkt. Hamis Andrea Kigwangalla – Waziri wa Maliasili na Utalii na Mhandisi Isack Aloyce Kamwelwe – Waziri wa Maji na Umwagiliaji.
Manaibu Waziri walioapishwa ni Joseph Sinkamba Kandege – Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI, George Joseph Kakunda – Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI, Kangi Alphaxard Lugola – Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Stella Alex Ikupa – Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Walemavu), Dkt. Mary Machuche Mwanjelwa – Naibu Waziri wa Kilimo, Abdallah Hamis Ulega – Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhandisi Atashasta Justus Nditiye – Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano na Elias John Kwandikwa – Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.
Manaibu Waziri wengine walioapishwa ni Subira Hamis Mgalu – Naibu Waziri wa Nishati, Stanslaus Haroon Nyongo – Naibu Waziri wa Madini, Josephat Ngailonga Hasunga – Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhandisi Stella Martin Manyanya – Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, William Tate Ole Nasha – Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Dkt. Faustine Engelbert Ndugulile – Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Juliana Daniel Shonza – Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Jumaa Hamidu Aweso – Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli amemuapisha Steven Nzohabonayo Kagaigai kuwa Katibu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Pamoja na kuapishwa katika nyadhifa hizo, Mawaziri, Manaibu Waziri na Katibu wa Bunge wamekula kiapo cha uadilifu kwa viongozi wa umma kilichoongozwa na Kamishna wa Maadili, Jaji Mstaafu Harold Nsekela.
Hafla ya kuapishwa kwa viongozi hao imefanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job Yustino Ndugai, Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. George Mcheche Masaju, Mawaziri na Makatibu Wakuu wa Wizara mbalimbali, Wajumbe wa Tume ya Utumishi wa Bunge na Kamati za kudumu za Bunge, viongozi wakuu wa vyombo vya Ulinzi na Usalama na Viongozi wa madhehebu ya Dini na vyama vya siasa.
Mara baada ya kuapishwa Mawaziri na Manaibu Waziri wamekabidhiwa nyaraka za kazi na kuanza kazi kwa kuhudhuria Kikao Maalum cha Baraza la Mawaziri kilichoongozwa na Mwenyekiti wake Mhe. Rais Magufuli.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
09 Oktoba, 2017
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 07 Oktoba, 2017 amefanya mabadiliko katika Baraza la Mawaziri kwa kuongeza idadi ya Wizara, kuteua Mawaziri na Naibu Mawaziri wapya na kuwahamisha Wizara baadhi ya Mawaziri na Naibu Mawaziri.
Katika mabadiliko hayo Mhe. Rais Magufuli ameongeza idadi ya Wizara na Mawaziri wake kutoka 19 hadi 21, na Naibu Mawaziri kutoka 16 hadi 21.
Iliyokuwa Wizara ya Nishati na Madini imegawanywa na kutakuwa na Wizara ya Nishati na Wizara ya Madini, na iliyokuwa Wizara Kilimo, Mifugo na Uvuvi imegawanywa na kutakuwa na Wizara ya Kilimo na Wizara ya Mifugo na Uvuvi.
Mhe. Rais Magufuli akiwa na Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa ametangaza mabadiliko hayo Ikulu Jijini Dar es Salaam na lifuatalo ni Baraza la Mawaziri baada ya kufanyiwa mabadiliko.
- Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.
I. Waziri – George Huruma Mkuchika
- Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).
I. Waziri - Selemani Said Jafo
II. Naibu Waziri - Joseph Sinkamba Kandege
III. Naibu Wazri - George Joseph Kakunda
- Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira.
I. Waziri - January Yusuf Makamba
II. Naibu Waziri - Kangi Alphaxard Lugola
- Ofisi ya Waziri Mkuu: Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu.
I. Waziri - Jenista Joackim Mhagama
II. Naibu Waziri - Anthony Peter Mavunde (Kazi, Vijana na Ajira)
III. Naibu Waziri - Stella Alex Ikupa (Walemavu)
- Wizara ya Kilimo.
I. Waziri - Dkt. Charles John Tizeba
II. Naibu Waziri - Dkt. Mary Machuche Mwanjelwa
- Wizara ya Mifugo na Uvuvi.
I. Waziri - Luhaga Joelson Mpina
II. Naibu Waziri - Abdallah Hamis Ulega
- Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.
I. Waziri - Prof. Makame Mbarawa Mnyaa
II. Naibu Waziri - Mhandisi Atashasta Justus Nditiye
III. Naibu Waziri - Elias John Kwandikwa
- Wizara ya Fedha na Mipango.
I. Waziri - Dkt. Philip Isdor Mpango
II. Naibu Waziri - Dkt. Ashatu Kijaji
- Wizara ya Nishati.
I. Waziri - Dkt. Medard Matogoro Kalemani
II. Naibu Waziri - Subira Hamis Mgalu
10. Wizara ya Madini.
I. Waziri - Angellah Kairuki
II. Naibu Waziri - Stanslaus Haroon Nyongo
- 11. Wizara ya Katiba na Sheria.
I. Waziri - Prof. Palamagamba John Aidan Mwaluko
Kabudi.
12. Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
I. Waziri - Dkt. Augustine Philip Mahiga
II. Naibu Waziri - Dkt. Susan Alphonce Kolimba
13. Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga (JKT).
I. Waziri - Dkt. Hussein Ali Mwinyi
14. Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
I. Waziri - Mwigulu Lameck Nchemba
II. Naibu Waziri - Mhandisi Hamad Yusuf Masauni
15. Wizara ya Maliasili na Utalii.
I. Waziri - Dkt. Hamisi Andrea Kigwangalla
II. Naibu Waziri - Josephat Ngailonga Hasunga
16. Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
I. Waziri - William Vangimembe Lukuvi
II. Naibu Waziri - Angelina Sylivester Mabula
17. Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji.
I. Waziri - Charles Paul Mwijage
II. Naibu Waziri - Mhandisi Stella Martin Manyanya
18. Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi.
I. Waziri - Prof. Joyce Lazaro Ndalichako
II. Naibu Waziri - William Tate Ole Nasha
19. Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.
I. Waziri - Ummy Ally Mwalimu
II. Naibu Waziri - Dkt. Faustine Engelbert Ndugulile
20. Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.
I. Waziri - Dkt. Harrison George Mwakyembe
II. Naibu Waziri - Juliana Daniel Shonza
21. Wizara ya Maji na Umwagiliaji.
I. Waziri - Mhandisi Isack Aloyce Kamwelwe
II. Naibu Waziri - Jumaa Hamidu Aweso
Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli amemteua Bw. Stephen Kagaigai kuwa Katibu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kabla ya Uteuzi huo, Bw. Stephen Kagaigai alikuwa Kaimu Karani wa Baraza la Mawaziri.
Bw. Stephen Kagaigai anachukua nafasi ya Dkt. Thomas D. Kashilila ambaye atapangiwa kazi nyingine.
Wateule wote wataapisha Jumatatu tarehe 09 Oktoba, 2017 saa 3:30 Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
07 Oktoba, 2017
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amesema Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kufanikisha utafutaji na upatikanaji wa mafuta yaliyopo katika bonde la Eyasi Wembere na ziwa Tanganyika hapa nchini ili Tanzania ianze kunufaika na rasilimali hiyo.
Mhe. Rais Magufuli amesema hay muda mfupi baada kupokea taarifa ya maendeleo ya utafiti wa mafuta katika maeneo ya bonde la ufa ya Eyasi Wembere na ziwa Tanganyika, iliyowasilishwa na timu ya wataalamu wa Tanzania na Uganda.
Timu hiyo imeelezea uwepo wa viashiria vya uhakika vya kijiolojia vinavyothibitisha kuwepo kwa mafuta katika maeneo ya Senkenke, Mwanzugi na Kining’inila katika bonde la Manonga, Wilaya ya Igunga Mkoani Tabora.
Katika mkutano huo uliohudhuriwa na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, Naibu Waziri wa Nishati na Madini Dkt. Medard Kalemani na Balozi wa Uganda hapa nchini Mhe. Richard Kabonero, timu ya wataalamu hao imesema miamba, uoto na uwepo wa bonde Eyasi Wembere katika mfumo mmoja wa bonde la Afrika Mashariki unaofanana na maeneo mengine yaliyothibitika kuwa na mafuta ni kiashiria muhimu cha kuwepo mafuta.
Kufuatia taarifa hiyo Mhe. Rais Magufuli amesema Serikali ya Awamu ya Tano ipo tayari kutekeleza shughuli zote zitakazowezesha kupatikana kwa mafuta katika bonde la Eyasi Wembere na ziwa Tanganyika na amewaagiza wataalamu wa Tanzania kuendelea kufanya kazi kwa ukaribu na wataalamu wa Uganda ambao wana uzoefu wa kupata mafuta katika ziwa Albert nchini humo.
Mhe. Rais Magufuli amewashukuru wataalamu wa Uganda wanaoshirikiana na wataalamu wa Tanzania katika kazi hii na amemuomba Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini wa Uganda Bw. Robert Kasande kumfikishia shukrani zake kwa Rais wa Uganda Mhe. Yoweri Kaguta Museveni kwa ushirikiano anautoa kwa Tanzania katika kufanikisha upatikanaji wa mafuta ya nchini Tanzania.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
05 Oktoba, 2017
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 05 Oktoba 2017, amemuapisha Meja Jen. Issa Suleiman Nassor kuwa Balozi wa Tanzania nchini Misri na Naibu Mkuu wa Jeshi la Polisi Abdulharaman Kaniki kuwa Balozi wa Tanzania nchini Zambia.
Akizungumza mara baada ya kula kiapo, Balozi Issa Suleiman Nassor amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kuonyesha imani kwake na kumteua kushika nafasi hiyo na amemuahidi kuendeleza na kukuza uhusiano uliopo kati ya Tanzania na Misri.
Balozi Nassor amemuahidi Mhe. Rais Magufuli kuwa atasimamia ipasavyo diplomasia ya uchumi ambayo kwa sasa ndio njia inayotumika duniani kukuza uhusiano wa kiuchumi baina ya mataifa mbalimbali.
Kwa upande wake Balozi Abdulrahman Kaniki amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kumteua kushika nafasi hiyo na ameahidi kuendeleza uhusiano wa muda mrefu kati ya Tanzania na Zambia ulioasisiwa na Hayati Baba wa Taifa Mwl. Julius Kambarage Nyerere na Dkt. Keneth Kaunda.
Balozi Kaniki amemuahidi Mhe. Rais Magufuli kuwa atafanyia kazi dhamira ya kuliendeleza Shirika la Reli la Tanzania na Zambia (TAZARA) ambalo limekuwa kiungo muhimu katika nyanja ya kiuchumi kati ya nchi hizi mbili.
Hafla ya kuapishwa kwa mabalozi hao imehudhuriwa na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Uhusiano wa Afrika Mashariki Dkt. Suzan Kolimba na viongozi wa vyombo vya Ulinzi na Usalama.
Jaffar Haniu
Naibu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
05 Oktoba, 2017
Dar es Salaam
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amepokea kwa mshtuko na masikitiko taarifa ya vifo vya watu 15 waliopoteza maisha baada ya lori walilokuwa wakisafiria kupinduka katika eneo la Ntembwa lililopo ndani ya hifadhi ya Lwafi Wilaya ya Nkasi Mkoani Rukwa.
Ajali hiyo imetokea jana tarehe 03 Oktoba, 2017 majira ya saa 2 usiku baada ya lori aina ya Fuso lililokuwa linatoka kijiji cha Mvimwa kuelekea kijiji cha Wampembe na likiwa limebeba mahindi na watu juu yake, kupinduka na kusababisha vifo hivyo na watu wengine 9 kujeruhiwa.
Kufuatia ajali hii Mhe. Rais Magufuli amemtumia salamu za rambirambi Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Kamishna Mstaafu Zelothe Stephen, familia za marehemu, ndugu, jamaa na marafiki wote walioguswa na vifo hivyo.
“Natambua hiki ni kipindi kigumu kwa wanafamilia wote waliopoteza ndugu zao katika ajali hii, natambua kuwa wamepoteza wapendwa wao na watu muhimu waliowategemea, nawapa pole sana kwa kufiwa na naungana nao katika maombi ili roho za marehemu zipumzishwe mahali pema peponi, Amina” Amesema Mhe. Rais Magufuli.
Mhe. Dkt. Magufuli pia amewaombea majeruhi wote wa ajali hii wapone haraka ili warejee katika afya njema na kuungana na familia zao katika maisha yao ya kila siku.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli amezitaka mamlaka zinahusika na masuala ya usalama barabarani kuongeza juhudi zitakazowezesha kukabiliana zaidi na matukio ya ajali za barabarani ili kuokoa maisha ya watu na mali.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
04 Oktoba, 2017