Taarifa kwa vyombo vya Habari ya zamani
Taarifa kwa vyombo vya habari
Jopo la Rais Kikwete lakutana na Mkurugenzi Mkuu wa WHO
Jopo la Watu Mashuhuri ambalo linaangalia jinsi gani dunia inavyoweza kujikinga na kukabiliana na majanga ya magonjwa ya milipuko katika siku zijazo chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, Alhamisi, Julai 16, 2015, limeendelea na kazi yake kwa kukutana na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Bi. Margaret Chan, lenye wajibu wa kusimamia sera na shughuli za afya duniani.
Kwa muda wa karibu saa mbili, wajumbe wa Jopo hilo, wamezungumza na Bi. Chan kwenye makao makuu ya WHO mjini Geneva kuhusu hasa jinsi gani WHO lilivyokabiliana na ugonjwa wa Ebola na uwezo wake wa kukabiliana na majanga yajayo duniani.
Wajumbe hao wa Jopo pia wamekutana na kuzungumza na Dkt. Isabelle Nuttall, mkurugenzi wa zamani wa Idara ya Maandalizi dhidi ya magonjwa duniani katika WHO na Dame Barbara Stocking ambaye ametoa ripoti ya awali kuhusu jinsi WHO ilivyojiandaa na kukabiliana na ugonjwa wa Ebola ambao katika miezi mitatu tu mwaka jana uliua watu 11,000 katika Guinea, Liberia na Sierra Leone.
Wajumbe wa Jopo hilo pia wamekutana na kuwaelezea mabalozi wanaowakilisha nchi zao katika Ofisi za Umoja wa Mataifa (UN) na mashirika ya kimataifa mjini Geneva katika makao makuu ya UN mjini humo.
Baadaye jioni, Rais Kikwete amewaongoza wajumbe wa Jopo kuhudhuria mchapalo ambao umeandaliwa kwa heshima yao na Mwakilishi wa Kudumi wa Shirikisho la Uswisi katika Umoja wa Mataifa mjini Geneva, Mheshimiwa Bruno Favel.
Wajumbe wa Jopo hilo lililoteuliwa Aprili 2, mwaka huu, na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) Mheshimiwa Ban Ki Moon na lilianza kazi yake Mei, mwaka huu, katika Makao Makuu ya UN mjini New York, Marekani.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
17 Julai 2015
Taarifa kwa vyombo vya habari
Wakubwa waunga mkono kazi ya Jopo la Rais Kikwete
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa Linalopendekeza Jinsi Dunia inavyoweza kukabiliana na majanga yajayo ya magonjwa ya milipuko, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete , Jumatano, Julai 15, 2015, ameongoza vikao vya Jopo hilo ambalo kazi yake imeungwa mkono na nchi 21 ambazo zilichangia mapambano dhidi ya ugonjwa wa Ebola.
Miongoni mwa mikutano ambayo Rais Kikwete ameiongoza katika Makao ya Umoja wa Mataifa (UN) mjini Geneva ni pamoja na yeye na wanajopo wenzake kutoa maelezo kuhusu maendeleo ya kazi yao kwa nchi ambazo zilichangia mapambano dhidi ya ugonjwa wa Ebola katika nchi za Guinea, Liberia na Sierra Leone.
Nchi hizo ambazo zimeonyesha kuunga mkono kazi ya Jopo hili katika mkutano huo ni Venezuela, Umoja wa Ulaya (EU), Uholanzi, Finland, Shirikisho la Russia (Russian Federation), Norway, China, Ubelgiji, India, Ujerumani, Marekani, Uswisi, Canada, Brazil, Denmark, Uingereza, Israel, Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Umoja wa Afrika (AU), Benki ya Dunia (WB), Jamhuri ya Korea na Japan.
Pamoja na kwamba wajibu mkuu wa Jopo hili siyo kuchunguza ugonjwa wa Ebola na madhara yake, bado ugonjwa huo ni msingi mkuu wa kazi ya Jopo hilo ambalo wajibu wake ni kutumia uzoefu wa Ebola kutoa mapendekezo ya jinsi dunia inavyoweza kukabiliana na majanga ya magonjwa ya milipuko katika siku zijazo.
Ugonjwa wa Ebola ambao ulilipuka katika nchi hizo tatu za Afrika Magharibi mwishoni mwa mwaka 2013 mpaka sasa umeua watu 11,000 katika nchi hizo na kusababisha mshtuko mkubwa duniani.
Hiyo ilikuwa mara ya 24 kwa ugonjwa huo kulipuka katika Afrika tokea ulipolipuka kwa mara ya kwanza mwaka 1976, miaka karibu 40 iliyopita, katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) wakati huo ikiitwa Zaire.
Hata hivyo, katika milipuko ya kwanza 23, ugonjwa huo uliua watu wachache zaidi kuliko mlipuko wa 24.
Jopo hilo limeambiwa kuwa tofauti na matarajio ya dunia kuwa ugonjwa huo ulikuwa unamalizika katika nchi hizo hasa katika Liberia, umeanza kupata kasi tena na nchi hizo tatu zinakisiwa kuwa na wagonjwa karibu 70.
Jopo hilo lenye Wajumbe sita liliteuliwa Aprili, mwaka huu, na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Mheshimiwa Ban Ki Moon na kufanya vikao vyake vya mwanzo Mei, mwaka huu, katika makao makuu ya UN, mjini New York, Marekani.
Mbali na kukutana na nchi zilizochangia mapambano dhidi ya Ebola, Rais Kikwete na Jopo lake limepata nafasi ya kumsikiliza aliyekuwa Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Kanda ya Afrika, wakati ugonjwa huo unalipuka Dkt. Luis Gomes Sambo wa Angola ambaye aliwaeleza wajumbe historia ya ofisi ya kanda hiyo iliyoko mjini Brazzaville, Jamhuri ya Congo, katika kukabiliana na ugonjwa huo.
Aidha, Wajumbe wa Jopo wamemsikiliza Mkurugenzi mpya wa Kanda, Dkt. Matshidizo Rebecca Moeti ambaye amezungumza kwa njia ya mkutanomtandao (teleconference) kutoka mjini Brazzaville. Dkt. Moeti alianza kazi yake Januari Mosi, mwaka huu, 2015.
Vile vile, Wajumbe wa Jopo wamesikiliza jitihada za Jamhuri ya Rwanda kukabiliana na magonjwa ya mlipuko kupitia kwa Waziri wa Afya wa nchi hiyo, Agnes Binagwaho ambaye naye alizungumza kwa mkutanomtandao kutoka Kigali, Rwanda.
Nje ya vikao hivyo, Rais Kikwete amekutana na kufanya mazungumzo na Katibu Mkuu Mstaafu wa UN, Mheshimiwa Kofi Annan. Katika mkutano huo kwenye Hoteli ya Intercontinental, viongozi hao wawili wamezungumzia masuala mbali mbali ya kimataifa, ikiwamo hali ya Burundi.
Rais pia amekutana kwa mazungumzo na Mtendaji Mkuu wa Kituo cha South Centre ambacho kina makao yake mjini Geneva, Dkt. Martin Kohr. Kituo hicho kilianzishwa chini ya uongozi wa Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, kwa nia ya utekelezaji wa Ripoti ya Kamisheni ya Nchi Zinazoendelea (South-South Commission), ambayo iliongozwa na Mwalimu.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
16 Julai, 2015
Taarifa kwa vyombo vya habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa linalochunguza jinsi dunia inavyoweza kujikinga na majanga ya magonjwa ya milipuko katika miaka ijayo, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, aliwasili mjini Geneva, Uswisi, usiku wa jana, Jumanne, Julai 14, 2015, kwa ajili ya kuendesha vikao vya Jopo hilo.
Vikao hivyo vitakuwa ni awamu ya pili kwa Jopo hilo ambalo liliteuliwa Aprili, mwaka huu, 2015 na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Mheshimiwa Ban Ki Moon.
Wajibu mkuu wa Jopo hilo ni kutoa mapendekezo ya kuimarisha mifumo ya kitaifa na kimataifa, ili kuweza kuzuia ama kudhibiti kwa uhakika zaidi majanga ya magonjwa ya milipuko kufuatia balaa la Ebola katika nchi za Liberia, Sierra Leone na Guinea ambalo limeua maelfu kwa maelfu ya watu.
Jopo hilo lilifanya vikao vyake kwa mara ya kwanza Mei, mwaka huu, katika makao makuu ya UN mjini New York, Marekani.
Vikao vya sasa vilivyoanza juzi, Jumatatu, Julai 13, 2015 vitachukua siku tano na vitafanyika kwenye Ofisi za UN na zile za Shirika la Umoja wa Mataifa ya Afya (WHO) mjini Geneva.
Mbali na Mwenyekiti Rais Kikwete, wajumbe wengine wa Jopo hilo ni Bwana Celso Amorim wa Brazil na aliyepata kuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi yake, Bi. Micheline Calmy-Rey ambaye ni Rais wa zamani wa Shirikisho la Uswisi, Narty Natalegawa ambaye alipata kuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Indonesia, Dr. Joy Phamaphi ambaye ni Katibu Mtendaji wa Umoja wa Viongozi wa Afrika katika Mapambano dhidi ya Malaria (ALMA) na waziri wa zamani wa afya wa Botswana na Dr. Rajiv Shah ambaye mpaka majuzi alikuwa Mtendaji Mkuu wa Shirika la Misaada ya Kimataifa la Marekani (USAID).
Hata hivyo, vikao vya sasa vitahudhuriwa na wajumbe wanne badala ya sita. Bwana Shaha atafuatilia vikao vya sasa kwa njia ya mkutanomtandao (tele-conference) na Bwana Natalegawa aliondoka mjini Geneva jana usiku kurejea nyumbani kuwahi sikukuu ya Idd El Fitri.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
15 Julai, 2015
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amewateua wasaidizi wake wawili. Uteuzi huo unaanza mara moja.
Katika uteuzi huo, Rais Kikwete amemteua Bwana Jumaa George Bwando kuwa Mnikulu. Bwana Bwando ni mtumishi wa miaka mingi wa Serikali.
Rais pia amemteua Bwana Martine Shigela kuwa Msaidizi wa Rais (siasa). Bwana Shigela anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Bwana Rajab Luhwavi ambaye karibuni aliteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu wa CCM (Bara)
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
9 Julai, 2015
Taarifa kwa vyombo vya habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amemteua Ndugu Laurean Rugambwa Bwanakunu kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Bohari ya Dawa (MSD).
Taarifa iliyotolewa Dar es salaam leo, Jumatatu, Julai 6, 2015 na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, inasema kuwa uteuzi wa Ndugu Bwanakunu unaanzia Juni 23, mwaka huu, 2015.
Kabla ya uteuzi wake, Ndugu Bwanakunu alikuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Ariel Glaser Paediatric AIDS Healthcare Initiative.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
6 Julai,2015
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete leo, Jumamosi, Julai 4, 2015, amepokea Hati za Utambulisho za Balozi mpya wa Qatar katika Tanzania, Mheshimiwa Abdallah Jassim Mohamed Al-Medady.
Katika mazungumzo na Balozi Al Medady baada ya kupokea hati zake za utambulisho, Ikulu, Dar es Salaam, Rais Kikwete amesema kuwa Tanzania itatafuta kufuata mfano mzuri wa Qatar katika matumizi mazuri ya mapato ya mauzo ya gesiasilia. Qatar ni moja ya nchi zinazoongoza duniani kwa uzalishaji wa gesiasilia.
“Kama kuna ubalozi hapa nchini utakuwa muhimu sana kwetu kwa kadri tunavyojaribu kuanza uzalishaji wa gesiasilia nchini ni ule wa kwako, Mheshimiwa Balozi. Hivyo, usishangae tukipiga hodi kuomba ushauri kuhusu raslimali hii muhimu.”
Rais Kikwete pia ameelezea matumaini yake kuwa Qatar itaendelea kufanya kazi vizuri na Serikali mpya ambayo itaundwa kufuatia Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka huu.
“Baadhi yetu tutakuwa tunastaafu katika miezi michache ijayo na kubakia kama raia wa kawaida. Ni matumaini yangu kuwa mtaendelea kufanya kazi na kuunga mkono Serikali ijayo kama mlivyotufanyia sisi. Tunawashukuru sana.”
Wakati huo huo, Rais Kikwete ameagana na Balozi Nasri Salim Abu Jaish wa Palestina ambaye amemaliza muda wa utumishi wake katika Tanzania.
Balozi Jaish ambaye alipata elimu yake ya juu katika Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam (UDSM) ameishukuru Tanzania kwa kuendelea kuunga mkono jitihada na mapambano ya Wapalestina kudai haki yao ya kuwa na taifa huru na linaloweza kujiendesha kiuchumi na kwa vigezo vingine vyote vya nchi huru.
Naye Rais Kikwete amemwambia Balozi Jaish kuwa msimamo wa Tanzania utaendelea kuwa ule ule kama ulivyoasisiwa mwaka 1967 chini ya uongozi wa Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere kufuatia Vita ya Siku Sita.
Balozi Jaish amemwambia Rais Kikwete kuwa anahamishiwa Addis Ababa, Ethiopia ambako atakuwa Balozi wa Palestina katika Ethiopia na katika Makao Makuu ya Umoja wa Nchi Huru za Afrika (AU).
Vile vile, Rais Kikwete amekutana na kuzungumza na Balozi Martin Aduki, Mjumbe Maalum wa Rais wa Congo Brazzaville, Mheshimiwa Sassou Nguesso.
Miongoni mwa mambo mengine, Mjumbe huyo maalum amewasilisha mwaliko wa kumwomba Rais Kikwete kuhudhuria mkutano maalum wa kujadili maendeleo ya mawasiliano ya digitali katika Afrika ambao utafanyika baadaye mwezi huu mjini Brazzaville. Marais wanane wanatarajiwa kuhudhuria mkutano huo.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
4 Julai, 2015
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete , Ijumaa, Julai 3, 2015, amepokea hati za utambulisho za Balozi wa Argentina katika Tanzania, Bi. Bibiana Lucila Johnes, mwenye makazi yake Nairobi, Kenya.
Katika mazungumzo baada ya kupokea hati hizo, Rais Kikwete amemkaribisha Balozi Johnes katika Tanzania na kuomba balozi asaidie kushawishi wawekezaji wa Argentina katika sekta ya maendeleo ya mifugo na ngozi kuja kuwekeza katika Tanzania.
“Argentina ni gwiji duniani katika sekta ya maendeleo ya mifugo na ngozi na Tanzania inaweza kunufaika sanaa na uwekezaji na utaalamu kutoka kwenu kwa sababu Tanzania ina mifugo mingi ambayo faida yake inaweza kuongezwa sana kwa uwekezaji wa msingi.”
Naye Balozi Johnes amemwambia Rais Kikwete kuwa chini ya mageuzi ya kisera ya Serikali ya Argentina, Bara la Afrika sasa ni eneo la msingi kabisa katika mahusiano ya kitaifa ya Argentina.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
4 Julai, 2015
Taarifa kwa vyombo vya habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amepokea kwa mshtuko na majonzi taarifa ya kifo cha Chifu wa Waluguru, Chifu Kingalu Mwanabanzi ambacho kimetokea asubuhi ya leo, Jumatano, Julai Mosi, 2015 Kitengo cha Moyo cha Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dar es Salaam.
Katika salamu zake kwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mheshimiwa Dkt. Rajabu Lutengwe, Rais Kikwete amesema kuwa amepokea taarifa cha kifo cha Chifu Kingalu kwa mshtuko na majonzi.
”Nimeshtushwa na taarifa za kifo cha Chifu Kingalu ambaye nimejulishwa kuwa kilitokea asubuhi ya leo katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili. Kwa hakika, kifo hiki kimeifanya jamii yetu kupoteza kiongozi aliyeendesha shughuli zake kwa busara kubwa,” amesema Rais Kikwete na kuongeza:
“Binafsi nilimjua Chifu Kingalu katika maisha yake. Alikuwa kiongozi mwenye busara na aliyetetea mila na tamaduni za watu wake. Alikuwa kiongozi mpenda watu na aliyejali sana maslahi na matakwa ya wafuasi wake. Nakutumia wewe Mkuu wa Mkoa wa Morogoro salamu zangu za rambirambi nikikupa pole kwa kuondokewa na mmoja wa viongozi wa kijamii katika eneo lako.”
“Aidha, kupitia kwako nawatumia wananchi wote wa Mkoa wa Morogoro na wanajamii wa Kiluguru kwa kuondokewa na kiongozi wa tamaduni na mila zao. Vile vile, nakuomba unifikishie pole zangu nyingi kwa wanafamilia ambao wamepoteza mhimili wao. Naungana nao katika msiba huu ambao pia ni msiba wangu. Naungana nao pia kumwomba Mwenyezi Mungu aiweke peponi roho ya Marehemu Chifu Kingalu Mwanabanzi. Amina.”
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
1 Julai,2015
Taarifa kwa vyombo vya habari
Rais Kikwete aiomba India kugharamia ujenzi wa reli ya Dar es Salaam
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ameiomba Serikali ya India kukubali kugharamia ujenzi wa reli katika Jiji laDar es Salaam ili kupunguza misongamano mikubwa ya magari na kuongeza usafisi wa usafiri katika Jiji hilo.
Ombi hilo la Serikali ya Tanzania limetolewa na Rais Kikwete asubuhi ya leo, Ijumaa, Juni 19, 2015, wakati alipokutana kwa mazungumzo rasmi na Waziri Mkuu wa India, Mheshimiwa Narendra Modi, ikiwa ni sehemu ya shughuli za Rais Kikwete kwenye ziara yake rasmi ya Kiserikali ya siku nne katika India kwa mwaliko wa Rais wa nchi hiyo, Mheshimiwa Pranad Mukherjee.
Katika mazungumzo hayo, Rais Kikwete amemweleza Waziri Mkuu Modi kuhusu jinsi wingi wa magari ulivyoongeza misongamano mikubwa ya magari na hivyo kupunguza sana ufanisi wa usafiri kwa mamilioni ya wakazi wa Jiji hilo. Inakadiriwa kuwa Mji wa Dar Es Salaam una wakazi zaidi ya milioni nne kwa sasa.
Katika maelezo yake, Rais Kikwete ameiomba Serikali ya Modi kufikiria uwezekano wa kugharamia ujenzi wa reli ya juu ya ardhi (siyo ya chini ya ardhi) kama njia ya uhakika zaidi ya kupunguza misongano.
Rais Kikwete amemwambia Waziri Mkuu kuwa tayari amezungumza na Kampuni ya Infrastructure Leasing and Financial Services (IFLS) ya India ambayo imeonyesha hamu ya kushiriki katika ujenzi wa reli hiyo kwa nia ya kuongeza ufanisi wa usafiri kwa wakazi wa Dar es Salaam.
Jana, Alhamisi, Juni 18, 2015, miongoni mwa watu wengine, Rais Kikwete alifanya mazungumzo na Mwenyekiti wa ILFS, Bwana Ravi Parthasarathy kuhusu ujenzi wa reli hiyo na Mwenyekiti huyo akaonyesha hamu kubwa ya kufanya hivyo ili mradi Serikali ya India ishauriwe na kukubali kugharamia mradi huo.
Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
19 Juni, 2015
Taarifa kwa vyombo vya habari
Serikali ya India imesema kuwa iko tayari kuongeza nafasi na fursa za raslimali fedha na nafasi kwa Tanzania katika maeneo mbalimbali yakiwemo elimu, afya, kilimo, ulinzi na mapambano dhidi ya ugaidi.
Aidha, Serikali ya India imesema kuwa itaanzisha utaratibu ambako Watanzania wanaoomba visa za kuingia India kwa ajili ya matibabu sasa wanaweza kuomba na kupata visa hizo kwa njia ya mtandao (e-visa).
Hatua hizo za Serikali ya India kwa Tanzania zimetangazwa leo, Ijumaa, Juni 19, 2015, wakati Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Mheshimiwa Narendra Modi alipokutana kwa mazungumzo rasmi ya Kiserikali na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ambaye yuko katika ziara rasmi ya siku nne nchini India kwa mwaliko wa Rais Pranab Mukherjee.
Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika Hyderabad, Waziri Mkuu ambaye ndiye kiongozi wa Serikali katika India alisema kuwa Serikali yake iko tayari kupokea na kutafakari maombi mapya ya Tanzania katika maeneo ya ushirikiano wa kijeshi kama Tanzania inahitaji kuimarisha zaidi majeshi yake na shughuli za ulinzi katika dunia ya sasa iliyobadilika sana.
Amesema kuwa India iko tayari kupokea na kutafakari maombi ya ushirikiano wa pamoja katika maeneo ya usalama wa bahari hasa katika kukabiliana na tishio la ugaidi katika Bahari ya Hindi.
Waziri Mkuu pia amesema kuwa India iko tayari kuongeza nafasi za masomo kwa Tanzania na wanafunzi wake. Mpaka sasa, kiasi cha wanafunzi 2,000 wanasoma katika vyuo vikuu na taasisi nyingine za elimu ya juu katika India.
“Tuko tayari kuongeza nafasi za masomo na elimu na katika maeneo mengine ya ujenzi wa uwezo wa Watanzania,” amesema Waziri huyo.
Kuhusu upatikanaji wa visa kwa Watanzania ambao wanataka kuingia katika India kwa ajili ya kupata matibabu, Mheshimiwa Modi amesema kuwa India imekubali kuwa Watanzania wanaotaka huduma za tiba, wataweza kuomba visa kwa kutumia njia ya mitandao na hivyo kupata visa haraka zaidi kuliko sasa.
Mara baada ya mazungumzo hayo, viongozi hao wawili wamehudhuria mkutano na waandishi wa habari ambako wameshuhudia utiaji saini mikataba minane ya ushirikiano kati ya Tanzania na India.
Mapema leo asubuhi, Rais Kikwete alipokelewa rasmi na Rais Mukherjee katika sherehe zilizofanyika kwenye Ikulu ya India ya Rashtrapati Bhavan, sherehe ambayo pia imehudhuriwa na Waziri Mkuu Modi.
Rais Kikwete amepigiwa mizinga 12 na kukagua gwaride kwa heshima yake katika sherehe hiyo iliyochukua kiasi cha dakika 10. Baada ya sherehe hiyo, Rais Kikwete ametembelea Jumba la Kumbukumbu Mahatma Gandhi la Rajghat lililoko mjini New Delhi.
Rais Kikwete pia amekutana kwa mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa India, Mheshimiwa Sashma Swaraj katika mazungumzo yaliyofanyika kwenye Hoteli ya Taj Palace ambako Rais Kikwete na ujumbe wake amefikia.
Rais Kikwete pia amekutana na kufanya mazungumzo na Makamu wa Rais wa India, Mheshimiwa Mohammad Hamid Ansari na Waziri wa Afya na Ustawi wa Familia, Mheshimiwa J.P Nadda.
Baadaye jioni, Rais Kikwete alitarajiwa kuhudhuria dhifa ya kitaifa iliyokuwa inaandaliwa kwa heshima yake na Rais Mukherjee.
Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
19 Juni, 2015
Taarifa kwa vyombo vya habari
Rais Jakaya Mrisho Kikwete ametuma salamu za rambirambi kwa Mkurugenzi wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Bw. Clement Mshana, wafanyakazi wake na waandishi wote kwa ujumla kufuatia kifo cha mtangazaji na mwandishi mwandamizi wa TBC Bi. Florence Dyauli.
“Pokea rambirambi zangu za dhati kwa kuondokewa na mwandishi mwandamizi na mahiri Bi. Florence” Rais amesema
“Mbali na uandishi na utangazaji wake mahiri, Bi. Florence alikua mzalendo wa kweli aliyetumikia taasisi hii ya serikali kwa uadilifu na upendo wa kweli, tutamkumbuka na tutaukosa mchango wake. Ni wajibu wetu kumuombea mapumziko mema kwa mwenyezi Mungu na kumshukuru kwa mchango wake alioutoa kwa moyo wa dhati”. Amesema Rais Kikwete na kuongeza kuwa:
“Hakika Florence tutamkumbuka, nawapa pole wafanyakazi wote wa TBC na waandishi wote kwa kuondokewa na mwenzao katika tasnia ya Habari”. Rais ameongeza.
“Salaam pia ziwafikie ndugu na jamaa wa Bi. Florence ambao msiba huu ni mkubwa sana kwao na unawagusa sana, naelewa machungu waliyonayo na huzuni, hata hivyo kwa pamoja ni wakati wa kuzidi kumuombea Marehemu katika safari yake ya mwisho”. Rais amesema na kuwatakia roho ya subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu kwao.
Bi. Florence ambaye amefariki jana 18 Juni, 2015 jijini Dar-es-Salaam alizaliwa Julai 27, 1961. Bi. Florence alianza kazi katika Radio ya Taifa, Radio Tanzania Dar-es-Salaam (RTD) na baadaye Televisheni ya Taifa (TVT) na kwa sasa TBC .
Mwenyezi Mungu ailaze Roho ya Marehemu mahali pema peponi, Amina.
……………………MWISHO……………………
Imetolewa na:
Premi Kibanga,
Mwandishi wa Habari wa Rais, Msaidizi,
Ikulu-DSM
19 Juni, 2015
Taarifa kwa vyombo vya habari
Kiwanda India chawazawadia wakulima wa Tanzania matrekta 10
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete , Alhamisi, Juni 18, 2015, amepokea matreka makubwa 10 ambayo yametolewa na Kampuni ya New Holland Agriculture ya India kama zawadi kwa mkulima wa Tanzania.
Matreka hayo aina ya TD5.90 yametolewa na Kampuni hiyo baada ya Rais Kikwete akifuatana na Mama Salma Kikwete kutembelea kiwanda hicho cha New Holland Agriculture kilichoko katika eneo la Greater Noida, nje kidogo ya Mji wa New Delhi, mji mkuu wa India, ambako Rais Kikwete anafanya ziara rasmi ya siku nne kwa mwaliko wa Rais Pranad Mukherjee.
Kiwanda hicho ambacho huzalisha matrekta ya kisasa kabisa 58,000 kwa mwaka kimekuwa kinafanya biashara na Tanzania tokea mwaka 2011 wakati kilipouza matrekta 700 kwa Shirika la Biashara la Jeshi la Kujenga Taifa la SUMA JKT. Mpaka mwisho wa mwaka huu, imepangwa kuwa shirika hilo la JKT litanunua matrekta mengine 300 kwa ajili ya kuboresha na kuleta mageuzi katika kilimo cha Tanzania.
Mbali na kuuza matrekta hayo, New Holland Agriculture ambacho soko lake kuu ni nchi za Ulaya na Marekani pia kimefundisha mafundi mchundo 26 kutoka JKT na walimu wa walimu watano tokea mwaka jana, 2014.
Pamoja na kwamba trekta la New Holland lilianza kuzalishwa na Kampuni yake mama ya CNH Industrial mwaka 1895, ilikuwa mwaka 1996 wakati New Holland Agriculture ilipoanzisha kiwanda katika Greater Noida, India. Kiwanda hicho kinamilikiwa kwa asilimia 100 na CNH Industrial.
Kampuni hiyo ya New Holland Agriculture ni moja ya makampuni ambayo yanaongoza dunia kwa kutengeneza vifaa vya kilimo na hasa matrekta ya kulimia na matrekta makubwa ya kuvunia mazao (harvesters).
Kampuni mama ya CNH Industrial ni kampuni kiongozi wa utengenezaji wa vifaa mbali mbali vya viwandani ikiwa inaendesha shughuli zake katika nchi 190 duniani na kutengeneza aina 12 za vifaa katika viwanda 62 na vituo vyake vya utafiti 48, shughuli ambazo kwa pamoja zinaajiri watu 71,000.
Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
19 Juni, 2015
Taarifa kwa vyombo vya habari
Watendaji wakuu makampuni ya India waimwagia sifa Tanzania
Watendaji wakuu wa makampuni makubwa ya India na Wafanyabiashara wengine wa nchi hiyo wameisifia Serikali ya Tanzania na sera zake za kuendeleza viwanda na kuvutia uwekezaji wakieleza utendaji wa Serikali katika eneo hilo kuwa ni wa uwazi mkubwa, wenye urafiki na unaovutia.
Aidha, watendaji wakuu hao wamesema kuwa Tanzania ni nchi nzuri kuwekeza kwa sababu ya amani, utulivu na utawala wa kisheria nchini humo.
Watendaji wakuu na wafanyabiashara hao wametoa pongezi hizo Alhamisi, Juni 18, 2015, wakati walipokutana kwa mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ambaye yuko katika ziara rasmi ya Kiserikali katika India kwa mwaliko wa Rais Pranad Mukherjee.
Katika mkutano huo uliofanyika kwenye Hoteli ya Taj Palace ambako Rais Kikwete ambaye anafuata na Mama Salma Kikwete, ndiko alikofikia, Watendaji wakuu hao, mmoja baada ya mwingine, wamesifia sera za Serikali ya Tanzania kuhusu uwekezaji na urafiki wa watendaji wake kwa wawekezaji.
Mara baada ya Rais Kikwete kutoa hotuba ya kusisimua kuelezea fursa za uwekezaji zinazopatikana katika Tanzania, Mwakilishi wa Kampuni ya airtel, Bwana Shirshirv Priyadarsh amemwambia Rais Kikwete:
“Sisi airtel, tumekuwa katika Tanzania kwa miaka mingi sasa.Tunaamni kuwa kuhusu suala la biashara na uwekezaji, Serikali yako Mheshimiwa Rais inaendeshwa kwa uwazi wa hali ya juu, pengine kuliko nchi nyingine yote ya Afrika.”
“ Kuna mambo makubwa matatu, uchumi wa Tanzania na sera zake za uwekezaji unaendeshwa kwa wazi mkubwa, Serikali na sera zake ni za kirafiki kwa uwekezaji na wawekezaji na pia ni sera zinazovutia mwekezaji yoyote kuwekeza katika uchumi huo.”
Naye Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Huduma za Tibabu ya Appolo amesema kuwa kwa sababu ya urahisi wa kufanya biashara katika Tanzania, kampuni hiyo itafungua mjini Dar Es Salaam, kliniki yake ya kwanza katika Tanzania ili kupunguza mzigo wa Watanzania wanaosaka huduma za tiba kulazimika kusafiri hadi India.
“Hatuna shaka kuwa ni rahisi kuwekeza na kuendesha shughuli katika Tanzania na hivyo katika miezi miwili ijayo, tutakuwa tunafungua kliniki yetu ya kwanza katika Tanzania,”amesema mama huyo ambaye alikuwa miongoni mwa watendaji wakuu wa makampuni 30 ya India kuhudhuria mkutano huo na Rais Kikwete.
Naye mwakilishi wa magari ya Kampuni ya Mahindra amesema kuwa kampuni hiyo imekuwa inaendesha shughuli zake katika Tanzania kwa muda sasa. “Kwa sababu ya kuridhishwa kwetu na sera nzuri za uwekezaji wa Tanzania sasa tunaomba kushirikiana na serikali kujikita kwa nguvu katika utengenezaji matrekta na kufungua viwanda vinavyotegemea mazao ya kilimo katika Tanzania.”
Kampuni ya magari ya Tata ambayo imekuwa katika Tanzania kwa miaka 20 sasa imesema kuwa sasa inataka kuanza kutengeneza mabasi katika Tanzania kwa ajili ya masoko ya Kusini mwa Afrika hasa Zimbabwe na Malawi.
Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
19 Juni, 2015
Taarifa kwa vyombo vya habari
JK: Tunazungumzia zaidi rushwa kwa sababu ya hatua za Serikali
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa Watanzania wamepata uelewa mkubwa wa rushwa na athari zake kwa sababu Serikali imechukua hatua nyingi za kujenga uwezo wa taasisi ambazo zinakabiliana na rushwa katika Tanzania kwa kiasi kikubwa na pia kuweka misingi thabiti ya kisheria ya kukabiliana na jambo hilo.
Aidha, Rais Kikwete amesema kuwa kazi ya kukabiliana haiwezi kuwa ya mtu mmoja, ya Rais pekee kwa kutoa maagizo na maelekezo bali kazi hiyo itafanikiwa vizuri zaidi kama kazi hiyo itafanywa na taasisi ambao zinazidi kuongeweza ukweli kila wakati.
Rais Kikwete alizungumzia suala hilo la rushwa usiku wa Jumatano, Juni 17, 2015, wakati alipokutana na kuzungumza na baadhi ya Watanzania wanaoishi nchini India kwenye Hoteli ya Taj Palace, mjini New Delhi, kwenye siku yake ya kwanza ya ziara yake rasmi ya siku nne nchini India kwa mwaliko wa Rais wa India, Mheshimiwa Pranad Mukherjee.
Akijibu maswali mbali mbali ya Watanzania hao, Rais Kikwete alisema: “ Kuna mwamko mkubwa zaidi kuhusu vita dhidi ya rushwa kwa sababu Serikali imeongeza sana uwezo wa taasisi zinazoongoza mapambano dhidi ya rushwa.”
“Tumeimarisha sana uwezo wa TAKUKURU, tumeongeza sana nguvu ya PPRA, tumepanua uwezo wa Ofisi ya Mthibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na kuhakikisha kuwa ripoti ya CAG inajadiliwa, tena kwa uwazi, ndani ya Bunge. Haya yote yameongeza uelewa na mwamko wa wananchi kupigana kwa nguvu zaidi na rushwa,” amesema Rais Kikwete na kuongeza:
“Kisheria hivyo hivyo taasisi hizo zimeongezewa nguvu. Hata makosa yenyewe ya ulaji rushwa yameongezwa kisheria kutoka manne ya mwaka 2005 hadi kufikia 24. Hili nalo la sheria limeziongezea taasisi zetu nguvu ya kufanya kazi ya kukabiliana na rushwa. Rushwa sasa inatambuliwa kwa urahisi zaidi kuliko zamani.”
Rais pia amesema kuwa ni makosa ya jinai kuwatoza malipo ya huduma mbali mbali nchini kwa fedha za kigeni na hasa dola. “Kwa wageni sasa, wanakuja na dola zao wakitaka kununua bidhaa mbali mbali nchini. Wao kulipa kwa dola ni barabara.”
Aliongeza: “Lakini kwa Watanzania hapana. Hawa wanastahili kulipia huduma mbali mbali kwa sarafu ya Tanzania. Huwezi kumtoza mzazi Mtanzania malipo ya ada ama karo ya mtoto wake katika fedha za kigeni. Lakini kwa mgeni, kwa nini tusimtoze kwa dola?”
Kuhusu ongezeko la ajali nchini, Rais Kikwete alisema kuwa ni kweli ajali zimeongezeka nchini kwa sababu mbali mbali ikiwamo kutokana na ongezeko kubwa la magari katika barabara zetu pamoja na uzembe na ulevi wa madereva.
“Mwaka 2005, Tanzania nzima ilikuwa na magari yaliyokadiriwa kufikia milioni 1.72. Lakini katika miaka 10 tu iliyopita, yameongeka magari 1.5 milioni. Hili ni ongezeko kubwa sana pamoja na jitihada zetu za kujenga na kupanua barabara zetu nchini,” alisema Rais Kikwete na kuongeza:
“Ni kweli tunahitaji kupanua barabara zetu, lakini madereva nao wanachangia sana ajali kwa ulevi na uzembe. Kwetu pale Chalinze, madereva wa malori wanasimamisha magari makubwa kunywa pombe, viroba. Baada ya kulewa kabisa ndiyo wanaingia katika magari yao wakidai kuwa pombe inawaongezea ufanisi wa kuendesha malori. Upuuzi gani huu?”
Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
19 Juni, 2015
Taarifa kwa vyombo vya habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete yuko njiani kwenda India ambako atafanya ziara rasmi ya Kiserikali ya siku nne katika Jamhuri ya India kwa mwaliko wa Rais wa India, Mheshimiwa Pranab Mukherjee. Ziara hiyo, inaanza rasmi jioni ya leo, Jumatano, Juni 17, 2015.
Wakati wa ziara yake, Rais Kikwete ambaye anafuatana na Mama Salma Kikwete, mbali na kukutana na Rais Mukherjee kwa mazungumzo rasmi ya Kiserikali, atakutana kwa mazungumzo na Makamu wa Rais, Mheshimiwa Mohammad Hamid Ansari na Waziri Mkuu Narendra Damordadas Modi, ambaye aliingia madarakani rasmi Mei 26, mwaka jana, 2014 akiwa Waziri wa 15 wa Jamhuri ya India baada ya chama chake cha Bharatiya Janata Party (BJP) kushinda uchaguzi mkuu.
Ziara hii itakuwa ya pili kwa Rais Kikwete kutembelea India katika miaka 10 ya uongozi wake. Mwaka 2008, Rais Kikwete, akiwa Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU), alitembelea India ambako alikuwa Mwenyekiti Mwenza wa Mkutano wa Kwanza wa Wakuu wa Nchi za Afrika na India (India-Africa Forum) uliofanyika mjini New Delhi, mji mkuu wa India pamoja na Waziri Mkuu wa India wakati huo, Mheshimiwa Manmohan Singh.
Wakati wa ziara yake, Rais Kikwete atatembelea miji ya New Delhi na Jaypur (Pink City of India) na miongoni mwa shughuli zake ni kukutana na Watanzania ambao wanaishi India, kukutana na wafanyabiashara wakubwa wa India wenye kutaka kuwekeza Tanzania na na kufungua Mkutano wa Kwanza wa Wafanyabiashara wa Tanzania na India (1st Indian-Tanzania Business Forum).
Mbali na wafanyabiashara, kiasi cha wanafunzi 2,500 wa Kitanzania wanasoma katika vyuo vikuu vya India kwa ufadhili wa Serikali za Tanzania na India. Hawa ni mbali na maelfu ya wanafunzi ambao wanajisomesha wenyewe katika vyuo vikuu vya nchi hiyo.
Rais pia atakutana kwa mazungumzo na Mtendaji Mkuu wa Shirika la Ndege la India, Air India, kwa nia ya kulishawishi shirika hilo kuanzisha tena safari za ndege kati ya nchi hizo mbili, atakutana na Mtendaji Mkuu wa Benki ya ICICI, benki kubwa binafsi kuliko zote katika India, ambayo inataka kuingia ubia na Benki ya Posta Tanzania, atakutana na Mkurugenzi wa Kampuni ya Infrastructure Leasing and Financial Services ambayo inataka kujenga barabara ya kisasa kabisa kati ya Dar es Salaam na Chalinze na miradi mikubwa ya maji.
Aidha, Rais Kikwete atakutana na kuzungumza na Mwenyekiti wa Kundi la Makampuni ya Hospitali za Apollo ambayo inataka kujenga hospitali kubwa na ya kisasa Kigamboni, Dar Es Salaam.
Rais Kikwete pia atatembelea kiwanda cha kutengeneza matrekta cha Fiat New Holland ambacho kimekuwa kinashirikiana kwa karibu na Kampuni ya Biashara ya Jeshi la Kujenga Taifa ya SUMA JKT na baadaye kutembelea Shirika la Taifa la Viwanda Vidogo la India.
Rais Kikwete ataungana na Waziri Mkuu Modi kushuhudia utiaji saini wa mikataba minne kati ya Tanzania na India katika maeneo ya utalii, maji na miundombinu.
Ziara ya Rais Kikwete katika India inatoa nafasi ya kuimarisha uhusiano wa kihistoria, wa karibu na wa kirafiki ambao una historia ndefu na ya karne nyingi na ambao uliimarishwa zaidi na uhusiano rasmi ambao ulianzishwa miaka 54 iliyopita. Kimsingi uhusiano huo umejengwa katika misingi ya biashara na mahusiano ya watu kwa watu.
India ndiyo nchi inayofanya biashara kubwa zaidi duniani na Tanzania. Mwaka 2013-14, biashara hiyo ilikadiriwa kufikia dola za Marekani bilioni nne. Mbali na uhusiano wa biashara, Watanzania wengi wamekuwa wanasaka huduma za afya na elimu katika India. Inakadiriwa kuwa tokea mwaka 1999 kiasi cha Watanzania 4,100 wamepata huduma za afya katika hospitali za Apollo pekee.
Inakadiriwa kuwa kuna wananchi kati ya 50,000 na 60,000 wenye asili ya India (PIO’s) ambao wanaishi na kufanya kazi katika Tanzania.
Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
17 Juni, 2015
Taarifa kwa vyombo vya habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa binafsi hana mgombea Urais ambaye anampendelea kwa sababu wagombea wote ni wa kwake na wa chama chake, isipokuwa anayo kura moja tu ambayo ataitumia mwezi ujao wakati wa vikao mbalimbali kuamua nani awe mgombea Urais wa Chama cha Mapinduzi (CCM) katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka huu, 2015.
Aidha, Rais Kikwete amesema kuwa hana tatizo na kujitokeza kwa wagombea wengi wa nafasi ya Urais zamu hii kupitia CCM kwa sababu huwezi kuwazuia watu kugombea nafasi hiyo kwa sababu ni haki yao.
Vile vile, Rais Kikwete amesema kuwa wingi wa wagombea zamu hii ni jambo zuri na ni ushahidi wa kiasi cha uhuru ambao umejengeka katika chama hicho na uthibitisho kuwa uongozi wa Tanzania katika miaka 10 iliyopita umekuwa wa mafanikio.
Rais Kikwete amesema hayo usiku wa kuamkia jana, Jumatatu, Juni 14, 2015 mjini Johannesburg, Afrika Kusini wakati anazungumza na Waziri Mdogo wa Mambo ya Nje wa Marekani anayeongoza Kitengo cha Masuala ya Afrika Bi. Linda Thomas-Greenfield.
Viongozi hao wawili walikuwa wanahudhuria Mkutano wa 25 wa Kawaida wa Nchi Wanachama wa Umoja wa Afrika kwenye Kituo cha Mikutano cha Sandton Covention Centre, Johannesburg, Afrika Kusini uliomalizika jana.
Mwanzoni tu mwa mazungumzo hayo, Bi. Lidsey alimwuliza Rais Kikwete: “Mheshimiwa Rais, je unaye mgombea yoyote ambaye unampendelea miongoni mwa utiriri wa wagombea?”
Rais Kikwete alimjibu: “Sina mgombea ninayempendelea, wagombea wote ni wa kwangu, ni wa Chama changu, isipokuwa ninayo kura moja ambayo kwa mujibu wa taratibu za haki katika Chama chetu nitaitumia katika vikao mbali mbali.”
Kuhusu kile kinachoitwa utiriri wa wagombea, Rais Kikwete amesema kuwa wingi wa wagombea ni jambo zuri kwa CCM. “Hiki ni chama kikubwa. Wingi unatupa nafasi ya kujadili kwa nafasi nani awe mgombea wetu. Isitoshe, tunaona wagombea wengi zamu hii kwa sababu ya wigo mkubwa wa uhuru ambao umejengeka katika nchi yetu katika miaka ya karibuni. Vile vile, wingi wa wagombea unathibitisha mafanikio yetu katika miaka 10 iliyopita kwa sababu tungeshindwa, watu wangeogopa kujitokeza kugombea nafasi hiyo.”
Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
16 Juni, 2015
Taarifa kwa vyombo vya habari
Rais Jakaya Mrisho Kikwete ametuma salamu za rambirambi kwa Waislamu wote nchini na Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA)) kufuatia kifo cha Sheikh Mkuu wa Tanzania Mufti Sheikh Issa Bin Shaaban Simba.
Marehemu Mufti amefariki leo 15/6/2015 asubuhi katika hospitali ya TMJ – DSM alipokuwa amelazwa akisumbuliwa na ugonjwa wa sukari na shinikizo la damu (pressure).
"Kifo kinaleta huzuni, hata hivyo Kifo hakizuiliki, hatuna budi kukikubali na ni wajibu wetu kumuombea Sheikh Mkuu kwa Mola wetu ampe mapumziko ya milele". Rais Kikwete ametuma salamu hizo za rambirambi kupitia kwa Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Sheikh Alhadi Mussa Salum.
"Nawaombea subra wana familia, ndugu, jamaa, waislamu wote na wana jamii kwani Mufti alikua kiongozi katika Jamii yetu'” Rais amesema na kueleza kuwa "Kamwe mchango wake hautasahaulika katika jamii yote kwa Ujumla na hakika sote tutamkumbuka" ameongeza.
Marehemu alijiunga na BAKWATA mwaka 1968 na amekuwa mwalimu wa chuo katika mikoa mbalimbali ya Mwanza, Bukoba na Mwaka 1970 alikuwa Shekhe wa Mkoa wa Shinyanga.
Rais amemuelezea Marehemu Mufti kama mwalimu katika jamii ambaye alikua na uzoefu wa hali ya juu na mwenye kupenda dini yake na kuitumia kwa manufaa ya jamii iliyomzunguka
"Amekua mwalimu imara na mtu wa kutumainiwa na kutegemewa katika uislamu na jamii kwa ujumla, hakika tutamkumbuka siku zote' Rais Kikwete ameongeza.
Shekhe Issa Bin Shaaban Simba alikuwa na uzoefu mkubwa ndani ya BAKWATA na aliwahi kukaimu nafasi ya mufti kwa siku 90, baada ya kifo cha Mufti Hemed mwaka 2002.
Baada ya hapo akasimamia mchakato wa uchaguzi wa Mufti Mkuu na baadaye 2003 akachaguliwa kuwa Mufti Mkuu wa Tanzania.
Mwenyezi Mungu ailaze roho yake pahali pema Peponi, Amina.
..................mwisho..........
Imetolewa na :
Premi Kibanga,
Mwandishi wa Habari wa Rais, Msaidizi,
Ikulu-DSM
15 Juni, 2015
Taarifa kwa vyombo vya habari
Rais Kikwete: Sera ya Nje itabakia ile ile
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa siasa ya nchi za nje na misingi mikuu ya kuongoza mahusiano ya Tanzania na nchi za kigeni hayatabadilika hata baada ya yeye kuondoka madarakani mwanzoni mwa Novemba, mwaka huu, 2015.
Aidha, Rais Kikwete amewahakikishia viongozi wa nchi wanachama wa Umoja wa Afrika (AU) kuwa yeye anaondoka madarakani lakini Tanzania waliyoizoea na kuijua itabakia pale pale na kuwaomba viongozi hao kumpa ushirikiano mkubwa mrithi wake kama walivyompa yeye.
Rais Kikwete ametoa uhakikisho huo mara mbili, Jumapili, Juni 14, 2015, wakati alipohutubia kuwaaga wakuu wenzake wa nchi wanachama wa Umoja wa Afrika (AU) wakati wa Mkutano wa 25 wa Kawaida wa Umoja wa Afrika uliofunguliwa kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Sandton Convention mjini Johannesburg, Afrika Kusini. Wakati wa mkutano ujao wa kawaida wa AU mjini Addis Ababa, Ethiopia, Januari, mwakani, Tanzania itakuwa na Rais mpya, Rais wa Tano.
Aidha, Rais Kikwete amerudia kauli na msimamo huo wa Tanzania wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Somalia, Mheshimiwa Hassan Sheikh Mahmoud ambako kiongozi huyo wa Somalia amemjulisha Rais Kikwete kuwa angependa kutembelea Tanzania baadaye mwaka huu.
Alisema Rais Kikwete kuwa misingi ya siasa za nchi za nje za Tanzania na misingi mikuu ya kuongoza mahusiano yake na nchi za nje yaliwekwa tokea Uhuru na hasa tangu kutungwa wa Sera ya Mambo ya Nje ya Tanzania mwaka 1972 na tokea wakati huo haijapata kubadilika hata kama wamebadilika viongozi mara nne sasa.
“Hatujapata kubadilisha misingi hiyo inayoelekeza kuwa mahusiano yatajengwa kuanzia nchi za jirani, zikifuatiwa na nchi za Afrika, nchi marafiki duniani na nchi nyinginezo.”
“Sina shaka kabisa kuwa misingi ya siasa za nje na misingi mikuu ya uongozi wa nchi yetu itabakia ile ile isipokuwa kama Rais ajaye atatoka chama kingine. Kitakachobadilika ni staili ya uongozi tu lakini misingi ya uongozi itabakia pale pale kwa sababu ni misingi mizuri, ni misingi ya busara ambayo imeongoza nchi yetu vizuri kwa miaka mingi.”
Ameongeza Rais Kikwete: “Ni matumaini yangu kuwa Watanzania tutachagua kiongozi mzuri atakayeendelea kutoa kipaumbele cha juu kwa masuala ya Afrika pamoja na uanachama na ushiriki wetu katika Umoja wa Afrika. Hii ni miongoni mwa misingi mikuu ya Sera ya Mambo ya Nje ya Tanzania tangu uhuru mpaka sasa. Nawaomba mumpe ushirikiano mkubwa kama mlionipatia mimi na hata kuzidi.”
Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
15 Juni, 2015
Taarifa kwa vyombo vya habari
Mafanikio yetu katika AU ni haya – Rais Kikwete
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ameelezea mambo makubwa saba ambayo Tanzania imeyasimamia kwa kusaidiana na nchi nyingine ama kuyaongoza katika miaka 10 wakati yeye alipokuwa Rais.
Amesisitiza kuwa mchango huo wa Tanzania kwa maendeleo ya Afrika umekuwa ni heshima kubwa kwa nchi yake.
Miongoni mwa shughuli hizo ni Tanzania, kama Mwenyekiti wa AU, kusimamia uanzishwaji wa ushirikiano wa kiuchumi kati ya Afrika na nchi za India, Uturuki na Umoja wa Ulaya
Jambo la pili, amesema Rais Kikwete ni kuongoza Operesheni ya Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Afrika kilichomwondoa madarakani Muasi Kanali Mohamed Bakar katika Kisiwa cha Anjouan na hivyo kulinda uhuru na umoja wa Visiwa vya Comoro.
Akiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Wakuu wa Nchi za AU kuhusu Mabadiliko ya Tabia Nchi (2012-2014), Tanzania iliwezesha kubuniwa na kuliwezesha Bara na msimamo kuhusu tabia nchi na mpango wa kuutekeleza – Climate Change Concept Paper and Climate Change Action Plan.
Tanzania pia ilipewa nafasi ya kuwa Mwenyeji wa Mahakama ya Watu na Haki za Binadamu ya AU na Bodi ya Ushauri dhidi ya Rushwa ya Umoja wa Afrika.
Rais Kikwete pia amesema kuwa pamoja na viongozi wengine wa Afrika, Tanzania ilifanikiwa kuanzisha Umoja wa Viongozi wa Afrika wa Kupambana na Malaria na Rais Kikwete mwenyewe kuwa Rais wake wa kwanza.
Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
15 Juni, 2015
Taarifa kwa vyombo vya habari
Watanzania wanaoishi nje ya Nchi wangependa serikali ijayo iendeleze na kudumisha juhudi za kuimarisha uchumi kuanzia pale ambapo Rais Jakaya Mrisho Kikwete ameishia katika utawala wake.
Jumuiya ya Watanzanzia wanaoishi nchini Uholanzi (TANE) wamemueleza Rais Jakaya Mrisho Kikwete katika risala yao iliyosomwa na Makamu Mwenyekiti wa Mpito Bwana Johannes Rwanzo, ambapo Rais amepata fursa ya kuzungumza na Watanzania hao jioni ya tarehe 8 Juni2015, katika Hoteli ya Crowne Plaza, mjini The Hague .
"Tunaomba serikali ijayo iendeleze pale utakapoishia". Amesema Bw. Rwanzo. “Tunajua kuna mambo mengi ambayo labda muda wa awamu mbili hautoshi kuyakamilisha, basi tungeomba mambo haya uweze kuyakabidhi kwenye utawala unaofuata ili waendeleze pale utakapokuwa umefikia" ameongeza.
Bw. Rwanzo ameyataja baadhi ya mambo ambayo yanahitajika kuendelezwa na awamu ijayo kuwa ni pamoja na juhudi za kupambana na umaskini nchini na ujenzi wa miundombinu.
Watanzania hao pia wamemuomba Rais Kikwete kuwa, pamoja na kustaafu, bado wangependa aendelee kutoa msaada kwa wananchi wa Tanzania kwani "Kustaafu sio mwisho wa kusaidia jamii".
Tangu kuingia madarakani, Rais Kikwete amekuwa na utaratibu wa kukutana na Watanzania wanaoishi nje ya Nchi kila anapofanya ziara katika Nchi mbalimbali na kuwaeleza maendeleo ya kisiasa, kiuchumi na kijamii.
Watanzania hao nao wamekuwa na jadi ya kumsomea risala, kumuuliza maswali kwa nia ya kupata ufafanuzi wa masuala muhimu na kumpa Zawadi za aina mbalimbali.
Rais Kikwete yuko katika ziara ya kikazi ya kuishukuru Nchi ya Uholanzi kwa misaada ya kimaendeleo na pia kuiomba iendelee kuisaidia Tanzania ili iweze kukamilisha na kuendeleza juhudi za kujenga na kuimarisha uchumi kwa nia ya kuleta maendeleo Tanzania.
Rais Kikwete amepata fursa ya kuwaeleza Watanzania kuhusu uchaguzi Mkuu ujao ambao ameahidi kuwa utasimamiwa vizuri ili Watanzania wapate nafasi ya kuchagua viongozi wanaowataka.
Rais pia amewaeleza Watanzania kuhusu juhudi mbalimbali za maendeleo ambazo amezifanya katika kipindi cha utawala wake ambazo zimechangia kukua kwa uchumi na Nchi kujijengea uwezo na kujiletea maendeleo.
Rais ametumia fursa hiyo kuelezea jitihada zilizofanyika katika ujenzi wa barabara, elimu, afya, maji na maendeleo katika teknolojia.
Rais Kikwete amemaliza ziara yake katika Nchi za Finland, Sweden na Uholanzi na anatarajia kuondoka Uholanzi tarehe 9 Juni,2015 asubuhi na kuwasili Dar es Salaam jioni.
...........Mwisho..........
Imetolewa na;
Premi Kibanga,
Mwandishi wa Habari wa Rais Msaidizi,
The Haque – Uholanzi.
9 Juni, 2015
Taarifa kwa vyombo vya habari
Rais Jakaya Mrisho Kikwete amezitaka Nchi wahisani kuongeza nguvu katika kusaidia kuendeleza Kilimo nchini Tanzania kwani sekta hiyo ndiyo inayotoa ajira kwa Watanzania wengi zaidi hasa katika maeneo ya vijijini.
Rais Kikwete amesema hayo leo tarehe 8 Juni, 2015, alipofanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Uholanzi Bw. Bert Koenders.
Rais Kikwete yuko nchini Uholanzi kufuatia mwaliko kutoka kwa Mfalme wa Uholanzi , Mfalme Willem-Alexander.Katika ziara yake ya siku 3, Rais Kikwete anatumia nafasi hii kuishukuru Uholanzi kwa misaada ya maendeleo ambayo imekuwa ikiipatia Tanzania na pia kuwaomba wahisani kuendelea kuisaidia Tanzania hata baada ya kipindi chake cha uongozi kumalizika.
"Nasikitika sikuweza kubadilisha na kukuza sekta ya kilimo hivyo watu wengi kuendelea kuwa maskini, ni sekta inayojumuisha watu wengi hivyo inahitaji kupewa msukumo zaidi". Rais amesema na kuongeza kuwa, "Kilimo ni sekta ambayo watu wengi wanaitegemea, lakini haikukua kwa kiwango cha kuridhisha na wala kupewa kipaumbele inavostahili".
Rais ameongeza na kuelezea jinsi sekta zingine zilivokua katika kipindi cha miaka 10 iliyopita. "Pamoja na kuendelea kukua kwa uchumi, bado tunahitaji kuongeza juhudi za kupunguza umaskini na ningependa muendelee kutusaidia hasa katika sekta ya kilimo hata baada ya kuondoka madarakani”.
Rais Kikwete amesema, misaada ya wahisani nchini Tanzania haijapotea kwani juhudi za kukuza uchumi zimefanikiwa kwa kiwango kikubwa ambapo mfumuko wa bei ambao kutokana na msukosuko wa uchumi wa Dunia mwaka 2011 ulifikia asilimia 18.6 na sasa umeshuka hadi asilimia 4.5 nchini Tanzania.
Hata hivyo Rais Kikwete amesema sekta ya Kilimo bado inahitaji msukumo zaidi na kupewa kipaumbele kwa lengo la kupunguza umaskini. "Tunahitaji Kilimo cha kisasa, wakulima kupata mikopo na kujenga maghala" amesema na kusisitiza kuwa hata baada ya kumaliza muda wake wa Urais, ataendelea kuipigania sekta hiyo ili iweze kutoa mchango wake wa kuondosha umaskini wa Watanzania walio wengi.
Waziri Koenders amemuahidi Rais Kikwete kuwa Uholanzi itaendelea kuisaidia Tanzania na kuahidi kuangalia na kufuatilia ombi la Rais Kikwete katika kukuza Kilimo nchini.
Katika mazungumzo yake Mfalme Willem-Alexander na pia Waziri Mkuu Mark Rute, Rais ametoa shukrani kwa misaada ya maendeleo na kuitaka Uholanzi kuendelea kuisaidia Tanzania na pia kuelezea kuhusu uchaguzi ujao ambao Tanzania itachagua Rais wa Awamu ya Tano.
.............Mwisho............
Imetolewa na;
Premi Kibanga,
Mwandishi wa Habari wa Rais Msaidizi,
The Haque-Uholanzi
8 Juni, 2015
Taarifa kwa vyombo vya habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia salamu za rambirambi Rais wa Jamhuri ya Watu wa China, Mheshimiwa Xi Jinping kuombeleza vifo vya zaidi ya watu 400 ambao wamepoteza maisha yao katika ajali ya boti ya kitalii, iliyozama katika Mto wa Yangtze mwanzoni mwa wiki hii.
Meli ya kitalii ya Eastern Star ilizama katika Mto wa Yangtze, karibu na mji wa Jianli, Jimbo la Kati la Hubei, Jumatatu usiku ikiwa na abiria 456 waliokuwa wanafanya safari ya kitalii ya siku 11 kutoka Nanjing kwenda Chongqing. Mpaka usiku wa jana, Ijumaa, Juni 5,2015, miili ya watu 369 ilikwishapatikana, watu 46 walikuwa hawajulikani walipo na 14 walikuwa wameokolewa.
Katika salamu zake za rambirambi, Rais Kikwete amemwambia Rais Jinping: “Nimepokea kwa mshtuko na masikitiko taarifa ya vifo vya mamia ya watu waliopoteza maisha yao katika ajali ya boti ya kitalii ya Eastern Star katika Jimbo la Hubei iliyotokea mwanzoni mwa wiki hii wakiwa katika safari kutoka Nanjing kwenda Chongqing.”
“Kwa hakika, haya ni maafa ya kitaifa. Kwa niaba ya Watanzania wenzangu, Serikali yangu na mimi mwenyewe, nakutumia wewe binafsi, Serikali yako na wananchi wote wa China salamu za dhati ya moyo wangu na naungana nanyi katika kuomboleza tukio hili la huzuni kubwa.”
Ameongeza Rais Kikwete katika salamu zake alizozituma usiku wa jana, Ijumaa, Juni 5, 2015: “Tanzania ikiwa nchi rafiki na China na Watanzania wote wanaungana na wenzao wa China kuwapa pole nyingi wote ambao wamepoteza wapendwa wao katika ajali hiyo.”
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
6 Juni, 2015
Taarifa kwa vyombo vya habari
Nchi ya Sweden imedhamiria kuukuza ushirikiano wake na Tanzania kwa Awamu mpya ambayo itaongeza uwekezaji na biashara zaidi.
Rais na Mtendaji Mkuu wa Muungano wa wafanyabiashara wa Sweden, Business Sweden, Bi Ylva Berg amemueleza Rais Kikwete katika mkutano wa Business Sweden na Rais Kikwete, jana tarehe 5, Juni,2015 katika Kituo cha Biashara (World Trade Centre) jijini Stockholm.
"Tunataka kushirikiana, kufanya biashara na uwekezaji na Tanzania hapa kwenye masuala ya nishati" amesema Bi Berg.
Sweden inachangia dola bilioni 1 katika Mfuko wa Nishati wa Rais Barack Obama wa Marekani maarufu kama Power Africa, ambao unalenga katika kuongeza idadi ya watu wanaotumia umeme barani Afrika.
Mpango huo unaanza kwa Nchi 6 ambazo ni Tanzania, Ethiopia, Ghana, Liberia, Kenya na Nigeria. Katika mkutano huo Rais Kikwete amewaeleza wafanyabiashara hao ambao pia ni wamiliki wa makampuni makubwa ya kimataifa kuwa sekta ya Nishati ni sekta inayokua kwa haraka sana nchini Tanzania.
"Tunahitaji wenza katika kukuza sekta ya Nishati, serikali haiwezi Peke yake". Rais amesema na kuwaeleza mahitaji ya nishati yaliyopo Tanzania na Nchi za jirani.
Rais Kikwete pia amefanya mazungumzo na Waziri wa Nyumba, Maendeleo ya Jiji na Mawasiliano Bw. Mehmet Kaplan, ambaye naye amefuatana na wafanya biashara wakubwa wa Sweden ili kupata picha kamili ya maendeleo na uwekezaji nchini Tanzania.
Rais ameelezea fursa zilizopo na kutoa changamoto kwa wafanyabiashara hao kuja kuwekeza Tanzania ili kuinua uchumi, kukuza ajira na hatimaye kuifanya Tanzania iweze kujitegemea na kuondokana na bajeti tegemezi.
Rais amemaliza ziara yake nchini Sweden kwa kutembelea Chuo cha Afya cha Karolinska ( Karolinska Institute ) ambacho kinashirikiana na Chuo cha Afya Muhimbili kwa zaidi ya miaka 20 sasa ambapo wataalamu wake kwa pamoja wanashirikiana katika shughuli za utafiti katika masuala ya Malaria na HIV.
KI Kama kinavyojulikana, zaidi ni Chuo cha 3 kwa ukubwa nchini Sweden na kinaongoza katika masuala ya utafiti. Mbali na ufadhili na ushirikiano na Muhimbili, KI pia inafanya utafiti kwa kushirikiana na Wizara ya Afya Zanzibar, ambapo juhudi zao kwa pamoja zimeweza kuondosha Malaria Zanzibar.
Rais Kikwete anatarajia kuondoka Usiku wa jana ambapo anatarajia kuanza ziara ya kikazi ya siku 3 nchini Uholanzi.
Imetolewa na;
Premiere Kibanga
Mwandishi wa Habari wa Rais Msaidizi,
Stockholm, Sweden
6 Juni, 2015.
Taarifa kwa vyombo vya habari
Rais mpya ajaye nchini Tanzania anakabiliwa na changamoto kubwa ya kuhakikisha Tanzania itaendelea kubakia kuwa moja kwa kudumisha Umoja wetu na Amani kwani Tanzania inatokana na muungano wa nchi mbili.
Rais Jakaya Kikwete ameyasema hayo jijini Stockholm - Sweden ambapo alikuwa akiongea na watanzania waishio Sweden mara baada ya kuwasili na kuanza ziara ya kikazi ya siku 3, kuanzia tarehe 3 - 5 Juni,2015.
"Hapa tulipofikia lazima kuhakikisha Taifa linakuwa moja, kuna vyama, na makabila mbalimbali, lazima uhakikishe Nchi inabaki moja". Rais amesisitiza.
Watanzania mbalimbali walioko nchini Sweden kwa ajili ya shughuli za kikazi, kimasomo na ambao wanaishi nchini Sweden, walifika kumpokea na kumsalimia Rais Kikwete ambapo pia wamemsomea risala ambayo pamoja na vitu vingine wametaka kujua kuhusu haki yao ya kupiga kura katika uchaguzi Mkuu ujao.
"Swala hili linategemea Tume ya Uchaguzi, likiwekewa utaratibu linawezekana. Taratibu zake hazijawekwa, lakini ninaamini kuwa uchaguzi ujao unakuwa uchaguzi wa mwisho ambao watanzania wanaoishi nje hawapigi kura". Rais amesema.
Rais Kikwete pia ameelezea matumaini yake kuwa Tanzania itapata kiongozi mzuri na kuelezea mafanikio ambayo serikali yake imeyapata na kutumaini kuwa yatadumishwa na kuendelezwa na Rais ajaye.
Mapema akisoma risala ya watanzania, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Watanzania Nchini Sweden Bw. Tengo Kilumanga, amempongeza Rais Kikwete kwa kuridhia na kuonesha nia ya dhati ya kumaliza kipindi cha uongozi wake na kuwa mfano bora katika ukanda wa Afrika Mashariki.
"Tunakupongeza mheshimiwa Rais, viongozi wengi katika Bara la Afrika huwa hawaagi, umefanya kitendo cha kishujaa sana. Viongozi wa Afrika huwa hawaagi kwa sababu siku ya kuondoka madarakani huwa haijulikani". Amesema Bwana Kilumanga. "Hii inaonesha wewe sio Mtu wa kupenda madaraka". Ameongeza.
Hii ni ziara ya kwanza ya Rais Kikwete ya kuaga Nchi wahisani na wenza katika maendeleo na Rais ameanzia Nchi za Nordic kwa sababu ya historia na uhusiano wa Nchi hizi kwa Tanzania tangu kupata Uhuru wake.
Rais Kikwete anaendelea na ziara yake nchini Sweden ambapo anatarajia kufanya mazungumzo na wafanyabiashara na wawekezaji mbalimbali kwa lengo la kuwahamasisha kuja kuwekeza nchini Tanzania.
Imetolewa na;
Premi Kibanga,
Mwandishi wa Habari wa Rais Msaidizi,
Stockholm - Sweden
4 June, 2015
Taarifa kwa vyombo vya habari
Serikali ya Sweden inaridhishwa na kiwango cha maendeleo ya kiuchumi ya Tanzania kwa kipindi cha miaka 10 iliyopita na inadhamiria kuinua ushirikiano baina yake na Tanzania ili kuleta maana zaidi katika maendeleo na kukua kwa uchumi kwa ujumla.
Waziri Mkuu wa Sweden Stefan Lofven amesema hayo jana tarehe 4, Juni, 2015 ofisini kwake alipokutana na Rais Kikwete. "Tumefikia kiwango kingine, tunahitaji kuanzisha awamu mpya ya Uhusiano wetu". Waziri Mkuu Lofven amesema.
Katika mazungumzo yao, viongozi hao wawili wamesema kuna umuhimu wa kuanzisha awamu nyingine ya maendeleo ambayo italeta maana zaidi ambapo Rais Kikwete amesema pamoja na ukweli kuwa uchumi wa Tanzania unakua kwa haraka, bado juhudi za kuondosha umaskini zinahitajika na zitafanikiwa kwa kuelekeza nguvu kwenye kilimo ambacho ndicho kinaajiri na kutegemewa na watanzania wengi zaidi hasa wanaoishi vijijini.
"Tumefikia awamu nyingine na ni awamu nzuri ya kudumisha uhusiano wetu, tunaweza kushirikiana kwenye nishati, kilimo ili kukuza uchumi zaidi". Waziri Mkuu Lofven amemuambia Rais Kikwete na Rais Kikwete akaongeza
"Pamoja na misaada hiyo, awamu nyingine ya uhusiano baina ya Nchi mbili hizi inahitaji pia kuona makampuni ya kutoka Sweden yanawekeza nchini Tanzania na pia kukuza biashara baina ya nchi mbili hizi ili hatimaye Tanzania iweze kujitegemea zaidi na kupunguza kutegemea misaada".
Mapema kabla ya kufanya mazungumzo na Waziri Mkuu Rais Kikwete amekutana na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika La Maendeleo Sweden (SIDA) Bwana Torbjorn Pettersson ambaye amemueleza Rais kuwa; Sweden imeridhishwa na kiwango cha maendeleo na juhudi za kupunguza umaskini nchini Tanzania, Uchumi wa Tanzania umekua kwa wastani wa asilimia 7, katika kipindi cha miaka 10 iliyopita, Pato la Taifa limekua kutoka sola za kimarekani bilioni 14.4 hadi kufikia dola bilioni 49.2 za kimarekani, wakati Pato la Mtu kwa mwaka 2005 lilikuwa dola 375 na mwaka 2014 limekua hadi dola 1038.
Rais Kikwete yuko nchini Sweden kuishukuru serikali ya Sweden na Watu wake kwa msaada wa maendeleo ambao umedumu tangu miaka ya 60. Nchi ya Sweden inaongoza kwa kuipatia Tanzania misaada ya maendeleo na ni kutokana na misaada hiyo Rais Kikwete ameishukuru Sweden kwa kuiwezesha Tanzania kuelekea kuwa Nchi yenye uchumi wa Kati (Middle Income Country) na kufuzu kutoka kundi la Nchi Masikini sana Duniani (Least Developed Country).
Rais Kikwete pia amefanya mazungumzo na Spika wa Bunge la Sweden Bwana Urban Ahlin pamoja na viongozi wa vyama mbalimbali vya siasa nchini Sweden na kuwashukuru kwa misaada ya maendeleo kwa takribani miaka 50 sasa.
Viongozi hao wamempongeza Rais kwa kufanya ziara ya shukrani na kuwaaga kwani ni mara chache kwa viongozi wengi wa Kiafrika kuaga na kuondoka madarakani.
Imetolewa na;
Premi Kibanga,
Mwandishi wa Habari wa Rais Msaidizi
Stockholm - Sweden.
4 June, 2015
Taarifa kwa vyombo vya habari
Serikali ya Sweden inaridhishwa na kiwango cha maendeleo ya kiuchumi ya Tanzania kwa kipindi cha miaka 10 iliyopita na inadhamiria kuinua ushirikiano baina yake na Tanzania ili kuleta maana zaidi katika maendeleo na kukua kwa uchumi kwa ujumla.
Waziri Mkuu wa Sweden Stefan Lofven amesema hayo jana tarehe 4, Juni, 2015 ofisini kwake alipokutana na Rais Kikwete. "Tumefikia kiwango kingine, tunahitaji kuanzisha awamu mpya ya Uhusiano wetu". Waziri Mkuu Lofven amesema.
Katika mazungumzo yao, viongozi hao wawili wamesema kuna umuhimu wa kuanzisha awamu nyingine ya maendeleo ambayo italeta maana zaidi ambapo Rais Kikwete amesema pamoja na ukweli kuwa uchumi wa Tanzania unakua kwa haraka, bado juhudi za kuondosha umaskini zinahitajika na zitafanikiwa kwa kuelekeza nguvu kwenye kilimo ambacho ndicho kinaajiri na kutegemewa na watanzania wengi zaidi hasa wanaoishi vijijini.
"Tumefikia awamu nyingine na ni awamu nzuri ya kudumisha uhusiano wetu, tunaweza kushirikiana kwenye nishati, kilimo ili kukuza uchumi zaidi". Waziri Mkuu Lofven amemuambia Rais Kikwete na Rais Kikwete akaongeza
"Pamoja na misaada hiyo, awamu nyingine ya uhusiano baina ya Nchi mbili hizi inahitaji pia kuona makampuni ya kutoka Sweden yanawekeza nchini Tanzania na pia kukuza biashara baina ya nchi mbili hizi ili hatimaye Tanzania iweze kujitegemea zaidi na kupunguza kutegemea misaada".
Mapema kabla ya kufanya mazungumzo na Waziri Mkuu Rais Kikwete amekutana na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika La Maendeleo Sweden (SIDA) Bwana Torbjorn Pettersson ambaye amemueleza Rais kuwa; Sweden imeridhishwa na kiwango cha maendeleo na juhudi za kupunguza umaskini nchini Tanzania, Uchumi wa Tanzania umekua kwa wastani wa asilimia 7, katika kipindi cha miaka 10 iliyopita, Pato la Taifa limekua kutoka sola za kimarekani bilioni 14.4 hadi kufikia dola bilioni 49.2 za kimarekani, wakati Pato la Mtu kwa mwaka 2005 lilikuwa dola 375 na mwaka 2014 limekua hadi dola 1038.
Rais Kikwete yuko nchini Sweden kuishukuru serikali ya Sweden na Watu wake kwa msaada wa maendeleo ambao umedumu tangu miaka ya 60. Nchi ya Sweden inaongoza kwa kuipatia Tanzania misaada ya maendeleo na ni kutokana na misaada hiyo Rais Kikwete ameishukuru Sweden kwa kuiwezesha Tanzania kuelekea kuwa Nchi yenye uchumi wa Kati (Middle Income Country) na kufuzu kutoka kundi la Nchi Masikini sana Duniani (Least Developed Country).
Rais Kikwete pia amefanya mazungumzo na Spika wa Bunge la Sweden Bwana Urban Ahlin pamoja na viongozi wa vyama mbalimbali vya siasa nchini Sweden na kuwashukuru kwa misaada ya maendeleo kwa takribani miaka 50 sasa.
Viongozi hao wamempongeza Rais kwa kufanya ziara ya shukrani na kuwaaga kwani ni mara chache kwa viongozi wengi wa Kiafrika kuaga na kuondoka madarakani.
Imetolewa na;
Premi Kibanga,
Mwandishi wa Habari wa Rais Msaidizi
Stockholm - Sweden.
5 Juni, 2015
Taarifa kwa vyombo vya habari
Rais mpya ajaye nchini Tanzania anakabiliwa na changamoto kubwa ya kuhakikisha Tanzania itaendelea kubakia kuwa moja kwa kudumisha Umoja wetu na Amani kwani Tanzania inatokana na muungano wa nchi mbili.
Rais Jakaya Kikwete ameyasema hayo jijini Stockholm - Sweden ambapo alikuwa akiongea na watanzania waishio Sweden mara baada ya kuwasili na kuanza ziara ya kikazi ya siku 3, kuanzia tarehe 3 - 5 Juni,2015.
"Hapa tulipofikia lazima kuhakikisha Taifa linakuwa moja, kuna vyama, na makabila mbalimbali, lazima uhakikishe Nchi inabaki moja". Rais amesisitiza.
Watanzania mbalimbali walioko nchini Sweden kwa ajili ya shughuli za kikazi, kimasomo na ambao wanaishi nchini Sweden, walifika kumpokea na kumsalimia Rais Kikwete ambapo pia wamemsomea risala ambayo pamoja na vitu vingine wametaka kujua kuhusu haki yao ya kupiga kura katika uchaguzi Mkuu ujao.
"Swala hili linategemea Tume ya Uchaguzi, likiwekewa utaratibu linawezekana. Taratibu zake hazijawekwa, lakini ninaamini kuwa uchaguzi ujao unakuwa uchaguzi wa mwisho ambao watanzania wanaoishi nje hawapigi kura". Rais amesema.
Rais Kikwete pia ameelezea matumaini yake kuwa Tanzania itapata kiongozi mzuri na kuelezea mafanikio ambayo serikali yake imeyapata na kutumaini kuwa yatadumishwa na kuendelezwa na Rais ajaye.
Mapema akisoma risala ya watanzania, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Watanzania Nchini Sweden Bw. Tengo Kilumanga, amempongeza Rais Kikwete kwa kuridhia na kuonesha nia ya dhati ya kumaliza kipindi cha uongozi wake na kuwa mfano bora katika ukanda wa Afrika Mashariki.
"Tunakupongeza mheshimiwa Rais, viongozi wengi katika Bara la Afrika huwa hawaagi, umefanya kitendo cha kishujaa sana. Viongozi wa Afrika huwa hawaagi kwa sababu siku ya kuondoka madarakani huwa haijulikani". Amesema Bwana Kilumanga. "Hii inaonesha wewe sio Mtu wa kupenda madaraka". Ameongeza.
Hii ni ziara ya kwanza ya Rais Kikwete ya kuaga Nchi wahisani na wenza katika maendeleo na Rais ameanzia Nchi za Nordic kwa sababu ya historia na uhusiano wa Nchi hizi kwa Tanzania tangu kupata Uhuru wake.
Rais Kikwete anaendelea na ziara yake nchini Sweden ambapo anatarajia kufanya mazungumzo na wafanyabiashara na wawekezaji mbalimbali kwa lengo la kuwahamasisha kuja kuwekeza nchini Tanzania.
Imetolewa na;
Premi Kibanga,
Mwandishi wa Habari wa Rais Msaidizi,
Stockholm - Sweden
5 Juni, 2015
Taarifa kwa vyombo vya habari
Uhusiano baina ya Tanzania na Finland ni wa kudumu na utaimarishwa na kutafutiwa namna ya kuukuza zaidi ya hapa ulipo sasa.
Rais Sauli Niinisto wa Finland amemueleza Rais Jakaya Mrisho Kikwete tarehe 2 Juni, Ikulu, jijini Helsinki wakati wa Mazungumzo baina ya viongozi hao.
"Uhusiano wetu ni wa muda mrefu, ni uhusiano ambao umedumu kwa miaka 50, tumekuwa na uhusiano ambao umeleta maendeleo ya kiuchumi kwa Tanzania". Rais Niinisto amesema, na kuongeza kuwa, "Hii inatupa nafasi ya kutafuta mbinu mpya za kuleta maendeleo na kukuza ushirikiano huu zaidi".
Rais Kikwete aliwasili Helsinki tarehe 1 Juni,2015 kwa ziara ya kikazi ya siku 3 ambapo pamoja na mambo mengine ametumia nafasi hiyo kumshukuru Rais Niinisto kwa mwaliko wake ambapo amemuelezea hali ya kisiasa, kiuchumi na kijamii nchini Tanzania.
Rais pia amemueleza mwenyeji wake kuhusu uchaguzi mkuu ujao nchini Tanzania na kuweka bayana kuwa, "Nimekuja kukushukuru pamoja na wananchi wa Finland kwa ujumla kwa mchango na misaada yenu ya maendeleo kwa Tanzania tangu nchi yetu ipate uhuru hadi leo na bado uhusiano wetu upo imara".
Rais Kikwete amesema na kuomba Finland kuendelea kuisaidia Tanzania katika jitihada zake za kukuza uchumi na kuletea watu wake maendeleo. Rais Kikwete pia anatumia ziara hii kuwaaga na kuwashukuru viongozi na washirika wa Tanzania katika maendeleo, ambao wametoa mchango mkubwa na msaada kwa serikali na wananchi wa Tanzania katika kipindi chake cha uongozi.
Rais Kikwete pia amefanya mazungumzo na Wabunge wa Finland ambao ni viongozi wa vyama vya siasa nchini humo, wakiongozwa na Spika wao Bi. Maria Lohela. Bi. Lohela amesema, Rais Kikwete ndiye kiongozi mkubwa wa nje kutembelea na kufanya mazungumzo na Wabunge hao ambao wameshika nyadhifa zao mpya kuanzia mwezi Aprili mwaka huu.
Rais Kikwete amemueleza Spika Lohela kuhusu kuisha kwa muhula wa Bunge la sasa nchini Tanzania ambapo, Spika Lohela amesema bunge la Finland linapenda kuendeleza ushirikiano na Bunge la Tanzania na hivyo kutoa mwaliko kwa wabunge wapya watakaochaguliwa katika uchaguzi wa Oktoba, mwaka huu.
Rais Kikwete pamoja na mambo mengine, ametembelea chuo Kikuu cha Aalto jijini Helsinki ambacho ni chuo cha 3 kwa ukubwa nchini Finland. Chuo cha Aalto kina utaratibu wa kubadilishana wanafunzi na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Rais Kikwete anatarajia kumaliza ziara nchini Finland tarehe 3 Juni,2015 kwa kukutana na kufanya mazungumzo na wafanyabiashara wa sekta mbalimbali kabla ya kuelekea nchini Sweden kuendelea na ziara yake ya kikazi kufuatia mwaliko kutoka kwa Waziri Mkuu wa Sweden Bwana Stefan Lofven.
..........Mwisho...........
Imetolewa na;
Premi Kibanga,
Mwandishi wa Habari wa Rais Msaidizi,
Helsinki - Finland
3 Juni, 2015
Taarifa kwa vyombo vya habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amepokea kwa mshutuko na masikitiko taarifa za kifo cha mbunge wa Jimbo la Ukonga, Dar es Salaam, Mheshimiwa Eugenia Mwaiposya ambaye ameaga dunia usiku wa kuamkia leo, Jumanne, Juni 2, 2015, mjini Dodoma ambako alikuwa anahudhuria Vikao vya Bunge.
Katika salamu zake za rambirambi kwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Anna Makinda, Rais Kikwete amesema: “Nimepokea kwa mshutuko na masikitiko taarifa za kifo cha Mbunge wa Jimbo la Ukonga, Mkoa wa Dar es Salaam, Mheshimiwa Eugenia Mwaiposya ambaye nimejulishwa ameaga dunia mjini Dodoma ambako alikuwa anaendelea kuhudhuria Vikao vya Bunge.”
Amesema Rais Kikwete: “Kwa hakika, taifa letu limepoteza kiongozi muhimu kutokana na kifo hiki. Mbunge Mwaiposya alikuwa mwakilishi hodari na mtetezi wa kuaminika wa wananchi wa Jimbo la Ukonga. Napenda kukutumia wewe Mheshimiwa Spika salamu zangu za rambirambi kwa kupoteza Mbunge mahiri sana. Aidha, kupitia kwako, nawatumia Wabunge wote salamu zangu za rambirambi kwa kuondokewa na mwenzao.”
Ameongeza Rais Kikwete: “Kupitia kwako, Mheshimiwa Spika, napenda pia kutuma salamu zangu kwa wananchi wa Jimbo la Ukonga ambao wamepoteza mwakilishi wao. Mheshimiwa vile vile, napenda kutoa pole nyingi kwa familia, ndugu na jamaa wa Mbunge Mwaiposya kwa kuondokewa na mama na mchangiaji mkubwa katika maisha yao. Wajulishe niko nao katika msiba huu mkubwa. Naelewa uchungu wao katika kipindi hiki na nawaombea subira ili waweze kuvuka kipindi hiki. Naomboleza nao na naungana nao katika kumwomba Mwenyezi Mungu aiweke peponi roho ya Mheshimiwa Eugenia Mwaiposya. Amina.”
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
2 Juni, 2015
Taarifa kwa vyombo vya habari
Rais Kikwete aanza ziara ya nchi tatu Ulaya
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete leo, Jumatatu, Juni Mosi, 2015 ameanza ziara rasmi ya wiki moja katika nchi tatu za Ulaya kwa mwaliko wa viongozi wa nchi hizo.
Rais Kikwete ambaye aliondoka nchini usiku wa jana, Jumapili, Mei 31, 2013 baada ya kumaliza kuendesha Mkutano wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuia ya Afrika Mashariki (EAC) kuhusu Burundi ameanzia ziara yake katika Finland ambako atakaa kwa siku tatu.
Baadaye, Rais Kikwete atatembelea nchi za Sweden na Uholanzi kabla ya kurejea nyumbani.
Katika Finland, Rais Kikwete miongoni mwa mambo mengine kesho Jumanne, Juni 2, 2015, atafanya mazungumzo rasmi ya Kiserikali na Rais wa nchi hiyo na baadaye atatembelea Bunge la nchi hiyo ambako atafanya mazungumzo na Wabunge.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
1 Juni, 2015