Taarifa kwa vyombo vya Habari ya zamani
Rais Akutana na Wanataaluma wa Vyuo Vikuu na Vyuo Vikuu Vishiriki vya Umma
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ameyapatia ufumbuzi matatizo makubwa na ya muda mrefu ambayo yamekuwa yanawakabili wahadhiri na wanataaluma wa Vyuo Vikuu na Vyuo Vikuu Vishiriki vya Umma nchini.
Katika kikao kilichofanyika Ikulu, Dar Es Salaam jana, Jumatano, Agosti 21, 2013 kwa muda wa saa sita kati ya Rais na Viongozi wa Muungano wa Wanataaluma wa Vyuo Vikuu na Vyuo Vikuu Vishiriki vya Umma nchini wakiongozwa na Mwenyekiti wao Prof. Remmy Assey kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine, na kuhudhuriwa pia na Makamu wa Rais Mheshimiwa Dkt. Mohamed Gharib Bilal na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Y. Sefue, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete aliamua na kuelekeza ifuatavyo:
(1) Serikali, kupitia Wizara ya Fedha, ihakikishe kuwa Bajeti ya Vyuo Vikuu na Vyuo Vikuu Vishiriki vya Umma ambayo imekuwa inapungua mwaka hadi mwaka inarejeshwa kwenye viwango vya zamani mapema iwezekanavyo, na kwamba bajeti hiyo isiwe inapungua mwaka hadi mwakakamailivyo sasa.
(2) Nyongeza ya fedha hizo itumike kuboresha mazingira na miundombinu ya kufundishia katika Vyuo Vikuu na Vyuo Vikuu Vishiriki vya Umma. Shughuli hiyo ianze kwa kufanyika tathmini ya kujua vipaumbele, na kuandaa mpango mahsusi wa utekelezaji.
(3) Madai ya wanataaluma yatokanayo na stahili zao, na ambayo yamehakikiwa yalipwe kwa awamu na kazi ya uhakiki wa madeni mengine iendelee.
(4) Serikali kupitia Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, ishirikiane na Viongozi wa Vyuo hivyo kupitia upya Muundo wa Utumishi (Scheme of Service) kwa ajili ya wanataaluma kwa lengo la kuuboresha kwa kuzingatia mahitaji maalum ya wanataaluma.
(5) Vyuo Vikuu vya Umma virejeshewe uhuru wa kuajiri wanataaluma moja kwa moja bila ya shughuli hiyo kufanywa na Sekretarieti ya Ajira Serikalini.
(6) Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma ikutane na Viongozi wa Muungano wa Wanataaluma haraka iwezekanavyo ili kupata ufumbuzi wa matatizo ya upandishaji vyeo wanataaluma na nyongeza za mishahara za kila mwaka.
(7) Utaratibu wa Mikopo ya Ujenzi wa Nyumba kwa ajili ya Watumishi wa Serikali ulioanzishwa na Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano waTanzania, uhusishe pia Wanataaluma wa Vyuo Vikuu. Aidha, Vyuo Vikuu na Vyuo Vikuu Vishiriki vyenye ardhi ya kujenga nyumba za kuishi wanataaluma vijadiliane na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii yenye wanachama kwenye vyuo hivyo ili kuona uwezekano wa Mifuko hiyo kujenga nyumba za kuishi za wanataaluma kwenye maeneo hayo.
(8) Mifuko ya Hifadhi ya Jamii na Mdhibiti wa Mifuko hiyo washirikiane haraka na Vyuo Vikuu na Vyuo Vikuu Vishiriki vya Umma pamoja na Serikali ili kulipatia ufumbuzi tatizo la uwasilishaji wa michango ya pensheni ya wanataaluma.
Rais na viongozi wa wanataaluma hao wamekubaliana kukutana tena baada ya miezi mitatu kupokea taaarifa ya utekelezaji na kufanya maamuzi kuhusu maeneo mengine yanayoendelea kuchambuliwa kwa kushirikiana kati ya Serikali, Uongozi wa Vyuo na Uongozi wa Muungano wa Wanataaluma.
Viongozi wa Muungano wa Wanataaluma wa Vyuo Vikuu na Vyuo Vikuu Vishiriki vya Umma nchini walimshukuru Rais kwa hatua hizi na maamuzi yake katika kushughulikia matatizo yao ya siku nyingi na kuahidi kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuyapatia ufumbuzi matatizo yaliyobaki.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
22 Agosti, 2013
Dkt. Stergomena Tax amependekezwa kuwa Katibu Mtendaji mpya
Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuia ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) mchana wa leo, Jumamosi, Agosti 17, 2013, wanatarajiwa kumdhibitisha Dkt. Stergomena Tax wa Tanzania kuwa Katibu Mtendaji mpya wa SADC.
Dkt. Tax ambaye kwa sasa ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki amependekezwa na Baraza la Mawaziri la SADC kuwa Katibu Mtendaji mpya kuchukua nafasi ya Dkt. Tomaz Augusto Salamao ambaye amemaliza muda wake wa utumishi wa Jumuia hiyo.
Dkt. Tax amependekezwa na Baraza la Mawaziri la SADC kuwa Katibu Mtendaji mpya kufuatia uchaguzi wa nafasi hiyo uliofanywa na Baraza hilo.
Katika uchaguzi, Dkt. Tax alipata wastani wa alama 79 wakati mpinzani wake, Mheshimiwa Peter G. Sinon, Waziri wa Serikali ya Shelisheli amepata wastani wa alama 72. Mheshimiwa Sinon ni Waziri wa Uwekezaji, Raslimali na Viwanda wa nchi hiyo.
Kwa mujibu wa Mkataba wa Kuanzishwa kwa SADC, Katibu Mtendaji wa Jumuia hiyo hupendekezwa na Baraza la Mawaziri na huthibitishwa na Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuia hiyo.
Dkt. Salamao amekuwa Katibu Mkuu wa SADC kwa miaka minane iliyopita baada ya kuwa ametumikia vipindi viwili vya miaka minne kila kipindi na kwa mujibu wa Mkataba wa SADC hawezi kuendelea kushika nafasi hiyo.
Pamoja na Dkt. Salamao, Naibu Katibu Mtendaji wa Jumuia hiyo kwa miaka minne iliyopita, Injinia Joao Samuel Caholo pia amemaliza muda wake. Hata hivyo, kwa sababu za kiufundi, nafasi yake haitaweza kujazwa kwenye mkutano wa sasa wa Jumuia hiyo.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
17 Agosti, 2013
Rais Banda amsifia Rais Kikwete kama Mwanademokrasia
Rais wa Jamhuri ya Malawi, Mheshimiwa Joyce Banda amemwelezea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete kama mwanademokrasia na kiongozi hodari anayepigania amani na utawala bora.
Aidha, Rais Banda amewaelezea wanawake maarufu wa Tanzania, Mama Gertude Mongella na Dkt. Asha Rose Migiro kama baadhi ya matunda ya juhudi za Jumuia ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kuleta usawa wa kijinsia katika eneo la Kusini mwa Afrika.
Rais Banda ametoa sifa hizo kwa Rais Kikwete na Watanzania hao wawili leo, Jumamosi, Agosti 17, 2013 wakati alipozungumza kwenye hotuba ya kupokea uongozi wa SADC kwenye Ufunguzi wa Mkutano wa Mwaka wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa SADC kwenye Kituo cha Mikutano cha Bingu wa Mutharika mjini Lilongwe, mji mkuu wa Malawi. Mkutano huo wa 33 wa wakuu wa nchi SADC ni wa siku mbili.
Akizungumza baada ya kuwa amepokea Uenyekiti wa SADC kutoka kwa Rais Armando Emilio Guebuza wa Mozambique, Rais Banda amesema kuwa uongozi wa Rais Kikwete wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC umethibitisha na kuonyesha dhahiri kuwa kiongozi huyo wa Tanzania ni mwanademokrasia anayepigania amani na utawala bora wakati wote.
“Wakati wa uongozi wake wa SADC-Troika, Rais Kikwete amejihusisha kwa karibu sana na ujenzi na utetezi wa demokrasia, utafutaji amani na jitihada za kuongeza kiwango cha utawala bora katika eneo letu la Afrika,” Mama Banda amewaambia mamia ya wasikilizaji kwenye ukumbi huo wa Bingu wa Mutharika.
Kuhusu Mama Mongella na Dkt. Asha Rose Migiro, Rais Banda amesema kuwa Watanzania hao wawili ni sehemu ya wanawake kadhaa katika eneo la SADC ambao wamefanikiwa kupata nafasi kubwa za uongozi kipindi ambako SADC imeelekeza nguvu zake katika kuleta usawa wa kijinsia.
Wakati wa uongozi wake wa SADC-Troika, Rais Kikwete amejihusisha sana na kutafuta suluhu na utatuzi wa migogoro ya kisiasa katika nchi za Zimbabwe, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Madagascar.
Rais Kikwete amemaliza muda wake wa uongozi wa Troika leo na nafasi yake inachukuliwa na Rais Hifikepunye Phohamba wa Namibia.
Mbali na Marais Kikwete, Banda na Guebuza, viongozi wengine ambao wamehudhuria mkutano na shughuli za leo ni pamoja na Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini, Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe, Rais Joseph Kabila Kabange wa DRC, Rais Khama Ian Khama wa Botswana, Dkt. Tom Thabane ambaye ni Waziri Mkuu wa Lesotho, Waziri Mkuu wa Mauritius na Makamu wa Rais wa Zambia, Mheshimiwa guy Scott.
Jumla ya nchi 14 zinawakilishwa katika Mkutano wa mwaka huu wa wakuu wa nchi wanachama wa SADC kati ya nchi 15 wanachama wa Jumuia hiyo. Madagascar haishiriki Mkutano huo kwa sababu ya kusimamishwa uanachama kwa sababu ya mgogoro wa kisiasa nchini humo.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
17 Agosti, 2013
Japan yatangaza sera mpya kwa Tanzania
Japan yatangaza sera mpya kwa Tanzania
- Sasa Tanzania kuwa nchi lengwa ya Japan
- Japan itasaidia Tanzania kuwa kitovu cha uwekezaji katika Afrika
- Kushiriki maboresho Reli ya Kati
- Kusaidia kupanua na kuboresha Bandari ya Dar Es Salaam
- Viwanda vya Japan kujengwa nchini kikiwemo cha kutengeneza pikipiki za Honda
- Ni matokeo ya Ziara ya Rais Kikwete Japan
JAPAN imeamua kuanzisha ushirikiano mkubwa zaidi na Tanzania ambako nchi hiyo itaifanya Tanzania kuwa nchi lengwa ya Japan na kuiwezesha kuwa kitovu cha biashara na uwekezaji katika Afrika kwa nia ya kuiwezesha kuwa na uchumi ulioimarika na wenye kuzalisha ajira nyingi kwa wananchi.
Uamuzi huo wa Japan ni matunda ya mazungumzo kati ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete na Waziri Mkuu wa Japan, Mheshimiwa Shinzo Abe yaliyofanyika Tokyo, Japan wakati Rais Kikwete alipotembelea nchi hiyo Juni, mwaka huu, 2013.
Uamuzi na msimamo mpya wa Japan umetangazwa rasmi leo, Jumamosi, Agosti 10, 2013 na Waziri wa Uchumi, Biashara na Viwanda wa nchi hiyo, Mheshimiwa Toshimistu Motegi alipokutana na kufanya mazungumzo na Rais Kikwete, Ikulu, Dar Es Salaam.
Kwa upande wa Tanzania, mazungumzo hayo yamehudhuriwa pia na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anashughulika na Uwekezaji na Uwezeshaji Mheshimiwa Mary Nagu, Waziri wa Viwanda na Biashara Mheshimiwa Dkt. Abdallah Kigoda na Waziri wa Uchukuzi Mheshimiwa Dkt. Harrison Mwakyembe.
Waziri Motegi amemwambia Rais Kikwete kuwa ametumwa na Waziri Mkuu Abe kufuatilia mazungumzo kati yao na kutangaza rasmi kuwa Japan imeiteua Tanzania kuwa nchi lengwa na kitovu cha uwekezaji wa Japan katika Afrika Mashariki na katika Afrika kwa jumla.
Waziri Motegi pia amemwambia Rais Kikwete kuwa pia amekuja Tanzania kutoa taarifa kuwa Japan iko tayari kushiriki katika kuboresha na kuifanya ya kisasa zaidi Reli ya Kati kwa kujenga njia ya kimataifa badala ya njia nyembamba ya sasa. Amesema kuwa Japan itatuma wataalam wake kuangalia jinsi gani ya kuanza kazi hiyo ya uboreshaji wa Reli hiyo.
Aidha, Mheshimiwa Motegi ametangaza kuwa Japan itashiriki katika upanuzi na uboreshaji wa Bandari ya Dar Es Salaam kwa kuifanya ya kisasa zaidi.
Waziri Motegi amesema kuwa katika azma ya Japan ya kuifanya Tanzania nchi ya mfano katika Afrika katika uwekezaji na uchumi ulioimarisha, amekuja na kundi la wafanyabiashara wa Japan ambao wanaendelea kufanya mazungumzo na wafanyabiashara wa Tanzania kuona jinsi gani wanavyoweza kusaidiana katika kuwekeza katika uchumi wa Tanzania.
Waziri pia amesema kuwa moja ya malengo ya uamuzi huo wa Japan ni kuhakikisha kuwa bidhaa ambazo kwa sasa zinanunuliwa moja kwa moja kutoka Japan zitazalishwa hapa nchini katika viwanda ambavyo vitajengwa na makampuni ya Japan.
Kwa kuanzia amesema kuwa makampuni mawili ya Honda na Panasonic yamekubali kujenga viwanda nchini kimoja kwa ajili ya kutengeneza pikipiki za Honda hapa hapa nchini na kingine kwa ajili ya kutengeneza vifaa vya umeme.
“Huu ni mwanzo tu Mheshimiwa Rais kwa sababu kama nilivyosema kuwa tunataka Tanzania kuwa nchi mfano ya uwekezaji wa Japan katika eneo hili la dunia na namna hiyo kwa pamoja tutakuwa tumeshirikiana katika kuongeza ajira kwa wananchi wa Tanzania,”Mheshimiwa Motegi amemwambia Rais Kikwete.
Waziri huyo pia amesema kuwa baadhi ya makampuni ya Japan yana mipango ya kuwekeza katika kilimo, na hasa kilimo cha pamba, na kuanzisha viwanda vya nguo hapa hapa nchini.
Wakati wa mazungumzo yao mjini Tokyo, Rais Kikwete alimtaka Waziri Mkuu Abe kuwekeza zaidi katika Afrika akisisitiza kuwa Japan ni moja ya mataifa makubwa duniani ambayo yamefanikiwa kupata soko kubwa katika Afrika na hasa soko la magari.
Uamuzi huo wa Japan na ziara ya Mheshimiwa Motegi inakuja wiki na miezi michache baada ya Tanzania kuwa imepokea viongozi wa mataifa mengi yakiwemo mataifa makubwa ya Marekani na China na inathibitisha ni kiasi gani siasa na sera za Tanzania zinavyokubalika duniani.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
10 Agosti, 2013
Rais Kikwete akutana na vijana wachoraji walioacha kutumia dawa kulevya
Rais Jakaya Mrisho Kikwete ameiagiza Wizara ya Afya kupitia kitengo cha magonjwa ya akili pamoja na Tume ya Kuratibu Udhibiti wa Dawa za Kulevya nchini kushirikiana na Kituo cha Ushauri Nasaha cha Pili Misana Foundation, ambacho kinawasaidia waathirika wa madawa ya kulevya ili kiweze kuwahudumia watu wengi zaidi hapa nchini.
Rais Kikwete amesema hayo leo Ikulu alipokutana na vijana walioachana na matumizi ya dawa za kulevya ambao wamepata ushauri nasaha na usaidizi kutoka katika kituo cha Pili Misana kilichopo Kigamboni jijini Dar es Salaam.“Jamii lazima ishiriki katika utatuzi wa jambo hili, ni tatizo kubwa na linamgusa kila mtu na inabidi wote tushiriki katika kulipiga vita” Mhe. Rais amesema na kumpongeza Bi. Pili Misana na Zacharia Hans Pope ambaye ndiye mfadhili wa kituo hicho ambacho tayari vijana wapatao 203 wamepatiwa huduma ya ushauri nasaha na kuweza kuachana na madawa ya kulevya na kurudia katika shughuli zao za kimaendeleo.
Rais Kikwete amesema tatizo la madawa ya kulevya ni la muda mrefu lakini hapo awali lilikuwa halisikiki sana kwa sababu jitihada za kuzuia madawa hayo zilikua hazitangazwi wala kufuatiliwa sana.“Sasa hivi juhudi mbalimbali za kupambana na madawa ya kulevya zinatangazwa na hivyo kusikika sana na pia taarifa nyingi zinazohusiana na madawa ya kulevya zinawekwa wazi kwa jamii” Mhe. Rais amesema na kueleza kuwa taarifa nyingi zinawekwa wazi na kutangazwa ili kushirikisha jamii katika kupambana na tatizo hili.
Kiasi cha vijana 35 leo wamefika Ikulu ambapo wametoka katika nyanja mbalimbali za kitaaluma, elimu na kijamii na pia umri tofauti kutoka miaka 14 hadi miaka 53. Kituo hicho kinahudumia watu wenye jinsia tofauti wake kwa waume kutoka sehemu mbalimbali nchini.
Rais Kikwete amesema Serikali inafanya jitihada kubwa sana za kuwasaidia vijana mbalimbali na bado itaendelea kutoa msaada huo, huku juhudi mbalimbali za kupambana na madawa hayo zikiendelea.
Naye mfadhili wa kituo hicho Bw. Zacharia Hans Pope ameitaka jamii kushiriki na kuwa karibu zaidi na vijana ili kuweza kusaidia katika mapambano ya madawa ya kulevya na athari zake nchini.