Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tovuti Rasmi ya Rais

Habari

SAMIA AZINDUA BANDARI KAVU YA KWALA


SERIKALI imezindua rasmi Kituo cha Kimataifa cha Lojistiki cha Kwala (Kwala International Logistics Centre), mradi wa kimkakati utakaopunguza gharama za usafirishaji, kuondoa msongamano wa malori jijini Dar es Salaam, na kuongeza ufanisi wa Bandari ya Dar es Salaam.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi mkoani Pwani leo, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema Kituo hicho ni suluhisho la muda mrefu kwa changamoto ya ongezeko la mizigo na meli bandarini.

“Ni wazi kuwa Kituo hiki ni jibu la kiu ya muda mrefu ya Tanzania kuwa na bandari kavu ya kisasa nje ya jiji la Dar es Salaam, hiyo kina umuhimu mkubwa,” amesema Rais Dkt. Samia.

Akieleza takwimu za matumizi ya Bandari ya Dar es Salaam, Rais Dkt. Samia amedokeza ongezeko la matumizi ya bandari hiyo kwa wastani wa asilimia 25 hadi 30 kila mwaka na kukua kwa shehena za mizigo kutoka tani milioni 23.69 mwaka 2023 hadi tani milioni 27.76 mwaka 2024, huku idadi ya meli ikiongezeka kutoka 1,860 hadi 1,990.

Ukuaji huu wa shughuli za bandari, amesema, umeongeza msongamano mkubwa wa malori jijini Dar es Salaam na mrundikano wa makasha bandarini, kwa kuwa usafirishaji mwingi wa mizigo hufanyika kwa njia ya barabara, hali inayopunguza ufanisi na ushindani wa Bandari ya Dar es Salaam kwa ujumla.

Rais Dkt. Samia ameeleza uwekezaji katika kituo cha Kwala kama sehemu ya kupanua bandari kwa kuhamishia shughuli kadhaa kutoka Dar es Salaam kwenda Kwala, hatua itakayoongeza wigo wa huduma na kuboresha kasi ya upakuaji na usafirishaji wa mizigo.

“Kituo hiki kitarahisisha upatikanaji wa huduma zote hapa Kwala na maboresho haya yataepusha gharama zilizokuwa zinasababishwa na ucheleweshaji wa mizigo,” amesema.

Kituo hiki kilichounganishwa na barabara kuu pamoja na reli ya kisasa ya SGR kipo kwenye mpango wa kuunganishwa na Bandari za Bagamoyo na Tanga, hatua inayolenga kuimarisha huduma za bandari na kuongeza mvuto wa Tanzania kama kitovu cha biashara ya kikanda na kimataifa.