Habari
SGR YA MIZIGO KULETA AHUENI GHARAMA ZA USAFIRISHAJI

TANZANIA imepiga hatua kubwa katika usafirishaji baada ya kuzindua rasmi safari za mizigo za treni ya umeme ya SGR kutoka Bandari ya Dar es Salaam hadi Kwala, hatua inayotarajiwa kupunguza gharama za uchukuzi, kuongeza ufanisi wa bandari, na kuchochea biashara na ukuaji wa viwanda.
“Hatua hii ni sehemu ya mkakati wa kitaifa wa kupunguza gharama za usafirishaji, kupunguza uchakavu wa barabara na kulinda mazingira,” amesema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan leo wakati wa uzinduzi rasmi wa tukio hilo, mkoani Pwani.
“Kwa kutumia treni ya umeme ya SGR, mzigo kutoka bandarini unaweza kufika Kwala ndani ya dakika 45 hadi saa moja, ikilinganishwa na wastani wa masaa matatu hadi matano kwa kutumia barabara,” aliongeza.
Akizungumzia mafanikio, Rais Dkt. Samia amesema mkakati huo utapunguza kwa zaidi ya asilimia 20 gharama za usafirishaji na kuongeza ushindani wa Bandari ya Dar es Salaam pamoja na kuchochea shughuli za kiuchumi katika maeneo yaliyopotiwa na njia ya reli.
Katika hatua nyingine, Rais Dkt. Samia amesema kuwa Serikali imewekeza Shilingi Bilioni 330.2 kwa ajili ya ununuzi wa mabehewa 1,430 ya mizigo ya treni ya SGR, na ameiagiza Wizara ya Uchukuzi na Shirika la Reli Tanzania (TRC) kuhakikisha mabehewa hayo yanatumika ilivyokusudiwa.
Rais Dkt. Samia pia ametoa rai kwa TRC kushirikiana na Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA) na kuwa mtoa huduma binafsi (open access operator) ili kufikia mtandao mpana zaidi wa mizigo.
Kadhalika, amehamasisha sekta binafsi ndani na nje ya nchi kuchangamkia fursa hiyo na kuwekeza katika usafirishaji wa abiria na mizigo kwa kununua vichwa na mabehewa yao wenyewe.
Kuanza kwa safari hizo kutaongeza mvuto wa Bandari ya Dar es Salaam, kupunguza muda wa upakuaji mizigo,na kutoa fursa zaidi za kibiashara.
Katika hatua nyingine, Rais Dkt. Samia ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa Kongani ya Viwanda ya Kwala (Kwala Industrial Park), mkoani Pwani inayotarajiwa kuwa kitovu kipya cha uchumi wa viwanda nchini.
Kongani hiyo yenye uwezo wa kuchukua viwanda 200 hadi kukamilika kwake inatarajia kuzalisha ajira za moja kwa moja 50,000 na zisizo za moja kwa moja 150,000. Hadi sasa, tayari viwanda saba vimeanza kazi na vitano zaidi vikiwa katika hatua za ujenzi.
Rais Dkt. Samia ameeleza kuwa uwepo wa kongani hiyo utavutia wawekezaji wa kimkakati katika miradi ya viwanda vya kuzalisha na kuongeza thamani ya bidhaa na kuahidi kuwa Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji ili kuvutia viwanda vipya, kuongeza ajira na kukuza uchumi wa Taifa.