Habari
TANZANIA YAKUMBUSHA MSINGI WA UKOMBOZI WA MSUMBIJI

TANZANIA imesema uhusiano kati yake na Jamhuri ya Msumbiji umejengwa juu ya msingi wa mapambano ya pamoja dhidi ya ukoloni na sio tu kwa sababu ya ukaribu wa kijiografia.
Hayo yameelezwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan alipoongoza rasmi Sherehe za Maadhimisho ya Miaka 50 ya Uhuru wa Jamhuri ya Msumbiji, zilizofanyika tarehe 25 Juni, 2025 katika Viwanja vya Machava, jijini Maputo.
Rais Dkt. Samia alisema Tanzania ilichukua jukumu la kihistoria kusaidia ukombozi wa Msumbiji kwa imani kuwa ukombozi wa taifa moja la Afrika ni ukombozi wa bara zima.
“Tanzania kuna Wamakonde, Wayao na Wamakua kama ilivyo Msumbiji. Kukataliwa uhuru kwa mmoja ni kukataliwa kwa wote,” alisema Rais Dkt. Samia.
Alifafanua kuwa Tanzania haikuunga mkono FRELIMO kwa misingi ya urafiki wa kawaida bali kwa kutambua hatari ya ukoloni kwa usalama wa kikanda.
“Uwepo wa ukoloni kwa Msumbiji ulikuwa ni tishio kwa uhuru wa Tanzania pia,” alisisitiza.
Rais Dkt. Samia alitaja maeneo ya Nachingwea, Bagamoyo na Zanzibar kama vituo muhimu vilivyotumika kutoa hifadhi na mafunzo kwa wapigania uhuru. Pia alikumbusha kuwa chama kikuu cha ukombozi cha nchini Msumbiji, FRELIMO, kilianzishwa rasmi jijini Dar es Salaam mwaka 1962.
“Tulitoa mafunzo ya kijeshi, tuliratibu misaada na kuwa wenyeji wa Jukwaa la Nchi za Mstari wa Mbele,” alieleza Rais. Dkt. Samia.
Alisema licha ya changamoto za kiuchumi, hujuma ya miundombinu na mashambulizi ya jeshi la wakoloni, Tanzania iliendelea kusimama imara na mstari wa mbele katika kusaidia harakati za ukombozi wa nchi ya Msumbiji.
Rais Dkt. Samia alielezea msaada wa Tanzania kwa Msumbiji kama jukumu la kindugu ambalo Tanzania ilibeba kuisaidia Msumbiji kupata uhuru wake, hata kama ingegharimu maendeleo ya Tanzania kwa muda.
“Tulikuwa tayari kuchelewesha maendeleo yetu ili kuhakikisha ndoto ya ukombozi inatimia,” alisema Rais Dkt. Samia.