Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan leo tarehe 17 Mei, 2021 amewaapisha Majaji wa Mahakama ya Rufani 7 na Majaji wa Mahakama Kuu 21 aliowateua tarehe 11 Mei, 2021.
Uapisho huo umefanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Makamu wa Rais Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango, Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, Spika wa Bunge Mhe. Job Yustino Ndugai, Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, Jaji Mkuu wa Zanzibar Mhe. Othman Makungu, Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi, viongozi wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama, viongozi wa Dini na viongozi wa taasisi mbalimbali.
Majaji wa Mahakama ya Rufani walioapishwa ni Mhe. Patricia Saleh Fikirini, Mhe. Penterine Muliisa Kente, Mhe. Dkt. Paul Faustine Kihwelo, Mhe. Lucia Gamuya Kairo, Mhe. Lilian Leonard Mashaka, Mhe. Issa John Maige na Mhe. Abraham Makofi Mwampashi.
Majaji wa Mahakama Kuu walioapishwa ni Mhe. Katarina Tengia Revocati Mteule, Mhe. Biswalo Eutropius Kachele Mganga, Mhe. Zahra Abdallah Maruma, Mhe. Devotha Christopher Kamuzora, Mhe. Messe John Chaba, Mhe. Lilian Jonas Itemba, Mhe. Awamu Ahmada Mbagwa, Mhe. Ayoub Yusuf Mwenda, Mhe. Nyigulila Robert Mwaseba, Mhe. John Francis Nkwabi, Mhe. Safina Henry Simfukwe.
Majaji wa Mahakama Kuu wengine walioapishwa ni Mhe. David Patrick Ngunyale, Mhe. Frank Habibu Mahimbali, Mhe. James Mutakyahwa Karayemaha, Mhe. Emmanuel Loitare Ngigwana, Mhe. Abdi Shabaan Kagomba, Mhe. Arafa Mpinga Msafiri, Mhe. Dkt. Ubena John Agatho, Mhe. Dkt. Eliamani Isaya Laltaika, Mhe. Dkt. Theodora Nemboyao Mwenegoha, Mhe. Mwanabaraka Saleh Mnyukwa.
Akizungumza baada ya kuwaapisha, Mhe. Rais Samia ameipongeza Mahakama ya Tanzania kwa kuongeza idadi ya Majaji wa Mahakama ya Rufani na Mahakama Kuu ambao watasaidia kupunguza mrundikano wa kesi na ucheleweshaji wa mashauri katika Mahakama hizo hali inayoleta dosari katika utoaji wa haki.
Mhe. Rais Samia amewataka Majaji hao kwenda kutekeleza wajibu wao kwa uaminifu, uadilifu, utu, imani na nafsi zao huku wakizingatia kiapo chao na amevitaka vyombo vinavyohusika katika upelelezi wa mashauri mbalimbali kuharakisha upelelezi huo ili mashauri yanayopelekwa Mahakamani yafanyiwe maamuzi haraka.
Ameipongeza Mahakama ya Tanzania kwa kazi kubwa wanayoifanya licha ya kukabiliwa na changamoto mbalimbali na ameahidi kuwa kadiri Serikali itakavyopata uwezo itashughulikia changamoto hizo.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amemshukuru Mhe. Rais Samia kwa kuwateua na kuwaapisha Majaji hao ambao wameongeza idadi ya Majaji wa Mahakama ya Rufani kutoka 17 hadi 24 na Majaji wa Mahakama Kuu kutoka 70 hadi 86.
Amesema ongezeko la Majaji wa Mahakama ya Rufani litasaidia kuongeza idadi ya mashauri yanayosikilizwa na kuamuliwa na majopo ya Majaji hao kutoka 1,620 hadi kufikia 2,268, na kupungua kwa mzigo wa mashauri kwa kila Jaji wa Mahakama Kuu kutoka mashauri 342 hadi 257.