Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tovuti Rasmi ya Rais

Habari

RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, MHE. SAMIA SULUHU HASSAN AZUNGUMZA KWA NJIA YA MTANDAO NA RAIS WA BARAZA LA UMOJA WA ULAYA MHE. CHARLES MICHEL.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, leo tarehe 12 Julai, 2021 amezungumza kwa njia ya mtandao na Rais wa Baraza la Umoja wa Ulaya Mhe. Charles Michel, Ikulu Jijini Dodoma.

 

Katika mazungumzo hayo, Mhe. Michel amempongeza Mhe. Rais Samia kwa hatua mbalimbali anazochukua tangu kushika hatamu ya uongozi na kumhakikishia kuwa Umoja wa Ulaya (EU) utaendelea kuwa mshirika muhimu na wa kimkakati wa maendeleo nchini Tanzania na kikanda.

 

Aidha, Mhe. Michel amempongeza Mhe. Rais Samia kwa jitihada anazochukua kupambana na ugonjwa wa Corona na kumueleza kuwa EU tayari inashirikiana na viwanda mbalimbali  vinavyozalisha chanjo barani Afrika kwa kuvijengea uwezo na kuongeza kuwa iwapo Tanzania itahitaji msaada huo EU iko tayari kuisaidia.

 

Kwa upande wake Mhe. Rais Samia ameshukuru Umoja wa Ulaya (EU) kwa ushirikiano katika masuala ya maendeleo ya jamii na kuwekeza katika miradi ya miundombinu kupitia Benki ya Uwekezaji ya EU ikiwa ni pamoja na Euro Milioni 50 zilizotolewa na Benki ya Uwekezaji ya EU kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa baadhi ya viwanja vya ndege vya mikoani.

Mhe. Rais Samia ameeleza kuwa katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita Tanzania na Umoja wa Ulaya zimesaini makubaliano ya msaada wa Euro Milioni 111.5 kwa ajili ya kuboresha miradi ya sekta ya nishati hususani  matumizi ya majiko banifu, uongezaji thamani  mazao ya nyuki, kuboresha mazingira ya biashara na kuimarisha usalama wa chakula.