Taarifa kwa vyombo vya Habari ya zamani
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amemteua Prof. William Anangisye kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB).
Prof. William Anangisye ni Mkuu wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Dar es Salaam (DUCE).
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
09 Agosti, 2017
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amemteua Prof. William Anangisye kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB).
Prof. William Anangisye ni Mkuu wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Dar es Salaam (DUCE).
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
09 Agosti, 2017
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 07 Agosti, 2017 amemaliza ziara ya kikazi ya siku 5 katika Mkoa wa Tanga kwa kuzungumza na wananchi wa Wilaya za Korogwe na Handeni pamoja na kufungua kituo cha mabasi cha Korogwe.
Kituo hicho chenye vyumba vya maduka 122 kimejengwa na Serikali ya Tanzania kwa gharama ya Shilingi Bilioni 4.023, na ni kati ya vituo vya mabasi 11 vinavyojengwa katika miji mbalimbali hapa nchini kwa gharama ya takribani Shilingi Bilioni 360.
Akizungumza na wananchi wa Korogwe muda mfupi kabla ya kufungua kituo hicho Mhe. Rais Magufuli amewapongeza wakandarasi waliojenga kituo hicho kwa kazi nzuri waliyoifanya na ameonya kuwa Serikali haitamvumilia mkandarasi yeyote atakayechelewesha ama kujenga mradi wa Serikali chini ya kiwango.
Mhe. Rais Magufuli amepokea ombi la Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Selemani Jafo kusamehewa kodi ya ongezeko la thamani (VAT) katika mradi huo na ameagiza miradi yote inayotekelezwa na Serikali ama kwa fedha za ufadhili isitozwe VAT.
“Haiwezekani miradi hii ni ya Serikali, au inatekelezwa kwa fedha za msaada ama mkopo nafuu halafu sisi wenyewe Serikali tunatoza VAT, kama kuna sheria tuzibadilishe, lakini kama kuna vifaa vimezuiwa kwa ajili ya VAT viachiwe ili miradi iendelee” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Mhe. Rais Magufuli amepokea kero ya uhaba wa maji na mgogoro wa kiwanda cha chai cha Bumbuli na ameahidi kuzifanyia kazi.
Wilayani Handeni Mhe. Rais Magufuli amezungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika eneo la Kibaoni na ametoa wiki 2 kwa wakandarasi waliokuwa wakijenga mradi wa mabwawa 3 ya maji kwa ajili ya Miji ya Manga, Mkata na Kwandugwa kurejea na kuendelea na kazi ya ujenzi wa mradi, vinginevyo wakamatwe na kuchukuliwa hatua za kisheria.
“Hela ya Serikali ninayoiongoza haiwezi kupotea bure, mradi huu ulitengewa Shilingi Bilioni 4.1, hawa wakandarasi walishalipwa Shilingi Bilioni 2.8 na ninafahamu kuwa hawapo kazini na mradi umesimama, nataka ndani ya wiki mbili wawe wamerudi na kuendelea na kazi, wasipofanya hivyo wakamatwe” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Pamoja na mradi huo Mhe. Rais Magufuli amewahakikishia wananchi wa Handeni kuwa Serikali imejipanga kutumia Shilingi Bilioni 200 kumaliza tatizo la maji katika Mji huo na vijiji vitakavyopitiwa na bomba la maji kutoka mto Pangani.
Mhe. Dkt. Magufuli pia amepokea kilio cha wananchi wa Handeni waliodai kuondolewa kikatili katika maeneo yao ya makazi na mashamba ili kumpisha mwekezaji wa uchimbaji wa madini na amewataka kutulia wakati anafanyia kazi kilio hicho.
Akiwa njiani Mhe. Rais Magufuli amesimamishwa katika vijiji vya Msima, Kwachaga na Manga ambako amesikiliza kero za wananchi juu ya ukosefu wa madaktari, uhaba wa maji na ukosefu wa umeme katika baadhi ya vijiji na amewahakikishia kuwa Serikali itatatua kero hizo kwa kuwa mipango ipo.
Katika Kata ya Kwachuma, Mhe. Rais Magufuli ameagiza kuondolewa kwa Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo ya Mazingara baada ya wananchi na Mkuu wa Wilaya ya Handeni Bw. Godwin Gondwe kudai amekuwa akitoa uamuzi usiotoa haki kwa wakulima pale wanapolalamikia mashamba yao ya mazao kuvamiwa na mifugo.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli amesimamishwa na wananchi wa Bunju “B” katika Wilaya ya Kinondoni Mkoani Dar es Salaam ambapo wafanyabiashara wadogo wamelalamikia kuondoshwa katika maeneo yao ya biashara, na Mhe. Rais amesitisha zoezi la kuwaondoa wafanyabiashara hao kwa siku 4 na ameahidi kumtuma Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Bw. Paul Makonda na wataalamu wengine kuchunguza malalamiko hayo ili kupata ufumbuzi.
Mhe. Rais Magufuli amerejea Jijini Dar es Salaam.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
07 Agosti, 2017
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli na Rais wa Jamhuri ya Uganda Mhe. Yoweri Kaguta Museveni leo tarehe 05 Agosti, 2017 wameweka jiwe la msingi la ujenzi wa mradi wa bomba la mafuta ghafi la Afrika Mashariki kutoka Hoima nchini Uganda hadi bandari ya Tanga nchini Tanzania.
Sherehe za uwekaji jiwe la msingi la mradi huo zimefanyika katika Kijiji cha Chongoleani Wilayani Tanga na kuhudhuriwa na Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan, Mke wa Rais Mhe. Mama Janeth Magufuli, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, Naibu wa Pili wa Waziri Mkuu wa Uganda Mhe. Dkt. Ali Kirunda Kivejinja, Mawaziri, Makatibu Wakuu, Wabunge na viongozi wa taasisi za Serikali za Tanzania na Uganda pamoja na wakuu wa mikoa ya Tanzania.
Bomba la kusafirisha mafuta hayo lenye urefu wa kilometa 1,445 ambapo kilometa 1,115 kati yake zitajengwa Tanzania, litakuwa na uwezo wa kusafirisha mapipa 216,000 kwa siku na ujenzi wake umepangwa kukamilika mwaka 2020 kwa gharama ya takribani Shilingi Trilioni 8 za Kitanzania.
Bomba hili litajengwa na kuendeshwa na kampuni za TOTAL ya Ufaransa, CNOOC ya China na TULLOW ya Uingereza, kwa ubia na Kampuni ya Taifa ya Mafuta ya Uganda (UNOC) na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC).
Akizungumza kabla ya kuweka jiwe la msingi Mhe. Rais Magufuli amemshukuru Mhe. Rais Museveni na Serikali yake kwa kufanikisha mradi huo na amemhakikishia kuwa Tanzania imejipanga kutoa ushirikiano wa kutosha pamoja na kuilinda miundombinu ya mradi huo.
Mhe. Rais Magufuli amewataka wananchi watakaonufaika na ajira zaidi ya 30,000 zitakazozalishwa na mradi huo kufanya kazi kwa juhudi, maarifa na uaminifu na pia ametoa wito kwa wananchi wa Tanga na mikoa yote itakayopitiwa na mradi huo kujipanga kunufaika na fursa mbalimbali za biashara zitakazotokana na mradi huo.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli amekubali ombi la Mhe. Rais Museveni la Tanzania kujenga bomba la kusafirisha gesi kwenda nchini Uganda kwa ajili ya kusaidia uzalishaji wa chuma, na pia amemshukuru kwa kukubali kutoa wataalamu waliogundua mafuta nchini Uganda kuja kushirikiana na wataalamu wa Tanzania kwa ajili ya kufanya utafiti wa mafuta katika ziwa Tanganyika na ziwa Eyasi magharibi mwa Tanzania.
Kwa upande wake Mhe. Rais Museveni amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa utayari wake wa kutekeleza mradi huo, na amesisitiza kuwa Tanzania na Uganda zinapaswa kushirikiana katika fursa zake mbalimbali ili kujenga uchumi imara na kuboresha maisha ya watu wake.
Mhe. Rais Museveni ametolea mfano wa mradi wa bomba la mafuta ghafi litakalojengwa na kueleza kuwa mafuta yatakayozalishwa yataziwezesha nchi hizi na nyingine za Afrika Mashariki kupata mafuta kwa gharama nafuu na hivyo kuimarisha huduma za usafirishaji na viwanda, na pia amesisitiza kuwa Tanzania iliyogundua gesi nyingi itaiuzia Uganda ili iitumie kuzalisha chuma kingi na kukiuza Tanzania.
Mhe. Rais Museveni pia ametoa wito kwa nchi za Afrika Mashariki kushirikiana zaidi na kujipanga kukabiliana na changamoto ya uwiano wa kibiashara usio na manufaa kwake, kutokana na takwimu kuonesha kuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki inauza kiasi kidogo cha bidhaa ikilinganishwa na bidhaa zinazoingia kutoka nje.
Mhe. Rais Museveni amemaliza ziara yake ya kikazi ya siku 2 hapa nchini na amerejea nchini Uganda, na Mhe. Rais Magufuli kesho anaendelea na ziara yake ya siku 5 hapa Mkoani Tanga ambapo atazindua kiwanda cha saruji cha Kilimanjaro, ataweka jiwe la msingi la upanuzi wa kiwanda cha maziwa cha Tanga (Tanga Fresh) na ataweka jiwe la msingi la ujenzi wa matanki ya kuhifadhia mafuta katika eneo la Raskazone hapa Mjini Tanga.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Tanga
05 Agosti, 2017
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ameelezea kutoridhishwa kwake na hatua zinazochuliwa na Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji dhidi ya watu waliouziwa viwanda na kisha kuvitelekeza na amemtaka Waziri wa Wizara hiyo Mhe. Charles Mwijage kuvinyang’anya na kuwapatia wawekezaji wanaoweza kuviendeleza.
Mhe. Rais Magufuli ametoa agizo hilo muda mfupi kabla ya kufungua kiwanda cha kuzalisha saruji cha Kilimanjaro kilichopo katika eneo la Maweni Mjini Tanga ambako leo ameendelea na ziara yake ya siku 5 Mkoani Tanga.
Mhe. Rais Magufuli amesema nchi nzima ina viwanda 197 vilivyotelekezwa baada ya kubinafsishwa takribani miaka 20 iliyopita, vikiwemo viwanda vilivyopo Mkoani Tanga lakini anashangaa kuona Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji havinyang’anyi licha ya kutoa maelekezo ya kufanya hivyo mara kadhaa.
Mhe. Rais Magufuli pia amewaagiza Wakuu wa Mikoa yote nchini kufanya tathmini ya viwanda vyote vilivyobinafsishwa katika maeneo yao ili kubaini ambavyo havifanyi kazi na kutafuta wawekezaji wengine wenye uwezo wa kuviendesha.
Kiwanda cha Saruji cha Kilimanjaro kina uwezo wa kuzalisha tani 300 za saruji kwa siku na kinatarajia kuongeza uzalishaji hadi kufikia tani 3,000 kwa siku mwaka ujao.
Baada ya kufungua kiwanda cha saruji cha Kilimanjaro Mhe. Rais Magufuli ameweka jiwe la msingi la upanuzi wa kiwanda cha kusindika maziwa cha Tanga (Tanga Fresh) ambacho kinatarajia kuongeza uzalishaji wa maziwa kutoka lita 50,000 kwa siku hadi kufikia lita 120,000 hatua ambao inatarajiwa kuongeza idadi ya wafugaji kutoka 6,000 hadi 12,000.
Kiwanda hicho kinamilikiwa na vyama vya ushirika vya wafugaji 24 kwa asilimia 42 na mwekezaji kutoka Uholanzi kwa asilimia 58 na upanuzi unaofanywa utaongeza uwekezaji kutoka Shilingi Bilioni 12 hadi kufikia Shilingi Bilioni 26.5.
Akiwa kiwandani hapo Mhe. Rais Magufuli ameiagiza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kukabidhi hati miliki ya kiwanda hicho kwa menejimenti ya kiwanda, na ameiagiza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) iliyokuwa ikidai kodi ya ongezeko la mtaji kuelekeza madai hayo kwa mmiliki wa awali wa kiwanda hicho aliyewauzia wakulima.
Mhe. Rais Magufuli amemuagiza Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mhe. Charles Mwijage kuchukua hatua dhidi ya kiwanda cha maziwa cha Arusha ambacho baada ya kubinafsishwa kimegeuzwa kuwa kituo cha kukusanyia maziwa na kuyasafirisha nje ya nchi kwa ajili ya kusindikwa.
Pia amemuagiza Waziri Mwijage kuwa nchi yoyote itakayozuia maziwa ya Tanzania nayo izuiwe kuingiza maziwa yake hapa nchini.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli ametoa siku 5 kwa Waziri wa Kilimo, Ufugaji na Uvivu Dkt. Charles Tizeba kufika kiwandani hapo na kushughulikia changamoto zinazokikabili kiwanda hicho.
Mhe. Rais Magufuli amefungua awamu ya kwanza ya mradi wa kituo cha matanki ya mafuta cha GBP kilichopo katika eneo la Raskazone Mjini Tanga ambacho kina uwezo wa kuhifadhi lita Milioni 122.6 na ambacho kinatarajia kupanuliwa hadi kufikia lita Milioni 300 ifikapo katikati ya mwaka ujao.
Mhe. Dkt. Magufuli amempongeza Mkurugenzi Mtendaji wa GBP Bw. Badar Sood kwa uwekezaji huo mkubwa wa Shilingi Bilioni 60 utakaojumuisha ujenzi wa kiwanda cha vilainishi na kiwanda cha kusindika gesi na amemhakikishia kuwa Serikali itaendelea kumuunga mkono wakati wowote.
Pia Mhe. Rais Magufuli amempongeza Bw. Sood kwa kulipa kodi ipasavyo ambapo katika mwaka miaka miwili iliyopita ameongeza malipo ya kodi kutoka Shilingi Bilioni 208.950 hadi kufikia Shilingi Bilioni 293.263 na amewahakikishia wawekezaji wote wanaolipa kodi ipasavyo kuwa wapo salama na Serikali itawalinda.
Mhe. Rais Magufuli ameelezea kutoridhishwa kwake na kusuasua kwa mchakato wa ununuzi wa mita za kupimia mafuta yanayoshushwa kutoka melini (Flow Meter) na ametaka Wizara zinazohusika katika mchakato huo kununua mita hizo haraka ili mafuta yanayoingia nchini yapimwe kwa usahihi na kukusanya kodi stahili.
Kesho Rais Magufuli atahitimisha ziara yake Mkoani Tanga kwa kuzungumza na wananchi wa Wilaya za Korogwe na Handeni.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Tanga
06 Agosti, 2017
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amesema Serikali imeanza kuchukua hatua dhidi ya watu waliouziwa mashamba makubwa Mkoani Tanga na kisha kuyatelekeza ambapo mpaka sasa hati miliki za ardhi 5 zenye zaidi ya ekari 14,000 zimefutwa.
Mhe. Rais Magufuli amesema hayo leo tarehe 03 Agosti, 2017 kwa nyakati tofauti wakati akizungumza na wananchi wa Mkata, Komkonga, Kabuku, Michungwani, Hale, Muheza na Pongwe katika Wilaya za Handeni, Muheza na Tanga ambako ameanza ziara ya kikazi ya siku 5 Mkoani wa Tanga.
Mhe. Rais Magufuli amefafanua kuwa Mkoa wa Tanga una mashamba 72 yaliyouzwa kwa watu mbalimbali na kwamba hatua za kunyang’anya mashamba yaliyotelekezwa zimeanza kuchukuliwa kwa mashamba 12 na tayari mashamba 5 ambayo hati zake zimeshafutwa, utaratibu unaendelea kuwagawia wananchi na wawekezaji watakaokuwa tayari kuyaendeleza kama ilivyokusudiwa.
Sambamba na hilo akiwa Mkata Wilayani Handeni, Mhe. Dkt. Magufuli ameagiza shamba la ekari 50 lililopo katika kijiji cha Kabuku na ambalo lililotolewa na wananchi kwa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kwa lengo la kujenga kiwanda miaka 7 iliyopita, lirejeshwe kwa wananchi na ametaka JKT ijenge kiwanda hicho katika eneo lake jingine lenye ukubwa wa zaidi ya ekari 9,000.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli ametoa siku 15 kufanyika kwa uchunguzi wa fedha kiasi cha Shilingi Milioni 500 zilizotolewa kwa ajili ya ujenzi wa majengo ya kituo cha afya cha Mkata, kufuatia kuwepo kwa taarifa za ufujaji wa fedha hizo na ameongeza kuwa Serikali itapeleka Shilingi Milioni 800 kwa ajili ya kuendeleza kituo hicho baada ya hatua stahiki kuchukuliwa.
“Siku 15 tuwe tumepata jibu ili fedha nyingine Shilingi Milioni 800 zije, kama huyo Mkandarasi hafai afukuzwe, kama kuna mtu hafai aondolewe, tuanze na ukurasa mpya, na ningeomba Mkuu wa Wilaya ulifuatilie hili ili asiponyoke mtu yeyote, na wewe una Mamlaka yote” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Kuhusu maji, Mhe. Rais Magufuli amesema Serikali imeanza kuchukua hatua dhidi ya tatizo hilo ikiwemo kutoa Shilingi Bilioni 2 kwa ajili ya kuupatia maji Mji wa Muheza na vijiji vingine na kwamba mradi mwingine wa Shilingi Bilioni 30 utatekelezwa ili kumaliza tatizo hilo.
Mhe. Rais Magufuli amewataka wananchi wa Tanga kujipanga kunufaika na fursa mbalimbali za ajira na biashara kufuatia mradi mkubwa wa ujenzi wa bomba la mafuta ghafi la kutoka Hoima nchini Uganda hadi bandari ya Tanga hapa Tanzania na amewahakikishia kuwa mradi huo utatoa mchango mkubwa katika maendeleo ya Tanga na Taifa kwa ujumla.
“Ndugu zangu wananchi wa Tanga nataka kuwahakikishia kuwa tunakwenda vizuri, tumepata mradi huu mkubwa na pia uchumi wetu unakwenda vizuri, hivi sasa nchi yetu ni kati ya nchi 5 duniani zenye uchumi unaokua kwa kasi na ni nchi ya 2 barani Afrika ikitanguliwa na Ethiopia” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Katika ziara hii Mhe. Rais Magufuli ameongozana na Mkewe Mama Janeth Magufuli, Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira Mhe. Januari Makamba na Wabunge wa Mkoa wa Tanga.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Tanga
03 Agosti, 2017
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 01 Agosti, 2017 amepokea hati za utambulisho wa Mabalozi watano walioteuliwa kuziwakilisha nchi zao hapa nchini.
Mabalozi waliowasilisha hati zao za utambulisho ni;
- Mhe. Nguyen Kim Doahn – Balozi wa Vietnam hapa nchini.
- Mhe. Prof. Ratlan Pardede – Balozi wa Indonesia hapa nchini.
- Mwadhama Askofu Mkuu Marek Solcynski–Balozi wa Vatican hapa nchini.
- Mhe. Dkt. Detlef Wachter – Balozi wa Ujerumani hapa nchini.
- Mhe. Richard Tumisiime Kabonero – Balozi wa Uganda hapa nchini.
Akizungumza na Mabalozi hao Mhe. Rais Magufuli amewapongeza kwa kuteuliwa kuziwakilisha nchi zao hapa nchini na amewahakikishia kuwa Serikali ya Awamu ya Tano itaendeleza na kuimarisha zaidi uhusiano na ushirikiano wake na nchi hizo ambazo ni marafiki wa muda mrefu na washirika wa maendeleo wa Tanzania.
Mhe. Rais Magufuli amewaomba Mabalozi hao kutilia mkazo diplomasia ya uchumi kwa kuongeza juhudi za kuhamasisha wafanyabiashara na wadau wengine wa maendeleo wa nchi hizo kushirikiana na Tanzania katika biashara na miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa viwanda, kilimo na huduma za kijamii.
Kwa upande wao Mabalozi waliowasilisha hati zao za utambulisho wamemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kuwapokea na wameahidi kuhakikisha uhusiano wa nchi zao na Tanzania unaendelezwa na kuimarishwa zaidi.
Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli amemuapisha Mhe. Benedict Martin Mashiba kuwa Balozi wa Tanzania nchini Malawi.
Mhe. Benedict Martin Mashiba anachukua nafasi ya Mhe. Victoria Richard Mwakasege ambaye amestaafu.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
01 Agosti, 2017
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akimuapisha Mhe. Benedict Mashiba kuwa Balozi wa Tanzania Nchini Malawi, Aidha Rais amepokea hati za Utambulisho kutoka kwa Ma
-
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amewasili Jijini Dar es Salaam leo tarehe 27 Julai, 2017 akitokea Mkoani Dodoma ambapo akiwa katika eneo la Tegeta Wilaya ya Kinondoni amezungumza na wananchi waliosimamisha msafara wake na kuwahakikishia kuwa Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kukabiliana na kero na kuimarisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi.
“Kwa sababu ni mara yangu ya kwanza kusimama hapa Tegeta, nianze kwa kuwashukuru sana, kwa kura nyingi mlizonipa ili niwe Rais wa Awamu ya Tano, nawashukuru CCM, nawashukuru CHADEMA, nawashukuru CUF, nawashukuru ACT na hata wale ambao hawana chama kwani wote kwa umoja wenu mlitanguliza maslahi ya Taifa na kumpa kura mtu ambaye atalisaidia Taifa, na mimi nitafanya kazi kwa nguvu zangu zote na kwa kumtanguliza Mwenyezi Mungu ili Watanzania wote hasa wanyonge ambao siku zote walikuwa wakionewa” amesema Mhe. Rais Magufuli
Baadhi ya juhudi alizozitaja kufanyika tangu aingie madarakani ni pamoja na kuondoa ada kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari, kuongeza mikopo ya wanafunzi wa vyuo vikuu kutoka Shilingi Bilioni 371 hadi kufikia Shilingi Bilioni 483, kukabiliana na vitendo vya rushwa na ufisadi na kulinda mali za umma hasa madini.
“Kwenye madini tumeibiwa sana, nchi yetu ni kati ya nchi zinazoongoza kwa kuibiwa, tumeibiwa kwa miaka 18, sasa imetosha” amesema Rais Magufuli.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli ameipongeza Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) kwa kuzuia udahili wa wanafunzi wote wa mwaka kwanza katika vyuo vikuu 19 na kuzuia udahili wa wanafunzi wa kozi 75 katika vyuo vikuu 22 kutokana na dosari zilizobainika wakati wa ukaguzi wa ubora vyuo hivyo uliofanyika Oktoba 2016.
“Ndugu zangu nchi hii ilishakuwa kila kitu hewa hewa, tumegundua wafanyakazi hewa zaidi ya 19,500, kulikuwa na mikopo hewa ya wanafunzi, na naipongeza TCU kwa kufungia baadhi ya vyuo kudahili wanafunzi, nafanya yote haya kwa ajili yenu, nataka tuwe na nchi nzuri” amebainisha Mhe. Rais Magufuli.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
27 Julai, 2017
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
TAARIFA KWA UMMA
Tarehe 05 Agosti, 2017 siku ya Jumamosi Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli na Rais wa Jamhuri ya Uganda Mhe. Yoweri Kaguta Museveni wataweka jiwe la msingi la Mradi wa bomba la kusafirisha mafuta ghafi la Afrika Mashariki kutoka Hoima nchini Uganda hadi bandari ya Tanga nchini Tanzania.
Mradi huu ni moja ya miradi mikubwa ambayo nchi yetu imeipata na kuanza kutekeleza tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani tarehe 05 Novemba, 2015. Ni mradi ambao uwekezaji wake ni mkubwa wa Dola za Marekani Bilioni 3.5 sawa na takribani Shilingi Trilioni 8 za kitanzania.
Urefu wa bomba hili ni kilometa 1,445 na kati ya hizo kilometa 1,115 zinajengwa Tanzania na mafuta ghafi yatakayosafirishwa ni mapipa 216,000 kwa siku.
Inatarajiwa wakati wa ujenzi wa mradi huu ajira takribani 10,000 zitazalishwa na Watanzania watakuwa wanufaika wakubwa wa ajira hizi. Nchi zetu za Tanzania na Uganda zitapata manufaa makubwa ya kiuchumi kutokana na kodi na tozo mbalimbali, mrahaba na shughuli nyingine za kibiashara zitakazoambatana na mradi huu.
Nachukua fursa hii, kuwaalika Watanzania wote kufuatilia matangazo ya moja kwa moja yatakayorushwa na vituo vya redio, televisheni na mitandao ya kijamii kwa siku hiyo ya Sherehe za uwekaji jiwe la msingi na pia kufuatilia matangazo mbalimbali na machapisho yatayotolewa na vyombo vyetu vya habari na mitandao ya kijamii kuelekea siku hiyo.
Kama ambavyo viongozi wa Mkoa wa Tanga wanafanya, tunataraji wananchi wa Tanga watajitokeza kwa wingi kuungana na Rais wao Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli na Rais wa Uganda Mhe. Yoweri Kaguta Museveni katika sherehe hii kubwa na kwa mradi huu mkubwa katika nchi zetu.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
28 Julai, 2017
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amewaagiza viongozi wa Manispaa ya Morogoro na viongozi wa Mkoa wa Morogoro kuwaacha wafanyabiashara ndogondogo wa Mji huo waendelee kufanya biashara zao katika eneo la kituo cha mabasi cha Msamvu.
Mhe. Rais Magufuli ametoa agizo hilo leo tarehe 27 Julai, 2017 baada ya msafara wake uliokuwa ukitoka Dodoma kuelekea Jijini Dar es Salaam kusimamishwa na wananchi wa Morogoro katika eneo la Msamvu na kumueleza kero ya kunyanyaswa na Manispaa ambao wamekuwa wakiwafukuza katika maeneo wanayofanyia biashara hasa baada kituo cha mabasi cha Msamvu kujengwa upya.
Mhe. Rais Magufuli amemuagiza Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro SACP - Ulrich Onesphory Matei kuhakikisha Askari Mgambo hawawasumbui wafanyabiashara ndogondogo na amewataka wafanyabiashara hao kutofanya vurugu wakati utaratibu mzuri unaandaliwa kwa ajili yao.
Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli amewataka watu wote waliobinafsishiwa viwanda mbalimbali katika mkoa wa Morogoro kuvirejesha Serikalini endapo wameshindwa kuviendeleza ili wapewe wawekezaji wanaoweza kuviendeleza na kuzalisha ajira.
“Ninarudia wito wangu niliokwisha kuutoa huko nyuma, kwamba wenye viwanda hapa Morogoro ambao wameshindwa kuviendesha, na leo nataja akiwemo Mbunge wa hapa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), narudia akiwemo Mbunge wa hapa wa CCM ambaye alibinafsishiwa viwanda vingi, kama ameshindwa kuviendesha avirudishe ili tuwape watu wengine kwa sababu vijana hawa wanakosa ajira, nazungumza kwa uwazi kwa sababu msema kweli ni mpenzi wa Mungu” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Pia Mhe. Rais Magufuli amewapongeza wakulima wa mazao Mkoani Morogoro kwa kuongeza uzalishaji wa mazao na amewataja wakulima wa Wilaya ya Kilosa kwa kuongeza uzalishaji kutoka asilimia 42 msimu uliopita hadi kufikia asilimia 82 katika msimu huu.
Kuhusu mradi wa ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa (Standard Gauge) Mhe. Rais Magufuli ametoa wito kwa wananchi wa Morogoro kujitokeza kupata ajira wakati wa ujenzi, lakini amewataka waliojenga katika hifadhi ya reli kuondoa majengo yao kwa hiari.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Morogoro
27 Julai, 2017
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 25 Julai, 2017 amekamilisha ziara yake ya kikazi ya siku 7 katika Mikoa ya Kagera, Kigoma, Tabora na Singida kwa kufungua barabara ya Itigi – Manyoni Mkoani Singida.
Barabara hiyo inayounganisha Mikoa ya Singida, Tabora na Kigoma ina urefu wa kilometa 89.3 na imejengwa gharama ya Shilingi Bilioni 114.692, fedha ambazo zimetolewa na Serikali ya Tanzania.
Akizungumza na wananchi wa Itigi katika sherehe za ufunguzi wa barabara hiyo Mhe. Rais Magufuli ambaye ameongozana na Mkewe Mama Janeth Magufuli, amesema Watanzania wana kila sababu ya kutembea kifua mbele kwa kuwa barabara hiyo pamoja na nyingine saba alizozifungua katika ziara hii zenye urefu wa jumla ya kilometa 707 zimejengwa kwa gharama ya Shilingi Bilioni 806, fedha zote zikiwa zimetolewa na Serikali ya Tanzania.
Mhe. Rais Magufuli amebainisha kuwa miradi mikubwa ya ujenzi wa barabara imetekelezwa na inaendelea kutekelezwa katika maeneo mbalimbali nchini na kwamba Serikali imeamua kuanzisha Wakala wa Barabara Vijijini kwa lengo la kuhakikisha barabara za vijijini zinajengwa kwa kiwango cha lami.
Kwa barabara ya Mkiwa – Itigi yenye urefu wa kilometa 57 na ambayo tayari zabuni ya ujenzi ilishatolewa kwa mkandarasi ili aijenge kwa kiwango cha lami kwa gharama ya Shilingi Bilioni 104, Mhe. Rais Magufuli ameiagiza Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kuupitia upya mkataba wa ujenzi wa barabara hiyo kwa kuwa kiwango cha fedha kilichopangwa ni kikubwa ikilinganishwa na gharama halisi.
Pia amemuagiza Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa Mnyaa kujadiliana na Mkandarasi anayejenga barabara hiyo ili aweze kuendelea kujenga barabara kutoka Itigi kuelekea Chunya hadi Makongorosi Mkoani Mbeya.
Pamoja na wananchi wa Itigi Mkoani Singida, Mhe. Dkt. Magufuli aliyetokea Tabora amezungumza na wananchi waliosimamisha msafara wake katika vijiji vya Kigwa, Kizengi na Tura Wilayani Uyui na amewataka kuendelea kuchapa kazi kwa juhudi na maarifa pamoja na kuzingatia uzalishaji mazao yanayostahimili ukame kama vile uwele, mtama, viazi na muhogo ili kuepuka tatizo la upungufu wa chakula.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli amewataka viongozi wote nchini kuhamasisha wananchi kufanya kazi hususani shughuli za kilimo ambacho ni uti wa mgongo wa Taifa, na ameonya kuwa kiongozi ambaye hatatekelezi agizo hilo atakuwa hafai na ataondolewa.
“Nawaagiza Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya hamasisheni watu kufanya kazi na kama kuna viongozi na watendaji wasiotekeleza wajibu huo katika maeneo yenu waondoeni mara moja” ameagiza Mhe. Rais Magufuli.
Viongozi wengine waliongozana na Mhe. Rais Magufuli katika ziara ya leo ni Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Hamis Kigwangalla, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu Prof. Norman Sigalla King na Wabunge wa Mkoa wa Singida.
Mhe. Rais Magufuli amewasili katika Ikulu ndogo ya Chamwino Mkoani Dodoma.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dodoma
25 Julai, 2017
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 24 Julai, 2017 ameweka jiwe la msingi katika miradi mikubwa miwili ambayo ni mradi wa maji kutoka ziwa Victoria kwenda miji ya Tabora, Igunga na Nzega na mradi wa ukarabati na upanuzi wa uwanja wa ndege wa Tabora, na amefungua barabara mbili za Tabora – Nyahua na Tabora – Puge – Nzega.
Mradi wa maji kutoka ziwa Victoria utatekelezwa kwa muda wa miezi 30 kwa gharama ya Shilingi Bilioni 600 ikiwa ni Mkopo kutoka Serikali ya India na utazalisha takribani lita Milioni 80 za maji kwa siku kwa ajili ya wakazi wa Tabora ambao kwa sasa wanahitaji lita Milioni 36 na pia utamaliza tatizo la maji katika miji ya Igunga, Nzega, Tinde, sehemu ya Wilaya ya Uyui, Shinyanga Vijijini na Vijiji 89 vilivyo kando ya mabomba ya mradi huo.
Mradi wa ukarabati na upanuzi wa uwanja wa ndege wa Tabora unatarajiwa kukamilika katika kipindi cha mwaka mmoja na nusu kuanzia sasa na ni miongoni mwa miradi inayotekelezwa kwa awamu tatu katika Mikoa ya Bukoba, Kigoma, Tabora na usanifu wa viwanja vingine 11 katika Mikoa mbalimbali nchini kwa gharama ya Shilingi Bilioni 69.7.
Barabara ya lami ya Tabora – Nyahua yenye urefu wa kilometa 85 imejengwa kwa gharama ya Shilingi Bilioni 123.773 na barabara ya Tabora – Puge – Nzega yenye urefu wa kilometa 114.9 imejengwa kwa gharama ya Shilingi Bilioni 160.515, fedha zote zikiwa zimetolewa na Serikali ya Tanzania.
Baada ya kuweka mawe ya msingi na kufungua miradi hiyo, Mhe. Rais Magufuli aliyeongozana na Mkewe Mama Janeth Magufuli amefanya mkutano wa hadhara katika uwanja wa Ali Hassan Mwinyi Mjini Tabora ambapo ameipongeza Wizara ya Maji na Umwagiliaji na Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa kutekeleza miradi hiyo, na pia amemuomba Balozi wa India hapa nchini Mhe. Sandeep Arya kumfikishia shukrani zake na za Watanzania kwa Waziri Mkuu wa India Mhe. Narendra Modi kwa kutoa mkopo wa Shilingi Bilioni 600 kwa ajili ya kufanikisha mradi huo wa maji na pia kutoa fedha nyingine Shilingi Trilioni 1.2 kwa ajili ya kutekeleza miradi mingine 17 hapa nchini.
Mhe. Rais Magufuli amemtaka Mkandarasi anayejenga mradi wa maji kutoka ziwa Victoria kuharakisha kazi hiyo na kuikamilisha kabla ya miezi 30 ili wananchi wa Tabora na maeneo yanayosubiri maji ya mradi huo waanze kunufaika mapema na pia ameiagiza Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kuongeza urefu wa njia ya kurukia ndege ya uwanja wa Tabora kutoka kilometa 1.9 waliyopanga hadi kufikia kilometa 2.5 na kujenga jengo kubwa zaidi la abiria litakaloweza kuchukua abiria laki 5 kwa mwaka badala ya abiria 50,000 kama ilivyopangwa hali itakayouwezesha uwanja huo kupokea ndege kubwa na ndogo.
Mhe. Rais Magufuli amewahakikishia wananchi wa Tabora kuwa Serikali yake imejipanga kutekeleza ahadi alizotoa ikiwemo kujenga reli ya kati kwa kiwango cha kisasa (Standard Gauge) itakayoanzia Dar es Salaam – Morogoro – Dodoma – Tabora hadi Kigoma ili kurahisisha usafiri na kukuza biashara ya ndani na nje ya nchi na amewataka wote waliojenga majengo katika hifadhi ya reli kujipanga kuondoa majengo yao kwa hiari kwa kuwa Serikali haitawalipa fidia yoyote.
Kuhusu kero mbalimbali ambazo wananchi wengi wamekuwa wakitaka kumweleza Rais katika mikutano na kwa kutumia mabango Mhe. Dkt. Magufuli amewaagiza viongozi wa Mikoa na Wilaya kutenga muda kila wiki kwa ajili ya kusikiliza kero hizo na ameonya kuwa kuendelea kwa vitendo hivyo kunaashiria kuwa viongozi wa maeneo husika hawatekelezi wajibu wao ipasavyo.
Pamoja na Mawaziri Prof. Makame Mbarawa Mnyaa na Mhandisi Gerson Lwenge mkutano huo umehudhuriwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu Prof. Norman Sigalla King na Wabunge wa Mkoa wa Tabora ambao wamemtaka Mhe. Rais Magufuli kutokatishwa tamaa na watu wanaobeza juhudi kubwa anazozifanya kuwapigania Watanzania, na wamemhakikishia kuwa Wabunge wote wenye nia njema na Tanzania wataendelea kumuunga mkono katika dhamira yake ya kuijenga Tanzania Mpya.
Kesho tarehe 25 Julai, 2017 Mhe. Rais Magufuli ataendelea na ziara yake Mkoani Singida ambako atafungua mradi wa barabara ya Manyoni – Itigi yenye urefu wa kilometa 89.3
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Tabora
24 Julai, 2017
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 23 Julai, 2017 ameweka jiwe la msingi la mradi wa maji wa Nguruka uliopo katika Wilaya ya Uvinza Mkoani Kigoma na kufungua miradi miwili ya barabara za Kaliua – Kazilambwa na barabara ya Tabora – Ndono – Urambo.
Mradi wa Maji wa Nguruka ambao utakamilika tarehe 31 Desemba, 2017 utagharimu Shilingi Bilioni 2.87 na ni miongoni mwa miradi 1,810 ya maji inayotekelezwa na Serikali kwa kutumia fedha za mfuko wa maji nchi nzima ambapo mpaka sasa miradi 1,333 kati yake imekamilika na miradi 477 ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji.
Barabara ya Kaliua – Kazilambwa ina urefu wa kilometa 56 imejengwa kwa gharama ya Shilingi Bilioni 61.86 na barabara ya Tabora – Ndono – Urambo yenye urefu wa kilometa 94 imejengwa gharama ya Shilingi Bilioni 118.96, fedha za miradi yote miwili zimetolewa na Serikali ya Tanzania.
Akizungumza na wananchi katika sherehe za miradi hiyo pamoja na wananchi waliokuwa wakisimamisha msafara wake katika vijiji vya Uvinza, Mpeta, Usinge, Isawima, Igagala, Ndono, Kalola na Ilolangulu, Mhe. Rais Magufuli aliyeongozana na Mkewe Mama Janeth Magufuli amemuagiza Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa Mnyaa kuhakikisha barabara za Urambo – Kaliua yenye urefu wa kilometa 28 inaanza kujengwa ndani ya mwezi mmoja na barabara ya Nyahua – Chaya yenye urefu wa kilometa 85 inaanza kujengwa ndani ya mwezi mmoja na nusu kwa kiwango cha lami.
Mhe. Rais Magufuli pia amewahakikishia wananchi wa Uvinza kuwa Serikali imeshapata fedha za kujenga barabara ya Uvinza – Malagarasi yenye urefu wa kilometa 50 na amemuagiza Waziri Mbarawa kuanza maandalizi ya ujenzi wa barabara ya Kazilambwa – Chagu yenye urefu wa kilometa 41.
Mhe. Rais Magufuli amesema Serikali imeweza kutekeleza miradi hiyo kwa fedha zake inazozipata kutokana na makusanyo ya kodi hivyo amewataka Watanzania kuhakikisha wanalipa kodi ipasavyo na wanadai risiti kila wanaponunua bidhaa na kwamba Serikali ya Awamu ya Tano itaendelea kukabiliana na mianya yote ya upotevu na matumizi mabaya ya fedha za Serikali.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli amewataka wananchi hao kuhifadhi mazingira kwa kujiepusha na vitendo vya ukataji miti katika maeneo ya hifadhi na kupunguza idadi kubwa ya mifugo inayozidi uwezo wa maeneo ya malisho waliyonayo na amekataa ombi la wananchi wa Kijiji cha Isawima waliotaka kuongezewa eneo la Kijiji hicho kwa kilometa 20 zaidi kuingia hifadhini.
Kuhusu tatizo la soko la tumbaku linalowakabili wakulima wa zao hilo mkoani Tabora Mhe. Dkt. Magufuli amewataka wakulima kuwa na subira kwa kuwa Serikali kupitia kwa Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa imeanza kushughulikia tatizo hilo.
Katika ziara ya leo Mhe. Rais Magufuli ameongozana na Mawaziri wawili Prof. Makame Mbarawa Mnyaa na Prof. Joyce Ndalichako, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge Kilimo, Mifugo na Maji Mhe. Daniel Nzanzugwanko na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu Mhe. Prof. Norman Sigalla King na Wabunge wa Mkoa wa Tabora ambao wamempongeza kwa kazi nzuri inayofanywa na Serikali na wamesema wanaunga mkono juhudi hizo.
Kesho tarehe 24 Julai, 2017 Mhe. Rais Magufuli ataendelea na ziara yake hapa Tabora ambapo ataweka jiwe la msingi la mradi wa maji kutoka ziwa Victoria, atafungua mradi wa upanuzi wa uwanja wa ndege wa Tabora eneo la Kaze-Hill, atafungua barabara za Tabora – Nyahua na Tabora – Nzega na atazungumza na wananchi katika uwanja wa Ali Hassan Mwinyi Mjini Tabora.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Tabora
23 Julai, 2017
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 22 Julai, 2017 ameweka jiwe la msingi la mradi wa maji safi na usafi wa mazingira wa Mji wa Kigoma ambao unatarajiwa kumaliza tatizo la uhaba wa maji katika mji huo ifikapo tarehe 30 Novemba, 2017.
Mradi huo utagharimu Shilingi Bilioni 42 na ni moja ya miradi mitano iliyotekelezwa katika miji ya Lindi, Sumbawanga, Babati, Mtwara na Kigoma kwa gharama ya Shilingi Bilioni 164 zikiwa ni ufadhili kutoka Serikali ya Ujerumani kupitia Benki ya Maendeleo ya Ujerumani (KfW) na Umoja wa Ulaya (EU).
Mhe. Rais Magufuli ameishukuru KfW na EU kwa ufadhili huo na ameiagiza Wizara ya Maji na Umwagiliaji kuhakikisha mradi wa maji wa Mji wa Kigoma ambao ulipaswa kukamilika tangu mwaka 2015, unakamilika ifikapo tarehe 30 Novemba, 2017 kama ilivyopangwa.
“Mkandarasi ameniambia mradi utakamilika tarehe 30 Novemba, 2017 na Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhandisi Gerson Lwenge umenihakikishia kuwa mradi utakamilika, nataka kuona mradi unakamilika, wananchi wa Kigoma wanataka maji, hawana haja ya kuendelea kumuona mkandarasi hapa, mradi huu umecheleweshwa sana” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Akizungumza na wananchi wa Kigoma katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa Lake Tanganyika Mjini Kigoma, Mhe. Rais Magufuli aliyeongozana na Mkewe Mama Janeth Magufuli, Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhandisi Gerson Lwenge, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa Mnyaa na Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi Prof. Joyce Ndalichako amewataka wananchi wa Kigoma kutoa ushirikiano wa karibu kwa Serikali katika kipindi hiki ambacho imeamua kuchukua hatua madhubuti za kuinua uchumi na kuondoa kero za wananchi.
Pamoja na kueleza kazi kubwa iliyofanywa na inayoendelea kufanywa kuboresha miundombinu ya barabara na kujenga reli ya kati kwa kiwango cha kisasa (Standard Gauge), Mhe. Dkt. Magufuli amesema Serikali ya Awamu ya Tano imeanza kutekeleza ahadi zake kwa wananchi ikiwemo kufuta tozo 80 katika mazao ya kilimo na tozo nyingine za mifugo na uvuvi ili kuwawezesha wakulima, wafugaji na wavuvi kunufaika na shughuli zao.
“Tumeamua kuwaondolea kero wakulima, sasa hivi ukiwa na mazao yasiyozidi tani moja hakuna kulipa ushuru” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Amebainisha kuwa Serikali imechukua hatua ya kuondoa kero katika huduma za afya kwa kuongeza fedha za bajeti ya dawa na vifaa tiba kutoka Shilingi Bilioni 31 hadi kufikia Shilingi Bilioni 250, imeongeza mikopo ya wanafunzi wa vyuo vikuu kutoka Shilingi Bilioni 373 hadi kufikia Shilingi Bilioni 483, imenunua ndege 6 kwa ajili ya kukuza utalii na kuongeza bajeti ya maendeleo hadi kufikia asilimia 40 ya bajeti nzima ya Serikali.
Katika Mkutano huo, Viongozi mbalimbali wakiwemo wabunge wa Mkoa wa Kigoma wamempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa kazi kubwa iliyofanywa na Serikali katika kipindi kifupi cha tangu aingie madarakani na wameahidi kuendelea kumpa ushirikiano ili kufanikisha dhamira yake ya kuijenga Tanzania mpya na kutatua kero za wananchi.
Kesho Mhe. Rais Magufuli anaendelea na ziara yake ambapo ataweka jiwe la msingi la mradi wa maji wa Nguruka uliopo katika Wilaya ya Uvinza Mkoani Kigoma, atafungua barabara ya Kaliua – Kazilambwa Mkoani Tabora na atafungua barabara ya Urambo – Ndono – Tabora Mkoani Tabora.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Kigoma
22 Julai, 2017
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 21 Julai, 2017 amezindua ujenzi wa barabara za Kibondo – Nyakanazi na Kidahwe – Kasulu, na amewahakikishia wananchi wa Mkoa wa Kigoma kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imejipanga kukamilisha ujenzi wa barabara yote ya Kidahwe – Nyakanazi yenye urefu wa kilometa 310 kama alivyoahidi.
Mhe. Rais Magufuli ameiagiza Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kutangaza zabuni ya ujenzi wa barabara ya Kasulu – Kibondo – Kakonko yenye urefu wa takribani kilometa 200 ndani ya kipindi cha mwezi mmoja kuanzia sasa.
Taarifa ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa Mnyaa imeeleza kuwa ujenzi wa barabara ya Kibondo – Nyakanazi yenye urefu wa kilometa 50 utagharimu Shilingi Bilioni 48.57 na barabara ya Kidahwe – Kasulu yenye urefu wa kilometa 63 utagharimu Shilingi Bilioni 66.331, fedha zote zinatolewa na Serikali ya Tanzania na miradi yote miwili imepangwa kukamilika ifikapo Septemba 2018.
Akizungumza na wananchi katika sherehe za uzinduzi wa ujenzi wa barabara hizo na wananchi waliokuwa wakisimamisha msafara wake katika vijiji vya Kakonko, Kibondo, Kifura, Busunzu, Mkuyuni, Mvugwe, Makere na Kasulu Mhe. Rais Magufuli aliyeongozana na Mkewe Mama Janeth Magufuli amesema Serikali imedhamiria kuimarisha barabara za ukanda wa magharibi ili kuchochea uchumi wa wananchi na kukuza biashara kati ya Tanzania na nchi jirani na ukanda huo.
Hata hivyo Mhe. Dkt. Magufuli ametaka wananchi ambao wamejenga nyumba katika hifadhi ya barabara ambayo ni meta 22.5 kila upande waondoe nyumba hizo kwa hiari kwa kuwa Serikali haitalipa fidia yoyote kwa waliojenga kwenye hifadh ya barabara.
Kuhusu tatizo la uhaba wa maji ambalo wananchi wameomba Serikali iwasaidie, Mhe. Rais Magufuli ameahidi kumtuma Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhandisi Gerson Lwenge kwenda katika maeneo yote yenye matatizo ya maji ili kupata ufumbuzi.
Katika mkutano wa hadhara uliohudhuriwa na maelfu ya wakazi wa Kasulu Mhe. Rais Magufuli amekubali ombi la wananchi kupatiwa sehemu ndogo ya hifadhi ya Kagerankanda ambayo wanaitumia kuzalisha mazao ya chakula na amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Brigedia Jenerali Mstaafu Emmanuel Maganga kupima eneo hilo na kuwagawia wananchi.
Akiwa njiani kuelekea Kigoma Mjini Mhe. Rais Magufuli amesimamishwa na wananchi wa Kibwigwa, Buhigwe na Manyovu, na amewahakikishia kuwa barabara ya Kasulu – Manyovu yenye kilometa 42 itajengwa kwa kiwango cha lami.
Katika ziara ya leo Mhe. Rais Magufuli ameongozana pia na Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi Prof. Joyce Ndalichako, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu Prof. Norman Sigalla King na Wabunge wa Mkoa wa Kigoma.
Kesho tarehe 22 Julai, 2017 Mhe. Rais Magufuli ataendelea na ziara yake hapa Mkoani Kigoma ambapo atazindua ujenzi wa mradi mkubwa wa usambazaji maji katika mji wa Kigoma na kuzungumza na wananchi Mjini Kigoma.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Kigoma
21 Julai, 2017
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Burundi Mhe. Pierre Nkurunziza leo tarehe 20 Julai, 2017 amefanya ziara ya Rasmi ya Kiserikali ya siku moja hapa nchini kwa mwaliko wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli.
Ziara hiyo imefanyika katika Wilaya ya Ngara Mkoani Kagera ambapo Mhe. Rais Nkurunziza amepokelewa rasmi kwa kupigiwa mizinga 21 na kukagua gwaride rasmi lililoandaliwa na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kwa heshima yake katika eneo la Lemela na baadaye mazungumzo rasmi na dhifa ya kitaifa iliyofanyika Mjini Ngara.
Baadaye viongozi hao wamezungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa Posta ya zamani Mjini Ngara.
Akizungumza katika mkutano huo, Mhe. Rais Magufuli aliyeongozana na Mkewe Mama Janeth Magufuli amemshukuru Mhe. Rais Nkurunziza kwa kukubali mwaliko wake na amemhakikishia kuwa Serikali yake ya Awamu ya Tano itaendeleza na kuimarisha zaidi uhusiano na ushirikiano wa kihistoria na kidugu na nchi ya Burundi hususani katika kukuza biashara na uwekezaji.
“Tanzania ni ndugu zako na Watanzania ni ndugu wa watu wa Burundi, umekuja kwa mazungumzo ya kiuchumi, tumezungumza mambo mengi ya kuimarisha biashara kati Tanzania na Burundi, katika takwimu za mwaka 2016 biashara kati ya Tanzania na Burundi ilikuwa na thamani ya Shilingi Bilioni 116.5, kiwango hiki ni kidogo kwa nchi ya Burudni ambayo ina watu zaidi ya Milioni 10 na Tanzania ambayo ina watu zaidi ya Milioni 52” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Halikadhalika Mhe. Rais Magufuli amesema Serikali ya Tanzania inaendelea na juhudi zake za kujenga reli ya kati kwa kiwango cha kisasa (Standard Gauge) ambayo itaunganisha bandari ya Dar es Salaam na nchi za Burundi na Rwanda na hivyo amemhakikishia Mhe. Rais Nkurunziza kuwa reli hiyo itakuwa kichocheo kikubwa cha uchumi wa Tanzania na nchi hizo.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli amempongeza Mhe. Rais Nkurunziza kwa juhudi zake za kusimamia amani nchini mwake na ametoa wito kwa wakimbizi wa Burundi ambao bado wapo nchini Tanzania kuitikia wito wa Rais wao aliyewataka warudi nchini Burundi ili wakaendelea kujenga Taifa lao kwa kuwa hali ni shwari.
Pia Mhe. Rais Magufuli amemuagiza Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Mwigulu Lameck Nchemba kusitisha utoaji wa uraia kwa wakimbizi hao ili utaratibu huo usitimiwe kama kigezo cha watu kuzikimbia nchi zao.
Kwa upande wake Mhe. Rais Nkurunziza amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa mwaliko wake na amesema Tanzania na Burundi ni ndugu na majirani ambao uhusiano na ushirikiano wake ulianza hata kabla ya uhuru.
Mhe. Rais Nkurunziza ametoa wito kwa wafanyabiashara wa Tanzania kwenda kufanya biashara Burundi na wafanyabisahara wa Burundi kuja Tanzania bila wasiwasi na amebainisha kuwa hali ya Burundi ni shwari kwani hata wakimbizi waliokimbilia Tanzania miaka miwili iliyopita wameanza kurejea nchi Burundi kwa hiari yao na wanaendelea na shughuli zao kama kawaida.
“Tunataka kuwajulisha wenzetu Watanzania na Warundi wenzetu ambao walikimbilia Tanzania, Burundi ya leo ni nchi yenye amani, tunawaalika Warundi wenzetu, kaka zetu na dada zetu ambao walikimbilia hapa Tanzania, warudi nchi kwao tujenge nchi yetu iwe na amani ya kudumu.
Tunapata faraja kwamba Warundi wenzetu ambao walikimbilia Tanzania miaka miwili iliyopita ambao wanafikia idadi ya 150,000 wameanza kurudi Burundi bila ya kupitia Shirika la Wakimbizi Duniani (UNHCR), kwa hiyo tunasema wote rudini nyumbani” amesema Mhe. Rais Nkurunziza.
Katika ziara hii Mhe. Rais Magufuli ameongozana na Mawaziri watano na Mhe. Rais Nkurunziza ameongozana na Mawaziri watano ambao pamoja na viongozi wengine wa taasisi na vyombo vya ulinzi na usalama wameshiriki mazungumzo rasmi.
Mhe. Rais Nkurunziza amemaliza ziara yake rasmi ya kiserikali ya siku moja hapa nchini na amerejea nchini Burundi.
Kesho tarehe 21 Julai, 2017 Mhe. Rais Magufuli ataendelea na ziara yake Mkoani Kigoma ambapo ataweka jiwa la msingi la ujenzi wa barabara ya Nyakanazi – Kibondo na barabara ya Kidahwe – Kasulu pamoja na kuzungumza na wananchi.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Ngara, Kagera
20 Julai, 2017
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Burundi Mhe. Pierre Nkurunziza leo tarehe 20 Julai, 2017 amefanya ziara ya Rasmi ya Kiserikali ya siku moja hapa nchini kwa mwaliko wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli.
Ziara hiyo imefanyika katika Wilaya ya Ngara Mkoani Kagera ambapo Mhe. Rais Nkurunziza amepokelewa rasmi kwa kupigiwa mizinga 21 na kukagua gwaride rasmi lililoandaliwa na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kwa heshima yake katika eneo la Lemela na baadaye mazungumzo rasmi na dhifa ya kitaifa iliyofanyika Mjini Ngara.
Baadaye viongozi hao wamezungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa Posta ya zamani Mjini Ngara.
Akizungumza katika mkutano huo, Mhe. Rais Magufuli aliyeongozana na Mkewe Mama Janeth Magufuli amemshukuru Mhe. Rais Nkurunziza kwa kukubali mwaliko wake na amemhakikishia kuwa Serikali yake ya Awamu ya Tano itaendeleza na kuimarisha zaidi uhusiano na ushirikiano wa kihistoria na kidugu na nchi ya Burundi hususani katika kukuza biashara na uwekezaji.
“Tanzania ni ndugu zako na Watanzania ni ndugu wa watu wa Burundi, umekuja kwa mazungumzo ya kiuchumi, tumezungumza mambo mengi ya kuimarisha biashara kati Tanzania na Burundi, katika takwimu za mwaka 2016 biashara kati ya Tanzania na Burundi ilikuwa na thamani ya Shilingi Bilioni 116.5, kiwango hiki ni kidogo kwa nchi ya Burudni ambayo ina watu zaidi ya Milioni 10 na Tanzania ambayo ina watu zaidi ya Milioni 52” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Halikadhalika Mhe. Rais Magufuli amesema Serikali ya Tanzania inaendelea na juhudi zake za kujenga reli ya kati kwa kiwango cha kisasa (Standard Gauge) ambayo itaunganisha bandari ya Dar es Salaam na nchi za Burundi na Rwanda na hivyo amemhakikishia Mhe. Rais Nkurunziza kuwa reli hiyo itakuwa kichocheo kikubwa cha uchumi wa Tanzania na nchi hizo.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli amempongeza Mhe. Rais Nkurunziza kwa juhudi zake za kusimamia amani nchini mwake na ametoa wito kwa wakimbizi wa Burundi ambao bado wapo nchini Tanzania kuitikia wito wa Rais wao aliyewataka warudi nchini Burundi ili wakaendelea kujenga Taifa lao kwa kuwa hali ni shwari.
Pia Mhe. Rais Magufuli amemuagiza Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Mwigulu Lameck Nchemba kusitisha utoaji wa uraia kwa wakimbizi hao ili utaratibu huo usitimiwe kama kigezo cha watu kuzikimbia nchi zao.
Kwa upande wake Mhe. Rais Nkurunziza amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa mwaliko wake na amesema Tanzania na Burundi ni ndugu na majirani ambao uhusiano na ushirikiano wake ulianza hata kabla ya uhuru.
Mhe. Rais Nkurunziza ametoa wito kwa wafanyabiashara wa Tanzania kwenda kufanya biashara Burundi na wafanyabisahara wa Burundi kuja Tanzania bila wasiwasi na amebainisha kuwa hali ya Burundi ni shwari kwani hata wakimbizi waliokimbilia Tanzania miaka miwili iliyopita wameanza kurejea nchi Burundi kwa hiari yao na wanaendelea na shughuli zao kama kawaida.
“Tunataka kuwajulisha wenzetu Watanzania na Warundi wenzetu ambao walikimbilia Tanzania, Burundi ya leo ni nchi yenye amani, tunawaalika Warundi wenzetu, kaka zetu na dada zetu ambao walikimbilia hapa Tanzania, warudi nchi kwao tujenge nchi yetu iwe na amani ya kudumu.
Tunapata faraja kwamba Warundi wenzetu ambao walikimbilia Tanzania miaka miwili iliyopita ambao wanafikia idadi ya 150,000 wameanza kurudi Burundi bila ya kupitia Shirika la Wakimbizi Duniani (UNHCR), kwa hiyo tunasema wote rudini nyumbani” amesema Mhe. Rais Nkurunziza.
Katika ziara hii Mhe. Rais Magufuli ameongozana na Mawaziri watano na Mhe. Rais Nkurunziza ameongozana na Mawaziri watano ambao pamoja na viongozi wengine wa taasisi na vyombo vya ulinzi na usalama wameshiriki mazungumzo rasmi.
Mhe. Rais Nkurunziza amemaliza ziara yake rasmi ya kiserikali ya siku moja hapa nchini na amerejea nchini Burundi.
Kesho tarehe 21 Julai, 2017 Mhe. Rais Magufuli ataendelea na ziara yake Mkoani Kigoma ambapo ataweka jiwa la msingi la ujenzi wa barabara ya Nyakanazi – Kibondo na barabara ya Kidahwe – Kasulu pamoja na kuzungumza na wananchi.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Ngara, Kagera
20 Julai, 2017
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ametoa siku 14 kwa wamiliki wa vituo vyote vya mafuta nchini kufunga na kutumia mashine za kielektroniki za kutolea risiti (Electronic Fiscal Petrol Printer).
Mhe. Rais Magufuli ametoa agizo hilo leo tarehe 19 Julai, 2017 wakati akizungumza na wananchi wa Biharamulo Mkoani Kagera muda mfupi kabla ya kufungua barabara ya lami ya Kagoma – Biharamulo – Lusahunga.
Mhe. Dkt. Magufuli ameiagiza Wizara ya Fedha na Mipango na Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kuhakikisha vituo vyote vya mafuta nchini vinatumia mashine hizo na kusisitiza kuwa wamiliki watakaokiuka agizo hilo vituo vyao vifungwe na kufutiwa leseni.
“Na kwa hili natoa siku 14, wale wenye vituo vya mafuta wote, uwe upo Chato, uwe Biharamulo, uwe Kagera, uwe Dar es Salaam hakikisha una hiyo mashine, ndani ya siku 14” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Mhe. Rais Magufuli pia amewataka wafugaji waliovamia hifadhi ya Burigi Mkoani Kagera kuondoa mifugo yao mara moja na amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Kagera Meja Jenerali Mstaafu Salum Kijuu kuendelea na operesheni ya kuondoa mifugo yote iliyovamia hifadhi hiyo na maeneo mengine yasiyoruhusiwa kupeleka mifugo.
Amewataka wafugaji kote nchi kuchunga mifugo yao katika maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya kulisha mifugo na ameonya kuwa vitendo vya wafugaji kuingiza mifugo yao katika hifadhi na mashamba ya wakulima havikubaliki.
“Mkuu wa Mkoa na Wakuu wa Wilaya simamieni hilo, ninajua bado kuna ng’ombe mle hifadhini, simamieni kwa kuzingatia sheria za hifadhi.
“Kwa hiyo wafugaji wajifunze namna ya kufuga, kama unaona una ng’ombe wengi na huwezi kuwatunza uza, hata mimi nimeuza ng’ombe wangu niliona wamekuwa wengi siwezi kuwatunza, viwanda vipo” amebainisha Mhe. Rais Magufuli.
Kuhusu kero ya uhaba wa maji inayowakabili wananchi wa Biharamulo, Mhe. Rais Magufuli ameelezea kusikitishwa na kasi ndogo ya utekelezaji wa mradi wa kupeleka maji katika mji huo na amemtaka Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji safi na Maji Taka Bukoba (BUWASA) Alen Mwita kuhakikisha mashine zilizonunuliwa zinafungwa na kuanza kutoa maji ifikapo tarehe 30 Julai, 2017.
Baada ya kuzungumza na wananchi wa Biharamulo katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kituo cha mabasi, Mhe. Rais Magufuli amefungua barabara ya Kagoma – Biharamulo – Lusahunga ambayo inaunganisha mawasiliano ya barabara kati ya mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Kigoma, Shinyanga na nchi jirani za Burundi, Rwanda na Uganda.
Barabara hiyo ina urefu wa Kilometa 154 na imejengwa kwa gharama ya Shilingi Bilioni 190.4 zilizotolewa na Serikali ya Tanzania.
Mapema leo asubuhi Mhe. Rais Magufuli ametembelea Seminari ya Mtakatifu Karoli Lwanga Katoke alikosoma elimu ya sekondari ambapo ameendesha harambee iliyofanikisha kupatikana mifuko 1,000 ya saruji na mabati 150 kwa ajili ya kuchangia ujenzi wa majengo ya Seminari hiyo, na pia ametoa Shilingi Milioni 1 kwa ajili ya kutengeneza dirisha la bweni alilolivunja wakati akiwa kidato cha pili pamoja na madirisha mengine yanayohitaji matengenezo.
Akiwa njiani kuelekea Ngara, Mhe. Rais Magufuli amesimamishwa na wananchi wa Nyakahura ambapo amewahakikishia kuwa Serikali itaifanyia matengenezo barabara ya Nyakahura – Rusumo – Ngara, ameahidi kumtuma Waziri wa Maji na Umwagiliaji kwenda kuangalia namna ya kutatua tatizo la maji na pia amechangia Shilingi Milioni 10 katika ujenzi wa majengo ya shule.
Kesho tarehe 20 Julai, 2017 Mhe. Rais Magufuli ataendelea na ziara yake Mkoani Kagera ambapo hapa Ngara atazungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara utakaofanyika mchana.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Ngara, Kagera
19 Julai, 2017
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amemtumia salamu za rambirambi Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Harrison George Mwakyembe kufuatia kifo cha mkewe Bi. Linah George Mwakyembe kilichotokea usiku wa tarehe 15 Julai, 2017.
Bi. Linah George Mwakyembe amefariki dunia katika hospitali ya Agha Khan Jijini Dar es Salaam alikokuwa akipatiwa matibabu.
Katika salamu hizo, Mhe. Rais Magufuli ameelezea kushtushwa na kusikitishwa na kifo hicho, na amesema yeye na familia yake wanaungana na familia ya Dkt. Mwakyembe katika kipindi hiki kigumu cha majonzi.
“Nakupa pole sana Dkt. Mwakyembe kwa kuondokewa na mkeo mpendwa Bi. Linah, natambua hisia za maumivu ulizonazo wewe na familia nzima, nyote nawaombea Mwenyezi Mungu awatie nguvu, awape subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha majonzi.
Namuombea Marehemu Linah George Mwakyembe apumzishwe mahali pema peponi, Amina” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli amesali Ibada ya Jumapili ya 15 ya mwaka wa Kanisa iliyofanyika katika Kanisa la Bikira Maria Parokia ya Chato Mkoani Geita na ameendesha harambee ya kuchangia ujenzi wa kanisa hilo.
Katika harambee hiyo Mhe. Rais Magufuli ambaye ameongozana na Mkewe Mama Janeth Magufuli amefanikiwa kuchangisha fedha taslimu kiasi cha Shilingi Milioni 13, ahadi Shilingi 920,000/=, mifuko ya saruji 33 na malori 2 ya mchanga.
Mhe. Rais Magufuli amewapongeza waumini wa Parokia ya Chato kwa hatua kubwa waliyopiga katika ujenzi wa kanisa kuu la Parokia hiyo na amewataka kuendelea kujitolea kukamilisha hatua za mwisho za ujenzi huo.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Chato, Geita
16 Julai, 2017
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 11 Julai, 2017 amemteua Prof. Florens D.A.M Luoga kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Prof. Florens D.A.M Luoga anachukua nafasi ya Bw. Bernard Mchomvu ambaye Bodi yake ilivunjwa na uteuzi wake kutenguliwa.
Prof. Florens D.A.M Luoga ni Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Taaluma)
Uteuzi wa Prof. Florens D.A.M Luoga unaanza mara moja.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Chato, Geita
11 Julai, 2017
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ameipongeza Taasisi ya Mkapa na Mfuko wa Dunia (Global Fund) kwa mchango wake wa kuunga mkono juhudi za Serikali za kuboresha huduma za kijamii kwa wananchi zikiwemo kujenga zahanati, nyumba za watumishi wa afya na shule.
Mhe. Rais Magufuli ametoa pongezi hizo leo tarehe 10 Julai, 2017 alipokuwa akizungumza na wananchi wa Chato Mkoani Geita muda mfupi baada ya Msarifu wa Taasisi ya Mkapa ambaye ni Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu Mhe. Benjamin William Mkapa kukabidhi nyumba 50 za watumishi wa afya kwa Mikoa ya Geita, Kagera na Simiyu zilizojengwa na taasisi hiyo.
Mhe. Dkt. Magufuli ametoa wito kwa taasisi nyingine zilizopo hapa nchini kuiga mfano mzuri uliooneshwa na Taasisi ya Mkapa kwa kufanya kazi zenye manufaa kwa wananchi na Taifa badala ya kuhamasisha mambo yasiyo na manufaa.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli amesema Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kuboresha huduma za Afya hapa nchini ikiwemo kuongeza bajeti ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na ametoa wito kwa wakurugenzi na watendaji wote wanaosimamia fedha hizo kuzitumia vizuri.
“Viongozi wetu wa halmashauri wa wilaya na mikoa msimamie miradi yetu kikamilifu, Watanzania hawa wana matumaini makubwa na Serikali yao, wamechoka kuonewa kila siku, na ndio maana nazungumza kila siku Serikali ninayoiongoza itakuwa upande wa wananchi, hasa wananchi wanyonge” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Pia Mhe. Rais Magufuli ameonya dhidi ya ubadhirifu wa fedha za umma unaofanywa katika miradi na huduma mbalimbali zinazotolewa na Serikali huku akibanisha kuwa Serikali inaendelea kufanya uhakiki wa pembejeo za ruzuku ambapo mpaka sasa katika mikoa 11 iliyowasilisha madai ya Shilingi Bilioni 50 imebainika kuwa madai halali ni Shilingi Bilioni 8.
Kwa upande wake Msarifu wa Taasisi ya Mkapa na Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu Mhe. Benjamin William Mkapa amempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali katika kuimarisha huduma za afya na amesema taasisi hiyo itaendelea kuunga mkono juhudi za Serikali kuimarisha huduma za afya kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ambao wamekuwa wakichangia gharama za kuboresha huduma hizo.
Mapema akitoa taarifa ya Taasisi ya Mkapa, Afisa Mtendaji Mkuu wa taasisi hiyo Dkt. Ellen Mkondya Senkoro amesema kati ya nyumba 50 zilizokabidhiwa leo, 20 zimejengwa Geita, 20 zimejengwa Simiyu na 10 zimejengwa Kagera na kwamba nyumba hizo ni kati ya nyumba zote 450 zenye thamani ya Shilingi Bilioni 26.5 zilizojengwa na taasisi hiyo tangu mpango ulipoanzishwa mwaka 2012.
Dkt. Senkoro ameongeza kuwa pamoja na kujenga nyumba hizo, Taasisi ya Mkapa imeajiri watumishi wa afya 1,100 na imejenga vituo 11 vya afya vinavyotoa huduma ya upasuaji nchini.
Nae Mwakilishi wa Mfuko wa Dunia (Global Fund) Bi. Matha Setembo amesema tangu mwaka 2003 hadi 2017 mfuko huo umeingia mikataba Serikali ya Tanzania yenye thamani ya Shilingi Trilioni 3.8 kwa ajili ya kupambana na ugonjwa wa Ukimwi, Kifua Kikuu na Malaria na kwamba kati ya mwaka 2018 – 2020 Mfuko huo umetenga takribani Shilingi Trilioni 1.3 kwa ajili ya Tanzania Bara na takribani Shilingi Bilioni 24.5 kwa ajili ya Zanzibar ili kukabiliana na magonjwa hayo.
Sherehe hizo zimehudhuriwa na Balozi wa Japan hapa nchini Mhe. Masaharu Yoshida ambaye amekabidhi kiwanda cha alizeti kwa chama cha ushirika cha msingi Chato, ameahidi kuwa Japan itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu ambaye amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kutoa kipaumbele kwenye huduma za afya ikiwemo kuongeza fedha za dawa na hivyo kuwezesha bei ya dawa katika vituo vya tiba kupungua kwa kati ya asilimia 15 na asilimia 80.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Chato, Geita
10 Julai, 2017
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ameridhia maombi ya kustaafu mapema kwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Prof. John Eudes Ruhangisa.
Taarifa iliyotolewa leo na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi imeeleza kuwa Mhe. Rais Magufuli ameridhia maombi ya kustaafu mapema kwa Prof. John Eudes Ruhangisa kuanzia leo 06 Julai, 2017.
Mhe. Prof. John Eudes Ruhangisa alikuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Shinyanga.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
06 Julai, 2017
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amemteua Bw. Waziri Waziri Kindamba kuwa Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL).
Taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi imeeleza kuwa Uteuzi wa Bw. Waziri Waziri Kindamba umeanza tarehe 04 Julai, 2017.
Kabla ya uteuzi huo, Bw. Waziri Waziri Kindamba alikuwa akikaimu nafasi hiyo.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
06 Julai, 2017
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, leo tarehe 4 Julai, 2017 amehitimisha ziara yake ya kikazi ya Siku Mbili Mkoani Mwanza kwa kuzindua mradi wa Uboreshaji wa huduma ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira katika kijiji cha Nyamazugo Wilayani Sengerema.
Mradi huo wa maji umetekelezwa chini ya mpango wa maji wa Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa ufadhili wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) kwa gharama ya shilingi bilioni 22.4. Mradi wa Maji Safi mjini Sengerema ulioanza tangu mwaka 2011 unatarajiwa kuwahudumia wakazi 138,000 ifikapo mwaka 2030.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa Mradi huo, Mhe. Rais Dkt. Magufuli amesema kukamilika kwa mradi huo kutamaliza tatizo la maji la muda mrefu kwa wakazi wa Sengerema na maeneo ya jirani.
Mhe. Rais Dkt. Magufuli amewataka wananchi wanaozunguka mradi huo kuutunza na kuhakikisha hawaharibu vyanzo vya maji katika eneo hilo la ziwa Victoria ikiwa ni pamoja na kuacha uvuvi haramu ambao umekuwa na madhara makubwa kwa wananchi.
Aidha, ameuagiza uongozi wa Mkoa wa Mwanza na Vyombo vya Dola kuchukua hatua kali dhidi ya watu wanaochafua vyanzo vya maji katika eneo la Ziwa Victoria.
Katika hafla hiyo ya Uzinduzi wa mradi wa maji Kada wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo - CHADEMA HamisiHussein Maarufu TABASAM, ameamua kuachana na chama chake na kujiunga na CCCM.
Mhe. Rais Dkt. Magufuli ameendelea kusisitiza msimamo wa Serikali kuwa hakuna mwanafunzi atakayepata ujauzito ataruhusiwa kuendelea na masomo na ameyataka Mashrika yasiyo ya Kiserikali ambayo yamekuwa yakipinga uamuzi huo kufungua Shule zao wenyewe ambazo zitawasomesha wanafunzi wanaopata ujauzito.
''Haiwezekani Serikali itoe pesa kuwasomesha wanafunzi halafu wapate mimba waendelee na masomo hilo haiwezekani, hizo NGOs zinazotetea hali hiyo zikitaka zijenge shule kwa ajili ya kuwasomesha wanafunzi watakaopata ujauzito''amesema Rais Magufuli.
Mhe. Rais Magufuli amezungumzia uamuzi wa Serikali kupeleka Miswada Mitatu ya dharura Bungeni kuwa unatokana na umuhimu wa hilo katika kutetea maslahi mapana ya nchi na kuhakikisha rasilimali za nchi zinawanufaisha wananchi.
Mhe. Rais Magufuli amewaonya wanachama wa Chama cha Mapinduzi CCM wenye nia ya kugombea nafasi mbalimbali katika Uchaguzi wa Chama hicho kutojihusisha na rushwa kwa vile rushwa ni adui wa haki, hivyo, atakayebainika kutumia rushwa atapoteza sifa ya kuwa Mgombea.
Akizungunzia ujenzi wa barabara ya kutoka Kamanga hadi Sengerama kwa kiwango cha lami, Mhe. Rais Dkt. Magufuli amesema kwa sasa Serikali imeshampata mkandarasi kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu na usanifu ili barabara hiyo ianze kujengwa katika kutimiza ahadi aliyoitoa wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.
Rais Magufuli pia amewataka Wakuu wa Mikoa na Wilaya nchni kufafanua kwa wananchi na kusimamia uamuzi wa Serikali wa kufuta tozo zaidi ya 80 katika mazazo ya Kilimo, tozo 7 za Mifugo na tozo 5 za Uvuvi ambao lengo lake ni kuwaondolea kero wananchi.
Aidha, amesema Serikali inafanya uchambuzi ili kubaini wale wote waliotoa pembejeo hewa na atakayebainika atachukuliwa hatua kali za kisheria.
Wakati huo huo, Mheshimiwa Rais Magufuli ameiagiza Wizara ya Nishati na Madini kusitisha utoaji wa leseni mpya za uchimbaji na halikadhalika leseni ambazo zimeisha muda wake. Ametoa maagizo hayo alipokuwa akizungumza na wananchi wa Geita ambao walizuia msafara wake katika maeneo mbalimbali wakati akiwa njiani kuelekea Chato.
Jaffar Haniu
Naibu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Sengerema,Mwanza
04 Julai 2017.
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, leo tarehe 3 Julai, 2017 amewasili mkoani Mwanza kwa ziara ya kikazi ya siku mbili na kupokelewa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. John Mongela pamoja na viongozi mbalimbali wa Mkoa wa Mwanza.
Akiwa mkoani hapa Mhe. Rais Magufuli atakuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa mradi wa uboreshaji wa huduma ya maji safi na usafi wa mazingira mjini Sengerema tarehe 4 Julai, 2017.
Katika Uwanja wa Ndege wa Mwanza Mhe. Rais Dkt. Magufuli amekutana na kamati ya amani ya viongozi wa dini na kuwashukuru viongozi hao kwa sala na dua zao na amewataka waendelee kuwahimiza waumini wao kuliombea Taifa ili liepukane na vitendo vya rushwa ambavyo ni adui wa maendeleo.
Akiwa njiani kutoka Uwanja wa Ndege wa Mwanza katika eneo la Bwiru kuelekea Ikulu ndogo ya Mwanza, Mhe. Rais Magufuli msafara wake umesimamishwa mara kwa mara na wananchi waliojaa barabarani na kuamua kuzungumza nao ambapo amewahakikishia kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imepania kupambana na ufisadi kwa lengo la kuwaletea maendeleo Watanzania bila kujali tofauti za dini au Siasa.
Aidha, amewahakikishia wananchi hao kuwa Serikali yake imedhamiria kuondoa kero mbalimbali ikiwa ni pamoja na kufuta baadhi ya kodi zenye kero na kuwapatia vitambulisho wafanyabishara wadogo wadogo, maarufu kama Wamachinga, ili waweze kufanya biashara zao bila kusumbuliwa.
Akiwa eneo la Nyamagana jijini Mwanza, Mheshimiwa Rais alitembea kwa miguu huku kuwasalimu wananchi waliokuwa wakimshangilia na kuzuia msafara wake. Rais Magufuli pia alikwenda Uwanja wa Mpira wa Nyamagana na kuungana na baadhi ya wananchi waliokuwa wakiangalia mechi ya mpira wa miguu kati ya timu ya Buhongwe na Nyamwaga.
Mhe. Rais Dkt. Magufuli pia amefurahishwa na maendeleo ya ujenzi wa barabara ya kutoka Uwanja wa Ndege wa Mwanza hadi katikakati ya jiji ambao gharama za ujenzi wake zilitokana na fedha zilizokuwa zimetengwa kwa ajili ya sherehe za Muungano.
Jaffar Haniu
Naibu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Mwanza
03 Julai 2017.
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 02 Julai, 2017 ameweka jiwe la msingi na kuzindua kazi za mradi wa ujenzi, ukarabati na upanuzi wa bandari ya Dar es Salaam utakaoiwezesha bandari hiyo kuhudumia meli kubwa na kuongeza kiasi cha mizigo ikilinganishwa na hali ilivyo hivi sasa.
Hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi imefanyika katika eneo la bandari hiyo Jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa Mnyaa, Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mhe. Charles Mwijage, Balozi wa Uingereza hapa nchini Mhe. Sarah Cooke na Mwakilishi wa Benki ya Dunia Bi. Bella Bird.
Ujenzi, ukarabati na upanuzi wa bandari ya Dar es Salaam umepangwa kufanyika kwa miezi 30 kuanzia sasa kwa gharama ya Shilingi Bilioni 926.2 ambapo kati yake Shilingi Bilioni 132 zinatolewa na Serikali ya Tanzania, Shilingi Bilioni 770 ni mkopo wa masharti nafuu kutoka Benki ya Dunia na Shilingi Bilioni 24 ni Msaada kutoka Shirika la Maendeleo la Uingereza (DFID).
Kazi za ujenzi, upanuzi na ukarabati huo zitafanyika katika gati namba 1 hadi gati namba 7 ambazo zinaendeshwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) na zitahusisha kujenga gati hizo, kuongeza kina cha bahari kwa kuongeza urefu kutoka wastani wa mita 12 hadi kufikia mita 15.5 na kukarabati miundombinu wezeshi ya bandari.
Mradi huu mkubwa utaiwezesha bandari ya Dar es Salaam kuongeza uwezo wa kuhudumia meli kubwa kutoka meli zenye urefu wa meta 243 na uwezo wa kubeba makontena kati ya 2,500 na 4000 hadi kufikia meli zenye urefu wa meta 320 na uwezo wa kubeba makontena kati ya 6,000 na 8,000 na pia kuongeza uwezo wa kuhudumia shehena za mizigo kutoka tani Milioni 18 za sasa hadi kufikia tani Milioni 28 ifikapo mwaka 2022.
Akizungumza kabla ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi huo, Mhe. Rais Magufuli amewashukuru wadau wa maendeleo walioshiriki kufanikisha mradi huo ambao ni Benki ya Dunia na DFID na amesema mradi huu ukikamilika utaiwezesha bandari kuwa ya mfano, na ametaka wakandarasi wanaojenga mradi huo waukamilishe haraka ikiwezekana kabla ya miezi 30 kuisha ili Tanzania na nchi za Rwanda, Uganda, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Zambia, Malawi na Zimbabwe zianze kunufaika mapema.
Mhe. Rais Magufuli amebainisha kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kuboresha bandari zote nchini lakini ameitaka TPA na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuongeza udhibiti wa mizigo inayoingia na kutoka kupitia bandari kwa kuhakikisha mizigo hiyo inakuwa halali na inalipiwa kodi ipasavyo.
Aidha, Mhe. Dkt. Magufuli amewataka Watanzania kuunga mkono juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali kupigania maslahi ya nchi na ameonya dhidi ya baadhi ya wanasiasa ambao wamekuwa wakibeza juhudi hizo pamoja na juhudi za kukabiliana na wahalifu ambao wanawaua raia wasio na hatia pamoja na askari polisi.
“Wajifunze kufunga midomo yao wakati Serikali inafanya kazi yake, na kwa ujumbe huu nataka Watanzania waelewe kuwa tuna mambo makubwa katika nchi hii tunayoshughulika nayo, na ndio maana wakati mwingine unakuta ni mzahamzaha tu, unakuta wakati mwingine mnashughulikia rasilimali za Watanzania zinazoibiwa, mtu mwingine anapinga hadharani” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Wakizungumza kabla ya hotuba ya Rais, Balozi wa Uingereza hapa nchini Mhe. Sarah Cooke na Mwakilishi wa Benki ya Dunia Bi. Bella Bird wamempongeza Mhe. Rais Magufuli na Serikali kwa juhudi kubwa zilifanyika kuongeza uwazi na ufanisi wa bandari, kudhibiti wizi, mizigo haramu na rushwa, na wameahidi kuendeleza uhusiano mzuri kati ya Serikali na vyombo wanavyoviwakilisha.
Nao Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu Mhe. Prof. Norman Sigalla King na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti Mhe. Hawa Ghasia wamempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa juhudi kubwa anazozifanya kuimarisha miundombinu na wameahidi kuendelea kuunga mkono juhudi hizo.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
02 Julai, 2017
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
“Kwa mshituko na masikitiko makubwa nimepokea taarifa za kifo cha Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) katika Kanda ya Afrika Kusini Dkt. Tonia Kandiero aliyefariki dunia ghafla jana usiku tarehe 28 Juni, 2017 akiwa ofisini kwake huko Pretoria Afrika Kusini”
Hii ni kauli ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli aliyoitoa leo tarehe 29 Juni, 2017 Ikulu Jijini Dar es Salaam muda mfupi baada ya kupokea taarifa za kifo cha Dkt. Tonia Kandiero ambaye kabla ya kuteuliwa kushika wadhifa wa Mkurugenzi Mkuu wa AfDB katika Ofisi za Kanda ya Afrika Kusini mwishoni mwa mwaka 2016 alikuwa Mwakilishi wa AfDB Tanzania.
“Nitamkumbuka Dkt. Tonia Kandiero kama mchapakazi hodari aliyetoa mchango mkubwa katika maendeleo ya nchi yetu, nikiwa Waziri wa Ujenzi nimeshirikiana nae kwa karibu kufanikisha utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo kwa nchi yetu ambayo imefadhiliwa na AfDB, ametoa mchango mkubwa kufanikisha ujenzi wa madaraja na barabara za Dodoma – Iringa, Dodoma – Babati, Namtumbo – Tunduru – Mtambaswala, Arusha – Taveta – Voi na pia alitoa mchango mkubwa katika kufanikisha miradi mingine ambayo ipo mbioni kutekelezwa ikiwemo ujenzi wa barabara ya Bagamoyo – Tanga – Mombasa, Mbinga – Mbambabay na Tabora - Katavi”.
Kufuatia kifo cha Dkt. Tonia Kandiero Mhe. Rais Magufuli amemtumia salamu za rambirambi Rais wa AfDB Dkt. Akinwumi Adesina, familia ya Dkt. Tonia Kandiero, wafanyakazi wote wa AfDB, ndugu, jamaa na marafiki wote walioguswa na msiba huu.
Dkt. Magufuli amemuombea marehemu Dkt. Tonia Kandiero apumzishwe mahali pema peponi, Amina.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
29 Juni, 2017
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 28 Juni, 2017 amekutana na timu ya wataalamu wa masuala ya umeme na ujenzi wa mabwawa ya maji ya kuzalisha umeme iliyotumwa na Waziri Mkuu wa Ethiopia Mhe. Hailemariam Desalegn kwa lengo la kubadilishana uzoefu na Tanzania.
Mhe. Rais Magufuli amesema timu hiyo inayoongozwa na Waziri wa Maji, Umwagiliaji na Umeme wa Ethiopia Dkt. Seleshi Bekele imekuja nchini kubadilishana uzoefu na timu ya wataalamu wa Tanzania ambayo inasimamia utekelezaji wa ujenzi wa mradi wa kuzalisha umeme katika maporomoko ya mto Rufiji (Stiegler’s Gorge Power Project).
Katika mazungumzo na timu hiyo yaliyofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam, Mhe. Rais Magufuli ameelezea nia yake ya kuhakikisha mawazo ya Baba wa Taifa Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere ya tangu mwaka 1980 juu ya kuzalisha umeme kutoka maporomoko ya mto Rufiji, yanatekelezwa haraka iwezekanavyo.
“Sasa hivi nchi yetu inazalisha megawatts 1,450 tu, lakini Stiegler’s Gorge itatuzalishia megawatts 2,100 umeme huo ni mwingi na utatusaidia katika viwanda, hivyo Serikali tumeamua kutekeleza mradi huu.
“Najua kutaanza kutokea vipingamizi mbalimbali, lakini naomba Watanzania tuwe na sauti moja, eneo litakalotumia ni Kilometa za mraba 1,350 ambalo ni sawa na asilimia 3 tu ya eneo lote la hifadhi ya Selous yenye ukubwa wa Kilometa za mraba 45,000” amesema Mhe. Rais Magufuli na kuongeza kuwa mradi huo utakuwa na faida nyingi zikiwemo uvuvi, maji kwa ajili ya wanyamapori na kilimo.
Kwa upande wake Waziri wa Maji, Umwagiliaji na Umeme wa Ethiopia Dkt. Seleshi Bekele amesema Ethiopia ambayo kwa sasa inazalisha megawatts 4,300 za umeme kwa kutumia maji, inayo miradi mingi ya kuzalisha umeme kwa kutumia maji ambayo itaiwezesha kufikia uzalishaji wa megawatts 17,000 ifikapo mwaka 2020 na kwamba yeye na watalaamu wa nchi wapo tayari kubadilishana uzoefu na Tanzania katika masuala ya umeme na ujenzi wa mabwawa ya maji ya kuzalisha umeme.
Mazungumzo hayo yamehudhuriwa na Katibu Mkuu Kiongozi Mhe. Balozi John Kijazi, Naibu Waziri wa Nishati na Madini wa Tanzania Dkt. Medard Kalemani na timu ya wataalamu wa Tanzania wanaosimamia utekelezaji wa ujenzi wa mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia maporomoko ya mto Rufiji (Stiegler’s Gorge Power Project).
Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli amekutana na wajumbe wa kamati mbili zilizofanya uchunguzi wa madini yaliyokuwamo kwenye makontena yenye mchanga wa madini katika maeneo mbalimbali hapa nchini, na kuwapongeza kwa kazi nzuri waliyoifanya.
Mhe. Rais Magufuli amesema timu hiyo imefanya kazi nzuri na yenye maslahi makubwa kwa Taifa na kwamba Serikali itahakikisha inafanyia kazi taarifa zilizotolewa na kamati hizo.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
28 Juni, 2017
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 27 Juni, 2017 ameagana na wafanyakazi wa iliyokuwa Ofisi ya Rais, Ufuatiliaji wa Utekelezaji wa Miradi (President’s Delivery Bureau - PDB) ambao wamehamishiwa katika ofisi na taasisi nyingine za Serikali kwa ajili ya kuendelea na utumishi wa umma.
Wafanyakazi hawa ndio walikuwa wakisimamia utekelezaji wa Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (Big Results Now - BRN).
Mhe. Rais Magufuli amekutana na wafanyakazi hao Ikulu Jijini Dar es Salaam ambapo amewashukuru kwa kazi nzuri waliyoifanya wakiwa PDB na amewataka kuendelea kulitumikia Taifa kwa juhudi na maarifa wakiwa katika ofisi nyingine walizopangiwa.
“Natambua kuwa nyie ni wafanyakazi wazuri wenye ujuzi na maarifa muhimu kwa ajili ya Taifa letu. Mmetoa mchango mkubwa mlipokuwa PDB nategemea mtaendelea hivyo na hata zaidi katika ofisi mbalimbali mlizopangiwa, mkachape kazi kwa kutanguliza maslahi ya Watanzania” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Mkutano huo umehudhuriwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma Mhe. Angellah Kairuki, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Dkt. Laurian Ndumbaro.
Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli amekutana na timu ya wataalam wa masuala ya umeme na ujenzi wa miundombinu ya mabwawa ya maji kwa ajili ya kuzalisha umeme na kujadiliana nao kuhusu utekelezaji wa mradi mkubwa wa uzalishaji wa umeme katika maporomoko ya mto Rufiji (Stiegler’s Gorge Power Project) ambao una uwezo wa kuzalisha Megawatts 2,100 za umeme.
Mhe. Rais Magufuli amekutana na wataalamu hao ikiwa ni utekelezaji wa nia yake ya kuhakikisha mradi huo unaanza kujengwa haraka iwezekanavyo na kuzalisha umeme mwingi utakaosaidia kuharakisha maendeleo hapa nchini, hususani ujenzi wa viwanda.
“Kesho Waziri Mkuu wa Ethiopia Mhe. Hailemariam Desalegn anawatuma wataalamu wake waliojenga mradi mkubwa wa bwawa la maji la kuzalisha umeme kule Ethiopia, wakiwa hapa mtakutana nao na mtabadilishana uzoefu, nataka na sisi tusichelewe, tuzalishe umeme utusaidie kwenye ujenzi wa viwanda” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
27 Juni, 2017