Taarifa kwa vyombo vya Habari ya zamani
Taarifa kwa vyombo vya habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete leo, Jumamosi, Mei 30, 2015 amekutana na kufanya mazungumzo na Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Unilever Duniani, Bwana Paul Poulman mjini Dar es Salaam.
Mazungumzo hayo yamefanyika Uwanja wa Ndege wa Dar es Salaam wakati Rais Kikwete aliporejea Dar es Salaam akitokea Dodoma kikazi na Bwana Poulman akitokea katika ziara ya Mikoa ya Njombe na Iringa, ambako alikuwa anakagua shughuli za Unilever wakati wa ziara yake nchini Tanzania.
Unilever inawekeza katika kilimo cha zao la chai katika Tanzania na hasa katika mikoa ya Njombe na Iringa, ambako inafanya kazi kwa karibu na wakulima wadogo wadogo wapatao 5,000 mbali na kuendesha mashamba yake yenyewe.
Katika mazungumzo hayo, Bwana Poulman amemwambia Rais Kikwete kuwa kampuni yake inalenga kuinua kipato cha wakulima wadogo wadogo 5,000 wa chai kwa kuinua ubora wa zao lao na kupanua eneo ambalo kampuni yake inalilima kwa sasa.
Bwana Poulman amesema kuwa katika jitihada zake za kupanua ukubwa wa mashamba na hivyo kuongeza kiwango cha uzalishaji wa zao la chai nchini, Unilever imepanda miche milioni 34 mipya ambayo kati yao milioni 20 imetolewa kwa wakulima wadogo wadogo.
Katika hatua nyingine za kuongeza uzalishaji wa chai nchini, Bwana Poulman amemwomba Rais Kikwete kusaidia kuboresha barabara za vijijini ambazo zinaelekea katika maeneo yaliko mashamba ya Unilever. Aidha, Bwana Poulman amemwomba Rais Kikwete kusaidia kuiwezesha Unilever kurudishiwa eneo lake la kilimo lililoko Ngwazi ili kampuni hiyo iweze kupanua shughuli zake.
Rais Kikwete amekubali kuwa Serikali yake itachukua hatua kufanikisha mambo hayo mawili na ameishukuru Unilever kwa kuonyesha imani kubwa kwa Tanzania kwa kuwekeza katika uchumi wake.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
30 Mei, 2015
Taarifa kwa vyombo vya habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amepokea kwa masikitiko na huzuni nyingi taarifa ya kifo cha mwanasiasa mkongwe nchini na aliyepigania uhuru wa Tanganyika, Ndugu Samwel Ntambala Ruangisa, ambaye aliaga dunia mwanzoni mwa wiki hii nchini Marekani ambako alikuwa anatibiwa.
Katika salamu za rambirambi ambazo amempelekea Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Mheshimiwa John Mongella kuomboleza kifo cha Mzee Ruangisa, ambaye pia alikuwa bado diwani katika Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba, Rais Kikwete amesema:
“Nimepokea taarifa za kifo cha Mzee Ruangisa kwa masikitiko na huzuni nyingi. Kwa zaidi ya nusu karne, Mzee Ruangisa amekuwa kiongozi wa kuigwa mfano katika nafasi zote ambazo zimepata kuzishikilia katika maisha yake kuanzia Ukuu wa Mkoa wa Ziwa Magharibi (sasa Kagera) na baadaye Mkoa wa Mara tu baada ya Uhuru wa Tanganyika mwaka 1961, Ubalozi, Uwaziri, Ubunge, Umeya na Udiwani. Katika kila nafasi aliyoishikilia, Mzee Ruangisa alionyesha uongozi wa kiwango cha juu. Kwa hakika, tumepoteza kisima cha uzoefu wa uongozi.”
Rais Kikwete ameongeza katika salamu zake za rambirambi: “Mkuu wa Mkoa nakutumia salamu zangu za rambirambi kuomboleza msiba huu na kupitia kwako naomba uwape pole wana-Kagera wote kwa kuondokewa na mzee wao wa siku nyingi. Aidha, naomba unifikishe pole zangu nyingi kwa wanafamilia wote ambao wamepoteza baba, babu na mhimili wa familia. Wajulishe kuwa niko nao katika kipindi hiki kigumu. Waambie naelewa machungu yao kwa sababu machungu yao ni machungu yangu. Vile vile, naungana nao katika kumwomba Mwenyeji Mungu, Mwingi wa Rehema, aiweke peponi roho ya Marehemu Samwel Ntambala Ruangisa. Amina.”
Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
IKULU,
DAR ES SALAAM.
27 Mei, 2015
Taarifa kwa vyombo vya habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete leo, Jumatano, Mei 27, 2015, amemwapisha Katibu Mkuu mpya, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Liberata Rutageruka Mulamula.
Aidha, katika sherehe fupi ya uapisho iliyofanyika Ikulu, Dar es Salaam, Rais Kikwete amemwapisha Balozi Hassan Simba Yahya kuwa Naibu Katibu Mkuu katika Wizara hiyo.
Katika sherehe hiyo iliyohudhuriwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mheshimiwa Bernard Membe, Rais Kikwete amemwapisha pia Ndugu Hemed Idd Mgaza kuwa Balozi mpya wa Tanzania nchini Saudi Arabia.
Kabla ya kuteuliwa kuwa Katibu Mkuu, Balozi Mulamula alikuwa Balozi wa Tanzania Washington, Marekani.
Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
IKULU,
DAR ES SALAAM.
27 Mei, 2015
Taarifa kwa vyombo vya habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ametuma salamu za rambirambi kuomboleza kifo cha aliyekuwa mtangazaji mashuhuri na maarufu wa iliyokuwa Redio Tanzania (sasa TBC Taifa), Ndugu Mshindo Mukeyenge ambaye alifariki dunia mwishoni mwa wiki na kuzikwa jana, Jumatatu, Mei 25, 2015.
Katika salamu alizomtumia Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Mkoa wa Dar Es Salaam, Mheshimiwa Sofia Mjema leo, Jumanne, Mei 26, 2015, Rais Kikwete amesema kuwa kifo cha Mzee Mukeyenge kimelinyang’anya “taifa letu hakina kubwa ya uzoefu wa utangazaji katika kipindi ambapo vijana wanaochipukia katika tasnia ya habari, na hasa utangazaji, walikuwa wanahitaji sana malezi, ushauri na uongozi wake.”
Rais Kikwete amemwelezea Mzee Mukeyenge kama Mtanzania aliyetoa mchango mkubwa katika ujenzi wa taifa letu kupitia kipaji chake cha utangazaji na kuwa mchango wake utaendelea kukumbukwa kwa miaka mingi ijayo.
“Aidha, tutaendelea kumkumbuka Ndugu Mshindo Mukeyenge kwa mchango wake mkubwa katika maendeleo ya michezo hapa nchini, na hasa mchezo wa soka, ambako alichangia kwa kulihabarisha taifa letu kupitia utangazaji wa mechi nyingi za soka za kitaifa ama kimataifa,” amesema Rais Kikwete.
Amemwambia Mkuu huyo wa Wilaya, “Kwa hakika nimepokea kwa huzuni taarifa za kifo cha Ndugu Mshindo Mukeyenge. Napenda kuungana nawe na wana-Temeke wote katika kuomboleza kifo cha mwenzetu. Aidha, napenda kukuomba unifikishie salamu zangu za rambirambi kwa wanafamilia na wote ambao wamepotelewa na mhimili wao. Wajulishe kuwa naungana nao katika machungu yao na katika kumwomba Mwenyezi Mungu aiweke pema peponi roho ya Marehemu Mshindo Mukeyenge. Amina”.
Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
26 Mei, 2015
Taarifa kwa vyombo vya habari
Rais ateua Makatibu Tawala Singida, Shinyanga
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amewateua makatibu tawala wa Mikoa ya Singida na Shinyanga kuanzia jana, Jumatatu, Mei 25, 2015.
Katika uteuzi huo, Rais Kikwete amemteua Ndugu Festo Luganda Kang’ombe kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida na Ndugu Abdul Rashid Dachi kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga.
Kabla ya uteuzi wake, Ndugu Kang’ombe alikuwa Mkurugenzi wa Halmashuri ya Kibaha, Mkoa wa Pwani wakati Ndugu Dachi alikuwa Katibu Tawala Msaidizi, Sekretarieti ya Mkoa wa Lindi.
Ndugu Kang’ombe anachukua nafasi ya Ndugu Liana Hassan ambaye amestaafu utumishi wa umma kwa mujibu wa sheria tokea Machi, mwaka huu, na Ndugu Dachi anachukua nafasi ya Ndugu Anselm Tarimo ambaye naye alistaafu utumishi wa umma kwa mujibu wa sheria Januari 22, mwaka huu, 2015.
Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
26 Mei, 2015
Taarifa kwa vyombo vya habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amemteua Bwana Anthony Peter Mavunde kuwa Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa, Mkoa wa Dodoma, kuanzia leo, Jumatatu, Mei 25, 2015.
Aidha, Rais Kikwete amefanya uhamisho wa wakuu 10 wa Wilaya kwa nia ya kuongeza ufanisi katika uongozi wa Wilaya mbali mbali nchini.
Katika mabadiliko hayo, Rais Kikwete amemhamisha Luteni Edward Ole Lenga kutoka Wilaya ya Mkalama, Mkoa wa Singida kwenda kuwa mkuu wa wilaya mpya ya Kyerwa, Mkoa wa Kagera. Luteni Lenga anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Luteni Kanali Benedict Kulikela Kitenga ambaye alifariki dunia Aprili 20, mwaka huu, 2015.
Wakuu wengine wa wilaya ambao Rais Kikwete amewahamisha ni Elizabeth Chalamila Mkwasa kutoka Wilaya ya Dodoma kwenda Wilaya ya Mvomero, Mkoa wa Morogoro, Dkt. Jasmine Tisike kutoka Wilaya ya Mpwapwa kwenda Wilaya ya Dodoma, Agnes Elias Hokororo kutoka Wilaya ya Namtumbo, Mkoa wa Ruvuma kwenda Wilaya ya Tunduru, mkoani humo humo na Fadhili Nkurlu kutoka Wilaya ya Misenyi, Mkoa wa Kagera kwenda Wilaya ya Mkalama.
Wengine ambao wamehamishwa ni Chande Bakari Nalicho kutoka Wilaya ya Tunduru kwenda Wilaya ya Namtumbo, Festo Shem Kiswaga kutoka Wilaya ya Mvomero kwenda Misenyi, Darry Ibrahim Rwegasira kutoka Wilaya ya Karagwe, Mkoa wa Kagera kwenda Wilaya ya Biharamulo, mkoani humo humo, Elias Choro John Tarimo kutoka Wilaya ya Biharamulo kwenda Chunya, Mkoa wa Mbeya na Deodatus Lukas Kinawiro kutoka Wilaya ya Chunya kwenda Wilaya ya Karagwe, Mkoa wa Kagera.
Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
25 Mei, 2015
Taarifa kwa vyombo vya habari
Tanzania itakuwa mwenyeji wa Mkutano wa Mpango wa Uendeshaji wa Shughuli za Serikali kwa Uwazi (Open Government Partnership - OGP), Kanda ya Afrika unaoanza kesho, Jumatano, Mei 20, 2015 katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere, Dar es Salaam na kufunguliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete.
Wajumbe 200 kutoka Serikalini, Asasi za Kiraia na Washirika wa Maendeleo kutoka ndani na nje ya Nchi wanatarjiwa kushiriki katika Mkutano huo wa siku nne na ambao Kaulimbiu yake ni “Kuimarisha Utawala Bora Unaozingatia Uwajibikaji na Uwazi (Enhancing Accountability Through Open Governance)
Washiriki hao ni pamoja na Mawaziri, kutoka ndani na nje ya nchi, Makatibu Wakuu, Wakuu wa baadhi ya Taasisi za Serikali, Washirika wa Maendeleo, Asasi za Kiraia kutoka ndani na nje ya nchi, wawakilishi kutoka Nchi wanachama wa OGP kutoka Bara la Afrika ambazo ni Kenya, Malawi, Afrika ya Kusini, Ghana, Liberia, Malawi, Siera Leone, Tunisia na wenyeji Tanzania.
Washiriki wengine ni pamoja na wawakilishi kutoka nchi za Botswana, Zambia, Uganda, Nigeria, Cote de Voire, Zimbabwe, Marekani. Washiriki wa Maendeleo ni pamoja na Benki ya Dunia, UNDP, UNICEF, UNESCO, MCC, USAID, DFID na JICA.
Mkutano huu ni wa kwanza wa OGP kufanyika nchini Tanzania lakini ni wa pili kufanyika katika Kanda ya Afrika. Mkutano wa kwanza ulifanyika Mombasa, Kenya mwaka 2013.
Mkutano huo unalenga Kuongeza uelewa zaidi wa Mpango wa Uendeshaji wa Shughuli za Serikali kwa Uwazi kwa kufanya majadiliano katika masuala mbalimbali kama vile uwajibikaji na utawala wa Serikali katika kutoa mrejesho kwa wananchi, uwazi katika masuala ya ardhi iliyopimwa kwa shughuli mbalimbali, uwazi katika masula ya bajeti na ushirikishwaji wa Asasi za Kiraia katika kuleta ufanisi Serikalini.
Aidha, Mkutano huo utatoa uzoefu wa utekelezaji wa OGP kutoka kwa nchi wanachama katika Bara la Afrika na nje ya Afrika kama vile taarifa za uwazi zinavyo imarisha uwajibikaji
Vile vile, Mkutano huo utawawezesha washiriki kupata maoni na mtazamo wa Asasi za Kiraia katika Usimamizi na utekelezaji wa shughuli za Serikali.
Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
19 Mei, 2015
Taarifa kwa vyombo vya habariMasahihisho katika taarifa ya Uteuzi wa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai na Mkurugenzi wa Intelijensia katika Jeshi la Polisi Rais wa Jamhur
Masahihisho katika taarifa ya Uteuzi wa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai na Mkurugenzi wa Intelijensia katika Jeshi la Polisi
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amemteua Kamishna wa Polisi (CP) Diwani Athumani Msuya, kuwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa makosa ya Jinai (Director of Criminal Investigation).
Kabla ya uteuzi huu CP Msuya alikuwa Kaimu Kamishna wa Kamisheni ya Intelijensia ya Jinai. CP Msuya anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Ndugu Isaya J. Mngulu ambaye amestaafu kwa mujibu wa Sheria.
Rais Kikwete pia amemteua Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) Valentino Mlowola kuongoza Idara ya Intelijensia ya Jinai, kujaza nafasi iliyoachwa na Kamishna Msuya.
Kabla ya Uteuzi huu, DCP Mlowola alikuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza. Uteuzi huu umeanza tarehe 3 Mei, 2015
Aidha, tunaomba radhi kwa makosa yaliyojitokeza katika taarifa ya awali tuliyowatumia tarehe 12 Mei, 2015.
Imetolewa na;
Premi Kibanga,
Mwandishi wa Habari wa Rais Msaidizi,
Ikulu – Dar es Salaam.
14 Mei, 2
Taarifa kwa vyombo vya habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amemteua Kamishna wa Polisi (CP) Diwani Athumani Msuya, kuwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa makosa ya Jinai (Director of Criminal Investigation).
Kabla ya uteuzi huu CP Msuya alikuwa Kaimu Kamishna wa kamisheni ya Intelijensia ya Jinai. CP Msuya anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Ndugu Robert S. Manumba ambaye amestaafu kwa mujibu wa Sheria.
Rais Kikwete pia amemteua Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) Valentino Mlowola kuongoza Idara ya Intelijensia ya Jinai, kujaza nafasi inayoachwa na Kamishna Msuya.
Kabla ya Uteuzi huu, DCP Mlowola alikuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza.
Uteuzi huu umeanza tarehe 3 Mei, 2015
…...Mwisho……
Imetolewa na;
Premi Kibanga,
Mwandishi wa Habari wa Rais Msaidizi,
Ikulu – Dar es Salaam.
12 Mei, 2015
Taarifa kwa vyombo vya habari
Rais Kikwete: Wekeni waambata kulinda maslahi ya wanafunzi wa Tanzania nje
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ameielekeza Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kuhakikisha kuwa Balozi mbali mbali za Tanzania nje ya nchi zinakuwa na Waambata wa Elimu kwa nia ya kukabiliana na kutatua matatizo ya wanafunzi wa Tanzania wanaosoma katika nchi mbali mbali duniani.
Aidha, Rais Kikwete amesema kuwa moja ya wajibu mkubwa wa mabalozi wanaoziwakilisha Tanzania nje ya nchi ni kutetea na kulinda maslahi ya Watanzania walioko katika nchi hizo, bila kujadili kama Watanzania hao wamepelekwa nje na Serikali ama wamekwenda huko kwa njia nyingine.
Rais Kikwete amefanunua mambo hayo wakati alipozungumza na viongozi wa wanafunzi wa Tanzania wanaosoma katika vyuo vikuu na vyuo vya elimu ya juu katika Algeria, nchi ambayo Rais Kikwete anaitembelea rasmi kwa siku tatu kuanzia jana, Jumamosi, Mei 9, 2015. Tanzania ina kiasi cha wanafunzi 370 katika Algeria kwa sasa.
Rais Kikwete alizungumza na viongozi hao wanafunzi kwenye siku ya kwanza ya ziara yake rasmi ya Kiserikali katika Algeria usiku wa jana, Jumamosi, Mei 9, 2015.
Akizungumza na viongozi hao wa wanafunzi, Rais Kikwete amesema kuwa Tanzania ina wanafunzi wengi katika nchi mbali mbali duniani, wanafunzi ambao wanahitaji huduma mbali mbali za kibalozi na hivyo ni lazima itafutwe namna ya kurejea katika utaratibu wetu wa zamani wa kuwa na Waambata wa Elimu katika balozi mbali mbali za Tanzania nchi za nje.
“Ni lazima tuwe na Waambata wa Elimu kwa ajili ya kushughulikia matatizo ya vijana ….wanafunzi wetu nje ya nchi. Kila ninapokwenda nakabiliana na matatizo kama haya mnayoniuliza nyie na mengine mengi na ya aina mbali mbali ya wanafunzi,” Rais Kikwete amwaambia wanafunzi hao mbele ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mheshimiwa Bernard Membe.
Kuhusu nafasi ya mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania katika nchi za nje, Rais Kikwete amesema kuwa ni shughuli muhimu ya kila balozi wa Tanzania katika nchi mbali mbali kushughulikia matatizo ya Watanzania.
“Mabalozi wetu kushughulikia matatizo ya Watanzania ni wajibu wao iwe ni wale Watanzania wanaopelekwa nje na Serikali ama wale ambao kwa njia moja ama nyingine wamejikuta nje ya nchi hata kama hawakupelekwa na Serikali. Huu ndio wajibu wa kila balozi wa Tanzania popote alipo,” amesema Rais Kikwete.
Rais Kikwete alianza ziara rasmi ya Kiserikali ya Algeria jana kwa mwaliko wa Rais Abdelaziz Bouteflika.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
10 Mei, 2015
Taarifa kwa vyombo vya habari
Rais Kikwete: Ni asilimia sita ya watoto walikuwa wanaingia sekondari 2005
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa ilikuwa ni lazima kuanzisha Shule za Sekondari za Kata nchini kwa sababu mwaka 2005 ni asilimia sita tu ya wanafunzi waliokuwa wanainga sekondari kutoka shule za msingi nchini.
Aidha, Rais Kikwete amesema kuwa katika miaka 10 iliyopita, yamekuwepo maendelea na mafanikio makubwa katika hali na hadhi ya shule hizo za sekondari za kata kiasi cha kwamba sasa shule hizo zimeanza kushindana na hata wakati mwingine kuzipiku shule binafsi na zile za serikali.
Rais Kikwete ametoa ufafanua huo usiku wa jana, Jumamosi, Mei 9, 2015, wakati alipozungumza na viongozi wa wanafunzi wa Tanzania wanaosoma katika vyuo vikuu na vyuo vya elimu ya juu katika Algeria kwenye siku ya kwanza ya ziara yake rasmi ya Serikali ya siku tatu katika nchi hiyo rafiki mkubwa na wa miaka mingi wa Tanzania.
Akijibu maswali ya wananchi hao , mojawapo likiwa kuhusu hali na hadhi ya sekondari za kata nchini, Rais Kikwete amesema kuwa ilikuwa ni lazima kuanzisha shule hizo kwa sababu nafasi za watoto wa shule kutoka shule za msingi hadi sekondari zilikuwa zinyu sana.
“Mwanzoni hali ilikuwa mbaya sana na hivyo uamuzi ulikuwa ni lazima kubadilisha hali hiyo. Ni asilimia sita tu ya watoto wetu walikuwa wanakwenda sekondari kutoka shule ya msingi katika nchi yenye watu wanaokaribia milioni 50 kwa sasa. Hali hii haikukubalika. Wajibu wetu, kama serikali, ilikuwa kutoa fursa kwa watoto wetu kupata nafasi nyingi zaidi za kuingia sekondari na tumefanikiwa sana katika hili,” alisema Rais Kikwete na kuongeza:
“Na wala siyo siri kuwa mwanzoni shule hizo zilikabiliwa na changamoto nyingi. Hatukuwa na walimu wa kutosha, vitabu vilikuwa havitoshi, Lakini sasa hali imebadilika. Walimu wa masomo ya sanaa sasa wanatosha na baadhi ya shule zina walimu wa ziada. Vitabu vimeanza kutosha.”
Aliongeaza Rais Kikwete: “Mwaka jana, kwa mfano, shule tatu bora za Mkoa wa Kilimanjaro, mkoa ambao umepiga hatua kubwa katika elimu, zilikuwa shule za kata na zote zilikuwa za Wilaya ya Mwanga.”
Rais Kikwete yuko katika Algeria kwa ziara rasmi ya Kiserikali ya siku tatu kwa mwaliko wa Rais Abdelaziz Bouteflika kuanzia jana, Jumamosi, Mei 9, 2015.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
10 Mei, 2015
Taarifa kwa vyombo vya habari
Rais aitisha kikao cha wakuu wa EAC kujadili Burundi
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Mkutano wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, ameitisha mkutano wa wakuu wenzake wa nchi hizo tano wa EAC, Jumatano ijayo, Mei 13, 2015, kujadili hali ilivyo katika Burundi, kwa kadri nchi hiyo inavyojiandaa kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu Juni 26, mwaka huu.
Rais Kikwete ametangaza habari ya kuitisha mkutano huo wakati alipozungumza na waandishi wa habari katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa (UN) kuwalezea matokeo ya mkutano wa wiki moja wa Jopo la Watu Mashuhuri Duniani linaloangalia jinsi dunia inavyoweza kukabiliana na majanga ya kiafya katika siku zijazo kufuatia balaa la ugonjwa wa Ebola katika Afrika Magharibi.
Rais Kikwete na wana-Jopo wenzake wamezungumza na waandishi wa habari leo, mjini New York, baada ya kuwa wamemaliza kikao cha kwanza cha Jopo lao lililoteuliwa na Katibu Mkuu wa UN, Mheshimiwa Ban Ki Moon, Aprili 2, mwaka huu, 2015, kupendekeza jinsi dunia inavyoweza kukabiliana na majangwa ya kiafya, na hasa ya magonjwa ya mlipuko, katika siku zijazo kufuatia balaa na athari za ugonjwa wa Ebola katika Afrika Magharibi.
Ugonjwa wa Ebola umeua watu karibu 10,000 katika kipindi kifupi katika nchi za Guinea, Liberia na Sierra Leone, hata kama ugonjwa huo ulijitokeza kwa mara ya kwanza mwaka 1976, karibu miaka 40 iliyopita katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC). Mpaka sasa ugonjwa huo hauna dawa inayojulikana dhahiri wala chanjo.
Katika maswali yaliyofuatia maelezo yake na ya wanajopo wenzake kuhusu kazi yao ya wiki moja, Rais Kikwete ameulizwa kuhusu hali ilivyo katika Burundi, na Tanzania, kama jirani inachukua hatua gani kukabiliana na hali hiyo katika nchi jirani.
Rais Kikwete amesema kuwa mara baada ya mawaziri wa nchi za nje wa Tanzania, Kenya, Uganda na Rwanda kuwa wametembelea Burundi majuzi, kwa maelekezo yake, na kumaliza ziara yao kwa kujionea hali ilivyo katika nchi hiyo, ameamua kuitisha Mkutano wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa EAC mjini Dar es Salaam Jumatano ijayo, Mei 13, 2015 ambako mawaziri hao watatoa ripoti yao ili ijadiliwe.
“Tumekubaliana kuwa sisi ndani ya EAC – Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi yenyewe tukutane Dar es Salaam, Jumatano ijayo, Mei 13, wiki ijayo, ili tujadiliane jinsi gani ya kuwasaidia ndugu zetu wa Burundi kuandaa uchaguzi wao kwa mafanikio wakihakikisha kuwa nchi yao inabakia na umoja, utulivu, usalama na amani bila misukosuko isiyokuwa na sababu,” Rais Kikwete amewaambia waandishi hao wa habari.
Ameongeza Rais Kikwete: “Baada ya hapo, tutaweza sasa kuwaelezea nyie waandishi wa habari kuhusu msimamo wa EAC na hata msimamo wa Tanzania kuhusu Burundi – tuwe na subira na tunaamini kuwa Burundi itaendelea kuwa ya utulivu na amani.”
Katika siku za karibuni kumekuwepo na hali ya mjadala mkali kuhusu maana halisi hasa ya Katiba ya Burundi, hususani katika kipengele kinachohusu vipindi vya kutumikia Urais. Baadhi wamekuwa wanadai kuwa kwa kutumikia miaka 10, Rais wa sasa, Mheshimiwa Pierre Nkurunziza amekamilisha mahitaji ya Kikatiba na wengine wakisema kuwa bado anayo haki ya kugombea kwa kipindi kimoja zaidi kwa sababu Rais amechaguliwa mara moja tu na wananchi.
Chama chake cha CNDD-FDD kimempitisha kuwa mgombea tena wa nafasi hiyo na wiki hii Mahakama ya Katiba ya nchi hiyo imesema kuwa Rais Nkurunziza anayo haki ya Kikatiba kuwania nafasi hiyo kwa mara nyingine.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
9 Mei, 2015
Taarifa kwa vyombo vya habari
Wawakilishi UN waunga mkono kazi ya Rais Kikwete na wenzake
Jumuiya ya Kimataifa katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa (UN) mjini New York imeelezea msimamo wake thabiti wa kuunga mkono kwa dhati na kwa kila hali kazi na jukumu ya Jopo la Watu Mashuhuri Duniani la Kukabiliana na Majanga Duniani linaloongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete.
Jumuiya hiyo imeeleza msimamo wake wa kuunga mkono Jopo hilo wakati Rais Kikwete na wana-Jopo wenzake walipopata nafasi ya kuwaelezea Wawakilishi wa Kudumu wa nchi mbali mbali duniani katika Umoja wa Mataifa kuhusu kazi iliyofanywa na Jopo hilo katika siku za mwanzo kabisa.
Jopo hilo lililotangazwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Mheshimiwa Ban Ki Moon Aprili 2, mwaka huu, limepewa jukumu ya kupendekeza jinsi gani dunia inavyoweza kukabiliana na majanga ya kiafya duniani, na hasa magonjwa ya milipuko, kama ilivyokuwa Ebola katika nchi za Afrika Magharibi za Guinea, Liberia bna Sierra Leone.
Baada ya wiki moja ya kazi kubwa mjini New York, Rais Kikwete na wajumbe wa Jopo hilo kutoka Brazil, Botswana, Indonesia, Uswisi na Marekani, wamekutana na Wawakilishi wa Kudumu wa mataifa mbali mbali katika UN kuwaelezea nini kimefanyika na nini kinatarajia kufanyika.
Baada ya maelezo ya wajumbe wa Jopo, mwakilishi wa Ubalozi wa Ujerumani katika UN alisema kuwa Ujerumani inaunga mkono moja kwa moja kazi ya Jopo hilo akisisitiza kuwa Kiongozi wa Ujerumani, Kansela Merkel amekubali kutoa kiasi cha dola za Marekani milioni moja kuunga mkono shughuli za Jopo hilo.
Mwakilishi wa Senegal alisema kuwa nchi yake inaunga mkono moja kwa moja kazi ya Jopo hilo lililoteuliwa na Katibu Mkuu wa UN, akisisitiza kuwa Senegal, kama Mwenyekiti wa Kamati ya Oslo ya Afya katika Umoja wa Mataifa itashirikiana na Jopo hilo moja kwa moja.
Mwakilishi wa Ufaransa amesema kuwa nchi yake inaunga mkono kazi ya Jopo moja kwa moja na kuwa ni uamuzi wa busara wa Katibu Mkuu wa UN kuunda Jopo hilo.
Mwakilishi wa Uingereza amepokea kwa mikono miwili uundwaji wa Jopo hilo, akisisitiza kuwa nchi hiyo itaendelea kuunga mkono jitihada za Jopo hilo kama ilivyoiunga mkono Sierra Leone wakati wa kukabiliana na Ebola.
Mwakilishi waLuxembourg amesema kuwa dunia inalitarajia Jopo hilo kuelekeza nguvu yake katika mapendekezo ya uongozi kuliko changamoto za kiufundi. Aidha, ameongeza kuwa nchi hiyo baada ya kushika Uenyekiti wa Umoja wa Ulaya (EU) itaongeza kazi yake katika kuchunguza athari za Ebola na kiini chake.
Mwakilishi wa Marekani amesema kuwa ni muhimu kwa Jopo kuweka msingi wake katika ugonjwa wa Ebola lakini katika magonjwa mengine ya mlipuko ili kuweza kupata uhakika zaidi wa athari za magonjwa hayo.
Naye, mwakilishi wa Uswisi amesema kuwa nchi yake inahitaji mapendekezo ya kisiasa kuliko yale ya kiufundi ama ya kimfumo. “Tunahitaji kazi kubwa ya kisiasa hapa kututoa katika matatizo ya sasa.”
Naye Mwalikishi wa Misri amesema kuwa nchi yake inaheshimu sana uteuzi wa Jopo hilo na kuamini kuwa Rais Kikwete ni kiongozi mwafaka katika kukabiliana na majanga ya kiafya duniani.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
9 Mei, 2015
Taarifa kwa vyombo vya habari
Ebola siyo ya mwisho, Rais Kikwete na Jopo lake waambiwa
Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Mheshimiwa J. Eliasson ameliambia Jopo la Watu Mashuhuri linaloongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete kuwa hakuna shaka duniani kuwa magonjwa ya milipuko, kama vile Ebola, yataendelea kuisumbua dunia katika miaka ijayo na hivyo ni lazima maandalizi yafanyike kukabiliana na hali hiyo.
Aidha, Naibu Katibu Mkuu huyo amelitaka Jopo hilo linaloangalia jinsi gani dunia inavyoweza kujiandaa na kukabiliana ipasavyo na milipuko ya magonjwa kama Ebola katika siku zijazo, kuangalia sababu za msingi za kusambaa kwa kasi sana kwa ugonjwa wa Ebola katika nchi za Afrika Magharibi za Guinea, Liberia na Sierra Leone kulinganisha na kasi ya kusambaa kwa ugonjwa huo katika nchi nyingine za Afrika zilizopata kukabiliwa na ugonjwa huo kama vile Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Uganda.
Mheshimiwa Eliasson aliyasema hayo , Jumatano, Mei 6, 2015 wakati alipokutana na kuzungumza na Jopo linaloongozwa na Rais Kikwete kwenye ofisi za Rais Kikwete kwenye Jengo la North Lawn Building katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa (UN) mjini New York.
Akizungumza na wajumbe wa Jopo hilo ambalo mbali na Rais Kikwete wanatoka nchi za Brazil, Botswana, Indonesia, Uswisi na Marekani, Bwana Eliasson amewataka wajumbe wa Jopo hilo kupendekeza jinsi ya kukabiliana na magonjwa ya milipuko katika siku zijazo kwa sababu Ebola siyo ugonjwa wa mwisho wa mlipuko kushambulia dunia.
“Nyie mnajua, kama mimi ninavyojua, kuwa katika dunia ya leo kutakuwepo na mlipuko mwingine, kutakuwepo na mara nyingine…itakuwepo Ebola nyingine ama ugonjwa unaofanana na Ebola. Hivyo, tunahitaji maandalizi ya kiwango cha juu kupambana na hali hiyo itakapojitokeza. Lenu ni Jopo linalojitegemea na hivyo tunaamini litakuja na mapendekezo ambayo yatatuwezesha kukabiliana na hali hiyo,” alisema Bwana Eliasson ambaye ni raia wa Sweden.
Kuhusu kasi ya kusambaa kwa ugonjwa wa Ebola katika nchi za Afrika Magharibi za Guinea, Liberia na Sierra Leone, Naibu Katibu Mkuu alisema kuwa ni vyema na ni jambo la msingi sana kwa Jopo hilo kuangalia kwa nini ugonjwa huo ulisambaa kwa kasi ya kutisha kuliko wakati mwingine wowote katika historia ya miaka 40, tokea ulipogunduliwa kwa mara ya kwanza katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
“Tunajua kuwa nyie kazi yenu siyo kuchunguza ugonjwa wa Ebola. Ugonjwa huu tunautumia tu kuweka msingi wa miaka ya mbele. Hivyo ni lazima kuangalia sababu za kiini kabisa za kwa nini ugonjwa huo ulisambaa kwa kasi kubwa katika nchi hizo tatu. Tunajua kuwa hizi ni baadhi ya nchi masikini zaidi duniani. Tunaambiwa kuwa idadi ya waliofariki baada ya kupata ugonjwa huo ilikuwa ni asilimia 60. Lakini kama ugonjwa huo huo ungelipuka katika nchi iliyoendelea kasi ya vifo ingekuwa asilimia 25 tu.”
Mheshimiwa Eliasson alikuwa mmoja wa viongozi na wataalam ambao tokea Jumatatu wiki hii wamekuwa wanakutana na kuzungumza na wajumbe wa Jopo hilo ambalo liliteuliwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN)Mheshimiwa Ban Ki Moon Aprili 2, mwaka huu, 2015.
Mheshimiwa Ban Ki Moon alilitaka Jopo hilo linalojitegemea kupendekeza jinsi gani ya kuimarisha mifumo ya kitaifa na kimataifa, ili kuzuia na kujenga uwezo wa kukabiliana ipasavyo na mabalaa ya kiafya, kwa kutilia maanani mafunzo ambayo yametokana na mlipuko wa Ebola katika nchi tatu za Afrika Magharibi ambao umeua watu karibu 10,000 katika muda mfupi.
Alhamisi, Mei 7, 2015 wajumbe wa Jopo hilo wameshinda wamejifungia wakijadiliana wenyewe kwenye Kituo cha Utulivu (Retreat Centre) cha Green Tree nje kidogo ya Jiji la New York.
Leo, Ijumaa, Mei 8, 2015 watakutana na kuwaelezea juu ya kazi yao Wawakilishi wa Kudumu wa Nchi Wanachama wa Umoja wa Mataifa na baadaye Rais Kikwete atakutana na kuhutubia mkutano wa waandishi wa habari, ikiwa ni kitendo cha mwisho cha mkutano huo wa kwanza wa Wajumbe wa Jopo hilo ambalo watakutana mara sita kabla ya kuwasilisha Ripoti yao kwa Mheshimiwa Ban Ki Moon Desemba mwaka huu.
Rais Kikwete na ujumbe wake, ataondoka mjini New York jioni ya leo kwenda Algiers, mji mkuu wa Algeria kuanza ziara rasmi ya kiserikali ya siku tatu katika nchi hiyo rafiki ya Afrika Kaskazini.
Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
8 Mei, 2015
Taarifa kwa vyombo vya habari
TAARIFA YA KUKAMILIKA KWA KAZI YA TUME YA UCHUNGUZI WA MALALAMIKO YALIYOTOKANA NA UTEKELEZAJI WA
OPERESHENI TOKOMEZA
___________________________________________
1.0 Utangulizi:
1.1 Tarehe 01/05/2014, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete aliunda Tume ya Uchunguzi kuhusu malalamiko yaliyotokana na utekelezaji wa Operesheni Tokomeza. Aliteua Makamishna watatu ambao ni Mhe. Balozi Jaji (Mst) Hamisi Amiri Msumi (Mwenyekiti wa Tume), Mhe. Jaji (Mst) Stephen Ernest Ntashima Ihema (Kamishna), Mhe. Jaji (Mst) Vincent Kitubio Damian Lyimo (Kamishna) na Ndugu Frederick Kapela Manyanda (Katibu wa Tume).
1.2 Operesheni Tokomeza ilikuwa Operesheni iliyobuniwa na Wizara ya Maliasili na Utalii kwa lengo jema na muhimu la kupambana na ujangili unaotishia urithi wetu wa wanyama pori, hususani tembo, faru, nyati, twiga, pundamilia n.k.
2.0 Hadidu Rejea kwa Tume
2.1 Kuchunguza namna Operesheni Tokomeza ilivyotekelezwa;
2.2. Kuchunguza iwapo maafisa waliotekeleza Operesheni Tokomeza walizingatia sheria, kanuni, taratibu na hadidu rejea walizopewa;
2.3. Kuchunguza iwapo maafisa waliotekeleza Operesheni Tokomeza walivunja sheria, kanuni, taratibu na hadidu rejea walizopewa;
2.4. Kuchunguza iwapo kuna watu waliokiuka sheria yoyote wakati wa utekelezaji wa Operesheni Tokomeza na iwapo hatua zilizochukuliwa na maafisa wa Operesheni Tokomeza dhidi ya wakosaji hao na mali zao zilikuwa sahihi;
2.5. Kupendekeza hatua zinazostahili kuchukuliwa dhidi ya maaafisa wa Operesheni Tokomeza waliokiuka sheria, kanuni, taratibu na hadidu rejea za Operesheni Tokomeza; na
2.6. Kupendekeza mambo yanayopaswa kuzingatiwa katika kupanga na kutekeleza Operesheni nyingine kama hii ili kuzuia na kuepuka malalamiko mengine kama yaliyotokea kwenye Operesheni Tokomeza.
3.0 Kukamilika kwa kazi ya Tume
3.1 Tume imekamilisha kazi yake na kukabidhi taarifa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, tarehe 10 Aprili, 2015. Kwa maagizo ya Rais tumeisoma na kuichambua taarifa hiyo vya kutosha. Kwa hakika Tume imefanya kazi kubwa sana, na nzuri sana ya uchunguzi na uandishi wa taarifa. Kazi imefanywa kwa weledi na umakini wa hali ya juu na kwa lengo dhahiri la kutenda haki. Katika siku 265, Tume ilitembelea wilaya 38 katika mikoa 20 na kuhoji jumla ya mashahidi 259. Mikoa iliyohusika ni Kigoma, Katavi, Rukwa, Mbeya, Kagera, Geita, Shinyanga, Simiyu, Mara, Lindi, Mtwara, Ruvuma, Iringa, Morogoro, Pwani, Tabora, Singida, Manyara, Arusha na Tanga.
3.2 Tume imejitahidi kuwahoji wote waliokuwa na malalamiko, kuwahoji mashuhuda, kuwahoji watuhumiwa, na kukusanya ushahidi wa aina mbalimbali ili ama kuthibitisha makosa pale yalipofanyika na kupendekeza hatua za kuchukua, au kujiridhisha kuwa tuhuma na malalamiko hayakuwa ya msingi. Kazi hiyo imefanywa vizuri na kurahisisha kazi ya Serikali ya kuchukua hatua zinazostahili.
4.0 Operesheni Tokomeza ilivyotekelezwa
4.1 Tume ilibaini kuwa katika kipindi cha mwezi mmoja cha utekelezaji wa Operesheni Tokomeza iliyoanza tarehe 4 Oktoba, 2013, mafanikio mengi yalipatikana, ikiwemo:
4.1.1 Watuhumiwa 1,030 wa makosa mbalimbali yanayohusu ujangili na uvunaji haramu wa misitu walikamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria;
4.1.2 Kukamatwa kwa meno ya 211 yenye uzito wa kilo 522, meno ya ngiri 11, mikia ya wanyama mbalimbali 36, ngozi za wanyama mbalimbali 21, pembe za swala 46, mitego ya wanyama 134, ng’ombe 7,621 waliokuwa wanachungwa ndani ya hifadhi na misitu, baiskeli 58, pikipiki 8 na magari 9;
4.1.3 Katika kipindi cha Operesheni kulikamatwa jumla ya bunduki za kijeshi 18, bunduki za kiraia 1,579, risasi 1,964, mbao vipande 27,913, mkaa magunia 1,242, magogo 858 na misumeno 60.
4.1.4 Operesheni ilifanikiwa kupunguza kasi ya mauaji ya tembo kutoka tembo wawili kwa siku hadi tembo wawili kwa mwezi wakati wa Operesheni;
4.2 Operesheni ilisitishwa rasmi tarehe 01/11/2013 ili kupisha uchunguzi wa malalamiko yaliyojitokeza. Baada tu ya kusitishwa kwa Operesheni wafugaji wengi wamerudisha mifugo yao katika maeneo ya hifadhi yaani Mapori ya Akiba, Hifadhi za Taifa, Hifadhi za Misitu na Maeneo Oevu na ujangili ukaanza kurejea. Aidha watuhumiwa waliokuwa wametoroka kukimbia Operesheni wameanza kurejea kwenye makazi yao.
5.0 Vitendo vya Ukiukwaji wa Sheria, Kanuni, Taratibu na Hadidu Rejea
5.1 Tume imebaini kuwa katika utekelezaji wa Operesheni kulikuwa na matukio ya ukiukwaji wa Sheria, Kanuni, Taratibu na Hadidu Rejea. Ukiukwaji huu umesababisha madhara kwa wananchi mbalimbali ikiwemo vifo, madhara ya mwili na kadhalika.
5.2 Tume ilichunguza matukio 15 ya vifo, na kuridhika kuwa vifo tisa (9) kati ya hivyo vilisababishwa na mateso ambapo watendaji kwenye Operesheni walitumia nguvu kubwa kupita kiasi dhidi ya watuhumiwa wakati wa ukamataji au kuhoji. Kabla ya vifo watu hao walikuwa chini ya ulinzi wa askari wa Operesheni na kuna ushahidi wa kitabibu (medical reports), ushahidi wa kimazingira na ushahidi wa kuona, unaohusisha vifo vya marehemu hao na mateso kutoka kwa askari wa Operesheni. Tume haikupata ushahidi wa kuhusisha vifo sita (6) vilivyobaki moja kwa moja na Operesheni Tokomeza.
5.3 Tume ilichunguza madai ya mateso yaliyosababisha madhara kwenye miili ya wahusika. Walalamikaji walieleza Tume kwamba waliteswa ili waoneshe silaha au nyara zilipofichwa au wakiri kujihusisha na ujangili au ujambazi na wataje washirika wao wa mtandao wa ujangili. Kulikuwa pia na malalamiko ya udhalilishwaji. Malalamiko hayo yalitoka kwenye wilaya ishirini na mbili (22) za mikoa mbalimbali. Yapo matukio ambayo walalamikaji waliweza kuleta mbele ya Tume uthibitisho wa kuteswa, na walionesha makovu na kutoa vyeti vya matibabu na PF 3 walizopewa baada ya kuumia.
5.4 Tume imebaini kuwepo matendo mbalimbali ya ukiukwaji wa sheria, kanuni, taratibu na hadidu rejea uliofanywa na baadhi ya askari wa Operesheni na maafisa wengine walioshiriki katika utekelezaji wake, ikiwemo matukio yanayoashiria rushwa na udanganyifu mbalimbali.
5.5 Tume ilishughulikia pia tuhuma za wizi, upotevu na uporaji wa mali. Walalamikaji wa kundi hili walieleza Tume kuwa wakati wa utekelezaji wa Operesheni, waliibiwa au kupoteza fedha na mali zao wakati na baada ya kukamatwa au kupekuliwa na askari wa Operesheni. Tume ilichunguza jumla ya matukio ishirini na tatu (23) ya aina hiyo na kubaini kuwa malalamiko mengi yalitokana na askari wa Operesheni kutofuata sheria, kanuni na taratibu za ukamataji, kuhoji na upekuzi maungoni mwa watuhumiwa na kwenye nyumba zao. Kasoro zilizoonekana ni pamoja na kutoshirikisha viongozi au watu huru katika upekuzi na kutojazwa hati za upekuzi mara baada ya upekuzi. Kasoro nyingine ni askari wengi kuingia kwenye nyumba kwa wakati mmoja. Aidha, Tume imebaini walalamikaji wengine waliongeza chumvi katika ushahidi wao kuhusu idadi ya mali na fedha zilizopotea au kuibiwa na hivyo ushahidi wao kutoaminika au kuthibitika.
5.6 Tume ilichunguza malalamiko ya kubakwa wakati wa utekelezaji wa Operesheni. Matukio yaliyochunguzwa na Tume yalikuwa katika Kijiji cha Iputi, Wilaya ya Ulanga, Mkoa wa Morogoro na Kijiji cha Mwantimba Wilaya ya Bariadi, Mkoa wa Simiyu na Wilayani Sikonge. Hata hivyo wote waliodai kubakwa hawakujitokeza mbele ya Tume kutoa ushahidi wao, hivyo Tume haikuweza kuchunguza malalamiko yao. Alijitokeza mlalamikaji mmoja Wilayani Ulanga, Morogoro, lakini Tume haikuridhika na maelezo yake, ambayo hayakutosheleza kubainisha kosa kwenye utekelezaji wa Operesheni Tokomeza.
5.7 Tume ilibaini kuwa wapo watuhumiwa waliofikishwa mahakamani na kutiwa hatiani na wengine kuachiwa. Tume imeona kuwa hatua hii ilikuwa sahihi kisheria. Lakini Tume ilibaini pia kuwa baadhi ya watuhumiwa hawakufikishwa mahakamani. Badala yake maafisa wa Operesheni walijichukulia mamlaka ya kutoa adhabu kwa watuhumiwa kama vile kukamata na kuzuia mali zao, kuchoma moto nyumba na mali zilizokuwa kwenye maeneo ya hifadhi, kuua au kujeruhi mifugo iliyokutwa kwenye maeneo ya hifadhi au kuuza kwa mnada ng’ombe waliokamatwa kwenye maeneo ya hifadhi. Hatua nyingine inayolalamikiwa ni kuchukua bunduki zinazomilikiwa kisheria.
5.8 Tume imebaini kwamba katika baadhi ya maeneo askari wa Operesheni walichoma nyumba moto kwa madai ya nyumba hizo kujengwa kwenye hifadhi. Malalamiko hayo yalitoka katika Wilaya za Mlele na Mpanda, Mkoa wa Katavi, Wilaya ya Momba, Mkoa wa Mbeya; Wilaya za Nkasi na Sumbawanga, Mkoa wa Rukwa; na Wilaya ya Simanjiro, Mkoa wa Manyara. Katika uchunguzi wa matukio haya Tume imebaini yafuatayo:
- Wanakijiji hawakupewa taarifa ya kutosha kuhamisha mali zao kabla ya kuchoma nyumba zao;
- Baadhi ya wanakijiji walipoteza vyakula na mali zao katika zoezi hilo la uchomaji moto;
- Kuna vijiji vilivyosajiliwa lakini sehemu ya vitongoji vyake viko ndani ya Hifadhi za Taifa;
- Kuna maeneo ya hifadhi au ushoroba (buffer zone) ambayo hayana alama za mipaka kati ya hifadhi au ushoroba na vijiji husika;
- Kuna nyumba ambazo hazikuwa kwenye eneo la hifadhi au ushoroba na hivyo zilichomwa moto kinyume cha sheria.
- Baadhi ya matukio na malalamiko ya kuchomewa moto nyumba yalitokea kabla ya Operesheni.
5.9 Uchunguzi wa Tume umebaini kuwepo kwa tatizo kubwa la wafugaji kutoka nje ya nchi na wafugaji wenyeji kuingiza mifugo yao katika Mapori ya Akiba, Hifadhi ya Misitu, Maeneo Oevu na Hifadhi za Taifa. Maeneo yaliyoathirika sana na tatizo hili ni Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Pori la Akiba la Kigosi – Moyowosi, Pori la Akiba la Maswa, Mapori ya Akiba ya Biharamulo – Burigi – Kimisi na Pori la Akiba la Kijereshi.
Katika baadhi ya maeneo imethibitika kwamba wapo ng’ombe waliouawa kwa kupigwa risasi baada ya kukutwa ndani ya hifadhi.
Aidha, Tume imeridhika kwamba kuna ng’ombe wa walalamikaji waliokamatwa na kuuzwa kwa mnada. Uuzaji wa ng’ombe katika tukio hili haukuzingatia utaratibu wa kisheria.
5.10 Tume ilipata ushahidi kwamba katika maeneo mbalimbali askari wa Operesheni walikamata au kuchukua bunduki, risasi pamoja na vitabu vyake hata kwa silaha zinazomilikiwa kihalali. Maeneo ambayo yalikuwa na malalamiko ya watu kuchukuliwa silaha zao ni mikoa saba (7) ambayo ni Katavi, Mbeya, Lindi, Morogoro, Tabora, Manyara na Pwani ambapo jumla ya watu sitini na mbili (62) walijitokeza mbele ya Tume kulalamika tukio hili.
6.0 Hatua Zitakazochukuliwa na Serikali
6.1 Baada ya kupitia kwa kina taarifa ya Tume, pamoja na mapendekezo ya Tume, Serikali itafanya yafuatayo:
6.1.1 Hatua za kimashtaka zitaendelea kwa shauri la mauaji ambalo upelelezi wake umekamilika na hatua za kiuchunguzi zitaendelea kwa mashauri mengine nane (8) ya mauaji ambayo upelelezi wake haujakamilika;
6.1.2 Hatua za kisheria na kiutawala zitachukuliwa dhidi ya watuhumiwa waliothibitika kuwatesa watu 15 wakati wa Operesheni;
6.1.3 Hatua za kiuchunguzi zinazofanywa na TAKUKURU kuhusu tuhuma za rushwa na udanganyifu zilizothibitika zitaendelea;
6.1.4 Silaha zinazodaiwa kumilikiwa kihalali zitafanyiwa uhakiki na ukaguzi wa kina kuhusu umiliki na matumizi yake na endapo hakutakuwa na sababu nyingine za kisheria za kuzuia urejeshwaji, wamiliki warejeshewe silaha zao kwa mujibu wa sheria na taratibu;
6.1.5 Mali ambazo zimethibitika kuchukuliwa wakati wa Operesheni kwa tuhuma za kuhusishwa na uvunaji haramu wa mazao ya misitu zirejeshwe endapo hakutakuwa na sababu za kisheria kuendelea kuzishikilia;
6.1.6 Serikali itafanya uhakiki wa vijiji ambavyo vimesajiliwa na vimo ndani ya hifadhi ili kutatua migogoro ya ardhi kati ya hifadhi na vijiji. Aidha, Serikali itahakikisha kunakuwa na ushirikiano wa karibu kati ya Msajili wa vijiji au mamlaka husika na Wizara ya Maliasili na Utalii ili kuepuka kusajili vijiji ndani ya maeneo ya hifadhi;
6.1.7 Wizara ya Maliasili na Utalii itatayarisha kanuni zitakazoweka utaratibu wa kuwaondoa watu waliovamia na kujenga makazi katika hifadhi;
6.1.8 Sheria zote zinazolinda maeneo ya hifadhi zitafanyiwa marekebisho ili kuongeza adhabu kwa kosa la kuingiza mifugo kwenye Hifadhi bila kujali uraia wa wamiliki wa mifugo hiyo;
6.2 Kwa vile Tume imejiridhisha na faida kubwa na mafanikio ya Operesheni Tokomeza, Serikali itaendelea na Operesheni kama hizo kadri itakavyojitajika ili kuokoa maliasili za Taifa, ikiwemo wanyama, hifadhi na misitu. Hata hivyo ushauri wa Tume juu ya kuboresha upangaji, usimamizi na utekelezaji wa Operesheni hizo itazingatiwa kikamilifu.
7.0 Mawaziri Waliojiuzulu
Tume ilijiridhisha kuwa Mawaziri wote waliojiuzulu, yaani Mhe. Dkt. Emmanuel J. Nchimbi, Mb., Mhe. Balozi Khamis Kagasheki, Mb., Mhe. Mathayo D. Mathayo, Mb., na Mhe. Shamsi V. Nahodha, Mb., hawakuhusika moja kwa moja na makosa yoyote ya utekelezaji kwenye Operesheni Tokomeza. Hivyo, waliwajibika kisiasa tu na hakuna hatua nyingine inayostahili dhidi yao.
Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
8 Mei, 2015
Taarifa kwa vyombo vya habari
MATOKEO YA UCHUNGUZI WA AWALI KUMHUSU NDUGU ELIAKIM
C. MASWI, KATIBU MKUU, WIZARA YA NISHATI NA MADINI
_________________________________________________
1.0 Utangulizi
1.1 Katika mkutano wake wa 16 na 17, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, pamoja na mambo mengine, lilijadili Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali iliyotokana na Taarifa ya Ukaguzi wa Akaunti ya Tegeta Escrow uliofanywa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali.
1.2 Baada ya majadiliano, Bunge lilipitisha maazimio kadhaa yaliyoelekezwa kwa Serikali kwa ushauri na utekelezaji. Mojawapo ya maazimio hayo yalimtaja Ndugu Eliakim C. Maswi, ambaye ndiye Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, kuwa amehusika kijinai au kimaadili katika miamala iliyotokea katika akaunti ya Tegeta Escrow.
1.3 Wakati anahutubia Taifa kupitia Wazee wa Dar es Salaam tarehe 22 Desemba, 2014, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alisema ifuatavyo:-
“Kuhusu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, kwa vile ni Mtumishi wa Umma, anatawaliwa na Sheria na Kanuni za Utumishi wa Umma. Hivyo, nimeshaelekeza Mamlaka kuchunguza tuhuma zake na hatimaye ikibainika ana makosa hatua za kinidhamu zitachukuliwa.”
1.4 Tuhuma dhidi ya Ndugu Eliakim C. Maswi zimeshughulikiwa katika ngazi mbili tofauti. Amechunguzwa na Sekretarieti ya Maadili ya Umma, kisha baada ya hapo alichunguzwa pia na Kamati ya Uchunguzi wa Awali iliyoundwa na mamlaka yake ya nidhamu.
2.0 Sekretarieti ya Tume ya Maadili
2.1 Kifungu 18 (2) (c) na (3) cha Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma kinaipa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma mamlaka na uwezo wa kuchunguza tuhuma yoyote ya kuvunjwa kwa maadili ya uongozi wa umma yanayotawaliwa na Sheria hiyo. Tuhuma dhidi ya Ndugu Eliakim C. Maswi zilizomo kwenye maazimio ya Bunge zinatawaliwa na Sheria hiyo.
2.2 Katika kutekeleza majukumu yake, Sekretarieti ya Maadili ya Umma ilifanya uchunguzi wa awali na kisha kumhoji Ndugu Eliakim C. Maswi tarehe 19 Desemba, 2014.
2.3 Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma haijabaini kuwepo kwa maslahi binafsi katika uamuzi uliofanywa na Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati na Madini wa kuruhusu fedha za Akaunti ya Tegeta Escrow kutolewa. Aidha, hawakubaini ukiukwaji wowote wa maadili ya viongozi wa umma uliofanywa na Ndugu Eliakim C. Maswi. Waliona kuwa yote aliyoyafanya yalizingatia matakwa ya Sheria, ushauri wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali pamoja na ridhaa ya TANESCO. Hivyo, Sekretarieti ya Maadili haikuona msingi wowote wa kuendelea na shauri la Ndugu Eliakim C. Maswi, na wamelihitimisha.
3.0 Kamati ya Uchunguzi wa Awali ya Mamlaka ya Nidhamu
3.1 Kwa mujibu wa Kifungu 4(3) (d) cha Sheria ya Utumishi wa Umma Na. 8 ya mwaka 2002 (kama ilivyorekebishwa) Katibu Mkuu Kiongozi ndiye Mamlaka ya Nidhamu ya Makatibu Wakuu.
3.2 Kwa kuzingatia Azimio husika la Bunge, na kwa maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Katibu Mkuu Kiongozi aliunda Kamati ya Uchunguzi wa Awali dhidi ya Ndugu Eliakim C. Maswi, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, chini ya Kifungu cha 36 cha Kanuni za Utumishi wa Umma za mwaka 2003 kinachotamka ifuatavyo:-
“Where it is necessary to institute disciplinary proceedings against a public servant, the disciplinary authority shall make preliminary investigations before instituting disciplinary proceedings.”
3.3 Kwa mamlaka aliyonayo chini ya Kanuni 35(2)(b) na Kanuni 37 ya Kanuni za Utumishi wa Umma za mwaka 2003, Katibu Mkuu Kiongozi alimpumzisha Bwana Eliakim C. MASWI kutekeleza majukumu yake ya kazi ya Katibu Mkuu ili kupisha uchunguzi wa awali. Uchunguzi wa awali ulifanyika chini ya Kanuni ya 36 ya Kanuni za Utumishi wa Umma zilizotajwa, pamoja na Kifungu 4(3) (d) cha Sheria ya Utumishi wa Umma Na. 8 ya mwaka 2002, kama ilivyorekebishwa.
3.4 Kwa mamlaka aliyonayo chini ya Kanuni zilizotajwa kwenye ibara 3.3 hapo juu, Katibu Mkuu Kiongozi aliteua Kamati ya Uchunguzi wa Awali na kuipa Hadidu za Rejea zifuatazo:
3.4.1 Kubainisha wajibu na madaraka halisi ya Katibu Mkuu, Wizaraya Nishati na Madini, kwenye uendeshaji wa TANESCO kwa ujumla, na hususan kwenye kufungua, kuendesha na hatimaye kufungwa kwa akaunti ya Tegeta Escrow.
3.4.2 Kubainisha na kupata maelezo ya kina juu ya kuhusika kwa Bwana Eliakim C. Maswi katika mchakato na mtiririko mzima wa akaunti ya Tegeta Escrow, tangu kufunguliwa hadi kufungwa.
3.4.3 Kubainisha na kupata maelezo ya kina iwapo kuna jambo lolote ambalo Bwana Eliakim C. Maswi alilifanya au ambalo alipaswa kulifanya lakini hakulifanya, linalomstahilisha achukuliwe hatua za nidhamu.
3.4.4 Kubainisha na kupata maelezo ya kina iwapo katika hatua yoyote ya mchakato na mtiririko wa tangu kufunguliwa hadi kufungwa kwa akaunti ya Tegeta Escrow, Bwana Eliakim C. Maswi alifanya jambo lolote linalodhihirisha matumizi mabaya ya mamlaka yake kama Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, kwa namna iliyosababisha hasara ya aina yoyote ile kwa Taifa la Tanzania.
3.4.5 Kubainisha na kupata maelezo ya kina iwapo katika hatua yoyote tangu akaunti ya Tegeta Escrow ilipofunguliwa hadi ilipofungwa, Bwana Eliakim C. Maswi hakuchukua tahadhari ya kutosha kulinda maslahi ya umma na kusababisha kupotea kwa fedha za umma kwa uzembe au matumizi mabaya ya madaraka.
3.4.6 Kubainisha iwapo kuna mahali popote katika mchakato wa akaunti ya Tegeta Escrow ambapo Bwana Eliakim Chacha Maswi alifanya jambo lolote linaloashiria kitendo cha kijinai, au kukiuka maadili ya viongozi wa umma.
3.4.7 Kuandaa taarifa ya uchunguzi wa awali kwa msingi wa Hadidu za Rejea zilizomo humu na kuiwasilisha kwa Katibu Mkuu Kiongozi. Taarifa hiyo, pamoja na mambo mengine, ipendekeze hatua za kuchukuliwa kwa kila eneo ambalo Kamati itabaini umuhimu wa hatua kuchukuliwa.
3.5 Mapendekezo ya Kamati ya Uchunguzi wa Awali
3.5.5 Kamati haijabaini kosa lolote ambalo linaweza kusababisha Ndugu Eliakim Chacha Maswi, Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati na Madini, kufunguliwa mashtaka ya kinidhamu kwa kukiuka Sheria ya Utumishi wa Umma Sura 298 ikisomwa pamoja na Kanuni zake za mwaka 2003 kwa kuruhusu Benki Kuu ya Tanzania kutoa fedha zilizokuwa katika Akaunti ya Tegeta Escrow.
4 Hitimisho la Uchunguzi wa Awali
4.4 Uchunguzi wa Awali uliofanywa na Sekretarieti ya Maadili umebaini kuwa Ndugu Eliakim C. Maswi hana makosa yoyote ya kimaadili katika mchakato wa fedha za akaunti ya Tegeta Escrow.
4.5 Hali Kadhalika Uchunguzi wa Awali uliofanywa na Kamati ya Uchunguzi wa Awali iliyoundwa na Katibu Mkuu Kiongozi umebaini kuwa Ndugu Eliakim C. Maswi, “hakutenda au kuhusika na jambo lolote linaloashiria vitendo vya jinai au kukiuka Maadili ya Viongozi wa Umma”.
4.6 Ushahidi wa vielelezo uliotolewa kwenye Sekretarieti ya Maadili na kwenye Kamati ya Uchunguzi wa Awali umejitosheleza kuthibitisha kwamba Ndugu Eliakim C. Maswi alitenda kazi yake kwa kiwango kinachoridhisha kwa kufanya mawasiliano na mamlaka mbalimbali na kwa nyakati tofauti kwa lengo la kuhakikisha na kujiridhisha kwamba kufungwa kwa Akaunti ya Tegeta Escrow kunafanyika kwa usahihi.
4.7 Hakuna ushahidi wowote kuwa Ndugu Eliakim C. Maswi alikuwa miongoni mwa waliopata mgao wa fedha au fadhila yoyote kutokana na kufungwa Akaunti ya Tegeta Escrow.
4.8 Kwa nafasi yake ya mamlaka ya nidhamu Katibu Mkuu Kiongozi, ameridhika kuwa Ndugu Eliakim C. Maswi hana makosa yoyote aliyoyafanya katika mchakato wa akaunti ya Tegeta Escrow yanayostahili adhabu. Hivyo, mchakato wa kinidhamu, kimaadili na kijinai dhidi yake umefikia mwisho wake. Mwenye mamlaka ya uteuzi atatafakari taarifa hizi na kuamua cha kufanya kuhusu ajira yake baadaye.
Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
8 Mei, 2015
Taarifa kwa vyombo vya habari
Mabalozi walielezea Jopo la Kikwete siasa ilivyohujumu mapambano dhidi ya Ebola
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete na wanajopo wenzake mashuhuri duniani ambao wanatafuta jinsi gani dunia inavyoweza kukabiliana vizuri zaidi na magonjwa ya milipuko katika siku zijazo, leo, Jumanne, Mei 5, 2015, wamekutana na Wawakilishi wa Kudumu katika Umoja wa Mataifa (UN) wa nchi tatu za Afrika Magharibi ambazo zimeathiriwa na ugonjwa wa Ebola.
Rais Kikwete na wanajopo wenzake wamekutana na mabalozi hao, ikiwa ni mwendelezo wa Jopo hilo, kukutana na kuwasikiliza watu mbali mbali katika vikao vyake kwenye Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York kwa nia ya kupata maoni na mawazo ya watu hao, hasa wale wanaokabiliana na ugonjwa wa Ebola katika nchi za Guinea, Liberia na Sierra Leone, nchi zinajulikana kama wanachama wa Manu River Union.
Tokea Jumatatu, Mei 4, 2015, Rais Kikwete na wanajopo wenzake kutoka nchi za Brazil, Botswana, Indonesia, Uswisi na Marekani wamekuwa wanasikiliza watu mbali mbali, wakiwemo wataalam wa magonjwa, madaktari na wasimamizi wa shughuli za kibinadamu katika maeneo ya majanga, ikiwa ni maandalizi ya kutoa mapendekezo yao ya kukabiliana na magonjwa ya milipuko katika siku zijazo kama walivyoombwa na Katibu Mkuu wa UN, Mheshimiwa Ban Ki Moon.
Kwa maelekezo ya Mheshimiwa Ban Ki Moon wakati anateua Jopo hilo, wanajopo wameombwa kutumia uzoefu na mafunzo yaliyopatikana katika kubabiliana na ugonjwa wa Ebola katika kuandaa Ripoti yao ya jinsi ya kukabiliana na magonjwa ya namna hiyo katika siku zijazo. Ripoti hiyo inatarajiwa kukabidhiwa kwa Mheshimiwa Ban Ki Moon Desemba mwaka huu, 2015.
Mwakilishi wa Guinea katika UN, Mheshimiwa Balozi Mamadi Toure amelieleza Jopo jinsi nchi hiyo iliyokuwa ya kwanza kugundua mgonjwa wa Ebola ilivyojikuta katika hali ya kuwa na uwezo mdogo wa kukabiliana na balaa la ugonjwa huo kwa sababu ya mfumo dhaifu wa sekta ya afya na miundombinu iliyokuwa imesambaratika wakati wa miaka mingi, zaidi ya miaka 20, ya utawala wa kijeshi nchini humo.
Balozi Toure ameeleza jinsi nchi hiyo ilivyokumbana na vikwazo vingi mwanzoni katika kukabiliana na ugonjwa huo ikiwa ni pamoja na ukosefu wa elimu kwa wananchi, ujinga wa baadhi ya wananchi na hata kuingizwa kwa siasa za upinzani katika jambo hilo ambako kulizuia ama kuchelewesha waathirika kwenda ama kupelekwa hospitali.
“Wananchi wa Guinea walikuwa hawakuandaliwa kiasi cha kutosha kukabiliana na ugonjwa huo ambao bado unaendelea katika nchi hiyo na nchi za jirani za Liberia na Sierra Leone. Kwa sababu ya upinzani wa kila aina na hasa wa kisiasa, ulitokea uhasama wa moja kwa moja wa wananchi kwa maofisa wa Serikali na wahudumu wa ugonjwa huo. Baadhi yao walishambuliwa na wananchi na kuna tukio moja ambako watu waliuawa,” amesema Balozi Toure.
“Ulikuwepo upinzani wa kisiasa na hata kidini, na yote mawili hayakusaidia kuzuia kusambaa haraka kwa ugonjwa huo. Watu walikataa kwenda hospitali kutibiwa, wagonjwa walifichwa ndani ya nyumba na hata watu waliposhauriwa kuacha kula nyama ya wanyapori bado walikataa. Kwa hakika ujinga, uongo na wananchi kudanganywa viliathiri sana jitihada za kukabiliana na ugonjwa huo haraka zaidi.”
Balozi huyo, kama walivyosema mabalozi wenzake wa Liberia na Sierra Leone, amesisitiza kuwa mwanzoni mwa ugonjwa huo hapakuwepo na uratibu wowote na hakuna mtu aliyejua jinsi gani ya kukabiliana na hali hiyo.
Hata hivyo, mabalozi wote watatu wamekubaliana kuwa ushirikiano kati ya viongozi wa nchi hizo tatu kwa nia ya kukabili ugonjwa huo kwa pamoja, umechangia sana kupunguza hali ya maambukizo ya ugonjwa huo katika nchi hizo tatu.
Jopo hilo linaendelea na kikao chake mjini New York leo.
Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
6 Mei, 2015
Taarifa kwa vyombo vya habari
Rais Kikwete atuma Mawaziri wa nchi nne Burundi
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete na Mwenyekiti wa Mkutano wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuia ya Afrika Mashariki (EAC) ametuma ujumbe wa mawaziri wa mambo ya nje wa nchi nne wanachama wa Jumuia hiyo kwenda Burundi kuchunguza hali ya kisiasa ilivyo nchini humo.
Aidha, Rais Kikwete amesema kuwa suluhisho la kisiasa la matatizo ya sasa ya Burundi yatapatikana kwa wananchi wa Burundi kuheshimimu Katiba na Sheria ya Uchaguzi na kuwa ni jukumu la jumuia ya kimataifa kuisaidia nchi hiyo kuvuka katika changamoto za sasa.
Rais Kikwete ameyasema hayo, Jumatatu, Mei 4, 2015 kwenye Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York wakati alipokutana na Katibu Mkuu wa Umoja huo, Mheshimiwa Ban Ki Moon ambaye alimwuliza Rais Kikwete kuelezea hali ilivyo Burundi mwishoni mwa kikao kati ya Ban Ki Moon na Wajumbe wa Jopo la Watu Maarufu Duniani ambalo limeteuliwa na Mheshimiwa Ban Ki Moon kutafuta njia za jinsi dunia inavyoweza kukabiliana vizuri zaidi na magonjwa ya milipuko katika siku zijazo.
Mheshimiwa Ban Ki Moon amemwambia Rais Kikwete: “Mheshimiwa Rais tuelezee kidogo hali ya Burundi kufuatia uamuzi wa Rais wa Burundi kugombea Urais kwa mara ya tatu…uamuzi huu unaweza kuendeleza hali ya machafuko na mauaji. Tunataka kujua maoni ya nchi jirani na Burundi na pengine wewe, Mheshimiwa Rais, ni mmoja wa watu wachache, wachache sana duniani ambao wanaweza kusaidia kubadilisha hali ilivyo katika Burundi.”
Rais Kikwete amemwambia Mheshimiwa Ban Ki Moon: “Kama unavyojua Mheshimiwa Katibu Mkuu kwa sasa mimi ni mwenyekiti wa EAC na nimeagiza mawaziri wa nje wa Tanzania, Kenya, Uganda na Rwanda kwenda Burundi kuzungumza na wadau wote muhimu na baada ya hapo watuletee ripoti na kutushauri jinsi tunavyoweza kusaidia katika Burundi.”
Rais Kikwete amesema kuwa mawaziri hao watakuwa wamemaliza kazi yao mwishoni mwa wiki hii na baada ya hapo EAC itaweza kujua nini la kufanya. “Aidha, kama unavyojua, Waziri wa Mambo ya Nje wa Burundi alikuwa Tanzania leo, akizungumza na Waziri wetu wa Mambo ya Mambo ya Nje kuhusu hali ya Burundi.”
Hata hivyo, Rais Kikwete amesema kuwa majawabu ya changamoto za sasa katika Burundi ni kwa wananchi wa Burundi kuongozwa na Katiba ya nchi na Sheria ya Uchaguzi ya nchi hiyo. “Kama kuna watu wanadhani kuwa uteuzi wa Rais wa Burundi kugombea tena urais nchini humo ni kuvunja sheria, basi wafuate mkondo wa sheria kuweza kupata ukweli na majawabu siyo kutumia nguvu”.
Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
5 Mei, 2015
Taarifa kwa vyombo vya habari
Tuna imani nanyi, Ban Ki Moon amwambia Rais Kikwete na wenzake
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) Mheshimiwa Ban Ki Moon amesema kuwa dunia ina imani kubwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete na wajumbe wengine wa Jopo la Watu Maarufu Duniani waliopewa jukumu la kutafuta jinsi dunia inavyoweza kukabiliana na magonjwa ya milipuko, kama vile Ebola, katika siku zijazo kuja na mapendekezo yao yanayolenga kuifanya dunia mahali bora zaidi pa kuishi.
Aidha, Mheshimiwa Ban Ki Moon amewaambia wajumbe hao kuwa uteuzi wao uliofanywa na yeye mwenyewe mwezi uliopita na umefanyika baada ya majina yao kuwa yamependekezwa na taasisi nyingine za kimataifa, mbali na Umoja wa Mataifa.
Mheshimiwa Ban Ki Moon ameyasema hayo, Jumatatu, Mei 4, 2015, wakati alipokutana na kuzungumza na wajumbe wa Jopo hilo ofisini kwake katika Makao Makuu ya UN mjini New York, muda mfupi kabla ya wajumbe hao kufanya kikao chao cha kwanza chini ya uenyekiti wa Rais Kikwete.
Akizungumza na wajumbe hao, Mheshimiwa Katibu Mkuu wa UN amesema kuwa dunia ina imani kubwa kuwa Jopo hilo litaweza kupendekeza njia bora zaidi za kukabiliana na magonjwa ya milipuko duniani kwa namna bora zaidi kuliko ilivyokuwa kwa mlipuko wa ugonjwa wa Ebola.
“Nawashukuru sana kwa kukubali uteuzi wangu. Dunia ina imani kubwa na uwezo wenu katika kutuwezesha sote kukabiliana kwa kujiamini zaidi na magonjwa ya milipuko katika siku zijazo,” Mheshimiwa Ban Ki Moon amewaambia wajumbe hao sita ambao wamepewa hadi Desemba mwaka huu kuwasilisha Ripoti kuhusu namna gani dunia inavyoweza kukabiliana vizuri zaidi na magonjwa ya milipuko.
Mbali na Rais Kikwete ambaye ni Mwenyekiti wa Jopo hilo, wajumbe wengine ni Bwana Celso Amorim wa Brazil, Bi. Micheline Calmy-Rey wa Uswisi, Bwana Marty Natalegwa wa Indonesia, Bi. Joy Phumaphi wa Botswana na Bwana Rajiv Shah wa Marekani.
Kuhusu uteuzi wao, Mheshimiwa Ban Ki Moon amesema kuwa uteuzi huo ulifanywa na yeye baada ya kushauriana na taasisi mbalimbali duniani na kukubaliana kuhusu uwezo wa Jopo hilo kuifanya kazi hiyo.
“Tunaweza kusema kuwa uteuzi huo umefanywa kwa pamoja na taasisi mbalimbali duniani – Umoja wa Mataifa, Benki ya Dunia na Shirika la Afya Duniani (WHO). Kwa hakika hii inaonyesha ni kiasi gani dunia ina imani nanyi katika uwezo wa kuifanya kazi hii,” amesema Mheshimiwa Ban Ki Moon.
Rais Kikwete amemshukuru Mheshimiwa Ban Ki Moon kwa uteuzi wa Jopo hilo akisisitiza kuwa uteuzi huo unaonyesha ni kiasi gani UN ina imani katika uwezo wa wajumbe wa Jopo kuifanya kazi hiyo vizuri.
Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
5 Mei, 2015
Taarifa kwa vyombo vya habari
Tuna imani nanyi, Ban Ki Moon amwambia Rais Kikwete na wenzake
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) Mheshimiwa Ban Ki Moon amesema kuwa dunia ina imani kubwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete na wajumbe wengine wa Jopo la Watu Maarufu Duniani waliopewa jukumu la kutafuta jinsi dunia inavyoweza kukabiliana na magonjwa ya milipuko, kama vile Ebola, katika siku zijazo kuja na mapendekezo yao yanayolenga kuifanya dunia mahali bora zaidi pa kuishi.
Aidha, Mheshimiwa Ban Ki Moon amewaambia wajumbe hao kuwa uteuzi wao uliofanywa na yeye mwenyewe mwezi uliopita na umefanyika baada ya majina yao kuwa yamependekezwa na taasisi nyingine za kimataifa, mbali na Umoja wa Mataifa.
Mheshimiwa Ban Ki Moon ameyasema hayo, Jumatatu, Mei 4, 2015, wakati alipokutana na kuzungumza na wajumbe wa Jopo hilo ofisini kwake katika Makao Makuu ya UN mjini New York, muda mfupi kabla ya wajumbe hao kufanya kikao chao cha kwanza chini ya uenyekiti wa Rais Kikwete.
Akizungumza na wajumbe hao, Mheshimiwa Katibu Mkuu wa UN amesema kuwa dunia ina imani kubwa kuwa Jopo hilo litaweza kupendekeza njia bora zaidi za kukabiliana na magonjwa ya milipuko duniani kwa namna bora zaidi kuliko ilivyokuwa kwa mlipuko wa ugonjwa wa Ebola.
“Nawashukuru sana kwa kukubali uteuzi wangu. Dunia ina imani kubwa na uwezo wenu katika kutuwezesha sote kukabiliana kwa kujiamini zaidi na magonjwa ya milipuko katika siku zijazo,” Mheshimiwa Ban Ki Moon amewaambia wajumbe hao sita ambao wamepewa hadi Desemba mwaka huu kuwasilisha Ripoti kuhusu namna gani dunia inavyoweza kukabiliana vizuri zaidi na magonjwa ya milipuko.
Mbali na Rais Kikwete ambaye ni Mwenyekiti wa Jopo hilo, wajumbe wengine ni Bwana Celso Amorim wa Brazil, Bi. Micheline Calmy-Rey wa Uswisi, Bwana Marty Natalegwa wa Indonesia, Bi. Joy Phumaphi wa Botswana na Bwana Rajiv Shah wa Marekani.
Kuhusu uteuzi wao, Mheshimiwa Ban Ki Moon amesema kuwa uteuzi huo ulifanywa na yeye baada ya kushauriana na taasisi mbalimbali duniani na kukubaliana kuhusu uwezo wa Jopo hilo kuifanya kazi hiyo.
“Tunaweza kusema kuwa uteuzi huo umefanywa kwa pamoja na taasisi mbalimbali duniani – Umoja wa Mataifa, Benki ya Dunia na Shirika la Afya Duniani (WHO). Kwa hakika hii inaonyesha ni kiasi gani dunia ina imani nanyi katika uwezo wa kuifanya kazi hii,” amesema Mheshimiwa Ban Ki Moon.
Rais Kikwete amemshukuru Mheshimiwa Ban Ki Moon kwa uteuzi wa Jopo hilo akisisitiza kuwa uteuzi huo unaonyesha ni kiasi gani UN ina imani katika uwezo wa wajumbe wa Jopo kuifanya kazi hiyo vizuri.
Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
5 Mei, 2015
Taarifa kwa vyombo vya habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, amemteua Balozi Liberata Rutageruka Mulamula kuwa Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa. Kwa sasa Balozi Mulamula ni Balozi wa Tanzania nchini Marekani na Mexico.
Rais Kikwete pia amemteua Balozi Hassan Simba Yahya kuwa naibu Katibu Mkuu katika Wizara hiyo ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa. Kwa sasa Balozi Yahya ni Mkurugenzi wa Idara ya Mashariki ya Kati Wizarani hapo.
Uteuzi huu umeanza tarehe 2 Mei, 2015
…………Mwisho…………
Imetolewa ;
Premi Kibanga,
Mwandishi wa Habari wa Rais Msaidizi,
Ikulu - Dar es Salaam.
4 Mei, 2015
Taarifa kwa vyombo vya habari
Big day for Kikwete as he chairs first UN High-Level Panel in New York
President Jakaya Mrisho Kikwete is having his big day in New York today, Monday, May 4, 2015, chairing his first meeting of United Nations Secretary-General’s High Level Panel on the Global Response to Health Crises.
The meeting is taking place at the Office of the Secretariat of the United Nations Secretary General’s High – Level Panel on the Global Response to Health Crises Conference Room on the North Lawn Building of the UN headquarters, where a temporary office has been set aside for President Kikwete.
The President who arrived in New York this morning after a long travel from Dar es Salaam, will chair this first meeting of the Panel for the next four days following the decision by United Nations Secretary-General, Ban Ki Moon, to appoint an independent High-Level Panel on the Global Response to Health Crises last month.
Other members of the panel include Mr. Celso Luiz Nunes Amorimo, former Minister of Foreign Relations (1993-1994 and 2003-2010) and Defence Minister of Brazil; Ms. Micheline Calmy-Rey, former President of the Swiss Confederation and Mr. Marty Natalegawa, former Foreign Minister of Indonesia and its Permanent Representative to the United Nations in New York.
Others are Ms. Joy Phumaphi, Excecutive Secretary of the African Leaders Malaria Alliance and Botswana’s former Minister for Health and Minister for Lands and Housing and Mr. Rajiv Shah, until January this year, Administrator of the United States Agency for International Development (USAID).
Panel members, appointed in the individual capacity, have been tasked by the UN Secretary General to make recommendations on how to strengthen national and international systems to prevent and manage future health crises taking into account lessons learned from the response to the outbreak of Ebola virus disease.
The Secretary-General decided to appoint the Panel following the outbreak of Ebola virus disease in West Africa, which escalated to become one of the largest global public heath crises in recent history, claiming thousands of lives and sickening many more with the devastating social-economic impacts. The spread of the disease in the epicentre countries of Guinea, Liberia and Sierra Leone has highlighted the importance and urgency of strengthening the architecture and management of global heath crises in order to better address future outbreaks.
Before their first meeting, Panel members were meeting Secretary General Ban Ki Moon, who has asked the panel to submit periodic progress reports and present its final report to the UN Secretary General at the end of December, this year, 2015. The Secretary General will then make the report available to the General Assembly, and undertake further action as appropriate.
In carrying out its work, the Panel will undertake a wide range of consultations, including with representatives from the affected areas and communities, the UN system, multilateral and bilateral financial institutions and regional development banks, non-government organizations, countries supporting the response effort, other Member States, health care providers, academic and research institutions, private sector and other experts.
The United Nations is providing a small secretariat for the Panel and the Panel can also draw on the Resource Group of senior and leading experts, which is to provide specialized advice to the Panel on technical and other issues as required.
Following this first meeting, the Panel will set out its working methods and programme of work, in consultation with the UN Secretary –General. The Panel is expected to hold a meeting every six weeks, with three meetings taking place in New York, one at UN offices in Switzerland, one at the African Union headquarters in Addis Ababa and one field meeting in the Ebola affected countries of Guinea, Liberia and Sierra Leone.
Issued by:
Directorate of Communications, State House,
Dar es Salaam
4th May, 2015
Taarifa kwa vyombo vya habari
Rais Kikwete aanza jukumu la kimataifa la kihistoria
- Aaanza kuongoza kikao cha kutafuta majawabu ya dunia kuhusu athari za magonjwa ya milipuko
- Akutana na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na wajumbe wa Jopo lake la Watu Maarufu Duniani
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ameanza kazi nzito leo, Jumatatu, Mei 4, 2015, mjini New York, kwa kuongoza Kikao cha Kwanza cha Mkutano wa Jopo la Watu Maarufu Duniani (High-Level Panel on the Global Response to Health Crises) lililoteuliwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kutafuta njia za kukabiliana na balaa la magonjwa ya milipuko katika miaka ijayo.
Mkutano huo wa kwanza wa Jopo hilo unafanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi za Sekretariati ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ya Jopo la Watu Maarufu Duniani kwenye Jumba la North Lawn Building katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa ambako Rais Kikwete atakuwa na ofisi zake za muda wakati anaongoza Jopo hilo.
Rais Kikwete ambaye amewasili New York asubuhi ya leo, Jumatatu, Mei 4, 2015 baada ya safari ndefu kutoka Dar es Salaam, ataendesha kikao cha Jopo hilo kwa siku nne mfululizo kufuatia uamuzi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Mheshimiwa Ban Ki Mooon, mwezi uliopita wa kuteua Jopo la Watu Wanaojitegemea na Maarufu Duniani kuunda Jopo la kutafuta njia ya kukabiliana na balaa la magonjwa ya milipuko katika miaka ijayo.
Wajumbe wengine wa Jopo hilo ni pamoja na Bwana Celso Luiz Nunes Amorimo, Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje (1993-1994 na 2003-2010) na Waziri wa zamani wa Ulinzi wa Brazil; Bi. Micheline Calmy-Rey, Rais wa zamani wa Muungano wa Uswisi na Bwana Marty Natalegawa, Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje na Mwakilishi wa Kudumu wa Indonesia katika Umoja wa Mataifa, mjini New York.
Wengine ni Bi. Joy Phumaphi, Katibu Mtendaji wa Taasisi ya Viongozi wa Afrika Kukabiliana na Malaria ya African Leaders Malaria Alliance na Waziri wa zamani wa Afya na Waziri wa Ardhi na Nyumba wa Botswana na Bwana Rajiv Shah, ambaye mpaka Januari mwaka huu alikuwa Mkuu wa Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani (USAID).
Wajumbe wa Jopo ambao wameteuliwa katika nafsi na uwezo wao wenyewe, wametakiwa na Katibu Mkuu Ban Ki Moon kutoa mapendekezo ya jinsi ya kuimarisha mifumo ya kitaifa na kimataifa ili kuzuia ama kuipa dunia uwezo zaidi wa kudhibiti mabalaa ya magonjwa ya milipuko katika siku zijazo kwa kutilia maanani mafunzo yaliyotokana na mlipuko wa Ebola.
Kwa hakika, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa aliteua Jopo hilo kufuatia mlipuko wa Ebola katika Afrika Magharibi, ambao haraka haraka ulitokea kuwa mmoja wa milipuko hatari zaidi duniani kwa afya ya umma katika historia ya dunia, ukisababisha ugonjwa kwa maelfu ya watu na kusababisha matatizo makubwa ya kijamii na kiuchumi. Kusambaa kwa ugonjwa huo katika Guinea, Liberia na Sierra Leone kumethibitisha umuhimu na uharaka wa kuimarisha mfumo na menejimenti ya mabalaa ya magonjwa ya mlipuko duniani, ili kuweza kukabiliana vizuri zaidi na milipuko ya namna hiyo katika siku zijazo.
Kabla ya kuanza kikao chao, Wajumbe wa Jopo wamekutana na kufanya mazungumzo na Katibu Mkuu Ban Ki Moon, ambaye tayari amewaomba kuwa wanatoa ripoti za mara kwa mara kuhusu kazi yao na hatimaye kutoa Ripoti ya Mwisho Desemba mwaka huu, 2015. Katibu Mkuu ataiwasilisha Ripoti hiyo kwenye Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwishoni mwa Desemba mwaka huu. Aidha, maamuzi mwafaka yatachukuliwa kutokana na mapendekezo ya Jopo hilo.
Katika kufanya kazi yake, Jopo litawasilisha na makundi mbali mbali ya watu, wakiwemo wawakilishi wa nchi na jamii zilizoathiriwa na Ebola, mifumo ya Umoja wa Mataifa, taasisi za fedha za kimataifa na kitaifa, taasisi za benki za maendeleo za kikanda, mashirika yasiyokuwa ya kimataifa, nchi zilizounga mkono mapambano dhidi ya Ebola, wafanyakazi wa afya, taasisi za kisomi na kitafiti, nchi nyingine wanachama wa UN, sekta binafsi na wataalam wengine.
Umoja wa Mataifa umetoa sekretarieti kwa ajili ya kusaidia kazi ya Jopo, ambalo pia lina uhuru wa kuwasilisha na kukutana na wataalam waandamizi wa kundi la Wataalam la Umoja wa Mataifa, ambalo hutoa ushauri wa kiufundi na masuala mengine kulingana na mahitaji ya Jopo.
Kufuatia mkutano huo wa kwanza, Jopo sasa linaweka mikakati ya namna ya kufanya kazi na mpango wa kazi kwa kushauriana na Katibu Mkuu. Jopo linatarajiwa kukutana kila baada ya wiki sita, mikutano mitatu ikiwa inafanyika New York, mmoja kwenye Ofisi za UN nchini Uswisi, mmoja kwenye Makao Makuu ya Umoja wa Afrika (AU) mjini Addis Ababa, Ethiopia na safari moja katika nchi zilizoathiriwa na Ebola za Guinea, Liberia na Sierra Leone.
Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
4 Mei, 2015
Taarifa kwa vyombo vya habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amemteua Ndugu Pius Msekwa kuwa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi.
Rais pia amemteua ndugu Daudi Rukiko Mayeji kuwa Mkurugenzi wa Jiji la Tanga. Kabla ya uteuzi huu, ndugu Mayeji alikuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilindi , Mkoani Tanga.
Uteuzi wa Ndugu Msekwa na wa Ndugu Mayeji umeanza tarehe 2 Mei, 2015
…….. Mwisho ……...
Imetolewa na;
Premi Kibanga,
Mwandishi wa habari wa Rais Msaidizi,
Ikulu – Dar es Salaam.
4 Mei, 2015
Taarifa kwa vyombo vya habari
Rais wa Jamhuri ya Muugano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amewateua Majaji wawili wa Mahakama Kuu ya Tanzania kuwa Majaji wa Mahakama ya Rufani. Taarifa iliyotolewa Dar es Salaam, Alhamisi, Aprili 30, 2015 na Ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi (KMK) imesema, uteuzi huu ulianza Jumamosi iliyopita, Aprili 24, 2015.
Taarifa hiyo imewataja Majaji hao kuwa ni Jaji Augustine Gherabast Mwarija na Jaji Stella Ester Augustine Mugasha, ambao wote wamekuwa Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania tokea walipoteuliwa Novemba 28, 2006.
Kabla ya uteuzi wake, Jaji Mwarija alikuwa Jaji Mfawadhi, Kitengo cha Biashara, Mahakama Kuu, Dar es Salaam. Kabla ya kuwa Jaji wa Mahakama Kuu alikuwa Msajili wa Mahakama ya Rufani kati ya mwaka 2003 na 2006.
Aliajiriwa kama Hakimu Mkazi Daraja la Tatu Februari 2, mwaka 1987, baada ya kupata Shahada ya Sheria mwaka 1986.
Naye Jaji Mugasha, kabla ya uteuzi wake, alikuwa Jaji Mfawidhi, Dar es Salaam. Alikuwa Jaji Mfawidhi, Mahakama Kuu, Kanda ya Arusha na awali Kanda ya Moshi tangu 2009 hadi alipohamishiwa Mahakama Kuu, Dar es Salaam.
Aliajiriwa kama Wakili wa Serikali mwaka 1983 baada ya kupata Shahada ya Sheria mwaka huo huo, 1983.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
30 Aprili, 2015
Taarifa kwa vyombo vya habari
Dangote amwambia Rais Kikwete: Tuko tayari kuzalisha saruji sasa
Tajiri mkubwa kuliko wote katika Afrika na mzalishaji mkubwa zaidi wa saruji barani, Bwana Aliko Dangote amemwambia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete kuwa ujenzi wa kiwanda cha saruji kikubwa kuliko vyote Tanzania unakamilika na kuwa Rais ataombwa kukifungua Agosti mwaka huu.
Bwana Dangote, raia wa Nigeria, alikutana na Rais Kikwete, Alhamisi, Aprili 30, 2015, Ikulu, mjini Dar es Salaam ambako tajiri huyo alikuwa amekuja kumweleza Rais Kikwete kuhusu maendeleo ya ujenzi wa kiwanda hicho kinachojengwa mjini Mtwara.
“Nimekuja kukujulisha Mheshimiwa Rais kuwa kazi yetu inakwenda vizuri na tutaanza uzalishaji wa saruji kwenye kiwanda chetu mjini Mtwara kuanzia Agosti mwaka huu, katika muda wa miezi miwili hivi ijayo. Wakati huo tutakuwa tayari kukuomba uje kutufungulia kiwanda chetu hiki,” Bwana Dangote alimwambia Rais Kikwete ambaye naye amekubali kufungua kiwanda.
Kiwanda hicho cha saruji kitakuwa kiwanda kikubwa zaidi kuliko kingine cha saruji chochote nchini. Kwa kuanzia kiwanda hicho kitakuwa na uwezo wa kuzalisha tani milioni tatu kwa mwaka, kiwango ambacho ni sawa na saruji inayozalishwa sasa na viwanda vyote vya sasa nchini.Kiwanda hicho kitakuwa na uwezo wa kuongeza uzalishaji hadi kufikia tani milioni tano kwa mwaka.
Baada ya kuwa amesikiliza, Rais Kikwete alimwuliza Bwana Dangote: “Je tunakuhudumia vizuri katika uwekezaji wako? Nini zaidi unataka tukufanyie?”
Bwana Dangote alisema kuwa bado shughuli zao zinakabiliwa na changamoto katika maeneo kadhaa ikiwa ni pamoja na jinsi ya kupata mawe ya mkaa kutoka Kiwanda cha Makaa ya Mawe cha Ngaka, mkoani Ruvuma, upatikanaji wa uhakika zaidi wa gesiasilia kwa ajili ya uzalishaji na upatikanaji wa madini aina ya gypsum kwa ajili ya uzalishaji.
Rais Kikwete ametoa maelekezo ya jinsi ya kutatua changamoto hizo kwa maofisa mbali mbali wa Serikali ambao walihudhuria mazungumzo hayo, akimwahidi mwekezaji huyo kuwa Serikali yake itahakikisha inatatua matatizo yote hayo, ili kukiwezesha kiwanda kuanza uzalishaji.
Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
2 Mei, 2015
Taarifa kwa vyombo vya habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, leo Jumanne, Aprili 28, 2014, amekuwa Mtanzania wa kwanza kuvuka rasmi Bahari ya Hindi kwa gari kwenda Kigamboni akitokea mjini Dar es Salaam.
Msafara wa Rais Kikwete ulivuka eneo hilo la maji kwa kutumia daraja la muda ambalo wahandisi wa ujenzi wa Kampuni ya China wanalitumia kwa ajili ya kujenga daraja kubwa na la kudumu na la kwanza la aina ya pekee katika eneo hilo.
Rais Kikwete alikuwa anakwenda na kurudi kutoka Kigamboni, ambako amekamisheni na kuruhusu kuanza kutumika kwa melivita mbili za Kamandi ya Maji ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania katika Kituo Kikuu cha Jeshi la Maji kilichopo eneo la Kigamboni.
Mwisho.
Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
28 Aprili,2015
Taarifa kwa vyombo vya habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, leo Jumanne, Aprili 28, 2015, ametoa kamisheni na kuruhusu kuanza kutumika kwa Melitiva mbili kwa ajili ya ulinzi wa pwani ya Tanzania.
Rais Kikwete ametoa kamisheni hiyo na kuruhusu kuanza kutumika kwa meli hizo, Melivita P77 Tanzania Navy Ship Mwitongo na Melivita P78 Tanzania Navy Ship Msoga katika Sherehe ya Utoaji Kamisheni iliyofanyika Makao Makuu ya Kamandi ya Jeshi la Maji la Tanzania Navy Base, Kigamboni, mjini Dar es Salaam.
Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi (CDF) Jenerali Davis Mwamunyange na Balozi wa China katika Tanzania, Balozi Lu Youching walikuwa miongoni mwa waliohudhuria sherehe hizo pamoja na wawakilishi wa kijiji cha Mwitongo, Butiama Mkoani Mara na Kijiji cha Msoga, Wilaya ya Bagamoyo, Mkoa wa Pwani ambavyo majina yake yametolewa kwa meli hizo mbili.
Akizungumza katika sherehe hizo, Jenerali Mwamunyange amesema uongozi wa Jeshi umeamua kuziita meli hizo mbili kubwa zaidi za kivita zilizopata kununuliwa nchini majina ya vijiji walikozaliwa viongozi wakuu wawili wa Tanzania, Mwalimu Nyerere na Rais Kikwete.
Rais Kikwete ameambiwa katika shehere hizo kuwa meli hizo kutoka Jamhuri ya Watu wa China, zitaongeza kwa kiwango kikubwa uwezo wa JWTZ kulinda mpaka wake ulioko katika Bahari ya Hindi na kuweza kukabiliana zaidi na vitendo vya uharifu, ugaidi na kulinda vizuri zaidi shughuli za utafutaji gesi na mafuta katika pwani hiyo ya Tanzania.
Akizungumza kabla ya kutoa kamisheni kwa meli hizo, Rais Kikwete ameishukuru Jamhuri ya Watu wa China kwa kuendelea kuiunga mkono Tanzania katika Nyanja ya kijeshi na Nyanja nyingine nyingi.
“Marafiki zetu wa China wamekuwa nasi kwa muda mrefu, wametuunga mkono tokea kuanzishwa kwa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania tokea Mwaka 1964. Kwa upande wa ulinzi wa majini, wamekuwepo tokea Mwaka 1971 walipotusaidia kuanzishwa kituo hiki cha Tanzania Naval Base hapa Kigamboni na kutoa boti 13 za ulinzi.”
Ameongeza Rais Kikwete: “Wamesaidia vifaa, wamesaidia utaalam na wataalam, wametoa mafunzo katika Chuo chetu cha Ubaharia cha hapa hapa. Kwa hakika hakuna marafiki kama wenzetu wa China, wananchi wake na Serikali yake kwa sababu wamesaidia sana maendeleo ya Jeshi letu. Karibuni wametusaidia kuanzisha kombania mbili za majeshi maalum ya majini na sasa meli hizi mbili ambazo zina uwezo wa kwenda kasi zaidi, uwezo wa kubeba silaha nyingi na kubwa zaidi na uwezo zaidi wa kulinda mipaka yetu”.
“Wako watu wanasema kuwa vifaa vya jeshi na ulinzi wa nchi yetu ni ghali. Ni kweli. Lakini sasa nani atatulindia nchi yetu? Ni sisi wenyewe na kazi ya ulinzi wa nchi haiweza kuwa kazi rahisi, wala nyepesi, wala isiyokuwa na gharama.”
Akifafanua hali ilivyo katika Pwani ya Tanzania, Rais Kikwete amesema: ”Miaka ya karibuni hapa yaliwahi kutokea majaribio 28 ya kuteka nyara meli katika eneo la maji la Tanzania, matano yalifanikiwa na mengine yakashindikana. Tuna shughuli za utafutaji wa mafuta na gesi, maharamia hufanya jitihada za kuzivuruga, lazima tuzilinde.”
Akitoa kamisheni hiyo, Rais Kikwete amesema: “Kwa kutumia nafasi yangu kama Amiri Jeshi Mkuu, natoa kamisheni na kuruhusu kuanza kutumika kwa melivita P77 Mwitongo na P78 Msoga. Mwenyezi Mungu azibariki melivita hizi pamoja na wafanyakazi wake wote.”
Wakati wa ukaguzi wa meli hizo, Rais Kikwete ameambiwa kuwa kila moja ya meli hizo ina uwezo wa kukaa baharini kwa muda wa siku saba bila kuhitaji kuongeza mafuta wala diseli na bila kuhitaji msaada wa huduma yoyote kwa ajili ya watumishi wake.
Mwisho.
Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
28 Aprili,2015
Taarifa kwa vyombo vya habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete leo, Jumanne, Aprili 28, 2015, amekutana na kufanya mazungumzo ya faragha na Rais wa 42 wa Marekani, Mheshimiwa Bill Clinton ambaye anafanya ziara nchini.
Baada ya mazungumzo hayo, viongozi hao walipata chakula cha mchana cha pamoja kabla ya kiongozi huyo wa Marekani kuondoka Ikulu, Dar es Salaam.
Katika mazungumzo hayo, viongozi hao wawili walizungumzia baadhi ya miradi ambayo inadhaminiwa na kugharimiwa na Taasisi ya Clinton Foundation katika nyanja ya afya na hasa katika maeneo ya utoaji wa dawa za kurefusha maisha kwa watu wanaoishi na virusi vya ukimwi, afya za akina mama na jinsi ya kupunguza vifo vya watoto wadogo chini ya miaka mitano na jitihada za kupambana na malaria, Nyanja ya kilimo hasa uzalishaji wa mbegu kwa wingi na kilimo cha soya.
Mwisho.
Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
28 Aprili,2014
Taarifa kwa vyombo vya habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho amepokea kwa majonzi na simanzi kubwa taarifa za kifo cha mmoja wa watumishi wa miaka mingi wa Serikali, Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (TPDF), Chama cha TANU na Kamati ya Ukombozi ya Umoja wa Africa – Liberation Committee of the African National Unity (OAU), Brigedia Hashim Mbita, kiongozi ambaye Rais Kikwete amemwelezea kama mmoja wa viongozi ambao wameifanyia nchi yetu mengi na kwa miaka mingi.
Rais Kikwete ambaye amepokea taarifa za msiba huo mara ulipotokea asubuhi ya leo, Jumapili, Aprili 26, 2015 wakati alipoingia tu Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, kuongoza maelfu kwa maelfu ya wananchi kuadhimisha miaka 51 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, ameuelezea msiba huo kama msiba wa simanzi kubwa.
“Ni wachache katika nchi yetu wanaoweza kulinganishwa na Mzee Hashim Mbita kwa kiwango cha utumishi uliotukuka, wa miaka mingi na usiokuwa na kasoro. Katika utumishi wa Serikali alipata kuwa Mwandishi wa Habari Mkuu wa Idara ya Habari na pia kuwa Mwandishi wa Habari wa Rais kabla na baadaye kuwa Balozi wa Tanzania katika Zimbabwe. Kazi zote alizifanya kwa ufanisi mkubwa sana,”amesema Rais Kikwete na kuongeza:
“Katika Chama cha TANU alikuwa Katibu Mtendaji wa Chama na katika Jeshi letu makini, Mzee Mbita alipata na kufikia cheo cha Brigedia Jenerali, yote mambo makubwa kweli kweli.”
Ameongeza Rais Kikwete: “Lakini ilikuwa katika nafasi ya Katibu Mtendaji wa Kamati ya Ukombozi ya Umoja wa Afrika ambako Mzee Mbita alikamilisha utumishi wake kwa kusimamia shughuli nzito ya kuwasaidia ndugu zetu Kusini mwa Afrika kwa miaka 20 mfululizo, miongo miwili, na kuweza kupata uhuru wao. Hakuna mpigania uhuru katika Mozambique, katika Zimbabwe, katika Namibia, katika Angola na hatimaye katika Afrika Kusini ukiondoa nchi nyingine kama Cape Verde, asiyejua mchango wa Mzee Mbita. Wote hawa amewatumia vizuri, kwa ufanisi, kama mlezi, kama kiongozi, kama kamanda hadi wakafanikisha kazi ya ukombozi. Huu ni mchango mkubwa kweli kweli.”
Ameongeza Rais: “Kitendo chake cha mwisho cha utumishi, kilikuwa kuongoza shughuli za Mradi wa Hashim Mbita wa Kuweka Kumbukumbu za Harakati za Ukombozi Kusini mwa Afrika na Kuenzi Viongozi Wakuu (Hashim Mbita Project to Honour Outstanding Leaders), kazi ambayo nayo aliifanya kwa uwezo na ufanisi mkubwa na ripoti yake tukaizindua mwaka jana pale Victoria Falls, Zimbabwe wakati wa Mkutano wa Mwaka wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).”
Ilikuwa kwenye Mkutano huo wakati Zimbabwe ilitangaza kumpa Mzee Mbita Nishani ya The Royal Order Munhumutapa yenye kutambua mchango wake katika harakati za ukombozi wa Zimbabwe. Mzee Mbita amekuwa raia wa sita wa kigeni, na wa kwanza asiyekuwa rais, kupata heshima hiyo ya juu kabisa ambayo hutolewa na Taifa la Zimbabwe kwa wageni ambao wamechangia Uhuru wa Zimbabwe.
Viongozi watano wa mwanzo kupata Nishani hiyo, mwaka 2005, walikuwa ni Marais na Viongozi Waanzilishi wa Kundi la Nchi za Frontline States dhidi ya Ukoloni na Ubaguzi wa Rangi, Marehemu Julius Kambarage Nyerere, Mzee Kenneth David Kaunda wa Zambia, Marehemu Sir Seretse Khama wa Botswana, Marehemu Samora Moises Machel wa Mozambique na Marehemu Augustinho Neto wa Angola,
Ameongeza Rais Kikwete: “Mzee Mbita ametibiwa ndani na nje ya nchi na kila alipolazwa hapa nchini nilikwenda kumwona hospitali. Majuzi tu nilikwenda kumwona kwenye Hospitali ya Jeshi letu pale Lugalo na tukazungumza vizuri sikujua itakuwa mara yangu ya mwisho kuzungumza naye. Naungana na familia ya Mzee Mbita katika kuomboleza kifo na msiba wa Mzee wetu huyu. Nawaomba watambue kuwa msiba wa Mzee Mbita ni msiba wetu sote, msiba wa taifa letu ambalo limepoteza busara yake wakati tulipokuwa tunahitaji zaidi.”
Ameongeza Rais: “Tayari nimeagiza Serikali na Jeshi washirikiane na familia ya Mzee Mbita katika kuandaa matanga na mazishi ya Mzee wetu huyu. Wakati tunaendelea na maandalizi, nawaomba wanafamilia wawe na utulivu na subira kwa kadri tunapopitia kipindi hiki kigumu na kwa pamoja tuendelee kumwomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehma kuiweka peponi roho ya Mzee Hashim Mbita. Amin.”
Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
26 Aprili, 2015