Viongozi wa Afrika wamuenzi Mwalimu Nyerere
- Jengo muhimu la Makao Makuu ya Umoja wa Afrika lapewa jina lake
- Hoja ya Mzee Mugabe yapokelewa kwa vifijo na nderemo
Umoja wa Nchi Huru za Afrika (AU) umetoa heshima pekee kwa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere na kumuenzi kwa kuamua kuwa moja ya majengo yake muhimu katika makao makuu ya Umoja huo mjini Addis Ababa, Ethiopia, litapewa jina la Mwalimu Julius Nyerere.
Mwalimu Julius Kambarage Nyerere anapewa heshima hiyo kubwa kwa mchango wake katika ukombozi wa Bara la Afrika na kuliondoa Bara la Afrika katika ukoloni.
Uamuzi wa kuliita Jengo la Baraza la Amani na Usalama (Peace and Security Council) la Umoja huo Mwalimu Julius Nyerere Hall ulifikiwa, Jumamosi, Januari 31, 2015, wakati wa kikao cha ndani cha marais wa nchi wanachama wa AU kilichofanyika makao makuu ya AU mjini Addis Ababa.
Akizungumza baadaye kwenye kikao hicho hicho, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete aliwashukuru viongozi wenzake, wakiongozwa na Mzee Mugabe, kwa kutoa heshima hiyo kubwa kwa mwanzilishi wa Taifa la Tanzania na kwa nchi ya Tanzania yenyewe.
Hoja ya kufanya uamuzi wa kuliita jengo hilo Mwalimu Julius Nyerere Hall ilitolewa ufafanuzi wa busara na wa kiwango cha juu kabisa na Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe ambaye ni Mwenyekiti Mpya wa Umoja wa Afrika.
Mzee Mugabe alichaguliwa na viongozi mwenzake kuwa mwenyekiti mpya juzi, Ijumaa, Januari 30, 2015 katika siku ya kwanza ya Mkutano wa 24 wa Kawaida wa AU.
Awali hoja hiyo iliwasilishwa na Rais wa Jamhuri ya Namibia Mheshimiwa Hifekepunye Phohamba katika kikao cha Baraza la Amani na Usalama la AU ambako iliungwa mkono bila kupigwa na yoyote.
Akizungumza kuunga mkono hoja hiyo ambayo mara tu baada ya kuwasilishwa ilipokelewa kwa vifijo na nderemo na wajumbe waliojaa katika Ukumbi wa Nelson Mandela Conference Hall, Rais Mugabe alielezea kwa kina na kwa undani kabisa mchango wa Mwalimu Nyerere katika ukombozi wa Afrika na jinsi yeye na Tanzania walivyobeba jukumu zito na mzigo mkubwa na mzito wa ukombozi wa Afrika.
Alisema Rais Mugabe: “Sote tulikuwepo pale Tanzania, kila mtu akiwa na kambi yake ya kufanyia mafunzo ya kijeshi. Wengine tukagawanyika pale pale, lakini shughuli za ukombozi zikaendelea. Sisi katika Zimbabwe tulikwenda pale chini ya Chama cha ZAPU lakini hatimaye kikazaliwa chama cha ZANU na hivyo tukawa na vyama viwili, Mozambique ilifika na chama kilichoongozwa na mchangiaji mmoja sikumbuki jina lake lakini hatimaye ikazaliwa Frelimo.”
Aliongeza: “Namibia walifika na chama cha SWANO lakini hatimaye kikazaliwa chama cha SWAPO na Afrika Kusini ilikuwa na vyama vya African National Congress (ANC) na Pan African Congress (PAC), Angola ilikuwa na vyama vitatu vya MPLA, UNITA na kile cha Holden Roberto na hata chama cha Guinea Bissau na Cape Verde kilikuwepo pale Tanzania.”
Alisema Rais Mugabe: “Kamati ya Ukombozi Kusini mwa Afrika (Liberation Committee) ilizaliwa na kufanyia kazi zake pale Dar Es Salaam. Sisi tulipewa kila kitu… chakula na mafunzo ya kijeshi. Tulianza bila kujua hata aina zipi za bunduki, lakini tukajifunza aina ya bunduki na mbinu za vita vya msituni na vita vya kawaida.”
Alisisitiza: “ Wakati sisi tunafanya mazoezi, Mwalimu Nyerere alihangaika dunia nzima kuomba fedha za kuendesha shughuli za ukombozi…alipata misaada kutoka China, kutoka Urusi wakati huo na nchi za Ulaya Mashariki, kutoka Algeria, kutoka Misri na hata kutoka hapa Ethiopia.”
Akizungumza katika lugha ya kuvutia ya Kiingereza na mifano mingi ya kuchekesha, Rais Mugabe alisema: “Naweza kuandika kitabu hata hapa hapa kuhusu mchango wa Mwalimu na Tanzania katika ukombozi wa Bara letu, hasa Kusini mwa Afrika. Mwalimu alibuni mbinu moja baada ya nyingine kufanikisha ukombozi na kufikia jinsi gani shughuli kubwa zaidi ya ukombozi wa Afrika Kusini ingeweza kufanikishwa.”
“Nchi gani ingeweza kubeba mzigo mkubwa kiasi hiki? Idadi ya vyama vya ukombozi na vijana wake na vurugu zao za kawaida, idadi ya wakimbizi kutoka nchi mbali mbali na wala siyo nchi tajiri. Kamwe hatutasahu mchango huu mkubwa wa waliyotufanyia… viongozi wale wote Mwalimu Nyerere, Kwame Nkrumah, Seko Toure, Gamal Abdu Nasser, Ben Bella….kamwe tusisahau historia hii ngumu ambayo viongozi wetu hawa waliipitia ili kulikomboa bara letu.”
Uamuzi huo wa Mkutano wa Viongozi wa Nchi Wanachama wa AU, una maana kuwa viongozi watatu maarufu wa Afrika wamepewa heshima katika majengo na eneo la makao makuu ya AU.
Ukumbi mkubwa wa mikutano kwenye makao makuu hayo unaitwa jina la Nelson Mandela Conference Hall, sanamu kubwa la Rais wa kwanza wa Ghana Hayati Kwame Nkrumah imesimamishwa mbele ya makao makuu hayo na sasa Jengo jipya la Baraza la Amani na Usalama la AU linapewa jina la Mwalimu Julius Nyerere Hall.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
1 Februari, 2015