Hotuba

- Jun 21, 2018
HOTUBA YA MHE. DKT. JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA WAKATI WA KUPOKEA GAWIO NA KUZINDUA UPATIKANAJI WA HUDUMA ZA SIMU NA VID...
Soma zaidiHotuba
HOTUBA YA MHE. DKT. JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA WAKATI WA KUPOKEA GAWIO NA KUZINDUA UPATIKANAJI WA HUDUMA ZA SIMU NA VIDEO CONFERENCE YA SHIRIKA LA SIMU (TTCL), DAR ES SALAAM,
TAREHE 21 JUNI, 2018
Mheshimiwa Prof. Makame Mbarawa,
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano;
Mheshimiwa Paul Makonda,
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam;
Mama Mary Sassabo, Katibu Mkuu anayesimamia
Sekta ya Mawasiliano kwenye Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano;
Mheshimiwa Mama Kate Kamba, Mweyekiti wa CCM wa Mkoa wa Dar es Salaam;
Waheshimiwa Wabunge wa Kamati ya Miundombinu;
Mheshimiwa Mhadisi Omary Nundu, Mwenyekiti wa TTCL;
Ndugu Waziri Kindamba, Mkurugenzi Mkuu wa TTCL;
Waheshimiwa Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama;
Waheshimiwa Viongozi mbalimbali mliopo hapa;
Ndugu Wafanyakazi wa TTCL;
Wageni Waalikwa wote, Mabibi na Mabwana:
RUDINI NYUMBANI – KUMENOGA!
Kwanza kabisa, napenda nimshukuru Mwenyezi Mungu aliyetuwezesha tukutane hapa tukiwa wenye afya njema. Aidha, napenda nimshukuru Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano pamoja na uongozi mzima wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (yaani TTCL) kwa kunialika kwenye tukio hili muhimu na la kihistoria hapa nchini. Ahsanteni sana.
Napenda nikiri kuwa leo najisikia kuwa mwenye furaha sana. Nina furaha kwanza kwa kupata fursa hii adimu ya kukutana na wafanyakazi wa Shirika letu la Mawasiliano. Pili, nina furaha kwa sababu, kama mlivyosikia, miaka miwili iliyopita, mwezi Juni mwaka 2016, tulifanya uamuzi wa kuirejesha TTCL Serikalini baada ya kununua asilimia 39 ya hisa zilizokuwa zikimilikiwa na Kampuni ya Bharti Airtel, kwa gharama ya shilingi bilioni 14.9. Wakati tukinunua hisa hizo, TTCL ilikuwa haijatoa gawio lolote kwa Serikali kwa kipindi cha miaka 15, tangu ilipoingia ubia na Kampuni ya Bharti Airtel mwaka 2001.
Lakini ndani ya kipindi kifupi cha miaka miwili tu, leo tupo hapa kushuhudia TTCL ikitoa gawio la shilingi bilioni 1.5 kwa Serikali. Haya ni mafanikio makubwa ambayo naamini kila mwenye kuitakia mema nchi yetu hana budi kufurahia; japokuwa mimi binafsi gawio hili limenifanya nijiulize maswali mengi sana. Nimejiuliza hivi wakati wa ubia kwa nini Shirika hili lilishindwa kutoa gawio kwa Serikali? Je, tulikuwa tukiibiwa? Je, usimamizi wa utendaji kazi haukuwa mzuri? Ama kulikuwa na hujuma? Mpaka sasa bado sijapata majibu, ingawa nimejifunza jambo moja kuwa sio kila ubia kwenye biashara ni mzuri.
Wageni Waalikwa wote, Mabibi na Mabwana;
Mbali na kupokea gawio, kama mlivyosikia, leo pia tunaishuhudia TTCL ikizindua huduma zake za mawasiliano kwa nchi nzima pamoja na huduma za mkutano mtandao (yaani video conference). Haya, kwa hakika, ni mafanikio makubwa sana, ambayo yanaonesha kuwa Shirika hili linazidi kukua. Na nimeambiwa kuwa katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, TTCL imefanikiwa pia kuongeza idadi ya wateja wake kutoka 247,000 hadi kufikia takriban laki nane hivi sasa. Hii inatupa moyo kwamba uamuzi wa kulirejesha Shirika hili Serikalini ulikuwa sahihi.
Hivyo basi, napenda nitumie fursa hii, kuipongeza Wizara, Bodi, Menejimenti pamoja na Watumishi wote wa TTCL kwa kuwezesha kupatikana kwa mafanikio haya. Bila ninyi mafanikio haya yasingepatikana. Hivyo, tembeeni kifua mbele. Nakumbuka wakati nawateua Mwenyekiti wa Bodi na Mkurugenzi Mkuu niliwapa maagizo ya kufanya mabadiliko kwenye Shirika hili. Mafanikio yaliyopatikana yanaonesha kuwa mlizingatia maelekezo yangu. Hongereni sana. Na hii inadhihirisha kuwa sisi Watanzania tukiamua, tunaweza.
Lakini zaidi ya hapo, kupitia kwa Bwana Kindamba, mafanikio haya ni uthibitisho kuwa, vijana wakipewa majukumu wanaweza sana. Na hii ndio sababu mara nyingi nimekuwa nikiteua vijana kushika nyadhifa mbalimbali Serikalini. Na kwa bahati nzuri, mpaka sasa, wengi niliowateua hawajaniangusha. Hivyo, naahidi nitaendelea kuwateua vijana kushika nafasi mbalimbali.
Waheshimiwa Viongozi;
Wageni Waalikwa wote, Mabibi na Mabwana;
Sekta ya mawasiliano na hasa mawasiliano ya simu, ni sekta nyeti ambayo imeleta mageuzi makubwa duniani katika kipindi cha hivi karibuni. Takwimu zinaonesha kuwa takriban watu bilioni 5 wanatumia simu za mikononi duniani hivi sasa. Hapa nchini kwetu, kwa takwimu za hivi karibuni, watu takriban milioni 40 wanatumia simu za mikononi. Sekta hii pia ni chanzo kikubwa cha mapato. Nakumbuka mwaka jana, tulipotembelewa na aliyekuwa Waziri Mkuu wa Ethiopia, Hailemariam Desalegn, alipata kunieleza kuwa mwaka 2016 Shirika la Simu la Ethiopia lilikusanya mapato yanayofikia Dola za Marekani bilioni 1.3, ambazo ziliwasaidia kujenga reli kutoka Addis Ababa hadi Bandari ya Djibouti.
Sambamba na hayo, sekta hii ya mawasiliano inatoa fursa nyingi za ajira. Mathalan, nimearifiwa kuwa TTCL imetoa ajira zipatazo 1,500 kwa Watanzania. Nchi yetu ina kampuni za simu takriban 8; hivyo ukijumlisha wauza vocha, watoa huduma za fedha kwa njia za mtandao, mafundi wa simu, n.k; unaweza kukadiria mwenyewe ni watu wangapi wamepata ajira kupitia sekta hii hapa nchini. Zaidi ya hapo, sekta hii ya mawasiliano ya simu imesaidia sana kuboresha maisha ya wananchi.
Hivi karibuni mlisikia kuwa nchi yetu iliibuka kidedea katika masuala ya uchumi jumuishi kwa Nchi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara. Moja ya mambo yaliyochangia kupatikana kwa mafanikio hayo ni kuongezeka kwa huduma za fedha kwa njia ya simu (T-Pesa, Tigo Pesa, M-Pesa, Airtel Money, n.k.). Na nimeambiwa kuwa hivi sasa wastani wa miamala ya fedha inayofanyika kwa njia ya simu nchini inafikia thamani ya shilingi trilioni 10 kwa mwezi. Hii imesaidia sana kuimarisha huduma za kifedha katika nchi yetu. Lakini, sekta hii pia imesaidia kuboresha huduma nyingine za kijamii, ikiwemo elimu na afya, kupitia huduma kama e-education, e-medicine, n.k.
Waheshimiwa Viongozi, Mabibi na Mabwana;
Ni kutokana na faida hizo za mawasiliano ya simu nilizozitaja, Serikali iliamua kufufua Shirika hili la Mawasiliano Tanzania. Mbali na kununua hisa kutoka Kampuni ya Bharti Airtel, tuliamua kulifutia Shirika hili madeni yenye thamani ya shilingi bilioni 100 ili yatumike kuwa sehemu ya mtaji. Na kupitia rasilimali zake, TTCL ilifanikiwa kukopa kiasi cha shilingi bilioni 96 kwa ajili ya kuongeza uwekezaji.
Vilevile, tuliiwezesha TTCL kupata masafa ya Megahezi 1,800 na 2,100 ili iweze kufunga mitambo ya mawasiliano ya teknolojia ya 2G (GSM), 3G (UMTS) na 4G (LTE) na hivyo kuondokana na teknolojia ya kizamani waliyokuwa wakitumia ya CDMA. Aidha, tuliikabidhi TTCL dhamana ya kusimamia na kuendesha Mkonga wa Taifa wa Mawasiliano na Kituo cha Kitaifa cha Kuhifadhi Kumbukumbu za Kimtandao (National Internet Data Centre). Hii imetuhakikishia usalama wa nchi yetu.
Nirudie tena kuwapongeza viongozi na watendaji wote wa TTCL kwa kazi kubwa na nzuri mnazofanya. Na binafsi nina imani, kutokana na kasi hii kubwa mnayokwenda nayo, baada ya kipindi kifupi kijacho, TTCL itakuwa imerejea kwenye hadhi yake na kuweza kutimiza malengo yaliyowekwa wakati wa kuanzishwa kwake mwaka 1993 kufuatia uamuzi wa kuligawa Shirika la Posta na Simu. Na ninafurahi Shirika la Posta nalo sasa limeanza kufanya kazi vizuri.
Nitumie fursa hii pia kuipongeza Kamati ya Bunge ya Miundombinu kwa kuishawishi Wabunge wengine kuridhia Sheria Mpya iliyoanzisha Shirika jipya la Mawasiliano la Tanzania. Aidha, nampongeza Mheshimiwa Spika, Naibu Spika pamoja na Wabunge wote wa Bunge letu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuiunga mkono Serikali katika jitihada mbalimbali za kuleta maendeleo kwa nchi yetu. Hivi sasa tumeleta mapendekezo Bungeni kuhusu kuanzisha Akanti Jumuishi ya Serikali (Single Akaunti) ili kupunguza gharama za uendeshaji. Hivi sasa tuna akaunti takriban 1,013. Zaidi ya hapo, Akaunti hii Jumuishi itasaidia kudhibiti matumizi ya fedha za Serikali. Nina imani kuwa Waheshimiwa Wabunge wataliunga mkono pendekezo hilo.
Waheshimiwa Viongozi;
Wageni Waalikwa wote, Mabibi na Mabwana;
Tumekuja hapa kupokea fedha. Na kama nilivyosema awali, leo mimi ni mtu mwenye furaha sana. Kwa hiyo sitapenda kuwachosha kwa hotuba ndefu. Hata hivyo, kabla ya kuhitimisha naomba mniruhusu niseme mambo machache ya mwisho.
Kwanza, ni kwenu wafanyakazi wa TTCL. Napenda kuwahimiza kuchapakazi kwa uzalendo na bidii. Nimewasifia kwa mafanikio makubwa mliyoyapata ndani ya kipindi kifupi. Lakini msibweteke. Bado mna safari ndefu ya kufikia malengo tuliojiwekea. Hivyo basi, nawasihi sana ongezeni bidii. Boresheni huduma zenu na kuhakikisha zinapatikana kwa gharama nafuu. Itunzeni miundombinu mliyonayo. Lakini zaidi ya hapo, jitahidini kuwa wabunifu katika kubuni bidhaa mpya kwa ajili ya soko.
Shirika la Simu la Ethiopia limeweza kubuni Huduma ya Taarifa za Masoko ya Bidhaa. Wakulima wengi nchini Ethiopia wanaipenda sana huduma hii kwa vile inawapa taarifa za bei za mazao yao kwa wakati (yaani real time). Nchini Ghana, walibuni huduma ya kugundua uhalali au ubora wa bidhaa. Mtu akinunua bidhaa tu, anaingiza code ya bidhaa hiyo kwenye simu yake na muda huo huo anagundua kama bidhaa hiyo ni halisi au feki? Na ninyi mnaweza kuanzisha huduma kama hizo na kubuni bidhaa nyingine za namna hiyo ili kupata wateja wengi zaidi.
Pili, napenda kuhimiza menejimeti ya TTCL kutokuwa na kigugumizi katika kukusanya madeni kwa wateja. Kumbukeni kuwa mko kwenye ushindani wa kibiashara. Msipokusanya madeni kutoka kwa wateja wenu, hamtaweza kushindana. Hivyo, hakikisheni mnakusanya madeni yenu kwa wakati. Msibembeleze mtu. Biashara haina kubembelezana.
Tatu, nafahamu kuwa hivi sasa Serikali ipo kwenye majadiliano kuhusu mgogoro wa kibiashara na Kampuni ya Bharti Airtel. Nina imani majadiliano hayo, kama yatakamilika kama tunavyotarajia, yatatoa fursa kubwa zaidi ya kuliimarisha zaidi Shirika letu la Mawasiliano. Hivyo basi, nazihimiza pande zote mbili kuongeza kasi ya majadiliano hayo ili muafaka upatikane mapema.
Nne, napenda nitumie fursa hii kutoa wito kwa Watanzania kuiunga mkono TTCL. Kama mlivyosikia, sasa TTCL inatoa huduma nchi nzima na huduma zake ni za kiwango cha juu kabisa. Hivyo basi, kama kaulimbiu ya TTCL inavyosema, nawasihi Watanzania “Rudini nyumbani – kumenoga”. Na katika hili, niseme tu kwamba nitashangaa sana, endapo Watumishi wenzangu tunaolipiwa huduma za simu na Serikali tutashindwa kujiunga na mtandao huu wa TTCL. Nitashangaa sana.
Lakini pia, nitashangaa endapo taasisi za Serikali na hata sekta binafsi zitashindwa kutumia huduma mpya ambayo tumeizindua muda mfupi ujao ya mkutano mtandao (video conference). Nitashangaa sana. Huduma hii itasaidia kupunguza gharama za kusafiri ama kukodisha kumbi za mikutano. Hivyo basi, nawasihi sana mjiunge na huduma hii inayotolewa na shirika letu la mawasiliano tena kwa gharama nafuu sana.
Tano, napenda kutumia fursa hii kuagiza taasisi na mashirika mengine yenye kustahili kutoa gawio kwa Serikali kufanya hivyo. Nafahamu kuwa kuna takriban mashirika na taasisi zipatazo mashirika 91 zenye kustahili kutoa gawio kwa Serikali. Lakini si zaidi ya mashirika au taasisi 50 ndio yamekuwa yakitoa gawio kwa Serikali. Mathalan, mwaka 2014/2015 ni mashirika 24 tu ndio yalitoa gawio lenye thamani yake ilikuwa shilingi bilioni 130.686. Mwaka 2015/2016 mashirika 25 yalitoa gawio la shilingi bilioni 249.3. Na baada ya kuanza kuwabana, mwaka jana (2016/2017) mashirika 38 yalitoa gawio Serikalini lenye thamani ya shilingi bilioni 677. Hii inadhirisha kuwa yapo mashirika mengi hayatoi gawio.
Hivyo basi, namuagiza Msajili wa Hazina kuhakikisha mashirika na taasisi zote zenye kustahili kutoa gawio kwa Serikali zinafanya hivyo. Yatakayoshindwa kufanya hivyo, viongozi wake wabadilishwe ama yafutwe. Naamini tukiyabana mashirika hayo, tutaweza kukusanya mapato mengi zaidi ambayo yatatuwezesha kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo na kuboresha huduma za jamii kwa wananchi wetu.
Waheshimiwa Viongozi;
Wageni Waalikwa wote, Mabibi na Mabwana;
Napenda kuhitimisha kwa kurudia tena kumshukuru Mheshimiwa Waziri Prof. Mbarawa pamoja na uongozi wa TTCL kwa kunialika kwenye tukio hili. Aidha, nawapongeza tena wafanyakazi wa TTCL kwa kazi nzuri na kubwa mnayoifanya. Napenda niwaahidi kuwa Serikali ipo pamoja nanyi, na tutaendelea kuwaunga mkono ili muweze kuongeza ushindani kwenye sekta hii ya mawasiliano nchini ili hatimaye wananchi wetu wanufaike kwa huduma bora zinazopatikana kwa gharama nafuu.
Mwisho lakini sio mwisho kwa umuhimu, nitumie fursa hii kuwapongeza TTCL kwa kutoa ajira ya ulinzi kwa Shirika la Suma-JKT.
Baada ya kusema hayo, sasa nipo tayari kupokea Hundi ya Gawio la Serikali la Shilingi Bilioni 1.5 kutoka TTCL.
Mungu Ibariki TTCL!
Mungu Wabariki Wafanyakazi wa TTCL!
Mungu Ibariki Tanzania!
“Ahsanteni sana kwa Kunisikiliza”

- May 19, 2018
HOTUBA YA MHE. DKT. JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA KWENYE SHEREHE ZA KUKABIDHI KOMBE LA MASHINDANO YA AFRIKA MASHARIKI KWA...
Soma zaidiHotuba
HOTUBA YA MHE. DKT. JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI,
RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA KWENYE SHEREHE ZA KUKABIDHI KOMBE LA MASHINDANO YA AFRIKA MASHARIKI KWA TIMU YA TAIFA YA VIJANA WENYE UMRI CHINI YA MIAKA 17 NA MSHINDI WA LIGI KUU YA TANZANIA BARA UWANJA TAIFA, DAR ES SALAAM, TAREHE 19 MEI 2018
Mheshimiwa Dkt. Harrison Mwakyembe, Waziri wa Habari,
Utamaduni, Sanaa na Michezo;
Mheshimiwa Juliana Shonza, Naibu Waziri wa Habari,
Utamaduni, Sanaa na Michezo;
Mheshimiwa Paul Makonda, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam;
Bwana Leodger Chillah Tenga, Mwenyekiti wa Baraza
la Michezo Tanzania (BMT);
Bwana Wallace Karia, Rais wa Shirikisho la Mpira
wa Miguu Tanzania (TFF);
Waheshimiwa Viongozi na Wachezaji wa Mpira
wa Miguu na Michezo mingine mliopo;
Ndugu Wadhamini, Washabiki na Wapenzi wa Michezo mliopo;
Ndugu Wananchi Wenzangu, Mabibi na Mabwana:
Awali ya yote, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kufika hapa. Aidha, namshukuru Mheshimiwa Waziri Dkt. Mwakyembe pamoja na Uongozi wa TFF kwa kunialika ili niweze kushiriki kwenye tukio hili la leo. Napenda kutumia fursa hii, hapa mwanzoni kabisa, kusema kuwa, mimi ni shabiki wa Timu ya Taifa, yaani Taifa Stars.
Nitumie fursa hii pia kuwapongeza wachezaji wa Timu za Simba na Kagera Sugar kwa burudani nzuri ambayo tumetoka kushuhudia muda mfupi uliopita. Kwa kweli mchezo ulikuwa mzuri. Timu zote zimejitahidi kuonesha uwezo wao wa kusakata kabumbu. Hongereni sana wachezaji wa Simba na Kagera Sugar. Lakini zaidi, naipongeza Timu ya Kagera Sugar kwa ushindi mlioupata.
Ndugu Washabiki na Wapenzi wa Michezo;
Kama mnavyofahamu, hivi karibuni Vijana wetu wa Serengeti Boys walifanikiwa kuchukua Kombe la Mashindano ya Afrika Mashariki kwa Vijana chini ya Umri wa Miaka 17 (CECAFA U17), ambayo yaliyofanyika nchini Burundi. Binafsi, nilikuwa nikifuatilia kwa karibu mashindano yale. Nilishuhudia mwenyewe jinsi vijana wetu walivyojituma na kucheza mchezo mzuri hadi kufanikiwa kuchukua Kombe.
Kutokana na ushindi huo mkubwa walioupata, nikaona ni vyema nikutane nao ili niwapongeze. Hivyo basi, napenda kutumia fursa hii kuwapongeza kwa dhati kabisa wachezaji pamoja na walimu wa Serengeti Boys kwa kututoa kimasomaso na kuchukua kombe hilo. Hongereni sana. Na bila shaka, huu ni mwanzo tu. Nina matumaini makubwa kuwa hata mwakani Kombe la Afrika litabaki hapa nchini.
Nitumie fursa hii pia kuipongeza Timu yetu ya Wasichana wanaoishi Mazingira Magumu ambayo ilishiriki Mashindano ya Kombe la Dunia nchini Urusi na kushika nafasi ya pili. Nao wameipeperusha vyema bendera ya nchi yetu na kututangaza kimataifa. Hongera sana kwa wachezaji, walimu na viongozi wa Timu hiyo. Wito wangu kwa TFF, Vyama vingine vya Michezo, Vilabu pamoja na Wadhamini mbalimbali, endeleeni kushirikiana katika kuibua vipaji na pia kuviendeleza. Wakati mwingine tumekuwa tunaibua vipaji lakini tunashindwa kuviendeleza. Binafsi, nitafurahi sana kama baadaye nitasikia vijana hawa wa Serengati Boys na Timu ya Taifa ya Watoto wanaoishi Mazingira Magumu wakichezea Timu zetu za Taifa ya Wakubwa au hata vilabu vikubwa vya hapa nchini ama nje ya nchi.
Waheshimiwa Viongozi, Mabibi na Mabwana;
Ukiachilia mbali ubingwa wa Serengeti Boys, nimekuja hapa kukabidhi Kombe la Ligi Kuu ya Tanzania Bara kwa Timu ya Simba. Mimi huwa nafuatilia fuatilia ligi mbalimbali, za hapa nyumbani lakini pia nje ya nchi. Katika ufuatiliaji wangu wa ligi mbalimbali duniani, jumamosi iliyopita, niligundua kuwa ni timu mbili tu ndizo zilikuwa zimechukua ubingwa bila kufungwa. Simba na Barcelona ya Hispania. Barcelona baadaye ikafungwa; lakini na leo Simba nayo wamefungwa. Hata hivyo, kwa namna walivyokuwa wamechukua ubingwa, na kwa kuwa kilikuwa kimepita kipindi kirefu bila ya wao kuchukua ubingwa, niliona nije kuwapongeza. Hivyo basi, napenda kutumia fursa hii kuwapongeza wachezaji, walimu na viongozi wa Simba, akiwemo Msemaji wao, Bwana Haji Manara, kwa kufanikiwa kuchukua ubingwa kwa stahili hii ya pekee. Nafahamu hii sio mara ya kwanza kwa Simba kuchukua ubingwa kwa staili hiyo. Walishawahi kufanya hivyo siku za nyuma.
Nazipongeza timu nyingine zilizoshiriki Ligi kwa kuonesha ushindani, lakini pia kwa kukubali matokeo. Nimefurahi kuwa Msimu huu hakuna Timu iliyokwenda FIFA kudai pointi. Napenda niseme pia kuwa ushindi ambao Timu ya Kagera Sugar leo umeipata umethibitisha kuwa Ligi ilikuwa ya ushindani; lakini pia unatoa changamoto kwa Timu ya Simba kujipanga vizuri zaidi kuweza kuiwakilisha vyema nchi yetu kwenye mashindano ya kimataifa. Na kwa kusema kweli, kwa kiwango hiki kilichooneshwa na Simba leo, endapo wataendelea hivi, hawawezi kufika mbali kimataifa. Ni lazima wajipange vizuri.
Ndugu Wapenzi wa Michezo;
Sababu ya tatu iliyoisukuma kukubali mwaliko wa kuja hapa ni kuunga mkono jitihada za viongozi wapya wa TFF. Kama mnavyofahamu, vyama vingi vya michezo, vikiwemo vilabu, vimekuwa na matatizo mengi ya uongozi. Vimekuwa vikikabiliwa na tuhuma za rushwa, ufisadi, wizi, matumizi mabaya ya madaraka, n.k. Pamoja na ukweli huo, bila shaka, wengi wenu, mtakubaliana nami kuwa, tangu uongozi mpya wa TFF umeingia madarakani umeonesha mabadiliko makubwa. Wanaonesha uadilifu na kujitahidi kufuata sheria na kanuni. Ni kweli, mapungufu bado yapo, lakini wanajitahidi.
Kutokana na jitihada walizoanza kuzifanya, nimeona nikubali mwaliko wao kwanza ili kuwaunga mkono, lakini pili, kuwapa moyo kuendelea na jitihada hizo. Na niwape moyo TFF, “endeleeni na jitihada hizo”. Serikali inawaunga mkono. Na napenda kutumia fursa hii, pia kuviomba vyama vingine vya michezo kuiga mfano huu ulioanza kuoneshwa na Viongozi wapya wa TFF. Tusiruhusu Vyama vyetu vya Michezo kuwa vichaka vya kujificha wahalifu.
Waheshimiwa Viongozi;
Ndugu Wanamichezo;
Mabibi na Mabwana;
Michezo ni burudani. Michezo ni afya. Michezo ni ajira. Lakini pia, katika dunia ya sasa, michezo ni biashara kubwa. Kwa kutambua hilo, Serikali ya Awamu ya Tano ninayoiongoza itaendeleza jitihada zilizoazishwa na Serikali zilizotangulia katika kukuza sekta ya michezo nchini. Na napenda kutumia fursa hii kuipongeza sana Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, chini ya Dkt. Mwakyembe, kwa jitihada mbalimbali inazofanya kuimarisha sekta ya michezo nchini.
Serikali inaahidi kuendelea kutenga bajeti kwa ajili ya michezo. Tutaendelea kutoa mafunzo na kuajiri wataalam wa michezo. Zaidi ya hapo, tutaendelea kujenga miundombinu ya michezo mbalimbali. Hivi karibuni, tunatarajia kuanza ujenzi wa Uwanja Mkubwa wa Kisasa kwenye Jiji la Dodoma kwa kushirikiana na marafiki zetu wa Morocco. Nitumie fursa hii kuzihimiza Halmashauri zote nchini kuendelea kutenga maeneo ya michezo na kuhakikisha hayavamiwi. Aidha, nakihimiza Chama changu (CCM) ambacho kinamiliki viwanja vingi nchini, nacho kuboresha viwanja vyake. Kwa Watanzania, hususan washabiki na wapenzi wa michezo nchini, nawasihi kuilinda miundombinu inayojengwa. Tukio kama lile la kung’oa viti uwanjani halipaswi kujirudia tena.
Sambamba na hayo, Serikali itaendelea kushirikiana, kwa hali na mali, na Vyama vyote vya Michezo katika kuziandaa Timu zetu za Taifa ili zituwakilishe vyema kwenye mashindano ya kimataifa. Mathalan, kama nilivyogusia awali, mwezi Aprili mwakani, nchi yetu itakuwa mwenyeji wa Mashindano ya Afrika ya Vijana chini ya umri wa Miaka 17. Napenda niahidi kuwa Serikali itashirikiana na TFF katika kufanikisha maandalizi ya mashindano hayo; lakini pia katika kuiandaa Serengeti Boys ili kombe hilo libaki hapa nchini, na kuweza kuhitimisha dhana kuwa sisi ni “kichwa cha mwendawazi”.
Niwaombe wadau na wadhamini mbalimbali kuendelea kushirikiana na Serikali pamoja na Vyama vya Michezo na Vilabu katika kuinua sekta ya michezo nchini. Mimi naamini, kama sote tukishirikiana, sekta ya michezo itazidi kukua na kuchangia maendeleo ya nchi yetu.
Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wanamichezo;
Sikuja hapa kuhutubia. Nimekuja hapa kuungana na Timu zetu ambazo zimeshinda mashindano mbalimbali. Timu ya Serengeti Boys, Timu ya Wasichana wanaoishi Mazingira Magumu pamoja na Timu ya Simba. Nazipongeza sana timu hizo zote kwa ushindi walioupata. Lakini, nitumie fursa hii pia kutoa wito kwa wanamichezo na Watanzania kwa ujumla kujipanga vizuri katika michezo. Kwa muda mrefu, tumekuwa wasindikizaji. Sasa tubadilike ili angalau timu zetu ziweze kushinda mashindano ya Afrika na kushiriki mashindano ya Kombe la Dunia. Watanzania wengi wanatamani kuona timu zao zikishinda na sio kila siku kuwa wasindikizaji. Hii ndio sababu nimekuja hapa kutoa hamasa kwa timu zetu zote. Na niseme tu kwamba, timu yoyote itakayoshinda, mimi nitaipongeza. Iwe Simba, Yanga, Kagera au timu nyingine yoyote ile, nitaipongeza. Ninachotaka mimi ni kuona timu zetu za michezo yote, zinashinda. Na kwa kweli, timu zetu zinao uwezo wa kushinda. Kinachohitajika ni kujiandaa na kujipanga vizuri.
Nihitimishe kwa kuishukuru tena Wizara na TFF kwa kunialika. Aidha, narudia tena kuzipongeza Timu za Serengati Boys, Timu ya Simba na Timu ya Wasichana wanaoishi Mazingira Magumu kwa ushindi walioupata. Nimefurahi kuwa leo Uwanja umejaa. Hongereni sana wapenzi na washabiki kwa kujitokeza kwa wingi.
Baada ya kusema hayo, sasa nipo tayari kutekeleza jukumu lililonileta la kukabidhi Kombe kwa timu zetu za Serengeti Boys, Timu ya Wasichana wanaoishi Mazingira Magumu pamoja na Simba Sports Club.
Mungu Ibariki Sekta ya Michezo nchini!
Mungu Ibariki Tanzania!
“Ahsanteni sana kwa kunisikiliza”

- May 07, 2018
HOTUBA YA MHESHIMIWA DKT. JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA KWENYE CHUO KIKUU CHA KILIMO CHA SOKOINE, MOROGORO, TAREHE 7 MEI,...
Soma zaidiHotuba
HOTUBA YA MHESHIMIWA DKT. JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA KWENYE CHUO KIKUU CHA KILIMO CHA SOKOINE, MOROGORO, TAREHE 7 MEI, 2018
Mheshimiwa Prof. Joyce Ndalichako;
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi;
Mheshimiwa Steven Kebwe,
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro;
Prof. Raphael Chibunda, Makamu Mkuu wa Chuo
Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA);
Prof. Lughano Kusiluka, Makamu Mkuu wa Chuo
Kikuu cha Mzumbe;
Rasi na Manaibu Rasi wa Chuo Kikuu cha SUA;
Viongozi Wengine wa Serikali mliopo;
Waheshimiwa Viongozi wa Dini mliopo;
Ndugu Wanajumuiya wa Chuo Kikuu Kilimo
Cha Sokoine (SUA)
Wageni Waalikwa wote, Mabibi na Mabwana:
Awali ya yote, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kufika hapa Chuo Kikuu cha Kilimo; Chuo ambacho kimepewa Jina la mmoja wa viongozi mahiri, shupavu na mtetezi wa wanyonge, aliyewahi kutokea katika nchi yetu, Hayati Edward Moringe Sokoine. Ingawa ametangulia mbele za haki, nina imani, kupitia jina la Chuo hiki, Watanzania wengi, kizazi kwa kizazi, wataendelea kumkumbuka na kumuenzi Kiongozi wetu huyo.
Napenda pia kutumia fursa hii kuwashukuru wana-SUA kwa mapokezi yenu mazuri. Nafahamu kuwa kama sio wote basi wengi weu hapa mlinipigia kura. Hivyo basi, kwa kuwa hii ni mara yangu kufika hapa tangu nimechaguliwa, napenda nitumie fursa hii kuwashukuru kwa dhati kabisa kwa kunichagua kuwa Rais wenu. Nasema “ahsanteni sana wana-SUA”. Niwaahidi tu kwamba sitowaangusha. Nitakuwa pamoja nanyina wakati wote.
Ndugu Wanajumuiya wa SUA;
Mabibi na Mabwana;
Tangu ijumaa iliyopita nimekuwa kwenye ziara ya Mkoa huu wa Morogoro. Nimepata fursa ya kukutana na kuzungumza na wananchi na halikadhalika kufanya shughuli mbalimbali za maendeleo. Nimeweka Jiwe la Msingi la Barabara ya Kidatu – Ifakara yenye urefu wa kilometa 66.9 inayojengwa kwa gharama ya shilingi bilioni 104.5. Nimeshiriki Uzinduzi wa Daraja la Kilombero lenye urefu wa mita 384, ambalo ni la nne kwa ukubwa nchini na ambalo wameamua kulipa jina la Magufuli.
Jana niliingia hapa Morogoro mjini, ambapo mchana nilizindua Stendi ya Kisasa ya Mabasi pale Msamvu. Leo asubuhi nilitakiwa niondoke kurudi Dar es Salaam. Sikuwa nimepangiwa kuja hapa SUA. Lakini, nikasema hapana; siwezi kumaliza ziara yangu bila kufika hapa SUA; Chuo Kikuu cha pekee cha Kilimo hapa nchini. Hii ndio maana mnaniona nipo hapa muda huu.
Ndugu Wananchi, Mabibi na Mabwana;
Nimekuja hapa kwa sababu kubwa tatu. Kwanza kuwasalimu wana-Jumuiya wa Chuo Kikuu hiki. Sababu ya pili iliyonileta hapa ni kutambua mchango mkubwa unaotolewa na Chuo hiki katika maendeleo ya nchi yetu. Hakuna shaka yoyote kuwa Chuo hiki, tangu kianzishwe tarehe 1 Julai, 1984 kimetoa mchango mkubwa katika maendeleo ya nchi yetu, kupitia kozi mbalimbali kinazofundisha na tafiti kilizofanya katika fani mbalimbali (sayansi ya kilimo, misitu, tiba ya mifugo, ufugaji wa samaki, maendeleo vijijini, utalii, ualimu, n.k.). Na mojawapo ya tafiti kubwa zilizowahi kufanywa na Chuo hiki, ambazo zinatambulika kimataifa, ni ule wa kuwafundisha panya kubaini mabomu na kuweza kugundua vimelea vya ugonjwa wa Kifua Kikuu.
Nitumie fursa hii, kukipongeza sana Chuo hiki kwa utafiti huo mkubwa ambao umeiletea sifa kubwa nchi yetu. Kwa hakika, mmetekeleza kwa vitendo dhamira ya Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, ya kuanzisha Chuo hiki. Nawapongezeni pia kwa ubunifu wenu wa kuongeza idadi ya kozi na fani mnazozifundisha. Nafahamu kuwa wakati Chuo hiki kinaanzishwa mwaka 1984, kilikuwa na vitivo vitatu tu; yaani kitivo cha kilimo, kitivo cha misitu na kitivo cha tiba ya mifuko. Sasa mmeongeza kozi nyingine, ikiwa ni pamoja na utalii, maendeleo vijijini, ualimu, n.k. Hongereni sana.
Ndugu Wanajumuiya wa SUA;
Sababu ya tatu iliyonisukuma kuja hapa leo ni kuwapa moyo na kuamsha ari na hamasa mpya kwenu ya kuendelea kujituma zaidi. Na katika hili, naomba nitaje maeneo machache, ambayo nitatamani sana Chuo hiki kiyape kipaumbele cha kutosha.
Eneo la kwanza ni kuendelea kufanya utafiti wa mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi. Ndugu zangu wana-SUA, mimi niliwahi kuwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi. Ninafahamu, kama tukiweka mkazo na kuisimamia vizuri sekta hizi za kilimo, mifugo na uvuvi, nchi yetu itapata maendeleo ya haraka. Hii ni kwa sababu takriban asilimia 70 ya Watanzania wanaendesha maisha yao kupitia shughuli za kilimo, mifugo na uvuvi. Aidha, nchi yetu inashika nafasi ya pili kwa kuwa na idadi kubwa ya mifugo Barani Afrika. Zaidi ya hapo, tunayo maeneo mengi yenye kufaa kufanya shughuli za uvuvi. Hivyo basi, ni wazi kuwa endapo tutaziwekea mkazo sekta hizi; tutapiga hatua kubwa kimaendeleo.
Sambamba na hilo, hivi sasa nchi yetu imejipanga kujenga uchumi wa viwanda kwa lengo la kuharakisha maendeleo na kukabiliana na tatizo la ajira. Viwanda tunavyovilenga kuvijenga ni vile vyenye kutumia malighafi zinazopatikana kwa wingi hapa nchini, hususan mazao ya kilimo, mifuko na uvuvi. Hii yote inafanya sekta hii ya kilimo, mifugo na uvuvi kuwa na umuhimu wa pekee kwa nchi yetu. Hii ndio sababu nakisisitiza sana Chuo hiki cha pekee cha Kilimo nchini kuendelea kufanya tafiti zaidi ili kuongeza uzalishaji wa mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi na hatimaye kuiwezesha nchi yetu kufanya mageuzi ya kiuchumi.
Nimefurahi wakati nikija hapa nimeona shamba lenu zuri la mfano. Nimeona mipapai midogo kabisa ikiwa tayari imezaa matunda. Hayo ni mafanikio makubwa. Na ni matumaini yangu kuwa utaalamu kama ule utasambazwa kwenye maeneo mengi ya nchi yetu. Tunataka wakulima wetu wajifunze mbinu za kisasa za kilimo ili waongeze uzalishaji. Na mahali pekee pa kujifunza mbinu hizo ni kwenye Chuo chenu hiki. Hakuna mahali pengine. Hii ndio sababu Serikali inakithamini sana Chuo hiki. Na nitumie fursa hii kuwahakikishia kuwa tutaendelea kuwathamini na kushirikiana kwa karibu na ninyi. Baadhi yenu mtakuwa mkifahamu kuwa, mimi, tangu nikiwa Waziri mpaka sasa nimekuwa Rais, nimekuwa nikiwaamini sana wasomi wa Chuo hiki na nimewateua kushika nyadhifa mbalimbali. Naahidi nitaendelea kuwatumia wasomi wa Chuo hiki. Na katika kudhihirisha dhamira ya Serikali ya kutaka kuona Chuo hiki kinachangia maendeleo ya kilimo nchini, leo niwaahidi kuwapatia fedha za kununua matrekta 10 mapya kwa ajili ya kufanya mafunzo ya vitendo.
Ndugu Wana-SUA;
Ukiachilia mbali utafiti wa mazao, eneo jingine ambalo nitafurahi kama mtalipa kipaumbele ni sekta ya utalii. Kama mnavyofahamu, nchi yetu ina vivutio vingi vya utalii. Na hivi sasa tumeanza kutekeleza mikakati mbalimbali ya kuikuza sekta hii ili iweze kutunufaisha zaidi kuliko ilivyo sasa. Tumejipanga kuanza kutangaza vivutio vyetu vyote, vikiwemo vya Ukanda wa Kusini, ambavyo ni karibu kabisa na hapa Morogoro. Sambamba na hayo, tunaimarisha miundombinu na huduma za usafiri, hususan usafiri wa ndege. Tunajenga viwanja vya ndege lakini pia tumenunua ndege mpya saba, tatu tayari zimeshawasili. Tumefanya hivyo kwa vile tunatambua kuwa ustawi wa sekta ya utalii kwa kiwango kikubwa inategemea usafiri wa anga. Takriban asilimia 70 ya watalii husafiri kwa kutumia ndege.
Kutokana na hatua tunazozichukua, ni wazi kuwa idadi ya watalii itaongezeka. Hii maana yake ni kwamba, nchi yetu itahitaji wataalam na watoa huduma wenye katika sekta ya utalii. Ni kwa sababu hiyo, narudia tena kukipongeza Chuo hiki kwa kuanzisha kozi ya utalii. Ombi langu kwenu endeleeni kuboresha elimu mnayoitoa na pia shirikianeni na mamlaka husika za utalii nchini katika kuibua na kutangaza vivutio vipya vya utalii. Vipo vivutio vingi ambavyo bado hatujavitangaza.
Waheshimiwa Viongozi;
Ndugu Wanajumuiya wa SUA;
Mabibi na Mabwana;
Moja ya vipaumbele vya Serikali ya Awamu ya Tano ni kuimarisha na kuboresha elimu nchini. Tangu tumeingia madarani tumechukua hatua mbalimbali kuendeleza jitihada zilizoanzishwa na Awamu zilizotangulia katika kuimarisha na kuiboresha sekta ya elimu nchini. Kama mjuavyo, elimu yetu imetoka mbali na kupitia kwenye changamoto nyingi. Hivyo basi, kwa upande wetu, tuliamua tuanze kwa kutoa elimu bila malipo kuanzia shule ya msingi hadi sekondari, ambapo kila mwezi tunatenga shilingi bilioni 23.868 kuigharamia. Tangu utaratibu huu uanze mwezi Desemba 2015 hadi mwezi Machi 2018, Serikali imetumia takriban shilingi bilioni 650.
Uamuzi huu wa kutoa elimu bila malipo umeongeza idadi ya wanafunzi wanaoanza darasa la kwanza na kidato cha kwanza maradufu. Mathalan, kwa upande wa shule ya msingi, idadi ya wanafunzi wanaoanza darasa la kwanza imeongezeka kutoka wastani wa watoto milioni 1 hadi kufikia milioni 2. Kwa upande wa sekondari idadi ya wanafunzi wanaodahiliwa kidato cha kwanza imeongezeka kwa wastani wa takriban asilimia 30. Hii maana yake ni kwamba watoto wengi, hususan kutoka familia masikini, walikuwa wakishindwa kupata elimu kwa kukosa ada au karo.
Kwa upande wa Elimu ya Juu, ninyi hapa mnafahamu vizuri, kuwa tumeongeza idadi ya wanafunzi wanaonufaika na mikopo kutoka 98,300 mwaka 2015 hadi kufikia takriban 124,000 hivi sasa. Hii imewezekana baada ya Serikali kuongeza bajeti ya mikopo kutoka shilingi bilioni 365. Mwaka wa Fedha 2015/2016 hadi kufikia shilingi bilioni 427 Mwaka 2017/2018. Na siku hizi fedha za mikopo zinatoka kwa wakati. Hata hivyo, ni ukweli kuwa, kutokana na rasilimali fedha kuwa ndogo na mahitaji kuwa makubwa, imefanya isiwe rahisi kutoa mikopo kwa wanafunzi wote. Hii ndio sababu tumeamua kuweka baadhi ya vigezo, ikiwemo uwezo wa familia ya mwanafunzi, masomo anayosomea, n.k. Kwa bahati nzuri, kama mlivyosikia, wanafunzi wa Chuo hiki cha Sokoine ni wanufaika wakubwa wa mikopo inayotolewa. Kati ya wanafunzi wapatao 8,000 wa Chuo hiki, zaidi ya wanafunzi wanafunzi 6,000 wamepata mikopo. Tumeamua kuwapatia mikopo wanafunzi wengi wa Chuo hiki kwa sababu hivi sasa nchi yetu inahitaji wataalamu wengi wa kilimo. Kupanga ni kuchagua.
Ndugu Wana-SUA, Mabibi na Mabwana;
Mbali na kuongeza wigo wa elimu kwa kuongeza idadi ya wanafunzi wa elimu msingi na vyuo vikuu, tunaboresha miundombinu mbalimbali ya taasisi zetu za kutolea elimu. Hivi sasa tupo kwenye utekelezaji wa mradi kabambe wa kukarabati shule za sekondari kongwe 88, zikiwemo Kilakala na Mzumbe zilizopo katika Manispaa hii ya Morogoro. Serikali pia imejenga na kukarabati miundombinu ya shule za msingi na sekondari za wananchi zipatazo 542, ambapo mpaka sasa tumetumia kiasi cha shilingi bilioni 88.402. Aidha, tumefanikiwa kumaliza kwa kiasi kikubwa tatizo la uhaba wa madawati kwenye shule nyingi za msingi na sekondari.
Kwa upande wa elimu ya juu, miradi mbalimbali ya miundombinu inaendelea. Mathalan, hapa SUA, kwenye bajeti ya mwaka huu, tumetoa shilingi bilioni 2 kwa ajili ya kujenga maabara kubwa (Multi-purpose Laboratory), ambayo ujenzi wake unatarajiwa kuanza mwezi Juni 2018. Tumetoa pia shilingi milioni 700 kwa ajili ya kujenga Mgahawa (Cafeteria) itakayochukua wanafunzi 400 kwa mpigo, ambayo nimeambiwa kuwa ujenzi wake unatarajiwa kukamilika mwezi Juni 2018. Vilevile, hapa SUA, kwenye bajeti ya Mwaka ujao wa Fedha (2018/2019) tumetenga shilingi bilioni 8 kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo. Na napenda nitumie fursa hii kumwagiza Waziri wa Elimu fedha zilizotengwa kwa ajili ya kujengea Hosteli katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, shilingi bilioni 2, nazo zihamishiwe hapa SUA ili zisaidie kupunguza kwenye Chuo hiki. Nitoe wito kwa uongozi wa Chuo, kuhakikisha wanatumia vizuri fedha zinazoletwa na Serikali kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya Chuo chenu.
Waheshimiwa Viongozi;
Ndugu Wanajumuiya wa SUA;
Mabibi na Mabwana;
Hivi punde nimetoka kusikiliza hoja mbalimbali kutoka kwa wana-Jumuiya wa Chuo hiki. Niseme tu kwa ujumla kuwa hoja zenu nimezipokea. Na kama mtakavyoona, baadhi tayari nimezijibu katika maelezo yangu, hususan kuhusu masuala mikopo na makazi ya wanafunzi. Hoja nyingine nadhani zipo ndani ya uwezo wenu wenyewe kuzitatua. Mathalan, masuala kama michango kuwa mingi kwa wanafunzi wa mwaka wa kwanza, suala la kubebana, n.k. Haya mnaweza kuyatatua ninyi wenyewe. Hivyo basi, nitatumia fursa hii kujibu au kutolea ufafanuzi baadhi ya hoja chache mlizowasilisha.
Kwanza, ni kuhusu suala la kuimarisha uhusiano na nchi ya Israeli, hususan katika masuala ya kilimo. Hili nakubaliana nalo na binafsi sina pingamizi kwa wataalam wetu kutembelea Israeli kwenda kujifunza. Na sio Israeli pekee, pamoja na nchi nyingine. Hatuwezi kuendelea endapo tutabaki tukijifungia tu sisi wenyewe hapa nchini. Hatuna budi tutoke nje ili kupata uzoefu kutoka kwa wenzetu. Na kwa bahati nzuri, nchi yetu ina marafiki wengi ambao wamekuwa wakitupatia fursa nyingi za masomo: Austaralia, China, Cuba, India, Urusi, Marekani, n.k. Lakini kwa bahati mbaya, fursa hizo hatujazitumia vizuri.Hivyo basi, nitoe wito kwa mamlaka husika kuhakikisha nchi yetu inanufaika na fursa hizo za elimu.
Suala la pili ambalo napenda kulizungumzia ni kuhusu madeni ya watumishi. Suala hili nimelieleza kwenye Sherehe za Mei Mosi hivi karibuni. Serikali ina dhamira ya dhati kabisa ya kulipa madeni yote inayodaiwa na watumishi wake. Tangu tumeingia madarakani, tayari tumelipa madai ya watumishi yenye thamani ya takriban shilingi bilioni 220.4. Tuendelea kulipa madeni yaliyosalia kwa kadri tutakavyokamilisha uhakiki. Kama mjuavyo, baadhi ya watumishi hawakuwa wakweli. Walitengeneza madeni mengi ya uongo. Hii ndio sababu inatulazimu tujiridhishe vizuri kabla ya kulipa madeni tunayodaiwa. Hivyo basi, nitoe wito kwa Mheshimiwa Waziri wa Elimu kuwasiliana na vyuo vyako vyote ili kupata madeni halali ya watumishi ili tuweze kuyalipa kwa haraka.
Tatu, ni kuhusu makazi na ofisi za watumishi. Suala hili nalo Serikali inalitambua. Hata hivyo, kutokana na uwezo mdogo wa kifedha na majukumu mengi tuliyonayo hivi sasa, imekuwa sio rahisi kuwapatia watumishi wetu wote makazi. Kama mnavyofahamu, Serikali ina watumishi wapatao laki 5. Hata hivyo, kupitia taasisi na mashirika yetu mbalimbali, tumekuwa tukiendelea kujenga nyumba za gharama nafuu maeneo mbalimbali nchini ili kuwawezesha watumishi kupanga au kununua. Hivyo basi, niwaombe watumishi kuchangamkia fursa hiyo. Aidha, nitumie fursa hii kuziomba taasisi za fedha, hususan benki, kujitahidi kutoa mikopo ya riba nafuu kwa watumishi ili kuwawezesha kununua na kujenga nyumba. Kuhusu tatizo la ofisi, niviombe vyuo vyote nchini kutumia vizuri fedha za malipo ya ada zinazobaki kwenye vyuo kutekeleza miradi ya maendeleo, ikiwemo ujenzi wa ofisi.
Hoja ya mwisho ambayo napenda kuijibu ni kuhusu suala la watumishi wa darasa la saba. Suala hili ni la kisheria na ni hivi majuzi tu Serikali imelitolewa ufafanuzi Bungeni. Lakini, kwa kifupi tu napenda kusema kuwa, Mwaka 2004, Serikali ilitoa Waraka ambao uliweka katazo la kuajiri watu wenye elimu chini ya kidato cha nne kwenye taasisi zake. Uamuzi huu ulifikiwa baada ya kujiridhisha kuwa nchi yetu ilikuwa na wahitimu wengi wa kidato cha nne na kuendelea. Hata hivyo, Waraka huo haukuwahusu watumishi wenye elimu ya darasa la saba ambao tayari walikuwa wameajiriwa. Wao waliendelea na kazi zao kama kawaida kwa vile Sheria hiyo mpya iliwakuta wakiwa tayari kazini. Pamoja na kutolewa kwa Waraka huo, wapo watu, ambao kwa njia za ujanja ujanja, ikiwemo kwa kutumia vyeti vya kughushi, waliajiriwa. Kufuatia zoezi tulilolifanya la uhakiki, tuliwabaini watumishi wa namna hiyo wapatao 14,000 na hivyo ikabidi tuwaondoe kazini. Huu ndio ufafanuzi ambao naweza kuutoa kuhusu suala hili; na kama nilivyosema, hili ni suala la Sheria hivyo sina mamlaka ya kuliingilia.
Waheshimiwa Viongozi;
Ndugu Wanajumuiya wa SUA;
Mabibi na Mabwana;
Kama nilivyosema, nimekuja hapa kuwasalimu lakini pia kuwapa moyo ili muendelee kujituma zaidi. Napenda kurudia tena kuwapongeza kwa kazi nzuri na kubwa mnayoifanya lakini pia nawashukuru kwa mapokezi yenu mazuri. Wito wangu kwenu wana-SUA, hususan wanafunzi, someni kwa bidii. Hili ndilo jukumu lililowaleta hapa. Serikali inawapa mikopo kutoka kwenye kodi tunazokusanya kwa wananchi maskini ili muweze kusoma vizuri na hatimaye muweze kulikombea Taifa letu kiuchumi.
Hivyo basi, narudia sana kuwasihi wanafunzi wa Chuo hiki kuitumia vizuri fursa hii adimu mliyopata. Nitawashangaa sana na kwa kweli sitasita kuchukua hatua kali endapo, badala ya kusoma, ninyi mtatumia muda wenu hapa kufanya mambo mengine ambayo hayaendani kabisa na masuala ya elimu: kushiriki kwenye migomo au kuendesha shughuli za kisiasa. Mkifanya hivyo, nitachukua hatua kali. Na hili siwatishi bali nawaeleza ukweli.
Baada ya kusema hayo, narudia tena kusema kuwa, nakipenda sana Chuo hiki, na Serikali itaendelea kukiimarisha ili kiweze kutimiza malengo ya kuanzishwa kwake.
Mungu Kibariki Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine!
Mungu Ibariki Tanzania!
“Ahsanteni sana kwa kunisikiliza”
.jpg)
- May 03, 2018
HOTUBA YA MHESHIMIWA DKT. JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, KWENYE UFUNGUZI WA BARABARA YA IYOVI - IRINGA –MAFINGA PAMOJA NA...
Soma zaidiHotuba
HOTUBA YA MHESHIMIWA DKT. JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, KWENYE UFUNGUZI WA BARABARA YA IYOVI - IRINGA –MAFINGA PAMOJA NA KIWANDA CHA KUTENGENEZA CHAKULA CHA KUKU (SILVERLANDS TANZANIA LTD)
IHEMI, IRINGA, TAREHE 3MEI, 2018
Mheshimiwa Profesa Makame Mbarawa,
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano;
Mheshimiwa Charles Mwijage, Waziri wa Viwanda,
Biashara na Uwekezaji;
Bibi Camilla Christensen, Naibu Balozi wa Denmark;
Mheshimiwa Amina Masenza, Mkuu wa Mkoa
wa Iringa na Wakuu wa Mikoa wote mliopo;
Waheshimiwa Makatibu Wakuu mliopo;
Mheshimiwa Suleiman Kakoso, Mwenyekiti wa Kamati
ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu;
Waheshimiwa Wabunge na Madiwani wote mliopo;
Viongozi wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama;
Mtendaji Mkuu na Wafanyakazi wa TANROADS;
Viongozi wengine wa Serikali, Vyama vya Siasa
na Dini mliopo;
Waheshimiwa Wageni Wote Waalikwa;
Ndugu Wananchi Wenzangu, Mabibi na Mabwana:
Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia uhai na kutuwezesha kukutana mahali hapa. Nawashukuru pia Waheshimiwa Mawaziri Prof. Mbarawa na Charles Mwijage, Uongozi wa Mkoa wa Iringa pamoja na Uongozi wa Kiwanda cha Silverlands Tanzania Ltd kwa kunialika kuja kuzindua barabara ya Iyovi – Iringa – Mafinga pamoja na Kiwanda cha Kutengeneza Chakula cha Kuku cha Silverlands Tanzania Ltd. Ahsanteni sana kwa kunialika.
Kwa namna ya pekee, napenda niwashukuru wananchi wa hapa Ihemipamoja na wakazi wote wa Wilaya hii ya Iringa Vijijini kwa mapokezi yenu mazuri. Hii ni mara yangu ya kwanza kuja hapa Ihemi tangu niwe Rais wa nchi yetu. Hivyo basi, napenda kutumia fursa hii kuwashukuru sana wana-Ihemi kwa kunipa kura nyingi za “ndiyo” zilizoniwezesha kuchaguliwa. Ahsanteni sana. Nawaahidi nitaendelea kufanya kazi kwa bidii ili kuwatumikia na kuiletea maendeleo nchi yetu.
Ndugu Wananchi Wenzangu, Mabibi na Mabwana:
Kama mtakavyokumbuka, moja ya ahadi kubwa tulizotoa wakati wa kampeni ilikuwa kujenga uchumi wa viwanda. Nakumbuka pia tulitaja na kuelezea sifa za viwanda tulivyolenga kuvijenga. Kwanza, vyenye kuajiri watu wengi ili kupunguza tatizo la ajira nchini. Pili, vyenye kutumia malighafi zinazopatikana kwa wingi hapa nchini ili mazao yetu na rasilimali nyingine tulizonazo zipate masoko. Tatu, ambayo bidhaa zake zinatumika kwa wingi hapa nchini na pia kuweza kuuzwa nje ya nchi. Lengo hapa ni kupunguza utegemezi wa kununua bidhaa kutoka nje, lakini pia kuipatia nchi yetu fedha za kigeni. Na nne, vyenye kutumia teknolojia ya kati ili iwe rahisi kwa wananchi wetu kujifunza.
Kiwanda cha Silverlands Tanzania Ltd kinazo sifa zote hizo nne nilizozitaja. Kinaajiri watu wengi. Tumesikia hivi punde kuwa Kiwanda kimetoa ajira zipatazo 938. Hii ni idadi kubwa. Kiwanda pia kinatumia malighafi nyingi za hapa nchini. Wamesema wenyewe hapa, asilimia 80 ya malighafi za Kiwanda chao zinapatikana hapa hapa nchini. Mahindi na Soya. Hii inamaanisha kuwa wakulima wa mazao hayo, hususan wa Wilaya hii ya Iringa Vijijini, hivi sasa wana uhakika wa soko la mazao yao. Aidha, bidhaa zinazozalishwa na Kiwanda (yaani chakula cha kuku) zinatumika kwa wingi hapa nchini. Kama mnavyofahamu, siku hizi Watanzania wengi wanafuga kuku. Lakini kama mlivyosikia, chakula cha kuku wanachozalisha, wanakiuza pia nje ya nchi. Wanauza Ethiopia, Kenya, Nigeria na Uganda. Hii maana yake ni kwamba Kiwanda cha Silverlands kinaingiza nchi yetu fedha za kigeni.
Napenda nitumie fursa kuwapongeza wamilikiwa Kiwanda cha Silverlandskwa kuamua kuwekeza kiasi cha Dola za Marekani milioni 71 hapanchini. Mmetoa ajira kwa Watanzania, mmewapa wakulima soko la mazao yao, mnaipatia Serikali yetu mapato kupitia kodi, na pia kuingiza fedha za kigeni nchini. Ninawashukuru na kuwapongeza sana. Aidha, nawapongeza kwa kuanzisha Kituo cha Mafunzo, ambapo mpaka sasa mmesema mmetoa mafunzo ya watu wapatao 895. Tunawashukuru na kuwapongeza sana. Na ninawahakikishia kuwa Serikali ipo pamoja nanyi. Ninafahamu kuwa yapo matatizo madogo kati ya Kiwanda na wananchi wa hapa, lakini nimefurahi Uongozi wa Kiwanda umeahidi kuyashughulikia. Hilo ni jambo zuri; na ni imani yangu kuwa Kiwanda hiki pia sasa kitaanza kulipa kodi kwa Serikali.
Napenda pia kuipongeza Wizara ya Viwanda kwa kuendelea kuwahamasisha wawekezaji wa hapa nchini na nje ya nchi kuwekeza kwenye sekta ya viwanda nchini. Vilevile, naupongeza uongozi wa Mkoa wa Iringa kwa kuweka mazingira mazuri yaliyowezesha Kiwanda cha Silverlands Tanzania Ltd kujengwa. Nimeambiwa Mkoa wa Iringa hivi sasa una jumla ya viwanda 2,663. Hongereni sana wana-Iringa. Endeleeni kuwavutia wawekezaji kwenye Mkoa wenu ili kusaidia kuondoa tatizo la ukosefu wa ajira, hususan kwa vijana.
Ndugu Wananchi Wenzangu, Mabibi na Mabwana:
Ili sekta yetu ya viwanda izidi kukua, kustawi na kushamiri, tunahitaji kufanya mambo mawili muhimu. Kwanza, kuimarisha upatikanaji wa nishati ya umeme. Umeme ni injini ya viwanda. Mitambo mingi ya viwandani inahitaji umeme ili iweze kufanya kazi. Pili, miundombinu ya usafiri. Ili malighafi ziweze kufika viwandani zinahitaji kusafirishwa. Na vilevile, ili bidhaa za viwandani ziweze kufika kwenye masoko, zinahitaji huduma ya usafiri. Mathalan, ili mahindi na soya yaweze kufika kwenye Kiwanda cha Silverlands inabidi yasafirishwe. Na vivyo hivyo, ili chakula cha kuku cha Kiwanda cha Silverlands kiweze kufika kwenye masoko, huduma ya usafiri inahitajika. Hii inadhihirisha kuwa miundombinu ya usafiri ni muhimu katika kujenga viwanda.
Ni kwa kutambua hilo, Serikali imeweka mkazo mkubwa katika kujenga miundombinu ya usafiri. Tunajenga reli. Tunapanua Bandari. Tunajenga viwanja vya ndege. Na halikadhalika, tunajenga barabara. Wiki iliyopita nilizindua Barabara ya Dodoma – Babati yenye urefu wa kilometa 251. Juzi tena (Jumapili) nimezindua Barabara ya Fufu – Migori – Iringa yenye urefu wa kilometa 189. Na leo nimefurahi kuja hapa Ihemikuzindua barabara hii ya Iyovi – Iringa – Mafinga yenye urefu wa kilometa 218.6. Nimefurahi sana.
Barabara hii ya Iyovi – Iringa – Mafinga ni muhimu sana, sio tu katika kujenga viwanda, bali pia katika kukuza uchumi wa nchi yetu. Kama mlivyosikia, Barabara hii ni sehemu ya Barabara Kuu ya TANZAM (Tanzania na Zambia) inayoanzia Dar es Salaam na kupita Mikoa ya Pwani, Morogoro, Iringa, Njombe, Mbeya na kuishia Tunduma, Mkoani Songwe, kwenye mpaka wa nchi yetu na Zambia, yenye urefu wa kilometa 918. Barabara hii pia inaungana na Barabara Kuu ya Kaskazini (The Great North) inayoanzia Cairo hadi Cape Town, ambayo inapita kwenye nchi 8. Kwa kuzingatia hilo, ni wazi kuwa, kukamilika kwa barabara hii kutafungua fursa nyingi za kiuchumi kwenye maeneo inakopita. Kuanzia biashara, kilimo, ufugaji, shughuli za misitu, n.k. Na kwa kuwa Barabara hii inapita kwenye maeneo ya vivutio vingi vya utalii, ikiwemo Hifadhi za Taifa za Ruaha, Mikumi, Selous, Milima ya Udzungwa, n.k., ni imani yangu kuwa watalii wengi watakuja. Kwa sababu hiyo, nawasihi sana wananchi wanaoishi kandokando ya barabara hii, kuchangamkia fursa. Itumieni barabara hii kuinua vipato vyenu na kuboresha hali yenu ya maisha. Hayo ndio malengo makuu ya Serikali kukopa fedha ili kujenga barabara hii.
Waheshimiwa Viongozi;
Wageni Waalikwa;
Ndugu Wananchi, Mabibi na Mabwana:
Kama mlivyosikia, ujenzi wa Barabara hii ya Iyovi – Iringa – Mafinga umegharimu shilingi bilioni 283.715. Fedha hizo ni mkopo kutoka kwa marafiki zetu wa Denmark. Mbali na kutufadhili mradi huu, Denmark tulishirikiana nao katika ukarabati wa barabara ya Ubungo – Mlandizi yenye urefu wa kilometa 65.7; Chalinze – Melela yenye urefu wa kilometa 129 pamoja na Chalinze – Segera – Tanga yenye urefu wa kilometa 245. Vilevile, Denmark wamefadhili ukarabati wa barabara za kiwango cha changarawe zenye urefu wa kilometa 900 hapa nchini.
Hivyo basi, napenda kutumia fursa hii, kwa niaba yangu binafsi na kwa niaba ya Serikali na Wananchi wa Tanzania, kutoa shukran zangu nyingi kwa Serikali na Wananchi wa Denmark kwa kutufadhili kutekeleza mradi huu pamoja na miradi mingine ya maendeleo. Tunawashukuru sana, tena sana. Nimefurahi kuona Naibu Balozi wa Denmark, Bibi Camilla yupo hapa. Tunaomba utufikishie shukrani zetu kwenye Serikali na Wananchi wa Denmark. Endeleeni kutuunga mkono. Misaada mtakayotupatia, tutaitumia vizuri. Hakuna senti itakayopotea.
Lakini kupitia kwako, Naibu Balozi, Bi. Camilla, naomba nichomekee jambo moja. Barabara hii mliyotufadhili imejengwa vizuri sana. Na napenda nitumie fursa hii kumpongeza sana Mkandarasi aliyeijenga. Hata hivyo, Barabara hii tatizo lake inapita katikati ya Mji wa Iringa na hivyo imeanza kusababisha msongamano wa magari. Zaidi ya hapo, kama unavyofahamu, kupitisha barabara kubwa kama hii katikati ya mji ni hatari. Hivyo basi, nitumie fursa hii, kuiomba Serikali ya Denmark kuona uwezekano wa kufadhili ujenzi wa Barabara ya Mzunguko ya takriban kilometa 12 ili magari makubwa yasilazimike kupita mjini. Ni imani yangu kuwa Serikali ya Denmark itakubali ombi letu, hata kama itakuwa mkopo.
Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi;
Wageni Waalikwa;
Ndugu Wananchi, Mabibi na Mabwana;
Nimekuja hapa kwa ajili ya kuzindua Kiwanda cha Silverlands Tanzania Ltd na Barabara ya Iyovi - Iringa –Mafinga yenye urefu wa kilometa 218.6. Nimetumia fursa hii pia kuwasalimu na kuwashukuru kwa kunipigia kura. Hata hivyo, kabla sijahitimisha hotuba yangu, naomba niseme maneno machache ya mwisho.
Kwanza, napenda kutumia fursa hii kuendelea kuwahamasisha Watanzania na pia watu kutoka nje kuja kuwekeza nchini. Nchi yetu ina fursa nyingi za kuwekeza kwenye sekta ya viwanda. Tuna sheria nzuri za kuwalinda wawekezaji. Na halikadhalika, tunalo soko kubwa la kuuzia bidhaa. Kama mjuavyo, sisi ni wanachama wa EAC na SADC, ambapo kwa pamoja, Jumuiya hizi zina idadi ya watu wapatao milioni 500. Hili ni soko kubwa la bidhaa.
Pili, wahimiza wananchi na watumiaji wa barabara nitakayoizindua hivi punde, kuhakikisha mnaitunza. Ujenzi wa miundombinu ya barabara kama hii unagharimu fedha nyingi. Hivyo, ni lazima tuzitunze. Aidha, barabara hii haipaswi kuwa chanzo cha ajali. Hivyo, nawasihi madereva kuwa waangalifu pindi wanapoendesha vyombo vya moto barabarani.
Tatu na mwisho, lakini sio mwisho kwa umuhimu, ni kwenu wana-Ihemi na wana-Iringa kwa ujumla. Fursa nyingi sasa zinakuja kwenye Mkoa wenu. Tumeanza kutekeleza mpango kabambe wa kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo katika Ukanda huu wa Kusini. Tunajenga Kiwanja cha Ndege cha Nduli. Barabara ndio kama hivi zinajengwa. Sambamba na hilo, hapa Iringa ni karibu kabisa na Dodoma, ambako Serikali imeamua kuhamishia Makao yake Makuu. Waswahili wanasema, “ukikaa karibu na uaridi lazima utanukia”. Hivyo, nawasihi mjiandae kutumia fursa ambazo Serikali inawaletea.
Lakini nina maombi mawili kwenu. Nawasihi muendelee kuiunga mkono Serikali, hususan kwa kudumisha amani na umoja wetu, kuchapa kazi kwa bidii na bila kusahau kulipa kodi. Ulipaji wa kodi ni muhimu sana. Aidha, nawasihi mjitahidi kujikinga na ugonjwa wa ukimwi. Hali ya ugonjwa huu katika Mkoa wenu sio ya kuridhisha sana.
Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana, napenda kuhitimisha hotuba yangu kwa kuwashukuru Waheshimiwa Mawaziri kwa kunialika kwenye shughuli hii. Nawapongeza Wamiliki wa Kiwanda cha Silverlands kwa kuamua kuwekeza hapa nchini. Aidha, naipongeza Wizara ya Ujenzi, TANROADS, wakiongozwa na Mhandisi Mfugalea, pamoja na Mkandarasi kwa kujenga Kiwanda hiki. Mwisho lakini sio kwa umuhimu, naushukuru uongozi wa Mkoa wa Iringa pamoja na wana-Iringa kwa ujumla kwa mapokezi yenu mazuri mliyonipa tangu nimewasili kwenye Mkoa wenu.
Baada ya kusema hayo, sasa nipo tayari kutekeleza jukumu lililonileta la kuzindua barabara ya Iyovi - Iringa – Mafinga yenye urefu wa kilometa 218.6 iliyojengwa kwa gharama za shilingi bilioni 283.715 kwa ufadhili wa Serikali ya Denmark.
Mungu Ibariki Iringa!
Mungu Ubariki Uhusiano kati ya Tanzania na Denmark!
Mungu Ibariki Tanzania!
“Ahsanteni sana kwa kunisikiliza”

- May 01, 2018
HOTUBA YA MHESHIMIWA DKT. JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, KWENYE SHEREHE ZA SIKUKUU YA WAFANYAKAZI DUNIANI IRINGA, TAREHE...
Soma zaidiHotuba
HOTUBA YA MHESHIMIWA DKT. JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA,
KWENYE SHEREHE ZA SIKUKUU YA WAFANYAKAZI DUNIANI
IRINGA, TAREHE 1 MEI, 2018
Mheshimiwa Kassim Majaliwa, Waziri Mkuu
wa Jamhuri Muungano wa Tanzania;
Mheshimiwa Job Ndugai, Spika wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania;
Ndugu Tumaini Nyamhokya, Rais wa Shirikisho
la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA);
Mheshimiwa Jenista Mhagama, Waziri wa Nchi,
Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi,
Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu;
Waheshimiwa Mawaziri wengine mliopo;
Mheshimiwa Balozi Mhandisi John Kijazi,
Katibu Mkuu Kiongozi;
Mheshimiwa Amina Masenza, Mkuu wa Mkoa wa Iringa pamoja na Wakuu wa Mikoa mingine
mliopo;
Mheshimiwa Aisha Nyerere, Jaji Mfawidhi wa Divisheni ya Kazi ya Mahakama Kuu;
Ndugu Wellington Chibebe, Mkurugenzi wa Shirika la Kazi Duniani (ILO), Ofisi ya Nchi za Afrika Mashariki;
Ndugu Jayne Nyimbo, Mwenyekiti wa Chama
cha Waajiri Tanzania (ATE);
Waheshimiwa Wabunge na Madiwani mliopo;
Waheshimiwa Mabalozi mliopo;
Ndugu Makatibu Wakuu mliopo;
Waheshimiwa Wakuu wa Wilaya mliopo;
Dkt. Yahya Msigwa, Katibu Mkuu wa Shirikisho
la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA);
Viongozi Wengine wa Vyama vya Wafanyakazi mliopo;
Viongozi Wengine wa Serikali mliopo;
Viongozi wa Vyama vya Siasa na Viongozi wa
Dini mliopo;
Ndugu Wafanyakazi Wenzangu;
Wageni Waalikwa wote;
Ndugu Wana-Iringa, Mabibi na Mabwana:
Kwanza kabisa napenda nitumie fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia afya njema na kutuwezesha kukutana hapa. Namshukuru pia Mheshimiwa Waziri Mhagama pamoja na Viongozi wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi nchini (TUCTA), wakiongozwa na Rais wake, Bwana Nyamhokya, kwa kunialika tena kushiriki kwenye maadhimisho haya ya Siku ya Wafanyakazi Duniani, au Mei Mosi, ambayo mwaka huu kitaifa yanafanyika hapa Iringa. Nawashukuru sana kwa kunialika.
Napenda pia kutumia fursa hii kuungana na wazungumzaji walionitangulia katika kutoa pole nyingi za misiba ya viongozi wa vyama vya wafanyakazi iliyotokea tangu tulipoadhimisha sherehe hizi mwaka jana. Vilevile, nawakumbuka wafanyakazi wote waliotutoka katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita. Tuzidi kuwaombea marehemu wote ili Mwenyezi Mungu azipumzishe roho za marehemu mahali pema peponi. Amina.
Ndugu Wafanyakazi na Ndugu Wananchi;
Hii ni mara yangu ya kwanza kuja Iringa tangu nichaguliwe kuwa Rais wa Awamu ya Tano wa nchi yetu. Hivyo basi, napenda kutumia fursa hii kuwashukuru wana-Iringa kutoka dini zote, makabila yote na vyama vyote kwa kunichagua kuwa Rais wenu. Nawashukuru sana wana-Iringa. Sina cha kuwalipa. Ninachowaahidi tu ni kwamba, nitashirikiana na viongozi wenzangu wa Serikali pamoja na wengine mliowachagua, wakiwemo Waheshimiwa Wabunge na Madiwani, katika kuhakikisha kuwa yale yote tuliyowaahidi tunayatekeleza. Na bila shaka, mtakubaliana nami kuwa, baadhi ya mambo tuliyoahidi tumeyatekeleza kwa mafanikio makubwa na mengine tunaendelea kuyatekeleza.
Ndugu Wafanyakazi Wenzangu;
Leo ni Mei Mosi. Ni Siku ya Wafanyakazi. Naamini wengi wetu hapa tunafahamu kwa nini kila mwaka dunia inaadhimisha Siku hii. Hivyo basi, napenda kutumia fursa hii kuwapongeza wafanyakazi wote nchini kwa kuadhimisha Siku hii muhimu. Aidha, nawapongezeni kwa mchango wenu mkubwa mnaoutoa katika kuiletea maendeleo nchi yetu. Hongereni sana wafanyakazi wa Tanzania.
Kwa hakika, mnafanya kazi kubwa. Mnastahili pongezi nyingi kwa mchango wenu mkubwa katika kuliletea maendeleo Taifa letu. Nitumie fursa hii, hapa mwanzoni kabisa, kuwahakikishia wafanyakazi wote nchini kuwa Serikali ya Awamu ya Tano inatambua mchango wenu na kuuthamini sana. Tunawapenda sana wafanyakazi. Tupo pamoja nanyi. Tutaendelea kushughulikia kero zenu zinazowakabili na kuboresha mazingira yenu ya kazi.
Ndugu Wafanyakazi Wenzangu,
Hivi punde tumetoka kusikia Risala nzuri ya TUCTA iliyosomwa na Katibu wake Mkuu, Bwana Msigwa. Kupitia Risala hiyo, TUCTA imeipongeza Serikali kwa kuchukua hatua mbalimbali za kuiletea maendeleo nchi yetu na halikadhalika kutatua baadhi ya kero za wafanyakazi nchini. Zaidi ya hapo, TUCTA imeeleza kuwa haitakuwa tayari kuwatetea wafanyakazi “mabazazi”, yaani wazembe, wavivu, watovu wa nidhamu, wajeuri, wala rushwa, mafisadi, wenye majungu, wafitini, walevi na wote wenye kufanana na sifa hizo. Nawashukuru sana TUCTA.
Ndugu zangu, nidhamu na uwajibikaji kwa mfanyakazi ni jambo la msingi sana. Kwenye hotuba yake ya Mei Mosi mwaka 1974, Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alisema, naomba nimnukuu “Mkulima asiyefanya juhudi katika shamba lake wakati wa kilimo anapunguza mapato ya nchi. Lakini angalau yeye anapata adhabu yake: hatopokea malipo yoyote, mazao yakikosekana au kuharibika kwa sababu ya uvivu wake. Kwa mfanyakazi ipo tofauti. Yeye hapati adhabu anayoipata mkulima. Yeye anaweza kuharibu kazi lakini mwisho wa mwezi anaendelea kupata mshahara wake kamili kama kawaida”, mwisho wa kunukuu.
Hii maana yake ni kwamba nidhamu katika kazi kwa mtumishi ni kitu cha muhimu na cha lazima. Mtumishi au mfanyakazi akiwa mzembe na mvivu, anakosa kutoa mchango katika maendeleo ya Taifa, lakini zaidi ya hapo, anakuwa mnyonyaji kupitia mshahara anaopokea. Hivyo basi, narudia tena kuwashukuru na kuwapongeza viongozi wa TUCTA kwa kuiunga mkono Serikali katika kusimamia nidhamu na uwajibikaji kwenye watumishi wa umma.
Ndugu Wafanyakazi Wenzangu,
Sambamba na pongezi walizotoa kwa Serikali na ahadi ya kutotetea ubazazi kwa wafanyakazi, Risala ya TUCTA imewasilisha hoja mbalimbali kwa Serikali. Baadhi ya hoja hizo zinahusu kero za wafanyakazi ambazo wameomba Serikali izishughulikie. Hoja nyingine ni mapendekezo yao kwa Serikali yenye lengo la kuiletea nchi yetu maendeleo zaidi. Kwa ujumla, niseme tu kwamba, hoja zenu zote ni sahihi. Serikali inazikubali na tunazipokea kwa ajili ya kuzifanyia kazi, ikiwa ni pamoja na zile zenye kuhusu Mikataba ya Kimataifa, Fomu za Polisi Na 3 (PF3), ushirikishwaji Wafanyakazi, uboreshaji elimu, masuala ya Walemavu, n.k. Kwa bahati nzuri, watendaji wakuu wa Serikali karibu wote wapo hapa. Naamini wamezisikia, watazichukua na kwenda kuzifanyia kazi. Hata hivyo, pamoja na kwamba tunazichukua hoja zenu zote, naomba mniruhusu na mimi nieleze baadhi ya mambo ambayo Serikali imefanya.
Ndugu Wafanyakazi;
Tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani imefanya mambo mengi yenye manufaa na faida kwa Wafanyakazi. Baadhi ya mambo hayo ni kama ifuatavyo;
(i) Tumefanikiwa kudhibiti mfumko wa bei za bidhaa muhimu nchini. Mathalan, wakati tunaingia madarakani, mwezi Novemba 2015, mfumko wa bei ulikuwa ni wastani wa asilimia 6.6. Tumefanikiwa kuishusha, na hivi sasa, kwa mujibu wa takwimu za mwezi Machi 2018, mfumko wa bei umefikia asilimia 3.9. Hii imekuwa njia nzuri ya kumsaidia mfanyakazi. Kama mnavyofahamu, unaweza kupandisha mshahara, lakini endapo bei za bidhaa zitapanda kiholela, uongezaji wa mishahara unakuwa hauna maana yoyote ile. Kwa sababu hiyo, Serikali itaendelea kufanya jitihada za kudhibiti mfumko wa bei za bidhaa muhimu zisipande kiholela ili kuwapa unafuu wafanyakazi na wananchi kwa ujumla, lakini pia tutahakikisha kuwa bidhaa zote muhimu, kama vile vyakula, mafuta na dawa zinapatikana maeneo yote na tena kwa urahisi zaidi.
(ii) Tunatoa elimu bure, ambapo kila mwezi tunatoa shilingi bilioni 23.8, sawa na shilingi bilioni 285.6 kwa Mwaka. Katika miaka miwili na nusu zimetolewa takriban shilingi bilioni 714. Elimu bila malipo imewanufaisha hadi wafanyakazi kwa vile watoto wenu nao sasa hawalipishwi ada na michango.
(iii) Tumelipa Madeni ya Mifuko ya Hifadhi za Jamii. Serikali ilikuwa ikidaiwa michango ya wafanyakazi, ambapo tangu mwaka 2013 ilikuwa haijalipwa au kulipwa kidogo. Madai yalifikia shilingi Trilioni 1.6. Lakini mpaka sasa tumelipa shilingi trilioni 1.4.
(iv) Tumelipa madeni ya Wazabuni na Wakandarasi kiasi cha shilingi trilioni 2. Kufuatiwa kulipwa kwa madeni hayo, wazabuni wameendelea kutoa huduma kwenye taasisi zetu. Aidha, wakandarasi wameendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo iliyokuwa imekwama; na kukamilika kwa miradi hiyo kumeleta na kutazidi kuleta manufaa kwa wafanyakazi.
(v) Madeni ya Ndani na Nje tunalipa kila mwezi takribani shilingi bilioni 900. Kwa miaka miwili na nusu tumelipa shilingi trilioni 2.7
(vi) Mishahara kila mwezi zinalipwa shilingi bilioni 564.501 baada ya kutoa Watumishi hewa. Awali tulikua tukilipa shilingi bilioni 777. Hii maana yake kwa mwaka tunalipa shilingi trilioni 6.77 na kwa miaka miwili na nusu tumelipa shilingi trilioni 16.935. Na bila shaka, mtakubaliana nami kuwa, siku hizi mishahara inalipwa kwa wakati.
(vii) Tunatekeleza miradi mbalimbali ya miundombinu na kuboresha huduma za jamii, ambapo kukamilika kwake kutaleta manufaa kwa nchi yetu, ikiwa ni pamoja na kwenu wafanyakazi. Miradi hiyo ni ujenzi wa SGR kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma unaotarajiwa kugharimu kiasi cha shilingi trilioni 7.06 na hadi sasa tumelipa shilingi trilioni 1.1. Miradi mingine mikubwa ni mradi wa kuzalisha umeme wa Stiglier’s Gorge; ununuzi wa ndege; ujenzi wa barabara na madaraja; miradi ya umeme; viwanja vya ndege; ujenzi wa meli; ujenzi wa miundombinu ya afya na elimu; mikopo elimu ya juu, ambapo mwaka huu wa fedha tunatumia shilingi bilioni 483; ujenzi wa Bandari kubwa Dar es salaam, Mtwara na Tanga (shilingi trilioni 1.1); miradi ya maji (takriban shilingi bilioni 600); ukarabati wa Reli ya Kati na Reli kutoka Tanga na Arusha; ujenzi wa Rada Dar es salaam, Mwanza, Songwe na Kilimanjaro; kusambaza vifaa vya maabara kwenye shule 1,696, n.k. Aidha, kuna miradi mingine mingi inayoendelea ikiwa ni pamoja na mradi wa Bomba la Mafuta; miradi ya kilimo, uvuvi na ufugaji. Miradi na shughuli zote hizi zinaigharimu Serikali fedha nyingi .
Sambamba na hayo, tangu tumeingia madarakani mwaka 2015, tumepata mafanikio makubwa katika kubadilisha taswira ya Utumishi wa Umma. Tulianza na zoezi la kuhakiki Watumishi wa Umma ili kuhakikisha kwamba Watumishi wa Umma wanakuwa wale wenye sifa stahiki. Tumefanikiwa kuondoa Watumishi hewa 19,708 na watumishi wenye vyeti feki 14,152. Haya ni mafanikio makubwa ambayo yametuwezesha kuokoa mabilioni ya shilingi, lakini pia tumeweza kubaki na watumishi wenye sifa ya kufanya kazi. Mazoezi haya mawili yamekamilika mwezi Oktoba mwaka 2017.
Kukamilisha kwa mazoezi hayo ya uhakiki, yametufanya tuanze kuajiri watumishi wapya. Mpaka sasa tumeajiri watumishi wapya 18,101 (walimu 6,495, watumishi wa afya 3752, watumishi wa Mambo ya Ndani 6164, Mahakama watumishi 200, Mafundi Sanifu wa Maabara 386, na watumishi wengine) na tunatarajia kuajiri watumishi wengine 22,150 kabla ya kumalizika kwa mwaka huu wa fedha. Aidha, tumeweza pia kuwapandisha madaraja (promotion) watumishi 88,016 mpaka hivi sasa. Tunategemea kukamilisha promosheni nyingine 25,504 kabla ya kumalizika kwa Mwaka huu wa Fedha. Hivyo, jumla, tutakuwa tumetoa promosheni 113,520 kabla ya mwezi Julai, mwaka huu 2018. Napenda kuwahakikishia kwamba Serikali itaendelea kuajiri watumishi wapya na kuwapandisha madaraja kadri bajeti inavyoruhusu.
Ndugu Wafanyakazi;
Kama mnavyojua, tofauti na ilivyokuwa zamani, siku hizi Serikali siyo mwajiri mkubwa. Sekta Binafsi ndiyo mwajiri mkubwa. Na katika hili, napenda kuipongeza sekta binafsi ya hapa nchini kwa kuendelea kutoa fursa nyingi za ajira kwa Watanzania. Wakati Serikali ya Awamu ya Tano inaingia madarakani, Sekta Binafsi ilikuwa na watumishi 2,334,969. Katika miaka miwili na nusu iliyopita, ajira hizo zilizoongezeka hadi kufikia 582,073, ambayo ni sawa na ongezeko la asilimia 24.9. Hili ni ongezeko kubwa la ajira.
Aidha, tukijumlisha na ajira za sekta isiyo rasmi, ajira zilizoongezeka zimefikia 1,826,743. Ongezeko hili ni kutokana na miradi mingi inayoendelea kutekelezwa, hususan kwenye miundombinu ya barabara, madaraja, reli, viwanja vya ndege na rada, bandari, miradi ya umeme, ujenzi wa shule na vyuo, miradi ya afya, miradi ya maji, viwanda, miradi ya gesi, pamoja na miradi katika sekta za kilimo, mifugo, uvuvi, madini na utalii, n.k. Haya ni mafanikio ya kujivunia ya Serikali ya Awamu ya Tano.
Tunaendelea kuboresha mazingira ya sekta binafsi ili izidi kustawi nchini na kutoa ajira nyingi kwa Watanzania. Kama mnavyojua, dhamira yetu ya Tanzania ya viwanda inaendelea kushika kasi. Viwanda vingi vimeanzishwa nchini na vinaendelea kuanzishwa. Kwa mujibu wa matokeo ya sensa ya viwanda iliyotolewa mwezi Juni 2017, viwanda vipya 3,306 vimejengwa, vikiwemo viwanda vya kati na vikubwa; na vingine vingi vinaendelea kujengwa. Katika Mkoa wa Pwani pekee, zaidi ya viwanda vikubwa 80 vinaendelea kujengwa hivi sasa. Hivi vyote maana yake ni ajira mpya kwa Watanzania.
Ndugu Wafanyakazi;
Kukamilika kwa mazoezi ya uhakiki pia kumeiwezesha Serikali kuanza kulipa malimbikizo ya madeni ya watumishi. Mpaka hivi sasa, tumeshalipa malimbikizo ya madeni ya mishahara ya watumishi 52,851 yenye thamani ya shilingi bilioni 68.323. Aidha, tumelipa madeni yasiyo ya mishahara yeye thamani ya shilingi bilioni 152.304. Hii imefanya jumla ya madeni yote ya watumishi tuliyolipa kufikia shilingi bilioni 220.627, ambapo mengi yalikuwa hayajalipwa tangu mwaka 2007.
Wizara ya Fedha kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma wanaendelea kuhakiki na kulipa madeni yaliyosalia kila mwezi. Napenda kuwahakikishia Watumishi wa Umma wote kwamba, yeyote mwenye madai halali atalipwa haki yake. Lakini mwenye madai ya uongo, hatolipwa kamwe.
Ndugu Wafanyakazi;
Kama nilivyosema, Serikali imefanya mambo mengi. Tumetoa ajira, tumelipa madeni yote niliyotaja; tunatoa elimu bure; tunatekeleza miradi mikubwa ya Reli, Bandari, Barabara, Maji, Umeme, Afya. Masuala haya yote yanategemea fedha kutoka mfuko mmoja tu. Sio rahisi kufanya mambo hayo yote, na pia kuweza kupandisha mishahara. Msema kweli ni mpenzi wa Mungu. Ni lazima tuchague. Na mimi kwa mtazamano wangu, nilidhani tuanze kwanza kutekeleza miradi hii mikubwa ya maendeleo ambayo itakapomalizika itatupatia fedha nyingi za kuweza kuongeza mishahara na kufanya mambo mengine ya maendeleo.
Kwa mfano, mimi naamini, tukijenga reli na ikianza kufanya kazi ya kubeba mizigo kwenda nchi za Burundi, Rwanda na pia kuhudumia nchi za DRC na Uganda, itatupatia fedha nyingi za kuweza kupandisha mishahara. Vivyo hivyo, tuktekeleza miradi ya barabara na umeme, tutapata fedha nyingi za kuweza kuongeza mishahara. Tukiongeza bajeti ya afya, wananchi watakuwa na afya njema na hivyo kuweza kushiriki kwenye shughuli mbalimbali za maendeleo. Kwangu mimi naona mambo hayo ni ya msingi zaidi kwa sasa kuliko kupeleka fedha mahali kwingine.
Nchi yetu imeazimia kujenga uchumi wa viwanda, lakini umeme tulionao ni takriban Megawati 1,500. Hivyo, kwangu mimi naona kutekeleza Mradi wa Umeme wa Stiglier’s Gorge utakaogharimu takriban shilingi trilioni 3 kuzalisha Megawati 2,100 ni muhimu zaidi kwa sasa kuliko kupeleka fedha hizo mahali kwingine. Kwangu mimi naona ni busara kutoa fedha za kujenga barabara za kuunganisha Mkoa wa Iringa na mikoa mingine pamoja na kujenga Uwanja wa Ndege wa Nduli ili utuletee watalii wengi, hususan katika kipindi hiki ambacho tumeamua kuifanya Iringa kuwa kitovu cha utalii kwenye Ukanda huu wa Kusini, kuliko fedha hizo kuzipeleka mahali kwingine. Kwangu mimi naona ni jambo jema kutoa fedha takriban shilingi bilioni 23.8 kwa mwezi kugharamia elimu bure ili watoto wengi wa maskini wapate elimu, kuliko kutumia fedha hizo kulipana mishahara. Kwangu mimi pia naona ni vizuri kutoa shilingi bilioni 483 kuwakopesha watoto wa maskini ili waweze kwenda kwenye Vyuo Vikuu, kuliko kutumia fedha hizo kujiongezea mishahara. Kupanga ni kuchagua.
Lakini, mbali na miradi hiyo ya maendeleo, nawaomba wafanyakazi mkumbuke kuwa, kwenye nchi yetu wapo pia wakulima, wafugaji na wavuvi, ambao nao wanahitaji maisha yaliyo bora. Hivyo, wakati tunajifikiria sisi, na wao pia tuwafikirie.
Pamoja na ukweli huo, matumaini bado yapo. Napenda nitumie fursa hii kuwahakikishia Wafanyakazi kuwa, baada ya kukamilisha mazoezi ya kuhakiki na kuanza kuajiri watumishi wapya, jambo kubwa ambalo sasa ni kipaumbele changu kwa watumishi wa umma ni kuboresha mishahara na maslahi mengine ya wafanyakazi. Nafarijika sana kwamba sasa tumeanza kukaa kwenye mstari, nidhamu imerejea, uadilifu unazidi kujengeka, mnafanya kazi kwa uzalendo na weledi, isipokuwa wachache ambao tutazidi kuwachukulia hatua stahiki. Tunaendelea kukamilisha ulipaji wa madeni ya watumishi. Lakini mwaka huu pia tutaendelea kutoa nyongeza ya mwaka ya mishahara (Annual increment). Naomba mniamini.
Ni bahati mbaya tu Katibu Mkuu wa TUCTA amenichomekea kuwa kwenye Sherehe za Mei Mosi mwaka jana niliahidi kupandisha mishahara. Hiyo sio kweli. Mwaka jana sikuahidi kupandisha mishahara. Na hotuba yangu ipo. Hata hivyo, leo ndio naweza kuahidi. Kama miradi hii itaenda vizuri, kama wafanyakazi mtaendelea kujituma na kuchapaka kazi kama mnavyofanya sasa, na kama Vyama vya Wafanyakazi vitaendelea kutoa ushirikiano wa kutosha kwa Serikali kama sasa, nawaahidi, na naomba mninukuu vizuri kuwa, kabla sijamaliza muhula wangu wa uongozi nitapandisha mshahara. Na nitakapopandisha, itakuwa kiwango kikubwa. Sio shilingi elfu 10. Narudia tena. Naomba wafanyakazi mniamini. Mimi ni mfanyakazi mwenzenu. Nilikuwa Mwalimu. Ninafahamu shida za wafanyakazi na kwa kweli ninawapenda sana wafanyakazi wenzangu. Kama ingekuwa inawezekana hata leo ningepandisha. Hata hivyo hali kwa sasa hairuhusu. Hivyo, narudia tena kuwasihi muwe wavumilivu na kuendelea kuchapa kazi kwa bidii ili tuweze kukuza uchumi wetu na hatimaye tutengeneze maisha bora ya baadaye. Mimi naamini kuwa miradi ya maendeleo tunayoitekeleza itakapokamilika, haitachukua muda mrefu kupandisha mishahara. Hata hivyo, kwa sasa, tutaendelea kuweka mkazo mkubwa katika kudhibiti mfumko wa bei.
Ndugu Wafanyakazi;
Mwaka jana katika risala yenu mliomba zoezi la kuunganisha mifuko likamilike mapema. Napenda kuwafahamisha kwamba zoezi hilo limekamilika baada ya Bunge kupitisha Sheria tarehe 31/01/2018 na mimi kuisaini tarehe 08/02/2018. Kilichobaki sasa ni kuanza kutumika kwa Sheria hiyo ambapo kutakuwa na mifuko miwili. Mfumko mmoja wa Watumishi wa Umma na mwingine kwa ajili ya Sekta Binafsi. Sheria iliyotungwa mbali na kuanzisha Mfuko wa Hifadhi ya Watumishi wa Umma (PSSSF) imefanya marekebisho katika Sheria ya Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (The National Social Security Fund Act) Sura ya 50 ili kuifanya NSSF kuhudumia Watumishi wa Sekta Binafsi wakiwemo Wakulima, Wafugaji, Wavuvi, Wajasiriamali wadogo (machinga na mama lishe).
Uunganishaji wa mifuko hii, unategemewa kurahisisha ulipaji wa mafao, kupunguza gharama za uendeshaji wa mifuko na hivyo kuboresha mafao ya wanachama. Katika kipindi hiki pia, kama nilivyoeleza hapo awali, tumeweza kulipa deni la shilingi trilioni 1.4 ya malimbikizo ya michango ya wanachama kwenye mifuko ya pensheni. Malipo haya yamewezesha wastaafu kuendelea kulipwa mafao yao kama wanavyostahili. Napenda kutumia fursa hii kuziagiza Mamlaka husika kukamilisha kwa haraka taratibu husika ili Mifuko hii ianze kazi mara moja; maana naanza kuona dalili za kuwepo kwa kigugumizi na kusuasua katika kukamilisha taratibu za kuanzisha Mifuko hiyo.
Ndugu Wafanyakazi,
Risala yenu pia imegusia suala la makato ya kodi ya mshahara (Pay As You Earn – PAYE); viwango vya mishahara, hususan ya kima cha chini; na vikao vya Bodi za Kima cha Chini cha Mishahara, Bodi za Mishahara pamoja na Chombo cha Ushauri (Labour Economic and Social Council – LESCO). Kuhusu suala hili, napenda kwanza niseme kuwa masuala haya ya maslahi kimsingi yanategemea pia uwezo wa kifedha wa Serikali. Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere aliwahi kusema ‘A calf can only suck the amount of milk her mother cow produces (yaani, ndama hunyonya kulingana na kiwango cha maziwa aliyonayo mama yake)”.
Lakini, pamoja na ukweli huo, Serikali kwa kile kidogo ilichonacho, imekuwa ikijitahidi sana kuboresha maslahi ya watumishi wake. Mathalan, kuhusu suala la PAYE, mwaka juzi tulipunguza kwa asilimia 2 kodi ya mshahara kutoka asilimia 11 hadi asilimia 9. Hii ilitufanya tufanikiwe kufikia malengo tuliyokubaliana (kati ya Serikali na Vyama vya Wafanyakazi) ya kuwa na kiwango cha tarakimu moja (single digit), miaka miwili kabla ya muda uliotakiwa.
Ndugu Wafanyakazi;
Kuhusu suala la ucheleweshaji wa kesi za Mahakama Kuu Kitengo cha Kazi, kama mlivyosikia hivi karibuni nimeteua Majaji 12 wa Mahakama Kuu. Hivyo basi, ni imani yangu kuwa uteuzi huo utapunguza tatizo lililokuwepo la uhaba wa majaji na hivyo kusaidia kupunguza kero ya ucheleweshaji wa kesi kwenye Mahakama Kuu Kitengo cha kazi.
Kuhusu suala la Watumishi wenye Vyeti vya Darasa la Saba, napenda tu niwakumbushe kuwa uamuzi wa Serikali kuendesha zoezi la ukaguzi wa vyeti ulilenga kulinda hadhi ya elimu nchini lakini pia kuamsha ari ya utendaji kazi kwa watumishi wenye sifa. Ni bahati mbaya tu katika kutekeleza zoezi hilo, yalitokea mapungufu. Lakini bahati nzuri, Serikali iliona mapungufu hayo, na kama mlivyosikia Waziri mwenye dhamana tayari ametoa msimamo wa Serikali Bungeni hivi majuzi. Kilichobaki sasa ni utekelezaji. Lakini, endapo bado mfanyakazi ataona ameonewa, namshauri afuate taratibu. Kama ambavyo nimekuwa nikisema, Serikali hii inawapenda wafanyakazi. Hatutaki kumwonea mfanyakazi yoyote. Hatutaki kuona mfanyakazi akinyanyasika. Na katika hili, napenda kurudia, kwa mara ya mwisho, agizo langu kuhusu kutomwamisha mtumishi kabla ya kumlipa fedha zake. Sitarudia tena kusema hili. Atakiuka agizo hili, hatutasita kumshughulikia. Na naomba Mheshimiwa Waziri Mkuu kulisimamia hilo.
Ndugu Wafanyakazi Wenzangu,
Kama nilivyosema, mbali na hoja hizo zilizohusu kero za wafanyakazi, Risala ya TUCTA pia imetoa mapendekezo na ushauri mbalimbali kwa Serikali kwa lengo la kuiletea nchi yetu maendeleo. Pendekezo lenu la kwanza linahusu umuhimu wa kutangaza vivutio vya utalii. Risala imeeleza kuwa Tanzania inashika nafasi ya pili kwa vivutio vya utalii duniani baada ya Brazil. Licha ya ukweli huo, idadi ya watalii wanaotembelea nchi yetu ni ndogo. Mmetaja sababu mojawapo yenye kusababisha hali hii kuwa ni kushindwa kwetu kutangaza vivutio vyetu. Hilo ni kweli kabisa. Lakini naomba niongeze sababu nyingine. Hatupati watalii wengi kwa vile, kwa muda mrefu, sekta ya usafiri wa anga nchini ilikuwa hoi bin taabani. Na kama mnavyofahamu, asilimia 70 ya watalii hutumia usafiri wa anga.
Kwa kutambua hilo, tumeanza kuchukua hatua za kutangaza vivutio vyetu mbalimbali na kuimarisha usafiri wa anga. Ninyi wana-Iringa mnafahamu vizuri. Mwezi Februari 2018, Mheshimiwa Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, alizindua mpango kabambe wa kutangaza vivutio vya Ukanda huu wa Kusini ujulikanao kwa jina la Resilient Natural Resorce for Tourism and Growth (REGROW), ambapo takriban Dola za Marekani milioni 150, ambazo ni sawa na takriban shilingi bilioni 330 zitatumika. Kama mnavyofahamu, Ukanda huu wa Kusini, kama ulivyo Ukanda wa Kaskazini, una vivutio vingi, ikiwemo Hifadhi ya Ruaha yenye kusifika kuwa na tembo wengi, Hifadhi ya Kitulo, au maarufu kama Bustani ya Mungu, ambayo ina maua ndwele ambayo hayapatikani mahali popote duniani, Maporomoko ya Kalambo ambayo ni ya pili Barani Afrika, maeneo ya kihistoria ya Kalenga na Isimila, n.k.
Sambamba na mkakati huo wa kutangaza vivutio, kama nilivyosema awali, tunaimarisha pia usafiri wa anga. Hivi sasa, tunajenga viwanja takriban 11 vya ndege kikiwemo kiwanja cha hapa Iringa, ambacho ujenzi wake utagharimu zaidi ya shilingi bilioni 90. Tumenunua pia ndege mpya 7, tatu tayari zimewasili na zimeanza kufanya kazi, na nyingi nne zinatarajiwa kuwasili baadaye mwaka huu, zikiwemo ndege kubwa mbili aina ya Boieng Dreamliner zenye uwezo wa kubeba watu 264. Tuna matumaini makubwa kuwa kutokana na hatua hizi, watalii wengi watatembelea nchi yetu na mchango wa sekta ya utalii, ambayo hivi sasa inaongoza kwa kuipatia fedha nyingi za kigeni nchi yetu, itazidi kuimarika.
Ndugu Wafanyakazi;
Kwenye Risala yenu pia mmegusia umuhimu wa kuwaelimisha wananchi kuhusu viwanda pamoja na kuwekeza kwenye miundombinu wezeshi. Serikali imekuwa ikijitahidi sana kuwaelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa viwanda na aina ya viwanda tunavyovitaka.
Kwa kifupi napenda kusema kuwa viwanda vina faida nyingi, ajira, mapato; n.k. Na kuhusu aina ya viwanda tunavyovilenga ni vile vyenye kuajiri watu wengi; vyenye kutumia malighafi zinazopatikana kwa wingi nchini; vyenye kutumia teknolojia ya kati; na ambavyo bidhaa zake zinahitajika kwa wingi hapa nchini lakini pia zinaweza kuuzwa nje ya nchi. Aina hizi za viwanda ni kama vile vya nguo, bidhaa za ngozi pamoja, usindikaji mazao ya kilimo, n.k. Kwa bahati nzuri, wana- Iringa ni wakulima wazuri wa mazao mbalimbali, hivyo wanayo nafasi kubwa katika kujenga Uchumi wa Viwanda nchini.
Ndugu Wafanyakazi;
Risala yenu pia imetoa ushauri kwa Serikali kuimarisha sekta ya elimu, hususan kuliangalia kwa makini suala la tofauti kubwa kati ya wavulana na wasichana kwenye taasisi za elimu; na halikadhali kusimamia suala la ubora wa elimu inayotolewa. Niseme tu kwamba suala la elimu ni ajenda muhimu ya Serikali ya Awamu ya Tano. Tangu tumeingia madarakani tumechukua hatua mbalimbali za kuboresha na kuimarisha sekta hii nyeti na muhimu kwa maendeleo ya nchi. Hatua hizo tayari nimezieleza hapo awali. Elimu bure, nyongeza kubwa ya bajeti ya mikopo ya wanafunzi wa vyuo vikuu kutoka shilingi bilioni 365 mwaka 2015/2016 hadi kufikia shillingi bilioni 427 Mwaka huu wa Fedha, ujenzi wa miundombinu mbalimbali ya elimu (shuleni, vyuoni na kwenye vyuo vikuu). Haya yote yamewezekana kufuatia uamuzi wa Serikali kuongeza bajeti ya elimu. Mwaka 2016/2017 tulitenga shilingi trilioni 1.36 na Mwaka huu wa Fedha shilingi trilioni 1.4. Hivyo basi, niwaombe wazazi kote nchini, kuwahimiza watoto wao, wa kike na wa kiume, kutumia fursa hiyo iliyotolewa na Serikali.
Kwa upande wa kuboresha elimu yenyewe, Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali. Mathalan, kwenye shule za sekondari tumesambaza vifaa vya maabara kwenye shule takriban 1,696. Tumewaajiri mafundi sanifu wa maabara wapatao 386. Aidha, katika Mwaka huu wa Fedha, mpaka sasa, tumewaajiri walimu takribani 6,500 wa shule za msingi na sekondari, wakiwemo walimu 3,728 wa masomo ya sayansi na hisabati. Kwa upande wa elimu ya juu, bila shaka, mlisikia hatua tuilizochukua za kufungia baadhi ya vyuo kudahili wanafunzi au kutodahili wanafunzi kwenye baadhi ya fani, baada ya kujiridhisha kuwa havina sifa. Tulifanya hivyo ili kuhakikisha tunalinda ubora wa elimu inayotolewa hapa nchini.
Ndugu Wafanyakazi Wenzangu,
Nimezungumza mengi sana. Na leo ni Siku ya Wafanyakazi. Hata hivyo, kama nilivyosema mwanzoni, leo ni mara yangu ya kwanza kufika Iringa tangu niingie madarakani. Kwa sababu hiyo, kabla sijahitimisha hotuba yangu, naomba kwa haraka haraka mniruhusu niseme mambo machache yenye kuhusu Mkoa huu wa Iringa. Tayari nimeeleza kuhusu Uwanja wa Ndege wa Nduli, tumepanga kupeleka umeme kwenye vijiji vyote 179 vya Mkoa huu ambavyo havina umeme kupitia REA Awamu ya Tatu.
Sambamba na hayo, tunaendelea kuboresha huduma za afya. Hivi sasa tunafanya ukarabati wa Hospitali ya Mkoa, na napenda kuwaahidi hata mgogoro wa kiwanja wa Hospitali hiyo, nao tutaushughulikia. Tumekamilisha upanuzi wa Hospitali ya Wilaya ya Iringa Manispaa, na hivi sasa tupo kwenye upanuzi wa Hospitali ya Wilaya ya Halmashauri ya Mafinga. Na kesho naenda kuweka Jiwe la Msingi la Ujenzi wa Wilaya Kilolo. Tunafanya ukarabati na upanuzi wa vituo vya Idodi (Iringa Vijijini); Kidabaga (Kilolo); Ihongole (Mafinga) na Malangali (Mufindi). Haya yote yamewazekana kutokana na Serikali kuongeza bajeti za Wizara ya Afya. Mwaka wa Fedha 2016/2017 tulitenga shilingi trilioni 1.8 na Mwaka huu wa Fedha (2017/2018) shilingi trilioni 2.2.
Kuhusu maji, nafahamu kuwa kuna Wilaya tatu za Mkoa huu zenye kukabiliwa na shida kubwa ya uhaba wa maji, ambazo ni Kilolo, Ilula na Mafinga. Lakini nafahamu pia kuwa hivi sasa kuna takriban miradi 14 yenye thamani ya shilingi bilioni 18.24 inayotekelezwa kwenye Mkoa huu. Aidha, wadau wa maendeleo wanatekeleza miradi mingine 10 kwa thamani ya shilingi bilioni 3.512. Kwenye barabara, TANROADS ilitengewa kiasi cha shilingi bilioni 17.948 kwa ajili ya kuhudumia barabara zake; na TARURA imetengewa shilingi bilioni 9.657 kwa ajili ya kuhudumia barabara zake. Vilevile, tupo mbioni kuanza ujenzi wa barabara ya lami kutoka Iringa mjini hadi Msembe katika Wilaya hii ya Iringa Vijijini yenye urefu wa kilometa 104, ambayo Mheshimiwa Waziri Mahiga ameilezea vizuri.
Mabibi na Mabwana; nafahamu ninyi wana-Iringa ni wakulima wazuri wa mazao mbalimbali. Mwezi Julai mwaka jana Serikali ilifuta tozo 87 za kilimo ili kuwapunguzia wakulima kero ya utitiri wa kodi. Aidha, tulipiga marufuku utozaji kodi wa mazao yanayosafirishwa kutoka Halmashauri moja kwenda nyingine, ambayo hayazidi tani moja. Ni matumaini yangu kuwa kwenye halmashauri hii hamlipishwi ushuru. Kwa marafiki zangu, Wamachinga na Mama Nitilie, Serikali imeanza kuwarasimisha wajasiliamali wadogo kwa kuwapatia vitambulisho maalum, ambavyo mtavilipia kwa kiasi kidogo. Lengo la kuanzisha vitambulisho hivyo ni kuwawezesha kufanya shughuli zenu bila kubughuziwa lakini pia kuchangia maendelea ya nchi yetu.
Ndugu Wafanyakazi wenzangu;
Napenda kuhitimisha kwa kurudia tena kuwashukuru kwa kunialika. Napenda niwahakikishie wafanyakazi kote nchini kuwa Serikali yenu inawathamini sana. Nawaahidi tutaendelea kuboresha mazingira yenu ya kufanyia pamoja na maslahi yenu, kadri uwezo wa kufanya hivyo utakavyokuwa ukiongezeka. Napenda niwapongeze Chama Cha Wafanyakazi wa Viwanda, Biashara, Taasisi za Fedha, Huduma na Ushauri (TUICO) kwa maandalizi mazuri ya shughuli hii. Nawapongeza pia waandamanaji kwa namna mlivyopendeza. Kwa hakika, shughuli zimefana sana.
Napenda pia kuwashukuru wageni wote waalikwa, wakiwemo Mabalozi, kwa kushiriki kwenye Siku hii muhimu. Mwisho lakini sio kwa umuhimu, napenda kuwashukuru wana-Iringa, mkiongozwa na Mkuu wenu wa Mkoa, Mheshimiwa Amina Masenza, Wakuu wa Wilaya pamoja na wana-CCM kwa mapokezi yenu mazuri. Napenda niwahakikishie kuwa yale yote tuliyoahidi, tutayatekeleza. Niwaombe tu tuendelee kudumisha amani na umoja wetu.
Mwisho kabisa, ni kuhusu suala la UKIMWI. Kwa mujibu wa matokeo ya utafiti uliotajwa na ofisi yetu ya Taifa ya Takwimu inaonesha kuwa Mkoa wa Iringa umeshika nafasi ya pili baada ya Njombe. Hapa maambukizi ni asilimia 11.2 wakati Njombe ni asilimia 11.6. Hii inatisha. Hivyo, nawaomba wana – Iringa kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa huu hatari. UKIMWI bado ni tishio.
Mungu Wabariki Wafanyakazi wa Tanzania!
Mungu Ibariki Tanzania!
“Ahsanteni sana kwa kunisikiliza”

- Apr 26, 2018
HOTUBA YA MHESHIMIWA DKT. JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, WAKATI WA SHEREHE ZA MIAKA 54 YA MUUNGANO, DODOMA, 26 APRILI, 20...
Soma zaidiHotuba
HOTUBA YA MHESHIMIWA DKT. JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, WAKATI WA SHEREHE ZA MIAKA 54 YA MUUNGANO, DODOMA, 26 APRILI, 2018
Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar
na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi;
Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan,
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Mheshimiwa Dkt. Akinwumi Ayodeji Adesina,
Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika;
Mheshimiwa Kassim Majaliwa,
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Mheshimiwa Balozi Seif Ali Iddi, Makamu wa Pili
wa Rais wa Zanzibar;
Mheshimiwa Job Ndugai,
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Mheshimiwa Zubeir Ali Maulid, Spika wa Baraza la Wawakilishi;
MheshimiwaMartin Ngoga, Spika wa Bunge
la Afrika Mashariki;
MheshimiwaProf. Ibrahim Juma, Jaji Mkuu wa Tanzania;
Mheshimiwa Omar Othman Makungu, Jaji Mkuu wa Zanzibar;
Waheshimiwa Mzee Mkapa, Rais Mstaafu wa Awamu
ya Tatu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Waheshimiwa Viongozi Wastaafu wote mliopo;
Waheshimiwa Wake wa Viongozi Wakuu,
mkiongozwa na Mama Fatuma Karume;
Waheshimiwa Mawaziri mliopo;
Mheshimiwa Balozi John Kijazi, Katibu Mkuu Kiongozi;
Mheshimiwa Dkt. Binilith Mahenge, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma;
Waheshimiwa Wabunge mliopo;
Waheshimiwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi mliopo;
Waheshimiwa Mabalozi na Viongozi wa Taasisi za Kimataifa;
Waheshimiwa Viongozi wa Vyama vya Siasa na Dini mliopo;
Wazee wa Mkoa wa Dodoma, Wageni Waalikwa wote;
Ndugu Wananchi Wenzangu, Mabibi na Mabwana:
Tarehe kama ya leo Mwaka 1964, Mataifa mawili ya Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar yaliungana na kuunda Taifa jipya, ambalo kwa sasa linajulika kwa jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Taifa hili jipya lilizaliwa baada ya aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar, Hayati Sheikh Abeid Amani Karume, na aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Tanganyika, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, kutia saini Hati ya Muungano kuunganisha nchi hizi mbili mwezi Aprili, 1964 na baadaye Hati hiyo kuridhiwa na Mabunge ya nchi zote mbili.
Mambo mengi yamewezesha kuwepo kwa Muungano huu. Kwanza, ni maono ya mbali ya waasisi wa Muungano, Mwalimu Nyerere na Mzee Karume, hususan kuhusu utengamano wa Bara la Afrika. Pili, ukaribu wa Kijiografia uliopo kati ya Tanganyika na Zanzibar. Tatu, ni mahusiano ya kidugu na urafiki baina ya wananchi wa Zanzibar na Tanganyika, ambayo yalichagizwa na lugha moja ya Kiswahili na mwingiliano wa masuala ya utamaduni. Na nne, uhusiano wa karibu na kirafiki uliokuwepo kati ya vyama vilivyopigania uhuru wa nchi zetu mbili, yaani Tanganyika African National Union (TANU) na Afro Shiraz Party (ASP).
Ndugu wananchi, Mabibi na Mabwana;
Napenda nitumie fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwanza kabisa kwa kutuwezesha kuiona siku ya leo; lakini pili kwa kuendelea kuulinda Muungano na Taifa letu kwa ujumla. Aidha, napenda kutumia fursa hii kuwapongeza Watanzania wote; wa dini zote, makabila yote, vyama vyote, rangi zote, waliopo hapa nchini na nje ya nchi, kwa kuadhimisha Sherehe hizi za Miaka 54 ya Muungano wetu na kuzaliwa Taifa letu. Happy Birthday Tanzania! Happy Birthday Watanzania wenzangu! Happy Birthday Muungano wetu!
Naomba pia mniruhusu niwashukuru wageni wetu mbalimbali, Waheshimiwa Mabalozi pamoja na Wawakilishi wa Taasisi za Kimataifa, ambao wamekuja kuungana nasi kwenye Sherehe hizi, ikiwa ni pamoja na Spika wa Bunge la Afrika Mashariki pamoja na Wabunge wote wa Afrika Mashariki. Lakini, kwa namna ya pekee kabisa, napenda nimshukuru na kumkaribisha Mgeni wetu, Mheshimiwa Dkt. Akinwumi Adesina, Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika, pamoja na ujumbe wake wote. Mheshimiwa Dkt. Adesina karibu sana nchini kwetu. Mimi pamoja na Wanazania wenzangu tumepokea kwa furaha kubwa ujio wako na tunakushukuru kwa sana kuungana nasi kwenye Maadhimisho haya
Ndugu wananchi, Mabibi na Mabwana;
Benki ya Maendeleo ya Afrika ni taasisi muhimu sana yenye kutoamchango mkubwa wa maendeleo kwa Bara letu. Inatoa ufadhili wa fedha lakini pia ushauri wa kitaalam. Kwa bahati nzuri, Tanzania ni miongoni mwa nchi waanzilishi na piawanufaika wakubwawa Benki hii. Mathalan, tangu imeanza kufanya shughuli zakehapa nchinimwaka 1971, tumenufaika na ufadhili wa kifedha yenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 3.457, ambapo kwa sasa wanatekeleza hapa nchini jumla ya miradi 25 yenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 1.986.
Kesho natarajia kuambatana na Mhe. Dkt. Adesina kwenda Kondoa kuzindua barabara ya Dodoma – Babati yenye urefu wa kilometa 251 ambayo tumeshirikiana na Benki ya Maendeleo Afrika kuijenga. Benki hii pia ndio waliotufadhili kujenga barabara ya Dodoma – Iringa yenye urefu wa kilometa 260, barabara ya Bububu – Mkokotoni yenye urefu wa kilometa 31 pamoja na kuboresha barabara za vijijini zenye urefu za urefu kilometa 21 Zanzibar.
Kwa niaba yangu binafsi na kwa niaba ya Serikali na Watanzania wote napenda kutumia fursa hii kutoa shukrani zangu nyingi Benki ya Maendeleo Afrika kwa ufadhili wanaotoa kwa nchi yetu. Baada ya kutokahapa Uwanjani, nitaenda kufanya mazungumzo na Dkt. Adesina. Na kwa jinsi ninavyomfahamu, nina uhakika, ataahidi mambo mengine mazuri kwa nchi yetu, ikiwemo miundombinu katika Manispaa ya Dodoma.
Waheshimiwa Viongozi;
Wageni Waalikwa;
Ndugu Watanzania wenzangu;
Mabibi na Mabwana;
Sio siri kuwa katika kipindi cha Miaka 54 ya Muungano wetu, nchi yetu imepata mafanikio mengi makubwa. Fanikio la kwanza na kubwa kabisa ni kudumisha na kuimarisha Muungano wenyewe. Wapo wenzetu wengi walijaribu kuunda Muungano kama wetu, lakini hawakufanikiwa. Sisi tumeweza, na leo Muungano wetu umefikisha miaka 54. Sambamba na hilo, tumeweza kuuimarisha. Mathalan, tumeongeza idadi ya maeneo ya ushirikiano. Mwaka 1964 wakati nchi zetu zinaungana, maeneo ya ushirikiano yalikuwa 11 tu. Lakini mpaka sasa tuna maeneo ya ushirikiano 22, na yote yameongezwa kwa mujibu wa sheria na kufikia maridhiano.
Vilevile, Muungano wetu umeifanya nchi yetu kuwa yenye sauti, nguvu, kujiamini na kuheshimika kimataifa. Tumeweza kulinda uhuru na mipaka yetu; na tunajiamulia mambo yetu sisi wenyewe. Zaidi ya hapo, Muungano wetu umeiwezesha nchi yetu kutoa mchango mkubwa katika masuala mbalimbali ya kimataifa, ikiwemo kusaidia harakati za ukombozi, kutetea haki za wanyonge pamoja na kusuluhisha migogoro sehemu mbalimbali duniani.
Halikadhalika, Muungano wetu umetuwezesha kupata mafanikio makubwa katika nyanja za kiuchumi, kisiasa na kijamii. Sio siri kuwa Tanzania ya leo sio ile ya mwaka 1964.Tumejenga miundombinu ya umeme pamoja na usafiri wa nchi kavu, anga na majini. Aidha, tumeimarisha na kuboresha upatikanaji wa huduma za jamii. Idadi ya taasisi za kutolea elimu na na huduma za afya nazo zimeongezeka maradufu. Haya ni baadhi tu ya mafanikio tuliyopata katika kipindi cha miaka 54 ya Muungano wetu. Yapo mengine mengi. Nikiyataja yote tutakesha.
Napenda kutumia fursa hii kwanza kabisa kuwashukuru na kuwapongeza waasisi wetu, Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere pamoja na Sheikh Karume kwa mchango wao mkubwa uliosaidia kupatikana kwa mafanikio haya. Nimefurahi kuona kuwa katika Sherehe hizi tunaye Mama Fatuma Karume. Tunawashukuru sana mama yetu pamoja na Mama Maria Nyerere kwa kuendelea kuunga mkono Muungano wetu.
Napenda pia kuwashukuru na kuwapongeza viongozi waliowafuatia kwa michango yao mbalimbali waliyoitoa. Natambua mchango wa Marais Wastaafu Mzee Mwinyi, Mzee Mkapa na Mzee Kikwete; Marais wote wa Zanzibar Wastaafu, Makamu wa Rais na Mawaziri Wakuu Wastaafu, pamoja na viongozi na wazee wote wastaafu ambao wametumikia Taifa kwa uaminifu na uadilifu mkubwa katika kuimarisha Muungano wetu. Tunawashukuru sana wazee wetu. Lakini kwa namna ya pekee kabisa, napenda niwashukuru Watanzania wote kwa michango yenu mbalimbali iliyowezesha kupatikana kwa mafanikio haya. Niseme tu kwamba, bila ninyi, mafanikio haya niliyoyataja kamwe yasingepatikana.
Ndugu Watanzania wenzangu, Mabibi na Mabwana:
Hakuna jambo zuri lenye kukosa kasoro. Muungano wetu pia changamoto zake. Lakini. kwa bahati nzuri, pande zote mbili za Muungano zimeweka utaratibu mzuri wa kushughulikia changamoto zilizopo. Nitumie fursa hii kumpongeza Makamu wa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan, Mwenyekiti wa Kamati ya kushughulikia masuala ya Muungano, kwa kazi kubwa na nzuri, ambayo Kamati yake inafanya kushughulikia changamoto zilizopo. Nawapongeza pia Mheshimiwa Waziri Mkuu pamoja n