Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tovuti Rasmi ya Rais

Habari

SERIKALI KUIMARISHA UWAJIBIKAJI, DIRA 2050


SERIKALI imedhamiria kutilia mkazo utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kwa kuimarisha mfumo wa uwajibikaji na upimaji wa matokeo ya kazi katika taasisi zote za umma.

Hayo yamebainishwa leo na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan wakati wa uzinduzi rasmi wa Dira hiyo jijini Dodoma, ambapo pia alisisitiza kuwa utekelezaji wa Dira 2050 hautakuwa na maana endapo hautafuatiliwa kwa uwazi, umakini na ufanisi.

Aidha, Rais Dkt. Samia ameielekeza Tume ya Taifa ya Mipango kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu kuandaa haraka mfumo wa kitaasisi wa ufuatiliaji na tathmini utakaoweka wazi majukumu, muda wa utekelezaji na njia za kupima mafanikio katika kila hatua ya utekelezaji.

“Kila taasisi ya Serikali italazimika kuwa na vigezo vya kupima utendaji (Key Performance Indicators - KPIs) vinavyoendana na malengo na shabaha ya Dira, alisema Rais Dkt. Samia.

Rais Dkt. Samia pia amedokeza kuwa mfumo huo utahakikisha kuwa taarifa za maendeleo zinawasilishwa kwa umma kwa wakati, hatua itakayosaidia kujenga uaminifu, kuongeza uwazi na kuhimiza ushiriki wa wananchi katika safari ya maendeleo ya Taifa.

“Tutapima kwa matokeo, si kwa maelezo. Ni lazima kila hatua tuone faida yake kwa wananchi,” alisisitiza.

Katika hatua nyingine, Rais Dkt. Samia ameiagiza Tume ya Kurekebisha Sheria na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuanza mchakato wa mapitio ya sheria ili kuziwezesha taasisi mbalimbali kutekeleza Dira hiyo kwa ufanisi, na kuongeza kuwa sera zote zisizolingana na mwelekeo wa Dira 2050 lazima zipitiwe na kufanyiwa marekebisho haraka.

Vilevile, Rais Dkt. Samia amesema ufanisi wa Dira hii unategemea ushirikiano kati ya Serikali Kuu, Serikali za Mitaa, sekta binafsi, asasi za kiraia, taasisi za dini na wananchi, na kutoa wito kwa taasisi zote za umma na binafsi kuchukua hatua mapema za kujiandaa kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi kabla ya mwezi Julai, 2026.

Kwa kauli mbiu ya Dira 2050 ya “Tanzania Tuitakayo”, Rais Dkt. Samia amesema sasa ni wakati wa kuondokana na mazoea na kuingia katika awamu mpya ya kupanga na kutekeleza maendeleo kwa weledi.

“Things cannot be business as usual. Lazima tubadilishe namna tunavyofanya kazi,” alisisitiza Rais Dkt. Samia.