Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ametoa wito kwa Makampuni ya simu kubuni teknolojia ya gharama nafuu itakayowezesha kila Mtanzania kupata huduma ya mawasiliano popote alipo nchini.
Rais Samia ametoa wito huo leo wakati wa utiaji saini mikataba ya upelekaji huduma za mawasiliano nchini kati ya Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) na watoa huduma za mawasiliano uliofanyika katika ukumbi wa Jakaya Kikwete.
Aidha, Rais Samia ameyataka Makampuni hayo kuleta teknolojia inayoendana na mazingira ya Tanzania kwa kuwa zipo changamoto zinazotokana na hali ya kijiografia na kipato kidogo cha wananchi katika baadhi ya maeneo.
Rais Samia pia amewataka Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (TARURA) kushirikiana na UCSAF na wakandarasi kuhakikisha njia zinapitika katika maeneo ya vijijini inapokwenda kujengwa minara hiyo.
Hali kadhalika, Rais Samia amewataka Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kuhakikisha kuwa minara inayokwenda kujengwa vijijini inapelekewa umeme ili faida inayokusudiwa ipatikane haraka.
Kwa upande mwingine, Rais Samia amesema kuwepo kwa huduma bora za mawasiliano hususan katika maeneo ya vijijini ni muhimu sana kiuchumi, kisiasa, kijamii, kiutamaduni na hata katika masuala ya ulinzi na usalama wa nchi yetu.
Miradi miwili iliyotiwa saini ni ya ujenzi wa minara 758 katika Kata 713 wenye gharama ya Shilingi bilioni 265.3 pamoja na mradi wa kuongeza uwezo wa minara 304 ya mawasiliano utakaogharimu kiasi cha Shilingi bilioni 10.2.