Hotuba
- Dec 13, 2016
HOTUBA YA MHE. DKT. JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA NA MWENYEKITI WA CHAMA CHA MAPINDUZI KWENYE MKUTANO WA HALMASHAURI KUU...
Soma zaidiHotuba
Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar na Makamu Mwenyekiti wa CCM - Zanzibar;
Mzee Philip Mangula, Makamu Mwenyekiti wa CCM - Tanzania Bara;
Ndugu Abdulrahman Kinana, Katibu Mkuu wa CCM;
Wajumbe wa Kamati Kuu;
Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa;
Ndugu Wana-CCM Wenzangu:
Napenda nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutupa uhai na kutukutanisha hapa tukiwa wazima. Aidha, nawashukuru ninyi wajumbe kwa kuja kwa wingi kuhudhuria Mkutano huu. Nawakaribisha Dar es Salaam. Nawakaribisheni sana hapa Ikulu. Jisikieni mko nyumbani. Hapa ni nyumbani kwenu.
Waheshimiwa Makamu Wenyeviti wa CCM Taifa;
Ndugu Katibu Mkuu;
Ndugu Wajumbe wenzangu wa NEC;
Leo ni mara yangu ya kwanza kuongoza Mkutano huu wa Halmashauri Kuu ya Taifa tangu nimechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Chama chetu mwezi Julai mwaka huu. Nakumbuka wakati napokea wadhifa wa Uenyekiti niliwashukuru Wajumbe wote kwa kunichagua. Lakini napenda, kwa mara nyingine tena, niwashukuru kwa dhati kabisa, wajumbe wote wa NEC kwa kunichagua kwa kishindo. Mlinipa kura zote.
Ahsanteni sana kwa imani kubwa mliyonionesha. Kama nilivyoahidi wakati ule, sitawaangusha.
Napenda kutumia fursa hii pia kumshukuru na kumpongeza Mwenyekiti Mstaafu wa Chama chetu, Mzee Kikwete, kwa uamuzi wake wa kung’atuka kabla ya muda wake ili kuniachia kijiti cha kuongoza Chama hiki. Uamuzi wake huo, ni kielezo kingine cha ubora na kukomaa kwa demokrasia kwenye Chama chetu. Nafurahi Mama Salma Kikwete yupo hapa. Natumaini atafikisha shukrani zangu kwake.
Ndugu Wajumbe wa NEC;
Katika hotuba yangu ya kupokea Uenyekiti nilieleza kwa kirefu masuala ambayo tutayapa kipaumbele katika Awamu hii ya uongozi. Nilieleza masuala mengi. Nisingependa nirudie. Lakini nitawakumbusha japo kwa haraka haraka.
- Kwanza, uimarishaji wa Chama katika ngazi zote pamoja na Jumuiya zake. Tunataka kuwa na Chama imara chenye uwezo wa kuisimamia Serikali na kutetea wanyonge. Hatutaki kuwa na Chama legelege cha watu walalamikaji. Sisi ndio tumepewa ridhaa na wananchi kuongoza hivyo hatuna budi kuhakikisha Serikali inatekeleza majukumu yake ipasavyo. Kwa maana nyingine, ninyi viongozi wa Chama mnapaswa kutoa maelekezo kwa Serikali kuhusu masuala mbalimbali.
- Pili, kuongeza idadi ya wanachama. Chama ni wanachama. Bila wanachama hakuna Chama. Hivyo, ni lazima tuhakikishe Chama chetu kina idadi kubwa ya wanachama, hususan vijana.
- Tatu, kuondoa rushwa katika Chama. Chama chetu ni miongoni mwa taasisi zinazotuhumiwa kwa vitendo vya rushwa nchini. Uwepo wa rushwa kwenye Chama chetu umekuwa ukijidhihirisha zaidi nyakati za uchaguzi. Ni lazima tutafute ufumbuzi wa gonjwa hili sugu. Hatutakuwa na msamaha na watoa na wapokea rushwa. Tutahakikisha Chama chetu kina viongozi na wanachama waadilifu.
- Nne, Chama kujitegemea kiuchumi. Tunataka Chama chetu kijitegemee kiuchumi. Haifai na ni aibu kwa Chama kikongwe kama chetu kutegemea fedha za ruzuku na watu binafsi kujiendesha. Tunazo rasilimali nyingi: mashamba, viwanja na vitega uchumi vya kila aina. Kinachohitajika ni kuhakikisha rasilimali hizo zinakinufaisha Chama chetu. Hivi sasa rasilimali zetu nyingi hatunufaiki nazo kutokana na usimamizi mbovu, ubadhirifu na kuingia mikataba isiyo na tija.
- Tano, kukomesha usaliti na kuvunja makundi. Wapo wanachama wachache ambao hukisaliti Chama chetu hasa nyakati za uchaguzi. Wapo pia wenye kuendekeza makundi hata baada ya uchaguzi kumalizika. Tutanataka kuikomesha tabia hii, ambayo inakidhoofisha sana Chama chetu. Napenda kutumia fursa hii kupongeza Kamati za Siasa za Wilaya na Mikoa ambazo zimechukua hatua dhidi ya watu waliotusaliti kwenye Uchaguzi mwaka jana.
- Sita, tunataka tuwe na Chama kilicho imara, hususan kwenye ngazi ya chini, ambako kuna wanachama wengi. Na sio Chama ambacho kipo kwa ajili ya viogozi wa juu pekee. Hivyo basi, katika awamu hii tunalenga kuwa na viongozi na vikao vichache vya ngazi ya juu.
- Saba, tunataka Chama chenye kuzingatia kanuni zake, ikiwemo Kanuni za Toleo la Mwaka 2012 ambazo zinaelekeza mwanachama kutokuwa na kofia mbili za uongozi katika Chama. Aidha, tunataka Chama chenye kuzingatia Katiba yake. Mathalan, vyeo katika Chama viwe ni vile tu vinavyotambulika kikatiba. Vile visivyotambuliwa Kikatiba, visiruhusiwe kama Mwenyekiti wa Wenyeviti, Makamanda au Walezi.
- Nane, Tunataka kanuni za Jumuiya za Chama ziendane na kanuni na matakwa ya Chama. Hivyo Jumuiya ni lazima zitekeleze majukumu yake kwa kuzingatia Katiba na Malengo ya Chama.
- Tisa, Tunataka kuwa na Chama kinachoongozwa na wanachama badala ya kuwa na mwanachama anayekiongoza Chama, na hivyo kufanya Chama kumfuta mwanachama badala ya mwanachama kukifuata Chama. Kwa hiyo, Chama ni lazima kiendelee kuwa mali ya wanachama badala ya Chama kuwa mali ya mwanachama.
Haya ni baadhi tu ya mambo ambayo tutayapa kipaumbele. Yapo mengine mengi. Lakini niseme tu kwamba itakuwa ni vigumu sana, mimi peke yangu, kutekeleza haya yote. Ni lazima tushirikiane. Na kwa kweli, mimi nawategemea ninyi katika kutekeleza mambo niliyoyataja. Hivyo, ni lazima tuwe kitu kimoja katika kukijenga Chama chetu.
Ndugu Wajumbe wa NEC;
Mwakani Chama chetu kitakuwa na jukumu moja kubwa: Kuchagua viongozi ambao wataongoza Chama chetu kwa kipindi cha miaka mitano ijayo. Zoezi la uchaguzi litaanza mwezi Februari na kukamilika mwezi Novemba 2017. Hili ni zoezi muhimu sana kwa vile uongozi tutakaouchagua ndio utakuwa na jukumu la kukipa Chama chetu ushindi kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa mwaka 2019 na Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2020. Tukichagua safu bora ya uongozi tutakuwa na uhakika wa ushindi wa kishindo kwenye chaguzi hizo. Tukichagua viongozi wabovu, tutapata shida kushinda.
Hivyo basi, napenda kutumia fursa hii kuhimiza Sekretarieti na Kamati za Siasa katika ngazi zote kuanza maandalizi ya uchaguzi huo, kwa kuwahamasisha wana-CCM kote nchini kujiandaa kushiriki uchaguzi huo. Aidha, napenda kutoa wito kwa wana-CCM wenzangu kuhakikisha tunachagua safu bora ya uongozi. Tuwachague viongozi wenye weledi, wachapakazi, waadilifu na wenye kukubalika kwenye jamii. Kamwe tusiwachague wala rushwa. Napenda kurudia onyo langu kuwa katika awamu hii hatutamsamehe mtu yeyote mwenye kutafuta uongozi kwa njia ya rushwa. Rushwa sasa basi kwenye Chama chetu. Aidha, naviagiza vyombo husika kuhakikisha kuwa wajumbe halali tu ndiyo wanashiriki uchaguzi. Pasiwe na mapandikizi. Tukipata taarifa za kuwepo kwa mapandikizi hatutasita kufuta uchaguzi.
Ndugu Wajumbe wa NEC;
Kwa mara nyingine tena, mwaka jana Watanzania walituamini na kutupa dhamana ya kuendelea kuliongoza taifa letu. Lakini kama mnavyofahamu, mwisho wa uchaguzi mmoja ndiyo mwanzo wa maandalizi ya uchaguzi unaofuata. Uchaguzi Mkuu mwingine utafanyika mwaka 2020. Hivyo basi, hatuna budi kujiandaa. Nafarijika kuona kuwa kwa upande wetu tumeanza kujiandaa kwa uchaguzi ujao, hususan kwa kuanza kutekeleza Ilani yetu ya Uchaguzi ya mwaka jana.
Kama mtakavyokumbuka, Ilani yetu ya Uchaguzi ya mwaka jana ilisheheni masuala mengi. Ilikuwa na ahadi nyingi. Tuliahidi kudumisha amani, muungano, umoja na mshikamano wetu. Tuliahidi kujenga uchumi wa viwanda ili kupambana na umaskini na tatizo la ajira. Tuliahidi kuboresha huduma za jamii, hususan elimu na afya. Tuliahidi kuzidisha mapambano ya kuondoa urasimu, uzembe, ubadhirifu na rushwa pamoja na kero nyingine zinazokabili wananchi. Tuliahidi kuongeza ukusanyaji wa mapato ya Serikali na kudhibiti matumizi yake. Tuliahidi kuimarisha uhusiano wetu na mataifa mengine pamoja na mashirika ya kimataifa.
Ndugu Wajumbe wa NEC;
Kama nilivyosema, utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2015 unakwenda vizuri. Nchi yetu ina amani. Mipaka yetu iko salama. Nchi ni tulivu. Vyombo vyetu vya ulinzi viko imara katika kukabiliana na tishio lolote la usalama. Muungano wetu nao upo imara. Umoja na mshikamano wa Watanzania unaendelea.
Hali ya uchumi wetu ni nzuri. Tumepanga uchumi mwaka huu ukue kwa asilimia 7.2 kutoka asilimia 7.0 mwaka jana. Dalili za kufikia azma hiyo zinaonekana. Uchumi katika robo ya pili ya mwaka huu ulikua kwa asilimia 7.9. Tumeweza kushusha mfumko wa bei kutoka asilimia 6.5 mwezi Januari mwaka huu hadi kufikia asilimia 4.5 mwezi uliopita. Tunaedelea na utekelezaji wa ahadi yetu ya kujenga uchumi wa viwanda ili kuwezesha nchi yetu kuwa ya kipato cha kati ifikapo mwaka 2025, kama ambavyo Dira yetu ya Taifa ya Maendeleo inavyoelekeza. Ili kujenga uchumi wa viwanda, inahitajika miundombinu imara ya usafiri na nishati ya umeme. Tunaendelea na kazi ya ujenzi wa miundombinu hiyo.
Katika bajeti ya mwaka huu, ambayo kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi yetu tumeelekeza asilimia 40 kwenye shughuli za maendeleo, tumetenga fedha nyingi kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya usafiri na umeme. Tunataka kuanza ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kimataifa (standard gauge), ambapo tumetenga shilingi trilioni 1. Reli hii itaunganisha nchi yetu na majirani zetu wa Rwanda na Burundi na hivyo kukuza shughuli za kiuchumi. Tunataka kununua meli mbili, moja Ziwa Victoria na nyingine Ziwa Tanganyika. Tunataka kununua ndege mpya ili kufufua Shirika letu la Ndege na kuboresha viwanja vya ndege. Tayari tumenunua ndege mpya sita na mbili zimeanza kufanya kazi. Taratibu za kununua ndege kubwa mbili zinaendelea. Hii itasaidia sana kukuza utalii nchini kwetu. Ni vigumu sana kukuza uchumi wa kitalii kama hatuna ndege. Sambamba na hatua hizo, tunaendelea na ujenzi wa miradi mbalimbali ya barabara na madaraja.
Miradi mikubwa miwili ya umeme inatekelezwa, ikiwemo upanuzi wa Mradi wa Kinyerezi I ili uwe na uwezo wa kuzalisha Megawati 335 kutoka Megawati 150 za sasa. Mradi mwingine ni Kinyerezi II ambao utakuwa na uwezo wa kuzalisha Megawati 240. Sambamba na miradi hiyo, tunatekeleza miradi mikubwa miwili ya kusafirisha umeme wa msongo wa Kv 400 wa kutoka Iringa-Dodoma-Singida-Tabora-Shinyanga wenye urefu wa kilometa 670 na kutoka Dar es Salaam – Tanga – Arusha wenye urefu wa kilometa 702. Katika bajeti ya mwaka huu, Serikali imetenga shilingi bilioni 534.4 kwa ajili ya kutekeleza miradi ya kusambaza umeme vijijini utakaotekelezwa na Wakala wa Nishati vijijini (REA). Aidha, wafadhili mbalimbali wameonesha nia ya kutuunga mkono kwa kuahidi kutoa zaidi ya shilingi bilioni 200.
Ndugu Wajumbe wa NEC;
Kuhusu huduma za jamii, tunaendelea kuboresha upatikanaji wa huduma za afya, elimu na maji. Tumetenga takriban shilingi trilioni 1.99 kwa ajili ya sekta ya afya. Nyingi ya fedha hizo tutazitumia katika kununulia madawa na vifaa tiba. Tumeongeza bajeti ya dawa kutoka shilingi bilioni 31 mwaka jana hadi kufikia shilingi bilioni 250 mwaka huu.
Kwenye elimu nako tumeanza kutoa elimumsingi bila malipo, ambapo kila mwezi tunatenga shilingi bilioni 18.77 kwa ajili ya kugharamia. Tumeongeza fedha za mikopo ya Elimu ya Juu kutoka shilingi bilioni 340 hadi kufikia shilingi bilioni 483. Matokeo ya hatua hizi ni kuongezeka kwa idadi ya wanafunzi wa darasa la kwanza na wale elimu ya juu imeongezeka. Wanafunzi wa darasa la kwanza wameongezeka kwa zaidi ya asilimia 84, wanafunzi wa sekondari kwa asilimia 26 na wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu wameongezeka kutoka wanafunzi 98,300 hadi kufikia takriban wanafunzi 125,000.
Tunaendelea kushughulikia kero mbalimbali za wananchi, ikiwemo urasimu katika utoaji huduma za umma na rushwa. Tunachukua hatua kali za “kuwatumbua” watumishi wa umma wazembe na wabadhirifu. Tumeanzisha Mahakama ya Mafisadi. Tumepunguza kero za kodi na tozo kwa wakulima. Wakulima wa korosho kwenye Mikoa ya Kusini ni mashahidi. Hivi majuzi nimewaagiza Wakuu wa Mikoa kuacha mara moja kuwabughuzi wafanyabiashara wadogo wadogo.
Tumeongeza ukusanyaji wa kodi kutoka wastani wa shilingi bilioni 850 hadi kufikia shilingi trilioni 1.2 kwa mwezi. Hii imewezekana baada ya kudhibiti mianya ya ukwepaji kodi. Tumedhibiti matumizi ya fedha za Serikali kwa kuzuia safari za nje, kuwaondoa takriban watumishi hewa 19,000 pamoja na kubaini kaya maskini hewa 55,000 waliokuwa wakipata misaada kutoka Mpango wa TASAF na wanafunzi hewa 65,000 wa shule za msingi. Tumepungua makato ya kodi kwa wafanyakazi kutoka asilimia 11 hadi 9.
Kuhusu masuala ya diplomasia, tumeendelea kukuza mahusiano yetu na mataifa ya nje pamoja na taasisi za kimataifa. Viongozi Wakuu wa Nchi mbalimbali wametutembelea kutoka Vietnam, India, Rwanda, Cuba, DRC, Morocco na Zambia. Mimi nimetembelea Rwanda, Uganda na Kenya. Katika ziara zote hizo, mkazo tumeweka katika ushirikiano wa kiuchumi.
Ndugu Wajumbe wa NEC;
Nina imani kabisa, kwa kasi hii tuliyoanza nayo tutaweza kutekeleza yale yote tuliyoyaahidi wakati wa kampeni. Niwaombe wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa mjivunie na kutangaza kwa wananchi mafanikio tuliyoyapata. Tuwahimize wananchi kushiriki kwenye shughuli za maendeleo. Tuwahimize wananchi pia kulipa kodi. Tutafute na kuwahamasisha wafanyabiashara kuwekeza kwenye sekta ya viwanda. Nafurahi wafanyabiashara wengi wameanza kuwekeza hapa nchini. Nawakaribisha wafanyabiashara kuja kuwekeza nchini na Serikali itaendelea kutoa vivutio mbalimbali.
Waheshimiwa Makamu Wenyeviti wa CCM Taifa;
Ndugu Katibu Mkuu;
Ndugu Wajumbe wenzangu wa NEC;
Siwezi kuhitimisha hotuba yangu bila kutoa shukrani zangu nyingi za dhati kwa Makamu wa Wenyeviti, Mheshimiwa Dkt. Shein na Mzee Mangula kwa ushirikiano mkubwa wanaonipa. Binafsi naendelea kujifunza mambo mengi kutoka kwao. Aidha, napenda nimshukuru Katibu Mkuu, Mzee wangu Kinana. Huyu ni nguzo na hazina muhimu sana kwenye Chama chetu. Nawashukuru pia wajumbe wa Kamati Kuu na Sekretarieti ya Chama kwa kazi kubwa mnayoifanya. Nawashukuru Wabunge na watumishi wa Serikali. Nawashukuru Watanzania wote kwa kuendelea kuiunga mkono Serikali. Nipo pamoja nanyi nyote. Tuendelee kushirikiana.
Napenda kuhitimisha kwa kusema kuwa tupo hapa kwa ajili ya kazi maalum. Katika mkutano wa leo tutaleta mapendekezo mbalimbali ya kuboresha muundo wa Chama chetu. Mapendekezo hayo hayamkusudii mtu bali kuboresha ubora wa Chama chetu. Hivyo basi, nawaombeni sana muyaunge mkono. Mkifanya hivyo, nina matumaini makubwa kuwa Chama chetu kitazidi kuimarika na kitaweza kuwatumikia vizuri Watanzania ambao wanakiamini sana.
Mungu Ibariki Tanzania!
Kidumu Chama cha Mapinduzi!
“Asanteni sana kwa Kunisikiliza”
- Dec 09, 2016
HOTUBA YA MHESHIMIWA DKT. JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, WAKATI WA SHEREHE ZA MIAKA 55 YA UHURU WA TANZANIA BARA UWANJA W...
Soma zaidiHotuba
Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan,
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar
na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi;
Mheshimiwa Kassim Majaliwa,
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Mheshimiwa Job Ndugai,
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Mheshimiwa Othman Chande, Jaji Mkuu wa Tanzania;
Waheshimiwa Mzee Mwinyi, Mzee Mkapa na Mzee Kikwete,
Marais Wastaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Mheshimiwa Mama Fatuma Karume;
Mheshimiwa Dkt. Gharib Bilal,
Makamu wa Rais Mstaafu wa Tanzania;
Mheshimiwa Amani Abeid Karume, Rais Mstaafu wa Zanzibar;
Waheshimiwa Mawaziri Wakuu Wastaafu wa Tanzania mliopo;
Waheshimiwa Mawaziri mliopo;
Mheshimiwa Balozi John Kijazi, Katibu Mkuu Kiongozi;
Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama;
Mheshimiwa Paul Makonda, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam;
Waheshimiwa Mabalozi na Viongozi wa Taasisi za Kimataifa;
Waheshimiwa Viongozi wa Vyama vya Siasa na Dini mliopo;
Waheshimiwa Wabunge;
Wageni waalikwa wote;
Wananchi Wenzangu, Mabibi na Mabwana:
Kwa mujibu wa ratiba ya leo, sipaswi kutoa hotuba. Hata hivyo, kutokana na umuhimu wa tukio la leo, imenibidi niwasalimu. Bila shaka, nyote mtakubaliana nami kuwa leo ni siku muhimu sana. Ni muhimu kwa sababu tunaadhimisha Sherehe za Miaka 55 ya Uhuru wa nchi yetu, ambao tuliupata tarehe 9 Desemba 1961. Baadhi yetu hapa wapo walioshuhudia tukio la kupata uhuru wa nchi yetu, wakiwemo Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili, Mzee Mwinyi na Mama Fatma Karume. Wakati huo mimi nilikuwa na umri wa miaka miwili tu. Lakini naamini wengi tuliopo hapa tumezaliwa baada ya uhuru.
Hivyo basi, Watanzania wote hatuna budi kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutupa uhai kuiona siku ya leo na kwa kuendelea kuilinda nchi yetu. Sambamba na kumshukuru Mwenyezi Mungu, tuwakumbuke pia wazee wetu wote ambao walijitoa muhanga kupigania uhuru wa nchi yetu, hususan wazee 17 waanzilishi wa Chama cha TANU, wakiongozwa na Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere. Kama isingekuwa ujasiri na ushupavu wao, huenda hadi leo tungekuwa bado tunatawaliwa. Kwa sababu hiyo, tunawashukuru sana wazee wetu hao.
Waheshimiwa Viongozi;
Mabibi na Mabwana;
Hii ni mara ya pili kwa Maadhimisho haya kufanyika tangu nimechaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mara ya kwanza ilikuwa mwaka jana, ingawa hatukufanya sherehe. Tuliadhimisha kwa kufanya usafi nchi nzima. Napenda nieleze kwa kifupi kwanini hatukufanya sherehe hizi mwaka jana. Sababu zilikuwa mbili. Kwanza, wakati tarehe za sherehe zinafika, mimi nilikuwa na mwezi mmoja tu madarakani. Wakati huo, hata safu ya uongozi nilikuwa bado sijaikamilisha. Hivyo, nikaona niahirishe kufanya Sherehe.
Sababu ya pili ni kwamba, kabla sijaahirisha, niliwauliza Kamati ya Maandalizi kuhusu gharama za kufanya sherehe. Wakaniambia shilingi bilioni 4. Nikawauliza kwa ajili ya nini? Wakaniambia ni kwa ajili ya posho na kuandaa hafla ya chakula. Nikawauliza Watanzania wote watapewa hiyo posho na kualikwa kwenye chakula? Wakasema hapana, posho ni kwa ajili ya Kamati ya Maandalizi na chakula ni kwa wageni waalikwa tu. Hivyo basi, baada ya kutafakari na kushauriana na wenzangu, tukakubaliana kuwa tusifanye sherehe. Fedha zilizopangwa kutumika kwenye Sherehe tukaamua zipelekwe kwenye ujenzi wa Barabara ya Ali Hassan Mwinyi kutoka eneo la Morocco hadi Mwenge. Tulifanya vile kwa kuwa tulitambua kuwa barabara ile itatumiwa na Watanzania wote. Sasa niwaulize Watanzania wenzangu, je tulikosea kutofanya Sherehe mwaka jana? Kama tulikosea mtusamehe.
Mwaka huu tumeamua tuadhimishe Sherehe hizi kwa sababu kubwa mbili. Kwanza kabisa, gharama zake ni ndogo. Baada ya hapa hapatakuwa na posho wala chakula. Lakini pili, tumeamua kufanya Maadhimisho haya kwa vile hii huenda ikawa ni mara ya mwisho sherehe hizi kufanyika hapa Dar es Salaam. Tunategemea kuanzia mwakani Maadhimisho haya yatakuwa yakifanyika Dodoma, ambako ndiko Makao Makuu ya nchi yetu. Hivyo basi, kwa wale wenzangu wapenda gwaride, itabidi msafiri kuja Dodoma.
Waheshimiwa Viongozi;
Mabibi na Mabwana;
Bila shaka mtakubaliana nami kuwa katika kipindi cha miaka 55 ya Uhuru wa nchi yetu, tumepata mafanikio mengi. Nafahamu wapo wenye kubeza mafanikio tuliyopata. Lakini ukweli ni kwamba tumepata mafanikio makubwa. Tanzania ya leo sio ile ya mwaka 1961. Tumelinda uhuru wa nchi yetu. Mipaka yetu ipo salama. Tunafanya mambo yetu wenyewe bila kuingiliwa. Wapo waliojaribu kutishia uhuru wetu lakini wameshindwa. Nchi yetu imebaki kuwa imara. Tumedumisha amani, umoja na mshikamano wa nchi yetu. Tangu tumepata uhuru, nchi yetu ina amani na wananchi wamebaki kuwa wamoja. Hatubaguani kwa misingi ya rangi, dini, kabila au itikadi. Tumejenga na kudumisha Muungano wetu. Ni vyema Watanzania wote tukajipongeza.
Aidha, tumeweza kujenga miundombinu mbalimbali ya kiuchumi, ikiwemo barabara, madaraja, vivuko, meli, reli, viwanja vya ndege, miradi ya umeme na maji n.k. Huduma za jamii kama vile afya na elimu, zimeboreshwa na kusogezwa karibu na wananchi. Baadhi yetu tunakumbuka jinsi ambavyo zamani ilitulazimu kutembea umbali mrefu kufuata huduma za shule au hospitali.
Nchi yetu pia inang’ara kimataifa kutokana na mchango wake katika harakati za ukombozi wa Bara la Afrika, kutafuta amani na kupinga uonevu duniani. Napenda kutumia fursa hii, kuwapongeza viongozi wa awamu mbalimbali za uongozi wa nchi yetu kwa kazi kubwa waliyoifanya na kuwezesha kupatikana kwa mafanikio haya. Aidha, nawapongeza Viongozi wa ngazi mbalimbali wa Serikali zetu mbili na watu wote waliotoa mchango kwa namna moja au nyingine. Nyote kwa pamoja, tunawapongeza na kuwashukuru sana.
Waheshimiwa Viongozi;
Wananchi wenzangu;
Mabibi na Mabwana;
Licha ya mafanikio tuliyoyapata, ni dhahiri kuwa bado zipo changamoto, ikiwemo kuendelea kwa matatizo ya umaskini, ukosefu wa ajira, upatikanaji wa huduma za jamii, rushwa n.k. Napenda kutumia fursa hii kuwahakikishia wananchi kuwa Serikali ya Awamu ya Tano itaendeleza jitihada zilizoanzishwa na Serikali za Awamu zilizotangulia katika kutatua changamoto hizo. Na kama nyote mnavyofahamu, Serikali hii iliingia madarakani mwezi Novemba mwaka jana baada ya kufanikiwa kushinda Uchaguzi Mkuu wa mwezi Oktoba. Wakati wa Kampeni za Uchaguzi Mkuu huo, tulinadi Ilani ya Uchaguzi wa CCM ambayo ilisheheni mambo mengi. Tuliahidi kujenga misingi imara ya kuifanya nchi yetu kuwa ya uchumi wa kati unaoongozwa na viwanda ifikapo mwaka 2025, kulingana na Dira yetu ya Taifa ya Maendeleo. Tuliahidi kupambana na uzembe na ubadhirifu Serikalini pamoja na kuboresha huduma za jamii, afya, elimu na maji.
Katika kutekeleza yale tuliyoyaahidi, tumeandaa Mipango, Mikakati na kuanza kuchukua hatua mbalimbali. Tayari tumekamilisha Mpango wa Miaka Mitano ya Maendeleo (2016/2017 – 2020/2021). Dhima kuu ya Mpango huu ni ujenzi wa uchumi wa viwanda. Tunataka kujenga uchumi wa viwanda ili kukabiliana na tatizo la umaskini na ukosefu wa ajira nchini. Utekelezaji wa Mpango huu umeanza mwezi Julai mwaka huu, ambapo imepitisha bajeti ya shilingi trilioni 29.5 kuanza kuutekeleza. Kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi yetu, Serikali imetenga asilimia 40 ya bajeti yote kutekeleza shughuli za maendeleo, ikiwemo ujenzi ya miundombinu ya usafiri na nishati ya umeme.
Tumetenga fedha nyingi kwenye ujenzi wa miundombinu ya usafiri na nishati kwa kutambua umuhimu wake katika ujenzi wa uchumi wa viwanda. Katika bajeti ya mwaka, tutaendelea na utekelezaji wa miradi umeme ya Kinyerezi I (kupanua uwezo wake kutoka Megawati 150 hadi kufikia Megawati 335) na Kinyerezi II utakaokuwa na uwezo wa kuzalisha Megawati 250.
Aidha, tumetenga shilingi trilioni 1 kuanza ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kimataifa (standard gauge) ambayo itaiunganisha nchi yetu na nchi za Burundi na Rwanda. Tumekwishanunua ndege sita mpya, ambapo ndege tatu ni aina ya Q400 Bombardier zenye uwezo wa kubeba abiria 76 kila moja. Kati ya ndege hizo tatu, mbili tayari zimewasili na kuanza kazi. Ndege mbili zitakuwa ni aina ya CS 300 zenye uwezo wa kubeba abiria 150 ambazo ni kwa mara ya kwanza zitatumika Barani Afrika. Tumeanza pia kufanya malipo ya kununua ndege kubwa aina ya Boeing 787 yenye uwezo wa kubeba abiria takriban 250. Tunaamini hatua hii itasaidia kukuza sekta ya utalii nchini.
Ndugu Wananchi;
Mabibi na Mabwana;
Sambamba na kujenga miundombinu ya uchumi, tunaendelea kuboresha sekta za afya na elimu. Kwenye elimu nako tumeanza kutoa elimumsingi bila malipo, ambapo kila mwezi tunatenga shilingi bilioni 18.777 kwa ajili ya kugharamia. Tumeongeza fedha za mikopo ya Elimu ya Juu kutoka shilingi bilioni 340 hadi kufikia shilingi bilioni 483. Matokeo yake idadi ya wanafunzi wa darasa la kwanza na elimu ya juu imeongezeka. Darasa la kwanza imeongezeka kwa zaidi ya asilimia 84, sekondari kwa asilimia 26 na wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu wameongezeka kutoka wanafunzi 98,300 hadi kufikia takriban wanafunzi 125,000. Na kuhusu afya, tumeongeza bajeti ya kununua dawa kutoka shilingi bilioni 31 mwaka jana hadi kufikia shilingi bilioni 250 mwaka huu.
Vilevile, tumeongeza ukusanyaji wa kodi kutoka wastani wa shilingi bilioni 850 hadi kufikia shilingi trilioni 1.2 kwa mwezi. Tumedhibiti mianya ya ukwepaji kodi na matumizi mabaya ya fedha za Serikali, hususan kwa kuzuia safari za nje zisizo na tija na kuwabaini watumishi hewa 19,000. Aidha, tumeanza kuondoa kero mbalimbali kwa wananchi, ikiwemo kupunguza utitiri wa kodi kwa wakulima na kiwango cha kodi wanacholipa wafanyakazi kutoka asilimia 11 hadi 9.
Nina matumaini makubwa kuwa, kutokana na hatua hizi tuazozichukua, azma yetu ya kuwa nchi ya uchumi wa kati unaoogozwa na viwanda ifikapo mwaka 2025 itawezekana. Na pia tutaweza kutimiza dhamira yetu ya kuboresha huduma za jamii na kuondoa kero mbalimbali kwa wananchi, ikiwemo uzembe kwa watumishi wa umma na rushwa. Ndiyo, ni lazima tukomeshe Rushwa. Rushwa ni kansa na pia ni adui wa haki na maendeleo. Kwa sababu hiyo, naahidi kuwa Serikali itaendelea kuchukua hatua za “kuwatumbua” watumishi wa umma wazembe na wabadhirifu. Na katika hili, nalishukuru Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kupitisha Sheria ya kuanzisha Mahakama ya Mafisadi.
Waheshimiwa Viongozi;
Wananchi wenzangu;
Mabibi na Mabwana;
Leo nilipanga niwasalimie tu. Hivyo basi, sitapenda kuwachosha kwa hotuba ndefu. Hata hivyo, kabla sijahitimisha hotuba yangu, naomba mniruhusu nieleze masuala mawili ya mwisho ambayo binafsi nitafurahi sana kama kila Mtanzania ataendelea kuyazingatia. Jambo la kwanza ni kuhusu umuhimu wa kudumisha Amani, Umoja na Mshikamano wetu. Kama mnavyofahamu, amani ni msingi wa maendeleo. Bila ya amani, hakuna maendeleo. Hivyo basi, leo tunapoadhimisha Sherehe hii ya Uhuru, napenda kuwahimiza Watanzania wote kuendelea kuilinda amani yetu na kuwafichua watu wenye nia ya kuhatarisha amani yetu. Sambamba na kulinda amani yetu, hatuna budi kudumisha umoja, mshikamano na muungano wetu, ambao ndiyo nguvu na silaha yetu kubwa kama taifa.
Jambo la pili, ni kuhusu kuchapa kazi kwa bidii. Kazi ni utu. Hivyo basi, kila mmoja wetu lazima afanye kazi kwa bidii ili kwenda sambamba na kaulimbiu yetu ya “Hapa Kazi tu”. Uwe mkulima, mfanyakazi, mfugaji, mvuvi au mfanyabiashara sote ni lazima tujipange kufanya kazi kwa bidii. Wazee wetu wa zamani walipambana na kutuletea uhuru. Sasa ni wajibu wetu kuchapakazi kwa bidii ili kulijenga Taifa letu. Hatuna mjomba wala shangazi kutoka nje kutuletea maendeleo.
Waheshimiwa Viongozi;
Wananchi wenzangu;
Mabibi na Mabwana;
Napenda nihitimishe kwa kusema tena kuwa leo ni siku ya furaha. na ya kihistoria kwa Taifa letu. Naipongeza Kamati ya Maandalizi kwa kufanikisha Maadhimisho haya. Sherehe zimefana sana. Navipongeza na kuvishukuru vikosi vyetu vya ulinzi na usalama kwa gwaride zuri ambalo tumeshuhudia. Mmeonesha umahiri mkubwa sana na kwa hakika nchi yetu ipo salama. Halikadhalika, nawashukuru wana-Dar es Salaam chini ya Mkuu Mkoa wenu, Paul Makonda, kwa kujitokeza kwa wingi kuhudhuria Maadhimisho haya. Navipongeza pia vikundi vyote vya burudani kwa kutuburudisha.
Mwisho lakini sio kwa umuhimu, nawashukuru wageni wetu waalikwa wote kwa kuja kuungana nasi katika Sherehe hizi. Nawashukuru sana Mabalozi kutoka nchi mbalimbali na taasisi za kimataifa. Nawaahidi kuwa tutaendelea kushirikiana nanyi. Napenda kurudia tena ahadi yangu kwa wananchi wote kuwa, Serikali ya Awamu ya Tano imejipanga kufanya kazi kwa manufaa ya Watanzania wote na kamwe hatutawaagusha. Tutafanya kazi pia kwa bidii bila ya kumbagua mtu yeyote.
Mungu Ibariki Tanzania!
Mungu Wabariki Watanzania!
“Ahsanteni Sana kwa kunisikiliza”
- Oct 03, 2016
HOTUBA YA MHE. DKT. JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, KWENYE TAMASHA LA MADHEHEBU YA BOHORA KUSHEHEREKEA MAADHIMISHO YA SIKUK...
Soma zaidiHotuba
Mtukufu Dkt. Syedna Mufaddal Saifuddin Saheb (TUS),
Kiongozi Mkuu wa Madhehebu ya Bohora Duniani;
Mheshimiwa Sheikh Abubakar Zubeir Ally,
Sheikh Mkuu na Mufti wa Tanzania,
Mheshimiwa Zainuddin Adamjee,
Kiongozi wa Madhehebu ya Bohora hapaTanzania;
Waheshimiwa Viongozi wa Dini na
Madhehebu Mbalimbali mliopo;
Viongozi wa Serikali mliopo;
Ndugu waumini wa Madhehebu ya Bohora
hapa nchini na kutoka nchi mbalimbali;
Ndugu wananchi, Mabibi na Mabwana;
Assalaam Eleykum!
Awali ya yote napenda nimshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa Rehema kwa kutupa uhai na kutukutanisha mahali hapa tukiwa wenye afya njema. Aidha, napenda kutumia fursa hii, kwa niaba yangu binafsi na kwa niaba ya Wananchi na Serikali kukukaribisha Mtukufu Dkt. Seydna Mufaddal Saifuddin Saheb(TUS) hapa Tanzania, hususan katika Jiji letu la Dar es Salaam. Watanzania wengi kama sio wote wamefurahi na kupokea kwa mikono miwili na moyo mkunjufu ujio wako hapa nchini.
Nakumbuka mara ya kwanza nilikutana na wewe, Mtukufu Dkt. Syedna Saifuddin tarehe 17 Agosti, 2016 pale Ikulu. Siku ile niliwasilisha kwako ombi la kufanya Maadhimisho haya ya Sikukuu ya Ashura hapa Dar es Salaam. Nashukuru ulikubali ombi langu. Lakini napenda kukiri kuwa sikutegemea kama ingewezekana kufanyika mwaka huu. Hii ni kwa sababu muda uliokuwa umebaki kufikia Maadhimisho haya ulikuwa mfupi sana. Hata hivyo, kwa jitihada zako imewezekana. Hivyo basi, napenda kwa mara nyingine tena kukushukuru kwa kukubali Maadhimisho haya kufanyika hapa Dar es Salaam mwaka huu. Nakushukuru pia kwa kuniruhusu kuingia mahali hapa patakatifu na kwa kunipa fursa ya kusema maneno machache. Ahsante sana Baba Mtukufu.
Napenda pia kutumia fursa hii kuwakaribisha wageni wetu wote kutoka nchi mbalimbali waliokuja hapa nchini kwa ajili ya Maadhimisho haya ya Ashura. Tunawakaribisheni sana hapa Dar es Salaam. Nawaombeni mjisikie mko nyumbani. Kwa ambao hawafahamu, Jiji la Dar es Salaam lilipewa jina hili na wafanyabiashara wa Kiarabu, ambao walikuwa wakifanya shughuli zao kwenye eneo hili karne kadhaa zilizopita, wakimaanisha Bandari Salama au Mji wa Amani. Hivyo basi, nina imani kubwa kuwa Maadhimisho haya yatafanyika katika mazingira ya amani na usalama. Napenda kuwahakikishia kuwa nchi yetu ni nzuri na ina amani. Tunavyo vivutio vingi vya kitalii, ikiwemo Mlima Kilimanjaro, Mbuga za Wanyama (Serengeti na Ngorongoro) pamoja na Visiwa vya Zanzibar vyenye utajiri mkubwa wa historia. Hivyo basi, nawaalika baada ya Maadhimisho haya, mtafute fursa ya kutembelea baadhi ya maeneo ili nanyi mjionee na kufurahia vivutio vya utalii vilivyopo hapa nchini.
Mheshimiwa Mtukufu Dkt. Syedna Saifuddin;
Mheshimiwa Mufti,
Ndugu Waumini;
Mabibi na Mabwana;
Tumekutana hapa kwa ajili ya Maadhimisho ya Sikukuu ya Ashura, ambayo pia ni maadhimisho ya kuanza kwa Mwaka Mpya wa Kiislamu. Nimeambiwa kuwa Sherehe za Ashura huadhimishwa kila mwaka duniani kote na waamuni wa Madhehebu ya Bohora. Mwaka huu Maadhimisho haya yameanza kuadhimishwa tarehe 2 Oktoba na yatadumu hadi tarehe 11 Oktoba. Nimeambiwa kwa waumini wa Madhehebu ya Bohora Sherehe za Ashura huadhimishwa kukumbuka kifo cha Mjukuu wa Mtume Muhammad (S.A.W), Imam Hussein bin Ali (A.S), aliyeuawa kwa kupigania dini takriban karne kumi na nne zilizopita. Nimearifiwa pia kuwa wakati wa maadhimisho hutolewa mawaidha na mafundisho mbalimbali kuhusu masuala ya kiroho na kiimani. Sambamba na masuala ya kiimani, mawaidha uweka pia mkazo kwenye masuala ya amani, umoja, mshikamano, haki na halikadhali masuala ya kijamii, uchumi na maendeleo kwa ujumla.
Hivyo basi, kwa niaba ya Wananchi wa Tanzania, Serikali na mimi mwenyewe binafsi, napenda kuwatakia Waamuni wote wa Madhehebu ya Bohora wa hapa nchini na duniani kote maadhimisho mema ya Sikukuu hii ya Ashura kwa mwaka huu. Wito wangu kwenu pokeeni na zingatieni mafundisho na mawaidha mbalimbali yatakayotolewa katika kipindi hiki na viongozi wenu, hususan kutoka kwa Kiongozi Mkuu Mtukufu Dkt. Syedna Saifuddin, kwa ajili ya kukua kiimani lakini pia kwa maendeleo na ustawi wa kila mmoja wenu na maeneo mnakoishi. Nawaombeni pia mtumie maadhimisho haya kutuombea sisi viongozi na taifa letu kwa ujumla.
Mheshimiwa Mtukufu Dkt. Syedna Saifuddin;
Mabibi na Mabwana;
Bila shaka, mtakubaliana nami kuwa dini ina mchango mkubwa sana katika ustawi na maendeleo ya taifa au jamii yoyote. Ili kudhihirisha hilo, waumini wa Dhehebu la Bohora wamekuwa wakitoa mchango mkubwa wa kimaendeleo hapa nchini. Wanashirikiana kwa karibu na Serikali katika masuala mbalimbali ya kiuchumi na kijamii. Nakumbuka hata kiongozi wa Jumuiya ya Bohora hapa nchini, rafiki yangu, Mheshimiwa Adamjee aliwahi kuwa Mbunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na alikuwa akitoa mchango mzuri wa mawazo kwa maendeleo ya taifa letu.
Lakini ninakumbuka pia kuwa mwezi Agosti mwaka huu Baba Mtukufu ulipokuja, ulitoa msaada wa Dola za Marekani elfu 53 katika kuunga mkono jitihada za Serikali yetu kukabiliana na changamoto ya upungufu wa madawati katika shule zetu. Aidha, mwezi Aprili mwaka huu Madaktari kutoka Hospitali ya Saifee ya nchini India walikuja hapa nchini na kutoa matibabu bure kwa wananchi kule Arusha, kwa ufadhili wa Madhehebu ya Bohora chini ya programu ya Project Good Health. Hii yote inadhihirisha kuwa dini zina mchango mkubwa katika shughuli za maendeleo hapa nchini. Hivyo basi, kwa niaba ya Serikali, napenda kuzishukuru dini zote kwa michango yao mbalimbali hapa nchini na nawaomba muendelee na moyo huo. Aidha, napenda kutumia fursa hii kukuhakikishia, Mtukufu Baba, kuwa Serikali ya Tanzania itaendelea kushirikiana na Dhehebu la Bohora hapa nchini.
Mheshimiwa Mtukufu Dkt. Syedna Saifuddin;
Mabibi na Mabwana;
Pamoja na pongezi hizo, napenda kutumia fursa hii kueleza kuwa Tanzania ni nchi yenye fursa mbalimbali za kiuchumi. Tunayo ardhi ya kutosha kwa ajili ya kilimo, rasilimali za maji (bahari, maziwa na mito) kwa ajili ya uvuvi, misitu, mifugo, madini na gesi. Aidha, Tanzania ni mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (East African Community – EAC) pamoja na ile ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (Southern African Development Community – SADC). Kwa pamoja Jumuiya zina idadi ya watu zaidi ya watu milioni 400 na hivyo tunalo soko kubwa la uhakika. Katika kipindi cha miaka mitano ijayo, nchi yetu imedhamiria kujenga uchumi wa viwanda. Hizi zote ni fursa nzuri za kuwekeza hapa nchini.
Hivyo basi, nakaribisha dini zote na wafuasi wenu wa ndani na nje ya nchi kutumia fursa zilizopo hapa nchini kuwekeza. Napenda kuwahakikishia kuwa Tanzania ni mahali salama kwa ajili ya uwekezaji. Hivyo karibuni sana. Nimefurahi sana kusikia Maadhimisho haya yamewaleta hapa nchini takriban waumini wa Bohora takriban elfu thelathini kutoka nchi mbambali. Naamini miongoni mwao wapo wafanyabiashara ambao baada Maadhimisho watapata muda wa kutafuta fursa za biashara na uwekezaji hapa nchini, ikiwa ni pamoja na kuingia ubia na Watanzania. Na kwa kuwa ninyi ni wacha Mungu, nina matumaini makubwa kuwa mkiamua kufanya biashara hapa nchini mtaiendesha kwa halali na wananchi maskini wa Tanzania watanufaika.
Mheshimiwa Mtukufu Dkt. Syedna Saifuddin;
Waheshimiwa Viongozi wa Dini mliopo;
Mabibi na Mabwana;
Kama nilivyosema awali tupo kwa ajili ya Maadhimisho ya Sikukuu ya Ashura na kuanza kwa Mwaka Mpya wa Kiislamu. Hivyo basi, naamini watu wengi wamekuja hapa wakiwa na shauku kubwa ya kusikiliza mawaidha na mafundisho mbalimbali kuhusiana na dini. Kwa sababu hiyo, haitakuwa busara kwangu kuwachosha kwa hotuba ndefu. Hata hivyo, kabla sijahitimisha napenda kutumia fursa hii nikueleze japo kwa kifupi hali ilivyo hapa nchini.
Kwa ujumla tunaendelea vizuri. Uchumi wetu mwaka huu unatarajia kukua kwa asilimia 7.2 kutoka asilimia 7.0 mwaka jana. Dalili za kufikia lengo hilo zimeanza kuonekana ambapo uchumi katika robo ya pili ya mwaka huu umekua kwa asilimia 7.9. Serikali yetu imeweka msisitizo wa kuifanya nchi yetu kuwa ya viwanda, ambapo tunataka ifikapo mwaka 2020 sekta hii iwe inatoa asilimia 40 ya ajira zote nchini. Hii ndiyo sababu tunawakaribisha wawekezaji kuja kushirikiana nasi kujenga viwanda hapa nchini.
Mheshimiwa Mtukufu Dkt. Syedna Saifuddin;
Waheshimiwa Viongozi wa Dini mliopo;
Mheshimiwa Mufti,
Ndugu Waaumini;
Wageni Waalikwa;
Mabibi na Mabwana;
Napenda kuhitimisha kwa kumshukuru tena Mtukufu Baba kwa kukubali Maadhimisho ya Ashura Mwaka huu hapa nchini. Tumefurahi umekuja na waumini kutoka mataifa mbalimbali duniani. Ombi langu kwako naomba uzidi kutuombea. Ombea nchi yetu, viongozi pamoja na wananchi wake. Nina imani kuwa kupitia maombi yako sisi tutasamehewa, haki itatawala na dunia itaponywa.
Napenda pia kutumia fursa hii kumpongeza kwa dhati kabisa Sheikh Abubakar Zubeir Ally, Sheikh Mkuu na Mufti wa Tanzania, kwa jitihada kubwa unazozifanya za kujenga umoja miongoni mwa madhehebu mbalimbali ya dini ya Kiislamu. Napenda pia kutoa shukrani zangu nyingi kwa viongozi wengine wa dini, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, BAKWATA na vyombo vya ulinzi ambao kwa pamoja wametoa ushirikiano katika kufanikisha Maadhimisho haya kufanyika katika hali ya utulivu.
Kabla sijaondoka mahali hapa patakatifu, nimekuja na zawadi ndogo. Zawadi hii ni kito kilichotengezwa na madini yanayopatika hapa Tanzania pekee yaitwayo, Tanzanite. Ninaomba nikukabidhi zawadi hii ili kila mahali utakapokuwa uwe ukiikumbuka nchi yetu.
Asanteni Sana kwa kunisikiliza!
“Assalam Aleykum”
- Sep 28, 2016
HOTUBA YA MHE. DKT. JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, KWENYE SHEREHE ZA KUZINDUA NDEGE MPYA DAR ES SALAAM, TAREHE 28 SEPTEM...
Soma zaidiHotuba
Mheshimiwa Job Ndugai, Spika wa Bunge la Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania;
Mheshimiwa Prof. Makame Mbarawa, Waziri wa Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano;
Waheshimiwa Mawaziri na Manaibu Waziri mliopo;
Mheshimiwa Balozi John Kijazi, Katibu Mkuu Kiongozi;
Mheshimiwa Paul Makonda, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam;
Mheshimiwa Dkt. Noman Sigala King, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu;
Waheshimiwa Wabunge mliopo na Mstahiki Meya wa Dar es Salaam;
Waheshimiwa Makatibu Wakuu mliopo hapa;
Mwenyekiti na Wajumbe wa Bodi ya ATCL na Mtendaji Mkuu wa ATCL;
Ndugu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania;
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania;
Wafanyakazi wa ATCL, TCAA, TAA na Bodi ya Utalii mliopo;
Waheshimiwa Wageni wote Waalikwa, Mabibi na Mabwana:
Napenda nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kukutana hapa kushuhudia tukio hili. Aidha, namshukuru Mheshimiwa Waziri Prof. Mbarawa kwa kunialika ili nishiriki katika hafla hii muhimu, ambayo inatoa dira ya wapi taifa letu linaelekea. Vilevile, kwa niaba yenu, napenda kutoa shukrani zangu nyingi kwa Kampuni ya Bombadier ya Canada ambayo imetengeneza ndege hizi mbili aina ya Bombardier Dash 8 Q400 zenye uwezo wa kubeba abiria 76 kila moja. Tunawashukuru sana kwa kutengeneza na kuzileta ndege hizi hapa nchini kwa wakati. Wametekeleza na kutimiza kaulimbiu yetu ya “hapa kazi tu”.
Wageni Waalikwa;
Mabibi na Mabwana;
Bila shaka mtakubaliana nami kuwa mambo mengi yamezungumzwa kuhusu ndege hizi. Wapo waliosema kuwa hazina spidi. Spidi yake ni kama bajaji. Lakini tumedhihirishiwa kuwa ndege hizi zina spidi. Zimesafiri umbali mrefu kutoka Canada kuja hapa nchini kwa kutumia siku chache tu. Wapo pia waliosema kuwa ndege hizi ni mbovu, za kizamani na hazitumiki duniani kwa sasa. Hilo nalo sio kweli. Ndege hizi zinatumika mahali pengi tu duniani. Marekani wanazo ndege zaidi ya 40 za namna hii, na hata Ethiopia pia wanazo. Wengine walilaumu uamuzi wetu wa kulipia kwa mkupuo. Sasa, kama unazo fedha kwa nini usilipe?
Napenda nitumie fursa hii kuwahakikishia Watanzania wenzangu kuwa ndege hizi ni nzuri, za kisasa na zinafaa katika mazingira yetu. Zinatumia mafuta kidogo na zina uwezo wa kutua kwenye viwanja vingi nchini. Na nina uhakika, ndege hizi sitatusaidia sana katika kurahisisha usafiri wa anga hapa nchini na pia kushusha gharama za usafiri wa ndege nchini. Kama mnavyofahamu, hivi sasa Serikali inafanya ukarabati wa viwanja vya ndege katika maeneo mengi nchini. Hivyo basi, uwepo wa ndege hizi utasaidia usafiri wa ndege kwenda maeneo hayo.
Wageni Waalikwa;
Mabibi na Mabwana;
Sambamba na kurahisisha usafiri, ndege hizi zitatusaidia sana katika kukuza sekta yetu ya utalii. Kama mnavyofahamu, moja ya njia ya kukuza sekta ya utalii katika nchi ni kuhakikisha kunakuwa na usafiri wa anga wa uhakika. Bila ya hivyo, ni vigumu sana kuwavutia watalii kutoka nje ya nchi. Hii ni kwa sababu, watalii wengi husafiri kwa kutumia usafiri wa anga. Mathalan, takwimu zinaonesha kuwa idadi ya watalii waliosafiri kwenye nchi mbalimbali duniani mwaka 2012 ilifikia bilioni 1, na bila shaka hivi sasa idadi hiyo itakuwa imeongezeka. Lakini jambo muhimu la kuzingatia ni kwamba kati ya watalii hao bilioni moja, zaidi ya nusu walisafiri wa kutumia usafiri wa anga. Huu ni uthibitisho tosha kuwa usafiri wa anga ni muhimu katika ukuzaji wa sekta ya utalii.
Hivyo basi, niwaombe Watanzania wenzangu kuunga mkono juhudi za Serikali za kufufua Shirika letu la Ndege, ambalo liliasisiwa na Baba wa Taifa letu, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Tuache kubeza kila jambo linalofanywa na Serikali. Tupende vitu vyetu. Ndege hizi ni za kwetu sote; na faida zake zitawanufaisha Watanzania wote. Na napenda kutumia fursa hii kuarifu kuwa, mbali na ndege hizi mbili, Serikali imepanga kununua ndege nyingine kubwa mbili, moja itakuwa na uwezo wa kubeba abiria 160 na nyingine abiria 240 na uwezo wa kusafiri umbali mrefu. Tukiwa na ndege hizi kubwa, tutaweza kuwaleta watalii hapa nchini moja kwa moja bila ya kupitia sehemu nyingine. Naishukuru sana Kamati ya Bunge ya Miundombinu kwa kuendelea kuunga mkono jitihada hizi za Serikali.
Wageni Waalikwa;
Mabibi na Mabwana;
Ndege hizi ni za Serikali lakini zitakodishwa kwa Shirika letu la Ndege la Tanzania (Air Tanzania Company Limited – ATCL), ambalo tumelifanyia mabadiliko makubwa ya uongozi. Tumesuka upya uongozi wake. Tumeunda Bodi mpya ambayo ni nzuri. Tumemwajiri Mtendaji Mkuu Mpya wa Shirika ambaye ana ueledi na uzoefu wa kutosha kwenye masuala ya usafiri wa ndege. Hivyo basi, nina matumaini makubwa kuwa uongozi huu mpya utafanya kazi kwa bidii ili kuleta mabadiliko katika Shirika letu.
Kama mnavyofahamu, Shirika letu la Ndege limekuwa likikabiliwa na changamoto nyingi. Lakini kubwa ilikuwa ni kushindwa kujiendesha. Lilikuwa linategemea ruzuku ya Serikali kujiendesha. Hali hii ya utegemezi kwa kiasi kikubwa ilisababishwa na baadhi ya watumishi wa Shirika kufanya vitendo vya ubadhirifu na hujuma. Mathalan, nimeambiwa kuwa ilikuwa ni kawaida kwa Shirika kutoa fedha za kununua mafuta ya ndege wakati hakuna safari zinazofanyika. Aidha, zipo taarifa kuwa kwenye Ofisi za Shirika kule Comoro ziliwahi kupotea takriban shilingi milioni 700 na mpaka leo hakuna hatua yoyote imechukuliwa dhidi ya watu waliohusika.
Vilevile, katika zoezi zima la ukatishaji tiketi, zipo taarifa kuwa baadhi ya wakatishaji tiketi walikuwa wakipewa fedha na mashirika mengine ya ndege kuacha kukata tiketi za Shirika. Wateja wakienda kuulizia tiketi walikuwa wakiambiwa kuwa ndege imejaa, kumbe si kweli. Ilifanyika hivyo kwa makusudi ili wasafiri waende kwenye mashirika mengine ya ndege.
Wageni Waalikwa;
Mabibi na Mabwana;
Nilizozitaja hapa ni baadhi tu ya changamoto zilizokuwa zikikabili Shirika. Zipo nyingine nyingi. Lakini niseme kwa dhati tu kuwa Serikali ina matarajio makubwa na uongozi huu mpya. Tuna imani kuwa uongozi mpya utafanya jitihada za kurekebisha changamoto nilizozitaja na nyingine ambazo sikuzitaja. Tunategemea kuwa mtajituma na kufanya kazi kwa bidii ili fedha za Watanzania ambazo zimetumika kununua ndege hizi zilete manufaa yaliyokusudiwa. Na kwa sababu hiyo, napenda kuusihi uongozi mpya kutosita kuchukua hatua zenye nia ya kuleta tija na faida kwenye Shirika, hata ikipidi kuwapunguza watumishi ili mbaki na wachache wanaohitajika.
Aidha, nawasihi mpanue wigo wa huduma zenu hadi nje ya nchi; na katika kutoa huduma, zingatieni sana suala la muda na ubora. Tambueni kuwa mko kwenye ushidani na si kila mtu atafurahi kuona mkifanikiwa. Hivyo, ni lazima muwe makini. Na katika hili, niseme tu kuwa binafsi sitarajii kuona Shirika linatoa kazi ya kukatisha tiketi kwa mawakala. Ninyi wenyewe mkijipanga vizuri mnaweza kuifanya kazi hiyo vizuri. Aidha, natoa wito kwenu, uongozi mpya, kuangalia uwezekano wa kufungua akaunti maalumu ya kutunza fedha ili mtakapopata faida, mzitumie kununua ndege nyingine na hivyo kukuza Shirika.
Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi;
Waheshimiwa Viongozi mliopo;
Wageni Waalikwa wote;
Mabibi na Mabwana;
Ningependa niishie hapa. Lakini kabla sijahitimisha hotuba yangu, napenda niseme kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kuleta maendeleo kwa taifa letu. Katika Mwaka huu wa Fedha, tutaanza ujenzi wa reli ya kati kutoka Dar es Salaam kwenda Mikoa ya Kigoma na Mwanza kwa kiwango cha kimataifa (standard gauge). Zabuni ya ujenzi huo tayari imetangazwa. Sambamba na ujenzi wa reli hiyo, Benki ya Dunia imekubali kutupa mkopo kwa ajili ya kuboresha huduma za reli iliyopo, ambapo tumeanza kwa kununua mabehewa mapya ambayo bila shaka baadhi yenu mmeyaona. Hizi ni baadhi tu ya jitihada za kuleta maendeleo ambazo tumeanza.
Mbali na hayo, hapa Dar es Salaam pia tuna mipango mingi ya kuendeleza na kuboresha Jiji hili, hususan kushughulikia tatizo sugu la msongamano wa magari barabarani. Kama mnavyofahamu, tumeanza ujenzi wa daraja la juu pale makutano ya TAZARA. Tunaendelea pia na mipango ya kujenga Daraja ya Juu pale Ubungo na jingine ambalo litapita juu ya Bahari ambalo litatoka Aga Khan hadi Coco Beach. Aidha, katika siku za usoni, tunatarajia kujenga reli ya kisasa ili kutoa huduma ya usafiri hapa Dar es salaam.
Sambamba na mipango hiyo ya maendeleo, tutaendelea kuchukua hatua za kuimarisha nidhamu Serikalini. Tunaendelea kuwashughulikia wabadhirifu na wala rushwa. Tutafanya hivyo kwa nia njema kabisa. Tunataka rasilimali za nchi hii ziwanufaishe Watanzania wote. Nyote ni mashahidi wa namna baadhi ya watu wachache walivyokuwa wakijinufaisha kupitia wafanyakazi hewa, wanafunzi hewa n.k. Hata hivi karibuni, kuna watu walitaka kujinufaisha kwa fedha za misaada ya waathirika wa tetemeko la ardhi kule Kagera. Tutawashughulikia watu wote wenye kuendekeza vitendo hivi.
Hivyo basi, naomba kutoa wito kwa wananchi wote kuendelea kuiunga mkono Serikali kwa hatua mbalimbali inazochukua. Nawaomba pia wanahabari kuendelea kuiunga mkono Serikali. Ninyi ni watu muhimu katika jamii hivyo fanyeni kazi yenu kwa makini na kizalendo. Kamwe msikubali kutumiwa na watu wabaya wasiyoitakia mema nchi yetu. Kumbukeni kuwa nchi hii ni yetu sote, ikikumbwa na matatizo hakuna atakayebaki salama. Sote tutaharibikiwa.
Baada ya maneno hayo, sasa natamka kuwa Ndege Mbili aina ya Bombadier Dash 8 Q400 zitakazotumiwa na Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) kutoa huduma ya usafiri wa anga nchini zimezinduliwa rasmi.
Mungu Ibariki ATCL!
Mugu Ibariki Tanzania!
‘Ahsanteni kwa kunisikiliza”
- Sep 08, 2016
HOTUBA YA MHESHIMIWA DKT. JOHN POMBE MAGUFULI, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA NA MWENYEKITI WA WAKUU WA NCHI WA JUMUIYA YA AFRIKA MASHARIKI WAKATI WA K...
Soma zaidiHotuba
Mheshimiwa Yoweri Kaguta Museveni, Rais wa Jamhuri ya Uganda;
Mheshimiwa Paul Kagame, Rais wa Jamhuri ya Rwanda;
Mheshimiwa William Ruto, Naibu Rais wa Jamhuri ya Kenya;
Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar
na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi;
Mheshimiwa Alain Aime Nyamitwe, Waziri wa Mambo
ya Nje wa Jamhuri ya Burundi;
Mheshimiwa Aggrey Tisa Sabuni, Mjumbe Maalum na
Mwakilishi wa Rais wa Sudan Kusini;
Mheshimiwa Balozi Dkt. Augustine Mahiga, Mwenyekiti
wa Baraza la Mawaziri wa EAC;
Waheshimiwa Mawaziri mliopo hapa;
Mheshimiwa Balozi Liberat Mfumukeko, Katibu Mkuu wa EAC;
Mheshimiwa Dan Kidega, Spika wa Bunge la Afrika Mashariki;
Mheshimiwa Jaji Dkt. Emmanuel Ugirashebuja,
Rais wa Mahakama ya Afrika Mashariki;
Waheshimiwa Makatibu Wakuu mliopo;
Waheshimiwa Mabalozi na Viongozi wa Taasisi za Kimataifa;
Wageni Waalikwa;
Mabibi na Mabwana;
Kwa niaba ya Serikali na Wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ninayo furaha kubwa kuwakaribisha wageni wote hapa nchini kwetu na hususan katika Jiji hili la Dar es Salaam. Kipekee kabisa, napenda kuwashukuru kwa dhati kabisa, Viongozi Wenzangu kwa kukubali mwaliko wangu wa kuhudhuria Mkutano huu Maalum. Uwepo wenu hapa leo ni ishara tosha ya mshikamano uliopo katika Jumuiya yetu. Aidha, huu ni uthibitisho wa azma tuliyonayo sisi viongozi wa Jumuiya kuhakikisha ukanda wetu unakuwa na amani, utulivu na maendeleo.
Kabla sijaendelea, napenda kutumia fursa hii pia kuipongeza Sekretarieti ya Jumuiya yetu chini ya uongozi mahiri wa Balozi Liberat Mfumukeko kwa maandalizi mazuri ya Mkutano huu. Sote tunafahamu, huu ni Mkutano wa Kwanza wa Jumuiya yetu unafanyika tangu Balozi Mfumukeko kuanza kazi ya Ukatibu Mkuu wa Jumuiya yetu hapo mwezi Aprili mwaka huu. Lakini kwa kile ambacho tumeshuhudia mpaka sasa, ni dhahiri kuwa Balozi Mfumukeko anastahili pongezi nyingi. Rai yangu kwake aendeleze mwanzo huu mzuri ili kuleta maendeleo kwa wananchi wetu na Jumuiya yetu kwa ujumla.
Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;
Mkutano huu Maalum unafanyika kwa ajili ya shughuli mahsusi. Kwa hakika, tumekutana hapa kujadili ajenda tatu muhimu kwa maendeleo ya Jumuiya yetu. Ajenda hizo ni: Ripoti ya Baraza la Mawaziri kuhusu masuala yanayohusu Sudan Kusini; Ripoti ya Rais Mstaafu Benjamini Mkapa ambaye ni Msuluhishi wa Mgogoro wa Burundi; na Ripoti ya Baraza la Mawaziri kuhusu Mkataba wa Ushirikiano wa Kiuchumi kati ya Jumuiya yetu na Jumuiya ya Ulaya. Napenda kutumia fursa hii, kupongeza kazi nzuri iliyofanywa na Baraza letu la Mawaziri wa Jumuiya chini ya Mwenyekiti wake Balozi Dkt. Mahiga katika kuandaa Mkutano huu. Mmefanya kazi kubwa sana na kwa hakika, mmeturahisishia sana kazi yetu katika Mkutano huu.
Waheshimiwa Viongozi, Mabibi na Mabwana;
Kama mnavyofahamu, Mkutano wa Kawaida wa 17 wa Wakuu wa Nchi wa Jumuiya yetu uliofanyika Arusha tarehe 2 Machi, 2016 kwa kauli moja ulipitisha uamuzi wa kukubali ombi la Sudan Kusini kuwa mwanachama wa Jumuiya yetu. Kulingana na uamuzi huo, tarehe 15 Aprili, 2016 katika ukumbi huu huu, mimi kwa wadhifa wangu wa Uenyekiti wa Jumuiya nikiwa pamoja na Mheshimiwa Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini, tulisaini Mkataba wa Sudan Kusini kujiunga na Jumuiya. Baada ya hapo, Serikali ya Sudan Kusini imewasilisha Hati ya Kuridhia (Instrument of ratification) Mkataba kwenye Sekretarieti ya Jumuiya. Hiyo inamaanisha kuwa hivi sasa nchi ya Sudan Kusini ni mwanachama kamili, mwenye haki zote na wajibu katika Jumuiya yetu. Nimeambiwa kuwa Sekretarieti kwa sasa inakamilisha Mpango Kazi kwa ajili ya kuiwezesha nchi hiyo kujumuishwa kwenye mipango na miradi ya Jumuiya.
Kwa niaba ya Jumuiya, napenda kwa mara nyingine tena kuipongeza Sudan Kusini kuwa mwanachama kamili wa Jumuiya yetu. Kwa heshima ya tukio hili, naomba tuwapongeze kaka na dada zetu wa Sudan Kusini kwa kupiga makofi mengi kufuatia nchi yao kujiunga rasmi kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Pamoja na furaha kubwa tuliyo nayo kuikaribisha Sudan Kusini kwenye Jumuiya, wananchi wa Afrika Mashariki tulishtushwa na kuhuzunishwa sana na taarifa za kuibuka upya kwa mapigano nchini humo. Napenda kutumia fursa hii, kuwaomba viongozi na wananchi wa Sudan Kusini kwa ujumla kuweka maslahi ya taifa lao mbele ili kumaliza mgogoro nchini humo. Suala hili ni muhimu sana kwa sababu kuimarika kwa amani na usalama kutaleta manufaa kwa wananchi wa nchi hiyo na kwenye ukanda wetu wote. Ni kwa sababu hii, napongeza kazi kubwa iliyofanywa na IGAD kurejesha amani na utulivu nchini Sudan Kusini. Na kwa bahati nzuri, nchi nyingi za Jumuiya yetu ni wanachama wa IGAD. Hivyo basi, nina uhakika kuwepo kwao katika IGAD, kumewezesha na kutaendelea kuwezesha mawazo na maoni yetu kuwasilishwa vizuri kwenye usuluhishi wa mgogoro huo.
Waheshimiwa Viongozi, Mabibi na Mabwana;
Kuhusiana na Burundi, kama ambavyo sote tunafahamu vizuri, nchi hiyo imekuwa kwenye mgogoro wa kisiasa kwa kipindi cha zaidi ya mwaka mmoja hivi sasa. Mgogoro huo umesababisha madhara mengi, ikiwa ni pamoja na kupoteza maisha ya wananchi wasio na hatia. Napenda kutumia fursa hii, kwa niaba ya Jumuiya, kutuma tena salamu nyingi za pole na rambirambi kwa Serikali, ndugu na wananchi wote wa Burundi kufuatia kifo cha mwakilishi wao kwenye Bunge la Afrika Mashariki, Marehemu Hafsa Mossi, aliyeuawa tarehe 13 Julai, 2016. Tunamwomba Mwenyezi Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi. Amina.
Licha ya changamoto zinazoendelea kuikabili Burundi, Jumuiya yetu imeendelea na jitihada za kurejesha amani nchini humo. Hii ndiyo sababu, katika Mkutano wetu wa 17 uliofanyika mwezi Machi 2016 mjini Arusha, tulimteua Rais Mstaafu wa Tanzania, Mheshimiwa Benjamin William Mkapa kuwa Mpatanishi wa Mazungumzo ya Amani ya Burundi. Mpatanishi amefanya mikutano kadhaa mjini Arusha na Brussels nchini Ubelgiji kwa kuwakutanisha wadau wakubwa katika mgogoro wa Burundi. Leo tumepokea Taarifa ya Msuluhishi ambayo imetoa mapendekezo kadhaa ya kumaliza mgogoro. Tumeyapokea na kuyakubali mapendekezo yote. Lakini kwa ujumla tu naweza kusema kuwa Taarifa tuliyoipokea inatoa matumaini ya kurejea kwa amani nchini Burundi.
Nampongeza kwa dhati Mheshimiwa Rais Mstaafu Benjamin Mkapa kwa jitihada zake za kuhakikisha amani ya kudumu inapatikana nchini Burundi. Nawahimiza wahusika nchini Burundi kutoa ushirikiano wa kutosha kwa Mpatanishi (Facilitator) na halikadhalika kwa Msuluhishi (Mediator), Rais Yoweri Kaguta Museveni wa Uganda. Niwaombe pia viongozi wenzangu wote tuendelee kutoa michango yetu ya hali na mali kuwasaidia ndugu zetu wa Burundi. Kurejea kwa amani nchini Burundi, kutawezesha Wana-Burundi kuelekeza nguvu zao kwenye shughuli za maendeleo kwa manufaa ya nchi yao na Jumuiya yetu kwa ujumla. Nitumie fursa hii pia, kuiomba Jumuiya ya Kimataifa kusaidia na kuunga mkono jitihada mbalimbali zinazofanywa na Msuluhishi.
Waheshimiwa Viongozi, Mabibi na Mabwana;
Naomba sasa nieleze suala la Mkataba wa Ubia wa Biashara kati ya Jumuiya yetu na Jumuiya ya Ulaya (EAC-EAC Economic Partnership Agreement – EPA). Kama mnavyofahamu, EPAs ni Mikataba ya Biashara baina ya Jumuiya ya Ulaya na nchi kutoka Afrika, Caribbean na Pacific. Lengo kuu la mikataba hii ni kuwezesha nchi maskini kutoka Afrika, Caribbean na Pacific kuingia kwenye uchumi wa dunia. Malengo mahususi ya EPA, ni kukuza ushirikiano wa kikanda, biashara ya bidhaa na maendeleo.
Majadiliano kati ya EAC na EU yalianza mwaka 2007. Majadiliano haya yalikamilika kwa kupatikana kwa EAC-EU-EPA, ambayo ilitarajiwa kukasainiwa mwaka huu. Kusainiwa na kuridhiwa kwa Mkataba huu, kutawezesha bidhaa kutoka Jumuiya ya Ulaya kuingia kwenye soko la Afrika Mashariki bila vikwazo chochote (free-access) na kwa upande wetu tutanufaika na viwango vya chini vya tozo (tariffs) zitakazotozwa bidhaa zitakazoingia kwenye soko la Jumuiya ya Ulaya. Napenda kukiri kuwa suala hili la EPA limechukua muda mwingi wa majadiliano yetu leo. Lilikuwa ni suala gumu kidogo.
Katika majadiliano yetu, yapo maswali mengi ambayo tulijiuliza, hususan kuhusu nini kitatokea au athari zipi zitatupata endapo Jumuiya yetu itasaini EPA. Baadhi ya maswali tuliyojiuliza ni haya yafuatayo:
Moja, Ni kwa namna gani Jumuiya yetu itaweza kulinda viwanda vya ndani na kukuza sekta ya viwanda katika mazingira ya ushindani mkubwa utakaotokana na kuruhusiwa kwa bidhaa nyingi za viwandani kutoka Jumuiya ya Ulaya kuingia katika soko la jumuiya yetu? Mathalan, Tanzania inalenga kujenga uchumi wa viwanda, lakini kupitia EPA, Tanzania italazimika kufungua soko lake kwa bidhaa nyingi za viwandani kutoka Jumuiya ya Ulaya. Je ufunguaji huu mkubwa wa soko letu kwa bidhaa kutoka Jumuiya ya Ulaya ambazo zimetengenezwa kwa gharama ya chini na teknolojia ya kisasa utakuwa na athari gani katika harakati za nchi yetu na Jumuiya yetu kwa ujumla kujenga na kukuza uchumi wa viwanda?
Pili, Je ni kwa namna gani tutaweza kuzuia Jumuiya yetu isigeuzwe kuwa soko la bidhaa za kilimo kutoka Ulaya? Na ni njia zipi tutazitumia kuwalinda wakulima wetu na sekta yetu ya kilimo kwa ujumla, ambayo kwa sasa ndiyo sekta kuu ya uchumi katika nchi zetu, hasa kwa kuzingatia ruzuku kubwa inayotolewa na Serikali za Ulaya kwa wakulima wake na pia kutokana na matumizi ya dhana za kisasa zinazotumiwa na wakulima wa Ulaya?
Tatu, Ni kwa namna gani tutaweza kukabiliana na tatizo la kukosekana kwa urari wa biashara kwa upande wetu, unaotokana na sisi kuendelea kuuza bidhaa ghafi kwenye soko la Ulaya?
Nne, Je, ni kwa namna gani nchi zetu katika Jumuiya zitaweza kuziba pengo la kuondoka kwa mapato ya kodi ambayo hivi sasa tunakusanya kutokana na bidhaa zinazoingia kutoka kwenye Jumuiya ya Ulaya? Mathalan, utafiti uliofanywa na Shirika la Utafiti wa Masuala ya Uchumi na Jamii (the Economic and Social Research Foundation) mwaka 2009 ulibainisha kuwa endapo Tanzania itatia saini EPA itapoteza takriban asilimia 45 ya mapato kutoka Jumuiya ya Ulaya katika kipindi cha miaka 20 tangu kusainiwa kwa EPA.
Tano, Je ni kwa kiwango gani uamuzi wa Uingereza kujitoa kwenye EU utaathiri EPA hasa kwa kuzingatia kuwa Uingereza ilikuwa ni soko kubwa la bidhaa nyingi kutoka kwenye Jumuiya yetu? Kwa mfano, takwimu zinaonesha kuwa kati ya bidhaa zote ambazo Tanzania ilipeleka katika Jumuiya ya Ulaya katika kipindi cha mwaka 2002 hadi 2014, asilimia 21 ya bidhaa hizo zilikwenda kwenye soko la Uingereza. Aidha, kwa mujibu wa takwimu nilizonazo, asilimia 28 ya bidhaa zote kutoka Kenya kwenda kwenye Jumuiya ya Ulaya zinauzwa kwenye soko la Uingereza. Tulijiuliza pia kama nchi za Marekani na Canada zimeanza kutafakari upya ushirikiano wake wa kibiashara na Jumuiya ya Ulaya baada ya uamuzi wa Uingereza kujitoa, iwejesisi tusitafakari suala hili?
Sita, Je ni namna gani tutaweza kushughulikia suala la Upendeleo Maalum (Most Favoured Nations Clause), ambapo katika Ibara 15 (2) ya EPA, nchi za EAC zinazuiwa kuingia kwenye ushirikiano wa kibiashara au kutoa upendeleo maalum kwa nchi zinazoibukia kiuchumi ambazo hazina ushirikiao na kiuchumi na Jumuiya ya Ulaya? Kipengele hiki kinakwenda kinyume na malengo ya kipengele wezeshi (Enabling clause) cha Shirika la Biashara Duniani (World Trade Organization) ambacho kinahimiza kutolewa kwa upendeleo maalum kwa nchi zinazoendelea na ushirikiano wa nchi za Kusini (South South Cooperation);
Saba, Je takwa la kwamba nchi za EAC zitoe fursa sawa za EPA kwa nchi na jumuiya zote zenye Mikataba ya Forodha na Jumuiya Ulaya lina athari gani kwa nchi zetu?
Nane; Je ni kwa namna gani tutashughulia suala la kukosekana kwa uhuru wa kisera katika kuweka kodi (Restrictions on Duties and Taxes on Exports)? Kama tunavyofahamu, kodi na tozo kwa bidhaa kwenda nje, hususan tozo kwenye bidhaa ghafi, ni njia mojawapo ya kuimarisha sekta ya viwanda na upatikanaji wa ajira. Kodi na tozo za namna hii kwa kiasi fulani zinawalazimisha wasafirishaji wa bidhaa ghafi kwenda nje kuongezea thamani bidhaa zao kabla ya kuzisafirisha kwenda nje ya nchi. Aidha, tozo na kodi hizo zinasaidia kuhakikisha uwepo usalama wa chakula katika nchi. Sasa je, uhuru wa kuweka kodi hizo ukiondoka kama ambavyo EPA inaelekeza, tutawezaje kusimamia suala la uongezaji thamani wa bidhaa ghafi kwenda nje na pia kuhakikisha usalama wa chakula katika nchi zetu?
Tisa, Ni njia zipi zitatumika kuzisaidia nchi ambazo, kwa kuendelea kubaki kwenye EPA, itathibitika dhahiri kuwa maslahi yake yanaathirika kwa kiwango kikubwa na hasa kwa kuzingatia kuwa EPA hautoi fursa kwa nchi moja peke yake kujitoa? (Mkataba unaitambua Jumuiya);
Kumi, Ipo haja gani kwa Burundi kusaini EPA wakati imewekewa vikwazo vya biashara na Jumuiya ya Ulaya?
Kwa hakika tulijiuliza maswali mengi na mjadala ulikuwa mzito. Lakini kama ilivyo kawaida katika Jumuiya yetu, kila linapotokea jambo lenye maslahi makubwa kwetu sote, hata kama ni ugumu kiasi gani, tumekuwa na utaratibu wa kufanya mazungumzo na mashauriano na hatimaye kuweza kufikia muafaka. Na wakati mwingine, hata kama tukishidwa kupata muafaka wa pamoja, tumekuwa tukitafuta njia ambayo itatusaidia kupata ufumbuzi. Kwa mara nyingine tena leo tumedhihirisha umoja na mshikamano wetu.
Baada ya mazungumzo ya marefu tuliyoyafanya kwa njia ya urafiki na uwazi mkubwa, tumeweza kupata njia ya kushughulikia suala la EPA. Mambo muhimu tuliyokubaliana kuhusu suala hili ni, kwanza, kujipa muda wa miezi mitatu kufanya mazungumzo zaidi kati yetu kwa lengo la kupata ufumbuzi na muafaka. Pili, kuiomba Jumuiya ya Ulaya kutoiadhibu Kenya kwa kuanza kutoza kodi bidhaa zake zitakazoingia kwenye soko lake ifikapo mwezi Januari 2017. Tatu, tumeiagiza Sekretarieti kuwasilisha uamuzi huu kwenye Jumuiya ya Ulaya. Na nne, baada ya miezi mitatu, tutakutana tena ili kufanya uamuzi wa pamoja wa Jumuiya yetu kuhusu suala la EPA. Haya ndiyo maamuzi yetu na nina imani Jumuiya ya Ulaya itatuelewa na kuyazingatia maombi yetu.
Waheshimiwa Viongozi;
Wageni Waalikwa;
Mabibi na Mabwana;
Itakuwa si jambo la busara kwangu kuhitimisha hotuba yangu bila kutoa pongezi zangu nyingi na za dhati kabisa kwa Mheshimiwa Christophe Bavivamo kutoka Rwanda, ambaye amechaguliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu mpya wa Jumuiya yetu. Nakupongeza sana Mheshimiwa Bavivamo. Nina imani kuwa mawazo, maono, mtazamo na uzoefu mpya unaokuja nao, utasaidia kusukuma mbele gurudumu la maendeleo katika jumuiya yetu. Kwa niaba ya Jumuiya, nakuahidi ushirikiano wa kutosha katika kutekeleza majukumu yako mapya ya Naibu Katibu Mkuu wa Sekretarieti ya Jumuiya.
Baada ya kusema hayo, naomba kuwakaribisha tena hapa nchini kwetu na nina imani kubwa kuwa, kwa muda mfupi mtakaokuwepo, mtalifurahia Jiji letu la Dar es Salaam.
“Ahsanteni sana kwa kunisikiliza”
- Jul 23, 2016
HOTUBA YA MHE. DKT. JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA NA MWENYEKITI WA CHAMA CHA MAPINDUZI KWENYE MKUTANO MKUU WA TAIFA WA...
Soma zaidiHotuba
Ndugu Mwenyekiti Mstaafu, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete;
Mzee Ali Hassan Mwinyi na Mzee Benjamini William Mkapa, Wenyeviti Wastaafu wa CCM;
Makamu Wenyeviti wa CCM, Dkt. Ali Mohamed Shein (kwa upande wa Zanzibar) na Mzee Philip Japhet Mangula (upande wa Tanzania Bara);
Makamu Wenyeviti Wastaafu mliopo hapa, Waasisi/Wazee Wastaafu wa CCM;
Katibu Mkuu, Ndugu Abdulrahman Kinana;
Wajumbe wa Kamati Kuu;
Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa;
Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa;
Viongozi wa Jumuiya mbalimbali za Chama;
Waheshimiwa Viongozi wa Vyama vya Siasa mliopo;
Waheshimiwa Mabalozi na Wawakilishi wa Taasisi mbalimbali za Kimataifa mliopo;
Wageni waalikwa, Mabibi na Mabwana:
KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI!
Awali ya yote, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutupa uzima na kutukutanisha hapa tukiwa na afya njema. Leo ni siku muhimu na ya kihistoria katika maisha yangu na kwa Chama chetu kwa ujumla. Ni siku ambayo wanaCCM kwa mara nyingine mmedhihirisha imani yenu kwangu kwa kunichagua kwa kura za kishindo kuwa Mwenyekiti wa Tano wa Chama chetu. Nawashukuru sana kwa heshima kubwa mliyonipatia na nawathibitishia kuwa nimeipokea heshima hii kwa moyo mkunjufu na unyeyekevu mkubwa.
Natambua kuwa jukumu mlilonipa siyo rahisi. Ni jukumu kubwa na zito. Lakini nina imani nitaliweza. Nitaliweza kwa sababu kwanza siko peke yangu. Nipo na ninyi wanaCCM wenzangu. Kwa kushirikiana nanyi tutatekeleza jukumu hili kwa pamoja. Pili, naamini nitaweza kwa sababu, uzuri wa Chama chetu ni kuwa kinaendeshwa kwa mujibu wa Katiba, Sheria, Kanuni na Taratibu. Hivyo, kwa kutumia miongozo hiyo nina imani kubwa kuwa kazi yangu haitakuwa ngumu. Jambo la muhimu itakuwa ni kufuata miongozo hiyo. Tatu, naamini nitaweza kwa sababu mimi siyo mgeni katika Chama. Nimekuwa mwanachama mwadilifu na mwaminifu wa CCM kwa takriban miaka arobaini, kipindi ambacho kimeniwezesha kukijua Chama. Najua kilikotoka, kinavyoendeshwa na wapi kinapaswa kuelekea. Hivyo basi, naahidi kutumia uwezo na uzoefu wangu wote kutekeleza majukumu yangu ya Chama na kamwe sitawaangusha.
Ndugu Mwenyekiti Mstaaf;
Ndugu Viongozi na WanaCCM wenzangu;
Sisi binadamu tumeumbwa kuwa watu wa kushukuru hasa tunapotendewa mambo mema na mazuri na wenzetu. Tukio hili la leo linatokea takriban mwaka mmoja tangu mliponichagua na kuniteua kuipeperusha Bendera ya Chama chetu katika kinyang’anyiro cha Urais kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana. Hata baada ya kunichagua, hamkuniacha peke yangu. Mliambatana na mimi bega kwa bega katika kipindi chote cha kampeni ili kuhakikisha Chama chetu kinaibuka na ushindi. Sote tunafahamu, Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana ulikuwa na ushindani na changamoto nyingi. Hata hivyo, tulishirikiana na kushikamana na hatimaye Chama chetu kilipata ushindi mkubwa na mimi kuchaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa hakika ushindi tulioupata ni matokeo ya juhudi za pamoja za wanaCCM wote. Binafsi najiona kuwa ni mwenye deni kubwa sana kwenu wanaCCM na Watanzania kwa ujumla. Sina cha kuwalipa. Lakini itoshe tu kusema kuwa nawashukuru sana, tena sana, kwa ushirikiano mkubwa mlionipa wanaCCM wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana. Kupitia kwenu, nawashukuru Watanzania wote wa vyama vyote, dini zote na makabila yote kwa kunichagua kuwa Rais wa Awamu ya Tano wa nchi yetu.
Nafahamu wakati wa kutoa shukrani si vizuri sana kutaja majina au kumshukuru mtu mmoja mmoja. Hii ni kwa sababu unaweza kumsahau mtu muhimu akajisikia vibaya. Hata hivyo, naomba mniruhusu niwashukuru angalau wachache kwa kuwataja majina.
Katika maisha yangu siwezi kusahau mchango mkubwa wa Mzee Ali Hassan Mwinyi. Mzee Mwinyi akiwa Mwenyekiti wa CCM ndiye alisimamia kikao cha Chama kilichoniteua mimi kwa mara ya kwanza kugombea Ubunge wa Jimbo la Biharamulo Mashariki mwaka 1995. Kama Mzee Mwinyi angekata jina langu siku ile, huenda leo mimi nisingekuwa hapa. Nakushuruku sana Mzee wangu Mwinyi maana huo ulikuwa ndiyo mwanzo wa safari yangu ya uongozi. Pili, ninamshukuru pia Mzee Benjamini William Mkapa ambaye aliniteua kuwa Naibu Waziri wa Ujenzi mwaka 1995 mara tu baada ya kuchaguliwa kuwa Mbunge. Mwaka 2000 akiwa Mwenyekiti wa CCM aliniteua kugombea Ubunge na nilipochaguliwa alinifanya kuwa Waziri kamili wa ujenzi hadi mwaka 2005. Nashukuru kwa kuniamini na kunipa nafasi ya kugombea Ubunge na kuniteua kwa nafasi ya Uwaziri tena bado nikiwa na umri mdogo. Mzee Mkapa ahsante sana.
Ninamshukuru Mzee Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete ambaye aliendelea kunilea katika uongozi kwa kuniteua kuwa Waziri wa Wizara mbalimbali, ikiwemo Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi; Wizara ya Mifugo na Maendeleo ya Uvuvi pamoja na Wizara ya Ujenzi. Kwa Mzee Kikwete mbali ya kupitisha jina langu kugombea Ubunge wakati akiwa Mwenyekiti wa CCM mwaka 2010 aliamua kujitishwa mzigo mzito wa kusimamia mchakato wote wa kumpata Mgombea Urais 2015, akaniamini hadi kuteuliwa na mikutano husika ya CCM. Kwa Mzee Kikwete pia nimejifunza mambo mengi lakini kubwa zaidi ni uvumilivu na ustamilivu. Nasema kwa dhati kabisa kuwa Mzee huyu ni mvumilivu na mstamilivu sana. Amesemwa mambo mengi kwa ajili yangu. Nakumbuka mara kadhaa aliniomba kunikabidhi Uenyekiti wa Chama lakini mimi nilikataa. Baadhi ya watu wakamzushia maneno kuwa ameng’ang’ania Uenyekiti lakini alibaki kimya. Binafsi sitasahau siku ile ya uteuzi wangu kuwa Mgombea Urais wa Chama chetu. Nakumbuka namna ambavyo baadhi ya wanachama walionesha utovu mkubwa wa nidhamu kwake lakini alibaki kuwa mtulivu na akashirikiana na viongozi wa Chama hatimaye mchakato wa kupata mgombea Urais ulikamilika kwa amani. Ni viongozi wachache wenye uvumilivu na ustahimilivu wa namna hii. Binafsi sina cha kumlipa zaidi ya kutoa ahadi ya kufanya kazi kwa bidii ili kumuenzi.
Mbali na viongozi hawa wakuu watatu, napenda pia kuwashukuru Makamu Mwenyekiti (Bara) Mzee Mangula; Makamu Mwenyekiti Zanzibar, Dkt. Shein; Katibu Mkuu Mzee Kinana; Manaibu Makatibu Wakuu kwa upande wa Bara na Zanzibar; Wazee Waasisi wa CCM upande wa Tanzania Bara na Zanzibar, Wajumbe wa Kamati Kuu na Halmashauri Kuu; Wajumbe wa Mkutano Mkuu na WanaCCM wote kwa kuonesha imani mkubwa kwangu. Naahidi nitaendelea kuwaenzi na kutafuta ushauri wenu katika uongozi wangu. Wazee pamoja na viongozi wengi wa CCM wameishi na kuona mengi katika uongozi. Sisi viongozi wa leo hatuna budi kuiga na kudumisha mambo mema kutoka kwenu. Ahsanteni sana WanaCCM wenzangu.
Ndugu Mwenyekiti Mstaafu;
Ndugu WanaCCM wenzangu;
Chama chetu ni kikongwe siyo tu hapa nchini bali pia Barani Afrika na duniani kwa ujumla. Mwakani kitafikisha miaka arobaini (40) tangu kilipozaliwa kufuatia kuunganishwa kwa vyama mama vilivyopigania uhuru wa nchi yetu vya TANU na Afro Shiraz Party. Mtakubaliana nami kuwa katika kipindi cha takriban miaka 40 ya uhai wake, Chama chetu kimepata mafanikio mengi. Kwa haraka haraka, nitaje baadhi ya mafanikio ya chama chetu, mengine yametajwa na Mwenyekiti Mstaafu:
- Kwanza, tumeendelea kuongoza dola ambalo ni lengo kuu la chama chochote cha siasa. Watanzania wameendelea kutuamini kwa kutupa dhamana kubwa ya kuongoza nchi yetu tangu mwaka 1977 wakati nchi yetu ilikuwa ikiendeshwa kwa mfumo wa chama kimoja hadi sasa katika mfumo wa vyama vingi ulioanza mwaka 1992;
- Pili, Chama chetu kimeendelea kuwa chama kinachoaminiwa katika Afrika na duniani kote kama chama kinachotetea na kinachoendelea kutetea uhuru, umoja na mshikamano kwa vyama vingine vya ukombozi katika Afrika na duniani kote.
- Tatu, Chama chetu kimeendelea kulinda na kudumisha Muungano wa nchi yetu. Muungano wetu upo tena ni imara na umebaki kuwa imara na mfano wa kuigwa duniani. Nitaendelea kuulinda Muungano huu kwa nguvu zangu zote;
- Nne, tumelinda na kudumisha amani na utulivu pamoja na umoja na mshikamano wa nchi yetu. Tanzania imeendelea kuwa kisiwa cha amani na watu wake ni wamoja licha ya tofauti za kisiasa, dini, kabila au maeneo wanakotoka;
- Tano, tumeendelea kuwaongoza Watanzania katika harakati za kuleta maendeleo katika nyanja za kiuchumi, kisiasa na kijamii kufuatana na mabadiliko mbalimbali yanayojitokeza ndani na nje ya nchi. Hali ya maisha ya Watanzania hivi sasa ni bora Zaidi kuliko ilivyokuwa mwaka 1977; na
- Sita, tumelea na kukuza demokrasia nchini. CCM kimeendelea kuwa babu na bibi, baba na mama, lakini pia kaka na dada wa vyama vyote nchini.
Kwa hakika haya ni mafanikio makubwa ya wanaCCM na Watanzania kwa ujumla. Wahenga husema “usione vyaelea, vimeundwa”. Hivyo basi, kila mwanaCCM hana budi kutembea kifua mbele na kujivunia mafanikio tuliyoyapata. Lakini hatupaswi kubweteka kwa vile bado tuna kazi kubwa ya kuhakikisha Watanzania wanapata maendeleo zaidi. Moja ya azimio la Mkutano Mkuu wa Taifa wa Pamoja wa TANU na Afro Shiraz Party uliofanyika mjini Dar es Salaam tarehe 21 Januari, 1977 wakati wa kuunganisha vyama vya TANU na Afro Shiraz Party na kuzaliwa kwa CCM lilikuwa, napenda kunukuu “Chama tunachokiunda tunataka kiwe chombo madhubuti katika muundo wake na hasa katika fikra zake na vitendo vya kimapinduzi vya kufutilia mbali aina zote za unyonyaji nchini, kupambana na jaribio lolote lile la mtu kumwonea mtu au shirika au chombo cha nchi kuonea na kudhalilisha wananchi, kudhoofisha uchumi au kuzorotesha maendeleo ya Taifa”, mwisho wa kunukuu. Endapo tukitathmini na kutafakari kwa kina azimio hili la tarehe 21 Januari, 1977, bila shaka mtakubaliana nami kuwa, licha ya mafanikio makubwa yaliyopatikana, bado Chama chetu na nchi yetu inakabiliwa na changamoto.
Changamoto hizo ni pamoja na kuendelea kwa tatizo la umaskini; ukosefu wa ajira; kuendelea kwa vitendo vya dhuluma, ufisadi, rushwa, ubadhirifu wa mali za umma; na pia kukosekana kwa huduma bora zaidi za kijamii, ikiwemo elimu, afya, maji na umeme. Hivyo basi, Chama chetu hakina budi kujipanga vizuri na kuchukua hatua mahsusi za kutatua changamoto zinazowakabili wananchi na taifa letu kwa ujumla. Tukishindwa kutatua changamoto hizo na kutimiza matarajio ya wananchi, tutapoteza mvuto na Watanzania watakosa imani na sisi. Hatupaswi kuruhusu hali hii kujitokeza. Tanzania imara na yenye mafanikio inatutegemea sisi.
Ndugu WanaCCM wenzangu;
Katika kipindi changu cha uongozi nimedhamiria kushirikiana na viongozi, watendaji na kila mwanachama katika ngazi zote ili kuhakikisha Chama chetu kinakuwa imara zaidi. Kwa kushirikiana nanyi, nitafanya kila jitihada kuhakikisha Chama chetu kinakwenda sambamba na hali ya sasa lakini bila kuathiri misingi madhubuti iliyojengwa na waasisi na viongozi wetu waliotangulia, yaani Baba wa Taifa letu, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Hayati Mzee Abeid Amani Karume. Ili kutekeleza azma hiyo natarajia kufanya mambo yafuatayo kwa kushirikiana nanyi:
Kwanza, Kuimarisha utendaji kazi wa Chama. Suala la kuimarisha utendaji wa chama ni muhimu sana. Kama alivyokuwa akisema Baba wa Taifa letu Mwalimu Nyerere kuwa “Chama legelege huzaa Serikali legelege”. Nitashirikiana nanyi kujenga Chama madhubuti chenye uwezo wa kuisimamia vizuri Serikali ili itekeleze ipasavyo majukumu yake, ikiwezekana tutapitia upya Katiba na Kanuni zetu ili kukidhi mazingira ya sasa na kuweza kuwatumikia wananchi ipasavyo. Sisi wanaCCM ndiyo tumepewa dhamana na Watanzania kuongoza nchi yetu hivyo tunao wajibu wa msingi wa kuisimamia vizuri Serikali ili itatekeleza majukumu yake ipasavyo. Tutahakikisha pia tunakuwa na safu bora ya uongozi katika ngazi zote kuanzia Shina hadi Taifa. Tutaangalia muundo (structure) wa Chama chetu katika ngazi mbalimbali na kuondoa vyeo visivyokuwa na tija katika Chama na hasa wakati huu wa mfumo wa vyama vingi. WanaCCM ni lazima tujiulize je ni kweli katika zama hizi bado tunahitaji mtoto wa miaka 8 hadi 15 kuwa chipukizi kwa ajili ya kumtumia kwenye siasa badala ya kumwacha asome? Kama akiwepo chipukizi wa CCM, chipukizi wa NCCR au Chadema ama TLP tutakuwa tunajenga nchi ya namna gani? Je bado kuna umuhimu wa kuwa na Makamanda wa Vijana ambao mara nyingi wenye kupewa vyeo hivyo ni wale wenye uwezo wa kifedha pekee? Je walezi kwenye Umoja wa Wanawake (UWT) bado wanahitajika? Je Washauri ndani ya Jumuiya ya Wazazi wanahitajika? Hii ni mifano tu. Tujiulize vyeo hivi vinawasaidiaje wananchi wa kawaida vijijini katika kutatua kero za ukosefu wa maji, barabara, madawati, huduma za afya n.k. Je si kweli vyeo hivi badala ya kutatua migogoro ya wananchi vimekuwa vyanzo vya migogoro ndani ya Chama hasa nyakati chaguzi zinapokaribia? Ni vyema basi wanaCCM tukatafakari na kujipima upya. Ni vyema sisi tuwe mfano wa kuongoza mabadiliko katika nchi yetu. Tutaziimarisha Jumuiya zetu za Chama yaani Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), Umoja wa Vijana CCM (UVCCM), na Jumuiya ya Wazazi kwa nguvu zote. Tutahakikisha tunakuwa na watendaji wenye sifa zinazohitajika sasa, wachapakazi na waadilifu. Nafahamu ili watendaji wafanye kazi vizuri wanahitaji maslahi bora na mazingira mazuri ya kufanya kazi. Nataka niwahakikishie kuwa tutafanya hivyo. Sitapenda kuona watendaji wetu wanakuwa ombaomba. Kwa bahati nzuri, Chama chetu kina rasilimali nyingi. Tutahakikisha rasilimali hizo zinatumika kwa manufaa ya Chama. Na hapa napenda kusema kuwa tutaunda kikosi kazi maalum kwa ajili ya kutambua na kuhakiki mali zote za Chama, tujue zinatumikaje, kina nani wanazitumia na mapato yanayoingia kwenye Chama ni kiasi gani. Hivyo, nitoe wito kwa Katibu Mkuu (CCM) nitakayemteua, Makatibu wote wa Mikoa, Wilaya, Kata hadi vijiji pamoja na viongozi wote wa Jumuiya za Chama kuorodhesha mali za Chama katika maeneo yao. Aidha, tutawahimiza wanachama wetu kulipa ada zao za kila mwaka tena kwa njia ya kieletroniki. Nina imani, tukiwa na safu bora ya uongozi, watendaji wa chama wachapakazi na waadilifu pamoja na rasilimali za kutosha, Chama chetu kitaweza kutekeleza majukumu yake vizuri, ikiwa ni pamoja na kuisimamia vyema Serikali.
Pili, Kuongeza idadi ya wanachama, wapenzi na mashabiki. Siasa ni mchezo wa idadi (Politics is a game of numbers). Nawapongeza Wenyeviti wa CCM wastaafu kwa jitihada kubwa mlizozifanya ya kuongeza wanachama, ambapo hivi sasa idadi yake inakaribia kuwa milioni 8.7. Chini ya uongozi wangu pia tutajitahidi kuongeza idadi ya wanachama, wapenzi na mashabiki. Tunahitaji kuwa na idadi kubwa ya watu kwenye upande wetu kwa ajili ya kuongeza idadi ya wanachama. Tunahitaji watu kwa ajili ya kupiga kura. Lakini kubwa zaidi, tunawahitaji watu kwa ajili ya kushiriki kwenye shughuli mbali za kimaendeleo. Hivyo basi, nitashirikiana nanyi katika kuhakikisha idadi ya wanachama, wapenzi na washabiki wa Chama chetu inaongezeka, hususan kwa kuvutia kundi la vijana. Na njia bora na rahisi ya kuwavuta watu kwenye Chama chetu ni kuhakikisha tunatekeleza ahadi zetu na wakati huo huo sisi viongozi na wanachama tujitahidi kuwa mfano bora wa kuigwa kwenye maeneo yetu, kwa maneno na vitendo vyetu.
Tatu, kuzidisha mapambano dhidi ya Rushwa, Ufisadi na upungufu wa maadili ya uongozi. Rushwa ni adui wa haki. Kwa kutambua hilo, Ibara ya 9 (h) na Ibara 132 (5)c ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania imekataza vitendo vya rushwa. Aidha, Ahadi namba 3 ya Mwanachama wa CCM inasema “Rushwa ni adui wa haki, sitapokea wala kutoa rushwa”. Vilevile, Kifungu Na. 18 (2) cha Katiba ya CCM inaeleza kuwa “itakuwa mwiko kwa kiongozi kupokea mapato ya kificho, kutoa au kupokea rushwa”.
Licha ya kuwepo kwa makatazo hayo ya kisheria na maadili, tatizo la rushwa bado ni kubwa hapa nchini. Cha kusikitisha zaidi ni kwamba Chama chetu CCM ni miongoni mwa taasisi ambazo tatizo la rushwa ni kubwa. Ni lazima niseme ukweli. Sisi sote ni mashahidi wa jinsi ambavyo tatizo hilo limekuwa likikiathiri Chama chetu na hasa nyakati za chaguzi mbalimbali ndani ya Chama. Mara nyingi fedha imekuwa kigezo cha mtu kupata uongozi. Mimi binafsi nilishuhudia hili wakati wa kinyang’anyiro cha kuwania nafasi ya kuwa Mgombea Urais kupitia Chama chetu mwaka jana. Vitendo vya rushwa vilikithiri sana. Vitendo vya rushwa vimesababisha Chama chetu kupoteza nafasi za Ubunge kwenye baadhi ya majimbo. Waingereza wana msemo usemao “You can’t give what you don’t have” (Huwezi kutoa usichokuwa nacho). Hii maana yake ni kwamba hatuwezi kuondoa tatizo la rushwa nchini kama sisi wenyewe wanaCCM tutakuwa tukiikumbatia rushwa. Hivyo basi, katika kipindi cha uongozi wangu wa Chama nimedhamiria kushirikiana nanyi katika kuhakikisha tunalikomesha tatizo hilo. Mtu yeyote atakayetumia rushwa kutafuta uongozi hataupata kamwe. Kwa bahati nzuri, Chama chetu kinazo Kanuni za Uongozi na Maadili ambazo zinaelekeza hatua za kuchukua kwa wanachama watakaokiuka maadili ya Chama. Mathalan, katika kupambana na rushwa wakati wa chaguzi mbalimbali za Chama, Kifungu Namba 6 (1) cha Kanuni za Uongozi na Maadili Toleo la Mwaka 2012 zinaelekeza kuwa Kiongozi yeyote atakayethibitika kuwa ameshinda uchaguzi kutokana na kitendo chochote cha rushwa atanyang’anywa ushindi alioupata na pia atazuiwa kugombea tena uchaguzi mwingine wowote kwa muda utakaoamuliwa na Halmashauri Kuu ya Taifa. Hivyo basi, kwa kuwa mwakani Chama chetu kitafanya Uchaguzi wa Viongozi wa ngazi mbalimbali, niwaombe wanaCCM wenzangu tuoneshe mfano kwenye uchaguzi huo kwa kujiepusha na vitendo vya rushwa, ikiwemo kutoa na kukusanya michango, misaada na zawadi kinyume cha taratibu za Chama; kununua kadi za wanachama; kuanza kampeni kabla ya muda uliowekwa rasmi, kutoa takrima n.k. Kwa atakayefanya vitendo hivyo, Chama chini ya uongozi wangu hakitamwonea aibu wala huruma. Nitahakikisha tunasimamia Katiba, Kanuni na Maadili ya Chama chetu ukurasa kwa ukurasa; kifungu kwa kifungu na kipengele kwa kipengele lengo likiwa ni kuhakikisha tunaendelea kuaminiwa na Watanzania.
Nne, Kukomesha Usaliti ndani ya Chama. Katika uongozi wangu nitahakikisha kuwa suala la usaliti ndani ya Chama linakomeshwa. Ndani ya Chama chetu pamekuwa na tabia kwa baadhi ya wanaCCM kusaliti Chama, asubuhi anakuwa CCM, usiku yuko Chama kingine. Wasaliti wa namna hii hawatakuwa na nafasi wakati wa uongozi wangu. Kama wapo wenye tabia wenye tabia hii ni vyema wakajirekebisha na kutubu kuanzia leo. La sivyo watupishe na kuondoka hata leo. Ni vyema kuishi na mchawi kuliko kukaa kuwa na msaliti. Tunahitaji kuwa na wanachama waadilifu wanaofuata Katiba, Kanuni na Maadili ya Chama chetu na siyo kuwa na wanachama ndumilakuwili. Hatuwahitaji wanachama ndumilakuwili ndani ya CCM. Hatuhitaji CCM pandikizi na wanaCCM maslahi ambao wapo CCM kwa sababu wanamwabudu mtu fulani kwa maslahi yao binafsi. Ninahitaji wanaCCM ambao siku zote, usiku na mchana; mvua na jua; njaa na shibe watabaki CCM bila kuyumba. Hiyo ndiyo CCM ya waasisi wetu Mwalimu Nyerere na Mzee Karume ninayoijua mimi.
Mimi ninaamini kama tukishirikiana katika kutekeleza mambo yote haya na mengineyo ambayo sikuyataja, Chama chetu kitaimarika na Watanzania wataendelea kutuunga mkono na kutuamini. Binafsi nataka kuona CCM inakuwa ya watu hasa wanyonge na si CCM ya viongozi pekee. Nataka CCM inayoaminika na si CCM inayodharaulika. Nataka CCM ya kufanya kazi na si CCM ya kuomba omba. Na pia nataka CCM inayojitegemea na si CCM inayotegemea wafadhili. Na kwa kuwa ninyi Wajumbe wa Mkutano Mkuu (chombo cha juu kabisa cha uamuzi katika Chama) mmenipa kazi hii, ninakwenda kufanya haya yote kwa niaba yenu.
Ndugu Viongozi na Ndugu WanaCCM wenzangu;
Wakati wa Kampeni za Uchaguzi Mkuu mwaka jana tulinadi Ilani yetu ya Uchaguzi ya Mwaka 2015 – 2020. Kwenye Ilani yetu tualiahidi mambo mengi. Tuliwaahidi Watanzania kuwa tutadumisha Muungano, amani na mshikamano wa nchi yetu. Tuliwaahidi kuboresha maisha yao. Tuliahidi kuboresha huduma za jamii, hususan afya, elimu na maji. Tuliwaahidi kujenga uchumi wa viwanda ili kukabiliana na tatizo la umaskini na ukosefu wa ajira. Tuliwahidi kuwaondolea kero mbalimbali ikiwemo rushwa, uonevu na dhuluma. Tuliwaahidi kuwa tutasimamia vizuri rasilimali za nchi. Tuliwaahidi kuimarisha miundombinu, hususan ya barabara, reli, bandari, nishati, usafiri wa anga, usafiri wa meli n.k. Watanzania walituamini na wakatupa tena ridhaa ya kuongoza nchi. Ndugu zangu wanaCCM ahadi ni deni. Ni lazima tutekeleze yale yote tuliyowaahidi kwenye Ilani yetu ya uchaguzi ili tuweze kujihakikishia tena ushindi kwenye Uchaguzi wa Mwaka 2020. Rais Mstaafu Mzee Mkapa alipata kusema “Mwisho wa Uchaguzi mmoja ndio mwanzo wa maandalizi ya uchaguzi mwingine”. Hivyo, ni lazima tujiandae.
Tangu Serikali ya Awamu ya Tano imeingia madarakani mpaka sasa imepita takriban miezi nane. Nafarijika kuwa katika kipindi hicho, tayari tumeanza kutekeleza baadhi ya mambo ambayo tumewaahidi Watanzania. Mambo hayo ni pamoja na utoaji wa elimu bure ambapo kila mwezi tunatenga bilioni 18.77. Hii imewezesha kuongeza wanafunzi waliojiandikisha darasa la kwanza kufikia milioni 1.9 mwaka 2016 kutoka milioni 1.02 mwaka 2015. Tumenunua ndege mpya mbili kutoka nchini Canada na zinatarajiwa kuwasili nchini mwezi Sepemba 2016. Tumeingia makubaliano na Serikali ya Uganda kujenga Bomba la Kusafirisha mafuta kutoka Hoima nchini Uganda hadi Bandari ya Tanga lenye urefu wa takriban kilometa 1,400 na linatarajiwa kutoa ajira zaidi ya 20,000 wakati wa ujenzi. Tumetangaza zabuni ili kuanza ujenzi wa reli mpya ya kisasa ya kiwango cha kimataifa (standard gauge) kutoka Dar es Salaam kwenda mikoa ya Mwanza na Kigoma na baadaye kuunganika na nchi za Rwanda na Burundi, ambapo katika bajeti ya mwaka huu (2016/2017) tumetenga Shilingi trilioni 1 kuanza ujenzi. Tumeongeza fedha za bajeti ya maendeleo kutoka asilimia 26 mwaka wa fedha 2015/2016 hadi asilimia 40 katika mwaka huu wa fedha (2016/2017). Tumeimarisha nidhamu ya watumishi wa umma, tumewaondoa watumishi hewa takriban 12,500 na bado tunaendelea kuwaondoa. Tumedhibiti matumizi ya Serikali na kuongeza ukusanyaji wa mapato hadi kufikia wastani wa shilingi trilioni 1.3 kwa mwezi. Licha ya hatua hizo tulizozichukua, ni dhahiri kuwa bado tuna safari ndefu katika kutimiza yale tuliyowaahidi Watanzania. Hivyo basi, napenda kutumia hadhara hii kuwaomba wanaCCM wenzangu kushirikiana kwa karibu na Serikali katika kuhakikisha ahadi zote tulizowaahidi wananchi wakati wa kipindi cha kampeni zinatekelezwa.
Mojawapo ya njia ya kuhakikisha ahadi zetu zinatekelezwa ni kwa sisi wanaCCM kujitahidi kufahamu mipango na mikakati mbalimbali ya Serikali. Mathalan, hivi karibuni tumepitisha Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano utakaotekelezwa kuanzia Mwaka 2016/2017 hadi 2020/2021. Mpango huu umejumuisha masuala yote tuliyoahidi kwenye Ilani yetu na umeainisha maeneo ya kipaumbele ya Serikali katika kipindi cha miaka mitano ijayo. Utekelezaji wa Mpango huu wa Maendeleo umeanza mwaka huu wa fedha ambapo Serikali imepanga kutumia kiasi cha Shilingi trilioni 29.5. Katika fedha hizo, asilimia 40 tumezielekeza kwenye shughuli za maendeleo, ikiwemo kujenga miundombinu wezeshi ya uchumi (miundombinu ya usafiri na nishati), kuboresha huduma za jamii, kama vile afya, elimu na maji n.k.
Naamini kama tutaifahamu na kuilewa vizuri mipango ya Serikali itakuwa rahisi kwetu kuwahamasisha wananchi wetu kushiriki kikamilifu kwenye shughuli za maendeleo, kama vile kilimo na ujenzi wa viwanda. Tutaweza pia kuwahamasisha kulipa kodi kwa ajili ya kugharamia mambo mbalimbali ya maendeleo ambayo Serikali imepanga kutekeleza. Bila kulipa kodi itatuwia vigumu kutekeleza ahadi tulizowaahidi wananchi. Aidha, kama tunaifahamu vizuri mipango ya Serikali tutaweza kufuatilia kwa karibu utekelezaji wake kwenye maeneo yetu, hususan kwenye halmashauri ambako fedha nyingi za Serikali zinaelekezwa. Hivyo basi, niombe kila mmoja wetu awe mtekelezaji wa kwanza wa Ilani ya Uchaguzi 2015 kwa kufanya kazi na pia kuwahamasisha Watanzania katika shughuli za maendeleo.
Ndugu Mwenyekiti Mstaafu;
Ndugu WanaCCM;
Wageni Waalikwa;
Mabibi na Mabwana;
Leo tupo Dodoma kushiriki kwenye Mkutano Mkuu Maalum wa CCM. Napenda kutumia mkutano huu kueleza masuala mengine mawili ya ziada. Jambo la kwanza. Hapa Dodoma ndio Makao Makuu ya Chama chetu pamoja na Serikali. Dodoma pia ni mji uliopo katikati ya nchi yetu. Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limekuwa likifanya vikao vyake hapa. Hata Chuo Kikuu kikubwa zaidi nchini kipo hapa Dodoma. Aidha, nimeamua maadhimisho ya Sherehe za Mashujaa mwaka huu yafanyike hapa Dodoma.
Hivyo basi, kwa kutambua umuhimu wa Dodoma na pia katika kutekeleza ndoto ya Baba wa Taifa letu, Hayati Mwalimu Nyerere ya kuhamishia Makao Makuu ya Serikali hapa Dodoma, napenda kutamka mbele ya Mkutano huu kuwa katika kipindi cha miaka mitano ya uongozi wangu, nitahakikisha kuwa Serikali inahamia hapa Dodoma. Nitoe wito kwa Mawaziri na watendaji wengine wa Serikali kujipanga kuhamia Dodoma. Hapa Dodoma kuna miundombinu ya kutosha hivyo naamini hapatokea visingizizio vya aina yoyote.
Jambo la pili ambalo napenda kulieleza ni kwamba leo hii nimepokea barua kutoka kwa Katibu Mkuu wa Chama chetu, Mzee Kinana. Barua hiyo imeeleza azma ya Mzee Kinana pamoja na wajumbe wote wa Sekretarieti ya sasa kutaka kujiuzulu ili kunipa nafasi ya kuunda Sekretarieti mpya. Baada ya kutafakari kwa kina maudhui ya barua hiyo na kuangalia majukumu makubwa yaliyopo mbele yetu, nimeamua kuwa Sekretarieti ya sasa chini ya Mzee Kinana iendelee. Kama kutakuwa na haja ya kufanya mabadiliko, nitaitisha Kikao cha Halmashauri Kuu kujadili suala hilo. Kwa sababu hiyo, kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa kilichopangwa kufanyika kesho kujadili suala hili hakitafanyika.
Ndugu Mwenyekiti Mstaafu;
Ndugu Viongozi;
Ndugu Wajumbe wa Mkutano Mkuu Taifa;
Wageni Waalikwa;
Mabibi na Mabwana;
Nafasi niliyopewa leo ni ya kutoa shukrani. Nafahamu tutapata fursa nyingine ya kuzungumza nanyi kwenye vikao na mikutano yetu kwa ajili ya kupeana mipango na mikakati mbalimbali ya kuimarisha Chama chetu na kuleta maendeleo kwa nchi yetu. Kwa sababu hiyo ningependa kuishia hapa. Hata hivyo, nitakuwa ni mnyimi wa fadhila kama nitahitimisha hotuba yangu bila kuwashukuru wageni wetu. Kwanza kabisa nawashukuru wawakilishi wa vyama vya siasa vya hapa nchini mliopo. Mmeonesha ukomavu mkubwa wa kisiasa. Siasa siyo uadui. Sisi sote ni Watanzania hivyo hatuna budi kudumisha umoja na mshikamano wa nchi yetu. Tuweke kando tofauti zetu za kisiasa na tushirikiane kwa pamoja kujenga nchi yetu. Maendeleo hayana vyama.
Nawashukuru pia wawakilishi wa vyama rafiki kutoka nje pamoja na Mabalozi mnaowakilisha nchi na taasisi mbalimbali za kimataifa mliopo hapa. Nawashukuru sana kwa kuja kujumuika nasi kwenye tukio hili la kihistoria. Napenda kuwahakikishia kuwa Chama cha Mapinduzi chini ya uongozi wangu, kitaendelea kushirikiana nanyi katika ngazi ya Chama na Serikali.
Aidha, napenda kuwashukuru watumishi wote wa Sekretarieti ya Chama chini ya kiongozi imara, mahiri na shupavu, Mzee Kinana, kwa kufanikisha mkutano huu. Mzee Kinana wewe kweli ni kiongozi. Sote tunafahamu kazi kubwa na nzuri iliyofanywa na Mzee Kinana tangu alipopewa nafasi ya Ukatibu Mkuu. Mara hii tena ameingoza Sekretarieti na kufanikisha Mkutano Mkuu huu Maalum. Nawashukuru pia Manaibu Makatibu Wakuu wa Bara na Zanzibar. Aidha, nazishukuru Kamati mbalimbali zilizoratibu maandalizi ya mkutano huu. Mmefanya kazi kubwa na nzuri.
Kwa namna ya pekee kabisa navishukuru vyombo vya ulinzi na usalama kwa kazi kubwa mliyoifanya ya kuhakikisha Mkutano huu unafanyika katika mazingira ya amani na usalama. Vilevile, nawashukuru ndugu zetu waandishi wa habari kwa kazi kubwa mliyoifanya ya kuripoti Mkutano wetu. Katibu Mkuu alipokuwa akitoa taarifa jana wakati wa Mkutano wa Halmashauri Kuu alisema waandishi wa habari walioomba kuripoti Mkutano huu ni 200 lakini nimeambiwa walijitokeza ni takriban 400. Hii inadhihirisha ukongwe na ukubwa wa Chama Cha Mapinduzi.
Halikadhalika, nawashukuru watoa huduma mbalimbali wa kwenye mkutano huu wahudumu, madereva pamoja na wenyeji wetu, wana-Dodoma kwa ukarimu wenu mkubwa mliotuonesha katika kipindi chote cha mkutano. Ahsanteni sana. Ninawashukuru pia Watanzania wote wakiwemo viongozi wa dini mbalimbali kwa kuendelea kuniombea mimi na taifa kwa ujumla. Navishukuru vikundi vya burudani vikiongozwa na Kikundi chetu cha Tanzania One Theatre (TOT) kwa kutuburudisha kwa nyimbo zenu maridadi.
Napenda kuhitimisha hotuba yangu kwa kurudia tena kutoa shukrani zangu nyingi kwa wanaCCM wenzangu kwa kunipa heshima kubwa ya kunichagua kwa kura nyingi kuwa Mwenyekiti wenu. Ombi langu kwenu, tuzidi kushirikiana katika kuimarisha Chama chetu ili Watanzania waendelee kutuamini. Uchaguzi uliopita umetudhihirishia kuwa penye umoja ushindi ni lazima. Hivyo, tuendeleze umoja wetu na tujiepushe kumtegemea mtu au kikundi cha watu wachache katika kufanya mambo yetu. Kila mara tukumbuke usemi wa Mwenyekiti wetu mstaafu, Mzee Kikwete, usemao: Chama kwanza, Mtu baadaye“. Chama chetu ni kikubwa. Tuna hazina kubwa ya viongozi wastaafu. Hivyo, tuendelee kushirikiana katika kuwatumikia Watanzania ili waendelee kutuamini.
Baada ya kusema hayo, namshukuru tena Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kumaliza Mkutano wetu salama na nawatakia kila mmoja wetu safari njema wakati tutakapokuwa tukirejea majumbani kwetu.
Mungu Kibariki Chama cha Mapinduzi
Mungu Ibariki Tanzania
Kidumu Chama Cha Mapinduzi“
“HAPA KAZI TU“
Ahsanteni kwa kunisikiliza“
- Jul 13, 2016
DONDOO KWENYE HAFLA YA UTOAJI WA MADAWATI YALIYOTOLEWA NA BUNGE LA TANZANIA VIWANJA VYA KARIMJEE, DAR ES SALAAM, 13 JULAI 2016
Soma zaidiHotuba
Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson, Naibu Spika wa Bunge la Tanzania;
Waheshimiwa Wajumbe wa Tume ya Bunge;
Waheshimiwa Mawaziri mliopo;
Mheshimiwa Paul Makonda, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam;
Waheshimiwa Wabunge mliopo;
Mheshimiwa Mstahiki Meya wa Jiji la Dar es Salaam;
Katibu wa Bunge pamoja na Watumishi wote wa Bunge;
Wageni waalikwa;
Mabibi na mabwana:
Nianze kwa kukushukuru Mheshimiwa Naibu Spika pamoja na uongozi mzima wa Bunge la Jamhuri ya Muungano kwa kunialika katika hafla hii ya ugawaji wa madawati. Aidha, nawashukuru wageni waalikwa wote pamoja na wananchi kwa ujumla kwa kujitokeza kwa wingi kushuhudia tukio hili muhimu na la kimaendeleo. Nimefurahi sana kuona kuwa miongoni mwetu hapa tupo viongozi wa vyama mbalimbali. Hivi ndivyo tunapaswa kuijenga nchi yetu. Tanzania ni yetu sote. Hivyo basi, kwa pamoja hatuna budi kushikamana katika kutatua changamoto zinazokabili Taifa letu. Maendeleo hayana chama.
Nitumie fursa hii pia, kwa kipekee kabisa, kuwashukuru Mheshimiwa Spika, Naibu Spika, Wenyeviti wa Kamati za Bunge pamoja na Wabunge wote wa Bunge la Jamhuri ya Muungano kwa uamuzi wenu wa kubana matumizi na kuweza kuokoa kiasi cha takriban shilingi bilioni 6. Aidha, nawashukuru kwa kuridhia wito wangu wa kuelekeza fedha hizo katika utengenezaji wa madawati. Kama mnavyofahamu, kufuatia uamuzi wa Serikali kuanza kutoa Elimumsingi bila malipo, idadi ya wanafunzi imeongezeka maradufu na hivyo kuibua tatizo la uhaba wa madawati katika shule zetu. Hivyo, madawati haya yaliyotengenezwa kutokana na uamuzi wenu wa kubana matumizi utasaidia kupunguza changamoto ya hii ya uhaba wa madawati.
Mheshimiwa Naibu Spika;
Waheshimiwa Wabunge;
Wageni Waalikwa;
Mabibi na Mabwana;
Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2015 -2020 iliahidi kuwa endapo Mgombea wake angeshinda, Elimumsingi, yaani darasa la kwanza hadi kidato cha nne, ingetolewa bila malipo. Bahati nzuri wananchi walituelewa na kutuchagua. Na kama usemi wa wahenga usemavyo, ahadi ni deni. Baada ya kuchaguliwa tu, Serikali ilianza mara moja kutekeleza ahadi ya kutoa elimumsingi bila malipo. Tangu mwezi Januari 2016, tumekuwa tukitenga shilingi bilioni 18.77 kila mwezi kwa ajili ya kugharamia elimu bila malipo, hususan ada, michango mbalimbali na ruzuku. Nafurahi utekelezaji wa elimumsingi bila malipo umeleta matokeo chanya. Idadi ya wanafuzi waliodahiliwa, hususan darasa la kwanza, imeongezeka maradufu kutoka wanafunzi 1,028,021 mwaka 2015 hadi kufikia 1,896,584 mwaka huu. Ongezeko hili ni sawa na asilimia 84.5.
Kama ilivyo kawaida jambo zuri lolote halikosi changamoto. Vivyo hivyo kutokana na kuongezeka kwa idadi ya wanafunzi, zimeibuka changamoto kadhaa kwenye shule zetu: uhaba wa madawati, vyumba vya madarasa na vyoo. Hata hivyo, tatizo la uhaba wa madawati lilijitokeza zaidi, ambapo upungufu wa madawati kwa shule za msingi na sekondari kwa ujumla ilikuwa madawati 1,355,398. Kati yake shule za msingi pekee upungufu ulikuwa ni madawati 1,166,548 na shule za sekondari 188,850.
Kwa kutambua ukubwa wa tatizo hilo, tarehe 15 Machi wakati nikiwaapisha Wakuu wa Mikoa niliwaagiza kushirikiana na Wakurugenzi wa Halmashauri na Wakuu wa Wilaya kuhakikisha wanatatua tatizo hilo la madawati. Aidha, mara kadhaa katika mikutano yangu ya hadhara nimekuwa nikiomba taasisi na mashirika ya umma na binafsi, vikundi na watu binafsi kuunga mkono jitihada za Serikali za kutatua tatizo hili la madawati.
Nafarijika kuona kuwa juhudi zetu zimezaa matunda. Hadi sasa hivi, zaidi ya madawati milioni moja, sawa na asilimia 88 ya mahitaji ya madawati kwa shule za msingi yametengenezwa na kwa shule za sekondari madawati yaliyotengenezwa ni asilimia 95.8. Jambo la kufurahisha zaidi ni kwamba halmashauri 25 zimeweza kufikia malengo kwa upande wa shule za msingi na halmashauri 46 kwa upande wa sekondari. Nawapongeza Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Viongozi wa Halmashauri hizo pamoja na wadau wote wa maeneo hayo kwa kufanikisha zoezi hilo. Navipongeza pia vyombo vya Habari, hususan Redio, Magazeti pamoja na vituo vya televisheni vya Channel Ten, TBC, Star Tv, Azam, ITV na Clouds kwa kuhamasisha wadau, taasisi na wananchi kuchangia zoezi hili la madawati. Nawashukuru wadau wote waliojitokeza kuchangia.
Mheshimiwa Naibu Spika;
Mabibi na Mabwana;
Kama nilivyodokeza hapo awali, fedha ambazo Bunge lilinikabidhi kwa kubana matumizi ni shilingi bilioni 6. Kutokana na fedha hizi, tunatarajia kutengeneza madawati takribani laki moja na ishirini, kwa gharama ya shilingi elfu hamsini kwa kila moja. Kwa kuzingatia umuhimu na uharaka wa zoezi hili, mara tu baada ya kukabidhiwa fedha hizi siku ile ya tarehe 11 Aprili, 2016 niliagiza kazi ya kutengeneza madawati wapewe Jeshi la Kujenga Taifa na Jeshi la Magereza. Leo nipo hapa kwa ajili ya hafla ya kugawa madawati 56,000 ya awamu ya kwanza kati ya madawati 60,000 ambayo yalitarajiwa kuwa yamekamilika kufikia tarehe 15 Julai, 2016. Nimeyaona madawati yaliyotengenezwa. Ni mazuri sana na yana ubora unaotakiwa. Nawapongezeni sana JKT na Magereza.
Pamoja na pongezi hizo, napenda niseme kwa wazi tu kuwa binafsi sijaridhishwa sana na kasi ya utengenezaji wa madawati haya. Kasi yake naiona ni ndogo sana, na hasa ukizingatia kuwa tunayo fedha na nguvu kazi ya kutosha. Watoto wetu wanateseka sana kwa kukaa chini na hivyo wanahitaji madawati haya kwa haraka. Ingefaa basi tuharakishe zoezi hili kwa kulifanya kuwa operesheni maalum. Nafahamu vyombo hivi vina uwezo mkubwa wa kukamilisha zoezi hili kwa haraka. Hivyo basi, nitoe wito kwa viongozi wa vyombo hivi kuhakikisha utengenezaji wa madawati haya unakamilika mapema iwezekanavyo.
Mheshimiwa Naibu Spika;
Waheshimiwa Wabunge;
Wageni Waalikwa;
Mabibi na Mabwana;
Kabla sijahitimisha hotuba yangu, napenda kurudia shukrani zangu nyingi kwa uongozi wa Bunge kwa msaada huu mkubwa wa madawati. Mchango wenu huu utapunguza sana kama sio kumaliza kabisa tatizo la madawati nchini. Niwaombe Waheshimiwa Wabunge mtakaokabidhiwa madawati haya leo mfikishe kwenye shule husika kwa wakati ili kuwawezesha watoto wetu kusoma katika mazigira mazuri.Nafahamu pamoja na jitihada zetu za kumaliza tatizo hili la madawati, bado shule zetu zinakabiliwa na changamoto nyingine, ikiwemo uhaba wa madarasa, ofisi za walimu na vyoo. Lakini kutokana na moyo ulioneshwa na Watanzania kote nchini katika zoezi hili la madawati, nina uhakika kabisa kuwa changamoto hizi nazo tutazimaliza.
Baada ya kusema hayo, napenda kuwashukuru wale wote walioshiriki katika kufanikisha tukio hili la leo la kukabidhi madawati yaliyotengenezwa na fedha za Bunge. Nawashukuru wananchi wote waliojitokeza kushuhudia tukio hili.
Mungu Ibariki Tanzania!
Mungu Libariki Bunge na Wabunge wote!
“Ahsanteni kwa kunisikiliza”.
- Jul 10, 2016
HOTUBA YA MHE. DKT, JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, WAKATI WA DHIFA YA KITAIFA ALIYOIANDAA KWA HESHIMA YA MHESHIMIWA NAREND...
Soma zaidiHotuba
Mheshimiwa Narendra Modi, Waziri Mkuu wa India;
Mheshimiwa Kassim Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Waheshimiwa Marais na Mawaziri Wakuu Wastaafu mliopo;
Waheshimiwa Mawaziri mliopo;
Waheshimiwa Mabalozi mliopo;
Waheshimiwa Viongozi wengine wa Serikali, Vyama na Dini mliopo;
Wageni Waalikwa;
Mabibi na Mabwana:
Awali ya yote, kwa niaba ya Serikali na Wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, napenda kukukaribisha Mheshimiwa Waziri Mkuu Narendra Modi pamoja na ujumbe wako hapa Dar es Salaam. Karibu sana nchini kwetu. Watanzania wengi walifurahi kusikia uamuzi wako wa kuijumuisha nchi yetu kwenye orodha ya nchi utakazozitembelea kwenye ziara yako hii ya pili hapa Barani Afrika. Hivyo, kwa hakika, wamepokea ujio wako kwa mikono miwili na moyo mkunjufu. Tutajitahidi kuhakikisha sio tu kwamba unaifurahia ziara yako hapa nchini bali pia kuifanya iwe ya mafanikio makubwa.
Wageni Waalikwa;
Mabibi na Mabwana;
Licha ya umbali uliopo kati Tanzania na India, nchi zetu mbili zina uhusiano mzuri tena wa muda mrefu. Sio tu kwamba tunaunganishwa na Bahari ya Hindi, bali pia uhusiano wetu ni wa kihistoria na kidugu. Zaidi ya miaka 1,000 iliyopita, wafanyabiashara kutoka India wakitumia mashua na ngalawa waliingia hapa nchini kwa minajili ya kuendesha shughuli zao za kibiashara. Walifikia katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu, ikiwemo Zanzibar na Kilwa. Baadhi yao walifanya biashara na kurejea India lakini wapo, tena wengi tu, waliolowea hapa nchini. Hawakurudi tena India. Huenda hii ndio sababu, miongoni mwetu hapa leo tunao Wabunge Kumi (10) wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambao wana asili ya India.
Uhusiano wetu ulizidi kukua baada ya Tanzania kupata uhuru, ukichagizwa zaidi na urafiki mkubwa uliokuwepo kati ya Baba wa Taifa letu, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Hayati Jawaharlal Nehru, Waziri Mkuu wa India wa wakati huo. Chini ya viongozi hawa, Tanzania na India zilikuwa mstari wa mbele katika kupinga ukoloni na ubaguzi wa rangi, hususan katika Bara la Afrika. Mahusiano hayo yaliendelezwa na viongozi waliofuatia katika awamu zote za uongozi wa mataifa yetu mawili. Uhusiano huu mzuri pia upo kwenye anga za kimataifa, hususan kupitia Umoja wa Mataifa, Jumuiya ya Madola, Jumuiya ya Nchi zisizofugamana na Upande Wowote, Jumuiya ya Nchi zinazopakana na Bahari ya Hindi (Indian Ocean Rim Association for Regional Cooperation) na hivi karibuni kupitia Jukwaa la Afrika na India lililoanzishwa mwaka 2008, ambapo kwenye kikao kilichoanzisha Jukwaa hilo, Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne wa Tanzania, Mzee Kikwete, ambaye nafurahi tuko naye hapa, alikuwa Mwenyekiti Mwenza.
Mabibi na Mabwana;
Uhusiano wetu mzuri katika ngazi ya kitaifa na kimataifa umeziwezesha nchi zetu kushirikiana vizuri kiuchumi. Na kwa hakika, naweza kusema kuwa India ni mdau wetu mkuu wa biashara. Biashara kati ya nchi zetu mbili imekuwa ikikua kila mwaka. Mathalan, mauzo ya bidhaa zetu kwenda India yameongezeka kutoka Dola za Marekani milioni 187 mwaka 2009 hadi kufikia Dola za Marekani Bilioni 1.29 mwaka 2015. Jambo la kufurahisha zaidi ni kwamba, tofauti na nchi nyingi ambazo tunafanya nazo biashara, urari wa biashara na India pia ni mzuri. Mathalan, kati ya Dola za Marekani Bilioni 3.5 ambazo ndio jumla ya thamani ya mauzo ya biashara kati ya nchi zetu kwa mwaka 2015, thamani ya bidhaa kutoka India ni Dola za Marekani Bilioni 2.4 wakati thamani ya mauzo ya Tanzania nchini India ni Dola za Marekani Bilioni 1.29. Aidha, uwekezaji kutoka India ambao umesajiliwa na Kituo chetu cha Uwekezaji una thamani ya Dola za Marekani Bilioni 2.4 na umezalisha ajira 54,176.
Ni dhahiri kuwa haya ni mafanikio makubwa. Sisi Watanzania hatuna budi kujivunia uhusiano wetu mzuri na India. Nina imani kuwa ziara hii ya Mheshimiwa Waziri Mkuu Modi hapa nchini itaimarisha zaidi uhusiano na ushirikiano wetu katika masuala ya kiuchumi. Nafurahi kuwa katika kikao chetu na Waziri Mkuu leo asubuhi, tumekubaliana kuimarisha ushirikiano kwenye sekta mbalimbali, ikiwemo TEHAMA, kilimo, viwanda vidogo vidogo, elimu, afya, maji nk. Waziri Mkuu pia ameahidi kuwa India itatoa kiasi cha Dola za Marekani milioni 500 kusaidia miradi mbalimbali ya maendeleo hapa nchini. Lakini jambo la kutia moyo zaidi ni kwamba Mheshimiwa Waziri Mkuu katika ujumbe wake ameambatana na Wafanyabiashara takriban 50. Wafanyabiashara hao wamekutana na wenzao wa Tanzania asubuhi hii na sina shaka, siku chache zijazo tutaanza kuona mafanikio ya ziara hii.
Mheshimiwa Waziri Mkuu;
Ziara yako hapa nchini inafanyika wakati nchi yako ikielekea kuadhimisha miaka 70 ya Uhuru wake mwezi ujao. Bila shaka, wengi kama si wote waliopo hapa watakubaliana nami kuwa katika kipindi cha miaka 70 iliyopita, India imepata mafanikio makubwa sana. India hivi sasa ni miongoni mwa nchi ambazo uchumi wake unakuwa kwa kasi kubwa. Ni miongoni mwa nchi zinazokua kwa kasi kiviwanda. Lakini pia mmepiga hatua kubwa katika masuala ya sayansi na teknolojia, hususan teknolojia ya habari. Mafanikio haya hayakujileta bali yametokana na kazi kubwa na nzuri iliyofanywa na viongozi wa India, ukiwemo wewe Mheshimiwa Waziri Mkuu, kwa kushirikiana na wananchi wenu. Napenda kutumia fursa hii kupitia kwako Mheshimiwa Waziri Mkuu kuwapongeza wananchi wa India kwa miaka 70 ya Uhuru wenu na pia kwa mafanikio makubwa mliyoyapata.
Nchi nyingi kama si zote za Afrika zimenufaika sana na mafanikio ya India. Sisi Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizonufaika na mafanikio mliyoyapata katika nyanja za elimu, afya, maji, kilimo, TEHAMA n.k; kupitia ama misaada ya moja kwa moja au kwa njia ya ushirikiano. Lakini sambamba na kutunufaisha, mafanikio yenu yametupa fursa sisi Watanzania na Waafrika kwa ujumla kujifunza masuala mbalimbali, ikiwemo Programu zenu kama vile Skill India, Digital India, 100 Smart Cities na pia program mpya uliyoianzisha ya Make in India. Napenda kukiri kuwa binafsi nimevutiwa sana na program hii ya Make in India ambayo inahimiza uwekezaji kwenye sekta ya viwanda vyenye kutumia malighafi, wataalamu/nguvu kazi kutoka ndani ya nchi. Programu hii imenivutia kwa vile dhima yake inafanana sana na Mpango wa Pili wa Miaka Mitano wa Maendeleo wa nchi yetu, ambao unalenga kujenga uchumi wa viwanda. Viwanda tunavyovilenga katika Mpango huu ni vyenye kutumia malighafi za ndani, nguvu kazi kubwa na kuzalisha bidhaa zenye kutumika zaidi ndani ya nchi. Hivyo basi, naamini tutaweza kubadilishana uzoefu katika kutekeleza Mipango hii.
Mheshimiwa Makamu wa Rais;
Mheshimiwa Rais wa Zanzibar;
Mheshimiwa Waziri Mkuu;
Waheshimiwa Marais na Mawaziri Wakuu Wastaafu mliopo;;
Waheshimiwa Wageni Waalikwa mliopo;
Mabibi na Mabwana:
Kama nilivyodokeza hapo juu, leo asubuhi mimi na Waziri Mkuu tulipata fursa ya kufanya mazungumzo rasmi. Tumezugumza mambo mengi. Tumejadiliana kwa kirefu na kukubaliana namna ya kuboresha na kuimarisha uhusiano na ushirikiano kati ya nchi zetu. Kwa sababu hiyo, nisingependa kuwachosha kwa hotuba ndefu. Na kwa hakika hapa sio mahali muafaka pa kutoa hotuba ndefu. Tupo hapa kwa ajili ya kufurahi na mgeni wetu, Waziri Mkuu Narendra Modi, pamoja na kusheherekea uhusiano mzuri na wa muda mrefu kati ya India na Tanzania.
Hivyo basi, kwa heshima na taadhima, niwaombe sote kwa pamoja tusimame na kisha tunyanyue glasi zetu ili tufurahie na mgeni wetu:
- Kwa ajili ya afya nzuri ya Waziri Mkuu Narendra Modi;
- Kwa ajili ya urafiki na uhusiano mzuri kati ya Tanzania na India.
“Ahsanteni kwa kunisikiliza”.
- Jul 06, 2016
HOTUBA YA MHE. DKT. JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, KWENYE BARAZA LA EID-EL-FITR, DAR ES SALAAM, TAREHE 6 AU 7 JULAI, 2016
Soma zaidiHotuba
Mheshimiwa Sheikh Mkuu na Mufti wa Tanzania,
Sheikh Abubakar Zubeir Ally;
Mheshimiwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa;
Mheshimiwa Rais Mstaafu Mzee Ali Hassan Mwinyi;
Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya BAKWATA;
Wajumbe wa Baraza la Ulamaa;
Waheshimiwa Masheikh na Viongozi wa BAKWATA;
Waheshimiwa Viongozi wa Dini na
Madhehebu Mbalimbali;
Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa,
Viongozi wenzangu wa Chama na Serikali;
Ndugu wananchi;
Wageni waalikwa,
Mabibi na Mabwana;
Assalaam Eleykum!
Eid-Mubarak!
Napenda nianze kwa kuungana na wote walionitangulia kuzungumza katika kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa Rehema kwa kutupa uhai na kutuwezesha kushiriki katika Baraza la Idd la mwaka huu. Aidha, nakushukuru sana Mheshimiwa Sheikh Mkuu na Mufti wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zubeir Ally, kwa kunialika kuja kujumuika nanyi katika siku hii adhimu ya kuhitimisha Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani. Binafsi najiona kuwa ni mtu mwenye bahati sana kupewa heshima hii kubwa ya kuwa Mgeni Rasmi kwenye Baraza hili la Idd. Nakushukuru sana Sheikh Mkuu na Mufti Sheikh Zubeir pamoja na uongozi mzima wa BAKWATA.
Hii ni mara yangu ya kwanza nashiriki kwenye Baraza la Idd tangu nimechaguliwa kuwa Rais wa Awamu ya Tano wa nchi yetu. Hivyo basi, napenda kutumia fursa hii pia kuwashukuru Masheikh pamoja na Waislamu kote nchini kwa ushiriki wenu mzuri kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana. Mtakumbuka ya kuwa uchaguzi mkuu wa mwaka jana ulikuwa na ushindani mkali. Hata hivyo, kutokana na maombi yenu pamoja na sala za Watanzania wa imani nyingine tuliweza kumaliza Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana salama. Kwa sababu hiyo, napenda kuwashukuru sana kwa sala zenu zilizowezesha nchi yetu kumaliza uchaguzi salama. Aidha, nawashukuru kwa kunipigia kura kwa wingi kuwa Rais wenu wa Awamu ya Tano. Ahsanteni sana.
Kama mtakavyokumbuka wakati wa Kampeni niliahidi kuwa endapo ningelichaguliwa kuwa Rais wa Tanzania ningefanya kazi kwa manufaa ya Watanzania wote bila kujali tofauti zao za dini, kabila, itikadi au rangi. Nilirudia ahadi hiyo wakati nikizindua Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Napenda kurudia tena ahadi hiyo leo. Mimi ni Rais wa Watanzania wote. Sitambagua mtu kwa misingi ya dini, kabila, rangi ama itikadi ya chama. Nitafanya kazi kwa faida na manufaa ya Watanzania wote. Hiyo ni ahadi yangu kwenu ndugu zangu Waislamu na Watanzania wote kwa ujumla. Na nitaendelea kumwomba Mwenyezi Mungu anisaidie kutimiza ahadi hiyo.
Waheshimiwa Masheikh na Ndugu Waislamu;
Tupo hapa kuadhimisha Sikukuu ya Eid El Fitr. Siku hii ni muhimu sana sio tu hapa nchini bali duniani kwa ujumla. Ni siku ambayo Waislamu duniani kote wanasheherekea kumalizika kwa Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani. Ingawa mimi sio Sheikh na wala si mwanazuoni lakini nafahamu kuwa Funga ya Ramadhani ni moja ya nguzo tano za Uislamu. Katika kipindi cha Mfungo, Waislamu hujinyima mambo mbalimbali, ikiwemo kuacha kula na kunywa mchana kutwa. Vilevile, waislamu hufanya ibada, na kujitahidi kutenda mambo mema na kujizuia kufanya vitendo viovu. Aidha, katika kipindi cha Mfungo, waislamu hufanya tafakari ya kiroho na kumrudia Mwenyezi Mungu Muumba na kuomba msamaha kwa mapungufu mbalimbali ya kiimani. Kwa ujumla, Kipindi cha Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani ni kipindi ambacho Waislamu hujinyima na kujitoa kutenda matendo mema ya kumpendeza Mungu.
Kwa kuzingatia maudhui hayo, mtakubaliana nami kuwa kushiriki katika Ibada ya Funga ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani sio suala rahisi. Ni jambo gumu. Yeyote anayeshiriki katika Ibada hii anastahili pongezi. Hivyo basi, kwa niaba ya Serikali na kwa niaba yangu binafsi, napenda kuwapongeza Waislamu wote walioshiriki na kumaliza salama ibada ya Funga ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani. Nina imani kuwa Mwenyezi Mungu mwingi wa Rehema amezikubali funga zenu na kusamehe madhambi yenu yote. Tumwombe Mwenyezi Mungu azidi kutupa uhai ili tuweze kushiriki tena Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani mwaka ujao. Amina.
Ndugu Waislamu;
Wakati nikiwapongeza kwa kumaliza Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani mwaka huu, napenda pia kuungana na Masheikh walionitangulia kuzungumza kuwasihi kwamba ucha Mungu mliouonyesha katika kipindi hiki cha mwezi Mtukufu wa Ramadhani muuendeleze. Usiishie jana baada ya kuandama kwa mwezi. Endeleeni kutenda matendo mema yenye kumpendeza Mwenyezi Mungu. Jiepusheni kutenda matendo mabaya yenye kumchukiza Mwenyezi Mungu. Endeleeni kuwasaidia watu wenye shida mbalimbali.
Kwa kufanya hivyo, naamini baraka na neema za Mwenyezi Mungu Muumba tulizozipata kipindi cha Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani zitaendelea kudumu nasi daima. Zaidi ya hapo ni kwamba, endapo mtaendeleza matendo mema ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani na Watanzania wa imani nyingine nao wakitenda matendo yaliyo mema, tutaweza kwa pamoja kupunguza kama sio kuondoa kabisa baadhi ya changamoto zinazoikabili nchi yetu hivi sasa, ikiwemo wizi, ubinafsi, rushwa, ufisadi, ujambazi n.k.
Mheshimiwa Mufti,
Ndugu Waislamu na Wananchi kwa ujumla;
Sikukuu kama hizi, mbali ya kufurahi na kusheherekea, zinatupa pia fursa ya kujikumbusha mambo mbalimbali yanayohusu mustakabali na ustawi wa taifa letu. Sisi Watanzania tunayo mambo mengi ambayo kwa kutumia sherehe kama hizi tunaweza kuyatafakari na kujikumbusha. Moja ya mambo ni suala la amani katika nchi yetu. Nina uhakika kabisa kuwa katika kipindi cha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani mliiombea nchi yetu amani. Hilo ni jambo jema sana. Amani ni suala muhimu sana. Bila ya amani hakuna maendeleo. Waasisi na wazee wa nchi yetu waliweka msisitizo katika amani. Hivyo, sisi nasi hatuna budi kuenzi na kuitunza amani yetu kwa manufaa yetu na vizazi vijazo. Kwa sababu hiyo, napenda kuahidi kuwa Serikali ya Awamu ya Tano itafanya kila jitihada katika kuhakikisha amani na utulivu vinadumu nchini.
Mheshimiwa Mufti,
Waheshimiwa Masheikh na Ndugu Waislamu;
Pamoja na kuwaelimisha wananchi kiroho na kuwasaidia waumini kiimani, jukumu jingine la dini ni kushirikiana na Serikali katika kujenga umoja na mshikamano katika Taifa na pia kuletea maendeleo kwa wananchi. Nafurahi hapa nchini taasisi za dini zimekuwa zikitekeleza majukumu haya yote vizuri. Hivi punde tumesikia Risala kutoka kwa Katibu Mkuu wa BAKWATA, Sheikh Suleiman Saidi Lolila. Ni Risala iliyosheheni mambo mengi. Imeeleza mipango na mikakati mingi na mizuri ambayo BAKWATA chini ya Sheikh Mkuu na Mufti Sheikh Zubeir imeanza au inataka kutekeleza. Baadhi ya mipango hiyo ni pamoja na azma ya Mufti Sheikh Zubeir kutaka kuwaunganisha Waislamu nchini. Hili ni jambo jema ambalo kila mwenye nia njema na Uislamu hana budi kuunga mkono.
Hivyo basi, napenda kutumia fursa hii kumpongeza kwa dhati kabisa Mheshimiwa Mufti kwa jitihada zake za kujenga umoja na mshikamano miongoni mwa Waislamu nchi. Nimeambiwa kuwa katika sherehe za leo, Mufti amewaalika Waislamu wa madhehebu yote. Hili ni jambo jema sana. Mitume wote waliokuja duniani walihimiza umoja na mshikamano miongoni mwa wanadamu. Hivyo basi, nampongeza sana Mheshimiwa Mufti kwa hatua alizoanza kuzichukua. Hivi punde tu amenidokeza kuwa mwezi ujao (Agosti 2016), Kiongozi wa Mabohora Duniani atakuja nchini. Nimemhakikishia kuwa nitakuwa tayari kukutana na Mgeni huyo.
Sambamba na kujenga umoja na mshikamano miongoni mwa Waislamu, Risala imeeleza mikakati ya BAKWATA katika shughuli mbalimbali za kijamii, hususan kwenye sekta ya elimu. Hili nalo ni jambo zuri sana. Nafahamu hii itakuwa si mara ya kwanza kwa BAKWATA kujishughulisha kwenye shughuli za kijamii. Mnayo miradi mingi ya kijamii mnayoisimamia, ikiwemo kwenye sekta ya afya, elimu, maji n.k. Watanzania wengi wamenufaika na huduma za kijamii zinazotolewa na taasisi na mashirika ya dini na madhehebu mbalimbali. Tunawashukuru sana kwa mchango wenu na tunawaomba mzidi kuendelea kuwahudumia Watanzania, hasa wa kipato cha chini.
Kwa upande wetu Serikalini, tutaendelea kushirikiana nanyi na ikibidi tutakuwa tayari kutoa misaada inayohitajika ili kuwawezesha kutimiza malengo mliyojiwekea. Nakumbuka wakati fulani nikiwa Waziri wa Ardhi, viongozi wa BAKWATA waliwahi kufika ofisini kwangu kwa ajili ya kufuatilia viwanja. Baadhi ya viwanja vilikuwa kwenye migogoro kwa sababu baadhi ya watu walijimilikisha au kuingia kwenye mikataba isiyokuwa na maslahi kwa Waislamu. Hivyo basi, napenda kutumia fursa hii kuwahakikishia kuwa Serikali itashirikiana nanyi katika kuhakikisha watu waliodhulumu mali za Waislamu wananyang’anywa kwa mujibu wa sheria. Serikali kamwe haitaruhusu watu wachache, kwa maslahi yao binafsi, wanufaike na mali za waislamu. Mali za Waislamu ni lazima ziwanufaishe waislamu wenyewe na vivyo hivyo kwa madhehebu mengine.
Mheshimiwa Sheikh Mkuu;
Ndugu Waislamu na Wananchi kwa ujumla;
Hivi sasa ni takriban miezi saba imepita tangu Serikali ya Awamu ya Tano imeingia madarakani. Katika kipindi hicho, yapo baadhi ya mambo ambayo tayari tumeanza kutekeleza, ikiwemo utoaji wa elimu bure, kurudisha nidhamu ya watumishi wa umma, kudhibiti matumizi ya Serikali, kuongeza ukusanyaji wa mapato n.k. Pamoja na hatua hizo, ni dhahiri kuwa bado tuna safari ndefu katika kutimiza yale tuliyoyakusudia na tuliyowaahidi Watanzania. Naomba niwahakikishie kwamba dhamira ya kuwatumikia kwa nguvu zetu zote na kwa kutumia vipaji vyote tulivyojaaliwa na Mwenyezi Mungu bado tunayo. Sababu tunayo na uwezo tunao kwani mamlaka mmetukabidhi.
Nawashukuru viongozi na waumini wa dini zote nchini kwa kuendelea kutuunga mkono na kuiombea Serikali yetu na sisi viongozi wake ili tutimize vyema wajibu. Maombi yenu yanazidi kutupa hamasa ya kuendelea kufanya kazi kwa bidii zaidi. Nawaombeni mzidi kutuombea na kamwe msichoke. Sisi mliotukabidhi dhamana ya kuongoza nchi tumedhamiria kuleta maendeleo kwa nchi yetu. Nchi yetu ina utajiri mkubwa wa rasilimali na hivyo hatupaswi kuwa maskini. Sambamba na kutuombea na kuliombea taifa, tunawaomba pia mzidi kuwahimiza wananchi kufanya kazi kwa bidii na kushiriki kikamilifu kwenye shughuli za maendeleo, hususan katika kutekeleza Mpango wetu wa Maendeleo wa Miaka Mitano ambao utekelezaji wake umeanza mwezi Julai 2016. Tusipofanya kazi hatutapa fedha. Fedha haiwezi kuja bila kufanya kazi. Tutafurahi na kwa hakika tupo tayari kupokea ushauri wenu kuhusu masuala mbalimbali kwa lengo la kuipatia nchi yetu maendeleo. Tanzania ni yetu sote na hivyo kila mtu anao wajibu wa kutoa mchango.
Mheshimiwa Sheikh Mkuu;
Wajumbe wa Baraza Ulamaa;
Ndugu Waislamu na Wananchi kwa ujumla;
Leo ni sikukuu. Ni siku ya furaha. Ni siku ambayo naamini kila mmoja wetu hapa anatamani kuwepo nyumbani kwake ili kuweza kujumuika na familia yake katika kufurahia sikukuu hii. Kwa kuzingatia hilo, haitakuwa busara kwangu kuendelea kuwachosha kwa hotuba ndefu. Lakini kabla sijahitimisha napenda kutoa mchango wangu mdogo kwa kijana aliyesoma utenzi na ambaye nimeambiwa kuwa anatarajiwa kwenda nchini Urusi hivi karibuni. Aidha, naahidi mbele ya hadhara hii kuwa nitatoa mchango mdogo kwa ajili ya kufanikisha safari ya waumini watakaokwenda Hija mwaka huu.
Baada ya kusema hayo, napenda kukushukuru tena Mheshimiwa Sheikh Mkuu na Mufti wa Tanzania kwa kunialika ili nishiriki kwenye shughuli hii muhimu. Nakushuru sana kwa heshima hii kubwa uliyonipa. Nawatakia Waislam na Watanzania wote kwa jumla sherehe njema ya Iddi. Iwe ni sherehe yenye furaha na faraja tele. Wito wangu kwa Watanzania wote, tusheherekee sikukuu hii kwa amani na utulivu.
Mungu Ibariki Afrika
Mungu Ibariki Tanzania
Eid Mubarak!
Assalam Aleykum.
Asanteni Sana kwa kunisikiliza!
- Jun 25, 2016
HOTUBA YA MGENI RASMI, MHESHIMIWA DKT. JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA WAKATI WA UZINDUZI WA MPANGO WA KUBORESHA USALAMA WA...
Soma zaidiHotuba
Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete,
Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Mheshimiwa Mwigulu Lameck Nchemba (Mb),
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi;
Mheshimiwa Injinia Hamad Yusuf Masauni,
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani wa Nchi;
Mheshimiwa Balozi John Kijazi,
Katibu Mkuu Kiongozi
Mheshimiwa Paul Makonda, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam;
Mheshimiwa Dkt. Idris Jala, Mwakilishi wa Waziri Mkuu wa Malaysia;
Ndugu Ernest Jumbe Mangu, Inspekta Jenerali wa Polisi;
Wakuu wa vyombo vya Ulinzi na Usalama;
Ndugu Abdulrahman Kaniki, Naibu Inspekta Jenerali wa Polisi;
Ndugu Said Mwema, Inspekta Jenerali wa Polisi Mstaafu;
Waheshimiwa Viongozi mbalimbali;
Waheshimiwa Mabalozi mliopo;
Makamada na Makamishna wa Jeshi la Polisi;
Viongozi wa Taasisi mbalimbali mliopo hapa;
Viongozi wa siasa na dini mliopo hapa;
Ndugu askari wa vyeo mbalimbali wa Jeshi la Polisi mliopo hapa;
Wageni waalikwa;
Mabibi na mabwana:
Napenda nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutupa afya njema na kutuwezesha sisi sote kujumuika hapa hii leo. Aidha, natoa shukrani zangu za dhati kwa Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Inspekta Jenerali wa Polisi pamoja na uongozi mzima wa Jeshi la Polisi kwa kunipa heshima ya kuwa Mgeni Rasmi katika shughuli hii muhimu ya uzinduzi wa Mpango wa Usalama wa Jamii.
Vilevile, nawashukuru wageni waalikwa na wananchi kwa ujumla kwa kuja kushuhudia tukio hili. Wahenga husema, “shughuli ni watu”. Hivyo, kujitokeza kwenu kwa wingi hapa kumefanikisha shughuli hii muhimu na bila shaka ni uthibitisho tosha kuwa ninyi pia mnakerwa na vitendo vya uhalifu. Napenda kutoa shukrani zangu yingi kwa wote waliofadhili Mpango huu wa Usalama wa Raia, hususan Benki za CRDB na NMB pamoja na Kampuni ya Super Doll. Mchango wenu tunauthamini sana.
Kipekee kabisa, napenda kuishukuru Serikali ya Malaysia, ambayo ni waasisi wa Mpango huu tutakaouzindua leo kupitia program yao ya Matokeo Makubwa Sasa (Big Result Now - BRN). Nawashukuru na kuwapongeza viongozi na wataalam wa Ofisi ya Rais ya Usimamizi wa Mpango wa BRN (Presidential Delivery Bureau) kwa kusimamia vizuri Mpango huu. Hongereni sana.
Wageni waalikwa;
Mabibi na mabwana;
Mara ya mwisho kuja kwenye Kiwanja hiki cha Biafra ilikuwa mwaka jana wakati wa Kampeni. Nilikuja hapa nikawaomba kura. Nawashukuru mliniamini na mkanipa kura nyingi zilizoniwezesha kuchaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa sababu hiyo, napenda kutumia fursa hii kuwashukuru kwa dhati kwa kunichagua kuwa Rais wenu wa Awamu ya Tano. Nawaahidi kuwa yote niliyoahidi kipindi cha kampeni nitayatekeleza na kamwe sitawaangusha.
Uchaguzi sasa umekwisha, hivyo basi, jukumu kubwa lililo mbele yetu hivi sasa ni kuleta maendeleo kwa nchi yetu. Tuondoe tofauti zetu za itikadi, dini au kabila tushikamane na kuchapakazi kwa bidii. Maendeleo hayana chama, dini au kabila. Sisi Watanzania wote kwa pamoja tunahitaji maendeleo. Tunahitaji kuona kero zetu mbalimbali zinazotukabili zinaondoka. Hivyo basi, binafsi nawaahidi kuwa nitakuwa Rais wa Watanzania wote. Sitambagua mtu kwa misingi ya dini, chama au kabila.
Wageni waalikwa;
Mabibi na mabwana;
Tupo hapa kwa ajili ya kushuhudia uzinduzi wa Mpango wa Usalama wa Raia ambao umebuniwa na Jeshi letu la Polisi. Huu ni Mpango kabambe unaolenga kupunguza kama sio kumaliza kabisa tatizo la uhalifu hapa nchini. Kupitia Mpango huu, Jeshi la Polisi litaanzisha Vituo vya Mawasiliano (Call Centres), kwa ajili ya kupokea taarifa za matukio mbalimbali ya uhalifu kutoka kwa wananchi. Kabla ya kuja hapa, nimetoka kuzinduzi mojawapo ya vitakavyokuwa Vituo vya Mawasiliano (Call Centre) pale kwenye Makao Makuu ya Jeshi la polisi. Katika Kituo hicho, nimeshuhudia vifaa na vitendea kazi vya kisasa. Nimeelezwa kuwa kupitia taarifa zitakazopokelewa kwenye Vituo hivyo, Jeshi la Polisi litaweza kutuma gari la doria kwenye eneo la tukio ndani ya dakika 15. Nimeambiwa magari ya doria yatafungwa vifaa maalum vya kuweza kuonekana mahali yalipo. Hii itawezesha askari waliopo kwenye Kituo Cha Mawasiliano kuelekeza magari ya doria kwa haraka kwenda kwenye eneo la tukio.
Sambamba na kuanzisha kituo cha Mawasiliano, Mpango huu pia utahusisha uanzishaji wa Vituo vya Polisi vya Kuhamahama (Mobile Police Stations). Kwa ujumla Mpango huu ni mzuri. Hivyo basi, napenda kutumia fursa hii kupongeza Jeshi la Polisi kwa kubuni Mpango huu wa Usalama wa Raia. Mimi naamini kuwa Mpango huu utasaidia juhudi zetu za kupambana na uhalifu hapa nchini kwetu.
Aidha, nitumie fursa hii kuwapongeza Viongozi, Makamanda, Askari wa Jeshi la Polisi kwa kazi kubwa na nzuri ya kusimamia amani na usalama hapa nchini kwa ujumla. Mnafanya kazi kubwa sana na Watanzania wengi wana imani kubwa nanyi. Sote ni mashahidi wa namna ambavyo Jeshi la Polisi lilisimamia vizuri usalama wa nchi yetu kipindi cha Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana. Mlisimamia amani na usalama nchini bila upendeleo wowote. Hivyo basi, napenda kutumia fursa hii kuwaahidi kuwa Serikali ya Awamu ya Tano itatoa ushirikiano wa kutosha kwenu ili mzidi kutekeleze majukumu yenu ipasavyo.
Inspekta Jenerali wa Polisi;
Ndugu Askari;
Licha ya pongezi hizo nilizozitoa kwenu ni dhahiri kuwa bado kuna changamoto. Na napenda kusema kwa dhati kabisa kuwa binafsi nimekuwa nikisononeshwa na kusikitishwa sana na vitendo vya uvamizi wa vituo vya polisi na vitendo vya ujambazi wa kutumia silaha ambavyo vimekuwa vikitokea hapa nchini. Vitendo hivyo sio tu kwamba vinatishia usalama wa wananchi wetu bali pia vinatia dosari Jeshi la Polisi. Hivyo basi, natoa wito kwa Viongozi wa Jeshi la Polisi kuhakikisha vitendo hivi vinakomeshwa mara moja.
Naamini kuwa kwa kutumia mbinu zenu mbalimbali, Jeshi la Polisi lina uwezo mkubwa wa kukomesha vitendo hivyo pamoja na uhalifu mwingine hapa nchini. Kwa bahati nzuri, mnao vijana wazuri, hodari, wazalendo na wachapakazi. Kinachohitajika ni kuwawezesha vijana hao, ikiwemo kuwapa motisha mbalimbali pale wanapofanya vitendo vya kishujaa. Na napenda kutumia fursa hii kuwahakikisha kuwa Serikali ya Awamu ya Tano itafanya kila jitihada ili kuboresha maslahi ya askari wa Jeshi la Polisi na vyombo vingine vya ulinzi na usalama.
Wageni waalikwa;
Mabibi na mabwana;
Mpango huu tunaouzindua leo unaanza kutekelezwa kwenye Wilaya hii ya Kinondoni ambayo kitakwimu ndiyo inaongoza kwa matukio ya uhalifu hapa nchini. Kwa takwimu zilizopo, Wilaya ya Kinondoni iliripoti matukio ya uhalifu 8410 (2012), 7924 (2013); 8095 (2014) na matukio 8804 (2015). Hivyo, matarajio yetu ni kwamba kuanza kutekelezwa mpango huu, matukio ya uhalifu katika Wilaya hii yatapungua katika miaka inayofuata. Na baada ya mpango huu kutekelezwa hapa Kinondoni, hatimaye utasambaa sehemu zote nchini.
Hata hivyo, napenda kusema kuwa ili mpango huu uweze kufanikiwa ni lazima Jeshi la Polisi liondoe kasoro ndogondogo zilizopo. Mathalan, utekelezaji wa Mpango huu unahitaji askari kuwa waadilifu na uaminifu kwa kiwango kikubwa. Kinyume chake, wananchi wanaweza kuwa wanapeleka habari kwenye vituo vyenu (call centres) lakini taarifa hizo zinaweza zisifanyiwe au zikatolewa kwa wahalifu. Hivyo basi, nitoe wito kwako inspekta Jenerali wa Polisi kuhakikisha askari watakaokuwepo kwenye vituo vya kupokea taarifa ni waaminifu na waadilifu. Ikiwezekana, askari hao wawe wanapewa posho maalum lakini pia hakikisheni mnalinda usalama wao kwa kutowafanya kutambulika kwa watu wa nje ya Jeshi lenu.
Ndugu Wananchi;
Mabibi na Mabwana;
Jukumu la kulinda na kudumisha ulinzi na usalama katika nchi ni jukumu letu sote. Licha ya kubuniwa kwa mpango huu kabambe, Jeshi la Polisi pekee haliwezi kukomesha uhalifu nchini. Ni lazima wananchi mtoe ushirikiano wa kutosha kwa Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa za uhalifu. Wahalifu wapo na wanaishi katika maeneo yetu. Hivyo, nawaomba msikae kimya mkiona uhalifu unafanyika mahali au kuna fununu za kufanyika kwa uhalifu kwenye maeneo yenu. Kwa bahati nzuri, katika Mpango huu tunaouzindua leo, Jeshi la Polisi limetoa namba za kupiga simu ili kuwasilisha taarifa za uhalifu. Namba zenyewe ni rahisi kabisa, yaani 111 au 112. Pigeni simu na mtoe taarifa kwa Jeshi la Polisi.
Mkifanya hivyo, mtakuwa mmesaidia juhudi za Jeshi la Polisi kukabiliana na uhalifu na bila shaka hali ya amani na usalama itaimarika hapa nchini. Sote hapa tunafahamu umuhimu wa usalama katika kufanikisha shughuli mbalimbali za maendeleo katika nyanja za siasa, uchumi au jamii. Binafsi ningependa kuona shughuli mbalimbali za kiuchumi, ikiwemo shughuli za maduka hadi nyakati za usiku, kama inavyofanyika kwenye nchi nyingine. Lakini huenda wenye maduka hapa nchini wanashindwa kufanya hivyo kutokana na kuhofia usalama wao na mali zao. Hivyo basi, narudia tena kutoa wito kwenu wananchi kutoa ushirikiano wa kutosha kwa Jeshi la Polisi ili kudhibiti vitendo vya uhalifu. Aidha, nitoe rai kwenu Jeshi la Polisi kuanza kuangalia uwezekano wa kufunga kamera kwenye maeneo mbalimbali, hususan katika miji ili kudhibiti uhalifu. Jambo hilo linawezekana na hasa kwa kuzingatia kuwa gharama zake si kubwa sana.
Sambamba na hilo, napenda kutumia fursa hii kuiagiza Mamlaka ya Mawasiliano nchini kushirikiana kwa karibu na Jeshi la Polisi katika kutekeleza Mpango huu wa Usalama wa Jamii tunaouzindua leo. Wakati nikiwa nazindua Kituo Cha Mawasiliano pale Makao Makuu ya Jeshi la Polisi nimeshuhudia kuwa simu zote zinazoingia kwenye Kituo zinarekodiwa na kutolewa nakala (printout). Kitendo hicho cha kurekodiwa na kutolewa nakala huchukua kama dakika mbili au zaidi. Ni kwa sababu hii, natoa wito kwa Mamlaka ya Mawasiliano kushirikiana na Jeshi la Polisi ili kuwezesha nakala za simu zinazopigwa kutolewa kwa haraka kuliko ilivyo sasa. Bahati nzuri Katibu Mkuu Kiongozi yupo hapa hivyo nategemea agizo hili litasimamiwa ipasavyo.
Mheshimiwa Waziri;
Inspekta Jenerali wa Polisi;
Ndugu Askari;
Wageni Waalikwa;
Mabibi na Mabwana;
Nimekuja hapa kwa ajili ya kuzindua Mpango wa Usalama wa Raia. Hivyo, sitapenda kuwachosha kwa hotuba ndefu. Hata hivyo, kabla sijahitimisha hotuba yangu, naomba mniruhusu kutoa pongezi nyingi kwa Mheshimiwa Rais Mstaafu, Mzee Jakaya Mrisho Kikwete na Inspekta Jenerali Mstaafu, Said Mwema pamoja na wote walioshiriki katika kubuni mpango huu. Binafsi naamini kama Mpango huu utasimamiwa vizuri, utakuwa ni mwarobaini wa changamoto za uhalifu hapa nchini.
Nalipongeza pia Jeshi kwa kazi kubwa mnayoifanya na nawaahidi tena kuwa Serikali ya Awamu wa Tano itashirikiana nanyi katika kuhakikisha mpango huu unafanikiwa ili hatimaye tuweze kutokomeza vitendo vya uhalifu hapa nchini. Vilevile, narudia kutoa shukrani zangu nyingi kwa wadhamini, Benki za CRDB na NMB pamoja na Kampuni ya Super Doll kwa kuunga mkono jitihada za Jeshi la Polisi za kupambana na uhalifu nchini. Wito wangu kwa Watanzania na taasisi nyingine igeni mfano wa makampuni haya kwa kutoa michango yenu ili kufanikisha mpango huu.
Mwisho lakini sio kwa umuhimu, napenda kuwashukuru wananchi wote mliojitokeza kuja mahali hapa. Nipo pamoja nanyi na kamwe sitawaangusha. Napenda kuwahakikishia kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kufanya kazi kwa nguvu zote kwa manufaa na ustawi wa wananchi wote na taifa kwa ujumla. Narudia wito wangu kwenu muendelee kutuunga mkono na kutuombea sisi Viongozi wenu. Kwa wanasiasa wenzangu, natoa rai kwenu kushirikiana na Serikali katika kuleta maendeleo kwa wananchi badala ya kuwa kikwazo. Binafsi sipo tayari kumruhusu mtu kunikwamisha kutekeleza yale niliyoyaahidi kipindi cha kampeni. Nitumie fursa hii kumpongeza Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mheshimiwa Makonda, kwa hatua anazozichukua hivi sasa kuwashughulikia wabadhirifu wa miradi mbalimbali ya barabara katika Jiji la Dar es Salaam. Naviagiza vyombo vyote vinavyohusika, ikiwemo Bodi za Usajili wa Makandarasi na Wahandisi pamoja na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kuchukua hatua dhidi ya wale wote waliohusika kutekeleza miradi ya barabara chini ya kiwango.
Baada ya kusema haya sasa natamka kuwa Mpango wa Usalama wa Raia umezinduliwa rasmi.
Mungu Libariki Jeshi la Wananchi Tanzania!
Mungu Ibariki Tanzania!
“Asanteni kwa kunisikiliza”
- Jun 23, 2016
HOTUBA YA MHESHIMIWA JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA KATIKA HAFLA YA KUPOKEA TAARIFA YA UCHAGUZI MKUU WA RAIS, WABUNGE NA MA...
Soma zaidiHotuba
Mheshimiwa Jaji (Mst) Damian Lubuva, Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi;
Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi;
Mheshimiwa Kassim Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Mheshimiwa Balozi Seif Ali Idd, Makamu wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar;
Mheshimiwa Zuber Ali Maulid, Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar;
Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson Mwansasu, Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Mheshimiwa Mohamed Chande Othman, Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Mheshimiwa Omar Othman Makungu, Jaji Mkuu wa Zanzibar;
Waheshimiwa Marais Wastaafu;
Waheshimiwa Mawaziri Wakuu Wastaafu;
Mheshimiwa Jecha Salum Jecha, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar;
Waheshimiwa Mawaziri;
Mheshimiwa Jaji Francis Mutungi, Msajili wa Vyama vya Siasa;
Waheshimiwa Wajumbe wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi;
Waheshimiwa Viongozi wa Vyama vya siasa;
Waheshimiwa wa Wawakilishi wa Asasi za Kiraia;
Mabibi na Mabwana.
Awali ya yote napenda kuchukua nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kukutana hapa leo tukiwa wazima. Aidha, napenda kutoa shukran zangu za dhati kwa Mwenyekiti na uongozi mzima wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa kunialika katika hafla hii fupi ya kunikabidhi Taarifa ya Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani uliofanyika hapa nchini mwezi Oktoba mwaka jana. Nimearifiwa kuwa tukio hili ni kwa mujibu wa utamaduni uliokuwekwa na Tume kwamba kila baada ya kumalizika Uchaguzi Mkuu, Tume huwasilisha Taarifa kwa Rais. Naipongeza Tume kwa kubuni na kuenzi utamaduni huu.
Kwa kipekee kabisa, napenda kuwashukuru Viongozi wa Serikali, Vyama vya Siasa na wageni wote waalikwa mliojitokeza kwa wingi mahali hapa. Uwepo wenu hapa ni kielelezo tosha kuwa mnatambua na kuthamini umuhimu wa tukio hili. Ahsanteni sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti,
Wageni Waalikwa;
Ndugu Viongozi;
Uchaguzi ni tukio muhimu katika nchi. Ni tukio linaloashiria kukua kwa demokrasia katika nchi. Kupitia uchaguzi, wananchi hupata fursa ya kuwachagua viongozi wanaowataka kwa hiari. Hata hivyo, uchaguzi usiposimamiwa vizuri unaweza kuwa chanzo cha mgogoro mkubwa na vurugu katika nchi. Ipo mifano mingi ya namna chaguzi katika nchi mbalimbali zimevuruga amani. Sina haja ya kuitaja.
Mwezi Oktoba mwaka jana nchi yetu ilifanya Uchaguzi wake Mkuu. Mtakubaliana nami kuwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana ulikuwa ni wa kipekee sana. Ulikuwa wa kipekee kwa sababu kubwa mbili. Mosi, uchaguzi huu ulikuwa ni wa kwanza kufanyika kwa kutumia Mfumo wa Kisasa wa Biometric Voter Registration (maarufu kama BVR). Hivyo, Tume ya Taifa ya Uchaguzi ililazimika kuboresha Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwa kutumia Mfumo wa BVR. Ili kufanya kazi hiyo, Tume iliomba kupata vifaa vya BVR vipatavyo 15,000. Lakini kutokana na ufinyu wa bajeti, vilipatikana vifaa 8,000 tu. Licha ya upungufu huo wa vifaa na pia ufinyu wa muda, Tume iliweza kukamilisha kwa ufanisi mkubwa zoezi la uandikishaji wapiga kura. Idadi ya wapiga kura walioandikishwa ilikuwa ni 23,161,440 sawa na asilimia 96.9 ya wapiga kura 23,901,471 waliokadiriwa. Nawapongeza sana Tume kwa kufanikisha zoezi hili.
Sababu ya pili ni kwamba Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana ulikuwa na ushindani mkali. Ulikuwa wenye mvuto na msisimko wa kipekee ndani na nje ya nchi yetu. Kutokana na hali ya ushindani iliyokuwepo, baadhi ya watu walionesha wasiwasi kuwa huenda amani na utulivu katika nchi ingepotea. Hata hivyo, tulimaliza uchaguzi kwa salama. Nchi yetu imebaki kuwa yenye amani na tulivu mkubwa. Bila shaka, kukamilika vizuri kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana ni matokeo ya kazi kubwa na nzuri iliyofanywa na Tume yetu ya Uchaguzi kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama, viongozi wa siasa pamoja na wananchi kwa ujumla.
Hivyo basi, kwa mara nyingine tena, napenda kutoa pongezi zangu nyingi kwako wewe Mheshimiwa Mwenyekiti, Jaji Mstaafu Lubuva pamoja na Sekretarieti ya Tume ikiongozwa na Mkurugenzi wa Uchaguzi, Ndugu Kailima Ramadhani, kwa kusimamia na kuendesha vizuri Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2015. Mlifanya kazi kubwa sana. Watazamaji wa Uchaguzi wengi kutoka ndani na nje ya nchi yetu wamekiri kuwa Uchaguzi wetu ulifanyika katika mazingira ya uwazi, uhuru, haki na amani. Aidha, nimearifiwa kuwa kutokana kusimamia vizuri zoezi la uandikishaji wapiga kura kwa njia ya kieletroniki (BVR), baadhi ya nchi zimeonesha nia ya kutaka kujifunza kutoka kwenu. Naipongeza sana Tume.
Mheshimiwa Mwenyekiti,
Hakuna kizuri kisicho na kasoro. Hivyo basi, naamini zipo baadhi ya kasoro zilijitokeza kwenye Uchaguzi wa mwaka jana. Jambo hili lisiwanyime raha. Ni suala la kawaida kabisa. Kama ambavyo wewe mwenyewe umetoka kusema hivi punde kuwa hakuna nchi hapa duniani imewahi kufanya uchaguzi bila ya kutokea kwa kasoro yoyote.
Pamoja na ukweli huo, natambua wametokea wakosoaji. Wakosoaji hao ni wa aina mbili. Kundi la kwanza ni la wakosoaji ambao wametaja mapungufu ya msingi kwa lengo la kuboresha chaguzi zetu zijazo. Naiomba Tume ipokee mapungufu waliyoyataja na kuyafanyia kazi ili uchaguzi ujao uwe bora zaidi. Kundi la pili ni la wakosoaji ambao kazi yao ni kukosoa. Hawa hata mngefanyaje wangekosoa tu. Hawana jema. Mtunzi wa Vitabu Maarufu wa Marekani, Ben Carson, alipata kusema, nanukuu “Even if you dance on water, Haters will accuse you of raising dust” (Hata ukicheza kwenye maji, wenye husda na wewe watasema unawatimulia vumbi), mwisho wa kunukuu.
Kwa wakosoaji wa namna hii, ili uchaguzi uonekane kuwa huru na haki ni lazima Chama Tawala kishindwe. Kikishinda, basi uchaguzi unakuwa sio huru. Ninyi wenyewe mmejionea wakati wanawalaumu ninyi kwa mapungufu yaliyojitokeza, kule Zanzibar wanailaumu ZEC kwa kufuta uchaguzi ambao ulidhihirika kuwa una mapungufu. Lakini mimi sishangai. Maana hii ndio imekuwa tabia yao. Wakosoaji wa namna hii nawafananisha na wale watu ambao wamekuwa wakizunguka kila siku sehemu mbalimbali ndani na nje ya nchi wakilaumu Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuingilia masuala ya ndani ya Zanzibar. Ndio watu hao hao wamekuwa wakijinasibu kuwa wanataka Tume huru ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC). Lakini cha kustaajabisha ni kwamba baada ya ZEC kufuta uchaguzi wa Zanzibar, wakanitaka mimi niingilie kati ili kutengua maamuzi ya ZEC. Wakajisahaulisha kuwa Zanzibar ina mamlaka yake na ZEC ni chombo huru ambacho maamuzi yake hayaingiliwi na mtu au chombo chochote.
Mimi niliwaambia hapana maana naheshimu Katiba na sheria. Naheshimu mamlaka ya Zanzibar na uhuru wa ZEC. Lakini niliwaahidi kwamba ningehakikisha Zanzibar inabaki kuwa salama na amani. Ninafurahi nimetekeleza ahadi yangu. Uchaguzi wa marudio Zanzibar umefanyika huku amani na utulivu ukiendelea. Nitumie fursa hii kuwapongeza ZEC na wananchi wa Zanzibar kwa kufanya uchaguzi wa marudio kwa usalama na utulivu mkubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Mabibi na Mabwana;
Uchaguzi sasa umekwisha. Lakini mtakubaliana nami kuwa mwisho wa uchaguzi mkuu mmoja ndio mwanzo wa maandalizi ya uchaguzi mwingine. Nafahamu ipo dhana iliyojengeka katika jamii yetu kuwa mwisho wa uchaguzi unaashiria pia mwisho wa kazi za Tume. Dhana hii si sahihi hata kidogo. Tume ya Uchaguzi ni taasisi ya kudumu. Kazi zake zinaendelea kama kawaida. Mathalan, kwa mujibu wa kifungu cha 15 (5) cha Sheria ya Tume ya Uchaguzi, sura ya 343, Tume inapaswa kuboresha Daftari la Kudumu la Wapiga Kura mara mbili kati ya uchaguzi mmoja na mwingine. Lakini pia Tume inao wajibu wa kuendelea kutoa elimu ya mpiga kura na pia kusimamia chaguzi ndogo ndogo zinazojitokeza. Kwa mantiki hiyo, niiombe Tume kuanza mapema maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.
Natambua zipo changamoto zinazokabili Tume katika kutekeleza majukumu yake hivi sasa. Mwenyekiti wa Tume amezitaja baadhi ya changamoto hizo hivi punde, ikiwemo ufinyu wa bajeti, ukosefu wa watumishi, uhaba wa vitendea kazi na ukosefu wa ofisi. Changamoto nyingine zinahusu masuala ya kisheria. Napenda kuwahakikishia kuwa Serikali imepokea changamoto hizi na tutazifanyia kazi. Tutatilia maanani pendekezo la Tume kuhusu kuanzisha Mfuko wa Uchaguzi. Mimi binafsi naliona pendekezo hili kuwa ni zuri sana. Mfuko huo ukianzishwa, utatoa fursa kwa Serikali na wadau wengine kuweza kuchangia kila mwaka na hivyo kupunguza tatizo la uhaba wa fedha kwa Tume, hasa nyakati za Uchaguzi Mkuu.
Lakini niseme tu kuwa kati ya changamoto mlizozitaja ipo moja ambayo imenigusa sana. Changamoto hiyo inahusu Tume kukosa jengo la ofisi. Mimi nilishuhudia ukubwa wa changamoto hii wakati nikichukua na kurudisha fomu za kuwania Urais mwaka jana. Nakiri kwa dhati kabisa kuwa mahali ilipo Ofisi ya Tume hivi sasa sio muafaka. Baya zaidi ni kwamba ofisi hiyo ipo kwenye jengo la kupanga. Tena sio kwenye jengo moja, mmepanga kwenye majengo matatu. Hii si sawa hata kidogo. Kwanza ni gharama. Nimearifiwa kuwa katika majengo matatu mliyopanga mnalipa takriban shilingi bilioni 1.3 kwa mwaka. Lakini kubwa zaidi ni kwamba kutokana na unyeti wa shughuli zake, Tume haipaswi kuwa kwenye jengo la kupanga. Hivyo, kama nilivyoahidi wakati Tume iliponikabidhi hundi ya kurejesha bakaa ya shilingi bilioni 12 ya bajeti ya mwaka wa fedha 2015/2016, nitahakikisha bakaa hiyo inarejeshwa kwa Tume ili ituike kwa ujenzi wa ofisi. Naamini fedha hizi zikitumika vizuri zitatosha kabisa kujenga jengo zuri na la kisasa. Lakini ningependa kurudia ombi langu kwa Tume kuwa, kama mtaona inafaa, basi jengo hilo la ofisi lijengwe kwenye Makao Makuu ya nchi yetu mjini Dodoma.
Mkijenga Dodoma mtakuwa mnatekeleza ndoto ya Baba wa Taifa letu ya kuhamishia Makao Makuu ya nchi yetu. Lakini kwa kuwa Dodoma ni katikati ya nchi itakuwa rahisi kwenu kufika kwenye maeneo mbalimbali ya nchi tena tena kwa haraka. Aidha, wadau wenu mbalimbali nao itawawia rahisi kuwafikia ninyi lakini pia mtasaidia kupunguza tatizo la foleni hapa Dar es Salaam.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Katika hotuba yako, umezungumza kwamba baada ya uchaguzi kumalizika, sasa Tume inataka kujielekeza kwenye suala mchakato wa Katiba Mpya ambao ulibaki kiporo kutokana na kuingiliwa na ratiba ya uchaguzi. Hilo ni jambo jema ambalo binafsi naunga mkono. Mchakato wa Katiba Mpya ulifikia mahali pazuri hivyo ni vyema tukaumalizia. Napenda kutumia fursa hii kuwashukuru Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete; Rais wa Zanzibar, Dkt. Ali Mohamed Shein; Mweyekiti wa Bunge la Katiba, Mzee Samweli Sitta na Makamu wake, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ambaye hivi sasa ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Mwenyekiti wa Tume ya Katiba Jaji Joseph Warioba kwa kazi kubwa waliyoifanya hadi kufikia hatua tulipo sasa. Naahidi kuhakikisha kumalizia sehemu iliyosalia. Hivyo, kama ulivyosema Mheshimiwa Mwenyekiti, nawaomba muanze kuchukua hatua mahsusi pamoja na taratibu zinazohitajika ili mtakapozikamilisha, Serikali iendelee na taratibu nyingine za kumalizia mchakato huo. Ni azma ya Serikali kuona mchakato huo unakamilika kwa muafaka ili kupata Katiba nzuri.
Wageni Waalikwa;
Mabibi na Mabwana;
Tupo hapa kwa ajili ya kushuhudia makabidhiano ya Taarifa ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2015. Hivyo, haitakuwa busara kwangu kuwachosha kwa hotuba ndefu. Hata hivyo, kabla sijahitimisha hotuba yangu napenda kusema jambo moja la mwisho.
Kama nilivyosema hapo awali sasa uchaguzi umekwisha. Ni kweli katika uchaguzi uliopita, kama ilivyo kawaida kwenye nchi za vyama vingi, watu mbalimbali kupitia vyama vyao walijitokeza kuwania nafasi mbalimbali za uongozi na baadhi yetu kuibuka washindi. Lakini kwa mtazamo wangu na bila shaka huu ni mtazamo wa Watanzania waliowengi kuwa katika uchaguzi huo hakuna aliyeshindwa. Watanzania wote kwa umoja wetu ni washindi. Hivyo, ni vyema sasa tukajielekeza kwenye kuchapa kazi ili kuleta maendeleo kwa nchi yetu. Tuache kuendeleza kampeni na siasa zisizo na tija. Itakuwa vyema kama siasa sasa zitahamia Bungeni ama kwenye vikao vya madiwani.
Watanzania wana uchu wa maendeleo. Watanzania wanataka maisha bora. Watanzania wanataka kuona kero zao mbalimbali zinaondolewa na Serikali iliyopo madarakani. Sisi tuliyopewa dhamana ya kuongoza Serikali kuna mambo tuliyowaahidi wananchi kuwa tutayatekeleza katika kipindi cha miaka mitano ijayo. Tunataka tutekeleze ahadi zetu. Sitakuwa tayari kuona mtu anatukwamisha kutekeleza yale tuliyowaahidi wananchi. Hivyo, nawaomba viongozi wenzangu, hususan viongozi wa siasa, tushirikiane katika kuwahamasisha wananchi wetu kufanya kazi ili azma ya nchi yetu ya kuwa na uchumi wa kati unaoongozwa na viwanda ifikapo mwaka 2025 itimie. Serikali kwa upande wake ipo tayari kushirikiana na kupokea ushauri wa kila Mtanzania ili kuhakikisha nchi yetu inapata maendeleo.
Mheshimiwa Mwenyekiti,
Waheshimiwa Viongozi;
Wageni Waalikwa;
Mabibi na Mabwana;
Napenda kuhitimisha hotuba yangu kwa kurudia kutoa pongezi kwa Tume kwa kusimamia vizuri Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana. Aidha, napenda kupongeza Vyombo vya Ulinzi na Usalama, wagombea wa nafasi mbalimbali, Viongozi wa Vyama, Viongozi wa Dini, Wana-Habari na wananchi kwa ujumla kwa ushiriki wenu mzuri uliowezesha nchi yetu kumaliza uchaguzi salama. Nawapongeza pia viongozi wa siasa waliohudhuria tukio hili la leo. Mmeonesha ukomavu mkubwa wa kisiasa. Siasa si uadui.
Kipekee kabisa nawapongeza Marais Kikwete na Dkt. Shein kwa kusimamia vizuri uchaguzi mkuu wa mwaka jana. Mwisho lakini sio kwa umuhimu, nawashukuru washirika wetu mbalimbali ambao kwa namna moja au nyingine walitoa michango ya hali na mali iliyowezesha Uchaguzi wa mwaka jana kufanyika kwa ufanisi, amani na utulivu. Tunatambua na kuthamini mchango wenu.
Mungu Ibariki Tume ya Taifa ya Uchaguzi!
Mungu Ibariki Tanzania!
“Asanteni Kwa Kunisikiliza”
- Jun 22, 2016
HOTUBA YA MHESHIMIWA JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA KATIKA KILELE CHA SHEREHE ZA MAADHIMISHO YA MIAKA 50 YA KUANZISHWA KWA...
Soma zaidiHotuba
Mheshimiwa Dkt. Servacius Likwelile, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango;
Mheshimiwa Prof. Benno Ndulu, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania;
Waheshimiwa Magavana wa Benki Kuu kutoka Nchi Wanachama wa SADC na EAC;
Waheshimiwa Magavana Wastaafu na Wajumbe wa Bodi ya Benki Kuu;
Wafanyakazi wa Benki Kuu mliopo;
Wageni Waalikwa;
Mabibi na Mabwana:
Napenda nianze kwa kutoa shukrani nyingi kwa Mheshimiwa Gavana wa Benki Kuu kwa kunipa mwaliko ili niweze kujumuika nanyi katika Maadhimisho haya ya Miaka 50 tangu kuanzishwa Benki Kuu ya Tanzania. Aidha, nawashukuru kwa kunipa fursa hii adimu ya kuzungumza katika hafla hii. Nafahamu hii si mara yangu ya kwanza kufika hapa tangu nimechaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwezi Oktoba mwaka jana. Nilishafika hapa mara moja. Lakini ziara ile ya kwanza haikuwa rasmi. ‘Nilivamia”. Hii ndio ziara yangu ya kwanza rasmi hapa. Hivyo, napenda kutumia fursa hii kuwashukuru kwa dhati kabisa kwa kunipa kura nyingi zilizoniwezesha kuchaguliwa kuwa Rais wa Awamu ya Tano ya nchi yetu. Ahsanteni sana.
Nitumie fursa hii pia kuwashukuru wageni waalikwa wote mliohudhuria kwa kukubali kutenga muda wenu na kuja hapa kujumuika nasi. Nimearifiwa miongoni mwa wageni waliopo hapa, wapo Magavana wa Benki Kuu au wawakilishi wao kutoka Nchi 20 Wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC). Karibuni sana Tanzania, hususan katika Jiji hili la Dar es Salaam.
Mheshimiwa Gavana;
Wageni Waalikwa;
Mabibi na Mabwana;
Tupo mahali hapa kwa ajili ya kuadhimisha Sherehe za Miaka 50 ya Benki Kuu ya Tanzania, ambayo ilianzishwa rasmi siku ya Jumatatu ya tarehe 14 Juni, 1966. Mtakubaliana nami kuwa kipindi cha miaka 50 ni kipindi kirefu kwa taasisi yoyote. Ukiangalia nyuma kwenye kumbukumbu za historia ya Benki hii ilivyokuwa siku ile ya tarehe 14 Juni, 1966 na ilivyo sasa, hutasita kutambua na kukiri kuwa Benki Kuu ya Tanzania imepata mafanikio makubwa. Hivi punde, Gavana Profesa Ndulu ametoka kueleza mafanikio kadhaa ambayo Benki imepata katika kipindi cha miaka 50 iliyopita. Kwa haraka haraka napenda kurudia kutaja mafanikio hayo ingawa mimi nimeyaweka katika makundi makubwa mawili:
Mosi, Kukua Kitaasisi: Wakati Benki hii ikianzishwa ilikuwa na ofisi moja tu hapa Dar es Salaam. Ofisi yenyewe ilikuwa ndogo yenye vitendea kazi vichache. Nimeambiwa kutokana na udogo wa ofisi, ilibidi fedha za za benki kuhifadhiwa Jeshini na kwenye Benki binafsi. Watumishi wa Kitanzania nao walikuwa wachache na hivyo kulazimu Benki kutumia wafanyakazi kutoka nchi marafiki, ikiwemo Uingereza, Ujerumani, Sweden, India n.k. Leo miaka 50 baadaye, Benki ina ofisi yake tena jengo lake ni miongoni mwa majengo ya kisasa kabisa hapa nchini. Aidha, Benki imefungua matawi sehemu mbalimbali ikiwemo Arusha, Dodoma, Mtwara, Mwanza na Zanzibar.
Pili, Utekelezaji wa Majukumu: Benki Kuu imekuwa na majukumu makubwa mawili tangu kuanzishwa kwake. Kati ya mwaka 1967 hadi katikati mwa miaka ya 1980, Benki Kuu ilijikita zaidi katika kutekeleza shughuli za maendeleo, ikiwemo kuelekeza nguvu kwenye ujenzi wa viwanda na kuimarisha kilimo. Hata hivyo, kutokana na changamoto zilizojitokeza na mageuzi ya kiuchumi yaliyofanyika kuanzia miaka ya 1990, jukumu la msingi la Benki Kuu ya Tanzania limekuwa ni kuandaa na kutekeleza sera ya fedha inayolenga kudhibiti mfumko wa bei na kujenga mfumo thabiti wa fedha kwa ajili ya ukuaji endelevu wa uchumi wa taifa. Majukumu mengine ambayo yamekuwepo tangu Benki Kuu ilipoanzishwa ni pamoja na kutoa sarafu ya nchi, kusimamia mabenki na taasisi za fedha, kusimamia na kudhibiti mifumo ya malipo nchini, kuhifadhi akiba ya nchi, ikiwemo fedha za kigeni pamoja na kutoa ushauri kuhusu masuala ya uchumi na fedha kwa Serikali. Mafanikio ya utekelezaji wa majukumu yaliyopatikana ni pamoja:
(i) Benki kuweza kutoa ushauri kwa Serikali na kusimamia mageuzi ya kiuchumi ya kuinusuru au kuikinga nchi yetu nyakati za misukosuko ya uchumi, mathalan wakati wa mdororo wa uchumi ulioikumba nchi miaka ya 1980, na hivi karibuni mdororo wa uchumi ulioikumba dunia mwaka 2008/09;
(ii) Benki imedhibiti mfumko wa bei nchini, ambapo katika miaka ya 1990 ulifikia 30%. Hivi sasa umepungua na kuwa wastani wa tarakimu moja kwa zaidi ya muongo mmoja uliopita;
(iii) Benki imewezesha ukuaji wa sekta ya fedha, hususan kuongezeka kwa huduma za kibenki, na mchango wake kwenye pato la taifa. Idadi ya benki imeongezeka maradufu kutoka benki 3 mwaka 1990 hadi kufikia 54 hivi sasa. Aidha, uwiano kati ya mikopo inayotolewa na benki na pato la taifa umeongezeka kutoka 4% mwaka 1995 hadi kufikia 23.1% mwaka 2015.
(iv) Benki imeweza kurahisisha upatikanaji wa fedha za kigeni nchini huku ikiendelea na jukumu lake la kuchapisha noti na kufua sarafu ya nchi.
Wageni Waalikwa;
Mabibi na Mabwana;
Sisi waswahili tunao msemo usemao “usione vyaelea, vimeundwa”. Mafanikio haya yote hayakujileta. Wapo watu ambao walijitoa na wanaendelea kujitoa kwa dhati kuyaleta. Baadhi yao ni ninyi watumishi wa Benki Kuu wa sasa na wastaafu mliopo hapa, mkiongozwa na Gavana wa sasa Profesa Ndulu na Gavana wa kwanza Mzee Edwin Mtei. Kwa niaba yao wote, naleta kwenu, pongezi zangu binafsi pamoja na za Serikali na Watanzania kwa ujumla, kwanza kwa kuwezesha Benki hii kutimiza nusu karne. Aidha, nawapongeza kwa mafanikio ambayo Benki imeyapata. Mmetoa mchango mkubwa sio tu kwa Benki hii bali kwa Taifa kwa ujumla. Hongereni sana. Nafahamu wapo ambao wametoa mchango kwenye Benki Kuu hii lakini wametangulia mbele za haki. Namwomba Mwenyezi Mungu aziweke roho zao mahali pema peponi. Amina.
Mheshimiwa Gavana na Wafanyakazi wa Benki Kuu;
Nimezungumza mafanikio mengi ya Benki Kuu ya Tanzania. Pamoja na mafanikio hayo, maadhimisho haya yanatoa fursa kwa Benki na taifa kwa ujumla kutafakari kwa kina changamoto zilizopo na kubuni mikakati ya kuzitatua. Mathalan, hivi sasa Benki Kuu ya Tanzania ina jukumu kubwa moja nalo ni kudhibiti mfumko wa bei na kujenga mfumo thabiti wa fedha kwa ajili ya ukuaji endelevu wa uchumi wa taifa. Benki Kuu na hata taasisi nyingi za fedha hazijihusishi moja kwa moja kwenye masuala ya ukuzaji uchumi. Lakini ukiangalia historia katika nchi zilizoendelea, kama Marekani, Uingereza, Japan, Korea Kusini utaona Benki Kuu zilitoa mchango mkubwa katika shughuli za uchumi, hususan kwenye kilimo, ujenzi wa nyumba na miundombinu.
Hivyo basi, si vibaya na sisi tukatafakari namna ambavyo Benki Kuu inavyoweza kushiriki kwenye shughuli za kiuchumi. Lakini ingefaa nieleweke kuwa ninaposema Benki Kuu kushiriki kwenye shughuli za kiuchumi sina maana kuwa ni lazima mshiriki moja kwa moja. Mnaweza kubuni mikakati au kutengeneza mazingira mazuri yatakayowezesha taasisi za fedha nchini, hususan mabenki binafsi na mifuko ya hifadhi ya jamii, kuona umuhimu wa kushiriki katika shughuli hizo. Mathalan, hivi sasa Serikali imeanzisha Benki ya Uwekezaji na Benki ya Maendeleo ya Kilimo. Hivyo, Benki Kuu inaweza kuweka masharti na kutengeneza mazingira wezeshi kwa mabenki binafsi nayo kutenga kiwango fulani cha mikopo wanayotoa kwa ajili ya shughuli za kilimo, mikopo ya nyumba na miundombinu. Kwa kufanya hivyo, nchi yetu itaweza kukuza uchumi kwa haraka na kukabiliana na tatizo la ukosefu wa ajira na umaskini.
Mheshimiwa Gavana na Wafanyakazi wa Benki Kuu;
Sambamba na kutafakari suala hilo la nafasi ya Benki Kuu katika shughuli za kiuchumi, yapo mambo mengine ambayo Benki Kuu haina budi kuchukua hatua za haraka kutafuta ufumbuzi wake au kurekebisha. Baadhi ya mambo hayo ni haya yafuatayo:
Mosi, kusimamia usambazaji wa huduma za fedha. Katika mafanikio ya Benki Kuu, nimetaja kuwa idadi ya mabenki na taasisi za fedha imeongezeka. Hata hivyo, idadi ya Watanzania wenye kupata huduma za kifedha ni ndogo sana ukilinganisha na idadi ya Watanzania. Sababu zipo nyingi lakini mojawapo kubwa ni kwamba taasisi nyingi za fedha zinafanya shughuli zake mijini wakati takriban asilimia 70 ya wananchi wanaishi vijijini. Hali hii kwa kiasi kikubwa inachangiwa na mabenki mengi kufanya zaidi biashara na taasisi za Serikali, hususan kupitia ununuzi wa dhamana na amana zinazotolewa na Benki Kuu. Cha kusikitisha zaidi ni kwamba fedha zinazotumiwa na mabenki hayo katika kununua dhamana na amana hizo ni zile zilizotunzwa katika benki hizo na taasisi mbalimbali za Serikali. Hii maana yake ni kwamba mabenki yamekuwa yakitumia fedha za Serikali kufanya biashara na Serikali lakini wanaonufaika ni wao. Na kwa kuwa utaratibu huu umekuwa ukiwanufaisha hawaoni umuhimu wa kusambaza huduma zao vijijini. Hivyo, wito wangu kwa Benki Kuu ni kwamba zihimizeni taasisi za fedha, ikiwemo mabenki, makampuni ya Bima na hata Mifuko ya Hifadhi, kupeleka huduma zao vijijini ambako Watanzania wengi wanaishi. Mkifanya hivyo, idadi ya wananchi wanaopata huduma za kibenki itaongezeka na pia itasaidia juhudi zetu za kuwaingiza wananchi katika mfumo rasmi na hatimaye kuwezesha Serikali kukusanya mapato kwa shughuli mbalimbali za maendeleo. Serikali kwa upande ilikwishaelekeza kufunguliwa kwa akaunti moja kwenye Benki Kuu ambayo taasisi zote za Serikali zitatunza fedha zao.
Pili, kushughulikia tatizo la Riba. Taasisi nyingi za fedha hapa nchini zimekuwa zikitoza riba kubwa ya mikopo. Hali hii imefanya Wajasiliamali wengi kuogopa kukopa kwenye taasisi za fedha kwa ajili ya kupanua biashara zao. Kwa wenye ujasiri wa kukopa wengi wao wanaishia kupata hasara ama kufilisiwa. Nafahamu zipo sababu nyingi zinazofanya viwango vya riba hapa nchini kuwa juu, mojawapo ikiwa ni kukosekana mfumo wa taarifa na kuwatambua wakopaji. Lakini kwa bahati nzuri Sheria ya Benki Kuu imeipa Benki hiyo mamlaka ya kuanzisha Mfumo wa Kumbukumbu za Mikopo na Madeni (Credit Reference System) ya wateja wa taasisi za fedha. Nitoe wito kwa Benki kufanyia kazi hili ili kusudi benki ziweze kushusha kiwango cha riba. Suala hili la riba kubwa pia limekuwa likisababishwa na tatizo nililoeleza hapo juu kuhusu mabenki kupenda kufanya biashara na taasisi ya Serikali zaidi ambako wamekuwa wakipata faida kubwa.
Tatu, kulinda thamani ya shilingi. Nafahamu Sheria ya Benki Kuu ya sasa hatoi nafasi ya moja kwa moja kwa Benki Kuu kulinda thamani ya sarafu yetu. Thamani ya shilingi inaamuliwa na nguvu za soko. Hata hivyo, zipo njia ambazo Benki Kuu inaweza kutumia katika kudhibiti kuporomoka kwa thamani ya shilingi yetu. Moja ya njia hizo ni kudhibiti matumizi ya fedha za kigeni, hususan Dola ya Marekani, hapa nchini. Jambo hili limekuwa likizungumzwa mara nyingi lakini hakuna hatua mahsusi zinazofanyika. Sijui kwa nini linashindikana maana nafahamu nchi nyingi zilizoendelea na zinazoendelea, zikiwemo za Afrika, ambazo zimefanikiwa katika kusimamia suala hili. Nitoe wito kwenu Benki Kuu mshirikiane na vyombo vingine vinavyohusika katika kuhakikisha suala hili linasimamiwa ipasavyo. Hii itasaidia sio tu kuzuia kuporomoka kwa thamani ya shilingi yetu bali pia kuzuia uwezekano wa nchi yetu kutumika kama sehemu ya kutakatisha fedha haramu kutoka kwa waharifu, wakiwemo magaidi na wafanyabiashara wa madawa ya kulevya.
Nne, kulinda usalama na ubora wa huduma. Maendeleo ya sayansi na teknolojia yameleta mageuzi makubwa kwenye sekta ya fedha, ikiwemo uwepo wa huduma za kieletroniki kama vile mashine za kutoa fedha (ATM) na huduma za kibenki kwa njia ya simu za viganjani (tigo pesa, M-pesa, airtel money n.k). Matumaini yangu ni kwamba Benki Kuu mmejipanga vizuri katika kuhakikisha kunakuwa na usalama wa huduma hizo lakini pia kuhakikisha Serikali inapata mapato yake stahiki. Mathalan, katika kipindi cha mwezi Machi 2016 pekee, shughuli za kibenki zilizofanyika (transactions) kwa njia ya simu za viganjani ni takriban shilingi trilioni 5.5 lakini sina hakika kama Serikali ilikusanya mapato yake yote yaliyotokana na shughuli hizo za kibenki. Nitoe wito kwa Benki Kuu mshirikiane na Mamlaka ya Mawasiliano katika kuhakikisha Serikali inakusanya mapato yake.
Tano, usimamizi na udhibiti wa Maduka ya kubadilishia fedha za kigeni (Bureau de Change). Ni vema Benki Kuu ikaimarisha usimamizi kuhusu uendeshaji wa maduka haya. Mnapaswa kufahamu uhalali wa fedha zinazobadilishwa na matumizi yake, ili maduka haya yasitumike kutakatisha fedha haramu au kutorosha fedha nje ya nchi na hatimaye kuharibu uchumi wetu.
Sita, suala la mfumko wa bei. Hivi punde nimewapongeza kuhusu kushuka kwa mfumko wa bei nchini. Hata hivyo, licha ya kushuka kwa mfumko wa bei hali ya maisha ya Watanzania wengi bado ni ngumu na huenda takwimu za kushuka kwa bei tunazowatangazia hawaoni umuhimu wake. Nitoe wito kwenu kujipanga vizuri katika kuhakikisha uchumi wa nchi unakua kwa kasi na wananchi waone manufaa ya takwimu tunazozitoa.
Mheshimiwa Gavana na Wafanyakazi wa Benki Kuu;
Nimeeleza mafanikio na changamoto za Benki Kuu katika kipindi cha miaka 50 iliyopita. Na huenda nimeeleza zaidi changamoto kuliko mafanikio. Nimefanya hivyo kwa makusudi kabisa kwa vile nataka msibweteke kwa kuwa nchi yetu bado inakabiliwa na changamoto nyingi. Nimefanya hivyo pia kwa kuwa nafahamu Benki Kuu chini ya uongozi mahiri wa Gavana Ndulu mnao uwezo mkubwa wa kuzitatua changamoto za kiuchumi zilizopo nchini.
Mimi naamini Benki Kuu mkiamua kusimamia haya niliyoyaeleza na mengineyo ambayo sikuyaeleza nchi yetu itaweza kupata maendeleo ya kiuchumi tena kwa haraka. Nasema hivyo, kwa sababu nchi yetu ina kila kitu. Tuna rasilimali za kutosha. Nchi yetu ipo kwenye eneo la kimkakati ambapo Bandari yetu inahudumia nchi nyingi za ukanda wetu ambazo hazina bahari. Aidha, nchi yetu ina amani na utulivu. Hivyo, nina imani kuwa kama kila mtu atatimiza wajibu wake ipasavyo nchi yetu itapata maendeleo.
Serikali kwa upande imejipanga kushirikiana na watumishi wa Benki Kuu pamoja na wafanyakazi wote nchini ili kuleta maendeleo ya haraka kwa nchi. Mtakumbuka wakati wa Sherehe za Mei Mosi, Serikali ilifanya uamuzi wa kupunguza kiwango cha kodi ya mapato kwa watumishi wa Serikali kutoka asilimia 11 hadi 9. Tulifanya hivyo kwa lengo la kutoa motisha kwa wafanyakazi. Kinyume na baadhi ya watu wanavyosema, Serikali ya Awamu ya Tano inawapenda na kuwathamini wafanyakazi wa Serikali. Na hapa napenda kufafanua uamuzi wa Serikali wa hivi karibuni wa kusimamisha ajira mpya na promosheni zote Serikalini. Uamuzi huu umetokana na kuwepo kwa tatizo kubwa la wafanyakazi hewa Serikalini ambao idadi yake ni zaidi ya 12,000 hivi sasa. Aidha, Serikali imebaini wapo wastaafu hewa zaidi ya 2000 ambao nao wanalipwa pensheni. Hivyo, ili kukabiliana na tatizo hili, Serikali imeamua kusitisha zoezi la kuajiri watumishi wapya na kutoa promosheni ili kujipa nafasi ya kushughulikia tatizo la wafanyakazi hewa. Nina imani zoezi hili litakamilika ndani ya kipindi cha miezi miwili na baada ya hapo taratibu za ajira mpya na promosheni zitaendelea kama kawaida.
Mheshimiwa Gavana;
Wageni Waalikwa;
Mabibi na Mabwana;
Tupo hapa kwa ajili ya kuadhimisha miaka 50 ya Benki Kuu. Nafahamu kwenye programu yenu mmeandaa mambo mengi ya kufanya, ikiwemo kongamano kwa ajili ya kujadili masuala mbalimbali. Hivyo, nisingependa kuwapunja muda wenu. Hata hivyo, kabla sijahitimisha hotuba yangu, ningependa kuzungumzia suala moja la mwisho.
Hivi karibuni, nchi yetu imekamilisha kuandaa Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano ambao utatekelezwa katika kipindi cha mwaka 2016/17 hadi mwaka 2020/21. Mpango huu unadhima ya kujenga uchumi wa viwanda ili kuchochea mageuzi ya kiuchumi na maendeleo ya watu. Utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo ya Taifa unatarajiwa kugharimu takriban shilingi trilioni 107, zikiwemo trilioni 59 kutoka Serikalini. Je Benki Kuu mmejipangaje katika kuhakikisha Mpango huu utatekelezwa?
Naamini mtakubaliana nami kuwa, moja ya changamoto kubwa ambayo nchi nyingi za Afrika inakabiliana nayo katika kutekeleza mipango na miradi mbalimbali ya maendeleo ni ukosefu wa fedha. Kutokana na kukosa fedha za kutosha, tumebaki tukitegemea sana mikopo na misaada kutoka kwa wahisani, ambayo katika miaka ya hivi karibu imepungua sana. Nyakati nyingine imekuwa ikitolewa kwa kuchelewa ama kwa masharti magumu sana. Hivyo, nchi zetu hazina budi kutafuta mbinu za kukabiliana na changamoto hii. Ni kwa sababu hii, nimefurahi sana kuona kuwa kaulimbiu ya kongamano lenu itahusu “Namna ya Kupata Fedha za Maendeleo na Athari za Mikopo na Misaada (Beyond Aid and Concessional Borrowing: New Ways of Financing Development in Africa and its Implications)”. Nina imani kuwa uwepo wa washiriki kutoka nchi za EAC na SADC, pamoja na Mtaalam Prof. Justin Lin kutoka nchi ya China, ambayo miaka kadhaa iliyopita ilikuwa inalingana na nchi nyingi za Kiafrika kimaendeleo lakini hivi sasa ni kinara miongoni mwa nchi zinazotoa misaada mingi, itasaidia kubadilishana uzoefu wa namna ya kukabili changamoto hii. Na mimi nitashukuru na kufurahi sana kama nitapata ripoti ya Kongamano lenu.
Mheshimiwa Gavana;
Menejimeti na Wafanyakazi wa Benki Kuu;
Wageni Waalikwa;
Mabibi na Mabwana;
Napenda kuhitimisha kwa hotuba yangu kwa kurudia kutoa pongezi nyingi kwa Benki Kuu kwa kazi kubwa na nzuri mliyoifanya katika kipindi cha miaka 50 iliyopita. Nawapongeza pia kwa mchango wa fedha mlioutoa kwa ajili ya kukabiliana na tatizo la madawati katika shule zetu. Wito wangu kwenu mzidi kuongeza juhudi ili miaka 50 ijayo iwe ya mafanikio makubwa ya kiuchumi kwa nchi yetu.
Mungu Ibariki Benki Kuu!
Mungu Ibariki Tanzania!
“Asanteni Kwa Kunisikiliza”
- Jun 02, 2016
HOTUBA YA MHESHIMIWA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA DK. JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI WAKATI WA KUWEKA JIWE LA MSINGI LA UJENZI WA MAKTABA MPYA YA CHUO KI...
Soma zaidiHotuba
Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais Mstaafu na Mkuu wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam;
Mheshimiwa Prof. Joyce Ndalichako, Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi;
Mheshimiwa Jaji Joseph Warioba, Makamu wa Kwanza wa Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Mheshimiwa Dkt. Mohamed Gharib Bilal, Makamu wa Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Mheshimiwa LU Youqing, Balozi wa China nchini Tanzania;
Mheshimiwa Ally Hapi, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni na Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam;
Mheshimiwa Mzee Pius Msekwa, Makamu Mwenyekiti Mstaafu wa Chama Cha Mapinduzi (Tanzania Bara);
Prof. Rwekaza Mukandala, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam;
Waheshimiwa Viongozi Waandamizi wa Serikali mliopo;
Makamu Wakuu wa Chuo Wastaafu mliopo;
Wahadhiri na Viongozi Waandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam;
Mwakilishi wa Kampuni ya Jiangsu Jiangdu kutoka China;
Ndugu Wanafunzi na Wanajumuiya ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam;
Wageni Waalikwa;
Mabibi na Mabwana:
Awali ya yote, napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwako Mheshimiwa Mkuu wa Chuo, Rais Mstaafu Jakaya Mrisho Kikwete na uongozi mzima wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam kwa kunikaribisha ili nijumuike nanyi katika shughuli hii muhimu ya uwekaji Jiwe la Msingi la Ujenzi wa Maktaba. Nimearifiwa kuwa Maktaba hii itakuwa ni ya aina yake hapa nchini, kwenye eneo letu la Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla. Nawashukuru sana kwa mwaliko wenu.
Nitumie fursa hii pia kuwashukuru wanajumuiya wote wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam na vyuo vingine nchini kwa kushiriki kikamilifu kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka jana. Aidha, napenda kutoa shukran zangu za dhati kwenu kwa kunipigia kura nyingi zilizoniwezesha kuchaguliwa kuwa Rais wa Awamu ya Tano. Ninawashukuru sana. Uchaguzi sasa umekwisha na napenda kuwaahidi kuwa sitawaangusha. Nitafanya kazi kwa kutumia elimu na nguvu zangu zote kwa ajili ya kuleta maendeleo nchini kwetu. Na kwa bahati nzuri elimu yangu nimeipata kwenye Chuo hiki.
Mheshimiwa Mkuu wa Chuo;
Wanajumuiya wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam;
Mabibi na Mabwana;
Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam kina historia kubwa. Hiki ni Chuo Kikuu cha kwanza hapa nchini na bado mpaka sasa ndicho kinaongoza kwa ubora wa elimu. Kimetoa mchango mkubwa kwa taifa letu, Afrika na duniani kwa ujumla. Viongozi wengi ndani na nje ya nchi yetu wamesoma kwenye Chuo hiki. Hivyo basi, kwenu ninyi wanafunzi mliopata fursa ya kusoma kwenye chuo hiki hamna budi kujiona kuwa ni wenye bahati sana.
Mkuu wa Chuo hiki, ambaye pia ni Rais Mstaafu wa nchi yetu, Mzee Kikwete, naye amesoma kwenye chuo hiki. Na napenda kusema hapa kuwa nilimteua kuwa Mkuu wa Chuo hiki kwa vile natambua kuwa anakifahamu vizuri Chuo hiki na ametoa mchango mkubwa katika maendeleo ya chuo hiki. Nipo hapa kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa Maktaba ya Chuo, ambayo fedha za ujenzi zilipatikana kutokana na jitihada kubwa alizozifanya yeye binafsi wakati akiwa Rais wa nchi yetu. Napenda kutumia fursa hii, kumshukuru na kumpongeza kwa dhati Mheshimiwa Mkuu wa Chuo na viongozi wengine ulioshirikiana nao katika kufanikisha kupatikana kwa fedha za ujenzi wa Maktaba hii. Nitumie fursa hii kuwahimiza wanafunzi kutumia vizuri Maktaba hii. Nina imani kuwa Maktaba hii itawanufaisha pia Watanzania wengine ambao si wanafunzi wa chuo hiki.
Mabibi na Mabwana;
Kama nilivyosema hapo awali, Maktaba hii itakuwa ni kubwa na ya kisasa. Nimearifiwa kuwa maktaba hii itahudumia jumla ya watu 2,600 kwa wakati mmoja, ikijumuisha eneo la kusomea lenye uwezo wa kuhudumia watu 1,800. Ujenzi wa Maktaba hii utagharamiwa kwa fedha za msaada (grant) kutoka Serikali ya China kiasi cha Dola za Marekani 41,280,000. Napenda kutumia fursa hii, kupitia kwa Mheshimiwa Balozi LU, kutoa shukrani zangu nyingi kwa Serikali ya China kwa kufadhili mradi huu. Kwa mara nyingine China imedhihirisha kuwa ni rafiki wa kweli wa Tanzania.
Urafiki wa Tanzania na China ni wa muda mrefu. China imetoa misaada mingi na kufadhili miradi mbalimbali hapa nchini kwetu tena bila kuwepo kwa masharti magumu. Serikali ya China ilitusaidia kujenga Reli ya TAZARA inayounganisha nchi yetu na nchi jirani ya Zambia. Hata hivi majuzi tu China imekubali kushirikiana na nchi zetu mbili kuanza kuikarabati reli ya TAZARA ili usafiri urejee kwenye hali yake ya kawaida. Aidha, Serikali ya China imekubali kushirikiana na nchi yetu kujenga reli ya kati kwa kiwango cha kimataifa yaani standard gauge kutoka Dar es Salaam kwenda mikoa ya Mwanza na Kigoma, ambayo hatimaye itaungana na reli kwenda nchi za Rwanda na Burundi. Katika ujenzi wa reli hiyo, Serikali yetu imetenga kiasi cha shilingi trilioni 1 kwenye bajeti ya mwaka ujao wa fedha kuanza ujenzi wa reli hiyo na Serikali ya China imekubali kutuongezea fedha za kukamilisha mradi huo. Napenda kuwashukuru tena ndugu zetu wa China kwa misaada yao na kuomba wadau wetu wengine wa maendeleo waige mfano huo wa China.
Ndugu Viongozi;
Ndugu Wanajumuiya wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam;
Mabibi na Mabwana;
Kipaumbele kimojawapo cha Serikali ya Awamu ya Tano ninayoingoza ni kuboresha na kuimarisha sekta ya elimu katika ngazi zote hapa nchini. Tangu tumeingia madarakani tayari tumeanza kuchukua hatua mbalimbali. Tumeanza kutekeleza ahadi yetu ya kutoa elimu bila malipo kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha nne, ambapo kila mwezi tunatenga kiasi cha shilingi bilioni 18.77 za kugharamia suala hilo. Baada ya kuanza kutoa elimu bila malipo idadi ya wanafunzi walioandikishwa kuanza darasa la kwanza imeongezeka maradufu kutoka 1,028,021 mwaka 2015 hadi kufikia 1,896,584 mwaka huu. Ongezeko hili, ambalo ni zaidi ya asilimia 84.5, limeibua changamoto kadhaa kwenye shule zetu, ikiwemo uhaba wa madawati na vyumba vya madarasa. Serikali itaendelea na jitihada za kurekebisha changamoto zilizojitokeza. Tunawakaribisha pia watu binafsi na wadau wengine kutoa michango yao ya hiari ili kuunga mkono jitihada za kurekebisha changamoto zilizojitokeza. Napenda kutumia fursa hii kuwashukuru Watanzania ambao wameitikia wito huu wa Serikali, kupitia kwa Wakurugenzi, Wakuu wa Wilaya na Wakuu wa Mikoa.
Kwa upande wa elimu ya juu nako tumeanza kuchukua hatua kwa kuongeza kiwango cha fedha kwa ajili ya mikopo ya wanafunzi. Baadhi yenu mnafahamu kuwa katika bajeti ya Mwaka wa Fedha 2015/2016 fedha iliyotengwa kwa ajili ya mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu ilikuwa ni takriban shilingi bilioni 340 kwa ajili ya kufadhili wanafunzi 98,300 tu. Baada ya Serikali ya Awamu ya Tano kuingia madarakani tuliongeza fedha hizo za mkopo hadi kufikia shilingi bilioni 473 na hivyo kuongeza idadi ya wanufaika hadi kufikia wanafunzi 124,358. Mpaka sasa tumeshatoa kiasi cha takriban shilingi bilioni 349 kwa ajili ya mikopo ya wanafunzi.
Ndugu Wanajumuiya wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam;
Nafahamu pametokea ucheleweshaji wa kutolewa kwa fedha za mkopo kwa robo ya muhula huu wa mwisho. Ucheleweshaji huo kimsingi ulitokana na kuchelewa kukamilika kwa zoezi la uhakiki wa wanafunzi wa vyuo vikuu. Kama unavyofahamu, nchi yetu imekuwa na changamoto ya kuwa na watumishi wasio waaminifu ambao wanatumia rasilimali za nchi ili kujinufaisha wenyewe, ikiwemo kwa kuingiza wafanyakazi hewa. Kwenye sekta ya elimu changamoto hii pia ipo. Wapo watumishi wanaotoa mikopo kwa wanafunzi hewa ama wakati mwingine mikopo hutolewa watu wasio na sifa.
Mathalan mtakumbuka miezi michache iliyopita Serikali ililazimika kufunga Kampasi za Chuo Kikuu cha St. Joseph za Songea na Arusha. Katika zoezi la kuwahamisha waliokuwa wanafunzi wa chuo hicho, ilibainika kuwa baadhi ya wanafunzi walikuwa hawana sifa hali ambayo iliyolazimu baadhi yao kurudishwa mwaka. Lakini cha kusikitisha zaidi ni kwamba miongoni mwa wanafunzi hao, walikuwepo wanafunzi 489 wa shahada ya ualimu ambao walikuwa wanapata mikopo ingawa sifa zao zilikuwa hazitoshi kusomea hata ualimu kwa ngazi ya cheti. Lakini wakati mikopo hii ikitolewa kwa wanafunzi hawa, walikuwepo wanafunzi wenye sifa waliokosa mikopo.
Ni kwa sababu hizo hizo, Serikali hivi karibuni ililazimika pia kusitisha ufundishaji wa Stashahada ya Elimu kwa wanafunzi zaidi ya 7802 waliokuwa wakisomea masomo ya Sayansi, Hisabati na Teknolojia kwenye Chuo Kikuu cha Dodoma. Nafahamu wapo baadhi ya wanasiasa wamejitokeza kujaribu kupotosha ukweli wa suala hili. Lakini ukweli ni kwamba Ripoti iliyoandaliwa na wataalam, akiwemo Dkt. Kitilya Mkumbo, ilishauri kuwa kutokana na miundombinu ya Chuo Kikuu cha Dodoma, uwezo wake ni kufundisha wanafunzi wa kozi hiyo maalum wasiozidi 1,800. Hata hivyo, ushauri huo haukutiliwa maanani. Badala yake idadi ya wanafunzi waliopelekwa chuoni hapo ilikuwa ni mara nne zaidi. Jambo la kusikitisha zaidi ni kwamba wanafuzi wengi waliopelekwa kuchukua kozi hiyo maalum hawakuwa na sifa zinazohitajika.
Kutokana na idadi ya wanafunzi kuwa kubwa, wahadhiri nao wakaanza kudai malipo ya ziada na hatimaye kuanza mgomo baridi. Kutokana na mgomo huo baridi, zikatokea taarifa kuwa wanafunzi nao wanajipanga kuanza mgomo. Kutokana na sababu hizo zote ndipo Serikali ikaamua kusitisha mafunzo hayo. Napenda kutumia fursa hii, kumpongeza Mheshimiwa Waziri Prof. Ndalichako kwa uamuzi aliochukua wa kusimamisha mafunzo hayo ili kulinda ubora wa elimu hapa nchini. Aidha, nawashukuru wanafunzi hao kukubali kuondoka kwenye eneo la shule kwa amani licha ya kuwepo kwa shinikizo kutoka kwa baadhi ya wanasiasa. Nina matumaini Wizara itakamilisha mapema zoezi la kuwachambua wanafunzi wenye sifa ili waweze kuhamishiwa kwenye vyuo vingine vya ualimu, ambavyo nimearifiwa kuwa vingi havina wanafunzi wa kutosha.
Nitumie fursa hii kutoa wito kwa wanasiasa wenzangu kuweka maslahi ya taifa mbele. Aidha, nitoe wito kwenu wanachuo kuacha kutumika na wanasiasa wasiolitakia mema taifa letu. Mmekuja hapa kusoma hivyo mnaowajibu wa kusoma kwa bidii. Niwaombe pia kuunga mkono hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali katika kuleta ustawi wa nchi yetu, ikiwemo hatua za kurudisha nidhamu nchini mwetu.
Nyote mnafahamu hapa nchini kwetu imezuka tabia ya watu kutoheshimu sheria na taratibu. Mifano ipo mingi lakini naweza kutoa mfano mmoja ulio hai wa hivi karibuni. Serikali hivi karibuni imekamilisha ujenzi wa barabara ya magari ya mwendo kasi. Mradi huo umegharimu zaidi ya shilingi bilioni 300 na lengo lake ni kuondoa kero ya foleni kwenye Jiji letu la Dar es Salaam. Hata hivyo, watu wameanza kuharibu miundombinu kwa kuitumia ndivyo sivyo, ikiwemo kufanya barabara hizo kuwa sehemu za malazi na huku baadhi ya madereva wa magari ya kawaida kuvamia barabara hizo. Cha kusikitisha haya yote yanafanyika huku mamlaka za usimamizi zikiangalia. Napenda kutumia fursa hii, kutoa wito kwa viongozi wa Dar es Salaam na Watanzania kwa ujumla kuheshimu sheria na taratibu za nchi.
Mheshimiwa Mkuu wa Chuo na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu;
Hivi punde mmetoka kueleza changamoto mbalimbali zinazokabili Chuo hiki. Changamoto hizi zimenigusa sana mimi kama kiongozi na mhitimu wa chuo hiki. Miongoni mwa changamoto zilizotajwa ipo moja ambayo imetiliwa mkazo zaidi ambayo ni uhaba wa mabweni. Binafsi naelewa madhara ya wanafunzi kuishi nje ya chuo na athari zake kwa elimu. Kwa kutambua hilo, naahidi kutoa shilingi bilioni 10 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa mabweni ya wanafunzi. Lakini ili fedha hizo zitolewa ni lazima Chuo kitafute eneo ndani ya eneo la sasa la chuo kujenga mabweni hayo. Siyo nje ya Chuo.
Natambua fedha hizi haziwezi kumaliza tatizo la uhaba wa mabweni kwa mara moja. Lakini nina imani fedha hizi zikitumiwa vizuri na kuongezwa fedha nyingine mnazozipata kutoka miradi mingine zitasaidia kupunguza uhaba wa mabweni kwa wanafunzi. Natoa wito kwa wadau wengine, hususan Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kufikiria kujenga mabweni ya wanafunzi kama ilivyofanyika kwa mradi wa Hosteli za Mabibo. Niwaombe viongozi, Mheshimiwa Waziri na Mkuu wa Chuo kuzungumza na viongozi wa mifuko hiyo ili iweze kusaidia katika kutatua tatizo hili. Nina imani kama watakubali kujenga tutaweza kupunguza tatizo hilo kwa kiwango kikubwa.
Mheshimiwa Mkuu wa Chuo;
Ndugu Wanajumuiya wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam;
Kuhusu changamoto nyingine zilizozitajwa, ikiwa ni pamoja na uhaba wa fedha za malipo ya masomo kwa wanataaluma, uhaba wa watumishi na uchakavu wa miundombinu, napenda kuwahakikishia kuwa nimezipokea changamoto hizo na ninaahidi kuwa zitashughulikiwa. Tutashughulikia kwa vile tunatambua kuwa, azma ya Serikali ya kujenga uchumi wa viwanda, inawategemea ninyi wana-taaluma. Bila ninyi ujenzi wa uchumi wa viwanda itakuwa ni ndoto.
Wito wangu kwenu tudumishe umoja na mshikamano, hususan kwa ajili ya maslahi mapana ya taifa letu. Tuondoe tofauti zetu na kila mmoja wetu ashiriki kikamilifu katika kujenga nchi yetu. Kwa bahati nzuri nchi yetu ina kila aina ya rasilimali zinazohitajika ili kupata maendeleo. Hivyo, mimi ninaamini kuwa kama sote tutashirikiana tutafanikiwa kuifanya nchi yetu kuwa mfano wa kuigwa.
Mheshimiwa Mkuu wa Chuo;
Waheshimiwa Viongozi mliopo;
Ndugu Wanajumuiya wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam;
Mabibi na Mabwana;
Napenda kuhitimisha hotuba yangu kwa kusisitiza tena umuhimu wa wanafunzi na Watanzania kwa ujumla kutumia maktaba ili kupata maarifa kuhusu taaluma mbalimbali. Naishukuru tena Serikali ya China kwa msaada huu na ninaahidi kuwa nchi yetu itaendelea kudumisha ushirikiano baina ya nchi zetu mbili na pia katika ngazi ya kimataifa.
Aidha, napenda kumpongeza Makamu wa Mkuu wa Chuo kwa kuendelea kukilea vizuri chuo hiki na hivyo kukifanya kubaki katika ubora wake. Vilevile, napenda kurudia ahadi yangu kwa wanafunzi kote nchini kuwa Serikali itahakikisha wanafunzi wanapata mikopo yao tena kwa wakati. Wito wangu kwenu wanafunzi muwe mnatoa nafasi kwa Serikali pindi panapotokea changamoto. Aidha, naomba uongozi wa Chuo nao kuwa mnawasilisha changamoto zenu mapema Serikalini ili zitatuliwe kwa haraka. Baadhi ya changamoto zinatokana na kuchelewa kuwasilishwa kwa taarifa. Kwa watumishi na Chuo tunatambua kuwa mnafanya kazi katika mazingira magumu lakini tutashirikiana ili kuboresha maslahi yenu.
Mwisho lakini sio kwa umuhimu napenda kutoa pongezi maalum kwa Prof. Mgaya. Huyu ni Mtanzania wa kweli. Baadhi ya watu walitaka kumwingizia maneno ya uongo lakini yeye alitoka hadharani na kueleza ukweli. Alikubali kuwa alikosea. Huo ndio uzalendo wa kweli.
Baada ya kusema hayo nawashukuru tena kwa kunialika kushiriki kwenye shughuli hii. Aidha, nawashukuru viongozi, wageni waalikwa na wananchi wote mliojitokeza kujumuika nasi katika shughuli hii.
“Mungu Kibariki Chuo Kikuu cha Dar es Salaam”
“Mungu Wabariki Viongozi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam”
Mungu Wabariki Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam”
“Mungu Ibariki Tanzania”
“Ahsanteni kwa kunisikiliza”
- May 31, 2016
HOTUBA YA MHE. DKT. JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, KWENYE HAFLA YA UTOAJI TUZO KWA WAZALISHAJI BORA WA VIWANDANI KWA MWA...
Soma zaidiHotuba
Dkt. Samuel Nyantahe, Mwenyekiti wa Shirikisho la Wenye Viwanda Tanzania;
Mheshimiwa Charles Mwijage (Mb), Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji;
Mheshimiwa Sospeter Muhongo (Mb), Waziri wa Nishati na Madini;
Makatibu Wakuu wa Wizara mbalimbali mliopo;
Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Viwanda;
Waheshimiwa Viongozi mliopo;
Waheshimiwa Mabalozi;
Wajumbe wa Baraza la Uongozi wa CTI;
Wenyeviti wa CTI waliomaliza muda wao;
Wanachama wa CTI;
Wageni Waalikwa;
Mabibi na Mabwana:
Napenda nianze kwa kuwashukuru Viongozi wa Shirikisho la Wenye Viwanda Tanzania kwa kunikaribisha kujumuika nanyi katika hafla hii ya Utoaji Tuzo za Rais kwa Viwanda vilivyofanya vizuri Mwaka 2015. Nawashukuru sana.
Hii ni mara yangu ya kwanza nakutana nanyi tangu nimechaguliwa kuwa Rais wa Awamu ya Tano wa nchi yetu. Napenda kutumia fursa hii kuwashukuru kwa kunipa kura nyingi kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka jana. Kura zenu ndizo zilizoniwezesha mimi kuchaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Narudia ahadi yangu niliyoitoa kipindi cha kampeni kuwa sitawaangusha.
Ndugu Mwenyekiti;
Viongozi mliopo;
Mabibi na Mabwana;
Mtakubaliana nami kuwa tangu kuanza kwa karne hii ya 21 tumekuwa tukisikia na kusoma taarifa mbalimbali za kusifu Bara letu la Afrika. Tunasikia maneno kama “Uchumi wa Afrika unakua kwa kasi”, “kati ya nchi 10 ambazo uchumi wake unakuwa kwa kasi 7 zinatoka Afrika”, “hii ni karne ya Afrika”. Ni dhahiri kuwa uchumi wa nchi za Afrika unakua kwa kasi kubwa. Kwa bahati nzuri moja ya nchi ambazo zinasifiwa kwa ukuaji uchumi wa kasi ni Tanzania. Sisi kama Watanzania na Waafrika tunapaswa kujipongeza.
Lakini wakati tukijipongeza, lipo swali la msingi ambalo sisi sote tunapaswa kujiuliza. Je, mambo gani yamefanya uchumi wa Afrika kuonekana unakua kwa kasi? Nini hasa kimebadilika kwenye nchi zetu? Ukiangalia kwa jicho makini utaona kuwa hakuna mabadiliko makubwa yaliyofanyika. Ni kweli hali ya amani na usalama imeimarika kwa kiasi kikubwa Barani kwetu. Aidha, kwenye baadhi ya nchi, ikiwemo Tanzania, kumetokea ugunduzi wa rasilimali mbalimbali za thamani, ikiwemo mafuta, gesi na madini mengine ya thamani. Ukiondoa mambo hayo, bado nchi zetu zinategemea kilimo kuwa uti wa mgongo wa uchumi. Mchango wetu kibiashara duniani ni chini ya 5%. Aidha, tunaendelea kuuza bidhaa ghafi kwenye soko la dunia na hivyo kufanya wastani wa mchango wa sekta ya viwanda kwenye pato la taifa katika nchi nyingi kuwa chini ya 15%, wakati kwenye nchi zilizoendelea ni kati ya 30 – 40%.
Hivyo basi, hatuna budi kubadilisha hali hii. Ni lazima tuhakikishe rasilimali tulizonazo tunazitumia vizuri. Tukumbuke kuwa baadhi ya rasilimali tulizonazo hazitadumu milele. Itafika wakati zitakwisha. Binafsi kama nitaulizwa ni kwa namna gani nchi za Afrika zinaweza kutumia vizuri rasilimali zake, jibu langu litakuwa moja tu. Nchi za Afrika zinapaswa kufanya mageuzi ya viwanda.
Ndugu Mwenyekiti;
Mabibi na Mabwana;
Sekta ya viwanda ni mhimili muhimu wa maendeleo ya kiuchumi duniani. Nchi nyingi duniani zimefanikiwa kupata maendeleo ya kiuchumi kupitia sekta ya viwanda, ikiwemo zile ambazo katika miaka ya 1960 na 1970 zilikuwa na uchumi sawa na Tanzania. Nchi hizo ni pamoja na China, India, Korea ya Kusini, Thailand, Malaysia, Vietnam na hata nchi jirani ya Mauritius, ambayo hivi sasa ni maarufu kwa kuzalisha sukari. Katika nchi hizo utagundua kuwa kasi ya ukuaji uchumi umetokana na ukuaji wa sekta ya viwanda. Mheshimiwa Waziri wa Viwanda ameeleza hivi punde kuwa viwanda vinasaidia kutengeneza ajira, kuongeza thamani ya mazao, kuongeza mapato ya serikali, kuchangia upatikanaji wa fedha nyingi za kigeni na pia kukuza sayansi na teknolojia kwenye nchi husika.
Ni kutokana na kutambua umuhimu wa sekta ya viwanda kwa maendeleo ya nchi, sikusita kukubali mwaliko wenu mara tu nilipoupata. Kama mtakavyokumbuka, ujenzi wa nchi ya uchumi wa viwanda ilikuwa ni ahadi yangu kubwa kipindi cha kampeni. Dhamira yangu hiyo bado ipo pale pale. Nafahamu kuwa hivi karibuni wametokea watu wanaosema kuwa mimi siwapendi wenye viwanda na matajiri. Maneno hayo ni uzushi ambao hauna ukweli wowote. Mimi nawapenda wenye viwanda nchini na naahidi nitawasaidia kwa nguvu zangu zote ili azma yetu ya kuwa na uchumi wa viwanda iweze kutimia.
Kwa bahati nzuri mipango ya ujenzi wa nchi ya viwanda tayari imeanza. Tumekamilisha kuandaa Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano utakaotekelezwa katika kipindi cha mwaka 2016/17 hadi mwaka 2020/21. Mpango huo umeeleza kuwa dhima yake kuu ni kujenga uchumi wa viwanda. Aina ya viwanda tunavyolenga kujenga ni vya uzalishaji (manufacturing industries), ambavyo hivi punde tutatoa tuzo kwa wazalishaji bora wa mwaka jana. Viwanda vya uzalishaji hutumia malighafi zinazopatikana kwa wingi ndani ya nchi, teknolojia ya kati, nguvu kazi kubwa na bidhaa zake zitatumika zaidi ndani ya nchi.
Malengo na matarajio yetu ni kwamba ifikapo mwaka 2020, sekta ya viwanda itachangia asilimia 15 ya pato la taifa kutoka asilimia 7.3 ya sasa, itatoa 40% ya ajira zote nchini na pia kuchangia upatikanaji wa fedha nyingi za kigeni. Mimi naamini jambo hili linawezekana na hasa ukizingatia kuwa nchi yetu imebarikiwa kuwa na mahitaji yote ya kujenga uchumi wa viwanda. Tunayo ardhi ya kutosha; nguvu kazi kubwa ya vijana; rasilimali za mifugo, misitu, samaki; pamoja na soko kubwa na la uhakika. Napenda kutumia fursa hii kuwapongeza wale wote wamejitoa kuwekeza kwenye sekta ya viwanda. Aidha, nawakaribisha na kuwahamasisha wawekezaji wengine wa ndani na nje kuwekeza kwenye sekta ya viwanda hapa nchini.
Wanachama wa CTI;
na Wamiliki wa Viwanda kwa ujumla;
Hivi punde tumetoka kusikiliza hotuba ya Mwenyekiti wenu, Dkt. Nyantahe, ambayo pamoja na masuala mengine ameelezea changamoto mbalimbali ambazo zinakwamisha ustawi wa sekta ya viwanda hapa nchini. Nisingependa kujibu changamoto mlizozitaja lakini itoshe tu kusema kuwa nimezisikia na tutachukua hatua mahsusi kuzishughulikia. Hata hivyo, napenda kueleza japo kwa uchache baadhi hatua, ambazo tumeanza kuchukua kujenga uchumi wa viwanda:
(i) Ujenzi wa Miundombinu ya Uchumi: Maendeleo na ustawi wa sekta ya viwanda kwa kiasi kikubwa hutegemea uwepo wa miundombinu ya uchumi ya uhakika, hususan miundombinu ya usafiri na nishati. Serikali imejipanga vizuri katika kuimarisha miundombinu ya usafiri, ikiwemo reli na barabara. Napenda kutumia fursa hii kuwaarifu kuwa katika mwaka ujao wa fedha, Serikali imetenga kiasi cha shilingi trilioni moja kwa ajili ya kuanza ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kimataifa (Standard Gauge Railway) kutoka Dar es Salaam kwenda mikoa ya Mwanza na Kigoma ambazo hatimaye zitaungana na reli zinazokwenda nchi za Burundi na Rwanda. Aidha, nchi yetu pamoja na Zambia zipo kwenye mazungumzo ya mwisho na Serikali ya China ili kuanza ukarabati wa reli ya TAZARA. Vilevile, tumepanga kuanza ujenzi wa barabara ya njia sita yenye urefu wa kilometa 128 kutoka Dar es Salaam hadi Chalinze ili kurahisisha usafirishaji wa bidhaa.
Sambamba na kuboresha na kuimarisha miundombinu ya usafiri, Serikali imeazimia kuondoa kero ya uhaba wa nishati ya umeme. Uwezo wa nchi yetu kuzalisha umeme hivi sasa ni MW 1,461.69. Tumejipanga kutekeleza miradi mingine ya umeme inayotumia gesi asilia, ikiwemo upanuzi wa Kinyerezi I (MW 185), mradi wa Kinyerezi II (MW 240) na Kinyerezi III itakayozalisha 300 MW. Aidha, tutaendelea na miradi mingine ya ufuaji umeme kwa kutumia vyanzo vingine, ikiwemo maji, jua, upepo na makaa ya mawe.
(ii) Suala la sheria na kodi/tozo: Katika kushughulikia suala hili Serikali imeunda Kamati ya Kitaifa (Regulatory Reform Committee) ambayo inaangalia kwa kina mazingira ya kufanya biashara na kutoa mapendekezo kwa Serikali. Kamati inafanya uchambuzi ili kubainisha sheria na tozo zisizo za lazima na zinazojirudia kwa lengo la kuzifuta au kuzipunguza. Nitoe wito kwenu Wafanyabiashara kuwasilisha kero zenu mbalimbali ambazo zinahitaji utatuzi wa haraka ili tuweze kuzishughulikia. Mimi nafahamu changamoto kubwa kwenye nchi yetu ni uwepo wa utitiri wa kodi sio tu kwenye sekta ya viwanda bali pia sekta nyingine, ikiwemo kilimo ambapo wakulima wanalalamikia kodi nyingi za mazao. Hivyo, ni vyema kama kodi hizi zitaangaliwa upya. Kwa bahati nzuri Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana yupo hapa hivyo nina imani ameipokea changamoto hii ya utitiri wa kodi na atachukua hatua mahsusi za kushughulikia. Mimi binafsi ningefurahi kuona wawekezaji kwenye sekta ya viwanda nchini wanapata unafuu mkubwa wa kodi na pia bidhaa zinazozalishwa nchini zinatozwa kodi ndogo kuliko zinazotoka nje.
(iii) Ukosefu wa mitaji na riba kubwa: Serikali inafahamu changamoto wanazozipata wawekezaji hasa wale wadogo na wa kati wanapotaka kukopa fedha kutoka katika mabenki. Riba kubwa na masharti magumu ya ukopaji ni baadhi ya changamoto zilizopo katika mabenki yetu. Nafahamu tatizo la kuwepo riba kubwa kwa kiasi fulani lilichangiwa na benki zetu kujikita zaidi kwenye ununuzi wa amana na dhamana za Serikali ambazo zinawapa faida kubwa za haraka. Matokeo yake benki zetu hazioni umuhimu wa kuwakopesha wafanyabiashara na wajasilimali. Tumeliona tatizo hilo na tayari tumeanza kuchukua hatua ya kukabiliana na tatizo hilo. Tuna imani mabenki sasa yataanza kutoa mikopo ya gharama nafuu kwa wafanyabiashara. Kwa upande wa Serikali, tumejipanga kuimarisha Benki ya Uwekezaji (TIB) kwa kuiongezea mtaji zaidi ili iweze kukopesha wawekezaji kwa riba nafuu na ya muda mrefu. Serikali pia itaangalia uwezekano wa kuanzisha Benki ya Maendeleo ya Viwanda (Industrial Development Bank) ili iweze kukopesha wawekezaji wengi zaidi katika sekta ya viwanda. Aidha, Serikali itaimarisha Mfuko wa Taifa wa Maendeleo ya Wajasiliamali (National Entrepreneurship Development Fund – NEDF) na Mfuko wa Dhamana na Mikopo kwa Wajasiriamali (Credit Guarantee Scheme) ili kuendelea kutoa mikopo kwa wajasiriamali wadogo na wa kati kwa lengo la kuanzisha, kukuza na kuendeleza viwanda vidogo na vya kati.
(iv) Mapambano dhidi ya rushwa: Rushwa ina athari katika kila sekta. Kwa kutambua hilo, tumeanza na tunaendelea kudhibiti mianya iliyokuwa inajitokeza katika usimamizi wa kodi katika bandari na mipaka ya nchi yetu. Lengo ni kulinda viwanda vya ndani na kuhakikisha kuwa tunaondoa ushindani usio wa haki. Nitoe onyo kwa watendaji wa Serikali ambao wanaendekeza vitendo vya rushwa kuacha mara moja. Atakayebainika kuendelea na vitendo hivyo na kukwamisha maendeleo ya viwanda nchini, sitasita kumchukulia hatua. Lakini wenye viwanda nanyi nawaomba muweke maslahi ya taifa mbele na kuacha kuendekeza vitendo vya rushwa. Sote tukishirikiaa tutashida vita hii.
Ndugu Mwenyekiti;
Wakati Serikali inashughulikia changamoto mlizozieleza, yapo baadhi ya mambo ambayo ninyi wenye viwanda mnapaswa kuchukua hatua. Mathalan, Tanzania ni mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC). Jumuiya hizi mbili kwa pamoja zina idadi ya watu takriban milioni 380. Hili ni soko kubwa, ambalo kama mngelitumia vizuri, mngeweza kuinua biashara zenu na pia kuchangia uchumi wa nchi yetu. Kwa nini tunashindwa kutumia fursa hii? Mathalan, mwezi uliopita Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini alikuja hapa nchini na katika mazungumzo yetu aliniomba kuhamasisha wafanyabiashara wa Tanzania kupeleka unga na mahindi nchini mwake. Hivyo basi, nitoe wito kwenu kuchangamkia fursa zinazotakana na nchi yetu kuwa mwanachama wa jumuiya hizo mbili.
Suala jingine linahusu ukwepaji wa kodi. Ukwepaji wa kodi una athari kubwa kwenye sekta ya viwanda. Kutokana na ukwepaji kodi, bidhaa kutoka nje zimekuwa zikifurika nchini na kuuzwa kwa bei ya chini. Matokeo yake bidhaa zinazozalishwa na viwanda vya ndani zinashindwa kuhimili ushindani na hatimaye kusababisha viwanda husika kushindwa kuendelea na uzalishaji. Mimi nina uhakika ninyi wenye viwanda mnawafahamu wakwepa kodi. Hivyo, niwaombe muwafichue watu wanaokwepa kodi ili kulinda viwanda vyenu lakini pia kuiwezesha Serikali kupata mapato inayostahili.
Ndugu Mwenyekiti;
Mabibi na Mabwana;
Tupo hapa kwa ajili ya kutoa tuzo kwa wazalishaji bora wa viwandani wa mwaka 2015. Hivyo, nafahamu kuwa shauku kubwa ya watu wengi hapa ni kutaka kujua washindi wa Tuzo ya Mzalishaji Bora Viwandani wa mwaka jana. Kwa sababu hiyo sitapenda kuendelea kuwachosha kwa hotuba ndefu. Lakini kabla ya zoezi la utoaji tuzo halijaanza, napenda kutoa pongezi zangu za dhati kwa wale wote walioshiriki katika kubuni wazo la kuanzisha tuzo hii. Nimearifiwa mashindano haya yalianzishwa mwaka 2005 kwa madhumuni ya kuleta ushindani kwa wenye viwanda ili kukuza sekta hiyo nchini. Vigezo vinavyotumika kumpata mshindi ni pamoja na:
(i) Kuangalia kiasi ambacho kiwanda kimeuza bidhaa zake nje;
(ii) Kuongeza uzalishaji;
(iii) Kutoa ajira, hususan kwa wanawake;
(iv) Kuboresha mazingira; na
(v) Kutoa huduma kwa jamii inayozunguka (Corparate Social Responsibility).
Nitumie fursa hii kuwapongeza wale wote watakaoibuka washindi kwa mwaka huu. Aidha, napenda kuwatia moyo wale wote ambao mwaka huu hawatafanikiwa. Ni imani yangu kuwa mkiongeza bidii huenda nanyi mwakani mtaibuka washindi.
Ndugu Mwenyekiti;
Waheshimiwa Mawaziri;
Viongozi mliopo;
Wageni Waalikwa;
Mabibi na Mabwana;
Napenda kuhitimisha hotuba yangu kutoa tena shukran zangu za dhati kwa Mheshimiwa Waziri na Mwenyekiti wa CTI kwa kunialika kushiriki kwenye hafla hii. Aidha, napenda kupongeza CTI kwa kazi kubwa mnayoifanya ya kuendeleza sekta ya viwanda hapa nchini. Mnafanya kazi kubwa sana. Nitumie fursa hii pia kuwapongeza pamoja na wadhamini wenu wakiongozwa na Benki M kwa kuandaa vizuri hafla hii. Wito wangu kwenu muangalie uwezekano kwenye miaka ijayo mashindano haya yashirikishe hata wale ambao si wanachama wa CTI. Aidha, muangalie uwezekano wa kuanzisha maonesho ambayo yatahusisha bidhaa zinazozalishwa na viwanda vya ndani tu ili kutoa fursa kwa walaji wa Tanzania na wa nje ya nchi kufahamu bidhaa zetu. Suala hili ni muhimu sana ili kuwahamasisha wananchi kupenda bidhaa za ndani. Nitumie fursa hii pia kuwahimiza Watanzania wenzangu kupenda bidhaa zinazozalishwa na viwanda vya ndani. Mkifanya hivyo, mtakuza sekta ya viwanda, mtaongeza fursa za ajira na kujenga uchumi wa taifa letu.
Mwisho lakini sio kwa umuhimu, napenda kumpongeza Mheshimiwa Rais Mstaafu Jakaya Mrisho Kikwete, ambaye alikuwa mlezi wa shirikisho hili kwa miaka 10 iliyopita. Nami ninapochukua jukumu hili la kuwa mlezi wenu, nawaahidi kuwasaidia kwa nguvu zangu zote na kuwapa ushirikiano wa kutosha ili ndoto yetu ya kuwa na Tanzania ya Viwanda itimie. Pamoja tutaweza.
Baada ya kusema hayo sasa nipo tayari kutekeleza jukumu lililonileta la kutoa tuzo kwa washindi wa Tuzo ya Rais ya Mwaka ya Wazalishaji Bora Viwandani.
Mungu Ibariki CTI!
Mungu Wabariki wenye Viwanda!
Mungu Ibariki Tanzania!
Mungu Ibariki Afrika!
“Ahsanteni sana kwa kunisikiliza”
- May 26, 2016
HOTUBA YA MHESHIMIWA DKT. JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, WAKATI WA KUFUNGUA MKUTANO WA MASHAURIANO WA BODI YA USAJILI WA...
Soma zaidiHotuba
Mheshimiwa Profesa Makame Mbarawa (Mb), Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano;
Mheshimiwa Paul Makonda, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam;
Eng. Joseph M. Nyamhanga, Katibu Mkuu (Ujenzi) Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano;
Eng. Consolata Ngimbwa, Mwenyekiti wa Bodi ya Usajili wa Makandarasi;
Wenyeviti wa Bodi mbalimbali hapa nchini;
Wajumbe wa Bodi ya Usajili wa Makandarasi;
Bw. Rhoben Nkori, Kaimu Msajili wa Bodi ya Usajili wa Makandarasi;
Ndugu Makandarasi;
Wadau wa Sekta ya Ujenzi;
Wageni Waalikwa;
Mabibi na Mabwana:
Awali ya yote, napenda kuwashukuru Mheshimiwa Waziri na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakandarasi kwa kunikaribisha kufungua mkutano huu wa Mashauriano. Kama mnavyofahamu nilikuwa Waziri wa Ujenzi kwa takriban miaka karibu 15. Moja ya taasisi nilizokuwa nazisimamia ni Bodi ya Wakandarasi. Hivyo, kuwepo mahali hapa najisikia furaha sana.
Napenda pia kutumia fursa hii kuwashukuru sana wakandarasi wote kwa kuniunga mkono kipindi cha Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana hadi kufanikiwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Niliahidi wakati wa kampeni kuwa sitawaangusha. Leo narudia tena kuwa sitawaangusha. Nayasema hayo huku nikifahamu fika kuwa nchi yetu inakabiliwa na changamoto nyingi. Lakini naamini tutashirikiana kwa pamoja kuzitatua na kuleta maendeleo nchini kwetu.
Wageni Waalikwa;
Mabibi na Mabwana;
Sekta ya Ujenzi ni moja ya sekta nyeti na muhimu katika kuleta maendeleo ya nchi kiuchumi. Kimsingi, hii ndiyo sekta mama ya maendeleo ya kiuchumi. Maendeleo ya sekta nyingine zote, ikiwemo kilimo, utalii, viwanda, biashara, madini n.k yategemea sekta ya ujenzi. Mathalan, Watanzania takriban asilimia 75 wanategemea kilimo kuendesha maisha yao ya kila siku. Lakini shughuli za kilimo zinahitaji zana, ambazo zinatengenezwa na makandarasi, ikiwemo matreka, maghala ya kuhifadhi chakula n.k. Hivyo hivyo, kwa sekta za uvuvi; utalii; viwanda; madini, ujenzi wa miundombinu ya usafiri, nishati na maji n.k. Hakuna shughuli yoyote ya kiuchumi inaweza kufanyika bila kutegemea wakandarasi na wahandisi. Hivyo basi, kwa ufupi, wakandarasi ni muhimu sana kwa maendeleo ya kiuchumi ya taifa lolote duniani, ikiwemo Tanzania.
Kwa kutambua umuhimu wa wakandarasi kwa maendeleo ya nchi yetu, sikusita kukubali mwaliko wa Mheshimiwa Waziri kujumuika nanyi hii leo. Ninafahamu endapo wakandarasi wakitetereka, azma ya nchi yetu kuwa nchi ya uchumi wa kati unaoongozwa na viwanda ifikapo mwaka 2025 itakuwa ngumu kuifikia.
Ndugu Makandarasi na Washiriki wa Mkutano huu;
Licha ya umuhimu wa wakandarasi katika maendeleo ya nchi, sekta ya ujenzi inakabiliwa na changamoto nyingi. Baadhi ya changamoto zinatokana na sababu za kimfumo na kisheria. Mathalan, hivi punde tumetoka kusikia kuwa nchi yetu ina wakandarasi 8,331 hivi sasa. Hii ina maana kuwa nchi yetu yenye takriban watu milioni 50, ina wastani wa mkandarasi mmoja katika kila watu 6000. Idadi hii ni ndogo sana ukilinganisha na nchi zilizoendelea. Kwa mfano, Japan ina wastani wa mkandarasi mmoja kwa kila watu 50. Hivyo basi, hatuna budi kufanya jitihada za kuongeza idadi ya wakandarasi nchini.
Changamoto nyingine inayokabili wakandarasi hapa nchini ni kukosa kazi. Tatizo hili linasababishwa na mambo mengi, mojawapo ikiwa ni gharama za ukandarasi kuwa juu. Nitoe mfano, hivi karibuni Idara ya Mahakama imetangaza zabuni ya kujenga mahakama za mwanzo na wilaya. Fedha iliyotengwa kutekeleza mradi huo ni shilingi bilioni 24, ambapo makadirio ya ujenzi wa mahakama moja ni shilingi milioni 200. Lakini cha kusikitisha gharama za ujenzi zilizotolewa na wakandarasi wengi wa ndani ni kati shilingi milioni 600 na bilioni 1.4. Ni dhahiri kwa gharama hizi, hata ile dhamira yetu ya kuwapa upendeleo maalum wakandarasi wa ndani, hasa kwa miradi inayotekelezwa kwa fedha za ndani, itakuwa ngumu kuitekeleza. Hivyo basi, niwaombe wakandarasi wazalendo kurekebisha hali hii ya kufanya gharama zenu kuwa juu.
Ndugu Makandarasi na Washiriki wa Mkutano huu;
Nafahamu kuwa wakati mwingine tatizo hili la gharama kuwa juu linasababishwa na upande wetu sisi Serikali. Baadhi ya watumishi wasio waaminifu wanadai rushwa kutoka kwenu kabla ya kutoa zabuni. Matokeo yake wakandarasi mnalazika kupandisha gharama ili kufidia fedha mnazotoa kwa ajili ya rushwa. Wito wangu kwenu badala ya kutoa rushwa, wafichueni watendaji waomba rushwa ili washughulikiwe. Kwa bahati nzuri, leo hapa tunaye Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU. Nilimwomba ahudhurie mkutano huu ili muweze kujadiliana naye kuhusu namna ya kukabiliana na rushwa katika sekta yenu. Nina imani mkishikiriana vizuri na TAKUKURU, tatizo la rushwa litapungua kama siyo kumalizika kabisa na hatimaye kazi za ukandarasi zitatolewa kwa kuzingatia uwezo.
Lakini sio rushwa pekee ndiyo inafanya gharama za ukandarasi kuwa juu. Lipo tatizo jingine la kuchelewa kutolewa kwa malipo ya kazi. Kwa bahati nzuri suala hili nalifahamu vizuri. Wakati nikiwa Waziri wa Ujenzi mara kadhaa nilishuhudia wakandarasi wakifanya kazi zao bila kufahamu lini watalipwa. Kutokana na hali hiyo, wakandarasi wakati mwingine walilazimika kuongeza gharama zao ili kuweka tahadhari endapo watachelewa kulipwa malipo yao au thamani ya fedha itashuka.
Napenda kutumia fursa hii kuwaarifu wakandarasi kuwa Serikali imeliona tatizo hili na tayari tumeanza kulishughulikia. Kama alivyosema Mheshimiwa Waziri, Serikali imeanza kulipa madeni yote iliyokuwa ikidaiwa na wakandarasi. Kiasi cha shilingi bilioni 650 tayari kimetolewa kuwalipa Makandarasi wa miradi mikubwa ya barabara. Aidha, tumetoa shilingi bilioni 462 kutoka Mfuko wa Babarara kuwalipa Makandarasi wa ndani wanaofanya kazi za matengenezo na ukarabati wa barabara. Tutaendelea kuwalipa madeni yenu. Hivyo, niwaombe nanyi muanze kushusha gharama zenu. Mkishusha gharama mtaweza kupata kazi nyingi na hivyo kupanda daraja na hatimaye kupata miradi mikubwa.
Ndugu Makandarasi na Washiriki wa Mkutano;
Pamoja na changamoto hizo za kimfumo na taratibu nilizozieleza, zipo nyingine ambazo mnazisababisha ninyi wenyewe. Mojawapo ya changamoto hizo ni kukosekana kwa umoja baina yenu. Nakumbuka wakati nikiwa Waziri nilijitahidi sana kuwahimiza kujenga umoja miongoni mwenu ili kuwawezesha kupata miradi mikubwa mtakayoitekeleza kwa pamoja (joint ventures). Hata hivyo, bado suala hili limekuwa gumu. Bila shaka, mnashindwa kujenga umoja kwa sababu ya ubinafsi na wivu.
Changamoto nyingine inayosababishwa na ninyi wenyewe ni ukiukaji wa maadili yenu. Hivi punde Msajili ametoka kusema kuwa ni kawaida kukuta leseni ya mkandarasi mmoja kutumiwa na mkandarasi mwingine, ambaye wakati mwingine anaweza kuwa hana sifa. Halikadhalika, wapo wakandarasi ambao wamesajili makampuni yao lakini hawana vifaa vya kufanyia kazi au hata ofisi maalum. Mambo haya yote kwa ujumla wake, yamekuwa na athari kubwa kwenu ninyi wakandarasi kwa kuwafanya msiaminike.
Hivyo basi, nitumie fursa hii kuwaomba tena ndugu zangu wakandarasi kujenga umoja miongoni mwenu. Nawaomba pia mjitahidi kulinda taaluma na maadili yenu ya kazi. Sambamba na kujenga umoja na kulinda taaluma, napenda kutoa wito kwenu kuunda timu maalum itayokuwa ikiwashauri namna ya kuomba kazi mbalimbali za ukandarasi. Nasema hivyo kwa kuwa wakati mwingine mnakosa kazi kwa kukosa utaalam wa kuomba kazi hizo.
Ndugu Makandarasi na Washiriki wa Mkutano;
Hivi punde Mwenyekiti wenu amewasilisha ombi maalum kwangu kuhusu wakandarasi wa ndani kupewa kipaumbele. Napenda kuwahakikishia kuwa nimelipokea ombi hilo na ninawaahidi kuwa nitalifanyia kazi. Nitawahimiza Mawaziri wote kulipa uzito unaostahili suala hili katika miradi inayotekelezwa kwenye Wizara zao. Hakuna sababu ya kushindwa kutekeleza suala hilo hasa kwa kuzingatia idadi ya wakandarasi wa ndani bado ni ndogo.
Mwenyekiti ameeleza hivi sasa hapa nchini kwetu idadi ya makandarasi kutoka nje ni asilimia 4 na wakadarasi wa ndani ni asilimia 96. Hata hivyo, miradi inayotekelezwa na wakandarasi wa ndani ni asilimia 46 tu, wakati wenzenu kutoka nje ambao idadi yao ni ndogo kuliko ninyi, wanatekeleza asilimia 56 ya miradi yote. Hivyo, hatuna budi kubadilisha hali hiyo kwa kutoa upendeleo maalum kwa wakandarasi wa ndani. Kwa kufanya hivyo tutakuwa tunawajengea uwezo wakandarasi wetu. Bahati nzuri nchi yetu inayo sheria ambayo inaelekeza kuwa kwa miradi ambayo thamani yake haizidi shilingi bilioni 10, kipaumbele kiwe kwa wakandarasi wa ndani. Aidha, tunayo mifano ya mahali ambapo tuliwahi kuwapa kazi wakandarasi wa ndani walifanya na matokeo yalikuwa ni mazuri. Mfano mzuri ni ujenzi wa Daraja la Mbutu ambalo wakandarasi wa ndani walishirikiana kujenga daraja hilo kwa gharama za takriban shilingi bilioni 11 wakati makadirio ya awali ilikuwa shilingi bilioni 20.
Ndugu Makandarasi na Washiriki wa Mkutano;
Kabla ya kuhitimisha hotuba yangu, napenda kueleza suala la mwisho. Hivi karibuni nchi yetu inatarajiwa kuanza utekelezaji wa miradi mikubwa, ikiwemo ujenzi wa Bomba la Mafuta kutoka Hoima nchini Uganda hadi Bandari ya Tanga. Aidha, tunatarajia kuanza ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kimataifa (Standard gauge) yenye urefu wa takriban kilometa 1, 200 kutoka Dar es Salaam kwenda mikoa ya Mwanza na Kigoma. Reli hii pia itaunganisha nchi yetu na nchi za Burundi na Rwanda. Kwenye bajeti ya mwaka ujao wa fedha 2016/2017 tumetenga kiasi cha shilingi trilioni moja ili kuanza ujenzi. Sambamba na miradi hiyo, ipo miradi mingine ya ujenzi ya viwanda, ikiwemo Kiwanda cha Mbolea kitakachojengwa Kilwa, ambacho kitakuwa kikubwa zaidi Barani Afrika.
Hii ni miradi mikubwa. Hata hivyo, sina hakika kama wakandarasi wetu wa ndani mmejipanga vizuri kutumia fursa za miradi hiyo mikubwa kutekelezwa hapa nchini. Nilidhani mngetumia mkutano huu kujadili fursa zitakazopatikana kutoka kwenye miradi hiyo lakini nimeangalia ajenda zenu sijaona mahali popote mtakapozungumzia miradi hiyo. Binafsi nitasikitika sana kama katika kutekeleza miradi hii hapatakuwa na mkandarasi yeyote wa Tanzania. Hivyo basi, rai yangu kwenu jipangeni vizuri ili nanyi mshikiri katika ujenzi wa miradi hii. Lakini ili kuwa na uhakika wa kupata kazi kwenye miradi, narudia tena ombi langu kwenu kujenga umoja na ushirikiano.
Mheshimiwa Waziri;
Mwenyekiti wa Bodi;
Ndugu Wakandarasi;
Wageni Waalikwa;
Mabibi na Mabwana;
Napenda kuhitimisha hotuba yangu kwa kuwashukuru tena Mheshimiwa Waziri na Mwenyekiti wa Bodi kwa kunialika. Napenda kuwahakikishia ndugu wakandarasi kuwa nipo pamoja nanyi. Nimeshirkiana nanyi kwa kipindi kirefu. Naamini mtampa Waziri mpya ushirikiano kama mlionipa mimi.
Mwisho lakini sio kwa umuhimu nautakia mkutano huu wa Mashauriano majadiliano mema. Nawasihi mjadili kwa kina na bila woga changamoto mbalimbali zinazowakabili na kubainisha njia za kuzitatua, ili kwenda sambamba na kaulimbiu ya mkutano wenu inayosema “Juhudi za makusudi za kukuza Uwezo wa Makandarasi Wazalendo kwa Maendeleo endelevu ya kiuchumi: changamoto na Mustakabali Wake” (Deliberate Capacity Building of Local Contractors for Sustainable Economic Development; Challenges and Way Forward). Binafsi nitafurahi kupata Ripoti ya Mkutano huu.
Baada ya kusema haya, sasa natamka kuwa Mkutano wa Mashauriano wa Bodi ya Usajili wa Makandarasi kwa Mwaka 2016 umefunguliwa rasmi.
AHSANTENI KWA KUNISIKILIZA
- May 16, 2016
HOTUBA YA MHE. DKT. JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA WAKATI WA KUWEKA JIWE LA MSINGI KWENYE MRADI WA UMEME WA KINYEREZI II, T...
Soma zaidiHotuba
Mheshimiwa Prof. Sospeter Muhongo, Waziri wa Nishati na Madini,
Mheshimiwa Balozi Masaharu Yoshida, Balozi wa Japan nchini,
Mheshimiwa Martha Mlata, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini;
Mheshimiwa Paul Makonda, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam;
Mheshimiwa Ramadhan Madabida, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Dar es Salaam;
Waheshimiwa Wabunge wa Mkoa wa Dar es Salaam mliopo hapa;
Katibu Mkuu na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini;
Mhandisi Felchesmi Mramba, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO;
Viongozi Mbalimbali mliopo hapa;
Wageni Waalikwa,
Ndugu Wananchi;
Mabibi na Mabwana.
Mheshimiwa Waziri nianze kwa kukushukuru kwa kunikaribisha kushiriki katika hafla hii ya kuweka Jiwe la Msingi la Ujenzi wa Mradi wa Kufua Umeme wa Kinyerezi II, ambao ukikamilika utaongeza megawati 240 kwenye Gridi ya Taifa. Mradi huu ni muhimu sana kwa ustawi na maendeleo ya taifa letu. Hivyo, napenda hapa mwanzoni kabisa kuwapongeza wewe, Mheshimiwa Waziri pamoja na watendaji wako katika Wizara, kwa kazi kubwa mnayoifanya ya kutekeleza miradi ya umeme kwa lengo la kuifanya nchi yetu kuwa na nishati ya umeme ya kutosha. Ninafahamu zipo changamoto nyingi zinazowakabili lakini mnajitahidi kuzishughulikia.
Hafla hii ya kuweka jiwe la msingi la kituo cha kufufua umeme unaotumia gesi asilia cha Kinyerezi II inafanyika miezi michache tu tangu kufanyika kwa uzinduzi wa Kituo cha Kufua Umeme cha Kinyerezi I mwezi Oktoba 2015. Kituo cha Kinyerezi I hivi sasa kinazalisha megawati 105. Tumearifiwa hivi punde kuwa ndani ya kipindi cha wiki mbili zijazo, Kituo cha Kinyerezi I kitakuwa na uwezo wa kuzalisha megawati 150. Miradi hii yote ni matokeo ya kukamilika kwa ujenzi wa Bomba la Gesi kutoka Mtwara, Lindi hadi Dar es Salaam uliojengwa kwa gharama ya Dola za Marekani bilioni 1.2.
Naomba mniruhusu kutumia fursa hii kuwashukuru wageni waalikwa na wananchi mliopo mahali hapa kwa kujitokeza kwa wingi kushuhudia uwekaji wa jiwe la msingi la mradi huu.
Ndugu Wananchi,
Mabibi na Mabwana;
Umeme ni maendeleo. Umeme ni kichocheo muhimu katika ukuaji wa uchumi wa Taifa lolote duniani. Matumizi ya nishati duniani hutumika kama kipimo cha maendeleo ya nchi husika. Umeme unasaidia kuongeza ufanisi wa shughuli za kiuchumi na kuboresha upatikanaji wa huduma za jamii kama vile afya, elimu na maji. Bila ya kuwepo kwa umeme wa uhakika, hata ndoto yetu ya kujenga uchumi wa viwanda haitaweza kutimia. Tukiwa na umeme wa uhakika tutaweza kujenga viwanda vidogo vidogo, vya kati na vikubwa na hivyo kutengeneza ajira kwa wananchi wetu.
Kwa mujibu ya takwimu zilizopo, uwezo wa nchi yetu wa kuzalisha umeme ni kati ya megawati 1200 hadi 1500 kwa mwaka. Na kama tulivyosikia hivi punde kutoka kwa Mheshimiwa Waziri, hivi sasa tunazalisha megawati 1025. Hii ina maana kuwa kila Mtanzania kwa sasa anatumia wastani wa watt 30 kwa mwaka. Tukijilinganisha na nchi nyingine, ambapo Kenya ni watt 40, China watt 490, Afrika Kusini watt 500 na Marekani watt 1683, utaona kuwa uwezo wetu wa kuzalisha nishati ya umeme bado upo chini. Hivyo, tunahitaji kuongeza jitihada zaidi za kuzalisha umeme.
Ndugu Wananchi,
Mabibi na Mabwana;
Wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu mwaka jana tulitoa ahadi ya kujenga uchumi wa viwanda. Lakini wakati tukiahidi hayo, tulifahamu pia kuwa ili kuweza kujenga uchumi wa viwanda ni lazima tuwe na umeme wa uhakika. Ni kwa sababu hiyo, leo nimefarijika sana kukaribishwa kuweka jiwe la msingi la Mradi wa Kufufua Umeme wa Kinyerezi II. Tukio hili linatokea takriban miezi mitatu tu baada ya mimi kuingia madarakani. Hii ni hatua nzuri.
Mradi huu wa Kinyerezi II unatekelezwa kwa ubia kati ya Serikali yetu na Japan. Gharama ya mradi huu ni Dola za Marekani milioni 344. Serikali ya Japan inagharamia 85% ya mradi na nchi yetu inachangia 15%. Wenzetu wa Japan walikwishatoa kiasi cha Dola za Marekani 292, lakini mradi huu ulikwama kuanza kutekelezwa kwa takriban miaka miwili kutokana na nchi yetu kukawia kuchangia. Kufuatia kuimarika na kuongezeka kwa ukusanyaji mapato tangu tulipoingia madarakani mwezi Novemba 2015, Serikali ilifanikiwa kutoa kiasi cha asilimia 15% kilichohitajika sawa na shilingi bilioni 120, mwezi Januari 2016. Kutolewa kwa fedha hizo ndiko kumewezesha mradi huu sasa kuanza kutekelezwa.
Kwa niaba ya Serikali na Watanzania kwa ujumla, napenda kutumia fursa hii kuishukuru Serikali ya Japan kwa kutupatia mkopo wa kutekeleza mradi huu. Nimefurahi kumwona Balozi wa Japan, Mheshimiwa Masaharu Yoshida yupo pamoja nasi katika shughuli hii. Nina imani atafikisha shukrani zetu kwenye Serikali yake.
Mheshimiwa Waziri;
Miradi mingi ya umeme iliyopo hapa nchini hivi sasa inaendeshwa kwa kutumia mitambo ya kukodisha. Umeme wa mitambo ya kukodisha umekuwa ukisababisha matatizo mengi kwa nchi yetu, ikiwemo gharama za uwendeshaji kuwa juu na hivyo kufanya bei ya umeme kuwa ghali. Sasa wakati umefika wa kuachana na utaratibu huo. Ndiyo. Ni lazima tuanze kutekeleza miradi ya umeme kwa kutumia mitambo yetu wenyewe. Hii ndio sababu nilianza hotuba yangu kwa kukupongeza Mheshimiwa Waziri kwa kuwa natambua kuwa mnafanya jitihada mbalimbali ili kuondokana na utaratibu wa zamani kukodisha mitambo.
Hatua mnazozichukua ni muhimu hasa kwa kuzingatia kuwa nchi yetu ina vyanzo vingi vya kuzalisha umeme, ikiwemo gesi asilia, makaa ya mawe, maji, upepo na madini ya uraium n.k. Kiwango cha gesi asilia tuliyonayo hivi sasa ni takriban futi za ujazo trilioni 57. Hivi karibuni tu ugunduzi mwingine wa gesi umefayika hapo Ruvu. Kutokana na utajiri huu wa gesi, nchi yetu haina sababu ya kuendelea kulalamikia tatizo la umeme. Kuna nchi nyingi duniani, hususan katika Bara la Ulaya, zinalazimika kusafirisha gesi masafa marefu kwa ajili ya kupata nishati ya umeme. Sisi tunayo gesi ya kutosha hapa hapa nyumbani. Wataalam tunao. Ni lazima tutumie gesi yetu kuzalisha umeme wa kutosha. Tukiwa na umeme wa kutosha, gharama za umeme zitashuka na hivyo kuwapunguzia ugumu wa maisha wananchi wetu.
Nimefarijika kusikia kuwa mmejipanga kuupanua Mradi wa Kinyerezi I ili uweze kuzalisha Megawati 335 kutoka Megawati 150 za sasa. Nyongeza hii ya Megawati 185 zikijumlishwa na hizi 240 zitakazotokana na mradi ambao tunaweka Jiwe la Msingi leo zitatuhakikishia kupata Megawati 425 katika kipindi cha takribani miaka miwili na nusu ijayo. Nafahamu ili kutekeleza mradi wa upanuzi wa Kinyerezi I, Mkandarasi anahitaji takriban Dola za Marekani milioni 20. Napenda kuwaahidi kuwa Serikali itafanya jitihada za kutafuta fedha hizo, ikiwezekana zipatikane ndani ya mwezi huu, ili mradi huo nao uanze kutelezwa mara moja. Tunataka nchi yetu iwe na umeme wa kutosha tena wa bei nafuu.
Wageni Waalikwa;
Mabibi na Mabwana;
Sambamba na miradi hiyo, nimearifiwa pia kuwa maandalizi ya ujenzi wa Mtambo ya Kinyerezi III wenye uwezo wa kuzalisha Megawati 600 (Megawati 300 Awamu ya I na Megawati 300 Awamu ya II) na Kinyerezi IV wenye uwezo wa Megawati 330, ambayo yote inatumia gesi asilia, yanaendelea vizuri. Aidha, kama alivyoeleza Mheshimiwa Waziri hivi punde, utekelezaji wa miradi ya umeme inayotumia vyanzo vingine vya umeme nayo inaendelea. Kukamilika kwa miradi hii yote kutawezesha nchi yetu siyo tu kuwa na umeme wa kutosha kwa matumizi ya ndani bali pia kuuza nchi za jirani.
Tukiweza kuuza umeme wetu nje tutapata fedha za kutekeleza miradi mingine ya maendeleo, kama vile ujenzi wa Bomba la Kusafirisha Mafuta kutoka Ziwa Albert nchini Uganda hadi Bandari ya Tanga, ambao unatarajiwa kuanza hivi karibuni na kuzalisha ajira za moja kwa moja takriban 21,500. Tukiwa na miradi mingi ya maendeleo kama hii tutaweza kukabiliana vizuri na changamoto ya ukosefu wa ajira inayokabili wananchi wetu.
Ndugu Wananchi;
Mabibi na Mabwana;
Nchi yetu inahitaji maendeleo. Kwa kutambua hilo, Serikali ya Awamu ya Tano ninayoingoza imejipanga kufanya kazi ya kuwaletea Watanzania maendeleo bila kujali tofauti za dini, kabila au itakadi za kisiasa. Tunafanya hivyo kwa vile tunaamini maendeleo hayana chama. Ombi langu kwa wananchi, endeleeni kuunga mkono hatua mbalimbali tunazozichukua katika kuwaletea maendeleo. Na katika hili, napenda kuwapongeza wananchi wa Kinyerezi kwa kukubali mradi huu kutekelezwa katika eneo lenu.
Nafahamu bado kuna changamoto kadhaa zinawakabili, ikiwemo baadhi yenu kutolipwa fidia. Napenda kuwahakikishia kuwa fedha zenu za fidia zipo na hivi karibuni mtalipwa kwa mujibu wa sheria za nchi yetu (Sheria ya Vijiji, Sheria ya Ardhi na Sheria ya Mipango Miji na Matumizi Bora ya Ardhi). Lakini kwa wale ambao wamegomea kupokea fidia zao, Serikali kamwe haitahangaika nao.
Mheshimiwa Waziri;
Ndugu Wananchi;
Mabibi na Mabwana;
Mradi huu upo Kinyerezi. Hapa Kinyerezi wapo vijana na akina mama. Hivyo basi, nina imani kuwa wananchi wa Kinyerezi watapewa kipaumbele katika kupata ajira kwenye mradi huu. Lakini nitumie fursa hii kuwaomba wanaKinyerezi watakaopata ajira katika mradi huu, kuwa waaminifu. Msishiriki kwenye vitendo viovu vya wizi wa vifaa vya ujenzi, mafuta ya transfoma, nyaya za umeme na vifaa vingine ama kuhujumu miundombinu ya mradi huu. Mtambue ya kuwa mradi huu ni wa Watanzania wote na utatunufaisha sote. Ukiiba vifaa vya ujenzi ufahamu kuwa wewe ni chanzo cha kuchelewesha maendeleo ya Watanzania. Mradi huu ukikamilika hata tatizo la maji hapa Kinyerezi litatatuliwa kwa haraka. Hivyo basi, kila mwananchi awe mlinzi wa mwenzake katika kuulinda mradi huu.
Sambamba na hilo, napenda kutoa wito kwa Wizara na TANESCO kuhakikisha mnamsimamia ipasavyo mkandarasi, Kampuni ya Sumitomo Corporation ya Japan, ili mradi huu sio tu ukamilike kwa wakati bali pia ubora unazingatiwe. Ikiwezekana mradi huu ukamilike hata kabla ya muda uliopangwa.
Mheshimiwa Waziri;
Ndugu Wananchi;
Mabibi na Mabwana;
Kabla ya kuhitimisha hotuba yangu, naomba niwashukuru tena washirika wetu wa maendeleo, hususan Serikali ya Japan, Benki ya Maendeleo ya Afrika pamoja na Benki ya Dunia ambao tumekuwa tukishirikiana nao katika kutekeleza miradi mbalimbali maendeleo nchini mwetu. Napenda kuwahakikishia washirika wetu kuwa fedha wanazotupatia zitatumika kwa malengo yaliyokusudia.
Baada ya kusema hayo, sasa nipo tayari kufanya kazi iliyonileta ya kuweka jiwe la msigi la mradi huu wa Kinyerezi II.
“AHSANTENI KWA KUNISIKILIZA”
- May 09, 2016
HOTUBA YA MHESHIMIWA DKT. JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA WAKATI WA UZINDUZI WA MAJENGO YA PPF PLAZA NA NSSF MAFAO HOUSE A...
Soma zaidiHotuba
Mheshimiwa Jenista Mhagama, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu;
Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango, Waziri wa Fedha na Mipango;
Mheshimiwa Felix Ntibenda, Mkuu wa Mkoa wa Arusha;
Bw. Erick Shitidi, Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu;
Waheshimiwa Wenyeviti na Wajumbe wa Bodi za PPF na NSSF;
Mheshimiwa Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Arusha;
Mheshimiwa Mstahiki Meya wa Jiji la Arusha;
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii;
Wakurugenzi Wakuu wa PPF na NSSF;
Waheshimiwa Wakuu wa Wilaya mliopo;
Waheshimiwa Madiwani;
Viongozi wa Serikali mliopo;
Ndugu Wafanyakazi wa PPF na NSSF;
Wageni Waalikwa;
Mabibi na Mabwana:
Napenda nianze hotuba yangu kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutupa afya njema na kutuwezesha kukutana mahali hapa tukiwa salama. Aidha, napenda kuwashukuru wananchi wa Arusha kwa mapokezi yenu mazuri tangu nilipowasili. Hii ni mara yangu ya tatu nakuja hapa Arusha tangu mmenichagua kuwa Rais wa Awamu ya Tano wan chi yetu. Lakini mara zote nimepata mapokezi makubwa. Ukarimu wenu unanipa moyo sana. Hivyo, nawashukuru sana wana-Arusha.
Napenda kutumia fursa hii pia kumpongeza Mstahiki Meya wa Jiji la Arusha kwa kazi kubwa anazozifanya katika kuunga mkono jitihada mbalimbali za Serikali, ikiwemo suala la wafanyakazi hewa, kama ambavyo yeye mwenyewe ameeleza hivi punde. Mimi na Mstahiki Meya tunatoka vyama tofauti lakini napenda kumpongeza kwa dhati kabisa kwa jitihada zake. Nafanya hivyo kwa kutambua kuwa sasa uchaguzi umekwisha. Jukumu kubwa ambalo lipo mbele yetu sote hivi sasa ni kuleta maendeleo kwa nchi yetu. Hivyo basi, natoa wito kwa wananchi wote kushikamana ili kutekeleza jukumu hilo kubwa ambalo lipo mbele yetu.
Ndugu Wananchi, Mabibi na Mabwana;
Hivi punde tutazindua majengo mawili yaliyojengwa na Mifuko miwili ya Hifadhi ya Jamii ya PPF na NSSF. Majengo haya ni mazuri na nina uhakika yataboresha mandhari ya Jiji letu la Arusha. Napenda kuipongeza Mifuko hii miwili ya Hifadhi ya Jamii kwa kuwekeza kwenye ujenzi wa majengo haya. Nimearifiwa kuwa wakati wa ujenzi wa majengo haya, Watanzania takriban mia mbili walipata ajira. Aidha, nafahamu kuwa wakati wa ujenzi, wapo wananchi waliopata ajira nyingine za muda mfupi. Nimefarijika zaidi kusikia kuwa makampuni ya Kitanzania yameshiriki katika ujenzi wa majengo haya. Nina imani makampuni hayo yamepata uzoefu wa kutosha. Hivyo basi, naipongeza sana Mifuko hii.
Ndugu Wananchi, Mabibi na Mabwana;
Pamoja na pongezi nilizozitoa, ni dhahiri kuwa yapo mambo ya kujiuliza. Tumeelezwa hivi punde kuwa ujenzi wa majengo haya mawili umegharimu zaidi ya shilingi bilioni sitini (60). Lakini tujiulize ni kwa namna gani majengo haya yatawanufaisha wananchi maskini na wasio na ajira? Viongozi wa Mifuko hii miwili wameeleza hivi punde kuwa majengo haya bado hayajapata wapangaji wa kutosha. Binafsi nafahamu pia kuwa majengo mengi ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii yaliyopo sehemu mbalimbali nchini, hayana wapangaji kwa sababu mbalimbali, ikiwemo gharama za kupanga kuwa juu. Matokeo yake Mifuko inapata hasara. Hivyo basi, nitoe wito kwa viongozi wa Mifuko hii kuwafikiria wananchi wa kipato cha chini kila mara wanapotaka kuwekeza.
Mimi naamini kama fedha zilizotumika kujenga majengo haya zingewekezwa kwenye sekta zinazowagusa wananchi wengi, zingeleta manufaa makubwa kwanza kwa mifuko yenyewe, lakini pia kwa wananchi na taifa kwa ujumla. Mathalan, nchi yetu ni ya pili kwa kuwa na idadi kubwa ya mifugo Barani Afrika baada ya Ethiopia. Aidha, nchi yetu inalima mazao mbalimbali, ikiwemo pamba, kahawa, matunda n.k. Kama fedha iliyotumika kujenga majengo haya ingeelekezwa kwenye kujenga viwanda vya ngozi na bidhaa zake au viwanda vya nguo ama vya kusindika matunda/mazao, wananchi wengi wangepata ajira, maisha yao yangeboreka, idadi ya wanachama kwenye mifuko hii ingeongezeka na nchi yetu ingepata mapato.
Ni kwa sababu hiyo, nimefurahi sana kusikia katika maelezo yaliyotolewa hivi punde na Waheshimiwa Mawaziri pamoja na viongozi wa Mifuko ya PPF na NSSF kwamba Mifuko ya Hifadhi ya Jamii sasa inataka kuelekeza nguvu kwenye sekta ya viwanda. Nawapongeza kwa hilo kwa vile azma hiyo inaenda sambamba na azma ya Serikali ya Awamu ya Tano inayolenga kuifanya nchi yetu kuwa ya nchi ya uchumi wa kati unaoongozwa na sekta ya viwanda.
Ndugu Wananchi;
Mabibi na Mabwana;
Sisi Watanzania, bila kujali tofauti zetu za dini, kabila au itikadi sote tunatamani kuona kero na shida zetu mbalimbali zinatatuliwa. Tunatamani kuondokana na umaskini na pia kuwa na maisha bora. Binafsi naamini kuwa mambo haya yote yanawezekana. Yanawekana kwa vile nchi yetu hii imebarikiwa kuwa na kila aina ya utajiri. Tunayo ardhi na maji ya kutosha, mifugo, misitu, wanyama, madini na gesi. Kama tungeweza kutumia vizuri rasilimali hizi tulizonazo, wananchi wangeondokana na umaskini walionao na nchi yetu ingepata maendeleo.
Hata hivyo, kwa bahati mbaya, licha ya utajiri wa rasilimali tulionao, ni watu wachache tu ndiyo wamekuwa wakinufaika. Watu hawa wachache ndiyo wameshilikia uchumi na kuhodhi kila biashara. Baadhi ya watu hawa pia ndiyo wamekuwa wakiwasababishia shida mbalimbali wananchi. Mathalan, nchi yetu hivi sasa inakabiliwa na tatizo la uhaba wa sukari. Tatizo hili kimsingi limesababishwa na baadhi ya wafanyabiashara wachache kwa maslahi yao binafsi. Wafanyabiashara hao wameamua kuficha sukari ili kusudi waweze kuuza sukari hiyo kwa bei waitakayo. Jambo la kusikitisha zaidi ni kwamba baadhi ya wafanyabiashara hao, wakati mwingine, wamekuwa wakiingiza sukari kutoka nje ambayo muda wake wa matumizi umepita. Ikifika hapa nchini, sukari hiyo inafungwa kwenye vifurushi au mifuko mipya na kisha kuingizwa sokoni na hivyo kuhatarisha maisha ya walaji.
Hatupaswi kuacha hali hii iendelee. Ni lazima tuibadilishe. Napenda kuwahakikishia kuwa Serikali ya Awamu ya Tano ninayoingoza imejipanga kurekebisha hali hii. Tutahakikisha rasilimali za umma zinawanufaisha wananchi wote. Tutahakikisha tunawashughulikia wale wote ambao wamekuwa wakitumia rasilimali za nchi kwa manufaa na maslahi yao binafsi. Hii ndiyo sababu, napenda kurudia tena wito wangu kwa viongozi wa Mifuko yote ya Hifadhi ya Jamii nchini kuangalia uwezekano wa kuwekeza kwenye sekta ya viwanda. Nawaahidi kuwa endapo mtaamua kuwekeza kwenye viwanda, Serikali itawapa ushirikiano wa kutosha, ikiwezekana kuwapa misamaha ya kodi. Tutafanya hivyo kwa sababu mimi naamini kuwa kama Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ingewekeza kwenye viwanda, mathalan vya sukari, shida ya uhaba wa sukari inayokabili nchi yetu hivi sasa isingekuwepo. Na hata kama ingekuwepo, basi hali isingekuwa kama ilivyo sasa. Tungeweza kuziba pengo hilo la uhaba wa sukari kwa kutoa vibali kwenu kuagiza sukari kutoka nje na bila shaka bei ya sukari ingeedelea kuwa chini.
Sambamba na kuomba mifuko ya hifadhi ya jamii kuwekeza kwenye viwanda, nawaomba wananchi wenzangu kuendelea kuunga mkono hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali katika kukabiliana na changamoto zinazoikabili nchi yetu. Suala hili ni muhimu kwa vile siyo watu wote wanafurahia hatua zinazochukuliwa na Serikali hivi sasa. Wapo baadhi ya watu wachache ambao wanajaribu kutuzuia. Lakini nina imani kama sisi sote tukiungana na kushikamana hakuna mtu atakayetukwamisha.
Waheshimiwa Viongozi;
Ndugu Wananchi;
Mabibi na Mabwana;
Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kama ikitumiwa vizuri inaweza kutoa mchango mkubwa katika maendeleo ya nchi. Nchi yetu ina mifuko ya hifadhi ya jamii saba (7), ambayo ni GEPF, LAPF, NSSF, NHIF, PPF,PSPF na WCF. Mifuko hii kwa pamoja ina mtaji wa shilingi trilioni 8.87. Baadhi ya Mifuko hii ya Hifadhi ya Jamii imeshiriki katika kutekeleza miradi mikubwa mbalimbali ya maendeleo hapa nchini, ikiwemo ujenzi wa Daraja la Mwalimu Julius Nyerere (Kigamboni), Ukumbi wa Bunge Dodoma na Chuo Kikuu Cha Dodoma. Utekelezaji wa miradi hii ni kielelezo tosha kuwa endapo Mifuko ya Hifadhi ya Jamii itatumiwa vizuri inaweza kuchochea maendeleo ya kiuchumi katika nchi. Hivyo basi, naipongeza mifuko yetu yote kwa mchango wao.
Pamoja na pongezi hizo, ni dhahiri kuwa mchango wa mifuko ya hifadhi kwenye maendeleo ya taifa letu kwa sasa bado ni mdogo. Mathalan, mifuko yote ya hifadhi iliyopo nchini kwa pamoja huchangia asilimia12 ya pato la taifa kwa mujibu wa takwimu za Benki Kuu za mwaka 2014. Kiwango hiki ni kidogo sana ukilinganisha na nchi nyingine, ambako mifuko ya hifadhi ya jamii huchangia hadi asilimia 40 ya pato la taifa. Hivyo basi, tunapaswa kuongeza bidii ili mifuko yetu ya hifadhi iweze kutoa mchango unaostahili kwenye maendeleo ya taifa, ikiwezekana na sisi tufikie asilimia 40 au zaidi.
Ndugu Wananchi, Mabibi na Mabwana;
Katika risala zilizosomwa na viongozi wa mifuko hii miwili tumesikia changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo. Moja ya changamoto hizo inahusu baadhi ya waajiri kushindwa kuwasilisha michango ya wafanyakazi wao kwa wakati. Napenda kurudia tena agizo langu nililolitoa kwenye Sherehe za Mei Mosi mwaka huu kwamba waajiri wote lazima wachangie kwenye mifuko hii. Na ninaposema waajiri wote ni pamoja na Serikali, kupitia Wizara ya Fedha. Bahati nzuri Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii, Mama Irene Isaka, upo hapa hivyo naamini agizo hili litasimamiwa ipasavyo.
Nafahamu Serikali ilikuwa inadaiwa takriban shilingi bilioni 700 kwenye mfuko wa PSPF kutokana na Wizara ya Fedha kushindwa kuwasilisha michango ya watumishi wa Serikali. Napenda kuwatarifu kuwa tumeanza kulipa deni hilo ambapo kiasi cha shilingi bilioni 500, tayari kimelipwa. Naamini malipo ya kiasi kilichobaki yatafanyika hivi karibuni. Hata hivyo, kutokana na zoezi la kuwaondoa watumishi hewa linaloendelea ambapo hadi hivi tumewabaini watumishi hewa takriban 1900, bila shaka deni lililobaki litapungua.
Nakubaliana pia na mapendekezo yaliyotolewa na viongozi wa mifuko kwamba kwa wale watakaoshindwa kuwasilisha michango yao wasilipwe mafao kwa mujibu wa sheria. Ndiyo, wasilipwe. Wakati sasa umefika mifuko yetu ya hifadhi ya jamii iendeshwe kisasa na sio kisiasa. Nafahamu wapo baadhi ya waajiri wamekuwa wakikusanya michango ya watumishi lakini hawaiwasilishi kwenye mifuko. Waajiri wa namna hiyo ni lazima watafutwe na kuwajibishwa ipasavyo.
Hata hivyo, napenda kutoa angalizo kuwa siyo kila kazi, waajiri wanatakiwa kuchangia kwenye mifuko ya hifadhi. Kazi nyingine ni za muda mfupi hivyo mwajiri hawalazimiki kumchangia mfanyakazi wake kwenye mifuko. Suala hili lazima lieleweke vizuri. Mimi binafsi nalifahamu suala hili vizuri kwa kuwa nilikuwa Waziri wa Ujenzi. Kwenye miradi mingi ya ujenzi, hususan barabara, watu walikuwa wakiajiriwa kwa muda mfupi. Waajiriwa wa namna hiyo hawakustahili kuchangiwa kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii.
Waheshimiwa Mawaziri;
Ndugu Viongozi na Wafanyakazi wa PPF na NSSF;
Wageni Waalikwa;
Mabibi na Mabwana;
Kabla sijahitimisha hotuba yangu, napenda kuwashukuru tena Waheshimiwa Mawaziri na viongozi wa PPF na NSSF kwa kunikaribisha kushiriki kwenye shughuli hii. Nawashukuru pia wananchi wa Arusha kwa mapokezi mazuri na ninawaahidi nipo pamoja nanyi na kamwe sitawaangusha. Na bahati nzuri mambo mazuri tayari yameanza kuonekana. Hivi majuzi nchi yetu imeingia makubaliano na Serikali ya Uganda kujenga bomba la mafuta kutoka Uganda hadi Bandari ya Tanga. Ujenzi wa Bomba hilo unatarajiwa kutoa ajira takriban elfu ishirini na tano na kuongeza pato la taifa kwa takriban asilimia 2.
Nitumie fursa hii pia kurudia tena wito wangu kwa Viongozi wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kuangalia uwezekano wa kuwekeza kwenye maeneo yenye tija na yenye kuhusisha watu wengi, hususan viwanda. Nimefurahi kusikia kwenye jengo la NSSF kutakuwa na kiwanda cha kukata tanzanite. Sio mbaya kama kwenye siku za usoni mtafikiria kujenga kiwanda cha tanzanite hapa hapa nchini ili nchi yetu iweze kunufaika ipasavyo na madini hayo kuliko ilivyo sasa.
Vilevile, napenda kuhimiza mifuko ya hifadhi pamoja na taasisi mbalimbali nchini kuhakikisha kuwa wakati mnapotekeleza miradi yenu mbalimbali mjitahidi kutoa kiupaumbele Watanzania. Ndio, ni lazima kipaumbele kiwe kwa Watanzania kwanza, hususan kwa zile kazi au miradi ambayo Watanzania wanamudu kuitekeleza. Hivyo, ndivyo nchi nyingine zinavyofanya. Na huo ndio muelekeo wa Serikali ya Awamu ya Tano.
Mwisho lakini sio kwa umuhimu, napenda kuwashukuru viongozi wa mifuko ya PPF na NSSF kwa mchango wenu wa madawati. PPF mmetoa madawati 2,000 na NSSF madawati 4,000. Nawashukuru sana kwa kuonesha mfano huu. Madawati haya yatatumiwa na watoto wetu waliopo shuleni. Kama mnavyofahamu, Serikali ilifanya uamuzi wa kutoa elimu bila malipo. Uamuzi huo umesababisha idadi ya wanafunzi kuongezeka maradufu na kuleta changamoto kadhaa, ikiwemo uhaba wa madawati. Hivyo basi, nitoe wito kwa taasisi na kila mwananchi atakayeguswa kushirikiana na Serikali katika kushughulikia changamoto mbalimbali zilizojitokeza kwenye shule zetu.
Baada ya kusema hayo, sasa nipo tayari kufanya uzinduzi wa majengo haya mawili ya PPF Plaza na NSSF Mafao House.
“Ahsanteni kwa kunisikiliza”
- May 01, 2016
HOTUBA YA MHESHIMIWA DKT. JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, KWENYE KILELE CHA SIKUKUU YA WAFANYAKAZI DUNIANI MEI MOSI 2016 IT...
Soma zaidiHotuba
Mhe. Samia Hassan, Makamu wa Rais;
Mhe. Kassim Majaliwa, Waziri Mkuu;
Ndugu Gratian Mukoba, Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA);
Mama Nortubunga Maskini, Makamu wa Rais wa TUCTA;
Mheshimiwa Jenista Mhagama, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu;
Mhe. Tulia Ackson, Naibu Spika;
Balozi Injinia John Kijazi, Katibu Mkuu Kiongozi;
Mheshimiwa Jordan Rugimbana, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma;
Waheshimiwa Mawaziri wote, na Waheshimiwa Wabunge mliopo;
Bi. Mary Kawar, Mkurugenzi wa Shirika la Kazi Duniani (ILO), Ofisi ya Nchi za Afrika Mashariki;
Waheshimiwa Mabalozi mliopo;
Waheshimiwa Majaji,
Mheshimiwa Almas Maige, Mwenyekiti wa Chama cha Waajiri Tanzania;
Dr. Aggrey Mlimuka, Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waajiri Tanzania (ATE);
Ndugu Nicholaus Mgaya, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA);
Viongozi wa Vyama vya Wafanyakazi;
Viongozi na Maafisa wa Serikali mliopo;
Wawakilishi wa Vyama vya Siasa mliopo; Mzee Mangula, Makamu Mwenyekiti wa CCM
Bwana Kimbisa (Mb), Mwenyekiti wa CCM Mkoa;
Wanahabari;
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Dodoma;
Ndugu Wananchi;
Ndugu Wafanyakazi;
Mabibi na Mabwana.
Awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutupa uhai na afya njema na kuweza kukutana hapa. Leo ni siku muhimu sana. Tupo hapa kwa ajili ya kuenzi na kuthamini mchango wa wafanyakazi wa Tanzania, wake kwa waume, walioko sekta binafsi na ya umma, na ambao kila siku tangu asubuhi hadi jioni wamekuwa wakivuja jasho kwa ajili ya maendeleo ya taifa letu.
Hii si mara yangu ya kwanza nashiriki Sherehe ya Siku ya Wafanyakazi, maarufu kama Mei Mosi. Nimeshiriki kwenye sherehe hizi mara kadhaa. Lakini leo nashiriki kipekee kabisa. Nashiriki kwa mara ya kwanza tangu nichaguliwe kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwezi Oktoba 2015. Hivyo, napenda kuchukua nafasi hii kuwashukuru Viongozi wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA) na Vyama vyote vya Wafanyakazi nchini kwa kunialika ili nijumuike nanyi kwenye Sherehe hizi za Siku ya Wafanyakazi Duniani mwaka huu. Aidha, napenda kuwashukuru wafanyakazi wote wa Tanzania kwa kunipa kura nyingi zilizoniwezesha kuchaguliwa kuwa Rais wa nchi hii. Naahidi kwenu kuwa sitawaangusha.
Nitumie fursa hii pia kuwapongeza sana wananchi wa Mkoa Dodoma chini ya Uongozi wa Mkuu wa Mkoa, Mheshimiwa Jordan Rugimbana kwa kukubali kuwa wenyeji wa Sherehe hizi pamoja na maandalizi mazuri mliyofanya kufanikisha sherehe hizi. Sherehe zimefana, hongereni sana! Nawashukuru pia wananchi wa Dodoma kwa kunipa kura nyingi wakati wa uchaguzi Mkuu wa mwaka jana.
Aidha, ninawashukuru sana Wafanyakazi na Wananchi wote mliojitokeza hapa leo kwa wingi ili kujiunga na wenzetu duniani kote kusherehekea siku hii muhimu ya Wafanyakazi Duniani.
Ndugu Wafanyakazi na Wananchi kwa ujumla;
Duniani kote wafanyakazi ni nguzo muhimu ya maendeleo. Hakuna taifa lolote duniani ambalo limeweza kuendelea bila kutegemea wafanyakazi wake. Hapa nchini, wafanyakazi wametoa mchango mkubwa kwa maendeleo ya taifa letu tangu kipindi cha ukoloni hadi sasa. Bila shaka wengi wetu hapa tunafahamu namna wafanyakazi na vyama vya wafanyakazi vilivyoshiriki kikamilifu katika harakati za ukombozi wa nchi yetu. Baada ya nchi yetu kupata uhuru, wafanyakazi wameendelea kutoa mchango mkubwa kwa maendeleo ya nchi yetu.
Nitumie fursa hii kuwapongeza wafanyakazi kote nchini kwa kazi kubwa na nzuri mnayoifanya kwa maendeleo ya taifa letu. Ninyi ndio mmejenga miundombinu mbalimbali tunayoitumia hivi sasa, ninyi ndio mnahakakikisha Watanzania wanapata huduma bora za elimu na afya lakini hata ulinzi na usalama wa taifa letu kwa kiwango kikubwa unategemea ninyi wafanyakazi. Hongereni sana wafanyakazi!
Ndugu Wafanyakazi na Wananchi kwa ujumla;
Kama nilivyotangulia kusema, hii ni sherehe yangu ya kwanza ya Mei Mosi tangu nimechaguliwa kuwa Rais wa Awamu ya Tano wa nchi yetu. Hivyo, napenda kutumia fursa hii adimu kuzungumza na wafanyakazi pamoja na wananchi kwa ujumla kuhusu masuala na mipango mbalimbali ambayo Serikali ya Awamu ya Tano ninayoingoza imepanga kutekeleza katika kipindi cha miaka mitano ijayo.
Serikali ya Awamu ya Tano imejipanga kuona nchi yetu inapata maendeleo kwa manufaa ya Watanzania wote. Tumejipanga kufanikisha utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2025 pamoja na Ilani ya Uchaguzi ya Chama Tawala. Sote tunafahamu kuwa Dira ya Taifa ya Maendeleo inalenga kuiwezesha nchi yetu kuwa ya uchumi wa kati unaongozwa na viwanda. Ili kutekeleza Dira ya Maendeleo na Ilani ya Uchaguzi ya Chama Tawala, tayari tumekamilisha Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano utakaotekelezwa katika kipindi cha mwaka 2016/17 hadi mwaka 2020/21.
Mpango huu unadhima ya kujenga uchumi wa viwanda ili kuchochea mageuzi ya kiuchumi na maendeleo ya watu. Lengo kuu la Mpango huu ni kuhakikisha rasilimali na fursa za nchi zinatumika vizuri ili kujenga uchumi wa viwanda na kupunguza umasikini. Baadhi ya malengo mahsusi ni kuimarisha kasi ya ukuaji mpana wa uchumi kwa manufaa walio wengi, kuongeza kasi ya kupunguza umaskini, kuongeza fursa ya ajira kwa wote, kuongeza upatikanaji na ubora wa huduma za jamii na kuongeza mauzo nje kwa bidhaa za viwandani.
Ndugu Wafanyakazi na Wananchi;
Baadhi ya masuala muhimu yaliyomo kwenye Mpango wa Maendeleo ambayo tutayatekeleza katika kipindi cha miaka mitano ijayo ni pamoja na kufufua viwanda na kujenga vipya, hususan vinavyotumia malighafi zinazopatikana kwa wingi hapa nchini, teknolojia ya kati, nguvu kazi na ambavyo bidhaa zake zitatumika zaidi hapa nchini, ikiwemo viwanda vya nguo na bidhaa za ngozi. Aidha, tunakusudia mazingira ya uzalishaji na uendeshaji biashara kwa kuhakikisha tunajenga miundombinu ya nishati ya umeme, reli, barabara, maji, madaraja, vivuko, bandari, viwanja vya ndege na TEHAMA. Tunalenga pia kuhakikisha kuwa panakuwepo ardhi kwa ajili ya uwekezaji na upatikanaji wa rasilimali-watu yenye ujuzi. Halikadhalika, tutaboresha sera, sheria, taratibu, uratibu na ushirikiano wa kitaasisi.
Maendeleo ya uchumi ni lazima yaende sambamba na maendeleo ya watu. Ili kuhakikisha hilo, vipaumbele vitakuwa ni kuhakikisha watu wanaondokana na umaskini, njaa na ukosefu wa ajira. Aidha, tutaboresha huduma za jamii, hususan afya na elimu, kwa kuhakikisha zinapatikana kwa uhakika na ubora unaostahili. Tutahakikisha watu wengi wanajiunga na mifuko ya hifadhi ya jamii na pia panakuwepo na usawa wa jinsia na watu wenye ulemavu, utawala bora, mipango miji na kuogeza juhudi za kukabiliana na athari za tabianchi.
Matumaini yetu ni kwamba utekelezaji wa Mpango huu utaleta matokeo chanya kwa nchi yetu kwa kukuza uchumi kutoka asilimia 7 mwaka 2015 hadi asilimia 10 mwaka 2020; kuongeza mapato ya yatokanayo na kodi kutoka asilimia 12.1 ya pato la taifa mwaka 2014/15 hadi asilimia 17.1 mwaka 2020; kuongezeka kwa kasi ya kupunguza umaskini ambapo pato la wastani kwa kila mwananchi litaongezeka kutoka wastani wa dola za Marekani 1,006 mwaka 2015 hadi 1,500 mwaka 2020; umaskini wa mahitaji ya msingi kupungua kutoka asilimia 28.2 mwaka 2011/12 hadi asilimia 16.7 mwaka 2020/21; huduma za msingi za afya na elimu zitaimarika; kuongezeka kwa mauzo nje ya nchi ya bidhaa za viwandani; kuongeza idadi ya watalii na kuongeza uwekezaji wa moja kwa moja kutoka dola la kimarekani bilioni 2.14 mwaka 2014/15 hadi bilioni 5 mwaka 2021. Hayo ndiyo malengo yetu.
Ndugu Wafanyakazi na Ndugu Wananchi
Utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo ya Taifa utagharimu takriban shilingi trilioni 107, zikiwemo trilioni 59 kutoka Serikalini.Kwa kuanza, kwenye bajeti ijayo, Serikali imetenga kiasi cha jumla ya shilingi trilioni 11.82 kwa ajili ya bajeti ya maendeleo sawa na asilimia 40 ya bajeti yote kutoka asilimia 26 mwaka uliopita. Kati ya fedha za bajeti ya maendeleo, shilingi 8.702 trilioni sawa na asilimia 74 ya bajeti ni fedha za ndani na fedha za nje ni shilingi 3.117 trilioni sawa na asilimia 26.
Kama mnavyoona, sehemu kubwa ya ugharamiaji wa mpango huu itafanyika kwa kutumia fedha za ndani. Hii ishara tosha kuwa tumedhamiria kufanikisha azma yetu ya kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2025 ili kuleta maendeleo nchini mwetu na kuwaondolea wananchi kero mbalimbali.
Ndugu Wafanyakazi na Ndugu Wananchi;
Bila shaka baadhi yenu mtashangaa kwa nini nimetumia Sherehe hii ya Wafanyakazi kuongelea malengo ya Serikali ya Awamu ya Tano katika kipindi cha miaka mitano ijayo. Jibu ni moja tu. Imenilazimu kueleza hayo yote ili sisi wafanyakazi wote hapa nchini tufahamu kazi kubwa iliyopo mbele yetu. Sisi ndio tunategemewa kuwaongoza Watanzania katika kutekeleza na kufikia malengo ya Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025. Hivyo, tunaposherehekea sikukuu hii ya wafanyakazi duniani hatuna budi kila mmoja wetu kujiuliza ni kwa namna gani tutachangia katika kufanikisha utekelezaji wa Mpango huu wa Maendeleo kwa nchi yetu. Kwa kifupi, naweza kusema kuwa mipango yote mizuri niliyoieleza hapo juu haiwezi kufanikiwa kama wafanyakazi hawatashiriki kikamilifu.
Hivyo basi, nitoe wito kwa wafanyakazi kote nchi kila mmoja kwa nafasi yake kujipanga vizuri katika kutekeleza Mpango huu. Ni lazima tufanye kazi kwa bidii na kujituma, ueledi mkubwa na uadilifu. Nchi yetu haitaweza kufikia uchumi wa kati unaoendeshwa kwa viwanda kama tutaendelea kulea uvivu, uzembe, ubadhirifu, rushwa, ukwepaji kodi, kutotimiza wajibu wetu na wafanyakazi hewa. Kwa kutambua hilo, Serikali yenu imeanza kuchukua hatua za kuimarisha nidhamu na uwajibikaji kwa watumishi Serikalini. Tayari tumeanza kuwashughulikia watumishi wachache ambao ni wazembe, wavivu, wala rushwa, wabadhirifu na wasio na maadili.
Nafahamu, watumishi wazembe na wabadhirifu ni wachache. Lakini watumishi hao ndio wamekuwa wakiharibu sifa nzuri ya watumishi wa umma. Hawa ndio wamekuwa wakirudisha nyuma gurudumu la maendeleo la nchi yetu. Hawa ndio wamekuwa wakinufaika na kunyonya jasho la wafanyakazi walio wengi wa Tanzania. Sasa mwisho wao umefika. Serikali ya Awamu ya Tano imejipanga kuwashugulikia popote walipo. Hatutawaonea aibu au huruma watumishi wa aina hii. Nimefurahi kusikia Vyama vya Wafanyakazi viko pamoja na Serikali na havitaunga mkono mtumishi mzembe, legelege na fisadi. Mmezidi kutupa nguvu zaidi ya kuendelea na jitihada tulizozianzisha za kurejesha nidhamu ya kazi kwenye utumishi wa umma. Niwaombe pia tushirikiane katika kushughulikia wafanyakazi hewa. Wafanyakazi hewa wameigharimu Serikali fedha nyingi ambazo zingeweza kuboresha maslahi ya wafanyakazi halali na kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo.
Hadi leo idadi ya wafanyakazi hewa waliopatikana ni 10,295. Kati ya wafanyakazi hao 8,373 ni kutoka Serikali za Mitaa na 1,922 ni wa Serikali Kuu. Kutokana na wafanyakazi hao hewa Serikali imekuwa ikilipa kiasa cha shilingi 11,603,273,799.41 kila mwezi sawa na shilingi 139,239,285,592.92 kwa mwaka sawa na shilingi 696,196,427,964.6 kwa miaka mitano. Fedha hizi zingeweza kujenga barabara za juu (flyovers) tano au kuboresha maslahi ya watumishi halali ama kuboresha huduma mbalimbali za jamii. Aidha, nafasi hizo hewa zingeweza kutoa ajira kwa wahitimu wa vyuo vikuu mbalimbali ambao wanatafuta kazi na hivyo kuleta manufaa kwa taifa.
Ndugu Wafanyakazi;
Wakati nikitoa rai kwa watumishi legelege, wabadhirifu na wala rushwa kubadilika, napenda pia kutumia fursa hii kuwapa moyo wafanyakazi wote ambao ni wachapakazi na ambao wanatekeleza majukumu yao kwa ueledi na uadilifu. Endeleeni kufanya kazi kwa kujiamini, kujituma bila ya kuwa wasiwasi wowote. Nafahamu wapo baadhi ya watu wamekuwa wakiwatisha na kuwaeleza kuwa Serikali ya Awamu ya Tano haijali wafanyakazi. Wapuuzeni watu hao. Hao ndio wale waliokuwa wakinufaika au kushirikiana na watumishi mafisadi, wala rushwa na wabadhirifu. Sasa wanatapatapa baada ya kuona Serikali inachukua hatua mahsusi kwa watumishi wa namna hiyo. Serikali ya Awamu ya Tano haitambuguzi mfanyakazi yeyote ambaye anajituma na kufanya kazi kwa ueledi na uadilifu. Nipende kusema tu Serikali yangu itawalinda na kuwatetea wafanyakazi waadilifu na wachapakazi.
Ndugu Wafanyakazi;
Wakati wa Kampeni na hata nikifungua Bunge niliwaahidi wafanyakazi wote wa umma na sekta binafsi kuwa ningeboresha maslahi na mazingira yenu ya kufanya kazi, ikiwemo kuongeza mishahara, kuwapatia vitendea kazi, pamoja na kulinda na haki za msingi za hifadhi ya jamii kama huduma za afya na malipo ya pensheni baada ya kustaafu kazi. Ahadi yangu hii bado ipo pale pale na nawaahidi tena sitawaangusha. Kwa bahati nzuri hata kaulimbiu ya Mei Mosi mwaka huu ambayo; “Dhana ya Mabadiliko Ilenge Kuinua Hali ya Wafanyakazi” inasisitiza umuhimu wa kuboresha maslahi na mazingira ya kazi ya wafanyakazi.
Kama alivyosema Katibu Mkuu wa TUCTA kuwa tangu tumeingia madarakani, tumeweza kuongeza ukusanyaji wa mapato kutokana na kuziba mianya mingi ya ukwepaji kodi na kudhibiti matumizi yasiyo ya lazima. Hata hivyo, sio dhamira yetu na bila shaka sio dhamira ya Watanzania walio wengi kuona fedha zote tunazokusanya tunazitumia kwa ajili ya kulipia mishahara watumishi tu. Nasema hivi ili mfahamu kwamba mapato haya yanawahitaji wengi sana. Wananchi walio wengi wamepata matumaini kuwa kutokana na kuongeza kwa mapato sasa huduma mbalimbali zitapatikana kwa ubora na uhakika. Hivyo, niwajibu wetu sisi mliotukabidhi kuongoza Serikali kuhakikisha tunatumia vizuri rasilimali za nchi kwa manufaa ya Watanzania wote. Na ninapenda kutumia fursa hii kuwahakikishia kuwa tutaelekeza fedha tunazozipata katika maeneo muhimu ambayo yanamgusa kila Mtanzania, wakiwemo wafanyakazi.
Ndugu Mwenyekiti wa TUCTA;
Ndugu Katibu Mkuu wa TUCTA;
Ndugu Wafanyakazi;
Hivi punde nimetoka kusikia risala yenu nzuri iliyosomwa na Katibu Mkuu wa TUCTA, Bwana Nicholas Mgaya. Sitaweza kujibu hoja zote zilizotajwa kwenye risala yenu. Lakini napenda kuwahakikishia kuwa Serikali imezipokea hoja zenu zote na tutazifanyia kazi. Hata hivyo, naomba mniruhusu nieleze japo kwa uchache baadhi ya hoja mliyotaja kwenye risala yenu:
Kwanza, kuhusu suala la kupunguza kodi ya mapato ya mshahara (PAYE) kwa wafanyakazi. Napenda kuwaarifu kuwa Serikali yangu kama nilivyoahidi wakati wa kampeni zangu nimeamua kuwapunguzia Wafanyakazi kodi ya Mapato ya Mishahara kutoka asilimia 11 ya sasa hadi asilimia 9 kuanzia mwaka wa fedha wa 2016/17 kutegemea Wabunge watakavyopitisha bajeti yetu. Tuna uhakika kwa kufanya hivyo, tutakuwa tumewapunguzia wafanyakzi mzigo mkubwa wa makato katika mishahara yao. Nimeamua kuanza na hili kwanza ili changamoto zilizopo sasa za kiuchumi tuweze kuzivuka na baadaye mambo yakiwa mazuri tutaangalia suala la kupandisha mishahara.
Pili, suala la tofauti ya mishahara. Tayari tumeanza kuchukua hatua kuhakikisha tunakuwa na mfumo wa mishahara ambao unazingatia vigezo vya uzito wa kazi na kupunguza tofauti kubwa ya malipo ya mshahara kwa kuoanisha mishahara ya watumishi wa Umma walioajiriwa Serikali Kuu, Serikali za Mitaa, Taasisi na Mashirika ya Umma. Tunataka Watumishi wa Umma wafaidi matunda ya kazi kwa kuzingatia uzito wa kazi wanazozifanya kwa misingi ya haki na usawa.
Aidha, kufuatia marekebisho ya Sheria ya Taasisi za Kazi Na.7 ya Mwaka 2004, tumeunda Bodi mbili za mishahara. Bodi ya mshahara katika Sekta Binafsi inayosimamiwa na Waziri mwenye dhamana ya masuala ya Kazi na Ajira, na Bodi ya Mshahara katika Utumishi wa Umma inayosimamiwa na Waziri mwenye dhamana ya Utumishi wa Umma. Majukumu ya Bodi hizi ni kufanya uchunguzi na kupendekeza kima cha chini cha mshahara katika sekta husika. Ni matarajio yetu kwamba bodi hizi zitatekeleza majukumu yake kwa weledi kwa kupendekeza viwango vinavyozingatia hali halisi ya uzalishaji, tija na uchumi wetu. Nilikwisha tamka sitarajii kuwa na mfanyakazi anayelipwa zaidi ya milioni 15 wakati wengine wanalipwa laki tatu kwa mwezi.
Tatu, suala la hifadhi ya jamii. Serikali ya Awamu ya tano inalenga katika kuhakikisha kwamba wananchi wengi zaidi watafaidika na mfumo wa hifadhi ya Jamii nchini kuliko ilivyo sasa. Kwa mfano tunataka wananchi wengi zaidi wajiunge na Bima ya Afya ili wawe na uhakika wa matibabu. Tunaendelea na juhudi ya kupanua wigo wa Mfuko wa Bima ya Afya vijijini (Community Health Fund) na pia kuwezesha wafanyakazi wengi wa sekta binafsi kujiunga na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (National Health Insurance Fund). Aidha, Mifuko ya Hifadhi ya Jamii imeanza kusajili wananchama toka sekta isiyo rasmi. Lengo la Serikali ni kuhakikisha kwamba wananchi wengi wanapata huduma za msingi za hifadhi ya jamii.
Kwa upande wa kuimarisha Mifuko ya hifadhi ya jamii pamoja nakuboresha malipo ya Pensheni, Serikali imekwishaelekeza Mifuko ya Hifadhi ya jamii kuachana na uwekezaji kwenye miradi isiyokuwa na tija. Wawekeze kwenye maeneo kama viwanda ili kuzalisha fursa za ajira na kujipatia wanachama zaidi. Aidha, ushauri wenu wafanyakazi kupitia shirikisho lenu la TUCTA kwa Serikali kuhusu kupunguza idadi ya Mifuko ya Pensheni nchini na matumizi yasiyo ya lazima umepokelewa na kukubalika. Lakini ni vyema mfahamu kwamba kutokana na historia tofauti ya kuanzishwa kwa mifuko ya hifadhi ya jamii iliyopo sasa, hatua zozote za marekebisho zinahitaji umakini mkubwa. Napenda niwahakikishie kwamba kazi ya kurekebisha mifuko ya Pensheni nchi tutaikamilisha ndani ya mwaka 2016/2017.
Nne, suala la Vyama vya Wafanyakazi. Napenda kutoa rai kwa waajiri kote nchini kutambua kwamba suala hili sio la hiari bali ni wajibu wao kuwaruhusu wafanyakazi kuanzisha na kujiunga kwenye vyama vya wafanyakazi sehemu za kazi bila ya kushurutishwa au kuchaguliwa chama cha kujiunga. Hivyo, waajiri wote wanaovunja takwa hili la sheria watachukuliwa hatua kali. Lakini pia nitoe wito kwenu Viongozi na wafanyakazi vyama hivyo visitumike kuchocheo migogoro ya kikazi, uzembe na uvivu kazini na wala visiwe vyama vya kisiasa kazini. Vyama hivyo vinapaswa kutumika kuimarisha uhusiano kati ya waajiri na waajiriwa, kuhamasisha utendaji kazi na kuleta utulivu sehemu za kazi.
Tano, suala la mikataba ya ajira. Waajiri wengi wamekuwa hawatekelezi matakwa sheria kama yalivyobainishwa katika Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini Na. 6 ya mwaka 2004 pamoja na marekebisho yake ambayo tumeyafanya mwaka 2015. Bado yapo malalamiko mengi ya wafanyakazi kutokuwa na mikataba ya kazi, kufanya kazi bila vifaa kinga, michango ya pensheni kuchelewa kuwasilishwa au kutowasilishwa kabisa kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii. Serikali ya Awamu ya Tano ninayoongoza haitavumilia ukiukwaji huu wa sheria.
Ili kuhakikisha waajiri wanatekeleza kwa hiari bila shurti sheria za kazi, tuanza kurekebisha tena Sheri ya Ajira na mahusiano kazini kwa kuanzisha adhabu za papo kwa papo ambapo waajiri watalazimika kulipa faini kwa kila kosa la kutotekeleza sheria za kazi. Pia, katika mwaka huu wa fedha, Serikali imetenga fedha kuajiri maofisa kazi zaidi wapatao 21 ili kuimarisha huduma za ukaguzi sehemu za kazi. Nitoe wito kwa Vyama vya wafanyakazi, kushirikiana kwa karibu na Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu). Aidha, ninaziagiza Mamlaka zinazohusika kusimamia utekelezaji wa Sheria za kazi kusimamia sheria husika bila woga kwa lengo la kuwalinda wafanyakazi wasiendelee kutumikishwa na kunyonywa.
Aidha, naziagiza mamlaka husika kushughulikia suala la ajira za wageni ambazo zinaweza kufanywa na wazawa. Hakuna nchi yoyote duniani ambayo jukumu lake kubwa ni kuwatafutia ajira wageni kazi ambazo ingeweza kufanywa na wazawa. Naagiza Wizara zote zisimamie hili suala kwa nguvu zote ili wazawa wapate ajira kwanza. Sambamba na hilo, wahusika wote mshirikiane pia kuwafichua wale wote watakaofanya kazi bila vibali. Nakumbuka zoezi hili lilianza sitaki kuamini kuwa ilikuwa ni nguvu za soda. Mheshimiwa Waziri tafadhali simamia hili.
Suala jingine ambalo nalo limekuwa ni tatizo sugu ni baadhi ya waajiri kushindwa kuwasilisha michango ya wafanyakazi wao kwenye mifuko ya hifadhi kwa wakati. Ingawa wafanyakzi wamekuwa wakikatwa kila mwezi lakini fedha hizo hazifiki kunakohusika. Tatizo hili pia linaihusu Serikali kutokana na Hazina kutopeleka michango. Hivyo, natoa wito kwa waajiri wote nchini kuwasilisha michango ya wafanyakazi wao kila mwezi bila kukosa. Hivyo, natoa wito kwa waajiri wote nchini kuwasilisha michango ya wafanyakazi wao kila mwezi bila kukosa.
Kwa upande wa Serikali tayari tumeanza kulishughulikia suala hili la michango kwa kutambua wafanyakazi wote halali ili michango yao iwasilishwe. Mathalan, kwenye Mfuko wa PSPF Serikali ilikuwa ikidaiwa shilingi takriban bilioni 710 bilioni lakini hadi sasa tumelipa takriban shilingi 500. Ni imani yangu kuwa michango ya inayotakiwa kulipwa na Serikali kwenye Mifuko ya Hifadhi itapungua kutokana na zoezi la kuwaondoa wafanyakazi hewa. Tunaomba Vyama vya Wafanyakazi vishirikiane na Serikali kufichua watumishi hewa.
Ndugu Mwenyekiti wa TUCTA;
Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu
Waheshimiwa Mawaziri na Waheshimiwa Wabunge mliopo;
Ndugu Katibu Mkuu wa TUCTA;
Wageni Waalikwa;
Ndugu Wafanyakazi;
Mabibi na Mabwana:
Napenda kuhitimisha hotuba yangu kwa kuwashukuru tena Viongozi wa TUCTA na Vyama vya Wafanyakazi nchini kwa heshima mliyonipa ya kushiriki kwenye Sherehe hizi. Aidha, napenda kurudia tena wito wangu kwa Wafanyakazi na wananchi wote kwa ujumla, tuendelee kufanya kazi kwa bidii, kwa nguvu zetu zote, kwa maarifa yetu yote na kwa kuzingatia misingi ya uwajibikaji na uadilifu ili tuweze kusukuma gurudumu la maendeleo ya nchi yenu. Tuachane na mazoea ya watu kuingia kazini asubuhi na kuondoka saa nne.
Tukumbuke ya kuwa kazi ni utu, kazi sio fursa ya kupata mshahara kwa manufaa ya familia zetu tu bali ni fursa nzuri ya kutoa mchago kwa taifa lako kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Mungu Wabariki Wafanyakazi Watanzania!
Mungu Ibariki Tanzania!
“Ahsanteni kwa Kunisikiliza”.
- Apr 19, 2016
HOTUBA YA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA MHESHIMIWA DKT. JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI KATIKA SHEREHE YA UZINDUZI RASMI WA DARAJA LA KIGAMBONI TAREHE 19 A...
Soma zaidiHotuba
Mheshimiwa Mhandisi Edwin Ngonyani, Naibu Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi;
Mheshimiwa Angela Kairuki, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Utumishi na Utawala Bora;
Mheshimiwa Anthony Mavunde, Naibu Waziri wa Nchi – Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu;
Mheshimiwa Paul Makonda, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam;
Mheshimiwa Dkt. Lu Youqing, Balozi wa Jamhuri ya Watu wa China;
Mheshimiwa Mohamed Yassir El Shawaf, Balozi wa Misri;
Mheshimiwa Ndugu Ramadhani Madabida, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam;
Mheshimiwa Prof. Norman Sigala, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu;
Waheshimiwa Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu pamoja na Sheria na Katiba;
Waheshimiwa Wabunge mliopo;
Mstahiki Meya wa Jiji la Dar es Salaam;
Makatibu Wakuu mliopo;
Wakuu wa Wilaya;
Waheshimiwa Madiwani;
Viongozi wa Serikali mliopo;
Viongozi wa Vyama vya Siasa;
Ndugu Wananchi, Mabibi na Mabwana:
Kwanza niaze kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kufika siku hii tukiwa salama. Aidha, napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa Viongozi wa Wizara husika, hususan Waheshimiwa Mawaziri, kwa kunialika kushiriki katika sherehe hii ya kihistoria kwa nchi yetu ya Uzinduzi wa Daraja la Kigamboni. Daraja hili ni la kipekee sio tu hapa nchini bali katika eneo zima la Afrika Mashariki. Nawapongeza waandaaji kwa maandalizi mazuri ya shughuli hii.
Hii ni mara yangu ya kwanza nafika katika Wilaya hii mpya ya Kigamboni tangu nimechaguliwa kuwa Rais wa Awamu ya Tano wa Nchi yetu. Nitumie fursa hii kuwashukuru wananchi wa Kigamboni kwa ushindi mkubwa mlionipa. Watu wa Kigamboni mmepata shida sana ya matatizo ya usafiri hadi kufikia baadhi ya wanasiasa kutaka kutumia tatizo hilo kuwa mtaji wao wa kisiasa. Lakini nawashukuru mlisimama imara na kunipa kura nyingi wakati wa uchaguzi. Kwa sababu hiyo, nimefarijika sana leo kuwepo mahali hapa kushuhudia uzinduzi wa daraja hili.
Niliwaahidi wakati wa kampeni kuwa sitawaangusha. Napenda kurudia tena leo kuwa sitawaangusha. Kama ilivyo serikali zilizotangulia, lengo la Serikali ya Awamu ya Tano ni kutatua kero za wananchi. Nafahamu kero ni nyingi na bila shaka hazitamalika kwa siku moja. Hata hivyo, naahidi kuwa Serikali ninayoingoza itajitahidi kupunguza kama sio kumaliza kabisa kero mbalimbali zinazowakabili wananchi hivi sasa.
Waheshimiwa Viongozi;
Ndugu Wananchi;
Mabibi na Mabwana;
Wazo la kujenga Daraja la Kigamboni liliibuka kwa mara ya kwanza mwaka 1933 wakati huo nchi yetu ikiwa chini ya utawala wa kikoloni wa Uingereza. Hata hivyo, kwa sababu mbalimbali mradi huu haukuweza kutekelezwa. Baada ya nchi yetu kupata uhuru, wazo la ujenzi wa Daraja hili liliibuka upya mwaka 1976 ambapo uamuzi wa kulijenga ulifikiwa. Kutokana na sababu mbalimbali, ikiwemo uhaba wa fedha, ujenzi wa daraja hili haukuanza kama ilivyotarajiwa. Hata hivyo, jambo lililodhahiri ni kwamba katika awamu zote za uongozi wa nchi yetu kulikuwa na nia na jitihada za makusudi za kujenga daraja hili. Mimi nimeifahamu historia hii kwa vile nilikuwa Waziri wa Ujenzi kwa takriban miaka 15.
Ndugu Wananchi;
Mabibi na Mabwana;
Daraja hili ni muhimu sana kwa wakazi wa Kigamboni. Bila shaka, baadhi yetu tunakumbuka kuwa miaka ya nyuma kidogo tumepoteza wapendwa wetu wengi kwa kukosekana kwa usafiri (kivuko) wa uhakika wa kwenda na kutoka Kigamboni. Watu walilazimika kuvuka kwa mitumbwi, ambayo wakati mwingine ilizama na kuleta maafa makubwa. Baadaye Serikali ilijitahidi kutatua tatizo hilo kwa kununua vivuko. Lakini kutokana na kasi ya maendeleo na kuongezeka kwa idadi ya watu, vivuko hivyo vilishindwa kukidhi mahitaji. Hivyo, daraja hili litasaidia sana kuondoa utegemezi wa kivuko kama njia ya usafiri kwa wakazi wa Kigamboni.
Sambamba na kutatua kero ya usafiri kwa wakazi wa Kigamboni, daraja hili kwa sababu, kwa mujibu ya Ramani ya Jiji (Master Plan), Kigamboni ndiko kumepangwa kutekelezwa shughuli mbalimbali za maendeleo ya Jiji la Dar es Salaam, ikiwemo Kituo cha Mabasi yaendayo mikoani. Shughuli hizo zilikwama kutokana na kutokuwepo kwa daraja la kuunganisha upande wa Kigamboni. Hivyo basi, kukamilika kwa daraja hili lenye urefu wa mita 680 na barabara unganishi ya urefu wa kilometa nne, ikiwemo barabara ya kilometa mbili na nusu ambayo tayari imekamilika, litawezesha shughuli za kimaendeleo kuanza kutekelezwa.
Aidha, daraja hili litafungua na kutangaza fursa za kiuchumi zilizopo kwenye eneo la Kigamboni, ikiwemo biashara na uwekezaji. Vilevile, daraja litawezesha kuanza ujenzi wa barabara ya kilometa 128 yenye njia sita na barabara za juu tano kutoka Kigamboni hadi Chalinze. Sambamba na shughuli hizo za kiuchumi, daraja hili litaboresha mandhari ya Jiji letu na kulifanya kuwa la kuvutia na la kisasa zaidi. Hivyo basi, nawahimiza wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla kutumia ipasavyo fursa za kiuchumi zitakazojitokeza kutokana na kukamilika kwa daraja hili ili kujiletea maendeleo.
Ndugu Wananchi;
Mabibi na Mabwana;
Kazi ya ujenzi wa daraja hili haikuwa rahisi. Ilikuwa ngumu sana. Hivi punde nimewaarifu kuwa wazo la kujenga daraja hili lilikuwepo tangu enzi ya ukoloni. Ujenzi ulipoanza pia tulikumbana na changamoto nyingi. Hivyo basi, nitumie fursa hii, kwa niaba yenu kumshukuru na kumpongeza kwa dhati kabisa Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete kwa kuridhia ujenzi wa daraja hili pale alipoweka jiwe la msingi mwezi Septemba 2012. Namshukuru pia kwa kuwa wakati huo mimi nilikuwa ni Waziri wa Ujenzi.
Aidha, napenda kutoa shukrani za dhati kwa uongozi mzima wa NSSF, akiwemo aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu Dkt. Ramadhani Dau, kwa kukubali kugharamia asilimia 60 ya ujenzi wa daraja hili. Nashukuru pia Kamati ya Ujenzi ikiongozwa na Mtendaji Mkuu wa TANROADS Mhandisi Patrick Mfugale pamoja na Mhandisi Karim Mataka wa NSSF. Wamefanya kazi nzuri na wanastahili pongezi nyingi. Hawa ndio walichora mchoro, kupanga na kusimamia ujenzi wa mradi huu. Kama nilivyosema awali, ujenzi wa daraja ulikuwa na changamoto nyingi. Lakini kwa kushirikiana na wasaidizi wao, wamefanya kazi hii kwa ubora na umahiri mkubwa. Ni kwa sababu hii, nimesikitika kuona vyombo vya habari havikutoa uzito unaostahili kwa tukio hili. Nimehuzunika pia kuona baadhi ya watu wanakosoa kuhusu gharama zilizotumika katika ujenzi wa daraja hili. Watanzania wenzangu, mimi nimekuwa Waziri wa Ujenzi kwa miaka mingi, nafahamu ujenzi wa madaraja makubwa kama haya unatumia fedha nyingi.
Wapo pia wanaokosoa kutokamilika kwa kipande kidogo cha barabara ya urefu wa kilometa moja na nusu kinachounganisha daraja hili kwa upande wa kigamboni. Napenda kuwaarifu kuwa ujenzi wake utaanza hivi karibuni kwa kutumia mkandarasi aliyejenga daraja hili. Wito wangu kwa Watanzania wenzangu tuwe na utaratibu na utamaduni wa kupenda na kuthamini vitu vyetu. Tunavyo vitu vingi vya kujivunia. Mathalani, tumejenga madaraja makubwa mengi, ikiwemo Daraja la Mkapa, Daraja la Kikwete pamoja na Daraja la Umoja. Hivyo, hatuna budi kujipongeza.
Nitumie fursa hii pia kueleza kuwa hivi karibuni Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi alikuja kwangu kuniomba daraja hili tunalolizindua leo kupewa jina langu. Nilikataa. Nilimkatalia kwa sababu daraja hili ni kiunganishi cha jiji la Dar es Salaam. Ninyi nyote mnafahamu katika nchi yetu hii kuna watu walifanya kazi kubwa ya kutuunganisha ili kuondoa tofauti zetu za rangi, dini na kabila. Kwa sababu hiyo, na bila shaka naamini mtaniunga mkono, nashauri Daraja hili lipewe jina la Baba wa Taifa letu, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ili kuenzi mchango wake katika kuwaunganisha Watanzania.
Wageni Waalikwa;
Mabibi na Mabwana;
Daraja hili limejengwa kwa ubia kati ya Serikali na sekta binafsi (NSSF). Kwa maana hiyo, fedha zilizotumika ni lazima zirudi kwa ajili ya kwenda kutekeleza miradi mingine ya maendeleo. Hivyo, katika kipindi hiki cha mwanzoni, watembea kwa miguu watapita bila malipo yoyote. Lakini kwa waendesha baiskeli, maguta na wenye magari watalazimika kulipa fedha kila watakapovuka kwenye daraja hili. Fedha zitakazopatikana zitatumika kuhudumia daraja hili, ikiwa ni pamoja na kufanya ukarabati wa miundombinu na kuwalipa mishahara watumishi, ambao nimearifiwa kuwa idadi yake itakuwa ni takriban 300.
Hivyo basi, niwaombe wahusika, hususan NSSF, kuandaa utaratibu mzuri kwa ajili ya watu kuanza kulipia. Aidha, niwaombe wakazi wa Dar es Salaam kutunza miundombinu ya daraja hili kwa kudumisha usafi ili liweze kudumu kwa muda mrefu. Aidha, viongozi wa Mkoa na NSSF hakikisheni mahali hapa panakuwa na usalama na sio kificho cha vibaka au sehemu ya kufanya biashara. Niwaombe wahusika wengine pia kuhakikisha miundombinu mingine inayohitajika, ikiwemo barabara zinazoungana na daraja hili pamoja na vituo kwa ajili ya abiria, vinajengwa mapema ili wananchi wasihangaike.
Waheshimiwa Mawaziri;
Wageni Waalikwa;
Mabibi na Mabwana;
Napenda kuhitimisha hotuba yangu kwa kutoa shukrani zangu tena kwa kualikwa kuwa Mgeni Rasmi kwenye shughuli hii. Aidha, nitumie fursa hii kuwashukuru na kuwapongeza Wakandarasi na Wasimamizi wote wa mradi huu kwa kazi kubwa na nzuri waliyoifanya kutekeleza mradi huu. Kwa kipekee kabisa nawashukuru na kuwapongeza wafanyakazi ambao walijitolea usiku na mchana kufanya kazi na kuhakikisha mradi huu unakamilika kwa wakati. Mwisho lakini sio kwa umuhimu nawapongeza tena wananchi wa Kigamboni kwa uvumilivu mkubwa mliouonesha kusubiria mradi huu. Nawaomba muendelee na uvumilivu huo na kushirikiana na viongozi wenu bila kujali tofauti zenu za kiitikadi ili kujiletea maendeleo.
Baada ya kusema hayo, sasa natangaza rasmi kuwa Daraja la Kigamboni limefuguliwa.
Mungu libariki Daraja la Kigamboni!
Mungu Ibariki Tanzania!
“Ahsanteni kwa kunisikiliza”
- Apr 16, 2016
HOTUBA YA MHE. DKT. JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA KATIKA HAFLA YA KUWEKAJI JIWE LA MSINGI LA UJENZI WA ‘FLYOVER’ KATIKA MA...
Soma zaidiHotuba
Mheshimiwa Prof. Makame Mbarawa (Mb), Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano;
Mheshimiwa Balozi Dkt. Augustine Mahiga (Mb), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika;
Mheshimiwa Paul Makonda, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam;
Mheshimiwa Prof. Norman Adamson Sigara, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu;
Mheshimiwa Balozi Masaharu Yoshida, Balozi wa Japan nchini,
Mheshimiwa Ramadhan Madabida, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Dar es Salaam;
Waheshimiwa Wabunge wa Mkoa wa Dar es Salaam mliopo hapa;
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano;
Bwana Toshio Nagase, Mwakilishi Mkuu wa Shirika la Ushirikiano wa Kimataifa la Japan (JICA) nchini Tanzania;
Viongozi Mbalimbali mliopo;
Wageni Waalikwa;
Ndugu Wananchi;
Mabibi na Mabwana:
Nianze hotuba yangu kwa kumshukuru Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa kunialika kushiriki katika shughuli hii muhimu na ya kihistoria ya kuweka Jiwe la Msingi la Ujenzi wa Barabara ya Juu (Flyover) ya kwanza hapa nchini kwenye eneo hili la TAZARA.
Aidha, nawashukuru pia wananchi waliojitokeza kushuhudia uwekaji wa jiwe la msingi la mradi huu. Kipekee kabisa, napenda kutumia fursa hii kuwashukuru Wana-Dar es Salaam kwa kunichagua kuwa Rais wenu wa Awamu ya Tano. Nawashukuru sana kwa ushindi mkubwa mlionipa.
Ndugu Wananchi;
Mabibi na Mabwana;
Mtakumbuka kuwa wakati tunaomba kura kipindi cha Kampeni za Uchaguzi Mkuu mwaka jana tuliahidi mambo mengi. Miongoni mwa mambo tuliyoahidi tukiwa hapa Dar es Salaam, na hasa mimi ilikuwa kwamba, endapo ningechaguliwa ningehakikisha barabara ya juu hapa TAZARA inajengwa ili kupunguza kero ya foleni lakini pia kubadilisha mandhari ya Jiji letu. Ahadi ni deni. Nina uhakika kwa Wana-Dar es Salaam leo ni ushahidi tosha kuwa tumeanza kutekeleza ahadi yetu. Nafahamu kuna baadhi ya watu walikuwa hawaamini kama jambo hili lingefanyika. Lakini hayawi hayawi yamekuwa. Ujenzi sasa unaanza.
Mradi huu ni muhimu sana hasa kwa wakazi wa Jiji letu la Dar es Salaam. Kwanza, kwa sababu mradi huu utapunguza kero ya foleni. Aidha, mradi huu utasaidia kuokoa fedha zilizokuwa zikipotea kutokana na tatizo la msongamano wa magari barabarani, ambapo inakadiriwa kuwa mwaka 2013 pekee nchi yetu ilipoteza kiasi cha shilingi bilioni 411.55. Halikadhalika, kwa kupunguza foleni hapa Dar es Salaam, tutaweza kuokoa maisha ya watu ambao wamekuwa wakipoteza maisha kwa ama kuchelewa kufika hospitalini kutokana na foleni au gari la zima moto kuchelewa kufika kwenye eneo la tukio.
Hivyo basi, kwa niaba ya Serikali, wananchi na kwa niaba yangu binafsi, napenda kuchukua fursa hii kuishukuru Serikali ya Japan kwa kukubali kufadhili kwa kiasi kikubwa ujenzi wa mradi huu. Wajapan ni marafiki wa kweli wa nchi yetu na wamekuwa wakitusaidia kwa takriban miaka 35 sasa. Hata Daraja la Salender limejengwa na Wajapan. Jambo la kufurahisha ni kuwa misaada ya Wajapan haina masharti magumu yasiyotekelezeka. Ahsanteni sana ndugu zetu wa Japan.
Katika mradi huu, Serikali ya Japan imetoa kiasi cha shilingi bilioni 93.44 wakati nchi yetu itatoa shilingi bilioni 8.3. Aidha, nchi yetu itagharamia baadhi ya kodi za ujenzi wa mradi huu. Hivyo, gharama za kutekeleza mradi wote huu ni takriban shilingi bilioni 100. Narudia tena kuwashukuru ndugu zetu wa Japan na nikuombe Mheshimiwa Balozi Yoshida ufikishe shukran zetu kwa Serikali yako kwa namna ambavyo mmekuwa mkitusaidia katika miradi mbalimbali ya maendeleo. Nitumie fursa hii pia kuwashukuru wafadhili wote ambao wamekuwa wakitusaidia na napenda kuwahakikishia kuwa misaada yenu tutaitumia kwa malengo yaliyokusudiwa.
Ndugu Wananchi;
Mabibi na Mabwana;
Kila mnapoona nchi tajiri inatoa msaada kutusaidia mfahamu kwamba fedha hizo zimetokana na wananchi wao kulipa kodi. Kwa hiyo fedha hizi zilizotolewa na Wajapan kutekeleza mradi huu ni fedha za walipa kodi wa Japan. Wameamua kuzileta Tanzania, ambako wananchi wake wengi wamekuwa wakikwepa kulipa kodi. Niwaombe basi Watanzania wenzangu tujitahidi kulipa kodi. Tukifanya hivyo, sisi wenyewe tutamudu kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo kama huu ambao tunaweka jiwe lake la msingi muda mfupi ujao.
Ndugu Wananchi;
Mabibi na Mabwana;
Sambamba na mradi huu wa Barabara ya Juu hapa TAZARA, Serikali pia inaendelea na utekelezaji wa miradi mingine mingi ya barabara hapa Dar es Salaam. Mradi wa Mabasi ya Mwendokasi Awamu ya Kwanza (BRT Phase I) ambao umegharimu takriban shilingi bilioni 388 zilizokopwa kutoka Benki ya Dunia tayari umekamilika. Mradi huu umechelewa kuanza kufanya kazi baada ya kubainika kuwa kuna watu wachache wanataka kujinufaisha. Hata hivyo, Serikali imefanikiwa kuzuia utapeli huo na hivyo muda wowote kuanzia sasa usafiri wa magari ya mwendokasi utaanza kufanya kazi baada ya Serikali kujiridhisha kuwa maslahi ya wananchi na Serikali yamelindwa.
Aidha, tumejenga barabara za mitaani zenye urefu wa takriban kilometa 28 kwenye maeneo mbalimbali hapa Dar es Salaam. Nitoe wito kwa viongozi wa mkoa, hususan Mameya kusimamia vizuri barabara hizo ili zisiharibike. Halmashauri zetu zinapata fedha za Mfuko wa Barabara. Mzitumie vizuri fedha hizo kwa kuzielekeza maeneo husika, hasa kutengeneza barabara za kwenye mitaa yetu.
Ndugu Wananch;
Mabibi na Mabwana;
Serikali ya Awamu ya Tano imejidhatiti kupunguza kama siyo kumaliza kabisa tatizo la msongamano wa magari hapa Dar es Salaam. Hii ni kwa sababu Jiji hili siyo tu kwamba ni kioo cha nchi yetu bali pia ni kiungo muhimu cha usafiri kwa nchi jirani ambazo zinatumia Bandari ya Dar es Salaam kusafirisha bidhaa zao, ikiwemo Rwanda, Uganda, DRC, Zambia na Malawi. Hivyo, tumepanga kutekeleza miradi mingine mingi, ikiwa ni pamoja na:
(i) Mradi wa Ujenzi wa Barabara ya Dar es Salaam hadi Chalinze yenye urefu wa kilometa 128 ambayo itakuwa ni ya “expressway”. Mradi huu upo kwenye hatua za mwisho za upembuzi yakinifu ambapo baada ya hapo wawekezaji wa kujenga barabara hiyo kwa njia ya Ubia kati ya Serikali na Sekta Binafsi (PPP) watapatikana. Barabara hii itakuwa ya njia sita kutoka Dar es Salaam katika eneo la Kigamboni ambako itaungana na Daraja la Kigamboni. Aidha, barabara hii itakuwa na makutano ya kisasa yenye barabara za juu (interchanges) tano (5) katika maeneo inapoungana na barabara nyingine.
(ii) Mradi wa ujenzi wa barabara za juu (Interchange) kwenye makutano ya Nelson Mandela, barabara za Morogoro na Sam Nujoma eneo la Ubungo (Ubungo Interchange) unaofadhiliwa na Benki ya Dunia ambapo zabuni za kumpata Mkandarasi zimetangazwa.
(iii) Ujenzi wa Daraja jipya la kutoka Hospitali ya Aga Khan hadi Ufukwe wa Coco lenye urefu wa takriban kilometa 7 ambao utagharamiwa kwa kutumia mkopo wa masharti nafuu kutoka Benki ya Exim. Utekelezaji wa mradi huu upo katika hatua ya maandalizi.
(iv) Mradi wa ujenzi wa miundombinu ya Mabasi ya Mwendokasi Awamu ya Pili (BRT Phase II) katika barabara za Kilwa, Chang’ombe na Kawawa na pia ujenzi wa barabara za juu (Flyovers) katika makutano ya barabara za Kilwa na Mandela (Uhasibu) na makutano ya barabara za Nyerere na Chang’ombe. Mradi huu ambao utagharamiwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika upo katika hatua ya maandalizi.
(v) Mradi wa ujenzi wa miundombinu ya Mabasi Yaendayo Haraka Awamu ya Tatu (BRT Phase III) katika barabara ya Nyerere hadi Gongo la Mboto, barabara ya Uhuru na barabara ya Azikiwe. Serikali inaendelea na mazungumzo na Benki ya Dunia kwa ajili ya kupata mkopo wa kugharamia mradi huu.
Sambamba na miradi hii ya barabara, Serikali pia inaendelea na mipango ya kujenga Reli ya Kati ya Kisasa kutoka Dar es Salaam kwenda mikoa ya Mwanza na Kigoma. Katika kutekeleza mradi huu, serikali imetenga kiasi cha shilingi trilioni moja katika bajeti ya mwaka ujao wa fedha ili kuanza ujenzi wakati huo huo mazungumzo na wafadhili wengine yakiendelea. Ili kupunguza tatizo la msongamano wa magari hapa Dar es Salaam, ujenzi wa reli hiyo utakapofika Ruvu, tutaanza kuitumia ili kuzuia magari makubwa ya mizigo kuja Dar es Salaam kufuata mizigo.
Lakini niseme pia kuwa siyo hapa Dar es Salaam pekee ambako miundombinu ya usafiri itaboreshwa. Kwenye bajeti ijayo, tumetenga fedha za kujenga barabara sehemu nyingine nchini, ikiwemo barabara ya kutoka Mtwara hadi Newala na kumaliza barabara ya Nyakanazi kwenda Kigoma. Aidha, tumepanga kununua ndege mbili kwa ajili ya Shirika letu la Ndege la Tanzania. Miradi hii mikubwa ya maendeleo itafanyika baada ya Serikali kufanya uamuzi wa makusudi kuongeza bajeti ya maendeleo kutoka asilimia 26 hadi 40 mwaka ujao wa fedha. Bajeti hiyo imeongezeka baada ya Serikali kuzidisha ukusanyaji wa mapato na kubana matumizi kwenye baadhi ya maeneo, ikiwemo safari za nje na matumizi mengine yasiyo ya lazima. Tumeongeza bajeti ya maendeleo ili kuondoa kero nyingi zinazowakabili wananchi na pia kuleta maendeleo ya haraka kwa nchi yetu.
Niwaombe Mawaziri na watumishi wengine kuwa wavumilivu katika kipindi hiki ambacho Serikali inaelekeza juhudi kubwa katika kutatua kero za wananchi na kusukuma mbele gurudumu la maendeleo. Aidha, napenda kutoa wito kwa wananchi wote kushikamana ili kuleta maendeleo nchini mwetu. Tuondoe tofauti zetu za kiitikadi maana maaendeleo hayana itikadi.
Ndugu Wananchi;
Mabibi na Mabwana;
Kabla sijahitimisha hotuba yangu, napenda kutumia fursa hii kusema masuala mengine machache kuhusu mradi huu tunaouzindua leo na miradi mingine ya namna hii kwa ujumla. Mradi huu unajengwa Dar es Salaam. Hivyo, bila shaka, utatoa ajira kwa wakazi wa Dar es Salaam. Hivyo, nitoe wito kwa wote watakaoajiriwa kwenye mradi huu kuwa waaminifu na kuacha vitendo vya wizi. Nawaomba pia kuachana na migomo isiyokuwa na msingi ili mradi huu umalizike kwa haraka. Aidha, nawahimiza wasimamizi na wakandarasi wa mradi huu kujitahidi ili mradi huu umalizike mapema, ikiwezekana hata kabla ya muda uliopangwa ili kuwapunguzia wananchi wa Dar es Salaam kero ya foleni, hasa kwa kuzingatia kuwa fedha za ujenzi wa mradi huu zipo.
Sambamba na kuulinda mradi hii, naomba wananchi wadumishe usafi kwenye Jiji letu ili miradi ya namna hii idumu muda mrefu. Natoa wito kwa viongozi wa Dar es Salaam kusimamia suala la usafi, ikiwezekana tungeni sheria ndogondogo kwa ajili ya kuwadhibiti watu wasiopenda usafi. Ni lazima Watanzania tubadilike. Ni lazima tuwe wasafi. Nafahamu wakati mwingine tatizo la uchafu hapa Dar es Salaam linatokana na sisi viongozi wenyewe kuwa wabinafsi. Tunatoa zabuni za usafi kwa kampuni zetu ambazo hazina uwezo wa kufanya kazi. Tubadilike kwa kuweka maslahi ya taifa mbele badala ya maslahi yetu binafsi.
Waheshimiwa Viongozi;
Wageni Waalikwa;
Mabibi na Mabanwa;
Napenda kuhitimisha kwa kutoa pongezi kwa Mheshimiwa Waziri kwa kazi kubwa unayoifanya ya kusimamia ujenzi wa miundombinu. Nawapongeza pia Watendaji na watumishi wote wa Wizara kwa kufanya kazi kwa kujituma. Mimi nilikuwa Waziri wa Ujenzi kwa takriban miaka 15 hivyo ninaifahamu Wizara hiyo. Naomba ushirikiano mlionipa mimi muuendeleze kwa Waziri wenu mpya. Nafahamu mna changamoto za madeni kutokana na miradi mikubwa tuliyoifanya siku za nyuma lakini nawaahidi Serikali italipa madeni hayo yote.
Baada ya kueleza maneno hayo, sasa nipo tayari kuweka Jiwe la Msingi la Mradi wa Barabara ya Juu katika Makutano ya TAZARA.
Mungu Ibariki Tanzania!
Mungu Wabariki Watanzania!
“Ahsanteni kwa kunisikiliza”