Taarifa kwa vyombo vya Habari ya zamani
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli na Rais wa Jamhuri ya Malawi Mhe. Prof. Arthur Peter Mutharika wamewaagiza Mawaziri wa nchi zote mbili kushughulikia haraka changamoto zinazosababishwa kusuasua kwa shughuli za kiuchumi ikiwemo biashara na miradi ya maendeleo.
Viongozi hao wametoa maagizo hayo leo tarehe 24 Aprili, 2019 katika Ikulu ya Lilongwe nchini Malawi katika siku ya kwanza ya Ziara Rasmi ya Kikazi ya siku 2 anayoifanya Mhe. Rais Magufuli hapa nchini Malawi kwa mwaliko wa Mhe. Rais Mutharika.
Baadhi ya maeneo ambayo Mawaziri wameagizwa kushughulikia haraka ni kuharakisha ujenzi wa Kituo cha Huduma za Pamoja za Mpakani (One Stop Border Post – OSBP) katika mpaka wa Songwe/Kasumulu, kuharakisha utiaji saini wa makubaliano ya ushirikiano katika masuala ya utalii, usafiri wa anga na kutatua changamoto zinazokikabili Kituo cha Mizigo cha Malawi (Malawi Cargo Center Ltd) kilichopo Jijini Dar es Salaam.
Aidha, Marais wote wawili wamekubaliana kutafuta mkopo nafuu wa fedha kwa ajili ya kutekeleza kwa pamoja mradi wa Bonde la Mto Songwe ambao utazalisha megawati 180 za umeme zitakazotumika kuendelea viwanda na matumizi mengine ya kijamii.
Mhe. Rais Magufuli amesisitiza kuwa Tanzania na Malawi zina kila sababu ya kutumia fursa mbalimbali zilizopo katika kukuza uchumi wa nchi hizo, kuimarisha ustawi wa jamii na kukuza zaidi biashara ikilinganishwa na hali ilivyo hivi sasa ambapo biashara kati ya nchi hizo ina thamani ndogo ya shilingi Bilioni 146.112 kwa mwaka kama iliyorekodiwa mwaka 2018.
Ameongeza kuwa Tanzania kwa upande wake imeendelea kuweka juhudi kubwa za kuimarisha miundombinu ya usafirishaji ikiwemo kuimarisha bandari hasa za Dar es Salaam na Mtwara, kujenga bandari kavu na kukamilisha ujenzi wa barabara ya Mtwara – Mbambabay (ushoroba wa Mtwara) ambayo itawawezesha wafanyabiashara wa Malawi kutumia bandari ya Mtwara ambayo ina umbali mfupi wa kilometa 820.
“Tumeamua kuimarisha bandari ya Mtwara ili kuiwezesha kupitisha tani 1,000,000 kwa mwaka ikilinganishwa na tani 400,000 za sasa, tunakamilisha ujenzi wa barabara ya Mbinga – Mbambabay ili ndugu zetu wa Malawi msilazimike kupitisha mizigo yenu Dar es Salaam, kwa hiyo natoa wito kwenu kuwa baada ya mwaka mmoja anzeni kutumia bandari ya Mtwara” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Katika Mazungumzo hayo Mhe. Rais Magufuli amempa pole Mhe. Rais Mutharika na wananchi wote wa Malawi kwa kupoteza ndugu zao na wengine kupata majeraha kufuatia mafuriko yaliyosababishwa na kimbunga cha Idai na amewatakia heri katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika mwezi Mei 2019.
Kwa upande wake Mhe. Rais Mutharika amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kuamua kufanya ziara yake ya kwanza nchini Malawi kwa nchi za Kusini mwa Afrika, na amempongeza kwa juhudi kubwa za kufanya mabadiliko ya kiuchumi nchini Tanzania.
Pia, Mhe. Rais Mutharika amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa msaada wa chakula, dawa na vifaa vya kujihifadhi vilivyotolewa na Tanzania kwa waathirika wa mafuriko ya kimbunga Idai, na pia amemshukuru kwa kutoa kiwanja kwa ajili ya ujenzi wa Ubalozi wa Malawi katika Jiji la Dodoma nchini Tanzania.
Mhe. Rais Magufuli ambaye ameongozana na Mkewe Mhe. Mama Janeth Magufuli amewasili Mjini Lilongwe leo asubuhi na mara baada ya mapokezi rasmi ameweka shada la maua katika mnara wa kumbukumbu ya aliyekuwa Rais wa Malawi Hayati Ngwazi Prof. Bingu Wa Mutharika uliopo katika viwanja vya Bunge la Malawi.
Katika mapokezi hayo Mhe. Rais Mutharika ameongozana na Mkewe Mhe. Prof. Mama Getrude Mutharika na baadaye leo jioni Mhe. Rais Magufuli atashiriki Dhifa ya Kitaifa iliyoandaliwa kwa heshima yake katika Ikulu ya Kamuzu Mjini Lilongwe.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Lilongwe
24 Aprili, 2019
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 25 Aprili, 2019 amemaliza Ziara Rasmi ya Kiserikali ya siku 2 Nchini Malawi kwa kufungua msimu wa soko la tumbaku na kuzungumza na wananchi katika eneo la Kanengo Mjini Lilongwe.
Kabla ya kuzungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara, Mhe. Rais Magufuli aliyeongozana na Mkewe, Mhe. Mama Janeth Magufuli pamoja na mwenyeji wake Rais wa Jamhuri ya Malawi Mhe. Prof. Arthur Peter Mutharika aliyeongozana na Mkewe Mhe. Prof. Getrude Mutharika wametembelea mnada wa tumbaku wa Lilongwe uliopo Kanengo.
Akizungumza na wananchi wakiwemo wadau wa tumbaku katika mkutano huo, Mhe. Rais Magufuli amempongeza Mhe. Rais Mutharika, Serikali anayoiongoza na wananchi wa Malawi kwa juhudi kubwa wanazozifanya katika kilimo cha mazao hususani zao la tumbaku ambalo linatoa ajira kwa asilimia 85 ya wananchi wote wa Malawi, linachangia fedha za kigeni kwa asilimia 60 na linachangia Pato la Taifa kwa asilimia 37.
Mhe. Rais Magufuli amepongeza utaratibu wa kuwa na siku rasmi ya ufunguzi wa msimu wa soko la tumbaku na kubainisha kuwa zao hilo sio tu lina umuhimu mkubwa nchini Malawi bali pia nchini Tanzania likiwa miongoni mwa mazao yanayochangia fedha nyingi za kigeni ambapo katika kipindi cha miaka 5 iliyopita limechangia Dola za Marekani Bilioni 1.333 (sawa na shilingi Trilioni 3 na Bilioni 270).
Mhe. Rais Magufuli ameongeza kuwa licha ya kuwa kilimo ni uti wa mgongo wa uchumi wa nchi za Afrika, sekta hii imeendelea kukabiliwa na changamoto nyingi zikiwemo teknolojia duni, ukosefu wa pembejeo na elimu duni ya ugani na hivyo ametoa wito kwa viongozi na wadau wote wa kilimo kufanyia kazi changamoto hizo na kulinda maslahi ya wakulima.
“Nchini Tanzania sekta ya kilimo inatoa usalama wa chakula kwa asilimia 100, inatoa ajira kwa asilimia 70, inatupatia asilimia 60 ya malighafi za viwandani, inachangia asilimia 30 ya Pato la Taifa na inatupatia fedha za kigeni kwa asilimia 25, hii yote inathibitisha kuwa kilimo ni sekta nyeti na muhimu sana Barani Afrika” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli ametoa wito kwa viongozi wa nchi za Afrika kuongeza mkazo katika ujenzi wa viwanda utakaosaidia kuongeza thamani ya mazao ya kilimo yanayozalishwa na wakulima na hivyo kuwaongezea kipato.
Tumbaku ni zao kuu la biashara nchini Malawi ambalo kwa msimu uliopita liliingizia Dola za Marekani Milioni 300 (sawa na shilingi Bilioni 713).
Akizungumza kabla ya kufunguliwa rasmi kwa msimu wa soko la tumbaku, Mhe. Rais Mutharika amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kukubali kufungua msimu wa soko la tumbaku wakati wa ziara yake rasmi ya kiserikali nchini humo, na amefafanua kuwa Serikali yake inatoa umuhimu na heshima kubwa kwa wakulima kwa kuwa uchumi wa Malawi unategemea kilimo.
“Kwetu sisi tumbaku ni zao la kimkakati, mwaka jana tulitunga sheria ya kuwalinda wakulima wa tumbaku na wawekezaji wa zao la tumbaku, tunaamini sasa uzalishaji na ubora wa tumbaku utaongezeka na wakulima watapata maslahi zaidi” amesisitiza Mhe. Mutharika.
Mhe. Rais Magufuli na Mhe. Rais Mutharika wametoa wito kwa wanunuzi wa tumbaku kutowanyonya wakulima wa zao hilo kwa kushusha bei ama kuwaingiza katika mikataba isiyo na maslahi kwao.
Mhe. Rais Magufuli ameagwa rasmi na mwenyeji wake Mhe. Rais Mutharika katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kamuzu Mjini Lilongwe, na baada ya kuondoka nchini Malawi amewasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Songwe Mkoani Mbeya Nchini Tanzania ambako ameanza ziara ya kikazi ya siku 8.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasilino ya Rais, IKULU
Mbeya
25 Aprili, 2019
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amewahakikishia wananchi wa Mbeya kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imejipanga kuhakikisha inatekeleza ahadi zote zilizopo katika Ilani ya Uchaguzi Mkuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2015 ili kujenga Tanzania bora zaidi.
Mhe. Rais Magufuli amesema hayo leo tarehe 25 Aprili, 2019 muda mfupi baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Songwe Mkoani Mbeya akitokea nchini Malawi alikokuwa katika Ziara Rasmi ya Kiserikali ya siku 2 kwa mwaliko wa Rais wa Jamhuri ya Malawi Mhe. Prof. Arthur Peter Mutharika.
Akiwasalimu maelfu ya wananchi wa Jiji la Mbeya waliojitokeza kumpokea na kumshangilia kuanzia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Songwe, Mbalizi, Iyunga, Nzovwe, Mafiati na Uzunguni, Mhe. Rais Magufuli amesema utekelezaji wa ahadi hizo unakwenda vizuri na ametaja baadhi ya maeneo yenye mafanikio makubwa kuwa ni kuimarishwa kwa huduma za afya ambapo hospitali 67 na vituo 352 vinajengwa nchini kote, kuimarishwa kwa elimu ambapo kila mwezi Serikali inatoa shilingi Bilioni 23.8 kwa ajili ya kutoa elimu bila malipo kuanzia shule ya msingi hadi sekondari, kuimarisha barabara zikiwemo barabara za Mkoa wa Mbeya, kuimarisha upatikanaji wa maji na maeneo mengine.
Akiwa Mbalizi wananchi wamemuomba awasaidie kutatua tatizo la maji ambapo baada ya maelezo ya Waziri wa Maji Mhe. Prof. Makame Mbarawa aliyeahidi kuwa Serikali itatoa shilingi Bilioni 3 kwa ajili ya kupeleka maji katika eneo hilo, Mhe. Rais Magufuli ametoa mwezi mmoja kwa Wizara ya Maji kuhakikisha ujenzi wa mradi huo unaanza na wananchi wanaondokana na tatizo la maji linalowakabili.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli amesema Serikali inaendelea kusambaza umeme katika vijiji vyote ambavyo havijapata huduma hiyo.
“Nataka niwahakikishie ndugu zangu wa Mbeya, tumejipanga kutekeleza Ilani ya Uchaguzi na tumedhamiria kuboresha maisha ya wananchi, naomba tuendelee kushikamana kusukuma mbele maendeleo, na maendeleo hayana chama” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Mhe. Rais Magufuli kesho ataendelea na ziara yake hapa Mkoani Mbeya ambapo atazungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara utakaofanyika katika uwanja wa Luanda Nzovwe Jijini Mbeya.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Mbeya
25 Aprili, 2019
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amemteua Dkt. Moses Mpogole Kusiluka kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Taifa ya Uongozi ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania (TASAF).
Dkt. Kusiluka ni Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Ikulu.
Wajumbe wa Kamati ya Taifa ya Uongozi ya TASAF ni;
- Balozi Zuhura Bundala
- Dkt. Dorothy O. Gwajima
- Dkt. Charles A. Mwamwaja
- Dkt. Ruth Rugwisha
- Dkt. Naftali B. Ng’ondi
- Mhandisi Hussein R. Mativila
- Bw. Richard Z. Shilambo
Taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi Mhe. Balozi John Kijazi imeeleza kuwa uteuzi huu umeanza tarehe 23 Aprili, 2019.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Mbeya
26 Aprili, 2019
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amesema Serikali itaendelea kuulinda Muungano wa Tanganyika na Zanzibar na ametoa wito kwa Watanzania wote kuendelea kudumisha amani, umoja na mshikamano.
Mhe. Rais Magufuli amesema hayo tarehe 26 Aprili, 2019 ambayo ni siku ya maadhimisho ya miaka 55 ya Muungano, wakati akihutubia maelfu ya wananchi wa Jiji la Mbeya katika uwanja wa Luanda, Nzovwe Jijini Mbeya akiwa katika siku ya pili ya ziara yake ya kikazi Mkoani hapa.
“Napenda kuwapongeza Waasisi wa Muungano wetu wakiongozwa na Baba wa Taifa, Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere na Hayati Sheikh Abeid Amani Karume kwa uamuzi wao wa busara.
Nataka kuwahakikishia kuwa tumejipanga kuulinda Muungano wetu na yeyote atakayethubutu kuuvunja atavunjika yeye” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Katika mkutano huo Mhe. Rais Magufuli amewapongeza wananchi wa Mkoa wa Mbeya kwa juhudi kubwa za uzalishaji mali hasa kilimo na amewapongeza viongozi wa Mkoa wa Mbeya wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa huo Mhe. Albert Chalamila kwa kusimamia vizuri shughuli za maendeleo ikiwemo ukusanyaji wa mapato ambapo katika masoko ya Jiji la Mbeya mapato hayo yameongezeka kutoka shilingi Bilioni 2.5 hadi shilingi Bilioni 5.
Mhe. Rais Magufuli amekubali ombi lililotolewa na Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Tulia Ackson ambapo ameagiza uwanja wa ndege uliopo Jiji Mbeya ubadilishwe matumizi na kuwa eneo la wafanyabiashara wadogo (Machinga), na ameiagiza Halmashauri ya Jiji la Mbeya kuliboresha eneo hilo kwa kuweka huduma muhimu.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli ameiagiza Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kufuatilia ujenzi wa uwanja wa ndege wa Songwe ambao ujenzi wake unaonekana kuwa na dosari ili ukamilike haraka kwa viwango vya kimataifa na kuwezesha ndege za aina zote kutua na kuruka.
Kuhusu miundombinu ya Jiji la Mbeya, Mhe. Rais Magufuli amesema Serikali imeanza mchakato wa kujenga barabara za mzunguko zenye urefu wa kilometa 40 ambazo zitasaidia kuondoa msongamano wa magari katikati ya Jiji na pia kusaidia kukabiliana na ajali zinazosababishwa na magari makubwa ya mizigo yaendayo nchi jirani kukatiza Jijini humo.
Katika mkutano huo, Mhe. Rais Magufuli ameagiza kuongezwa kwa muda uliowekwa kwa Watanzania kusajili laini zao za simu hadi kufikia Desemba mwaka huu na ameitaka Mamlaka ya vitambulisho vya Taifa (NIDA) kuharakisha mchakato wa utoaji wa vitambulisho hivyo kwa Watanzania sambamba na usajili wa laini za simu kwa kuwa usajili wa laini hizo unafanywa kwa kutumia vitambulisho vya Taifa.
Mhe. Rais Magufuli ameiagiza Wizara ya Viwanda na Biashara kufuatilia kiwanda cha nyama cha Mbeya ambacho kilianzishwa enzi za Baba wa Taifa Hayati Mwl. Nyerere na baadaye kikatelekezwa.
Mapema kabla ya hotuba ya Mhe. Rais Magufuli, Mawaziri walioongozana nae pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mhe. Albert Chalamila wameeleza juhudi kubwa zilizofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano tangu ilipoingia madarakani na mipango mahususi ya kutatua kero mbalimbali ikiwemo kutekeleza mradi wa maji wa shilingi Bilioni 3 utakaomaliza tatizo la maji katika Jiji la Mbeya, kuletwa shilingi Bilioni 18.8 kwa ajili ya kutoa elimu bila malipo, kuletwa shilingi Bilioni 2.137 kwa ajili ya ukamilishaji wa majengo ya shule, vijiji 580 kupatiwa umeme, vituo vya afya 14 kujengwa kwa thamani ya shilingi Bilioni 6.7 na kupatiwa shilingi Bilioni 14.4 za mradi wa uboreshaji wa Jiji la Mbeya.
Mapema kabla ya Mkutano huo Mhe. Rais Magufuli amefungua jengo la Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) lililopo Uzunguni Jiji Mbeya ambalo ujenzi wake umegharimu shilingi Bilioni 13 na litatumika kutoa huduma za mfuko huo na kupangisha.
Kesho Mhe. Rais Magufuli ambaye ameongozana na Mkewe Mhe. Mama Janeth Magufuli ataendelea na ziara yake hapa Mkoani Mbeya ambapo atazindua barabara ya Mbeya – Chunya na ataweka jiwe la msingi la ujenzi wa barabara ya Chunya – Makongorosi.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Mbeya
26 Aprili, 2019
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 27 Aprili, 2019 amefungua barabara ya lami ya Mbeya – Chunya na ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa barabara ya lami ya Chunya – Makongolosi, zote zikiwa ni sehemu ya barabara kuu ya Mbeya – Makongolosi – Rungwa yenye urefu wa kilometa 528.
Ujenzi wa barabara ya lami ya Mbeya – Chunya yenye urefu wa kilometa 72 umegharimu shilingi Bilioni 140 na ujenzi wa barabara ya Chunya – Makongolosi uliopangwa kukamilika Januari 2020 utagharimu shilingi Bilioni 62.7, fedha zote zimetolewa na Serikali ya Tanzania.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mhandisi Patrick Mfugale amesema barabara hizo ni sehemu ya barabara kuu ya Mbeya – Makongolosi – Rungwa yenye urefu wa kilometa 528 na amebainisha kuwa ujenzi wa barabara ya Chunya – Makongolosi umefikia asilimia 33.2.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika Mjini Chunya, Mhe. Rais Magufuli amewapongeza wananchi wa Chunya kwa kutatuliwa kero kubwa ya barabara ya Mbeya – Chunya ambayo baada ya kukamilika kwa kiwango cha lami imerahisisha usafiri wa abiria na mizigo, kuokoa muda mwingi waliokuwa wakiupoteza barabarani na kuepusha ajali zilizowapata kutokana na ubovu wa barabara.
“Inawezekana ndugu zangu wa Chunya mmeanza kusahau kuwa katika barabara hii mlikuwa mnapata ajali nyingi na mlikuwa mnatumia siku nzima kusafiri kutoka Chunya kwenda Mbeya, sasa barabara ya lami imekamilika, natoa wito kwenu muitunze na muitumie vizuri kuinua shughuli za kiuchumi” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Mhe. Rais Magufuli amesema lengo la Serikali ni kuhakikisha barabara hiyo inaendelea kujengwa hadi itakapounganishwa na Mikoa ya Singida na Tabora.
Katika mkutano huo, Mhe. Rais Magufuli ametoa wiki 1 kwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mhe. Albert Chalamila na Waziri wa Madini Mhe. Dotto Biteko kuhakikisha soko la madini ya dhahabu linaanzishwa Wilayani Chunya ili kukabiliana na utoroshaji wa madini hayo unaodaiwa kufanywa na wachimbaji wa dhahabu.
Mhe. Rais Magufuli ametoa onyo kwa viongozi wote wa Mikoa hapa nchini ambao hawajaanza kutekeleza maelekezo ya kufungua masoko ya madini na amebainisha kuwa uwepo wa masoko hayo utawasaidia wachimbaji kutonyonywa na kuongeza mapato ya Serikali.
Kuhusu tatizo la maji linaloukabili Mji wa Chunya licha ya kupatiwa mradi wa shilingi Milioni 992, Mhe. Rais Magufuli ameiagiza Wizara ya Maji kutafuta fedha za dharura kwa ajili ya kusambaza maji hayo kwa wananchi, na ameitaka Wizara hiyo kuifuatilia miradi yote iliyotekelezwa kati ya mwaka 2013 na 2018 yenye thamani ya shilingi Bilioni 117 ambapo imebainika kuwa kati ya fedha hizo ni shilingi Bilioni 17 tu ndizo zimetekeleza miradi inayofanya kazi.
Kwa upande wa afya, Mhe. Rais Magufuli ameiagiza Wizara ya Afya kuiboresha Hospitali ya Wilaya ya Chunya na pia amechangia shilingi Milioni 200 kwa ajili ya uboreshaji wa Hospitali hiyo na shilingi Milioni 200 kwa ajili ya uboreshaji wa Kituo cha Afya cha Makongolosi.
Mhe. Rais Magufuli amempongeza Hakimu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya Mhe. Michael Clarence Mteite, Vyombo vya Dola na viongozi wa Mkoa wa Mbeya kwa kusimamia haki na kuhakikisha mtuhumiwa Idd Said Sekeni aliyemlawiti mtoto wa miaka 6 anasakwa na anatumikia adhabu yake ya kifungo cha maisha jela. Pia ameonya dhidi ya vitendo vya unyanyasaji na udhalilishaji ikiwemo mauaji yanayoambatana na imani za kishirikina na ametaka Vyombo vya Dola kuwasaka na kuwachukulia hatua wote wanaojihusisha na vitendo hivyo.
Akiwa njia kutoka Jijini Mbeya kwenda Chunya, Mhe. Rais Magufuli amewasalimu wananchi wa Kijiji cha Chalangwa na kuwachangia shilingi Milioni 5 katika mradi wao wa ujenzi wa vyumba 5 vya madarasa, akiwa njiani kutoka Chunya kwenda Jijini Mbeya amesimama katika Kijiji cha Mwansekwa na kuchangia shilingi Milioni 10 kwa ajili ya ujenzi wa Shule ya Sekondari na akiwa Iganzo amewahakikishia wananchi wa Mbeya kuwa Serikali itahakikisha viwanda vilivyotelekezwa vinafufuliwa.
Mhe. Rais Magufuli ambaye katika ziara ya leo ameongozana na Mkewe Mhe. Mama Janeth Magufuli, Naibu Spika Mhe. Dkt. Tulia Akson, Mawaziri na Wabunge kesho atashiriki Ibada ya kumsimika Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Mbeya Mhashamu Askofu Gervas John Mwasikwabhila Nyaisonga itakayofanyika katika Uwanja wa Sokoine Jijini Mbeya.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Mbeya
27 Aprili, 2019
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ametoa wiki 1 kwa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Wizara ya Viwanda na Biashara kukamilisha taratibu za uwekezaji kwa kampuni Sugar Investment Trust (SIT) ya Mauritius ambayo imecheleweshwa kuwekeza katika uzalishaji wa sukari tangu mwaka 2017.
Mhe. Rais Magufuli ametoa maagizo hayo tarehe 17 Aprili, 2019 Ikulu Jijini Dar es Salaam baada ya kukutana na kufanya mazungumzo na Mwenyekiti wa Kampuni hiyo Bw. Gansam Boodram aliyeongozana na Balozi wa Mauritius hapa nchini Mhe. Jean Pierre Jhumun.
Katika mazungumzo hayo Bw. Boodram ameeleza kuwa yupo tayari kulima ekari 25,000 za mashamba ya miwa kwa ajili ya uzalishaji wa sukari na kwamba uwekezaji huo utawezesha kuzalishwa kwa tani 125,000 za sukari, ajira za kudumu 3,000 na ajira za muda 5,000 lakini amekwama kuendelea kutokana na kusubiri majibu ya Serikali kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuhusu upatikanaji wa eneo la uzalishaji wa miwa na ujenzi wa kiwanda cha sukari.
Mhe. Rais Magufuli ameagiza ufanyike uchambuzi wa haraka katika maeneo ya Bonde la Mto Rufiji Mkoani Pwani, Eneo la shamba la Mkulazi Mkoani Morogoro na eneo la Kibondo Mkoani Kigoma ili mwekezaji huyo apatiwe na kuanza mara moja uwekezaji kwa kuwa nchi inahitaji kuongeza uzalishaji wa sukari utakaomaliza upungufu wa tani zaidi ya 100,000 ambazo kwa sasa zinaagizwa kutoka nje ya nchi.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli amemuagiza Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara Dkt. Edward Mhede kufuatilia makubaliano ya ushirikiano katika uvuvi kati ya Tanzania na Mauritius ambayo hayajatiwa saini tangu mwaka 2017 licha ya wawekezaji wa Mauritius kuonesha nia ya kutaka kuwekeza katika uvuvi na viwanda vya samaki.
Mhe. Balozi Jhumun amemueleza Mhe. Rais Magufuli kuwa Mauritius inao uzoefu mkubwa katika uvuvi na viwanda vya samaki na kwamba kwa kuitikia wito wake wa kuhamasisha wawekezaji kuja hapa nchini, amefanikiwa kupata kampuni zilizotayari kufanya uwekezaji huo baada ya makubaliano kati ya Tanzania na Mauritius kutiwa saini.
Mhe. Rais amezionya taasisi za Serikali kikiwemo Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kwa kutoharakisha taratibu za kuwawezesha wawekezaji kuwekeza na amemhakikishia Mhe. Balozi Jhumun kuwa atafuatilia kuhakikisha uwekezaji wa kampuni ya SIT unafanyika.
“Ndugu zangu watendaji wa Serikali badilikeni, achene kukwamisha wawekezaji, fanyeni maamuzi na kama yanawashinda toeni taarifa kwenye mamlaka za juu” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
17 Aprili, 2019
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 11 Aprili, 2019 amefungua barabara ya lami ya Mafinga – Nyigo – Igawa na amezungumza na wananchi wa Mtwango, Makambako, Wanging’ombe, Nyololo, Mafinga, Tanangozi na Iringa Mjini.
Barabara ya lami ya Mafinga – Nyigo – Igawa yenye urefu wa kilometa 138.7 inayounganisha Mikoa ya Iringa, Njombe na Mbeya ni sehemu ya barabara kuu ya Dar es Salaam Tunduma (TANZAM) na imekarabatiwa kwa gharama ya shilingi Bilioni 232 na Milioni 601, fedha ambazo zimetolewa kwa mkopo nafuu kutoka Benki ya Dunia na Serikali ya Tanzania.
Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mhandisi Chrispianus Ako amesema barabara ya Mafinga – Nyigo – Igawa ambayo awali ilijengwa mwaka 1972 ilihitaji ukarabati mkubwa uliohusisha kuongeza upana kutoka kati ya meta 6.75 na 8.3 hadi kufikia meta 11 hadi meta 13 na kuongeza unene wa tabaka la lami hadi kufikia Milimeta 90 ili kuiwezesha kupitisha magari yenye uzito mkubwa, upana zaidi na kuweka njia za waenda kwa miguu.
Mhandisi Ako ameongeza kuwa Benki ya Dunia imefadhili ujenzi wa barabara hiyo kupitia Mradi wa Kuboresha Biashara na Usafirishaji wa Kusini mwa Bara la Afrika (SATTFP) na kwamba kupitia mradi huo upembuzi yakinifu na usanifu unaendelea kufanywa kwa barabara ya Igawa – Tunduma yenye urefu wa kilometa 218 na barabara ya mchepuko katika Jiji la Mbeya yenye urefu wa kilometa 48.9.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhe. Isack Kamwelwe amesema Serikali inakarabati barabara za Kanda ya Nyanda za Juu Kusini ili kufungua fursa nyingi za uchumi na kijamii ikiwa ni pamoja na kusafirisha abiria na bidhaa kwenda na kutoka Nyanda za Juu Kusini na nchi jirani za Malawi, Zambia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Kabla ya kufungua barabara hiyo, Mhe. Rais Magufuli amezungumza na wananchi wa Mtwango Wilayani Njombe waliokuwa wamekusanyika kwa maelfu kando ya barabara kuu ya Makambako - Njombe ambapo baada ya kuelezwa na Mbunge wa Lupembe Mhe. Joram Hongoli kuhusu mgogoro wa wakulima wa chai na mwekezaji aliyeuziwa kiwanda cha chai cha Lupemba amewataka wakulima hao wasubiri kwa mwezi mmoja ili Serikali ipitie nyaraka za ubinafsishaji wa kiwanda hicho na kutoa uamuzi.
Pamoja na kuchangia shilingi Milioni 5 kwa ajili ya ujenzi wa mabweni ya Shule ya Sekondari Sovi iliyopo Mtwango, Mhe. Rais Magufuli amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Njombe na viongozi wote wa Mkoa huo kuwasaka watu wote wanaowapa ujauzito wanafunzi na kuwafikisha katika vyombo vya sheria.
Katika Mkutano wa hadhara uliofanyika katika Mji wa Makambako Wilayani Njombe Mhe. Rais Magufuli amepokea shukrani za wananchi kutoka kwa Mbunge wa Jimbo la Makambako Mhe. Deo Sanga (Jah People) kwa kupatiwa shilingi Milioni 400 zilizojenga kituo cha Afya, Shilingi Bilioni 1.5 za ujenzi wa hospitali ya Wilaya na malipo ya fidia ya shilingi Bilioni 3.
Mhe. Rais Magufuli amewahakikishia wananchi wa Makambako kuwa kilometa 6 za barabara za lami katika mji huo zitajengwa, tatizo la upungufu wa maji litakwisha baada ya kutekelezwa kwa mradi utakaogharimu shilingi Bilioni 45 na amewataka Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhe. Prof. Makame Mbarawa na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhe. Isack Kamwelwe kubaki Makambako ili watatue tatizo la maji la eneo la Manga na kumaliza tatizo la madai ya fidia katika kituo cha ukaguzi wa pamoja cha Idofi (One Stop Inspection Center) ikiwa ni pamoja na kupunguza ukubwa wa eneo lililopangwa ambalo lina urefu wa kilometa 2.
Mhe. Rais Magufuli ameishukuru Benki ya Dunia kwa kutoa fedha za mkopo nafuu kwa barabara ya Mafinga – Nyigo – Igawa pamoja na miradi mingine hapa nchini, lakini ametoa wito kwa benki hiyo kufanya uamuzi haraka juu ya miradi ambayo Tanzania imeomba kukopeshwa fedha ili kujua kama fedha itatolewa ama haitatolewa.
Mhe. Rais Magufuli pia ameitaka TANROADS na Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kufuatilia utendaji kazi wa kitengo cha Wahandisi wanaofanya makadirio ya gharama za miradi ya ujenzi wa barabara kutokana na baadhi ya barabara kujengwa kwa gharama kubwa kupita kiasi ikilinganishwa barabara nyingine.
Akiwa njiani kwenda Iringa Mjini, Mhe. Rais Magufuli amesimama na kuzungumza na wananchi wa Nyololo, Mafinga, Ifunda, Tanangozi na Iringa Mjini ambapo Wabunge wa maeneo hayo wamemshukuru kwa Serikali kutoa fedha za ujenzi wa Hospitali za Wilaya, Vituo vya Afya na kutenga fedha kwa ajili ya kuimarisha upatikanaji wa maji.
Mjini Mafinga Mhe. Rais Magufuli amekutana na umati wa maelfu ya wananchi na amejibu maombi ya Mbunge wa jimbo hilo Mhe. Cosato Chumi kuhusu zuio la malori yanayobeba mbao kusafiri baada ya saa 12 jioni ambapo ameagiza Wizara ya Maliasili na Utalii kufanya mchato wa kubadili sheria na kanuni zinazoweka zuio hilo ili malori yaruhusiwe kusafirisha mbao kwa saa 24.
Mjini Iringa alikokutana na maelfu ya wananchi kandokando mwa barabara Mhe. Rais Magufuli amempongeza Mkuu wa Mkoa Mhe. Ali Hapi na viongozi wenzake kwa juhudi zao za kushughulikia kero za wananchi na pia ameagiza mkandarasi anayejenga soko la Iringa Mjini lililotengewa shilingi Bilioni 3.7 awe amemaliza kazi hiyo ndani ya mwezi 1 na nusu.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Iringa
11 Aprili, 2019
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amefungua Hospitali ya Mkoa wa Njombe na kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa barabara ya Njombe – Moronga – Makete akiwa katika siku ya 2 ya ziara yake ya kikazi Mkoani Njombe.
Hospitali ya Mkoa wa Njombe imejengwa katika eneo la Wikichi Mjini Njombe na awamu ya kwanza ya ujenzi wa majengo ya hospitali hiyo yaliyohusisha jengo la huduma za wagonjwa (OPD) imegharimu shilingi Bilioni 3 na Milioni 629 fedha zote zimetolewa na Serikali ya Tanzania.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu ameeleza kuwa wizara yake imeandaa watumishi 119 watakaotoa huduma katika hospitali hiyo na kwamba katika awamu ya pili ya ujenzi wa majengo ya hospitali hiyo, Serikali imetenga shilingi Bilioni 5.7 kwa ajili ya kuendeleza miundombinu yake.
Ameongeza kuwa Wizara ya Afya imejipanga kuhakikisha Hospitali ya Mkoa wa Njombe pamoja na hospitali zote za rufaa nchini zinakuwa na Madaktari Bingwa wa kada muhimu za kipaumbele na inatumia shilingi Bilioni 2.5 kila mwaka kusomesha Madaktari Bingwa ambao wana mkataba wa kufanya kazi katika hospitali za Serikali kwa miaka mitatu baada ya masomo yao.
Mhe. Rais Magufuli ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa barabara ya Njombe - Moronga – Makete yenye urefu wa kilometa 107.4 ambayo inaunganisha Makao Makuu ya Mkoa wa Njombe na Wilaya ya Makete.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhe. Isack Kamwelwe amesema ujenzi wa barabara hii umegharimu shilingi Bilioni 224.563, fedha zote zikiwa zimetolewa na Serikali ya Tanzania na kwamba kujengwa kwake kutawawezesha wananchi wa Njombe kusafirisha bidhaa zao kwenda Mbeya na kuufikia uwanja wa ndege wa Songwe ambao Serikali imetoa shilingi Bilioni 3.5 ili kuimarisha miundombinu itakayouwezesha kupokea ndege za mizigo katika miezi minne ijayo.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa Sabasaba Mjini Njombe, Mhe. Rais Magufuli amewapongeza wananchi wa Njombe kwa juhudi kubwa wanazozionesha katika uzalishaji wa mazao hasa ya chakula na kueleza kuwa Serikali itaendelea kuunga mkono juhudi zao kwa kuhakikisha miundombinu inaboreshwa na huduma mbalimbali za kijamii zinatolewa.
Kuhusu kituo cha mabasi cha Njombe ambacho ujenzi wake ulianza tangu mwaka 2013 na haujakamilika mpaka sasa, Mhe. Rais Magufuli ambaye amewaita viongozi wa Mji wa Njombe na Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Josephat Kandege kutoa maelezo ya kwa nini ujenzi huo haujakamilika, ametoa siku 30 kuanzia leo kuhakikisha kituo hicho kinakamilika.
Hata hivyo, Mhe. Rais Magufuli ameiagiza bodi ya wakandarasi nchini kumchunguza Mkandarasi Masasi Construction Co. Ltd ambaye alipewa zabuni ya kujenga kituo hicho kwa awamu ya kwanza na ya pili na baadaye akatimuliwa kutokana na dosari zilizojitokeza ili hatua za kisheria zichukuliwe.
Kuhusu Hospitali ya Mkoa, Mhe. Rais Magufuli ameagiza ianze kutumika ndani ya miezi miwili na amewapongeza wananchi Njombe kwa kupata hospitali hiyo.
Kesho tarehe 11 Aprili, 2019 Mhe. Rais Magufuli ambaye ameongozana na Mkewe Mhe. Mama Janeth Magufuli, atamaliza ziara yake Mkoani Njombe kwa kufungua barabara ya Mafinga – Igawa na kuzungumza na wananchi katika mji wa Makambako.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Njombe
10 Aprili, 2019
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 09 Aprili, 2019 ameanza ziara yake ya kikazi ya siku 3 Mkoani Njombe akitokea Mkoani Ruvuma ambapo amezindua Kituo cha Afya cha Madaba Wilayani Songea na amefungua kiwanda cha chai cha Kabambe kilichopo Lwangu Mjini Njombe.
Ujenzi wa Kituo cha Afya cha Madaba Wilayani Songea umehusisha jengo la wodi ya wazazi, maabara, jengo la upasuaji, nyumba ya mtumishi, chumba cha kuhifadhi maiti, kichomeo cha taka na vifaa tiba kwa gharama ya shilingi Milioni 665.5 fedha ambazo zimetolewa kwa ushirikiano wa Serikali ya Tanzania na Mfuko wa Pamoja wa Wadau wa Sekta ya Afya.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali katika sekta ya afya na ametaja baadhi ya mafanikio kwa Mkoa wa Ruvuma kuwa ni kuongezeka kwa bajeti ya dawa kutoka shilingi Milioni 845 hadi kufikia shilingi Bilioni 3 na kuongezeka kwa idadi ya akina mama wajawazito wanaojifungulia katika vituo vya tiba kutoka asilimia 63 hadi 82.
Mhe. Ummy Mwalimu amewashukuru wadau wa huduma za afya kwa kuendelea kuchangia shilingi Bilioni 130 kila mwaka na kubainisha kuwa wiki iliyopita wametoa sehemu ya fedha hizo kiasi cha shilingi Bilioni 50 ambazo zimesambazwa katika vituo vya tiba kwenye Mikoa yote hapa nchini kupitia utaratibu mpya wa kupeleka fedha moja kwa moja kwenye vituo husika.
Mbunge wa Jimbo la Madaba Mhe. Joseph Mhagama amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa jinsi Serikali inavyowahudumia wananchi wake na amebainisha kuwa vijiji vyote vya Jimbo hilo isipokuwa vitatu vimepatiwa umeme, vituo vya afya 2 vimepatiwa shilingi Milioni 900 na miradi mingine ya maji yenye thamani ya shilingi Bilioni 1 na Milioni 900.
Akizungumza na wananchi wa Madaba katika sherehe za uzinduzi wa kituo chao cha afya, Mhe. Rais Magufuli amewashukuru wadau wa afya wote waliochangia ujenzi wa kituo hicho na pia amewapongeza viongozi wa Wilaya ya Songea kwa kusimamia vizuri ujenzi.
Mhe. Rais Magufuli amewataka viongozi na watumishi wa Wizara ya Afya kuhakikisha fedha zinazotengwa kwa ajili ya miradi zinaelekezwa katika miradi husika na amebainisha kuwa Serikali itaendelea kuhakikisha inaimarisha huduma za afya kwa Watanzania wote.
Sherehe hizo zimehudhuriwa na Mabalozi na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa yanayochangia katika Mfuko wa Pamoja wa huduma za Afya hapa nchini na kwa niaba yao Balozi wa Denmark hapa nchini Mhe. Einar Jensen ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa kutilia mkazo huduma za afya ikiwemo kujenga hospitali mpya 67 na vituo vya afya 352 ambapo 210 kati yake vimechangiwa na mfuko huo.
Mkoani Njombe ziara ya Mhe. Rais Magufuli imeanza kwa kufungua kiwanda cha chai cha Kabambe kinachomilikiwa na kampuni ya Unilever Tanzania katika eneo la Lwangu Mjini Njombe.
Kiwanda hiki ambacho kilianza kujengwa Januari 2017 kinasindika tani 50 za chai kwa siku (na kina uwezo wa kusindika hadi tani 150), kimeajiri wafanyakazi 700 na kinawahudumia wakulima wadogo wa chai 3,000.
Mkurugenzi Mtendaji wa Unilever Tanzania Bw. David Minja amemueleza Mhe. Rais Magufuli kuwa kiwanda hicho ni moja ya viwanda vya Unilever Tanzania vilivyoajiri Watanzania 7,000 na kuwanufaisha watu 40,000 na kwamba Unilever Tanzania imewekeza kiasi cha shilingi Bilioni 49.6 katika viwanda na hivyo kuunga mkono sera ya viwanda.
Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Joseph Kakunda amesema kiwanda hicho ni kati ya viwanda 36 vya chai hapa nchini na ni kati ya viwanda 108 vilivyoanzishwa katika mwaka 2018/19.
Mwekezaji wa kiwanda cha chai cha Kabambe Sir Ian Wood kutoka Wood Foundation amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kukifungua kiwanda hicho na amesema anaamini kiwanda hicho kitasaidia kuinua kipato cha wakulima kama ambavyo viongozi wa Njombe wakiwemo viongozi wastaafu walimuomba kuwekeza.
Akizungumza baada ya kufungua kiwanda na kujionea mitambo ya kisasa ya kusindika chai inavyofanya kazi, Mhe. Rais Magufuli ameipongeza kampuni ya Unilever Tanzania kwa uwekezaji huo na ametoa wito kwa wakulima wa Mkoa wa Njombe kuongeza uzalishaji wa chai kutoka asilimia 20 ya chai wanayopeleka kiwandani hapo hivi sasa hadi kufikia asilimia 70 iliyopangwa kutoka kwa wakulima wadogo.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli amekemea tabia ya baadhi ya viongozi na watendaji wa Serikali ambao wamekuwa wakiwakwamisha wawekezaji wanaotaka kujenga viwanda na amemuomba Balozi wa Uingereza hapa nchini Mhe. Sarah Cooke na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda na Biashara kumjulisha pale watakapobaini mwekezaji amekwamishwa.
“Ndio maana nimeamua kuitoa TIC (Kituo cha Uwekezaji Tanzania) kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara na kuipeleka Ofisi ya Waziri Mkuu, na huko nako nikiona mambo hayaendi nitaitoa na kuileta ofisini kwangu, nataka mtu anayetaka kuwekeza akija leo, kesho aoneshwe eneo la kujenga kiwanda, sio kumzungushazungusha” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Mhe. Rais Magufuli ameelezea furaha yake ya kuona Tanzania ya Viwanda inafanikiwa ambapo katika kipindi cha miaka 3 viwanda 3,500 vimejengwa na Watanzania wengi wanaendelea kupata ajira.
Kesho tarehe 10 Aprili, 2019 Mhe. Rais Magufuli ambaye ameongozana na Mkewe Mhe. Mama Janeth Magufuli ataendelea na ziara yake Mkoani Njombe ambapo ataweka jiwe la msingi la ujenzi wa Hospitali ya Mkoa na ataweka jiwe la msingi la mradi wa ujenzi wa barabara ya lami ya Njombe – Makete na kuzungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Njombe
09 Aprili, 2019
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 08 Aprili, 2019 ameendelea na ziara yake Mkoani Ruvuma kwa kutembelea shamba la Gereza la Kitai lililopo Wilayani Mbinga na kuzindua kiwanda cha kuchakata mahindi cha Kikosi cha Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) 842KJ - Mlale Wilayani Songea.
Akiwa Gereza la Kitai, Mhe. Rais Magufuli ametembelea shamba la mahindi lenye ukubwa wa ekari 650 linalolimwa kwa kutumia wafungwa wa gereza hilo na ambalo linatarajiwa kuzalisha tani 780 za mahindi katika msimu huu.
Kamishna Jenerali wa Magereza Faustine Kasike amemueleza Mhe. Rais Magufuli kuwa mahindi yatakayovunwa katika shamba hilo yatatumika kulisha Magereza ya Mikoa 3 (Ruvuma, Lindi na Mtwara) yenye wafungwa 2,000 na kubainisha kuwa kupitia mkakati wake wa uzalishaji wa mazao katika Magereza 10 Jeshi hilo linatarajia kuvuna tani 15,135.75 za mahindi, mpunga na maharage msimu huu baada ya kupanua mashamba yanayolimwa kutoka ekari 1,950 hadi kufikia ekari 5,395.
Akizungumza na Askari, Maafisa wa Magereza na wananchi wa Kitai, Mhe. Rais Magufuli amelipongeza Jeshi la Magereza kwa kuitikia wito wake wa kuhakikisha linawatumia wafungwa ipasavyo katika uzalishaji na ametoa matrekta 2 kwa Gereza la Kitai ili yasaidie kupanua mashamba ya mazao katika eneo la ekari zaidi ya 7,000 zilizopo katika gereza hilo.
Hata hivyo Mhe. Rais Magufuli amelitaka Jeshi la Magereza kuwahamisha wafungwa waliopo katika magereza yasiyokuwa na shughuli za uzalishaji na kuwapeleka katika magereza yenye shughuli za uzalishaji mali likiwemo gereza la Kitai ambalo lina wafungwa 233 ikilinganishwa na uwezo wake wa kuchukua wafungwa 370 ilihali baadhi ya Mikoa hapa nchini ina idadi kubwa ya wafungwa kupita uwezo wake na hawafanyi kazi zozote za uzalishaji mali.
“Nimeambiwa katika Magereza yetu wapo wafungwa kama 18,000 na Mahabusu 19,000 nataka wafungwa hawa watumike kuzalisha mali badala ya kukaa Magerezani halafu Serikali iwe inatoa fedha kwa ajili ya kuwalisha, Magereza mengine yaige mfano wa Gereza la Kitai.
Nataka wafungwa watumike kwelikweli na kama kuna suala la kisheria, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ipeleke mapendekezo ya mabadiliko ya sheria Bungeni” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Mhe. Rais Magufuli amelielekeza Jeshi la Magereza liwatumie wafungwa kujenga makazi ya askari pamoja na miundombinu ya huduma za kijamii katika maeneo hayo, pia baada ya kuelezwa na wanafunzi wa Shule ya Msingi Kitai kuwa shule hiyo inakabiliwa na uhaba wa matundu ya vyoo amechangia shilingi Milioni 5.
Baada ya kutoka Gereza la Kitai, Mhe. Rais Magufuli amezindua kiwanda cha kuchakata mahindi cha Jeshi la Kujenga Taifa (842KJ) Mlale Wilayani Songea ambacho kina uwezo wa kuchakata tani 5,280 kwa mwaka na amepokea gawio la Serikali kutoka Shirika la Suma-JKT la shilingi Milioni 700.
Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jen. Venance Mabeyo amesema ujenzi wa kiwanda hicho pamoja na viwanda vingine vilivyo chini ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ) vinajengwa ili kuunga mkono sera ya viwanda na kutekeleza majukumu ya jeshi hilo wakati wa amani na kwamba pamoja na kutekeleza wajibu huo JWTZ inaendelea kuhakikisha mipaka ya nchi ipo salama.
Waziri wa Ulinzi na JKT Mhe. Dkt. Hussein Mwinyi amesema katika kuongeza uzalishaji wa mazao Serikali imejipanga kuhakikisha wanafunzi wanaojiunga na JKT wanatumika ipasavyo kuzalisha mali ikiwemo mazao yatakayotumika kwa chakula cha Majeshi na kuuza ili kupata fedha.
Akizungumza baada ya kuzindua kiwanda hicho Mhe. Rais Magufuli amempongeza Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jen. Venance Mabeyo na Mkuu wa JKT Mej. Jen Martin Busungu kwa kazi nzuri zinazofanywa na Jeshi hilo na ameelezea kufurahishwa kwake na namna Jeshi linavyotekeleza maagizo linayopewa ikiwemo ujenzi wa viwanda, ujenzi wa ukuta Mererani, ujenzi wa nyumba Dodoma, uinuaji wa kivuko cha MV Nyerere katika ziwa Victoria na ukusanyaji wa korosho za wakulima na ametaka Majeshi mengine yaige mfano huo.
“Najisikia raha sana kuwa na Jeshi la namna hii, najisikia raha kuongoza vikosi vya ulinzi kama nyinyi, na mimi nawaahidi kuwa Serikali itahakikisha Jeshi linakuwa imara na maslahi yenu yanaboreshwa” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Mhe. Rais Magufuli ameishukuru Suma-JKT kwa kutoa gawio la Serikali la shilingi Milioni 700 na ametoa wito kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira kuyachunguza mashirika ya umma ambayo hayatoi gawio kwa Serikali ili hatua zichukuliwe kurekebisha dosari zitakazobainika.
Mhe. Rais Magufuli aliyeongozana na Mkewe Mhe. Mama Janeth Magufuli kesho tarehe 09 Aprili, 2019 atamaliza ziara yake Mkoani Ruvuma kwa kuzindua Kituo cha Afya cha Madaba Wilayani Songea na ataanza ziara yake ya siku 3 katika Mkoa wa Njombe kwa kufungua kiwanda cha chai cha Unilever kilichopo Lwangu, Mjini Njombe.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Songea
08 Aprili, 2019
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 09 Aprili, 2019 ametengua uteuzi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa Mkoani Ruvuma Dkt. Oscar Albano Mbyuzi.
Kufuatia uamuzi huo, Mhe. Rais Magufuli amemteua Bw. Jimson Peter Mhagama kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa.
Uteuzi wa Bw. Mhagama unaanza mara moja leo tarehe 09 Aprili, 2019.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Songea
09 Aprili, 2019
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 07 Aprili, 2019 ameendelea na ziara yake katika Wilaya ya Mbinga Mkoani Ruvuma ambapo ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa barabara ya lami ya Mbinga – Mbambabay na kuzungumza na wananchi.
Ujenzi wa barabara ya Mbinga – Mbambabay yenye urefu wa kilometa 67 utagharimu shilingi Bilioni 134 zilizotolewa kwa mkopo nafuu kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) na Serikali ya Tanzania na unakamilisha barabara nzima ya ushoroba wa maendeleo wa Mtwara (Mtwara Development Corridor) yenye urefu wa kilometa 1,020.
Kabla ya kuzungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa Masumuni Mjini Mbinga, Mhe. Rais Magufuli amewaongoza wananchi kusimama kwa dakika 1 kumkumbuka na kumuombea Hayati Abeid Amani Karume ambapo leo ni kumbukumbu ya siku ya kifo chake.
Mhe. Rais Magufuli ameishukuru AfDB kwa kutoa mkopo wa ujenzi wa barabara hiyo na amemtaka mkandarasi anatekeleza kazi hiyo (China Henan Internatinal Cooperation Group Co. Ltd - CHICO) kukamilisha ujenzi kabla ya kuisha kwa mwaka 2020 badala ya mwaka 2021 kama ilivyopangwa.
Amewapongeza wananchi wa Mikoa ya Ruvuma, Lindi na Mtwara kwa kufanikisha ndoto ya kukamilishwa kwa barabara ya kuanzia bandari ya Mtwara hadi bandari ya Mbambabay na kubainisha kuwa itaongeza fursa za uchumi kwa wananchi na Taifa ikiwemo kuwahakikishia soko la ndani na nje ya nchi kwa mazao ya wakulima.
Katika mkutano huo, Mhe. Rais Magufuli amejibu kero za wananchi zilizotolewa na Mbunge wa Mbinga Mjini Mhe. Sixtus Mapunda kwa kuagiza vyombo vya dola kuchunguza na kuchukua hatua dhidi ya wote waliohusika kuifilisi Benki ya Wananchi wa Mbinga ambayo ilikuwa ikiwasaidia wananchi hasa wakulima.
Mhe. Rais Magufuli amewataka viongozi wa wilaya ya Mbinga wakiwemo Wabunge kuwafichua watu waliohusika kuwadhulumu wakulima wa kahawa katika msimu uliopita ili Serikali ichukue hatua.
Aidha, amempongeza Waziri wa Kilimo Mhe. Japhet Hasunga kwa hatua zinazochukuliwa na wizara yake kuanzisha mnada wa kahawa Wilayani Mbinga, hatua ambayo itawasaidia wakulima kupata soko la uhakika na kuepusha dhuluma na wizi.
“Nataka niwahakikishie ndugu zangu kuwa katika awamu yangu mafisadi hawatapenya, tumefanikiwa kuondoa watumishi hewa, kaya masikini hewa zilizokuwa zinapewa fedha za TASAF na tutaendelea kusimamia nidhamu ya kazi na kusimamia kila senti ya Serikali” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Mhe. Rais Magufuli amezungumzia zoezi la ugawaji wa vitambulisho vya wajasiriamali ambapo amewaonya viongozi wa Mikoa na Wilaya ambao hawagawi vitambulisho hivyo licha ya wananchi kuvihitaji na pia ametaka viongozi hao wasiwalazimishe watu kuvinunua.
“Viongozi wa Mikoa na Wilaya ambao hamgawi vitambulisho maana yake mnapingana na maelekezo yangu, na ndugu zangu wajasiriamali ambao hamfanyi juhudi za kupata vitambulisho hivyo najua itafika siku wale ambao hawana vitambulisho watazuiwa kufanya biashara, ikifika hapo sitawatetea” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Mapema akimkaribisha Mhe. Rais Magufuli Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Isack Kamwelwe amesema pamoja na kujenga barabara ya Mtwara – Mbambabay, Serikali ya Awamu ya Tano imeanza kufanya mazungumzo na Benki ya Dunia kwa ajili ya kupata fedha za kujenga kilometa 11 za barabara ya mchepuko katika Mji wa Songea itakayoepusha magari makubwa kukatiza katikati ya mji, kukarabati barabara ya Songea – Njombe. Serikali pia imetoa fedha kiasi cha shilingi Bilioni 5 kwa ajili ya kuanza mara moja ukarabati wa uwanja wa ndege wa Songea ili uweze kupokea ndege kubwa katika kipindi cha miezi 6 ijayo.
Kesho tarehe 08 Aprili, 2019 Mhe. Rais Magufuli ambaye ameongozana na Mkewe Mhe. Mama Janeth Magufuli ataendelea na ziara yake hapa Mkoani Ruvuma ambapo atatembelea shamba la mahindi la gereza la Kitai Wilayani Mbinga na kuzindua kiwanda cha kusaga mahindi cha Kikosi cha Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Mlale Wilayani Songea.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Mbinga
07 Aprili, 2019
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 05 Aprili, 2019 ameendelea na ziara yake Mkoani Ruvuma ambapo amefungua barabara ya lami ya Tunduru – Matemanga – Kilimasera – Namtumbo na amezindua Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) cha Wilaya ya Namtumbo.
Ujenzi wa barabara ya lami ya Tunduru – Matemanga – Kilimasera – Namtumbo yenye urefu wa kilometa 193 umegharimu ya shilingi Bilioni 173.3, fedha ambazo zimetolewa na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Shirika la Maendeleo la Japan (JICA) na Serikali ya Tanzania.
Barabara hiyo pamoja na madaraja yake ni sehemu ya ujenzi wa barabara ya lami ya ushoroba wa Mtwara (Mtwara Development Corridor) unaounganisha bandari ya Mtwara na bandari ya Mbambabay iliyopo katika Mkoani Ruvuma.
Akizungumza katika sherehe za ufunguzi wa barabara hiyo zilizofanyika katika Mji wa Tunduru, Mhe. Rais Magufuli ameishukuru AfDB na JICA kwa kufadhili ujenzi wa barabara hiyo na amewapongeza wananchi wa Mkoa wa Ruvuma kwa kuondokana na adha kubwa ya usafiri waliyokuwa wakiipata kutokana na ubovu wa barabara.
Katika sherehe hizo Mhe. Rais Magufuli amempongeza Mkuu wa Wilaya ya Tunduru Mhe. Juma Homera kwa juhudi kubwa za kusukuma mbele maendeleo ya wilaya hiyo na amemuagiza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Selemani Jafo kutenga shilingi Milioni 200 kwa ajili ya kusaidia uboreshaji wa Hospitali ya Wilaya ya Tunduru na pia amemuagiza Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhe. Prof. Makame Mbarawa kutafuta suluhisho la uhakika la upatikanaji wa maji ya kutosha kwa ajili ya Mji huo.
Kuhusu kiwanda cha kubangua korosho cha Tunduru (Korosho Africa) kilichopo Mjini Tunduru ambacho kimedaiwa kubangua korosho kwa kiwango kidogo ikilinganishwa na uwezo wake Mhe. Rais Magufuli ameiagiza Wizara ya Kilimo na Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kuhakikisha kiwanda hicho kinaongeza ubanguaji wa korosho hadi kufikia uwezo wake wa juu wa tani 10,000 kwa mwaka na ameelekeza kuwa mwekezaji huyo auziwe korosho kwa bei nafuu ya shilingi 3,800 kwa kilo.
Akiwa njiani kuelekea Songea Mjini Mhe. Rais Magufuli amesikiliza kero za wananchi wa Matemanga, Huria, Mchomoro, Namtumbo Mjini, Litola na Lumecha ambapo amewaagiza Mawaziri kuhakikisha huduma za afya katika vituo vya afya zinaimarishwa, umeme unapatikana haraka na kutafuta suluhisho la changamoto ya tatizo la maji.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli amewahakikishia wananchi hao kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kujengwa kwa kiwango cha lami barabara ya Lumecha – Londo – Ifakara ambayo inaunganisha Mkoa wa Ruvuma na Mkoa wa Morogoro na kwamba kazi ya ujenzi wa madaraja imeanza kufanyika.
Mjini Namtumbo, Mhe. Rais Magufuli amezindua Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) kilichojengwa na Serikali ya Tanzania kwa gharama ya shilingi Bilioni 6.5 na ambacho kitakuwa na uwezo wa kutoa mafunzo kwa wanafunzi 600 wa kozi ndefu na fupi kwa mwaka.
Mhe. Rais Magufuli ameelezea kutoridhishwa kwake na gharama kubwa zilizotumika ikilinganishwa na thamani ya majengo yaliyojengwa na ameitaka VETA na viongozi wote wa Serikali kutambua umuhimu wa kubana matumizi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Mafunzo ya Ufundi, Mhe. Joyce Ndalichako amesema pamoja na chuo cha VETA Namtumbo, Serikali imejenga vyuo vingine vya VETA katika Mikoa ya Njombe, Rukwa, Geita na Simiyu. Pia imejenga vyuo vya maendeleo ya jamii 20 ambavyo vitaongezeka hadi kufikia 34 ifikapo mwaka 2020.
Mhe. Rais Magufuli ambaye ameongozana na Mkewe Mhe. Mama Janeth Magufuli kesho tarehe 06 Aprili, 2019 ataendelea na ziara yake hapa Mkoani Ruvuma ambapo atazindua mradi wa kusafirisha umeme mkubwa kutoka Makambako hadi Songea, ataweka jiwe la msingi Kituo cha Mabasi na ujenzi wa barabara za lami za Manispaa ya Songea na atazungumza na wananchi katika Mkutano wa hadhara utakaofanyika katika uwanja wa Majimaji.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Songea
05 Aprili, 2019
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 04 Aprili, 2019 ameanza ziara ya kikazi ya siku 6 katika Mkoa wa Ruvuma akitokea Mkoani Mtwara.
Akiwa njiani kutoka Wilaya ya Nanyumbu Mkoani Mtwara kwenda Tunduru Mkoani Ruvuma, Mhe. Rais Magufuli amesalimiana na wananchi wa Vijiji vya Michiga, Nakapanya na Namiungo ambako amewahakikishia kuwa Serikali itanunua korosho zote za wakulima, zikiwemo zilizokusanywa kwa mtindo wa Kangomba baada ya waliofanya makosa hayo kukiri na kuomba radhi.
Katika Kijiji cha Nakapanya, Mbunge wa Jimbo la Tunduru Kaskazini Mhe. Ramo Makani ametoa maelezo juu ya tatizo la maji linalokikabili kijiji hicho na vijiji vingine vya Wilaya ya Tunduru na Mhe. Rais Magufuli ametoa maagizo kwa wataalamu na viongozi kuangalia namna ya kuvuna maji ya mvua kwa kutumia mabwawa makubwa badala ya kuendelea kutegemea kupata maji kutoka mbali.
Mhe. Rais Magufuli amelazimika kutembelea jengo la soko la Kijiji cha Nakapanya baada ya wananchi kulalamikia kuwa Mahakama imewazuia kutumia jengo hilo kutokana na kujengwa jirani na jengo la Mahakama ya Mwanzo na baada ya kujionea hali halisi ameagiza jengo hilo la soko lianze kutumika kuanzia kesho tarehe 05 Aprili, 2019 na ameagiza viongozi wa Wilaya ya Tunduru wahakikishe mazingira ya jengo hilo yanaboreshwa.
Kuhusu jengo la Mahakama ya Mwanzo lililopo jirani na soko hilo na ambalo ni chakavu, Mhe. Rais Magufuli ametoa shilingi Milioni 10 kisha kuendesha harambee iliyofanikisha kupatikana jumla ya shilingi Milioni 22 za kujengea jengo jipya la Mahakama ya Mwanzo ya Nakapanya na ameelekeza kuwa jengo hilo lijengwe mahali pengine.
Mhe. Rais Magufuli pia amezungumza na wananchi wa Kijiji cha Namiungo ambapo Diwani wa Kata ya Namiungo Mhe. Salima Limbalambala ameomba Serikali iwasaidie wananchi hao kupata Kituo cha Afya, na Mhe. Rais Magufuli amemuagiza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Suleimani Jafo kutenga shilingi Milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya cha Namiungo.
Kesho Mhe. Rais Magufuli ambaye ameongozana na Mkewe Mhe. Mama Janeth Magufuli ataendelea na ziara yake hapa Mkoani Ruvuma ambapo atafungua barabara ya Tunduru – Matemanga – Kilimasera – Namtumbo na atazindua mradi wa ujenzi wa Chuo cha Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) Wilayani Namtumbo.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Tunduru
04 Aprili, 2019
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 04 Aprili, 2019 amemaliza ziara yake ya siku 3 Mkoani Mtwara kwa kufungua Kituo cha Afya cha Mbonde kilichopo katika Wilaya ya Masasi na kufungua barabara za Mangaka – Nakapanya – Tunduru na Mangaka - Mtambaswala.
Kituo cha Afya cha Mbonde kilichojengwa kwa gharama ya shilingi Milioni 500 ni miongoni mwa Vituo vya Afya vipya 13 vilivyojengwa Mkoani Mtwara na ni miongoni mwa Vituo vya Afya vipya 352 vilivyojengwa nchi nzima katika kipindi cha miezi 18 iliyopita vikiwa na uwezo wa kutoa huduma za matibabu mbalimbali ikiwemo matibabu ya upasuaji.
Akiwa kituoni hapo, Mhe. Rais Magufuli amejionea miundombinu yake ikiwemo wodi za kulala wagonjwa, maabara, vyumba vya upasuaji vyenye vifaa vya kisasa na majengo mapya.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kuendelea kutilia mkazo uwekezaji katika miundombinu ya kutolea huduma za afya pamoja na kutoa maelekezo yenye manufaa ikiwemo kuagiza ununuzi wa vifaa ufanyike moja kwa moja kutoka kwa watengenezaji moja kwa moja, hali iliyosaidia kuokoa gharama za ununuzi zikiwemo mashine za usingizi ambazo zimenunuliwa kwa shilingi Milioni 50 badala ya shilingi Milioni 100 kwa kila mashine moja.
Nae Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Selemani Jafo amesema Serikali ya Awamu ya Tano imefanikiwa kujenga Vituo vya Afya 352 na hospitali 67 nchi nzima katika kipindi cha miezi 18 ikilinganishwa na hospitali 77 zilizokuwa zimejengwa tangu Uhuru, na kwamba katika bajeti ijayo vituo vya afya vingine 27 vitajengwa katika maeneo mbalimbali nchini.
Akizungumza baada ya kufungua Kituo cha Afya cha Mbonde Mhe. Rais Magufuli amewapongeza wananchi wa Masasi kwa kupata kituo hicho na ameeleza kuwa Serikali imetumia shilingi Bilioni 184 kujenga vituo vyote 352 nchi nzima kwa lengo la kuhakikisha Watanzania wanapata huduma za uhakika za matibabu jirani na maeneo wanayoishi.
Mhe. Rais Magufuli ameipongeza Wizara ya Afya na TAMISEMI kwa kuhakikisha ujenzi wa vituo vya afya unafanyika vizuri na amebainisha kuwa pamoja na kujenga miundombinu hiyo pia imejenga nyumba 306 za watumishi wa afya, imeajiri madaktari 11,200 na kuimarisha huduma za matibabu ya kibingwa katika hosptali ya Taifa Muhimbili na hospitali nyingine za rufaa hali iliyowezesha nchi jirani kuitegemea Tanzania kwa matibabu.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli amekubali ombi la Mbunge wa Lulindi Mhe. Jerome Bwanausi la kujengwa kwa kilometa 40 za barabara ya lami kati ya Mpeta na Newala na pia ameahidi kutoa gari la wagonjwa kwa ajili ya kituo cha afya cha Mbonde baada ya gari lililokuwepo kuchomwa moto wakati wa vurugu.
Mhe. Rais Magufuli ameiagiza Wizara ya Kilimo na Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kuhakikisha viwanda vyote vya korosho vilivyobinafsishwa lakini havifanyi kazi vinanyang’anywa haraka na amemtaka Naibu Katibu Mkuu wa Viwanda Bw. Ludovick Nduhiye kutoondoka Mtwara mpaka ahakikishe agizo hilo limetekelezwa.
Kabla ya kuondoka Masasi kuelekea Nanyumbu Mhe. Rais Magufuli ametembelea Ofisi ya Chama Cha Mapinduzi ya Wilaya ya Masasi ambayo ilikumbwa na kadhia ya kuchomwa moto na waandamanaji mwaka 2013 ambapo amechangia shilingi Milioni 20 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa ofisi mpya, amechangia shilingi Milioni 5 kwa Shule ya Msingi Mkuti na ametoa wito kwa wananchi wa Masasi kujiepusha na mihemko ya hasira inayosababisha uharibifu wa mali.
Mhe. Rais Magufuli pia amechangia shilingi Milioni 5 kwa shule ya Sekondari Mikangaula kwa ajili ya kuimarisha miundombinu ya shule hiyo na ameagiza shule hiyo iwekewe umeme ndani ya miezi 2.
“Nitawapa shilingi Milioni 5 zikawasaidie kujenga miundombinu ya shule, na umeme mtapata, lakini nitoe wito kwenu na kwa wanafunzi wote Tanzania kusoma kwa juhudi kwa sababu sasa hivi elimu inatolewa bila malipo na mkifika vyuo vikuu mtapata mikopo” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Akiwa Mangaka Wilayani Nanyumbu Mhe. Rais Magufuli amefungua barabara ya lami ya Mangaka – Nakapanya – Tunduru yenye urefu wa kilometa 137 na ambayo imejengwa kwa gharama ya shilingi Bilioni 126.3 na barabara ya lami ya Mangaka – Mtambaswala yenye urefu wa kilometa 65.5 na imejengwa kwa gharama ya shilingi Bilioni 56.2.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Isack Kamwelwe amesema kukamilika kwa barabara hizo pamoja na miradi mingine ya barabara kuu kumefikisha jumla ya kilometa 957 (kupitia Mingoyo) na hivyo kukamilisha mpango wa ujenzi wa barabara za lami za ushoroba wa kusini unaounganisha Mbambabay mpaka Mtwara.
Barabara hizo zimejengwa kwa ushirikiano wa Serikali ya Tanzania na Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB) na Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Japan (JICA).
Akizungumza na wananchi wa Nanyumbu katika sherehe za ufunguzi wa barabara hizo Mhe. Rais Magufuli amewashukuru Marais Wastaafu Mhe. Benjamin William Mkapa na Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kwa kukubali mawazo yake ya kujengwa barabara hizo akiwa Waziri wa Ujenzi na pia ameishukuru AfDB na JICA kwa ufadhili mkubwa walioutoa kufanikisha ujenzi wa barabara hizo.
Mhe. Rais Magufuli amewapongeza wananchi wa Mikoa ya Mtwara, Lindi na Ruvuma kwa kufanikiwa kupata barabara hizo na hivyo kuondokana na adha ya hali mbaya ya barabara iliyowasumbua kwa miaka mingi na kusababisha shughuli nyingi za kiuchumi kudorola.
Kuhusu ujenzi wa barabara ya Mnivata – Tandahimba – Newala – Masasi, Mhe. Rais Magufuli ameiagiza Wizara ya Fedha na Mipango na Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kuwasilisha andika la kuomba ufadhili wa ujenzi wa barabara hiyo Jumatatu ijayo (08 Aprili, 2019) baada ya Balozi wa Japan hapa nchini Mhe. Shinichi Goto na Mwakilishi wa JICA Bw. Yasunori Onishi ambao wamehudhuria sherehe hiyo kuonesha utayari wa kutoa fedha.
Mhe. Rais Magufuli ametoa siku 5 kwa Baraza la Taifa la Menejimenti ya Mazingira (NEMC) kutoa vibali kwa mwekezaji anayesubiri kibali ili aweze kusafirisha tani Milioni 1 za makaa ya mawe kwenda nje ya nchi kupitia bandari ya Mtwara
Katika salamu zake za kumuaga Mhe. Rais Magufuli Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mhe. Gelasius Byakanwa amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa ziara yake Mkoani Mtwara na ameahidi kuwa maelekezo yote aliyoyatoa yatatekelezwa.
Mhe. Rais Magufuli amewashukuru wananchi wa Mtwara kwa mapokezi na kujitokeza kwa wingi katika mikutano na katika miradi aliyoiweka mawe ya msingi na kuifungua na ameongeza kuwa “najua baadhi yenu mlijitokeza kutaka tusalimiane kandokando ya barabara lakini sikufanikiwa kwa kuwa nisingeweza kukutana nanyi usiku, lakini tambueni kuwa tupo pamoja na nawapenda sana”.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Nanyumbu
04 Aprili, 2019
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt John Pombe Magufuli amewaagiza viongozi wote nchini kuhakikisha wanaondoa vikwazo vyote dhidi ya wawekezaji ambao wana dhamira ya dhati ya kuwekeza katika maeneo mbalimbali ya kuimarisha uchumi, kuzalisha ajira, kuongeza mapato ya Serikali na kustawisha maisha ya wananchi.
Mhe. Rais Magufuli ametoa maagizo hayo muda mfupi kabla ya kufungua kiwanga cha kubangua korosho cha Yalin Cashewnut Company Ltd kilichopo eneo la Msijute Mtwara Vijijini ambako leo ameanza ziara ya siku 3 Mkoani Mtwara.
Maagizo hayo yamekuja baada ya Meneja Mkuu wa kiwanda hicho Bw. Suleiman Milanzi kueleza kuwa wamiliki wa kiwanda hicho walishindwa kuanza ubanguaji wa korosho mwezi Desemba 2018 kama ilivyopangwa na sasa wataanza ubanguaji huo Mei 2019 baada ya kukutana na urasimu na gharama kubwa za kupata umeme ambapo wamelazimika kununua transifoma kwa gharama ya shilingi Milioni 27 na kulipia gharama kubwa za kuingiza maji ambapo walitakiwa kulipia shilingi Milioni 100.
Mhe. Rais Magufuli ameliagiza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kurejesha fedha alizotumia mwekezaji huyo kununua transifoma na amewataka viongozi wa Mkoa na Wizara husika kuhakikisha kiwanda kinapatiwa maji haraka iwezekanavyo, huku akibainisha kuwa hakutarajia kuona mwekezaji huyo akikwamishwa ilihali viongozi wa Mkoa, Wizara, viongozi wa siasa na halmashauri wapo na wanajua jinsi Serikali inavyotilia mkazo ajenda ya ujenzi wa viwanda.
Akiwa kiwandani hapo Mhe. Rais Magufuli ameambiwa kuwa tayari kiwanda hicho kimenunua tani 100 za korosho kwa bei ya shilingi 4,100 kwa kilo kwa ajili ya ubanguaji wa majaribio na kwamba baada ya majaribio hayo kiwanda kitakuwa na uwezo wa kubangua tani 10,000 na baadaye kitaongeza ubanguaji hadi kufikia zaidi ya tani 40,000 kwa mwaka kwa kutegemea upatikanaji wa malighafi yaani korosho ghafi.
Wamiliki wa kiwanda hicho pia wamekubali kununua tani 30,000 za korosho za msimu huu kwa bei ya shilingi 3,700 kwa kilo na Mhe. Rais ameagiza mwekezaji huyo auziwe korosho anazohitaji pamoja na wanunuzi wengine watakaokuwa tayari kununua korosho zilizonunuliwa na Serikali na kuhifadhi katika maghala kwa bei hiyo.
Mhe. Rais Magufuli amewapongeza wakulima wa Mtwara, Lindi na maeneo mengine yanayozalisha zao hilo huku akisisitiza kuwa Serikali haiwezi kuliacha zao la korosho bila usimamizi wa karibu kwa kuwa licha ya kuwaingia kipato wakulima na kuzalisha ajira kwa Watanzania wengi, limekuwa chanzo muhimu cha mapato ya Serikali kwani katika mwaka 2016/17 liliingiza kipato cha shilingi Bilioni 616 na mwaka 2017/18 liliingiza shilingi Trilioni 1 na Bilioni 207.
Akitoa maelezo ya awali Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mhe. Joseph Kakunda amesema kiwanda cha Yalin Cashenut Company Ltd ni kati ya viwanda 108 vilivyojengwa katika mwaka 2018/19 ambapo kati yake 11 ni vya kubangua korosho na kwamba viwanda hivyo vipya vimeajiri wafanyakazi 2,836.
Nao Wabunge wa Mkoa wa Mtwara Mhe. George Mkuchika (Newala Mjini) na Hawa Ghasia (Mtwara Vijijini) wamemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa dhamira yake ya kuwasaidia wakulima wa korosho wa Mkoa huo, kupanua uwanja wa ndege wa Mtwara Mjini, kujenga barabara na kutekeleza miradi mingine mikubwa ya kuuinua mkoa huo kimaendeleo.
Mhe. Rais Magufuli ambaye ameongozana na Mkewe Mhe. Mama Janeth Magufuli kesho tarehe 03 Aprili, 2019 ataendelea na ziara yake hapa Mtwara ambapo pamoja na kuzungumza na wananchi ataweka jiwe la msingi katika mradi wa ujenzi wa barabara ya Mtwara – Mnivata na ataweka jiwe la msingi la mradi wa uboreshaji wa miundombinu ya Chuo cha Ualimu Kitangili Wilayani Newala.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Mtwara
02 Aprili, 2019
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 02 Aprili, 2019 ameanza ziara ya kikazi ya siku 3 Mkoani Mtwara ambapo mara baada ya kuwasili ameweka jiwe la msingi katika upanuzi wa uwanja wa ndege wa Mtwara na kuzungumza na wananchi.
Uwanja huo unafanyiwa upanuzi ikiwa ni miaka 67 tangu ulipojengwa mwaka 1952 ambapo upanuzi unahusisha kuongeza upana wa njia ya kurukia kutoka meta 30 hadi 45, kuongeza urefu wa njia ya kurukia kutoka meta 2,258 hadi 2,800, kujenga maegesho mapya ya ndege, kujenga barabara na maegesho ya magari, kuweka vifaa vya zimamoto na usalama, kujenga uzio na kuweka mfumo wa umeme wa akiba.
Upanuzi huo umeanza Juni 2018 na utakamilika Septemba 2020 kwa gharama ya shilingi Bilioni 50.4, fedha ambazo zimetolewa na Serikali ya Tanzania.
Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mhandisi Christianus Ako amesema upanuzi huo ukikamilika utauwezesha uwanja wa ndege wa Mtwara kupokea ndege za daraja 4E ambapo ndege kubwa na ndogo zitakuwa na uwezo wa kutua na kuruka.
Akizungumza katika sherehe hizo Mhe. Rais Magufuli amesema Serikali ya Awamu ya Tano imemua kuupanua uwanja huo ili kufungua fursa nyingi zaidi za kiuchumi katika mkoa wa Mtwara na kwamba upanuzi kama huo unafanywa katika viwanja vingine 11 hapa nchini.
Kuhusu kuchelewa kuanza kwa kazi za upanuzi huo kutokana na Mkandarasi M/S Beijing Construction Engineering Group Company Ltd kutopatiwa sehemu ya malipo ya awali, Mhe. Rais Magufuli ametoa siku 5 kwa Mawaziri wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano na Wizara ya Fedha na Mipango kuhakikisha asilimia 15 ya awali ambayo ni sawa na shilingi Bilioni 7 zinalipwa, lakini amemuonya Mkandarasi huyo kuhakikisha anafanya kazi vizuri (usiku na mchana) na kwa kuzingatia muda kwa kuwa taarifa zinaonesha Mkandarasi huyo hajafanya kazi ya kuridhisha katika uwanja wa ndege wa Mwanza.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli amezungumzia ununuzi wa korosho uliofanywa na Serikali baada ya wanunuzi binafsi kutaka kununua korosho kwa bei ya chini ya shilingi 2,000 na kueleza kuwa baada ya Serikali kuamua kununua korosho hizo kwa shilingi 3,300 kwa kilo, jumla ya tani 156,865 zenye thamani ya shilingi Bilioni 578.7 kutoka kwa wakulima 373,149 zimenunuliwa na hivyo kuwaokoa wakulima hao wasipoteze mapato makubwa.
Kufuatia baadhi ya wenye korosho zinazozidi kilo 1,500 kukiri na kuomba radhi baada ya kushindwa kuuza korosho zao kwa Serikali kutokana na kuzikusanya kwa njia zisizokubalika (Kangomba), Mhe. Rais Magufuli amekubali kuwasamehe na ameagiza Wizara ya Fedha na Mipango kutoa shilingi Bilioni 50 katika siku 2 zijazo ili waanze kulipwa.
Hata hivyo ameonya kuwa watakaoruhusiwa kuuza ni wale wanaozimiliki korosho hizo dosari nyingine na ametaka mchezo wa kununua korosho kwa mtindo wa Kangomba ukome.
“Najua kuna watu 18,000 wakiwemo wale wasiokuwa na mashamba 780 hawajalipwa, nimeshatoa maagizo zitolewe shilingi Bilioni 50 ili waanze kulipwa, nafanya hivi kwa sababu wamekiri na wameomba radhi kwa kufanya kangomba, sasa msirudie tena mchezo huu, achene kuwanyonya wakulima” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Katika mkutano huo Mhe. Rais Magufuli amewaonya viongozi wa Mkoa wa Mtwara kuacha kugombana wao kwa wao na badala yake amewataka washirikiane kusukuma mbele gurudumu la maendeleo la mkoa huo. Pia amewaomba viongozi wa Dini wasaidie kuwaunganisha viongozi hao.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Mtwara
02 Aprili, 2019
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 01 Aprili, 2019 amemuapisha Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango atakayeshughulikia sera Bw. Adolf Hyasinth Ndunguru na Naibu Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Hafla ya kuapishwa kwa viongozi hao imehudhuriwa na Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba Kabudi, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Ashatu Kijaji, Makatibu Wakuu, Viongozi Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama na wafanyakazi wa Wizara ya Fedha na Mipango.
Akizungumza baada ya kuwaapisha, Mhe. Rais Magufuli ameitaka TRA na Wizara ya Fedha na Mipango kupanua uwigo wa kodi kwa kuongeza idadi ya walipa kodi na kuibua vyanzo vipya vya mapato, pamoja na kujenga mazingira rafiki kwa watu wengi zaidi kulipa kodi ili kuongeza makusanyo ya kodi.
Mhe. Rais Magufuli ameelezea kutoridhishwa kwake na utendaji wa TRA ambayo mpaka sasa inakusanyaji kodi kwa walipa kodi Milioni 2 na Laki 7 tu kati ya Watanzania wote zaidi ya Milioni 55, na amesema kwa mtindo huo TRA itakuwa inazidi kuwakamua walipa kodi wachache wakati ingeweza kupanua uwigo wa kodi na kuweka viwango vya kodi vinavyolipika na vitakavyowavutia watu wengi zaidi kulipa kodi.
“Ukienda mipakani wafanyabiashara wanafungua maduka upande nchi za wenzetu na sio upande wa Tanzania, na sababu ni kwamba wakifungua upande wa Tanzania wanasumbuliwa na TRA, wekeni viwango vya kodi vinavyolipika ili watu wengi waweze kulipa kodi badala ya kukwepa” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Mhe. Rais Magufuli ameelezea kutofurahishwa na mrundikano wa kesi za kodi mahakamani na ametaka tatizo hilo lifanyiwe kazi kwa kuwa linasababisha kodi nyingi kutolipwa kwa kusubiri mivutano ya kesi.
Amempongeza Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji kwa ufuatiliaji mzuri wa fedha za bajeti zinazoelekezwa katika miradi mbalimbali na kuchukua hatua zinazostahili ikiwemo kuzirejesha hazina na kuzielekeza mahali pengine zinapohitajika.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli amemtaka Naibu Katibu wa Fedha na Mipango Mkuu Bw. Ndunguru na Naibu Kamishna Mkuu wa TRA Bw. Mbibo kwenda kurekebisha dosari zote zilizopo katika ofisi zao ikiwa ni pamoja na kuwaondoa watumishi wanaoonekana kuwa kikwazo cha kutekeleza mipango ya Serikali.
Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan amesema viongozi hao wanatarajiwa kufanya vizuri zaidi katika nafasi walizopewa hivi sasa hasa ikizingatiwa kuwa wanakwenda kufanya kazi katika ofisi zenye mchango mkubwa katika uchumi wa nchi.
Nae Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Ashatu Kijaji na Kamishna Mkuu wa TRA Bw. Charles Kichere wamemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa uteuzi wa viongozi hao na wameahidi kwenda kusimamia kwa ukaribu zaidi utekelezaji wa fedha za bajeti na kufanyia kazi changamoto ya kupanua uwigo wa kodi na kuongeza idadi ya walipa kodi.
Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli akiwa na Mkewe Mhe. Mama Janeth Magufuli wametoa heshima za mwisho kwa mwili wa Marehemu na kutoa mkono wa pole kwa familia ya Mbunge wa Iringa Mjini Mhe. Mch Peter Msigwa ambaye amefiwa na Dada yake Tryphosa Simon Sanga aliyefariki dunia tarehe 30 Machi, 2019 kwa ajali ya gari Jijini Dar es Salaam.
Wakiwa nyumbani kwa Marehemu Kimara Stopover, Jijini Dar es Salaam, Mhe. Rais Magufuli na Mama Janeth Magufuli wameungana na wanafamilia kumuombea Marehemu apumzike mahali pema peponi, Amina.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
01 Aprili, 2019
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amemteua Bw. Adolf Hyasinth Mohondela Ndunguru kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango anayeshughulikia Sera.
Bw. Ndunguru ameteuliwa kushika nafasi ya Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango (Sera) ambayo ilikuwa wazi.
Kabla ya uteuzi huo Bw. Ndunguru alikuwa Naibu Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Kufuatia Uteuzi huo, Mhe. Rais Magufuli amemteua Bw. Msafiri Lameck Mbibo kuwa Naibu Kamishna Mkuu wa TRA.
Kabla ya Uteuzi huo Bw. Mbibo alikuwa Meneja wa TRA Mkoa wa Kilimanjaro.
Uteuzi wa viongozi hao unaanza mara moja leo tarehe 31 Machi, 2019.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
31 Machi, 2019
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 28 Machi, 2019 ametembelea hanga la matengenezo ya ndege la Shirika la Ndege la Taifa (ATCL) katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam na kukagua marekebisho ya ndege ya Serikali aina ya Foker 50 ambayo inabadilishwa matumizi ili itumike kusafirisha abiria kama zinavyotumika ndege nyingine za ATCL.
Katika ziara hiyo ya kushtukiza Mhe. Rais Magufuli ameshuhudia kazi ya ufungaji wa viti 48 vya abiria ukiwa umekamilika na mafundi wa kupaka rangi wakiwa wanakamilisha kuchora picha ya mnyama Twiga anayetumiwa kama nembo ya ndege za ATCL.
Mhe. Rais Magufuli ameelezwa kuwa kazi ya marekebisho ya ndege hiyo imechukua muda wa siku 7 na mafundi wanakabidhi ndege leo, tayari kwa matumizi.
Tarehe 23 Desemba, 2018 wakati wa mapokezi ya ndege mpya ya Serikali aina ya Airbus A220-300 Jijini Dar es Salaam, Mhe. Rais Magufuli aliagiza ndege 2 za Serikali (Foker 50 na Foker 28) zilizokuwa zikitumiwa na viongozi zibadilishwe matumizi ikiwa ni pamoja na kupakwa rangi ya ATCL ili zitumiwe na Watanzania wote kwa kusafirisha abiria.
Hata hivyo mapema leo asubuhi akipokea taarifa ya utendaji kazi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mhe. Rais Magufuli ameeleza kusikitishwa kwake na kitendo cha viongozi na watendaji wa Serikali kutaka kupeleka ndege (Foker 50) Afrika Kusini ili ikabadilishwe rangi ambako ingetumia gharama kubwa ya kiasi cha zaidi ya shilingi Milioni 328 badala ya kazi hiyo kufanyika hapa hapa nchini.
Mhe. Rais Magufuli amesema alilazimika kuingilia kati mchakato huo na kuagiza marekebisho hayo ikiwemo kupaka rangi za ATCL yafanyike hapa hapa Tanzania na zoezi hilo limefanikiwa kwa gharama ya shilingi Milioni 7 ikilinganishwa na shilingi Milioni 328 endapo ndege hiyo ingepelekwa Afrika Kusini.
Akiwa uwanjani hapo Mhe. Rais Magufuli amemuagiza Mtendaji Mkuu wa ATCL Mhandisi Ladislaus Matindi kuhakikisha fedha zote zilizoanza kutolewa kwa ajili ya kuipeleka ndege hiyo Afrika Kusini zikiwemo posho za marubani na wahudumu wa ndege, gharama za mafuta na malipo ya awali ya matengenezo zirudishwe.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli ameagiza mafundi 6 waliofanya kazi ya upakaji wa rangi ya ndege hiyo kwa makubaliano ya kulipwa shilingi Milioni 2 waongezwe fedha nyingine shilingi Milioni 10 kama motisha ya kuonesha moyo wa uzalendo, kufanya kazi kwa wakati na kuokoa fedha nyingi ambazo Serikali ingetoa kwa ajili ya kupeleka ndege Afrika Kusini.
Akitoa maelezo kwa Mhe. Rais Magufuli, Mhandisi Matindi amekiri kuwa endapo ndege hiyo ingepelekwa Afrika Kusini marekebisho yangetumia muda usiopungua siku 14 na gharama zingekuwa sio chini ya shilingi Milioni 328, na amemhakikishia Mhe. Rais Magufuli kuwa fedha zilizotolewa zimerejeshwa.
Mhandisi Matindi ameongeza kuwa baada ya kukamilika kwa matengenezo hayo ATCL inatarajia kuwa ndege hiyo itaanza mara moja kutoa huduma za usafiri wa anga katika kituo cha Mtwara na kufuatiwa na Iringa, Mpanda na baadaye Songea, Pemba na Tanga.
Mhe. Rais Magufuli pia ametembelea hanga la ndege za Jeshi la Polisi na kushuhudia helkopta na ndege zilizopo, ambapo amelipongeza jeshi hilo kwa utunzaji mzuri wa ndege zake.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
28 Machi, 2019
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 28 Machi, 2019 ametembelea hanga la matengenezo ya ndege la Shirika la Ndege la Taifa (ATCL) katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam na kukagua marekebisho ya ndege ya Serikali aina ya Foker 50 ambayo inabadilishwa matumizi ili itumike kusafirisha abiria kama zinavyotumika ndege nyingine za ATCL.
Katika ziara hiyo ya kushtukiza Mhe. Rais Magufuli ameshuhudia kazi ya ufungaji wa viti 48 vya abiria ukiwa umekamilika na mafundi wa kupaka rangi wakiwa wanakamilisha kuchora picha ya mnyama Twiga anayetumiwa kama nembo ya ndege za ATCL.
Mhe. Rais Magufuli ameelezwa kuwa kazi ya marekebisho ya ndege hiyo imechukua muda wa siku 7 na mafundi wanakabidhi ndege leo, tayari kwa matumizi.
Tarehe 23 Desemba, 2018 wakati wa mapokezi ya ndege mpya ya Serikali aina ya Airbus A220-300 Jijini Dar es Salaam, Mhe. Rais Magufuli aliagiza ndege 2 za Serikali (Foker 50 na Foker 28) zilizokuwa zikitumiwa na viongozi zibadilishwe matumizi ikiwa ni pamoja na kupakwa rangi ya ATCL ili zitumiwe na Watanzania wote kwa kusafirisha abiria.
Hata hivyo mapema leo asubuhi akipokea taarifa ya utendaji kazi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mhe. Rais Magufuli ameeleza kusikitishwa kwake na kitendo cha viongozi na watendaji wa Serikali kutaka kupeleka ndege (Foker 50) Afrika Kusini ili ikabadilishwe rangi ambako ingetumia gharama kubwa ya kiasi cha zaidi ya shilingi Milioni 328 badala ya kazi hiyo kufanyika hapa hapa nchini.
Mhe. Rais Magufuli amesema alilazimika kuingilia kati mchakato huo na kuagiza marekebisho hayo ikiwemo kupaka rangi za ATCL yafanyike hapa hapa Tanzania na zoezi hilo limefanikiwa kwa gharama ya shilingi Milioni 7 ikilinganishwa na shilingi Milioni 328 endapo ndege hiyo ingepelekwa Afrika Kusini.
Akiwa uwanjani hapo Mhe. Rais Magufuli amemuagiza Mtendaji Mkuu wa ATCL Mhandisi Ladislaus Matindi kuhakikisha fedha zote zilizoanza kutolewa kwa ajili ya kuipeleka ndege hiyo Afrika Kusini zikiwemo posho za marubani na wahudumu wa ndege, gharama za mafuta na malipo ya awali ya matengenezo zirudishwe.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli ameagiza mafundi 6 waliofanya kazi ya upakaji wa rangi ya ndege hiyo kwa makubaliano ya kulipwa shilingi Milioni 2 waongezwe fedha nyingine shilingi Milioni 10 kama motisha ya kuonesha moyo wa uzalendo, kufanya kazi kwa wakati na kuokoa fedha nyingi ambazo Serikali ingetoa kwa ajili ya kupeleka ndege Afrika Kusini.
Akitoa maelezo kwa Mhe. Rais Magufuli, Mhandisi Matindi amekiri kuwa endapo ndege hiyo ingepelekwa Afrika Kusini marekebisho yangetumia muda usiopungua siku 14 na gharama zingekuwa sio chini ya shilingi Milioni 328, na amemhakikishia Mhe. Rais Magufuli kuwa fedha zilizotolewa zimerejeshwa.
Mhandisi Matindi ameongeza kuwa baada ya kukamilika kwa matengenezo hayo ATCL inatarajia kuwa ndege hiyo itaanza mara moja kutoa huduma za usafiri wa anga katika kituo cha Mtwara na kufuatiwa na Iringa, Mpanda na baadaye Songea, Pemba na Tanga.
Mhe. Rais Magufuli pia ametembelea hanga la ndege za Jeshi la Polisi na kushuhudia helkopta na ndege zilizopo, ambapo amelipongeza jeshi hilo kwa utunzaji mzuri wa ndege zake.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
28 Machi, 2019
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 28 Machi, 2019 amemuapisha Mhe. Valentino Mlowola kuwa Balozi wa kwanza wa Tanzania nchini Cuba.
Hafla ya kuapishwa kwa Mhe. Balozi Mlowola imefanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, Katibu Mkuu Kiongozi Mhe. Balozi John Kijazi, Mawaziri, Makatibu Wakuu, Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Prof. Adelardus Kilangi, Viongozi Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama, viongozi wa Madhehebu ya Dini, Viongozi wa vyama vya siasa na viongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam.
Akizungumza baada ya kumuapisha Mhe. Balozi Mlowola, Mhe. Rais Magufuli amesema Serikali imeamua kuanzisha Ubalozi wa Tanzania nchini Cuba kwa kutambua uhusiano na ushirikiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na nchi hiyo ambao ulianzishwa na Baba wa Taifa Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere, na pia kunufaika zaidi na fursa zilizopo nchini Cuba zikiwemo utalaamu na ujuzi wa uzalishaji wa miwa na sukari, uzalishaji wa dawa, ufundishaji wa madaktari, elimu na fursa nyingine.
“Nakupongeza kwa kukubaliwa na Cuba kuiwakilisha Tanzania katika nchi yao, sasa nataka ukafanye kazi, nataka tunufaike na Cuba ambao ni watalaamu wa kuzalisha miwa na sukari, waje wajenge viwanda vya sukari hapa Tanzania ili tukabiliane na upungufu wa sukari inayozalishwa hapa nchini” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Kwa upande wake Mhe. Balozi Mlowola ameahidi kwenda kufanya kazi kwa juhudi na maarifa na kuhakikisha malengo ya Mhe. Rais Magufuli pamoja na matarajio ya Watanzania yanafikiwa.
Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli amepokea taarifa ya utendaji kazi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) ya mwaka 2017/18 iliyowasilishwa kwake na Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU Kamishna Diwani Athumani.
Katika taarifa hiyo Kamishna Diwani Athumani amesema TAKUKURU imepata mafanikio makubwa katika kuzuia na kupambana na rushwa katika mwaka 2017/18 na ametaja baadhi ya mafanikio hayo kuwa ni kuokoa fedha za Serikali kiasi cha shilingi Bilioni 70.3 ambazo zingepotea kutokana na vitendo vya rushwa, kurudisha shilingi Bilioni 13.1 zilizotokana na matukio ya ukwepaji wa kodi na kesi kubwa 3 za wakweji wa kodi ambazo kufunguliwa katika Mahakama Kuu kitengo cha rushwa na uhujumu uchumi zenye thamani ya shilingi Bilioni 27.7.
Mafanikio mengine ni kuongezeka kwa kesi za rushwa zilizofunguliwa katika mahakama mbalimbali kutoka kesi 435 za mwaka 2016/17 hadi kesi 495 ambapo kati yake kesi 296 zimeamriwa na katika kesi 178 watuhumiwa wamepata adhabu ya vifungo mbalimbali, sawa na asilimia 60.1 ukilinganisha na asilimia 41 iliyofikiwa mwaka 2016/17.
Akizungumzia taarifa hiyo Mhe. Rais Magufuli amempongeza Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU na timu yake kwa juhudi kubwa wanazozionesha katika mapambano dhidi ya rushwa na ameitaka taasisi hiyo kuendelea kufichua mianya yote ya vitendo vya rushwa nchini.
Ametoa mfano wa mianya hiyo kuwa ni pamoja na kuwepo kwa walipa kodi wenye mashine za kutolea risiti (EFD) zisizotambuliwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), madai ya kughushi ya marejesho ya kodi (Tax Refunds) na ukwepaji mkubwa wa kodi unaofanywa na baadhi ya wafanyabiashara akiwemo mfanyabiashara mmoja aliyekwepa kulipa zaidi ya shilingi Bilioni 8.3 kutokana na kuingiza nchini magari 176.
Mhe. Rais Magufuli pia amemtaka Kamishna Diwani Athumani kuhakikisha anawachukulia hatua wafanyakazi wa TAKUKURU ambao wanakiuka maadili ikiwemo kujihusisha na rushwa, akiwemo mtumishi mmoja ambaye anayedaiwa kujikusanyia zaidi ya shilingi Bilioni 1.4 kwa kuwauzia watumishi wa TAKUKURU viwanja hewa.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli amekubali ombi la Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. George Mkuchika aliyeomba TAKUKURU isaidiwe kufungua ofisi katika wilaya mpya 21.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
28 Machi, 2019
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amemteua Dkt. Richard Faustine Sambaiga kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali.
Taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi, Mhe. Balozi John Kijazi imeeleza kuwa uteuzi wa Dkt. Sambaiga umeanza tarehe 23 Machi, 2019.
Dkt. Sambaiga ni Mhadhiri Mwandamizi, Idara ya Sosholojia ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Bi. Rukia Masasi ambaye amemaliza muda wake.
Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli kesho tarehe 28 Machi, 2019 atamuapisha Mhe. Balozi Mteule Valentino Mlowola kuwa Balozi wa Tanzania nchini Cuba.
Mhe. Balozi Mteule Mlowola ataapishwa Ikulu Jijini Dar es Salaam, kuanzia saa 3:30 asubuhi.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
27 Machi, 2019
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amemteua Mhandisi Julius Ndyamukama kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA).
Mhandisi Ndyamukama anachukuwa nafasi ya Bw. Richard Mayongela ambaye uteuzi wake umetenguliwa na anatakiwa kuripoti Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano ambako atapangiwa kazi nyingine.
Kabla ya uteuzi huo Mhandisi Ndyamukama alikuwa Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Dar es Salaam, na ndiye alikuwa msimamizi mkuu wa ujenzi wa majengo namba 3 (Terminal 3) ya uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam ambayo yapo katika hatua za mwisho kukamilika.
Uteuzi wa Mhandisi Ndyamukama unaanza tarehe 26 Machi, 2019.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
26 Machi, 2019
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 25 Machi, 2019 amekutana na kuwapongeza wachezaji wa Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) kwa kufanikiwa kufuzu kucheza fainali za michuano ya soka Barani Afrika kwa mwaka 2019 (AFCON-2019) na pia amempongeza bondia Hassan Mwakinyo ambaye juzi alishinda pambano lake dhidi ya bondia Sergio Gonzalez wa Argentina lililofanyika Jijini Nairobi nchini Kenya.
Hafla ya kuwapongeza wanamichezo hao imefanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, Viongozi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF), Kamisheni ya Ngumi Tanzania (TPBRC) na Kamati ya Ushindi ya Taifa Stars iliyoongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Paul Makonda.
Akizungumza katika hafla hiyo Mhe. Rais Magufuli ameelezea kufurahishwa kwake na matokeo ya mchezo wa jana ambapo Taifa Stars iliifunga Timu ya Taifa ya Uganda (The Cranes) katika uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam kwa magoli 3-0 na ameahidi kuwa Serikali itaendelea kuunga mkono juhudi za wanamichezo wote kwa kuwa mafanikio yao yanaliletea Taifa sifa na heshima na pia yanatangaza fursa mbalimbali ikiwemo utalii, biashara na uwekezaji.
Mhe. Rais Magufuli amewapongeza wachezaji wa Taifa Stars, viongozi wa TFF, Kamati ya Ushindi ya Taifa Stars na Watanzania wote kwa kuungana pamoja kuishangilia timu yao katika mchezo wa jana bila kujali tofauti zao za kidini, itikadi za kisiasa, makabila na kanda wanazotoka.
“Kwa kweli jana nilifurahi sana jinsi mlivyokuwa mnacheza na jinsi mlivyofunga magoli, Watanzania wanataka furaha, sio kufungwafungwa kama mlivyofungwa kule Lesotho, ile iliniuma sana hadi nilipanga kuwa sitaita tena timu kuja hapa Ikulu, lakini sasa safi.
Nataka niwahakikishie Serikali ipo na nyinyi na ni matarajio yangu kuwa mtajiandaa vizuri ili mkafanye vizuri katika michuano ya AFCON huko Misri, sasa vita imeanza” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Mhe. Rais Magufuli ametoa changamoto kwa wadau wote wa michezo kuhakikisha wanasimamia uboreshaji wa miundombinu ya michezo, wanajipanga vizuri kwa michezo mbalimbali ya kuiwakilisha nchi, wanarekebisha dosari zote zilizosababisha kusuasua kwa Tanzania katika michezo ya kimataifa na ameipongeza TFF kwa kufanikiwa kurejesha mgao wa fedha za maendeleo kutoka Shirikisho la Soka Duniani (FIFA).
Aidha, ameiagiza Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kufuatilia uendeshaji wa uwanja wa Taifa ili kujiridhisha juu ya mapato na matumizi ya fedha za uwanja huo pamoja na kuangalia ubora wake kutokana na kuwepo kwa taarifa kuwa maeneo yanayoharibika hayafanyiwi matengenezo inavyopaswa.
Mhe. Rais Magufuli amempongeza bondia Hassan Mwakinyo kwa ushindi alioupata hapo juzi baada ya kumpiga kwa knockout bondia Sergio Gonzalez wa Argentina katika pambano lisilo la ubingwa lilifanyika Jijini Nairobi nchini Kenya, pamoja na mapambano mengine ambayo alishinda na amemtaka kuendelea kufanya vizuri katika mapambano mengine ili kuipatia sifa Tanzania.
“Nafahamu kuwa unazo changamoto nyingi ambazo hukusema hapa, lakini nakupongeza sana, juzi umemtandika yule jamaa mpaka akakaa chini na huwa nakuona unavyofanya mazoezi makali kwa kutumia matairi, wewe ni kijana safi sana” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Mhe. Rais Magufuli ameipongeza kampuni ya Serengeti Breweries Limited ambayo ni wadhamini wa timu ya Taifa Stars na SportPesa ambao ni wadhamini wa bondia Hassan Mwakinyo kwa mchango wao mkubwa wa kuendeleza michezo.
Katika hafla hiyo Mhe. Rais Magufuli amekubali maombi yaliyotolewa na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ya kusaidiwa maandalizi ya michuano ya AFCON kwa vijana wa chini ya miaka 17 iliyopangwa kuanza tarehe 14 Aprili, 2019 hadi tarehe 28 Aprili, 2019 Jijini Dar es Salaam huku Tanzania ikiwakilishwa na timu ya Serengeti Boys, ambapo amesema Serikali itatoa shilingi Bilioni 1 kusaidia maandalizi hayo.
Halikadhalika Mhe. Rais Magufuli ametoa zawadi ya kiwanja kimoja cha kujenga nyumba Jijini Dodoma kwa kwa kila mchezaji wa Taifa Stars, Bondia Hassan Mwakinyo, mchezaji wa zamani na Nahodha wa Taifa Stars Leodgar Tenga na mchezaji wa zamani na mfungaji wa bao lililoiwezesha Tanzania kucheza robo fainali ya AFCON mwaka 1980 Peter Tino ambaye pia amezawadiwa shilingi Milioni 5.
Kwa upande wao wachezaji wa Taifa Stars ambao wameongozwa na Nahodha Msaidizi Himid Mao na bondia Hassan Mwakinyo wamemshukuru Mhe. Rais Magufuli na Serikali kwa ushirikiano mkubwa walioupata hadi kufikia mafanikio hayo na wamemuahidi kuendelea kufanya vizuri katika michezo inayofuata.
Rais wa TFF Bw. Wallace Karia na Mwenyekiti wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT) Bw. Leodgar Tenga wamesema baada ya kufuzu kucheza fainali za AFCON sasa Taifa Stars inaelekeza nguvu zake kujiandaa na michuano hiyo mikubwa Barani Afrika na pia wameelezea matumaini makubwa ya Tanzania kufanya vizuri katika michuano ya AFCON kwa vijana wa chini ya miaka 17 ambapo Tanzania itawakilishwa na timu ya Serengeti Boys, michuano ya AFCON kwa wanawake ambapo Tanzania inawakilishwa na Twiga Stars na kufanya vizuri kwa timu ya Taifa ya Soka chini ya miaka 20 (Ngorongoro Heros) ambayo tarehe 31 Machi, 2019 itacheza na Eritrea Mjini Asmara.
Pamoja na kuwapongeza wachezaji wa Taifa Stars na Bondia Hassan Mwakinyo Mhe. Rais Magufuli amekula chakula cha mchana na wachezaji hao.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
25 Machi, 2019
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Kansela wa Ujerumani Mhe. Angela Merkel jana tarehe 20 Machi, 2019 amezungumza kwa njia ya simu na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli na kumhakikishia kuwa Ujerumani ipo tayari kukuza zaidi uhusiano wake na Tanzania hususani kusaidia juhudi za kuimarisha uchumi.
Mhe. Angela Markel amempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano katika kujenga mazingira mazuri ya uwekezaji ikiwemo kupambana na rushwa na kuimarisha miundombinu.
Kufuatia mafanikio hayo Mhe. Angela Markel amesema Ujerumani itawaleta wafanyabiashara watakaowekeza katika maeneo mbalimbali ya kuimarisha uchumi ikiwemo kujenga kiwanda cha kuzalisha mbolea ambacho kitakuwa kikubwa kuliko vyote Barani Afrika.
Mhe. Angela Merkel amesema Ujerumani imedhamiria kuunga mkono juhudi za ujenzi wa viwanda nchini Tanzania na kwamba ana matumaini kuwa kiwanda kikubwa cha mbolea kitakachojengwa nchini Tanzania kitasaidia kuongeza kipato cha wananchi na kuimarisha kilimo kwa Tanzania na nchi nyingine za Afrika.
Ametoa wito wa kuimarishwa kwa Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano (Joint Permanent Comission – JPC) na amemwalika kwa mara ya pili Mhe. Rais Magufuli kutembelea Ujerumani, ziara ambayo itatanguliwa na ziara ya Mawaziri wa Tanzania kukutana na Mawaziri wa Ujerumani.
Kwa upande wake Mhe. Rais Magufuli amemshukuru Mhe. Angela Merkel kwa kumpigia simu na kueleza dhamira yake ya kukuza zaidi uhusiano wa Tanzania na Ujerumani na amebainisha kuwa Tanzania itahakikisha inajenga mazingira mazuri katika maeneo yote ya ushirikiano yakiwemo biashara na uwekezaji.
Mhe. Rais Magufuli amempongeza Mhe. Angela Markel kwa uongozi wake wa zaidi ya miaka 13 akiwa Kansela wa Ujerumani na amemhakikishia kuwa Tanzania itadumisha na kukuza zaidi ushirikiano huo kwa manufaa ya pande zote mbili.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
21 Machi, 2019
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 21 Machi, 2019 amekutana na kufanya mazungumzo na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar Mhe. Sheikh Mohammed bin Abdulrahman J.A. Al Thani, Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Viongozi hao wamezungumzia uhusiano na ushirikiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na Qatar na dhamira yao ya kuhakikisha uhusiano na ushirikiano huo unaendelezwa na kukuzwa zaidi hususani katika masuala ya uwekezaji katika gesi, madini, utalii na miundombinu ya barabara, bandari, nishati, reli na huduma za kijamii.
Mhe. Rais Magufuli amemshukuru Mhe. Sheikh Mohammed kwa kuja kwake hapa nchini pamoja ujumbe wa wawekezaji wenye dhamira ya kuwekeza nchini Tanzania na amemuomba ampelekee salamu za shukrani kwa Mtawala wa Taifa la Qatar Sheikh Tamim bin Hamad Al Thani kwa kuendeleza uhusiano na Tanzania.
Mhe. Rais Magufuli amesema Tanzania inazo fursa nyingi za uwekezaji zikiwemo uchakataji wa gesi, madini, utalii na usafiri wa anga hivyo amemuomba Sheikh Mohammed kuwahamasisha wafanyabiashara wa Qatar kushirikiana na Tanzania kuwekeza katika maeneo hayo.
“Natambua kuwa Qatar mna utalaamu wa kuchakata gesi na sisi tunayo gesi nyingi, kwa hivyo nawakaribisha mje tushirikiane kuwekeza katika sekta ya gesi, na pia natambua kuwa nyie ni wanunuzi wakubwa wa dhahabu, sisi tunayo dhahabu nyingi na hivi sasa tumeanzisha vituo vya ununuzi wa dhahabu, nawakaribisha mje mnunue dhahabu na tutawapa ushirikiano wote mtaouhitaji” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli ameiomba Qatar kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo ikiwemo uzalishaji wa nishati ya umeme, ujenzi wa reli, barabara na madaraja na pia amemualika Mtawala wa Qatar Sheikh Tamim bin Hamad Al Thani kufanya ziara hapa Tanzania.
Kwa upande wake Naibu Waziri Mkuu wa Qatar Sheikh Mohammed amemshukuru Mhe. Rais Magufuli na Serikali yake kwa kuendelea kushirikiana na Qatar katika masuala mbalimbali na kubainisha kuwa Qatar inathamini uhusiano huo.
Sheikh Mohammed ameahidi kuwa Qatar ipo tayari kufanyia kazi maombi yaliyotolewa na Mhe. Rais Magufuli na pia kuzileta kampuni za nchi hiyo kuja kuwekeza katika maeneo yenye fursa zenye manufaa kwa pande zote mbili.
Nae Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi amesema baada ya kukutana na Mhe. Rais Magufuli, yeye na Sheikh Mohammed watakua na mazungumzo ya kina kuhusu maeneo ya ushirikiano.
Mazungumzo ya viongozi hao yamehudhuriwa na Balozi wa Tanzania nchini Qatar Mhe. Fatma Rajab na Balozi wa Qatar nchini Tanzania Mhe. Abdullah Jassim Mohammed Al Medadi.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
21 Machi, 2019
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 16 Machi, 2019 amekutana na Mjumbe Maalum wa Rais ambaye ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Uganda Mhe. Sam Kutesa aliyewasilisha ujumbe kutoka kwa Rais wa Uganda Mhe. Yoweri Kaguta Museveni.
Baada ya mazungumzo hayo yaliyofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam, Mhe. Sam Kutesa amesema pamoja na kuwasilisha barua kutoka kwa Mhe. Rais Museveni amezungumza na Mhe. Rais Magufuli kuhusu uhusiano na ushirikiano mzuri na wa kidugu uliopo kati ya Tanzania na Uganda.
Mhe. Sam Kutesa amefafanua kuwa mazungumzo yao yamejielekeza zaidi katika uhusiano wa kiuchumi hususani usafirishaji wa bidhaa za kwenda nchini Uganda kupitia bandari za Dar es Salaam na Tanga.
Ameongeza kuwa Mhe. Rais Magufuli amemhakikishia kuwa Tanzania itaendelea kuboresha miundombinu ya usafirishaji wa bidhaa za kwenda nchini Uganda na ametaja baadhi ya juhudi hizo kuwa ni kuimarisha reli ya kati, kukarabati mabehewa 400 ambapo 50 kati yake yamekamilika na kwamba ni matumaini kuwa juhudi hizo zitawawezesha wafanyabiashara wa Uganda kusafirisha mizigo yao bila kikwazo.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
16 Machi, 2019
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 16 Machi, 2019 amefanya ziara ya kushtukiza katika mradi wa ujenzi wa nyumba za makazi ya Askari Magereza wa gereza la Ukonga Jijini Dar es Salaam na kuagiza mradi huo ukabidhiwe kwa Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ).
Mhe. Rais Magufuli ametoa maagizo hayo baada ya kubaini kuwa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) imeshindwa kutekeleza mradi huo kwa wakati, licha ya Serikali kutoa shilingi Bilioni 10 za ujenzi.
Ametaka wataalamu wa TBA waliokuwa wakisimamia mradi huo pamoja na Askari Magereza waondoke na kuwapisha JWTZ.
“Kwa hiyo hapa nisimuone mtu wa TBA, nisimuone mtu wa Magereza kuja kusimamia, muwaache Jeshi la Wananchi wafanye kazi zao, siku watakapokuja kunikabidhi na mimi nitawakabidhi Magereza, kwa hiyo watu wa TBA kuanzia leo nimewafukuza hapa” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Mhe. Rais Magufuli ameelezea kutoridhishwa na utendaji kazi wa TBA katika mradio huo ambao ulianza zaidi ya miaka 2 iliyopita kwa kushirikisha Jeshi la Magereza ambalo lilikuwa linaisadia TBA katika kazi za ujenzi, na ametaka TBA na Jeshi la Magereza wabadilike katika utekelezaji wa majukumu yao.
“Nataka kila mlipo watu wa Magereza mfanye kazi, msimamie watu, kama ni ng’ombe muwafuge vizuri wazalishe vizuri hadi muuze mazao nje, kama ni kilimo mlime kwelikweli, muwe ni jeshi la kuzalisha, hii ni aibu kuleta jeshi jingine la wananchi kuja kuwajengea nyumba nyinyi, wakati nyumba mnakaa nyinyi, mlitakiwa muwe mmeshapanga mkakati kwamba TBA wamesuasua, ngoja tufyatue matofari, tuanze kujenga” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Mkuu wa Utawala wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Kanali Charles Mbuge amesema JKT itakamilisha ujenzi huo ndani ya kipindi cha miezi 2 na nusu kuanzia kesho na kwamba kazi zitafanywa usiku na mchana.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli ameitaka TBA kutoa maelezo ya namna fedha zilizotolewa na Serikali kiasi cha shilingi Bilioni 10 zilivyotumika, na ameonya kuwa endapo itabainika matumizi ya fedha hizo hayaendani na kazi zilizofanyika hatua kali zitachukuliwa.
Katika mradi huo, ujenzi wa majengo 12 ya makazi ya Askari Magereza yaliyopangwa kuwa na ghorofa 4 kila moja ulioanza Desemba 2016 umefikia asilimia 45 tu na unaendelea kwa kusuasua.
Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli amefanya ziara ya kushtukiza katika mradi wa ujenzi wa majengo ya makazi wa Magomeni Kota Jijini Dar es Salaam na kuelezea kusikitishwa na hali ya kusuasua kwa ujenzi huo ulioanza Aprili 2017.
Mhe. Rais Magufuli ameshuhudia ujenzi wa majengo yenye ghorofa 3 ukiwa umefikia asilimia 36 na kazi za ujenzi zikiwa zimesimama kwa muda usiojulikana.
Mmoja wa wananchi wanaosubiri kukamilika kwa ujenzi wa nyumba hizo Mzee Omary Mpimbila amemueleza Mhe. Rais Magufuli kuwa wamekuwa wakifanya juhudi za kufuatilia hatma ya majengo hayo kutoka TBA na Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano lakini mpaka sasa hawajapatiwa majibu ya sababu za kutelekezwa kwake.
Mhe. Rais Magufuli ameahidi kuchukua hatua za haraka kuhakikisha ujenzi huo unaendelea na wakazi wa Magomeni Kota wanapatiwa makazi kama walivyoahidiwa.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
16 Machi, 2019