Taarifa kwa vyombo vya Habari ya zamani
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, amemteua Bwana Samwel William Shelukindo kuwa Balozi na pia kuwa Msaidizi wa Rais (Diplomasia).
Kabla ya uteuzi huu, Bwana Samwel William Shelukindo alikuwa Mkuu wa Utawala kwenye Ubalozi wa Tanzania Mjini Addis Ababa Ethiopia.
Uteuzi huu unaanza tarehe 01 Oktoba, 2014.
“Mwisho”
Imetolewa na;
Premi Kibanga,
Mwandishi wa Habari wa Rais Msaidizi,
Ikulu – Dar es Salaam.
02 Oktoba, 2014
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais amteua Bw. Mwaseba kuwa Naibu Kamishna Mkuu TRA
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amemteua Bwana Lusekelo Mwaseba kuwa Naibu Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Taarifa iliyotolewa Ikulu, Dar Es Salaam, leo, Jumatano, Oktoba Mosi, 2014, na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, imesema kuwa uteuzi huo unaanza leo.
Kabla ya uteuzi wake, Bwana Mwaseba alikuwa Kamishna wa Uchunguzi katika Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
1 Oktoba, 2014.
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais ataja hatua saba za kupunguza msongamano wa magari Dar
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ametaja hatua saba ambazo Serikali yake imeanza kuzichukua ama inakusudia kuzichukua ili kukabiliana na msongamano wa magari katika Jiji la Dar Es Salaam.
Aidha, Rais Kikwete amesema kuwa msongamano wa magari ni ishara ya ubora wa maisha ya wananchi na ustawi wa Watanzania kwa sababu miaka 20 ama hata 10 iliyopita, Jiji la Dar Es Salaam halikuwa na msongamano. “Sasa kila mtu ana gari, naambiwa nyumba nyingine zina magari matatu – la baba, la mama na la watoto.”
Hata hivyo, Rais Kikwete ameonya kuwa, kama ilivyo katika miji yote mikubwa duniani, ni jambo lisilowezekana kumaliza tatizo la msongamano wa magari katikati ya Jiji la Dar Es Sslaam (Central Business District), hasa kwa kutilia maanani kuwa hakuna shaka kuwa watu wataendelea kununua magari na huwezi kuvunja nyumba zote katikati ya Jiji ili kupanua barabara.
Rais Kikwete ambaye alikuwa anazungumza leo, Jumatano, Oktoba Mosi, 2014, wakati akizindua rasmi Barabara kisasa ya Mwenge -Tegeta kwenye Barabara ya New Bagamoyo Road, amezitaja hatua hizo za kukabiliana na msongamano wa magari katika Mji wa Dar Es Salaam kuwa ni pamoja na ujenzi wa njia ya Mabasi Yaendayo Kasi (DART), ambao awamu yake ya kwanza inakaribia kukamilika pamoja na uanzishwaji wa huduma za kisasa za usafiri wa treni katika maeneo mbali mbali ya jiji hilo.
“DART inalenga kuwashawishi wananchi kupunguza matumizi ya magari binafsi na kutumia zaidi usafiri wa umma. Na hili litawezekana ikiwa mabasi yenyewe yatakuwa mazuri na huduma ikawa bora,” amesema Rais Kikwete na kuongeza:
“Usafiri wa treni ambao nausema mimi ni usafiri wa treni za kisasa zenye mabehewa ya kubeba abiria mijini siyo ule wa sasa ambako mabehewa ya kwenda Kigoma na Mwanza ndiyo yanatumika kubeba abiria kati ya Dar Es Salaam na Tabata.”
Hatua ya tatu ambayo Rais Kikwete ameitaja ni kujengwa kwa barabara za juu kwa juu (flyovers) katika maeneo ya TAZARA na Ubungo, yenye msongamano wa watu wengi, na ujenzi wa barabara 12 za kuzunguka Jiji (Ring Roads) na nyingine za kuunganisha maeneo ya jiji hilo kama vile upanuzi wa Barabara ya Uhuru kuwa njia mbili kila upande badala ya njia moja ya sasa.
Aidha, Rais Kikwete amezitaja hatua nyingine kuwa ni ujenzi wa Daraja jipya la Salender ambalo litapitia baharini, usafiri wa kivuko kipya kutoka Bagamoyo hadi Dar Es Salaam na ujenzi wa miji midogo ya kisasa inayojitegemea katika maeneo ya Kigamboni, Mabwepande na Luguruni.
Rais Kikwete amesema kuwa baadhi ya hatua hizo zinazochukuliwa ama zinalengwa kuchukuliwa na Serikali zimekuwa zinakabiliwa na siasa nyingi za kupinga miradi hiyo kutoka kwa baadhi ya viongozi na wanasiasa nchini ambao amewaita “watu wenye upeo mfupi”.
“Kiongozi anayehubiri upinzani wa maendeleo kwa sababu za siasa ni kiongozi mbovu. Huyu ni mtu mwenye uongozi mbovu, na ana upeo mfupi, usiiona mbali, kwa sababu kiongozi mzuri hawezi kuhubiri siasa za kupinga maendeleo ya wananchi wake.”
Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
1 Oktoba, 2014.
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais azindua Barabara ya Mwenge-Tegeta
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete leo, Jumatano, Oktoba Mosi, 2014, amezindua rasmi Barabara ya Kisasa ya Mwenge-Tegeta ambayo ni sehemu ya Barabara ya New Bagamoyo Road, mjini Dar Es Salaam.
Barabara hiyo yenye urefu wa kilomita 12.9 imegharimu kiasi cha Sh. bilioni 77.85, fedha ambazo zimetolewa na Serikali ya Japan kupitia Shirika lake la Maendeleo ya Kimataifa la JICA. Serikali ya Tanzania imechangia asilimia 7.64 katika gharama za ujenzi wa Barabara hiyo.
Rais Kikwete amefanya uzinduzi huo katika eneo la Makutano ya Kambi ya Jeshi ya Lugalo na Barabara ya Kawe katika sherehe iliyoshuhudiwa na mamia ya wananchi. Alikuwa ni Rais Kikwete ambaye aliweke jiwe la msingi la ujenzi wa Barabara hiyo Aprili 4, mwaka 2011.
Barabara hiyo ni awamu ya kwanza ya ujenzi wa Barabara itokayo Makutano ya Barabara ya Kawawa, Kinondoni hadi Tegeta. Ujenzi wa awamu ya pili wa kilomita 4.3 kati ya Mwenge na Makutano ya Barabara ya Kawawa, unatarajiwa kuanza wakati wowote baada ya mipango yote ya ujenzi huo kukamilika.
Barabara hiyo ya Mwenge-Tegeta inalenga kupunguza msongamano wa magari katika eneo la kaskazini mwa Dar Es Salaam na pia ni sehemu ya bararaba kuu inayounganisha Jiji la Dar Es Salaam na Mkoa wa Pwani, kupitia Wilaya ya Bagamoyo, na kuunganisha mikoa hiyo na mikoa ya kaskazini mwa Tanzania.
Akizungumza kwenye sherehe hiyo ya uzinduzi wa Barabara hiyo iliyojengwa na Kampuni ya Konoike kutoka pia Japan, Balozi wa Japan katika Tanzania, Mheshimiwa Masaki Okada amesema kuwa ujenzi wa barabara hiyo ulichelewa kukamilika mwaka jana, kama ilivyopangwa, kwa sababu ya wajenzi kukabiliwa na matatizo ya mafuriko makubwa yaliyotokea mwaka 2011.
Mbali na kutaja misaada mingi katika sekta ya miundombinu na hasa barabara ambayo imefadhiliwa na Japan katika miaka mingi iliyopita, Mheshimiwa Okada amesema kuwa Japan sasa iko tayari kuanza ujenzi wa Barabara ya Gerezani-Bendera Tatu, Dar Es Salaam, utakaogharimu Sh. bilioni 18.5, msaada kutoka Japan.
Aidha, Balozi huyo amewaomba radhi Watanzania kutokana na ucheleweshaji wa kuanza kwa ujenzi wa barabara ya juu kwa juu –flyover- katika eneo la TAZARA, Dar Es Salaam, ambao utagharimu Sh. bilioni 53 ambazo zinatolewa na Serikali ya Japan kupitia Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la JICA.
Amesema kuwa ujenzi huo umechelewa kwa sababu makandarasi wa Kijapan ambao walitakiwa kujenga flyover hiyo wanakabiliwa na kazi nyingi huko nyumbani za kujenga upya miundombinu iliyoharibiwa na tetemeko na kimbunga cha Great East Japan Earthquake and Tsunami, kilichotokea Machi 2011 na kusababisha uharibifu mkubwa mno.
Aidha, amesema kuwa wajenzi hao pia wanalazimika kufanya kazi usiku na mchana ili kukamilisha miundombinu ya kuiwezesha Japan kuandaa Michezo ya Olimpiki ambayo imepangwa kufanyika nchini humo mwaka 2020.
Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
1 Oktoba, 2014.
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Ushirikishi wa Mataifa mbalimbali duniani katika maendeleo na utatuzi wa matatizo yanayozikumba nchi hizo, ndiyo njia kuu na ya kipekee katika karne ya leo ya kukabiliana na changamoto zake.
Rais Jakaya Mrisho Kikwete amesema hayo jana tarehe 26 Septemba, 2014 katika Chuo Kikuu cha Rutgers, katika mji wa New Jersey, nchini Marekani.
"Mataizo mengi yanayoikabili duniani kwa sasa yana sura ya kimataifa, leo hii hakuna tatizo la nchi moja, sababu utandawazi umeinua majukumu ya watendaji mbalimbali na kuyafanya ya kimataifa" ameongeza.
Rais Kikwete amealikwa Chuoni hapo kutoa mhadhara kuhusu umuhimu wa ushiriki wa kimataifa katika utatuzi wa matatizo na changamoto za kimataifa, pamoja na kushuhudia kutiwa saini kwa Mkataba wa Makubaliano ya Ushirikiano kati ya Chuo Kikuu cha Rutgers na Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).
Akitolea mfano suala hili, Rais ameeleza jinsi matatizo na changamoto mbalimbali zinavyotatuliwa kwa pamoja na Jumuiya ya kimataifa katika nyanja za Afya, Uchumi, Tabia nchi, Siasa na Kijamii.
Rais pia ametolea mfano utekelezaji wa Malengo ya Milenia (MDGs) na kusema utekelezaji wa MDGs umekuwa mfano wa jinsi gani ubia wa kimataifa una mchango mkubwa katika utatuzi wa changamoto mbalimbali duniani. Ushiriki huu ni ule wa Serikali mbalimbali, Mashirika ya Kimataifa, Mashirika yasiyo ya kimataifa na ya kijamii.
"Tanzania imefaidika sana katika Nyanja zote za Maendeleo, imeshirikiana na wabia mbalimbali wa Maendeleo kama Shirika la Maendeleo la Marekani (USAID), Global Fund, Bill and Melinda Gates, Clinton Foundation na mengineyo.
Rais amesema ni katika mantiki hiyo hiyo ya ushirikiano ambapo vyuo vikuu vikishirikiana, vitafaidika katika utafiti, kubadilishana uzoefu, elimu, sayansi na teknolijia. Chini ya ushirikiano huu kati ya Rutgers na UDOM vitashirikiana katika kubadilishana wanafunzi na walimu katika jitihada za kuboresha elimu, ujuzi na tafiti mbalimbali.
Chuo cha Rutgers pia tayari kina ushirikiano na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na mashirika mbalimbali kwa kubadilishana wanafunzi.
Rais Kikwete amemaliza ziara yake ya kikazi nchini Marekani ambapo anatarajia kuondoka Marekani Tarehe 28 Septemba, 2014 kurejea jijini Dar es Salaam.
..........Mwisho..........
Imetolewa na;
Premi Kibanga,
Mwandishi wa Habari wa Rais Msaidizi
New York - Marekani
27 Septemba, 2014
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Tanzania iko tayari kushirikiana na wanachama wote wa Umoja wa Mataifa (UN) kufikia makubaliano ya Malengo ya Maendeleo mapya baada ya Malengo ya Milenia (MDGs) ya sasa kufikia mwisho wake ifikapo mwaka 2015.
Rais Kikwete amesema hayo wakati akihutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA) jana tarehe 25 Septemba, 2014 jijini New York, Marekani.
Agenda ya kikao cha Baraza Kuu la UN mwaka huu ni "Delivering on and Implementing a Transformative Post 2015 Development Agenda" ambapo amesema anatarajia majadiliano yatatoa nafasi kwa nchi kupanga mipango ya baadae kwa manufaa ya vizazi vijavyo.
"Tutumie muda huu kuendeleza mafanikio na mafunzo kutoka nchi mbalimbali na pia tujifunze kutokana na changamoto za kushindwa kufikia malengo ya Milenia, na kuzitumia kama viashiria vya ajenda ya Maendeleo baada ya Mwaka 2015". Rais amesisitiza.
Rais ameiasa dunia kuwa wakati huu ambapo inajadili ajenda ya Maendeleo baada ya Mwaka 2015, isisahau malengo ya milenia ambayo hayajakamilika na kuyaweka vizuri katika ajenda mpya ya baada ya malengo ya sasa kufikia tamati mwaka ujao.
Pamoja na kwamba dunia inazungumzia ajenda mpya ya baada ya mwaka ujayo amezitaka nchi kuhakikisha na kuongeza kasi ya utekelezaji katika kipindi cha siku 461 zilizobakia kufikia mwisho.
Pamoja na umuhimu wa MDGs Rais Kikwete amezungumzia suala la Tabia Nchi na kuzitaka nchi zote duniani kukusanya nguvu katika suala hili ili kuiokoa dunia kutokana na majanga ya Tabia Nchi.
Masuala mengine ni kuhusu Mageuzi katika UN, ambapo Rais Kikwete amesema kusuasua kwa mazungumzo ya kuleta Mageuzi kunakatisha tamaa na kuomba yafufuliwe. Masuala mengine ni kuhusu hali ya usalama duniani ambapo ugaidi umechukua mkondo wa kutishia amani duniani na kuzitaka nchi zote kupambana na ugaidi.
Masuala mengine ni pamoja na suala la muda mrefu la uhasama baina ya Israeli na Palestina ambalo limedumu kwa muda mrefu hivyo kuutaka Umoja wa Mataifa kulitafutia suluhu ya kudumu.
Suala lingine ni la Sahara Magharibi ambalo pia limedumu kwa muda mrefu bila ufumbuzi, suala la vikwazo kwa nchi ya Cuba ambavyo navyo vimekuwepo kwa muda mrefu sana, hivyo kuutaka Umoja wa Mataifa kutafuta utatuzi wa kudumu.
Rais Kikwete pia amezungumzia ugonjwa wa Ebola ambao tayari umeua watu wapatao 2,400 na bado haujadhibitiwa. Rais amesema ugonjwa wa Ebola ni tishio kwa nchi zilizoathirika, jirani na dunia kwa ujumla.
"Juhudi za pamoja zinahitajika kwani ndiyo njia sahihi, naamini kuna teknolojia na rasilimali za utaalamu na fedha ambavyo kwa pamoja,tunaweza kushinda tishio la ugonjwa huu" amesema.
Rais amezitaka juhudi zaidi zifanyike katika kuudhibiti, kwa kuwa ugonjwa huu ni hatari na unaweza kuwa janga la dunia.
...........Mwisho..............
Imetolewa na;
Premi kibanga,
Mwandishi wa Habari wa Rais Msaidizi,
New York -Marekani
26 Septemba, 2015
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Tanzania inatarajiwa kupata sheria ya Uhuru wa kupata Habari ifikapo Mwezi Februari, Mwaka 2015.
Rais Jakaya Mrisho Kikwete amesema hayo jana tarehe 24 Septemba, 2014 jijini London alipokuwa mmoja wa wazungumzaji katika mkutano unaohusu Uwazi na ushirikiano kati ya serikali na jamii (Open Government Partnership-OGP).
Rais Kikwete amesema, rasimu ya muswaada wa Uhuru wa kupata Habari uko katika hatua ya mwisho ambapo wadau mbalimbali wanashauriana na kutoa maoni tayari kupelekwa bungeni.
"Muswaada huo unatarajiwa kusomwa kwa mara ya kwanza Mwezi Novemba mwaka huu, na kufikia Mwezi Februari mwakani sheria mpya ya kupata Habari itakua tayari" amesema.
Mwezi Oktoba Mwaka 2013 katika mkutano wa OGP jijini London, Rais Kikwete alitangaza nia na ujasiri ulioko Serikalini kuhakikisha kuwa Tanzania inakuwa na sheria ya Uhuru wa Habari.
Rais amesema, Uhuru wa Habari ni muhimu kwa wananchi kwa sababu "Ni haki yao ya msingi na kuwawezesha wananchi kufanya maamuzi yanayofaa kuhusu maisha yao" na kuongeza kuwa "Ni muhimu wananchi kujua serikali yao inafanya nini kwa niaba yao" amesisitiza.
Akizungumza katika mkutano huo, Rais Barack Obama wa Marekani amesema OGP ni ubia kati ya Serikali na Wananchi wake. "Hakuna nchi yenye
majibu yote kwa suala hili la Uwazi katika Serikali, tunahitaji kujifunza kutoka kwa kila mmoja" na kuongeza kuwa ni jambo jema kwa serikali kuimarisha ushirikiano na taasisi za kijamii.
Viongozi wengine waliochangia katika mkutano huo ni pamoja na Indonesia , Afrika ya Kusini na Ufaransa. Rais Kikwete yuko jijini New York kuhudhuria Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UN) ambapo pamoja na mambo mengine anahudhuria mikutano mingine yenye maslahi kwa Tanzania.
Wakati huo huo, Rais Kikwete amekutana na Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza Bwana Gordon Brown ambaye pia ni Mjumbe Maalum wa UN kuhusu Elimu ambaye amemshukuru na kumsifu Rais Kikwete kwa kusimamia Elimu nchini Tanzania.
"Tunataka kukusaidia kufikia malengo ya milenia, tunajivunia mafanikio makubwa uliyoyapata katika elimu" amesema Bw. Brown katika kikao hicho ambacho kimehudhuriwa na wabia wa maendeleo ambao kwa pamoja wanataka kusaidia Serikali katika kuleta maendeleo na kunyanyua zaidi kiwango cha Elimu nchini.
Wabia hao ni pamoja na Shirika la Global Education, Shirika la Watoto Duniani (UNICEF), Shirika la Misaada la Marekani (USAID), wawakilishi wa Serikali ya Uingereza na Benki ya Dunia.
Wengine ni kutoka Global Business Coalition na Dubai CARES ambao kwa pamoja wanataka kuinua kiwango cha Elimu ya Msingi na Sekondari kwa kusaidia na kuchangia ili kuboresha zaidi na kuinua kiwango cha elimu nchini.
Tarehe 25 Septemba, 2014, Rais Kikwete atahutubia Baraza la Umoja wa Mataifa ambapo hotuba hiyo itaonekana moja kwa moja kupitia UN webcast.
......Mwisho......
Imetolewa na;
Premi Kibanga,
Mwandishi wa Habari wa Rais Msaidizi,
New York - Marekani
25 Septemba, 2014
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Mabadiliko ya Tabia Nchi duniani yanahatarisha Uhai na Maendeleo ya Binadamu, ikiwemo kurudisha nyuma au kufuta kabisa Maendeleo ya Kiuchumi na Kijamii yaliyokwishapatikana.
Rais Jakaya Mrisho Kikwete amesema hayo jana tarehe 23 Septemba, 2014, jijini New York , Marekani wakati akihutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, ambapo amewakilisha msimamo wa bara zima la Afrika kuhusu suala zima la Tabia Nchi.
Rais Kikwete ametahadharisha kuwa kama hali iliyopo sasa hivi haitashughulikiwa, madhara yake yatakuwa makubwa hivyo dunia inapaswa kuchukua hatua za kukabiliana na Tabia Nchi.
Rais Kikwete anasema, Afrika inaamini kuwa hali hii inaweza kubadilishwa kwa sababu wazalishaji wakubwa wa hewa ya ukaa ni nchi zilizoendelea ambazo zina teknolijia, ujuzi wa kiufundi, na uwezo wa kifedha kuchukua hatua zinazostahili.
"Sote tunajua kuwa hiki ndicho kimetamkwa na Mkataba wa Kyoto na itifaki zak , na tunachosisitiza hapa ni kuwa, makubaliano haya yaheshimiwe na kutekelezwa" Amesema.
Pamoja na mambo mengine, Mkataba wa Kyoto umezitaka nchi ambazo zinazalisha kwa wingi hewa ya ukaa, kuchukua majukumu zaidi ya kupambana na athari za Tabia Nchi. Katika utaratibu huo, nchi za Afrika zinachangia kiasi kidogo sana cha hewa ya ukaa na uchafuzi wa Mazingira kwa ujumla.
Mkutano huo kuhusu Tabia Nchi umeongozwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) Bw. Ban Ki Moon.
Mapema akihutubia Baraza la UN Rais Baraka Obama wa Marekani amesema kuwa tishio la Tabia Nchi ni la dunia nzima na kuelezea kuwa madhara ya Tabia Nchi yanaongezeka haraka kuliko hata hatua zake za kukabiliana nayo na hivyo dunia inatakiwa kuchukua hatua za haraka na kuahidi kuwa Marekani itazisaidia nchi zinazoendelea kupambana na athari za mabadiliko ya hali ya hewa.
Viongozi wakuu duniani wamekwisha wasili jijini New York Marekani ambapo Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa litaanza kusikiliza hotuba na misimamo ya nchi wanachama kuanzia leo tarehe 24 - 27 Septemba, 2014 na mijadala inatarajiwa kuanzia tarehe 29 Septemba.
Masuala makubwa yatakayojadiliwa katika kikao cha Baraza Kuu la UN mwaka huu ni pamoja na kuzungumzia changamoto mbalimbali duniani zikiwemo za umaskini, njaa, usalama na mabadiliko ya Tabia Nchi.
Rais Kikwete anatarajiwa kuhutubia Baraza hilo tarehe 25 Septemba,2014 kati ya Saa 11 hadi Saa 1 na nusu usiku, (Tanzania iko mbele kwa masaa 7). Hotuba hiyo inaweza kuonekana moja kwa moja kupitia UN webcast.
----Mwisho----
Imetolewa na;
Premi Kibanga,
Mwandishi wa Habari wa Rais Msaidizi,
New York – Marekani
24 Septemba, 2014
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais Jakaya Mrisho Kikwete jana tarehe 22 Septemba, 2014 aliongoza mikutano miwili mikubwa ya viongozi wa Afrika kuandaa agenda ya pamoja itakayo wasilishwa kwenye mkutano wa Umoja wa Mataifa (UN) kuhusu Tabia Nchi utakaofanyika leo tarehe 23 Septemba, 2014, chini ya uenyekiti wa Katibu Mkuu wa UN Bw. Ban Ki Moon.
Rais Kikwete ndiye atawakilisha msimamo na agenda ya Afrika kwa niaba ya viongozi wenzake wote wa Afrika.
Rais Kikwete ni Mratibu wa Kamati ya Viongozi wakuu wa Serikali za Afrika kuhusu Tabia Nchi (Coordinator of the Committee of African Heads of State and Government on Climate Change (CAHOSCC) ambapo viongozi wameandaa hoja kuu ambazo zinatarajiwa kuwasilishwa kwenye mkutano huo wa UN.
Afrika inatarajia kuhamasisha UN, nchi zilizoendelea na dunia kwa ujumla kuchukua hatua zaidi za kupunguza athari za Tabia Nchi hasa katika bara la Afrika ambalo linaathirika zaidi hata pamoja na kuwa na mchango mdogo katika uchafuzi wa Mazingira.
Mkutano wa UN kuhusu Tabia Nchi unatazamiwa kuwa mkubwa zaidi kuwahi kufanyika kuhusu Mabadiliko ya Tabia Nchi Duniani , ambapo Afrika itapata nafasi ya kuwasilisha hoja zake na ujumbe mzito ambao unatarajiwa kuwa utaleta mabadiliko na mtazamo mpya katika suala hili la Tabia nchi.
Afrika inakabiliwa na changamoto nyingi za Tabia nchi ambazo pia zina athari kubwa katika uchumi wa nchi hizo.
"Afrika inatakiwa kuwa wazi kuhusu Tabia nchi, kuwe na ujumbe wa kisiasa na Afrika inatakiwa ipate haki yake kutokana na athari kubwa inayolikumba bara la Afrika kutokana na suala la Tabia Nchi"
Rais Kikwete amesema kwenye mkutano "Afrika inatoa asilimia 3 tu ya hewa ya ukaa duniani, lakini inachukua tani zipatazo bilioni 60 za gesi hiyo" amesema Rais Kikwete na kuongeza kuwa “suala hili lazima liziamshe nchi za Afrika na kutafuta njia za kukabiliana nalo kwani ni suala linalotishia uhai” .
Rais Jakaya Mrisho Kikwete yupo Nchini Marekani kuhudhuria mikutano mbalimbali ya viongozi wa Dunia ikiwemo Baraza Kuu la UN ambapo anatarajiwa kuhutubia Baraza hilo tarehe 25 Septemba, 2014, mchana.
-------Mwisho--------
Imetolewa na;
Premi Kibanga,
Mwandishi wa Habari wa Rais Msaidizi,
New York - Marekani
23 Septemba, 2014
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ameondoka nchini usiku wa jana, Jumatatu, Septemba 15, 2014, kuanza ziara ya wiki mbili katika Marekani ambapo atahutubia Mkutano wa 69 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UN General Assembly) New York.
Mbali na kuhutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York, Rais Kikwete pia atahudhuria mikutano muhimu katika mji mkuu wa Marekani, Washington, D.C.
Mjini New York, Rais Kikwete atashiriki katika mikutano mikubwa zaidi ya 10 ikiwa ni pamoja na kuhutubia Baraza Kuu wakati wa Majadiliano ya Jumla ( General Debate) yaliyopangwa kufanyika Septemba 24 hadi 27 na Septemba 29 hadi Oktoba Mosi, mwaka huu, 2014.
Rais Kikwete amepangwa kuwa kiongozi wa 12 duniani kuhutubia Baraza hilo mchana wa Alhamisi ijayo, Septemba 25, 2014. Mkutano wa 69 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa utaanza Septemba 16 hadi Desemba 24, mwaka huu, 2014.
Miongoni mwa mikutano mingine muhimu ambayo Rais Kikwete atashiriki ni pamoja na kuwa mwenyekiti wa Kamati ya Wakuu wa Nchi Wanachama wa Umoja wa Afrika (AU) Kuhusu Mazingira (CAHOSC) na Mkutano wa Wakuu wa Nchi Kuhusu Mazingira ulioitishwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Mheshimiwa Ban Ki Moon.
Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
16 Septemba , 2014.
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais Kikwete akagua utayari wa Tanzania kukabiliana na Ebola
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete leo, Jumanne, Septemba 9, 2014, amekagua huduma na vifaa, pamoja na maandalizi ya kukabiliana na ugonjwa hatari wa Ebola, ili kujiridhisha na utayari wa Tanzania dhidi ya tishio kubwa la ugonjwa huo.
Mara tu baada ya kutua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar Es Salaam, akitokea Dodoma, Rais Kikwete amekwenda moja kwa moja kukagua vifaa, huduma na maandalizi ya jinsi Tanzania inavyojiandaa kubaini na kushughulikia wagonjwa wa Ebola, ambao wanaweza kupitia kwenye Uwanja huo.
Rais Kikwete ameonyeshwa Kamera na Mashine za Kuchanganua Picha (Scanners) ambazo tayari zimefungwa kwenye eneo ambalo abiria hulitumia kuingilia katika Uwanja huo.
Rais Kikwete ameelekeza kuboreshwa kwa taratibu na huduma ili kuhakikisha kuwa wasafiri hawapotezi muda mwingi kwa kujipanga foleni ili waweze kukaguliwa.
“Ugonjwa huo usiwe ni kikwazo kwa abiria kupita kwenye Uwanja wetu huu. Tutengeneze mfumo na utaratibu ambao unawezesha wasafiri kupita katika eneo hilo kama ambavyo imekuwa siku zote, lakini wakati huo mashine zetu zikiwa tayari kugundua haraka ni msafiri yupi ana matatizo ama dalili za ugonjwa huo.”
Amesisitiza Rais Kikwete: “Tusitengeneze mfumo ambao unazalisha msongamano ndani ya Uwanja wa Ndege. Napenda kuona kuwa wasafiri wanaendelea kuutumia Uwanja wetu bila msongamano na ucheleweshwaji wowote. Abiria wasipate taabu kwa sababu ya Ebola.”
Mpaka sasa hakuna hata kesi moja ya Ebola imethibitishwa katika Tanzania, lakini maandalizi ya kiwango cha juu yamekuwa yanafanywa, ili kujenga utayari wa kukabiliana na tishio la ugonjwa huo ambao unaendelea kuua maelfu ya watu katika nchi za Afrika Magharibi za Liberia, Sierra Leone, Guinea, Senegal na Nigeria pamoja na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Aidha, ugonjwa Ebola haujapata kuingia katika Tanzania katika historia ya ugonjwa huo ambao asili yake ni DRC, ambako mgonjwa wa kwanza alipatikana eneo la Mto Ebola.
Baada ya kumaliza ukaguzi wake kwenye Uwanja wa Ndege, Rais Kikwete ametembea, akaona na akaelezwa kuhusu maandalizi ya kukabiliana na ugonjwa huo kwenye Kituo Kikuu cha Kuwatenga na Kuwahudumia Wagonjwa wa Ebola (Ebola Isolation Centre) katika Mkoa wa Dar Es salaam kwenye Hospitali ya Wilaya ya Temeke.
“Nimeanzia Uwanja wa Ndege. Nia yangu ni kuona utayari wetu katika kukabiliana na ugonjwa hatari wa Ebola, kuona jinsi gani mifumo yetu inavyofanya kazi, kwa ujumla wake, kukabiliana na janga hili hatari sana,” amesema Rais Kikwete ambaye amefuatana na Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Mheshimiwa Seif Rashid na Mkuu wa Mkoa wa Dar Es Salaam, Said Mecky Sadiq.
Baada ya kukagua huduma mbali mbali kwenye Kituo hicho ikiwa ni pamoja na kuona wodi zinazoandaliwa kwa ajili ya wagonjwa na kuelezwa hatua zinachukuliwa, Rais Kikwete ametoa maagizo kadhaa ikiwa ni pamoja na kutengenezwa mazingira bora zaidi na eneo zuri la watumishi wa afya wa Kituo hicho, kuhakikisha kuwa mfumo wa maji unafanya kazi vizuri na kukarabati vyoo na bafu.
Amesisitiza Rais Kikwete: “Nataka kuona kituo chenye viwango vya kuweza kuhudumia watu wa tamaduni zote na watu wa hadhi zote – kuanzia aliyevaa lubega hadi kwa yule mwenye suti ya sehemu tatu. Aidha, wekeni sehemu ya kupika chakula kwa ajili ya wagonjwa.”
Kwenye Kituo hicho ambacho awali kilijengwa kama Kituo cha Kupokea na Kuhudumiwa Wagonjwa wa ugonjwa wa Kipindupindu, Rais Kikwete ameelezwa kuwa kila mgonjwa mmoja wa Ebola ataweza kuhudumiwa na wafanyakazi wanne wa sekta ya afya, ambao nguo na magauni yao yatachomwa moto kila wanapomaliza kumhudumia mgonjwa.
Aidha, ameelezwa kuwa tayari wanataaluma 1,200 wamepewa mafunzo ya kuhudumia mgonjwa wa Ebola katika Mkoa wa Dar Es Salaam, kwamba vifaa vyenye thamani ya Sh. milioni 119 tayari vimenunuliwa na kuwa daktari mmoja ametumwa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo (DRC) kupata uzoefu wa kukabiliana na ugonjwa huo.
Waziri Rashid amemwambia Rais Kikwete kuwa kitaifa maandalizi yanaendelea na kuwa mpaka sasa Kamera na Mashine za Kuchanganua Picha tayari zimefungwa katika Viwanja vya Ndege vya Dar Es salaam, Zanzibar, Kilimanjaro na Mwanza na kwenye vituo vya mipaka ya Tanzania na nchi za Uganda, Rwanda, Burundi na Zambia.
Aidha, Waziri amesema kuwa maagizo yametolewa kwa hospitali zote nchini kuwa na vyumba maalum vya kuwatenga na kuwahudumia wagonjwa wa Ebola.
Wiki iliyopita, akizungumza na viongozi na wazee wa Mkoa wa Dodoma kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Chuo cha Mipango, Dodoma, Rais Kikwete ambaye alikuwa amemaliza ziara ya mkoa huo, alizungumzia tishio la ugonjwa huo na hatua zinazochukuliwa na Serikali kukabiliana nalo.
Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
9 Septemba , 2014.
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete leo, Jumatano, Septemba 10, 2014, amefanya mazungumzo ya faragha na mgeni wake, Rais Yoweri Kaguta Museveni wa Uganda, Ikulu, Dar Es salaam.
Rais museveni ambaye alikuwa kwenye ziara ya siku moja ya kikazi katika Tanzania, aliwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere kiasi cha saa 4 na dakika 10 asubuhi na kupokelewa na mwenyeji wake, Rais Kikwete.
Mazungumzo kati ya viongozi hao wawili, yalianza saa tano unusu asubuhi na kuchukua kiasi cha saa moja na dakika 15.
Rais Museveni aliondoka Ikulu baada ya chakula cha mchana na aliagana na mwenyeji wake, Rais Kikwete kwenye Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere, Dar Es salaam, kabla ya kupanda ndege yake kurejea nyumbani.
Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
10 Septemba , 2014.
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ameelezea huzuni na masikitiko yake makubwa kufuatia vifo vya watu 36 vilivyotokea katika ajali ya barabarani Wilayani Butiama, Mkoa wa Mara, ambako pia watu 79 wameuamia, baadhi yao vibaya.
Mara baada ya kupata taarifa hiyo iliyotokea leo, Ijumaa, Septemba 5, 2014, Rais Kikwete ambaye yuko katika ziara ya kikazi ya siku tatu Mkoani Arusha, amemtumia salamu za rambirambi Mkuu wa Mkoa wa Mara, akielezea huzuni na masikitiko yake .
“Nimehuzunishwa mno na kusikitishwa sana na taarifa hii ya kutisha ya vifo vya watu 36 ambavyo vimetokea leo wakati mabasi mawili yalipogongana ana kwa ana katika eneo la Sabasaba, Wilaya ya Butiama, mkoani mwako. Nakutumia salamu zangu za rambirambi pamoja na wananchi wote wa Mkoa wa Mara kuomboleza vifo vya Watanzania wenzetu ambao wameaga dunia yetu ghafla katika ajali hii,” amesema Rais Kikwete na kuongeza:
“Nakuomba uwafikishie wafiwa wote pole zangu nyingi sana, ukiwajulisha kuwa niko nao katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo. Aidha, napenda uwajulishe kuwa naungana nao kumwomba Mwenyezi Mungu aziweke pema roho za marehemu.”
“Aidha, naungana nanyi wana-Mara kuwapa mkono wa pole na kuwaombea wote walioumia katika ajali hiyo waweze kupona haraka ili wapate nafasi ya kuendelea na shughuli zao za maendeleo.”
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
5 Septemba, 2014
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Jeshi la Wananchi ni Kimbilio la Wananchi - Rais
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (TPDF) ni kimbilio kuu la Watanzania wote kutokana na mahusiano mazuri ambayo yamekuwepo kati ya Jeshi hilo na wananchi katika miaka 50 iliyopita.
Aidha, Rais Kikwete amesema kuwa Watanzania wanayo imani na matumaini makubwa kuwa Jeshi hilo litaendelea kutii viapo vyake, kuilinda Katiba ya nchi na kuwalinda wananchi wenyewe wakati wote na kusaidiana nao wakati wa majanga.
Rais Kikwete ameyasema hayo leo, Ijumaa, Septemba 5, 2014, wakati alipozungumza na maofisa na wapiganaji wa Jeshi hilo baada ya kushuhudia Zoezi la Medani kuadhimisha miaka 50 ya Jeshi hilo katika eneo la Langururusu, Wilaya ya Monduli, Mkoa wa Arusha.
Katika Zoezi la Medani, maelfu ya wanapiganaji wa TPDF, wameshiriki katika Operesheni Maliza Matata ambako wapiganaji hao wameikomboa sehemu ya ardhi ya nchi yao ya Waungwana ambayo ilikuwa imetekwa na askari wa nchi jirani ya Matata.
Matata ilivamia eneo la Waungwana baada ya nchi hiyo ya Waungwana kutetea maslahi ya nchi nyingine jirani ya Mavuno ambayo husumbuliwa mno na mara kwa mara na nchi ya Matata kwa sababu ya kuwa na utajiri mkubwa na raslimali nyingi.
Katika hotuba yake, Rais Kikwete amewaambia mamia ya askari na wananchi waliohudhuria Sherehe hizo za miaka 50 ya Jeshi: “Wananchi wa Tanzania wanayo mapenzi makubwa na Jeshi letu, maana hili ni Jeshi lao na linatokana na wao. Wameishi na Jeshi hili vizuri na wamenufaika na huduma za kijamii zinazotolewa na Jeshi lao.”
Rais amewaambia askari hao: “Kutokana na hali hiyo, wananchi wanayo matumaini makubwa kuwa mtaendelea kutii viapo vyenu, mtailinda Katiba ya nchi na mtaendelea kuwalinda wakati wote na kusaidiana nao wakati wa majanga. Nyinyi ni kimbilio la Watanzania wote.”
Rais Kikwete amesema kuwa kazi kubwa na nzuri ambayo imefanywa na TPDF imemfanya yeye kama Amiri Jeshi Mkuu kutembea kifua mbele iwe ndani ama nje ya nchi.
“Ninapotembelea mara kwa mara vikosi vyenu na kujionea kazi zenu na utayari wenu kivita, hujisikia vizuri kama Amiri Jeshi Mkuu wenu, natembea kifua mbele kote niendako, maana mnanipa raha ndani ya nchi na mnanipa heshima kubwa nje ya nchi. Nina imani kuwa kwa sasa Jeshi letu lipo katika kiwango cha juu cha utayari kivita kwa vifaa na watu.”
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
5 Septemba, 2014
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais Kikwete: Haya ndiyo mafanikio ya JWTZ
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, amelisifia Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kwa kutaja mafanikio yake makuu katika miaka 50 ya uhai wake, akisisitiza kuwa ni Jeshi imara na bora linaongozwa na misingi ya uzalendo, utii na nidhamu ya hali ya juu.
Rais pia amesema kuwa kwa amani, utulivu na usalama ambao umekuwepo katika Tanzania kwa miaka 50 iliyopita umechangiwa sana na Jeshi la Wananchi wa Tanzania. JWTZ lilizaliwa Septemba Mosi, 1964.
Akizungumza na maelfu ya wapiganaji na wananchi kwenye Sherehe za Miaka 50 ya Jeshi hilo kwenye eneo la Langururusu, Wilaya ya Monduli, Mkoa wa Arusha leo, Ijumaa, Septemba 5, 2014, Rais Kikwete amesema kuwa uzalendo na nidhamu ni mambo ambayo yanalitofautisha JWTZ na majeshi mengine mengi duniani mambo yaliyoyashinda majeshi ya nchi nyingi hususan katika Afrika.
Rais Kikwete alikuwa anazungumza baada ya kushuhudia Zoezi la Medani la Operesheni Maliza Matata ambalo limeshirikisha mamia ya wapiganaji na maofisa ambako zimetumika silaha za moto kwa njia ya ndege za kivita, vifaru, makombora na risasi.
Zoezi hilo limeshirikisha maofisa na askari kutoka Makao Mkuu ya Jeshi, Kamandi ya Majeshi ya Nchi Kavu, Kamandi ya Jeshi la Anga, Kamandi ya Jeshi la Maji, Jeshi la Kujenga Taifa na Jeshi la Akiba.
Rais Kikwete amewaambia wapiganaji nao na maofisa wao ambao walikuwa ni pamoja na wakuu waliopita wa Jeshi hilo kuwa moja ya mafanikio makubwa ya Jeshi hilo ni kusimamia na kutekeleza majukumu yake iwe ni wakati wa amani ama wakati wa vita, tena kwa weledi mkubwa.
Rais Kikwete ameyataja mafanikio machache ya Jeshi hilo kuwa ni pamoja na kushiriki na kufanikisha harakati za Ukombozi Barani Afrika kwa kufundisha majeshi ya Vyama vya Ukombozi, na kushiriki moja kwa moja kwenye vita vya Ukombozi mwa Kusini mwa Bara la Afrika katika Mozambique, Angola, Zimbabwe, Namibia na Afrika Kusini.
Rais pia amesema kuwa JWTZ limelinda uhuru na mipaka ya nchi kwa vitendo kwa kuyapiga majeshi ya uvamizi ya Idd Amin na kuweka historia kwa kuwa Jeshi lililopigana na jeshi la nchi nyingine na kuliangamiza kabisa.
Mheshimiwa Kikwete pia amesema kuwa JWTZ limeshiriki kikamilifu kwenye operesheni za kulinda amani katika nchi za Liberia, Darfur (Sudan), Lebanon, Ivory Coast, Visiwa vya Shelisheli, Visiwa vya Comoro na hivi karibuni kuyapiga na kuyatoa katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) majeshi ya waasi wa M23.
Rais pia amesema kuwa JWTZ limeshiriki kikamilifu shughuli za uokoaji na hususan katika majanga ya ajali kama za Meli za MV Bukoba na kule Zanzibar na kwenye majanga ya mafuriko katika sehemu mbali mbali nchini.
Rais amesema kuwa mamilioni ya Watanzania wamenufaishwa na huduma za elimu na afya ambazo Jeshi hilo linazitoa kupitia shule na hospitali zinazomilikiwa na Jeshi na pia limeshiriki katika kukuza elimu ya kujitegemea kwa vijana kupitia Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU).
Rais Kikwete amesema kuwa katika miaka yote 50, JWTZ halijawahi kuacha malengo yake makuu ya kuanzishwa kwake. “Limebakia la ulinzi wa wanchi siyo uvamizi. Limebakia Jeshi linalotokana na Wananchi wa Tanzania kwa ajili ya Wananchi wa Tanzania. Limebakia Jeshi la Ukombozi na kulinda amani lililotumika kwenye harakati za Ukombozi wa Afrika na kulinda amani duniani”.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
5 Septemba, 2014
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ameelezea huzuni na masikitiko yake makubwa kufuatia vifo vya watu 36 vilivyotokea katika ajali ya barabarani Wilayani Butiama, Mkoa wa Mara, ambako pia watu 79 wameuamia, baadhi yao vibaya.
Mara baada ya kupata taarifa hiyo iliyotokea leo, Ijumaa, Septemba 5, 2014, Rais Kikwete ambaye yuko katika ziara ya kikazi ya siku tatu Mkoani Arusha, amemtumia salamu za rambirambi Mkuu wa Mkoa wa Mara, akielezea huzuni na masikitiko yake .
“Nimehuzunishwa mno na kusikitishwa sana na taarifa hii ya kutisha ya vifo vya watu 36 ambavyo vimetokea leo wakati mabasi mawili yalipogongana ana kwa ana katika eneo la Sabasaba, Wilaya ya Butiama, mkoani mwako. Nakutumia salamu zangu za rambirambi pamoja na wananchi wote wa Mkoa wa Mara kuomboleza vifo vya Watanzania wenzetu ambao wameaga dunia yetu ghafla katika ajali hii,” amesema Rais Kikwete na kuongeza:
“Nakuomba uwafikishie wafiwa wote pole zangu nyingi sana, ukiwajulisha kuwa niko nao katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo. Aidha, napenda uwajulishe kuwa naungana nao kumwomba Mwenyezi Mungu aziweke pema roho za marehemu.”
“Aidha, naungana nanyi wana-Mara kuwapa mkono wa pole na kuwaombea wote walioumia katika ajali hiyo waweze kupona haraka ili wapate nafasi ya kuendelea na shughuli zao za maendeleo.”
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
5 Septemba, 2014
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Jeshi la Wananchi ni Kimbilio la Wananchi - Rais
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (TPDF) ni kimbilio kuu la Watanzania wote kutokana na mahusiano mazuri ambayo yamekuwepo kati ya Jeshi hilo na wananchi katika miaka 50 iliyopita.
Aidha, Rais Kikwete amesema kuwa Watanzania wanayo imani na matumaini makubwa kuwa Jeshi hilo litaendelea kutii viapo vyake, kuilinda Katiba ya nchi na kuwalinda wananchi wenyewe wakati wote na kusaidiana nao wakati wa majanga.
Rais Kikwete ameyasema hayo leo, Ijumaa, Septemba 5, 2014, wakati alipozungumza na maofisa na wapiganaji wa Jeshi hilo baada ya kushuhudia Zoezi la Medani kuadhimisha miaka 50 ya Jeshi hilo katika eneo la Langururusu, Wilaya ya Monduli, Mkoa wa Arusha.
Katika Zoezi la Medani, maelfu ya wanapiganaji wa TPDF, wameshiriki katika Operesheni Maliza Matata ambako wapiganaji hao wameikomboa sehemu ya ardhi ya nchi yao ya Waungwana ambayo ilikuwa imetekwa na askari wa nchi jirani ya Matata.
Matata ilivamia eneo la Waungwana baada ya nchi hiyo ya Waungwana kutetea maslahi ya nchi nyingine jirani ya Mavuno ambayo husumbuliwa mno na mara kwa mara na nchi ya Matata kwa sababu ya kuwa na utajiri mkubwa na raslimali nyingi.
Katika hotuba yake, Rais Kikwete amewaambia mamia ya askari na wananchi waliohudhuria Sherehe hizo za miaka 50 ya Jeshi: “Wananchi wa Tanzania wanayo mapenzi makubwa na Jeshi letu, maana hili ni Jeshi lao na linatokana na wao. Wameishi na Jeshi hili vizuri na wamenufaika na huduma za kijamii zinazotolewa na Jeshi lao.”
Rais amewaambia askari hao: “Kutokana na hali hiyo, wananchi wanayo matumaini makubwa kuwa mtaendelea kutii viapo vyenu, mtailinda Katiba ya nchi na mtaendelea kuwalinda wakati wote na kusaidiana nao wakati wa majanga. Nyinyi ni kimbilio la Watanzania wote.”
Rais Kikwete amesema kuwa kazi kubwa na nzuri ambayo imefanywa na TPDF imemfanya yeye kama Amiri Jeshi Mkuu kutembea kifua mbele iwe ndani ama nje ya nchi.
“Ninapotembelea mara kwa mara vikosi vyenu na kujionea kazi zenu na utayari wenu kivita, hujisikia vizuri kama Amiri Jeshi Mkuu wenu, natembea kifua mbele kote niendako, maana mnanipa raha ndani ya nchi na mnanipa heshima kubwa nje ya nchi. Nina imani kuwa kwa sasa Jeshi letu lipo katika kiwango cha juu cha utayari kivita kwa vifaa na watu.”
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
5 Septemba, 2014
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ameelezea huzuni na masikitiko yake makubwa kufuatia vifo vya watu 36 vilivyotokea katika ajali ya barabarani Wilayani Butiama, Mkoa wa Mara, ambako pia watu 79 wameuamia, baadhi yao vibaya.
Mara baada ya kupata taarifa hiyo iliyotokea leo, Ijumaa, Septemba 5, 2014, Rais Kikwete ambaye yuko katika ziara ya kikazi ya siku tatu Mkoani Arusha, amemtumia salamu za rambirambi Mkuu wa Mkoa wa Mara, akielezea huzuni na masikitiko yake .
“Nimehuzunishwa mno na kusikitishwa sana na taarifa hii ya kutisha ya vifo vya watu 36 ambavyo vimetokea leo wakati mabasi mawili yalipogongana ana kwa ana katika eneo la Sabasaba, Wilaya ya Butiama, mkoani mwako. Nakutumia salamu zangu za rambirambi pamoja na wananchi wote wa Mkoa wa Mara kuomboleza vifo vya Watanzania wenzetu ambao wameaga dunia yetu ghafla katika ajali hii,” amesema Rais Kikwete na kuongeza:
“Nakuomba uwafikishie wafiwa wote pole zangu nyingi sana, ukiwajulisha kuwa niko nao katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo. Aidha, napenda uwajulishe kuwa naungana nao kumwomba Mwenyezi Mungu aziweke pema roho za marehemu.”
“Aidha, naungana nanyi wana-Mara kuwapa mkono wa pole na kuwaombea wote walioumia katika ajali hiyo waweze kupona haraka ili wapate nafasi ya kuendelea na shughuli zao za maendeleo.”
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
5 Septemba, 2014
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais Kikwete aungana na wenzake Mkutano wa Ugaidi
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete leo, Jumanne, Septemba 2, 2014, ameungana na viongozi wengine wa Afrika na wajumbe kutoka nchi mbali mbali duniani kuhudhuria Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika (AU) kujadili hatari na athari za ugaidi katika Bara la Afrika na namna ya kukabiliana nao.
Katika Mkutano huo kwenye Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Kenyatta – Kenyatta International Convention Centre (KICC) mjini Nairobi, Kenya umefanyika chini ya uenyekiti wa Mwenyekiri wa sasa wa Baraza hilo, Mheshimiwa Idrisa Deby, Rais wa Chad.
Nchi zote 15 wanachama wa Baraza hilo zimewakilishwa katika Mkutano huo wa siku moja na miongoni mwa Marais ambao walihudhuria mbali na Rais Kikwete na Rais Deby ni Rais Yoweri Museveni wa Uganda, Mheshimiwa Goodluck Jonathan, Rais wa Nigeria, Rais wa Somalia, na mwenyeji wa Mkutano huo, Mheshimiwa Uhuru Kenyatta, Rais wa Kenya.
Rais Kikwete ambaye aliwasili mjini Nairobi usiku wa jana, Jumatatu, Septemba Mosi, 2014, baada ya kukatisha kwa muda ziara yake ya kikazi katika Mkoa wa Dodoma, alitarajiwa kuhutubia Mkutano huo baadaye jioni ya leo.
Kikao cha ufunguzi cha mapema asubuhi, wajumbe walisikia hotuba kutoka kwa viongozi wanne wakianza na Rais Deby ambaye alitoa hotuba ya ufunguzi akifuatiwa na Rais Jonathan ambaye alizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU) Mheshimiwa Mohamed Abdulaziz, Rais wa Mauritania ambaye hakuweza kuhudhuria Mkutano huo.
Rais Jonathan ambaye nchi yake imeathirika mno kutokana na ugaidi wa Kikundi cha Boko Haram amesema kuwa ugaidi unashamiri katika Afrika kwa sababu ya kuongezwa nguvu na uhalifu mwingine wa kimataifa kama vile biashara ya dawa za kulevya, ujangili, biashara ya binadamu, biashara ya fedha haramu.
Amesema kuwa dunia na Afrika inahitaji mbinu nyingine za kukabiliana na ugaidi kwa sababu ya uhalifu huo kusaidiwa na uhalifu wa aina nyingine na ambazo unavuka mipaka ya nchi mbali kwa urahisi zaidi.
Naye Rais Kenyatta ambaye pia nchi yake imeathiriwa mno na ugaidi wa Kikundi cha El Shaabab, amesema kuwa Bara zima la Afrika linakabiliwa na ugaidi zikiwa nchi za eneo la Sahel za Chad, Mali na Libya, eneo la Afrika Mashariki ambalo linasumbuliwa na ugaidi wa El Shaabab na eneo la nchi za Nigeria na Cameroun, ambazo zinasumbuliwa na Boko Haram na eneo la Afrika ya Kati ambazo zinasumbuliwa na ugaidi wa Lord’s Army.
Naye Makamu Mwenyekiti wa Kamisheni ya Afrika, Balozi Erasto Mwencha amesema kuwa uteuzi wa Jiji la Nairobi kuandaa Mkutano huo ni mwafaka kabisa kutokana na madhara ambayo Jiji hilo na nchi ya Kenya kwa jumla imekuwa inapitia kwa sababu ya mashambulizi ya ugaidi.
“Kwa pamoja tumekuja hapa kuelezea mshikamano wetu na ukaribu wetu kwa Kenya, wananchi wake na Serikali yake kutokana na mashambulzi ambayo yamekuwa yanaikumba nchi hii,” amesema Balozi Mwencha.
Mkutano huo pia umesikiliza Ripoti ya Mwenyekiti wa Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika kuhusu aina, athari, hatari ya ugaidi na namna nchi hizo zinaweza, kwa pamoja, kukabiliana na kushinda balaa hilo.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
2 Septemba, 2014
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amewasili Nairobi, Kenya, usiku ya jana, Jumatatu, Septemba Mosi, 2014,kuhudhuria Mkutano Maalum wa Wakuu wa Nchi zinazounda Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika (AU) ambako Tanzania ni mwanachama.
Mkutano huo wa siku moja ambao utajadili ugaidi na athari zake kwa nchi za Afrika umepangwa kufanyika leo, Jumanne, Septemba 2, 2014 kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Kenyatta na kuhudhuriwa na viongozi mbali mbali akiwamo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Mheshimiwa Ban Ki Moon.
Mwisho!
Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
02 Septemba, 2014.
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Serikali yajenga maelfu ya miradi ya maji
SERIKALI ya Rais Jakaya Mrisho Kikwete imeanza ujenzi na utekelezaji wa Miradi 1,555 ya Maji nchi nzima katika jitihada za kukabiliana na hatimaye kumaliza tatizo la uhaba wa huduma ya maji safi na salama kwa wananchi, Waziri wa Maji, Mheshimiwa Profesa Jumanne Maghembe ametangaza leo, Ijumaa, Agosti 29, 2014.
Akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Chunyu, Wilaya ya Mpwapwa, Mkoa wa Dodoma, kabla ya kumkaribisha Rais Kikwete kuzindua mradi wa maji katika kijiji hicho, Profesa Maghembe amesema kuwa Mradi wa Maji wa Chunyu ni moja ya miradi hiyo 1,555 inayojengwa pote nchini ili kuwapatia Watanzania wote maji safi na salama.
Waziri Maghembe amemwambia Rais Kikwete na wananchi hao wa Chunyu kuwa kati ya miradi hiyo, miradi 230 tayari imekamilika na inatoa huduma ya maji kwa wananchi milioni mbili katika mikoa mbali mbali ya Tanzania.
Ameongeza Mheshimiwa Maghembe: “Miradi mingine 538 inaendelea kujengwa katika Vijiji 540 na imepangwa kuwa imekamilika katika muda wa miezi sita ijayo ili ianze kutoa huduma ya maji kwa wananchi milioni nne. Miradi mingine 525 inafanyiwa maandalizi na inatarajiwa kuanza kujengwa katika mwezi mmoja ujao, Oktoba, mwaka huu.”
Waziri Maghembe amesema kuwa miradi hiyo 525 inayoanza kujengwa Oktoba, mwaka huu, inepangwa kukamilika Machi mwakani, 2015, na hivyo kuiwezesha Serikali kutimiza lengo lake la kutoka huduma ya maji kwa safi na salama watu milioni 7,250,000 nchini.
Rais amefungua Mradi wa Maji wa Chunyu, kijiji kilichoko kilomita 27 kutoka mjini Mpwapwa na kilomita 92 kutoka mjini Dodoma, ikiwa ni sehemu ya ziara ya Rais Kikwete katika Mkoa wa Dodoma ambayo ilianza jana, Alhamisi, Agosti 28, 2014.
Rais Kikwete ameanza ziara ya kikazi katika Mkoa wa Dodoma baada ya kumaliza ziara kama hiyo katika Mkoa wa Morogoro. Rais alianzia ziara yake ya Dodoma katika Wilaya ya Kongwa, jana, Alhamisi, Agosti 28, 2014.
Kati ya kumaliza ziara ya Morogoro na kuanza ile ya Dodoma, Rais Kikwete alisafiri kwenda Ngara, Mkoa wa Kagera, ambako aliungana na Rais Pierre Nkurunzinza wa Burundi katika Uzinduzi wa Uimarishaji Mpaka wa Kimataifa kati ya Tanzania na Burundi, shughuli iliyofanyika upande wa Tanzania wa Kijiji cha mpakani cha Mugikomero.
Mradi wa Chunyu, moja ya vijiji 93 vya Wilaya ya Mpwapwa, utatoa huduma ya maji safi na salama kwa wananchi wapatao 3,912 waishio katika vitongoji saba vya kijiji hicho. Mradi huo ulianza kujengwa Oktoba, mwaka jana, 2013 na kukamilika Juni mwaka huu.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
29 Agosti, 2014
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Ujenzi wa Daraja la Gulwe waanza, Rais aweka jiwe la msingi
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete leo, Ijumaa, Agosti 29, 2014, ameweka jiwe la msingi kwenye mradi mwingine mkubwa wakati wa ziara yake ya kikazi ya Mkoa wa Dodoma iliyoanza rasmi jana, Alhamisi, Agosti 28, 2014.
Rais Kikwete ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa Daraja la Gulwe, lililoko katika Mto Kinyasungwi, Wilaya ya Mpwapwa kwenye Barabara ya Mpwapwa-Gulwe-Kibakwe hadi Chipogolo, kiasi cha kilomita 124.
Jiwe hilo la msingi ni la pili kwa mradi kubwa kuwekwa na Rais Kikwete katika ziara yake ya Mkoa wa Dodoma baada ya jana, Alhamisi, kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa barabara ya lami kutoka Mbande-Kongwa Junction-Kongwa lenye urefu wa kilomita 11.6. Barabara hiyo ni sehemu ya barabara ya Mbande-Kongwa Junction-Kongwa-Mpwapwa-Mbande lenye urefu wa kilomita 101.
Daraja hilo kubwa lenye urefu wa mita 42 litasaidiwa na makalvati tisa ili kupitisha maji katika bonde ambalo lina historia ya mafuriko. Pamoja na Daraja hilo, pia itajengwa barabara ya lami lenye urefu wa kilomita 1.53. Daraja hilo linajengwa katika eneo lenye urefu wa nusu kilomita.
Daraja hilo ni kiungo muhimu kati ya Mji wa Mpwapwa na maeneo ya Gulwe, Kibakwe, Rudi na Chipogo ambavyo ni maarufu kwa uzalishaji wa mazao ya chakula kama vile mahindi, mtama, karanga na ufuta. Aidha, daraja hili ni kiungo muhimu kati ya Mji wa Mpwapwa na Barabara Kuu ya Iringa - Dodoma ambayo inajengwa kwa kiwango cha lami.
Serikali ya Rais Kikwete iliamua kujenga daraja jipya la Gulwe baada ya daraja la zamani kubomolewa na mafuriko yaliyotokea Desemba 2009 baada ya mvua kubwa iliyonyesha nchini na kuharibu barabara na madaraja mengi nchini.
Kufuatia mafuriko hayo, Benki ya Dunia iliikopesha Tanzania dola za Marekani milioni 15 ili kuiwezesha Tanzania kukabiliana na dharura hizo za mafuriko chini ya mpango wa Benki hiyo wa TSSP.
Madaraja yaliyojengwa chini ya fedha hizo za Benki ya Dunia ni pamoja na Daraja la Ruhekei la Wilaya ya Nyasa, Mkoa wa Ruvuma, ambalo Rais Kikwete alilizindua mwezi uliopita, Julai, mwaka huu.
Daraja hilo na barabara hiyo ya lami, vinavyojengwa kwa ubia wa makampuni ya hapa nyumbani Afriq Engineering and Construction na MS Kashere Enterprises Limited, zinagharimu Sh. bilioni 3.3. Ujenzi umepangwa kuchukua miezi 12 na mpaka sasa kazi hiyo imekamilika kwa asilimia 40.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
29 Agosti, 2014
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Waziri Magufuli: Rais kuzindua miradi mikubwa 25
Wizara ya Ujenzi imetangaza kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete atazindua rasmi miradi mikubwa 25 ya barabara na madaraja inayoandaliwa na kukamilishwa katika kipindi chake cha uongozi kabla ya kumaliza muda wake wa urais.
Waziri wa Ujenzi, Mheshimiwa John Pombe Magufuli ametangaza habari hiyo leo, Alhamisi, Agosti 28, 2014, kwenye sherehe ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa Barabara ya Mbande-Kongwa Junction-Kongwa, Mkoani Dodoma, yenye kilomita 16.5, ilifanyika katika eneo la Kongwa Junction, Wilaya ya Kongwa.
Ujenzi wa barabara hiyo ni moja ya miradi mingi ya barabara na madaraja yanayojengwa nchini kwa sasa na barabara hiyo imeanza kwa ujenzi wa kilomita tano kutoka Kongwa Junction hadi Kongwa inayogharimu kiasi cha sh bilioni 2.909 zinazotolewa na Serikali ya Tanzania.
Barabara hiyo ni sehemu ya Barabara ya Mbande-Kongwa Junction-Mpwapwa yenye urefu wa kilomita 50, barabara ambayo inapangwa kujengwa hadi kibakwe.
Barabara ya Mbande-Kongwa Junction-Kongwa imeanishwa kwenye Ilani ya CCM ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 lakini kwa maana ya kufanyiwa upembuzi yakinifu na usanifu na siyo kwa madhumuni ya kujengwa wakati huu. Ujenzi wake umeanza kwa sababu usanifu wake umekamilika mapema.
Waziri Magufuli amewaambia wananchi kwenye sherehe hiyo kuwa Rais Kikwete ambaye chini ya uongozi wake zinajengwa barabara zenye urefu wa kilomita 11,154, anatarajiwa kuzidua miradi hiyo 25 kabla ya kumaliza uongozi wake mwishoni mwa mwaka ujao kwa sababu imejengwa chini yake yeye.
Miradi hiyo ambaye ameitaja Waziri Magufuli ni Barabara za Bariadi-Lamadi, Uyovu-Bwanga, Bagamoyo-Msata, Usagara-Kisesa Bypass, Bwanga-Biharamulo,Kyaka –Bugene, Mbeya-Lwanjilo, Lwanjilo-Chunya na Nzega-Puge.
Miradi mingine ni barabara za Puge-Tabora, Tabora-Nyahua, Ndono-Urambo, Simiyu/Mara Border –Musoma, Bulamba-Kisorya, Makutano-Natta, Sumbawanga-Kanazi, Sumbawanga-Matai-Bandari ya Kasanga, Kanazi-Kizi-Kibaoni, Sitalike-Mpanda, Dodoma-Mayamaya na Magole –Turiani.
Madaraja ambayo yamo kwenye programu hiyo ni Daraja la Kigamboni,Daraja la Sibiti, Daraja la Mbutu, Daraja la Malagarasi na Daraja la Kilombero.
Waziri Magufuli pia ametangaza miradi ya ujenzi wa barabara ambayo imegharimiwa na kutekelezwa kwa asilimia 100 na Serikali ya Tanzania ambayo ujenzi wake kwa kiwango cha lami umekamilika ikiwa ni pamoja na Barabara ya Korogwe-Handeni, Handeni-Mkata,Kyamyorwa-Buzirayombo, Bizoyambo-Geita na Mwandiga-Manyovu.
Nyingine ni Somanga-Matandu, Mbwemkuru –Migoyo, Nangurukuru-Mbwemkuru, Tarekea-Rongai-Kamwanga, Tarekea-Rombo Mkuu, Babati-Bonga, Dodoma-Manyoni, Singida - Manyoni, Kigoma-Kidahwe, Dumila-Rudewa, Tabora-Ndono, Tabora-Ndono na Kagoma Biharamulo-Lusahuga na upanuzi wa Barabara ya Kilwa.
Madaraja yanahusika ni Daraja la Kigamboni, Daraja la Kilombero, Daraja la Sibiti na Daraja la Mbutu.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
28 Agosti, 2014
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Serikali yajenga maelfu ya miradi ya maji
SERIKALI ya Rais Jakaya Mrisho Kikwete imeanza ujenzi na utekelezaji wa Miradi 1,555 ya Maji nchi nzima katika jitihada za kukabiliana na hatimaye kumaliza tatizo la uhaba wa huduma ya maji safi na salama kwa wananchi, Waziri wa Maji, Mheshimiwa Profesa Jumanne Maghembe ametangaza leo, Ijumaa, Agosti 29, 2014.
Akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Chunyu, Wilaya ya Mpwapwa, Mkoa wa Dodoma, kabla ya kumkaribisha Rais Kikwete kuzindua mradi wa maji katika kijiji hicho, Profesa Maghembe amesema kuwa Mradi wa Maji wa Chunyu ni moja ya miradi hiyo 1,555 inayojengwa pote nchini ili kuwapatia Watanzania wote maji safi na salama.
Waziri Maghembe amemwambia Rais Kikwete na wananchi hao wa Chunyu kuwa kati ya miradi hiyo, miradi 230 tayari imekamilika na inatoa huduma ya maji kwa wananchi milioni mbili katika mikoa mbali mbali ya Tanzania.
Ameongeza Mheshimiwa Maghembe: “Miradi mingine 538 inaendelea kujengwa katika Vijiji 540 na imepangwa kuwa imekamilika katika muda wa miezi sita ijayo ili ianze kutoa huduma ya maji kwa wananchi milioni nne. Miradi mingine 525 inafanyiwa maandalizi na inatarajiwa kuanza kujengwa katika mwezi mmoja ujao, Oktoba, mwaka huu.”
Waziri Maghembe amesema kuwa miradi hiyo 525 inayoanza kujengwa Oktoba, mwaka huu, inepangwa kukamilika Machi mwakani, 2015, na hivyo kuiwezesha Serikali kutimiza lengo lake la kutoka huduma ya maji kwa safi na salama watu milioni 7,250,000 nchini.
Rais amefungua Mradi wa Maji wa Chunyu, kijiji kilichoko kilomita 27 kutoka mjini Mpwapwa na kilomita 92 kutoka mjini Dodoma, ikiwa ni sehemu ya ziara ya Rais Kikwete katika Mkoa wa Dodoma ambayo ilianza jana, Alhamisi, Agosti 28, 2014.
Rais Kikwete ameanza ziara ya kikazi katika Mkoa wa Dodoma baada ya kumaliza ziara kama hiyo katika Mkoa wa Morogoro. Rais alianzia ziara yake ya Dodoma katika Wilaya ya Kongwa, jana, Alhamisi, Agosti 28, 2014.
Kati ya kumaliza ziara ya Morogoro na kuanza ile ya Dodoma, Rais Kikwete alisafiri kwenda Ngara, Mkoa wa Kagera, ambako aliungana na Rais Pierre Nkurunzinza wa Burundi katika Uzinduzi wa Uimarishaji Mpaka wa Kimataifa kati ya Tanzania na Burundi, shughuli iliyofanyika upande wa Tanzania wa Kijiji cha mpakani cha Mugikomero.
Mradi wa Chunyu, moja ya vijiji 93 vya Wilaya ya Mpwapwa, utatoa huduma ya maji safi na salama kwa wananchi wapatao 3,912 waishio katika vitongoji saba vya kijiji hicho. Mradi huo ulianza kujengwa Oktoba, mwaka jana, 2013 na kukamilika Juni mwaka huu.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
29 Agosti, 2014
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Burundi awashukuru Watanzania
Rais wa Jamhuri ya Burundi, Mheshimiwa Pierre Nkurunzinza ameishukuru Tanzania na Watanzania wote kwa mchango wao mkubwa katika kuleta amani na utulivu katika Burundi, akisisitiza kuwa hakuna nchi nyingine duniani imechangia amani katika Burundi kuliko Tanzania.
Aidha, Rais Nkurunzinza amesema kuwa pamoja na kwamba nchi hizo mbili zina mpaka, bado Tanzania imeruhusu maelfu kwa maelfu ya wakimbizi kutoka Burundi kuingia katika Tanzania bila kufuata taratibu za mipaka na uhamiaji kwa sababu ya matatizo yaliyokuwa yanawakabili wananchi hao wa Burundi.
Rais wa Burundi alikuwa anazungumza leo, Jumatano, Agosti 27, 2014, wakati wa sherehe kubwa ya Uzinduzi wa Upimaji na Uwekaji Mawe Kimataifa kati ya Tanzania na Burundi iliyofanyika upande wa Tanzania Kijiji cha Mugikomelo mpakani kwa nchi hizo na kuhudhuriwa na maelfu na maelfu ya wananchi wa Tanzania na Burundi.
Akizungumza na wananchi hao, Rais Nkurunzinza amesema: “Tunawashukuru sana Watanzania. Ni ndugu zetu. Tunawashukuru kwa kutuunga mkono wakati wa matatizo yetu na kutusaidia kumaliza matatizo hayo.”
Ameongeza: “Sisi katika Burundi tumepitia matatizo mengi, matatizo mbali mbali. Kuliko nchi nyingine yoyote duniani, Tanzania imekuwa nasi wakati wote wa matatizo. Jitihada za kutusaidia zilianzishwa na Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere lakini zimeendelea na kuendelezwa na viongozi wengine wa Tanzania.”
Rais Nkurunzinza amesisitiza kuwa wakati wote Burundi ilipokuwa na matatizo, Tanzania iliwaruhusu wakimbizi kuingia nchini humo kwa maelfu bila kujali taratibu za mipaka na uhamiaji. “Kuna wakati wakimbizi zaidi ya milioni moja wa Burundi waliingia Tanzania. Mpaka kati ya nchi hizo ulikuwepo wakati wa matatizo yetu haya, lakini bado Tanzania ilituachia kuingia Tanzania.”
Ameongeza Rais huyo wa Burundi: “Tunajua kuwa tuliharibu vitu vingi lakini mlituvumilia. Hakuna la maana la kuwalipeni isipokuwa kuwaombeni mpokee shukurani zetu za dhati. Kwa sababu ya mchango wenu mkubwa sasa matatizo ya Burundi yameisha.”
Uwekaji mawe kwenye mpaka wa kimataifa kati ya nchi hizo umefanyika kufuatia mchakato mrefu ambako wataalam wa nchi hizo wamepima theluthi moja tu – yaani kilomita 120 – za mpaka kati ya nchi hizo mbili ikiwa ni zoezi la kwanza la namna hiyo kufanyika katika mpaka huo tokea Agosti 5, mwaka 1924, miaka 90 iliyopita, wakati Tume ya Mipaka ya Uingereza na Ubelgiji (Anglo-Belgian Border Commission) ilipoitiliana saini Mkataba wa mpaka kati ya nchi hizo mbili.
Mpaka kati ya Tanzania na Burundi una urefu wa kilomita 451 ikiwa nchi ya tano yenye urefu mkubwa zaidi kati ya nchi nane jirani na Tanzania.
Nchi ya kwanza kuwa na mpaka mrefu zaidi na Tanzania ni Kenya yenye mpaka wa kilomita 769, ikifuatiwa na Mozambique kilomita 756, Malawi kilomita 475, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kilomita 473, Burundi, Uganda kilomita 396, Zambia kilomita 388 na Rwanda kilomita 217.
Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
27 Agosti , 2014.
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Marais Kikwete na Nkurunzinza washuhudia uhakiki wa mpaka wa nchi zao
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amezitaka Mamlaka zote zinazohusika na Uhakiki Mipaka na Uwekaji Mawe katika Mpaka wa Kimataifa wa Tanzania na Burundi na mipaka mingine kati yaTanzania na nchi nyingine unakamilika mapema iwezekanavyo.
Aidha, Rais amesema kuwa Tanzania inapima mpaka wake na Burundi na mipaka yake na nchi nyingine jirani siyo kwa sababu ya kuwepo kwa migogoro na nchi jirani bali kwa sababu ya kuwahakikishia wananchi wa nchi zote wanaoishi mipakani kujua ni sehemu gani na mazingira yapi wanafanyia shughuli zao za maendeleo.
Rais Kikwete ameungana na Rais wa Burundi, Mheshimiwa Pierre Nkurunzinza leo, Jumatano, Agosti 27, 2014 kuzindua Zoezi la Upimaji na Uwekaji Mawe ya Mpaka kati ya Tanzania na Burundi katika sherehe kubwa na ya kusisimua iliyofanyika upande wa Tanzania wa Kijiji cha Mpakani cha Mugikomero.
Rais Kikwete amewasili Mugikomero saa 8:15 mchana akitokea Uwanja wa Ndege wa Mchauru, mjini Geita ambako ndege yake imetua saa nne kamili asubuhi ikitokea mjini Dodoma kujiunga na Rais Nkurunzinza ambaye alitangulia kuwasili kwenye kijiji hicho.
Rais Kikwete amekielezea kitendo cha Uzinduzi wa Zoezi hilo kuwa ni kielelezo tosha cha uhusiano mwema, udugu na urafiki uliopo kati ya Tanzania na Burundi, nchi mbili ambazo pamoja na Rwanda zilikuwa nchi moja zilikuwa chini ya Utawala wa Wajerumani ikijulikana kama German East Africa.
Nchi hizo zilitengana baada ya Ujerumani kushindwa katika Vita Kuu ya Pili ya Dunia ambako Tanganyika iliwekwa chini ya utawala wa Waingereza wakati Burundi na Rwanda ziliwekwa chini ya himaya ya Ubelgiji.
Akifafanua umuhimu wa kuhakiki mpaka, Rais Kikwete amesema kuwa mara ya mwisho kwa Mpaka wa Kimataifa wa Tanzania na Burundi kuhakikiwa na mkataba kusainiwa kati ya nchi hizo ilikuwa Agosti 5, mwaka 1924, miaka 90 iliyopita.
“Kama zilivyo nchi nnyingine za Afrika, Tanzania na Burundi zilirithi mpaka uliopo kutoka kwa waliokuwa watawala wetu enzi za ukoloni. Mpaka huu haujafanyiwa marekebisho wala kuimarishwa tangu nchi zetu zipate uhuru zaidi ya miaka 50 iliyopita. Katika kipindi hicho yamekuwepo mabadiliko mengi likiwemo ongezeko la watu, shughuli za maendeleo katika maeneo ya mpakani na hata alama za mipaka zimekuwa vigumu kutambulika ama kwa sababu ya kuchakaa au mawe yameng’olewa,” amesema Rais Kikwete.
Ameongeza pia kuwa baada ya kutambua vyanzo vya migogoro na utata miongoni mwa baadhi ya nchi za Afrika, Umoja wa Afrika (AU) katika Kikao cha Wakuu wa Nchi za Serikali kilichofanyika Accra, Ghana Juni 27, mwaka 2007, uliamua kuwa nchi zote zishirikiane kuimarisha mipaka yao ifikapo mwaka 2012. Muda huo uliongezwa hadi 2017.
Rais Kikwete amesema kuwa zoezi hilo ambako katika awamu ya kwanza kilomita 120 za mpaka zimepimwa na kuwekewa mawe ya utambuzi wa mpaka, halikuwa rahisi kwa sababu mpaka wa Tanzania na Burundi ni mrefu, kiasi cha kilomita 450, sawa na urefu kati ya Dar Es Salaam na Lindi.
“Isitoshe mpaka hauko mijini, maeneo mengi yako misituni kwenye mabonde na milima. Ni vigumu kuyafikia. Kwa upande wetu, mpaka uko katika mikoa miwili ya Kagera na Kigoma na katika wilaya tano, nne zikiwa katika Mkoa wa Kigoma na moja ikiwa Ngara, Mkoa wa Kagera. Isitoshe, hatuna mfadhili na zoezi hili tumeligharimia sisi wenyewe,” amesema Rais Kikwete.
Rais Kikwete amewambia wananchi kuwa mbali na zoezi na Burundi, nchi ya Tanzania inaendelea na zoezi kama hili kwa nchi nyingine jirani, akisisitiza kuwa mpaka wa Tanzania na nchi za Kenya, Mozambique, Comoro na Shelisheli katika Bahari ya Hindi umefikisha na Mikataba kutiwa saini.
Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
27 Agosti , 2014.
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Wanafunzi wa Chuo Kikuu Mzumbe waunga mkono Bunge Maalumu la Katiba
Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Mzumbe cha Morogoro wameunga mkono mchakato wa Bunge Maalumu la Katiba wakisema kuwa wanaridhishwa na hatua iliyofikiwa na mwendo mzima wa Bunge hilo na kuwa mwafaka unawezekana kuhusu vipengele viliyobakia na kupatikana kwa theluthi mbili za kupitisha Katiba Mpya.
Wanafunzi hao wameeleza msimamo wao huo jioni ya leo, Jumatatu, Agosti 25, 2014, chuoni hapo kwenye risala ambayo wameisoma hadharani mbele ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ambaye ametembelea chuo hicho ikiwa sehemu ya ziara yake ya siku saba Mkoani Morogoro.
Katika risala hiyo iliyosomwa na Rais wa Chama cha Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Bwana Boniface Maige Juma, wanafunzi hao wamesema kuwa ni vyema mchakato huo ukaungwa mkono na kila Mtanzania ili kuuwezesha kuleta neema na matarajio yanayokusudiwa.
Amesema Bwana Juma: “Mheshimiwa Rais, tunaridhishwa sana na hatua iliyofikiwa na Bunge Maalum la Katiba. Tunaamini kuwa mwafaka unawezekana kwa vipengele vingine vya Rasimu ya Katiba. Aidha, tunaamini kuwa theluthi mbili za kupitisha Katiba Mpya zinawezekana kupatikana.”
Akijibu risala hiyo, Rais Kikwete amewaambia mamia kwa mamia ya wanazuoni, watumishi wengine wa chuo hicho na wanavijiji vya jirani na chuo: “Maoni yenu ndiyo maoni yangu. Ni jambo la kusikitisha kuwa tofauti hizi za viongozi wa siasa zinaleta mfarakano wa namna hii. Tokea mwanzo niliwaambia kuwa wakijiruhusu kushindana na kuviziana katika mchakato huo watakwama.”
Ameongeza Rais Kikwete: “Aidha, niliwaambia kuwa Katiba inayotafutwa siyo Katiba ya CCM, ama ya CHADEMA, ama ya NCCR, ama ya CUF. Niliwaambia kuwa hii ni Katiba ya wananchi wa Tanzania. Ni vyema tukakubaliana kuwa yenye kutugawa tukayaacha kwa sasa na kukubali kwa yale ambayo hatuna tofauti.”
Kuhusu madai kuwa Rais Kikwete anakataa kukutana na wajumbe wa Bunge hilo ambalo wanaendelea kususia shughuli za Bunge hilo, Rais Kikwete amesema: “Mimi sina tatizo la kukutana nao. Wanajua jinsi ya kukutana nami, ili tuweze kutafuta namna ya kumaliza tofauti hizi.”
Hata hivyo, Rais Kikwete ameongeza kuwa ana matumaini kuwa mchakato huu utaweza kuwapatia Watanzania katiba mpya.
“Mimi naishi kwa matumaini. Naamini kuwa tutafika mwisho vizuri. Mchakato ni mgumu lakini barabara ndefu haikosi kona. Tukidhamiria kweli kweli tutafika tuendako vizuri.”
Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
25 Agosti , 2014.
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Tunafikiria kufuta ada sekondari – Rais Kikwete
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ametangaza rasmi kuwa Serikali inaangalia uwezekano wa kufuta ada katika shule zake za sekondari, kama namna ya kuboresha Sera ya Elimu na kuhakikisha kuwa kila mwanafunzi anayeanza darasa kwanza anamaliza kidato cha nne.
Aidha, Rais Kikwete amesema kwamba Serikali yake iliibua mpango wa ujenzi wa sekondari za kata kwa sababu nafasi za wanafunzi kuingia sekondari zilikuwa zimekuwa finyu kiasi cha kwamba ni asilimia kati ya sita na 10 ya watoto wote waliokuwa wanamaliza shule za msingi mwaka 2005 walikuwa wanaingia sekondari wakati anaingia madarakani.
Rais Kikwete pia amesema kuwa pamoja na kejeli nyingi zilizoelekezwa kwa shule za sekondari za kata kiasi cha kuitwa Yeboyebo katika miaka ya mwanzoni ya shule hizo, bado zimekuwa na mafanikio makubwa, ambayo ni sehemu ya mafanikio makubwa ya jumla ya Sekta ya Elimu katika miaka karibu tisa ya uongozi wake.
Rais Kikwete alikuwa anazungumza jioni ya leo, Jumatano, Agosti 25, 2014, na wanajumuia ya Chuo Kikuu cha Mzumbe cha Morogoro na wakazi wa vijiji vya jirani na chuo hicho ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kikazi katika Mkoa wa Morogoro iliyoanza Agosti 20.
Katika hotuba yake ya kusisimua, Rais Kikwete ametumia muda wa kutosha kuelezea historia ya maendeleo ya elimu nchini, mabadiliko ya mwelekeo wa elimu na sera ambazo zimeongoza mageuzi makubwa katika elimu chini ya uongozi wake.
Rais Kikwete amewaambia mamia kwa mamia ya wanazuoni hao na watumishi wengine wa Chuo hicho pamoja na wanavijiji wa jirani kuwa Serikali wakati wote imekuwa inasaka kubuni sera za kuendeleza elimu nchini na wakati wote kuboresha sera hizo.
“Kwa mfano sasa hivi tunaangalia jinsi gani ya kufuta karo katika shule zetu zote za sekondari za Serikali kama namna ya kuhakikisha kuwa kila mtoto anayeanza darasa la kwanza anakuwa na nafasi ya kumaliza sekondari kwa maana ya kidato cha nne bila kulazimika kuacha shule kwa sababu ya ada,”amesema Rais Kikwete na kuongeza:
“Tunaangalia kuondoa ada hii ambako wazazi wanalipa Sh. elfu ishirini kwa shule za kutwa na Sh. elfu sabini kwa shule za bweni, ili watoto wetu waingie darasa la kwanza na kwenda moja kwa moja hadi kidato cha nne bila ya wasiwasi wa kukwamishwa na ada.”
Akielezea historia ya kuanzishwa kwa Shule za Sekondari za Kata, Rais Kikwete amesema kuwa wakati Serikali yake inaingia madarakani, hali ya watoto kuingia sekondari kutoka shule za msingi ilikuwa mbaya kiasi cha kwamba ni asilimia kati ya sita na 10 iliyokuwa inasonga mbele kwa sababu shule za sekondari zilikuwa chache.
“Kwa miaka mingi, tulikuwa hatukujenga shule mpya za sekondari, na kama mnavyojua wakoloni wa Kiingereza ndio kabisa hawakujenga shule. Kazi hiyo waliwaachia Wamisionari. Kwa hiyo wakati tunaingia madarakani, hali ilikuwa mbaya ndiyo maana tukaja na Sera ya Shule za Kata.”
Kwa mujibu wa takwimu rasmi, zilikuwepo jumla ya shule za sekondari 1,745 mwaka 2005 zikiwemo shule 1202 za Serikali na sasa ziko jumla ya shule za sekondari 4,576 zikiwemo shule 3,528 za Serikali.
Kuhusu maendeleo ya shule za sekondari za kata, Rais Kikwete amesema kuwa zimekuwa na mafanikio makubwa kama ambavyo Sekta ya Elimu nzima imekuwa na mafanikio makubwa.
Rais Kikwete ameelezea baadhi ya mafanikio hayo kama vile upanuzi mkubwa wa elimu ya msingi na uandikishaji wa watoto kuingia shule, upanuzi wa elimu ya sekondari, ongezeko kubwa la wanafunzi wa shule za sekondari, upanuzi wa elimu ya juu ambako sasa kuna vyuo vikuu 51, vikiwemo 15 vya umma, ongezeko la fedha za mikopo ya elimu kutoka sh bilioni 16 mwaka 2005 na kufikia bilioni 345 kwa sasa, kuongezeka kwa wakopaji kutoka wanafunzi 16,000 mwaka 2005 hadi kufikia 95,000 kwa sasa.
Rais Kikwete amesema kuwa kwa sasa Serikali yake inapambana na changamoto zilizojitokeza kutokana na kupanuka sana kwa elimu nchini na kuwa moja ya changamoto hizo ni ukosefu wa walimu wa masomo ya sayansi ambapo sasa imefikia kikomo kwa sababu, sasa wapo karibu wa kutosha wa masomo hayo kwa shule za sekondari zote nchini.
Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
25 Agosti , 2014
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ameupa wiki moja uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa, Mkoa wa Morogoro, kuwapatia viwanja vya kujenga nyumba wahanga wa mafuriko ya kiasi cha miaka minne iliyopita mjini Kilosa.
Rais Kikwete ametoa agizo hilo leo, Jumapili, Agosti 24, 2014 wakati alipozungumza na wananchi wa Kilosa katika mkutano wa hadhara uliofanyika mjini Kilosa baada ya kutembelea Wilaya hiyo kukagua na kuzindua miradi ya maendeleo.
Rais Kikwete amerejea Mkoani Morogoro asubuhi ya leo kuendelea na ziara yake ya siku saba mkoani huo baada ya kuikatisha jana, Jumamosi, Agosti 23, 2014, kwenda kwenye Chuo cha Uongozi wa Kijeshi, Monduli, Mkoani Arusha, ambako alikwenda kutoa kamisheni kwa maofisa wapya wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (TPDF).
Baada ya kuwa amelalamikiwa kwa maneno na kwa mabango na wahanga hao kuwa hawajapatiwa viwanja vya kujenga nyumba za kudumu baada ya kuwa wameahidiwa viwanja hivyo na Rais Kikwete mwenyewe wakati alipowatembelea kufuatia mafuriko ya Mto Mkondoa miaka minne iliyopita, Rais Kikwete amesema:
“Ni jambo la kusikitisha kuwa bado ahadi zangu kwenu hazijatimizwa. Niliahidi mambo mawili wakati nilipokuja kuwaoneni – moja niliahidi kuwa tutawapatia viwanja vya kuweza kujenga nyumba za kudumu na pili niliwaahidi kuwasaidia kujenga nyumba. Sasa tuanze na la kwanza,”alisema Rais Halmashauri hiyo kujieleza mbele ya wananchi hao kuhusu ahadi hizo.
Baada ya kuambiwa kuwa vimepimwa viwanja 800 katika Halmashauri hiyo, Rais Kikwete aliamuru kuwa kiasi cha viwanja 400 vitengwe kwa ajili ya wahanga hao wa mafuriko.
“Katika muda wa wiki moja, yaani kuanzia kesho Jumatatu hadi kufikia Ijumaa, nataka taratibu zote kuwa zimekamilika na kila mtu kuwa ameonyeshwa kiwanja chake. Tutazingumzia habari ya ujenzi baadaye,” alisema Rais Kikwete.
Mapema asubuhi, Rais Kikwete ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa Mradi wa Kufua Umeme katika eneo la Msolwa, Wilaya ya Kilosa, mradi ambao unajengwa na Shirika la Watawa wa Madonda Matakatifu ya Yesu la Stigmatine Fathers and Brothers la Kanisa Katoliki ambalo lilianza shughuli zake katika Wilaya ya Kilosa Novemba 1989.
Mradi huo wa Yovi Mini Hydropower Project unajengwa kwenye milima na maporomoko ya Mto Yovi na unalenga kuzalisha megawati kati ya moja na 2.3 kwa ajili ya mamia kwa mamia ya watumiaji katika eneo hilo ikiwamo shule maarufu na ya mfano ya sekondari ya Msolwa St. Gaspar iliyofunguliwa na Shirika la Stigmatine mwaka 1994.
Mradi huo ambao unagharimu Sh. bilioni tisa utaondoa gharama kubwa za kuzalisha umeme kwa mafuta ya dizeli, utawezesha Shule ya Msolwa kuwa na umeme wa uhakika, utawezesha wananchi za vijiji vya Kisanga, Msolwa na Madizini kupata umeme wa uhakika kwa bei nafuu na utaunganishwa moja kwa moja kwenye gridi ya taifa katika jitihada za kupunguza tatizo la umeme nchini.
Gharama za umeme huo ambao utaanza kuzalishwa Januari mwakani zimechangiwa na Serikali ya Tanzania kupitia Mradi wa Umeme Vijiji – REA- na wananchi wa eneo hilo ambao wametoa eneo kwa ajili ya ujenzi wa mradi.
Rais Kikwete anaendelea na ziara yake katika Mkoa wa Morogoro leo.
Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
24 Agosti,2014
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ameupa wiki moja uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa, Mkoa wa Morogoro, kuwapatia viwanja vya kujenga nyumba wahanga wa mafuriko ya kiasi cha miaka minne iliyopita mjini Kilosa.
Rais Kikwete ametoa agizo hilo leo, Jumapili, Agosti 24, 2014 wakati alipozungumza na wananchi wa Kilosa katika mkutano wa hadhara uliofanyika mjini Kilosa baada ya kutembelea Wilaya hiyo kukagua na kuzindua miradi ya maendeleo.
Rais Kikwete amerejea Mkoani Morogoro asubuhi ya leo kuendelea na ziara yake ya siku saba mkoani huo baada ya kuikatisha jana, Jumamosi, Agosti 23, 2014, kwenda kwenye Chuo cha Uongozi wa Kijeshi, Monduli, Mkoani Arusha, ambako alikwenda kutoa kamisheni kwa maofisa wapya wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (TPDF).
Baada ya kuwa amelalamikiwa kwa maneno na kwa mabango na wahanga hao kuwa hawajapatiwa viwanja vya kujenga nyumba za kudumu baada ya kuwa wameahidiwa viwanja hivyo na Rais Kikwete mwenyewe wakati alipowatembelea kufuatia mafuriko ya Mto Mkondoa miaka minne iliyopita, Rais Kikwete amesema:
“Ni jambo la kusikitisha kuwa bado ahadi zangu kwenu hazijatimizwa. Niliahidi mambo mawili wakati nilipokuja kuwaoneni – moja niliahidi kuwa tutawapatia viwanja vya kuweza kujenga nyumba za kudumu na pili niliwaahidi kuwasaidia kujenga nyumba. Sasa tuanze na la kwanza,”alisema Rais Halmashauri hiyo kujieleza mbele ya wananchi hao kuhusu ahadi hizo.
Baada ya kuambiwa kuwa vimepimwa viwanja 800 katika Halmashauri hiyo, Rais Kikwete aliamuru kuwa kiasi cha viwanja 400 vitengwe kwa ajili ya wahanga hao wa mafuriko.
“Katika muda wa wiki moja, yaani kuanzia kesho Jumatatu hadi kufikia Ijumaa, nataka taratibu zote kuwa zimekamilika na kila mtu kuwa ameonyeshwa kiwanja chake. Tutazingumzia habari ya ujenzi baadaye,” alisema Rais Kikwete.
Mapema asubuhi, Rais Kikwete ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa Mradi wa Kufua Umeme katika eneo la Msolwa, Wilaya ya Kilosa, mradi ambao unajengwa na Shirika la Watawa wa Madonda Matakatifu ya Yesu la Stigmatine Fathers and Brothers la Kanisa Katoliki ambalo lilianza shughuli zake katika Wilaya ya Kilosa Novemba 1989.
Mradi huo wa Yovi Mini Hydropower Project unajengwa kwenye milima na maporomoko ya Mto Yovi na unalenga kuzalisha megawati kati ya moja na 2.3 kwa ajili ya mamia kwa mamia ya watumiaji katika eneo hilo ikiwamo shule maarufu na ya mfano ya sekondari ya Msolwa St. Gaspar iliyofunguliwa na Shirika la Stigmatine mwaka 1994.
Mradi huo ambao unagharimu Sh. bilioni tisa utaondoa gharama kubwa za kuzalisha umeme kwa mafuta ya dizeli, utawezesha Shule ya Msolwa kuwa na umeme wa uhakika, utawezesha wananchi za vijiji vya Kisanga, Msolwa na Madizini kupata umeme wa uhakika kwa bei nafuu na utaunganishwa moja kwa moja kwenye gridi ya taifa katika jitihada za kupunguza tatizo la umeme nchini.
Gharama za umeme huo ambao utaanza kuzalishwa Januari mwakani zimechangiwa na Serikali ya Tanzania kupitia Mradi wa Umeme Vijiji – REA- na wananchi wa eneo hilo ambao wametoa eneo kwa ajili ya ujenzi wa mradi.
Rais Kikwete anaendelea na ziara yake katika Mkoa wa Morogoro leo.
Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
24 Agosti,2014