Taarifa kwa vyombo vya Habari ya zamani
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amezindua barabara ya Tunduma – Laela – Sumbawanga yenye urefu wa kilometa 223.2 ambayo ni sehemu ya barabara kuu katika ushoroba wa magharibi unaoanzia Tunduma – Mpanda – Kigoma – Nyakanazi wenye urefu wa kilometa 1,286.
Ujenzi wa barabara hiyo umegharimu shilingi Bilioni 373 na Milioni 949 kwa ufadhili wa mfuko wa changamoto za milenia (MCC) na kukamilika kwake kumesaidia kuinua shughuli za kiuchumi katika ukanda wa nyanda za juu kusini na ukanda wa magharibi, na pia kumeunganisha usafiri kati ya Tanzania na nchi jirani za Malawi, Zambia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Burundi, Rwanda na Uganda.
Akizungumza katika sherehe za uzinduzi wa barabara hiyo zilizofanyika katika Mji Mdogo wa Laela Wilayani Sumbawanga, Mhe. Rais Magufuli amewapongeza wananchi wa Mikoa yote inayonufaika na barabara hiyo na amewahakikishia kuwa Serikali inayo dhamira ya dhati ya kuhakikisha barabara kuu zote za ukanda wa magharibi zinajengwa kwa kiwango cha lami.
Ameishukuru Marekani kupitia MCC kwa ufadhili wa mradi huo, Rais Mstaafu Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kwa mradi huo kutekelezwa katika kipindi chake na ameipongeza Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano pamoja na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kwa usimamizi wa ujenzi wa barabara hiyo, na pia amewataka wananchi na watumiaji wa barabara hiyo kutunza miundombinu yake kwa kutochimba mchanga kando ya barabara na madaraja, kutomwaga mafuta barabarani na kutoiba alama za barabarani.
Katika mkutano huo, Mhe. Rais Magufuli ameelezea kuchukizwa na taarifa za kuchomwa moto mitambo ya umeme jua ya mradi wa maji wa Mji Mdogo wa Laela uliogharimu shilingi Bilioni 1.7 na ameagiza waliohusika kukamatwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria.
Aidha, baada ya kupokea malalamiko dhidi ya mkandarasi Fally Enterprises Ltd aliyepatiwa zabuni ya kujenga mradi huo pamoja na miradi mingine ambayo inadaiwa kutofanya kazi kama ilivyotarajiwa licha fedha zake kulipwa, Mhe. Rais Magufuli ametoa siku 7 kwa vyombo vya dola kumkamata, kuchunguza na kumfikisha katika vyombo vya sheria, na pia ameiagiza Wizara ya Maji kuwachunguza na kuwachukulia hatua za kisheria maafisa wote wa wizara waliohusika kumpa zabuni mkandarasi huyo.
Halikadhalika, Mhe. Rais Magufuli ameelezea kuchukizwa na taarifa ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Kangi Lugola juu ya Askari Polisi 9 waliokuwa wakijihusisha na vitendo vya rushwa na kuwabambikiza kesi wananchi, na amemuagiza Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini IGP-Simon Sirro kumsimamisha kazi Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Sumbawanga ACP-Polycarp Urio kwa kutowasilisha taarifa ya maelekezo ya Waziri Lugola aliyeagiza Askari Polisi hao wahamishwe kituo cha kazi.
Pia, Mhe. Rais Magufuli ametoa mwezi 1 kwa Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga Vijijini ambayo ofisi zake zipo Sumbawanga Mjini kuhamia katika Mji Mdogo wa Laela ili kutoa huduma jirani na wananchi na ameelekeza kuwa mtumishi yeyote ambaye hatatii agizo hilo afukuzwe kazi mara moja.
Sambamba na agizo hilo, Mhe. Rais Magufuli ametoa mwezi 1 kwa ofisi zote za taasisi za umma zilizopo kwenye majengo ya kupanga, kuhamia katika majengo ya Serikali ili kuokoa fedha za Serikali ambazo zimekuwa zikitumika kulipia gharama za kupanga katika majengo yasiyo ya Serikali.
Kwa TANROADS Makao Makuu ambayo ofisi zake zipo katika jengo la kupanga lililopo Morocco Jijini Dar es Salaam, Mhe. Rais Magufuli ametoa siku 5 kwa ofisi hizo kuhamia katika majengo ya Serikali.
Akiwa njiani kutoka Tunduma Mkoani Songwe kwenda Sumbawanga Mkoani Rukwa, Mhe. Rais Magufuli amesimama kuwasalimu wananchi wa Vijiji vya Chiwanda, Ndalambo, Ikana na Lwasho Wilayani Momba, na Vijiji vya Ikosi, Mpui, Kaengesa, Mkonda na Tamasenga Wilayani Sumbawanga ambako amewataka kutumia uwepo wa barabara nzuri ya lami kuongeza uzalishaji wa mazao kwa kuwa sasa wana uhakika wa kuyafikia masoko ya ndani na nje ya nchi.
Mhe. Rais Magufuli ambaye ameongozana na Mawaziri amesema Serikali imechukua hatua madhubuti za kuhakikisha Watanzania wanapata umeme, elimu bila malipo, wanaboreshewa huduma za matibabu na kwamba pamoja kuimarisha zaidi huduma hizo, imeanza kushughulikia tatizo la maji ambalo linayakabili maeneo mengi ikiwa ni pamoja kuwashughulikia wakandarasi na maafisa wa Serikali wanaohujumu miradi hiyo.
Kesho tarehe 07 Oktoba, 2019, Mhe. Rais Magufuli ambaye ameongozana na Mkewe Mama Janeth Magufuli ataendelea na ziara yake Mkoani Rukwa ambapo atazindua mradi wa maji na usafi wa mazingira wa Mji wa Sumbawanga, atazindua Msikiti wa Istiqaama Community of Tanzania uliopo Sumbawanga Mjini na atazungumza na wananchi katika Mkutano wa hadhara utakaofanyika katika uwanja wa Nelson Mandela Mjini Sumbawanga.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Sumbawanga
06 Oktoba, 2019
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 07 Oktoba, 2019 ameendelea na ziara yake Mkoani Rukwa ambapo amezindua mradi wa maji safi na usafi wa mazingira wa Mji wa Sumbawanga na Msikiti wa Jumuiya ya Istaqaama Tanzania uliopo Mjini Sumbawanga.
Mradi wa maji safi na usafi wa mazingira wa Manispaa ya Sumbawanga umetekelezwa kwa ushirikiano wa Serikali ya Tanzania, Serikali ya Ujerumani kupitia Shirika la Maendeleo la Ujerumani (KFW) na Umoja wa Ulaya (EU) kwa gharama ya shilingi Bilioni 35 na umehusisha kuongeza uzalishaji wa maji kutoka lita Milioni 7.5 kwa siku zilizokuwa zikizalishwa kwa kutumia miundombinu ya zamani hadi kufikia lita Milioni 20 ambazo ni zaidi ya mahitaji ya wakazi 70,932 wa Mji huo wanaohitaji lita Milioni 13 kwa siku.
Waziri wa Maji, Prof. Makame Mbarawa amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa Serikali ya Awamu ya Tano kutoa kipaumbele katika utekelezaji wa miradi ya maji ambapo kwa sasa zaidi ya miradi 547 ikiwemo 468 ya maji vijijini na 79 ya maji mijini yenye thamani ya shilingi Trilioni 3.98 ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji.
Msikiti mpya wa Istiqaama Bomani uliopo Mjini Sumbawanga una uwezo wa kuchukua waumini 650 kwa mara moja, na umejengwa pamoja na kuchimba kisima cha maji kinachotoa huduma kwa wananchi.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Istiqaama Tanzania, Sheikh Seif Ally Seif amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kutengua agizo la kusitisha ujenzi wa Msikiti huo lililotolewa na Manispaa ya Sumbawanga na hivyo kuruhusu Jumuiya hiyo iendelee na ujenzi ambao umekamilika kwa asilimia 100.
Baada ya kuzindua miradi hiyo, Mhe. Rais Magufuli amezungumza na wananchi wa Manispaa ya Sumbawanga katika uwanja wa Nelson Mandela ambapo ameishukuru Serikali ya Ujerumani na Umoja wa Ulaya kwa kufadhili ujenzi wa mradi wa maji wa Mji huo na ameagiza Wizara ya Maji kutafuta fedha za kutekeleza mradi mwingine wa usambazaji maji kwa wananchi.
Ameipongeza Jumuiya ya Istiqaama kwa kujenga Msikiti mzuri katika Manispaa ya Sumbawanga ambapo pamoja na kuchangia shilingi Milioni 5 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya Msikiti, amewataka Waislamu kuutumia Msikiti huo kudumisha amani, upendo, umoja na kuhimiza maendeleo ya wananchi.
Kufuatia Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Selemani Jafo kueleza kuwa kuna Halmashauri za Wilaya 30 ambazo ofisi zake zipo katika Makao Makuu ya Mikoa, Mhe. Rais Magufuli ametoa mwezi mmoja kwa Halmashauri hizo kuhamia katika maeneo ya halmashauri zao vinginevyo zitafutwa.
Kuhusu mgogoro kati ya Manispaa ya Sumbawanga na wafanyabiashara wa soko la Mandela waliokuwa wanadai kuzuiwa kuendeleza ujenzi wa vibanda vya biashara kwa madai ya Manispaa ya Sumbawanga kutafuta fedha za kujengea soko la kisasa, Mhe. Rais Magufuli ameagiza wafanyabiashara hao waruhusiwe mara moja kuendelea na ujenzi huo na amemuagiza Waziri wa TAMISEMI kutoa shilingi Milioni 300 zitakazosaidia kukamilisha ujenzi wa soko hilo.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli amewapongeza wananchi wa Rukwa kwa uzalishaji mkubwa wa mazao na ameahidi kuwa kwa kutambua juhudi zao katika maendeleo Serikali itahakikisha uwanja wa ndege wa Sumbawanga unajengwa, barabara za kuunganisha Mkoa huo na Mikoa mingine pamoja na nchi zinajengwa na ameutaka uongozi wa Mkoa huo kushughulikia kero za wananchi.
Ameelezea kuchukizwa na takwimu za idadi kubwa ya wanafunzi wa shule wanaopata ujauzito ambapo takwimu zinaonesha mwaka 2018 wanafunzi 229 walipata ujauzito na hivyo amewataka wazazi na viongozi wa Dini kusimamia vizuri utoaji wa malezi kwa watoto wao, na viongozi wa Mkoa wa Rukwa kuchukua hatua za kukomesha tatizo hilo.
Kesho tarehe 08 Oktoba, 2019, Mhe. Rais Magufuli ambaye ameongozana na Mkewe Mama Janeth Magufuli ataendelea na ziara yake ambapo atazindua barabara ya Sumbawanga – Kanazi, ataweka jiwe la msingi la ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Nkasi, atazindua Kituo cha Afya cha Namanyere na atazindua uandikishaji orodha ya wapiga kura wa Mamlaka za Serikali za Mitaa 2019.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Sumbawanga
07 Oktoba, 2019
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 05 Oktoba, 2019 ameweka mawe ya msingi katika miradi miwili ya ujenzi wa Hospitali ya Mji wa Tunduma na ujenzi wa barabara ya lami ya Mpemba – Isongole inayounganisha Tanzania na Malawi.
Jengo la Hospitali ya Mji wa Tunduma yenye hadhi ya Hospitali ya Wilaya linajengwa kwa gharama ya shilingi Bilioni 4.9 ambapo mpaka sasa ujenzi wake umegharimu shilingi Bilioni 2.2.
Barabara ya Mpemba – Isongole ina urefu wa kilometa 50.3, inajengwa kwa kiwango cha lami kuunganisha Tanzania na Malawi kwa gharama ya shilingi Bilioni 109.439 na ujenzi wake umefikia asilimia 48.
Akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika Mjini Tunduma, Mhe. Rais Magufuli amempongeza Meneja wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) katika Mkoa wa Songwe kwa ujenzi bora wa jengo la Hospitali ya Mji wa Tunduma na ameagiza fedha zilizobaki kwa ajili ya kukamilisha mradi huo zitolewe haraka ili hospitali ikamilike na kuanza kutoa huduma kwa wananchi.
Mhe. Rais Magufuli amesema kujengwa kwa hospitali hiyo pamoja na hospitali ya Uhuru Mkoani Dodoma kunafanya idadi ya hospitali mpya zinazojengwa tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani kufikia 69 na kwamba lengo la kujengwa kwa hospitali hizo pamoja na vituo vya afya vipya 352 kunalenga kuwaondolea Watanzania adha ya kupata matibabu.
Kuhusu ujenzi wa barabara ya Mpemba – Isongole, Mhe. Rais Magufuli ameelezea kutoridhishwa na kasi ndogo ya mkandarasi China GEO Engineering anayejenga barabara hiyo ambaye ameanza kazi mwaka 2017 na ameagiza kuanzia sasa kazi za ujenzi zifanyike usiku na mchana ili mradi ukamilike kwa wakati, vinginevyo hatua zichukuliwe dhidi ya mkandarasi huyo.
Mhe. Rais Magufuli pia ameelezea kutofurahishwa na gharama kubwa za ujenzi wa barabara hiyo ambapo wastani wa kilometa 1 ni takribani shilingi Bilioni 2 na hivyo ametaka kuanzia sasa asiwe anaalikwa kuweka mawe ya msingi ama kufungua miradi ambayo gharama zake za ujenzi ni kubwa kupita kiasi.
Wakizungumza katika mkutano huo Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe. Selemani Jafo na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Ummy Mwalimu wamemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa uwekezaji mkubwa anaoufanya katika sekta ya afya hali iliyosaidia kusogeza huduma za matibabu jirani na wananchi, kupunguza vifo vya akina mama wajawazito wakati wa kujifungua na kuimarisha upatikanaji wa dawa.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhe. Isack Kamwelwe amesema pamoja na kujengwa kwa kiwango cha lami kwa barabara ya Mpemba – Isongole, Serikali imejenga barabara nyingine zaidi ya 10 katika ukanda wa Nyanda za Juu Kusini zikiwemo Sumbawanga – Kanazi (km 75), Kanazi – Kizi – Kibaoni (km 76.7), Sitalike – Mpanda (km 36.7), Sumbawanga – Matai – Kasanga (km 112), Mbeya – Lwanjilo (km 36), Kikusa – Ipinda – Matema (km 39.1), Lwanjilo – Chunya (km 36), Chunya – Makongorosi (km 39), Njombe – Moronga (km 53.9), Njombe – Makete (km 53.5), Lusitu – Mawengi (km 50) na daraja la Momba (lenye urefu wa meta 84).
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Tunduma
05 Oktoba, 2019
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli na Rais wa Jamhuri ya Zambia, Mhe. Edgar Chagwa Lungu tarehe 05 Oktoba, 2019 wamezindua Kituo cha Huduma za Pamoja Mpakani (One Stop Border Post) cha Tunduma(Tanzania)/Nakonde (Zambia).
Miundombinu mpya ya kituo hicho upande wa Tunduma (Tanzania) imejengwa kwa gharama ya shilingi Bilioni 14 zilizotolewa kwa ufadhili kutoka Trade Mark East Africa (TIMEA).
Akizungumza katika sherehe za uzinduzi huo, Mhe. Rais Magufuli amemshukuru Mhe. Rais Lungu kwa kuitikia mwaliko wake wa kuja kuzindua kituo hicho na kumhakikishia kuwa Tanzania inatarajia kuwa kujengwa kituo hicho kutachochea uchumi wa Tanzania na Zambia kwa kuokoa muda na gharama kubwa zinazotumika mpakani.
Mhe. Rais Magufuli ametoa wito kwa maafisa wa forodha, uhamiaji na huduma nyingine za mpakani hapo kuhakikisha vikwazo vyote vinaondolewa ili kutowakwamisha wananchi wa pande hizo mbili kuongeza kasi ya biashara.
Amefafanua kuwa baada ya kufanya kazi kubwa ya kupigania ukombozi wa Mataifa mbalimbali ya Afrika, Baba wa Taifa la Tanzania Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere na Muasisi wa Taifa la Zambia Mzee Kenneth Kaunda walijielekeza katika ukombozi wa kiuchumi kwa kuanzisha miradi mikubwa ya bomba la Mafuta la Tanzania na Zambia (TAZAMA - lenye urefu wa kilometa 1,710) ambao unaendelea vizuri na reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA - yenye urefu wa kilometa 1,860) ambayo haifanyi vizuri jambo ambalo linahitaji kufanyiwa kazi kwa nguvu.
Mhe. Rais Magufuli ameeleza dhamira yake ya kuhakikisha TAZARA inaondoka katika hali ya sasa ambapo usafirishaji wake wa mizigo umeshuka kutoka tani 601,229 hadi kufikia tani 128,105 hali ambayo itasaidia kuongeza biashara kati ya Tanzania na Zambia na kupunguza gharama za usafirishaji.
Kwa upande wake, Mhe. Rais Lungu amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kumwalika na kwa kuhakikisha kituo hicho kinajengwa na kukamilika kwa kuwa mpaka wa Tunduma/Nakonde ambao hupitisha magari takribani 600 kwa siku ni moja ya mipaka yenye shughuli nyingi katika nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Africa (SADC).
Mhe. Rais Lungu ameungana na Mhe. Rais Magufuli kuwataka maafisa wanaotoa huduma katika mpaka wa Tunduma/Nakonde kutokuwa kikwazo kwa wafanyabiashara hasa wafanyabiashara wadogo ambao ndio tegemeo kubwa la ustawi wa nchi, na ameahidi kuwa yeye na Mhe. Rais Magufuli hawatakubali kumuacha nyuma mtu yeyote.
Baada ya kuzindua kituo cha huduma za pamoja mpakani, Mhe. Rais Magufuli na Mhe. Rais Lungu wamefanya mkutano wa hadhara katika Mji wa Nakonde nchini Zambia ambapo Mhe. Rais Magufuli amewahakikishia wananchi wa Zambia kuwa Watanzania ni ndugu, majirani na marafiki zao.
Mhe. Rais Magufuli ametangaza kutoa msaada wa tani 25 za mbegu za korosho zenye thamani ya shilingi Milioni 125 kwa Zambia zitakazosaidia kufufua zao la korosho nchini humo ili kuinua kipato cha wananchi, na pia ametoa msaada wa shilingi Milioni 5 kwa shule ya Sekondari Nakonde.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli ameshauri Zambia ijenge barabara ya lami ya kuanzia mpakani kwenda Zambia kama ambavyo Tanzania imefanya na Mhe. Rais Lungu amesema tayari Serikali ya nchi hiyo imetoa zabuni ya ujenzi wa barabara hiyo kati ya Nakonde na Isoko.
Kesho tarehe 06 Oktoba, 2019, Mhe. Rais Magufuli ambaye ameongozana na Mkewe Mama Janeth Magufuli ataendelea na ziara yake ambapo atazindua barabara ya lami ya Tunduma – Sumbawanga.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Tunduma
05 Oktoba, 2019
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ameanza ziara ya kikazi ya siku 9 katika Mikoa ya Songwe, Rukwa na Katavi ambapo tarehe 04 Oktoba, 2019 ameweka jiwe la msingi katika mradi wa upanuzi wa huduma za maji na kuzindua kiwanda cha kukoboa kahawa cha GDP katika Mji wa Vwawa, Wilaya ya Mbozi Mkoani Songwe.
Mradi wa upanuzi wa huduma za maji katika Mji wa Vwawa utaongeza uzalishaji wa maji kutoka lita Milioni 1 hadi kufikia lita Milioni 2 kwa gharama ya shilingi Bilioni 1 na Milioni 550 na Mhe. Rais Magufuli ameongeza shilingi Milioni 100 za kununulia pampu ili kuongeza uzalishaji wa maji hayo hadi kufikia uzalishaji wa lita Milioni 3 kwa siku.
Mhe. Rais Magufuli ameagiza mradi huo ukamilike ifikapo tarehe 30 Oktoba, 2019 na amewahakikishia Watanzania kuwa Serikali inayo dhamira ya dhati ya kuhakikisha tatizo la maji linashughulikiwa ipasavyo.
Waziri wa Maji Prof. Makame Mbarawa amesema pamoja na kutekeleza mradi huo, Serikali itachimba visima 3 vitakavyowezesha uzalishaji wa maji katika Mji wa Vwawa kuongezeka hadi kufikia lita Milioni 8 kwa siku na kwamba kwa Mkoa mzima wa Songwe Serikali inatekeleza miradi 18 ya maji kwa gharama ya shilingi Bilioni 18.8.
Kiwanda cha kukoboa kahawa cha GDM chenye uwezo wa kukoboa tani 10 za kahawa kwa saa kinamilikiwa na Bw. Gervas Mwangoka ambaye amewezeshwa na Serikali kupitia Benki ya Biashara ya TIB iliyomkopesha shilingi Bilioni 7.
Mhe. Rais Magufuli amempongeza Bw. Mwangoka kwa uwekezaji huo na ametoa wito kwa Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) kushirikiana na GDM kupanua kiwanda hicho ili kiongeze zaidi kiwango cha ukoboaji wa kahawa.
Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Innocent Bashungwa amesema kiwanda hicho kimefikisha idadi ya viwanda 28 vinavyokoboa kahawa ya wakulima hapa nchini na ameahidi kuendelea kushirikiana na Wizara ya Kilimo na wawekezaji mbalimbali kuongeza idadi ya viwanda vya kuongeza thamani ya mazao.
Akiwa njiani kutoka uwanja wa ndege wa Songwe kuelekea Vwawa, Mhe. Rais Magufuli amezungumza na wananchi wa vijiji vya Nanyala, Lumbira, Mahenje na Mlowo ambapo ametoa mwezi mmoja kwa viongozi wa Mkoa wa Songwe na Wizara husika kuumaliza mgogoro wa ardhi kati ya Kijiji cha Nanyala na Kampuni ya Saruji ya Mbeya kufuatia wananchi kulalamika kuwa mgogoro huo unasababisha kukosa maeneo ya kufanyia shughuli zao za uzalishaji mali.
Katika Kijiji cha Mahenje, Mhe. Rais Magufuli amechangia shilingi Milioni 5 kwa ajili ya ujenzi wa majengo ya shule ya Sekondari Mahenje na shilingi Milioni 3 kwa ajili ya shule ya msingi Mahenje, na pia amefungua jengo la Mahakama ya Wilaya ya Mbozi lililopo Mlowo.
Mkutano wa hadhara umefanyika Mji wa Vwawa ambapo Mhe. Rais Magufuli amewapongeza wananchi wa Songwe kwa juhudi kubwa za uzalishaji mali hasa katika mazao ya chakula, na amekubali ombi la Mkoa huo kumegewa sehemu ya eneo linalomilikiwa na Kituo cha Utafiti wa Kilimo ili litumike kujenga Kituo cha Mabasi na Soko ambapo ameagiza ekari 50 zimegwe kwa ajili hiyo.
Mhe. Rais Magufuli amempongeza Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brigedia Jenerali Mstaafu Nicodemus Mwangela kwa kuokoa shilingi Bilioni 2.3 kati ya shilingi Bilioni 6.5 zilizotengwa kwa ajili ya ujenzi wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa na ameagiza fedha zilizookolewa zitumike kumalizia majengo zaidi ya 1,500 ya shule yanayohitaji fedha za umaliziaji.
Amempongeza Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Dkt. Edwin Mhede kwa kuandika historia ya ukusanyaji wa juu wa mapato katika mwezi Septemba 2019 ambapo ulifikia shilingi Trilioni 1 na Bilioni 767 na kwamba ukusanyaji huo mkubwa wa mapato pamoja na udhibiti wa wizi na ufisadi ndio unaoiwezesha Serikali kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo ikiwemo umeme, reli, ndege, barabara na kutoa elimu bila malipo hali iliyouwezesha Mkoa wa Songwe kupatiwa shilingi Bilioni 251 za miradi ya maendeleo katika kipindi cha miaka 3 iliyopita.
Mhe. Rais Magufuli ametoa wito kwa Watanzania kuwa makini dhidi mabeberu na vibaraka wao, wanaotumia mbinu mbalimbali kutaka kuvuruga mwelekeo mzuri wa Tanzania na ameomba Watanzania wamwelewe anaposhughulikia maendeleo na kutatua kero.
“Adui hajalala, hili nataka mlitambue, kila unapopiga hatua mbele ujue kuna maadui 10 nyuma, sisi kama Taifa la Tanzania hatuwezi kuwakwepa, lakini tuchape kazi, tumtangulize Mungu wetu kwa maendeleo ya nchi yetu, na niwaombe wale wengine ambao wamejitoa ufahamu kwa kutokutambua wao ni Watanzania, Mungu akawaguse, akawabadilishe mawazo yao, wakaishi kama walivyo Watanzania wengine, wakatambue kuwa hawana Taifa jingine zaidi ya Tanzania” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Kesho Mhe. Rais Magufuli ambaye ameongozana na Mkewe Mama Janeth Magufuli, ataendelea na ziara yake hapa Songwe ambapo yeye na Rais wa Jamhuri ya Zambia Mhe. Edgar Chagwa Lungu watazindua Kituo cha Huduma za Pamoja Mpakani cha Tunduma na Nakonde (One Stop Border Post).
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Vwawa, Songwe
04 Oktoba, 2019
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 01 Oktoba, 2019 amemuapisha Dkt. Wilson Mahera Charles kuwa Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na Kanali Wilbert Augustine Ibuge kuwa Balozi.
Hafla ya kuapishwa kwa viongozi hao imefanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Makamu wa Rais, Mhe. Samia Suluhu Hassan, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Mhe. Angellah Kairuki na Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Mhe. Jaji Mstaafu Semistocles Kaijage.
Akizungumza baada ya kuwaapisha, Mhe. Rais Magufuli amewatakia heri viongozi walioapishwa na kuwataka wafanye kazi kwa kumtanguliza Mwenyezi Mungu na kwa maslahi ya Taifa.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
01 Oktoba, 2019
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Ufafanuzi.
- Aliyehamishwa kituo cha kazi kutoka Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro na kwenda kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Itigi Mkoani Singida ni Bw. John Kulwa Magalula.
Uhamisho huu umefanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 01 Oktoba, 2019.
----------------------
- Aliyeteuliwa kuwa Katibu Tawala wa Wilaya ya Ilala ni Bi. Charangwa Selemani Makwiro.
Uteuzi huu umefanywa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Kepteni Mstaafu George Huruma Mkuchika kuanzia leo tarehe 01 Oktoba, 2019.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
01 Oktoba, 2019
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 01 Oktoba, 2019 amefanya uteuzi na kuwahamisha vituo vya kazi Wakurugenzi wa Halmashauri za Manispaa na Wilaya, na pia amefanya uteuzi wa Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi na Mkuu wa Itifaki (Chief of Protocal).
Wakurugenzi Watendaji walioteuliwa ni kama ifuatavyo;
- Mhe. Rais Magufuli amemteua Bw. Ndaki Stephano Muhuli kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Siha Mkoani Kilimanjaro. Kabla ya uteuzi huo Bw. Ndaki Stephano Muhuli alikuwa Katibu Tawala wa Wilaya ya Kiteto Mkoani Manyara.
- Mhe. Rais Magufuli amemteua Bi. Rehema Said Bwasi kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro. Kabla ya uteuzi huo Bi. Rehema Said Bwasi alikuwa Katibu Tawala wa Wilaya ya Korogwe Mkoani Tanga.
- Mhe. Rais Magufuli amemteua Bi. Sheillah Edward Lukuba kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro Mkoani Morogoro. Kabla ya uteuzi huo Bi. Sheillah Edward Lukuba alikuwa Katibu Tawala wa Wilaya ya Ilala Mkoani Dar es Salaam.
- Mhe. Rais Magufuli amemteua Bw. Mohamed Mavura kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti Mkoani Pwani. Kabla ya uteuzi huo Bw. Mohamed Mavura alikuwa Afisa katika Makao Makuu ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).
- Mhe. Rais Magufuli amemteua Bw. Ezekiel Henrick Magehema kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kyela Mkoani Mbeya. Kabla ya uteuzi huo Bw. Ezekiel Henrick Magehema alikuwa Afisa Tarafa wa Malangali Mkoani Iringa.
- Mhe. Rais Magufuli amemteua Bi. Diana Sono Zacharia kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Butiama Mkoani Mara. Kabla ya uteuzi huo Bi. Diana Sono Zacharia alikuwa Afisa Tarafa wa Ukerewe Mkoani Mwanza.
- Mhe. Rais Magufuli amemteua Bi. Hanji Godigodi kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi Mkoani Songwe. Kabla ya uteuzi huo Bi. Hanji Godigodi alikuwa Afisa Elimu Taaluma wa Mkoa wa Dar es Salaam.
- Mhe. Rais Magufuli amemteua Bw. Said H. Magaro kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Uyui Mkoani Tabora. Kabla ya uteuzi huo Bw. Magaro alikuwa Afisa Tarafa wa Msata Mkoani Pwani.
- Mhe. Rais Magufuli amemteua Bi. Hawa Lumuli Mposi kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi Mkoani Morogoro. Kabla ya Uteuzi huo Bi. Hawa Lumuli Mposi alikuwa Afisa Tarafa wa Ifakara Mkoani Morogoro.
10. Mhe. Rais Magufuli amemteua Bw. Godwin Justin Chacha kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Rombo Mkoani Kilimanjaro. Kabla ya Uteuzi huo Bw. Chacha alikuwa Afisa Tarafa wa Maswa Mkoani Simiyu.
Wakurugenzi Watendaji waliohamishwa vituo vya kazi ni kama ifuatavyo;
- Mhe. Rais Magufuli amemhamisha aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro na kumpeleka kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Itigi Mkoani Singida.
- Mhe. Rais Magufuli amemhamisha aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti Mkoani Pwani Bi. Advera Ndebabayo na kumpeleka kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Arusha.
Katika hatua nyingine, Mhe. Rais Magufuli amemteua Dkt. Wilson Mahera Charles kuwa Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC). Kabla ya uteuzi huo Dkt. Wilson Mahera Charles alikuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Arusha.
Dkt. Wilson Mahera Charles anachukua nafasi ya Bw. Athuman Kihamia ambaye atapangiwa kazi nyingine.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli amemteua Kanali Wilbert Augustine Ibuge kuwa Balozi na Mkuu wa Itifaki (Chief of Protocal) wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Kanali Ibuge anachukua nafasi ya Mhe. Balozi Grace A. Martin ambaye atapangiwa majukumu mengine ya Kibalozi.
Uteuzi wa viongozi hao unaanza leo tarehe 01 Oktoba, 2019.
Wakati huo huo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Kepteni Mstaafu George Huruma Mkuchika amefanya uteuzi wa Makatibu Tawala wa Wilaya (DAS) wawili kama ifuatavyo;
- Mhe. Kepteni Mstaafu Mkuchika amemteua Bw. Charangwa Selemani Makwiro kuwa Katibu Tawala wa Wilaya ya Ilala Mkoani Dar es Salaam. Bw. Makwiro anachukua nafasi ya Bi. Sheillah Edward Lukuba ambaye ameteuliwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro.
- Mhe. Kepteni Mstaafu Mkuchika amemteua Bw. Thomas Salala kuwa Katibu Tawala wa Wilaya ya Mtwara. Kabla ya uteuzi huo Bw. Thomas Salala alikuwa Katibu wa Mkuu wa Mkoa wa Kagera.
Uteuzi wa Makatibu Tawala wa Wilaya hao unaanza leo tarehe 01 Oktoba, 2019.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
01 Oktoba, 2019
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amefanya uteuzi wa viongozi mbalimbali kama ifuatavyo;
Kwanza, Mhe. Rais Magufuli amemteua Prof. Blasius Bavo Nyichomba kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT). Prof. Nyichomba ni Profesa Mshiriki wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
Pili, Mhe. Rais Magufuli amemteua Dkt. Rosemarie Nyigulila Mwaipopo kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Uendeshaji ya Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru. Dkt. Mwaipopo ni Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
Tatu, Mhe. Rais Magufuli amemteua Prof. Longinus Kyaruzi Rutasitara kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA).
Nne, Mhe. Rais Magufuli amewateua Bi. Rhoda M. Ngamilanga na Bi. Devotha Christopher Kamuzora kuwa Makamu Wenyeviti wa Baraza la Rufani za Kodi.
Tano, Mhe. Rais Magufuli amemteua Prof. Yunus D. Mgaya kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR). Prof. Mgaya anashika wadhifa huo kwa kipindi kingine cha miaka 2.
Taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi, Mhe. Balozi John Kijazi imeeleza kuwa uteuzi wa viongozi hao umeanza leo tarehe 26 Septemba, 2019.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
26 Septemba, 2019
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 30 Septemba, 2019 amepokea taarifa ya utekelezaji wa ushauri alioutoa tarehe 22 Septemba, 2019 kuhusu kuwasamehe washtakiwa wa makosa ya uhujumu walio tayari kukiri makosa yao, kuomba msamaha na kurejesha fedha na mali.
Akitoa taarifa hiyo Ikulu Jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) Biswalo Mganga amesema kwa kipindi cha siku 7 zilizotolewa, washtakiwa 467 wameandika barua na kuomba kurudisha jumla shilingi Bilioni 107 na Milioni 842.
DPP Mganga amefafanua kuwa kati ya fedha hizo wapo washtakiwa waliotayari kulipa hivi sasa kiasi cha shilingi Bilioni 13 na Milioni 602 pamoja kukabidhi Serikalini madini yakiwemo dhahabu na Tanzanite yenye jumla ya kilo 35, na pia wapo washtakiwa waliotayari kulipa shilingi Bilioni 94 na Milioni 240 kwa awamu.
Ameongeza kuwa pamoja na fedha hizo, wapo washtakiwa wengine wawili walioitikia zoezi hili na hivyo kukiri makosa yao Mahakamani ambapo mmoja wao amelipa shilingi Bilioni 1 na Milioni 37 na amekabidhi Serikalini gramu 2,123.64 za madini ya vito yenye thamani ya shilingi Milioni 36.5.
Aidha, DPP Mganga amemuomba Mhe. Rais Magufuli aongeze siku kwa watuhumiwa kuwasilisha barua zao za kuomba msamaha na kurejesha fedha na mali kutokana na baadhi yao kushindwa kufanya hivyo kwa kipindi kifupi cha siku 7 kutokana na sababu mbalimbali.
Mhe. Rais Magufuli amempongeza DPP Mganga na timu yake kwa kazi nzuri waliyofanya katika utekelezaji wa ushauri huo na pia kwa namna wanavyoiwakilisha vizuri Serikali katika kesi mbalimbali Mahakamani.
Mhe. Rais Magufuli ameelezea kufurahishwa na mwitikio wa washtakiwa wengi kujitokeza kuomba msamaha na kurejesha fedha na mali wanazodaiwa kuhujumu, na ameagiza washtakiwa wote waliofanya hivyo waanze kuachiwa kutoka Magerezani waliokokuwa wanashikiliwa.
Amekubali kuongeza siku 7 kwa DPP kuendelea kupokea barua za washtakiwa ambao wapo tayari kuomba msamaha na kurejesha fedha na mali na ameonya kuwa baada ya muda huo hakutakuwa na msamaha mwingine na kwamba kutolewa kwa msamaha huo hakuna maana kuwa makosa ya uhujumu uchumi yamefutwa.
“Nafahamu wapo wengine wanadanganywa na Mawakili wao kuwa wakikubali ndio watakuwa wamejifunga, hapana, wakisamehewa wamesamehewa, lakini sio lazima kuomba msamaha wakitaka kuendelea kubaki Magerezani ni shauri yao.
Lakini wale ambao wameomba msamaha na wamelipa waachieni hata leo, na wasirudie tena kufanya makosa hayo” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Ameitaka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Magereza na Jeshi la Polisi kuendelea kushirikiana na Ofisi ya DPP katika utekelezaji wa zoezi hilo.
Amebainisha kuwa fedha zitakazokusanywa kutoka kwa washtakiwa hao zitalinufaisha Taifa kwa kwenda kutumika katika maendeleo ya wananchi ikiwemo ujenzi wa hospitali na barabara na kwamba ni matarajio yake kuwa washtakiwa watakaoachiwa watakwenda kushiriki ujenzi wa Taifa kwa njia zilizo halali.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
30 Septemba, 2019
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 16 Septemba, 2019 amefungua kiwanda kikubwa cha utengenezaji wa mabomba kiitwacho Pipe Industries Co. Ltd kilichopo Vingunguti Jijini Dar es Salaam na kuagiza miradi yote itumiayo mabomba ikiwemo miradi ya maji na miundombinu mbalimbali kutumia mabomba yanayozalishwa hapa nchini.
Kiwanda hicho cha kipekee katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati kinazalisha mabomba aina ya High Density Polyethylene Pipe (HDPE), Poly Vinyl Chloride (PVC) na Grass Reinforced Plastic Pipes (GRP) ambayo ni maalum kwa ajili ya usambazaji wa maji safi na salama, miundombinu ya maji taka, miradi ya ujenzi, kilimo cha umwagiliaji na migodi ya madini.
Mkurugenzi Mkuu wa kiwanda hicho Bw. Seif Ally Seif amesema ujenzi wa kiwanda hicho umegharimu zaidi ya shilingi Bilioni 120 na unakwenda sambamba na dira ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kujenga viwanda na kuongeza usambaza wa maji kwa wananchi ifikapo mwaka 2025.
Bw. Seif amesema kiwanda hicho kina uwezo wa kuzalisha tani 25,000 za mabomba aina ya HDPE na PVC, na tani 40,000 za mabomba aina ya GRP kwa mwaka lakini kutokana na changamoto za kukosekana kwa soko kinazalisha tani 8,000 za mabomba ya HDPE na PVC, na tani 5,000 za mabomba aina ya GRP kwa kutumia teknolojia ya kisasa inayozalisha mabomba yenye ubora wa hali ya juu unaotambulika kimataifa.
Ameongeza kuwa kiwanda hicho kitapanuliwa katika awamu ya pili kwa kuongeza uwekezaji wa shilingi Bilioni 150 ambapo licha ya kuongeza uzalishaji, idadi ya watu watakaopata ajira itaongezeka kutoka 215 wa sasa hadi kufikia 500.
Akizungumza katika sherehe za ufunguzi wa kiwanda hicho, Mhe. Rais Magufuli amewapongeza Wakurugenzi wa kiwanda hicho Bw. Seif Ally Seif na Nassor Ally Seif kwa uwekezaji huo na ameagiza miradi yote ya Serikali itumie mabomba yanayozalishwa hapa nchini ili kuvilinda viwanda vya ndani ambavyo vinachangia katika mapato ya Serikali kwa kulipa kodi na kuzalisha ajira kwa wananchi.
Amewaagiza viongozi na watendaji wa Serikali kuhakikisha wakandarasi wanaojenga miradi ya Serikali wanatumia mabomba yanayozalishwa hapa nchini vinginevyo wakandarasi hao wasipewe zabuni za ujenzi, lakini pia ametaka viwanda vinavyozalisha mabomba hapa nchini kuhakikisha mabomba hayo yana ubora na yanauzwa kwa bei nafuu.
Kuhusu ucheleweshaji wa majibu ya sampuli za bidhaa za mionzi zinazopita katika bandari ya Dar es Salaam unaosababisha waingizaji wa bidhaa hizo kutozwa adhabu ya kuzidisha muda wa utunzaji wa mizigo (Storage charges), Mhe. Rais Magufuli ameagiza wizara, na taasisi huzika ziwasiliane kuondoa kikwazo hicho cha biashara.
Amempongeza Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Innocent Bashungwa kwa hatua alizochukua kuboresha utendaji kazi wa wizara hiyo ikiwemo soko la korosho ambapo kwa muda mfupi baada ya kuteuliwa kushika wadhifa huo amefanikiwa kupata soko la korosho zenye thamani ya shilingi Bilioni 130 na kwamba korosho zingine pia zipo mbioni kuuzwa.
Kuhusu baadhi ya watu ambao wamekuwa wakipinga juhudi za kuwaletea maendeleo Watanzania ikiwemo kushabikia vitendo vya kuhujumu miradi mikubwa ya Serikali, Mhe. Rais Magufuli amewataka Watanzania kuwapuuza watu hao kwa kuwa wameshindwa kutambua kuwa miradi inayotekelezwa ni mali ya Watanzania wote bila kujali tofauti zao na inagharimiwa kwa fedha za walipa kodi wa Tanzania.
“Inashangaza kuona Watanzania wenzetu wanashabikia kukamatwa kwa ndege ya Serikali, unajiuliza hivi hawa wapo sawa sawa kweli? Na mimi nataka kuwahakikishia Watanzania hatutarudi nyuma, wao watapinga au watashirikiana na mabeberu kutuyumbisha lakini tusijali tusonge mbele.
Hizi ndege tunazonunua sio za Magufuli ni za Watanzania wote, zinasaidia wagonjwa, zinaleta watalii na watu wengine wanawahi kwenye shughuli zao” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
16 Septemba, 2019
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amewaagiza viongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam, Halmashauri ya Manispaa ya Ilala na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kuhakikisha ujenzi wa machinjio ya ng’ombe, mbuzi na kondoo ya Vingunguti Jijini Dar es Salaam unafanyika usiku na mchana ili ukamilike haraka.
Mhe. Rais Magufuli ametoa agizo hilo leo tarehe 16 Septemba, 2019 alipofanya ziara ya kushtukiza katika machinjio hiyo na kujionea hali mbaya ya miundombinu inayotumika hivi sasa na kasi ndogo ya ujenzi wa jengo la machinjio mpya.
Mhe. Rais Magufuli ametembelea machinjio hiyo akitokea katika kiwanda cha kutengeneza mabomba kiitwacho Pipe Industries Co. Ltd baada ya kupata taarifa kuwa kazi ya ujenzi huo inasuasua licha ya Serikali kutoa shilingi Bilioni 14 tangu mwaka uliopita.
Pamoja na kutaka kazi za ujenzi zifanyike usiku na mchana, Mhe. Rais Magufuli pia ameagiza watumiaji wa machinjio ya Vingunguti kutolipa ushuru wowote kuanzia sasa mpaka hapo Manispaa ya Ilala itakapokamilisha ujenzi wa machinjio mpya.
“Kuanzia sasa ni marufuku mtu yoyote kuwatoza ushuru hapa, haiwezekani muwe mlipa ushuru halafu hamuoni fedha mnazolipa zinafanya kazi gani, ni lazima viongozi mjifunze kuwekeza ndipo mwende kukusanya ushuru” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli alipozungumza na watumiaji wa machinjio ya Vingunguti muda mfupi baada ya kutembelea eneo linapojengwa jengo jipya na kujionea hali ya machinjio ya sasa.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli ametaka ujenzi wa jengo la machinjio hiyo uwe umekamilika ifikapo mwezi Desemba, 2019 badala ya mwezi Juni 2020 iliyopangwa.
Mwenyekiti wa wanaotumia machinjio hiyo Bw. Joel Meshack ameishukuru Serikali kwa kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa machinjio hiyo na amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kuingilia kati kwa kuwa hata wao walikuwa hawaridhishwi na kasi ndogo ya ujenzi.
Watumiaji wa machinjio hiyo wameongeza kuwa wanaamini kujengwa kwa machinjio ya kisasa katika eneo hilo kutasaidia kuongeza viwango vya nyama na thamani ya ngozi ambayo kwa sasa inauzwa kwa bei ya kutupa kutokana na maandalizi mabaya.
“Mhe. Rais tunakushukuru umekuja, hali ya machinjio yetu sio nzuri hata nyama tunayotoa hapa tunashindwa kuipeleka Super Market, ngozi ya mbuzi inauzwa hadi shilingi 200 na ngozi ya ng’ombe tunauza shilingi 3,000 tu kutokana na miundombinu duni ya kuchinjia, sisi tunaamini ikijengwa machinjio ya kisasa ubora utaongezeka na tutapata kipato kizuri” amesema Bw. Mtaga Motogambogo.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
16 Septemba, 2019
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 16 Septemba, 2019 amezindua mfumo wa rada za kuongozea ndege katika vituo vya Dar es Salaam na Kilimanjaro.
Sherehe za uzinduzi huo zimefanyika katika eneo la rada ndani ya uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) Jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Mawaziri, Makatibu Wakuu, Mabalozi wanaoziwakilisha nchi mbalimbali hapa nchini, Wabunge na Wakuu wa Mikoa ya Dar es Salaam, Kilimanjaro na Arusha.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) Bw. Hamza Said Johari amesema TCAA ilianza mchakato wa ununuzi wa rada 4 za kiraia mwaka 2016/17 kwa kutumia mkandarasi Thales LAS France SAS kutoka Ufaransa kwa gharama ya shilingi Bilioni 67.3 ambapo usimikaji wa rada hizo unafanyika katika vituo vya Dar es Salaam, Mwanza, Kilimanjaro na Songwe, na pia vituo vidogo vya Zanzibar na Arusha.
Bw. Johari amefafanua kuwa rada za vituo vya Dar es Salaam na Kilimanjaro zimekamilika kwa asilimia 100, rada ya Mwanza imefikia asilimia 90 na rada ya Songwe imefikia asilimia 40, na kwamba rada za vituo vidogo vya Zanzibar na Arusha zimekamilika kwa asilimia 100.
Amebainisha kuwa utekelezaji wa mradi wa kuweka mfumo wa rada za kuongozea ndege unaiwezesha nchi kudhibiti anga lake lote tofauti na hapo awali ambapo nchi iliweza kudhibiti anga kwa asilimia 25 tu na kwamba kutokana na uwekezaji huo nchi itajihakikishia usalama zaidi wa anga lake, itaongeza mapato kwa takribani shilingi Bilioni 16 zaidi ya makusanyo ya sasa, kuongoza ndege nyingi kwa wakati mmoja, kupunguza muda wa kuruhusu ndege kati ya moja na nyingine, kupunguza kazi ya kuongoza ndege na kukidhi matakwa ya kimataifa.
Akizungumza katika sherehe hizo Mhe. Rais Magufuli amempongeza Mkurugenzi Mkuu wa TCAA Bw. Hamza Said Johari kwa utendaji kazi wake mzuri ambapo licha ya kusimamia vizuri mchakato wa utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa rada, amefanikiwa kuongeza ukusanyaji wa mapato ya mamlaka hiyo kutoka shilingi Bilioni 40 hadi kufikia shilingi Bilioni 71 na kwamba mwaka huu mapato hayo yanatarajiwa kufikia shilingi Bilioni 82.
Mhe. Rais Magufuli amesema Serikali ya Awamu ya Tano imefanikiwa kutekeleza mradi huu kwa gharama nafuu ya shilingi Bilioni 67.3 ikilinganishwa na yaliyotokea katika mradi uliopita ambao ulizingirwa na vitendo vya ufisadi hali iliyosababisha Maafisa wa Uingereza walioshiriki kuuza rada hiyo kujiuzulu na akashangazwa na Maafisa waliohusika katika sakata hilo upande wa Tanzania kutojiuzulu hadi sasa.
Amewahakikishia Watanzania kuwa Serikali ya Awamu ya Tano itaendelea kusimamia utekelezaji wa miradi inayotumia fedha za umma kwa uadilifu mkubwa na kwa manufaa ya Watanzania wote.
“Mradi huu utaboresha huduma zetu za usafiri wa anga, na utatuhakikishia usalama wa anga letu, sasa tutakuwa tunaliona anga letu lote” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Mhe. Rais Magufuli amezungumzia hatua kubwa ambayo Tanzania imepiga katika usafiri wa anga ikiwemo matokeo mazuri ya kufufua Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) ambalo sasa limeshika soko la ndani kwa asilimia 75 ikilinganishwa na asilimia 3 kabla ya kununuliwa kwa ndege mpya 6.
Katika salamu zake, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job Yustino Ndugai amesema Watanzania wana kila sababu ya kuipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kwa usimamizi na matumizi mazuri ya fedha za umma huku akitolea mfano wa kiasi cha shilingi Bilioni 67.3 zilizotumika kutekeleza mradi huu wa kununua rada kubwa 4 na ndogo 2, ilihali huko nyuma fedha kiasi cha takribani shilingi Bilioni 230 zilizotumiwa vibaya na kulazimu Serikali ya Uingereza kuzirudisha kwa Serikali ya Tanzania na ilikuwa zitumike kununua rada moja tu.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Isack Kamwelwe amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa Serikali kutoa fedha za kutekeleza mradi wa rada wa kusimika rada hizo na amesema kwa mujibu wa mkataba mkandarasi atawajibika kutoa vipuri vya rada hizo kwa miaka 3 na kuhakikisha vipuri vinapatikana kwa miaka 15.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
16 Septemba, 2019
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ametoa shilingi Milioni 10 kwa Timu ya Taifa ya mpira wa miguu kwa watu wenye ulemavu inayojiandaa kushiriki mashindano ya mpira wa miguu kwa watu wenye ulemavu Afrika (CANAF) yaliyopangwa kuanza tarehe 01 Oktoba, 2019 katika Mji wa Benguela nchini Angola.
Katibu wa Rais, Bw. Ngusa Samike amekabidhi fedha hizo kwa viongozi na wachezaji wa timu hiyo leo tarehe 22 Septemba, 2019 katika studio za Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) ambalo limekuwa likitangaza taarifa za timu hiyo kuomba msaada ili ifanikishe safari ya kwenda kushiriki katika mashindano hayo.
Bw. Samike amewasilisha ujumbe wa Mhe. Rais Magufuli ambaye amewapongeza viongozi na wachezaji wa timu hiyo kwa dhamira yao ya kuiwakilisha nchi katika mashindano hayo na amewatakia heri na ushindi.
Mhe. Rais Magufuli ametoa wito kwa Watanzania wengine watakaoguswa kuisadia timu hiyo kufanya hivyo na kwa timu zingine zinazoiwakilisha Tanzania nje ya nchi kwa kuwa zinaitangaza Tanzania.
“Kwa watu wenye ulemavu kushiriki michezo pia ni tiba, kwa hivyo nawapongeza kwa kushiriki michezo na mashindano haya naamini jamii itaendelea kutilia mkazo walemavu kushiriki michezo” amesema Bw. Samike.
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu kwa Watu wenye Ulemavu (TAFF) Bw. Peter Sarungi na Mwenyekiti wa Chama cha Wenye Ulemavu Bw. Hamad Komboza wamemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kutoa msaada huo na kwa kuendelea kuwatambua na kuwathamani watu wenye ulemavu.
Wamesema timu hiyo yenye wachezaji 13, walimu 5 na viongozi 2 itaondoka tarehe 28 Septemba, 2019 kuelekea nchini Angola ambako inakwenda kushiriki mashindano hayo kwa mara ya kwanza na wameahidi kufanya vizuri.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TBC Bi. Matha Swai amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa moyo wake wa upendo wa kuchangia watu mbalimbali wenye uhitaji kila anapowaona kupitia vyombo vya habari na amehidi kuwa TBC itaendelea kutimiza jukumu lake la kuwatangaza watu hao ili watu mbalimbali wenye mapenzi mema wawaone na kuwasaidia.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
22 Septemba, 2019
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amemteua Jaji Mstaafu Mathew Pauwa Mhina Mwaimu kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora.
Taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi, Mhe. Balozi John Kijazi imeeleza kuwa sambamba na uteuzi wa Mwenyekiti, Mhe. Rais Magufuli amemteua Bw. Mohamed Khamis Hamad (Wakili wa Serikali katika Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka Zanzibar) kuwa Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora.
Pamoja na uteuzi huo, Mhe. Rais Magufuli ameteua Makamishna wa Tume hiyo kama ifuatavyo;
- Dkt. Fatma Rashid Khalfan. (Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Zanzibar).
- Bw. Thomas Masanja (Mhadhiri wa Sheria, Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino – SAUT).
- Bi. Amina Talib Ali (Afisa Mwandamizi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar).
- Bw. Khatib Mwinyi Chande (Mhadhiri Msaidizi Chuo Kikuu Huria Tanzania – OUT)
- Bw. Nyanda Josiah Shuli (Afisa Mwandamizi wa Wizara ya Fedha na Mipango).
Uteuzi huu umeanza tarehe 19 Septemba, 2019.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
22 Septemba, 2019
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 20 Septemba, 2019 amefanya uteuzi wa viongozi mbalimbali.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi Mhe. Balozi John Kijazi uteuzi huo ni kama ifuatavyo;
- Mhe. Rais Magufuli amemteua Bw. Loata Sanare kuwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro.
Bw. Sanare anachukua nafasi ya Dkt. Kebwe Stephen Kebwe ambaye uteuzi wake umetenguliwa.
- Mhe. Rais Magufuli amemteua Bw. Mussa Maselle kuwa Mkuu wa Wilaya ya Malinyi Mkoani Morogoro.
Kabla ya uteuzi huo Bw. Maselle alikuwa Msaidizi wa Mkuu wa Mkoa wa Geita.
- Mhe. Rais Magufuli amemteua Bw. Tixon Tuyangine Nzunda kuwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (anayeshughulikia Bunge na Waziri Mkuu).
Kabla ya uteuzi huo Bw. Nzunda alikuwa Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa – TAMISEMI (aliyekuwa akishughulikia Elimu)
- Mhe. Rais Magufuli amemteua Dkt. Ally Possi kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.
Kabla ya uteuzi huo, Dkt. Possi alikuwa Naibu Wakili Mkuu wa Serikali.
- Mhe. Rais Magufuli amemteua Bw. Gabriel Pascal Malata kuwa Naibu Wakili Mkuu wa Serikali.
Kabla ya Uteuzi huo, Bw. Malata alikuwa Kamishna wa Kazi katika Ofisi ya Waziri Mkuu.
- 6. Mhe. Rais Magufuli amemteua Bi. Mary Maganga kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango (anayeshughulikia Utawala).
Kabla ya uteuzi huo, Bi. Maganga alikuwa Kamishna wa Bajeti wa Wizara ya Fedha na Mipango.
- Mhe. Rais Magufuli amemteua, Mhandisi Anthony Damian Sanga kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji.
Kabla ya uteuzi huo, Bw. Sanga alikuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira wa Jiji la Mwanza.
- Mhe. Rais Magufuli amemteua Bw. Alphayo J. Kidata kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Mtwara.
Bw. Kidata anachukua nafasi ya Dkt. Jilly Elibariki Maleko ambaye ameteuliwa kuwa Balozi.
- Mhe. Rais Magufuli amemteua Mhandisi Emmanuel Kalobelo kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro.
Kabla ya uteuzi huo Bw. Kalobelo alikuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na anachukua nafasi ya Bw. Cliford Tandali ambaye amestaafu.
10. Mhe. Rais Magufuli amemteua Dkt. Khatibu Kazungu kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Kilimanjaro.
Kabla ya uteuzi huo, Dkt. Kazungu alikuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango na anachukua nafasi ya Mhandisi Aisha Amour ambaye ameteuliwa kuwa Balozi.
Wateule hao wote wataapishwa Jumapili tarehe 22 Septemba, 2019 saa 9:00 alasiri, Ikulu Jijini Dar es Salaam.
UHAMISHO.
Mhe. Rais Magufuli amefanya uhamisho wa Wakuu wa Wilaya wawili ambapo aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Tarime Mkoani Mara Mhandisi Charles Kabeho amehamishwa kituo cha kazi na kuwa Mkuu wa Wilaya ya Chato Mkoani Geita, na aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Chato Mkoani Geita Mhandisi Mtemi Msafiri Simeoni amehamishwa kituo cha kazi na kuwa Mkuu wa Wilaya ya Tarime Mkoani Mara.
Mhe. Rais Magufuli amefanya uhamisho wa Naibu Makatibu Wakuu wawili ambapo aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Bw. Nicholaus Merinyo William Mkapa amehamishwa na kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, na aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Bw. Mathias Bazi Kabunduguru amehamishwa na kuwa Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, TAMISEMI (anayeshughulikia Elimu).
MABALOZI.
Mhe. Rais Magufuli amefanya uteuzi wa Mabalozi 12 watakaoiwakilisha Tanzania katika vituo vya Abu Dhabi (Falme za Kiarabu), Bujumbura (Burundi), Brussels (Ubelgiji), Cairo (Misri), Harare (Zimbabwe), Kuwait City (Kuwait), Pretoria (Afrika Kusini), Riyadh (Saudi Arabia), Tokyo (Japan), Umoja wa Mataifa - Geneva (Switzerland), Umoja wa Mataifa – New York (Marekani) na Abuja (Nigeria).
Walioteuliwa kuwa Mabalozi kwa ajili ya vituo hivyo ni Bw. Mohammed Mtonga (Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa Serikali Mstaafu), Bi. Jilly Elibariki Maleko (aliyekuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Mtwara), Dkt. Benson Alfred Bana (ambaye ni Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam), Meja Jenarali Mstaafu Anselm S. Bahati, Prof. Emmanuel D. Mbennah (ambaye ni Makamu Mkuu wa Chuo, Chuo Kikuu cha Mtakatifu John), Bi. Maimuna Tarishi (Katibu Mkuu Mstaafu), Meja Jenerali Mstaafu Gaudence Milanzi (Katibu Mkuu Mstaafu), Bw. Ali Jabir Mwadini (ambaye ni Kansela Mkuu, Ubalozi Mdogo wa Tanzania-Dubai), Dkt. Modestus Francis Kipilimba (Mkurugenzi Mkuu Mstaafu, Idara ya Usalama wa Taifa), Bw. Jestas Abuok Nyamanga (Mkurugenzi wa Ulaya na Amerika, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki), Prof. Kennedy Godfrey Gastorn (Katibu Mkuu wa Taasisi ya Kimataifa ya Ushauri wa Kisheria wa Asia na Afrika - Asian-African Legal Consultative Organization) yenye Makao Makuu New Delhi, India.
Tarehe ya kuapishwa kwa Mabalozi hao na vituo vyao vya kazi itatangazwa baada ya taratibu za kidiplomasia kukamilika.
Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli amewapandisha vyeo na kuwateua Maafisa 3 kuwa Mabalozi.
Wateule hao ni Bw. Stephen Patrick Mbundi ambaye ni Mkurugenzi wa Idara ya Ulinzi, Siasa na Usalama katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Ali Sakila Bujiku ambaye ni Msaidizi wa Rais na Dkt. Mussa Lulandala ambaye ni Msaidizi wa Rais.
Mabalozi Wateule hao wataendelea kutekeleza majukumu yao hapahapa nchini na wataapishwa Jumapili tarehe 22 Septemba, 2019 saa 9:00 alasiri Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
20 Septemba, 2019
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania katika nchi mbalimbali duniani wamempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kwa utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati ambayo inajengwa kwa fedha za Watanzania.
Mabalozi hao 43 ambao wapo hapa nchini tangu tarehe 13 Agosti, 2019 wametoa pongezi hizo leo tarehe 22 Agosti, 2019 walipokutana na kuzungumza na Mhe. Rais Magufuli Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Wametoa pongezi hizo baada ya kutembelea mradi wa ujenzi wa bwawa la Nyerere litakalozalisha megawati 2,115 katika mto Rufiji, mradi wa ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa (standard gauge railway) unaoanzia Dar es Salaam hadi Dodoma, jengo la 3 la abiria katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam Jijini Dar es Salaam, mradi wa ujenzi wa barabara za juu katika makutano ya barabara ya Morogoro na Sam Nujoma (Ubungo Interchange), mradi wa upanuzi wa bandari ya Dar es Salaam, mradi wa usambazaji wa gesi (Taifa Gas), mradi wa udhibiti wa mawasiliano Tanzania na mradi wa ujenzi wa daraja la Tanzanite (New Selander Bridge) katika bahari ya Hindi.
Kwa upande wa Zanzibar wametembelea mradi wa ujenzi wa jengo la biashara na makazi (shopping mall) eneo la Michenzani, mradi wa ujenzi wa jengo la 3 la abiria katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Sheikh Abeid Amani Karume, mradi wa ujenzi wa nyumba za kisasa wa Fumba Wilaya ya Magharibi, mradi wa ujenzi wa barabara ya Kaskazini - Bububu – Mkokotoni na mradi wa ujenzi wa bandari ya mafuta na gesi katika eneo la Manga Pwani.
Mabalozi hao wameeleza kuwa utekelezaji wa miradi hiyo pamoja na juhudi nyingine kubwa zinazofanywa na Serikali katika nyanja mbalimbali za huduma za jamii zimeleta heshima kwa nchi na machoni mwa Jumuiya ya Kimataifa, na kwamba zimedhihirisha kufikiwa kwa malengo ya Tanzania kuingia katika uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.
Pia wamempongeza kwa kuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kwa kipindi cha mwaka mmoja na wameahidi kuongoza vyema katika mikutano ya Mabalozi wa SADC katika nchi wanazowakilisha kwa kuzingatia mwelekeo ambao Mhe. Rais Magufuli ameutoa katika Mkutano wa 39 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC uliofanyika tarehe 17-18 Agosti, 2019 Jijini Dar es Salaam.
Akizungumza baada ya kuwasilikiza Mabalozi hao, Mhe. Rais Magufuli amewapongeza kwa kazi wanazozifanya katika nchi wanazoiwakilisha Tanzania na amewataka waendelee kutekeleza majukumu yao kizalendo na kwa kutanguliza maslahi ya Tanzania.
Pamoja na kueleza kuhusu hali ya uchumi wa nchi, juhudi za kuwapelekea maendeleo Watanzania na juhudi za kujenga uwezo wa kujitegemea, Mhe. Rais Magufuli amewataka Mabalozi hao kutafuta wawekezaji watakaowekeza katika miradi yenye manufaa hapa nchini.
“Nataka Mabalozi mtuletee miradi ya maendeleo, ifike mahali Balozi ujiulize kwa kuwa kwangu Balozi nimepeleka nini nyumbani? Nimewezesha kujengwa kiwanda? Kujengwa barabara? Kujenga daraja au jengo fulani?” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Mhe. Rais Magufuli amewasisitiza Mabalozi hao kuhakikisha wanasimamia na kufuatilia kwa karibu masuala wanayoamini yana manufaa kwa nchi ikiwemo uwekezaji na kwamba wasikubali kukwamishwa na viongozi ama wizara yoyote.
“Nataka muwe very aggressive, na ukiona mtu anakukwamisha mimi nipo niandikieni uone kama hatakwama yeye, mimi nataka kuona vitu sio maneno maneno” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Kuhusu changamoto mbalimbali walizomueleza, Mhe. Rais Magufuli ametoa wito kwa Mabalozi hao kuzishughulikia pale ambapo wao wenyewe wana uwezo na amemtaka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kufanyia kazi taarifa wanazopelekewa na Mabalozi hao kwa wakati.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
22 Agosti, 2019
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ametoa wito kwa Mataifa ya Afrika kutafsiri vizuri dhana ya uhuru na kujiepusha na masalia ya fikra za kikoloni za kuamini kuwa watawala wa zamani wa Mataifa ya Afrika ndio wenye uwezo wa kusaidia kusimamia na kuendeleza rasilimali zilipo katika Bara la Afrika.
Mhe. Rais Magufuli ametoa wito huo leo tarehe 29 Agosti, 2019 Ikulu Jijini Dar es Salaam alipohutubia Mkutano wa 6 wa Jukwaa la Uongozi Afrika unaohudhuriwa na Marais Wastaafu Mhe. Benjamin William Mkapa (Tanzania), Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete (Tanzania), Mhe. Thabo Mbeki (Afrika Kusini), Mhe. Hassan Mohamud (Somalia), Mhe. Hery Rajaonarimampianina (Madagascar), Mabalozi, Wawakilishi wa Kimataifa na washiriki wa Jukwaa la Uongozi Afrika.
Mhe. Rais Magufuli amefafanua kuwa dhana ya uhuru haiwezi kutenganishwa na kujitegemea kwani bila kujitegemea uhuru wa Taifa husika utakuwa mikononi mwa linayemtegemea.
“Maana hasa ya kupigania uhuru ilikuwa ni kurejesha rasilimali na hasa maliasili zetu lakini pia kuwa na maamuzi kamili kuhusu namna ya kuzisimamia na kuzitumia kwa manufaa yetu ili kuleta ukombozi wa kiuchumi, na hii ndio maana pekee ya kulinda uhuru wa kisiasa.
Tusijidanganye watawala wetu wa zamani hawawezi kugeuka kwa usiku mmoja na kuwa wajomba zetu au wakombozi wetu kiuchumi, utegemezi huu ndio umeimarisha mizizi na misingi ya ukoloni mamboleo, ni lazima tuamke” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Ametaja sababu ya 2 inayosababisha usimamizi mbaya wa rasilimali za Bara la Afrika kuwa ni tafsiri potofu ya msingi wa maendeleo kwa kudhani fedha ni msingi wa maendeleo hali iliyosababisha viongozi wake kuzunguka katika Mataifa tajiri kuomba misaada na mikopo ambayo inawezekana inatokana na rasilimali za Afrika, badala ya kuelekeza nguvu katika kusimamia na kutumia rasilimali zilizopo huku akisisitiza maneno ya Baba wa Taifa Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere aliyesema ili tuendelee tunahitaji watu, ardhi, siasa safi na uongozi bora.
Sababu nyingine ni ukosefu wa ubunifu na teknolojia ya viwanda ambavyo vitaongeza thamani ya bidhaa za Afrika na kuzalisha ajira, migogoro na hali tete ya kisiasa inayosababishwa na mabeberu wanaotaka kuendelea kutumia maliasili za Afrika kwa manufaa yao, watendaji na viongozi wa Afrika kuingia mikataba mibovu na wawekezaji bila kujali maslahi ya Afrika kutokana na kukosekana kwa uzalendo na uharibifu wa maliasili unaosababishwa na uharibifu wa mazingira na mabadiliko ya tabia nchi.
Mhe. Rais Magufuli amelipongeza Jukwaa la Uongozi Afrika kwa kuja na kauli mbiu isemayo “Kuimarisha Usimamizi Bora wa Maliasili kwa ajili ya Mageuzi ya Kijamii na Kiuchumi Afrika” na kubainisha kuwa kauli mbinu hiyo inaonesha umuhimu wa kujenga mifumo mipya ya kusimamia na kutumia rasilimali kwa manufaa ya watu wake.
Ametaja baadhi ya hatua zilizoanza kuchukuliwa na Tanzania katika kusimamia matumizi bora ya maliasili ili kufikia mageuzi ya kijani na kiuchumi kuwa ni kutunga sheria ya kulinda utajiri na rasilimali za Tanzania ya mwaka 2017, kupitia upya na kurekebisha mikataba ya uchimbaji wa madini isiyokuwa na manufaa kwa Taifa, kuweka msukumo mkubwa katika ujenzi wa viwanda na ukuzaji wa teknolojia ya viwanda na kudhibiti uharibifu wa maliasili za misitu na kulinda baionowai.
Hatua nyingine ni kutekeleza miradi mikubwa ya kuzalisha nishati ya umeme ukiwemo mradi mkubwa wa kujenga Bwawa la Nyerere katika mto Rufiji utakaozalisha megawati 2,115 za umeme, kuongeza maeneo ya uhifadhi kwa kuongeza Hifadhi za Taifa 3 mpya, kudhibiti nidhamu ya watumishi wa umma, kudhibiti ufisadi na ubadhirifu na kwamba matokeo ya hatua hizo yameanza kuonekana.
Washiriki wa mkutano huo unaofanyika kwa siku 2 wakiwemo Marais Wastaafu wameeleza umuhimu wa viongozi wa Afrika kutoa kipaumbele katika masuala muhimu yanayowahusu na kwa kushirikiana na kubadili mtazamo na fikra za utegemezi.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
29 Agosti, 2019
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 02 Septemba, 2019 amekutana na Watendaji takribani 3,800 wa Kata zote hapa nchini katika viwanja vya Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Katika Mkutano huo, Mhe. Rais Magufuli amesikiliza maoni, changamoto na ushauri kutoka kwa Watendaji Kata wa Mikoa yote hapa nchini na kutoa majibu na maelekezo mbalimbali kwa watendaji na viongozi wa Serikali.
Mhe. Rais Magufuli amewapongeza Watendaji wa Kata kwa kuiwakilisha vizuri Serikali katika Kata zao na amewahakikishia kuwa Serikali inatambua na inathamini uwepo wao na majukumu wanayoyatekeleza.
Amewaagiza viongozi wa Wilaya, Mikoa na Wizara kuhakikisha Watendaji wa Kata hawanyanyaswi wakati wakitekeleza majukumu yao ya kusimamia ulinzi na usalama, maendeleo ya wananchi na kutekeleza maelekezo mbalimbali ya Serikali na kwamba hatosita kuchukua hatua dhidi ya viongozi na watendaji wakiwemo Maafisa Utumishi na Wakurugenzi wenye tabia ya kufanya unyanyasaji huo.
Hata hivyo, Mhe. Rais Magufuli amewataka Watendaji wa Kata kutowanyanyasa wananchi hasa wanyonge, kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria na taratibu na kuhakikisha wanawatembelea wananchi ili kusikiliza na kutatua kero zao badala ya wananchi hao kusubiri mpaka watembelewe na viongozi wa Kitaifa.
Amewataka kufuatilia na kutoa taarifa juu ya miradi yote ya maendeleo inayotekelezwa katika Kata zao katika sekta mbalimbali zikiwemo elimu, afya, maji, barabara na miundombinu mingine pamoja na kusimamia vizuri ardhi.
“Usikubali mradi unatekelezwa kwenye kata yako wewe hujui, na usikubali mradi uhujumiwe kwenye kata yako na wewe upo, ukiona fedha zinachezewa toa taarifa, Mtendaji wa Kata ndio mwakilishi wa Rais kwenye Kata yako, wewe ndio bosi kwenye kata” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Mhe. Rais Magufuli amewataka Watendaji wa Kata kuhakikisha wanawasimamia watumishi wote wa Serikali katika Kata zao, kujiepusha na vitendo vya rushwa na kushirikiana kwa karibu na Watendaji wa Vijiji katika utekelezaji wa majukumu mbalimbali ya Serikali.
Katika michango yao, Watendaji wa Kata wamemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kuandika historia ya kuwaita kwa mara ya kwanza na kuzungumza nao katika Ikulu ya Dar es Salaam, na kwa uongozi mahiri wa Serikali ya Awamu ya Tano ambayo imejenga matumaini makubwa ya kujenga uchumi na kuimarisha hali ya maisha ya wananchi.
Watendaji wa Kata hao wamemuahidi Mhe. Rais Magufuli kuongeza juhudi na maarifa katika utekelezaji wa majukumu yao na kuhakikisha mipango ya Serikali hususani miradi ya maendeleo katika ngazi ya Kata inafanikiwa.
Pamoja na kutoa ushauri katika masuala mbalimbali wamemueleza changamoto mbalimbali wanazokutana nazo katika utumishi wao ambapo Mhe. Rais Magufuli ameahidi kuzishughulikia.
“Nimefurahi sana kuzungumza nanyi leo, kwa nilivyowasikia nina imani kubwa sana na nyinyi, nyinyi ni wapiganaji mnaotosha kuhakikisha nchi yetu inasonga mbele, nchi yetu inakwenda vizuri na kwa mambo tunayoyafanya lazima watakuwepo wa kutaka kuturudisha nyuma, nawaambia msijali tembeeni kifua mbele na kachapeni kazi” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Mkutano huo umehudhuriwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Kept. George Huruma Mkuchika, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Selemani Jafo, Katibu Mkuu Utumishi Dkt. Laurian Ndumbaro, Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Ikulu Dkt. Moses Kusiluka, Katibu Mkuu TAMISEMI Mhandisi Joseph Nyamuhanga na Naibu Katibu Mkuu Utumishi Dkt. Francis Michael.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
02 Septemba, 2019
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amemteua Prof. Fredrick Cassian Kahimba kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Uhandisi na Usanifu Mitambo Tanzania (TEMDO).
Taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi Mhe. Balozi John Kijazi imeeleza kuwa uteuzi wa Prof. Kahimba umeanza tarehe 31 Agosti, 2019.
Kabla ya uteuzi huo, Prof. Kahimba alikuwa Profesa Mshiriki na Naibu Makamu Mkuu wa Chuo (Utawala na Fedha), Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) Mkoani Morogoro.
Prof. Kahimba amechukua nafasi hiyo iliyokuwa wazi.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
02 Septemba, 2019
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amefungua mkutano wa mashauriano wa wadau wa sekta ya ujenzi hapa nchini na kuwahakikishia Wakandarasi, Wahandisi, Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi kuwa Serikali itaendelea kuchukua hatua madhubuti za kuwajengea uwezo wa kutekeleza miradi mingi na mikubwa hapa nchini.
Mkutano huo wa siku 2 umefunguliwa leo tarehe 04 Septemba, 2019 katika ukumbi wa Diamond Jubilee Jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na wajumbe 4,390 kutoka Bodi ya Usajili wa Wakandarasi (CRB), Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB), Bodi ya Usajili wa Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi (AQRB) na Wadau wa huduma za bidhaa za ujenzi chini ya kauli mbiu “Wajibu wa wadau wa sekta ya ujenzi katika kufikia uchumi wa viwanda endelevu kwa ustawi wa jamii”.
Katika hotuba yake, Mhe. Rais Magufuli amesema katika kutekeleza sheria inayotaka miradi yenye thamani ya chini ya shilingi Bilioni 10 kutolewa kwa Wakandarasi wa ndani, katika mwaka uliopita miradi 1,068 yenye thamani ya shilingi Bilioni 267.7 iliyotolewa na Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (TARURA) ilitekelezwa na Wakandarasi wa ndani na kwamba mwaka huu Serikali imetenga fedha nyingine shilingi Bilioni 278.13 kupitia TARURA ambazo miradi yake itatekelezwa na Wakandarasi wa ndani.
Amesema pamoja na kuwapa Wakandarasi wa ndani miradi mikubwa mfano ujenzi wa barabara ya lami ya Rudewa – Kilosa, Urambo – Kaliua na Kimara – Kibaha, Serikali imelipa madeni ya wakandarasi ambapo katika mwaka 2016/17 zimelipwa shilingi Bilioni 557 na mwaka 2017/18 zimelipwa shilingi Bilioni 833.65.
Ameongeza kuwa kampuni za Wakandarasi wa ndani zimeendelea kupata kipaumbele katika utekelezaji wa miradi ya maji ambapo katika mwaka uliopita zimepata miradi yenye thamani ya shilingi Bilioni 386.34 na kwa upande wa miradi ya nishati ya umeme zimepata miradi yenye thamani ya shilingi Bilioni 996.
“Tunafanya hivyo ili kuimarisha uwezo wa wataalamu wetu na kampuni za hapa nchini, na pia kwa lengo la kuhakikisha fedha zetu zinabaki nchini ili zisaidie kuimarisha uchumi wetu” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Hata hivyo, Mhe. Rais Magufuli amewakosoa Wakandarasi na Wahandisi hao kwa vitendo vyao vya kutoshirikiana katika utekelezaji wa majukumu na miradi, na ametoa wito kwao kujitafakari na kuchukua hatua zitakazosaidia kuondoa dosari hizo.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli amezitaka kampuni za ukandarasi kufanya kazi zao kwa kuzingatia sheria, taratibu na uadilifu wa taaluma yao ikiwemo kujiepusha na vitendo vya rushwa na upangaji wa gharama kubwa za miradi huku akitolea mfano wa uamuzi wa Serikali kujenga majengo yake bila kutumia wakandarasi ili kuokoa fedha nyingi.
“Serikali imejenga vituo vya afya 352 kwa shilingi Bilioni 184, endapo ujenzi huo ungefanywa na Wakandarasi tungetumia shilingi Trilioni 1, ujenzi wa darasa 1 umetumia shilingi Milioni 20 lakini tungetumia Wakandarasi tungejenga kwa shilingi Milioni 50 hadi 60, halikadhalika ujenzi wa bweni bila Wakandarasi umegharimu shilingi Milioni 75 tena likiwa na fenicha lakini tungetumia Wakandarasi tungetumia shilingi Milioni 170, sasa kwa gharama kubwa kama hizi ni lazima mjitathmini na mjirekebishe” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Mhe. Rais Magufuli amewataka Wakandarasi hao kuacha kulalamika na badala yake kutumia fursa ya uwepo wa miradi mbalimbali inayotekelezwa hapa nchi kuomba kazi na kuzifanya vizuri na amewahakikishia kuwa changamoto mbalimbali ambazo wameomba zitatuliwe, Serikali itazifanyia kazi.
Ametoa wito kwa taasisi za elimu kuongeza fursa za mafunzo kwa Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi ambao amesema idadi yao ni ndogo (chini ya 2,000) ikilinganishwa na idadi ya Watanzania zaidi ya Milioni 50 huku akiwataka Watanzania kuwatumia wataalamu hao katika ujenzi badala ya kujenga holela.
Wenyeviti wa Bodi za CRB, ERB, AQRB pamoja na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu wamempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa namna anavyotilia mkazo ujenzi wa miundombinu mikubwa ambayo ni nguzo muhimu ya uchumi hasa tunapoelekea katika uchumi wa kati unaotegemea viwanda na wameahidi kumuunga mkono katika jitihada hizo.
Baada ya ufunguzi wa mkutano huo Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe ametoa tangazo rasmi la Serikali kuwa Ndege ya Tanzania aina ya Airbus 220-300 iliyokuwa ikishikiliwa nchini Afrika Kusini kwa agizo la Mahakama imeachiwa.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
04 Septemba, 2019
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ametangaza siku 3 za maombolezo ya Kitaifa kufuatia kifo cha Rais Mstaafu na Baba wa Taifa la Zimbabwe Ndg. Robert Gabriel Mugabe kilichotokea leo tarehe 06 Septemba, 2019 nchini Singapore alikokuwa akipatiwa matibabu.
Katika siku 3 za maombolezo zinazoanzia leo 06 Septemba, 2019 hadi 08 Septemba, 2019 bendera zitapepea nusu mlingoti.
Leo asubuhi, Mhe. Rais Magufuli ambaye ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) amemtumia salamu za rambirambi Rais wa Jamhuri ya Zimbabwe Mhe. Emmerson Mnangagwa, familia ya Mzee Robert Gabriel Mugabe, wananchi wa Zimbabwe, Waafrika na wote walioguswa na musiba huu.
Katika salamu hizo Mhe. Rais Magufuli amesema “Nimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo cha Rais Mstaafu na Baba wa Taifa la Zimbabwe Mzee Robert Gabriel Mugabe. Afrika imepoteza mmoja wa viongozi jasiri, shupavu, mwanamajumui wa Afrika (Pan-Africanist) na aliyekataa ukoloni kwa vitendo, Mungu aiweke roho yake mahali pema peponi, Amina.”
Mhe. Rais Magufuli ameongeza kuwa Hayati Robert Gabriel Mugabe aliipenda Tanzania, alijenga uhusiano na ushirikiano wa karibu, kidugu na kirafiki na Tanzania tangu enzi za uongozi wa Baba wa Taifa la Tanzania Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere na kwamba Afrika itamkumbuka kwa jinsi alivyoshirikiana na viongozi mbalimbali kupinga ukoloni na ukandamizaji wa haki za Waafrika.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
06 Septemba, 2019
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli na Rais wa Jamhuri ya Uganda, Mhe. Yoweri Kaguta Museveni wamehutubia Kongamano la Kwanza la Wafanyabiashara wa Tanzania na Uganda lililofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam na kusisitiza umuhimu wa wafanyabiashara hao kuongeza biashara baina ya nchi hizo.
Kongamano hilo limehudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Mawaziri, Makatibu Wakuu, Mabalozi na Wafanyabiashara takribani 2,000 wa Tanzania na Uganda na limeambatana na maonesho ya bidhaa na huduma.
Katika hotuba yake, Mhe. Rais Magufuli amewataka Wafanyabiashara wa Tanzania na Uganda pamoja na wadau wengine wakiwemo viongozi kujiuliza kwa nini biashara kati ya Tanzania na Uganda ni ndogo wakati nchi hizi majirani zinazo fursa nyingi na kubwa za kufanya biashara na kukuza uchumi.
Amefafanua kuwa licha ya biashara kati ya nchi hizo kuongezeka kutoka shilingi Bilioni 116.7 mwaka 2017 hadi kufikia shilingi Bilioni 388.5 mwaka 2018 bado wafanyabiashara wa nchi hizo wanapaswa kuongeza zaidi na ametoa wito kwa watendaji na viongozi wa pande zote mbili kuondoa vikwazo ambavyo vinakwamisha biashara.
Mhe. Rais Magufuli ametaja baadhi ya juhudi zilizofanywa na Tanzania katika kuboresha mazingira ya biashara kati ya Tanzania na Uganda kuwa ni kuboresha miundombinu ya usafirishaji ambayo ni barabara, reli na kivuko, kujenga kituo cha pamoja cha huduma za mpakani (One Stop Border Post), kupunguza vizuizi vya barabarani hadi kufikia vitatu, kuimarisha usafiri wa anga na kuimarisha kituo cha uwekezaji Tanzania (TIC).
Amewaagiza Mawaziri na watendaji wa Serikali kushughulikia malalamiko ambayo yanatolewa na Serikali badala ya kuyaacha yakiathiri ustawi wa biashara.
Kuhusu ujenzi wa bomba la mafuta la kuanzia Hoima nchini Uganda hadi Bandari ya Tanga nchini Tanzania, Mhe. Rais Magufuli amesema yeye na Mhe. Rais Museveni wamekubaliana kuwa mradi huo utatekelezwa na amewashangaa watendaji wanaokwamisha kuanza kwa ujenzi.
Amewataka wataalamu wanaoshiriki majadiliano ya uwekezaji katika mradi huo kutanguliza maslahi ya wananchi kwa kuacha kung’ang’ania masharti ambayo hayazingatii manufaa mapana ya mradi huo.
“Idadi ya watu watakaopata ajira katika mradi huu ni zaidi ya 20,000, sisi viongozi ni lazima tutengeneze ajira kwa watu wetu, kwa hiyo bomba hili halitakiwi kucheleweshwa, haijalishi kwamba kuna sababu za wawekezaji ni lazima tuwezeshe mradi huu kutekelezwa” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Mhe. Rais Magufuli ametoa wito kwa wafanyabiashara wa Uganda wenye nia ya kufanya biashara na kuwekeza nchini Tanzania kuja wakati wowote na ametaja baadhi ya fursa zilizopo kuwa ni pamoja na ununuzi wa kahawa, madini na kujenga viwanda.
Kwa upande wake, Mhe. Rais Museveni amesema biashara ndogo kati ya Tanzania na Uganda inasababishwa na uelewa mdogo wa baadhi ya watu ambao hawajui kama biashara huleta ustawi wa jamii na Taifa.
Mhe. Rais Museveni ametoa wito kwa wananchi wa Tanzania na Uganda kuongeza uzalishaji wa bidhaa mbalimbali ili bidhaa hizo ziweze kuuzwa na kununuliwa baina ya nchi hizo sanjali na kuimarisha matumizi ya teknolojia ya kisasa katika uzalishaji.
Amewakaribisha wafanyabiashara kwenda kuwekeza na kufanya biashara nchini Uganda lakini amesema Serikali yake haitapokea uwekezaji wa gharama kubwa katika miradi ya umeme, reli na benki za maendeleo kwa kuwa maeneo hayo yanapaswa kuwekezwa kwa gharama ambazo wananchi watamudu.
Mhe. Rais Museveni amempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa (standard gauge railway-SGR) kwani utasaidia usafirishaji wa mizigo ya kwenda Uganda na nchi nyingine za Burundi, Rwanda na Kongo Mashariki kwa gharama nafuu.
Kuhusu mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta, Mhe. Rais Museveni amesema mradi huo utatekelezwa.
Mhe. Rais Magufuli ambaye ameongozana na Mkewe Mama Janeth Magufuli na Mhe. Rais Museveni ambaye ameongozana na Mkewe Mama Janeth Museveni wametembelea mabanda ya maonesho na kushuhudia bidhaa na huduma zitolewazo na kampuni na mashirika ya Tanzania na Uganda.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
06 Septemba, 2019
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli na Rais wa Jamhuri ya Uganda, Mhe. Yoweri Kaguta Museveni leo tarehe 06 Septemba, 2019 wamefungua jengo la Taasisi ya Mwalimu Nyerere lililopo Posta Jijini Dar es Salaam.
Jengo hilo lenye ghorofa 29 lina ofisi za Taasisi ya Mwalimu Nyerere zinazojumuisha chuo na maktaba itakayokuwa na machapisho mbalimbali ya Baba wa Taifa Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere na kitega uchumi cha hoteli ya nyota tano yenye vyumba 256.
Ujenzi wa jengo hilo lenye ukubwa wa eneo la mita za mraba 63,000 umegharimu Dola za Marekani Milioni 150 sawa na takribani shilingi Bilioni 341.7 zilizotolewa kwa mkopo kutoka kampuni ya China Railway Construction Engineering Group (CRJE) na Benki ya Dunia kupitia shirika la fedha la kimataifa (IFC).
Akizungumza baada ya ufunguzi, Mhe. Rais Magufuli ameipongeza Taasisi ya Mwalimu Nyerere kwa kufanikisha kujengwa kwa jengo hilo na pia amewashukuru wadau wote waliofanikisha mradi huo wakiwemo kampuni ya CRJE na IFC.
Pamoja na kufurahishwa na mradi huo, Mhe. Rais Magufuli amemuelezea Hayati Mwl. Nyerere kuwa alichukia kuona watu wakionewa hasa wanyonge, alipenda umoja na mshikamano na alikuwa na sifa ya kujiamini, kujitegemea na kutokubali kuingiliwa na Taifa jingine, hivyo ametoa wito kwa viongozi na wananchi kumuenzi Baba wa Taifa kwa kufuata nyayo zake.
Ameahidi kuwa Serikali itashirikiana na Taasisi ya Mwalimu Nyerere katika utekelezaji wa majukumu yake kama yalivyoasisiwa na Hayati Mwl. Nyerere mwenyewe na amesisitiza kuwa Tanzania haitaruhusu mambo yake kuamliwa na Taifa jingine.
Mhe. Rais Magufuli ameelezea kusikitishwa na tabia za baadhi ya watu (tena wa ndani ya nchi) ambao wamekuwa wakibeza kazi nzuri zilizofanywa na Hayati Mwl. Nyerere na ameahidi kuendeleza maono na miradi ambayo alianzisha ama alitaka kuitekeleza ikiwemo mradi wa ujenzi wa bwawa la kuzalisha umeme katika mto Rufiji, ufufuaji wa shirika la ndege la taifa (ATCL) na ujenzi wa viwanda.
Kwa upande wake, Mhe. Rais Museveni pamoja na kuwashukuru wadau wote waliochangia ujenzi wa jengo hilo ameuelezea mchango wa Hayati Mwl. Nyerere katika ukombozi wa nchi nyingi za Afrika na kwamba hata yeye alikuwa mfuasi wake tangu mwaka 1963 na akajionea mchango wake mkubwa katika nchi mbalimbali ikiwa ni pamoja kumvurusha Idd Amin Dada aliyevamia Kagera mwaka 1978 na kupigania uhuru wa Afrika Kusini.
Mhe. Rais Museveni amesema Mwl. Nyerere ameacha somo kubwa la ushirikiano na hivyo amesisitiza umuhimu wa nchi za Afrika kushirikiana katika kustawisha uchumi na jamii.
Makamu mwenyekiti wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere Mhe. Jaji Mstaafu Joseph Sinde Warioba amemshukuru Mhe. Rais Museveni kwa mchango wake wa hali na mali katika kufanikisha ujenzi wa jengo hilo na kwa jinsi alivyo karibu na taasisi hiyo.
Amesema Mwl. Nyerere alianzisha taasisi hiyo ili ishirikiane na Serikali, taasisi mbalimbali na wananchi kwa ujumla kwa lengo la kuenzi misingi ya maisha na maendeleo ya watu wote, na pia ameishukuru Serikali kwa kuisaidia taasisi hiyo ikiwemo kutoa kiwanja lilipojengwa jengo hilo ambacho kina thamani ya shilingi Bilioni 11.4.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere Mzee Joseph Butiku amesema Mwl. Nyerere alitaka taasisi hiyo ijielekeze katika kudumisha, kuimarisha, kutetea na kuenzi ujumbe wa amani, umoja na maendeleo yenye tija kwa watu wote na yanayotokana na juhudi za watu wenyewe.
Amesisitiza malengo ya taasisi kuwa ni kufanya kazi ambazo Mwl. Nyerere mwenyewe alishirikiana na Watanzania wenzake na alikuwa akizifanya kipindi cha uongozi wake tangu alipoanzisha chama cha TANU na baada ya hapo alivyoshirikiana na viongozi wenzake wa Tanzania, Afrika na Dunia kwa ujumla katika jitihada za kulinda na kudumisha amani, umoja na maendeleo ya watu wote na hasa wanyonge.
Sherehe za ufunguzi wa jengo hilo zimehudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais Mstaafu Mhe. Benjamin William Mkapa, Rais Mstaafu Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Mke wa Rais Magufuli Mama Janeth Magufuli, Mke wa Rais Museveni Mama Janeth Museveni, Makamu wa Rais Mstaafu Mhe. Dkt. Mohammed Gharib Bilal, Mke wa Baba wa Taifa Mama Maria Nyerere, Mke wa Rais wa Kwanza wa Zanzibar Mama Fatma Karume, Mke wa Rais Mstaafu Kikwete Mama Salma Kikwete, Mawaziri, Makatibu Wakuu, Mabalozi, viongozi wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama, viongozi wa Dini, Viongozi wa Siasa na viongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
06 Septemba, 2019
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 10 Septemba, 2019 amemjulia hali Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam Mhashamu Yuda Thaddaeus Ruwa’ichi ambaye amelazwa katika Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI) Jijini Dar es Salaam.
Baba Askofu Mkuu Ruwa’ichi alipatwa na ugonjwa wa kiharusi juzi huko Moshi Mkoani Kilimanjaro ambako alianza kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Kilimanjaro (KCMC), na kisha kupelekwa MOI ambako amefanyiwa upasuaji wa kichwa na anaendelea na matibabu.
Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Ubongo na Mishipa ya Fahamu wa MOI Prof. Joseph Kahamba amesema baada ya kufanyiwa upasuaji huo hali ya Baba Askofu Ruwa’ichi imeanza kuimarika.
Mhe. Rais Magufuli pamoja na Madaktari na Wauguzi wa MOI wamemuombea Baba Askofu Ruwa’ichi ili apone haraka na kuendelea na majukumu yake ya kila siku.
Akiwa katika wodi hiyo ya wagonjwa mahututi, Mhe. Rais Magufuli amewajulia hali wagonjwa wengine waliofanyiwa upasuaji wa kichwa na kuelezea kufurahishwa na maendeleo makubwa yaliyopatikana katika taasisi ya MOI ambayo sasa inatoa matibabu ya upasuaji mkubwa ambayo hayakuwa yanapatikana hapa nchini.
Prof. Kahamba amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa Serikali kufanya uwekezaji mkubwa katika taasisi ya MOI katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita ikiwemo kukamilisha jengo, kuongeza vitanda vyote vinavyohitajika katika vyumba vya upasuaji na chumba cha wagonjwa mahututi (ICU), kununua vifaa vipya vya uchunguzi kama vile MRI, CT-Scan, Digital x-ray, Ultrasound na sasa mipango inaendelea kununua kifaa kiitwacho Endovascular Neurosuite ambacho kinagharimu shilingi Bilioni 7.5 hali iliyoiwezesha MOI kufikia viwango vya kimataifa.
Mhe. Rais Magufuli amewapongeza Madaktari na Wauguzi wa MOI kwa kazi kubwa wanayoifanya na ameahidi kutoa shilingi Bilioni 1.5 kwa taasisi hiyo kwa ajili ya kununulia vipandikizi kwa ajili ya wagonjwa wanaopatiwa matibabu baada ya kuvunjika.
Mkurugenzi Mtendaji wa MOI Dkt. Respecious Boniface amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kutoa fedha hizo na kumhakikisha kuwa zitasaidia katika matibabu ya Watanzania wengi.
Akiwa njiani kurejea Ikulu, Mhe. Rais Magufuli ametembelea Kituo cha Polisi cha Selander Bridge na kuzungumza na Askari wa Kituo hicho ambapo ameagiza WP 4160 Beatrice Kayuni Mlanzi kupandishwa cheo kutoka Koplo na kuwa Sajenti baada ya kuonesha utimilifu katika kazi.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
10 Septemba, 2019
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amemteua Dkt. John Stanslaus Ndunguru kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Ardhini (LATRA).
Taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi Mhe. Balozi John Kijazi imeeleza kuwa uteuzi wa Dkt. Ndunguru umeanza tarehe 09 Septemba, 2019.
Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli amemteua Prof. Antony Manoni Mshandete kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA).
Prof. Mshandete ni Naibu Makamu Mkuu wa Chuo (Taaluma, Utafiti na Ubunifu), Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela (NM-AIST) kilichopo Mkoani Arusha.
Uteuzi huu umeanza tarehe 09 Septemba, 2019.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
11 Septemba, 2019
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amemteua na kumuapisha Kamishna Diwani Athuman Msuya kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa.
Uteuzi wa Kamishna Diwani Athuman Msuya umeanza leo tarehe 12 Septemba, 2019 na ameapishwa leo Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Kabla ya uteuzi huo, Kamishna Diwani Athuman Msuya alikuwa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).
Akizungumza baada ya kumuapisha, Mhe. Rais Magufuli amemtaka Kamishna Diwani Athuman Msuya kuchapa kazi kwa juhudi na maarifa na kwa kuweka mbele maslahi ya Taifa.
Kamishna Diwani Athuman Msuya anachukua nafasi ya Dkt. Modestus Kipilimba ambaye atapangiwa kazi nyingine.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
12 Septemba
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amefungua maonesho ya 4 ya wiki ya viwanda ya Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) na kuhimiza nchi wanachama kutilia mkazo utekelezaji wa Mkakati wa SADC wa Maendeleo ya Viwanda wa kuanzia mwaka 2015 – 2063.
Ufunguzi huo umefanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Mawaziri na Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu Wakuu, Mabalozi, Wabunge, Sekretarieti ya SADC, viongozi kutoka sekta binafsi na washiriki wa maonesho ya viwanda kutoka nchi mbalimbali.
Mhe. Rais Magufuli ambaye amengozana na Mkewe Mama Janeth Magufuli amesema pamoja na kuwepo kwa Mkakati wa SADC wa Maendeleo ya Viwanda bado kasi ya ukuaji wa viwanda ni ndogo na hivyo kusababisha viwanda kuendelea kutoa mchango mdogo katika maendeleo ya kiuchumi kwa nchi za SADC.
Amebainisha kuwa nchi za SADC zimeendelea kuwa wazalishaji wa malighafi na nguvu kazi kwa ajili ya mataifa mengine huku zenyewe zikiwa waagizaji wa bidhaa za viwandani kutoka nje ilihali zikipangiwa bei ya kuuza na kununua bidhaa hizo, hali inayodidimiza wakulima na kurudisha nyuma juhudi za kupata maendeleo ya kiuchumi.
Mhe. Rais Magufuli ameongeza kuwa kutokana na kutokuwa na viwanda urari wa biashara kati ya Afrika na mabara mengine umekuwa sio mzuri na ametolea mfano wa mwaka 2017 ambapo thamani ya biashara kati ya Afrika na Umoja wa Ulaya ilikuwa ni shilingi Trilioni 708 (Euro Bilioni 280) ambapo Afrika ilinunua bidhaa za shilingi Trilioni 376.7 (Euro Bilioni 149) na ikauza bidhaa za shilingi Trilioni 331 (Euro Bilioni 131), lakini asilimia 60 ya bidhaa ilizouza zilikuwa ghafi na hivyo kuwa na thamani ndogo.
“Hii inathibitisha kwamba sisi Afrika tunazalisha bidhaa ambazo hatuzitumii na tunatumia bidhaa ambazo hatuzizalishi, ni lazima tubadilishe mwelekeo huu ili tuzalishe bidhaa ghafi, tuzisindike au kutengeneza viwandani na tuzitumie” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Ili kuepukana na changamoto hii inayosababisha upotevu wa fedha za kigeni, Mhe. Rais Magufuli ametoa wito kwa nchi za SADC kutekeleza kwa vitendo nguzo 3 za Mkakati wa SADC wa Maendeleo ya Viwanda ambazo ni kuhimiza maendeleo ya viwanda kama kichocheo cha mageuzi ya kiuchumi na kiteknolojia, kuongeza ushindani wa bidhaa za viwandani na kutumia mtangamano wa kikanda na jiografia yetu (yenye watu takribani Milioni 350) kwa maendeleo ya viwanda na uchumi.
Mhe. Rais Magufuli ametoa wito kwa nchi za SADC kuweka kipaumbele katika uhawilishaji wa teknolojia ya viwanda vya ndani ya Jumuiya na ndani ya Afrika pamoja na kuuziana malighafi na bidhaa zingine miongoni mwa nchi wanachama ili kukuza mitaji na kuendeleza viwanda vya ndani ya SADC na Afrika nzima, kukuza na kuendeleza ubunifu wa watu wa Afrika pamoja na kuhamasisha matumizi ya teknolojia rahisi na kujenga mazingira wezeshi kwa ajili ya kukuza sekta ya viwanda.
Maeneo mengine ni kuondoa vikwazo vyote vinavyochelewesha maendeleo ya sekta ya viwanda na kuhimiza sekta binafsi kuchangamkia fursa za kuwekeza katika viwanda badala ya kubaki ikilalamikia changamoto inazokumbana nazo.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli ameeleza juhudi mbalimbali zilizofanywa na Tanzania katika kuendeleza viwanda kuwa ni pamoja na kuongeza uzalishaji wa umeme ikiwemo mradi mkubwa wa kuzalisha megawati 2,115 katika mto Rufiji, kujenga miundombinu ya reli, barabara, bandari, viwanja vya ndege na kuhamasisha ujenzi wa viwanda ambapo kati ya mwaka 2015 na sasa viwanda zaidi ya 4,000 vimejengwa.
Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Innocent Bashungwa, Katibu Mtendaji wa SADC Dkt. Stergomena Tax na Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF) Bw. Salum Shamte wamempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa jitihada kubwa za kujenga mazingira wezeshi ya ujenzi wa viwanda hapa nchini, na wametoa wito kwa nchi zote za SADC kutilia mkazo uboreshaji wa mazingira wezeshi na wadau mbalimbali kujitokeza kuwekeza katika viwanda.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
05 Agosti, 2019
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amepokea kwa mshtuko na masikitiko makubwa taarifa ya vifo vya watu zaidi ya 60 na majeruhi takribani 70 walioungua kwa moto baada ya lori lililokuwa na shehena ya mafuta kupata ajali na kisha kulipuka moto Mjini Morogoro.
Ajali hiyo imetokea leo tarehe 10 Agosti, 2019 majira ya saa 2 asubuhi ambapo lori hilo lililokuwa linatoka Dar es Salaam limepinduka jirani na Kituo Kikuu cha Mabasi cha Msamvu baada ya dereva wa lori kumkwepa mwendesha pikipiki na kisha mafuta yaliyokuwa yakimwagika kushika moto na kuunguza watu waliokuwa wanayachota.
Mhe. Rais Magufuli ametoa pole kwa familia, ndugu, marafiki na wote waliopoteza jamaa zao katika ajali hii na pia amewaombea majeruhi wapone haraka.
“Nimeumia sana kusikia idadi kubwa ya Watanzania wenzetu waliopoteza maisha katika ajali hii, natoa pole kwa wote walioguswa na vifo hivi hasa familia za Marehemu wote, nawaombea Marehemu wapumzike mahali pema peponi na majeruhi wote wapone haraka” amesema Mhe. Rais Magufuli na kumuagiza Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Kebwe Steven Kebwe kufikisha salamu zake za pole kwa familia na wote walioguswa na vifo hivyo.
Mhe. Rais Magufuli ameagiza Wizara zote zinazohusika kushughulikia ajali hii na ametaka Hospitali ya Mkoa wa Morogoro kwa kushirikiana na Hospitali ya Taifa Muhimbili kuhakikisha majeruhi wote wanapatiwa matibabu ili kuokoa Maisha yao.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli ameelezea kusikitishwa kwake na vitendo vya watu kuvamia magari yanayopata ajali kwa lengo la kujipatia bidhaa mbalimbali zilizobebwa na magari hayo na ametaka vitendo hivyo vikome.
“Baadhi ya magari haya yanabeba mafuta ambayo ni hatari kama ilivyotokea Morogoro, yapo magari yanabeba kemikali za sumu, yapo magari yanabeba milipuko nakadhalika, nawaomba sana tuache tabia hii” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
10 Agosti, 2019
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ametangaza siku 3 za Maombolezo ya Kitaifa kuanzia leo Jumamosi tarehe 10 Agosti, 2019 kufuatia vifo vya watu zaidi ya 60 vilivyosababishwa na ajali ya kuungua kwa moto wakati wakichota mafuta yaliyokuwa yakimwagika baada ya lori la mafuta kupinduka Mjini Morogoro.
Ajali hiyo imetokea leo majira ya saa 2 asubuhi ambapo lori lenye shehena ya mafuta ya petroli limepinduka jirani na Kituo Kikuu cha Mabasi cha Msamvu Mjini Morogoro wakati dereva alipokuwa akijaribu kumkwepa mwendesha pikipiki.
Pamoja na zaidi ya watu 60 kufariki dunia watu wengine takribani 70 wamejeruhiwa na wanapatiwa matibabu katika hospitali ya Mkoa wa Morogoro na Hospitali ya Taifa Muhimbili Jijini Dar es Salaam.
Mhe. Rais Magufuli amemtuma Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa kumwakilisha katika mazishi ya Marehemu wa ajali hiyo yanayotarajiwa kuanza kesho Jumapili tarehe 11 Agosti, 2019.
Katika kipindi cha maombolezo bendera zote zitapeperushwa nusu mlingoti.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
10 Agosti, 2019