Taarifa kwa vyombo vya Habari ya zamani
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 16 Mei, 2017 amefanya ziara katika ofisi za Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) ambapo amekagua miundombinu ya shirika hilo na kuzungumza na wafanyakazi.
Mhe. Rais Magufuli amejionea jinsi miundombinu ya shirika hilo inavyokabiliwa na changamoto mbalimbali za uchakavu na teknolojia duni na amesema Serikali itafanyia kazi changamoto hizo ikiwa ni pamoja na kujenga majengo mapya ya studio za kisasa za kurushia matangazo katika makao makuu ya nchi Mjini Dodoma.
Hata hivyo Mhe. Dkt. Magufuli ambaye hivi karibuni ametoa Shilingi Bilioni 3 kwa ajili ya kuisaidia TBC amemtaka Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo Dkt. Ayub Rioba kutumia fedha hizo kutatua matatizo ya uhaba na uchakavu wa vifaa vya uzalishaji wa vipindi na urushaji wa matangazo, kununua vyombo vya usafiri na kufanya ukarabati wa majengo.
Kuhusu maslahi ya wafanyakazi amewahakikishia kuwa Serikali itaboresha stahili zao kwa mujibu wa utaratibu uliopo na papohapo amemuagiza Dkt. Rioba kulipa mara moja malimbikizo ya posho zote ambazo wafanyakazi hao wanadai kuanzia Mwezi Oktoba 2016, zilizofikia shilingi Bilioni 1 na milioni 285.
Mhe. Rais Magufuli ametaka wafanyakazi wa TBC kufanya kazi kwa juhudi, maarifa na ubunifu wa hali ya juu ili matangazo ya chombo hicho cha Taifa yawavutie Watanzania wengi, na kiwe chombo kinachoongoza nchini.
“Msemaji wa Serikali mkubwa ni TBC1 na Redio ya Taifa, nyinyi hamuwezi mkawa kama vyombo vingine ambavyo vina malengo yao ya kufanya biashara, nyinyi kazi yenu ni kutoa taarifa sahihi kwa Watanzania bila kubagua vyama vyao, bila kubagua dini zao, bila kubagua makabila yao, huo ndio uwe msimamo mkuu.
“Mmetoa mchango mkubwa sana kwenye Taifa hili, hilo ni lazima niseme, hata vipindi vyenu ukiviangalia ni vizuri vinaeleza mpaka maisha ya vijijini, na mimi ni shabiki mkubwa sana wa TBC, lakini tatizo lenu mnashindwa kwenda na wakati wa sasa” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli amemuagiza Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe aliyekuwepo katika ziara hiyo kuuangalia Mkataba kati ya TBC na Star Times na kuchukua hatua zinazostahili endapo itabainika kuwa mkataba huo hauna manufaa.
Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Fedha Duniani (IMF) Bw. Tao Zhang na kuishukuru IMF kwa kuendelea kuwa wadau wa maendeleo wa Tanzania.
Mhe. Rais Magufuli amemueleza Bw. Tao Zhang kuwa Tanzania inatekeleza mpango wa pili wa maendeleo utakaoiwezesha kuwa nchi ya uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025 na hivyo ameiomba IMF kushirikiana na Tanzania kutekeleza miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa miundombinu, uwekezaji katika viwanda na kuwahamasisha wadau wengine kuwekeza hapa nchini.
Kwa upande wake Bw. Tao Zhang amempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa kazi kubwa anayoifanya kusimamia uchumi wa Tanzania na amesema uchumi wa Tanzania umeendelea kukua vizuri tangu miaka 20 iliyopita ukichagizwa na uwepo wa sera nzuri na mipango imara ya mageuzi, na kwamba anaamini kuwa uongozi mzuri wa Mhe. Rais Magufuli akishirikiana na wadau wa maendeleo wataendelea kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazoukumba uchumi duniani.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
16 Mei, 2017
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ameridhia maombi ya kuacha kazi kwa viongozi wafuatao;
- Ndg. Saidi Meck Sadiki - Aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro.
- Ndg. Aloysius Kibuuka Mujulizi - Aliyekuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Mwenyekiti wa Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania.
- Ndg. Upendo Hillary Msuya - Aliyekuwa Jaji wa Mahakama Kuu Tanzania.
Taarifa iliyotolewa leo tarehe 16 Mei, 2017 na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi imeeleza kuwa Mhe. Rais Magufuli ameridhia maombi ya kuacha kazi kwa viongozi hao kuanzia tarehe 15 Mei, 2017.
Gerson Msigwa,
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU,
Dar es Salaam,
16 Mei, 2017.
Taarifa kwa vyombo vya habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, leo tarehe 15 Mei, 2017 ameivunja rasmi Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu Dodoma (CDA) na ameagiza mali na shughuli zote zilizokuwa zikifanywa na CDA zihamishiwe Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma.
Mhe. Rais Magufuli ameivunja CDA kwa kutia saini hati ya Amri ya Rais ya kuivunja Mamlaka hiyo Ikulu Jijini Dar es Salaam, tukio ambalo limeshuhudiwa na Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Vangimembe Lukuvi, Waziri wa Sheria na Katiba Mhe. Prof. Palamagamba John Aidan Mwaluko Kabudi, Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Antony Mavunde, Katibu Mkuu Kiongozi Mhe. Balozi John Kijazi, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Bw. Jordan Rugimbana na viongozi mbalimbali wa wizara.
Mhe. Rais Magufuli amesema ameamua kuivunja CDA na kuhamishia majukumu yake katika Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma ili kuondoa mkanganyiko wa utoaji wa huduma kwa wananchi uliokuwa ukisababishwa na mgongano kati ya vyombo hivyo viwili na pia kuendana na mahitaji ya sasa ambayo yamedhihirisha kuwa hakuna haja ya kuwepo kwa CDA.
Kufuatia uamuzi wa kuivunja CDA, Mhe. Dkt. Magufuli pia ameivunja Bodi ya CDA, aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa CDA Mhandisi Paskasi Muragili atapangiwa kazi nyingine na ameagiza wafanyakazi wote wa Mamlaka hiyo wahamishiwe Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma na ofisi nyingine za Serikali kadiri inavyofaa.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli ameagiza hati zote za kumiliki ardhi zilizokuwa zikitolewa na CDA kwa ukomo wa umiliki wa miaka 33 zibadilishwe na kufikia ukomo wa umiliki wa miaka 99 kama ilivyo katika maeneo mengine nchini ili kuwavutia wawekezaji hasa wa viwanda.
“Wananchi wa Dodoma wamelalamikia tatizo hili kwa muda mrefu sana, hata nilipokuwa kwenye kampeni zangu za uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 walilalamika sana, sasa nimetekeleza niliyowaahidi, naamini kwa uamuzi huu malalamiko ya wananchi yatapata utatuzi na pia tutakuwa tumeondoa kikwazo cha umiliki wa muda mfupi wa ardhi uliosababisha wawekezaji kushindwa kujenga viwanda Dodoma.
“Sasa majukumu yote yanahamishiwa Manispaa ya Dodoma, sitaki kuendelea kusikia visingizio, mkajipange mambo yaende vizuri” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa wamemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa uamuzi huo na wameahidi kusimamia kwa ukaribu mchakato wa kuhamisha majukumu ya CDA kwenda Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma.
Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu Dodoma (CDA) ilianzishwa kwa Amri ya Rais ya tarehe 01 Aprili, 1973 na kutangazwa kupitia tangazo la Serikali namba 230 na imevunjwa rasmi leo tarehe 15 Mei, 2017 kwa Amri ya Rais na kuchapishwa katika gazeti la Serikali.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
15 Mei, 2017
Taarifa kwa vyombo vya habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ameitumia salamu za rambirambi familia ya mmoja wa Waasisi wa Taifa la Tanzania Ndg. Paul Sozigwa aliyefariki dunia leo tarehe 12 Mei, 2017 Jijini Dar es Salaam.
Katika Salamu hizo Mhe. Rais Magufuli amesema Marehemu Paul Sozigwa atakumbukwa kwa utumishi wake uliotukuka kwa Taifa, uchapakazi na uadilifu.
“Natambua kuwa Marehemu Paul Sozigwa ni miongoni mwa Waasisi wa Taifa letu ambao walijitoa kwa dhati kuipigania nchi yetu kabla na baada ya uhuru, alishirikiana na Waasisi wengine wa Taifa letu akiwemo Baba wa Taifa Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere, kukabiliana na changamoto mbalimbali zilizolikabili Taifa letu baada ya uhuru zikiwemo kupiga vita umasikini, ujinga na maradhi ndani ya Chama na Serikali, hakika tutazienzi juhudi zake” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli ameitumia salamu za rambirambi familia ya aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Ndg. Said Mwambungu aliyefariki dunia leo tarehe 12 Mei, 2017 katika hospitali ya Taifa Muhimbili Jijini Dar es Salaam.
Mhe. Rais Magufuli amesema Marehemu Saidi Mwambungu atakumbukwa kwa uchapakazi wake, busara, uongozi mahiri, na uzalendo wake kwa Taifa alipokuwa kiongozi ndani ya Serikali na katika Chama Cha Mapinduzi (CCM).
“Ndg. Said Mwambungu alikuwa ni kiongozi wa aina yake, moyo wake wa upendo ulimwezesha kufanikiwa katika kazi zake nyingi, siku zote alipigania maendeleo ya wananchi na hakushindwa kutatua jambo kwa njia ya mazungumzo, hakika tutaukumbuka na kuuenzi mchango wake” amefafanua Mhe. Rais Magufuli.
Mhe. Rais Magufuli amewapa pole nyingi wanafamilia, wanachama wa CCM, na wananchi wote walioguswa na vifo hivyo na amewaombea wapumzike mahali pema peponi, Amina.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
12 Mei, 2017
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Afrika ya Kusini Mhe. Jacob Gedleyihlekisa Zuma amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali yake ya Awamu ya Tano kwa kuanza ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa (Standard Gauge) na ameahidi kuunga mkono ujenzi huo.
Mhe. Rais Zuma ametoa kauli hiyo wakati wa mazungumzo rasmi na alipokuwa akizungumza na wananchi wa Tanzania na Afrika Kusini kupitia vyombo vya habari Ikulu Jijini Dar es Salaam, ikiwa ni katika ziara yake rasmi ya kiserikali ya siku mbili hapa nchini kwa mwaliko wa Mhe. Rais Magufuli.
Mhe. Rais Zuma amesema anatambua kuwa ujenzi wa reli ya kati utaleta manufaa makubwa kwa Tanzania na nchi za maziwa makuu na hivyo amekubali ombi la Mhe. Rais Magufuli la kuwahamasisha wafanyabiashara na wawekezaji wa Afrika ya Kusini kushirikiana na Tanzania kufanikisha mradi huo mkubwa.
Wakiwa katika Mazungumzo rasmi viongozi hao wamezindua rasmi Tume ya Pamoja ya Marais (Bi-National Commission-BNC) kwa kufanya kikao cha kwanza cha tume hiyo tangu ianzishwe mwaka 2011 ambapo wamepokea makubaliano yaliyofikiwa katika kikao cha tume ngazi ya mawaziri.
Kabla ya kuzungumza na wananchi kupitia vyombo vya habari Mhe. Rais Magufuli na Mhe. Rais Zuma wameshuhudia utiaji saini wa hati tatu za ushirikiano kati ya Tanzania na Afrika Kusini ambazo ni Muhtasari wa makubaliano ya Mkutano wa Tume ya Pamoja ya Marais, Makubaliano ya Ushirikiano katika Masuala ya Bioanuwai na Uhifadhi na Makubaliano ya Ushirikiano katika Sekta ya Uchukuzi.
Akizungumzia makubaliano na mazungumzo yao Mhe. Rais Magufuli amemshukuru Mhe. Rais Zuma kwa kuitikia mwaliko wake na kukubali kuendeleza na kuongeza zaidi ushirikiano na uhusiano kati ya nchi yake na Tanzania hususani kuwahimiza wawekezaji na wafanyabiashara kuja kuwekeza nchini Tanzania katika sekta mbalimbali zikiwemo Kilimo, Ujenzi wa Miundombinu, Utalii, Madini na Afya kwa kutumia uwezo mkubwa uliopo Afrika Kusini.
Mhe. Rais Magufuli amesema hivi sasa biashara kati ya Tanzania na Afrika Kusini kwa mwaka ni Shilingi Trilioni 2.4, uwekezaji wa Afrika Kusini hapa nchini ni Dola za Marekani Milioni 803.15 uliozalisha ajira 20,916 na kwamba kiwango hicho kinaweza kuongezeka zaidi endapo ushirikiano utaimarishwa zaidi.
“Na ili tufanikiwe kukuza biashara tumekubaliana kuondoa vikwazo na kuwahamasisha wafanyabiashara na wawekezaji wa nchi zetu mbili kutumia fursa ya uhusiano na ushirikiano mzuri wa kirafiki na kidugu uliopo kati ya nchi zetu kufanya kazi pamoja” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Mhe. Dkt. Magufuli ameongeza kuwa Tanzania itapeleka walimu wa lugha ya Kiswahili ambayo inazungumzwa na watu takribani milioni 120 ili wakafundishe lugha hiyo katika vyuo vya Afrika ya Kusini na hivyo kuimarisha zaidi ushirikiano.
Kwa upande wake Mhe. Rais Zuma amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kumualika kufanya ziara rasmi ya kiserikali hapa nchini na amesema nchi yake itahakikisha makubaliano yote ya Tume ya Pamoja ya Marais yanatiliwa mkazo na kutekelezwa kwa kuzingatia muda uliopangwa.
Mhe. Rais Zuma amesema Afrika Kusini inatambua na kuheshimu mchango mkubwa wa Tanzania kwa ukombozi wa nchi mbalimbali za Afrika ikiwemo Afrika Kusini ambayo Hayati Baba wa Taifa Mwl. Julius Kambarage Nyerere alishirikiana na Waasisi wa Taifa hilo walioongozwa na Hayati Mzee Nelson Mandela kupigania Ukombozi na Uhuru na kwamba anafurahi kuona Tanzania bado inatoa mchango mkubwa kupigania Amani katika Bara la Afrika.
“Mhe. Rais Magufuli naomba nikuhakikishie kuwa Afrika Kusini itaendeleza na kuimarisha zaidi uhusiano wake na ndugu na marafiki zake Tanzania katika kujenga uchumi kwa manufaa ya wananchi na pia kupigania amani kwa kuwa bila amani na usalama hakuna maendeleo” amesema Mhe. Rais Zuma.
Pamoja na kufanya mazungumzo rasmi, viongozi hawa watashiriki mkutano wa wafanyabiashara wa Tanzania na Afrika Kusini (Business Forum) unaofanyika katika ukumbi wa Kimataifa wa Julius Nyerere na jioni Mhe. Rais Zuma atahudhuria dhifa ya kitaifa iliyoandaliwa kwa heshima yake na mwenyeji wake Mhe. Rais Magufuli Ikulu Jijini Dar es Salaam kabla ya kurejea Afrika Kusini baadaye leo.
Gerson Msigwa,
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU,
Dar es Salaam,
11 Mei, 2017.
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ametoa magari mapya matatu ya kubebea wagonjwa kwa Wabunge watatu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili kuwasaidia wananchi wa maeneo yao ya ubunge.
Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi amekabidhi magari hayo aina ya Land Cruiser Hardtop kwa niaba ya Rais Ikulu Jijini Dar es Salaam kwa Mbunge wa Nkasi Kaskazini Mkoa wa Rukwa Mhe. Ally Keissy, Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Tabora Mhe. Munde Tambwe na Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Shinyanga Mhe. Lucy Mayenga.
Akizungumza baada ya makabidhiano hayo, Balozi Kijazi amesema Mhe. Rais Magufuli ametoa magari hayo baada ya kuguswa na kilio cha muda mrefu cha Wabunge hao waliokuwa wakiomba wananchi wao wapatiwe magari ya wagonjwa.
“Mhe. Rais ameamua kuwakabidhi nyinyi haya magari kutokana na vilio vyenu ambavyo amekuwa akivisikia mara kwa mara, Mhe. Keissy umekuwa hata ukitafuta miadi ya kuja kumuona Mhe. Rais kwa suala hili, Waheshimiwa Wabunge wamekuwa wakiyazungumza haya kwa muda mrefu.
“Tunafahamu kila Mbunge katika jimbo lake anahitaji kupata huduma kama hii, na huduma kama hii ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM, kwa hiyo sisi Serikali kila tunapopata uwezo basi tunasaidia pale tunapoweza kufikia kwa wakati ule, tulishatoa magari mengine matatu kama haya Chalinze na vituo vingine vya Morogoro.” Amesema Balozi Kijazi
Balozi Kijazi amewapongeza Wabunge hao kwa kupata magari hayo kwa ajili ya wananchi wao na amewasihi kuhakikisha yanatunzwa vizuri ili yadumu muda mrefu na yawahudumie wananchi wote bila kujali dini, kabila, itikadi zao za kisiasa wala makundi.
Kwa upande wao Mhe. Ally Keissy, Mhe. Munde Tambwe na Mhe. Lucy Mayenga wamemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kuitikia kilio chao cha kuwasaidia wananchi magari ya kubebea wagonjwa, na wamempongeza kwa kazi nzuri ya kuwapigania Watanzania wote hasa wenye shida na pia kwa juhudi kubwa za kuleta maendeleo.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
09 Mei, 2017
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 06 Mei, 2017 amezindua Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) na kuongoza Mkutano wa 10 wa Baraza hilo uliofanyika katika ukumbi wa Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Baraza hili ni la tatu na mkutano huu ni wa kwanza kuongozwa na Mhe. Rais Magufuli tangu aingie madarakani ambapo tofauti na mikutano mingine, Mhe. Rais Magufuli ameendesha majadiliano ya pamoja ambapo wajumbe wa baraza na wawakilishi wengine kutoka sekta binafsi wamepata fursa ya kutoa maoni, mapendekezo na dukuduku, kisha kupatiwa majibu kutoka kwa Mawaziri, Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa na Mhe. Rais.
Miongoni mwa yaliyojitokeza ni kuiomba Serikali kuendelea kushirikiana na sekta binafsi katika upangaji na utekelezaji wa mipango, sera na sheria mbalimbali za uwekezaji na biashara, kuendelea kuondoa vikwazo na urasimu ambao unachangia kupunguza ufanisi katika biashara na uwekezaji, kuongeza vivutio vya uwekezaji na kuendelea kushirikisha sekta binafsi katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ujenzi, utalii na viwanda.
Aidha, wawakilishi wa sekta binafsi wameipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kwa juhudi kubwa inazozifanya kujenga miundombinu muhimu kwa uwekezaji na biashara kama vile ujenzi wa reli, barabara, meli na ununuzi wa ndege, kukabiliana na rushwa, kusimamia mpango wa ujenzi wa viwanda, kujenga nidhamu na uwajibikaji wa watumishi wa umma na kujenga uhusiano mzuri na mataifa mbalimbali duniani.
Pamoja na majibu yaliyotolewa na Mawaziri ambao ni wajumbe wa Baraza la Taifa la Biashara, Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa amewaahidi wawakilishi wa sekta binafsi waliohudhuria mkutano huo kuwa Serikali itahakikisha maoni yao yote yanafanyiwa kazi ili Taifa liweze kunufaika na rasilimali zake na kusonga mbele kimaendeleo.
“Naomba niwahakikishie kuwa hisia zenu tumezipata, maoni yenu tutayazingatia na tutahakikisha tunayafanyia kazi haraka iwezekanavyo ili kwa pamoja tufanye kazi ya kuijenga nchi yetu” amesema Mhe. Majaliwa.
Mhe. Rais Magufuli amewapongeza wajumbe wa Baraza la Taifa la Biashara pamoja na Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) inayoongozwa na Mwenyekiti wake Dkt. Reginald Mengi kwa juhudi kubwa zinafanywa kuendeleza biashara na uwekezaji nchini na amewaahidi kuwa Serikali ya Awamu ya Tano itaendelea kuwathamini na kushirikiana na wawekezaji na wafanyabiashara kwa manufaa ya Taifa.
Mhe. Rais Magufuli ameelezea kufurahishwa na maoni, mapendekezo na dukuduku alizozipata kutoka kwenye mkutano huo na amewakikishia kuwa Serikali anayoiongoza itafanyia kazi maoni yote yaliyotolewa ikiwemo kuondoa usumbufu unaosababishwa na uwingi wa taasisi zinazomhudumia na kumtoza mfanyabiashara na mwekezaji, kuongeza vivutio, kuboresha mifumo ya ukusanyaji wa kodi mbalimbali na kuishirikisha sekta binafsi katika mipango na utekelezaji wa miradi.
Kuhusu tatizo la ucheleweshaji wa mizigo bandarini Mhe. Rais Magufuli ameagiza kuanzia Jumatatu tarehe 08 Mei, 2017 taasisi zote zinazotoa huduma katika bandari ya Dar es Salaam ziungane na Mamlaka ya usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kutoa huduma kwa muda wote wa saa 24.
“Kama alivyosema Waziri Mkuu, tunataka kufanyia kazi maoni yenu mara moja, kuanzia Jumatatu nataka taasisi zote za pale bandarini zitoe huduma saa 24, haiwezekani bandarini kwetu mizigo ichukue siku 13 kuitoa bandarini wakati bandari za wenzetu majirani inatoka baada ya siku 3, tutashindana vipi?” amehoji Mhe. Rais Magufuli.
Hata hivyo Mhe. Dkt. Magufuli amewataka wafanyabiashara na wawekezaji wajirekebisha kwa kasoro ambazo baadhi yao wanazo ikiwemo ukwepaji wa kodi, kupandisha viwango vya bei kwa huduma wanazotoa Serikalini, kujihusisha na rushwa, kutaka faida kubwa isiyostahili bila kuwajali wananchi na kutochangamkia fursa za uwekezaji za ndani na nje ya nchi licha ya juhudi zake za kuwaleta viongozi na wafanyabiashara kutoka nchi mbalimbali.
“Nataka mjiulize amekuja Waziri Mkuu wa India, amekuja Rais wa Vietnam, amekuja Rais wa Uturuki, amekuja Rais wa Kongo (DRC), amekuja Rais wa Zambia, amekuja Rais wa Uganda, amekuja Mfalme wa Morocco na wengine wengi, tumenufaikaje? Mbona wao wanakuja kuwekeza hapa nyie kwa nini hamuendi kwao?” amehoji Mhe. Rais Magufuli.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
06 Mei, 2017
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amepokea kwa mshtuko na masikitiko makubwa taarifa ya vifo vya wanafunzi 32 wa darasa la saba, walimu 2 na dereva wa gari la shule ya msingi iitwayo Lucky Vicent ya Arusha vilivyotokea leo saa 3 asubuhi baada ya gari walilokuwa wakisafiria kupata ajali katika eneo Rhotia Marera, Wilaya ya Karatu Mkoani Arusha.
Wanafunzi na walimu hao walikuwa wakitoka shuleni kwao kwenda shule ya msingi iitwayo Tumaini kwa ajili ya kufanya mtihani wa ujirani mwema na walipofika katika eneo la Rhotia Marera basi walilopanda liliacha njia na kisha kutumbukia korongoni ambako limesababisha vifo hivyo na majeruhi watatu.
Kufuatia ajali hii, Mhe. Rais Magufuli amemtumia salamu za rambirambi Mkuu wa Mkoa wa Arusha Bw. Mrisho Gambo na kueleza kuwa ajali hiyo imezima ndoto za watoto waliokuwa wakijiandaa kulitumikia Taifa na imesababisha uchungu, huzuni na masikitiko makubwa kwa familia za marehemu na Taifa kwa ujumla.
“Ndg Mkuu wa Mkoa wa Arusha Bw. Mrisho Gambo naomba unifikishie pole nyingi kwa wazazi, ndugu, jamaa na marafiki wote wa wanafunzi, walimu na dereva waliopoteza maisha, hiki ni kipindi kigumu kwetu sote, na uwaambie naungana nao katika majonzi na maombi.
“Muhimu kwa sasa tuwaombee marehemu wote wapumzishwe mahali pema, majeruhi wapone haraka na wote walioguswa na msiba huu wawe na moyo wa subira, ustahimilivu na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu” Amesema Mhe. Rais Magufuli.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
06 Mei, 2017
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amemteua Prof. Egid Beatus Mubofu kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS).
Taarifa iliyotolewa leo tarehe 04 Mei, 2017 na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi imeeleza kuwa uteuzi wa Prof. Egid Beatus Mubofu umeanza tarehe 02 Mei, 2017.
Prof. Egid Beatus Mubofu aliyekuwa akikaimu nafasi hiyo amechukua nafasi iliyoachwa wazi na Bw. Joseph B. Masikitiko ambaye uteuzi wake umetenguliwa.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
04 Mei, 2017
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, leo tarehe 02 Mei 2017, amemaliza ziara ya siku Tatu mkoani Kilimanjaro, ambapo akiwa mkoani hapa pamoja na mambo mengine alikuwa mgeni rasmi katika Maadhimisho ya siku ya Wafanyakazi Duniani - Mei Mosi.
Katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Kilimanjaro - KIA, Rais Magufuli ameagwa na viongozi mbalimbali wa mkoa huo wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Mhe. Said Mecki Saidick.
.
Jaffar Haniu,
Naibu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU,
Moshi, Kilimanjaro.
02 Mei, 2017
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, leo tarehe Mosi Mei, 2017 amesema Serikali ya Awamu ya tano imepanga kufanya nyongeza ya kawaida ya kila mwaka katika mishahara yaani Annual increment, ambayo ilikuwa imesimama kwa muda mrefu ikiwa ni pamoja na promosheni.
Rais Magufuli ametoa ahadi hiyo katika Sherehe za siku ya Wafanyakazi duniani zilizofanyika katika Uwanja wa Chuo cha Ushirika Moshi mkoani Kilimanjaro.
Amesema uamuzi wa Serikali wa kuanza kutoa promosheni unatokana na kukamilika kwa zoezi la uhakiki wa Wafanyakazi hewa zaidi ya wafanyakzi kumi 19,000 walibainika kuwa wafanyakazi hewa.
''Yale mambo yote yaliyokuwa pending ikiwa ni pamoja na promosheni kwa sababu tulishindwa, unaweza kupromoti mfanyakazi hewa hayupo,kwa sababu tungetoa promosheni wakati kuna wafanyakazi 19,000 hewa,maanake tungepromoti na 19,000 na siajabu na watu waliowaandika mule ndio wangeletwa katika mapendkezo ya promosheni'' amesema Rais Magufuli.
Aidha, Rais Magufuli amewaonya watumishi ambao wamekuwa wakidanganya umri wa kustaafu ili waendelee kufanya kazi kwa muda mrefu na kuwa siku zao sasa zimekwisha.
Katika hatua nyingine Rais Magufuli amepiga marufuku uhamisho wa Wafanyakazi bila kuwalipa stahili zao kutokana na kuwepo na tabia ya kuwahamisha wafanyakazi bila kuzingatia taratibu hasa za malipo ya uhamisho.
''Sasa niwaombe wafanyakazi yeyote akihamishwa hakuna kuhama mpaka umelipwa pesa ya uhamisho,kuanzia juu mpaka chini,yeyote atakaye kuhamisha mwambie nipe hela yangu ya uhamisho ninapoenda akishindwa usihame kaa hapohapo ufanye kazi'' Amesema Rais Magufuli.
Amesema viongozi wengine wamekuwa wakiwahamisha wafanyakazi kwa maslahi binafsi au visasi kutokana na maendeleo wanayowapata wafanyakzi
Rais Mgufuli amewahakikishia wafanyakazi kuwa Serikali ya awamu ya Tano itaendelea kuwajali na kuwa karibu nao katika kutimiza dhana ya utatu ya ushirikiano kati ya Serikali, Wafanyakazi na Waajiri kwa lengo la kuleta maendeleo.
Aidha, Rais Magufuli amewaeleza wafanyakazi mipango mbalimbali anayofanywa na Serikali katika kuwaletea maendeleo ikiwa ni pamoja na ununuzi wa ndege mpya ,ujenzi wa Reli ya kisasa, utoaji elimu bila malipo na uboreshaji wa miundombinu katika kuwaletea maendeleo wananchi.
Sherehe za Mei Mosi zilizofanyika katika mkoa wa Kilimanjaro pia zimehudhuriwa na Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa, Spika wa Bunge Mhe. Job Ndugai, Mawaziri, Manaibu Mawaziri, Wabunge na viongozi mbalimbali wa Chama na Serikali ambapo kauli mbiu inasema,'' Uchumi wa Viwanda uzingatie kulinda Haki, Maslahi na Heshima ya Mfanyakazi''.
Jaffar Haniu
Naibu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Moshi, Kilimanjaro
1 Mei, 2017
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, leo tarehe 30 Aprili 2017, amekutana na kuzungumza na viongozi wa dini wa madhehebu mbalimbali na kuuagiza viongozi wa mkoa wa Kilimanjaro kutatua kero zinazowakabili wananchi wa mkoa huo.
Rais Magufuli ametoa agizo hilo kufuatia malalamiko ya baadhi ya viongozi wa dini kueleza kero zinazowakabili ikiwa ni pamoja na manyanyaso yanayofanyiwa na wafanyakazi wa Wakala wa Maegesho ya magari mkoani humo.
Kufuatia malalamiko hayo, Rais Magufuli amemuagiza Kamanda wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini TAKUKURU kuchunguza mkataba uliongiwa kati ya Manispaa ya Moshi na Wakala wa Maegesho ya magari mkoni humo ili kujua uhalali wake kwani kumekuwa na ubadhirifu mkubwa wa upotevu wa mapato yatokanayo na makusanyo ya maegesho hayo.
'' Uangalie ule mkataba wa parking wa hapa Moshi,kama kuna ufisadi wowote peleka Mahakamani,lakini haya ya administration kayaangalie wasinyanyase watu, huwezi hata ukamuona sheikh unafunga gari lake,ukimuona Mchungaji na kola yake unafunga tu ni ushetani,sasa saa nyingine wale vijana wanaofanya ile kazi wanajisahau, hawaheshimu utu wa Watanzania'' amesema Rais Magufuli.
Pia amemuagiza Mkurugenzi wa Manisapaa ya Moshi kutoa kibali cha Ujenzi wa Kituo cha Uchunguzi wa maradhi kilichoombwa na mwananchi mmoja mkoani humo ili aweze kuendelea na ujenzi huo kutokana na kutopewa kibali hicho kwa muda mrefu.
Katika hatua nyingine, Rais Magufuli amesema kutokana na Serikali kuzuia unywaji wa pombe aina ya viroba idadi ya vifo katika mkoa wa Pwani imepungua kutoka 80 hadi 20 na hata ajali za pikipiki maarufu Bodaboda nazo zimepungua nchini.
Aidha, Rais Magufuli ametaka uongozi wa Wilaya ya Hai kufanya kazi bila kutishwa na madiwani ikiwa ni pamoja na kubadili sheria ndogondogo wilayani humo ili kupunguza kero za utitiri wa ushuru kwa wananchi.
Rais Magufuli ametoa maagizo hayo wakati alipokutana na viongozi wa dini wa mkoa wa Kilimanjaro, Vyama vya Siasa na watendaji wa Serikali mkoani humo na kula nao chakula cha mchana kilichoandaliwa na mkoa wa Kilimanjaro.
Jaffar Haniu
Naibu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU.
Moshi, Kilimanjaro.
30 Aprili, 2017.
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, leo tarehe 30 Aprili 2017, ameungana na waumini wa dini ya Kikristo kusali ibada ya Jumapili katika Kanisa la Kiaskofu, Jimbo Katoliki la Moshi ,Parokia ya Kristo Mfalme na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Moshi Mjini, Dayosisi ya Kaskazini mkoani Kilimanjaro na kuwataka waumini wa makanisa hayo na Watanzania kwa ujumla kuendeleza amani iliyopo nchini kwa kuwa ndio chachu ya Maendeleo.
Rais Magufuli amesema hatua zinazochukuliwa na Serikali ya awamu ya Tano zina lengo la kuwaletea wananchi maendeleo ya kweli ya taifa linalomuamini MUNGU.
'' Napenda muniamini kuwa mimi nipo kwa niaba yenu, najua huu Urais si wangu, Urais mnao ninyi mlioamuwa nitumike kama mtumishi kwa wakati huu, nawaomba sana muendelee kuniweka katika sala zenu ili kazi hii ya Urais isinipe kiburi, nikawe mtumishi wa watu'' Amesema Rais Magufuli.
Rais Magufuli amewashukuru waumini wa makanisa hayo mawili na watanzania kwa ujumla kwa kusimama pamoja kuliombea Taifa amani iliyowezesha wananchi kupiga kura kwa amani katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 na kutokana na sala zao Mwenyezi MUNGU akamuwezesha kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Aidha, Rais Magufuli ametoa msaada wa mifuko 100 ya Saruji kusaidia maendeleo ya kanisa Katoliki na Shilingi Milioni Moja kwa Kwaya ya Kanisa hilo ili irekodi nyimbo zake, halikadhalka katika Kanisa la KKKT, Mheshimiwa Rais ametoa mifuko 150 ya Saruji kwa ajili ya kuchangia maendeleo ya Kanisa hilo na Shilingi milioni Moja kwa Kwaya ya Kanisa hilo.
Nae Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu Mhe. Jenista Mhagama amemuunga mkono Rais Magufuli kwa Kuchangia Mifuko hamsini ya Saruji ambapo Mkuu wa Mkoa wa kilimanjaro Mhe. Said Meck Sadick amechangia mifuko hamsini ya Saruji na Shilingi laki Tano.
Kwa upande wake Askofu wa Jimbo Katoliki la Moshi ,Parokia ya Kristo Mfalme Askofu Isaac Amani amemshukuru Rais Magufuli kwa uwamuzi wa kusali kanisani hapo na kuwataka waumini wa kanisa hilo na Tanzania kwa ujumla kuendelea kumuombea yeye pamoja na Serikali yake ili iweze kuwatumikia Watanzania katika kuwaletea maendeleo na kuifanya Tanzania kuwa nchi ya mfano kwa Bara la Afrika.
Kwa upande wake Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania - KKKT, Askofu Dr Fredrick Shoo amewataka waamini wa kanisa hilo na watanzania kwa ujumla kutokuwa na hofu kwa mambo yanayofanywa na Rais hususani katika kupambana na maovu, dhuluma na ufisadi vikiwemo na badala yake Watanzania wabadilike na kujijengea mazoea ya kufanya kazi halali na kuwa waaminifu na kuwa wazalendo kwa Taifa lao.
Aidha, Askofu Shoo amemuomba Dkt Magufuli kuangalia uwezekano wa kupunguza kodi hususani kwa taasisi za kidini zinzotoa huduma za kijamii zikiwemo zile za Elimu na Afya.
Akijibu Maombi hayo Rais Dkt Magufuli amewaeleza waamini na watanzania kwa ujumla kuwa Serikali inathamini michango ya huduma za kijamii zinazotolewa na Taasisi za dini na kuahidi kuliangalia suala hilo.
Jaffar Haniu
Naibu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU.
Moshi, Kilimanjaro.
30 Aprili, 2017.
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, leo tarehe 29 Aprili 2017, ameuagiza Uongozi wa Mkoa wa Dodoma kuunda kamati itakayoshughulikia suala la kubadilisha hati ya umiliki wa ardhi katika mkoa huo kutoka miaka 33 hadi miaka 99.
Rais Magufuli ametoa agizo hilo katika Uwanja wa Ndege wa Dodoma wakati alipokutana na viongozi mbalimbali wa mkoa huo wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Jordan Rugimbana, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job Ndugai na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa.
Kamati hiyo itahusisha wajumbe kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Ofisi ya Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano,Mkurugenzi wa Halmashauri ya mji wa Dodoma na Mkurugenzi wa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu Dodoma - CDA.
Rais Magufuli amesema mji wa Dodoma pekee ndio wenye matatizo makubwa ya umiliki wa ardhi kutokana na hati zake kutolewa kwa miaka 33 badala ya miaka 99 kama ilivyo miji mingine nchini kitu kunachorudisha nyuma maendeleo ya mji huo ikiwa ni pamoja na uwekezaji.
'' Dodoma bado kuna tatizo moja kubwa, katika viwanja vyote vinavyotolewa hapa hati zake ni za miaka 33, huwezi ukajenga nchi ya viwanda,huwezi ukamvutia muwekezaji ambaye hati yake ni miaka 33 na wakati anataka kwenda kukopa benki umpe garantii ya miaka 33,nafikiri hii sheria tulikosea sana na nafikiri hii ni moja ya sheria ambayo ilifanya hata viwanda vingi visijengwe hapa Dodoma'' amesema Rais Magufuli.
Katika hatua nyingine, Rais Magufuli ameridhia ombi la Chuo Kikuu cha Dodoma kusamehewa kulipa kodi ya ardhi ya zaidi ya shilingi Bilioni Mbili iliyokuwa inadaiwa na CDA na kuagiza kutodaiwa tena kwa kuwa chuo hicho hakifanyi biashara bali hutoa huduma kwa jamii.
''Chuo kikuu cha Dodoma hakifanyi biashara ,kipo pale kwa ajili ya kutoa elimu kwa watanzania na wengi wao ni watoto wa masikini ,ardhi zote kwa mujibu wa sheria namba nne na namba tano ya mwaka 1999 na sheria nyingine zote za ardhi zikiwemo zile za mabadiliko za mwaka 2007 mwenye Mamlaka makubwa ya kusimamia ardhi ni Rais,kulingana na misingi hiyo ili mradi tu hili lisichukuliwe kwa kila Taaasisi lakini nimetoa special offer kwa Chuo Kikuu cha Dodoma lile deni lisamehewe , wasidaiwe na wala wasiwadai tena'' amesema Rais Magufuli.
Rais Magufuli pia ameagiza Ujenzi wa Uwanja wa mkubwa wa michezo mkoani humo unaofadhiliwa na Mfalme wa Morocco ujengwe karibu na eneo la Nane Nane mkoani Dodoma.
Aidha, Rais Dkt. Magufuli amesema kuwa anataka uwanja huo uwe mkubwa na wa kisasa utakaokidhi mahitaji ya kimataifa katika kipindi cha zaidi ya miaka 100 ijayo na hivyo atasimamia mwenyewe ujenzi huo.
Kwa upande wa ujenzi wa Uwanja wa ndege wa Dodoma, Rais Magufuli ameagiza kufanywa tathmini ya nyumba zitakazo bomolewa kwa ajili ya upanuzi wa Uwanja huo ili kulipwa fedha zao mara moja hali itakayopelekea Uwanja huo ukidhi mahitaji ya kutua ndege za kimataifa.
Katika hatua nyingine Rais Magufuli amewashukuru Wananchi wa Mkoa wa Dodoma kwa ukarimu na makaribisho makubwa hususan katika sherehe za maadhimisho ya miaka 53 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar yaliyofanyika tarehe 26 Aprili mkoani humo.
Amesema Wananchi wa Dodoma wameonyesha ukarimu na uvumilivu wa hali ya juu hata pale mvua ilipokuwa inanyesha waliendelea kushuhudia sherehe hizo ni kitu ambacho cha kuigwa na wananchi wa mikoa mingine nchini.
Rais Magufuli ameondoka mkoani Dodoma kuelekea mkoa wa Kilimanjaro, ambapo pamoja na mambo mengine atakuwa mgeni rasmi katika sherehe za sikukuu ya wafanyakazi Duniani, Mei Mosi.
Jaffar Haniu
Naibu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Chamwino, Dodoma
29 Aprili, 2017
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, leo tarehe 29 Aprili 2017, ameuagiza Uongozi wa Mkoa wa Dodoma kuunda kamati itakayoshughulikia suala la kubadilisha hati ya umiliki wa ardhi katika mkoa huo kutoka miaka 33 hadi miaka 99.
Rais Magufuli ametoa agizo hilo katika Uwanja wa Ndege wa Dodoma wakati alipokutana na viongozi mbalimbali wa mkoa huo wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Jordan Rugimbana, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job Ndugai na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa.
Kamati hiyo itahusisha wajumbe kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Ofisi ya Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano,Mkurugenzi wa Halmashauri ya mji wa Dodoma na Mkurugenzi wa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu Dodoma - CDA.
Rais Magufuli amesema mji wa Dodoma pekee ndio wenye matatizo makubwa ya umiliki wa ardhi kutokana na hati zake kutolewa kwa miaka 33 badala ya miaka 99 kama ilivyo miji mingine nchini kitu kunachorudisha nyuma maendeleo ya mji huo ikiwa ni pamoja na uwekezaji.
'' Dodoma bado kuna tatizo moja kubwa, katika viwanja vyote vinavyotolewa hapa hati zake ni za miaka 33, huwezi ukajenga nchi ya viwanda,huwezi ukamvutia muwekezaji ambaye hati yake ni miaka 33 na wakati anataka kwenda kukopa benki umpe garantii ya miaka 33,nafikiri hii sheria tulikosea sana na nafikiri hii ni moja ya sheria ambayo ilifanya hata viwanda vingi visijengwe hapa Dodoma'' amesema Rais Magufuli.
Katika hatua nyingine, Rais Magufuli ameridhia ombi la Chuo Kikuu cha Dodoma kusamehewa kulipa kodi ya ardhi ya zaidi ya shilingi Bilioni Mbili iliyokuwa inadaiwa na CDA na kuagiza kutodaiwa tena kwa kuwa chuo hicho hakifanyi biashara bali hutoa huduma kwa jamii.
''Chuo kikuu cha Dodoma hakifanyi biashara ,kipo pale kwa ajili ya kutoa elimu kwa watanzania na wengi wao ni watoto wa masikini ,ardhi zote kwa mujibu wa sheria namba nne na namba tano ya mwaka 1999 na sheria nyingine zote za ardhi zikiwemo zile za mabadiliko za mwaka 2007 mwenye Mamlaka makubwa ya kusimamia ardhi ni Rais,kulingana na misingi hiyo ili mradi tu hili lisichukuliwe kwa kila Taaasisi lakini nimetoa special offer kwa Chuo Kikuu cha Dodoma lile deni lisamehewe , wasidaiwe na wala wasiwadai tena'' amesema Rais Magufuli.
Rais Magufuli pia ameagiza Ujenzi wa Uwanja wa mkubwa wa michezo mkoani humo unaofadhiliwa na Mfalme wa Morocco ujengwe karibu na eneo la Nane Nane mkoani Dodoma.
Aidha, Rais Dkt. Magufuli amesema kuwa anataka uwanja huo uwe mkubwa na wa kisasa utakaokidhi mahitaji ya kimataifa katika kipindi cha zaidi ya miaka 100 ijayo na hivyo atasimamia mwenyewe ujenzi huo.
Kwa upande wa ujenzi wa Uwanja wa ndege wa Dodoma, Rais Magufuli ameagiza kufanywa tathmini ya nyumba zitakazo bomolewa kwa ajili ya upanuzi wa Uwanja huo ili kulipwa fedha zao mara moja hali itakayopelekea Uwanja huo ukidhi mahitaji ya kutua ndege za kimataifa.
Katika hatua nyingine Rais Magufuli amewashukuru Wananchi wa Mkoa wa Dodoma kwa ukarimu na makaribisho makubwa hususan katika sherehe za maadhimisho ya miaka 53 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar yaliyofanyika tarehe 26 Aprili mkoani humo.
Amesema Wananchi wa Dodoma wameonyesha ukarimu na uvumilivu wa hali ya juu hata pale mvua ilipokuwa inanyesha waliendelea kushuhudia sherehe hizo ni kitu ambacho cha kuigwa na wananchi wa mikoa mingine nchini.
Rais Magufuli ameondoka mkoani Dodoma kuelekea mkoa wa Kilimanjaro, ambapo pamoja na mambo mengine atakuwa mgeni rasmi katika sherehe za sikukuu ya wafanyakazi Duniani, Mei Mosi.
Jaffar Haniu
Naibu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Chamwino, Dodoma
29 Aprili, 2017
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, leo tarehe 28 Aprili 2017, amepokea taarifa ya uhakiki wa vyeti kwa Watumishi wa Umma katika ukumbi wa Chimwaga mkoani Dodoma na kuiagiza Wizara ya fedha kuwaondoa katika orodha ya Watumishi wa Umma na kusimamisha mishahara ya Watumishi 9,932 waliobainika kutumia vyeti vya kugushi.
Idadi ya watumishi hao imebainika baada ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mheshimiwa Angela Kairuki kukabidhi taarifa ya zoezi la uhakiki wa vyeti kwa watumishi wa Umma zaidi ya laki nne kwa Rais Magufuli, zoezi ambalo liliendeshwa na Serikali kuanzia mwezi Oktoba mwaka 2016.
Rais Magufuli pia amewataka Watumishi 9,932 waliobainika kutumia vyeti vya kugushi kujiondoa wenyewe katika utumishi wa Umma kabla ya tarehe 15 Mei 2017 na baada ya muda huo hatua za kisheria zitachukuliwa ikiwa ni pamoja na kufikishwa katika vyombo vya sheria.
'' Kwa hiyo Waziri Mkuu upo hapa na Waheshimiwa Mawaziri wote mnaohusika, hawa watu 9932 mshahara wao wa mwezi huu ukatwe na waondoke mara moja kwenye Utumishi wa Umma kuanzia leo, watakao baki mpaka tukiingia mwezi wa tano tuwapeleke kwa mujibu wa sheria ili kusudi wakafungwe hiyo miaka saba'' amesema Rais Magufuli.
Pia Rais Magufuli ameiagiza Wizara ya Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala bora kutangaza nafasi hizo 9,932 upya ili wenye sifa stahiki waweze kuomba
Aidha, Rais Magufuli ameiagiza Tume inayofanya uhakiki wa vyeti kwa Watumishi wa Umma kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu kuendelea na uchunguzi wa Watumishi wa Umma 1538 waliobainika kutumia vyeti vyenye utata hadi Mei 15, 2017
'' hawa wenye vyeti vya utata kwa maana kuwa vyeti vyao vinatumiwa na watu zaidi ya mmoja, Wizara ya Utumishi muhakikishe kufika tarehe 15 muwe mmeshajua ni nani mwenye cheti chake, na mshahara wa mwezi huu wasipewe kwanza mpaka atakayepatikana mwenye cheti halali'' amesema Rais Magufuli.
Pia ameagiza uchunguzi ufanyike kwa watumishi 11,596 wenye vyeti vya Utaalumu bila kuwasilisha vyeti vya kidato na Sita kwa kuwa sio fani zote zinazohitaji kuwa na vyeti vya kidato cha Sita ili kusomea utaalamu husika na kuagiza kulipwa mishahara yao kama kawaida.
Katika hatua nyingine, Rais Magufuli amezindua maadhimisho ya miaka kumi tangu kuanzishwa kwa Chuo kikuu cha Dodoma.
Rais magufuli amewaelezea Wanajumuiya ya Chuo Kikuu cha Dodoma mipango mbalimbali inayofanywa na Serikali katika kuboresha maisha ya Watanzania na kukuza Uchumi ikiwa ni pamoja na kuimarisha Miundombinu ya Usafiri kwa kununua ndege mpya Sita na Ujenzi wa Reli ya kisasa.
Mheshimiwa Rais amesema hatua ya Serikali kuimarisha huduma za jamii inatokana na mafanikio ya Serikali kudhibiti upotevu wa mapato na hivyo kuwataka wananchi kuunga mkono jitihada za Serikali ili kukamilisha malengo ya Tanzania ya viwanda.
Jaffar Haniu
Naibu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Chamwino, Dodoma
28 Aprili, 2017
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, kesho tarehe 28 Aprili 2017, atapokea Taarifa ya zoezi la uhakiki wa vyeti kwa Watumishi wa Umma katika Ukumbi wa Chimwaga Mkoani Dodoma.
Taarifa hiyo itawasilishwa kwa Mheshimiwa Rais na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mheshimiwa Angellah Kairuki.
Zoezi la uhakiki wa vyeti kwa Watumishi wa Umma liliendeshwa na Serikali kuanzia Mwezi Oktoba mwaka 2016.
Jaffar Haniu,
Naibu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU,
Chamwino, Dodoma.
27 Aprili, 2017
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, leo tarehe 26 April 2017, ameongoza maelfu ya Watanzania katika sherehe za miaka 53 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar zilizofanyika katika Uwanja wa Jamhuri Mjini Dodoma.
Akizungumza mara baada ya kukagua gwaride la vikosi vya ulinzi na Usalama lililoandaliwa kwa heshma yake, Rais Magufuli amewahakikishia watanzania kuwa yeye na Rais wa Zanzibara Dkt. Ali Mohamed Shein wataendelea kuulinda Muungano kwa nguvu zao zote na kwamba atakayejaribu kuuvunja atavunjika yeye.
''Muungano ndio silaha yetu. Ni nguvu yetu. Mimi na mwenzangu Dkt. Shein tutaulinda Muungano kwa nguvu zote. Yeyote atakayejaribu kuuvunja atavunjika yeye'' amesema Rais Magufuli.
Aidha Dkt. Magufuli amewataka watanzania kuendelea kudumisha amani iliyopo nchini kwani amani ndio chachu ya maendeleo yanayopatikana nchini.
Rais Magufuli amesema Tanzania imeweza kufikisha miaka 53 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwa sababu ya amani iliyopo nchini iliyowezesha kupatikana mafanikio makubwa ikiwa ni pamoja na kuunganisha mataifa yetu mawili na kuuunda taifa moja lenye nguvu.
Aidha amesema Muungano wa Tanganyika na Zanzibar umewezesha kupatikana mafanikio makubwa katika nyanja za kiuchumi, kisiasa na kijamii.
Mhe. Rais ametaja mafanikio mengine yaliyopatikana kutokana na Muungano ni kukua kwa uchumi na kukabiliana na matatizo ya umasikini na ukosefu wa ajira,kuimarisha miundombinu ya usafiri wa anga, majini,reli na nchi kavu.
Aidha Muungano umeimarisha na kuboresha upatikanaji wa huduma za jamii ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa idadi ya shule na hospitali pamoja na kukua kwa demokrasia nchini.
Kwa mara ya kwanaza katika historia ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar Maadhimisho ya Sherehe za Muungano zinafanyika mkoani Dodoma makao makuu ya Serikali ikiwa ni ishara tosha kuwa Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na chama cha Mapinduzi imedhamiria kwa dhati kuhakikisha makao makuuu ya Serikali yanakuwa Dodoma.
''Niwahahakikishie wana Dodoma na Watanzania kwa ujumla kwamba Serikali sasa tumefika Dodoma na hatutarudi tena, na kama tulivyoahidi mwaka 2020 Serikali yote itakuwa imehamia hapa'' amesema Rais magufuli.
Sherehe za miaka 53 ya Muungano zimehudhuriwa na viongozi mbalimbali ikiwa ni pamoja na wajane wa viongozi waasisi wa Muungano mke wa hayati Mwalimu Julius Nyere Mama Maria Nyerere na hayati Abeid Aman Karume, Mama Shadya Karume,Makamu wa Rais Mama Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, na viongozi wa chama na serikali.
Kauli mbiu ya Sherehe za Muungano mwaka huu ni ''Miaka 53 ya muungano,Tuuulinde na kuuimarisha, Tupige vita Dawa za Kulevya na Kufanya Kazi kwa Bidii''
Jaffar Haniu
Naibu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dodoma
26 Aprili, 2017
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, leo tarehe 21 Aprili, 2017 amemteua Mhandisi Benjamin Joel Mchwampaka kuwa Kamishna wa Madini.
Taarifa iliyotolewa leo na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi imeeleza kuwa uteuzi wa Mhandisi Benjamin Joel Mchwampaka umeanza tarehe 19 Aprili, 2017.
Kabla ya uteuzi huo, Mhandisi Benjamin Joel Mchwampaka alikuwa Kamishna Msaidizi sehemu ya uchimbaji mdogo wa madini.
Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli amemteua Dkt. Adelardus Kilangi kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (Petroleum Upstream Regulatory Authority -PURA).
Dkt. Adelardus Kilangi ni Mkurugenzi wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino Tanzania (SAUT) kampasi ya Arusha.
Uteuzi wa Dkt. Adelardus Kilangi umeanza tarehe 19 Aprili, 2017.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
21 Aprili, 2017
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amemteua Prof. Raphael Tihelwa Chibunda kuwa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA).
Taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi, Ikulu Jijini Dar es Salaam imeeleza kuwa Uteuzi wa Prof. Raphael Tihelwa Chibunda unaanza leo tarehe 24 Aprili, 2017.
Kabla ya uteuzi huo Prof. Raphael Tihelwa Chibunda alikuwa Mkurugenzi Msaidizi, Idara ya Sayansi na Teknolojia katika Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia.
Prof. Raphael Tihelwa Chibunda anachukua nafasi ya Prof. Gerald Monela ambaye amemaliza muda wake.
Wakati huo huo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amewasili Mjini Dodoma ambako pamoja na mambo mengine atakuwa mgeni rasmi katika Sherehe za maadhimisho ya miaka 53 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Katika uwanja wa ndege wa Dodoma, Mhe. Rais Magufuli amepokelewa na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job Ndugai, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Sera, Bunge, Kazi, Ajira na Walemavu Mhe. Jenister Mhagama na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Jordan Rugimbana
Sherehe za Muungano mwaka huu, zitafanyika katika Uwanja wa Jamhuri ikiwa ni mara ya kwanza kufanyika katika makao makuu ya nchi Mjini Dodoma.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
24 Aprili, 2017
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, leo tarehe 20 Aprili, 2017 amekutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) na kuwahakikishia kuwa Serikali ya Awamu ya Tano itaendeleza na kuimarisha zaidi ushirikiano kati yake na wafanyakazi kwa manufaa ya Taifa.
Katika Mazungumzo hayo yaliyofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam, Mheshimiwa Rais Magufuli amesema pamoja na kuimarisha ushirikiano huo, Serikali ipo tayari kupokea maoni na ushauri wowote utakaotolewa na vyama vya wafanyakazi wenye lengo la kuboresha maslahi ya wafanyakazi na kuongeza tija kazini.
Mhe. Rais Magufuli amesema Serikali inatambua changamoto mbalimbali zinazowakabili wafanyakazi na itaendelea kuchukua hatua za kukabiliana nazo kama ambavyo imeanza kufanya hivyo.
“Nataka kuwahakikishia nyinyi viongozi wa TUCTA na wafanyakazi wote kuwa Serikali ya Awamu ya Tano inawapenda wafanyakazi na ipo tayari kuwapigania, jambo la msingi tutangulize maslahi ya Taifa, kawaambieni wafanyakazi wachape kazi na Serikali itawalinda” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Kwa upande wao Viongozi wa TUCTA wakiongozwa na Rais wa Shirikisho hilo Bw. Tumaini Nyamhokya wamempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa juhudi kubwa zinazochukuliwa na Serikali yake kujenga uchumi imara, kuimarisha utendaji kazi wa watumishi wa Serikali, kupambana na rushwa, kuondoa watumishi hewa na kulipa madeni ya watumishi.
Viongozi hao wameahidi kushirikiana na Serikali katika kusimamia haki na wajibu wa wafanyakazi na wameomba Serikali iendelee kufanyia kazi masuala mbalimbali ya wafanyakazi ikiwemo kuwalipa stahili zao na kuboresha mazingira ya kazi.
Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli amepokea barua yenye ujumbe wa Rais wa Jamhuri wa Rwanda Mhe. Paul Kagame iliyowasilishwa kwake na Mjumbe Maalum ambaye ni Waziri wa Elimu wa Rwanda Dkt. Musafiri Papias Malimba.
Pamoja na kupokea barua hiyo, Mhe. Rais Magufuli na Dkt. Musafiri Papias Malimba wamezungumzia masuala mbalimbali ya ushirikiano kati ya Tanzania na Rwanda ikiwemo katika sekta ya elimu hususani maendeleo ya sayansi na teknolojia.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli ameipongeza Rwanda kwa kuamua lugha ya Kiswahili ianze kufundishwa katika shule zake na ameahidi kuwa Tanzania ipo tayari kutoa walimu wa kwenda kufundisha lugha hiyo.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
20 Aprili, 2017
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli na Mkewe Mama Janeth Magufuli leo tarehe 16 Aprili, 2017 Sikukuu ya Pasaka, wameungana na Waumini wa Kanisa la Africa Inland – Tanzania Dayosisi ya Pwani Pastorate ya Magomeni kusali Ibada ya Pasaka.
Katika Ibada hiyo Askofu wa Kanisa la Africa Inland – Tanzania Baba Askofu Charles Salalah ameongoza maombi ya kumuombea Mhe. Rais Magufuli ili aendelee kutekeleza majukumu yake ya kuiongoza nchi vizuri na amempongeza kwa kazi kubwa ya kurekebisha mambo yote yasiyofaa nchini ikiwemo kuwaondoa viongozi wanaotumia madaraka yao vibaya na kufuja mali za umma.
“Mhe. Rais unafanya kazi kubwa ya kutumbua majipu, majipu unayoyatumbua wewe ni majipu madogomadogo yaliyotokana na jipu kuu ambalo ni dhambi za mwanadamu, na jipu hili lilitumbuliwa na Bwana Yesu, kwa hiyo sisi Wakristo wenzako na waumini wengine tunakuombea sana na tunakuunga mkono katika kazi hii nzito ya kutumbua majipu haya madogomadogo ya watumishi hewa, mishahara hewa, mikopo hewa na mengine mengi” amesema Askofu Charles Salalah.
Akizungumza katika Ibada hiyo Mhe. Rais Magufuli amewashukuru Wakristo wa Kanisa la Africa Inland na waumini wa madhehebu mengine ya dini kwa kuendelea kumuombea na ameomba maombi hayo yaendelee, na pia waiombee nchi iendelee kuwa na amani, umoja, mshikamano na watu wachapa kazi.
Mapema asubuhi Mhe. Rais Magufuli ameshiriki Ibada ya Pasaka katika Kanisa la Mtakatifu Petro lililopo katika Parokia ya Oysterbay Jijini Dar es Salaam ambapo katika salamu zake za Pasaka Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo amesema baraka zilizoletwa na Yesu Kristo aliyefufuka ni kwa ajili ya watu wote wakristo na wasio wakristo na amemtakia heri Mhe. Rais Magufuli ili matumaini ya baraka hizo ziwafikie Watanzania wote.
Amemuombea Mhe. Rais Magufuli kuwa imara katika changamoto na machungu anayokutana nayo katika uongozi akisema “Yesu Kritso akuimarishe na akutie nguvu ili matumaini tunayoyadhimisha leo yawafikie Watanzania wote”
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
16 Aprili, 2017
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Hatimaye Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ametekeleza ahadi yake ya kukabiliana na uhaba wa mabweni kwa wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambapo leo tarehe 15 Aprili, 2017 amefungua mabweni mapya ya wanafunzi wa chuo hicho yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 3,840.
Mhe. Rais Magufuli alitoa ahadi ya kujenga mabweni hayo tarehe 02 Juni, 2016 na ujenzi ukaanza tarehe 01 Julai, 2016 ambapo Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) kwa kushirikiana na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) wamejenga majengo 20 yenye ghorofa 4 kila moja kwa gharama ya Shilingi Bilioni 10, na pia wamejenga uzio wa kuzunguka majengo hayo na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kimenunua vitanda, makabati, meza, viti na magodoro kwa ajili ya wanafunzi wote 3,840.
Sherehe za ufunguzi wa majengo hayo zimefanyika ndani ya eneo la mradi na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Mke wa Rais Mama Janeth Magufuli, Mawaziri, Wabunge, Makatibu Wakuu, Wasomi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na viongozi mbalimbali wa Serikali na vyama vya siasa.
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Prof. Rwekaza Mukandala na Rais wa Serikali ya wanafunzi wa chuo hicho (DARUSO) Bw. Erasmi Leon wamemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kutekeleza ahadi yake tena kwa muda mfupi wa chini ya miezi 8, na wamemuhakikishia kuwa Jumuiya ya chuo hicho inamuunga mkono katika jitihada zake za kujenga Tanzania imara chini ya kauli mbiu ya “Hapa Kazi Tu”.
Pamoja na kuelezea furaha yake ya kufanikiwa kwa ujenzi wa mabweni hayo, Mhe. Rais Magufuli ameipongeza TBA na Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kwa juhudi kubwa zilizofanyika kuharakisha ujenzi huo na kwa gharama nafuu, na ametaka mradi huo uwe mfano wa kuigwa kwa miradi mingine itakayotekelezwa nchini kote.
“Nilipowaambia wataalamu wanipe makadirio ya gharama za ujenzi wa mradi huu waliniambia utagharimu kati ya Shilingi Bilioni 150 hadi 170, nikamuita Mtendaji Mkuu wa TBA Bw. Mwakalinga nikamuambia kuna Bilioni 10 za kujenga mabweni haya.
“Sasa naambiwa kwenye miaka ya 2000 kulijengwa mabweni ya wanafunzi kule Mabibo, mabweni yale yanachukua wanafunzi 4,000 na yaligharimu Shilingi Bilioni 27, sisi hapa tumejenga mabweni mwaka 2017 yanachukua wanafunzi 3,840 na yamegharimu Shilingi Bilioni 10, sasa hapo mtapiga mahesabu wenyewe” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Aidha, Mhe. Dkt. Magufuli ameagiza wanafunzi watakaoishi katika mabweni hayo mapya walipie Shilingi 500/= kwa siku badala ya Shilingi 800/= na amewahakikishia Watanzania kuwa Serikali ya Awamu ya Tano itaendelea kuwapigania wanyonge na masikini kwa kuhakikisha wanapata haki ya elimu ikiwemo mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu.
Mhe. Rais Magufuli amekubali mwaliko wa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako wa kwenda kufungua Kampasi ya Mloganzila ya Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) lakini ameagiza chuo hicho kitakapofunguliwa wanafunzi wote wanasomea masomo ya tiba katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam wahamishiwe Mloganzila.
Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli ametekeleza ahadi yake ya kuwajengea nyumba wakazi wa Magomeni Kota Jijini Dar es Salaam ambapo leo ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa nyumba 644 za wakazi hao waliovunjiwa nyumba zao na kubaki bila makazi.
Mhe. Rais Magufuli alitoa ahadi ya kuwajengea nyumba wakazi hao tarehe 09 Septemba, 2016 na ujenzi ukaanza tarehe 01 Oktoba, 2016 ambapo TBA inaendelea na kazi ya kujenga majengo matano yenye ghorofa 8 na 9 na yatakayokuwa na jumla ya nyumba 652, majengo ya biashara na bustani vitakavyokamilika mwaka huu kwa gharama ya Shilingi Bilioni 20.
Mhe. Dkt. Magufuli amepongeza maendeleo ya ujenzi huo na baada ya kuelezwa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi kuwa kuna maeneo mbalimbali nchini yenye nyumba zaidi ya 5,000 zilizo katika maeneo kama Magomeni Kota, ameahidi kuwa Serikali ya Awamu ya Tano itaendelea kutekeleza Ilani ya Uchaguzi Mkuu ya CCM ya kuwapatia makazi bora wananchi kwa kuwajengea nyumba katika maeneo hayo.
“Nyumba hizi zikikamilika wapatieni hawa wakazi wa Magomeni Kota waliovunjiwa nyumba wakae bure kwa miaka mitano na baada ya hapo ndipo muwauzie kwa utaratibu mtakaouweka, lakini Mhe. Lukuvi najua nchi nzima kuna maeneo yana nyumba kama hizi za Magomeni kota 5,331 nilishaagiza nyumba hizo zirudishwe Serikalini na wewe mwenyewe umeahidi kuwa utaleta hati zake mwezi ujao, siku zote tulikuwa tunajenga nyumba kwa ajili ya wafanyakazi, sasa tutaanza kujenga nyumba kwa ajili ya watanzania, uwe mfanyakazi, uwe muuza chipsi uwe nani una haki ya kupata nyumba” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
15 Aprili, 2017
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amepokea kwa mshtuko na masikitiko makubwa taarifa za vifo vya Askari Polisi 8 waliouawa kwa kushambuliwa na watu wenye silaha jana jioni tarehe 13 Aprili, 2017 katika eneo la Jaribu Mpakani, Wilaya ya Kibiti Mkoani Pwani.
Askari Polisi hao walikuwa wakitoka kubadilishana doria na wameshambuliwa kwa kupigwa risasi wakiwa wanasafiri kwa gari katika barabara ya Dar es Salaam – Lindi.
Mhe. Rais Magufuli amemtumia salamu za rambirambi Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP-Ernest Mangu, familia za askari wote waliouawa, Askari Polisi wote na Watanzania wote walioguswa na vifo hivyo.
“Nimeshtushwa na nimesikitishwa sana na vifo vya askari wetu 8 ambao wamepoteza maisha wakiwa wanalitumikia Taifa, naungana na familia za marehemu wote, Jeshi la Polisi na Watanzania wote katika kipindi hiki kigumu cha huzuni na majonzi ya kuondokewa na vijana wetu shupavu.
“Namuomba Mwenyezi Mungu atupe moyo wa subira, uvumilivu na ustahimilivu” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Aidha, Mhe. Dkt. Magufuli amelaani tukio hilo na matukio yote ya kuwashambulia askari polisi ambao wanafanya kazi kubwa na muhimu ya kulinda raia na mali na ametaka Watanzania wote watoe ushirikiano katika kukomesha vitendo hivyo.
Mhe. Rais Magufuli amewaombea marehemu wote wapumzishwe mahali pema peponi, Amina.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
14 Aprili, 2017
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, leo tarehe 12 Aprili, 2017 ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa sehemu ya kwanza ya reli ya kati kwa kiwango cha kisasa (Standard Gauge) itakayoanzia Dar es Salaam hadi Morogoro, yenye urefu wa kilometa 300 zinazojumuisha vituo vya kupishana treni na vituo vya abiria na mizigo.
Sherehe za uwekaji jiwe la msingi zimefanyika Pugu Jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo, Mke wa Rais Mama Janeth Magufuli, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa Mnyaa, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Bajeti Mhe. Hawa Ghasia, Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Miundombinu Mhe. Prof. Norman Sigalla King, Mabalozi wa nchi mbalimbali, wawakilishi wa taasisi za kimataifa na viongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam.
Reli inayojengwa itakuwa na uwezo wa kubeba mizigo yenye uzito wa tani 35 kwa ekseli moja, itasafirisha abiria kwa mwendokasi wa hadi kilometa 160 kwa saa, mizigo kwa mwendokasi wa hadi kilometa 120 kwa saa na itakuwa na uwezo wa kusafirisha jumla ya tani milioni 17 za mizigo kwa mwaka, ikilinganishwa na reli nyembamba iliyopo sasa iliyojengwa mwaka 1912 ambayo inasafirisha abiria kwa mwendokasi wa kilometa chini ya 30 kwa saa, inabeba tani 13 kwa ekseli moja na ina uwezo wa kubeba jumla ya tani milioni 5 tu za mizigo kwa mwaka.
Sehemu ya kwanza ya ujenzi wa reli hiyo inayofanywa na kampuni ya Yapi Merkezi ya Uturuki kwa kushirikiana na Motaengil Africa imepangwa kuchukua muda wa miezi 30 kuanzia sasa kwa gharama ya Shilingi Trilioni 2.7 na itafuatiwa na sehemu nyinyine nne zitakazounganisha reli kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza kwa urefu wa jumla ya kilometa 1,219.
Akitoa taarifa kwa Mhe. Rais, Mtendaji Mkuu wa Kampuni hodhi ya rasilimali za reli nchini (RAHCO) Bw. Masanja Kadogosa amesema reli hiyo itakuwa na uwezo wa kubeba treni inayovuta mabehewa 100 ya mizigo yenye urefu wa kilometa 2 kwa mpigo na kwamba mizigo itakayobebwa na treni moja ni sawa na mizigo ambayo ingebebwa na malori 500.
Ameongeza kuwa kupitia reli hiyo abiria wataweza kusafiri kati ya Dar es Salaam na Morogoro kwa muda wa saa 1 na dakika 25
Mhe. Rais Magufuli amesema Watanzania wana kila sababu ya kujivunia kuanza kwa ujenzi wa reli hiyo kwa kuwa itasaidia kurahisisha usafiri wa abiria na mizigo ndani ya nchi na kwenda nchi jirani za Rwanda, Burundi, Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, itazalisha ajira za moja kwa moja kwa Watanzania 600,000 na itasadia kuimarisha uchumi.
Mhe. Dkt. Magufuli amesema pamoja na kuanza kwa ujenzi wa kilometa 300 za kuanzia Dar es Salaam hadi Morogoro, Serikali imeelekeza jitihada zake kuanza ujenzi wa sehemu ya pili ya kuanzia Morogoro hadi Dodoma yenye urefu wa kilometa 336 na kwamba Serikali ya Uturuki imeonesha nia ya kushirikiana na Tanzania kujenga sehemu hiyo.
Kwa wakazi wa Dar es Salaam, Mhe. Rais Magufuli amesema katika kipindi kifupi Serikali ya Awamu ya Tano imechukua hatua madhubuti za kuboresha Jiji kama alivyoahidi zikiwemo kujenga barabara za juu katika makutano ya barabara maeneo ya TAZARA na Ubungo (Flyover), kujenga daraja la baharini litakalounganisha Agha Ghan na Coco Beach, kujenga barabara za mzunguko (Ring roads) na kununua ndege kwa ajili ya Shirika la Ndege Tanzania (ATCL).
Pamoja na kuwapongeza wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kupitisha bajeti iliyowezesha kuanza kwa ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa, Mhe. Rais Magufuli amewaomba Watanzania wote kuendelea kuunga mkono juhudi hizi kubwa na muhimu kwa maendeleo na amewataka kujiepusha na mijadala isiyo na tija katika maendeleo.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
12 Aprili, 2017
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, leo tarehe 11 Aprili, 2017 amewaapisha wajumbe wa Kamati Maalum ya pili ya wachumi na wanasheria itakayochunguza mchanga wenye madini ulio katika makontena yaliyopo maeneo mbalimbali nchini.
Walioapishwa ni Mwenyekiti wa kamati hiyo Prof. Nehemiah Eliachim Osoro na wajumbe wake ambao ni Prof. Longinus Kyaruzi Rutasitara, Dkt. Oswald Joseph Mashindano, Bw. Casmir Sumba Kyuki, Bw. Andrew Wilson Massawe, Bw. Gabriel Pascal Malata, Bw. Usaje Bernard Usubisye na Bi. Butamo Kasuka Philip.
Akizungumza baada ya kuwaapisha wajumbe wa kamati hii, Mhe. Rais Magufuli amesema ameunda kamati hiyo ili ifanye uchunguzi wa kina utakaobaini aina ya madini yaliyo ndani ya mchanga huo, thamani yake, kiwango cha kila aina ya madini, uzito wa mchanga unaowekwa ndani ya makontena na pia kujua ni makontena mangapi yamepitishwa tangu mwaka 1998.
“Kafuatilieni makontena mangapi yametoka hapa nchini na kupelekwa nje ya nchi tangu mwaka 1998, na kama hayo makontena yana madini aina ya dhahabu, shaba na silva mkafuatilie tujue zimepelekwa tani ngapi za dhahabu, tani ngapi za shaba na tani ngapi za silva, je makontena mangapi yanapita kila mwezi? Makontena 1,000 au mangapi? na je zilikuwa na thamani ya kiasi gani? Je tumelipwa kiasi gani cha fedha?
“Na nyie wanasheria mfanye uchunguzi juu ya kinachofanyika na muone sheria zinasema? Tujue utekelezaji wa sheria kama unafanyika inavyotakiwa? Tunataka hoja hizi zipate majibu” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Mhe. Rais Magufuli amesisitiza kuwa wakati umefika kwa Tanzania kunufaika na rasilimali zake na kwamba Serikali haiwezi kukubali madini yaendelee kuondoka bila kuleta manufaa kwa wananchi.
Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli amepokea ripoti ya mwaka 2015/2016 ya utendaji kazi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) iliyowasilishwa kwake na Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU Kamishna Valentino Mlowola.
Taarifa hiyo imewasilishwa kwa Mhe. Rais Magufuli kwa mujibu wa sheria ya TAKUKURU na imeeleza kuhusu mafanikio ya kuzuia na kupambana na rushwa, mfumo wa utendaji kazi wa TAKUKURU na changamoto zilizojitokeza.
Katika maelezo yake mafupi kwa Mhe. Rais Magufuli, Kamishna Mlowola amesema kutokana na nia thabiti ya Serikali ya Awamu ya Tano kukabiliana na rushwa wananchi wameitikia kwa wingi kutoa taarifa za vitendo vya rushwa na kumekuwa na ongezeko kubwa la kesi za rushwa ambazo zinafikishwa mahakamani.
Aidha, Kamishna Mlowola amesema katika kipindi cha tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani fedha za umma zilizookolewa na TAKUKURU zimeongezeka kutoka Shilingi Bilioni 7 hadi kufikia Shilingi Bilioni 53 huku kukiwa na mafanikio makubwa katika kudhibiti mianya ya ukwepaji wa kodi na matumizi mabaya ya fedha za miradi ya maendeleo.
Mhe. Rais Magufuli ameipongeza TAKUKURU kwa mafanikio makubwa iliyoyapata na ameahidi kuwa Serikali itaendelea kuunga mkono juhudi hizo ili kufanikisha vita dhidi ya rushwa.
Hata hivyo, ameitaka taasisi hiyo kuhakikisha wote wanabainika kujihusisha na vitendo vya rushwa wanachukuliwa hatua zinazostahili na kwamba kama mapungufu ya kisheria ishirikiane na vyombo husika kurekebisha sheria hizo.
“Rushwa tukiiacha iendelee tutakwama, kwa hiyo niwaombe Watanzania na vyombo vyote vinavyohusika vitoe ushirikiano mkubwa kwa TAKUKURU, lakini nitoe wito kwenu TAKUKURU, sijaona watu wakifungwa sana kwa makosa ya rushwa.
Mtu anashikwa na ushahidi lakini akipelekwa mahakamani ushahidi haupelekwi au unafichwa kwa makusudi au anayeendesha kesi anaamua kutokuusema halafu aliyeshikwa na rushwa anaachiwa, wananchi wanawajua wanaojihusisha na rushwa, ifike mahali watu wanaokutwa na makosa ya rushwa wafungwe” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
11 Aprili, 2017
Taarifa kwa vyombo vya habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 10 Aprili, 2017 ameteua wajumbe wa kamati maalum ya pili itakayofanya uchunguzi wa madini yaliyomo kwenye mchanga wenye madini ulio ndani ya makontena yaliyopo katika maeneo mbalimbali hapa nchini.
Kamati hiyo inajumuisha wachumi na wanasheria na imetanguliwa na kamati ya kwanza iliyoundwa na wataalamu wa masuala ya jiolojia, kemikali na uchambuzi wa kisayansi.
Taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi imewataja wajumbe wa kamati hiyo kuwa ni;
- Prof. Nehemiah Eliachim Osoro
- Prof. Longinus Kyaruzi Rutasitara
- Dkt. Oswald Joseph Mashindano
- Bw. Gabriel Pascal Malata
- Bw. Casmir Sumba Kyuki
- Bi. Butamo Kasuka Philip
- Bw. Usaje Benard Usubisye
- Bw. Andrew Wilson Massawe
Wajumbe hao wataapishwa na Mhe. Rais Magufuli kesho tarehe 11 Aprili, 2017 saa 3:00 asubuhi Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
10 Aprili, 2017
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 06 Aprili, 2017 amefanya mazungumzo na Balozi wa Umoja wa Ulaya hapa nchini Mhe. Roeland Van de Geer na kuushukuru umoja wa nchi hizo kwa kutoa msaada wa Euro Milioni 205 sawa na takribani Shilingi Bilioni 500 kwa ajili ya kuunga mkono juhudi za maendeleo hapa nchini kwa kipindi cha miaka 4 kuanzia mwaka huu.
Mhe. Rais Magufuli amesema kutolewa kwa fedha hizo kumethibitisha uhusiano na ushirikiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na Umoja wa Ulaya na kwamba pamoja na kutoa fedha hizo umoja huo unatarajia kutoa fedha nyingine kiasi cha Euro Bilioni 1.2 kwa ajili ya kuendeleza viwanda, kilimo na uzalishaji wa nishati.
“Nimefurahi sana kwamba uhusiano na ushirikiano wetu unajikita kushughulikia mambo ya msingi kwa Watanzania, nakuhakikishia kuwa fedha mnazotoa zitatumika vizuri na zitatoa mchango mkubwa katika maendeleo yetu” amesema Mhe. Dkt. Magufuli.
Nae Mhe. Balozi Roeland Van de Geer amempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa uongozi wake mzuri na dhamira yake ya kujenga uchumi na kusimamia utawala bora ikiwemo mapambano dhidi ya rushwa, na pia amemuahidi kuwa nchi wanachama wa umoja huo zitaendeleza na kuimarisha zaidi ushirikiano wake na Tanzania.
Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli amefanya mazungumzo na Balozi wa Israel hapa nchini Mhe. Yahel Vilan na kumhakikishia kuwa Tanzania imedhamiria kuimarisha na kukuza zaidi uhusiano na ushirikiano wake na Israel hususani katika masuala ya uwekezaji, biashara, utalii na uboreshaji wa huduma za kijamii.
Mhe. Rais Magufuli amesema ili kufanikisha dhamira hiyo Tanzania imefungua ubalozi nchini Israel na amemuomba Mhe. Yahel Vilan kupeleka ujumbe kwa Waziri Mkuu wa Israel Mhe. Benjamin Netanyahu kuwa Tanzania itafurahi kuona Israel inafungua ubalozi wake hapa nchini.
“Naamini uhusiano na ushirikiano wetu utaongeza manufaa zaidi kwa nchi zetu na watu wake, nimefurahishwa sana na taarifa kuwa watalii wataanza kuja kwa ndege moja kwa moja kutoka Tel Aviv Israel na hivi karibuni ndege yenye watalii zaidi ya 200 itakuja nchini kwetu, nawakaribisha sana watalii na wawekezaji kutoka Israel” amesema Rais Magufuli.
Kwa upande wake Mhe. Balozi Yahel Vilan pamoja na ujumbe wake amemueleza Mhe. Rais Magufuli kuwa wamefurahishwa na ziara waliyoifanya hapa nchini iliyowawezesha kukutana na viongozi mbalimbali na ameahidi kuwa Serikali ya Israel itajenga jengo la wagonjwa mahututi (ICU) katika Hospitali ya Benjamin Mkapa Mkoani Dodoma kuanzia mwishoni mwa mwaka huu.
Mhe. Balozi Yahel Vilan amemhakikishia Mhe. Rais Magufuli kuwa Israel itaendelea kushirikiana kwa karibu na Tanzania kwa kuunga mkono juhudi mbalimbali za maendeleo ikiwemo ujenzi wa viwanda, kilimo na kuimarisha huduma za matibabu kwa wananchi.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasilino ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
06 Aprili, 2017
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 04 Aprili, 2017 amefanya mabadiliko madogo katika safu ya Makatibu Wakuu.
Taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi imeeleza kuwa Mhe. Rais Magufuli amemteua Prof. Kitila Alexander Mkumbo kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji.
Prof. Kitila Alexander Mkumbo anachukua nafasi ya Mhandisi Mbogo Futakamba ambaye amestaafu.
Kabla ya Uteuzi huu Prof. Kitila Alexander Mkumbo alikuwa Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
Mhe. Rais Magufuli amemteua Dkt. Leonard Akwilapo kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.
Kabla ya Uteuzi huo Dkt. Leonard Akwilapo alikuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.
Kufuatia uteuzi huo aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Bi. Maimuna Tarishi amehamishwa na kuwa Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Bunge).
Bi. Maimuna Tarishi anachukua nafasi iliyoachwa na Mussa Uledi ambaye uteuzi wake ulitenguliwa.
Mhe. Rais Magufuli amemteua Dkt. Ave Maria Semakafu kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ambako anajaza nafasi iliyoachwa na Dkt. Leonard Akwilapo ambaye ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara hiyo.
Kabla ya Uteuzi huo Dkt. Ave Maria Semakafu alikuwa Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS).
Wateule hao wataapishwa kesho tarehe 05 Aprili, 2017 saa 3:00 Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
04 Aprili, 2017
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amemtumia salamu za rambirambi Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job Ndugai kufuatia kifo cha Mbunge wa Viti Maalum wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Mhe. Dkt. Elly Marko Macha.
Mhe. Dkt. Elly Marko Macha amefariki dunia tarehe 31 Machi, 2017 katika hospitali ya New Cross iliyopo Wolverhampton nchini Uingereza alikokuwa akipatiwa matibabu.
Mhe. Dkt. Magufuli ameelezea kusikitishwa na kuhuzunishwa na kifo cha Mbunge huyo ambaye ameondoka katika kipindi ambacho Taifa lilikuwa bado linahitaji mchango wake.
Katika salamu hizo, Mhe. Rais Magufuli amempa pole Mwenyekiti wa CHADEMA Mhe. Freeman Mbowe, Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wanachama wa CHADEMA kwa kuondokewa mwanachama wao na amesema anaungana nao katika kipindi hiki kigumu cha majonzi.
Aidha, Mhe. Dkt. Magufuli amemuomba Spika wa Bunge Mhe. Job Ndugai kumfikishia salamu za pole kwa familia ya marehemu, ndugu, jamaa na marafiki wote walioguswa na msiba huo.
“Mhe. Job Ndugai natambua kuwa kifo cha Mhe. Dkt. Elly Marko Macha kimeleta mshtuko na huzuni kubwa sio tu kwa Bunge bali pia kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki, naomba kuwapa pole wote walioguswa na sote tumuombee marehemu apumzishwe mahali pema peponi, Amina” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
31 Machi, 2017