Habari
SAMIA KUCHOCHEA THAMANI YA PAMBA MASWA

SERIKALI imeendelea kuonesha dhamira yake ya kukuza sekta ya viwanda kwa kuwahimiza wawekezaji kutumia malighafi za ndani, hususan zao la pamba, katika kuongeza thamani ya mazao na kuleta ajira kwa wananchi.
Hayo yamebainishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan alipozungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara wilayani Maswa, tarehe 18 Juni 2025, ikiwa sehemu ya muendelezo wa ziara yake ya kikazi mkoani Simiyu.
Rais Dkt. Samia alisema Serikali itaendelea kushirikiana na wawekezaji waliowekeza kwenye viwanda vya kuchakata pamba nchini.
Aidha, Rais Dkt. Samia alisisitiza kuwa ni ndoto ya Serikali kuona pamba inayolimwa nchini inazalisha nyuzi na bidhaa nyingine za viwandani kupitia viwanda vya ndani. Alieleza kuwa Serikali imekaribisha wawekezaji kupanua mitaji na teknolojia katika mnyororo mzima wa thamani wa zao hilo muhimu kiuchumi kwa mikoa ya kanda ya ziwa.
“Tunataka kuona viwanda vinavyotumia pamba yetu vinazidi kuongezeka. Serikali ipo tayari kushirikiana na kila mwekezaji anayetaka kuongeza thamani ya mazao ya Watanzania,” alisema Rais Dkt. Samia.
Akizungumzia maendeleo ya kiuchumi ya mkoa wa Maswa, Rais Dkt. Samia alieleza kuwa katika msimu wa kilimo 2024/2025, wilaya hiyo inatarajia kuvuna tani 60,438 za pamba, kati ya tani 278,358 zinazotarajiwa kuzalishwa katika mkoa mzima wa Simiyu.
Takwimu hizo, alisema, zinaonesha uwezo mkubwa wa uzalishaji ambao unahitaji kuunganishwa na miundombinu ya uchakataji ili kuwapa wakulima soko la uhakika.
Katika hatua nyingine, Rais Dkt. Samia alizindua rasmi kiwanda cha kuchambua pamba cha Shree Rajendra Agro Industry Limited, chenye thamani ya zaidi ya Shilingi Bilioni 12, chenye uwezo wa kupokea tani 350 za pamba mbegu kwa siku.