Rais wa Jamhuri ya Burundi Mhe. Évariste Ndayishimiye amewasili nchini kwa ziara ya kitaifa ya siku 3 yenye lengo la kuimarisha uhusiano baina ya nchi yake na Tanzania.
Mara baada ya kuwasili katika viwanja vya Ikulu, Chamwino mkoani Dodoma, Mhe. Rais Ndayishimiye amepokelewa na mwenyeji wake Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan na kukagua gwaride la heshima lililoandaliwa kwa ajili yake pamoja na kupigiwa mizinga 21.
Mhe. Rais Ndayishimiye amefanya mazungumzo na mwenyeji wake Mhe. Rais Samia pamoja na kuzungumza na waandishi wa habari kuhusu masuala mbalimbali ya uhusiano na ushirikiano wa nchi hizi mbili.
Katika mazungumzo na waandishi wa habari, Mhe. Rais Samia amesema Tanzania inaridhishwa na uhusiano mzuri na wa kidugu uliopo kati yake na Burundi na kusisitiza kuwa uhusiano huo utadumishwa.
Mhe. Rais Samia amempongeza Mhe. Rais Ndayishimiye kwa jitihada zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali yake katika kuimarisha hali ya amani na utulivu pamoja na kuimarisha umoja wa kitaifa wa Warundi.
Pia, Mhe. Rais Samia amempongeza Mhe. Ndayishimiye kwa hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali yake katika kuimarisha uchumi ikiwemo mapambano dhidi ya rushwa, kuondoa tozo kwenye sekta ya kilimo pamoja na kutoa mikopo kwa wanawake na vijana.
Aidha, Mhe. Rais Samia ameeleza kuwa Serikali ya Tanzania inaungana na Burundi kulaani matukio ya kigaidi yaliyotokea tarehe 18 na 20 Septemba, 2021 nchini Burundi na kusababisha vifo vya watu 9 na wengine kujeruhiwa pamoja na uharibifu wa mali.
Mhe. Rais Samia amesema Tanzania inaendelea na utekelezaji wa makubaliano yaliyofikiwa wakati wa Mkutano wa Sita wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano (JPC) uliofanyika Kigoma tarehe 3 hadi 5 Machi, 2021 na kuishukuru Burundi kwa hatua ya utekelezaji wa makubaliano hayo.
Amemhakikishia Mhe. Rais Ndayishimiye kuwa Tanzania itaendelea kushirikiana na Burundi katika kulinda na kuimarisha ulinzi hususan kwenye mipaka ya nchi hizi mbili.
Kuhusu ushirikiano katika sekta ya biashara na Uwekezaji, Mhe. Rais Samia amesema biashara kati ya Tanzania na Burundi inaendelea kushamiri na kuongezeka.
Kwa upande wake Rais wa Jamhuri ya Burundi Mhe. Évariste Ndayishimiye amemshukuru Mhe. Rais Samia kwa mualiko wa kuja kutembelea Tanzania katika ziara hiyo ambayo amesema inazidi kuimarisha uhusiano wa kidugu baina ya mataifa hayo uliokuwepo kwa muda mrefu.
Mhe. Rais Ndayishimiye amempongeza Mhe. Rais Samia kwa kuongoza nchi vizuri na kuonyesha mfano bora kwa wanawake kuwa wanaweza wanapopata nafasi.
Aidha, Mhe. Ndayishimiye ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa kupitia majukwaa mbalimbali ya kimataifa kuitetea kupata haki na kuipigania kuondolewa vikwazo na Jumuiya za Kimataifa ambapo Burundi inategemea vikwazo hivyo vitakwisha hivi karibuni.
Vilevile, Mhe. Nadyishimiye amemuhakikishia Mhe. Rais Samia kuwa kiwanda cha kuzalisha mbolea cha ITRACOM, kilichopo Nala Jijini Dodoma kitatoa ajira sawa kwa raia wa Burundi na Tanzania na kitapunguza uhaba wa mbolea hapa nchini pindi kitakapokamilika.
Pia. Mhe. Rais Ndayishimiye ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa kuipatia eneo kwa ajili ya ujenzi wa bandari kavu katika eneo la Kwala Ruvu mkoani Pwani na Katosho Kigoma ambazo zitasaidia kupunguza gharama za usafirishaji wa mizigo na kuongeza tija katika uzalishaji.
Mhe. Rais Ndayishimiye anatarajiwa kuhudhuria Dhifa ya Kitaifa leo jioni iliyoandaliwa kwa heshima yake na Mwenyeji wake Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan, katika viwanja vya Ikulu Chamwino mkoani Dodoma.