Taarifa kwa vyombo vya Habari ya zamani
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ameeleza mshituko na masikitiko yake kufuatia kifo cha Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar Es salaam (UDSM), Balozi Fulgence Kazaura kilichotokea nchini India usiku wa jana, Jumamosi, Februari 22, 2014.
Katika salamu zake za rambirambi kwa Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Mheshimiwa Dkt. Shukuru Kawambwa, Rais Kikwete amesema: “Nimepokea kwa mshituko, masikitiko na huzuni taarifa ya kifo cha Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Balozi Flugence Kazaura, ambacho nimejulishwa kuwa kimetokea katika Kituo cha Matibabu ya Kansa katika mji wa Chennai, nchini India.”
“Kwa hakika, kifo cha Mzee Kazaura siyo kwamba kimekipokonya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kiongozi hodari na mwenye visheni kubwa, lakini kifo hicho kimeondolea Tanzania mmoja wa watumishi hodari wa umma. Mzee Kazaura pia alikuwa mtumishi mwaminifu na mwadilifu kwa nchi yake na sote tunaendelea kwa kumkumbuka kwa sifa hizo na mchango wake mkubwa katika utumishi wa umma,” amesema Rais Kikwete na kuongeza:
“Alithibitisha sifa hizo katika nafasi zote alizozishikilia katika maisha yake tokea alipokuwa Katibu Mkuu katika wizara mbali, hadi alipokuwa Balozi wa Tanzania Makao Makuu ya Umoja wa Ulaya (EU) na nchini Ubelgiji, hadi alipoteuliwa Mshauri Maalum wa Uchumi wa Rais, hadi alipokuwa Naibu Katibu Mkuu wa Jumuia ya Afrika Mashairiki (EAC) katika uongozi mbali mbali za Bodi za mashirika ya umma na binafsi na hata kwenye nafasi yake Ukuu wa Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam kwa miaka tisa. Tutaendelea kumkumbuka.”
Ameongeza Rais Kikwete: “Nakutumia wewe Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dkt. Shukuru Kawambwa salamu zangu za rambirambi kufuatia msiba huu mkubwa. Aidha, kupitia kwako naitumia jumuia nzima ya Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam pole nyingi kwa kuondokewa na kiongozi wao.”
“Nakuomba pia unifikisshie salamu zangu za pole nyingi kwa familia ya Mzee Kazaura. Wajulishe kuwa naungana nao katika kuomboleza kifo cha Mzee wetu huyu na kwamba msiba wao ni msiba wangu pia. Pia naomba wajue kuwa naungana nao katika kumwomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, aiweke mahali pema peponi roho ya Marehemu Fulgence Kazaura. Amina.”
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
23 Februari, 2014
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete usiku wa jana, Jumamosi, Februari 22, 2014, aliongoza harambee ya kupatikana kwa zaidi ya sh milioni 600 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya kisasa vya matibabu kwa ajili ya Wodi ya Watoto katika Hospitali ya Taifa, Muhimbili, Dar Es Salaam.
Katika halfa hiyo iliyofanyika kwenye Hoteli ya Golden Tulip, Dar Es Salaam, Rais Kikwete pia ameahidi kuendeleza kuongoza jitihada za kupatikana kwa kiasi cha sh milioni 328 ambazo zinahitaji kukamilisha hesabu ya sh. 929, 915,000 ambazo ndizo zilikuwa lengo la halfa ya jana.
Halfa hiyo pia iliwakutanisha viongozi wakuu wa awamu tatu za uongozi wa juu wa Tanzania ambako Rais wa Pili wa Tanzania, Mzee Ali Hassan Mwinyi na Rais wa Tatu za Tanzania, Mzee Benjamin William Mkapa walikuwa wenyeji wa halfa hiyo kwa nyadhifa zao kama walezi wa Chama cha Madaktari wa Watoto Tanzania (PAT).
Uchangiaji katika halfa hiyo ulikuwa wa aina tatu – kuna fedha taslimu milioni 55.4 zilizochangwa moja kwa moja, kuna ahadi za uchangiaji na kuna wachangiaji walioamua kuwa watatoa fedha za kununua vifaa mbali mbali vinavyohitajika katika Wodi hiyo ambayo gharama yake inakadiriwa kufikia dola za Marekani 570,500.
Katika halfa hiyo, Ikulu ya Rais Kikwete imetoa mchango wa kununua mashine iitwayo Infant Radiant Warmer yenye thamani ya dola za Marekani 15,300 wakati Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) inayoongozwa na Mama Salma Kikwete imechangia ununuzi wa mashine iitwayo Compressor Nebulizer ambayo gharama yake ni dola za Marekani 12,000.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
23 Februari, 2014
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Ubalozi wa Tanzania katika Rwanda usiku wa jana, Jumatano, Januari 29, 2014 ulitoa taarifa kwa vyombo vya habari ikikanusha habari za uongo na uzushi ambazo ziliandikwa mwishoni mwa wiki na gazeti la Serikali ya Rwanda la News of Rwanda.
Ifuatayo ni taarifa kamili iliyotolewa na Kaimu Balozi wa Tanzania nchini Rwanda, Mheshimiwa Francis Mwaipaja:
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
30 Januari, 2014
STATEMENT ON CLAIMS BY THE NEWS OF RWANDA
The Embassy of Tanzania in Rwanda is deeply saddened by malicious and untrue reports, published over the weekend by the Rwanda Government Owned Newspaper, The News of Rwanda, in which it accuses the President of the United Republic of Tanzania, HE Jakaya Mrisho Kikwete, of supporting and holding meetings with members of rebel groups opposed to the Government in Kigali.
Indeed, these reports are nothing but a bunch of dangerous lies fabricated by editors of this publication with obvious malicious intent to attack the person of the President of a friendly neighbouring country and create an impression that Tanzania is working with enemies and groups opposed to the Government of Rwanda.
The News of Rwanda, which has gained uneviable notoriety of reporting and publishing malicious, dangerous and perpetual propaganda, quoting unnamed sources claims, among other things, that two founding members of the Rwanda National Congress (RNC) including Dr. Theogene Rudasingwa met secretly in Dar es Salaam with top commanders of the Democratic Forces for Liberation of Rwanda (FDLR).
Given the enormity and dangerous nature of these reports, the Embassy of Tanzania in Rwanda would like to make the following clarification:
- That the so called founding members of Rwanda National Congress, Dr. Rudasingwa and adviser Condo Gervais together with top commanders of FDLR, namely Lt. Col Wilson Irategeka and Col Hamadi were not in Tanzania last week. Indeed, our records do not show that they have visited Tanzania in the recent years.
- That, there was no meeting of any kind at any official residences of President Kikwete, either in Dar es Salaam or in Dodoma or anywhere. Indeed, President Kikwete has never met any of those people mentioned anywhere – in Tanzania or outside. Moreover, on the day that News of Rwanda claims that the meeting took place, Thursday 23rd, this month, the President was not even in the country – he was in Davos attending the meeting of the World Economic Forum (WEF).
- That, the former Prime Minister of Rwanda Faustin Twagiramungu was also not in Tanzania on any or the same mission and did not attend the meeting with representatives of RNC and FDLR as no meeting of such nature took place in Dar es Salaam or anywhere in Tanzania as alleged by this paper. The Immigration Department in Tanzania does not have a record of such people entering or exiting the country.
- That, The Tanzania Immigration Department has never issued any travel document to any Rwandan citizen including those claimed in the News of Rwanda that they travelled to Mozambique using Tanzanian passports on or around December 20th 2013. It is not the business of Tanzania to issue travel documents to citizens of other countries.
- That it is also untrue that the so-called, “insider establishment” in Tanzania is providing the base for organization and facilitation for travel for FDLR fighters. It is open secret that there is no presence of even a single FDLR fighter in Tanzania. The News of Rwanda should know better where these fighters are based and operate from.
As mentioned earlier, this report and other similar reports published in recent weeks by the News of Rwanda are not only untrue, baseless and mere fabrication but also dangerous and threatening to the excellent and sound diplomatic and social relations between our two neighbouring countries, both of which are members of the East African Community (EAC).
President Kikwete is deeply hurt by these lies and his humble advice to the editors of this publication is to stop fabricating untrue claims which potentially could create and fuel animosity and confusion among the people of our two neighbouring and friendly countries. At a time when President Kikwete and President Paul Kagame of Rwanda had agreed in Kampala to foster friendly relations, such newspaper claims can only sour the atmosphere and President Kikwete would like to know what the editors of the publication are up to?
The Embassy of Tanzania in Rwanda does not take lightly these allegations by the News of Rwanda given the position that this publication occupies in Rwanda.
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Nigeria Mheshimiwa Goodluck Jonathan amemwalika Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete kuhudhuria Mkutano wa Taasisi ya Uchumi Duniani Afrika (WEF-Africa) unaofanyika katika mji mkuu wa Nigeria wa Abuja mwezi Mei mwaka huu.
Rais Jonathan ametoa mwaliko huo kwa Rais Kikwete wakati viongozi hao wawili walipokutana na kufanya mazungumzo leo, Alhamisi, Januari 23, 2014, kwenye Hoteli ya Intercontinental, Davos, Uswisi, ambako viongozi hao wanahudhuria wa Mkutano wa Mwaka huu wa Taasisi ya Uchumi Duniani –WEF.
Rais Kikwete amekubali mwaliko huo wa kuhudhuria Mkutano huo uliopangwa kufanyika Mei 7-9 mwaka huu mjini Abuja, Nigeria.
Mkutano huo kati ya viongozi hao wawili umehudhuriwa na Mawaziri wa Nigeria wa Mambo ya Nje na Fedha na Uchumi.
Nigeria inakuwa nchi ya nne katika Afrika kuandaa mkutano huo. Kwa miaka mingi, mkutano huo wa WEF-Africa ulikuwa unafanyika Cape Town, Afrika Kusini mpaka Tanzania ilipofanikiwa kuwa nchi ya kwanza ya Afrika nje ya Afrika Kusini kuandaa Mkutano huo mwaka 2010.
Tokea wakati huo, Ethiopia imeandaa mkutano huo na sasa Nigeria.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
23 January, 2014
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Marekani Mheshimiwa Barack Obama amemwalika Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete kuhudhuria Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika ambao anauandaa katika mji mkuu wa Marekani, Washington baadaye mwaka huu.
Mkuu wa Shirika la Misaada ya Maendeleo ya Kimataifa la Marekani (USAID), Bwana Rajiv Shah amewasilisha mwaliko huo wa Rais Obama kwa Rais Kikwete wakati wa mkutano wao uliofanyika leo, Alhamisi, Januari 23, 2014, katika Ukumbi Mkuu wa Mikutano ya Taasisi ya Uchumi Duniani (WEF) Davos, Uswisi.
Bwana Shah amemwambia Rais Kikwete kuwa Rais Obama amemwalika Rais Kikwete kuwa miongoni mwa viongozi wa Afrika ambao watahudhuria Mkutano wa wakuu wa nchi za Afrika na Rais Obama uliopangwa kufanyika Agosti 5-6 mwaka huu mjini Washington.
Bwana Shah amemwomba Rais Kikwete kusaidia kutoa mchango wa mawazo kuhusu jinsi gani ya kufanikisha mkutano huo ambao unazungumzia jinsi Marekani inavyoweza kuongeza kasi ya kusambaza umeme katika Afrika chini ya Mpango wa Marekani wa Power Africa.
Aidha, Bwana Shah amemwomba Rais Kikwete kusaidia mawazo yake ya jinsi ya kusaidia ajenda ya pili ya kikao hicho ambayo ni jinsi ya kuongeza mafanikio ya Mpango wa Kuboresha Kilimo katika Afrika wa Grow Africa ambao unaungwa mkono kwa kiasi kikubwa na Marekani.
Hii ni mara ya tatu kwa Rais Obama kumwalika Rais Kikwete kushiriki katika shughuli za kiongozi huyo wa Marekani na za Serikali yake. Miezi mitatu tu baada ya kushika madaraka mwaka 2008, Rais Obama alimwalika Rais Kikwete kuwa kiongozi wa kwanza wa Afrika kutembelea Ikulu ya Rais Obama na kufanya mazungumzo naye.
Ilikuwa kwenye mkutano wao ambako Rais Obama alimwuliza Rais Kikwete nini utawala wake Rais Obama ungeweza kulifanyia Bara la Afrika na Rais Kikwete akamwambia Rais Obama kuwa njia rahisi zaidi ya kusaidia Bara la Afrika ni kusaidia kuendeleza kilimo kwenye bara hilo ambako mamilioni kwa mamilioni ya watu wanategemea kilimo kwa maisha yao. Rais Obama aliukubali ushauri huo ambao anautekeleza kwa njia nyingi kwa sasa.
Rais Obama pia alimwalika Rais Kikwete kuwa miongoni mwa viongozi watatu wa Afrika kuhudhuria Mkutano wa Wakuu wa Nchi Tajiri na Zenye Viwanda Vingi Zaidi wa G-8 uliofanyika Camp David, Maryland, eneo la mapumziko ya mwishoni mwa wiki la viongozi wa Marekani.
Rais Kikwete amekubali mwaliko huo wa sasa akisema kuwa atawasilisha mapendekezo yake ya jinsi ya kufanikisha mkutano huo muda siyo mrefu kuanzia sasa.
Bwana Shah amemwambia Rais Kikwete kuwa mawazo yake yatasaidia kuongeza kasi ya jitihada za Marekani na nchi za Afrika katika kusambaza umeme na kuboresha kilimo kwenye Bara hilo.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
23 January, 2014
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Kifungu 20 (2) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sura 83, Toleo la 2013 inamtaka Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuchapisha kwenye Gazeti la Serikali Rasimu ya Katiba ndani ya siku thelathini (30) baada ya kukabidhiwa rasimu hiyo na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Taarifa iliyotolewa leo na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue inaeleza kwamba, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, alikabidhiwa Rasimu ya Katiba tarehe 30 Desemba, 2013, na ataichapisha kwenye Gazeti la Serikali litakalotolewa Ijumaa, tarehe 24 Januari 2014.
Aidha, kifungu 22 (1) (c) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sura 83, Toleo la 2013, kinampa madaraka Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushauriana na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, kuteua wajumbe 201 wa Bunge Maalumu la Katiba kutoka miongoni mwa majina yanayopendekezwa kwao na makundi yaliyotajwa ndani ya Sheria hiyo.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, anakusudia kukamilisha uteuzi wa Wajumbe hao baada ya kushauriana na Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, mwanzoni mwa wiki ijayo na majina hayo kuchapishwa kwenye Gazeti la Serikali kama kifungu 22 (3) cha Sheria iliyotajwa inavyomtaka kufanya.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
22 Januari, 2014
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia Salamu za Rambirambi Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mheshimiwa Perseko Kone kutokana na vifo vya watu wazima 12 na mtoto mmoja wa miezi minne vilivyotokea tarehe 20 Januari, 2014 kufuatia kugongana uso kwa uso kwa gari aina ya Toyota Noah lililokuwa limebeba abiria likitokea Itogi kwenda Singida na lori katika eneo la Isuna Mkoani Singida.
“Nimeshtushwa, nimesikitishwa na kuhuzunishwa mno na taarifa za vifo vya watu 13 akiwemo mtoto wa miezi minne waliofariki papo hapo katika eneo la ajali tarehe 20 Januari, 2014 baada ya gari aina ya Toyota Noah walilokuwa wakisafiria kutoka Itigi kwenda Singida kugongana uso kwa uso na lori katika eneo la Isuna”.
Rais Kikwete amesema inatia simanzi kuona ajali zikiendelea kutokea na kupoteza maisha ya watu wasio na hatia na hususan mtoto mdogo kama huyu wa miezi minne, kusababisha ulemavu wa kudumu kwa baadhi ya watu na uharibifu wa mali kutokana na makosa ya binadamu katika uendeshaji wa vyombo vya moto.
“Kufuatia ajali hiyo ya kusikitisha, ninakutumia wewe Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mheshimiwa Perseko Kone salamu zangu za rambirambi kutokana na msiba huo, na kupitia kwako, naomba unifikishie salamu zangu za rambirambi na pole nyingi kwa familia zote zilizopoteza wapendwa wao katika ajali hiyo. Nawaomba wanafamilia wawe na moyo wa uvumilivu, subira na ujasiri hivi sasa wanapougulia machungu ya kupotelewa na ndugu zao”, amesema Rais Kikwete kwa masikitiko.
Aidha Rais Kikwete amesema anamuomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema azipokee na kuzilaza Mahala Pema Peponi Roho za Marehemu wote, na amewahakikishia wafiwa kuwa yuko pamoja nao katika kuomboleza msiba huu mkubwa.
Vilevile amemtakia ahueni kijana mmoja majeruhi wa ajali hiyo na aweze kupona haraka na kurejea katika hali yake ya kawaida na kuungana tena na ndugu na jamaa zake.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
20 Januari, 2014
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete leo, Jumamosi, Januari 18, 2014, amefanya uteuzi wa Makatibu Tawala wapya wa mikoa mitano na kuhamisha makatibu tawala wengine na Wakurugenzi wa Majiji nchini.
Taarifa ya Katibu Mkuu Kiongozi (KMK), Balozi Ombeni Sefue iliyotolewa jioni ya leo, Ikulu, Dar Es Salaam inasema kuwa uteuzi na uhamisho huo unaanza leo hii.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Makatibu Tawala wapya ni Ndugu Wamoja A. Dickolangwa ambaye ameteuliwa kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Iringa ambako alikuwa Kaimu Katibu Tawala; Ndugu Abdallah D. Chikota ambaye ameteuliwa kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Lindi. Kabla ya hapo, alikuwa Mkurugenzi wa Halmashauri wa Wilaya ya Newala na Ndugu Symthies E. Pangisa ambaye ameteuliwa kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Rukwa. Kabla ya uteuzi wake, Ndugu Pangisa alikuwa Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Mtwara.
Wengine ni Ndugu Alfred C. Luanda ambaye ameteuliwa kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Mtwara. Kabla ya uteuzi wake, alikuwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Tabora na Ndugu Jackson L. Saitabau ambaye ameteuliwa kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Njombe. Kabla ya hapo, alikuwa Katibu Tawala Msaidizi wa Mkoa wa Arusha.
Taarifa hiyo iliwataja waliohamishwa kuwa ni Ndugu Beatha Swai aliyekuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani na sasa anahamishiwa Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI; Ndugu Sipora J. Liana ambaye alikuwa Mkurugenzi wa Jiji la Arusha anahamishiwa Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI; Ndugu Benedict Ole Kuyan ambaye alikuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Tanga anahamishiwa Mkoa wa Mara na Ndugu Salum M.Chima ambaye alikuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Rukwa anahamishiwa Mkoa wa Tanga.
Wengine waliohamishwa ni Ndugu Mgeni Baruani ambaye alikuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Njombe anahamishiwa Mkoa wa Pwani; Ndugu Juma R. Iddi ambaye alikuwa Mkurugenzi wa Jiji la Mbeya anahamishiwa Jiji la Arusha kama Mkurugenzi; Eng. Omari Chambo ambaye alikuwa Katibu Mkuu, Wizara ya Uchukuzi anahamishiwa Mkoa wa Manyara kama Katibu Tawala wa Mkoa huo na Dkt. John Ndunguru aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Ujenzi anahamishiwa Mkoa wa Kigoma kama Katibu Tawala wa Mkoa huo.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
18 Januari, 2014
Taarifa kwa vyombo vya Habari
KWA WAHARIRI WOTE
TUNAPENDA KUWAJULISHENI KUWA PRESS CONFERENCE YA KATIBU MKUU KIONGOZI ILIYOKUWA IFANYIKE LEO SAA TANO ASUBUHI, JUMAPILI, JANUARI 19, 2014, , SASA ITAFANYIKA LEO, JANUARI 19, 2014, SAA NANE MCHANA KATIKA UKUMBI WA MAWASILIANO - IKULU.
TUNAOMBA RADHI KWA MABADILIKO HAYO.
ASANTENI
SALVA RWEYEMAMU
MKURUGENZI WA MAWASILIANO
IKULU,
DAR ES SALAAM.
19 JANUARI, 2014
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano waTanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, amewahamisha na kuwateua baadhi ya Mawaziri na Naibu Mawaziri kama ifuatavyo:-
1.0 OFISI YA RAIS
Hakuna mabadiliko.
2.0 OFISI YA MAKAMU WA RAIS
2.1 Waziri wa Nchi (Muungano) - Hakuna mabadiliko
2.2 Mhe. Eng. Dr. Binilith Satano MAHENGE (Mb)
Waziri wa Nchi (Mazingira).
2.3 Mhe. Ummy Ali MWALIMU (Mb)
Naibu Waziri
3.0 OFISI YA WAZIRI MKUU
Hakuna mabadiliko
4.0 WIZARA
4.1 WIZARA YA FEDHA
4.1.1 Mhe. Saada Mkuya SALUM (Mb)
Waziri wa Fedha
Mhe. Mwigulu Lameck NCHEMBA (Mb)
Naibu Waziri wa Fedha
4.1.2 Mhe. Adam Kighoma Ali MALIMA (Mb)
Naibu Waziri wa Fedha
4.2 WIZARA YA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA
Hakuna mabadiliko
4.3 WIZARA YA KATIBA NA SHERIA
4.3.1 Mhe. Dkt. Asha-Rose Mtengeti MIGIRO (Mb)
Waziri wa Katiba na Sheria
4.3.2 Naibu Waziri - Hakuna mabadiliko
4.4 WIZARA YA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI
Hakuna mabadiliko
4.5 WIZARA YA VIWANDA NA BIASHARA
4.5.1 Waziri - Hakuna mabadiliko
4.5.2 Mhe. Janet Zebedayo MBENE (Mb)
Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara
4.6 WIZARA YA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA
Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi (Mb)
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa
4.7 WIZARA YA UJENZI
Hakuna mabadiliko
4.8 WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI
4.8.1 Mhe. Mathias Meinrad CHIKAWE (Mb)
Waziri wa Mambo ya Ndani
4.8.2 Naibu Waziri - Hakuna Mabadiliko
4.9 WIZARA YA AFYA NA USTAWI WA JAMII
4.9.1 Mhe. Dkt. Seif Seleman RASHIDI (Mb)
Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii
4.9.2 Mhe. Dkt. Kebwe Stephen KEBWE (Mb)
Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii
4.10 WIZARA YA ELIMU NA MAFUNZO YA UFUNDI
4.10.1 Waziri: Hakuna mabadiliko
4.10.2 Mhe. Jenista Joakim MHAGAMA (Mb)
Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi
14.11 WIZARA YA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA NA WATOTO
14.11.1 Waziri: Hakuna mabadiliko
14. 11.2 Mhe. Dkt. Pindi Hazara CHANA (Mb)
Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto
14.12 WIZARA YA MAENDELEO YA MIFUGO NA UVUVI
14.12.1 Mhe. Dkt. Titus Mlengeya Dismas KAMANI (Mb)
Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi
14.12.2 Mhe. Kaika Saning’o TELELE (Mb)
Naibu Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi
14.13 WIZARA YA KAZI NA AJIRA
Hakuna mabadiliko
14.14 WIZARA YA MAWASILIANO, SAYANSI NA TEKNOLOJIA
Hakuna mabadiliko
14.15 WIZARA YA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI
14.15.1 Waziri - Hakuna mabadiliko
14.15.2 Mhe. George Boniface Taguluvala SIMBACHAWENE (Mb)
Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
14.16 WIZARA YA MAJI
14.16.1 Waziri - Hakuna mabadiliko
14.16.2 Mhe. Amos Gabriel MAKALLA (Mb)
Naibu Waziri wa Maji
14.17 WIZARA YA KILIMO, CHAKULA NA USHIRIKA
14.17.1 Waziri - Hakuna mabadiliko
14.17.2 Mhe. Godfrey Weston ZAMBI (Mb)
Naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika
4.18 WIZARA YA UCHUKUZI
Hakuna mabadiliko
4.19 WIZARA YA HABARI, VIJANA, UTAMADUNI NA MICHEZO
4.19.1 Waziri - Hakuna mabadiliko
4.19.2 Mhe. Juma Selemani NKAMIA (Mb)
Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo
4.20 WIZARA YA MALIASILI NA UTALII
4.20.1 Mhe. Lazaro Samuel NYALANDU (Mb)
Waziri wa Maliasili na Utalii
4.20.2 Mhe. Mahmoud Hassan MGIMWA (Mb)
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii
4.21 WIZARA YA NISHATI NA MADINI
4.21.1 Waziri - Hakuna mabadiliko
4.21.2 Naibu Waziri (Madini) - Hakuna mabadiliko
4.21.3 Mhe. Charles Muhangwa KITWANGA (Mb)
Naibu Waziri (Nishati)
Balozi Ombeni Y. Sefue
KATIBU MKUU KIONGOZI
Ikulu
DAR ES SALAAM
19 Januari, 2014
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ametangaza kuwa kesho, Jumatatu, Januari 13, 2014, itakuwa ni Siku ya Mapumziko (Public Holiday) kwa Watanzania wote kusheherekea miaka 50 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.
Rais Kikwete ameutangaza uamuzi huo mjiniZanzibarambako leo ameungana na Watanzania na Wazanzibari wote kusheherekea miaka 50 ya Mapinduzi Matukufu yaZanzibarya Januari 12, mwaka 1964.
Mapinduzi hayo yaliyoongozwa na mwasisi wa Zanzibar na Taifa la Tanzania, Hayati Abeid Amaan Karume yalifanikiwa kuung’oa madarakani utawala dhalimu wa Sultan na kuwawezesha kwa mara ya kwanza katika historia Waafrika walio wengi kujitawala ndani ya nchi yao wenyewe.
Yalikuwa ni Mapinduzi yaZanzibaryaliyofungua njia ya kuzaliwa kwa Muungano waTanganyikanaZanzibar– miezi mitatu baada ya Mapinduzi hayo – Aprili 26, 1964.
Naye Rais waZanzibarna Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mheshimiwa Ali Mohamed Shein ametangaza kuwa kesho itakuwa Siku ya Mapumziko Tanzania Visiwani kusheherekea miaka 50 ya Mapinduzi yaZanzibar.
Rais Shein alitangaza mapumziko hayo wakati alipohutubia wananchi kwenye Uwanja wa Michezo wa Amaan mjiniZanzibarkatika kusherehekea miaka 50 ya Mapinduzi.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amemteua Mhandisi Paul Mhangilwa Masanja kuwa Kamishna wa Madini nchini.
Taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Obeni Y. Sefue mjini Dar Es salaam leo, Ijumaa, Januari 17, 2014, imesema kuwa uteuzi huo wa Bwana Masanja ulianza jana, Januari 16, 2014.
Taarifa hiyo imesema kuwa kabla ya uteuzi wake, Mhandisi Masanja alikuwa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA).
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
17 Januari, 2014
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amewapandisha vyeo Maafisa Wakuu wanne wa Jeshi la Polisi Tanzania.
Aidha, Rais Kikwete amefanya uteuzi wa nafasi za madaraka katika Jeshi hilo kufuatia mabadiliko ya muundo wa Jeshi la Polisi Tanzania.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Ikulu, Dar Es salaam leo, Jumanne, Desemba 3, 2013 na Kaimu Katibu Mkuu Kiongozi, Dr. Florens Turuka waliopandishwa vyeo kuwa Kamishna wa Polisi (CP) na ambao wote walikuwa ni Naibu Kamishna wa Polisi ni DCP Ernest Mangu, DCP Thobias Andengenye, DCP Abdulrahaman Kaniki na DCP Hamdan Omari Makame.
Rais pia amempandisha cheo SACP Athuman Diwani kuwa Naibu Kamishna wa Polisi.
Walioteuliwa katika nafasi za madaraka katika Jeshi la Polisi ni CP Clodwing Mtweve ambaye anakuwa Kamishna wa Fedha na Utaratibu wa Ugavi na Usafirishaji wa Watu na Vitu (Logistics), CP Paul Chagonja ambaye anakuwa Kamishna wa Operesheni na Mafunzo, CP Isaya Mungulu ambaye anakuwa Mkurugenzi wa Uchunguzi wa Makosa ya jinai (DCI), CP Mussa Ali Mussa ambaye ameteuliwa kuwa Kamishna wa Polisi Jamii.
Wengine ni CP Hamdan Omari Makame ambaye anakuwa Kamishana wa Polisi, Zanzibar; CP Ernest Mangu ambaye anakuwa Mkurugenzi wa Usalama wa Jinai, CP Thobias Andengenye ambaye anakuwa Kamishna wa Utawala na Utumishi, CP Abdulrahman Kaniki ambaye anakuwa Kamishna wa Uchunguzi wa Ushahidi wa Jinai na CP Abdulrahman Diwani ambaye anakuwa Naibu Mkurugenzi wa DCI.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
3 Desemba, 2013
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amemteua Engineer Felchesmi Mramba kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO).
Taarifa iliyotolewa Ikulu, Dar Es Salaam leo, Jumatatu, Desemba 2, 2013, na Kaimu Katibu Mkuu Kiongozi, Dkt. Florens Turuka inasema kuwa uteuzi huo umeanza leo hii.
Kabla ya uteuzi wake, Eng. Mramba alikuwa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hilo la TANESCO.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
2 Desemba, 2013
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Mbunge wa Jimbo la Bariadi Mashariki, Mheshimiwa John Momose Cheyo wa Chama cha UDP na Mwenyekiti wa Taifa wa Chama hicho ametoa zawadi maalum kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete.
Mheshimiwa Cheyo ametoa zawadi hiyo kwa Mheshimiwa Rais katika sherehe maalum iliyofanyika asubuhi ya jana, Alhamisi, Novemba 28, 2013, mjini Bariadi Mkoani Simiyu wakati wa halfa ya kutawazwa kwa Rais Kikwete kuwa Mtemi wa Kabila la Kisukuma.
Hafla hiyo ya kutawazwa kwa Rais Kikwete ndilo lilikuwa tukio la kwanza katika siku ya tatu ya ziara ya siku tano ya Rais Kikwete katika Mkoa wa Simiyu, shughuli ambayo imehudhuriwa na mamia kwa mamia ya wakazi wa Bariadi.
Wakati wa hafla hiyo, ilitangazwa kuwa Mheshimiwa Cheyo, kwa niaba ya wananchi wa Wilaya ya Itilima, alikuwa amemzawadia Rais Kikwete ng’ombe mitamba miwili kutoka shamba la mifugo la Mabuki. Mheshimiwa Cheyo mwenyewe hakuwepo kwenye tukio hilo kutokana na matatizo ya afya yake.
Kwenye hafla hiyo, Rais Kikwete ametawazwa kuwa Mtemi wa Kabila la Wasukuma na amepewa jina la Ng’humbubanhu, jina ambalo lina maana ya “Mtu wa Watu, Kimbilio la Watu, Mwenye Upendo na Watu”.
Kwenye halfa hiyo, mke wa Rais Kikwete, Mama Salma Kikwete ametawazwa kuwa Mke wa Mtemi na kupewa jina la Mgole Mbula, jina ambalo lina maana ya malkia wa mvua.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
28 Novemba, 2013
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa mwanasiasa anayeamua kupigana kwa sababu ya upinzani ama ushabiki wa kisiasa basi huyo siasa zimemshinda na ni vyema atafute shughuli nyingine ya kufanya.
Aidha, Rais Kikwete amewataka Wakuu wote wa Wilaya nchini ambako kuna dalili za upungufu ama tayari kuna ukosefu wa chakula wawasilishe haraka taarifa za upungufu huo Serikalini ili hatua zichukuliwe kuwafikishia wananchi chakula mapema.
Rais Kikwete ameyasema hayo leo, Ijumaa, Novemba 29, 2013, wakati alipohutubia mkutano mkubwa wa hadhara mjini Meatu katika siku ya tatu ya ziara yake ya siku tano katika Mkoa wa Simiyu ambako leo ametembelea wilaya za Bariadi, Itilima na Meatu.
Amesema kuwa tofauti ya vyama siyo sababu ya kutosha ya kugombanisha na kupiganisha watu kwa sababu mwanasiasa ambaye anaamua kupigana na mpinzani wake kwa sababu ya ushabiki wa upinzani ana matatizo kwenye akili yake.
“Kuwapo kwa tofauti ya vyama siyo sababu ya kugombana na ikitokea ukaona mwanasiasa anapigana na mwenzake kwa sababu ya tofauti za siasa basi ujue huyo ana matatizo kwenye akili yake. Mwanasiasa anayepigana kwa sababu ya tofauti za siasa basi huyo siasa zimemshinda, aende akalime muhogo,” amesema Rais Kikwete.
Rais Kikwete alikuwa anajibu malalamiko ya Mbunge wa Meatu, ambaye alikuwa amedai kuwa washabiki wa Chama cha Mapinduzi (CCM) ambao alidai walikuwa wamewapiga washabiki wa chama chake cha CHADEMA walikuwa wanalindwa na wanasiasa wa CCM hata kama amekiri kuwa wako mahakamani.
Baada ya kusikia malalamiko hayo, Rais Kikwete amesema: “Ukiona mwanasiasa anapigana kwa sababu ya ushabiki wa siasa ujue kuwa amefilisika. Huyu siasa imemshinda, aende kulima muhogo. Ugomvi ama lugha za damu itamwagika na nchi haitatawalika hazina nafasi katika siasa. Ushindani wetu siyo wa ngumi bali wa nguvu ya hoja kwenye majukwaa.”
Amesisitiza Rais Kikwete: “Mwanasiasa anayeanzisha ugomvi, awe wa CCM ama wa CHADEMA, huyu siasa zimemshinda. Akafanye shughuli nyingine. Kubwa ni kwamba mtu wa namna hiyo anastahili kukamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.”
Kuhusu malalamiko ya wananchi kuhusu uhaba na ukosefu wa chakula ambayo Rais Kikwete ameelezwa njiani wakati anasafiri kutoka Wilaya ya Bariadi kwenda Wilaya ya Meatu kupitia Wilaya ya Itilima, Rais amesema:
“Nyinyi viongozi hamjanieleza jambo hili lakini wananchi wamelalamika sana njia nzima. “Wanasema wanakabiliwa na upungufu na uhaba wa chakula kwa sababu ya ukame. Nawataka viongozi wa Wilaya hii yenye historia ya ukame na wilaya nyingine nchini kuandaa haraka taarifa za hali ya chakula na kuziwakilisha Ofisi ya Waziri Mkuu kwa ajili ya kufanyiwa kazi.”
Ameongeza Rais Kikwete: “Viongozi changamkieni kuleta taarifa. Lakini nataka jifunzeni kuacha kulima mahindi – maeneo yenye mvua kidogo mahindi hayastawi mnapoteza jasho lenu bure. Limeni mtama unastahili ukame vizuri zaidi.”
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
29 Novemba, 2013
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ameagiza vyombo vya Serikali vinavyosimamia na kuendesha operesheni dhidi ya majangili wanaoua wanyamapori kutoonea wala kudhulumu watu wakati wanaendesha operesheni hiyo - Operesheni Tokomeza.
Aidha, Rais Kikwete amesisitiza tena kuwa pamoja na matatizo yanayodaiwa kutokea wakati wa hatua ya mwanzo ya operesheni hiyo, bado Serikali itaendelea na operesheni hiyo yenye lengo la kukabiliana na majangili wanaua wanyama na hasa tembo na faru ili kupata pembe za wanyama hao.
Rais Kikwete pia amewataka wananchi na hasa wafugaji kutokuingiza na kulisha ng’ombe katika hifadhi za taifa kwa sababu wanyama pekee wanaotakiwa kulishwa katika maeneo hayo ni wanyamapori tu.
Rais Kikwete ameyasema hayo jioni ya jana, Alhamisi, Novemba 28, 2013, wakati alipohutubia maelfu ya wananchi kwenye Kituo cha Mabasi cha Meatu mjini Meatu akiwa kwenye siku ya tatu ya ziara yake ya tano katika Mkoa wa Simiyu.
Baada ya kuwa amesikiliza malalamiko ya baadhi ya wakazi wa wilaya hiyo kuwa baadhi ya maofisa wa Serikali wanaoendesha Operesheni hiyo wanaonea watu na kutaifisha mifugo yao, Rais Kikwete aliagiza:
“Maagizo yangu siyo kuonea watu, siyo kudhulumu watu. Operesheni hii itaendelea lakini tusionee watu. Nataka kuona operesheni hii ikiendeshwa kwa madhumuni yake ambayo ni kupambana na majangili na wala siyo kuonea watu.”
Rais amewataka wananchi wote ambao wanayo malalamiko ya kweli ya kukamatwa na kutaifishwa kwa mifugo yao, wawasilishe rasmi malalamiko yao Serikalini.
“Kama kweli mtu ameonewa, ng’ombe wake wamekamatwa na kutaifishwa na maofisa wa Serikali atueleze kwa ndani malalamiko yake. Tajeni jina la mtu ambaye alidhulumu, tajeni idadi ya ng’ombe waliochukuliwa na eneo ambako walichukuliwa, mtu mwenye ukweli wa namna hiyo ana haki ya kudai na atalipwa.”
Rais Kikwete leo, Ijumaa, Novemba 29, 2013, atakatisha ziara yake katika Mkoa wa Simiyu kwenda Kampala, Uganda ambako kesho atahudhuria mkutano wa mwaka huu wa viongozi wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
29 Novemba, 2013
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano waTanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amependekeza hatua saba za msingi za kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi kwa kupunguza uzalishaji wa gesijoto na kuongeza fedha za kukabiliana na hali hiyo duniani.
Aidha, Rais Kikwete amesema kuwa ni siri ya wazi kuwa Afrika inateseka zaidi kwa kukabiliwa na changamoto nyingi na za kila aina kutokana na mabadiliko ya tabia nchi pamoja na ukweli kuwa inachangia kidogo sana katika kuzalisha gesijoto na kuharibu mazingira.
Akizungumza kwenye ufunguzi wa Mkutano wa Kimataifa wa Mabadiliko ya Tabia Nchi wa COP19/CMP9 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa wa Michezo wa Poland, mjini Warsaw, jioni ya leo, Jumanne, Novemba 19, 2013, Rais Kikwete amewaambia mamia ya washiriki wa Mkutano huo kuwa dunia inahitaji kuchukua hatua saba za msingi kukabiliana na hali hiyo.
Hatua hizo ni zifuatazo:
(a) Kukubaliana kuhusu njia za msingi za kitaasisi za jinsi ya kuzifidia nchi kutokana na upotevu unaotokana na mabadiliko ya tabia nchi.
(b) Kukubaliana kuhusu ni taasisi ipi itasimamia shughuli zinazohusiana na misitu. Taasisi itakayohakikisha na kusimamia namna ipi nchi masikini zinavyoweza kufidiwa kifedha kutokana na upunguzaji wa gesijoto.
(c) Kukubaliana kuhusu misingi, masharti na maelekezo ambayo yatasimamia hatua za kupunguza gesijoto katika nchi zilizoendelea.
(d) Hatua na njia ambazo zitaongoza nchi zilizoendelea kupunguza gesijoto zinatakiwa kukubaliwa na kuelezwa waziwazi.
(e) Kuna umuhimu wa haraka wa kuupatia Mfuko wa Mazingira wa Kijani fedha za kuanzisha na kuimarisha Mfuko huo. Kwa sasa ni Mfuko mtupu. Lazima tuhakikishe kuwa unajazwa ipasavyo. Aidha, lazima tukubaliane namna gani kiasi cha dola za Marekani Bilioni 100 zilizokubaliwa kuchangwa kila mwaka zitakavyopatikana na kugawanywa.
(f) Kituo cha Teknolojia ya Mazingira na Mtandao kitafute jinsi ya kuondoa vikwazo katika masuala yanayohusiana na uhamishaji wa teknolojia kutoka nchi tajiri kwenda nchi zinazoendelea na kumaliza changamoto zinahusiana na Haki Miliki.
(g) Kwenye COP hii tunahitaji kukubaliana kuhusu baadhi ya mambo yanayohusiana na upunguzaji wa gesijoto.
Rais Kikwete alikuwa anazungumza kwa niaba ya viongozi wa Umoja wa Afrika (AU) katika nafasi yake akiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Viongozi wa Afrika kuhusu Mabadiliko ya Tabia Nchi (CAHOSCC).
Rais Kikwete amekuwa Mwenyekiti wa Kamati hiyo tokea Januari, mwaka huu, 2013, wakati alipochaguliwa na viongozi wenzake kushika nafasi hiyo kufuatia kifo cha aliyekuwa anashikilia nafasi hiyo, Waziri Mkuu wa Ethiopia, Mheshimiwa Meles Zenawi, Septemba, mwaka jana.
Viongozi wengine ambao wamezungumza katika Mkutano huo wa ufunguzi ambao Mwenyekiti wake alikuwa ni Rais wa COP 19 Mheshimiwa Marcin Korolec, Waziri wa Mazingira wa Poland ni Waziri Mkuu wa Poland, Mheshimiwa Donard Tusk na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Mheshimiwa Ban Ki Moon.
Wengine ni Rais wa Mkutano wa 68 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Mheshimiwa Balozi John Williams Ashe ambaye ni Balozi wa Antigua na Barbuda katika Umoja wa Mataifa na Katibu Mtendaji wa Mkataba wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabia Nchi wa Umoja wa Mataifa (UNFCC), Mheshimiwa Christiana Figueres.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
19 Novemba, 2013
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete jioni ya leo, Alhamisi, Novemba 14, 2013, amekuwa mmoja wa viongozi wa kwanza na wachache kukutana kwa mazungumzo na Rais Mahinda Rajapaksa wa Sri Lanka katika Makazi Rasmi ya Rais wa nchi hiyo ya Temple Trees mjini Colombo, mji mkuu wa nchi hiyo.
Rais Kikwete akifuatana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mheshimiwa Bernard Membe na Balozi wa Tanzania nchini Sri Lanka, Mheshimiwa John Kijazi amezungumza na Mheshimiwa Rajapaska kwa kiasi cha dakika 35.
Rais Kikwete amekuwa miongoni mwa viongozi watatu ambao wamekutana na Rais Rajapaksa leo miongoni mwa viongozi wengi ambao kesho wanaanza Mkutano wa Wakuu wa Serikali wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Madola (CHOGM).
Viongozi wengine wa Nchi na Serikali waliokutana na Rais Rajapaksa, ambaye ni mwenyeji wa Mkutano wa Jumuiya ya Madola, ni Waziri Mkuu wa Malaysia, Datuk Seri Najib Tunku Razak na Waziri Mkuu wa Pakistan, Mheshimiwa Muhammad Nawaz Sharif.
Katika mazungumzo kati ya Rais Kikwete na Rais Rajapaksa, viongozi hao wawili wamejadili masuala yanayohusu uhusiano kati ya Tanzania na Sri Lanka na masuala ya kimataifa ukiwamo mkutano wa Jumuiya ya Madola wenyewe unaoanza kesho, Ijumaa, Novemba 14, 2013.
Rais Kikwete amemshukuru Rais Rajapaksa kwa kutuma wataalam wa zao la nazi ambao karibuni walikuja Tanzania kuangalia na kushauri kuhusu ugonjwa wa minazi ambao unashambulia zao hilo nchini. Wataalam hao tayari wamerejea Sri Lanka kufanya utafiti na vipimo vya kisayansi matokeo ya uchunguzi wao.
“Mheshimiwa Rais umeahidi na umetimiza. Kama ulivyoahidi wakati wa ziara yako katika Tanzania, wataalam wamekuja na sasa tunasubiri matokeo ya uchunguzi wao na ushauri wao,” Rais Kikwete amemwambia Rais Rajapaksa.
Rais Kikwete pia amemshukuru Rais Rajapaksa kwa kushawishi makampuni ya Sri Lanka kuwekeza katika shughuli za viwanda vya nguo na miradi midogo ya kuzalisha umeme.
Rais Kikwete pia amemshukuru Rais Rajapaksa kwa mwaliko wake wa kushiriki mkutano wa Jumuiya ya Madola na pia akampongeza kwa kuandaa vizuri mikutano ya mwanzo ya Jumuiya hiyo iliyotangulia Mkutano wa Wakuu wa Serikali wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Madola (CHOGM).
“Naomba radhi pia kuwa sikuweza kufika mapema ili kufanya ziara rasmi kama tulivyokuwa tumekubaliana ulipotutembelea nyumbani. Wewe unajua mambo ya uongozi, shughuli zimekuwa nyingi kidogo kuliko kawaida,” amesema Rais Kikwete.
Naye Mheshimiwa Rajapaksa amemshukuru Rais Kikwete kwa kusaidia kuongeza hamasa ya viongozi wa Afrika kushiriki katika Mkutano wa mwaka huu wa Jumuiya ya Madola.
“Aidha, tunakushukuru wewe binafsi kwa kusafiri safari ndefu kuja kuhudhuria mkutano huu. Asante sana”.
Rais Kikwete na Mama Salma Kikwete wamewasili nchini Sri Lanka asubuhi ya leo kutokea nyumbani tayari kuhushuria Mkutano huo wa Jumuiya ya Madola.
Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ameshtushwa na kufadhaishwa na taarifa za kifo cha Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Dkt. Sengondo Mvungi kilichotokea jana, Jumanne, Novemba 12, 2013 kwenye Hospitali ya Milpark, Johannesburg, AfrikaKusini.
Katika salamu za rambirambi ambazo amemtumia Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Joseph Sinde Warioba, Rais Kikwete amesema kuwa amepokea kwa mshtuko mkubwa na fadhaha taarifa za kifo cha Dkt. Mvungi. “Kwa hakika ni taarifa iliyonisumbua na kunipa huzuni nyingi.”
Rais Kikwete amesema kuwa hakuna shaka kuwa katika maisha yake Dkt. Mvungi ametoa mchango mkubwa katika maendeleo ya Tanzania kwa namna mbalimbali na kuwa kifo kimemfika wakati Taifa la Tanzania lilikuwa bado linahitaji busara, hekima na mchango wake katika mchakato mzima wa kusaka Katiba mpya.
“Kuanzia alipokuwa mwandishi wa habari katika Magazeti ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya Uhuru na Mzalendo, hadi uhadhiri wake katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, hadi uwakili katika Kampuni ya South Law Chambers, hadi uongozi wake katika Chama cha NCCR-Mageuzi, hadi uamuzi wake wakugombea Urais wa Tanzania mwaka 2005 na sasa akiwa Mjumbe wa Tume ya Katiba, Dkt. Mvungi ametoa mchango wake mkubwa sana katika maendeleo ya nchi yetu. Na hili hatutalisahau,” amesema Rais Kikwete.
“Kwa masikitiko makubwa, nakutumia wewe Jaji Joseph Warioba, Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba salamu za rambirambi za dhati ya moyo wangu nikiombeleza kifo cha Dkt. Mvungi. Nakupa pole nyingi wewe Mwenyekiti, wajumbe wa Tume na wafanyakazi wote wa Tume kwa kuondokewa na mwenzenu. Naungana nanyi kuomboleza msiba huo mkubwa.”
“Aidha, kupitia kwako, natuma pole nyingi kwa wana-familia, ndugu, marafiki na majirani wa Dkt. Mvungi kwa kuondokewa na mhimili, msimamizi wa familia na ndugu. Wajulishe kuwa nikonao katika msiba huu mkubwa. Wajulishe kuwa msiba wao ni msiba wangu pia. Muhimu waelewe kuwa binafsi naelewa machungu yao katika kipindi hiki kigumu na namwomba Mwenyezi Mungu awape subira waweze kuvuka kipindi hiki kigumu kwasababu yote ni mapenzi yake.”
Amemalizia Rais Kikwete: “Napenda kuungana nao katika kumwomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, aiweke mahali pema roho ya Marehemu Dkt. Sengondo Mvungi. Amina.”
Wakati huohuo Rais Kikwete ametuma salamu za rambirambi kwa familia ya Marehemu Musa Hillal Samizi ambaye alifariki tarehe 11 Novemba,2013 hapa Dar es Salaam.
Rais amemwelezea marehemu Samizi kama kada mahiri na mtumishi mwaminifu katika uhai wake.
Rais amesema “Marehemu Samizi atakumbukwa kwa upendo, ushirikiano na uchapakazi wake katika kazi na katika nafasi mbalimbali ambazo aliwahi kushika ndani ya Chama cha Mapinduzi na Serikalini”.
Marehemu Samizi aliwahi kushika nyadhifa mbalimbali zikiwemo Ubunge wa Jimbo la Kigoma Mjini,Katibu Msaidizi wa Chama cha Mapinduzi Makao Makuu Dodoma, Afisa Utumishi NBC, Mjumbe wa NEC, Mjumbe wa Bodi MECCO, SHIHATA, Serengeti Safari Lodge pamoja na Mkuu wa Wilaya za Handeni, Kasulu, Tabora na Moshi kabla ya kustaafu Mwaka 2012 alipostaafu.
Mungu ilaze mahali pema Roho ya marehemu Samizi. Amen.
Mwisho.
Imetolewana;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
13 Novemba, 2013
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais Jakaya Mrisho Kikwete ameondoka jioni ya leo tarehe 13 Novemba,2013 kuelekea Colombo , Sri-Lanka kuhudhuria kikaocha siku tatu (3) cha Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Madola(Commonwealth Heads of Government Meeting – CHOGM) kinachotarajiwa kuanza tarehe 15-17 November,2013.
Sri-Lanka inachukua uenyekiti wa Jumuiya ya Madola kwa kipindi cha miaka miwili ijayo kutoka Australia.
Pamoja na Kikao cha CHOGM Rais Kikwete anatarajia kuhudhuria kikao cha viongozi na baadhi ya wafanyabiashara .
Kwa mara ya kwanza Malkia wa Uingereza hatahudhuria Kikaocha Sri-Lanka na badala yake atawakilishwa na mwanae Prince Charles.
CHOGM ni Kikao kinachofanyika kila baada ya miaka miwiliambacho ujumbe wa mwakani “Growth with Equity: Inclusive Development” ujumbe ambao unasisitiza Ukuaji na Maendeleo yatakayokuwa na faida na usawa kwa jamii nzima kwa lengo la kupunguza pengo lililopo kati ya maskini na matajiri katika jamii.
Pamoja na agenda hiyo, viongozi hao watapata nafasi yakuzungumzia hali ya kisiasa na kiuchumi katika nchi za Jumuiya ya Ulaya, mabadiliko ya hali ya hewa na biashara baina ya mataifa.
Kikao cha viongozi kitafanyika baada ya kufanyika kwa baadhi ya vikao vya makundi mbalimbali katika Jumiya ikiwemo Vijana,Wafanya biashara, makundi maalum na cha Mawaziri.
Mwisho.
Imetolewa na;
Premi Kibanga,
Mwandishi wa Habari wa Raisi Msaidizi,
Ikulu – Dar es Salaa
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ameirudishia Kampuni ya Nyamigogo Grand Vezir Holdings ya Mkoani Geita zawadi ya gramu 227 za dhahabu safi akielekeza kuwa zawadi hiyo itumike kuwasaidia watoto yatima.
Rais Kikwete ametoa maelekezo hayo leo, Jumatatu, Novemba 11, 2013, baada ya kukabidhiwa zawadi ya dhahabu hiyo wakati wa sherehe ya kuzindua mgodi wa uchenjuaji dhahabu wa kampuni hiyo nje kidogo ya mji mdogo wa Kharuma ambako ndiko makao makuu ya wilaya mpya ya Nyang’hwale, Mkoa wa Geita.
Gramu hizo 227 ambazo ni sawa na aunzi nane zina thamani ya Sh. milioni 16 kwa bei ya sasa ya soko la dhahabu duniani.
Baada ya kukabidhiwa zawadi hiyo, Rais Kikwete ameuliza: “Sasa nifanye nini na zawadi hii? Nawarudishieni hii dhahabu, iuzeni popote mnakotaka na fedha itakayopatikana tutawapa watoto yatima.”
Akizungumza na wananchi katika mgodi huo, Rais Kikwete ameupongeza uongozi wa mgodi huo akisema kuwa umeongeza thamani ya dhahabu na ya maisha ya wananchi katika eneo hilo nje ya mji mdogo wa Kharuma.
Hata hivyo, Rais Kikwete ameushauri uongozi wa mgodi huo kufanya jitihada za kuboresha teknolojia inayotumika. “Mmefanya vizuri sana na mgodi huu ni mradi wa maana sana kwa kuongeza thamani ya dhahabu na kuboresha maisha ya wananchi katika eneo hili. Ubunifu huu unastahili pongezi.”
Ameongeza Rais Kikwete: “Lakini lazima tuboreshe teknolojia. Teknolojia inayotumika kwenye mgodi huu bado ni ya zamani kidogo. Hii ni sawa na hadithi ya mtu mwenye chongo katika jamii ya vipofu watupu. Yeye anaonekana kama mfalme.”
Mgodi wa Nyamigogo ambao ni mgodi wa marudio kwa maana ya kwamba unazalisha dhahabu kutokana na mchanga ambao huko nyuma umepata kufuliwa na kutoa dhahabu, ulianzishwa mwaka 2011 na mpaka sasa zimewekezwa kiasi cha Sh.bilioni 1.6 katika uendelezaji wa mgodi huo.
Risala ya uongozi wa mgodi huo inasema kuwa mgodi huo unaozalisha kiasi cha gramu kati ya 500 na 600 kwa mwezi na unaajiri watu 45 wakiwemo wanawake 10.
Tokea kuanzishwa kwake, mgodi huo umekuwa unaunga mkono shughuli za jamii inayouzunguka ikiwa ni pamoja na kujenga zahanati na madarasa ya shule katika vijiji viwili.
Rais Kikwete amezindua mgodi huo ikiwa sehemu ya kukagua na kuzindua miradi ya maendeleo katika ziara yake rasmi ya kikazi katika Mkoa wa Geita, moja ya mikoa minne ambayo aliianzisha mwaka jana. Mikoa mingine ni Simiyu, Njombe na Katavi.
Ziara hiyo ya siku tano inamalizika kesho, Jumanne, Novemba 12, 2013, na mbali ya kuzindua mgodi huo, Rais Kikwete leo amepokea ripoti ya maendeleo ya Wilaya ya Nyang’hwale na kuhutubia mkutano wa hadhara katika mji mdogo wa Kharuma uliohudhuriwa na mamia kwa mamia ya wananchi.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
11 Novemba, 2013
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia Salamu za Rambirambi Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Anne Semamba Makinda kuomboleza kifo cha Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Shughuli za Bunge, Bwana Anselm Lyatonga Mrema kilichotokea usiku wa tarehe 10 Novemba, 2013 katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma alikokuwa amepelekwa kwa matibabu ya ugonjwa wa shinikizo la damu.
“Nimepokea kwa mshtuko na masikitiko makubwa taarifa za kifo cha Mtumishi wa Ofisi yako ya Bunge, Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Shughuli za Bunge, Bwana Anselm Lyatonga Mrema kilichotokea usiku wa tarehe 10 Novemba, 2013 katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma alikokuwa amepelekwa kwa matibabu akisumbuliwa na shinikizo la damu”, amesema kwa masikitiko Rais Kikwete katika Salamu zake za Rambirambi.
“Nilimfahamu Marehemu Anselm Lyatonga Mrema, enzi za uhai wake, kama Mtumishi Mwaminifu, Mwadilifu na Mchapakazi Hodari aliyejituma kikamilifu katika utekelezaji wa majukumu yake, sifa ambazo zilimfanya apande cheo kutoka kuwa Katibu Msaidizi Mwandamizi wa Bunge na kuwa Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Shughuli za Bunge”, ameongeza kusema Rais Kikwete.
“Kutokana na msiba huo mkubwa, ninakutumia wewe Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Anne Semamba Makinda pamoja na Watumishi wote wa Bunge Salamu zangu za Rambirambi kwa kuondokewa na Mtumishi muhimu ambaye mchango wake katika Utumishi wa Bunge na Taifa kwa ujumla ulikuwa bado unahitajika sana”, amesema Rais Kikwete.
Rais Kikwete amemuomba Spika wa Bunge kumfikishia Salamu zake za Rambirambi na pole nyingi kwa Familia ya Marehemu Anselm Lyatonga Mrema kwa kupotelewa na Kiongozi na mhimili muhimu wa familia. Amewahakikishia Wanafamilia kuwa yuko pamoja nao katika kuomboleza msiba wa Mpendwa wao.
Amewaomba wawe na moyo wa uvumilivu na ujasiri katika kipindi chote cha maombolezo kwa kutambua kuwa yote ni mapenzi yake Mola. Aidha Rais Kikwete amesema anamuomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema aipokee na kuilaza Mahala Pema Peponi Roho ya Marehemu Anselm Lyatonga Mrema, Amina.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
11Novemba, 2013
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amevitaka vyombo vya habari vya Tanzania kuonyesha ukomavu katika kuisaidia nchi kujenga mahusiano na nchi nyingine badala ya kuandika na kutangaza habari za uhusiano kwa ushabiki na utiaji chumvi.
Wito huo wa Rais Kikwete unafuatia uandishi wa habari za mkutano kati ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Tanzania Mheshimiwa Bernard Membe naWaziri wa Mambo ya Nje wa Kenya, Mheshimiwa Amina Mohammed uliofanyika jana, Jumapili, Novemba10, 2013, mjini Dar es Salaam.
Baada ya mkutano huo, Mheshimiwa Amina Mohammed aliwaeleza waandishi wa habari kuwa Kenya sasa imeelewa vizuri msimamo wa Tanzania kuhusu mchakato wa utengamano ndani ya Jumuia ya Afrika Mashariki (EAC), hatua ambayo imepongezwa na Rais Kikwete.
Kufuatia hatua hiyo muhimu na sahihi ya Kenya, baadhi ya magazeti yaliyochapishwa leo nchini yametoka na vichwa vya habari kama vile “Kenya yaiangukia Tanzania” na “Kenya yasalimu amri”, vichwa vya habari ambavyo havisemi ukweli, siyo sahihi na ni vya uchochezi na uzandiki.
Ni vichwa vya habari ambavyo haviitendei haki Tanzania wala Kenya. Rais Kikwete hakufurahishwa, na kwahakika, amesikitishwa na vichwa hivyo vya habari.
Tanzania, kupitia hotuba ya Rais Kikwete Bungeni Alhamisi iliyopita ilitoa hoja za kuimarisha Jumuia ya Afrika Mashariki. Kenya imeelewa hoja hiyo ya Tanzania na imefanya uamuzi sahihi na wenye manufaa kwa Jumuia yetu.
Hivyo, ni wajibu wa vyombo vya habari nchini kuchangia katika kuimarisha Jumuia badala ya kuandika habari za utengamano kwa namna ya ushabiki usiokuwa na maana na usio na mashiko.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
11Novemba, 2013
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amefanya uteuzi wa wakuu wa Shirika la Utafiti wa Maendeleo ya Viwanda (TIRDO), Mhifadhi Mkuu wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro na Mkurugenzi wa Makumbusho ya Taifa.
Katika uteuzi huo, Rais amemteua Prof. Mkumbukwa Madundo Angelo Mtambo kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utafiti wa Maendeleo ya Viwanda (TIRDO).
Rais pia amemteua Bwana Freddy Safiel Manongi kuwa Mhifadhi Mkuu wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, ambaye hivi sasa ni kaimu Mkuu wa Chuo cha Wanyamapori cha Mweka na pia amemteua Prof. Audax Zephania Philip Mabula kutoka chuo kikuu cha Dar es Salaam kuwa Mkurugenzi wa Makumbusho ya Taifa.
Uteuzi huu umeanza rasmi mwishoni mwa Mwezi Octoba mwaka huu.
Imetolewa na;
Premi Kibanga,
Mwandishi wa Habari wa Rais Msaidizi,
Ikulu - Dar es Salaam.
11 Novemba, 2013
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia Salamu za Rambirambi Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji Mstaafu, Mheshimiwa Damian Z. Lubuva kufuatia kifo cha aliyewahi kuwa Mjumbe wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi na Wakili wa Kujitegemea, Jaji Mstaafu, Mheshimiwa Hillary Mkate kilichotokea nyumbani kwake Kinondoni Jijini Dar es Salaam tarehe 1 Novemba, 2013.
“Nimeshtushwa, nimesikitishwa na kuhuzunishwa sana kutokana na taarifa za kifo cha Jaji Mstaafu, Mheshimiwa Hillary Mkate ambaye amewahi kuitumikia Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kwa uadilifu mkubwa, na hivyo kutoa mchango stahiki katika kuiongoza Tume hiyo kufanya kazi zake kikamilifu”, amesema kwa masikitiko Rais Kikwete katika Salamu zake za Rambirambi.
Rais Kikwete amesema alimfahamu Marehemu Jaji Hillary Mkate, enzi za uhai wake, kama kiongozi mwadilifu na mchapakazi hodari ambaye alitumia vipaji vyake vyote alivyojaaliwa na Mwenyezi Mungu kutoa haki kwa wananchi mbalimbali waliokuwa wakizitafuta haki zao kutokana na sababu mbalimbali.
“Kutokana na msiba huu mkubwa, Ninakutumia wewe Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji Mstaafu, Mheshimiwa Damian Lubuva, Watumishi wote wa Mahakama na Wanasheria kote nchini kwa kuondokewa na mwenzao, Jaji Mstaafu na Wakili wa Kujitegemea, Mheshimiwa Hillary Mkate. Namuomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema aipokee na kuilaza Mahala Pema Peponi Roho ya Marehemu, Amina”, ameongeza kusema Rais Kikwete.
Aidha Rais Kikwete amemuomba Jaji Mstaafu, Mheshimiwa Damian Lubuva kumfikishia Salamu zake za Rambirambi na pole nyingi kwa Familia ya Marehemu Jaji Mstaafu, Hillary Mkate kwa kupotelewa na Kiongozi na Mhimili wa Familia.
Amewahakikishia Wanafamilia hao kuwa yuko pamoja nao katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo ya mpendwa wao. Amewaomba wawe na moyo wa uvumilivu, utulivu na subira katika kuomboleza msiba huu kwa vile yote ni Mapenzi yake Mola.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
4 Novemba, 2013
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ameondoka nchini jioni ya jana, Jumatatu, Oktoba 28, 2013, kwenda London, Uingereza, kwa ziara ya kikazi ya siku nne ambako atahudhuria Mkutano wa Kimataifa wa Serikali Uwazi (Open Government) uliotishwa na Serikali ya Waziri Mkuu wa Uingereza, Mheshimiwa David Cameroun.
Mkutano huo wa siku mbili utafanyika keshokutwa Jumatano na Alhamisi kwenye Ukumbi wa Queen Elizabeth 2 mjini London.
Miongoni mwa mambo makuu ambayo mkutano huo utazungumzia ni Serikali Uwazi na Ajenda ya Maendeleo Baada ya Mwaka 2015 wakati muongo wa utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo ya Milenia (Millenium Development Goals) unafikia mwisho.
Masuala mengine ambayo yatazungumzwa katika mkutano ambao Rais Kikwete anaambatana na Mawaziri wake watatu ni pamoja na uwazi katika manunuzi ya umma, uwazi katika mikataba, haki ya kupata habari, uwazi katika ukaguzi wa fedha za umma, uwazi wa Serikali na vyombo vya habari, uwazi katika mikataba ya maliasili, uwazi katika maendeleo ya nchi zinazoendelea.
Mawaziri wanaoambatana na Rais Kikwete katika ziara hiyo ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Mheshimiwa Bernard Membe, Waziri wa Sheria na Katiba Mheshimiwa Mathias Chikawe na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utawala Bora Serikali ya Mapinduzi, Zanzibar Mheshimiwa Mwinyihaji Makame.
Rais Kikwete anatarajia kurejea nyumbani Jumamosi, Novemba 2, 2013.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
29 Oktoba, 2013
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia Salamu za Rambirambi Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mheshimiwa Bernard Membe kufuatia kifo cha Mwanadiplomasia na Mwanasiasa Mkongwe, Balozi Isack Sepetu aliyefariki dunia tarehe 27 Oktoba, 2013 katika Hospitali ya TMJ ya Jijini Dar es Salaam alikopelekwa kwa matibabu ya ugonjwa wa Kisukari na Kiharusi.
Marehemu Balozi Isack Sepetu, enzi za uhai wake, aliwahi kushika nyadhifa mbalimbali za juu Serikalini kuanzia miaka ya Sabini ambapo aliwahi kuteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje katika Serikali ya Awamu ya Kwanza, Waziri wa Habari, Utangazaji na Utalii katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
Katika miaka ya Tisini, aliteuliwa kuwa Waziri wa Nchi, Mipango na Uchumi katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar iliyoongozwa na Dr. Salmin Amour. Akiwa Balozi wa Tanzania, Marehemu aliiwakilisha nchi katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) na uliokuwa Muungano wa Nchi za Kisovieti za Kisoshalisti za Urusi (USSR) ambayo kwa sasa ni Russia.
“Nimepokea kwa mshtuko na masikitiko makubwa taarifa za kifo cha Mwanasiasa na Mwanadiplomasia Mashuhuri, Balozi Mstaafu, Mheshimiwa Isack Sepetu aliyefariki dunia katika Hospitali ya TMJ Jijini Dar es Salaam alikopelekwa kwa matibabu ya ugonjwa wa Kisukari na Kiharusi tarehe 27 Oktoba, 2013”, amesema Rais Kikwete katika Salamu zake za Rambirambi.
Rais Kikwete amesema alimfahamu Marehemu Balozi Isack Sepetu, enzi za uhai wake, kama Mwanasiasa na Kiongozi mwenye bidii na uwezo mkubwa wa uongozi ambaye alidhihirisha uaminifu na uadilifu wake katika nyadhifa mbalimbali alizowahi kushikilia katika Awamu zote za Uongozi Tanzania Bara na Zanzibar. Balozi Sepetu aliwahi pia kuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa nafasi ya kuteuliwa na Mwenyekiti wa Chama, na kukitumikia Chama kwa uaminifu na uadilifu mkubwa.
“Natambua hata baada ya kustaafu, Marehemu Balozi Isack Sepetu aliendelea kuaminiwa katika utumishi wake, na hivyo kuteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Vitega Uchumi Zanzibar (ZIPA) katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein, na pia Mjumbe wa Bunge la Afrika Mashariki hadi mauti yalipomkuta”, amesema Rais Kikwete, na kuongeza,
“Kutokana na msiba huo mkubwa, ninakutumia wewe Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mheshimiwa Bernard Membe Salamu zangu za Rambirambi kwa kumpoteza Mwanadiplomasia na mmoja wa Viongozi shupavu katika nchi yetu, Marehemu Balozi Isack Sepetu”.
“Kupitia kwako, naomba pia Salamu zangu za Rambirambi na pole nyingi ziwafikie Wanafamilia ya Marehemu kwa kumpoteza Kiongozi na Mhimili Madhubuti wa Familia. Nawaomba wote wawe na moyo wa uvumilivu na subira katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo kwani yote ni mapenzi yake Mola”.
Rais Kikwete amewahakikishia Wanafamilia ya Marehemu Balozi Isack Sepetu kuwa yuko pamoja nao katika kipindi chote cha majonzi kufuatia kifo cha mpendwa wao. Namuomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema aipokee na kuilaza Mahala Pema Peponi Roho ya Marehemu Balozi Isack Sepetu, Amina.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
28 Oktoba, 2013
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa ni wajibu wa Halmashauri nchini kuhakikisha kuwa zinawabana wafanyabiashara kulipa kodi baada ya kununua mazao ya wakulima katika halmashauri hizo.
Rais Kikwete ameshangaa wakati wa ziara yake kusikia malalamiko ya viongozi wa Mkoa wa Njombe kuwa wafanyabiashara wanaonunua zao la pareto katika Mkoa huo wamekuwa wanakataa kulipa ushuru.
“Komesheni ujinga huu wa watu kununua pareto ya wakulima bila kulipa ushuru na kodi kwa Halmashauri. Mnajinyima wenyewe raslimali muhimu ya maendeleo yenu kwa kushindwa kuwalazimisha watu kulipa kodi,” alisema Rais Kikwete jana, Jumatano, Oktoba 23, 2013 mjini Njombe wakati anazungumza na viongozi wote wa Mkoa huo wakati anamaliza na kujumuisha ziara yake ya siku saba katika Mkoa huo.
Alisema Rais Kikwete: “Mtapata wapi fedha za kuendesha halmashauri zetu kama mnashindwa kutoza kodi na ushuru kwa watu wanaofanya biashara. Hakuna Serikali duniani inayoendeshwa bila kutoza kodi. Hakuna. Haipo duniani.”
Rais Kikwete amesema: “Kwa kuwatoza wafanyabiashara wakubwa wanaonunua mazao kodi kunazisaidia Halmashauri na hata Serikali Kuu kuondokana na ulazima wa kuwatoza wananchi wa kawaida kodi ndogo ambazo sisi tunaziita kodi za kero na tumezifuta.”
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
24 Oktoba, 2013
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa Serikali yake itakomesha kero ya wanafunzi na watoto wa shule nchini kuchangia vitabu vya kiada katika masomo yao.
Aidha, Rais Kikwete amesema kuwa wajibu wa kuhimiza ujenzi wa maabara za sayansi katika shule nchini siyo tu matakwa ya Rais bali suala hili linatakiwa kuwa wajibu wa kufa na kupona kwa kila kiongozi katika ngazi zote za uongozi kwa sababu nchi haiwezi kuendelea bila wanasayansi.
Vile vile, Rais Kikwete amewaagiza viongozi wote katika ngazi zote na hasa kwenye ngazi ya wilaya na halmashauri kutenga katika bajeti zao fedha za kujenga nyumba za walimu kwa nia ya kuboresha mazingira ya kazi ya walimu nchini.
Rais Kikwete amesema na kutoa maagizo hayo jana, Jumatano, Oktoba 23, 2013, alipozungumza na uongozi wa Mkoa wa Njombe wakati anakamilisha na kujumuisha ziara yake ya siku saba katika Mkoa huo kwenye Ukumbi wa Halmashauri ya Mji wa Njombe.
Rais ambaye alizungumza masuala mengi kuhusiana na aliyoyaona wakati wa ziara hiyo alijielekeza kwa muda mrefu katika masuala ya elimu na nafasi ya viongozi katika kusuma mbele sekta ya elimu kama mkombozi mkuu wa Watanzania.
Kuhusu kupatikana kwa vitabu vya kiada kwa watoto na wanafunzi nchini, Rais Kikwete amewaambia viongozi hao wa Njombe:
“Nimeilekeza Wizara ya Elimu na Mafunzo ya ufundi kuwasilisha kwangu bajeti inayotakiwa kutuwezesha sisi, kama Taifa, kuhakikisha kuwa kila mtoto wetu na mwanafunzi wa nchi yetu hii anakuwa na kila kitabu cha kiada kwa kila somo.”
“Hili ni jambo ambalo tumelizungumza kwa muda mrefu. Hakuwezi kamwe kuendelea kuahirisha majawabu ya suala hili. Nataka kujua itatugharimu kiasi gani kwa kila mtoto na mwanafunzi nchini kuwa na kitabu chake cha kiada kwa kila somo. Tumepata msaada wa marafiki wetu. Tunawashukuru. Lakini sasa wakati umefika kwa sisi wenyewe kuelekeza nguvu zetu zote kumaliza tatizo hilo,” amesema Rais Kikwete na kusisitiza:
“Ilikuwa wanafunzi 10 kwa kitabu kimoja, tumeshuka hadi wanafunzi watatu kwa kitabu kimoja. Hili halitoshi na hali hii haikubaliwi ni lazima iwe ni mwanafunzi mmoja na kitabu kimoja, kitabu chake.”
Kuhusu ujenzi wa maabara ya sayansi katika kila sekondari nchini na umuhimu wa kufundisha masomo ya sayansi nchini, Rais Kikwete amesema “ni lazima tujenge hizi maabara haraka, ni lazima tuongeze kasi yetu ya kufundisha masomo ya sayansi na ni lazima tukabiliane na uhaba wa walimu wa kufundisha sayansi nchini.”
“Maendeleo ya nchi huletwa na wanasayansi. Na kama mfumo wa elimu wa nchi yoyote hautoi nafasi ya kutosha kulea na kujenga wanasayansi basi nchi hiyo inapiga hatua ya kurudi nyuma. Kwenye hili, tayari tumeachwa na treni na wala suala hili siyo matakwa ya Rais bali ni suala la kufa na kupona kwa viongozi wote wa ngazi zote,” amesema Rais Kikwete.
Ameongeza: “Siyo kila mtu katika nchi yetu atakuwa mwanasiasa. Hawa tayari tunao wa kutosha na wengine kazi yao sasa ni kusababisha ghasia nchini. Tunahitaji wanasayansi zaidi – tunahitaji madaktari, tunahitaji wahandisi. Ni lazima tuwekeze ipasavyo katika eneo hili kwa sababu tukikosea sasa tutakuwa tumekosa hatua moja kubwa na muhimu katika jitihada za kujiletea maendeleo.”
Amesema kuwa anatambua matatizo yaliyoko katika ufundishaji wa masomo ya sayansi nchini na kuwa kwa sababu hiyo ameitisha mkutano wa wadau wote wanaohusika na elimu na eneo la sayansi nchini ambao utafanyika Novemba 3, mwaka huu, kwa nia ya kutafuta majawabu ya matatizo hayo.
Tanzania inahitaji walimu 44,007 wa sayansi katika shule zake za sekondari. Waliopo kwa sasa ni walimu 17,059 na hivyo kuwepo na upungufu wa walimu 26,948 wakati vyuo vyote nchini vina uwezo wa kuhitimisha walimu 2,100 kwa masomo ya sayansi kila mwaka.
Kuhusu ujenzi wa nyumba za walimu, Rais Kikwete amesema kuwa kila kiongozi popote alipo ni lazima awe na mpango kabambe wa kuhimiza ujenzi wa nyumba za walimu na kuweka katika bajeti yake ya kila mwaka fedha za ujenzi huo.
“Kwenye ngazi ya taifa tumetoa Sh. Milioni 500 kwa kila Halmashauri nchini mwaka huu kama namna ya kuanza kukabiliana na tatizo hilo. Mwaka huu wa fedha, tunaanza kwa majaribio na Halmashauri 40 na ile ya Makete katika Mkoa huu wa Njombe ni mojawapo. Tutaendelea kutoka fedha kila mwaka huu kwa nia ya kumaliza tatizo hili.”
Ameongeza: “Sasa kwenye kila ngazi ya wilaya, kaeni chini mtafakari jinsi gani ya kuzitumia fedha hizo vizuri ili ziweze kujenga nyumba nyingi. Natambua kuwa kwenye sehemu nyingine shughuli hii itakuwa ngumu unapokuwa na madiwani ambao pia ni wakandarasi. Lakini hii tutakabiliana nalo.”
Ameelekeza kuwa mbali na kuzitumia fedha hizo vizuri, pia ametaka kila Halmashauri nchini kutenga fedha katika bajeti zao za ujenzi wa nyumba za walimu.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
24 Oktoba, 2013