TAMKO LA MHE. DKT. JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA KWA WATANZANIA KUHUSU UGONJWA WA HOMA YA MAPAFU UNAOSABABISHWA NA KIRUSI AINA YA KORONA,
DODOMA, TAREHE 22 MACHI, 2020
Ndugu Watanzania wenzangu; Habari za muda huu. Nimelazimika kuzungumza nanyi muda huu ili kueleza suala moja muhimu linaloikabili nchi yetu na dunia nzima kwa sasa kwa ujumla. Kama nyote mnavyofahamu, kwa takriban miezi mitatu sasa, dunia imeingia kwenye taharuki kubwa kufuatia kuibuka kwa ugonjwa wa Homa ya Mapafu inayosababishwa na Kirusi aina ya Korona (COVID – 19).
Ugonjwa huu umesababisha athari mbalimbali, hususan kwenye nyanja za afya na uchumi. Kiafya, kwa mujibu wa takwimu za leo, ugonjwa huu tayari umewapata watu zaidi ya 260,000 kwenye nchi zaidi ya 160 duniani, ambapo mpaka sasa takriban watu 11,000 wamepoteza maisha. Kiuchumi, ugonjwa huu umeziathiri zaidi sekta ya biashara, uzalishaji, usafiri wa anga pamoja na utalii.
Awali, Shirika la Afya Duniani (World Health Organization – WHO) liliutangaza ugonjwa huu kuwa Dharura ya Kimataifa (yaani Global HealthEmergency). Hata hivyo, kutokana na kasi ya kusambaa kwake, tarehe 11 Machi, 2020; WHO iliutangaza ugonjwa huu kuwa Janga la Kimataifa (yaani Global Health Pandemic).
Ndugu Watanzania; kufuatia kuibuka kwa ugonjwa huu, Serikali ilianza kuchukua hatua mbalimbali za kuzuia usiingie nchini; na pia kujipanga kukabiliana nao au kuzuia usisambae, endapo ungeingia. Wizara yetu ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ilianza kutoa elimu kwa wananchi kuhusu namna ya kujihadhari na kujikinga na ugonjwa huu, kupitia vyombo mbalimbali vya habari. Nitumie fursa hii kuipongeza Wizara na pia kuvishukuru vyombo vya habari pamoja na watu mbalimbali walioshirikiana na Serikali kutoa elimu kwa wananchi juu ya ugonjwa huu.
Sambamba na kutoa elimu, Serikali ilitoa mafunzo ya kuwaandaa madaktari na wauguzi ili kukabiliana na ugonjwa huu. Aidha, tulichukua hatua za kuimarisha maeneo yetu ya mipaka pamoja na maeneo ya kuingia nchini, hususan katika Viwanja vyetu vya Ndege vya Dar es salaam, Kilimanjaro, Zanzibar na Mwanza, ambapo tumepeleka wataalamu pamoja na vifaa vya kuwapima wasafiri wanaoingia nchini. Vilevile tumetenga maeneo ya kuhifadhi wagonjwa watakaobainika kuambukizwa ugonjwa huo.
Ndugu Watanzania wenzangu; mpaka sasa, nchi yetu imebaini wagonjwa (12) ambao wamethibitika kuambukizwa ugonjwa huu wa korona. Kati yao wanne (4) ni raia wa nje na wanane (8) ni raia wa Tanzania. Wagonjwa wote, isipokuwa mmoja, ametoka kwenye nchi zilizokuwa zimebainika kuwa na maambukizi ya ugonjwa huo. Kwa bahati nzuri, wagonjwa wote wanaendelea vizuri na tunamshukuru Mwenyezi Mungu hadi sasa hatujapata kifo chochote kinachotokana na Korona. Vipimo vya leo vyote vinaonesha hakuna aliyekutwa na maambukizi (negative). Hata mgonjwa wetu wa kwanza kupatikana na ugonjwa huu naye ameonesha negative. Napenda niwashukuru na kuwapongeza madaktari pamoja na wauguzi wetu ambao wanaendelea kujitoa kuwachunguza na kuwahudumia wagonjwa hao.
Ndugu Watanzania; kufuatia kuingia kwa ugonjwa huo hapa nchini, Serikali imeendelea kutoa maelekezo mbalimbali ya kukabiliana na ugonjwa huo. Kwanza, kama mtakavyokumbuka, nilitangaza kuzuia shughuli za ukimbizaji Mwenge wa Uhuru mwaka huu na kuelekeza fedha zilizokuwa zimetengwa kwa shughuli hiyo, takriban shilingi bilioni moja, zipelekwe Wizara ya Afya ili ziongeze jitihada za kusaidia kukabiliana na ugonjwa wa korona. Aidha, tarehe 17 Machi na tarehe 18 Machi, 2020, kwa nyakati tofauti, kupitia kwa Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mhe. Ummy Mwalimu, Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Serikali ilitoa Matamko yenye maelekezo ya kuimarisha hatua za kukabiliana na ugonjwa huu.
Maelekezo hayo yalihusu uamuzi wa Serikali wa kuzifunga shule zote za awali, msingi pamoja na sekondari kwa kipindi cha mwezi mmoja (yaani siku 30). Tumevifunga pia vyuo vyote vya elimu ya juu na kati kwa mwezi mmoja. Sambamba na hayo, Serikali imesitisha mikusanyiko yote ya ndani na nje isiyo ya lazima, ikiwemo mikutano, semina, warsha, matamasha ya muziki na shughuli nyingine za kijamii. Vilevile, tumezuia michezo yote inayohusisha watu wengi kwa kipindi cha mwezi mmoja, ikiwemo ligi na mashindano mbalimbali
Ndugu Watanzania wenzangu; kwa lengo la kuimarisha zaidi mikakati yetu ya kukabiliana na ugonjwa huu; napenda nitumie fursa hii kutangaza hatua nyingine ambazo Serikali imeamua kuzichukua, kama ifuatavyo:
Kwanza, tumeamua kuimarisha Kamati ya Kitaifa ya kukabiliana na Ugonjwa huu, ambayo sasa itakuwa chini ya Waziri Mkuu akisaidiwa na Waziri wa Afya. Wajumbe wengine watachaguliwa na Waziri Mkuu kulingana na umuhimu wao.
Pili, kuanzia kesho tarehe 23 Machi, 2020 wasafiri wote watakaongia nchini kutoka kwenye mataifa yaliyoathirika zaidi na ugonjwa huu, watalazimika kufikia sehemu za kujitenga(self isolation) na kukaa huko kwa siku 14 kwa gharama zao wenyewe. Maelekezo haya yatawahusu pia Watanzania wanaotoka kwenye nchi hizo ambao walikwenda kwa shughuli mbalimbali.
Tatu, naelekeza Wizara ya Afya pamoja na mamlaka nyingine husika, kuhakikisha Maabara yetu ya Taifa inaimarishwa kwa kupatiwa vifaa vya kisasa vya uchunguzi. Aidha, naagiza maeneo yote ya vituo vinavyotumiwa na watu kuingia nchini, yapelekewe vifaa vya ukaguzi na pia kujikinga kwa ajili ya watumishi. Katika hilo, navihimiza pia vyombo vyetu vya ulinzi na usalama navyo kuimarisha ulinzi wa mipaka yetu yote ili kuzuia watu kuingia nchini kiholela bila kufanyiwa uchunguzi.
Nne, Serikali kuanzia sasa imesitisha kutoa vibali vya kusafiri kwa watumishi kwenda kwenye nchi zilizoathirika na ugonjwa wa Korona. Aidha, tunawasihi na kuwashauri wananchi ambao hawana shughuli za lazima sana za kutembelea nchi hizo, pamoja na maeneo mengine, yakiwemo ya ndani ya nchi, kuahirisha safari zao kwa sasa.
Ndugu Watanzania wenzangu; sambamba na hatua hizo, napenda kutumia fursa hii kurudia wito wangu kwa Watanzania kuzingatia maelekezo yote yanayotolewa na wataalam kuhusu namna ya kujikinga na ugonjwa huu. Wataalamu wetu tayari wametueleza kuwa virusi vya korona huambukizwa endapo mtu mwenye navyo atapiga chafya au kukohoa na majimaji yake kuingia kwa mtu mwingine kupitia mdomo, pua ama macho. Aidha, mtu anaweza kuambukizwa virusi hivyo endapo atashikana mikono na mtu mwenye maambukizi au kushika mahali penye maambukizi kama vile meza, vitasa, simu, n.k. na kisha kujishika kwenye pua, mdomo na macho. Kwa sababu hiyo, nawasihi sana Watanzania wenzangu kuachana na tabia ya kushikana mikono au kushika mdomo, pua na macho. Aidha nawahimiza kujitahidi kunawa mikono yetu kwa sabuni na maji yanayotiririka mara kwa mara ili kujikinga na ugonjwa huu.
Halikadhalika, nawasihi Watanzania wenzangu tujiepushe na mikusanyiko ya watu wengi isiyo ya lazima. Hata hivyo, natambua kuwa, kwenye baadhi ya maeneo huenda mikusanyiko isiepukike, ikiwemo kwenye hospitali, masoko, maduka, stendi, kambi, misikiti, makanisa na kwenye vyombo vya usafiri wa umma. Natoa wito kwa wahusika wanaosimamia maeneo hayo kuhakikisha wanachukua tahadhari zote muhimu ili maeneo hayo yasiwe chanzo cha kuenea kwa ugonjwa huu. Aidha, nawasihi wananchi watakaokwenda katika maeneo hayo au kutumia vyombo vya usafiri wa umma na wenyewe kuchukua tahadhari kama inavyoshauriwa na wataalamu.
Nitumie fursa hii pia kuwasihi Watanzania kuacha kufanya utani/mzaha na pia kujiepusha na tabia ya kutoa taarifa za uzushi na upotoshaji ambazo zinaweza kusababisha taharuki kwenye jamii. Watu watakaobainika wakifanya mzaha, hatua zichukuliwe dhidi yao. Taarifa zote muhimu kuhusu ugonjwa huu zitatolewa na Serikali kupita kwa Waziri Mkuu, Waziri wa Afya na Msemaji Mkuu wa Serikali.
Ndugu Watanzania wenzangu; ni wazi kuwa ugonjwa huu umeleta taharuki hapa nchini na duniani kwa ujumla. Hata hivyo, napenda nitumie fursa hii kuwatoa hofu Watanzania dhidi ya ugonjwa huu. Hofu zingine tunazitengeneza sisi wenyewe bila sababu. Nawasihi Watanzania tuepuke hofu zisizo na msingi. Binafsi naamini, kwa jinsi tulivyojipanga na endapo kila Mtanzania atazingatia maelekezo yaliyotolewa na wataalamu, nchi yetu itaweza kuushinda ugonjwa huu; kama ambavyo tumewahi kushinda maadui wengine ambao walijaribu kutaka kuidhuru nchi yetu. Jambo la msingi kwetu ni kuendelea kushikamana kama Taifa.
Na katika hilo, napenda niseme kuwa, pamoja na kuibuka kwa ugonjwa huu, nawahimiza Watanzania wenzangu tuendelee kuchapa kazi kwa bidii ili kuijenga nchi yetu. Ugonjwa huu kamwe usiwe sababu ama kigezo cha kuacha kufanya kazi. Badala yake utupe hamasa zaidi ya kuchapa kazi kwa bidii. Kama mnavyojionea wenyewe, tangu ugonjwa huu uanze, kila nchi imekuwa ikichukua tahadhari yake wenyewe. Hii inatufundisha kuwa shida inapotokea usitegemee atatokea mtu wa kukusaidia. Ni lazima upambane mwenyewe. Hivyo basi, nawahimiza Watanzania wenzangu, katika kipindi hiki ambacho nchi yetu na dunia inapambana na ugonjwa huu, tuendelee pia kuchapa kazi kwa bidii ili kuijenga nchi yetu. Wakulima watumie mvua zinazoendelea kulima kwa bidii mazao mbalimbali; waliopo viwandani nao waendelee kufanya kazi; na vivyo hivyo, kwa wafugaji, wavuvi, wafanyabiashara, wafanyakazi, n.k. Kila mtu aendelee kufanya kazi. Miradi mbalimbali inayotekelezwa katika maeneo mbalimbali nayo iendelee kutekelezwa kwa nguvu zote. Kamwe tusiruhusu Ugonjwa huu wa Korona kuharibu uchumi wetu. Shughuli zote za uchumi na uzalishajini lazima ziendelee.
Mwisho lakini sio kwa umuhimu, napenda kutumia fursa hii kutoa wito kwa viongozi wa dini na madhehebu mbalimbali nchini kuendelea kuliombea Taifa letu. Tofauti na nyakati nyingine, huu ndiyo wakati hasa ambao sisi kama Taifa inatubidi tuwe karibu zaidi na Mwenyezi Mungu. Na kimsingi, hivyo ndivyo vitabu vyote vitakatifu vinavyotufundisha. Tunapopatwa na shida au majanga, hatuna budi kumuomba Mwenyezi Mungu. Mathalan, kwa wenzangu Wakristo wanafahamu, kwenye Kitabu cha 2 Nyakati 7:14,wana wa Israeli walipopatwa na janga la ugonjwa wa tauni, Mwenyezi Mungu aliwakumbusha kumwomba, ambapo alisema, ‘’ ikiwa watu wangu walioitwa kwa Jina langu watajinyenyekesha na kuomba na kunitafuta uso na kuziacha njia zao mbaya, basi nitasikia toka mbinguni na kuwasamehe dhambi zao na kuiponya nchi yao’’. Lakini hata kwa ndugu zangu Waislamu, nimeambiwa kwenye Korani Tukufu, kwenye Kitabu cha Al-Baqarah, sura ya pili, mstari wa 155, Mwenyezi Mungu anasema, “Tutakutieni katika hofu au msukosuko kidogo; hofu ya njaa, mali, au kuwanyima nafsi, na matunda au mazao”. Lakini, katika mstari huo huo Mwenyezi Mungu anaahidi habari njema, kwa watakaokuwa na subira, uvumilivu au kuendelea kujinyenyekeza kwa sala na toba.
Hii inatukumbusha umuhimu wa kuomba pindi tunapopata majanga mbalimbali.Hivyo, narudia tena kuwasihi Viongozi wetu wa dini kuendelea kuliombea Taifa letu; lakini pia muwahimize waumini wenu kusali ili kuiombea nchi yetu. Kamwe tusikubali shetani kupitia Korona, atuvuruge na kumsahamu Mwenyezi Mungu. Huu ndio wakati wa kupambana na shetani korona kwa nguvu zote. Nina imani Mungu wetu siku zote atakuwa upande wetu na mapambano haya yetu dhidi ya korona tutayashinda
Mungu Ibariki Tanzania
Mungu Ibariki Afrika
‘’Ahsanteni sana kwa Kunisikiliza’’