Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ameshuhudia utiaji saini wa mikataba ya Miradi ya Maji wa Miji 28 katika hafla iliyofanyika Ikulu, Chamwino.
Mikataba hiyo imesainiwa kati ya Serikali ya Tanzania na makampuni ya JW INFRA Ltd, AFCONS Infrastructures Ltd, Larsen & Toubro, Megha Engineering and Infrastructures Ltd, China Civil Engineering Construction Corporation (CCECC) na Jandu Plumbers Limited.
Aidha, miji itakayonufaika na Miradi hiyo ni pamoja na Handeni, Korogwe, Muheza, Pangani, Kilwa, Masoko, Nanyumbu, Ifakara, Chunya, Rujewa, Wangingo'mbe, Makambako, Njombe, Kiomboi, Singida, Manyoni na Chemba.
Miji mingine ni Chamwino, Mugumu, Kasulu, Mpanda, Sikonge, Urambo, Kaliua, Kayanga, Geita, Chato, Mafinga pamoja na ukanda wa Makonde.
Utekelezaji wa Miradi hiyo ni asilimia 8 ya mikakati ya Serikali ya usambazaji wa huduma ya maji safi na salama maeneo ya mijini na vijijini.
Rais Samia amesema Serikali itaendelea kutekeleza miradi ya maji ili hadi kufika mwaka 2025 huduma ya usambazaji wa maji safi na salama ifikie asilimia 85 vijijini na asilimia 95 mijini.
Vile vile, Rais Samia ameitaka Wizara ya Maji kuisimamia vyema miradi ya maji pamoja na Wakandarasi wanaopewa kujenga ili iwe na manufaa kwa pande zote mbili.