Taarifa kwa vyombo vya Habari ya zamani
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amewapongeza wananchi wa Chato Mkoani Geita kwa kuitikia wito wa Serikali wa kuongeza juhudi katika kazi za uzalishaji mali hali iliyoiwezesha Wilaya hiyo kupiga hatua kubwa za kimaendeleo.
Mhe. Rais Magufuli ametoa pongezi hizo tarehe 01 Julai, 2019 wakati akiwasalimu wananchi hao katika eneo la Njiapanda, muda mfupi baada ya kutua katika Uwanja wa Ndege wa Chato akitokea Jijini Dar es Salaam.
Amefafanua kuwa akiwa angani kabla ya kutua amefurahishwa kuona jinsi wananchi wa Chato walivyochangamka kimaendeleo kwa kujenga nyumba za kuishi za kisasa, majengo ya biashara, majengo ya huduma za jamii na mashamba ya mazao mbalimbali.
“Nawapongeza sana wananchi wa Chato, mnachapa kazi kwelikweli na maendeleo yanaonekana, Chato inabadilika. Nilishasema asiyefanya kazi na asile, kwa hiyo tuendelee kushikamana kufanya kazi na kujenga nchi yetu” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Mhe. Rais Magufuli ametoa wito kwa Watanzania wote kuendelea kuchapa kazi kwa juhudi na maarifa, kushikamana na kutobaguana ili kwa pamoja waijenge Tanzania ambayo ina rasilimali nyingi.
Kabla ya kuwasalimu wananchi wa Njiapanda, Mhe. Rais Magufuli amewasalimu na kuwashukuru wananchi wanaofanya kazi za ujenzi katika uwanja wa ndege wa Chato.
Mhe. Rais Magufuli amewasili leo katika Kijiji cha Mlimani Wilayani Chato kwa Mapumziko.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Chato
01 Julai, 2019
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 25 Juni, 2019 amezindua ghala na mitambo ya gesi ya mitungi inayotumika kupikia (Liquefied Petroleum Gas – LPG) inayomilikiwa na kampuni ya Watanzania iitwayo Taifa Gas Tanzania Limited katika Wilaya ya Kigamboni Jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taifa Gas Tanzania Limited Bw. Hamisi Ramadhani ameeleza kuwa uwekezaji mkubwa wa upanuzi wa ghala na mitambo ya gesi iliyopo Kigamboni umefanyika kuanzia mwaka 2016 hadi mwaka 2018 ambapo umeongeza uwezo wake kutoka tani 1,650 hadi kufikia tani 7,650.
Uwekezaji huu umekwenda sambamba na ujenzi wa maghala na mitambo ya gesi katika Mikoa 20 hapa nchini kwa gharama ya shilingi Bilioni 150 na hivyo kuifanya Taifa Gas Tanzania Limited kuwa kampuni kubwa zaidi ya uwekezaji kwa idadi ya mitambo na kwa ukubwa wa ghala lenye mitambo ya kisasa kuliko yote Mashariki na Kusini mwa Afrika.
Bw. Hamisi Ramadhani ameongeza kuwa uwekezaji huu umezalisha ajira za moja kwa moja 260 na zisizo za moja kwa moja 3,500 na kwamba pamoja na kuuza Tanzania kampuni hiyo inasambaza gesi katika nchini za Uganda, Rwanda, Burundi, DRC na Sudani Kusini.
Mwenyekiti wa Bodi ya Taifa Gas Tanzania Limited Bw. Rostam Azizi amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kuweka na kusimamia mazingira yenye usawa kwa wafanyabiashara na wawekezaji wote na kwamba kutokana na mazingira mazuri ya kufanyia biashara anatarajia kuongeza uwekezaji wa miradi mingine yenye thamani ya shilingi Bilioni 500 katika miaka 3 ijayo.
“Msimamo wako thabiti dhidi ya matendo ya zamani ya ujanjaujanja katika biashara na uwekezaji, na ukwepaji wa kodi, ndivyo ambavyo leo hii vimetufanya baadhi yetu ambao kwa miaka tuliamua kuwekeza mitaji nje ya Tanzania, kupata moyo wa kuanza tena kurejesha mitaji hapa nyumbani” amesisitiza Bw. Rostam Azizi huku akitoa wito kwa wafanyabiashara wenzake kutambua kuwa milango ya uwekezaji Tanzania iko wazi kwa uwekezaji madhari wanafuata sheria, taratibu na kanuni za nchi.
Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Medard Kalemani ameeleza kuwa kufuatia juhudi mbalimbali zilizofanywa na Serikali kuanzia mwaka 2015 hadi sasa sekta ya nishati imepata mafanikio makubwa ikiwemo kuongezeka kwa Watanzania wanaotumia gesi ya kupikia kutoka Milioni 1 hadi Milioni 2.5, kuongezeka kwa uwezo wa nchi kupokea gesi kutoka tani 220,000 hadi tani 617,000 (ongezeko la asilimia 240), kampuni 8 za gesi ya kupikia kuajiri Watanzania 12,000 na uzalishaji wa umeme kuongezeka kutoka megawati 1,280 hadi kufikia megawati 1,601.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Mhe. Rais Magufuli ameipongeza kampuni ya Taifa Gas Tanzania Limited kwa uwekezaji huo na Wizara ya Nishati kwa kusimamia vizuri sekta ya nishati nchini ikiwemo kuongeza upatikanaji wa gesi ya kupikia kwa Watanzania, kuongeza usambazaji wa umeme kutoka vijiji 2,018 mwaka 2015 hadi kufikia vijiji 7,318 hivi sasa na kwa kuhakikisha matatizo ya kukatika umeme yaliyokuwepo awali yanapungua kwa kiasi kikubwa.
Mhe. Rais Magufuli amewahakikishia Watanzania kuwa Serikali itaendelea kuchukua hatua madhubuti za kuongeza uzalishaji wa umeme kupitia miradi mikubwa ikiwemo miradi ya Mto Rufiji na Mto Ruhuji Mkoani Njombe ili kufikia megawati 5,000 zitakazowezesha kupunguza bei ya umeme na kukuza viwanda.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli ameipongeza sekta binafsi kwa uwekezaji uliofanywa katika sekta ya gesi ulioongeza uzalishaji wa gesi ya kupikia kutoka tani 17,000 mwaka 2015 hadi kufikia tani 92,500 hivi sasa na amewakaribisha wafanyabiashara na wawekezaji wengine wa ndani na nje ya nchi kuja kuwekeza hapa nchi kwa kuwa Serikali ipo tayari kushirikiana nao.
Ametoa wito kwa Taifa Gas Tanzania Limited na wawekezaji wengine wa sekta ya gesi kupanua huduma zao hadi vijijini ili Watanzania waondokane na matumizi ya mkaa na kuni katika kupikia na badala yake watumie gesi.
“Uwekezaji huu uliofanywa na Taifa Gas Tanzania Limited ni uthibitisho kuwa Serikali inapenda sekta binafsi, tunataka wawekezaji wa kweli sio maneno maneno, na wewe Rostam Azizi kama kuna wawekezaji huko walete, na umeniambia kiwanda chako cha ngozi kilichopo Morogoro kitakuwa tayari baada ya miezi 3, nitakuja” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Kuhusu changamoto mbalimbali za Wilaya ya Kigamboni ikiwemo mradi mkubwa wa nyumba zilizojengwa na Shirika la Hifadhi ya Jamii la NSSF uitwao Dege, Mhe. Rais Magufuli amesema pamoja na kwamba mradi huo umezingirwa na ufisadi, Serikali inasubiri Mamlaka husika ikiwemo NSSF na wananchi kutoa maoni ya nini kifanyike.
Sherehe za uzinduzi wa ghala na mitambo ya gesi ya Taifa Gas Tanzania Limited zimehudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo viongozi wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama, viongozi wa Dini, viongozi wa vyama vya siasa, wawekezaji mbalimbali na viongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa huo Mhe. Paul Makonda.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
25 Juni, 2019
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) Mhe. Felix Antoine Tshisekedi amemaliza Ziara ya Kitaifa ya siku 2 aliyoifanya hapa nchini kwa mwaliko wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli.
Mhe. Tshisekedi ameagwa na mwenyeji wake Mhe. Rais Magufuli katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam na kuelekea nchini Burundi.
Mapema leo asubuhi Mhe. Rais Tshisekedi ametembelea mradi wa ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa (Standard Gauge Railway) katika eneo la Vingunguti Jijini Dar es Salaam na baadaye akatembelea Bandari ya Dar es Salaam ambayo hutumika kupitisha mizigo ya DRC.
Akiwa Ikulu Jijini Dar es Salaam Mhe. Rais Tshisekedi amefanya mazungumzo na mwenyeji wake Mhe. Rais Magufuli na baadaye viongozi hao wamezungumza na wananchi kupitia vyombo vya habari.
Mhe. Rais Magufuli amemshukuru Mhe. Rais Tshisekedi kwa kufanya Ziara ya Kitaifa hapa nchini na kwa dhamira yake ya kukuza na kuimarisha zaidi uhusiano na ushirikiano kati ya DRC na Tanzania hususani katika uchumi.
Mhe. Rais Magufuli amesema kiwango cha biashara kinachofanywa kati ya Tanzania na DRC ni kidogo ikilinganishwa na ukubwa wa uhusiano na fursa zilizopo kati ya nchi hizo, ambapo katika mwaka uliopita biashara kati ya Tanzania na DRC ilikuwa na thamani ya shilingi Bilioni 305.375, wafanyabiashara wa DRC walikuwa wamewekeza nchini Tanzania miradi 8 yenye thamani ya shilingi Bilioni 13.144 na kukiwa na Watanzania wachache ambao wameweka nchini DRC.
Amefafanua kuwa japo kuwa sekta ya usafirishaji inaridhisha kidogo kwa DRC kuongeza mizigo inayopita Bandari ya Dar es Salaam kutoka tani Milioni 1.176 ya mwaka 2017 hadi kufikia tani Milioni 1.78 ya mwaka 2018, kuna haja ya kuchukua hatua madhubuti zaidi za kukuza biashara na uwekezaji ikiwemo kuondoa vikwazo, kutumia fursa mbalimbali zilizopo ikiwemo madini, uvuvi, kilimo, ujenzi wa viwanda na kulitumia ipasavyo soko la nchi hizo lenye jumla ya watu Milioni 140.
Kwa upande wa Tanzania, Mhe. Rais Magufuli amesema pamoja na kujenga reli ya kati (SGR), kupanua Bandari ya Dar es Salaam, kuanzisha huduma za pamoja za bandari kwa saa 24 (siku zote 7 za wiki) na kuimarisha miundombinu ya barabara katika njia 8 za kuingia na kutoka DRC, Tanzania imeongeza muda wa kusubiri bandarini kutoka siku 24 hadi 30 kwa mizigo ya DRC, imeondoa katazo la ufunguaji makontena na kufuta tozo ya kusindikiza mizigo hadi mpakani mwa Tanzania na DRC.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli amesema Tanzania itaikarabati meli ya MV. Liemba inayotoa huduma kati ya Tanzania (Kigoma) na DRC, itajenga meli mpya mbili ambapo moja itakuwa na uwezo wa kubeba abiria 600 na mizigo tani 400 na ya pili itakuwa meli ya mizigo yenye uwezo wa kubeba tani 2,000 na ameafiki mapendekezo ya Mhe. Rais Tshisekedi ya reli ya kati ya Tanzania kujengwa kutoka Isaka – Rusumo – Kigali hadi Mashariki ya Kongo ili kufikisha mizigo moja kwa moja nchini DRC.
Mhe. Rais Magufuli amewataka Mawaziri na Wataalamu wa Tanzania na wenzao wa DRC (watakaoteuliwa) ndani ya mwaka huu, kuitisha kikao cha Kamati ya Pamoja ya Ushirikiano (Joint Permanent Commission – JPC) ambacho hakijawahi kufanyika tangu mwaka 2002 ili kujadili na kurejesha maeneo muhimu ya ushirikiano ikiwemo ushirikiano katika usafiri wa anga kati ya Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) na Shirika la Ndege la Congo (Congo Airways).
Mhe. Rais Magufuli amemtakia heri Mhe. Rais Tshisekedi katika uongozi wake na amemshauri kusimama kidete kutatua matatizo ya wananchi wa DRC huku akisisitiza kuwa kwa utajiri wa DRC, uchumi wa nchi hiyo haupaswi kukua kwa kiwango kidogo cha asilimia 4.
Kwa upande wake, Mhe. Rais Tshisekedi amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kumwalika kufanya Ziara ya Kitaifa hapa nchini na amebainisha kuwa lengo la ziara yake ni kuimarisha na kukuza zaidi udugu, urafiki na uhusiano wa kihistoria uliopo kati ya Tanzania na DRC.
Mhe. Tshisekedi amesema katika mazungumzo yake na Mhe. Rais Magufuli wamekubaliana kuwa bila amani jitihada za maendeleo katika eneo lote la maziwa makuu hazitafanikiwa, hivyo wana kila sababu ya kuhakikisha kunakuwa na amani ya kudumu pamoja na kutumia vizuri fursa mbalimbali za kukuza uchumi ukiwemo ukanda wa ziwa Tanganyika wenye urefu wa kilometa 554.
Amesema ana matumaini kuwa JPC itakayofanyika itatatua changamoto zote za kukuza biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na DRC na ameahidi kufanya kazi kwa ushirikiano wa karibu na Mhe. Rais Magufuli.
Pamoja na kumshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa ahadi yake ya kuunga mkono ombi la DRC kujiunga katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, Mhe. Rais Tshisekedi ameahidi kuhudhuria Mkutano wa 39 Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) utakaofanyika mwezi Agosti mwaka huu hapa Tanzania na amebainisha kuwa anaamini kuwa SADC ni jumuiya yenye fursa na manufaa makubwa ya kiuchumi.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
14 Juni, 2019
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 13 Juni, 2019 amekutana na wabunifu wawili wa kuzalisha umeme kwa kutumia maji ya mito kutoka Mkoani Njombe na kuagiza wataalamu wa wizara na taasisi zinazojihusisha na sayansi, teknolojia na uvumbuzi kuwafuatilia na wabunifu na wavumbuzi mbalimbali ili kuwaunga mkono katika kuboresha kazi zao.
Wabunifu waliokutana na Mhe. Rais Magufuli Ikulu Jijini Dar es Salaam ni John Akani Fute na Jairos Ngairo ambao wamebuni miradi ya kuzalisha umeme kwa kutumia maji yanayotiririka mtoni, kusukuma maji kwa kutumia pampu zisizotumia umeme na kusaga nafaka kwa kutumia machine zinazoendeshwa na maji ya mto. Bwana Fute amebuni mradi unaozalisha kilowati 28 na Bw. Ngairo anazalisha kilowati 15 za umeme.
Mkutano huo umewahusisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati Dkt. Hamis Mwinyimvua, Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Leonard Akwilapo, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara Bw. Ludovick Nduhiye pamoja na viongozi na wataalamu wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC).
Mhe. Rais Magufuli amewapongeza wabunifu hao kwa kuzalisha umeme wa gharama nafuu unaowanufaisha wananchi na ameagiza TANESCO na COSTECH kuwaunga mkono ambapo TANESCO itatoa shilingi Milioni 30 na COSTECH shilingi Milioni 20 kwa wabunifu hao, na pia timu ya wataalamu itaondoka kesho kwenda Njombe ilipo miradi hiyo kwa ajili ya kutoa ushauri wa kitaalamu na kuiboresha.
Mhe. Rais Magufuli ameelezea kutofurahishwa na vitendo vya wataalamu kuwakatisha tamaa na kuwatisha wabunifu wa vitu mbalimbali vinavyowasaidia wananchi kama ambavyo Bw. John Fute (Pwagu) na Bw. Jairos Ngairo wamekuwa wakifanyiwa na badala yake ametaka wabunifu hao waungwe mkono kwa ushauri wa kitaalamu na kuwawezesha kuongeza tija.
Mhe. Rais Magufuli ameipongeza TBC kwa kufuatilia kazi za ubunifu na uvumbuzi kupitia makala yake ya Hadubini (Habari kwa Kina) ikiwemo makala ya ubunifu wa mradi huo wa umeme iliyoandaliwa na waandishi wa Habari Bi. Tatu Abdallah na Bi. Zaituni Mkwama na ameagiza Wizara na Taasisi za Serikali kufuatilia taarifa zinazotangazwa na vyombo vya habari na kuchukua hatua katika maeneo yanayozihusu.
Ameiagiza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kufuatilia jengo la ghorofa 3 linalodaiwa kutelekezwa na raia mmoja wa kigeni huko Kunduchi Jijini Dar es Salaam ambalo limebaki mikononi mwa mlinzi ambaye anatishwa na wajanja wanaotaka kujimilikisha kwa nguvu. Taarifa hii pia ilitangazwa na TBC kupitia makala ya Hadubini.
“Nakupongeza sana Mkurugenzi Mkuu wa TBC, Dkt. Ayub Rioba na wafanyakazi wa TBC kwa kazi nzuri mnayoifanya, angalau nyinyi mnathubutu kujituma hadi vijijini kufuatilia mambo haya muhimu kwa jamii, nataka wizara na taasisi ambazo zina wataalamu na wasomi ziigeni mfano huu” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Wakizungumza katika mkutano huo, Bw. Fute na Bw. Ngairo wamemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kuwapa shilingi Milioni 5 ikiwa ni kutambua ubunifu wao na wameahidi kwenda kuboresha zaidi kwa kushirikiana na wataalamu wa Serikali.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
13 Juni, 2019
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amempongeza Rais wa Jamhuri ya Zimbabwe Mhe. Emmerson Mnangagwa kwa hatua madhubuti za kufanya mageuzi ya kiuchumi katika nchi hiyo na ametoa wito kwa Jumuiya ya Kimataifa kuondoa vikwazo vilivyowekwa dhidi ya Zimbabwe.
Mhe. Rais Magufuli amesema hayo tarehe 28 Mei, 2019 wakati akitoa hotuba katika Dhifa ya Kitaifa iliyoandaliwa na Mhe. Rais Mnangagwa kwa heshima yake na kufanyika Ikulu Jijini Harare.
Mhe. Rais Magufuli amesema katika kipindi kifupi cha tangu Mhe. Rais Mnangagwa aingie madarakani hali ya uchumi imeanza kuimarika ambapo kwa sasa uchumi wa Zimbabwe unakua kwa wastani wa asilimia 3.5, mwaka ujao unatarajiwa kukua kwa wastani wa asilimia 4.2 na mwaka unaofuata kuongeza hadi wastani wa asilimi 4.4.
Kufuatia hali hiyo ameisihi Jumuiya ya Kimataifa kuondoa vikwazo mbalimbali vilivyowekwa dhidi ya Zimbabwe kwa kuwa vikwazo hivyo vinawaumiza wananchi wa Zimbabwe wakiwemo watoto na wanawake.
Katika hotuba hiyo, Mhe. Rais Magufuli kwa mara nyingine amewapa pole Rais na wananchi wote wa Zimbabwe kwa kupoteza watu takribani 400 waliofariki dunia katika mafuriko yaliyosababishwa na Kimbunga Idai kilichoikumba Zimbabwe Machi 2019. Amesema Watanzania wanaungana na ndugu zao Wazimbabwe katika majonzi ya kuondokewa na jamaa zao na wanawaombea kwa Mwenyezi Mungu aziweke roho zao mahali pema peponi, Amina.
Kuhusu uhusiano wa Tanzania na Zimbabwe ulioasisiwa na Baba wa Taifa Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere na Mzee Robert Mugabe, Mhe. Rais Magufuli amesema Tanzania inatambua na inathamini uhusiano huu wa kihistoria na kidugu na amebainisha kuwa jukumu lililopo sasa ni kuelekeza nguvu nyingi zaidi katika uhusiano na ushirikiano wa kiuchumi utakaoziwezesha Tanzania na Zimbabwe kuongeza biashara na uwekezaji.
Mhe. Rais Magufuli amebainisha kuwa katika mazungumzo yake ya faragha na Mhe. Rais Mnangagwa leo mchana wamekubaliana kusimamia ipasavyo makubaliano yaliyopo katika Kamati ya Pamoja ya Kudumu (Joint Permanent Commission – JPC) kwa manufaa ya nchi zote mbili.
“Mhe. Rais Mnangagwa ujio wangu hapa Zimbabwe ni kuthibitisha kuwa urafiki wetu bado upo imara na sisi Tanzania tumejipanga kuuimarisha zaidi, tunataka tufanye biashara zaidi na nyinyi ndugu zetu wa Zimbabwe ili tukuze uchumi wa nchi zetu na kuongeza kipato cha wananchi wetu” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Kwa upande wake, Mhe. Rais Mnangagwa amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kukubali mwaliko wake, na amemthibitishia kuwa yeye na wananchi wa Zimbabwe wanatambua kuwa Watanzania ni ndugu zao waliojitolea kwa dhati katika ukombozi wao wakiongozwa na dhamira ya dhati ya Hayati Mwl. Nyerere.
Amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kuwa kiongozi wa kwanza katika nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kutoa msaada wa chakula, dawa na vifaa vya kujihifadhi wakati Zimbabwe alipokumbwa na mafuriko yaliyosababishwa na Kimbunga Idai mwezi Machi 2019.
Mhe. Rais Mnangagwa amesema msaada huo uliwagusa Wazimbabwe wengi na kuwakumbusha umuhimu wa kuchukua tahadhari dhidi ya majanga na mabadiliko ya tabia nchi.
Amesisitiza kuwa daima Zimbabwe itabaki kuwa rafiki na ndugu wa kweli wa Tanzania na hivyo amemhakikishia Mhe. Rais Magufuli kuwa nchi hiyo ipo tayari kukuza zaidi ushirikiano wa kiuchumi kwa kuongeza biashara na uwekezaji pamoja na kushirikiana katika usafiri wa anga.
Amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kumpa mbinu mbalimbali za kiuongozi ikiwemo kuondoa watumishi hewa ambao wamekuwa mzigo mkubwa kwa Serikali na ameahidi kudumisha ushirikiano kati ya chama chake ZANU-PF na Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Dhifa hiyo ya Kitaifa imehudhuriwa na Makamu wa Rais wa Zimbabwe Mhe. Constantino Chiwenga, Mke wa Rais wa Zimbabwe Mhe. Amai Auxillia Mnangagwa, Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara Ndg. Philip Mangula, viongozi wa ZANU-PF, Mawaziri wa Tanzania na Zimbabwe na Mtoto wa Baba wa Taifa na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Ndg. Makongoro Nyerere.
Kesho (29 Mei, 2019), Mhe. Rais Magufuli atamaliza ziara yake hapa nchini Zimbabwe kwa kufanya mazungumzo rasmi na mwenyeji wake Mhe. Rais Mnangagwa na kutembelea na kuweka shada la maua katika eneo la kumbukumbu ya mashujaa wa ukombozi wa Zimbabwe.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Harare
28 Mei, 2019
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amemteua Bw. Mohammed Abdallah Mtonga kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL).
Bw. Mtonga anachukuwa nafasi ya Dkt. Omari Rashid Nundu ambaye ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya kampuni ya simu za mkononi ya Airtel Tanzania.
Uteuzi wa Dkt. Omari Rashid Nundu katika nafasi hiyo unafuatia makubaliano yaliyofikiwa kati ya Serikali ya Tanzania na kampuni ya Bharti Airtel International juu ya uendeshaji wa kampuni ya simu za mkononi ya Airtel Tanzania ambapo Mwenyekiti wa Bodi ya Airtel Tanzania anapaswa kuteuliwa na Serikali ya Tanzania.
Kwa mujibu wa makubaliano hayo Afisa Mkuu wa Ufundi (Chief Technical Officer – CTO) pia anateuliwa na Serikali ya Tanzania, na aliyeteuliwa kushika nafasi hiyo ni Dkt. Prosper Godfrey Mafole.
Wajumbe wengine watakaoiwakilisha Serikali katika Bodi ya Airtel Tanzania ni Bw. John Marato Sausi na Bw. Lekinyi Ngariapusi Mollel.
Uteuzi huu unaanza leo tarehe 12 Juni, 2019.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
12 Juni, 2019
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 08 Juni, 2019 amemteua Mhe. Innocent Lugha Bashungwa kuwa Waziri wa Viwanda na Biashara.
Mhe. Bashungwa anachukua nafasi ya Mhe. Joseph George Kakunda ambaye uteuzi wake umetenguliwa.
Kabla ya uteuzi huo, Mhe. Bashungwa alikuwa Naibu Waziri wa Kilimo.
Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli amemteua Bw. Edwin Mhede kuwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Bw. Mhede anachukua nafasi ya Bw. Charles Edward Kichere ambaye uteuzi wake umetenguliwa.
Kabla ya uteuzi huo Bw. Mhede alikuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara.
Uteuzi wa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara utafanywa baadaye.
Kufuatia uamuzi huo, aliyekuwa Kamishna Mkuu wa TRA Bw. Charles Edward Kichere ameteuliwa kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Njombe.
Bw. Kichere anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Bw. Erick Shitindi ambaye amestaafu.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
08 Juni, 2019
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amewapongeza Watanzania kwa kuitikia wito wa Serikali wa kuacha kutumia mifuko ya plastiki ambayo ina madhara makubwa katika mazingira na viumbe hai wakiwemo binadamu.
Mhe. Rais Magufuli ametoa pongezi hizo tarehe 03 Juni, 2019 wakati akizungumza na wafanyabiashara wa soko la samaki la Feri Jijini Dar es Salaam baada ya kufanya ziara ya kushtukiza sokoni hapo na kujionea wafanyabiashara na wanunuzi wa samaki wakitumia mifuko mbadala.
Mhe. Rais Magufuli amempongeza Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. January Makamba, Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya wote ambao wamesimamia utekelezaji wa maelekezo aliyoyatoa tangu mwaka 2016 kuhusu kuondoa matumizi ya mifuko ya plastiki kwa mujibu wa sheria.
Hata hivyo, Mhe. Rais Magufuli amewataka wafanyabiashara kutotumia mwanya huo kuuza mifuko na vifungashio mbadala kwa bei kubwa na badala yake amewataka wafanyabiashara hao pamoja na wawekezaji wa ndani na nje kujenga viwanda vya kutengeneza mifuko na vifungashio kwa kutumia malighafi zinazopatikana hapa nchini.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli ametoa wito kwa wananchi kujenga utamaduni wa kuwa na vifaa vya kubebea bidhaa wanazozinunua madukani na masokoni ili kuepuka gharama kununua vifungashio ama mifuko mbadala.
Mhe. Rais Magufuli ameziagiza mamlaka zinazohusika, kuhamasisha utengenezaji wa mifuko na vifungashio mbadala hapahapa nchini ili kuongeza ajira katika viwanda vya kutengenezea bidhaa hizo badala ya kuacha wafanyabiashara wakigeuza nchi kuwa mahali pakuingiza bidhaa hizo kutoka nje ya nchi.
Akiwa katika soko hilo la Feri, Mhe. Rais Magufuli amenunua samaki kutoka kwa wafanyabiashara wadogo wanaotumia vitambulisho vya wajasiriamali na amewapongeza kwa juhudi zao za kujitafutia kipato halali.
Ameiagiza Manispaa ya Kinondoni kupunguza tozo ya pango kwa wapaa samaki kutoka shilingi 1,000 hadi shilingi 500 kwa siku na ameitaka manispaa hiyo kutenga shilingi Milioni 10 kutoka kwenye makusanyo ya soko hilo kujenga jengo jingine la wafanyabiashara wasiouza samaki kama vile Mama Lishe, Baba Lishe na wauza bidhaa zingine ambao hawanufaiki na jengo la wauza samaki ambalo mwaka jana alichangia shilingi Milioni 20.
Mhe. Rais Magufuli amekagua maendeleo ya ujenzi wa jengo la wauza samaki ambalo alilichangia shilingi Milioni 20 mwaka jana ambapo ameagiza Manispaa ya Ilala ifanye ukaguzi wa gharama zilizotumika kutokana na kuwepo wasiwasi wa matumizi mabaya ya fedha.
Ameiagiza Manispaa ya Ilala na Menejimenti ya soko la Feri kuweka utaratibu wa kuwapokea wafanyabiashara wanaoingiza samaki sokoni hapo kwa muda wote wa saa 24, kuweka umeme na maji katika jengo mojawapo la wafanyabiashara wa samaki ndani ya siku 5 na kuingiza umeme katika jengo la huduma ya Msalaba Mwekundu (Red Cross) lililopo sokoni hapo.
Huku wakimshangilia Wafanyabiashara wa soko la Feri wamemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa jinsi anavyowapigania Watanzania wanyonge wakiwemo wafanyabiashara wadogo na wamemhakikishia kuwa watatekeleza maagizo yake ya kutotumia mifuko ya plastiki kama inavyoelekezwa katika sheria ya usimamizi wa mazingira ya mwaka 2004 na kanuni zake.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
03 Juni, 2019
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 28 Mei, 2019 amewasili katika Jiji la Harare nchini Zimbabwe ambapo anafanya Ziara Rasmi ya Kitaifa ya siku 2 kwa mwaliko wa Rais wa Zimbabwe, Mhe. Emmerson Mnangagwa.
Katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Robert Mugabe, Mhe. Rais Magufuli amepokelewa rasmi na mwenyeji wake, Mhe. Rais Mnangagwa kisha kukagua gwaride rasmi lililoandaliwa kwa ajili yake na kupigiwa mizinga 21.
Baadaye leo, Mhe. Rais Magufuli atakuwa na mazungumzo ya falagha na mwenyeji wake, Mhe. Rais Munangagwa na kisha atahudhuria Dhifa ya Kitaifa iliyoandaliwa na Mhe. Rais Mnangagwa kwa heshima yake.
Kesho, Mhe. Rais Magufuli atafanya mazungumzo rasmi na mwenyeji wake na kisha atatembelea na kuweka shada la maua katika eneo la mashujaa wa ukombozi wa Zimbabwe.
Katika ziara hii Mhe. Rais Magufuli ameongozana na viongozi mbalimbali wakiwemo Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara Ndg. Philip Mangula, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi, Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Luhaga Mpina na Waziri wa Kilimo Mhe. Japhet Hasunga.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Harare
28 Mei, 2019
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amesema Tanzania itaiuzia Zimbabwe tani 700,000 za mahindi kufuatia nchi hiyo kukabiliwa na upungufu wa chakula.
Mhe. Rais Magufuli ametoa ahadi hiyo muda mfupi baada ya kufanya mazungumzo rasmi kati yake na Rais wa Jamhuri ya Zimbabwe, Mhe. Emmerson Mnangagwa yaliyofanyika Ikulu Jijini Harare.
Ameeleza kuwa katika msimu uliopita Tanzania ilipata ziada ya chakula ya tani Milioni 3.3 baada ya kuvuna tani Milioni 16.8 ambapo kati yake mahitaji ya nchi ni tani Milioni 13.5.
Katika mazungumzo hayo, Mhe. Rais Magufuli ameikaribisha Zimbabwe kujifunza jinsi Tanzania inavyotoa mafunzo ya kujenga Taifa kwa vijana kupitia Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na amebainisha kuwa JKT inasaidia vijana kuwa wazalendo wa kweli, kuwa na nidhamu na wakakamavu.
Mhe. Rais Magufuli pia ameelezea kutofurahishwa kwake na kutofanyika kwa Kamati ya Kudumu ya Pamoja (Joint Permanent Commission – JPC) tangu mwaka 1998 hali iliyosababisha kukosekana kwa msukumo wa kutosha wa kutekeleza maeneo muhimu ya uhusiano yenye kuimarisha uchumi wa pande zote na hivyo ametaka Mawaziri na Wataalamu kufanya kikao cha JPC ndani ya mwezi mmoja.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli amesisitiza kuwa Tanzania itaendelea kuwa rafiki wa kweli wa Zimbabwe na ameahidi kuwa tayari kuwaleta walimu watakaofundisha lugha ya Kiswahili katika shule na vyuo vya Zimbabwe.
Halikadhalika, Mhe. Rais Magufuli ametoa wito kwa wafanyabiashara na wawekezaji wa Tanzania na Zimbabwe kuongeza biashara kati ya nchi hizo ikilinganishwa na hali ilivyo hivi sasa ambapo kiwango cha biashara katika nchi hizo ni shilingi Bilioni 22.578 tu.
Kwa upande wake, Mhe. Rais Mnangagwa amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa utayari wake wa kutoa mahindi kwa ajili ya kusaidia upungufu wa chakula nchini Zimbabwe na amesisitiza kuwa Wazimbabwe watafurahi kupata chakula kutoka kwa ndugu zao Watanzania.
Kuhusu maeneo mengine ya ushirikiano ambayo Mawaziri walijadiliana kabla ya mazungumzo hayo, Mhe. Rais Mnangagwa amesema Zimbabwe ipo tayari kuyatekeleza na kukamilisha maeneo mapya yatakayokubalika na kutiwa saini makubaliano yake.
Baadhi ya maeneo hayo ni pamoja na Zimbabwe kuitumia bandari ya Mtwara katika kusafirisha mizigo yake, kushirikiana katika utalii na usafiri wa anga, kubadilishana utaalamu katika kilimo, mifugo na uvuvi.
Baada ya mazungumzo hayo viongozi hao wamekutana na Waandishi wa Habari na kuwaeleza juu ya yaliyojiri wakati wa mazungumzo.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Harare
29 Mei, 2019
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 26 Mei, 2019 amekutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Afrika Kusini, Mhe. Cyril Ramaphosa, Ikulu Jijini Pretoria.
Katika Mazungumzo hayo, Mhe. Rais Magufuli amempongeza Mhe. Rais Ramaphosa kwa kuapishwa kuwa Rais wa Awamu ya Tano wa Afrika Kusini na amemhakikishia kuwa Tanzania itadumisha uhusiano na ushirikiano wa kidugu na kihistoria na nchi hiyo ulioasisiwa na Baba wa Taifa Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere na Hayati Nelson Mandela kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha ANC (African National Congress).
Mhe. Rais Magufuli amemshukuru, Mhe. Rais Ramaphosa kwa kumkaribisha kufanya nae mazungumzo siku moja baada ya kuapishwa kuwa Rais wa Awamu ya Tano wa Afrika Kusini na amebainisha kuwa anatarajia uhusiano wa Tanzania na Afrika Kusini utaimarishwa zaidi katika masuala ya uchumi na kukuza lugha ya Kiswahili.
Kwa upande wake, Mhe. Rais Ramaphosa amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kuhudhuria sherehe za kuapishwa kwake, na amemhakikishia kuwa Afrika Kusini inatambua mchango mkubwa wa Tanzania katika ukombozi wa Taifa hilo na kwamba katika kipindi chake cha uongozi wake atauendeleza na kuuza zaidi uhusiano huo.
Mhe. Rais Ramaphosa amesema kufuatia uamuzi wa Afrika Kusini kuanza kufundisha lugha ya Kiswahili, nchi yake itachukua walimu wa Kiswahili kutoka Tanzania ili watumike kufundisha somo hilo katika shule za msingi na sekondari.
Aidha, Mhe. Rais Ramaphosa ameahidi kufanya Ziara Rasmi ya Kitaifa nchini Tanzania kabla ya Mkutano wa 39 wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) uliopangwa kufanyika mwezi Agosti 2019 nchini Tanzania. Na pia atahudhuria mkutano huo.
Kabla ya mazungumzo hayo Mhe. Rais Magufuli ambaye ameongozana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi amemkabidhi Mhe. Rais Ramaphosa zawadi ya vitabu vya kusoma na kufundishia lugha ya Kiswahili kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
Mhe. Rais Magufuli na Mhe. Rais Ramaphosa wamefanya mazungumzo hayo ikiwa ni kabla Mhe. Rais Ramaphosa hajatangaza Baraza lake la Mawaziri.
Mhe. Rais Magufuli kesho ataondoka nchini Afrika Kusini na kuelekea nchini Namibia ambako atafanya Ziara Rasmi ya Kitaifa kwa mwaliko wa Rais wa Namibia Mhe. Hage Geingob.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Pretoria
26 Mei, 2019
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 21 Mei, 2019 amepokea gawio la Serikali la shilingi Bilioni 2.1 kutoka Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) baada ya Shilika hilo kupata faida ya shilingi Bilioni 8.3 katika kipindi cha mwaka 2018/19.
Hafla ya kukabidhiwa kwa gawio hilo imefanyika Makao Makuu ya TTCL yaliyopo katika Jengo la Extelecom, Posta Jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Aloyce Kamwelwe, Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dkt. Bashiru Ally Kakurwa, Viongozi Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama, Wabunge na viongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa huo Mhe. Paul Makonda.
Mkurugenzi Mkuu wa TTCL Bw. Waziri Kindamba amemueleza Mhe. Rais Magufuli kuwa uwekezaji na mageuzi yaliyofanywa na Serikali kwa shirika hilo tangu mwaka 2016 yameliwezesha kujiimarisha na kuanza kutoa gawio ambapo mwaka jana lilizalisha faida na kutoa gawio la Serikali la shilingi Bilioni 1.5 na mwaka huu limetoa gawio la shilingi Bilioni 2.1 baada ya mapato kuongezeka kutoka shilingi Bilioni 107.4 hadi kufikia shilingi Bilioni 119.4.
Mwenyekiti wa Bodi ya TTCL Mhandisi Omari Nundu amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa jitihada kubwa zilizofanywa na Serikali kuimarisha TTCL zikiwemo kulipatia fedha, kutoa shilingi Bilioni 14.9 kwa ajili ya kununua hisa zote za mbia ili TTCL imilikiwe na Serikali kwa asilimia 100 na kulipigania kwa kila namna hali iliyosaidia kulinusuru.
“Mhe. Rais tunakushukuru sana kwa kuitetea TTCL, bila wewe ingekuwa imekufa, tunakuahidi kuendelea kupiga hatua ikiwemo kupanua uwigo wetu katika soko la mawasiliano” amesema Mhandisi Nundu.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Mhe. Selemani Kakoso amempongeza Mhe. Rais Magufuli na Serikali anayoiongoza kwa uwekezaji mkubwa unaofanywa kwenye miundombinu ya mawasiliano ikiwemo kuinusuru TTCL, kufufua Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), kupigania hisa za Serikali kwenye kampuni ya simu za mkononi ya Airtel, kuwekeza katika teknolojia ya kudhibiti mapato ya Serikali kupitia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na kujenga meli mpya katika maziwa.
Msajili wa Hazina Bw. Athumani Mbuttuka amesema pamoja na gawio lililotolewa na TTCL, Hazina imekwishapokea gawio la shilingi Bilioni 367.21 kwa mwaka 2018/19 kutoka mashirika na kampuni za umma ambazo Serikali ina hisa chache, na kwamba hadi kufikia tarehe 30 Aprili, 2019 Ofisi ya Hazina imekusanya shilingi Bilioni 602 ikiwa ni asilimia 101 ya makisio ya mwaka 2018/19 ambayo yalikuwa shilingi Bilioni 597.76.
Aidha, amebainisha kuwa katika kipindi cha miaka 3 iliyopita makusanyo ya gawio yameongezeka kutoka shilingi Bilioni 119.2 hadi kufikia shilingi Bilioni 339.48 sawa na ongezeko la asilimia 185 na kuongeza kuwa “Hili ni ongezeko kubwa, na unastahili pongezi kubwa Mhe. Rais”.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Aloyce Kamwelwe amemhakikishia Mhe. Rais Magufuli kuwa Wizara hiyo imejipanga kuhakikisha TTCL inazidi kuwa imara na huduma zake zinawafikia Watanzania wengi.
Akizungumza baada ya kupokea mfano wa hundi ya gawio la shilingi Bilioni 2.1, Mhe. Rais Magufuli ameipongeza TTCL kwa hatua kubwa ilizopiga katika kipindi kifupi na ameeleza kuwa kabla ya kuanza kutoa gawio mwaka jana shirika hilo lilikuwa likipata hasara ya shilingi Bilioni 15 kila mwaka kwa kipindi cha miaka 15 jambo ambalo halikubaliki.
Mhe. Rais Magufuli ameelezea kufurahishwa kwake na juhudi za TTCL kuongeza wateja kutoka Milioni 1.8 mwaka jana hadi kufikia Milioni 2.2, kuanzisha kampuni ya huduma za kifedha ya T-Pesa yenye wateja 400,000, mawakala 14,000 na mtaji wa shilingi Bilioni 6 na kuanzisha huduma ya kuhakiki pembejeo za wakulima.
Mhe. Rais Magufuli ameagiza fedha za ruzuku ambazo hutolewa na Serikali kwa Mfuko wa Mawasiliano kwa kampuni zote za simu kwa ajili ya kujenga minara katika maeneo yasiyokuwa na huduma za mawasiliano zielekezwe kwa TTCL pekee ili shirika hilo la umma lijenge minara yake badala ya kukodi kutoka kwa kampuni binafsi ambako hulipa kati ya shilingi Milioni 700 na Milioni 800 kila mwezi.
Pia, Mhe. Rais Magufuli ameelezea kutofurahishwa na taasisi na viongozi wa Serikali ambao hawajaitikia wito wa kutumia huduma za mawasiliano za TTCL na amemuagiza Mkurugenzi Mkuu wa TTCL Bw. Waziri Kindamba kumpelekea orodha ya Mawaziri wanaotumia simu za TTCL.
Kuhusu utoaji wa gawio la Serikali, Mhe. Rais Magufuli amemuagiza Msajili wa Hazina kuhakikisha taasisi zote zinazopaswa kutoa gawio la Serikali zinafanya hivyo vinginevyo zifutwe.
Mapema kabla ya kuanza kwa hafla hiyo, Mhe. Rais Magufuli ametumia moja ya huduma zinazotolewa na TTCL ambayo ni Mkutano Luninga (Video Conference) ambapo amezungumza mubashara na Wakuu wa Mikoa 5 wakiwa katika Mikoa yao na kupokea taarifa mbalimbali za Mikoa hiyo.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
21 Mei, 2019
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD) umetenga shilingi Bilioni 127.3 kwa ajili ya kufadhili miradi ya kilimo nchini Tanzania kwa kipindi cha miaka 3 kuanzia mwaka 2020.
Rais wa IFAD, Mhe. Gilbert Fossoun Houngbo amesema hayo leo tarehe 20 Mei, 2019 Ikulu Jijini Dar es Salaam alipokutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli.
Pamoja na kutenga fedha hizo, Mhe. Houngbo ambaye ni Waziri Mkuu Mstaafu wa Togo amempongeza Mhe. Rais Magufuli na Serikali anayoiongoza kwa juhudi kubwa anazozifanya katika kukuza uchumi ikiwemo utekelezaji mzuri wa miradi inayofadhiliwa na IFAD, kutilia mkazo umuhimu wa uwekezaji usiokuwa tegemezi, unaolinda utu, unaozalisha kipato kwa wananchi na unaojenga misingi endelevu ya kujitegemea.
Amebainisha kuwa baada ya kutenga fedha hizo, IFAD inasubiri upande wa Tanzania kuainisha maeneo mahususi ya miradi ya kilimo ambako fedha zitaelekezwa na ameeleza kuwa ana matumaini miradi hiyo itafanikiwa kwa kuzingatia kuwa Tanzania ni nchi yenye amani na namna Serikali ilivyo na dhamira ya maendeleo.
Mhe. Rais Magufuli ameishukuru IFAD kwa ushirikiano wake mzuri na Tanzania na amemhakikishia Mhe. Houngbo kuwa ushirikiano na uhusiano huo ulioanza mwaka 1978 utadumishwa kwa maslahi ya Watanzania.
Mhe. Rais Magufuli amesema fedha zilizotengwa katika mpango huo wa miaka 3 zitaelekezwa katika maeneo yenye maslahi mapana ya sekta ya kilimo ikiwemo kuwezesha matumizi ya zana bora za kilimo katika uzalishaji, kuzalisha mbegu bora za mazao, kutatua changamoto ya masoko ya mazao, kuboresha ufugaji na ameipongeza IFAD kwa kutoa fedha pasipo kuweka masharti ya maeneo zinakopaswa kuelekezwa.
Mhe. Rais Magufuli ameiagiza Wizara ya Kilimo kuharakisha mchakato wa kuainisha maeneo yatakayopokea fedha hizo ili utekelezaji wa mpango huo uanze.
Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Ushirikiano wa Maendeleo ya Kimataifa wa Sweden, Mhe. Peter Eriksson.
Baada ya mazungumzo hayo, Mhe. Peter Eriksson amempongeza Mhe. Rais Magufuli na Serikali yake kwa mafanikio makubwa katika mapambano dhidi ya rushwa na ameeleza dhamira ya Sweden kuimarisha zaidi uhusiano na ushirikiano wake na Tanzania.
Mazungumzo hayo yamehudhuriwa na Balozi wa Sweden hapa nchini Mhe. Anders Sjöberg na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi.
Katika hatua nyingine, Mhe. Rais Magufuli amemuapisha Mhe. Dkt. Mpoki Mwasumbi Ulisubisya kuwa Balozi wa Tanzania nchini Canada.
Hafla ya kuapishwa kwa Mhe. Balozi Ulisubisya imefanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi na Viongozi Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
20 Mei, 2019
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ameipongeza Taasisi ya Al-Hikma kwa kuandaa mashindano ya Qur’aan Tukufu yaliyojumuisha nchi mbalimbali za Afrika, na kwa kushirikiana na Serikali katika utoaji wa huduma mbalimbali za kijamii.
Mhe. Rais Magufuli ametoa pongezi hizo leo tarehe 19 Mei, 2019 wakati akihutubia katika Mashindano Maalum ya 20 ya Qur’aan Tukufu Afrika yaliyohusisha washiriki kutoka nchi 18 za Afrika na kufanyika katika Uwanja Mkubwa wa Taifa Jijini Dar es Salaam.
Mhe. Rais Magufuli amesema pamoja na kujenga Misikiti 50 hapa nchini, Serikali inatambua kuwa Taasisi ya Al-Hikma imesaidia jamii kwa kuchimba visima vya maji 110, imejenga shule 1 ya msingi na shule 2 za Sekondari na inawasomesha watoto yatima 400.
Kutokana na mchango huo, Mhe. Rais Magufuli ameishukuru taasisi hiyo pamoja na taasisi zingine mbalimbali zinazomilikiwa na Madhehebu ya Dini ambazo zimekuwa zikitoa mchango mkubwa katika kuhudumia jamii kwenye sekta za elimu, afya na kutoa misaada ya kibinadamu.
Kufuatia maombi yaliyotolewa na Taasisi ya Al-Hikma, Mhe. Rais Magufuli amemuagiza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe. Selemani Jafo kuhakikisha taasisi hiyo inapatiwa hati ya umiliki wa eneo ililoomba libadilishiwe matumizi kwa ajili ya kujenga Kituo cha Afya kitakachotoa huduma kwa wananchi wote ifikapo Ijumaa (24 Mei, 2019).
Aidha, Mhe. Rais Magufuli amewapongeza washiriki wote wa mashindano hayo ya Qur’aan Tukufu, Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA), Serikali ya Saudi Arabia na wadau mbalimbali kwa kufanikisha mashindano hayo ambayo licha ya kuimarisha misingi ya kumcha Mwenyezi Mungu, yanaimarisha uhusiano baina ya Tanzania na Saudia Arabia pamoja na Mataifa yote yanayoshiriki.
Amemtaka Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa wa Saudi Arabia Mhe. Dkt. Swalehe Al-Sheikh (ambaye amehudhuria katika mashindano hayo) kufikisha salamu zake kwa Mfalme wa Saudi Arabia, ambapo pamoja na shukrani kwa uhusiano mzuri wa Tanzania na Saudia Arabia ameomba nchi hiyo ijenge Msikiti mkubwa hapa nchini kwa ajili ya Waislamu kufanya Ibada zao.
Mhe. Rais Magufuli amewatakia heri Waislamu wote katika Mwezi Mtukufu wa Ramadhani na amezitaka mamlaka za Serikali kuchukua hatua dhidi ya wafanyabiashara wenye tabia ya kupandisha bei za vyakula wakati wa Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.
Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili, Alhaji Dkt. Ali Hassan Mwinyi amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kuungana na Waislamu katika mashindano hayo na amewataka Watanzania kuendelea kumuombea kutokana na kazi nzuri anazozifanya za kusukuma mbele gurudumu la maendeleo kwa kasi kubwa na kudumisha umoja wa Watanzania.
Nae Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amesema uwepo wa Mhe. Rais Magufuli katika mashindano hayo na hotuba aliyoitoa imedhihirisha dhamira yake ya kuimarisha umoja na mshikamano kwa Watanzania wote na kwamba Waislamu wote wamefarijika sana.
Mhe. Rais Magufuli amekabidhi zawadi kwa washindi wa mashindano hayo ambapo aliyeibuka mshindi wa kwanza ni Mouhamed Diallo (Senegal), wa pili ni Faruq Kabiru Yakubu (Nigeria), wa tatu ni Shamsuddin Hussein Ally (Zanzibar), wa nne ni Idrissa Ousmane (Niger) na wa tano ni Sumaiya Juma Abdallah (Pwani, Tanzania).
Pamoja na viongozi hao, mashindano hayo yamehudhuriwa na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, Makamu wa Rais Mstaafu Mhe. Dkt. Mohamed Gharib Bilal, Mawaziri, Mabalozi wa nchi mbalimbali na viongozi mbalimbali wa Madhehebu ya Dini na vyama vya siasa.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
19 Mei, 2019
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amemteua Mhe. Benjamin William Mkapa (Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania) kuwa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).
Mhe. Mkapa ameteuliwa kushika wadhifa huo kwa kipindi cha pili mfululizo.
Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli amemteua Prof. Ignas Aloys Rubaratuka kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA).
Prof. Rubaratuka ameteuliwa kushika wadhifa huo kwa kipindi cha pili mfululizo.
Uteuzi wa viongozi hao umeanza tarehe 10 Mei, 2019.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
14 Mei, 2019
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) Mhe. Dkt. Akinwumi Adesina ameipongeza Tanzania kwa ukuaji mzuri wa uchumi wa wastani wa asilimia 7 kwa mwaka na hivyo kuendelea kuwa miongoni mwa nchi zenye uchumi unaokua kwa kasi kubwa Duniani.
Mhe. Dkt. Adesina ametoa pongezi hizo leo tarehe 15 Mei, 2019 Ikulu Jijini Dar es Salaam muda mfupi baada ya kukutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kuhusu ushirikiano kati ya benki hiyo na Tanzania katika maeneo mbalimbali ya maendeleo.
Mhe. Dkt. Adesina amempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa dhamira yake njema na msimamo wake wa kuwapigania Watanzania na amemtaka kuendelea na mwelekeo huo ambao umeendelea kuimarisha uchumi kwa ukuaji wa wastani wa asilimia 7 ikilinganishwa na wastani wa ukuaji wa uchumi wa dunia wa asilimia 3.5.
Halikadhalika amempongeza kwa ushirikiano na nchi jirani kama vile Uganda na hivyo kufanikisha ujenzi wa mradi mkubwa wa bomba la kusafirisha mafuta ghafi lenye urefu wa kilometa 1,443 kati ya Hoima nchini Uganda na bandari ya Tanga nchini Tanzania kwa kushirikisha sekta binafsi.
Aidha, Mhe. Dkt. Adesina amesema wamezungumzia kuhusu kilimo na kwamba AfDB ipo tayari kusaidia kutatua tatizo la masoko ya mazao yanayozalishwa katika kanda mbalimbali za Tanzania na kuongeza thamani.
Kuhusu miradi mingine ya maendeleo amesema kwa hivi sasa AfDB imetoa ufadhili kwa miradi yenye thamani ya shilingi Trilioni 4.55 na kwamba hivi karibuni benki hiyo imeidhinisha ufadhili kwa miradi ya ujenzi wa barabara za mzunguko (ring road) za Jiji la Dodoma zenye urefu wa kilometa 110, ujenzi wa uwanja wa ndege wa kimataifa wa Msalato Mkoani Dodoma, na pia ameipongeza Tanzania kwa kuanza mradi mkubwa wa ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa kati ya Dar es Salaam na Dodoma kwa kutumia fedha zake na ameahidi kuwa benki hiyo itaunga mkono mradi huo hasa kwa ujenzi wa kuanzia Isaka kwenda Kigali nchini Rwanda na hivyo kunufaisha nchi nyingine za Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Kwa upande wake, Mhe. Rais Magufuli amemshukuru Mhe. Dkt. Adesina kwa ushirikiano mkubwa ambao AfDB inautoa kwa Tanzania na amemhakikishia kuwa Tanzania itahakikishia fedha zinazotolewa na benki hiyo zinatekeleza miradi iliyokusudiwa kwa uhakika na inaleta matokeo yanayotarajiwa.
Mhe. Rais Magufuli amesema pamoja na miradi hiyo AfDB pia imekubali kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya lami ya Mpanda – Tabora yenye urefu wa kilometa 359, kujenga awamu ya pili ya mradi wa miundombinu ya mabasi yaendayo haraka (BRT) kati ya Kariakoo na Mbagala Jijini Dar es Salaam na kujenga njia ya umeme ya msongo wa kilovoti 400 kati ya Sumbawanga – Mpanda – Kigoma – Nyakanazi.
Kuhusu AfDB kusaidia ujenzi wa reli ya kati kwa kipande cha kuanzia Isaka mpaka Kigali Mhe. Rais Magufuli amesema ufadhili huo utasaidia kuharakisha usafirishaji wa madini yaliyopo katika kanda ya kati na magharibi mwa Tanzania.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
15 Mei, 2019
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ametengua uteuzi wa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi Mkoani Songwe Bw. Adelius Kazimbaya Makwega na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Uyui Mkoani Tabora Bi. Hadija Makuwani.
Mhe. Rais Magufuli ametengua uteuzi wa Wakurugenzi hao kuanzia leo tarehe 16 Mei, 2019.
Mhe. Rais Magufuli ametangaza uamuzi huo katika kikao cha kazi kati yake na Wakuu wa Mikoa, Makatibu Tawala wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Makatibu Tawala wa Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri za Majiji, Manispaa, Miji na Wilaya kilichofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Wakurugenzi wa Halmashauri hizo watateuliwa baadaye.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
16 Mei, 2019
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Magufuli amewataka Wakuu wa Mikoa, Makatibu Tawala wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Makatibu Tawala wa Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri za Wilaya, Miji, Manispaa na Majiji kujenga ushirikiano na uhusiano mzuri baina yao ili kurahisisha utekelezaji wa majukumu yao.
Mhe. Rais Magufuli ametoa maelekezo hayo leo tarehe 16 Mei, 2019 katika kikao cha kazi kati yake na viongozi hao kilichofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam, na kuhudhuriwa na Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, baadhi ya Mawaziri na Makatibu Wakuu.
Mhe. Rais Magufuli amewaonya baadhi ya viongozi hao ambao wamekuwa na migogoro baina yao na hivyo kuathiri utendaji kazi na amesema endapo vitendo hivyo vitaendelea hatasita kuchukua hatua ikiwa ni pamoja kuwaondoa katika nyadhifa zao.
Pamoja na kuwataka kuwa waadilifu na wenye nidhamu kazini, Mhe. Rais Magufuli amewataka kusimamia kwa ukaribu miradi yote ya maendeleo inayotekelezwa katika maeneo yao, kusimamia ukusanyaji wa mapato yote ya Serikali, kusimamia ulinzi na usalama na kusimamia rasimali za umma.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli amewapongeza viongozi hao kwa kazi nzuri wanazozifanya zinazowezesha mipango na mikakati mbalimbali ya Serikali kwenda vizuri na amewahakikishia kuwa anawaamini na anatarajia wataendelea kufanya vizuri katika utekelezaji wa majukumu yao.
“Ni matumaini yangu baada ya kikao hiki cha leo sote tutakwenda kwa mwelekeo mzuri zaidi, nendeni mkachape kazi, mimi ndiye niliyewaweka kwenye nafasi hizo na ninafuatilia utendaji kazi wa kila mmoja wenu, sitarajii kusikia tena hamuelewani miongoni mwenu” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Katika kikao hicho Mhe. Rais Magufuli amesikiliza kero na changamoto mbalimbali ambazo zinawakabili viongozi hao katika maeneo yao ya kazi na ameahidi kwenda kuzishughulikia.
Kabla ya kuanza kwa kikao hicho, Mhe. Rais Magufuli amemuapisha Mhe. Juma Zuberi Homera kuwa Mkuu wa Mkoa wa Katavi.
Mhe. Homera pia amekula kiapo cha uadilifu kwa viongozi wa umma kilichoongozwa na Kamishna wa Maadili Mhe. Jaji Mstaafu Harold Nsekela.
Baada ya kikao hicho, viongozi hao wamekula futari na Mhe. Rais Magufuli aliyoiandaa kwa ajili yao.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
16 Mei, 201
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Serikali ya Shirikisho la Ujerumani kupitia Mpango wa Kusaidia Majeshi Rafiki imekubali kuongeza kipindi cha kutoa misaada kwa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kwa miaka 4 zaidi kuanzia mwaka 2021 hadi 2024 ambapo pamoja na mambo mengine itajenga Hospitali kubwa ya Kijeshi yenye kiwango cha “Level 4” Mkoani Dodoma.
Balozi wa Ujerumani hapa nchini Mhe. Dkt. Detlef Wäechter akiwa na ujumbe kutoka Wizara ya Ulinzi na Wizara ya Mambo ya Nje ya Ujerumani ametangaza uamuzi huo tarehe 09 Mei, 2019 Ikulu Jijini Dar es Salaam alipokutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli.
Pamoja kujenga hospitali hiyo Mhe. Dkt. Wäechter amesema katika ushirikiano huo Ujerumani kupitia Timu ya Ushauri ya Wataalamu wa Kijeshi (GAFTAG) itaongeza mafunzo na vifaa vya ulinzi wa amani, itaendelea kufundisha madaktari wa Jeshi na kutoa vifaa vya matibabu na kutoa mafunzo ya ulinzi wa amani.
Katika ushirikiano wa sasa utakaoishia 2021, kati ya mwezi Juni 2017 na Machi 2019, Ujerumani imejenga Hospitali ya Kanda huko Monduli Mkoani Arusha ambayo imewekewa vifaa tiba vinavyotumia teknolojia ya kisasa na itakayotumiwa kama Hospitali ya Rufaa ikisaidiana na Hospitali ya Kijeshi ya Lugalo iliyopo Jijini Dar es Salaam. Ujenzi wa hospitali hiyo umegharimu shilingi Bilioni 5 na Milioni 947 ambapo shilingi Milioni 346.8 kati yake zimetolewa na Serikali ya Tanzania.
Ufadhili mwingine uliotolewa ni upanuzi na uboreshaji wa Chuo cha Sayansi na Tiba cha Lugalo, ujenzi wa karakana za Jeshi katika Mikoa ya Dar es Salaam, Dodoma, Shinyanga na Mwanza, ujenzi wa idara ya dharura ya Hospitali Kuu ya Jeshi Lugalo, ujenzi wa mabweni ya wanafunzi katika Hospitali ya Kanda iliyopo Bububu - Zanzibar, uboreshaji wa Hospitali za Kanda zilizopo Zanzibar, Mbeya, Mwanza na Tabora, msaada wa magari na vifaa tiba.
Mhe. Rais Magufuli ameishukuru Ujerumani kwa kuendeleza na kuukuza uhusiano na ushirikiano na Tanzania na amemhakikishia Mhe. Balozi Wäechter kuwa Serikali ya Tanzania itahakikisha misaada yote inayotolewa inaleta manufaa yaliyokusudiwa.
Mazungumzo hayo yamehudhuriwa na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mhe. Dkt. Hussein Mwinyi, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jen. Venance Mabeyo na Katibu wa Kwanza wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Bw. Malte Loknitz aliyeongoza ujumbe wa Maafisa kutoka Wizara ya Ulinzi na Wizara ya Mambo ya Nje ya Ujerumani pamoja na Mshauri wa GAFTAG hapa nchini Luteni Kanali Thomas Nalbach.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
09 Mei, 2019
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 29 Aprili, 2019 ameendelea na ziara yake ya kikazi Mkoani Mbeya ambapo amefunguwa kiwanda cha maparachichi Wilayani Rungwe, ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa barabara ya lami ya Katumba – Mbambo – Tukuyu na barabara ya lami ya Kikusya – Ipinda – Matema.
Kiwanda maparachichi kinachomilikiwa kwa ushirikiano wa Kampuni ya Chai (TATEPA), Kanisa la Moravian Tanzania na Wakulima zaidi ya 5,000 wa maparachichi wa Wilaya ya Rungwe kina uwezo wa kufungasha tani 60 za maparachichi kwa siku, kimezalisha ajira kwa watu 20,000 na wengine zaidi ya 100,000 wananufaika na uwepo wake, na uwekezaji wake umegharimu shilingi Bilioni 25.
Akizungumza baada ya kufungua kiwanda hicho, Mhe. Rais Magufuli ameipongeza Bodi ya Wakurugenzi wa kiwanda hicho na wakulima wa maparachichi wa Rungwe na ametoa wito kwa wakulima hao kuongeza juhudi katika uzalishaji na mwekezaji kuongeza bei ya ununuzi wa maparachichi ili kumnufaisha zaidi mkulima.
Baada ya kufungua kiwanda hicho, Mhe. Rais Magufuli amesalimiana na maelfu ya wananchi wa Katumba na kuwajulisha kuwa Serikali imeamua kuirejesha Shule ya Sekondari Ndembela kwa Kanisa la Waadventista Wasabato baada ya Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe kushindwa kulipa fidia kwa wakati na pia ametoa shilingi Milioni 5 kuchangia ujenzi wa shule nyingine ya Sekondari Ntuso inayojengwa na wananchi katika eneo hilo.
Kwa eneo la Katumba na Kijiji cha Suma ambako wananchi wamemuomba kusaidiwa upatikanaji wa maji na umeme, Mhe. Rais Magufuli amemtaka Waziri wa Maji Mhe. Prof. Makame Mbarawa kuhakikisha vijiji hivyo vinapata maji na amewahakikishia wananchi hao kuwa Serikali imejipanga kuvipatia umeme vijiji vyote nchini ifikapo mwaka 2021 kupitia mradi wa awamu ya 3 ya usambazaji wa umeme vijijini na mijini (REA-III).
Katika Mji wa Busokela Mhe. Rais Magufuli ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa barabara ya lami ya Katumba – Busokelo – Tukuyu yenye urefu wa kilometa 81.3 ambapo kilometa 10 kati yake ujenzi wake umekamilika kwa gharama ya shilingi Bilioni 9.1.
Akizungumza na wananchi wa Busokelo, Mbambo, Ntaba na Ipinda Mhe. Rais Magufuli amesema kwa kutambua juhudi kubwa za wananchi katika kilimo cha ndizi, kakao, mpunga, viazi mviringo na maparachichi, Serikali itaijenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami na ametoa wito kwa wananchi hao kuongeza juhudi katika uzalishaji wa mazao hayo na kuyapeleka katika masoko yenye bei nzuri.
Ameiagiza Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kuanza mchakato wa ujenzi wa barabara hiyo bila kuchelewa.
Mhe. Rais Magufuli ameweka jiwe la msingi la barabara ya lami ya Kikusya – Ipinda – Matema katika eneo la Tenende Wilayani Kyela ambayo ina urefu wa kilometa 39.1 na ambayo ujenzi wake utagharimu shilingi Bilioni 65.5.
Kabla ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa barabara hiyo, Mhe. Rais Magufuli amezungumza na wananchi wa Ipinda ambao kwa niaba yao Mbunge wao wa Jimbo la Kyela Mhe. Harrison Mwakyembe ameshukuru kwa kujengewa barabara hiyo na kuomba Serikali iwasaidie kutatua tatizo la maji.
Waziri wa Maji Mhe. Prof. Makame Mbarawa na Waziri wa TAMISEMI Mhe. Suleiman Jafo wamewahakikishia wananchi wa Ipinda kuwa Serikali itatatua tatizo la maji la Mji huo katika kipindi kifupi kijacho na itapeleka vifaa katika Kituo cha Afya cha Ipinda ambacho kimejengwa kwa ubora wa hali ya juu.
Katika ziara ya leo, Mhe. Rais Magufuli amepokea malalamiko ya wananchi juu ya kutozwa ushuru kwa mazao yaliyo chini ya uzito wa tani moja, na amewaonya viongozi wa Wilaya kuzingatia matakwa ya sheria yanayowataka wasitoze ushuru huo na pia ametoa maelekezo kwa Halmashauri ambazo bado zinatekeleza sheria ndogo za kutoza ushuru huo kufanya marekebisho.
Aidha, baada ya kupokea malalamiko ya wananchi wa Tenende juu ya kutokamilishwa kwa kituo chao cha afya ambacho ujenzi wake ulioanza tangu mwaka 2010 haujakamilika, Mhe. Rais Magufuli ameielekeza TAMISEMI kutoa shilingi Milioni 50 kwa ajili ya kuendeleza ujenzi huo na ameuagiza uongozi wa Wilaya ya Kyela kuhakikisha kinakamilika ili kianze kutoa huduma kwa wananchi.
Kesho Mhe. Rais Magufuli ataendelea na ziara yake Mkoani Mbeya ambapo atahutubia mkutano wa hadhara katika uwanja wa John Mwakangale Mjini Kyela, ataweka jiwe la msingi la ujenzi wa nyumba za walimu, mabweni na maabara katika Chuo cha Ualimu Mpuguso na kuzungumza na wananchi wa Tukuyu.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Kyela
29 Aprili, 2019
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 06 Mei, 2019 amekutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi wa Idara ya Afrika wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) Bw. Abebe Aemro Selassie Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Baada ya mazungumzo hayo Bw. Selassie amesema aliomba kukutana na Mhe. Rais Magufuli ili kuzungumzia masuala mbalimbali yanayohusu uhusiano wa muda mrefu kati ya Tanzania na IMF na jinsi shirika hilo linavyoshiriki katika kutoa ushauri wa kiuchumi.
Bw. Selassie amempongeza Mhe. Rais Magufuli na Serikali anayoiongoza kwa juhudi kubwa zinazofanywa kuwekeza katika miradi mikubwa ikiwemo miundombinu itakayopunguza gharama za nishati ya umeme.
Kuhusu kuvuja kwa taarifa za ukuaji wa uchumi, Bw. Selassie amesema IMF itatuma timu ya wataalamu wake itakayokutana na timu ya wataalamu wa Wizara ya Fedha na Mipango ya Tanzania kwa lengo la kupitia maeneo yote yaliyoanishwa katika matazamio ya ukuaji uchumi ya IMF na yale ya Serikali ya Tanzania.
“Mimi na Mhe. Rais Magufuli tumekubaliana kuwa IMF na Tanzania watabaki kuwa wadau wanaoaminiana, tunaona fursa nyingi na muhimu katika nchi hii ikiwemo mipango mizuri ambayo Mhe. Rais Magufuli ameianzisha.
Katika wiki zijazo, tutaendelea na mazungumzo na kuendelea kufanya kazi kwa ukaribu na Serikali ya Tanzania na tutaleta timu ya wataalamu watakaokuja kujadiliana na Serikali ya Tanzania ili kutazama maeneo yote yaliyofanyiwa mageuzi makubwa na kuyawianisha na ukuaji wa uchumi” amesema Bw. Selassie.
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Mpango amewahakikishia Watanzania kuwa wizara yake imejipanga kutoa ufafanuzi wa maeneo yote ambayo yanapaswa kuwemo katika taarifa ya IMF ya ukuaji wa uchumi wa Tanzania ikiwemo utelezaji wa miradi mikubwa ya kiuchumi.
“Ili uchumi wa nchi ukue ni lazima uwe unawekeza, na bahati nzuri sana Mhe. Rais amemueleza mgeni wake jinsi tunavyowekeza kwenye miundombinu hususani ujenzi wa reli ya kati, jinsi tunavyowekeza katika ujenzi wa bwawa kubwa litakalotupatia megawati 2,100 za umeme na pia miradi ya barabara na viwanda vingi vilivyojengwa, haya ndio yanayokuza uchumi na sisi tunaamini kabisa wenzetu hawakuyazingatia kabisa katika taarifa ya awali (iliyovuja)” amesema Mhe. Dkt. Mpango.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi amewatoa shaka wawekezaji kutoka nchi mbalimbali kuendelea kuwa na imani na mazingira ya uwekezaji ya Tanzania na amewataka Watanzania kutokua na hofu kwamba wawekezaji watapungua kwani wawekezaji hao wanaendelea kuja.
“Nashukuru kwamba hata wawekezaji wenyewe hawana hofu kwani hata baada ya taarifa hiyo kuwa imevujishwa bado wengi wameendelea kuja na kuonesha nia ya kufanya kazi na sisi, na nashukuru Shirika la Fedha la Kimataifa kwa kuja kuzungumza na sisi, hiyo ni dalili kuwa shirika hili bado lipo nasi na bado tunaendelea na mazungumzo, wale ambao walidhani pana ugomvi mkubwa kati ya Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na Tanzania walikuwa wamekosea kabisa, na msimamo wa Tanzania utafahamika baada ya mazungumzo kuanza na kuweza kuwapitisha katika miradi mikubwa ya maendeleo ambayo inafanyika” amesema Mhe. Prof. Kabudi.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
06 Mei, 2019
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 30 Aprili, 2019 ameendelea na ziara yake Mkoani Mbeya ambapo ameweka jiwe la msingi katika mradi wa ujenzi na ukarabati wa majengo ya Chuo cha Ualimu Mpuguso kilichopo katika Wilaya ya Rungwe na amezungumza na wananchi wa Kyela, Mpuguso na Tukuyu.
Katika Chuo cha Ualimu Mpuguso ambacho majengo yake yaliyojengwa tangu mwaka 1926 yalikuwa chakavu, mradi huo unahusisha ujenzi wa majengo ya nyumba za walimu 13, mabweni 2 yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 308, vyumba 16 vya madarasa, kumbi 2 za mikutano na mihadhara, maabara 2 za sayansi, maktaba 1 na matundu 12 ya vyoo. Vilevile mradi huo unahusisha ukarabati wa nyumba 4 za walimu, mabweni 2, matundu 7 ya vyoo na bafu 7.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Leonard Akwilapo amesema mradi huo utagharimu shilingi Bilioni 9.6 fedha ambazo zinatolewa na Serikali ya Tanzania na Serikali ya Canada, na kwamba Chuo cha Ualimu Mpuguso ni kati ya vyuo 4 vya ualimu vinavyojengewa majengo mapya na kukarabatiwa kwa jumla shilingi Bilioni 36 na Milioni 475. Vyuo vingine ni Ndala (Tabora), Kitangali (Mtwara) na Shinyanga.
Akizungumza na wananchi baada ya kuweka jiwe la msingi la Chuo cha Ualimu Mpuguso, Mhe. Rais Magufuli ameipongeza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa ujenzi na ukarabati wa chuo hicho na amebainisha kuwa Serikali imechukua hatua ya kukarabati vyuo hivyo vikongwe kwa kutambua mchango wake mkubwa katika kuandaa walimu wanaotekeleza mchango mkubwa kufundisha wanafunzi.
Mhe. Rais Magufuli amebainisha kuwa pamoja na kujenga na kukarabati majengo ya vyuo hivyo Serikali imechukua hatua nyingine madhubuti za kuboresha elimu nchini ikiwemo kutoa ruzuku ya shilingi Bilioni 23.8 kwa ajili ya kutoa elimu ya msingi na sekondari bila malipo, kuongeza fedha za mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu kutoka shilingi Bilioni 365 (wanafunzi 98,000) hadi shilingi Bilioni 473 (wanafunzi 125,000) na kuajiri walimu wapya zaidi ya 18,000.
Mapema leo asubuhi, Mhe. Rais Magufuli amezungumza na wananchi wa Kyela katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa John Mwakangale ambapo amewapongeza wananchi wa Kyela kwa juhudi zao kubwa katika kilimo na amebainisha kuwa Serikali inaunga mkono juhudi hizo ikiwemo kutoa shilingi Bilioni 102 kwa Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) ili kuwakopesha wakulima.
“Natoa wito kwenu wakulima wa Kyela, nendeni mkakope Benki ya Kilimo ili mlime kisasa na mzalishe mazao mengi, takwimu zinaonesha Mbeya imekopa kiasi kidogo cha shilingi Milioni 799.9 tu ikilinganishwa na Mikoa mingine ambayo imekopa hadi zaidi ya shilingi Bilioni 30, mnajichelewesha nyinyi wewe wenyewe” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Amewaagiza viongozi wa Mkoa wa Mbeya na Wilaya ya Kyela kuwalinda wakulima kwa kuhakikisha mazao yao yaliyochini ya tani 1 hayatozwi ushuru, na wafanyabiashara wadogo (Machinga) wenye vitambulisho hawabughudhiwi, na pia ameagiza vyombo vya dola kuchunguza na kumchukulia hatua za kisheria Afisa ushirika wa Wilaya hiyo ambaye anakabiliwa na tuhuma za kughushi nyaraka.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli amewataka wananchi wa Kyela kuendelea kushirikiana na wananchi wenzao wa nchi jirani ya Malawi, na ameahidi kuwa katika kipindi chake cha uongozi atahakikisha uhusiano na ushirikiano kati ya Tanzania na Malawi unaimarishwa ikiwemo kutekeleza miradi miwili ya ujenzi wa Kituo cha Pamoja cha huduma za Mpakani cha Kasumulu na mradi wa Bonde la Mto Songwe utakaozalisha megawati 180 za umeme.
Pia ameiagiza Wizara ya Viwanda na Biashara kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo kuhakikisha kiwanda cha kakao kinajengwa Wilayani Kyela ili kusindika kakao nyingi inayozalishwa na wakulima wa Wilaya hiyo.
Katika Mkutano huo, Mhe. Rais Magufuli amechangia shilingi Milioni 5 kwa ajili ya ujenzi mpya wa Msikiti ulioondolewa katika hifadhi ya barabara na ameendesha harambee ya kuchangia ujenzi huo na kufanikiwa kukusanya shilingi Milioni 20.2.
Akiwa njiani kutoka Kyela kwenda Mbeya Mjini, Mhe. Rais Magufuli amesalimiana na wananchi wa Ushirika na Tukuyu ambapo amemuagiza Waziri wa TAMISEMI Mhe. Selemani Jafo kutoa shilingi Bilioni 1 kwa ajili ya kuboresha Hospitali ya Wilaya ya Tukuyu kufuatia hospitali hiyo kukabiliwa na uchakavu na kuelemewa kutoa huduma kwa wagonjwa wa kutoka Wilaya 3 zilizokaribu nayo.
Mhe. Rais Magufuli pia ameagiza kusitishwa mara moja kwa tozo ya shilingi 50,000 wanayotozwa Wamachinga waliopanga katika majengo ya masoko yaliyopo katika Mji wa Tukuyu, na amemuagiza Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya kuwasaka waliofyeka mazao katika shamba la migomba na mahindi la Maria Nyasika na kisha kuwafikisha Mahakamani.
Mhe. Rais Magufuli kesho ataendelea na ziara yake hapa Mkoani Mbeya ambapo atakuwa mgeni rasmi katika Sherehe za Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi (Mei Mosi) zitakazofanyika katika uwanja wa Sokoine Jijini Mbeya.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Mbeya
30 Aprili, 2019
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amewapongeza wafanyakazi wote kote nchini kwa juhudi kubwa wanazozifanya katika kazi na amewahakikishia kuwa Serikali itaendelea kuboresha zaidi mazingira ya kazi, kupanua uwekezaji katika miradi ya maendeleo na kutatua kero za wafanyakazi ili kulinda maslahi yao.
Mhe. Rais Magufuli amesema hayo katika sherehe za maadhimisho ya siku ya wafanyakazi (Mei Mosi) zilizofanyika katika uwanja wa Sokoine Jijini Mbeya, muda mfupi baada ya kupokea maandamano ya wafanyakazi na kusikiliza risala ya wafanyakazi iliyosomwa na Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) Dkt. Yahaya Msigwa.
Mhe. Rais Magufuli amesema kwa kutambua kuwa wafanyakazi wana mchango mkubwa katika ujenzi wa uchumi wa Taifa, Serikali itaendelea kuimarisha mazingira ya kazi na hivyo ameridhia bodi ya mishahara kukutana ilimradi isitumie vibaya fedha za umma, kupunguza viwango vya kodi ya mshahara (PAYE) kwa wafanyakazi wote na kuwajali wafanyakazi wote wakiwemo wenye elimu ya Darasa la Saba.
“Nataka kuwahakikishia ndugu zangu wafanyakazi, Serikali ninayoiongoza inawapenda wafanyakazi, hata hili la wafanyakazi wa Darasa la Saba nataka kuwajulisha kuwa kati ya wafanyakazi wote 525,506 walioajiriwa na Serikali wafanyakazi 98,615 wana elimu ya Darasa la Saba, Serikali haiwabagui wafanyakazi wenye elimu ya Darasa la Saba” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Mhe. Rais Magufuli ameyapokea mapendekezo ya TUCTA kuhusu Serikali kutilia mkazo ujenzi wa viwanda katika maeneo ya uzalishaji wa mazao, kuwekeza zaidi katika uchumi wa bahari ikiwemo kununua meli kubwa za uvuvi katika bahari kuu na kutangaza vivutio vya utalii ili kuongeza uwigo wa ajira na kuongeza mapato ya Serikali ambayo yatawanufaisha Watanzania wote wakiwemo wafanyakazi.
Pamoja na kuahidi kufanyia kazi mapendekezo hayo, Mhe. Rais Magufuli amesema Serikali imeamua kuelekeza fedha nyingi katika miradi itakayochochea uchumi na kuwanufaisha Watanzania wote wakiwemo wafanyakazi na ametaja baadhi ya miradi hiyo kuwa ni Ujenzi wa reli ambao utagharimu shilingi Trilioni 7.026 (kati ya Dar es salaam na Dodoma), kuanza ujenzi wa mradi wa umeme wa mto Rufiji utakaozalisha megawati 2,100 kwa gharama ya shilingi Trilioni 6.5 na ununuzi wa ndege 8 kwa ajili ya kukuza utalii na kurahisisha usafiri.
Maeneo mengine yaliyoelekezewa fedha nyingi ni kukarabati na kujenga meli mpya katika maziwa makuu ya Victoria, Tanganyika na Nyasa kwa gharama ya shilingi Bilioni 287.9, kupanua bandari 3 za Dar es Salaam, Mtwara na Tanga kwa gharama ya shilingi Trilioni 1.2 na kupanua viwanja vya ndege 11.
“Na kwa taarifa yenu jana (tarehe 30 Aprili, 2019) Benki ya Maendeleo Afrika – AfDB imeidhinisha mkopo kwa Tanzania shilingi Bilioni 415.3 zitakazotumika kujenga kilometa 110 kuzunguka Jiji la Dodoma na itakuwa ni barabara ya njia nne” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli amesema Serikali imeamua kuelekeza fedha nyingine nyingi katika miradi ya huduma za jamii ikiwemo ujenzi wa Hospitali za Wilaya 67 uliogharimu shilingi Bilioni 105, kujenga na kukarabati Vituo vya Afya 352 kwa shilingi Bilioni 184.67 na vifaa vyake vya shilingi Bilioni 41.6 pamoja na kuongeza bajeti ya dawa kutoka shilingi Bilioni 31 hadi 270.
Miradi mingine ni maji ya Ziwa Victoria kwenda Miji ya Nzega, Igunga, Tabora na Sikonge pamoja na mradi wa maji wa Jiji la Arusha yote ikigharimu shilingi Trilioni 1 na mradi wa maji katika Miji 28 hapa nchini utakaogharimu shilingi Trilioni 1.2.
Na katika elimu, Mhe. Rais Magufuli amesema Serikali inatoa shilingi Bilioni 23.8 kila mwezi kwa ajili ya kutoa elimu bila malipo, imeongeza mikopo ya elimu ya juu kutoka shilingi Bilioni 365 hadi 473 na fedha nyingine nyingi kuelekezwa katika miradi ya kusambaza umeme, kilimo, ufugaji na mawasiliano.
Kwa upande wa wafanyakazi, Mhe. Rais Magufuli amesema baada ya uhakiki kufanyika Serikali imetoa nyongeza ya mshahara ya shilingi Bilioni 72.8 kwa wafanyakazi 505,985, imelipa malimbikizo ya mishahara ya shilingi Bilioni 75.5 kwa wafanyakazi 50,386, imelipa shilingi Bilioni 29.5 kwa wafanyakazi 118,989 waliopandishwa madaraja, imelipa shilingi Bilioni 291.3 kwa madai ya wafanyakazi yasiyo ya mshahara na kwamba wafanyakazi wengine 193,166 watapandishwa madaraja mwaka ujao wa fedha.
Halikadhalika, Mhe. Rais Magufuli amesema Serikali imeinusuru mifuko ya hifadhi ya jamii kwa kulipa deni la shilingi Trilioni 1.5 ambazo Serikali haikuwa inawasilisha kwa mifuko hiyo tangu mwaka 2012, imeridhia kuendelea na kikokotoo cha zamani kwa malipo ya wafanyakazi wanaostaafu ambao ni mzigo mkubwa na kwamba pamoja na hayo yote pia imewajengea walimu nyumba 11,077, watumishi wa wizara ya afya nyumba 301 na katika mwaka ujao wa fedha itaajiri wafanyakazi wapya 45,000.
Kufuatia majukumu hayo mazito Mhe. Rais Magufuli amewataka wafanyakazi kuwa na subira katika ombi lao la kuongezewa mishahara na ameahidi kuwaongezea mishahara hiyo kabla hajamaliza kipindi chake cha uongozi.
“Nawasihi ndugu wafanyakazi kuendelea kuchapa kazi kwa bidii ili kuiletea maendeleo nchi yetu, Wazee wetu wa zamani walijitoa mhanga kuikomboa nchi yetu kisiasa, ni jukumu letu kizazi cha sasa kujitoa mhanga kuikomboa nchi yetu kiuchumi” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Sherehe za Mei Mosi mwaka huu zimehudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Mke wa Rais Mhe. Mama Janeth Magufuli, Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassa, Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, Spika wa Bunge Mhe. Job Ndugai, Naibu Spika Mhe. Dkt. Tulia Ackson, Mawaziri, Mabalozi, Viongozi Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama, Wakuu wa Mikoa, Wabunge na viongozi wa Mkoa wa Mbeya wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa huo Mhe. Albert Chalamila.
Kesho, Mhe. Rais Magufuli ataendelea na ziara yake hapa Mkoani Mbeya ambapo atafungua Hospitali ua Uamsho wa Wakristo Tanzania (UWATA) na kuzungumza na wananchi wa Wilaya ya Mbarali katika uwanja wa Barafu Mjini Rujewa.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Mbeya
01 Mei, 2019
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amemuagiza Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mhe. Albert Chalamila na viongozi wa Wilaya ya Mbarali kumpelekea orodha ya wananchi waliogawiwa ekari 6,028 zilizorejeshwa kutoka kwa wawekezaji waliouziwa na Serikali mashamba ya mpunga katika Wilaya ya Mbarali.
Mhe. Rais Magufuli ametoa maagizo hayo tarehe 02 Mei, 2019 katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa Barafu Mjini Rujewa baada ya kubaini kuwepo kwa madai ya wananchi yanayoonesha kuwa ugawaji wa mashamba hayo ulifanyika kwa dosari.
Kabla ya hotuba ya Mhe. Rais Magufuli, Mhe. William Lukuvi ameeleza kuwa baada ya kupokea maelekezo ya Mhe. Rais mwaka 2016 yaliyomtaka kushughulikia kero ya wananchi wa Mbarali waliodai kuporwa maeneo yao na wawekezaji, yeye pamoja na viongozi wa Mkoa wa Mbeya na Wilaya ya Mbarali walifanyia kazi maelekezo hayo na kufanikiwa kubaini kuwa mwekezaji wa shamba la Kapunga Rice Farm alikuwa amezidisha eneo la ekari 4,675 na mwekezaji wa shamba la Highland Estate Ltd alizidisha ekari 1,352.9 katika hati zao za umiliki.
Mhe. Lukuvi amesema baada ya kubaini hivyo Wizara ilifanya mabadiliko ya hati za umiliki wa mashamba hayo na ekari zilizozidi kurejeshwa kwa wananchi kama ilivyoelekezwa na Mhe. Rais Magufuli.
Pamoja na kuagiza apatiwe orodha ya wananchi waliogawiwa mashamba hayo Mhe. Rais Magufuli amempongeza mwekezaji wa shamba la Highland Estate Ltd ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Mbarali Mhe. Haroon Mulla Pirmohamed kwa kuachia sehemu ya shamba iliyozidi na kwa kutoa matrekta madogo (Power Tillers) 102 kwa vijiji vyote vya Jimbo la Mbarali, lakini amewaonya watu wanaofanya udalali wa kuwakodisha wakulima mashamba kwa gharama kubwa ikilinganishwa na kiwango kilichowekwa na wawekezaji hao.
Mhe. Rais Magufuli amewaonya wananchi wa Mbarali kuacha majungu dhidi ya viongozi akiwemo Mbunge na amewasihi kushikamana na kujielekeza kuijenga Wilaya yao ya Mbarali.
Kuhusu vijiji 33 vilivyomo katika eneo la hifadhi ya bonde la Mto Ruaha kulingana na Tangazo la Serikali namba 28, Mhe. Rais Magufuli amesema tume ya Mawaziri 8 aliowatuma kufanya tathmini ya maeneo yote yaliyopo katika hifadhi hapa nchini imeshawasilisha taarifa yake, na amewahakikishia kuwa Serikali itafanya maamuzi yatakayozingatia maslahi ya wananchi wa Mbarali.
“Nataka niwaambie ndugu zangu wa Mbarali, Serikali mliyoiweka madarakani kamwe haiwezi kuwaonea, naomba mtuamini tufanyie kazi ripoti ya Mawaziri na tutaleta majibu, lakini kile kijiji cha Machimbo ambacho wananchi wake walidai fidia na wakalipwa takribani shilingi Milioni 800, hao itabidi waondoke” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli amewataka wananchi waliochepusha maji ya Mto Ruaha na kuyaelekeza katika mashamba yao bila vibali kuacha kufanya hivyo kwa kuwa wanasababisha kupungua kwa maji yanayokwenda katika mabwawa ya Mtera na Kidatu ambayo yanazalisha umeme unaoingizwa katika Gridi ya Taifa kwa ajili ya Watanzania wote.
Mhe. Rais Magufuli amewahakikishia wananchi wa Mbarali kuwa Serikali inazo taarifa juu ya kero zao mbalimbali zikiwemo ukosefu wa maji, huduma zisizoridhisha katika vituo vya kutolea tiba, kukatikakatika kwa umeme, rushwa na ufisadi na kuendelea kutozwa kwa ushuru kinyume cha sheria, na kwamba zinafanyiwa kazi.
Mawaziri walioongozana na Mhe. Rais Magufuli katika ziara hiyo wamewaeleza wananchi wa Mbarali kuwa Serikali inaendelea kuboresha huduma mbalimbali ikiwemo kutoa shilingi Bilioni 1.5 kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya, kutoa shilingi Bilioni 1.5 kwa ajili ya ujenzi wa Chuo cha Ufundi (VETA), kutoa shilingi Bilioni 4.2 kwa ajili ya kujenga maghala 7 ya kuhifadhia mazao Mkoani Mbeya yakiwemo 5 yanayojengwa Mbarali na kununua mitambo 25 ya kuvunia mpunga.
Akiwa Njiani kuelekea Mbarali, Mhe. Rais Magufuli amesalimiana na wananchi wa Inyala, Ilongo, Mswiswi, Igurusi, Chimala, Mabadaga na Igawa ambapo ameiagiza Wizara ya Maji kushughulikia tatizo la maji linaloyakabili maeneo hayo na amemuagiza Waziri wa Kilimo Mhe. Josephat Hasunga kuchukua hatua dhidi ya wataalamu wa Kurugenzi ya Umwagiliaji ya Wizara hiyo ambao wamehusika katika ujenzi wa miradi 5 ya mabwawa ya umwagiliaji ambayo licha ya Serikali kutoa fedha nyingi miradi hiyo haifanyi kazi.
Kabla ya kuelekea Mbarali leo asubuhi Mhe. Rais Magufuli amefungua Hospitali ya Uamsho wa Wakristo Tanzania (UWATA) katika kata ya Mwakibete Jijini Mbeya iliyogharimu shilingi Bilioni 3.3 na amepongeza juhudi zinazofanywa na UWATA katika kutoa huduma za kijamii ikiwemo matibabu na elimu.
Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Prof. Joyce Ndalichako amesema Serikali huchangia katika vituo vya afya binafsi nchini ikiwemo Hospitali hiyo ya UWATA ambapo kati ya Julai 2018 na Machi 2019 imechangia shilingi Bilioni 38.4 kwa ajili ya mishahara ya watumishi, vifaa na dawa.
Akiwa Hospitali hapo Mhe. Rais Magufuli amechangia shilingi Milioni 5 kwa shule ya Sekondari Mwakibete kwa ajili ya ununuzi wa madawati, na Naibu Spika Mhe. Dkt. Tulia Ackson ameunga mkono kwa kuchangia shilingi Milioni 2 na Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Mbeya na Naibu wa Menejimenti ya utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa amechangia shilingi Milioni 1.
Kesho, Mhe. Rais Magufuli atamaliza ziara yake hapa Mkoani Mbeya ambapo ataweka jiwe la msingi la mradi wa ujenzi wa Maktaba ya Chuo Kikuu cha Teknolojia Mbeya (MUST) na atazindua upanuzi wa kiwanda cha saruji cha Mbeya.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Mbeya
02 Mei, 2019
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 03 Mei, 2019 amemaliza ziara yake ya kikazi ya siku 9 Mkoani Mbeya kwa kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa jengo la maktaba ya Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST) na kuweka jiwe la msingi la upanuzi wa Kiwanda cha Saruji Mbeya.
Jengo la maktaba la MUST ambalo ni la ghorofa 3, litakuwa na ofisi 24 na uwezo wa kuchukua wasomaji 2,500 kwa mara moja ikilinganishwa maktaba iliyopo hivi sasa ambayo inachukua wasomaji 150 tu. Ujenzi huu utagharimu shilingi Bilioni 5.523.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Prof. Joyce Ndalichako amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kutoa kipaumbele katika elimu na amebainisha kuwa pamoja na kujengwa kwa maktaba hiyo Serikali imetoa shilingi Milioni 482.6 kwa ajili ya kujenga vyumba vya madarasa vya chuo hicho, imetoa fedha nyingine shilingi Milioni 702 kwa ajili ya kukarabati majengo ya MUST Kampasi ya Rukwa inayotarajiwa kuanzishwa hivi karibuni na imetoa shilingi Milioni 483 kwa ajili ya kujenga mabweni ya wanafunzi 600 katika Kampasi hiyo ya Rukwa.
Prof. Ndalichako ameongeza kuwa katika jitihada za kuboresha miundombinu ya vyuo vya elimu ya juu Serikali imetoa shilingi Bilioni 10.2 kwa ajili ya kujenga mabweni ya Chuo Kikuu Mzumbe Mkoani Morogoro, imetoa shilingi Bilioni 3 kwa ajili ya kujenga jengo la taaluma na utawala na shilingi Milioni 488.3 kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu ya Kampasi ya Tegeta Jijini Dar es Salaam.
Maeneo mengine ni Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) ambako imetoa shilingi Bilioni 9.7 kwa ajili ya ujenzi wa Maabara Mtambuka na Kafteria na katika Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi (MUHAS) ambako imetoa shilingi Bilioni 12 kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha umahiri cha magonjwa ya moyo na mishipa ya damu.
Akizungumza na wanafunzi na wafanyakazi wa Vyuo Vikuu vilivyopo Mkoani Mbeya, Mhe. Rais Magufuli amewapongeza viongozi wa MUST kwa lengo lao la kupanua udahili wa wanafunzi kutoka 4,630 wa sasa hadi kufikia 15,000 ifikapo mwaka 2025 lakini ameelezea kutoridhishwa kwake na kasi ndogo ya ujenzi wa jengo hilo la maktaba ulioanza mwaka 2015.
Mhe. Rais Magufuli ameahidi kuwa Serikali itatoa kiasi cha shilingi Bilioni 2.9 zilizobaki kwa ajili ya kukamilisha ujenzi huo ndani ya mwezi huu na amekikosoa chuo hicho kwa kutumia wakandarasi wa nje kujenga jengo la maktaba wakati chuo chenyewe kinao wahandisi ambao wamekuwa wakitumika kujenga majenga mbalimbali ya Serikali ikiwemo shule kongwe 15, Vyuo vya Ualimu 15, Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi 18, hospitali na majengo ya wizara Mkoani Dodoma.
Akijibu maombi ya Mwenyekiti wa Baraza la MUST Mhe. Zakia Megji na Makamu Mkuu wa chuo hicho Prof. Aloys Mvuma, Mhe. Rais Magufuli amesema Serikali itahakikisha chuo hicho kinaimarishwa ili kutimiza ndoto ya Baba wa Taifa Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere aliyetaka Taifa liwe na chuo imara cha sayansi na teknolojia, na kutokana na dhamira hiyo ametoa shilingi Bilioni 5 kwa ajili ya ujenzi wa mabweni ya wanafunzi, na amemuagiza Prof. Ndalichako kuhakikisha wizara inatafuta fedha kwa ajili ya kununua vifaa vya kufundishia na kujifunzia wanafunzi.
Mhe. Rais Magufuli amemuagiza Mkurugenzi wa Jiji la Mbeya SSP. James Kasusura kuhakikisha mkandarasi aliyepewa zabuni ya shilingi Bilioni 10.4 kwa ajili ya kujenga barabara za lami za Jiji la Mbeya zikiwemo kilometa 2 za barabara ya kuungia chuo hapo anafanya kazi usiku na mchana ili barabara hiyo ikamilike haraka badala ya kuleta visingizio vya mvua.
Kuhusu madai ya kuchelewesha kwa uthibitisho wa Ithibati ya kuanzishwa kwa mitaala ya chuo hicho pamoja na vyuo vingine hapa nchini kutoka Tume ya Vyuo Vikuu nchini (TCU), Mhe. Rais Magufuli ametoa siku 10 kwa TCU kutoa majibu ya maombi ya Ithibati ya Mitaala iliyoombwa na MUST na ameelezea kutoridhishwa na ucheleweshaji huo usiozingatia juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali kuwekeza katika elimu.
“Haiwezekani tangu mwaka 2015 mpaka leo hakuna kibali, najitahidi kuteua wasomi lakini wananiangusha, Waziri Ndalichako shughulikia jambo hili nataka hao TCU waje hapa na ndani ya siku 10 watoe majibu, kama ndio waseme na kama ni hapana waseme” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Amekipongeza Chuo Kikuu cha MUST kwa kuanzisha mafunzo ya ufundi mchundo na usadifu na amewaonya wanafunzi wa chuo hicho kuelekeza jitihada zao katika masomo badala ya masuala yasiyo ya msingi ikiwemo mahusiano ya kimapenzi ambayo huishia kuharibu mienendo yao ya masomo na kuwakwaza wazazi na walezi wao. Amesisitiza “Nawasihi wanangu Someni”.
Akiwa Njiani kwenda Kiwanda cha Saruji, Mhe. Rais Magufuli amekutana na wananchi wa Songwe Mbeya Vijijini, ambapo amemuagiza Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Joseph Kakunda kuchukua hatua haraka dhidi ya mwekezaji aliyeuziwa kiwanda cha nguo cha Mbeya tangu mwaka 2001 na hajakiendeleza mpaka leo licha ya kutoa ahadi za kufunga mitambo ya kuzalisha bidhaa nyingine.
Mawaziri walioongozana na Mhe. Rais Magufuli wamejibu kero za wananchi waliokusanyika katika eneo hilo ambapo wameahidi kushughulikia tatizo soko la zao la pareto, kusaidia ujenzi wa Kituo cha Afya na kuimarisha barabara.
Mhe. Rais Magufuli ameweka jiwe la msingi la upanuzi wa Kiwanda cha Saruji cha Mbeya kinachomilikiwa na Serikali kwa asilimia 25, Mfuko wa Hifadhi ya Jamii wa NSSF kwa asilimia 10 na mwekezaji Lafarge Holcim kwa asilimia 65 ambapo upanuzi huo utakaogharimu shilingi Bilioni 105 utaongeza uzalishaji wa saruji kutoka tani 400,000 kwa mwaka hadi kufikia tani 1,100,000.
Pamoja na kuipongeza menejimenti ya kiwanda hicho inayoongozwa na Bi. Ilse Boshoff kwa kiwanda hicho kuendelea kuzalisha saruji baada ya kubinafsishwa mwaka 2003 na kuajiri wafanyakazi 203, Mhe. Rais Magufuli ameitaka kuanza kutoa gawio kwa Serikali.
Mhe. Rais Magufuli pia amekipongeza kiwanda hicho kwa kuzalisha kwa wingi malighafi ya saruji iitwayo Clinker na ametoa wito kwa viwanda vingine kununua Clinker kutoka kiwanda hicho na sio kuagiza kutoka nje ya nchi ambako Serikali imepiga marufuku.
Kuhusu tatizo la kukatika kwa umeme mara kwa mara ambalo Meneja Mkuu wa Kiwanda hicho Bi. Isle Boshoff amelalamikia kuwa husababisha hasara kubwa ikiwemo hasara ya shilingi Bilioni 6.5 waliyoipata mwaka jana, Mhe. Rais Magufuli amemuagiza Waziri wa Nishati na Madini Mhe. Dkt. Medard Kalemani kushughulikia tatizo hilo na pia ameagiza Meneja wa Shirika la Umeme (TANESCO) katika Mkoa wa Mbeya Mhandisi Benedict Bahati kushushwa cheo na kuondolewa katika Mkoa wa Mbeya kutoka na kutoshughulikia tatizo hilo.
Mhe. Rais Magufuli aliyeongozana na Mkewe Mhe. Mama Janeth Magufuli amerejea Jijini Dar es Salaam.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Mbeya
03 Mei, 2019
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 29 Aprili, 2019 ameendelea na ziara yake ya kikazi Mkoani Mbeya ambapo amefunguwa kiwanda cha maparachichi Wilayani Rungwe, ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa barabara ya lami ya Katumba – Mbambo – Tukuyu na barabara ya lami ya Kikusya – Ipinda – Matema.
Kiwanda maparachichi kinachomilikiwa kwa ushirikiano wa Kampuni ya Chai (TATEPA), Kanisa la Moravian Tanzania na Wakulima zaidi ya 5,000 wa maparachichi wa Wilaya ya Rungwe kina uwezo wa kufungasha tani 60 za maparachichi kwa siku, kimezalisha ajira kwa watu 20,000 na wengine zaidi ya 100,000 wananufaika na uwepo wake, na uwekezaji wake umegharimu shilingi Bilioni 25.
Akizungumza baada ya kufungua kiwanda hicho, Mhe. Rais Magufuli ameipongeza Bodi ya Wakurugenzi wa kiwanda hicho na wakulima wa maparachichi wa Rungwe na ametoa wito kwa wakulima hao kuongeza juhudi katika uzalishaji na mwekezaji kuongeza bei ya ununuzi wa maparachichi ili kumnufaisha zaidi mkulima.
Baada ya kufungua kiwanda hicho, Mhe. Rais Magufuli amesalimiana na maelfu ya wananchi wa Katumba na kuwajulisha kuwa Serikali imeamua kuirejesha Shule ya Sekondari Ndembela kwa Kanisa la Waadventista Wasabato baada ya Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe kushindwa kulipa fidia kwa wakati na pia ametoa shilingi Milioni 5 kuchangia ujenzi wa shule nyingine ya Sekondari Ntuso inayojengwa na wananchi katika eneo hilo.
Kwa eneo la Katumba na Kijiji cha Suma ambako wananchi wamemuomba kusaidiwa upatikanaji wa maji na umeme, Mhe. Rais Magufuli amemtaka Waziri wa Maji Mhe. Prof. Makame Mbarawa kuhakikisha vijiji hivyo vinapata maji na amewahakikishia wananchi hao kuwa Serikali imejipanga kuvipatia umeme vijiji vyote nchini ifikapo mwaka 2021 kupitia mradi wa awamu ya 3 ya usambazaji wa umeme vijijini na mijini (REA-III).
Katika Mji wa Busokela Mhe. Rais Magufuli ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa barabara ya lami ya Katumba – Busokelo – Tukuyu yenye urefu wa kilometa 81.3 ambapo kilometa 10 kati yake ujenzi wake umekamilika kwa gharama ya shilingi Bilioni 9.1.
Akizungumza na wananchi wa Busokelo, Mbambo, Ntaba na Ipinda Mhe. Rais Magufuli amesema kwa kutambua juhudi kubwa za wananchi katika kilimo cha ndizi, kakao, mpunga, viazi mviringo na maparachichi, Serikali itaijenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami na ametoa wito kwa wananchi hao kuongeza juhudi katika uzalishaji wa mazao hayo na kuyapeleka katika masoko yenye bei nzuri.
Ameiagiza Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kuanza mchakato wa ujenzi wa barabara hiyo bila kuchelewa.
Mhe. Rais Magufuli ameweka jiwe la msingi la barabara ya lami ya Kikusya – Ipinda – Matema katika eneo la Tenende Wilayani Kyela ambayo ina urefu wa kilometa 39.1 na ambayo ujenzi wake utagharimu shilingi Bilioni 65.5.
Kabla ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa barabara hiyo, Mhe. Rais Magufuli amezungumza na wananchi wa Ipinda ambao kwa niaba yao Mbunge wao wa Jimbo la Kyela Mhe. Harrison Mwakyembe ameshukuru kwa kujengewa barabara hiyo na kuomba Serikali iwasaidie kutatua tatizo la maji.
Waziri wa Maji Mhe. Prof. Makame Mbarawa na Waziri wa TAMISEMI Mhe. Suleiman Jafo wamewahakikishia wananchi wa Ipinda kuwa Serikali itatatua tatizo la maji la Mji huo katika kipindi kifupi kijacho na itapeleka vifaa katika Kituo cha Afya cha Ipinda ambacho kimejengwa kwa ubora wa hali ya juu.
Katika ziara ya leo, Mhe. Rais Magufuli amepokea malalamiko ya wananchi juu ya kutozwa ushuru kwa mazao yaliyo chini ya uzito wa tani moja, na amewaonya viongozi wa Wilaya kuzingatia matakwa ya sheria yanayowataka wasitoze ushuru huo na pia ametoa maelekezo kwa Halmashauri ambazo bado zinatekeleza sheria ndogo za kutoza ushuru huo kufanya marekebisho.
Aidha, baada ya kupokea malalamiko ya wananchi wa Tenende juu ya kutokamilishwa kwa kituo chao cha afya ambacho ujenzi wake ulioanza tangu mwaka 2010 haujakamilika, Mhe. Rais Magufuli ameielekeza TAMISEMI kutoa shilingi Milioni 50 kwa ajili ya kuendeleza ujenzi huo na ameuagiza uongozi wa Wilaya ya Kyela kuhakikisha kinakamilika ili kianze kutoa huduma kwa wananchi.
Kesho Mhe. Rais Magufuli ataendelea na ziara yake Mkoani Mbeya ambapo atahutubia mkutano wa hadhara katika uwanja wa John Mwakangale Mjini Kyela, ataweka jiwe la msingi la ujenzi wa nyumba za walimu, mabweni na maabara katika Chuo cha Ualimu Mpuguso na kuzungumza na wananchi wa Tukuyu.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Kyela
29 Aprili, 2019
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amesema Serikali ya Awamu ya Tano itaendelea kushirikiana na Madhehebu yote ya Dini kwa kuwa inatambua mchango mkubwa wa madhehebu hayo katika kutoa mafundisho ya kiroho na kiimani yanayosaidia wananchi kuwa raia wema pamoja na mchango mkubwa unaotolewa na madhehebu hayo katika utoaji wa huduma za kijamii na maendeleo.
Mhe. Rais Magufuli amesema hayo leo tarehe 28 Aprili, 2019 katika Ibada ya kumsimika Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Mbeya Mhashamu Askofu Mkuu Gervas John Mwasikwabhila Nyaisonga iliyofanyika katika uwanja wa Sokoine Jijini Mbeya na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Maaskofu, Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Tulia Ackson, Mawaziri na viongozi wa Mkoa wa Mbeya wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa huo Mhe. Albert Chalamila.
Pamoja na kuendeleza ushirikiano na Madhehebu yote ya Dini nchini, Mhe. Rais Magufuli amewapongeza wananchi wa Mbeya kwa Jimbo lao kupandishwa hadhi na kuwa Jimbo Kuu Katoliki na kumpata Askofu Mkuu wa Kwanza, na pia ametoa wito kwa Maaskofu na viongozi wote wa Madhehebu ya Dini nchini kuliombea Taifa ili liendelee kukua kiuchumi na kuepukana na majanga mbalimbali.
“Endeleeni kuwaombea Watanzania wazidi kuwa raia wema, waachane na vitendo vya wizi, ubadhilifu, rushwa, unyang’anyi, ubakaji, mauaji na ushirikina” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Mhe. Rais Magufuli amewahakikishia Maaskofu na Watanzania wote kwa ujumla kuwa uchumi wa nchi unakwenda vizuri.
Akizungumza kwa niaba ya Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), Makamu wa Rais wa TEC Mhashamu Askofu Flavian Matindi Kassala amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kuungana nao katika Ibada hiyo na amemhakikishia kuwa Kanisa Katoliki linathamini ushirikiano wake na Serikali.
Mhashamu Askofu Kassala amemhakikishia Mhe. Rais Magufuli kuwa Maaskofu wataendelea kuliombea Taifa na kumuombea yeye ili avuke vikwazo vyote katika juhudi zake za kuliendeleza Taifa.
Askofu Mkuu mpya wa Jimbo Kuu Katoliki la Mbeya Mhashamu Gervas John Mwasikwabhila Nyaisonga amesimikwa na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo kuwa Askofu Mkuu wa Kwanza wa Jimbo hilo ambalo sasa litaundwa pamoja na Majimbo Katoliki ya Mpanda na Iringa.
Mhe. Rais Magufuli ambaye ameongozana na Mkewe Mhe. Mama Janeth Magufuli kesho ataendelea na ziara yake hapa Mkoani Mbeya ambapo atafungua kiwanda cha maparachichi Wilayani Rungwe, ataweka jiwe la msingi la ujenzi wa barabara ya lami ya Katumba – Mbambo – Tukuyu na ataweka jiwe la msingi la ujenzi wa barabara ya lami ya Kikusya – Matema.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Mbeya
28 Aprili, 2019
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 24 Aprili, 2019 ameondoka hapa nchini na kwenda nchini Malawi ambako anafanya Ziara Rasmi ya Kiserikali ya siku 2 kwa mwaliko wa Rais wa Jamhuri ya Malawi Mhe. Prof. Arthur Peter Mutharika.
Mhe. Rais Magufuli akiwa na Mkewe Mhe. Mama Janeth Magufuli ameondoka katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam na atapokelewa rasmi na mwenyeji wake katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kamuzu Mjini Lilongwe.
Akiwa Mjini Lilongwe Mhe. Rais Magufuli ataweka shada la maua katika mnara wa kumbukumbu ya aliyekuwa Rais wa Malawi Hayati Bingu Mutharika, kisha atafanya mazungumzo na mwenyeji wake Mhe. Rais Mutharika, na jioni atahudhuria Dhifa ya Kitaifa aliyoandaliwa kwa heshima yake na Mhe. Rais Mutharika.
Hapo kesho Mhe. Rais Magufuli akiwa na mwenyeji wake Mhe. Rais Mutharika atamaliza ziara yake kwa kufungua msimu wa Soko la Tumbaku na kuzungumza na wadau wa zao hilo na baadaye atarejea nchini Tanzania ambako ataanza ziara ya kikazi ya siku 8 katika Mkoa wa Mbeya.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
24 Aprili, 2019
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli na Rais wa Jamhuri ya Malawi Mhe. Prof. Arthur Peter Mutharika wamewaagiza Mawaziri wa nchi zote mbili kushughulikia haraka changamoto zinazosababishwa kusuasua kwa shughuli za kiuchumi ikiwemo biashara na miradi ya maendeleo.
Viongozi hao wametoa maagizo hayo leo tarehe 24 Aprili, 2019 katika Ikulu ya Lilongwe nchini Malawi katika siku ya kwanza ya Ziara Rasmi ya Kikazi ya siku 2 anayoifanya Mhe. Rais Magufuli hapa nchini Malawi.
Baadhi ya maeneo ambayo Mawaziri wameagizwa kushughulikia haraka ni kuharakisha ujenzi wa Kituo cha Huduma za Pamoja za Mpakani (One Stop Border Post – OSBP) katika mpaka wa Kasumulu, kuharakisha utiaji saini wa makubaliano ya ushirikiano katika masuala ya utalii, usafiri wa anga na kutatua changamoto zinazokikabili Kituo cha Mizigo cha Malawi (Malawi Cargo Center Ltd).
Aidha, Marais wote wawili wamekubaliana kutafuta mkopo nafuu wa fedha kwa ajili ya kutekeleza kwa pamoja mradi wa Bonde la Mto Songwe ambao utazalisha megawati 180 za umeme zitakazotumika kuendelea viwanda na matumizi mengine ya kijamii.
Mhe. Rais Magufuli amesisitiza kuwa Tanzania na Malawi zina kila sababu ya kutumia fursa mbalimbali zilizopo kwa kukuza uchumi wa nchi hizo, kuimarisha ustawi wa jamii na kukuza zaidi biashara ikilinganishwa na hali ilivyo hivi sasa ambapo biashara kati ya hizo ina thamani ndogo ya shilingi Bilioni 146.112 iliyorekodiwa mwaka 2018.
Ameongeza kuwa Tanzania kwa upande wake imeendelea kuweka juhudi kubwa za kuimarisha miundombinu ya usafirishaji ikiwemo kuimarisha bandari hasa za Dar es Salaam na Mtwara, kujenga bandari kavu na kukamilisha ujenzi wa barabara ya Mtwara – Mbambabay ambayo itawawezesha wafanyabiashara wa Malawi kutumia bandari ya Mtwara ambayo ina umbali mfupi wa kilometa 820.
“Tumeamua kuimarisha bandari ya Mtwara ili kuiwezesha kupitisha tani 1,000,000 kwa mwaka ikilinganishwa na tani 400,000 za sasa, tunakamilisha ujenzi wa barabara ya Mbinga – Mbambabay ili ndugu zetu wa Malawi msilazimike kupitisha mizigo yenu Dar es Salaam, kwa hiyo natoa wito kwenu kuwa baada ya mwaka mmoja anzeni kutumia bandari ya Mtwara” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Katika Mazungumzo hayo Mhe. Rais Magufuli amempa pole Mhe. Rais Mutharika na wananchi wote wa Malawi kwa kupoteza ndugu zao na wengine kupata majeraha kufuatia mafuriko yaliyosababishwa na kimbunga cha Idai na amewatakia heri katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika mwezi ujao.
Kwa upande wake Mhe. Rais Mutharika amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kuamua kufanya ziara yake ya kwanza nchini Malawi kwa nchi za Kusini mwa Afrika, na amempongeza kwa juhudi kubwa kufanya mabadiliko ya kiuchumi nchini Tanzania.
Pia, Mhe. Rais Mutharika amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa msaada wa chakula, dawa na vifaa vya kujihifadhi vilivyotolewa na Tanzania kwa waathirika wa mafuriko ya kimbunga Idai, na pia amemshukuru kwa kutoa kiwanja kwa ajili ya ujenzi wa Ubalozi wa Malawi katika Jiji la Dodoma nchini Tanzania.
Mhe. Rais Magufuli ambaye ameongozana na Mkewe Mhe. Mama Janeth Magufuli amewasili Mjini Lilongwe leo asubuhi na mara baada ya mapokezi rasmi ameweka shada la maua katika mnara wa kumbukumbu ya aliyekuwa Rais wa Malawi Hayati Ngwazi Prof. Bingu Wa Mutharika uliopo katika viwanja vya Bunge.
Katika mapokezi hayo Mhe. Rais Mutharika ameongozana na Mkewe Mhe. Mama Getrude Mutharika na baadaye leo jioni Mhe. Rais Magufuli atashiriki Dhifa ya Kitaifa iliyoandaliwa kwa heshima yake katika Ikulu ya Kamuzu Mjini Lilongwe.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Lilongwe
24 Aprili, 2019
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ameongeza muda wa miaka 3 kwa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) iliyokuwa imalize muda wake leo tarehe 23 Aprili, 2019.
Taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi Mhe. Balozi John Kijazi imeeleza kuwa Mwenyekiti na Wajumbe wote wa bodi hiyo wameongezewa muda hadi tarehe 23 Aprili, 2022.
Bodi hiyo inaongozwa na Mwenyekiti, Mhe. Jaji Mstaafu Thomas Mihayo na wajumbe 6 kama ifuatavyo;
- Bw. Augustine Kungu Olal.
- Bi. Zabein Muhaji Mhita.
- Bw. Richard Rugimbana.
- Bw. Mark Leveri.
- Bw. Ally Hussein Laay.
- Bw. Ibrahim Mussa.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
23 Aprili, 2019