Habari
TANZANIA KUWA KITOVU CHA UTAFITI WA URANI AFRIKA MASHARIKI

TANZANIA imeandika historia mpya katika sekta ya madini leo baada ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuzindua Kiwanda cha Majaribio cha Uchenjuaji wa Madini ya Urani kilichopo Namtumbo, Mkoa wa Ruvuma.
Rais Dkt. Samia amesema hatua hiyo ni sehemu ya safari ya kujenga uchumi wa kisasa unaotegemea maarifa, teknolojia na rasilimali za ndani, huku ikilenga kuimarisha nafasi ya Tanzania katika ramani ya dunia.
“Tanzania itakuwa kwenye ramani ya dunia kama moja kati ya wachangiaji 10 wakubwa zaidi wa malighafi hii muhimu ya nishati safi,” amesema Rais Dkt. Samia na kuongeza kuwa urani ni miongoni mwa madini ya kimkakati duniani, yakitumika kuzalisha nishati ya nyuklia, tiba za saratani, na tafiti za kisayansi.
Kwa kuzindua mradi huu, Tanzania inajiweka katika nafasi ya kuwa kitovu cha utafiti na uchakataji wa urani kwa Afrika Mashariki na Kati.
Aidha, amefafanua kuwa mradi huu ni sehemu ya utekelezaji wa Dira 2050 ya kuifanya Tanzania kuwa taifa lenye viwanda na uchumi wa kati ngazi ya juu unaojitegemea, na kwamba unalenga kuhakikisha urani inachakatwa ndani ya nchi ikizingatia usalama wa kiafya, kimazingira na kufuata viwango vya kimataifa, hatua itakayoongeza mchango wa sekta ya madini katika uchumi wa Taifa na kupunguza utegemezi wa mauzo ya malighafi ghafi nje ya nchi.
Tanzania ni miongoni mwa nchi chache barani Afrika zenye akiba kubwa ya urani. Taarifa za kitaalamu zinaonesha kuwa maeneo ya Mto Mkuju, Namtumbo, yana akiba ya takriban tani 60,000 za urani, hazina yenye thamani kubwa kiuchumi, kisayansi na kimkakati.