Hotuba
- Apr 24, 2018
HOTUBA YA MHESHIMIWA DKT. JOHN POMBE MAGUFULI, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA KWENYE BUNGE LA AFRIKA MASHARIKI DODOMA, TAREHE 24 APRILI, 2018
Soma zaidiHotuba
HOTUBA YA MHESHIMIWA DKT. JOHN POMBE MAGUFULI,
RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
KWENYE BUNGE LA AFRIKA MASHARIKI
DODOMA, TAREHE 24 APRILI, 2018
Mheshimiwa Martin Ngoga, Spika wa Bunge
la Afrika Mashariki;
Mheshimiwa Job Ndugai, Spika wa Bunge
la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Mheshimiwa Kassim Majaliwa, Waziri Mkuu
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Mheshimiwa Dkt. Ali Kivenjija, Naibu wa Pili
wa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Uganda,
ambaye pia ni Waziri wa Afrika Mashariki
na Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri la
Jumuiya ya Afrika Mashariki;
Waheshimiwa Mawaziri mliopo;
Waheshimiwa Wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki;
Waheshimiwa Wabunge wa Bunge
la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Mheshimiwa Dkt. Liberat Mfumukeko, Katibu Mkuu
wa Jumuiya ya Afrika Mashariki;
Mheshimiwa Balozi John Kijazi, Katibu Mkuu Kiongozi;
Mheshimiwa Binilith Mahenge,
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma;
Waheshimiwa Mabalozi pamoja na Wakuu
wa Taasisi za Kimataifa mliopo;
Wadau Mbalimbali wa Maendeleo mliopo;
Waheshimiwa Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi
na Usalama;
Waheshimiwa Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana:
Najisikia furaha na heshima kubwa kusimama mbele yenu leo kuhutubia kwa mara ya kwanza Bunge la Afrika Mashariki, ambalo nalo linafanyika hapa Dodoma kwa mara ya kwanza. Nakushukuru Mheshimiwa Ngoga, Spika wa Bunge la Afrika Mashariki, kwa kunialika; lakini pia nawashukuru Wabunge wote wa Bunge hili la Afrika Mashariki kwa uamuzi wenu wa kufanya kikao hiki hapa Dodoma.
Kwa hakika, mmefanya uamuzi mzuri sana. Baadhi yenu mnafahamu kuwa moja ya sababu zinazotajwa kusababisha kuvunjika kwa Jumuiya yetu ya mwanzo ya Afrika Mashariki mwaka 1977, ilikuwa ushiriki mdogo wa sekta binafsi na wananchi. Wananchi walio wengi hawakuifahamu vizuri Jumuiya yetu. Hivyo basi, utaratibu huu wa kufanya vikao vya Bunge hili sehemu tofauti tofauti ndani ya Jumuiya unatoa fursa kwa wana-Afrika Mashariki wote kuifahamu vyema Jumuiya yao, shughuli inazofanya pamoja na manufaa yake.
Kwa sababu hiyo, napenda kurudia tena kupongeza uamuzi huu wa kufanya kikao hapa Dodoma. Na niseme tu kwamba hamjakosea kuamua kufanya kikao chenu hapa Dodoma. Hapa ni katikati mwa nchi yetu. Ni Makao Makuu ya Serikali pamoja na Chama Tawala, Chama Cha Mapinduzi (CCM). Sambamba na hilo, wananchi wa Dodoma ni wakarimu. Lakini hapa Dodoma kuna sifa nyingine. Hapa ni maarufu sana kwa kuzalisha zabibu tamu zaidi duniani, ambayo hata ukinywa mvinyo wake huwezi kupata “hangover”. Kwa hiyo, unaweza kufanya mkutano mchana, jioni ukapata mvinyo na kesho yake ukaendelea na Mkutano kama kawaida. Haya yote yanafanya Dodoma iwe sehemu nzuri sana ya kufanyia Mikutano. Hivyo basi, ni imani yangu kuwa Waheshimiwa Wabunge wa Afrika Mashariki mmefurahia uwepo wenu hapa Dodoma.
Waheshimiwa Viongozi;
Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;
Nimetangulia kusema kuwa hii ni mara yangu ya kwanza kuhutubia Bunge hili tangu nichaguliwe kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwezi Oktoba 2015. Lakini, nafahamu pia kuwa Bunge hili la Nne la Afrika Mashariki, nalo ni jipya. Limeanza kazi mwezi Desemba 2017. Hivyo basi, napenda kutumia fursa hii kuwapongeza Wabunge wote wa Bunge hili la kwa kuchaguliwa kwenu. Hakuna shaka, mmechaguliwa kwa vile wana-Afrika Mashariki wana imani kubwa juu yenu. Wana uhakika kuwa mtawawakilisha vyema katika kusukuma mbele gurudumu la maendeleo la Jumuiya yetu. Niwaombe sana msiwaangushe.
Naomba pia mniruhusu kutumia fursa hii, kwa namna ya pekee kabisa, kumpongeza Mheshimiwa Ngoga kwa kuchaguliwa kuwa Spika wa Bunge hili. Kwa bahati nzuri, yeye ni Spika wa Tano wa Bunge la Afrika Mashariki. Na mimi ni Rais wa Awamu ya Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hivyo basi, namuahidi kumpa ushirikiano wa kutosha katika kipindi chote cha uongozi wake wa Bunge hili.
Mheshimiwa Spika na Waheshimiwa Wabunge;
Wakati ninapowapongeza kwa kuchaguliwa, napenda mtambue kuwa jukumu lililo mbele yenu ni kubwa sana. Ninyi ni Wawakilishi na pia ni sauti ya wana-Afrika Mashariki wote. Hili ni jukumu kubwa. Lakini, zaidi ya hapo, kama mnavyofahamu, mmechaguliwa katika kipindi cha kipekee sana. Kipindi ambacho Jumuiya yetu imepiga hatua kubwa za kimaendeleo lakini pia inakabiliwa na changamoto nyingi.
Kama mjuavyo, Ukanda wetu wa Afrika Mashariki hivi sasa unasifika kwa ukuaji uchumi wa kasi duniani. Aidha, tumefanikiwa kwa kiwango kikubwa kuondoa vikwazo vya biashara na uwekezaji. Hii imefanya biashara na uwekezaji miongoni mwa Nchi Wanachama kuongezeka maradufu. Mathalan, kabla ya kuanza kwa Umoja wa Forodha (Customs Union) mwaka 2005 biashara yetu (yaani intra-East African trade) ilikuwa na thamani ya Dola za Marekani bilioni 1.8. Lakini, tangu tuanzishe Umoja wa Forodha na kuanza kutekeleza Itifaki ya Soko la Pamoja (Common Market), biashara yetu imeongezeka hadi kufikia zaidi ya Dola za Marekani bilioni 5 hivi sasa. Zaidi ya hapo, idadi ya wanachama nayo inaongezeka, na kuna nchi nyingi tu zinatamani kujiunga nasi.
Haya, bila shaka, ni mafanikio makubwa. Hivyo basi, ninyi Waheshimiwa Wabunge wa Bunge la Nne la Afrika Mashariki mnao wajibu mkubwa kwanza wa kuhakikisha mafanikio haya yanalindwa lakini pili yanaendelezwa kwa nguvu zaidi. Na katika hilo, nimefurahi kusikia kuwa kwenye kikao chenu hiki, pamoja na masuala mengine, mmejadili Miswada miwili muhimu; mmoja kuhusu Taasisi ya Fedha ya Jumuiya (East African Monetary Institute) na mwingine kuhusu Takwimu (Statistics Bill). Kama mnavyofahamu, Jumuiya yetu imeweka hatua nne za ushirikiano. Utekelezaji wa hatua mbili za mwanzo, yaani Umoja wa Forodha na Soko la Pamoja, kama nilivyoeleza awali unaendelea. Sasa tunaelekea hatua ya tatu, ambayo ni Ushirikiano wa Masuala ya Kifedha (Monetary Union). Ili kufikia hatua hiyo, miswada hii miwili mliyoijadili ni muhimu sana. Hivyo basi, nawapongeza sana kwa kuijadili miswada hiyo.
Sambamba na hilo, nimeambiwa kuwa kabla ya kuja hapa Dodoma, mmetembelea miradi mbalimbali ya maendeleo kwenye Jumuiya yetu kwa lengo la kujielimisha na kujionea wenyewe utekelezaji wake. Hapa nchini, mmetembelea Bandari ya Dar es Salaam, Kituo cha Ukaguzi wa Magari pale Vigwaza, Zanzibar; lakini pia mmeshiriki kwenye zoezi la upandaji miti katika Chuo Kikuu cha Dodoma. Hili nalo ni jambo jema. Moja ya majukumu mliyonayo ni kusimamia utekelezaji wa maamuzi na miradi ya maendeleo. Hivyo basi, nawapongeza kwa kuamua kutembelea maeneo hayo ili kujionea utekelezaji wa miradi hiyo ya maendeleo.
Mheshimiwa Spika na Waheshimiwa Wabunge
wa Bunge Afrika Mashariki;
Kama nilivyosema awali, mbali na mafanikio yaliyopatikana, Jumuiya yetu pia inakabiliwa na changamoto kadha wa kadha. Tuna matatizo ya migogoro, ambayo imekuwa ikigharimu maisha ya watu wengi. Vikwazo vya biashara na uwekezaji pia bado vipo. Kuna changamoto za kutoaminiana. Changamoto hizi na nyingine ambazo sikuzitaja, ninyi Wabunge, mkiwa sauti na wawakilishi wa wana-Afrika Mashariki wote, mnao wajibu wa kuzitafutia majibu ili kuzimaliza, na hatimaye kuweza kuimarisha utengamano wa Jumuiya yetu na halikadhalika kujenga umoja miongoni mwa viongozi, watendaji na wana-Afrika Mashariki wote kwa ujumla.
Kama mjuavyo, sisi wana-Afrika Mashariki ni kitu kimoja. Hivyo, tunapaswa kupendana. Sisi ni ndugu. Mheshimiwa Spika Ngoga ni raia wa Rwanda lakini nafahamu ameishi na kusoma hapa nchini hadi Chuo Kikuu. Lugha yetu pia ni moja, na nimefurahi Mheshimiwa Spika Ngoga umesisitiza umuhimu wa kutumia lugha ya Kiswahili kwenye shughuli zetu badala ya kuendelea kutumia za Mataifa mengine. Haya yote yonadhihirisha kuwa sisi ni ndugu. Nimefurahi hata hapa mmekaa kama ndugu na watu wanaopendana. Hivi ndivyo haswaa inapaswa iwe. Hatupaswi kutengana, bali kushirikiana katika kuleta maendeleo kwa nchi zetu pamoja na Jumuiya yetu kwa ujumla. Tusipofanya hivya hivyo, tutawaangusha wananchi wetu ambao wanatuamini.
Mheshimiwa Spika na Waheshimiwa
Wabunge wa Afrika Mashariki
Ukiachilia mbali changamoto hizo nilizozitaja, zipo changamoto nyingine mbili zenye kuikabili Jumuiya yetu ambazo naomba mniruhusu nizielezee kidogo. Changamoto ya kwanza, ni ukosefu wa viwanda. Nchi zetu zina utajiri mkubwa wa rasilimali. Tuna madini, mifugo, bidhaa za kilimo, uvuvi, misitu, n.k. Kwa bahati mbaya, utajiri huo bado haujatunufaisha vya kutosha. Na moja ya mambo yenye kusababisha hali hii ni kukosekana kwa viwanda kwenye nchi zetu. Matokeo yake tumekuwa tukiuza rasilimali hizo nje ya nchi huku zikiwa ghafi na hivyo kutukosesha mapato ya kutosha. Kama mnavyofahamu, bei ya bidhaa ghafi kwenye soko la dunia mara nyingi huwa zipo chini. Mbali na upotevu huo wa mapato, tatizo jingine, ambalo mimi naliona kuwa kubwa, ni kwamba, kwa kuuza rasilimali ghafi nje ya nchi, maana yake tunapeleka fursa za ajira kwa watu wa mataifa mengine. Kama tungekuwa na viwanda vyetu vya kuchakata, kusindika au kuongeza thamani rasimali hizo, fursa hizo za ajira zingeenda kwa wananchi wetu.
Ni kwa kutambua hilo, Serikali ninayoiongoza imeweka mkazo mkubwa sana kwenye suala la ujenzi wa viwanda. Na nafurahi mwitikio umekuwa mkubwa. Wawekezaji wengi, wakiwemo kutoka Nchi Wanachama wa Afrika Mashariki, hivi sasa wanawekeza kwenye sekta ya viwanda hapa nchini. Nitumie fursa hii, kuwaomba Waheshimiwa Wabunge wa Afrika Mashariki kulipa mkazo suala hili la ujenzi wa viwanda, hususan kwa kuhakikisha Sera na Sheria zinazotungwa kwenye Jumuiya yetu pamoja na Nchi Wanachama zinawavutia wawekezaji wengi, lakini pia zinalinda viwanda vyetu. Ndio! Ni lazima tulinde viwanda vyetu. Tusipofanya hivyo, vitakufa. Jumuiya yetu ina watu wapatao milioni 170. Hili ni soko kubwa kwa viwanda vyetu.
Mheshimiwa Spika na Waheshimiwa Wabunge;
Changamoto ya pili ambayo ningependa kuielezea inahusu uimarishaji wa miundombinu, hususan ya usafiri na nishati ya umeme. Miundombinu hii ni muhimu sana katika kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi miongoni mwa Mataifa. Hata suala la kukuza sekta ya viwanda haliwezi kufanikiwa endapo nchi zetu hazitaboresha au kuimarisha miundombinu hii. Lakini, kwa bahati mbaya, tafiti nyingi zilizofanyika miaka ya nyuma kidogo iliyopita zilionesha kuwa Ukanda wetu wa Afrika unakabiliwa na matatizo ya miundombinu ya usafiri na nishati ya umeme. Hii imefanya gharama za usafiri na umeme kuwa juu. Mathalan, tafiti zilionesha kuwa gharama za usafiri kwenye Ukanda wetu ni mara 4 hadi 5 ukilinganisha na nchi za Asia Mashariki, Marekani na Ulaya; na zinachangia kuongeza gharama za bidhaa kwa asilimia 40.
Sekta ya umeme pia ina matatizo. Mathalan, kwa mujibu wa Power Africa, mwaka 2015, nchi zote sita wanachama wa Afrika Mashariki, ukijumlisha Sudan Kusini, zilikuwa na takriban Megawati 6,500. Nadhani sio lazima mtu awe mtaalam wa hesabu au uchumi ili kufahamu kuwa kiwango hiki cha umeme ni kidogo kuweza kuhimili mahitaji ya uchumi wa kisasa. Na mbaya zaidi ni kwamba, hata bei ya umeme nayo ipo juu ukilinganisha na maeneo mengine duniani. Hali hii imechangiwa na mambo mengi; mojawapo nchi zetu kushindwa kutelekeleza miradi ya umeme kwa kutumia vyanzo vilivyopo. Tumekuwa tukiwategemea sana wawekezaji kutoka nje ambapo wengi wanataka kupata faida kubwa.
Mheshimiwa Spika na Waheshimiwa Wabunge;
Pamoja na changamoto za miundombinu nilizozitaja, ni wazi kuwa katika miaka ya hivi karibuni, Nchi Wanachama zimejitahidi sana kuimarisha miundombinu. Kwa mfano, kwenye barabara, hivi sasa mtu anaweza kutoka hapa Dodoma kwenda Kampala, ama Kigali au Nairobi kwa barabara ya lami. Na barabara nyingi bado zinaendelea kujengwa. Sisi Tanzania hivi sasa tunaendelea na ujenzi barabara za kuungaisha mikoa ya Tabora, Rukwa na Kigoma ambazo zitarahisisha usafiri kati yetu na wenzetu wa Burundi na Rwanda. Aidha, tunajenga barabara ya Nyakanazi hadi Kidahwe ambayo itaboresha usafiri kati yetu na wenzetu wa Uganda.
Ukiachilia mbali barabara, hivi sasa ndani ya Jumuiya yetu kuna miradi mingi mikubwa ya miundombinu ya usafiri inatekelezwa; na baadhi inatekelezwa kwa ushirikiano wa Nchi Wanachama. Mathalan, Kenya tayari wamekamilisha ujenzi wa reli ya kisasa kutoka Bandari ya Mombasa kwenda Nairobi, ambayo inalenga kuboresha usafiri kwenye Ushoroba wa Kaskazini (Northern Corridor). Sisi Tanzania tumeanza kutekeleza mradi wa kupanua Bandari ya Dar es Salaam pamoja na ujenzi Reli ya Kati kwa kiwango cha kimataifa (standard gauge) ili kuboresha usafiri kwenye Ushoroba wa Kati (Central Corridor) ambao unahudumia nchi za Burundi, Rwanda, Uganda na pia nchi ya DRC. Tunakarabati meli zetu na tumeanza kutengeneza meli mpya kubwa kwa ajili ya kuboresha usafiri kwenye Ziwa Victoria. Kama mnavyofahamu, Ziwa hili ni kiungo muhimu cha usafiri kwenye Jumuiya yetu, hususan kwa nchi zinazozunguka Ziwa hilo (Tanzania, Kenya na Uganda). Inakadiriwa kuwa takriban watu milioni 40 wanaishi karibu na Ziwa hili.
Kwenye miundombinu ya usafiri pia tunashirikiana na wenzetu wa Uganda kutekeleza mradi mkubwa wa Bomba la Kusafirisha Mafuta (East African Oil Pipeline) kutoka Hoima hadi Bandari ya Tanga. Tumenunua ndege mpya 6 na tunapanua viwanja vyetu vya ndege 11 ili kuwezesha ndege kubwa kutua. Tunategemea hatua hizi zitaboresha usafiri wa anga sio tu hapa nchini bali kwenye Ukanda mzima wa Afrika Mashariki.
Kuhusu nishati ya umeme; kama mnavyofahamu, nchi yetu imegundua kiasi kikubwa cha gesi. Takriban futi za ujazo trilioni 57. Tumeanza kutumia gesi hiyo kutekeleza miradi ya kuzalisha umeme. Vilevile, tupo mbioni kuanza ujenzi wa mradi mkubwa wa kufufua umeme kwa kutumia maji wa Stiglier’s Gorge, ambao utazalisha takriban Megawati 2,100. Tunataka kwanza tuwe na umeme mwingi ambao ikibidi tutauza hadi kwa Nchi nyingine Wanachama; lakini pili tunalenga kupunguza uzalishaji wa umeme wa mafuta ili kuifanya bei ya umeme nayo iwe chini. Sambama na hayo, tunashirikiana na Nchi nyingine Wanachama kutekeleza baadhi ya miradi. Tunatekeleza na wenzetu wa Kenya mradi wa kusafirisha umeme wa msongo wa kilovoti 400 unaoanzia Zambia, kupita hapa Tanzania na kuelekea Kenya. Tunatekeleza na Uganda mradi wa kufufua umeme wa Kikagati – Murongo. Aidha, tupo kwenye majadiliano na Rwanda pamoja na Uganda kutekeleza mradi wa kuzalisha umeme pale Songezi.
Ni imani yangu kuwa miradi hii, pamoja na ile inayotekelezwa kwenye Nchi nyingine Wanachama itakapokamilika; tutakuwa tumefanikiwa kuimarisha huduma ya usafiri na upatikanaji umeme kwenye nchi zetu. Na hilo likitokea, sio tu tutakuza sekta ya viwanda, bali pia tutaimarisha Jumuiya yetu na kukuza uchumi kwenye nchi zetu. Ombi langu kwa wana-Afrika Mashariki tuendelee kujiamini. Mimi naamini, tukijiamini, tutaweza. Hivi punde, nimeeleza kuhusu ujenzi wa reli, ununuzi wa ndege na ujenzi wa meli mpya; haya yote tunayafanya kwa fedha zetu wenyewe. Naamini hata nchi nyingine zinaweza kufaya hivyo. Nitumie fursa hii pia kutoa wito kwa Sekretarieti ya Afrika Mashariki, kupitia kwa Katibu Mkuu wake ambaye nimefurahi yupo hapa, kuendelea kuratibu na kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa miradi mbalimbali ya miundombinu kwenye Jumuiya. Baadhi ya miradi inachukua muda mrefu kutekelezwa, ukiwemo wa Barabara ya Bagamoyo – Horohoro – Malindi.
Sambamba na hayo, nawasihi Waheshimiwa Wabunge wa Afrika Mashariki nanyi kulipa kipaumbele suala hili la ujenzi wa miundombinu. Kama mnavyofahamu, ujenzi wa miundombinu unahitaji fedha nyingi. Kwenye Mkutano wa Wakuu wa Nchi kuhusu Miundombinu uliofanyika mapema mwaka huu Jijini Kampala ilielezwa kuwa nchi za Afrika Mashariki zinahitaji angalau Dola za Marekani bilioni 78 ili kuboresha na kuimarisha miundombinu. Hiki ni kiasi kikubwa. Hivyo basi, ninyi Waheshimiwa Wabunge mnao wajibu wa kuwashawishi na kuwahamasisha wawekezaji kutoka ndani na nje ya Jumuiya yetu kuwekeza kwenye eneo hili la miundombinu. Nimefurahi leo hapa tunao Waheshimiwa Mabalozi na Wawakilishi wa Taasisi za Kimataifa. Ninaamini wataendelea kutuunga mkono katika eneo hili.
Mheshimiwa Spika wa Bunge la Afrika Mashariki;
Nimeongea mengi. Lakini, kabla sijahitimisha hotuba yangu, naomba uniruhusu niseme mambo machache ya mwisho.
Jambo la kwanza, napenda kutumia fursa hii kueleza kuwa Tanzania ikiwa miongoni mwa waanzilishi wa Jumuiya hii itaendelea kuwa mwanachama mwaminifu. Tutaendelea kushirikiana na Nchi wengine Wanachama katika kutimiza dira na malengo ya Jumuiya hii. Tutaheshimu na kutekeleza maamuzi mbalimbali ambayo kama Nchi Wanachama tutayafikia kwa pamoja. Na katika hili, napenda kuarifu kuwa mwaka jana nchi yetu iliridhia Itifaki ya Jumuiya kuhusu Masuala ya Amani na Usalama (Protocol on Peace and Security). Mapema mwaka huu, nchi yetu imezindua Pasipoti Mpya ya Kielektroniki ya Afrika Mashariki ya Tanzania, kama ilivyoamualiwa na Jumuiya yetu. Hii yote inathibitisha kuwa Tanzania inaheshimu maamuzi ya Jumuiya hii.
Pili, Jumuiya yetu inazidi kukua. Hivi sasa ina Nchi Wanachama sita; na idadi ya watu wapatao milioni 170, kama ilivyoeleza. Hii imeziongezea nguvu nchi zetu. Na kama tukiendelea kushikamana, nina imani, Jumuiya yetu itazidi kuimarika, sauti yake itaongezeka na tutaheshimika kimataifa. Ninyi Wabunge wa Afrika Mashariki ni kiungo muhimu katika kuhakikisha hili linafanikiwa. Mkiwa wawakilishi wa wananchi mnayo nafasi kubwa ya kuwaunganisha wana-Afrika Mashariki wote; lakini pia kuwaelimisha na kuwatahadharisha dhidi ya watu wenye nia mbaya na Jumuiya yetu. Ni wajibu wenu kuwaelimisha wananchi ili umoja na mshikamano wetu uzidi kudumu kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho. Baba wa Taifa letu na mmoja wa waasisi wa Jumuiya hii, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, aliwahi kusema, naomba nimnukuu “Unity will not make us rich, but it can make it difficult for Africa and the African peoples to be disregarded and humiliated”. Mwisho wa kunukuu.
Suala la tatu na mwisho, lakini sio mwisho kwa umuhimu; nadhani nitafanya makosa kama nitahitimisha hotuba yangu bila kueleza japo kwa ufupi hali ilivyo hapa nchini. Kwa ujumla, nchi yetu inaendelea vizuri. Kama mnavyofahamu, tu miongoni mwa nchi tano ambazo uchumi wake unakua kwa kasi Barani Afrika. Mwaka jana uchumi ulikua kwa asilimia Kisiasa, kama mnavyoona nchi yetu ni tulivu na ina amani. Muungano wetu pia unazidi kuimarika. Kesho kutwa unafikisha miaka 54. Kwa kuwa bado mtakuwa hapa Dodoma, nitumie fursa hii kuwaalika Sherehe za Muungano wetu, ambao ni wa pekee Barani Afrika, ambazo kwa bahati nzuri zitafanyika hapa Dodoma.
Mheshimiwa Spika wa Bunge la Afrika Mashariki;
Waheshimiwa Wabunge wa Afrika Mashariki
Waheshimiwa Viongozi mliopo;
Wageni Waalikwa Wote, Mabibi na Mabwana;
Naomba nihitimishe kwa kuwashukuru Wabunge wa Afrika Mashariki kwa kunialika kuhutubia Bunge lenu. Narudia tena, Serikali ninayoingoza itatoa ushirikiano wa kutosha kwa Bunge hili. Namshukuru pia Mheshimiwa Spika Job Ndugai pamoja na Wabunge wote wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuridhia shughuli hii ifanyike hapa kwenye eneo lenu. Na hii inadhihirisha uhusiano mzuri uliopo kati ya Bunge hili la Afrika Mashariki pamoja na Mabunge ya Nchi Wanachama.
Napenda pia kutumia fursa hii kuwashukuru na pia kuwapongeza Vyombo vya Ulinzi na Usalama pamoja na Wananchi wa Mkoa wa Dodoma wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa, Mheshimiwa Dkt. Binilith Mahenge, kwa kuwapokea vizuri wageni wetu na kwa kuhakikisha amani na utulivu vinaendelea kudumishwa.
Waheshimiwa Viongozi, nilifundishwa na Mbunge wa hapa Dodoma kuwa wanasiasa huwa tuna mwisho na mwisho kabisa. Sasa naomba niseme la mwisho kabisa. Na hapa naomba ninukuu maneno mengine ya Mwalimu Nyerere aliyosema kwenye Sherehe za Miaka 50 Uhuru wa Ghana, nanukuu, “Kizazi changu kiliongoza jitihada za kuleta uhuru wa kisiasa wa Bara letu. Kizazi cha sasa cha Waafrika hakina budi kuchukua kijiti pale tulipoishia, na kwa nguvu mpya, kusukuma mbele maendeleo ya Bara letu”, mwisho wa kunukuu. Kwa kutumia maneno hayo ya Mwalimu Nyerere, napenda nitoe wito kwenu ninyi Waheshimiwa Wabunge na wana-Afrika Mashariki wote kushikamana na kushirikiana, na kwa pamoja tushike kijiti na kuendeleza pale walipoishia waasisi na viongozi wetu waliotangulia.
“Mungu Libariki Bunge la Nne la Afrika Mashariki”
“Mungu Ibariki Jumuiya Yetu ya Afrika Mashariki”
“Ahsanteni Sana kwa Kunisikiliza”
- Apr 23, 2018
HOTUBA YA MHE. DKT. JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, KWENYE UFUNGUZI WA JENGO LA PSPF NA OFISI ZA MAKAO MAKUU YA BENKI YA...
Soma zaidiHotuba
HOTUBA YA MHE. DKT. JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI,
RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA,
KWENYE UFUNGUZI WA JENGO LA PSPF NA OFISI
ZA MAKAO MAKUU YA BENKI YA NMB
DODOMA, TAREHE 23 APRILI, 2018
Mheshimiwa Job Ndugai, Spika wa Bunge
la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Mheshimiwa Mizengo Peter Pinda, Waziri Mkuu
Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Mheshimiwa Jenista Mhagama, Waziri wa Nchi
Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi
Vijana, Ajira na Walemavu;
Mheshimiwa Dkt. Ashatu Kijaji, Naibu
Waziri wa Fedha na Mipango;
Mheshimiwa Dkt. Binilith Mahenge,
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma;
Waheshimiwa Wabunge mliopo;
Waheshimiwa Makatibu Wakuu mliopo;
Waheshimiwa Wazee wa Mkoa wa Dodoma;
Waheshimiwa Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi
na Usalama mliopo;
Wenyeviti wa Bodi za PSPF na NMB;
Mheshimiwa Makongoro Nyerere,
Mwakilishi wa Mama Maria Nyerere;
Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania;
Mama Irene Isaka, Mkurugenzi Mkuu Mamlaka
ya Usimamizi ya Mifuko ya Jamii
Bwana Adam Mayingu,
Mkurugenzi Mkuu wa PSPF;
Mama Ineke Bussemaker,
Mkurugenzi Mkuu wa NMB;
Waheshimiwa Viongozi wengine wa Serikali,
Vyama vya Siasa na Dini mliopo;
Ndugu Wafanyakazi wa NMB na PSPF mliopo;
Wageni Waalikwa wote, Mabibi na Mabwana:
Awali ya yote, napenda nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutupa uhai na kutuwezesha kukutana hapa. Aidha, nawashukuru Waheshimiwa Mawaziri Wahusika kwa kunialika kwenye hafla hii ya uzinduzi wa Jengo la PSPF pamoja na Ofisi za Makao Makuu ya NMB na Tawi lake la Kambarage hapa Dodoma.
Napenda pia niwashukuru wana-Dodoma pamoja na wageni waalikwa wote kwa kujitokeza kwa wingi kushuhudia tukio hili. Nimefurahi kumwona Spika wa Bunge, Waziri Mkuu Mstaafu Mzee Pinda pamoja na wazee wengine wa Dodoma. Lakini, nimefarijika zaidi kuona kuwa katika hafla hii tunaye Ndugu Makongoro Nyerere, Mwakilishi wa Mama Maria Nyerere. Ahsante sana kwa kujumuika nasi.
Waheshimiwa Viongozi;
Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;
Kama nilivyotangulia kusema, tupo hapa kwa ajili ya kufanya matukio makubwa mawili. Kwanza, kuzindua Jengo hili la PSPF, lijulikanalo kwa jina la Dodoma Plaza; na pili, kuzindua Makao Makuu ya NMB hapa Dodoma pamoja na Tawi la Kambarage.
Napenda nitoe pongezi nyingi kwa PSPF kwa kujenga jengo hili zuri na la kisasa kabisa hapa Dodoma. Limeboresha na kupendezesha mandhari ya hapa Dodoma, ambako ni Makao Makuu ya Nchi yetu. Nimefurahi kusikia kuwa Jengo hili limesanifiwa na ujenzi wake kusimamiwa na Watanzania; na kwamba takriban Watanzania 250 walipata ajira wakati wa ujenzi. Zaidi ya hapo, nimefurahi sana kusikia takriban asilimia 98 ya Jengo hili tayari limepangishwa. Nafahamu kuwa ipo baadhi ya Mifuko ya Jamii imejenga majengo kama haya lakini yamekosa wapangaji. Ninyi inaonekana mlifanya utafiti wa kutosha kabla ya kujenga jengo hili. Hivyo, hongereni sana PSPF.
Kwa upande wa NMB, nanyi nawapongeza sana. Kama mnavyofahamu, mimi ni mteja wenu; tena wa muda mrefu. Zaidi ya hapo, kama mjuavyo, Serikali inamiliki asilimia 32 ya hisa kwenye Benki hii. Nikiwa kama mteja wenu na Kiongozi wa Serikali ambayo ina hisa asilimia 32, huwa najisikia furaha sana kila nikiona Benki hii inazidi kufanikiwa. Napenda kutumia fursa kuipongeza NMB kwa kuwa Benki namba moja kwa kufikisha huduma zake sehemu kubwa ya nchi yetu, ikiwemo vijijini. Mkurugenzi Mtendaji, Mama Bussemaker ameeleza kuwa, kupitia matawi yake 216, ATMs 800 na Mawakala 6,000; Benki hii imeweza kufikisha huduma sehemu kubwa ya nchi yetu, takriban asilimia 98 ya Wilaya za nchi yetu. Na asilimia 60 ya huduma hizo zipo maeneo ya vijijini. Hongera sana NMB. Ninyi mmejitofautisha na benki nyingine ambazo huwa zinafanya kazi maeneo ya mijini pekee.
Sambamba na hilo, napenda kuwapongeza NMB kwa kufungua Ofisi za Makao Makao na kuanzisha Tawi ambalo mmeliita Kambarage, jina la Baba wa Taifa letu. Huu ni uamuzi wa busara, na niwaambie tu kuwa hamjakosea kulipa Tawi lenu Jina la Kambarage. Kwanza, kwa sababu historia benki yenu kimsingi ilianzia 1967 ambapo Serikali iliyoongozwa na Baba wa Taifa ilianzisha Benki ya Taifa ya Biashara (National Bank of Commerce – NBC) baada ya kutaifisha benki zilizokuwepo. Mwaka 1997, NBC iligawanywa na kuundwa taasisi tatu, yaani NBC Holding Corporation, NBC (1997) na Benki hii ya NMB, ambayo ilibinafishwa mwaka 2005 na kuendelea mpaka sasa. Pili, kama mnavyofahamu, mwaka 1973, wakati Baba wa Taifa akiwa Rais wa nchi yetu, Serikali ilifanya uamuzi wa kuhamia Dodoma. Hivyo, kuliita Tawi lenu la hapa Dodoma jina la Baba wa Taifa ni jambo sahihi kabisa. Na napenda nitumie fursa hii kumshukuru Mama yetu, Mama Maria Nyerere, kwa kuridhia Tawi hili kupewa jina la Baba wa Taifa. Ni matumaini yangu kuwa wafanyakazi wa Tawi hili watamuezi Baba wa Taifa kwa vitendo. Watachapa kazi kwa bidii na uadilifu mkubwa.
Waheshimiwa Viongozi;
Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;
Benki pamoja na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii inatoa mchango mkubwa katika maendeleo ya nchi yetu. Kwanza, kupitia huduma za kifedha inazotoa kwa wananchi. Inakadiriwa kuwa Watanzania wapatao milioni 4.7 wana akaunti za benki ambazo huzitumia kuhifadhi fedha zao. Benki pia zinatoa mikopo kwa wananchi na hivyo kusaidia kupunguza umaskini. Kwa upande wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii, takwimu zinaonesha kuwa hivi sasa ina wanachama milioni 2.2 nchini. Wanachama hao hunufaika na huduma mbalimbali za kifedha zinazotolewa na Mifuko hiyo, ikiwemo mafao ya uzeeni, pensheni, mikopo, n.k.
Pili, Mifuko ya Hifadhi na Benki inachangia kukuza uchumi wa nchi. Mathalan, hivi punde tumesikia kuwa PSPF imewekeza kwenye Kiwanda cha Sukari Kagera, Kiwanda cha Nguo cha 21st Century kilichopo Morogoro na wanaendelea kushirikiana na mifuko mingine kufufua kiwanda cha maturubai, ambacho nacho kipo Morogoro. Kupitia viwanda hivi, Serikali inapata mapato, ambayo yanatumika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo na kuboresha huduma za jamii. Kwa upande wa Benki, tumesikia kuwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, NMB imelipa kodi kwa Serikali kiasi cha shilingi bilioni 402. Aidha, mwaka jana (2017), NMB imetoa kwa Serikali gawio la shilingi bilioni 16.525. Wamewawezesha wakulima wadogo wadogo wapatao 800,000 na kutoa misaada mbalimbali ya kijamii, ambapo mwaka jana pekee, walitoa shilingi bilioni 1.4 kwa ajili ya kununua madawati 6,000 na kompyuta 300. Na hivi punde tu hapa wamekabidhi shilingi milioni 50 za msaada. Mambo hayo yote kwa ujumla wake yanachangia kukuza uchumi.
Pamoja na ukweli huo, napenda niseme jambo moja kwa NMB. Kama mlivyosema ninyi wenyewe, mwaka jana mlitoa gawio la shilingi bilioni 16.525. Lakini mimi nimefuatilia na miaka ya nyuma, kuanzia mwaka 2010. Katika kufuatilia huko, nikagundua kuwa kwa kipindi cha miaka mitatu mfululizo, kuanzia 2014/2015 hadi 2016/2017, mmekuwa mkitoa gawio linalofanana, yaani shilingi bilioni 16.525. Hii kwa kweli imenishtua na kunikwaza. Nimejiuliza hivi ni kweli kwa miaka yote hiyo faida ilikuwa ikifanana? Sikupata majibu ya uhakika. Hivyo basi, niuombe Uongozi wa NMB kuliangalia suala hili; na ni matumaini yangu kuwa gawio la mwaka huu wa fedha (2017/2018) litakuwa tofauti. Nitumie fursa hii pia kutoa wito kwa Watendaji wa Serikali wanaotuwakilisha kwenye NMB nanyi kufuatilia kwa karibu.
Mabibi na Mabwana, faida ya tatu ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii na Benki ni kutoa fursa za ajira kwa wananchi. Wapo Watanzania wengi ambao wameajiriwa kwenye Benki na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii. Mathalan, nimeambiwa kuwa, hivi sasa, Mifuko yetu ya Hifadhi ya Jamii ina watumishi wapatao 2,000, bila kujumlisha wafanyakazi waliopo kwenye miradi iliyoazishwa na mifuko hii. Kwa upande wa NMB, tumesikia kuwa wenyewe wana watumishi wapatao 3,400 na kama nilivyosema awali, ina mawakala 6,000. Nchi yetu ina benki zaidi ya 50 kwa hiyo mnaweza kukadiria fursa za ajira zilizotolewa.
Hizi ni baadhi tu ya faida za taasisi za kifedha ambazo zinachangia maendeleo ya nchi yetu. Hivyo basi, napenda kutumia fursa hii, kuzipongeza taasisi zote za fedha nchini kwa michango yao kwenye maendeleo ya nchi yetu. Kwa namna ya pekee, naipongeza sana PSPF pamoja na mifuko mingine ya hifadhi nchini kwa kuitikia vizuri wito wa Serikali wa kujenga viwanda. Nimearifiwa kuwa kwa pamoja, Mifuko ya Hifadhi ya Jamii, ipo kwenye hatua mbalimbali za kutekeleza miradi ya viwanda 16. Aidha, nazipongeza benki ambazo zimekuwa zikitoa mikopo kwa wawekezaji mbalimbali kujenga viwanda nchini.
Waheshimiwa Viongozi;
Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;
Licha ya faida hizo pamoja na pongezi hizo nilizozitoa, ni ukweli usiopingika kuwa sekta ya fedha nchini bado inakabiliwa na changamoto nyingi. Lakini nitataja kubwa mbili. Kwanza, ni uchanga wa sekta yenyewe. Ni kweli kuwa hivi sasa tuna benki zaidi ya 50 na tulikuwa na takriban Mifuko ya Hifadhi ya Jamii saba. Lakini hii haiondoi ukweli kuwa sekta ya fedha nchini bado ni changa. Mathalan, nimeeleza hapo awali kuwa hivi sasa ni takriban Watanzania milioni 4.7 tu ndio wana akaunti za benki na wanachama wa Mifuko ni milioni 2.2. Kwa nchi yenye idadi ya watu milioni 55, idadi hii ni ndogo sana. Lakini zaidi ya hapo, kwa taarifa nilizonazo, Mifuko yetu ya Hifadhi ya Jamii ina ukwasi wenye thamani ya shilingi trilioni 12.23 na ukwasi wa Benki zetu zote hauzidi shilingi trilioni 30. Hiki ni kiasi kidogo sana cha ukwasi kwa kuzingatia ukubwa wa nchi yetu na mahitaji tuliyonayo. Hivyo basi, taasisi za fedha hazina budi kujiimarisha, hususan kwa kuongeza idadi ya wanachama ili hatimaye kuweza kukuza mitaji iliyonayo.
Changamoto ya pili, ambayo mimi naiona ni ubora wa huduma zinazotolewa na taasisi za fedha nchini. Nimeeleza hapo awali kuwa, ukiondoa Benki hii ya NMB, benki nyingi zimejikita zaidi mijini na kuacha maeneo ya vijijini ambako ndiko kuna Watanzania wengi. Takriban asilimia 70 ya Watanzania wanaishi vijinini. Lakini, zaidi ya hapo, riba kwenye benki zetu zipo juu sana. Kwa upande wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii, nako kuna matatizo ya ucheleweshaji wa malipo lakini pia hata viwango vya mafao vinalalamikiwa kuwa vipo chini. Na hii ndio sababu iliyoifanya Serikali kuamua kuiunganisha Mifuko ya Hifadhi ya Jamii iliyopo na kuunda Mifuko miwili, yaani National Social Security Fund (NSSF) na The Public Service Social Security Fund (PSSSF), ambao utahudumia watumishi wa umma.
Tumeamua kuunda mifuko hii miwili ili kuondoa utitiri wa mifuko uliokuwepo na ushindani usio na tija baina ya mifuko hiyo, ambao ulikuwa ukiongeza gharama za uendeshaji na kusababisha wanachama kulipwa mafao madogo. Hivyo basi, tuna imani kuwa, baada ya kuuganisha mifuko hiyo na kuunda miwili, sasa aina na viwango vya mafao vitaongezeka. Na binafsi nadhani, suala hili la kuunganisha mifuko, linafaa pia kuigwa na benki zetu. Nimefurahi kusikia kuwa baadhi ya benki, hususan zenye kusuasua katika utendaji kazi, zimeanza taratibu za kuungana. Hili ni jambo zuri.
Waheshimiwa Viongozi;
Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;
Nimekuja hapa kuzindua Jengo la PSPF na kufungua Ofisi za Makao Makuu NMB hapa Dodoma pamoja na Tawi la Kambarage. Hata hivyo, kabla sijahitimisha hotuba yangu, naomba mniruhusu niseme maneno machache ya mwisho. Kwanza, narudia tena kuwapongeza wafanyakazi wa NMB na PSPF kwa kazi nzuri mnayoifanya. Endeleeni kujituma. Serikali ipo pamoja nanyi. Nitumie fursa hii kuwahimiza Watanzania kujiunga na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii lakini pia kufungua akaunti za benki kwa ajili ya usalama wa fedha zenu.
Suala jingine, ni kwa watani zangu wa Dodoma. Kwanza, nimemsikia kilio chenu kupitia Mbunge wenu kuhusu adha ya kodi na tozo mbalimbali, ambazo zimekuwa zikiathiri biashara ya mchuzi wa zabibu. Kwa bahati nzuri Mawaziri, Watendaji wa Serikali pamoja na Waheshimiwa wako hapa. Bila shaka wamesikia; na nina imani wataenda kulifanyia kazi suala hilo. Nitumie fursa hii pia kuwaarifu wana-Dodoma kuwa sasa mambo mazuri mengi yanakuja kwenye Mkoa wenu. Mwezi Machi mwaka huu nilikutana na Bwana Ricardo Tadeu, Makamu wa Rais wa Kampuni ya AB INBEV, ambayo inamiliki asilimia 57 ya hisa za TBL. Aliniambia kuwa TBL imepaga kujenga kiwanda hapa Dodoma kwa gharama ya Dola za Marekani milioni 100. Hivyo, nawasihi wana-Dodoma kuchangamkia fursa zinazokuja. Kwa upande wake, Serikali itaendelea kuimarisha miundombinu na kuboresha huduma za jamii. Nitumie fursa hii kuwapongeza viongozi wa Mkoa wa Dodoma kwa jitihada wanazozifanya za kuufanya Mji wa Dodoma kuwa wa kisasa.
Suala la mwisho ni kuhusu ombi la Mwenyekiti wa Bodi ya PSPF kuhusiana na viwanja vilivyopo karibu na eneo hili. Katika hili, napenda niwe tu mkweli. Suala hili siwezi kuliingilia. Namini wenye viwanja hivyo wamevipata kihalali. Hivyo basi, kama mnataka kuwaondoa, ni vyema ninyi wenyewe mzungumze nao. Wakikubali, wawauzie au muwape viwanja maeneo mengine. Lakini hilo ni lenu ninyi wenyewe. Mimi siwezi kuliingilia.
Baada ya kusema hayo sasa nipo tayari kutekeleza jukumu lililonileta hapa la kuzindua Jengo la Dodoma Plaza, lenye thamani ya shilingi bilioni 37.02 mali ya PSPF, pamoja na Ofisi za Makao Makuu ya NMB na Tawi la NMB Kambarage hapa Dodoma.
Munngu Ibariki PSPF!
Mungu Ibariki NMB!
Mungu Ibariki Sekta ya Fedha Nchini!
Mungu Ibariki Tanzania!
“Ahsanteni sana kwa kunisikiliza”
- Apr 11, 2018
HOTUBA YA MHE. DKT. JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA KWENYE UZINDUZI WA TAASISI YA JAKAYA MRISHO KIKWETE DAR ES SALAAM, TA...
Soma zaidiHotuba
HOTUBA YA MHE. DKT. JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI,
RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
KWENYE UZINDUZI WA TAASISI YA JAKAYA
MRISHO KIKWETE
DAR ES SALAAM, TAREHE 11 APRILI, 2018
Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, Rais Mstaafu
wa Awamu ya Nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
na Mwenyekiti wa Taasisi ya Jakaya Mrisho Kikwete;
Mheshimiwa Mzee Ali Hassan Mwinyi,
Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili wa Jamhuri
ya Muunganowa Tanzania;
Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Waheshimiwa Wake wa Viongozi mliopo;
Waheshimiwa Mawaziri mliopo;
Waheshimiwa Mabalozi na Wakuu wa Taasisi
za Kimataifa mliopo;
Waheshimiwa Wadhamini wa Taasisi ya
Jakaya Mrisho Kikwete kutoka
Mataifa mbalimbali;
Waheshimiwa Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama;
Waheshimiwa Wabunge mliopo;
Waheshimiwa Wawakilishi wa Asasi za Kiraia mliopo;
Wageni Wote Waalikwa, Mabibi na Mabwana:
Awali ya yote, napenda nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutupa uhai na kutuwezesha kukutana hapa katika hafla hii. Aidha, kwa namna ya pekee kabisa, napenda nimshukuru sana Mheshimiwa Rais Mstaafu, Mzee Jakaya Mrisho Kikwete kwa kunialika kushiriki naye katika hafla hii ya kuzindua taasisi yake inayojulikana kwa jina la Jakaya Mrisho Kikwete Foundation. Nakushukuru sana Mzee Kikwete.
Napenda pia kuwakaribisha wageni mbalimbali hapa Ikulu. Ningependa niwaarifu kuwa Ukumbi huu ambapo tupo leo, ulijengwa wakati wa Uongozi wa Rais Mstaafu Mzee Kikwete. Hivyo, alivyonialika kwenye Ukumbi mwingine kuzindua Taasisi yake; nilisema hapana, na kumwambia tutafanya kwenye Ukumbi huu, ambao aliujenga. Nashukuru alikubali, na nawashukuru pia wageni wote kwa kuhudhuria kwa wingi.
Kwa mliotoka nje ya Tanzania, ambao wengi wenu ni wadhamini wa Taasisi ya Jakaya Mrisho Kikwete, karibuni sana hapa Tanzania. Nchi yetu ni tulivu, ina amani na watu wake ni wakarimu sana. Aidha, nchi yetu ina vivutio vingi vya utalii. Mbuga za Serengeti na Ngorongoro, Visiwa vya Zanzibar, Mlima Kilimanjaro na vigine vingi. Ni imani yangu kuwa kabla hamjaondoka mtapata fursa ya kutembelea baadhi ya vivutio hivyo.
Waheshimiwa Viongozi;
Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;
Kama mnavyojua, tupo hapa kwa ajili ya kuzindua Taasisi ya Jakaya Mrisho Kikwete. Napenda kutumia fursa hii, hapa mwanzo kabisa, kumpongeza kwa dhati, Mheshimiwa Rais Mstaafu, Mzee Kikwete, kwa uamuzi wake wa kuanzisha Taasisi hii. Sote hapa tunafahamu, Mzee Kikwete ametoa mchango mkubwa sana kwa nchi yetu; tangu akiwa mtumishi wa Chama, Jeshini na kwenye Wizara mbalimbali alizoziongoza. Lakini alitoa mchango mkubwa zaidi, wakati akiwa Rais wa nchi yetu, kuanzia mwaka 2005 hadi aliponiachia mimi kijiti mwaka 2015. Aliitumikia kwa uadilifu na uaminifu mkubwa nchi yetu. Najua sisi wanadamu hatuna kawaida ya kuwasifu watu wakati wakiwa hai. Lakini leo mimi naomba nimsifu Mzee Kikwete akiwa hai.
Alisimamia vizuri mageuzi ya kiuchumi; ujenzi wa miundombinu; uboreshaji wa huduma mbalimbali za jamii, hususan afya, elimu na maji; ukuzaji wa demokrasia; na pia aliitangaza vyema nchi yetu kimataifa. Watanzania tutaendelea kumkumbuka kwa kusimamia ujenzi wa Shule za Kata, Chuo Kikuu cha Dodoma, Hospitali ya Mloganzila, ujenzi wa miundombinu, ikiwemo barabara na Bomba la Gesi, n.k. Kwa hakika, umetufanyia mambo mengi sana. Tunakushukuru sana; na nina uhakika, mchango wako, utaendelea kukumbukwa vizazi hadi vizazi.
Waheshimiwa Viongozi;
Mabibi na Mabwana;
Pamoja na mchango mkubwa ambao tayari ameutoa kwa nchi yetu, Mzee huyu, baada ya kustaafu; kutokana na mapenzi makubwa aliyonayo kwa nchi yetu na Bara letu la Afrika, na baada ya kuona bado ana nguvu za kutosha na kwa kutambua uzoefu mkubwa alionao. Kama mnavyofahamu, Mzee Kikwete, mbali na kuwa Rais wa nchi yetu, ameshika nyadhifa mbalimbali ndani na nje ya nchi. Amekuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC); Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC); Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU); Mjumbe wa Jopo la Watu Mashuhuri la Kumshauri Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu kukabiliana na Majanga ya Afya, ikiwemo Ebola; Mjumbe wa Jopo la Kumshauri Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Lishe; Jopo la Kumshauri Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Afya ya Wanawake, Watoto na Vijana; Balozi wa Heshima wa Chanjo Duniani; aliwahi kuwa Mjumbe wa Kamati ya Usuluhishi wa Mgogoro wa Cote d’Ivoire na hivi sasa ni Mwakilishi wa Umoja wa Afrika kwenye Mgogoro wa Libya.
Kwa kuzingatia hayo yote, Mzee Kikwete, ameona aendelee kuitumia nchi yetu na Bara letu zima la Afrika; kupitia Taasisi hii aliyoianzisha. Nakupongeza sana Mzee Kikwete. Kwa hakika, umefanya jambo jema. Umeiga mifano ya watangulizi wako, Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, Mzee Mwinyi na Mzee Mkapa; ambao nao baada ya kustaafu wameendelea kutoa michango yao kwa njia mbalimbali, ikiwemo kuanzisha taasisi kama hii. Na hii inapaswa kuwa changamoto kwa wastaafu na wazee wengine. Kustaafu sio mwisho wa kutoa mchango kwa Taifa lako. Kustaafu ni hatua tu. Kila mtu, ambaye Mwenyezi Mungu amemjalia umri mrefu, itafika wakati atastaafu. Mimi pia Mwenyezi Mungu akinipa umri, na ukomo wangu wa kuongoza nchi yetu kwa mujibu wa Katiba ukifika, nitastaafu. Na kwa kweli sifikirii na wala sina mpango wa kuongeza muda. Muda ukifika nitaachia kijiti kwa mwingine, na kuungana na watangulizi wangu akina Mzee Mwinyi, Mzee Mkapa na Mzee Kikwete.
Waheshimiwa Viongozi, Mabibi na Mabwana;
Tumesikia hivi punde kuwa Taasisi hii ya Jakaya Mrisho Kikwete itajishughulisha na masuala makubwa manne. Kwanza, masuala ya afya. Sisi sote hapa tunafahamu umuhimu wa sekta ya afya. Taifa haliwezi kupata maendeleo endapo wananchi wake hawatakuwa na afya njema. Eneo la pili, ambalo Taasisi hii itashughulikia, ni masuala ya maendeleo ya vijana. Kama tujuavyo, vijana ni kundi rika muhimu katika jamii na Taifa kwa ujumla. Uhai wa Taifa lolote lile upo mikononi mwa vijana. Hii ni kwa sababu vijana wapo wengi. Mathalan, hapa nchini ni takriban asilimia 60. Zaidi ya hapo, vijana wana nguvu na uthubutu. Lakini, licha ya ukweli huo, ni wazi kuwa, duniani kote, kundi hili la vijana ndilo lenye kukabiliwa na matatizo mengi, ikiwemo ukosefu wa ajira, elimu na ujuzi, pamoja na changamoto nyingine za kimalezi (mmong’onyoko wa maadili, dawa za kulevya, n.k.). Hivyo basi, mikatati ya makusudi inahitajika kushughulikia changamoto mbalimbali zenye kuwakabili vijana.
Eneo la tatu, ambalo tumeambiwa Taasisi hii itashughulikia ni kilimo. Sote hapa tunafahamu umuhimu wa sekta ya kilimo kwa maendeleo ya nchi. Uchumi wa nchi nyingi za Afrika unategemea sekta hii ya kilimo. Nikitoa mfano wa hapa nchini, sekta hii imeajiri takriban asilimia 70 ya Watanzania. Inatuhakikishia usalama wa chakula. Inachangia takriban asilimia 25 ya Pato la Taifa na asilimia 30 ya mauzo ya nje. Sekta ya kilimo pia inatoa takriban asilimia 60 ya malighafi kwa ajili ya viwanda vyetu. Hii yote inadhihirisha kuwa sekta ya kilimo ni muhimu. Hivyo, nimefurahi kuona Taasisi hii itashughulika pia na vijana.
Eneo la nne, ni utawala bora na amani. Hili nalo ni eneo muhimu sana. Hivyo basi, nimefurahi kuona kuwa Taasisi ya Jakaya Mrisho Kikwete imeamua kushughulikia pia eneo hili la Utawala Bora na Amani.
Kwa ujumla, niseme tu kwamba, maeneo yote manne ambayo Taasisi ya Jakaya Mrisho Kikwete imechagua kuyashughulikia ni muhimu sana. Na bila shaka, mtakubaliana nami kuwa, maeneo hayo manne ni ya kipaumbele kwa Serikali nyingi za Afrika hivi sasa, ikiwemo Serikali ninayoingoza. Hivyo basi, nakupongeza sana Mzee Kikwete kwa kuchagua kwa umakini maeneo hayo. Na nimefurahi kuona kuwa kaulimbiu ya Taasisi hii inasema “Transforming Lives Through Collaboration”, yaani “Kuboresha Maisha ya Watu kwa Ushirikiano na Wadau Wote”. Hii ina maana kuwa Taasisi hii imeazimia kufanya kazi kwa kushirikiana na si kushindana na Serikali. Hili ni jambo jema. Na napenda nitumie fursa hii nikuhakikishie Mzee Kikwete kuwa Serikali ninayoingoza inaunga mkono Taasisi yako na tutashirikiana nayo kwa kwa karibu, kwa hali na mali, katika kutekeleza malengo iliyojiwekea.
Mheshimiwa Rais Mstaafu, Mzee Kikwete;
Umeeleza hivi punde kuwa, japokuwa Taasisi yako itashughulikia mambo manne, lakini mmepanga kuanza na suala la afya, na hasa mtaelekeza nguvu katika mapambano dhidi ya vifo vya akina mama wajawazito na watoto chini ya umri wa miaka mitano. Hili ni jambo jema sana. Kama nilivyosema awali, sekta ya afya ni nyeti na muhimu kwa maendeleo ya Taifa lolote. Lakini, zaidi ya hapo, sote hapa tunafahamu kuwa vifo vya akina mama wajawazito na watoto chini ya umri wa miaka mitano ni miongoni mwa changamoto kubwa zenye kulikabili Bara letu. Takwimu zinaonesha kuwa Nchi za Afrika zilizopo Kusini mwa Jangwa la Sahara ndizo zinakabiliwa zaidi na changamoto ya vifo vya wajawazito na watoto wenye umri chini ya miaka mitano.
Nitumie fursa hii kukupongeza sana Mzee Kikwete. Wakati wa Uongozi wako nchi yetu ilipata mafanikio makubwa katika eneo hili. Tuliweza kupunguza idadi ya vifo vya watoto chini ya umri wa miaka mitano kutoka 112 mwaka 2004/2005 hadi kufikia 67 mwaka 2014/2015, kwa kila watoto 1,000. Aidha, vifo vya wajawazito vilipungua kutoka wastani wa vifo 800 mwaka 2004/2005 hadi kufikia 432 mwaka 2014/2015, kwa kila vizazi hai 100,000. Hongera sana Mzee Kikwete.
Serikali ya Awamu ya Tano ninayoingoza imejipanga kuendeleza mafanikio haya. Na nimefurahi Waziri wa Afya yupo hapa. Suala la kupunguza vifo vya wajawazito na watoto wa chini ya miaka mitano tumeliweka kuwa miongoni mwa vipaumbele vya Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2016/2017 – 2020/2021). Kupitia Mpango huo, tunalenga kupunguza vifo vya watoto wa chini ya miaka mitano kutoka 67 hadi 45 kwa kila watoto 1,000, na vifo vya wajawazito kutoka 432 hadi kufikia 250, kwa kila vizazi hai 100,000. Na tayari tumeanza kuchukua hatua. Mathalan, ili kukabiliana na tatizo la vifo vya akina mama wajawazito, hivi sasa tunavipanua na kuviboresha takriban vituo vya afya 208 nchi nzima ili kuviwezesha kutoa huduma dharura za upasuaji. Hatua hii bila shaka itasaidia kupunguza vifo vya wajawazito wakati wa kujifungua.
Kuhusu vifo vya watoto chini ya umri wa miaka 5, hivi sasa watoto wote wanapata huduma za chanjo bure; na dawa za chanjo zipo za kutosha. Ni matumaini yetu kuwa, kutokana na hatua hizi na nyingine nyingi tunazozichukua, na kwa kushirikiana na wadau wengine, ikiwemo Taasisi ya Jakaya Mrisho Kikwete, tutaweza kukabiliana na changamoto ya vifo vya wajawazito na watoto wenye umri chini ya miaka mitano. Dying while giving life is unacceptable. Vilevile, vifo vya watoto wetu wadogo havikubaliki. Ni lazima tushirikiane kuzuia vifo hivyo.
Mheshimiwa Rais Mstaafu, Mzee Kikwete;
Waheshimiwa Viongozi mliopo;
Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana:
Hapa sio mahali pa hotuba. Tupo hapa kwa ajili ya kushuhudia uzinduzi wa Taasisi ya Rais wetu mstaafu ya Jakaya Mrisho Kikwete. Hata hivyo, kabla sijahitimisha hotuba yangu naomba niseme masuala machache ya mwisho.
Jambo la kwanza, napenda kurudia tena kukupongeza Mheshimiwa Rais Mstaafu Mzee Kikwete kwa kuanzisha Taasisi hii na napenda nikuahidi tena kuwa Serikali ninayoingoza itashirikiana na karibu sana na Taasisi yako. Nawaomba pia wadau mbalimbali waiunge mkono Taasisi hii. Nawashukuru na kuwapongeza wadhamini waliojitolea kumsaidia Rais wetu Mstaafu katika kuendesha Taasisi hii. Niwaombe pia Mabalozi, hususan wa nchi za Afrika, mlioshiriki katika uzinduzi huu, kuitangaza Taasisi kwenye nchi zenu. Kama mlivyosikia, Taasisi hii sio kwamba itaendesha shughuli hapa Tanzania pekee bali kwenye Bara zima la Afrika. Hivyo, nawasihi muitangaze na kuiunga mkono.
Jambo la pili, napenda kuahidi kuwa Serikali ya Awamu ya Tano itashirikiana na taasisi zote za kiraia zinazofanyakazi hapa nchini zenye lengo la kuwaletea maendeleo Watanzania. Hata hivyo, niwe mkweli, Serikali ninayoingoza, kamwe; haitashirikiana au kuifumbia macho taasisi yoyote ya kiraia yenye malengo ya kuvuruga amani ya nchi yetu au kuharibu maadili ya Watanzania. Taasisi kama ambayo Mheshimiwa Rais Mstaafu amezitolea mfano hivi punde, ambazo zinafadhiliwa ili kuvuruga amani na utulivu ndani ya nchi, kamwe hatutaziuga mkono.
Jambo la tatu na la mwisho, lakini sio mwisho kwa umuhimu, napenda kutoa shukrani zangu kwa Mheshimiwa Kikwete. Nafahamu nimemshukuru mara kadhaa. Lakini, nitaendelea kufanya hivyo kila wakati nikipata nafasi. Bila ya Mzee huyu, huenda leo mimi nisingekuwa Rais. Hivyo, namshukuru sana. Lakini pia, nawashukuru viongozi wengine wastaafu, Mzee Mwinyi, Mzee Mkapa, Mzee Karume, Makamu wa Rais Mzee Bilal, Mawaziri Wakuu Wastaafu, Makamu Wenyeviti wastaafu wa CCM kwa kunilea na kuniongoza. Sina cha kuwalipa zaidi ya kusema ahsanteni. Naahidi nitaendelea kuwaenzi. Niwaombe Watanzania wote tuendelee kuwaenzi wazee na wastaafu wetu. Na niseme tu kuwa, binafsi, kila ninapokutana na Marais wastaafu, Mzee Mwinyi, Mzee Mkapa, Mzee Kikwete, Mzee Karume pamoja na viongozi wengine wastaafu, huwa najisikia faraja sana. Wanaifundisha na kuniongoza. Na hii ndio sifa yetu kubwa sisi Watanzania. Sio kwenye nchi nyingi, utakuta viongozi wastaafu; au viongozi wastaafu na waliopo madarakani; wanakutana na kukaa pamoja. Sehemu nyingine jambo hili haliwezekani kabisa. Na mifano ipo mingi.
Baada ya kusema hayo, sasa ninayo furaha kutamka kuwa Taasisi ya Jakaya Mrisho Kikwete imezunduliwa Rasmi. Naitakia mafanikio mema na makubwa Taasisi hii.
Mungu Mbariki Rais Mstaafu Jakaya Mrisho Kikwete!
Mungu Wabariki Marais na Viongozi wengine Wastaafu!
Mungu Ibariki Taasisi ya Jakaya Mrisho Kikwete!
Mungu Zibariki Taasisi zote za Kiraia zenye nia njema na Nchi yetu!
Mungu Ibariki Tanzania!
“Ahsanteni sana kwa kunisikiliza”
- Apr 07, 2018
HOTUBA YA MHE. DKT. JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA KWENYE UZINDUZI WA NYUMBA ZA ASKARI POLISI ARUSHA, TAREHE 7 APRILI, 2018
Soma zaidiHotuba
HOTUBA YA MHE. DKT. JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA KWENYE UZINDUZI WA NYUMBA ZA ASKARI POLISI ARUSHA, TAREHE 7 APRILI, 2018
Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba,
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi;
Mheshimiwa Mhandisi Hamad Masauni;
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi;
Mheshimiwa Mrisho Gambo,
Mkuu wa Mkoa wa Arusha;
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani;
Mheshimiwa Simon Sirro, Inspekta Jenerali
wa Polisi pamoja na Wakuu wa Vyombo
vya Ulinzi na Usalama mliopo;
Waheshimiwa Viongozi wengine wa Serikali mliopo;
Viongozi wa Vyama vya Siasa na Dini mliopo;
Maafisa na Askari wa Jeshi la Polisi;
Waheshimiwa Wageni Wote Waalikwa;
Ndugu wana- Habari;
Wananchi wa Arusha, Mabibi na Mabwana:
Nitumie fursa hii, kwanza kabisa, kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyetupa uhai na kutuwezesha kukutana siku ya leo. Kama mnavyofahamu, tarehe kama ya leo, miaka 46 iliyopita, nchi yetu ilimpoteza mmoja wa viongozi mahiri na shupavu, Hayati Mzee Abeid Aman Karume, ambaye aliuawa kwa kupigwa risasi tarehe 7 Aprili, 1972 wakati akiwa anacheza bao na marafiki zake kwenye Makao Makuu ya Ofisi ya CCM Kisiwandui, zilizopo Unguja, Zanzibar.
Kwa heshima yake, naomba sote tusimame kwa dakika moja ili tuweze kumkumbuka Kiongozi wetu huyu, ambaye alikuwa mwanamapinduzi na mtetezi mkubwa wa wanyonge. Tuzidi kumwombea kwa Mwenyezi Mungu aipumzishe roho yake mahali pema peponi. Amina.
Ndugu Wananchi, Mabibi na Mabwana;
Wakati anauwawa, Hayati Mzee Karume alikuwa Rais wa Zanzibar na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Wazanzibar na Watanzania kwa ujumla, tunamkumbuka Hayati Mzee Karume kwa mambo mengi. Yeye ndiye aliongoza Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya tarehe 12 Januari, 1964 ambayo ndiyo yalihitimisha utawala wa Sultan na vibaraka wake. Aidha, Mzee Karume pamoja na Hayati Baba wa Taifa letu, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, ndio walioasisi Muungano wa nchi yetu; Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Wao ndio waliosaini Hati za Muungano baada ya kufikia makubaliano ya kuziunganisha nchi zao mbili, yaani Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar. Hii maana yake ni kwamba, bila ya jitihada za Hayati Mzee Karume, huenda Zanzibar bado ingekuwa ipo chini ya utawala wa Sultan, kupitia vibaraka wake; na huenda pia Taifa jipya la Tanzania, ambalo baadaye mwezi huu linafikisha miaka 54, lisingezaliwa.
Ndugu Wananchi, Mabibi na Mabwana;
Ukiachilia mbali mchango huo mkubwa alioutoa, Wazanzibar na Watanzania kwa ujumla tutaendelea kumkumbuka Hayati Mzee Karume kwa uamuzi wake wa kugawa ardhi bure kwa wananchi pamoja na kujenga nyumba kwa ajili ya watu wasiojiweza. Leo hii ukienda Zanzibar, utaziona nyumba zilizojengwa na Hayati Mzee Karume wakati wa uongozi wake.
Kwa kutambua mchango mkubwa alioutoa Mzee Karume kwa nchi yetu, Serikali iliamua tarehe 7 Aprili ya kila mwaka iwe siku ya mapumziko (Karume Day). Lengo ni kuwapa Watanzania fursa ya kumkumbuka lakini pia kutafakari namna ya kuenzi maisha yake. Hivyo basi, leo tunapoadhimisha miaka 46 ya Kifo cha Mzee Karume, nawasihi Watanzania tuenzi maisha yake, hususan kwa kulinda uhuru wetu, kudumisha amani na umoja wetu, pamoja na kuchapa kazi kwa bidii. Haya ndiyo mambo ambayo Mzee Karume aliyapigania sana enzi za uhai wake.
Waheshimiwa Viongozi, Mabibi na Mabwana;
Kama nilivyoeleza hivi punde kuwa, moja ya mambo ambayo sisi Watanzania tutaendelea kumkumbuka Mzee Karume, ni uamuzi wake wa kuwajengea wananchi nyumba. Nami leo nimefurahi kuja hapa Arusha, ambapo pamoja na kuiadhimisha Siku hii ya Karume Day, muda mfupi uliopita, nimepata fursa ya kuzindua nyumba 31 za Jeshi la Polisi. Inspekta Jenerali wa Polisi Simon Sirro ameeleza hivi punde kuwa tarehe 27 Septemba, 2017 jumla ya nyumba 13 za askari polisi ziliteketea kwa moto; na kuziacha takriban familia 14 bila makazi ya kuishi.
Kufuatia tukio hilo la kusikitisha, Serikali pamoja na kuzitafutia makazi ya muda familia hizo, ilitoa shilingi milioni 250 kwa ajili ya kujenga nyumba mpya 13. Na kama mlivyosikia, Wafanyabiashara wa Mkoa wa Arusha nao walichangishana na kufanikiwa kupata fedha za kujenga nyumba 18. Hivyo, leo nimezindua jumla ya nyumba 31. Hii ina maana kuwa janga lile la moto, pamoja na kwamba lilituhuzunisha sana, limeleta neema. Kwa “Kisukuma” hii unaweza kusema “It was a blessing in disguise”. Ziliungua nyumba 13, lakini sasa zimejengwa nyumba 31.
Waheshimiwa Viongozi, Mabibi na Mabwana;
Nitumie fursa hii kuwashukuru wananchi wa Arusha, kwanza kwa misaada mbalimbali mliyotoa wakati lilipotokea janga la moto. Nimeambiwa kuwa, wana-Arusha mlitoa chakula, maji, dawa, n.k., kwa waathirika. Nawashukuru na kuwapongeza sana.
Pili, na kwa namna ya pekee kabisa, napenda nitoe shukrani zangu nyingi kwa wananchi waliochangisha fedha zilizowezesha kujengwa kwa nyumba hizo 18. Ahsanteni sana wananchi wa Arusha. Na napenda kusema kuwa, kupitia kwenu wana-Arusha, mimi binafsi nimejifunza jambo, na hasa baada ya kufahamu kuwa nyumba hizi 31 zimejengwa kwa takriban shilingi milioni 700. Nimebaini kuwa kama nikitoa shilingi bilioni 10, na fedha hizo zikasimamiwa na kutumika vizuri, tunaweza kujenga nyumba nyingi kwenye mikoa mbalimbali nchini na hivyo kupunguza tatizo la makazi kwa askari wetu.
Na kwa kweli baada ya kufahamu hilo, na pia baada ya kusikia maelezo mazuri kutoka kwa Inspekta Jenerali wa Polisi na kushuhudia maonesho ya kijasiri kutoka kwa askari wetu wa Jeshi la Polisi, napenda kutumia fursa hii kuahidi kuwa Serikali itatoa shilingi bilioni 10 kwa Jeshi la Polisi ili ziweze kuzitumia kujenga nyumba za askari wa ngazi za chini katika mikoa mbalimbali nchini. Niwaombe Wakuu wa Mikoa mingine pamoja na wananchi kwa ujumla, wakiwemo Waheshimiwa Wabunge, nanyi kuangalia uwezekano wa kusaidia jitihada za Serikali za kupunguza tatizo la makazi kwa askari wetu. Mimi wakati nikiwa Mbunge nakumbuka niliwahi kutoa shilingi milioni 25 kutoka Mfuko wa Jimbo kuchangia ujenzi wa nyumba za askari kwenye Jimbo langu.
Ndugu Wananchi, Mabibi na Mabwana;
Jeshi letu la Polisi linapaswa kuungwa mkono kutokana na kazi nzuri na kubwa linayoifanya. Nchi yetu ipo salama na ina amani kutokana na kazi nzuri inayofanywa na Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama. Kama isingekuwa vyombo vyetu vya ulinzi na usalama, huenda amani tunayojivunia hivi sasa isingekuwepo. Na hii ndio maana huwa nawashangaa sana baadhi ya watu, wakiwemo wanasiasa wenzangu, ambao kila siku hawachoki kubeza na kulikebehi Jeshi letu la Polisi. Huwa nawashangaa sana.
Ninyi wananchi ni mashahidi; miezi michache tu iliyopita, katika Mkoa wa Pwani, sehemu za Ikwiriri, Kibiti na Rufiji, watu walikuwa wakiuawa kila kukicha. Jumla ya watu 59, (raia 42 na askari 17) waliuawa. Na jambo la kushangaza na kusikitisha ni kwamba, wengi waliouawa walikuwa viongozi wa Serikali na Chama cha Mapinduzi. Lakini kutokana na kazi nzuri iliyofanywa na askari wetu wa Jeshi letu la Polisi pamoja na vyombo vingine vya ulinzi na usalama, hivi sasa vitendo hivyo vimekomeshwa. Hali ni shwari; na wananchi wanaendelea na shughuli zao kama kawaida.
Nitumie fursa hii kulipongeza sana Jeshi la Polisi kwa kufanikiwa kukomesha vitendo hivyo vya uhalifu. Napenda niwahakikishie kuwa Watanzania wengi wanathamani na kutambua kazi yenu. Kebehi zinazotolewa dhidi yenu na watu wachache zisiwayumbishe au kuwakatisha tamaa. Serikali ipo pamoja nanyi. Tutaendelea kuliboresha Jeshi lenu pamoja na vyombo vingine vya ulinzi na usalama, hususan kwa kuwapatia vifaa na zana za kisasa. Zaidi ya hapo, tutaendelea kuboresha mazingira yenu ya kazi pamoja na maslahi yenu. Inspekta Jenerali wa Polisi ameeleza baadhi ya mambo ambayo Serikali inafanya katika kuliboresha Jeshi la Polisi.
Ndugu Wananchi, Mabibi na Mabwana;
Nitumie fursa hii kujibu pia baadhi ya maombi ambayo hivi Inspekta Jenerali wa Polisi amewasilisha kupitia Risala yake. Niseme tu kwamba maombi yenu yote nimeyapokea na Serikali itayafanyia kazi. Lakini kuhusu ombi lenu la kupewa kibali cha kuajiri askari wapya, niziagiza mamlaka husika kutoa kibali kwa Jeshi la Polisi kuajiri askari wapya 1,500. Hata hivyo, nitoe wito kwa Jeshi la Polisi, kuhakikisha watakaoajiri wawe ni wale tu waliohitimu vizuri mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT). Na kuhusu ombi la kupandishwa vyeo Maafisa wa Polisi, nawagiza mkakamilishe uchambuzi wenu wa ndani na kisha mniletee mapendekezo ya askari wanaostahili kupandishwa vyeo. Lakini hapa pia nitoe angalizo, msimpendelee au kumwonea mtu yeyote. Majina mtakayoleta yawe ni wale tu ya wanaostahili kupandishwa.
Sambamba na hayo, napenda kutumia fursa hii kuwahimiza Viongozi wa Jeshi la Polisi kurekebisha kasoro ndogo ndogo chache zilizopo ndani ya Jeshi lenu, ambazo zimekuwa zikichafua sifa yenu nzuri. Wapo askari wachache; wachache sana, ambao wanalichafua Jeshi lenu. Wanapenda kuchukua rushwa, wanawanyanyasa wananchi, ikiwemo kuwabambikizia wananchi kesi. Rekebisheni mapungufu haya, kwanza, kwa kuongeza umakini katika kuajiri; pili, imarisheni mafunzo mnayotoa kwa askari; na tatu, kwa wale wachache watakaothibitika kufanya vitendo vyenye kulichafua Jeshi lenu, msisite kuwachukulia hatua kali za kinidhamu. Nimefurahi Inspekta Jenerali umeeleza baadhi ya hatua za kinadhamu mnazozichukua kwa baadhi ya askari wanaokiuka miiko na maadili ya Polisi. Endeleni kuchukua hatua hizo.
Waheshimiwa Viongozi;
Ndugu Wananchi;
Mabibi na Mabwana;
Leo ni Siku ya Kumbukumbu ya Hayati Mzee Karume. Nimeitumia siku hii pia kufanya uzinduzi wa nyumba 31 za Jeshi la Polisi hapa Arusha. Hata hivyo, haitakuwa vyema kuhitimisha hotuba yangu bila kuwaeleza wana-Arusha mipango na mikakati mbalimbali ambayo Serikali yenu inaitekeleza kwa lengo la kuleta maendeleo kwa nchi yetu.
Tangu tuingie madarakani, takriban miaka miwili na nusu iliyopita, Serikali ya Awamu ya Tano, kwa nia ya kuendeleza jitihada zilizofanywa na Awamu zilizotangulia, imechukua hatua mbalimbali zenye lengo la kuleta maendeleo kwa nchi yetu. Tumeimarisha nidhamu kwenye utumishi wa umma; tumeongeza mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi pamoja na biashara haramu ya dawa za kulevya. Aidha, tumeimarisha usimamizi na ulinzi wa rasilimali zetu, ikiwemo madini na maliasili mbalimbali. Bila shaka, jana mmeshuhudia nimezindua Ukuta pale Mererani ili kudhibiti wizi na utoroshaji wa madini yetu ya Tanzanite.
Sambamba na hayo, tumeongeza ukusanyaji mapato. Kwa mujibu wa Takwimu zilizotolewa mara ya mwisho na Mamlaka ya Mapato (TRA), mwezi Desemba 2017, tulikusanya shilingi trilioni 1.6. Haijawahi kutokea nchi yetu kukusanya mapato makubwa ya kodi kiasi hicho. Na napenda kutumia fursa hii kuwapongeza wana-Arusha na Watanzania kwa ujumla kwa kuitikia vizuri wito wa Serikali wa kulipa kodi. Nchi yetu ni lazima tuijenge sisi wenyewe. Hatuna mjomba wala shangazi wa kuja kutujengea.
Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;
Kutokana na kuongeza ukusanyaji mapato, tumeweza kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo na kuboresha huduma za jamii. Tayari mmesikia kuhusu hatua tunazochukua kwenye afya na elimu. Lakini tunajenga pia barabara. Hapa Arusha, tayari tumekamilisha ujenzi wa barabara ya njia nne yenye urefu wa kilometa 14.1 kutoka Sakina hadi Tengeru, kwa gharama ya shilingi bilioni 72.09; na ujenzi wa Barabara ya Mchepuko wa Kusini “Southern Bypass” unaendelea. Vilevile, kwenye Barabara ya Mto wa Mbu – Ngarasero hadi Loliondo, tumeanza ujenzi wa kipande cha Waso – Sale chenye urefu wa kilometa 49 kwa gharama ya shilingi bilioni 87. Halikadhalika, TARURA imetengewa takriban shilingi bilioni 6.28 kufanya ukarabati wa barabara mbalimbali za mijini na vijijini katika Mkoa huu wa Arusha, ambazo hazipo chini ya TANROADS.
Tunakarabati njia ya reli kutoka Tanga kuja hapa Arusha ili kurahisisha usafiri na usafirishaji. Tunapanua bandari zetu kuu za Dar es Salaam, Mtwara na Tanga kwa gharama ya takriban shilingi trilioni 1.2. Tunataka wananchi wa Arusha wapokee mizigo yao katika Bandari ya Tanga na waisafirishe kwa reli hadi hapa. Tunavipanua pia viwanja vyetu vikubwa vya ndege vya Dar es Salaam na KIA kwa gharama ya shilingi bilioni 650. Tunatumia fedha nyingine takriban shilingi bilioni 500 katika kujenga au kufanya marekebisho ya viwanja vya ndege 11 kwenye Mikoa mbalimbali ili kutekeleza Sera yetu ya Usafirishaji, ambayo inaelekeza kila Mkoa kuwa na Kiwanja cha Ndege. Tumenunua pia ndege mpya sita. Tunachukua hatua hizi ili kukuza sekta ya utalii nchini. Ninyi wana-Arusha mnafahamu vizuri, asilimia 70 ya Watalii duniani hutumia usafiri wa anga. Hivyo basi, bila kuimarisha usafiri wa anga ni vigumu kukuza sekta ya utalii.
Sambamba na hayo, tunatekeleza pia miradi ya maji karibu kwenye kila mkoa nchini. Mathalan, hapa Arusha, tunatekeleza mradi mkubwa wa kuchimba visima virefu 56 kwa gharama ya shilingi bilioni 476, ambazo tumekopeshwa kwa masharti nafuu na Benki ya Maendeleo ya Afrika. Mkuu wa Mkoa amenieleza suala la kodi ya ongezeko la thamani ambalo linachelewesha utekelezaji wa mradi huo. Tatizo hilo tutalishughulikia ili mradi huo uweze kukamilika.
Waheshimiwa Viongozi;
Ndugu wana-Arusha, Mabibi na Mabwana;
Mbali na kutekeleza miradi ya maendeleo na kuboresha huduma za jamii, tunaendelea kushughulikia kero nyingine zenye kuwakabili wananchi wetu, hususan wananchi wa kipato cha chini. Tumepunguza utitiri wa kodi kwenye kilimo, mifugo na uvuvi. Tumeanza usajili wa wajasiliamali wadogo (mama lishe, machinga, n.k) kwa kuwapatia vitambulisho maalum vitakavyowawezesha kuendesha shughuli zao kwa uhuru bila kubughudhiwa.
Haya ni baadhi tu ya mambo ambayo tumetekeleza katika kipindi cha miaka miwili na nusu iliyopita. Yapo mengine mengi, ambayo kwa sababu ya muda siwezi kutaja. Hivyo basi, nitumie fursa kuwasihi wana-Arusha na Watanzania kuendelea kuiunga mkono Serikali, hususan kwa kudumisha amani na umoja wetu na bila kusahau kuchapa kazi kwa bidii. Amani ndio msingi wa maendeleo. Nawapogeza wana-Arusha hivi sasa mpo mstari wa mbele katika kudumisha amani. Hii imefanya hata shughuli za kiuchumi, ikiwemo utalii na ujenzi wa viwanda, ziendelee kustawi na kushamiri. Nimeambiwa mpaka sasa mmejenga viwanda vipya 46. Hongereni sana wana-Arusha.
Nawasihi muendelee kudumisha amani, lakini pia toeni ushirikiano kwa viongozi wenu wote. Maendeleo hayana chama. Hii ndio sababu ilinifanya kabla ya kuanza kuhutubia niwape fursa Waheshimiwa Wabunge wote wa Arusha kueleza shida na kero zilizopo kwenye majimbo yao. Na napenda nitumie fursa hii kuwahakikishia Waheshimiwa Wabunge wote kuwa kero zenu nimezichukua na tutazishughulikia. Lakini niwe mkweli, suala la kuwapa ng’ombe Wafugaji wa Kimasai ambalo Mbunge wa Longido amenieleza, hilo Serikali haitafanya kwa vile hilo sio jukumu la Serikali. Jukumu la Serikali ni kuwawekea wananchi mazingira mazuri ya kuendesha shughuli zao za maendeleo, ikiwemo kutekeleza miradi ya maji, kujenga barabara, n.k., lakini sio kutoa ng’ombe bure. Hilo, kwa kweli, hatutafanya.
Waheshimiwa Viongozi;
Mabibi na Mabwana;
Nimezungumza mengi. Naomba nihitimishe kwa kurudia tena kuwaomba Watanzania kuitumia Siku hii ya Kumbukumbu ya Hayati Mzee Karume kutafakari mchango wake na kuuenzi. Aidha, napenda kuwashukuru tena viongozi wa Jeshi la Polisi kwa kunialika kuzindua nyumba 31 za askari polisi hapa Arusha. Nawapongezeni pia kwa kazi nzuri na kubwa mnazozifanya. Nawapongeza pia wale wote walioshiriki kwenye maonesho na burudani mbalimbali. Kila mtu aliyeko hapa, amefurahi. Hongereni na tunawashukuru sana.
Wito wangu kwenu endeleeni kuchapa kazi kwa bidii. Msimuogope au kumwonea mtu yeyote. Vilevile, jitahidini kurekebisha kasoro ndogo ndogo zilizomo kwenye Jeshi letu. Na katika hili, napenda niseme kuwa lipo jambo jingine moja ambalo huwa naona kila mara likifanywa na viongozi wa Jeshi la Polisi japokuwa huwa halinifurahishi sana. Jambo lenyewe ni kuwaona askari polisi wakishiriki shughuli za uchomaji wa mashamba ya bangi. Mimi nadhani hiyo sio kazi ya Jeshi la Polisi. Kazi yenu ni kuwakamata wahalifu. Hivyo basi, badala ya ninyi kuchoma bangi, hakikisheni mnawakamata wahusika ili wao wenyewe ndio wafanye kazi ya kuchoma mashamba hayo. Mkifanya ninyi mnalidhalilisha Jeshi lenu.
Mwisho lakini sio mwisho kwa umuhimu, napenda nitumie fursa hii kuwashukuru wana-Arusha, mkiongozwa na Mkuu wenu wa Mkoa, Mrisho Gambo, kwa mapokezi yenu makubwa. Tangu nimechaguliwa kuwa Rais nimekuja Arusha mara nyingi. Lakini, mara zote nimepata mapokezi mazuri. Ahsanteni sana wana-Arusha.
Baada ya kusema hayo: Mungu Libariki Jeshi la Polisi!
Mungu Wabariki Wana-Arusha!
Mungu Ibariki Tanzania!
“Ahsanteni sana kwa kunisikiliza”
- Apr 03, 2018
HOTUBA YA MHE. DKT. JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA KWENYE UZINDUZI WA MRADI WA KUFUFUA UMEME WA KINYEREZI II, DAR ES SALAAM...
Soma zaidiHotuba
HOTUBA YA MHE. DKT. JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA KWENYE UZINDUZI WA MRADI WA KUFUFUA UMEME WA KINYEREZI II, DAR ES SALAAM, TAREHE 3 APRILI, 2018
Mheshimiwa Medard Kalemani, Waziri wa Nishati;
Waheshimiwa Mawaziri mliopo;
Mheshimiwa Paul Makonda,
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam;
Mheshimiwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati;
Bwana Hiroyuki Kubota, Mwakilishi wa Balozi
wa Japan nchini;
Waheshimiwa Wabunge mliopo mkiongozwa na
Mbunge wa hapa Mheshimiwa Bonna Kaluwa;
Dkt. Alexander Kyaruzi, Mwenyekiti wa Bodi
ya Wakurugenzi ya TANESCO;
Dkt. Tito Mwanuka, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO;
Mwakilishi Mkuu wa Shirika la Maendeleo la Japan (JICA);
Mwakilishi Mkazi wa Benki ya Sumitomo Mitsui
Corporation ya Japan;
Waheshimiwa Viongozi wengine wa Serikali mliopo;
Waheshimiwa Viongozi wa Vyama vya Siasa na Dini mliopo;
Waheshimiwa Wageni wengine Waalikwa;
Wananchi Wenzangu, Mabibi na Mabwana:
Awali ya yote, napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kukutana hapa. Aidha, namshukuru Mheshimiwa Waziri na Viongozi wa Wizara ya Nishati kwa kunialika kuja kuzindua Mradi huu wa Kufufua Umeme Megawati 240 kwa kutumia gesi asilia hapa Kinyerezi. Ahsanteni sana. Nawashukuru pia wananchi wa Kinyerezi kwa kujitokeza kwenu kwa wingi kushuhudia tukio hili, licha ya mvua nyingi kuendelea kunyesha. Ahsanteni sana wana-Kinyerezi.
Naomba pia mniruhusu nitumie fursa hii, hapa mwanzoni kabisa, niipongeze Wizara ya Nishati pamoja pamoja na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kwa kazi nzuri mnayoifanya. Waswahili husema “mnyonge mnyogeni lakini haki yake mpeni”. Siku hizi, TANESCO, mnajitahidi sana kufanya kazi. Hongereni sana. Endeleeni hivyo hivyo. Serikali ipo pamoja nanyi. Nampongeza Mkandarasi, Kampuni ya Sumitomo Corporation ya Japan, kwa kuutekeleza mradi huu kwa haraka. Kama tulivyosikia, Mradi huu, ambao unatekelezwa kwa kutumia teknolojia ya kisasa ya combined cycle (yaani gesi na mvuke unaozalishwa na mtambo wa kufufua umeme), awali ulipangwa kukamilika mwezi Septemba 2018, lakini leo mwezi Aprili 2018, tayari. Hongera sana kwa Kampuni ya Sumitomo. Mmetekeleza kwa vitendo dhana yetu ya “Hapa Kazi Tu”. Nawapongeza na kuwashukuru pia kwa kutoa ajira nyingi kwa Kitanzania. Nimeambiwa kuwa kati ya wafanyakazi takriban 2,000 wa Kampuni hii ambao wameshiriki kwenye utekelezaji wa Mradi huu, asilimia 95 ni Watanzania. Hii maana yake ni kwamba fedha nyingi za kutekeleza Mradi huu zimebaki hapa nchini. Tunawashukuru sana.
Waheshimiwa Viongozi, Mabibi na Mabwana;
Umeme ni injini na mhimili muhimu katika ukuzaji uchumi na kuboresha maisha ya binadamu. Umeme unachochea shughuli za uzalishaji na hivyo kutoa fursa za ajira na kuboresha maisha ya watu. Azma na dhamira yetu ya kujenga uchumi wa viwanda haiwezi kutimia bila ya kuwa na umeme wa kutosha na wa uhakika. Ni kwa sababu hiyo, inatia moyo sana kuona kuwa, pamoja na matatizo tuliyonayo ambayo nitayaeleza muda mchache ujao, hali ya umeme nchini sio mbaya sana. Mmesikia hivi punde kuwa mahitaji ya umeme nchini hivi sasa ni Megawati 1,051, lakini tunaozalisha ni Megawati 1,513.3. Haya ni mafanikio makubwa ambayo hatuna budi kujipongeza.
Hata hivyo, pamoja na takwimu hizo za kutia matumaini, ni wazi kuwa jitihada za makusudi zinahitajika ili tuweze kuwa na umeme unaokidhi mahitaji ya uchumi wa kisasa. Mathalan, sisi leo tunajivunia kuwa na Megawati 1,513.3; lakini yapo Mataifa mengine, wakiwemo marafiki zetu wa karibu, ambao wana umeme mwingi zaidi. Kwa mfano, wenzetu wa Ethiopia wana takriban Megawati 4,300 na hivi sana wanakamilisha ujenzi wa Bwawa la kuzalisha Megawati nyingine 6,000. Hii peke yake inaonesha kuwa jitihada za makusudi zinahitajika ili kuongeza uzalishaji wa umeme nchini.
Lakini ukiachilia mbali mfano huo, utafiti uliofanywa na Ofisi yetu ya Takwimu mwaka 2015, ulionesha kuwa asilimia 36.6 tu ya Watanzania ndio walikuwa wameunganishwa na umeme, bila shaka, hivi sasa itakuwa imeongezeka. Zaidi ya hapo, Watanzania wengi, takriban asilimia 60 wanatumia mkaa, kuni au mafuta ya taa kupata nishati. Hali hii imechangawia na bei ya umeme nchini kuwa juu na hasa kwa kuwa umeme wetu mwingi vado unazalishwa kwa kutumia mafuta (dizeli); na kama mnavyofahamu baadhi ya mikataba ya kuzalisha umeme tuliyoingia ni mibovu. Athari za kutumia kuni na mkaa zinafahamika. Kwanza, inachangia kuharibu mazingira, ambapo katika nchi yetu inakadiriwa kuwa kila mwaka tunapoteza hekta 400,000 za misitu. Pili, matumizi ya kuni na mkaa yana athari nyingi za kiafya.
Waheshimiwa Viongozi, Mabibi na Mabwana:
Ni kutokana na sababu hizo, uzalishaji wa umeme imekuwa kipaumbele cha Serikali ya Awamu ya Tano. Na hii ndio sababu leo nimefurahi kuja hapa kuzindua mradi huu wa Kinyerezi II ambao utaongeza kwenye Gridi yetu ya Taifa Megawati 240. Nitumie fursa hii kuishukuru Serikali ya Japan kwa kushirikiana nasi katika kutekeleza mradi huu. Kama mlivyosikia, gharama za mradi huu ni Dola za Marekani milioni 344, sawa na shilingi bilioni 758. Serikali yetu imetoa Dola za Marekani milioni 51.6 sawa na takriban shilingi bilioni 120, na wenzetu wa Japan wametupatia Mkopo wa Masharti nafuu wa Dola za Marekani milioni 292.4. Tunawashukuru sana. Nimefurahi kuona kuwa katika shughuli hii tunaye Mwakilishi wa Balozi wa Japan, Bw. Kubota, pamoja na Wawakilishi wa Shirika la Maendeleo la Japan (JICA) na Benki ya Maendeleo ya Japan. Tunaomba mtufikishie shukrani zetu nyingi kwa Mfalme, Waziri Mkuu pamoja na Wananchi wote wa Japan.
Waheshimiwa Viongozi, Mabibi na Mabwana:
Mbali na mradi huu wa Kinyerezi II, hivi sasa tunafanya upanuzi wa Kinyerezi I ili kuuongezea wa kuzalisha umeme kutoka Megawati 150 za sasa hadi kufikia Megawati 325. Mradi huu ambao unatekelezwa na Serikali kwa asilimia 100 kwa gharama ya Dola za Marekani milioni 188, takriban shilingi bilioni 400, nao nimeambiwa unatarajia kukamilika mwakani (2019). Miradi mingine ya kuzalisha umeme kwa kutumia gesi asilia ambayo ipo kwenye hatua mbalimbali ni Kinyerezi III utakaozalisha Megawati 600, Kinyerezi IV Megawati 330, Mradi wa Mtwara Megawati 300, Somanga Fungu Megawati 330, n.k. Lakini, zaidi ya hapo, hivi sasa tupo mbioni kuanza utekelezaji wa Mradi mkubwa wa kuzalisha umeme wa maji wa Stiglier’s Gorge, ambao utatoa Megawati 2,100. Ni matumani yangu kuwa Wizara ya Nishati itakamalisha mapema taratibu za kumpata Mkadarasi wa kutekeleza mradi huo.
Lengo letu ni kwamba, ikifika mwaka 2020, nchi yetu iwe na angalau Megawati 5,000. Na tukiweza kutimiza lengo hilo, tutaanza kuwabana TANESCO nao wapunguze bei ya umeme. Nchi yetu ina vyanzo vingi vya kuzalisha umeme, ikiwemo gesi asilia, maji, jua, upepo, makaa ya mawe, nyuklia, n.k. Hivyo, haiwezekani bei ya umeme iendelee kuwa juu. Nitumie fursa hii kukaribisha makampuni au watu binafsi kuwekeza kwenye sekta ya umeme nchini. Lakini nitoe angalizo kwamba hatutakuwa tayari kushirikiana na wawekezaji matapeli na wenye nia ya kujinufaisha wao zaidi.
Waheshimiwa Viongozi, Mabibi na Mabwana:
Kama mjuavyo, ili umeme uweze kumfikia mtumiaji una hatua tatu muhimu. Hatua ya kwanza, ni kufufua au kuzalisha umeme wenyewe. Pili, usafirishaji; na tatu ni usambazaji. Hivyo basi, mbali na mipango na mikakati ya kuzalisha au kufufua umeme ambayo nimetoka kuielezea hivi punde, Serikali pia inatekeleza miradi mikubwa ya kusafirisha umeme. Hivi karibuni tumekamilisha mradi wa kusafirisha umeme wa msongo wa kilovoti 400 kutoka Iringa hadi Shinyanga umbali wa wa kilometa 632. Miradi ya msongo wa kilovoti 400 kutoka Singida - Namanga umbali wa kilometa 414; Mbeya – Nyakanazi msongo wa kilovoti 400; na Makambako – Songea kilovoti 250 nayo inaendelea.
Kuhusu miradi ya usambazaji umeme, hivi sasa tupo kwenye utekelezaji wa Mradi mkubwa wa Kupeleka Umeme Vijijini Awamu ya Tatu ambapo tunalenga ikifika mwaka 2020/2021 vijiji vyote nchini viwe vimefikiwa na miundombinu ya umeme. Hadi kufikia mwezi Desemba 2016 takriban vijiji 4,395 kati ya 12,268 tayari vilikuwa vimefikiwa na miundombinu ya umeme. Hivyo, Awamu hii ya Tatu utafikisha kwenye vijiji vilivyosalia ambavyo idadi yake ni 7,873. Ni matumaini yangu kuwa kutokana na hatua tunazochukua, baada ya muda mfupi ujao, nchi yetu itakuwa sio tu na umeme wa kutosha, bali pia umeme wa uhakika na wenye kupatikana kwa gharama nafuu. Na hii ndio moja ya sababu iliyonisukuma kuigawa Wizara ya Nishati na Madini ili kuwa Wizara ya Nishati peke yake na Madini peke yake.
Waheshimiwa Viongozi, na Ndugu Wananchi;
Nimekuja hapa kwa ajili ya kuzindua Mradi wa Kufufua Umeme Megawati 240 wa Kinyerezi unaotumia teknolojia ya kisasa ya combined cycle. Tayari nimemshukuru Mheshimiwa Waziri kwa kunialika. Nimeipongeza Wizara, TANESCO pamoja na Mkandarasi kwa kumaliza mradi mapema. Nimewashukuru marafiki zetu wa Japan kwa kutupatia mkopo wa masharti nafuu; na nimeeleza mikakati tuliyonayo ya kuimarisha upatikanaji wa umeme nchini. Hata hivyo, kabla sijahitimisha, napenda nieleze masuala machache ya mwisho.
Kwanza, napenda kuhimiza Wizara ya Nishati, kupitia TANESCO na REA, kuongeza kasi ya kuunganishia wananchi umeme. Niwaombe wananchi nanyi mchangamkie fursa za kuunganishiwa umeme. Serikali imepunguza gharama za kuunganisha umeme kwa kiwango kikubwa. Sambamba na hilo, naziomba taasisi za umma na binafsi, za hapa nchi na nje ya nchi, kuongeza kasi au kuchangamkia fursa ya kusambaza gesi asilia kwa wananchi ili kupunguza athari za matumizi ya mkaa na kuni nchini. Changamkieni pia fursa za kusambaza umeme wa jua.
Pili, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO ameeleza kuwa channgamoto kubwa iliyokumba mradi huu ni kodi na tozo mbalimbali ambazo zimeongeza gharama za mradi kutoka Dola za Marekani milioni 344 hadi kufikia Dola za Marekani milioni 356.2. Nitumie fursa hii kurudia wito wangu kwa taasisi za Serikali kufanya kazi kwa karibu na kwa ushirikiano, hususan katika kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo kama hii. Hivi majuzi nilikuwa Bohari ya Dawa kupokea msaada wa magari 181 kutoka Global Fund; nao waliilalamikia Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) kuwa kikwazo cha kutoa dawa bandarini. Magari ya Polisi yalikwama muda mrefu Bandari kwa sababu ya kodi. Niziombe basi, taasisi za Serikali kufanya kazi kwa ushirikiano; lakini bila kuathiri utendaji wenu.
Tatu, ni kwenu watani zangu wa Dar es Salaam. Serikali inahamia Dodoma, lakini dhamira yetu ya kuifanya Dar es Salaam kuwa Jiji la Kisasa bado ipo pale pale. Kama tulivyoahidi wakati wa kampeni, hivi sasa tunaendelea na ujenzi wa madaraja ya juu pale TAZARA na Ubungo ili kupunguza tatizo la foleni. Mwaka huu pia tunatarajia kuanza ujenzi wa Awamu ya Pili ya miundombinu ya magari ya mwendokasi kutoka Kariakoo kwenda Mbagala. Ujenzi wa Kiwanja cha Ndege unaendelea vizuri, na kama mlivyosikia jana tumeipokea ndege yetu nyingine mpya. Ujenzi wa Reli ya Kisasa kwenda Morogoro na Dodoma unaendelea. Bandari ya Dar es Salaam nayo inapanuliwa. Vilevile, Serikali imepata Mkopo kutoka Benki ya Dunia wenye thamani ya shilingi bilioni 660 ambazo zitatumika kujenga barabara zenye urefu wa kilometa 210, masoko, Stendi ya Mabasi pamoja mifereji mikubwa ya kilometa 40, ikiwemo katika Bonde la Msimbazi. Miradi hii imepangwa ikamilike mwaka 2020.
Kuhusu elimu, Mkoa wa Dar es Salaam unatengewa wastani wa shilingi bilioni 1 kila mwezi kwa ajili ya elimu bila malipo. Mwaka huu wa fedha, tayari umepokea shilingi bilioni 7.27; na tangu mpango huu uanze, umeshapokea shilingi bilioni 25.84. Sambamba na fedha hizo za elimu bila malipo, katika Mwaka huu wa Fedha, Mkoa umepokea shilingi bilioni 3.5 ili kujenga na kukarabati miundombinu, ambapo jumla ya shule za msingi 4 na sekondari 12 zinakarabatiwa, zikiwemo shule kongwe za Azania, Jangwani na Tambaza.
Kuhusu afya, ninyi ni mashahidi upatikanaji wa dawa katika vituo vya kutolea huduma za afya unazidi kuimarika. Ujenzi wa miundombinu unaendelea. Hospitali za Rufaa za Mkoa za Amana, Mwananyamala na Temeke zimeboreshewa miundombinu. Tunajenga hospitali za Wilaya ya Konondoni (Mabwepande) na Ilala (Kivule). Vituo vya afya vya Kimbiji (Kigamboni), Mtoni Kijichi, Charambe navyo vinakarabatiwa ili viwe na uwezo wa kutoa huduma za dharura, hususan upasuaji kwa wajawazito. Hospitali za Kitaifa zilizopo hapa Dar es Salaam, ikiwemo Muhimbili tunaendelea kuiboresha. Na kama mnavyofahamu, Hospitali ya Mloganzila nayo imeanza kazi na hivyo kupunguza mzigo kwa Muhimbili.
Haya niliyosema ni baadhi tu ya mambo ambayo tuliahidi na tumeanza kuyatekeleza. Niwaombe wana-Dar es Salaama na Watanzania kwa ujumla, endeleeni kuiunga mkono Serikali, lakini tushirikiane kuitunza amani yetu. Tusikubali watu wachache, kwa maslahi yao binafsi, watuondoe katika ajenda yetu ya maendeleo au watufarakanishe kwa misingi ya ukabila, udini, ukanda, n.k. Niliapa kuilinda amani ya nchi yetu, naahidi nitailinda kwa nguvu zangu zote.
Baada ya kusema hayo, sasa nipo tayari kutekeleza jukumu lililonileta hapa la Kuzindua Mradi wa Kufufua Umeme wa Kinyerezi utakaozalisha Megawati 240.
Mungu Ibariki Miradi yetu ya Umeme!
Mungu wabariki Wana-Dar es Salaam!
Mungu Ibariki Tanzania!
“Ahsanteni sana kwa kunisikiliza’
- Apr 02, 2018
HOTUBA YA MHE. DKT. JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, KWENYE HAFLA YA UZINDUZI WA MRADI WA KUSIMIKA MFUMO WA RADA NNE ZA KU...
Soma zaidiHotuba
HOTUBA YA MHE. DKT. JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI,
RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA,
KWENYE HAFLA YA UZINDUZI WA MRADI WA KUSIMIKA MFUMO WA RADA NNE ZA KUONGOZA NDEGE
KWENYE VIWANJA VYA JULIUS NYERERE,
KILIMANJARO, MWANZA NA SONGWE
DAR ES SALAAM, TAREHE 2 APRILI, 2018
Mheshimiwa Prof. Makame Mbarawa, Waziri wa Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano;
Mheshimiwa Dkt. Sira Ubwa, Waziri wa Ujenzi,
Mawasiliano na Usafirishaji wa Zanzibar;
Waheshimiwa Mawaziri na Manaibu Waziri mliopo;
Mheshimiwa Paul Makonda, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam
pamoja na Wakuu wa Mikoa mingine mliopo;
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu;
Waheshimiwa Wabunge mliopo hapa;
Waheshimiwa Makatibu Wakuu mliopo hapa;
Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama;
Ndugu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania;
Viongozi na Wafanyakazi wa TCAA, ATCL, TAA;
Waheshimiwa Viongozi wengine wa Serikali,
Vyama vya Siasa na Dini mliopo;
Waheshimiwa Wageni wote Waalikwa, Mabibi na Mabwana:
Kwanza kabisa, napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kukutana hapa kushuhudia tukio hili. Aidha, namshukuru Mheshimiwa Waziri Prof. Mbarawa kwa kunialika katika hafla hii ya Uzinduzi wa Mradi wa Mfumo wa Rada kwa ajili ya kuongoza ndege kwenye Viwanja vyetu vya Julius Nyerere (Dar es Salaam), Kilimanjaro (KIA), Mwanza pamoja na Songwe. Ahsante sana Mheshimiwa Waziri.
Waheshimiwa Viongozi, Mabibi na Mabwana;
Rada ni chombo au nyenzo muhimu sana sio tu kwa ajili ya usafiri wa anga, bali pia usalama na maendeleo ya nchi kwa ujumla. Licha ya ukweli huo, nchi yetu hivi sasa ina rada moja tu ya kiraia, ambayo inatumika kuongozea ndege. Rada hiyo ipo hapa kwenye Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere hapa Dar es Salaam; na ina uwezo wa kuhudumia asilimia 25 tu ya anga letu. Na kwa bahati mbaya, uwezo wa Rada hiyo ambayo ilinunuliwa mwaka 2002 ili itumike kwa kipindi cha miaka 12, nao umepungua sana kutokana na uchakavu. Hii imefanya baadhi ya mashirika ya ndege yasite kufanya shughuli zao hapa nchini.
Ni kutokana na hali hiyo, leo nimefurahi sana kuja hapa kuweka Jiwe la Msingi la Mradi huu wa Usimikaji Mfumo wa Rada Nne kwenye Viwanja vyetu vya hapa Dar es Salaam, Kilimanjaro, Mwanza na Songwe. Kwa hakika, nimefurahi sana. Na nimefurahi kwa sababu, sasa nina hakika kuwa Mradi huu utakapokamilika, tutakuwa na uwezo wa kuliona anga letu lote pamoja na anga za nchi jirani, hususan Burundi na Rwanda, ambazo Shirika la Kimataifa la Anga (ICAO) limetukasimu. Hii pia itaimarisha usalama wa nchi yetu; itarahisisha shughuli za uongozaji ndege na pia itaiongezea nchi yetu mapato. Hivi sasa tunapoteza wastani wa shilingi bilioni 1.2 ya tozo ya kuongozea ndege kwa mwaka kutokana na ICAO kukasimu sehemu ya anga la nchi yetu kwa majirani zetu wa Kenya. Hivyo, nina uhakika kuwa Mradi huu ukikamilika, sehemu hiyo tutarejeshewa na tutaweza kukusanya fedha tunazozipoteza.
Napenda kutumia fursa hii kuipongeza Mamlaka ya Usafiri wa Anga nchini kwa kuanza kutekeleza mradi huu. Kama mlivyosikia, Mradi huu utagharimu takriban shilingi bilioni 67.3. Asilimia 45 ya fedha hizo zinatoka kwenye vyanzo vya ndani vya Mamlaka, ambavyo wamepata baada ya kuamua kujibana. Serikali Kuu imewaunga mkono kwa kuwaongezea asilimia 55 iliyobaki. Hii maana yake ni kwamba fedha zote za kutekeleza mradi huu zimetolewa na Serikali. Hongereni sana TCAA. Nahimiza taasisi nyingine nazo ziige mfano wenu.
Nitutumie fursa hii pia kuwapongeza viongozi na wafanyakazi wa TCAA kwa kazi nzuri mnayoifanya ambayo inailetea sifa nchi yetu. Hivi punde Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano ameeleza kuwa mmevuka lengo la usalama ICAO la asilimia 60 kwa kupata asilimia 64.35. Nawapongezeni sana kwa kuvuka lengo hilo tena kwa kipindi kifupi sana. Mwaka 2013 mlipata asilimia 37.8. Hongereni sana. Nikuhakikishie Mheshimiwa Waziri kuwa nitakuwa tayari kumpokea Rais wa ICAO wakati wowote ili niweze kupokea tuzo ambayo TCAA imepata.
Waheshimiwa Viongozi, Mabibi na Mabwana;
Kama alivyogusia Mheshimiwa Waziri kuwa Mradi huu wa Rada ni sehemu ya miradi mingi inayotekelezwa nchini kwa lengo la kuboresha na kuimarisha usafiri wa anga. Kama mnavyofahamu, katika dunia ya sasa usafiri wa anga ni muhimu sana, hususan katika masuala ya biashara (ikiwemo kusafirisha maua, mbogamboga, minofu ya samaki na nyama) na pia kukuza sekta ya utalii. Zaidi ya asilimia 70 ya watalii duniani wanatumia usafiri wa anga. Na kama mjuavyo, nchi yetu ni miongoni mwa nchi zinazoongoza kwa kuwa na vivutio vingi vya utalii, na katika kipindi kifupi kijacho, tumejipanga kuongeza idadi ya watalii wanaotembelea nchi yetu kutoka milioni 1.3 ya sasa hadi milioni 5. Kwa sababu hiyo, uimarishaji wa usafiri wa anga ni jambo lisilokwepeka.
Hivyo basi, mbali na Mradi huu wa Rada, tumenunua ndege mpya sita. Tatu tayari zimewasili, ikiwemo moja ambayo itawasili baadaye leo. Ndege nyingine tatu zinatarajiwa kuwasili baadaye mwaka huu, ikiwemo ndege kubwa ya Boeing Dreamliner yenye uwezo wa kubeba watu 262. Mbali na ununuzi wa ndege, tunafanya upanuzi wa viwanja vikubwa vya Dar es Salaam na Kilimanjaro kwa gharama ya takriban shilingi bilioni 650. Aidha, tunafanya upanuzi wa viwanja vingine 11 vya mikoani kwa gharama ya shilingi bilioni 500. Ni matumaini yangu kuwa miradi hii ikikamilika, usafiri wa anga nchini utaimarika. Na kama mnavyofahamu, tunaendelea pia kuimarisha usafiri wa reli, maji na barabara.
Mheshimiwa Waziri, Mabibi na Mabwana;
Nimekuja hapa kwa ajili ya kuweka Jiwe la Msingi la Mradi wa Rada. Hata hivyo, kabla sijahitimisha hotuba yangu, naomba nieleze masuala mawili ya mwisho.
Mosi, nazihimiza Wizara, Mamlaka ya Viwanja vya Ndege na Msimamizi wa Mradi huu kuhakikisha mnamsimamia kwa karibu Mkandarasi, Kampuni ya Thales Las France SAS, ili mradi huu ukamilike mapema, ikiwezekana kabla ya muda uliopangwa. Niombe pia Mamlaka ya Usafiri wa Anga kuhakikisha mnaandaa wataalam wa kutosha kwa ajili ya kuendesha na kutunza Rada tunazojenga. Nimefurahi kusikia kuwa wataalam takriban 33 tayari wapo Ufaransa kwa ajili ya mafunzo.
Pili, naziagiza mamlaka husika kuimarisha ulinzi na usalama kwenye viwanja vyetu. Hakikisheni viwanja vyote vinakuwa na vifaa vya kisasa vya ukaguzi wa abiria lakini pia mipaka ya viwanja vyote ilindwe. Tukio la aibu na la kusikitisha lililotokea Mwanza halipaswi kujirudia tena.
Tatu, katika maelezo yako Mheshimiwa Waziri umeeleza wasiwasi wako kuwa ujenzi wa Mradi huu unaweza kuchelewa kukamilika kwa sababu ya tatizo la fedha linalokabili ujenzi wa jengo jipya la kuongeza ndege katika Uwanja wa Ndege wa Mwanza. Napenda kuiagiza Wizara ya Ujenzi kumsimamia kwa karibu Mkandarasi anayetekeleza ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Mwanza. Amekuwa akisuasua sana na kutoa visingizio vingi. Fedha za kutekeleza mradi huo zipo. Hivyo basi, narudia tena kuwaagiza kumsimamia Mkandarasi huyo kwa karibu. Mradi huo umechelewa sana kukamilika; hivyo tusiruhusu uendelee kuchelewa na kukwamisha ujenzi wa Rada.
Suala la nne na la mwisho, napenda nitumie fursa hii kuwaarifu wana-Dar es Salaam na Watanzania kwa ujumla kuwa nchi yetu inaenda vizuri. Tupo vizuri. Mwaka jana (2007) uchumi wetu ulikua kwa asilimia 7 na hivyo kuifanya nchi yetu kuwa miongoni mwa nchi tano ambazo uchumi wake unakuwa kwa kasi kubwa Barani Afrika. Na hii pia ndio imetuwezesha kununua ndege sita, tunajenga reli, tunajenga barabara, tunatekeleza miradi ya umeme, tunaboresha huduma za afya, elimu na maji. Tusingekuwa vizuri kiuchumi tusingeweza kufanya mambo hayo yote kwa mpigo. Nitumie fursa hii kuwapongeza Watanzania wote kwa kuendelea kulipa kodi. Miradi hii yote tumeweza kuitekeleza kutokana kodi zenu. Hivyo, endeleeni kulipa kodi, lakini pia chapeni kazi kwa bidii, na bila kusahau tuzidi kudumisha amani na mshikamano wetu. Serikali, kwa upande wake, ipo imara katika kuhakikisha amani ya nchi yetu inaendelea kudumu.
Mheshimiwa Waziri wa Uchukuzi;
Waheshimiwa Viongozi,
Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;
Nihitimishe hotuba yangu kwa kukushukuru tena Mheshimiwa Waziri kwa kunialika. Aidha, narudia tena kuipongeza Wizara, Mamlaka ya Usafiri wa Anga pamoja na taasisi nyingine zilizopo chini ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa kazi nzuri na kubwa mnazoendelea kuzifanya. Hongereni sana. Endeleeni kufanya kazi kwa kujituma. Serikali ipo pamoja nanyi.
Mabibi na Mabwana; Baada ya kusema hayo, sasa nipo tayari kutekeleza jukumu lililonileta hapa la kuweka Jiwe la Msingi la Mradi wa Mfumo wa Rada kwa ajili ya Viwanja vya Ndege vya Julius Nyerere, Kilimanjaro, Mwanza na Songwe utakaogharimu shilingi bilioni 67.3, ambazo zote zitatolewa na Serikali yetu.
Mungu Ubariki Mradi huu wa Ujenzi wa Rada!
Mungu Ibariki Tanzania!
“Ahsanteni sana kwa kunisikiliza”
- Mar 26, 2018
HOTUBA YA MHESHIMIWA DKT. JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, KWENYE HAFLA YA UZINDUZI WA MAGARI MAPYA 181 YA BOHARI YA DAWA YA...
Soma zaidiHotuba
HOTUBA YA MHESHIMIWA DKT. JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, KWENYE HAFLA YA UZINDUZI WA MAGARI MAPYA 181 YA BOHARI YA DAWA YALIYOTOLEWA NA MFUKO WA DUNIA
WA KUPAMBANA NA UKIMWI, MALARIA NA KIFUA KIKUU
DAR ES SALAAM, TAREHE 26 MACHI, 2018
Mheshimiwa Ummy Mwalimu, Waziri wa Afya,
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto;
Waheshimiwa Manaibu Mawaziri mliopo;
Bwana Linden Morrison, Mwakilishi wa Mtendaji Mkuu
wa Mfuko wa Dunia wa Kupambana na UKIMWI,
Kifua Kikuu na Malaria (Global Fund);
Waheshimiwa Wabunge mliopo;
Mheshimiwa Paul Makonda,
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam;
Dkt. Mpoki Ulisubisya, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya,
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto;
Ndugu Makatibu Wakuu mliopo;
Bwana Laurean Rugambwa Bwanakunu,
Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Dawa;
Viongozi wengine wa Serikali, Vyama vya Siasa
pamoja na Viongozi wa Dini mliopo;
Ndugu Wafanyakazi wa Bohari ya Dawa;
Wageni waalikwa wote, Mabibi na Mabwana:
Awali ya yote, napenda nimshukuru Mwenyezi Mungu aliyetupa uzima na kutuwezesha kukutana hapa. Aidha, namshukuru Mheshimiwa Waziri wa Afya kwa kunialika kwenye tukio hili muhimu la Uzinduzi wa Magari 181 ya Bohari ya Dawa, ambayo nchi yetu imepatiwa msaada na Mfuko wa Dunia wa Kupambana na UKIMWI, Kifua Kikuu na Malaria (Global Fund. Ahsante sana Mheshimiwa Waziri kwa kunialika.
Napenda pia nitumie fursa hii, hapa mwanzoni kabisa, kutoa shukrani zangu nyingi kwa Global Fund kwa kutoa msaada huu wa magari 181 kwa Bohari yetu ya Dawa. Nimeambiwa kuwa baada ya kupata magari haya, ambayo thamani yake ni shilingi bilioni 20.75, sasa Bohari ya Dawa itakuwa na jumla ya magari 213 kutoka 32 iliyokuwa nayo awali. Hii, bila shaka, itaongeza ufanisi na utendaji kazi wa Bohari yetu ya Dawa, hususan katika kusambaza dawa na vifaa tiba sehemu mbalimbali nchini. Hivyo basi, tunawashukuru sana Global Fund kwa kutupatia msaada huu.
Lakini niseme tu kwamba, hii sio mara ya kwanza kwa Global Fund kutupatia msaada. Tangu Mfuko huu uanzishwe mwaka 2003, nchi yetu imenufaika na misaada yenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 1.9, sawa na zaidi ya shilingi trilioni 4, hadi kufikia mwezi Julai 2017. Kama mnavyofahamu, Mfuko huu ndio pia umetoa fedha kwa ajili ya kujenga nyumba 480 za watumishi wa afya sehemu mbalimbali nchini, kupitia Taasisi ya Benjamin William Mkapa.
Ukiachilia mbali misaada hiyo, mwezi Julai mwaka jana, Mfuko huu uliidhinisha kiasi kingine cha Dola za Marekani milioni 591, takriban shilingi trilioni 1.1, kitakachotumika hadi mwaka 2020, kwa ajili ya kupambana na magonjwa ya UKIMWI, Kifua Kikuu, Malaria pamoja na kuboresha na kuimarisha huduma za afya nchini. Tunawashukuru sana marafiki zetu hawa wa Global Fund. Nimefurahi kuona kuwa katika hafla hii tunaye mwakilishi wa Global Fund, Bwana Morrison. Kwa niaba yangu binafsi, na kwa niaba ya Serikali na Watanzania wote, naomba utufikishie shukrani zetu nyingi kwa uongozi wa juu wa Global Fund. Tunawasihi mzidi kuunga mkono jitihada zetu za kupambana na UKIMWI, Kifua Kikuu, Malaria pamoja na kuboresha na kuimarisha sekta ya afya nchini. Tunaahidi kuitumia vizuri misaada yenu.
Waheshimiwa Viongozi;
Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;
Sekta ya afya ni nyeti na muhimu kwa maendeleo ya Taifa lolote. Bila kuiimarisha sekta hii ni ndoto kupata maendeleo. Hata azma na dhamira yetu ya kuwa nchi ya uchumi wa kati wenye kuongozwa na viwanda ifikapo mwaka 2025, haiwezi kutimia kama hatutaweka mkazo kwenye sekta ya afya. Hii ni kwa sababu, ili kufikia azma hiyo, tunahitaji wananchi wenye afya njema; watakaoweza kushiriki kikamilifu shughuli za kiuchumi na uzalishaji, kama vile ujenzi wa viwanda, kilimo, uvuvi, ufugaji, utalii, biashara, n.k.
Kwa kuzingatia hilo, na kwa nia ya kuendeleza jitihada zilizofanywa na awamu zilizotangulia, Serikali ya Awamu ya Tano imetoa kipaumbele kikubwa kwenye sekta ya afya. Hivi sasa sekta ya afya ni miongoni mwa zinazoongoza kwa kutengewa fedha nyingi. Mathalan, katika Mwaka wa Fedha 2015/2016 ilitengewa shilingi trilioni 1.8, Mwaka wa Fedha 2016/2017 shilingi trilioni 1.9 na Mwaka huu wa Fedha imetengewa shilingi trilioni 2.2. Moja ya maeneo yaliyonufaika zaidi na ongezeko hili la bajeti ni eneo la dawa na vifaa tiba. Bajeti ya kununua dawa imeongezeka maradufu, kutoka shilingi bilioni 31 Mwaka wa Fedha 2015/2016 hadi kufikia shilingi bilioni 251 Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mwaka huu wa Fedha (2017/2018) imefikia shilingi bilioni 269.
Nitumie fursa hii kuwapongeza sana Wizara ya Afya pamoja na Bohari ya Dawa kwa kazi nzuri ya kuhakikisha dawa zinapatikana nchini. Niwapongeze pia uamuzi wa kuanza kununua dawa na vifaa tiba moja kwa moja kutoka kwa wazalishaji. Uamuzi huo umesaidia sana kudhibiti bei za dawa nchini. Sina shaka, ufanisi na utendaji kazi wenu mzuri ndio umewesha Bohari yetu ya Dawa kukasimiwa jukumu la kununua dawa, vifaa tiba na vitendanishi kwa niaba ya nchi zote za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC). Hongereni sana Bohari ya Dawa. Ni matumaini yangu kuwa magari haya 181 mliyopewa na Global Fund, yataboresha zaidi utendaji wenu wa kazi, na hasa katika kuhakikisha upatikanaji na usambazaji dawa nchini. Na katika hili, niwahimize Bohari ya Dawa kuendelea kufungua Maduka ya Dawa sehemu mbalimbali nchini ili kuongeza uhakika dawa nchini.
Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;
Ukiachilia mbali eneo la dawa, Serikali inaendelea na ujenzi pamoja na ukarabati wa miundombinu ya vituo vya kutolea huduma za afya. Tumejenga vituo vipya vya kutolea huduma za afya vipatavyo 268 na hivyo kuifanya nchi yetu kuwa na vituo vya kutolea huduma za afya vipatavyo 7,284. Vituo vingine vya kutoa huduma za afya vinaendelea kujengwa sehemu mbalimbali nchini, ikiwemo ujenzi wa Hospitali za Mikoa mipya ya Njombe, Geita, Katavi na Simiyu. Sambamba na ujenzi wa vituo hivyo vipya, hivi sasa tunaboresha vituo vya afya 204 nchi nzima. Moja ya malengo ya uboreshaji huo ni kuviwezesha vituo hivyo kufanya upasuaji wa dharura lengo likiwa kupunguza vifo vya akimama wajawazito na mtoto kutoka wastani wa vifo 556 katika kila vizazi hai 100,000 hivi sasa hadi kufikia angalau vifo 292 mwaka 2020. Naziipongeza Wizara ya Afya na TAMISEMI kwa kusimamia ujenzi wa vituo hivyo.
Tumeendelea pia kuimarisha huduma za kibingwa kwenye Hospitali zetu za Rufaa za Muhimbili, Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete, Taasisi ya Mifupa (MOI), Taasisi ya Saratani ya Ocean Road pamoja na hospitali za rufaa za Bugando, Mbeya na KCMC. Aidha, tunaziimarisha Hospitali zetu za Benjamini Mkapa iliyopo Chuo Kikuu cha Dodoma pamoja na Hospitali yetu ya kisasa kabisa ya Mloganzila, ambayo niliizindua mwezi Novemba 2017. Ni wazi kuwa hatua hizi tunazozichukua sio tu zitaboresha na kuimarisha sekta ya afya nchini, bali pia zitaiwezesha nchi yetu kufikia azma yake ya kuwa nchi ya uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.
Mheshimiwa Waziri wa Afya;
Waheshimiwa Viongozi;
Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;
Jukumu langu leo ni kuzindua magari haya 181 yaliyotolewa na Global Fund kwa Bohari yetu ya Dawa. Hata hivyo, kabla sijatekeleza jukumu hilo, naomba mniruhusu niseme masuala machache ya mwisho.
Suala la kwanza ni kuhusu utunzaji wa magari haya. Kama mlivyosikia, magari haya yamegharimu fedha nyingi. Hivyo basi, Bohari ya Dawa mnao wajibu wa kuhakikisha magari haya yanatunzwa. Hakikisheni mnatafuta madereva makini ili magari haya yatumike kwa muda mrefu. Nitashangaa sana na kwa kweli nitasikitika sana, endapo baada ya mfupi kupita, nitasikia magari haya yameharibika.
Pili, naendelea kuhamasiha taasisi na wafanyabiashara kuwekeza kwenye viwanda vya dawa nchini. Kama ambavyo mmesikia, Serikali imeongeza bajeti ya dawa hadi kufikia shilingi bilioni 269. Ukijumlisha na michango kutoka kwa wafadhili mbalimbali, bajeti ya dawa hivi sasa inafikia takriban shilingi bilioni 460, kama ambavyo Mheshimiwa Waziri amesema. Zaidi ya hapo, kama nilivyogusia awali, Bohari yetu ya Dawa imepewa dhamana na Global Fund kununua dawa kwa ajili ya nchi zote za SADC. Lakini, pamoja na mafanikio hayo, inasikitisha kuona kuwa asilimia 94 ya dawa ambazo Bohari ya Dawa inanunua zinatoka nje ya nchi. Kama tungekuwa na viwanda vya dawa, fedha nyingi zingebaki hapa nchini na Watanzania wangepata ajira. Ni kwa sababu hii nazidi kukihimiza ujenzi wa viwanda vya dawa nchini. Na nitumie fursa hii kutoa wito kwa Wizara ya Afya kubuni mkakati wa kuwahamasisha wafanyabiashara na wataalam wa hapa nchi kujenga viwanda vya dawa. Serikali itakuwa tayari kuwaunga mkono.
Tatu, pamoja na jitihada zinazofanywa na Serikali za kuimarisha upatikanaji dawa nchini, ninazo taarifa kuwa wakati mwingine Bohari ya Dawa imekuwa ikikumbana na vikwazo katika kuingiza dawa nchini kutoka taasisi mbalimbali za Serikali. Kwa kweli, mimi huwa nashangaa sana. Inakuwaje taasisi moja ya Serikali inaikwamisha taasisi nyingine. Taasisi za Serikali hazipaswi kukwamishana katika utendaji kazi. Zinao wajibu wa kufanya kazi kwa ukaribu na ushirikiano. Hivyo basi, napenda kutumia fursa hii kuzihimiza taasisi za Serikali kuacha kukwamishana. Na niseme tu kwamba, Serikali haitavumilia kuona taasisi yake moja ikikwamisha shughuli za taasisi nyingine. Hilo likitokea, hatutasita kuchukua hatua. Lakini kuhusu suala hili la Bohari ya Dawa, naagiza Wizara ya Wizara ya Afya kulishughulikia na hasa kwa sababu, kwa mujibu wa taarifa nilizonazo, kikwazo kikubwa cha uingizaji dawa kimekuwa Mamlaka ya Chakula na Dawa (TDFA), ambayo nayo ipo chini ya Wizara ya Afya. Hili ni suala lenu la ndani; hivyo hamna budi kulishughulikia ninyi wenyewe.
Waheshimiwa Viongozi;
Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;
Napenda kuhitimisha kwa kumshukuru tena Mheshimiwa Waziri kwa kunialika. Aidha, narudia tena kuwashukuru Global Fund kwa kutupatia msaada huu wa magari pamoja na misaada mingine wanayotoa kwa nchi yetu. Nawapongezeni tena Bohari ya Dawa kwa kazi nzuri na kubwa mnayoifanya, lakini pia nawahimiza kutunza magari haya.
Baada ya kusema hayo, sasa nipo tayari kuzindua magari 181 yenye thamani ya shilingi bilioni 20.75 ambayo yametolewa na Mfuko wa Dunia wa Kupambana na UKIMWI, Kifua Kikuu na Malaria.
Mungu Ibariki Global Fund!
Mungu Ibariki Bohari ya Dawa!
Mungu Ibariki Tanzania!
“Ahsanteni sana kwa kunisikiliza”
- Mar 14, 2018
HOTUBA YA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, DKT. JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI KWENYE HAFLA YA KUWEKA JIWE LA MSINGI LA UJENZI WA RELI MPYA YA KISASA (STAND...
Soma zaidiHotuba
HOTUBA YA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, DKT. JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI KWENYE HAFLA YA KUWEKA JIWE LA MSINGI LA UJENZI WA RELI MPYA YA KISASA (STANDARD GAUGE RAILWAY – SGR) STESHENI YA IHUMWA, DODOMA, TAREHE 14 MACHI, 2018
Mheshimiwa Kassim Majaliwa, Waziri Mkuu
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Mheshimiwa Tulia Ackson, Naibu Spika wa Bunge
la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Mheshimiwa Mizengo Pinda, Waziri Mkuu Mstaafu
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Mheshimiwa Philip Mangula, Makamu Mwenyekiti
wa Chama Cha Mapinduzi – Bara;
Mheshimiwa Prof. Makame Mbarawa,
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano;
Waheshimiwa Mawaziri mliopo hapa;
Mheshimiwa Dkt. Binilith Mahenge,
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma;
Waheshimiwa Makatibu Wakuu mliopo hapa;
Waheshimiwa Wabunge mliopo;
Mheshimiwa Balozi wa Uturuki nchini;
Waheshimiwa Mabalozi na Wawakilishi wa Taasisi za Kimataifa;
Waheshimiwa Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama;
Profesa John Kandoro, Mwenyekiti wa Bodi
ya Shirika la Reli Tanzania;
Bwana Masanja Kadogosa, Mkurugenzi Mtendaji
wa Shirika la Reli Tanzania;
Waheshimiwa Viongozi wengine wa Serikali mliopo;
Waheshimiwa Viongozi wa Vyama vya Siasa na Dini mliopo;
Viongozi na Wafanyakazi wa Makampuni
ya Yapi, Merkezi (Uturuki) na Mota Engil ya Ureno;
Wafanyakazi wa Shirika la Reli nchini;
Ndugu Wananchi, Wana-Habari, Mabibi na Mabwana:
Awali ya yote, napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kukutana hapa leo hii. Aidha, napenda kuushukuru Uongozi wa Wizara ya Ujenzi pamoja na Shirika la Reli nchini kwa kunialika kushiriki kwenye tukio hili muhimu na la kihistoria la kuweka Jiwe la Msingi la Mradi wa Reli ya Kisasa (Standard Gauge) kutoka Morogoro hadi Dodoma (Makutopora), umbali wa kilometa 422. Nakumbuka, tarehe 12 Aprili mwaka jana, mlinialika kuweka Jiwe la Msingi la Awamu ya Kwanza la Mradi huu pale Pugu, Dar es Salaam. Na leo mmenialika tena, nawashukuruni sana.
Napenda pia kutumia fursa hii kuwashukuru wananchi wa hapa Ihumwa, maeneo jirani pamoja na Mkoa mzima wa Dodoma kwa kujitokeza kwa wingi kushiriki katika tukio hili. Nimepita hapa Ihumwa mara nyingi, lakini sikuwa nikifahamu kuwa Kitongoji hiki ni kikubwa. Leo nimejionea mwenyewe; na kwa namna mlivyojitokeza kwa wingi kwenye tukio hili, napenda kuwaahidi kuwa Serikali itajenga barabara kutoka pale Barabara Kuu (Dar –es Salaam – Dodoma) hadi hapa stesheni. Waziri wa Ujenzi yupo hapa, hivyo basi, ni matumaini yangu kuwa amenisikia.
Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi;
Waheshimiwa Viongozi, Mabibi na Mabwana;
Ni jambo lililo wazi kuwa miundombinu imara ya usafiri ni kichocheo muhimu cha ukuaji uchumi katika nchi. Bila kuwa na miundombinu hiyo, ni ndoto kupata maendeleo. Moja ya changamoto kubwa zenye kulikabili Bara la Afrika ni kukosekana kwa miundombinu imara na ya uhakika ya usafiri.
Hali hii inasababisha gharama za usafiri kuwa juu ukilinganisha na Mabara mengine. Tafiti zinaonesha kuwa gharama za usafiri katika Bara la Afrika ni kubwa kuliko maeneo mengine duniani. Mathalan, wastani wa bei ya kusafirisha kontena moja la futi 20 kwenye nchi za Afrika Mashariki, umbali usiozidi kilometa 1,500, ni Dola za Marekani 5,000. Bei hii ni sawa kabisa na gharama ya kusafirisha kontena lenye ukubwa kama huo kutoka China hadi Tanzania, umbali wa kilometa 9,000.
Kwa ujumla, tafiti zinaonesha kuwa kukosekana kwa miundombinu imara ya usafiri kunashusha Pato la nchi za Afrika kwa asilimia 2 na kuongeza gharama za usafirishaji kwa asilimia 40. Hii ndio moja ya sababu inayozifanya nchi zetu zishindwe kushindana na nchi za Mabara mengine katika masuala ya biashara, uwekezaji na halikadhalika maendeleo ya viwanda. Ni kwa sababu hiyo, leo nimefurahi sana kuja hapa Ihumwa kuweka Jiwe hili la Msingi la Awamu ya Pili ya Mradi wa Reli hii ya Kisasa kutoka Morogoro hadi Dodoma, ambayo nchi yetu imeamua kuijenga kwa fedha zake yenyewe. Nimefurahi sana.
Waheshimiwa Viongozi, Mabibi na Mabwana;
Kuna njia kuu nne za usafiri. Usafiri wa anga, maji, barabara na reli. Hata hivyo, tafiti zimethibitisha kuwa usafiri wa njia ya reli ni bora, salama, wa haraka na nafuu zaidi ukilinganisha na njia nyingine, hususan katika kusafirisha shehena kubwa ya mizigo na idadi kubwa ya abiria. Ripoti ya Benki ya Maendeleo ya Afrika ya Mwaka 2015 kuhusu Usafiri wa Reli (Rail Infrastructure in Africa: Financing Policy Option) inaeleza kuwa, napenda kunukuu kwa Kiswahili,“Rail Transport is critical to supporting economic development and, unless this mode of transport is developed, Africa may not realize its full potential in exploiting its abundant natural resources and wealth”, mwisho wa kunukuu. (Nikinukuu maneno hayo kwa lugha yetu adhimu ya Kiswahili, Ripoti hiyo ya AfDB inasema kuwa, Usafiri wa reli ni mhimili muhimu kwa maendeleo ya kiuchumi na, endapo usafiri huu hautaboreshwa au kuimarishwa, Afrika kamwe haitaweza kutumia rasilimali na utajiri ilionao). Hii inadhihirisha kuwa usafiri wa njia ya reli ni muhimu kwa maendeleo ya kiuchumi.
Kwa bahati nzuri, nchi yetu inazo njia kuu mbili za usafiri wa reli. Reli ya Kati iliyojengwa enzi za ukoloni, kati ya mwaka 1899 na 1929; na ile ya TAZARA inayounganisha nchi yetu na ndugu zetu wa Zambia, ambayo ilijengwa miaka ya 1970 kwa msaada wa marafiki zetu wa China. Hata hivyo, utendaji kazi wa reli hizi sio wa kuridhisha sana kutokana na uwekezaji mdogo, ubovu wa miundombinu, uchakavu wa vitendea kazi, ikiwemo vichwa vya treni na mabehewa, pamoja na matatizo ya uongozi yaliyokuwepo.
Naupongeza uongozi mpya ukiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji, Bwana Masanja Kadogosa pamoja na watumishi wote wa Shirika la Reli kwa kuanza kuchukua hatua za kuboresha na kuimarisha usafiri wa reli nchini, hususan Reli ya Kati. Mmeanza kufanya ukarabati wa reli kutoka Tanga hadi Arusha. Mapato pia yameanza kuongezeka. Hii inadhihirisha kuwa Watanzania tukiamua tunaweza. Siku za nyuma, tuliwahi kukodisha Shirika hili kwa Kampuni kutoka nje, lakini matokeo hayakuwa mazuri. Lilizidi kudidimia. Hivyo basi, naipongeza Wizara, uongozi mpya wa Shirika na watumishi wote kwa jitihada mnazozifanya za kuliimarisha Shirika hili.
Waheshimiwa Viongozi;
Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;
Ujenzi wa reli hii mpya na ya kisasa, ambayo itatumia umeme na dizeli, utaongeza tija na ufanisi katika usafiri wa reli nchini. Kwa haraka haraka, naomba nitaje baadhi ya faida zitakazoletwa na reli hii.
Faida ya kwanza, reli hii itarahisisha usafiri wa mizigo na abiria. Tumesikia hivi punde kuwa mwendokasi wa reli hii itakuwa kilometa 120 kwa treni za mizigo na kilometa 160 kwa saa kwa treni za abiria. Hii ina maana kuwa mtu ataweza kusafiri kutoka Dar es Salaam hadi hapa Dodoma kwa kutumia saa 3 tu, kutoka wastani wa saa 5 hadi 6 zinazotumika hivi sasa kwa usafiri wa gari na saa 12 zinazotumika sasa kwa kutumia reli. Aidha, mtu atasafiri kwa kutumia saa 9 tu hadi Mwanza kutoka saa 36 za reli ya sasa. Ni dhahiri kuwa hii itarahisisha huduma za usafiri sio tu hapa nchini bali pia kwenda nchi jirani.
Aidha, reli hii itaongeza biashara hapa nchini pamoja na nchi za jirani. Kama mnavyofahamu, nchi yetu inapakana na takriban nchi 8, ambapo 6 hazina Bahari; hivyo, kutegemea kupitishia mizigo yao kwenye Bandari zetu. Inakadiriwa kuwa reli hii itakuwa na uwezo wa kusafirisha tani milioni 17 kwa mwaka, ukilinganisha na tani milioni 5 za sasa. Hii, bila shaka, itaongeza mapato kwenye Bandari yetu ya Dar es Salaam, lakini pia itaimarisha biashara, hususan kati ya nchi yetu na nchi zinazohudumiwa na Ushoroba wa Kati (Central Corridor), yaani Burundi, DRC, Rwanda na Uganda.
Vilevile, ujenzi wa reli hii utasaidia kutunza barabara zetu. Kama mnavyofahamu, tumepiga hatua kubwa katika ujenzi wa barabara za lami. Mikoa mingi tayari imeunganishwa kwa barabara za lami. Mathalan, Mkoa wa Dodoma hivi sasa umeunganishwa na Mikoa ya Manyara, Morogoro, Singida na Iringa kwa lami. Hata hivyo, barabara zetu, wakati mwingine, zimekuwa zikiharibika mapema kutokana na kutumika kusafirisha mzigo mkubwa. Hivi punde tumesikia kuwa reli hii ya kisasa itakuwa na uwezo wa kubeba mzigo wa takriban tani 10,000 kwa mara moja, sawa na malori (semi trailers) 500 yenye uwezo wa kubeba tani 20. Hii, bila shaka, itasaidia sio tu kutunza barabara zetu, bali pia kupunguza gharama za kukarabati barabara hizo mara kwa mara.
Halikalidhalika, ujenzi wa reli hii utasaidia kukuza sekta nyingine za kiuchumi. Kama mnavyofahamu, ustawi wa sekta zote za kiuchumi (kilimo, uvuvi, ufugaji, viwanda, madini, utalii, n.k.) unategemea miundombinu ya usafiri. Ni vigumu sana kukuza sekta hizo za kiuchumi bila kuwa na miundombinu imara ya usafiri.
Sambamba na hayo, ujenzi wa reli hii ya kisasa utatoa ajira. Inakadiriwa kuwa jumla ya ajira 30,000 za moja kwa moja na nyingine 600,000 zisizo za moja kwa moja zitatolewa wakati wa ujenzi wa reli hii. Hii itasaidia kupunguza tatizo la ajira nchini. Zaidi ya hapo, reli hii itasaidia kupunguza uharibifu wa mazingira. Kama mnavyofahamu, reli hii itakuwa pia inatumia umeme, ambao hautoi hewa ya ukaa kwa wingi, na hivyo kusaidia kutunza mazingira yetu.
Ndugu Wananchi, Mabibi na Mabwana;
Hizi ni baadhi tu ya faida za ujenzi wa reli hii. Zipo nyingine nyingi. Hivyo basi, sisi Watanzania hatuna budi kujivuna na kujipongeza kwa kutekeleza mradi huu. Ndio; sisi Watanzania ni lazima tujivune. Tuna kila sababu ya kujivuna. Nchi yetu imebarikiwa sana. Ni kubwa, na kama mlivyosikia hivi majuzi imetangazwa kuwa, hivi sasa tumefikia takriban milioni 54. Hii inatuongezea nguvu na sauti kimataifa, lakini pia ni mtaji mkubwa katika harakati zetu za kujiletea maendeleo. Wenzetu wa China wametumia fursa kama hii (ukubwa wa nchi na idadi ya watu, bilioni 1.3) kujiletea maendeleo. Hivyo basi, na sisi tunaweza kutumia fursa hii kuharakisha maendeleo kwenye nchi yetu.
Hata hivyo, ni wazi kuwa, ukubwa wa nchi na idadi ya watu peke yake, sio hoja. Ni kwa namna gani tunatumia ukubwa wa nchi na idadi ya watu tuliyonayo ndio jambo la msingi zaidi. Nchi ya Denmark ni ndogo na ina idadi ya watu wapatao milioni 5. Lakini, nchi hii ni tajiri na wanatoa misaada hadi kwa nchi yetu. Hii imewezekana kwa vile wamejipanga vizuri na wanajituma katika kufanya kazi. Ndio sababu na mimi kila wakati nimekuwa nikiwasisitiza Watanzania kufanya kazi. Maendeleo si lelemama. Hakuna njia ya mkato katika kutafuta maendeleo. Usipofanya kazi, kila siku utakuwa unalalamika kuwa “vyuma vimebana”.
Hivyo basi, napenda kutumia fursa hii kuwahimiza Watanzania wenzangu tuzidi kuchapa kazi. Mbali na ujenzi wa reli hii, hivi sasa tunatekeleza au tupo mbioni kuanza kutekeleza miradi mikubwa ya miundombinu, ikiwemo Mradi wa Bomba la Mafuta kutoka Hoima nchini Uganda hadi Bandari ya Tanga; Mradi wa Kufufua Umeme wa Stiglier’s Gorge na Usambazaji wa Umeme Vijijini (REA); Upanuzi wa Bandari za Dar es Salaam, Mtwara na Tanga; upanuzi wa viwanja vya ndege, ujenzi wa barabara; utengenezaji wa meli katika Ziwa Victoria na Maziwa mengine; n.k. Miradi hii itatoa ajira nyingi, zaidi ya milioni moja. Hivyo basi, nawasihi sana Watanzania tuzichangamkie.
Waheshimiwa Viongozi;
Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;
Nimekuja hapa kwa ajili ya kuweka Jiwe la Msingi la Mradi huu wa Reli ya Kisasa kutoka Dar es Salaam kwenda Mikoa ya Mwanza na Kigoma; na hatimaye kuelekea nchi za Burundi na Rwanda. Nimetumia muda mwingi kueleza umuhimu na faida za mradi huu. Hata hivyo, kabla sijahitimisha hotuba yangu, napenda kueleza mambo manne ya mwisho.
Jambo la kwanza, ni kuhusu utekelezaji wa mradi huu. Natoa wito kwa Wizara ya Ujenzi, Mshauri Msimamizi pamoja na Mkandarasi kuhakikisha Mradi huu unakamilika kwa wakati. Nimefurahi kuwa ujenzi wa Awamu ya Kwanza kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro unaendelea vizuri. Hakikisheni miradi hii yote inakamilika mapema iwezekanavyo, ikiwezekana kabla ya muda uliopangwa. Watanzania wana hamu kubwa ya kuona mradi huu unakamilika.
Pili, napenda kutumia fursa hii kuwahimiza Watanzania wote kuendelea kulipa kodi ili kutekeleza miradi ya maendeleo kama hii, pamoja na kuboresha huduma mbalimbali za jamii. Kama mnavyofahamu, ujenzi wa reli hii kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza, yenye urefu wa kilometa 1,219 na ambao utajengwa kwa awamu tano, utagharimu takriban shilingi trilioni 15. Katika awamu hizi mbili za mwanzo, yaani kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro na Morogoro hadi Dodoma umbali wa kilometa 722, Serikali itatumia takriban shilingi trilioni 7.062. Ukiachilia mbali mradi huu, Serikali inatekeleza miradi mingine mingi ya maendeleo, kama nilivyoitaja hapo awali, ikiwemo ujenzi wa barabara. Hapa Dodoma tumepanga kujenga barabara ya mzunguko yenye urefu wa kilometa 100.
Tunafanya upanuzi wa bandari zetu kubwa za Dar es Salaam, Mtwara na Tanga. Tumepanga kununua meli mpya kubwa kwenye Ziwa Victoria. Tunafanya ukarabati wa viwanja vya ndege takriban 11 nchini. Tumenunua ndege mpya sita. Tunajiandaa kuanza utekelezaji wa mradi mkubwa wa umeme wa Stiglier’s Gorge pamoja na kutekeleza Awamu ya Tatu ya Kupeleka Umeme Vijijini, ambapo tunataka ifikapo mwishoni mwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 tuwe tumefikisha huduma hiyo kwenye vijiji vyote ambavyo havijafikiwa na huduma ya umeme, takriban 7800 nchi nzima, vikiwemo vilivyopo katika Mkoa huu wa Dodoma. Tunatekeleza miradi mikubwa ya maji katika mikoa yote nchini, ikiwemo hapa Dodoma.
Sambamba na hayo, kama mnavyofahamu, hivi sasa tunatoa elimu bila malipo kuanzia shule ya msingi hadi Sekondari, ambapo kila mwezi tunatenga takriban shilingi bilioni 23.8. Tumeongeza idadi ya wanafunzi wanaopata mikopo ya vyuo vikuu hadi kufikia takriban 123,000, ambapo katika Mwaka huu wa Fedha tumetenga shilingi bilioni 427.544. Aidha, tunaendelea kuboresha huduma za afya, hususan kwa kujenga miundombinu. Kwenye kila Mkoa tunapeleka fedha kwa kujenga au kukarabati miundombinu. Ninyi wana-Dodoma ni mashahidi. Tunafanya upanuzi wa Hospitali yenu ya Mkoa na kukarabati vituo vitano vya afya, vikiwemo vya Makole na Bahi. Tumeongeza pia bajeti ya kununulia dawa na vifaa tiba, ikiwemo katika Hospitali ya Rufaa ya Benjamin Mkapa iliyopo Chuo Kikuu cha Dodoma, ambayo Serikali imeipatia vifaa vya kisasa kama MRI, CT-Scan pamoja na vifaa vya kupandikiza figo na kufanya upasuaji bila kuchana.
Miradi na shughuli hizi zote zinahitaji fedha. Tena nyingi. Na Serikali inapata fedha kupitia kodi. Hivyo, napenda kutumia fursa hii kuwasihi Watanzania wote kuendelea kulipa kodi. Baadhi ya wafanya biashara wanatoa risiti za thamani ndogo ukilinganisha na gharama halisi za bidhaa. Hivyo, nawasihi wafanya biashara kutoa risiti halali, lakini pia nawahimiza wananchi kudai risiti kila wakati mnaponunua bidhaa au huduma yoyote ile. Lakini, nitumie fursa hii pia kuziomba mamlaka husika, hususan Wizara ya Fedha na Mamlaka ya Kodi nchini (TRA) kutafakari viwango vya kodi zetu nchini. Kwenye baadhi ya maeneo nadhani vipo juu sana na kusababisha kudorora kwa shughuli za biashara na halikadhalika maendeleo ya viwanda. Viwango vya juu vya kodi, ndivyo pia vinawafanya baadhi ya wananchi watafute mbinu za kukwepa kulipa kodi na hivyo kuikosesha Serikali mapato. Hivyo basi, naziomba mamlaka husika kulitafakari kwa kina suala hili la kodi. Mimi naamini, kama tutapunguza utitiri na kuweka viwango vyenye kustahili au kulingana na shughuli na vipato vya Watanzania, sio tu wananchi wengi watahamasika na kuona fahari kulipa kodi, bali pia tutastawisha shughuli za biashara na maendeleo ya viwanda nchini.
Jambo la tatu, napenda kuwahimiza Watanzania wenzangu kuendelea kuilinda na kudumisha amani yetu. Mheshimiwa Waziri Mkuu amelielezea suala hili vizuri. Hivyo basi, itoshe tu kusema kuwa amani ndio msingi wa maendeleo katika Taifa lolote. Bila ya amani, hakuna maendeleo. Tuendelee kuitunza amani yetu tuliyoachiwa na waasisi wetu, wakiongozwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Tusikubali kuchonganishwa na watu wasioitakia mema nchi yetu kwa kisingizio chochote kile. Na napenda kutumia fursa hii kuvipongeza vyombo vya ulinzi na usalama kwa kazi kubwa mnayoifanya ya kulinda amani yetu.
Waheshimiwa Viongozi;
Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;
Jambo la nne na la mwisho, lakini sio kwa umuhimu, ni kwenu watani zangu Wagogo. Fursa sasa zinakuja katika Mkoa wenu. Reli hii inajengwa na itapita kwenye Mkoa wenu. Serikali inahamia Dodoma; ambapo mimi pia natarajia kuhamia mwaka huu. Viwanda vingi navyo vimeanza kujengwa. Mathalan, nafahamu kuwa Mifuko yetu ya Hifadhi ya Jamii imepanga kutekeleza miradi kadhaa ya viwanda hapa Dodoma, ikiwa ni pamoja na kufufua Kiwanda cha kusindika nafaka na kukamua mafuta cha National Milling Corporation (NMC), Kiwanda cha kutengeneza matofali na vigae, na Kiwanda cha Kusindika Juisi na Mvinyo wa Zabibu ambacho kitajengwa Chinangali, Chamwino.
Sambamba na hayo, tunatarajia kuanza ujenzi wa Kiwanja kikubwa cha michezo hapa Dodoma mjini kwa ufadhili wa marafiki zetu wa Morocco. Wataalam wetu wanatarajia hivi karibuni kwenda Morocco kupeleka mchoro wa Kiwanja. Tunatarajia pia kuanza ujenzi wa Kiwanja Kikubwa cha Ndege eneo la Msalato ili ndege kubwa ziweze kutua hapa Dodoma. Hizi ni fursa kwenu, hivyo basi, nawasihi mjipange vizuri kuzitumia, hususan katika kupambana na umaskini pamoja na tatizo la ajira.
Mheshimiwa Waziri;
Waheshimiwa Viongozi mliopo;
Wageni Waalikwa;
Ndugu Mabibi na Mabwana;
Napenda kuhitimisha hotuba yangu kwa kukushukuru tena Mheshimiwa Waziri kwa kunikaribisha kwenye hafla hii. Aidha, napenda kurudia tena kuwahimiza kuhakikisha Mradi huu unakamilika kwa wakati.
Nawashukuru pia wananchi na viongozi mbalimbali kwa kujitokeza kwa wingi kwenye tukio hili. Nakushukuru pia Mheshimiwa Spika pamoja na Wabunge kwa kupitisha bajeti ya ujenzi wa reli hii. Nawashukuru wana-habari pamoja na vikundi mbalimbali vya burudani.
Baada ya kusema hayo, sasa nipo tayari kutekeleza jukumu lililonileta la kuweka Jiwe la Msingi la Awamu ya Pili ya Mradi wa Reli ya Kisasa kutoka Morogoro hadi Dodoma (Makutopora), ambao utagharimu shilingi trilioni 4.3 ambazo zote zitatolewa na Serikali.
Mungu Ibariki Reli yetu ya Kisasa!
Mungu Wabariki wana-Dodoma!
Mungu Ibariki Tanzania!
“Ahsanteni sana kwa kunisikiliza”
- Feb 09, 2018
HOTUBA YA MHESHIMIWA DKT. JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA KWENYE HAFLA ALIYOINDAA KWA AJILI YA MABALOZI NA VIONGOZI WA TAASI...
Soma zaidiHotuba
HOTUBA YA MHESHIMIWA DKT. JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA KWENYE HAFLA ALIYOINDAA KWA AJILI YA MABALOZI NA VIONGOZI WA TAASISI
ZA KIMATAIFA KUKARIBISHA MWAKA MPYA 2018
IKULU, DAR ES SALAAM, 9 FEBRUARI, 2018
Mheshimiwa Dkt. Augustine Mahiga, Waziri wa Mambo ya Nje
na Ushirikiano wa Afrika Mashariki;
Mheshimiwa Brahin Salem Buseif, Balozi wa Saharawi
na Kaimu Kiongozi wa Mabalozi nchini;
Waheshimiwa Mabalozi na Wawakilishi wa Taasisi
na Mashirika ya Kimataifa;
Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana:
Habarini za Jioni. Karibuni sana hapa Ikulu. Nawashukuru, Waheshimiwa Mabalozi, kwa kukubali mwaliko wangu wa kuhudhuria hafla hii, ambayo kwenye utamaduni wa kidiplomasia, imezoeleka duniani kote. Tanzania na sisi tumekuwa tukifanya hafla hii kila mwaka; na bila shaka, tutaendelea kuifanya. Hata hivyo, napenda kuwaarifu kwamba, mwaka huu, huenda utakuwa wa mwisho kwa hafla hii kufanyika hapa Dar es Salaam. Tunatarajia, kuanzia mwakani, kufanyia Dodoma, Makao Makuu ya nchi yetu.
Hivyo basi, niwaombe, Waheshimiwa Mabalozi, mwakani, mjiandae kuja Dodoma, ambako viongozi wengi wa Serikali tayari wamehamia, ikiwa ni pamoja na Mawaziri, Waziri Mkuu na Makamu wa Rais. Mimi pia natarajia kuhamia mwaka huu. Hivyo, nawasihi na nyie muanze kufikiria kuhamia Dodoma. Dodoma ni pazuri na ni katikati mwa nchi yetu. Naupongeza Umoja wa Mataifa na mashirika yake kwa kuanza mchakato wa kuhamia Dodoma, ambapo mwezi Desemba 2017, walifungua Ofisi za Muda. Hongereni sana Umoja wa Mataifa; na napenda kutumia fursa hii kuwaarifu kuwa Serikali imeamua kugawa bure viwanja vyenye ukubwa wa Ekari 5.5 kwa kila Ofisi ya Kibalozi iliyopo nchini. Hivyo, nawahimiza kuchangamkia fursa hiyo.
Waheshimiwa Mabalozi;
Wawakilishi wa Mashirika na Taasisi za Kamataifa;
Hivi sasa ni takriban mwezi mmoja na siku kadhaa umepita tangu kuanza kwa Mwaka Mpya 2018. Kwa utamaduni wetu sisi Watanzania, mwaka ukianza, hadi mwezi Machi, huwa tunaendelea kupeana heri ya mwaka mpya. Hivyo basi, kwa niaba yangu binafsi na kwa niaba ya Serikali na Wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, napenda kutumia fursa hii, kuwawatakia heri ya Mwaka Mpya wa 2018, ninyi Waheshimiwa Mabalozi na Wawakilishi wa Taasisi za Kimataifa, familia pamoja na watumishi wenu. Aidha, naomba mnifikishie salamu zangu za Heri ya Mwaka Mpya 2018 kwa Wakuu wa Nchi pamoja na Taasisi na Mashirika, ambayo mnayawakilisha vizuri hapa nchini.
Nafahamu kuwa, kwa baadhi yenu, hii ni mara ya kwanza kushiriki katika hafla hii hapa Tanzania. Napenda nirudie tena kuwakaribisha sana nchini kwetu. Tanzania ni nchi nzuri; watu wake ni wakarimu na ina vivutio vingi vya utalii. Nina uhakika, mmeshasikia kuhusu Visiwa vya Zanzibar, Mlima Kilimanjaro, pamoja na Mbuga za Serengeti na Ngorongoro. Lakini, mbali na vivutio hivyo vinavyotambulika ulimwenguni kote, tunavyo vivutio vingine vingi vizuri. Mti mrefu zaidi Barani Afrika upo hapa nchini, tena karibu kabisa na Mlima Kilimanjaro. Aidha, tuna Hifadhi ya Taifa ya Ruaha ambayo ni kubwa zaidi nchini na inasifika kwa kuwa na tembo wengi. Vilevile, tunayo Hifadhi ya Taifa ya Kitulo ambayo inasifika kwa kuwa na aina nyingi za maua ya ndwele ya asili ambayo hayapatikani sehemu nyingine yoyote duniani; na halikadhalika Maporomoko ya Mto Kalambo, kule Rukwa, ambayo ni ya pili kwa kuwa na kina kirefu Barani Afrika, baada ya yale ya Tugale yaliyopo nchini Afrika Kusini. Hivyo basi, nawahimiza, mkipata muda, tembeleeni vivutio hivyo ili mjionee uzuri wa Tanzania. Tunawaomba pia muwahamasishe wananchi wenu kuja kutembelea vivutio vyetu.
Waheshimiwa Mabalozi;
Wawakilishi wa Mashirika na Taasisi za Kamataifa;
Bila shaka, mtakubaliana nami kuwa, duniani kote, katika kipindi cha mwanzo wa mwaka kama hiki; ni jambo la kawaida kufanya tafakari ya masuala ya mwaka uliopita na kupanga mikakati ya mwaka mpya. Kwetu sisi Tanzania, Mwaka 2017, ulikuwa wenye mafanikio makubwa katika ngazi ya kitaifa na kimataifa; japo changamoto nazo zilikuwepo.
Mathalan, katika ngazi ya kitaifa, mwaka jana, tuliendelea kutekeleza Mpango wetu wa Maendeleo wa Miaka mitano wa 2016/17 – 2020/2021, unaolenga kuifanya nchi yetu kuwa ya uchumi wa kati unaoongozwa na viwanda ifikapo mwaka 2025, kama ambavyo Dira ya Taifa ya Maendeleo inavyoelekeza. Na katika kutekeleza Mpango wetu, tuliweka pia mkazo katika kushughulikia matatizo yaliyokuwa yakitukwamisha katika kupiga hatua za kimaendeleo. Kama mjuavyo “Ukitaka kupata maendeleo, badala ya kuongeza tu bidii, jambo la kwanza unatakiwa kushughulikia au kurekebisha mambo yanayokukwamisha kupata maendeleo”. Mathalan, ukitaka kujitosheleza kifedha, njia nzuri sio kuongeza bidii ya kutafuta fedha, bali unatakiwa kwanza kudhibiti matumizi ya kile kidogo unachokipata. Na vilevile, ukitaka kupungua unene, njia nzuri sio kuanza kufanya mazoezi, bali ni kuacha kufanya mambo yanayosababisha uwe mnene.
Kwa kuzingatia hilo, mwaka 2017, tuliendelea kushughulikia matatizo yenye kuikwamisha nchi yetu kupata maendeleo. Tulizidisha mapambano dhidi ya rushwa, wizi na uporaji wa rasilimali zetu. Kama mnavyofahamu, miongoni mwa mambo yanayozikwamisha nchi za Afrika kupata maendeleo ya haraka kiuchumi, Tanzania ikiwemo, ni vitendo vya rushwa, ukwepaji kodi na uporaji wa rasilimali. Ripoti ya Jopo la Umoja wa Afrika lililoongozwa na Rais wa Zamani wa Afrika Kusini, Thabo Mbeki, iliyotolewa mwaka 2015, ilibainisha kuwa katika kipindi cha miongo mitatu iliyopita nchi za Afrika, Tanzania ikiwemo, zimepoteza takriban Dola za Marekani trilioni 1.8, wastani wa Dola za Marekani bilioni 50 – 80 kwa mwaka. Aidha, Ripoti hiyo iliendelea kueleza kuwa, hivi sasa, nchi za Afrika, kila mwaka, zinapoteza wastani wa Dola za Marekani bilioni 150 kutokana na rushwa, wizi, ukwepaji kodi na uporaji wa rasilimali.
Hivyo basi, katika mwaka 2017, tumeendelea kuchukua hatua za kudhibiti vitendo hivyo. Tumepitisha sheria ya kulinda na kusimamia rasilimali zetu ili ziweze kuinufaisha nchi yetu. Ni wazi kuwa hatua hii huenda haikuwafurahisha baadhi ya watu, lakini ilitulazimu tuichukue ili kuleta maendeleo ya kiuchumi kwa nchi yetu. Sambamba na hilo, tumeendelea kuziba mianya ya ukwepaji kodi, na hivyo kuweza kuongeza ukusanyaji mapato. Mathalan, katika kipindi cha mwezi Julai hadi Desemba 2017, tulifanikiwa kukusanya kodi kiasi cha shilingi trilioni 7.87, sawa ongezeko la asilimia 8.45 ukilinganisha na mapato ya kipindi kama hicho mwaka 2016. Lakini, kubwa zaidi ni kwamba, mwezi Desemba 2017, mapato ya kodi yaliyokusanywa ni shilingi trilioni 1.66. Kiwango hiki ni kikubwa zaidi kuwahi kukusanywa hapa nchini.
Kutokana na hatua tunazozichukua, uchumi wetu umeendelea kuimarika. Katika nusu ya kwanza ya mwaka 2017, uchumi ulikua kwa asilimia 6.8, na hivyo kuifanya nchi yetu kuongoza katika Ukanda wetu wa Afrika Mashariki, lakini pia kuwa miongoni mwa nchi tano ambazo uchumi wake unakua kwa kasi kubwa Barani Afrika. Tulifanikiwa pia kudhibiti mfumko wa bei, ambapo mwezi Desemba 2017 ulifikia asilimia 4. Kwa ujumla, wastani wa mfumko wa bei nchini mwaka jana ulikuwa chini ya asilimia 5.5, kiwango ambacho ni cha chini ukilinganisha na nchi nyingi za Afrika. Akiba ya fedha za kigeni nayo imeongezeka; na tumeweza kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo pamoja na kuboresha huduma za jamii, hususan zile zenye kuwagusa wananchi wengi kama vile afya, elimu na maji. Na hii, bila shaka, ndio moja ya sababu iliyoifanya nchi yetu itajwe kuongoza kwa uchumi shirikishi kwa nchi za Kusini mwa Bara la Afrika.
Waheshimiwa Mabalozi;
Wawakilishi wa Mashirika na Taasisi za Kamataifa;
Mbali na kushughulikia matatizo ya rushwa, wizi, ukwepaji kodi, n.k.; tumeendelea kushughulikia changamoto nyingine zilizokuwa zikikwamisha maendeleo ya nchi yetu. Kama mnavyofahamu, ukiachilia mbali vitendo vya rushwa pamoja na wizi na ubadhirifu wa rasilimali, changamoto nyingine kubwa inayokabili Bara la Afrika, ni tatizo la kukosekana kwa miundombinu imara ya usafiri na nishati ya umeme. Mathalan, kwa mujibu wa Ripoti ya Maendeleo ya Afrika (Africa Progress Report) ya mwaka 2015, watu zaidi ya milioni 600, ambao ni takriban nusu ya watu wote wa Bara la Afrika, hawatumii umeme. Takwimu pia zinaonesha kuwa nchi za Kusini mwa Bara la Afrika, zote kwa pamoja, ukiondoa Afrika Kusini, zinatumia umeme kidogo ukilinganisha na nchi ya Hispania. Aidha, matatizo haya ya umeme yanachangia kushusha kwa asilimia 2.4 Pato la Afrika. Lakini, ukiachilia mbali umeme, gharama za usafirishaji Barani Afrika ni kubwa ukilinganisha na Mabara mengine kutokana na ama kukosekana au udhaifu wa miundombinu ya usafiri. Mambo haya yote kwa pamoja, ndio yanasababisha mchango wa Bara la Afrika kibiashara na uwekezaji duniani kuwa mdogo sana.
Kwa kutambua hilo, tumeendelea kuchukua hatua za kuimarisha miundombinu ya usafiri pamoja na upatikanaji wa umeme. Sehemu kubwa ya nchi hivi sasa imeunganishwa kwa barabara; na nyingine zinaendelea kujengwa. Aidha, mwaka 2017 tumeanza ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kimataifa (standard gauge) kutoka hapa Dar es Salaam kwenda Mikoa ya Mwanza na Kigoma. Reli hii baadaye itaungana na reli za kwenda nchi za Burundi na Rwanda. Ujenzi wa kipande cha Dar es Salaam hadi Dodoma chenye urefu wa kilometa 712 tayari umeanza na utagharimu kiasi cha shilingi trilioni 7.062, zote zitatolewa na Serikali yetu. Aidha, hivi karibuni, wakati wa ziara ya Rais Kagame wa Rwanda, tumekubaliana kuanza ujenzi wa kipande cha kutoka Isaka kwenda Kigali nchini Rwanda. Sambamba na hayo, tunaendelea na upanuzi wa viwanja vya ndege vikubwa vya Dar es Salaam, Zanzibar, Kilimanjaro pamoja na vingine takriban 11 katika mikoa mbalimbali lengo likiwa kukuza sekta yetu ya utalii. Vilevile, tunafanya upanuzi mkubwa na kuboresha utendaji wa bandari zetu kuu za Dar es Salaam na Mtwara kwa gharama ya takriban shilingi trilioni 1.1. Tunatekeleza miradi hii kwa vile takriban asilimia 90 ya shehena ya mizigo inayokuja hapa nchini upitia kwenye bandari hizi. Aidha, Bandari ya Dar es Salaam inategemewa na nchi nyingine majirani. Tunaiboresha pia Bandari ya Tanga, hususan baada ya nchi yetu pamoja na Uganda kuingia makubaliano ya kutekeleza mradi mkubwa wa Bomba la Mafuta kutoka Hoima nchini Uganda hadi Bandari ya Tanga. Ujenzi wa Bomba hilo lenye urefu wa kilometa 1,415 utaanza mwaka huu, ambapo, kama mtakavyokumbuka, mwaka jana, mimi na Rais Museveni wa Uganda tuliuwekea jiwe la msingi.
Kuhusu umeme, tunaendelea na utekelezaji wa miradi mikubwa ya kuzalisha, kusafirisha na kusambaza umeme. Mwaka 2017, tumeanza Awamu ya Tatu ya kupeleka Umeme Vijiji, ambapo tunatarajia kufikisha umeme kwenye vijiji 7,873. Lengo letu ni kwamba, ifikapo Mwaka wa Fedha 2020/2021, vijiji vyote nchini viwe vimefikiwa na miudombinu ya umeme. Tunatekeleza pia miradi mikubwa ya kuzalisha umeme, hususan kwa kutumia gesi yetu asilia. Aidha, mwaka huu, tunatarajia kuanza utekelezaji wa mradi mkubwa wa kuzalisha umeme wa kutumia maji wa Stiglier’s Gorge, ambao utazalisha Megawati 2,100. Tunataka ikifika mwaka 2020, nchi yetu angalau iwe Megawati 5,000 kutoka Megawati 1,460 za sasa. Nafahamu kumekuwa na maneno maneno kuhusu mradi wetu wa Stiglier’s Gorge; ukihusishwa na uharibifu wa mazingira katika Hifadhi ya Taifa ya Ruaha. Ukweli ni kwamba, hakutakuwa na uharibifu wowote. Tumefanya tathmini ya kina ya mazingira, na tumeweka mikakati ya kudhibiti uharibifu. Zaidi ya hapo, mradi huu, utatekelezwa katika eneo dogo sana. Ni chini ya asilimia 4 ya eneo zima la Hifadhi ya Ruaha. Hivyo, hakuna uwezekano wowote wa kuathiri mazingira ya eneo hilo.
Waheshimiwa Mabalozi;
Wawakilishi wa Mashirika na Taasisi za Kamataifa;
Kuhusu azma yetu ya kujenga viwanda, ninyi Waheshimiwa Mabalozi mnafahamu vizuri kuwa hakuna nchi duniani kote imewahi kupata maendeleo ya kiuchumi bila kutegemea viwanda. Mnafahamu pia kuwa, sekta ya viwanda ni muhimu katika kupiga vita umaskini na tatizo la ajira. Hivyo basi, mwaka 2017 tumeendelea na jitihada za kujenga uchumi wa viwanda nchini. Na napenda kuwaarifu kwamba, katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, takriban viwanda 3,500 vimejengwa. Na vingine vingi vinaendelea kujengwa. Naishukuru sekta binafsi ya hapa nchini na kutoka nje kwa namna ilivyoitikia vizuri wito wa Serikali yetu wa kujenga viwanda. Nafahamu kuwa wapo baadhi ya watu ambao wanaeneza uzushi kuwa sisi hatupendi sekta binafsi. Hiyo sio kweli hata kidogo. Tunaipenda sekta binafsi na tunathamini na kutambua mchango wao. Na tunafahamu vizuri kuwa katika dunia ya sasa sekta binafsi ni mhimili muhimu katika kujenga uchumi.
Kwa sababu hiyo, tutaendelea kushirikiana na sekta binafsi ya hapa nchini na ile ya nje. Tutaendelea pia kushughulikia vikwazo mbalimbali vinavyoikabili sekta hii, ikiwa ni pamoja na kurekebisha sera na sheria zetu pale inapobidi; kuongeza vivutio vya uwekezaji na biashara; kushughulikia matatizo ya urasimu, rushwa, utitiri wa kodi, n.k. Hivyo basi, nahimiza sekta binafsi kuendelea kuwekeza hapa nchini. Na niwaombe Waheshimiwa Mabalozi, nanyi wahimizeni wafanyabishara kutoka nchi zenu kuja kuwekeza hapa nchini. Nchi yetu ina fursa nyingi za uwekezaji. Ukiachilia mbali sekta ya viwanda, tuna fursa kwenye sekta za kilimo, mifugo, uvuvi, utalii, ujenzi wa miundombinu, huduma, n.k. Aidha, nchi yetu ina soko kubwa. Tunapakana na nchi takriban 8, lakini pia sisi ni wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na halikadhalika Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika, ambazo kwa pamoja zina idadi ya watu wapatao milioni 500. Hili ni soko kubwa kwa mwekezaji yeyote.
Waheshimiwa Mabalozi;
Wawakilishi wa Mashirika na Taasisi za Kamataifa;
Kimataifa, mwaka 2017, nchi yetu imeendelea kushiriki kikamilifu kwenye masuala mbalimbali katika ngazi ya Kikanda, Bara na duniani kwa ujumla. Kama mjuavyo, msingi mkuu wa Sera yetu ya Mambo ya Nje ni kuimarisha ujirani mwema, ushirikiano wa kikanda na kimataifa. Hivyo, tumeendelea kutekeleza Sera hiyo. Mimi pamoja na viongozi wenzangu, tumefanya ziara na kushiriki kwenye mikutano mbalimbali ya kimataifa. Binafsi, mwaka jana, nilihudhuria Mkutano wa Umoja wa Afrika na kutembelea nchi ya Uganda. Aidha, tulipata bahati ya kutembelewa na viongozi kadhaa wa nchi na taasisi za kimataifa, ikiwa ni pamoja na Waziri Mkuu wa Ethiopia, Hailemariam Dessalegn; Rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma; Rais wa Uganda, Yoweri Museveni; Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia, Kanda ya Afrika, Dkt. Makhtar Diop; Rais wa Benki ya Dunia, Dkt. Jim Yong Kim; na Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), Mhe. Tao Zang; pamoja na viongozi wengine wengi. Wakati wa ziara hizo, tuliweza kufikia makubaliano mbalimbali yenye lengo la kuimarisha ushirikiano, hususan kwenye nyanja za kiuchumi.
Mwaka jana pia, tumeendelea kushirikiana na nchi pamoja na taasisi nyingine za kimataifa katika kushughulikia changamoto mbalimbali zinazokabili Kanda, Bara na dunia yetu kwa ujumla. Na moja ya changamoto hizo ni suala la migogoro. Kama mnavyofahamu, tangu imepata uhuru, mwaka 1961, nchi yetu imekuwa mstari wa mbele katika kutafuta amani Barani Afrika na duniani. Tumeshiriki na tunaendelea kushiriki katika harakati za usuluhishi wa migogoro ya Burundi, DRC, n.k. Tunafarijika kuona kuwa amani nchini Burundi inaendelea kuimarika; na tunaendelea kuwahimiza wahusika kwenye migogoro nchini DRC, Sudan Kusini, n.k., kumaliza tofauti walizonazo ili kuweza kurejesha amani kwenye nchi zao.
Mbali na ushiriki wetu katika usuluhishi wa migogoro, nchi yetu, hivi sasa, ina vikosi kwenye misheni za kulinda amani nchini DRC, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Lebanon, Sudan na Sudan Kusini. Nitumie fursa hii, kuzishukuru nchi na taasisi za kimataifa zilizotutumia salamu za rambirambi na pole kufuatia tukio lililotokea tarehe 8 Desemba 2017 la kuuawa kwa askari wetu 15 na wengine 43 kujeruhiwa, wakati wakiwa katika jukumu la kulinda amani nchini DRC. Tukio hili, kwa hakika, liliacha majonzi na simanzi kubwa kwa Watanzania. Hata hivyo, napenda niseme kuwa, kama Taifa, halijatukatisha tamaa wala kutuyumbisha. Tutaendelea kushiriki katika harakati za kutafuta amani mahali popote duniani, na tutaendelea kushiriki kwenye misheni za kulinda amani. Tunaushukuru Umoja wa Mataifa kwa kuunda Timu kuchunguza chanzo cha tukio la tarehe 8 Desemba, 2017. Tunaihimiza Timu iliyoundwa kukamilisha mapema uchunguzi wake, ili chanzo kijulikane, wahusika wafahamike na hatimaye sheria ifuate mkondo wake.
Waheshimiwa Mabalozi;
Wawakilishi wa Mashirika na Taasisi za Kamataifa;
Katika mwaka huu wa 2018, Tanzania itaendelea kutekeleza Mpango wake wa Maendeleo wa Miaka Mitano. Tutazidisha mapambano dhidi ya rushwa na ubadhirifu. Tutaendelea kuimarisha miundombinu ya kiuchumi, hususan ya usafiri na nishati ya umeme. Tutaboresha huduma mbalimbali za kijamii, hususan elimu, afya a maji.
Sambamba na hayo, tutaendelea kushiriki kwenye masuala mbalimbali ya kimataifa. Tutakuwa wanachama waaminifu wa taasisi za Kikanda, katika Bara na kimataifa, ambazo sisi ni wanachama. Tutaendelea kushiriki kwenye usuluhishi wa migogoro; na vikosi vyetu vitandelea kushiriki kwenye misheni za kulinda amani. Vilevile, tutaendelea kutekeleza mipango na malengo mbalimbali ya kikanda, kibara na kidunia, ikiwemo Ajenda ya Umoja wa Afrika ya 2063 na Ajenda ya Umoja wa Mataifa ya Malengo Endelevu ya 2030. Na moja ya malengo ya dunia tuliyopanga kutekeleza, ni kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka 2030 tuwe tumezuia maambukizi mapya ya Virusi Vya Ukimwi (VVU). Na katika kufikia azma hii, tumeanzisha Mfuko wa Udhamini wa Ukimwi, ambapo tumelenga kukusanya kiasi cha shilingi trilioni 6 katika kipindi cha miaka mitano ijayo. Hivyo basi, tunawaomba mtuunge mkono.
Waheshimiwa Mabalozi;
Wawakilishi wa Mashirika na Taasisi za Kamataifa;
Nafahamu, katika hafla kama hii, hotuba huwa haziwi ndefu. Lakini leo, nimeeleza mengi. Nimefanya hivyo, kwa kuwa, kama nilivyosema awali, hii huenda itakuwa mara ya mwisho kwa sherehe hizi kufanyika hapa Dar es Salaam. Mwakani ni Dodoma. Na kwa sababu hiyo, kabla sijahitimisha hotuba yangu, naomba mniruhusu nieleze masuala matatu ya mwisho.
Suala la kwanza; muda mfupi uliopita, nimeeleza kuwa Tanzania itaendelea kushiriki kwenye misheni za kulinda amani. Na napenda kusisitiza tena kuwa tutaendelea kushiriki kwenye misheni hizo. Hata hivyo, wakati nikisisitiza hilo, napenda kueleza masikitiko yetu kuhusu uamuzi wa Umoja wa Mataifa kuanza kutekeleza sera ya kupunguza gharama kwenye misheni za kulinda amani. Ni kweli, uendeshaji wa misheni za kulinda amani ni gharama kubwa. Lakini, ni ukweli pia usiopingika kuwa, hakuna gharama inayozidi uhai wa watu na umuhimu wa amani. Tanzania tunauona uamuzi huu wa kupunguza gharama utadhoofisha jitihada za kutafuta amani kwenye maeneo yenye migogoro; na kuhatarisha maisha ya walinda amani pamoja na raia wasio na hatia wanaoishi kwenye maeneo yenye migogoro. Hivyo basi, tunauomba Umoja wa Mataifa pamoja na Nchi Tano Wanachama wa Kudumu wa Umoja wa Mataifa kutafakari upya uamuzi huo.
Suala la pili, ni kuhusu uamuzi wetu wa hivi karibuni wa kujitoa kwenye Mpango wa Majaribio wa Kutafuta Suluhu ya Kudumu ya Tatizo la Wakimbizi (Comprehensive Refugee Response Framework – CRRF). Kwanza kabisa, napenda kueleza kuwa, nchi yetu, tangu imepata Uhuru mwaka 1961, imekuwa ni miongoni mwa nchi zenye kupokea wakimbizi wengi. Mpaka sasa tunaendelea kuwapokea; na bila shaka, tutaendelea kuwapokea; lakini wale tu wenye kustahili na kwa kuzingatia sheria za kimataifa. Nchi yetu pia imeweka historia duniani kwa kuwa ya kwanza kutoa uraia kwa wakimbizi wapatao 150,000 kwa wakati mmoja. Hakuna nchi imewahi kufanya hivyo. Hata hivyo, kutokana na sababu za usalama, tumelazimika kujitoa kwenye Mpango wa CRRF, ambao pamoja na masuala mengine, unaelekeza kutolewa kwa ardhi kwa ajili ya wakimbizi, kuwaruhusu kutembea mahali popote na kutoa vibali vya ajira. Tumeamua kujitoa kwa sababu tunadhani kuwa, katika kipindi hiki cha sasa ambacho dunia inakabiliwa na changamoto za usalama, ikiwemo ugaidi, kushamiri kwa biashara ya binadamu na makosa mengine ya kimataifa, utekelezaji wa Mpango huu unaweza kuleta madhara makubwa ya kiusalama kwa nchi yetu. Lakini, mbali na hilo, tumesita kuendelea na Mpango huu kutokana na uzoefu tulioupata wakati tulipotoa uraia kwa wakimbizi 150,000. Wakati tunatoa uraia, jumuiya ya kimataifa iliahidi ingetoa fedha za kuwapatia makazi na masuala mengine muhimu. Lakini, mpaka sasa, hakuna fedha iliyotolewa; na badala yake tumeanza kushawishiwa kukopa fedha za kuwahudumia wakimbizi. Hali hii imetukatisha tamaa; na tunaona itakuwa ni kuibebesha mzigo mkubwa Serikali yetu. Hivyo basi, tunaiomba jumuiya ya kimataifa ituelewe.
Suala la tatu na la mwisho ni kuhusu taarifa za kukamatwa kwa meli zenye kupeperusha bendera ya Tanzania, ambazo zimejihusisha kwenye matukio ya uhalifu. Taarifa hizi kwa hakika zimetusikitisha sana sisi kama Taifa, kwa sababu zinachafua jina na sifa nzuri ya nchi yetu. Hata hivyo, ningependa kufafanua kuwa, kimsingi, meli hizo si za kwetu; zimesajiliwa tu hapa Tanzania. Kama mnavyofahamu, usajili wa meli za nje ni jambo la kawaida na linafanywa na nchi mbalimbali duniani. Hata hivyo, kutokana na matatizo yaliyojitokeza, Serikali imeamua kuchukua hatua. Tumesitisha usajili wa meli zote 470 zilizosajiliwa hapa nchini zenye kupeperusha bendera yetu, na tumeanza kufanya uchunguzi wa kina kuthibitisha uhalali wa shughuli zao. Zile zitakazobainika kukiuka sheria na taratibu, tutazifutia usajili. Sambamba na hilo, tumesitisha usajili wa meli mpya kutoka nje mpaka pale itakapotangazwa tena. Tumechukua hatua hizo, ili nchi yetu isitumike kuwa kichaka cha kujificha wahalifu.
Waheshimiwa Mabalozi;
Wawakilishi wa Mashirika na Taasisi za Kamataifa;
Napenda kuhitimisha hotuba yangu, kwa kurudia tena kuwashukuru kwa kuhudhuria hafla hii. Aidha, nawashukuru kwa namna ambavyo nchi zenu na mashirika mnayowakilisha yanavyoshirikiana vizuri na nchi yetu katika nyanja mbalimbali: kiuchumi, kisiasa, kijamii, kiulinzi na usalama, n.k. Mchango wenu ni mkubwa sana. Bila ninyi, huenda mambo mengi tuliyotekeleza mwaka jana, yasingewezekana. Hivyo basi, tunawashukuru sana; na kupitia kwenu, tunaendelea kuziomba nchi na taasisi mnazoziwakilisha ziendelee kutuunga mkono. Kwa upande wetu, tutazidi kuimarisha uhusiano wetu na nchi, mashirika na taasisi zenu.
Baada ya kusema hayo, napenda kurudia tena kuwatakia Heri ya Mwaka Mpya 2018. Uwe mwaka wa Amani na Mafanikio.
“Ahsanteni kwa kunisikiliza”
- Feb 01, 2018
HOTUBA YA MHE. DKT JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, MGENI RASMI, MAADHIMISHO YA SIKU YA SHERIA, DAR ES SALAAM, TAREHE 1 FE...
Soma zaidiHotuba
HOTUBA YA MHE. DKT JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA,
MGENI RASMI, MAADHIMISHO YA SIKU
YA SHERIA, DAR ES SALAAM,
TAREHE 1 FEBRUARI, 2018
Mheshimiwa Prof. Ibrahim Juma, Jaji Mkuu
wa Tanzania;
Mhe. Tulia Akson Mwansasu (Mb), Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Mheshimiwa Omar Othman Makungu, Jaji Mkuu wa Zanzibar;
Mheshimiwa Prof. Palamagamba Kabudi (Mb),
Waziri wa Sheria na Katiba;
Waheshimiwa Mawaziri na Manaibu Waziri mliopo;
Mheshimiwa Balozi John Kijazi,
Katibu Mkuu Kiongozi;
Mhe. Paul Makonda, Mkuu wa Mkoa
wa Dar es Salaam;
Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu mliopo;
Mheshimiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali;
Waheshimiwa Majaji Wakuu Wastaafu;
Waheshimiwa Majaji wa Mahakama ya Rufaa,
Mheshimiwa Jaji Kiongozi;
Waheshimiwa Majaji wa Mahakama Kuu;
Mheshimiwa Msajili Mkuu na Mtendaji Mkuu wa Mahakama;
Naibu Rais wa Chama cha Wanasheria Tanzania Bara;
Mkurugenzi wa Mashtaka;
Waheshimiwa Viongozi wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama;
Waheshimiwa Mabalozi na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa;
Waheshimiwa Wageni wetu kutoka Guatemala;
Waheshimiwa Wasajili, Mahakimu na Mawakili;
Waheshimiwa Viongozi wa Vyama vya Siasa na Dini mliopo;
Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;
Awali ya yote, napenda na mimi niungane na walionitangulia katika kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutupa uhai na kutuwezesha kukutana hapa leo. Tulikutana mara ya mwisho kwenye sherehe kama hizi, mwaka jana 2017; nakumbuka ilikuwa tarehe 2 Februari. Naamini kuna wenzetu tulikuwa nao mwaka jana, lakini leo hatunao. Hatuna budi kuwakumbuka wote waliotutoka. Hivi karibuni, tumeondokewa na mwanafamilia mwenzetu, Jaji Mstaafu wa Mahakama ya Rufaa, Mheshimiwa Robert Kisanga. Wakati wa uhai wake, Jaji Kisanga alitoa mchango mkubwa kwa Mahakama na Taifa kwa ujumla. Hivyo basi, tunawaombea wote waliotutoka wapumzike mahali pema peponi. Amina.
Napenda pia kutumia fursa hii kuushukuru uongozi wa Mahakama chini ya Mheshimiwa Prof. Ibrahim Juma, Jaji Mkuu wa Tanzania, kwa kunialika kwenye Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini. Hii ni mara yangu ya tatu kushiriki kwenye Siku ya Sheria tangu nimechaguliwa kuwa Rais wa nchi yetu. Nimefurahi kuona kuwa miongoni mwetu leo, tunaye pia Naibu Spika wa Bunge, Mheshimiwa Tulia Akson. Huu ni uthibitisho tosha kuwa mihimili yetu mitatu ya Dola ina mahusiano mazuri na inafanya kazi kwa ushirikiano mkubwa. Sisi sote ni kitu kimoja. Lengo letu ni moja: kuleta maendeleo kwa nchi yetu. Lakini zaidi ya hapo, kama Mheshimiwa Jaji Mkuu alivyosema, sisi sote ni wadau muhimu wa Siku hii ya Sheria. Bunge ndilo lenye kutunga sheria; Mahakama inazitafsiri; na sisi Serikali (Utawala) ndio wenye jukumu la kusimamia utekelezaji wake. Hivyo basi, nakushukuru tena Mheshimiwa Jaji Mkuu kwa kutualika kushiriki katika siku hii muhimu.
Mheshimiwa Jaji Mkuu;
Waheshimiwa Viongozi;
Mabibi na Mabwana:
Ni wazi kuwa Maadhimisho ya Siku ya Sheria ni muhimu sana. Ni muhimu, kwanza kabisa, kwa sababu ya umuhimu wenyewe wa sheria. Hivi punde tu Mheshimiwa Jaji Mkuu ameeleza kuwa sheria ni muhimu katika kudumisha amani na pia kuleta maendeleo kwa wananchi na nchi kwa ujumla. Lakini zaidi ya hapo, sheria ni muhimu katika kutoa haki. Na kama mjuavyo, haki ni hitaji kubwa katika jamii. Nikinukuu usemi mmoja wa Kiingereza unasema, “Justice is the great interest of man on earth”. Hivyo basi, kwa kuadhimisha Siku hii ya Sheria, maana yake ni kwamba nchi yetu inatambua umuhimu wa sheria katika kusimamia haki, kudumisha amani na kuleta maendeleo katika nchi.
Lakini ukiachilia hilo la umuhimu wa sheria, Maadhimisho haya ya Siku ya Sheria ni muhimu kwa vile yanatoa fursa kwa vyombo vinavyohusika na masuala ya sheria na utoaji haki (yaani Mahakama, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jeshi la Polisi, Magereza, TAKUKURU, Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Mawakili, n.k.) kukutana na kufanya tafakuri ya masuala mbalimbali, wanajadili mapungufu na mafanikio waliyopata katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita; na kupanga mikakati ya mwaka mpya, ikiwemo kurekebisha mapungufu yaliyojitokeza pamoja na kuboresha au kuimarisha mafanikio yaliyokwishapatikana.
Napenda kutumia fursa hii kuvipongeza vyombo vyote vinavyohusika na masuala ya sheria na haki nchini kwa kazi kubwa na nzuri ya kusimamia sheria na kutoa haki kwa kipindi cha mwaka mmoja uliopita. Na kwa namna ya pekee kabisa, naipongeza Mahakama ya Tanzania kwa kazi kubwa na nzuri iliyofanya ya kutoa haki. Kama sote tujuavyo, Mahakama ndio chombo pekee cha kutoa haki nchini. Mheshimiwa Jaji Mkuu ameeleza kuwa katika mwaka uliopita Mahakama iliweza kupunguza kwa kiwango kikubwa mlundikano wa kesi au mashauri, hususan katika Mahakama za Mwanzo, Wilaya na Hakimu Mkazi. Mathalan, Mahakama za Mwanzo hadi kufikia mwezi Desemba mwaka jana zilibakiwa na mashauri 14 yaliyozidi umri wa miezi 6 (kipindi ambacho kinatafsiriwa na mahakama kuwa mlundikano). Na kwa kuzingatia kuwa zaidi ya asilimia 70 ya mashauri yote ya mahakama, yanafunguliwa kwenye ngazi ya Mahakama za Mwanzo, ni wazi kuwa haya ni mafanikio makubwa. Lakini nafahamu, bila ya kupata ushirikiano kutoka vyombo vingine, Mahakama peke yake isingeweza kupata mafanikio haya. Hivyo basi, navipongeza vyombo vilivyofanikisha kupatikana kwa mafanikio haya. Hongereni sana.
Mheshimiwa Jaji Mkuu pamoja na Viongozi
wa Vyombo vingine vya kusimamia sheria na haki:
Licha ya mafanikio mliyopata mwaka jana pamoja na pongezi nilizozitoa kwenu hivi punde, jambo moja lipo dhahiri: Usimamizi wa sheria na mfumo wa utoaji wa haki nchini bado unakabiliwa na matatizo mengi. Na moja ya matatizo hayo ni kupungua kwa uadilifu kwa watumishi wachache wa vyombo vyetu vyenye dhamana ya kusimamia sheria na kutoa haki. Nasema ni wachache kwa vile nafahamu kuwa watumishi wengi wa vyombo hivi ni wazuri na waadilifu. Lakini, hawa wachache, hatupaswi kuwaacha kwa kuwa matendo yao yanavichafua sana vyombo vyetu. Hawa ndio wanaowadai rushwa na kuwabambikiza kesi wananchi; wanachelewesha upelelezi na kuharibu ushahidi; na pia ndio wenye tabia ya kutoa hukumu za upendeleo au kuchelewa kuandika hukumu. Naipongeza Tume ya Utumishi wa Mahakama, ambayo ipo chini ya Jaji Mkuu, kwa kuwachukulia hatua za kinidhamu, ikiwemo kuwafukuza au kuwastaafisha, watumishi wa mahakama wapatao 112 ambao walibainika kuhusika na vitendo vya rushwa na kukiuka maadili.
Nafahamu, miongoni mwa waliostaafishwa wapo Mahakimu 27, wakiwemo 14 ambao wamefukuzwa kazi. Awali, Mahakimu hawa wote walishinda kesi mahakamani, lakini baadaye Tume iliamua kuwastaafisha. Mbali na Mahakimu, watumishi wengine 67 wa Mahakama nao walifukuzwa kazi. Hongera sana Jaji Mkuu. Tume imetekeleza kwa vitendo kauli aliyowahi kutoa Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, nanukuu “kazi ya ujaji au uhakimu inahitaji uadilifu wa hali ya juu. Kama Jaji au Hakimu sio mwaminifu au mwadilifu kazi hiyo haimfai, akatafute kazi nyingine”, mwisho wa kunukuu. Narudia tena kukupongeza Mheshimiwa Jaji Mkuu na nakusihi kuendelea kuwachukulia hatua kali watumishi wa Mahakama wasio waadilifu, ikiwemo kulifuatilia kwa karibu suala la baadhi ya watumishi wa Mahakama kuomba vibali vya kwenda likizo nje ya nchi kila mwaka. Suala hili halitoi picha nzuri kwa Mahakama. Utafiti uliofanywa na Taasisi isiyo ya Serikali ya TWAWEZA hivi karibuni umebaini kuwa rushwa nchini imepungua kwa asilimia 85 ukilinganisha na miaka 5 iliyopita. Hata hivyo, Jeshi la Polisi na Mahakama bado mnaongoza kwa vitendo vya rushwa. Utafiti huu haupaswi kupuuzwa. Hivyo basi, nakuomba Mheshimiwa Jaji Mkuu kuendelea kuzidisha mapambano dhidi ya rushwa. Aidha, navihimiza vyombo vingine, (Polisi, TAKUKURU, Magereza, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mwendesha Mashtaka, n.k) navyo kuiga mfano ulioanza kuoneshwa na Mahakama katika kupiga vita rushwa pamoja na vitendo vingine vya ukiukwaji wa maadili.
Mbali na suala la uadilifu, tatizo la ucheleweshaji wa kesi bado lipo ama katika kufanya upelelezi, kusikiliza au katika kutoa maamuzi. Jaji Mkuu ameeleza jitihada zinazofanywa na Mahakama kutatua tatizo la mlundikano wa kesi; na nimempongeza. Lakini tatizo bado lipo. Yeye mwenyewe ameeleza kuwa kufikia mwezi Desemba 2017, Mahakama za Wilaya na Hakimu Mkazi, zilikuwa na jumla ya mashauri 2,334 ambayo zina umri zaidi ya mwaka mmoja. Na amekiri pia kuwa kwenye Mahakama Kuu na Mahakama kuna mlundikano mkubwa zaidi. Ni kweli kuwa baadhi ya kesi zinachelewa kwa sababu zinazoelezeka, lakini nyingine hazina sababu za msingi. Unaweza kukuta ushahidi wote upo; lakini utasikia upelelezi bado unaendelea; au kunakuwa na kusuasua kwenye kusikiliza au kutoa maamuzi ya kesi husika. Pale Ikulu huwa napokea malalamiko mengi ya wananchi kuhusu ucheleweshaji wa kesi, kwa vile wanadhani naweza kuingilia kati. Lakini huwa nawajibu sina mamlaka hayo. Sana sana tu huwa nawashauri waendelee kufuatilia mahakamani. Lakini hata ninyi wenyewe mmeona hivi karibuni, baada ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kuanza kuwasikiliza wananchi wenye madai mbalimbali, idadi kubwa ya watu imejitokeza. Hii inadhihirisha kuwa bado tuna matatizo makubwa kwenye mfumo wetu wa utoaji haki. Hivyo basi, niviombe vyombo husika kuliwekea mkakati maalum suala hili la ucheleweshaji wa kesi, ikiwa ni pamoja na kupanga mikakati ya kuwabaini na kuwashughulikia wanaozichelewesha kwa uzembe au kutaka kujipatia rushwa.
Nasema hivyo, kwa sababu ucheleweshaji wa kesi una athari nyingi kuanzia kwa mtu mmoja mmoja, kwenye jamii na nchi kwa ujumla. Ninyi Wanasheria mna msemo wenu “Haki iliyocheleweshwa ni sawa na Haki iliyonyimwa”. Lakini mbali na kunyima haki, ucheleweshaji wa kesi umechangia kuvuruga amani na utulivu kwenye baadhi ya maeneo na kusababisha watu kupoteza maisha au kupata majeraha ya kudumu. Vilevile, kuna athari nyingi za kiuchumi. Mathalan, kwa taarifa nilizonazo ni kwamba, kuna kesi 139 zenye kuhusiana na masuala ya kodi zilizofunguliwa kwenye Baraza la Kodi (Tax Appeals Board) na Baraza la Usuluhishi wa Kodi (Tax Appeals Tribunal). Kesi hizi, ambazo zimefunguliwa kati ya mwaka 2009 hadi 2015, zina thamani ya shilingi bilioni 169.1 na Dola za Marekani milioni 38.2. Endapo kesi hizi zingetolewa uamuzi, huenda baadhi yake Serikali ingeshinda na kupata fedha kwa ajili ya kutekeleza shughuli mbalimbali za maendeleo. Lakini, mbali na kuiokosesha Serikali mapato, ucheleweshaji wa kesi umefanya baadhi ya makampuni, zikiwemo benki, kufilisika. Na hii ni moja ya sababu zinazofanya riba za mikopo ya benki zetu kuwa juu. Wenye Benki wana hofu kuwa wakikopesha inawezekana mkopo usirudishwe, na hata aliyeshindwa kurejesha mkopo, akishitakiwa huenda ikachukua muda mrefu hukumu kutolewa. Badala yake, wanaamua kupandisha riba, ili mtu mmoja akishindwa kurejesha mkopo, aweze kufidiwa na mwenzie.
Mheshimiwa Jaji Mkuu;
Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana:
Nafahamu kuwa matatizo niliyoeleza sio mageni. Sote tunayafahamu na mara kwa mara tumekuwa tukiyajadili. Mimi mwenyewe niliyazungumza mwaka juzi kwenye Sherehe kama hizi, mwaka jana nikayazungumza tena; na leo nimeyarudia. Nimefanya hivyo kwa makusudi kabisa. Lengo langu nilitaka tukumbushane ili kwa pamoja tuyatafutie majibu yake. Kuna hadithi inayomhusu Mwanasayansi mmoja Maarufu Duniani, Dkt. Albert Einstein. Siku moja alikuwa akisimamia Mtihani wa Fizikia kwenye darasa lake. Mmoja wa wanafunzi akamuuliza: “Dkt. Einstein, mtihani huu mbona kama wa mwaka jana?” Dkt. Einstein akamjibu “Ndio ni kama wa mwaka jana, lakini mwaka huu natarajia kuwa majibu yatakuwa tofauti.” Hivyo basi, na mimi nimeamua kuzungumzia tena mapungufu haya ili tuendelee kuyatafutia ufumbuzi wake, ikiwezekana majibu mapya kulingana na dunia ya sasa.
Na kwa sababu hiyo, nimefurahi sana kusikia kuwa kaulimbiu ya Maadhimisho ya Siku ya Sheria Mwaka huu inasema “Matumizi ya TEHAMA katika Utoaji Haki kwa Wakati na kwa Kuzingatia Maadili”. Kaulimbiu hii ni nzuri sana. Jaji Mkuu, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali pamoja na Makamu Rais wa Chama Cha Wanasheria wameeleza vizuri na kwa kirefu suala la TEHAMA. Lakini, na mimi niseme tu kwa ufupi kwamba, TEHAMA ina nafasi kubwa katika kushughulikia matatizo mengi yanayokabili mfumo wa usimamizi wa sheria na utoaji haki nchini. TEHAMA itaongeza kasi ya utoaji haki (mathalan kupitia video conference); itadhibiti uzembe na vitendo vya ukiukwaji wa maadili kwa watumishi, ikiwemo majalada kupotea na vitendo vya rushwa. Aidha, TEHAMA itapunguza gharama za uendeshaji Mahakama na kuimarisha ukusanyaji wa mapato. Hivyo basi, nawapongeza Mahakama kwa kaulimbiu hii na kwa kuanza kufanya kazi kwa njia ya TEHAMA. Endeleeni hivyo hivyo. Na sisi Serikali tutaendelea kuwaunga mkono.
Mbali na matumizi ya TEHAMA, Mahakama na vyombo vingine havina budi kutekeleza mikakati mingine ya kushughulikia mapungufu yaliyopo kwenye mfumo wetu wa sheria na utoaji haki. Mathalan, mwaka jana (2017), Serikali ilipitisha Sheria kuhusu Msaada wa Kisheria (Legal Aid Act) ili kuwasaidia wananchi kupata msaada wa kisheria na hatimaye kurahisisha shughuli za utoaji haki. Lakini, jambo la kusikitisha ni kwamba, mpaka sasa kanuni za Sheria hiyo bado hazijakamilika. Na ni miezi takriban tisa sasa imepita. Hivyo basi, napenda kutumia fursa hii, kuagiza vyombo husika, hususan Wizara ya Sheria na Katiba pamoja na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, kuhakikisha kuwa ndani ya mwezi mmoja ujao, kanuni hizo ziwe tayari zimekamilika.
Sambamba na hayo, ni vizuri kama Mahakama itaendelea kuhimiza utaratibu wa kuwa na mahakama za kuhama hama (mobile courts). Wakati nikiwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi nilishuhudia ufanisi wa mahakama za kuhama hama. Endeleeni pia kuhimiza usuluhishi. Usuluhishi utapunguza sio tu mlundikano wa kesi bali pia idadi ya wafungwa kwenye Magereza yetu. Wakati wa Sherehe za Uhuru mwaka jana nilieleza kuwa nchi yetu ilikuwa na takriban wafungwa takriban 38,000. Wafungwa wanaigharimu Serikali fedha nyingi. Mathalan, katika kipindi cha miaka minne iliyopita, Serikali ilitenga kiasi cha takriban shilingi bilioni 100 kwa ajili ya kuwatunza na kuhudumia wafungwa. Mwaka wa Fedha 2014/2015 zilitengwa shilingi bilioni 22.3; Mwaka 2015/2016 shilingi bilioni 21.6; Mwaka 2016/2017 shilingi bilioni 27.3 na Mwaka huu wa Fedha shilingi bilioni 19.8. Hiki ni kiasi kikubwa ambacho kingeweza kutumika katika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo.
Hivyo basi, nadhani sasa wakati umefika wa kuanza kuweka msisitizo katika adhabu mbadala, hususan kwa makosa madogo madogo. Najua sheria zipo, kinachohitajika ni kuweka utaratibu na mikakati ya kuzisimamia. Sambamba na hilo, Jeshi la Magereza hamna budi kuweka mikakati itakayowezesha kujitegemea kwa kuwatumia vizuri wafungwa. Hii pia itawasaidia wafungwa kuweza kujitegemea pindi wakimaliza vifungo vyao. Hivi majuzi nilitoa msamaha kwa wafungwa; lakini nimesikitika kusikia kuwa baadhi yao tayari wamekamatwa kwa uhalifu. Hii inaonesha kuwa wakiwa jela wafungwa hawapati mafunzo ya kutosha. Hivyo, ipo haja kwa Magereza kuangalia upya mafunzo inayotoa kwa wafungwa. Tunataka mtu akifungwa, wakati akitoka awe amebadilika na kuwa mtu mwema.
Waheshimiwa Viongozi;
Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana:
Katika hotuba yake, Mheshimiwa Jaji Mkuu ameeleza baadhi ya changamoto zinazoikabili Mahakama. Ametaja uhaba wa vifaa na vitendea kazi, uhaba wa miundombinu, upungufu wa watumishi (Majaji), maslahi, n.k. Serikali inafahamu changamoto hizi. Na bila shaka, mnatambua jitihada tunazozichukua katika kuzishughulikia. Katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, Serikali imetoa takriban shilingi bilioni 40 ili kuiwezesha Mahakama kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo, ikiwemo ujenzi wa miundombinu, ambayo hivi punde Mheshimiwa Jaji Mkuu ameitaja. Ujenzi wa Mahakama Kuu mbili (Kigoma na Mara); za Hakimu Mkazi 5 na za Wilaya 16.
Naipongeza Mahakama kwa kusimamia vizuri miradi hiyo. Aidha, nawapongeza kwa kuanza kutekeleza mpango wa kuhamia Dodoma. Nawaahidi kuwa mtakapokuwa tayari kuanza ujenzi Dodoma, Serikali itawaunga mkono.
Nitumie fursa hii pia kuwashukuru washirika wetu mbalimbali wa maendeleo, ambao tunashirikiana nao katika kuboresha Mahakama zetu. Benki ya Dunia imekuwa ikifadhili miradi mingi ya Mahakama. Nimefurahi kuona Mwakilishi wa Dunia yupo hapa. Tunawashukuru sana. Endeleeni kutuunga mkono, hususan katika masuala haya ya sheria na utoaji haki; na halikadhalika katika mapambano dhidi ya rushwa.
Kuhusu changamoto ya uhaba wa watumishi (Majaji) pamoja na maslahi yenu, Serikali imezichukua na itazifanyia kazi. Tutasubiri kupokea mapendekezo yenu ya majaji wapya pamoja na maboresho ya maslahi yenu. Lakini, ningependa niseme kwamba, katika kushughulikia changamoto hizi, tutazingatia uwezo wa Serikali.
Mheshimiwa Mkuu;
Waheshimiwa Viongozi mliopo;
Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana:
Nihitimishe hotuba yangu kwa kuushukuru tena uongozi wa Mahakama kwa kunialika kwenye shughuli hii muhimu. Aidha, nawapongeza kwa kazi kubwa mnayoifanya. Ombi langu kwenu, shirikianeni na vyombo vingine, katika kushughulikia mapungufu yaliyopo katika mfumo wetu wa kutoa haki na kusimamia sheria. Kila mmoja wetu, akatimize wajibu wake katika kuwatumikia Watanzania.
Mungu Ibariki Siku ya Sheria!
Mungu Ibariki Mahakama ya Tanzania!
Mungu Ibariki Tanzania!
“Ahsanteni sana kwa kunisikiliza”
- Jan 31, 2018
HOTUBA YA MHE. DKT. JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, KWENYE HAFLA YA UZINDUZI WA PASIPOTI YA KIELEKTRONIKI DAR ES SALAAM,...
Soma zaidiHotuba
HOTUBA YA MHE. DKT. JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI,
RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA,
KWENYE HAFLA YA UZINDUZI WA PASIPOTI YA KIELEKTRONIKI
DAR ES SALAAM, TAREHE 31 JANUARI, 2018
Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Mheshimiwa Dkt. Ali Mohammed Shein, Rais wa Zanzibar
na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi;
Mheshimiwa Kassim Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania;
Mheshimiwa Balozi Seif Ali Iddi, Makamu wa Pili
wa Rais wa Zanzibar;
Mheshimiwa Prof. Ibrahim Juma, Jaji Mkuu wa Tanzania;
Mheshimiwa Othman Makungu, Jaji Mkuu wa Zanzibar;
Mheshimiwa Zubeir Ali Maulid, Spika wa Baraza
la Wawakilishi Zanzibar;
Mheshimiwa Tulia Akson Mwansasu, Naibu Spika
wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Waheshimiwa Marais Wastaafu wa Serikali zetu mbili,
Mzee Mwinyi na Mzee Karume;
Mheshimiwa Mwigulu Nchemba, Waziri wa Mambo ya
Ndani ya Nchi pamoja na Mawaziri na Manaibu
Mawaziri wengine mliopo;
Mheshimiwa Balozi John Kijazi, Katibu Mkuu Kiongozi;
Mheshimiwa Abdulhamid Yahya Mzee, Katibu Mkuu
Kiongozi wa Serikali ya Zanzibar;
Mheshimiwa Paul Sherlock, Balozi wa Ireland, pamoja
na Mabalozi wengine mliopo;
Mheshimiwa Paul Makonda, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam;
Waheshimiwa Wabunge mliopo;
Mheshimiwa Mstahiki Meya wa Jiji la Dar es Salaam;
Waheshimiwa Makatibu Wakuu mliopo;
Dkt. Anna Peter Makakala, Kamishna Mkuu wa Uhamiaji;
Waheshimiwa Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama mliopo;
Mwakilishi wa Kampuni ya HDI Global;
Waheshimiwa Viongozi Wengine wa Serikali mliopo;
Waheshimiwa Viongozi wa Vyama vya Siasa na Dini mliopo;
Ndugu Watumishi wa Idara ya Uhamiaji mliopo;
Wageni wote Waalikwa, Mabibi na Mabwana:
Kwanza kabisa, naungana na walionitangulia kuzungumza katika kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutupa uhai na kutuwezesha kukutana hapa leo. Aidha, natoa shukrani zangu nyingi kwa Mheshimiwa Mwigulu Nchemba, Waziri wa Mambo ya Ndani pamoja na Kamishna Mkuu wa Uhamiaji, Dkt. Makakala, kwa kunialika katika tukio hili muhimu na la kihistoria kwa nchi yetu. Ahsanteni sana.
Napenda pia, hapa mwanzoni kabisa, kuwapongeza Watumishi wa Idara ya Uhamiaji kwa kazi mnazofanya. Kwa hakika, mnafanya kazi kubwa na nzuri. Hivi punde, Kamishna Mkuu wa Uhamiaji ameeleza baadhi ya mafanikio mliyopata katika kipindi kifupi kilichopita. Mmeanza kutumia mfumo wa ukusanyaji mapato kwa njia ya kielektroniki katika Ofisi zenu za Makao Makuu zilizopo hapa Dar es Salaam na Zanzibar. Aidha, mmeanza kutumia Mfumo wa Kuhakiki Hati za Vibali vya Ukaazi (e -Verification System) na pia mmeitikia wito wa Serikali wa kuhamia Dodoma. Hongereni sana Idara ya Uhamiaji kwa mafanikio hayo.
Ndugu Wananchi;
Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;
Sio siri kuwa Idara hii ya Uhamiaji ni nyeti na muhimu katika nchi yoyote. Ni muhimu kwanza katika suala la ulinzi na usalama; lakini pia ni muhimu kwa maendeleo ya kiuchumi ya nchi. Kamishna Mkuu wa Uhamiaji ameeleza baadhi ya majukumu ya Idara yetu ya Uhamiaji kwa mujibu wa Sheria. Na baadhi ya majukumu hayo ni: (i) kutoa pasipoti na hati nyingine za kusafiria kwa raia wa Tanzania; (ii) kutoa hati za ukaazi kwa raia wa kigeni waliokidhi matakwa ya sheria; na (iii) kuratibu maombi ya wageni wanaoomba uraia wa Tanzania. Haya ni majukumu makubwa ambayo yanadhihirisha unyeti na umuhimu wa Idara hii.
Lakini pamoja na unyeti na umuhimu nilioueleza, ni wazi kuwa katika miaka ya hivi karibuni, Idara hii ililegalega kiasi. Ninyi nyote hapa ni mashahidi wa namna nchi yetu ilivyogeuka kuwa uchochoro wa wahamiaji haramu. Kila siku vyombo vya habari vilikuwa vikiripoti. Pasipoti zetu nazo zilikuwa zikigawiwa kiholela na wakati mwingine kuangukia kwa wahalifu, wakiwemo wafanyabiashara wa dawa za kulevya. Hii imeharibu sana taswira ya nchi yetu, na hivyo kufanya baadhi ya Watanzania kupata taabu kuingia kwenye baadhi ya nchi. Wengine wamepewa Pasipoti za Tanzania huku wakimiliki Pasipoti za nchi nyingine, kinyume kabisa cha sheria ya nchi yetu. Sambamba na hayo, vibali vya ukaazi pamoja na uraia wa nchi yetu navyo vilitolewa bila kuzingatia taratibu. Kuna raia wengi wa kigeni wamepata uraia bila kuwa na sifa stahiki na baadhi wameweza hadi kushika nyadhifa muhimu Serikalini. Wapo pia waliopewa vibali vya ukaazi kiujanjaujanja; wengine hawana sifa yoyote. Lakini zaidi ya hapo, ukusanyaji wa mapato ya viza na vibali vya ukaazi nao ulikuwa hauridhishi. Fedha nyingi zilikuwa zikipotea. Haya ni baadhi ya mapungufu yaliyokuwepo katika Idara hii, ambayo yalifanya watu wengi waione kuwa imeshindwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo.
Na hii ndio moja ya sababu zilizonisukuma mimi kufanya mabadiliko ya uongozi wa Idara hii. Nikamteua mwanamama, Dkt. Makakala, kuwa Kamishna Mkuu. Nimemteua mwanamama kwa makusudi. Kama mnavyofahamu, akinamama ni waaminifu. Na nashukuru hajaniangusha. Ameanza vizuri. Ameeleza hivi punde kuwa mwaka jana pekee, Idara ya Uhamiaji imekamata takriban wahamiaji haramu 15,068. Siku za nyuma idadi ya waliokatwa ilikuwa ndogo. Hivyo basi, nakupongeza sana Kamishna Mkuu. Nafahamu kuwa bado kuna mapungufu; lakini natambua jitihada ulizoanza kuzichukua. Nakuhimiza uendelee kushughulikia mapungufu yaliyosalia bila ya uoga wowote. Na nawasihi watumishi wa Idara ya Uhamiaji kuendelea kumpa ushirikiano wa kutosha.
Ndugu Wananchi, Mabibi na Mabwana;
Tumekutana hapa kwa shughuli maalum. Kufanya Uzinduzi wa Pasipoti ya Kielektroniki (e-Passport) ya Tanzania. Bila shaka, sote tunaifahamu posipoti pamoja na umuhimu na kazi zake. Baadhi yetu tunazo. Lakini, kwa ujumla, niseme tu kwamba, Pasipoti ni nyaraka inayomwezesha mtu kusafiri kutoka nchi moja kwenda nyingine. Kwa kawaida, nyaraka hii hutolewa na nchi kwa raia wake, na kwa maana hiyo hutumika pia kumtambulisha mtu uraia wake. Lakini, wakati mwingine, nchi inaweza kutoa pasipoti hata kwa mtu asiye raia wake (mathalan, mwekezaji au mtaalam wa jambo fulani). Aidha, katika zama za sasa, zipo baadhi ya taasisi zenye kutambulika kimataifa, ambazo nazo hutoa pasipoti kwa watumishi wake. Baadhi ya taasisi hizo ni Jumuiya yetu ya Afrika Mashariki, Umoja wa Afrika, Umoja wa Mataifa, n.k.
Kwa kuzingatia hayo yote, ni dhahiri kuwa tukio hili la leo ni muhimu sana. Ni muhimu kwanza kutokana na umuhimu wa Pasipoti nilioueleza hivi punde; lakini pili kwa sababu Pasipoti hii tunayoizindua leo ni ya pekee sana. Kama mnavyofahamu, nchi yetu nayo ina Pasipoti yake. Pasipoti hii imekuwepo na tumekuwa tukiitumia kwa muda mrefu sasa. Mfumo uliotumika kuitengeneza ni wa kizamani na haikuwekewa usalama wa kutosha. Hii ndio sababu imekuwa rahisi kwa baadhi ya kuighushi. Zaidi ya hapo, taarifa zilizomo kwenye Pasipoti ya zamani ilikuwa ni lazima zisomwe kwenye mashine. Hii ndio sababu, Watanzania wakitaka kutembelea baadhi ya nchi, walilazimika kwanza kuzituma Pasipoti zao kwenda nchi hizo au kwenye Balozi za jirani, ili kupata viza.
Pasipoti tunayoizindua leo, kama nilivyosema, ni ya kielektroniki. Ina alama nyingi za usalama (security features). Hii itasaidia kupunguza kama sio kuondoa kabisa uwezekano wa kughushiwa. Zaidi ya hapo, kwa kuwa Pasipoti hii ni ya kielektroniki, baadhi ya taarifa zake zitaweza kusomeka kwenye mifumo ya kielektroniki bila kulazimika kuipeleka Pasipoti yenyewe. Hii itaokoa muda, itapunguza gharama na uwezekano wa kupotea pindi Pasipoti zinaposafirishwa kwenda nje ya nchi kwa ajili ya kuomba viza.
Waheshimiwa Viongozi;
Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;
Hivi punde Kamishna Mkuu ameeleza kuwa uzinduzi wa Pasipoti hii ya Kielektroniki ya Tanzania inaashiria kuanza kwa utekelezaji wa mradi mkubwa wa Uhamiaji Mtandao (e-Immigration), ambao umepangwa kutekelezwa kwa awamu nne. Baada ya kuzindua Pasipoti hii, Awamu inayofuata, ambayo ni ya pili, itahusu kufunga mfumo wa Viza ya Kieletroniki (e-Visa) pamoja na Hati ya Ukaazi ya Kielektroniki. Awamu ya tatu itahusu Usimamizi wa Mipaka kwa njia ya Kielektroniki (e-Border Management System); na Awamu ya Nne itahusu kupanua huduma za uhamiaji mtandao kwenye Ofisi za Balozi zetu pamoja na Wilaya zenye shughuli nyingi za kiuhamiaji.
Napenda kutumia fursa hii, kuipongeza Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Idara ya Uhamiaji pamoja na taasisi nyingine zilizohusika kwa kuanza kutekeleza mradi huu wa Uhamiaji Mtandao. Mimi naufahamu vizuri Mradi huu na nimekuwa nikiufuatilia kwa karibu. Haikuwa jambo rahisi kufikia hatua hii. Kamishna Mkuu wa Uhamiaji ameeleza hivi punde kuwa gharama za mradi huu ni Dola za Marekani milioni 57.82, sawa na takriban shilingi bilioni 127.2. Lakini, awali ulipangwa kutekelezwa kwa Dola za Marekani milioni 226, zaidi ya shilingi bilioni 400. Ikabidi tuingilie kati ndipo tukaipata Kampuni ya HDI Global ya Marekani, ambayo ilikubali kuutekeleza kwa kiasi hicho cha Dola za Marekani milioni 57.82. Kama alivyosema Kamishna Mkuu, Kampuni ya HDI Global ni ya kimataifa na imekidhi viwango vyote.
Hivyo basi, naishukuru Kampuni hii kwa kubali kutekeleza mradi huu kwa gharama nafuu. Aidha, naishukuru sana Serikali ya Ireland kwa ushirikiano waliotupa kumpata Mkandarasi huyu. Nimefarajika kuona kuwa Balozi wa Ireland, Mheshimiwa Sherlock, pamoja na Mwakilishi wa Kampuni ya HDI Global tunao hapa. Tunawashukuru sana. Vilevile, nawashukuru na kuwapongeza Watanzania wote kwa kuwezesha kuanza utekelezaji wa mradi huu. Fedha zote za kutekeleza mradi huu zinatolewa na Serikali. Na kama mnavyofahamu, Serikali inapata fedha kupitia kodi zenu mnazolipa. Hivyo basi, hongereni sana Watanzania. Na nawasihi muendelee kulipa kodi ili kuiwezesha Serikali kutekeleza miradi ya maendeleo kama hii pamoja na kuboresha huduma mbalimbali za jamii.
Nawasihi pia kuendelea kuunga mkono mradi huu. Hivi punde imeelezwa kuwa pasipoti hii mpya ya kielektroniki itapatikana kwa gharama za shilingi 150,000. Bei hii ipo juu kuliko bei ya sasa. Lakini Mheshimiwa Waziri ameeleza vizuri kuwa bei hii imezingatia gharama za utengenezaji pamoja na ukubwa na ubora pasipoti hii mpya. Pasipoti hii itakuwa na kurasa nyingi kuliko ya zamani; na pia, kama ilivyoelezwa, bei hii ipo chini ukilinganisha na bei ya Pasipoti kama hii kwenye nchi nyingine. Hivyo basi, hatuna budi tuikubali na hasa kwa kuzingatia kuwa ongezeko hili la bei limetokana na maboresho tuliyofanya katika kuimarisha usalama wa Pasipoti zetu. Na niwaombe pia Watanzania wenzangu, tukipata Pasipoti hizi tuzilinde na kuzitunza; kwani kuna taarifa kuwa baadhi ya watu walipewa Pasipoti, wakaziuza na kisha kusingizia kuwa zimepotea. Naamini ujanja kama huo hauwezi kufanyika kwenye Pasipoti zetu mpya kwa vile zimeongezewa alama za usalama.
Waheshimiwa Viongozi;
Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;
Jukumu langu leo ni kuzindua Pasipoti ya Kielektroniki ya Tanzania. Hivyo, sitapenda kuwachosha kwa hotuba ndefu. Lakini, kabla sijahitimisha hotuba yangu, ninayo masuala mengine machache ambayo ningependa niyaeleze.
Suala la kwanza linahusu umuhimu wa kutekeleza kwa wakati na kusimamia kwa umakini mkubwa mradi huu. Kama ilivyoelezwa, mradi huu una awamu nne, ambazo zote zimepangwa kukamilika ndani ya mwaka huu wa 2018. Hivyo basi, hakikisheni mnakamilisha kama ilivyopangwa. Tunataka kuona wananchi wetu pamoja na wageni wanaotutembelea wanapata huduma nzuri za kiuhamiaji na tena za haraka. Nimefurahi kusikia kuwa katika kutekeleza Mradi huu, wadau karibu wote wanaohusika na masuala ya uhamiaji (NIDA, RITA, Jeshi la Polisi, Idara ya Wakimbizi, Bodi ya Utalii, BRELA, TRA, n.k.) wameshirikishwa, na kutakuwa na mfumo wa mawasiliano. Hii, bila shaka, itaongeza ufanisi na kasi ya utendaji kazi.
Kwa sababu hiyo, nitashangaa kama, pamoja na kuanza kwa mradi huu, wananchi watachukua muda mrefu kupata Pasipoti zao au kupata majibu ya kutopewa kwa kukosa vigezo. Nitashangaa, kama malalamiko ya upatikanaji viza yataendelea kusikika, kama ilivyotokea wakati wa Sherehe za Waumini wa Madhehebu ya Bohora mwaka juzi na wakati wa ujio wa Timu ya Everton ya Uingereza mwaka jana. Nitashangaa, kama vibali vya ukaazi vitatolewa kiholela na kwa watu wasio na sifa. Nitashangaa pia kama ukusanyaji wa mapato hautaongezeka. Nitashangaa sana. Lakini, ningependa pia kusema kuwa, katika kutekeleza mradi huu, kuweni sana makini, hususan katika masuala yanayohusu usalama na uraia wa nchi yetu. Na katika hili, nawapongeza Idara ya Uhamiaji kwa kuanzisha zoezi la utambuzi wa watu wasio raia nchini. Zoezi hili liwe endelevu, na lifanyeni kwa kushirikiana na mamlaka nyingine ili kuwatambua wote wanaoishi nchini bila vibali, wenye kufanya kazi bila vibali vya kazi na ukaazi au wanaofanya kazi zinazoweza kufanywa na Watanzania. Hivi majuzi wameingia wakimbizi zaidi ya 1,000 kutoka DRC; lakini nimeambiwa walioripoti Kambini wahafiki 1,000. Wengine watakuwa wameingia mitaani. Watafuteni na kuwakamata.
Suala la pili, ambalo linahusiana na hilo la kwanza, ni kuhusu uadilifu na uaminifu. Ni kweli kabisa kuwa Mfumo huu wa Uhamiaji Mtandao ni mzuri sana. Lakini, kama mjuavyo, mfumo kama mfumo peke yake hauwezi kuleta matokeo tunayoyataka. Ufanisi wa Mfumo huu utategemea sana uadilifu na utendaji kazi wa watumishi wa Idara hii. Natambua kuwa bado wapo watumishi wa Idara hii ambao hawataki kubadilika. Wanaendelea na utaratibu wa zamani wa kuendekeza vitendo vya rushwa. Kwa bahati nzuri, watu hao sio wengi. Ni wachache. Lakini, vitendo vyao vinaichafua sana Idara hii nyeti na muhimu katika nchi. Hivyo basi, Kamishna Mkuu hakikisha watu hawa unawashughulikia bila woga. Wakati mwingine, huwa nashangaa sana kuona wakimbizi haramu wanakamatwa baada ya kuwa wamepita kwenye maeneo mengi ya nchi. Ifike wakati sasa, ikibainika mhamiaji haramu alivuka eneo fulani bila kukamatwa, mathalani Mkoa fulani; basi kiongozi wa Mkoa husika achukuliwe hatua. Ashushwe cheo au hata kufukuzwa kazi. Ndio, wafukuzwe tu. Wapo Watanzania wengi tu wazalendo wanatafuta kazi.
Suala la tatu, ni kuhusu changamoto zinazoikabili Idara ya Uhamiaji alizosema Kamshna Mkuu. Upungufu wa vitendea kazi, vifaa, n.k. Serikali inatambua changamoto zenu zote na baadhi tumeanza kuzishughulikia. Mtakumbuka kuwa ni hivi majuzi tu Serikali imenunua nyumba 103 za watumishi wa Uhamiaji kule Dodoma kwa gharama ya takriban shilingi bilioni 3. Kuhusiana na suala la kuhamia Dodoma, nawaahidi kuwapatia shilingi bilioni 10 kwa ajili ya ujenzi wa Ofisi ya Makao Makuu Dodoma. Nawaahidi pia kuwa Serikali itaendelea kutatua changamoto zenu nyingine, ikiwemo kuboresha maslahi yenu, kadri uwezo wetu kifedha utakavyozidi kuimarika. Kama nilivyosema awali, Idara ya Uhamiaji ni nyeti na muhimu kwa usalama, ustawi na maendeleo ya nchi kwa ujumla.
Suala la nne na la mwisho, lakini sio kwa umuhimu, ni kwa wana-Dar es Salaam. Nawashukuru sana kwa kujitokeza kwa wingi kwenye shughuli hii. Nawahakikishia Serikali yenu imejipanga kuwaletea na kutatua shida zenu mbalimbali. Mathalan, nafahamu moja ya kero kubwa katika Jiji hili, ni suala la msongamano wa magari barabarani. Tumeanza kuchukua hatua. Tunajenga madaraja ya juu pale TAZARA na Ubungo, yote kwa pamoja, kwa gharama ya takriban shilingi bilioni 290.45. Aidha, mwaka huu (2018) tunatarajia kuanza ujenzi Awamu ya Pili ya mradi wa Barabara za Mabasi ya Mwendokasi kutoka mjini hadi Mbagala (Kilwa Road) yenye urefu wa kilometa 20.3. Halikadhalika, mwezi Februari, 2018 tunatarajia kuanza upanuzi wa Barabara ya Morogoro kuwa ya njia sita kutoka Kimara hadi Kiluvya, urefu wa takriban kilometa 16. Na kama mnavyofahamu, tumeanza ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kimataifa kuanzia hapa Dar es Salaam kuelekea Dodoma, umbali wa takriban kilometa 712 ambapo kiasi cha shilingi trilioni 7.062 kinatarajiwa kutumika; chote kitatolewa na Serikali. Reli hii, ambayo itaelekea Mikoa ya Mwanza na Kigoma na kisha kuungana na reli za kwenda Burundi na Rwanda, ikikamilika itarahisisha sana usafiri kati ya hapa Dar es Salaam, jiji kubwa la biashara, na Dodoma, Makao Makuu ya nchi yetu.
Sambamba na hayo, tunaboresha huduma nyingine za kijamii, ikiwemo maji, afya na elimu. Mwezi Juni, 2017 nilizindua mradi wa Maji wa Ruvu Juu pale Mlandizi kwa ajili ya Jiji la Dar es Salaam na maeneo ya jirani. Hivi sasa tunatekeleza mradi wa kuchimba visima virefu vya Mpera na Kimbiji kwa ajili ya kusambaza kwenye maeneo ambayo kwa sasa hayana mtandao wa mabomba. Miradi hii yote itaboresha upatikanaji wa huduma za maji. Kwenye afya, tunaendelea kuboresha hospitali zetu za Taifa zilizopo hapa Dar es Salaam: Muhimbili na Taasisi ya Saratani ya Ocean Road. Aidha, hivi majuzi tu nilizindua Hospitali kubwa na ya kisasa ya Mloganzila, ambayo inaipunguzia mzigo Hospitali yetu ya Taifa ya Muhimbili. Mpaka sasa zaidi ya wagonjwa 140 tayari wamehamishiwa Mloganzila. Tutaendelea kuijengea uwezo Hospitali hii ya Mloganzila. Vilevile, tunaziboresha hospitali zetu za Wilaya: Amana, Mwananyamala na Temeke pamoja na vituo vya afya vipatavyo vitano katika Jiji hili, vikiwemo viwili katika Wilaya hii ya Temeke (Yombo Vituka na Maji Matitu) ili kuviwezesha kutoa huduma ya dharura za upasuaji, hususan kwa akinamama wajawazito. Kwenye elimu, ninyi nyote mnafahamu mambo tunayofanya ya kupanua wigo na kuboresha elimu nchini, kuanzia elimu ya msingi hadi chuo kikuu.
Nina imani, kwa hatua hizi tunazochukua, Jiji la Dar es Salaam litazidi kuwa bora. Wito wangu kwenu wananchi endeeleni kuiunga mkono Serikali, hususan kwa kudumisha amani na umoja, kuchapa kazi kwa bidii na bila kusahau kulipa kodi.
Waheshimiwa Viongozi;
Ndugu Wananchi;
Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;
Nimezungumza mengi. Napenda niishie hapa. Nawashukuru tena wenyeji wa shughuli hii kwa kunialika. Aidha, nawashukuru wenzangu tuliohudhuria hafla hii pamoja na wana-Dar es Salaam. Ahsanteni sana kwa kujitokeza kwa wingi kwenye tukio hili muhimu na la kihistoria kwa nchi yetu.
Baada ya kusema hayo, sasa nipo tayari kutekeleza jukumu lililonileta la kuzindua Pasipoti ya Kielektroniki ya Tanzania.
Mungu Ibariki Pasipoti ya Kielektroni ya Tanzania!
Mungu Ibariki Idara ya Uhamiaji!
Mungu Wabariki Wana-Dar es Salaam!
Mungu Ibariki Tanzania!
“Ahsanteni sana kwa kunisikiliza”
- Dec 20, 2017
HOTUBA YA MHE. DKT. JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, WAKATI WA UWEKAJI JIWE LA MSINGI LA UJENZI WA OFISI YA TAIFA YA TAKW...
Soma zaidiHotuba
Mheshimiwa Kassim Majaliwa, Waziri Mkuu
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Dkt. Philip Mpango, Waziri wa Fedha na Mipango;
Waheshimiwa Mawaziri na Manaibu Mawaziri mliopo;
Mheshimiwa John Malecela, Waziri Mkuu Mstaafu;
Mheshimiwa Dkt. Binilith Mahenge, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma;
Mheshimiwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dodoma;
Mheshimiwa Hawa Ghasia, Mwenyekiti wa Kamati
ya Bunge ya Bajeti;
Mheshimiwa Ian Myles, Balozi wa Canada nchini;
Mheshimiwa Mama Bella Bird, Mwakilishi
wa Benki ya Dunia nchini;
Waheshimiwa Wabunge na Mstahiki Meya
wa Manispaa ya Dodoma;
Ndugu Mkurugenzi Mkuu pamoja na Watumishi
wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu;
Waheshimiwa Viongozi mbalimbali mliopo hapa;
Wageni Waalikwa wote, Mabibi na Mabwana:
Napenda nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, Muumba wetu, kwa kutupa uhai na kutuwezesha kukutana hapa leo. Aidha, naushukuru uongozi wa Wizara ya Fedha pamoja na Ofisi ya Taifa ya Takwimu kwa kunialika kwenye hafla hii ya kuweka Jiwe la Msingi la Ujenzi wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu hapa Dodoma, ambako ndiko Makao Makuu ya Nchi yetu. Ahsanteni sana.
Aidha, napenda kutumia fursa hii kuwashukuru wageni wote waalikwa pamoja na wananchi wa Dodoma kwa kujitokeza kwa wingi kushuhudia tukio hili. Nina uhakika kuwa mmejitokeza kwa wingi sio tu kwa sababu mnafahamu manufaa ya Jengo hili kujengwa hapa Dodoma, Makao Makuu ya Nchi yetu; bali pia kwa kuwa mnatambua umuhimu wa takwimu kwa maendeleo ya nchi.
Waheshimiwa Viongozi;
Wananchi Wenzangu, Mabibi na Mabwana;
Nafahamu kuwa wengi wetu hapa tunajua umuhimu wa takwimu. Hata hivyo, napenda kutumia fursa hii kusisitiza kuwa takwimu ni muhimu. Na ni muhimu katika nyanja zote. Iwe kiuchumi, kisiasa, kijamii na halikadhalika kiulinzi na usalama; na hata kiutamaduni.
Takwimu, na hasa zikiwa sahihi, zinaiwezesha Serikali kutambua mahitaji ya nchi au wananchi; kuweka malengo na kuandaa mipango ya maendeleo; pamoja na kufuatilia utekelezaji wake. Mathalan, kupitia takwimu za idadi ya watu, Serikali inatambua kiasi gani cha fedha kinachotakiwa kutengwa kwa ajili ya kununua dawa; au kufahamu mahali gani shule au kituo cha afya kijengwe.
Sambamba na hayo, takwimu zinaliwezesha Taifa kujipima limefikia hatua gani kimaendeleo, hususan kwa kutumia vigezo mbalimbali, ikiwemo pato la taifa, wastani wa umri wa kuishi, kiwango cha vifo kwa makundi mbalimbali (watoto wachanga, akinamama wajawazito) n.k. Zaidi ya hapo, takwimu ni muhimu kwa nchi kama yetu kwa ajili ya kufahamu utajiri na rasilimali tulizonazo, kama vile madini, gesi, mafuta, wanyama pori, mifugo, rasilimali za kwenye maji, n.k.
Hivyo basi, kwa ujumla, naweza kusema kuwa, takwimu ni muhimu sio tu katika nyanja zote, bali pia katika ngazi zote. Iwe ngazi ya mtu mmoja mmoja, familia, taasisi ya Serikali au isiyo ya Serikali; na Taifa kwa ujumla. Hii ndio sababu kuna usemi wa Kiingereza usemao “Without good statistics, the development process is blind”. Tafsiri ya Kiswahili isiyo rasmi ya usemi huu ni kwamba “bila ya takwimu sahihi, ni vigumu kupata maendeleo”.
Waheshimiwa Viongozi, Mabibi na Mabwana;
Ni kutokana na ukweli huo, napenda kutumia fursa hii kuipongeza Ofisi ya Taifa ya Takwimu kwa kazi kubwa na nzuri mnayoifanya katika kuandaa takwimu mbalimbali nchini. Hongereni sana. Napenda pia kutumia fursa hii, kuwapongeza kwa uamuzi wenu wa kujenga Ofisi hii hapa Dodoma. Kama mnavyofahamu, Serikali imedhamiria kwa dhati kabisa kuhamia Dodoma. Hivyo basi, ujenzi wa Jengo hili, ambalo, bila shaka litaboresha mandhari ya Mji wa Dodoma, unaenda sambamba na azma ya Serikali ya kuhamia Dodoma. Nimefurahi kusikia kuwa kazi ya ujenzi wa Jengo hili umekuwa ukitoa wastani wa ajira za moja kwa moja zipatazo 120 kwa siku; na kwamba kazi ya usanifu, ushauri na usimamizi inafanywa na Wataalam wa Tanzania. Hili ni jambo zuri kwa vile linawajengea uwezo wataalam wetu wa ndani.
Lakini, kwa namna ya pekee, napenda kutumia fursa hii kutoa shukrani zangu nyingi kwa washirika wetu mbalimbali, ambao wameufadhili mradi huu utakaogharimu kiasi cha Shilingi Bilioni 11.6 hadi kukamilika. Tunaishukuru Benki ya Dunia, Shirika la Maendeleo la Uingereza (DfID) na Shirika la Maendeleo la Canada. Tunawashukuru sana; na nimefurahi kuona wawakilishi wa Taasisi hizi tuko nao hapa. Pokeeni shukrani zetu nyingi, na tunawaomba muendelee kutuunga mkono. Nawahakikishia kuwa kila senti mtakayotupatia tutaitumia vizuri. Hakuna hata senti moja itakayopotelea kwenye mifuko ya watu.
Waheshimiwa Viongozi;
Wananchi Wenzangu, Mabibi na Mabwana;
Mwanzoni mwa hotuba yangu nimeeleza kuwa takwimu ni muhimu kwenye masuala mbalimbali ya maendeleo, ikiwemo kutambua ukuaji uchumi wa Taifa. Hivyo basi, kwa kuwa leo nimekuja hapa kuweka Jiwe la Msingi la Ofisi ya Takwimu; na kwa kuwa nipo hapa Dodoma, Makao Makuu ya Nchi; napenda kutumia fursa hii, kueleza kwa kifupi tu hali ya ukuaji uchumi wa nchi yetu kwa kutumia takwimu mbalimbali.
Kwa ujumla, napenda kusema tu kuwa, ukuaji wa uchumi wetu unaendelea vizuri. Mathalan, katika nusu ya kwanza ya mwaka huu, uchumi ulikua kwa kasi ya asilimia 6.8. Kasi hii imeiwezesha nchi yetu kuongoza katika eneo la Afrika Mashariki, lakini pia kuifanya kuwa miongoni mwa nchi ambazo uchumi wake unakua kwa kasi barani Afrika. Aidha, mfumko wa bei umeendelea kuwa chini, ambapo mwezi Novemba 2017 umefikia asilimia 4.4. Na hii inamaanisha kuwa ugumu wa maisha umepungua kinyume na baadhi ya watu wanavyosema kuwa “vyuma vimekaza”. Wengi ambao kwao vyuma vimekaza ni wale ambao walizoea fedha za bure, ikiwemo kupitia watumishi hewa, safari za nje, semina, n.k. Kwa wenye kujituma, vyuma haviwezi kukaza. Mathalan, kwa mkulima wa korosho ambaye bei imeongezeka kutoka wastani wa shilingi 2,000 kwa kilo hadi shilingi 4,000, unadhani kwake vyuma vitakaza? Lakini pia tujiulize, hivi kweli inawezekana kwa mtu wa kule kwetu Chato, ambako bei saruji imeshuka kutoka wastani wa shilingi 27,000 hadi shilingi 15,000 kwa mfuko iwe vyuma kwake vimekaza?
Mbali na kupungua kwa mfumko wa bei, akiba ya fedha za kigeni za nchi yetu imeongezeka. Hivi sasa imefika Dola za Marekani bilioni 5.82. Kiasi hiki cha fedha kinatuwezesha kununua nje bidhaa na huduma kwa miezi mitano. Kiwango kilichowekwa na Jumuia ya Afrika Mashariki ni angalau miezi minne. Hizi ni baadhi tu ya takwimu zinazoonesha kuwa uchumi wetu unaendelea vizuri. Nafahamu kuwa wapo watu wanaojaribu kupotosha ukweli huo; lakini nawaomba Watanzania muwapuuze watu hao na badala yake mziamini takwimu zinazotolewa na Ofisi yetu ya Takwimu, ambayo hivi punde Mwakilishi wa Benki ya Dunia, Mama Bella Bird, ameisifu kuwa ni mojawapo ya taasisi bora Barani Afrika.
Wananchi Wenzangu, Mabibi na Mabwana;
Ni dhahiri kuwa takwimu za ukuaji uchumi pekee kama haziendi sambamba na maendeleo na ustawi wa maisha ya watu hazina umuhimu wowote. Upo usemi wa Kiingereza usemao “You cannot feed the hungry on statistics (Huwezi kumlisha au kumshibisha mtu mwenye njaa kwa takwimu)”. Aidha, Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, aliwahi kusema kuwa “Maendeleo ya Uchumi ni lazima yafungamanishwe na Maendeleo ya Watu”. Kwa kutambua hilo, Serikali inafanya kila jitihada ili kuhakikisha kuwa maendeleo ya kiuchumi yaliyopatikana yanawiana na maendeleo na ustawi wa maisha ya watu. Hii ndio sababu, tumeweka mkazo mkubwa katika kuboresha huduma za jamii, ambazo zinawagusa wananchi wengi.
Mathalan, kama mnavyofahamu, hivi sasa tunatoa elimu bila malipo kuanzia shule ya msingi hadi sekondari. Mpaka kufikia mwezi Novemba 2017, Serikali imetumia kiasi cha shilingi bilioni 535 tangu utaratibu huu uanze mwezi Desemba 2015. Mkoa wa Dodoma pekee umepokea kiasi cha shilingi bilioni 16.6. Bila shaka, mtakubaliana nami kuwa, utaratibu huu umewezesha watoto wengi kutoka familia maskini kupata fursa ya elimu. Na hii inathibitishwa na ongezeko kubwa la wanafunzi wanaoanza darasa la kwanza na kidato cha kwanza. Na kama mnavyofahamu, njia rahisi ya kumsaidia mtu maskini, ni kumpa elimu.
Sambamba na elimu, tumeboresha huduma za afya nchini, ambapo tumeongeza bajeti ya dawa pamoja na kununua vifaa vya uchunguzi, vitanda, magodoro na mashuka; na halikadhalika tumeajiri watumishi wapya wa afya. Mathalan, nimeambiwa kuwa upatikanaji wa dawa muhimu kwenye Mkoa huu, umefikia asilimia 90 hivi sasa. Aidha, hapa Dodoma tumekamilisha jengo la wodi ya akina mama katika Hospitali ya Mkoa kwa gharama ya shilingi milioni 600, na tunatarajia kuanza ukarabati na ujenzi wa miundombinu mingine ya hospitali hiyo kwa gharama ya takriban shilingi bilioni 2.5. Vilevile, jumla ya vituo 5 vya afya, kikiwemo cha Makole na Bahi, tumevikarabati kuviwezesha kutoa huduma za dharura, ikiwemo upasuaji kwa akina mama wajawazito. Uboreshaji wa vituo hivyo umegharimu shilingi bilioni 2.5.
Sambamba na hayo, Hospitali ya Benjamin Mkapa nayo imeanza kutoa huduma; ambapo Serikali imeipatia vifaa vya kisasa kama MRI, CT-Scan pamoja na vifaa vya kupandikiza figo na kufanya upasuaji bila kuchana mwili. Vilevile, hivi sasa tupo kwenye mazungumzo na marafiki zetu wa Israel ili kuanzisha kitengo cha Huduma za Wagonjwa Mahututi cha Kisasa katika Hospitali ya Benjamin Mkapa. Hatua hizi, bila shaka, zimeimarisha upatikanaji wa huduma ya afya hapa Dodoma.
Tunachukua pia hatua za kuboresha upatikanaji wa huduma ya maji. Kwenye kila Mkoa hivi sasa kuna miradi ya maji inayotekelezwa. Hapa Dodoma, tumetekeleza miradi kadhaa ya maji, ukiwemo Mradi wa kupeleka maji Chuo Kikuu cha Dodoma. Lakini sambamba na miradi hiyo, tupo mbioni kuanza ujenzi wa mradi wa mkubwa wa maji wa Bwawa la Farkwa kwa gharama ya Dola za Marekani milioni 420, zaidi ya shilingi bilioni 920, ambapo mpaka sasa usanifu na mchoro wake umekamilika. Bwawa hili litakapokamilika, linatarajiwa kuondoa kabisa tatizo la maji katika Wilaya za Bahi, Chemba, Chamwino na hapa Manispaa.
Hizi ni baadhi tu ya hatua tunazochukua kuhakikisha maendeleo ya kiuchumi tuliyoyapata tunayatafsiri kwenye maisha ya watu. Lakini mbali na hatua hizi za kuboresha huduma za jamii, tumeelekeza nguvu katika kuimarisha miundombinu ya usafiri na umeme, ambayo nayo ni muhimu sana sio tu katika kukuza uchumi bali pia kuleta ustawi katika maisha ya wananchi. Tunajenga reli ya kisasa kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza; tunatekeleza miradi mikubwa ya umeme.
Waheshimiwa Viongozi;
Wananchi Wenzangu, Mabibi na Mabwana;
Jukumu langu leo ni kuweka Jiwe la Msingi la Jengo hili. Hivyo, nisingependa kuwachosha kwa hotuba ndefu. Hata hivyo, kabla sijahitimisha, ninayo masuala kama manne ambayo ningependa niyaseme.
Suala la kwanza, kama mtakavyokumbuka, mwanzoni mwa hotuba yangu nimeeleza kuhusu umuhimu wa takwimu. Lakini ili takwimu ziwe muhimu ni lazima ziwe sahihi. Hivyo basi, napenda kutumia fursa hii kuhimiza Ofisi ya Takwimu kuendelea kuandaa taarifa zenu kwa weledi mkubwa. Aidha, natoa wito kwa wananchi na Taasisi zote za Serikali kutoa ushirikiano wa kutosha kwa Ofisi ya Taifa ya Takwimu pindi wakihitaji taarifa mbalimbali. Sambamba na hayo, natoa onyo kwa wale watu wote wenye kutoa takwimu za uongo au upotoshaji. Naziagiza mamlaka husika kuchukua hatua dhidi ya watu wa namna hiyo. Sheria ya Takwimu kifungu Namba 37 kifungu kidogo cha 3 hadi cha 5 kinatamka wazi kwamba mtu au Taasisi akitoa takwimu za uongo au kusababisha wananchi kushindwa kutoa ushirikiano kwa ofisi ya Taifa ya Takwimu, adhabu yake ni kifungo cha miezi sita hadi miaka mitatu, ama kulipa faini kati ya shilingi milioni moja hadi shilingi milioni kumi; au adhabu zote kwa pamoja. Nimefurahi kusikia kuwa mchakato wa kuifanyia marekebisho sheria hiyo ili kuiongezea makali umeanza. Haiwezekani taasisi za kitaifa na kimataifa zenye wajibu wa kutoa takwimu zitoa takwimu fulani, halafu ajitokeze mtu mwingine aseme kuwa ana takwimu nyingine zinazotofautiana na hizo. Jambo hili halikubaliki.
Suala la pili, napenda pia kutumia fursa hii kurudia wito wangu nilioutoa hivi majuzi wakati nafungua tawi la CRDB kwa Wizara ya Fedha pamoja na Benki Kuu kuhusu kuimarisha usimamizi wa Benki, matumizi ya Dola, pamoja na usajili wa makampuni ya Simu na Benki kwenye mfumo wa ukusanyaji mapato kwa njia ya Kielectroniki. Mheshimiwa Waziri wa Fedha, hakikisha suala hili linatekelezwa kabla ya mwisho wa mwaka huu. Na pia Mheshimiwa Waziri fuatilia suala la umiliki wa Kampuni ya Simu ya Airtel, ambalo kwa taarifa zilizopo, ni mali ya Serikali.
Suala la tatu, mwezi Juni mwaka huu, wakati nikiwa pale Kijitonyama kuzindua Kituo cha Data na Mfumo wa Ukusanyaji Mapato kwa njia ya Kielektroniki niliagiza kuwa Taasisi zote za Serikali kutumia Kituo cha Data cha Taifa na kuachana na utaratibu wa kila taasisi kutengeneza Kituo chake. Mheshimiwa Waziri katika taarifa yake ameeleza kuwa Ujenzi wa Jengo hili utahusisha pia ujenzi wa kanzidata. Hivyo basi, natoa wito kwenu kutafakari suala hili vizuri. Kama hakuna sababu za msingi za kujenga kanzidata yenu wenyewe, ni vyema mtumie Kituo cha Data cha Taifa, ambacho kina viwango vya kimataifa na Serikali ilitumia fedha nyingi kuwekeza.
Suala la nne, ni kwa wana-Dodoma wote. Dodoma sasa inafunguka. Fursa nyingi za kiuchumi zinakuja, hususan kutokana na uamuzi wa Serikali kuhamishia Makao Makuu hapa Dodoma. Aidha, kuna miradi mingi na mikubwa imepangwa kutekelezwa hapa Dodoma, ikiwemo ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kimataifa, kutoka Dar es Salaam kupita hapa Dodoma kuelekea mikoa ya Mwanza na Kigoma. Ujenzi wa kipanda cha Reli hii kutoka Dar Es Salaam mpaka hapa Dodoma (Makutupora) chenye urefu wa takriban kilometa 712 kimeanza kujengwa kwa gharama ya shilingi trilioni 7.062 ambazo zote zitatolewa na Serikali. Sambamba na hayo nafahamu kuwa Mifuko yetu ya Hifadhi ya Jamii imepanga kutekeleza miradi kadhaa ya viwanda hapa Dodoma, ikiwa ni pamoja na kufufua Kiwanda cha kusindika nafaka na kukamua mafuta cha National Milling Corporation (NMC), Kiwanda cha kutengeneza matofali na vigae, na Kiwanda cha Kusindika Juisi na Mvinyo wa Zabibu ambacho kitajengwa Chinangali, Chamwino. Hivyo basi, nawasihi sana wana-Dodoma kujipanga vizuri kutumia fursa hizo.
Mwisho kabisa, nawashukuru tena kwa kunikaribisha. Aidha, nawapongeza tena Ofisi ya Takwimu kwa kazi nzuri mnayoifanya. Nawashukuru pia tena washirika kwa misaada yenu mbalimbali mnayotupatia. Naomba muendelee na moyo huo.
Mabibi na Mabwana; baada ya kusema hayo, sasa nipo tayari kutekeleza jukumu lililonileta la kuweka Jiwe la Msingi la Jengo la Ofisi ya Taifa ya Takwimu hapa Dodoma.
Mungu Ibariki Ofisi ya Taifa ya Takwimu!
Mungu Ibariki Dodoma!
Mungu Ibariki Tanzania!
“Ahsanteni sana kwa kunisikiliza”
- Dec 18, 2017
HOTUBA YA MHE. DKT. JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA NA MWENYEKITI WA CCM KWENYE UFUNGUZI WA MKUTANO MKUU WA TISA WA TAIFA W...
Soma zaidiHotuba
Ndugu Dkt. Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar
na Makamu Mwenyekiti wa CCM - Zanzibar;
Ndugu Philip Mangula, Makamu Mwenyekiti
wa CCM- Tanzania Bara;
Ndugu Wenyeviti na Makamu Wenyeviti
Wa CCM wa Taifa Wastaafu mliopo;
Ndugu Abdulrahman Kinana, Katibu Mkuu wa CCM;
Ndugu Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Ndugu Kassim Majaliwa, Waziri Mkuu
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Mheshimiwa Balozi Seif Ali Iddi, Makamu wa Pili
wa Rais wa Zanzibar;
Waheshimiwa Mawaziri Wakuu Wastaafu mliopo;
Ndugu Wake za Viongozi Wastaafu mkiongozwa
na Mama Maria Nyerere na Fatuma Karume;
Ndugu Wajumbe wa Kamati Kuu;
Ndugu Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa;
Ndugu Viongozi Wastaafu mliopo;
Ndugu Wawakilishi wa Vyama Rafiki
na Shindani vya CCM mliopo;
Ndugu Viongozi na Wazee Wastaafu wa CCM mliopo;
Ndugu Wageni Wetu Wote Waalikwa: Viongozi wa
Serikali na Dini mliopo;
Ndugu Wajumbe wa Mkutano Mkuu;
Ndugu Wana-CCM Wenzangu; Mabibi na Mabwana:
CCM OYEE! MAPINDUZI, DAIMA!
Awali ya yote, napenda nimshukuru Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, kwa kutujulia uhai na kutuwezesha kukutana hapa Dodoma leo. Aidha, napenda kutumia fursa hii kuwakaribisha ndugu wajumbe pamoja na wageni wote waalikwa katika Mkutano huu Mkuu wa Tisa wa Taifa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) unaofanyika hapa Dodoma; Makao Makuu ya Chama chetu pamoja na Serikali. Karibuni sana.
Natambua kuwa baadhi yenu mmelazimika kusafiri umbali mrefu kuja kuhudhuria Mkutano huu. Hivyo basi, napenda nitumie fursa hii kuwapa pole ya safari. Bila shaka, mmesafiri umbali mrefu kuja kuhudhuria Mkutano kwa kuwa mnafahamu umuhimu wake, lakini pia hii ni ishara ya mapenzi ya kweli mliyonayo kwa Chama hiki. Na ningependa kutumia fursa hii kuwapongeza wajumbe wote wa Mkutano huu kwa kuchaguliwa kwenu. Hongereni sana.
Ndugu Wajumbe wa Mkutano Mkuu na Wana-CCM Wenzangu;
Mkutano huu unafanyika zikiwa zimepita takriban wiki 3 tangu nchi yetu ifanye Uchaguzi Mdogo wa Madiwani katika kata 43. Na kama mtakavyokumbuka, katika uchaguzi huo, Chama chetu kilishinda viti vya udiwani 42. Hivyo basi, napenda kutumia fursa hii, hapa mwanzoni kabisa, kutoa pongezi nyingi kwa wanachama, wapenzi na mashabiki wa CCM kwa ushindi mkubwa tuliopata.
Kwa tathmini yangu binafsi, ushindi huu tuliopata umetokana na mambo makubwa manne. Kwanza kabisa, ni matokeo ya uungwaji mkono mkubwa na kukubalika kwa Chama chetu miongoni mwa Watanzania. Pili, unatokana na uimara na ukomavu wa Chama chenyewe. Sio siri kuwa Chama hiki ni kikongwe. Mwaka huu kimetimiza miaka 40 tangu kianzishwe. Hakuna Chama kikongwe kama hiki hapa nchini. Kimeongoza Dola tangu kimeanzishwa mwaka 1977 na tangu kurejeshwa kwa Mfumo wa Vyama vingi nchini 1992. Kina mashina, matawi, pamoja na wanachama, wapenzi na washabiki nchi nzima. Na katika kudhihirisha kuwa Chama hiki ni kikubwa na kikongwe, ni katika kudhihirisha hili, ninyi wenyewe mnajionea hapa viongozi wakuu wastaafu wa Chama na Serikali wapo hapa. Tunaye hapa Mzee Mwinyi, Mzee Mkapa, Mzee Kikwete, Mzee Karume, Mzee Malecela, Mzee Msekwa, Mzee Msuya, Mzee Dkt. Salim na Mzee Pinda. Hii inadhihirisha kuwa Chama hiki ni kikongwe na kina hazina kubwa.
Sababu ya tatu, iliyotufanya tushinde Uchaguzi huu ni kwamba tunatekeleza kwa vitendo mambo tuliyoahidi wakati wa Kampeni kupitia Ilani yetu ya Uchaguzi ya Mwaka 2015 – 2020. Na nne, tumeshinda kwa vile hivi sasa wana-CCM tuna umoja. Na tunashirikiana. Hivyo basi, napenda kurudia tena kuwapongeza wana-CCM kote nchini kwa ushindi tuliopata.
Ndugu Wajumbe wa Mkutano Mkuu;
Mabibi na Mabwana;
Kama nilivyotangulia kusema kuwa huu ni Mkutano Mkuu wa Tisa wa Taifa wa Chama chetu. Mkutano Mkuu wa CCM wa Taifa ndiyo kikao kikubwa zaidi kuliko vyote vya Chama; na kina madaraka ya mwisho kwa mujibu wa Katiba. Kwa kuzingatia hilo, na kwa kuwa Chama chetu ni Chama Tawala, ni dhahiri kuwa Mkutano huu ni muhimu sana. Maamuzi yatakayofanywa na Mkutano huu yatakuwa na athari (impact) sio tu kwenye Chama chetu bali Taifa letu kwa ujumla.
Ndugu Wajumbe wa Mkutano Mkuu na Wana-CCM Wenzangu;
Kama mnavyofahamu, Mkutano huu una ajenda kubwa tatu. Kwanza, utapokea na kujadili Taarifa ya Kazi za Chama itakayotolewa na Halmashauri Kuu ya CCM Taifa na kutoa maelekezo ya mipango ya utekelezaji wa Siasa ya CCM kwa kipindi cha miaka mitano ijayo. Aidha, Mkutano huu utapokea na kujadili Taarifa za Serikali zote mbili (yaani Muungano na Zanzibar) kuhusu utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi pamoja na uongozi wa Serikali na Nchi kwa ujumla. Vilevile, Mkutano huu utafanya uchaguzi wa Mwenyekiti wa CCM Taifa; Makamu wake wawili, mmoja wa Zanzibar na mwingine Tanzania Bara; pamoja na Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa.
Na kwa mujibu wa ratiba iliyopo, Taarifa ya Kazi za Chama itawasilishwa na Katibu Mkuu wa Chama, Ndugu Abdulrahaman Kinana. Aidha, Taarifa za Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi na Uendeshaji wa Serikali zitawasilishwa na Waziri Mkuu, Mheshimiwa Kassim Majaliwa, kwa upande wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Balozi Seif Ali Idd kwa upande wa Serikali ya Zanzibar. Kwa sababu hiyo, hotuba yangu haitagusia sana masuala hayo. Nitajikita zaidi katika suala la uchaguzi wa Chama chetu na nitaeleza baadhi ya mambo ambayo natamani sana kuona Chama hiki kikifanya katika kipindi cha miaka mitano ijayo.
Ndugu Wajumbe wa Mkutano Mkuu;
Mabibi na Mabwana;
Kama mnavyofahamu, tangu mwezi Aprili mwaka huu Chama chetu pamoja na Jumuiya zake zote tatu (Umoja wa Wazazi, Umoja wa Wanawake na Umoja wa Vijana) kimekuwa kwenye zoezi muhimu la uchaguzi. Tulianza uchaguzi kwenye ngazi ya mashina, kisha tukaelekea kwenye ngazi ya tawi, kata, wilaya na mkoa; na kwenye Jumuiya, uchaguzi tayari umekamilika hadi katika ngazi ya Taifa. Nimefarijika sana kuona kuwa katika zoezi hili la uchaguzi wagombea wengi walijitokeza, tena wengi sana. Hii inathibitisha ukukomavu wa demokrasia ndani ya Chama chetu.
Baada ya kukamilisha uchaguzi wa Chama kuanzia ngazi ya shina hadi mkoa; na kwa upande wa Jumuiya hadi ngazi ya Taifa; sasa tunakwenda kuhitimisha zoezi la uchaguzi wa Chama katika ngazi ya Taifa. Kama nilivyotangulia kusema, Mkutano huu utamchagua Mwenyekiti wa CCM Taifa; Makamu Wenyeviti wawili, pamoja na Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa. Na nawaomba ndugu wajumbe mchague kwa umakini. Usimchague mtu kwa sababu ya urafiki, udini, ukabila, ukanda, au kwa kutegemea kupata maslahi fulani fulani binafsi. Zaidi ya hapo, kamwe! Narudia tena, kamwe, msimchague mtoa rushwa. Ahadi Namba 3 ya mwana- CCM inasema, nanukuu, “rushwa ni adui wa haki sitapokea wala kutoa rushwa”, mwisho wa kunukuu.
Ndugu zangu wana-CCM, Chama chetu kimedhamiria kwa dhati kabisa kupambana na rushwa. Hivi majuzi mmesikia wenyewe tulitengua matokeo ya kura za maoni ya kupata mgombea wa Ubunge kule Singida baada ya kupatikana kwa tuhuma za rushwa. Na niwahakikishie kuwa, hata kwenye uchaguzi huu, endapo itathibitika kuna wagombea wameshinda kwa kutoa rushwa, hatutasita kutengua. Rushwa ni kansa. Rushwa ni adui wa haki. Ninyi wenyewe ni mashahidi kuwa kuna wakati ilikuwa vigumu kwa mtu kwenye Chama chetu kupata uongozi bila kutumia rushwa. Lakini, nimeshukuru sana Mwenyekiti Mstaafu Mzee Kikwete, kama isingekuwa uimara wake mimi nisingepata nafasi hivyo. Ahsante sana Mzee Kikwete. Hivyo basi, nawasihi sana wana-CCM wenzangu, msimchague mtoa rushwa. Badala yake, chagueni watu waadilifu, wachapakazi, wasio endekeza makundi na wenye mapenzi ya dhati kwa Chama chetu.
Ndugu Wana-CCM wenzangu;
Nafahamu kuwa jukumu langu leo ni kufungua Mkutano wetu. Lakini kabla sijafanya hivyo, ninayo masuala mawili ambayo ningependa kueleza. Suala la kwanza, linahusu zoezi la uchaguzi tulilolifanya ndani ya Chama chetu mwaka huu. Kwenye uchaguzi wowote ule kuna kushinda au kushindwa. Hivyo basi, wakati tunaelekea kuhitimisha zoezi la uchaguzi kwenye Chama chetu, ninalo ombi moja kwenu. Uchaguzi huu tulioufanya kwenye Chama chetu kuanzia mwezi Aprili 2017 hadi mwezi huu wa Desemba 2017 usiwe chanzo cha mifarakano au kuvurugika kwa umoja na mshikamano ulioanza kujengeka ndani ya Chama chetu. Bali utuimarishe na kutufanya kuwa wamoja zaidi.
Tuwapongeze wale walioshinda; na napenda kutumia fursa hii kuwapongeza wale wote waliochaguliwa kushika nyadhifa mbalimbali za uongozi kwenye Chama pamoja na Jumuiya zake. Hongereni sana. Ushindi mlio upata ni uthibitisho wa imani kubwa waliyonayo wana-CCM juu yenu.
Kwa wale ambao kura hazikutosha, msikate tamaa au kuwa wanyonge. Kama nilivyosema, kwenye uchaguzi wowote kuna kushinda na kushindwa. Safari hii kura hazikutosha; lakini huenda kwenye uchaguzi ujao, nanyi mkaibuka washindi. Hivyo, jambo la msingi kwenu hivi sasa ni kuchapakazi kwa bidii na kuwaunga mkono viongozi waliochaguliwa. Na niwaombe sana ndugu wajumbe na wana-CCM kwa ujumla, sasa tuyavunje makundi yote tuliyoanzisha wakati wa Uchaguzi. Uchaguzi umekwisha. Wakati wa kampeni umekwisha. Sasa, tunatakiwa tuchape kazi ili kukiimarisha zaidi Chama chetu. Napenda kutumia fursa hii kueleza kuwa, kamwe; narudia tena, kamwe, Chama hakitamvumilia mtu yeyote mwenye kuendeleza makundi. Awe ni kiongozi aliyechaguliwa, awe mgombea aliyeshindwa ama mwanachama wa kawaida.
Ndugu Viongozi;
Ndugu Wajumbe wa Mkutano Mkuu;
Mabibi na Mabwana;
Suala la pili ambalo ningependa kueleza linahusu maono niliyonayo ya namna ambayo natamani Chama chetu kifanye kazi katika kipindi cha miaka mitano ijayo. Na hili, nitalieleza kwa kirefu kidogo. Hivyo, nawaomba ndugu wajumbe mnivumilie kiasi.
Ndugu wajumbe na wana-CCM wenzangu, Mkutano wetu huu Mkuu wa Tisa wa Taifa unafanyika katika mazingira ya kipekee sana. Ni ya kipekee kwa sababu, kwanza, unafanyika katika kipindi ambacho Chama chetu kimetimiza miaka 40. Pili, unafanyika wakati nchi yetu imetimiza miaka 25 tangu kurejeshwa kwa Mfumo wa Vyama vingi. Na tatu, ambalo nadhani ni kubwa na muhimu zaidi ni kwamba, Mkutano huu unafanyika katika mwaka ambao Chama kimeanza kutekeleza Awamu ya Nne ya Mradi wa kuimarisha na kujenga uhai wa Chama.
Kama mnavyofahamu, ukiachilia mbali suala la ukongwe na kukomaa kidemokrasia, kama ambavyo nimeeleza awali; sifa nyingine muhimu na kubwa zaidi ya CCM, ni utaratibu wake wa kujitathmini na kujikosoa mara kwa mara, na kisha kufanya mageuzi yanayokwenda sambamba na wakati na hali halisi. Ni kutokana na ukweli huo, tangu imeanzishwa mwaka 1977, CCM imetekeleza awamu tatu za miradi ya kujenga na kuimarisha Chama. Mradi wa kwanza ulitekelezwa kati ya mwaka 1985 hadi 1987, ambapo Mwenyekiti wa wakati huo, Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, alizunguka nchi nzima kwa lengo la kukiimarisha Chama, hususan katika ngazi za chini.
Na wakati akihitimisha Awamu hiyo ya Kwanza, Baba wa Taifa alitangaza kuzindua Awamu ya Pili ya Mradi wa kuimarisha Chama, ambao pamoja na masuala mengine, ulihimiza Chama katika ngazi zote na kujenga itikadi; kuwa na mpango kazi unaotekelezwa; na kuimarisha mfumo wa nidhamu na demokrasia ndani ya Chama. Awamu ya Tatu ya Mradi wa kujenga na kuimarisha Chama ilianza kufuatia hotuba aliyotoa mtangulizi wangu, Mwenyekiti Mstaafu, Mzee Kikwete, wakati wa kupokea Uenyekiti wa Chama hapa hapa Dodoma tarehe 25 Juni, 2006. Msisitizo katika Awamu hii ilikuwa kujenga uongozi imara kwa kuhakikisha kuwa nafasi zote za uongozi ndani ya Chama zinakamilika; na viongozi wanakuwa mfano wa kuigwa kwa kuonesha njia.
Ndugu Wajumbe wa Mkutano Mkuu;
Mabibi na Mabwana;
Wakati Chama kikiendelea kutekeleza Awamu ya Tatu ya uimarishaji Chama, kutokana na mabadiliko na changamoto mbalimbali, haja ya kukifanyia Chama chetu mageuzi makubwa ya kimfumo, muundo na utendaji ilijitokeza. Hivyo basi, kufuatia majadiliano ya kina na ya muda mrefu yaliyofanyika; na hususan baada ya Chama kutazama itikadi yake, mwenendo wake, matendo yake, dhamira yake, malengo yake pamoja na kuangalia nidhamu ya viongozi wake. Na baada ya Chama kusikiliza sauti ya wanachama na wananchi kwa ujumla. Kama mnavyofahamu, Chama hiki ni cha wananchi wote. Hatimaye, mwezi Machi mwaka huu (2017), Chama chetu kilikubali kufanya mageuzi kupitia Mkutano Mkuu.
Mageuzi yaliyofanyika yamejikita katika mawanda makubwa matatu: mfumo, muundo na utendaji. Msingi mkuu wa mageuzi haya ni kukirejesha Chama kwa wanachama ili kukifanya kuwa kimbilio la wananchi. Na malengo mahususi ya mageuzi tuliyofanya ni kuongeza tija na ufanisi katika utendaji wa Chama, uwajibikaji miongoni mwa viongozi; pamoja na kupunguza gharama za uendeshaji wa Chama.
Mambo muhimu yaliyozingatiwa katika mageuzi haya ni kupunguza idadi ya vikao na wajumbe wa vikao ili kuondoa urasimu, kuongeza tija ya vikao husika na halikadhalika kupunguza gharama. Kwa kuwakumbusha tu, tumepunguza idadi ya wajumbe wa Mkutano huu Mkuu kutoka 2,422 hadi 1,706. Tumepunguza wajumbe wa Halmashauri Kuu kutoka 388 hadi 163; na Kamati Kuu kutoka 34 hadi 26. Tumefanya hivyo, ili viongozi watumie muda mwingi kushughulikia matatizo ya wanachama na wananchi kwa ujumla, badala ya kutumia muda mwingi kukaa ofisini na kushiriki kwenye vikao.
Tunaamini kuwa, endapo Chama kitaweza kushughulikia vizuri matatizo ya wananchi, kitaweza kuwavuta watu wengi zaidi kujiunga nacho. Katika mageuzi tuliyofanya pia, tumefuta utaratibu wa mtu mmoja kuwa na vyeo zaidi ya kimoja. Tumefuta vyeo ambavyo havikuwepo Kikatiba (kamanda, mlezi, n.k). Mageuzi tuliyoyafanya pia yamehimiza uadilifu na uwajibikaji miongoni mwa viongozi na wanachama, pamoja na kusisitiza Chama chetu kujitegemea kiuchumi. Ili kuhakikisha kuwa mageuzi tuliyofanya yanapata msingi wa kisheria, tumelazimika kuifanyia marekebisho Katiba ya Chama pamoja na Jumuiya zake.
Ndugu Wajumbe wa Mkutano Mkuu;
Mabibi na Mabwana;
Sio siri kuwa mageuzi tuliyoyafanya mwaka huu ni makubwa sana. Na ni lazima tuyasimamie. Na watu wa kwanza ambao watawajibika kuyasimamia ni viongozi ambao wamechaguliwa kushika nafasi mbalimbali hivi karibuni. Napenda kutumia fursa hii kuwasisitiza viongozi wote wa Chama waliochaguliwa kwenda kusimamia mageuzi tuliyoyafanya. Na niseme tu kuwa binafsi nitafurahi sana endapo viongozi waliochaguliwa wataweza kusimamia masuala makubwa manne, ambayo Mkutano huu ukiridhia unaweza kuyafanya kuwa ndiyo malengo makuu ya Mradi wa Awamu ya Nne ya kujenga na kuimarisha Chama.
Suala la kwanza kabisa, ni kukiimarisha Chama chetu kwa kuongeza idadi ya wanachama. Kama mnavyofahamu, lengo kuu la Chama chochote cha siasa ni kushinda uchaguzi na kushika Dola. Na katika nchi ya kidemokrasia kama yetu, mtaji pekee wa kufanikisha hili ni kwa Chama kuhakikisha kinakuwa na idadi kubwa ya wanachama, wapenzi na washabiki. Hivyo basi, viongozi mliochaguliwa, jukumu lenu la kwanza, ni kuhakikisha kuwa mnaongeza idadi ya wanachama, wapenzi na washabiki wa Chama chetu katika maeneo yenu. Tunataka ikifika wakati wa uchaguzi, washindani wetu, wasiambulie chochote.
Jambo la pili, ambalo naomba viongozi waliochaguliwa kulisimamia ipasavyo, ni katika kuhakikisha kuwa Chama chetu kinajitegemea kiuchumi. Chama chetu ni kikubwa na kikongwe. Hivyo, ni aibu kwa Chama hiki kuwa tegemezi. Kwa sababu hiyo, natoa wito kwa viongozi wote waliochaguliwa kuhakikisha Chama chetu kinajitegemea kiuchumi. Hivyo, tuwahimize wanachama waliopo kwenye maeneo yenu kulipa ada zao za mwaka. Na njia nzuri ya kuwashawishi wanachama kulipa ada ni kuhakikisha kunakuwa na uwazi katika ukusanyaji na matumizi wa mapato. Watu wanataka waone fedha zao wanazotoa zimeenda na kufanya nini. Sambamba na kuweka uwazi kwenye mapato na matumizi, jengeni utamaduni wa kuwatembelea wanachama. Msikae ofisini kuwasubiri wanachama walete michango. Na niwaombe wana-CCM wenzangu tujitahidi kulipa ada zetu za mwaka. Zama za kusubiria matajiri watulipie ada zetu wakati wa kampeni, zimepitwa na wakati. Ni lazima sisi wenyewe tujitoe. Chama kitajengwa na wenye chama, siyo matajiri wachache.
Njia nyingine ya kuhakikisha Chama kinajitegemea kiuchumi ni kusimamia vizuri rasilimali za Chama. Kama ambavyo nimesema mara kadhaa, Chama hiki kina rasilimali nyingi: viwanja vya michezo, majengo, mashamba, n.k.; lakini kwa bahati mbaya, kwa muda mrefu, rasilimali hizi hazijakinufaisha Chama chetu. Hii imetufanya, tutegemee zaidi ruzuku na michango ya wahisani. Mathalan, mapato ya Chama kwa mwaka wa fedha 2014/2015 ilikuwa takriban shilingi bilioni 29.35. Kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 21.95 ni ruzuku na michango ya hiari. Mwaka 2015/2016, mwaka wa uchaguzi, mapato yalikuwa shilingi bilioni 73.19, ambapo ruzuku na michango ya hiari ni shilingi bilioni 56.82; na katika mwaka 2016/2017, mapato yalikuwa shilingi bilioni 40.01, ambapo ruzuku na michango ya hiari ni shilingi bilioni 27.56. Hii inadhihirisha kuwa uwezo wetu wa kujitegemea ni mdogo. Ni lazima turekebisha hali hii, na kwa bahati nzuri tumeanza kuchukua hatua, ikiwemo kufanya uhakiki wa mali zetu zote, halikadhalika tupo mbioni kuanzisha mfumo wa kielektroniki utakaokiwezesha Chama kutambua na kusimamia rasilimali na mali zake zote, mapato na kusimamia uendeshaji kwa ujumla. Hivyo basi, niwaombe viongozi wapya mkaendeleze jitihada zilizoanzishwa.
Sambamba na hilo, viongozi wapya hamna budi kubuni miradi mipya. Na katika hili, niseme tu kwamba, itakuwa aibu kwa Chama chetu, ambacho Serikali yake inahubiri ujenzi wa uchumi wa viwanda, tutashindwa hadi ikifika mwaka 2020 kuanzisha angalau kiwanda kimoja.
Tatu, nawasihi sana viongozi wapya, kila mtu mahali pake alipo, ahakikishe kuwa Chama chetu kinakuwa kiungo kati ya Serikali na wananchi. Chama, hususan Chama tawala kama chetu, kinao wajibu wa msingi wa kuwaeleza na kuwafafanulia wananchi umuhimu wa utekelezaji mipango na hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali. Zaidi ya hapo, kinao wajibu wa kuchukua maoni, mapendekezo na kero mbalimbali za wananchi na kuziwasilisha Serikalini. Niwe mkweli, hivi sasa, Chama chetu hakitekelezi vizuri jukumu hili. Tumekuwa hodari sana wa kufanya kampeni na kuhakikisha Chama kinashinda uchaguzi. Lakini, baada ya hapo, huwa tunajiweka pembeni, ama kwa kuvaa sura ya Userikali au kwa kuwaogopa watendaji wa Serikali. Nilisema kwenye Mkutano Mkuu uliopita, viongozi wa Chama hawapaswi kuwaogopa watendaji wa Serikali, hususan katika kutetea maslahi ya wananchi wanyonge.
Katika kusisitiza umuhimu wa Chama chetu kuwa kiungo kati ya Serikali na wananchi, napenda ninukuu maneno yafuatayo, ambayo Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliyatamka tarehe 7 Juni, 1968 alipohutubia Mkutano Mkuu wa Chama cha Uganda People’s Congress, na nitanukuu kwa lugha yetu adhimu ya Kiswahili:“Kazi ya Chama kilicho imara ni kuwa daraja linalowaunganisha wananchi na Serikali yao. Ni wajibu wa Chama kuwasaidia wananchi kuelewa Serikali yao inafanya nini na kwanini; na kuwashawishi wananchi kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Serikali yao, ikiwemo kuondoa umaskini wao....Zaidi ya hapo, Chama kina jukumu au wajibu wa kuwasemea wananchi (The Party must speak for the people)”, mwisho wa kunukuu.
Hivyo basi, nawasihi sana viongozi wapya, nendeni makatekeleze jukumu hili ipasavyo. Pongezeni pale inapobidi kupongeza, na kosoeni inapobidi. Na ili muweze kutekeleza jukumu hili vizuri, hakikisheni kuwa mnakuwa karibu na wananchi, lakini pia mnaifahamu vizuri mipango ya Serikali na mikakati ya kutekeleza mipango hiyo, ikiwemo bajeti zinazotengwa. Nitashangaa na kwa kweli nitasikitika, kama nitaona wananchi wanadai kufahamishwa mapato na matumizi ya Serikali ya Kijiji, huku Mwenyekiti wa CCM wa Shina au Tawi yupo; nitashangaa wananchi walalamike kuhusu ubadhirifu katika ujenzi wa kituo cha afya au shule wakati Mwenyekiti wa CCM na Kamati ya Siasa ya Kata wapo; na vilevile nitashangaa wananchi kushindwa kuelewa umuhimu wa kununua ndege, kujenga reli ya standard gauge na mradi wa umeme wa Stiglier’s Gorge wakati kuna Mwenyekiti wa CCM Wilaya, Mkoa na Wajumbe wa Halmashauri Kuu na Mbunge wa CCM. Nitashangaa sana. Na niwaombe viongozi wa Serikali kutoa ushirikiano na ufafanuzi kwa viongozi wa Chama. Lakini ningependa pia kusema kuwa wana-CCM mkitaka kukosoa jambo linalofanywa na Serikali, mkumbuke kuwa ninyi ni Chama Tawala. Mnazo njia nyingi za kufikisha mapungufu mnayoyaona kwenye Serikali. Kuna usemi ambao Umoja wa Wazazi hupenda kuutumia, usemao “Uchungu wa Mwana, Aujuaye Mzazi”. CCM Oyeee! Mapinduzi, Daima mbele!
Jambo la nne, na la mwisho lakini sio kwa umuhimu, ambalo ningependa viongozi wapya mlipe mkazo unaostahili, ni uadilifu. Na uadilifu unapaswa kuanza na ninyi. Kiongozi anapaswa kuwa mfano wa kuigwa kwa wanachama na wananchi kwa ujumla. Haifai, na kwa kweli, kamwe Chama hakitamvumilia kiongozi au mwanachama wa CCM mwenye kutuhumiwa au kujihusisha na vitendo vya rushwa, utapeli, wizi, ubadhirifu, ujambazi, ulevi uliopindukia, kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya, n.k. Upo usemi wa enzi usemao “Mke wa Mfalme hapaswi hata kuhisiwa kuwa anachepuka”. Hivyo basi, kama kuna viongozi wa namna hiyo wamechaguliwa, ni vyema wakajirekebisha.
Ndugu Wajumbe wa Mkutano Mkuu;
Mabibi na Mabwana;
Kama nilivyotangulia kusema, taarifa ya Utekelezaji wa Ilani na uendeshaji wa Serikali zitawasilishwa na Waziri Mkuu na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar. Hata hivyo, napenda nitumie fursa hii kueleza mambo machache kuhusiana na masuala hayo. Kwanza kabisa, kama mnavyofahamu, jukumu kubwa la Serikali zetu mbili ni kuhakikisha amani, umoja na Muungano wa nchi yetu unadumishwa. Hii pia ni moja ya ahadi zilizopo kwenye Ilani yetu ya Uchaguzi. Bila shaka, mtakubaliana nami kuwa Serikali zetu mbili zimeweza kutekeleza jukumu na ahadi hii kikamilifu. Nchi yetu ipo salama na ina utulivu. Muungano wetu upo imara. Na watanzania tumeendelea kuwa wamoja. Watu wachache waliojaribu kutishia amani, Muungano na umoja wetu tumewadhibiti kikamilifu.
Suala la pili ambalo ningependa kuzungumzia ni kuhusu utekelezaji wa ahadi kubwa ya uchaguzi ya kujenga nchi ya uchumi wa kati unaoongozwa na viwanda ifikapo mwaka 2025. Ahadi hii nayo tunaitekeleza vizuri. Uchumi wetu unaendelea kuimarika, ambapo nchi yetu ni miongoni mwa nchi chache barani Afrika ambao uchumi wake unakua kwa kasi. Aidha, mfumuko wa bei unaendelea kushuka, ambapo mwaka huu mwezi Novemba ulishuka kumefikia asilimia 4.4. Vilevile, akiba ya fedha za kigeni imefikia Dola za Marekani milioni 5,820.4 mwezi Septemba 2017. Kiasi hiki kinaiwezesha nchi yetu kulipia gharama ya kununua bidhaa kwa miezi mitano. Hii ina maana kwamba leo hii Watanzania tunaweza kukaa bila kufanya kazi yoyote kwa miezi mitano na tukaendelea kupata huduma kama kawaida. Lakini hii haimanisha kwamba watu waache kufanya kazi. Ni lazima tuendelee kufanya kazi. Kama maandiko matakatifu yanavyosema, asiye fanyakazi na asile. Nanyi mnafahamu kuwa mtu asiye kula maana yake atakufa.
Kuhusu ujenzi wa Viwanda, kwa kipindi cha miaka 2 iliyopita takriban Viwanda vipya 3,306 vimejengwa, na hizi ni takwimu za mwezi Juni 2017. Lakini jambo la kufurahisha zaidi ni kwamba viwanda vingine vinajengwa na hata vile vya zamani vimeanza kufufuliwa. Mathalan, Mifuko yetu ya Hifadhi ya Jamii (NSSF, ZSSF, PSPF, GEPF, Bima ya Taifa ya Afya, LAPF na WCF) hivi sasa inatekeleza miradi takriban 15 ya viwanda, ambavyo nimeambiwa kuwa vitazalisha takriban ajira 350,000. Baadhi ya miradi ni ulimaji wa mashamba ya Miwa na ujenzi wa Viwanda vya Sukari vya Mkulazi na Mbigiri mkoani Morogoro, ambako pia kutakuwa na uzalishaji wa umeme utakaoingizwa kwenye Gridi ya Taifa; Ufufuaji wa Vinu vya Kusindika Nafaka na Ukamuaji Mafuta vya Shirika la Usagishaji la Taifa (National Milling Corporation – NMC) vilivyopo hapa Dodoma, Iringa na Mwanza; Ufufuaji wa Kiwanda cha Bidhaa za Ngozi pale Karanga, Moshi Mjini; Kiwanda cha Katani na Agave Syrup itokanayo na mabaki ya mkonge Mkoani Tanga; Kiwanda cha Madawa TPI Arusha; Kiwanda cha Kutengeneza Matofali ya Kuchoma na Vigae hapa Dodoma; Kiwanda cha Kusindika Tangawizi Kilimanjaro; Kiwanda cha Nyama cha Nguru Ranch Morogoro; Kiwanda cha Mvinyo wa Zabibu hapa Dodoma; Kiwanda cha bidhaa za hospitali (pamba na maji tiba) Simiyu, n.k. Naipongeza Mifuko hii kwa kuitikia wito wa Serikali wa kujenga viwanda. Na hii ndio sababu nahimiza Chama chetu nacho kushiriki katika utekelezaji wa ahadi hii.
Ndugu Viongozi;
Ndugu Wajumbe wa Mkutano Mkuu;
Wageni wetu Waalikwa;
Mabibi na Mabwana;
Nimezungumza mengi. Hivyo basi, napenda nihitimishe hotuba yangu kwa kuwashukuru wajumbe wa Mkutano huu kwa kuhudhuria kwa wingi. Aidha, napenda kutumia fursa hii kuwashukuru, Makamu wangu wawili, Mheshimiwa Dkt. Shein na Mzee Mangula kwa ushirikiano mkubwa walionipa tangu nilipochaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Chama chetu mwezi Julai mwaka jana. Nimejifunza na naendelea kujifunza mambo mengi kupitia kwao. Lakini, kwa namna ya pekee, namshukuru Mzee Kinana pamoja na Sekretarieti ya Chama kwa ujumla kwa kunisadia katika kutenda kazi za Chama na kufanya mageuzi mbalimbali. Nakushukuru sana Mzee Kinana. Na ni matarajio yangu kuwa Mzee huyu ataendelea kunisaidia katika kazi.
Napenda pia kutumia fursa hii, kuwashukuru wageni wetu waalikwa, Wawakilishi pamoja na Mabalozi mnaowakilisha Vyama Rafiki vya CCM kutoka nchi mbalimbali. Tunawashukuru sana kwa kushiriki nasi katika Mkutano huu. Napenda pia kuwashukuru wawakilishi wa vyama shindani mliohudhuria Mkutano huu. Mmeonesha ukomavu mkubwa wa kisiasa. Licha ya tofauti zetu za kiitikadi, lengo letu sisi sote ni kuijenga nchi yetu. Hii ndio sababu nimefarijika sana kwa kuja kuhudhuria Mkutano huu. Ahsanteni sana. Maendeleo hayana Chama japo naamini kuwa maendeleo ya kweli yataletwa na CCM.
Nitumie fursa hii pia kuwashukuru viongozi wetu wastaafu, wakiwemo Wenyeviti na Makamu Wenyeviti Wastaafu, Makatibu Wakuu Wastaafu, pamoja na na wazee wetu wengine, wakiwemo mama zetu wapendwa, Mama Maria Nyerere na Mama Fatuma Karume kwa kuja kushiriki nasi kwenye Mkutano huu. Tunawashukuruni sana.
Mwisho lakini sio kwa umuhimu, napenda kuwashukuru viongozi na wanachama wapya ambao wamejiunga na Chama chetu hivi karibuni. Na napenda kuwaarifu kuwa wapo wengi wanaotamani sana kujiunga na Chama chetu.
Baada ya kusema hayo, sasa natamka rasmi kuwa Mkutano Mkuu wa Tisa wa Taifa wa Chama Cha Mapinduzi umefunguliwa rasmi hapa Dodoma. Nawatakia wajumbe wenzangu Mkutano mwema na maamuzi ya busara.
Kidumu Chama Cha Mapinduzi!
Mapinduzi, Daima!
Mungu Wabariki Wajumbe wa Mkutano huu!
Mungu Ibariki CCM!
Mungu Ibariki Tanzania!
“Ahsanteni sana kwa kunisikiliza”
- Dec 14, 2017
HOTUBA YA MHESHIMIWA DKT. JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA WAKATI WA UFUNGUZI WA MKUTANO MKUU WA CHAMA CHA WALIMU TANZANIA (...
Soma zaidiHotuba
Mheshimiwa Mwalimu Leah Ulaya, Kaimu Rais
wa Chama Cha Walimu Tanzania;
Mheshimiwa Kassim Majaliwa, Waziri Mkuu
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Mheshimiwa Job Ndugai, Spika wa Bunge
la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Mheshimiwa Seleman Jafo, Waziri wa Nchi
Ofisi ya Rais – TAMISEMI;
Mheshimiwa Prof. Joyce Ndalichako, Waziri wa Elimu
na Mafunzo ya Ufundi;
Mheshimiwa George Mkuchika, Waziri wa Nchi,
Ofisi ya Rais – UTUMISHI;
Mheshimiwa Jenista Mhagama, Waziri wa Nchi,
Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu;
Waheshimiwa Mwalimu Janet Magufuli,
Mke wa Rais, na Mwalimu Mary Majaliwa, Mke wa Waziri Mkuu;
Mheshimiwa Binilith Mahenge, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma;
Waheshimiwa Wabunge mliopo;
Mheshimiwa Makatibu Wakuu mliopo;
Mheshimiwa Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama
vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA);
Ndugu Katibu Mtendaji wa Tume ya Utumishi wa Walimu;
Waheshimiwa Viongozi wa Vyama vya Wafanyakazi
mliohudhuria kutoka Ndani na Nje ya Tanzania;
Ndugu Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa
wa Chama Cha Walimu Tanzania;
Waheshimiwa Viongozi mbalimbali mliopo;
Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana:
Awali ya yote napenda niwashukuru sana walimu kwa kunikaribisha. Kwangu mimi, leo ni siku ya pekee sana. Na nakiri kwamba nimefurahi sana. Nimefurahi, kwanza, kwa kupata fursa hii adhimu ya kuzungumza nanyi walimu wenzangu. Kama mnavyofahamu, mimi ni mwalimu. Mke wangu naye ni mwalimu. Nazijua shida na raha za ualimu. Hivyo basi, kuwepo mahali hapa, ni faraja kubwa kwangu. Lakini, jambo la pili lililonifurahisha ni kwamba, sasa nimetambua kuwa Chama Cha Walimu kimedhamiria kufanya kazi na Serikali. Ahsanteni sana walimu wenzangu. Na napenda kutumia fursa hii kuwahikikishia kuwa Serikali itashirikiana na ninyi kwa karibu.
Kabla sijaendelea zaidi, napenda nami niungane nanyi katika kutoa salamu zangu za pole kwa familia, ndugu na jamaa wa Marehemu Alhaji Yahya Msulwa, aliyekuwa Katibu Mkuu wa CWT, ambaye aliaga dunia tarehe 17 Novemba, 2017, wakati akiwa kwenye maandalizi ya Mkutano huu. Sambamba na hilo, kama mnavyofahamu, leo nchi yetu imeiaga rasmi miili ya askari wetu mashujaa 14 waliouawa hivi karibuni nchini DRC wakiwa katika ulinzi wa amani. Hivyo basi, naomba tuzidi kuwaombea mashujaa wetu roho zao zipumzike mahali pema pepoi. Aidha, tuwaombee mashujaa wengie waliojeruhiwa kwenye tukio hilo ili wapone kwa haraka. Amina.
Waheshimiwa Viongozi;
Ndugu Walimu Wenzangu;
Leo ni mara yangu ya kwanza kukutana rasmi na walimu tangu nimechaguliwa kuwa Rais wa Awamu ya Tano ya Nchi yetu. Hivyo basi, napenda kutumia fursa hii kuwashukuru walimu kote nchini kwa kura nyingi mlizonipa zilizoniwezesha kuibuka mshindi kwenye Uchaguzi Mkuu uliopita. Ahsanteni sana walimu wenzangu. Nawaahidi kufanya kazi kwa bidii kwa manufaa ya Watanzania wote.
Napenda pia kutumia fursa hii, kutoa shukrani zangu nyingi kwa uongozi wa CWT kwa uamuzi wenu wa kuhamishia Mkutano huu hapa Dodoma. Kama mnavyofahamu, Mkutano huu awali ulipangwa kufanyika Arusha. Lakini baadaye, mliamua kuuhamishia hapa Dodoma. Nawashukuru sana. Hapa Dodoma ndio Makao Makuu ya nchi yetu. Hapa pia ni Makao Makuu ya Ofisi za Bunge. Aidha, hapa ni mahali ambako, chuo kikubwa zaidi katika eneo zima la Afrika Mashariki na Kati, Chuo Kikuu cha Dodoma, kipo. Hivyo basi, nina imani kuwa Wajumbe wa Mkutano wamefurahi kuja kufanya mkutano wao hapa Dodoma.
Waheshimiwa Viongozi;
Ndugu Wajumbe wa Mkutano;
Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;
Sekta ya elimu ni nyeti na muhimu katika jamii na pia kwa maendeleo ya Taifa lolote. Sisi Waswahili tuna msemo usemao “Elimu ni Ufunguo wa Maisha”. Marafiki zetu Wachina nao wana msemo usemao, naomba niunukuu kwa Lugha yetu adhimu ya Kiswahili, “Ukitaka kuwekeza kwa mwaka mmoja, panda mpunga; Ukitaka kuwekeza kwa miaka kumi, panda miti; lakini ukitaka kuwekeza katika maisha, wekeza kwenye elimu”. Hii yote ni katika kudhihirisha kuwa elimu ni muhimu kwa mtu mmoja mmoja, katika jamii na kwa maendeleo ya nchi kwa ujumla.
Na bila shaka, kwa kutambua umuhimu huo, Serikali za Awamu zote za nchi yetu, ya kwanza hadi ya sasa, imeweka mkazo mkubwa katika kukuza na kuboresha sekta hii. Juzi kwenye Maadhimisho ya Sherehe za Uhuru nimeeleza kuwa wakati tunapata Uhuru, mwaka 1961, baada ya utawala wa Kikoloni uliodumu kwa takriban miaka 76, nchi yetu ilikuwa na shule za msingi 3,100. Lakini katika kipindi cha miaka 56 ya Uhuru wetu, tumeweza kujenga shule za msingi mpya 14,279 na hivyo kutufanya tuwe na jumla ya shule za msingi 17,379. Katika kipindi hicho Shule za sekondari zilikuwa 41, lakini hivi sasa zipo 4,817. Tulikuwa na Chuo Kikuu kimoja, lakini leo hii tuna vyuo vikuu 48.
Mtakubaliana nami kuwa haya ni mafanikio makubwa sana. Hivyo basi, napenda kutumia fursa hii kutoa pongezi zangu nyingi kwa viongozi wa awamu zote za nchi yetu kwa kufanikisha kupatikana kwa mafanikio haya. Pamoja na pongezi hizo nilizozielekeza kwa viongozi watangulizi wangu, upo usemi usemao “unaweza kuwa na shule, chuo au chuo kikuu bila ya kuwepo kwa majengo, vitabu, madawati, maabara, chaki na kalamu; lakini kamwe huwezi kuwa na shule au chuo bila ya walimu”. Kwa maana hiyo, pongezi nyingi zaidi inafaa ziwaendee ninyi walimu. Hivyo basi, kwa niaba yangu binafsi na kwa niaba ya Serikali na wananchi wote wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania napenda kutumia fursa hii kutoa pongezi nyingi sana kwenu walimu kwa kazi kubwa na nzuri mnayoifanya ya kuwaelimisha Watanzania. Kwa hakika, walimu mnafanya kazi kubwa sana. Hongereni na ahsanteni sana.
Waheshimiwa Viongozi;
Ndugu Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CWT;
Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;
Kama nilivyotangulia kusema hapo awali, Serikali za Awamu zilizotangulia zimefanya juhudi kubwa za kukuza na kuendeleza sekta ya elimu nchini. Kwa lengo la kuendeleza mafanikio hayo, na sisi Serikali ya Awamu ya Tano tunachukua hatua mbalimbali za kupanua wigo na kuboresha sekta ya elimu. Kama mnavyofahamu, hivi sasa tunatekeleza elimu bila malipo kuanzia shule ya msingi hadi sekondari, ambapo awali tulikuwa tukitenga shilingi bilioni 18.77 kwa mwezi kugharamia, lakini kuanzia mwezi Julai 2016 tuliongeza fedha hizo hadi kufikia shilingi bilioni 23.868. Hii maana yake ni kwamba, tangu utaratibu huu uanze mwezi Desemba 2015 hadi Novemba 2017, Serikali imetumia kiasi cha takribani shilingi bilioni 535.
Ninyi walimu ni mashahidi wazuri. Uamuzi wa Serikali wa kuanzisha elimu bila malipo, umeleta mafanikio makubwa sana, hususan katika kuongeza idadi ya wanafunzi wanaoanza darasa la kwanza na kidato cha kwanza. Lakini, kutokana na ongezeko hilo la wanafunzi, zilijitokeza changamoto, ikiwemo upungufu wa madawati, vyumba vya madarasa, pamoja na vifaa na vitendea kazi vingine. Kutokana na matatizo hayo, Serikali ilianza kuchukua hatua ili kushughulikia.
Tulishirikiana na wadau mbalimbali, wakiwemo wananchi, na kuweza kupunguza kwa takriban asilimia 95 tatizo la madawati kwenye shule zetu za msingi na sekondari nchini kote. Aidha, katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, Serikali imejenga na kukarabati miundombinu katika shule za msingi na sekondari 365, zikiwemo shule za sekondari kongwe 88; kwenye halmashauri 129. Miundombinu hiyo ni nyumba za walimu 12, vyumba vya madarasa 1,435, mabweni 261, majengo ya utawala 11, mabwalo 6, matundu ya vyoo 2,832, maktaba 4, na visima vya maji safi 4. Aidha, katika bajeti ya Mwaka huu wa Fedha 2017/2018, Serikali, kupitia bajeti ya Halmashauri, imetenga shilingi bilioni 126.65 kwa ajili ya kujenga na kukarabati miundombinu ya shule za msingi na sekondari, itakayojumuisha nyumba za walimu 2,364; madarasa 6,636; vyoo 9,355; madawati 118,921; mabweni 157; hosteli 176 na maabara zipatazo 1,817. Waheshimiwa Mawaziri wahusika hakikisheni haya yanatekelezwa.
Sambamba na hayo, tumeanza kuchukua hatua mbalimbali za kuboresha elimu yenyewe. Ninyi walimu ni mashahidi, mwaka huu wa 2017 tumegawa vifaa vya maabara kwenye shule za sekondari 1,696 pamoja na vifaa vya wanafunzi wenye mahitaji maalum katika shule za msingi 213 na shule za sekondari 22.
Ukiachilia mbali Elimu ya Msingi na Sekondari, Serikali pia inaboresha Elimu ya Juu, hususan kwa kutoa mikopo kwa wanafunzi. Idadi ya wanafunzi wa Chuo Kikuu wanaopewa mikopo imeongezeka kutoka 98,300 mwaka 2015 hadi kufikia takriban 124,000 hivi sasa. Hii imewezekana baada ya Serikali kuongeza bajeti ya mikopo kutoka shilingi bilion 373 hadi kufikia shilingi bilion 483. Wanafunzi walimu wanaonufaika na mikopo ya elimu ya juu ni 22,867, ambapo mwaka huu Serikali itatumia shilingi billion 79.63 kuwagharamia. Na ninyi wenyewe ni mashahidi kuwa hivi sasa mikopo inatolewa kwa wakati; na hata rufaa za mikopo hivi sasa zinashughulikiwa mapema. Wito wangu kwa walimu wanaopata mikopo; wakimaliza, wakubali kufanya kazi kwenye vituo wanavyopangiwa.
Ndugu Wajumbe wa Mkutano;
Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;
Mbali na kupanua wigo na kuboresha sekta ya elimu, tunafanya jitihada za kuboresha maslahi na kushughulikia kero mbalimbali za walimu. Hivi punde mmemsikia Kaimu Katibu Mkuu wa CWT akiipongeza Serikali kwa jitihada inazofanya kuboresha maslahi ya walimu na kushughulikia kero mbalimbali zinazowakabili. Mathalan, ameipongeza Serikali kwa kutoa Waraka wa Muundo Mpya wa Watumishi wa Walimu; Upandishwaji madaraja ya Walimu; uanzishaji wa Tume ya Utumishi wa Walimu, n.k.
Lakini, licha ya hatua hizo, Serikali pia imefanya mambo mengine mengi ya kuboresha maslahi na kushughulikia kero za walimu. Mathalan, awali nilieleza kuwa Serikali iliongeza kiwango cha ruzuku inayopelekwa kwenye shule kutoka shilingi bilioni 18.77 hadi shilingi bilioni 23.868 kwa mwezi. Kiasi kilichoongezeka ni mahususi kwa ajili ya kutoa posho za madaraka kwa Wakuu wa Shule na Waratibu wa Elimu Kata. Tangu utaratibu huu uanze tayari tumetoa shilingi bilioni 86.56. Niwaombe watu wanaopewa, posho hizo ziwaongezee motisha ya kufanya kazi kwa maslahi ya Taifa. Aidha, naziagiza mamlaka za uteuzi kutoa vyeo kwa watu wenye sifa na wenye kustahili.
Sambamba na hilo la kutoa posho, tangu tumeingia madarakani, tumetoa kiasi cha shilingi bilioni 56.92 kulipia madeni ya walimu, ambapo kiasi cha shilingi bilioni 14.23 tumelipa madeni ya mshahara na shilingi bilioni 42.69 ni madeni yasiyo ya mshahara. Kadri tutakavyokamilisha uhakiki wa madeni, tutalipa madeni yote halali.
Mheshimiwa Kaimu Rais wa CWT,
NduguWajumbe wa Mkutano;
Licha ya jitihada mbalimbali zilizofanywa na Serikali katika kuimarisha sekta ya elimu na kuboresha maslahi ya walimu nchini, ni dhahiri kuwa sekta ya elimu na ninyi walimu wenyewe bado mnakabiliwa na matatizo kadhaa. Mathalan, tuna upungufu wa madarasa, vyoo, nyumba za walimu, madawati na maabara.
Sambamba na matatizo hayo, hivi punde, Kaimu Katibu Mkuu wa CWT, katika Risala yake, ameeleza matatizo na kero mbalimbali zenye kuwakabili walimu. Ametaja suala la upandishaji vyeo kwa wakati; suala la walimu waliopandishwa madaraja mwaka jana na kisha kusitishwa; malipo ya walimu wastaafu; suala la posho ya kufundishia (teaching allowance); upungufu wa walimu wa masomo ya sayansi; n.k. Amezungumzia pia hofu mliyonayo walimu kuhusu uwezekano wa kupungua kwa mafao ya kustaafu kufuatia uamuzi wa kuiunganisha mifuko ya hifadhi ya jamii ili ibaki miwili.
Kama nilivyotangulia kusema hapo awali, mimi ni mwalimu. Hivyo basi, hata kabla sijawa Rais, nilikuwa nikizifahamu shida na matatizo mbalimbali yanayowakabili walimu wa Tanzania. Na kama nilivyosema, Mke wangu, naye ni mwalimu; na amekuwa kila mara akinikumbusha kuhusu masuala ya walimu. Lakini, mbali na yeye, kwa bahati nzuri viongozi wengi niliowateua kushika nyadhifa mbalimbali ni walimu. Waziri Mkuu ni mwalimu. Mke wake ni mwalimu Hapa pia tunao Mawaziri Mhagama na Prof. Ndalichako, ambao wote ni walimu. Na wote hawa wamekuwa wakiwatetea sana. Lakini zaidi ya hapo, Makamu wa Rais, Mama Samia, naye ni mtetezi mkubwa sana wa walimu. Kwa hiyo, viongozi wote wamekuwa wakiwatetea sana ninyi walimu.
Na niseme tu kuwa, kutokana na kazi kubwa ambayo ninyi walimu mnayoifanya, ni haki yenu kutetewa na kwa kweli Serikali inao wajibu wa kuhakikisha inashughulikia shida na kero zenu. Mimi binafsi natamani sana; tena sana, kuona shida mbalimbali za walimu zinaisha kabisa. Hata haya, matatizo mliyonieleza leo ningetamani sana nitoe majibu yake yote hapa hapa ili yaweze kushughulikiwa mara moja. Lakini, hilo ni jambo lisilowezekana. Kama mnavyofahamu, uwezo wa Serikali bado mdogo na majukumu iliyonayo ni mengi. Mbali na kushughulikia sekta ya elimu, tunawajibika kushughulikia masuala ya afya, maji, umeme, barabara, ulinzi, n.k., ambayo yote haya ni muhimu kwa nchi, lakini pia ni muhimu hata kwenu ninyi walimu. Walimu mnahitaji huduma bora za afya, mnahitaji maji, umeme, barabara, ulinzi na usalama, n.k.
Kwa sababu hiyo, Serikali inawajibika kuhakikisha kuwa kidogo kinachopatikana, tunakigawa kwenye sekta zote muhimu. Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, alipata kusema, nanukuu, “Ndama hunyonya kiwango cha maziwa ambacho mama yake anacho”. Hivyo, nawasihi sana walimu wenzangu, kwa kile kidogo tunachokileta kwenu mkipokee na kuiona dhamira nzuri ya Serikali ya kushughulikia shida na kero zenu mbalimbali. Napenda tu niwahakikishie kuwa Serikali inatambua kero zenu zote na kadri uwezo wa Serikali kifedha utakavyokuwa ukiongezeka, tutaendelea sio tu kuboresha maslahi yenu bali sekta ya elimu kwa ujumla.
Mheshimiwa Kaimu Rais wa CWT,
Ndugu Wajumbe wa Mkutano huu;
Pamoja na maelezo hayo, napenda kutolea ufafanuzi baadhi ya hoja zilizotolewa na Kaimu Katibu Mkuu katika Risala yake. Moja ya hoja aliyoizungumza ni uhaba wa walimu wa sayansi nchini. Ni kweli kuwa tatizo hili lipo na limeongezeka baada ya Serikali kuanza kutoa elimu bila malipo, ambapo idadi ya wanafunzi kwenye shule zetu imeongezeka. Serikali inachukua hatua mbalimbali kushughulikia tatizo hili. Mwaka huu pekee tumeajiri walimu wa masomo ya sayansi na hisabati wapatao 3,462. Aidha, walimu wengine wapatao 15,135, wakiwemo wa sayansi, wanatarajiwa kuajiriwa wakati wowote baada ya vyeti vyao kuhakikiwa na kuthibitishwa uhalali wake.
Vilevile, tunaendelea kupanua wigo wa kuzalisha walimu. Mathalan, kati ya wanafunzi 22,867 wanaosomea ualimu niliowataja awali na ambao Serikali inawapa mikopo ya vyuo vikuu, wanafunzi 13,510 ni wa masomo ya sayansi na hesabu. Zaidi ya hapo, Serikali ipo katika ukarabati wa vyuo vyake takriban 20 na ujenzi wa vyuo 3. Ujenzi na ukarabati huu utakapokamilika, utaongeza idadi ya udahili wa wanafunzi wa ualimu kutoka 20,535 hadi kufikia wanafunzi takriban 30,000. Hatua hizi, bila shaka, zitapunguza tatizo la uhaba wa walimu.
Hata hivyo, nafahamu kuwa wakati mwingine, tatizo la uhaba wa walimu linatokana na mgawanyo usio linganifu. Shule nyingi za mijini zina walimu wengi kuliko mahitaji yake. Hivyo niziombe Mamlaka husika kuliangalia suala hili kwa umakini. Lakini huu usiwe mwanya wa kuwahamisha walimu bila kufuata utaratibu. Agizo langu kuhusu kutomhamisha mwalimu mpaka atakapolipwa stahiki zake liko pale pale. Lakini pia nitoe wito kwenu walimu; mkipangiwa kazi mahali, mkubali kwenda.
Suala jingine ambalo Kaimu Katibu Mkuu amelizungumzia ni hofu mliyonayo kuhusu uwezekano wa kupungua kwa malipo ya mkupuo baada ya kuunganisha mifuko ya hifadhi ya jamii. Hakuna kitakachopungua. Lengo la Serikali kuiunganisha mifuko ya jamii na kubakisha miwili ni kuongeza ufanisi na tija katika mifuko hiyo. Kama mnavyofahamu, kutokana na mifuko kuwa mingi, ililazimu kila mfuko kutumia fedha nyingi kutafuta wanachama. Jambo hili liliongeza gharama za uendeshaji kwenye mifuko hiyo na hivyo kusababisha mifuko hiyo kutoa mafao madogo ya kustaafu kwa wanachama wake. Sasa tumeamua kuwa na mifuko miwili tu; mmoja kwa ajili ya watumishi wa umma na mwingine sekta binafsi. Hii itasaidia sio tu kuondoa ushindani usio na tija, bali pia unatarajia kuiwezesha mifuko hii kutoa mafao mazuri zaidi kwa wanachama wake wanaostaafu. Hivyo basi, napenda kuwatoa hofu walimu wenzangu kwamba mafao hayatapungua. Lakini sambamba na hilo, sheria ya kuunganisha mifuko bado haijatungwa. Mswada umesomwa mara moja Bungeni. Na sasa maoni ya wadau mbalimbali yanaendelea kupokelewa. Hivyo, na ninyi CWT mnayo nafasi ya kuendelea kutoa maoni yenu ili kuboresha mswada huo.
Kuhusu suala la posho ya kufundishia (teaching allowance), mtakumbuka kuwa kwa mujibu wa Waraka wa Watumishi wa Serikali Na.1 wa mwaka 1996 kuhusu Mfumo, Miundo na Ngazi Mpya za Mishahara kwa Watumishi wa Serikali kuanzia tarehe 1 Julai, 1996 posho zote zilijumuishwa katika mishahara. Lengo lilikuwa kuboresha mishahara na mafao ya uzeeni ya Watumishi. Kufuatia utekelezaji wa Waraka huo, nyongeza halisi ya mshahara wa kima cha chini baada ya kujumuishwa posho katika mishahara ilikuwa ni asilimia 55.2; na nyongeza halisi ya kima cha juu baada ya kujumuishwa posho katika mshahara ilifikia asilimia 36.9. Hii ndio sababu posho ya kufundishia waliyokuwa wakipewa walimu, iliondolewa. Pamoja na maelezo hayo, natambua umuhimu wa posho hii. Hivyo, napenda kurudia tena kadri mama ndama atakapoongeza maziwa, tutaangalia uwezekano wa kurejesha posho hii ili kuwapa motisha walimu wetu. Hivyo, nawaomba Watanzania tuchape kazi kwa bidii ili kuongeza uwezo wetu kiuchumi.
Kuhusiana na suala la mafunzo kwa walimu, Serikali inafahamu umuhimu wa kuwapatia mafunzo endelevu ya mara kwa mara walimu wetu. Na kwa kweli tumekuwa tukifanya hivyo. Jumla ya walimu 5,920 wa masomo ya sayansi, hisabati na kiingereza wamepata mafunzo hivi karibuni. Na tutaendelea kutoa mafunzo hayo.
Mheshimiwa Kaimu Rais wa CWT,
Ndugu Wajumbe wa Mkutano huu;
Suala jingine ambalo ningependa nilizungumzie ni kuhusu madeni mbalimbali ya walimu. Serikali inatambua uwepo wa madeni hayo. Na tumekuwa tukiyalipa. Kama nilivyosema awali, tangu tumeingia madarakani tayari tumelipa madeni ya walimu yenye thamani ya shilingi bilioni 56.92. Lakini, madeni bado yapo. Hivi punde Kaimu Katibu Mkuu wenu ameeleza kuwa hivi sasa walimu wanaidai Serikali kiasi cha shilingi bilioni 25.6. Napenda, kwanza kabisa, kuwapongeza viongozi wa CWT kwa kuwa wakweli. Nakumbuka kuwa kuna wakati aliwahi kujitokeza mmoja wa viongozi wa CWT na kusema kuwa walimu wanaidai Serikali takriban shilingi trilioni 1.5. Hivyo, nawapongeza sana viongozi wa sasa wa CWT kwa kuwa wakweli. Na kwa kuwa mmeonesha uungwana na mmekuwa wakweli, napenda kuwahakikishia kuwa mara tu tutakapomaliza kuhakiki deni hili, tutawalipa mara moja.
Lakini pia ningependa kutumia fursa hii kueleza kuwa, Serikali imekuwa ikichelewa kulipa madeni yenu pamoja na ya watumishi wengine wa umma, kutokana na kuwepo kwa matatizo kadhaa, ikiwemo tatizo la watumishi hewa na wenye vyeti feki. Hii ndio sababu mwaka jana tuliamua kusitisha zoezi la upandishaji vyeo na madaraja kwa watumishi; na tukaanzisha zoezi la uhakiki kwa watumishi wote wa Serikali. Zoezi la uhakiki mpaka sasa limetuwezesha kubaini watumishi hewa wapatao 19,706, ambao walikuwa wakiigharimu Serikali kiasi cha shilingi bilioni 19.848 kwa mwezi, sawa na shilingi bilioni 238.17 kwa mwaka. Aidha, tumeweza kubaini watumishi wenye vyeti feki wapatao 12,000, wakiwemo walimu 3,655. Baada ya kukamilisha zoezi hili, Serikali mwezi Novemba 2017, imewapandishaji vyeo watumishi 59,967, wakiwemo walimu na ambao marekebisho ya mishahara yao itaanza kutolewa kuanzia mwezi huu. Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 159.33 kwenye bajeti ya mwaka huu kwa ajili ya marekebisho hayo ya mishahara.
Na kuhusu zoezi la uhakiki wa madeni, lenyewe bado linaendelea. Na kimsingi, zoezi hili ni endelevu. Hata hivyo, nawahakikishia kuwa kadri tutakavyokuwa tunakamilisha uhakiki wa madeni tunayodaiwa, tutayalipa. Wito wangu kwenu walimu wenzangu, endapo unafahamu kuwa katika madeni uliyowasilisha Serikalini kuna udanganyifu, ni vyema ujaze upya. Na niwaombe viongozi wa CWT kupitia tena madeni yote ya walimu ili kujiridhisha; na mkijiridhisha pelekeni madeni hayo kwa viongozi wa Wilaya na Mikoa, nao wakijiridhisha na kuweka saini zao; baada ya hapo madeni hayo yawasilishwe kwa Waziri Mkuu. Nawaahidi kuwa, Serikali ikijiridhisha kuwa madeni hayo ni sahihi, tutayalipa mara moja. Lakini nitoe onyo kwamba, endapo itatokea mtu ameidhinisha madeni yenye udanganyifu, naye tutawachukulia hatua.
Kuhusiana na hoja zenu nyingine mlizoziwasilisha, ikiwemo upandishaji wa vyeo kwa wakati; Serikali kutoa mikopo ya ujenzi wa nyumba isiyo na riba; uhaba wa vifaa vya kufundishia; kushirikishwa katika mabadiliko yoyote ya mitaala; masomo ya TEHAMA; Serikali imepokea hoja zenu zote na tutashirikiana nanyi katika kuzitafutia ufumbuzi. Nafahamu baadhi ni masuala ya kiutendaji tu na hayahitaji gharama yoyote; hivyo, naziagiza mamlaka husika kushughulikia kwa haraka. Na kwa yale yenye kuhitaji fedha, tutaendelea kuyashughulikia taratibu, kadri uwezo wa Serikali kifedha utakavyokuwa ukiimarika.
Waheshimiwa Viongozi;
Mheshimiwa Kaimu Rais wa CWT,
Ndugu Wajumbe wa Mkutano;
Jukumu langu leo ni kufungua tu Mkutano wenu. Lakini kabla sijatekeleza suala hili, ninalo suala moja la mwisho ambalo ningependa kulizungumza. Nafahamu kuwa, kwenye Mkutano huu, pamoja na mambo mengine, mtafanya uchaguzi wa Rais wa CWT kuziba nafasi iliyoachwa wazi na Rais wenu Mstaafu, Mwalimu Gratian Mukoba. Napenda kutumia fursa hii kuwasihi sana walimu wenzangu, kuchagua kwa umakini mkubwa. Chagueni mtu atakayeshughulikia masuala yenu. Na kamwe msichague mtu mwenye nia ya kuitumia CWT kutekeleza maslahi yake binafsi.
Sio siri kuwa kuna wakati mliwachagua watu ili wawaongoze na kuwatumikia, lakini hawakufaya hivyo. Badala yake, walitumia Chama hiki kutekeleza maslahi yao binafsi. Na walitumia Chama chenu kujinufaisha. Niwaulize walimu wenzangu, hivi mnafahamu fedha za michango mnazokatwa kila mwezi zinatumikaje? Au mmeshawahi kujiuliza kuhusu utendaji kazi wa Benki yenu na ni namna gani inawanufaisha? Sina hakika kama mnafahamu. Lakini niwaambie, kwa taarifa nilizonazo, Benki yenu haifanyi vizuri, na ni miongoni mwa Benki ambazo wakati wowote inaweza kufungwa. Nakumbuka wakati fulani nilialikwa kwenda kuizindua lakini sikwenda, baada ya kujiridhisha kuwa Benki hiyo haifanyi vizuri na haipo kwa maslahi ya walimu. Ni watu wachache tu ndio wananufaika nayo. Hivyo basi, nawasihi tena walimu wenzangu, katika uchaguzi huu, msichague watu wenye nia ya kujinufaisha kupitia CWT.
Lakini zaidi ya hapo, msiwachague watoa rushwa. Rushwa ni ugonjwa. Ni kansa. Ukimchagua mtoa rushwa hutoweza kamwe kumuuliza michango yenu ya kila mwezi inatumikaje; na utashindwa kumuuliza manufaa yaliyopatikana kwenye Benki yenu. Hivyo basi, narudia tena kuwasihi walimu wenzangu katika uchaguzi huu chagueni vizuri. Chagueni watu watakaowatetea na kuwasemea matatizo yenu. Na kamwe msimchague mtu ambaye lengo lake ni kuigombanisha CWT na Serikali. Mapambano mara nyingi hayajengi. Na niwashauri walimu wenzangu, wakati mwingine, mkitaka kufanikisha jambo, tumieni ule usemi usemao, “If you want to win an enemy, join him and work with him…” Siwapigii kampeni; lakini kwa dhati kabisa nawapongeza viongozi wa sasa wa CWT kwa kuonesha nia ya kweli ya kuwatetea na kushughulia shida za walimu. Wameonesha kuwa wapo tofauti na wapo tayari kufanya kazi na Serikali. Huo ndio unapaswa kuwa muelekeo wa CWT hivi sasa. Mimi naamini kuwa kama Serikali na CWT tukiwa kitu kimoja tutaweza kushughulikia matatizo mengi yanayowakabili walimu tena kwa haraka.
Mheshimiwa Kaimu Rais wa CWT,
Waheshimiwa Viongozi mliopo;
Ndugu Wajumbe wa Mkutano;
Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;
Napenda kuhitimisha hotuba yangu kwa kuushukuru tena uongozi wa CWT kwa kunikaribisha kufungua Mkutano huu. Aidha, kwa namna ya pekee, naushukuru uongozi wa Chuo Kikuu cha Dodoma kwa kukubali kuwa wenyeji wa Mkutano huu. Tunawashukuru sana na tunawashukuru pia walimu wanafunzi wa Chuo hiki kwa kujitokeza kwenu kwa wingi kwenye ufunguzi wa Mkutano wa CWT.
Halikadhalika, nawashukuru viongozi wa vyama vya wafanyakazi kwa kuhudhuria kwenye Mkutano huu. Na vilevile, nawashukuru wageni wote waalikwa kutoka ndani na nje kwa kuamua kutenga muda wenu kuja kushiriki kwenye Mkutano huu. Mwisho lakini sio kwa umuhimu, wajumbe wa Mkutano huu, na nawaomba mfikishe salamu kwa walimu wote nchini kuwa Serikali ipo pamoja nao.
Baada ya kusema hayo, sasa natamka rasmi kuwa nimeufungua Mkutano Mkuu Maalum wa Taifa wa CWT. Nawatakia Mkutano mwema.
Mungu Ibariki CWT!
Mungu Wabariki Walimu Wote!
Mungu Ibariki Tanzania!
“Ahsanteni sana kwa kunisikiliza”
- Dec 13, 2017
HOTUBA YA MHE. DKT. JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, KWENYE UFUNGUZI WA TAWI JIPYA LA BENKI YA CRDB DODOMA, TAREHE 13 DESEMB...
Soma zaidiHotuba
Mheshimiwa Job Ndugai, Spika wa Bunge
la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango, Waziri wa Fedha na Mipango;
Mheshimiwa Dkt. Binilith Mahenge, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma;
Mheshimiwa Tulia Ackson, Naibu Spika wa
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Mheshimiwa John Malecela, Waziri Mkuu
Mstaafu wa Tanzania;
Ndugu Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania;
Ndugu Ally Hussein Laay, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi
wa Benki ya CRDB;
Dkt. Charles Kimei, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB;
Waheshimiwa Viongozi mbalimbali mliopo hapa;
Waheshimiwa Wazee wa Mkoa wa Dodoma;
Wageni Waalikwa wote, Mabibi na Mabwana:
Awali ya yote, napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu, Muumba wetu kwa kutupa afya njema na kutuwezesha kukutana hapa leo. Napenda pia, kwa namna ya pekee kabisa, kuushukuru uongozi wa Wizara ya Fedha na Mipango pamoja na Benki ya CRDB kwa kuniliaka kushiriki kwenye tukio hili la kuzindua Tawi la Benki yenu hapa Dodoma.
Napenda kukiri kuwa nimefurahi sana kushiriki kwenye hafla hii. Nimefurahi kwa sababu kwanza mimi ni mteja wa Benki ya CRDB kwa muda mrefu; tangu nikiwa Mwanafunzi wa Chuo Kikuu. Zaidi ya hapo, hapa Dodoma ndio Makao Makuu ya nchi yetu. Ni hivi karibuni tu tumefanya maamuzi makubwa ya kuhakikisha Serikali yote inahamia Dodoma ifikapo mwaka 2020. Kama mnavyofahamu, Waziri Mkuu pamoja na Viongozi na Watendaji wa Wizara tayari wamehamia. Aidha, Makamu wa Rais naye anatarajiwa kuhamia mwezi huu; na mimi nitahamia mwakani.
Ni dhahiri kuwa, kutokana na uamuzi huu wa kuhamia Dodoma, idadi ya watu katika Mji huu hapa itaongezeka sana. Na huduma za taasisi kama za benki zitahitajika zaidi. Hivyo basi, napenda kutumia fursa hii kuushukuru na kuupongeza uongozi wa Benki hii kwa uamuzi wenu wa kufungua Tawi hili hapa Dodoma. Kwa kufungua Tawi hili, mmeunga mkono uamuzi wa Serikali wa kuhamia Dodoma. Ahsanteni sana.
Waheshimiwa Viongozi;
Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;
Sekta ya benki ni muhimu sana katika maendeleo ya nchi. Ni muhimu kwanza kabisa katika ukuzaji uchumi. Sekta ya benki inatoa mchango mkubwa katika pato la taifa. Mathalan, mwaka 2014, sekta hii ilichangia asilimia 3.4 ya pato la taifa; mwaka 2015 na mwaka jana 2016 ilichangia asilimia 3.6. Aidha, benki zinachangia ukuaji uchumi kupitia ulipaji wa kodi kwa Serikali. Hivi punde mmetoka kumsikia Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB, Dkt. Kimei, akisema kuwa katika kipindi cha miaka 10 iliyopita Benki yake imelipa kodi zaidi ya shilingi bilioni 800 na hivyo kuiwezesha kushinda tuzo ya kuwa mlipaji kodi bora mara kadhaa. Hongereni sana CRDB.
Lakini mbali na kukuza uchumi, sekta ya benki ni muhimu katika kupiga vita umaskini. Benki zinashiriki katika kupiga vita umaskini, kupitia kwanza mikopo inayoitoa kwa wananchi, hususan wafanyabiashara na wajasiliamali wadogo kama vile machinga na mama lishe. Pili, zinachangia kupiga vita umaskini kwa namna inavyoshiriki katika kukuza sekta nyingine. Kama mnavyofahamu, sekta ya benki ni muhimu sekta nyingine zote. Iwe viwanda, kilimo, uvuvi, ufugaji, ujenzi, biashara, usafirishaji; na hata sekta za huduma kama afya, elimu, maji, n.k. Kwa mfano, benki ikitoa mkopo wa mtaji wa kujenga kiwanda; kupitia mkopo huo, wananchi watapata ajira wakati wa ujenzi na baada ya kiwanda kukamilika. Fikiria pia benki ikitoa mkopo kwa ajili ya ujenzi wa barabara; wakati wa ujenzi wa barabara hiyo wananchi wanapata ajira, lakini pia ikikamilika itapunguza gharama na usafiri kwa wananchi, na hivyo kusaidia kupunguza umaskini.
Sambamba na hayo, sekta ya benki ni umuhimu kwa vile inatoa ajira za moja kwa moja. Mathalan, nimeambiwa kuwa Benki hii imetoa ajira kwa Watanzania wapatao 3,200. Lakini pia sekta ya benki ni muhimu kwa vile inawasaidia wananchi kutunza amana (fedha) kwa usalama, na wakati wowote wakihitaji, wanapewa. Tena kwa siku hizi, kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia, hata ukihitaji fedha zako usiku wa manane unazipata kwa njia ya ATMs au Simu kiganjani.
Waheshimiwa Viongozi;
Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;
Kwa kuzingatia hayo yote, ni dhahiri kuwa sekta ya benki ni muhimu kwa maendeleo ya Taifa lolote. Na kwa sababu hiyo, inatia moyo kuona kuwa kwa takriban miongo mitatu iliyopita, sekta ya benki imezidi kuimarika hapa nchini. Mathalan, mwaka 1990, nchi yetu ilikuwa na benki 3 tu, lakini kwa sasa nchi yetu ina zaidi ya benki 58. Na jambo la kufurahisha zaidi ni kwamba miongoni mwa benki zinazofanya vizuri ni Benki hii ya CRDB, ambayo kwa takriban asilimia 86 zinamilikiwa na Watanzania (asilimia 40 watu binafsi, asilimia 21 Serikali na mifuko ya pensheni ina asilimia 15).
Hivi punde, Mkurugenzi Mtendaji Dkt. Kimei, ameeleza mafanikio ambayo Benki hii imepata tangu kuanzishwa kwake mwaka 1996. Baadhi ya mafanikio aliyoyataja ni kuongezeka kwa rasilimali zake kutoka thamani ya shilingi bilioni 54 hadi kufikia shilingi trilioni 5.5; kupanua wigo wa benki kutoka matawi 19 hadi 260, ukiachilia mbali ATMs 600 ilizonazo, Mawakala 3,000, SACCOS shirikishi 455 na matawi ya kutembea 21. Benki pia imetoa mikopo yenye thamani ya shilingi trilioni 3.5; ambapo shilingi trilioni 1 zimekwenda kwenye sekta mbili za kilimo na viwanda. Aidha, kama nilivyosema awali, benki imelipa kodi ya shilingi bilioni 800 na kutoa ajira 3,200 kwa Watanzania. Vilevile, mwaka huu, baada ya kuwabana sana hatimaye wametoa gawio la shilingi bilioni 19 kwa Serikali. Na natumaini wataendelea kutupa gawio letu kila mwaka. Hivyo basi, napenda kutumia fursa hii, kwa dhati kabisa, kutoa pongezi nyingi sana kwa Benki hii chini ya Dkt. Kimei kwa kazi kubwa inazofanya kwa ajili ya kukuza uchumi lakini pia kupiga vita umaskini katika nchi yetu.
Mtakumbuka kuwa Benki hii kihistoria ilikuwa ikimilikiwa kwa asilimia 100 na Serikali, wakati huo ikijulikana kama Tanzania Rural Development Bank (TRDB). Mwaka 1996 ilibinafsishwa ili kuongeza ufanisi wake. Kwa mfano mzuri uliooneshwa na Benki hii, ni dhahiri kuwa kama mashirika na taasisi zote zilizobinafsishwa zingefanya kazi kama Benki hii, nchi yetu ingekuwa imepiga hatua kubwa za kimaendeleo. Lakini mashirika na viwanda vingi vilivyobinafsishwa, hivi sasa havifanyi kazi.
Waheshimiwa Viongozi;
Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;
Jukumu langu leo ni kufungua benki hii. Hata hivyo, kabla sijatekeleza jukumu hilo, ninayo masuala machache ya kueleza. Suala la kwanza kabisa, ni malalamiko kuhusu kupungua kwa kasi ya ukuaji wa mikopo kwa sekta binafsi. Serikali inalitambua suala hili, na kupitia Benki Kuu, imechukua hatua mbalimbali kulishughulikia. Mathalan, Mwezi Aprili, mwaka huu tuliamua kupunguza kiwango cha kisheria cha sehemu ya amana inayotakiwa kuwekwa benki kuu na benki za Biashara kutoka asilimia 10 hadi asilimia 8. Sambamba na hilo, tumeshusha riba ya Benki Kuu (discount rate) mara mbili kutoka asilimia 16 hadi 12 mwezi Machi 2017, na mwezi Agosti tukaishusha tena hadi asilimia 9. Pamoja na hayo, tumetoa mikopo maalum kwa benki za biashara na halikadhalika Benki Kuu inanunua fedha za kigeni kwenye soko la jumla la benki ili kuongeza ukwasi wa shilingi kwenye uchumi. Hatua nyingine tulizochukua ni kuendelea mazingira ya biashara na uwekezaji ili kuongeza chachu katika shughuli za uchumi.
Kutokana na hatua hizi, hali ya ukwasi imeanza kuimarika na kusaidia kupunguza riba katika soko la fedha baina ya benki (IBCM rate) kutoka asilimia 13.69 mwezi Desemba 2016 hadi asilimia 3.29 mwezi Novemba 2017. Aidha, riba katika soko la dhamana za Serikali zimepungua kutoka wastani wa asilimia 15.12 mwezi Desemba 2016 hadi asilimia 8.76 mwezi Novemba 2017. Kwa matokeo haya, tuna matumaini makubwa kuwa kasi ya ukuaji wa mikopo kwa sekta binafsi utazidi kuimarika katika siku za hivi karibuni.
Suala jingine ambalo ningependa kuzungumzia ni kuhusu benki kushiriki kwenye shughuli za maendeleo. Kama nilivyosema hapo awali, sekta ya benki ni muhimu kwenye sekta zote, ikiwemo viwanda na kilimo. Hivyo basi, napenda kutoa wito kwa benki zote nchini kuangalia wa kutenga fedha nyingi za mikopo kwenye sekta hizi mbili. Kama mnavyofahamu, nchi yetu kwa sasa imedhamiria kujenga uchumi wa viwanda; na miongoni mwa viwanda tunavyolenga kuvijenga ni vile vinavyotumia zaidi malighafi za hapa nchini, hususan mazao ya kilimo. Hivyo basi, naziomba benki kuunga mkono dhamira hiyo ya Serikali. Nimefurahi kusikia kuwa ninyi CRDB mmekuwa mkitenga asilimia 15 kwa ajili ya sekta ya viwanda, na mwakani mmepanga kuongeza hadi kufikia asilimia 20, sawa na shilingi bilioni 700. Hongereni sana. Na naziomba benki nyingine ziige mfano wenu.
Napenda pia kuzungumzia kidogo suala la benki kupanua wigo wa mtandao wenu. Ni kweli kuwa idadi ya benki imeongezeka hapa nchini. Lakini kwa bahati mbaya, benki nyingi zipo Dar es Salaam na kwenye baadhi ya miji mikuu ya mikoa na wilaya. Mathalan kwa taarifa za mwaka 2015 asilimia 36.3 ya matawi yote ya Benki yalikuwa Dar es Salaam asalimia 7.1 Arusha, asilimia 6.5 Mwanza, asilimia 5.4 Mbeya na asilimia 4.6 Moshi. Ni benki chache tu ndizo zina matawi kwenye vijijini. Hivyo, natoa wito kwenu kusambaza huduma zenu hadi vijijini, ambako Watanzania wengi wanaishi. Na ninaposema kusambaza huduma hadi vijijini simaanishi kwamba lazima mjenge majengo, ninachomaanisha ni kwenu ninyi kubuni njia mbalimbali za kufikisha huduma za kibenki kwa wananchi waliopo vijijini, ikiwemo kuanzisha matawi mengi zaidi ya kutembea, kuingia ubia na mawakala (Bank Agents), kuanzisha huduma za kifedha za kwa njia za mtandao (Sim Banking, Internet Baking n.k.) kama ambavyo ninyi CRDB na baadhi ya Benki nyingi mmeanza kufanya.
Nina imani mkiweza kufikisha huduma zenu hadi vijijini, sio tu mtawasaidia wananchi kupata huduma za kibenki bali pia itawaongezea benki nchini ukwasi wa kutosha. Kwa mujibu wa taarifa ya Benki Kuu ya Tanzania ya mwaka 2015, ukwasi wa benki zote nchini mwaka 2014 ulikuwa una thamani ya shilingi trilioni 22.5. Kiasi hiki bado ni kidogo sana ukilinganisha na mahitaji makubwa ya fedha (mikopo) yaliyopo hapa nchini. Mathalan, Mpango wetu wa Taifa wa Maendeleo wa miaka mitano, ambao tumeanza kuutekeleza katika mwaka wa fedha 2016/2017 unahitaji kiasi cha shilingi trilioni 107. Hivyo, nawahimiza benki kusambaza huduma zenu kwenye maeneo ya vijijini ili muweze kuongeza ukwasi katika benki zenu. Aidha, nawakaribisha wawekezaji wengine kuja kuwekeza kwenye sekta hii ya benki hapa nchini.
Jambo jingine ambalo ningependa kuzungumzia ni kuhusu tatizo la riba za mikopo kuendelea kuwa juu. Riba za mikopo hapa nchini bado zipo juu. Natambua kuwa tatizo hili linasababishwa na mambo mengi, ikiwemo kutokuwepo kwa taarifa za kutosha za wakopaji, wasiwasi wa benki kutolipwa na wakopaji na hivyo kuongeza gharama za ufuatiliaji, n.k. Pamoja na matatizo hayo, Serikali imechukua hatua mbalimbali, ambazo binafsi nilidhani zingeweza kushusha kiwango cha riba nchini ili kuwawezesha wananchi, hususan wa kipato cha chini kuchukua mikopo. Mojawapo ya hatua hizo ni kuanzisha Mfumo wa Kuhifadhi Taarifa za Wakopaji ( yaani Credit Reference Bureau) ambao unaziwezesha benki zote kuwatambua wakopaji na kuweza kuchukua tahadhari stahiki. Aidha, tunaendelea kutoa vitambulisho vya taifa ambavyo kwa sasa vina taarifa nyingi. Hivyo, basi naziomba benki kuanza kupunguza viwango vya riba. Aidha, naihimiza Benki Kuu kukamilisha zoezi la kutangaza Sera ya Riba (Policy Rate), ambayo itazifanya taasisi za kifedha kuwa na riba zinazowiana na sera hiyo. Vilevile, napenda kutumia fursa hii kuwahimiza wananchi kuwa na utamaduni wa kurejesha mikopo. Dawa ya deni ni kulipa. Na niiombe Mahakama ya Biashara kuharakisha kesi zinazohusiana na madeni ya mikopo.
Mbali na hayo, napenda kutoa wito kwa Wizara ya Fedha na Benki ya Kuu kudhibiti matumizi ya ya fedha za kigeni (Dola) nchini. Na jambo hili, liende sawia na kuongeza usimamizi kwa Maduka ya Kubadilisha Fedha (Bureau De Change). Ni lazima tuondokane na utaratibu wa matumizi holela ya fedha za kigeni nchini; lakini pia Maduka ya Kubadilisha Fedha yasitumike kuwa sehemu za kutakatisha fedha zisizo halali kutoka nje. Aidha, natoa wito kwa Benki Kuu kuongeza usimamizi katika uanzishaji na uendeshaji wa shughuli za Kibenki hapa nchini. Kabla Benki haijaanzishwa wamiliki wake wafuatiliwe kwa makini; na halikadhalika, benki inayoshindwa kujiendesha ifutwe hata kama ni ya Serikali.
Sambamba na hayo, mtakumbuka kuwa mwezi Juni mwaka huu, nikiwa pale Kijitonyama kuzindua Kituo cha Data na Mfumo wa Ukusanyaji Mapato kwa njia ya Kielektroniki, niliagiza kuwa benki zijiunge na Mfumo huo wa kukusanya mapato kwa njia ya kielektroniki. Na nakumbuka Kamishna wa TRA aliahidi kuwa hadi mwezi Desemba makampuni yote ya benki na simu yatakuwa yamejiunga. Hivi sasa tupo katikati ya mwezi Desemba, lakini kwa taarifa nilizonazo ni benki chache tu ndizo tayari zimejiunga na mfumo huo. Benki nyingi pamoja na baadhi ya Makampuni ya Simu bado hazijajiunga na mfumo huo. Napenda kurudia tena agizo langu kwa benki na kampuni zote za simu kuhakikisha zinajiunga na mfumo huo kabla ya mwaka huu kwisha. Kwa kampuni ya simu au benki itakayoshindwa kutekeleza agizo hili, taratibu husika zifanyike, ikiwezekana makampuni au benki hizo zifungiwe kufanya kazi nchini.
Jambo la mwisho ambalo ningependa kulisema ni kutoa wito kwa Watanzania wote kutumia huduma za kibenki hususan kwa kufungua akaunti za benki. Mbali na usalama, benki inasaidia mtu kupanga matumizi yake vizuri. Unakuwa huwezi kutumia fedha ovyo. Lakini, nawasihi na nanyi wamiliki wa Benki kuimarisha mifumo yenu ya usalama ili kukabiliana na vitendo vya wizi kwa njia za mtandao. Aidha, wachukulieni hatua watumishi wenu ambao sio waaminifu.
Waheshimiwa Viongozi;
Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;
Napenda kuhitimisha hotuba yangu kwa kuushukuru tena uongozi wa CRDB kwa kunikaribisha na kwa zawadi ya hundi ya kiasi cha shilingi milioni 100 mliyonikabidhi. Hundi hii mmenikabidhi hadharani. Hivyo basi, na mimi naikabidhi kwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma ili fedha hizo zikatumike kwa ya kujenga Wodi katika Hospitali ya Mkoa. Siku moja nitakuja kuikagua hiyo wodi.
Mwisho kabisa lakini sio kwa umuhimu napenda kuwapongeza LAPF kwa kujenga jengo hili hapa Dodoma. Jengo ni zuri sana.
Baada ya kusema hayo, sasa nipo tayari kutekeleza jukumu lililonileta la kufungua Tawi la Sita la Benki ya CRDB hapa Dodoma.
Mungu Ibariki CRDB!
Mungu zibariki Benki zote nchini!
Mungu wabariki wana-Dodoma!
Mungu Ibariki Tanzania!
“Ahsanteni sana kwa kunisikiliza”
- Dec 09, 2017
HOTUBA YA MHESHIMIWA DKT. JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, KWENYE SHEREHE ZA MIAKA 56 YA UHURU WA TANZANIA BARA, DODOMA, TA...
Soma zaidiHotuba
Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi;
Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Mheshimiwa Kassim Majaliwa, Waziri Mkuu
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Mheshimiwa Balozi Seif Ali Iddi, Makamu wa Pili
wa Rais wa Zanzibar;
Mheshimiwa Job Ndugai, Spika wa Bunge
la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Mheshimiwa Zubeir Ali Maulid, Spika wa Baraza la Wawakilishi;
Mheshimiwa Prof. Ibrahim Juma, Jaji Mkuu wa Tanzania;
Mheshimiwa Omar Othman Makungu, Jaji Mkuu wa Zanzibar;
Waheshimiwa Marais Wastaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mzee Mwinyi, Mzee Mkapa na Mzee Kikwete;
Waheshimiwa Viongozi Wakuu Wastaafu wa Serikali zetu mbili mliopo, Mzee Bilal, Mzee Malecela, Mzee Kificho;
Waheshimiwa Wake wa Viongozi Wakuu mliopo, mkiongozwa na Mama Maria Nyerere na Mama Fatuma Karume;
Waheshimiwa Mawaziri mliopo;
Mheshimiwa Dkt. Binilith Mahenge, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma;
Mheshimiwa Balozi John Kijazi, Katibu Mkuu Kiongozi;
Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama;
Waheshimiwa Wabunge;
Waheshimiwa Mabalozi na Viongozi wa Taasisi za Kimataifa;
Waheshimiwa Viongozi wa Vyama vya Siasa na Dini mliopo;
Wageni waalikwa wote;
Wananchi Wenzangu, Mabibi na Mabwana:
Kabla ya kuanza hotuba yangu, naomba sote tusimame kwa dakika moja kuwaombea mashujaa wetu, askari 14, waliouawa wakiwa katika jukumu la kulinda amani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) juzi. Tunamwomba Mwenyezi Mungu aziweke roho za marehemu mashujaa wetu mahali pema peponi na kuwaponya askari waliojeruhiwa. Amina.
Baada ya utangulizi huo, napenda nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, Muumba wetu, kwa kutujalia uzima na kutuwezesha kuiona siku hii adhimu kwenye historia ya nchi yetu. Siku kama ya leo ya Jumamosi, tarehe 9 Desemba mwaka 1961, Jamhuri ya Tanganyika, hivi sasa Tanzania Bara, ilipata Uhuru wake. Uhuru huu ulihitimisha utawala wa kikoloni uliodumu nchini kwa takriban miaka 76; ikijumuisha miaka 33 ya Utawala wa Ujerumani na miaka mingine 43 ya Utawala wa Uingereza.
Kama mnavyofahamu, harakati za kutafuta Uhuru wa nchi yetu ziliongozwa na Chama cha Tanganyika African National Union (TANU), ambacho mwaka 1977 kiliungana na Chama cha Afro Shiraz (ASP), ambacho kiliongoza mapinduzi matukufu ya Zanzibar ya mwaka 1964, na kuunda Chama Cha Mapinduzi (CCM), Chama Tawala. Hii ndiyo historia yenyewe. Haiwezi kubadilika. Uhuru wa nchi yetu uliletwa na Vyama Mama vya CCM, yaani TANU na ASP. Hivyo basi, leo tunaposheherekea Miaka 56 ya Uhuru wa Tanganyika (Tanzania Bara), hatuna budi kuwashukuru na kuwapongeza Wazee wetu 17, ambao mwezi Julai 1954, wakiongozwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, walianzisha Chama cha TANU. Tunawakumbuka pia wananchi wote, ambao kabla na wakati wa Chama cha TANU, walishiriki katika harakati za kutafuta uhuru wa nchi yetu. Nafahamu wengi wao tayari wametangulia mbele za haki; hivyo, kwa niaba ya Watanzania wote, namwomba Mwenyezi Mungu azipumzishe roho zao mahali pema peponi. Amina!
Ndugu wananchi,
Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana:
Ni ukweli usiopingika kuwa, katika kipindi cha Miaka 56 ya Uhuru wa nchi yetu, tumepata mafanikio makubwa. Ndio! tumepata mafanikio makubwa, tena sana tu. Nafahamu wapo watu ambao wakisikia kauli hiyo huwa wanaumia; lakini huo ndio ukweli. Nchi yetu imepiga hatua kubwa za maendeleo tangu kupata Uhuru. Naomba nitoe mifano michache. Wakati tunapata Uhuru, baada ya utawala wa takriban miaka 76 ya Kikoloni, nchi yetu ilikuwa na mtandao wa barabara wenye urefu kilometa 33,600. Kati ya barabara hizo ni kilometa 1,360 tu ndio zilikuwa na lami. Kwa sasa tuna mtandao barabara wenye kilomita 122,500, ambapo kilometa 80,000 zipo chini ya TAMISEMI na zinahudumiwa na TARURA; kilometa 36,000 zipo chini ya TANROADS, na kilometa 6,500 zipo chini ya Hifadhi za Wanyama za Taifa (TANAPA). Aidha kati ya Mtandao huo wa barabara, kilometa 12,679.55, ni za lami. Sambamba na hayo, kuna jumla ya kilometa 2,480 zinazoendelea kujengwa kwa kiwango cha lami na barabara nyingine zenye urefu wa kilometa 7,087 zipo kwenye hatua mbalimbali za maandalizi kwa ajili ya kujengwa kwa kiwango cha lami. Vilevile, tumejenga madaraja makubwa 17, na mengine 14 yapo kwenye hatua mbalimbali.
Ukiachilia mbali ujenzi wa barabara, wakati tunapata Uhuru, nchi yetu ilikuwa na vituo vya kutolea huduma za afya 1,095 (hospitali 98, vituo vya afya 22 na zahanati 975), leo hii tuna vituo 7,293 (hospitali 178, vituo vya afya 795 na zahanati 6,285). Wakati tunapata Uhuru tulikuwa na Shule za Msingi 3,100 hivi sasa zipo 17,379; shule za sekondari zilikuwa 41 hivi sasa zipo 4,817; na tulikuwa na Chuo Kikuu kimoja tu, lakini leo vipo 48. Madaktari waliosajiliwa walikuwa 403, ambapo kati yao Watanganyika walikuwa 12 tu, leo tuna madaktari 9,343. Mwaka 1961, Wahandisi wazalendo walikuwa wawili (2) tu; lakini hadi kufikia mwezi Juni 2017 nchi yetu imefikisha wahandisi 19,164. Makandarasi nao walikuwa wawili tu (2), lakini hivi sasa wakandarasi waliosajaliwa wamefikia 9,350. Halikadhalika, wakati tunapata Uhuru, wastani wa umri wa mtu kuishi ulikuwa miaka 37, leo hii wastani ni miaka 61. Mifano ipo mingi. Siwezi kuitaja yote leo.
Itoshe tu kusema kuwa katika kipindi cha miaka 56 ya uhuru wetu, tumepiga hatua kubwa za kimaendeleo kwenye nyanja mbalimbali, ikiwemo huduma za jamii, ulinzi, umeme, kilimo, utalii, biashara, mifugo, uvuvi, demokrasia, diplomasia, utamaduni, n.k. Zaidi ya hapo, na pegine kubwa zaidi ni kwamba, katika kipindi cha miaka 56 ya Uhuru, tumeweza kulinda na kudumisha amani, umoja na Muungano wetu.
Hivyo basi, napenda kutumia fursa hii, kuwashukuru na kuwapongeza kwa dhati kabisa Viongozi wa Awamu zote za Serikali zetu mbili, ya Muungano na ya Zanzibar, kwa mafanikio makubwa yaliyopatikana katika kipindi cha miaka 56 ya Uhuru wa nchi yetu. Na nimefarijika sana kuona kuwa viongozi wastaafu wa nchi yetu, Mzee Mwinyi, Mzee Mkapa, Mzee Kikwete, Mzee Bilal, Mzee Malecela tunao hapa. Na niwaambie ndugu zangu Watanzania kuwa mambo kama haya ya kuwaona viongozi wastaafu wakishiriki kwenye tukio kama hili kwa pamoja ni nadra sana Duniani. Sio kwenye nchi zote jambo kama hili linawezekana. Kwenye nchi nyingine haiwezekani. Hivyo basi, nawasihi Watanzania wenzangu tuzidi kudumisha amani na umoja wetu. Na mimi namuomba Mwenyezi Mungu siku moja niweze kuhudhuria tukio kama hili nikiwa nimeungana na viongozi wengine wastaafu.
Lakini mbali na kuwapongeza viongozi wastaafu kwa mafanikio yaliyopatikana, napenda kuwapongeza Watanzania wote: wakulima, wafanyakazi, wavuvi, wafugaji, wafanyabiashara, wasanii, n.k.; kwa michango yenu ya hali na mali iliyowezesha kupatikana mafanikio niliyoyataja na mengine ambayo sikuyataja. Bila ya ninyi kujitoa, mafanikio haya kamwe yasingepatikana. Navipongeza pia vyombo vyetu vya ulinzi na usalama (JWTZ, Polisi, Usalama wa Taifa, Magereza, Uhamiaji, Zimamoto, n.k.), kwa kushiriki kikamilifu na kufanikisha kupatikana kwa mafanikio haya. Napenda kuwahakikishia vyombo vyote vya ulinzi kuwa Serikali yenu ipo pamoja nanyi na tutaendelea kushughulikia changamoto mbalimbali zinawakabili.
Ndugu wananchi,
Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana:
Sherehe za Uhuru wa Tanzania Bara mwaka huu zinafanyika hapa Dodoma. Hapa Dodoma ndio Makao Makuu ya Nchi yetu. Na zitaendelea kufanyika hapa. Napenda niwahakikishie ndugu Watanzania kuwa Serikali ya Awamu ya Tano itaendeleza mambo yote mazuri yaliyopatikana, na kutekeleza mambo mengine mapya kwa lengo la kuhakikisha kuwa Watanzania wote wanafaidi matunda ya uhuru.
Ombi langu kwa Watanzania endeleeni kuziamini Serikali zetu mbili, za Muungano na ya Zanzibar. Mimi na mwenzangu Dkt. Shein, tunaahidi kuwa tutasimamia na kutekeleza mambo yote tuliyowaahidi, ikiwemo ahadi zilizomo kwenye Ilani yetu ya Uchaguzi. Na kutekeleza hayo, hatutambagua mtu kwa misingi ya dini, kabila, itikadi ya kisiasa, jinsia au rangi. Daima tutakuwa watumishi wenu.
Ndugu wananchi,
Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana:
Leo wakati tunaadhimisha Sherehe za Miaka 56 ya Uhuru wa Tanzania Bara, napenda kuwakumbusha Watanzania wenzangu kuwa Ibara ya 45 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatoa mamlaka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutoa msamaha kwa wafungwa wa makosa mbalimbali. Kwa faida ya hadhira hii, napenda kuinukuu Ibara hiyo, kama ifutavyo:
45 (1) bila kuathiri masharti mengineyo yaliyomo katika Ibara hii, Rais anaweza kutenda lolote kati ya mambo yafuatayo:-
(a) kutoa msamaha kwa mtu yeyote aliyepatikana na hatia mbele ya mahakama kwa kosa lolote, na aweza kutoa msamaha huo ama bila ya masharti au kwa masharti, kwa mujibu wa sheria;
(b) kumwachilia kabisa au kwa muda maalum mtu yeyote aliyehukumiwa kuadhibiwa kwa ajili ya kosa lolote ili mtu huyo asitimize kabisa adhabu hiyo au asitimize adhabu hiyo wakati wa muda huo maalum;
(c) kuibadilisha adhabu yoyote aliyopewa mtu yeyote kwa kosa lolote iwe adhabu tahafifu;
(d) kufuta adhabu yote au sehemu ya adhabu yoyote aliyopewa mtu yeyote kwa ajili ya kosa lolote au kufuta adhabu yote au sehemu ya adhabu ya kutoza, au kuhozi (au kuchukua) kitu cha mtu mwenye hatia ambacho vinginevyo kingechukuliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano.
(2) Bunge laweza kutunga Sheria kwa ajili ya kuweka utaratibu utakaofuatwa na Rais katika utekelezaji wa madaraka yake kwa mujibu wa Ibara hii.
(3) Masharti ya Ibara hii yatatumika kwa watu waliohukumiwa na kuadhibiwa Tanzania Zanzibar na kwa adahabu zilizotolewa Tanzania Zanzibar kwa mujibu wa sheria iliyotungwa na Bunge inayotumika Zanzibar, halikadhalika, masharti hayo yatatumika kwa watu waliohukumiwa na kuadhibiwa Tanzania Bara kwa mujibu wa sheria.
Sambamba na Ibara hii inayompa Rais mamlaka ya kutoa msamaha, nimesoma pia Presidential Affair Act ya mwaka 1962 cap 9 of Tanzania.
Ndugu Watanzania wenzangu;
Hivi sasa nchi yetu ina wafungwa wapatao 39,000, ambapo wanaume ni takriban 37,000 na wanawake ni 2,000. Kati ya wafungwa waliopo magerezani, wafungwa 522 wamehukumiwa adhabu ya kifo, ambapo wanaume ni 503 na wanawake ni 19. Idadi ya wafungwa waliofungwa kifungo cha maisha ni 666, ambapo wanaume ni 655 na wanawake 11.
Hivyo basi, kwa mujibu wa mamlaka niliyopewa na Katiba kupitia Ibara ya 45, nimeamua kutoa msamaha kwa wafungwa 8,157. Kati ya wafungwa hao niliowapa msamaha, wafungwa 1,828 watatoka leo na waliosalia 6,329 watapunguziwa vifungo vyao vya kukaa gerezani na kutoka kulingana na vifungo vyao. Vilevile, kwa kutumia Ibara hiyo ya 45, nimetoa msamaha kwa wafungwa 61 waliokuwa wamehukumiwa kunyongwa. Halikadhalika, nimeamua kutoa msamaha kwa wafungwa kutoka Familia ya Nguza (Nguza Vicking na Johnson Nguza). Wengi niliowapa msamaha, hususan waliohukumiwa kunyongwa na kufungwa vifungo virefu, wametumikia vifungo vyao kwa muda mrefu na wameonesha tabia njema na kujutia makosa yao.
Waheshimiwa Viongozi;
Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana:
Nimeeleza mambo mengi; mengi sana. Hivyo, napenda niishie hapa. Lakini kabla sijahitimisha, napenda nitoe shukrani zangu nyingi kwa Kamati ya Maandalizi kwa kufanikisha Sherehe hii. Sherehe zimefana sana. Hongereni sana wana-Kamati. Tunavishukuru pia vyombo vya ulinzi na usalama, vikundi vya burudani, chipukizi na waandishi wa habari kwa kufanikisha sherehe hii.
Kwa namna ya pekee, napenda kuwashukuru wageni wetu waalikwa waliokuja hapa kushiriki nasi katika shughuli hii muhimu na ya kihistoria kwa taifa letu.Tunawashukuru Mabalozi na Wawakilishi wa Taasisi mbalimbali za Kimataifa. Napenda niwahakikishie kuwa Tanzania itaendelea kushirikiana na Mataifa yenu pamoja na Taasisi mnazoziwakilisha.
Napenda pia kuwashukuru wana-Dodoma wote, mkiingozwa na Mkuu wenu wa Mkoa, Mheshimiwa Mahenge, kwa ukarimu mkubwa mliotuonesha na kwa kujitokeza kwa wingi kwenye Sherehe hizi. Nimejionea mwenyewe kuwa watu wengi wapo nje. Hii ina maana kuwa mnahitaji uwanja mpya. Na kwa bahati nzuri, rafiki zetu wa Morocco wamekubali kutujengea Uwanja Mpya hapa Dodoma, ambapo Jiwe la Msingi tunatarajia kuliweka mwezi Machi au Aprili 2018. Sambamba na hilo, napenda kuwahakikishia wana-Dodoma kuwa dhamira ya Serikali kuhamia Dodoma ipo pale pale. Hakuna kurudi nyuma. Makamu wa Rais atahamia kabla ya mwisho wa Mwaka huu, na mimi nitahamia mwakani. Tutaendelea kuboresha miundombinu pamoja na upatikanaji wa huduma za jamii hapa Dodoma, hususan kwa kuwa hivi sasa mji huu ndio kioo cha nchi yetu. Ahadi yetu ya kujenga barabara ya mzunguko, uwanja wa michezo, njia ya reli kutoka kitongoji cha Chalinze hadi hapa mjini pamoja na kuboresha huduma za maji na afya zipo pale pale. Nawaomba muendelee kutuamini. Na kamwe hatutawaangusha.
Mwisho lakini sio kwa umuhimu, napenda kurudia tena kuwashukuru viongozi wastaafu kwa kuja kujumuika nasi kwenye sherehe hizi. Aidha, navishukuru vyombo vyetu vya ulinzi na usalama kwa kazi kubwa na nzuri wanazofanya kuhakikisha nchi yetu inaendelea kuwa kisiwa cha amani. Wito wangu kwa Watanzania tuendelee kuenzi na kudumisha tunu za Amani, Muungano pamoja na Umoja na Mshikamano, ambazo tumeachiwa na waasisi wetu, Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere na Mzee Abeid Karume.
Mungu Ibariki Tanzania!
Mungu Wabariki Watanzania!
“Ahsanteni Sana kwa kunisikiliza”
- Nov 25, 2017
HOTUBA YA MHESHIMIWA DKT. JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, KWENYE UFUNGUZI WA HOSPITALI YA TAALUMA NA TIBA YA CHUO KIKUU CHA...
Soma zaidiHotuba
Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Mheshimiwa Mohamed Gharib Bilal, Makamu wa Rais
Mstaafu pamoja na Mheshimiwa Mizengo Peter Pinda,
Waziri Mkuu Mstaafu;
Mheshimiwa Anna Makinda, Spika Mstaafu wa Bunge
la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Mheshimiwa Prof. Joyce Ndalichako, Waziri wa Elimu,
Sayansi na Teknolojia;
Mheshimiwa Ummy Mwalimu, Waziri wa Afya,
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto;
Mheshimiwa Seleman Said Jafo, Waziri wa Nchi,
Ofisi ya Rais - TAMISEMI
Mheshimiwa Song Geum Yong, Balozi wa Jamhuri
ya Korea ya Kusini;
Waheshimiwa Wakuu wa Mikoa ya Dar es Salaam na Pwani;
Waheshimiwa Wabunge mliopo;
Waheshimiwa Makatibu Wakuu mliopo;
Prof. Apolinary Kamuhabwa, Makamu Mkuu wa Chuo cha Afya
na Sayansi Shirikishi cha Muhimbili;
Waheshimiwa Mabalozi na Wawakilishi wa Taasisi
za Kimataifa mliopo;
Mwenyekiti wa Baraza la Chuo, Maprofesa pamoja na
Wana-Jumuiya wote wa Chuo Kikuu cha Afya na
Sayansi Shirikishi Muhimbili;
Viongozi wengine wa Serikali, Vyama vya Siasa
pamoja na Viongozi wa Dini mliopo;
Ndugu Wananchi wa Mloganzila na maeneo jirani;
Wageni waalikwa, Mabibi na Mabwana:
Napenda nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyetupa uzima na kutuwezesha kukutana hapa leo. Aidha, namshukuru Mkuu wa Chuo, Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili, Mzee Ali Hassan Mwinyi, pamoja na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako, kwa kunialika kwenye tukio hili la ufunguzi wa Hospitali hii ya Taaluma na Tiba ya Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi cha Muhimbili, hapa Mloganzila. Hili ni tukio muhimu sana kwa maendeleo ya nchi yetu; hivyo basi, ninawashukuru sana kwa kunialika.
Napenda pia kutumia fursa hii kuwashukuru Wana-Jumuiya wa Hospitali hii pamoja na wananchi wa hapa Mloganzila na maeneo jirani, kwanza, kwa kujitokeza kwenu kwa wingi kushuhudia tukio hili. Lakini pili, kwa mapokezi yenu mazuri.
Waheshimiwa Viongozi;
Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;
Afya njema ni msingi mkubwa wa maendeleo katika Taifa. Nchi ambayo wananchi wake hawana afya njema kamwe haiwezi kupata maendeleo. Hii ni kwa sababu mwananchi asiye na afya njema hawezi kushiriki kwenye shughuli za ujenzi wa Taifa, kama vile kilimo, ufugaji, uvuvi, biashara, lakini pia kufanya kazi ofisini, viwandani, migodini, n.k.; na kama atashiriki, basi mchango wake utakuwa mdogo sana.
Hii, bila shaka, ndio sababu Awamu zote za Uongozi wa nchi yetu, kuanzia Awamu ya Kwanza hadi sasa, zimekuwa zikiweka mkazo mkubwa katika kuboresha huduma za afya hapa nchini. Na mimi leo nafurahi kuja hapa Mloganzila kufungua Hospitali hii ya Taaluma na Tiba ya Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi cha Muhimbili. Kama ambavyo mmesikia, Hospitali hii, ambayo ilianza kujengwa mwezi Machi 2014 na kukamilika mwezi Agosti 2016, ni kubwa na pia ya kisasa. Ina uwezo wa kulaza wagonjwa 571 na kuhudumia wagonjwa wengine wa nje. Ujenzi wake pamoja na vifaa umegharimu takriban Dola za Marekani milioni 94.5, sawa na Shilingi za Tanzania bilioni 206.7. Kati ya fedha hizo, Serikali yetu ilitoa Dola za Marekani milioni 18 sawa na takriban shilingi bilioni 39.4; na kiasi kingine, Dola za Marekani 76.5, sawa na takriban shilingi bilioni 167.3 ni mkopo wa masharti nafuu kutoka kwa marafiki zetu wa Korea Kusini.
Napenda kutumia fursa hii, kuishukuru sana Serikali ya Korea Kusini kwa kutupatia mkopo wa masharti nafuu uliotuwezesha kujenga hospitali hii. Korea Kusini ni marafiki zetu. Wametekeleza miradi mbalimbali nchini. Aidha, hivi karibu, Serikali ya Korea inatarajia kufadhili ujenzi wa Daraja la kupita Juu ya Bahari kutoka Aga Khan hadi ufukwe wa Coco Beach umbali wa takriban kilometa 7.1. Kama hiyo haitoshi, kampuni kutoka Korea Kusini itaanza ujenzi wa meli kwa ajili ya kutoa huduma kwenye Ziwa Victoria. Hivyo, tunawashukuru sana marafiki kwa kukuza ushirikiano. Na nimefurahi Balozi wa Korea Kusini, Mheshimiwa Song Yong yupo hapa. Tafadhali, naomba sana utufikishie shukrani zetu nyingi kwa Serikali pamoja na wananchi wa Korea Kusini. Lakini niseme tu kwamba katika kukuza na kuimarisha zaidi uhusiano wetu na Korea Kusini na sisi tumefungua Ubalozi nchini humo hivi karibuni.
Sambamba na kuishukuru Serikali ya Korea kwa ufadhili wao, napenda, kwa namna ya pekee kabisa, kumshukuru na kumpongeza sana Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, Rais Mstaafu wa Awamu wa Nne kwa kuridhia kuanza kwa ujenzi wa Hospitali hii wakati wa uongozi wake. Mimi nataka niwaeleze ukweli, bila Rais mstaafu Kikwete, Hospitali hii isingejengwa. Yeye ndio aliyeasisi wazo la kujengwa kwa Hospitali hii. Sisi wengine tulikuwa tunatekeleza maelekezo yake. Nakumbuka nikiwa Waziri wa Ardhi alinipa maelekezo ya kufuatilia upatikanaji wa eneo hili. Aidha, nikiwa Waziri wa Ujenzi aliniagiza kujenga barabara ya kuja hadi hapa. Nafurahi niliweza kutekeleza maelekezo yake. Eneo hili lenye ukubwa wa ekari 3,800 lilipatikana na barabara ilijengwa na kukamilika. Lakini, nasema kwa dhati kabisa kuwa, sifa zote kuhusiana na ujenzi wa Hospitali hii ziende kwa Mheshimiwa Kikwete. Napenda pia kuwashukuru na kuwapongeza Mkandarasi, Kampuni ya Kolon Global Corporation ya Korea Kusini, pamoja na Wasimamizi wa mradi kwa kukamilisha ujenzi wa Hospitali hii.
Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;
Kama ambavyo Mheshimiwa Ndalichako ameeleza, Hospitali imejengwa kwa madhumuni makubwa matatu. Kwanza, kufundishia wataalam wa masuala ya afya kwa ngazi ya stashahada, shahada, pamoja na shahada za uzamili na uzamivu. Pili, kutoa huduma za afya za kibingwa kwa magonjwa mbalimbali. Na tatu, kufanya tafiti kuhusu namna ya kuboresha tiba na huduma za kinga. Hospitali tayari imekamilika, hivyo, hatua inayofuata sasa ni kuanza ujenzi wa miundombinu ya kufundishia, hususan kumbi za mihadhara (lecture halls), maktaba, maabara, hosteli na cafeteria.
Napenda kuwahakikishia kuwa Serikali imedhamiria kwa dhati kuhakikisha miundombinu hiyo inajengwa ili kuifanya Hospitali hii itekeleze majukumu yake ipasavyo. Nimeambiwa kuwa ujenzi wa miundombinu hiyo utagharimu shilingi bilioni 13.32. Na kama alivyosema Mheshimiwa Waziri Ndalichako tayari Mkandarasi, Wakala wa Majengo ya Serikali (TBA), amelipwa malipo ya awali kiasi cha shilingi bilioni 3.9. Hivyo, natoa wito TBA kuanza mara moja ujenzi wa mradi miundombinu inayohitajika ili kukiwezesha Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi cha Muhimbili kudahili wanafunzi wengi zaidi, kutoka 3,000 wa sasa hadi kufikia 15,000; na hivyo kupunguza tatizo la uhaba wa watumishi wa afya katika hospitali zetu.
Waheshimiwa Viongozi;
Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;
Kukamilishwa na kufunguliwa rasmi kwa Hospitali hii ya Mloganzila ni sehemu tu ya jitihada kubwa zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano za kuboresha huduma za afya hapa nchini. Tangu tumeingia madarakani miaka miwili iliyopita, tumejenga na kuboresha miundombinu mbalimbali kwa ajili ya kutoa huduma za afya. Tumejenga vituo vipya vya kutoa huduma za afya vipatavyo 268 na hivyo kufanya nchi yetu kuwa na vituo vya kutoa huduma za afya vipatavyo 7,284. Vituo vingine vya kutoa huduma za afya vinaendelea kujengwa sehemu mbalimbali nchini, ikiwemo ujenzi wa Hospitali za Mikoa mipya ya Njombe, Geita, Katavi na Simiyu. Sambamba na ujenzi wa vituo hivyo vipya, hivi sasa tunaviboresha vituo vya afya 170 kwa gharama ya shilingi bilioni 161.9 ili kuviwezesha kutoa huduma ya uzazi wa dharura. Lengo la uboreshaji huu ni kupunguza vifo vya mama na mtoto kutoka wastani wa vifo 556 katika kila vizazi hai 100,000 vya sasa hadi kufikia angalau vifo 292 mwaka 2020. Tumekamilisha pia ujenzi wa nyumba 220 kwa ajili ya watumishi wa afya.
Mbali na ujenzi wa miundombinu, tumeendelea na uimarishaji wa huduma za kibingwa kwenye Hospitali zetu za Rufaa za Muhimbili, Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete, Taasisi ya Mifupa (MOI), Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (na napenda nimhakikishie Mheshimiwa Waziri wa Afya kuwa tutampatia fedha kwa ajili ya kununua Scan aliyoomba) pamoja na hospitali za rufaa za Bugando, Mbeya na KCMC. Uboreshaji huu ni pamoja kuanzisha huduma za kupandikiza vifaa vya kuongeza usikivu (cochlea implant). Tumeziongezea pia vifaa, vifaa tiba na vitendanishi. Mathalan, kwenye Hospitali ya Taifa ya Muhimbili tumeongeza vitanda vya ICU kutoka 21 hadi kufikia 75, na vitanda kwa ajili ya wagonjwa wa kusafisha figo vimeongezeka kutoka 27 hadi 42. Tumeongeza pia vyumba vya upasuaji kutoka 13 hadi kufikia 20. Kwa upande wa Taasisi ya Saratani ya Ocean Road tumeiongezea vifaa na vitanda vya wagonjwa kutoka 40 hadi 100; wakati Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete hivi sasa ina uwezo wa kufanya upasuaji wa wagonjwa watatu kwa siku kutoka mmoja hapo awali.
Sambamba na hatua hizo, Serikali imeongeza bajeti ya dawa na vifaa tiba, kutoka shilingi bilioni 31 kwenye Mwaka wa Fedha 2015/2016 hadi kufikia shilingi bilioni 251 mwaka 2016/2017; na Mwaka huu wa Fedha Serikali imetenga shilingi bilioni 269 kwa ajili hiyo. Matokeo yake upatikanaji wa dawa muhimu katika Bohari Kuu ya Dawa na vituo vya Serikali vya kutoa huduma za afya umeongezeka. Jambo la kutia moyo zaidi ni kwamba bei ya dawa na vifaa nayo imeanza kupungua, hususan kufuatia uamuzi wa Serikali wa kuanza kununua moja kwa moja kutoka kwa wazalishaji badala ya kupitia kwa madalali. Mathalan, bei ya dawa ya chanjo ya homa ya ini (hepatitis B Vaccine) imepungua kutoka shilingi 22,000 hadi shilingi 5,300; dawa ya kupambana na maambukizi ya bacteria (Amoxicillin/clavulanic Acid Potassium 625 mg) yenye vidonge 15 bei yake imepungua kutoka shilingi 9,800 hadi shilingi 4,000. Aidha, bei ya shuka za hospitalini imepungua kutoka shilingi 22,200 hadi shilingi 11,100. Hii ni mifano michache tu.
Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;
Licha ya hatua tunazozichukua, na ambazo zinatia moyo, natambua kuwa bado sekta yetu ya afya inakabiliwa na matatizo kadhaa. Moja ya matatizo hayo, ni uhaba wa watumishi wa afya. Na tatizo hili kimsingi lina sura kubwa mbili. Sura ya kwanza, ni uhaba wa watumishi wenyewe. Nchi yetu bado ina mahitaji makubwa ya watumishi wa afya. Tulionao ni 89,842 kati ya 184,901 wanaohitajika. Hivyo, tuna upungufu wa watumishi wa afya takriban 95,059. Serikali inalifahamu hili ndio maana tayari tumetoa vibali vya ajira zipatazo 3,410 (madaktari 258 na wataalam wa kada mbalimbali za afya 3,152) ili kupunguza pengo la watumishi wa afya lililopo, na hasa baada ya kuondolewa watumishi wenye vyeti vya kughushi. Aidha, tumevifanyia ukarabati na upanuzi vyuo vyetu vya uuguzi na ukunga vya Nzega, Mirembe, Mtwara na Tanga pamoja vyuo vya maafisa tabibu Musoma na Mpanda. Matokeo yake udahili wa wanafunzi wa afya imeongezeka hadi kufikia 13,632 na hivyo kuvuka lengo lililowekwa la kudahili wanafunzi 10,000 ifikapo mwaka 2017. Aidha, hivi sasa Serikali inatoa mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 54.26 kwa wanafunzi wanaosomea masuala ya afya wapatao 10,189. Lakini sio kwamba tunataka kuongeza idadi tu. Hapana. Tunahimiza pia ubora wa wataalam wanaozalishwa kwenye vyuo vyetu. Hii ndio sababu Serikali iliamua kuvisimamisha baadhi ya vyuo kudahili wanafunzi kwa mwaka huu baada ya kujiridhisha kuwa havina uwezo.
Sura ya pili ya tatizo la uhaba wa watumishi wa afya hapa nchini, linatokana na mgawanyo usio mzuri wa watumishi wenyewe. Mathalan, nimeambiwa kuwa takriban asilimia 60 ya madaktari wote nchini, wapo hapa Dar es Salaam. Na ni asilimia 40 tu ndio wapo Mikoani. Nafahamu kuwa tatizo hili linasababishwa na mambo mengi, ikiwa ni pamoja na hospitali nyingi kubwa kuwepo hapa Dar es Salaam lakini kuwepo na mazingira mazuri ya kufanyia kazi. Hata hivyo, natambua pia kuwa suala la Wizara ya Afya kusimamia Hospitali za Kibingwa na Maalum pekee, na hospitali nyingine kuanzia ngazi ya mkoa kuwa chini ya TAMISEMI nalo linachangia kuwepo kwa mgawanyo usiowiana wa madaktari kati ya hapa Dar es Salaam na Mikoani; na halikadhalika kati ya Hospitali za Kibingwa na zisiso za Kibingwa.
Napenda nitoe mifano michache. Hospitali ya Taifa ya Muhimbili yenye takriban vitanda 1,600, ina jumla ya madaktari bingwa, madaktari wanafunzi na wahadhiri wa Chuo Kikuu cha Muhimbili wapatao 532. Hii maana yake ni kwamba kila daktari anahudumia vitanda vitatu. Lakini katika Mkoa wa Tabora daktari 1 alikuwa akihudumia wagonjwa 208,329, kwa mujibu wa Sensa ya Mwaka 2012. Mfano mwingine ni wa hapa hapa Dar es Salaam. Hospitali ya Manispaa ya Temeke yenye kuhudumia wastani wa wajawazito wanaojifungua 100 kwa siku ina madaktari bingwa wa akinamama wawili. Lakini Hospitali ya Taifa ya Muhimbili yenye kuhudumia wastani wa akinamama wanaojifungua kati ya 40 hadi 50 kwa siku, ina madaktari bingwa 40; ukiachilia mbali madaktari wanafunzi waliopo. Hii inadhihirisha kuwa hakuna mgawanyo mzuri wa madaktari wachache tulionao. Ni kweli, tunahitaji kuwa na madaktari bingwa wengi katika hospitali zetu. Lakini, haina maana kuwa na madaktari wengi kwenye Hospitali za Kibingwa wakati hospitali nyingine za kawaida, zenye kuhudumia watu wengi, hazina madaktari. Tukiruhusu hali hii kuendelea, wananchi wengi wataendelea kukosa huduma za afya; na hata wakipewa rufaa kwenda hospitali za rufaa au kibingwa wanakuwa tayari wamechelewa na watashindwa kutibika.
Hivyo, niziombe Mamlaka husika kulitafakari suala hili kwa kina, ikiwezekana, kuangalia uwezekano wa Hospitali za Mikoa nazo ziwe chini ya Wizara ya Afya. TAMISEMI ibaki kusimamia hospitali za Wilaya, vituo vya afya na zahanati. Nina imani kuwa hii itasaidia kuboresha huduma katika Hospitali za Rufaa za Mikoa na hivyo kuipunguzia mzigo Hospitali ya Taifa ya Muhimbili. Lakini, sambamba na hilo, niwaombe madaktari nao kuwa wazalendo pindi wakipangiwa kwenda kufanya kazi Mikoani na Wilayani. Serikali imeanza kuboresha maslahi ya watumishi wa afya wanaofanya kazi kwenye Hospitali za Mikoa na Wilaya, ambapo, mathalan, katika Hospitali za Rufaa za Mikoa, daktari bingwa alikuwa akilipwa shilingi 2,000 kwa ajili ya kumuona mgonjwa ambaye ni mwanachama wa Mfuko wa Taifa wa Bima, lakini sasa analipwa shilingi 15,000. Daktari wa kawaida alikuwa akilipwa shilingi 2,000 lakini sasa analipwa shilingi 7,000. Katika Hospitali za Wilaya, daktari alikuwa akilipwa shilingi 1,000 lakini sasa analipwa shilingi 7,000. Tumefanya hivyo ili kuwavutia madaktari kwenda kufanya kazi katika Hospitali za Mikoa na Wilaya nchini.
Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;
Ukiachilia mbali suala la uhaba wa watumishi wa afya, nchi yetu bado ina upungufu wa miundombinu ya kutolea huduma za afya, hususan zahanati, vituo vya afya, hospitali za wilaya, nyumba za watumishi, n.k. Kama nilivyoeleza hapo awali, Serikali inaendelea na jitihada za kujenga miundombinu hiyo. Lakini nawakaribisha watu binafsi, makampuni na mashirika ya dini kuendelea kuunga mkono jitihada hizo.
Tatizo la tatu ambalo mimi naliona lenye kuikabili sekta yetu ya afya ni kukosekana kwa viwanda vya kuzalisha madawa hapa nchini. Dawa nyingi tunaagiza kutoka nje kwa gharama za juu. Kama tungekuwa na viwanda vingi vya kuzalisha dawa hapa nchini, nina uhakika bei ya dawa ingekuwa chini zaidi na hospitali zetu zingekuwa na dawa za kutosha. Hivyo basi, napenda kurudia wito wangu kwa wafanyabiashara, makampuni na mashirika mbalimbali kuwekeza kwenye viwanda vya madawa na vifaa tiba hapa nchini. Soko lipo, tena ni kubwa. Mmesikia kuwa tumeongeza bajeti ya dawa, lakini pia washirika wetu mbalimbali wameendelea kutufadhili kwa kutupatia fedha za kununulia dawa. Mathalan, Global Fund wametupatia takriban Dola za Marekani milioni 300 kwa ajili hiyo. Lakini sambamba na hayo, mnafahamu kuwa sisi ni wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), ambazo zina takriban nchi 18. Kama hiyo haitoshi, hivi karibuni taasisi yetu ya Bohari Kuu ya Madawa imekabidhiwa jukumu la kununua dawa kwa niaba ya nchi zote za SADC. Hivyo, soko lipo. Kilichobaki ni kwa wafanyabiashara na wataalam wetu kujipanga vizuri katika kutumia fursa hiyo ya kuwa na soko kubwa la dawa. Nimefurahi kusikia kuwa Hospitali hii ya Mloganzila imetenga eneo mahususi kwa ajili ya ujenzi wa viwanda vya dawa. Na nina imani mtakuwa mmetenga pia eneo maalum kwa ajili ya kulima mimea mbalimbali kwa ajili ya kufanya utafiti wa madawa, ambayo yalikuwa ndio mawazo ya Mzee Kikwete. Napenda pia kutumia fursa hii kuushauri Mfuko wa Bima ya Afya kujielekeza katika mwelekeo huo wa ujenzi wa viwanda vya madawa.
Tatizo jingine ambalo naliona ni wananchi wetu wengi kushindwa kujiunga na Mifuko ya Bima ya Afya. Kama mnavyofahamu, gharama za afya huwa ni kubwa na ugonjwa mara nyingi hutokea bila kutarajia. Hali hii inafanya wananchi wengi kushindwa kumudu gharama za matibabu, licha ya kwamba Serikali imejitahidi sana kupunguza gharama za matibabu. Mifuko ya Bima ya Afya (NHIF na CHF) ina nafasi kubwa ya kuwasaidia wananchi kupunguza gharama za matibabu. Lakini kwa bahati mbaya, idadi ya wananchi waliojiunga na mifuko hii ni ndogo. Hivyo basi, nitumie fursa hii kuwaomba wananchi kote nchini kujiunga na Mifuko ya Bima ya Afya ili iwasaidie pindi wanapokumbwa na magonjwa au kuuguliwa na ndugu au jamaa. Gharama za kujiunga na mifuko ya bima ya afya sio kubwa, ni ndogo.
Waheshimiwa Viongozi;
Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;
Nimeeleza masuala mengi. Lakini kabla sijahitimisha hotuba yangu, ninayo masuala mengine madogo ya kueleza. Jambo la kwanza, ni kuhusu utunzaji wa miundombinu hii. Kama mlivyosikia, ujenzi wa miundombinu na ununuzi wa vifaa kwa ajili ya Hospitali hii hapa Mloganzila umegharimu fedha nyingi. Hivyo basi, nawasihi sana wafanyakazi na watumishi wa hapa muitunze. Na niziombe mamlaka husika za hospitali zote nchini kuhakikisha vifaa kwenye Hospitali za Serikali vinatunzwa. Kitunze kidumu.
Jambo la pili linaihusu Hospitali hii. Hospitali hii inakabiliwa na changamoto kadhaa, ikiwemo uhaba wa watumishi. Wanaohitajika ni takriban 950, lakini waliopo ni wachache kutokana na vibali vichache vya ajira na uhaba wa watumishi wenyewe wa afya. Hata hivyo, kwa taarifa nilizonazo ni kuwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, ukijumuisha Taasisi ya Moi pamoja na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete, ina takriban vitanda 1,940. Aidha, madaktari na watumishi kwa pamoja idadi yao inafikia 3,812. Wodi ya Mwaisela peke yake ina vitanda 244 na kuhudumia wagonjwa wa nje wapatao 400. Wodi hii pia imekuwa ikihudumiwa na madaktari bingwa wapatao 75, wakisaidiwa na madaktari wanafunzi takriban 20 na wauguzi wapatao 69. Lakini, kama nilivyosema, Hospitali hii ya Mloganzila ina vitanda 571, ambavyo havina wagonjwa na inakabiliwa na changamoto ya watumishi.
Nimekuwa nikijiuliza kama Hospitali ya Taifa ya Muhimbili yenye kukabiliwa na ufinyu wa nafasi za kulaza wagonjwa ina watumishi wengi kama nilivyoeleza, kwanini basi tusiwahamishe baadhi ya madaktari na wagonjwa kutoka Muhimbili kuja hapa, na hivyo kuweza kupiga ndege wawili kwa jiwe moja. Kwanza, kupunguza uhaba wa watumishi katika Hospitali hii ya Mloganzila. Na pili kupunguza mrundikano wa wagojwa kwenye Hospitali yetu ya Taifa ya Muhimbili. Vilevile, Hospitali hii itaweza kuhudumia watu wengi zaidi kuliko sasa na wanafunzi pia wataweza kujifunza vizuri zaidi. Halikadhalika, tutaipunguzia Serikali gharama kwa vile watumishi watakaohamishiwa hapa kutoka Muhimbili tayari ni waajiriwa wa Serikali; na kwa kuwa Hospitali hii ipo hapa Dar es Salaam hata gharama za uhamisho hazitakuwepo. Hivyo basi, nitoe wito kwa wahusika wote, hususan Wizara ya Elimu na Chuo cha Muhimbili, Wizara ya Afya na Hospitali ya Muhimbili, Taasisi za Moi na ya Moyo ya Jakaya Kikwete pamoja na wahusika wengine, kukutana na kulitafakari suala hili vizuri ili uwekezaji huu ulete manufaa yaliyokusudiwa.
Suala jingine lenye kufanana na hili nililotoka kulizungumzia ni kuhusu ushirikiano miongoni mwa taasisi zenye kusimamia Hospitali hii. Kama nilivyoeleza hapo awali, Hospitali hii ina jukumu la kufundisha wataalam wa afya na pia kutoa huduma za afya, hususan za kibingwa kwa wananchi. Inafahamika kuwa jukumu la kusimamia sekta ya afya lipo Wizara ya Afya na Wizara ya Elimu inashughulikia sekta ya elimu. Kwa maana hiyo, ili Hospitali hii iweze kutekeleza majukumu yake yote mawili ipasavyo ni lazima Wizara hizi mbili pamoja na watendaji wake zifanye kazi kwa karibu na kwa ushirikiano. Nimefurahi kusikia kuwa Waheshimiwa Mawaziri wa Afya na Elimu wanashirikiana; japo sina hakika kama hali iko hivyo hadi kwa watendaji wao. Endapo hapatakuwa na ushirikiano, upo uwezekano wa Hospitali hii kushindwa kutekeleza majukumu yake, ikajikita kwenye jukumu moja, mathalan la kufundisha wataalam na kuacha jukumu la kutoa huduma za afya kutokana na ama utashi wa viongozi wa Hospitali wenyewe au kwa kukosa bajeti ya kutoa huduma ya afya kutoka Wizara ya Afya. Hivyo basi, natoa changamoto kwa wahusika wote kuhakikisha washirikiana ili Hospitali hii itekeleze majukumu yake yote mawili ipasavyo; jukumu la kufundisha wataalam na jukumu la kutoa huduma za afya kwa wananchi. Wizara ya Elimu itoe bajeti ya kufundishia kwa Hospitali hii Wizara ya Afya itenge bajeti itakayoiwezesha Hospitali hii kutoa huduma za afya kwa wananchi, kwa sababu wao ndio wenye jukumu la kusimamia sekta ya afya. Huu ndio wito wangu kwa mamlaka zenye kusimamia Hospitali hii.
Suala la tatu linahusu ulipaji wa fidia kwa wananchi waliokuwa wakiishi katika eneo hili. Historia ya eneo hili ipo wazi. Kabla ya kumilikishwa kwenye Hospitali hii, eneo hili, tangu mwaka 1946 lilikuwa chini ya milki ya Serikali, kupitia kwanza Tanganyika Packers na baadaye Kampuni ya Biashara ya Mifugo Tanzania (KABIMITA) chini ya Wizara ya Maji na Maendeleo ya Mifugo. Eneo hili lilitumika kwa ajili ya kufuga, kutunza na kunenepesha mifugo (holding ground) kabla ya kuuzwa au kuchinjwa. Wakati huo hapakuwa na wananchi waliokuwa wakiishi. Baada ya KABIMITA kuacha kulitumia, wananchi walianza kuishi na kuliendeleza, na hatimaye likasajiliwa vijiji vya ujamaa vya Kwembe (1980) na Mloganzila (1993); lakini umilki ardhi ulibaki kuwa Serikalini ndio maana tulipotaka kujenga Hospitali hii, hatukupata taabu kulichukua. Hata hivyo, kwa busara na huruma ya Serikali iliamua kuwa wananchi waliokuwa wakiishi hapa walipwe fidia ya mandelezo waliyoyafanya. Kiasi cha takriban shilingi bilioni 8.07 kililipwa kwa watu 1,919 waliofanyiwa tathmini kati ya mwaka 2008 – 2010. Aidha, mwaka 2011 Serikali iliwalipa fidia wananchi wengine 619 kiasi cha shilingi bilioni 1.61. Hivyo basi, nitumie fursa hii kusema kuwa Serikali haitalipa tena fidia kwenye eneo hili. Na wala wasipite watu kuwadanganya kuwa kuna fidia nyingine. Kama nilivyosema, fidia tayari ilishalipwa. Lakini nafahamu kuwa wapo wakazi wawili waligomea malipo yao, lakini hundi zao zipo; wakati wowote wakiwa tayari wanaweza kuzifuata kwenye Wizara husika. Fidia iliyotolewa ni kwa mujibu wa sheria na taratibu za nchi yetu.
Mheshimiwa Rais Mstaafu Mzee Mwinyi;
Waheshimiwa Viongozi;
Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;
Napenda kuhitimisha kwa kuwashukuru tena viongozi wa Hospitali hii pamoja na Wizara husika kwa kunikaribisha kwenye shughuli hii. Nawashukuru pia Mheshimiwa Makamu wa Rais Mstaafu, Dkt. Bilal pamoja na Waziri Mkuu Mstaafu Mzee Mizengo Pinda, ambao kwa kushirikiana na Rais Mstaafu Mzee Kikwete walifanikisha ujenzi wa Hospitali. Aidha, namshukuru pia Mheshimiwa Mama Anna Makinda, Spika Mstaafu ambaye Bunge aliloliongoza ndilo lilipitisha bajeti ya kujenga Hospitali hii. Na narudia tena kuishukuru Serikali ya Korea Kusini ambao walitupatia mkopo wa ujenzi wa Hospitali hii ya kisasa; pamoja na wengine wote waliofanikisha. Napenda kuwahakikishia viongozi wa Hospitali hii pamoja na wananchi kwa ujumla kuwa Serikali ya Awamu ya Tano itaendelea kufanya kila jitihada kuhakikisha hospitali hii ya kisasa inakuwa bora sio tu hapa nchini bali Barani Afrika.
La mwisho kabisa, hususan kwa wananchi wa maeneo haya, hivi karibuni Serikali imeanza maandalizi kwa ajili ya ujenzi wa barabara kutoka Ubungo hadi Kibaha. Ili kutekeleza mradi huo, nyumba zilizokuwa zimejengwa kwenye hifadhi ya barabara zimebomolewa kwa mujibu wa sheria. Ujenzi wa barabara hiyo yenye urefu wa kilometa 16 utaanza wakati wowote kuanzia sasa.
Baada ya kusema hayo, sasa nipo tayari kutekeleza jukumu lililonileta hapa Mloganzila la kuifungua rasmi Hospitali ya Taaluma na Tiba ya Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi cha Muhimbili.
Mungu Ibariki Hospitali Hii!
Mungu Wabariki Wana-Mloganzila!
Mungu Ibariki Tanzania!
“Ahsanteni sana kwa kunisikiliza”
- Oct 18, 2017
HOTUBA YAMHESHIMIWA DKT. JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA KWENYE MAADHIMISHO YA KUMBUKUMBU YA BABA WA TAIFA, MWALIMU JULIUS N...
Soma zaidiHotuba
HOTUBA YAMHESHIMIWA DKT. JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA KWENYE MAADHIMISHO YA KUMBUKUMBU YA BABA WA TAIFA, MWALIMU JULIUS NYERERE PAMOJA NA SHEREHE ZA KILELE CHA MBIO ZA MWENGE NA WIKI YA VIJANA KITAIFA MKOANI MJINI MAGHARIBI, TAREHE 14 OKTOBA, 2017
Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi;
Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Mheshimiwa Kassim Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Mheshimiwa Balozi Seif Ali Iddi, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar;
Mheshimiwa Zubeir Ali Maulid, Spika wa Baraza la Wawakilishi;
Mheshimiwa Moudline Cyrus Castico, Waziri wa Kazi, Uwezeshaji, Vijana, Wazee, Wanawake na Watoto wa Zanzibar;
Mheshimiwa Jenista Muhagama, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu- Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu;
Ndugu Mwakilishi wa Familia ya Baba wa Taifa, Mheshimiwa Makongoro Nyerere;
Mama Yetu Mpendwa, Mama Fatuma Karume;
Waheshimiwa Mawaziri na Manaibu Mawaziri mliopo;
Waheshimiwa Mabalozi mliopo;
Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi pamoja na Wakuu wa Mikoa wote mliopo;
Mheshimiwa Viongozi wa Vyama vya Siasa mkiongozwa na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mjini Magharibi;
Waheshimiwa Wabunge na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi mliopo;
Waheshimiwa Viongozi wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama;
Ndugu Makatibu Wakuu na Manaibu Makatibu Wakuu mliopo;
Waheshimiwa Viongozi wa Dini mliopo;
Ndugu Waandishi wa Habari;
Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana:
Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, Muumba wetu, ambaye ametuwezesha kukutana katika siku hii muhimu. Kama mnavyofahamu, Siku hii imebeba mambo makubwa mawili, au naweza kusema matatu. Kwanza, tunakumbuka kifo cha Baba wa Taifa letu, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, ambaye tarehe kama ya leo, miaka 18 iliyopita, alitutoka hapa duniani. Na Pili, kulingana na maelekezo ya Waraka wa Baraza la Mawaziri Na. 11 wa Mwaka 2002, Siku ya leo pia ni kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru kwa mwaka huu na Wiki ya Vijana Kitaifa.
Hivyo basi, napenda kutumia fursa hii kuwashukuru Waheshimiwa Mawaziri husika kwa kunialika kwenye shughuli hii muhimu. Kama mnavyofahamu, hii ni mara yangu ya kwanza kushiriki kwenye shughuli hii tangu nimechaguliwa kuwa Rais wa Awamu ya Tano. Mwaka jana, sherehe hizi zilipofanyika kule Simiyu, nilimwomba Mheshimiwa Rais Dkt. Ali Mohamed Shein Rais wa Serikali ya Zanzibar aniwakilishe, ambapo alifanya kazi hiyo vizuri sana huko Bariadi. Hivyo, kwa hakika kabisa, nimefurahi sana kushiriki kwenye shughuli hii.
Nitumie pia fursa hii kuwashukuru wananchi wa Mkoa wa Mjini Magharibi na Zanzibar kwa ujumla kwa mapokezi yenu mazuri. Aidha, nawashukuru kwa kujitokeza kwenu kwa wingi katika shughuli hii. Kama msemo wa Kiswahili usemavyo ”shughuli ni watu”. Hivyo, nasema, ahsanteni sana.
Waheshimiwa Viongozi,
Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;
Kama nilivyotangulia kusema, moja ya mambo yaliyotukutanisha hapa leo ni kukumbuka kifo cha Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, ambacho kilitokea London, Uingereza, siku kama ya leo mwaka 1999. Tangu wakati huo, kila mwaka, ifikapo tarehe 14 Oktoba, tunafanya maadhimisho haya. Tutafanya hivyo pia mwakani na naamini tutafanya hivyo kwa miaka mingi ijayo kama si katika kipindi chote cha uhai wa Taifa letu.
Lakini, Watanzania wenzangu, tujiulize, hivi ni kwanini hasa tunamkumbuka Mwalimu Nyerere? Je, ni kwa sababu tu Siku hii imetamkwa kwenye sheria? Au tuna sababu za msingi za kumkumbuka? Tusipojiuliza maswali hayo, tutaendelea kuiadhimisha Siku hii kwa mazoea na hatimaye itapoteza umuhimu wake. Lakini niseme tu kuwa, nijuavyo mimi ni kwamba, Siku hii iliamriwa kuwa Siku ya Kitaifa ili kuwapa Watanzania fursa ya kujikumbusha mchango mkubwa na usiosahaulika uliotolewa na Mwalimu Nyerere katika nchi yetu. Na katika kujikumbusha huko, tujifunze na kutumia mafunzo tunayoyapata katika kusukuma mbele maendeleo ya nchi yetu.
Mabibi na Mabwana;
Nafahamu kuwa Watanzania wengi wanamfahamu au wamewahi kusikia habari za Mwalimu Nyerere. Baadhi walishiriki naye katika shughuli mbalimbali. Wengine walimuona wakati akiwa Rais. Wapo pia waliomfahamu kupitia vitabu au simulizi mbalimbali. Hata hivyo, kwa kuzingatia umuhimu wa siku hii, na kwa kuwa hii ni mara ya kwanza kushiriki kwenye maadhimisho haya tangu niwe Rais, nimeona ni jambo jema kumzungumzia kidogo Mwalimu Nyerere. Hii ni kwa sababu, sisi wenyewe, lakini hasa vijana na watoto wetu, wanahitaji kumfahamu vizuri mtu huyu tunayemkumbuka leo na pia kufahamu kwa nini tunafanya hivyo.
Ndugu Watanzania, Mabibi na Mabwana;
Historia ya uongozi wa Mwalimu Nyerere ni ndefu sana. Lakini niseme tu kuwa tunamkumbuka kwa sababu, kwanza, alikuwa kiongozi mzalendo. Mwalimu Nyerere alianza uongozi wa kisiasa mwaka 1953 alipochaguliwa kuwa Rais wa Tanganyika African Association (TAA). TAA ndio iliyozaa Chama cha Tanganyika African National Union (TANU), ambacho ndicho kilichoongoza harakati za kupigania uhuru wa nchi yetu.
Katika kipindi hicho cha mwanzoni kabisa cha uongozi wake kisiasa, Mwalimu Nyerere alionesha uzalendo wa hali ya juu na kuthamini kwake utu na usawa wa binadamu. Wakati anachaguliwa kuwa Rais wa TAA na baadaye TANU, alikuwa anafundisha St.Francis College, hivi sasa inajulikana kama Shule ya Sekondari Pugu. Umbali wa kutoka Pugu hadi kwenye Ofisi za TAA/TANU kwenda na kurudi ilikuwa kama kilometa 46. Na enzi hizo hapakuwa na usafiri wa daladala kama ilivyo sasa. TAA/TANU haikuwa na usafiri na hata fedha za kumlipa mshahara. Lakini kwa uzalendo wake, Mwalimu Nyerere alitumia fedha zake kujigharamia usafiri na wakati mwingine kulazimika kutembea kwa miguu. Alifanya hivyo kwa kujitolea. Tujiulize leo, ni viongozi wangapi wa Serikali na hata kwenye vyama wameweza kujitolea kiasi hicho?
Lakini kama hiyo haitoshi, mwaka 1955, alipotakiwa na Mwalimu Mkuu wa St.Francis College kuchagua ama kuendelea na kazi au kuacha kujihusisha na shughuli za kisiasa, Mwalimu Nyerere aliamua kuacha kazi na kubaki kuwa kiongozi wa TANU; kazi ambayo alikuwa halipwi mshahara wowote. Aliamua hivyo ili aendelee kuongoza harakati za kudai uhuru. Sijui kama tunafahamu maisha aliyoishi Mwalimu Nyerere na familia yake baada ya kuacha kazi; lakini, nina uhakika, yalikuwa magumu sana.
Kitu pekee kilichomsukuma kufanya uamuzi huo ni uzalendo wake. Isingekuwa hivyo, angetafuta kazi nyingine nzuri ya mshahara mzuri, kwa maana alikuwa msomi mzuri; na wasomi wa kiwango chake, wakati huo walikuwa wakihitajika sana. Je, tujiulize ni wangapi hivi leo wanaweza kufanya uamuzi wa kizalendo kama huo uliofanywa na Baba wa Taifa? Leo hii kuna Watanzania wangapi ambao kwa sababu tu wanalipwa vizuri kwenye makampuni ya wageni wanakofanya kazi, wanaisaliti nchi kwa vitendo vya wizi? Je, kuna viongozi wangapi waliopewa dhamana na wananchi lakini kwa sababu ya ubinafsi na kukosa uzalendo, wamekubali kusaini mikataba isiyo na tija kwa nchi? Je, tuna viongozi wangapi ambao wametanguliza maslahi yao binafsi mbele kuliko maslahi ya Tanzania? Majibu mnayo.
Ndugu Watanzania, Mabibi na Mabwana;
Sifa ya pili ya Mwalimu Nyerere alikuwa kiongozi asiye mbinafsi na mwenye kuthamini utu na usawa wa binadamu. Hili linadhihirishwa kwa jinsi yeye na familia yake walivyoishi. Waliishi maisha ya kawaida sana kama Watanzania wengine. Hakujilimbikizia mali wala hakuishi maisha ya anasa na kifahari. Kuna mtu niliwahi kumsikia akisema”kama Mwalimu Nyerere angekuwa mbinafsi au mpenda utajiri angeweza kuchukua fukwe yote ya Msasani ili iwe yake”. Na kweli angeweza, maana kuna mifano mingi tu ya viongozi wengi wa zama zake, na hata wa sasa, wanafanya hivyo. Lakini hakufanya hivyo. Yeye, Mama Maria, watoto na ndugu zake wengi waliishi na wanaendelea kuishi maisha ya kawaida kabisa, sawa na Watanzania wengi, licha ya kuwa Rais kwa takriban miaka 23.
Mfano mwingine unaodhihirisha kuwa Mwalimu Nyerere hakuwa mbinafsi bali mwenye kuthamini utu na usawa wa binadamu, ni jambo alilolifanya mwanzoni tu mwa uongozi wake akiwa Rais wa Tanzania. Baada ya nchi yetu kupata uhuru, baadhi ya wasomi waliokabidhiwa madaraka walianza kutoa shinikizo kwa Serikali kutaka kuongezewa mishahara na marupurupu. Mwalimu Nyerere hakukubaliana kabisa na madai hayo na hakusita kuikemea tabia hiyo ya ubinafsi kwa ukali na uwazi kabisa.
Hakuishia hapo. Ili kuonesha mfano, yeye mwenyewe, aliamua kupunguza mshahara wake ili kuwakumbusha wasomi hao kuwa haiwezekani kwa watu wachache kuongezana mishahara wakati wananchi wengi masikini hawapati huduma muhimu za afya, elimu na maji kutokana na ukosefu wa fedha. Tujiulize, je, sisi tuko tayari kuacha mishahara hewa? Je, mishahara tunayoipata tunaifanyia kazi? Je,nasi tupo tayari kujipunguzia, au kuacha kushinikiza kuongezwa kwa mishahara na marupurupu yetu ili kuiwezesha Serikali kuboresha huduma za jamii kwa manufaa ya Watanzania wote? Nasema hayo sio kwa sababu sitaki mishahara iongezwe. La hasha. Ninachotaka kusema ni kwamba kabla ya kudai nyongeza ya mishahara ni lazima kwanza kufahamu uwezo wa Serikali; lakini pia tutambue kuwa kuna Watanzania wenzetu wengi tu wanaohitaji kuboreshewa huduma.
Nafahamu kuwa huku Zanzibar mishahara ya watumishi wa kima cha chini imeongezwa kutoka Shilingi laki moja na nusu hadi shilingi laki tatu. Na kwa upande wa kule Bara, baada ya kukamilisha zoezi la uchambuzi wa watumishi hewa na wenye vyeti vya kughushi, Serikali imewapandisha vyeo watumishi 59,967 na kurekebisha mishahara yao, ambapo kiasi cha shilingi bilioni 159.33 kimetengwa kwenye bajeti ya mwaka huu. Mishahara mipya ya watumishi hao inatarajiwa kuanza kulipwa mwezi huu. Endapo tusingefanya uchambuzi, Serikali ingepoteza takriban shilingi bilioni 89 kwa mwaka kwa kuwalipa watumishi hewa na wenye vyeti feki.
Ndugu Watanzania, Mabibi na Mabwana;
Sifa nyingine ya Mwalimu Nyerere alikuwa mpenda amani, umoja na mshikamano. Wakati wa harakati za kudai uhuru, aliwahimiza Watanganyika kutotumia nguvu, licha ya kuwepo kwa vitendo vya uchokozi na hila chafu zilizofanywa na wakoloni. Hii ndio moja ya sababu, zilifanya nchi yetu kupata uhuru kwa njia ya amani. Aidha, licha ya kuwa Tanganyika ilikuwa na takriban makabila 121 na dini mbalimbali, alifanikiwa kuwaunganisha wananchi wote katika harakati za kudai uhuru wa nchi yao.
Mwalimu Nyerere pia alikuwa muumini mzuri wa Muungano. Tanganyika ilipokaribia kupata uhuru, alikuwa tayari kuchelewesha uhuru huo kuzisubiri nchi nyingine za Afrika Mashariki (Kenya, Uganda na Zanzibar) ili uhuru huo upatikane kwa pamoja na kuwezesha kuundwa kwa taifa moja la Shirikisho la Afrika Mashariki. Lakini hata pale ilipodhihirika kuwa suala hilo haliwezekani, mwaka 1964, Baba wa Taifa pamoja na shujaa mwingine wa nchi yetu, Hayati Mzee Abeid Aman Karume, waliasisi Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kuunganisha Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar. Na mwaka 1977, viongozi hao waliasisi Muungano wa vyama vya TANU na Afro Shiraz Party, na kuunda CCM, Chama Tawala, ambacho kimebaki kuwa miongoni mwa vyama vikongwe duniani. Hii inadhihirisha kuwa Mwalimu Nyerere alikuwa mpenda muungano. Tujiulize je, vitendo vyetu leo vinalenga kudumisha amani ya nchi yetu au kuivunja? Je, sisi hatuna udini au ukabila? Je, maneno na vitendo vyetu vinadumisha au vinahatarisha Muungano wetu? Haya ni maswali muhimu kujiuliza Watanzania wote tunapoadhimisha siku hii ya Mwalimu Nyerere.
Wheshimiwa Viongozi, Mabibi na Mabwana;
Kiongozi yoyote ana sifa kubwa moja; kuwa na maono (vision). Mwalimu Nyerere alikuwa ni kiongozi mwenye maono, tena makubwa na ya mbali sana. Alijua kuwa anataka kujenga Taifa huru na linalojitegemea. Taifa la watu wenye kujali na kuheshimu utu wa kila mmoja. Hayo ndio maono yake. Lakini, kama mnavyofahamu, maono peke yake bila mikakati, ni ndoto. Mwalimu Nyerere alibuni na kusimamia utekelezaji wa mikakati ya kutekeleza maono yake. Ndani ya miaka michache tu baada ya nchi yetu kupata uhuru, Mwalimu Nyerere alibaini kuwa huwezi kujenga Taifa huru na linalojitegemea kama njia kuu za uzalishaji zitamilikiwa au kusimamiwa na wageni au watu binafsi peke yake. Ni lazima Serikali ishiriki kikamilifu. Na huo ndio ukweli wenyewe. Nchi zote zilizofanikiwa kiuchumi duniani, Serikali zao zilishiriki moja kwa moja katika shughuli za kiuchumi. Hivyo basi, aliona upo umuhimu wa kujenga misingi itakayoiwezesha Serikali kushiriki kikamilifu kwenye shughuli za uzalishaji; na hapo ndipo Azimio la Arusha likazaliwa mwaka 1967.
Mbali kuweka miiko ya kuwabana viongozi kutumia nafasi zao kujilimbikizia mali, Azimio la Arusha liliipa nguvu Serikali ya kuzuia viwanda, mashirika na makampuni ya kibepari kutorosha rasilimali zetu kwenda nje ya nchi. Lakini pia, kupitia Azimio la Arusha, Serikali ilijenga viwanda pamoja na kuanzisha mashirika na makampuni mengine mapya. Tukawa na viwanda vingi tu, vikiwemo vya nguo, viatu, matairi, vifaa vya kilimo, chuma, n.k.; na hivyo tukapunguza utegemezi wa kuagiza bidhaa hizo kutoka nje. Shirika letu la ndege lilikuwa na uwezo wa kutoa huduma ndani na nje ya nchi. Nakumbuka tulikuwa na ndege 9; mbili aina ya Boeing, Fokker 3 na Twin Otters 4. Aidha, Serikali ikaanzisha Shirika la Nyumba (NHC), ambalo lilikuwa na nyumba zipatazo 6,000 kwa ajili ya wananchi wa kipato cha chini. Na huku Zanzibar, Hayati Mzee Karume, akajenga majengo ya ghorofa sehemu mbalimbali ikiwa ni pamoja na pale Michenzani.
Sambamba na hayo, Serikali iliweka mkazo kwenye elimu, ambapo ilitolewa bure bila ubaguzi, kuanzia shule ya msingi hadi chuo kikuu. Mwalimu Nyerere aliamini kuwa ukitaka kumkomboa mtu mnyonge ni lazima umpe elimu. Vilevile, alihimiza watu kufanya kazi kwa bidii kwa kutumia kaulimbiu za “uhuru na kazi”, “siasa ni kilimo”, n.k. Hii ni baadhi tu ya mikakati iliyotumiwa na Mwalimu Nyerere katika kujenga Tanzania aliyotaka. Lakini pia, kwa kutambua hali halisi ya nchi yetu wakati huo, Baba wa Taifa, aliwahi kutamka, nanukuu “madini yetu tuliyonayo ni vema tukayaacha mpaka Watanzania watakapokuwa na ufahamu wa kutosha wataamua kuyachimba”, mwisho wa kunukuu.
Pamoja na misingi hiyo mizuri iliyowekwa na Baba wa Taifa, kupitia Azimio la Arusha, miaka michache tu baada ya Mwalimu Nyerere kung’atuka Azimio la Arusha lilikatupwa. Sasa sijui ilitokea kwa makusudi au bahati mbaya. Mimi sijui, ila ukweli ni kwamba, tulilitupa. Na baada ya kulitupa tukaanza kuuza mashirika na viwanda vyetu, hata vile vilivyojiendesha kwa faida, kwa matarajio kwamba tutakaowauzia wangeviendesha kwa ufanisi zaidi. Lakini haikuwa hivyo. Viwanda na mashirika mengi tuliyoyabinafsisha, sasa yamekufa. Leo viko wapi viwanda vya nguo, ngozi, nyama, matairi n.k? Kwa takwimu nilizonazo, jumla ya viwanda 197 vilivyoanzishwa na Mwalimu Nyerere hivi sasa havipo; vimekufa. Na hapa ndipo mara nyingi mimi huwa najiuliza, ni nani hasa aliyeturoga sisi Watanzania? Kwa nini tuliamua kuuza viwanda vyetu? Ilikuwaje tukaruhusu Shirika letu la Ndege libaki na ndege moja kutoka 9 zilizokuwepo? Kwanini Shirika letu la Nyumba lishindwe kujenga nyumba za wananchi wa kipato cha chini? Hivi wananchi wana namna hiyo hivi sasa hawapo? Au hawahitaji tena makazi mazuri na ya gharama nafuu? Lakini swali kubwa ninalojiuliza kila wakati ni kwanini tuliliacha Azimio la Arusha wakati maudhui na misingi yake, binafsi, mpaka leo, naiona kuwa ni mizuri. Ndio, ni mizuri. Tunachoweza kujadiliana ni kuhusu mikakati ya utekelezaji wake kwa nyakati za sasa, lakini maudhui na misingi yake bado ni mizuri.
Waheshimiwa Viongozi,
Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;
Jitihada za Baba wa Taifa kutetea wanyonge, kupigania umoja, amani, haki na usawa, hazikuishia tu hapa nchini. Zilivuka hadi nje ya mipaka ya nchi yetu. Tanzania, chini ya uongozi wa Mwalimu, ilikuwa mstari wa mbele kwenye harakati za ukombozi wa Bara la Afrika. Ilikuwa Makao Makuu ya Kamati ya Ukombozi ya OAU; na pia ilitoa hifadhi na mafunzo kwa vyama vya ukombozi vya Afrika Kusini, Angola, Msumbiji, Namibia na Zimbabwe, hadi nchi hizo zilipopata uhuru. Kama hiyo haitoshi, jana niliongea na Rais Yoweri Museveni wa Uganda ambaye aliniambia kuwa bila Mwalimu Nyerere huenda yeye asingekuwa Rais wa Uganda hivi sasa.
Mbali na kutoa mchango kwenye harakati za ukombozi, Baba wa Taifa alikuwa miongoni mwa waanzilishi wa OAU, sasa Umoja wa Afrika, na pia Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC). Tanzania pia chini ya uongozi wa Mwalimu Nyerere, ilikuwa mtetezi wa haki za wanyonge duniani kote. Mathalan, tulikuwa mstari wa mbele kutetea haki ya Jamhuri ya Watu wa China kupata uanachama kwenye Umoja wa Mataifa. Zaidi ya hapo, Mwalimu Nyerere alishiriki kwenye usuluhishi wa migogoro Barani Afrika. Na katika kudhihirisha hilo, wakati anafariki alikuwa Msuluhishi wa mgogoro wa Burundi.
Huyo ndiye Mwalimu Julius Kambarage Nyerere: Mpigania Uhuru; Mwanafrika halisi (Pan-Africanist); Mpenda Amani, Haki, Umoja na Usawa; Rais wa TAA na TANU; Waziri Mkuu wa kwanza wa Tanganyika; Rais wa Jamhuri ya Tanganyika; Rais wa Kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mwenyekiti wa kwanza wa CCM; Baba wa Taifa letu, ambaye leo tunakumbuka kifo chake na kusheherekea maisha yake. Kwa ujumla, naweza kusema kuwa Mwalimu Nyerere alikuwa miongoni mwa viongozi bora kuwahi kutokea sio tu hapa nchini, bali pia Barani Afrika na duniani kwa ujumla. Vijana na watoto wetu hawana budi kumfahamu mtu huyu wa aina yake katika historia ya nchi. Tuwafundishe watoto wetu fikra za Mwalimu Nyerere. Tuwasimulie kazi na mambo aliyoyasimamia. Na Watanzania wote kwa ujumla, hatuna budi kuenzi mambo mazuri aliyotuachia Baba wa Taifa letu. Nyerere oyeeee!!!!!
Waheshimiwa Viongozi,
Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;
Hayo niliyoeleza na maswali niliyouliza lengo lake sio kumtuhumu mtu yeyote. Nimeeleza na kuuliza maswali hayo kwa lengo la kumpa kila Mtanzania, fursa ya kutafakari ili kubaini wapi tulijikwaa au kukosea; na hatimaye tutafute njia ya kujisahihisha. Ni wazi kuwa, Baba wa Taifa, kama binadamu, alikuwa na mapungufu yake. Hata hivyo, mimi naamini kuwa endapo kila Mtanzania ataamua kwa dhati ya moyo wake kuenzi mambo mazuri ya Mwalimu Nyerere, nchi yetu itapata maendeleo makubwa tena kwa haraka.
Na katika hili, napenda nitumie fursa hii kuwathibitishia, kwa niaba ya mwenzangu Mheshimiwa Rais Shein, kuwa Serikali zetu mbili zimejipanga kuhakikisha zinaendelea kusimamia masuala na misingi mizuri iliyoachwa na waasisi wetu, Mwalimu Nyerere na Mzee Karume, pamoja na viongozi waliofuata wa nchi yetu. Ni dhahiri kuwa kuvaa viatu vyao sio jambo rahisi. Lakini, nina imani kuwa, kwa ushirikiano wenu, tutaweza kuyasimamia na kuyatekeleza haya. Mathalan, moja ya ndoto za Baba wa Taifa ilikuwa kuhamishia Makao Makuu ya nchi yetu, Dodoma. Uamuzi wa kuhamia Dodoma ulifanyika tangu mwaka 1973, lakini utekelezaji wake ulikuwa ukilegalega kwa sababu mbalimbali. Sisi tumeamua kuhamia Dodoma. Na tayari tumeshaanza kuhamia huko. Mawaziri, Makatibu Wakuu na baadhi ya watendaji kutoka Wizara zote tayari wameshamia. Waziri Mkuu naye amehamia. Makamu wa Rais atahamia mwaka huu; na mimi nitahamia mwakani. Hii inadhihirisha kuwa tumedhamiria kwa dhati kumuenzi Baba wa Taifa kwa vitendo na siyo maneno.
Sambamba na hilo, Serikali zetu mbili zitaendelea kuimarisha Umoja, Mshikamano na Muungano wetu. Tutadumisha pia amani yetu. Yeyote atakayejaribu kuhujumu Muungano wetu au kuvuruga amani yetu, tutapambana naye kwa nguvu zetu zote; na kwa vyovyote vile, atambue kuwa kamwe hatoshinda.
Zaidi ya hapo, tutaendeleza harakati za kujiletea maendeleo ya kiuchumi. Tutaimarisha na kuboresha miundombinu muhimu ya kiuchumi, hususan ya usafiri na nishati. Na katika hili, tumeamua kwa dhati kabisa kufufua Shirika letu la Ndege, ambalo kama nilivyoeleza awali, wakati wa Baba wa Taifa lilikuwa likifanya vizuri sana. Tayari tumenunua ndege mpya sita; mbili tayari zimewasili na zinatoa huduma. Na zile nyingine, napenda niwahakikishie kuwa nazo zitakuja. Aidha, tumeamua kutekeleza mradi mkubwa wa umeme wa Stiglier’s Gorge, ambao nao ulibuniwa tangu enzi za Baba wa Taifa. Sisi tumeamua kuutekeleza. Mradi huu utakapokamilika utazalisha takriban Megawati 2,100. Tumeshatangaza zabuni; na nimearifiwa kuwa makampuni 79 yamejitokeza kuomba zabuni ya kujenga mradi huo.
Tutaendelea kupanua wigo na kuboresha huduma za jamii, hususan afya, elimu na maji. Kwa bahati nzuri, Serikali zetu mbili kila mwaka zimekuwa zikiongeza bajeti kwenye sekta hizo. Aidha, tutaimarisha usimamizi wa rasilimali zetu. Kama mnavyofahamu, nchi yetu ina rasilimali nyingi: madini, mafuta, gesi, misitu, maeneo ya hifadhi na wanyamapori, pamoja na rasilimali za kwenye bahari, maziwa na mito. Lakini ninyi ni mashahidi, rasilimali hizi bado hazijatunufaisha. Ni watu wachache tu humu nchini na wengine kutoka nje, ndio wenye kunufaika nazo.
Napenda kuwaahidi kuwa katika kipindi changu cha uongozi, kamwe sitaruhusu hali hiyo kundelea. Nitashirikiana na mwenzangu Rais Shein pamoja na ninyi wananchi katika kuhakikisha rasilimali zetu zinatunufaisha. Tayari tumeshaanza kuchukua hatua mbalimbali. Kule Bara, kwa mfano, mwezi Julai mwaka huu, tulishapitisha sheria ya kulinda rasilimali zetu, hususan madini. Aidha, tumedhibiti biashara ya madini; na matokeo yake tumeanza kuyaona. Mathalan, kufuatia agizo langu nililolitoa mwezi Machi, 2017 kuhusu kuimarisha usimamizi wa rasilimali zetu, hususan madini, uzalishaji umeongezeka tofauti na tulivyokuwa tukiambiwa awali. Nitatoa mifano michache. Kabla ya agizo langu, almasi iliyozalishwa mwezi Januari 2017, ilikuwa carats 18,808.1; Februari 2017 carats 11,260.8; na mwezi Machi 2017 carats 15,743. Na niaka ya nyuma nayo, hali ilikuwa ni hivyo. Lakini baada ya agizo, uzalishaji umeongezeka. Mwezi Juni 2017 tulizalisha carats 28,889.7; mwezi Julai 2017 carats 27,578.75; Agosti 2017 carats 32,753; na Septemba 2017 carats 27,578.75. Na sio almasi pekee ndio uzalishaji umeongezeka. Uzalishaji wa Tanzanite piaumeongezeka.
Huu ni mwanzo tu. Tutachukua hatua hizi tulizozianza kwenye rasilimali zetu zote, ikiwemo gesi, utalii, misitu na baharini; ambako pia tumekuwa tukiibiwa sana. Na kuhusu rasilimali za maji, tayari tumeshaunda Chombo cha kusimamia uvuvi kwenye Bahari Kuu (Deep Sea Fishing Authority), ambacho kwa bahati nzuri Makao Makuu yake yapo huku Zanzibar.
Watanzania wenzangu, Mabibi na Mabwana;
Nafahamu kuwa kutokana na hatua tunazozichukua, wamejitokeza baadhi ya watu wanaowapotosha wananchi kwa kuwaambia kuwa hali ya uchumi wetu inadorora. Huo ni uzushi. Ukweli ni kwamba uchumi wetu unazidi kuimarika. Mwaka huu unatarajiwa kukua kwa asilimia 7.1, na hivyo kuifanya nchi yetu kushika nafasi ya tatu Barani Afrika. Sambamba na hilo, mfumuko wa bei unazidi kupungua. Mwezi Julai, mfumuko wa bei ulikuwa asilimia 5.2, lakini mwezi Agosti ulishuka hadi kufikia asilimia 5.0. Na matokeo yanaonekana. Bei za bidhaa nyingi zimeshuka. Mathalan, mfuko mmoja wa saruji hivi sasa unauzwa kwa wastani wa shilingi 10,500 kutoka wastani wa shilingi 15,000; mafuta ya kupikia yameshuka kutoka wastani wa shilingi 3,095 kwa lita hadi shilingi 2,863; mafuta ya taa yameshuka kutoka wastani wa shilingi 2,862 kwa lita hadi shilingi 1,925. Mifano ipo mingi.
Kama hiyo haitoshi, ujenzi wa viwanda unaendelea vizuri. Nafahamu kuna watu wanaobeza kuhusu ujenzi wa viwanda; lakini kweli ni kwamba vinajengwa. Mathalan, mwaka 2015 vilikuwepo viwanda 49,243, lakini hadi kufikia mwanzoni mwa mwaka huu, vimeongezeka hadi kufikia viwanda 52,549. Hii inamaanisha kwamba tangu tumeingia madarakani vimejengwa viwanda vipya 3,306. Halikadhalika, uwekezaji unazidi kuongezeka. Kwa mujibu wa Ripoti ya Uwekezaji Duniani (World Investment Report) ya mwaka 2017 iliyotolewa na Shirika la Umoja wa Mataifa linalosimamia Biashara na Maendeleo (UNACTAD), mwaka 2016 nchi yetu ilisajili miradi yenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 1.35, na hivyo kuongoza katika eneo letu la Afrika Mashariki. Aidha, kwa mujibu wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), hadi kufikia mwezi Septemba mwaka huu, tulikuwa tumesajili miradi 271 yenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 1.496 itakayotoa ajira zipatazo 22,000. Hii inadhihirisha kuwa uchumi wa nchi yetu unakwenda vizuri.
Licha ya ukweli huo, natambua kuwa, kutokana na hatua tunazozichukua za kuwabana mafisadi na wabadhirifu wa mali za umma, wapo wananchi wa kawaida kabisa, ambao sio wezi wala mafisadi, wanaothirika. Chukua mfano, umemkamata mwizi wa fedha za umma. Mwizi huyo kama alikuwa anatumia fedha alizoziiba kujenga nyumba zake, ni lazima ujenzi wa nyumba hizo utasimama. Ujenzi ukisimama, atakayeathirika sio huyo mwizi pekee, bali wajenzi waliokuwa wakijenga nyumba, mama lishe waliokuwa wakiwapikia wajenzi, bodaboda waliokuwa wakiwabeba wajenzi, wauza maji, soda n.k. Hili nalifahamu. Lakini kama kweli tunataka kupambana na wizi na ubadhirifu pamoja na kuleta maendeleo kwa nchi yetu, athari hizi hatuwezi kuzikwepa. Mabadiliko ya aina yoyote ile, lazima yana athari kama hizi. Lakini jambo la kututia moyo ni kwamba, athari hizi mara nyingi huwa ni za kipindi kifupi. Baada ya muda, zinakwisha. Kuna usemi usemao “Mabadiliko ni magumu mwanzoni, yanakuwa machungu yanapofikia katikati, lakini mwishoni matokeo yake ni mazuri na matamu”.
Hivyo, nawaomba wananchi mtuvumilie katika kipindi hiki cha mpito. Baada ya muda mfupi, mambo yatakuwa mazuri. Lakini hata kama hayatakuwa mazuri hivi karibuni, watoto na wajukuu wetu watanufaika. Na huo ndio uzalendo. Uzalendo maana yake ni kuwa tayari kujitolea kwa faida ya wengi au vizazi vijavyo. Waasisi na wazee wetu walifanya hivyo. Walijitolea kupigania uhuru wa nchi yetu, lakini tunaofaidi matunda ya uhuru ni sisi. Hivyo, na sisi hatuna budi kujitoa ili vizazi vyetu vijavyo vinufaike. Mimi pamoja na mwenzangu, Rais Shein, tumeamua kujitoa kuleta maendeleo ya nchi yetu. Hivyo, nawaomba wananchi mtuunge mkono. Je, mko tayari kutuunga mkono? Ahsanteni sana.
Waheshimiwa Viongozi;
Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;
Wageni Waalikwa;
Kama nilivyosema awali, Siku ya leo pia tunaadhimisha Kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru kwa mwaka huu wa 2017. Mwenge wa Uhuru ni moja ya tunu za nchi yetu, na uliasisiwa na Baba wa Taifa. Hata kabla ya nchi yetu kupata uhuru, Baba wa Taifa alitamka maneno yafuatayo katika Bunge la Kikoloni tarehe 22 Oktoba Mwaka 1959, nanukuu,”Sisi Watanganyika tunataka kuwasha Mwenge na kuuweka juu ya Mlima Kilimanjaro, umulike hata nje ya mipaka yetu, ulete matumaini pale ambapo hakuna matumaini, upendo pale ambapo pana chuki, heshima ambapo pamejaa dharau”, mwisho wa kunukuu. Tamko hili, mbali na kuamsha zaidi hamasa na kuchochea harakati za nchi yetu kudai uhuru; lilibeba falsafa nzito inayotoa taswira ya Taifa ambalo Baba wa Taifa alitaka kulijenga: Taifa lenye amani, linalojitegemea na lenye kuheshimu misingi ya utu, haki na usawa wa binadamu.
Azma ya kuwasha Mwenge ilitimia kwenye mkesha wa Uhuru, tarehe 9 Desemba, 1961, ambapo marehemu Kapteni Alexander Nyirenda, na wenzake, waliupandisha Mwenge wa Uhuru katika kilele cha Mlima Kilimanjaro. Na tangu mwaka 1964, kila mwaka, Mwenge wa Uhuru umekuwa ukikimbizwa nchi nzima, kuzunguka Mikoa yote ya Tanzania Bara na huku Zanzibar, Halmashauri zote za Wilaya, Vijiji pamoja na Mitaa mbalimbali ili kuendelea kukumbushana misingi ambayo juu yake nchi yetu imejengwa na inaendelea kujengwa; na pia nafasi ya nchi yetu mbele ya mataifa na watu wa mataifa wengine.
Katika kukumbushana huku, mbio za Mwenge huambatana na shughuli za ujenzi na uzinduzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo ambayo shabaha yake ni kukuza utu na ustawi wa watanzania. Kila Mwaka, Mwenge huzindua miradi mbalimbali. Mathalan, katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, Mwenge wa Uhuru umezindua jumla ya miradi 6,838 yenye thamani ya takriban shilingi trilioni 2.51; wastani wa miradi 1,367.6 kwa mwaka, ambayo thamani yake kwa wastani ni shilingi milioni 500. Mwaka huu pekee (2017), miradi iliyozinduliwa ni 1,512 yenye thamani ya shilingi trilioni 1.1. Miradi ambayo imekuwa ikizinduliwa na Mwenge inahusu sekta za afya, elimu, kilimo, maji, mawasiliano, mazingira, ujenzi, uwezeshaji, uvuvi na viwanda.
Sambamba na hilo, kila mwaka, mbio za Mwenge wa Uhuru zimekuwa na kaulimbiu yake, ambapo mwaka huu inasema“Shiriki Kukuza Uchumi wa Viwanda kwa Maendeleo ya Nchi Yetu”. Nawapongeza waliobuni kaulimbiu hiyo ambayo inakwenda sambamba na Dira ya Maendeleo ya Taifa letu na pia dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kujenga Tanzania ya viwanda ifikapo mwaka 2025. Nimefarijika zaidi kusikia kuwa katika Mbio za Mwenge mwaka huu, jumla ya viwanda 148 vimeziduliwa. Viwanda hivyo vimejengwa kwa gharama ya shilingi bilioni 468.46 na vinatarajiwa kuzalisha ajira 13,370. Pamoja na ajira hizo, nina uhakika kuwa viwanda hivyo vitaingizia nchi fedha za kigeni na kuipatia Serikali yetu mapato kupitia kodi; na hatimaye kusaidia kupunguza umaskini nchini. Hii ndiyo sababu tumekuwa tukihimiza ujenzi wa viwanda. Na hizi ni baadhi ya faida za Mwenge.
Watanzania Wenzangu;
Licha ya dhana na falsafa nzuri pamoja na faida za Mwenge nilizozitaja, wapo watu wanaoupinga na kutaka ufutwe. Mimi nawashangaa sana wanaosema ufutwe! Sijui ni watu wametokea sayari gani? Wakati mwingine huwa najiuliza hivi hawa nao kweli ni sehemu ya historia ya nchi hii? Najiuliza hivyo kwa sababu, kama kweli wewe ni Mtanzania na unaifahamu kidogo historia ya nchi hii pamoja na ya Baba wa Taifa na Mzee Karume, huwezi kuthubutu kutamka kuwa eti Mwenge ufutwe. Huwezi! Mwenge wa Uhuru ni tunu tuliyoachiwa na waasisi wa Taifa hili. Na kamwe mimi siwezi kukubali Mwenge ufutwe. Niwaombe Watanzania wenzangu tuwapuuze, tuwazomee na kuwasuta wote wanaosema Mwenge ufutwe. Tunazo sababu nyingi za kukataa Mwenge wetu kufutwa, lakini kwa ajili ya muda, nitataja kama tatu hivi.
Kwanza, Mwenge wa Uhuru hautafutwa kwa sababu unachochea maendeleo. Kama mlivyosikia, wakati wa Mbio za Mwenge za Uhuru Mwaka huu, miradi mbalimbali ya maendeleo imezinduliwa. Natambua kuwa mojawapo ya hoja zinazotolewa na wenye kuupinga Mwenge wetu ni suala la gharama. Lakini mimi nafahamu kuwa katika mbio za Mwenge mwaka huu, Serikali ilitenga shilingi milioni 463 kugharamia. Sasa ukilinganisha kiasi hicho na miradi 1,512 iliyozinduliwa yenye thamani inayokaribia shilingi trilioni 1.1, ni dhahiri kuwa hoja ya gharama haina mashiko? Lakini nafahamu kuwa wapo watakaosema kuwa miradi hiyo ingeweza kuzinduliwa hata bila ya Mwenge. Huenda hilo ni kweli. Lakini tujiulize, je kama Mwenge usingekuwepo, viongozi wa vijiji, kata, tarafa, wilaya na hata mikoa kweli wangekuwa wanahagaika kila mwaka kubuni miradi, kama ilivyo sasa? Nadhani majibu mnayo.
Lakini ukiachilia mbali hilo, Mwenge wa Uhuru pia unatumika kufichua maovu. Hivi punde nimepokea taarifa ya Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka huu, ambayo pamoja na masuala mengine, imefichua ubadhirifu kwenye utekelezaji wa baadhi ya miradi. Hii ndio kazi nyingine ya Mwenge wa Uhuru. Na napenda kutumia fursa kumhakikishia Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka huu na Watanzania kwa ujumla kuwa Serikali itafuatilia miradi hiyo na kuwachukulia hatua stahiki watakaohusika na ubadhirifu huo.
Pili, Mwenge wa Uhuru unawaunganisha Watanzania na kuimarisha Muungano wetu. Kama nilivyogusia hapo awali, Mwenge wa Uhuru uzunguka nchi nzima, Tanzania Bara na Visiwani. Wanaokimbiza Mwenge wanatoka pande zote mbili za Muungano. Kwa kufanya hivyo, Mwenge unatuunganisha Watanzania na kuimarisha Muungano wetu. Na kila unapopita mahali, unatoa matumaini mapya (kupitia miradi) na kusambaza upendo miongoni mwa Watanzania.
Tatu, na muhimu zaidi, ni kwamba Mwenge wa Uhuru ni alama ya uhuru na utaifa wetu. Kama mnavyofahamu, kila nchi hapa duniani ina alama zake za Taifa. Na sisi ni hivyo hivyo. Moja ya alama yetu ni Mwenge wa Uhuru. Nyingine ni Wimbo ya Taifa, Bendera ya Taifa, n.k. Hivyo kuufuta Mwenge wa Uhuru ni sawa na kufuta historia na alama inayotambulisha utaifa wetu.
Zaidi ya hapo ningependa kuwataarifu Watanzania wenzangu kuwa Mwenge au alama zinazofanana na Mwenge hazipo tu hapa nchini. Zipo nchi na taasisi za kimataifa zenye alama kama hii ya Mwenge wetu wa Uhuru. Baadhi ya nchi hizo ni majirani zetu wa Kenya, Msumbiji na Rwanda. Aidha, ninyi nyote hapa ni mashahidi, nchi yetu mara kadhaa imekuwa ikipokea Kifimbo cha Malkia wa Uingereza, Mwenge wa Olimpiki, Kombe la Dunia, n.k; lakini sijawahi, hata siku moja, kusikia watu wakipinga vifimbo hivyo kuja nchini au kutaka vifutwe. Sana sana tu, baadhi ya wanaoupinga Mwenge wetu, ndio hao hao wamekuwa mstari wa mbele kwenda kuvipokea vifimbo hivyo. Binafsi, siwapingi wao kwenda kupokea vifimbo hivyo. Acha waende, hakuna ubaya. Ubaya ni pale wanapoupinga Mwenge wetu, huku wakiona fahari kupokea vifimbo hivyo.
Hivyo basi, kwa niaba ya mwenzangu Mheshimiwa Rais Dkt. Shein, napenda kurudia tena kuwaambia watu hao kuwa, katika kipindi chetu cha uongozi, Mwenge wa Uhuru utaendelea kuwepo. Na niwaombe Watanzania wote wenye mapenzi mema na nchi yetu, mtuunge mkono.
Ndugu Viongozi,
Ndugu Wananchi, Mabibi na Mabwana;
Jambo la tatu ambalo limetukutanisha hapa leo ni kuadhimisha kilele cha Siku ya Vijana Kitaifa. Kama mnavyofahamu, duniani kote, vijana ndio uhai wa Taifa. Hii ni kwa sababu wapo wengi; wana nguvu na uthubutu. Hivyo basi, katika Siku hii ya kilele cha Sherehe ya Wiki ya Vijana Kitaifa, napenda kuwahimiza vijana kote nchini kushiriki kikamilifu katika shughuli za ujenzi wa Taifa letu. Mtambue ya kuwa Taifa hili ni lenu. Na maendeleo yake yanawategemea ninyi.
Lakini ili kijana aweze kushiriki kikamilifu kwenye shughuli za ujenzi wa Taifa na kutoa mchango wenye tija kwa nchi, hana budi, kujiendeleza kielimu kila wakati na kujiepusha na vitendo vitakavyopunguza uwezo wake, ikiwemo matumizi ya dawa za kulevya na ngono zembe. Na huo ndio wito wangu mwingine kwenu vijana wa Tanzania leo mnapoadhimisha kilele cha Wiki ya Vijana Kitaifa.
Waheshimiwa Mawaziri;
Waheshimiwa Viongozi mbalimbali mliopo,
Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;
Nimesema mengi. Lakini kabla sijahitimisha hotuba yangu, napenda kuwashukuru tena Mawaziri husika kwa kunialika kwenye tukio hili. Aidha, nawashukuru tena wananchi wa Mjini Magharibi na Zanzibar kwa ujumla kwa mapokezi yenu mazuri na pia kwa kujitokeza kwa wingi kwenye tukio hili. Lakini shukrani za pekee ziende kwenye makundi yafuatayo:
Kwanza, kwa waandaji wa tukio hili. Shughuli imefana sana. Hongereni sana. Pili, natoa shukrani kwa viongozi wa dini wote ambao wametuombea dua na kuliombea Taifa letu. Tatu, natoa shukrani na pongezi nyingi sana kwa wakimbiza Mwenge wetu wa Uhuru mwaka huu wakiongozwa na Amour Hamad Amour. Mmefanya kazi kubwa sana. Hatuna cha kuwalipa.
Napenda pia kutoa shukrani zangu nyingi kwa vyombo vya ulinzi na usalama kwa kuhakikisha usalama unakuwepo hapa uwanjani na sehemu zote ambazo Mwenge ulipita. Nawashukuru pia Vijana wa Halaiki kwa kutuburudisha. Mmetia fora. Mwisho lakini sio kwa umuhimu, navishukuru vyombo vya habari vyote vilivyoripoti tukio hili. Tunawashukuru sana.
Mwisho kabisa, kama mnavyofahamu, mimi pamoja na kuwa Rais, ni Mwenyekiti wa CCM. Natambua kuwa hapa kuna wana-CCM wengi. Na hivi sasa Chama chetu kipo kwenye zoezi muhimu la uchaguzi. Hivyo basi, napenda niwatakie wana-CCM wote uchaguzi mwema. Wito wangu kwenu, chagueni viongozi bora, wenye uwezo wa kuongoza, wasio makundi na wala kujihusisha na vitendo vya rushwa; ili Chama chetu kibaki kuwa imara. Mara zote tukumbuke wosia wa Baba wa Taifa wakati aking’atuka mwaka 1985, kuwa “Bila CCM imara, nchi itayumba”. Kidumu Chama cha Mapinduzi.
Napenda kuhitimisha kwa moja ya kauli za Baba wa Taifa, aliyoitoa kwenye Sherehe za Miaka 40 ya Uhuru wa Ghana zilizofayika tarehe 6 Machi, 1997 mjini Accra, nanukuu “Kizazi changu kiliongoza jitihada za kuleta uhuru wa kisiasa wa Bara letu. Kizazi cha sasa cha Waafrika hakina budi kuchukua kijiti pale tulipoishia, na kwa nguvu mpya, kusukuma mbele maendeleo ya Bara letu”, mwisho wa kunukuu. Hivyo basi, leo tunapokumbuka maisha ya Baba wa Taifa pamoja na falsafa ya Mwenge wa Uhuru, sisi Watanzania wa kizazi cha sasa, hatuna budi kukumbushana kuchukua kijiti kilichoachwa na waasisi wetu ili kulipeleka Taifa letu mbele zaidi, hasa kiuchumi.
Mungu Ibariki Familia ya Baba wa Taifa!
Mungu Ibariki Familia ya Mzee Karume pamoja na Waasisi wote!
Mungu Ubariki Mwenge wa Uhuru!
Mungu Wabariki Vijana wote wa Tanzania!
Mungu Ibariki Tanzania!
“Ahsanteni sana kwa kunisikiliza”
- Oct 03, 2017
HOTUBA YA MHESHIMIWA DKT. JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA WAKATI WA UFUNGUZI WA MKUTANO MKUU WA 33 WA JUMUIYA YA TAWALA ZA M...
Soma zaidiHotuba
Mheshimiwa Kassim Majaliwa, Waziri Mkuu
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Gulamhafeez Mukadamu, Mwenyekiti wa ALAT
na Mstahiki Meya wa Manispaa ya Shinyanga,
Mheshimiwa Stephen Peter Mhapa, Makamu Mwenyekiti wa ALAT
na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa,
Mheshimiwa Seleman Jafo, Naibu Waziri wa Nchi
Ofisi ya Rais-TAMISEMI;
Mheshimiwa Paul Makonda, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam;
Waheshimiwa Wabunge mliopo hapa;
Wastahiki Mameya wa Majiji na Manispaa pamoja na
Waheshimiwa Wenyeviti wa Halmashauri za Miji na Wilaya;
Waheshimiwa Madiwani wa Dar es Salaam, mkiongozwa
na Mstaiki Meya Isaya Mwita;
Mstahiki Meya wa Zanzibar pamoja na Viongozi mbalimbali
kutoka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar;
Mhandisi Mussa Iyombe, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais – TAMISEMI;
Prof. Faustin Kamuzora, Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais;
Bwana Abdallah Ngodu, Kaimu Katibu Mkuu wa ALAT;
Wakurugenzi wa Majiji, Manispaa, Miji na Halmashauri za Wilaya;
Wawakilishi wa Jumuiya za Serikali za Mitaa kutoka
Nchi za Afrika Mashariki mliopo;
Wawakilishi wa Wadhamini kutoka Makampuni
na Mashirika ya Serikali na Yasiyo ya Kiserikali,
Wawakilishi wa Vikundi vya Wajasiriamali;
Ndugu Waandishi wa Habari;
Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana:
Napenda nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, Muumba wetu, ambaye ametupa uhai na kutuwezesha kukutana hapa. Aidha, nakushukuru sana Mwenyekiti wa Jumuiya ya Tawala za Serikali za Mitaa Tanzania (Association of Local Government Authorities of Tanzania – ALAT), Mheshimiwa Mukadamu, kwa kunialika kufungua Mkutano huu Mkuu wa 33 wa ALAT. Nasema Ahsante sana.
Natambua baadhi yenu hapa mmesafiri umbali mrefu kuja kuhudhuria Mkutano huu, ambao awali ulipangwa kufanyika Jijini Mbeya, lakini siku za mwishoni ukalazimika kuhamishiwa hapa Dar es Salaam. Hivyo basi, kwanza, napenda kuwapa pole kwa uchovu wa safari. Lakini pili, kama mnavyofamu, mimi pamoja na kuwa na majukumu ya Urais, nina dhamana kwenye Wizara ya TAMISEMI; hivyo basi, napenda niwakaribishe wajumbe wote hapa Dar es Salaam na katika Mkutano huu wa 33 wa ALAT. Karibuni sana ndugu wajumbe.
Napenda pia hapa mwanzoni kabisa nimshukuru Mwenyekiti wa ALAT Taifa kwa salamu za pongezi alizozitoa kwangu, hususan kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Awamu ya Tano wa nchi yetu. Namshukuru pia kwa pongezi zake kuhusu utendaji kazi wa Serikali ya Awamu ya Tano. Nasema ahsante sana. Mmezidi kutupa moyo wa kuendelea kufanya kazi kwa bidii. Lakini nami ningependa kutumia fursa hii kuwapongeza, wewe Mheshimiwa Mwenyekiti na Makamu wako, Wastahiki Mameya wa Majiji na Manispaa pamoja na Wenyeviti wa Halmashauri zote nchini kwa kuchaguliwa kwenu. Napenda niwaahidi kuwa Serikali ya Awamu ya Tano itashirikiana nanyi kwa karibu katika kuhakikisha tunaleta maendeleo kwa wananchi na nchi yetu kwa ujumla.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Ndugu Wajumbe, Mabibi na Mabwana;
Kwangu mimi, Mkutano huu ni muhimu sana. Ni muhimu kwa sababu, kama mnavyofahamu, ALAT ni chombo kinachounganisha pamoja mamlaka na wadau mbalimbali wanaohusika na masuala ya Serikali za Mitaa hapa nchini. Na sote hapa tunatambua kuwa Serikali za Mitaa ni mamlaka ambazo zipo karibu zaidi na wananchi. Kwa sababu hiyo, binafsi naona kuwa hii ni fursa nzuri kwangu kuzungumza kwa kina na Watanzania wenzangu; na hasa kwa kuzingatia kuwa hii ni mara yangu ya kwanza kuhudhuria Mkutano huu wa ALAT, tangu nimechaguliwa kuwa Rais wa Awamu ya Tano wa nchi yetu. Hivyo basi, nina imani Mheshimiwa Mwenyekiti pamoja na ndugu wajumbe mtaniruhusu, kabla ya kuzungumzia masuala yaliyotuleta hapa, kueleza hatua mbalimbali ambazo tumechukua tangu tumeingia madarakani pamoja na mipango na mikakati tuliyonayo ya kuleta maendeleo kwa nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti na Ndugu Wajumbe;
Tangu tumeingia madarakani, takriban miezi 23 iliyopita, tumefanya mambo mengi ya kuleta maendeleo kwa nchi yetu. Mtakumbuka, tulianza kwanza kuimarisha ukusanyaji wa mapato na kudhibiti ubadhirifu wa mali za umma. Tulibana mianya ya ukwepaji kodi na hivyo kutuwezesha kuongeza ukusanyaji wa mapato kutoka wastani wa shilingi bilioni 850 kwa mwezi hadi kufikia shilingi trilioni 1.3. Sambamba na kuongeza ukusanyaji mapato, tuliamua kudhibiti ubadhirifu wa mali za umma. Tumezuia safari za nje, warsha na semina zisizo na tija. Hivi majuzi tu mmesikia kuwa ujumbe wetu kwenye Mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ulikuwa na watu watatu tu na walituwakilisha vyema.
Kutokana na kuongeza mapato na kubana matumizi, hivi sasa tunawalipa mishahara ya watumishi wetu kwa wakati. Aidha, tumeweza kulipa madai mbalimbali ya watumishi, ikiwa ni pamoja na michango yao kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii. Zaidi ya hayo, tumeweza kuongeza bajeti yetu ya maendeleo kutoka wastani wa asilimia 26 hadi kufikia wastani wa asilimia 40 hivi sasa.
Hii ndiyo imetuwezesha kupanua wigo na kuboresha huduma mbalimbali za jamii, hususan elimu, afya na maji. Kama mnavyofahamu, kwenye elimu, baada ya kuingia madarakani, tulianza kutoa elimu bila malipo kuanzia shule ya msingi hadi sekondari, ambapo mwanzoni tulikuwa tukitenga kila mwezi shilingi bilioni 18.77. Mwezi Julai 2016, kiasi hicho kiliongezwa hadi kufikia shilingi bilioni 23.868, na hivyo kufanya hadi mwezi Agosti mwaka huu, kuwa tumetumia kiasi cha shilingi bilioni 465.6 kugharamia elimu bila malipo. Matokeo yake, bila shaka, nyote hapa mnafahamu. Idadi ya wanafunzi wanaoanza darasa la kwanza na kidato cha kwanza imeongezeka maradufu; darasa la kwanza kwa takriban asilimia 90 na kidato cha kwanza takriban asilimia 25. Tumeongeza pia idadi ya wanafunzi wa elimu ya juu wanaopata mikopo kutoka 98,300, wakati tunaingia madarakani, hadi kufikia takriban 125,000. Hii imewezekana baada ya kuongeza bajeti ya mikopo kutoka shilingi bilioni 365 hadi kufikia shilingi bilioni 483.
Kwenye afya, nako tumeimarisha na kuboresha upatikanaji wa huduma hiyo. Tumeongeza bajeti ya kununua madawa kutoka shilingi bilioni 31 wakati tunaingia madarakani hadi kufikia shilingi bilioni 269, mwaka huu wa fedha. Hii imeongeza sana upatikanaji wa madawa kwenye hospitali zetu, na hasa baada ya Serikali kuanza utaratibu wa kununua dawa moja kwa moja kutoka kwenye viwanda zinakozalishwa. Aidha, Serikali imegawa katika kila halmashauri vifaa tiba, ikiwemo vitanda ya kawaida, vitanda vya kujifungulia, magodoro na mashuka, ambavyo thamani yake kwa ujumla ni shilingi bilioni 3.58. Halikadhalika, katika kuboresha Huduma za Afya ya Mama na Mtoto, Serikali ilipata fedha jumla ya shilinigi bilioni 161.9 kutoka Benki ya Dunia pamoja na wadau wengine wanaosaidia sekta ya afya kwenye Mfuko wa Pamoja (Busket Fund). Fedha hizo zimepangwa kutumika kuboresha vituo vya afya 170 ili kuviwezesha kutoa huduma za uzazi za dharura kwa lengo la kuokoa maisha ya mama na mtoto; na zinatumwa moja kwa moja katika vituo vya afya husika katika mwaka huu wa fedha.
Kuhusu sekta ya maji, miradi mingi ya maji hivi sasa inatekelezwa sehemu mbalimbali nchini. Karibu kwenye mikoa yote kuna miradi mikubwa ya maji inatekelezwa. Mathalan, mwezi Machi 2017, nilikuwa Mkoa wa Lindi ambapo nilitoa maelekezo ya kukamilishwa kwa haraka mradi wa maji wa Ng’apa wenye thamani ya shilingi bilioni 32, ambao nimeambiwa unaendelea kukamilika. Mwezi Juni mwaka huu, nilizindua Mradi wa Maji wa Ruvu Juu pale Mlandizi kwa ajili ya kuhudumia Jiji hili la Dar es Salaam na sehemu za Mkoa wa Pwani. Aidha, mwezi Julai, nilizindua mradi mkubwa wa maji pale Sengerema wenye thamani ya shilingi bilioni 22.4. Mwezi Julai pia niliweka Mawe ya Msingi kwenye mradi wa maji wa Kigoma wenye thamani ya shilingi bilioni 42 na Mradi Mkubwa wa Maji kutoka Ziwa Victoria kwenda miji ya Nzega, Tabora na Igunga wenye thamani ya shilingi ya shilingi bilioni 550. Juzi mmeshuhudia Mheshimiwa Waziri Mkuu akizindua mradi wa maji kule Longido wenye thamani ya shilingi bilioni 16; lakini nafahamu pia mradi wa maji wa Musoma umekamilika na unasubiri kuzinduliwa. Halikadhalika, nafahamu kuwa kuna mradi mkubwa wa maji unatekelezwa katika jiji la Arusha wenye thamani ya shilingi bilioni 476, na wakati wowote tutaanza utekelezaji wa mradi mwingine mkubwa wenye thamani ya shilingi bilioni 250 kwa ajili ya miji ya Bariadi, Legangabilili, Maswa, Meatu na Busega. Kama hiyo haitoshi, mwezi Julai mwaka huu, Serikali ya India ilitupatia mkopo wa masharti nafuu wenye thamani ya Dola za Marekani milioni 500, sawa na takriban shilingi trilioni 1.2, kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maji kwenye miji 17, ikiwemo Zanzibar. Kwa ujumla, miradi mingi inatekelezwa sehemu mbalimbali nchini. Hivyo basi, nina imani kuwa baada ya muda mfupi, tutakuwa tumepunguza kwa kiasi kikubwa tatizo la maji nchini. Nitoe wito kwenu viongozi wa Serikali za Mitaa kuendelea kuwahamasisha wananchi kutunza mazingira pamoja na vyanzo vya maji. Bila kufanya hivyo, itafika wakati tutakuwa na miundombinu mizuri isiyotoa maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti na Ndugu Wajumbe;
Mbali na kuboresha huduma za jamii, tumeweza kuimarisha miundombinu ya kiuchumi, hususan usafiri na nishati. Tumeanza ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kimataifa kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza na Kigoma na kisha nchi za Burundi na Rwanda, kwa fedha zetu wenyewe. Ujenzi wa kipande cha kilometa 300 kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro tayari umeanza, ambapo kiasi cha shilingi trilioni 2.74 kitatumika. Na hivi majuzi (ijumaa), tumesaini mkataba wa kuanza ujenzi wa kipande cha kilometa 412 kutoka Morogoro hadi Dodoma (Makutopora) kwa thamani ya shilingi trilioni 4.328; na hivyo gharama za ujenzi kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma kufikia shilingi trilioni 7.062.
Tunafanya upanuzi wa Bandari zetu za Mtwara na Dar es Salaam. Mwezi Machi mwaka huu, niliweka Jiwe la Msingi la Upanuzi wa Bandari ya Mtwara kwa thamani ya shilingi bilioni 130. Aidha, mwezi Julai mwaka huu, niliweka Jiwe la Msingi la Upanuzi wa Bandari ya Dar es Salaam, ambao thamani yake ni shilingi bilioni 926.2. Kama hiyo haitoshi, wakati nikiwa Tanga katika sherehe za kuweka Jiwe la Msingi la Mradi wa Bomba la Mafuta kutoka Hoima nchini Uganda hadi Bandari ya Tanga, nilimwagiza Waziri wa Ujenzi kuanza taratibu za kutafuta mkandarasi wa kupanua Bandari ya Tanga kwa thamani ya shilingi bilioni 16. Vilevile, tumetengeneza meli mbili za Mv. Iringa na Mv. Ruvuma, ambazo zinatoa huduma katika Ziwa Nyasa. Aidha, tupo katika hatua za mwisho za kupata wakandarasi kwa ajili ya ukarabati wa meli mbili za Mv. Victoria na Butiama pamoja na ununuzi wa meli mpya kwa ajili ya Ziwa Victoria.
Sambamba na hayo, tunakamilisha upanuzi wa Viwanja Vikubwa vya Ndege vya Mwalimu Julius Nyerere kwa gharama ya shilingi bilioni 560 na Kilimajaro kwa thamani ya shilingi bilioni 91. Aidha, tunaendelea na ukarabati wa viwanja takriban 11 vya ndege sehemu mbalimbali nchini, ikiwemo Mwanza (shilingi bilioni 90); Mtwara (shilingi bilioni 46); Shinyanga (shilingi bilioni 49.2); Sumbawanga (shilingi bilioni 55.9); Musoma (shilingi bilioni 21), Songea (shilingi bilioni 21) na Iringa (shilingi bilioni 39). Tumenunua ndege mpya sita, mbili tayari zimewasili na kuanza kazi, kwa ajili ya kutoa huduma ya usafiri na kukuza sekta ya utalii. Kama mnavyofahamu, ukuaji na ustawi wa sekta ya utalii kwa kiasi kikubwa unategemea uwepo na ubora wa usafiri wa anga katika nchi. Vilevile, ujenzi wa barabara unaendelea vizuri. Tangu tumeingia madarakani tumeshajenga takriban kilometa 1,500 za lami kwa thamani ya shilingi trilioni 1.8. Na nyingi bado tunaendelea kuzijenga. Nikianza kuzitaja tunaweza kumaliza kesho. Lakini kwa kuwa leo tupo hapa Dar es Salaam, niseme tu kuwa, moja ya barabara tunayotarajia kuanza kujenga hivi karibuni ni barabara ya njia sita kutoka Dar es Salaam hadi Chalinze. Aidha, tunaendelea na ujenzi wa barabara za juu pale TAZARA (shilingi bilioni 94.031) na Ubungo (shilingi bilioni 177.424); na muda si mrefu tutaanza ujenzi wa Awamu ya II, III na III za miundombinu ya magari ya mwendokasi kwa thamani ya shilingi bilioni 891. Tunajenga miundombinu hii ili kupunguza tatizo la msongamano wa magari katika Jiji hili.
Kuhusu umeme, nako tunaendelea vizuri. Lakini tunafahamu kuwa mahitaji ya umeme nchini bado ni makubwa. Hivyo, tunaendelea na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kuzalisha umeme, ikiwemo Kinyerezi I na II, ambayo kwa pamoja inatarajiwa kuzalisha Megawati 565, kwa kutumia gesi yetu asilia. Miradi hii kwa ujumla ina thamani ya shilingi trilioni 1.2. Aidha, maandalizi kwa ajili ya miradi ya Kinyerezi III na IV, ambayo itazalisha takriban Megawati 600, inaendelea vizuri. Tumeanza pia maandalizi ya ujenzi wa mradi mkubwa wa kuzalisha umeme wa maji pale Stiglier’s Gorge, ambao utazalisha Megawati 2,100. Tunataka, hadi kufikia mwaka 2020, nchi yetu iwe na angalau Megawati 5,000 kutoka Megawati 1,460 za sasa. Sambamba na hilo, tunaendelea na jitihada za kupeleleka umeme vijijini. Mpaka sasa, tumeshapeleka umeme kwenye vijiji zaidi ya 4,000. Aidha, mwaka huu tumeanza Awamu ya Tatu ya Mpango wa Umeme vijijini. Lengo letu ni kufikisha miundombinu ya umeme kwenye vijiji vipatavyo 7,873 ifikapo mwaka 2020/21. Katika bajeti ya mwaka huu, tumetenga shilingi bilioni 469.09 kuanza kutekeleza mradi huo. Tunataka dhana ya viwanda inasambae hadi vijijini.
Mheshimiwa Mwenyekiti na Ndugu Wajumbe;
Mbali na kuongeza ukusanyaji mapato na kudhibiti matumizi, tumeimarisha nidhamu na kurejesha heshima kwenye utumishi wa umma. Tumewachukulia hatua za kinidhamu baadhi ya watumishi wazembe na wala rushwa. Zaidi ya hapo, tumewaondoa takriban watumishi hewa wapatao 20,000, ambao walikuwa wakiigharimu Serikali takriban shilingi bilioni 19.848 kwa mwezi; na kwa mwaka shilingi bilioni 238.176. Vilevile, tumewaondoa watumishi wenye vyeti feki wapatao 12,000, ambao kwa mwaka waligharimu Serikali shilingi bilioni 142.9. Tumefanya hivyo ili kurudisha nidhamu na kuenzi elimu na ueledi katika utumishi wa umma. Mtakubaliana nami kuwa, uwepo wa watumishi hewa na wenye vyeti feki ulikuwa ukizorotesha na kupunguza ufanisi katika utoaji huduma kwenye taasisi za umma. Aidha, uwepo wa watumishi wenye vyeti feki ulikuwa unapunguza heshima na hadhi ya elimu na ujuzi, na hivyo, kushusha ari na morali miongoni mwa watumishi wenye sifa.
Sambamba na hilo, tumejitahidi kuondoa kero mbalimbali, ambazo zilikuwa zikiwasumbua wananachi. Mathalan, tumeondoa kero za utitiri wa kodi kwa wakulima, wafugaji na wavuvi. Tumefuta tozo 80 kwa wakulima, tozo 7 kwa wafugaji na tozo 5 kwa wavuvi. Tumepiga marufuku kutoza kodi mazao yanayosafirishwa kutoka Halmashauri moja kwenda nyingine, ambayo uzito wake hauzidi tani moja. Na kwa kuwa tozo hizi nyingi tulizozifuta zilikuwa zikisimamiwa na ninyi watu wa Serikali za Mitaa, niwaombe kupitia vikao vyenu, mkafanye taratibu za kuzifuta kama bado hamfanya hivyo. Lakini, kama hiyo haitoshi, kwa wakulima pia, kufuatia uamuzi wa Serikali wa kuanzisha utaratibu wa kununua mbolea kwa pamoja (Bulk Procurement System – BPS), tumeweza kupunguza bei ya mbolea ya kupandia na kukuzia kuanzia mwezi uliopita (Septemba). Mathalan, Mkoani Lindi, bei ya mfuko mmoja wa mbolea ya kupandia imeshuka kutoka shilingi 100,000 hadi kufikia shilingi 51,000. Mikoa mingine bei zimepungua kutegemeana na gharama za usafirishaji. Na huu ni mwanzo tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti na Ndugu Wajumbe;
Baada ya kuchukua hatua za kuimarisha ukusanyaji wa mapato na kudhibiti matumizi; kuboresha huduma za jamii; kuimarisha miundombinu ya uchumi; kurejesha heshima ya utumishi wa umma na kushughulikia baadhi ya kero zinazowakabili wananchi wetu; ambazo kimsingi, bado tunaendelea nazo, sasa tumeanzisha vita ya uchumi. Kama mnavyofahamu, nchi yetu ni tajiri. Tuna rasilimali za kila aina. Tunayo madini misitu, rasilimali za misitu na majini, n.k. Aidha, nchi yetu inashika nafasi ya pili kwa vivutio vya utalii duniani baada ya Brazil. Lakini pamoja na kuwa na rasilimali nyingi kiasi hicho, bado hazijatunufaisha. Wanaonufaika ni watu wengine.
Kutokana na hali hiyo, tumeamua kuchukua hatua za makusudi kulinda rasimali zetu. Mlisikia kuwa tuliunda Tume za kuchunguza biashara ya madini na vito vya thamani. Matokea yake, kila mmoja wetu hapa amesikia. Lakini kwa kifupi, tulikuwa tunaibiwa sana. Kwa sababu hiyo, mwezi Julai 2017 tulipitisha Sheria za kulinda rasilimali zetu, hususan madini. Aidha, kwa lengo hilo hilo la kulinda rasilimali zetu, hivi majuzi nikiwa Mererani niliagiza kuanza mara moja kwa ujenzi wa uzio kuzunguka eneo lenye rasilimali nyingi ya madini ya Tanzanite, ili kudhibiti vitendo vya wizi. Nafurahi ujenzi huo tayari umeanza. Lakini niseme tu kuwa huu ni mwanzo tu. Hatutaishia kwenye madini pekee. Tutaenda pia kwenye rasilimali zetu nyingine, ikiwemo za utalii, misitu na za majini. Tunataka kuona, rasilimali za nchi yetu, zinatunufaisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti na Ndugu Wajumbe;
Katika kuchukua hatua hizi, ni dhahiri kuwa wapo watu walioathirika na kuumia. Na natambua kuwa wapo watu wanalalamika. Lakini kwangu mimi, hili ni jambo la kawaida, kama kweli tunahitaji maendeleo. Maendeleo hayaji kirahisi. Maendeleo sio lelemama. Maendeleo ni mapambano. Hivyo basi, niwaombe Watanzania wenzangu tujidhatiti katika harakati za kuleta maendeleo kwa nchi yetu. Waingereza wana usemi wao usemao “No Pain, No Gain” au “No sweet without sweat”. Lakini ningependa kusema tu kuwa watu wengi wanaolalamika hivi sasa ni wale waliokuwa wakinufaika na mfumo ulikuwepo zamani. Huwezi kutegemea mmiliki wa benki iliyokuwa ikinufaika kwa kufanya biashara na Serikali afurahie hatua tunazozichukua; Haiwezekani mtu aliyekuwa akilipwa mishahara na posho za watumishi hewa afurahie hatua tunazochukua; Huwezi kutegemea mtu aliyekuwa akikwepa kodi afurahie hatua tunazozichukua; Huwezi kutegemea mtu aliyezoea kusafiri nje kila wiki afurahie hatua tunazozichukua; huwezi kutegemea mtu aliyepata ajira kwa kutumia cheti feki alichokinunua Kariakoo afurahie hatua tunazozichukua. Lakini pia huwezi kutegemea mtu aliyekuwa akinufaika na fedha za pembejeo hewa (ambapo katika Halmashauri 140 zilizofanyiwa uchunguzi, imebainika kuwa zilitolewa pembejeo hewa zenye thamani ya shilingi bilioni 57.963) na kaya masikini hewa (56,000) kupitia TASAF, afurahie hatua tunazozichukua. Ni dhahiri kuwa watu waliokuwa wakinufaika, watalalamika.
Hivyo basi, binafsi sishitushwi sana na malalamiko yanayotolewa na baadhi ya watu. Natambua, ukitumbua mtu jipu ni lazima atalalamika. Sana sana tu, kelele zinazopigwa hivi sasa zinatuongezea nguvu zaidi ya kuendelea na jitihada tulizozianza, ambazo kwa hakika kabisa, naweza kusema sio tu zinaungwa mkono na wananchi walio wengi bali pia zimeanza kuleta matokeo chanya ya kiuchumi kwa nchi yetu. Kama mnavyofahamu, nchi yetu ni miongoni mwa nchi zinaongoza kwa ukuaji uchumi Barani Afrika hivi sasa, ambapo mwaka huu uchumi wetu unatarajiwa kukua kwa asilimia 7.1. Hii inafanya nchi yetu kushika nafasi ya tatu. Sambamba na hilo, tumeweza kudhibiti mfumko wa bei. Mathalan, mwezi Julai, mfumko wa bei ulikuwa asilimia 5.2, lakini mwezi Agosti ulishuka hadi kufikia asilimia 5.0. Hii ni dalili njema. Lakini zaidi ya hapo, kinyume na baadhi ya watu wanavyosema, nchi yetu imeendelea kung’ara katika kuwavutia wawekezaji wengi. Hivi majuzi mmemsikia Mkurugenzi Mkuu wa Kituo Cha Uwekezaji (Tanzania Investment Centre – TIC) akieleza kuwa mwaka uliopita nchi yetu iliongoza kwa kuvutia wawekezaji wengi kwenye Ukanda wetu wa Afrika Mashariki. Tathmini hii inaenda sambamba na Ripoti ya African Economic Outlook Toleo la 16 iliyotolewa kwa pamoja na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), ambayo inataja nchi yetu kuwa miongoni mwa nchi kumi bora Barani Afrika kwa kuvutia wawekezaji mwaka 2016. Na hiki ni kielezo kuwa hatua tunazochukua ni nzuri na mwelekeo wetu ni mzuri. Na huenda hii ndio sababu viongozi wengi wa nje wanatembelea nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Ndugu Wajumbe, Mabibi na Mabwana;
Niliona nianze na hayo ili kuwapa taswira halisi ya hali ilivyo hapa nchini. Na kwa kuwa ninyi mko karibu zaidi na wananchi na mnashirikiana nao kwenye mambo mengi, nina uhakika kuwa mtaenda kuwafafanuliwa kuhusu hatua hizi tunazozichukua. Baada ya kusema hayo, sasa naomba nizungumzie masuala yanayohusu Mkutano huu wa leo.
Kwanza kabisa, napenda kuipongeza ALAT pamoja na mamlaka za Serikali za Mitaa kote nchini kwa kazi kubwa mnazofanya katika kuleta maendeleo kwa nchi yetu. Mafanikio mengi ya Serikali niliyoyataja hapo awali, yamepatikana kutokana na jitihada mnazozifanya ninyi lakini pia ushirikiano mnaotupa sisi wa Serikali Kuu. Kwa kutumia vyanzo vyenu vya mapato, mmeweza kutekeleza miradi mingi ya maendeleo, ikiwemo ujenzi wa shule, hospitali, vituo vya afya, zahanati, miradi ya maji pamoja na barabara. Aidha, mara nyingi, ninyi ndio mmekuwa wasimamizi wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali Kuu kwenye maeneo yenu. Kwa sababu hiyo, sina budi, kuwapongeza.
Lakini pamoja na pongezi hizo, hampaswi kuridhika na mafanikio yaliyopatikana. Kama mnavyofahamu, nchi yetu bado ina safari ndefu ya kufikia kule tunakotamani. Mathalan, nimeeleza hapo awali kuwa Serikali hivi sasa inatekeleza elimu bila malipo, lakini ukiachilia mbali tatizo la uhaba wa madawati ambalo tumelipunguza kwa kiwango kikubwa, bado tuna upungufu wa madarasa, maabara, vyoo, nyumba za walimu, n.k. Hivyo basi, Mamlaka za Serikali za Mitaa, hazina budi, kubuni mikakati ya kushughulikia matatizo hayo. Aidha, kwa kuwa mko karibu na wananchi, mnao wajibu wa kuwahimiza wananchi kupeleke watoto wao mashuleni ili wanufaike na fursa iliyotolewa na Serikali ya kutoa elimu bila malipo.
Kwenye afya pia, bado kuna upungufu mkubwa ya miundombinu, ikiwemo hospitali, vituo vya afya, zahanati, nyumba za watumishi, n.k. Huko nako hamna budi kubuni mikakati ya kushughulikia matatizo hayo. Aidha, kwa kuwa hivi sasa Serikali imeongeza upatikanaji wa madawa kwenye hospitali zetu, niwaombe waheshimiwa Madiwani na Wakurugenzi mwendelee kuhamasisha wananchi kujiunga na mifuko ya bima za afya ili kupata matibabu bila vikwazo. Vilevile, hakikisheni mnasimamia vyema fedha na matumizi ya dawa, ikiwemo kuanzisha mifuko ya dawa (Drug Revolving Fund) kwa kila Halmashari, ili kuhakikisha upatikanaji endelevu wa fedha za dawa.
Sambamba na hayo, ili kuhakikisha mnakuwa na uwezo wa kutosha wa kuboresha huduma za jamii nilizozitaja na kutekeleza miradi ya maendeleo, hamna budi kuimarisha ukusanyaji wa mapato. Nafahamu hii ni changamoto kubwa inayozikabili mamlaka za Serikali za Mitaa. Na kimsingi, nionavyo mimi, tatizo sio kwamba hakuna vyanzo vya mapato. Hapana. Hali hii inatokana na sababu kubwa mbili. Kwanza, fedha nyingi zinazokusanywa hupotelea kwenye mifuko ya “wajanja” wachache. Pili, watendaji wengi wanakosa ubunifu katika kubuni vyanzo endelevu vya mapato. Ndio maana kila siku utaona wanaongeza tozo kwenye mazao ya wakulima, wavuvi au wafugaji. Hivyo basi, nitoe wito kwenu kuhakikisha mnatengeneza mifumo madhubuti ya ukusanyaji mapato, hususan ukusanyaji mapato kwa njia ya kielektroniki. Na katika hili, ningependa kuwasisitiza kutumia Wakala wa Serikali Mtandao katika kutengeneza mifumo yenu ya ukusanyaji kodi. Aidha, nawahimizeni kubuni vyanzo endelevu vya mapato.
Halikadhalika, kuhakikisheni mnasimamia vizuri fedha mnazokusanya na zile zinazotolewa na Serikali Kuu kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo. Natambua hivi sasa suala la hati chafu limepungua kwenye halmashauri nyingi. Lakini hii haimanishi kuwa ubadhirifu na wizi umekwisha kwenye Halmashauri zetu. Ubadhirifu bado upo. Imethibitika kuwa mara nyingi taarifa za vitabuni hazifanani na hali halisi ya utekelezaji wa miradi na kazi (value for money). Kwa maneno mengine, kazi inayofanyika hailingani na thamani halisi ya fedha inayotumika. Hivyo basi, nawaomba ndugu wajumbe mlipe suala hili la usimamizi wa fedha za Serikali kipaumbele kinachostahili. Miradi inayotekelezwa ni lazima iendane na thamani ya fedha zinazotolewa. Na katika hili, msisite kuwachukuliwa hatua za kinidhamu au kuwatumbua wale wote wakatakaojihusisha na ubadhirifu wa fedha zinazotolewa kwa ajili ya maendeleo ya wananchi. Lakini niwaombe na ninyi kuacha mtindo wa kutoa zabuni kwenye makampuni yenu au ya washirika wenu, ambayo hayana uwezo wa kutekeleza miradi husika.
Masuala mengine ambayo ningetamani sana kuona mnayapa kipaumbele kwenye maeneo yenu ni kudhibiti migogoro na makundi kwenye halmashauri zetu. Haipendezi kuona, kwenye Halmashauri, kuna kundi la Meya na Naibu Meya; ama kundi la Mwenyekiti na Mkurugenzi. Hali hii inazorotesha utendaji na kupunguza kasi ya kuwapelekea maendeleo wananchi. Nawasihi pia muendelee kushughulikia kero mbalimbali zinazowakabili wananchi, hasa wananchi wa kipato cha chini, ikiwemo, kama nilivyosema awali, utitiri wa kodi kwa wakulima, wafugaji na wavuvi; na halikadhalika ukosefu wa maeneo ya biashara kwa wafanyabiashara wadogo. Vilevile, nawasihi muendelee kuwahimiza wananchi kuhusu umuhimu wa kudumisha amani na umoja wetu, kulipa kodi na kuchapa kazi kwa bidii. Nina imani, sote tukifanya haya, nchi yetu itapata maendeleo, tena kwa haraka.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Katika risala yako umeeleza kuhusu mipango yenu mbalimbali na kuwasilisha baadhi ya maombi. Kwa ujumla, niseme tu kuwa nimeyapokea maombi yenu yote. Lakini nakiri kuwa nimefarijika sana kusikia azma yenu ya kuhamishia Makao Makuu yenu kutoka hapa Dar es Salaam kwenda Dodoma, Makao Makuu ya nchi yetu. Nawapongezi sana kwa kuunga mkono dhamira ya Serikali ya kuhamia Dodoma. Na napenda kutumia fursa hii kuwahakikishia kuwa, kama nilivyoahidi kwenye hotuba yangu ya kupokea wadhifa wa kuwa Mwenyekiti wa CCM mwezi Julai mwaka jana, hadi kufikia mwaka 2020, Serikali yote itakuwa imehamia Dodoma. Kama mnavyofahamu, tayari Waziri Mkuu, Mawaziri, Makatibu Wakuu na baadhi ya watendaji wa Wizara wameshahamia Dodoma. Makamu wa Rais anatarajia kuhamia mwaka huu. Na mimi natarajia kuhamia mwakani. Hivyo basi, narudia tena, kuwashukuru kwa uamuzi wenu wa busara wa kuhamia Dodoma. Na kuhusu jengo mnalotaka kujenga Dodoma kwa ajili ya ofisi na kitega uchumi, wakati ukifika, Serikali kulingana na uwezo wake wa kifedha, itaangalia uwezekano wa kuwaunga mkono.
Kwenye Risala yako pia umeeleza suala la ucheleweshaji wa fedha za maendeleo kutoka Serikali Kuu, suala la uhaba wa watumishi wa Serikali za Mitaa na pia posho za Waheshimiwa Madiwani. Serikali inatambua masuala hayo yote. Tutaendelea kuhimiza HAZINA kutoa fedha za maendeleo kwa haraka. Kama mnavyofahamu, tangu tumeingia madarakani, tumejitahidi sana kuhakikisha fedha zinatolewa kwa wakati. Mathalan, katika Bajeti ya mwaka 2014/2015 fedha za maendeleo zilizotengwa kwenda kwenye halmashauri (Serikali za Mitaa) ni shilingi bilioni 339.8 lakini zilizotoka zilikuwa shilingi bilioni 250.2 sawa na asilimia 62; mwaka 2015/16 zilitengwa shilingi bilioni 296.3, zikatolewa shilingi bilioni 168.8 sawa na asilimia 57; mwaka 2016/17 zilitengwa shilingi bilioni 256.7, zilizotolewa ni shilingi 251.5 sawa na asilimia 98. Na katika mwaka huu wa fedha, tumetenga shilingi bilioni 308.6, na napenda niwahakikishie fedha zote zitatolewa. Sambamba na hilo, mwaka huu, tumeanzisha Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (TARURA), ambayo imetengewa shilingi bilioni 246, ukiachilia mbali fedha zilizoahidiwa na wafadhili mbalimbali, ikiwemo Benki ya Dunia. Hivyo basi, sina shaka, tatizo la fedha za maendeleo litazidi kupungua.
Kuhusu tatizo la uhaba wa watumishi baada ya kuwaondoa watumishi wenye vyeti feki, Serikali mwaka huu imepanga kuajiri watumishi wapya wapatao 52,000, wakiwemo watumishi wa afya, walimu na watumishi wa kada nyingine. Hivyo basi, nina imani kuwa hii itapunguza uhaba wa watumishi kwenye Serikali za Mitaa. Ombi langu tu msiajiri watumishi wasio na sifa. Lakini niwe mkweli ombi lenu la kuongeza posho kwa madiwani, kidogo litaiwia Serikali vigumu kulitekeleza kwa wakati huu. Kama nilivyosema hapo awali, kwa sasa, Serikali imeelekeza nguvu zake katika kuboresha huduma za jamii na kujenga miundombinu ya kiuchumi. Hivyo basi, niwaombe Waheshimiwa Madiwani mtuelewe katika hili. Aidha, nawaombeni mzidi kuwahamisha Watanzania kuchapa kazi kwa bidii na kulipa kodi ili kuongeza uwezo wetu wa kifedha. Uwezo wetu ukiimarika, Serikali kamwe haitasita kuboresha maslahi sio tu yenu ninyi Waheshimiwa Madiwani bali pia watumishi wote wa umma.
Umeeleza pia kuhusu ombi la kutaka kuridhiwa kwa Mkataba wa Umoja wa Afrika kuhusu Ugatuaji Madaraka (The African Union Charter on Principles and Values on Decentralization, Local Governance and Local Development) pamoja na ombi la kutaka nchi yetu kuwa Makao Makuu ya Jumuiya ya Tawala za Serikali ya Mitaa kwa Kanda ya Afrika. Maombi haya nayo tumeyapokea. Nitaziagiza taasisi husika kupitia Mkataba huo na endapo haukinzani na Katiba na Sheria zetu, uweze kuridhiwa na Bunge letu. Na kuhusu ombi la nchi yetu kuwa Makao Makuu, natambua faida za kuwa mwenyeji wa Taasisi hiyo. Hata hivyo, kabla ya kukubali kuipokea taasisi hiyo, ni vyema tathmini ikafanyika kuhusu mahitaji ya fedha yanayotakiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Siwezi kuhitimisha hotuba yangu bila kugusia kaulimbiu ya Mkutano huu, ambayo inasema “Ardhi kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa ni chachu ya Maendeleo, Halmashauri zitenge ardhi kwa ajili ya Uwekezaji wa Viwanda Vidogo na Vikubwa”. Kama mnavyofahamu, kipaumbele kikubwa cha Serikali ya Awamu ya Tano ni ujenzi wa Viwanda. Na ili kujenga viwanda, unahitaji ardhi. Hivyo, kaulimbiu hii ni nzuri na imekuja kwa wakati muafaka. Kwenye ziara zangu maeneo mengi nchini, nimekuwa nikihimiza wakurugenzi, Wakuu wa Wilaya na Mikoa kutenga maeneo na kuweka miundombinu rafiki ili kuwavutia wawekezaji kujenga viwanda. Hivyo basi, kwa mara nyingine napenda kurudia tena wito huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Mheshimiwa Naibu Waziri wa TAMISEMI;
Ndugu Wajumbe, Mabibi na Mabwana;
Nimezungumza mengi. Napenda kuhitimisha hotuba yangu kwa kukushukuru tena Mwenyekiti wa ALAT kwa kunialika kufungua Mkutano huu. Napenda kuwahakikishia tena kuwa Serikali ya Awamu ya Tano ipo pamoja nanyi. Nitafuatilia Mkutano huu, na yote mtakayokubaliana, nawaahidi kuwa Serikali itayazingatia na kuyatekeleza. Wito wangu kwenu, mjadiliane kwa amani na uwazi.
Baada ya kusema hayo, sasa natamka kuwa Mkutano wa 33 wa Jumuiya ya Tawala za Serikali za Mitaa (ALAT) umefunguliwa rasmi.
Mungu Ibariki ALAT!
Mungu Zibariki Mamlaka zote za Serikali za Mitaa Nchini!
Mungu Ibariki Tanzania!
“Ahsanteni sana kwa kunisikiliza”
- Aug 23, 2017
HOTUBA YA MHE. DKT. JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, KWENYE HAFLA YA KUWEKA JIWE LA MSINGI LA MRADI WA KUBORESHA BANDARI Y...
Soma zaidiHotuba
Mheshimiwa Prof. Makame Mbarawa, Waziri wa Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano;
Waheshimiwa Mawaziri na Manaibu Waziri mliopo;
Mheshimiwa Balozi John Kijazi, Katibu Mkuu Kiongozi;
Mheshimiwa Paul Makonda, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam;
Mheshimiwa Dkt. Noman Sigala King, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu;
Mheshimiwa Hawa Ghasia, Mwenyekiti wa Kamati ya
Kudumu ya Bunge ya Bajeti;
Mheshimiwa Sarah Cooke, Balozi wa Uingereza nchini;
Mheshimiwa Mama Bella Bird, Mwakilishi wa Benki ya Dunia;
Mwakilishi wa Trade Mark East Africa;
Waheshimiwa Wabunge mliopo na Mstahiki Meya wa Dar es Salaam;
Waheshimiwa Makatibu Wakuu mliopo hapa;
Mwenyekiti na Wajumbe wa Bodi ya Mamlaka ya Bandari Tanzania;
Ndugu Mkurugenzi Mkuu na Wafanyakazi wa Mamlaka
ya Bandari Tanzania;
Waheshimiwa Wageni wote Waalikwa, Mabibi na Mabwana:
Nianze kwa kuungana na wote walionitangulia kuzungumza katika kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutupa uhai na kutuwezesha kushuhudia tukio hili. Aidha, napenda nitoe shukrani zangu nyingi kwa Mheshimiwa Waziri, Prof. Mbarawa, pamoja na uongozi mzima wa Mamlaka ya Bandari Tanzania kwa kunipa heshima ya kuwa Mgeni Rasmi katika hafla hii ya kuweka Jiwe la Msingi la Mradi wa Kuboresha Bandari ya Dar es Salaam. Ahsanteni sana.
Mbele yangu hapa nawaona wageni. Namwona Mheshimiwa Balozi Cooke wa Uingereza; Mama Bird, Mwakilishi wa Benki ya Dunia nchini; pamoja na wawakilishi wa Shirika la Maendeleo la Uingereza (DFID) na Trade Mark East Africa, ambao kwa pamoja wametoa mchango wao katika kufadhili mradi huu. Tunawashukuru sana kwa ujio wenu lakini pia kwa kutuunga mkono katika kuutekeleza mradi huu muhimu.
Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;
Tukio hili la uwekaji Jiwe la Msingi la mradi wa kuboresha Bandari ya Dar es Salaam ni muhimu sana kwa maendeleo na ustawi wa nchi yetu. Ni muhimu kwa sababu Bandari ya Dar es Salaam ni lango kuu la biashara na pia ni kitovu cha uchumi sio tu kwa nchi yetu bali pia kwa baadhi ya nchi jirani. Takwimu zinaonesha kuwa asilimia 90 ya shehena za mizigo inayoingia na kutoka hapa nchini inapita kwenye Bandari hii. Aidha, nchi takriban 6 hupitisha mizigo yao katika Bandari hii. Nchi hizo ni Burundi, DRC, Malawi, Rwanda, Uganda na Zambia. Lakini kama hiyo haitoshi, hivi majuzi tu tumeanza ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kimataifa (standard gauge). Ufanisi na manufaa ya reli hiyo yatategemea sana utendaji kazi mzuri wa Bandari hii.
Kwa kuzingatia mambo hayo yote, ni dhahiri kuwa uboreshaji huu ni umuhimu kwa nchi yetu pamoja na nchi nyingine jirani zinazotumia Bandari hii. Uboreshaji huu utaongeza shehena ya mizigo inayopita katika Bandari hii na hivyo kuipatia Serikali yetu mapato mengi kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo na pia kuboresha huduma za jamii. Hivyo basi, napenda nitoe pongezi nyingi kwa Wizara pamoja na Mamlaka ya Bandari Tanzania kwa kuanza kutekeleza mradi huu.
Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;
Kama mlivyosikia hivi punde, mradi huu utatekelezwa kwa awamu mbili. Awamu ya kwanza, ambayo leo tunaweka jiwe la msingi, itahusisha uboreshaji wa Gati Na. 1-7 na Gati la kuhudumia magari (Roll-on-Roll off Berth –RORO). Awamu ya pili ya mradi huu, itahusisha kuongeza kina na kupanua lango la kuingilia Bandarini, mzunguko wa kugeuzia meli (Turning Basin), pamoja na kujenga kujenga Gati mpya Na. 12-15.
Gharama za utekelezaji wa mradi huu kwa awamu zote mbili ni Dola za Marekani milioni 421, sawa na takriban Shilingi za Tanzania bilioni 926.2. Kati ya fedha hizo, Serikali ya Tanzania itatoa Dola za Marekani 63.4; Benki ya Dunia itatoa Dola za Marekani milioni 345.2; na Serikali ya Uingereza kupitia Shirika lake la Maendeleo (DFID) itatoa Dola za Marekani milioni 12.4. Hivyo basi, napenda kurudia tena kuwashukuru washirika wetu hawa ambao wamekubali kutuunga mkono katika kutekeleza mradi huu muhimu kwa maendeleo ya nchi yetu.
Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;
Kama mlivyosikia, awamu ya kwanza ya mradi huu, awali, ilipangwa kutekelezwa kwa miezi 36. Lakini baada ya mashauriano yaliyofanyika, Mkandarasi, Kampuni ya China Harbour Construction kutoka China, amekubali kukamilisha mradi huu kwa kipindi cha miezi 28. Hili ni jambo jema sana. Sidhani kama kulikwa na sababu za msingi za kufanya mradi huu uchukue muda mwingi kiasi hicho kuutekeleza. Kampuni iliyopewa kandarasi ya kuutekeleza ni kubwa; lakini fedha pia zipo. Hivyo, nimefurahi kusikia muda wa kutekeleza mradi huu umepunguzwa.
Kukamilika mapema kwa mradi huu kutaiwezesha Bandari ya Dar es Salaam kupokea meli nyingi na kubwa; na hivyo kupunguza ucheleweshaji. Hii pia itasaidia Bandari yetu kushindana na Bandari nyingine katika Ukanda wetu. Kama mnavyofahamu, katika siku za hivi karibuni, zimekuwepo taarifa zakupungua mizigo katika Bandari hii. Moja ya sababu zinazochangia hali hiyo ni kwamba kina cha Bandari yetu ni kidogo. Hii inafanya meli kubwa zishindwe kuja au zilazimike kutumia muda mrefu kusubiri. Bila shaka, nyote hapa mnafahamu, katika dunia ya sasa ya ushidani, hakuna mfanyabiashara aliye tayari kupotezewa muda. Hivyo, mradi huu utakapokamilika, utaondoa tatizo la ucheweleshaji katika Bandari yetu. Kama utatokea, basi labda usababishwe na watendaji wetu, ambao ningependa tu kusema kuwa Serikali kamwe haitawavumilia.
Lakini mbali na kuondoa tatizo la ucheleweshaji, mradi huu utakuza biashara na shughuli nyingine za kiuchumi kati yetu na nchi nyingine. Kama nilivyosema awali, Bandari hii inatumiwa na mataifa jirani takriban saba. Na mnafahamu pia kuwa nchi yetu ni mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), ambazo kwa pamoja zina watu wapatao milioni 600. Hivyo, mradi huu utakapokamilika, utakuza biashara kati yetu sio tu na mataifa yanayotumia Bandari yetu bali pia na nchi zote wanachama wa EAC na SADC. Hii ni kwa sababu, Bandari ni kichocheo muhimu cha kukuza biashara miongoni mwa mataifa. Takriban asilimia 90 ya shehena ya mizigo duniani husafirishwa kwa usafiri wa majini, ambapo Bandari ni kiungo muhimu.
Ndugu Viongozi mliopo;
Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;
Jukumu langu leo ni kuweka Jiwe la Msingi la Awamu ya Kwanza ya Mradi wa Upanuzi na Uboreshaji wa Bandari ya Dar es Salaam. Hivyo basi, sitapenda kuwachosha kwa hotuba ndefu sana. Hata hivyo, kabla sijahitimisha hotuba yangu, napenda nizungumze masuala manne ya mwisho.
Kwanza kabisa, napenda kuwahakikishia kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kwa dhati kabisa kuboresha na kuimarisha miundombinu ya usafiri hapa nchini. Mbali na kuboresha Bandari ya Dar es Salaam, tunaboresha na kupanua Bandari zetu za Mtwara na Tanga na halikadhalika kwenye Maziwa Makuu ya Victoria, Tanganyika na Nyasa. Tunaendelea pia na ujenzi na ukarabati wa viwanja vya ndege na barabara. Tunafanya hivyo kwa vile tunatambua kuwa huduma na miundombinu imara ya usafiri na usafirishaji ni muhimu sio tu katika kukuza biashara bali pia katika ukuaji wa sekta nyingine za uchumi, ikiwemo kilimo, viwanda, utalii, ufugaji, uvuvi, n.k.
Suala la pili ni kwa ndugu zangu wa Mamlaka ya Bandari na Bodi yake. Nawapongeza kwa hatua mnazochukua katika kuboresha na kuongeza ufanisi wa Bandari yetu. Lakini hamna budi kuzidisha juhudi hasa katika usimamizi wa Bandari Kavu Binafsi (ICDs). Bandari hizi kavu zilianzishwa kwa makusudi ya kusaidia pale mizigo inapozidi hapa Bandarini. Lakini kwa taarifa nilizonazo ni kwamba, siku hizi hata kabla ya mizigo kujaa hapa Bandarini, inapelekwa kwenye Bandari hizo Kavu, ambako kuna dalili za ukwepaji kodi. Nimeambiwa pia kwamba mara nyingi mizigo inayopelekwa huko husemekana kuwa inasafirishwa kwenda nje lakini mingi hushushwa hapa hapa nchini. Nitoe wito kwa Mamlaka ya Bandari, Mamlaka ya Mapato pamoja na vyombo vingine husika kushughulikia suala hili la Bandari Kavu na pia ukwepaji wa kodi unaofanyika kupitia Bandari kavu hizo.
Suala la tatu, napenda kuihimiza Mamlaka ya Bandari kuimarisha ulinzi na usalama wa hapa Bandarini, hususan kuhusu mizigo inayoteremshwa. Nimearifiwa kuwa hivi majuzi vimeshushwa vichwa vya treni vipatavyo 15 lakini mpaka sasa havijulikani mmiliki wake. Shirika la Reli limevikana. Sasa mimi najiuliza inawezekanaje vichwa vya treni viletwe na kushushwa hapa bila kufahamika mmiliki wake. Na kama hilo limewezekana, je haitawezekana pia kwa watu wenye nia mbaya na nchi yetu kuleta vitu vyenye kuhatarisha usalama wetu? Hivyo basi, niwaombe Mamlaka ya Bandari kuimarisha usalama wa Bandari yetu. Na kuhusu tukio hili la vichwa vya treni, niviombe vyombo vya dola kulichunguza ili kuweza kumbaini mmiliki wake.
Suala la nne na la mwisho ni kuhusu wana-siasa wenzangu, ambao wamekuwa wakiibuka kuzungumzia mambo wasiofahamu undani wake. Mathalan, hivi karibuni kuna wanasiasa wamejitokeza kujaribu kuwatetea watu wanaoshikiliwa kwa makosa ya kuhatarisha amani na usalama wa taifa letu. Nawasihi wanasiasa wa namna hiyo kuacha kutafuta sifa na umaarufu usio na tija. Ninyi ndugu zangu hapa nyote ni mashahidi kuwa katika muda mfupi uliopita, nchi yetu imewapoteza askari pamoja na wananchi wasio na hatia zaidi ya 30. Lakini jambo la kusikitisha ni kwamba wanasiasa hao hawakuwahi kulaani na kukemea mauaji hayo; lakini badala yake wanaibuka kuwatetea watu ambao inaaminika kuwa wanahusika na vitendo hivyo vya mauaji. Hii inatia mashaka kuwa huenda hata wanasiasa hao pia wanahusika, hasa kwa kuzingatia kuwa ukiondoa askari, walengwa wa mauji hayo ni watu kutoka chama kimoja tu. Nitoe wito kwa wanasiasa wenzangu tuchunge ndimi na kauli zetu. Amani ya nchi yetu ni muhimu sana. Tusiichezee. Maendeleo haya tunayoyaona na kuyatamani leo kamwe hayawezi kupatikana kama amani itapotea. Hivyo, tuiache Serikali itekeleze majukumu yake. Kinyume na hapo, hatutawavumilia wanasiasa wa namna hiyo. Nilichaguliwa kuwa Rais wa Tanzania, na hivyo nawajibika kulinda amani na usalama wa nchi yetu kwa nguvu zangu zote. Naviomba vya ulinzi na usalama visiwaogope au kuwaonea aibu wanasiasa wa namna hiyo. Lakini zaidi, nawaomba Watanzania wote, bila kujali tofauti zetu za dini, kabila au vyama, kuilinda amani yetu na pia kuweka mbele maslahi ya taifa letu.
Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi;
Waheshimiwa Viongozi mliopo;
Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;
Napenda kuhitimisha hotuba yangu kwa kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge wote, lakini hasa Wabunge wa Kamati za Miundombinu na Bajeti kwa kuiunga mkono Serikali. Upauzi na uboreshaji wa Bandari hii umezungumzwa kwa muda mrefu, hata hivyo, utekelezaji wake ulikuwa ukikwama kutokana na sababu mbalimbali, ikiwemo ukosefu wa fedha. Lakini baada ya Kamati hizi mbili kuupitisha mradi huu pamoja na bajeti yake, sasa tunautekeleza. Nazipongeza sana Kamati hizi mbili kwa uamuzi wenu huo wa kijasiri.
Naomba pia mniruhusu kuwashukuru tena washirika wetu katika mradi huu kwa kutuunga mkono. Aidha, nawashukuru Mabalozi wote mliojitokeza kuhudhuria shughuli. Hii inadhihirisha kuwa mnatambua umuhimu wa mradi huu. Tunawashukuru sana na napenda niwaahidi kuwa tutaendelea kushirikiana nanyi kwa karibu.
Mwisho lakini sio kwa umuhimu, napenda kuwashukuru tena viongozi wa Wizara pamoja na Mamlaka ya Bandari kwa kunialika kwenye tukio hili. Aidha, nawapongezeni kwa kazi nzuri mnayoifanya. Endeleeni kujituma. Ongezeni mapambano dhidi ya rushwa. Vitendo vya rushwa na wizi viwe mwiko katika Bandari. Zaidi ya hapo zingatieni muda. Msiwacheleweshe wateja wenu. Mkiyafanya hayo, nina imani kuwa Bandari hii itatoa huduma bora na kuchangia maendeleo ya nchi yetu; na hata maslahi ya wafanyakazi wake pia yataboreshwa.
Baada ya kusema hayo, sasa nipo tayari kutekeleza shughuli iliyonileta ya kuweka Jiwe la Msingi la Mradi wa Kuboresha Bandari ya Dar es Salaam.
Mungu Ibariki Bandari ya Dar es Salaam!
Mungu Zibariki Bandari Zetu Zote!
Mungu Ibariki Tanzania!
“Ahsanteni sana kwa kunisikiliza”