Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tovuti Rasmi ya Rais

Habari

SGR YAJA NA FURSA MPYA ZA UCHUMI MASWA


RAIS Dkt. Samia Suluhu Hassan amewataka wakulima na wakazi wa Wilaya ya Maswa, mkoani Simiyu kuchangamkia fursa zitakazotokana na ujenzi wa reli ya kisasa (SGR), akisema mradi huo utabadilisha kwa kiasi kikubwa mfumo wa usafirishaji wa mazao na bidhaa katika ukanda huo.

Akihutubia mkutano wa hadhara katika wilaya hiyo tarehe 18 Juni 2025, Rais Dkt. Samia alisema kuwa Maswa imepata nafasi ya kipekee kwa kuteuliwa kuwa kituo cha kushushia na kupakia mizigo cha reli ya SGR katika eneo la Malampaka, na hivyo kutoa wito kwa wananchi kujiandaa ipasavyo kunufaika na fursa hiyo ya kitaifa.

"Ni wakati wetu sasa wa kuongeza uzalishaji, kuongeza thamani ya mazao yetu na kufikia masoko ya mbali kwa kutumia usafiri nafuu wa reli hii," alisema Rais Dkt. Samia, akisisitiza umuhimu wa wakulima na wafanyabiashara kujipanga mapema ili kunufaika na miundombinu hiyo ya kisasa.

Rais Dkt. Samia aliongeza kuwa pamoja na usafiri wa uhakika wa bidhaa, mradi wa reli hiyo unaleta fursa nyingine nyingi ikiwemo ajira za muda, zabuni za ujenzi, na huduma za kijamii zitakazokuwa zinahitajika wakati na baada ya ujenzi kukamilika.

Aidha, aliwataka viongozi wa wilaya hiyo kuweka mikakati ya kuwawezesha wananchi kuingia katika minyororo ya thamani ya biashara zitakazochochewa na uwepo wa kituo hicho cha mizigo, ikiwa ni pamoja na kuboresha mazingira ya uzalishaji.

Rais Dkt.Samia ameweka bayana kuwa dhamira ya Serikali ni kuhakikisha kuwa miundombinu mikubwa kama reli ya SGR inatoa manufaa ya moja kwa moja kwa wananchi kupitia ukuaji wa shughuli za kilimo, biashara na viwanda vidogo.