Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tovuti Rasmi ya Rais

Habari

Tuzo la Rais Kikwete lakadhibiwa Washington Apokea Waziri Bernard Membe kwa niaba katika sherehe ya kuvutia


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete usiku wa leo, Jumatano, Aprili 9, 2014, ametunukiwa Tuzo ya Utumishi Bora wa Umma Barani Afrika katika sherehe kubwa iliyofanyika kwenye Hoteli ya St. Regis kwenye mji mkuu wa Marekani wa Washington.

 

Tuzo hiyo ambayo imepokelewa, kwa niaba ya Rais Kikwete, na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Mheshimiwa Bernard Membe imetolewa na jarida maarufu la kimataifa la African Leadership Magazine kwa Rais Kikwete kwa kuwa “Kiongozi wa Afrika aliyetoa mchango mkubwa zaidi katika maendeleo ya kiuchumi ya wananchi wake kwa mwaka 2013.”

 

Pamoja na Rais Kikwete, Waafrika wengine ambao wamepewa heshima kwenye sherehe hiyo ni Dkt. Kingsley Moghalu, Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Nigeria na Bwana John Kennedy Opara, Katibu Mtendaji wa Tume ya Mahujaji Wakristo wa Nigeria ambaye pia ni mshauri wa Rais Gooluck Jonathan wa nchi hiyo kuhusu mahusiano ya kidini nchini Nigeria.

 

Tuzo hiyo imekabidhiwa kwa Mheshimiwa Membe, kwa niaba ya Rais Kikwete, na Balozi wa Nigeria katika Marekani, Profesa Ade Adefuye ambaye naye ametoa Tuzo hiyo kwa niaba ya Rais Jonathan ambaye, kama alivyo Rais Kikwete, hakuweza kuhudhuria sherehe hiyo ya kuvutia.

 

Jarida la African Leadership Magazine ambalo huchapishwa mjini London, Uingereza na mjini Washington, lilimchagua Rais Kikwete kushinda Tuzo hiyo kwa mwaka 2013 baada ya wasomaji na wadau wake wengine wa Jarida hilo kuwa wamemchagua kwa njia ya kura ya maoni Rais Kikwete kama kiongozi aliyetoa mchango mkubwa zaidi kwa maendeleo ya wananchi wake katika Bara la Afrika. Rais Kikwete anamfuatia Rais wa Sierra, Mheshimiwa Ernest Bai Koroma, ambaye alishinda Tuzo hiyo mwaka 2012.

 

Awali, Rais Kikwete alikuwa akabidhiwe Tuzo hiyo tokea Desemba mwaka jana, lakini kutokana na kuingiliana kwa shughuli za Rais, sherehe hiyo iliahirishwa hadi mwaka huu.

 

Akizungumza kabla ya kukabidhi Tuzo hiyo kwa Mheshimiwa Membe, Balozi Adefuye wa Nigeria katika Marekani amemwelezea kwa undani anavyomfahamu Rais Kikwete akisisitiza kuwa kiongozi huyo wa Tanzania ni kielelezo cha rika jipya la viongozi wa Afrika ambao dira na visheni yao ni maendeleo ya Bara la Afrika na wananchi wake.

 

“Kwa niaba ya Nigeria, kwa niaba ya Bara la Afrika, nawasilisha kwenu Mwafrika wa wakati huu, mtoto maarufu wa Tanzania na mtoto maarufu wa Bara la Afrika – Rais Jakaya Mrisho Kikwete,” amesema Dkt. Adefuye katika sherehe iliyotangazwa na kuonyeshwa moja kwa moja na mitandao mbali mbali ya kijamii duniani.

 

Sherehe hiyo imehudhuriwa na watu mbali mbali mashuhuri wakiwamo baadhi ya mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao katika Marekani, Naibu Spika wa Bunge la Tanzania Mheshimiwa Job Ndugai ambaye yuko Washington kwa shughuli za kikazi, Mwakilishi katika Bunge la Wawakilishi wa Jimbo la Georgia katika Marekani, Bi. Dee Dawkins-Haigler ambaye pia ni mwenyekiti wa wabunge weusi katika Bunge hilo na Balozi wa Tanzania katika Marekani Mheshimiwa Liberata Mulamula.

           

Aidha, akizungumza katika hotuba yake ya utangulizi mwanzoni wa sherehe hiyo, Mchapishaji wa Jarida la African Leadership Magazine, Dkt. Ken Giami ameeleza jinsi Rais Kikwete alivyochaguliwa kwa kishindo na wasomaji na wadau wengine wa Jarida hiyo kutokana na mafanikio yake katika uendeshaji na utawala bora wa Tanzania pamoja na mafanikio yake katika ustawi wa kiuchumi wa wananchi wa Tanzania wakati wa kipindi chake cha uongozi.

Imetolewa na:

Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,

Ikulu,

DAR ES SALAAM.

 

9 Aprili, 2014