Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 09 Desemba, 2017 amewaongoza Watanzania kusherehekea maadhimisho ya miaka 56 ya Uhuru wa Tanzania Bara katika uwanja wa Jamhuri Mjini Dodoma.
Sherehe hizo zimehudhuriwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Balozi Seif Ali Idd, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job Yustino Ndugai, Spika wa Baraza la Wawakilishi Mhe. Zubeir Ali Maulid, Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, Spika wa Bunge wa Bunge la Morocco Mhe. Hakim Benchamach, Marais wastaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na viongozi wengine wastaafu na wanaoongoza taasisi mbalimbali.
Pamoja na kukagua gwaride rasmi na kupigiwa mizinga 21 kwa heshima yake, Mhe. Rais Magufuli, viongozi mbalimbali na wananchi wameshuhudia maonesho mbalimbali yaliyofanywa na kikundi cha komandoo, askari wa kupambana na ugaidi, ndege za kivita, gwaride la wanafunzi, ngoma za asili, kwaya na muziki wa wasanii wa kizazi kipya (Bongo Fleva) walioimba wimbo maalum wa uzalendo kwa Tanzania.
Akizungumza katika sherehe hizo Mhe. Rais Magufuli ametoa msamaha kwa wafungwa 8,157 ambao ni sehemu ya wafungwa wote 39,000 waliopo magerezani wakitumikia vifungo mbalimbali.
Kati ya wafungwa hao, 6,329 wamepunguziwa adhabu na 1,828 wameachiwa huru kuanzia leo wakiwemo 61 waliohukumiwa kunyongwa na waliokuwa wakitumikia vifungo vya maisha, na amewataja miongoni mwao kuwa ni Mganga Matonya aliyefungwa gerezani kwa miaka 44 na mwenye umri wa miaka 85, wanamuziki Nguza Viking (Babu Seya) na mwanae Johnson Nguza (Papii Kocha)
“Nawapa msamaha wafungwa hawa kwa mujibu wa ibara ya 45 ibara ndogo ya 1 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayonipa mamlaka hayo, nimeamua kufanya hivi kwa sababu baadhi ya wafungwa wanaotumikia vifungo vya maisha ni wazee sana na wangine wameonesha mwenendo mzuri wa kitabia wakiwa gerezani”
“Na hawa niliowapa msamaha sio wale waliojihusisha na mauaji ya watu wenye ualbino na waliofungwa kwa kuhusika katika ujambazi” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Hata hivyo Mhe. Rais Magufuli ameonya kuwa msahama alioutoa usitafsiriwe kwa kuhalalisha watu kujihusisha katika uhalifu na amesisitiza kuwa vyombo vya dola vitaendelea kusimamia sheria.
Mhe. Rais Magufuli amewapongeza Watanzania wote kwa kufikisha miaka 56 ya Uhuru na kubainisha kuwa katika kipindi hicho nchi imepiga hatua kubwa katika maendeleo ikiwemo kuongezeka mtandao wa barabara kutoka kilometa 33,600 hadi kufikia kilometa 150,946, kati yake kilometa za lami zikiwa zimeongezeka kutoka 1,360 hadi 12,679.55.
Aidha, ameongeza kuwa Wakala wa barabara nchini (TANROADS) inaendelea na ujenzi wa barabara nyingine za lami zenye kilometa 2,480 na barabara nyingine za lami zenye urefu wa kilometa 7,087 zipo katika maandalizi ya kuanza ujenzi.
Maeneo mengine ambayo Tanzania imepiga hatua ni kuongezeka kwa shule za msingi kutoka 3,100 hadi 17,379, shule za sekondari kutoka 41 hadi 4,817, vyuo vikuu kutoka 1 hadi 48, Madaktari waliosajiliwa kutoka 403 hadi 9,343, Wahandisi waliosajiliwa kutoka 2 hadi 19,164 na Wakandarasi kutoka 2 hadi 9,350.
“Kwa hiyo ndugu zangu tumepiga hatua kubwa sana, hata wastani wa maisha yetu umepanda kutoka miaka 37 hadi 61 na pia idadi yetu imeongeza kutoka watu Milioni 9 hadi Milioni 52” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dodoma
09 Desemba, 2017