Taarifa kwa vyombo vya Habari ya zamani
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt Jakaya Mrisho Kikwete amefanya uteuzi katika Mahakama kama ifuatavyo;
Rais amemteua Bi. Katarina Revocati kuwa Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania (Chief Registrar). Kabla ya uteuzi huu, Bi. Revocati alikuwa Msajili wa Mahakama ya Rufani.
Rais pia amemteua Ndugu John Rugalema Kahyoza kuwa Msajili wa Mahakama ya Rufani na kabla ya uteuzi huu, Ndugu Kahyoza alikuwa Msajili wa Mahakama Kuu.
Mwingine aliyeteuliwa ni Ndugu Ilvin Claud Mugeta ambaye anakuwa Msajili wa Mahakama Kuu. Kabla ya Uteuzi huu ndugu Mugeta alikua Mkurugenzi wa Ukaguzi na Maadili.
Uteuzi huu umeanza tarehe 3 Oktoba, 2015.
MWISHO
Imetolewa na:
Premi Kibanga,
Mwandishi wa Habari wa Rais, Msaidizi
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
19 Oktoba, 2015
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
RAIS – SALAM ZA RAMBI RAMBI – MHE. DEO FILIKUNJOMBE
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ameeleza mshituko wake mkubwa na huzuni yake nyingi, akiomboleza kifo cha Mbunge wa Ludewa, Mkoa wa Njombe, Mheshimiwa Deo Filikunjombe ambaye alifariki katika ajali ya helikopta usiku wa kuamkia Ijumaa, Oktoba 16, 2015 katikati ya Hifadhi ya Wanyamapori ya Selous, Mkoa wa Morogoro.
Katika salamu zake za rambirambi kwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Anna Semamba Makinda, Rais Kikwete amesema “Nimeshtushwa mno na taarifa za kifo cha Mheshimiwa Deo Filikunjombe. Kwa hakika, ni msiba ulionihuzunisha sana.”
Rais Kikwete amemweleza Mama Makinda: “Tumempoteza kijana hodari na mmoja wa wabunge mahiri ambao mchango wao katika Bunge letu tukufu na katika shughuli za uongozi wa nchi yetu na wananchi wake zilikuwa zinajionyesha dhahiri. Ni kifo ambacho kimetuachia pengo kubwa la uongozi na kimetokea wakati bado Bunge lako tukufu, Chama chetu cha CCM na wananchi wa Ludewa walikuwa bado wanahitaji uongozi na mchango wake.”
Ameongeza Rais Kikwete: “Nakutumia wewe Spika wa Bunge letu tukufu salamu zangu za rambirambi na kupitia kwako kwa Wabunge wote kwa kuondokewa na mwenzao. Aidha, kupitia kwako nawatumia wananchi wa Ludewa salamu zangu nyingi za rambirambi kwa kumpoteza Mbunge wao aliyewatumikia vizuri na kwa moyo wote kwa kipindi chote cha miaka 10 ya Ubunge wake.”
“Aidha, nakuomba unifikishie pole zangu nyingi kwa familia ya Mheshimiwa Filikunjombe pamoja na ndugu na marafiki wa familia hiyo. Naelewa machungu ya familia kwa kuondokewa na mhimili wao. Wajulishe Wabunge, wajulishe Wana-Ludewa na ijulishe familia ya Marehemu Filikunjombe kuwa niko nao katika maombolezo ya msiba huu mkubwa kwa sababu msiba wao ni msiba wangu. Napenda pia wajue kuwa naungana nao katika kumwomba Mwenyezi Mungu aiweke pema peponi roho ya Marehemu Deo Filikunjombe. Amen.”
Wakati huo huo, Rais Kikwete Jumamosi asubuhi, Oktoba 17, 2015, aliungana na mamia ya wananchi na waombolezaji kuuaga mwili wa Mheshimiwa Filikunjombe katika shughuli iliyofanyika kwenye Hospitali Kuu ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) Lugalo, mjini Dar es Salaam.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
19 Oktoba, 2015
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais akutananaMjumbeMaalumwaRais Kabila
RaiswaJamhuriyaMuunganowa Tanzania, MheshimiwaJakayaMrishoKikweteJumamosiOktoba 17, 2015, alikutananakufanyamazungumzona Bwana Emmanuel Adrupiako, MshaurinaMjumbeMaalumwaRaiswaJamhuriyaKidemokrasiaya Congo (DRC), Mheshimiwa Joseph Kabila Kabange.
MkutanohuouliofanyikaIkulu, Dar es Salaam, ulichukuakiasi cha nususaanaviongozihaowawiliwalijadilimasualayanayohusuuhusianokatiya Tanzania na DRC napiamasualayanayohusuhalikatikaukandawaAfrikaMasharikina Kati.
Imetolewana:
KurugenziyaMawasilianoyaRais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
19 Oktoba, 2015
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete Alhamisi, Oktoba 15, 2015 ameungana na maelfu kwa maelfu ya wananchi wa Wilaya ya Handeni, Mkoa wa Tanga na wa kutoka nje ya wilaya hiyo kumzika Mheshimiwa Dkt. Abadllah Omari Kigoda, Waziri wa Viwanda na Biashara na Mbunge wa Jimbo la Handeni kwa miaka mingi.
Dkt. Kigoda ambaye alifariki dunia mwanzoni mwa wiki katika Hospitali ya Apollo ya mjini New Delhi, India ambako alikuwa anatibiwa tokea mwezi uliopitwa, amezikwa nyumbani kwake mjini Handeni.
Rais Kikwete ambaye alifuatana na Mama Salma Kikwete amewasili mjini Handeni kwa helikopta saa tisa mchana, akitokea Dodoma ambako amefanya ziara ya kikazi yenye shughuli nyingi ya siku tatu, na akaenda moja kwa moja kujiunga na maelfu kwa maelfu ya waombolezaji kwa ajili ya mazishi ya waziri wake huyo.
Mapema asubuhi ya leo mwili wa Waziri Kigoda uliagwa rasmi kwenye Viwanja vya Karimjee mjini Dar es Salaam katika shughuli ambayo iliongozwa na Makamu wa Rais, Dkt. Mohammed Gharib Bilal kabla ya mwili huo kusafirishwa kwa barabara kupelekwa Handeni.
Dkt. Kigoda ambaye amefariki akiwa na umri wa miaka 62, alizaliwa Novemba 25, mwaka 1953, katika Wilaya ya Korogwe, Mkoa wa Tanga na amekuwa Mbunge wa Jimbo la Handeni tokea mwaka 1995 mfululizo.
Rais Kikwete amerejea mjini Dar es Salaam jioni baada ya kumalizika kwa mazishi hayo.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
16 Oktoba, 2015
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete Alhamisi, Oktoba 15, 2015, amekitumia Chama cha Siasa cha National League for Democracy (NLD) salamu za rambirambi kuomboleza kifo cha Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho, Mheshimiwa Dkt. Emmanuel Makaidi ambaye ameaga dunia katika Hospitali ya Mkoa wa Lindi .
“Nimepokea kwa huzuni na masikitiko taarifa za kifo cha Mwenyekiti wetu wa NLD, Mheshimiwa Emmanuel Makaidi, ambaye nimejulishwa kwa amepoteza maisha mchana wa leo mjini Lindi.”
Amesema Rais Kikwete: “Nawatumieni salamu zangu za rambirambi viongozi wa NLD na wana-NLD wote kwa msiba huu mkubwa ambao umekinyang’anya chama chenu kiongozi mkuu wa miaka mingi.”
Ameongeza: “Kwa hakika, NLD imepoteza mhimili wake. Taifa letu pia limepoteza kiongozi mzuri na shupavu wa siasa katika kipindi ambacho alihitajika zaidi kuliko wakati mwingine wowote. Wakati wote wa maisha yake ameonyesha uongozi wa hali ya juu na uzalendo kwa nchi yake tokea alipokuwa kiongozi hodari wa michezo hadi alipolitumia taifa letu kama Mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba.”
“Naungana nanyi katika maombolezo na pia nawaombeni mnifikisheni pole zangu nyingi kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki wa Dkt. Makaidi kwa kuondokewa na mhimili wa familia na rafiki mzuri. Aidha, naungana nanyi katika kumwomba Mwenyezi Mungu aiweke pema peponi roho ya marehemu Dkt. Emmanuel Makaidi.”
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
16 Oktoba, 2015
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
NDUGU WAHARIRI,
Kilele cha mbio za mwenge wa uhuru , kumbukumbu ya Baba wa Taifa , Mwalimu JULIUS Nyerere na wiki ya vijana Kitaifa,
Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete katika hotuba yake amezungumzia idadi ya watu watliojiandikisha kupiga kura .
Kwa uhakiki ni kuwa wapiga kura 22,751, 292 kwa upande wa Bara na 503,193 waZanzibar.
Hii ndiyo idadi kamili ambayo imo kwenye hotuba ya Mheshimiwa Rais na hii ndiyo idadi kamili kama ilivyotolewa na Tume ya UchaguziTanzania.
Asanteni
Imetolewa na Premi Kibanga,
Mwandishi wa Habari wa Rais, Msaidizi
Dodoma
13 Oct, 2015
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amepokea kwa mshtuko na huzuni nyingi taarifa za kifo cha Waziri wa Viwanda na Biashara, Mheshimiwa Dkt. Abdallah Omari Kigoda ambaye aliaga dunia jana, Jumatatu, Oktoba 12, 2015 katika Hospitali ya Apollo mjini New Delhi, India, ambako alikuwa amelazwa kwa matibabu tokea Septemba 19, mwaka huu. Alikuwa na umri wa miaka 62.
Katika salamu za rambirambi ambazo amemtumia Waziri Mkuu Mheshimiwa Mizengo Peter Kayanza Pinda, Rais Kikwete amesema: “Kwa hakika, nimeshtushwa na kuhuzunishwa mno na taarifa za kifo cha Waziri Kigoda ambacho nimetaarifiwa kuwa kimetokea India ambako alikuwa anapata matibabu tokea mwezi uliopita.”
Ameongeza Rais Kikwete katika salamu zake hizo za rambirambi: “Kama unavyojua, namfahamu vizuri Mheshimiwa Kigoda. Alikuwa Waziri wangu. Nimefanya kazi naye kwa karibu na kwa miaka mingi ndani ya Serikali yetu. Alikuwa mtumishi hodari, mtumishi mwaminifu na mwadilifu kwa wananchi wa Tanzania, na hasa wananchi wa Jimbo la Handeni, ambao aliwawakilisha kwa miaka mingi akiwa Mbunge wao. Tutakosa utumishi wake mahiri sana.”
“Nakutumia wewe Mheshimiwa Pinda, Waziri Mkuu wa nchi yetu salamu za rambirambi za dhati ya moyo wangu kuomboleza kifo cha Mheshimiwa Kigoda. Aidha, kupitia kwako namtumia rambirambi nyingi Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Anna Semamba Makinda na Wabunge wote kwa kuondokewa na mwenzao.”
Ameongeza Rais Kikwete: “Nakuomba pia unifikishe salamu zangu za rambirambi kwa wananchi wa Jimbo na Wilaya ya Handeni ambao wamepoteza Mbunge wao aliyewatumikia kwa ustadi mkubwa kwa miaka mingi. Aliwawakilisha vizuri na kujali sana maslahi yao. “
Amesisitiza Rais Kikwete: “Kupitia kwako, Waziri Mkuu pia naitumia familia, ndugu, jamaa na marafiki wa Mheshimiwa Kigoda kwa kuondokewa na mhimili wa familia na rafiki yao mpenzi. Yajulishe makundi yote hayo kuwa niko nao katika msiba huu mkubwa, uchungu wao ni uchungu wangu na majonzi yao ni majonzi yangu. Nawaombea kwa Mwenyezi Mungu awape subira na nguvu ya uvumilivu katika kipindi hiki kigumu na cha majonzi. Pia naungana nao kumwomba Mwenyezi Mungu aiweke pema peponi roho ya Dkt. Abdallah Omari Kigoda”. Amen.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
13 Oktoba, 2015
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa michezo ya Tanzania inadumaa na kushindwa kuendelea kwa sababu ya uongozi mbaya na viongozi ambao wanajali zaidi vyeo kuliko kuendeleza michezo.
Aidha, Rais Kikwete amesema kuwa sababu kubwa ya pili inayudumaza michezo katika Tanzania ni kushindwa kwa viongozi kukubali ukweli kuwa wanamichezo lazima walelewe na kuanza kupewa mafunzo wakati bado wadogo na wenye umri wa chini.
Rais vile vile amesema kuwa ili kuweka msingi wa ulezi wa wanamichezo bora wa Tanzania, ametoa “ofa” yake ya mwisho kwa wanamichezo kwa kuwajengea Kituo cha Kulea Vipaji vya Watoto Wadogo kilichojengwa eneo la Kidongo Chekundu, Mnazi Mmoja, Dar es Salaam.
Rais Kikwete ameyasema hayo usiku wa kuamkia leo, Jumanne, Oktoba 13, 2015, alipozungumza katika halfa rasmi iliyoandaliwa na wanamichezo wa Tanzania kutambua mengi ambayo kiongozi huyo ameifanyia sekta ya michezo katika miaka 10 ya uongozi wake na kumuaga.
Katika halfa hiyo ambayo msimamizi wake mkuu kilikuwa ni Chama cha Waandishi wa Michezo Tanzania (TASWA) kwenye Ukumbi wa Mlimani City mjini Dar es Salaam, Rais Kikwete ameelezea mapenzi na ushiriki wake katika michezo maishani mwake akisisitiza:
“Kwa rekodi yangu mimi ni mpenzi wa michezo na mwanamichezo. Hivyo nchi yetu isipofanya vizuri katika michezo mbali mbali ni jambo linalonisononesha sana.”
Ameongeza: “Kwa maoni yangu yapo matatizo mawili makubwa katika uendeshaji wa michezo yetu. Tatizo kubwa la kwanza ni viongozi ambao wanaingia katika uongozi wa michezo kwa heshima tu ya kutafuta vyeo na kutunisha CV zao. Wengine wanaitwa wenyeviti, wengine wanaitwa marais. Jambo kubwa hapa siyo kuwa na cheo, isipokuwa ni jambo gani unalifanya kwa kutumia cheo hicho…kwa hakika maelezo ya kwa nini tunaendelea kufanya vibaya katika michezo siyaelewi kabisa mimi.”
Rais Kikwete ametoa mfano wa maamuzi mabaya yanayofanywa na viongozi wa michezo nchini: “Nimesema mimi kuwa Serikali italipia makocha wa michezo. Lakini viongozi wetu wa michezo hata hawaelewi hata maana halisi ya makocha wazuri. Sisi tunaleta makocha wao wanawaondoa. Ukweli ni kwamba ukipata mwalimu mzuri mambo ya michezo yatakwenda vizuri.”
“Hakuna mbadala wa mwalimu mzuri na ndiyo maana Serikali ilisema kuwa italipia makocha. Kama klabu zina walimu wazuri ni dhahiri utapata wachezaji wazuri. Kama huna mwalimu mzuri huwezi kupata timu nzuri…huwezi kuvuna usichopanda.”
Amesisitiza Rais Kikwete: “Matatizo yetu yako kwenye uongozi. Kuna kitu mahali katika uongozi wetu wa michezo hakiendi vizuri. Na hili lazima nyie watu wa michezo mlitafutie majawabu yake. Kazi hiyo haiwezi kuwa ya Rais wa nchi.”
Rais Kikwete ameongeza kuwa tatizo kubwa la pili ni kwamba Tanzania haiwekezi ipasavyo kuendeleza na kulea vipaji vya watoto, tokea wakiwa wadogo. “Klabu zetu hazitaki kuwekeza katika watoto wadogo. Kazi yao ni kupora wachezaji kutoka timu nyingine wakati wote. Mfano mzuri ni jinsi miaka ya 1970, klabu ya Yanga ilivyowekeza katika watoto ambao walikuja kuwa wachezaji hodari sana wa Tanzania.”
Amesema Rais Kikwete: “Nawashukuru kwa kuniaga na kutambua tuliyoyafanya kwa pamoja wakati wa kipindi changu cha uongozi kwenye eneo la michezo. Na mimi nimeamua kutoa “ofa” yangu ya mwisho kwa wanamichezo wa Tanzania kwa kuwajengea Kituo cha kufundisha na kulea vipaji vya watoto wa Tanzania katika michezo mbali mbali”.
Kituo hicho kinachojulikana kama Kikwete Sports Park (KSP) kitafunguliwa rasmi Jumamosi wiki hii, Oktoba 17. Fedha za ujenzi wa Kituo hicho zimetolewa na Kampuni ya Umeme ya Symbion Power na kitaendeshwa na watalaam wa klabu ya soka ya Ligi Kuu ya England, Sunderland ambayo pia itatoa makocha wa soka. NBA ya Marekani itatoa makocha wa mpira wa kikapu.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
13 Oktoba, 2015
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Tutakidhi mahitaji yote ya saruji Tanzania – Alhaj Dangote
- Dangote Group yafungua viwanda vinne Afrika katika miezi minne tu
- Ni katika Tanzania, Ethiopia, Zambia na Cameroon
- Yasema imewekeza Tanzania kwa sababu ya sera nzuri za Serikali na mazingira bora ya uwekezaji
Tanzania itaanza kujitegemea kwa saruji karibuni, bila kulazimika kuagiza bidhaa nje, kufuatia kuzinduliwa kwa kiwanda kikubwa zaidi cha kuzalisha saruji kuliko kingine chochote katika Afrika Mashariki kilichojengwa katika eneo la Msijute, Mtwara Vijijini, Mkoa wa Mtwara ikiwa ni uwekezaji wa mabilioni ya fedha wa Kampuni ya Dangote Group ya Nigeria.
Aidha, Kampuni hiyo imesema kuwa imechagua kuwekeza Tanzania katika ujenzi wa Kiwanda hicho na huduma za upakiaji na upakuaji mizigo katika eneo lenye ukubwa wa hekta 25 katika Kijiji cha Mgao, kilichoko karibu na kiwanda hicho, kwa gharama ya dola za Marekani milioni 600 kwa sababu ya sera nzuri za Serikali na mazingira mazuri na rafiki ya kufanyia biashara yaliyojengwa na Serikali ya Tanzania.
Kampuni hiyo pia imesema kuwa Kiwanda hicho ndicho kimejengwa kwa kasi zaidi na kwa muda mfupi zaidi miongoni mwa viwanda vyote vya saruji ambavyo vimejengwa na Kampuni hiyo katika Bara la Afrika. Ujenzi wa Kiwanda hicho umechukua miezi 30 tu, miaka miwili unusu, tokea ujenzi huo ulipoanza Mei 27, mwaka 2013, kufuatia mkataba uliotiwa saini kati ya Kampuni hiyo na Serikali ya Tanzania.
Vile vile, Kampuni hiyo imetangaza kuwa imeamua kuwekeza zaidi katika Tanzania, na zamu hii, katika sekta ya kilimo ambako Dangote Group imeanza majadiliano na Serikali kwa ajili ya kuwekeza katika uzalishaji wa sukari.
Kiwanda hicho kilichozinduliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete umefanywa Jumamosi, Oktoba 10, 2015 ni Kiwanda cha nne cha saruji kuzinduliwa na Kampuni ya Dangote Group katika Bara la Afrika katika miezi minne tu iliyopita na wala siyo cha mwisho kuzinduliwa na Kampuni hiyo mwaka huu.
Akizungumza katika sherehe ya uzinduzi, Rais na Mtendaji Mkuu wa Dangote Group, Alhaj Aliko Dangote amesema kuwa kiwanda hicho ambacho kitazalisha saruji tani za ujazo milioni tatu kwa mwaka ni kiwanda kikubwa zaidi cha saruji katika Afrika Mashariki na kitakidhi mahitaji ya bidhaa hiyo nchini na kubakiza kiasi cha kutosha kwa ajili ya kuuza nje.
“Tutakapofikia kiwango cha juu kabisa cha uzalishaji wetu, Kiwanda hiki kitaiwezesha Tanzania kujitegemea kwa mahitaji ya saruji na kubakiza kiasi kikubwa tu kwa ajili ya kuuza katika masoko ya nje,” Alhaj Dangote amemwambia Rais Kikwete na mamia ya wananchi waliohudhuria sherehe ya uziduzi huo ambao walikuwa ni pamoja na wafanyabiashara 172 kutoka Nigeria ambao Alhaji Dangote aliwaalika katika sherehe hiyo.
Miongoni mwa wageni hao pia walikuwepo kwenye sherehe hizo ni Mwakilishi wa Serikali ya Nigeria, Alhaj Mallam Nasir Ahmad el Rufai, Gavana wa Jimbo la Kaduna, Wajumbe wa Bodi ya Dangote Group na mabinti zake Dangote watatu ambao karibu wote wamepanda ndege zao binafsi jioni ya leo baada ya shughuli hiyo kurejea kwao Nigeria.
Kuhusu uamuzi wa Makampuni ya Dangote kuwekeza katika Tanzania, Alhaji Dangote amesema: “Tunamshukuru sana Rais Kikwete. Serikali yake ilitengeneza mazingira rafiki ya kutuwezesha kuwekeza. Jambo kubwa kwetu sisi wafanyabiashara ni kuwepo kwa mazingira rafiki ya uwekezaji. Kwa hakika, Tanzania ni moja ya nchi rafiki zaidi kwa ajili ya kuvutia uwekezaji katika Afrika. Mageuzi ambayo nchi hii imefanya katika sekta mbali mbali na kukua kwa uhakika kwa uchumi, ni mambo yaliyotuongoza kuichagua Tanzania kama nchi yetu ya kuwekeza.”
Ameongeza kuwa Dangote Group imeamua kuwekeza katika Kiwanda hicho katika Tanzania kwa sababu inataka kuchangia katika ujenzi wa miundombinu ya Tanzania, kupanua fursa za ajira na kushiriki katika maendeleo ya jumla. Kiwanda hicho kinatarajia kutoa ajira 1,500 za moja kwa moja na 9,000 zisizokuwa za moja kwa moja.
“Visheni yetu pia ni kuwekeza katika uchumi ambazo zina uwezo wa kurudisha gharama za uwekezaji huo kwa uhakika na kuwa ujenzi wa Kiwanda hicho utazidi kuimarisha uhusiano kati ya nchi rafiki za Tanzania na Nigeria.”
Kuhusu mipango yake ya kuiwezesha Afrika kujitegemea kwa uzalishaji wa saruji na kupunguza idadi ya fedha za kigeni zinazotumiwa na nchi za Afrika kuagiza saruji kutoka nje, Alhaj Dangote amesema: “Kiwanda hiki ni moja ya miradi yetu yenye mafanikio ambayo inaendelea kujengwa katika nchi 18 za Afrika kwa mujibu wa mkakati wetu wa uwekezaji katika Bara la Afrika.”
Ameongeza: “Agosti mwaka huu, tumezindua viwanda viwili vipya katika Zambia na Cameroon. Na mwezi Juni, mwaka huu, tulifungua kiwanda chetu katika Ethiopia. Kabla ya mwisho wa mwaka huu, tutazindua viwanda vyetu vingine katika baadhi ya nchi nyingine za Afrika zikiwemo Senegal na Afrika Kusini. Tunaamini ipasavyo katika uwezo wa kiuchumi wa Afrika na maendeleo ya baadaye ya Bara la Afrika.”
Ameongeza Alhaj Dangote: “Vile vile mwezi Agosti mwaka huu mjini Lagos, tuliwekeana saini makubaliano ya kiasi cha dola za Marekani bilioni 4.34 na Kampuni ya Sinoma International Engineering kwa ajili ya ujenzi wa viwanda vingine 10 vya saruji katika nchi nyingine za Afrika na katika nchi ya Nepal iliyoko Bara la Asia. Uwezo wa jumla wa kuzalisha tani za ujazo milioni 25 kwa mwaka. Miradi hii ikikamilika katika miaka michache ijayo, Dangote Group itakuwa na uwezo wa kuzalisha tani za ujazo milioni 81 kwa mwaka na hivyo kuifanya Kampuni yetu kuwa moja ya kampuni kubwa zaidi za uzalisha saruji duniani.”
Kampuni ya saruji ya Dangote Cement Plc ndiyo kampuni kubwa zaidi katika Nigeria na Afrika Magharibu nzima katika Soko la Hisa la Nigeria (NSE) tokea ilipoandikishwa kwenye Soko hilo Oktoba mwaka 2010. Kampuni hiyo inasudia kujisajili kwenye masoko ya hisa ya Johannesburg (Afrika Kusini) na London (Uingereza).
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
11 Oktoba, 2015
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete , Jumamosi, Oktoba 10, 2015 amezindua mtambo mkubwa na miundombinu ya kisasa kabisa ya kuchakata na kusafirisha gesiasilia katika uwekezaji mkubwa ambako Serikali imewekeza kiasi cha dola za Marekani bilioni 1.33, sawa na sh trilioni 2.926, na kukamilisha uhakika wa kuongeza upatikanaji wa gesi kwa ajili ya matumizi ya uzalishaji na matumizi ya umeme viwandani, majumbani na kwenye magari.
Rais Kikwete amezindua mtambo huo katika eneo la Madimba, kilomita 25 kutoka mjini Mtwara, na kwa kuzindua miundombinu hiyo, Serikali sasa imekamilisha uunganishaji wa maeneo yanayozalisha gesiasilia kwa sasa ya Mnazi Bay na Songo Songo yanayotarajiwa kuzalisha gesi baadaye ya Ntorya, Kiliwani Kaskazini (Songo Songo) katika Mkoa wa Mtwara na Mkuranga katika Mkoa wa Pwani pamoja na gesi itakayotoka Bahari ya Hindi.
Akizungumza katika sherehe kubwa ya uzinduzi iliyohudhuriwa na mamia kwa mamia ya wananchi, mabalozi, wawekezaji katika sekta ya gesiasilia nchini, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Dr. James Mataragio amemwambia Rais Kikwete kuwa fedha za kuwekeza katika mradi huo mkubwa zimetokana na mchango wa Serikali ya Tanzania na mkopo kutoka Serikali ya Watu wa China kupitia benki yao ya EXIM.
Miundombinu hiyo iliyozinduliwa na Rais Kikwete inahusisha mitambo ya Madimba yenye uwezo wa kusafisha gesi futi za ujazo milioni 210 kwa siku, mitambo mingine kama hiyo katika eneo la Songo Songo yenye uwezo wa kusafisha gesi futi za ujazo zipatazo milioni 140 kwa siku, bomba lenye urefu wa kilomita 18 kutoka eneo la Mnazi Bay, Msimbati hadi Madimba na bomba la kusafirisha gesiasilia kutoka Mabimba hadi Kinyerezi mjini Dar es Salaam lenye urefu wa kilomita 477.
Aidha, mitambo hiyo ni pamoja na bomba la kusafirishia gesi la kilomita 29 kutoka Bahari ya Hindi hadi Songo Songo hadi Somanga Fungu na bomba lenye urefu wa kilomita 28 kutoka Kinyerezi hadi Ubungo hadi Tegeta kwa ajili ya kuzalisha umeme zaidi nchini.
Ujenzi wa miundombinu hiyo ulianzishwa na Rais Kikwete wakati shughuli rasmi ya utandazaji bomba kutoka Madimba hadi Dar es Salaam Novemba 21 mwaka 2012 wakati alipoweka jiwe la msingi katika ujenzi wake eneo la Kineyerezi Dar es Salaam na hivyo kuwezesha wakandarasi wakuu kuanza kazi ya ujenzi wa miundombinu hiyo ambayo inamilikiwa kwa asilimia 100 na Serikali ya Tanzania kupitia TPDC.
Wakandarasi wakuu watatu ni makampuni matatu kutoka China ambayo ni Kampuni ya China Petroleum Technology and Development Corporation (CPTDC), China Petroleum Pipeline Bureau (CPP) na China Petroleum Engineering Company (CPE). Makampuni hayo yote matatu ni tanzu ya Shirika la Mafuta la China la China National Petroleum Company (CNPC).
Mkurugenzi huyo wa TPDC ambayo inashiriki katika Mradi wa miundombinu hiyo kupitia kampuni yake tanzu ya GASCO amesema kuwa uzinduzi wa miundombinu unaifanya Tanzania kuingia katika orodha ya nchi zenye nishati ya gesiasilia duniani. “Na siyo ya kutosha tu bali ya kukidhi mahitaji muhimu kwa uwekezaji mkubwa, wa kati na hata wa kijasiriamali na hivyo kuwa na msingi mkuu na muhimu wa kuchochea maendeleo ya viwanda na ukuaji wa uchumi wa kasi zaidi.”
Akizungumza katika sherehe hizo, Rais Kikwete ametaka wote wanaohusika na huduma ya umeme kuhakikisha wanakomesha kukatika kwa umeme nchini kwa sababu sasa hakuna sababu ya kuwepo kwa tatizo hilo nchini.
Aidha, ameitaka TPDC kutimiza wajibu wake wa kijamii kwa kuwajengea wananchi huduma za afya, zahanati, shule na mahitaji mengine madogo wakazi wa maeneo ambako gesi hiyo inatoka na hata katika maeneo ambako bomba lao kuu linapitia.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
11 Oktoba, 2015
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete , Jumamosi, Oktoba 10, 2015, amefungua kiwanda kikubwa zaidi cha kuzalisha saruji kuliko kingine chochote katika Afrika Mashariki kinachomilikiwa na Kampuni ya Dangote Group ya Nigeria ambayo Mwenyekiti na Rais wake, Alhaji Aliko Dangote ndiye tajiri mkubwa zaidi Barani Afrika.
Uzinduzi huo umefanyika kwenye kiwanda hicho kipya kilichoko eneo la Msijute, Mtwara Vijijini, Mkoa wa Mtwara kiasi cha kilomita 20 kutoka mjini Mtwara kwenye Barabara ya Mtwara-Lindi na kuhudhuriwa na wafanyabiashara kiasi cha 170 kutoka Nigeria ambao wamehudhuria sherehe hiyo kama wageni wa Alhaj Dangote.
Aidha, ujumbe huo wa Dangote Group umeongozwa na Mheshimiwa Mallam Nasir Ahmad El Rufai, Gavana wa Jimbo la Kaduna ambaye pia ameiwakilisha Serikali ya Nigeria ambayo imekuwa inawaasa wafanyabiashara wake kusambaza uwekezaji wao katika Bara la Afrika na hasa katika nchi zenye utulivu wa uhakika kama Tanzania.
Kiwanda hicho kipya pia kinatarajia kuajiri watu 1,500 katika ajira ya moja kwa moja na watu 9,000 kwa ajira isiyokuwa ya moja kwa moja
Kiwanda hicho ambacho kitazalisha tani za ujazo milioni tatu kwa mwaka kimegharimu dola za Marekani milioni 600, ikiwa ni uwekezaji mkubwa zaidi kutoka nje kuingizwa katika uchumi wa Tanzania na ambacho uzalishaji wake unatarajiwa kushusha kwa kiasi kikubwa bei ya bidhaa muhimu ya saruji nchini ambayo katika baadhi ya maeneo ya Tanzania mfuko wa kilo 50 wa saruji unagharimu kiasi cha sh. 20,000.
Uzalishaji wa saruji wa kiwanda hicho ni mkubwa kuliko uzalishaji wa viwanda vyote vya saruji vilivyoko nchini kwa sasa na kuwepo kwake kutabadilisha uchumi wa Mkoa wa Mtwara na kuchangia kwa kiasi kikubwa ukuaji wa uchumi wa Tanzania ambayo inatumia kiasi cha tani za kimetriki milioni tatu kwa shughuli za ujenzi wa nyumba, madaraja na barabara.
Sherehe hizo za ufunguzi wa kiwanda hicho ambacho kimejengwa katika muda mfupi sana wa miaka miwili unusu pia zimehudhuriwa na Waziri Mkuu wa Chad na Mawaziri kutoka nchi za Malawi na Mozambique. Aidha, Alhaj Dangote amefuatana na watoto wake watatu wa kike na wajumbe wa Bodi ya Dangote Group katika sherehe hizo.
Akizungumza katika sherehe hizo za kufana zilizofanyika kwenye eneo la kiwanda hicho kikubwa, Rais Kikwete amesema kuwa kiwanda hicho kimezinduliwa wakati mwafaka kwa sababu sekta ya ujenzi imekuwa kwa kiasi kikubwa katika miaka 10 iliyopita na kwa sasa inachangia asilimia 12.5 katika Pato la Taifa kutoka asilimia saba.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
11 Oktoba, 2015
Taarifa kwa vyombo vya habari
Rais Jakaya Mrisho Kikwete amempongeza Rais Filipe Jacinto Nyusi wa Msumbiji kwa kuwa tayari kufanya mazungumzo yanayolenga kuleta Amani nchini Msumbiji. Rais Kikwete ametoa pongezi hizo wakati wa mkutano wa hadhara mjini Pemba katika Mkoa wa Cabo Delgado.
"Mheshimiwa Rais, na mimi nawaunga mkono wale wanaokushawishi ufanye mazungumzo, mwenyezi Mungu yuko upande wako na Tanzania iko nyuma yako" Rais amesema na kuwaambia wananchi wa Msumbiji
"Naomba wananchi mumuunge mkono Rais Nyusi katika mazungumzo na Dhlakama".
Mazungumzo hayo kati ya Chama Tawala cha FRELIMO na chama cha Upinzani cha Renamo kinachoongozwa na Alphonse Dhlakama yanalenga katika kutafuta amani ya kudumu nchini Msumbiji.
Juhudi hizo zilianza April 2013 lakini mwezi Agosti, 2015 kiongozi huyo wa RENAMO aliyasitisha ghafla na tangu hapo amekua akikataa mualiko wa Rais Nyusi wa kufufua mazungumzo yao.
Rais Nyusi ameeleza nia yake ya kuyafufua mazungumzo hayo na pia kuelezea nia yake ya kujumuisha vyama vingine vya siasa na mashirika yasiyo ya kiserikali.
Katika mkutano huo Rais Kikwete ameelezea nia yake ya kuendeleza urafiki na ushirikiano baina ya nchi hizi kwa nia ya kuleta maendeleo.
Akizungumza katika Mkutano huo Rais Nyusi amemuelezea Rais Kikwete kuwa mfano bora wa kuigwa katika kanda na Afrika kwa ujumla.
"Rais Kikwete anaondoka madarakani baada ya kipindi chake cha miaka 10, anatufundisha kuheshimu sheria na taratibu" Amesema Rais Nyusi nakumueleza kuwa "Natambua mchango wake na kumuambia ana pahala pakuishi Msumbiji"
Rais Kikwete pia amekutana na Watanzania wanaoishi Cabo Delgado ambao wana umoja wao unaojulikana kama Jumuiya ya Watanzania Cabo Delgado (JUCAWA) ambapo wamemuomba Rais kuwasaidia kufungua ubalozi mdogo Mkoani humo kwani kuna watanzania wengi na changamoto nyingi ambazo zote inabidi kupelekwa mjini Maputo kutafutiwa ufumbuzi. Rais Kikwete amekubali ombi lao hilo na kuahidi kulifanyia kazi.
Rais Kikwete na Ujumbe wake wamerejea Mkoani Mtwara ambapo tarehe 10 Oktoba, 2015 anatarajia kufungua kiwanda cha sementi cha Dangote pamoja na shughuli zingine za kiserikali.
.....................Mwisho............
Imetolewa na:
Premi Kibanga,
Mwandishi wa Habari wa Rais, Msaidizi,
Pemba-Msumbiji
9 Oktoba, 2015
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais Jakaya Mrisho Kikwete amewaasa wabunge wa Bunge la Msumbiji kufanya mazungumzo ili kumaliza tofauti zao.
Rais Kikwete ametoa ushauri huo jana tarehe 8 Oktoba wakati wa mazungumzo na Spika wa Bunge la Msumbiji Bibi Veronica Macamo ofisini kwake.
"Fanyeni mazungumzo, haiwezekani mkarudia vita tena baada ya miaka 22 , hatutapenda mrudi kwenye uwanja wa vita, hivyo ni muhimu mkafanya mazungumzo" Rais amewaasa wabunge katika kikao chake na Spika.
"Nyinyi wabunge lazima mtambue nafasi zenu na wajibu wenu wa kutokurudia vita tena, nyinyi ni wawakilishi wa watu na watu wanahitaji maendeleo sio vita" Rais Kikwete ameelezea.
Rais Kikwete amewaasa wabunge wasikubali nchi yao kuingia katika vita na badala yake wakae pamoja na kuweka makubaliano ambayo yatakubalika kwa vyama vyote na hatimaye kuwaepushia wananchi wa Msumbiji kuingia kwenye vita kwa mara nyingine.
Kikao cha Rais na Spika Macao ambaye anatoka Chama Tawala cha Ukombozi wa Msumbiji, The Mozambique Liberation Front (FRELIMO) pia kimehudhuriwa na wabunge wa vyama vya Mozambique Democratic Movement (MDM) na Mozambican National Resistance (RENAMO) ambavyo vinaunda Bunge la Msumbiji.
Rais Kikwete yupo nchini Msumbiji kwa ziara ya Kiserikali ya siku 2 kufuatia mualiko kutoka kwa Rais Filipe Jacinto Nyusi.
Mara baada ya kuwasili Maputo, Rais Kikwete amefanya mazungumzo na mwenyeji wake ambapo Rais Nyusi amemshukuru Rais Kikwete kwa msaada wake na kumueleza kuwa Msumbiji inathamini sana uhusiano baina ya nchi mbili hizi na kueleza nia yake ya kukuza uhusiano huu katika Nyanja za kibiashara na katika kupambana na maovu mbalimbali baina ya nchi hizi.
Baadae Rais Kikwete alipata heshima ya kupewa Ufunguo wa mji wa Maputo na kutangazwa Rais wa jiji hilo na Meya wa Maputo Ndugu David Simango.
"Una haki zote za raia wa Maputo, una haki ya kuingia wakati wowote, nakutakia kujisikia upo nyumbani ambapo siku zote utapendwa na kukaribishwa." Amesema Meya Simango mara baada ya kumkabidhi Rais Kikwete Ufunguo huo.
Ufunguo wa Mji wa Maputo ndiyo, heshima ya juu zaidi katika jiji la Maputo.
Rais pia ametembelea na kufanya mazungumzo kwenye ofisi za Chama Tawala cha FRELIMO na kuongea na wanachama wake.
Jana usiku, Rais Nyusi alimuandalia Rais Kikwete na Ujumbe wake chakula cha jioni kwa Heshima ya Rais Kikwete ambaye pia katika mazungumzo yao, Rais Kikwete ameaga na kueleza kuwa Tanzania inatarajia kupata kiongozi mwingine baada ya uchaguzi wa tarehe 25 Oktoba ,2015 lakini mahusiano na sera za nchi kwa Taifa la Msumbiji utaendelea na hatimaye kuimarika zaidi.
Leo asubuhi, Rais Kikwete anatarajia kuelekea mji wa Pemba, katika jimbo la Cabo Delgado ambapo anatarajia kufanya mkutano wa hadhara na baadae kukutana na Watanzania wanaoishi katika jimbo hilo kabla ya kuelekea Mkoani Mtwara kuendelea na shughuli za kitaifa.
.....................Mwisho................
Imetolewa na:
Premi Kibanga,
Mwandishi wa Habari wa Rais, Msaidizi,
Maputo-Msumbiji
9 Oktoba, 2015
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais kikwete ateuliwa Tume ya Elimu Duniani
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ameteuliwa kuwa Mjumbe wa Tume ya Kimataifa ya Kuchunguza Jinsi ya Kugharimia Elimu Duniani – The International Commission on Financing Global Education Opportunity.
Tume hiyo, inayoongozwa na Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza, Mheshimiwa Gordon Brown ambaye pia ni Mjumbe Maalum wa Umoja wa Mataifa (UN) wa Elimu Duniani ina jumla ya wajumbe 30, wakiwemo marais na mawaziri wakuu wa zamani, wataalum wa elimu, wafanyabiashara kutoka sekta binafsi na wawakilishi wa mashirika yasiyokuwa ya kiserikali (NGO’s) duniani.
Tume hiyo imeteuliwa na viongozi watano duniani wakishirikiana na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na ilitambulishwa kwa mara ya kwanza katika mkutano uliofanyika Septemba 29, mwaka huu, 2015 mjini New York, Marekani.
Rais Kikwete alihudhuria mkutano huo wa kwanza wakati wa ziara hiyo Marekani ambako pia alikuwa anaongoza Jopo ya Watu Mashuhuri Duniani ambao wanaangalia jinsi dunia inavyoweza kujiandaa vizuri zaidi dhidi ya magonjwa ya milipuko.
Viongozi walioteua Tume hiyo ni Mheshimiwa Erna Solberg ambaye ni Waziri Mkuu wa Norway, Mheshimiwa Michelle Bachelet Rais wa Chile, Mheshimiwa Irina Bokoba ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa UNESCO, Mheshimiwa Peter Mutharika Rais wa Malawi na Mheshimiwa Joko Widodo Rais wa Indonesia.
Tume hiyo ya Elimu itawasiliana na kukutana na viongozi mbali mbali duniani, wabuni sera za elimu na watafiti wa masuala ya elimu ili kuiwezesha Tume hiyo kujenga hoja zinazokidhi umuhimu wa kuwepo kwa upatikanaji wa fedha za kutosha na uwekezaji katika kuleta usawa katika upatikanaji wa nafasi za elimu kwa watoto wa kike na kiume.
Aidha, Tume hiyo italenga kuangalia jinsi gani dunia inavyoweza kuongeza uwekezaji katika elimu katika muda mfupi na katika muda mrefu na itapendekeza aina ya uwekezaji na hatua za kuchukuliwa.
Pia, Tume hiyo itapendekeza njia za kuwashawishi wakuu wa nchi na Serikali, mawaziri wa fedha, uchumi, elimu na ajira, magavana wa majimbo na serikali za mitaa pamoja na viongozi wa kibiashara na wawekezaji kuchukua hatua za kuwezesha ongezeko kubwa la fedha katika sekta ya elimu.
Miongoni mwa watu ambao watatumikia kwenye Tume hiyo pamoja na Rais Kikwete ni Rais wa zamani wa Mexico Mheshimiwa Felipe Calderon, Rais wa zamani wa Kamisheni ya Ulaya Mheshimiwa Jose Manuel Barroso, Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Dangote Group Bwana Aliko Dangote, Waziri Mkuu wa zamani wa Australia Mheshimiwa Julia Gillard, Rais wa Benki ya Dunia Mheshimiwa Jim Kim, na Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Alibaba Group ya China, Bwana Jack Ma.
Wengine ni Mama Graca Machel wa Mozambique, Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Econet Wireless Group ya Zimbabwe Bwana Strive Masiyiwa, Mwanamuziki Shakira Mebarak, Waziri wa zamani wa fedha wa Marekani na Rais wa Heshima wa Chuo Kikuu cha Harvard Bwana Lawrence Summers na Bi. Helle Thorning Schmitt, waziri mkuu wa zamani wa Denmark.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
08 Oktoba, 2015
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ameondoka nchini asubuhi ya leo, Alhamisi, Oktoba 8, 2015 kwenda Mozambique kwa ziara rasmi ya Kiserikali ya siku mbili nchini humo kwa mwaliko wa Rais wa nchi hiyo, Mheshimiwa Filipe Nyusi.
Akiwa nchini Mozambique, Rais Kikwete atatumia nafasi hiyo kuuaga rasmi uongozi wa nchi hiyo na wananchi wa Mozambique wakati anajiandaa kustaafu urais wa Tanzania na kukabidhi madaraka kwa Rais wa tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika wiki chache zijazo.
Tanzania na Mozambique ni nchi ambazo zimekuwa marafiki wakubwa na wa damu kwa miaka mingi tokea wakati wapiganaji wa Chama cha Frelimo walipokuwa wakipigania uhuru wa nchi hiyo dhidi ya wakoloni wa Kireno tokea nchini Tanzania ambako chama hicho kilianzishwa mwaka 1964.
Rais Kikwete anatarajiwa kurejea nyumbani kesho baada ya kuwa amemaliza ziara hiyo.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
08 Oktoba, 201
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ametuma salamu za rambirambi na maombolezo kumlilia Mwenyekiti wa Chama cha Siasa cha Democratic Party (DP), Mchungaji Christopher Mtikila, ambaye alipoteza maisha katika ajali ya gari iliyotokea alfajiri ya leo, Jumapili, Oktoba 4, 2015, katika Kijiji cha Msolwa, Wilaya ya Bagamoyo, Mkoa wa Pwani.
Katika salamu zake za rambirambi kwa Chama cha DP, Rais Kikwete amesema: “ Nimepokea kwa huzuni kubwa taarifa za kifo cha Mwenyekiti wenu na Mtanzania mwenzetu, Mchungaji Christoher Mtikila ambaye nimeambiwa amepoteza maisha katika ajali ya gari Mkoani Pwani akiwa njiani kurejea mjini Dar es Salaam akitokea kwao Njombe.”
“Kwa hakika, kifo cha Mchungaji Mtikila ni pigo kubwa kwa Chama cha Democratic Party ambacho kimempoteza kiongozi wake mkuu. Aidha, kifo hicho ni pigo kwa medani za siasa katika Tanzania na kimetunyang’anya mmoja wa viongozi hodari na wazalendo, aliyekuwa na msimamo thabiti na usioyumba katika kutetea mambo ambayo aliyaamini katika maisha yake yote,” amesema Rais Kikwete na kuongeza:
“Ni jambo la kusikitisha pia kuwa tunampoteza Mchungaji Mtikila katika kipindi cha mchakato muhimu wa kisiasa nchini ambako mchango wake ulikuwa unahitajika sana. Hakika, tutamkosa mwenzetu katika uwanja wa siasa za nchi yetu.”
Ameendelea Rais Kikwete, “Nawatumieni nyie wana-democratic Party salamu za dhati ya moyo wangu na pole nyingi kwa kuondokewa na kiongozi wetu mkuu, wa miaka mingi na wenye uzoefu wa uongozi wa chama cha siasa.”
“Aidha kupitia kwenu, napenda kuitumia pole zangu nyingi familia ya Mchungaji Mtikila. Nawapa pole sana wanafamilia, ndugu na marafiki na napenda wajue kuwa niko nao katika kipindi hiki cha majonzi ya kuondokewa na mhimili wa familia. Naungana nao katika majonzi. Aidha, naungana nao katika kumwomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, aiweke pema roho ya Mchungaji Christopher Mtikila. Amen”.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
04 Oktoba, 2015
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Nchi nne duniani leo, Jumatano, Oktoba 7, 2015, zimemtakia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete heri ya siku ya kuzaliwa na maisha marefu na bora. Rais Kikwete alizaliwa Oktoba 7, mwaka 1950.
Nchi hizo - Ubelgiji, Hispania, Mozambique na Uganda - zimeelezea heri hizo wakati mabalozi wateule wa nchi hizo nne walipowasilisha Hati za Utambulisho kwa Rais Kikwete kuwa mabalozi wa nchi zao katika Tanzania.
Mabalozi hao waliowasilisha Hati za Utambulisho ni Mheshimiwa Paul Cartier wa Ubelgiji, Mheshimiwa Felix Costardes Artieda wa Hispania, Mheshimiwa Monica Patricio Clemente wa Mozambique na Mheshimiwa Dorothy Samali Hyuha wa Uganda.
Akizungumza baada ya kupokea Hati za Utambulisho kutoka kwa Mheshimiwa Cartier mbali na kumtakia Rais Kikwete heri ya siku ya kuzaliwa amempongeza pia Rais Kikwete kwa kazi nzuri ya kuongoza Jopo ya Watu Mashuhuri Duniani Kuhusu Afya – High Level Panel on Global Heath.
Rais Kikwete amemwomba Balozi huyo mpya kuifanyia Tanzania kazi moja: Kuyashawishi makampuni zaidi ya Ubelgiji kuja kuwekeza katika Tanzania. “Shughuli yako kubwa iwe ni kushawishi makampuni kutoka Ubelgiji kuja kuwekeza katika Tanzania,” amesema Rais Kikwete.
Rais Kikwete pia amemwomba balozi huyo kuangalia jinsi gani Tanzania, Ubelgiji na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) zinavyoweza kushirikiana kutengeneza upya lango la kuthibiti maji kutoka Ziwa Tanganyika katika eneo la Moba kwa sababu uharibifu wa lango hilo unasababisha Ziwa Tanganyika kupoteza maji mengi na hivyo kina cha Ziwa hilo kupungua sana katika miaka michache iliyopita.
Katika mazungumzo yake na Balozi Artieda wa Hispania, Rais Kikwete amesema kuwa anafurahi kwamba amemaliza muhula wake wa uongozi wa Tanzania na yuko tayari kustaafu kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Sikumaliza matatizo yote ya Watanzania, na wala hakuna Rais ambaye amepata kumaliza matatizo yote na hatapatikana duniani, lakini kwa hakika nimetoa mchango wangu katika maendeleo ya nchi yake na watu wake. Naondoka nikiwa mtu mwenye furaha sana.”
Katika mazungumzo yake na Balozi Clemente baada ya kuwa amepokea Hati za Utambulisho za Balozi huyo, Rais Kikwete amesema kuwa uhusiano wa Tanzania ni wa kihistoria na wa kipekee kabisa duniani.
“Ni uhusiano wa miaka mingi, uhusiano wa watu na watu, uhusiano na Serikali na Serikali, uhusiano wa chama kwa chama. Lengo letu iwe ni kuuendeleza uhusiano huo na kuufikisha kwenye ngazi tofauti na ya juu kabisa.”
Akizungumza na Balozi Hyuha wa Uganda, Rais Kikwete amemtaka balozi huyo mpya kuzidi kuimarisha uhusiano kati ya Tanzania na Uganda, uhusiano ambao Rais Kikwete ameuelezea kama uhusiano maalum.
Rais Kikwete amemwambia Balozi Hyuha ambaye naye alimtakia heri ya siku ya kuzaliwa: “Uganda ni moja ya marafiki wetu wa karibu zaidi na wanaoaminika zaidi. Sisi ni marafiki, sisi ni ndugu na tuna uhusiano maalum kati yetu. Hivyo, Mheshimiwa Balozi hapa karibu nyumbani, jisikie uko nyumbani na usijione mpweke katika nchi yako.”
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
07 Oktoba, 2015
Taarifa kwa vyombo vya habari
Serikali ya Kenya na watu wake wameelezea shukrani zake kwa Rais Jakaya Mrisho Kikwete kwa urafiki na ushirikiano thabiti aliouonyesha kwa watu wa Kenya katika kipindi cha miaka 10 ya uongozi wake. Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya amesema hayo tarehe 5 Oktoba, 2015 katika Ikulu ya Nairobi wakati wa mazungumzo ya kiserikali.
"I thank you, and on behalf of People of Kenya for your friendship and Cooperation that was reflected during your 10 years as President" Rais Kenyatta amemueleza Rais Kikwete wakati wa mazungumzo yao jijini Nairobi.
"Chini ya uongozi wako Kenya na Tanzania zimeongeza ushirikiano baina yao katika miundombinu, biashara, uwekezaji, sekta binafsi na biashara ambapo imeongezeka na kuifanya Tanzania kuwa soko kubwa la Kenya" Rais Uhuru amesema.
Rais Kikwete yuko nchini Kenya kwa Ziara ya kiserikali ya siku tatu, ambapo pamoja na mambo mengine , Rais Kikwete atahutubia Bunge la Kenya na kukutana na wafanyabiashara wa nchini Kenya.
Mara baada ya kuwasili jumapili jioni Rais Kikwete alikutana na Watanzania waishio nchini Kenya na kula nao chakula cha usiku katika Hoteli ya Villa Rosa Kempisky. Watanzania hao wamemshukuru Rais na kumpongeza kwa mafanikio yanayoshuhudiwa nchini.
Akisoma risala yao Makamu mwenyekiti wa umoja wa Watanzania waishio nchini Kenya, Bw Cleophas Tesha amesema mafanikio hayo yametokana na juhudi binafsi za Rais Kikwete na Serikali ambayo ameisimamia kwa miaka yote 10.
"Kwa Umakini wako katika kusimamia maslahi ya wananchi, uimara wako bila kushinikizwa, tunakupongeza kwa kuweka nchi yetu katika ramani ya dunia". Amesema Bw. Tesha "Tunaamini bado Taifa litaendelea kutumia ujuzi wako". Leo Usiku Rais Kikwete na ujumbe wake watahudhuria dhifa ya Kitaifa iliyoandaliwa kwa heshima yake.
Kesho tarehe 6 Rais Kikwete anatarajia kuhutubia Bunge la Kenya na wananchi wake ambapo anatarajia kuwaaga rasmi Rais Kikwete na ujumbe wake wanatarajia kuondoka Nairobi kurudi Dar-es-Salaam.
............................Mwisho...............................
Imetolewa na:
Premi Kibanga,
Mwandishi wa Habari wa Rais, Msaidizi
Nairobi-Kenya
5 Oktoba, 2015
Taarifa kwa vyombo vya habari
RAIS KIKWETE AANZA ZIARA RASMI KENYA
- Aungana na Rais wa Kenya kufungua barabara itayounganisha Tanzania na Kenya.
- Kuhutubia Bunge na kutembelea Kaburi la Hayati Jomo Kenyatta
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete leo, Jumapili, Oktoba 4, 2015 ameanza ziara rasmi ya Kiserikali ya siku tatu katika Jamhuri ya Kenya kwa mwaliko wa Rais wa Jamhuri ya Kenya, Mheshimiwa Uhuru Muigai Kenyatta ambako miongoni mwa shughuli nyingine atahutubia Bunge la Kenya.
Rais Kikwete ameanza ziara yake kwa kuungana na Rais Kenyatta kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa Barabara ya Taveta-Mwatate ambayo ni sehemu ya barabara inayounganisha Tanzania na Kenya ikianzia Arusha-Holili-Taveta-Mwatate. Barabara hii itaunganisha eneo la kaskazini mwa Tanzania na Bandari ya Mombasa, Kenya.
Hii ni ziara ya pili rasmi kwa Rais Kikwete katika Kenya. Miaka mitatu iliyopita, Rais kikwete alifanya ziara rasmi katika Kenya kwa mwaliko wa Rais Mwai Emilio Kibaki na Rais Kikwete ataitumia ziara ya sasa kuwaaga wananchi wa Kenya baada ya miaka 10 ya uongozi ambako ameimarisha sana uhusiano kati ya Tanzania na Kenya ikiwa ni pamoja na kusaidia kusuluhisha mgogoro mkubwa wa kisiasa uliosababisha machafuko na mauaji ya mamia ya wananchi wa Kenya kufuatia Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2009.
Mbali na kuwaaga wananchi wa Kenya katika nafasi yake kama Rais wa Tanzania, Rais Kikwete pia atawaaga viongozi na wananchi wa Kenya kwenye nafasi yake kama Mwenyekiti wa Jumuia ya Afrika Mashariki (EAC).
Aidha, mbali na kuhutubia Bunge la Kenya wakati wa ziara yake, Rais Kikwete atatembelea na kuweka shada la maua kwenye kaburi ya Hayati Jomo Kenyatta, Rais wa kwanza na muasisi wa Taifa la Kenya.
Rais Kikwete pia atafanya mazungumzo rasmi ya Kiserikali na mwenyeji wake, Rais Kenyatta; atahutubia Chama cha Wafanyabiashara wa Kenya na atatembelea Kiwanda cha Dawa cha Universal kilichoko eneo la Kikuyu.
Katika tukio lake la kwanza, Rais Kikwete na mwenyeji wake kwa pamoja wameanzisha rasmi ujenzi wa Barabara ya Arusha-Holili-Taveta-Mwatate kwa kiwango cha lami kwa kuweka jiwe la msingi wa ujenzi wa kipande cha Taveta-Mwatate chenye urefu wa kilomita 98.4 na kilomita nyingine tisa za lami ambazo zitajengwa katika mji wa Taveta.
Barabara ya Taveta-Mwatate ambayo ujenzi wake utachukua miezi 36 ilianza kujengwa Mei 17, mwaka jana, 2014, inatarajiwa kukamilika Mei 17, mwaka 2017, kwa gharama ya shilingi za Kenya bilioni 8.4 ambazo zimetolewa na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) na Serikali ya Kenya. Tayari kilomita 34 za barabara hiyo zimejengwa kwa lami.
Akizungumza katika sherehe hiyo, Mwakilishi wa AfDB, Bwana Gabriel Negatu amesema kuwa barabara hiyo ni sehemu ya mtandao wa barabara za kuunganisha nchi wanachama wa Jumuia ya Afrika Mashariki (EAC). Moja ya barabara hizo ya Arusha-Namanga-Athi River tayari imekamilika na kufunguliwa rasmi na viongozi wa EAC.
Bwana Negatu amesema kuwa AfDB imezitengea Tanzania na Kenya dola za Marekani bilioni 1.5 kwa ajili ya miradi ya miundombinu na kuwa kati ya hizo tayari dola milioni 218 zimetolewa, milioni 112 zikiwa zimetolewa kwa Tanzania na milioni 106 zimetolewa kwa Kenya.
Mwisho.
Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
04 Oktoba, 2015
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais waJ amhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amemteua Ndugu Francis M. Mwakapalila kuwa Mhasibu Mkuu wa Serikali kuanzia juzi, Alhamisi, Oktoba 1 , 2015.
Ndugu Mwakapalila anachukua nafasi ya Bibi Mwanaidi Mtanda ambaye amestaafu kazi kwa mujibu wa sheria.
Kabla ya uteuzi wake kuwa Mhasibu Mkuu wa Serikali, Ndugu Mwakapalila alikuwa Naibu Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
03 Oktoba, 2015
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amewataka wafanyabiashara na sekta binafsi nchini kuishi vizuri na Serikali kwasababu pande zote zinategemeana na kuhitajiana.
“Ni wajibu wenu kuishi vizuri na Serikali, mkianza kusemana na kushambuliana, mnaweza kabisa msipate ama hata kupoteza kuungwa mkono na Serikali,” Rais Kikwete aliwaambia wafanyabiashara wa Tanzania.
Rais Kikwete alikuwa anazungumza wakati wa Chakula cha Usiku kilichoandaliwa na wafanyabiashara wa Tanzania kupitia Taasisi ya Tanzania Private Sector Foundation (TPSF) kwenye halfa ya kumwaga Rais Kikwete kwenye hoteli ya Serena, Dar es Salaam, usiku wa kuamkia leo, Jumamosi, Oktoba 3, 2015.
Aliwaambia wafanyabiashara hao: “Hapa nazungumzia suala la mahusiano na kuishi vizuri na Serikali yenu. Nyie ni watu muhimu sana, lakini mkibakia peke yenu bila kuungwa mkono na Serikali, shughuli zenu zitakwenda kwa taabu sana.”
Alisisitiza: “Pande zote zinahitajiana. Nyie hamuwezi kusonga mbele bila msaada wa serikali na Serikali hivyo hivyo haiwezi kwenda bila ushirikiano na sekta binafsi kwasababu shabaha ya pande zote mbili ni moja – yaani kuwatoa Watanzania katika umasikini na kuwasidia watu wetu kuishi maisha bora zaidi.”
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
03 Oktoba, 2015
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Wafanyabiashara wa Tanzania wamemwagia sifa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, kwa kuinua uchumi wa Tanzania katika sekta mbalimbali katika miaka 10 ya uongozi wake, kupitia hatua zake mbalimbali alizozichukua katika kipindi hicho cha ustawi wa kasi zaidi kuliko wakati mwingine katika historia ya Tanzania.
Wafanyabiashara hao pia wameipongeza Serikali yake kwa kukubaliwa kupata awamu ya pili ya mabilioni kwa mabilioni ya fedha za misaada za Millennium Challenge Coprporation(MCC) ya Marekani na pia kwa kufanikiwa kwenye kigezo cha Serikali yake kuchukua hatua za kwelikweli kupambana na rushwa. Tanzania itapata karibu sh. trilioni moja katika awamu hiyo.
Sifa hizo za wafanyabiashara zilimwaga usiku wa jana, Ijumaa, Oktoba 2, 2015, wakati wa Chakula cha Usiku ambacho wafanyabiashara hao walimwandalia Rais Kikwete kupitia Taasisi yao yaTanzania Private Sector Foundation (TPSF) kwenye Hoteli ya Serena mjini Dar es Salaam.
Pongezi hizo za Rais Kikwete ziliogozwa na Mwenyekiti wa TPSF, Bwana Reginald Mengi, ambaye amemshukuru Rais kwa mafanikio yake katika ujenzi wa miundombinu ya barabara, viwanja vya ndege na reli; mawasiliano, kuboresha mazingira ya kufanyia biashara na kulinda utulivu na amani nchini.
“Napenda nikupongeza Mheshimiwa Rais hasa kwa mambo mawili ya karibuni. Moja ni mafanikio ya Serikali yako kupata awamu ya pili ya mabilioni ya fedha za MCC baada ya kuwa Tanzania imeonyesha dhamira thabiti ya kukabiliana na rushwa,” alisema Mengi na kuongeza:
“Pili, napenda kukupongeza kwa kuchaguliwa kwako kuwa miongoni mwa watu mashuhuri duniani watakaotafuta njia za kufuta kabisa ugonjwa wa malaria duniani ukiwa kwenye kundi moja na matajiri wakubwa sana duniani”. Siyo kupunguza bali kuufuta ugonjwa huo unaoua watu wetu wengi. Tunajua umeshiriki sana katika mitandao ya kukabiliana na ugonjwa huo kama vile ALMA, Malaria No More, lakini hii ya kujaribu kufuta kabisa ugonjwa huo ni kubwa sana.”
Baraza la Kilimo Tanzania (ACT) lilimshukuru Rais Kikwete kwa ulezi wake wa shughuli za kilimo nchini nakusema kuwa anaondoka madarakani wakati dalili za mageuzi makubwa katika sekta hiyo zimeanza kujitokeza wazi wazi nchini.
Chama cha Wana-Mabenki Tanzania (TBA) kimesema kuwa mafanikio katika shughuli za kibenki yanajionyesha wazi wazi kutokana na sera nzuri za miaka 10 ya uongozi wa Rais Kikwete.
“Takwimu hazidanganyi Mikopo ya kibiashara nchini imeongezeka kutoka bilioni 1,600 mwaka 2005 hadi kufikia bilioni 14,000 kwa sasa. Matawi ya mabenki nchini yameongezeka kutoka 400 hadi 600 kwasasa na watumishi katika sekta hiyo wameongezeka kutoka 9,000 hadi kufikia 15,000 na sasa nchini zipo benki zaidi ya 52,” alisema mwakilishi wa TBA
Nacho Chama cha Utalii Tanzania kimesema kuwa mafanikio katika sekta hiyo ni dhahiri kabisa kiasi cha kwamba sekta hiyo sasa inaongoza katika kuiingizia Tanzania fedha za kigeni.
Alisema mwakilishi wake: “Idadi ya watalii wanaotembelea Tanzania imeongezeka kutoka watalii 612,754 mwaka 2005 hadi kufika watalii 1,138,000 mwaka jana. Hili ni ongezeko la zaidi ya asilimia 80. Tanzania sasa inapata kiasi cha dola za Marekani bilioni mbili kutokana na utalii zikilinganishwa na dola milioni 747.2 mwaka 2005. Hili ni ongezeko la asilimia 163. Ajira zimeongezeka kutoka 500,000 mwaka 2005 hadi kufikia 1,200,000 kwasasa. Tuseme nini zaidi yahapo?”
Chama cha Wafanyabiashara Wanawake katika Tanzania nacho kimetoa pongezi na sifa nyingi kwa mafanikio ya miaka 10 ya uongozi wa Rais Kikwete katika kuwezesha wanawake nchini.
Mwenyekiti wake, Bi. Anna Matinde alisema: “Umeanzisha Benki ya Wanawake ambayo ni kimbilio la wanawake wajasiriamali, umeteua akinamama wengi katika nafasi za uongozi, umetupa Spika wa Bunge wa kwanza mwanamke, umetuachia Katiba Inayopendekeza 50-50. Umetuwezesha sana Mhe. Rais.”
Mwenyekiti wa Chama cha Madini Tanzania, Balozi Ami Mpungwe alisema kuwa Rais Kikwete anaondoka madarakani akiwa ameanzisha michakato ya kutekelezwa kwa miradi mikubwa ya madini Tanzania ambayo itabadilisha kabisa sura ya Tanzania.
“Mhe. Rais umekuwa mdau wa madini kwa miaka mingi- tokea ulipoingia Serikalini mwaka 1988. Kwasababu hiyo unaijua sana sekta hii na ndiyo maana umeanzisha michakato ya miradi mikubwa ya madini – mradi wa madini ya nickel wa Kabanga, Ngara, mradi wa urani wa Mantra, mradi wa graphite, mradi wa uchimbaji chuma na makaa ya mawe kule Liganga na Mchuchuma. Yote haya yatabadilisha sana sura ya nchi yetu na maisha ya wananchi wake.”
Rais wa Chama cha TCCIA amesema kuwa shughuli za biashara kikiwemo kilimo na uuzaji nje mazao zimeongezeka sana katika miaka 10 ya uongozi wa Rais Kikwete.
“Mauzo yetu ya nje ya mazao ya kilimo sasa yamefikia dola za Marekani bilioni tano kutoka bilioni 1.6 mwaka 2005, mapato ya bidhaa za nje kuvuka Tanzania kuingia nchi jirani yamepanda kutoka dola za Marekani bilioni 1.2 mwaka 2005 hadi kufikia dola bilioni tisa kwa sasa. Mauzo yetu katika nchi za Jumuia ya Afrika Mashariki yamefikia thamani ya dola za Marekani milioni 569 kutoka dola milioni 162 mwaka 2005, mauzo yetu katika nchi za SADC yamepanda kutoka dola milioni 445 hadi kufikia dola bilioni 1.2. Umeinua sana shughuli za kilimo.”
Makundi hayo mbalimbali, likiwemo Baraza la Taifa la Biashara Tanzania (TNBC) yamempa zawadi mbalimbali na hati za kutambua mchango wa Rais Kikwete katika uongozi wa Tanzania.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
03 Oktoba, 2015
Taarifa kwa vyombo vya habari
Kituo cha kisasa cha michezo kufunguliwa Dar mwezi ujao
- Kinaitwa Jakaya M. Kikwete Park na kitafunguliwa na Rais Kikwete
- Ni cha kwanza cha aina yake nchini na kitafundisha watoto wadogo michezo (Bonyeza blog kwa habari picha)
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete mwezi ujao, Alhamisi, Oktoba 17, 2015, atazindua rasmi Kituo cha Michezo cha Kisasa cha Jakaya M. Kikwete Youth Park (JMK Park), Kidongo Chekundu, Dar es Salaam, kituo cha kwanza cha aina yake nchini chenye kulenga miongoni mwa mambo mengi kuanza kulea wanamichezo tokea wakiwa wadogo.
Rais Kikwete alikubali kuzindua Kituo hicho wakati wa mazungumzo kati yake na Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Umeme ya Symbion Power, Bwana Paul Hinks kwenye Hoteli ya JW Marriot Essex House, mjini New York, Marekani ambako Rais alikuwa anafanya ziara rasmi ya kikazi. Rais Kikwete alikiwekea Kituo hicho jiwe la msingi mwaka jana.
Katika mkutano huo, uliofanyika jana, Jumanne, Septemba 29, 2015, Bwana Hinks alimweleza Rais Kikwete kuwa ujenzi wa Kituo hicho sasa umekamilika tayari kwa uzinduzi na hivyo kuongeza thamani kubwa kwenye eneo ambalo miaka ya nyuma lilikuwa gereji ya kutengenezea magari.
Kituo hicho cha JMK Park kimegharimu kiasi cha dola za Marekani milioni mbili na ni matokeo ya ushirikiano ya Kampuni ya Symbion Power ya Marekani, Klabu ya Soka la Ligi Kuu ya Uingereza ya Sunderland AFC na Taasisi ya Grasshopper Soccer.
Baada ya uzinduzi huo, Kituo hicho kitafunguliwa kwa umma kwa mara ya kwanza Jumamosi ya Oktoba 19, 2015, na hivyo kukiwezesha kuanza shughuli zake, shughuli kubwa ikiwa ni kulea watoto wa kike na kiume kwa kupitia michezo.
Kwa mujibu wa mipango ya sasa, Kituo hicho kitaanza kwa kutoa mafunzo ya michezo ya soka, mpira wa kikapu (basketball), netiboli, mpira wa wavu (volleyball) na mpira wa magongo (hockey), michezo ambayo viwanja vyake vya kisasa kabisa vimekamilika kujengwa.
Kuhusu soka, JMK Park kitaanza kutoa mafunzo ya mchezo huo kuanzia Januari 2016 kwa timu za watoto wa chini ya umri wa miaka 16 na miaka 14 na pia kitatoa mafunzo maalum kwa watoto wadogo zaidi wa kati ya miaka 10 na 11.
Mafunzo hayo yatatolewa na makocha wenye weledi na uzoefu kabisa ambao watatolewa na Klabu ya Sunderland.
Kuhusu mpira wa kikapu, mafunzo yataanza kutolewa kwa watoto wa kiume wa kati ya miaka 12 na 15 kutoka shule 30 za msingi katika Mkoa wa Dar es Salaam ambazo zitaunda timu 30 zitakazoshiriki katika ligi ya mchezo huo kila mwaka. Mafunzo ya mchezo huo kwa ajili ya watoto wa kike, utaanza katika mwaka wa pili wa kufunguliwa kwa Kituo hicho.
Kituo hicho ambacho kitafunguliwa kila siku kwa mwaka mzima pia kitatoa nafasi kwa watu wazima wapenzi wa michezo kukitumia kwa mujibu wa taratibu zitakazotangazwa baadaye na wahusika.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
30 Septemba, 2015
Taarifa kwa vyombo vya habari
Rais Kikwete ajiunga na matajiri wa Marekani kufuta malaria duniani
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ameombwa na amekubali kujiunga na kundi la watu mashuhuri duniani wakiwemo viongozi wa Afrika, matajiri wa Marekani na watu wengine mashuhuri katika kutafuta majawabu ya kufuta ugonjwa wa malaria duniani kwa kuanzia na Bara la Afrika.
Ombi kwa Rais Kikwete kujiunga na kundi hilo ambalo litaongozwa na tajiri mkubwa zaidi duniani, Bwana Bill Gates, liliwasilishwa kwa mara ya kwanza kwake wiki iliyopita na Mjumbe Maalum wa Umoja wa Mataifa wa Kupambana na Malaria, Bwana Ray Chambers, tajiri mwingine wa Marekani.
Ombi hilo liliwasilishwa kwake katika mkutano na Bwana Chambers kwenye Hoteli ya JW Marriot, Essex House, mjini New York, Marekani, ambako Rais Kikwete alikuwa amefikia wakati wa safari yake ya shughuli nyingi katika Marekani na akalikubali ombi hilo.
Katika mkutano wa kwanza wa kukutanisha wadau wa wazo hilo duniani kwenye chakula cha usiku kilichoandaliwa Jumatatu, Septemba 28, 2015, mjini New York, ilielezwa kuwa baada ya jitihada za kupunguza kwa kiwango kikubwa cha malaria duniani, na hasa katika Bara la Afrika kufanikiwa, sasa jitihada zinaelekezwa katika kufuta kabisa ugonjwa huo katika Bara hilo.
Miongoni mwa watu waliohudhuria chakula cha usiku ni Rais Kikwete, mabwana Bill Gates na Ray Chambers, Rais wa Liberia Mama Ellen Johnson Serliaf, Waziri Mkuu wa Ethiopia Mheshimiwa Hailemarian Desalegn na Katibu Mtendaji wa Umoja wa Viongozi wa Afrika wa Kupambana na Malaria, Mama Joy Phumaphi.
Waziri Mkuu Desalegn ndiye mwenyekiti wa sasa wa Umoja wa Viongozi wa Afrika Katika Kupambana na Malaria (Alma) na Mama Serliaf ndiye mmoja wa makamu mwenyekiti wakati Rais Kikwete akiwa mwenyekiti.
Miaka 10 iliyopita, Rais Kikwete na Bwana Chambers walijadiliana na kukubaliana kuanzisha Alma na walikuwa viongozi hao wawili ambao walibuni wazo la kusambaza mamilioni kwa mamilioni ya vyandarua vya kupambana na malaria katika Afrika. Katika Tanzania, kila familia ilipewa vyandarua vya kupambana na malaria kwa mujibu wa ukubwa wa familia.
Bwana Ray Chambers aliongoza mapambano ya kupunguza malaria katika Afrika ambapo vifo vyake vimepungua kwa asilimia 70 katika miaka 10 iliyopita, lakini chini ya mpango wa sasa Bwana Gates ataongoza mpango wa kufuta kabisa malaria duniani kwa kuanzia na Bara la Afrika.
Rais Kikwete ameondoka Marekani usiku wa Jumanne, kurejea nyumbani baada ya ziara ambayo ilishirikisha shughuli zake kama Mwenyekiti wa Jopo la Watu Mashuhuri Duniani kupendekeza jinsi gani dunia inaweza kujiandaa vizuri zaidi kukabiliana ma magonjwa ya milipuko kufuatia majanga ya ugonjwa wa Ebola.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
30 Septemba, 2015
Taarifa kwa vyombo vya habari
JK kwa Wabunge wa Marekani: Fungeni masoko ya kimataifa ya pembe za ndovu na ujangili utaisha
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ametoa changamoto kwa Wabunge wa Bunge la Marekani kufunga masoko ya pembe za ndovu na faru duniani, kama njia yenye uhakika ya kukomesha ujangili dhidi ya wanyamapori katika nchi za Afrika na kwa haraka zaidi.
Aidha, Rais Kikwete amewataka Wabunge hao kuzisaidia nchi za Afrika kifedha, ili kukomesha ujangili huo kwa sababu Wabunge hao tayari wameitangazia dunia kuwa wanazo fedha za kutosha kwa ajili ya kukabiliana na majanga ya ujangili.
Rais Kikwete alitoa changamoto hizo usiku wa Jumatatu, Septemba 28, 2015, wakati alipohutubia Umoja wa Wabunge wa Bunge la Marekani ambao wanalenga kulinda na kuhifadhi wanyamapori na uhifadhi duniani, kujenga umoja wa kisiasa wa kukabiliana na ujangili na kutafuta majawabu ya changamoto zinazokabili uhifadhi unaojulikana kama International Conservation Caucus Foundation (ICCF) Group.
Akizungumza nao mjini New York, Marekani, ambako Rais alikuwa anafanya ziara ya kikazi na mbele ya baadhi ya marais wenzake wa nchi za Afrika wanaokabiliana na ujangili na wanaofanya kazi kwa karibu na ICCF Group, Rais Kikwete alisema kuwa kama kweli Wabunge wa Marekani wakiamua kutumia nguvu za taifa lao kubwa duniani kufunga masoko ya meno ya ndovu na pembe za faru basi tatizo hilo litamalizika haraka.
ICCF inafanya kazi kwa karibu na nchi za Tanzania, Kenya, Uganda, Sudan Kusini, Zambia, Malawi, Gabon, Botswana, Mozambique, Namibia, Congo-Brazaville na Afrika Kusini na marais Peter Mutharika wa Malawi na Rais Ali Omar Bongo wa Gabon walikuwepo kwenye halfa hiyo iliyohutubiwa na Rais Kikwete.
Katika hotuba yake, Rais Kikwete amewaambia Wabunge hao wa Marekani kuwa nchi za Afrika pamoja na kufanya jitihada kubwa kukabiliana na kile alichokielezea kama”kiwango cha juu kabisa cha uendawazimu" lakini zina ukomo wa uwezo wa kifedha na nguvu katika kukomesha ujangili bila kusaidiwa na nchi kubwa kama Marekani.
“Nyie kama wabunge wa Marekani mna uwezo mkubwa sana kama ilivyo nchi yenu. Fungeni masoko ya pembe za ndovu na faru. Wanunuzi mnawajua nyie wenyewe kuliko hata mimi. Wengi wenu mna fedha na nguvu nyingi kuliko sisi katika Afrika kumaliza tatizo hili. Sisi ni hadithi ya mkufu kukatikia pabovu. Timizeni wajibu wenu na kwa kweli ujumbe wangu mkubwa kwetu usiku wa leo ni fungeni masoko haya na tatizo litaisha sana,” alisema Rais Kikwete na kuongeza:
“Nimemsikia mama pale akisema kuwa ICCF ina kiasi cha dola bilioni 13.2 za kufanya kazi ya kukabiliana na ujangili duniani. Tunahitaji fedha hizi. Mnatamba kuwa mnayo fedha nyingi lakini sisi tulioko kwenye uwanja wa mapambano hatuzioni fedha hizo. Tupeni fedha tufanye kazi.”
Rais Kikwete alikuwa anazungumzia risala ya ICCF iliyokuwa imeeleza kuwa ICCF inazo fedha kiasi cha dola bilioni 13.2 za kukabiliana na changamoto za ujangili.
Rais Kikwete pia ametoa historia ya jinsi Tanzania imetoa kipeumbele kwa shughuli za hifadhi tokea uhuru mwaka 1961 na jinsi ambavyo imehangaika kukabiliana na ujangili katika miaka hiyo yote wakati mwingine kwa kulazimika kutumia Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (TPDF) kuendesha operesheni maalum kuokoa wanyamapori.
“Wakati wa uhuru, Tanzania ilikuwa na tembo wanaokadiriwa kufikia 150,000 lakini ilipofikia mwishoni mwa miaka ya 1970 na mwanzoni mwa miaka ya 1980, walikuwa wamebakia tembo 50,000 tu. Tuliendesha operesheni maalum kuokoa wanyamapori hao na baada ya operesheni hiyo idadi ikapanda hadi kufikia tembo 110,000.”
Aliongeza Rais Kikwete: “Lakini ukaanza uendawazimu mwingine wa kiwango cha juu kabisa wa kuua wanyamapori kwa sababu ya pembe zao. Hesabu yetu ya mwisho ilionyesha kuwa tulikuwa tumebakiwa na tembo 43,000 tu. Tunaendesha operesheni nyingi.” Alisema Rais Kikwete na kuongeza:
“ Ushahidi unaonyesha kuwa tumesimamisha uendawazimu kwa sasa hasa katika ukanda wa Kaskazini wa utalii. Tatizo sasa limebakia katika mfumo wa mazingira wa Selous-Ruaha. Hili tunaendelea kupambana nalo kwa sababu mtandao wa ujangili ni mkubwa sana. Sasa na nyie tusaidieni kwa vitendo.”
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
30 Septemba, 2015
Taarifa kwa vyombo vya habari
Benki ya Dunia: Tanzania yaongoza duniani kutoa huduma za pesa kwa simu
Tanzania ni nchi ya kwanza duniani kutoa huduma za pesa, kutoa mikopo na kutoa riba kwa kutumia mawasiliano ya simu, Benki ya Dunia imesema na kuongeza kuwa Tanzania ni moja ya masoko makubwa zaidi duniani ya kutoa huduma ya fedha kwa njia ya simu.
Benki hiyo ya Dunia pia imesema kuwa Serikali ya Tanzania imewekeza kwa kiwango cha juu katika mfumo wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT) ikilinganishwa na nchi nyingine duniani na kulingana na uwezo wake.
Benki hiyo pia imesema kuwa nchi jirani ya Kenya inaongoza kwa kutuma pesa kupitia mfumo wa M-Pesa katika eneo ambalo miaka michache iliyopita lilikuwa eneo la kujidai la nchi tajiri tu duniani.
“Huu ni mfano kutoka Afrika ambao unaweza kuigwa na nchi zote duniani,” amesema Profesa Kaushik Basu, Mchumi Mkuu wa Benki ya Dunia (WB) wakati akiwasilisha kwa ufupi tu yaliyomo katika Ripoti ya Benki hiyo ya World Development Report ambayo itatolewa hivi karibuni.
Profesa Basu alikuwa anazungumza jana, Jumatatu, Septemba 28, 2015 kwenye Mkutano wa Wakuu wa Nchi uliozungumzia Hali ya Enzi za Digitali (Digital Age) uliofanyika kwenye Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa (UN), ikiwa ni sehemu ya majadiliano kuhusu Malengo ya Maendeleo Mapya (SDG’s) ambayo yanachukua nafasi ya Malengo ya Maendeleo ya Milenia (MDG’s) ambayo muda wake wa utekekezaji wa miaka 15 umefikia mwisho mwaka huu.
Akizungumza katika mkutano huo uliohudhuriwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Estonia Mheshimiwa Toomas Hendrik Ilves na Rais wa Benki ya Dunia (WB) Dkt. Jim Kim, Profesa Kaushik alisema:
“Tuko katikati ya mapinduzi makubwa ya teknolojia, ambayo athari zake bado ni ngumu sana hata kubashiri. Na hizi ni shughuli ambazo miaka michache iliyopita zilikuwa hata hazina jina, lakini sasa inteneti na teknolojia ya digitali inabadilisha maisha ya kijamii na kisiasa ya binadamu,” alisema Profesa Basu.
Aliongeza: “Chukulia takwimu hizi – kuna kiasi cha utafuta habari kwenye google kiasi cha bilioni 4.2 kwa siku moja, kila sekunde watu wanatuma tweet 6,000 na rekodi ilikuwa Agosti mwaka 2013 wakati zilipotumwa tweet 143,199 kwa sekunde wakati ilikuwa inaonyeshwa filamu moja ya sanaa.”
Aliongeza: “Mfumo wa uwekaji na utumaji pesa wa M-Pesa katika Kenya sasa unashindana na mifumo ya siku nyingi ya nchi matajiri duniani. Kila watu wazima 1,000 kuna akaunti 700 katika Kenya ikiwa ni ongezeko 103 kutoka mwaka 2013.”
“Jirani na Kenya kuna mfano mwingine wa mafanikio makubwa zaidi duniani katika nchi jirani ya Tanzania. Tanzania imewekeza sana katika ICT na katika mfumo wa kuhamisha na kusambaza fedha. Sasa Tanzania ni soko kubwa zaidi duniani la kutuma fedha kwa njia ya simu,” alisema Profesa Kaushik.
Aliongeza: “Tanzania sasa ni nchi ya kwanza duniani kutoa huduma ya pesa, kutoa mikopo na kutoa riba kwa njia ya simu. Hii ni mifano ambayo nchi zote duniani zinaweza kuiga kutoka Afrika.”
Wakati huo huo, Rais Kikwete leo, Jumanne, Septemba 28, 2015, amekutana na kufanya mazungumzo na Malkia wa Uholanzi, Malkia Maxima wa Uholanzi, Mke wa Mfalme Willem-Alexander kuhusu jinsi gani ya kuzidi kuisaidia Tanzania kuongeza kasi yake katika kuboresha huduma za pesa kupitia ICT.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
29 Septemba, 2015
Taarifa kwa vyombo vya habari
Tanzania yatangaza hatua tano za kuendeleza haki za wanawake na usawa wa kijinsia
- Yaahidi kufanya mabadiliko makubwa ya kisera na kisheria
- Miongoni mwa Sheria zitakazohusika ni Sheria ya Ndoa na Sheria ya Urithi
- Ni katika utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu - SDG’s
Tanzania imeahidi kuchukua hatua tano muhimu za kutetetea na kuendelea haki za wanawake kati ya sasa na mwaka 2030, ikiwa ni pamoja na kufanya mabadiliko makubwa ya kufuta sheria zinazokandamiza wanawake na kutunga sheria za kuleta usawa wa kijinsia, yote katika utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG) mapya kwa manufaa ya wanawake wa Tanzania.
Miongoni mwa hatua hizo itakuwa ni pamoja na kufuta ama kufanya mabadiliko ambayo yanaendeleza vitendo vya kiutamaduni ambavyo kwavyo vinaendeleza ubaguzi wa wanawake kama vile Sheria ya Ndoa, Sheria ya Urithi na kutunga Sheria ya Kukomesha Ukatili dhidi ya wanawake.
Msimamo huo wa Tanzania umeelezwa Jumapili, Septemba 27, 2015 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete alipozungumza katika Mkutano wa Usawa wa Jinsia na Uwezeshaji wa Akinamama: Dhamira ya Kuchukua Hatua uliohudhuriwa na wakuu wa nchi mbali mbali duniani kwenye Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa (UN) mjini New York, Marekani.
Rais Kikwete ameuambia mkutano huo ulioitishwa kwa pamoja na Jamhuri ya Watu wa China, Denmark, Mexico na Kenya kuwa hatua ya pili ambayo Tanzania inakusudia kuchukua ni kuridhia makubaliano yote ya kimataifa kuhusu haki za akinamama hasa Makubaliano ya Kimataifa Juu ya Kukomesha Aina Zote za Ubaguzi Dhidi ya Wanawake – Convention on the Elimination of All Forms of Discrimination Against Women (CEDAW).
Hatua nyingine ambazo Rais Kikwete amesema kuwa Tanzania itachukua katika miaka 15 ijayo ili kuhakikisha usawa wa kijinsia nchini ni zifuatazo:
- Kuendeleza na kuunga mkono upatikanaji wa raslimali fedha zinazolenga kuongeza usawa wa kijinsia kwa mujibu wa Ajenda ya Kugharimia Maendeleo ya Addis Ababa, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha zinatolewa pesa za kutekeleza mipango ya kitaifa na ya Serikali za mitaa za kukomesha ukatili dhidi ya wanawake.
- Kuhakikisha utekelezaji wa uwakilishi wa uongozi wa asilimia 50-50 kati ya wanawake na wanaume katika nafasi zote za maamuzi kwenye ngazi zote.
- Kupatikana na kutumiwa kwa data na habari za ukweli katika utunzi wa sera na utoaji maamuzi ya kukomesha ubaguzi wa kijinsia.
- Kutunga na utekelezaji mfumo wa uwajibikaji na ufuatiliaji wa haki za kijinsia na haki za akinamama zilizokubaliwa kitaifa na kwenye ngazi ya Serikali za mitaa.
Rais Kikwete pia amewaambia wajumbe wa mkutano huo kuhusu hatua za kisera na kisheria ambazo zimechukuliwa na Tanzania katika miaka ya karibuni kujenga usawa wa kijinsia, ikiwa ni pamoja na Sheria ya Ardhi ya mwaka 1999 na marekebisho yake ya mwaka 2004 ambayo yanawapa akinamama nafasi na haki ya kupata, kushikilia, kutumia na kumiliki ardhi.
Hatua nyingine ni kuwapa wanawake nafasi za maamuzi na uongozi katika nyanja za kisiasa na maisha ya umma. Katika kutekeleza hilo, idadi ya wabunge wanawake imeongezeka kutoka asilimia 21.5 ya wabunge wote mwaka 2005 hadi kufikia asilimia 34.5 mwaka huu, mawaziri wanawake wameongezeka kutoka sita mwaka 2005 hadi kufikia 26 mwaka huu na idadi ya majaji wanawake imeongezeka kutoka wanane mwaka 2005 hadi kufikia 41 mwaka huu.
Rais Kikwete amesema kuwa hatua nyingine zilizochukuliwa na Serikali ni kupunguza vifo vya wanawake wakati uzazi, kutunga Sheria dhidi ya ukatili wa kijinsia na ukatili dhidi ya wanawake na watoto; kuanzishwa kwa uandaaji wa Bajeti inayotilia maanani mahitaji ya wanawake na kuongeza uwezekaji wa kiuchumi wa akinamama kupitia kuanzishwa kwa Benki ya Wanawake Tanzania (TWB) yenye kulenga kutoa mikopo ya masharti nafuu kwa akinamama wafanyao biashara ndogo ndogo na za kati.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
28 Septemba, 2015
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
JK: Kampeni zinaendeshwa kwa uhuru wa kumwaga kabisa
- Afafanua kuwa Tanzania inataka mchakato utakaozaa uchaguzi huru na wa haki
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete , Ijumaa, Septemba 25, 2015 amemwambia Kiongozi wa Ujerumani, Kansela Angele Merkel kuwa upo uhuru mkubwa na usiokuwa kifani kwa vyama vyote ya siasa kufanya kampeni zake kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu uliopangwa kufanyika Oktoba 25, mwaka huu, 2015.
Aidha, Rais Kikwete amemwambia Kansela Merkel kuwa Jopo la Watu Mashuhuri Duniani linalotafuta kufanya mapendekezo ya jinsi dunia inavyoweza kujiandaa vizuri zaidi kwa magonjwa ya milipuko, sasa linakaribia kumaliza kazi yake na lipo katika hatua ya kuandaa mapendekezo kuhusu nini dunia ifanye katika siku zijazo.
Rais Kikwete amekutana na kuzungumza na Kansela Merkel katika mkutano uliofanyika kwenye Ubalozi wa Ujerumani kwenye Umoja wa Mataifa (UN) mjini New York na kumuona Mama Merkel mwenyewe. Viongozi hao wawili wapo New York, Marekani kuhudhuria shughuli za mwaka huu za Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (United Nations General Assembly (UNGA).
Katika mazungumzo hayo, Kansela Merkel alitaka kujua kutoka kwa Rais Kikwete kuhusu mwenendo mzima wa Kampeni za Uchaguzi Mkuu zinazoendelea nchini na uhuru unaotolewa kwa kila chama kufanya kampeni zake.
“Kama unavyojua Mheshimiwa Kansela tuko katikati ya Kampeni ya Uchaguzi Mkuu. Kampeni zinakwenda vizuri. Tunao wagombea wa urais nadhani kiasi cha wanane hivi na kila chama kinaendesha kampeni zake kwa uhuru mkubwa na usiokuwa na kifani. Tunataka mchakato ambao utazaa uchaguzi huru na wa haki na hivyo ni muhimu kwa kila chama kuendesha shughuli zake za kampeni kwa uhuru,” Rais Kikwete amemwambia Mama Merkel.
Rais pia amemwambia Kansela Merkel kuhusu baadhi ya mambo makubwa ya kampeni yakiwemo mambo yanayohusu masuala ya huduma za kijamii kama vile afya, elimu na mapambano dhidi ya umasikini. “Kampeni zote kwenye ngazi zote – ngazi ya urais, ngazi za wabunge na ngazi za Serikali za mitaa zinakwenda vizuri kwa uhuru wa kumwaga kabisa.”
Rais Kikwete pia ametumia mkutano wake na Kansela Merkel kumweleza Mama huyo kuhusu kazi ya Jopo ya Watu Mashuhuri Duniani kuhusu Matatizo ya Afya akisisitiza kuwa baada ya hatua ya kuwasilikiza watu mbali mbali, sasa Jopo limeanza kuandaa maoni yake na mapendekezo.
Jopo hilo ambalo liliteuliwa Aprili mwaka huu na Katibu Mkuu wa UN Mheshimiwa Ban Ki Moon kufuatia majonzi makubwa yaliyosababishwa na ugonjwa wa Ebola katika nchi za Guinea, Liberia na Sierra Leone, linatarajiwa kukabidhi ripoti yake kwa Mheshimiwa Ban Ki Moon Desemba mwaka huu.
Ujerumani ni moja ya nchi zinazoongoza dunia katika kuunga mkono na kugharimia shughuli za Jopo hilo na pia imewekeza fedha nyingi katika kugharimia uboreshaji wa mifumo ya afya katika nchi za Guinea, Liberia na Sierra Leone.
Baadaye usiku, Rais Kikwete alikuwa mmoja wa viongozi wa nchi nane duniani ambao wamehudhuria chakula cha usiku ambacho kimeandaliwa na Kansela Merkel kwa ajili ya viongozi ambao wanaunda kundi la nchi ambazo zimekubali kubeba wajibu wa kuhakikisha utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (Sustainable Development Goals –SDG) ambayo yanachukua nafasi ya Malengo ya Maendeleo ya Milenia (MDG) ambayo muda wake wa utekelezaji wa miaka 15 umemalizika.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
26 Septemba, 2015
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Tanzania kuongoza utekelezaji wa malengo mapya ya maendeleo duniani.
- Imeteuliwa mongoni mwa nchi nane tu duniani kufanya kazi hiyo
- Rais Kikwete amesema kuwa Tanzania iko tayari kuifanya kazi hiyo
Tanzania ni moja ya nchi nane duniani zilizoteuliwa katika kundi la nchi zitakazoongoza mapambano ya dunia ya utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (Sustainable Development Goal – SDG’s) ambayo yanachukua nafasi ya Malengo ya Maendeleo ya Milenia (Millennium Development Goals –MDG’s) ambayo muda wake wa utekelezaji wa miaka 15 umemalizika mwaka huu. Nchi hizo zinajulikana kama High Level Support Group.
Tanzania imechaguliwa kuwa miongoni mwa nchi hizo nane duniani katika dhamira ya kisiasa ambayo inaongozwa na nchi za Sweden na Ujerumani ili kuhakikisha kuwa SDG’s zinapata mafanikio makubwa zaidi katika kukabiliana na changamoto za duniani ukiwemo umasikini. Kazi kubwa ya nchi hizo itakuwa ni kuongoza mapambano ya kutafuta utashi wa kisiasa duniani kwa ajili ya utekelezaji wa malengo hayo.
Nchi nyingine duniani mbali na Tanzania, Sweden kwa ajili hiyo ya kisiasa ni Brazil, Liberia, Tunisia, Colombia na Timor ya Mashariki.
Kazi ya nchi hizo ambayo itakuwa ni ushawishi na kuongoza mapambano ya utekelezaji wa SDG’s imezinduliwa usiku wa Ijumaa, Septemba 25, 2015 katika halfa maalum iliyoandaliwa na Waziri Mkuu wa Sweden Mheshimiwa Stefan Lofven kwenye Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa (UN) mjini New York, Marekani.
Kama ilivyokuwa kwa MDG’s, malengo ya SDG’s yamejadiliwa na kukubaliwa na nchi wanachama wa UN ambayo ndiyo msimamizi mkuu wa malengo hayo muhimu katika kukabiliana na changamoto kuu duniani ukiwamo umasikini na shughuli za tabianchi.
Katika halfa hiyo, viongozi wa nchi hizo nane, wameonyesha na kuthibitisha dhamira yao ya kuongoza mapambano ya kisiasa ya kutekeleza SDG’s kwa kutia saini azimio maalum ambako kila nchi imejithibitisha dhamira yake katika mapambano hayo.
Viongozi ambao wametia saini azimio hilo ni Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Waziri Mkuu wa Sweden Mheshimiwa Lofven; Mheshimiwa Angela Merkel, Kansela wa Ujerumani; Mheshimiwa Dilma Rousseff, Rais wa Brazil na Mama Ellen Johnson Sirleaf, Rais wa Jamhuri ya Liberia.
Viongozi wengine ambao wametia saini azimio hilo ni Mheshimiwa Juan Manuel Santos, Rais wa Colombia; Mheshimiwa Taur Matan Rauk, Rais wa Timor Mashariki na Waziri Mkuu wa Tunisia, Mheshimiwa Habib Essid ambaye amemwakilisha Rais wake.
Akizungumza katika halfa hiyo, Rais Kikwete amesema kuwa utekelezaji wa MDG’s umeonyesha dhahiri kuwa masuala makuu yanayoongoza mafanikio ya shughuli hiyo ni upatikanaji wa fedha za kutosha kutekeleza malengo hayo na kuwepo kwa mfumo thabiti wa kufuatia utekelezaji. “Na haya mawili, kwa pamoja, yalitegemea sana utashi wa kisiasa wa utekelezaji wa malengo hayo.”
“Nimesimama hapa kukuambia yale ambayo nilikuambia nchini Sweden tulipokutana kiasi cha miezi mitatu iliyopita, kwamba naunga mkono wazo la kuanzishwa kwa kundi la nchi hizi nane na niko tayari kutoa utumishi wangu kwa kazi hii sasa na katika siku zijazo baada ya kuwa nimestaafu kutoka kwenye uongozi wa nchi yangu.”
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
26 Septemba, 2015
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Sasa ni Rasmi: Tanzania kupata mabilioni mengine ya MCC
- Yafaulu mtihani wa kupata bilioni 992.8 za kuboresha sekta ya umeme
- Yafanikiwa baada ya kutimiza masharti yote likiwemo la kupambana na rushwa
- Zitaanza kutolewa mwakani baada ya kupigiwa kura na Bodi ya MCC
Tanzania imetimiza masharti yote ya kupatiwa raundi ya pili ya fedha za maendeleo kutoka Shirika la Maendeleo ya Milenia la Millennium Challenge Corporation (MCC) la Marekani na itaanza kupata na kunufaika na mabilioni hayo ya fedha baada ya wajumbe wa Bodi ya MCC kupiga kura ya kuidhinisha kutolewa kwa fedha hizo chini ya Mpango wa MCC-2.
Habari hizo njema zimetangazwa Jumamosi, Septemba 26, 2015, kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, na Mtendaji Mkuu wa MCC, Bi. Dana J. Hyde katika mkutano uliofanyika katika Hoteli ya JW Marriot Essex House, New York, na kuhudhuriwa na watumishi waandamizi wa MCC akiwamo Bwana Kamran Khan, Makamu wa Rais wa Operesheni za MCC. Rais Kikwete yuko New York kuhudhuria shughuli za mwaka huu za Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.
“Hongera Mheshimiwa Rais kwa sababu nchi yako, Tanzania imetimiza masharti yote ya kupata fedha nyingine chini ya mpango wa MCC - 2, ikiwa ni pamoja na uongozi wa MCC kuridhika kuwa Tanzania inachukua hatua za dhati kupambana na rushwa,” Bi. Hyde amemwambia Rais Kikwete na viongozi wengine wa Tanzania akiwamo Waziri wa Nchi za Fedha wa Zanzibar, Mheshimiwa Yusuf Omar Mzee.
Bi. Hyde amemwambia Rais Kikwete kuwa Bodi ya MCC, katika mkutano wake wa Septemba 17, mwaka huu na chini ya Mwenyekiti wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Bwana John Kerry, imeafiki kuhusu kipengele pekee kilichokuwa kimebakia katika masharti ya kupata fedha za MMC kuwa ni kweli Tanzania inakabiliana ipasavyo na rushwa na kuchukua hatua stahiki kukabiliana na janga hilo la rushwa.
MCC imetoa taarifa ya kuthibitisha kuwa Tanzania imetimiza masharti ya kuiwezesha kufaulu kupata raundi ya pili ya fedha za maendeleo na pia imetoa taarifa ya kuthibitisha kuwa ni kweli Bodi ya MCC imeridhishwa na hatua zinazochukuliwa kukabiliana na rushwa.
Tofauti na fedha nyingi zinazotolewa na wafadhili wengi duniani, fedha za MCC hazitakiwi kurudishwa na nchi inayopewa fedha hizo na pia nchi husika hupewa uhuru wa kuchagua aina ya miradi ya maendeleo ambayo inaitaka igharimiwe na fedha hizo.
Miongoni mwa wajumbe wengine wa Bodi ya MCC ni pamoja na Waziri wa Fedha wa Marekani ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Bodi, Mwakilishi wa Biashara wa Marekani duniani, Mwendeshaji Mkuu wa Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani (USAID), nafasi ambayo kwa sasa anaikaimu Bwana Alfonsi Lenhardt, Mtendaji Mkuu wa MCC Bi. Hyde na Rais wa Taasisi ya International Republican Institute (IRI) Balozi Mark Green.
Mabalozi Lenhardt na Green walikuwa mabalozi wa Marekani katika Tanzania wakati wa majadiliano, upitishaji na utekelezaji wa MCC–1.
Bi Hyde amesema sasa linalobakia ni kwa wajumbe wa Bodi kupelekewa muhtasari wa kuidhinisha mabilioni hayo kwa Tanzania ambayo chini ya mpango wa uwekezaji wa MCC–2 yatakwenda katika kuboresha huduma za umeme katika Tanzania ikiwa ni pamoja na kusambaza umeme katika vijiji vingi zaidi nchini. Kiasi cha asilimia 46 ya Watanzania kwa sasa wanapata umeme kutoka asilimia 10 ya mwaka 2005 na sehemu kubwa ya asilimia hiyo imetokana na msaada wa MCC-1.
Chini ya Mpango huo wa pili wa MCC, Tanzania itapatiwa kiasi cha dola za Marekani milioni 472.8 (sawa na sh. bilioni 992.80). Kwa kutilia maanani kiasi cha dola milioni 698 (sawa na sh. trilioni 1.46) ambazo zilitolewa chini ya MCC-1 basi Tanzania itakuwa imepata jumla ya dola za Marekani trilioni 2.45 za maendeleo kutoka Marekani katika kipindi cha miaka 10 tu iliyopita. Fedha za MCC-2 zitaanza kutolewa mwakani, 2016.
Kiasi kilichotolewa kwa Tanzania wakati wa MCC-1 ndicho kilikuwa kiasi kikubwa zaidi ambacho kimepata kutolewa na Marekani chini ya Mpango huo wa Millennium Challenge Corporation na kwa kupita MCC-2 Tanzania itakuwa ni nchi ambayo itakuwa imepata kiasi kubwa cha fedha za maendeleo chini ya MCC duniani.
Fedha zilizotolewa chini ya MCC -1 zilitumika kujenga Barabara za Tunduma-Sumbawanga, Tanga-Horohoro na Namtumbo-Songea-Mbinga.
Aidha, fedha hizo zilitumika kujenga upya mfumo wa huduma za maji kwa ajili ya miji ya Dar es Salaam na Morogoro na zilitumika kusambaza umeme katika vijiji vya mikoa 10 ya Tanzania Bara.
Fedha hizo vile vile zilitumika kutandaza njia ya pili ya kusafirisha umeme chini ya Bahari ya Hindi kati ya Bara na Tanzania Visiwani na pia zilitumika kujenga barabara zote kuu za Kisiwa cha Pemba na baadhi ya barabara za Unguja kwa kiwango cha lami.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
27 Septemba, 2015