Taarifa kwa vyombo vya Habari ya zamani
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
JK: Tutakomesha ugomvi wa wafugaji na wakulima.
Asisitiza kuwa tatizo ni wafugaji kulisha ng’ombe mashambani
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ameahidi kuwa Serikali yake italipatia ufumbuzi wa kudumu tatizo sugu la ugomvi kati ya wakulima na wafugaji katika Mkoa wa Morogoro ambalo kimsingi linasababishwa na wachungaji kuingiza mifugo yao katika mashamba ya wakulima.
Aidha, Rais Kikwete amewataka wachungaji kuacha mara moja tabia yao ya kuingiza na kulisha ng’ombe wao katika mashamba ya wakulima akisisitiza kuwa hicho ndicho chanzo cha ugomvi kati ya makundi hayo mawili.
Rais Kikwete ambaye anafanya ziara ya siku saba katika Mkoa wa Morogoro ametoa ahadi ya kutafuta ufumbuzi wa kudumu wa ugomvi kati ya makundi hayo baada ya kulalamikiwa kila aliposisima na wananchi kuhusu tabia ya wafugaji kuingiza na kulisha ng’ombe wao katika mashamba ya wakulima.
Akiwa njiani kutoka Ifakara, Wilaya ya Kilombero kwenda Wilaya ya Morogoro, Rais Kikwete ameshuhudia mwenyewe malalamiko hayo ya wananchi dhidi ya tabia hiyo ya wafungaji ambao wengi wao siyo wakazi ama wenyeji wa Mkoa wa Morogoro.
Baada ya kujaribu kuwaeleza wananchi katika maeneo mbali mbali kuhusu chanzo cha ugomvi huo na nini hasa ufumbuzi wa suala hilo, Rais Kikwete amewaambia wananchi katika Kijiji cha Mgalegole-Mngazi, eneo la Duthumu, Tarafa ya Bwakira: “Nakwenda sasa kutafuta ufumbuzi wa kudumu wa tatizo hili. Ni lazima tukomeshe tatizo hili.”
Amesisitiza Rais Kikwete: “Kimsingi, huu ni ugomvi usiostahili kwa sababu kila mmoja kati ya makundi haya anamhitaji mwenzake. Wafugaji wanahitaji chakula…ugali na mchele..kutoka kwa wakulima. Nao wakulima wanahitaji kitoweo…nyama kutoka kwa wafugaji. Kubwa hapa ni wafugaji kuacha kulisha ng’ombe kwenye mashamba ya watu wengine.”
Ameongeza Rais Kikwete: “Mnawaachia watoto kuchunga ng’ombe. Wanaingiza mifugo katika mashamba ya watu. Wakiwauliza mnawapiga, mnawajeruhi. Acheni mambo haya.”
Rais Kikwete ameanzia ziara yake ya leo kwa kuweka jiwe la msingi katika upanuzi wa Kituo cha Afya Kibaoni, mjini Ifakara, ambacho kinapanuliwa kuwa Hospitali ya Wilaya na baadaye akakabidhi madawati 278 kwa shule 17 za msingi za Tarafa za Mang’ula na Kidatu katika Wilaya ya Kilombero. Madawati hayo yametolewa na Shirika la Taifa la Hifadhi (TANAPA).
Baada ya hapo, Rais Kikwete ambaye anafuatana na Mama Salma Kikwete katika ziara hiyo amepanda treni ya Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA) kwenda Kisaki, Wilaya ya Morogoro, ambako amelakiwa na mamia kwa mamia ya wananchi.
Baadaye, Rais Kikwete amezindua Mradi wa Maji wa Duthumu ambao umefadhiliwa na wanachama wa Lions Clubs za Sweden na pia kuzindua vifaa na huduma ya upasuaji katika Kituo cha Afya katika eneo hilo.
Katika mji mdogo wa Mtamba, Rais Kikwete amezindua soko jipya la kisasa na kuzungumza na wananchi ambako aliahidi kuwa Serikali imeanza kufanya upembuzi yakinifu wa ujenzi wa Barabara ya Bingwa-Mvua kwa kiwango cha lami.
Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
22 Agosti,2014
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais Kikwete aweka historia nyingine: Asafiri kwa treni ya TAZARA
kwa mara ya kwanza
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, leo, Alhamisi, Agosti 21, 2014, ameweka historia nyingine katika ziara yake ya Mkoa wa Morogoro wakati aliposafiri kwa treni ya Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA), ikiwa ni mara yake ya kwanza kutumia usafiri huo katika kipindi chake cha Urais.
Rais Kikwete, akifuatana na Mama Salma Kikwete, amesafiri kilomita 143 ndani ya Behewa la Kirais (Presidential Coach) la T-One kwa kiasi cha saa tatu na dakika 25 akitokea stesheni ya Ifakara katika Wilaya ya Kilombero kwenda Stesheni ya Kisaki, Wilaya ya Morogoro.
Rais Kikwete akiandamana na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mheshimiwa Joel Bendera na Waziri wa Ujenzi, Mheshimiwa John Pombe Magufuli, amepanda treni hiyo kiasi cha saa 4:45 asubuhi mjini Ifakara na kushuka 8:10 mchana wakati alipowasili Kisaki. Kwa muda mwingi alikuwa katika Chumba cha Mikutano (Conference Room) cha Behewa la Kirais hilo ambalo pia lina huduma nyingine nyingi za Kirais.
Rais Kikwete anakuwa Rais wa tatu wa Tanzania kutumia Behewa hilo na kusafiri ndani ya treni ya TAZARA. Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, ambaye TAZARA ilibuniwa na kujengwa chini ya uongozi wake, alitumia Behewa hilo na treni hiyo mara mbili, mara ya kwanza ikiwa mwaka 1976 aliposafiri na mgeni wake, aliyekuwa Rais wa Sierra Leone, Mheshimiwa Siaka Stevens.
Rais wa Pili, Mzee Ali Hassan Mwinyi pia alitumia Behewa hilo na usafiri wa TAZARA mara mbili wakati Rais wa Tatu, Mheshimiwa William Mkapa hakupata kutumia Behewa hilo wala usafiri wa TAZARA.
Hiyo ilikuwa mara ya pili kwa Rais Kikwete kuweka historia katika ziara yake ya siku saba katika Mkoa wa Morogoro iliyoanza jana, Jumatano, Agosti 20, 2014.
Katika siku yake ya kwanza jana, msafara wa Rais Kikwete, uliweka historia kwa kuwa magari ya kwanza kuvuka Mto Kilombero kwa kutumia daraja, ukiwa unatokea Wilaya ya Ulanga kuingia Wilaya ya Ifaraka ambako Rais aliweka jiwe la msingi la ujenzi wa daraja kamili kwenye Mto huo.
Msafara huo, ulivuka Mto huo kwa kutumia daraja jembamba la chuma ambalo linatumiwa kama daraja la muda na mafundi wa Kampuni ya Kichina ambayo inajenga daraja kubwa na la kweli kweli kwenye Mto huo linalogharimu Sh. bilioni 56 zinazotolewa na Serikali ya Tanzania.
Kutokana na adha ya karne na karne ambayo wananchi wa wilaya hizo mbili wamekuwa wanaipata kuvuka Mto Kilombero kwa kivuko na hata mitumbwi, wananchi wa maeneo hayo wamelipachika Daraja hilo jina la Daraja la Ukombozi.
Daraja la Mto Kilombero ni moja ya madaraja makubwa matatu ambayo Rais Kikwete, katika kampeni yake ya Urais ya mwaka 2005, aliahidi kuyajenga na ambayo yaliwekwa katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010.
Madaraja mengine ni lile la Kigamboni, Dar Es Salaam, ambalo ujenzi wake unaendelea na Daraja la Mto Malagarasi Mkoani Kigoma ambalo ujenzi wake umekamilika.
Madaraja hayo matatu, na mengine mawili, ya Kirumi kwenye Mto Mara na la Rufiji ni madaraja ambalo yalikuwa yamepangwa kujengwa katika Mpango wa Kwanza wa Taifa wa Maendeleo. Daraja la Kirumi lilijengwa wakati wa uongozi wa Mwalimu Nyerere na lile la Rufiji lilijengwa wakati wa uongozi wa Mzee Mkapa. Matatu yaliyobakiwa yamejengwa wakati wa Uongozi wa Rais Kikwete.
Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
21 Agosti,2014
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia Salamu za Rambirambi Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Mheshimiwa Fatma Mwasa kufuatia ajali ya barabarani iliyotokea tarehe 19 Agosti, 2014 katika Kijiji cha Mlogolo, Wilaya ya Sikonge Mkoani Tabora.
Ajali hiyo iliyotokea katika Kijiji cha Mlogolo Wilayani Sikonge, ilihusisha basi la abiria la Kampuni ya Sabena lililokuwa likitokea Mbeya kwenda Mwanza ambalo lililogongana uso kwa uso na basi lingine la Kampuni ya AM Coach lililokuwa likitokea Mwanza na kusababisha vifo vya watu 19 na kujeruhi wengine 81.
“Nimeshtushwa na kusikitishwa na ajali hii iliyogharimu maisha ya watu 19 na wengine 81 kujeruhiwa” amesema Rais.
“Pokea Salamu zangu za Rambirambi kutokana na ajali hiyo, na kupitia kwako naomba unifikishie Salamu za Rambirambi na pole kwa wafiwa wote kwa kupotelewa ghafla na wapendwa wao. Namuomba Mwenye Mungu, Mwingi wa Rehema azipokee na kuzilaza Roho za Marehemu wote mahala pema peponi, Amina”.
Rais Kikwete amewaomba wafiwa wote wawe na moyo wa uvumilivu na ujasiri wakati huu ambao ni mgumu sana kwao wanapoomboleza vifo vya ndugu na jamaa zao.
Aidha amesema anawaombea kwa Mola majeruhi wote wa ajali hiyo waweze kupona haraka na kurejea tena katika hali zao za kawaida na kuungana tena na familia, ndugu na jamaa zao.
Kwa mara nyingine Rais Kikwete ameendelea kusisitiza umakini na usimamizi mzuri wa Sheria ya Usalama Barabarani kutoka kwa mamlaka zinazohusika, ili maisha ya wananchi wasio na hatia yasiendelee kupotea na kusababisha simanzi kwa familia, na kupotea kwa nguvu kazi muhimu ya Taifa.
Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
21 Agosti,2014
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais Kikwete aandika historia: Aanzisha ujenzi Daraja la Kilombero
Historia imeandikwa jioni ya leo, Jumatano, Agosti 20, 2014 katika Mkoa wa Morogoro na katika Tanzania. Kwa mara ya kwanza tokea enzi na enzi, magari yameweza kuvuka Mto wa Kilombero, moja ya mito mikubwa zaidi nchini, mpakani mwa Wilaya za Ulanga na Kilombero katika Mkoa wa Morogoro.
Magari hayo ya msafara wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete yamevuka Mto Kilombero kwa kutumia daraja dogo la muda ambalo wajenzi wa daraja kwenye mto huo wamelijenga kwa ajili ya kurahisisha kazi yao ya ujenzi wa daraja hilo kubwa. Daraja hilo la muda la chuma lina uwezo wa kubeba tani 100.
Rais Kikwete na msafara wake wa magari kiasi ya 20 umevuka Mto Kilombero kwa kutumia magari ukitokea Wilaya ya Ulanga kuingia katika Wilaya ya Kilombero kwa ajili ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa daraja hilo katika sherehe iliyofanyika upande wa mto wa Wilaya ya Kilombero, kilomita kiasi cha saba unusu kutoka mjini Ifakara.
Rais Kikwete ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa Daraja la Mto Kilombero kwenye siku yake ya kwanza ya ziara yake ya siku saba katika Mkoa wa Morogoro.
Rais Kikwete ameanzia ziara hiyo katika Kijiji cha Mwaya ambako amezindua Mradi wa Kusambaza Umeme Vijijini na pia kuzindua Mradi wa Mfumo wa Huduma za Afya za Masafa (Telemedicine).
Daraja hilo linalojengwa kwenye Mto Kilombero unakamilisha ujenzi wa madaraja matano makubwa nchini ambayo yalikuwa yamepangwa kujengwa katika Mpango wa Kwanza wa Taifa wa Maendeleo mwaka wa fedha wa 1967-1968 lakini likashindikana kujengwa kwa miaka 47 iliyopita mpaka sasa.
Daraja hilo linalogharimu Sh. bilioni 55.8 ambazo zote zinatolewa na Serikali ya Tanzania linajengwa na Kampuni ya China Railway 15 ya China, lina madaraja mawili – kubwa ambalo lina urefu wa mita 384 na dogo lenye urefu wa mita 120, litakuwa pia na makaravati 35, na njia ya watu kupita kwa mguu na baiskeli.
Daraja hilo lenye uwezo wa kubeba tani 180 kwa wakati mmoja, pia litajengwa pamoja na barabara ya lami ya kilomita 9.5, ikiwa ni kilomita saba unusu upande wa Ifakara na kilomita mbili upande wa Wilaya ya Ulanga.
Akizungumza kwenye sherehe hiyo iliyohudhuriwa na mamia kwa mamia ya wananchi pamoja na kwamba Rais Kikwete alikawia kidogo kufika darajani hapo kwa sababu ya shughuli za uzinduzi wa miradi mingi kwenye Wilaya ya Ulanga, Mtendaji Mkuu wa Tanroads, Mhandisi Patrick Mufugale amesema kuwa ujenzi wa daraja hilo umechelewa kidogo kwa sababu ya tuta na daraja la mwanzo la muda kuchukuliwa na maji wakati wa mafuriko ya mwaka huu.
Amesema kuwa kutokana na tukio hilo, ujenzi wa sasa umefanyiwa marekebisho makubwa ambayo yataliwezesha tuta la sasa kuweza kuhimili aina yoyote ya mafuriko makubwa hata kwa miaka 100 ijayo.
Baada ya kushindikana kujengwa kwa miaka mingi, Rais Kikwete, wakati akiwa Mgombea Urais wa Chama cha Mapinduzi (CCM) katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005 aliahidi ujenzi wa daraja hilo. Aidha, ujenzi huo uliwekwa katika Ilani ya CCM ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010.
Akizungumza na wananchi baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa daraja hilo na kupanda Mti wa Kumbukumbu, Rais alikumbusha historia ya ujenzi wa daraja hilo akisema kuwa katika Mpango wa Kwanza wa Taifa wa Maendeleo, Serikali iliamua kujenga madaraja matano makubwa nchini.
Amesema kuwa madaraja hayo ni Daraja la Kirumi kwenye Mto Mara, Daraja la Mto Rufiji, Daraja la Kigamboni, Dar Es Salaam; Daraja la Mto Kilombero na Daraja la Mto Malagarasi.
Amesema kuwa kati ya madaraja hayo, Uongozi wa Awamu ya Kwanza ulijenga Daraja la Kirumi kwenye Mto Mara na Uongozi wa Awamu ya Tatu ukajenga darala la Mto Rufiji.
“Sisi tuliamua kujenga madaraja matatu makubwa – Kigamboni na kwenye Mito Malagarasi na Kilombero. Lile la Malagarasi limekamilika, lile la Kigamboni linakamilika na litakuwa tayari Juni, mwakani, wakati leo tumeweka jiwe la msingi kwenye Ujenzi wa hili la Kilombero ambalo ujenzi wake tayari umeanza.”
Rais Kikwete ambaye ameanza ziara ya Mkoa wa Morogoro leo, kesho ataendelea na ziara yake katika Wilaya za Morogoro
Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
20 Agosti,2014
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, Jumatano, Agosti 20, 2014 ameanza ziara ya Mkoa wa Morogoro kwa kuzindua Mfumo wa Huduma za Afya za Masafa – telemedicine – katika Kituo cha Afya cha Mwaya, Wilaya ya Ulanga, ambako mtoto mchanga wa kike wa umri wa saa chache amepewa jina la Salma, mke wa Rais Kikwete.
Rais Kikwete ambaye amewasili Kijiji cha Mwaya, kwa helikopta akitokea Dar es Salaam, kuanza ziara hiyo ya siku saba Mkoani Morogoro, ameanza kwa kuzindua Mradi Mkubwa wa Kusambaza Umeme Vijijini Morogoro kabla ya kwenda kwenye Kituo cha Afya cha Mwaya.
Kwenye Kituo hicho cha afya, Rais Kikwete ameambiwa na Daktari Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dkt. Godfrey Mtei kuwa mradi umethibisha uwezo mkubwa wa kuokoa maisha ya akinamama waja wazito wakati wa kujifungua, kutokana na wataalam kubadilisha ujuzi na utaalam kwa njia ya mtandao wa internet na simu wakati wa kuwazalisha akinamama.
Dkt. Mtei amesema kuwa tokea mwaka 2010 kiasi cha akinamama 13,674 wamejifungulia katika vituo vya afya vitatu vya Mwaya, Mtimbira na Mlimba ambavyo viko katika Mfumo huo katika Mkoa wa Morogoro na kati ya hao 1,360 wamejifungua kwa upasuaji na vimetokea vifo tisa tu katika kipindi hicho chote.
Mfumo huo unatekelezwa kwa pamoja kati ya Serikali ya Tanzania na Shirika Lisilokuwa la Kiserikali la World Lung Foundation ambalo linafadhiliwa, miongoni mwa taasisi nyingine, na Bloomberg Philanthropies, unatekelezwa katika Mikoa ya Pwani, Morogoro na Kigoma.
Miongoni mwa mambo mengine, World Lung Foundation linagharimia vifaa kama simu, kompyuta mpakato (laptops), moderms, linatoa mafunzo kwa watumishi wawili wawili kutoka kila moja ya vituo vya afya ambako Mfumo huo unaendeshwa na kutoa gharama ya vituo kuunganishwa kwenye mtandao.
Aidha, chini ya Mpango wa Kuboresha Huduma za Afya ya Uzazi na Mtoto, Shirika hilo pia linajenga vyumba vya upasuaji ikiwa ni pamoja na kutoa tiba stahiki, wadi za wazazi, uboreshaji wa mifumo ya maji na umeme kwa kuweka jenereta na sola, kujenga nyumba za watumishi na kutoa mafunzo mahsusi kwa watumishi wapatao 106.
Mara baada ya kuzindua Mfumo huo, Rais Kikwete ambaye anafuatana na Mama Salma Kikwete amemtembelea wodini mtoto wa kike ambaye amezaliwa leo hii chini ya Mfumo huo. Mama yake mtoto huyo ameamua kumpa mtoto huyo jina la Salma (la Mama Kikwete) mara baada ya Mama Salma kumbeba na kumfurahia mtoto huyo.
Kwenye makao makuu ya Wilaya ya Ulanga ya Mahenge, Rais Kikwete amezindua Hosteli ya wasichana katika Shule ya Sekondari ya Nawenge na pia kupokea madawati 100 kwa ajili ya shule ya msingi ya Epanko ambayo yametolewa na Kampuni ya Kibaran Resources ya Australia ambayo inafanya maandalizi ya uchumbaji wa madini ya uno – graphite – katika wilaya hiyo. Shule ya Sekondari ya Nawenge ina wanafunzi 475 na walimu 26. Aidha, Rais Kikwete amezindua mradi wa maji wa mjini Mahenge ambao umegharimiwa na Serikali kwa kiasi cha sh. milioni 433.7. Mradi huo umejengwa kutokana na ahadi ya Rais Kikwete ya mwaka 2008 wakati alipotembelea Wilaya ya Ulanga.
Rais Kikwete pia amesimama Kijiji cha Lupiro ambako amezindua maghala ya kuhifadhi mchele baada ya kuwa umepukuchuliwa kutoka kwenye mpunga na kuhutubia mkutano wa hadhara ambako wananchi wametoa kilio chao kutokana na ukosefu la soko la uhakika la mchele.
Baada ya Lupiro, Rais Kikwete ameingia katika Wilaya ya Kilombero ambako ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa Daraja la Mto Kilombero ambalo ujenzi wake umekuwa unazungumzwa na kupangwa kutokea mwaka wa fedha wa 1967-1968.
Rais Kikwete leo, Alhamisi, Agosti 21, 2014 anaendelea na ziara yake katika Mkoa huo wa Morogoro kwa kutembelea Wilaya ya Morogoro.
Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
21 Agosti,2014
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia Salamu za Rambirambi Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, National Electoral Commission (NEC) kufuatia taarifa za kifo cha aliyekuwa Mwenyekiti wa Kwanza wa Tume hiyo, Jaji Mstaafu, Mheshimiwa Lewis Makame kilichotokea katika Hospitali ya AMI Trauma Centre Jijini Dar es Salaam tarehe 18 Agosti, 2014.
“Nimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo cha Jaji Mstaafu wa Mahakama ya Rufaa Tanzania na Mwenyekiti wa Kwanza wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) chini ya Mfumo wa Vyama Vingi vya Siasa, Mheshimiwa Lewis Makame ambaye amelitumikia Taifa letu katika Utumishi wa Umma kwa uaminifu, uadilifu, bidii na umahiri mkubwa”, amesema kwa masikitiko Rais Kikwete katika Salamu zake.
Katika utumishi wake, Marehemu Jaji Lewis Makame, enzi za uhai wake, alikuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania kabla ya kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufaa na baadaye Mwenyekiti wa NEC ambayo aliiongoza kwa miaka 17 mfululizo hadi alipostaafu mwaka 2011. Uongozi wake ulichangia sana kuimarisha amani, utulivu, umoja na mshikamano wa kitaifa katika mazingira mapya ya demokrasia ya vyama vingi vya siasa hapa nchini.
“Ni kwa kutambua kipaji kikubwa cha uongozi alichokuwa nacho Marehemu Jaji Lewis Makame, Taifa letu limepoteza mtu muhimu sana kwani hata baada ya kustaafu kwake alikuwa bado anahitajika sana kutokana na mchango wake wa ushauri katika mambo mengi yanayohusu maendeleo ya nchi yetu”, amesema Rais Kikwete na kuongeza,
“Kutokana na msiba huu mkubwa, nakutumia Salamu za Rambirambi kwa kumpoteza aliyekuwa Kiongozi Mahiri wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi. Kupitia kwako, naomba Salamu zangu za Rambirambi na pole nyingi ziifikie Familia ya Marehemu kwa kumpoteza Kiongozi na Mhimili Madhubuti. Namuomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema aipokee na kuilaza Mahala Pema Peponi Roho ya Marehemu, Jaji Lewis Makame, Amina”, amesema Rais Kikwete akiomboleza msiba huu.
Amewahakikishia Wanafamilia kuwa yuko pamoja nao katika kuomboleza msiba huu mkubwa, na anamuomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema awape moyo wa uvumilivu, ujasiri na subira Wanafamilia wote, ndugu na jamaa wa Marehemu, ili waweze kuhimili machungu ya kuondokewa na Mpendwa wao kwa kutambua kuwa yote ni Mapenzi yake Mola.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
19 Agosti, 2014
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Msichana wa Kitanzania ashinda mashindano ya Insha ya SADC
- Ni Neema Steven kutoka Shule ya Sekondari ya Naboti, Njombe
- Awabwaga washindani 39 wa kanda mbali na wa nyumbani
Mtoto wa Kitanzania,msichana Neema Steven Mtwanga, ameibuka kinara katika Mashindano ya Utunzi wa Insha katika nchi wanachama wa Jumuia ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) kwa kushika nafasi ya kwanza miongoni mwa washindani 39 waliowania Tuzo ya Utunzi wa Insha hiyo kwa Mwaka 2014.
Msichana Neema Steven Mtwanga, 16, kutoka Shule ya Sekondari ya Naboti, Mkoa wa Njombe, ametunukiwa Tuzo ya ushindi huo katika Mkutano wa 34 wa Kawaida wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa SADC ulioanza leo katika Hoteli ya Elephant Hills Resort, Victoria Falls, Zimbabwe.
Nafasi ya pili imeshikwa na Kudzai Ncube kutoka Shule ya Sekondari ya Mazowe nchini Zimbabwe na nafasi ya tatu imeshikwa na Manxoba Msibi kutoka Shule ya Sekondari ya Etjendlovu katika Swaziland.
Kwa ushindi huo, Neema Steven Mtwanga ambaye yuko kidato cha nne, amezawadiwa hundi ya dola za Marekani 1500 ambayo ni sawa na shilingi milioni 2.3 na amelipiwa gharama zote za kumwezesha kushiriki katika Mkutano wa Wakuu wa Nchi za SADC na kukabidhiwa zawadi hiyo. Aidha, Neema amepewa zawadi ya ipad kwa ajili ya matumizi yake ya teknolojia ya mawasiliano na habari.
Mashindano hayo ya Insha ya Mwaka 2014 yalianzishwa rasmi Oktoba, 2013 ambako washindani walitakiwa kuandika Insha kuhusu mada: “Climate Change is having adverse effect on the socio-economic development in the Region. What should the Education Sector do to mitigate the impact on the youth” – Mabadiliko ya Tabia Nchi yanaathiri maendeleo ya kijamii na kiuchumi ya Kanda ya SADC. Nini Sekta ya Elimu ifanye kupunguza athari hizo kwa vijana?
Insha 39 zilipokelewa kutoka nchi 13 kati ya nchi 15 wanachama wa SADC ikiwa ni Insha tatu kwa kila nchi. Insha zilipokelewa kutoka Tanzania, Angola, Botswana, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Lesotho, Malawi, Mauritius, Mozambique, Namibia, Afrika Kusini, Swaziland, Zambia na Zimbabwe.
Majaji wa kupitia na kuamua washindi wa Insha hizo walitoka Tanzania, Zambia na Zimbabwe na walikutana mjini Gaborone, Botswana, Julai, mwaka huu kupitia Insha zote na kutoa uamuzi wa nani washindi.
Ujumbe wa Tanzania kwenye Mkutano huo wa SADC umepokea kwa furaha ushindi wa msichana Neema ukieleza kuwa ushindi huo umeiletea Tanzania heshima kubwa katika eneo la SADC na nje ya eneo hilo.
Mwisho!
Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
17 Agosti,2014
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Tanzania yatamba Zimbabwe
- Brigedia Hashim Mbita atunukiwa Tuzo la Monomtapa
- Ripoti yake kuhusu Ukombozi wa Kusini mwa Afrika yazinduliwa
Zimbabwe imemtunukia Mtanzania, Katibu Mtendaji wa zamani wa Kamati ya Ukombozi ya Afrika, Brigedia Jenerali Hashim Mbita, Tuzo ya juu kabisa ambayo hutolewa na Taifa la Zimbabwe kwa watu wachache sana duniani, tuzo ambayo pia inaambatana na zawadi ya dola za Marekani laki moja – sawa na shilingi milioni 160.
Rais Robert Gabriel Mugabe amemtunuku tuzo hiyo Brigedia Mbita kutokana na mchango wake wa kuitoa Zimbabwe katika minyororo ya ukoloni katika nafasi yake kama Katibu Mtendaji wa Kamati ya Ukombozi ya Afrika ambayo aliingoza kwa miaka zaidi ya 20 tokea 1972 hadi 1994 wakati Afrika Kusini ilipofuta Ubaguzi wa Rangi.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete alikuwa miongoni mwa viongozi wa Nchi Wanachama wa Jumuia ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) walioshuhudia tukio hilo kwenye Hoteli ya Elephant Hills Resort, Victoria Falls, Zimbabwe ambako viongozi hao wanakutana katika Mkutano wa 34 wa mwaka wa Viongozi wa SADC.
Hiyo ni mara ya kwanza kwa Taifa la Zimbabwe kutunuku tuzo hiyo kubwa na ya heshima zaidi kuliko nyingine yoyote ya Nishani ya Royal Order of Monomtapa kwa binadamu ambaye siyo Rais ama siyo Rais wa zamani. Nishani hiyo inapata jina lake kutoka kwa Mtawala wa eneo ambalo sasa ni Zimbabwe kabla ya wakoloni wa Kiingereza hawajaitawala nchi hiyo.
Maelezo ya Mzee Mbita yaliwasilishwa na Katibu Kiongozi wa Serikali ya Zimbabwe na Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo na Brigedia Mbita anakuwa binadamu wa sita kutunukiwa tuzo hiyo.
Watunukiwa wengine ambao mpaka sasa wamepata tuzo hiyo ni viongozi waanzilishi wa Umoja wa Nchi za Mstari wa Mbele katika Ukombozi wa Afrika (Frontline States) ni Mwalimu Julius Nyerere, Hayati Augustino Neto wa Angola, Hayati Samora Machel wa Mozambique, Hayati Sir Seretse Khama wa Botswana na Rais Kenneth Kaunda wa Zambia.
Akikabidhi nishani hiyo, Rais Mugabe amemwelezea Mzee Mbita kama “kiongozi wa kijeshi na mkombozi ambaye alitoa mchango usiopimika na kuonyesha nia thabiti kwa ukombozi wa nchi zetu Kusini mwa Afrika. Ni mtu ambaye amesaidia jitihada za ukombozi katika kanda yetu na nje yake akitujengea misingi ya kuungwa mkono kijeshi, kisiasa na kidiplomasia.”
Ameongeza Rais Mugabe: “Huyu ndiye alikuwa kinara wa mapambano yetu yote kuanzia kwenye ustawi wetu, kupata sare za kivita, kuhakikisha safari zetu zinapangwa vizuri na kutupa ushauri wa kijeshi – huyo ndiye alikuwa Brigedia Komredi Hashim Mbita”.
Rais Mugabe ambaye ametunuku nishani hiyo kwa nafasi yake kama Rais wa Zimbabwe, Amirijeshi mkuu wa nchi hiyo ambaye anabeba nishani ya Grand Master of the Zimbabwe Order of Merit amesikitishwa na ukweli kuwa Mzee Mbita hakuweza kuhudhuria nafasi hiyo kwa sababu ya kudorora kwa afya yake.
Badala yake nishani hiyo imepokelewa kutoka kwa Mzee Mugabe na Bi. Sheila Hashim Mbita, mtoto wa kwanza wa Brigedia Mbita ambaye ameishuku sana Zimbabwe na Rais Mugabe kwa uamuzi wao wa kumtunukia baba yake.
“Baba yangu ameshindwa kuhudhuria sherehe hii muhimu sana kwake, lakini alifurahi sana alipopewa habari za nishani hii. Mimi nikiwa mtoto wa kwanza katika familia namwakilisha baba yangu na familia yote,” amesema Bi. Sheila.
Ameongeza Bi. Sheila, “sisi kama familia tukiongozwa na baba yetu tunathamini sana nishani hii. Baba yangu aliingoza kwa muda mrefu ofisi ya Kamati ya Ukombozi wa Kusini mwa Afrika tokea mwaka 1972 hadi ilipofungwa mwaka 1994 baada ya Afrika Kusini kushinda siasa za Ubaguzi wa Rangi”.
Brigedia Hashim Mbita alikuwa Katibu Mtendaji wa tatu na wa mwisho wa Kamati ya Ukombozi wa Kusini mwa Afrika ambaye pia aliiongoza kamati hiyo kwa muda mrefu zaidi kuliko mwingine yoyote.
Brigedia Mbita ni mtumishi wa umma mstaafu, ofisa wa jeshi, mwandishi wa habari na mwanasiasa ambaye kwa nyakati mbali mbali kabla ya kuwa Katibu mtendaji wa Kamati ya Ukombozi, alifanya kazi kama Ofisa Habari wa Mkoa, Ofisa Mkuu wa Habari wa Serikali, Mwandishi wa Habari wa Rais, Balozi, Katibu Mwenezi na Katibu Mtendaji wa Taifa wa chama cha siasa cha TANU.
Mwisho!
Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
17 Agosti,2014
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amewasili Victoria Falls, Zimbabwe, kuhudhuria Mkutano wa 34 wa Kawaida wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuia ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).
Rais Kikwete, mara baada ya kuwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa mji wa kitalii wa Victoria Falls, ameingia katika kikao cha kwanza ambacho ni mkutano wa nchi wanachama wanaounda Asasi ya Siasa na Ulinzi ya SADC (Troika Organ). Kikao hicho, kama ulivyo Mkutano wenyewe wa SADC, kinafanyika kwenye Hoteli ya Elephants Hills.
Mkutano wenyewe ambao utafanyika chini ya Rais Robert Gabriel Mugabe wa Zimbabwe ambaye ndiye mwenyeji wa Mkutano huo, umaanza asubuhi ya leo, Jumapili, Agosti 17, 2014.
Sherehe hiyo ya ufunguzi itaanza kwa hotuba ya Katibu Mtendaji wa SADC, Dkt. Stergomena Lawrence Tax, Mtanzania, ikifuatiwa na hotuba ya Rais Mugabe mwenyewe ambaye atakuchukua Uenyekiti wa SADC kwenye siku hiyo ya kwanza ya Mkutano huo.
Mkutano pia utahutubiwa na Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AU), Dkt. Nkosazana Dlamini-Zuma na Marais wapya wawili wa Nchi wanachama wa SADC. Marais hao ni Profesa Arthur Peter Mutharika wa Malawi ambaye pia ni Mwenyekiti wa SADC anayemaliza muda wake na Rais Hery Rajaonarimampianina wa Madagascar.
Kwenye mkutano huo pia Mradi wa Kitabu cha Hashim Mbita wa Tanzania utawasilishwa kwa marais na Meneja wa Mradi huo ambao shahaba yake ni kuweka kumbukumbu ya Historia ya Ukombozi wa Nchi za Kusini mwa Afrika. Aidha, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Utafiti wa Kupambana na Umasikini (REPOA), Profesa Samuel Wangwe atawasilisha mada kuu ya Mkutano huo wa 34 ambayo kimsingi ni kuangalia jinsi gani nchi za SADC zinavyoweza kujiboresha kiuchumi.
Mkutano huo wa siku mbili unamalizika Jumatatu, Agosti 18, 2014.
Mwisho!
Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
17 Agosti,2014
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
SADC yaishukuru Tanzania kwa mchango wa ukombozi
Aidha, SADC yashukuru na kumpongeza Mzee Hashim Mbita
Jumuia ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) imeishukuru na kuipongeza tena Tanzania kwa mchango wake mkubwa na wa hali na mali uliofanikisha jitihada za mapambano ya ukombozi yaliyoleta uhuru kwa nchi za Kusini mwa Afrika.
Aidha, SADC imemshukuru na kumpongeza aliyekuwa Katibu Mtendaji wa Kamati ya Ukombozi ya Afrika, Brigedia Hashim Mbita wa Tanzania, kwa mchango wake na uongozi wake wa mapambano ya ukombozi, iwe katika nyanja ya kuviwezesha vyama vya ukombozi kwa hali na mali, raslimali na ushauri.
Pongezi hizo kwa Tanzania zilitolewa usiku wa jana, Jumamosi, Agosti 16, 2014, na Kikao cha Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC – SADC Troika- kilichofanyika kwenye Hoteli ya Elephant Hills Resort, Victoria Falls, Zimbabwe, chini ya Uenyekiti wa Rais Hifikepunye Phohaba wa Namibia.
Mkutano huo wa SADC Troika ulihudhuriwa na wanachama wa Asasi hiyo – nchi za Namibia, Lesotho na Tanzania. Nchi za Afrika Kusini, Madagascar na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) zilishiriki kama waalikwa maalum wa kikao hicho.
Akizungumza kwenye mkutano huo kwa niaba ya nwenzake, Rais Pohamba alisema: “Tunawashukuru wananchi wa Tanzania kwa mchango wao wa kiuchumi, kijeshi na kimkakati katika kuunga mkono kwa hali na mali jitihada za mapambano ya ukombozi wa nchi zetu.”
Aliongeza Rais Pohamba: “Sote tunaijua Tanzania, sote tunawajua Watanzania. Kwa pamoja walitoa jasho na damu na sisi wenyewe katika kutafuta ukombozi wa nchi zetu. Tutaendelea kukumbuka na kuenzi mchango wao mkubwa na usiosahaulika kwa ustawi wa nchi zetu.”
Kuhusu Mzee Mbita, ambaye Ripoti yake ya shughuli za ukombozi ilitarajiwa kuwasilishwa kwenye Mkutano wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa SADC, Rais Pohamba alisema: “Brigedia Mbita alifanya kazi mchana na usiku kufanikisha shughuli za ukombozi wa Kusini mwa Afrika. Tunamshukuru sana kwa uongozi wake na mchango wake mkubwa katika kuleta uhuru wa nchi zetu.”
Aliongeza: “Brigedia Mbita ni raia wa Tanzania na alikuwa Katibu Mtendaji wa Kamati ya Ukombozi Kusini mwa Afrika iliyokuwa na makao makuu yake mjini Dar es Salaam. Alichapa kazi kweli kweli na chini ya uongozi wake, vyama vya ukombozi vilipata misaada ya hali na mali, misaada ya kiroho na ushauri wa kijeshi kwa sababu yeye mwenyewe alikuwa mtu wa shughuli za jeshi.” Mzee Mbita aliongoza Kamati ya Ukombozi tokea mwaka 1974 hadi ilipomaliza shughuli zake.
Akizungumza kwa ufupi sana katika kikao hicho, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete alimpongeza sana Brigedia Mbita akisema kuwa alifanya kazi nzuri na kubwa na “tunampogeza kwa kazi nzuri sana ya kuandaa Ripoti hiyo.”
Ripoti hiyo inayojulikana kama Mradi wa Hashim Mbita iliongozwa na Meneja wa Mradi, Profesa Arnold Temu wa Tanzania na imechapishwa na Kampuni ya Mkuki na Nyota, pia ya Tanzania, ambayo Mtendaji Mkuu wake, Mzee Walter Bgoya ameandamana na mwakilishi wa Mzee Mbita kwenye mkutano huo.
Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
17 Agosti,2014
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Tanzania yatamba Zimbabwe
- Brigedia Hashim Mbita atunukiwa Tuzo la Monomtapa
- Ripoti yake kuhusu Ukombozi wa Kusini mwa Afrika yazinduliwa
Zimbabwe imemtunukia Mtanzania, Katibu Mtendaji wa zamani wa Kamati ya Ukombozi ya Afrika, Brigedia Jenerali Hashim Mbita, Tuzo ya juu kabisa ambayo hutolewa na Taifa la Zimbabwe kwa watu wachache sana duniani, tuzo ambayo pia inaambatana na zawadi ya dola za Marekani laki moja – sawa na shilingi milioni 160.
Rais Robert Gabriel Mugabe amemtunuku tuzo hiyo Brigedia Mbita kutokana na mchango wake wa kuitoa Zimbabwe katika minyororo ya ukoloni katika nafasi yake kama Katibu Mtendaji wa Kamati ya Ukombozi ya Afrika ambayo aliingoza kwa miaka zaidi ya 20 tokea 1972 hadi 1994 wakati Afrika Kusini ilipofuta Ubaguzi wa Rangi.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete alikuwa miongoni mwa viongozi wa Nchi Wanachama wa Jumuia ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) walioshuhudia tukio hilo kwenye Hoteli ya Elephant Hills Resort, Victoria Falls, Zimbabwe ambako viongozi hao wanakutana katika Mkutano wa 34 wa mwaka wa Viongozi wa SADC.
Hiyo ni mara ya kwanza kwa Taifa la Zimbabwe kutunuku tuzo hiyo kubwa na ya heshima zaidi kuliko nyingine yoyote ya Nishani ya Royal Order of Monomtapa kwa binadamu ambaye siyo Rais ama siyo Rais wa zamani. Nishani hiyo inapata jina lake kutoka kwa Mtawala wa eneo ambalo sasa ni Zimbabwe kabla ya wakoloni wa Kiingereza hawajaitawala nchi hiyo.
Maelezo ya Mzee Mbita yaliwasilishwa na Katibu Kiongozi wa Serikali ya Zimbabwe na Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo na Brigedia Mbita anakuwa binadamu wa sita kutunukiwa tuzo hiyo.
Watunukiwa wengine ambao mpaka sasa wamepata tuzo hiyo ni viongozi waanzilishi wa Umoja wa Nchi za Mstari wa Mbele katika Ukombozi wa Afrika (Frontline States) ni Mwalimu Julius Nyerere, Hayati Augustino Neto wa Angola, Hayati Samora Machel wa Mozambique, Hayati Sir Seretse Khama wa Botswana na Rais Kenneth Kaunda wa Zambia.
Akikabidhi nishani hiyo, Rais Mugabe amemwelezea Mzee Mbita kama “kiongozi wa kijeshi na mkombozi ambaye alitoa mchango usiopimika na kuonyesha nia thabiti kwa ukombozi wa nchi zetu Kusini mwa Afrika. Ni mtu ambaye amesaidia jitihada za ukombozi katika kanda yetu na nje yake akitujengea misingi ya kuungwa mkono kijeshi, kisiasa na kidiplomasia.”
Ameongeza Rais Mugabe: “Huyu ndiye alikuwa kinara wa mapambano yetu yote kuanzia kwenye ustawi wetu, kupata sare za kivita, kuhakikisha safari zetu zinapangwa vizuri na kutupa ushauri wa kijeshi – huyo ndiye alikuwa Brigedia Komredi Hashim Mbita”.
Rais Mugabe ambaye ametunuku nishani hiyo kwa nafasi yake kama Rais wa Zimbabwe, Amirijeshi mkuu wa nchi hiyo ambaye anabeba nishani ya Grand Master of the Zimbabwe Order of Merit amesikitishwa na ukweli kuwa Mzee Mbita hakuweza kuhudhuria nafasi hiyo kwa sababu ya kudorora kwa afya yake.
Badala yake nishani hiyo imepokelewa kutoka kwa Mzee Mugabe na Bi. Sheila Hashim Mbita, mtoto wa kwanza wa Brigedia Mbita ambaye ameishuku sana Zimbabwe na Rais Mugabe kwa uamuzi wao wa kumtunukia baba yake.
“Baba yangu ameshindwa kuhudhuria sherehe hii muhimu sana kwake, lakini alifurahi sana alipopewa habari za nishani hii. Mimi nikiwa mtoto wa kwanza katika familia namwakilisha baba yangu na familia yote,” amesema Bi. Sheila.
Ameongeza Bi. Sheila, “sisi kama familia tukiongozwa na baba yetu tunathamini sana nishani hii. Baba yangu aliingoza kwa muda mrefu ofisi ya Kamati ya Ukombozi wa Kusini mwa Afrika tokea mwaka 1972 hadi ilipofungwa mwaka 1994 baada ya Afrika Kusini kushinda siasa za Ubaguzi wa Rangi”.
Brigedia Hashim Mbita alikuwa Katibu Mtendaji wa tatu na wa mwisho wa Kamati ya Ukombozi wa Kusini mwa Afrika ambaye pia aliiongoza kamati hiyo kwa muda mrefu zaidi kuliko mwingine yoyote.
Brigedia Mbita ni mtumishi wa umma mstaafu, ofisa wa jeshi, mwandishi wa habari na mwanasiasa ambaye kwa nyakati mbali mbali kabla ya kuwa Katibu mtendaji wa Kamati ya Ukombozi, alifanya kazi kama Ofisa Habari wa Mkoa, Ofisa Mkuu wa Habari wa Serikali, Mwandishi wa Habari wa Rais, Balozi, Katibu Mwenezi na Katibu Mtendaji wa Taifa wa chama cha siasa cha TANU.
Mwisho!
Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
17 Agosti,2014
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete asubuhi ya leo, Ijumaa, Agosti 15, 2014, amewaapisha Majaji 20 wapya wa Mahakama Kuu ya Tanzania ambao aliwateua mwanzoni mwa wiki hii katika hafla iliyofanyika Ikulu, Dar Es Salaam.
Halfa hiyo iliyofanyika Ikulu, Dar Es Salaam ilihudhuriwa pia na Makamu wa Rais Mheshimiwa Mohamed Gharib Bilal, Waziri Mkuu Mheshimiwa Mizengo Pinda, Jaji Mkuu wa Tanzania Mheshimiwa Mohamed Chande Othman, Waziri wa Katiba na Sheria Mheshimiwa Asha Rose Migiro na Jaji Mkuu wa Zanzibar Mheshimiwa Omar Othman Makungu.
Majaji hao wapya wa Mahakama Kuu ya Tanzania ni pamoja na akinamana wanane na uteuzi huo wa Mheshimiwa Rais Kikwete umeshirikisha wanasheria kutoka Serikalini, Taasisi za Umma, Jumuia ya Afrika Mashariki, Sekta Binafsi na Asasi za Kiraia.
Majaji hao wapya ambao wameapishwa leo ni Jaji Penterine Muliisa Kente, Jaji Benedict Batholomew Mwingwa, Jaji Eliezer Mbuki Feleshi, Jaji John Eudes Ruhangisa, Jaji Winfrida Beatrice Korosso, Jaji Lilian Leonard Mashaka, Jaji David Eliad Mrango, Jaji Edson James Mkasimongwa, Jaji Mohamed Rashid Gwae na Jaji Firmin Nyanda Matogoro.
Wengine ni Jaji Leila Edith Mgonya, Jaji Barke Mbaraka Abdou Sehel, Jaji Awadhi Mohamed, Jaji Lugano J. Mwandambo, Jaji Rose Ally Ibrahim, Jaji Paul Kihwelu, Jaji Modesta Opiyo Makopolo, Jaji Amour Said Khamisi, Jaji Mary Caroline Levira na Jaji Salma Maghimbi.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
15 Agosti, 2014
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amemteua Dkt. Charles Msonde kuwa Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Mitihani Tanzania (NECTA).
Taarifa iliyotolewa Ikulu, Dar es Salaam jioni ya jana, Alhamisi, Agosti 14, 2014, na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue inasema kuwa uteuzi huo ulianza juzi, Jumatano, Agosti 13, 2014.
Kabla ya uteuzi wake, Dkt. Msonde alikuwa Kaimu Katibu Mtendaji wa Baraza hilo hilo la mitihani.
Dkt. Msonde anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Dkt. Joyce Ndalichako, ambaye amerudi kuendelea na kazi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam baada ya kumaliza likizo yake ya kujinoa (Sabbatical Leave).
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
15 Agosti, 2014
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
JK: Tunakwamishwa na uzalishaji na matumizi madogo mno ya umeme
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa moja ya sababu kubwa zinazokwamisha maendeleo makubwa zaidi na ya haraka zaidi ya Afrika ni uzalishaji mdogo na matumizi ya chini mno ya umeme.
Aidha, Rais Kikwete amesema kuwa hali hiyo inaeleza jinsi ongezeko la uzalishaji na matumizi ya umeme linavyoweza kuharakisha maendeleo ya Afrika na kuleta manufaa ya dhahiri kwa kila familia na kwa kila Mwafrika.
Rais Kikwete ameyasema hayo jana, Jumatano, Agosti 6, 2014, wakati alipozungumza kwenye Mkutano wa Kwanza wa Wakuu wa Nchi za Bara la Afrika uliofanyika chini ya uenyekiti wa Rais Barack Obama, ambaye ni mwenyeji wa Mkutano huo.
Rais Kikwete amewaambia wakuu wa nchi hizo kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani kuwa ni dhahiri kuwa bila ongezeko kubwa la uzalishaji na matumizi ya umeme Bara la Afrika halitatoka kwenye uduni.
Rais amesema kuwa kwa mujibu wa Ripoti ya Kanda ya Shirika la Umoja wa Mataifa Mazingira (UNEP) “Efficient Lighting in Sub Saharan African Countries” matumizi ya umeme katika Bara zima la Afrika ni asilimia 31 tu na hivyo kulifanya Bara la Afrika kutumia asilimia tatu tu ya umeme wote duniani.
Rais Kikwete amesema kuwa ili kuelewa udogo wa matumizi ya umeme ya Bara la Afrika ni kuangalia matumizi ya nishani hiyo kwa kila mkazi wa Bara hilo na yule wa Marekani. Amesema kuwa wakati kila raia wa Marekani anatumia kilowati 13, 246 katika Afrika wastani ni kilowati 440.
Ameongeza Rais Kikwete: “Ukiondoa Afrika Kusini, matumizi ya umeme kwa kila raia wa Afrika yanateremka na kufikia kilowati 160 tu.”
Amefafanua Rais Kikwete: “Uzalishaji wa jumla wa umeme wa Bara la Afrika ni gigawati 63 ambazo ni sawa na umeme unaozalishwa na nchi moja tu ya Ulaya – Hispania. Ukiondoa Afrika Kusini, nchi zinazobakia wa Afrika zina uwezo wa kuzalisha gigawati 28 tu, kiasi ambacho kinazalishwa na nchi moja tu ya Marekani Kusini ya Argentina.”
Rais Kikwete ambaye alikuwa anafafanua jinsi utoaji huduma ulio dhahiri unavyoweza kunufaisha wananchi na kujenga mazingira ya taasisi zisizokuwa za kiserikali kushamiri, ametaja mambo mengine ya msingi ambayo ni lazima yawepo ili wananchi waweze kunufaika ikiwemo elimu, ushamiri wa sekta binafsi, sera sahihi za kiuchumi, uwekezaji katika ujenzi wa miundombinu na uboreshaji wa kilimo.
Pia Rais Kikwete ametaja mambo mengine muhimu yanayoweza kusaidia kuboresha maisha ya wananchi kuwa ni uendelezaji na matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano pamoja na kulea na kukuza demokrasia, utawala bora na utawala wa sheria.
Rais Kikwete ambaye yuko katika ziara ya kikazi ya siku tisa katika Marekani, anaondoka mjini Washington, D.C., leo kwenda Houston ambako atafungua na kushiriki katika mkutano wa uwekezaji katika uchumi wa Tanzania.
Mwisho!
Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
07 Agosti, 2014
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
JK: Nataka kuwa Rais wa mwisho kuongoza Tanzania masikini
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa anataka na anatamani kuwa Rais wa mwisho wa Tanzania kuongoza nchi ambayo ni maskini na hivyo atatumia muda wake uliobakia katika uongozi kuelekeza nchi kwenye mwelekeo huo.
Aidha, Rais Kikwete amesema kuwa jambo la msingi kabisa la kama Watanzania watanufaika na ugunduzi wa gesi asili ama watabakia katika hali yao ya sasa ya umasikini ni aina ya uongozi ambao nchi hiyo itaupata, uongozi wenye uwezo wa kufanya maamuzi sahihi kwa kadri nchi inavyozidi kusonga mbele.
Rais Kikwete pia anasema kuwa Tanzania inatarajia kuanza kupokea mapato yake ya kwanza kutokana na raslimali ya gesi asilia katika miaka sita ijayo, kuanzia Mwaka 2020.
Rais Kikwete ameyasema hayo jana, Jumatatu, Agosti 4, 2014, wakati alipozungumza kwenye Kituo cha Kimataifa cha Maendeleo (Centre for Global Development) mjini Washington,D.C., Marekani, ambako alizungumzia Hali ya Baadaye ya Tanzania kufuatia Ugunduzi wa Gesi – Future of Tanzania following the Discoveries of Gas.
Rais Kikwete yuko nchini Marekani kwa ziara rasmi ya siku tisa ambako miongoni mwa mambo mengine atahudhuria Mkutano wa Kwanza wa Viongozi wa Marekani na Afrika ulioitishwa na Rais Barack Obama wa Marekani na unaoanza leo, Jumanne, Agosti 5, 2014.
Rais Kikwete ameuambia mkutano kwenye Kituo hicho kuwa anataka kufanya kila linalowezekana katika kipindi chake kilichobakia cha uongozi kuhakikisha kuwa anaanzisha na kuanza kujenga taasisi na kuweka kanuni sahihi za kuweza kusimamia raslimali ya gesi asilia .
“Nitafanya kila linalowezekana kuhakikisha kuwa Watanzania na nchi yao wananufaika kutokana na mapato ya raslimali kutokana na gesi asilia. Nataka na natamani kuwa Rais wa mwisho wa Tanzania kuongoza nchi masikini. Raslimali ya gesi inatoa nafasi na fursa kubwa kwa nchi yetu kuondokana na umasikini. Mimi nimeongoza nchi masikini, lakini nataka mrithi wangu kuongoza nchi yenye ustawi na utajiri,” amesema Rais Kikwete na kuongeza:
“Hivyo, dhamira na shughuli yangu kubwa kati ya sasa na mwisho wa kipindi changu cha uongozi ni kuiongoza nchi yetu kuelekea kwenye njia hiyo ambako gesi italeta ustawi na utajiri na maisha bora zaidi kwa wananchi wetu.”
Hata hivyo, Rais Kikwete amesema kuwa ili Watanzania wanufaike na mapato ya gesi ni muhimu kuwepo na uongozi imara ambao utakuwa tayari kuchukua maamuzi sahihi kwa kadri nchi inavyosonga mbele. “Jambo la kutia moyo ni kwamba Tanzania ni demokrasia, na ushiriki wa umma kutaja kujua nini kinaendelea uko juu sana.”
Tanzania imekuwa inatafuta gesi na mafuta tokea miaka ya 1950 na ugunduzi wa kwanza ulikuwa Mwaka 1974 katika Kisiwa cha Songo Songo kilichoko Mkoa wa Lindi na Mnazi Bay katika Mkoa wa Mtwara mwaka 1982.
Hata hivyo, ilikuwa kuanzia Mwaka 2010 wakati ugunduzi mkubwa wa gesi ulipofanyika kwenye eneo la bahari, ugunduzi ambao mpaka sasa umefikia futi za ujazo trilioni 50.5.
Mwisho!
Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
05 Agosti, 2014
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Maono hasi yanaipotosha sekta binafsi ya Marekani kuhusu Afrika – Rais Kikwete
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ameitaka sekta binafsi na wafanyabiashara wa Marekani kujifunza kutoka kwa wenzao wa Bara la Asia, ambao wameongeza uwekezaji wao katika Afrika kwa sababu wanapata habari sahihi na za kweli kuhusu Afrika kutoka kwa vyombo vyao vya habari.
Aidha, Rais Kikwete amesema kuwa pingamizi kubwa la kufanya biashara kati ya Marekani na Afrika siyo tena Bahari ya Atlantic ama umbali bali ni maono hasi yanayojengwa na vyombo vya habari vya Marekani kuhusu Bara la Afrika.
Rais Kikwete ameyasema hayo jana, Jumatatu, Agosti 4, 2014 wakati wa sherehe ya kuwekwa kwa Rais Kikwete katika Jumba la Mashujaa wa Uongozi wa Afrika la Jarida la African Leadership – African Leadership Hall of Fame – kwenye Jengo la National Press Club mjini Washington, D.C., Marekani ambako Rais anafanya ziara ya siku tisa.
Sherehe hiyo ya kumwingiza Rais Kikwete kwenye Africa Leaderrship Hall of Fame imefanyika wakati wa Chakula cha Mchana cha 5th African Business Leadership Award Luncheon kwenye Jumba hilo la National Press Club.
Rais Kikwete anakuwa kiongozi wa tatu wa Afrika kutunukiwa heshima hiyo kubwa. Marais waliotangulia kupewa heshima hiyo ni Rais wa Sierra Leone na Rais wa Namibia.
Akizungumza kabla ya kukabidhiwa medali na cheti cha kutunukiwa heshima hiyo, Rais Kikwete amesema kuwa ni jambo la kusikitisha kuwa vyombo vya habari havijali sana maendeleo mazuri ya Bara la Afrika. “Matokeo yake ni kwamba sekta binafsi ya Marekani imefanywa kuamini kuwa Bara la Afrika ni bara hatari sana kuwekeza.”
Ameongeza Rais Kikwete: “Mara nyingi, Afrika inaonekana kama nchi moja badala ya Bara moja, na hivyo tatizo katika nchi moja kwa urahisi sana linafanywa tatizo la nchi zote na kwa namna hasi. Hii ni tofauti na Bara la Asia, ambako vyombo vya habari huelezea picha nzuri za matukio ya Afrika. Hii ndiyo maana kuna ongezeko la uwekezaji wa sekta binafsi ya Asia katika Afrika leo kuliko ilivyokuwa miaka 10 iliyopita.”
Rais Kikwete ameongeza: “Hivyo, pingamizi kubwa ya kufanya biashara kati ya Afrika na Marekani siyo Bahari ya Atlantic wala umbali kati ya maeneo hayo. Pingamizi ni maono hasi. Tunayo kila sababu ya kumshukuru Rais Obama kwa uongozi wake na dhamira yake kubadilisha gurudumu hili la historia.”
Ameongeza: “Uamuzi wake kuitisha Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika na kuiwekea Sekta Binafsi ya Marekani ushiriki muhimu katika Mkutano huo ni uamuzi wa kimapinduzi. Afrika imekuwa inasubiri fursa hii ya kufanya biashara na Marekani kwa muda mrefu. Na tumedhamiria kutumia fursa hii kwa kadri inavyowezekana.”
Rais Kikwete amelishukuru Jarida la The African Leadership kwa mchango wake mkubwa wa kujenga uhusiano kati ya Afrika na Marekani.
Aidha, Rais Kikwete amelishukuru Jarida hilo kwa kumtunuku tuzo ya Kiongozi Bora wa Kusukuma Maendeleo Mwaka 2013 – The Most Impactful African Leader of the Year Award 2013, tuzo ambayo Rais Kikwete alipewa Aprili 9, 2014. Tuzo hiyo ilipokelewa kwa niaba ya Rais Kikwete na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mheshimiwa Bernard Membe.
Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
05 Agosti, 2014
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Sina muda kujadili upuuzi huu kuhusu Ridhiwani – Rais Jakaya Kikwete
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa ni mkusanyiko wa upuuzi mtupu madai kuwa yeye Rais alishiriki kumwokoa mtoto wake, ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Chalinze Mheshimiwa Ridhiwani Kikwete ambaye alikuwa amekamatwa na madawa ya kulevya nje ya nchi.
Aidha, Rais Kikwete amesema kuwa Urais ni taasisi kubwa sana nchini na hivyo yeye akiwa Rais hawezi kujiingiza katika ubishani na watu wa mtaani, kama ambavyo wanataka baadhi ya watu wanamsukuma ili ashiriki katika maneno hayo ya mitaani.
“This is nonsense – ni mkusanyiko wa upuuzi. Sina muda wala siwezi kupoteza nguvu yangu kujadili upuuzi na ujinga wa namna hiyo,” amesema Rais Kikwete usiku wa Jumamosi, Agosti 2, 2014, wakati alipozungumza na Watanzania wanaoishi katika Marekani kwenye Hoteli ya Marriot Washington, mjini Washington D.C.
Rais Kikwete ambaye yuko katika ziara ya kikazi ya siku tisa katika Marekani alitoa majibu hayo baada ya kuwa ameulizwa kuhusu madai yaliyotolewa Julai Mosi, mwaka juzi, 2012 na Katibu Mkuu wa Chama cha CHADEMA, Wilbroad Slaa, madai hayo yamempeleka mahakamani.
Amesema Rais Kikwete: “Hatuwezi sisi kujiingiza katika shughuli ya kupoteza muda kwa kushiriki upuuzi na ujinga. Haya ni maneno ya kipuuzi yanayosemwa na watu ambao kazi yao usiku na mchana ni kuota jinsi ya kuyumbisha ajenda yetu ambayo imefanikiwa sana katika kubadilisha hali ya maisha ya Watanzania.’
Amesisitiza Rais Kikwete: “Urais ni taasisi kubwa sana. Rais wa nchi yetu hawezi kujiingiza katika ubishani na watu wa mitaani. Kwanza huyo Ridhiwani amemfikisha Slaa kortini na mpaka leo hata kesi yenyewe haijatajwa.”
Kuhusu swali jingine aliloulizwa kuhusu suala hilo, kuwa Rais Kikwete alitia saini mikataba 12 na uongozi wa Jamhuri ya Watu wa China kama sehemu ya masharti ya kuachiwa kwa Ridhiwani, Rais Kikwete amesema:
“Naipenda nchi yangu kiasi cha kwamba siwezi kufikiria hata kuiweka rehani. Haya ni maneno ya kipuuzi tu, yenye kutafuta kututoa kwenye ajenda zetu nzuri. Hatuna muda nayo, sisi tunaelekeza nguvu zetu kwenye mambo ya maana ya kuleta mabadikio katika ustawi wa Watanzania.”
Mwisho!
Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
04 Ag2014
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
JK: Mchakato wa Katiba ni sawa na barabara yenye kona
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ameueleza mchakato wa kutafuta Katiba mpya nchini na changamoto zake kama barabara ndefu yenye kona.
Aidha, Rais Kikwete amesema kuwa mchakato huo, kimsingi, unatakiwa kuongozwa na ukweli kuwa Katiba ni kuhusu wananchi wenyewe na maisha yao na wala siyo tu mchakato huo kuongozwa na idadi ya Serikali – mbili ama tatu.
Rais pia amesema kuwa ni dhahiri kuwa yapo mengi ambayo hayajakaa sawasawa katika mchakato mzima hasa kuhusu jinsi Katiba mpya itakavyolinda maisha ya wananchi na kusaidia kuboresha ustawi wao.
Rais Kikwete ameyasema hayo usiku wa Jumamosi, Agosti 2, 2014, kwenye Hoteli ya Marriot Washington, mjini Washington wakati alipokutana, akazungumza na kujadili na Watanzania wanaoishi katika Marekani hasa kutoka maeneo ya jiji la Washington D.C., na majimbo ya Virginia, Maryland, California na New York.
Akiwaeleza Watanzania kuhusu hali ilivyo nchini – kisiasa na kichumi – Rais Kikwete amesema kuwa ni kweli kuwa mchakato wa kutafuta Katiba mpya umekuwa unakabiliwa na changamoto kadhaa katika siku za karibuni.
Rais Kikwete amewaambia Watanzania hao: “Najua kuwa mchakato wa Katiba umekuwa na changamoto katika siku za karibuni lakini kwangu mimi mchakato huo ni sawa na barabara ndefu ambayo haikosi kona. Kona zitakuwepo lakini mimi ni mtu ambaye anaishi kwa matumaini na ni matumaini yangu kuwa mchakato huo utaendelea na hatimaye kufikia mwisho vizuri kama tunavyotarajia wote.”
Rais Kikwete ameongeza: “Aidha, naamini kuwa yapo mengi kuhusu Katiba ambayo hayajapata muda wa kutosha wa kuyajadili katika Bunge la Katiba. Kimsingi, Katiba ni Katiba ya wananchi, ni Katiba kuhusu maisha yao na ustawi wao. Hili jambo sijaona kama linaonekana sana katika mjadala wa Katiba.”
Ameongeza: “Mchakato wetu kwa muda mrefu umekuwa kuhusu idadi ya Serikali, ziwe mbili ama ziwe tatu. Kwangu mimi, idadi ya Serikali ni muhimu, lakini naamini kuwa Katiba iwe ni kuhusu maisha yenyewe ya wananchi na ustawi wao lakini mwelekeo mzima wa Mchakato huo usiwe kuhusu idadi ya Serikali tu.”
Rais Kikwete amesema kuwa anajua kuwa yamekuwepo maneno mengi kuhusu Katiba lakini akaongeza kuwa anaamini majawabu ya changamoto na matatizo ya sasa ya mchakato huo yatapatikana.
“Najua kuwa maneno yamekuwa mengi lakini siyo ndiyo demokrasia ya wazi inavyofanya kazi lakini sisi katika Serikali hatuna wasiwasi na hali hiyo. Ndiyo mambo yanavyotakiwa kuwa katika nchi ambako demokrasia inafanya kazi. Yale mambo yanayotusumbua kwa sasa yanazungumzwa na vyama vyetu na naamini majawabu yatapatikana.”
Wakati huo huo, Rais Kikwete amerudia kusema kuwa Serikali inaandaa utaratibu wa kisheria ambao utalinda mapato yatakayotokana na mauzo ya rasilimali ya gesi nchini kwa kizazi cha sasa cha Watanzania na vizazi vijavyo.
“Tutahakikisha kuwa tunaanzisha Mfuko Maalum kulinda fedha zitakazotokana na mauzo ya gesi. Raslimali hii pamoja na fedha ambazo zinatokana na rasilimali hiyo siyo mali ya kizazi chetu tu bali ni mali ya vizazi vijavyo vya Watanzania”.
Mwisho!
Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
04 Agosti,2014
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amewataka Watanzania waishio nje ya nchi na wanaotaka kuona Tanzania inakubali kuanzisha mfumo wa uraia pacha kutumia muda wao kujenga hoja za jambo hilo badala ya kupoteza muda kwenye mijadala ya blogu na kulaumi watu wengine.
Rais Kikwete amewataka Watanzania hao kusema ili wasikike kwa sababu, kimsingi, hoja ya uraia pacha haina nguvu miongoni mwa Watanzania wanaoishi Tanzania bali hoja hii inatokana zaidi na msukumo wa Watanzania wanaoishi nje ambao kwa bahati mbaya hawafanyi jitihada za kutosha kutetea hoja yao.
Rais Kikwete ameyasema hayo usiku wa Jumamosi, Agosti 2, 2014, wakati alipokutana, akazungumza na kujibu maswali ya Watanzania wanaoishi Marekani, hasa katika maeneo ya jiji la Washington D.C., na majimbo ya Virginia, Maryland, New York na hata California katika mkutano uliofanyika katika Hoteli ya Marriot Washington, mjini Washington D.C..
Rais Kikwete yuko katika ziara ya siku tisa katika Marekani ambako miongoni mwa mambo mengine atahudhuria Mkutano wa Kwanza wa Marekani na Afrika ambao shughuli zake zinaanza leo Jumatatu. Mkutano huo, umeitishwa na Rais Barack Obama wa Marekani na unahudhuriwa na viongozi wa nchi 47 kutoka Afrika.
Rais Kikwete amewaambia Watanzania hao kuacha kupoteza muda kujadili mambo yasiyokuwa na maana na badala yake kuelekeza nguvu zao katika kujenga hoja yenye nguvu zaidi ya uraia pacha, jambo ambalo ni moja ya mambo yatakayojadiliwa katika mchakato wa Katiba mpya.
“Mnashinda kwenye blogu mkijadili mambo ambayo wenzenu nyumbani wana uwezo mkubwa zaidi kuyajadili kuliko nyie. Mnajiingiza katika mambo ambayo sisi nyumbani tuna uwezo mkubwa nayo kuliko nyie. Kwa mambo haya, sisi tunatosha zaidi. Mnaacha kujadili mambo yanayohusu maisha yenu – kama hili la uraia pacha na mnajiingiza katika mambo yasiyowahusu,” amesema Rais Kikwete na kuongeza:
“Kwa sasa upo huu mjadala wa uraia pacha ni hoja yenu. Nyie badala ya kushiriki katika mjadala huu kwa njia zote, mnashinda kujadili mambo ambayo hayana maana. Kwanza hoja ya uraia pacha siyo hoja ya watu wengi nyumbani, siyo jambo linalowahusu. Hata rasimu sina uhakika kama mmeisoma vizuri na kujua nini kimependekezwa – lakini hata huo muda hamna. Kazi yenu mnashinda mnajadili mambo yasiyokuwa na maana – nani kavaa nguo fupi, nani kafanya nini, haya ndiyo mambo yanayochukua muda wetu.”
Rais Kikwete amesisitiza: “Ushauri wangu ni kwamba tumieni muda wetu kusaidia kusukuma hoja yenu hii muhimu – ambayo kama mnavyojua imeingizwa katika rasimu kwa mapendekezo ya CCM kwa sababu suala hilo halikuwemo katika rasimu ya kwanza.”
Mwisho!
Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
04 Agosti, 2014
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais Kikwete awasili Marekani kwa Mkutano wa Barack Obama
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amewasili katika mji mkuu wa Marekani wa Washington D.C., kwa ziara ya siku tisa katika Marekani, ambako miongoni mwa mambo mengine, atahudhuria Mkutano wa Kwanza wa Kihistoria wa Viongozi wa Bara la Afrika na Marekani (USA-Africa Leader’s Summit) ulioitishwa na Rais Barack Obama.
Mkutano huo wa siku mbili utafanyika Agosti 5-6 ukianza na Mkutano wa Biashara kati ya Afrika na Marekani (US-Africa Business Forum) Agosti 5, utakaofanyika kwenye Hoteli ya Mandrin Oriental na kufuatiwa na Mkutano wenyewe wa US-Africa Leader’s Summit utaofanyika kwenye Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani (State Department) siku inayofuata.
Kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Dulles mjini Washington, Rais Kikwete amepokelewa na Balozi wa Tanzania katika Marekani, Mheshimiwa Liberata Mulamula na maofisa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani.
Kwenye ziara hiyo, Rais Kikwete ameandamana na Mama Salma Kikwete ambaye naye atakuwa na program tofauti wakati wa ziara hiyo, kama watakavyokuwa wake wa viongozi wengine wa Afrika wanaohudhuria Mkutano huo.
Mkutano huo wa kwanza wa aina yake kati ya Kiongozi wa Marekani na Viongozi wa Afrika umepangwa kuhudhuriwa na viongozi kutoka nchi 47 ambazo zote zimealikwa na Rais Obama kushiriki Mkutano huo.
Mbali na shughuli zake nyingi za mjini Washington, Rais Kikwete atasafiri kwenda Dallas, Jimbo la Texas, ambako atakutana na Rais wa 43 wa Marekani, Mheshimiwa George W. Bush, kabla ya kuendelea na safari katika mji mwingine mkubwa wa jimbo hilo wa Houston.
Mjini Houston, Rais Kikwete atafanya mkutano wa kimkakati wa kibiashara na wafanya biashara maarufu mbali mbali hasa wa sekta ya gesi na mafuta kabla ya kumaliza ziara yake.
Miongoni mwa shughuli zake, Mama Salma Kikwete atahudhuria Mkutano wa Wake wa Marais wa Afrika na Mke wa Rais wa Marekani, Michelle Obama utakaofanyika kwenye Kituo cha John F. Kennedy. Mkutano huo utahudhuriwa pia na Mke wa Rais George W. Bush, Mama Laura Bush.
Rais Kikwete pia atahudhuria Mkutano wa Wake za Marais wa Nchi Wanachama wa Jumuia ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) na pia atakutana na akinamama wa Tanzania wanaoishi mjini Washington D.C., na majimbo jirani ya Maryland na Virginia.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
2 Agosti, 2014
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Tuna sifa pekee za uwekezaji Barani Afrika,
Rais Kikwete awaambia Wamarekani
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ameyataka makampuni na wafanyabiashara wa Marekani kuongeza uwekezaji wao katika Tanzania, akisema kuwa Tanzania inao uwezo wa kupokea zaidi ya mara 10 uwekezaji wa sasa wa makampuni ya Marekani katika Tanzania wa dola za Marekani bilioni 4.5.
Aidha, Rais Kikwete amesema kuwa Tanzania ina uwezo mkubwa zaidi wa kufanya biashara kubwa zaidi na Marekani kuliko biashara ya sasa kati ya nchi hizo mbili yenye thamani ya dola za Marekani milioni 328.8.
Rais Kikwete ameyasema hayo katika taarifa yake maalum anayoitoa mwishoni mwa wiki hii akikaribisha Mkutano wa Kwanza na wa Kihistoria wa Viongozi wa Marekani na Afrika (USA-Africa Leaders Summit) ulioitishwa na Rais Barack Obama wa Marekani na unaofanyika kwa siku tatu kuanzia Jumatatu, Agosti 4, 2014 mjini Washington D.C. Nchi 47 za Afrika zimealikwa kushiriki Mkutano huo.
Katika taarifa yake hiyo kwa vyombo vya habari, ambayo pia imetolewa sambamba na Taarifa Rasmi ya Tanzania (Tanzania National Statement) kuhusu mkutano huo, Rais Kikwete amesema:
“Wakati huu wa Mkutano wa Viongozi wa Marekani na Afrika naungana na viongozi wenzangu wa Afrika kumpongeza, kwa namna ya pekee, Mheshimiwa Barack Obama, Rais wa Marekani , kwa kubuni wazo na kuandaa Mkutano huu wa kihistoria wa wakuu wa nchi.”
Ameongeza Rais Kikwete katika kuukaribisha Mkutano huo, “Mkutano huu wa wakuu wa nchi ni ushahidi wa wazi kuthibitisha dhamira ya Rais Obama katika kukuza uhusiano kati ya Afrika na Marekani na pia kuchangia kuongeza kasi ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii ya Afrika, kwa kufuta umasikini katika Bara letu.”
Rais Kikwete ameongeza na kusisitiza: “Aidha, mkutano huu unatoa nafasi nzuri sana kwa Bara la Afrika kuelezea hadithi yake kuhusu maendeleo ambayo Bara letu linayapata na kupitia katika maeneo ya kijamii, kiuchumi na kisiasa na kiusalama. Pia Mkutano huo unatoa nafasi nadra sana kwa Bara la Afrika kuwajulisha kwa undani kabisa wafanyabiashara wa Marekani kuhusu fursa za kibiashara na uwekezaji kwenye nchi zetu.”
Akifafanua kuhusu hali ya uwekezaji na uhusiano wa kibiashara kati ya Tanzania na Marekani, Rais Kikwete amesema kuwa Tanzania iko tayari kufanya biashara na Marekani.
“Kwa hakika, tayari, kuna wawekezaji kadhaa pamoja na wafanyabiashara ambao wanaendesha shughuli zao katika Tanzania. Hata hivyo, tunaamini kuwa uhusiano huu wa uwekezaji na biashara unaweza kuwa mkubwa zaidi kuliko ilivyo sasa.”
Rais Kikwete pia ameyataja maeneo ambako makampuni ya Marekani yanaweza kuwekeza, tena kwa haraka, yakiwemo ya utafutaji wa gesi na mafuta, uchimbaji wa madini, kilimo na viwanda vya kilimo, uzalishaji wa viwandani, teknolojia ya habari na mawasiliano na uzalishaji na usambazaji wa umeme.
Maeneo mengine ambayo Rais Kikwete ameyataja kuwa tayari kwa uwekezaji wa makampuni ya Marekani ni pamoja na ujenzi na uendeshaji wa bandari, ujenzi wa mtandao wa reli na hasa Reli ya Kati na utalii.
Mbali na fursa hizo za uwekezaji, Rais Kikwete amesema kuwa Tanzania inazo sifa za ziada kwa ajili ya wawekezaji ikiwa ni pamoja na hali ya amani na utulivu, mazingira rafiki ya kufanyia biashara, jiografia ya Tanzania yenyewe, soko kubwa na linalofikika bila vikwazo kupitia Jumuia ya Afrika Mashariki na Jumuia ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) ambazo kwa pamoja zina soko ya watu kiasi cha milioni 400 na nguvukazi yenye ujuzi.
Rais Kikwete amemalizia taarifa yake kwa kusema: “Mwisho, napenda kusema kuwa Tanzania inayo furaha kubwa sana kuhusishwa na Mkutano huu wa Kihistoria wa Wakuu wa Nchi. Tunayo matarajio makubwa kuhusu matokeo ya Mkutano wa Kwanza wa Wakuu wa Nchi wa Marekani na Afrika.”
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
3 Agosti, 2014
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia salamu za rambirambi Mkuu wa Mkoa
wa Dodoma Dkt. Rehema Nchimbi kufuatia ajali iliyotokea tarehe 30 Julai, 2014 katika
eneo la Pandambili, Wilayani Kongwa na kuua watu wapatao 18.
Katika ajali hiyo, watu 13 walifariki katika eneo la ajali, na majeruhi wapatao 56
walifikishwa hospitalini. Kati ya majeruhi hao hadi sasa waliolazwa ni 30 na wengine
wameruhusiwa baada ya kupata matibabu.
Rais amemuomba Dkt. Nchimbi kumfikishia rambirambi zake za dhati kwa ndugu
na jamaa waliopoteza wapendwa wao katika ajali hiyo, na kuwapa pole majeruhi wote
na kuwatakia kupona haraka ili warejee kwenye shughuli zao za kila siku.
“ Natoa Pole za dhati kwa wale wote walioondokewa na wapendwa wao katika
ajali hii na pia kuchukua nafasi hii kuwapa pole majeruhi wote na kuwaombea kupona
haraka na kurudi katika shughuli zao za kila siku”. Rais amesema katika salamu zake
kwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma.
“Hakika ni jambo la kusikitisha sana kuondokewa na wananchi wetu katika ajali ,
natoa wito wangu kwa madereva wote na wote wanaotumia vyombo vya moto kuwa
makini wanapokuwa barabarani “. Rais amesema na kuongeza kuwa;
“Kila dereva anaetumia chombo cha moto, ana wajibu wa kulinda maisha yake
na ya watumiaji wengine kwa kuwa makini na muangalifu awapo barabarani, kwani
ajali hizi zinarudisha nyuma maendeleo ya taifa na ya wananchi kwa ujumla” Rais
amesema na kuvitaka vyombo vya ulinzi na usalama barabarani kutolegeza kamba
katika kuwachukulia hatua madereva wasio makini na wazembe wakati wote”.Rais
amesisitiza.
Taarifa kutoka Mkoani Dodoma zinasema ajali hiyo ya jana (30 Julai, 2014)
ilisababishwa na Lori ambalo lilitaka kupita lori jingine na hivyo kwenda kugongana uso
kwa uso na Basi la Moro Best lililokuwa likitokea Mpwapwa kuelekea Dar es Salaam.
......Mwisho......
Imetolewa na;
Premi Kibanga,
Mwandishi wa Habari wa Rais Msaidizi,
Ikulu – Dar es Salaam.
30 Julai, 2014
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais Kikwete atunukiwa Tuzo jingine la kimataifa
- Zamu hii ni la kuwa Nyota wa Demokrasia Afrika
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete kwa mara nyingine ametunukiwa tuzo la kimataifa – zamu hii kwa kuwa mshindi waTuzo la Nyota wa Demokrasia Afrika 2014 – Icon of Democracy Award Winner for 2014 in Africa.
Kwa mujibu wa barua aliyoandikiwa Rais Kikwete na kupokelewa Ikulu, Dar Es Salaam, Rais Kikwete amekuwa mshindi wa kwanza, na kwa mbali kabisa, katika mchuano na marais watatu wa Afrika ambao walifikia mwisho mwa mchuano wa kuwania tuzo hilo.
Katika barua hiyo, Mchapishaji na Mhariri Mkuu wa Jarida hilo, Pastor Elvis Iruh, akizungumza kwa niaba ya Kamati ya Tuzo 2014, amesema kuwa uongozi wa Rais Kikwete umekuwa ni hadithi ya kusifiwa ya mafanikio katika Bara ambako hadithi za namna hiyo siyo nyingi.
Tuzo hilo hutolewa na Jarida la The Voice na mwaka jana mshindi alikuwa ni Rais Bai Koroma wa Sierra Leone ambaye alikuwa ni mshindi wa pili wa Tuzo hiyo ambalo ilitolewa kwa mara ya kwanza kwa Rais wa Kwanza wa Zambia, Mzee Kenneth Kaunda.
Sherehe maalum ya kukabidhi tuzo hiyo imepangwa kufanyika Oktoba 17, mwaka huu, 2014, katika Hoteli ya Van der Valk, iliyoko Almere, Uholanzi.
Miongoni mwa sifa nyingine, Rais Kikwete anatunukiwa Tuzo hiyo kwa sababu ya kuwa msimamizi mzuri na wa kweli wa demokrasia, kuendelea kuhakikisha kuwa amani, utulivu na maendeleo vinaendelea kupatikana katika eneo la Afrika ambalo limepitia vipindi vingi vya migogoro na matatizo.
Aidha, gazeti hilo linasema kuwa Rais Kikwete amekuwa kiongozi wa mfano, kimataifa na kikanda, na linatoa mfano wa mchango wake katika kusuluhisha mgogoro mkubwa wa kisiasa nchini Kenya kufuatia uchaguzi mkuu wa 2007.
Rais Kikwete pia anasifiwa kwa mchango wake katika kusimamia maendeleo ya Tanzania katika nyanja mbali mbali – kilimo, elimu, miundombinu, maendeleo ya viwanda, utalii na pia mchango wake katika kuendeleza vijana na kutoa nafasi nyingi kwa akinamama kushika nafasi nyingi za uongozi.
Jarida la The Voice pia limempongeza Rais Kikwete kwa kuimarisha Umoja na Muungano wa Tanzania na kutoa nafasi kwa wananchi kujadili na kukubaliana kuhusu Katiba mpya ya Tanzania.
Aprili mwaka huu, Rais Kikwete alitunukiwa tuzo la kuwa kiongozi mwenye mchango mkubwa zaidi katika maendeleo ya Afrika kwa mwaka 2013 – The Most Impactful Leader in Africa 2013.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
30 Julai,2014
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete leo, Jumatatu, Julai 28, 2014, amekutana kwa mazungumzo na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Atomiki na Nishati (IAEA) Mheshimiwa Yakuya Amano.
Katika mazungumzo yao Ikulu, Dar Es Salaam, viongozi hao wawili wamebadilisha mawazo ya jinsi IAEA linavyoweza kuisaidia Tanzania kuongeza uzalishaji wa mbegu mpya ya mpunga ambayo utafiti wake ulifanyika Tanzania Visiwani na kuendeshwa na Shirika hilo.
Aidha, Rais Kikwete na mgeni wake wamezungumzia jinsi Shirika hilo linavyoweza kusaidia Tanzania kupata utaalam wa kutunza matunda na mboga kwa muda mrefu zaidi bila kuharibika ama kuoza kwa kutumia utalaamu wa mionzi.
Mheshimiwa Amano, raia wa Japan ambaye amekuwa Mkurugenzi Mkuu wa IAEA tokea Desemba mosi mwaka 2009, amemwambia Rais Kikwete kuwa baada ya kutembelea Tanzania huko nyuma ameipenda nchi kiasi cha kuamua zamu hii kuja kutembelea kwa mapumziko.
Mheshimiwa Amano ni Mkurugenzi Mkuu wa tano tokea kuanzishwa kwa Shirika hilo lenye makao yake makuu mjini Vienna, Austria, mwaka 1957.
Rais Kikwete kwa upande wake amemshukuru Mheshimiwa Amano kwa misaada ambayo Shirika lake limekuwa linatoa kwa taasisi za Tanzania ikiwamo Hospitali ya Ocean Road na Shirika la Uthibiti wa Dawa na Chakula (TDFA).
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
28 Julai, 2014
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Kero ya karne ya maji yamalizika Masasi na Nachingwea
Kero ya miaka mingi ya uhaba mkubwa wa maji kwa wakazi wa miji ya
Masasi, Mkoa wa Mtwara na Nachingwea, Mkoa wa Lindi, hatimaye imemalizika
kufuatia kuzinduliwa kwa mradi mkubwa ambao unatoa huduma ya maji kwa
wakazi wa miji hiyo.
Aidha, mradi huo, unaojulikana kama Mradi wa Majisafi wa Masasi –
Nachingwea, utatoa maji pia kwa baadhi ya vijiji vya Wilaya ya Ruangwa, Mkoa
wa Lindi pia, na vijiji vingine ambako mradi huo unapitia.
Mradi huo mkubwa wenye uwezo wa kutoa lita za ujazo za maji milioni
13.6 kwa siku kutoka chanzo cha maji cha chemichemi ya Mbwinji iliyoko Milima
ya Makonde katika Wilaya ya Newala, umezinduliwa rasmi na Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete leo, Alhamisi,
Julai 24, 2014, katika sherehe kubwa zilizofanyika katika miji hiyo miwili ya
Masasi na Nachingwea.
Mradi huo ulioanza kujengwa Februari 2011 na kukamilika Julai mwaka
jana, umejengwa chini ya Program ya Maendeleo ya Sekta ya Maji kwa gharama
kubwa ya kiasi cha sh. bilioni 31 na unaendeshwa na Mamlaka ya Majisafi na
Usafi wa Mazingira Masasi-Nachingwea (MANAWASA).
Gharama za mradi huyo zimetolewa kwa pamoja na Serikakli ya Tanzania
na mfuko wa wafadhili ambao wanahisa sekta ya maji ikiwamo Benki ya Dunia
na wafadhili wengine wengi.
Kwa mujibu wa maelezo ya Mhandisi Nuntufyo David Mwamsojo, mbali
na mradi huo kuwa na uwezo wa kuzalisha lita za ujazo milioni 13.6, mahitaji ya
mji wa Masasi kwa sasa ni mita za ujazo milioni mbili tu na yale ya Nachingwea
ni milioni 1.25 kwa hiyo kuuacha mradi huo kubakia na uwezo mkubwa wa
kuhudumia miji hiyo kwa miaka mingi ijayo.
Alisema kuwa huduma ya maji, kufuatia kukamilika kwa mradi huo,
inawafikia wakazi 83,128 kati ya wakazi 102,696 sawa na asilimia 81 ya wakazi
wote wa mji wa Masasi wakati kwa mji wa Nachingwea mradi unatoa huduma
kwa wakazi 49,471 kati ya wakazi 77, 207 ambayo ni sawa na asilimia 64.
Mpaka sasa wateja 2,101 wameunganishiwa maji kutoka mradi huo katika
mji wa Masasi wakiwemo wateja 1,721 wapya wakati katika mji wa Nachingwea
wateja zaidi ya 900 wameunganishiwa huduma ya maji ya mradi huo mpya
wakiwemo 371 wapya.
Kukamilika kwa mradi huo kunatimiza ahadi ambayo Rais Kikwete aliitoa
wakati wa Kampeni ya uchaguzi Mkuu na hivyo kuwawezesha wakazi wa
maeneo hayo kuboresha maisha yao kwa kuwa na maji safi na salama.
Akizungumza katika sherehe zote mbili za Masasi, wakati wa asubuhi
na Nachingwea, wakati wa mchana, Rais Kikwete ametoa maombi mawili kwa
wakati wa mji huo.
Kwanza, amewataka wakazi wa maeneo hayo kulinda chanzo cha maji
hayo katika Milima ya Makonde katika Wilaya ya Newala, na pili ni kulinda
miundombinu ya kusambaza maji hayo popote ilipo.
“Mimi kama mnavyojua, niliishi Nachingwe kati ya mwaka 1986 na 1988
kabla ya kuhamishiwa Masasi, hivyo mimi siyo mgeni kwa tatizo kubwa la
maji lililokuwa linawakabili wananchi. Nalielewa vizuri. Nimeishi nalo. Hivyo,
ninaposema nafurahi kwamba tumemaliza tatizo hilo, maneno hayo yanatoka
ndani ya dhati ya moyo wangu,” amesema Rais Kikwete.
Rais Kikwete, wakati huo akiwa Meja Kikwete, alikuwa Katibu wa CCM
wa Wilaya ya Nachingwea kabla ya kuhamishiwa Wilaya ya Masasi na hatimaye
kuchaguliwa kuwa Naibu Waziri wa Maji, Nishati na Madini mwaka 1989.
Rais Kikwete ambaye alikuwa katika ziara ya siku sita katika Mkoa wa
Ruvuma na siku moja moja katika mikoa ya Lindi na Mtwara amerejea Dar Es
salaam jioni ya leo.
Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu- Dar es Salaam.
24 Julai,2014
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Gazeti la Mawio la leo,Alhamisi, Julai 17, 2014, limeandika kwenye
ukurasa wake wa kwanza habari yenye kichwa cha habari: “JK, Ukawa wateta”.
Imedaiwa katika habari hiyo kuwa mkutano huo kati ya Rais na ujumbe
wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) ulifanyika Ikulu, Dr es Salaam, wiki
iliyopita usiku, kutokana na ombi la Rais.
Habari hizi siyo za kweli. Rais Kikwete hajapata kukutana na kufanya
majadiliano na ujumbe wa UKAWA kuhusu mchakato wa Katiba Mpya iwe ndani
ama nje ya Ikulu, iwe usiku ama mchana, iwe ndani ama nje ya nchi. Na kwa sababu
hajapata kukutana nao ni dhahiri pia kuwa hajapata kuwaomba wakutane naye.
Hata hivyo, Mheshimiwa Rais anaendelea kuamini kwamba ni muhimu
kwa UKAWA kurejea Bungeni ili kukamilisha kazi ya kuunda Katiba Mpya
inayosubiriwa kwa hamu na Watanzania wote. Aidha, Rais anaunga mkono
jitihada zinazofanywa na watu mbali ili hatimaye UKAWA warudi Bungeni.
Mwisho!
Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
17 Julai,2014
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Saidieni watu kutoka kwenye umasikini, Rais awaagiza viongozi
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya
Mrisho Kikwete amezitaka taasisi za Serikali kuongeza kasi ya kupunguza
umasikini miongoni mwa wananchi, akisisitiza kuwa wananchi wamekaa katika
umasikini kwa muda mrefu mno kupita kiasi.
Rais Kikwete amesema kuwa wanachotarajia wananchi kutoka kwa
taasisi za Serikali ni kusaidiwa kutoka kwenye umasikini kwa kasi kubwa zaidi
kwa sababu wamekaa katika hali ya umasikini kwa muda wa kupita kiasi.
Rais Kikwete ametoa maelekezo hayo leo, Jumapili, Julai 20, 2014,
wakati alipokagua shamba la kisasa la zao la buni kwenye kijiji cha Lipokela,
Wilaya ya Songea, ikiwa ni moja ya shughuli zake katika siku ya nne ya ziara
yake ya siku sita katika Mkoa wa Ruvuma.
Rais Kikwete amesimama kwenye shamba hilo akiwa njiani kutoka
Wilaya ya Mbinga kuelekea Wilaya ya Songea ambako leo amefungua soko
la kimataifa katika kijiji cha Mkenda, kilicho mpakani kabisa mwa Tanzania
na Mozambique. Baadaye, Rais amekagua daraja kwenye Mto wa Ruvuma
ambalo linaunganisha Tanzania na Mozambique.
Rais Kikwete ametoa maelekezo hayo baada ya kuambiwa kuwa
pamoja na kwamba shamba hilo, pengine ni kubwa kuliko jingine lolote la buni
nchini, limefanikiwa kupata miche 3,000,000 ya buni za kisasa ambayo lilihitaji
lakini wakulima wa kawaida wa zao hilo la kahawa wanashindwa kupatiwa
kiasi hicho hicho cha miche ya buni.
“Kwanini tunashindwa kupata miche milioni tatu kwa ajili ya wananchi
ambayo wenyewe mmesema kuwa gharama yake yak uizalisha ni shilingi
milioni 900? Kwanini tunashindwa kupata miche ya kutosha ili wakulima wetu
wapande na kuongeza kipatoc hao?”Rais Kikwete amemwuuliza Profesa
James Teri, Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Utafiti ya Kahawa Tanzania
(TACRI).
Ameongeza Rais Kikwete: “Hatuwezi kuwabakiza wananchi wetu katika
umasikini kwa miaka mingine 30 kwa sababu tu hatuna uwezo wa kuzalisha
miche ya kutosha. Hatuwezi kufanya hivyo, wameishi kiasi cha kutosha katika
umasikini.”
Amesisitiza Rais Kikwete: “Kazi yetu ni kuwatoa watu wengi zaidi katika
umasikini kwa haraka kubwa zaidi kwa sababu wamechelewa mno. TACRI
inaweza kufanya hivyo kwa kuwapa wananchi mbegu bora zaidi ya buni, ili
waondokane na mibuni ya zamani ambayo uzalishaji wake ukochini. Hivyo,
nataka kujua tunaweza kufanya nini kufanikisha hili siyo kuniambia habari
ya changamoto ambazo TACRI inakumbana nazo katika kutimiza majukumu
Ameongeza Rais Kikwete: “Siridhiki na kasi ya kujaribu kuwatoa watu
wetu katika umasikini. Nahitaji kupata miche milioni tatu kwa ajili ya wananchi
wetu. Kama iliwezekana kulipatia shamba hilo miche milioni tatu kwa nini
isiwezekane kwa wananchi?”
Shamba hilo kubwa la mibuni (inayozalisha kahawa) ni mali ya Kampuni
ya AVIV, ambayo ni kampuni tanzu ya Kampuni ya Olam International,
ambayo inaendesha shughuli za biashara katika nchi 65 duniani.
Olam iliingia Tanzania miaka 20 iliyopita na shughuli zake kubwa ni
katika mazao ya korosho na kiwanda cha kuchambua pamba kilicho Bunda,
Duniani, Olam ina mashamba ya mibuni katika nchi tano ambazo ni
Tanzania, Zambia, Ethiopia, Laos na Brazil.
AVIV ambayo inapanda mibuni ya kuzalisha kahawa yaa ina ya Arabica
ilipanda miche ya kwanza miaka mitatu iliyopita na inakaribia kuvuna kwa
mara ya kwanza. Katika kijiji hicho cha Lipokela, AVIV ina ardhi yenye ukubwa
wa hekta 2,000.
Rais Kikwete anaendelea na ziara yake katikaMkoa wa Ruvuma leo kwa
kutembelea na kukagua shughuli za maendeleo katika Wilaya ya Namtumbo.
Mwisho!
Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
20 Julai,2014
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ameitaka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) nchini kuhakikisha kuwa kesi za rushwa dhidi ya watu mbali mbali inazozipeleka mahakama zinakuwa na nafasi kubwa ya kufanikiwa kwa maana ya washitakiwa kukutwa na makosa.
Aidha, Rais Kikwete ameitaka Taasisi hiyo kuwa karibu na umma akisema kuwa TAKUKURU na umma ni sawa na maji na samaki kwa sababu Taasisi hiyo haiwezi kufanikiwa bila ushirikiano na umma.
Rais pia amesema kuwa Serikali yake inakusudia kutunga sheria ya kuwalinda watoa habari kwa TAKUKURU ili kufanikisha zaidi kazi ya Taasisi hiyo.
Rais Kikwete ameyasema hayo leo, Alhamisi, Julai 17, 2014, kwenye siku yake ya kwanza ya ziara rasmi ya siku sita mkoani Ruvuma ambako ameanzia ziara yake katika Songea Mjini.
Katika siku yake ya kwanza leo, Rais Kikwete ambaye anafuatana na Mama Salma Kikwete, amezindua ghala kubwa la kuhifadhia chakula lililojengwa na Wakala wa Taifa wa Kuhifadhji Chakula (NFRA), amezindua nyumba za bei nafuu ambazo zimejengwa katika eneo la Mkuzo na Shirika la Taifa la Nyumba (NHC), amefungua rasmi Ofisi za TAKUKURU za Mkoa wa Ruvuma na pia amehutubia mkutano mkubwa wa hadhara kwenye Uwanja wa Majimaji wa Songea.
Akizindua ofisi hiyo ya TAKUKURU, Rais Kikwete ameipongeza Taasisi hiyo kwa kazi nzuri ambayo imekuwa ikiboreka kila mwaka lakini akasisitiza kuwa wakati umefika kwa TAKUKURU kufiksha mahakamani kesi zile ambazo zina nafasi kubwa ya kutuhumiwa kukutwa na hatia. "ni vyema tuhakikishe kuwa kesi zinazokwenda mahakamani zinakuwa na mpangilio mzuri na nafasi kubwa ya Serikali kushinda kesi hizo."
Ameongeza Rais Kikwete: "Ni vyema pia kuwa pamoja na mafanikio yote ya TAKUKURU ni lazima taasisi hiyo iongeze ushirikiano wake na umma. TAKUKURU na umma ni sawa na samaki na maji kwa sababu kama ilivyo kuwa samaki hawezi kuishi nje ya maji, hivyo hivyo TAKUKURU haiwezi kufanikiwa bila ushirikiano na umma, bila kupata habari kutoka umma."
Ofisi hiyo ya TAKUKURU ya Mkoa wa Songea imegharimu sh. bilioni 1.18 na imejengwa kwa kiasi cha miezi 20 ikiwa ni sehemu ya sera ya Serikali ya kujenga ofisi tatu za mikoa kila mwaka ili kuondoa uhaba wa ofisi za kufanyika kazi za Taasisi hiyo.
Kwenye uzinduzi za nyumba za NHC, Rais Kikwete ameambiwa kuwa katika eneo hilo la Mkuzo, shirika hilo limejenga kiasi cha nyumba 18 za kuuza na zimejengwa kwa gharama ya sh. milioni 676.
Rais Kikwete pia ameambiwa kuwa nyumba hizo zimejengwa katika kutekeleza kaulimbiu ya NHC ya "Nyumba yangu, Maisha yangu" ambayo mpaka sasa inatekelezwa katika mikoa 14. Ujenzi wa nyumba hizo ulianza Januari mwaka jana na unakamilika mwezi ujao, Agosti, 2014.
Nyumba hizo, ameambiwa Rais Kikwete, kuwa zitauzwa kwa gharama ya kati ya sh. milioni 33 na 44 bila kodi ya VAT lakini ambayo inaongezeka na kuwa kati ya milioni 44 na 52 kwa kutegemea ukubwa wa nyumba - kuanzia ya vyumba viwili hadi nyumba vitatu. Rais Kikwete anaendelea na ziara yake mkoani humo.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
17 Julai, 2014
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete Jumatatu Julai 14, 2014 amekutana na kundi la wasanii kutoka Marekani lililowasili nchini usiku wa Alhamisi, Julai 10, 2014, kwa ajili ya kuendesha mafunzo kwa wasanii wa Tanzania kwenye Ukumbi wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT) mjini Dar es Salaam.
Wasanii hao ni pamoja na Terrence J. (Jenkins), mwendeshaji wa kipindi cha muziki kwenye televisheni ya E! Entertainment, mwigizaji wa filamu na mtunzi wa vitabu na Revi Shelton, Mtendaji wa Shughuli za Muziki katika Kampuni ya Outlet Media Group.
Wengine ni Chaka Zulu, Mtendaji wa Shughuli za Muziki kutoka Kampuni ya Disturbing The Peace Records na Davis Banner, mwigizaji, mwanamuziki, mtunzi na msimamizi wa shughuli za muziki ambaye amepata kushinda tuzo maarufu ya Grammy.
Kiasi cha wasanii 250 walishiriki semina hiyo inayoitwa Mafunzo ya Uendelezaji Usanii. Hiyo ilikuwa ni kutimiza ahadi aliyotoa Rais Kikwete kwa wasanii wa Tanzania kuwa atachangia kuinua kiwango cha ujuzi na weledi wao kwa kuwaandalia mafunzo yatayoendeshwa na magwiji wa sanaa kutoka Marekani sasa imetimia.
Akizindua Kampeni ya Uzalendo kwa Vijana inayoendeshwa na Muungano wa Wasanii Tanzania kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma mwezi uliopita, Juni 14, 2014, Rais Kikwete aliahidi kuchangia kuinua kiwango cha usanii na weledi wa wasanii wa Tanzania kwa kusaidia kuandaa mafunzo yatakayoendeshwa na wasanii maarufu kutoka Marekani.
Mbali na kuendesha shughuli za mafunzo ya wasanii ambazo wamekuwa wakizifanya kwa makundi madogo madogo tokea walipowasili nchini, pia wanamuziki hao wa Marekani na kundi la wapiga picha watatembelea sehemu mbali mbali nchini, hasa kwenye vivutio vya watalii, ambako watapiga picha na kuandaa vipindi vya kuitangaza Tanzania katika vyombo vya habari vya Marekani.
Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
15 Julai,2014
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais Jakaya Mrisho Kikwete ameipongeza Ujerumani kwa kutwaa Kombe la Dunia mwaka huu.
Rais Kikwete ametoa pongezi hizo kwa Balozi mpya wa Shirikisho la Jamhuri ya Ujerumani Mheshimiwa Egon Kochanke ambaye amewasilisha Hati zake za Utambulisho leo asubuhi Ikulu .
“Naipongeza Ujerumani kwa kuibuka washindi natumaini tutashirikiana vyema katika masuala ya utamaduni hasa hasa katika kuinua kiwango cha soka nchini Tanzania na kuzisaidia klabu za Tanzania kuanzisha shule maalum kwa ajili ya mpira wa miguu nchini.” Rais amesema na kuishukuru Ujerumani kwa misaada mbalimbali katika sekta za Maji, Utalii, Usafiri wa majini na maeneo mengine ya maendeleo.
Rais pia amepokea Hati za Mabalozi Richard Stuart Man wa New Zealand na Bw. Claude Morel wa Ushelisheli ambao wana makazi yao Pretoria, Afrika ya Kusini na Balozi Sander Kocsis wa Hungary mwenye makazi yake Nairobi , Kenya.
Baadae leo mchana, Rais Kikwete amekabidhi Bendera ya Taifa kwa Timu ya Michezo ya Jumuiya ya Madola, inayotarajiwa kufanyika Glasgow kuanzia tarehe 23 Julai hadi tarehe 3 Agasti mwaka huu.
Hafla ya kuiaga Timu hiyo imefanyika katika Uwanja wa Taifa jijini na kuhudhuriwa na Waziri wa Mambo ya Nje, Mhe. Bernard Membe na Naibu waziri, Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Mhe. Juma Nkamia.
Timu ya Tanzania inatarajiwa kuondoka kesho tarehe 16 Julai,2014 kuelekea Scotland ambapo inatarajiwa kushiriki katika Riadha, Ngumi, Mpira wa Meza, Judo, Kuogelea, Baiskeli na Kunyanyua vitu vizito.
Rais amewaambia washiriki waende wakijua kuwa wana deni la kutunza heshima binafsi kama wachezaji na heshima ya Nchi na Taifa kwa ujumla.
“Siri ya mafanikio ni maandalizi mazuri na tumewekeza sana kwenye mafunzo na maandalizi yenu na hivyo safari hii maandalizi yalikuwa mazuri, hivyo mna deni kubwa” Rais amesema.
………………………………………….Mwisho…………………………………………
Imetolewa na;
Premi Kibanga,
Mwandishi wa Habari wa Rais Msaidizi,
Ikulu - Dar-es-Salaam,
15 Julai, 2014