Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tovuti Rasmi ya Rais

Habari

TUMIENI KALAMU ZENU KULINDA AMANI, MSHIKAMANO; SAMIA AWAASA WANAHABARI


WAANDISHI wa habari nchini wameaswa kutumia taaluma zao kulinda mshikamano wa kitaifa na kudumisha amani katika kipindi cha kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwezi Oktoba, 2025.

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam katika Kongamano la Amani la Umoja wa Maimamu Tanzania (UMATA), Rais Dkt. Samia alisema vyombo vya habari vina nafasi ya kipekee katika kujenga taswira ya taifa na kuimarisha utulivu wa kisiasa.

“Tangu mwaka 2021 tumechukua hatua mbalimbali kuimarisha uhuru wa vyombo vya habari. Ni wajibu wa wanahabari kutumia uhuru huo kwa weledi, hususan tunapoelekea kipindi hiki cha uchaguzi, kuhakikisha wanajenga badala ya kubomoa amani iliyopo,” alisema.

Rais Dkt. Samia pia alibainisha mchango wa Serikali katika kukuza sekta ya habari nchini, ambapo alieleza kuwa Serikali imeondoa vikwazo kadhaa vilivyokuwa vikikwamisha tasnia ya habari, hatua iliyolenga kuongeza uwazi na uhuru wa kujieleza.

Pamoja na hayo, alionya kuwa uhuru huo unapaswa kwenda sambamba na wajibu wa kitaifa wa kulinda amani na umoja wa Watanzania, akitolea mfano wa baadhi ya mataifa yaliyopoteza amani na utulivu kutokana na taarifa zisizo sahihi au lugha ya kichochezi inayosambazwa kupitia vyombo vya habari.