Taarifa kwa vyombo vya Habari ya zamani
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 10 Agosti, 2016 ameanza ziara ya siku mbili katika mikoa ya Geita na Mwanza baada ya kumaliza mapumziko mafupi nyumbani kwake Chato Mkoani Geita.
Jijini Mwanza Rais Magufuli amepokelewa na maelfu ya wananchi waliokuwa wakisimamisha msafara wake tangu alipoingia kupitia kivuko cha Busisi - Kigongo na baadaye kupita Usagara, Buhongwa, Mkolani, Nyegezi, Mkuyuni na Igogo ambako pamoja na kuwahakikishia kuwa Serikali yake imejipanga kukabiliana na kero mbalimbali za wananchi na kuwaletea maendeleo, amesitisha agizo la Jiji la Mwanza la kuwataka wafanyabiashara wadogo maarufu kwa jina la Machinga kutofanya biashara zao katikati ya Jiji ifikapo tarehe 20 Agosti, 2016.
Pamoja na kusitisha agizo hilo, Dkt. Magufuli amewaagiza viongozi wa Jiji la Mwanza na Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela kutafuta na kuandaa maeneo ambayo wafanyabiashara hao watayatumia kwa ajili ya kufanyia biashara zao.
"Na mtakapowatafutia maeneo ya biashara wapelekeni sehemu ambazo ni nzuri, msiwapeleke sehemu ambazo hazina biashara, hawa wamachinga wanaendesha maisha yao kwa kutumia biashara hizi" Amesema Rais Magufuli.
Aidha, Rais Magufuli amewahakikishia wananchi wa Mwanza kuwa Serikali imeanza kufanya usanifu na upembuzi yakinifu ikiwa ni maandalizi ya kuanza ujenzi wa daraja kubwa litakalounganisha eneo la Busisi Wilayani Sengerema na Kigongo Wilayani Misungwi ili kuondoa adha ya wananchi kuvuka eneo hilo kwa kutegemea vivuko, na pia itahakikisha inanunua meli moja katika ziwa viktoria kama ilivyoahidi.
Kabla ya kuingia Jijini Mwanza Rais Magufuli amehutubia mkutano wa hadhara katika Mji wa Sengerema na pia amezungumza na wananchi wa Sima Wilayani Sengerema na Kasamwa Wilayani Geita ambako amewahakikishia kuwa Serikali yake itaongeza msukumo katika kutatua tatizo la uhaba wa maji katika maeneo hayo kwa kusambaza maji ya kutoka ziwa Viktoria huku akiwataka viongozi halmashauri husika kutumia rasilimali za halmashauri kutatua tatizo hilo la maji katika maeneo ambayo hayatapitiwa na mradi mkubwa wa maji ya kutoka ziwa Viktoria.
Katika hatua nyingine Mhe. Rais Magufuli amewaagiza viongozi wa Mikoa ya Mwanza na Geita kutafakari sababu zilizosababisha kufa kwa Chama Kikuu cha Ushirika cha NYANZA na viwanda vya kuchambua pamba (Ginneries) ili kupanga namna ya kuvifufua.
Rais Magufuli ametoa agizo hilo leo alipokuwa akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Kasamwa kilichopo Wilayani Geita na ameahidi kuwa Serikali yake ipo tayari kuunga mkono juhudi za wakulima kwa kuanzisha viwanda vya kuongeza thamani ya mazao yao ikiwemo zao la pamba.
Rais Magufuli atakamilisha ziara yake ya siku mbili kesho tarehe 11 Agosti, 2016 kwa kuweka jiwe la msingi katika Daraja la watembea kwa miguu na kuzungumza na wananchi wa Mwanza katika Uwanja wa Furahisha.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Mwanza
10 Agosti, 2016
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 07 Agosti, 2016 ametembelea Msikiti na Makanisa yaliyopo Chato Mjini Mkoani Geita na kuendelea kuwasihi Watanzania kuombea amani na utulivu katika nchi bila kujali tofauti za dini, makabila na kanda wanazotoka.
Rais Magufuli ametoa ujumbe huo mara baada ya kusali ibada ya Jumapili katika Kanisa Katoliki la Bikira Maria Parokia ya Chato, na baadaye kutembelea Kanisa la Anglikana la Mtakatifu Stephano Parokia ya Chato, Kanisa la African Inland Church la Chato na kumalizia katika Msikiti wa Omar Bin -L-Khattab wa Chato.
Dkt. Magufuli amesema pamoja na Watanzania wote kuungana kuombea amani na utulivu pia hawana budi kutekeleza kwa vitendo Maandiko Matakatifu ya Biblia yasemayo "Asiyefanya kazi na asile" kwa kuhakikisha kila mmoja anachapakazi kwa juhudi na maarifa ili kuharakisha maendeleo ya Taifa.
"Ndugu zangu nawashukuru sana, muendelee kuliombea taifa hili, taifa letu ni la umoja, sisi wote ni Watanzania, tuendelee kumuomba mola wetu, kudumisha amani yetu, kujenga umoja wetu kwa dini zote, makabila yote na vyama vyote, kwa sababu mola wetu anatupenda sisi sote" Amesema Rais Magufuli.
Aidha, mara baada ya kuwasalimu waumini wa Kanisa Katoliki la Bikira Maria Parokia ya Chato, Rais Magufuli ameendesha harambee ya kuchangia ujenzi wa jengo jipya la Kanisa hilo ambapo amefanikiwa kukusanya Shilingi Milioni moja za papo kwa papo.
Tayari Dkt. Magufuli alishachangia ujenzi huo kwa kutoa Shilingi Milioni kumi tarehe 03 Aprili, 2016 na ametoa wito kwa watu mbalimbali kujitokeza kuchangia ujenzi wa Kanisa hilo.
Katika Msikiti wa Omar Bin-L-Khattab na Makanisa ya Anglikana na African Inland Church Rais Magufuli amechangia Shilingi Milioni tano kwa kila moja kwa ajili kuendeleza na kukarabati majengo.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU.
Chato
07 Agosti, 2016
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amewaagiza viongozi wote wa kuanzia ngazi ya Mkoa hadi Kitongoji hapa nchini kufuatilia matumizi ya fedha zinazotolewa na Serikali kwa ajili ya kutoa elimu bila malipo kwa lengo la kudhibiti mianya ya matumizi mabaya ya fedha hizo.
Rais Magufuli ametoa maagizo hayo leo tarehe 01 Agosti, 2016 katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa Mnadani na kuwajumuisha wananchi wa Katoro na Buseresere Mkoani Geita.
Katika agizo hilo Dkt. Magufuli amewaonya walimu ambao wameanza kufanya udanganyifu kwa kuandikisha idadi kubwa ya wanafunzi kuliko idadi halisi kwa lengo la kupata mgao mkubwa wa fedha za ruzuku na amesema Serikali itachukua hatua kali dhidi ya yeyote atakayebainika kufanya hivyo.
"Ninafahamu mgao wa fedha hizo hutolewa kulingana na idadi ya wanafunzi waliopo, wapo baadhi ya walimu ambao wameanza kuandika wanafunzi hewa katika shule zao, ili kusudi aletewe hela nyingi kuliko idadi ya wanafunzi waliopo, wanafunzi kama wapo laki nne yeye anasema shule yangu hii ina wanafunzi laki tano, ili kusudi hela zikija za wanafunzi laki tano, za wanafunzi laki moja wagawane.
"Napenda nitoe wito kwa walimu Tanzania nzima, mnatafuta matatizo, narudia mnatafuta matatizo, msijaribu kula hela ya Serikali" Amesema Rais Magufuli.
Pamoja na agizo hilo, Rais Magufuli pia ametaka viongozi wa ngazi zote katika Mikoa kuhakikisha wana takwimu za idadi ya wanafunzi katika shule zote zilizopo katika maeneo yao ili kurahisisha ufuatiliaji wa fedha hizo na amesema kuwa kuanzia sasa ataanza kutembelea shule kwa kushitukiza na kwamba kiongozi atakayeonekana kutojua takwimu itakuwa ni uthibitisho kuwa hatoshi kuendelea na wadhifa alionao.
"Na nitoe wito kwa viongozi wa Mikoa, Mkuu wa Mkoa, Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi, Makatibu Tarafa, Watendaji wa Kata, Wenyeviti wa Vijiji, kila mmoja awe na idadi ya wanafunzi waliopo katika shule zao, hatutaki kuwapunja wanafunzi hela ambayo wanatakiwa kupata, lakini pia hatutaki kutoa hela ambayo haitakiwi" Amesisitiza Rais Magufuli.
Mhe. Rais Magufuli ambaye ametumia mkutano huo kueleza juhudi mbalimbali zilizofanywa na Serikali yake ya Awamu ya Tano, kutekeleza ahadi yake ya kujenga Tanzania Mpya pia amewataka viongozi na watendaji wa Serikali kutekeleza wajibu wao kwa kutembelea wananchi wanaowaongoza badala ya kukaa muda mwingi ofisini huku akisisitiza ofisi hizo kuwepo katika maeneo yenye shughuli husika.
Aidha, Dkt. Magufuli amekosoa utaratibu unaotumiwa na Halmashauri nyingi za Majiji, Manispaa, Miji na Wilaya kutumia mawakala katika ukusanyaji wa mapato ya Halmashauri akisema mawakala hao wamekuwa wakitumia utaratibu huo kukusanya fedha nyingi na kisha kuwasilisha kiasi kidogo katika Halmashauri husika.
"Hivi kwa nini Halmashauri msingekuwa na maafisa wenu wazuri na mkawa na mashine za kielektroni kwa ajili ya kukusanya fedha? Amehoji Dkt. Magufuli na kuongeza kuwa "tena mawakala wengine ndio hao hao wamekuwa wakikusanya kodi hata kwa wananchi wanyonge wenye vibiashara vidogo vya kuuza mchicha bila hata kuwaonea huruma"
Rais Magufuli ambaye ameongozana na Mkewe Mama Janeth Magufuli amemaliza ziara yake ya siku nne katika Mikoa ya Singida, Tabora, Shinyanga na Geita na yupo nyumbani kwake Chato Mkoani Geita kwa mapumziko mafupi.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Chato
01 Agosti, 2016
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amesema serikali yake haitagawa chakula cha bure kwa wananchi wanaopatwa na tatizo la njaa pasipo kuwa na sababu za msingi na badala yake amewataka watanzania wajikite kufanya kazi kwa juhudi na maarifa ikiwa ni pamoja na kuzalisha chakula cha kutosha.
Rais Magufuli amesema hayo leo tarehe 31 Julai, 2016 wakati akihutubia mikutano ya hadhara na kuzungumza na wananchi waliosimamisha msafara wake akiwa njiani kutoka Mkoani Tabora kuelekea Shinyanga na baadaye Geita anakoendelea na ziara yake.
Pamoja na kuwahimiza wananchi kuzalisha chakula cha kutosha ili kuondokana na njaa Rais Magufuli amesema serikali yake itajikita kuhakikisha inashughulikia tatizo la uhaba wa maji, ujenzi wa miundombinu hususani barabara na reli, kuimarisha huduma za matibabu, elimu na kutengeneza ajira.
Akiwa Isaka Mkoani Shinyanga Rais Magufuli amesema serikali haitalipa fidia kwa wananchi waliopatwa na maafa ya mafuriko yaliyobomoa nyumba zao mwezi Machi mwaka 2015 na badala yake itajielekeza kutatua tatizo kubwa la uhaba wa maji katika mji huo ambao una makutano ya reli ya kati ya kutoka Dar es Salaam kwenda nchi za Burundi na Rwanda.
Katika Mji wa Kagongwa Rais Magufuli amepokea kilio cha wananchi dhidi ya vitendo vya ujambazi na ametoa siku tano kwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Shinyanga kuhakikisha watu wanaojihusisha na ujambazi wanakamatwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria.
Mjini Kahama, Dkt. Magufuli ameiagiza Wizara ya Nishati na Madini kushirikiana na Mbunge wa Kahama Mhe. Jumanne Kishimba kukokotoa mahesabu vizuri na kubaini kodi ambayo Serikali inastahili kulipwa baada ya Mbunge huyo kudai kuna kiasi kikubwa cha kodi hakijakusanywa kama ambavyo sheria inaelekeza.
Aidha, Rais Magufuli amesema serikali itahakikisha wawekezaji wanaochimba madini wanaacha kusafirisha mchanga wenye madini kwa lengo la kwenda kuchakata nje ya nchi na badala yake ametaka uchakataji huo ufanyike hapa hapa nchini.
Dkt. Magufuli amezungumza na wananchi vijiji vya Segese na Bukoli na kuwahakikishia kuwa Barabara ya Kahama, Segese, Kakola hadi Geita yenye urefu wa kilometa 146 itajengwa kwa kiwango cha lami kama alivyoahidi.
Mjini Geita, Rais Magufuli amepokea kilio cha wananchi wanaodai kuwekewa zuio la kutumia mawe yenye mabaki ya madini ya dhahabu (Magwangala) kwa lengo la kusaga na kuchenjua ili kupata dhahabu, na ametoa wiki tatu kwa Wizara ya Nishati na Madini kwa kushirikiana na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kufanya tathimini na kuwaruhusu wachimbaji wadogo kutumia Magwangala.
Rais Magufuli pia ameiagiza Bodi ya Pamba hapa nchini kuhamisha ofisi zake zilizopo Jijini Dar es salaam na kuzileta katika Mikoa ya kanda ya ziwa ambako uzalishaji wa zao la pamba unafanyika.
Dkt. Magufuli amewaonya viongozi na watendaji wa bodi hiyo dhidi ya vitendo vya usambazaji wa mbegu za pamba zisizoota na amesema ikitokea tena watachukuliwa hatua.
Kesho tarehe 01 Agosti, 2016 Rais Magufuli ambaye ameongozana na Mkewe Mama Janeth Magufuli anatarajia kukamilisha ziara yake ya siku nne katika Mikoa ya Singida, Tabora, Shinyanga na Geita.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Geita
31 Julai, 2016
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 30 Julai, 2016 ameendelea na ziara yake katika Mkoa wa Tabora akitokea Mkoa wa Singida.
Kabla ya kuingia Mkoani Tabora, Rais Magufuli amezungumza na wananchi wa Mji wa Misigiri katika Wilaya ya Iramba ambapo amemuagiza Meneja wa Wakala wa Barabara katika Mkoa wa Singida kuhakikisha mkandarasi anayejenga daraja la Sibiti anarejea kazini mara moja kukamilisha ujenzi wa daraja hilo.
Rais Magufuli amesema serikali yake imejipanga kumlipa fedha mkandarasi huyo na hivyo hakuna sababu ya kuendelea kusimamisha ujenzi huo.
Mkoani Tabora, Rais Magufuli amezungumza na wananchi waliosimamisha msafara wake katika vijiji vya Nanga na Ziba na amefanya mikutano ya hadhara katika miji ya Igunga na Nzega ambako amewahakikishia wananchi kuwa serikali yake itahakikisha inatekeleza ahadi zilizopo katika Ilani ya Uchaguzi Mkuu ya Mwaka 2015.
Katika mkutano wa hadhara uliofanyika Igunga, Rais Magufuli amepokea malalamiko ya wananchi kuhusu kutoanza kutumika kwa kituo cha mabasi na soko na amewaagiza viongozi wa Mkoa wa Tabora kuhakikisha kituo cha mabasi cha Igunga na soko la Igunga vinaanza kutumika kuanzia Jumatatu ijayo ya tarehe 01 Agosti, 2016.
Kuhusu kero ya maji, Dkt. Magufuli amesema Tanzania imepata mkopo wa dola za kimarekani Milioni 268.35 kutoka nchini India ambazo zitatumika kutekeleza mradi wa kusambaza maji ya ziwa Viktoria katika Miji ya Tabora, Igunga, Nzega, Sikonge na Uyui pamoja na vijiji vilivyopo kandokando mwa bomba kuu kuanzia mwaka huu ambapo watu milioni moja na laki moja (1,100,000) watanufaika.
Dkt. Magufuli ameongeza kuwa pamoja na juhudi hizo Serikali imefanya usanifu na upembuzi yakinifu kwa ajili ya kutekeleza mradi wa kusambaza maji ya kutoka mto Malagarasi kwa ajili ya Miji ya Urambo, Kaliua na Nguruka pamoja na vijiji vilivyopo kandokando mwa bomba kuu ambako watu laki sita (600,000) watanufaika.
Aidha, Rais Magufuli amepiga marufuku wakulima wadogo kutozwa ushuru wa mazao watokapo na mazao mashambani.
"Ninapenda tukusanye kodi, lakini sio kukusanya kodi kutoka kwa watu masikini, mtu ametoka shambani na magunia yake mawili au hata matano halafu nyinyi mnamtoza kodi.
"Mimi sipendi kuwanyanyasa hawa watu wanyonge, mtu akiwa na mazao lori zima hapo sawa lakini sio kwa mtu mnyonge mwenye gunia moja" Amesema Rais Magufuli.
Kuhusu maombi ya Mkoa wa Tabora kutaka kuanzishwa Mkoa mwingine kutokana na ukubwa wa baadhi ya Wilaya Rais Magufuli amesema haioni umuhimu wa kuanzisha Mikoa mipya hapa nchini kwa sasa, na badala yake fedha zitaelekezwa katika huduma kwa wananchi kama vile maji, barabara, miundombinu na huduma za afya.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Nzega
30 Julai, 2016
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 29 Julai, 2016 ameanza ziara ya siku nne katika mikoa ya Singida, Tabora, Shinyanga na Geita akitokea mkoani Dodoma, ambapo amezungumza na wananchi kwa lengo la kuwashukuru kwa kumpigia kura katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana na kueleza juhudi zinazofanywa na serikali katika kutatua kero za wananchi na kuwaletea maendeleo.
Akiwa Mkoani Singida, Rais Magufuli aliyeongozana na mkewe Mama Janeth Magufuli amewasihi watanzania kufanya kazi kwa juhudi na kujiepusha na vitendo vya vurugu vinavyohamasishwa na baadhi ya wanasiasa huku akionya kuwa serikali yake haitamvumilia mtu yeyote ambaye atathubutu kuchochea vurugu ikiwemo maandamano kinyume cha sheria.
"Sitaki nchi hii iwe ya vurugu, watakaoleta vurugu mimi nitawashughulikia kikamilifu bila huruma, na wasije wakanijaribu, mimi ni tofauti sana na kama wapo watu wanaowatumia wakawaeleze vizuri, mimi sijaribiwi na wala sitajaribiwa.
"Wananchi hawa wana shida, na siasa nzuri ni wananchi washibe, siasa nzuri ni wananchi wetu wapate dawa" Amesema Rais Magufuli.
Kuhusu hatua mbalimbali zilizochukuliwa na Serikali yake ya awamu ya tano tangu aingie madarakani Rais Magufuli ametaja baadhi ya hatua hizo kuwa ni kufuta ada kwa shule za msingi na sekondari, kutoa mikopo kwa wanafunzi wa vyuo vikuu zaidi ya laki moja na kuongeza fedha za miradi ya maendeleo katika bajeti ya serikali kutoka asilimia 26 ya mwaka 2015/2016 hadi kufikia asilimia 40 katika bajeti ya mwaka huu 2016/2017.
Hatua nyingine ni kuondoa wafanyakazi hewa 12,500 katika orodha ya waliokuwa wanalipwa mshahara na serikali, kudhibiti upotevu wa mapato serikalini, kutenga shilingi Trilioni moja kwa ajili ya kuanza ujenzi wa Reli ya kati kwa kiwango cha kisasa yaani Standard gauge na pia akazungumzia hatua zilizochukuliwa dhidi ya wala rushwa na wanaojihusisha na ufisadi kwa kuunda mahakama ya mafisadi huku akiapa kuwa katika kipindi chake hakuna fisadi atakayeendelea kutamba.
Akiwa njiani Rais Magufuli amewasalimu wananchi wa Ikungi na baadaye amefanya mkutano wa hadhara Singida Mjini ambako amesisitiza kuwa serikali yake haiko tayari kumvumilia mtu yeyote atakayekwamisha utekelezaji wa Ahadi na Ilani ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2015.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Singida
29 Julai, 2016
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli ametengua uteuzi wa Mwenyekiti wa Bodi ya Mfuko wa Barabara (Road Fund Board) Dkt. James Munanka Wanyancha.
Taarifa ya Katibu Mkuu Kiongozi iliyotolewa leo Mjini Dodoma imeeleza kuwa Rais Magufuli ametengua uteuzi huo kuanzia leo tarehe 28 Julai, 2016.
Kufuatia kutenguliwa kwa uteuzi huo, Rais Magufuli amemteua Bw. Joseph Odo Haule kuwa Mwenyekiti mpya wa Bodi ya Mfuko wa Barabara.
Uteuzi wa Bw. Joseph Odo Haule umeanza leo tarehe 28 Julai, 2016.
Kabla ya uteuzi huo Bw. Joseph Odo Haule alikuwa Meneja wa Mfuko wa Barabara (Road Fund).
Wajumbe wengine wa Bodi ya Mfuko wa Barabara wanaendelea katika nafasi zao.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dodoma
28 Julai, 2016
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli amemuapisha Bw. Oliva Paul Joseph Mhaiki kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC).
Aidha, Rais Magufuli amemuapisha Mwl. Winifrida Gaspar Rutaindurwa kuwa Katibu wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC).
Rais Magufuli alifanya uteuzi wa Mwenyekiti na Katibu wa Tume ya Utumishi wa Walimu tarehe 15 Julai, 2016.
Viongozi hawa wanakuwa wa kwanza kuongoza Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) tangu Tume hiyo ilipoundwa kwa mujibu wa sheria ya Tume ya Utumishi wa Walimu Namba 25 ya mwaka 2015 ikiwa na majukumu ya kusimamia na kuratibu masuala yanayohusu utumishi wa walimu.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dodoma
27 Julai, 2016
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 26 Julai, 2016 amekutana na kufanya mazungumzo na Makamu wa Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) Dkt. Frannie Leautier katika Ikulu ya Chamwino Mkoani Dodoma, ambapo ameishukuru benki hiyo kwa mchango wake mkubwa katika maendeleo ya Tanzania hususani kutoa mikopo iliyowezesha ujenzi mkubwa wa barabara.
Pamoja na kuishukuru AfDB Rais Magufuli ameiomba benki hiyo kuendelea kushirikiana na Tanzania katika utekelezaji wa mipango na miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo mpango mkubwa wa uzalishaji wa nishati ya umeme utakaofanikisha ujenzi wa viwanda, ujenzi wa barabara zinazounganisha ndani na nje ya Tanzania na kuunga mkono juhudi za kukabiliana na rushwa.
Kwa upande wake Makamu wa Rais wa AfDB Dkt. Frannie Leautier amempongeza Rais Magufuli kwa juhudi kubwa alizozianza katika kujenga uchumi wa Tanzania, kukabiliana na rushwa na kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya serikali na ameahidi kuwa benki hiyo itaendelea kuunga mkono juhudi hizo kwa kutoa mikopo ya masharti nafuu itakayofanikisha mipango na miradi mbalimbali ya Tanzania.
"Tanzania ni nchi ambayo inapata fedha kuliko nchi zote za Afrika katika mpango wa AfDB kupitia Mfuko wa Maendeleo wa Afrika, hizi ni fedha ambazo zinatolewa kwa mkopo nafuu zaidi kuliko mikopo mingine" Amesema Dkt. Frannie Leautier.
Dkt. Frannier Leautier amebainisha kuwa AfDB inatarajia kuwa Tanzania itanufaika kupitia vipaumbele vitano vya benki hiyo ambavyo ni kusaidia uzalishaji wa nishati, utangamano wa bara la Afrika, maendeleo ya viwanda, usalama wa chakula na kuboresha hali ya maisha.
Aidha, Makamu wa Rais huyo wa AfDB amesema kuanzia mwakani benki hiyo imepitisha miradi mikubwa mitatu kwa ajili ya Tanzania ambayo ujenzi wa nyumba ya makazi, utoaji wa mikopo vijijini kwa ajili ya kuendeleza kilimo na maeneo ya uchumi kupitia benki ya CRDB na kukiendeleza Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Nelson Mandela kilichopo Arusha ambapo benki hiyo itatoa Dola za Marekani Milioni 4.
Mazungumzo hayo yamehudhuriwa na Mwakilishi Mkazi wa AfDB Dkt. Tonia Kandiero, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Ashatu Kijaji.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dodoma
26 Julai, 2016
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amemteua Dkt. Samuel M. Nyantahe kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC).
Taarifa ya Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi imeeleza kuwa Uteuzi huu umeanza tarehe 20 Julai, 2016.
Kabla ya uteuzi huo Dkt. Samuel M. Nyantahe alikuwa Mwenyekiti wa Shirikisho la Wenye Viwanda Tanzania (CTI).
Dkt. Samuel M. Nyantahe anachukuwa nafasi iliyoachwa wazi na Dkt. Chrisant Majiyatanga Mzindakaya ambaye amejiuzulu wadhifa huo.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dodoma
25 Julai, 2016
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amewasihi Watanzania kuwaenzi Mashujaa kwa kudumisha Amani, Umoja na Utulivu uliojengwa na mashujaa hao.
Rais Magufuli ametoa rai hiyo leo tarehe 25 Julai, 2016 wakati wa maadhimisho ya kumbukumbu ya siku ya Mashujaa, yaliyofanyika katika uwanja wa Mashujaa Mjini Dodoma.
Pamoja na kutoa rai hiyo Rais Magufuli ameahidi kuwa atahakikisha azma ya Serikali kuhamia Dodoma inatekelezwa kabla ya kuisha kwa kipindi chake cha uongozi wa miaka mitano.
"Tunapoadhimisha siku ya Mashujaa hatuwezi kumsahau Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Baba wa Taifa alisema makao makuu yawe Dodoma, haiwezekani sisi watoto wake, sisi wajukuu wake tupinge kauli ya Mzee huyu.
"Kwa hiyo nilikwishazungumza na leo narudia hili katika siku ya Mashujaa, mlinichagua ndugu zangu wa Dodoma kwa kipindi cha miaka mitano, hadi sasa miezi minane imepita, nimebakiza miaka minne na miezi minne, nataka kuwathibitishia kuwa katika kipindi cha miaka minne na miezi minne iliyobaki nitahakikisha serikali yangu pamoja na mimi tunahamia Dodoma bila kukosa" amesema Rais Magufuli.
Kufuatia maelekezo hayo ya Mhe. Rais, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa ameagiza Mawaziri wote waanze mara moja kuhamia Dodoma na kwamba yeye mwenyewe atakuwa amehamia Dodoma ifikapo mwezi Septemba mwaka huu.
Viongozi wengine waliohudhuria maadhimisho hayo ni Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein, Rais Mstaafu wa awamu ya Pili Alhaji Ali Hassan Mwinyi, Mke wa Rais Mama Janeth Magufuli, Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Tulia Ackson, Spika wa Baraza la Wawakilishi Mhe. Zubeir Ali Maulid, Mawaziri Wakuu wastaafu Mhe. John Samwel Malecela na Mhe. Mizengo Kayanza Peter Pinda, Mabalozi na wanadiplomasia kutoka nchi mbalimbali, Viongozi wa vyombo vya ulinzi na usalama, Viongozi wa vyama vya siasa na dini, maafisa na askari waliopigana vita mbalimbali.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dodoma
25 Julai, 2016
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Benki ya Exim ya China imekubali kutoa mkopo wenye masharti nafuu wa dola za Marekani Bilioni 7.6 sawa na zaidi ya Shilingi Trilioni 16 za kitanzania kwa ajili ya kugharamia ujenzi wa mradi mkubwa wa reli ya kati hapa nchini kwa kiwango cha kisasa (Standard Gauge) unaotarajiwa kuanza katika mwaka huu wa fedha.
Rais wa Benki ya Exim ya China Bw. Liu Liang amemueleza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 20 Julai, 2016 katika Ikulu ndogo ya Chamwino Mkoani Dodoma kuwa pamoja na kutoa fedha hizo zitakazofanikisha ujenzi wa kilometa 2,190 za reli ya kati benki hiyo itashirikiana na Tanzania katika kubadilishana uzoefu na utaalamu katika ujenzi na uendeshaji wa reli.
Pamoja na kukubali kutoa fedha hizo, Rais huyo wa Benki ya Exim ya China amempongeza Rais Magufuli na serikali yake kwa dhamira ya dhati ya kuiletea nchi maendeleo ikiwemo kuharakisha ujenzi wa reli ya kati na ameahidi kuwa benki yake itatoa ushirikiano wa karibu katika kufanikisha mradi huo na miradi mingine ya maendeleo.
"Kuhusu huu mradi wa reli ya kati tuna mtazamo chanya, tunauona ni mradi mzuri na tutatoa ushirikiano wowote utakaohitajika. Tunaamini kuwa kwa ushirikiano na serikali ya Tanzania mchakato wa utekelezaji wa mradi huu utafanyika kwa mafanikio na kwa kuzingatia muda" Amesema Rais Magufuli.
Kwa upande wake Rais Magufuli amemshukuru Rais wa Benki ya Exim ya China Bw. Liu Liang kwa kukubali kutoa fedha hizo na amemuhakikishia kuwa Tanzania imedhamiria kutekeleza mradi huo ambao tayari ujenzi wake umepangwa kuanza katika mwaka huu wa fedha kwa kutumia fedha za ndani kiasi cha shilingi Trilioni 1 zilizotengwa katika bajeti.
Rais Magufuli amebainisha kuwa kutekelezwa kwa mradi huo kutasaidia kuinua uchumi wa Tanzania na nchi jirani zisizopakana na bahari zikiwemo Uganda, Rwanda, Burundi, na Congo.
"Kwa hiyo kukubali kwao ambako ilikuwa ni kitu kikubwa, inaonesha kwamba juhudi za Tanzania kwenda haraka haraka zinakubalika kimataifa, na wenzetu hawa wachina wana pesa nyingi.
"Na kule kuaminika kwamba tunakopeshwa kwa masharti nafuu, riba yake ni ndogo na huku kwetu ni mafanikio makubwa, kwa hiyo mizigo mingi tutakuwa tunaisafirisha, tutaendeleza reli yetu na bandari zetu" Amesema Rais Magufuli.
Mradi wa ujenzi wa reli ya kati utahusisha ujenzi wa reli kwa kiwango cha kisasa (Standard Gauge) kutoka Dar es salaam-Tabora-Isaka-Mwanza, Tabora-Mpanda-Kalemela, Tabora-Uvinza-Kigoma na Isaka-Keza-Msongati.
Mazungumzo kati ya Rais Magufuli na Rais wa benki ya Exim ya China yamehudhuriwa na Balozi wa China hapa nchini Dkt. Lu Youqing, Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa Mnyaa, Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt. Suzan Kolimba.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dodoma
20 Julai, 2016
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amemteua Prof. Sylvester Michael Mpanduji kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwanda Vidogo (SIDO).
Taarifa iliyotolewa leo Ikulu Jijini Dar es salaam na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi imeeleza kuwa uteuzi wa Prof. Sylvester Michael Mpanduji umeanzia leo tarehe 18 Julai, 2016.
Kabla ya uteuzi huu Prof. Sylvester Michael Mpanduji alikuwa Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA).
Prof. Sylvester Michael Mpanduji anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Mhandisi Omary Jumanne Bakari ambaye uteuzi wake umetenguliwa.
Wakati huo huo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amemteua Dkt.Winnie Mpanju-Shumbusho kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Benjamini Mkapa - Dodoma.
Kabla ya Uteuzi huo, Dkt. Winnie Mpanju-Shumbusho alikuwa Mkurugenzi Mkuu Msaidizi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) lenye makao yake makuu Mjini Geneva nchini Uswisi na alimaliza mkataba wake tangu Mwezi Desemba 2015.
Uteuzi wa Dkt. Winnie Mpanju-Shumbusho umeanza leo tarehe 18 Julai, 2016.
Dkt. Winnie Mpanju-Shumbusho anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Dkt. Donan William Mmbando ambaye ameomba kupumzika kutokana na sababu binafsi.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es salaam
18 Julai, 2016
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amewaagiza viongozi wa Jeshi la Polisi Tanzania kuwaondoa watumishi wote wasiokuwa askari polisi na ambao wamekuwa wakijihusisha na vitendo vya ukiukwaji wa taratibu na ufujaji wa fedha za umma ili kulinda heshima, nidhamu na uadilifu ndani ya jeshi hilo.
Rais Magufuli ametoa maelekezo hayo leo tarehe 18 Julai, 2016 muda mfupi baada ya Naibu Makamishna wa Polisi 25 na Makamishna Wasaidizi Waandamizi wa Polisi 35 kula kiapo cha uadilifu kwa viongozi wa umma, Ikulu Jijini Dar es salaam.
Pamoja na kutoa agizo la kutaka wasio askari polisi kuondolewa katika utumishi wa jeshi la polisi, Rais Magufuli pia ameagiza jeshi hilo lichukue hatua dhidi ya wote wanaokabiliwa na tuhuma za wizi wa fedha wakiwemo wanaodaiwa kuiba mabilioni ya shilingi zilizotolewa kwa ajili ya ununuzi wa sare za askari mwaka jana 2015.
"Mnajua kupeleleza, mna vyombo vyote, ofisi ya IGP (Inspekta Jenerali wa Polisi) ipo palepale, ofisi ya DCI (Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai) ipo palepale, Makamishna wote mnazunguka mnakwenda palepale, mwizi mnae palepale, mnashindwa kumshika.
"Kama mnafikiri kuwa na raia katika jeshi la polisi wanawaharibia kazi zenu hamisheni raia wote na wapelekeni utumishi, kwani hakuna mhasibu ambaye ni askari polisi? hakuna mhandisi ambaye ni askari polisi? hakuna afisa tawala ambaye ni askari polisi? Mimi nafikiri kama matatizo ya wizi na wafanyakazi hewa yanaletwa na raia waliomo ndani ya jeshi la polisi na majeshi yetu mengine, IGP kaorodheshe raia wote wanafanya kazi Jeshi la Polisi ili waondolewe na tuwapangie kazi nyingine uraiani" Amesema Rais Magufuli
Hata hivyo Rais Magufuli amelipongeza Jeshi la Polisi kwa kazi nzuri linayofanya iliyoliwezesha kujenga imani kubwa kwa watanzania na ametaka viongozi wa Jeshi hilo wawaongoze askari walio chini yao vizuri, wawatie moyo na waache vitendo vya kuwakatisha tamaa kwa kuwaadhibu ama kuwatisha pale wanapochukua hatua stahiki dhidi watu wanaovunja sheria.
"Sasa mimi niwaombe nyinyi, wale wadogo mnaowaongoza mkawape mamlaka ya kutimiza wajibu wao, hata kama ameshika gari la IGP liache lishikwe IGP atakwenda kujieleza mwenyewe, hata akishika gari la RPC afanye hivyohivyo, hata akishika gari la Waziri au gari la Rais mwacheni atekeleze wajibu wake, sheria ni msumeno, tunawanyima nguvu hawa wa chini wanapotimiza wajibu wao kwa mujibu wa sheria halafu unamwambia liachie, ukifanya hivyo aliyeshikwa anatoka pale akiwa anatamba kwelikweli na yule askari unamvunja nguvu ya kufanya kazi" Amesisitiza Rais Magufuli.
Rais Magufuli pia amelitaka jeshi hilo kuungana na vyombo vingine vya serikali katika kutekeleza shughuli zake zikiwemo kusimamia ukusanyaji wa mapato ya serikali bandarini, katika sekta ya utalii na maeneo mengine, kukabiliana na vitendo vya rushwa na kuondoa watumishi hewa.
Tukio hili la Naibu Makamishna wa Polisi na Makamishna Wasaidizi Waandamizi wa Polisi kula kiapo cha uadilifu kwa viongozi wa umma limeongozwa na Kamishna wa Maadili Jaji Mstaafu Salome Kaganda na limehudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Mwigulu Lameck Nchemba, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora Mhe. Anjellah Kairuki, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Hamad Yusuf Masauni, Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. George Mcheche Masaju, Makatibu Wakuu na Viongozi wa vyombo vya Ulinzi na Usalama.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es salaam
18 Julai, 2016
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Kuna ujumbe umesambazwa kupitia mitandao ya kijamii ukieleza kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amemthibitisha Kaimu Mkurugenzi wa Mwasiliano ya Rais Ikulu Bw. Gerson Msigwa katika cheo hicho na kwamba amemteua Bw. Jerry Murro kuwa Msaidizi wa Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu.
Ujumbe huo wenye kichwa cha habari kilichoandikwa "BREAKING NEWS" unasomeka hivi, nanukuu.
"Mhe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amemthibitisha Ndg Geryson Msigwa kuwa mkurugenzi wa mawasiliano Ikulu huku msaidizi wake akiwa ni aliyekuwa msemaji wa Klabu ya Yanga Ndg Jerry Muro" Mwisho wa kunukuu.
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu inapenda kukanusha taarifa hiyo na kuwataka wananchi kuipuuza.
Ifahamike kuwa uteuzi wowote unaofanywa na Mhe. Rais Magufuli hutangazwa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu ama kupitia Mamlaka rasmi za serikali. Pia huwekwa katika tovuti rasmi ya Ikulu ambayo ni www.ikulu.go.tz
Kwa sasa Mhe. Rais John Pombe Magufuli hajafanya uthibitisho wa Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu Bw. Gerson Msigwa na wala hajamteua Bw. Jerry Cornel Murro kuwa Msaidizi wa Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu kama ilivyoenezwa. Pia hana mpango wa kufanya uteuzi huo.
Ikulu inawaomba wananchi wote kuzipuuza taarifa hizo na kuendelea na shughuli zenu za kila siku. Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu Bw. Gerson Msigwa ataendelea kuwapa taarifa kutoka Ikulu kupitia utaratibu rasmi ambao umekuwa ukitumika.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es salaam
17 Julai, 2016
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amemteua Prof. Longinus Kyaruzi Rutasitara kuwa Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCAA).
Prof. Longinus Kyaruzi Rutasitara anachukuwa nafasi iliyoachwa wazi na Dkt. Nyamajeje Calleb Weggoro ambaye muda wake umemalizika.
Uteuzi huu umeanza tarehe 16 Julai, 2016.
Kwa mujibu wa sheria ya Mamlaka ya usafiri wa anga ya mwaka 1977 Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka hiyo huteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambapo Mwenyekiti akitoka Tanzania Bara, Makamu Mwenyekiti hutoka Tanzania Zanzibar na kinyume chake.
Wakati huo huo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amempandisha cheo Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Kedmon Andrew Mnubi kuwa Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP).
SACP Kedmon Andrew Mnubi pamoja na makamishna wengine 59 ambao Rais Magufuli amewapandisha vyeo kuanzia tarehe 16 Julai, 2016 watakula kiapo cha uadilifu kwa viongozi wa umma kesho jumatatu tarehe 18 Julai, 2016 Ikulu Jijini Dar es salaam saa tatu asubuhi.
Rais Magufuli atakuwepo wakati Makamishna wote 60 wakila kiapo cha uadilifu kwa viongozi wa umma, zoezi ambalo litaendeshwa na Kamishna wa Maadili Jaji Mstaafu Salome Kaganda.
Wote wakaohudhuria tukio hili wanatakiwa kufika Ikulu kabla ya saa mbili na nusu asubuhi na wataingia kupitia lango kuu la mashariki (lango la baharini).
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es salaam
17 Julai, 2016
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kwa mamlaka aliyopewa amefanya uteuzi wa viongozi na watendaji wa taasisi mbalimbali za Serikali, na pia amewapandisha vyeo maafisa wa Jeshi la Polisi Tanzania.
Uteuzi huo ni kama ifuatavyo;
- 1. Mhe. Augustino Lyatonga Mrema.
- Ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Taifa ya Parole kwa kipindi cha miaka mitatu, kuanzia leo tarehe 16 Julai, 2016.
- Mhe. Augustino Lyatonga Mrema anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Jaji Mstaafu Mhe. Eusebia Nicholaus Munuo ambaye muda wake umemalizika.
- 2. Prof. William R. Mahalu
- Ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete. Uteuzi huu umeanza leo tarehe 16 Julai, 2016.
- 3. Prof. Mohamed Janabi
- Ameteuliwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete. Uteuzi huu umeanza tarehe 15 Julai, 2016.
- 4. Prof. Angelo Mtitu Mapunda
- Ameteuliwa kuwa Kamishna wa Tume ya Utumishi wa Mahakama kwa kipindi cha miaka mitatu. Uteuzi huu umeanza tarehe 15 Julai, 2016.
- 5. Bi. Sengiro Mulebya
- Ameteuliwa kuwa Kamishna wa Tume ya Utumishi wa Mahakama kwa kipindi cha miaka mitatu. Uteuzi huu umeanza tarehe 15 Julai, 2016.
- 6. Bw. Oliva Joseph Mhaiki
- Ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC). Uteuzi huu umeanza tarehe 15 Julai, 2016.
- 7. Mwl. Winifrida Gaspar Rutaindurwa
- Ameteuliwa kuwa Katibu wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC). Uteuzi huu umeanza tarehe 15 Julai, 2016.
- 8. Dkt. Charles Rukiko Majinge
- Ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya wadhamini ya Hospitali ya Taifa Muhimbili. Uteuzi huu umeanza leo tarehe 16 Julai, 2016.
- 9. Dkt. Julius David Mwaiselage
- Ameteuliwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taasisi ya Saratani ya Ocean Road. Uteuzi huu umeanza tarehe 15 Julai, 2016.
Kupandishwa Vyeo
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amewapandisha vyeo maafisa 25 wa Jeshi la Polisi kutoka cheo cha Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) na kuwa Naibu Kamishna wa Polisi (DCP).
Waliopandishwa vyeo hivyo ni kama ifuatavyo;
- Essaka Ndege Mugasa
- Adamson Afwilile Mponi
- Charles Ndalahwa Julius Kenyela
- Richard Malika Revocatus
- Geofrey Yesaya Kamwela
- Lucas John Mkondya
- John Mondoka Gudaba
- Matanga Renatus Mbushi
- Frasser Rweyemamu Kashai
- Ferdinand Elias Mtui
- Germanus Yotham Muhume
- Fulgence Clemence Ngonyani
- Modestus Gasper Lyimo
- Mboje John Shadrack Kanga
- Gabriel G.A. Njau
- Ahmed Zahor Msangi
- Anthony Jonas Rutashubulugukwa
- Dhahir Athuman Kidavashari
- Ndalo Nicholus Shihango
- Shaaban Mrai Hiki
- Simon Thomas Chillery
- Leonard Lwabuzara Paul
- Ahmada Abdalla Khamis
- Aziz Juma Mohamed
- Juma Yussuf Ally
Aidha, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amewapandisha vyeo maafisa wa Jeshi la Polisi wengine 34 kutoka cheo cha Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) na kuwa Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP).
Waliopandishwa vyeo hivyo ni kama ifuatavyo;
- Fortunatus Media Musilimu
- Goyayi Mabula Goyayi
- Gabriel Joseph Mukungu
- Ally Omary Ally
- Edward Selestine Bukombe
- Sifael Anase Mkonyi
- Naftari J. Mantamba
- Onesmo Manase Lyanga
- Paul Tresphory Kasabago
- Dadid Mshahara Hiza
- Robert Mayala
- Lazaro Benedict Mambosasa
- Camilius M. Wambura
- Mihayo Kagoro Msikhela
- Ramadhani Athumani Mungi
- Henry Mwaibambe Sikoki
- Renata Michael Mzinga
- Suzan Salome Kaganda
- Neema M. Mwanga
- Mponjoli Lotson
- Benedict Michael Wakulyamba
- Wilbroad William Mtafungwa
- Gemini Sebastian Mushi
- Peter Charles Kakamba
- Ramadhan Ng'anzi Hassan
- Christopher Cyprian Fuime
- Charles Philip Ulaya
- Gilles Bilabaye Muroto
- Mwamini Marco Lwantale
- Allute Yusufu Makita
- Kheriyangu Mgeni Khamis
- Nassor Ali Mohammed
- Salehe Mohamed Salehe
- Mohamed Sheikhan Mohamed
Maafisa hawa wa Jeshi la Polisi Tanzania wamepandishwa vyeo kuanzia tarehe 15 Julai, 2016.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es salaam
16 Julai, 2016
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amezindua mpango wa ugawaji wa madawati yanayotengenezwa kutokana na fedha zilizotolewa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania baada ya kubana matumizi katika bajeti yake.
Uzinduzi huo umefanyika leo tarehe 13 Julai, 2016 katika viwanja vya Karimjee Jijini Dar es salaam ambapo Rais Magufuli amekabidhi madawati 537 kwa mbunge wa jimbo la Ilala Mheshimiwa Mussa Azan Zungu kwa niaba ya wabunge wa majimbo yote ya Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar ambayo yatagawiwa idadi hiyohiyo ya madawati kwa kila jimbo.
Madawati hayo 537 ni sehemu ya madawati 61,385 ambayo yametengenezwa katika awamu ya kwanza na yatafuatiwa na madawati mengine 60,000 yatakayogawiwa katika awamu ya pili na yote kwa ujumla yatagharimu shilingi bilioni 4 ambazo zilitolewa na Bunge tarehe 11 Aprili, 2016 baada ya kubana matumizi katika bajeti yake, ikiwa ni kuitikia wito wa Mhe. Rais John Pombe Magufuli.
Mikoa itakayonufaika katika awamu ya kwanza ya ugawaji wa madawati hayo ni Dar es salaam, Pwani, Morogoro, Lindi, Mtwara, Ruvuma, Iringa, Njombe, Mbeya, Songwe, Rukwa, Katavi, Unguja, Pemba na Tanga.
Akizungumza katika hafla hiyo, Rais Magufuli amewashukuru na kuwapongeza wabunge kwa kutoa mchango huo na pia amewapongeza wadau wengine ambao wameitikia wito wake wa kuchangia madawati kwa lengo la kuondoa tatizo la wanafunzi kukaa chini.
Rais Magufuli amesema baada ya kuanza kutekeleza ahadi ya kuondoa ada kwa shule za msingi na sekondari, idadi ya wanafunzi waliojiandikisha kuanza darasa la kwanza imeongezeka kutoka wanafunzi 1,282,100 hadi kufikia wanafunzi 1,896,584 sawa na ongezeko la asilimia 84.5 hali iliyosababisha upungufu wa madawati 1,400,000 lakini tatizo hilo limetatuliwa kwa kiasi kikubwa ambapo mpaka sasa zaidi ya madawati 1,000,000 yametengenezwa.
Aidha, Dkt. Magufuli amelitaka Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na Jeshi la Magereza kuongeza kasi katika utengenezaji wa madawati ili yakamilike haraka na kuanza kutumika.
Hafla hiyo imehudhuriwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa, Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Tulia Ackson, Wabunge wa kamati ndogo ya tume ya huduma za bunge, Viongozi wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) na Jeshi la Magereza pamoja na wanafunzi wa shule ya msingi Bunge.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es salaam
13 Julai, 2016
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amewataka wakurugenzi wa halmashauri zote za Majiji, Manispaa, Miji na Wilaya hapa nchini kufanya kazi za kuwaletea maendeleo wananchi na kuondoa kero zinazowakabili kwa kujiamini, uadilifu na uaminifu.
Dkt. Magufuli ameyasema hayo leo tarehe 12 Julai, 2016 Ikulu Jijini Dar es salaam muda mfupi kabla ya wakurugenzi hao wa halmashauri kula kiapo cha uadilifu kwa viongozi wa umma, zoezi ambalo limeendeshwa na Ofisi ya Rais Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma.
Mhe. Rais Magufuli amesema katika kutekeleza jukumu hilo la kuwaletea wananchi maendeleo na kuondoa kero zinazowakabili, wakurugenzi hao hawana budi kuhakikisha wanatekeleza kwa vitendo ahadi ambazo serikali ya awamu ya tano imezitoa, wakiongozwa na Ilani ya Uchaguzi Mkuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2015 - 2020.
Aidha, amesema wakurugenzi wote wa halmashauri wana wajibu wa kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na amewataka kutosita kuchukua hatua dhidi ya watendaji ambao wamejigeuza kuwa miungu watu na wanawanyanyasa wananchi.
"Wapo watendaji wa kata ambao ni miungu watu, wanachonganisha wananchi na serikali, katumieni madaraka mliyonayo kuwaondoa kazini" Amesema Rais Magufuli
Mhe. Rais Magufuli pia amewataka wakurugenzi hao kusimamia ipasavyo ukusanyaji wa mapato ya serikali na ametumia nafasi hiyo kuagiza wizara zote kuanza kutumia mashine za kielektroniki (EFD) katika ukusanyaji wa mapato kwenye taasisi zote ambazo zinakusanya maduhuli.
Dkt. Magufuli amewasisitiza wakurugenzi hao kuhakikisha wanasimamia vizuri fedha zinazotolewa na serikali kwa ajili ya utoaji wa elimu ya msingi na sekondari bila malipo, ambapo kila mwezi serikali hutoa shilingi bilioni 18.777 na ametaka tabia ya wakurugenzi wa halmashauri kushirikiana na wafanyabiashara ama wanasiasa kujinufaisha kupitia zabuni za serikali ikome.
Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa ambao walikuwepo wamewataka wakurugenzi hao wa halmashauri kuwa watumishi bora, kusimamia vizuri rasilimali za halmashauri na kushirikiana na viongozi wa mkoa na wilaya katika halmashauri zao.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es salaam
12 Julai, 2016
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi anapenda kuwataarifa wakurugenzi wa Halmashauri za Majiji, Manispaa, Miji na Wilaya walioteuliwa tarehe 07 Julai, 2016 kuwa watakapofika Ikulu Dar es salaam kwa ajili ya kula kiapo cha uadilifu wa uongozi wa umma siku ya Jumanne tarehe 12 Julai, 2016 wahakikishe wanakuja na nakala zao halisi za vyeti vya kitaaluma (Original Academic Certificates).
Ieleweke kuwa uhakiki wa vyeti halisi vya kitaaluma (Original Academic Certificates) unafanywa kwa lengo la kujiridhisha baada ya mchakato wa kawaida wa uhakiki kufanywa kwa kutumia vyeti visivyokuwa halisi (Photocopies).
Uhakiki huu wa vyeti utaanza saa mbili asubuhi na wahusika wote mnaombwa kuingia Ikulu kwa kupitia geti kuu la lililopo upande wa mashariki (Upande wa Baharini)
Tafadhali zingatia maelekezo haya.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es salaam
09 Julai, 2016
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amemteua Dkt. Leonard Lutegama Maboko kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS).
Taarifa ya Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi imeeleza kuwa uteuzi huu umeanza tarehe 07 Julai, 2016.
Kabla ya uteuzi huu Dkt. Leonard Lutegama Maboko alikuwa Mkurugenzi wa Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya binadamu Mbeya (NIMR Mbeya).
Dkt. Leonard Lutegama Maboko anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Dkt. Fatma Mrisho ambaye mkataba wake umemalizika tangu tarehe 30 Juni, 2016.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es salaam
08 Julai, 2016
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Tunapenda kufanya marekebisho madogo katika majina yaliyopo kwenye orodha ya wakurugenzi wa Halmashauri za Majiji, Manispaa, Miji na Wilaya ambapo Dkt. Leonard Moses Massale ametangazwa kuwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma.
Jina hilo limeingizwa katika Orodha ya Wakurugenzi wa halmashauri kwa makosa, na kwa sababu hiyo Dkt. Leonard Moses Massale anaendelea kuwa Mkuu wa wilaya ya Ilemela Mkoani Mwanza.
Kufuatia marekebisho hayo, uteuzi wa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma utatangazwa baadaye.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es salaam
07 Julai, 2016
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 07 Julai, 2016 amefanya uteuzi wa wakurugenzi wa halmashauri za majiji 5, Manispaa 21, Miji 22 na Wilaya (DC) 137 za Tanzania Bara.
Uteuzi huo umetangazwa na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhandisi Mussa Iyombe ambapo kati ya wakurugenzi wote 185 walioteuliwa, 65 wameteuliwa kutoka orodha ya wakurugenzi wa zamani na 120 ni wakurugenzi wapya.
Orodha ya wakurugenzi walioteuliwa kulingana na mikoa yao ni kama ifuatavyo;
ARUSHA
- Arusha Jiji - Athumani Juma Kihamia
- Arusha DC - Dkt. Wilson Mahera Charles
- Karatu DC - Banda Kamwande Sonoko
- Longido DC - Jumaa Mohamed Mhiwapijei
- Meru DC - Kazeri Christopher Japhet
- Monduli DC - Stephen Anderson Ulaya
- Ngorongoro DC - Raphael John Siumbu
DAR ES SALAAM
- Dar es salaam Jiji - Siporah Jonathan Liana
- Kinondoni Manispaa - Aron Titus Kagurumjuli
- Temeke Manispaa - Nassibu Bakari Mmbaga
- Ilala Manispaa - Msongela Nitu Palela
- Kigamboni Manispaa - Stephen Edward Katemba
- Ubungo Manispaa - Kayombo Lipesi John
DODOMA
- 1. Dodoma Manispaa - (Uteuzi utafanywa baadaye)
- Kondoa DC - Kibasa Falesy Mohamed
- Kondoa Mji - Khalifa Kondo Mponda
- Mpwapwa DC - Mohamed Ahamed Maje
- Kongwa DC - Mhandisi Ngusa Laurent Izengo
- Chemba DC - Semistatus Hussein Mashimba
- Chamwino DC - Athuman Hamis Masasi
- Bahi DC - Rachel Marcel Chuwa
GEITA
- Bukombe DC - Dionis Maternus Nyinga
- Chato DC - Mhandisi Joel Bahahari
- Geita DC - Ally Abdallah Kidwaka
- Geita Mji - Modest J. Apolinaly
- Mbogwe DC - Mahwago Elias Kayandabila
- Nyang'wale DC - Carlos K. Gwamagobe
IRINGA
- Iringa Manispaa - William Donald Mafwele
- Mafinga Mji - Saada S. Mwaruka
- Mufindi DC - Riziki Salas Shemdoe
- Iringa DC - Robert Mgendi Magunya
- Kilolo DC - Aloyce Kwezi
KAGERA
- Biharamulo DC - Wende Israel Ng'ahala
- Bukoba DC - Abdulaaziz Jaad Hussein
- Bukoba Manispaa - Makonda Kelvin Stephen
- Karagwe DC - Godwin Moses Kitonka
- Kyerwa DC - Shedrack M. Mhagama
- Missenyi DC - Limbe Berbad Maurice
- Muleba DC - Emmanuel Shelembi Luponya
- Ngara DC - Aidan John Bahama
KATAVI
- Mlele DC - Alex Revocatus Kagunze
- Mpimbwe DC - Erasto Nehemia Kiwale
- Mpanda DC - Ngalinda Hawamu Ahmada
- Mpanda Manispaa - Michael Francis Nzyungu
- Nsimbo DC - Joachim Jimmy Nchunda
KIGOMA
- Buhigwe DC - Anosta Lazaro Nyamoga
- Kakonko DC - Lusubilo Joel Mwakabibi
- Kasulu DC - Godfrey Msongwe Masekenya
- Kasulu Mji - Fatina Hussein Laay
- Kigoma Ujiji - Manispaa - Judethadeus Joseph Mboya
- Kigoma DC - Hanji Yusuf Godigodi
- Kibondo DC - Shelembi Felician Manolo
- Uvinza DC - Weja Lutobola Ng'olo
KILIMANJARO
- Manispaa ya Moshi - Michael Nelson Mwandezi
- Hai DC - Yohana Elia Sintoo
- Siha DC - Valerian Mwargwe Juwal
- Same DC - Shija Anaclaire
- Mwanga DC - Golden A. Mgonzo
- Rombo DC - Magreth Longino John
- Moshi DC - Emalieza Sekwao Chilemeji
LINDI
- Kilwa DC - Bugingo I. N. Zabron
- Lindi DC - Samwel Warioba Gunzar
- Lindi Manispaa - Jomaary Mrisho Satura
- Liwale DC - Justine Joseph Monko
- Nachingwea DC - Bakari Mohamed Bakari
- Ruangwa DC - Andrea Godfrey Chezue
MANYARA
- Babati Mji - Fortunatus Hilario Fwema
- Hanang DC - Bryceson Paul Kibasa
- Mbulu DC - Festi Fungameza Fwema
- Mbulu Mji - Anna Philip Mbogo
- Simanjiro DC - Yefred Edson Myezi
- Kiteto DC - Tamim Kambona
- Babati DC - Hamis Iddi Malinga
MARA
- Manispaa ya Musoma - Fidelica Gabriel Myovela
- Bunda DC - Amos Jeremiah Kusaja
- Bunda Mji - Janeth Peter Mayanja
- Butiama DC - Solomon Kamlule Ngiliule
- Musoma DC - Flora Rajab Yongolo
- Serengeti DC - Juma Hamsini Seph
- Rorya DC - Charles Kitanuru Chacha
- Tarime DC - Apoo Castro Tindwa
- Tarime Mji - Hidaya Adam Usanga
MBEYA
- Busokelo DC - Eston Paul Ngilangwa
- Chunya DC - Sofia Kumbuli
- Kyela DC - Mussa Joseph Mgata
- Mbarali DC - Kivuma Hamis Msangi
- Mbeya DC - Ameichiory Biyengo Josephat
- Mbeya Jiji - Zacharia Nachoa Ntandu
- Rungwe DC - Loema Isaya Peter
SONGWE
- Momba DC - Adrian Jovin Jungu
- Tunduma Mji - Valery Alberth Kwemba
- Mbozi DC - Edna Amulike Mwaigomole
- Ileje DC - Haji Mussa Mnasi
- Songwe DC - Elias Philemon Nawela
MOROGORO
- Gairo DC - Agnes Martin Mkandya
- Kilombero DC - Dennis Lazaro Londo
- Ifakara Mji - Francis Kumba Ndulane
- Kilosa DC - Kessy Juma Mkambala
- Morogoro DC - Sudi Mussa Mpili
- Morogoro Manispaa - John Kulwa Magalula
- Mvomero DC - Florent Laurent Kyombo
- Ulanga DC - Audax Christian Rukonge
- Malinyi DC - Marcelin Rafael Ndimbwa
MTWARA
- Mtwara DC - Omari Juma Kipanga
- Mtwara Mikindani Manispaa - Beatrice Dominic Kwai
- Masasi Mji - Gimbana Emmanuel Ntayo
- Masasi DC - Mkwazu M. Changwa
- Nanyumbu DC - Hamis Hassan Dambaya
- Newala DC - Mussa Mohamed Chimae
- Newala Mji - Andrew Frank Mgaya
- Tandahimba DC - Said Ally Msomoka
- Nanyamba Mji - Oscar Anatory Ng'itu
MWANZA
- Mwanza Jiji - Kiomoni Kibamba Kiburwa
- Ilemela Manispaa - John Paul Wanga
- Kwimba DC - Pendo Anangisye Malabeja
- Magu DC - Lutengano George Mwalwiba
- Misungwi DC - Eliud Leonard Mwaiteleke
- Ukerewe DC - Tumaini Sekwa Shija
- Buchosa DC - Crispian Methew Luanda
- Sengerema DC - Magesa M. Boniphace
NJOMBE
- Njombe Mji - Iluminata Leonald Mwenda
- Makambako Mji - Paul Sostenes Malala
- Makete DC - Francis Emmanuel Namaumbo
- Njombe DC - Monica Peter Kwiluhya
- Ludewa DC - Ng'wilabuzu Ndatwa Ludigija
- Wanging'ombe DC - Amina Mohamed Kiwanuka
PWANI
- Bagamoyo DC - Azimina A. Mbilinyi
- Chalinze DC - Edes Philip Lukoa
- Kibaha DC - Tatu Seleman Kikwete
- Kibaha Mji - Jenifer Christian Omolo
- Kisarawe DC - Mussa L. Gama
- Mafia DC - Erick Mapunda
- Mkuranga DC - Mshamu Ally Munde
- Kibiti DC - Alvera Kigongo Ndabagoye
- Rufiji DC - Salum Rashid Salum
RUKWA
- Kalambo DC - Simon Ngagani Lyamubo
- Sumbawanga DC - Nyangi John Msemakweli
- Sumbawanga Manispaa - Hamid Ahmed Njovu
- Nkasi DC - Julius M. Kaondo
RUVUMA
- Mbinga DC - Gumbo Samanditu Gumbo
- Mbinga Mji - Robert Kadaso Mageni
- Namtumbo DC - Christopher Michael Kilungu
- Nyasa DC - Oscar Albano Mbuzi
- Songea DC - Simon Michael Bulenganija
- Madaba DC - Shafi Kassim Mpenda
- Tunduru DC - Abdallah Hussein Mussa
- Songea Manispaa - Tina Emelye Sekambo
SHINYANGA
- Kishapu DC - Stephen Murimi Magoiga
- Msalala DC - Berege Sales Simon
- Shinyanga DC - Mark Emmanuel Malembeka
- Kahama Mji - Anderson David Msumba
- Shinyanga Manispaa - Lewis Kweyemba Kalinjuna
- Ushetu DC - Michael Augustino Matomola
SIMIYU
- Bariadi DC - Abdallah Mohamed Malela
- Bariadi Mji - Melkizedek Oscar Humbe
- Itilima DC - Mariano Manyingu
- Maswa DC - Fredrick Damas Sagamiko
- Busega DC - Anderson Njiginya
- Meatu DC - Said F. Manoza
SINGIDA
- Ikungi DC - Rustika William Turuka
- Iramba DC - Linno Pius Mwageni
- Mkalama DC - Martin Msuha Mtanda
- Manyoni DC - Charles Edward Fussi
- Itigi DC - Luhende Pius Gerald
- Singida DC - Rashid Mohamed Mandoa
- Singida Manispaa - Kizito L. Brava
TABORA
- Igunga DC - Revocatus Lubigili Kuuli
- Kaliua DC - John Marco Pima
- Nzega DC - Jacob James Mtalitinya
- Nzega Mji - Phillimon Mwita Magesa
- Sikonge DC - Simon Saulo Ngatunga
- Tabora Manispaa - Bosco Addo Ndunguru
- Urambo DC - Magreth Nakainga
- Tabora -Uyui - Hadija Maulid Makuani
TANGA
- Tanga Jiji - Daudi R. Mayeji
- Korogwe DC - George John Nyaronga
- Korogwe Mji - Jumanne Kiangoshauri
- Muheza DC - Luiza Osmin Mlelwa
- Handeni Mji - Keneth K. Haule
- Handeni DC - William Methew Mafukwe
- Pangani DC - Sabas Damian Chambasi
- Mkinga DC - Mkumbo Emmanuel Barnabas
- Bumbuli DC - Peter Isaiah Nyalali
- Kilindi DC - Clemence Andagile Mwakasenda
- Lushoto DC - Kazimbaya Makwega Adeladius
Wakurugenzi wote walioteuliwa wanatakiwa kufika Ikulu Jijini Dar es salaam siku ya Jumanne tarehe 12 Julai, 2016 saa tatu asubuhi kwa ajili ya kula kiapo cha ahadi ya uadilifu kwa viongozi wa umma.
AIDHA, tunapenda kutoa ufafanuzi kuwa makatibu tawala wa wilaya wote ambao majina yao yamejitokeza katika orodha ya wakurugenzi wa halmashauri za Majiji, Manispaa, Miji na wilaya, Mhe. Rais Magufuli ameamua kuwabadilishia majukumu na sasa watatumikia vyeo vyao vya ukurugenzi badala ya vyeo vya Ukatibu Tawala wa Wilaya.
Kufuatia mabadiliko hayo, nafasi za Makatibu Tawala wa Wilaya ambao wameteuliwa kuwa Wakurugenzi wa Halmshauri zitajazwa baadaye.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es salaam
07 Julai, 2016
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 07 Julai, 2016 amemteua Bw. Deogratius John Ndejembi kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Mkoani Dodoma.
Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi amesema Bw. Deogratius John Ndejembi anachukua nafasi iliyoachwa na aliyeteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Bw. John Ernest Palingo ambaye amehamishiwa Wilaya ya Mbozi katika Mkoa wa Songwe.
Uhamisho wa Bw. John Ernest Palingo kwenda Wilaya ya Mbozi, umefanywa baada ya Mhe. Rais Magufuli kuridhia maombi ya Bw. Ally Masoud Maswanya aliyeteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Mbozi, kuomba uteuzi wake utenguliwe kutokana na sababu binafsi.
Bw. Deogratius John Ndejembi atakula kiapo cha ahadi ya uadilifu kwa viongozi wa umma siku ya Jumanne tarehe 12 Julai, 2016 Ikulu Jijini Dar es salaam.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es salaam
07 Julai, 2016
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amempongeza Mufti wa Tanzania Sheikh Aboubakar Zubeir bin Ali kwa juhudi zake za kuwaunganisha waislamu wote na kupanua uwigo wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) kutoa huduma za kijamii na ameahidi kuwa serikali ya awamu ya tano itaunga mkono juhudi hizo.
Rais Magufuli ameyasema hayo leo tarehe 06 Julai, 2016 wakati akihutubia Baraza la Eid el-Fitr kwa mara ya kwanza tangu achaguliwe kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, lililofanyika kitaifa katika viwanja vya Karimejee Jijini Dar es salaam.
Dkt. Magufuli amesema kitendo cha kuwaunganisha waislamu wote katika Baraza la Eid el-Fitr kinafungua ukurasa mpya na ni moja ya hatua muhimu za kuimarisha amani, umoja na mshikamano miongoni mwa waislamu wa makundi mbalimbali pamoja na watanzania wengine waisio waislamu.
Aidha Rais Magufuli amezungumzia juhudi zinazofanywa na BAKWATA katika kuimarisha taasisi zake zinazotoa huduma za kijamii na kulinda mali zake akisema serikali itahakikisha mali zote za waislamu zinakuwa salama na kwamba wote waliodhulumu mali za waislamu watazirejesha.
Awali akisoma taarifa, Katibu Mkuu wa BAKWATA Alhaji Suleiman Said Lolila amesema BAKWATA inakusudia kupanua huduma za kijamii kwa lengo la kuwahudumia wananchi ikiwemo kujenga chuo kikuu Mkoani Dodoma na pia amempongeza Rais Magufuli kwa juhudi zake za kuondoa umasikini huku akimtaka asikatishwe tamaa na wachache watakaoudhika kwa kuguswa na hatua zinazochukuliwa.
Nae Mufti wa Tanzania Sheikh Aboubakar Zubeir Ali pamoja na kumshukuru Rais Magufuli kwa kuongoza bila ubaguzi amewataka watanzania kuungana na juhudi za serikali kupinga matendo maovu ikiwemo rushwa na ufisadi na pia amelaani ndoa za jinsia moja akisema ni kinyume na maadili ya dini.
Baraza la Eid el-Fitr pia limehudhuriwa na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa, Rais Mstaafu wa awamu ya pili Alhaji Ali Hassan Mwinyi, mabalozi na wabunge.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es salaam
06 Julai, 2016
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli kwa mamlaka aliyonayo kwa mujibu wa kifungu cha 48 cha sheria ya tafsiri za sheria (Interpretation of Laws Act) Sura 1, leo tarehe 5 Julai, 2016 ametengua uteuzi wa Mwenyekiti wa Bodi ya Benki ya Maendeleo ya TIB Prof. William Lyakurwa.
Kufuatia hatua hiyo, kwa mujibu wa mamlaka aliyonayo chini ya kifungu cha 9 (2) cha ya Sheria ya mashirika ya umma (Public Corporations Act) Sura 257, Mhe. Rais amemteua Prof. Palamagamba J. A. M. Kabudi kushika nafasi ya Mwenyekiti wa Bodi ya Benki ya Maendeleo ya TIB kwa kipindi cha miaka mitatu.
Kufuatia mabadiliko hayo, Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Isdor Mpango kwa mamlaka aliyonayo kwa mujibu wa kifungu cha 48 cha sheria ya sheria ya tafsiri za sheria (Interpretation of Laws Act) Sura 1, ametengua uteuzi wa Wajumbe Bodi ya Benki ya Maendeleo ya TIB. Aidha, kwa mujibu wa mamlaka aliyonayo chini ya kifungu cha 9 (1) cha ya Sheria ya mashirika ya umma (Public Corporations Act, Sura 257) Mhe. Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Isdor Mpango ameteua wajumbe wapya wa Bodi wafuatao kwa kipindi cha miaka mitatu:
- Brig. Gen (Rtd) Mabula Mashauri
- Dkt. Razack B. Lokina
- Bi. Rose Aiko
- Prof. Joseph Bwechweshaija
- Bw. Said Seif Mzee
- Dkt. Arnold M. Kihaule
- Bw. Maduka Paul Kessy
- Bw. Charles Singili
Uteuzi wa Mwenyekiti na Wajumbe wapya wa Bodi unaanza tarehe leo 5 Julai, 2016.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es salaam
05 Julai, 2016.
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amemtumia salamu za rambirambi Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job Ndugai kufuatia kifo cha Mbunge Mstaafu wa Jimbo la Kilindi Mkoani Tanga Mhe. Beatrice Shelukindo kilichotokea jana tarehe 02 Julai, 2016.
Mhe. Beatrice Shelukindo ambaye amewahi kuwa Mbunge Bunge la Afrika Mashariki na baadaye kuwa Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa vipindi viwili mfurulizo hadi alipostaafu mwaka jana 2015, amefariki dunia akiwa nyumbani kwao Njiro Mkoani Arusha.
Katika salamu zake Rais Magufuli amesema taifa limempoteza mtu aliyetoa mchango mkubwa katika maendeleo hususani alipokuwa Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akiwawakilisha wananchi wa Jimbo la Kilindi na Mkoa wa Tanga.
“Mhe. Beatrice Shelukindo alikuwa kiongozi shupavu, ambaye siku zote alisimama kidete kupigania maendeleo ya wananchi na kutetea rasimali za taifa.
“Kupitia kwako Mhe. Spika Job Ndugai naomba unifikishie salamu zangu za pole kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki wote wa marehemu na pia kwa wabunge wote wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania” Amesema Rais Magufuli.
Dkt. John Pombe Magufuli pia amewaombea wote walioguswa na kifo cha Mhe. Beatrice Shelukindo kuwa na moyo wa subira na uvumilivu katika kipindi hiki cha kuondokewa na mpendwa wao na amemuombea marehemu apumzishwe mahali pema peponi, amina.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es salaam
03 Julai, 2016
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amezitumia salamu za pole familia, ndugu, jamaa na marafiki wa watu 12 waliopoteza maisha kufuatia ajali mbili zilizotokea katika eneo moja la VETA Dakawa, Tarafa ya Dumila, Wilaya ya Kilosa Mkoani Morogoro.
Ajali ya kwanza imetokea majira ya saa 11:30 jioni ya tarehe 30 Juni, 2016 ambapo watu 5 wamefariki dunia kufuatia malori mawili, mojawapo likiwa na shehena ya mafuta kugongana na kisha kuwaka moto, na ajali ya pili ikatokea hapohapo majira ya saa 10:00 alfajiri ya tarehe 01 Julai, 2016 baada ya basi la kampuni ya Otta High Class kuligonga lori la mafuta lililokuwa likiungua moto na kusababisha vifo vya watu 7 mpaka sasa.
Katika salamu zake kupitia kwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Steven Kebwe, Rais Magufuli amesema amepokea kwa mshituko na masikitiko taarifa za vifo vya watu hao ambao licha ya taifa kupoteza nguvu kazi muhimu, ndugu, jamaa na marafiki wamepoteza watu waliowategemea na wapendwa wao.
“Ndugu Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Steven Kebwe naomba unifikishie salamu zangu za pole kwa wote waliopatwa na msiba na uwaambie naunga nao katika kipindi hiki kigumu cha majonzi.
“Pia nawaombea wawe na moyo wa uvumilivu na ustahimilivu na Mwenyezi awapumzishe marehemu wote mahali pema peponi, Amina” amesema Rais Magufuli.
Rais Magufuli pia amewaombea majeruhi wote waliolazwa hospitali na wale wanaoendelea kupata matibabu wakiwa majumbani, kupona haraka ili waendelee na kazi zao za kila siku.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es salaam
02 Julai, 2016
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amewahakikishia wafanyabiashara wa Rwanda kuwa bandari ya Dar es salaam ni salama kwa wao kupitisha mizigo na ameahidi kuwa Serikali ya Tanzania inaendelea kuchukua hatua za kuiboresha bandari hiyo na kurahisisha biashara kati ya nchi hizi mbili.
Rais Magufuli ametoa kauli hiyo leo tarehe 01 Julai, 2016 alipokuwa akizungumza na wananchi wa Tanzania na Rwanda kupitia vyombo vya habari wakati wa ziara rasmi ya kiserikali ya Rais wa Jamhuri ya Rwanda Mhe. Paul Kagame inayofanyika kwa siku mbili hapa nchini.
Dkt. Magufuli amesema pamoja na kuchukua hatua kadhaa za kuboresha bandari ya Dar es salaam kwa manufaa ya wafanyabiashara wanaopitisha mizigo, Tanzania imeamua kuipatia Rwanda eneo la kujenga bandari kavu kwa ajili ya mizigo ya wafanyabiashara wake na pia Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) itafungua ofisi Mjini Kigali nchini Rwanda ikiwa ni juhudi za kurahisisha na kuongeza biashara kati ya nchi hizi mbili.
Aidha, Rais Magufuli amesema kwa kutambua umuhimu wa reli ya kati kwa uchumi wa Tanzania na Rwanda, Tanzania imetenga shilingi Trilioni moja katika bajeti mpya ya serikali kwa ajili ya kuanza ujenzi wa Reli hiyo kwa kiwango cha kisasa yaani “Standard Gauge” na kwamba ni matarajio kuwa wadau wengine wa maendeleo watajitokeza kuunga mkono juhudi za ujenzi wa reli hiyo hapa Tanzania na nchini Rwanda huku akidokeza kuwa China imeonesha nia ya kuunga mkono mradi huo.
Dkt. Magufuli ameongeza kuwa serikali yake pia imechukua hatua madhubuti za kulifufua shirika la ndege la Taifa na kwamba tayari mipango imefanywa kuhakikisha ndege mbili aina Bombadier Q400 zinanunuliwa na zitatua hapa nchini kabla ya mwisho wa mwezi Septemba Mwaka huu 2016.
Kwa upande wake Rais wa Jamhuri ya Rwanda Mhe. Paul Kagame amemshukuru Rais Magufuli kwa kumualika kufanya ziara rasmi ya kiserikali hapa nchini na amemhakikishia kuwa serikali yake itaendeleza na kuimarisha zaidi ushirikiano uliopo kati ya nchi yake na Tanzania kwa manufaa ya wananchi wa nchi zote mbili.
Majira ya jioni Rais Kagame akiwa na mwenyeji wake Rais Magufuli, amefungua rasmi maonesho ya 40 ya kimataifa ya Biashara Dar es salaam yanayofanyika katika viwanja vya Sabasaba vilivyopo Barabara ya Kilwa, Wilaya ya Temeke, Mkoani Dar es salaam.
Akizungumza kabla ya kuzindua rasmi maonesho hayo, Rais Kagame ametoa wito kwa Tanzania na Rwanda pamoja na nchi nyingine za Jumuiya ya Afrika Mashariki kushirikiana na sekta binafsi katika kutumia fursa nyingi za kibiashara zilizopo baina yake na kuwaletea manufaa wananchi.
Nae Rais Magufuli amezipongeza nchi takribani 30 zilizojitokeza kushiriki katika maadhimisho hayo zikiwemo kampuni zaidi ya 650 na wadau zaidi ya 2,000 na amesisitiza umuhimu wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki zenye watu takribani milioni 165 na nchi nyingine za Jumuiya ya maendeleo kusini mwa Afrika (SADC) kuongeza biashara baina yake kwa kuwa hivi sasa kiwango cha biashara baina ya nchi hizo ni cha chini mno.
Baada ya kufungua maonesho hayo, Rais Kagame na mwenyeji wake Rais Magufuli wametembelea mabanda mbalimbali ya maonesho ya bidhaa na huduma katika viwanja vya Sabasaba na baadaye Rais Kagame atahudhuria dhifa ya Kitaifa iliyoandaliwa na mwenyekiji wake Rais John Pombe Magufuli Ikulu Jijini Dar es salaam.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es salaam
01 Julai, 2016
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 29 Juni, 2016 amewaapisha wakuu wa Mikoa watatu aliowateua Jumapili iliyopita tarehe 26 Juni, 2016.
Wakuu wa Mikoa walioapishwa leo Ikulu Jijini Dar es salaam ni Dkt. Binilith Satano Mahenge ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Dkt. Charles Ogesa Mlingwa ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Mara na Bi. Zainab Rajab Telack ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga.
Hafla ya kuapishwa kwa wakuu hao wa Mikoa imehudhuriwa na Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama na wakuu wa wilaya wateule ambao waliteuliwa na Rais Magufuli Jumapili iliyopita tarehe 26 Juni, 2016.
Aidha, miongoni mwa wakuu wa wilaya 139 walioteuliwa, Rais Dkt. John Pombe Magufuli amefanya mabadiliko madogo katika wilaya tatu ambapo ametengua uteuzi wa Mkuu wa Wilaya ya Rombo Mteule Mhe. Fatma Hassan Toufiq na badala yake amemteua Bi. Agness Elias Hokororo kuwa Mkuu wa Wilaya hiyo, ametengua uteuzi wa Mkuu wa wilaya ya Serengeti Mteule Bw. Emile Yotham Ntakamulenga na badala yake amemteua Bw. Nurdin Hassan Babu kuwa Mkuu wa Wilaya hiyo na ametengua uteuzi wa Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Mteule Bw. Fikiri Avias Said na badala yake amemteua Bw. Miraji Mtaturu kuwa Mkuu wa wilaya hiyo.
Akizungumza katika hafla hiyo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amewataka wakuu wa wilaya wateule kwenda kuchapa kazi na kutatua kero za wananchi katika wilaya zao huku wakizingatia kufanya kazi kwa uadilifu na uaminifu.
Rais Magufuli pia amewataka kusimamia ukusanyaji mapato ya serikali na matumizi ya fedha na rasilimali nyingine za umma, kuhakikisha wananchi wapo salama na pia kuhakikisha wananchi wanafanya kazi za uzalishaji mali.
"Katika kazi hizi wapo watakaowakejeli, katika kazi hizi wapo watakaowadhihaki, nyinyi kavumilieni na mmuweke Mungu mbele na mkawaweke watanzania mbele, mkafanye kazi kadiri Mungu atakavyokuwa amewaongoza.
"Nataka kuwahakikishia tunawaunga mkono kwa nguvu zote, mkafanye kazi bila uwoga wowote, katembeeni kifua mbele, kwa sababu tumewaamini wala msiwe na wasiwasi, ukifanya kitu kizuri kwa dhamira yako iliyo njema kitazaa matunda mazuri, ukifanya kitu kwa unafiki hakitafanikiwa" Amesema Rais Magufuli
Katika hafla hiyo, wakuu wa mikoa walioapishwa na wakuu wa wilaya wateule wamekula kiapo cha ahadi ya uadilifu kwa viongozi wa umma, zoezi ambalo limeongozwa na Kamishna wa Maadili Jaji Mstaafu Salome Kaganda.
Katika hatua nyingine, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amekutana na kufanya Mazungumzo na mwenyekiti mwenza wa taasisi ya Bill and Melinda Gates ya Marekani Bi. Melinda Gates ambapo Rais Magufuli amemuhakikishia mwenyekiti mwenza huyo kuwa serikali ya awamu ya tano itaendeleza na kuimarisha zaidi uhusiano wake na taasisi hiyo ambayo imekuwa ikishirikiana na Tanzania katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya Afya, Uongozi na Kilimo.
Kwa upande wake Bi. Melinda Gate amempongeza Rais Magufuli kwa kazi kubwa anayoifanya katika kukabiliana na rushwa na kuongeza ukusanyaji wa mapato ya serikali, na pia kwa nia yake thabiti ya kuinua sekta ya kilimo inayotegemewa na idadi kubwa ya watanzania na ameahidi kuwa taasisi ya Bill and Melinda Gates itaendelea kushirikiana na Serikali ya awamu ya tano katika kuongeza tija ya uzalishaji wa mazao ya kilimo.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es salaam
29 Juni, 2016