Taarifa kwa vyombo vya Habari ya zamani
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Waziri Mkuu wa Shirikisho la Jamhuri ya Kidemokrasi ya Ethiopia Mhe. Hailemariam Dessalegn ameondoka nchini leo kurejea nchini mwake Ethiopia baada ya kumaliza ziara yake rasmi ya kiserikali hapa nchini aliyoifanya kwa mwaliko wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli.
Katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam, Mhe. Hailemariam Dessalegn ameagwa na mwenyeji wake Mhe. Rais Magufuli aliyeongozana na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa.
Akiwa nchini Mhe. Hailemariam Dessalegn amefanya mazungumzo na mwenyeji wake Mhe. Rais Magufuli Ikulu Jijini Dar es Salaam, amehudhuria dhifa ya kitaifa iliyoandaliwa na Mhe. Dkt. Magufuli kwa heshima yake na leo asubuhi ametembelea bandari ya Dar es Salaam ambapo amesema nchi yake ipo tayari kuitumia bandari hiyo sambamba na kuanzisha kituo cha huduma za usafirishaji wa mizigo kwa ndege (Cargo Hub) katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere kupitia shirika lake la ndege la Ethiopia Airline.
Emmanuel Buhohela
Kaimu Mwandishi wa Habari wa Rais Msaidizi
Dar es Salaam
01 Aprili, 2017
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 01 Aprili, 2017 amewaapisha wajumbe wa kamati maalum ya kuchunguza kiwango na aina ya madini yaliyomo kwenye mchanga wenye madini ulio ndani ya makontena yaliyopo katika maeneo mbalimbali hapa nchini.
Hafla ya kiapo kwa wajumbe wa kamati hiyo imefanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. George Mcheche Masaju, Katibu Mkuu Kiongozi Mhe. Balozi John Kijazi, Kamishna wa Maadili Mhe. Jaji Harold Nsekela na viongozi wa vyombo vya ulinzi na usalama.
Kamati hiyo ya wanasayansi 8 walioteuliwa na Mhe. Rais Magufuli tarehe 29 Machi, 2017 inaongozwa na Mwenyekiti wake Prof. Abdulkarim Hamis Mruma na itafanya kazi ya uchunguzi kwa siku 20 kisha kuwasilisha ripoti yake kwa Mhe. Rais.
Akizungumza baada ya kuwaapisha, Mhe. Rais Magufuli amesema ameamua kuunda kamati hiyo yenye wasomi waliobobea katika masuala ya jiolojia, kemikali na uchambuzi wa kisayansi ili wawawakilishe Watanzania zaidi ya Milioni 50 ambao wanataka kujua ukweli kuhusu rasilimali yao ya madini.
“Hivi sasa duniani kuna vita nyingi na vita mojawapo ni vita ya uchumi, kwa hiyo tunawatuma nyinyi mwende mkapigane vita hii katika sekta hii ya madini, mkawawakilishe Watanzania zaidi ya Milioni 50, mkapate ukweli wote na wala msikubali kuyumbishwa na mtu yeyote, tumieni utaalamu wenu, busara zenu, uzalendo wenu kwa Taifa na upendo wenu kwa Watanzania hasa masikini wenye shida nyingi” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Mhe. Dkt. Magufuli amewahakikishia kuwa Serikali itatoa kila aina ya ushirikiano kufanikisha kazi hiyo na ametaka wawe huru kutumia vitendea kazi vyovyote vinavyohitajika zikiwemo maabara mbalimbali za taasisi za Serikali na nyinginezo.
“Nendeni popote mnapohitaji kufanya kazi tutawapa ushirikiano, fungueni makontena popote yalipo, chukueni sampuli na mkazipime mjue kilichomo na naviagiza vyombo vya dola vihakikishe hakuna mtu atakayewakwamisha” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli
Aidha, Mhe. Dkt. Magufuli amesema baada ya kuunda kamati hii ya wanasayansi ataunda kamati nyingine ya wachumi na wanasheria kwa ajili ya kufanya tathmini na kuiangalia sera na sheria ya madini kwa lengo la kupata taarifa zaidi juu ya biashara ya madini hapa nchini.
Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na Kiongozi Mkuu wa Jumuiya ya Kihindu ya BAPS Swaminarayan Sanstha Duniani Mtukufu Mahant Swami Maharaj ambaye yupo nchini kwa ziara ya siku 7.
Pamoja na kumshukuru kwa ujio wake hapa nchini, Mhe. Rais Magufuli amemhakikishia kuwa Serikali ya Tanzania itaendeleza na kuimarisha zaidi uhusiano na ushirikiano wake na Jumuiya hiyo na amewaalika wafanyabiashara walio chini ya Jumuiya hiyo kuja nchini Tanzania kuwekeza katika viwanda, kilimo na shughuli nyingine za biashara na uwekezaji.
“Nimefurahishwa sana na ujio wako Mtukufu Mahant Swami Maharaj, sisi Tanzania tumekuwa tukishirikiana na Jumuiya ya Hindu tangu miaka mingi, nitafurahi kama mtaungana na juhudi za Serikali ya Tanzania kujenga viwanda, njooni mjenge viwanda na Serikali itawapa ushirikiano wowote mtakaohitaji” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Mtukufu Mahant Swami Maharaj ambaye amefanya dua ya kuliombea Taifa na Rais, amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kukutana nae na amemhakikishia kuwa uhusiano na ushirikiano kati ya Jumuiya hiyo na Tanzania ulioanzishwa tangu enzi za utawala wa Awamu ya Kwanza ya Tanzania unaendelezwa na kukuzwa zaidi.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
01 Aprili, 2017
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Waziri Mkuu wa Shirikisho la Kidemokrasia la Jamhuri ya Ethiopia Mhe. Hailemariam Dessalegn amemhakikishia Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kuwa nchi yake ipo tayari kuimarisha na kukuza zaidi uhusiano na ushirikiano wake na Tanzania utakaosaidia kuleta manufaa makubwa zaidi kiuchumi na kukabiliana na umasikini wa wananchi wa nchi zote mbili.
Mhe. Hailemariam Dessalegn ametoa kauli hiyo leo Ikulu Jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na wananchi wa Tanzania na Ethiopia kupitia vyombo vya habari muda mfupi baada ya kuwasili nchini kwa ziara rasmi ya kiserikali ya siku mbili, anayoifanya kwa mwaliko wa Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli.
Miongoni mwa maeneo ambayo Mhe. Hailemariam Dessalegn amesema atatilia mkazo ni ushirikiano katika usafiri wa anga ambapo ameahidi kuwatuma wataalamu kutoka Shirika la Ndege la Ethiopia kuja nchini kushirikiana na Wataalamu wa Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) ili kuimarisha utendaji kazi na kuikuza ATCL.
“Shirika letu la ndege la Ethiopia ni shirika linaloendeshwa kwa faida Barani Afrika, lina ndege 96 na linatarajia kununua ndege nyingine 42, ndege zake zinatua katika viwanja 92 duniani kote na viwanja 42 ndani ya Ethiopia, hivyo nitawaleta viongozi wa shirika hili ili waje washirikiane na ATCL kuweka mkakati wa namna ya kuiendeleza ATCL na kuiwezesha kufanya kazi kwa faida” amesema Mhe. Hailemariam Dessalegn.
Pia amesema Shirika la Ndege la Ethiopia kwa kushirikiana na ATCL litaufanya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam kuwa kituo chake cha mizigo (Cargo Hub) na hivyo kuwezesha mizigo ya ukanda wa Afrika Mashariki na maeneo jirani kutumia uwanja huo kusafirisha mizigo yake duniani kote.
Mhe. Rais Magufuli na Mhe. Hailemariam Dessalegn ambao kabla ya kuzungumza na wananchi wamefanya mazungumzo rasmi, wamesema wamekubaliana kuwa Tanzania na Ethiopia zibadilishane uzoefu juu ya uzalishaji wa nishati ya umeme kwa kutumia maji ambapo Mhe. Hailemariam Dessalegn ameahidi kuwatuma wataalamu wa nchi yake kuja nchini Tanzania kutoa uzoefu wa namna Ethiopia ilivyoweza kuzalisha kiasi kikubwa cha umeme kwa kutumia maji ukiwemo mradi mkubwa unaoendelea kujengwa uitwao Grand Ethiopian Renaissance Dam (GERD) ambao unatarajiwa kuzalisha megawatts 6,470 za umeme.
“Mhe. Waziri Mkuu tutafurahi sana kushirikiana nanyi katika suala la uzalishaji wa nishati ya umeme kwa sababu hata sisi tunaweza kuzalisha umeme mwingi katika maporomoko ya maji ya Stiegler’s Gorge yaliyopo katika mto Rufiji” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Viongozi hao wamekubaliana kushirikiana kufanya mapinduzi ya kilimo na mifugo, hasa ikizingatiwa kuwa Ethiopia inaongoza kwa idadi kubwa ya ng’ombe barani Afrika na Tanzania inashika nafasi ya pili na kwamba juhudi hizo zitakwenda sambamba na kujenga viwanda vingi vitakavyoongeza thamani ya mazao.
“Naamini kuwa tukishirikiana katika kilimo na mifugo, tutaweza kutumia teknolojia za kisasa katika uzalishaji wa mazao ikiwemo ngozi na nyama na tutatumia mashirika yetu ya ndege kuyafikia masoko mbalimbali duniani na hivyo kukuza uchumi na kuwaongezea wakulima wetu kipato” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Aidha, viongozi hawa wamekubaliana kushirikiana kwa kubalishana uzoefu juu ya namna sekta mbalimbali zitakavyoleta manufaa ya kiuchumi zikiwemo huduma za benki, madini na gesi, elimu na mawasiliano hususani simu.
Mhe. Rais Magufuli amesema ziara ya Waziri Mkuu Mhe. Hailemariam Dessalegn imekuwa ya manufaa makubwa kwa Tanzania na amesisitiza kuwa wakati umefika wa kukuza biashara kati ya nchi hizi ambazo kwa sasa thamani ya biashara kati yake ni Dola za Marekani milioni 2.24 tu.
Kabla ya kuzungumza na wananchi kupitia vyombo vya habari, viongozi hao wameshuhudia utiaji saini wa mikataba 3 ambayo ni Mkataba wa Mkakati wa ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Ethiopia, Mkataba wa kuanzishwa Kamisheni ya Pamoja ya Kuduma kati ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Ethiopia na Hati ya Makubaliano ya Ushirikiano katika sekta ya utalii kati ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Ethiopia.
Waziri Mkuu wa Shirikisho la Kidemokrasia la Jamhuri ya Ethiopia Mhe. Hailemariam Dessalegn amewasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam leo asubuhi na kupokewa na mwenyeji wake Mhe. Rais Magufuli aliyeongozana na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa na akiwa uwanjani hapo amepigiwa mizinga 19, amekagua gwaride lililoandaliwa kwa heshima yake na ameshuhudia burudani ya ngoma za asili.
Jioni hii, Mhe. Hailemariam Dessalegn atahudhuria dhifa ya kitaifa iliyoandaliwa kwa heshima yake na Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
31 Machi, 2017
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, leo tarehe 29 Machi, 2017 ameteua kamati ya wataalamu watakaofanya uchunguzi kwa lengo la kubaini kiwango cha madini kilichomo katika makontena yenye mchanga wa madini yanayoshikiliwa katika maeneo mbalimbali hapa nchini.
Taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi imeeleza kuwa kamati hiyo yenye wajumbe 8, inatakiwa kuanza kazi haraka iwezekanavyo.
Wajumbe wa Kamati hiyo ni;
- Prof. Abdulrahman Hamis Mruma
- Prof. Justianian Rwezaura Ikingula
- Prof. Joseph Bushweshaiga
- Dkt. Yusuf Ngenya
- Dkt. Joseph Yoweza Philip
- Dkt. Ambrose Itika
- Mohamed Zengo Makongoro
- Hery Issa Gombela
Wajumbe wote wa kamati hii wanatakiwa kufika ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi, Ikulu Jijini Dar es Salaam Ijumaa tarehe 31 Machi, 2017 saa 4:00 asubuhi.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
29 Machi, 2017
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 27 Machi, 2017 amepokea ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa mwaka wa fedha unaoishia tarehe 30 Juni, 2016 Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Ripoti hiyo imewasilishwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Prof. Mussa Juma Assad katika hafla iliyohudhuriwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa.
Ripoti hiyo imegusa maeneo mbalimbali yakiwemo ukaguzi wa hali ya hesabu za Serikali, misamaha ya kodi, ukusanyaji wa kodi na maduhuli ya Serikali, uandaaji na utekelezaji wa bajeti, hali ya deni la Taifa, usimamizi wa rasilimali watu, usimamizi wa mali na madeni ya Serikali na usimamizi na uendeshaji wa taasisi za umma zikiwemo taasisi muhimu za kifedha na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO).
Prof. Mussa Juma Assad amesema pamoja na hatua kubwa iliyopigwa na Serikali katika kuzingatia taratibu za fedha bado kuna mapungufu mbalimbali ambayo yameendelea kujitokeza na ameshauri hatua zichukuliwe kukabiliana nayo ikiwemo kudhibiti mianya ya upotevu wa fedha za umma katika madini, kuiepusha TANESCO kununua umeme wa gharama kubwa, matumizi mabaya ya misamaha ya kodi na kuongeza mashine za kutoa risiti (EFD).
Akizungumza baada ya kupokea ripoti hiyo, Mhe. Rais Magufuli ameipongeza Ofisi ya CAG kwa kazi nzuri inayofanya na ameahidi kuwa Serikali itaendelea kushirikiana kwa karibu na ofisi hiyo ili kukabiliana na mianya yote inayosababisha upotevu wa fedha za umma.
Hata hivyo Mhe. Rais Magufuli amemuagiza CAG kufanya ukaguzi wa kina katika sekta ya madini na kubaini mianya yote ambayo inasababisha nchi kukosa mapato makubwa hususani katika misamaha ya kodi, mikataba mbalimbali na ulipaji wa kodi.
“Haiwezekani Watanzania wanakosa dawa hospitali wakati dhahabu zao zinaondoka, Watanzania wanakosa maji wakati dhahabu zao zinaondoka, Watanzania wanakosa umeme wakati dhahabu zao zinaondoka, Watanzania wanakosa barabara wakati dhahabu zao zinaondoka, nataka ukakague kwa kina hii sekta ya madini ili watanzania wajue chao nini na kama kinapatikana sawasawa?” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Mhe. Dkt. Magufuli pia amemuagiza Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Majaliwa kuitisha kikao cha pamoja kitakachomkutanisha CAG na Mawaziri wote, Makatibu Wakuu wa wizara zote, Gavana wa Benki Kuu na Wakuu wa taasisi za umma ili kila mmoja aambiwe hali ya hesabu katika taasisi yake na kuchukua hatua.
“Mhe. Waziri Mkuu ukaongoze hicho kikao na wewe CAG uwaambie kila mmoja katika eneo lake juu ya dosari zake, sitaki kuona dosari zinajirudia zilezile kila wakati” amefafanua Mhe. Rais Magufuli.
Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, CAG anapaswa kuwasilisha ripoti ya hesabu za Serikali kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kabla ya tarehe 31 Machi ya kila mwaka, na baada ya hapo ripoti hiyo huwasilishwa bungeni katika kikao kinachofuata.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
27 Machi, 2017
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, leo tarehe 25 Machi, 2017 amemteua Bw. Charles Edward Kichere kuwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Kabla ya Uteuzi huo Bw. Charles Edward Kichere alikuwa Naibu Kamishna Mkuu wa TRA.
Bw. Charles Edward Kichere anachukua nafasi ya Bw. Alphayo Kidata ambaye ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu, Ikulu.
Kufuatia uteuzi huo, nafasi ya Naibu Kamishna Mkuu wa TRA itajazwa baadaye.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
25 Machi, 2017
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ametengua uteuzi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini Prof. Justin Ntalikwa kuanzia leo tarehe 26 Machi, 2017.
Nafasi ya Katibu Mkuu wa wizara hiyo itajazwa baadaye.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
26 Machi, 2017
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, leo tarehe 24 Machi, 2017 amewaapisha Mawaziri wawili, Katibu Mkuu Ikulu, Mabalozi wanne na Kamishna wa Tume ya Mahakama, Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Walioapishwa ni Mhe. Dkt. Harrison George Mwakyembe aliyeapishwa kuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Prof. Palamagamba Aidan John Mwaluko Kabudi aliyeapishwa kuwa Waziri wa Mambo ya Katiba na Sheria, na Bw. Alphayo Kidata aliyeapishwa kuwa Katibu Mkuu – Ikulu.
Wengine ni Mhe. Sylvester Mabumba aliyeapishwa kuwa Balozi wa Tanzania nchini Comoro, Mhe. Dkt. Abdallah Possi aliyeapishwa kuwa Balozi wa Tanzania nchini Ujerumani, Mhe. Job Masima aliyeapishwa kuwa Balozi wa Tanzania nchini Israel na Mhe. Jaji Stella Esther Mugasha aliyeapishwa kuwa Kamishna wa Tume ya Mahakama.
Akizungumza baada ya kuwaapisha viongozi hao, Mhe. Rais Magufuli amewataka kuchapa kazi kwa juhudi, maarifa na kwa kutanguliza maslai ya Taifa na pia amewasihi kutobabaishwa na kauli ama vitendo vyovyote vya kuwavunja moyo.
Mhe. Rais Magufuli pia amewasihi waandishi wa habari na wamiliki wa vyombo vya habari kufanya kazi zao kwa weledi na kwa kutanguliza maslai ya Taifa badala ya kutoa kipaumbele katika masuala ya migogoro na mambo mengine yasiyo na manufaa kwa wananchi na Taifa kwa ujumla.
“Nchi yetu huko nje ina sifa kubwa sana, juzi tu hapa amekuja Rais wa Benki ya Dunia na amekubali kutupatia Shilingi Trilioni 1.74 na pia Benki ya Dunia ipo katika mchakato wa kutupatia fedha zingine Shilingi Trilioni 2.8 kwa ajili ya miradi mbalimbali ya maendeleo, haya ndio mambo muhimu ya kuandika lakini hebu angalia siku iliyofuata jinsi magazeti yalivyoandika” amehoji Mhe. Rais Magufuli.
Aidha, amewaonya wamiliki wa vyombo vya habari ambavyo vimekuwa vikiandika habari za uchochezi na amemtaka Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe kuhakikisha vyombo vya habari vinafanya kazi kwa kufuata sheria na havitumiwi kuvuruga nchi.
Kabla ya kuwaapisha viongozi hao, Mhe. Rais Magufuli amepokea hati za utambulisho za Mabalozi 6 walioteuliwa kuziwakilisha nchi zao hapa nchini.
Mabalozi hao ni Balozi wa Cyprus hapa nchini mwenye makazi yake Mjini Muscat - Oman Mhe. Andreas Panayiotou, Balozi wa Bangladesh hapa nchini mwenye makazi yake Mjini Nairobi – Kenya Mhe. Meja Jenerali Abdul Kalam Mohammad Humayun Kabir na Balozi wa Nepal hapa nchini mwenye makazi yake Mjini Pretoria – Afrika Kusini Mhe. Amrit Bahaur Rai.
Wengine ni Balozi wa Ecuador hapa nchini mwenye makazi yake Mjini Addis Ababa – Ethiopia, Balozi wa New Zealand hapa nchini mwenye makazi yake Mjini Pretoria – Afrika Kusini na Balozi wa Jamhuri ya Kongo mwenye makazi yake Mjini Kigali – Rwanda Mhe. Michael Gerrard Burrel.
Katika mazungumzo yake na Mabalozi hao Mhe. Rais Magufuli amewapongeza kwa kuteuliwa kuziwakilisha nchi zao hapa nchini na amewahakikishia kuwa Tanzania itaendeleza na kuimarisha uhusiano na ushirikiano na nchi hizo, huku akitilia mkazo ushirikiano katika masuala ya uwekezaji, biashara na kubadilishana uzoefu katika uzalishaji mali hususani kilimo.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
24 Machi, 2017
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, leo tarehe 23 Machi, 2017 amemteua Bw. Alphayo Kidata kuwa Katibu Mkuu, Ikulu.
Bw. Alphayo Kidata anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Bw. Peter Ilomo ambaye amestaafu.
Kabla ya uteuzi huo Bw. Alphayo Kidata alikuwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na nafasi hiyo itajazwa baadaye.
Uteuzi wa Bw. Alphayo Kidata unaanza mara moja na ataapishwa kesho tarehe 24 Machi, 2017 Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
23 Machi, 2017
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 23 Machi, 2017 amefanya ziara ya kushtukiza katika bandari ya Dar es Salaam kwa lengo la kufuatilia utekelezaji wa maelekezo aliyoyatoa kwa nyakati tofauti juu ya kudhibiti udanganyifu wa mizigo inayoingia na kutoka nchini kupitia bandari hiyo ikiwemo usafirishaji wa mchanga wa madini kwenda nje ya nchi.
Katika ziara hiyo Mhe. Rais Magufuli ameshuhudia makontena 20 ya mchanga wenye madini kutoka kwenye migodi iliyopo kanda ya ziwa ambayo yamezuiliwa kusafirishwa nje ya nchi tangu alipotoa agizo la kupiga marufuku usafirishaji wa mchanga nje ya nchi tarehe 02 Machi, 2017.
Pamoja na kushuhudia makontena hayo, Mhe. Rais Magufuli amemuagiza Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini IGP - Ernest Mangu na vyombo vingine vya dola kuhakikisha mchanga wa madini unashikiliwa popote ulipo, mpaka hapo uchunguzi wa kina utakapofanyika kubaini ukweli.
“Nataka niwaambie nchi yetu inachezewa mno, nimekuja kuyaona haya makontena kama yapo, na kweli nimeyaona, sasa utaratibu utakapokamilika nataka Watanzania na dunia nzima ione kilichomo humu ndani kama ni mchanga kweli ama dhahabu” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Akiwa bandarini hapo Mhe. Dkt. Magufuli pia ameshuhudia udanganyifu mwingine unaofanywa na wafanyabiashara wanaoagiza mizigo kutoka nje ya nchi baada ya kuoneshwa makontena ambayo nyaraka zinaonesha yamebeba mitumba ya nguo na viatu wakati ndani yake kila kontena moja limebeba magari matatu ya kifahari.
Maafisa wa bandari ya Dar es Salaam na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wamemueleza Mhe. Rais Magufuli kuwa kufuatia maelekezo aliyoyatoa ya kuhakikisha mizigo yote inakaguliwa kwa mitambo ya mionzi (Scanning Machines) wamefanikiwa kubaini udanganyifu mwingi unaofanywa na wafanyabiashara wanaoingiza nchini na kusafirisha nje ya nchi mizigo mbalimbali yakiwemo makontena 10 ambayo yamepatikana yakiwa na magari ya kifahari ilihali nyaraka zake zikionesha yana mitumba ya nguo na viatu.
Mhe. Rais Magufuli amewapongeza maafisa na wafanyakazi wa bandari ya Dar es Salaam na TRA kwa kazi nzuri wanayofanya kudhibiti upotevu wa fedha za umma bandarini hapo na amewataka kuendelea kutekeleza wajibu wao kwa uzalendo na kujiepusha na rushwa.
“Leo mmenifurahisha sana, ninawatia moyo endeleeni kuwakamata wote wanaofanya udanganyifu huu na muwachukulie hatua kali za kisheria, lakini msimuonee mtu na msipokee rushwa, tunataka watu wajifunze kuwa hapa sio shamba la bibi” amesisitiza Rais Magufuli.
Aidha, ametoa wito kwa vyombo vyote vinavyoshughulikia udhibiti wa mizigo inayoingia na kutoka kupitia bandari ya Dar es Salaam na bandari nyingine hapa nchini, kuendelea kushirikiana ili kukomesha vitendo vyote vya udanganyifu ambavyo vinasababisha nchi kupoteza mapato mengi.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
23 Machi, 2017
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, leo tarehe 23 Machi, 2017 amefanya mabadiliko madogo katika Baraza la Mawaziri.
Katika Mabadiliko hayo, Mhe. Rais Magufuli amemteua Prof. Palamagamba Aidan John Mwaluko Kabudi kuwa Waziri wa Katiba na Sheria.
Aidha, Mhe. Dkt. Magufuli amemteua Dkt. Harrison George Mwakyembe kuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.
Uteuzi huu unaanza mara moja.
Wateule wote wataapishwa kesho Mchana tarehe 24 Machi, 2017 Ikulu, Jijini Dar es Salaam.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
23 Machi, 2017
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, leo tarehe 22 Machi, 2017 amekutana na kufanya mazungumzo na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China (CPC) na Katibu wa Kamati ya CPC ya Manispaa ya Beijing nchini China Mhe. Guo Jinlong.
Katika Mazungumzo hayo Mhe. Guo Jinlong amewasilisha salamu za Rais wa China na Katibu Mkuu wa CPC Mhe. Xi Jinping ambaye amempongeza Mhe. Dkt. Magufuli kwa juhudi zake za kuimarisha uchumi wa Tanzania, kupambana na rushwa na kufanya mageuzi yenye lengo la kukiimarisha Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa manufaa ya Watanzania.
Mhe. Guo Jinlong amesema uhusiano na ushirikiano mzuri kati ya China na Tanzania ulioasisiwa na Mwenyekiti Hayati Mao Tse-tung na Baba wa Taifa Hayati Mwl. Julius Nyerere utaendelezwa na kuimarishwa zaidi na kwa namna ya kipekee ameishukuru Tanzania kwa kuiunga mkono China katika masuala ya kimataifa.
Aidha, Mhe. Guo Jinlong ameahidi kuwasilisha katika Kamati Kuu ya CPC ombi la Tanzania kuikaribisha China kushirikiana katika ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa (Standard Gauge) kwa kipande cha kuanzia Morogoro hadi Dodoma na pia ombi la kulikaribisha Shirika la Ndege la China kuanzisha safari za moja kwa moja kati ya Beijing na Dar es Salaam ili kukuza utalii, uwekezaji na biashara.
“Nimefurahi sana kwa kutupokea vizuri na ninakuhakikishia kuwa tutaendelea kushirikiana na Tanzania katika maeneo mbalimbali ya uhusiano wetu ikiwemo kuendeleza kilimo na viwanda nchini Tanzania” amesema Mhe. Guo Jinlong.
Kwa upande wake Mhe. Rais Magufuli amemshukuru Mhe. Guo Jinlong kwa kuja nchini Tanzania na kumletea ujumbe wa Mhe. Rais Xi Jinping.
Mhe. Dkt. Magufuli amesema Tanzania itaendelea kuuthamini na kuukuza uhusiano na ushirikiano wake na China na amemuomba Mhe. Guo Jinlong kuwashawishi wawekezaji na wafanyabiashara wa China kuja Tanzania kuwekeza katika sekta mbalimbali hususani viwanda, ujenzi wa miundombinu ya usafiri na majengo na kuendeleza kilimo.
“Naomba unipelekee ujumbe kwa Mhe. Rais Xi Jinping kuwa namkaribisha sana Tanzania na namhakikishia kuwa Tanzania ipo tayari wakati wowote kushirikiana na China katika maendeleo na mambo mengi yenye manufaa kwa wananchi wa pande zote mbili” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli ameshuhudia utiaji saini wa mikataba mitatu ya misaada iliyotolewa na Serikali ya China kwa Tanzania ambayo ni msaada wa upanuzi wa Shule ya Polisi Tanzania iliyopo Moshi Mkoani Kilimanjaro, msaada wa Dola za Marekani 300,000 kwa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na msaada Dola 20,000 kwa ajili ya kuunga mkono jitihada za Serikali kupambana na dawa za kulevya.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
22 Machi, 2017
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, leo tarehe 20 Machi, 2017 ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa barabara za juu kwenye makutano ya barabara za Morogoro, Mandela na Sam Nujoma eneo la Ubungo Jijini Dar es Salaam (Ubungo Interchange).
Sherehe za kuweka jiwe la msingi katika mradi huo zimefanyika kando ya makutano ya barabara hizo na kuhudhuriwa na Rais wa Benki ya Dunia Mhe. Dkt. Jim Yong Kim, Mke wa Rais Mama Janeth Magufuli, Mawaziri wa Tanzania, Balozi wa China hapa nchini Mhe. Dkt. Lu Youqing, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu Mhe. Prof. Norman Sigala King na viongozi wengine wa Wizara na Mkoa wa Dar es Salaam wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa huo Bw. Paul Makonda.
Ujenzi wa barabara hizo utagharimu Shilingi Bilioni 188.71 ambapo kati yake Shilingi Bilioni 186.725 ni mkopo wenye masharti nafuu kutoka Benki ya Dunia na Shilingi Bilioni 1.985 zitatolewa na Serikali ya Tanzania, na mradi huo utakaochukua muda wa miezi 30 unatekelezwa kwa lengo la kupunguza msongamano wa magari katika jiji la Dar es Salaam.
Akizungumza katika sherehe hizo, Rais wa Benki ya Dunia Mhe. Dkt. Jim Yong Kim amempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa kazi nzuri anayofanya katika uongozi wake iliyomjengea sifa nzuri duniani kote.
“Nilivutiwa na hotuba za Mwalimu Julius Nyerere hasa aliposema bila uhuru hakuna maendeleo na bila maendeleo utapoteza uhuru wako, kwa maana hiyo Nyerere aliona kuwa maendeleo ndio njia pekee ya kulifanya Taifa kuwa imara na kujitawala na kuwawezesha watu kujua mwelekeo wa maisha yao.
“Nipo hapa kwa sababu viongozi wengi wa Afrika na wengine wengi duniani, wameniambia unatakiwa kwenda Tanzania, kuona kile anachofanya Rais Magufuli, ikiwemo kuzuia rushwa na kujenga uchumi wa nchi ambayo ni huru” amesema Dkt. Jim Yong Kim.
Kwa upande wake Mhe. Rais Magufuli ameishukuru Benki ya Dunia kwa kuunga mkono juhudi za maendeleo za Tanzania na ameahidi kuwa Tanzania itaendelea kushirikiana na benki hiyo kwa kuendelea kukopa na kulipa madeni yake.
Mhe. Dkt. Magufuli amesema ataendelea kutekeleza ahadi yake ya kukabiliana na msongamano wa magari katika Jiji la Dar es Salaam ambapo pamoja na kujengwa kwa barabara za juu katika makutano ya Ubungo, maandalizi yanaendelea kujenga njia ya barabara 6 za kuanzia Dar es Salaam hadi Chalinze Mkoani Pwani, kujenga kilometa 305 za reli ya kati kwa kiwango cha kisasa (Standard Gauge) kuanzia Dar es Salaam hadi Morogoro, kujenga bandari kavu katika eneo la Ruvu Mkoani Pwani na kujenga daraja la Salenda litakalounganisha Agha Khan na Coco Beach kupitia baharini.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli ametoa wito kwa wananchi wa Dar es Salaam na Watanzania kwa ujumla kuunga mkono juhudi hizo nzuri na muhimu kwa maendeleo, na kuachana na ushabiki usio na manufaa unaochochewa na baadhi ya watu kupitia mitandao ya kijamii na baadhi ya vyombo vya habari.
Amewataka wakandarasi watakaojenga barabara za juu katika makutano ya Ubungo kuharakisha ujenzi huo, ikibidi kumaliza kabla ya miezi 30 na pia amewasihi wananchi watakaopata kazi katika mradi huo kuwa waaminifu na waadilifu wakati wote wa ujenzi.
“Tujielekeze katika masuala ya msingi na ya maendeleo, tuache kujielekeza katika udaku, tunapoteza muda mwingi katika masuala ambayo yanatupotezea muda” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Pamoja na kuweka jiwe la msingi Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli na Mhe. Dkt. Jim Yong Kim wameshuhudia utiaji saini wa miradi 3 itakayopatiwa mkopo nafuu kutoka Benki ya Dunia ambayo ni mradi wa ujenzi wa miundombinu ya usafiri katika Jiji la Dar es Salaam, mradi wa kusambaza maji safi, mazingira na ukusanyaji wa maji taka, na mradi wa uendelezaji wa miji ya Arusha, Dodoma, Kigoma, Mbeya, Tanga, Mwanza na Mtwara, yote ikiwa na thamani ya Jumla ya Shilingi Trilioni 1.74.
Mhe. Rais Magufuli amesema pamoja na mkopo wa Shilingi Trilioni 1.74 Tanzania inatarajia kunufaika na mkopo mwingine wa Shilingi Trilioni 2.79 zitakazotumika katika miradi ya endelezaji bandari ya Dar es Salaam, umeme, gesi, kilimo, afya na elimu kwa Tanzania Bara na Zanzibar.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
20 Machi, 2017
Taarifa kwa vyombo vya habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, leo tarehe 19 Machi, 2017 amekutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein, Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Mazungumzo hayo yamehudhuriwa na Waziri wa Nishati na Madini Prof. Sospeter Mwijarubi Muhongo, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mhandisi Kahitwa Bishaija na Meneja Mwandamizi wa Fedha wa TANESCO Bw. Sadock Mugendi.
Wakati huo huo, Waziri wa Nishati na Madini Prof. Sospeter Mwijarubi Muhongo amewatoa hofu wananchi wa Zanzibar kuwa hawatakatiwa umeme baada ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) kuanza kulipa deni inalodaiwa na TANESCO.
Prof. Muhongo amesema tayari SMZ imeanza kulipa kiasi cha Shilingi Bilioni 10 na itaendelea kulipa deni hilo mpaka litakapomalizika.
Aidha, Prof. Muhongo ametoa wito kwa wadaiwa sugu wote wa TANESCO kulipa madeni yao katika kipindi cha siku 5 zilizobaki kwa kuwa wasipolipa watakatiwa umeme.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
19 Machi, 2017
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Tanzania imekubali ombi la kuipatia Kenya madaktari 500 watakaoisaidia nchi hiyo kukabiliana na tatizo la uhaba wa madaktari katika vituo vyake vya tiba hasa baada ya kutokea kwa mgomo wa madaktari nchini humo.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amekubali kutoa madaktari hao leo tarehe 18 Machi, 2017 Ikulu Jijini Dar es Salaam, baada ya kufanya mazungumzo na ujumbe wa viongozi wa Wizara ya Afya ya Kenya uliotumwa na Rais wa nchi hiyo Mhe. Uhuru Kenyatta.
Kiongozi wa ujumbe huo ambaye ni Waziri wa Afya wa Kenya Mhe. Dkt. Cleopa Mailu amemueleza Mhe. Rais Magufuli kuwa baada ya kutokea mgomo wa madaktari pamoja na uamuzi wa nchi hiyo kugatua madaraka katika sekta ya afya, imebainika kuwa nchi hiyo ina upungufu mkubwa wa madaktari ambao hauwezi kumalizwa kwa kutegemea madaktari wanaosomeshwa nchini humo bali kupata madaktari kutoka nje ya nchi.
Mhe. Dkt. Cleopa Mailu aliyeongozana na Gavana wa Kisumu Mhe. Jack Ranguma amesema Kenya ipo tayari kuwalipa stahili zote madaktari 500 watakaopatiwa kutoka Tanzania ikiwa ni pamoja na mishahara na nyumba za kuishi.
Nae Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii nchini Tanzania Mhe. Ummy Mwalimu amesema Wizara yake ipo tayari kutoa madaktari hao haraka iwezekanavyo kwa kuwa Tanzania inao madaktari wengi wazuri ambao wamemaliza masomo yao na hawajapata ajira, na wengine wamemaliza mikataba yao ya kazi na bado wana uwezo wa kufanya kazi.
“Kwa hiyo nitoe wito kwa madaktari wote Tanzania ambao hawapo katika utumishi wa umma, hawapo katika hospitali teule na ambao hawapo katika hospitali za mashirika yasiyo ya kiserikali wanaolipwa na Serikali, waombe nafasi hizi.
Vigezo vikubwa ambavyo tutaviangalia ni kwanza awe amemaliza mafunzo ya vitendo (Internship) na pili awe amesajiliwa na Baraza la Madaktari la Tanganyika, kwa hiyo leo hii tutatoa tangazo na tumefurahi sana kwa sababu tunao madaktari wa kutosha ndani ya nchi na tunaweza kuwapeleka Kenya” amesema Mhe. Ummy Mwalimu.
Kwa upande wake Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Magufuli amesema Tanzania imekubali ombi hilo kwa kuwa Kenya ni ndugu, jirani na rafiki wa kweli wa Tanzania na amemtaka Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Mhe. Ummy Mwalimu kuharakisha mchakato wa kuwapata madaktari hao ili wawahi kwenda Kenya kutekeleza jukumu hilo.
“Matatizo ya Kenya ni matatizo ya Tanzania, tutawapatia madaktari hao 500 ili wakatoe huduma ya matibabu kwa ndugu zetu waliopo Kenya, na kwa kuwa mmenihakikishia kuwa madaktari wangu mtawalipa mishahara inavyotakiwa, mtawapa nyumba za kuishi, na mtahakikisha wanafanya kazi katika mazingira mazuri na salama mimi sina tatizo na naamini mambo yatakwenda vizuri” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
18 Machi, 2017
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo Mkoani Pwani Alhaji Majid Mwanga kuwasaka, kuwakamata na kuwafikisha katika vyombo vya sheria wafugaji wote wanaodaiwa kuhusika katika matukio ya kuwashambulia kwa viboko wananchi wa Kijiji cha Fukayosi kilichopo Wilayani humo.
Mhe. Dkt. Magufuli aliyekuwa akisafiri kwa gari kutoka Dodoma kwenda Jijini Dar es Salaam ametoa agizo hilo leo tarehe 17 Machi, 2017 aliposimama katika kijiji hicho baada ya kuona wananchi wengi wakiwa wamekusanyika kando ya Ofisi ya Kata.
Baada ya kusimamisha msafara wake, Mhe. Rais Magufuli aliwaita wananchi waliokuwa wamekusanyika huku wakiwa wameshika mabango yaliyoandikwa ujumbe wa kutaka wafugaji wa jamii ya Wamang’ati waondolewe na kisha akatoa nafasi kwa baadhi yao kueleza dukuduku lao.
Wananchi hao ambao ni wakulima na mfugaji mmoja aliyejitokeza wakaeleza kuwa Wamang’ati wamekuwa wakiwanyanyasa kwa kuingiza mifugo katika mashamba yao ya mazao na wakithubutu kuwakataza wamekuwa wakichapwa viboko na baadhi kuuawa.
Katika majibu yake, pamoja na kutaka wote wanaodaiwa kuwashambulia wananchi kwa viboko wakamatwe Mhe. Rais Magufuli amemtaka Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo kukomesha mara moja vitendo vya wafugaji kuwapiga wakulima na wakulima kuwapiga wafugaji, na pia kukomesha vitendo vya wafugaji kulisha mifugo yao katika mashamba ya wakulima.
“Kuanzia leo isitokee mfugaji kumpiga mkulima, mkulima kumpiga mfugaji wala mfugaji kulisha mifugo yake kwenye mashamba ya wakulima, na suala hili nitalifuatilia mimi mwenyewe.
“Kwa hiyo Mkuu wa Wilaya na Viongozi mlishughulikie hili kabla mimi sijawashughulikia nyinyi, wale waliopiga watu, nataka wote wakamatwe na wafikishwe kwenye vyombo vya sheria” amesema Mhe. Dkt. Magufuli.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
17 Machi, 2017
Taarifa kwa vyombo vya habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amelifuta agizo lililotolewa jana tarehe 16 Machi, 2017 na Waziri wa Katiba na Sheria Dkt. Harrison Mwakyembe linalotoa sharti la kuwa na cheti cha kuzaliwa kwa watu wote watakaofunga ndoa kuanzia tarehe 01 Mei, 2017.
Mhe. Rais Magufuli amefuta agizo hilo leo wakati akizungumza na Waandishi wa Habari muda mfupi kabla ya kuondoka katika Ikulu ya Chamwino Mkoani Dodoma na kurejea Jijini Dar es Salaam.
Mhe. Dkt. Magufuli amesema Serikali haiwezi kuruhusu sharti hilo kutumika kwa kuwa litawanyima haki ya kuoa na kuolewa Watanzania wengi ambao hawana vyeti vya kuzaliwa, huku utaratibu wa kupata vyeti hivyo ukiwa bado unakabiliwa na changamoto nyingi kwa wanaohitaji.
Amesema mpaka sasa idadi ya Watanzania walio na vyeti vya kuzaliwa ni chini ya asilimia 20 huku wengi wao wakiwa ni wananchi waishio vijijini ambako ni vigumu kupata vyeti hivyo, na wengine wakiwa ni waliozaliwa kabla ya kuanza kutolewa kwa vyeti vya kuzaliwa nchini mwaka 1961.
“Kwa hiyo ndugu zangu Watanzania msiwe na wasiwasi wowote, endeleeni na utaratibu wenu wa kuoa na kuolewa kama kawaida na kama kuna kifungu chochote cha sheria kinachomlazimisha mtu awe na cheti cha kuzaliwa ndipo aoe ama aolewe nitamuelekeza Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Harrison Mwakyembe apeleke Bungeni kikarekebishwe” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Mhe. Rais Magufuli ametoa wito kwa wanasheria kuziangalia vizuri sheria zinazohusiana na kuzaliwa na kifo na kuoa na kuolewa ili zisilete mkanganyiko kwa wananchi.
Hata hivyo Mhe. Rais Magufuli ametoa wito kwa Watanzania kuendelea kupata vyeti vyao vya kuzaliwa kama kawaida na amewataka viongozi wote kuwahamasisha wananchi kuwa na vyeti hivyo.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mkurugenzi wa Mawasilino ya Rais, IKULU
Chamwino
17 Machi, 2017
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 16 Machi, 2017 ametembelea eneo la ujenzi wa Ikulu Chamwino Mkoani Dodoma na kuwahakikishia wananchi kuwa atahamia Dodoma hivi karibuni kama alivyoahidi.
Mhe. Rais Magufuli ambaye ameongozana na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenister Joakim Mhagama na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi amesema pamoja na majengo ya Ikulu Serikali itajenga miundombinu mingine zikiwemo reli na barabara za lami zitakazounganisha maeneo ya vijiji vinavyozunguka Ikulu na mji wa Serikali.
Pia Mhe. Dkt. Magufuli amewahakikishia wananchi kuwa wote watakaoguswa na shughuli za ujenzi wa miundombinu ya Serikali na wanaostahili kulipwa fidia watalipwa, na ametoa wito kwa wananchi hao kutumia fedha za fidia watakazolipwa kujenga makazi bora na kujipanga kufanya shughuli zenye manufaa kwao.
“Hapa sasa watakuja watu wengi, wafanyakazi na wageni maana tayari Mabalozi wa nchi mbalimbali nao watajenga ofisi zao hapa, sasa na nyinyi mjipange kufanya biashara, mtapata soko la kuuza mazao na bidhaa nyingine, mkipata fedha ziwasaidie kwa manufaa na sio kuzichezea” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Kwa upande wake Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa amesema utekelezaji wa Serikali kuhamia Dodoma unakwenda vizuri ambapo mpaka sasa viongozi wakuu wa wizara zote na wafanyakazi 2,069 wameshahamia Dodoma na wengine wanaendelea kuhamia Dodoma.
Mhe. Majaliwa ameongeza kuwa atasimamia utekelezaji wa maagizo ya Mhe. Rais Magufuli aliyeagiza kujengwa kwa reli itakayounganisha eneo la Bwigili na Dodoma mjini ili kurahisisha usafiri wa watu pamoja na kuharakisha ujenzi wa barabara za kuzunguka mji wa Dodoma na barabara za kuunganisha mji wa Serikali na Dodoma Mjini.
Wakiwa katika eneo hilo, Mhe. Rais Magufuli na Waziri Mkuu Mhe. Majaliwa wameshiriki ufyatuaji wa matofari yatakayotumia katika ujenzi wa majengo ya Ikulu.
Mapema kabla ya kutembelea eneo hilo, Mhe. Rais Magufuli amepokea taarifa ya mapendekezo ya ujenzi wa Mji wa Serikali wa Makao Makuu Dodoma kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu Mhandisi Paskasi Muragili na kuagiza ujenzi wa Mji huo uzingatie maslai ya Taifa.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Chamwino
16 Machi, 2017
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ametengua uteuzi na kumsimamisha kazi Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Bunge) Bw. Uledi Abbas Mussa.
Taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi imeeleza kuwa kutenguliwa kwa uteuzi na kusimamishwa kazi kwa Bw. Uledi Abbas Mussa kunaanzia tarehe 15 Machi, 2017.
Hatua hiyo imechukuliwa ili kupisha uchunguzi zaidi dhidi ya Bw. Uledi Abbas Mussa kufuatia kutozingatiwa kwa taratibu zinazotakiwa katika kushughulikia masuala ya uwekezaji.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Chamwino
15 Machi, 2017
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 13 Machi 2017, amekutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein Ikulu ya Chamwino mjini Dodoma.
Dkt. Magufuli amesema katika mazungumzo yao wamezungumza mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kumtakia heri Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein kufuatia leo kuwa siku yake ya kuzaliwa.
Kwa upande wake Rais Dkt. Ali Mohamed Shein amesema anamshukuru Rais Dkt.Magufuli kwa kumtakia heri katika siku yake muhimu ya kuzaliwa na hivyo wamekutana kubadilishana mawazo katika kuhakikisha wanajenga nchi na kusonga mbele.
''Siku ya kuzaliwa ni siku ya furaha lazima ikumbukwe lazima isherehekewe, mimi siku yangu ya kuzaliwa sisherehekei sana lakini huwa nafurahi sana na leo nimefurahi sana'' amesema Dkt. Shein.
Dkt.Shein amesema ametumia siku yake ya kuzaliwa kumtembelea Rais Dkt.Magufuli ili waweze kubadulishana mawazo kwani wana kazi kubwa ya kujenga nchi.
Jaffar Haniu
Naibu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dodoma
13 Machi, 2017
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 13 Machi 2017, amekutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein Ikulu ya Chamwino mjini Dodoma.
Dkt. Magufuli amesema katika mazungumzo yao wamezungumza mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kumtakia heri Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein kufuatia leo kuwa siku yake ya kuzaliwa.
Kwa upande wake Rais Dkt. Ali Mohamed Shein amesema anamshukuru Rais Dkt.Magufuli kwa kumtakia heri katika siku yake muhimu ya kuzaliwa na hivyo wamekutana kubadilishana mawazo katika kuhakikisha wanajenga nchi na kusonga mbele.
''Siku ya kuzaliwa ni siku ya furaha lazima ikumbukwe lazima isherehekewe, mimi siku yangu ya kuzaliwa sisherehekei sana lakini huwa nafurahi sana na leo nimefurahi sana'' amesema Dkt. Shein.
Dkt.Shein amesema ametumia siku yake ya kuzaliwa kumtembelea Rais Dkt.Magufuli ili waweze kubadulishana mawazo kwani wana kazi kubwa ya kujenga nchi.
Jaffar Haniu
Naibu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dodoma
13 Machi, 2017
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, ametuma salamu za rambirambi kwa familia ya mmoja wa Waasisi wa Taifa na Waziri Mstaafu Bw. George Kahama kufuatia kifo cha kiongozi huyo kilichotokea leo tarehe 12 Machi, 2017.
Bw. George Kahama amefariki dunia akiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili Jijini Dar es Salaam alikokuwa akipatiwa matibabu.
Katika Salamu zake Mhe. Rais Magufuli amesema Taifa limempoteza mmoja wa watu waliotoa mchango mkubwa katika kupigania uhuru, maendeleo na ustawi wa jamii ya watanzania akiwa katika nyadhifa mbalimbali za uongozi hususani kuwa miongoni mwa Mawaziri katika Baraza la kwanza la Mawaziri ambapo alishika wadhifa huo kwa awamu tatu za uongozi wa Tanzania.
“Sir George Kahama alikuwa kiongozi shupavu, mzalendo, mwanasiasa mahiri, aliyewapenda Watanzania na aliyejitoa kushirikiana na viongozi wenzake akiwemo Baba wa Taifa Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere kupigania uhuru, kujenga misingi ya Taifa likiwemo Azimio la Arusha, kujenga misingi ya uchumi wa ujamaa na kujitegemea na mengine mengi, kwa hakika hatutamsahau”
“Japo kuwa Sir. George Kahama ametangulia mbele za haki, sisi viongozi tuliopo tutamuenzi kwa kuhakikisha tunaendeleza juhudi za kuipigania Tanzania aliyoshiriki kuijenga, na pia tunamuombea kwa Mwenyezi Mungu aipumzishe roho yake mahali pema peponi, Amina” amesema Mhe. Rais Magufuli katika salamu hizo.
Pamoja na familia ya Marehemu Bw. George Kahama, Mhe. Dkt. Magufuli amewapa pole nyingi wanachama wote wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Wabunge, Ndugu, Jamaa na Marafiki wote walioguswa na msiba huo.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dodoma
12 Machi, 201
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, leo tarehe 07 Machi, 2017 amewasili Mkoani Dodoma ambako pamoja na mambo mengine ataongoza Kikao cha Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa, Mkutano wa Halmashauri Kuu ya Taifa na Mkutano Mkuu Maalum wa Chama Cha Mapinduzi.
Mhe. Dkt. Magufuli ambaye ni Mwenyekiti wa CCM ataongoza kikao na mikutano hiyo kuanzia tarehe 10 - 12 Machi, 2017 Mjini Dodoma.
Mhe. Rais Magufuli akiwa na Mkewe Mama Janeth Magufuli amewasili katika Ikulu ya Chamwino Mkoani Dodoma akitokea Mkoani Morogoro ambako jana tarehe 06 Machi, 2017 alizindua uwanja wa kisasa wa ndegevita wa Ngerengere.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dodoma
07 Machi, 2017
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, leo tarehe 06 Machi, 2017 amezindua uwanja wa kisasa wa ndegevita wa Ngerengere uliopo Mkoani Morogoro, uliofanyiwa ukarabati mkubwa baada ya miundombinu ya uwanja uliojengwa tangu mwaka 1970 kuharibika.
Sherehe ya uzinduzi wa uwanja huo imefanyika uwanjani hapo na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Mke wa Rais Mama Janeth Magufuli, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, Balozi wa China hapa nchini Mhe. Dkt. Lu Youqing, Viongozi wa vyombo vya ulinzi na usalama na Wakuu wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania wastaafu.
Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali Venance Salvatory Mabeyo amesema ukarabati wa uwanja huo ulioanza tarehe 15 Julai, 2013 umegharimu Shilingi Bilioni 137 na Milioni 631 ikiwa ni ufadhili wa Serikali ya China na umehusisha kujenga upya njia ya kuruka na kutua ndege yenye urefu wa mita 3,000 upana wa mita 45 na unene wa sentimeta 45.
Jenerali Mabeyo ameongeza kuwa uwanja huo ni miongoni mwa viwanja bora zaidi duniani kwa sasa na una uwezo wa kutumiwa na ndege za aina zote zilizo chini ya Boeing 777 huku akibainisha kuwa pamoja na ndege za kivita pia unaweza kutumiwa na ndege za kawaida za abiria kwa dharula.
Nae Balozi wa China hapa nchini Mhe. Dkt. Lu Youqing amesema kujengwa kwa uwanja huo kumeimarisha zaidi uhusiano na ushirikiano kati ya Tanzania na China na amempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa kuendeleza uhusiano huo.
Pamoja na kuzindua uwanja huo, Mhe. Rais Magufuli ameshuhudia maonesho ya ndege za kivita zilizorushwa kwa mbinu mbalimbali za kivita, kutoa heshima na kutua katika uwanja huo.
Katika hotuba yake, Mhe. Rais Magufuli amelipongeza Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kwa kazi kubwa linayofanya na pia amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Watu wa China Mhe. Xi Jinping na Serikali yake kwa msaada mkubwa iliyoutoa kujenga uwanja huo.
“Mhe. Balozi Lu Youqing naomba unipelekee shukrani zangu za dhati Mhe. Rais wa China kwa kutoa msaada huu mkubwa wa kujenga uwanja wa ndegevita wa Ngerengere, najua China imetusaidia kujenga Reli ya TAZARA, Kiwanda cha Urafiki na Uwanja wa Mpira, hii yote inathibitisha uhusiano wetu mzuri, urafiki na undugu” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Aidha, Mhe. Dkt. Magufuli ameahidi kujenga barabara ya lami ya kuunganisha Kamandi ya Jeshi la anga ya Ngerengere na barabara kuu ya Dar es Salaam – Morogoro.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Morogoro
06 Machi, 2017
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 05 Machi, 2017 amemaliza ziara yake ya kikazi ya siku 4 katika mikoa ya Pwani, Lindi na Mtwara.
Kabla ya kuondoka Mjini Mtwara na kurejea Jijini Dar es Salaam Mhe. Rais Magufuli amefanya mkutano wa hadhara katika Uwanja wa Mashujaa Mjini Mtwara ambapo amesema Serikali ya Awamu ya Tano imejipanga kuhakikisha inasukuma maendeleo ya Mtwara na Lindi kwa nguvu kubwa kwa manufaa ya wananchi.
Amesema Serikali imedhamiria kutilia mkazo juhudi za uendelezaji wa bandari ya Mtwara, ujenzi wa barabara, uimarishaji wa miundombinu ya nishati ya umeme, ujenzi wa viwanda vikubwa na usimamizi mzuri wa shughuli za kilimo ambavyo vitasaidia kukuza uchumi, kuzalisha ajira na kuboresha maisha ya watu.
Mhe. Rais Magufuli amewapongeza viongozi na wananchi wa Mkoa wa Mtwara kwa mafanikio yaliyopatikana katika soko la korosho lililopita na ameagiza wale wote waliohusika kufuja fedha za wakulima wachukuliwe hatua.
Aidha, Mhe. Dkt. Magufuli amesema Tanzania itaendeleza uhusiano na ushirikiano wake mzuri na nchi jirani ya Msumbiji na ametaka suala la wahamiaji haramu wanaoondolewa nchini humo wakiwemo Watanzania lisikuzwe huku akisisitiza kuwa Serikali haiwezi kuwatetea watu wanaishi katika nchi nyingine bila kufuata sheria.
Kuhusu Mkoa wa Mtwara kufanya vibaya kielimu, Mhe. Rais Magufuli amewataka wananchi wa Mtwara kubadilika kwani juhudi za Serikali kuwapelekea maendeleo hazitakuwa na maana kama wananchi watakuwa hawana elimu.
"Nimeambiwa hapa watu wanapenda sana disco na ngoma, watoto badala ya kusoma wanacheza disco, hapo tunakwenda pabaya" amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Mkutano wa Mhe. Rais Magufuli Mjini Mtwara umedhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi, Waziri wa Nishati na Madini Prof. Sospeter Muhongo, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa, Waziri wa Fedha na Mipango Dr. Philip Mpango, Wabunge na viongozi wa taasisi.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Mtwara
05 Machi, 2017
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ametoa siku 7 kwa Wizara ya Nishati na Madini kumega eneo lenye makaa ya mawe katika eneo la Ngaka lililopo Wilaya ya Mbinga Mkoani Ruvuma na kuipatia kampuni ya Dangote ili iweze kuzalisha yenyewe makaa ya mawe kwa ajili ya kiwanda chake cha saruji kilichopo Mkoani Mtwara.
Mhe. Rais Magufuli ametoa agizo hilo leo tarehe 05 Machi, 2017 wakati wa uzinduzi wa magari 580 ya kusafirishia saruji ya Kampuni ya Dangote uliofanyika kiwandani hapo na kuhudhuriwa na Waziri wa Nishati na Madini Prof. Sospeter Mwijarubi Muhongo, Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Isdor Mpango na Mmiliki wa kiwanda cha Dangote Alhaji Aliko Dangote.
Pamoja kuagiza kampuni ya Dangote ipatiwe eneo la kuchimba makaa ya mawe, Mhe. Dkt. Magufuli ameitaka Wizara ya Nishati na Madini kuhakikisha inafikisha gesi katika kiwanda hicho haraka iwezekanavyo lengo likiwa kuondoa vikwazo vya uhaba wa makaa ya mawe na ukosefu wa gesi ambavyo vimekuwa vikisababisha uzalishaji wa saruji kusimama mara kwa mara.
Mhe. Rais Magufuli pia ameitaka kampuni ya saruji ya Dangote kuwasiliana moja kwa moja na Serikali pale inahitaji huduma yoyote badala ya kuwatumia watu wa kati ambao wamekuwa wakisababisha kuongezeka kwa gharama za uendeshaji na bidhaa na hivyo kuathiri uzalishaji wa saruji wa kiwanda hicho.
Kabla ya kuzindua rasmi magari hayo Mhe. Rais Magufuli amepokea kero za madereva ambao walifanya usaili wa kuomba kazi ya kuendesha magari hayo tangu miezi miwili iliyopita, ambapo wamemueleza kuwa menejimenti ya kiwanda hicho haijawaita kazini mpaka leo licha ya kuwepo kwa malori mapya wanayopaswa kuendesha, huku Menejimenti ikiendelea kutumia malori ya watu binafsi kupitia kampuni za kati ambazo ndizo zimekuwa zikitumika kutoa huduma nyingi kwa kiwanda.
Kufuatia malalamiko hayo Mhe. Dkt. Magufuli amemshauri mmiliki wa kiwanda hicho Alhaji Aliko Dangote kuiangalia vizuri Menejimenti yake na kuitaka iachane na wafanyabiashara wa kati ikiwemo kampuni moja iliyotaka kupewa zabuni ya kupokea gesi kutoka Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) kisha kuzalisha umeme na kuiuzia Dangote.
"Ndugu Alhaji Aliko Dangote, iangalie vizuri Menejimenti yako, inawatumia watu wa kati na ndio hao wanaosababisha matatizo, na mimi nimeshaiagiza wizara hakuna kuuza gesi kwa watu wa kati, tunataka tukuletee gesi wewe mwenyewe na uzalishe umeme wewe mwenyewe" amesisitiza Rais Magufuli.
Kwa upande wake Alhaji Aliko Dangote ameelezea kufurahishwa kwake na uwekezaji wa kiwanda hicho uliogharimu Dola za Marekani Milioni 650 na kwamba kiwanda hicho kitakachozalisha tani Milioni 2 za saruji mwaka huu kinatarajia kufikia uzalishaji wa tani Milioni 3 mwaka ujao, kuzalisha ajira 20,000 huku kikiwa kimesaidia kupunguza bei ya saruji nchini kutoka Shilingi 15,000/- kwa mfuko mmoja kilo 50 hadi kufikia Shilingi 10,000/-.
Alhaji Aliko Dangote ameongeza kuwa tangu kampuni yake ianze kuuza saruji bei ya bidhaa hiyo sokoni imeshuka kutoka Shilingi 15,000/- kwa mfuko mmoja wa kilo 50 hadi kufikia Shilingi 10,000/- na kwamba imeamua kununua magari ya kusafirisha saruji ili iweze kusambaza saruji hiyo nchi nzima kwa gharama nafuu ambayo watanzania wengi wataimudu.
Nae Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango amesema licha ya kuzalisha ajira, tangu kampuni hiyo ianze shughuli zake imeshalipa kodi kiasi cha Shilingi Bilioni 46.139 na kodi inatarajiwa kuongezeka kadiri uzalishaji unavyopanda.
Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli amezindua kituo cha kupooza umeme cha Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kilichopo mjini Mtwara ambacho kinajengwa kwa fedha na wataalamu wa TANESCO kwa gharama ya Shilingi Bilioni 16, mradi ambao utahusisha ujenzi wa njia ya umeme ya kilovoti 132 kutoka Mtwara hadi Lindi na hivyo kumaliza tatizo la kukatika kwa umeme katika Mji wa Lindi.
Mhe. Dkt. Magufuli amempongeza Waziri wa Nishati na Madini Prof. Sospeter Mwijarubi Muhongo, Menejimenti na wafanyakazi wa TANESCO kwa kazi nzuri wanayofanya iliyowezesha usambazaji wa umeme kuongezeka hadi kufikia asilimia 46 ya nchi nzima, lakini ametoa maagizo kwa TANESCO kuwakatia umeme wote wenye madeni bila kujali kama ni taasisi ya umma ama binafsi.
Mapema leo asubuhi Mhe. Rais Magufuli amesali ibada ya Diminika ya kwanza ya Kwaresma katika Kanisa la Watakatifu wote, Jimbo Katoliki la Mtwara ambako amechangia Shilingi Milioni 1 na mifuko 200 ya saruji kwa ajili ya ujenzi wa uzio wa Kanisa na ukarabati wa Kanisa na amewataka wananchi wa Mtwara kushikamana kuiombea nchi na kufanya kazi kwa ajili ya maendeleo ya mkoa na Taifa zima.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Mtwara
05 Machi, 2017
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, ameitaka Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kuachana na utaratibu wa kutoa zabuni za uendeshaji wa bandari kwa kampuni binafsi ambazo huingia mikataba isiyo na manufaa kwa nchi na kusababisha uwepo mianya ya upotevu wa fedha za umma.
Mhe. Rais Magufuli ametoa agizo hilo leo tarehe 04 Machi, 2017 muda mfupi kabla ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa gati namba 2 ya bandari ya Mtwara ambayo ujenzi wake unatarajiwa kuchukua muda wa miezi 21 kuanzia sasa.
"Kwa sababu mmeamua kuichimba hii bandari ili kuongeza kina mpaka mita 15 kwa kutumia fedha zetu, sitegemei TPA na Wizara kuingia tena mkataba na wawekezaji wengine, kwa sababu imekuwa ni kawaida hapa Tanzania, tunatumia fedha zetu halafu wanakuja watu wengine kufanya biashara na fedha zetu kana kwamba nchi hii haina wasomi, na wanaokuja kuendesha kweli wanaiba" amesema Mhe. Rais Magufuli.
Mapema Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa amesema gati namba 2 itakayojengwa katika bandari ya Mtwara itakuwa na urefu wa mita 350 na ujenzi wake utagharimu Shilingi Bilioni 137.5 zote zikiwa zimetolewa na Serikali ya Tanzania.
Nae Mkurugenzi Mkuu wa TPA Mhandisi Deusdedit Kakoko amesema imelazimu kuongeza gati katika bandari ya Mtwara baada ya kuwepo ongezeko la mizigo inayosafirishwa kupitia bandari hiyo ambapo kiwango cha mizigo inayohudumiwa kinatarajiwa kuongezeka kutoka tani 273,886 mwaka 2015/2016 hadi kufikia tani 388,000 mwaka 2016/2017 kiwango ambacho kinakaribia ukomo wa uwezo wa bandari hiyo yenye uwezo wa kuhudumia tani 400,000 kwa mwaka.
Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli amefungua Kituo cha Biashara cha Benki ya NMB Mjini Mtwara na kutoa maagizo kwa Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango kutoa maelekezo ili fedha zote za Serikali zipitie Benki ya NMB ambayo licha ya hisa zake kumilikiwa na Serikali kwa asilimia 32 imekuwa ikitoa gawio kwa Serikali kila mwaka ambapo mwaka 2016 ilitoa Shilingi Bilioni 16.5 na mwaka huu inatarajia kutoa zaidi ya kiwango hicho cha gawio.
"Na nikuombe Waziri, kwa sababu wewe ndio unayesimamia fedha za Serikali, toa maelekezo ili fedha zote zipitie benki ya NMB, labda kama kutakuwa na umuhimu sana wa kupitia benki nyingine" amesema Mhe. Rais Magufuli.
Mhe. Rais Magufuli ambaye ameipongeza benki ya NMB kwa kujikita kutoa huduma za kibenki kwa wananchi wa kawaida na wafanyakazi nchi nzima ametoa wito kwa benki zote nchi kupunguza viwango vya riba ili Watanzania wengi waweze kukopa na kufanya shughuli za uzalishaji mali.
Katika hatua nyingine, Mhe. Rais Magufuli amefungua jengo la Benki Kuu ya Tanzania (BOT) Mjini Mtwara ambalo limejengwa kwa gharama ya Shilingi Bilioni 31 na linatoa huduma za Benki Kuu katika kanda ya kusini inayojumuisha Mikoa ya Mtwara, Lindi na sehemu za Mikoa ya Pwani na Ruvuma.
Pamoja na kumpongeza Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete kwa kuridhia ujenzi wa jengo hilo na kuipongeza BOT kwa kufanikisha ujenzi huo na kusimamia vizuri uchumi wa nchi, Mhe. Rais Magufuli ameitaka benki hiyo kuu kuchukua hatua kali dhidi ya benki ambazo zimekuwa zikikiuka maadili na taratibu za kibenki ikiwemo kushiriki njama za kuiba fedha za Serikali kupitia mikopo na utakatishaji wa fedha.
Aidha, amemtaka Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania Prof. Benno Ndulu aandae utaratibu utakaozibana benki zinazofanya biashara hapa nchini ili zilazimike kuwakopesha wananchi, kupunguza viwango vya riba na kuendeleza shughuli za uzalishaji mali.
Mhe. Rais Magufuli pia amefungua nyumba 40 za makazi za Rahaleo zilizojengwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Mjini Mtwara kwa gharama ya Shilingi Bilioni 10.5 na ameipongeza NHC kwa kazi nzuri ya ujenzi wa nyumba za makazi ya wananchi katika maeneo mbalimbali nchini.
Akiwa katika mradi huu Mhe. Dkt. Magufuli ameagiza kuanzia sasa Mkoa, Wilaya ama Kiongozi yeyote atakayeomba kujengewa makazi na NHC ahakikishe eneo lililoandaliwa kwa ajili ya kujengwa makazi hayo linafikishiwa barabara, umeme na maji na ameitaka NHC kuacha kutumia wakandarasi katika ujenzi wa majengo yake na badala yake waunde vikosi kazi vya ujenzi kwa kutumia wataalamu waliopo ndani ya nchi ili kuzalisha ajira zaidi na kupunguza gharama za ujenzi wa majengo.
Mhe. Dkt. Magufuli ambaye leo ameingia Mkoani Mtwara akitokea Mkoani Lindi amesimamishwa na wananchi wa Kijiji cha Mnolela Kilichopo Lindi Vijijini ambapo baada ya kupokea kero ya Kijiji hicho kushindwa kumalizia jengo la zahanati aliamua kulikagua na kisha akatoa mchango wa Shilingi Milioni 15, zitakazojumlishwa na Shilingi Milioni 10 zitakazotolewa na Mbunge wa Jimbo la Mtama Mhe. Nape Nnauye na Shilingi Milioni 30 zitakazotolewa na Halmashauri ya Wilaya ya Lindi Vijijini, na ameagiza ujenzi huo ukamilike ndani ya miezi 3 kuanzia sasa.
Halikadhalika, Mhe. Rais Magufuli amesimamishwa na kuzungumza na wananchi wa Kijiji cha Madangwa kilichopo Lindi Vijijini ambapo baada ya kupokea kero ya ubadhirifu wa fedha za wakulima wa Korosho ameuagiza uongozi wa Mkoa wa Lindi kuwasaka viongozi wote wa vyama vya ushirika wanaotuhumiwa kula fedha za wakulima na kuwachukulia hatua za kisheria.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Mtwara
04 Machi, 2017
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, amewaahidi wananchi wa Lindi kuwa Serikali itawapatia kivuko kitakachosaidia kurahisisha usafiri wa watu na mizigo kati ya Lindi Mjini na eneo la Kitunda ambalo kwa sasa linafikika kwa njia ya mzunguko wa kilometa 80 kwa kutumia barabara.
Mhe. Rais Magufuli ametoa ahadi hiyo wakati akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa Ilulu Mjini Lindi ikiwa ni siku yake ya pili ya ziara ya kikazi ya siku 4 katika mikoa ya Pwani, Lindi na Mtwara.
Kivuko hicho kitasaidia kupunguza muda wa safari kutoka saa 1.30 zinazotokana na kusafiri kwa gari kutoka Lindi kupitia Mnolela hadi Kitunda hadi kufikia dakika 10 zitakazotumika kuvuka bahari kwa kutumia kivuko.
Mbali na ahadi hiyo ya kivuko Mhe. Dkt. Magufuli amewahakikishia kuwa Serikali yake imedhamiria kuibadili Lindi kwa maendeleo ikiwemo kujenga viwanda, mojawapo ikiwa ni kiwanda kitakachojengwa hivi karibuni na wawekezaji kutoka Ujerumani na ambacho kitazalisha ajira zaidi ya 10,000.
Kuhusu tatizo la kukatika kwa umeme linaloukabili Mji wa Lindi, Mhe. Rais Magufuli amesema tatizo hilo litakwisha baada ya mradi wa kuunganisha njia ya umeme kutoka Mtwara uliopangwa kugharimu Shilingi Bilioni 16 utakapokamilika.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli ameuagiza uongozi wa Mkoa wa Lindi kushughulikia haraka migogoro ya ardhi iliyojitokeza na kuwachukulia hatua watu wote waliofuja fedha za wakulima.
Mkutano huo wa hadhara umehudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhandisi Gerson Lwenge, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Nape Nnauye, baadhi ya Wabunge wa Mkoa wa Lindi na Mbunge Mteule wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Mama Salma Kikwete ambaye amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kumteua kuwa Mbunge na amemuahidi kuchapa kazi.
Mhe. Rais Magufuli kesho ataendelea na ziara yake Mkoani Mtwara.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Lindi
03 Machi, 2017
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, ameagiza kushikiliwa kwa hati za kusafiria za mwakilishi wa kampuni ya ukandarasi ya Overseas Infranstructure Alliance Private Limited ya India Bw. Rajendra Kumar pamoja na wasaidizi wake mpaka hapo kampuni hiyo itakapokamilisha ujenzi wa mradi wa maji wa Ng'apa Mjini Lindi ambao ulipaswa kuwa umekamilika tangu tarehe 17 Machi, 2015.
Mhe. Rais Magufuli ametoa agizo hilo leo tarehe 03 Machi, 2017 alipotembelea mradi huo ambao unatarajiwa kuzalisha zaidi ya lita za ujazo milioni 5 za maji kwa siku kwa ajili ya wakazi wa Mji wa Lindi ambao wanakabiliwa na tatizo kubwa la maji.
Mhe. Dkt. Magufuli ameelezea kusikitishwa na usimamizi mbaya wa mradi huo ambao tayari kiasi cha Shilingi Bilioni 21.8 zimetolewa kati ya Shilingi Bilioni 29 zilizopangwa kutumika hadi kukamilika kwake, na ameonya kuwa endapo mradi huo hautakamilika katika kipindi cha miezi 4 kuanzia sasa atachukua hatua dhidi ya wanaopaswa kuusimamia.
"Ikipita miezi minne nisilaumiwe, hatuwezi kukubali wananchi wa Lindi wanashida ya maji, fedha zimetolewa, mkandarasi anaamua kupeleka fedha India, mradi umecheleweshwa kwa miaka miwili na mkandarasi hayupo kwenye eneo la ujenzi halafu mnaopaswa kumsimamia mnamuangalia tu wakati sheria zipo, kwa nini hamkumfukuza muda wote huu?" amehoji Mhe. Rais Magufuli.
Mapema akitoa maelezo kuhusu mradi huo Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhandisi Gerson Lwenge amesema mradi huo unatekelezwa kwa mkopo kutoka Benki ya Maendeleo ya Ujerumani (KFW) na Jumuiya ya Ulaya (EU) ambapo hadi sasa umefikia asilimia 85 na kwamba mkandarasi amesimamisha kazi kutokana na kuishiwa fedha.
Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) na ameiomba bodi hiyo ishirikiane na Tanzania kutekeleza miradi mikubwa ya uzalishaji wa umeme na ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa "Standard Gauge".
Pamoja na kutoa ombi hilo Mhe. Dkt. Magufuli ameipongeza benki hiyo kwa kutoa mikopo nafuu iliyowezesha kutekelezwa kwa miradi mingi ya maendeleo hapa nchini hususani ujenzi wa barabara lakini ameomba mchakato wa upatikanaji wa mikopo hiyo urahisishwe na kuharakishwa ili miradi mingi zaidi itekelezwe kwa wakati.
"Hapa Tanzania AfDB imefanya mambo makubwa sana, tunaipenda sana benki hii kwa sababu imetuwezesha kujenga barabara nyingi zikiwemo ya Iringa - Dodoma inayounganisha Cape Town Afrika Kusini hadi Misri, barabara ya Namtumbo - Tunduru - Masasi na nyingine nyingi, kwa kweli hawa ni wadau muhimu wa maendeleo" amesema Mhe. Rais Magufuli.
Akizungumza baada ya kikao hicho kiongozi wa Bodi ya Wakurugenzi waliokutana na Mhe. Rais Magufuli katika Ikulu ndogo ya Lindi Bi. Lekhethe Mmakgoshi amempongeza Mhe. Dkt. Magufuli kwa juhudi zake za kuleta mageuzi ya kiuchumi nchini Tanzania na ameahidi kuwaAfDB itaendelea kuwa mshirika muhimu wa maendeleo ya Tanzania ikiwemo kufanyia kazi maombi aliyoyatoa kwa Bodi hiyo.
Nae Dkt. Namajeje Weggoro ambaye ni mmoja wa wakurugenzi hao anayewakilisha nchi saba za Afrika ikiwemo Tanzania amesema Tanzania ni nchi inayoongoza kwa kupata mikopo mingi kutoka AfDB na ameongeza kuwa maombi yaliyotolewa na Mhe. Rais Magufuli yatapewa kipaumbele.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Lindi
03 Machi, 2017
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, ameweka jiwe la msingi la kiwanda cha kutengeneza vigae (Tiles) cha Kampuni ya Goodwill Tanzania Ceramic Limited kilichopo katika Wilaya ya Mkuranga Mkoani Pwani.
Kiwanda hicho kikubwa Afrika Mashariki na Kati ambacho ujenzi wake umegharimu Dola za Marekani Milioni 50 kwa awamu ya kwanza kitakuwa na uwezo wa kuzalisha mita za mraba 80,000 za vigae kwa siku, kitazalisha ajira za moja kwa moja 1,000 na ajira zisizo za moja kwa moja 2,000.
Akizungumza kabla ya kuweka jiwe la msingi la kiwanda hicho Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na uwekezaji Dkt. Adelhelm Meru amesema pamoja na kiwanda hicho, tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani jumla ya viwanda 2,169 vinavyojumuisha viwanda vidogo, vya kati na vikubwa vimesajiliwa na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) na vipo katika hatua mbalimbali za kukamilika.
Nae Balozi wa China hapa nchini Mhe. Dkt. Lu Youqing amempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa kutilia mkazo juhudi za kukuza uchumi zilizowezesha Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zenye uchumi unaokuwa kwa kasi kubwa Barani Afrika na amebainisha kuwa China itaendelea kushirikiana na Tanzania kuendeleza uwekezaji nchini Tanzania ikiwemo kujenga viwanda.
"Mhe. Rais kwa mujibu wa takwimu za TIC mpaka mwisho wa Juni 2016 uwekezaji wa moja kwa moja kutoka China umefikia Dola za Marekani Bilioni 6.6 na umezalisha ajira za moja kwa moja kwa Watanzania 150,000 na zisizo za moja kwa moja 450,000 na kiwanda hiki cha Goodwill Tanzania Ceramic Limited kimejengwa na wawekezaji kutoka China, vipo viwanda vingine vingi vinajengwa, Mbunge wa Mkuranga ameniambia kuwa kuna viwanda zaidi ya 50 vya Wachina vinavyojengwa hapa Mkuranga, nimefurahi sana kuona karibu kila sekta Watanzania wanafurahia ushirikiano wa Tanzania na China" Amesema Balozi Dkt. Lu Youqing.
Akizungumza baada ya kutembelea kiwanda hicho, Mhe. Rais Magufuli ameishukuru Menejimenti ya kiwanda hicho kwa uwekezaji huo na ameelezea kufurahishwa kwake na kutumika kwa teknolojia ya kuyeyusha mchanga wa kutengenezea vigae.
Kufuatia kujionea mwenyewe teknolojia hiyo, Dkt. Magufuli amepiga marufuku usafirishaji wa mchanga wa madini nje ya nchi na ametaka mchanga wote ufanyiwe uyeyushaji hapa hapa nchini.
"Nchi hii tumechezewa vya kutosha, sasa nyinyi hapa mnayeyusha mchanga kwa kuuchemsha hadi nyuzi joto 1,000 wakati wengine wanasafirisha mchanga nje ya nchi wakati uchemshaji wake hauhitaji kufika hata nyuzi joto 1,000, naiagiza Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji na Wizara ya Nishati na Madini kuwa kuanzia sasa ni marufuku kusafirisha mchanga nje ya nchi" amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Baada ya kuweka jiwe la msingi la kiwanda cha kampuni ya Goodwill Tanzania Ceramic Limited Mhe. Rais Magufuli ameendelea na ziara yake kwa kuzungumza na wananchi wa Ikwiriri na kupokea kero zao ambapo amewaagiza Mamlaka ya Maji katika Mji huo kuhakikisha mradi wa maji uliojengwa na kukamilika tangu mwaka 2015 kwa gharama ya Shilingi Bilioni 5, unaanza kutoka maji kabla ya mwisho wa Mwezi huu na pia amepiga marufuku utozaji wa ushuru kwa wafanyabiashara wadogowadogo wa mazao.
Mhe. Rais Magufuli pia amepokea kero za wananchi wa Somanga, Nangurukuru na Mchinga Moja na huko kote amewataka wananchi kufanya kazi kwa bidii ikiwemo kuzalisha mazao ya chakula cha kutosha huku akiweka bayana kuwa Serikali haitatoa chakula cha msaada kwa watakaopatwa na njaa ilihali wanaweza kuzalisha chakula katika maeneo yao.
"Najua mmezoea kusikia maneno mazuri mazuri kuwa hakuna atakayekufa kwa njaa, sasa mimi nasema usipofanya kazi, usipolima mazao na kupata chakula wakati mvua inanyesha Serikali haitatoa chakula cha bure kwa wenye njaa, ni lazima tufanye kazi, sasa hivi mvua zinanyesha limeni mazao ya chakula" amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Aidha, Mhe. Dkt. Magufuli amewaagiza viongozi wa Mkoa wa Lindi kushughulikia migogoro ya wakulima na wafugaji iliyoanza kuibuka mkoani humo, ameahidi kutoa Shilingi Milioni 20 kusaidia ujenzi wa Zahanati ya Somanga, amewaagiza Viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa kujenga kituo cha mabasi cha Nangurukuru na pia amemuagiza Mganga Mkuu wa Mkoa wa Lindi kwa kushirikiana na Mbunge wa Jimbo la Mchinga Mhe. Hamidu Bobali kuhakikisha anapeleka Daktari katika kijiji cha Mchinga Moja ili kutatua kero ya wananchi kukosa huduma ya matibabu.
Mhe. Rais Magufuli ataendelea na ziara yake kesho tarehe 03 Machi, 2017 hapa Mkoani Lindi.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Lindi
02 Machi, 2017