Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ametoa wito kwa viongozi wa Serikali kuanza kutumia matokeo ya Sensa katika kupanga miradi na mipango jumuishi ya maendeleo endelevu kwa wananchi.
Rais Samia ametoa wito huo uwanja wa Jamhuri wakati akizindua matokeo ya mwanzo ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 pamoja na Mwongozo wa Kitaifa wa Matumizi ya Matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022.
Aidha, Rais Samia ametangaza kuwa Tanzania ina idadi ya watu 61,741,120 ambapo watu 59,851,347 wapo Tanzania Bara na watu 1,889,773 wapo Zanzibar.
Kati ya watu 61,741,120, wanawake ni 31,687,990 sawa na asilimia 51 na wanaume ni 30,053,130 sawa na asilimia 49.
Kwa kipindi cha miaka kumi iliyopita Tanzania ilikuwa na watu 44,928,923, hivyo kuna ongezeko la watu 16,812,197 sawa na ongezeko la asilimia 3.2 kwa mwaka kati ya mwaka 2012 na mwaka 2022.
Rais Samia amesema Serikali imeandaa Mwongozo wa Kitaifa wa Matumizi ya Matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 ili utumike katika kutunga na kutekeleza sera na mipango ya maendeleo ya kisekta katika ngazi zote za utawala.
Kufanyika kwa Sensa ya Watu na Makazi, Sensa ya Majengo, na Sensa ya Anwani za Makazi ya mwaka 2022 kumeifanya Tanzania kuandika historia kwa kuwa takwimu hizo zitawezesha kufuatilia na kutathmini Sera za Mipango Miji na kuwafikia wananchi kwa urahisi zaidi ili kuwapatia huduma za kijamii.