Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, amesema malengo makuu ya kuwepo kwa mfumo wa Demokrasia ya vyama vingi vya siasa nchini ni kuongeza kasi ya kuleta maendeleo kwa wananchi.
Mhe. Rais Samia amesema hayo tarehe 15 Desemba, 2021 wakati akifungua mkutano wa wadau wa siasa unao jadili hali ya demokrasia ya vyama vingi vya siasa nchini Tanzania, unaofanyika Jijini Dodoma.
Mhe. Rais Samia amesema fursa ya kuwa na jukwaa la kutoa mawazo mbadala lisiwe kibali cha kuendesha siasa za chuki, uhasama, na zinazokwamisha maendeleo ya wananchi.
Amesema tukiendesha siasa za namna hiyo itakuwa ni kinyume na malengo ya kuanzishwa kwa mfumo wa demokrasia ya vyama vingi vya siasa, kwasababu hata katika nchi za ambazo ndio waasisi wa mfumo huo wanazipa kipaumbele shughuli za maendeleo kuliko malumbano ya kisiasa.
Aidha, amesema siasa za maneno yasiyo na staha, kusema uongo, lugha za dhihaka, maneno ya kashfa, kuchochea watu wasishiriki katika shughuli za Maendeleo, kutotii sheria, uchonganishi baina ya wananchi hazina tija yoyote bali ni ukiukwaji wa kanuni za ushindani.
Mhe. Rais Samia amewakumbusha wadau wa siasa kwamba Tanzania ni moja tu duniani ambayo ni taifa huru lililojengwa katika misingi ya amani, upendo na mshikamano na linaloongozwa kwa misingi ya Katiba na Sheria zilizotungwa na Bunge na sio utashi wa mataifa ya nje.
Pia, Mhe. Rais Samia amesema demokrasia ya vyama vingi vya siasa nchini itakuwa na maana kama amani, utulivu na umoja wa kitaifa utadumishwa na kuwaletea maendeleo wananchi.
Vile vile, Mhe. Rais Samia ameviasa vyama vya siasa na taasisi za kiraia kuheshimu sheria, kanuni na taratibu ili uhuru uwe na maana iliyokusuiwa na amani iweze kutamalaki.
Mhe. Rais Samia amevishauri vyama vya siasa na taasisi za kiraia nchini kuwa kunapotokea tatizo lolote katika mfumo, kasoro au mambo kutokwenda sawa, njia nzuri ni kufanya majadiliano yatakayokuja na majawabu na sio malumbano.
Akijibu ombi la Mwenyekiti wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) Mhe. Zitto Kabwe kuhusu kutoa msamaha kwa Kiongozi mmoja wa Kisiasa, Mhe. Rais Samia amesema demokrasia ni kuheshimu sheria, unapoheshimu sheria ndipo demokrasia inapokua, lakini pia ndipo inapoleta heshima, heshima ya mtu inakuja kwa kuheshimu sheria za nchi, unapovunja sheria za nchi heshima yako haitaheshimiwa, Serikali haitakuheshimu lakini lazima ujue kwamba unapotumia uhuru wako mwisho wa uhuru wako huanza heshima ya mtu mwingine.
Aidha, Mhe. Rais Samia amewaomba viongozi wa Vyama vya Siasa, kuacha kufikiria mambo yaliyopita, bali watazame mbele kwa matumaini, waweke nguvu zao pamoja kuijenga Tanzania mpya na amesisitiza kuwa kama mkuu wa Nchi ana jukumu na wajibu wa ulezi na kama mlezi anatakiwa kuwa mvumilivu, msikivu na mwenye kusamehe.
Amesema yupo tayari kusikiliza viongozi wenzake, washawishiane kusameheana, kwa kuwa anajua kuna mengi ya kusikiliza, madukuduku, hasira, malalamiko, nongwa, yanayotokana na uchanga wa demokrasia.
Mhe. Rais Samia amesema wanachama wa vyama vya siasa na viongozi wao wana uhuru wa kufanya kazi zao za kichama na kisiasa, huku wakitumia Vyombo vya habari vilivyo huru kujitangaza na kunadi sera zao, ispokuwa suala la msingi ni kufuata sheria za nchi na kuhakikisha wanafanya siasa ambazo hazicheleweshi ama kuvuruga maendeleo ya nchi.
Pia, Mhe. Rais amemtaka Msajili wa Vyama vya Siasa pamoja na Vyama vya Siasa kukaa na kujadiliana katika Mkutano huo namna bora ya kufanya shughuli zao za mikutano ya kisiasa bila kuvunja sheria za nchini.