Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amewataka Viongozi katika maeneo yaliyogunduliwa madini kusimamia vyema miradi hiyo ili itekelezwe ipasavyo na kulinufaisha taifa.
Rais Samia ametoa tamko hilo leo Ikulu, Chamwino wakati wa utiaji saini ya makubaliano baina ya Serikali na kampuni za uchimbaji madini za Evolution Energy Minerals Limited, EcoGraf Limited, na Peak Rare Earth Limited zote kutoka Perth Australia.
Aidha, Rais Samia amewataka Viongozi na taasisi za Serikali kushirikisha wananchi katika maeneo ya migodi ili waweze kutoa huduma mbalimbali.
Rais Samia pia amesema madini ya Kinywe na adimu yaliyogunduliwa ni madini muhimu ya kimkakati duniani ambapo yanahitajika katika teknolojia mpya za kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.
Vile vile, Rais Samia amesema katika siku zijazo Tanzania itakuwa kitovu cha uzalishaji na usafishaji wa madini hayo na hivyo kuweza kuvutia uwekezaji mahiri na kuendelea kunufaika na fursa zilizojitokeza.
Hali kadhalika, Rais Samia amesema kutokana na juhudi zilizofanywa na Serikali, ukuaji wa Sekta ya Madini na mchango wake katika pato la taifa umeendelea kuimarika na unatarajia kuwa zaidi ya 10% kama inavyoainishwa kwenye Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025.
Madini hayo ya kipekee na adimu kupatikana yamegundulika katika maeneo ya Chilalo Wilayani Lindi, Epanko Wilayani Ulanga, na Nguala Wilayani Songwe.