Taarifa kwa vyombo vya Habari ya zamani
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amemteua Mhandisi (Eng.) Bashir J. Mrindoko kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji kwa kumpandisha cheo kutoka nafasi ya Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo.
Aidha, Rais Kikwete amemhamisha Mhandisi Mbogo Paulo Futakamba, Naibu KatibuMkuu, Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika kwenda Wizara ya Maji kujaza nafasi iliyoachwa na Mhandisi Bashir Mrindoko.
Taarifa iliyotolewa Dar es Salaam leo, Jumanne, Oktoba 15, 2013, na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue imesema kuwa vile vile Rais Kikwete amemteua Mhandisi Raphael Leyan Daluti kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika kuchukua nafasi ya Mhandisi Futakamba.
Kabla ya uteuzi wake, Mhandisi Daluti alikuwa Mkurugenzi wa Idara ya Umwagiliaji naHuduma za Ufundi katika Wizara hiyo ya Kilimo, Chakula na Ushirika.
Balozi Sefue amesema katika taarifa yake kuwa uteuzi na uhamisho huo umeanza Oktoba 13, mwaka huu, 2013.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
15 Oktoba, 2013
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Tanzania na Marekani zimeimarisha mahusiano yao katika kipindi cha miaka minne iliyopita kutokana na uhusiano na ushirikiano mzuri wa balozi anaemaliza muda wake nchini Mh. Alfonso Lenhardt.
“Asante kwa kazi nzuri uliyoifanya katika kipindi chote cha miaka minne uliyoitumikia hapa Tanzania. Mambo mengi na makubwa yenye kuleta maendeleo na manufaa kwa Tanzania yamefanyika hapa nchini na umeyasimamia na kuyafanikisha ipasavyo” .
Rais Jakaya Mrisho Kikwete amemueleza Balozi Lenhardt leo alipofika Ikulu kuaga na kumshukuru Rais na serikali yake kwa ushirikiano alioupata katika kipindi chake cha ubalozi hapa nchini.
Rais Kikwere amesema ushirikiano wa nchi hizi mbili umekua na kuimarika zaidi na anatarajia kuwa balozi ajaye naye atakuwa na mchango mkubwa katika kuendeleza na kuimarisha zaidi mahusiano baina ya nchi hizi.
Naye balozi Lenhart amesema Tanzania iko moyoni mwake na ataendelea kuwa balozi wa Tanzania popote alipo .
“ Nikushukuru wewe mheshimiwa Rais na serikali yako kwa ushirikiano mzuri na utayari wa kunisikiliza na kunisaidia wakati wote nilipohitaji ushauri wako, umekuwa msaada mkubwa kwangu. Asante kwa ushirikiano wako na siku zote nitaendelea kuwa balozi wa Tanzania kwani Tanzania iko moyoni mwangu”.
Mapema Balozi Lenhardt alipata nafasi ya kumtakia Rais Kikwete siku njema ya Kuzaliwa na kumpatia zawadi kama kumbukumbu ya siku hii ya leo na mara baada ya mazungumzo Rais na balozi wakapata nafasi ya kula chakula cha mchana pamoja na mama Salma Kikwete na Mama Jacqueline Lenhardt, ambaye ni mke wa balozi Lenhardt.
Imetolewa na;
Premi Kibanga,
Mwandishi wa Habari wa Rais Msaidizi,
Ikulu,
Dar es Salaam.
07 October, 2013
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amewataka viongozi nchini kuacha mara moja tabia ya kuruhusu watu wachache kukalia maeneo makubwa ya ardhi bila kuyaendeleza akisisitiza kuwa kufanya hivyo ni kuzuia maendeleo.
Aidha, Rais Kikwete amewataka viongozi wa Wilaya ya Kisarawe katika Mkoa wa Pwani kukutana na watu wote wanaomiliki maeneo makubwa ya ardhi wilayani humo na kuwataka kuelezea mipango yao ya kuiendeleza ardhi hiyo vinginevyo wayang’anywe ardhi hiyo.
Rais Kikwete alitoa maagizo hayo jana, Jumapili, Oktoba 6, 2013, wakati alipokuwa akipokea taarifa ya maendeleo ya Wilaya hiyo akiwa katika siku yake ya nne ya ziara ya mkoa wa Pwani kukagua na kuzindua miradi ya maendeleo.
Rais Kikwete amesema kuwa raslimali kuu ya maendeleo katika Wilaya ya Kisarawe, na kwa hakika nchi nzima, ni ardhi.
“Sasa nyie viongozi, kuna watu mmewapa ardhi, tena wengine maeneo makubwa sana ya ardhi, hawayaendelezi. Watu hawa wanazuia maendeleo ya wilaya yenu na wananchi wenu. Nyie viongozi mnazuia maendeleo ya watu wetu hawa masikini. Wabaneni hawa kwa sababu wengi wao ni walanguzi tu na wala hawana nia ya kuendeleza ardhi wanayomiliki,” alisema Rais Kikwete na kuongeza:
“Wabaneni watu hawa waifanyie ardhi mambo ambayo walioombea. Vingine wairudishe ardhi hii ili itumiwe na wengine kuiendeleza wilaya yenu.”
Amesisitiza Rais Kikwete: “Msiwaachie watu hawa, wabaneni waiendeleza ardhi. Siyo nia ya Serikali kuwanyang’anya ardhi wanayomiliki lakini ni lazima watupe mipango yao ya namna wanakusudia kuiongezea ardhi hiyo thamani. Pale Mtwara kuna mtu alikuwa anashikilia eneo kubwa bila kuliendeleza. Viongozi wa Mtwara wakaleta mapendekeza kwangu tuchukue sehemu ya ardhi hiyo kwa ajili ya ujenzi wa kiwanda cha saruji. Sasa kiwanda hicho kimeanza kujengwa.”
Hata hivyo, Rais Kikwete amesema kuwa inawezekana viongozi katika sehemu mbali mbali wanashindwa kuchukua hatua kuhusu ardhi kwa sababu na wao ni sehemu ya wamiliki. “Na wengine wamo katika chumba hiki, lakini kama mnafanya hivyo na nyie mnakwamisha maendeleo ya watu wenu. Ardhi ni raslimali kubwa sana ya maendeleo na kamwe haiwezi kuachwa bila kuongezewa thamani.”
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
7 Oktoba, 2013
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Leo, Jumatatu, Oktoba 7, 2013, zimetungwa habari, zikaingizwa kwenye Mitandao ya Kijamii na kusambazwa sana zikidai kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ametia saini Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ambao ulipitishwa na Bunge katika Kikao chake cha mwezi uliopita.
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu inapenda kufafanua kama ifuatavyo:
(a) Kwanza, Ofisi ya Rais, Ikulu haijapokea Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba. Inawezekana Muswada huo umekwishakutumwa kutoka Bungeni lakini haujamfikia Mheshimiwa Rais. Hivyo, kama haujamfikia, Mhe. Rais hawezi akawa ameutia saini
(b) Pili, Muswada huo ukimfikia Mheshimiwa Rais, inatarajiwa kuwa atautia saini kwa sababu Muswada huo umepitia katika mchakato sahihi na halali wa Kikatiba kwa maana ya kufikishwa Bungeni na Serikali, Kujadiliwa na hatimaye kupitishwa na Bunge.
(c) Tatu, kama yapo marekebisho ambayo yanaonekana yanafaa kufanywa katika Sheria hiyo, basi yatafanywa na Bunge baada ya Mhe. Rais kuwa ametimiza matakwa ya Kikatiba ya kutia saini Muswada ambao umepitishwa na Bunge kwa kufuatia mchakato sahihi na halali wa Kikatiba.
(d) Nne, na wala hii haitakuwa mara ya kwanza kwa Sheria kupitishwa na Bunge, ikatiwa saini na Mhe. Rais na baadaye kufanyiwa marekebisho na Bunge baada ya kuonekana umuhimu wa kufanya marekebisho hayo. Mwishoni mwa mwaka 2012, Sheria ya Marekebisho ya Katiba ilipitia njia hiyo.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
7 Oktoba, 2013
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Ofisi ya Rais, Ikulu, na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) leo, Jumatatu, Oktoba 7, 2013, zimetiliana saini mkataba ambako UNDP itaunga mkono jitihada za Serikali za kuanzisha Kitengo cha Kuharakisha Huduma za Kilimo (ADD) ndani ya Kitengo cha Rais cha Kuharakisha Huduma kwa Wananchi (Presidential Delivery Burea – (PDB).
Chini ya makubaliano hayo yaliyotiwa saini Ikulu, Dar Es Salaam, UNDP itaipatia PDB kiasi cha dola za Marekani milioni 9.5 ambazo zimetolewa kwa pamoja na Taasisi ya Bill and Melinda Gates ya Marekani na UNDP yenyewe.
Waliotia saini waraka wa makubaliano ambao unajulikana kama “Catalyzing Agricultural Developmenmt in Tanzania – Agricultural Delivery Division ni Katibu Mkuu Ikulu, Bwana Peter Ilomo kwa niaba ya Ofisi ya Rais, Ikulu na Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa na Mwakilishi Mkazi wa UNDP, Bwana Alberic Kacou.
Fedha hizo zitatumika kutoa msaada wa kiufundi na kusaidia kuanzishwa kwa Kitengo kipya cha ADD.
Akizungumza kwenye hafla hiyo fupi, Bwana Kacou amesema kuwa chini ya makubaliano hayo, fedha hizo zitatumika kwa kipindi cha miaka mitatu na ameishukuru PDB, Ofisi ya Rais na Ofisi ya Waziri Mkuu kwa uongozi wao ambao umewezesha UNDP, Bill and Melinda Gates Foundation, kuunga mkono jitihada hizo za Serikali.
Serikali ya Tanzania imeanzisha PDB kwa nia ya kuharakisha huduma kwa wananchi katika sekta sita muhimu kwa maendeleo ya wananchi.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
7 Oktoba, 2013
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Ofisi ya Rais, Ikulu, imeanza mawasiliano na viongozi wa vyama vya siasa nchini vyenye hoja kuhusu Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba uliopitishwa karibuni na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa nia ya kuandaa mkutano kati ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete na viongozi wa vyama hivyo.
Mawasiliano hayo yameanza leo, Jumatatu, Oktoba 7, 2013, kufuatia maelekezo ya Rais Kikwete kwa Ofisi ya Katibu wa Rais.
Kufuatia matukio yaliyotokea Bungeni wakati wa kujadiliwa na kupitishwa kwa Muswada huo mwezi uliopita, na maneno na kauli mbali mbali ambazo zimetolewa na wabunge wa vyama vya upinzani na wadau wengine kufuatia kupitishwa kwa Muswada huo na Bunge, Rais Kikwete katika hotuba yake kwa wananchi Ijumaa iliyopita, Oktoba 4, 2013, alisema kuwa hoja na kauli za wanaopinga Muswada huo zinazungumzika kwa nia njema ya kutafuta mwafaka katika mchakato wa kutafuta Katiba Mpya.
Kwa mujibu wa maandalizi hayo, Ofisi ya Rais, Ikulu inaangalia uwezekano wa kuitisha mkutano huo Jumapili ya Oktoba 13 ama Jumanne ya Oktoba 15, mwaka huu.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
7 Oktoba, 2013
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amerejea nchini mchana wa leo, Jumatatu, Septemba , 2013, baada ya ziara ya kikazi yenye mafanikio makubwa katika Marekani na Canada.
Miongoni mwa shughuli nyingine nyingi katika ziara hiyo, Rais Kikwete alihutubia Kikao cha 68 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UN) mjini New York.
Rais Kikwete ambaye aliondoka nchini Jumapili ya Septemba 15 alianzia safari yake mjini San Francisco, Marekani, ambako miongoni mwa mambo mengine alizindua Ubalozi Mdogo wa Tanzania katika Jimbo la California.
Rais pia alikutana na kuzungumza na Jumuia ya Watanzania katika Jimbo hilo na kukaribishwa katika Jiji la Vallejo katika sherehe za miaka 20 za uhusiano wa kimji kati ya Jiji hilo na mji wa Bagamoyo.
Ziara ya Rais Kikwete San Francisco ilifuatiwa na ziara ya mjini Washington ambako shughuli zake kubwa zilikuwa kukutana na viongozi wa Bunge la Marekani na pia kuhudhuria Hafla ya Chakula cha Usiku cha Taasisi ya Kulinda Hifadhi na Mazingira ya Bunge la Marekani (ICCF) ambako alitunukiwa tuzo maalum za Mtunzaji Mazingira Bora wa Mwaka.
Aidha, Rais Kikwete alishuhudia utiaji wa saini mikataba ya kufungua Ofisi Ndogo za Ubalozi wa Tanzania katika majimbo mbali mbali ya Marekani.
Baada ya hapo, Rais Kikwete alikwenda Canada ambako alitunukiwa Shahada ya Uzamivu ya Udaktari wa Sheria na Chuo maarufu na kikongwe cha Canada cha Guelph ambacho ni maarufu duniani kwa shughuli na utafiti wa kilimo.
Kufuatia ziara hiyo ya Canada, Rais Kikwete alikwenda New York ambako alikuwa na shughuli nyingi ikiwa ni pamoja na kuhutubia Kikao cha 68 cha Baraza Kuu la UN Ijumaa ya wiki iliyopita, akakutana na Katibu Mkuu wa UN Mheshimiwa Ban Ki Moon, akashiriki kikao maalum cha wakuu wa nchi kujadili hali ya Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) kilichoitishwa na Mheshimiwa Ban Ki Moon.
Akiwa mjini New York, Rais Kikwete pia alikuwa kiongozi pekee wa Afrika aliyealikwa kushiriki katika Mkutano wa Rais wa Marekani Mheshimiwa Barack Obama na taasisi zisizokuwa za kiserikali duniani na pia alihudhuria Halfa Maalum iliyoandaliwa na Rais Obama alipomaliza kuhutubia Kikao cha 68 cha Baraza Kuu la UN.
Aidha, Rais Kikwete alishiriki Mkutano wa Mwaka wa Taasisi ya Clinton Global Initiative na pia akawa mzungumzaji rasmi katika Mkutano wa Kupambana na Ujangili Duniani uliotishwa na Rais Ali Omar Bongo Ondemba wa Gabon.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
30 Septemba, 2013
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ametangaza kuwa ataliamrisha Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kuongoza mapambano dhidi ya ujangili wa tembo na faru na ukataji haramu wa miti kwa shughuli za biashara ambao umefikia kiwango kikubwa Tanzania.
Aidha, Rais Kikwete amesema kwamba sekta ya utalii katika Tanzania sasa imeanza kutishiwa kweli kweli na uuaji wa wanyama hao na biashara haramu ya meno ya tembo na faru na kuwa tishio hilo ni kubwa kwa sababu sekta ya utalii inachangia kiasi cha asilimia 17 katika Mapato ya Taifa na inaajiri kiasi cha watu 300,000.
Rais Kikwete ametangaza uamuzi huo makini jioni ya leo, Alhamisi, Septemba 26, 2013 wakati alipozungumza kwenye Mkutano wa Viongozi wa Nchi na Serikali kuhusu biashara haramu ya wanyama na bidhaa zake pamoja na biashara haramu ya bidhaa za miti na mbao.
Rais Kikwete ameuambia Mkutano huo ulioandaliwa na Rais Ali Omar Bongo Ondimba wa Gabon na Serikali ya Ujerumani kwenye Makao Makao ya Umoja wa Mataifa kuwa mwaka 1960, Tanzania ilikuwa na tembo kiasi cha 350,000 lakini kutokana na ujangili idadi hiyo ya tembo ilishuka hadi 110,000 ilipofika mwaka 2009. Kuhusu faru, Rais Kikwete amesema kuwa mwaka 1974 walikuwepo faru 700 katika Tanzania na sasa wako chini ya 100 kwa sababu ya vitendo vya kijangili.
“Katika miaka ya 1980 na 1990 wakati wa kilele cha ujangili katika mikonga ya wanyama, tulilazimika kutumia jeshi kutuliza hali hiyo. Tuliona matokea mazuri na tulikuwa na utulivu wa aina fulani. Lakini katika miaka minne iliyopita, tumeshuhudia kuongezeka kwa vitendo vya ujangili kwa ari na kasi mpya. Kwa mfano kati ya mwaka 2010 na Julai, mwaka, 2013, zaidi ya tembo 1,386 waliuawa katika Tanzania.”
Ameongeza Rais Kikwete: “Tumechukua hatua kali za kupambana na ujangili ikiwa ni pamoja na sera, sheria na kanuni za kupambana na ujangili. Aidha, tumetia saini mikataba mbali mbali ya kimataifa ya kupambana na ujangili huu.” Amesema Rais Kikwete na kuongeza:
“Vile vile, tumechukua hatua za kukamata majangili na hata kukamata silaha zinazotumika katika ujangili. Kati ya mwaka 2010 hadi katikati ya mwaka huu, 2013, jumla ya majangili 5,189 wametiwa mbaroni na silaha kiasi cha 1,952 zimekamatwa. Isitoshe, vipande vya 3,788 vya meno ya tembo vimekamatwa vikiwa na uzito wa kilo 10,756 zilikamatwa nchini. Nimeamuru Jeshi la Wananchi wa Tanzania kukabiliana na hali hiyo na naamini kuwa tutapata mafanikio makubwa zaidi katika operesheni inayoandaliwa.”
Hata hivyo, Rais Kikwete amesema kuwa bado shughuli za kupambana na ujangili, zinakabiliwa na changamoto nyingi ikiwa ni pamoja na mahitaji ya watumishi 4,800 wapya kwa ajili ya kupambana na ujangili hata kama wameajiriwa wafanyakazi 500 tu mwaka huu.
“Pamoja na kwamba tuna matatizo ya watumishi, bado pia tuna matatizo ya raslimali fedha. Bajeti ya sasa ya dola za Marekani 6.9 milioni kwa ajili ya Idara ya Wanyamapori haitoshi kutimiza yote haya. Tunahitaji dola za Marekani milioni 19.4 kwa ajili ya shughuli hiyo na nyongeza ya dola milioni 30 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa na ujenzi wa nyumba za wafanyakazi. Tukiachiwa pekee yetu hatuna uwezo. Tunaomba twende pamoja katika hili.”
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
26 Septemba, 2013
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa Mifuko ya Hifadhi nchini itaendelea kuchangia maendeleo ya Tanzania kwa kugharimia miradi mbali mbali nchini lakini kwa namna ya kuilinda ili Serikali isije kuua bata wa dhahabu anayetaga mayai ya dhahabu.
Rais pia amesema kuwa Mifuko ya Hifadhi yote katika Tanzania ni salama kabisa na hatairajiwi kukumbwa na changamoto za ukwasi hadi mwaka 2040 ikitokea kunakuwepo na hitilafu katika uendeshaji wa Mifuko hiyo ama baadhi yake.
Rais pia amesema kuwa misaada inayotolewa na Shirika la Misaada ya Maendeleo la Marekani la Millennium Challenge Corporation (MCC) ni ya aina yake duniani kwa sababu wanufaika wakubwa wa misaada hiyo wanapewa uhuru wa kuamua ni miradi gani ndani ya nchi igharimiwa na misaada ya MCC.
Vile vile, Rais amezitaja sekta kubwa ambako wawekezaji kutoka Marekani wanaweza kuweza mitaji yao kama njia ya kuongeza uwekezaji wao katika Tanzania na hivyo kusaidia kukuza kwa kasi zaidi uchumi wake.
Rais Kikwete alikuwa akizungumza leo, Alhamisi, Septemba 26, 2013, kwenye Hoteli ya Hyatt, mjini New York, Marekani katika Mkutano wa Uwekezaji wa nchi chache za Afrika na wafanyabiashara wa Marekani ulioandaliwa na MCC yenyewe na kufanyika chini ya uenyekiti wa Mtendaji Mkuu wa Shirika hilo, Bwana Daniel W. Yohannes.
Mkutano huo ambao kaulimbiu yake ilikuwa, “Africa’s Economic Transformation” umehudhuriwa na viongozi wa nchi nne ambazo zilizonufaika na awamu ya kwanza ya miradi mikubwa ya MCC, Tanzania ikiwa ndiyo nchi iliyopewa fedha zaidi za Shirika hilo duniani za kiasi cha dola za Marekani 698 ambazo zimeingizwa katika miradi ya miundombinu ya barabara, usambazaji umeme vijiji, ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Mafia na usambazaji wa huduma ya maji katika Jiji la Dar Es Salaam na Manispaa ya Morogoro.
Tanzania sasa imeanza majadiliano na MCC kuhusu awamu ya pili ya msaada wa Shirika hilo.
Mbali na Rais Kikwete, viongozi wengine ambao wamehudhuria Mkutano huo ni Rais Armando E.Guebuza wa Mozambique, Waziri Mkuu wa Lesotho Mheshimiwa Tom Thabane na Waziri Mkuu wa Morocco Mheshimiwa Abdalleh Benkiane.
Akijibu maswali katika Mkutano huo baada ya kuwa ametoa hotuba yake, Rais Kikwete amesema kuwa hakuna shaka kuwa Mifuko ya Hifadhi nchini imeanza kuchangia kwa kiasi kikubwa miradi ya maendeleo na itaendelea kufanya hivyo kwa namna ya kuifanya mifuko yenyewe endelevu.
“Hakuna shaka kuwa Mifuko ya Hifadhi Tanzania sasa imeanza kuchangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya nchi yetu. Kwa kiasi kikubwa ilikuwa fedha ya Mifuko hiyo iliyosaidia kujenga Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) na inachangia miradi mingine mingi,” amesema Rais Kikwete na kuongeza:
“Isitoshe, mifuko yetu yote ni salama na ina afya nzuri. Haitarajiwi kuwa inaweza kupata matatizo kwa miaka mingi ijayo hadi mwaka 2040 na matatizo yatatokea tu kama tukiendesha mambo yetu vibaya. Tunaitumia mifuko yetu vizuri na kwa manufaa ya maendeleo ya nchi yetu. Tutaitumia vile vile kwa namna endelevu yaani tusije tukaua bata wa dhahabu ambaye anataga mayai ya dhahabu.”
Kuhusu misaada ya MCC, Rais Kikwete amesema kuwa “misaada hiyo ni ya aina yake duniani kwa sababu ina uhuru. Nchi inayopewa msaada inapewa uhuru wa kuamua yenyewe ni miradi gani igharimiwe na msaada unaotolewa na MCC. Ni modeli nzuri na aina yake duniani.”
Amesisitiza Rais Kikwete: “Nani angekubali kugharimia barabara za Namtumbo hadi Songea? Nani angegharimia barabara ya kutoka Tunduma hadi Sumbawanga? MCC imekubali kutupa fedha ya kugharimia miradi hiyo baada ya kuwa sisi wenyewe tumefanya uamuzi”.
Rais Kikwete ameongeza: “Isitoshe, MCC inachukua muda mfupi kufanya maamuzi. Hata pale ambako sisi tunaopewa pesa tunalazimika kupata kibali cha matumizi ama kufanya mabadiliko kwenye maamuzi kuhusiana na miradi inayogharimiwa na MCC, uamuzi unachukuliwa kwa haraka bila ucheleweshaji ambao tunakumbana nao katika mahusiano yetu na baadhi ya mashirika ya kimataifa.”
Kuhusu nafasi za uwekezaji katika Tanzania, Rais Kikwete amewaambia wawekezaji hao kuwa nafasi ziko katika sekta za ujenzi wa miundombinu ya barabara, reli, bandari za Mtwara na Tanga, na umeme; sekta ya utafutaji na uchimbaji wa gesi na utoaji wa huduma kwa sekta hiyo mpya katika Tanzania; uwekezaji katika sekta ya uvuvi; uwekezaji katika sekta ya kilimo na viwanda vinavyotegemea kilimo; uwekezaji katika utalii iwe Tanzania ama Tanzania Visiwani.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
26 Septemba, 2013
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete jioni ya leo, Alhamisi, Septemba 26, 2013, ametembelea Ubalozi wa Kudumu wa Kenya Umoja wa Mataifa(UN), New York, Marekani na kutia saini Kitabu cha Rambirambi kufuatia vifo vya watu 69 na mamia kujeruhiwa katika shambulio la kigaidi mjini Nairobi mwishoni mwa wiki.
Rais Kikwete amewasili kwenye Ubalozi wa Kudumu wa Kenya Umoja wa Mataifa, Jengo 866 UN Plaza, kiasi cha saa 8:30 kamili baada ya kutembea kwa mguu na walinzi wake kutoka Makao Makuu ya UN yaliyoko karibu kwenda Ubalozini ambako alipokelewa na Balozi Koki Muli Grignon, Naibu Mwakilishi wa Kudumu wa Kenya UN kwa niaba ya Balozi Macharia Kamau ambaye yuko nje ya Marekani.
Baada ya kuwa ametia saini Kitabu cha Rambirambi, Rais Kikwete amezungumza kwa ufupi na wafanyakazi wa Ubalozi huo na kupiga nao picha akisema kuwa amekwenda kwenye Ubalozi huo kuelezea majonzi na hasira yake kufuatia vifo vya watu hao pamoja na kujeruhiwa kwa mamia ya watu katika shambulio la kigaidi lilitokea Jumamosi, wiki iliyopita, katika Kituo cha Maduka cha Westgate, eneo la Westlands, Nairobi.
“Siku ile ya tukio nilikuwa natokea Canada kuja Marekani na nililiona tukio hilo kwenye televisheni, bado nikiwa Canada. Nilimpigia simu Rais Kenyatta na kuzungumza naye. Nilimweleza masikitiko yangu na hasira yangu kwa shambulio hilo dhidi ya watu wasiokuwa na hatia na raia wasiokuwa na ujuzi wowote wa kupigana,” Rais Kikwete amesema na kuongeza:
“Nilimweleza Rais Kenyatta masikitiko na hasira yangu kuhusu kitendo hicho. Nilimwelezea utangamano wa Watanzania na Wakenya katika tukio hilo. Nilimwambia kuwa wananchi wa nchi zote mbili wako pamoja katika kipindi hiki kigumu, ni majirani na watu wale wale. Nilimwambia kuwa tutaendelea kushirikiana katika kupambana na ugaidi kwa sababu wakati wa tukio hilo la Septemba mwaka 1998, Nairobi na Dar ES Salaam wote waliathirika.”
Ameongeza: ”Nilimwambia Rais Kenyatta kuwa Tanzania iko tayari kusaidia katika kuchangia mawazo na raslimali kutafuta suluhisho la tukio hili kama msaada wetu ungehitajika. Nilimtakia yeye na wananchi wa Kenya kuwa na moyo wa uvumilivu na subira katika kipindi hiki kigumu.”
Naye Balozi Koki Muli Grignon amemwambia Rais Kikwete: “Kwa niaba ya wafanyakazi wote wa Ubalozi wa Kenya Umoja wa Mataifa, nataka kukuelezea kuwa umetupa heshima kubwa sana kwa kuja hapa, umetupa hamasa na ari. Pamoja tutapambana kukomesha ugaidi katika eneo letu la Afrika Mashariki. Ujio wako umetushangaza, umemshangaza kila mtu kwenye Ubalozi. Hatukutarajia kabisa. Tunakushukuru sana Mheshimiwa Rais.”
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
26 Septemba, 2013
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa Serikali yake inalifanyia mageuzi muhimu na marekebisho makubwa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kwa nia ya kuharakisha jitihada za Serikali kusambaza umeme kwa wananchi wengi zaidi.
Aidha, Rais Kikwete amesema kuwa Serikali imechukua hatua nyingi na kali za kupambana na rushwa kwa nia ya kukomesha vitendo hivyo katika Tanzania na kuinua kiwango cha utawala bora.
Rais Kikwete ameyasema hayo leo, Jumatano, Septemba 25, 2013 wakati alipokutana na kuzungumza na ujumbe wa Shirika la Misaada ya Maendeleo la Marekani la Millennium Challenge Corporation (MCC) ukiongozwa na Mtendaji Mkuu wake, Bwana Daniel W Yohannes.
Ujumbe huo umekutana na Rais Kikwete katika Hoteli ya JW Marriott mjini New York ambako Rais Kikwete amefikia kwa ziara yake ya kikazi katika Marekani ambako miongoni mwa mambo mengine atahutubia Mkutano wa 68 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UN) ulioanza jana, Jumanne, Septemba 24, 2013.
Katika mazungumzo hayo, Bwana Yohannes amemwelezea Rais Kikwete kuhusu maendeleo ya ombi la Tanzania kuingizwa katika awamu ya pili ya misaada ya Serikali ya Marekani kupitia MCC chini ya Akaunti ya Milenia Tanzania (MCA(T)). Nchi nyingine za Afrika ambazo maombi yao yanafikiriwa katika awamu hiyo ya pili ni Morocco, Mozambique na Lesotho.
Tanzania ndiyo nchi iliyopokea sehemu kubwa zaidi ya msaada wa MCC duniani katika awamu ya kwanza ambako ilipewa kiasi cha dola za Marekani milioni 698 ambazo zimeingizwa katika miradi mikubwa ya ujenzi wa barabara, usambazaji wa umeme vijijini, miradi ya maji na ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Mafia.
Serikali ya Tanzania imeamua kuwa fedha za awamu ya pili ya MCC zitaingizwa kupanua zaidi huduma za umeme na ujenzi wa barabara za vijiji kwa nia ya kuongeza idadi ya Watanzania wanaopata huduma za umeme na kwa nia ya kuboresha barabara za vijijini katika maeneo yanayozalisha mazao kwa wingi zaidi.
Serikali ya Rais Kikwete imeliweka suala la usambazaji umeme kwa Watanzania mijini na vijijini miongoni mwa maeneo yake ya kipaumbele. Wakati anaingia madarakani mwaka 2005, ni asilimia 10 tu ya Watanzania waliokuwa wanapata umeme. Katika miaka saba iliyopita, asilimia hiyo imepata hadi kufikia 21 ikiwa ni asilimia 11 zaidi kuliko katika miaka yote 50 ya Uhuru. Lengo la sasa ni kuifikisha asilimia 30 ama zaidi mwaka 2015.
Katika mazungumzo hayo na Rais Kikwete, Bwana Yohannes ametaka kujua ni hatua zipi Serikali inazichukua kurekebisha changamoto zinazoikabili TANESCO na hatua gazi zinachukuliwa kuzidi kukabiliana na matatizo ya rushwa.
Rais Kikwete amemweleza Bwana Yohannes: “Kama unavyojua, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limepitia safari ngumu na kukabiliwa na changamoto nyingi lakini sasa tumeamua katika Serikali kulifanyia mageuzi muhimu na marekebisho makubwa kwa maana ya muundo wake na pia kuangalia viwango vya malipo ambayo Shirika hilo linawatoza wateja wake. Mageuzi haya katika TANESCO ni muhimu sana na yameanza kufanyika na kwa hakika Serikali imedhamiria kukayamilisha mageuzi hayo katika muda mfupi iwezekanavyo.”
Kuhusu rushwa, Rais Kikwete amemwambia Bwana Yohannes, “Jitihada zetu katika kupambana na rushwa zinaendelea. Tumeimarisha taasisi inayohusika na kuzuia na kupambana na rushwa.Tumeimarisha mtandao wa kukabiliana na balaa hili na Serikali yangu imewafikisha mahakamani waliopata kuwa viongozi na maofisa waandimizi wa umma katika Serikali kujibu mashitaka ya rushwa na matumizi mabaya ya madaraka.”
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
25 Septemba, 2013
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete jioni ya jana, Jumanne, Septemba 24, 2013, ameendesha kikao chake cha kwanza kama Mwenyekiti wa Kamati ya Viongozi wa Nchi za Umoja wa Afrika Kuhusu Mazingira (CAHOSCO).
Rais Kikwete aliendesha kikao hicho kwenye Ofisi za Ubalozi wa Kudumu wa Umoja wa Afrika (AU) katika Umoja wa Mataifa mjini New York, Marekani. Ubalozi wa Kudumu wa AU una hadhi ya watazamaji katika UN.
Rais Kikwete alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Viongozi wa Nchi Wanachama wa AU mwanzoni mwa mwaka huu kuhusu Mazingira kufuatia kifo cha aliyekuwa mwenyekiti wa Kamati hiyo Mheshimiwa Meles Zenawi, Waziri Mkuu wa zamani wa Ethiopia aliyefariki na kuzikwa Septemba, mwaka jana, 2012.
Kikao hicho kilihudhuriwa na nchi zote wanachama wa Kamati ya Mazingira ya AU ikiwa ni pamoja na Mozambique ambayo iliwakilishwa na Mheshimiwa Rais Armando Guebuza, Waziri Mkuu wa Ethiopia Mheshimiwa Haile Mariam Deselengy pamoja na mawaziri na wawakilishi wa nchi za Algeria, Uganda, Senegal, Swaziland, Mauritius na Jamhuri ya Congo.
Kikao hicho kilikuwa kinajadili namna ya kukubaliana kuhusu msimamo wa Afrika utakaowakilishwa katika Mkutano wa Dunia wa Mazingira wa Novemba mwaka huu nchini Poland.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
25 Septemba, 2013
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa hakuna shughuli za biashara haramu ya binadamu inayofanywa katika Tanzania bali barabara za Tanzania na ardhi yake inatumiwa kupitisha biashara hiyo.
Hata hivyo, Rais Kikwete amesema kuwa Serikali yake itaendelea kushirikiana na nchi jirani kuhusu chimbuko la biashara hiyo na katika kuchukua hatua za kukomesha vitendo hivyo haramu.
Rais Kikwete ametoa msimamo huo wa Tanzania leo, Jumatano, Septemba 25, 2013, wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na ujumbe wa Shirika la Misaada ya Maendeleo la Marekani la Millennium Challenge Corporation (MCC) ukiongozwa na Mtendaji Mkuu wake, Bwana Daniel W. Yohannes.
Ujumbe huo ulikutana na Rais Kikwete katika Hoteli ya JW Marriott, mjini New York, ambako amefikia kwa ziara yake ya kikazi nchini Marekani na Bwana Yohannes na wenzake walikuwa wanamwelezea Rais Kikwete maendeleo ya ombi la Tanzania la awamu ya pili ya misaada ya maendeleo baada ya kumalizika kwa awamu ya kwanza.
Katika mazungumzo hayo, Bwana Yohannes ametaka kujua hatua ambazo zinachukuliwa na Serikali ya Rais Kikwete kukabiliana na baadhi ya mambo yanayojitokeza kuwa changamoto katika utekelezaji wa miradi ya MCC kupitia Shirika la Tanzania la Millennium Challenge Account Tanzania – MCA (T).
Baadhi ya changamoto ambazo Bwana Yohannes amezitaja ni pamoja na nini kinafanyika kuhusu TANESCO, kuhusu juhudi za kupambana na rushwa na jinsi gani ya kukabiliana na biashara haramu ya binadamu.
Rais Kikwete ametoa majibu ya changamoto zote tatu na kumweleza Bwana Yohannes kuwa biashara haramu ya binadamu haifanyiki wala kuanzia katika Tanzania na kuwa inaanzia Ethiopia, inapitia Kenya, Tanzania, Malawi na kwenda hadi Afrika Kusini.
“Wanakusanya watu katika Ethiopia na kuna mtu anapewa fedha na watu hao wanaokusanywa. Wanakuja Kenya na kuna mtu wa kuwapokea na kuwahudumia, wanakuja Arusha na hatimaye wanaingia Malawi na Afrika Kusini. Katika Tanzania wanapita tu na kuna wakati tulipata kukamata Waethiopia kiasi cha 19,000 na tukawarudisha kwao kwa gharama yetu,” amesema Rais Kikwete na kuongeza:
“Kutoka Ethiopia watu hawa wamekuwa kama mto usiokauka maji. Hivyo, sisi katika Tanzania tunafanywa kama njia ya kupitia tu. Ni kweli wako mawakala lakini kwa hakika biashara hii haifanyiki katika Tanzania. Inafanyika kwingine na nchi yetu inafanywa kama njia tu. Kuna wakati nilipata kuzungumza na viongozi wa Ethiopia na Kenya kuhusu suala hilo lakini bado tutaendelea kulifuatilia.”
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
25 Septemba, 2013
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Marekani Mheshimiwa Barack Obama ametoa pongezi na sifa kwa Tanzania kwa kuwa miongoni mwa nchi chache duniani ambazo zimetia saini mkataba wa Ushirikiano wa Serikali Zinazoendeshwa kwa Uwazi ambao unalenga kujenga na kuendeleza nafasi ya taasisi zisizokuwa za Kiserikali katika utawala bora, uwazi na uwajibikaji katika uendeshaji wa Serikali.
Rais Obama ametoa pongezi hizo kwa Tanzania leo, Jumatatu, Septemba 23, 2013, wakati akizungumza katika mkutano maalum aliouandaa mwenyewe Rais Obama kuzungumzia nafasi za Serikali katika kuunga mkono na kuendeleza asasi na taasisi zisizokuwa za Kiserikali na kuzishirikisha zaidi katika kuboresha shughuli za utawala bora uliofanyika kwenye Hoteli ya Hilton, mjini New York, Marekani.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete alikuwa miongoni mwa viongozi wachache duniani walioalikwa kushiriki mkutano huo maalum ambao pia ulishirikisha wawakilishi wa asasi zisizokuwa za Kiserikali 300.
Baadhi ya nchi nyingine za Afrika zilizoalikwa na kushiriki katika mkutano huo ni pamoja na Liberia, Ghana, Benin, Libya, Tunisia, Senegal, Afrika Kusini na Botswana.
Shabaha kuu ya mkutano huo wa saa moja ilikuwa ni kutafuta namna ya kuongeza kiwango cha kuungwa mkono kwa taasisi na asasi hizo na jinsi gani ya kuzilinda ili kuziwezesha kufanya kazi kwa ufanisi zaidi.
Aidha, mkutano huo ulilenga kuzitaka Serikali ambazo zinaweka vikwazo kwenye utendaji wa asasi hizo kuondoa vikwazo hivyo haraka ambavyo vinahujumu utendaji kazi na mchango wa asasi hizo katika uendeshaji wa utawala bora.
Katika hotuba yake ya ufunguzi wa mkutano huo, Rais Obama amezisifia nchi kama Tanzania ambazo zimetia saini makubaliano ya Ushirikiano wa Serikali Wazi ambayo yanalenga kupandisha nafasi ya asasi zisizokuwa za Kiserikali katika Utawala Bora,Uwazi na Uwajibikaji katika Serikali.
Amesema kuwa binafsi alikuwa ameamua kukutana na viongozi wa asasi zisizokuwa za kimataifa wakati wa ziara yake ya karibu katika Afrika ambako miongoni mwa nchi nyingine alitembelea Tanzania.
Rais Obama alifurahi sana kukutana na Rais Kikwete. Rais Obama alimkumbatia Rais Kikwete akimwelezea kama “kaka wa karibu na rafiki mzuri” kauli na kitendo ambacho kiliwashangaza mamia ya watu waliokuwa kwenye ukumbi.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
23 Septemba, 2013
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ameitaka Jumuia ya Kimataifa kufanya kila linalowezekana kumaliza mzozo wa kisiasa na mapigano katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), ili kutoa nafasi kwa wananchi wa Congo kuishi katika amani na kujitafutia maendeleo.
“Hawa ni watu walioteseka sana na kwa muda mrefu, wana haki ya kupata amani, wana haki ya kupata muda wa kupumzika kutokana na vita na mapigano,” Rais Kikwete ameuambia mkutano wa pili wa wakuu wa nchi zilizotia saini mkataba wa kutafuta amani, usalama na ushirikiano katika DRC chini ya Umoja wa Mataifa (UN).
Katika mkutano huo, uliofanyika leo, Jumatatu, Septemba 23, 2013, kwenye Umoja wa Mataifa mjini New York chini ya Uenyekiti wa Katibu Mkuu wa UN, Mheshimiwa Ban Ki Moon kama ulivyokuwa mkutano wa kwanza uliofanyika Februari 24, mwaka huu, 2013, mjini Addis Ababa, Ethiopia, Rais Kikwete amewaambia viongozi wenzake wa nchi wanachama wa Umoja wa Nchi za Maziwa Makuu (ICGLR) na wengine waliotia saini mkataba huo:
“Nadhani hatua zilizochukuliwa mpaka sasa kuhusu DRC ni nzuri na mchakato wa kutafuta amani nchini humo unakwenda vizuri. Ni muhimu tukafikia mwisho wa tatizo hili kwa sababu wananchi wa DRC wametesema mno na kwa muda mrefu. Wana haki ya kupata amani, wana haki ya kupata muda wa kutosha wa kufanya mambo ya maana kama ya maendeleo yao badala ya kukaa na kufikiria vita,” Rais Kikwete amesema kwenye mkutano huo.
Rais Kikwete amesema kuwa siri ya kufanikiwa katika DRC ni kutekeleza yale yote ambayo nchi hizo zimekubaliana kutekeleza katika DRC akisisitiza: “La msingi ni kila mmoja wetu kutekeleza yale yote tuliyokubaliana. Hiyo ndiyo siri ya kuleta amani na utulivu katika DRC.”
Mbali na Rais Kikwete, mkutano huo wa leo umehudhuriwa na Rais Yoweri Museveni wa Uganda ambaye pia ni Mwenyekiti wa ICGLR, Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini, Rais Joseph Kabila Kabange wa DRC, Rais Paul Kagame wa Rwanda, Rais Joyce Banda wa Malawi ambaye ni Mwenyekiti wa Jumuia ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AU) Mheshimiwa Nkosazana Dlamini-Zuma, na Katibu Mkuu wa UN ambaye alikuwa mwenyekiti wa mkutano huo.
Aidha, mkutano huo umehudhuriwa na Makamu wa Rais na wawakilishi wa Jamhuri ya Congo (Congo-Brazzaville), Zambia, Angola na Sudan Kusini.
Kwenye mkutano huo, wasemaji wengi wamesisitiza kuwa hakuna amani ya kweli katika DRC na nchi za Maziwa Wakuu bila viongozi wa nchi hizo kukubali kuzungumza na kukubaliana na vikundi mbali mbali ambavyo vinapigana dhidi ya baadhi ya nchi hizo.
Baadaye leo, Rais Kikwete amehudhuria mkutano wa Baraza la Uongozi la Umoja wa Kutafuta Usalama wa Chakula na Ushirikiano wa Grow Africa uliofanyika kwenye Ofisi za Taasisi ya Uchumi Duniani (WEF) uliofanyika kwenye ofisi za taasisi hiyo katika Marekani mjini New York.
Rais alizungumza kwa ufupi katika mkutano huo ambako alitaka wafadhili wa miradi ya kilimo katika Afrika kuongeza kasi ya kutoa fedha za kuleta mageuzi ya kilimo katika Bara la Afrika kwa sababu kila mmoja wa wadau anatekeleza majukumu yake kwa haraka zaidi kuliko wafadhili.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
23 Septemba, 2013
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa hakuna uporaji wowote wa ardhi unaofanywa na Serikali yake dhidi ya ardhi ya wananchi na hasa wakulima wadogo.
Aidha, Rais Kikwete amesema Serikali ya Tanzania haiwezi kupora ardhi ya wananchi na hasa wakulima wadogo kwa sababu sera za kilimo za Serikali zinalenga kumlinda mkulima mdogo na kumwezesha kujikomboa kutoka kwenye umasikini.
Rais Kikwete alitoa msimamo huo, kwa mara nyingine tena, mwishoni mwa wiki wakati alipozungumza na wana-jumuia ya Chuo Kikuu cha Guelph cha Toronto, baada ya kuwa ametunukiwa Shahada ya Uzamivu ya Heshima ya Sheria na Chuo hicho maarufu cha Canada.
Katika hotuba yake ya kupokea na kukubali shahada hiyo, Rais Kikwete ambaye alizungumzia maendeleo na changamoto za kilimo katika Afrika alisema kuwa kamwe Serikali ya Tanzania haiwezi kupora ardhi ya wakulima wadogo wadogo kwa sababu sera ya Serikali katika mipango yote mikubwa ya kilimo ni kumlinda na kumtetea mkulima mdogo.
“Hakuna uporaji wa ardhi unaofanywa na Serikali katika Tanzania kama inavyodaiwa na baadhi ya watu. Uporaji wa ardhi ya mkulima mdogo hauwezi kutokea katika Tanzania kwa sababu sera za Serikali ni kuhakikisha kuwa mkulima mdogo anakuwa mtu wa kwanza kunufaika na kufaidika na sera za kilimo za Serikali,” alisema Rais Kikwete na kuongeza:
“Mkulima mdogo yuko katikati ya mipango na sera za Serikali, na kwa kweli ndiye mtu muhimu zaidi katika mipango ya kilimo ya Serikali. Kazi ya wakulima wakubwa ambao tunawakaribisha kuwekeza katika Tanzania ni kuunga mkono shughuli za kilimo za wakulima wadogo kwa maana kweli kweli ya uwezeshaji.”
Rais Kikwete amesema kuwa kwa kadri Serikali inavyokaribisha wakulima wakubwa kuwekeza katika kilimo na uchumi wa Tanzania, ni dhahiri kuwa Serikali itaendelea kuwalinda na kuwatetea wakulima wadogo ambao watashirikiana na wakulima wakubwa katika kuboresha kilimo cha Tanzania.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
23 Septemba, 2013
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete jana, Ijumaa, Septemba 20, 2013, ametunukiwa Shahada ya Uzamivu (PHD) ya Udaktari wa Sheria (Honorary Degree of Doctor of Law (Honoris Cause) na Chuo Kikuu cha Guelph cha Toronto, Canada, katika sherehe ya kufana iliyohudhuriwa na mamia ya wasomi wa Chuo hicho wakiwemo wanafunzi na wahadhiri na Wana-jumuia ya Watanzania waishio Canada.
Naye Rais Kikwete ameitunuku Shahada hiyo kwa “Wananchi wote wa Tanzania na hasa wakulima wadogo ambao wanapigana kufa na kupona kuboresha maisha yao kupitia kilimo.”
Hiyo ni heshima ya juu kabisa ambayo Chuo Kikuu kinaweza kutoa kwa mwanadamu na Rais Kikwete anakuwa Mtanzania wa kwanza kutunukiwa Shahada hiyo katika historia ya zaidi ya miaka 100 ya Chuo hicho, maarufu kwa utafiti wa kilimo na magonjwa ya wanyama.
Maandamano maalumu ya kutunuku Shahada hiyo yameingia katika Ukumbi wa Kumbukumbu ya Vita – War Memorial Hall – kwenye Chuo hicho uliokuwa umefurika watu na baada ya nyimbo za taifa za Tanzania na Canada, Makamu Mkuu wa Chuo hicho na Kaimu Rais wa Chuo hicho, Dkt. Maureen Mancuso amefungua rasmi Baraza la Kutunuku Shahada.
Katika maelezo ya uamuzi wa Chuo hicho kutunuku Shahada hiyo kwa Rais Kikwete, Profesa Dkt. Kevin Hall amewaambia mamia ya wageni waliohudhuria sherehe hiyo kuwa Chuo hicho kimeamua kutoa Shahada hiyo kwa kutambua mchango wake katika kuendeleza, kuboresha na kuleta mageuzi katika kilimo cha Tanzania na Afrika.
“Tumeshuhudia kwa namna isiyokuwa ya kawaida kabisa jinsi gani Rais Kikwete amekuwa sauti isiyochoka ya kusemea kilimo cha Afrika na kuishawishi dunia katika kusaidia kuleta mageuzi na mapinduzi ya kijani katika Bara hili muhimu sana kwa kukabiliana na changamoto zinazokabili kilimo katika Bara la Afrika,” amesema Dkt. Hall ambaye ni Makamu wa Rais wa Chuo hicho anayesimamia shughuli za utafiti.
Ameongeza: “Kwa miongo mingi hatujashuhudia kiongozi mmoja wa Afrika akijitokeza kwa namna isiyofichika kabisa kukabiliana na chagamoto zinazokabili shughuli inayoajiri watu wengi sana na ambayo ni tegemeo kubwa la maisha ya mamilioni ya watu. Rais Kikwete tunakushukuru kwa mchango wako mkubwa katika kuleta mapinduzi ya kilimo katika Afrika kupitia progamu zako kama vile Kilimo Kwanza na SACGOT.”
Dkt. Mancuso amemvalisha Rais Kikwete skafu yake kuashiria tunuku ya Shahada ya Uzamivu kiasi cha saa 10 na nusu kamili na akamkaribisha kutoa hotuba yake ya kukubali heshima hiyo kubwa ya Chuo cha Guelph.
Rais Kikwete, kama kawaida yake anapozungumzia shughuli za kilimo, ametoa hotuba ya kusisimua ambayo ilizungumzia hali ya kilimo katika Tanzania na Afrika, changamoto kuu za kilimo na hatua ambazo zinachukuliwa kukabiliana na hali hiyo.
Akizungumzia umuhimu wa kilimo katika Tanzania amesema kuwa asilimia 75 ya Watanzania wanaishi maeneo ya mashambani na kutegemea kilimo kwa maisha yao na kuwa hata wale wanaoishi mijini uhai wao unategemea kilimo kwa njia nyingi.
“Kilimo kinatupa chakula tunachokula, mali ghafi ya viwanda vyetu, mapato yetu ya fedha za kigeni na ajira kwa ajili ya watu wetu. Kilimo kinaingiza asilimia 25 ya Pato la Taifa, asilimia 34 ya mapato yetu ya fedha za kigeni, asilimia 95 ya chakula chetu na kinaajiri asilimia 75 ya watu wetu. Kwa ufupi basi, maendeleo ya uchumi na ustawi wa wetu unategemea kilimo.”
Rais amesema kuwa “pamoja na umuhimu huo wa kilimo kwa Tanzania na Afrika, bado kilimo cha Bara hilo kinabakia cha jadi, kilicho duni na chenye sifa ya uzalishaji mdogo. Niruhusuni nitoe takwimu kufafanua hoja hii. Katika Tanzania hekta moja ya mahindi inazalisha tani 1.3, wastani wa Afrika ni tani 1.9, katika China ni tani 5.7 na hapa Canada naambiwa ni tani 10. Hivyo hivyo, kwa uzalishaji wa mpunga na pamba.”
Rais pia ametoa sababu ya uduni wa kilimo cha Afrika akisema kuwa moja ya sababu zake ni ukosefu wa teknolojia ya kutosha ya uzalishaji ambako bado jembe la mkono ndiyo zana kuu ya uzalishaji. Pili, alisema kuwa wakulima wanategemea sana mvua badala ya umwagiliaji, tatu, hakuna mbegu bora za kutoa mazao mengi zaidi, nne, kuna matumizi madogo zaidi ya mbolea, tano, kuna matumizi kidogo ya dawa za kukabiliana na magonjwa ya mazao, sita, wakulima wengi hawana uelewa wa kutosha wa mbinu za kisasa za kilimo na saba, hakuna njia rahisi za wakulima kupata mikopo kwa ajili ya kuendeleza kilimo chao.
“Angalia takwimu hii. Kwa wastani, mkulima wa Tanzania anatumia kilo 13 za mbolea kwa hekta moja, wastani wa Afrika ni kilo nane kwa hekta. Lakini katika Uholanzi ni kilo 577. Matumizi ya mbolea ni kidogo kwa sababu ya upatikanaji na bei yake kubwa. Mbolea ni ghali mno kwa mkulima,” amesema Rais Kikwete.
Baada ya kufafanua hali halisi, Rais Kikwete ameelezea hatua ambazo Serikali yake inachukua kukabiliana na hali hiyo ikiwa ni pamoja na kuanzisha Mpango Mkubwa wa Kuendeleza Kilimo wa ASDP na program za kutekelezaji wake kama vile Kilimo Kwanza na SACGOT.
Ameeleza jinsi Serikali yake ilivyopandisha bajeti ya kilimo kutoka sh. bilioni 233.2 mwaka 2005/6 hadi kufikia sh. trilioni 1.1 za sasa, jinsi mfuko wa ruzuku ulivyoongezewa bajeti kutoka sh. bilioni 8.5 mwaka 2005/6 hadi sh. bilioni 157.8 za sasa, uagizaji wa trekta ambao umeongezeka mara tatu kutoka matrekta 5,308 mwaka 2005/6 hadi kufikia matreka 14,668 kwa mwaka 2012/13.
Rais Kikwete pia amekishukuru Chuo Kikuu cha Guelph kwa kuanzisha na kudumisha ushirikiano wa karibu na taasisi na vyuo vikuu vya Tanzania kikiwamo Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine cha Morogoro na Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM). Ametaka ushirikiano huo udumishwe na kuendelezwa.
Kabla ya sherehe za tunuku, Rais Kikwete ametembelea na kujionea baadhi ya shughuli za utafiti za Chuo hicho ukiwamo utafiti wa mazao na utafiti wa magonjwa ya wanyama.
Shahada Uzamivu hiyo ni ya saba kutolewa kwa Rais Kikwete tokea aanze kuongoza Tanzania miaka minane iliyopita. Vyuo vikuu vingine ambavyo vimemtunuku Shahada za Uzamivu Rais Kikwete ni Chuo Kikuu cha St.Paul cha Minnesota, Marekani; Chuo Kikuu cha Kenyatta, Nairobi, Kenya; Chuo Kikuu cha Fatih cha Uturuki, Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam (UDSM), Chuo Kikuu cha Sayansi na Afya cha Muhimbili (MUHAS) na Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) na sasa Chuo Kikuu cha Guelph.
Rais Kikwete ambaye alikuwa katika ziara ya siku tatu ya kikazi katika Canada anaondoka leo, Jumamosi, Septemba 21, 2013 kwenda mjini New York, Marekani kwa ajili ya shughuli za Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwaka huu. Kabla ya kuwasili Canada, Rais Kikwete alitembelea Jimbo la California kwa siku mbili, mjini Washington,D.C., zote za Marekani kwa siku mbili pia.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
21 Septemba, 2013
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete usiku wa Jumatano, Septemba 18, 2013, alitunukiwa heshima ya pekee duniani ya kupatiwa Tuzo ya Mhenga ya Taasisi ya Kimataifa ya Hifadhi ya Bunge la Marekani (ICCF) katika sherehe ya kufana ya Chakula cha Usiku iliyofanyika kwenye ukumbi maarufu wa Andrew Mellon mjini Washington, D.C.
Rais Kikwete ametunukiwa Tuzo la Mhenga ambayo ni Tuzo ya Mtunzaji Bora wa Hifadhi wa Mwaka wa ICCF kwa kutambua na kuheshimu mchango wake mkubwa na uliotukuka katika jitihada za Uongozi wake na wa Tanzania kuhifadhi wanyama, mbunga na maeneo ya hifadhi ya wanyama pamoja na mazingira.
Hiyo ilikuwa mara ya kwanza kwa Tuzo hiyo kutolewa kwa yoyote kwa jina la Mhenga (Neno la Kiswahili lenye maana ya Mtu wa Kale) na mamia kwa mamia ya watu wakubwa nchini Marekani, wakiwamo Maseneta, Wajumbe wa Bunge la Wawakilishi la Marekani, Wafanyabiashara Maarufu, Watunzaji Hifadhi hodari duniani na Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AU) Mama Dkt. Nkosazana Dlamini Zuma walihudhuria sherehe hiyo ya kuvutia ya Chakula cha Jioni.
Baadhi ya watu maarufu waliozungumza ama kutoa Tuzo nyingine katika sherehe za Chakula hicho ambako walihudhuria wageni zaidi ya 500 na ambako washereheshaji walikuwa ni pamoja na aliyekuwa Balozi wa Marekani katika Tanzania Mheshimiwa Mark Green pamoja na Mbunge wa Bunge la Wawakilishi la Marekani, Mheshimiwa Allen Boyd ni pamoja na Seneta Lindsey Graham ambaye alizungumzia Sera za Misaada ya Nje ya Marekani.
Wengine waliozungumza ama kutoa Tuzo ni pamoja na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Mama Hillary Clinton ambaye alizungumza kwa njia ya video, Mwakilishi Jim Moran, Mwakilishi Betty McCollum, Seneta Saxby Chambliss, Seneta Rob Portman na Mwakilishi Ed Royce.
ICCF ina nchi wanachama 46 duniani na 40 kati ya hizo ziliwakilishwa katika Sherehe hiyo ya aina yake ikiwamo Kenya kutoka Afrika, Jordan kutoka Mashariki ya Kati na Colombia kutoka Marekani Kusini.
Sherehe za mwaka huu za kutoa Tuzo za ICCF ambayo ndiyo taasisi maarufu zaidi katika Bunge la Marekani ikiwa na maseneta 31 kutoka vyama vyote vikuu vya Marekani vya Democrat na Republican, Gavana mmoja wa Jimbo Mheshimiwa Sam Brownback wa Jimbo la Kansas na chama cha Republican na Wabunge wa Baraza la Wawakilishi 128 ziliongozwa na kaulimbiu isemayo: “Hifadhi katika Afrika: Usalama, Demokrasia na Maendeleo”.
Mwenyekiti wa Sherehe za mwaka huu za Tuzo za ICCF Dkt. Cristian Samper alikuwa ni Rais na Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Wildlife Conservation Society ambaye amefuata katika nyayo za wenyeviti wengine wa shughuli hiyo waliopita ambao ni Marais wa zamani wa Marekani Bill Clinton na George Herbert Walker Bush, Malkia Noor wa Jordan, Waziri wa Fedha wa Marekani Mheshimiwa Hank Paulson, Mawaziri wa Mambo ya Ndani wa zamani wa Marekani Mheshimiwa Bruce Babbit na Mheshimiwa Dirk Kempthorne.
Na mbali na Rais Kikwete, wageni wengine maalum wa Sherehe za mwaka huu za Tuzo za ICCF walikuwa ni Mama Zuma, Mtawala Mkuu wa Shirika la Misaada ya Maendeleo ya Kimataifa ya Marekani Dkt. Rajiv Shah, na Dkt. Naoko Ishii, Mwenyekiti na Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Global Environment Facility.
Mbali na Rais Kikwete, viongozi wengine waliopata kutunukiwa Tuzo ya juu ya ICCF ni Waziri Mkuu wa Uingereza Mheshimiwa Tony Blair, Rais wa zamani wa Mexico Mheshimiwa Felipe Calderon, Waziri Mkuu wa Norway Jens Stoltenberg na Prince Albert wa Pili wa Monaco.
Akimtambulisha na kumkaribisha Rais Kikwete kupokea Tuzo hiyo, Mwanzilishi na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya ICCF, Mheshimiwa David Barron alimwelezea Rais Kikwete kuwa ni rafiki wa hifadhi, mtu ambaye ametoa mchango mkubwa katika kulinda hifadhi katika nchi Tanzania na katika Afrika.
“Hatuwezi kutumia upande usiofaa wa akili yetu kufikiria. Hakuna shaka kuwa Rais Kikwete ana ari kubwa ya hifadhi ya wanyama, ya mazingira na ya dunia yetu kwa jumla na amethibitisha ukweli huo. Ni rafiki mkubwa tuliyenaye katika Afrika. Naomba tumkaribishe usiku wa leo.”
Akizungumza baada ya kuwa amepokea Tuzo la Mhenga, Rais Kikwete alisema kuwa shughuli za hifadhi katika Tanzania na Afrika zinakabiliwa na changamoto kuu tatu ambazo ni mgongano kati ya hifadhi ya wanyama na ongezeko la watu ambako watu wameongezeka na wanadai ardhi zaidi ya kilimo na kufanyia shughuli zao nyingine, na mgongano kati ya binadamu na wanyama kwa maana wanyama kuharibu mazao na mali za watu.
Rais Kikwete alisema kuwa changamoto ya tatu ni ujagili dhidi ya wanyama, ukataji haramu wa miti jambo ambalo “limefikia kiwango cha kutisha kabisa na lisilovumilika.”
Hata hivyo, Rais Kikwete aliihakikishia dunia kuwa Tanzania itaendelea kulinda kwa njia zote, ikiwa ni pamoja na kutumia jeshi, mbuga za wanyama, hifadhi za wanyama na maeneo ya wanyama. Tanzania ina mbuga 17 za wanyamapori, maeneo ya hifadhi 28, maeneo 43 ya kulinda wanyamapori na maeneo 38 ya kuthibiti wanyamapori.
Tokea mwaka 1961 wakati wa Uhuru, Tanzania imetenga kiasi cha asilimia 30 ya eneo lake lote kwa ajili ya hifadhi ikiwa ni pamoja na hekta 12.5 milioni za misitu.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
19 Septemba, 2013
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete leo, Ijumaa, Septemba 20, 2013, anatunukiwa Shahada ya Uzamivu (PHD) na Chuo Kikuu cha Guelph cha Canada kwa kutambua mchango na uongozi wake katika kuleta mageuzi ya kilimo katika Afrika.
Viongozi wa Chuo hicho wanasema kuwa wamefanya uamuzi wa kumtunuku Rais Kikwete kutokana na jitihada zake za kukabiliana na changamoto zinazokabili kilimo, jitihada zake za kuleta usalama wa chakula na pia majaribio makubwa ya kuongeza matumizi ya technolojia katika kilimo cha Tanzania na Afrika.
Rais Kikwete ambaye amewasili hapa usiku wa jana, Alhamisi, Septemba 19, 2013 akitokea Washington, D.C., Marekani ambako alikuwa kwa siku mbili akitokea Jimbo la California atakuwa Mtanzania wa kwanza kutunukiwa shahada ya juu kabisa katika historia ya Chuo hicho.
Chuo cha Guelph ni moja ya vyuo vikuu vinavyoheshimiwa zaidi katika Canada na duniani katika Nyanja za kilimo na kilianzishwa rasmi kama Chuo cha Kilimo cha Jimbo la Ontario Mei Mosi, mwaka 1874.
Chuo hicho ambacho kimejipatia umaarufu kutokana na ubora wa shughuli zake za utafiti kimekuwa katika mstari wa mbele kutafuta majawabu ya changamoto zinazoikabili dunia katika masuala ya kilimo, raslimali za maji, matatizo makubwa ya magonjwa ya mimea, matatizo ya ukuaji haraka wa miji duniani na changamoto za biashara za kimataifa.
Katika miaka ya karibuni kufuatia tishio kubwa kimataifa la ongezeko la bei za vyakula duniani na hasa katika nchi masikini, mabadiliko ya tabianchi, ongezeko la uchafuzi wa hali ya hewa, uharibifu wa mazingira, changamoto za upatikanaji wa maji safi na salama duniani, kazi ya Chuo hicho imeongezeka sana.
Chuo hicho kimeichagua Tanzania kama nchi ya kufanya nayo kazi katika Afrika kukabiliana na changamoto hizo na kimemtambua Rais Kikwete kutokana na mchango wake mkubwa katika sekta ya kilimo katika miaka yote ya uongozi wake na mipango yake ya kuboresha kilimo katika Tanzania kama ASDP, Kilimo Kwanza na SAGCOT ambayo yote inasifiwa sana kimataifa.
Chuo hicho kina mahusiano ya karibu na Vyuo Vikuu vya Dar es Salaam, Sokoine cha Mzumbe - Morogoro na UDOM - Dodoma. Kati ya mwaka jana na mwaka huu, Chuo hicho kimetiliana saini Makubaliano ya Ushirikiano (MOU) na Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine cha Mzumbe - Morogoro na Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).
Mara nne kati ya Januari, mwaka jana, 2012 na Juni, mwaka huu, 2013, uongozi wa Chuo hicho ukiongozwa na Rais na Makamu Mkuu wa Chuo, Dkt. Alastair Summerlee na Makamu wa Rais wa Utafiti Dkt. Kevin Hall umetembelea Tanzania na kukutana na viongozi wa Serikali pamoja na wale wa Vyuo Vikuu vya Dar Es Salaam na Sokoine cha Mzumbe, Morogoro.
Mbali na ujumbe ambao unaongozana na Rais Kikwete, sherehe za kutunukiwa kwa Kiongozi Mkuu huyo wa Tanzania pia zitahudhuriwa na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Mheshimiwa Dkt. Shukuru Kawambwa, Jumuia ya Watanzania wanaoishi Canada pamoja na maofisa wa Ubalozi wa Tanzania nchini humo.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
20 Septemba, 2013
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa maslahi ya makampuni ya Marekani yanayotaka kuwekeza katika Tanzania hayataathiriwa na kuwepo kwa China katika uchumi wa Tanzania kwa sababu China siyo moja ya wawekezaji wakuu katika uchumi wa Tanzania kwa sasa.
Rais Kikwete amesema kuwa miongoni mwa wawekezaji wakuu wa uchumi wa Tanzania, China inashikilia nafasi ya 10 huku Uingereza ikiwa inaongoza katika kuwekeza katika Tanzania.
Aidha, Rais Kikwete amesema kuwa China ni miongoni mwa nchi zinazoongoza kwa misaada ya maendeleo kwa Tanzania lakini siyo katika makampuni ya nchi hiyo kuwekeza katika uchumi wa Tanzania na hivyo nchi hiyo haiwezi kuwa tishio kwa uwekezaji wa makampuni ya Marekani.
Rais Kikwete ametoa ufafanuzi huo mchana wa Jumatano, Septemba 18, 2013, wakati alipokutana katika mkutano wa kikazi na Mwenyekiti wa Kamati Ndogo ya Mahusiano ya Nje na Bajeti ya Miradi ya Maendeleo ya Bunge la Marekani mjini Washington, D.C., pamoja na baadhi ya wajumbe wa kamati yake.
Katika mkutano huo, Rais Kikwete aliulizwa jinsi gani fedha ya Jamhuri ya Watu wa China katika uchumi wa Tanzania inavyoathiri uwekezaji wa makampuni ya Marekani.
“Napenda kuwahakikisheni kuwa hakuna athari yoyote. China inashikilia nafasi ya 10 katika uwekezaji katika nchi yetu na hivyo siyo miongoni mwa nchi zinazoongoza katika uwekezaji. Nchi ya kwanza kabisa ni Uingereza ikifuatiwa na Kenya, India na Afrika Kusini. Hizi ndizo nchi kubwa nne.”
Ameongeza Rais Kikwete: “China iko zaidi katika kutoa misaada ya maendeleo ambako kwa kweli huko ni miongoni mwa nchi zinazoongoza siyo kwenye uwekezaji. Walitujengea TAZARA, wamejenga Uwanja wa Taifa, sasa wanajenga Bomba la Mafuta kutoka Mtwara hadi Dar Es Salaam, watajenga Bandari ya Bagamoyo…yote hii ni kwenye misaada ya maendeleo.”
“Ni msaada wa maendeleo wa China kwa nchi yetu kama tunavyopokea misaada ya nchi nyingine na kama China inavyotoa misaada kwa nchi nyingine. Hivyo, kwa kweli hakuna tishio lolote kwa uwekezaji wa Marekani kutoka kwa Wachina katika Tanzania, sijui nchi nyingine. Kwa Marekani nadhani mtu wa kumwogopa katika uwekezaji katika Tanzania ni Uingereza.”
Wakati huo huo, Rais Kikwete ametoa rambirambi kwa Serikali na Bunge la Marekani kufuatia mauaji ya watu 12 yaliyofanywa na kijana mmoja mwenye umri wa miaka 34 kwenye Kambi Moja ya Jeshi la Maji la Marekani mjini Washington, D.C.,mwanzoni mwa wiki hii.
“Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kwa niaba ya nchi yangu, Serikali na mimi binafsi kutoa salamu zangu za rambirambi kufuatia tukio hili la kusikitisha sana ambako watu wasiokuwa na hatia wamepoteza maisha yao.”
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
20 Septemba, 2013
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ameiambia Kamati ya Bunge la Marekani kuwa Tanzania haijafukuza mkimbizi hata mmoja kutoka nchini na wanaondolewa katika Tanzania ni wahamiaji haramu walioingia na kuishi nchini bila kufuata taratibu na sheria za Uhamiaji.
Rais amesema kuwa kamwe Tanzania ambayo imekuwa kimbilio kubwa la wakimbizi katika historia haiwezi kamwe kuwafukuza nchini wakimbizi kwa kuwa haina sababu ya kufanya hivyo, na hata kama sababu ingekuwepo, ingefanya hivyo kwa kufuata taratibu za kimataifa.
Msimamo huo wa Tanzania umeelezwa kwa mara nyingine tena mchana wa leo, Jumatano, Septemba 18, 2013 wakati alipokutana katika mkutano wa kikazi na Mwenyekiti wa Kamati Ndogo ya Mahusiano ya Nje na Bajeti ya Miradi ya Maendeleo, Mheshimiwa Kay Granger na baadhi ya wajumbe wa Kamati yake.
Katika mkutano huo uliofanyika katika Bunge la Marekani, mjini Washington D.C., Rais Kikwete amesema kuwa umekuwepo upotoshaji kuhusu amri ya Serikali ya kuwaondoa nchini wahamiaji haramu ambao wanaishi nchini kinyume cha sheria.
Akijibu swali ambalo aliulizwa na mmoja wa wajumbe wa Kamati hiyo, Rais Kikwete amesema: “Tuna wakimbizi 264,000 kutoka nchi za Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) ambao wote wako katika makambi yao mkoani Kigoma. Hakuna mkimbizi ambaye amefukuzwa.”
Ameongeza: “Hata kama tungetaka waondoke nchini tunajua taratibu za kuwaondoa wakimbizi kwa sababu Tanzania ina uzoefu wa miaka mingi wa kuwapokea, kuwatunza na kuwajali wakimbizi. Tungewasiliana kwanza na Umoja wa Mataifa na nchi ambazo walitokea wakimbizi hao kabla ya kuwashauri kurudi makwao. Wote wako makambini na hivyo suala la kuwafukuza nchini halipo.”
Amesisitiza Rais Kikwete: “Watu ambao tunawaondoa sisi ni wahamiaji haramu katika mikoa ya Kagera, Kigoma na Geita. Wengine wamekuwa nchini kwa muda. Kuna wakati waliambiwa kuweka vizuri ukaaji wao nchini kisheria lakini hawakufanya hivyo. Hawa hatuna jingine la kuwafanyia, ni lazima waondoke. Tuliwapa wiki mbili za kuondoka wenyewe, tumeongeza tena muda wa wiki mbili. Kiasi cha wahamiaji haramu 34,000 waliondoka wenyewe, sasa waliobakia tunawasaka katika operesheni maalum.”
Alisema kuwa baada ya kumalizika kwa muda huo, sasa Serikali imeanzisha operesheni maalum ya kuwaondoa wale ambao hawakuondoka nchini wenyewe. “Na operesheni hii itaendelea hadi tutakapomaliza tatizo hili la wahamiaji haramu ambao wanashutumiwa kwa vitendo vya ujambazi, utekaji nyara mabasi, uvamizi wa misitu ya asili na hifadhi kwa malisho na kuingiza maelfu kwa maelfu ya mifugo katika maeneno tengefu katika mikoa ya Kagera, Kigoma na Geita.”
Baada ya mkutano huo, Rais Kikwete ameshiriki chakula cha mchana ambacho kiliandaliwa kwa ajili yake na Taasisi ya Kimataifa ya Hifadhi ya Bunge la Marekani ya International Conservation Caucus Foundation (ICCF) katika ukumbi wa chakula wa Wabunge ndani ya Bunge hilo.
Rais Kikwete ambaye yuko katika ziara ya kikazi katika Marekani amewasili mjini Washington D.C., mapema leo asubuhi akitokea mjini San Francisco ambako alikuwa na ziara ya siku mbili katika Jimbo la California.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
18 Septemba, 2013
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amemteua Bi. Jacqueline M. Maleko kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE).
Kulingana na Katibu Mkuu Kiongozi (KMK) Balozi Ombeni Y. Sefue, uteuzi huo ulianza Septemba 10, mwaka huu, 2013.
Kabla ya uteuzi huu, Bi. Maleko alikuwa Mkurugenzi Msaidizi, Idara ya Masoko, Wizara ya Viwanda na Biashara, kabla ya kuteuliwa kukaimu nafasi hiyo ya Mkurugenzi Mkuu wa TanTrade.
“Mwisho”
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
DAR ES SALAAM.
18 Septemba, 2013
Rais kikwete aanza ziara za Marekani na Canada
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ameondoka nchini leo, Jumapili, Septemba 15, 2013, kwenda Marekani na Canada kwa ziara za kikazi ambako miongoni mwa shughuli zake nyingine nyingi atahutubia Mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UN) mjini New York.
Ziara ya Rais Kikwete itaanzia katika Jiji la San Francisco, Jimbo la California, ambako atakuwa na ziara ya siku mbili na ambako atafungua Ubalozi Mdogo wa Tanzania katika jimbo hilo kubwa zaidi kuliko mengine katika Marekani na pia kukutana na Jumuia ya Watanzania waishio katika Jimbo hilo. Rais pia atakutana na kufanya mazungumzo na Meya Osby Davis wa Mji wa Vallejo.
Jumatano, Rais Kikwete atakuwa mjini Washington, D.C., kwa siku moja ambako atakutana na viongozi wa Bunge la Marekani kwa chakula cha mchana, atahudhuria sherehe ya kutiwa saini kwa mikataba ya kufunguliwa kwa Balozi Ndogo za kuwakilisha Tanzania katika sehemu mbali mbali za Marekani na pia atahudhuria dhifa ya mwaka ya Kamati Ndogo ya Bunge la Marekani kuhusu hifadhi za wanyama na ardhi.
Alhamisi, Rais Kikwete atakwenda mjini Toronto, Canada ambako siku ya pili atatunukiwa Shahada ya Heshima ya Uzamivu (PHD) ya Sheria na Chuo Kikuu cha Guelph.
Baada ya hapo, Rais Kikwete atarejea tena katika Marekani zamu hii mjini New York ambako atakuwa na shughuli nyingi akianza na kuhudhuria halfa ya taasisi ya kupambana na ugonjwa wa malaria duniani ya Roll Back Malaria, na baadaye kuhudhuria shughuli ya namna ya kuongeza kiwango cha Lishe duniani. Aidha, Rais Kikwete atahudhuria Mkutano wa Nchi Wanachama wa Maziwa Makuu na pia kukutana kwa mazungumzo na Rais Alassane Quattara wa Cote d’Ivore.
Vile vile akiwa mjini New York, Rais Kikwete atahudhuria halfa rasmi itakayoandaliwa na Rais Barack Obama wa Marekani kwa ajili ya viongozi mbali mbali duniani na Jumanne ijayo asubuhi atahudhuria ufunguzi wa Kikao cha 66 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ambacho kitahutubiwa na Katibu Mkuu wa Umoja huo, Mheshimiwa Ban Ki Moon na baadaye kuhudhuria Chakula cha Mchana ambacho kitaandaliwa na Katibu Mkuu huyo kwa ajili ya viongozi mbali mbali duniani wanaohudhuria Kikao hicho.
Rais pia atakutana kwa mazungumzo na Mheshimiwa Daniel Yohannes, Mtendaji Mkuu wa Millennium Challenge Corporation (MCC), inayogharimia miradi ya mabilioni ya fedha katika sekta ya miundombinu katika Tanzania, atakutana kwa mazungumzo na Katibu Mkuu Ban Ki Moon, atahudhuria Mkutano wa Mwaka wa Taasisi ya Clinton Global Foundation ambayo inagharimia miradi mbali mbali katika Tanzania.
Rais Kikwete atahutubia Kikao cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa saa tisa mchana (saa za Marekani) Septemba 26, mwaka huu, 2013 ambako atazungumzia Ajenda ya Maendeleo Duniani baada ya mwaka 2015.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
15 Septemba, 2013
Rais Kikwete azindua mtambo wa kufua umeme,Nyakato,Mwanza
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete jana, Jumapili, Septemba 8, 2013, alizindua mtambo wa kufua umeme kiasi chamegawati 60 katika eneo la Nyakato mjini Mwanza, umeme ambao utachangia kwa kiwango kikubwa kupunguza shida ya umeme katika Mkoa wa Mwanza na mikoa ya jirani.
Aidha, Rais Kikwete ameiagiza Wizara ya Nishati na Madini na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuanza mara moja maandalizi ya kupeleka umeme kwenye machimbo ya madini ya nikeli yaliyoko Kabanga, Ngara, Mkoa wa Kagera.
Vile vile, Rais Kikwete amesema kuwa Serikali yake itaharakisha mipango ya kujenga reli hadi kwenye eneo hilo kama maandalizi ya kuanza kuchimbwa kwa madini hayo ambayo ni mazito na kuyasafirisha kwa barabara kwenda bandarini Dar Es Salaam kutaharibu kwa haraka barabara zinazojengwa kwa gharama kubwa nchini.
Akizungumza kabla ya kuzindua mtambo huo, Rais Kikwete ameitaka Wizara ya Nishati na Madini kuharakisha mipango ya kuunganisha eneo la Kabanga, Ngara, Mkoani Kagera kwenye Gridi ya Taifa ili uzalishaji wa madini ya nikeli usije kukwamishwa na ukosefu wa umeme. Amesema kuwa mgodi huo utahitaji umeme mwingi kiasi cha megawati 40.
Rais amesema kuwa Serikali yake itahakikisha inafikisha reli kwenye eneo la Kabanga mapema ili kuhakikisha kuwa nikeli inayozalishwa inasafirishwa kwa reli badala ya barabara. Amesema kuwa madini hayo ni mazito mno na kuyasafirisha kwa barabara kutaharibu kabisa na katika muda mfupi barabara ambazo zinajengwa nchini kwa gharama kubwa.
Mtambo wa Umeme wa Nyakato wenye uwezo wa kuzalisha megawati 60 ulianza kujengwa mwaka jana, 2012, baada ya Serikali ya Tanzania kuwekeana mkataba wa ujenzi na Kampuni ya Semco and Rolls Royce ya Norway mwaka 2011 wakati maandalizi ya ujenzi huo yalipoanza.
Gharama za ujenzi wa mtambo huo ambazo ni shilingi bilioni 130 (Euro milioni 48.7 na dola za Marekani 15.9) zimelipwa kwa asilimia 100 na Serikali ya Tanzania.
Akizungumza na wananchi kwenye sherehe ya uzinduzi huo, Rais Kikwete amesema kuwa umeme siyo anasa bali ni moja ya vigezo vya msingi na muhimu kabisa vya maendeleo.
“Vipo vigezo vingi vya maendeleo ya nchi na binadamu, lakini moja ya vigezo hivyo ni umeme. Na ukiangalia matumizi ya umeme kwa kila nchi yanaonesha kiwango cha maendeleo cha nchi hiyo. Katika Marekani, kwa mfano, kila mwananchi anatumia kiasi cha kilowati 12,000 kwa wastani. Sisi katika Tanzania ni kilowati 89 tu na wastani wa Bara la Afrika ni kilowati 150,” amesema Rais Kikwete na kuongeza:
“Nc hi yetu ya Tanzania ina umeme kiasi cha megwati 1,450 tu wakati katika Afrika Kusini ni megawati 45,000 na unaweza kuona tofauti ya maendeleo. Hivyo, ni muhimu sana kwetu kuongeza kiwango cha kuzalisha umeme katika nchi yetu.”
Katika siku ya tatu ya ziara yake kukagua miradi ya maendeleo katika Mkoa wa Mwanza, Rais Kiwete pia amefungua Kituo cha Polisi cha Nyakato ambacho kimegharimu shilingi milioni 450, Serikali ikiwa imechangia kiasi cha asilimia 20 cha gharama hizo.
Kituo hicho cha kisasa kilianza kujengwa mwaka 2003 lakini ujenzi wake ukawa unakwamakwama kutokana na ukosefu wa bajeti hadi uongozi wa polisi wa Mkoa wa Mwanza ulipoamua kukijenga kituo hicho kwa njia ya kuishirikisha jamii na ikaundwa Kamati ya Ujenzi chini ya uenyekiti wa Bwana Alfred Wambura.
Akizungumza kwenye sherehe ya ufunguzi wa kituo hicho, Rais Kikwete ameahidi kuwa atajenga nyumba moja kwa ajili ya makazi ya polisi. Kituo hicho kina jumla ya askari polisi 65.
Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
09 Septemba, 2013
Rais Kikwete ahudhuria mkutano wa Asasi ya Ulinzi, Usalama na Siasa wa Jumuia ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC Troika)
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amewasili mjini Windhoek, Namibia, jioni ya leo, Jumatano, Septemba 11, 2013, kuhudhuria Mkutano wa Asasi ya Ulinzi, Usalama na Siasa (SADC Troika Organ) wa Jumuia ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC).
Mkutano huo wa siku ,moja unaofanyika baadaye jioni ya leo katika Ikulu ya Namibia mjini Windhoek unahudhuriwa na wakuu wa nchi wanachama wa Troika pamoja na waalikwa kutoka Tanzania, Lesotho, Malawi, Afrika Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na wenyeji Namibia.
Mkutano huo unafanyika chini ya Uenyekiti wa Rais Hifikepunye Phohamba wa Namibia ambaye mwezi uliopita alikabidhiwa Uenyekiti wa Asasi hiyo na Rais Kikwete ambaye aliiongoza kwa mwaka mmoja.
Mbali na Rais Phohamba na Rais Kikwete, viongozi wengine wanaohudhuria mkutano huo ni Rais Joyce Banda wa Malawi ambaye ni Mwenyekiti wa SADC, Rais Joseph Kabila Kabange wa DRC na Waziri Mkuu wa Lesotho Mheshimiwa Tom Thabane.
Hata hivyo, kama mwenyekiti aliyepita, Tanzania inabakia kuwa Mjumbe wa Troika pamoja na Nambia na Lesotho ambayo ni Makamu Mwenyekiti wa sasa wa Asasi hiyo.
Afrika Kusini na DRC zinahudhuria Mkutano huo kama waalikwa hasa kwa sababu moja ya ajenda kuu za kikao hicho ni kujadili hali ilivyo katika Mashariki mwa nchi hiyo ambako majeshi ya Serikali ya Rais Kabila majuzi yalipambana na waasi wa kikundi cha M23 ambacho kinataka kuiangusha Serikali hiyo.
Rais Kikwete na ujumbe wake amewasili mjini Windhoek jioni ya leo akitokea mjini Mwanza ambako asubuhi ya leo amemaliza ziara yake yenye mafanikio makubwa ya siku tano katika Mkoa huo kukagua na kuzindua miradi ya maendeleo.
Kabla ya kuondoka mjini Mwanza, Rais Kikwete amezungumza na viongozi wa Mkoa huo kwenye majumuisho ya ziara yake hiyo.
Kikao hicho pia kitakuwa cha kwanza kwa Katibu Mtendaji mpya wa SADC, Dkt. Stergomena Lawrence Tax wa Tanzania ambaye alichaguliwa mwezi uliopita kushika nafasi hiyo iliyoachwa na Dkt. Tomaz Salamao.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
IKULU,
DAR ES SALAAM.
11 Septemba, 2013
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amewasili mjini Windhoek, Namibia, jioni ya leo, Jumatano, Septemba 11, 2013, kuhudhuria Mkutano wa Asasi ya Ulinzi, Usalama na Siasa (SADC Troika Organ) wa Jumuia ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC).
Mkutano huo wa siku ,moja unaofanyika baadaye jioni ya leo katika Ikulu ya Namibia mjini Windhoek unahudhuriwa na wakuu wa nchi wanachama wa Troika pamoja na waalikwa kutoka Tanzania, Lesotho, Malawi, Afrika Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na wenyeji Namibia.
Mkutano huo unafanyika chini ya Uenyekiti wa Rais Hefepunye Phohamba wa Namibia ambaye mwezi uliopita alikabidhiwa Uenyekiti wa Asasi hiyo na Rais Kikwete ambaye aliiongoza kwa mwaka mmoja.
Mbali na Rais Phohamba na Rais Kikwete, viongozi wengine wanaohudhuria mkutano huo ni Rais Joyce Banda wa Malawi ambaye ni Mwenyekiti wa SADC, Rais Joseph Kabila Kabange wa DRC na Waziri Mkuu wa Lesotho Mheshimiwa Tom Thabane.
Hata hivyo, kama mwenyekiti aliyepita, Tanzania inabakia kuwa Mjumbe wa Troika pamoja na Nambia na Lesotho ambayo ni Makamu Mwenyekiti wa sasa wa Asasi hiyo.
Afrika Kusini na DRC zinahudhuria Mkutano huo kama waalikwa hasa kwa sababu moja ya ajenda kuu za kikao hicho ni kujadili hali ilivyo katika Mashariki mwa nchi hiyo ambako majeshi ya Serikali ya Rais Kabila majuzi yalipambana na waasi wa kikundi cha M23 ambacho kinataka kuiangusha Serikali hiyo.
Rais Kikwete na ujumbe wake amewasili mjini Windhoek jioni ya leo akitokea mjini Mwanza ambako asubuhi ya leo amemaliza ziara yake yenye mafanikio makubwa ya siku tano katika Mkoa huo kukagua na kuzindua miradi ya maendeleo.
Kabla ya kuondoka mjini Mwanza, Rais Kikwete amezungumza na viongozi wa Mkoa huo kwenye majumuisho ya ziara yake hiyo.
Kikao hicho pia kitakuwa cha kwanza kwa Katibu Mtendaji mpya wa SADC, Dkt. Stergomena Lawrence Tax wa Tanzania ambaye alichaguliwa mwezi uliopita kushika nafasi hiyo iliyoachwa na Dkt. Tomaz Salamao.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
IKULU,
DAR ES SALAAM.
11 Septemba, 2013
Rais Kikwete Amemhamishia Eng. Iyombe Wizara ya Ujenzi.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amemhamisha Engineer Ibrahim Iyombe, aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kwenda kuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi.
Taarifa iliyotolewa Dar es Salaam leo, Alhamisi, Agosti 22, 2013 na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue imesema kuwa Eng. Iyombe anachukua nafasi ya Engineer John Stanslaus Ndunguru ambaye atapangiwa kazi nyingine.
Aidha, taarifa imesema kuwa uhamisho huo unaanza mara moja.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
22 Agosti, 2013
Rais- Uteuzi wa Nyamajeje Calleb Weggoro
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amemteua Dkt. Nyamajeje Calleb Weggoro kuwa Msaidizi wa Rais, Masuala ya Ushirikiano wa Kikanda.
Taarifa iliyotolewa leo, Alhamisi, 29 Agosti, 2013 mjini Dar es Salaam na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Y. Sefue inasema kuwa uteuzi huo umeanza jana Agosti 28, mwaka huu, 2013.
Kabla ya uteuzi huu, Dkt. Nyamajeje Calleb Weggoro alikuwa Mkurugenzi wa Sekta za Uzalishaji (Productive Sectors) katika Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
“Mwisho”
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
29 Agosti, 2013
Rais- Uteuzi wa Sylvester Ambokile Mwakinyule
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amemteua Ndugu Sylvester Ambokile Mwakinyule kuwa Kamishna Mkuu, Idara ya Uhamiaji.
Taarifa iliyotolewa leo, Alhamisi, 29 Agosti, 2013 mjini Dar es Salaam na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Y. Sefue inasema kuwa uteuzi huo umeanza jana, Agosti 28, mwaka huu, 2013.
Ndugu Mwakinyule anachukua nafasi ya Ndugu Magnus Ulungi ambaye atapangiwa kazi nyingine.
Kabla ya uteuzi wake, Ndugu Sylvester Ambokile Mwakinyule, alikuwa Naibu Kamishna wa Uhamiaji na Mwambata wa Uhamiaji katika Ubalozi wa Tanzania, London, Uingereza
“Mwisho”
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
29 Agosti, 2013
Rambirambi Moses Kulola
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete ameshtushwa na kuhuzunishwa na taarifa za kifo cha Kiongozi wa Kanisa la Evangelistic Assemblies of God Tanzania (EAGT) Askofu Mkuu Moses Kulowa ambaye ameaga dunia asubuhi ya leo, Alhamisi, Agosti 29, 2013 katika Hospitali ya AMI iliyoko Masaki mjini Dar Es Salaam akiwa na umri wa miaka 84.
Rais kikwete ameelezea mshtuko na huzuni yake katika Salamu za Rambirambi alizomtumia Katibu Mkuu wa Kanisa hilo Bwana Brown Mwakipesile kufuatia kifo cha Askofu Mkuu Kulowa.
“Nimeshtushwa, nimesikitishwa na kuhuzunishwa sana na taarifa za kifo cha Mtumishi wa Mungu wa muda mrefu na Askofu Mkuu wa Kanisa la Evangelistic Assemblies of God Tanzania (EAGT), Marehemu Moses Kulola kutokana na maradhi yaliyomfanya wakati fulani apelekwe hadi India kupatiwa matibabu” amesema Rais Kikwete.
Rais Kikwete amesema alimfahamu Marehemu Askofu Moses Kulola kwa miaka mingi wakati wa enzi za uhai wake, kama Mtumishi Hodari wa Kiroho aliyejitoa vilivyo katika kuwahudumia Waumini wa Kanisa lake ambapo mahubiri yake yametoa mchango mkubwa katika kuimarisha imani za Waumini wake na kusaidia kwa kiasi kikubwa katika kudumisha amani na utulivu wa nchi yetu.
Aidha Rais Kikwete amesema kifo cha Askofu Mkuu, Moses Kulola kimeacha pengo kubwa siyo tu kwa Waumini wa Kanisa lake hapa nchini, bali pia miongoni mwa wapenda amani kote nchini na kwingineko duniani kwa vile enzi za uhai wake, Marehemu aliweza kufikisha ujumbe muhimu wa kiimani kupitia mahubiri yake kwa watu wa mataifa mbalimbali ndani na nje ya Bara la Afrika.
“Kwa niaba yangu mwenyewe na Serikali ninayoingoza, ninakutumia wewe Katibu Mkuu wa Kanisa la Evangelical Assembies of God Tanzania, Bwana Brown Mwakipesile na Waumini wote wa Kanisa hilo Salamu za Rambirambi kutoka dhati ya moyo wangu kwa kumpoteza Kiongozi muhimu wa Kiroho. Ninawajulisha kuwa niko nanyi katika wakati huu mgumu kwa sababu msiba wenu ni msiba wetu pia. Sala na mioyo yetu iko nanyi wakati wa maombolezo ya kifo cha Kiongozi huyo shupavu wa dini. Nawaomba wote muwe wavumilivu na wenye subira kwani yote ni Mapenzi yake Mola”, amesema Rais Kikwete.
“Vilevile kupitia kwako, naomba unifikishie Salamu zangu za Rambirambi na pole nyingi kwa familia, ndugu na jamaa wa Marehemu, Askofu Mkuu, Moses Kulola kwa kumpoteza Baba, Kiongozi Shupavu na Mhimili wa familia. Natambua fika kwamba hiki ni kipindi kigumu sana kwao cha maombolezo. Natambua machungu yenu wakati huu na naungana nanyi katika kumwomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema aiweke peponi roho ya Marehemu Moses Kulowa. Amina.”
Mazishi ya Marehemu, Askofu Mkuu wa Kanisa la Evangelistic Assemblies of God Tanzania (EAGT) yatafanyika mjini Mwanza Jumatano ijayo tarehe 4 Septemba, 2013. Heshima za mwisho kwa mwili wa Kiongozi huyo zitatolewa siku ya Jumamosi tarehe 31 Agosti, 2013 katika Kanisa la EAGT karibu na Hospitali ya Temeke kuanzia saa 2.00 asubuhi hadi saa 6.00 mchana.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
29 Agosti, 2013