Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tovuti Rasmi ya Rais

Habari

Tunajenga Jeshi siyo kwa nia ya uchokozi bali ulinzi wa mipaka yetu Rais


Tunajenga Jeshi siyo kwa nia ya uchokozi bali ulinzi

wa mipaka yetu – Rais

 

 

 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa Tanzania inaimarisha Jeshi lake – Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), siyo kwa nia ya kumchokoza mtu ama nchi yoyote, bali kwa nia ya kulinda mipaka yake kwa sababu kila hatua ya maendeleo ina changamoto tofauti za ulinzi wa nchi.

 

Aidha, Rais Kikwete amesema kuwa siyo uharibifu kutumia fedha nyingi kujenga Jeshi, kama ambavyo baadhi ya watu wamekuwa wanadai, kwa sababu ni wajibu wa kila nchi kuhakikisha kuwa Jeshi lake linakuwa katika utayari wa kukabiliana na uchokozi wa aina yoyote.

 

Rais vile vile amesema kuwa uchumi wa Tanzania, na hasa uchumi mpya wa gesiasilia, ambayo ndiyo itakuwa msingi mkuu wa uchumi na maendeleo ya Tanzania lazima ulindwe kwa njia yoyote na kwa nguvu zote.

 

Rais Kikwete aliyasema hayo Jumatatu, Oktoba 19, 2015 wakati alipozungumza katika Sherehe ya Kukamilisha Mradi wa Ukarabati wa Uwanja wa Ndege wa Kurushia Ndegevita na Sherehe ya Kufungua Mradi wa Kuongeza Urefu wa Uwanja wa Ndegevita katika Kituo cha Kijeshi cha Kamandi ya Anga cha Ngerengere, Mkoa wa Morogoro.

 

Rais aliwaambia walioshuhudia sherehe hiyo akiwemo Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali Davis Mwamunyange na Balozi wa Jamhuri ya Watu wa China katika Tanzania Mheshimiwa Dkt. Lu Youquing kuwa Tanzania inajenga Jeshi lake vizuri kwa ajili ya ulinzi wa mipaka yake.

 

“Hatujengi Jeshi letu kwa nia ya kumchokoza yeyote ama nchi yoyote. Tunajenga Jeshi letu kwa nia ya kulinda mipaka yetu. Na kweli huwezi kujua, katika dunia yetu hii wakorofi na wachokozi wapo. Kwa sasa hawapo lakini huwezi kusema kuwa hawatakuwepo milele. Inawezakana mtu akaamua kutuchokoza na hivyo lazima tuwe tayari kulinda mipaka yetu. Iddi Amin alikurupuka hivyo hivyo.”

 

Rais kikwete aliongeza: “Na wala tusije kujidanganya. Kutumia fedha nyingi kujenga Jeshi letu siyo ubadhirifu wa fedha. Ni jambo la lazima kabisa. Ni matarajio yangu kuwa sera za namna hiyo zitaendelea, hata chini ya uongozi ujao, hata kama baadhi ya watu wanaweza hata wakaanza kufikiria sera ya kupunguza matumizi ya kijeshi….yatakuwa ni makosa makubwa.”

 

Rais Kikwete pia ameishukuru nchi ya Jamhuri ya Watu wa China kwa kuisaidia Tanzania katika masuala ya ulinzi, akisisitiza kuwa katika ujenzi wa Jeshi la Tanzania hakuna nchi rafiki kama China duniani. “Ni wajibu wetu kuwajua na kuwashukuru marafiki zetu wa kweli.”

 

China ndio inagharimia miradi hiyo miwili ya maboresho ya Uwanja wa ndegevita wa Ngerengere ambao ukikamilika utakuwa na uwezo wa kuhudumia hata ndege kubwa za abiria ikitokea hali ya dharura katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere wa Dar es Salaam.

 

Imetolewa na:

Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,

Ikulu,

DAR ES SALAAM.

21 Oktoba, 2015