Taarifa kwa vyombo vya Habari ya zamani
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 22 Desemba, 2019 ameungana na waumini wa Kanisa Katoliki Parokia ya Bikira Maria Chato Mkoani Geita kusali Dominika ya 4 ya Majilio na ametumia nafasi hiyo kuwatakia heri ya Krismasi na Mwaka Mpya Watanzania wote.
Katika salamu hizo, Mhe. Rais Magufuli amesema tunapoelekea katika sikukuu ya Krismasi na Mwaka Mpya Wakristo na Waumini wa madhehebu mengine mbalimbali wanalo jukumu la kuendelea kuombea amani, upendo na umoja kwa wanadamu wote bila kubaguana.
“Niwaombe ndugu zangu wa Chato na Watanzania kwa ujumla, tusherehekee sikukuu ya Krismasi kwa amani na upendo mkubwa, lakini pia tuukaribishe Mwaka Mpya kwa amani na upendo mkubwa wa Kristo, mwaka unaokuja uwe mwaka wa mafanikio, uwe mwaka wa maendeleo, uwe mwaka wa kujenga umoja wetu kwa Watanzania wote, uwe mwaka wa amani na upendo na uwe mwaka wa kuendeleza Taifa letu katika maendeleo ya kweli” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli amewapongeza Waumini wa Parokia ya Bikira Maria Chato kwa kazi kubwa ya upanuzi wa Kanisa wanayoendelea nayo ambayo naye alichangia upanuzi wake mwaka 2016.
Misa Takatifu hiyo imeongozwa na Paroko wa Parokia hiyo Padre Henry Mulinganisa.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Chato
22 Desemba 2019
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, tarehe 18 Desemba, 2019 amefungua Mahakama ya Wilaya ya Chato, ameweka mawe ya msingi ya jengo Jeshi la Zimamoto la Wilaya ya Chato na Msikiti, na amefungua madarasa na mradi wa maji katika Shule ya Msingi Chato ambayo alisoma elimu yake ya msingi.
Jengo la Mahakama ya Wilaya ya Chato lililogharimu shilingi Milioni 913 ni moja ya Majengo 26 ya Mahakama Kuu, Mahakama za Hakimu Mkazi wa Mkoa, Mahakama za Wilaya na Mahakama za Mwanzo zilizojengwa katika maeneo mbalimbali hapa nchini ikiwa ni utekelezaji wa Mpango wa Miaka 5 wa Mahakama ya Tanzania ulioanza 2016/17 hadi 2020/21 ambao umelenga kuboresha miundombinu ya mahakama kwa kukarabati, kumalizia na kujenga majengo mapya.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa Serikali ya Awamu ya Tano kutoa shilingi Bilioni 40.8 zilizofanikisha utekelezaji wa miradi 55 ya ujenzi inayojumuisha miradi 12 iliyokuwa imekwama, 29 iliyojengwa na kukamilika na 14 inayoendelea kujengwa, na ameeleza kuwa huo ni uthibitisho wa dhamira yake ya kweli ya kuhakikisha Mahakama inapata majengo ya kisasa ili kutimiza jukumu lake la kikatiba la utoaji wa haki.
Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amebainisha kuwa kwa sasa Mahakama ya Tanzania inajiandaa kuanza ujenzi wa Makao yake Makuu Jijini Dodoma, kujenga majengo jumuishi (majengo yatakayojumuisha huduma za Mahakama Kuu, Mahakama za Hakimu Mkazi, Mahakama ya Wilaya na Ofisi za Wadau) na kujenga majengo mengine 33 ya Mahakama za Wilaya na Mahakama za Mwanzo, miradi yote ikiwa inagharamiwa na Serikali ya Tanzania.
Jengo la Zimamoto Wilaya ya Chato ambalo ujenzi wake umefikia asilimia 60 kwa gharama ya shilingi Milioni 713.6 linatarajiwa kukamilika Februari 2020 kwa gharama ya jumla ya shilingi Milioni 943, kiasi ambacho ni kidogo ikilinganishwa na endapo lingejengwa kwa utaratibu wa zabuni za wakandarasi ambapo ungegharimu shilingi Bilioni 1.6.
Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Thobias Andengenye amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa Serikali ya Awamu ya Tano kutoa shilingi Bilioni 108.743 ambazo zimesaidia kulipa madeni makubwa ya wazabuni, watumishi na mishahara hali iliyoamsha morali na ari ya kazi kwa wafanyakazi.
Amesema katika kipindi cha miaka minne jeshi hilo limepata mafanikio makubwa ikiwemo kujenga jengo la Makao Makuu Dodoma kwa shilingi Bilioni 2.656, kupata magari ya zimamoto 18, magari ya uokoaji 3, gari 1 la wagonjwa na boti 1, kuwapandisha vyeo Maafisa na Askari 683, kukusanya maduhuli ya Serikali kiasi cha shilingi Bilioni 73.264 na kushiriki kikamilifu katika matukio ya moto 5,367 na matukio 2,060 ya uokoaji.
Msikiti (Masjid Al Huda) ambao ujenzi wake utakamilika Desemba 2020 kwa ghamara ya shilingi Bilioni 1.6 ukiwa na uwezo wa kuchukua waumini 3,000 watakaoingia ndani na 6,000 wakaokuwa nje, unajengwa kwa ufadhili wa Taasisi ya Al Hikma baada ya kuombwa na Mhe. Rais Magufuli kufanya hivyo kwa ajili ya Waislamu wa Chato.
Rais wa Taasisi ya Al Hikma Sheikh Shareef Abdulqadir Al – Ahdal amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa upendo wake kwa Watanzania wa Madhehebu yote ya Dini na ameahidi kuwa Tasisi hiyo itaendelea kushirikiana na Serikali katika masuala mbalimbali ya kutoa huduma kwa jamii.
Jengo la madarasa 3 na ofisi 2 za walimu limejengwa katika Shule ya Msingi Chato ikiwa ni mchango wa Mhe. Rais Magufuli kwa shule hiyo ambayo alisoma kati ya mwaka 1967 na 1974 na mradi wa kisima cha maji katika shule hiyo ni kati ya visima 8 vilivyochimbwa Wilayani Chato na Taasisi ya Kiislamu chini ya ufadhili wa Rais wa Falme za Kiarabu (UAE) kwa gharama ya shilingi Milioni 340.3.
Akizungumza na wananchi wa Chato waliojitokeza katika ziara hiyo, Mhe. Rais Magufuli amempongeza Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma kwa hatua kubwa za maendeleo ya Mahakama na ameahidi kuwa Serikali itaendelea kutekeleza dhamira yake ya kuhakikisha inaimarisha Mahakama ili itende vyema jukumu lake la kutoa haki kwa Watanzania wote.
Amesema katika miaka minne ya uongozi wake Serikali imeongeza Majaji wa Mahakama ya Rufani 11, Majaji wa Mahakama Kuu 39 na Mahakimu 396 na hivyo kuongeza idadi ya watumishi hao kutoka 700 hadi kufikia 938.
Hata hivyo ametoa wito kwa vyombo vyote vinavyohusika kuendelea kutekeleza mpango wa kupunguza mrundikano wa wafungwa na mahabusu magerezani na amempongeza Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) Mhe. Biswalo Mganga na vyombo washirika kwa kuwaachia mahabusu 751 katika Mikoa 3 baada ya kubaini kuwa walikuwa na makosa madogo madogo ama kubambikizwa kesi.
Mhe. Rais Magufuli amelipongeza Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kwa mafanikio makubwa lililoanza kuyapata ikiwemo kujenga majengo mazuri kwa gharama nafuu, kuanza kuunda magari ya zimamoto hapahapa nchini kwa kushirikiana na Shirika la Nyumbu, kushiriki katika matukio ya uzimajimoto na uokoaji na ameahidi kuwa Serikali itaendelea kuliimarisha jeshi hilo.
Mhe. Rais Magufuli ameishukuru Taasisi ya Kiislamu (Islamic Foundation) na Rais wa UAE Mtukufu Khalifa bin Zayed Al Nahyan kwa kufadhili mradi wa maji wa visima 8 kikiwemo cha shule ya Msingi Chato na Taasisi Al Hikma kwa kukubali ombi lake la kujenga Msikiti wa Wilaya ya Chato, na ameahidi kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na madhehebu yote ya Dini katika kutoa huduma kwa jamii.
Waziri wa Maji Mhe. Prof. Makame Mbarawa amesema pamoja na kuwepo wadau mbalimbali wa maendeleo wanaosaidia juhudi za kukabiliana na changamoto za upatikanaji wa maji hapa nchini, Serikali ya Awamu ya Tano imechukua hatua madhubuti za kukabiliana na changamoto hizo ambapo hivi sasa inatekeleza miradi 350 ya maji yenye thamani ya shilingi Trilioni 3.5 na tayari upatikanaji wa maji kwa Watanzania umepanda kutoka wastani wa asilimia 56 hadi kufikia asilimia 71.
Mhe. Rais Magufuli amewataka Watanzania kutunza miundombinu ya maji inayojengwa na Serikali na wadau mbalimbali kote nchini badala ya kuiba vipuri na mitambo kama walivyofanya miaka ya nyuma, na pia amewataka Watanzania wanaoathiriwa na maji ya mvua zinazonyesha baada ya kujenga katika mikondo ya maji kutoilaumu Serikali kwa kuwa madhara yanayowapata yanasababishwa na wao wenyewe kuziba njia za maji.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli amerejea kauli yake kuwa hatarajii kuongeza hata siku moja baada ya kumaliza kipindi chake cha uongozi kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na amesisitiza kuwa mafanikio yanayopatikana sasa yanatokana na baraka za Mwenyezi Mungu ambaye atabariki kupatikana kwa kiongozi mwingine atakayefanya vizuri.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Chato
18 Desemba, 2019
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 09 Desemba, 2019 ameungana na Watanzania wote katika maadhimisho ya miaka 58 ya Uhuru wa Tanzania Bara yaliyofanyika kwa mara ya kwanza katika uwanja wa CCM Kirumba Jijini Mwanza.
Sherehe za maadhimisho hayo zimehudhuriwa na maelfu ya wananchi na viongozi mbalimbali wakiwemo Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Ali Mohamed Shein, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Balozi Seif Ali Idd, Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job Yustino Ndugai, Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Mhe. Zubeir Ali Maulid na Jaji Mkuu wa Zanzibar Mhe. Omar Othman Makungu.
Viongozi wengine ni Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili Mhe. Dkt. Ali Hassan Mwinyi, Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu Mhe. Benjamin William Mkapa, Mawaziri Wakuu Wastaafu, Mawaziri, Mabalozi wa nchi mbalimbali, viongozi wakuu wa vyombo vya Ulinzi na Usalama, Wabunge, viongozi wa Dini, viongozi wa vyama vya siasa na viongozi wa taasisi mbalimbali.
Sherehe za maadhimisho hayo zimepambwa kwa gwaride rasmi lililoandaliwa na Majeshi ya Ulinzi na Usalama, maonesho ya ndege vita, helkopta, zimamoto na burudani za kwaya, ngoma za asili, dansi na Bongofleva.
Katika hotuba yake, Mhe. Rais Magufuli amewapongeza Watanzania wote kwa kuadhimisha miaka 58 ya tangu Tanzania Bara ipate Uhuru na amewashukuru waasisi wa Taifa wakiongozwa na Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere kwa juhudi kubwa walizozifanya kupigania uhuru kupitia chama cha TANU na hatimaye uhuru kupatikana tarehe 09 Desemba, 1961.
Mhe. Rais Magufuli amesema Watanzania wana kila sababu ya kujipongeza kwa kuendelea kudumisha amani, umoja na mshikamano katika kipindi chote cha miaka 58 na amewapongeza Marais wa awamu zote nne zilizotangulia kwa kuiongoza Tanzania kwa mafanikio.
Ameyataja baadhi ya mafanikio ambayo Tanzania imeyapata baada ya Uhuru kuwa ni kuongezeka kwa barabara za lami kutoka kilometa 1,360 hadi kilometa 12,679.55 ilihali nyingine zaidi ya 2,000 zikiwa katika ujenzi, kuongezeka kwa vituo vya tiba (Hospitali, Vituo vya Afya na Zahanati) kutoka 1,098 hadi 7,293, kuongezeka kwa Shule za Msingi kutoka 3,100 hadi 17,379 na kuongezeka kwa Shule za Sekondari kutoka 41 hadi kufikia 4,817.
Maendeleo mengine ni kuongezeka kwa Vyuo Vikuu kutoka 1 hadi kufikia 48, Madaktari waliosajiliwa kutoka 403 (Watanganyika wakiwa 12) hadi kufikia 9,400, Wahandisi kutoka 2 hadi 19,164, Wakandarasi kutoka 2 hadi kufikia 9,350 na pia wastani wa umri wa mtu kuishi kuongezeka kutoka miaka 37 hadi kufikia miaka 61.
Mhe. Rais Magufuli amesema katika kusukuma mbele gurudumu la maendeleo Serikali ya Awamu ya Tano anayoiongoza imedhamiria kuimarisha zaidi uchumi kwa kujenga viwanda ambavyo kwa miaka minne vimejengwa zaidi ya 4,000, kuimarisha miundombinu kwa kufufua reli na kujenga reli ya kisasa (standard gauge), kujenga barabara, kupanua na kuboresha bandari, kujenga na kukarabati meli 5, kununua ndege 11, kujenga viwanja vya ndege 11, kujenga Bwawa la Nyerere litakalozalisha megawati 2,115 za umeme, kusambaza umeme katika vijiji vyote vya Tanzania, kuongeza Hifadhi za Taifa, kuinua uvuvi na kuimarisha usimamizi wa maliasili hasa madini.
Amewashukuru Watanzania wote na wadau mbalimbali wa maendeleo kwa kuiunga mkono Serikali katika juhudi hizi na ameahidi kuwa Serikali itaendelea kuhakikisha uchumi wa Tanzania unakuwa, huduma za kijamii zinaboreshwa na Watanzania wananufaika na rasilimali za nchi yao.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli ameeleza kusikitishwa na kuwepo kwa idadi kubwa ya Wafungwa 17,547 na Mahabusu 18,256 waliopo Magerezani na hivyo ameamua kutoa msamaha kwa idadi kubwa ya wafungwa 5,533 ambao wanapaswa kuachiwa huru kuanzia kesho tarehe 10 Desemba, 2019.
Ameipongeza Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) na Mahakama kwa kuwaachia huru Mahabusu 601 waliokuwa wakikabiliwa na kesi za uhujumu uchumi baada ya kutekeleza masharti ya msamaha alioutoa na ametaka wasirudie kufanya makosa.
Kabla ya kumaliza hotuba yake, Mhe. Rais Magufuli amemkaribisha Rais wa Zanzibar, Marais Wastaafu, Mawaziri Wakuu Wastaafu na viongozi wa vyama vya siasa kuwasalimu Watanzania ambapo wamesisitiza umuhimu wa kudumisha amani, umoja na mshikamano, kumuunga mkono Mhe. Rais Magufuli na Serikali anayoiongoza, kuchapa kazi na wamempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa uongozi mzuri na mafanikio makubwa ya kiuchumi yaliyopatikana kwa kipindi kifupi cha miaka minne ya uongozi wake.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Mwanza
09 Desemba, 2019
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 08 Desemba, 2019 ameungana na Waumini wa Parokia ya Epiphania Bugando Jijini Mwanza kusali Misa Takatifu ya Dominika ya 2 ya Majilio iliyoongozwa na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Mwanza Mhashamu Renatus Nkwande.
Katika mahubiri yake, Baba Askofu Mkuu Nkwande amesema sawia na kipindi hiki cha Majilio ambapo Wakristo wanakumbushwa kufanya toba na kufanya matendo mema, Watanzania wanapaswa kujitafakari juu ya matendo yao na kuachana na matendo yamchukizayo Mwenyezi Mungu yakiwemo mauaji, wizi na ubinafsi.
Baba Askofu Mkuu Nkwande amesema inasikitisha kusikia wapo baadhi ya Watanzania wanaoiba na kujilimbikizia mali, ilihali Watanzania wenzao wanapata taabu kwa ukosefu wa huduma za kijamii kutokana na rasilimali nyingi kukumbatiwa na watu wachache.
Amemuombea Mhe. Rais Magufuli na viongozi wote Serikali kuendelea kutekeleza majukumu yao vizuri kama ambavyo wameanza, na amempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa kuhimiza watu kufanya kazi, kuwa waadilifu na kuacha wizi.
“Mhe. Rais jipe moyo, endelea na kazi hiyo kwa sababu Watanzania tunafurahia unachokifanya na tunakuunga mkono” amesema Baba Askofu Mkuu Nkwande.
Katika salamu zake, Mhe. Rais Magufuli ambaye alisali katika Kanisa hilo kwa mara ya mwisho mwaka 1978 akiwa kidato cha nne, amemshukuru Baba Askofu Nkwande kwa mahubiri mazuri yanayohimiza kuepuka dhambi na kutenda yaliyo mema na amewataka Watanzania kuzingatia ujumbe huo.
Mhe. Rais Magufuli ambaye ameongozana na Mkewe Mama Janeth Magufuli amechangia shilingi Milioni 5 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba ya Padre wa Parokia hiyo na ameongoza harambee iliyofanikisha kupatikana kwa shilingi 12,650,000/= kwa ajili ya ujenzi huo.
Baadaye leo Mhe. Rais Magufuli ataweka jiwe la msingi mradi wa ujenzi wa meli na chelezo katika Ziwa Victoria hapa Jijini Mwanza.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Mwanza
08 Desemba, 2019
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 07 Desemba, 2019 ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa daraja la Kigongo – Busisi lenye urefu wa kilometa 3.2 na upana wa mita 28.45 ambalo litakalounganisha mawasiliano ya barabara kati ya Mikoa ya Mwanza na Geita kukatiza Ziwa Victoria.
Sherehe za uwekaji jiwe la msingi zimefanyika katika eneo la Kigongo, Wilaya ya Misungwi Mkoani Mwanza na kuhudhuriwa na wananchi na viongozi mbalimbali wakiwemo Spika wa Bunge Mhe. Job Yustino Ndugai, Mawaziri na Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu Wakuu, viongozi wakuu wa vyombo vya Ulinzi na Usalama, Wakuu wa Mikoa ya Mwanza, Geita na Kagera, Wabunge, viongozi wa taasisi mbalimbali, viongozi wa Dini na viongozi wa vyama vya siasa.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mhandisi Patrick Mfugale amesema ujenzi wa daraja hilo pamoja na barabara unganishi zenye urefu wa kilometa 1.66 umepangwa kukamilika mwezi Julai 2023 kwa gharama ya jumla ya shilingi Bilioni 699, fedha zote zinatolewa na Serikali ya Tanzania.
Daraja hilo refu kuliko yote Afrika Mashariki, na la 6 kwa urefu Barani Afrika litakuwa mbadala wa vivuko vya MV Misungwi, MV Sengerema na MV Mwanza, na litajengwa kwa teknolojia ya madaraja marefu inayoitwa Extra Dosed Bridge ambapo litajengwa juu ya nguzo 67 zikiwemo nguzo 3 zenye urefu wa meta 40 na umbali wa meta 160 kutoka nguzo moja hadi nyingine.
Mhandisi Mfugale amebainisha kuwa daraja hilo linalojengwa na wakandarasi China Civil Engineering Construction Corporation na China Railway 15 Group Corporation litaondoa adha ya usafiri wa wananchi, mizigo na magari ambayo kwa sasa huvushwa kwa vivuko, na kwamba baada ya ujenzi idadi ya magari yanayovuka kwa siku inatarajiwa kuongezeka kutoka 1,600 hadi 10,200 kwa siku na muda kuvuka utapungua kutoka saa 2:30 hadi dakika 4.
Akizungumza katika sherehe hizo, Mhe. Rais Magufuli amewapongeza wananchi wa Kanda ya Ziwa hususani Mikoa ya Mwanza na Geita kwa ujenzi wa daraja hilo ambalo litakuwa utatuzi wa kero ya miaka mingi, iliyosababisha vifo kutokana na ajali za majini na wagonjwa kucheleweshwa hospitali, kuchelewa kwa biashara na safari za wananchi, na kwamba kukamilika kwake kutakuwa chachu ya kukua kwa uchumi wa kanda hiyo na Tanzania kwa ujumla.
Mhe. Rais Magufuli ambaye ameongozana na Mkewe Mama Janeth Magufuli amesema kuanza kwa ujenzi wa daraja hilo ni uthibitisho kuwa Tanzania sio masikini na kwamba tukiamua tunaweza, hivyo ametoa wito kwa Watanzania wote kutembea kifua mbele kwa kuwa daraja hilo litaharakisha biashara kati ya Tanzania na nchi jirani za Rwanda, Burundi, Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Amewataka wakandarasi wanaojenga daraja hilo kufanya kazi usiku na mchana ili waweze kumaliza ujenzi kabla ya muda uliopangwa kwa kuwa Watanzania wanalihitaji daraja hilo haraka, na ametoa wito kwa wananchi wa Mwanza na Geita kujitokeza kupata ajira katika kazi za ujenzi, kuuza bidhaa mbalimbali vikiwemo vyakula na amewakumbusha Watanzania wote kuendelea kulipa kodi kwa kuwa mradi huo pamoja na miradi mingine ya ujenzi wa reli, barabara, majengo, maji, afya na umeme inatekelezwa kwa fedha za Watanzania wenyewe.
Mhe. Rais Magufuli amempongeza Mtendaji Mkuu wa TANROADS Mhandisi Patrick Mfugale kwa mchango wake mkubwa wa kusanifu madaraja makubwa, madaraja madogo na barabara, jukumu ambalo anaendelea nalo kwa kushirikiana na Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Aloyce Kamwelwe amesema pamoja na ujenzi wa daraja la Kigongo - Busisi, Serikali imejenga madaraja makubwa 77 na madaraja madogo 8,020 na kwamba ujenzi wa madaraja mengine makubwa 6 unaendelea ambayo ni Wami (Pwani), Magara (Manyara), Sukuma (Mwanza), Kitengule (Kagera), Msingi (Singida), Ruhuhu (Ruvuma) na Selander (Dar es Salaam).
Spika wa Bunge, Mhe. Job Yustino Ndugai amempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa Serikali ya Awamu ya Tano kuandika historia nyingine kubwa ya kujenga daraja refu kuliko yote Afrika Mashariki na ameahidi kuwa Bunge litaendelea kuunga mkono juhudi hizo kwa kupitisha fedha za ujenzi wa mradi huo na miradi mingine ya maendeleo katika bajeti ya Serikali.
Kesho tarehe 08 Desemba, 2019 Mhe. Rais Magufuli ataendelea na ziara yake hapa Mkoani Mwanza kwa kuweka jiwe la msingi la mradi wa ujenzi wa meli na chelezo katika ziwa Victoria.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Mwanza
07 Desemba, 2019
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amewataka viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chato Mkoani Geita kuanza mara moja upanuzi wa majengo ya Hospitali ya Wilaya ya Chato kwa kuwa Serikali imeshatoa shilingi Bilioni 1 kwa ajili ya ujenzi huo.
Mhe. Rais Magufuli ambaye hakufurahishwa na taarifa za viongozi wa halmashauri hiyo kupoteza muda mwingi wakibishana juu ya upanuzi huo licha ya fedha za ujenzi kutolewa tangu mwezi Julai 2019, ameonya kuwa Serikali haiwezi kuvumilia kuona watu wakipata shida kwa uzembe wa viongozi wachache wa Halmashauri.
Amemuagiza Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe. Selemani Jafo na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chato Bw. Eliud Mwaiteleke kuhakikisha ujenzi wa majengo hayo unafanyika na kwa gharama zinazostahili.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli amemtaka Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo Dkt. Ligobeth Kalisa kuhakikisha mashine ya x-ray inafanya kazi muda wote na wananchi wanapatiwa huduma kwa wakati. Amesisitiza kuwa “sio sawa kwa Hospitali ya Wilaya kukosa huduma za x-ray, eti kwa sababu ya hakuna mikanda ya kupigia picha”.
Mhe. Rais Magufuli ametoa maagizo hayo leo tarehe 06 Desemba, 2019 aliwatembelea na kuwapa pole wagonjwa waliolazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Chato akiwemo Mzee Zephania Petro Kanoge ambaye ndiye aliyemhamasisha kuingia katika siasa mwaka 1995.
Mzee Kanoge na mwenzake marehemu Constantine Misungwi walimfuata Mhe. Rais Magufuli mara mbili Jijini Mwanza alikokuwa akifanya kazi katika Chama Kikuu cha Ushirika cha Nyanza wakimtaka agombee Ubunge, licha ya kukataa wazee hao waling’anga’ania hadi alipokubali na wakabeba jukumu la kumfanyia kampeni kwa kutumia pikipiki hadi aliposhinda Uchaguzi Mkuu.
Mhe. Rais Magufuli amemshukuru Mzee Kanoge kwa mchango wake mkubwa katika Maisha yake ya siasa na amemuombea apone haraka ili aweze kurejea nyumbani na kuungana na familia yake.
Akiwa hospitalini hapo, Mhe. Rais Magufuli amewaona wagonjwa wengine pamoja na wanawake na watoto waliofika kupata chanjo ambapo amewahakikishia kuwa Serikali imeanza kuchukua hatua madhubuti za kuboresha huduma za afya ikiwemo ujenzi wa vituo vya afya na hospitali mpya kote nchini, na kuongeza bajeti ya dawa kutoka shilingi Bilioni 31 hadi kufikia shilingi Bilioni 270.
Mhe. Rais Magufuli pia amekwenda eneo la Ginnery ambako ametoa pole kwa familia ya Mzee Mariganya Nghwenge aliyefariki dunia juzi tarehe 04 Desemba, 2019. Mzee Marigana anakumbukwa kwa ukulima wake hodari ambapo mwaka 1967 alizalisha mihogo mingi ukiwemo mhogo mkubwa alioutumia kumuonesha Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere alipotembelea Chato na kuzungumza na wananchi.
Mjini Chato, Mhe. Rais Magufuli amewasalimu wananchi waliokuwa wamesimama kando mwa barabara, na waliokuwa wakiendelea na biashara zao madukani ambapo wananchi hao wamemuombea, wamempongeza kwa uongozi madhubuti ulioonesha mabadiliko makubwa katika kipindi kifupi na wamemtakia heri katika majukumu yake.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Chato
06 Desemba, 2019
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ametoa shilingi Bilioni 10 kwa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kwa ajili ya kuanza ujenzi wa Makao Makuu ya Ulinzi wa Taifa katika eneo la Kikombo Jijini Dodoma.
Mhe. Rais Magufuli ametoa fedha hizo leo tarehe 25 Novemba, 2019 baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa mradi huo na ameagiza milima yote inayozunguka eneo la Makao Makuu ya Ulinzi wa Taifa lenye ukubwa wa ekari 5,567 imilikiwe na JWTZ kwa ajili ya shughuli za ulinzi.
Kuhusu madai ya fidia, Mhe. Rais Magufuli amemuagiza Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma Bw. Godwin Kunambi kuwalipa fidia ya shilingi Bilioni 3 na Milioni 339 wananchi 1,500 wa Kata ya Kikombo ambao ardhi yao imechukuliwa na JWTZ kwa ajili ya Makao Makuu ya Ulinzi wa Taifa, kuanzia tarehe 01 Desemba, 2019.
Pamoja na agizo hilo, Mhe. Rais Magufuli amewatahadharisha wananchi wa Kikombo kujiepusha na matapeli wanaowahamasisha kudai fidia wasiyostahili kwa mujibu wa sheria ama kudai ardhi isiyo yao.
Mhe. Rais Magufuli pia ameiagiza Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kujenga kwa kiwango cha lami kilometa 18 za barabara inayounganisha Makao Makuu ya Ulinzi wa Taifa na barabara kuu ya Dodoma – Morogoro.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli amekubali ombi la Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jen. Venance Salvatory Mabeyo aliyeomba Serikali ibebeba jukumu la kulipa deni la takribani shilingi Trilioni 1 ambalo JWTZ inadaiwa baada ya kujengewa nyumba 6,064 za makazi ya Askari katika maeneo mbalimbali nchini, badala ya Askari kukatwa posho zao ili kupata fedha za kulipia deni hilo kama ilivyowekwa katika mkataba wa ujenzi.
“Nakuhakikishia hakuna kukatwa Askari yeyote, hilo deni litabebwa na Serikali, kabla sijaja hapa nimeshamwelekeza Waziri wa Fedha na Katibu Mkuu, na nafikiri kesho au keshokutwa wataanza kulipia hilo deni ambalo limeanza kuiva, tutaanza kulipa Dola za Marekani zaidi ya Milioni 25 (sawa na shilingi Bilioni 56 na Milioni 948). Mkataba ni kweli ulikosewa, nafikiri ilikuwa ni mwaka 2012/13 lakini siwezi kukubali makosa ya namna hiyo yakafanyika katika kipindi changu” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli amewapongeza Maafisa na Askari wa JWTZ kwa kazi nzuri ya kulinda mipaka ya nchi na kushiriki katika operesheni za kulinda amani katika Mataifa mbalimbali, majukumu ambayo yamelijengea heshima jeshi hilo na Tanzania.
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jen. Venance Salvatory Mabeyo wamemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa maelekezo yake ya kujengwa Makao Makuu ya Ulinzi wa Taifa katika eneo la Kikombo ambayo yanajengwa na jeshi lenyewe.
Mapema kabla ya kuweka jiwe la msingi la mradi huo, Mhe. Rais Magufuli ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa uwanja wa maadhimisho ya kitaifa katika eneo la Chamwino.
Ujenzi wa uwanja huo utakamilika Januari 2020 ukiwa na uwezo wa kuchukua watu 5,000 kwa gharama ya shilingi Bilioni 2, na awamu ya pili itahusisha ujenzi wa ukumbi wa mikutano, jengo la watu mashuhuri na jengo la kupumzikia watu.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Chamwino
25 Novemba, 2019
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 24 Novemba, 2019 amepokea kiasi cha shilingi Trilioni 1.05 zinazotokana na gawio na michango kutoka taasisi, mashirika ya umma na kampuni ambazo Serikali ina hisa.
Hafla ya kupokea gawio na michango hiyo imefanyika Ikulu ya Chamwino Mkoani Dodoma na kuhudhuriwa na Mke wa Rais Mama Janeth Magufuli, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job Yustino Ndugai, Mawaziri na Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu Wakuu, Viongozi Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama, Mabalozi, Kamati ya Bunge ya Uwekezaji Mitaji ya Umma (PIC), viongozi wa Dini na viongozi wa Mkoa wa Dodoma wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa Dkt. Binilith Mahenge.
Katika taarifa yake Msajili wa Hazina Bw. Athuman Mbuttuka amesema fedha za gawio na michango iliyowasilishwa leo kwa Mhe. Rais Magufuli ni ya mwaka wa fedha wa 2018/19 na imetoka katika taasisi, mashirika ya umma na kampuni 79 kati ya taasisi, mashirika ya umma na kampuni zote 266 ambazo Serikali imewekeza mitaji, na kwamba kiasi hicho kimeongezeka kutoka shilingi Bilioni 161.04 zilizokusanywa katika mwaka 2014/15.
Bw. Mbuttuka amebainisha kuwa mafanikio ya kuongezeka kwa makusanyo hayo yametokana na juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano za kuhakikisha taasisi, mashirika ya umma na kampuni ambazo Serikali ina hisa zinaendeshwa kwa tija na kuzalisha gawio, ambapo idadi ya taasisi, mashirika ya umma na kampuni zinazotoa gawio na michango zimeongezeka kutoka 24 mwaka 2014/15 hadi kufikia 79 mwaka 2018/19.
Amebainisha kuwa maelekezo ya Mhe. Rais Magufuli pia yamesaidia kuongeza hisa za Serikali katika kampuni ya Airtel kutoka 40 hadi 49, kuongeza hisa za kampuni UDART hadi asilimia 85, kurudisha umiliki wa hisa kwa asilimia 25 katika kampuni ya MECO kutoka asilimia 2, na majadiliano yanaendelea kwa kampuni nyingine.
Bw. Mbuttuka ameongeza kutokana na maelekezo ya Mhe. Rais Magufuli, Wizara ya Fedha kwa kushirikiana na ofisi yake zimenusuru mali za Serikali zilizokuwa hatarini kutoweka ambapo katika mikoa 10 iliyopitiwa, Serikali imetambua mali 531 na kufanikiwa kurejesha Serikalini majengo 337, viwanja 140, mashamba makubwa 10, maghala 41 na mali zingine 3 pamoja na kurejesha umiliki wa asilimia 100 katika kampuni ya Songwe Water Company Ltd na asilimia 40 kwa kampuni ya Liquid Storage Company Ltd.
Akizungumza baada ya kupokea gawio, Mhe. Rais Magufuli amezipongeza taasisi, mashirika ya umma na kampuni 79 zilizotoa gawio na michango kwa Serikali na ametoa siku 60 kwa taasisi, mashirika ya umma na kampuni 187 ambazo hazikutoa gawio na michango, kutoa gawio na michango hiyo vinginevyo bodi zake zitavunjwa na uteuzi wa watendaji wakuu kutenguliwa.
Mhe. Rais Magufuli amefafanua kuwa Serikali imewekeza mitaji ya kiasi cha shilingi Trilioni 59.6 katika taasisi, mashirika ya umma na kampuni 266 ikitarajiwa kuwa zitaendeshwa kwa tija badala ya kuwa tegemezi kwa Serikali ama kuendeshwa kwa hasara.
Amemuagiza Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango kuhakikisha taasisi, mashirika ya umma na kampuni hizo 187 zinawasilisha gawio lake ndani ya muda huo vinginevyo achukue hatua.
Mhe. Rais Magufuli ameeleza kuwa utendaji kazi wa taasisi hizo ni moja kati ya vyanzo muhimu vinavyopaswa kuchangia katika maendeleo ya nchini ikiwemo miradi mikubwa inayotekelezwa nchini, na amerejea kauli yake kuwa kutokana na fursa zilizopo hapa nchini zikiwemo maji, ardhi, madini, gesi, mifugo na nguvu kazi, hakuna sababu ya Watanzania kujiona masikini.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli amesema pamoja na kuongezeka kwa gawio na michango kutoka taasisi hizo bado makusanyo kutoka vyanzo vya kikodi na visivyo vya kikodi hayatoshi na hivyo ametoa wito kwa taasisi hizo pamoja na wadau wengine kuongeza juhudi katika uzalishaji na ukusanyaji wa kodi.
Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango ameahidi kufanyia kazi maelekezo ya Mhe. Rais Magufuli huku akibainisha kuwa kwa sasa bajeti ya Serikali inategemea mapato ya ndani kwa asilimia 70 na amesisitiza kuwa uchumi wa Tanzania utajengwa na Watanzania wenyewe.
Kesho tarehe 25 Novemba, 2019 Mhe. Rais Magufuli ataweka jiwe la msingi la ujenzi wa uwanja wa maadhimisho ya kitaifa Ikulu Chamwino, ataweka jiwe la msingi la mradi wa ujenzi wa Makao Makuu ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ) katika eneo la Kikombo, ataweka jiwe la msingi mradi wa ujenzi wa jengo la Bodi ya Usajili wa Wakandarasi (CRB) na ataweka jiwe la msingi katika mradi wa ujenzi wa Ofisi ya Makao Makuu ya Idara ya Uhamiaji Jijini Dodoma.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Chamwino
24 Novemba, 2019
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 24 Novemba, 2019 ameungana na Waumini wa Kanisa Katoliki Parokia ya Mtakatifu Maria Imakulata, Chamwino – Ikulu Mkoani Dodoma, kusali Misa Takatifu ya Dominika ya mwisho ya mwaka C, ambayo ni sherehe ya Bwana Yesu Kristo.
Misa Takatifu imeongozwa na Paroko wa Parokia hiyo Padre Laurent Lelo.
Akiwasalimu Waumini wenzake kabla ya Misa hiyo kuisha, Mhe. Rais Magufuli amewashukuru kwa kumpokea baada ya kuhamia Chamwino Mkoani Dodoma na amewashauri Waumini wenzake kupanua Kanisa la Mtakatifu Maria Imakulata kwa kuwa anaamini baada ya Ofisi ya Rais Ikulu kuhamia Chamwino idadi ya Waumini itaongeza na Kanisa lililopo halitatosha.
Pamoja na ushauri huo ameendesha harambee ya kuchangisha fedha kwa ajili ya upanuzi wa Kanisa ambapo amefanikiwa kukusanya shilingi 20,265,000/- ikiwemo shilingi 10,000,000 aliyochangia yeye mwenyewe na shilingi 1,000,000 aliyochangia Mkewe Mama Janeth Magufuli.
Mhe. Rais Magufuli ambaye pia amechangia shilingi Milioni 2 kwa kwaya ya kanisa hilo, pia ameahidi kuwachangia Waislamu wa Chamwino kwa kuwa anaamini nako idadi ya waumini itaongezeka.
Mhe. Rais Magufuli amewatakia heri Watanzania wote ambao leo wanapiga kura za kuwachagua viongozi wa Serikali za Mitaa na ameeleza kuwa yeye hakupiga kura kwa sababu katika Kijiji cha Chamwino ambako alijiandikisha, mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) amepita bila kupingwa na hivyo uchaguzi haukuwepo.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Chamwino
24 Novemba, 2019
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 23 Novemba, 2019 amemuagiza Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini IGP – Simon Sirro kumsimamisha kazi Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Shinyanga ACP – Richard Abwao na Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa wa Shinyanga SSP - John Rwamlema kufuatia tuhuma za utovu wa nidhamu na kuhusika katika uhujumu uchumi zinazowakabili.
Halikadhalika, Mhe. Rais Magufuli amemuagiza Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Dkt. Edwin Mhede kumsimamisha kazi Meneja wa TRA Mkoa wa Shinyanga Bw. Jumbe Lazarous Samson kutokana na tuhuma za kuhusika katika uhujumu uchumi.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli amemuagiza Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa kufanya uchunguzi wa kina juu ya tuhuma zinazowakabili viongozi hao.
Wakati huo huo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kesho tarehe 24 Novemba, 2019 atapokea gawio, michango na ziada ya Serikali kutoka mashirika, kampuni na taasisi mbalimbali ambazo zinamilikiwa na Serikali.
Hafla ya kupokea gawio, michango na ziada hiyo itafanyika Ikulu ya Chamwino Mkoani Dodoma kuanzia saa 4:00 asubuhi na kurushwa moja kwa moja na vyombo vya habari vya Redio, Televisheni na Mitandao ikiwemo youtube channel ya Ikulumawasiliano.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Chamwino
23 Novemba, 2019
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt John Pombe Magufuli tarehe 22 Novemba 2019 ameweka mawe ya msingi katika miradi minne ya ujenzi wa majengo ya Serikali Mkoani Dodoma.
Majengo yaliyowekwa mawe ya msingi ni Hopsitali ya Uhuru inayojengwa katika eneo la Maduka Wilayani Chamwino, nyumba 118 za makazi ya Askari Polisi, Soko Kuu na Kituo Kikuu cha Mabasi cha Dodoma vinavyojengwa katika eneo la Nzuguni Jijini Dodoma.
Ujenzi wa jengo la Hospitali ya Uhuru utakamilika Aprili 2020 kwa gharama ya shilingi Bilioni 3.9 ambapo Mhe. Rais Magufuli amempongeza Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Selemani Jafo kwa kukabidhi kazi ya ujenzi wa hospitali hiyo kwa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) baada ya kutoridhishwa na kasi ndogo ya Wakala wa Majengo Tanzania (TBA).
Ujenzi wa nyumba 88 zilizopo Dodoma ambazo ni kati ya nyumba 118 za makazi ya Askari Polisi utakamilika Desemba 31, 2019 kwa gharama ya shilingi Bilioni 2 na Milioni 728, ambapo Mhe. Rais Magufuli amewahakikishia Askari Polisi kuwa Serikali itaendelea kuboresha mazingira yao ya kazi kwa kuwa anatambua kazi kubwa na nzuri inayofanywa na jeshi hilo pamoja na vyombo vingine vya ulinzi na usalama katika kulinda amani, usalama wa raia na mali zao.
Akizungumza na Askari na wananchi waliojitokeza katika eneo la Nzuguni zinapojengwa nyumba hizo, Mhe. Rais Magufuli amesema kutokana na kazi nzuri inayofanywa na Jeshi la Polisi ameamua jengo la Wizara ya Maji na Umwagiliaji lililopangwa kutumiwa na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira (DUWASA) kukabidhiwa kwa Jeshi la Polisi kwa ajili ya makao makuu ya hilo.
Jengo hilo la ghorofa 4 lina vyumba 157, ukarabati wake umefikia asilimia 95 na Mhe. Rais Magufuli amemtaka Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini IGP Simon Sirro kuanza kulitumia wakati ukarabati ukikamilishwa.
Ujenzi wa Soko Kuu utakamilika Februari 2020 kwa gharama ya shilingi Bilioni 14.4 ambapo Mhe. Rais Magufuli pamoja na kuwapongeza viongozi wa Jiji la Dodoma amependekeza soko hilo liitwe Soko Kuu la Ndugai, ikiwa ni kutambua mchango wa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job Yustino Ndugai katika kuongoza Bunge la 11 linaloidhinisha bajeti ya utekelezaji wa miradi mingi ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Tano likiwemo soko hilo.
Ujenzi wa Kituo Kikuu cha Mabasi cha Dodoma utakamilika Februari 2020 kwa gharama ya shilingi Bilioni 24. Fedha hizo pamoja na za ujenzi wa Soko Kuu zimetolewa kwa mkopo kutoka Benki ya Dunia.
Kituo hiki kitakuwa na uwezo wa kuchukua mabasi 250, magari madogo 600, bajaji 150, bodaboda 250 na kutumiwa na watu 6,000 kwa mpigo, na pia kitaunganishwa kwa miundombinu ya reli inayoungana na reli ya kati, na reli ya kwenda uwanja wa ndege wa kimataifa wa Msalato ambao unaanza kujengwa kwa gharama ya shilingi Bilioni 500.
Akizungumza na wananchi mara baada ya kuweka jiwe la msingi la kituo hicho, Mhe. Rais Magufuli aliyeongozana na Mkewe Mama Janeth Magufuli amewashukuru wananchi wa Dodoma kwa kuwapokea wafanyakazi na viongozi mbalimbali akiwemo yeye mwenyewe, Makamu wa Rais na Waziri Mkuu ambao tayari wameshahamia Dodoma na pia amewapongeza kwa maendeleo ya kasi kubwa yanayofanyika Mkoani humo.
“Nafarijika kuona Serikali yote sasa imehamia Dodoma, huu ni uthibitisho kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kikiahidi kinatekeleza, niliahidi kuwa Serikali itahakikisha mandhari ya Dodoma yanaboreshwa na sasa mnaona nyinyi wenyewe, kila mahali panajengwa majengo mazuri, hata siku nilipotangaza Dodoma kuwa Jiji kuna watu walibeza lakini sasa wote ni mashahidi, Dodoma inapendeza” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Mhe. Rais Magufuli amesema pamoja na kujengwa kwa Soko Kuu na Kituo Kikuu cha Mabasi, Serikali inajenga miradi mingine mikubwa ikiwemo barabara za mzungumzo za njia 4 zenye urefu wa kilometa 110 kwa shilingi Bilioni 415, eneo la kuegeshea malori, dampo la taka, eneo la kupumzikia, uwanja wa ndege wa kimataifa wa Msalato na Hospitali ya Uhuru.
Ametoa wito kwa wananchi wa Dodoma kuchapa kazi, kuchangamkia fursa za maendeleo zinazokuja kutokana na kuhamia kwa Makao Makuu ya Serikali ikiwemo kuzalisha mazao mengi kwa ajili ya kuuza.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli amewatahadharisha wananchi dhidi ya matapeli wanaowadanganya ili waanzishe migogoro ya ardhi dhidi ya Serikali na ameonya kuwa watakaostahili kulipwa kwa mujibu wa sheria watalipwa na wasiostahili hawatalipwa.
Baada ya kuweka mawe ya msingi katika miradi hiyo, Mhe. Rais Magufuli amekabidhi jengo la DUWASA kwa Jeshi la Polisi Nchini kwa ajili ya Makao Makuu ya jeshi hilo na amekabidhi iliyokuwa Ofisi ya TAMISEMI iliyopo katikati ya Jiji la Dodoma kwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt. Binilith Mahenge kwa ajili ya kuwa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa. Ofisi za DUWASA na TAMISEMI zimehamishiwa katika eneo la Mji wa Serikali Mtumba.
Kesho tarehe 23 Novemba, 2019 Mhe. Rais Magufuli atawaapisha Mabalozi 4 aliowateua hivi karibuni, kuanzia saa 3:00 asubuhi katika Ikulu ya Chamwino, Dodoma.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Chamwino
22 Novemba, 2019
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 21 Novemba, 2019 ametunukiwa Shahada ya Heshima ya Udaktari wa Falsafa katika Sayansi (Doctor of Science Honoris Causa) ya Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).
Mhe. Rais Magufuli aliyeongozana na Mkewe Mama Janeth Magufuli ametunukiwa shahada hiyo na Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma Mhe. Benjamin William Mkapa (Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu) katika sherehe za mahafali ya 10 ya chuo hicho zilizofanyika katika ukumbi wa Chimwaga Jijini Dodoma.
Sherehe hizo zimehudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa aliyeongozana na Mkewe Mama Mary Majaliwa, Mawaziri, Wabunge, Mabalozi wa nchi mbalimbali, Viongozi Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama, Wakuu wa Mikoa, viongozi wa Dini, viongozi wa siasa na wasomi.
Wasifu wa Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli uliosomwa na Prof. Davis George Mwamfupe umeeleza kuwa Chuo Kikuu cha Dodoma kimeamua kumtunuku Shahada ya Heshima ya Udaktari wa Falsafa Mhe. Rais Magufuli kwa kutambua mchango wake mkubwa katika maendeleo ya Tanzania kwa kipindi kifupi cha miaka 4 ya uongozi wake kwenye sekta za elimu, nishati, miundombinu, uchukuzi, maji, mawasiliano, maliasili, utalii, afya, madini na kilimo.
UDOM imeeleza kuwa kazi kubwa iliyofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Mhe. Rais Magufuli katika kutekeleza Dira ya Maendeleo ya 2025 inayoelekeza Tanzania kuingia katika uchumi wa kati imefanywa kwa mafanikio makubwa na imetaja baadhi ya maeneo ya mafanikio kuwa ni utoaji wa elimu bila malipo kwa shule za msingi na sekondari, kujenga miundombinu na kuongeza mikopo ya wanafunzi wa vyuo vikuu, kuongeza uzalishaji wa nishati ya umeme na kuanza ujenzi wa Bwawa la Nyerere, kujenga barabara, reli ya kisasa (SGR), bandari na viwanja vya ndege.
Maeneo mengine ni kuongeza upatikanaji wa maji ambapo hadi Februari 2019 miradi 65 ya maji iliyowanufaisha Watanzania Milioni 25.36 imetekelezwa, kuunganisha Zanzibar na mkongo wa Taifa na kuweka mfumo wa kusimamia mawasiliano (TTMS), kununua ndege 11 kwa ajili ya kuimarisha usafiri wa anga na kukuza utalii, kudhibiti ujangili, kuboresha sekta ya afya (kwa kujenga hospitali 69, vituo vya 352, kuongeza bajeti ya dawa kutoka Shilingi Bilioni 31 hadi Bilioni 270 na kununua vifaa tiba), kusimama na kuongeza mapato ya madini na kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula hali iliyoweza kuwepo chakula cha kutosha na cha ziada.
Akizungumza baada ya kutunukiwa shahada hiyo, Mhe. Rais Magufuli amekishukuru Chuo Kikuu cha Dodoma kwa kumtunuku shahada hiyo na amebainisha kuwa awali haikuwa rahisi kwake kukubali kutunukiwa shahada ya Udaktari wa Falsafa pasipo kuisomea darasani, lakini baadaye alikubali kwa kuwa anaamini shahada hiyo imetolewa kwa kutambua kazi kubwa iliyofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi wake.
“Kutokana na maisha niliyokulia sikuwahi kuzoea vitu vya burebure (dezo), na hapa dunia nimejifunza kuwa hakuna kitu cha bure, hata hivyo nimetambua kuwa shahada hii imetolewa kwa kutambua mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Tano kwa miaka 4, hivyo hii ni heshima kwa Watanzania wote, wafanyakazi, wakulima, wafugaji na wavuvi hasa wanaolipa kodi” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Mhe. Rais Magufuli amewashukuru viongozi wote nchini, Chama Cha Mapinduzi (CCM), vyombo vya Ulinzi na Usalama, viongozi wa Dini, viongozi wa Siasa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ushirikiano wao mkubwa katika kuhakikisha nchi inakua na amani na utulivu, na miradi ya maendeleo inatakelezwa kwa mafanikio makubwa.
Pamoja na kueleza mafanikio yaliyopatikana katika maeneo mbalimbali ambayo Serikali ya Awamu ya Tano imetilia mkazo, Mhe. Rais Magufuli amewataka Watanzania wote kuendelea kushikamana katika kujenga nchi na kutokubali kuyumbishwa na changamoto za mabeberu na vibaraka wao waliopo ndani ya nchi, ambao wamekuwa wakitumika kukwamisha juhudi za Serikali katika maendeleo na safari ya kuufikia uchumi wa kati ifakapo mwaka 2025.
Amewapongeza wahitimu wa UDOM wa mwaka huu na ametoa wito kwa wasomi hapa nchini kuendelea kufanya tafiti mbalimbali zinazojielekeza kutatua changamoto za Watanzania, na kwamba tafiti hizo zisiwe tegemezi kwa watu wa nje ambao ndio huchagua ajenda za utafiti huku akibainisha kuwa Serikali itaendelea kuchangia mfuko wa utafiti.
Kesho tarehe 22 Novemba, 2019 Mhe. Rais Magufuli ataweka jiwe la msingi la mradi wa ujenzi wa Hospitali ya Uhuru katika eneo la Maduka Chamwino, ataweka jiwe la msingi la mradi wa ujenzi wa nyumba 118 za askari polisi katika eneo la Nzuguni, ataweka jiwe la msingi la mradi wa ujenzi wa Kituo Kikuu cha Mabasi cha Dodoma katika eneo la Nzuguni, ataweka jiwe la msingi la mradi wa ujenzi wa Soko Kuu la Dodoma katika eneo la Nzuguni na kisha atazungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Chamwino, Dodoma.
21 Novemba, 2019
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amemteua Dkt. Mussa Daniel Budeba kuwa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (Geological Survey of Tanzania - GST).
Taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi, Mhe. Balozi John Kijazi imeeleza kuwa uteuzi wa Dkt. Budeba umeanza leo tarehe 15 Novemba, 2019.
Kabla ya uteuzi huo, Dkt. Budeba alikuwa Mhadhiri wa Idara ya Uhandisi wa Kemikali na Madini ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
15 Novemba, 2019
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 12 Novemba, 2019 amezindua kitabu cha maisha binafsi ya Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Benjamin William Mkapa kiitwacho “My Life, My Purpose” (yaani Maisha Yangu, Kusudio Langu).
Sherehe za uzinduzi wa kitabu hicho zimefanyika katika ukumbi wa Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein, Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili Mhe. Dkt. Ali Hassan Mwinyi na Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete.
Wengine ni Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job Yustino Ndugai, Mawaziri Wakuu Wastaafu, Mawaziri, Majaji Wakuu Wastaafu, viongozi wakuu wa vyombo vya Ulinzi na Usalama, Mabalozi, Wabunge, viongozi wastaafu waliofanya kazi na Mhe. Mkapa akiwa Rais, viongozi wa Taasisi mbalimbali na viongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa, Mhe. Paul Makonda.
Katika hotuba yake, Mhe. Rais Magufuli amempongeza Mhe. Rais Mstaafu Mkapa kwa kuandika kitabu kuhusu maisha yake kuanzia alipozaliwa mwaka 1938 katika Kijiji cha Lupaso, Wilaya ya Masasi Mkoani Mtwara, safari yake ya masomo, siasa na uongozi alipokuwa Rais wa Awamu ya Tatu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kati ya mwaka 1995 na mwaka 2005, kwa kuwa kitabu hicho kitawasadia Watanzania na watu wengine duniani kujifunza na kufahamu mchango mkubwa alioutoa kwa Taifa la Tanzania na katika Jumuiya ya kimataifa katika masuala ya maendeleo na uongozi.
Mhe. Rais Magufuli amekiri kuwa Mhe. Rais Mstaafu Mkapa ni mfano wake wa kuigwa na amemshukuru kwa mchango wake mkubwa katika safari yake ya siasa na uongozi kuanzia mwaka 1995 alipomnadi katika kampeni za Uchaguzi Mkuu akigombea Ubunge, alipomteua kuwa Naibu Waziri wa Ujenzi na baadaye Waziri wa Ujenzi, alipokubali ushauri wake akiwa katika nyadhifa hizo na alipomtia moyo katika uamuzi wake wa kugombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 2015.
Ametaja moja ya ushauri ulioungwa mkono na Mhe. Rais Mstaafu Mkapa kuwa ni Serikali ya Tanzania kuanza kujenga barabara za lami kwa kutumia fedha za ndani kwa kutenga shilingi Bilioni 1 kila mwezi, na kusimamia kwa karibu utendaji wa Wizara hali iliyopelekea aitwe jina la utani la Askari wa Mwamvuli.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli amempongeza Mhe. Rais Mstaafu Mkapa kwa mchango wake mkubwa katika maendeleo ya uchumi wa Tanzania na kupiga vita umasikini kwa kuanzisha mikakati mbalimbali ikiwemo Mkakati wa Kukuza na Kuondoa Umasikini Tanzania (MKUKUTA), Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania (MKURABITA), Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania (TASAF) na Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi (MMEM).
Mhe. Rais Magufuli ameelezea kufurahishwa na juhudi zilizofanywa na Mhe. Rais Magufuli katika kukuza uchumi, kuondokana na utegemezi na kudumisha amani, na kwamba ni kutokana na hilo hata Serikali ya Awamu ya Tano anayoiongoza inasimamia mwelekeo huo.
Pamoja na kuipongeza Taasisi ya Uongozi kwa kuandika kumbukumbu za viongozi, ameitaka taasisi hiyo kuchapisha kitabu cha maisha binafsi ya Mhe. Rais Mstaafu Mkapa kwa lugha ya Kiswahili ili Watanzania wengi waweze kusoma, na ametoa wito kwa viongozi wengine wakiwemo wa ngazi za chini kuandika vitabu kuhusu maisha yao.
Kwa upande wake Mhe. Rais Mstaafu Mkapa, amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kukubali kuzindua kitabu chake na amempongeza kwa msimamo wake wa kuhakikisha Tanzania inajitegemea hasa katika maendeleo.
Mhe. Rais Mstaafu Mkapa amewashukuru wote walioshiriki katika uandaaji na uchapishaji wa kitabu cha maisha yake binafsi na amesema pamoja na kuandika kuhusu maisha yake, katika kitabu hicho ameeleza jinsi alivyofanya kazi na kumfahamu Baba wa Taifa Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere ambaye fikra zake bado zipo hai na zina mashiko mpaka sasa.
Uzinduzi wa kitabu cha maisha binafsi ya Rais Mstaafu Mkapa, umekwenda sambamba na maadhimisho ya miaka 81 ya tangu kuzaliwa kwake, ambapo viongozi waliohudhuria sherehe hizo wamepata nafasi ya kumpongeza, kumtakia afya njema na maisha marefu na pia wameshiriki nae chakula cha mchana kilichoandaliwa kwa heshima yake na Mhe. Rais Magufuli.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
12 Novemba, 2019
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amezishukuru nchi za Nordic kwa uhusiano na ushirikiano wake mzuri na nchi za Afrika ikiwemo Tanzania na ametoa wito kwa nchi hizo kujielekeza zaidi katika ushirikiano wa kiuchumi.
Mhe. Rais Magufuli amesema hayo tarehe 08 Novemba, 2019 alipohutubia Mkutano wa 18 wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Afrika na Nordic uliofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam.
Akizungumza katika mkutano huo ambao umehudhuriwa na Mawaziri 29 wa nchi za Afrika na Mawaziri 5 wa nchi za Nordic ambazo ni Norway, Sweden, Denmark, Finland na Iceland, Mhe. Rais Magufuli amesema Afrika inakumbuka mchango mkubwa uliotolewa na nchi za Nordic kabla na baada ya harakati za ukombozi wa nchi nyingi za Afrika, ambapo zilichangia huduma za kijamii na kiuchumi kama vile afya, elimu, kilimo, sayansi na teknolojia, nishati, mazingira pamoja na kulinda amani na usalama.
Ametolea mfano wa Tanzania ambapo nchi za Nordic zimechangia ujenzi wa Kituo cha Elimu Kibaha, Chuo cha Utafiti wa Kilimo Uyole, vyuo mbalimbali vya ufundi na kampeni za kufuta ujinga katika miaka ya 70.
Hata hivyo, Mhe. Rais Magufuli amesema kuna haja ya kubadilisha mwelekeo na kuingia katika mwelekeo wa kisiasa unaojikita katika ushirikiano wa kiuchumi kupitia biashara na uwekezaji.
Amesisitiza kuwa kwa kuwa nchi za Nordic zenye watu wapatao Milioni 27 zina uchumi mkubwa unaofikia pato la mwaka la Dola za Marekani Trilioni 1.7 ikilinganishwa na nchi za Afrika zenye watu Bilioni 1.2 na pato la mwaka la Dola za Marekani Trilioni 2.334, Afrika inapaswa kujifunza kutoka Nordic na amezikaribisha nchi za Nordic kuja kuwekeza Afrika katika viwanda vitakavyoongeza thamani ya mazao, kuzalisha ajira na kulipa kodi kwa ajili ya maendeleo.
Amebainisha kuwa Afrika ina fursa nyingi za uwekezaji ikiwemo eneo la ukubwa asilimia 30 ya eneo lote duniani linalofaa kwa kilimo, ukanda wa pwani ya bahari wenye urefu wa kilometa 30,500, mifugo, misitu, wanyamapori, mafuta, gesi, utalii na uchumi wake unaokua vizuri kwa wastani wa asilimia 4.1.
Mhe. Rais Magufuli ametoa wito kwa nchi za Afrika kujenga mazingira mazuri yatakayovutia uwekezaji kutoka nchi za Nordic na amesema kwa kutambua hilo Serikali ya Tanzania imechukua hatua madhubuti za kuvutia uwekezaji huo zikiwemo kuwa na sheria za kuwalinda wawekezaji, kutekeleza mkakati wa kurekebisha na kuboresha mazingira ya biashara (The Blue Print) na kutenga kanda maalum kwa ajili ya ujenzi wa viwanda na uwekezaji.
Hatua zingine ni kujenga na kuboresha miundombinu ya usafiri na usafirishaji kama vile barabara, reli, bandari, viwanja vya ndege, kujenga meli, kununua ndege pamoja na kutekeleza mradi mkubwa wa ujenzi wa Bwawa la Nyerere litakalozalisha megawati 2,115 za umeme.
Baada ya kuhutubia mkutano huo, Mhe. Rais Magufuli amefanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Sweden Mhe. Ann Linde, Waziri wa Mambo ya Nje wa Norway Mhe. Ine Marie Eriksen Søreide na Waziri wa Mambo ya Nje wa Finland Mhe. Pekka Haavisto.
Mhe. Rais Magufuli amewaomba Mawaziri hao kupeleka salamu zake kwa Wakuu wa Nchi zao na amewahakikishia kuwa Tanzania ipo tayari wakati wote kuendeleza na kukuza zaidi uhusiano uliopo, mkazo zaidi ukiwa katika biashara na uwekezaji.
Mawaziri hao wamempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa jitihada kubwa za kujenga uchumi kuelekea uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025 na kupiga vita rushwa na pia wamemuahidi kuendelea kushawishi kampuni za nchi zao kuja kuwekeza Tanzania ikiwemo kampuni kubwa ya Equinor ya Norway ambayo inakamilisha maandalizi ya kuwekeza nchini Tanzania kiwanda cha kusindika gesi (LNG) kitakachogharimu Dola za Marekani Bilioni 20 (sawa na shilingi Trilioni 45.555).
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
08 Novemba, 2019
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 04 Novemba, 2019 amemuapisha Bw. Charles Edward Kichere kuwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Bw. Kichere ataanza kazi kesho tarehe 05 Novemba, 2019 baada ya Prof. Mussa Juma Assad kumaliza muda wake.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli amewaapisha Majaji 12 wa Mahakama Kuu aliowateua jana tarehe 03 Novemba, 2019 ambao ni Mhe. Jaji Elizabeth Yoeza Mkwizu, Mhe. Jaji Joachim Charles Tiganga, Mhe. Jaji Augustine Karichuba Rwizile, Mhe. Jaji Fredrick Kapela Manyanda, Mhe. Jaji Deo John Nangela na Mhe. Jaji Angela Antony Bahati.
Wengine ni Mhe. Jaji Edwin Elias Kakolaki, Mhe. Jaji Kassim Ngukah Robert, Mhe. Jaji Angaza Ernest Mwipopo, Mhe. Jaji Ephery Kisanya Sedekia, Mhe. Jaji Dkt. Zainab Diwa Mango na Mhe. Jaji Said Mashaka Kalunde.
Mhe. Rais Magufuli amemuapisha Bi. Katarina Tengia Revocati kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Njombe.
Pia, Mhe. Rais Magufuli amemuapisha Kanali Francis Ronaldo Mbindi kuwa Kamishna wa Kazi katika Ofisi ya Waziri Mkuu.
Mhe. Rais Magufuli amemuapisha Jaji Mstaafu Mathew Pauwa Mhina Mwaimu kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora na amemuapisha Bw. Mohamed Khamis Hamad kuwa Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora.
Mhe. Rais Magufuli amewaapisha Makamishna watano wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora ambao ni Dkt. Fatma Rashid Khalfan, Bw. Thomas Paul Masanja, Bi. Amina Talib Ali, Bw. Khatib Mwinyi Khatib Mwinyichande na Bw. Nyanda Josiah Shuli.
Halikadhalika, Mhe. Rais Magufuli amemuapisha Mhandisi Aisha Amour kuwa Balozi wa Tanzania nchini Kuwait.
Hafla ya kuapishwa kwa viongozi hao imefanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job Yustino Ndugai, Mawaziri na Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu Wakuu, viongozi wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama, Majaji wa Mahakama ya Rufani, Majaji wa Mahakama Kuu na viongozi wa taasisi mbalimbali zinazohusiana na masuala ya sheria.
Akizungumza baada ya kuwaapisha, Mhe. Rais Magufuli ametoa wito kwa viongozi hao kufanya kazi zao kwa mujibu wa sheria, kutimiza wajibu wao kwa uhuru na haki na kuwatumikia Watanzania vizuri hasa wanyonge.
Amemtaka Kamishna wa Kazi Kanali Francis Ronald Mbindi kuhakikisha anashughulikia tatizo la utoaji holela wa vibali vya kazi kwa wageni ambao wamekuwa wakiingia nchini na kufanya kazi ambazo zinaweza kufanywa na Watanzania.
Mhe. Rais Magufuli amemtaka CAG Bw. Kichere kufanya kazi kwa uhuru na kuzingatia mipaka ya kazi yake, pamoja na kushughulikia dosari zilizopo ndani ya Ofisi ya CAG ikiwemo watumishi kulipwa posho isivyo halali.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma na Spika wa Bunge Mhe. Job Yustino Ndugai wamewapongeza viongozi wote walioapishwa na wamewataka kutumia imani ya Mhe. Rais Magufuli kwao, kwa kutekeleza majukumu yao kwa tija, uadilifu na kukidhi matarajio ya watu.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
04 Novemba, 2019
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 03 Novemba, 2019 amefanya uteuzi wa viongozi mbalimbali.
Taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi, Mhe. Balozi John Kijazi imewataja walioteuliwa kama ifuatavyo;
- Mhe. Rais Magufuli amemteua Bw. Charles Edward Kichere kuwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (Controller and Auditor General – CAG).
Bw. Kichere anachukuwa nafasi ya Prof. Mussa Juma Assad ambaye kipindi chake cha miaka 5 katika nafasi hiyo kinakwisha kesho tarehe 04 Novemba, 2019.
Kabla ya Uteuzi huo Bw. Kichere alikuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Njombe.
- Mhe. Rais Magufuli amemteua Bi. Katarina Tengia Revocati kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Njombe.
Kabla ya uteuzi huo Bi. Katarina Tengia Revocati alikuwa Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania na anachukua nafasi ya Bw. Charles Edward Kichere ambaye ameteuliwa kuwa CAG.
- Mhe. Rais Magufuli amemteua Mhandisi Aisha Amour kuwa Balozi wa Tanzania nchini Kuwait.
Kabla ya Uteuzi huo, Mhandisi Aisha Amour alikuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Kilimanjaro.
- Mhe. Rais Magufuli amemteua Kanali Francis Ronald Mbindi kuwa Kamishna wa Kazi katika Ofisi ya Waziri Mkuu.
Kanali Francis Ronald Mbindi anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Bw. Gabriel Pascal Malata ambaye hivi karibuni aliteuliwa kuwa Naibu Wakili Mkuu wa Serikali (Deputy Solicitor General)
Aidha, Mhe. Rais Magufuli amefanya uteuzi wa Majaji 12 wa Mahakama Kuu. Walioteuliwa ni;
- Dkt. Zainabu Diwa Mango.
Kabla ya uteuzi huu Dkt. Zainab Diwa Mango alikuwa Wakili wa Serikali Mkuu katika Ofisi ya Taifa ya Mashtaka.
- Bw. Edwin Elias Kakolaki.
Kabla ya uteuzi huu Bw. Edwin Elias Kakolaki alikuwa katika Ofisi ya Kupambana na Kuzuia Dawa za Kulevya Nchini.
- Dkt. Deo John Nangela.
Kabla ya uteuzi huu Dkt. Deo John Nangela alikuwa katika Ofisi ya Tume ya Ushindani (Fair Competition Commission - FCC).
- Bw. Fredrick Kapela Manyanda.
Kabla ya uteuzi huu Bw. Fredrick Kapela Manyanda alikuwa katika Ofisi ya Taifa ya Mashtaka.
- Bi. Elizabeth Yoeza Mkwizu.
Kabla ya uteuzi huu Bi. Elizabeth Yoeza Mkwizu alikuwa Naibu Msajili wa Mahakama ya Rufani.
- Augustine Karichuba Rwizile.
Kabla ya uteuzi huu Bw. Augustine Karichuba Rwizile alikuwa Naibu Msajili wa Mahakama.
- Bw. Ephery Sedekia
Kabla ya uteuzi huu Bw. Ephery Sedekia alikuwa Katibu wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (Attorney General – AG).
- Bw. Angaza Mwaipopo.
Kabla ya uteuzi huu Bw. Angaza Mwaipopo alikuwa katika Ofisi ya Rais, Ikulu.
- Bw. Joachim Charles Tiganga.
Kabla ya uteuzi huu Bw. Joachim Charles Tiganga alikuwa Naibu Msajili Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.
- Bw. Kassim Ngukali Robert.
Kabla ya uteuzi huu Bw. Kassim Ngukali Robert alikuwa katika Ofisi ya Kitengo cha Kudhibiti Fedha Haramu cha Wizara ya Fedha na Mipango.
- Bw. Said Mashaka Kalunde.
Kabla ya uteuzi huo, Bw. Said Mashaka Kalunde alikuwa katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
- Bi. Angela Antony Bahati.
Kabla ya uteuzi huo, Bi. Angela Antony Bahati alikuwa Katibu Msaidizi wa Tume ya Kurekebisha Sheria.
Wateule hawa wote pamoja na Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti na Makamishna 5 wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora ambao waliteuliwa hivi karibuni wataapishwa kesho tarehe 04 Novemba, 2019 saa 3:30 asubuhi, Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
03 Novemba, 2019
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 03 Novemba, 2019 amemuelekeza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Selemani Jafo kufanya mabadiliko kwa Halmashauri ya Mji wa Ifakara na Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero, zilizopo katika Mkoa wa Morogoro kama ifuatavyo;
- Halmashauri ya Mji wa Ifakara iongezwe idadi ya Kata, kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero.
Makao Makuu yawe Ifakara Mjini.
- Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero ibadilishwe jina, na iitwe Halmashauri ya Wilaya ya Mlimba.
Makao Makuu yawe Mngeta kama ilivyoamuliwa na Baraza la Madiwani.
Mhe. Rais Magufuli amewasisitiza viongozi wa halmashauri kutowayumbisha wananchi na watumishi kuhusu utekelezaji wa maelekezo hayo.
Mhe. Rais Magufuli amemuagiza Mhe. Waziri Jafo kusimamia utekelezaji wa maelekezo hayo kwa mujibu wa sheria
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
03 Novemba, 2019
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ameagiza Wizara ya Fedha na Mipango kutoa shilingi Bilioni 40 kwa ajili ya kumalizia madeni yote ya wakulima wa korosho yaliyobaki baada ya Serikali kununua korosho za wakulima katika msimu wa mwaka 2018/19.
Mhe. Rais Magufuli ametoa maagizo hayo leo tarehe 01 Novemba, 2019 Ikulu Jijini Dar es Salaam alipokutana na viongozi wa Wizara, Mikoa, Wilaya na Taasisi za Serikali ambazo zinahusika katika uzalishaji na mauzo ya zao la Korosho.
Mkutano huo umehudhuriwa na Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa.
Pamoja na kuagiza Wizara ya Fedha na Mipango itoe fedha hizo kesho tarehe 02 Novemba, 2019 Mhe. Rais Magufuli amewaagiza viongozi wa Mikoa na Wilaya kuhakikisha fedha hizo zinawafikia wakulima na sio vinginevyo, na pia kuhakikisha wanalipwa wakulima wanaostahili kupata malipo hayo.
Mhe. Rais Magufuli ameelezea kutoridhishwa kwake na utendaji kazi wa Wizara ya Kilimo na viongozi wa Mikoa na Wilaya ambao katika maeneo yao kumetokea wizi mkubwa wa fedha za wakulima kupitia vyama vya msingi vya ushirika (AMCOS) hali iliyosababisha wakulima wengi kuishi maisha duni.
Mhe. Rais Magufuli amesema amesikitishwa kuona viongozi wa Wizara, Mikoa na Wilaya hawajachukua hatua madhubuti dhidi ya watu wanaowaibia wakulima mpaka alipoamua kumtuma Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Brig. Jenerali John Mbungo ambaye kwa muda mfupi amebaini kuwepo wizi wa shilingi Bilioni 1.23 na tayari amefanikisha kurejeshwa kwa shilingi Milioni 375 katika Mkoa wa Lindi pekee.
Amewataka viongozi wa Wizara ya Kilimo, Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya kubadilika na kuhakikisha haki za wakulima zinalindwa ipasavyo kwa kurejesha fedha zilizoibwa na kuzuia mianya yote ya wizi.
“Nataka mfanye kazi, hakuna mtu wa kuwanyanyasa, nendeni mkashughulikie kero za wakulima, mna vyombo vya ulinzi na usalama nendeni mkavisimamie, kinyume na hapo nitakuona hutoshi kwenye nafasi hiyo” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Kuhusu minada ya korosho, Mhe. Rais Magufuli ametaka utaratibu uliowekwa wa kufungua mnada kuanzia saa 2:00 asubuhi hadi saa 10:00 Jioni na kisha kufungua masanduku yenye zabuni kwa uwazi mara baada ya saa 10 jioni uheshimiwe, ili kuepusha njama za upangaji wa bei.
Viongozi wa Mikoa na Wilaya wamemuahidi Mhe. Rais Magufuli kuwa wanakwenda kusimamia maelekezo yake na kuhakikisha haki za wakulima zinalindwa.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
01 Novemba, 2019
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 28 Oktoba, 2019 amepokea hati za utambulisho za Balozi wa Umoja wa Ulaya (EU) hapa nchini Mhe. Manfred Fanti, Balozi wa Finland hapa nchini Mhe. Riitta Swan na Balozi wa Rwanda hapa nchini Mhe. Mej. Jen. Charles Karamba, Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na Mhe. Rais Magufuli baada ya kuwasilisha hati zake za utambulisho Mhe. Balozi Manfred Fanti ameishukuru Tanzania kwa kumpokea kuja kuiwakilisha EU hapa nchini na amesema katika kuendeleza na kukuza zaidi uhusiano na ushirikiano na EU na Tanzania atajielekeza zaidi katika masuala ya maendeleo kwa kuwa anaamini kuna mambo mengi na mazuri ya kufanya yatakayoiwezesha Tanzania kuingia katika uchumi wa kati kama ilivyopanga.
Mhe. Balozi Fanti ameongeza kuwa anaamini katika mazungumzo ya pamoja kati ya Tanzania na EU katika masuala mbalimbali na kwamba katika kipindi chake anatarajia kutilia mkazo miradi ya kuzalisha nishati ya umeme kupitia Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na utekelezaji wa miradi mingine iliyopo katika makubaliano ya 11 ya mkataba wa mfuko wa maendeleo ya EU uliotengewa shilingi Trilioni 1.583 yanatekelezwa.
Mhe. Rais Magufuli amempongeza Mhe. Balozi Fanti kwa msimamo wake wa kuimarisha na kukuza zaidi uhusiano wa Tanzania na EU na amesema Tanzania inatambua uhusiano mzuri na wa kihistoria uliopo kati yake na EU na kwamba ipo tayari kushirikiana na Balozi huyo katika utekelezaji wa masuala yenye maslahi kwa pande zote mbili.
Kwa upande wake Balozi wa Finland hapa nchini Mhe. Riitta Swan pamoja na kushukuru kwa kupokelewa amempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa mafanikio makubwa katika kupambana na rushwa na amesema katika kipindi chake hapa nchini atahakikisha maeneo ya uhusiano kati ya Tanzania na Finland yanaimarishwa ikiwemo mradi wa utunzaji wa mazingira, kuboresha mifumo ya ukusanyaji wa kodi kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na utawala bora.
Mhe. Rais Magufuli amemshukuru kwa dhamira yake ya kukuza zaidi ushirikiano na uhusiano na Tanzania na amesema Tanzania itakuwa tayari kutoa ushirikiano wowote atakaouhitaji.
Nae Balozi wa Rwanda hapa nchini Mhe. Mej. Jen. Charles Karamba ameishukuru Tanzania kwa kumkaribisha na amemhakikishia Mhe. Rais Magufuli kuwa katika kipindi chake cha Ubalozi atahakikisha matarajio ya Rais wa Rwanda Mhe. Paul Kagame kukuza zaidi uhusiano wa Tanzania na Rwanda yanafanikiwa.
Mhe. Rais Magufuli amemkaribisha Mhe. Balozi Karamba na kumtaka ahakikishe biashara kati ya Tanzania na Rwanda inakuwa zaidi ikiwemo kutekelezwa kwa makubaliano yake na Mhe. Rais Kagame ya Rwanda kutumia bandari ya Tanga katika upokeaji na usafirishaji wa mizigo ya kwenda na kutoka Rwanda.
“Sisi ni ndugu na ni wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Mwenyekiti wetu ni Rais wa Rwanda Mhe. Paul Kagame, hatuna sababu ya kupoteza muda, nataka usukume sana suala la kuongeza biashara kati ya Tanzania na Rwanda ili nchi zetu zinufaike zaidi” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
28 Oktoba, 2019
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli l tarehe 23 Oktoba, 2019 amekutana na viongozi wa Taasisi ya Mashauriano ya Kisheria kwa Nchi za Asia na Afrika (AALCO) ambao wanahudhuria mkutano wa 58 unaofanyika hapa nchini kwa siku 5 ukiwakutanisha wajumbe kutoka nchi wanachama 49 na mashirika mbalimbali.
Viongozi wa AALCO waliokutana na Mhe. Rais Magufuli ni Rais wa AALCO aliyechaguliwa katika mkutano huu Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga (Waziri wa Sheria na Katiba, Tanzania), Makamu wa Rais wa AALCO aliyechaguliwa katika mkutano huu Prof. Mohamad Shalaldeh (Waziri wa Sheria wa Palestina), Katibu Mkuu wa AALCO Prof. Kennedy Gastorn (Tanzania) na Naibu Makatibu Wakuu wa AALCO watatu ambao ni Bw. Yukihiro Takeya (Japan), Bi. Wang Liyu (China) na Dr. Ali Garshasbi (Iran).
Mhe. Rais Magufuli amewashukuru na kuwakaribisha wajumbe wa AALCO nchini Tanzania na amewahakikishia kuwa Serikali inatambua kazi inayofanywa na taasisi hiyo tangu ijiunge nayo mwaka 1965 na kuwa mwanachama kamili kuanzia mwaka 1973.
Mhe. Rais Magufuli amesisitiza umuhimu wa AALCO kutekeleza malengo ya taasisi hiyo kama alivyoelezwa na viongozi hao, na ametoa wito wa kuendelea kuzitetea nchi wanachama hasa zinazowekewa vikwazo mbalimbali.
Ametolea mfano wa Zimbabwe ambayo imewekewa vikwazo kwa miaka mingi hali inayosababisha wananchi wa Zimbabwe kuteseka.
Rais wa AALCO Mhe. Balozi Mahiga na Katibu Mkuu Mhe. Prof. Kennedy Gastorn wamemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kupata fursa ya kukutana nae na wameahidi kuwa AALCO itaendelea kutekeleza majukumu yake kwa maslahi ya Asia na Afrika.
Mazungumzo hayo yamehudhuriwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Sheria na Katiba Mhe. Amon Mpanju.
Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China (CPC) Ndg. Guo Yezhou, Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Mhe. Rais Magufuli amemshukuru Ndg. Yezhou kwa kutembelea hapa nchini kwa mara ya pili na pia ameishukuru China kwa kuendeleza ushirikiano na uhusiano mzuri na Tanzania ikiwemo mchango mkubwa wa chama cha CPC ambacho kinajenga Chuo cha Uongozi cha Mwalimu Julius Nyerere katika Wilaya ya Kibaha Mkoani Pwani kwa ajili ya kutoa mafunzo ya uongozi kwa nchi 6 zenye vyama vya ukombozi vilivyoshirikiana na CPC ambazo ni {Tanzania (CCM), Afrika Kusini (ANC), Zimbabwe (ZANU-PF), Msumbiji (FRELIMO), Angola (MPLA) na Namibia (SWAPO)}.
Mhe. Rais Magufuli pia amemuomba Ndg. Yezhou kufikisha shukrani zake kwa Rais wa China na Mwenyekiti wa CPC Mhe. Xi Jinping kwa kutoa tuzo kwa Waziri Mkuu Mstaafu wa Tanzania Mhe. Dkt. Salim Ahmed Salim ikiwa ni kutambua mchango wake katika kuiwezesha China kuwa mwanachama wa Umoja wa Mataifa.
Mhe. Rais Magufuli amemhakikishia kuwa Sera za Tanzania kuhusu China hazijabadilika na amesema Tanzania itaendelea kushirikiana na China katika jitihada mbalimbali za maendeleo.
Mazungumzo hayo yamehudhriwa na Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Ndg. Bashiru Ally Kakurwa na Balozi wa China hapa nchini Mhe. Wang Ke.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
23 Oktoba, 2019
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amemtaka Waziri wa Maji Prof. Makame Mbarawa kuchukua hatua dhidi ya wataalamu wa wizara hiyo wanaochelewesha utekelezaji wa miradi ya maji licha ya Serikali kutoa fedha za miradi hiyo.
Mhe. Rais Magufuli ametoa agizo hilo leo tarehe 16 Oktoba, 2019 alipokuwa akizungumza na wananchi wa Masasi Mkoani Mtwara baada ya Mkurugenzi wa Maji Bw. Nuntufye Mwamsojo kueleza kuwa ujenzi wa chujio ya maji kwa ajili ya mji huo unasuburi kufanyika kwa upembuzi yakinifu uliopangwa kuchukua muda wa miezi 6.
Mhe. Rais Magufuli aliyechukizwa na mipango ya ucheleweshaji miradi amesema wataalamu wa Wizara ya Maji hawana sababu za msingi za kutumia muda mrefu kufanya upembuzi yakinifu wakati wananchi wana tatizo la maji na hivyo ametoa wiki mbili kwa upembuzi huo kukamilika na ujenzi wachujio kuanza mara moja.
“Waziri Mbarawa unafanya kazi nzuri sana, lakini nataka uwe mkali, hawa wataalamu wako wa maji wizarani wanakuangusha, nenda ukawashughulikie hata kama ni kuwafukuza wafukuze, wananchi hawawezi kuendelea kukosa maji halafu wataalamu wanaleta lugha za upembuzi yakinifu miezi 6 kwa ajili ya chujio ya maji?” amehoji Mhe. Rais Magufuli.
Akiwa njiani kutoka Ruangwa kwenda Lindi Mjini kupitia Masasi Mkoani Mtwara Mhe. Rais Magufuli amesimama na kuzungumza na wananchi wa Ikungu, Nachingwea, Naipanga, Lukuledi, Chigugu na Ndanda ambapo amewahakikishia kuwa Serikali itawalipa wakulima wa korosho ambao hawajalipwa fedha zao kuanzia Jumanne ijayo tarehe 22 Oktoba, 2019.
Naibu Waziri wa Kilimo Mhe. Hussein Bashe amesema maandalizi ya kuwalipa wakulima hao yamekamilika ambapo shilingi Bilioni 53.6 zimeandaliwa kumaliza madeni ya wakulima wa korosho yaliyobaki na pia amebainisha kuwa Serikali imeanza kuchukua hatua dhidi ya viongozi wa vyama vya ushirika waliowaibia wakulima ili wafikishwe katika vyombo vya kisheria.
Mjini Nachingwea Mhe. Rais. Magufuli amelazimika kukagua eneo linapojengwa soko na eneo kilipohamishwa kituo cha mabasi baada ya wananchi wa Mji huo kuwalalamikia viongozi wa Wilaya kuwa wameshindwa kukamilisha miradi hiyo licha ya Serikali kutoa fedha.
Baada ya ukaguzi huo, Mhe. Rais Magufuli amewaonya Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea Bi. Rukia Muwango na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Nachingwea Bw. Bakari Mohammed Bakari kutokana na kutotekeleza majukumu yao ipasavyo na amemtaka Mkuu wa Mkoa wa Lindi Bw. Godfrey Zambi kufuatilia maagizo anayoyatoa kwa viongozi wa Mkoa huo.
Akiwa katika Kijiji cha Chigugu Wilayani Masasi, Mhe. Rais Magufuli amemuagiza Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Brig. Jen. John Mbungo kumuondoa Kamanda wa TAKUKURU Mkoani wa Mtwara Bw. Steven Mafipa na kufanya uteuzi mwingine wa Kamanda wa TAKUKURU wa Mkoa huo kutokana na kushindwa kuwashughulikia viongozi wawili wa chama cha msingi cha ushirika (AMCOS) wanaodaiwa kuwaibia fedha wakulima wa korosho wa Chigugu.
Mhe. Rais Magufuli amemuagiza Brig. Jen. Mbungo kufanya uteuzi huo leo ili kesho tarehe 17 Oktoba, 2019 mteule huyo aripoti katika kituo chake cha kazi na kwenda moja kwa moja kushughulikia malalamiko ya wakulima wanaodai kuibiwa fedha na viongozi wa vyama vya msingi vya ushirika.
Mhe. Rais Magufuli amempa siku 5 Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mtwara Blasius Chatanda kuwakamata watuhumiwa Salum Chilundu na Juma Mpopo ambao wametanjwa na Diwani wa Kata ya Chigugu Mhe. Amina Mpandula kuwa wamehusika katika wizi wa fedha za wakulima wa korosho kupitia AMCOS.
Akiwa Ndanda, Mhe. Rais Magufuli amepokea maombi ya wanafunzi wa shule kongwe ya sekondari ya Ndanda ambao wameomba Serikali isaidie kukarabati miundombinu ya shule hiyo na kujenga bwalo la chakula ambapo ameagiza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kutoa shilingi Milioni 100 kwa ajili hiyo.
Halikadhalika, Mhe. Rais Magufuli amemtaka Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mhe. Gelasius Byakanwa na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile kubaki Ndanda ili kufuatilia madai ya wananchi waliolalamikia kutozwa fedha nyingi za matibabu wanapokwenda kutibiwa katika Hospitali ya Ndanda ambayo ni Hospitali Teule ya Wilaya ya Masasi (DDH) na ameonya kuwa endapo itathibitika kuwa madai ya wananchi ni kweli Serikali itajenga hospitali ya Serikali itakayoweza kutoa huduma kwa gharama nafuu.
Mhe. Rais Magufuli pia ameahidi kuwa Serikali itatoa shilingi Milioni 100 kwa ajili ya upanuzi wa zahanati ya Naipanga, ametoa shilingi Milioni 10 kwa shule ya Lukuledi Maalum (ambayo ina wanafunzi viziwi) kwa ajili ya kutatua changamoto za shule hiyo likiwemo tatizo la maji na amechangia shilingi Milioni 9 kwa shule za Sekondari Mbemba na Sekondari Isdor Shirima na Shule ya Msingi Chigugu.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Lindi
16 Oktoba, 2019
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 20 Oktoba, 2019 amewaapisha viongozi 3 aliowateua hivi karibuni kushika nyadhifa mbalimbali.
Hafla ya kuapishwa kwa viongozi hao imefanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Makamu wa Rais, Mhe. Samia Suluhu Hassan, Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, Waziri wa Katiba na sheria Mhe. Balozi Augustine Mahiga na Viongozi Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama.
Walioapishwa ni Bw. Mathias Kabunduguru aliyepishwa kuwa Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Bw. Gerald Geofrey Mweli aliyeapishwa kuwa Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Bw. Ali Bujiku Sakila aliyeapishwa kuwa Balozi.
Akizungumza baada ya kuwaapisha, Mhe. Rais Magufuli amewataka viongozi hao kwenda kuchapa kazi katika ofisi zao kwa kutanguliza maslahi ya Taifa, kuzingatia haki na sheria na bila kuyumbishwa na maneno ya kuwakatisha tamaa.
Amempongeza aliyekuwa Mtendaji Mkuu wa Mahakama Bw. Hussein Katanga kwa utendaji wake akiwa katika nafasi hiyo na amemtaka Mtendaji Mkuu wa Mahakama Bw. Kabunduguru kuendeleza mageuzi makubwa yaliyofanyika katika Mahakama ukiwemo mradi wa kuboresha Mahakama unaofadhiliwa na Benki ya Dunia.
Mhe. Rais Magufuli amemtaka Bw. Mweli kwenda kushirikiana na viongozi wenzake wa TAMISEMI na hasa katika kushughulikia maslahi ya Walimu na wafanyakazi wa wizara hiyo.
Mhe. Rais Magufuli amewataka viongozi wote Serikalini kushughulikia kwa karibu kero mbalimbali zinazowakabili wananchi na ametolea mfano wa Wakulima wa Mkoa wa Mtwara ambako hivi karibuni amefanya ziara na kubaini kuwa viongozi wa vyama vya msingi vya ushirika 32 wamekula fedha za wakulima kiasi cha zaidi ya shilingi Bilioni 1.2 na baada ya maelekezo yake Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) imefanikisha kurudishwa kwa shilingi Milioni 255 na viongozi 92 kukamatwa.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
20 Oktoba, 2019
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 19 Oktoba, 2019 amefanya uteuzi wa viongozi mbalimbali kama ifuatavyo;
- Mhe. Rais Magufuli amemteua Bw. Mathias Kabunduguru kuwa Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania. Kabla ya uteuzi huo Bw. Kabunduguru alikuwa Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) anayeshughulikia Elimu.
Bw. Kabunduguru anachukua nafasi ya Bw. Hussein Katanga ambaye ameteuliwa kuwa Balozi.
- Mhe. Rais Magufuli amemteua Bw. Godfrey Gerald Mweli kuwa Naibu Katibu Mkuu TAMISEMI (anayeshughulikia Elimu). Kabla ya uteuzi huo Bw. Mweli alikuwa Mkurugenzi wa Mipango wa Wizara ya Sheria na Katiba.
- Mhe. Rais Magufuli amemteua Bw. Hashim Abdallah Komba kuwa Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea. Kabla ya uteuzi huo Bw. Komba alikuwa Katibu Tawala wa Wilaya ya Iringa.
Bw. Komba anachukua nafasi ya Bi. Rukia Muwango ambaye uteuzi wake umetenguliwa.
- Mhe. Rais Magufuli amemteua Bw. Hassan Abbas Rungwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Nachingwea.
Bw. Rungwa anachukua nafasi ya Bw. Bakari Mohammed Bakari ambaye uteuzi wake umetenguliwa na atapangiwa kazi nyingine.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
19 Oktoba, 2019
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ameiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kufanya uchunguzi kwa miradi 107 yenye thamani ya shilingi Bilioni 90.28 iliyobainika wakati wa mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka huu (2019) kuwa na dosari mbalimbali zikiwemo kutekelezwa chini ya ubora, kutokamilika, matumizi mabaya ya fedha za umma na udanganyifu.
Mhe. Rais Magufuli ametoa maagizo hayo leo tarehe 14 Oktoba, 2019 katika sherehe za kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru, Kumbukumbu ya Baba wa Taifa Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere na Wiki ya Vijana zilizofanyika Kitaifa katika uwanja wa Ilulu Mjini Lindi.
Mhe. Rais Magufuli amekabidhi kitabu cha taarifa ya miradi hiyo kilichowasilishwa kwake na Kiongozi wa Mbio za Mwenge mwaka huu Bw. Mzee Mkongea Ali kwa Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU Brig. Jen. John Mbungo na kumuagiza wote wakaobainika kuhusika katika dosari za miradi hiyo kufikishwa Mahakamani ili sheria zichukue mkondo wake.
Katika taarifa hiyo Bw. Mzee Mkongea Ali amesema udanganyifu mkubwa umebainika katika miradi ya maji na amesisitiza kuwa endapo fedha nyingi zilizotolewa na Serikali kwa ajili ya kutatua tatizo la maji zitasimamiwa vizuri, tatizo hilo litapata ufumbuzi.
Amebainisha kuwa yeye na wakimbiza Mwenge wa Uhuru wenzake wamebaini kazi kubwa inayofanywa na Serikali ikiwemo miradi mikubwa ya maendeleo inayotekelezwa katika maeneo mbalimbali nchini, kuongezeka kwa nidhamu katika utumishi wa umma na kujengwa kwa miundombinu muhimu ya kuvutia uwekezaji mambo ambayo ni muhimu kwa maendeleo.
Kabla Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa hajasoma risala ya wananchi wa Tanzania, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenister Mhagama amesema mwaka huu Mwenge wa Uhuru umekimbizwa kwa miezi 7 katika jumla ya kilometa 26,274 ambapo umeweka mawe ya msingi, kufungua na kuzindua miradi ya maendeleo 1,390 yenye thamani ya shilingi Trilioni 4 na Bilioni 750 iliyopo katika Mikoa 31 na Halmashauri 195.
Kuhusu kumbukumbu ya Baba wa Taifa Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere, Mhe. Rais Magufuli amewataka Watanzania kuendelea kumuenzi kwa kutekeleza kwa vitendo misingi ya Uhuru na Azimio la Arusha ambalo linahimiza watu kuchapa kazi kwa juhudi na maarifa, elimu kwa wote hasa elimu ya ufundi, kupiga vita umasikini na ukosefu wa ajira, kujenga miundombinu, uzalendo na nidhamu kwa watumishi wa umma.
Ameahidi kuwa Serikali ya Awamu ya Tano itajitahidi kwa kadri iwezavyo kumuenzi Baba wa Taifa na ametaja baadhi ya juhudi zilizofanywa kwa vitendo kuwa ni kupambana na rushwa ambapo Mahakama ya kushughulikia Ufisadi imeanzishwa, watumishi hewa takribani 20,000 na wafanyakazi wenye vyeti feki 14,000 wameondolewa katika utumishi wa umma, kutoa shilingi Bilioni 23.8 kwa ajili ya elimu bila malipo kwa shule za msingi na sekondari, kutoa shilingi Bilioni 470 kwa mwaka kwa ajili ya mikopo ya elimu ya juu, kuboresha huduma za afya ambapo hospitali mpya 69 na vituo vya afya 352 vinajengwa na kuongeza bajeti ya dawa kutoka shilingi Bilioni 31 hadi kufikia shilingi Bilioni 270.
Maeneo mengine ni kuboresha upatikanaji wa huduma za maji Mijini na Vijijini ambapo takribani shilingi Trilioni 2 zinatumika, kuhimiza ujenzi wa viwanda ambapo viwanda takribani 4,000 vimejengwa, kuanza ujenzi wa mradi mkubwa wa ujenzi wa Bwawa la Mwl. Nyerere litakalozalisha megawati 2,115 za umeme ambapo shilingi Trilioni 6.5 zinatumika, kujenga reli ya kisasa (standard gauge railway – SGR) ambapo shilingi Trilioni 7.3 zinatumika, kujenga viwanja vya ndege 11, kununua ndege 11, kupanua bandari ambapo takribani shilingi Trilioni 1 zinatumika, kununua meli mpya na kukarabati za zamani.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli amesema Serikali ya Awamu ya Tano inamuenzi Baba wa Taifa kwa kuhakikisha inasimamia vizuri rasilimali na maliasili zikiwemo misitu, wanyamapori na madini kupitia sheria mpya ya mwaka 2017 ambayo imewezesha kuongezeka kwa mapato ya madini kutoka shilingi Bilioni 191 mwaka 2016/17 hadi kufikia shilingi Bilioni 335 mwaka 2018/19, kuanzisha Hifadhi za Taifa 4 ikiwemo Hifadhi ya Taifa ya Nyerere baada ya kumega Pori la Akiba la Selous na kuimarisha sekta ya Kilimo.
Kuhusu vijana, Mhe. Rais Magufuli ameipongeza Serikali ya Awamu ya Nne iliyoongozwa na Rais Mstaafu Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kwa kurejesha mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa kwa vijana na ameahidi kuwa Serikali ya Awamu ya Tano itaendeleza mafunzo hayo.
Sherehe hizo zimehudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Balozi Seif Ali Idd, Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, Spika wa Baraza la Wawakilishi Mhe. Zubeir Ali Maulid, Mawaziri wa Tanzania Bara na Zanzibar, Mabalozi, Wakuu wa Mikoa na viongozi wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama.
Kesho tarehe 15 Oktoba, 2019 Mhe. Rais Magufuli ambaye ameongozana na Mkewe Mama Janeth Magufuli ataendelea na ziara yake Mkoani Lindi ambapo atazindua barabara za Mji wa Ruangwa, ataweka jiwe la msingi la ujenzi wa ghala la mazao la Kijiji cha Lipande Wilayani Ruangwa na atahutubia mkutano wa hadhara Mjini Ruangwa.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Lindi
14 Oktoba, 2019
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 12 Oktoba, 2019 amemaliza ziara yake ya kikazi ya siku 9 katika Mikoa ya Songwe, Rukwa na Katavi kwa kuzindua safari za ndege za Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) za Dar es Salaam – Mpanda (Mkoani Katavi).
Hafla ya uzinduzi wa safari hizo imefanyika katika uwanja wa ndege wa Mpanda na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Mke wa Rais Mama Janeth Magufuli, Mawaziri, Wabunge, viongozi wa Dini, viongozi wa vyama vya siasa na viongozi wa Mkoa wa Katavi wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa huo Mhe. Juma Homera.
Mkurugenzi Mtendaji wa ATCL Mhandisi Ladislaus Matindi amesema shirika hilo litaanza kwa kufanya safari moja kwa wiki na baadaye mwaka huu litaongeza hadi safari tatu kwa wiki kutokana na mahitaji makubwa ya usafiri wa ndege kwa wakazi wa Katavi, Mikoa jirani na nchi jirani.
Akizungumza na wananchi waliojitokeza kushuhudia tukio, Mhe. Rais Magufuli ameipongeza ATCL kwa kuitikia wito alioutoa siku 3 zilizopita, alipoagiza shirika hilo kuanza safari za kwenda Mpanda ndani ya wiki 1 baada ya kupokea maombi ya wananchi.
Mhe. Rais Magufuli ameelezea dhamira ya Serikali kuendelea kuimarisha usafiri wa anga kwa wananchi na kukuza uchumi kupitia utalii, biashara, uwekezaji na kwamba pamoja na ndege nyingine mpya 1 kuja baadaye mwaka huu, Serikali imenunua ndege zingine 3 kwa lengo la kuimarisha zaidi usafiri wa anga.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli amezungumzia zoezi la uandikishaji orodha ya wapiga kura wa Mamlaka ya Serikali za Mitaa 2019 ulioanza tarehe 08 Oktoba, 2019 na utamalizika tarehe 14 Oktoba, 2019 ambapo ameonya kuwa viongozi wa Mikoa na Wilaya ambao Mikoa na Wilaya zao hazitafanya vizuri katika uandikishaji huo wasimlaumu kwa hatua atakazochukua.
Halikadhalika, Mhe. Rais Magufuli amezungumzia utekelezaji wa ushauri alioutoa kwa watu wanaokabiliwa na mashtaka ya uhujumu uchumi ambapo amesema hadi sasa watu 138 wameachiwa huru baada ya kuomba msamaha na kurejesha Mabilioni ya fedha na kwamba zoezi hilo linaendelea kwa wengine takribani 500 walioomba msamaha huo.
Baada ya kuzindua safari za ndege za ATCL, Mhe. Rais Magufuli akiwa na Mkewe Mama Janeth Magufuli amesafiri kwa ndege ya ATCL aina ya Bombardier Dash 8 - Q400 kutoka Mpanda Mkoani Katavi kwenda Dodoma ambako atajiandikisha katika orodha ya wapiga kura wa Serikali za Mitaa 2019.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Mpanda
12 Oktoba, 20
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 11 Oktoba, 2019 ameendelea na ziara yake Mkoani Katavi ambapo ameweka jiwe la msingi la mradi wa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme ya msongo wa kilovoti 132 kutoka Tabora hadi Katavi, ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Tanganyika na ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa barabara ya lami ya Mpanda – Ifukutwa – Vikonge.
Mradi wa umeme utakaokamilika miezi 10 ijayo, unahusisha ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme yenye urefu wa kilometa 379 na ujenzi wa kituo cha kupooza na kusambaza megawati 100 za umeme, kiasi ambacho ni kikubwa ikilinganishwa na matumizi ya sasa ya Mkoa wa Katavi unaotumia megawati 5.
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani amesema mradi huo ambao utagharimu shilingi Bilioni 135.3 utasaidia kupunguza gharama kubwa za uzalishaji wa umeme katika Mkoa wa Katavi ambao unatumia shilingi Bilioni 6.8 kwa mwaka kuzalisha umeme kwa kutumia jenereta la mafuta ikilinganishwa na mapato ya shilingi Bilioni 1.4, na utauwezesha Mkoa huo kuunganishwa na Gridi ya Taifa.
Pamoja na kuwahakikishia wananchi wa Katavi kuwa vijiji vyote 172 na vitongoji 1,444 vya Mkoa huo vitapatiwa umeme, Dkt. Kalemani amesema Serikali itatekeleza awamu ya pili ya mradi huo utakaohusisha ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme ya msongo wa kilovoti 400 yenye urefu wa kilometa 1,372 kutoka Iringa – Mbeya – Tunduma – Sumbawanga – Mpanda – Kigoma hadi Nyakanazi.
Dkt. Kalemani amefafanua kuwa mradi huo utagharimu Dola za Marekani Milioni 576 sawa na takribani shilingi Trilioni 1 na Bilioni 312 na utawezesha kuunganishwa katika Gridi ya Taifa kwa ukanda wa nyanda za juu kusini, magharibi na kaskazini magharibi ambao unatumia umeme unaozalishwa kwa majenerata ya mafuta.
Hospitali ya Wilaya ya Tanganyika ambayo inajengwa katika Kijiji cha Majalila ni miongoni mwa hospitali mpya za hadhi ya Wilaya 69 zinazojengwa hapa nchini ambapo Serikali imetoa shilingi Bilioni 1.5 kwa kila moja, na kwa Mkoa wa Katavi hospitali zingine 2 zinajengwa katika Halmashauri za Wilaya ya Mpimbwe na Mlele.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe. Selemani Jafo amesema Serikali imetenga fedha zingine shilingi Bilioni 33.5 kwa ajili ya kuongeza shilingi Milioni 500 kwa kila Hospitali mpya ya Wilaya ili kuimarisha uwekaji wa vifaa.
Ujenzi wa barabara ya lami ya Mpanda – Ifukutwa – Vikonge yenye urefu wa kilometa 37.6 ambao ni sehemu ya barabara kuu ya Tunduma – Sumbawanga – Mpanda – Kigoma – Nyakanazi yenye urefu wa kilometa 1,286 utagharimu shilingi Bilioni 58 na Milioni 979 hadi utakapokamilika Machi 2020.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mhandisi Patrick Mfugale amesema jumla ya kilometa 530 za barabara za ukanda wa magharibi kuanzia Tunduma – Sumbawanga – Mpanda – Uvinza – Nyakanazi ujenzi wake umekamilika na kilometa zingine 597 za barabara za lami ujenzi wake upo katika hatua mbalimbali za ujenzi.
Akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika Majalila Wilayani Tanganyika, Mhe. Rais Magufuli amewapongeza wananchi wa ukanda wa magharibi mwa Tanzania kwa kupata miundombinu hiyo ya umeme, barabara na matibabu na hivyo ametoa wito kwa wananchi hao kuongeza uzalishaji mali kwa kuchapa kazi zaidi ili Serikali iendelee kuwapelekea maendeleo kwa kutumia fedha za ndani.
Mhe. Rais Magufuli amempongeza Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika Bw. Salehe Mhando na viongozi wenzake Wilayani humo kwa kusimamia vizuri maendeleo ya Wilaya yao hasa ujenzi wa Hospitali ya Wilaya na Vituo vya Afya, lakini amewaagiza kuhakikisha ifikapo tarehe 30 Oktoba, 2019 wanahamisha ofisi zao kutoka Mjini Mpanda na kwenda Majalila ambako ndio Makao Makuu ya Wilaya, na ameagiza jina la Halmashauri ya Wilaya hiyo libadilishwe na kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika badala ya Halmashauri ya Wilaya ya Mpanda Vijijini.
Amemuagiza Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhe. Isack Kamwelwe kutangaza zabuni ya kilometa 50 za ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami kuanzia Vikonge kuelekea Uvinza na kubainisha kuwa Serikali itaendelea kujenga barabara hiyo mpaka ikamilike.
Kuhusu mradi wa umeme, Mhe. Rais Magufuli ameipongeza Wizara ya Nishati na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kwa kutumia mafundi wake kujenga njia ya Umeme ya Tabora – Katavi hali inayosaidia kuokoa fedha nyingi ambazo zingelipwa kwa wakandarasi na ameelezea kufurahishwa kwake na kazi ya usambazaji wa umeme ambapo idadi ya vijiji vilivyounganishwa umeme kupitia mradi wa umeme vijijini (REA) imeongezeka kutoka vijiji takribani 2,000 mwaka 2015 hadi kufikia vijiji 8,100 hivi sasa na pia TANESCO kutotegemea ruzuku ya Serikali ikilinganishwa na hapo awali ilipokuwa inapewa shilingi Bilioni 200 kwa mwaka.
Mhe. Rais Magufuli amewataka wakimbizi wa Burundi waliopo Mkoani Katavi kuacha kujihusisha na vitendo vya uhalifu ikiwemo ujambazi, na ameagiza kuanzia sasa Mkoa wa Katavi kuwa chini Brigedi ya Tabora ya Jeshi la Ulinzi la Watanzania Tanzania (JWTZ) na uwanja wa ndege wa Mlibanzi uliopo katika msitu wa Tongwe kuwa chini ya Jeshi.
Pia Mhe. Rais Magufuli amesema Serikali imetenga shilingi Bilioni 40 kwa ajili ya kujenga bandari ya Kalema Mkoani humo, na sambamba na hilo amemuagiza Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Luhaga Mpina kuanza mchakato wa kujenga kiwanda cha samaki jirani na bandari hiyo.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Mpanda
11 Oktoba, 2019
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amesema Watanzania wana kila sababu ya kutangaza na kujivunia mafanikio makubwa yaliyopatikana katika kipindi kifupi cha miaka minne iliyopita na ameahidi kuendelea kusimamia rasilimali za Taifa ili ziwanufaishe zaidi.
Mhe. Rais Magufuli ameyasema hayo tarehe 10 Oktoba, 2019 wakati akihutubia wananchi wa Mkoa wa Katavi katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa Azimio Mjini Mpanda.
Amesema juhudi kubwa zilizofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano kubana mianya ya wizi, ufisadi, rushwa, matumizi mabaya ya ofisi na mali za umma na kudhibiti nidhamu kwa watumishi wa umma zimesaidia kuokoa fedha nyingi ambazo zimetumika kutekeleza miradi mingi ya maendeleo ikiwemo ile ambayo ilionekana kutowezekana.
Mhe. Rais Magufuli ametaja baadhi ya miradi hiyo kuwa ni ujenzi wa Bwawa la kuzalisha umeme la Nyerere ambao utagharimu shilingi Trilioni 6.5, ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa (standard gauge railway – SGR) utakaogharimu shilingi Trilioni 7.2, ununuzi wa ndege, ujenzi wa barabara na madaraja makubwa, ujenzi wa vituo vya afya na Hospitali za Wilaya, ujenzi wa miundombinu ya elimu na kutoa shilingi Bilioni 23.8 kila mwezi kwa ajili ya kugharamia elimu bila malipo kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari.
“Ni lazima tujiulize maswali sisi Watanzania bila uoga na bila kumuonea mtu, kama tumeongeza ukusanyaji mapato kutoka Bilioni 850 hadi Trilioni 1.3 na mwezi uliopita tumekusanya shilingi Trilioni 1.7, kama tumejenga Vituo vya Afya 352 kwa mpigo, tumejenga Hospitali za Wilaya 69 wakati tangu tupate uhuru tulikuwa na Hospitali za Wilaya 77 tu, hela hizo zilikuwa zinakwenda wapi? Ukweli unabaki palepale, kama tumenunua ndege na sasa zitakuwa 11 kwa nini hatukununua miaka 50 iliyopita? Nyerere alipoondoka aliacha ndege, zote zimepotea, zipo wapi? Hilo nalo ukisema ni nongwa ndugu zangu, ukitaka kupima maendeleo ni lazima ujue mahali ulipotoka, mahali ulipo na mahali unapokwenda, hicho ndicho kipimo cha maendeleo cha kila mtu, treni ilikua inakufa mpaka tukabinafsisha kwa watu wengine, hapa Mpanda mlikuwa hamuoni treni, leo treni inakuja, ndugu zangu mnasahau? Amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Amewataka viongozi wote wa Serikali, siasa, Dini na taasisi binafsi kuyatangaza mafanikio hayo makubwa ili Watanzania wajue nchi yao inakokwenda na wapate moyo zaidi wa kuendelea kuijenga kwa kuchapa kazi kwa juhudi na maarifa.
Mhe. Rais Magufuli amempongeza Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mhe. Juma Homera kwa juhudi kubwa alizozifanya kusimamia maendeleo ya Mkoa huo katika kipindi kifupi cha miezi 4 tangu ateuliwe kuongoza Mkoa huo ambapo amefanikiwa kusimamia uanzishaji wa soko la madini na hivyo kuongeza ukusanyaji wa mapato kutoka shilingi laki 6 kwa mwezi hadi kufikia shilingi Milioni 148, kusimamia masoko ya mazao ya tumbaku, pamba na mahindi, kutatua kero za wananchi ikiwemo migogoro ya ardhi na mkakati wa kuanzisha viwanda.
Mhe. Rais Magufuli ameahidi kuwa Serikali itatoa fedha za kujenga kiwanda cha kuchambua pamba (Ginnery) katika Mkoa wa Katavi ambacho kitagharimu shilingi Bilioni 1.6 lakini amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Katavi na Wizara ya Kilimo kuhakikisha wakulima wa pamba ambao hawajapata malipo ya kilo Milioni 6 za pamba wanalipwa ndani ya siku 7.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli ameiagiza Wizara ya Maji na Mkoa wa Katavi kufuatilia miradi ya maji ambayo utekelezaji wake unasuasua Mkoani humo ikiwemo miradi 9 yenye thamani ya shilingi Bilioni 3.109.
Mhe. Rais Magufuli ameelezea kusikitishwa na taarifa baadhi ya wakimbizi wa kutoka nchi jirani wanaodaiwa kujihusisha na vitendo vya uhalifu Mkoani Katavi na ametoa wito kwa wakimbizi hao kuacha vitendo hivyo na Vyombo vya Dola kuhakikisha uhalifu huo unakomeshwa.
Kabla ya mkutano huo, Mhe. Rais Magufuli amefungua barabara ya lami ya Sitalike – Mpanda yenye urefu wa kilometa 36.9 ambayo imegharimu shilingi Bilioni 39.8 (fedha zote zimetolewa na Serikali ya Tanzania) na pia ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa barabara ya Tabora (Usesula) – Konga – Mpanda yenye urefu wa kilometa 342.9 ambayo itakapokamilika Machi 2021 itagharimu shilingi Bilioni 450.
Pia Mhe. Rais Magufuli amefungua Kituo Kikuu cha Mabasi cha Mkoa wa Katavi kiitwacho Mizengo Pinda, ambacho ujenzi wake umegharimu shilingi Bilioni 4.4 na amewapongeza wananchi wa Manispaa ya Mpanda kwa kupata kituo hicho pamoja na kujengewa barabara mpya za Mjini zenye urefu wa kilometa 7.7 kwa gharama ya shilingi Bilioni 8 hali inayoufanya Mji huo kuwa nadhifu.
Kesho tarehe 11 Oktoba, 2019 Mhe. Rais Magufuli ambaye ameongozana na Mkewe Mama Janeth Magufuli ataendelea na ziara yake Mkoani Katavi ambapo ataweka jiwe la msingi la mradi wa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme ya msongo wa kilowati 132 kutoka Tabora kwenda Mpanda, ataweka jiwe la msingi la ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Tanganyika na ataweka jiwe la msingi la ujenzi wa barabara ya Mpanda – Vikonge.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Mpanda
10 Oktoba, 2019
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 09 Oktoba, 2019 ameendelea na ziara yake katika Mkoa wa Katavi ambapo amefungua barabara ya lami ya Kanazi – Kizi – Kibaoni yenye urefu wa kilometa 76.6 na daraja la Kavuu (lenye urefu wa meta 85.3 na upana wa meta 4.6) lililopo katika barabara ya Majimoto – Inyonga.
Ujenzi wa barabara ya Kanazi – Kizi – Kibaoni ambao ni sehemu ya barabara kuu ya Sumbawanga – Namanyere – Mpanda yenye urefu wa kilometa 245 umegharimu shilingi Bilioni 102.364, fedha zote zimetolewa na Serikali ya Tanzania.
Ujenzi wa daraja la Kavuu ambalo linaunganisha Makao Makuu ya Halmashauri ya Wilaya ya Mpimbwe na Wilaya ya Mlele Mkoani Rukwa, umegharimu shilingi Bilioni 3.6, fedha zote zimetolewa na Serikali ya Tanzania.
Akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika Kibaoni Wilayani Mlele, Mhe. Rais Magufuli amewapongeza wananchi wa Mkoa wa Katavi kwa juhudi kubwa katika uzalishaji wa mazao ya chakula na amewaahidi kuwa Serikali itaendelea kuboresha miundombinu ya barabara na madaraja na kuimarisha zaidi huduma za kijamii ikiwemo kusambaza zaidi umeme na maji.
Mhe. Rais Magufuli ameiagiza Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kuanza maandalizi ya ujenzi wa barabara ya Kibaoni – Sitalike yenye urefu wa kilometa 71 ambayo ni kipande kilichobaki kuunganisha Mkoa wa Rukwa na Katavi kupitia Hifadhi ya Taifa ya Katavi.
Amefafanua kuwa Serikali imedhamiria kuhakikisha barabara kuu kwa kiwango cha lami kutoka Mpanda – Uvinza – Nyakanazi unakamilika ili ukanda wa nyanda za juu kusini unaoiunganisha Tanzania na nchi za Zambia, Malawi hadi Afrika Kusini uunganishwe na ukanda wa magharibi unaounganisha Tanzania na nchi za Burundi, Rwanda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Uganda.
Kuhusu migogoro ya ardhi, Mhe. Rais Magufuli amesema Serikali imeamua vijiji 920 kati ya 975 hapa nchini vilivyopo katika maeneo ya hifadhi kutoondolewa katika maeneo hayo, kufuta mapori ya akiba 12 (yenye jumla ya ekari 707,659.95) na Misitu 7 (yenye jumla ya ekari 46,715) na kumega maeneo katika hifadhi 14 ili kuwawezesha wananchi kupata maeneo ya kuishi, kilimo na ufugaji na kwamba katika uamuzi huo vijiji 60 vilivyonufaika ni vya Mkoa wa Katavi.
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. William Lukuvi amefafanua kuwa pamoja na hatua hiyo, wataalamu wa ardhi watapita katika vijiji hivyo ili kutoa elimu ya matumizi bora ya ardhi ili kuepusha migogoro inayoweza kujitokeza baina ya wananchi.
Hata hivyo, Mhe. Rais Magufuli ameonya kuwa baada ya Serikali kuchukua uamuzi huo, haitarajii kuona wananchi wanaendelea kuvamia maeneo ya hifadhi na amewataka wananchi wa Katavi kutumia maeneo hayo kuzalisha zaidi mazao mbalimbali ili kujiongezea kipato.
Akiwa njiani kutoka Namanyere katika Wilaya ya Nkasi Mkoani Rukwa kuelekea Mpanda Mkoani Katavi, Mhe. Rais Magufuli amesalimiana na wananchi wa Kizi (Nkasi) na Mirumba (Mlele) na baadaye amesalimiana na wananchi wa Sitalike Wilayani Mpanda ambapo amewahakikishia kuwa vitongoji vya Igalukilo, Kabenga, Kaloleni na Situbwike havitaondolewa katika maeneo ya hifadhi kufuatia uamuzi wa Serikali wa kuvirasimisha vitongoji hivyo.
Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli ametembelea Hifadhi ya Taifa ya Katavi na kisha kuzungumza na Maafisa na Askari Wanyamapori wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) ambapo amewapongeza kwa kazi nzuri ya kuhifadhi wanyamapori ikiwemo kukabiliana na ujangili hali iliyowezesha kuongezeka kwa idadi wanyama wakiwemo wale waliokuwa hatarini kutoweka.
Mhe. Rais Magufuli amemtaka Kamishna wa Uhifadhi wa TANAPA Dkt. Allan Kijazi kuchimba mabwawa ya kuvuna maji mengi zaidi ya mvua yatakayowasaidia wanyama hasa viboko wakati wa kiangazi kikali pamoja na kujipanga kuzuia wanyama wakali wanaoweza kuvamia makazi ya watu na kuhatarisha maisha ya wananchi.
Kesho tarehe 10 Oktoba, 2019 Mhe. Rais Magufuli ambaye ameongozana na Mkewe Mama Janeth Magufuli ataendelea na ziara yake hapa Mkoani Katavi ambapo atazindua Kituo cha Mabasi cha Mkoa wa Katavi, ataweka jiwe la msingi la ujenzi wa barabara ya Mpanda – Sitalike na kuhutubia mkutano wa hadhara katika uwanja wa Azimio Mjini Mpanda.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Mpanda
09 Oktoba, 2019
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 08 Oktoba, 2019 amefungua barabara ya Sumbawanga – Kanazi, ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Nkasi, amefungua Kituo cha Afya Nkomolo na kuzindua uandikishaji katika orodha ya wapiga kura wa Mamlaka za Serikali za Mitaa (2019) ulioanza leo hapa nchini.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mhandisi Patrick Mfugale amesema ujenzi wa barabara ya Sumbawanga – Kanazi yenye urefu wa kilometa 75 ambayo ni sehemu ya barabara ya Sumbawanga – Kanazi – Mpanda yenye urefu wa jumla ya kilometa 245, uliogharimu shilingi Bilioni 100.7 umekamilika mwaka 2017 na barabara hiyo imekabidhiwa mwaka 2018.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Selemani Jafo amesema Hospitali ya Wilaya ya Nkasi ambayo inajengwa kwa ghamara ya shilingi Bilioni 1 na Milioni 500 ni moja kati ya hospitali mpya 69 zenye hadhi ya Wilaya zinazojengwa hapa nchini na kwamba katika bajeti ya mwaka huu Serikali imetenga fedha za ujenzi wa Hospitali zingine 27 na kufanya jumla ya hospitali zenye hadi ya wilaya zilizojengwa katika Awamu ya tano kufikia 96.
“Mhe. Rais tunakushukuru na kukupongeza sana kwa kutoa kipaumbele katika ujenzi wa miundombinu ya kutolea huduma za afya, kwa miaka miwili tu unajenga Hospitali za Wilaya 96 wakati nchi yetu tangu ipate uhuru ilifanikiwa kujenga Hospitali za Wilaya 77 tu hadi mwaka 2015” amesema Mhe. Jafo katika Mkutano wa hadhara uliofanyika Mjini Namanyere, Wilaya ya Nkasi Mkoani Rukwa.
Kituo cha Afya Nkomolo kilichojengwa kwa gharama ya shilingi Milioni 500 tayari kimeanza kutoa huduma na kimefunguliwa kwa niaba ya vituo vingine 10 vya Mkoa wa Rukwa ambavyo vimejengwa katika Wilaya zote za Mkoa huo.
Mhe. Rais Magufuli amezindua uandikishaji katika orodha ya wapiga kura wa Mamlaka za Serikali za Mitaa ambao umeanza nchini kote leo tarehe 08 Oktoba, 2019 hadi tarehe 14 Oktoba, 2019 na amewataka Watanzania kujitokeza kwa wingi kujiandikisha ili waweze kushiriki kupiga kura na kuchagua viongozi wanaowafaa katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika tarehe 24 Novemba, 2019.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara Mjini Namanyere, Mhe. Rais Magufuli amewapongeza wananchi wa Nkasi na Mkoa mzima wa Rukwa kwa maendeleo makubwa ya kuimarishwa kwa miundombinu ya barabara, hospitali, vituo vya afya, umeme na huduma nyingine na amewahakikishia kuwa Serikali itaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya kuboresha zaidi maisha ya wananchi.
Mhe. Rais Magufuli ambaye akiwa njiani kutoka Sumbawanga kwenda Namanyere Wilayani Nkasi amesalimiana na wananchi wa Ntendo, Nkundi, Milundikwa, Kasu na Chala amewataka wataalamu wa Wizara ya Maji kubadilika na kubuni mbinu za kutatua matatizo ya maji yanayowakabili wananchi, ikiwemo kuvuna maji ya mvua katika mabonde yaliyopo katika maeneo mengi yenye tatizo la ukosefu wa maji.
Akiwa katika mkutano huo wa hadhara, Mhe. Rais Magufuli amesikiliza kilio cha Mama Mjane aitwaye Felista Mkombo ambaye aliibiwa ng’ombe 25 lakini Askari Polisi walimwachia mtuhumiwa na baadaye akafanikiwa kutoroka, ambapo ameagiza Polisi wakiongozwa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Rukwa Mathias Nyange na Mkuu wa Wilaya ya Nkasi Mhe. Said Mtanda kumlipa Mama huyo shilingi Milioni 15 kama fidia kutokana na kutoshughulikia vizuri tatizo lake.
Mhe. Rais Magufuli ameelezea kusikitishwa na namna viongozi wa Mkoa wa Rukwa wasivyoshughulikia kero za wananchi na mara baada ya kumaliza hotuba yake ameagiza viongozi hao wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa Mhe. Joachim Wangabo kubaki mkutanoni hapo ili wasikilize kero za wananchi wote waliokuwa wamebeba mabango na kumpatia taarifa.
“Tatizo la Mkoa huu viongozi hamshughulikii kero za wananchi, kila mahali wananchi wanalalamika na hata hapa kuna mabango mengi ya wananchi wenye kero mbalimbali, sasa nataka mbaki hapa muwasikilize na mnipe taarifa” ameagiza Mhe. Rais Magufuli.
Amempongeza Mbunge wa Nkasi Mhe. Ally Kessy kwa jinsi anavyoshughulikia kero za wananchi na kufuatilia miradi ya maendeleo na amemuahidi kuwa Serikali itachukua hatua kutatua kero hizo pamoja kuwachukulia hatua watumishi wa umma ambao wamekuwa wakishirikiana na wakandarasi kuiba fedha za miradi.
Kesho tarehe 09 Oktoba, 2019, Mhe. Rais Magufuli ambaye ameongozana na Mkewe Mama Janeth Magufuli ataendelea na ziara yake ambapo atafungua barabara ya Kanazi – Kizi – Kibaoni.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Namanyere, Nkasi
08 Oktoba, 2019